Story

My Past - Sehemu ya 8.

Friday, May 26, 2017 naomimwakanyamale 0 Comments

E
lvin alibaki ameinamisha kichwa pale mlangoni. “Pole na majukumu Elvin. Umekula?” Mama yake, alijaribu kumsemesha baada ya kumuona mwanae amekwamia mlangoni. “Nimekula mama. Vipi wewe?” “Nimeshinda vizuri.” “Baba amesharudi?” Elvin alimuhoji mama yake. “Amerudi muda sio mrefu. Ameingia kuoga ili aje kula. Njoo ule kidogo.” “Nimeshiba mama. Asante.”  “Umekula wapi usiku huu Elvin!?” Irene alidakia. “Nilikuwa na hamu ya chips za kwa Manyanya nikaenda kununua.” Elvin alijibu akionekana amechoka. “Umeenda kula wapi? Maana sikuoni nazo hapo.” Elvin alimtizama Irene kwa muda akaingia ndani akaenda kukaa kwenye makochi alipokuwepo yeye Irene. Mama yake alikuwa amekaa sehemu yakulia chakula.
“Unasemaje Irene?” Elvin alimuuliza Irene. “Nilipokupigia simu nilikuuliza maswali hujanijibu, ukanikatia simu. Na hapa napo nimekuuliza swali pia hujajibu. Nikuelewe vipi?” “Unajua kabisa siwezi kukukatia simu Irene. Nilikuaga nikakwambia tutaonana baada ya muda mfupi, ukasema sawa.” “Hilo sio swala la msingi. Lakini nimeingiwa na wasiwasi Elvin, kwani hunitaki tena? Maana hunitafuti. Nikikutumia ujumbe, hujibu.” Irene alianza kulia huku akiongea na kulalamika. Aliongea mambo mengi bila kumpa nafasi Elvin yakuongea. Alieleza jinsi anavyompenda na kumuhitaji maishani. Jinsi anavyomfahamu yeye tokea wakiwa watoto. Irene alijieleza kwa muda mrefu, huku Mama Mwasha na mume wake wakiwa mezani wakila, Elvin alibaki ameegemeza kichwa chake kwenye kochi akimsikiliza.
Ukweli macho yake yalikuwa yakimwangalia Irene, lakini akili zake zilikuwa kwa Bella. Alifurahia jinsi alivyomuacha usiku huo. Japokuwa alimuacha anatisha sana usoni, lakini alifurahia kitendo cha kuomba pamoja na Bella. Alifurahia ule utulivu anaoupata anapokuwa na Bella. Elvin alitabasamu moyoni huku akimwangalia Irene, aliyekuwa akilia kidogo, na kuongea sana. “Kwa hiyo wewe unasemaje?” Irene alimuuliza Elvin, akawa kama ndio anamshtua kutoka mawazoni. “Hivi Irene, wewe huwa unasali?” Wazazi wake walishangaa hilo swali alilouliza Elvin, halikuwa likifanana kabisa na shutuma nyingi alizotupiwa mtoto wao na Irene. Kumbe Elvin hakuwa amesikia jambo hata moja. “Kusali?” Irene akauliza kwa mshangao sana.
“Namaanisha wewe binafsi, ukiwa peke yako, huwa unapata muda wakuongea na Mungu?” Irene alibabaika sana. “Naenda kanisani, kwani vipi?”  “Ila ukiwa peke yako, wewe na Mungu wako, iwe chumbani au popote pale, unapata muda wakuzungumza na Mungu?” Irene alinyamaza. “Nakushauri uanze. Itakusaidia sana.” Elvin alimaliza na kusimama akataka kuondoka. Aliwaacha wazazi wake wamepigwa na butwaa. Kumbe Eli alikuwa jikoni, akaanza kucheka sana. “Sasa maana yake nini?” Irene aliuliza kwa mshangao .

“Eli atoa siri ya Irene.”
Eli alijitokeza pale sebuleni akiwa anaendelea kucheka. Alicheka huku akipiga makofi nakufanya watu wote wamgeukie yeye wakiwa na mshangao. “Yaani Dogo ilikuwa kidogo tu, uingizwe choo cha kike. Kidogo tu.” Eli aliendelea kucheka. Kaka zake Elvin wote walizoea kumwita Elvin, Dogo. “Hapa nimeshaingiza bia zangu za bureeee, zinanisubiri kesho baa. Niliwaambia washikaji, Irene hawezi kufanikiwa. Si mmemuona Dogo alivyochomoka kimungumungu? Wewe Irene nakuambia kweli, huyu Dogo, mdogo wangu mimi, kichwa yake ipo vizuri. Hiko kichwa hukiwezi kabisa wewe Irene.” “Wewe Eli vipi!?” “Hilo ndilo tatizo lako. Una maneno mengi sanaaaa, halafu huna akili ya kufikiria na kumuelewa mtu. Unaongea sana. Yaani mimi mwenyewe mshinda baa kwenye kelele, nilikuwa jikoni nakusikiliza lakini kichwa kilishaanza kuniuma kwa kukusikiliza. Unafikiri utashinda vipi kwa mtu kama Elvin asiyeweza kelele? Wewe umejiingiza kwenye mashindano na wenzako bila kufikiria, na kumjua Elvin. Huwezi kufanikiwa hata kidogo. Nishawaangalieni sana mahusiano yenu, ndio maana kule baa, niliwaambia ukishinda wewe leo, mimi nawanywesha pombe mwezi mzima, buree, nawalipia mimi. Hata mtu mjinga wa kupita kiasi, akikaa na Elvin siku moja tu, atajua kelele hawezi kabisa. Uliza kila mtu humu ndani, Dogo huyu hawezi kelele, zilimshinda kabisa. Wewe hushangai tangia umeanza kuongea, kajibu mara mbili tu. Ya kwanza kama unakumbuka na kama unaakili ya kufikiria amekuita muongo.” “Wala hajaniita muongo.” “Ndio maana nakwambia wewe mapepe, akili yako haijatulia. Husikilizi watu wakiongea, na ndio maana umeshindwa kabisa kuishi na Elvin ambaye ni mtu rahisi sana kuishi naye. Wewe hushangai mwenzako kwa nini kakutupia kwa Mungu wako aliyekuleta hapa duniani? Elewa wewe mtoto. Hapo ndio anakwambia yeye kakunawia mikono, Mungu peke yake aliyekuumba wewe kijitu cha ajabu, peke yake ndio anakuweza.” Eli akaanza kucheka tena.
“Yaani Dogo anakajiukorofi kake ka chinichini huyu! Eti anamuuliza shetani kama anasali! Mama umemuona Elvin lakini?” Eli aliendelea kucheka. “Naomba ukalale Eli.” Mama yake alitaka aondoke. “Ngoja kwanza mama, huyu mtoto wa Banda mimi namjua na habari zake zote na wenzake zinajulikana. Yaani mimi zimenifikia nikiwa baa. Atawasumbueni sana huyu. Hawa mademu wote wanao wazunguka hakuna mtoto wa kuoa hata mmoja, hamuoni mimi nawakambia?” “Kwanza hatukutaki?” Irene alijibu kwa kiburi. Eli alizidi kucheka. Elvin alibaki amesimama anamsikiliza kaka yake.
 “Sasa mimi ngoja niwaambie ukweli wote juu ya hawa watoto. Kwanza nyinyi kwa nini hamshangai leo mimi nimerudi mapema? Nimekuja kushuhudia. Nilipoambiwa tu mchezo umeanza, Irene ameenda kumfuata Elvin, na wakasema safari hii Irene lazima ashinde, mimi nikawaapia, nikawaambia Irene hamuwezi Elvin, hata afanyaje. Wakasema mbona Irene amempigia simu Elvin wakutane na Elvin hajakataa? Ngoja kwanza nikuulize Elvin. Eti huyu mtoto hajakutumia ujumbe anakwambia anakupenda na amekumiss?” Elvin alishtuka kidogo, Irene akanywea kama sio yeye.
“Simmeona alivyopoa kama sio yeye! Mimi nawaambia nafahamu mambo yote. Wewe Dogo ule ujumbe si hukujibu?” Elvin alikuwa kimya akishangaa. “Basi hayo majibu yako ya ule ujumbe uliotumiwa, ulikuwa unasubiriwa na hawa watoto wa kishua kweli. Unaambiwa simu yake huyu ilikuwa imewekwa mezani tokea amekutumia ujumbe wanasubiri jibu kutoka kwako. Walipoona kimya nasikia wakaanza kumzomea huyu mwanamke wako. Akawahakikishia kuwa wewe huwezi kuchomoa kwake hata iweje. Alipoona kimya, ndio maana akakupigia simu ili mkutane. Ulipokubali mkutane hapa nyumbani, akaanza kutamba kwa wenzake, eti ashakunasa, kwa kuwa umekubali mkutane. Washikaji pale baa wakaanza kushangilia, eti umeshanaswa. Mimi nikawakatalia kata kata. Tulipomaliza tu kuwekeana dau na washikaji, nikawaambia ngoja sasa mimi niende nikarikodi kila kitu mje kushukudia kichwa cha Dogo. Nikatoka zangu baa, nikaja zangu kukaa jikoni nisikilize mchezo mzima, wakati simu yangu nimetegesha hapo kwenye kochi alilokuwa amekaa Irene, ili kuanzia kesho nipate pombe za bure.” “Muongo Eli. Unaongea pombe tupu tu hapo.” “Sikatai kama mimi mlevi. Lakini kama mimi nimuongo, Elvin akane kama hajapokea ujumbe kutoka kwako na hakukujibu mpaka ulipompigia. Sio wewe uliyekuwa ukizunguka siku nzima kumsaka Elvin, kuanzia kazini kwake mpaka hapa nyumbani, bila mafanikio mpaka jioni hii ndio Elvin amepokea simu yako? Na wala sikuwa na Dogo. Sasa yote hayo kama mimi muongo, ningeyajuaje?” Wote wakabaki kimya wakishangaa.
“Habari zako zote nimezipata leo Irene. Wewe mchafu sana.” Eli alimsogelea kidogo. “Mimi si unaniita mlevi, sikatai nakunywa kwa pesa yangu, sigombani na mtu, nina marafiki wengi kuliko adui. Wewe una maadui wengi kuliko marafiki. Rafiki zako wenyewe wamechoshwa na wewe, wanakuanika kila mahali.” “Wala, best zangu hawawezi.” “Si ndivyo wanavyo kudanganya. Nikuulize swali ili ujue hao unaowaita best zako ndio wanatoa siri zako?” “Uliza.” Irene alijibu bila woga.
Eli alianza kucheka sana. “Yaani leo utaumbuka wewe! Tatizo lako wewe jeuri na hutaki kushindwa. Haya twende kazi. Swali moja tu. Hujalala na Phil wewe?” Irene akanyamaza. Eli akaanza kucheka. “Ona sura yako. Nitakuletea kioo mimi ujione. Junior Masha mwenyewe anajidai rafiki yake Elvin, lakini ashakugonga zaidi ya mara moja. Unabisha?” Irene akanyamaza. Elvin alishtuka sana. “Junior!?” “Sasa je? Muulize demu wako huyo, na muulize Junior kwa nini alikuja kukwambia kama Phil na yeye alijishindia kwa Irene. Unafikiri eti alikuja kumsemelea huyu bure? Alikasirika Irene alipolala na Phil. Waongo wote hawa pamoja na baba zao wenye hela zao za wizi. Kwanza kwenda kwenu usilete mashetani yako hapa.” Hasira zilishaanza kumpanda Eli.
“Nakwambieni mimi habari zote za hawa watoto wanaojidai wakishua ninazo. Hawana lolote hawa, wanakazi ya kuzungukana zungukana humo kwa humo. Wanakulana wenyewe kwa wenyewe. Ndio maana mimi sigusi kabisa huko. Heri nikajinywee zangu pombe, nifurahi nikirudi nilale.” “Pombe sio nzuri Eli.” Baba yake aliingilia. “Najua wewe mtu wa Mungu baba, utapinga tu. Lakini niangalie mimi na hao wanao watatu. JJ hana raha hata kidogo na ndoa yake, sababu ya kumuozesha mtoto wa rafiki yenu. Mwanamke kutwa anadai hiki anataka kile, JJ halali kwa kufanya kazi mridhishe yule mwanamke, lakini wapi. Haya huyu mtoto wenu mzuri Elvin, oneni  anavyosemwa sasa hivi mtaani sababu ya huyu mtoto! Tena warafiki yenu pia. Mmekaa tu hapo, nyinyi kama wazazi mnasikiliza huyu mtoto anaongea kama cherehani tena bila adabu, hata hamshangai kuwa huyu mtoto ni mtoto wa namna gani! Atakuja kuwa mkwe wa namna gani huyu? Msichana hana aibu! Tangia mwenzie anaingia hapa, anaongea tu. Sasa badala nyinyi, baba na mama, mumshauri Elvin, mnataka kelele hiyo ndio akaishi nayo mpaka kifo! Hivi nyinyi baba na mama mnatupenda lakini au?” Eli aliendelea kwa wazazi wake.
“Wewe mwenyewe mama umemuona Elvin ameingia, kitu cha kwanza, umempa pole, ukamuuliza chakula. Huyu mtoto tokea mwenzake ameingia hapa ni lawama tu. Maneno mengii halafu wewe mwenyewe mchafuu. Kwanza toka nyumbani kwetu, toka nenda kwenu. Kawaambie mashoga zako na huu mtego wa pili umeshindwa hapa nyumbani kwa Mzee Mwasha.” Eli alimsogelea karibu zaidi Irene kama kutaka kumtoa nje.
“Ngoja kwanza Eli. Umesema mtego wa pili?” Elvin akauliza. “Kumbe! Tatizo lako Dogo hutaki kujichanganya, hujui mambo. Wewe hukushangaa alivyokimbizwa hospitalini siku ile eti amekunywa sumu, kwa nini kwa muda mfupi tu hospitali nzima ilikuwa imejaa, mashoga zake na wazazi wao? Kundi zima lakina baba lilikuwepo pale. Wewe hutumii akili habari hizo zilifika saa ngapi wakati mgonjwa anafika tu hospitali na watu wanafika? Hujajiuliza? Basi ule ulikuwa mtego mwingine. Wote walikuwa kwenye simu, wanasubiri tu Irene adanganye amekunywa sumu, halafu kila mtoto amtaarifu mzazi wake, watu wajae pale hospitalini kujulikane ni tatizo kubwaa, ligeuke kuwa gumzo ili Elvin ajisikie vibaya na nyinyi baba na mama mumlazimishe Elvin amuoe huyu, ili yeye apate sifa kwa rafiki zake. Kwanza wala hakupendi huyu msichana. Anatafuta sifa kwa rafiki zake, ili yeye ndio awe mshindi, awe amekupata wewe. Wanakuwinda kweli wenzako hawa. Wewe peke yako ndio hujagonga msichana hata mmoja kwenye kundi lao, sasa huyu Irene ndio ameapa, yeye ndio atakuwa msichana wa kwanza kukufikisha kitandani. Huoni anavyokung’ang’ani? Sasa nenda kawaambia wazazi wako na mashoga zako, mimi kaka yake Elvin, nimesema kwenye hii nyumba wameshindwa, wamempata JJ, yeye ndio kafara yetu. Hatuwataki na wala hatuoi tena huko kwenye kundi lenu. Toka zako hapa. Nenda kajiuze nyumba nyingine sio hapa. Kwenda zoko, shetani wa mchana wewe. Toka.” Irene alianza kulia.
Eli alizidi kumsogelea huku anapepesuka kwa kulewa. “Nimekwambia chukua kipochi chako nenda kwenu kwenye gorofa lenu la uwizi. Na mtakuja kufilisiwa siku si nyingi. Toka.” “Eli wewe! Hebu nyamaza.” “Kwani wewe mama hujui baba yake huyu mwizi? Habari zote tunazipata baa.” “Hapana Eli usiseme hivyo.” “Sawa mama. Mbona huendi wewe? Nitakupiga mtama mimi. Vitoto vina sifa mbaya hivi! Kila mwanaume mwenye pesa mjini anawajua. Kazi yao kujikondesha, vyembamba hata nyama havina. Halafu kuvaa uchi na kuongea kingereza kirefuuu, kichwani hamna kitu. Kwenda na ukirudi tena hapa nakuchapa makofi.” Elvin alikuwa kimya kabisa akishangaa usaliti wa marafiki zake.
“Inamaana wote walikuwa wakijua kuwa Junior Masha anamahusiano na Irene, halafu hakuna aliyeniambia!?” Elvin aliwaza kwa sauti.  “Wanafiki wote hawa watoto. Wakike na wakiume, hamna wenye nafuu. Wanajua kutapanya pesa za baba zao, hakuna cha ziada wanachojua kufanya. Wewe ukishasikia wanasafiri kama kundi kwenda kwenye mapumziko mahali, ujue ndio uchafu wanao enda kufanya huo. Huyu atalala na huyu, kesho yule anarudi kulala na huyu. Junior Masha huyo anayejidai rafiki yako mpenzi, ndio mbaya kuliko wote. Kwa kuwa anawahonga pesa nyingi, kashalala na kundi lote la kina Irene. Ila nasikia hapo kwa Irene ndipo anapo rudiarudia. Lakini kawamaliza wote hao. Uongo Irene?” Irene alikuwa bado analiana. “Acha uchuro hapa nyumbani kwetu. Ngoja nikusindikize kwa nguvu.” Eli alichukua funguo za gari za Irene na pochi yake, akamsukumizia Irene nje huku anacheka. “Kesho utakuta habari zako zote mtaani, mpaka kwa mama yako mzazi atapata haya mazungumzo yetu. Ndio mkome kutufuata watoto wa Mzee Mwasha.” Eli alifunga mlango akarudi ndani.  
“Ngoja mimi nikalale.” Eli alimsogelea mama yake akiwa ametulia kabisa kama sio yeye. Mama yake alibaki akimwangalia. “Nimeharibu nini?” Eli alimuuliza mama yake. “Usingemwita baba yake mwizi.” “Basi mama yangu nimekosa. Wameniudhi sana hawa watoto. Wanataka kumchezea Dogo bwana, wakati Dogo ametulia! Ngoja nikalale. Kesho tutaongea vizuri, si unajua nimekunywa kidogo? Lakini usifikiri nimelewa, naondoka tu kwa kuwa nakujua wewe mama yangu kipenzi huwa hupendi hata harufu ya pombe. Ngoja nikajifungie chumbani kwangu mpaka kesho. Sitaki kukuudhi. Sawa mama?” “Ni kweli Eli. Naomba kesho uwahi nyumbani nina mazungumzo na wewe.” “Usiwe na wasiwasi mama yangu. Tutapanga vizuri kesho asubuhi nikiamka. Kabla sijaenda kazini nitakuja kukuaga chumbani kwako, ndio uniambie muda kamili unaotaka niwepo hapa nyumbani. Au nimekosea?” “Ni sawa kabisa. Kabla ya kwenda kazini uje kuniaga.” “Ndio maana nakupenda mama yangu. Wewe ndio mwanadamu pekee unayenielewa hapa duniani.” Alimbusu mama yake akaondoka. Elvin na baba yake walikuwa kimya kabisa wakimsikiliza Eli na mama yake. Eli alipoondoka, baba yake alimgeukia Elvin. “Pole sana Elvin.” “Naomba na mimi nikalale. Usiku mwema.” Elvin naye akaondoka bila yakuongeza kitu.
**********************************
Bella alimka akiwa na nguvu, aliamua kumtumia Mzee Masha zile picha alizojipiga bafuni. Alituma picha zote akiwa amevimba sana uso na ujumbe. ‘Hii ndio shukurani yako kwangu baada ya kutumia mwili wangu utakavyo. Na isingekuwa Elvin kuniwahisha hospitalini wakati tupo safarini, labda sasa hivi ningekuwa nimekufa. Lakini nakuapia Masha, Ipo siku Mungu atakulipa kabla hujafa.’  Bella alilia kidogo akaingia bafuni kuoga akarudi kukaa kitandani akiwaza.

**********************************

Elvin alirudi kuwaona asubuhi hiyo. “Ric bado amelala!?” “Anachoka sana na hiyo michezo yake. Njoo ukae hapa.” Bella alijisogeza ili Elvin akae pale kitandani. Elvin alikaa, Bella akabaki akimwangalia. “Nini nimekuudhi Elvin?” Bella alimuuliza kwa upole sana baada yakumuona ameingia na sura ambayo hakuzoea kuiona usoni mwake. “Kwa nini?” Elvin alishtuka kidogo, hakujua kama uso wake ulionyesha tofauti. “Unaonekana hukulala vizuri. Jiegemeze hapo ulale kidogo, nitakuamsha baaaye kidogo apate kifungua kinywa.” Bila kubisha, Elvin alijivuta chini kidogo, akapitiwa na usingizi, pembeni ya Bella. Ni kweli hakuwa amelala vizuri. Bella alibaki akimwangalia.
**********************************

Kwa muda mfupi aliokuwa amekaa na Elvin, hasa safari yao ya mapumzikoni, Bella alijikuta kwa mara ya kwanza anampenda mwanaume kimapenzi. Alijitahidi kupingana na hisia zake, kutokana na maisha anayoishi kwa wakati ule, lakini alishindwa. Ndio kwa mara ya kwanza alishikwa na mwanaume akapata furaha moyoni. Ndiye mtu pekee aliyemfanya alale kwa haraka na ndiye mtu pekee aliyeweza kumfanya acheke sana, mbali na Eric. Alibaki akimtizama, mpaka na yeye alipopitiwa na usingizi pembeni yake.
**********************************

Elvin aliendelea kuwa akija pale hotelini kuanzia asubuhi na kuondoka usiku akimuuguza Bella, mpaka Bella alipopona kabisa akabaki alama kidogo ambazo aliweza kuzificha kwa kupaka foundation. Japokuwa alikuwa amepata sababu ya kumuuguza Bella, lakini pia alifurahia muda na mambo aliyokuwa akifanya na Bella kila awapo naye pale hotelini. Ule utulivu aliokuwa akiupata, hisia za mapenzi zilizokuwa zikitembea katikati yao, yeye na Bella, tena bila kuingiliwa na mtu yeyote, kwani hata Eric hakuwa na muda nao, furaha yake ilikuwa nikujua wapo pale pembeni yake, yeye akiwa anaendelea na michezo yake, kwa hiyo Elvin alianza kuchukia masaa yanavyokimbia, na usiku unavyoingia kwa haraka, na kuagana na Bella kipindi hicho cha usiku anapotakiwa kurudi nyumbani kwao na kumuacha Bella pale hotelini. Alikuwa akichelewa sana kurudi nyumbani, na aliamka asubuhi sana kuwahi kurudi hotelini hapo, tena wakati mwingine bila ya kuonana na wazazi wake, tabia ambayo wazazi wake hawakuizoea kuina kutoka kwa Elvin.

**********************************

Siku ya ijumaa nayo haikukawia kufika, muda wa Eric kurudi shule nao ukawadia, wawili hao wakiwa wanashinda kitandani hapo, kwa kisingizio cha kuuguzana, na Bella kuwa na mdogo wake. Elvin akiwa chumbani kwao, akiangalia movie na Bella, Bella ilibidi kuweka kando hisia zake, ili maisha mengine yaendelee. “Vin!” Bella alimuita. Elvin alifurahia sana jinsi Bella alivyomuita. Alimgeukia na tabasamu usoni. “Naomba nikuache na Ric mara moja, niende nikakate tiketi za ndege ya Arusha. Anatakiwa awe amefika shuleni siku ya Jumapili, lakini nataka awahi kwenda jumamosi ili apate angalau siku moja yakutoa hiyo michezo yake kichwani kabla hajaanza kuingia darasani.” “Ungependa niwasindikize Arusha?” “Ningefurahi sana.” Elvin alimuona vile Bella alivyofurahia wazo la kwenda naye Arusha.
“Basi twende wote, mimi ndio nitakata tiketi.” “Ninazo pesa Elvin. Naomba mimi ndio nikate tiketi.” “Unapata wapi hela Bella? Naomba uniambie ukweli.” “Nimeahidi kukwambia Elvin, naomba uendelee kuwa mvumilivu.” “Lakini mimi sipo huru, au siwezi kutumia pesa ambazo sijui zinatoka wapi. Siwezi Bella. Hata hapa hotelini nakuja kwa kuwa wewe ulikuwa mgonjwa, lakini inanitia wasiwasi sana. Mnaishi maisha ya gharama sana. Ambayo hayaendani na uhalisia wa maisha. Sijisikii huru kuwa kwenye mazingira kama haya, Bella. Unisamehe, lakini ndivyo nilivyo. Ni heri kukosa kuliko kuwa navyo vingi ambavyo najua havitokani na njia sahihi. Siwezi kuishi nje ya kile ninachoweza kutengeneza. Kwa hiyo kama kweli unataka kwenda na mimi Arusha, naomba mimi ndio ni gharamie hiyo safari.” Bella alibaki ameinama chini. Elvin alimuona akifuta machozi.
“Usinielewe vibaya Bella, sikuhukumu kwa lolote, kwa kuwa sijui ni nini kilichokupelekea kufika ulipo sasa hivi, lakini siwezi kuwa na wewe kwenye maisha ambayo sielewi. Siwezi kujiingiza kwenye kitu nisichokielewa.” “Kwa hiyo hututaki tena?” Bella aliuliza huku akilia. “Hapana Bella. Sijasema hivyo na wala nisingekuwa hapa kama namaanisha hivyo. Ila ninachotaka uelewe, najua kiasi cha pesa unachoingiza, nimeona maisha unayoishi sasa, kaviendani kabisa. Najua una pesa nyingi sana, ambazo sijui unatoa wapi Bella, na umeshindwa kuniambia kabisa. Siwezi kuanza kuzitumia na wewe. Naomba tunapokuwa wote, tuishi maisha ya kwetu. Yanayoendana na sisi, na uwezo wangu. Itanirahisishia sana mimi kuwa karibu na wewe. Unafikiri utaweza Bella?” “Nitaweza Elvin.” “Asante. Basi twende tukakate tiketi.” “Naona itakugarimu sana Elvin, naomba nichangie kidogo.” Bella alifuta machozi.
“Wewe unatakiwa kulipa ada na mambo mengine ya shule ya Ric. Acha mimi nilipie tiket. Tunarudi lini?” “Huwa tukifika Arusha, namzungusha anunue vitu atakavyohitaji shuleni, na tunatembea kidogo ndipo nampeleka shule. Mpaka kurudi mjini inakuwa imeshafika jioni, huwa nalala, kesho yake ndio narudi huku Dar. Lakini najua wewe una majukumu mengi, unaweza kugeuza siku hiyohiyo.” “Sawa, twendeni.” Ilibidi Bella kumtoa Eric Headphones masikioni na kumpokonya zile rimoti ndipo aliposhtuka.
“Nini Bella?” “Kesho unarudi shule. Twende tukakate tiketi.” “Kwani nilazima twende wote? Naomba uniache utanikuta.” “Ric jamani! Ujue sitakununulia game nyingine tena kama hizo game zinachukua nafasi yangu! Tokea nikupe hizo game, hatujapata tena muda na mimi. Unashindwa hata kuniangalia!” “Basi Bella, samahani. Twende wote. Unataka twende wapi tena?” Bella alitabasamu. “Kukata tiketi.” “Haya twende. Tutaenda na Elvin?” “Ndiyo. “Utanisindikiza shuleni pia, Elvin? Ili ukapafahamu ninaposoma?” “Tutaenda wote Ric.” Eric alifurahi sana.
“Nitakuonyesha viwanja ninavyocheza mpira wa miguu na kikapu. Bella amekwambia kuwa mimi ndio wananitegemea shuleni?” Eric aliendelea kujisifia njia nzima yeye ndio alikuwa akiongea, Elvin na Bella walikuwa wakicheka tu.
“Nikwambie kitu Elvin?” Eric aliendelea. “Ehe.” “Yupo msichana mmoja wakizungu, ananipenda kweli!” “Ric wewe!” Bella alishtuka sana. “Lakini nimemwambia kama ulivyoniambia Bella. Usiwe na wasiwasi, sijasahau.” “Na usisahau.” Elvin alikuwa akicheka. “Kwani wewe Ric, ulimwambia nini huyo msichana?” Elvin aliuliza huku anacheka. “Kama Bella alivyoniambia.” “Kwa hiyo ukamwambiaje?” Elvin alishamuona Eric ana akili za kitoto sana, akataka kuendelea kumsikiliza tu.  “Nimemwambia Bella ameniambia nisubiri kwanza, nisiwe na msichana yeyote.” Elvin alizidi kucheka.
“Kwani Bella si ndivyo ulivyoniambia? Au nimekosea?” “Ndiyo. Hakuna kuwa na msichana sasa hivi.” Bella alijibu bila kufikiria. “Ngoja kwanza Ric. Sasa huyo msichana anamfahamu Bella?” Ric alifikiria kidogo. “Atakuwa hamfahamu Bella, eeh?” Eric aliuliza huku akifkiria. “Nikifika shuleni nitamwambia Bella ni nani.” Eric alipata wazo jingine. “Au fanya hivi, watakapo kuwa wasichana wanakufuata, wewe waambie hapana. Waambie mimi sitaki kuwa na mahusiano sasa hivi.” “Eti eeh Elvin? Itanipunguzia maswali ya kutaka kumjua Bella.” Bella alikuwa akicheka huku akitingisha kichwa. “Yaani Ric huyu, bado mtoto sana.” “Hapana Bella. Mimi nimeelewa. Unajua kila nikimaliza kucheza huwa wananifuata wananiambia wananipenda. Halafu sio huyo msichana wakizungu tu, na wengine huwa wananiletea  kadi na zawadi. Sasa badala yakuwaambia Bella amenikataza, nitawaambia kwa kifupi kama alivyosema Elvin. Hapana.” “Safi sana Ric. Sasa wakikuuliza kwa nini, utasemaje?” Elvin aliuliza kumchokoza tu.
“Ndio hapo sasa nitawaambia Bella amenikataza.” Elvin na Bella walikuwa wakicheka mpaka wanafuta machozi. “Au nimekosea?” Eric alikuwa haelewi kwa nini wanamcheka. “Tukirudi hotelini, tutaongea vizuri Ric. Mimi na wewe. Sawa?” “Sawa Elvin. Ili unieleweshe vizuri?” “Ndiyo. Ili nikueleweshe vizuri kwa nini unatakiwa usubiri. Usiwe kwenye mahusiano ya mapenzi sasa hivi, sio kusema tu ‘Bella amenikataza’.” “Watakuwa hawanielewi, eeh?” Ric aliuliza kwa nia nzuri kabisa. “Tutaongea vizuri, usiwe na wasiwasi. Vipi na masomo lakini?” “Najitahidi. Bella amesema nikifeli tu, atanitoa kwenye michezo. Kwa hiyo najitahidi kusoma pia ili nibaki kwenye michezo, haswa mpira wa kikapu. Mimi ndio team leader wao, lakini namasomo najitahidi japo sijawahi kuwa mtu wa kwanza darasani, lakini sijawahi kufeli. Bella anaangalia mitihani yangu anasema najitahidi sana. Si nasema ukweli Bella?” “Ndiyo Ric. Unajitahidi sana darasani.” Eric alifurahi sana.

Bella na Elvin, jijini Arusha.”
Safari ya Arusha ilikuwa nzuri sana. Vilijaa vicheko kati yao, huku wakiendelea kuzunguka jijini hapo. Walizunguka kumnunulia Eric vitu vyake vya shule, Elvin alikuwa akimwangalia vile Bella anavyo mwaga pesa kwa mdogo wake bila kufikiria. Kila kitu alichotaka Eric, Bella alinunua bila hata kufikiria mara mbili. Walikuwa wakizungushwa na taksii mjini, mpaka jioni walipompeleka Eric shuleni kwao. Elvin alibaki akitoa macho jinsi hiyo shule ilivyokuwa nzuri na ya kisasa. Viwanja vya mpira vya kisasa, mazingira yote yalikuwa mazuri sana.
“Unalipa ada kiasi gani hapa?” Ilibidi Elvin amuulize Bella. “Milioni 22. Kwa mwaka.” Bella alijibu bila kufikiria. Elvin alishtuka sana. Alibaki akimtizama Bella, ambaye hakuwa na wasiwasi kabisa. Walizungushwa kwenye hiyo shule, kila mtu alionekana kumfurahia Eric. Kweli waliona vitoto vingi vya kike vikimkimbilia na kumkumbatia Eric, huku wakimwambia walikuwa na hamu naye. Eric kama kawaida yake alikuwa akicheka tu. Mwishowe walipoona giza limeingia, wakamuga na kumuacha Eric akiwa ameungana na rafiki zake, wakisimuliana likizo ilikuwaje, wao wakaondoka kutafuta hoteli.
Njia nzima Bella alikuwa kimya kabisa akiangalia dirishani. Elvin alimuona jinsi alivyokosa raha. Bella yule wazamani alirudi usoni. Alipooza sana. Dereva alisimamisha taksii mbele ya hoteli. “Naamini hapa mtapapenda.” Dereva aliwageukia kuwataarifu wamefika. “Naomba nilipe Elvin, tafadhali. Nilishatenga pesa ya usafiri kabisa.” Walikuwa wamezunguka na hiyo taksii, karibu siku nzima. Bella alijua watakuwa wanadaiwa pesa nyingi sana, asingependa kumtia Elvin garama zaidi. Alihakikisha yeye ndiye analipia, wakashuka.
Walibabaika sana walipofika mapokezi, hawakujua kama wachukue chumba kimoja au viwili. “Vyovyote tu vile, Elvin.” Bella alibabaika. “Utakuwa sawa?” “Ndiyo.” Alijibu tu, lakini hakujua atakuwa sawa akiwa peke yake chumbani au wakiwa wawili. Elvin alibaki akimwangalia kwa muda. “Nitachukua chumba kimoja chenye vitanda viwili.” Bella akatabasamu. “Asante.” Elvin akalipia chumba, wakapewa funguo, wakaondoka na mizigo yao pale mapokezi.
“Kumbe ulitaka nichukue chumba kimoja, kwa nini sasa hukuniambia?” Elvin aliuliza wakati wanapandisha ngazi kuelekea chumbani kwao. “Eti Bella?” “Nahofia Elvin. Hunifahamu vizuri, au hutufahamu vizuri, usije ukanielewa vibaya.” Walingia ndani wakakuta chumba kizuri sana. Kisafi na kina kila kitu ambacho wangekitaka kwa usiku huo. Bella aliweka vitu vyake kwenye kitanda kimojawapo akabaki akiwaza. “Mbona huna raha sasa?” Bella alitabasamu. “Tumezunguka sana leo, naona nimechoka. Labda nikaoge kwanza nitajisikia vizuri.” Bella alingia kuoga akatoka akiwa ameshavaa nguo za kulalia. “Hatutoki kwenda kula.” “Hapana Elvin. Mimi nitawahi tu kulala.” “Njoo kwanza.” Elvin alipigapiga kitanda chake kumuashiria Bella aende akakae hapo.
“Vipi mbona furaha yote imeisha?” Bella alianza kulia. “Usilie bwana. Niambie una nini?” “Sina maisha bila Ric, Elvin. Naishi kwa ajili ya yule mtoto. Maisha yangu yamejaa mateso makali sana, angalau nikiwa na Ric, najio…” Bella alizidi kulia. “Natamani kama ningekuwa naishi naye kila siku.” “Kwa nini sasa umempeleka shule ya bweni, tena huku Arusha, wakati Dar kuna shule nzuri sana?” Bella alifikiria kidogo kwa muda. Kisha akafuta machozi.
“Kwa mara ya kwanza, Bella aamua kuwa muwazi kwa Elvin.”
“Nikwambie kitu Elvin?” “Unaweza kuniambia kitu chochote kile Bella.” “Hutanikimbia?” “Siwezi Bella. Najua umepita kwenye maisha magumu sana. Siwezi kukuhukumu. Hata hivyo nashangaa sana, haya maisha unayoishi, shule anayosoma Ric, vyote ni vya gharama sana. Kila kitu chako ni cha gharama. Natamani kujua ulifanikiwa vipi!” “Sijafanikiwa Elvin. Nipo kwenye kifungo kikali sana. Usinione hivi natembea lakini ujue natembea kwa ajili ya Ric. Huu muonekano wa nje ni sababu ya Ric tu, lakini ndani nimeoza, nikama mzoga. Ninafanyiwa mambo mabaya sana. Yaani mimi mwenyewe nikikaa najifikiria nawezaje kuamka siku ya pili na kutembea, sielewi. Ile kazi mliyonipa na baba yako ni sehemu pekee ninayoweza kusimamisha hofu yangu kwa muda, nikasahu maisha yangu kwa masaa machache nikiwa pale kazini wakati Ric akiwa hayupo.” Bella aliendelea.
 Umeshawahi kuwa na hofu ya kurudi kwenye nyumba unayoishi?” Elvin alimwangalia Bella kwa kumuhurumia sana. “Basi ndio mimi. Kila ninapotoka kazini nikifikiria narudi nyumbani, mwili mzima unatetemeka, au kama sasa hivi Ric amerudi shule inabidi nirudi nyumbani.” “Sikuelewi Bella. Ric alisema pale ndio nyumbani kwenu.” “Ndivyo ninavyomwambia yeye. Lakini kama sasa hivi akiwa yeye hayupo, siwezi kuishi pale, narudi huko nyumbani.” “Sielewi Bella.” Bella alivuta pumzi kwa nguvu sana. Akasogea kujiegemeza kitandani. Elvin alimsogelea ili kumsikiliza kwa makini.
Mama alipofariki, nilikwambia tulienda kuzika kijijini. Kila mtu alitukataa kutuchukua ili watusaidie.” “Baba yenu yuko wapi?” “Hata sijui. Unajua hata Ric mwenyewe hafahamu kuwa sisi sio watoto wa baba mmoja? Mama aliugua sana. Kipindi cha karibia kifo chake alikuwa akiongea mambo mengi sana, alikuwa kama amechanganyikiwa. Sasa sijui ni kweli au la, lakini alikuwa akiropoka kwamba Ric ana baba yake na mimi nina baba yangu.” “Hukumuuliza baba zetu wako wapi?” “Yaani Elvin sijui ni mshtuko wa maisha au vipi, sikuwa hata na wazo la kumuuliza. Nilimuuguza sana mama. Tena nikiwa na hofu sana asije kufa akatuacha. Nilikuwa nikiogopa maisha baada ya kifo chake. Sikujua itakuaje hatima yetu mimi na Ric. Kwa hiyo akili yangu ilikuwa ni kuhangaika apone na si vinginevyo. Halafu hakuwa na biashara wala hakuwa ameajiriwa. Kwa hiyo maisha yakaanza kuwa magumu, akawa ananituma kuuza baadhi ya vitu vyake huku au kule, ilimradi tu tuweze kuishi. Sasa alipochanganyikiwa na mimi nilikuwa kama nimechanganyikiwa, maana nilikuwa sijui chakufanya tena. Hela hakuna, na maisha yalikuwa yanatakiwa yaendelee. Kilikuwa kipindi kigumu sana, sitakaa nisahau.” Bella alianza kutokwa machozi.
“Mama aliugua sana, Elvin. Sana. Ilifikia kipindi, ilikuwa ni mtu wakumgeuza tu. Hali ilikuwa mbaya kweli! Aligeuka akawa mweusi wakati alikuwa na rangi kama hii yetu, mimi na Ric. Alijawa mapele, halafu mbaya zaidi akawa ametusahau kabisa. Hakuwa akimtambua Eric wala mimi.” Bella alizidi kulia.
“Pole Bella. Pole sana. Lakini nini kilitokea baada ya kuachwa kijijini?” Bella akajitahidi kutulia ili aendelee kumsimulia Elvin. “Kama nilivyokwambia, maisha ya kule kijijini yalitushinda tukaja mjini kwenye nyumba tuliyokuwa tukiishi na mama. Lakini tukakuta kila kitu kimechukuliwa. Ikabidi tukakae na Kaka Mat, kwenye chumba chake, mtaa wa Kigogo. Maisha yalikuwa magumu sana Elvin. Kaka Mat alikuwa akitupenda sana. Alikuwa akileta chakula kila akipata mteja kwenye taksii, lakini shule kwa Ric ndio ilikuwa shida. Hakuwa akielewa chochote darasani, sababu ya lugha. Tokea tunaanza shule ya chekechea wote wawili tulianzishwa hizi shule za kingereza kitupu. Sasa kule shuleni akawa anashindwa kabisa kuelewa. Ukimwamsha asubuhi aende shule, analia sana. Anasema wenzake wanamcheka shuleni kwa kuwa hajui kusoma wala kuandika. Kumbe ni sababu ya lugha ya Kiswahili. Hatukuwahi kujifunza kwa Kiswahili. Kwa hiyo wakawa wakimuona mjinga, wakati kwa asili yeye anaakili nzuri tu darasani.” Bella akaendelea.
“Akaanza kuwa anazunguka mtaani kucheza, kuanzia asubuhi mpaka jioni. Na kama unavyopajua Kigogo, wale mateja wa pale Kigogo wakaanza kumtumia. Wewe unamjua Ric, hawezi kukataa hata akiambiwa kitu cha hatari kiasi gani. Tuliishi pale kwa muda mrefu sana bila mabadiliko yeyote ya kifedha. Mwishowe nikaona anaweza kuharibikiwa kabisa.” Bella akatulia kidogo.
“Nikaamua kwenda kuomba msaada kwa rafiki yangu kipenzi, ambaye tulikuwa naye karibu kabla ya kifo cha mama. Tulipofika pale, nikawaelezea kwa ufupi maisha yetu ya wakati huo, nikawaambia tunaomba watusaidie msaada wowote, kwani mazingira ya kule tunapoishi ni hatarishi kwetu. Yule mama na mtoto wake, ambaye ndio huyo rafiki yangu, wakatufukuza vibaya sana. Tukaambiwa tuondoke, huku yule rafiki yangu akinisanifu, kwamba nilikuwa muongo nilimdanganya nyumba tuliyokuwa tukiishi mikocheni ilikuwa yetu. Ukweli Elvin, hata mimi sikuwa nikijua kama pale ilikuwa ni nyumba ya kupanga. Kwa kuwa nilikuwa siulizi au simuulizi mama. Maadamu maisha yalikuwa yakienda vizuri tu, basi. Tena mama alijitahidi sana kutulea kwenye maisha ya hali ya juu sana, tulifanana na watoto wa matajiri. Na mama alikuwa na upendo sana, nahisi ndicho kilichonifanya nishindwe hata kuwahi kumuuliza baba yangu yuko wapi, na hakuwahi hata kuzungumzia.”
“Basi, tulipofukuzwa pale nyumbani kwa rafiki yangu wakati tupo njiani akatusimamisha dereva wao. Akasema ametumwa aje atuchukue atupeleke mahali. Niliingiwa na wasiwasi kidogo, nikamuuliza ni nani amemtuma? Maana tulifukuzwa muda mfupi sana uliopita halafu tena tunatumiwa gari! Akasema tupande kwenye gari kama tunataka msaada. Tukapanda. Lakini Elvin, najuta mpaka leo. Najuta na kulaani ile siku nilipokubali kupanda lile gari.” Bella alikuwa akilia huku akijifinya na kujipigapiga.
“Natamani wakati tumesimama pale tunaongea na yule dereva, gari nyingine ingekuja ikatugonga tukafa mimi na Eric, au hata radi ingetupiga tukafa pale pale kabla hatujaingia kwenye ile gari. Najuta Elvin, najuta sana.” Elvin alimvuta mikono yake, kwani Bella alikuwa akijiminya kwa nguvu sana na kwa uchungu, kama kujiadhibu. “Pole Bella.” “Kupanda kwangu kwenye lile gari, ndio ukawa mwanzo wa mateso yangu. Siku napanda kwenye lile gari, ndio siku nilipomuuza Enabella aliyezaliwa na Tunu na kukubali auwawe kila siku. Ndipo mateso yangu yalipoanza rasmi.” Bella alilia sana, kisha akatulia baada ya Elvin kumtuliza.
“Tulipelekwa kwenye ile hoteli, Ric anapopaita nyumbani. Kwenye chumba kilekile, nakuanza kuhudumiwa kama watoto wa mfalme.” “Na nani?” “Mara ya kwanza alikuwa anakuja dereva tu. Kwa muda mrefu sana dereva alikuwa akituhudumia, siku moja akaja sasa huyo baba mwenyewe. Cha kwanza akatuambia anataka atusaidie, atamsomesha Eric. Yeye ndio alimtafutia Eric hii shule. Kumbe shida yake ni kututenganisha mimi na mdogo wangu ili anitumie mimi.” Elvin alikunja uso kidogo.
“Ric alipooenda shule tu, ndipo manyanyaso, masimango vipigo vilipoanza kwangu. Tena bila kosa. Yule baba alinichukua mpaka Dubai, na kufanya mapenzi na mimi. Sijawahi kuumia roho kama siku ile. Maumivu ya mwili hayakuzidi ya moyoni, Elvin. Alinifanyia mapenzi kikatili sana, tena kilazima. Hapakuwa na kuombwa. Alinihesabia misaada anayonipa, nakuniambia lazima alale na mimi. Unakumbuka tulikutana Dubai nikiwa naumwa?” Elvin alishtuka sana. “Mzee Masha!?” “Ndio kipindi kile yule baba alitoa utoto wangu tena kikatili sana. Sikuwahi hata kuwa na wazo la kuwa na mwanaume. Tena mtoto wake Zera, alikuwa na wanaume wengi tu, wakati tupo marafiki lakini mimi sikuwa hata na wazo lakuanza mapenzi kwa wakati ule. Mama alinisihi sana nisubiri.”
“Eti yule baba alikuja kuniambia alikuwa akinitamani tokea naenda kulala nyumbani kwake na mwanae! Fikiria Elvin, yule baba alivyomkatili, anawezaje kunitamani mtoto ninayelingana na mtoto wake? Tena nilikuwa mtoto mdogo kweli. Alinitoa pale Dubai, akatafuta nyumba ambayo ndiyo naishi naye mpaka sasa. Alinitafutia mama mtu mzima ili kunifundisha mambo ya ndoa. Nilikuwa ninalia Elvin, nilikuwa sitaki kujifunza. Mwishowe yule mama akaamua kuwa ananisemelea kwa Masha kuwa sitaki kujifunza kila anapokuja pale nyumbani, huwa nalia wakati wote yeye anaponifundisha. Masha alikuwa akinivuta mpaka chumbani kwetu, ananipiga na kunilazimisha nirudi kwa yule mama, kwenye chumba kingine, nijifunze mpaka nielewe. Nyumba yenyewe imezungushiwa ukuta na kuna walinzi mlangoni.”
“Siku moja alipoondoka nikajaribu kuruka ukuta ili nitoroke, nikakamatwa na wale walinzi, jamani yule baba aliporudi alinipiga kama mwizi.” Bella alivua kiblauzi alichokuwa amevaa kumuonyesha alama za mikanda ya suruali iliyoachwa mwilini mwake. “Ona huko mgongoni hizo alama. Na yule baba anajua kupiga, sijawahi kuona. Alipotosheka akaniambia, siku nikitoroka tena ndio mwisho wa maisha ya Eric. Yaani nikitoroka tu, nijue nimemuua Ric. Na akaniambia lazima nijifunze kila kitu nielewe, lasivyo kitakachompata Ric, nisimlaumu. Bella alitulia kidogo huku akilia na kufuta machozi.
“Mzee Masha anafahamika sana kwa ukorofi. Kuua kwake sio shida. Nasikia alishaua mtu pale nyumbani kwake, tena kwa risasi. Nasikia kuwa walipata shida ya bomba linaloingiza maji nyumbani kwao. Akatafutiwa kijana wakwenda kutengeneza. Nasikia huyo kijana akaanza kuzunguka kwenye nyumba ya Masha bila kujua kumbe ile nyumba ina kamera kila mahali. Akafika mpaka chumbani kwa Masha na mkewe akijidai anaangalia kama maji yanatoka mpaka ndani, akaiba vitu vya thamani akavificha mfukoni. Kumbe Masha alikuwa akimfuatilia. Akamfuata mpaka chumbani kwake, akamkuta yule jamaa. Akamuuliza kama amechukua kitu chochote pale ndani, nasikia Jamaa akakataa. Kama unavyojua ukorofi wa Masha, akaanza kumpiga, jamaa wakati anajitetea, Masha akatoa risasi yake akammaliza.” Bella alishtuka sana. “Mungu wangu Elvin! Hakufungwa?” Bella akauliza kwa mshtuko.
“Nani wakumfunga Masha hapa mjini? Kwanza anaakili sana. Tukio zima lilikuwa likirekodiwa kwenye kamera zake. Halafu yeye mwenyewe ndiye aliwapigia simu polisi, pale pale akiwa na maiti chumbani kwake kuwataarifu tukio zima la wizi. Na pesa alizo nazo, na ushahidi huo wa jamaa kuingia chumbani kwake, tena akakutwa na dhahabu alizokuwa amezificha kwenye mifuko yake, kesi iliisha bila tatizo. Tena yeye ndio alionekana mshindi. Masha anajulikana sana hapa mjini. Mpaka wazee wanamwita yeye Mzee kwa pesa yake na ukorofi. Sidhani kama ana kitu anachoogopa hapa duniani. Anaogopewa sana. Na tangia tukio hilo la mauaji, nasikia hakuna mwizi anayekajaga kwake.” Elvin alimmaliza nguvu zote Bella.
 “Sasa hebu endelea, ulifanyaje na huyo mama mwalimu wako?” “Ndio ikabidi kuanza hiyo shule na huyo mama, mpaka aliporidhika huyo mama kuwa nimeelewa ndipo akaondoka. Nikabakia mimi na yeye. Si unajua mkewe hayupo? Basi mimi nimegeuka kuwa kama mkewe. Hataki nifanye kazi yeyote ile, yaani kazi yangu nikumuhudumia yeye tu. Anaweza akakuamulia akufungie mahali, utakesha ukimridhisha yeye, bila kukujali wewe.” Elvin alishangaa kidogo.
 “Anawezaje kufanya mapenzi kwa muda wote huo!?”  “Nilikuja kugundua kuwa huwa anatumia madawa ya kuongeza nguvu za kiume. Kama juzi hapa nilipovimba sura, tukashindwa kwenda kijijini kwenye kaburi la mama, alikuja akachukua chumba palepale hotelini tena pembeni ya chumba chetu, nilikesha naye. Tena nimkatili yule baba, hana huruma hata kidogo. Siku nzima alinifungia pale chumbani nikimridhisha yeye bila kunijali mimi. Ikabidi kumdanganya Ric ili niwe naye yeye tu. Zaidi ya masaa 24, nilikuwa naye. Hakuniachia mpaka dereva alipomgongea kumwambia atachelewa ndege. Na hapo karibu na mwisho alinipiga na bado akaendelea kunitumia, ndio akaondoka bila hata kuomba msamaha.” Elvin alikuwa akishangaa na kumuhurumia sana Bella.
“Siku ile ulipokuja kunitoa kwenye gari nikiwa nimepoteza fahamu, ukanipeleka hospitalini, nikalazwa zaidi ya majuma mawili, ukawa na mimi hospitalini, alinipiga akaniacha hapo sakafuni navuja damu.” “Kwa nini!?” “Nilichelewa kurudi nyumbani nikijua yupo safarini. Ilikuwa hivi, wakati natoka kazini, Joo aliniomba nimsogeze kwake. Sasa mimi sikuwa na wasiwasi nilijua yupo kwa familia yake, nikampeleka Joo mpaka kwenye kituo cha Tazara. Na siku ile mvua ilikuwa inanyesha sana, mpaka kufika nyumbani ilikuwa saa nne na nusu usiku. Jamani Mzee alinipiga yule. Kama anaua nyoka, huku amenishikia bastola kuwa ataniua kabla mimi sijamuua kwa magonjwa. Aliniacha pale sakafuni navuja damu. Nilikaa pale mpaka asubuhi ndipo nikajivuta mpaka nje ya chumba, nikapiga simu getini kumuomba mlinzi aingie ndani anibebe mpaka kwenye gari ili niwahi hospitalini. Haikuwa mara ya kwanza kupigwa lakini ile ya siku ile alinipiga mateke mengi nikajua nimevunjika ndani, nikajiambia nilazima nitibiwe lasivyo nitakufa nimuache Ric peke yake.” Bella alipata pakutolea dukuduku lake.
 “Mara nyingine huwa akinipiga nikijiona hali siyo mbaya sana, najitibu tu palepale nyumbani mpaka napona.” “Mungu wangu Bella! Kwa nini huondoki?” “Nakwenda wapi Elvin? Ameapa kifo peke  yake ndicho kitatutenganisha mimi na yeye. Na amesema, endapo atanihisi tu kama nina mwanaume, ataniua na yeye ajiue. Ameniapia hatakaa aniache tena. Eti ameniambia hawezi tena kuishi bila mimi. Siku aliyoniacha pale sakafuni nikiwa navuja damu, sijitambui, alirudi wakati nipo hospitalini, yeye alijua nimetoroka. Unajua alienda kumchukua Ric shuleni akamfungia mahali? Ndio maana nilipoambiwa Ric amechukuliwa na watu wasiojulikana, ilibidi kukimbia kutoka pale hospitalini kurudi nyumbani huko ninakoishi naye ili amwachie Ric. Na kweli niliporudi tu nyumbani, usiku ule ule alimuachia Ric. Alisema mimi nikiwa ndani na yeye, Ric atakuwa nje. Lasivyo nisije mlaumu kwa lolote litakalompata Ric.” Elvin alibaki ametoa macho huku ameweka mikono kichwani.
“Angalia hizi picha.” Elvin alichukua simu ya Bella nakujiona yeye na Bella. “Nani amekutumia hizi picha?” “Ni yeye mwenyewe. Nafuatiliwa kila niendapo Elvin. Hata hapa tulipo sitashangaa kama kuna mtu na yeye amechukua chumba hapahapa ili kuniangalia ninachofanya. Hata wewe imebidi nikuombee ruhusa, na amekubali kwa kuwa anakuamini sana. Na nilimwambia Ric ndio anakutaka.” “Sasa huogopi tumelala chumba kimoja?” “Sijui Elvin. Wakati mwingine akili inachoka nashindwa kufikiria. Nitajua siku atakayonikabili. Nimejua hawezi kuniua, bado ananihitaji sana. Yupo kama mwehu akiniona. Akili yake inakuwa haifanyi kazi kabisa. Hapa ameniambia nikimrudisha tu Ric shule, natakiwa kurudi nyumbani.” “Sasa kwa nini huishi na Ric kwenye hiyo nyumba?” “Elvin wewe? Kweli mdogo wangu aone uchafu ninao fanyiwa! Ajue kuwa naishi na libaba kama lile! Nitakuwa simsaidii kabisa kimaadili. Hata yeye nimempiga marufuku asithubutu hata kuonana na Ric, akae naye mbali kabisa.” “Kwa nini?” “Mchafu vile! Atamsogelea Ric amwambie nini? Hana kitu chochote chema kinachoweza kumfaa Ric maishani.” “Isipokuwa pesa yake.” Elvin alimalizia nakumuumiza Bella.
“Lakini Elvin, naitolea josho hiyo pesa. Naistahili jamani. Acha tu na mimi niitumie.” “Hapana Bella. Wewe ni wathamani kubwa sana. Hakuna pesa inayoweza kununua utu wako isipokuwa mapenzi ya kweli.” Bella alishangaa sana. Sina thamani Elvin. Mimi nikama jalala lakutupia huzuni na kila aina ya uchafu wa yule baba.” “Hapana Bella. Yeye ndivyo anavyotaka uamini hivyo ili azidi kukukandamiza. Amekufunga kwa mapesa mengi na kukupa mavitu ya thamani huku akikutishia uhai wako na wa Ric ili kukuonyesha hakuna njia ya kutoka kwake, au hakuna maisha mengine zaidi ya hayo anayokupa yeye.” Elvin alirudi kukaa vizuri.
“Kuwa mkweli Bella, ni watoto wa ngapi Wakitanzania umewaona pale kwenye ile shule anayosoma Ric?” “Wachache sana, tena wanahesabika.” “Swali jingine, ile shule inatoa elimu nzuri?” “Sana.” “Sasa kwa nini unafikiri wazazi wengine hawapeleki watoto wao kwenye shule inayotoa elimu nzuri kama ile, tena inayokuza vipaji kwa namna ile?” “Sababu ya gharama.” “Basi ndio ujue Bella, na wewe unaishi maisha ambayo sio yako. Ile ni shule ya watoto wa mabalozi, tena watoto wao wanasomeshwa na serikali zao, pamoja na wafanyabiashara wakubwa sana hapa nchini. Ona gari alilokupa au unalotembelea, hata mkewe haendeshi gari kama hilo. Jitazame mavazi yako na vitu vyako kwa ujumla. Anataka kukupumbaza akili zako kwa vitu vya thamani ili ushindwe kabisa kujitoa huko. Hebu jiulize Bella, ni wasichana wangapi umekutana nao wako kama wewe?” Bella alinyamaza.
“Kila ukitokezea mahali, wewe unaonekana watofauti kwa nje, jinsi ulivyopambwa kwa vitu vya thamani, lakini ujue na ndani pia uko wa tofauti sana na wasichana wenzako. Wanaonekana wakawaida sana, lakini wenzako wanafuraha na amani. Anakuzungusha nchi na sehemu mbalimbali hapa duniani huku anakutishia kifo, au anakupiga karibu ya kukuua, itakusaidia nini? Utakaa hivyo mpaka lini?” “Labda mpaka Ric amalize shule.” “Ndio utafanyaje?” “Sijui Elvin. Maisha ninayoishi sasa hivi ni kwa ajili ya Ric tu. Nimeshakufa nikiwa hai.” Bella alizidi kulia.
“Sio kweli Bella. Hiyo ni kauli ya mtu aliyekubali kushindwa. Nimekuona ukiwa kwenye hali ya kufa, ukaweza kusimama na ukapona. Sijawahi kukutana na msichana jasiri kama wewe Bella. Mungu amekuwekea nguvu ya tofauti sana ndani yako. Hiyo nguvu inayokutoa kwenye kifo na kukurudishia uzima, unaweza kuitumia na ukaishi ukiwa huru.” “Nafanyaje?” “Anza kufanyia kazi fikra zako wewe mwenyewe kwanza. Rudisha thamani ya mwili wako wewe mwenyewe. Haijalishi ni mambo mangapi mabaya anayokufanyia, lakini kila ukiamka, jiambie wewe ni wa thamani, hujafa, uzuri huo wa nje ndio uliopo ndani, na unastahili vitu vizuri zaidi. Ukisharudisha uhai wako wa ndani, kubaliana na maisha jinsi yalivyo. Sasa hivi unaishi maisha ya juu sana, ambayo sio yako. Unalipia hayo maisha uliyopewa na kitu cha thamani sana, utu wako. Ni kama mtu anayekubali kubadilishana, alumasi kwa bati. Utu wako wewe ni alumasi Bella, usiwahi kusahau hilo na usikubali mtu akwambie vinginevyo.” Bella aliinama chini nakuzidi kulia.
“Hujanielewa Elvin, yule baba analala na mimi kama mbwa.” “Nimekuelewa Bella, lakini hayo yote hayapotezi uthamani wako. Hata akufanyie nini, wewe ni wathamani sana Bella. Na kamwe usiishi maisha sababu ya Ric. Utafanyaje kesho ukisikia Ric amelala usiku akaamka amekufa?” “Na mimi nitakufa Elvin.” “Hapana Bella. Lazima ukubali kuwa uhai wa Eric unashikiliwa na Mungu sio Mzee Masha. Hakuna jinsi wewe unaweza kumlinda Ric, ukafanikiwa. Mungu anampenda Ric kuliko hata wewe unavyompenda. Hufikii hata nusu ya upendo wa Mungu kwa Ric. Anamfikiria na kumlinda. Hata kama Mzee Masha akimkamata na kutaka kumuua, kama Mungu hajaruhusu, hawezi kumfanya chochote akafanikiwa. Lazima uweke Imani yako kwa Mungu Bella, sio kwako. Kamwe huwezi kumlinda Ric. Ushafikiria kama ukifa leo Ric atafanyaje?” “Naogopa kufikiria hivyo, Elvin.” “Wala usiogope, kwa kuwa Mungu aliyemleta Ric hapa duniani anajua jinsi ya kumlinda bila wewe, lakini wewe ndio unataka kumpa maisha yasiyo yake.” Bella alikunja uso kidogo nakujifuta machozi. “Kivipi?” “Maisha mnayoishi siyo yenu Bella. Umekubali kuuza utu wako kwa kitu kisicho cha thamani.” “Nifanyaje?” “Anzeni kuishi wewe na Ric, kwa kadiri ya kipata chako.” Bella aliinama akifikiria.
“Pale kazini unalipwa vizuri Bella. Ric anaweza kusoma shule za kingereza za pale pale mjini, zinazolingana na kipato chako. Tafuta nyumba, ukiona huwezi, pangisha hata chumba kimoja kama mnavyoishi pale hotelini na mdogo wako, mwambie Ric ukweli, kwamba maisha yamebadilika, aelewe maisha yakoje, muishi kutokana na kipato chenu. Rudisha mali za watu Bella, ili uwe huru. Utashangaa amani utakayopata ukiwa na kidogo lakini unakifanyia kazi halali.” “Mzee Masha ataniua.” “Hawezi kama ukianza kumuonyesha unajithamini. Anza taratibu. Sikwambii sasa hivi unatakiwa kwenda kumtoa Ric shule, hapana. Kwa kuwa umeshamlipia ada ya mwaka mzima, mwache amalizie. Mzee Masha akikupa ada nyingine, mwambie hapana, nataka kumsomesha mdogo wangu mimi mwenyewe. Mrudishie kadi zake za benki, acha kumuomba pesa. Ishi kutokana na mshahara wako. Taratibu utaona na yeye anakuheshimu. Ni ngumu, lakini najua utaweza.”
“Wala sio ngumu Elvin. Ni kwa kuwa sikuwa nimepata hilo wazo. Mimi na Ric, tunajua kulala njaa. Haitamsumbua Ric kuona anarudi kusoma Dar, kwanza atafurahi kuwa karibu na mimi. Mimi ndio nilimlazimisha akasome bweni.” “Ndio maana nakwambia Bella, sijawahi kukutana na mtu kama wewe. Ni vile shida zilikuziba macho ukashindwa kujiona. Muonyeshe unajitambua, utaona hata yeye atakuheshimu. Usikubali akupige halafu na wewe umekaa tu unalia. Atakuua kweli! Muonyeshe unajithamini na hufurahii anayokufanyia na lazima aache.”
 “Nimekuelewa Elvin. Na ninakushukuru sana. Najiona ni kama nimetua mzigo mzito sana. Ningejua ningekushirikisha mapema.” “Hujachelewa Bella. Naamini huu ni muda mwafaka. Kama nilivyokwambia, usiache kuomba. Inawezekana nikawa nimekwambia kwa sehemu tu, lakini ukiomba msaada wa Mungu atakusaidia zaidi.” “Tunaweza kuomba tena na leo?” “Leo itakuwa zamu yako Bella.” “Lakini sijui jinsi ya kuomba.” “Hakuna kanuni. Wewe fanya kama nilivyofanya jana, kisha mwambie Mungu kile ambacho unataka akusaidie.” Bella na Elvin walishikana mikono wakaanza kuomba pamoja. Lakini Bella alikuwa akilia sana, akijiona vile allivyomchafu mbele za Mungu, Elvin alimsaidia, wakaomba mpaka wakamaliza.
“Nataka kulala Elvin.” “Nisubiri na mimi nikaoge tuje tulale kwa pamoja.” Elvin alitoka bafuni, Bella alikuwa ameshahamia kwenye kitanda chake. Alimfunika vizuri, na kubaki akimtizama. Bella akatabasamu. “Asante Elvin.” Elvin alitabasamu huku akimtizama Bella aliyekuwa amejiegemeza kichwa kwenye mto, na amemfunika kwa mablangeti. “Nikwambie kitu Bella?” Bella alicheka kidogo. “Kitu gani hicho kinachokufanya wewe mwenyewe ucheke?” “Wewe ni mzuri sana, ndio maana Mzee wa watu anachanganyikiwa.” “Elvin wewe!” Bella alimpiga kofi kidogo. “Kweli tena. Wewe ni mzuri wa kila kitu, hata moyo wako ni mzuri sana. Una upendo. Hata Joo anakusifia sana.” “Asante Elvin.” Bella alicheka kwa aibu, lakini Elvin aliona dimpozi zake, akazishika. “Ukicheka hivi ndio unapendeza zaidi, kuliko ukianza kununa.” “Basi kuanzia sasa hivi nitakuwa nacheka.” Elvin alikuwa amekaa pembeni ya kitanda cha Bella wakiongea. Alijaribu kumtania kidogo, Bella alikuwa akicheka sana.
“Nimefurahi umeweza kujua ukweli juu yangu Elvin, na bado umeuona uthamani wangu. Niliogopa sana kukwambia, nilijua ukijua uchafu wangu utanikimbia.” “Hapana Bella. Umezidi kunifanya nitake kuwa na wewe karibu zaidi, nimeona umeniamini kuniambia ukweli wote.” “Kwa hiyo utazidi kuwa karibu na mimi? Yaani namaanisha karibu na sisi.” Bella alijishtukia, Elvin akacheka. “Nitakuwa na wewe Bella. Usiogope. Najua umekubali kuanza safari yenye changamoto, nitakuwepo karibu kukushika mkono ili usianguke peke yako.” Bella alifurahi sana. Machozi ya furaha yalianza kuchirizika pembeni ya macho yake. “Nakushuru Elvin.” Elvin alimfuta taratibu huku akitabasamu. “Nimekwambia ukianza kuweka sura ya majonzi, unatisha.” Bella akacheka. Waliendelea kuongea, mwishowe waliagana, Elvin alirudi kulala kitandani kwake. Waliendelea kuongea mambo mawili matatu, mpaka Elvin alipomuona Bella anasinzia. Akazima taa wakalala.
**********************************
Ni kweli hakuna uhuru ulio sahihi kama uhuru wa fikra. Bella alifungua macho yake asubuhi hiyo akiwa kitandani mwake, akaanza kuhisi kitu cha tofauti na siku nyingine kila alipokuwa akiamka. Alihisi mwili wake unaelea angani, furaha ilijaa moyoni mwake, tabasamu kubwa lilipamba uso wake. Alibaki akifikiria ni nini kimemtokea. ‘Nini kimebadilika?’ Bella akajiuliza. Alijaribu kujipigapiga kujua kama yupo usingizini, akasikia maumivu kidogo akacheka. Wazo lilimjia yupo chumba kimoja na Elvin. Aligeuka kwa haraka kuhakiki mawazo yake, alimuona Elvin yupo kitanda cha pembeni yake akiwa amelala. Bella akacheka. ‘Nipo huru.’ Bella alijiambia. ‘Sina cha kuficha tena mbele ya Elvin, anajua uchafu wangu wote na amebaki kuwa rafiki yangu.’ Bella aliwaza. Alikumbuka maombi aliyoomba usiku uliopita na Elvin. ‘Hata Mungu amenisamehe. Lakini nitaendelea kuishi na Mzee Masha!’ Bella alijisuta moyoni. ‘Elvin amesema nimuachie Mungu.’ Bella aligeuka akalala kifudifudi na kujaribu kumuomba Mungu akiwa peke yake bila msaada wa Elvin.
“Mungu! Elvin amesema utanisikiliza na umenisamehe. Nimeamini kutokana na furaha niliyonayo sasa. Najua nimekosea kukubali kulala na Mzee Masha. Natamani kubadilisha maisha yangu, lakini sijui kitu chakufanya. Elvin amesema wewe unaweza kunisaidia. Naomba unisaidie, na umlinde Ric. Asante kwa ajili ya rafiki mpya uliyenipa, Elvin. Msaidie na yeye ili Mzee Masha asimdhuru. Mmmmmm! Bella alifikiria tena kidogo. Sijui niseme nini tena… ooh Mungu, tusaidie mimi na Ric tupate nyumba nzuri, na sisi kwa mara nyingine tena tuwe na kwetu. Amina.”
Bella alimaliza kuomba, akashangaa jinsi ilivyokuwa rahisi. Akatamani arudie tena, lakini akakumbuka Elvin alimwambia Mungu hana tatizo la kusikia wala kuona. ‘Atakuwa amenisikia.’ Bella alijiambia. Nikikumbuka tena kitu kingine nitamwambia tena Mungu.’ Bella alitabasamu. Elvin bado alikuwa amelala.
Akatoka kitandani kwake akinyata. Kilikuwa ni kipindi cha baridi sana katika jiji hilo la Arusha. Bella alivaa soksi zake harakaharaka akanyata mpaka bafuni. Akachukua kitaulo kidogo cha kujisugulia mwili akakilowesha maji ya baridi huku akicheka kimyakimya, alipohakikisha ni chabaridi sana, akarudi akinyata kurudi chumbani. Alisogea taratibu mpaka kitandani kwa Elvin, akamfunua shuka taratibu, kwa tahadhari kubwa, akamuwekea kile kitambaa cha baridi, pembeni ya mgongo wake, kisha akakimbilia chini ya uvungu, huku akicheka akiwa amefunga mdomo. Alimsikia Elvin akiruka pale kitandani, akaona kile kitaulo kimetupwa chini.
“Bella!” Alimsikia Elvin akiita kwa sauti. “Nikikukamata, utaoga maji ya baridi leo.” Alibaki akicheka pale chini ya uvungu wa kitanda huku amejifunga mdomo wake ili Elvin asijue alipo. Aliona miguu ya Elvin akielekea bafuni kumtafuta baada ya kumkosa pale kitandani, na kutupa mablangeti yote chini. “Heri uendelee kujificha Bella. Naenda kukujazia maji kwenye sinki la kuogea, tena maji ya baridi matupu. Nitakuloweka leo, ukae huko siku nzima.” Bella aliendelea kucheka taratibu. Alipomkosa bafuni, alitoka akasimama katikati ya chumba akifikiria, Bella aliendelea kucheka.
Kama aliyepata wazo, Elvin aliinama moja kwa moja chini ya uvungu wa kitanda chake. “Nimekukamata, sijakukamata?” Bella alicheka kwa nguvu sana. Elvin alimvuta miguu yake kumtoa uvunguni. Bella alikuwa akicheka sana. Alimzidi mahesabu Elvin, akaweza kumkimbia. Walizungushana kwenye hicho chumba wakikimbizana, mara wapande juu ya vitanda, mara juu ya makochi, huku Bella akicheka sana. “Nitakukamata tu Bella.” “Nisikilize kwanza Elvin, mimi nia yangu ilikuwa nzuri, kutaka kukuamsha tuwahi uwanja wa ndege, tusiachwe na ndege.” “Hapana Bella, ungeniamsha kwa kuniita tu.” “Usingenisikia Elvin. Maji baridi pekee ndiyo yamekusaidia kumka. Tena badala ya kutafuta kunilipizia, ulitakiwa unishukuru.” “Nimepata wazo.” Elvin alirudi bafuni akachukua kikombe cha karatasi kilichokuwa kimetengwa maalumu kwa ajili ya kupigia mswaki, akachota maji ya baridi kutoka kwenye sinki akaenda kumnwagia Bella. “Sikubali Elvin. Kwa nini unimwagie maji badala ya kile kitaulo?” Bella alikimbia bafuni ili kuwahi kikombe kingine achote maji, lakini Elvin alimuwahi akaingia na kuchukua vikombe vyote akanyanyua mikono juu. “Najua wewe nimrefu siwezi kukufikia. Lakini kumbuka Mungu amenipa mikono.” Bella alianza kumwagia Elvin maji ya baridi na mikono yake, huku Elvin na yeye akimwagia. Walikuwa wakicheka sana mpaka machozi. “Ujue Bella wewe unaakili za kitoto sana!” “Hata wewe Elvin. Kwa nini umelipiza wakati nia yangu ilikuwa nzuri? Ona tulivyojaza maji hapa bafuni.” “Ona unavyotetemeka.” “Hata wewe unatetemeka.” “Kosa ni lako Elvin.” “Twende tukajifunike blangeti tupate joto.” Bella alikimbia mpaka kitandani kwa Elvin akachukua blangeti la Elvin akachanganya na lake akaenda kitandani kwake akajifunika.
“Muone! Sababu ya uchokozi, umeshindwa hata kufikiria, umepanda kitandani na nguo mbichi.” “AAAAAaaaaah!” Bella alilalamika Elvin alibaki kucheka. Alijifungia chooni, Elvin akaoga haraka haraka akabadili nguo akiwa hukohuko bafuni. “Fanya haraka Elvin, nakufa na baridi huku.” “Uliyataka mwenyewe, uvumilie mpaka nimalize.” Bella alikuwa akicheka tu. Wote walipooga na kuvaa nguo kavu, walirudi kitandani na kusahahu kama wanatakiwa kuwahi uwanja wa ndege.
“Niambie Elvin, nafikiria namba gani?” Bella alimtaka Elvin afikirie, mara tu baada yakupanda kitandani kwake alipokuwepo amejifunika Elvin. “Mmmmmmhhhhh!” Elvin alianza kufikiria mwishowe akasema, “Mbili.” Bella alishtuka sana. “Elvin wewe! Umejuaje?” “Nimefikiria akili zako zinawaza nini, nikakumbuka ni Ric tu. Kwa hiyo ndio mtu wa pili unayemfikiria, mbali na wewe baada ya kuipata nafsi yako.” “Umejuaje kama nimepata nafsi yangu?” Bella aliuliza huku akicheka sana. “Sijawahi kukuona ukiwa na furaha hiyo tokea nakufahamu Bella. Ulipokuja ofisini kwa mara ya kwanza, nilikuona ni dada wa hali ya juu sana. Lakini kadiri nilipokuwa nikikaa na wewe, ndivyo jinsi nilivyokugundua kwanza wewe bado ni mtoto sana, na japokuwa unaonekana una kila kitu, akili nzuri, mavazi mazuri, gari la kifahari, kila kitu chako kwa nje hakikuwahi kuwa na kasoro, hata pale kazini walijaribu kukuharibia sana, lakini kila kitu chako hakikuwa na kasoro, lakini kila nilipokuwa nikikuangalia, niliona jinsi ndani ulivyokuwa umepotea. Ndio maana tokea mwanzo nilitaka kukudadisi mambo kadhaa ili nijue nini kinakusibu, lakini ulifanikiwa kufunga milango yote, mtu yeyote asifahamu kinachoendelea moyoni mwako.” “Nilikuwa naogopa Elvin. Niliogopa nikikwambia au nikiwa karibu na wewe, Mzee Masha angekudhuru au nilijua ungenielewa vibaya sana kujua ninamahusiano na mume wa mtu, tena Mzee anayeweza kunizaa.” Elvin akacheka.
 “Sasa hofu imeisha?” “Wewe ndio umeondoa hofu yangu baada ya kukuona bado unanithamini wakati unajua maisha machafu ninayoishi. Halafu hofu kwa Mzee Masha ndio imeisha kabisaa. Simuogopi tena.” “Akirudi akasema atakuua.” “Acha aniue Elvin. Unakumbuka wakati tupo mapumzikoni katika wishing zangu, nilisema natamani niwe mtoto tena? Nimekuja kuamini leo asubuhi, hakuna atakayeweza kukamilisha hiyo shauku yangu isipokuwa mimi mwenyewe. Leo asubuhi nimeamka kama Enabella, sio Bella mwanamke wa Mzee Masha. Nimejisikia nipo huru. Nimepata muda mzuri na wewe. Sihitaji kujiweka kifungoni Elvin. Nimeamua kuishi siku moja moja. Kuanzia leo asubuhi, kesho zangu zote nimemuachia Mungu.” “Uliomba tena?” Bella alicheka. “Ndiyo. Niliamka nikamwambia Mungu kila kitu. Najisikia uhuru wa ajabu Elvin. Najisikia furaha ambayo sijawahi kuisikia kabla.” Elvin alicheka.
“Safi sana. Ndio maana nakwambia wewe ni jasiri Bella. Wakati wote una uwezo mkubwa sana wakujifufua wewe mwenyewe. Na hiyo ni nguvu aliyokupa Mungu. Wengine wangehitaji muda mrefu sana kuwatoa kwenye hiyo hali yako, lakini ona wewe ilivyokuchukua muda mfupi! Sasa unajua nini Bella?” “Nini?” “Hicho ni kitu Mungu ameweka ndani yako, ili pia uwe msaada kwa wengine.” “Elvin wewe!?” “Kweli Bella. Hicho ni kitu cha tofauti sana ulichonacho Bella. Watu wengi wanaishi wakionekana hai usoni lakini wapo kwenye vifungo vikali sana. Jipe tu muda, utakuja kuona.” “Nani atakubali kufarijiwa na mtu kama mimi? Kwanza watu wakija kujua ukweli, watanihesabu kama mwizi wa mume wa watu. Hawawezi kunisikiliza hata kidogo.” “Kila mtu ana maisha aliyoishi huko nyuma Bella. ‘Every one has past history’. Nyingine za kutisha, na wengine kama sisi tulibahatika tukalelewa na wazazi wacha Mungu, tukabahatisha kukua katika mazingira fulani yaliyotuepusha na hatari. Halafu kuna watu kama nyinyi Mungu aliwaumba na mioyo ya tofauti, akakubali kuwapitisha kwenye mapito fulani, magumu sana, ambayo ni wewe peke yako Bella ndiye umeweza kuyamudu, hakuna mwanadamu mwingine anaweza kuishi kwenye maisha kama yako, isipokuwa wewe Bella. Wengi wangeshakufa, lakini jiangalie wewe jinsi ulivyo mpaka leo unaendelea, na umeweza kuamka asubuhi na kuweka furaha moyoni kwangu.” Bella alikuwa akilia.
 “Wewe huhitaji furaha kutoka kwangu Elvin. Maisha yako yanaeleweka.” Elvin alicheka na kufikiria kidogo. “Sio kweli Bella. Napitia kwenye kipindi kigumu sana. Unakumbuka nilikuja hotelini ukaniuliza ni nini kinanisumbua, kisha ukaniambia nilale?” Bella alivuta kumbukumbu. “Nimekumbuka. Halafu hukuniambia.” “Basi ulinisaidia sana pale uliponiambia nilale. Usiku uliopita sikuwa nimelala hata kidogo kwa mawazo.” “Nini tatizo?” “Ni mkusanyiko wa mambo  mengi Bella. Nilikesha nikiwaza jinsi nilivyosalitiwa na watu ambao niliwahesabu marafiki ambao ni kama ndugu, nilijiona vile nilivyokuwa mjinga na kipofu kutokuona mambo ambayo hata Mungu mwenyewe alionionyesha mbele ya macho yangu lakini sikutaka kuona. Nilijichukia sana kwa maamuzi mengine ambayo nilichukua kwenye maisha bila hata kumuomba Mungu. Wakati maisha yangu yote nimekuwa nikiwa mtu wa kumuomba Mungu katika kila kitu. Lakini kunajambo nililifanya, bila hata kumshirikisha Mungu, nimefanya kama nilivyoona waliotangulia wakifanya, yaani kama desturi yetu, na mimi nikajiingiza humo, limenigeuka vibaya sana. Limenichafulia jina langu, mbaya zaidi limechafua akili zangu. Hivi kuwa hapa na nyinyi, angalau kumenisaidia sana.” “Pole Vin. Sasa, unaweza kubadilisha?” Bella alimuuliza kwa kumuhurumia.
 “Kubomoa ni kazi rahisi sana Bella, lakini kujenga inachukua muda mrefu. Sizungumzii kujenga jina langu tena, hiyo hainisumbui hata kidogo, nafikiria kujijenga mimi mwenyewe na mahusiano niliyodhani ni imara kumbe ni mabovu sana. Nimejua ukweli, nafikiria sasa na simama wapi bila kuharibu mahusiano ambayo yamejengwa na wazazi wetu! Sijui Bella. Lakini nipo kwenye wakati mgumu sana na hapa wazee wanasubiri jibu langu. Ninatakiwa kutoa maamuzi yangu haraka sana ili kupunguza machafuko yanayo endelea. Kikao cha wazee kinafanyika mara moja kwa mwezi, na baba ameniambia kikao hicho kikifanyika wazee wametaka kuniona ili kusikia maamuzi yangu. Kwa hiyo uniombee Bella. Nikipindi kigumu sana, sikuwahi kufikiria naweza kufika hapa.” Bella alijilaza pembeni ya Elvin. “Pole Elvin. Najua Mungu atakusaidia.” Elvin alimfunika shuka na blangeti Bella. Wote wakapitiwa tena na usingizi wakiwa wamelala kitandani kwa Bella.
Bella alishtuka akiwa amejificha kwenye mbavu za Elvin. Baridi ilikuwa kali. Akavuta simu yake kuangalia muda. “Elvin! Elvin!” Elvin alifungua macho. “Tumechelewa ndege.” “Oooh noo. Tumepitiwa na usingizi.” Elvin alijibu huku akijitoa kwa shida ndani ya yale mablangeti. “Mwenzako natakiwa kazini kesho. Twende tukaangalie kama tunaweza kupata ndege nyingine.” Walivaa harakaharaka na kuwahi uwanja wa ndege.
Hawakupata ndege nyingine na walikataliwa kurudishiwa pesa, kwa kuwa kosa lilikuwa ni la kwao. Bella alianza kucheka. “Unacheka nini sasa? Ujue pesa ndio imekwenda hivyo!” “Tukaangalie kama tunaweza kupata basi lakutufikisha Dar.” “Sasa hivi?” “Ndiyo Elvin. Wewe mwenzangu uko likizo, mimi natakiwa kazini kesho. Unataka Mzee Mwasha anifukuze kazi?” “Nitakuombea ruhusa. Acha tuondoke na ndege ya kesho.” “Hapana Elvin. Nimekosa kazini kwa muda mrefu sana. Lazima kesho niwepo kazini.” “Basi tufanye hivi, mpigie Mzee Mwasha simu, mwambie kesho utachelewa kazini. Tuondoke na ndege ya kwanza kesho asubuhi, na kwa kuwa umeacha gari yako uwanja wa ndege wa Dar, tukitua tu, tunaenda moja kwa moja ofisini. Nitakusaidia kazi zako zote.” “Kweli Elvin? Sio tunafika pale unaanza kutoa udhuru.” “Lini nimewahi kukuahidi kitu halafu sijafanya?” Bella alicheka huku akifikiria. “Kweli hujawahi.” “Haya, tuulize tiketi ya kesho.”
Elvin alimgeukia muhudumu waliyemkuta pale. “Tunaomba tiketi ya ndege ya kwanza kabisa ya kesho asubuhi.” “Ngoja niangalie kama mtapata nafasi.” Muhudumu alijibu. “Mimi nitalipia.” Bella alinong’ona. “Umesahau Bella.” “Nini tena?” Elvin akamwangalia. “Kuishi kutokana na kipato chako. Mshahara wako hautoshi kupanda ndege na kumtunza Ric.” Bella alipooza gafla. “Umeamua jambo zuri Bella. Usirudi nyuma. Anza kuishi maisha yako sasa. Mimi napata mshahara mkubwa kuliko wewe, na sina majukumu mengi kama wewe. Acha nilipie mimi.” “Asante Elvin.” Walipata tiketi zao wakarudi hotelini.
“Kwa hiyo Elvin, unashauri nisitumie tena hizi kadi za Mzee Masha? Zina pesa nyingi sana.” Bella aliuliza kwa upole mara walipoingia chumbani kwao na kukaa kwenye kochi. “Uamuzi ni wako Bella. Lakini lazima ukubali kujitunza wewe mwenyewe kwa kipato chako. Tokea ulipoamua kubadili maisha yako, inamaana ukubali kurudi kwenye uhalisia wa mambo. Wewe huna uwezo wa maisha hayo anayokudanganyia Mzee Masha. Na akiona umejitambua na ukaheshimu maamuzi yako na kuyasimamia, hata iweje na yeye ataanza kukuheshimu. Sasa hivi hawezi kukuheshimu kwa kuwa kila akikuangalia anaona pesa yake tu, hakuoni wewe kama Enabella. Lazima afike mahali aweze kutofautisha pesa yake na utu wako.” Bella alijiegemeza kwa Elvin taratibu. “Nimekuelewa Elvin.” Bella alitulia. “Najua ni ngumu kwa kuwa ameshakuzoeza vibaya, lakini Bella, utaweza tu.” Bella alibaki kimya. Walikaa pale kila mtu akiwaza lake. “Nasikia njaa Elvin.” “Twende tukatafute chakula.”

 “Elvin na Bella warudi Dar wakiwa wenye furaha.”
Bella na Elvin waliweka historia ya namna yake wakati wapo jijini Arusha. Kila walipokuwa wakitizamana walicheka. Walipata muda mzuri sana wa pamoja. Ni kama Bella alifungua ukurasa mpya wa maisha, na Elvin ni kama alifanikiwa kumrudisha Enabella wa zamani, tena mwenye vitu vingi sana ndani yake. Lakini alijawa na utoto wakupita kiasi. Kila Elvin alipokuwa akimsikiliza, alishindwa kuamini kama ni Bella yule yule. Alikuwa mcheshi sana, na alimfanya Elvin acheke kila wakati kwa vituko. Alikuwa na michezo midogo midogo yenye mitego ndani yake, aliyokuwa akikusudia kumkamata Elvin. Kama siyo swali la mahesabu basi alimpa kitendawili chakumfanya Elvin afikirie majibu kwa makini sana. Alimwambia anatoa maswali yake mtandaoni.
Walitua jijini bado ilikuwa mapema sana. “Unataka nikurudishe kwanza nyumbani kabla sijaenda ofisini?” Bella aliuliza wakati wanashuka kwenye ndege. “Twende wote tu ofisini. Naona likizo imeisha, nishapumzika vyakutosha, na mimi nipo tayari kuanza kazi.” Bella alifurahi sana. Waliongozana mpaka ofisini.
Wakati wanaingia tu, walimkuta Mama Mwasha, Mzee Mwasha na Irene pale mapokezi. Bella na Elvin walishtuka, kwani waliingia wakiwa wanacheka sana huku wakifuta machozi. Bella ndio alijisahau kwa kucheka, maana alikuwa akimcheka Elvin kwa sauti ya juu, tena huku akilitaja jina lake. Walisimama gafla, vicheko vikakoma, watu wote walio wakuta pale ndani, walibaki wakiwatizama wao, maana waliingia wakiwa wanapiga kelele za vicheko. Tangia wakiwa nje, Bella na Elvin walikuwa wakikimbizana kuwahi nani atafungua mlango wa kwanza. Wakabaki wakitizamana. Ilikuwa bado asubuhi, Elvin hakuwa amelala nyumbani kwao na ndio anaingi na Bella wakiwa wanafuraha sana asubuhi hiyo.
**********************************

Haya… nini kitaendelea?
Usikose Sehemu ya 9

0 comments: