Story
“Shikamooni.” Bella aliamua kusalimia. “Marahaba
Bella. Naona watu wa masoko wamekwama, wanahitaji masaada wako.” “Ngoja niende
huko sasa hivi.” Bella alimjibu Mzee Mwasha na kuondoka, akimuacha Elvin na
familia yake.
My Past - Sehemu Ya 9.
“Shikamooni.” Bella aliamua kusalimia. “Marahaba
Bella. Naona watu wa masoko wamekwama, wanahitaji masaada wako.” “Ngoja niende
huko sasa hivi.” Bella alimjibu Mzee Mwasha na kuondoka, akimuacha Elvin na
familia yake.
“Nilijua ungerudi jana.” Mama Mwasha alimwongelesha Elvin. “Tulichelewa ndege. Nilimpigia simu baba
kumwambia, nikataka kuongea na wewe, akasema ulisha lala. Vipi unajisikiaje?”
“Vizuri. Nimeona nije kukaa na baba yako huku, kule nyumbani najiona mpweke.”
“Mnaweza kurudi nyumbani ukapumzike, mimi
nitakuwepo hapa.” “Mbona baba yako ameniambia umechukua likizo ya siku kumi,
zimeshaisha?” “Naona akili zimetulia. Nimepumzika vyakutosha. Naona nipo tayari
kuanza kazi.” Elvin alijibu huku akimuangalia baba yake. Alibaki akishangaa
kumuona Irene pale hasa baada ya mazungumzo yake na Eli.
“Naona uanze kazi kesho Elvin, ili leo ukapate muda wa mazungumzo
na Irene. Amekuja hapa, amesema anataka kuzungumza na wewe.” Mzee Mwasha alijaribu
kumshauri Elvin. Lakini Elvin alikunja uso. “Tangia
lini umeanza kunipangia kitu chakufanya!?” Elvin alionyesha kukasirika
kidogo. “Yaani ikitokea Irene ananitaka
kwa muda na wakati wake yeye, natakiwa kuacha kila kitu nifwatize ratiba zake!?”
“Nafikiri ingekuwa vizuri ukamsikiliza Elvin.” “Hapana baba, hatuwezi kuishi
kwa mtindo huo. Siwezi kuendelea kuishi kutokana na kile Irene anachotaka.
Nimeshaishi hivyo kwa muda mrefu sana, nafikiri inatosha. Na ninaomba na wewe
asikuingize huko, atatuvuruga sana.” Irene alianza kulia.
“Nimekwambia baba, Elvin amebadilika sana. Najua yote hayo ni
sababu ya Bella.” “Umeanza Irene.
Tafadhali hili ni eneo la kazi. Bella anafanya kazi hapa, anajiheshimu na anaheshimika
na wafanyakazi wengine. Acha kumuharibia sifa yake kwa tuhuma zisizo za kweli.
Najua huwezi kujizuia kuongea, naomba uondoke tutazungumza nikitoka kazini,
kila mtu anatusikiliza sisi.” “Hukuwa hivi Elvin.
Tulikuwa na matatizo yetu, lakini wakati wote tulikaa chini tukatatua pamoja. Lakini
tangia aje Bella, mambo yamebadilika.”
“Hebu acha tuhuma za kijinga Irene. Bella alikuwa na wewe wakati unamahusiano
ya siri ya kimapenzi na marafiki zangu, Junior na Phil? Nafikiri ni wakati
muafaka uanze kuwajibika na makosa yako. Acha kutupia watu lawama. Lini
unampango wakujirekebisha, Irene? Naomba uondoke tafadhali. Acha kufanya fujo
hapa kazini. Umeshaharibu vyakutosha, acha kuendelea kuharibu. Na ninakuomba
kabisa, acha kuingiza wazazi wangu katika hili. Tulianza mahusiano yetu tukiwa
mimi na wewe, naomba tumalize hivyo.” “Tunamaliza!?
Kwani ndio tunaachana Elvin? Kumbuka tulipotoka mimi na wewe.” Elvin alifungua mlango
wa ofisini kwake, akaingia na kufunga mlango. Aliwaacha wazazi wake na Irene
palepale.
“Nilikwambia baba JJ, nimapema sana. Mpeni Elvin muda jamani! Ona
ulivyomnyima mtoto raha. Amekuja na furaha yake, umeharibu kila kitu. Ni juzi
tu ndio amejua kuwa wewe Irene ulikuwa sio mwaminifu kwenye mahusiano yenu,
akaumia sana. Halafu leo mnataka kumlazimisha! Na yeye ni binadamu. Naomba
mumuache. Haraka hiyo uliyonayo Irene ni ya nini?” “Kwa hiyo Mama Mwasha unasema anayonifanyia Elvin ni sawa?” “Hebu kuwa na utu kidogo Irene! Wewe uliyomfanyia Elvin unaona ni
sawa? Uchafu wote ule uliomfanyia, unataka leo ageuke tu aseme yamekwisha!?
Mwache mwenzio afikirie. Hivyo unavyomfuatilia kila siku humpi muda
wakufikiria, unazidi kumsukumia mbali.” “Kwa
hiyo unasema nimpe muda wa kuendelea kuwa na Bella? Unafikiri mimi mjinga? Mnataka
eti nikae tu nyumbani wakati najua Bella anamchukua mwanaume wangu!?” Irene alikuwa akiongea kwa nguvu sana, kila mtu alikuwa akisikia.
Elvin alitoka ofisini kwake na kumsogelea Irene.
“Siku nyingine nikikusikia unaongea na mama
yangu hivyo..” “Utanifanya nini Elvin? Eeh? Utanifanya nini?” “Toka Irene
tafadhali. Naomba uondoke.” “Kwa hiyo unanifukuza?” “Unaning’ang’ania nini
Irene? Kwani mwanaume nipo peke yangu? Au kama alivyosema Eli unataka
kuthibitishia watu wewe nimshindi? Naomba uniache kabisa, na leo ndio iwe
mwisho kunitafuta tafadhali.” “Kwa hiyo na uchumba wetu?” “Nimekwambia basi,
Irene. Huna nidhamu kwa yeyote yule. Unaongea na kila mtu vile unavyotaka wewe!
Wewe utakuwa mke wa namna gani, bwana? Naomba
uondoke Irene, tafadhali. Toka.” “Unafikiri huyo Bella ndio mwanamke atakaye
kufaa? Tutakuona.” Irene aliendelea.
“Na Bella! Bella! Najua unanisikia. Utapaona mjini pachungu wewe.
Wewe si unatumia huo uzuri wako kuchukua wanaume za watu, tutakufundisha adabu.
Utaukimbia huu mji.” Irene alihakikisha anatoa watu ofisini kwa kelele. Wafanyakazi
walioweza kutoka walitoka kuangalia kulikoni, maana Irene alikuwa akipayuka
kama mwehu. Alifanya fujo zakutosha kabla hajaondoka. Alimtukana sana Bella,
akamgeukia Elvin na wazazi wake, tena kwa sauti ya juu, hakuna aliyetaka
kumgusa asije akazua kesi nyingine. Wote walibaki wakimtizama, mpaka alipochoka
ndipo alipoondoka. Elvin alirudi ofisini kwake.
***************************************
Irene aliweza kuharibu
hali ya hewa ya pale ndani. Furaha yote kati ya Bella na Elvin iliisha. Mama
Mwasha aliendelea kulalamika. “Naomba uwe
unanisikiliza baba JJ. Unaona sasa?” “Sikujua kama huyu mtoto ni mkorofi kwa
kiasi hicho bwana. Twende nyumbani ukapumzike.” “Hapana Mwasha. Umeshachafua akili
ya mtoto, lazima tumuache akiwa sawa. Ulimuona jinsi alivyoingia? Alikuwa na
furaha sana, ona sasa hivi alipoondoka hapa.” “Basi nenda kanisubiri ofisini
kwangu, wakati naenda kuzungumza naye.” Mama Mwasha alikuwa na matatizo ya
moyo. Baada ya kuugua sana na kufanyiwa vipimo vingi ndipo walipogundua moyo
wake ni mkubwa. Kwa hiyo walikuwa wakimwangalia kwa karibu sana. Afya yake
ilikuwa ikibadilika mara kwa mara.
Mzee Mwasha aligonga
ofisini kwa Elvin. Elvin alimkaribisha. “Unauhakika
utaweza kubaki, au unataka tuwe wote?” “Nipo sawa baba. Wewe rudi nyumbani na
mama ili akapumzike. Nitawaona jioni.” Mzee Mwasha alisimama pale kwa muda.
“Elvin! Nia yangu ni nzuri mwanangu.
Nataka uwe na furaha.” “Naelewa baba. Usiwe na wasiwasi, kila kitu kitakuwa
sawa tu. Nyinyi nendeni nyumbani mkapumzike. kukitokea chochote kile ambacho
kinakuhitaji wewe mwenyewe, nitakupigia.” “Asante.” Mzee Mwasha akatoka,
lakini Elvin alikuwa amekasirika sana. Alishindwa kufanya kazi kabisa, alibaki
amekaa tu ofisini kwake mpaka muda wa chakula cha mchana. Alimtuma mfagizi
akanunue chakula na kumwambia akilete ofisini mwake. Kilipokuja alipiga simu
ofisi za masoko akitaka Bella afike ofisini kwake.
Baada ya muda Bella
aligonga ofisini kwa Elvin. “Vipi kazi
huko?” “Ni vitu vidogo tu, naamini nitamaliza kabla siku ya kazi haijaisha.”
“Njoo tule.” “Asante Elvin, lakini hapana.” “Kwa nini?” Bella aliingia
ndani na kufunga mlango. “Samahani Elvin,
nafikiri kwa sasa inabidi nikae mbali na wewe kidogo. Watu wananifikiria
vibaya. Hata muda mrefu haujapita tangia tumalize kelele za Lily, yule dada wa masoko,
akinilalamikia nakuganda sana, wakati kila mtu hapa ofisini anajua
yeye anakupenda sana. Leo Irene anaonyesha kuwa mimi ndio sababu ya matatizo
yenu. Nafikiri turudishe mahusiano kama ya zamani, iwe ni kazi tu.” “Unafanya
hivyo kwa ajili yako mwenyewe Bella, au kwa ajili yao?” Bella akanyamaza. “Unajua nini Bella, uwamuzi ni wako. Fanya
vile unavyoona inafaa, sitakusumbua tena.” “Kwangu sio usumbufu Elvin, nia
yangu ni nzuri.” “Sawa.” Elvin alijibu kwa kifupi, akasimama akatupa kile
chakula chote kwenye ‘trash can’ nakutoka nje. Bella
alisimama pale ofisini kwa Elvin kwa muda mrefu akiwaza mwishowe alitoka kurudi
kuendelea na kazi.
***************************************
Mambo yalibadilika sana
kwa Elvin na Bella, mbali na maswala ya kazi ni kweli Elvin hakumuongelesha
kitu kingine chochote Bella. Ilikuwa salamu, na kumpa maagizo kitu gani cha
kufanya kama kipo, na kama ni wajibu wa kawaida tu wa Bella, Elvin hakusogea
kabisa ofisini kwake. Bella alianza kuwa na hamu na Elvin. Alikumbuka wakati
mzuri waliokuwa nao wakati wapo Arusha, nakutamani kutokee sababu waongee tena,
lakini hapakuwepo. Alikuwa na maswali mengi sana yakumuuliza afanye nini kwa
wakati ule juu ya mahusino yake na Mzee Masha lakini aliogopa kumsogelea, kwani
Elvin alionyesha sura ya kazi wakati wote. Siku zilizidi kwenda hali haikuwahi
kubadilika kati yao.
***************************************
Bella aliamua kutafuta
bahasha akaweka kadi za Mzee Masha, ili asitumie kabisa. Akaanza kujinyima sana.
Alianza kuona hata shida kuendeshea ile gari. Kwani lile gari lilikuwa
likimgharimu sana kwa upande wa mafuta na matengenezo. Akawa analiacha nyumbani
ili kubania pesa yake, na kaunza kupanda daladala. Haikuwa rahisi hata kidogo
kwa Bella. Aliacha kadi mbili zilizokuwa na pesa za kutosha, moja ilikuwa ni ya
dolla akaunti na nyingine ya pesa ya kitanzania. Alikuwa akiamka asubuhi na
mapema kuwahi daladala ambazo alikuwa akizifuata mbali sana na alikuwa karibu
wa mwisho kutoka ofisini ili kusubiria watu wapungue posta mpya ili apate
daladala ya kurudi kwake.
Alipoona mateso
yanazidi, alianza kutafuta vyumba karibu na kazini kwake. Alimshirikisha Joo
uhitaji wake, Joo akamwambia yupo mtu anaweza kusaidia kupata nyumba za msajili
wa majumba. Akamtafuta yule dalali na kuongea naye. Alimwambia ampe muda ili
kumtafutia sehemu nzuri karibu na mjini. Bella alikuwa akichoka sana sababu ya
kutembea. Wakati mwingine aliishia kulala sebleni kwenye makochi, nakushindwa
kabisa kufika chumbani kwake sababu ya kuchoka.
“Masha atua jijini,
akisubiriwa na Talaka yake kutoka kwa Bela”
Siku moja ya ijumaa
alipotoka kazini, Bella alikuwa amechoka sana, mvua ilimnyeshea, alijaa matope
kila mahali kwani magari mengine yalimpita njiani na kumwagia maji machafu.
Alipofika tu nyumbani kwake, akapanda kwenye makochi akiwa bado amevaa viatu
vyake, na kukumbatia pochi, vilevile mchafu akapitiwa na usingizi. “Bella! Bella!” Alishtukia Mzee Masha
anamwamsha. “Nimechoka T, naomba niache
nilale.” “Unalalaje kwenye makochi wewe!? Twende ukalale ndani.” “Sitaki.”
“Umekuwa mbishi wewe! Hebu jione ulivyojaa taka. Unanuka Bella, na mimi unajua
siwezi kukaa sehemu chafu.” Bella alisimama na kwenda moja kwa moja bafuni,
akaoga nakurudi kujitupa kitandani.
“Wewe Bella vipi? Hutujaonana muda wote huo, nimerudi kukuona
halafu unanifanyia ukorofi.” “Nakuomba unyamaze, T. Kama nikunipiga au mambo
mengine iwe kesho. Sasa hivi nimechoka siwezi hata kujisogeza.” Bella aligeukia upande
mwingine na kupotelea usingizini. Mzee Masha alishangaa sana.
Kama kawaida yake, kabla
ya kufika nyumbani alishakunywa dawa za kuongeza nguvu za kiume ili akifika
nyumbani, aweze kulala na Bella. Mzee Masha alikesha akizunguka ndani ya ile
nyumba, mpaka palipokuwa panapambazuka. Kwa kuwa hali yake ilikuwa mbaya,
ilimbidi kumbaka tu Bella akiwa usingizini. Bella alilia siku hiyo kuanzia
mwanzo mpaka mwisho. “Hizi ni siku za
hatari T, kwa nini unafanya hivyo? Nikishika mimba?” “Si tutaitoa!” “Yaani uue mtoto! Kwa
nini?” “Niko kwenye kipindi
kigumu sana na familia yangu, siwezi kuongeza mtoto mwingine sasa hivi.” “Wewe ni shetani Masha.” Mzee Mwasha alianza kucheka.
Bella alienda jikoni na
kuchukua mwiko na kurudi nao chumbani nakuanza kumpiga nao Mzee Masha. “Unataka nikuumize tena Bella. Acha ukorofi
usio na sababu.” Bella aliendelea kumpiga kila mahali huku akilia. “Nimekwambia acha Bella. Nikisimama hapa
nitakuumiza ulie wewe.” “Huwezi kuniumiza
zaidi ya hivi. Umenibaka! Wewe ni shetani.”
“Sijakubaka, nimechukua haki yangu.” “Huna
haki juu ya mwili wangu. Mimi sio mkeo.”
“Acha ujinga wako. Hebu rudi kitandani ulale.” Bella alitaka kumpiga
tena, lakini Mzee Masha alichukua ule mwiko na kuuvunja. “Nimekwambia panda kitandani.” “Sipandi
na chukua….” Bella alienda kwenye droo alipokuwa ameweka ile bahasha iliyokuwa
na kadi zote za benki na funguo za gari, akamtupia Mzee Masha. “Maskini mkubwa wewe. Chukua vitu vyako uone kama sitaweza kuishi.” Mzee Masha aliokota ile
bahasha huku akicheka.
“Sasa hapa maskini ni mimi au wewe?” Bella alikuwa akilia
kwa hasira sana. Mzee Masha alifungua ile bahasha akakuta zile kadi za benki. “Utarudi kuziomba hizi kadi wewe mwenyewe.
Wewe kubali hasira za kijinga zikutawale. Na kama kweli hutaki hili gari, mimi
nitaliuza kesho.” “Nimekwambia sina shida na vitu vyako.” “Mbona nimekukuta
hapa sasa? Kama huna shida na vitu vyangu?” Bella aliingia bafuni kuoga.
Alitoka, akachukua pochi
yake akaweka mswaki na dawa ya mswaki na nguo za ndani akataka kutoka. “Nakwambia ukitoa huo mguu tu hapo nje ya
geti, kitakachompata mdogo wako usinilaumu.” Bella alicheka. “Unajua nini Mzee Masha, kwanza
nitakushukuru sana kama utamuua. Itanirahisishia maisha yangu. Nakushauri uende
ukamchukue sasa hivi wewe mwenyewe. Mpige risasi, mnyonge, fanya kile
unachotaka. Wote tutakufa siku moja. Acha kuwa mjinga kunitishia maisha.”
Bella alirudi ndani kuchukua vitu vyake baadhi. “Na kwa taarifa yako, picha zile nilizokutumia wewe ukiwa umenipiga na
kuniumiza mwili wangu, na zile nyingine ulizonipiga mpaka nikalazwa nikafanyiwa
upasuaji, nimezitengenezea video, kisha nikazituma na kwa watu wengine.
Nimewaambia wasiponisikia kwa siku mbili tu, au Ric akipotea tu wakufuate wewe.
Sijui utajificha wapi uso wako! Na uangalie email yako. Nimekutumia hiyo video
niliyojirekodi maisha yangu yote kuanzia ulipojidai unatusaidia ukaishia
kunitoa bikra yangu, vipigo na picha zote ulivyokuwa umeniharibu mwili wangu, vyote
vipo kwenye hiyo video. Na vyote hivyo viko kwa watu zaidi ya mmoja. Nimekutaja
jina lako, mkeo na watoto wako wote. Sasa niguse tena uniumize, nikaongeze
ushahidi, au niue unitupe, watu wasambaze ile video. Utapaona mjini pachungu.”
Bella aliendelea kukusanya vitu vyake vyote bila wasiwasi.
“Acha hivyo vitu vyote ni mali yangu.” “Acha upumbavu Masha. Hata
mimi hivi vyote ni jasho langu. Umesahau ulivyokuwa unanibaka? Umesahahu
ulipotoa bikra yangu bila ridhaa yangu? Umesahau jinsi ulivyokuwa
ukinidhalilisha? Matusi na kushikashika mwili wangu hata mbele ya dereva wako,
ukiwa umeniamuru niwe na kuja kukupokea kutoka uwanja wa ndege? Kwa hiyo hili
ni jasho langu.” Mzee Masha alikuwa haamini.
“Tena wakati nafungasha, ili usibaki unashangaa ngoja nikuwashie
video niliyojirikodi.” Bella alimuwashia Mzee Masha ile video akiwa anaongea amekaa
kwenye kochi huku picha zake akiwa amemjeruhiwa vibaya sana zikipita. Bella
alimalizia. “Utakapokuwa
unaangalia video hii ujue Mzee Masha ametufanyia kitu kibaya sana, mimi na
mdogo wangu Eric. Naomba haki itendeke. Enabella.”
Wakati Mzee Masha
anaangalia ile video, wazo lilimjia Bella. Alijiandikia cheki ya pesa nyingi
sana, akamgeukia Mzee Masha. “Na hiki ndio
kiinua mgongo changu baada ya kustaafu ajira yako.” Bella alimpokonya
funguo za gari mkononi, akapandisha vitu vyote vya thamani kwenye gari yake. “Tena nilitaka niondoke bila kitu kwako.
Lakini nimeona ni ujinga. Umenitesa vyakutosha, umechukua usichana wangu, hivi
vitu havifikii hata nusu ya vitu ulivyochukua kwangu. Gari yako utaikuta
hotelini.” Kama utani Bella alijikuta yupo huru.
Alitoka pale getini huku
akitetemeka, asiamini ule ujasiri aliutoa wapi. Machozi yaliendelea kumtoka.
Aligeuka nyuma kuangalia kama kuna mtu anamfuata, lakini hakuona mtu
anayemfuatilia. Alikwenda moja kwa moja mpaka benki. Akatoa zile pesa
alizojiandikia kwa haraka sana ili kuwahi Masha asiizuie ile hundi. Akazibadili
zile pesa kwenda kwenye pesa za kitanzania, akaziweka kwenye akaunti yake
aliyokuwa amefungua kwa jina lake yeye na Ric.
“Bella aanza maisha mapya, bila Masha.”
Alibaki akiwaza sehemu
ya kwenda. Akaamua kumpigia tena yule dalali, lakini dalali alimwambia ana sehemu
nzuri sana, ambayo amepata mteja aliyekubali kumlipa yeye pesa nyingi zaidi ya
Bella. Bella alimbembeleza na kumuahidi kumuongezea pesa zaidi kama atampa yeye
hiyo sehemu siku hiyo hiyo, akakubali. Siku hiyo hiyo Bella akapata sehemu ya kuishi
kwenye nyumba za msajili wa majumba, eneo la Ocean Road. Hakuwa na kitanda wala
kochi lakini Bella alikuwa na furaha yakupindukia. Alitupa nguo zake zote chini
na kulala palepale sakafuni siku nzima huku akilia kwa furaha.
Ilipofika jioni
alirudisha gari ya Mzee Masha hotelini, akaacha na simu yake ndani ya hiyo
gari, akatafuta taksii yakumrudisha nyumbani kwake. Alijawa na furaha sana. Aliingia
bafuni kuoga tena na tena kutoa harufu ya Mzee Masha mwilini mwake. Alisimama
katikati ya bomba la maji, yakiwa yanamwagikia. Bella alijisafisha sana mpaka
roho yake iliporidhika.
Alipata sehemu ya vyumba
vitatu, akaanza kupigia mahesabu pesa aliyonayo na majukumu makubwa yanayo
mkabili. “Kwanza lazima kuwa na ada ya Ric ili asiache kwenda shule, na mimi mwenyewe
ni lazima nirudi shule. Halafu lazima kununua gari itusaidie mimi na Ric.
Siwezi kumrudisha Ric kwenye maisha ya daladala. Lakini lazima kununua vitanda
na tv,vyombo, jiko,…” Bella alianza kuingiwa na wasiwasi kila
alipopanga mahesabu ya pesa aliyonayo na majukumu mazito yanayomkabili. Wasiwasi
ulizidi kumuingia. Ndio alikuwa ametoka kulipia kodi ya mwaka mzima. ‘Au nimefanya haraka kuondoka kwa Mzee
Masha? Ningesubiri kwanza wakati nipo kwake ningekuwa nanunua vitu taratibu
mpaka ningejaza hii nyumba ndio ningeondoka. Sina hata kitanda!’ Bella
aliendelea kuwaza usiku huo akiwa peke yake. ‘Najua nikirudi kwa Masha
atanipokea.’ Bella alianza kushawishika. ‘Lakini hapana, inabidi nifanye kama alivyonishauri Elvin. Nitaweza
tu. Hatua ndogondogo kama mtoto mdogo. Nianze kutafuta shule ya Eric kwanza.’
Bella alipata muda mzuri sana wakuwaza akiwa peke yake. Weekend ile alilala
chini kwenye nguo zake kwani hakuwa hata na kabati, lakini alipata muda wa
kuwaza na kufanya mipango mingi sana.
***************************************
Siku ya jumatatu aliamka
asubuhi na mapema kuwahi kazini. Alijitahidi kufanya kazi zake harakaharaka
akaamua kumfuata Elvin kumuomba ruhusa awahi kutoka. Aligonga ofisi ya Elvin,
akakaribishwa, lakini Elvin alikuwa kwenye simu. Ilimbidi akae asubirie. Baada
ya muda Elvin akamaliza. “Samahani Elvin,
naomba niwahi kutoka kidogo.” Elvin alibaki akimwangalia. “Nikiwahi kumaliza mapema naweza kurudi
kazini.” Bella aliongeza baada ya kumuona Elvin ametulia kama anatafakari. “Naomba urudi Bella. Mambo ya muhasibu
hayajakaa vizuri.” “Nitajitahidi kuwahi kurudi, na nikirudi nitahakikisha namaliza
kila kitu.” “Sawa.” Bella alitoka na kuanza kuzungukia shule za sekondari.
Alijitahidi kutafuta
shule nzuri lakini ambazo hatalipia pesa nyingi. Alitembea siku hiyo, jua
likimchoma, bila kula wala kunywa maji. Viatu alivyokuwa amevaa vilikuwa vya
juu, kwa hiyo alikuwa amechoka na alianza kutokwa na malengelenge miguuni.
Hakuwepo Kaka Mat, wala gari la Mzee Masha, au dereva wa Masha. Bella
alikumbuka usemi wa Mzee Masha akimwambia anatakiwa ashukuru yale maisha
aliyompa. ‘Nikweli nilikwa nikiishi
maisha ambayo sio yangu.’ Bella alijiambia.
Baada ya kuhangaika
sana, alipata shule. Hakutaka kufanya kosa, aliamua kulipa ada ya mwaka mzima
ili asije ishiwa. ‘Siwezi kununua
gari sasa hivi, itabidi kumfundisha Ric kupanda daladala kila asubuhi ili
kutunza pesa.’ Bella aliwaza wakati ametoka kulipia kila kitu
kilichohitajika shuleni kwa Eric. Alianza kutembea akiwa amechoka sana, akirudi
ofisini.
***************************************
Alifika ofisini akiwa
amechelewa. Muda wa kazi ulishaisha. “Umechelewa
Bella. Nataka kufunga mlango niwahi kurudi nyumbani.” Bella alikuwa
amechoka sana. “Samahani Elvin, imechukua
muda mrefu zaidi ya nilivyotegemea. Naomba unifungie humuhumu ndani ili
nimalize hii kazi leo kabla ya kesho.” Elvin alimgeukia ili kumwangalia
kwani alikuwa ameinamia meza ya mapokezi akisaini makaratasi fulani, na alikuwa
akiongea naye bila kumtizama. Bella alikuwa akitokwa na jasho, nywele zilikuwa
zimevurugika, amejawa vumbi na usoni hakuonekana na furaha hata kidogo.
“Ukirudi asubuhi nitakuwa nimesharekebisha kila kitu, na watakuwa
tayari kuendelea na kazi.” Elvin alimwangalia kwa muda. “Tunaweza
kuongea ofisini kwangu?” Elvin alihoji huku akimshangaa. “Ndiyo. Naomba nikaoshe uso kwanza. Nitarudi
muda sio mrefu.” Aliondoka kwenda kujisafisha kidogo na kumuacha Elvin bado
akimtizama.
Bella alimkuta Elvin
ofisini kwake. “Najua nimechelewa Elvin,
samahani sana.” “Mbona kama ulikuwa
unalia?” Bella alinyamaza huku akijaribu kuzuia machozi yake. “Ulienda wapi?” “Kutafuta shule ya Ric.
Nataka akimaliza mwaka huu asirudi tena kule kwenye ile shule ya Arusha.”
“Umepata sasa shule?” “Nimefanikiwa kupata, na nimelipia garama zote kabisa.”
“Gari yako iko wapi?” “Ile ya Mzee Masha?” “Ndiyo Bella. Si ndio ulikuwa
unatumia?” “Nilimrudishia mwenyewe. Sasa hivi sina gari.” Elvin
alimwangalia kidogo. “Kwa hiyo unakujaje
kazini?” “Natumia daladala.” Elvin alimuhurumia, hakuwa amemuangalia Bella
kwa muda mrefu sana tokea siku walipokuwa wametoka safari, Arusha. Alikuwa
amekonda, alionekana anapitia wakati mgumu sana.
“Kwa hiyo daladala zinafika mpaka huko kwenu?” “Kule nilikokuwa
nikiishi na Mzee Masha, zilikuwa haziingii ndani, nilikuwa nikitembea. Lakini
nimehama, sasa hivi naishi hapa karibu. Sio mbali sana na kwenye daladala kama
nitataka kupanda daladala, lakini huwa wakati mwingine natembea tu mpaka hapa
kazini.” “Umehama kwa Mzee Masha!?” “Ndiyo.” Elvin alikuwa haamini,
hakujua kama Bella angechukua ushauri wake nakuufanyia kazi kwa haraka vile.
Alijisikia vibaya kumuacha peke yake hasa baada ya kumwambia aachane na Mzee
Masha. Ni kama alimtoa mahali fulani, akamuacha njia panda.
“Kwa hiyo siku hizi unaishi peke yako?” “Ndiyo. Nilipoachana na
Masha, nilitafuta sehemu yakuishi mimi na Ric. Akirudi safari hii ndio mwisho
wa maisha ya bweni. Tutakuwa tukiishi wote. Asante kwa ushauri Elvin. Nimeweza
kujikomboa na Mzee Masha.” “Hongera Bella. Najisikia vibaya naona kama
nimekutelekeza.” Bella alitabasamu kinyonge akainama. “Sasa unaonaje maisha?” “Kwa kweli nimagumu sana. Lakini najua
nitazoea. Kama jumamosi hii itabidi niende Arusha kwa basi ili nikamuone Ric.”
“Nakupongeza Bella. Mwanzo utakuwa mgumu sana, lakini kwa vile ninavyokufahamu,
najua utaweza tu.” “Naamini hivyo. Naweza kwenda kuendelea na kazi?” “Umesema
nikufungie humu ndani!?” “Nataka nimalizie kabisa kwenye idara hiyo ya uhasibu,
ili kesho nione vitengo vyote vinaonekanaje. Kama vitahitaji marekebisho au la,
ili nisikucheleweshee ripoti mwishoni mwa mwezi.” “Umekula?” “Muda wachakula
umenikuta barabarani nazunguka kutafuta shule. Lakini hamna neno, nitatengeneza
chai hapo jikoni nitakuwa sawa tu.” “Sawa.” Bella alitoka pale na kuingia
kwenye ofisi ya muhasibu. Kazi za pale ofisini pekee ndizo ziliweza kuchukua
akili za Bella, kutoka kwenye shida zake na kumfanya azame pale kazini akitaka
amalize haraka na kwa ufasaha. Hata hivyo hakuwa na kitanda kwa hiyo makochi ya
pale ofisini yangemfaa tu.
***************************************
Wakati akili zake
zimezama na kusahahu hata alipo, huku akifanya kazi zake, alisikia mlango
mkubwa ukifunguliwa. Aliangalia saa, ilishakuwa saa nne usiku. “Elvin!” Bella aliita kutaka
kuhakikisha. “Ni mimi Bella.” “Umesahau
nini?” “Nimekuja kukuangalia na kukuletea chakula. Njoo jikoni.” Bella
alipumua kwa nguvu, akaanza kujisikilizia. Kweli njaa ilishaanza kumuuma.
Alitoka pale na kuelekea jikoni. Elvin alionekana alishafika nyumbani akaoga na
kubadilisha nguo za kazi.
“Asante kwa chakula. Njaa ilishaanza kuniuma sema nikaipuuza.” Bella alikaa chini na
kuanza kula. “Mbona wewe huli?” “Nimekula
nyumbani na mama.” Bella alifikiria kidogo. “Nimekumiss
Vin!” Bella aliongea kinyonge sana. “Wewe
si ulinifukuza, Bella?” “Nilikosea
Elvin. Nahisi siku ile niliingiwa na hofu. Sikufikiria wakati naongea. Naomba
unisamehe. Lakini nia yangu ilikuwa nzuri. Sikutaka mimi ambaye nimeshaishi maisha
yangu yote ndio niwe sababu ya kukugombanisha na mchumba wako.” “Umeshaishi maisha
yako yote!?” Bella alicheka kwa kujidharau.
“Nimebakiza
nini Elvin? Nawezekana nikawa mdogo wa umri kwenu, lakini nimeshaishi maisha
yote, kama mama aliyekula chumvi nyingi. Mimi sio kama wewe au Irene, ambao
bado maisha mazuri tena yenye ahadi nyingi yanawasubiri mbeleni. Sikutaka
mimi ndio niwe kizuizi cha kuwafanya msifikie ndoto yenu.” “Wewe huwezi kuzuia
chochote Bella. Hata hivyo na mimi nahisi nilikuwa na hasira na nilikuwa kwenye mshtuko.
Sikutegemea kumuona Irene siku ile, tena baada ya kujua uchafu mwingi
alionifanyia. Tulipokuwa Arusha, nilipata wakati mzuri sana. Nikajua nimepata
rafiki mwingine hasa baada ya kugundua marafiki zangu wakaribu wote walikuwa na
mahusiano ya kimapenzi na Irene. Nilimshukuru Mungu kuona angalau umeweza
kufanya akili zangu zitulie. Nikajisifia nimeweza kuamsha kitu kipya ndani yako.
Sasa kuja hapa na wewe unaniambia unaomba tukae mbali mbali, hasira za
kusalitiwa na kukataliwa zikanisumbua sana. Nilijua umenikataa Bella.
Nilijichukia na kuumia sana.” “Pole Elvin, lakini sikukusudia kukuumiza. Na
sikujua mambo yaliyokuwa yakiendelea kati yako wewe na Irene. Naomba nisamehe.”
“Yameisha Bella!” “Kwa hiyo tutarudi kuwa marafiki?” Bella aliuliza huku
akicheka. “Nilikuwa nakumbuka kweli hicho
kicheko chako.” Wote walianza kucheka, ile hali ya uzuni ikaisha kabisa.
Wakarudi ofisini kwa muhasibu na kuanza kufanya kazi pamoja mpaka walipomaliza
saa saba ya usiku.
“Twende nikurudishe nyumbani kwako.” Bella alianza kucheka. “Ujue hakuna hata kochi.” “Unalala wapi
sasa?” “Kwenye nguo zangu.” “Bella!” “Kweli. Nabania pesa kwa ajili ya shule ya
Ric na mimi nataka nirudi shule. Sitaki kuja kuishiwa hela halafu Ric
akateseka.” “Ndio maana ulitaka
kulala humu ndani nini? Ili ulalie sofa za Mzee Mwasha.” Bella alikuwa
akicheka. “Kesho lazima ununue kitanda
Bella. Huwezi kuishi maisha ya namna hiyo wakati mshahara unaingia.” “Naogopa
kuishiwa.” “Halafu ndio unajisifia umekula chumvi nyingi, wakati muoga wa
maisha hivyo! Acha uoga. Maisha ni hatua Bella. Tena umeanza vizuri ukiwa na
kazi. Anza kununua vitu vya msingi. Kitanda, tv, jiko na vyombo.” “Hela itaisha
wewe Elvin!” Elvin alianza kucheka.
“Kweli kazi itakuwepo. Kwahiyo unataka kulala chini, halafu pesa
unaweka benki?” “Sasa je? Kwa ajili ya Ric.” “Nilikwambia, lazima uanze
kujithamini wewe mwenyewe kwanza, Bella. Usipojitunza wewe mwenyewe, utafika
mahali utachoka na kushindwa hata kumsaidia Ric. Unahitaji kula vizuri, kulala sehemu
nzuri ili uweze kufikiria. Kesho tunaenda kununua vitanda.” “Haya bwana.” Elvin alimuendesha
Bella mpaka kwake.
Kwa mara ya
kwanza, Elvin nyumbani kwa Bella.
“Kweli sio mbali bwana.
Halafu ni pazuri!” “Unafikiri Ric
atapapenda?” “Kwa jinsi nilivyoongea na Ric, anaonekana anataka sehemu
atakapopaita nyumbani, basi. Namuona Ric sio mpenda makuu.” “Karibu ndani
sasa.” Elvin alifurahi sana kuona Bella amechukua hatua.
“Hongera sana Bella. Naomba mimi ninunue Tv na kitanda, kama
pongezi yangu kwako. Umefanya kitendo cha kijasiri sana.” “Asante Elvin.
Angalau na mimi nina kwangu.” “Uliwezaje lakini kutoka kwa Mzee Masha?” “Njoo
ukae hapa chini nikusimulie.” Bella alimsimulia Elvin kila kitu. “Daah pole sana Bella.” “Asante. Hapa
nasubiri ikifika zaidi ya mwezi nikapime kama sikushika mimba.” “Utafanyaje sasa kama umeshika mimba?”
“Sijui Elvin. Yaani sielewi kabisa. Namwachia Mungu.” “Safi sana. Hiyo ndio
inayotakiwa.” Walikaa pale wakiongea na kucheka mpaka ilipokuwa saa 9
usiku.
“Lala Bella. Nitakuja kukuchukua asubuhi twende kazini.” “Kweli
Elvin?” Elvin alicheka. “Nitakufuata
bwana. Usiku mwema.” “Sema asubuhi njema.” Alimuacha Bella anajiandaa
kulala, wote wakiwa na furaha yakurudisha mahusiano yao.
***************************************
Bella alimfanya Elvin
kuwa mtu wake wakaribu sana. Alikuwa akimwambia kila kitu bila kumficha. Kwa
hiyo Elvin alijua maisha ya Bella kwa undani sana, na wakati wote aliweza
kumshauri vizuri. Alimsaidia kununua vitu vya ndani vya muhimu ambavyo alijua
angevihitaji. Bella alimtajia kiwango cha pesa alichonacho benki, Elvin
alimsaidia kupanga matumizi, ikamsaidia Bella kuishi bila hofu. Urafiki kati
yao ulirudi, ikawa ngumu kumtenganisha Elvin na Bella. Waliongozana kila
mahali, walikula chakula pamoja. Kuanzia cha asubuhi mpaka jioni. Kama haikuwa nyumbani
kwa Bella, basi ofisini. Furaha kati yao ilitawala, tena safari hii bila hofu
ya Masha wala Irene.
***************************************
“Lazima urudi chuoni umalize mitihani yako
Bella.” “Kweli.” Elvin alimsindikiza Bella
chuoni. Akafanikiwa kupata tarehe ya karibu ya kufanya mitihani yake, na kwa kuwa
Mzee Masha alishalipia ada nzima, Bella aliweza kufanya ile mitihani bila
gharama ya ziada. Hatimaye alipata cheti.
***************************************
“Itabidi kuendelea kusoma,
Bella.” “Sio sasa hivi Elvin. Ada ya hicho chuo ni kubwa sana. Nitashindwa
kumsomesha Ric, na sitaweza kuishi mjini vizuri. Natamani tuwe na gari. Hata
kama siyo ya thamani sana, basi ya kawaida tu ili kutusaidia kuzunguka hapa
mjini kwa urahisi.” Elvin alikuwa akiongea na Bella nyumbani kwake siku hiyo jioni
baada yakutoka kazini. “Si utasubiria
chakula ili tule wote?” Bella alikuwa akipika. “Sijamuona mama siku mbili hizi, nataka leo niwahi nyumbani kidogo kabla
hajalala. Maana kila nikirudi usiku anakuwa amelala na kila nikiondoka asubuhi
ili nikuwahi wewe huku, anakuwa bado hajaamka.” “Hamna shida. Nisalimie wote.
Nitakuona kesho Elvin.” Kilikuwa kipindi kizuri sana kwa Elvin ambacho
hajawahi kukipitia kwenye maisha yake. Alikuwa mtoto mkimya na mwenye maadili
yote. Akakutana na Bella mcheshi na mpenda kucheka sana. Kila kitu alikifanyia
utani na kumfanya Elvin acheke. Elvin alishasahau kabisa usaliti wa marafiki
zake. Akawa haendi tena kwenye vikao vyao vya watoto wa marafiki wa baba yake.
Kila alipokuwa akipigiwa simu kuwa wenzake wanakutana mahali kwa ajili ya
tafrija fulani, Elvin alitoa udhuru. Muda mwingi walitumia na Bella.
***************************************
“Nataka kukufundisha kitu Elvin.” “Isiwe tu
uchokozi.” Bella alicheka. “Nataka kukufundisha mambo ya IT.”
“Utanicheka bure. Mimi na kompyuta vitu viwili tofauti.” “Utaelewa bwana. Mimi
mwalimu mzuri.” Siku za jumamosi ambazo wafanyakazi wengine hawakuwa wakija
kazini, Elvin alimfuata Bella na kwenda naye kazini. Alimfundisha mambo mengi
sana. Akawa msaada mkubwa kwenye maisha ya Elvin. Mambo mengine Bella
alimshauri Elvin kama utani tu, lakini kila Elvin alipofanyia kazi,
alifanikiwa. Baba yake alikuwa akishangaa sana. Kwa muda mfupi sana Mzee Mwasha
aliweza kulipa madeni ya watu, angalau akarudisha heshima kwa Wazee
wenzake.
“Bella kwa familia ya
Mwasha.”
Siku moja ya jumamosi
wakati Elvin yupo nyumbani kwa Bella akiangalia mpira, alipigiwa simu.
Alionyesha kushtuka sana. “Lazima
niondoke Bella. Mama ameanguka chooni, baba anasema hali mbaya. Na baba naye
nimemuacha nyumbani akiwa hajisikii vizuri.” “Pole Elvin. Naomba unijulishe
hali itakavyokuwa.” Elvin akaondoka. Bella alisubiri simu ya Elvin mpaka
usiku, lakini hakupiga, akaamua atume ujumbe. ‘Nina
wasiwasi Elvin, naomba nijulishe hali ya mama ikoje?’ Elvin akapiga. “Pole Bella.
Nimechanganyikiwa ndio maana nimeshindwa kukupigia simu.” “Nini tena? Hali ya
mama ni mbaya sana?” Bella akauliza. “Siyo
nzuri. Tumemleta hapa hospitalini na baba naye amefika hapa amezidiwa. Nipo
peke yangu. Eli hapokei simu. Kaka JJ amesafiri. Nimemuomba mkewe aje ili akae
na mama, anasema mtoto wao mgonjwa, hawezi kuja leo mpaka kesho.” “Pole Elvin.
Basi ngoja nichukue taksii nije kukaa na mama.” “Unauhakika? Maana akiwa kwenye
hali hii hawezi kuamka, kila kitu ni hapohapo kitandani.” “Usiwe na wasiwasi.
Nitakuwepo kusaidiana na manesi. Nakuja sasa hivi.” “Asante Bella.” Wakaagana kwa makubaliano Bella
amfuate hospitalini.
Bella alifika pale na
kukuta Mama Mwasha ndio anabadilishwa nguo sababu ya kujisaidia. Hakufurahia
kabisa jinsi wale wauguzi walivyokuwa wakiongea naye, nikama walikuwa
wakimlaumu, kwa nini hakuwaita wakati anataka kujisaidia? Na hiyo ilikuwa mara
ya tatu. Mama Mwasha alijitetea kwa shida kidogo kwamba ni kama hata hakuwa
akijua kama anataka kwenda chooni. “Sasa
hivi mimi nipo dada yangu. Hatutakusumbua tena. Akijisaidia nitambadilisha mimi
mwenyewe. Naomba tu unielekeze kwa kupata mashuka ya kubadili mpaka hiyo kesho
tutakapo mnunulia diaper.” Bella aliingilia. “Na ukiondoka nani atambadilisha?” “Nitakuwa naye hapa, sitaondoka.” Yule
muuguzi alitoka akionekana kuchefukwa na harufu ya kinyesi cha mtu mzima.
“Pole mama. Utapona.” Bella alimuona Mama Mwasha akitokwa na machozi.
“Sikujua mwanangu.” Alijibu kwa shida
kidogo. “Wala usijali mama. Nitakuwepo
kukusaidia. Utakuwa salama. Wewe lala tu, mimi nipo hapa, ukiwa na shida yeyote
utaniambia.” Mama Mwasha alikuwa hawezi hata kujisogeza kila apatwapo na
ile hali. Elvin alipiga simu, lakini Bella alikata akamtumia ujumbe. ‘Mama amelala,Vin. Hatuwezi kuongea.
Lakini usiwe na wasiwasi anaendelea vizuri.’ ‘Asante Bella.’ Elvin alijibu. ‘Vipi baba?’ Bella naye akauliza. ‘Anasinzia
hapa.’ Bella alituma picha ya kisanamu kinachocheka. ‘Akilala nitakuja kuwaona.’ Bella
akajibu.’Sawa.’
Ilipofika asubuhi
madakatri walimruhusu Mzee Mwasha huku akiwa amepewa masharti ya kupumzika
kabisa. Elvin alimrudisha baba yake nyumbani, na kurudi ofisini akiwa
amemuachia Bella majukumu ya mama yake.
***************************************
Usiku ule Bella hakulala
kabisa. Hali ya Mama Mwasha haikuwa nzuri. Alikuwa akimbadili mara kwa mara.
Ilipofika asubuhi mkwewe, yaani mke wa mtoto wake wa kwanza JJ, Diva, alifika
hospitalini hapo kumuona mama mkwe wake. Alikuwa amevaa kiofisi, alionekana
anafanya kazi nzuri, na hata ukimwangalia usoni alionekana ni dada aliyesoma na
anajielewa. Chumba kizima kilijaa manukato yake, alionekana na umbile dogo
dogo, isingekuwa rahisi kujua hata kama ana mtoto mmoja. “Vipi anaendeleaje?” Aliuliza mara tu alipoingia. “Usiku hakulala, hali ilikuwa sio nzuri.
Ndio anapitiwa na usingizi sasa hivi.” “Basi nitarudi baadaye. Nina vikao vingi
sana ofisini na vyote nategemewa mimi.” “Sawa.” Yule dada hakutaka kabisa
kumuamsha Mama Mwasha, akatoka. Hakuwa ameleta hata chupa ya uji au maji ya
kunywa kwa mgonjwa.
Bella alikaa pale
akisinzia mpaka Elvin alipokuja. “Pole
Bella. Nakuona ulivyo choka, lakini itabidi uvumilie tu. Nimekuletea chakula,
narudi ofisini. Siunajua ule mzigo wa Unganda ndio unaondoka leo?” “Wewe nenda
wala usijali. Kukitokea tatizo lolote nitakujulisha.” Elvin alimsogelea mama
yake akambusu, lakini alikuwa amelala. “Nitawaona
baadaye.” Elvin naye akatoka.
***************************************
Ilipofika jioni kabisa,
Elvin alirudi pale hospitalini akiwa na baba yake na Eli. Eli alibaki
amemkodolea macho Bella. “Kwani hivi
viumbe kweli huwa vipo hapa duniani!?” Eli aliongea kwa mshangao sana mbele
ya wazazi wake na Elvin, akiwa anamshangaa Bella. “Uliniambia hajanywa kabisa.” Mzee Mwasha aliongea kwa sauti ya
chini akimlaumu Elvin, aliyempitia kaka yake huko alipokuwa na kumleta
hospitalini. “Sijanywa bwana! Mbona
hamniamini?” Kumbe Eli alimsikia baba yake. “Mimi namshangaa huyu kiumbe. Sijawahi kuonana nao uso kwa uso viumbe
kama hawa, isipokuwa magazetini tu, tena wamechorwa kama vikatuni. Au wewe
Elvin husomagi katuni nini? Au kumbuka gazeti la San, wanachoraga wasichana
kama huyu hapa.” Eli alikuwa akiongea huku akiendelea kumwangalia Bella
bila kukwepesha macho. “Mama mgonjwa Eli.
Si nimekwambia?” Elvin alimshtua kaka yake. “Kweli bwana. Huyu mtoto kanichanganya kabisa nikamsahau mama yangu.”
Eli alimsogelea mama yake. Bella aliomba kuongea na Elvin wakatoka nje kidogo.
“Nanuka Elvin. Na sijabeba hata nguo za kubadili. Naomba nirudi
nyumbani nikaoge na kuchukua vitu vya muhimu.” “Nisubiri tutaenda wote.
Nafikiri shemeji anakuja. Leo atalala na mama ili na wewe ukapumzike.” Bella na Elvin walirudi
ndani. Baada ya muda mfupi tu Mke wa JJ, Diva akaingia. “Yaani nimechoka. Tokea asubuhi nazunguka kwenye vikao.” Akavuta
kiti akakaa. “Shikamoo baba.” “Marahaba mama. Pole na kazi.” Mzee
Mwasha alijibu. “Asante. Cheo kimenijia
na majukumu. Hivi kesho kutwa natakiwa kusafiri kwenda South Africa kwenye kikao.”
Kila mtu alinyamaza kumsikiliza. Aliongea mambo mawili matatu yanayomuhusu yeye
na kazi yake, mpaka harufu mbaya ilipoanza kuenea mle ndani. Bella alijua ni
Mama Mwasha amejisaidia tena, akawa akitafuta jinsi yakumtoa kila mtu mle ndani
ili ambadilishe.
“Mbona kunanuka?” Diva alianza kulalamika. Bella alimnong’oneza
Elvin kumuomba awatoe watu pale ili ambadili. “Baba na Eli naomba tusubiri hapo nje kidogo.” Mzee Mwasha alielewa,
hakuuliza chochote akatoka yeye wa kwanza, Eli akafuata nyuma Elvin.
Bella alisogea pale
kitandani na kuanza kumfunua. “Kumbe ni
yeye amejisaidia!” “Ndiyo. Naona
anamchafuko wa tumbo.” “Sasa kwa nini huiti wauguzi?” Diva aliuliza huku
amekunja uso na amekaa palepale. “Sipendi
jinsi wanavyo muhudumia. Wanakuwa kama wanamlaumu wakati ni mgonjwa.”
“Wanachoka!” Diva alidakia. “Ndio
maana naona ni vizuri kuwapokea vitu kama hivi ambavyo tunaweza kufanya
wenyewe.” Bella alimbadilisha Mama Mwasha, safari hii alimvalisha diaper
alizokuwa amezileta Elvin. Maongezi yote hayo waliyokuwa wakiongea, Mzee Mwasha
na wanae walikuwa wakisikiliza wakiwa nje.
“Chumba chote kimejaa harufu mbaya! Heri tufungue hayo madirisha.” Diva aliendelea kulalamika.
Bella alitoa zile nguo nje, akarudi kuosha mikono yake, baada ya kutupa zile
gloves alizokuwa amevaa wakati wakumbadilisha Mama Mwasha, akafungua madirisha
na mlango.
Walipoona milango
inafunguliwa Mzee Mwasha na wanae wakarudi ndani. “Asante sana Bella.” Mzee Mwasha akashukuru. Bella alitabasamu. “Jamani mimi naomba nitangulie nyumbani
nikaangalie watoto. Kama mnavyojua JJ hayupo nyumbani, watoto wako na dada tu.
Na kama mnavyojua wasichana wa kazi siku hizi. Ukute alishaondoka watoto
wameachwa peke yao.” Akasimama. “Mama
pole sana. Nitawaona kesho.” Alitoka bila hata kugeuka nyuma. Elvin
alimgeukia Bella. “Naona turudi kwenye
ule mpango wako wa mwazoni.” Bella akacheka. “Ndio twende sasa hivi, wakati baba yupo hapa.” Bella alinong’ona
lakini Mzee Mwasha alisikia. “Na wewe
mama unaondoka?” “Nitarudi baada ya muda mfupi sana. Nataka nikaoge na kubadili
nguo. Sitakawia.” Bella alijibu na tabasamu usoni. “Haya mama. Nashukuru sana.” Mzee Mwasha alikuwa ni kama
aliyeishiwa maneno kwa Bella. “Baba!
Namsindikiza, tutarudi sasa hivi.” Elvin aliaga. “Kwa nini mimi nisimsindikize? Eti Dogo? Ili wewe ubaki tu hapa na mama.”
Eli aliongeza. “Twende Bella.” Elvin
hakutaka kumjibu kaka yake, akatoka nje Bella akafuata.
***************************************
Bella alimuuguza Mama Mwasha
kwa muda wa siku sita akiwa peke yake usiku na mchana. Mzee Mwasha alikuwa
akija mida ya asubuhi nakumfanya Bella apate muda wa kulala kidogo kwenye kochi
wakati Elvin akiwa kazini. Waliendelea hivyo mpaka madaktari walipoona anaweza
kwenda kutumia dawa nyumbani.
Siku hiyo anaruhusiwa,
JJ na mkewe walikuwa wamekuja hospitalini.
“Pole sana mama yangu. Ndio nimeingia sasa hivi. Amekuja kunipokea Diva,
nikamwambia tupitie hapa moja kwa moja.” “Asante. Pole na safari.” Mama
Mwasha alijibu. Hawakuwa wamemuona mkewe tokea alipoaga siku ile usiku. “Na mimi nilisafiri. Nilikuwa na mkutano
South Africa.” Diva aliongeza lakini hakuna aliyejibu na yeye hakuonekana
kujali. “Vipi mama. Wamekwambiaje?”
“Nimeruhusiwa, wamesema nikaendelee na dawa tu nyumbani nikisubiri kwenda
India.” “Wanachosubiri nini kukupeleka huko India?” “Si unajua tunasubiri
foleni baba.” “Foleni ya nini tena?” “Tumeomba
msaada wa serikali, na unajua tupo wengi na mimi mzee. Kwa hiyo mpaka zamu
yangu ije ifike sio kitu cha leo hicho.” JJ alikaa kimya kwa muda.
“Kwani ni kiasi gani? Eti baba?” “Sijui ila wanasema ni pesa
nyingi.” “Si dhani kama kuna pesa nyingi ya kushindwa kumsaidia mama. Itakuwa
hamna sababu ya sisi wote kufanya kazi kama tutashindwa kumsaidia mama apone.
Ngoja nikaongee na daktari wake, nijue gharama. Na Eno anakuja kesho. Tutapanga
vizuri. Lakini lazima ukatibiwe mapema mama. Mimi sikujua kuwa tatizo ni pesa!” JJ aliendelea
kushangaa.
“Mi naona ukaulize gharama kwanza babe. Inaweza kuwa pesa nyingi
sana, ikalazimu kusubiria huo msaada wa serikali.” Mkewe, Diva alishauri. “Wewe unaongea nini!? Yaani mama akae
anateseka eti tunasubiri msaada wa serikali wakati uwezo tunao?” “Unajuaje sasa
kama uwezo tunao wakati hujajua gharama?” “Zitapatikana tu hizo pesa. Hata iweje, mama hawezi kuendelea na hali
hiyo.” JJ na mkewe waliendelea kubishana pale mbele za watu. “Mimi nashauri kaka ukaulize tu ili tujue.
Tunaweza tukawa tunaogopa gharama kumbe ni kitu kinachoweza kufanywa hata na
mtu mmoja tu.” Elvin aliongeza.
“Mtu mmoja huyo, awe hana majukumu. Sisi tuna mambo mengi sana.” Mkewe JJ alijibu tena. “Unajua sikuelewi Diva!” “Usichoelewa nini?”
“Mbona kama swala la mama yangu kutibiwa kwako sio muhimu!?” “Nimuhimu sana.
Lakini tusiende kichwa kichwa, halafu mwishowe tukabaki tunaangaliana hata ada
ya watoto hamna.” JJ akatoka bila hata yakumjibu mkewe.
Eli alikuwa amekasirika
sana. Aliamua anyamaze. Bella alikuwa amekaa kimya kabisa kwenye kona
akiwasikiliza ndugu hao. Ulipita ukimya wa muda, mwishowe Bella aliamua kuanza
kukusanya vitu tayari kwa kuondoka. “Nikusaidie
nini Bella?” Elvin alitaka kumsaidia Bella. “Kuliko kuzungukwa na mizigo humu ndani wakati tulisha ruhusiwa, labda
wewe uanze kuweka vitu kwenye gari.” Bella alijibu huku akiendelea
kukusanya. Eli alisaidiana na mdogo wake Elvin kurudisha vitu kwenye gari.
Wakati wanamalizia JJ akarudi.
“Umeona baba! Tulikuwa tukiogopa bure kumbe wala sio pesa nyingi
kabisa. Tukiwa na milioni 50, mama anaweza kwenda na muuguzi na akafanyiwa
vipimo vyote, tena kama atatakiwa kufanyiwa upasuaji hiyo hiyo pesa itatosha
kabisa.” “Hee!” Mkewe alishtuka. “Nini?”
JJ akamgeukia mkewe na kumuuliza. “Nashangaa
hiyo pesa.” “Kwamba ni kubwa au ndogo?” JJ akaendelea kuhoji. “Hapo inabidi vikao vya nguvu vifanyike.”
“Ili kupata hiyo milioni 50 tu au vikao vya nini?” “Kumbe wewe mwenzangu unaona
ndogo?” “Acha kuwa mbinafsi Diva. Utalinganisha hiyo pesa na uhai wa mtu? Hata
sisi wenyewe tukiamua kulipia hayo matibabu tunaweza.” “Kwa nini iwe sisi tu!?”
“Sijasema sisi tu ndio tulipie. Nimesema
hata sisi tungeamua kulipia hiyo pesa yote tungeweza. Tutachangia wote.” “Labda
hivyo.” Diva mke wa JJ alisikika kuridhika.
“Sasa jamani, naona tuondoke.” Mzee Mwasha aliamua
kuaga. “Mlisharuhusiwa?” JJ akauliza.
“Ameruhusiwa na ameandikiwa dawa za
kutumia nyumbani.” Elvin akajibu. “Sasa
mnafanyaje hapa?” JJ akauliza. “Kivipi?”
“Nani anamsaidia mama?” “Bella anatusaidia kukaa na mama. Imekuwa kama Mungu
amemleta kwa wakati huu. Tangia mama yako aanze kuumwa yeye ndio alikuwa naye
hapa. Siunajua afya yangu na mimi ilikorofisha? Nilishindwa kabisa kukaa hapa
na mama yenu. Alikuwa akishinda huyu binti hapa na mama yenu usiku na mchana.”
JJ alikunja uso. “Wewe Diva sinilikupigia
simu ukaniambia unaenda hospitalini kumuona mama?” “Kumbe?” “Mbona sielewi?” “Nilikuja. Sasa usichoelewa nini?” Diva
akajibu kwa ukali huku na yeye kama hamuelewi mumewe.
“Sikiliza kaka JJ na mkeo. Naomba mkaongelee mambo yenu nyumbani
kwenu. Mama anaumwa.” Eli alikuwa na hasira sana. “Katika
hiyo milioni 50, ninayo million 10 kamili hata kesho naweza kuwapa, halafu tano
nitaongeza wishoni mwa week hii. Kama kaka ulivyosema, mama akatibiwe.
Anateseka sana.” Kila mtu alibaki akimwangalia Eli cha pombe. “Nyinyi vipi? Tatizo lenu mnaniona mimi
mlevi sana, lakini nakunywa kwa akili. Halafi sihongi mwanamke, nalala na kula
bure, kazi nzuri ninayo, mnafikiri mimi sina hela? Tuheshimiane jamani. Mimi
kesho namkabidhi Mzee Mwasha milioni 10, mwisho wa week nampa 5. Sawa baba?”
“Asante Eli. Asante Sana.” Mzee Mwasha akashukuru.
“Mimi naomba niwe wa mwisho baba. Watakapokomea wenzangu, mimi
nitamalizia.” “Hee! Wewe JJ vipi? Wakikomea milioni 20?” “Mimi nitamaliza hizo
30.” JJ alijibu kwa hasira. “Unasema
tu.” Diva alijibu kwa kujiamini sana. “Twende
mama, nikusindikize kuingia kwenye gari.” JJ alimsogelea mama yake karibu. “Tunakwenda wote?” Mama Mwasha akauliza.
“Nitakuja nyumbani baadaye, mama. Naomba
nikasalimie watoto kidogo, sijawaona muda.” “Hamna neno, hata kesho unaweza
kuja.” “Unakumbuka supu yangu ilivyo nzuri?” Mama Mwasha alitoa tabasamu. “Sasa ndio nataka kuja kukupikia, iwe ndio
chakula chako cha usiku.” “Haya, nitasubiri.” JJ alimnyanyua mama yake
kutoka kitandani na kumuweka kwenye kigari cha kusukuma cha hospitali,
{Wheelchair}.
“Eli! Asante sana mdogo wangu kwa mchango. Umejitahidi sana.” JJ alikuwa akiongea na
Eli huku akimsukuma mama yake kutoka hapo chumbani. “Na dada
mdogo unaitwa nani tena?” JJ akauliza. “Naitwa
Enabella, au Bella.” “Asante sana mdogo wangu kutusaidia kumuuguza mama.”
“Asante kushukuru.” Bella alijibu kwa heshima sana. JJ naye alionekana ni
mtu anayejielewa na pesa ilionekana wazi ipo. Alifanana sana na baba yao.
Walipompandisha mama yao
kwenye gari, Elvin alimgeukia kaka yake. “Kwa
hiyo mmesema mtarudi jioni?” “Nakwenda kuwaona watoto tu, halafu nitarudi.”
“Sawa. Nilitaka kumrudisha Bella nyumbani kwake akapumzike kidogo. Maana tangia
mama amelazwa hapa, hajarudi nyumbani kwake.” “Hamna shida kabisa, mimi na Diva
tutakuja kumpokea. Nenda kapumzike Enabella. Asante sana.” JJ alimpa mkono.
“Asante.” Bella alijibu huku akitoa
tabasamu. “Bella mwanangu!” Mzee Mwasha
alimsogelea Bella. “Nakushukuru mama.
Mungu akubariki.” “Asante.” Bella alijibu tena kwa heshima huku akimpa mkono
Mzee Mwasha.
“Dogo! Mimi naweza kumpeleka Bella na gari yangu, ili na wewe
ukapumzike kidogo.” Eli alimgeukia Elvin. “Naomba
twende nyumbani Eli. Tafadhali sana.” Mama yake aliwahi kabla Elvin
hajajibu. “Mbona mpo hivi nyinyi watu wa
nyumba ya Mzee Mwasha? Nifanyaje sasa? Mnanilalamikia kila siku hamjawahi
kuniona na mwanamke. Haya, sasa hivi nimemuona Bella, nataka kumchangamkia
mnaanza kuweka vipingaamizi. Nifanyaje sasa?” “Naomba twende Eli.” Mama Mwasha alirudia.
“Bella akinikubali, nakuahidi naacha pombe mama. Na jumapili
tutakuwa tunaenda wote kanisani. Nakuapia kwa Mungu mama yangu. Kwanza wewe
mbona hushangai siku hizi sinywi?” Wote walibaki wakimwangalia Eli. Bella
aliinama. JJ alikuwa akicheka sana. “Umeacha
kwanywa Eli?” “Kweli kaka, sijanywa tangia nimuone huyu mtoto. Muulize Dogo.
Ilikuwa natoka kazini nakuja hapa kwa mama.” “Si kawaida yako Eli, mama
akiiumwa huwa hunywi.” “Kaka nakwambia safari hii ni sababu ya Bella, sio mama.
Huyu mtoto akinikubali, nitakuwa siendi baa. Mimi itakuwa kazini, halafu nawahi
kurudi nyumbani kwa Bella. Au unasemaje Bella?” Eli aliuliza. JJ alizidi kucheka. “Twende ukapumzike Bella.” Elvin
hakutaka kuchangia kitu alimgeukia Bella akaongoza njia.
“Daah!” Eli aliweka mikono kichwani. “Umemuona
jinsi Dogo anavyonibania, kaka?” “Tatizo unaanza kwa pupa Eli. Taratibu mdogo
wangu.” “Etii!??” “Hutakiwi kuwa na
haraka.” “Uzoefu kaka. Tatizo sina uzoefu na hawa viumbe kabisa.” “Hutakiwi
haraka.” JJ aliendelea kuongea huku anacheka. “Nimekuelewa kaka. Napunguza kasi. Lakini nakuambia ukweli kaka yangu,
akinikubali huyu mtoto, mwaka huu huu natangaza ndoa.” JJ alikuwa akicheka
sana. Mzee Mwasha alitingisha kichwa akaingia kwenye gari. “Tatizo lako baba huniamini kabisa.” “Naomba turudishe nyumbani Eli.
Mama akapumzike.” “Haya kaka, ngoja niwarudishe wazazi nyumbani.” “Lakini si
jioni nitakukuta?” JJ alimuuliza Eli akijua lazima atakuwa yupo baa, kwa
kuwa mama yake ameruhusiwa, na anaendelea vizuri.
Siku zote Eli akisikia
mama yake mgonjwa, hakuwa akienda baa wala hagusi pombe, anabaki akimuuguza
mama yake mpaka apone. “Inategemea saa
ngapi. Nataka nipite kwa washikaji kidogo tukasherekee kupona kwa mama.”
“Hapana Eli. Mama hajapona vizuri. Utasherekea akipona kabisa.” “Daah! Huo
mtihani kaka. Nina kama siku sita sijanywa kabisa kaka yangu. Hapa nilipo akili
haifanyi kazi vizuri. Ngoja basi nipate hata mbili, nitawahi kurudi. Sichelewi
utanikuta nyumbani.” JJ alitingisha kichwa nakuondoka huku akicheka, kurudi
kumfuata mkewe aliyeondoka katikati ya mazungumzo. Alirudi kukaa kwenye gari
akimsubiria mumewe. Eli aliondoka na wazazi wao, Elvin alimrudisha Bella
nyumbani, JJ akaondoka na mkewe.
***************************************
“Nakushukuru sana Bella.”
“Na wewe usianze Elvin. Mtaendelea kushukuru mpaka lini?” “Daah! Sikutegemea.”
“Nini sasa?” “Basi bwana.” Bella alitabasamu. “Nataka
nikifika tu nilale. Ninahamu na usingizi wa kitandani.” “Ndio uzime simu
kabisa.” “Nani wakunipigia? Ni wewe tu na Ric ndio mna namba yangu.” “Basi
nitakupigia baadaye.” “Si umesema nikalale?” Elvin akacheka. “Nitakupigia kukuangalia unaendeleaje.”
“Mmmh! Haya tutaona kama hata hiyo baadaye itafika kabla hujanipigia simu.”
Wote walikuwa wakicheka. Elvin alimsindikiza Bella mpaka ndani kabisa.
Wakaongea mambo machache ya kazini.
“Umeona faida ya kujifunza kazi zangu? Sasa hivi ningekuwa
nasubiriwa na kazi nyingi sana.” “Tena nimekuwa mtaalamu kukuzidi wewe Bella.” Bella alianza kucheka. “Mwanafunzi hawezi kumpita mwalimu bwana. Kuna
mambo mengine sijakwambia.” “Si utaenda kukagua kazi yangu? Utaona kama utakuta
kosa hata moja. Ila kutengeneza ripoti ndio bado hujanifundisha, na huko wala
sijagusa. Nimekuachia mwenyewe.” “Haya Elvin.” Waliagana kisha Elvin
akaondoka. Bila kupoteza muda, Bella alioga na kujitupa kitandani. Alilala kama
mtu aliyekufa.
***************************************
“Bella! Bella!” Bella alishtuka
katikati ya ndoto. “Vipi Elvin!”
“Samahani, imebidi niingie tu mpaka chumbani ulikuwa hufungui mlango.” “Saa ngapi sasa hivi?” “Saa
tatu usiku.” Bella alikaa. “Nimelala
muda mrefu! Tokea tulipotoka hospitalini.” Bella alifikiria kidogo
akashtuka. “Oooh No. Kwa nini upo hapa?
Mama mzima?” “Tunaomba msaada wako bwana. Nimekuja kukuchukua.” “Nini tena?”
“Shemeji ambaye tulitegemea aje kumsaidia mama amesema hataweza kuja leo. Ndio
tukaona turudi tu kwako tukuombe uje msaidie mama kidogo, bado hana nguvu ya
kufanya mambo mengi na baba naye mgongo unauma na kama unavyotuona sisi wote
watoto wakiume, hatuwezi kumsafisha. Ni kwa muda mfupi tu, akipata nguvu na
wewe utapumzika.” “Usijali Elvin. Ngoja nichukue vitu baadhi nitakavyohitaji
ndio tuondoke.” “Unataka nikusaidie nini?” “Kwanza umekula? Maana nakujua Elvin, mambo yakishapandana kidogo
tu, na kula hutaki.” “Tutaenda kula wote tukifika nyumbani.” “Nani amepika sasa
wakati mama mgonjwa.” “JJ yupo
nyumbani. Mzuri sana wakupika. Naona mama alihamishia ujuzi wake kwake. Kwa
hiyo amepika chakula kingi tu, twende tukale.” Bella alichukua kibegi
kidogo akaweka vitu vyake wakatoka na Elvin.
Kwa mara ya Kwanza, Bella
nyumbani kwa Mwasha.
Walifika, Elvin akamkaribisha ndani. “Pole sana Enabella, najua tunakusumbua.
Lakini tuvumilie dada yetu.” “Hapo tena kaka JJ unaharibu bwana. Dada tena!
Mwite shemeji.” Eli alimkatiza kaka yake. “Nilikwambia punguza kasi Eli.” “Daah! Tatizo
kila nikimuona huyu mtoto nachanganyikiwa kabisa kaka. Nasahau. Basi karibu
Enabella. Karibu sana.” Wote walicheka mpaka Bella mwenyewe. Mzee Mwasha
alitoka akionekana anamaumivu. “Pole.”
Bella alimuwahi. “Asante mama. Afadhali
umekuja. Naona mama yako anakuhitaji humo ndani.” “Sawa. Nipeleke Elvin.”
Bella alimgeukia Elvin. “Ningechaguliwa
mimi bwana! Mbona mimi sina bahati jamani?” Eli alilalamika. Bella alicheka
na kumfuata Elvin nyuma.
Walimkuta Mama Mwasha
amelala kitandani akihangaika. “Pole
mama.” “Naona nipunguze kula.” Mama Mwasha aliongea kinyonge na aibu kidogo.
“Kwa nini mama?” “Naona najichafua tu.
Mara ya kwanza nimejitahidi kujisafisha, Mzee Mwasha amenipeleka bafuni,
tumeishia kuchafua bafu zima.” Mama Mwasha alianza kulia. “Ni nini hiki jamani?” “Pole
mama. Usijali, nimapito tu utapona.” “Nahisi
ninatatizo jingine jamani, sio moyo. Haja inatoka bila kujua!” Elvin alimsogelea mama
yake. “Usilie mama bwana! Tutampigia simu
daktari wako tumuulize ili tujue vizuri. Bella yupo hapa kukusaidia. Usiwe na
wasiwasi. Hawezi kukuacha ukachafuka tena.” Mama Mwasha alijawa aibu sana. “Unisamehe Bella mwanangu.”
“Usiwe na wasiwasi mama. Na wala huhitaji kuomba radhi. Sasa hivi wewe unatakiwa
kuangalia afya yako tu. Utapona na utakuwa sawa kabisa. Mimi nipo hapa na wewe,
kila kitu kitakuwa sawa.” “Asante Bella.” Mama Mwasha alikuwa
akiongea kwa shida kidogo.
“Naomba Elvin utupishe.” Bella alimgeukia Elvin na kuongea naye kwa
sauti ya chini huku akicheka. “Unanifukuza?”
“Toka bwana, Vin.” “Uje kula lakini.”
“Nitakuja, ngoja nimalizane na mama.”
Bella alibaki na Mama Mwasha. “Tuangalie
kama unahitaji kubadilishwa.” “Naomba nioge kabisa Bella mwanangu. Nilipokuwa
na Mwasha naona nimejipaka uchafu kila mahali.” “Wazo zuri. Na tubadilishe haya
mashuka.” “Asante sana Bella.” Bella alimsaidia Mama Mwasha kusimama, ni
kweli alikuwa amejichafua. Alimsaidia kuoga, akambadilisha nguo, akamvalisha na
dieper nyingine safi, akatandika kitanda vizuri na kuweka kila kitu sehemu
yake. Kwa muda mfupi hali ya hewa ya pale chumbani ikabadilika.
Mama Mwasha alibaki
akishangaa jinsi Bella alivyokuwa akifanya bila kinyaa na kwa haraka. “Inabidi ujilaze mama. Nikuletee nini?”
“Mmmh! Naona niache kula mwanangu. Najisaidia hovyo kweli! Kila nikila chakula
hakikai tumboni.” “Usiache kula kwa sababu hiyo mama. Mwili wako unahitaji
chakula kingi. Usiwe na wasiwasi juu ya usafi. Ukijichafua nitakubadilisha tena
bila shida.” Bella alitabasamu kumfanya atulie na kumuondoa wasiwasi. “Sasa nikuletee nini?” “Supu. JJ
ametengeneza supu nzuri sana.” “Haya. Basi jilaze kidogo, upumzike.
Nitakusaidia kukaa nitakapo rudi na hiyo supu.” “Asante Bella.” Bella
alicheka na kutoka na yale mashuka machafu.
“Kazi ya kufua hiyo ni yangu, Bella.” Eli alipokea yale
mashuka machafu. “Asante.” Bella
alitabasamu kisha akamgeukia Elvin. “Vin!”
Bella aliita na kufanya kila mtu amgeukie Elvin. “Bwana Dogo na jina amebadilishwa bwana! Umesikia kaka?” Wote
walianza kucheka. “Bella! Na mimi naomba
nibadilishe jina. Nichagulie zuri kama la Vin.” “Ona ulivyoharibu jina la watu.
Mwenyewe Bella hatamki hivyo.” JJ aliongeza kuchokoza. “Daah! Kumbe na wewe kaka umemsikia Bella? Itabidi tuanze shule. Bella
awe mwalimu wangu anifundishe kutamka hilo jina Viiin. Viini au VIIIn!”
“Jina fupi tu, lakini lishakuwa gumu!” JJ
aliendelea kutaniana na Eli. “Eebwana we
kaka! Sijui nimepatia? Eti Bella?” “Tatizo ni sauti Eli.” “Hapo na mimi nakukubalia
kaka. Sauti ya Bella ndio inatamka utamu.” Bella alikuwa akicheka sana vile
Eli alivyokuwa akijaribu kutamka Vin.
“Ulikuwa unasemaje Bella?” Elvin aliuliza huku akitingisha kichwa na
kucheka vile kaka zake walivyokuwa wakiwatania. “Mama anataka supu.” “Kazi ya kumlisha mama, hiyo ni yangu. Wewe kaa
chini ule.” JJ alisimama kwenda kumtayarishia mama yake chakula. Alishangaa
jinsi wanavyofanya kazi kwa ushirikiano. “Kaa
ule.” Elvin alimshtua Bella. “Kwani
hapa hamna msichana wa kazi?” Bella alinong’ona akimuuliza Elvin. “Sisi hatukukuzwa na msichana wa kazi Bella.
Mama huwa anafanya kazi zake mwenyewe na sisi tukimsaidia. Ila kweli kazi ya
kufua na pasi ni kazi ya Eli. Anapenda sana kufua, ila kazi za ofisini zilipoanza
kuwa nyingi alimtafuta kijana wakufua, huwa anakuja mara mbili kwa juma, anafua
na kupiga pasi. Usafi wa ndani tunasaidiana.” Bella alishangaa kidogo.
“Kwa hiyo kupika JJ?” “Yeye huyo anapenda jikoni sana. Akipika
kila mtu lazima atakula. Mjuzi wa mapishi kama mama. Kula uone alivyompishi
mzuri.” “Na wewe kazi yako ni nini?” Elvin alicheka. “Mimi kiziwanda bwana. Nipo potepote. Wananituma kuanzia asubuhi mpaka
jioni. Hata sijui kazi yangu ni nini humu ndani. Lakini sipendi kabisa kufua.”
Waliendelea kula pale mezani Elvin akiongea na Bella. “Unaonekana umechoka Elvin.” “Sana. Nimezunguka sana leo.” “Basi uwahi
kulala.” “Maadamu wewe upo, na umelala kidogo, sitakuwa na wasiwasi. Najua mama
yupo kwenye mikono salama. Hivi nilikwambia asante?” “Sitaki Elvin.” “Haya
bwana. Twende nikakuonyeshe chumbani kwako.” “Nahamia hapahapa nini?” Wote
walicheka.
Nyumba ya Mzee Mwasha
ilikuwa kubwa sana. Japokuwa ilikuwa ina ramani ya kizamani lakini waliitunza
nyumba yao vizuri sana. Ilikuwa safi na vitu vizuri. “We Elvin!” Elvin alikuwa akitaka kutoka. “Sasa nitajuaje kama mama ananihitaji?” “Ni sawa nikimwambia baba
akupigie simu kila wakikuhitaji?” “Una
akili sana.” Bella alijibu huku akijitupia kitandani. “Wewe mwambie baba apige wakati wowote mimi nitaenda.” “Haya. Ndio
ulale sasa.” “Sina usingizi. Nataka nipitie mambo machache kwenye laptop yangu
ndipo nilale. Na mimi nikiwa na shida nitakupigia.” “Sawa sawa. Na mimi nikiamka nitakuja kukuangalia.” Waliagana Elvin
akaondoka.
***************************************
Haukuwa usiku wenye
hekaheka nyingi. Bella aliamshwa mara moja tu, kwenda kumbadilisha Mama Mwasha,
wakati mwingine alilala tu. Aliamua kumtumia Elvin ujumbe, kwani aliamka na
kukuta nyumba iko kimya kabisa, hakujua kama watu wapo au walitoka. ‘Bado umelala?’ ‘Angalia saa.’ Elvin alijibu. Ilishakuwa saa tano asubuhi. Bella akapiga. “Uko wapi sasa?” “Nimekuja
huku uwanja wa ndege, kumpokea Eno.” “Nimepitiwa na usingizi, nikamsahau
mgonjwa wangu! Sasa amekula?” “Usijali. Baba alisema tusikuamshe. Nilimpa uji
kabla ya kuondoka, muulize kama anasikia njaa umpe matunda.” “Na chakula cha
mchana je?” Bella aliuliza. “JJ anakuja sasa hivi,
atarekebisha. Usiwe na wasiwasi.” “Kwa hiyo nikagonge chumbani kwa baba na
mama?” Elvin alianza kucheka. “Usicheke
bwana. Kumetulia sana. Kama wamelala je?” “Hawajalala. Nimetoka kuongea na mama
muda sio mrefu.” “Haya. Baadaye basi.” Bella alijisikia vibaya kulala kwa muda mrefu tena ugenini
alipoenda kuuguza!
Alikwenda kugonga. “Karibu
Bella.”
Mzee Mwasha aliitika. “Shikamooni.” “Marahaba
Bella. Ulilala salama?” Bella alicheka kwa aibu. “Nimelala sana mpaka nimemsahau mama!” “Ndio
vizuri umepumzika. Naona hana tatizo lolote. Nenda kaangalie chakula ule.” “Sio mama angeoga kwanza?” Bella aliuliza kiuungwana. “Ningeshukuru Bella. Naona nitajisikia vizuri.” Mama Mwasha akajibu. “Basi twende ukaoge, halafu ndio na mimi nikaoge.” Bella alimsaidia kusimama, akaingia naye bafuni.
Alimkalisha kwenye kiti na kumsaidia kuoga mpaka alipomaliza.
“Kwani uzoefu wa kuuguza ulipata wapi Bella?” Ilibidi Mama Mwasha amuulize.
Bella akacheka. “Kabla ya kifo cha mama,
aliugua kwa muda mrefu sana na hatukua na msaada wowote ule, mimi tu ndio
nilikuwa nikimuuguza.” “Aliugua nini?” “UKIMWI.” Bella alijibu kwa upole
sana. “Pole Bella.” “Lakini nashukuru
Mungu, hospitalini walinifundisha jinsi ya kumuuguza.” Bella akatulia
kidogo, kama anayefikiria. “Mama yangu
aliugua sana. Sana. Alikuwa kwenye mateso makali sana, mpaka anakufa alikuwa
amechanganyikiwa kabisa. Hakuwa akitutambua tena.” “Una ndugu wangapi?”
Mama Mwasha aliendelea kuhoji wakati Bella anampaka mafuta.
“Tulizaliwa wawili tu, mimi na mdogo wangu Eric.” “Baba yenu yuko
wapi?” “Mama ndiye alikuwa akitulea, hatukuwahi kumuona baba yetu.” “Ndugu wa
mama je?” “Hawakuwa na maelewano mazuri na mama. Kwa hiyo hata baada ya kifo
chake, hakuna aliyetaka kutuchukua ili atusaidie. Tukabaki mimi na Ric tu.”
“Pole sana Bella.” Bella alicheka. “Asante.
Lakini tumeshazoea maisha ya sisi wawili tu, japo tunamkumbuka sana mama yetu.
Alikuwa mtu mzuri sana.” “Basi
utakuwa umechukua kwa mama yako.” Bella alicheka tena. “Sidhani. Mama alikuwa mkarimu wa kupitiliza. Alikuwa tayari atoe kila
kitu ampe mtu, yeye akose. Furaha yake ilikuwa ni kumuona mtu mwingine
anafuraha.” Waliendelea kuongea wakiwa wawili kwenye chumba kidogo
kilichokuwa na nguo, wakati Mama Mwasha amekaa na Bella akimsaidia kuvaa.
“Ngoja nikuchane na nywele kabisa, uzidi kupendeza.” “Mmmh!
Nimeshazeeka Bella mwanangu. Na maradhi haya ndio yananinyima raha kabisa.
Nazidi kuchanganyikiwa.” “Pole mama. Utapona usiwe na wasiwasi.” “Sijui Bella
mwanangu.” “Unajua nini mama? Nimejifunza kitu fulani katika maisha. Kila mwanadamu
anakuwa na kipindi fulani kwenye maisha ambacho ni kigumu sana, hakuna jinsi
akaeleza mtu mwingine akaelewa. Lakini huwa kinapita mama. Inaweza
kuchukua muda usiotegemea, lakini itaisha mama yangu. Vumilia tu.” Mama Mwasha alimshangaa
sana Bella. Alionekana ni mtoto lakini aliweza kufanya mambo makubwa sana.
Hakujua hekima hiyo aliipata wakati wakumuuguza mama yake, au baada ya kifo.
“Asante
sana Bella. Unanipa moyo sana, wewe hujui tu.” Bella alicheka. “Kweli mwanangu. Niliingiwa hofu sana na
hawa watoto wakiume watupu niliozaa! Nikajiambia ndio nafikia hatua naogeshwa
na Eli!? Nikamwambia Mungu anisitiri aibu yangu. Sasa wewe kuja, na wala
hunionei kinyaa, kweli Mungu atakulipa.” “Amina mama. Ona ulivyopendeza.”
Bella alimchana nywele vizuri na kumvalisha gauni alilojua halitamsumbua. Mama
Mwasha aliugua kwa muda mrefu sana. Hata alipolazwa hospitalini hakuwa na
nguvu. Ni mtu aliyekuwa kwenye uangalizi wa daktari kwa karibu sana, kila
wakati.
***************************************
“Mama yuko wapi?” Eno aliingia chumbani
kwa wazazi wake. Mzee Mwasha alikaa. “Mbona
hamna hata salamu bwana? Kama hujaniona?” Eno akacheka. “Samahani baba. Akili na mawazo yote yapo
kwa mama.” “Yupo hapo ndani anavaa.” “Mama Mwasha!” Eno akaita. “Nakusikia.” “Toka basi.” Bella aliona
uso wa Mama Mwasha jinsi ulivyofunguka kwa furaha. “Nakuja kukubeba.” Mama Mwasha akacheka. “Njoo.” Eno alifungua mlango akaenda kumkumbatia mama yake. “Pole sana mama.” “Nimefurahi umekuja Eno,
mwanangu.” Eno akambusu kichwani.
“Ona ulivyokonda! Hauli nini?” “Nakula. Msalimie Bella.” Ndipo Eno
alipoinua macho yake kumtizama Bella.
Alibaki ameduwaa kama
kwa dakika moja. “Hujambo Bella?”
“Sijambo, shikamoo.” Eno alikuwa bado kwenye mshangao. “Mbona hivyo! Mnafahamiana?” Eno hakutaka kusema mengi. “Nahisi nimemfananisha. Twende sebleni.
Nimekuletea zawadi nyingi sana.” Mama Mwasha akacheka. “Kama umeleta viatu tena, siwezi kutembea.” Eno akambeba. “Ni kwa muda tu. Utapona mama. Urudie enzi
zako.” “Sijui Eno.” “Wewe mwenyewe ulitufundisha tusikate tamaa, mbona wewe
unakata tamaa sasa? Utapona bwana.” Eno alikuwa akiongea na mama yake huku amembeba,
wakielekea sebleni.
***************************************
Bella aliamua kwenda
kuoga, akatoka akiwa anaonekana ametulia na sura ya uchovu imeisha. Nyumba
nzima ilikuwa ikinukia. “JJ akiwa jikoni,
utajua tu. Tunakula saa ngapi?” “Acha haraka Eno. Tulia kitawekwa mezani sasa
hivi.” Watoto wote walikuwa hapo siku hiyo. Ulijaa utani wakiwachokoza wazazi
wao. Bella alikuwa amekaa kwenye meza ya chakula ameinamia kompyuta yake.
“Eno!” Eli akaita. Eno akamgeukia. “Ushasikia
kuwa naoa?” Eno alianza kucheka sana. “Tatizo
lako wewe Eno, dharau zimekuzidi.” “Nionyeshe shemeji basi.” “Unataka kuonyeshwa
mara ngapi? Pombe nishaacha. Jumapili naenda kanisani na baba. Au unasemaje
baba?” Mzee Masha alitingisha kichwa kama anayesikitika. “Baba na wewe unanitosa!? Mimi kondoo mpya.”
“Sasa na Bella akikukataa? Kanisani tena basi na unarudia pombe?” Mzee
Mwasha akamuliza. “Baba naye kwa
maswali yake! Bella wangu baba. Hawezi kunikataa. Dogo nitamuweka sawa
anisaidie kunichongea kwa Bella. Au unasemaje Elvin?” “Bella huyu hapa. Wewe
anza kupanga maneno tu.” Elvin akajibu. “Zaidi
ya haya?” “Hapo bado hujasema kitu Eli.” “Daah! Kama ndio hivyo, basi bwana.
Mnataka mpaka jasho linitoke ndio nioe? Mimi ndio maana mambo ya wanawake
yamenishinda. Bora bia. Unakamua chupa zako taratiiibu, usiku ukifika unalala.”
“Tatizo una haraka Eli mdogo wangu.
Nimekwambia taratibu.” JJ alichangia wakati wanapanga chakula mezani.
Waliendelea kutaniana wakicheka. “Lakini
kaka, Bella mwenyewe si unamuona anavyo changanya? Nashindwa kuvumilia.”
Wote walikuwa wakicheka.
***************************************
Walikaa mezani wote
wakaanza kula. “Jamani naomba nichukue
nafasi hii kumshukuru Bella. Najua kazi anazofanya yeye alitakiwa afanye Diva,
mke wangu lakini tangia jana kichwa kinamuuma.” “Mkeo muongo kaka.” Eli akadakia.
“Eli! Naomba nyamaza.” “Sawa mama.” Eli
akanyamaza. “Ni kweli JJ. Bella amekuwa
msaada mkubwa sana.” Mzee Mwasha alieleza kazi alizokuwa akifanya Bella, mchana
na usiku, tena bila kuchoka. Kila mtu alimshukuru na kumpa mkono Bella. “Sasa ndio tuungane kumfanya Bella asiondoke
humu ndani. Akimalizana na mama, mimi naoa kabisa.” “Utamuweka wapi?” JJ
akamuuliza Eli. “Sasa Kaka na wewe mbona
kama huoni mbali? Ndio tunabaki humuhumu ndani kuendelea kumlea mama!” “Umegoma
kujenga kabisa?” JJ akamuuliza tena. “Nyinyi
wote mnajenga. Sasa mnataka nani aje abaki na mama humu ndani? Mimi ndio
nimejitolea kubaki humu ndani.” Waliendelea kucheka mpaka JJ alipotaka
kuzungumza tena.
“Eno! Inabidi kumpeleka mama India akatibiwe. Nimeuliza gharama,
wanasema milioni 50 itatosha.” “Mimi nitaitoa hiyo pesa.” Kila mtu akamgeukia
Eno. “Unataka kutoa yote peke yako!”
“Ndiyo. Maana nyinyi wote mpo hapa karibu, mnamsaidia baba na mama. Mimi nipo
mbali. Mnakumbuka ule mchango wa biashara ya baba wa wakati ule? Nyinyi
mlichanga, mimi sikuwa na pesa. Sasa hivi nalipwa vizuri sana tu, acha na mimi
nisaidie.” “Daah! Milioni 15 yangu imepona. Tena nilikuwa nimeshawandikia Mzee
Mwasha hundi ya milioni 10 kabisa. Ngoja niirudishe. Asante Eno.” Walianza kucheka
tena.
“Asante sana Eno mwanangu.” Mzee Mwasha aliongeza. “Na Eli nashukuru kwa moyo wa utayari.” “Asante baba.” Wote walijibu.
“Nawashukuru wanangu. Mungu awabariki.”
Aliongeza mama yao. “Amina mama.” Wote
waliitikia kwa pamoja tena.
“Sasa kaka JJ, uanze kufuatilia hiyo safari na huyo nesi
atakayekwenda na mama.” Eno alitoa wazo. “Nitaenda
kuongea naye jumatatu.” “Kama hiyo pesa itatosha, naomba niende na Bella pia.”
Mama Mwasha aliongea kinyenyekevu. “Naona
Bella ameshanielewa. Hawa manesi nirahisi kunichoka na kunifanyia mambo mabaya.
Kama pesa itatosha lakini, sitaki niwaumize wanangu.” “Hamna shida mama. Kama
Bella atakuwa tayari kwenda, tutamkatia na yeye tiketi.” “Eti Bella?” JJ
akamgeukia Bella. “Naomba niongee na
Elvin kwanza.” Bella akajibu. “Kwa
nini usiongee na mimi Bella?” Eli alimchokoza tena Bella. “Elvin ndio bosi wangu kule kazini.”
Bella alijibu huku akicheka na kuinama chini. “Baba na mimi naomba kazi kwenye kampuni yako. Hata bure mimi nitafanya
tu. Huna haja yakunilipa.” Kila mtu alianza kucheka tena.
***************************************
Wakati wanaongea na
kucheka, aliingia Diva, Mama yake Diva, na yeye alikuwa mmoja wa kundi hilo la
kina mama Mwasha, Mama Banda, Mama Danny na kina mama wengine. Waliingia
wakakaa. Eli, Elvin na Bella walikuwa wamebaki mezani, wakati wazazi wao, JJ na
Eno walipohamia sebleni kuongea na wageni. “Pole
sana Mama Mwasha. Unaendeleaje?” “Nashukuru Mungu sasa hivi nina nafuu.” “Pole
sana.” Kimya cha muda kilitanda.
“Bella! Njoo uwasalimie marafiki zetu. Mungu ametupa mtoto
mwengine jamani. Amekuwa msaada kweli kipindi cha kuugua kwa mke wangu.
Bila yeye sijui tungefanyaje.” Mzee Mwasha alivunja ukimya. “Kwa kuwa hana kazi ndio maana.” Diva
akajibu kwa kiburi. Bella alisimama kwenda kusalimia. “Shikamo…” “Hee! Huyu mtoto si ndio Enabella? Au nimechanganya jina?” Mama
Banda, yaani mama yake Irene, akauliza kwa mshangao mkubwa. “Ndio jina lake. Kwani vipi?” Mzee
Mwasha akajibu. “Wewe Mama Mwasha si ndio shoga yake kipenzi Mama Masha!? Leo mbona kumgeuka mwenzio!?
Unakula sahani moja na mke mwenzie!?” Mama Banda aliuliza kwa mshangao
sana.
“Kwani mtoto mwenyewe ndiye huyu, mke mdogo wa Masha?” Mama Danny akauliza. “Kumbe! Si niliwaambia nyinyi ni katoto
kadogoo? Basi ndio huyu, aliyemchanganya Mzee Masha. Unaambiwa Masha kabadilika
kama siye yeye kwa huyu mtoto. Hasikii la wazee wenzake wala haoni vile
anavyotesa familia yake. Na nasikia ukitaka ugomvi naye, muingilie mambo yake
na huyu mtoto! Sijui kamfanyaje Masha? Itabidi atoe hiyo siri kwa ulimwengu
mzima wanao mjua Masha.” Wote walicheka kwa kejeli.
Bella alitamani ardhi
ipasuke apotee pale pale. “Naye kajaliwa
uso wa mbuzi! Hana aibu? Anazunguka humu humu! Na si ndio huyuhuyu kavunja
uchumba wa Irene na Elvin?” Mama mwingine akauliza. “Ndiye yeye huyu huyu. Hana atakaye mbakisha.” Mama Banda, yaani
mama yake Irene akadakia. “Atawachanganya
huyu mtoto, mpaka mshikane mashati. Naona na JJ naye anatoa shukurani zake
haziishi.” Diva aliongeza. “Sijui
kachanganywa na hicho kiuno!” Diva alicheka kwa dharau. “Diva! Angalia mdomo wako wewe!” JJ alijibu. “Kumbe uongo? Asante gani zisizoisha? Asubuhi asubuhi umeamkia hapa ili
uje umuone huyu mtoto! Sasa ukae utulizane. Ushaambiwa mkewe Masha. Na
akikusikia atakupiga risasi. Maana hakawii yule.” Diva alikuwa akiongea huku
anamcheka mumewe.
***************************************
Bella amekamatwa. Mbele ya washitaki wake, katika nyumba hiyo ya
Mwasha wanaojiheshimu. Nini kitaendelea?
Usiache kufuatilia na kutoa mchango wako hapo chini.
Barikiwa.
0 comments: