Story

is mine - ni wangu Part 1 {Sehemu 1 - 12}

Wednesday, January 02, 2019 naomimwakanyamale 0 Comments



H

akujua kama ni laana au mkosi unaomwandama katika maisha yake. Kila akijiangalia“Sasa kasoro yangu mimi ni nini?” Niswali lililokuwa likimuumiza sana Nanaa, binti aliyekulia kwenye nyumba ya dada wa mama yake, tokea anazaliwa mpaka anakua. hakuona tofauti kubwa aliyonayo na wasichana wengi wanao tamkwa ni warembo. Alijua kwa hakika wakiitwa wasichana wazuri, na yeye akakisimama, hawezi akaambiwa akae. Hata umbile halikuwa na tofauti sana na maumbile ya wasichana wengine wanaofanya wanaume washindwe kujizuia kuwasindikiza kwa macho. Hata ngozi yake ya mwili, si wanaume tu walioisifia kuwa ana rangi nzuri, tena moja mwili mzima, bali hata wasichana wenzake walitaka kujua ni nini anatumia kinachomfanya kuwa na rangi nzuri kiasi hicho.



*****************************************************



Mama yake Nanaa, Wini, alishika mimba akiwa mwanafunzi wa sekondari ya shule ya wasichana Weru Weru. Wini akiwa binti mdogo wa kidato cha tatu tu, ndipo alipotimiza kusudi zima la kuletwa Nanaa duniani. Ugumu ulikuja kwa Wini, asijue tumbo hilo analipeleka wapi kwa kuwa alikuwa akilelewa na mama ambaye alishawapa msimamo wake tokea wanakuwa. Alishajiwekea misingi na kanuni ambazo aliwahakikishia hazitawahi kuvunjika. Mojawapo ni kutoleta nyumbani kwake mtoto nje ya ndoa, zaidi mtoto huyo akiwa hana majibu yakutosheleza. Kama baba yake.



Haikuwa bure. Mama yake Wini na Maria ambaye ndio dada mkubwa, alishakuwa gumzo pale kijijini. Hakutaka watoto hao watimize kile watu wanachosema juu ya uzazi wake. Baada ya kashfa nyingi akichekwa hapo kijijini, Kirua Vunjo, hapo hapo Moshi. Ilimbidi mama huyo kuangukia kanisani. Alishika dini bila kupenda. Kanisani ikawa ndio kimbilio pekee. Masista na mapadri, wakageuka kuwa rafiki zake hapo kijijini baada ya kuachwa na mumewe.



Nyumbani kwa Ulimali, yaani baba yake Wini na Maria, na mkewe huyo mkubwa, ilikuwa huzuni kila mwaka. Kama sio mimba ya mama huyo kuharibika. Basi mtoto aliyebahatika kuzaliwa, atakaa siku chache tu, kabla ya kutimiza hata mwezi, tena mara zote wanakuwa watoto wakike, hufariki bila hata ugonjwa. Maria ambaye ni dada yake Wini, mama yake mkubwa Nanaa, ndiye alizaliwa wa kwanza. Hapakuwa na shida. Mara tu baada ya mama huyo kuolewa, akampata Maria. Mzee Ulimali akajipa moyo akijua mtoto atakayefuata, atakuwa wa kiume kama alivyotarajia. Miaka ikazidi kwenda. Vifo vya watoto wa kike vikaongozana, mpaka Mzee huyo akakata tamaa.



Alitafuta mke mwingine. Hakutaka kwenda mbali sana. Alioa hapo hapo kwenye kijiji cha Kirua Vunjo. Lakini safari hii alipata mke upande wa kaskazini, na kumuacha mkewe mkubwa upande wa kusini. Alibahatika kuoa binti mdogo tu. Mkewe huyo wa pili akaanza kwa kuzaa watoto wa kiume mapacha, jambo lililomfurahisha huyo mzee, nakuamua kuachana kabisa na mkewe wa kwanza, ambaye alikuwa na uzazi wa shida, tena wa watoto wakike watupu ambao Mzee Ulimali hakuwataka. Aliwaita hasara.



Wakati Mzee Ulimali anaondoka rasmi kwa mkewe, alimuacha akiwa mjamzito. Mkewe hakutaka kumwambia kwa kuhofia historia kujirudia. Asije akamwambia ni mjamzito, baada ya siku chache mimba ikaharibika, au akaja kuzaa mtoto mwingine wa kike, tena asikae muda mrefu, akafa. Akaamua anyamze na ujauzito wake. Akaachwa na mtoto mmoja tu wa kike, Maria. Ndipo baada ya miezi tisa kutimia, hatimaye ndipo akazaliwa mama Nanaa, yaani Wini, ambaye naye alibahatika kifo cha utotoni. Wini mwenyewe alipatikanika au alizaliwa wakati baba yake alishakimbia nyumba hiyo, aliyosema ina mkosi.



Mama huyo alizalia hospitali ya serikali ya hapo hapo Kirua Vunjo kusini. Akasaidiwa kulea watoto wake hao wawili wa kike na kanisa katoliki la Uchira, yeye kama mwajiriwa wa kanisani hapo. Kanisani kukawa ndio kimbilio pekee kwa mama huyo. Kusali na kwenda kwenye misa, kwao haikuwa ni swali. Ratiba za kanisani zilijulikana nyumbani humo kama wanavyojua majina yao. Kuanzia jumatatu mpaka jumatatu. Asubuhi mpaka jioni. Kipindi cha kwa resma, kufunga halikuwa ni jambo la mjadala. Kulipikwa chakula cha usiku tu wakati wakufungua.



Dini na maadili yake ndio ulikuwa wimbo ndani ya ile nyumba. Mama huyo alisisitiza kufuatwa bila kukwepa au kukosea. Watoto wake wote walishapitia mafunzo ya komunyo ya kwanza na kipaimara na wakafuzu. Waliijua katekisimu ukurasa kwa kurasa. Walijua Sala za kuombea mambo mbali mbali na mtakatifu nani anasaidia nini ili wamuombe, halafu huyo mtakatifu awaombee kwa Mungu. Kama ni safari, basi walijua wazi, mtakatifu Christopher ndiye mtakatifu sahihi wa kuwa naye safarini. Ikija kwenye kusali rozari, hapo hawakuhitaji hata kufikiria. Walijua wapo kifungu gani, wamtaje nani au watamke nini, bila shida yeyote na bila kukosea. Kwa kuwa sala ilikuwa sehemu ya maisha yao.



Akitaka kusisitizia jamii kuwa yeye hatetereki kwa kuachwa na mumewe sababu ya kuzaa watoto wakike watupu, ambao ni Maria, na Mama yake Nanaa, ambaye ndio Wini, mama huyo wakichaga, alipapambana kufa na kupona kulea binti zake kimaadili na kusomesha. Alimpa mtoto huyo jina la Wini baada ya kufanikiwa kushinda kifo, na kuzaa akiwa na umri wa utu uzima. Sista aliyekuwa akimsaidia kipindi alipojifungua mtoto huyo, ambaye walikuwa marafiki, alimshauri ampe jina hilo la Wini. Kwani alishakaa muda mrefu sana bila kushika mimba baada ya kuzika watoto wengi, wakati Maria mtoto wake wa kwanza akiwa ameshakuwa binti mkubwa tu. Kumpata mama yake Nanaa, aliyefanikiwa mpaka kutoka naye hospitalini akiwa hai, ulikuwa ushindi mkubwa sana kwake. Hata aibu ya kuwa ni mtoto wa kike, iliisha. Baada ya kutoka naye, akarudi naye nyumbani. Mwezi ukapita mtoto huyo akiwa bado hai, ndipo alipombatiza jina la Wini. Lakini akiwa hana mume tena, na anajulikaana anamkosi.



Watu walisubiri kifo cha Wini, lakini wakashangaa akikuwa mpaka akafaulu vizuri sana kwenda shule ya wasichana Weru Weru sekondari. Mtoto huyo alijulikana pale kijijini kama anaakili sana. Aliwaendesha wakaka aliokuwa nao darasani, kitu kilichofuta machozi ya mama yake.



Mama huyo alifanya kila aliwezalo kutunza binti hao waliokuwa na tofauti kubwa sana ki umri. Hakuwa masikini wala tajiri. Alifanikiwa kuwapa wanae maisha ya kawaida tu. Dada mkubwa alibahatika kupata mume akiwa binti mdogo baada ya kuhitimu chuo chake cha ualimu, akaolewa kwa heshima kubwa sana pale kijijini, wakati bado mama yake Nanaa, Wini yupo shuleni.



************************************************



Mara baada ya Wini kushika mimba, hapakuwa na mjadala. Mama yake alimfukuza nyumbani kimya kimya, kuepusha aibu. Hatimae yale yaliyokuwa yamezungumzwa na baba yao na watu wengine yakatimia. ‘watoto wa kike ni bure kabisa. Wanaishia kuzaa nyumbani tu!’ Ndio usemi huo aliokuwa akiusema baba yao mpaka kuondoka kwake. Akiwa anaficha aibu hiyo, mama yake alimtoa yule binti bila kutaka kujua anakwenda wapi na huku akimuonya asije wahi kurudi tena pale kijijini bila ya ndoa au na huyo aliyempa mimba. “Ukirudi hapa uwe na baba wa huyo mtoto, tena akiwa anakuja kulipa mahari. Akuoe.” Ndivyo alivyoagwa Wini nyumbani kwao.



Wini alitoka kijijini kwao na kuhamia mjini akiwa bado binti mdogo, asiyejua maisha. Akajitupa jijini Moshi akijaribu kupambana na maisha bila mafanikio. Alitoka kwao akidhania angeweza kuishi peke yake, lakini akagundua maisha si rahisi kama alivyodhani. Aliona vile mama yake akihangaika na kazi za shamba na hapo kanisani ambako aliajiriwa, akajua ingekuwa rahisi kwake.



Wakati anakua, alimuona wakati mwingine mama yake akibeba parachichi na ndizi kwenda kuuza kwenye uzio wa kanisani na mashuleni. Kwa pesa chache alizokuwa ametoka nazo nyumbani, na yeye akaiga. Hakuhitaji mtaji mkubwa kununua sinia na parachichi. Akaanza huku akijiwekea mikakati kama alivyomuona mama yake akifanya wakati anamlea yeye na dada yake kabla ya kuolewa. Ndivyo alivyojua na yeye atapambana mpaka mtoto wake akue.



Mambo hayakuwa marahisi hivyo. Alianza kutanga tanga jijini Moshi, akitafuta pakuishi bila mafanikio. Kufunga na kufungua akajikuta ni omba omba mkamilifu, asijue chakufanya mtaani. Jua mvua vyote vilikuwa vyake. Hakuna aliyekuwa akimuona yeye kama yeye. Cha kwanza walilitambua tumbo. Binti mdogo, mrembo, mjamzito.



Kwake siku hazikuwa zikikimbia kama alivyokuwa akisikia kwa watu wengine wakilalamika. Aliweza kuhesabu sekunde, dakika, saa, siku, juma, mwezi akiwa hana tumaini. Maisha yale duni aliyokuwa akiona wanaishi nyumbani kwao na kutamani maisha ya wengine, gafla akageuka kuyatamani sana. Alikuwa akilia nakutamani arudishe siku nyuma ili awepo nyumbani kwao. Hata nyumba ya mama yao akaanza kuona ilikuwa jumba la kifahari, akatamani arudi, lakini alikumbuka jinsi alivyotolewa kwa siri pale kijijini.



************************************************



Ilikuwa ni alfajiri sana. Mama yake alimpandisha kwenye gari ya kwanza iliyokuwa inapita pale kijijini kwao, ili hata mtu asimuone baada ya usiku uliopita kupata uhakika Wini ni mjamzito. Hakutaka kujua aliyempa mimba wala hakutaka mjadala. Baada ya kuona mabadiliko kwa mwanae huyo aliyekuwa yupo likizo, wakati anakaribia kurudi shuleni, ilibidi kumuuliza. Kwa kuwa alikuwa mkali sana, ilimbidi Wini akiri kuwa yeye ni mjamzito. Mama yule hakutaka kesi. Alimwambia aende kulala. Wini akijua yamekwisha, alishangaa anaamshwa kukiwa hata hapajapambazuka. Akaambiwa akaoge, ndipo alipopewa maneno yake ya mwisho, na kuagwa rasmi hapo nyumbani asiamini kama kweli yamemkuta.



************************************************



 Kitanda cha kawaida sana alichokuwa akilalia nyumbani kwao, akaanza kukiona kilikuwa cha thamani kubwa kila inapofika usiku na kutafuta pakujilaza. Hofu ya kubakwa kila siku usiku anapolala huko mtaani, ikamfanya anze kutanga tanga kila siku usiku akibadili sehemu za kulala ili wahuni wasijue usiku huo alipo. Alihangaika kila sehemu  mpaka dada yake mkubwa alipomchukua na kumuhifadhi nyumbani kwake.



Tena alimuhifadhi kwa kuwa watu walikuwa wakimsema na kumtaka msaidie mdogo wake aliyekuwa akitangatanga mtaani na ujauzito. Hakujulikana anaishi wapi, lakini alionekana akizunguka mchana akitafuta kazi au msaada kwa ndugu jamaa na marafiki.



Ndipo habari zikamfikia dada yake, yaani Maria. Alipotolewa nyumbani, mama yake alitangazia kila mtu kuwa Wini alikwenda kwa dada yake huko mjini. Akitoka huko atarudi shuleni moja kwa moja, hatarudi tena pale kijijini. “Dada yake amemwita huko mjini, kabla hajarudi shuleni.” Huo ndio ukawa usemi wa mama yao kwa kila aliyemuulizia Wini pale kijijini. Kwa hiyo kwa pale kijijini ikawa mama huyo ametoa balaa hilo, la aibu kwa muda. Hakuna aliyejua kama Wini alikuwa mjamzito.



Isipokuwa majiraji wa chache wa dada yake pale pale mjini. Walikuwa wakimuona Wini akimfuata dada yake kazini kuomba msaada hata wa pesa ya kwenda kula. Mwanzoni Maria alidanganya walimu wenzake kuwa hamfahamu ni nani. Lakini ikawa ngumu. Rangi zao za mwili zilifanana sana. Wakachukua umbile linalofanana na mama yao. Kuanzia urefu na muonekano mzima wa nje. Maria na Wini walifanana kwa asilimia kubwa, japo Wini alikuwa mdogo sana kwa Maria.



Wini alikuwa akihangaika. Akiona amekwama kabisa, njaa imemlemea, alikuwa akikimbilia kazini kwa dada yake aliyekuwa akimsema sana ndipo anamsaidia vijisenti kidogo. Dada yake alipoacha kazi, akahamia kuomba msaada pale nyumbani kwake. Wakati mwingine alikuwa akifika hapo nyumbani kwa dada yake kwa kujiiba. Anajificha mpaka ahakikishe shemeji yake hayupo ndipo anamfuata msichana wa kazi, ataomba hata kiporo. Akishakula, anaondoka kwa haraka sana ili shemeji yake asimkute nyumbani kwake kwani alishampiga marufuku yeye na dada yake. Akikataa kabisa Wini kukimbilia pale. Alimtaka Wini arudi nyumbani kwao, akaombe msamaha, atulie kijijini baada ya kushindwa shule kuliko vile anavyotangatanga mjini. Na hapo ndipo majirani na wafanyakazi wenzake Maria, ndipo walipomuona Wini na kujua kama ni ndugu na Maria.



************************************************



Lakini huo haukuwa wakati wa dada yake, Maria, kumkaribisha mtu yeyote aende kuishi nyumbani kwake. Kwanza ndio na yeye alikuwa kwenye bed rest ya mimba aliyokuwa ameitafuta kwa takribani miaka 10, tena kwa shida sana.



Dada huyo ambaye alikuwa kwenye ndoa ya muda mrefu, alijaliwa mtoto wa kwanza wa kiume. Wakamwita James. James alikaa akiwa mtoto wa pekee kwa muda mrefu sana huku wazazi wakihangaika kutafuta watoto wengine lakini baba yake, au mumewe Maria akiwa hana pressure sana, kwani tayari analo dume lake, James. Shuguli ilikuwa kwa Maria akitaka watoto wengine. Alikumbuka shida alizokuwa akimuona mama yake akipata wakati akitafuta watoto, akazidi kuchanganyikiwa. Hakutaka apitie huko. Lakini angalau yeye alitanguliza mtoto wa kiume. Ikawa nafuu kwenye ndoa.



 James alipatikanika mwaka wa kwanza tu baada ya wazazi wake kufunga ndoa. Ilikuwa faraja kubwa sana. Baada tu ya kujifungua James, Mama yake na Wini akiwa bado mdogo, walifika hapo mjini kumsaidia kumlea Maria. Baada ya siku chache alimchukua Maria na mwane huyo mchanga James, na kurudi naye kumlea kipindi hicho cha uzazi pale kijijini. Wakaomba James abatizwe pale pale kijijini kwa bibi yake. Angalau tu kusuta watu na kuwaonyesha watu kuwa hakuwa na uzazi mbaya. Mume wa Maria alikuwa na kazi nzuri. Alijijenga mjini maeneo ya Majengo. Kwa hiyo muda Maria yupo pale kijijini analelewa uzazi, ndio Wini naye yupo binti mdogo tu. Baba yake James akaweka heshima pale kijijini. Kulikuwa kukimwagwa vyakula hapo. Na siku ya ubatizo wa James, kukachinjwa na ng’ombe, watu wakaalikwa. Wakala na kunywa mbege mpaka wakachoka. Bia zakueleweka zilikuwepo.



Ukweli Maria alimpa heshima mama yake. Maria ukawa ndio mfano anaoimbiwa Wini tokea anakuwa mpaka anafukuzwa kwao. Ni kweli Maria alifanana zaidi na mama yao hasa, tabia. Wote walikuwa wazungumzaji sana. Na walipendana na mama yake kama marafiki. Ukiwakuta Maria anazungumza na mama yake, utafurahi. Ungejua ni marafiki walio shibana. Kwa mshahara wake wa ualimu, hakuacha kumsaidia mama yake kumtunza Wini. Tena alipoolewa na mume mwenye uwezo. Ndio kila mtu alijua. Maisha ya mama huyo yakaleta aghueni kubwa sana.



************************************************



Lakini baada ya kumzaa James. Kipenzi cha bibi yake. Maria alikaa miaka 10, akihangaika kila mahali kutafuta watoto. Huku akikumbuka kashfa na adha ya mama yake aliyomuona akipitia mpaka baba yao kuwakimbia, wakati anakuwa. Hofu ya kuolewa mke wa pili au kukimbiwa, ikaanza kumtesa. Mama yao alizunguka kila mahali na Maria, kuhakikisha anashika mimba ya pili. Hakuta kile alichopitia yeye, ndio Maria apitie. Alihakikisha kule kote alikoshindwa kupita yeye kusaka mtoto, ndiko anakompitisha Maria ili kumsaidia kupata mtoto. James akageuka kuwa mtoto wa bibi kipindi hicho mama yake anahangaika na uzazi.



************************************************



Mwaka huo mama yake Nanaa anafukuzwa nyumbani, ndio na dada yake naye alikuwa ameshika mimba. Akawa radhi kuacha kazi na kuchukua bed rest ya ujauzito wa mtoto aliyemtafuta kwa shida sana. Wakati Wini anahamia kwa dada yake akiwa na mimba ya miezi 6 anaelekea 7, dada yake ndio alikuwa amebakisha siku chache ajifungue.



Wakati mtoto wake wakiume James alishatimiza miaka 10 anatafuta 11, ndipo akajifungua mtoto mwingine wa kike. Wakampa jina la Viola. Na ndipo baada ya miezi mitatu baadaye, binti huyo mdogo, yaani mama yake mdogo James na Viola, Wini, akiwa hajulikani mwenye mimba hiyo ni nani, akapatwa uchungu mida ya saa tatu usiku.



Alihangaika mwenyewe chumbani akitaka asisumbue wenye nyumba wake. Hasa shemeji yake aliyetamka wazi wazi na yeye hamtaki mle ndani. Lakini muda wa mtoto kutoka au kuzaliwa ukifika, umefika tu. Hauchagui mazingira wala ulipo. Haujali hali ya mama aliyonayo wakati ule. Akitakiwa kutoka duniani, lazima atoke. Alihangaika mpaka usiku sana chupa ikapusuka akiwa peke yake chumbani. Alishtuka alipoona damu zinatoka, ndipo akaenda kumgongea dada yake. Akakimbizwa hospitalini. Akaingizwa chumba cha kujifungulia, lakini binti huyo mdogo, yaani mama yake Nanaa hakufanikiwa kutoka humo kwenye chumba cha kujifungulia, akiwa hai. Hata hakubahatika kumnyonyesha Nanaa. Alipata matatizo ya uzazi, akafariki wakati daktari wa zamu alipokuwa akimsaidia kumtoa mtoto. Damu chache aliyokuwa nayo Wini, iliendelea kumwagika mpaka mauti ilipomfika.



*****************************************************



Ndipo ilipobidi Maria, dada yake Wini arudi na huyo mtoto, nyumbani bila kutarajia. Jina hilo la Nanaa, Wini alimuachia James, mtoto wa dada yake. James alikuwa akijisogeza sana karibu na Wini wakati yupo nyumbani kwao. Siku moja alimfuata mama yake mdogo, akamuuliza mtoto akizaliwa ataitwa nani, akamwambia Nanaa. Baada ya mtoto kurudishwa nyumbani, Maria akiwa amechanganyikiwa. Hajui chakufanya na huyo mtoto asiye na mama wala baba, ndipo James akawaambia wasimwite tu mtoto, anaitwa Nanaa. Kila mtu alimshangaa James. Lakini alionekana anauhakika na huyo mtoto. Ndipo kuanzia hapo akaanza kuitwa Nanaa.



Alilelewa kwa shida sana kwani alikuwa ameingilia penzi la mtoto aliyetafutwa kwa shida na mume wa Maria alikuwa akimuhesabia Wini siku ili atoke nyumbani kwake. Alimruhusu Wini kujifungua tu, kisha akamwambia mkewe baada ya hapo anataka Wini aondoke na mtoto wake. Wakati Viola mtoto wao anatimiza miezi mitatu ndio Nanaa alizaliwa na kuachwa akiwa hajulikani baba, ila mama aliyefariki. Kwa hiyo ikabidi siku za mwanzoni na yeye kunyonyeshwa kama Viola na mama huyo ambaye aliona mtoto wake anapunjwa. Huku mumewe akimlaumu mkewe kumpokea Wini, mama yake Nanaa tokea mwanzoni. Kila Nanaa alipokuwa akilia wakati mdogo, mumewe alitoka nje kabisa akisema hataki kusikia sauti ya mtoto huyo. Alimlaumu mkewe kuleta matatizo ndani ya ile nyuma.



Nanaa alikataliwa hata kwa bibi yake. Mama yake Maria na Wini alikataa kata kata huyo mtoto kurudishwa pale kijijini. Alikataa hata kumtambua kama ni mjukuu wake. Baba yake James, ambaye ni mume wa Maria, alikuwa akimsimanga mkewe, mchana na usiku. “Kama hata mama yake mzazi alimfukuza, kwa nini wewe ulimpokea? Huyo binti ni tatizo mke wangu. Unajitafutia balaa.” Hayo ndiyo maneno aliyokuwa akiyapata kutoka kwa mumewe wakati wa uhai wa Wini. Tena mbele yake. Mbaya zaidi ni pale mdogo wake alipofariki.



Ni kweli balaa likatokea. Akaachiwa mtoto ambaye hawakujua pakumpeleka. Mumewe alisema sana. Kwani hata mazishi ya Wini ni kama yalifanywa na rafiki za dada yake. Mumewe alikataza kabisa maswala ya msiba nyumbani kwake. Maiti ya Wini iliagwa katika hospitali ya taifa KCM na kupelekwa makaburini. Alizikwa kimya kimya, bila ibada wala mama yake kuwepo. Ni kama alitupwa tu, habari ikaisha.



Baada ya kuzunguka na huyo mtoto akitaka amtoe pale ndani na kushindwa, ndipo ikabidi amlee Nanaa mle mle ndani. Lakini kwa shida sana. Mumewe alikataa kumsaidia kabisa. Hakutaka hata shilingi yake kumtunza huyo mtoto aliyejua ni balaa ambalo mkewe amelileta ndani ya hiyo nyumba. Watu walisema mama yake Nanaa alikufa sababu ya kulaaniwa na mama yake. Kwa hiyo hata Nanaa, amebeba mkosi.



*****************************************************



Kwa shida, dhiki na mateso, Nanaa akakua. Alikula chakula kama watu wote mle ndani. Alinunuliwa nguo pale inapolazimu, hasa sare za shule. Lakini mara nyingi alivaa nguo za watoto wa mama yake mkubwa pale zinapokuwa ndogo kwao au mama huyo anapotaka kubadilisha nguo za mwanae Viola, ndipo alipopewa Nanaa. Kwa Nanaa hakuona shida, kwani alikuwa akikua akiona hivyo. Na tangia anapata uelewa wake, akiwa mtoto mdogo sana, mama huyo alihakikisha anamuelewesha Nanaa na kuelewa kuwa pale alipo anasaidiwa tu. Kwa hiyo Nanaa alikuwa akijua anasaidiwa tu. Na alisimuliwa vile alivyokuwa ikimlazimu mama huyo kukesha kumlea yeye, badala ya kupumzika na mumewe. Kwa hiyo kila alichokuwa akipewa Nanaa, alishukuru sana na kufurahia.



Alishajua hastahili chochote mle ndani. Yeye anasaidiwa tu. Tena aliaminishwa pale alipo ni sehemu ya thamani sana kwake, kwani alikataliwa kila mahali. Hata bibi yake alimkataa. Alimuona hata akifika pale hataki kumgusa wala hata kuzungumza naye. Alikaa naye mbali kabisa huku akimkaripia kila akimsogelea. Alimuona bibi yake vile anavyompenda Viola, mjukuu wake aliyemuhangaikia sana mpaka kushikwa mimba yake. James ndio alikuwa kipenzi kabisa cha bibi huyo. Na hata Nanaa alijua. Yale mazingira yote yakamfanya kuelwa na kujua ni kweli pale alipo ni sehemu sahihi, na yale ni maisha anayopaswa kuyatumikia vizuri.



Usingemkuta akilalamika kama anateswa. Hakujua maisha mengine zaidi ya yale aliyokuwa akiishi pale kwa mama yake mkubwa. Kwa hiyo akajua inamlazimu kuishi vile. Tena alitakiwa kushukuru sana. Ila kadiri alivyozidi kukua na kuona mapenzi anayopewa Viola na wazazi wake, kitu kipya kikaanza kujengeka ndani yake. Ikaanza kuibua shauku ya kutaka kupendwa na kuthaminiwa na yeye kama Viola. Lakini hakuacha kukumbushwa bahati aliyoipata baada ya mama yake kumuacha na mama yake mkubwa kumpokea. Kwa upande mwingine, ikabidi awe mpole.



*******************************************************************



Walipofikisha miaka miwili tu, Viola akiwa amemtangulia kwa miezi 3, mama mkubwa akapata mimba ambayo hakutegemea. Akazaa mtoto wa kike mwingine ambaye alimwita Vai. Hapo ndipo Nanaa alipokuwa mtu mzima gafla. Akaanza kutumwa hiki na kile kumsaidia mama mkubwa kulea mtoto huyo mchanga. Baada ya muda mfupi mtoto huyo mdogo, aliyekuwa akilingana kabisa na watoto wake akageuka kuwa mtumwa, akiwatumikia wanae wote mle ndani. Nanaa akageuka kuwa mkubwa kuliko hata James. Alibeba majukumu makubwa kuliko wenzake, na akalinganishwa na msichana wa kazi.



Nanaa alisoma shule za kawaida za serikali, lakini wenzake walisoma shule za kulipia. Walikuwa wakifuatwa na basi la shule pale nyumbani, yeye ilimlazimu kuamka mapema kama anavyoamka msichana wa kazi pale nyumbani, ambaye alikuwa akilala naye chumba kimoja. Anaandaa kifungua kinywa na kusaidia usafi, baada ya kula ndipo awahi shuleni akitembea kwa miguu. Na jioni anapotoka shule, ilimlazimu kusaidia kazi za pale ndani. Ikiwemo kupika, kunyoosha nguo za wazazi wa mle ndani, na ndugu zake kama alizilifua siku hiyo asubuhi, na kuwawekea vyumbani kwao, na kusaidia kazi nyingine za mle ndani.



Kama ungelimuuliza Nanaa kuwa anateswa, asingesema anateswa. Aliambiwa anawajibika kufanya yote hayo ili baba yake mkubwa asije kutafuta msichana mwingine wa kazi, akachukua nafasi ya kuishi yeye mle ndani. Kwa hiyo alipambana kwa kadiri ya uwezo wake kuonyesha hamna kazi ya kuhitajika msichana wa kazi wa pili mle ndani. Yeye na msichana wa kazi, wanatosha kabisa, kumudu kazi zote za mle ndani. Mwanzoni majukumu ya kuwahudimia wenzake yalimlemea sababu ya umri mdogo na kazi nyingi. Lakini kadiri siku zilivyozidi kwenda na umri uliposegea, akaweza kumudu majukumu yake vizuri, hakuona shida tena. Alijipendekeza kwa kadiri ya uwezo wake ili kuwafurahisha walezi hao ambao baba mwenye nyumba hakuwa hata na muda naye.



************************************************



Mida ya jioni walikuwa na utaratibu wa kula pamoja, na kila mwenye habari zake huo ndio muda wakuziongea na kucheka kabla ya kwenda kulala. Kina Viola walikuwa wao ndio wenye habari za kuvutia kwani walisoma shule za kisasa na walikutana na watoto wa matajiri, lakini sio Nanaa. Kwanza anakuwa amechoka, na pili alikuwa akiomba wamalize mazungumzo hayo mapema ili wakamalizie kazi za siku hiyo na wao wapumzike. Yeye Nanaa na dada wa kazi ndio walikuwa wa mwisho kulala ili kuhakikisha sinki la jikoni halilali na vyombo vichafu na jikoni panaachwa pasafi kila siku.



Muda wa kuangalia tamthilia ukifika, watu wote walikusanyika sebleni wanaangalia tamthilia pamoja. Mama yake mkubwa alikuwa mcheshi sana, maneno mengi hayakuwa yakimwisha. Basi huo nao ukawa muda wake wa kuchekesha kila mtu mle ndani. Baada ya watoto wake kukua, alijitupia kwenye biashara. Hakuweza kurudi tena kwenye kazi yake ya mwanzoni, ya ualimu.



Alikuwa na maduka ya nguo na vipodozi anayomiliki hapo mjini. Kwa hiyo alikutana na watu wengi tofauti tofauti na vituko vingi alivyokuwa akisimulia arudipo nyumbani kila siku. Mumewe alikuwa meneja wa kampuni ya kahawa pale pale jijini Moshi. Aliweza kuongeza kipato hapo nyumbani, nakufanya maisha ya familia yake kuwa mazuri. Lakini alihakikisha pesa yake au jasho lake linakwenda kwa wanae aliowazaa yeye tu, na si vinginevyo.



Alijulikana kama mwanaume mbahili, lakini si kwa watoto wake. Tokea Nanaa anazaliwa na kuletwa pale nyumbani, alishawekeana makubaliano na mkewe, huyo mtoto wa nyongeza sio jasho lake na yeye hatahusika kwa lolote. Kwa hiyo Nanaa aliishi pale, lakini akihudumiwa na mama yake mkubwa huku akikumbushwa mara kwa mara tokea mtoto anasaidiwa tu. Na kila pesa iliyotumika kwake kibinafsi, aliambiwa ni kiasi gani na ni jinsi gani ilivyomgarimu mama yake mkubwa. Iwe ni ada au michango midogo midogo aliyotakiwa kupeleka shuleni. Tena shule yenyewe ilikuwa ya bure ya serikali.



Lakini ilikuwa lazima awekwe chini na kuelezwa ugumu wa pesa alionao huyo mama. Majukumu mazito yanayomkabili yeye kama mama mwenye watoto watatu wenye mahitaji kama yake Nanaa, lakini anawanyima wanae, au anajinyima yeye, au anashindwa kumsaidia mama yake mzazi kule kijijini, inabidi apewe pesa hiyo yeye ambaye baba yake hakujulikana na mama yake alishafariki bila hata kuacha usia wowote ule. Kwa hiyo Nanaa alikuwa akikuwa akijijua yeye ni mzigo kwa mama yake mkubwa, na inamgarimu sana kuwepo pale na kumsaidia.



*******************************************************************



 Japokuwa hapakuwa na mateso ya moja kwa moja ambayo mtu anaweza kulalamika kuwa anateswa, lakini yale maisha yaliendelea kuibua shauku mbali mbali ndani ya Nanaa. Akitamani kuwa na chake au mtu anayemuhitaji, asiyemuona mzigo wala kumlalamikia kwa kila kitu. Ni kweli hakuwa akiteswa kwani alitakiwa kufanya kazi kama watoto wengi wanavyokuzwa, japo wenzake hawakuwa wakifanya kazi pale nyumbani. Alitakiwa kuamka asubuhi na mapema, kama mtoto mwingine yeyote anayepewa malezi mazuri ya kufundishwa maisha, japo ilimlazimu yeye kuamka kuwaandalia mazingira mazuri wenzake kina Viola na Vai, wenye umri mmoja au wakubwa kidogo, ili waende shule wakiwa hawajachoka.



Alikwenda shule kwa kutembea tofauti na wenzake, lakini hilo pia aliambiwa ni baba yao ndio anawalipia usafiri wa kuwaleta na kuwarudisha shule, yeye Mama Mkubwa hana pesa ya kumsomesha huko wanakosoma wenzake, kwa kuwa inabidi kununua chakula cha kutosha na yeye ale vizuri na alale vizuri. Nanaa hakuwahi kulalamika. Akaelewa ni kweli anatakiwa kuwa mtu wa shukurani. Tena wakati mwingine alifanya kwa ziada ili kumfurahisha mama yake mkubwa. Alijitahidi sana kufanya kazi pale ndani ili kumfanya Mama Mkubwa akitoka kazini apate muda wa kupumzika tu. Kila alipokuwa akirudi nyumbani, Nanaa alimuwahi na kikombe cha chai, au maji na ikitokea kuna juisi, basi alimpa Mama Mkubwa hiyo juisi na tabasamu kubwa usoni lililojaa unyenyekevu huku akitoa pole na kupokea mkoba.



Alijitahidi sana asiwe tatizo mle ndani ya nyumba. Kila wakati alikumbushwa yaliyompata mama yake. Akajitahidi kutulia kabisa. Hasa katika mapenzi. Japo Mama Mkubwa alisharuhusu kama kuna mmoja wao amepata mwanaume, basi ahakikishe huyo mwanaume anafahamika hapo nyumbani. Alitoa ruhusa ya kuletwa pale nyumbani afahamike. Aliwaambia binti zake kuwa hiyo itasaidia kuongeza heshima kwa huyo mwanaume. Kwa hiyo hata kama alikuwa na wazo la kumchezea tu, kama mama yake Nanaa alivyochezewa, basi huyo mwanaume ataogopa.



*******************************************************************



Japokuwa ni kama walilingana na Viola mtoto wa mama yake mkubwa, lakini mwenzake alimpita mbali sana kimakuzi. Alizungumza lugha ya kingereza kwa ufasaha. Alikuwa binti mwenye kujiamini. Alisoma shule nzuri. Alijua kuzungumza mbele za watu bila shida na alishaleta wanaume pale kwao kama marafiki, tena vijana wazuri tu na wanaonekana wasomi kama yeye mwenyewe Viola na Vai. Na Nanaa alihusika katika matayarisho ya pale ndani ikitokea Viola na mdogo wake wanataja siku ya wanaume zao kufika hapo nyumbani.



Nanaa alikuwa akiwatamania wenzake waliofanikiwa kupata wazazi wanaowapenda na kuwajali, na pia isitoshe, walibahatika kupata wanaume wazuri. “Na mimi nikija kumpata mwanaume wangu kama huyo kaka, nitampenda sana. Nitahakikisha tunaoana naye ili tukizaa watoto wetu tuwalee wenyewe wasihangaike au kusumbua watu kama mimi. Tutaishi kwenye nyumba yetu nzuri na watoto wetu wazuri, tuta..” Ni mikakati aliyokuwa akijiwekea Nanaa kila siku alipokuwa akikaribisha wanaume wa Viola na Vai.



Alikuwa akimshangaa Viola vile anavyochezea bahati. Alipata bahati ya wanaume waliompenda lakini hakuwa kuridhika. Hawakukosa kasoro. Akaishia kuwabadilisha mchana na usiku huku akieleza vituko vyao na kuwafanya hata mama yake acheke, kama jambo la kawaida tu.



*******************************************************************



Mpaka Nanaa anamaliza kidato cha nne, katika shule za kutwa. Hakuwa akimjua mwanaume kimapenzi. Alipata vishawishi vingi. Zikiwemo lifti za kurudishwa nyumbani. Walimu na wanafunzi wa shuleni hapo Old Moshi sekondari. Wakimpa ahadi nyingi zakuvutia, lakini Nanaa akafunga moyo. Akakana nafsi yake, akamaliza kidato cha 4. Alifaulu kwenda kidato cha 5. Akachaguliwa katika shule ya wasichana Ashira.



Ilikuwa furaha kubwa moyoni mwa Nanaa. Angalau anakwenda kuanza maisha sehemu nyingine, mbali na nyumbani hapo kwa mama yake mkubwa. Akaanza kuonja ladha ya maisha mapya. Akafurahia utulivu aliokuwa akipata mbali na kelele za pale ndani kwa kina Viola ambazo alikuja kujua upo uwezekano wa kuishi mahali pengine na ukafurahia maisha mengine mbali na maisha aliyoaminishwa ndio maisha pekee hapa duniani. Shule akawa mkombozi wa kwanza wa Nanaa. Ikampa ladha ambayo hakutarajia. Moyo wake ukapenda na kuthamini zaidi elimu. Akajiambia shule ndio mkombozi wake.



Akaanza kupendeza na kuvutia. Shule hiyo iliyokuwepo juu kabisa ya kimlima kikali cha Marangu, kwake ilikuwa ni mbingu ndogo. Hakuwa akitamani shule zifungwe. Hakuwa akielewa wanafunzi wengine waliokuwa wakilalamikia maisha ya pale shuleni. Alituliza akili zake zote shuleni. Baada ya muda mfupi tu, akapata na rafiki ambaye ndio aliongeza ladha nzuri zaidi ya maisha hapo shuleni. Aliitwa Anni. Wakaanza kuongozana kila mahali na Anni.



Nanaa na Alex.

Siku moja Anni alitembelewa na kaka yake Alex. Akamtambulisha Nanaa kwa kaka yake. Alex akampenda sana Nanaa. Akaanza kutafuta sababu za kuwepo Shuleni hapo kwa kisingizio anakwenda kwa dada yake. Kila wazazi walipotaka kumtumia kitu Anni shuleni, Alex akawa mtu mzuri sana wakujitolea kwenda Ashira kupeleka mahitaji ya dada yake. Hakujali mlima huo wa Marangu kufika shuleni hapo, nia ni kumuona na Nanaa. Ukaanza urafiki kati ya Nanaa na Alex pia.



Safari za Alex kumtembelea Anni dada yake Ashira zikawa nyingi. Nyumbani kwa kina Alex na Anni ilikuwa Arusha. Kwa hiyo Alex akapata sababu nzuri sana ya kila siku za jumamosi kuwepo kwenye shule hiyo ya wasichana Ashira, tena akigaramiwa na wazazi wao, wakijua anakwenda kumtembelea Anni, binti yao mdogo.



Hisia za kimapenzi zikaanza. Nanaa akavutiwa na ujio wa mara kwa mara wa Alex kwenda kuwatembelea. Lakini Alex alisisitiza huwa anakwenda pale maalumu kwa ajili yake yeye. Nanaa akaona ni upendo ulioje? Arusha mpaka Marangu! Tena kupandisha kilima kikali kile ili kumfikia yeye tu, hakika Alex akawa ni kijana mwenye mapenzi ya dhati.



Shauku kubwa ya Nanaa, ilikuwa kupata mtu atakayeonyesha anamuhitaji. Hakujali sura wala umbile. Yeyote yule atakayemuhitaji, basi alijiapia kujitoa kwake. Sasa kumpata Alex aliyeonyesha utayari wa kuvunja ratiba zake zote, ili awe naye. Ilimgusa sana. Akajua yeye ndio atakuwa mwanaume wakumtoa pale nyumbani kwa mama yake mkubwa. Amuoe, kisha wakaishi naye popote kule Mungu atakapowajalia. Ampunguzie mzigo mama yake mkubwa na kuepuka chuki ya baba yake mkubwa ambayo wala hakuhitaji kuificha. Alimuonyesha kila mtu waziwazi, kuwa hataki kujihusisha na huyo mtoto.



Mahusiano ya mapenzi yakaanza. Nanaa akamwaga moyo wake wote kwa Alex, akionyesha wazi yupo tayari kufanya lolote kwa kijana huyo. Kama ulishaona wanawake desparate hapa duniani, basi Nanaa aliwashikia bendera. Akawa kama aliyechanganyikiwa na Alex. Naye Alex akaonyesha kumuhitaji vilivyo. Kwa mara ya kwanza, Nanaa akapata mtu baki, mbali na kaka yake James, anayempenda na kumjali. Akapata faraja ya ajabu moyoni. Akapata mwanaume wa kwanza, mbali na James, anayeweza kukaa naye na kumsikiliza. Mwanadamu anayefunga safari, kupandisha mlima mkali wa Marangu, kwenda kumuona yeye! Kwake lilikuwa jambo la faraja sana.



Anni alipokuja kugundua, akaamua awe anawapa nafasi. Alex anapokuja shuleni, anafikia Ashira B, atajificha sehemu ambayo alikuwa akikutana na Anni na Nanaa. Anni  atamsalimia kaka yake na kuchukua mizigo yake, na kuwapisha. Yakaanza mabusu yakuagana. Akifika tu shuleni hapo, wa kwanza kuitwa ni Nanaa, ndipo ataitwa mdogo wake. Yakaja na mabusu ya kukaribishana. Moto wa mapenzi ukawaka ndani yao. Wakaona hawatosheki kwa mabusu. Tena mbaya zaidi mabusu yenyewe hayakuwa ya muda mrefu sababu ya mazingira. Wote waliona hamna sababu yakusubiri tena, wakakubaliana kipindi cha likizo fupi, kabla Nanaa hajarudi nyumbani, watafute chumba mahali, watumie siku hiyo kuridhishana, kisha jioni ndipo aende nyumbani akijidai ndio ametoka shuleni.



Na ikawa hivyo. Nanaa akiwa hamjui kabisa mwanaume kwa umri huo akiwa kidato cha 5, akaamua kugawa bikra yake kwa Alex. Haikumsumbua wala dhamira haikumuuma kwani walikubaliana kuona mara Alex atakapo maliza chuo. Alex alikuwa chuo cha uhasibu Arusha. Ndio alikuwa mwaka wa 1, wakati Nanaa yupo kidato cha 5. Kwa hiyo Nanaa alikuwa amejitoa kwa moyo mweupe kwa mwanaume atakayekuwa mumewe pindi atakapo maliza chuo hicho. “Hata hivyo sifanyi kosa kama mama. Mimi nafahamika na Anni dada yake. Halafu Alex sio muhuni kama mwanaume aliyemrubuni mama. Mimi nitakuwa mwangalifu, sio kama mama. Siwezi shika mimba.” Hayo ndio maneno aliyokuwa akijifariji nayo Nanaa anapokwenda kujifungia nyumba za wageni na Alex.



Kwa kuwa hakukamatwa mara ya kwanza, basi wakajenga mazoea ya kukutana mahali, nakutumia siku nzima kufanya mapenzi, ndipo Nanaa anarudi nyumbani. Mwaka wao wa kwanza wa mapenzi ukaisha vizuri. Nanaa anapokuwa likizo, basi mawasiliano hayakukauka. Alex akiwa jijini Arusha, Nanaa nyumbani kwao Majengo, hapo hapo jijini Moshi. Wakati mwingine akiwa likizo, Alex alikuja Moshi kumtembelea Nanaa.



Siku za kufungua shule zinapofika, Alex alimsubiria Nanaa mjini, akiwa ameshachukua chumba mahali. Nanaa anakwenda hapo. Wanatumia siku hiyo wakiwa wawili, kisha jioni Nanaa anakwenda shuleni, au analala mpaka kesho yake ndipo anakwenda shuleni. Na siku za kufunga shule hivyo hivyo. Alex alimfuata mpaka shuleni. Anamchukua asubuhi hiyo, wanakwenda Moshi mjini. Wanachukua chumba kwenye nyumba za kulala wageni. Mpaka jioni ndipo Nanaa anarudi nyumbani na kuendelea kwenda kumtembelea Alex hapo hotelini. Atamtumikia mwanaume huyo bila kuchoka, mpaka anapoondoka kurudi kwao Arusha.



Penzi likakolea. Alex akawa anapata anachokitaka kwa Nanaa, japo kwa upande wa Nanaa, yeye mapenzi hayakuwa muhimu. Hakujali kama anafurahia yale mapenzi. Ilimradi alipata mtu atakayemtoa kwenye yale maisha. Ni kweli hapakuwa na shaka kama watakuja kuona pindi watakapomaliza shule. Alex alishamuhakikishia maisha mazuri mara baada ya kuona. Basi Nanaa alitoa mwili wake kwa Alex kama mumewe huku akiwa mwangalifu asishike mimba, asije zaa kabla ya kufunga ndoa. Wakachagua majina ya watoto wao. Wakapanga idadi na jinsia ya watoto watakao zaa. Penzi likaendelea mpaka Nanaa alipomaliza kidato cha 6. Akaona ndio muda muafaka na yeye kupeleka mwanaume nyumbani kwao.



***************************************************



Wakati Nanaa anapanga kumpeleka Alex nyumbani, alikuwa ndio anajiandaa kwenda kumaliza mwaka wa mwisho chuoni. Nanaa na Viola ndio walikuwa wamemaliza kidato cha sita, wapo nyumbani wanasubiria matokeo yao. Baada ya kumaliza tu shule yake ya kidato cha sita, Viola akaenda jijini Dar kumtembelea James, kaka yake. Alikaa kwa muda kidogo tu, ndipo Vai naye baada ya kufunga shule akamfuata Viola dada yake. Wote waliondoka huku wakimringishia Nanaa kuwa wanaenda jijini Dar, kwenye starehe. Yeye anatakiwa abaki asaidie kazi za mle ndani.



Nanaa alitamani sana na yeye aongozane nao, angalau akapaone tu Dar, au atoke nje ya mkoa wa Kilimanjaro, lakini mama mkubwa alimkatalia. Kwanza alimwambia hana pesa ya kumpa ya nauli halafu anamajukumu pale nyumbani. Hawezi kumruhusu asafiri. Nanaa akaridhika. Akabaki mle ndani akifanya kazi. Siku Alex alizoweza kwenda kumtembelea, basi Nanaa ilimlazimu kutoroka nyumbani mida ya mchana ambayo mama yake mkubwa yuko kwenye majukumu yake ya kila siku, anakwenda kumuhudumia Alex huko hotelini.



*****************************************************



Maisha yakaendelea. Nanaa akitafuta wakati mtulivu wakumtambulisha Alex kwa mama mkubwa. Kila mama mkubwa aliporudi nyumbani, hakuacha kueleza starehe wanazopata wanae huko jijini Dar kwa kaka yao James na vile kaka yao anavyowafurahia. Ikawa hamna nafasi ya mtu mwingine kuzungumzwa pale ndani, wala kusikilizwa. Ni matambo ya mama mkubwa tu, kwa wanae huko jijini Dar.



Siku wasiyotarajia, kabla hata shule ya Vai haijafungua, akaona Viola na Vai wanarudishwa pale nyumbani na kaka yao James. Alimuona James akizungumza na mama mkubwa, lakini hakujua kulikoni. Lakini akamuona kaka James akiondoka bila mmoja wao.



 Nanaa akafurahi kuona wamerudi, akajiambia ule ndio wakati wa kumtambulisha kwao Alex, ili wasiendelee kumdharau. Ilikuwa ndio kwa mara ya kwanza na yeye Nanaa ana habari njema kama wenzake ya kupeleka mwanaume anayempenda nyumbani kwao. Kwa muonekano Alex hakuwa mbaya. Aliweza kutambulishwa kokote bila shida. Swala la kuwa analafudhi ya kiarusha ikawa ni mojawapo ya kivutio kwa Nanaa. Wala hakujali. Na ukichanganya pesa ya wazazi wake, basi Nanaa alijua lazima ataweka heshima hapo nyumbani.

Tofauti na matarajio yake, alijua angesifiwa baada ya kutoa habari hizo. Lakini walimcheka sana. Wakijua kwa ushamba alionao kwa wanaume, ataleta kituko mle ndani. Wasijue Alex ni mtoto wa mjini na Nanaa sio mshamba kama wanavyodhani. Alishakuwa na huyo mwanaume kwa takribani miaka miwili sasa. Na Nanaa hakuwa bikra kama walivyodhani. Alex alikuwa akifaidi penzi lake kwa siri kwa muda mrefu tu.



Viola apokonya penzi la Nanaa, ampora Alex.



V

iola alichanganyikiwa baada ya Alex kufika hapo nyumbani. Alitawala mazungumzo yote, huku akionyesha uzoefu wa mambo kadhaa. Alitaka kujua malengo yake baada ya kumaliza chuo. Nini kilimpelekea kusomea mambo ya mahesabu. Changamoto gani anapata katika kusomea fani hiyo. Viola akiwa amechangamka, aliendelea kuhoji maswali mengi yamsingi ambayo hata Nanaa mwenyewe hakuwahi kumuuliza Alex.



Alipoona mapokezi ni mazuri nyumbani kwa kina Nanaa, akaanza kumtembelea kila jumamosi. Analala hotelini na kuondoka siku ya jumapili au jumatatu asubuhi. Furaha na amani vikatawala kwa muda. Kila anapokuja nyumbani basi Viola hakukosa mazungumzo ya msingi kwa Alex. Gafla akageuka yeye kuwa msichana wa maana kwa Alex kuliko Nanaa. Mara Nanaa akaanza kuona mawasiliano yanakuwa mazito kati yao. Alex akaacha kuonekana pale nyumbani lakini Viola furaha kwake ikaongezeka. Akaanza kudanganya kwa baba yake huku mama akimkingia kifua kuwa kila siku za ijumaa huwa anamtuma kijijini kwa bibi yake na kurudi jumapili usiku au jumatatu na wakati mwingine alimuaga baba yake kuwa anakwenda kutafuta chuo mikoa mingine basi na kupotea zaidi pale nyumbani.



Alitangaza pale nyumbani kwao kuwa, kwa mara ya kwanza maishani amepata mwanaume wa ndoto yake. Alisema ameshatambulishwa mpaka upande wa huyo mwanaume ni watu wenye uwezo sana. Ilikuwa furaha kwa Mama Mkubwa, kwani ni kweli Viola alibadilika. Kila aliporudi safari alirudi na vitu vipya na vya maana, akiwa amejawa furaha.



Juhudi za kumtafuta Alex ziliendelea huku akiambiwa yupo na hili au lile atapiga simu baadaye. Vicheko vilitawala mle ndani, asijue anayechekwa ni yeye. Maswali ya kuulizwa Alex alipo huku akichekwa hayakuisha, na yeye hakushindwa kumtafutia sababu ya kuwapa ndugu zake ili tu kuonyesha yeye na Alex wapo vizuri, ila Alex ametingwa tu. Asijue linalo endelea.



“Atakuwa kapata mwanamke mwingine anayempenda.” Mdogo wake Viola, yaani Vai alikuwa akimwambia Nanaa huku akimcheka Nanaa pale alipokuwa akimtetea Alex kuwa yupo busy. “Hapana. Alex ni mwaminifu sana. Ni ubusy tu.” Nanaa aliongea kwa uhakika, akimtetea mpenzi wake mbele ya Viola ambaye ndio alikuwa amerudi kutoka safari ya siku tatu ambayo Nanaa alimsikia mama yake akimwambia baba mkubwa kuwa amemtuma Viola kijijini kwa bibi yao . “Ubusy huo ubusy gani bwana!? Wewe kubali kuwa umeachwa. Sababu hazikuishi!” “Amesema atakuja ijumaa ijayo.” Wakamcheka kwa sauti ya juu, na kugonga mikono wakimcheka Nanaa bila huruma akiwa amewapelekea chakula cha mchana, pale pale sebleni walipokuwa wakiangalia luninga. Viola alimtaka awapalekee chakula pale pale, akisema kwa nyodo kuwa amechoshwa na usiku mrefu, uliopita, uliokuwa umejaa starehe nyingi. Hakutaka kunyanyuka na kwenda kula mezani.



 “Sasa mnacheka nini?” Nanaa aliuliza wakati Viola ameenda kuongea na simu yake nje. “Njoo nikuonyeshe anapokuwaga Alex.” Vai alimwita Nanaa. Alitoa simu na kuanza kumuonyesha picha za Alex akiwa na Viola, na nyingine hata wao walikuwepo. “Hizi za jumamosi ya juzi. Niliwafuata hotelini, Alex akatutoa. Wenzio wapo kwenye mipango ya harusi, hata mama anajua. Hapa wanasubiri Alex amalize tu chuo, aje kutoa mahari.” Nanaa alihisi yupo ndotoni. “Na kwa taarifa yako zaidi, Viola kaamua kumbebea mimba kabisa ili asije badili mawazo. Kwa hiyo andika maumivu.” Nanaa alikaa chini. “Yaani Viola amembembea mimba mpenzi wangu!?” Nanaa aliuliza na kufanya amcheke zaidi. “Sema aliyekuwa mpenzi wako, wewe Nanaa. Mbona huelewi?” Nanaa alinyanyuka na kuondoka.



****************************************************



Visa vikaanza. “Sasa unanuna nini? Kama mwenzio amebahatika kupata mwanaume mzuri si ushukuru Mungu, badala ya kumnunia? Kama hakuwa andiko lako, basi. Maana mwenzio tayari mjamzito.” Mama Mkubwa alikuwa akiongea na Nanaa alipomkuta jikoni akiosha vyombo. “Huna shukurani wewe mtoto.” “Mbona mimi sijasema kitu, mama mkubwa?” “Mbona Viola anasema humsalimii? Akikuita msaidie, huendi. Mama yako alikuja hapa na ujauzito wako, tukamsaidia bila kujali alikobebea mimba. Hatujui kama ilikuwa mimba ya mume wa mtu au la. Lakini nikamsaidia bila kujali. Leo mwenzio amebahatika, unamfanyia roho mbaya!? Shukurani yako iko wapi wewe?” Gafla kitendo cha Viola binti aliyemaliza kidato cha 6 tu, nakushika mimba, kikaonekana cha kusifiwa.



Kazi ya kumuhudumia Viola, mjamzito, ikampata Nanaa. Alex anapokuja kumsalimia Viola mpenzi wake, pia Nanaa alitakiwa amuhudumie huyo Alex, tena bila kinyongo. Alitakiwa aonyeshe heshima kwa Alex kama shemeji yake. Hakuruhusiwa kumsemesha, ila kumtengea kinywaji na chakula kisha kuondoka. Viola alimpiga marufuku Nanaa mbele ya Alex kuwa asimtafute tena mpenzi wake, hawataki usumbufu.



 ******************************************************



Matokeo yakumaliza kidato cha sita yalipotoka, Nanaa akapata daraja la pili, Viola daraja la nne. Ni kama hapakuwa na jambo zuri lililokuwa limemtokea Nanaa. Mama Mkubwa aliumia sana. Akabaki kuzungumza kwa mafumbo.  “Katika maisha huwezi kupewa vyote. Heri yako mwanangu umebahatika kuolewa na mwanaume anayekupenda. Wakwe zako wanakujali na unatarajia mtoto.” Hayo ni maneno kutoka kwa Mama Mkubwa. Hapakuwa na pongezi kwa Nanaa, ila manyanyaso. Hapo ndipo alipoona upendeleo wa wazi wazi na kujiona kweli yeye si mtoto wa pale ndani.



Wenzake walianza kutuma maombi ya vyuo mbali mbali lakini Nanaa alishindwa. Kwani aliacha kupewa pesa, akawa yupo tu nyumbani akimtumikia Viola mchana na usiku. Hakuna hata aliyezungumzia mambo yake ya shule tena, bali majukumu. Ampikie nini Viola au alipewa ratiba ya siku nzima ya jinsi ya kumuhudumia Viola. Napo hapo alilala akiwa hoi. Maana mara nyingi Viola alibadili mawazo ya kila chakula alichotaka Nanaa ampikie. Anaweza kutaka ndizi na nyama ya ng’ombe. Nanaa anapompikia na kumpelekea, anaweza kusema hakitaki tena kile chakula, anataka chakula kingine au kumlazimu kufuata aina ya chips fulani mbali sana na hapo nyumbani, tena pengine ni usiku. Ilimradi tu, atumikiwe na mwenzie.



******************************************************



James mtoto mkubwa wa mama Mkubwa, alikuwa amemaliza chuo na kuajiriwa jijini Dar. Aliishi Dar kwa muda mrefu tu. Tokea yupo chuo mpaka ameajiriwa. Kwa umri, aliwapita mbali sana dada zake. Halafu kwa asili James alibeba haiba ya kiutu uzima. Alijiheshimu sana. Kwa hiyo hata hapo nyumbani aliheshimiwa kama anavyoheshimiwa baba yao.



Alifika nyumbani hapo mida ya usiku. Aliwaambia ilimbidi kwenda kazini asubuhi ndipo akaanza safari. Kwa muda mfupi tu alipoingia pale ndani, akahisi mambo hayakuwa sawa. Ilikuwa saa tano na nusu usiku wakati anamaliza kula. Alikuta watu wote wakimsubiria kasoro Viola. Kama kawaida, Nanaa ndiye aliyekuwa akimuhudumia kaka yake. Wakati anatoa vyombo na kusafisha meza, James akaongea kwa sauti. “Nina hamu sana na supu ya makongoro ya Kiboriloni. Kesho asubuhi ujiandae Nanaa. Nataka unipeleke.” Nanaa akafurahi sana kusikia atapata muda wa faragha na mkombozi wake.



****************************************************



Halikuwa jambo la ajabu kwao kwa James kumtaka Nanaa ndio amsindikize. James alijulikana anampenda sana Nanaa, kama ndio dada wakuzaliwa tumbo moja. Wakati mwingine alifika hapo nyumbani kwenda kumuona tu Nanaa. Hata hivyo, yeye ndiye aliyekuwa amemlea Nanaa, kama yaya wake, tokea anatolewa hospitalini baada ya kifo cha mama yake. James ndiye aliyetoa hilo jina la Nanaa, akisema ndilo jina mama yake alimwambia huyo mtoto akizaliwa atamwita hivyo. Ndiye aliyejua kula na vaa ya Nanaa, tokea hata Nanaa hajakatika kitovu cha kuzaliwa.



****************************************************



Kwa uongeaji ule, ndio alikuwa akitangaza kuwa Nanaa hatakuwepo asubuhi ya siku inayofuata. Kwa maana nyingine, alikuwa akimtaka mama yake asimpangie Nanaa majukumu mazito yatakayomchelewesha yeye na Nanaa kutoka. Ujumbe ulifika bila shida. Nanaa akaachwa bila jukumu lolote kwa siku inayofuata. Hata hivyo mtetezi wake alikuwepo. Hakuna anayemgusa wala kumsema. Aliachwa kabisa.



Wakaagana na kwenda kulala. Aliamka asubuhi nakufanya shuguli chache kumsaidia msichana wa kazi ambaye ndio rafiki yake wa karibu.  Ndiye waliyekuwa wakilala naye na kuzungumza mambo mengi. Kwanza ni kama wote walikuwa kwenye nafasi moja wakitumika humo ndani kuanzia asubuhi mpaka usiku wanapomaliza kazi zote. Walijikuta wapo karibu kwa kuwa iliwalazimu kufanya kazi pamoja ili kupata muda wakupumzika.



Alipomaliza shuguli zake za asubuhi, akarudi chumbani kujiandaa. Akamsikia James anamwita kwa sauti. “Nipo huku chumbani kaka.” “Twende!” Nanaa akatoka. Wakasalimiana kidogo, wakatoka wao wawili tu. Mdogo wake wa mwisho, Vai alipotaka na yeye aongozane nao, James alimkatalia bila kung’ata maneno tena mbele ya wazazi wao. Akisema waziwazi anataka muda na Nanaa tu.



****************************************************



“Vipi?” James alimtupia swali mara tu baada ya kukaa. Kutokana na makuzi aliyokuzwa yakuto kusikilizwa pale anapoishi. Yeye kama msikilizaji wa mambo ya watu na kupokea amri tu, Nanaa hakuwa muongeaji sana. Wakati wote alikuwa kimya akisikiliza au kucheka tu. Na ilimlazimu kuwa mtaratibu ili asiingie matatizoni, lakini si kwa kaka yake James. Hakuwahi kumficha James jambo. Na yeye ndiye alikuwa akimsikiliza Nanaa. Alijua maisha magumu ya Nanaa, kwani alizaliwa James akiwa na akili timamu. Alimuona vile mama yake Nanaa alipokuja pale nyumbani kwao akiwa mjamzito. Manyanyaso aliyokuwa akiyapata kutoka kwa wazazi wake na Nanaa mwenyewe, yote hayo James aliyajua kwa kuyaona.



Kwa hiyo akajenga upendo wa ajabu sana kwa Nanaa. Alimkingia kifua Nanaa tokea mtoto mpaka amekuwa. Na wote walijua. Ukitaka kumuudhi James, mguse Nanaa. Hapo ndipo alimbadilikia kila mtu mpaka hata mama yake mzazi. Baba yake ndio hakutaka ukaribu na Nanaa kabisa. Usingeweza kuwakuta wawili hao sehemu moja wakiwa wanazungumza. Kama watakuwa kwenye banda la ng’ombe wakifanya kazi, basi kutakuwa kimya kabisa. Kila mmoja akifanya kazi yake. Na ilikuwa mara chache sana. Ni kama alikuwa akimkwepa Nanaa.



******************************************************



 Wakati Nanaa na Viola walipokuwa wachanga kabisa, alipoona Nanaa analia sana na hakuna wakumbembeleza, James akajifunza kumbembeleza mpaka akajua mbinu zote za kumtuliza Nanaa. Akatatua kero kubwa sana iliyokuwepo kwa wazazi wake. Kwa hiyo kila Nanaa alipokuwa akilia, yeye ndio aliitwa kumbembeleza au walimsikia akikimbia kutafuta kilio cha mtoto huyo. Hata kama ni usiku, James akimsikia tu analia, ataamka na kuhakikisha anamtuliza Nanaa mpaka anatulia. Akajifunza mambo yote ya watoto wachanga. Hakupata shida.



Kwa kuwa tayari alimuona mama yake akimlea mdogo wake Viola. Na kwa kuwa uhitaji wa malezi ya Nanaa ulitokea, James akaongeza umakini kwenye kutizama kila kitu mama yake anachomfanyia mtoto huyo mchanga, ambaye alimtafuta kwa shida sana na kumlea kwa mapenzi yote, Viola. Akaiga kila kitu na kuhamishia kwa mtoto huyo aliyekuwa ameachwa mkiwa, Nanaa. Kwa muda mfupi sana, akamudu kila kitu na Nanaa akajisikia salama mikononi mwa James, mtoto wa kiume, mwenye umri wa miaka 11 tu. Akawa kama ndiye mama yake.



Akajua kumlisha. Kumbadilisha nguo na nepi, pamoja na kumsafisha. Kila alipomuona ameachwa bila uangalizi mzuri, James alichukua hatua kwa haraka sana bila kuuliza. Kama akimkuta amelowa au amejichafua, basi James mwenyewe ndiye aliyekuwa akihusika. Akilia Nanaa, James hakupata shida. Alishajua hata na sauti zakumtuliza mtoto. Sauti ipi aitumie wapi, neno lipi lakuzungumza wapi. Kama alivyomuona mama yake anamfanyia mdogo wake Viola. Na Nanaa akamtambua James. Kwa sauti, harufu yake na sura. Akishikwa tu na James, alitulia kwa haraka sana. Ikajulikana James ndio kazi anayopenda na kufurahia. Kwa hiyo kila Nanaa alipotakiwa kuhudumiwa, aliitwa James.



Jioni alipokuwa akitoka shule, alifanya kazi zake za shule kwa haraka ili apate muda na mtoto. Alijua kitu baba yake anachotaka ni kufaulu vizuri shuleni na kwenye maisha. Sasa ili asimtenganishe na Nanaa, James akaongeza juhudi zaidi shuleni ili kusiwe na lawama. Maana baba yake alishamtahadharisha kuwa atakuwa mjinga kama akiendelea kuwa kama mama wa Nanaa. Alimlaumu sana mama yake kumruhusu James kuwa karibu na marehemu Wini kutokea mwanzoni. Akahisi James hatakuwa kama watoto wengine wakiume. Hakuwa na muda na marafiki wala michezo ile ya watoto wa umri wake.



Maisha yake yalibadilika mara Nanaa alipozaliwa. Alibeba sura ya utu uzima, na majukumu yakamwingia. Na kwa kuwa alipendwa sana hapo nyumbani, aliendekezwa tokea mdogo. Mpaka baba yake alikuwa akimsikiliza sana James. Alipoona hatari ya Nanaa kugawiwa kwa watu wa nje tokea mtoto, akawaomba wazazi wake wasihangaike tena kumgawa Nanaa, akawaahidi kuwa yeye atamuhudumia. Hayo aliyaongea akiwa bado na umri ule ule miaka 11. Baba yake alipomuuliza swala la shule. Akaahidi kuleta matokeo mazuri sana nyumbani.



Na kweli, Mungu akamfanikisha sana katika hilo eneo. James akazidi kufaulu shuleni. Wakakosa chakuzungumza. Kila alipotoka shule, alikimbilia ndani kwa Nanaa. Atamchukua Nanaa na kuanza kucheza naye wakati anakula. Kama akimkuta kama nepi imejaa, au mchafu na njaa. Atamsafisha na kumlisha kwanza ndipo na yeye akae chini ale. Wakati anafanya kazi zake za shule, atamuacha Nanaa pembeni yake akicheza. Na hapo hutamsikia Nanaa akilia. Kutakuwa na utulivu wa namna yake. James anafanya kazi zake za shule huku akizungumza naye kumfanya atulie na kucheka. Nanaa akaijua sauti ya James na kumsikiliza kwa  makini sana kama mtoto kwa mama.



Siku ambazo haendi shuleni, ndio ikawa salama kwa Nanaa. Kuanzia asubuhi utamkuta Nanaa msafi sana. Atasafishwa na James, na kulishwa. Nanaa akawa akimfahamu James hata akipita kwa mbali. Kama akiwa anacheza mahali, akimuona tu James, au akisikia sauti yake hata kwa mbali, mambo yote yatasimama. Atatambaa na kumfuata popote anapoenda au alipo. Alipoanza kutembea ndio ikawa zaidi. Angalau mama mkubwa akawa anapata msaada wa mtu mwingine kumtoa Nanaa karibu yake na mwanae.



****************************************************



Ilikuwa huzuni na uchungu kati ya James na Nanaa pale James alipofaulu na kuchaguliwa katika shule ya bweni ya wavulana Iliboru. Ilididi James kwenda kuanza kusoma kidato cha kwanza shuleni huko na kumuacha Nanaa akiwa bado anamuhitaji James. Kila alipokuwa akipata nafasi, alirudi kwenda kumuona Nanaa. Wakati mwingine alidanganya shuleni ni mgonjwa sana, ili arudi nyumbani awe na Nanaa angalau kwa siku chache tu.



Rafiki zake wote James walimfahamu Nanaa. Hakuna jinsi James ataongea stori zake, asisimulie habari za mdogo wake kipenzi Nanaa. Lakini anapoanza kumuelezea, au jinsi anavyomuelezea Nanaa, utafikiri ni mama anaeleza habari za mtoto wake. Mungu alitengeneza connection ya ajabu sana kati ya James na Nanaa. Hata Nanaa alipovunja ungo, mtu aliyemwambia ni James. James ndiye aliyekuwa akimtunza kwa karibu tokea zamani. Kila alipokuwa akipewa pesa zake za matumizi, alimgawia Nanaa kiasi na kumnunulia vitu vidogo vidogo alivyojua anahitaji. Yeye ndio alikuwa akimnunulia mpaka nguo za ndani. Kwa hiyo alipomwambia tu James kuwa amevunja ungo, akakimbilia dukani kwenda kumletea pedi. Kila alipokuwa mwezini James alijua na kuwa akimnunulia mahitaji yake yote, kumsitiri dada yake huyo, asiaibike.



Kila shule zilipokuwa zikifungwa iwe likizo ndefu au fupi, James alikimbilia nyumbani kuwa na Nanaa. Wakakuwa wakiwa na mahusiano ya kipekee na kila Nanaa alipopewa nguo za James amfulie, alihakikisha anampa pesa kidogo kama shukurani tofauti na wengine ambao walikosoa kila kitu Nanaa alichokuwa akiwafanyia.



Na hata Nanaa alipokuwa akipika, James alipita jikoni kuomba supu ya nyama kabla haijaungwa na kukaa naye jikoni akizungumza naye hili au lile ndipo aende kwenye mizunguko yake. Kwa hiyo ikajenga tabia. Kila anapochemsha nyama, Nanaa alimuwekea James supu na nyama kidogo pembeni, ndipo anapounga mchuzi wa nyumba nzima. Hata kama alichemsha maharage, basi alimuwekea mchuzi wake pembeni kabla hajaunga. James akawa ndio kiongozi wa Nanaa. Kwani alimlea tokea anakuwa. Tena alimlea kwa karibu. Ile ya kumuogesha na kumbadilisha mpaka nepi. Kwa hiyo alifuata mahusia ya James na ndiye akawa kama mzazi wa pekee kwake.



****************************************************



“Ni nini kinaendelea?” James akamuuliza tena Nanaa, wakiwa kwenye kimgahawa hicho, pembeni ya soko hilo kubwa la Kiboriloni, wakipata supu. Nanaa alimueleza James kila kitu. Kuanzia mahusiano ya wizi aliyokuwa nayo na Alex. Muda alioutumia kwenye mahusiano, makubaliano yote waliyokuwa wamekubaliana, vile alivyompeleka pale nyumbani na kuishia mikononi kwa Viola.



“Naumia sana kaka yangu. Alex na mama mkubwa ndio wananiumiza zaidi. Alex kwa kunigeuka. Ahadi zote alizonipa mimi ndizo hizo hizo anazitimiza kwa Viola. Mama mkubwa akijua wazi ubaya alionifanyia Alex na Viola, amewapa baraka zake zote. Yaani mimi ndio nadeki matapishi ya Viola! Yaani namuhudumia kwa ujauzito aliopewa na aliyekuwa mpenzi wangu! Si sawa kaka. Na ninahisi ananifanyia makusudi kabisa. Viola anaweza kunipigia simu usiku, wakati nimelala, eti niamke nikampelekee maji ya kunywa chumbani kwake. Siku akikosa yeye usingizi, najikuta ninakesha naye usiku kucha mpaka yeye alale. Nikishindwa kuamka mapema akiniita, anakwenda kulalamika kwa mama mkubwa, basi hiyo siku itakuwa mbaya sana kwangu.” Nanaa alikuwa akiongea huku anatokwa machozi.



James aliumia sana. “Unajua sikuwa najua kama Viola ni mjamzito!? Ndio maana ananikwepa sana. Hataki hata kupishana na mimi tokea jana nilipofika pale nyumbani. Nikajua labda ni kwa kuwa niliwafukuza kule kwangu na kuwarudisha huku nyumbani. Tena kwa hasira sana na kumuonya mama wasiwahi kurudi tena Dar, nyumbani kwangu. Sasa nikashangaa leo asubuhi mama ananiambia eti Viola amepata safari ya gafla, amesafiri. Kumbe ananificha ujauzito wake! Kwa nini mama anatoa baraka zake kwa Viola mtoto mdogo? Na shule?” James aliuliza kwa hasira kidogo.



Akiwa anataka kuuliza kwa nini aliwafukuza Viola na Vai, nyumbani kwake Dar, akaona ni heri aeleze shida zake kabla James hajaondoka hopo mjini Moshi kurudi kwake jijini Dar. “Matokeo yetu yametoka, kaka. Yeye amepata daraja la 4, mimi la pili. Kinachoniuma zaidi ni kule kusimangwa mimi na matokeo yangu, halafu yeye anapewa sifa zote. Wenzangu wote wameanza kutuma maombi ya chuo kaka, lakini mimi nimeshindwa. Sina pesa kaka. Mama mkubwa anasema amefika mwisho, na Vai naye anatakiwa aende shule. Wakati najua wazi Vai amekataa shule.” “Nini?” James alizidi kuchanganyikiwa. Asiamini yanayo endelea hapo nyumbani kwao. Wazazi aliojua ni wakali sana kwake na Nanaa, ni kama wamebadilika kabisa. Au sio hao wanao lea wadogo zake.



“Vai ameacha shule. Wamekuja kugundua hata mitihani ya kidato cha nne hakufanya. Alikuwa anadanganya kuwa anasubiri matokeo, kumbe alishaacha shule muda mrefu tu. Aliwaandikia barua shuleni kwao. Akijidai yeye ndio mzazi, kuwa anahamishwa shule. Akafanya taratibu zote za uhamisho. Akatoa namba ya simu ya mwanaume wake, huko shuleni, akijidai baba mkubwa amebadili namba na anataka ahame shule akamalizie kidato cha nne shule nyingine. Sijui aliandika shule gani huko ya bweni. Barua zilipokuwa zikija pale nyumbani za uhamisho aliokuwa ameshugulikia wakati anamaliza muhula wa kwanza wa kidato cha nne, akawa anazifungua mwenyewe, anazichoma moto. Kwa hiyo shuleni wakajua wamewasiliana na wazazi wake na wamekamilisha taratibu zote za uhamisho, kumbe ni yeye. Shule zikafungua ili amalizie hiki kidato cha nne, akawa anatoka nyumbani asubuhi kama kawaida. Tena akiwa amevaa sare zake za shule na kurudi jioni. Hakuna aliyekuwa akijua alipokuwa anaenda, lakini mpaka akamaliza muhula. Ada akawa amepewa, na michango isiyoisha akawa anaomba pesa hapo nyumbani kwa baba mkubwa, halafu anarudisha risiti za shule kama kawaida. Kumbe hata shuleni kwenyewe hakuwa akienda katika kipindi chote hicho mpaka wenzake wakamaliza kidato cha 4. Baba Mkubwa alimpiga karibu ya kumuua. Akatoroka pale nyumbani kama mwezi, akarudi. Amesema kabisa yeye hataki shule.” James alibaki kimya kwa muda. Nanaa alimuona amebadilika mpaka sura yake.



 “Wewe unataka kuendelea na shule?” “Natamani kaka. Sina jinsi nyingine ya kujikwamua maishani ila shule. Halafu sio kama nimefaulu sana, nahofia kukosa nafasi za chuo kama nitaendelea kuchelewa. Mwaka huu watu wamefaulu sana.” James alifikiria tena kidogo. “Jiandae, wakati naondoka kesho kutwa, tunaondoka wote.” Nanaa hakuamini. “Lakini Mama mkubwa hawezi kukubali, kaka. Nani atafanya kazi pale ndani? Yule dada wa kazi anakaribia kuondoka. Amesema mwezi huu ndio mwisho, na yeye anaenda kuolewa.” “Usiwe na wasiwasi. Wewe jiandae. Mambo mengine niachie mimi.”  Wakatoka pale James akiwa amekasirika na kuumia sana moyoni, lakini akawa mtulivu mbele ya Nanaa.



Alimwambia wakazunguke madukani kidogo. “Una kitu chochote unahitaji?” James alimuuliza Nanaa. “Nina shida na begi, kaka. Sitakuwa na sehemu ya kubebea vitu vyangu.” “Unataka begi kubwa au dogo?” James aliuliza tena. “Kwani nitarudi lini?” Nanaa aliuliza kwa wasiwasi kidogo akitamani kuambiwa asirudi tena pale kwa mama yake mkubwa. “Wewe tu.” James alijibu kwa kifupi na mafumbo. “Kwa hiyo hata nikitaka kuishi na wewe huko huko ni sawa?” James alicheka. “Mpaka utakapo pata kwako. Sio ubweteke.” “Mbona nakuelewa kaka. Ulisema hakuna kutulia mpaka nipate changu.” “Kumbe bado unakumbuka? Endelea kupambana. Sasa chagua begi unalotaka na kitu kingine kimoja kama zawadi yako ya kufaulu kidato cha sita.” “Kweli kaka? Kwani hapo ndio nimefaulu?” James alicheka. “Umefaulu vizuri tu. Hutasumbuka sana kupata chuo. Hongera.” Nanaa aliipokea hiyo pongezi kwa shingo upande akijua vile James alivyo na akili ya darasani, akajua pale anampa tu moyo. Wakati wote alikuwa akipata alama za A tu. Hakumbuki vinginevyo.



Kila matokeo yake yalipokuwa yakitoka. Ripoti zake zilipokuwa zikitumwa nyumbani, baba yake alikuwa akizifungua na kumkabidhi James mwenyewe. Na yeye alikuwa lazima ampelekee Nanaa amuonyeshe. Wakati wote alimwambia Nanaa, na yeye anaweza kufaulu vile vile. Alikuwa akimuonyesha mpaka mitihani yake. Vile alivyokuwa akifaulu vizuri. Nanaa akawa anapata moyo, anajua ataweza tu.







Tumaini jipya kwa Nanaa.

Hakujua kaka yake alifanyaje. Au aliongea nini na mama yake mkubwa, lakini wakati wamekaa mezani wote wakila, James akaingia na baba yake usiku ambao kesho yake walijua anaondoka. Alikuja siku ya ijumaa usiku, jumamosi hiyo ndio alikuwa anazunguka na Nanaa mjini. Jumapili walipotoka kanisani, alimuomba baba yake amsindikize kwa bibi yake huko kijijini. Walishinda huko kwa bibi yake siku nzima ndipo wakarudi usiku, akasema anaondoka siku ya jumatatu asubuhi.



Akamwita Nanaa. “Nataka leo uwahi kulala, tunaondoka asubuhi sana kesho. Hakikisha unabeba vitu vyako vyote. Nataka ukifika kule utulize mawazo shuleni. Sio tena safari za kurudi huku kufuata vitu ulivyosahau.” Nanaa alitamani kushangilia, lakini palikuwa na ukimya mkubwa sana hapo, kila mtu akiwasikiliza.



“Unanisikia Nanaa?” James aliuliza. “Nimesikia kaka.” “Haya, naomba umalize kula hapo, kisha unyanyuke. Nenda moja kwa moja kwenye gari na wala si jikoni kuanza kuosha vyombo au kuanza shuguli tena. Chukua begi nililokununulia la zawadi yako ya kufaulu vizuri kidato cha sita. Lipo nyuma kabisa ya gari. Kakusanye vitu vyako vyote. Weka kwenye hilo begi, halafu uje uniite. Nitalibeba usiku huu huu, nikalifungie kwenye gari. Bakisha nguo za kuvaa kesho safarini tu. Mizigo yote italala kwenye gari. Umesikia?” “Sawa kaka.” Chakula hakikulika tena kwa furaha. Hakutegemea kama ataruhusiwa kuondoka kwenye ile nyumba.



James anaingia na kumtangazia uhuru! Ahadi ya maisha mapya na kutimiziwa ndoto za kuendelea na shule! Bado kwake ilikuwa ni ndoto. Pale pale akasimama. “Chukua funguo za gari hizi hapa.” James akamrushia Nanaa fungua. Akadaka. “Nilikwambia begi lipo kwenye trunk?” “Ndiyo, kaka.” Nanaa akaitikia kwa furaha zote. “Haya, God’s speed! Fanya kwa haraka uwahi kulala. Nataka tuwahi sana kuondoka. Kesho mchana, natakiwa niwepo ofisini kwangu.” Sio kwamba ni begi jipya ambalo Nanaa hakulijua. Ni lile lile alilomnunulia walipoenda naye madukani. Lakini walikubaliana walifiche mpaka safari itakapokuwa tayari.



Nanaa alikimbilia kwenye gari ya kaka yake. Ilikuwa ni gari aina ya Toyota RAV4, ya kisasa ya mwaka 2017. Ya rangi ya silver. Safiii. Ikionekana inatunzwa vizuri. Nanaa alimjua kaka yake kwa usafi. Akafungua gari huku haamini kama kweli kwa mara ya kwanza maishani atatoka katika ule mji wa Kilimanjaro. “Mmmh! Ngoja nijitulize kwanza. Chochote chaweza tokea, nikazuiliwa kuondoka na kaka. Mungu nisaidie.” Nanaa akawaza. Akatoa begi lake akarudi ndani akiwa mtulivu kama hakuna kinachoendelea rohoni mwake.



 Akarudisha funguo  kwa kaka yake, akakimbilia chumbani. Alikusanya kila kitu chake mpaka jiwe la kusugulia miguu, akaweka kwenye kilo begi. Hata hivyo hakuwa na vitu vingi sana. alishakwenda shule zote alizowahi kusoma akachukua matokeo yake, akisubiria muujiza wa kupata pesa aanze kutuma maombi vyuoni. Lakini akashindwa mpaka James alipokuja na kumwambia wanaondoka wote. Alivitazama vile vyeti, akaviweka kifuani, asiamini kama yale makaratasi aliyoyakumbatia, ambavyo ndio vyeti vyake vya tokea shule ya msingi, ndio vimefanyika tiketi ya kumtoa hapo kwenye hiyo nyumba. “Naenda Dar mimi Nanaa, mtoto wa Wini! Kweli shule umekuwa mkombozi wangu.” Nanaa aliendelea kuwaza. Akavibusu vile vyeti. Akavitazama kana kwamba vitazungumza jambo lolote. Akajicheka na kuviweka ndani ya hilo begi.



Aliporidhika kuwa vitu vyake vyote vipo ndani ya hilo begi, akatoka nalo. “Nilikwambia uniite Nanaa. Wewe vipi? Utavunja mgongo.” James alisimama kwa haraka mara alipomuona Nanaa anatoka na begi lake. “Nimeona sio zito.” “Ngoja nikusaidie. Wewe nenda kaoge, upumzike. Mimi nitaliweka kwenye gari. Asubuhi ya saa 10, nitakuja kukugongea. Uwe tayari. Hata chai tutakunywa njiani, usije kuamka na kuanza kupika tena.” Nanaa akacheka. “Muone alivyo furahi.” “Asante kaka.” “Si unakumbuka nilikwambia shule itakutoa chini na kukuketisha na wakuu? Sasa hayo ndio matunda yake. Hongera sana.” James aliendelea kujivunia Nanaa mbele ya wazazi wake, Vai na msichana wa kazi. “Asante kaka, nimeona.” Nanaa akaitika huku anacheka. Ile nyumba ikageuka kuwa kama kuna msiba. Watu wote walikuwa kimya wakimsikiliza James na Nanaa. Nanaa alikuwa anacheka mpaka dimpozi zake zilikuwa zikionekana.



******************************************************



Hakuna aliyeweza kumgusa Nanaa, kama James akiwepo. Walishamjua anamtetea Nanaa tokea mtoto. Alimzungushia wigo wa ulinzi na utetezi ambao huwezi hata kumuonya Nanaa, akiwepo yeye. Hakuna aliyemuona anastahili kuzungumza na Nanaa ipasavyo. Alijua ni uonevu tu kwake. Lakini yeye mwenyewe alikuwa akizungumza naye sana. Na mara nyingine alikuwa mkali sana kwake lakini hakutaka mtu mwingine aingilie. Alikuwa akisema hakuna anayemfahamu Nanaa, kwa hiyo huwezi kurekebisha kitu usichokifahamu. Kaka huyo mtulivu, aliyebeba haiba ya utu uzima, watu waliujua ukali wake James, pale unapomgusa Nanaa. Aligeuka kuwa kama mbogo, na mama yake alijua. Kila anapokuwepo James, Nanaa aliachwa kabisa.



******************************************************



Msichana wa kazi alimfuata Nanaa chumbani huku analia. “Unaniacha Nanaa! Na mimi naondoka kesho tu, wewe ukiondoka.” Nanaa alianza kucheka. “Ukiondoka watachanganyikiwa.” Nanaa alishabikia. Wala hakumkataza asiondoke. Usiku huo ukawa wakuagana. Nanaa alikuwa amechagua zawadi ya taulo kubwa jeupe. Ndilo aliloomba kaka yake amnunulie. Kwani alikuwa akijifutia khanga wakati wote kila akimaliza kuoga. Kwa hiyo akatamani taulo jipya. Akajimbia zawadi yake ya kufaulu kidato cha 6, kutoka kwa kaka yake ni taulo tu. Na kweli James akamnunulia pamoja na hilo begi. Kwa hiyo usiku huo wa furaha, Nanaa alioga na kujifutia taulo jipya, kubwa na jeupe. Tayari moyo wake ukaanza kuonja raha ya kule aendako.



******************************************************



James alikuja kumgongea Nanaa saa 11:30 asubuhi. “Mbona umepooza tena?” James alimuuliza Nanaa. “Ingia huku chumbani kaka.” Nanaa akamvuta mkono James, akaingia ndani akafunga mlango. “Ujue nimeamka asubuhi kujiandaa, sijamkuta Maria, huyu dada wa kazi! Nimeenda kumwangalia mpaka kwenye banda la ng’ombe, hayupo. Nimerudi humu ndani kuangalia begi lake. Ona. Hamna vitu vyake hata kimoja. Ametoroka. Jana alikuwa analia hapa kuwa namuacha peke yake, hataweza kazi.” Nanaa alikuwa ananong’ona. “Sasa hayo sisi hayatuhusu. Twende ukawaage. Tuondoke sasa hivi.” Nanaa akaanza kucheka taratibu. “Kaka wewe! Nani atawasaidia kazi? Ujue Vai na Viola hawajui hata kuosha vyombo?” “Najua. Si walikuja kuishi na mimi Dar. Sasa unataka kubaki uwasaidie?” “Akuuu!” Nanaa akajibu kwa kukataa huku akipandisha mabega. James akacheka. “Ndio tuondoke sasa.” Wakatoka.



Nanaa aondoka Moshi ahamia jijini Dar kutimiza ndoto zake.

Hakuwa akiamini wakati kaka yake akitoa gari pale kwenye nyumba aliyolelewa na kukuzwa kwa masimango mengi. Asiamini kama siku hiyo ndio mwanzo wa kuachana na Viola, Alex, baba mkubwa na mama mkubwa. Nanaa alibaki akiangalia dirishani huku machozi yakimtoka. Hewa safi iliyokuwa imeenea humo ndani ya gari ya kaka yake, ilimtuliza roho yake na kujua kwa hakika anaenda kuanza maisha mapya na mazuri.



Njia nzima alikuwa akijaribu kuainisha aina ya changamoto ambazo labda atapambana nazo huko jijini Dar, akajikuta anajiaminisha kuwa ataweza tu. “Kama nimeweza kuishi pale kwa mama mkubwa, naamini hakuna nitakaposhindwa kuishi.” Nanaa aliendelea kuwaza wakati kaka yake akiendelea kukanyaga mafuta kuwahi jijini Dar. Maisha yakaanze kwa Nanaa na yeye awahi kazini siku hiyo ya jumatatu.































































Nanaa Jijini.

N

anaa alitua jijini Dar akiwa na James, ambaye alikodisha nyumba ya vyumba viwili na alikuwaakitumia gari ya kampuni akiwa jijini. Gari yake hiyo aliitumia siku za weekend tu kwenye shuguli zake binafsi. Alibahatika kazi kwenye kampuni moja ya simu kama muhandisi. Alisomea mambo ya “Eletronics Engineering”. Kwa hiyo alikuwa na kazi nzuri, na maisha yakueleweka. Lakini kwa kuwa alikuwa na akili ya maendeleo, bado alikuwa kwenye kuwekeza. Kwa hiyo hakuwa na pesa nyingi mkononi. Lakini alijitahidi kuishi maisha ya kawaida tu kama mtu msomi mwenye mshahara mzuri.



Alikuwa na kijana aliyekuwa akifika kumsaidia usafi nyumbani hapo, lakini Nanaa akaanza kushika usukani. Alimfulia, akampikia kaka yake na bado aliweza kufanya usafi ndani na nje ya hiyo nyumba ndogo, bila shida. Kwa kuwa walikuwa wakielewana tokea zamani, furaha na amani havikukosekana ndani ya hiyo nyumba yao.



James alitoka asubuhi na mapema, na kurudi usiku. Wakati mwingine alichelewa kurudi na kumkuta Nanaa alishalala, ila ameachiwa chakula mezani. Alimsaidia Nanaa kufanya maombi ya kujiunga katika vyuo mbali mbali pale jijini, na kumsisitiza kuomba na chuo kikuu cha Dodoma na Mzumbe. “Huwezi jua utabahatika wapi. Tupia ndoano kila mahali.” James alimtia moyo. Na kweli Nanaa alituma maombi kwenye vyuo vingi tofauti tofauti. Akafanikiwa kupata nafasi katika chuo kikuu cha Mlimani. James alimsaidia kufuatilia mkopo, Nanaa akapata mkopo wa asilimia 80, James akaahidi kumalizia.



Nanaa, Chuo Kikuu Cha Mlimani.

Shule ya Nanaa ikaanza. Akabadilika, kama siye Nanaa aliyekuwa akiishi mkoani Kilimanjaro. Akanoga na kuiva kwa joto la jijini Dar. Nanaa huyu ni Nanaa aliye huru. Anayejifikiria mwenyewe. Kutoka kwenye manyanyaso mengi. Kazi nyingi mfululizo, leo yupo hosteli! Peke yake. Anajiwazia yeye tu. Kuanzia akiamka asubuhi mpaka usiku anakwenda kulala, jukumu lake likawa ni shule na yeye peke yake. Pesa ikaanza kuingia. Kutoka  bodi ya mikopo na kwa kaka yake. Akaanza urembo wa nywele na kucha. Akatafuta sehemu wanazouza mitumba, akaanza kuvaa vizuri. Akawa anapendeza na kuvutia.  Wakati wote utakaomuona Nanaa, alikuwa msafi. Kuanzia kichwa ambacho alikisuka wakati wote. Kama si rasta, basi alishonea weaving. Hakuacha nywele zake hivi hivi. Alizaliwa na kipilipili kikavu sana. Kwa hiyo wakati wote alizisuka nywele zake. Miguuni na mikononi, safi wakati wote.



Urembo, uzuri na unadhifu wa Nanaa haukujificha kwenye macho ya wengi. Hata wenzake wakaanza kumsifia kuanzia rangi ya mwili wake, umbile na kila kitu mwilini mwake kilipewa sifa. Wanaume wakaanza kuvutiwa. Kila mmoja aliyebahatika kumuona, alitaka na kuota kumiliki penzi la Nanaa. Kuanzia wenzake wa mwaka wa kwanza mpaka wa ngazi za juu. Kila mmoja akajitosa kwa wakati wake. Wakimtaka Nanaa aliyeumizwa, kimapenzi. Huku akiwa na hofu ya kuumizwa tena, lakini bado shauku ya kuja kuwa na kwake na wake, haikumwisha moyoni. Ni kweli Alex alimuumiza, “lakini si wanaume wote ni wabaya bwana!” Nanaa alijiambia.



Haiba yake ya kupenda kucheka na kuwa msikilizaji mkubwa ikawavuta hata wa kina dada wa darasani kwao. Akajikuta ameingizwa katikati ya marafiki wawili wa muda mrefu. Zena na Tia. Waliokuwa wameanza urafiki wao tokea shule ya sekondari. Wakatengeneza kundi dogo la marafiki watatu. Akawa Nanaa, Zena na Tia. Na wote wakajikuta wamepata chumba kimoja ‘main campas’, Hall 3. Lakini siku za weekend mara moja moja na likizo Nanaa alikuwa akirudi nyumbani kwa James. Kipindi cha mitihani alikuwa akipotea kabisa hapo nyumbani. Lakini James alikuwa akielewa na kufurahia juhudi za dada yake. Alimsisitiza kutulia na kuweka akili chuoni.



Nanaa na penzi la Zac chuoni.

Kadiri siku zilivyozidi kwenda ndivyo alivyozidi kusitasita kwenye njia mbili katika kufungua moyo kwa mwanaume mwingine. Lakini Zac akawazi wenzake. Yeye akawa king’ang’anizi kweli kweli. Hodi na zawadi tofauti tofauti na za mara kwa mara kwa Nanaa, chumbani kwao hazikukoma.  Kama Zac hakumkuta chumbani hapo, basi aliacha zawadi hizo chini ya mto anao lalia Nanaa, kitandani kwake. Ilimradi tu kuonyesha kumjali na kuwa anamfikiria wakati wote.



Zac alikuwa mwaka wa mwisho, wakati Nanaa ndio yupo mwaka wa kwanza. Hilo nalo likaongeza nafasi ya kuanza kufikiriwa yeye na Nanaa zaidi ya wengine wote. Nanaa akaanza kumpigia mahesabu. “Naona huyu atanifaa. Si kwa kujali huku!” Nanaa alijiambia huku akicheka moyoni na tabasamu kubwa usoni, mara baada ya kurudi chumbani kwao na kina Tia kumwambia anamzigo chini ya mto, kitandani mwake. Uliokuwa umeachwa na Zac masaa machache yaliyopita.



Wenzake wote walikaa huku wamemkodolea macho, kuona kile alichokuwa ameletewa safari hiyo. Nanaa akatoa kwa madaha yote. Zilikuwa chocolate nzuri aina ya ‘Godiva’.  Zilibeba umbo la moyo mkubwa na ndani yake zilipangwa chocolate 32 zenye ladha tofauti tofauti ikiwemo caramels, dark chocolate, milk chocolate na truffles. Kila mtu alitoa macho. Hata Nanaa mwenyewe alishangaa. Ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kuletewa zawadi ya chocolate. Kwake pia yalikuwa mageni. Akajisikia vizuri mbele za wenzake. Akaanza kuwagawia ili nao waonje.



“Kweli huyu ndio wakunioa. Kwanza atamaliza chuo mapema, kabla yangu. Atapata kazi, na kutafuta sehemu yetu ya kuishi pamoja mara baada ya harusi yetu. Yaani hapa namaliza chuo, naenda kwangu sio narudi tena kwa kaka.” Nanaa akaendelea kumpigia mahesabu usiku huo huku akila chocolate zake.



Ujumbe wa shukurani kwa chocolate nzuri alizofurahia yeye na wenzake kwa Zac, ndio ukawa mwanzo wa mawasiliano na penzi zito kati yao. Shule na mapenzi vikaanza kwenda pamoja. Zac alionekana kumpenda sana Nanaa. Kama kwa mara ya kwanza, Nanaa akapata mwanaume anayemjulia. Hakutaka amuone Nanaa akiwa mnyonge. Wakati wote alipokuwa naye, alimuweka mikononi mwake. Popote na mbele ya yeyote, alimkumbatia Nanaa na kunyesha mvua ya mabusu.



Nanaa alipoona Zac ni mwaname wakueleweka, akamsimulia kaka yake, James juu yake. “Mbona sasa humleti nyumbani?” James aliuliza. “Tumepanga akimaliza chuo, ndio tujitambulishe rasmi kwa pande zote.” Nanaa aliongea na tabasamu usoni. “Kumbe mpo serious?” James alishangaa kidogo. “Huyu anaelekea kaka. Ameapa kunioa, na ananipenda sana na kunijali kuliko nilivyowahi kufikiria. Naamini safari hii Mungu amenifuta machozi.” James aliuona uso wa dada yake vile ulivyojaa furaha ukionyesha kutulia, akajua ni kweli amepata kijana wakueleweka.



************************************************



Lakini hakuachana na rafiki zake hao wawili. Zena na Tia. Urafiki ukanoga. Alipokuwako Tia, ndipo utampata Zena na Nanaa. Waliongozana kila mahali. Wakati Nanaa yupo na Zac, Zena hakuwa amepata mwanaume bado, na Tia alikuwa na mpenzi wake, Evan aliyekuwa akisoma SUA, mjini Morogoro. Wakati mwingine alikuwa akija jijini kutembea nyumbani kwao na kuona rafiki zake pia hapo Chuo kikuu Mlimani na IFM. Tia, Nanaa na Zena hawakuacha kujumuika na Evan na kundi la marafiki zake. Kama ni siku za weekend, basi watatoka kwenda kumbi na sehemu za starehe pamoja, wao kama kundi.



Ikitokea kama wanatoka siku za weekend au kwenye vilikizo vifupi ambavyo kaka yake anajua angekuwepo nyumbani kwake, na Nanaa akajua kuwa watachelewa kurudi, au watapanga kwenda mahali watachelewa, basi alimtaarifu kaka yake, na kuishia kulala chuoni bila kurudi nyumbani kwa kaka yake. Na mara nyingi Evan anapokuwa jijini, basi Tia ambaye na yeye alifaulu kutokea shule ya wasichana Iringa, na wazazi wake walikuwa wakiishi Iringa mjini, alitumia siku hizo bila shida, kulala popote anapotaka Evan mpaka Evan atakaporudi chuoni.



Evan na Tia.

Evan mtoto wa jijini. Alizaliwa hapo hapo Dar. Lakini shule ya secondary alisomea Tosamaganga, huko huko Iringa. Enzi hizo shule hizo mbili, Iringa girls na Tosamaganga walikuwa maswahiba. Ikitokea kuna mziki kwenye shule hiyo ya wasichana wa sekondari ya Iringa, basi shule ya wanaume watakayo karibishwa ni Tosamaganga. Na hivyo hivyo upande wa shule hiyo ya bweni ya wavulana, Tosamaganga. Wasichana wao walijulikana kama ‘Iringa girls’.



Wakati Tia na Zena wanakaribishwa kidato cha 5, kama ilivyo ada. Sherehe nzuri ya shule ilifanyika. Shule ya wanaume Tosamaganga ikakaribishwa ili kuja kucheza mziki shuleni hapo. Na hapo ndipo Evan na Tia walipokutana kwenye mziki. Yeye Evan akiwa kidato cha 6. Japokuwa wote wawili hawakuwa na watu wakucheza nao, washamba kabisa. Zena mtoto aliyetoka kwenye nyumba ya wazazi walioshika dini, Tia mtoto hapo hapo Iringa. Lakini hakuwahi hata kuingia Club. Wakakusudia siku hiyo wasipitwe. Japo waingie kuosha macho. Kujua kinachofanyikaga humo ndani ya mziki.



Walipofika kwenye mziki ndipo Evan akatokea na kumuomba Tia, pale pale ukumbini wacheze pamoja. Zena na Tia waliangaliana na kucheka kwa aibu. Kisha Tia akamgeukia tena Evan na kuuliza akiwa hana uhakika sana, kwani hata wao wenyewe walijua kati ya wasichana wote waliokuwepo pale ndani, wao walikuwa wasichana wa kawaida sana kuliko wenzao. “Unamaanisha mimi?” Tia aliuliza huku akijinyooshea kidole huku akijicheka. Evan alicheka kwa kujiamini. Mikono mfukoni. “Ndiyo. Nimeomba tucheze wote.” Tia alimgeukia Zena kwa mshangao. Akiwa haamini.



Evan hakuwa amekurupuka hata kidogo. Yeye na marafiki zake, walishamuona Tia na Zena wakiwa wamekaa peke yao wanacheka kitoto huku wakishangaa jinsi wengine wanavyocheza. Walionekana ni wasichana wenye mambo ya kitoto. Evan aliwaambia wenzake anakwenda kuzungumza na mmoja wao bila kuamua ni yupi kabla. Lakini kadiri alipokuwa akiwasogelea, ndipo macho yake yakavutiwa na Tia.







Zena na Tia.

Tia na Zena walikutana siku ya kwanza kabisa walipowasili shuleni hapo. Zena akiwa anatokea jijini Dar, na Tia hapo hapo mjini Iringa. Wote waliletwa na baba zao. Wakati wazazi wakilipia ada ya shule, wakajikuta wamebaki wao peke yao. Ikabidi wasalimiane. Wakajikuta wote wanapenda kucheka hata pasipo sababu. Kule tu kujitambulisha mimi naitwa Zena, natokea Dar, tayari cheko. Bila kujijua na Tia naye akaanza kucheka wasijue wanacheka nini. Mvua ilikuwa ikitaka kunyesha. Wazazi walipomaliza taratibu zote za kuwasajili watoto wao wakataka kuwaaga. Baba yake Zena kuwahi usafiri ili akajipumzishe hotelini, na baba yake Tia kwenye gari lake.



Walipotoka na kukuta watoto wao wakicheka kama ndege, ikabidi wafahamiane. Mzee Hiza, ambaye ndiye baba yake Zena aliposema anakimbilia hotelini kabla hajalowa, ndipo baba yake Tia, Mzee Sonzigwa alipomwambia, kamwe mkewe hatamsamehe, kama akisikia aliacha mgeni akalale hotelini na si nyumbani kwao. Hapo ndipo Zena alipojua wapi Tia alipata utundu. Mzee huyo alikuwa mzungumzaji tofauti na baba yake, Mzee Hiza, swala 5. Alikuwa mtulivu sana. Kikubwa alichoweza kufanya ni kushukuru na kucheka tu.



Mzee Sonzigwa alimchukua baba yake Zena, wakaondoka na kuwaacha Tia na Zena wakipelekwa bwenini na kiranja aliyekuwepo zamu siku hiyo. “Baba yako anaonekana mpole!” Tia alisifia. “Sasa ngoja uje ukutane na mkewe. Ndio utauliza walikutana wapi.” Tia akacheka. “Kwani yukoje?” Tia alihoji huku akijiandaa kucheka. “Unamjua kasuku?” Tia aliangua kicheko bila kutoa jibu. “Basi ndio Mama Hiza. Hakuna asiyemjua pale mtaani kwetu. Kwanza hakujaliwa aibu. Hana cha mgeni wala mwenyeji. Akianza jambo, hamalizi. Mshari, hujawahi ona. Usithubutu ukamuanza. Utajuta.” Tia alizidi kucheka. “Sasa baba yako anasemaje?” “Kama vile ulivyomuona. Yeye ilimradi aswali. Basi. Anabaki akimsikiliza tu mkewe. Humuwezi mama Hiza. Watoto wote wanao anza kuongea pale mtaani wanajua kutamka mama Hiza.” Urafiki ukanoga kati yao. Wakajikuta darasa moja mpaka wakafaulu chuo kikuu. Hawakufanya kosa. Wakahakikisha wapo chumba kimoja hapo Hall 3. Na kukusudia kumuongeza Nanaa kwenye kundi lao.



************************************************



Kwa kuwa walikuwa watundu sana na wachokozi, hawakuacha kumtania Nanaa. Walipenda umbile lake na hawakuacha kumtupia neno kila Nanaa anapoingia darasani kana kwamba hawakuwa wakitoka chumba kimoja. Mbaya zaidi, awe amechelewa na wao  wawe wamewahi lecture. Wataanza, “Jamani mmemuona Nanaa ameingia?” “Nanaa wa ukweli.” Tia atarusha neno jingine kumuunga mkono shoga yake Zena.



 “Nanaa wakuvutia bwana!” Zena ataongeza. “Hana atakachoweka mwilini, Nanaa kikamchukiza.” “Nanaa Mashallah!” “Nanaa wa dimpozi.” “Nanaa wa mitego!” “Nanaa wakuumiza mioyo!” “Nanaa ndoto ya wengi!” Zena na Tia watapokezana maneno huku watu wakicheka, na Nanaa akicheka na kutingisha kichwa. “Hivi nyinyi mlifikaje hapa Mlimani?” Mara zote Nanaa aliwauliza.



************************************************



Siku moja, kabla ukaribu wao haujachanganya. Bali kulala chumba kimoja tu. Wakimuona Nanaa akiwasikiliza na kucheka wakiwa chumbani, na darasani kuwa kama hayupo. Zena na Tia walimwandikia Nanaa barua, na kuamua kuisoma mbele ya darasa zima wakati profesa aliyetakiwa kuingia kwenye kipindi, kuahirisha kipindi hicho. “Jamani! Kuna barua rasmi kwa Nanaa. Sisi kama wapenzi wa Nanaa, tutaisoma.” Zena aliongea kwa sauti kufanya wale waliokuwa wanataka kutoka darasani wasubiri na kuwasikiliza. Nanaa alijiweka sawa, akabaki akiwatizama. Tia na Zena walijulikana kwa vituko. Swali likawa, wakiwa wao wawili peke yao, wanaweza kuzungumza kitu cha maana?



“Kwa Nanaa! Kutokana na tabia ya wanaume wa hapa mjini, kupenda wasichana kama wewe. Na mimi ndugu yako Zena, kushindwa kubahatika kumvutia hata mmoja wao. Kamati ya Tia na Zena, imetafakari kwa kina. Imefikia maamuzi yafuatayo.” Tia na Zena wakatizamana. Wote wakiwa wamesimama mbele ya ukumbi huo wa lecture. Wakaweka sura za kazi. Tia akiwa msomaji, Zena akampa maji, kama kusafisha koo, kisha Tia akaendelea. “Tumeazimia yafuatayo. Nanaa atakuwa rafiki wa Zena. Haraka iwezekanavyo. Tia akiwa katikati yao. Kwa haraka sana, ni lazima Nanaa ahakikishe kila anapokwenda kula, maktaba, au kutembea kokote kule, lazima Tia na Zena wawepo.” “Umesahau kuweka, endapo ataweza kuniunganisha na kaka yake, basi afanye hivyo mara moja. Ili kunusuru hali ya upweke, na kunitoa nyumbani kwa mama Hiza.” Zena aliingilia na kuongezea huku akiwa uso usio na masihara hata kidogo. Watu walizidi kucheka.



Wakiwa mwaka huo huo wa kwanza, tena wote wakiwa wageni hapo chuoni. Watu wakiwa bado wanaogopana hapo darasani. Wakipeana heshima. Hawajuani vizuri. Zena na Tia, binti hao waliokwishajulikana ni watundu wa kupindukia. Walinyimwa hofu kwa yeyote, wakafanikiwa kumvuta Nanaa katikati yao na kumfanya rafiki. Maisha yakazidi kuleta ladha kwa Nanaa. Marafiki waliomfanya acheke wakati wote na mpenzi Zac! Hakuna jinsi ungemwambia Nanaa amekosea maisha au alizaliwa kwa bahati mbaya, akakubali.



************************************************



Evan alipokuwa akija kwa Tia hapo chuoni, alikutana na Zena na Nanaa. Utundu mwingi, maneno yasiyoisha na stori nyingi vuliwavutia hata rafiki wa Evan pia. Wakikosekana kina dada hao kati yao, lazima wauliziwe ndipo kikao kinanoga. Evan alikuwa akifika chuoni hapo na gari la baba yake akiwa na rafiki zake. Basi kitawekwa kikao mahali. Watacheka mpaka wanaagana au wakati mwingine aliwatoa wote watatu na kwenda kukutana na marafiki zake huko club. Starehe zinaendelea.



Mwanzoni Nanaa alijitahidi kutolemea upande mmoja. Lakini akajikuta upande wa Zac unaanza kupendelewa zaidi kadiri siku zilivyozidi kwenda na penzi lilivyozidi kuwa zito. Ikawa ikimlazimu wakati mwingi wa weekend, ambapo alizoea kuwepo na kina Tia na Zena, kuwepo Mabibo hosteli ambako alikuwa akiishi Zac mpenzi huyo mpya.



Walipokuwa wakimlalamikia, alijitahidi kutoka nao japo kwa masaa machache na kurudi kwa Zac. Ikitokea wamechelewa kutoka kwenye starehe, Nanaa na Zena watarudishwa hosteli. Siku inayofuata kama bado ni weeked, basi Zena atarudi kwa mama Hiza, Nanaa kwa kaka yake au kwa Zac. Wakati Tia akitumia siku hizo, mchana na usiku na Evan. Maisha yakaendelea.



Wakati mwingine watatu hao walipochoka na kusoma, walikwenda kwa Mama Hiza kwenda kucheka. Wakazoeleka nyumbani kwa kina Zena. Na kila walipokuwa wakiondoka mama Hiza, mjuzi wa vitafunio hakuacha kuwatengenezea vitu kadhaa vya kurudi navyo chuoni. Walimpenda mama huyo kwa stori nyingi na vichekesho. Wakati mwingine wa weekend kabla hawajatawanyika, walimpigia simu kujua kama yupo nyumbani au la. Basi akiwaambia yupo, wote wataingia kwenye gari mpaka Tankibovu, nyumbani kwa kina Zena. Kwenda kumsalimia mama huyo, japo kwa dakika chache tu ndipo Nanaa aende kwa kaka yake au Zac. Tia aende kwa Evan au alale hapo hapo na Zena mpaka jumapili usiku.



Basi hapo mama Hiza atawasimulia habari za mtaa mzima. Nani kaachika, nani kafumaniwa, nani anamuhisi mchawi wake. Nani anayejidai anaswali sana lakini mmbeya. Habari zote za mtaani hapo atawasimulia kina Zena mpaka watakapo ondoka. Na alikuwa na uwezo mkubwa sana wakusimulia. Hata jambo likiwa dogo kwa namna gani, lakini mama huyo atalikuza kwa kadiri ya muda wao. Atalisimulia jambo hilo kwa mbwembwe zote, nakuwafanya wacheke mpaka watoe machozi. Na wakati wote mumewe hubaki kimya akimsikiliza na kumtizama kama yuko karibu nao. Maisha yakawa mazuri na yakupendeza.



************************************************



 Wakati wanakaribia kumaliza mwaka, wakiwa wanakaribia mitihani, Nanaa kumaliza mwaka wa kwanza, Zac kumalizia mwaka wake wa tatu na wa mwisho chuoni hapo, Nanaa kama kawaida yake, alifika nyumbani kwa James siku ya ijumaa baada ya mtihani wake uliokuwa umemlaza macho. Alimsaidia kusafisha na kumpikia kama kawaida huku akimsubiri kaka yake arudi kutoka kazini. James alirudi nyumbani kutokea kazini akidhani Nanaa atalala siku hiyo, lakini kumbe alifika tu kuaga.



Hivi nimekuja kukuona na kukuaga, kaka yangu. Mitihani imekaribia. Baada ya siku 8 tu, tunaanza mitihani ya kufunga mwaka. Hutaniona kwa majuma matatu na siku kadhaa. Nataka nikatulie kabisa chuoni. Ila nikimaliza tu mitihani, nitarudi hapa nyumbani.” “Si leo ulale? Nitakupeleka kuona movie.” “Acha nijikaze kaka yangu. Nikimaliza mitihani tutazurula wote mpaka uchoke wewe.” James akacheka, Nanaa akachukua mkoba wake na kutoka.



************************************************



Nia ya Nanaa haikuwa kurudi hostel kusoma kama alivyomuaga kaka yake. Ilikuwa kwenda kumsurprise mpenzi wake Zac aliyekuwa akimtegemea siku inayofuata ya jumamosi. Walikubaliana kutoka pale hostel na kwenda kujifungia mahali. Wakatumie siku ya jumamosi na jumapili pamoja kabla hawajaingia kipindi hicho kigumu cha mitihani ambacho alijua itakuwa ngumu kuonana mara kwa mara. Nanaa alikwenda mpaka hostel za Mabibo ambako alikuwa akiishi Zac, bila hata kumtaarifu mpenzi wake kuwa anakwenda siku hiyo si kesho yake kama walivyokuwa wamekubaliana.



Nia alitaka kumfurahisha kwani siku iliyopita alimbembeleza sana Nanaa, waanze mapumziko yao siku hiyo ya ijumaa, lakini Nanaa akakataa akimwambia ana mtihani mmoja siku hiyo ya ijumaa mchana na angekuwa na vipindi mfululizo mpaka usiku, kwa hiyo atakuwa amechoka sana. Akamuomba mpenzi wake aliyekuwa amemwambia anahamu naye sana, amvumilie mpaka kesho yake ili apumzike usiku huo. Wakikutana awe na nguvu. Kwa shingo upande Zac akakubali. Lakini baada ya mtihani huo wa mchana, maprofesa wa vipindi vya jioni wakaahirisha vipindi. Ndipo Nanaa akaonelea aende kwa kaka yake. Amsaidie kazi na kwenda kumsuprise mpenzi wake. Waanze mapumziko mapema.



************************************************



Zac alikuwa na rafiki mfanyakazi. Bachela, aliyekuwa akiishi peke yake kwenye nyumba yake hiyo Makongo juu. Mara nyingi aliwaachia chumba kimoja watumie hapo hapo nyumbani kwake kila walipohitaji. Kwa hiyo weekend hiyo, Nanaa na Zac walipanga kuwepo huko.



************************************************



Alishuka kwenye daladala na lengo la kuelekea moja kwa moja chumbani kwa Zac na rafiki yake akiwa amejawa furaha zote akimfikiria vile Zac atakavyofurahi kumuona usiku huo wala si kesho yake. Wakati anakaribia jengo ambalo lina chumba chao akakutana na rafiki yake Zac ambaye anaishi naye chumba kimoja, Felix. Wakasalimiana na Felix na kutaniana kidogo, kisha wakaongozana moja kwa moja chumbani kwao huku wakiongea na kucheka.



Walipofika mlango wa chumbani kwao, wakasikia mziki mkubwa ndani. Kitu ambacho si kawaida yao. “Jamaa katoka nini? Maana namjua Zac, hapendi kelele.” Felix aliongea huku akifungua mlango. “Labla aliacha radio wazi kukuashiria yupo maeneo ya karibu.” Nanaa aliongeza huku akiwa na shauku ya mlango ufunguliwe waangalie ndani. Na alijiambia yupo tayari kusubiri kama Zac hatakuwepo. “Atakuwa ameenda kufuata chakula hapo Cafe.” Felix Akaongeza baada ya kufanikiwa kufungua mlango na funguo na kuchomoa funguo mlangoni ili waingie ndani.



Alipomaliza kuchomoa funguo, wakaingia ndani bila hata kugonga wakijua kwa kelele zile, Zac asiyependa kelele, hawezi kuwepo ndani. Wote walibaki wameduwaa mara baada ya kuingia na kumkuta Zac  na msichana mwingine aliyekuwa kwenye kundi moja la kujisomea na Zac wapo kitandani, uchi na wao wakiwashangaa.



************************************************



Huyo msichana hakuwa mgeni kwa Nanaa. Walifahamiana na Nanaa. Nanaa alimfahamu kwa jina moja tu la Ndina. Mara nyingi Nanaa alimkuta na Zac na marafiki zao wengine wakijisomea pamoja. Kama hawakuwa maktaba pamoja, basi chini ya mdigrii wakisoma. Hata mara nyingine aliwakuta cafeteria wakila pamoja mara baada ya  lectures au wakiwa wamemaliza kujisomea.



Zac hakuwahi kusita kumbusu Nanaa mbele yake huyo dada na marafiki zake wengine. Walishawazoea na kuwaelewa. Kwani mara nyingine Nanaa alipowakuta mahali wakisoma, Zac alitengeneza nafasi pembeni yake, nakumtaka Nanaa akae hapo akimsubiria wakati wao wanamalizia kusoma. Basi hapo Zac ataendelea kusoma na wenzake huku amemkumbatia Nanaa. Mara nyingine alimtupia mabusu ya hapa na pale. Ilimradi tu, kuonyesha mapenzi kwa Nanaa. Na kundi lao zima walimfahamu Nanaa kuwa ni wa Zac rafiki yao. Kwa hiyo hata alipokuwa akimkuta Zac na Ndina peke yao, haikumsumbua kwani waliheshimiana sana.



Ndina alikuwa msichana wa kawaida sana ukimlinganisha na Nanaa. Hakuwa na vitu vya ajabu ambavyo mtu au hasa wanaume wengi wa kiafrika wanaweza kuvitaja na kuvisifia kama jinsi Nanaa alivyo. Mara nyingi Nanaa alipokutana naye mara baada ya salamu, hapakuwa na maongezi mengi. Kwani Zac alimtawala Nanaa wakati wote.



************************************************



Nanaa alibaki ametoa macho huku maswali mengi aliyotamani kuuliza yakibakia kupiga kelele ndani yake bila mtu wa pembeni yake kusikia. Ndina alishavuta shuka pembeni yake akajifunika nakubaki kimya. Felix yeye aliweza kusogelea radio iliyokuwa na mziki mkubwa, kelele nyingi zaidi pale ndani, akaizima. Nanaa alimwangalia wakati akisogelea radio. Chuki ikamwingia. “Inamaana hata Felix alikuwa akijua? Mbona haonekani kushtuka ila kusikitika tu?” Nanaa akaanza kujisikia vibaya, akijihisi ni mjinga mbele ya kundi zima lakina Zac. Swali la kuwa aliyeingilia mapenzi ya mwenzake, likaanza kukosa jibu kwa Nanaa. Ni yeye au Ndina?



“Nilijua wewe ni wangu Zac!” Ndilo neno pekee aliloweza kutoka mdomoni mwa Nanaa. Aliongea kwa masikitiko makubwa kutoka moyoni. Zac alijua historia ya Nanaa na Alex. Vile alivyomsaliti. Akamuahidi kumuenzi na kumpa mapenzi ya kweli. Hakutaka kuendelea kujidhalilisha pale mbele yao, akaamua kutoka.



************************************************



Haikuwa mara ya kwanza kwa Nanaa kumsaprizi Zac. Lakini lilikuwa ni jambo ambalo hata Zac alikuwa akilitegemea hasa siku za ijumaa. Alijua wazi Nanaa huwa anakwenda kwenye chumba hicho kumsubiria endapo atachelewa kurudi hapo Mabibo hostel. Naye Zac hakuwa akichelewa. Kila ijumaa baada ya vipindi, aliwahi kurudi hostel akijua aidha atamkuta Nanaa au atamsubiri. Mara nyingi walitumia usiku wa ijumaa pamoja. Kisha siku ya jumamosi, Nanaa alikuwa akirudi kwa kaka yake kama kawaida.



Kwa kuwa nyumbani kwa kina Felix ilikuwa hapo hapo jijini, basi mara nyingi walijikuta wapo peke yao hapo chumbani. Basi siku hizo za Ijumaa walikuwa wakizitumia chumbani hapo, kitanda hicho hicho alichomkuta Ndina yupo uchi usiku huo aliomkatalia yeye Zac na kumwambia atakuwa amechoka mpaka kesho yake ndipo wakajifungie Makongo juu kwa rafiki yake mwingine Zac, ambapo walikuwa wakipata uhuru wote.



************************************************



Nanaa alitoka hapo asijue ni kama alimfumania Zac na Ndina, au alibahatika kujua ukweli. Hakujua kama amekamatwa na wivu au aibu. Chuki au amejidhalilisha. Kila alipojifananisha na Ndina, bado alijiona ni bora kuliko yeye. Mawazo yakampeleka vile anavyojituma kitandani kumridhisha Zac, “na bado analala na Ndina!? Kwa..”  Nanaa akataka kujinyeshea mvua ya maswali, lakini akasikia sauti ya Zac ikimwita kwa mbali kama anayemkimbiza.



Kwa haraka sana alijionya hata asisimame. Akaongeza mwendo akielekea zilipo daladala, barabarani bila hata kugeuka. Kumbe baada ya kutoka tu pale chumbani, ni kama akili ikamrudia Zac waliokuwa kimya pale kitandani na Ndina. Felix aligeuka na kuendelea na shuguli zake pale pale chumbani. Wala hakutoka kuwapa nafasi. Akavuta suruali yake. Akavaa kwa haraka na kuanza kumkimbiza Nanaa bila shati. Kifua kikiwa wazi kabisa.



Alimuona Nanaa akiongeza mwendo kwa mbali kukiwa na giza tayari. Aliendelea kumkimbiza bila viatu mpaka kituo cha daladala akiomba msamaha na kusema ni bahati mbaya. Lakini Nanaa hakujibu kitu.  Akapanda ndani ya daladala huku akikumbuka vile alivyosalitiwa na Alex pia, daladala iliondoka, Zac akiwa amepiga magoti nje ya daladala hiyo akiomba Nanaa ashuke ili wazungumze. Hakumjibu kitu, alibaki ameinama nakushindwa hata kumwangalia Zac nje ya dirisha. Wasafiri wengine walibaki wakichungulia dirishani wakishangazwa na Zac.



************************************************



Hazikuwa siku nyingi zilizopita tokea Nanaa na Zac wawe na wakati mzuri wa pamoja. Ilikuwa weekend iliyopita tu, pale James alipomwambia Nanaa amsindikize au warudi wote nyumbani, mkoani Kilimanjaro, Moshi, kusalimia wazazi. Nanaa akamkatalia kaka yake na kumsihi sana aende yeye mwenyewe, yeye atakuja kurudi kwa mama yake mkubwa wakati mwingine.



Kwa kuwa ilikuwa katikati ya muhula, James akaonelea ni sawa kumuacha. Asimlazimishe na kuishia kuchanganywa na mama yake mara baada ya kufika huko kwao. Nanaa akashindwa shule. James alisafiri yeye mwenyewe. Aliondoka siku hiyo ya Jumamosi alfajiri sana. Nanaa akampigia simu Zac na kumuelezea kila kitu. Zac akamuomba wakutane Makongo juu kwa rafiki yake, kwa kuwa Felix alikuwepo pale hosteli. Hakwenda kwao. Kwa kuwa James alikuwa akirudi siku ya jumatatu, Nanaa aliondoka hapo nyumbani siku ya jumamosi asubuhi na kwenda kujifungia na Zac mpaka siku ya jumatatu ndipo alipotoka hapo na kwenda kwenye kipindi kilichokuwa kikianza saa nne asubuhi.

 ************************************************



Nanaa aliondoka, lakini akiwa ameumia kupita alivyowahi kuumizwa kabla. Moyo ulikuwa unauma kama umechomwa mkuki. “Mbona alionekana kuridhishwa na penzi langu. Wakati wote aliniambia mimi ni mzuri kitandani. Anapenda jinsi ninavyomfanyia kitandani. Na umbo langu linazidi kumsisimua kila nikiwa mtupu mbele zake.” Nanaa aliendelea kuwaza hapo ndani ya hiyo daladala asijue ashuke wapi! Arudi kwa kaka yake au hostel.



************************************************

Kilichokuwa kikimuumiza Nanaa ni vile alivyokuwa amejitoa kwa Zac. Alikuwa muaminifu sana kwake. Hata rafiki wa Evan, Terry aliyekuwa akisoma IFM alipokuwa akimtongaza Nanaa, alikataa kata kata, huku akijigamba anaye mpenzi. Alimwambia Terry kuwa si kwamba anaye tu mpenzi, bali mume. Nanaa alijisifia siku hiyo mbele ya kundi hilo walipokuwa wamekwenda beach ya Kigamboni, kupumzika. “Nampenda Zac. Na yeye ananipenda kwa dhati. Sijaona wala hakuna mwanaume kama Zac.” Nanaa alijisifu mbele ya marafiki hao wakiume wa Evan. Wote walimsikiliza na kufunga kinywa wakijua ule ujumbe ulitoka kwa Nanaa ukiwa hauna hila, ila ulimuumiza sana Terry.

Terry mtoto wa mama. Rafiki wa karibu sana na Evan. Watoto wa jiji. Lakini walicheza kwa tahadhari. Wakilindana wasije wakapitiliza starehe, wakawaumiza wazazi wao. Wote walitoka kwenye familia zenye hali nzuri inayoenda kwenye nzuri sana. Wazazi wasomi. Baba yake Evan alikuwa daktari katika hospitali kubwa ya Muhimbili, wakati baba yake Terry alikuwa daktari katika hospitali binafsi waliyokuwa wameanzisha yeye na marafiki zake. Wote walitoka kwenye familia ambazo hazikuwa zikilia shida. Wazazi wanaoamini katika professinals, na wao walikuwa wasomi. Kwa hiyo hata watoto wao walijua elimu ndio kila kitu. Hawakuzidisha starehe na kusahau shule hata kidogo.

*****************************************************

Tokea mara ya kwanza Tia anamtambulisha Nanaa kwenye kundi hilo. Yeye akiwa mgeni. Kwani Zena na Tia walishawahi kutoka nao mara kadhaa kabla ya Nanaa. Walisha alikwa kwenye shuguli mbali mbali za wadogo zao huko majumbani kwao. Iwe ni communion ya kwanza au kipaimara cha mmoja wa wadogo zao kwenye kundi hilo la kina Evan, Tia na Zena pia walialikwa. Kwa hiyo walijikuta wanafahamiana na wote kwenye kundi hilo kabla ya Nanaa kujiunga nao, lakini Terry hakuonyesha hata uhitaji wa mwanamke mpaka alipokuja Nanaa.

Ilikuwa ni birthday ya mmpenzi wake Tia, Evan ndipo Nanaa alipokwenda na yeye. Walianzia nyumbani kwa kina Evan. Walikuwa ndugu, jamaa na marafiki wakaribu wa wasomi hao, wazazi wa wakina Tery na Evan. Walikula na kunywa. Lakini Nanaa akaona jambo la pekee na ndipo akaja kuelewa baadaye, ni kwa nini kina Evan na Terry, japokuwa ni watoto wenye uwezo wa kujitosheleza majumbani kwao, lakini bado wamebaki kuwa ni vijana wenye kiasi. Kabla ya kukata keki, wazee hao na wake zao, pamoja na ndugu. Walimtaka Evan aelezee alipo, anapofikiria kwenda. Changamoto anazokabiliana nazo kwa wakati huo. Ni hatua gani amechukua mpaka hapo. Na nini anampango wa kufanyia kazi. Basi hapo ndipo ataulizwa maswali na kuomba ashauri wenzake. Na kuelezea makosa aliyoyafanya, na kushauri wasipite alikopita yeye au wasifanye kosa kama alilofanya yeye.

Nanaa aliona ni kitu cha ajabu jinsi wazee hao wanavyofanya kwa vijana wao, lakini akavutiwa sana. Walikuwa ni wakina baba wa makamu, na walionekana wasomi tu. Wake zao hivyo hivyo. Lugha ya kingereza ndiyo iliyokuwa ikitumika kati yao. Hata watoto wadogo kabisa walikuwa wakitumia lugha hiyo kuashiria wote wanasoma kwenye shule za maana na kingereza kwao sio lugha ya kujidaia. Ndio lugha ya mawasiliano kati yao.

Terry alimganda sana Nanaa jioni hiyo. Alimfuata kila mahali na kutaka azungumze naye. Nanaa aliamua amuwahi mapema kabla hawajaagana. “Ninaye mpenzi wangu. Anaitwa Zac. Anamaliza chuo mwaka huu. Tunampango wa kuoana.” Terry alitabasamu. “Nilitaka kukukaribisha kwenye birthday yangu na mimi jumamosi ijayo.” “Mmmh! Ningependa kuja, lakini kuanzia ijumaa nitakuwa na Zac. Weekend hii nimeshindwa kwenda, kwahiyo weekend ijayo lazima tuwe wote.” Nanaa alikataa kwa kujitetea. “Haitakuwa siku nzima. Ni jumamosi jioni. Ukiweza kufika, nitafurahi kukuona Nanaa.” “Naomba nisikuahidi Terry. Huwa nikiwa na Zac, hapendi niende mahali. Nakuwa naye mpaka jumapili jioni. Nashukuru kwa mwaliko lakini.” Nanaa alitoa tabasamu na kuondoka.



*****************************************************

Terry alikuwa mwaka wa pili kwenye chuo cha IFM. Ulishapita mwaka, tokea asalitiwe na mpenzi wake. Akaapa hatapenda tena. Lakini hata wenzake waliona tofauti pale alipotokea Nanaa. Alikuwa akihangaika kupita walivyomzoea. Evan alimshauri awe muwazi kwa Nanaa, kuliko vile anavyojifanya kuwa katuni mbele za marafiki zake kila anapomuona Nanaa.

*****************************************************

Siku ya birthday yake ilikuwa mbaya zaidi, kwani Nanaa mpaka sherehe inaisha, Nanaa hakuwa ametokea. Alitoka na kwenda kukaa nje, nyuma ya nyumba yao. Wakati wenzake wakifurahia ndani, wakila na kucheza Terry alikuwa nje mpaka watu wote wakatawanyika pale ndani nyumbani kwao. Hawakuwa wamemuona Terry. Alijichukia kumpenda msichana ambaye kwanza alikuwa mgeni kwake. Hamfahamu. Pili tayari anajua yupo na mpenzi wake. Tena mwanaume anayetarajia kumuoa. Hicho ndicho kilimuuma zaidi. Lakini alishindwa kujisaidia. Anampenda Nanaa.

*****************************************************

Kidogo wivu ukaanza kwa Zena ambaye aliona anamstahili Terry. Kwanza yeye kama ndiye wakwanza aliyemfahamu Terry kabla yake. Kila walipokuwa wakikutana kwenye kundi hilo ambalo Tia ndiye alimkaribisha na kukutana na kina kaka hao. Palikuwepo na mazungumzo ya pamoja. Ukweli hapakuwepo na mazungumzo binafsi kati ya Zena na Terry. Japo Zena alishaonyesha kumpenda sana Terry. Kwanza alijua ni yeye peke yake kwenye kundi lile ambaye hana msichana. Halafu ni Terry jamani! Nani asimpende?

Analishwa na kutuzwa vizuri na mama yake. Hana mawazo ya kufikiria pesa, kama watu wengi. Mtoto wa mama. Hawezi kutoka nyumbani mpaka mama yake ahakikishe amekula na ananguo safi. Akitoka mama akiwa kazini, basi atapigiwa simu kuulizwa. Na pengine kuambiwa apitie ofisini kwa mama, akachukue pesa za matumizi. Gari anayotembelea ni ya nyumbani. Hajui hata kama huwa inafanyiwa matengenezo. Hilo lilikuwa jukumu la dad au mama.

Kwa nini usimpende Terry? Ngozi nzuri. Anaongea lugha ya kingereza na tabasamu zuri usoni. Akionyesha ametulia. Hana shida ya kumnunulia mtu yeyote zawadi kutoka kwenye pesa ya ziada anayopewa nyumbani. Hawazi kutaliwa nini, wala kulipa garama yeyote. Ni yeye tu. Kila ijumaa anarudi nyumbani na nguo chafu za juma nzima. Zinafuliwa na kupigwa pasi ndipo zirudi tena hosteli. Shida hamna. Ila sasa ni mapenzi. Alisalitiwa, akampenda Nanaa mchumba wa mtu, ambaye anamuumiza moyo wake.



Zena alia wivu.

Wivu ulimsumbua Zena kwani alishamwambia Tia na Nanaa juu ya hisia zake kwa  Terry. Hasira ilimpanda zaidi pale alipowakuta Nanaa na Terry wakizungumza na kucheka upande wa baa wakati wote wamekaa baharini walipokuwa Kigamboni juma moja baada ya birthday ya Terry. Nanaa alitoka upande wa baharini akiwaaga anakwenda maliwatoni. Baada ya muda kidogo, Zena akamuona Terry na yeye  amesimama anaondoka kuelekea upande aliokwenda Nanaa. Akajua wazi anayemfuata ni Nanaa. Kwani Terry alionyesha wazi kuvutiwa na Nanaa. Hakuacha kumuuliza maswali mbele yao na kuchangia chochote Nanaa anachozungumza.

Wakati Nanaa anatoka chooni, akamuona Terry. Alimfanyia ishara ya kumwita, Nanaa akamfuata pale alipomkuta amekaa upande wa baa kama anaagiza vinywaji. Kwa kuwa Terry alimwalika kwenye birthday yake na hakwenda, Nanaa akaona huo ndio wakati mwafaka wakuomba radhi na kuuliza mambo yalikwendaje siku hiyo. Akiwa hajui jinsi alivyomuumiza Terry, Nanaa aliongea kama jambo la kawaida huku akitaka michapo ya siku hiyo.

Wakiwa kwenye mazungumzo, hata hawajafika mbali, Zena naye akawasogelea.  Akiwa hajui hili wala kile kinachoendelea si kwa Zena tu ambaye ni rafiki kipenzi, hata Terry pia. Nanaa akatoa ahadi isiyo na hatia. “Basi kwa malipizi, itabidi nikutoe kwa chakula cha mchana. Tusherehekee birthday yako. Nitakuletea zawadi. Ili ujue sikuwa nimekusudia kukosa birthday yako.” Nanaa aliongea huku akicheka. “Nilishamwambia ilikuwa ni weekend ya Zac. Ulikuwa kwa mpenzi wako.” Zena aliongeza. “Afadhali unitetee Zena shoga yangu. Terry anajua nilikimbia.” Nanaa aliongeza.

“Tusirudi nyuma, tukaharibu ahadi ya kunitoa.” Terry aliongeza. Nanaa akacheka. “Hilo tu? Usijali. Nakutafutia siku yako maalumu.” Nanaa akaongeza akijua ni utani kabisa, akacheka na kuondoka. Aliwaacha pale Zena na Terry. Wala asijue walirudi baada ya muda gani pale kwenye kundi. Asijue kama Zena alirudi akiwa na furaha au la. Kwa kuwa muda ulikuwa umeshakwenda, hata Zena alipowaambia Tia na Nanaa waondoke, Nanaa hakuona kuna jambo la ajabu. Walishakula. Wakaongea na kucheka. Ilishakuwa jioni. Akaona sawa waondoke. Asijue kinachoendelea.



*****************************************************

Halikuwa kosa la Nanaa. Kwani wakati Zena anawaambia jinsi anavyompenda Terry, wakiwa chumbani kwao. Kila mmoja kitandani kwake, yeye Nanaa alikuwa aki chat na Zac. Ukweli alikuwepo pale, lakini mawazo hayakuwepo pale hata kidogo. Alikuwa akipata jumbe za mapenzi kutoka kwa Zac. Akisifia penzi alilompa kabla hawajaagana siku hiyo ya jumapili. Zac alimwambia alifurahishwa na hiki na kile, ilimradi tu kumfurahisha Nanaa. Kwa hiyo akili ya Nanaa ikawa imezama kwenye simu yake akifurahia zile jumbe, huku akifikiria na yeye maneno mazuri ya mapenzi ya kurudisha kwa Zac wakati Zena akiendelea na yeye kueleza hisia zake kwa Terry. Hata hakuwa akiwasikiliza Tia na Zena. Kwanza alijua ni mazungumzo yao binafsi marafiki hao aliowakuta. Na yeye alikuwa amechoshwa na mapenzi ya kuanzia ijumaa usiku mpaka jumapili hiyo anarudi hosteli.

*****************************************************

Siku hiyo walipotoka Kigamboni, Terry na Evan ndio waliokuwa wakiwarudisha hosteli kwa gari. Nanaa aliomba ashushwe kwa kaka yake, mtaa wa Kijitonyama. Karibu sana na Usalama wa Taifa,  badala ya hosteli. Yeye Zena alipelekwa mpaka kwenye kituo cha daladala karibia na kwao. Asingethubutu kuonekana kwao anarudishwa na wanaume. Wakati wote wakijua Tia atabaki na Evan kama kawaida yao mpaka siku inayofuata ya jumapili. Evan akirudi chuoni SUA, mjini Morogoro ndipo Tia anarudi hosteli.

Wakati Nanaa anashuka, aliwaaga kwa kicheko asijue kinachoendelea. Aliwaacha Zena, Tia, Terry na Evan kwenye gari. Mazungumzo yote ndani ya gari baada ya kushuka Nanaa, ilikuwa Terry akifurahia ahadi yakutolewa na Nanaa. Hata Tia aliumia sana. Asiamini Nanaa anawezaje kumfanyia hivyo Zena. Tena baada ya kuwaambia wazi vile anavyojisikia kwa Terry. Halafu tayari Nanaa alikuwa na mpenzi wake Zac!

Tia akaona vile Zena alivyoumia, akamwambia Evan waonane kesho ili yeye awe na Zena usiku huo. Akaamua akalale na shoga yake nyumbani kwao, ili amfariji. Evan hakuwa na tatizo. Akawashusha kituoni, na hapo ndipo wakapata nafasi ya kumsema vizuri Nanaa. “Tabia yake mbaya.” Zena alianza kutupa shutuma. “Hatosheki na wanaume!” Tia akamuunga mkono shoga yake Zena. “Amesahau sisi ndio tumemtambulisha kwao? Ametawala kundi zima sasa hivi, utafikiri yeye ndio mwenyeji wetu jamani!” Zena alilalama. “Hukumuona vile alivyokuwa akijishaua kwa Terry. Niliwakuta peke yao kule upande wa baa. Nanaa akijinadi.” Mashoga hao waliongea mapungufu yote ya Nanaa, wakakubaliana kumtema tu.

 Mkakati wa jumatatu kumtoa kwenye urafiki rasmi ukapangwa wakiwa hapo hapo kwenye kituo cha daladala cha Tangibovu karibu sana na kwa kina Zena. Wakaadhimia kufuta kabisa urafiki na wala wasiongozane naye popote ili inapofika siku ya kukutana na kundi la kina Evan, Nanaa asiwepo. Baada ya kuafikiana na mikakati yao juu ya Nanaa ambaye gafla amekuwa adui, ndipo wakaelekea nyumbani kwa kina Zena ambako ni kama kwa kina Tia pia. Kwa kuwa wazazi wa Tia walishakuja kumkabidhi Tia rasmi hapo kwa wazazi wa Zena, basi Tia hakumuhitaji Zena kufika kwa mama Hiza. Akawa ameshazoeleka pale nyumbani. Urafiki wa wazazi uliokuwa unaelekea kwenye undugu kati ya familia hizo mbili ukawa umeshakomaa.

*****************************************************

Akiwa hajui lolote Nanaa alirudi hosteli siku inayofuata ya jumapili akiwa na tabasamu lake lote. Akawakuta Tia na Zena chumbani kwao. Akaona wote wamenuna. Nanaa akaanza kuwatizama kwa zamu na kucheka. “Mbona kama mmeninunia? Nimefanyaje tena!?” Nanaa aliwauliza huku akiwatizama kwa zamu. Ndipo Zena alipomjibu kwa jazba vile walivyokerwa na tabia yake yakutaka kumpora Terry wake. Wakashangaa Nanaa anacheka sana. Wakatulia kidogo.

“Unacheka nini sasa? Unafikiri mazuri?” Zena aliuliza akiwa amepunguza jazba. “Kumbe unamtaka Terry?” Nanaa aliuliza huku anacheka. “Kumbe?” Zena alijibu. “Aiii! Mimi sina hata shida naye. Wewe tafuta neno baya lolote la kunichafua kwa huyo Terry, halafu mwambie unampenda.” Wakaangaliana. “Kweli?” “Sasa mimi wa nini huyo Terry? Zac mwenyewe ananishinda. Terry nitamuweka wapi mimi na ratiba ngumu ya Zac? Ijumaa mpaka jumapili ananitaka kitandani mpaka nimkimbie weekend nyingine sababu ya kaka.” Tia na Zena wakajiweka sawa.

“Tena kukusaidia tu Zena, mimi niache kuja kwenye mikusanyiko yenu kwa muda. Akishajiona mpo naye tu, lazima atakuchangamkia. Kwanza unalipa shoga yangu.” Roho ilisuuzika. Zena akaanza kucheka. “Sasa kwa nini hukuniambia tokea mwanzo? Mimi hata sikuwa na wazo. Kwanza mbona nilishamwambia Terry kuwa ninaye Zac?” “Niliwaambia.” “Basi mimi hata sikuwa na wazo. Labda akili yangu haikuwepo. Sasa mlipanga kuninunia mpaka lini!?” Nanaa aliuliza kwa kuwasuta. “Wala hatukuwa tumekununia.” “Mmmh! Aibu zenu wanawake.” Vicheko na mikakati yakumpata Terry ikaendelea jioni hiyo mpaka wakaamua kutoka na kwenda kujisomea.

Nanaa baada ya kusalitiwa kwa mara ya Pili.

Alitoka pale Mabibo hosteli moyo na mwili ukiwa kama umekufa ganzi. Asielewe anatatizo gani. Kama uzuri, alisifiwa mpaka na wanawake wenzake. Kwa hakika Ndina haoni ndani. “Nilijua Zac ni wangu!” Nanaa aliendelea kuwaza. Mapenzi aliyokuwa akionyeshwa na Zac, kwa hakika Nanaa alijua amefika. Sifa zilizokuwa zikimwagiwa kwake, kuanzia umbile na mambo wanayofanya pamoja, hakuwahi hata kuhisi kama Zac anaweza kugusa mwanamke mwingine. Faraja aliyokuwa akimpa! Mbele za watu alimkumbatia na kumbusu. Ni kama alikuwa akitangazia uma wote, kuwa Nanaa ni wake.Anarudishaje sura yake kwa watu waliokuwa wakiyajua mapenzi yale? Anaishije tena bila penzi zito la Zac?

Zikiwa zimebaki siku chache za mitihani, Nanaa akijaribu kujifikiria hatima yake kimapenzi, alishindwa kusoma kabisa. Kila akiinamia vitabu, badala yakuona maandishi, macho yalimuona Zac na Ndina pale kitandani. Akaamua awekeze muda mwingi wakujisomea kwenye makundi ya wenzake wanao soma pamoja. Lakini pia haikusaidia. Mawazo yaligoma kuwepo pale. Yalisambaa kwenye jumbe za mapenzi alizokuwa akitumiwa na Zac. Simu za kutakiwa usiku mwema kila siku na maneno matamu kutoka kwa Zac. Si asubuhi si mchana, Zac aliwasiliana naye. Hata akiwa kwenye vipindi, aliweza kumtumia ujumbe Nanaa kuwa anamfikiria yeye. Leo anaishije bila hayo maisha matamu yaliyokuwa yamejaa faraja?Mitihani yakumaliza mwaka wa kwanza ilimalizika kwa shida mno. Matokeo yalitoka lakini yalikuwa mabaya sana kwa Nanaa. Alifeli masomo mawili nakutakiwa kuyarudia. Na yale masomo aliyokuwa amefaulu ni kama alikuwa kwenye mstari wa kufeli kabisa. Yote alipata alama ya “C”.

*****************************************************

Ile hali ya kumfumania Zac ilimuathiri sana kiasi ya kwamba hakujua kama hata akirudia ile mitihani anaweza kufaulu. James alijua kuna tatizo tu. Nanaa alikuwa ni kama amepigwa na kibumbuwazi wakati wote. Wakiwa wamekaa sehemu, macho yake yakiangalia kitu, hayatatoka hapo hata kwa nusu saa. Ndipo James ikabidi kumuuliza taratibu huku akimsihi asimfiche. Akawa mtu wa kwanza kumsimulia kilichompata. Hakuwa na ujasiri wa kumwambia mtu yeyote. Hata Zena na Tia hakuwa amewaambia. Ila walijua kuna tatizo. Kwani hapakuwa tena na simu za usiku wala za asubuhi kutoka kwa Zac. Simu ya Nanaa ilikuwa imefungwa kipindi chote cha maandalizi na wakati wa mitihani. Hawakumuona hata akisoma ujumbe.



James alimuona vile alivyoumia. Alimuelezea kwa kuumia sana tofauti na vile alivyokuwa amemueleza juu ya kusalitiwa na Alex. “Kwa hakika huyu nilijua ni wangu!” Nanaa alimalizia kwa kaka yake huku amenyong’onyea pale kwenye kochi. Ilibidi James achukue nafasi ya umama na kuanza kumtia moyo ili asiharibikiwe zaidi. James akiwa ameumia sana, alizungumza naye kwa upendo kama mama au dada yake anayempenda sana. Akamkumbusha wajibu alionao kwa wakati ule wa kwanza ni shule, ndipo ije ndoa kama Mungu atamjalia mwanaume atakayemthamini. Alimwambia kwa wakati huo ni lazima kutuliza mawazo na kufanya ile mitihani.



Mungu akamsaidia tena kipindi hicho kigumu cha machungu na kusalitiwa kikapita. Angalau akaanza kulala mpaka asubuhi bila kugeuka geuka kitandani. Nanaa alipata nafuu, akarudisha akili shuleni, akaanza kujiandaa kurudia mitihani hiyo wakati wenzake wakiwa likizo.



*****************************************************

Tia na Zena wao walifaulu vizuri tu. Tena kwa alama za juu sana. Walihakikisha habari zinamfikia Nanaa. Ili ajue wao wamempita kielimu. Kwa hiyo hawakuwepo kwenye kundi la wanao takiwa kurudia mitihani. Baada yakumaliza mitihani, Tia alibaki jijini kwa muda. Akarudi kuishi  nyumbani kwa kina Zena. Walihakikisha wanajua kinachoendelea. Tena kutoka kwa rafiki wa Karibu wa Zac.



Vicheko viliwajaa kujua kilichompata Nanaa. “Yako wapi!? Yako wapi shoga yangu?” Zena alicheka mara baada ya kukata simu waliyokuwa wameweka kwenye ‘loud speaker’ wakimsikiliza rafiki wa Zac, akieleza mkasa mzima. “Kitanda hakiangalii kiuno chembamba, wala rangi ya mwili. Ukilalia tu, mchezo unachezwa.” Tia alizidi kupasua mbavu huku machozi yakimtoka kwa furaha ya kumcheka Nanaa. “Alivyoshushuka! Ndio maana kujidai kote kulimwisha.” “Alikuwa hawezi hata kututizama.” “Kwa mabusu yale na zawadi! Hata mimi ningenyong’onyea.” Wakaendelea kupokezana. “Kawa mdogoooo! Eti Zac atanioa. Yako wapi? Ndoa Bongo?” Zena akaongeza huku akicheka na kuongeza. “Halafu Zac alivyomshenzi, umeona mwanamke aliyelala naye? Ndio ujue havichagui sura wala umbile.” Walizidi kucheka na kugonga mikono wakifurahia anguko la penzi la waliyemwita shoga yao.



“Lakini hizo sio habari njema sana kwangu, Tia.” Akili ilimrudia Zena wakiwa wanamcheka mwenzao. “Zena bwana! Eti havichagui kiuno.” Tia aliongeza na kuzidi kucheka akiunga mkono hoja ya shoga yake Zena. “Subiri kwanza Tia. Terry akijua kama sasa hivi Nanaa hana mtu si ndio atahamisha majeshi kwake?” Zena aliingiwa na hofu ya gafla. “Ataambiwa na nani huyo Terry? Hakuna kumtafuta tena Nanaa. Akakae huko huko kwao. Anaweza kurudi na hasira, akatembea na wanaume zetu wote. Akuu! Atuondolee balaa lake na mkosi. Hata simu zake hakuna kupokea tena.” Tia aliongea kwa hakika akijihami.



 Mikakati ya kumkwepa Nanaa ikakamilika. Kipindi hicho kabla Tia hajarudi kwao, akiwa jijini kwa kina Zena, walihakikisha wanamkwepa kabisa Nanaa. Hawakumpigia tena simu. Kwa hiyo kila walipokuwa wakitoka, hawakutaka kumwambia Nanaa. Evan alikuwa akienda kuwachukua wao wawili tu. Na kila Terry alipouliza alipo Nanaa, walimwambia yupo na Zac. Utulivu ukawepo. Zena akaendelea kujisogeza kwa Terry bila uwepo wa Nanaa.



Nanaa & Jamal.



Maisha ya kuamka asubuhi nakujisomea yakaanza tena. Wakati mwingine anarudi chuoni kusoma na kukutana na wenzie wanaorudia mitihani hiyo. Wanasoma pamoja. Akichoka anapanda daladala mpaka maktaba ya jiji, anaanza kujisomea tena. Ile ilikuwa kama njia yakutoa uchovu na kubadili mazingira kuanza upya. Kisha jioni anarudi nyumbani. Akaendelea kufanya hivyo akiongeza bidii ili kutimiza lengo. Ilikuwa ni lazima amalize chuo.



Akiwa kwenye maandalizi hayo, akajikuta anakutana na kijana mmoja hapo hapo kwenye hiyo maktaba. Eneo analopenda kujificha yeye kusoma, ndilo huyo kijana naye alikuwa akipendelea kwenda hapo. Nanaa alimuona akitua vitabu vyake na kuanza kujisomea. Hakuwahi kumuona na mtu yeyote, ila yeye tu akijisomea. Wakajikuta kila siku kwenye kona hiyo wao wawili tu. Kila mmoja kimya, akisoma kivyake.



*****************************************************

Wakaanza kusalimiana kila mmoja wao anapomkuta mwenzake na kuagana kila mmoja wao anapoondoka na kumuacha mwenzake. Ikabidi kufahamiana majina. Nanaa akajitambulisha kwa Jamal. Siku hiyo nayo ikapita kwa kujuana majina tu.



“Naona haya ndio maeneo yako ya kujidai! Hukosi!” Nanaa akatabasamu. Akanyanyua uso akiwa amezama kitabuni. Alijua ni Jamal tu ndiye aliyezoea kuwepo hapo, japo siku hiyo alichelewa kidogo.  “Inanilazimu. Nimeshikwa. Lazima kurudia mitihani.” Nanaa akawa muwazi. “Pole. Inatokea kabisa. Lakini kwa juhudi hizo, lazima utapita tu.” Jamal akamtia moyo. “Nashukuru. Na hayo ndio maombi yangu.” Ikawa siku ya kwanza angalau kumuongelesha kidogo. Akavuta kiti sehemu yake, Jamal akapotelea kwenye vitabu vyake.



Siku nyingine, Jamal aliingia na kumkuta tena Nanaa alishaingia hapo maktaba. Akamsalimu na kuvuta kiti pembeni yake. “Vipi?” “Safi tu. Habari za kutwa?” Nanaa naye akatoa salamu. “Nzuri, namshukuru muumba.” Jamal akajibu, Nanaa akatabasamu. “Mbona na wewe huishi kuja hapa?” Na yeye siku hiyo Nanaa akauliza. “Elimu ya utuuzimani. Tulikimbia shule wakati vijana, sasa hivi maisha yanaturudisha huku.” Jamal akajibu kwa kifupi. Nanaa akacheka lile jibu. Kwani Jamal hakuwa hata na dalili ya uzee. “Haya bwana. Hongera.” Nanaa hakuhoji zaidi. Akaishia hapo.

*****************************************************

Taratibu wakaanza kutoka muda mmoja. Jamal anapanda gari yake na kuondoka, Nanaa anaelekea kituo cha daladala kusubiri usafiri wa kumshusha kituo kilichopo karibu na nyumbani kwa kaka yake.  Baada ya siku mbili, Jamal akajitolea kumsindikiza kituo cha daladala na kumsubiri mpaka apande kwenye daladala ndipo na yeye aondoke. Alimwambia hajisikii vizuri kumuacha tu bila kuwa na uhakika amepata usafiri na kuondoka pale salama. Nanaa akamwangalia kwa tabasamu, akakubali kusindikizwa. Napo hapakuchukua siku zaidi ya mbili. Baada ya kusubiri kituoni kwa muda mrefu siku ya tatu, Jamal akaona amsogeze tu, japo hakuwa akielekea pande hizo.



Nanaa hakuona sababu. “Daladala huwa zinachelewa tu. Lakini nitapata usafiri. Wewe usijali. Nenda tu, mimi nitaendelea kusubiria.” Nanaa alijaribu kukataa lifti hiyo. Lakini Jamal akasisitiza. “Siwezi kukuacha mrembo kama wewe barabarani hapa na kiza hichi. Ukipatwa na janga? Vijana wamjini hawawezi kujizuia kwa mrembo kama wewe. Acha nikusogeze japo mpaka karibu na nyumbani.” Nanaa akacheka. Wakaongozana mpaka kwenye gari ndogo ya kawaida tu ya Jamal.

*****************************************************

Lifti zikaendelea. Ikajengeka tabia ya kurudishwa mpaka kituo cha daladala karibu kabisa na nyumbani kwa kaka yake. Hapakuwa na mazungumzo mengi humo garini. Kila mmoja akiongea kwa kujiwinda. Lakini Jamal uzalendo ukamshinda. Akaamua kuvunja ukimya. Alimwambia alivutiwa naye, na angependa wazidi kufahamiana zaidi.



Ukweli Nanaa alikuwa ni dada mwenye vitu vya kuvutia macho ya mtu yeyote kwa haraka. Hakuwa gumzo la jiji, lakini ukifanikiwa kuwa naye karibu, lazima utavutiwa tu. Nanaa akacheka kwa aibu kidogo wakati anakaribia kushushwa kituoni. “Ni sawa baada ya kusoma siku ya jumamosi, tukaelekea nyumbani kwangu?” Tayari uchu ulishamlemea Jamal. Kumbeba Nanaa kwenye gari lake na kukaa pembeni yake na kuyaona mapaja yaliyotulia kitini kila akibadili gia, halikuwa jambo rahisi. Rangi nyeupe usoni aliyokuwa akiiona ikiwaka, akajua ndivyo atakavyokuta ndani pindi atakapomfunua. Anavumiliaje tena?



“Sitakuchelewesha. Nitakurudisha hapa muda kama huu.” Jamal akasisitiza. “Hee! Kwa hiyo unataka nishinde kwako siku nzima!? Maana unajua siku za jumamosi huwa namaliza kusoma mapema.” Nanaa alihoji na tabasamu la soni, usoni. “Nakuahidi kutokuchoka.” Nanaa akainama kwa muda kama anayefikiria.



“Ana nyumba na gari! Ngoja nikajionee. Huwezi jua.” Nanaa akawaza. Akanyanyua sura na kumtizama Jamal aliyekuwa akisubiria jibu lake. “Lakini sitakaa sana.” “Ukitaka nikurudishe wakati wowote ule, utaniambia. Lakini ukitaka kulala pia, sitakuwa na neno.” “We Jamal!” Nanaa akashangaa kwa pozi. “Hakuna neema kubwa kama kumiliki Kito cha thamani kwenye maisha ya mwanadamu yeyote yule hapa duniani. Nitakuwa nimenyimwa shukurani, na Mungu hatanikumbuka tena, kama nikikataa baraka ya uwepo wako nyumbani mwangu. Sasa Mungu anipe nini tena?” Nanaa akamtizama kama kuhakiki yale maneno, akabaki natabasamu asijue ajibu neno gani kwa maneno mazito kama yale. Jamal alijua wazi amekubaliwa.



*****************************************************

Siku hiyo ya jumamosi Nanaa akawahi kufika hapo maktaba akiwa na shauku ya kumkuta Jamal. Mpaka inafika saa sita kasoro, Jamal hakuwepo. Wasiwasi ukampata Nanaa. Akajuta kujirahisisha kwa kiasi kile. “Kwa nini nilimkubalia?” Akajilaumu huku ameinamia vitabu vyake. Mara akasikia mtu anamgusa begani. Akageuka. “Jamal!” “Ahadi ni deni Nanaa. Saa sita ndio hii. Nimekuja kukuchukua.” Nanaa akacheka kwa furaha. “Mbona hukuja tokea asubuhi?” “Si kwa ugeni nilio nao mimi.” Jamal alijibu na kumfanya Nanaa acheke. “Kwa hiyo ulikuwa ukijiandaa na ugeni?” Nanaa akauliza. “Kumbe!? Sio mgeni wangu anafika nyumbani, hamna chakula wala maji! Sikulelewa hivyo.” Jamal alikuwa na lafudhi iliyomvutia Nanaa. Lafudhi ya watu wa pwani. Nanaa akatabasamu na kurudi kukusanya vitu vyake vyote vilivyokuwepo hapo mezani. Jamal akamsaidia kubeba, na kutoka pale maktaba.



Nanaa nyumbani kwa Jamal.

Jamal akaendesha mpaka nyumbani kwake Temeke. “Huku ndiko nilikopata sehemu ya kuishi.” Jamal aliongea wakati anamfungulia Nanaa mlango. Nanaa ambaye hachagui sura ila mtu tu wakuwa naye, hakuona shida. Ilikuwa nyumba ndogo tu. Kwa haraka Nanaa akajua anaishi peke yake. Palikuwa pasafi sana. Nanaa akaona asiwe mchoyo wa sifa. “Jamal wewe unaonekana ni msafi sana.” “Subiri mpaka uangalie kila mahali ndipo usifie. Unaweza ukajuta baadaye.” Nanaa akacheka.



Akaingia na kutaka kukaa. “Twende nikutembeze kila mahali. Sitaki tena siku nyingine ukawa mgeni humu.” “Kwani unampango wa kunikaribisha tena?” Nanaa akauliza kwa tabasamu. “Hata! Nataka siku nyingine na mimi uje unikaribishe.” “Humu humu ndani?” Nanaa akauliza huku akicheka. “Kumbe? Na mimi nataka siku nyingine nikirudi, nisikute makochi yakinitizama. Bali nikukute na wewe kitini unanisubiri.” Nanaa akacheka sana. Jamal aliongea kwa lafudhi iliyozidi kumfurahisha Nanaa.



“Au hutaki?” “Sijui.” Nanaa akajibu kwa aibu. “Yaani unataka leo ndio iwe mwisho!? Haiwezekani Nanaa. Nimekukaribisha hapa kwa kuwa nimekuheshimu na ninakuona ni mtu utakayenifaa. Si ningekukaribisha tu hata baa? Kukuleta hapa kwangu, ujue nimekuheshimu sana.” “Nakushukuru.” Nanaa akasuuzika roho. Mungu ampe nini tena? Nyumba, gari na Jamal anayemtangazia wenyeji mchana kweupee!



 “Twende sasa nikuonyeshe kila mahali. Au njaa inakuuma?” “Hapana. Nipo sawa tu.” “Kwa hiyo unaniruhusu nikutengee chakula baadaye?” “Hamna shida.” Nanaa alijibu kwa kuridhika kabisa kitu kilichomfurahisha Jamal aliyekuwa akimezea mate mapaja aliyokuwa akiyaona ndani ya gauni. Sasa hivi yapo ndani ya nyumba yake. Nanaa si mtoto!



Akarudi kumshika mkono kumuongoza atakapo yeye Jamal. Bila hiana, Nanaa akafuata kwa tabasamu. Walifanikwa kuona chumba cha kwanza, choo cha wageni wakaishia chumbani kwa Jamal. Humo ndipo alipojua ni kweli Jamal alikuwa na uchu naye. Chumba kile kisafi, Jamal alikitumia ipasavyo kukata kiu. Na Nanaa naye hakumzuia. Akajituma ipasavyo. Hapakuwepo tena na Zac wakumfanya ashindwe kumvulia nguo Jamal. Akamkumbuka Terry, akajiambia kama angekuwepo wakati ule, yeye ndio angefaidi. Lakini akakumbuka uchu wa Zena kwa Terry. Akaona ajiachie tu. Akahangaika siku nzima kumfurahisha Jamal kwenye kitanda hicho bila hata kujali hisia zake.

*****************************************************

 Nanaa akaanza kujifikiria ndio anakuwa mama wa ile nyumba, na kwa usafiri ule aliokuwa nao Jamal, sio pabaya sana kuanzia maisha. Hakuona chakupoteza kama akitoa penzi lake kwa Jamal, pengine atamvutia zaidi. Na kweli, hapakuwa na jinsi ungesema Jamal hakumfurahia Nanaa siku hiyo pale kitandani. Nanaa alitoa ujuzi wake wote siku ile kumfurahisha Jamal bila hata kujijali yeye. Alijituma kwa kadiri ya uwezo wake. Yale aliyokuwa akimfanyia Zac, ndio alipewa Jamal siku ile tena kwa juhudi huku akiongeza mautundu, asije kukimbiwa tena. Kwa Nanaa alikuwa ni kama yupo kazini. Lengo moja tu, ndoa. Awe na kwake, aepukane na kuishi au kuwa mzigo kwa mtu. Yeyote mwenye mafanikio kidogo ya maisha, huyo alimfaa. Hapakuwa na vigezo eti mwanaume mrefu. Sijui kifua kipana. Rangi sijui iweje! Hapana. Bora mwanaume, basi.



*****************************************************

Mapenzi yakachanganya, ratiba za maktaba zikaanza kuongezeka. Siku ambazo Jamal haendi kazini, siku hizo za jumamosi, Nanaa alifika nyumbani kwake asubuhi. Walipata kifungua kinywa pamoja, mapenzi kidogo, kisha kujisomea. Ikifika jioni, mapenzi tena yakuagana, ndipo anamrudisha Nanaa nyumbani kwao.



Mambo yakaenda vizuri, wakiwa wanatumia muda mwingi kusoma na mapenzi. Hapakuwa na maongezi mengi sana kati yao, kwani Jamal alionekana kumtaka zaidi Nanaa kitandani kuliko kitu kingine. Kile kitendo chakuonyeshwa anahitajika na mtu, kilimfariji sana Nanaa. Simu na ujumbe wakutakiwa usiku mwema, huku akiambiwa ni jinsi gani anasubiriwa kesho yake wakafanye hiki au kile havikuisha. Pengo la Zac likazibika kwa haraka sana. Yale aliyokuwa akifanyiwa na Zac, akakutana nayo kwa Jamal. Tena akimsifia vilivyo huku akimlaumu kumuacha akiwa bado anamuhitaji kwa mapenzi zaidi.



*****************************************************

Muda wa Nanaa wa kurudia mitihani yake ikafika. Akafanya akiwa ametulizwa kwenye penzi la Jamal aliyekuwa akimpa vihela vya hapa na pale vyakujikimu. Matokeo yakatoka, yale masomo akawa ameyafaulu, akaendelea mwaka wa pili na penzi la Jamal.



*****************************************************

 Urafiki ukarudi kati yake na marafiki zake, Zena na Tia, kwani Nanaa aliwaambia juu ya Jamal baada yakumuona anapilika pilika zisizoisha. Kama hakuwepo kwenye simu, basi anakuja kuchukuliwa na kuondoka. Ndipo Tia akamuuliza kulikoni. Ikabidi kuwaambia habari za kuvutia za mpenzi mpya mwenye gari na nyumba, si kama Zac.



 Zena akapata habari ya kuzidi kumchafua Nanaa kwa Terry, ili kumvuta kwake. Nanaa hakuwa akitoka nao tena, kwani alikuwa akija kuchukuliwa mara baada ya kipindi chao cha mwisho siku ya ijumaa. Kila alipokuwa akitoka kwenye lecture siku hiyo ya ijumaa, alimkuta Jamal akimsubiri nje. Alikuwa akimchukua siku za ijumaa anakuwa naye nyumbani kwake mpaka jumatatu asubuhi wakati Jamal akienda kazini ndipo anamshusha chuoni.



Nyumbani kwa kaka yake alikuwa akienda siku ya jumapili. Atakaa naye kidogo, na kumuaga. Kulala nyumbani kwa kaka yake akapunguza. Kama siku hiyo ya jumapili akienda kumtembelea kaka yake akapakuta pachafu, basi atamsaidia kusafisha na kufua. Akishaacha kila kitu sehemu yake na chakula, ndipo anaondoka kurudi kwa Jamal mpaka siku inayofuata, jumatatu.



Ilimbidi kuongeza juhudi ya kusoma hizo siku za kati kati ya juma. Maana siku hizo anazokuwepo kwa Jamal, kuanzia hiyo ijumaa jioni mpaka jumatatu asubuhi wanapotoka hapo kwa Jamal, Nanaa alikuwa mke kweli kweli. Kujituma kumpikia na penzi kitandani. Kufua na kufanya usafi kwenye kijinyumba hicho kidogo, ambacho Nanaa alishajiona ni mama mwenye nyumba. Yaani yupo kwake.



Asubuhi ya jumatatu pia Jamal alimuaga kwa kujiridhisha kweli kweli akimwambia kwa kujifidia kwa siku hizo ambazo Nanaa hatakuwepo hapo. Walifanya penzi la kufidia jumanne, jumatano na alhamisi. Ijumaa usiku alirudishwa kitandani hapo. Na jumatatu asubuhi alitoa sex ya nguvu ndipo wanapooga, nakuanza siku. Jamal kazini, Nanaa chuoni. Maisha yakaendelea.



*****************************************************

Penzi alilokuwa akipewa Jamal halikuwa kama la Zac. Kwani Zac alipewa kwenye hosteli na nyumbani kwa rafiki yake. Hapakuwa na uhuru. Alipewa penzi la kimya kimya sababu walijua wapo wanachuo wengine wanapita nje ya chumba chao, au walijua wapo wanachuo wengine chumba cha jirani. Wakiwa nyumbani kwa rafiki yake Zac, pia iliwalazimu kuwa wastaarabu japo walijua anajua kinachoendelea huko chumbani. Lakini hapo kwa Jamal, Nanaa alikuwa huru.



Kwanza ni nyumba anayoishi peke yake. Majirani wapo mbali. Jamal hakuwa na maneno mengi. Alimuonyesha wazi anamtaka kitandani tu. Kila asubuhi anapokuwepo hapo nyumbani kwake, nilazima amwamshe kwa kumtaka kimapenzi. Tena penzi la haja. Jamal hakuwa mvivu hata kidogo katika hilo eneo. Kitu kilichomlazimu Nanaa mwenyewe kujituma kweli kweli hata kama ni asubuhi. Ndipo aamke akaandae kifungua kinywa. Na baada ya hapo tena warudi tena kitandani.



*****************************************************

Alimshangaa vile Jamal alivyokuwa mkimya. Hakuwa akizungumza sana. Kama sio wanafanya mapenzi, basi wanaangalia mpira. Mechi za timu za nchi za bara la Ulaya au tamthilia za hapo hapo nyumbani. Alikuwa na mikanda mingi sana ya filamu ambayo walikuwa wakiangalia kila wanapokuwa pamoja. Na alimuonyesha wazi, pindi anapoangalia vitu vyake kwenye luninga, angependa kusikia na maneno. Kwa hiyo kunakuwa na utulivu wa aina yake.



*****************************************************

Siku moja ya jumapili wakati Jamal anaogo na Nanaa yupo kitandani, baada ya shuguli nzito hapo kitandani. Tena Nanaa akiwa anaugulia maumivu kwa mapenzi ya muda mrefu. Simu ya Jamal ikaanza kuita akiwa yupo bafuni. Nanaa akiwa hoi hapo kitandani, akigugumia maumivu ya michubuko mingi aliyoipata katikati ya tendo, nakushindwa hata kusema, au kumwambia Jamal ili tu kumfurahisha. Alibaki hapo kitandani akigugumia maumivu sehemu za siri huku akiitazama simu ya Jamal iliyokuwa ikiita na kukata.



*****************************************************

Tokea siku ya ijumaa wanafika hapo nyumbani mpaka siku hiyo ya jumapili, Jamal alionekana anataka kufanya mapenzi tu. Tangia anamchukua Nanaa chuoni, Nanaa alishamuona hayupo sawa. Alipoingia kwenye gari akajua kuna tatizo. Nanaa alimsalimia kama kawaida. Akarudisha salamu kwa kifupi tu. Baada ya kuona amekuwa kimya sana au mzito wa maongezi, akaamua na yeye anyamaze. Walipofika tu nyumbani siku hiyo ya ijumaa, akamshusha nakutoka kufuata chakula. Hakutaka Nanaa apike. Alimwambia aoge, nakumsubiria.



Ndipo mapenzi yakaanza bila maongezi mengi. Kila alipomuuliza kulikoni, alimbusu, na kuanza tena  mapenzi. Jumamosi nayo ikawa hivyo hivyo. Anatoka kwenda kununua chakula. Baada ya muda anarudi, kazi inaendelea. Kwa ukavu ule aliokuwa akikutana nao kwa Nanaa nakuendelea kufanya naye mapenzi bila kujali, wala kutaka kumlainisha kwanza, japo Nanaa alishamjua si mtu wa kujali anachojisikia yeye wanapokuwa kwenye mapenzi, lakini siku ile alizidisha. Hapakuwa na mapumziko marefu wala maongezi. Wakati wote alitaka Nanaa amchezee na kuanza mapenzi tena na tena. Nanaa alijua lipo jambo. Alimchubua vilivyo. Mpaka inafika siku hiyo ya jumapili, Nanaa hakuwa na hamu tena yakuwepo pale.



Mara hiyo ya mwisho kabla yakuingia bafuni kuoga na kumuacha hapo kitandani, Nanaa alihangaika naye sana ili kumfikisha. Alishasahau hata walianza saa ngapi. Alifanya naye huku akigugumia na kujikaza sana. Alishamuomba Mungu wake amkumbuke kipindi kile, Jamal amalize, apumzike. Mpaka anafanikiwa, Nanaa hakuwa na hamu. Alilala pale kitandani akiwa hoi na maumivu makali. Akiwaza kama amuage Jamal na kumwambia amepata zarula anatakiwa kuondoka, au amwambie ukweli kama anavidonda vinavyompa maumivu makali sana. Hataweza kufanya tena mapenzi siku ile. “Ataniona sifai. Heri niendelee kujikaza, lakini nimkwepe mapenzi leo. Angalau nijiuguze mpaka tena ijumaa ijayo atakapokuja kunichukua. Nitakuwa nimepona.” Simu ya Jamal ikaita tena na kumtoa kwenye mawazo.

Nanaa alizwa tena!

Akamwita Jamal mara kadhaa kumuuliza kama ampelekee simu hiyo huko uko bafuni au ajibu yeye, lakini Jamal hakusikia. Ikaita mara tatu, kisha ujumbe ukaingia. ‘Mtoto bado ni mgonjwa, mume wangu. Pesa uliyonitumia haijatosha matibabu na chakula. Uliniahidi kuja leo. Mpaka sasa hujafika na simu hupokei. Nimeamua kwenda kwenu ili wanisaidie. Mama yako ameamua kumrudisha Fatma hospitalini, Barabara ya kwanza, ili afanyiwe vipimo upya. Homa ipo juu sana. Hapa tulipo tupo hospitalini. Naomba upokee simu mume wangu. Unatutia wasiwasi, hasa baba.’ Nanaa alikaa kwa mshtuko.



Wakati anafikiria na kurudia ule ujumbe, Jamal akaingia pale chumbani. “Mbona umeshika simu yangu bila ruhusa!? Unatafuta nini?” Jamal aliiuliza kwa hasira. “Kwa nini hukuniambia kama umeoa na unafamilia!?” Nanaa aliuliza. “Uliuliza?” Jamal akajibu kwa kuuliza swali nakumfanya Nana ashindwe chakujibu. Alitamani kulaumu, lakini akakumbuka hamfahamu Jamal hata kidogo. Ni kweli hakudanganywa. Alitamani kulia. Lakini akajisuta moyoni. Anamlilia nani pale? Jamal hakuonyesha kufumaniwa hata kidogo.



Alichukua simu yake kutoka kwa Nanaa bila shida. Akavaa pensi yake, akatoka pale chumbani bila hata maelezo ya ziada kwa Nanaa. Bila kupoteza muda wala kuoga, Nanaa akavaa harakaharaka, akakusanya vitu vyake nakutoka. Alikutana na Jamal nje akizungumza na simu, akampita na kuondoka bila ya kumuaga.



Kwa kutumia pesa alizokuwa amepewa na Jamal siku chache zilizopita, akachukua taksii kurudi chuoni. Hakutaka hata kupeleka sura yake kwa kaka yake. “Vipi Jamal? Mbona umerudi leo badala ya kesho?” Zena alimrushia swali mara alipofika chumbani kwao. Aliwakuta wakiangalia tamthilia, kila mmoja akiwa kitandani kwake. “Wewe Nanaa? Si huwa unarudi jumatatu asubuhi!?” Nanaa alijitupa kitandani kwake, akalala bila kujibu kitu.



*****************************************************

Kwanza alikuwa na madonda ya penzi alilokuwa akilitoa tokea siku ya ijumaa alipochukuliwa hapo chuoni. Kwa hiyo alikuwa na maumivu makali sana. Alijichukia na kujidharau sana vile alivyokuwa akivumulia, ili kumridhisha Jamal. Alijinyima raha yeye, ili kumpa raha mume wa mtu! Kwa kipi? Kwa nini?  Nanaa aliendelea kujutia.



Pili alijichubua yeye mwenyewe donda la moyoni. Kwa haraka gani jamani!? Hata muda wakutosha haukuwa umepita tokea atendwe na Zac, akajitupa kwa Jamal. Bila kumfahamu Jamal, siku ya kwanza tu kukaribishwa nyumbani kwake, tayari kitandani, tena kwa sarakasi kibao! Nikulogwa au ujinga ulioje! Haraka hiyo ya kujigawa hivyo kama karanga za kwenye kapu zinazoonjeshwa kwa kila mtu, ili zinunuliwe hata kwa wasiokuwa na lengo nazo, ni za nini!?



Hayo yote yakazua ububu. Hakujua awaeleze nini wenzake. Walishamshuhudia akiwa kwenye mahusiano ya mapenzi na wanaume wawili. Kwa muda mfupi mfupi, ndani ya mwaka mmoja, tena walijua ni mahusiano mazito. Kwani Nanaa alikuwa akihama kabisa na kwenda kuwaridhisha hao wanaume zake huko huko watakapo wao. Halafu mahusiano yote hayakudumu! Anawaambia nini wao waliokuwa wakimsifia uzuri wa kila kitu? Alijua hata marafiki zake watamshangaa nakuhisi anakasoro kubwa.



*****************************************************

Tia bado alikuwa kwenye mahusiano na Evan. Na hakuwahi kumsikia akimlalamikia huyo Evan hata mara moja. Habari za Evan zilizokuwa zikiletwa humo chumbani, ni sifa zake tupu. Vile anavyojua kumjali, basi. Tena Tia msichana wa kawaida kabisa. Hakuna cha rangi nyeupe wala umbo namba 6 au 8. Hakuna alikopita wanaume wakageuka au hata kuhisi kama amepita msichana wa ajabu. Lakini alitangaza kuenziwa na mwanaume aliyeanza naye tokea yupo kidato cha 5. Sasa yupo chuoni mwaka wa pili. Tena sio na mwanaume wa kijijini. Evan. Mtoto wa jijini. Ametoka kwenye familia ya wasomi, wenye exposure. Anajua warembo na sifa zake. Lakini Tia alijisifu vile alivyotulia kwake.



*****************************************************

Alinyamaza pale kitandani, akijuta kwa nini aliwasaidia kutafuta chumba. Tena kuwafanya waishi nao chumba kimoja. Kama asingekuwa kuwasaidia kuwatafutia chumba, wala wasingeishi chumba kimoja. Usiku huo angekuwa na watu wengine. Wasiojua historia yake ya mapenzi. Wala si Zena na Tia. Na wala wasingejua kinachoendelea. Nanaa akajuta sana.



*****************************************************



 Kipindi Nanaa yupo hapo chuoni akijiandaa na kurudia mitihani yake, Zena alimtafuta na kumuomba awasaidie kutafuta chumba kwa kuwa yeye alikuwa maeneo ya hapo chuoni, na walijua kuna matron alikuwa akimpenda sana Nanaa, wakajua wakimpanga vizuri Nanaa, watapa chumba hapo hapo main campus’, wanapopapenda, tena kwenye sehemu nzuri.



*****************************************************

 Alinyanyuka kwenda kuoga baada ya maumivu kuendelea. Akaona akajisafishe labda maumivu yatatulia. Akanywa na dawa na kurudi kulala huku mikakati mikali ikiendelea kichwani mwake. Alishahangaika akidhani atapata mwanaume atakayempenda na kumthamini, akaishia kujidhalilisha. Alishagawa penzi kwa wanaume hao, lakini hakuna aliyeona uthamani wake. “Mhhh! Inatosha sasa.” Nanaa alijisemea moyoni. “Labda kweli shule ndio itakuwa mkombozi wangu pekee. Mapenzi yamenikataa. Nitulie, nishike moja. Shule tu.” Nanaa aliazimia moyoni.



*****************************************************

Alipopona tu madonda aliyoachiwa na Jamal. Tena alijiuguza kwa kujipaka mafuta kila wakati bila kumwambia mtu. Huku asijue kama inasaidia au la! Kama anajiongezea sumu mwilini au la! Kila alipooga na kujisafisha, alipaka mafuta mpaka akapona. Maswali ya hofu yalipita kichwani mwake akijiuliza mbali na madonda yale, ni nini kingine Jamal alichomuachia!? Yalimtesa sana. Mwishowe akaona asijichoshe na maswali ambayo anaweza kupata majibu yake.



Nanaa ambaye hakujua kama ni mchaga au vipi, akapiga moyo konde mpaka hospitali ya kulipia. Mbele ya daktari aliyemkuta siku hiyo akamwambia shida yake ni moja tu, kujua kama ameathirika au la! Alipomuuliza kwa nini hakwenda kwenye vituo vya ushari nasaha, akasema moyo wake ulimtuma hapo. Hataki kuulizwa maswali wala hataki kushauriwa. Yeye anataka kupimwa UKIMWI, apewe majibu yake, basi. Mengine atajua mbele ya safari.



Kwa kuwa ilikuwa ni hospitali ya kulipia, pesa yake tu. Nanaa akapimwa. Alikaa pale akisubiri matokeo yake huku mawazo yakizunguka huku na kule. Yalipotoka na kuambiwa hajaathirika, akatoka pale bila kuaga. Akajiwekea mikakati yake. Akajiambia lazima kuitimiza hata iweje.



*****************************************************

Na kweli Nanaa aliamua kutulia na shule tu. Aliachana na kila aina ya marafiki na vishawishi vitakavyoingilia shule yake, akatuliza mawazo shuleni tu. Muda wa kuwepo hapo hosteli ukapungua. Akaanza kuishi nyumbani kwa kaka yake zaidi labda kuweo na test au kipindi cha mitihani. Alifanya hivyo ili kupunguza kero za wanaume walioanza kumfuata mpaka pale chumbani anakoishi na kina Tia.Walipojua tu Nanaa ameachwa tena na Jamal, Tia na Zena wakaanza kumkwepa huku wakimcheka waziwazi. Nanaa akajua. Akaamua kujitenga nao kabisa.



Wakiwa wanamsengenya Nanaa kwa mafumbo bila kujua Evan dereva wao aliyekuwa akiwaendesha anawasikiliza. Zena na Tia wakiwa wamekaa kiti cha nyuma wakicheka bila habari. Wakajikuta wanaropoka jina la Nanaa na kusema kuwa ameachwa tena. Evan hakuchelewesha zile habari. Wakiwa wamesimama kwenye mataa, Evan akamtumia ujumbe Terry kwa haraka sana. ‘Naona Mungu amesikia sala zako. Nanaa hana mtu tena. Nasikia ameachana na huyo mwanaume mwingine. Changamka. Huu ndio wakati wako kabla hajakupiku mwingine.’ Evan alituma ule ujumbe pale pale wakati Zena na Tia wanaendelea kumcheka Nanaa.



*****************************************************

Terry akamtafuta Evan, wakapanga weekend inayofuata, lazima Evan arudi jijini ili kumsindikiza hosteli, kwenye chumba cha Tia na Zena wakijua ndipo watakapompata Nanaa, kwa kuwa walijua wakipanga kuwaita Zena na Tia mahali, Nanaa hatakwenda.



Na kweli ijumaa usiku Evan alitoka chuoni SUA akaenda moja kwa moja nyumbani kwa kina Terry. Wakazungumza na kupanga asubuhi na mapema waamkie chuo kikuu cha Mlimani. Ili tu Terry ambaye alikuwa akisubiri muujiza wake, akamuone Nanaa. Na kweli Evan rafiki watokea utotoni mwa Terry akawasili nyumbani kwao. Akamchukua, safari ya Mlimani ikaanza. Njiani alikuwa kimya. Evan alijua wazi anapanga hoja zake pindi atakapofanikiwa kumkuta Nanaa ambaye hawakuwa wamemuona kwa kipindi kirefu. Kila alipokuwa akimuulizia, Zena alimtinga na majibu aliyodhani yatavunja moyo wa Terry, lakini asijue ndio alikuwa akiongeza shauku ya Terry kuja kummiliki Nanaa.



Mungu alikuwa upande wao, walifika kwenye chumba cha kina Tia, saa nne asubuhi. Wakamkuta kweli Nanaa yupo. Lakini alikuwa kwenye simu. Mtu wa upande wa pili akiongea, ambaye alikuwa James. Nanaa alishawasalimia kwa kuwapungia mkono mara walipoingia chumbani hapo, akiwa na simu sikioni imeshikiliwa na mkono wa shoto. Wakulia ndio ulifanikiwa kuwapungia wakati wanaingia, akaendelea kukusanya baadhi ya vitu huku akizungumza kwenye simu.



Terry alijawa na furaha baada ya kumkuta Nanaa hapo ndani na kupata tabasamu lililosindikizwa na dimpozi nzuri za Nanaa. Akafarijika moyoni. Wakaendelea kusalimiana na Zena na Tia wakati Nanaa bado yupo kwenye simu. Ndipo wakasikia Nanaa akijibu, “Pole sana kaka yangu. Basi nakuja kukusaidia. Labda uji utakaa tumboni.” Hapo hapo Nanaa akachukua kijibegi chake kama pochi. Akawapungia tena mkono. Safari hii alikuwa akiwaaga, akatoka akiwa bado anazungumza kwenye simu.



*****************************************************

Haikuwa weekend nzuri hata kidogo kwa Terry. Pale pale alibadilika. “Twendeni basi.” Zena aliongea kwa sauti ya kuchangamka. Kwani waliingia na ofa ya kuwachukua na kuwapeleka kwenye kifungua kinywa. Terry alishabadilika mpaka alionekana usoni. “Hata mimi nipo tayari.” Tia naye aliongea huku akimsogelea Evan mpenzi wake. “Naombeni niwe muwazi. Mimi sitaongozana na nyinyi. Nilimfuata Nanaa, naona na yeye ameondoka. Sina kawaida ya kwenda kupata kifungua kinywa asubuhi asubuhi kwenye mabaa. Kwanza mimi sio mlevi, na pili kwetu wanakuwa na kifungua kinywa kizuri sana zaidi ya mahoteli mengi sana hapa mjini.” Akiwa na hasira, Terry akatoka.



Zena aliumia sana. Hapo hapo na yeye akakubaliana na matokeo. Kuwa hata iweje, Terry hawezi kumpenda. Wala hatawahi kuwa wake. “Nilidhani Terry atakuwa wangu!” Zena aliwaza moyoni, akiwa amejawa simanzi usoni. Japokuwa alishamuonyesha wazi kuwa anamtaka awe mpenzi wake, lakini Terry hakuonyesha kumtaka hata kidogo. Akakubali pia kosa halikuwa la Nanaa. Nanaa alishajitoa kwao muda mrefu sana. Na alikuwa na uhakika Nanaa na Terry hawakuwa wakiwasiliana hata kidogo. Kumuwekea kinyongo Nanaa alijua ni kumuonea tu.

Nanaa mwenyewe alishamruhusu amchafue vile atakavyo kwa Terry ili tu kumvutia kwake. Alielewa maumivu aliyonayo Terry kwa wakati ule, ‘kupenda asipopendwa!’ Inauma. Akamuhurumia kwani na yeye ndipo alipokuwepo kwa wakati huo. Alitamani ingekuwa vinginevyo ili mambo yawe tofauti. Lakini mapenzi ni kitu cha ajabu. Akaamua awaache tu Tia na Evan watoke wao peke yao. Yeye akabaki.



Nanaa ahama hostel na kurudi kwa kaka yake.

Akiwa njiani yale yaliyokuwa yakiendelea pale chumbani akiwa anazungumza na kaka yake kwenye simu yakamjia. Akakumbuka jinsi Zena alivyobabaika mara Evan na Terry walipoingia. “Bado Zena anaonekana hajafanikiwa kwa Terry.” Nanaa akawaza. “Inabidi nijiweke nao mbali kabisa. Hata pale chumbani nihame. Nisije nikarudi, akapata sababu yakunichukia zaidi.” Nanaa alishajua wanamchukia. Hakutaka wamrushie yeye lawama. Akakusudia kutulia nyumbani kwa kaka yake moja kwa moja. “Hakuna kulala kwengine tena isipokuwa kwa kaka tu.” Nanaa akakusudia kuhama kwenye hicho chumba ambacho ni kama yeye ndio aliwakaribisha wenzake. Akaanza kuhamisha kitu kimoja baada ya kingine bila kuaga.



 Sio wanafunzi wa mwaka wa tatu wala wa kwanza waliokuwa wakimtafuta Nanaa tu. Hata wenzake wa darasa moja walimtafuta. Alikuwepo kama hayupo. Akiwa mahali alinyamaza kimya kama hayupo. Kwanza angezungumza nini wakati habari zake zilishasambazwa kila mahali na kina Zena na Tia. Wakidhani wanamuharibia zaidi, kumbe ndio wanaamsha wale waliokata tamaa kwenda kujaribu bahati zao na wao kwa Nanaa.



Lakini Nanaa alikusudia. Alikataa katakata swala la shule na mapenzi. Hata uwe na pesa na kumuahidi kumpa yeye gari, Nanaa asingekubali tena. Waliposhindwa kwa Nanaa mwenyewe, waliwafuata marafiki zake ili wawasaidie kuwatongozea Nanaa. Alipoona fujo za Zena na Tia zanazidi. Wanachukua pesa zawatu kwa lengo la kugawa namba yake kwa watu asiowafahamu, akabadili namba na kuhamisha vitu vyake vyote pale chumbani. Maana wakati mwingine wa mchana, alikuwa akirudi kujipumzisha pale chumbani kwao, na ndipo hapo kina Zena hutoa habari kwa wanaume kuwa yupo chumbani. Akaamua kukusanya kila kitu chake mpaka kalamu. Na kweli akaacha kabisa kulala nje na nyumbani kwa kaka yake. Ikawa ni nyumbani kwa kaka yake James ambaye alikuwa kama ndiye ndugu wa pekee na mzazi wake Nanaa. Basi. Iwe karibu ya mitihani au la, Nanaa alihakikisha usiku analala nyumbani kwa kaka yake. Ikitokea anachelewa kumaliza kujisomea na wenzake, alimsihi James awe anamfuata chuoni ili arudi naye nyumbani.



*****************************************************

Hakika Nanaa hakuwa ametania. Alikusudia. Mpaka kina Tia wakaanza kuwa na hamu naye na kuanza kujirudi. Lakini aliyeng’atwa na nyoka, kang’atwa tu. Nanaa akawa makini kwa kila mtu anayemsogelea. Hakuonyesha hasira, lakini aliishi na kila mtu kwa tahadhari. Maisha yake ikawa shule, na nyumbani. Zena na Tia ndio waliobaki kusumbuliwa na wanaume. Na ndio waliokuwa wakipokea hongo ili kusaidia kumtongoza Nanaa, lakini Nanaa alibaki akiwacheka. “Mtakuja kubembwa juu juu nyinyi! Endeleeni kupokea pesa za watu.” “Sasa kama huyu kaka mwingine kwa nini unamkataa?” Tia  alimuuliza. “Hana lolote. Anataka anivue nguo tu, ili aniangalie hili tako likiwa halina nguo. Anichezee aje kuniumiza moyo wangu. Sitaki.” “Bwana huyu kaka anachanganywa na miguu yako.” “Sio miguu tu. Anasema anapenda kiuno cha Nanaa.” Zena alidakia. “Basi mpeni pole. Mwambieni ataendelea kukiona kwenye gauni tu, lakini hatawahi kuniweka kitandani.” “Basi nenda hata kazungumze naye, Nanaa shoga yetu. Tumekula pesa yake.” Nanaa alicheka sana. “Mtajijua wenyewe. Aliyewaambia mpokee nani? Nishamaliza kazi ya kuvulia wanaume nguo. Kama hawakubahatika kipindi kile cha mgao, wapeni pole. Waambieni Nanaa ameshamaliza mgao.” Akawacheka na kuondoka mapema kabla giza halijaingia kuwahi kwa kaka yake.



*****************************************************

Nanaa akajituliza mpaka mwaka huo wa pili ulipoisha. Hapakuwa na mapenzi tena. Alishakinahiwa. Jamal ndio alimchefua kabisaa. Mawazo yakawa shuleni, na Mungu akamfanikisha hapo. Hakukamatwa somo hata moja. Na yeye akawa amefaulu vizuri sana. Tena kwa alama za “A” tupu. Kwa hakika hata James akafurahi na kujisifu kwa wenzake. Lakini Nanaa akatakiwa kwenda field kabla yakurudi chuo kumalizia mwaka wake wa mwisho.

Wapi akafanye field hiyo? Akaanza kuhangaika kutafuta maofisi ambayo angefanya field hiyo lakini angalau wamlipe pesa kidogo ya kumsaidia hata nauli na hata wakiweza kumuajiri mpaka chuo kifungue, lakini akakosa. Hapo ndipo ikambidi azungumze na kaka yake. Ili amsaidie kumtafutia sehemu yakufanya field. James akamwambia ampe muda kidogo wa kutafuta.

Baaada ya kama siku mbili akamwambia amefanikiwa kumpatia kazi mahali. Amepata ahadi ya kazi kwa muda ambao muhasibu wa hiyo ofisi atakapokuwa likizo ya uzazi. Nanaa alifurahi sana na kumshukuru Mungu wake.

Nanaa Mchakato wa Field!

Siku ya jumamosi asubuhi Nanaa alisikia watu wakicheka na James sebleni kwao. Ndio na yeye alikuwa ameingia tu chumbani kwake baada ya kumaliza shuguli zake. Akaona atoke aangalie ni kina nani wanaomfanya kaka yake acheke hivyo. Alikuta ni mtu na mkewe. Wakitaniana sana na James. Akajua lazima watakuwa marafiki wa James. “Njoo Nanaa usalimie na uongee vizuri na Grace. Ndiye atakuwa bosi wako. Hakikisha unamuelewa usibaki unayashangaa hayo macho yake, akamaliza kuongea hujaelewa kitu.” Nanaa akamtizama Grace vizuri. Kweli alikuwa na macho yakuvutia. Akacheka.

“Usicheke mtoto wa kichaga. Tumekuja mjini kuzisaka pesa. Changamka na usipumbazwe na hayo macho na sauti hiyo, ukashindwa kuomba pesa kubwa. Maana wakati tupo pale chuo kikuu cha Mlimani, huyo Grace alizungusha vichwa vya wasomi wenye shahada zao, wafanyakazi, maprofesa,  na wafanyabiashara wa jiji. Watu wazima tukabaki kama wehu. Muulize Danny. Mimi mwenyewe nilitaka kuoa, lakini nikashindwa. Kila alipokuwa akiniangalia, maneno yalikuwa hayatoki. Mwenzangu Danny akaamua kufa kiume, lakini karibia tumkimbize Mirembe kwa kuchanganywa na Grace.” Wote walianza kucheka tena. Lakini Nanaa akawa ameshapata utambulisho wakujitosheleza. Danny ni mume wa Grace bosi wake. Marafiki wa kaka zake waliosoma pamoja.

“Achana nao hao. Wanapenda kunichokoza tu. Tutaelewana Nanaa, usiogope.” Grace alijibu huku akicheka. “Ashindwe kuelewa Danny mpaka leo, ataelewa mdogo wangu huyo? Kwanza hayo macho kwa mara ya kwanza yakikuangalia unakuwa kama unapumbaa hivi! Sasa Danny ndio alikuwa anatuchosha. Pesa hana, anamtaka Grace. Ukiangalia mgongo wa Grace, Danny alikuwa anazidi kuchanganyikiwa. Basi tukajua pakumpatia Danny. Tukitaka kumchanganya, tunamtisha, tunamwambia tumemuona Grace amepakizwa kwenye gari zuri sana, halafu huoni ndani, vioo vyeusi. Basi weee, Danny anapagawa!” James aliongeza nakuwafanya wazidi kucheka.

“Nakwambia nilipambana mpaka nikafanikiwa.” Danny aliongeza. “Na usifikiri akikwambia alipambana anadanganya? Nilikuwa sina raha. Alikuwa ananisumbua kupita maelezo. Yaani namgombesha mbele za watu, labda asubuhi, lakini mchana utamuona huyo amerudi. Angekuwa hasomei Eletronics huyu, watu wangesema hana akili vizuri.” Grace alijibu kwa sauti yake ya upole. “Mimi nakwambia vile ulivyokuwa ukinigombesha huku unanifukuza, nilikuwa nasikia raha. Nilikuwa narudi kwa kina James nawaambia Grace ameniongelesha.” Walizidi kucheka.

“Yaani anagombeshwa, lakini yeye anasikia raha! Danny mjinga sana huyu. Yaani mpaka tulikuwa tunamuhurumia.” “Halafu sasa suruali yake ni moja tu ya jinsi. Tisheti tu ndio alikuwa anabadili. Marafiki zangu walikuwa wananicheka. Halafu alivyo sasa Danny, anakufuata mpaka kwenye lecture, mbele za watu. Eti ananijulia hali! Nilikuwa nakasirika mpaka basi.” Grace aliwafanya wazidi kucheka. Mvumilivu hula mbivu. Huoni niliibuka mimi mshindi? Namiliki chombo mwenyewe. Nimewapiga bao watu na pesa zao.” Mumewe akajisifia.

“Hawa wawili hawa, na wenzao wenye akili kama zao, walisoma sekondari pamoja. Wakachaguliwa hapo chuo kikuu cha Mlimani. Wakawa chuo kimoja, mwaka mmoja, darasa moja, na sasa hawa wawili katika kundi lao, wanafanya kazi sehemu moja. Hawana jipya. Wananikera na macho yangu, sina raha. Huyo James kaka yako, na wenzake, walikuwa wanamsindikiza Danny kunitongaza. Basi James na wenzake walikuwa wanasimama mbali kidogo, wanatuangalia mimi na Danny tunavyoongea. Walikuwa wananiudhi kundi lao hawa! Sina hamu. Twende mwaya Nanaa tukazungumze hapo nje. Maana yule muhasibu wangu amepitisha siku za kujifungua, muda wowote ule anaweza akajifungua, nikabaki nahangaika. Ofisi yenyewe sio kubwa, lakini yeye ndiye anamajukumu mengi.” Wakatoka nje. Kuzungumza.

*****************************************************

Grace alizungumza naye taratibu. Kwa kumsikiliza tu, Nanaa akavutiwa na bosi Grace. “Sasa upo tayari kuanza kazi lini?” Grace aliuliza. “Hata kesho. Sina kitu chakufanya sasa hivi.” “Mbona wewe utanifaa. Ndio vizuri uanze mapema akuelekeze kila kitu, ili ikitokea anajifungua, tusikwame.” Nanaa akafurahi sana. Wakakubaliana mshahara, Grace na mumewe wakaondoka.

*****************************************************

 “Naona ulivyofurahi.” James alimchokoza dada yake. “Kasema atanilipa.” Nanaa alijibu huku akicheka. “Ni watu wazuri sana, hawana shida. Ninauhakika utafurahia kufanya kazi na Grace. Ni dada muungwana sana.” “Ni kweli ulitaka kumuoa? Mzuri kweli.” James akacheka. “Hapana. Huwa tunapenda kumchokoza tu. Danny, mumewe ni mtundu sana. Halafu Grace ni mpole. Wakati mwingine tunamchokoza tu ili aongee. Tokea shule huwa tunapenda vile anavyoongea kwa upole. Usipomchokoza Grace, hazungumzi hata. Atabaki kimya tu.” “Kwa hiyo Danny ni rafiki yako tokea zamani?” “Danny ni mtu wa watu sana. Alikuwa au tuseme ni  rafiki wa kila mtu. Alituunganisha marafiki tuliokuwa tukisoma pamoja tokea sekondari. Tukajikuta tunakundi letu. Utakuja kuwaona wengine. Danny hawezi kupoteza mtu. Mmoja wetu akipotea tu, atamtafuta mpaka tujue alipo. Mwishowe tumejikuta lazima kukutana mara kwa mara. Tulipotezana kwa muda, yeye alipoamua kurudi chuoni kufanya shahada ya pili. Akawa kimyaa. Alipomaliza akatukusanya tena. Ameajiriwa pale ofisini kwetu. Hata mwaka hajamaliza pale kazini, lakini kila mtu anamfahamu. Mpaka wafagizi wanamjua Danny. Kila anapopita anatengeneza marafiki anaowafanya wawe karibu yake. Mtundu sana na haishiwi maneno.” Waliendelea kuzungumza wakicheka vituko vya Danny alivyokuwa akisimulia James.

Nanaa aanza field.

Nanaa akaanza kazi kipindi huyo muhasibu anafunga mahesabu na kutengeneza ripoti ya mwezi. Walifanya kama siku mbili tu, Nanaa akiweka juhudi na kuuliza maswali mengi kadiri awezavyo. Akijua ile si field tu, sasa ni kama kazi. Na kama akiongeza juhudi, ni sehemu anayoweza kurudi kuomba ajira pindi atakapomaliza chuo.  Mshahara wa mwanzoni tu ulimvutia. Akajua akirudi na vyeti, basi mambo yake yatakuwa safi.

Kabla huyo muhasibu hajakamilisha ripoti, na Nanaa kuona inakuaje mpaka mwisho, chupa ya uchungu ikavunjika wakiwa ofisini. Wote walifurahi kwa kuwa huyo mtoto alikuwa akisubiriwa na watu wote pale ofisini lakini sio Nanaa. Nanaa alitaka waendelee kuwa naye ili amfundishe mpaka mwisho ili asije haribu, lakini ndio katikati ya mafundisho, chupa ikavunjika. Grace alimkimbiza hospitalini huku akiwa amempigia simu mumewe awafuate hospitalini. Nanaa alibaki pale hajui chakufanya.

*****************************************************

Alikaa hapo mpaka jioni wakati anakaribia kufunga, akasikia sauti ya mtu akiongea nje ya ofisi yao, akiwa mapokezi.  “Sasa hivi siwezi kufanya kitu cha maana G. Nimechoka na nina mambo mengi. Akili haijatulia. Kwa nini nisije siku ya jumamosi?” Alimsikia mtu akiongea taratibu kama Grace. Lakini huyu sauti yake ilikuwa nzito, nzuri ya kiume. Akasikia kimya kama mtu anayesikiliza upande wa pili. “Bwana wewe ni muoga tu, G. Unaweza.” “Siwezi. Wewe msaidie.” Nanaa alishtukia yule mtu amefungua mlango amemsimamia mbele ya meza yake na sauti ya Grace ikasikika kutoka kwenye sauti. Moyo wa Nanaa ukapasuka. Akabaki kimya asijue kwa nini.

“Labda jumamosi. Leo nitakuharibia kazi. Jumamosi akili itakuwa imetulia, au usubiri baada ya week ijayo.” Yule kaka aliendelea kuongea kwenye simu huku akivuta kitabu cha invoice mbele ya meza ya yule muhasibu, akaanza kuangalia taratibu. “Kwanza wala huna transanctions nyingi! Acha uvivu G. Fanya mwenyewe.” Waliendelea kuzungumza, Grace akisikika akimsisitiza yeye ndio afanye. “Basi nitakuja hiyo siku ya jumamosi, wewe zungumza naye muelewane. Nikifanya leo, nitamchanganya tu.” Grace aliendelea kuzungumza upande wapili. “Sawa. Hamna shida.” Akaitikia na kukata simu, na kumuangalia Nanaa.















Geb!

N

anaa hakuhitaji utambulisho, alijua wazi ni kaka yake Grace, bosi wake. Walifanana sana na Grace. Macho yao yalikuwa yakifanana sana. Makubwa kiasi na yakusinzia. Aliongea kwa utulivu kama Grace, yaani haiba ya utulivu kama Grace. Mweusi na nywele nyingi zilizoonekana alifanya juhudi za makusudi kuzitengenezea mustachi mzuri kuzunguka midomo yake na usoni. Nanaa alibaki akimtizama.

“Naitwa Geb, kaka yake Grace.” Akampa Nanaa mkono na kuendelea. “Alitaka nimalizie kazi ya muhasibu wake, lakini leo nimechoka sana. Nikisema nikae hapa, nitashindwa kukuelekeza vizuri. Ingekuwa nafanya peke yangu, hapo sawa. Lakini inaonekana G, anataka nikufundishe na wewe.” “Kwani ni ngumu sana? Naweza kukuangalia wakati wewe unafanya. Huna haja yakuongea sana.” Nanaa aliuliza, yule kaka akakaa kwenye kompyuta ya yule muhasibu na kuanza kuangalia bila kujibu kwa muda.

Huyu mwenzako nilitumia karibia mwaka mzima kumuelekeza kutengeneza hii ripoti tu. Mpaka kipindi fulani nikawa natengeneza mwenyewe. Nafikiri kama nikuweza vizuri, amefanikisha kama ripoti mbili za mwisho, nyingine zote ilikuwa lazima nizirekebishe sana. Ni kama nilikuwa nafanya mwenyewe tu.” Aliendelea kuperuzi kwenye kompyuta ya huyo muhasibu huku Nanaa amekaa meza ya pembeni isiyokuwa na kompyuta.

“Yaani mpaka hapa tu, naona nitahitaji siku nzima. Vitu vingi sana havijakamilika.” Aliendelea kuperuzi huku Nanaa akiwa kimya. “Daah! Kuko hovyo sana.” Aliendelea kuzungumza mwenyewe huku akiendelea kuperuzi.

Akaingia dereva wa hiyo kampuni. “Mzima bosi?” Geb alisalimia. “Kumbe mkuu mwenyewe upo hapa?” “Nipo.” Geb alijibu akarudisha macho kwenye kompyuta. “Kama upo basi ipo neema. Maana nina mzigo hapa, natakiwa kumkabidhi muhasibu kisha anikatie kiasi.” “Usinitie matatizoni bwana. Mimi sina pesa. Na sitaki kukaa na pesa ya mtu.” Geb alijibu huku akiendelea kuangalia kompyuta kwa makini.

“Unanikatalia bure bosi wangu. Najua wewe huna shida na pesa ndogo ndogo hizi.” “Unamuongelea Geb wa jana, leo hali mbaya. Mpigie simu bosi wenu umuulize chakufanya.” Yule dereva aliendelea kuzungumza na Geb wakionekana kufahamiana. Kwani walitaniana kidogo, mwishowe Grace akampigia simu Nanaa. “Pokea pesa kutoka kwa huyo dereva, kisha uumpe elfu 10. Hakikisha mnaandikishiana na anaweka saini sehemu kuthibitisha amepokea hiyo pesa na amekupa hiyo pesa.” “Sawa nitafanya hivyo. Kwani hutarudi tena?” Nanaa akauliza. Nitakuwepo hapo kesho. Geb bado yupo?” “Yupo.” “Sawa. Analalamika amechoka, hawezi kukusaidia kufunga mahesabu. Anataka kuja kufanya jumamosi. Utaweza?” “Saa ngapi?” “Atakwambia mwenyewe. Hapendi kufanya kazi siku za jumamosi asubuhi asubuhi, kwa hiyo haitakuwa asubuhi sana, usiogope.” Nanaa akacheka kidogo. “Sawa.” Alimuelekeza kidogo Nanaa, wakaagana.

*****************************************************

Baada ya makabidhiano, yule dereva aliondoka na kumuacha Nanaa na Geb pale ofisini. Geb alipiga simu kitengo cha stoo kuomba transction zote. “Mbona nilishatuma!?” Kijana aliyekuwepo kwenye kitengo hicho akajibu. “Ni sawa kama nikikuomba utume tena?” Geb aliomba kiustarabu sana. Nanaa akabaki akimwangalia kwa kujiiba. “Sawa. Nitafanya hivyo.” “Asante sana na samahani kwa usumbufu.” “Hamna shida.” Akakata simu na kusimama.

*****************************************************

 “Nilikwambia naitwa Geb?” “Ndiyo.” “Samahani. Akili zimechoka. Sasa bosi wako ameniambia huwa hufanyi kazi siku za jumamosi. Mimi nitakuwepo hapa asubuhi ya saa nne. Ukiweza kuja kutizama ninachofanya ni sawa. Ukishindwa, nitakuelekeza wakati mwingine. Haina haraka.” “Sawa.” Geb alimtizama kwa macho yaliyomfanya Nanaa abaki ameduwaa, asijue kama aliulizwa swali na kama alijibu sahihi. Akakumbuka kaka yake alimwambia asili ya macho yale yakikuangalia kwa mara ya kwanza, hupumbaza.  

Nanaa akajiweka sawa baada ya kuona bado anamtizama. “Si umesema jumamosi utakuwa hapa, saa nne ya asubuhi?” Nanaa akauliza kama kupata uhakika. “Ndiyo. Na wewe umesema sawa. Sasa, sawa hiyo nitegemee utakuja au utataka kujifunza wakati mwingine?” “Nitajitahidi kuwepo.” Nanaa aliongeza. “Basi usiku mwema. Tutaonana Mungu akipenda.” Geb akatoka. Ndipo Nanaa akapumua kwa nguvu kama aliyepata aghueni. Alihisi tokea Geb amtazame ni kama alishindwa kupumua tena. Akabaki anababaika. “Si kwa macho yale. Daah!” Nanaa alijiambia huku akijicheka.

*****************************************************

Isivyo kawaida yake, Nanaa ambaye hakuwahi hata kumfikiria mwanaume kwa umbile, akajikuta anabaki na taswira ya Geb. Kutoka kwenye kuapa hataki tena mwanaume, lakini akajisikia shauku ya kutamani jumamosi ifike haraka akamuone tena Geb. Hiyo ilikuwa siku ya jumatano Geb alipowatembelea pale ofisini. “Hivi hata jina nilimtajia kweli? Sijui ameoa au anampenzi? Daah! Yule akikutamkia ndoa, unasamehe hata mahari.” Nanaa aliwaza wakati amejilaza kitandani kwake. Alitamani Geb arudi tena pale ofisini au ajue habari zake zaidi, lakini hakujua amuulize nani.

*****************************************************

Siku ya jumamosi ilipofika, Nanaa alimka asubuhi na mapema nakuanza kujiandaa. Kila nguo siku hiyo haikumpendeza. Alivaa yakumbana, “Mmh! Ataona najirahisisha sana.” Akavua na kuvaa kubwa kidogo. “Hii hapana. Hata kiuno changu hakionekaniki! Wakati hiki ndicho kinawachanganya wengi!” Akacheka na kuvua. Alihangaika kuvua na kuvaa, mpaka akaishia kuvaa gauni la kawaida tu kwa kuwa muda ulikuwa umeisha, akaona atachelewa na kuonekanika sio msomi.

 Alitoka akiwa na haraka, akabahatisha daladala mpaka ofisini. Akakuta walinzi tu, na watu wa stoo waliokuwa wakipokea na kutoa mizigo. Aliingia ofisini kwa muhasibu akakaa akisubiri mpaka saa nne na nusu ndipo akamsikia Grace na Geb wanaingia.Walipita moja kwa moja ofisini hapo alipo Nanaa, wakiwa na mtoto mzuri sana wakiume, mwenye macho yanayo fanana na wao. Rangi yake pia alikuwa mweusi kama wao. Nanaa akabaki akijiuliza kama ni mtoto wa Geb au Grace.

Alimsalimia Nanaa kwa heshima akabaki anamwangalia. Nana akacheka. “Wewe vipi Fili?” Grace akamuuliza Fili. Akampa ishara ya ainame ili amnong’oneze. Grace akacheka na kuinama kumpa sikio. Yule mtoto ambaye alimtaja kama Fili, akamnong’oneza kitu Grace nakumfanya acheke sana. Akatoa simu na kupiga, kisha akaweka sauti kubwa.

Alipopokea tu, Grace akaanza. “James! Umepata shemeji.” “Nani?” Upande wa pili aliuliza ambaye ni James, kaka yake Nanaa. “Fili amesema Nanaa ni mchumba wake.” Wote walicheka mpaka Geb. “Kwa kuwa naonana na Danny jioni, mwambie Fili nimemkabidhi. Nitamalizana na dad hukohuko.” Ndipo Nanaa akajua kuwa yule ni mtoto wa Grace wala si Geb. Roho ikatulia. “Labda bado hajaoa.” Nanaa akawaza kwa haraka huku akicheka.

Nanaa alikuwa akicheka kwa aibu kwani bado Grace alikuwa akicheka huku akimwangalia mwanae. Akampigia simu Danny mumewe na kumsimulia. “Mwanao anataka kumuoa Nanaa.” “Sasa huko ndiko kuingizana umaskini. Mwambie kabla hajafikiria kuoa atafute kwanza kazi, ili apate pesa ya kumlipa James ya mahari. James atataka nyumba yangu bure.” Grace aliendelea kucheka na mumewe akilalamika.

Baada ya muda Danny akamuunganisha James kwenye simu wakawa wote watatu. “Hapa nishaanza kutafuta mteja wa nyumba yangu ile mbavu za mbwa. Mahari ya Nanaa ni mjengo wako Danny.” James aliongea mara baada ya kupokea simu. “Si nilikwambia Grace? Mtoto anataka kuniingiza umaskini huyo! Mahari yenyewe si umesikia?” “Acha kumuogopesha mwanangu bwana James. Hata kwa mkopo sisi tutaoa tu.” Grace alimtetea mwanae. “Tena Grace uishie hapo hapo. Mwambie Fili kama anamtaka Nanaa, awe na pesa yake. Mtoto anataka vitu vizuri huyo! Hajui vizuri garama?” Wote wakacheka. “Mpango wangu ilikuwa nimepeleke huyo Fili kijijiniii. Nikamchukulie mke kwa joo mbili, basi.” Danny aliongeza. Waliendelea kutaniana, huku vicheko vikiendelea. Ikabidi Grace awaage.

*****************************************************

Akamgeukia Nanaa. “Huyu anaitwa Geb. Mdogo wangu.” “Kaka yako bwana.” Geb alimkatisha. “Kwa kupenda ukubwa huyu! Mimi ndio mkubwa, nimempita kwa lisaa lizima.” Ndipo Nanaa akajua kuwa ni mapacha. “Kwani ukiniita kaka unapungua wapi, G?” “Haya. Na hivi unanisaidia, acha niwe mpole. Huyu ni Geb, anko wa Fili. Ndiye anayenisaidia mambo ya mahesabu kwenye maisha yangu yote. Usifikiri ni hapa ofisini tu.” Nanaa akacheka kidogo kama asiyesadiki. “Usifikiri nakutania. Nachukia sana hesabu, lakini yeye ni mtaalamu sana wa mambo ya mahesabu tokea watoto yeye ndio alikuwa mwalimu wangu. Halafu huwa achoki kufundisha. Atakuelekeza mpaka wewe mwenyewe ndio utachoka. Nitakuacha naye hapa. Ukichoka wewe uondoke tu, maana yeye anaweza kulala hapahapa.” “Siwezi kulala bwana. Saa kumi jioni mwisho. Naenda mazoezini.” Geb alidakia tena huku macho yakiwa kwenye makabrasha yaliyokuwepo hapo juu ya meza.

“Haya Nanaa, kazi kwako. Mtumie vizuri kumuuliza maswali yote, ili jumatatu ukiachiwa ofisi, usipate shida.” “Sawa, asante.” Nanaa alishukuru. “Nitakuja baadaye kumchukua Fili twende wote mazoezini. Au unasemaje?” Geb alimtizama Fili, akampa 5. “Ewaa. Ujiandae na uvae kabisa ile jezi yako na viatu. Nikija tu, tunaondoka.” Wakaona Fili anababaika wala hafurahii tena kwenda mpirani na anko. “Nini?” Geb akamuuliza Fili. “Unabaki naye?” Fili akauliza nakuwafanya wote wacheke. “Yaani huyu mtoto kama Danny!” Geb alicheka huku anatingisha kichwa. “Nanaa yupo kazini. Anatoka jioni. Ukimtaka umtafute kesho, hafanyi kazi. Sawa?” Geb alimjibu Fili. “Sawa.” Fili alijibu kwa kuridhika kwa ahadi ya kuonana na Nanaa kesho yake.



“Tutamtafuta kesho?” Wakati wanatoka walimsikia Fili akimuuliza mama yake na kumfanya Nanaa na Grace wacheke. “Wewe Nanaa umemchanganya mwanangu. Wala hakuwa hivi.” Grace aliongea huku akifungua mlango wakutoka nje ya ofisi, wakasikia wakifunga nakutoka.

*****************************************************

Palipita hali ya ukimya kidogo, Geb akiendelea na shuguli zake, na Nanaa akifikiria chakufanya. “Nimeshajisahau! Naendelea bila kukuonyesha. Sogeza kiti uone jinsi ninavyokusanya kila kitu, na kupangilia mpaka kupata ripoti nzima.” Nanaa alisogeza kiti na kukaa naye meza moja, kazi ikaanza. Kulikuwa na utulivu wa namna yake pale ofisini. Mara kadhaa Geb alitaka kujua kama bado wapo pamoja au alimuacha mbali, na mara zote Nanaa alisema anaelewa.

“Kama una swali lolote, usisite kuniuliza.” Geb alimgeukia kuona kama bado Nanaa yupo au alishahama pale. Yale macho alitamani yaendelee kumuangalia kwa muda. “Naelewa.” Nanaa alijibu kwa utulivu. “Na ujue mwezi ujao hii ndio kazi utatakiwa kufanya. Kwa hiyo uelewe kweli kweli. Ukiwa na swali uliza. Usisite. Na hakuna swali dogo au kubwa. Yote ni ya msingi.” “Sawa.” Nanaa alijibu.

*****************************************************

Waliendelea na kazi, ilipofika saa 7:30 mchana, Grace akampigia kaka yake. “Nikuletee chakula?” “Nataka nimalize kabisa. Nikila sasa hivi nitapata uvivu.” “Ndio maana hunenepi.” “Niwekee chakula changu, nikirudi nitakuja kula.” “Mama anasisitiza uwahi kurudi. Usikae huko ukajisahau kula.” “Sasa unataka nikumalizie kazi yako au unataka nije kula?” Grace alisikika akicheka.

“Liz amesema atakuja baadaye.” “Mfanye anisubiri, asiondoke mpaka nije.” “Changamsha mikono sasa.” “Sitachelewa.” “Vipi Nanaa?” “Yupo. Anaonekana kuelewa.” “Mruhusu akale.” “Sawa. Nitakuona baadaye, lakini usisahau kumfanya Liz anisubiri.” “Nitampa hiyo kazi Danny. Amuongeleshe mpaka umkute.” Geb alicheka kidogo, akakata simu.

*****************************************************

Hapo hapo baada ya Nanaa kusikia kuna Liz, alichafukwa na roho yake. Hasira za kusalitiwa zikampanda. Kumbukumbu za juhudi zake kujitoa kwa wanaume nakuishia kujidhalilisha zikamjia. Akaamua atoke pale. “Vipi!?” Geb aliuliza baada ya kuona Nanaa anavuta kiti chake kwa nguvu na kusimama bila taarifa. “Ni muda wa kula, si ndio?” Nanaa aliuliza kishari kidogo. Geb akabaki akimtizama. “Nakwenda kula.” Nanaa akaaga nakutoka bila kuongeza wala kujibiwa.

Hakuna chakula kilichopita kooni, akajikuta akitokwa na machozi asijue ni kwa nini. Aliingia chooni akakaa humo kwa muda, akarudi tena jikoni akatengeneza chai, lakini akaishia kuimwaga kwenye sinki. Alishikwa na hasira za ajabu, akashindwa kujizuia. Chuki kwa wanaume ikamwingia, akaamua kurudi ofisini.

Alifungua mlango akapokelewa na macho matulivu ya Geb. “Kwema?” Geb aliuliza kwa utulivu. “Najisikia vibaya, naondoka naenda kupumzika.” Alijibu kwa kifupi. Akachukua kipochi chake, nakutoka. Geb alibaki ameshangaa. Lakini lilikuwa jukumu lake kumaliza kazi aliyokuwa amepewa na dada yake. Akabaki akifanya ile kazi, asielewe kilichompata mwanafunzi wake. Kilikuwa kitendo cha muda mfupi. Hakujua kama ni maumivu ya gafla au alikuwa nayo kwa muda mrefu! Anamuuliza nani na Nanaa alishaondoka?

*****************************************************

Nanaa alitoka pale akarudi nyumbani. Akashukuru kutomkuta James nyumbani, akaingia chumbani kwake nakuanza kulia. Alilia kana kwamba Geb alikuwa mpenzi wake akamfumania. Na wala hakuwahi kulia vile hata alivyowafumania wapenzi wake wote. Alilia kwa kusononeka kutoka moyoni, huku akikubali kushindwa.

Alilia kukosa ambacho wala hakuwahi kumiliki na wala hakuwa akimfahamu Geb. Labda ni juhudi alizoweka kwenye kuvaa akitaka kumfurahisha? Ni kweli Nanaa kwa mara ya kwanza amependa? Amependaje mtu kwa kumuona tu? Hamfahamu Geb. “Sasa kwa nini nilie wakati hanifahamu na mimi simfahamu? Anamaisha yake na mimi ninayo yangu. Huu ni ujinga.” Nanaa aliwaza na kujikashifu. Akaamua kulala.

*****************************************************

Sababu ya kulia muda mrefu, alipitiwa na usingizi mzito mpaka akaamshwa na simu ya James. “Pole. Nasikia uliondoka kazini ukiwa unaumwa. Vipi?” James aliuliza. “Sasa hivi najisikia vizuri. Nilipatwa na kizunguzungu cha gafla, tumbo lilikuwa linauma.” “Unataka nije nikupeleke hospitalini?” “Hapana kaka yangu. Nimepumzika angalau sasa hivi najisikia vizuri.” “Pole sana.” “Asante.” Ukimya ulizuka kidogo.

“Unauhakika utakuwa sawa bila kwenda hospitalini?” Bado James alionyesha wasiwasi. “Usiwe na wasiwasi. Nikijisikia vibaya nitakupigia. Lakini sasa hivi najisikia vizuri.” “Basi nitamjulisha na Grace. Amenipigia simu akiwa na wasiwasi.” Nanaa alijisikia vibaya sana kwa jinsi alivyoondoka, hata yeye hakujua kilichompata. “Naomba uniombee msamaha. Niliondoka gafla.” “Afadhali uliwahi kuondoka kuliko kuzidiwa ofisini. Basi pumzika, usihangaike na kupika. Mimi nitakula hukuhuku, nitakuletea na wewe.” “Asante. Lakini usiwe na wasiwasi, nipo sawa tu.” “Sawa. Basi endelea pumzika, nitakuona baadaye.” Nana alivuta pumzi akajirudisha kulala vizuri.

*****************************************************

Wakati amejilaza ujumbe ukaingia. ‘Vipi, unaendeleaje? Geb.’ Nanaa aliusoma ule ujumbe na kuufuta pale pale bila hata kutaka kujibu. “Hayamuhusu.” Nanaa alijisemea na kuiweka simu yake pembeni kwa hasira. Akarudi kulala mpaka James alipokuja kumgongea kuwa amerudi na chakula. Aliamka kula na kurudi kulala. Siku inayofuata alilala karibia siku nzima. Aliamka jioni na kujikuta peke yake, James hayupo. Akapika na kuosha vyombo, akarudi chumbani kwake.

Ilipofika usiku akasikia sauti ya Grace, Danny na James wakiingia huku wakicheka sana. “Nenda kamuamshe tujue anaendeleaje?” Alimsikia Grace akimtuma James. “Unawasiwasi wakupoteza mfanyakazi nini?” Danny aliuliza huku akimcheka mkewe. “Ninavyomuhitaji huyo Nanaa! Sitaki yule dereva awe analala na pesa. Ataanza kuzitumia. Nenda bwana James.” Alimsikia James akisogelea chumba chake huku anacheka. “Nanaa! Bosi wako amekufuata.” Nanaa akafungua mlango. “Nilikwambia uwaambie najisikia vizuri, kaka. Wasiwe na wasiwasi.” “Wewe njoo uwasalimie, labda wataridhika.” Nanaa akatoka kuelekea sebleni. “Tumekuletea na mchumba wako. Labda utapona.” Grace alimuwahi Nanaa mara alipotokea, akacheka. Fili alikuwa amepakatwa na Geb kwenye kochi dogo, wametulia kimya. Halafu Grace na Danny wamekaa kwenye kochi kubwa.

“Nimepona. Nilimwambia kaka James akwambie, ili usiwe na wasiwasi.” “Afadhali. Pole sana. Tulikuwa tunamwambia James, tunaanza kupunguza mahari, tumekuletea icecream.” Nanaa alicheka, akaenda kupokea kopo dogo la Vanilla Ice cream. “Sijui kama utapenda. Tumechukua tu.” “Asanteni sana kwa kujali, na poleni kwa usumbufu.” “Hamna shida. Kwanza ndio tumepata sababu ya kuja hapa.” Danny alidakia nakumfanya James acheke.

“Sasa unataka nini hapa kwetu?” James akauliza huku akicheka. “Si basi tu. Kwani hujawahi kuona wale watu wasiopenda kwao?” Danny aliongeza nakufanya wote wacheke kasoro Geb, alibaki akimbembeleza Fili aliyekuwa amelala kifuani kwake. Aliendelea kupitisha mkono wake mgongoni kwa Fili taratibu. Nanaa alijifanya kama hajamuona na wala na yeye hakuzungumza chochote, alibaki kimya tu akibembeleza mtoto.

 Jumatatu!

Alifika ofisini siku ya jumatatu akaendelea na shuguli zake kama kawaida. Ilipofika mchana, alisikia sauti ya Geb akiwa ameingia hapo ofisini akiongea na dada yake wakiwa mapokezi. “Utakuwa hunidai.” Alimsikia Geb akimwambia Grace. “Mbona nakushukuru. Nimeipitia ripoti nzima, naona mambo sio mabaya.” “Lakini bado nikiangalia nafikiri unaweza kutengeneza faida kubwa zaidi, G.” “Umeniambia. Tupate basi muda tuzungumze zaidi ili unishauri chakufanya.” Geb aliaga, akaondoka bila hata kusogelea ofisi ya Nanaa, akamsikia Grace anakuja ofisini kwake. Geb ametuletea bank statement ya mwezi uliopita. Naomba uitunze, atakuja kudai wakati wakutengeneza ripoti.” “Sawa.” Nanaa aliipokea na kuiweka kwenye faili lake.

Ijumaa ya pili tokea afute ujumbe wa Geb.

Yalipita majuma mawili mfululizo bila kumuona Geb pale ofisini wala hakutuma tena ujumbe. Alitamani kumfahamu zaidi kama anakofanya kazi, na mambo mengine mengi lakini akaishia kujiambia haina sababu. Siku ya ijumaa wakati anakaribia kutoka, akiwa anarudisha mafaili mengine pale mapokezi, akamuona Grace anaongea na simu kwenye mlango wakutokea nje ya ofisi. “Nanaa!” Grace akamwita. Nanaa akamsogelea. Kesho ni birthday ya mchumba wako. Tutamfanyia sherehe ndogo tu. Unaweza kuja na James kama huna kitu kinachokufunga.” “Saa ngapi?” “Saa kumi na nusu jioni. James anafahamu hoteli ambayo huwa tunafanyia. Nitamwambia mje naye.” “Anapenda zawadi gani?” Nanaa akauliza. “Mmh! Wala usihangaike. Anamichezo mingi sana, naona hata mingine hachezei. Wewe njoo tu.” “Nije mikono mitupu!?” Grace akacheka. “Basi njoo nyumbani uje unisaidie kuandaa zawadi zakuwapa watoto watakao hudhuria hiyo party, halafu tutaondoka wote kuelekea huko kwenye sherehe na hizo zawadi.” “Hapo sawa.” Wote wakacheka. “Mnakaa wapi?” “Nitamtuma Danny au James wakulete nyumbani. Usiwe na wasiwasi. Utafikishwa tu.” Nanaa alifurahia kuona amepata kitu chakufanya siku inayofuata.

Jumamosi ya siku ya birthday ya Fili.

Siku inayofuata, siku ya jumamosi ambayo amealikwa kwenye shuguli ya Fili, aliamka asubuhi na mapema akiwa amejawa furaha. Akafua nguo zake na kaka yake. Akasafisha nyumba, baada ya kuandaa kifungua kinywa, akabaki amekaa chumbani kwake akimsubiria James aamke ili ajue ni saa ngapi atampeleka nyumbani kwa Grace. Alimsikia James ameamka, anamwita. Akatoka. “Nahisi Grace atakutaka mapema. Danny amenipigia kuniambia msichana wao wa kazi ameondoka leo asubuhi.” “Utanipeleka?” “Ngoja nile kwanza. Nimeamka na njaa. Nitakupeleka kwenye saa tano hivi.” Nanaa alirudi chumbani kwenda kujitayarisha, akamuacha James anapata kifungua kinywa huku akiongea na kucheka kwenye simu.

*****************************************************

Ilipofika saa tano na nusu, Geb alifika. “Niambie Muhashamu wa jimbo!” James alimchokoza. “Nipo kaka. Nimetumwa kumfuata Nanaa.” “Pole kwa usumbufu. Kuna mahali natakiwa kwenda sasa hivi. Nikaona mpaka nimalize huko, nije nimchukue hapa na kumleta huko kwenu, nitachelewa.” “Hamna shida.” Geb alijibu.

James alienda kumwita Nanaa ambaye tayari mapigo ya moyo yalikuwa yakimwenda mbio baada yakusikia sauti ya Geb ndani ya nyumba yao. “Nilimuomba Grace amtume mtu akufuate. Kunamahali natakiwa kwenda. Geb ndio amekuja kukuchukua. Tutaonana jioni kwenye shuguli.” “Hamna shida.” Nanaa alitoka akamkuta Geb amekaa kwenye kochi akimsubiri.

Hakuwa amemuongelesha tokea siku alipomuacha ofisini, tena kwa hasira na hata alipofika siku ile akiwa na familia ya dada yake, Nanaa hakumsalimia. “Habari yako?” Nanaa akasalimia. “Nzuri.” Geb akajibu kwa ufupi tu. “Mimi nipo tayari.” Nanaa akaongeza, Geb akasimama. “Sasa kaka?” Geb alimgeukia James. “Tutaonana jioni. Acha mimi nikasake pesa kwanza.” “Sawa. Baadaye basi.” Geb aliaga nakutoka, Nanaa akamfuata nyuma baada ya kuagana na kaka yake.

*****************************************************

Alikutana na gari ya rangi ya silver, aina ya ‘Cadillac Escalade, SUV’ ikisubiri nje. Nanaa alibaki ametoa macho. Hakuwahi kuona gari nzuri vile. Akabaki anashangaa. Alisikia Terry na Evan pamoja na marafiki zake wakishindana kutajiana aina ya magari ambayo ndio ndoto zao. Na kama endapo watafanikiwa kimaisha watanunua magari hayo. Nanaa hakuwa hata anaelewa hayo majina. Hakuwa kwenye ulimwengu huo wakuwaza aina ya magari wakati hata pa kulala ilikuwa shida. Hakujua aina ya magari, na hakuona umuhimu wa mtu kupoteza pesa nyingi eti kwa ajili ya kununua tu gari, mpaka alipokutana na ile gari pale nje. Ndipo akaelewa kwa nini kuna aina ya magari, na watu wanapenda aina fulani.

Wazo la kwanza alifikiria kama angepiga picha kwenye lile gari. “Hata nikipiga picha itasaidia nini? Niache ushamba.” Nanaa alijisuta. “Khaaa! Sio kwa uzuri huu wa gari jamani!” Alibaki akikodoa macho. Geb alipoona amezubaa pale nje, akarudi upande wa abiria. Mlango wa mbele, akamfungulia mlango. “Karibu.” Akamkaribisha kama kumshtua na kumtaka waondoke. “Asante.” Akasogea. Tayari miguu ilikuwa ikicheza. “Ndani litakuaje? Hizi nguo haziendani na hili gari hata kidogo.” Nanaa aliendelea kuwaza wakati anasogelea mlango. Akaingia, Geb akafunga mlango.

Geb alijua wazi Nanaa amebabaika na lile gari. Alitegemea. Akamcheka moyoni kwani alishindwa kuzuia mshangao wake. Alishangaa mpaka mdomo aliacha wazi. Geb hakujua kama Nanaa alijijua jinsi alivyoachama mdomo na kutoa macho baada ya kuona lile gari. Alicheka tena moyoni, akatulia tu usoni.

Alimsubiri ajifunge mkanda ndipo aondoe gari. Nanaa hakujua hata kama anatakiwa kujifunga mkanda. Akabaki ametulia kwenye kitu huku akishangaa ile dashboard. Akagundua safari haijaanza. Wapo pale pale. Akamgeukia dereva wake. “Nasubiri ufunge mkanda.” Haraka sana, Nanaa akajiangalia gauni alilokuwa amevaa. Lilikuwa la lastiki kiunoni. Ni kweli lilikuwa na vijinyuzi vyembamba pembeni. Vyakupitishia mkanda wa gauni. Lakini Nanaa hakuwa amevaa mkanda. Alivaa bila mkanda. Lilikuwa la kuchanua chini. Kigauni cheusi. Polka dots za gold. Kilikuwa kina mikono mifupi iliyoshuka chini kidogo ya mabega. Kilimwagika vizuri sana chini ya kiuno.

“Sikupataga mkanda unaofanana na hili gauni.” Nanaa alijitetea. Bado Geb alikuwa akimtizama wakati anajiangalia na kuendelea kuvuta lile gauni na kulikusanya chini ya mapaja kama kulikalia. “Kwa hiyo hapa sina mkanda.” Aliendelea kujieleza, akionekana kupaniki tayari. “Namaanisha mkanda wa gari. Kwa ajili ya usalama wako.” Geb aliongea kiungwana. “Oooh! Mkanda wa gari. Nil..nil …nilifikiri..” Akaanza kupambana kuvuta mkanda wa hilo gari pembeni ya hicho kiti alichokuwa amekalia. “Nikusaidie?” Geb aliuliza baada yakuona anatumia nguvu nyingi kwa kuvuta mkanda ambao hata Fili huwa anavuta bila shida.

*****************************************************

Nanaa alijisikia aibu mara mbili. Sio kosa lake. Amepanda wapi gari zuri hivyo? Kaka yake James ana gari nzuri. Lakini ni ya kawaida tu, na huwa Nanaa mwenyewe hapandi mara kwa mara kwa kuwa James anatumia gari ya ofisini siku za kazi, na hawaongozani na Nanaa. Wanafanya kazi pande mbili tofauti za Dar. Ofisi za kina James zipo njia yakuelekea Kawe kutokea Morocco. Na ofisi ya kina Nanaa, ipo Kariakoo Karibu na Fire. Siku za weekend James anakuwa na mishuguliko yake na gari yake, Nanaa anabaki nyumbani. Akiwa na safari basi daladala itahusika.

Mwanaume mwingine aliyekuwa naye na mwenye gari alikuwa Jamal. Jamal alikuwa na gari aina ya Mark 2. Nayo ilikuwa ya kawaida sana.  Tena ilionekana ni ya zamani. Jamal aliinunua kwa mfanyakazi mwenzake akiwa ameshaitumia kwa miaka mingi tu. Na huyo mfanyakazi mwenzake alinunua used ya Japan. Vioo vilishaharibika. Hakumbuki hata kama lilikuwa na mkanda. Milango ya hilo gari ya Jamal ilikuwa lazima ufunge kwa nguvu. Tena wakati mwingine mara mbili au tatu.

*****************************************************

Nanaa aliendelea kupambana na mkanda wa kiti chake mpaka alipochoka. Akakubali kushindwa. Geb alikuwa ametulia kimya, akimsubiria achoke ndipo amsaidie. Kwa kuwa alijua kwa uvutaji ule, lazima mikanda iji lock. Kwa hiyo alimuacha apambane mpaka achoke ndipo arudie tena kuuliza kama angetaka msaada. “Naona mikanda mibovu.” Nanaa aliongea kwa upole, baada ya kupambana na ule mkanda na kushindwa.

Geb alimsogelea. Mapigo ya Nanaa yalianza kwenda kasi. “Ananipa pole kwa kunibusu!?” Aliwaza harakaharaka huku mapigo ya moyo yakienda kasi wakati Geb akijivuta upande wake. Akanyoosha mkono kwa tahadhari kama asiyetaka kumgusa. Akavuta ule mkanda kwa urahisi sana, akamfunga. Nanaa alivuta pumzi kwa nguvu. Akajiweka sawa pale kitini huku aibu imemlemea.

*****************************************************

Kwenye nyumba aliyopangisha kaka yake, hapakuwa na geti. Kwa hiyo ilikuwa rahisi kuingia na kutoka bila shida. Hakujua aseme nini tena. Alishajidhalilisha vyakutosha. “Sio kosa langu. Sijazaliwa kwenye magari. Hata yeye kuna mambo hajui. Kwani yeye ni Mungu kuwa anajua kila kitu? Wala sio jambo la ajabu nililolifanya.” Nanaa alijitetea kwenye nafsi yake. “Lakini nisingesingizia kuwa mikanda ni mibovu! Gari yenyewe inaonekana mpya. Lazima nibadili mazungumzo. Kuondoa hii aibu.” Akawaza kama ajieleze juu ya ujumbe ambao hakujibu au vile alivyomuacha pale ofisini bila maelezo ya kutosha, na pia akamfuata nyumbani kwao, akashindwa hata kumsalimia. “Labda nitulie tu.” Nanaa aliwaza.

*****************************************************

Akajifunga mkanda wake na yeye, kisha akaondoa gari. Geb hakuongeza neno wala kuuliza swali, aliendelea kuendesha akiwa ametulia kimya kana kwamba yupo peke yake kwenye lile gari. “Itakuwa gari ya dada yake hii. Grace anapesa sana.” Nanaa alianza kuwaza wakati Geb akiendelea kuendesha. Akakumbuka ripoti ya mwezi uliopita ilivyoonyesha faida kubwa waliyoingiza. “Hakika Mungu amembariki yule dada.” Nanaa akaendelea kuwaza.

Alishangaa kuona wanapita Ubungo, wakielekea njia ya Mabibo hosteli. Akamkumbuka Zac, mpenzi wake wazamani. Kidogo akaanza kukosa raha. Akajiweka sawa na kugeukia dirishani. Akaegemeza kichwa vizuri hapo dirishani, akabaki akiangalia nje ya dirisha. Mawazo yalimpeleka moja kwa moja mpaka siku alipomfumania Zac. “Mmmh!” Alipumua kwa nguvu huku ameshika shavu. Geb alimtizama, lakini akagundua Nanaa hakuwepo pale kimawazo hata kidogo. Macho yake yalikuwa nje ya lile gari.

*****************************************************

Mawazo yakampeleka siku ya kwanza akitolewa bikra na Alex. Akakumbuka yale maumivu. Akakusanya miguu yake pamoja. Akakumbuka ule utayari baada ya kujishauri kwa muda mrefu kama amkubalie Alex au la. Alex alikuwa mkubwa kwake. Lakini wakati wote alimbembeleza wafanye mapenzi. Ili asimpoteze au akaenda kuridhishwa na mwingine, Nanaa aliyekuwa na shauku ya kutoka kwa mama yake mkubwa. Akaamua kumpa Alex bikra yake. Akamruhusu yeye ndio awe mwanaume wake wa kwanza.

Akiwa anavuja damu pale kitandani wakati Alex amekimbilia dukani kununua pedi, Nanaa aliendelea kugugumia maumivu. Kwani ni kama Alex hakuwa amemuelewa Nanaa, pale alipokuwa akimsihi afanye taratibu. “Naomba uwe mwangalifu Alex. Mwenzio sijawahi kufanya mapenzi.” Akiwa amejawa hofu, binti huyo wa sekondari alimsihi Alex aliyekuwa chuoni. Akiwa na tumaini la kuja kuolewa. Lakini Alex alimwingilia kama aliyekuwa anapambana. Na bado Nanaa alivumilia mpaka mwisho wa Alex akapiga bao. “Nilijua kwa hakika Alex anganioa! Nilijua ni wangu! Lakini aliamua kuzaa na Viola! Nina kasoro gani mbaya hivyo inayowafanya wanaume kunikimbia?” Hakukumbuka kufurahishwa kimapenzi na Alex hata mara moja. Na wakati wote Alex hakuonyesha kama anajali furaha ya Nanaa kwenye tendo hilo. Ilimradi yeye amefanikiwa, aliishia kumshukuru kwa juhudi zake.

Mawazo yakamrudisha kwa Jamal. “Jamal ndio alinionyesha ni kama alikuwa akipunguza haja zake tu mwilini mwangu. Hapakuwa na penzi lolote pale. Hata nilipomwambia ninafahamu kuwa ana mke, hakuonyesha kujali hisia zangu. Mbona sina bahati!? Ni nini wanakutana nacho huko kwenye mwili wangu kinachowachefua na kushindwa kunithamini?” Nanaa aliendelea kuwaza na kuumia moyoni.

*****************************************************

Walikutana na foleni kubwa kwenye njia yakuingilia Tabata. Wakasimama. Ndipo Nanaa akajua wanaelekea Tabata. Alishindwa kuuliza wanaelekea Tabata ipi, kwani hakuwa amemuongelesha chochote dereva wake, tokea amfunge mkanda. “Hivi nilisema hata asante kweli?” Nanaa alijiuliza na kujichukia. “Ustarabu ni kitu kidogo Nanaa jamani! Hata asante hukusema!” Akajisuta kidogo. “Nitakuwa nimesema bwana.” Akajitetea nafsini mwake. “Hata kama sikusema, nani alimwambia anifuate na mgari wa ajabu? Kwanza abiria huwa hawatakiwi kufunga mkanda. Ajali ikitokea? Au kwa nini basi mikanda iliwekwa kwenye viti vyote!?” Nanaa aliendelea kupambana na mawazo yake.

*****************************************************

Simu ya Geb ilianza kuita. Nanaa akagutuka, na kujiweka sawa. Alishangaa mlio unalilia kwenye spika za gari. Akatulia kidogo. “Huo sio mziki bwana! Hata kama ni ushamba sio kwa kiasi hiki. Niache kujifanya mjinga wakupita kiasi.” Akaona Geb anabonyeza kwenye kitufe kilichopo kwenye usukani wa hilo gari. “Kuna foleni kweli. Lakini tupo njiani tunakuja.” Geb aliongea. “Amejuaje aliyempigia?” Nanaa akajiuliza huku akitafuta kusoma kama kuna sehemu iliandikwa jina la mpigaji. “Mbona anazungumza naye bila mwenzie kujitambulisha? Au namba imetokea mahali ndio akajua? Lakini wapi sasa!? Mbona haweki simu masikioni!?” Nanaa aliendelea kujiuliza.

 “Kama hutajali naomba upitie matunda sokoni. Nilimtuma Danny, amesahau.” Alikuwa ni Grace. Nanaa akatambua sauti ya bosi wake. “Lakini amemjuaje mpigaji? Maana ameanza kuongea moja kwa moja baada ya kupokea tu!” Akaanza kuchungulia kwa makini kwenye dashboard kuona kama kuna mahali kunaonyesha namba au jina. “Hamna shida. Tunaweza kupitia sokoni. Lakini ujue tutazidi kuchelewa. Kuna foleni kubwa kweli.” Geb alijibu. “Ni afadhali mchelewe lakini mje na hayo matunda. Fili ameshaanza kuulizia juisi yake. Nimemzungusha lakini naona anaanza kunibadilikia.” “Sawa.” Geb alijibu na kukata simu. Walikuwa wakizungumza kwa kutumia spika ya gari, kwa hiyo hata Nanaa alikuwa akiwasikiliza. Grace aliongea kwa utulivu kama Geb. “Watakuwa wanaishi wote na dada yake.” Nanaa aliwaza.

“Naona twende hapo Buguruni sokoni, itakuwa karibu zaidi.” Geb alimgeukia Nanaa, macho yao yakagongana. “Sawa.” Nanaa alijibu na kukwepesha macho kwa haraka. “Lakini alijuaje aliyempigia?” Bado Nanaa aliendelea kujiuliza lakini hakutaka kujiabisha zaidi. Aliona Geb anahama upande mwingine kurudi barabarani ili kuelekea Buguruni sokoni. “Kwani huko kwao hakuna magenge wanayouza matunda!?” Nanaa alijiuliza.



Zena kwa Nanaa tena.

Simu yake ikaanza kuita. Yake haikutolea mlio kwenye spika za gari, bali kwenye kipochi chake kidogo alichokuwa amekipakata. Akaitoa ikiwa imeshakatika. Aliposoma jina la aliyempigia. Akaguna kwa sauti. “Mmmh!” Geb akamtizama. Ikaanza kuita tena. “We Zena? Umekosea namba au ulitaka kunipigia mimi!?” Nanaa aliuliza mara baada ya kupokea. “Nanaa naye!?” “Nini?” “Nakupigia wewe bwana. Za siku?” “Nzuri.” Nanaa alijibu, wazi alionekana yupo kwenye mshangao.

 “Sasa mbona hata huniulizi na mimi?” “Nipo bado kwenye mshangao Zena. Siamini kama umenipigia mimi simu.” “Hamna bwana. Nimekuwa na hamu na wewe. Ulishaanza field?” “Wewe Zena? Hebu acha kunidanganya bwana. Niambie una shida gani?” “Nakujulia hali tu shoga yangu.” “Yameanza lini? Kwani Tia ameenda wapi?” “Nanaa naye?” “Zena? Usinifanye mimi mtoto mdogo. Najua unashida. Wewe niambie tu.” “Mpaka naona aibu.” Nanaa akacheka. “Aibu ya nini sasa? Wewe niambie. Mimi nilielewa. Wala usijali.” “Mmmh Nanaa wewe! Kweli?” “Kabisa Zena. Wala usijali. Niliwaelewa kabisa wewe na Tia. Usijali. Niambie.” Walifika sokoni.

 Geb aliegesha gari. Akabaki ametulia kwenye kiti chake bila hata kufungua mlango wala kuzima gari. Nanaa hakuwa ameelewa ule ukimya. “Naomba usubiri kwanza Zena.” Akamgeukia Geb baada ya kubonyeza sehemu ya MUTE ili Zena upande wa pili asisikie. “Tumefika sokoni. Unaweza kunisubiri tu kwenye gari. Nitajitahidi kuwahi kurudi.”, “Hutataka msaada?” Nanaa akauliza. Geb akafikiria kidogo. “Hapana. Nitarudi baada ya muda mfupi sana. Nisubiri tu.” Akashuka na kumuacha Nanaa ndani ya gari.

Akaendelea na Zena. “We Zena?” “Kwani uko wapi?” “Buguruni sokoni. Kwani vipi?” Nanaa akauliza. “Kwanza nikuombe radhi shoga yangu. Nilikukosea.” Nanaa akacheka. “Mbona kama huamini?” “Nakusikiliza.” “Umenisamehe?” “Wewe Zena? Nimekwambia nilielewa. Mbona kama nahisi shida yako ni kubwa sana? Unanianzia mbalii!” “Wala sio uongo shoga yangu. Nimepata mwanaume.” Nanaa akaanza kucheka.

“Usicheke bwana! Sasa Tia yupo mbali. Jamaa mwenyewe anaonekana yupo vizuri. Natamani anioe.” “Hongera Zena.” Nanaa alimpongeza mwenzie bila hila. “Lakini nataka uje leo tutoke wote. Na yeye akiwepo. Kisha kwenye mazungumzo yetu, nitagusia maswala ya ndoa kwa ujumla, halafu wewe naomba uulize maswali kwa makini. Kama swala la kumpima na mengineyo. Sitaki kupoteza naye muda.” “Ujue una kichaa wewe Zena?” “Nisaidie shoga yangu. Mimi kama namuogopa.” “Sasa utaolewaje na mwanaume unayemuogopa? Mtazungumzaje mkisha oana? Au utataka nihamie kwenu?” Zena aliendelea kumbembeleza Nanaa, huku akimsikiliza hoja zake. Baada ya muda Geb akarudi na mifuko mingi sana ya matunda.

*****************************************************

Akafungua mlango wa nyuma. “Subiri kwanza Zena.” Nanaa akamuweka tena kwenye Mute na kumgeukia Geb. “Naweza kukusaidia? Naweza hata kuyapakata hapa mbele.” Nanaa aliuliza. “Haina haja. Nitayaweka tu hapa kwenye boksi kubwa, yasikuchafue wala kuchafua gari.” Geb akajibu. Akaanza kuyapanga huko nyuma ya gari kwa uangalifu huku Nanaa akimtizama akiwa amegeuka nyuma, akabaki akimtizama vile anavyoyapanga kwa makini. “Anaogopa kuchafua gari ya dada yake. Wala sio mimi.” Nanaa alijisemea moyoni.

“Labda atakuwa hana kazi ya maana, ndio maana dada yake anamtumatuma.” Nanaa aliendelea kuwaza. “Wakati mwenzake anasoma na kujiendeleza sijui yeye alikuwa wapi!? Kweli duniani watu hawafanani. Yaani hawa ni mapacha, mmoja kafanikiwa, mwingine mzurulaji. Atakuwa na kazi ya kujitengeneza kama mtoto wa kike, na kulala na kila mwanamke anayempitia. Mwanaume gani kucha zimelingana kama anafanya kazi saluni ya kutengeneza kucha! Ananukia kama mtoto wa kike! Mimi mwenyewe mwanamke lakini sinukii hivyo. Nywele utafikiri anafanya kazi kwenye saluni ya kinyozi! Ndevu zimejipanga mstari, utafikiri askari wa Uingereza! Basi kazi yake itakuwa ndio hiyo tu. Kujitengeneza na kuzunguka na gari ya dada yake. Na macho hayo, wanawake watakuwa wanapangwa mstari mpaka wanachoka.” Nanaa aliendelea kuwaza huku akimwangalia Geb aliyekuwa ameinama nyuma ya gari akiendelea kupanga matunda.

*****************************************************

 “We Nanaa!? Akamsikia Zena anaita. Akakumbuka kama amemsahau shoga yake kwenye simu. “Zena?” “Uko wapi wewe? Mbona sikuelewi?” “Nimekwambia nipo Buguruni sokoni.” “Mbona patulivu hivyo? Soko hilo soko gani?” “Nipo ndani ya gari na wewe.” Zena akaanza kucheka. “Siku hizi shoga yangu umepata bwana mwenye gari lenye AC?” “Leta dharau zako, uone kama nitakusaidia.” Geb akafungua sehemu nyingine kwenye boksi, pale pale nyuma ya gari alipokuwepo akatoka na chupa mbili za maji. Akarudi ndani ya gari, akafungua ile chupa ya maji, akamkabidhi Nanaa. “Naona jua kali sana. Karibu maji.” “Asante.” Nanaa alishukuru akapokea yale maji yaliyokuwa baridi. “Karibu.” Geb naye akajibu.

“Asante ya nini na wewe Nanaa?” Zena akauliza upande wa pili wa simu. “Siongei na wewe.” Geb akakunja uso. “Sio wewe. Samahani ni...” Nanaa aliongea huku akinyoosha kidole kwenye simu. Geb akaelewa. “Nani? Uko na nani wewe Nanaa?” Zena aliendelea kudadisi upande wa pili wa simu. “Nimesahau kuikausha hiyo chupa. Chukua hii napkins itakusaidia kuikausha hiyo chupa, usilowe.” “Asante.” Baadhi ya matone kutoka kwenye chupa aliyopewa ya maji ya kunywa, yalishaanza kumdondekea Nanaa. Akapokea zile napkins. Geb akafunga mkanda, akaondoa gari.

*****************************************************

 “Mbona unasena asante kila mara? Umepata bwana mwanajeshi nini? Naona nidhamu imeongezeaka.” “Zena! Naomba nikupigie simu baadaye.” “Nanaa wewe! Tafadhali shoga yangu.” “Si umtafute Tia?” “Tia yuko mbali na ameshaanza field. Hawezi kuja.” “Nitakufikiria.” “Acha kunifanyia hivyo Nanaa. Kwanza Terry anakutafuta.” “Mmmh! Mimi ndio wakula makombo?” Nanaa akauliza. “Sio makombo. Terry alinikataa kabisa. Anakutaka wewe.” “Naona umesahau shida yako wewe.” “Basi. Naacha habari za Terry. Njoo basi leo nyumbani tuzungumze.” “Kuna mahali nakwenda jioni.” “Mbona sasa hivi mapema tu. Njoo kabla hujakwenda huko. Tupange mambo yetu vizuri. Tena anabest yake na yeye hajaoa. Ukikubali tutoke wote, nitamwambia aje naye. Mambo yao safi. Siwezi kukuunganisha kwa wanafunzi kama kina Terry.” Nanaa akacheka.

“Akikusikia Tia.” Zena na yeye akacheka. “Hawana hela bwana. Kutwa chips mayai! Mtoko huu ni wa uhakika shoga yangu. Tutaenda kwenye mahoteli makubwa ya maana. Usijivunge. Au ushapata bwana?” “Wapi? Nipo tu.” “Basi njoo nyumbani tuzungumze vizuri. Lazima kieleweke.” “Nitakuja baadaye.” “Ndio maana nakupenda.” “Acha kunidanganya. Nitakuwa siji.” “Nanaa naye!?” Nanaa akacheka kidogo. “Haya Zena. Nashukuru kunikumbuka. Nitakuona baadaye.” Alimsikia Zena akipiga kelele za kushangilia. Nanaa akacheka na kukata simu.

Alibaki na tabasamu usoni. Gafla akakumbuka mazungumzo yake na Zena. Tabia yake yakumuunganisha na wanaume. “Mungu wangu! Sijui amenielewa huyu?” Nanaa akawaza. Akaamua kumtumia ujumbe Zena baada ya kufikiria tena kidogo. ‘Sina uhakika kama umenielewa vizuri Zena. Naomba usiniunganishe na yeyote, yule. Hata aweje. Bado nipo mapumzikoni. Naomba nikusaidie ishu yako tu, basi. Sitaki mwanaume kwa sasa.’ ‘Nanaa naye!’ ‘Kweli tena Zena. Tafadhali sana. Nimeamua hivyo na naomba ibaki hivyo. Nitakuja kwa ajili yako, basi.’ ‘Lakini…’ Wakaendelea kujibizana kwa jumbe, mpaka wakawekana sawa. Baada ya majibizano hayo na kuridhika kuwa Zena ameelewa, hatamtafutia mwanaume, akarudisha simu yake kwenye pochi.

Alishangaa kuona wamesimama mbele ya geti kubwa tu. Akajua wamefika. Akajua ameongea na Zena kwa muda mrefu, au hawakuwa wakikaa mbali sana. Labda maeneo ya Tabata ya mwanzoni. Pia hakuuliza. Geti likafunguliwa, wakaingia ndani. Nyumba ilionekana bado mpya. Kulimwagwa vitofali vizuri. Kuanzia getini mpaka mlangoni. Baiskeli ndogo ilikuwa pembeni, akajua itakuwa ya Fili.

Kwa mara ya kwanza, Nanaa nyumbani kwa Bosi wake.

“Karibu.” Geb alimkaribisha. Nanaa akafungua mkanda. “Asante. Nikusaidie nini?” “Nisubiri tu twende wote ndani. Nitabeba tu mwenyewe, sio vitu vingingi.” Geb alitoa boksi zima. Lilikuwa ni boksi la plastiki, lenye mishikio miwili. Lilionekana ni maalumu kwa kubebea vitu kama hivyo. Akafunga mlango akamkaribisha ndani. Wakaongozana mpaka ndani sebleni.

“Karibu Nanaa, nipo huku jikoni. Msichana wa kazi ameondoka leo asubuhi, amefiwa. Natayarisha chakula cha mchana, tukishakula ndio tuanze kufunga zawadi.” Nanaa akamfuata Geb kule jikoni kulikosikika sauti ya Grace. “Asante na pole na shuguli.” Nanaa akaingia. “Asante mwaya.” Grace alijibu na tabasamu.

“Mama yuko wapi?” Geb aliuliza mara baada yakutua mzigo. “Alikuwa anasinzia hapa, Fili amempa nyanya, kala nusu, nusu amekufunikia hapo kwenye meza. Ameniambia ukija uile.” Grace akamjibu, Geb akanawa mikono akasogelea ile sahani. “Halafu nimempatia maparachichi.” “Atafurahi kweli. Alikuwa ananiambia anahamu nayo.” “Tena nimepata yale mazuri anayopenda.” Geb aliendelea kukila kile kipande cha nyanya huku akiongea na dada yake.

“Fili yuko wapi?” Nanaa naye akauliza. “Yupo na bibi yake huko chumbani. Na anavyopenda kuongea mwanangu yule, sijui kama mama atakuwa ameweza kulala!” Nanaa akacheka. “Ngoja nikamwangalie mama. Nitakuja kukusaidia kutengeneza juisi.” Geb alitaka kutoka. “Ungenielekeza tu mimi, nitatengeneza.” Nanaa alimuwahi. “Anza basi kuosha matunda mawili mawili kutoka kwenye hilo boksi. Nikirudi nitakutolea tangawizi na Blenda, nikuonyeshe tunavyosaga. Ni rahisi tu.” Geb alitoka akamuacha Nanaa anaanza kuosha matunda.

 “Pole.” “Nimeshazoea. Wasichana huwa hawakai hapa kwangu, sijui kwa nini! Mwanzoni nilifikiria wanalemewa na kazi, tukawa tunawasaidia, lakini wapi. Nikafikiri ni sababu ya Fili.” “Kwa nini Fili?” “Mtoto ni mtundu huyo, hujawahi kuona. Yupo kama baba yake. Akianza kuongea mpaka kichwa kinauma na anataka umsikilize. Nahisi ndio maana wanatukimbia, wanachoka. Nikataka kumuanzisha shule mapema ili niwe natoka naye asubuhi na kurudi naye jioni, ili kuwafanya wasichana wa kazi wasitukimbie, lakini Danny hataki aanze shule kabla yakufikisha miaka 5. Kwa hiyo wasichana wa kazi wakitukimbia, inabidi wote tupeane zamu ya kubaki naye hapa. Lakini bibi yake ndio huwa anakuwa naye zaidi, kwa kuwa hachoki.” Nanaa akacheka.

Kweli tena. Bibi yake anatabia kama za Geb. Huwa hawachoshwi na kelele nyingi, wanawezana naye. Kwa hiyo muda mwingi hata tukiwa na mfanyakazi, bibi yake huwa anachelewa kwenda kwenye shuguli zake. Anamuhudumia Fili. Anahakikisha amemuogesha, anamuacha amekula ndio anaondoka, ili Msichana wa kazi asiwe anahusiki na mtoto, nayo pia haikusaidia.” “Poleni.” Nanaa akaona ampe tu pole.

“Haya na anko wake pia akaanza kazi ya kufua nguo zote. Mara mbili kwa week. Tena wakati mwingine akiona nguo nyingi anafua mpaka usiku na kukunja nguo zote, anampangia Fili kabatini kwake, na mimi nakuwa napika chakula cha usiku mara nyingi, ili tu kumpunguzia msichana wa kazi majukumu, lakini pia naona hawakai. Sasa sijui itakuaje, lakini kwa kuwa ametimiza miaka mitano, ni heri aanze tu shule, nitachanganyikiwa bure.” “Pole. Na Danny?” Nanaa aliuliza baada yakuona dad mtoto hayupo kwenye ratiba ya ulezi.

“Huyo sitaki akae na mwanangu siku nzima. Mwanangu anakuwa hana raha. Mkali sana kwa Fili. Anamlea kama mtumzima bwana! Hapana. Yaani nikimuacha mwanangu na Danny hata masaa mawili tu, tumbo linauma. Kila saa nampigia simu au naomba Geb arudi aje awaangalie. Najikuta kazi zenyewe zilizonipeleka ofisini sifanyi, nina kazi yakumpigia simu Danny, kumkumbusha umri wa Fili. Ndio tumeona tuache kumpa yeye hiyo kazi ya ulezi tubaki nayo sisi tu.” Nanaa alikuwa akicheka sana.

*****************************************************

 Geb akarudi akiwa amembeba Fili mabegani. “Usimuweke hapo juu bwana. Ataanguka. Si unamjua hawezi kutulia?” “Nimemtoa kule kwa mama ili apumzike kidogo. Anaruka ruka tu kitandani mama hawezi kulala.” “Tulia basi kidogo Fili mwanangu. Huchoki? Au nimpigie simu dad arudi aje akuchukue?” “Hapana mama. Natulia” “Basi tulia. Tumalize kazi haraka ili tuwahi kwenye birthday yako.” Tayari Grace alionekana kulemewa. Alishika hiki na kuacha nusu.

“Mwache bwana. Mimi si nipo? Hawezi kuanguka. Haya nenda kamsalimie Nanaa, halafu uje ukae hapa kwenye meza.” Alienda kusimama mbele ya Nanaa akabaki akimtizama huku anacheka. “Anajua kuchanganyikiwa vibaya huyu! Sasa unacheka nini badala usalimie?” Mama yake alidakia huku akiendelea na shuguli zake. “Hapo anataka uiname, akubusu.” Geb aliongeza, wakacheka. Fili alienda kuvuta kiti mpaka karibu ya Nanaa, akapanda na kumfikia Nanaa. “Ningeinama tu.” Nanaa akacheka. “Uiname umpunguzie shuguli? Anapenda shuguli huyo!” Grace akaongeza. Fili akambusu shavuni kisha akamkumbatia. “Asante Fili.” Nanaa alishukuru na tabasamu la aibu usoni. Hakuzoea.

“Karibu. Umekuja kuishi na mimi?” Fili akamuuliza Nanaa. “Nitakuchukua twende tukaishi wote kwangu.” “Afadhali. Umchukue moja kwa moja. Lakini James anaweza kumrudisha usiku huyo.” Grace aliongeza na kufanya Nanaa acheke. “Wewe ndio uje uishi hapa kwetu.” Fili akaendelea. “Kwa nini?” “Dad amesema nisubiri mpaka nisome, nipate mahela mengiiiii.” Fili alionyesha ukubwa wa pesa anazotakiwa awe nazo kwa kupanua vimikono vyake. “Halafu ndio amesema nikishapata pesa niende kwa anko James, tumlipe hela, nikuchukue. Lakini amesema nikikuchukua nisirudi tena hapa, nikupeleke kwangu.” Walicheka sana.

“Yaani Danny jamani!” Grace alilalamika. “Lakini wewe ukija hapa sasa hivi, usimwambie kama mimi ndio nimekwambia uje tuishi wote hapa. Wewe umwambie umeamua kuja kuishi hapa na mimi, wala sijakuita. Halafu hawezi kukufukuza.” Fili aliongeza na kuwafanya wote wazidi kucheka, Geb alikuwa akitingisha kichwa. “Hapa kazi ipo. Akili ya ujanja ujanja kama baba yake. Wewe! Tulikwambia nini juu ya kusema uongo?” “Hapo anko nitakuwa mimi sijadanganya. Nanaa atakuwa ndio amekuja hapa.” Fili akajitetea.

“Kwa hiyo unamfundisha Nanaa kusema uongo?” “Hapana anko.” “Na hapo pia unasema uongo. Si umemfundisha aje hapa asikutaje kwa dad wako kama wewe ndio umemkaribisha?” Fili alinyamaza kidogo kisha akauliza. “Kwani huo ni uongo?” “Sasa je? Hakuna kusema uongo.” “Basi Nanaa. Usiseme tena. Samahani anko.” “Haya, nenda kacheze, usubiri mpaka upate hela kama alivyokwambia dad, ndio utaenda kumlipa anko James, umchukue Nanaa, umpeleke kwako sio hapa. Sawa?” Fili alipooza. “Sawa anko. Kwani utamwambia dad?” Akauliza kwa upole. “Ukirudia tena kumfundisha Nanaa kusema uongo, ndio nitamwambia.” “Mimi sirudii tena. Usimwambie dad wangu.” “Ujue nitakuwa nakusikiliza kila neno unaloongea. Usirudie tena. Haya nenda.” Alishuka kwenye kiti, akatoka.

*****************************************************

 “Afadhali umemuweza. Fili anaongea jamani! Halafu hasahau jambo kama anko wake. Hapo ataenda kumsimulia kila mtu kuwa anataka kuoa lakini dad amemwambia atafute kwanza pesa.” Wote waliendelea kucheka wakati Grace anasimulia vituko vya mwanae, Geb anatengeneza juisi. “Sasa si atarudi tena kwa bibi yake?” Nanaa aliwakumbusha, Geb akatoka kwa haraka kwenda kumtafuta, akarudi amemshika. “Alishafika chumbani kwa bibi yake nakuanza kumsimulia habari zake zisizo isha. Nimekwambia kaa hapa.” Geb alimpandisha tena juu ya meza. “Msimulie Nanaa badala ya bibi.” Fili akaanza kusimulia huku akiruka ruka hapo juu ya meza.

“Utaumia Fili mwanangu. Tulia basi.” “Naweza kuruka hapa, mama. Juu mpaka chini. Muulize anko.”  Fili alimchonganisha anko wake. “Wewe Fili?” Geb alimshtua huku akimkonyeza anyamaze lakini hakunyamaza. “Namwambia ukweli mama yangu. Mwenzio anko sio muoga. Ananiruhusu nipande halafu niruke.” Nanaa alicheka sana. “Geb jamani!” Grace alilalamika. “Hawezi kuumia bwana. Huyu ni spider man. Acha hofu.” “Usikubali awe anaruka.” “Hana neno bwana. Kwanza hapo pafupi.” Geb alitetea. Alikuwa akimruhusu kuruka kwa siri, akiona mama yake hayupo. Alikuwa akivaa nguo zake za spieder man na kumuomba anko wake aruke kama spider man.

 “Kwani ni lazima aruke? Tafuta mchezo mwingine. Umesikia Fili?” “Spider man lazima aruke mama.” “Hapana Fili mwanangu. Mwambie dad au anko wakutafutie kazi nyingine za spider man, ufanye. Kuliko kuruka. Ukivunjika, mama ataumia sana.” “Basi mama yangu. Nitaruka kidogo tu.” Geb na Nanaa wakacheka. “Kwani lazima kuruka Fili? Acha tu mwanangu. Utaumia.” Mama yake alisisitiza huku akimpa juisi aliyokuwa ametengeneza Nanaa. Alimuwekea kwenye chupa yake maalumu yenye picha za spider man, akaanza kunywa, ndio akanyamaza. Geb alimbeba na kutoka naye pale jikoni akabaki Nanaa na Grace wakimalizia usafi.

*****************************************************

Grace alipanga chakula mezani, akamwita kila mtu aje kula. Wakati wamekaa mezani ili wale, mama yao naye akatoka chumbani. Umbile alifanana sana na Grace kama alijizaa huyo mwanamke, hata rangi alifanana na watoto wake lakini sio yale macho. Nanaa akasimama. “Nilikuwa naambiwa mchumba umefika.” Yule mama alitoa mkono na kumpa Nanaa, wote wakacheka. “Naona sasa hivi kila mtu anamfahamu Nanaa. Kila anayepiga simu, anakaribishwa kwenye birthday na kuambiwa Nanaa atakuwepo. Mwanangu amependa jamani.” Grace alidakia. Wote wakacheka. “Shikamoo mama.” Nanaa alisalimia huku akicheka. “Marahaba. Karibu sana.” Yule mama alikaa.

*****************************************************

 “Mbona sahani yako haina nyama?” Mama yao alimuuliza Geb. “Nimeshakula zote.” Geb akajibu. “Chukua na hizi zangu.” “Kula bwana mama. Nikitaka nitaongeza. Mbona bado zipo tu nyingi.” “Basi chukua hii moja.” Walibishana kwa muda, mwishowe Geb akachukua nyama kutoka kwenye sahani ya mama yake. “Hajawahi kukua huyo kwa mama. Utawazoea tu. Mama akila kitu, anataka na mwanae ale. Hata kama hayupo nyumbani, anakula nusu, nusu anamuwekea.” Grace akamwambia Nanaa, Nanaa akacheka kidogo na kuinama. “Mvivu sana wakula huyu. Usipomsisitiza kula, ndio basi tena. Hizo nyama zilizofanikiwa kuingia huko tumboni ndio kashamaliza hapo. Huo mdomo hautapitisha tena kitu kingine.” Mama yao aliongeza, Nanaa alicheka tena kidogo na kuinamia sahani yake tena, akaendelea kula bila yakuongeza neno.

 “Watakuwa wanamdekeza ndio maana hataki kutoka nyumbani kwa dada yake, akaishi peke yake ajitegemee. Amenikalia kudeka!” Nanaa akawaza. Wakala lakini hawakuwa wakizungumza sana, mpaka Danny alipoingia ndio akaanza kuongea nakuwafanya wote waanze kucheka. Kitu kidogo, Danny alikikuza, akakisimulia kwa mbwembwe nyingii na kuwafanya wote wacheke. Fili alianza kusinzia, Grace akambeba kwenda kumuogesha ili amlaze angalau apate usingizi wa mchana. Nanaa alitoa vyombo pale mezani wakisaidiana na Geb kurudisha jikoni.

“Acha niwasaidie tu kusafisha. Sio vingi.” Nanaa alitaka Geb ampishe pale kwenye sinki. “Ni vyakupanga tu hapo kwenye mashine. Huwa mashine inatusaidia kuosha. Labda sufuria ndio zakuziosha. Ngoja nikuonyeshe.” Geb alisuuza kidogo, akavipanga vyote kwenye mashine iliyomtoa macho Nanaa, hakuwahi kuona mashine yakuoshea vyombo. Ili kuepuka mshangao usoni, akaamua aanze kuosha sufuria. “Sasa kwa nini wasichana wa kazi hawakai kama kuna mpaka mashine za kuoshea vyombo!?” Nanaa aliwaza.

*****************************************************

Simu ya Geb iliita. Akatoa mfukoni na kupokea. “Vipi?” Aliuliza. “Nimetoka kazini, nimechoka.” Akasikia sauti ya kike upande wa pili. “Njoo upumzike hapa kwetu.” “Fili anakelele bwana.” Yule msichana alilalamika, Geb akacheka. “Ameenda kulala, hatakusumbua.” “Acha tu niende kwangu. Nipumzike, nikiamka ndio nijiandae kuja kwenye birthday yake.” “Njoo basi, angalau nikuone, Liz.” Geb alimbembeleza. “Kwani una hamu na mimi?” Liz akauliza. “Si ndio maana nataka uje?” Liz alisikika akicheka. “Niache nikalale kidogo, Geb. Nimechoka. Tukitoka kwenye sherehe tutakuwa wote, mpaka utanifukuza.” “Sawa mama. Baadaye basi. Ulale unono.” Liz alisikika akicheka tena. “Asante.” Wakakata simu.

*****************************************************

Mara Grace akaingia.  “Usingehangaika kuosha hayo masufuria, Geb angeosha tu.” “Hamna shida. Kwanza namalizia.” “Basi ukimaliza uje tukae hapo sebleni, tupumzike kidogo. Fili amelala.” “Mbona Fili mwenyewe sio mtundu wa hivyo?” Geb na Grace waliangaliana wakacheka. “Kweli. Nipeni mimi siku za jumamosi niwe nakaa naye.” “Kama ulikuwa unatania ujue ndio imekula kwako. Na hivi sina msichana wa kazi, jumamosi ijayo asubuhi na mapema, nakuletea kwako.” Nanaa alicheka. “Kweli tena, wewe mlete tu. Ndugu yangu ana mtoto wa kiume, yule mtoto ndio mtundu. Wakati kaka akiwa anakwenda au alipokuwa akija nyumbani kusalimia, huwa kaka anachoka. Anasemaga ameshaona watoto watundu, lakini pale mwisho.” “Mtoto wa Viola?” Grace akauliza na kumfanya Nanaa kushangaa kidogo.

“Kumbe unawafahamu dada zake James?” Wakacheka. “Alishawahi kufika hapa. Zamani kabla ya kupata mtoto. Alimpenda sana Geb, lakini tatizo la Geb kazubaa. Sasa hivi angekuwa na mtoto mkubwa tu na Viola.” Nanaa alitulia kidogo kama anawaza. “Tena hata Vai pia alishafika hapa. Walikuja kumtembelea kaka yao hapa Dar, James akawaleta waje watusalimie.” “Kumbe! Sikuwa nafahamu kama mnafahamiana vizuri hivyo!” “Sana tu.” Grace akaitika bila shaka. Nanaa alikosa raha asijue ni kwa nini. Alikausha mikono, akabaki amesimama kama aliyeduwaa.



*****************************************************

Kumbukumbu za mateso pale nyumbani kwa mama yake mkubwa zilimjia. Vile Viola alivyompokonya mwanaume wake, akazaa naye, huku akipongezwa na mama yake bila kujali machungu aliyomsababishia. Alimkumbuka Alex, ahadi walizokuwa wamewekeana, majina ya watoto waliokuwa wameamua kuwapa pindi watakapo jaliwa watoto hao. Lakini akaishia kuzaa na Viola.

Alex alifanikiwa kulipa mahari kama alivyoahidi, Viola akabaki akimsubiri amalize chuo ili wafunge ndoa, lakini walikuja kusikia Alex alioa mwanamke mwingine, kwa haraka sana, mara tu baada yakumaliza chuo chake. Ilimchukua zaidi ya miaka miwili kwa Nanaa kuja kurudi nyumbani kwa mama yake mkubwa, Moshi. Kila James alipokuwa akienda kusalimia, Nanaa alikataa kurudi. Alimuomba ampe kwanza muda wakupona. James alikuwa akimletea habari zote ya kinachoendelea nyumbani kwao, lakini Nanaa hakuwa akienda kusalimia na alikata mawasiliano kabisa.

Yalikuwa ni majuma machache sana yaliyopita kabla yakuanza kazi kwa Grace ndipo alipoona ni vyema kuungana na James, kwenda kusalimia nyumbani kwao. Siku alipokwenda kusalimia, alijuta. Asubuhi ya siku inayofuata baada ya kutua tu Moshi, Mama yake mkubwa aliimwita kutoka chumbani alipokuwa amelala na kumtaka aende hapo sebleni kwa mazungumzo. Nanaa alivaa, akaosha uso, na kwenda kukaa alipokuwa amekaa yeye na watoto wake. Bila hata kujua linaloendelea kwenye maisha ya Nanaa ambaye hawakuwa wameonana kwa zaidi ya miezi 24, tena waliachana katika hali ya machungu, yule mama alianza kumsema sana Nanaa.

 James na baba yake walikuwa wametoka, kwa hiyo alimsema vile atakavyo. Alimsema Nanaa bila kupumzika tena akitumia maneno machafu ambayo asingethubutu kumsema mtoto wake aliyemzaa. Alimsema vile alivyonyimwa shukurani. Amefanikiwa kidogo tu na kusahau alipotoka. “Usifikiri hapo ulipo umefika mwenyewe. Hata hapo unapoishi sasa hivi ni kwa James, mtoto wangu. Tulimsomesha na kumtunza kwa jasho letu. Sasa hivi wewe usiye na shukurani ndio unafaidi jasho la mtoto wangu. Umekuwa mzigo kwenye maisha yake mpaka anashindwa kumsomesha mdogo wake, anakusomesha tu wewe mtu baki. Hunashukurani kabisa. Umeondoka hapa, unashindwa hata kunijulia hali! Mwenzio anashindwa kusaidia nyumbani kwao, kwa kuwa wewe umekuwa mzigo kwake! Unajidai msomi kwa kuwa umefika chuo kikuu! Tutakuona utafika wapi.” Alimsema Nanaa mpaka aliposikia gari ya mumewe wakirudi nyumbani na James, ndipo akanyamaza na kubadilika kuwa mwema kwake kana kwamba sio yeye na kubadili mazungumzo mara James alipoingia tu ndani.

*****************************************************

 “Nanaa amemshauri Vai mrudi naye Dar na yeye akatafute shule asome.” Alimuwahi James kabla hajakaa, na tabasamu usoni. James alipoona sura ya Nanaa alijua kilichokuwa kikiendelea na kujua ule ulikuwa uongo. “Mbona baba ameniambia kuwa Vai anataka kuolewa? Sasa anasoma lini na kuolewa lini?” James aliuliza huku akikaa. “Kwani mtu akiolewa hawezi kurudi shule?” “Nini kinaanza sasa?” James akauliza tena. “Vyote vinaweza kwenda kwa wakati mmoja.” Mama yake akamjibu. “Basi kama ndio hivyo akasomee kwake na mumewe amsomeshe.” James alijibu.

“Mwanaume mwenyewe hana pesa. Sijui tutaishije?” Vai akaongeza. “Nanaa twende nikakuonyeshe kitu.” James hakutaka kuingilia kabisa. Alishawazira wadogo zake. Alichukia vile mama yao anavyowakingia kifua, hata walipokuwa wakikosea, hakutaka waonywe. “Sasa utaondoka na Vai, ili aanze kujiandaa na safari?” Mama yake alirudia tena. “Hapana.” James alijibu bila hata kufikiria. Kama aliyekuwa ameshaandaa jibu tayari.

“Kwa nini!?” Mama yao akauliza kwa mshangao na hasira. “Yaani upo radhi kumsaidia huyu mtu baki na sio mdogo wako, ambaye ni damu yako?! Tumeshamsaidia huyo Nanaa vyakutosha. Ni wakati sasa atafute maisha yake, apishe nafasi ya wenzie wapate msaada. Kwanza bibi yako anashida.” “Nimeshazungumza na bibi na nimeshamtumia pesa za matumizi.” “Sasa nini kinachokushinda kumchukua Vai?” James akarudi kukaa kwenye kochi.

“Unakumbuka Viola na Vai walishakuja Dar ili waishi na mimi? Unakumbuka kuwa mimi ndiye niliwarudisha? Nilikueleza sababu zote za kwa nini nawarudisha nyumbani. Nilishindwa kuishi nao. Nafasi niliyotaka kuwapa wao, sasa hivi nimempa Nanaa na anaitumia vizuri. Nanaa amekuwa msaada kwangu. Tunaheshimiana. Hawa watoto wako walinitia aibu kwa marafiki zangu, mpaka ikabidi niwafukuze. Kila mwanaume walikuwa wanamtongoza wao. Mpaka waume za marafiki zangu, walikuwa wakiwatongoza. Kama rafiki zangu wangekuwa watu wasio na ndoa za kueleweka, si wangevunja ndoa zao? Na pia hawana uwezo wakufanya kazi za nyumbani kama Nanaa. Wakati naishi nao, Viola na Vai, ilinilazimu kuwatafutia msichana wa kazi wakuwahudumia wao, wakati wao wamekaa tu, wanaangalia tv, mchana na usiku. Shule walikataa, wakaishia kuniingiza hasara zakulipa ada bila wao kuhudhuria darasa hata moja. Nanaa amekubali kusoma. Anahangaika na shule, amebakiza kidogo tu amalize.” James alijieleza kwa kituo bila jazba, ili mama yake aelewe.

“Watu wanabadilika James. Dada zako wamebadilika sana.” “Basi watafute chuo hapahapa Moshi waanze kusoma. Kama baba ameshindwa kuwasomesha, mimi nitatuma hiyo pesa itakayohitajika ya ada.” “Sijashindwa kumsomesha hata mmoja wao hapo. Muulize Viola kama sijambembeleza ajikaze arudi shule. Tena nilimwambia nitamsaidia kumtafuta mtu wakumlelea mtoto wake, wakati anasoma, lakini amekataa. Ni week iliyopita tu nilimkumbusha tena, akakataa. Jana pia nilizungumza nao wote wawili kutaka warudi shule, lakini wamekataa. Sijashindwa kuwasomesha hata kidogo.” Baba yao aliingilia. “Nanaa twende.” James akasimama na kutoka nje kumsubiria Nanaa.

*****************************************************

Alikumbuka yale maneno yote. Akakumbuka vile Grace naye alivyosema anawafahamu vizuri sana. Aibu na hofu ikaanza kumwingia. “Sasa sijui walimtaka mume wa Grace, Danny!? Aibu gani hii! Kumbe muda wote nipo hapa wananiangalia tu, kumbe wanazijua habari zetu! Sijui niage niondoke?” Nanaa alibaki ameduwaa, huku Grace na Geb wakizungumza pale pale jikoni, akasikia wanacheka. Akashtuka.

 “Twende basi.” Grace alitoka pale jikoni, akamfuata nyuma, wakaenda kukaa pale sebleni, Nanaa akiwa amepotelea kwenye mawazo. Zile kumbukumbu za maneno ya mama yake mkubwa zilishamuharibia utulivu wa moyoni. Akabaki kimya nakushindwa kuchangia lolote. Geb naye alitoka akaenda kukaa pale akisaidia kufunga zawadi.

*****************************************************

Mara waliona mlango unafunguliwa. “Liz!” Geb alishangaa. “Si ulisema una usingizi?” “Nimekubali ile ofa ya kuja kulala hapa hapa. Shikamoo bibi wa Fili.” Liz alimgeukia mama yao nakusalimia. “Marahaba. Karibu.” Alijibu kwa ufupi tu mama huyo akanyamaza. “Njaa inauma, nina usingizi, sijui nifanye lipi niache lipi?” “Nilikwambia napika. Chakula tumekirudisha sasa hivi kwenye friji. Wewe nenda kale ndio ukalale.” Grace alijibu, Geb akasimama, Liz akambusu midomoni. “Twende nikusindikize ukale, ndio ulale.” Wakaondoka na Geb kuelekea jikoni, akamsikia Liz akiongea na kucheka akiwa na Geb huko huko jikoni. Akajua ni wapenzi.

“Liz! Liz!” Grace akaita. “Nimesahau kukutambulisha kwa Nanaa. Njoo.” Liz alitoka. “Huyo ndio Nanaa.” “Mchumba wa Fili?” Liz aliuliza na kuamsha kicheko. “Amemng’ang’ania! Kabla hajalala alikuwa anamfundisha Nanaa uongo wakumwambia baba yake ili ahamie hapa.” “Aje amlee?” Liz akauliza. “Naona. Maana wasichana wa kazi wote wanamkimbia. Lakini Geb akamgombesha aache uongo, naona akapooza mpaka akapata usingizi.” Wakacheka tena.

“Sasa Nanaa ujiandae. Mume yule hamna kulala sababu ya maneno mengi. Sura ya upole kama mama yake. Akikuangalia hivi na macho yake yale, utafikiri ni malaika ambaye hajaanza kuongea. Lakini ngoja afungue mdomo, ndio utajua ni mtoto wa Danny. Jana amenipigia simu ananieleza habari zako, mpaka nikapitiwa na usingizi. Mtoto hachoki! Kila nikimuaga ananiita, Anti Liz, nimekwambia Nanaa ni mzuri?” Namwambia ulishaniambia zaidi ya mara hamsini, anasema “Ndio unatakiwa usisahau sasa”.”  Kila mtu alikuwa anacheka. “Sasa Nanaa ujiandae. Hajuagi kuongea kwa kifupi huyo mumeo, na hachoki.” Liz akarudi jikoni, baada ya kula wakaongozana na Geb chumbani.

*****************************************************

Japokuwa alikuwa akicheka, lakini moyoni alishakosa amani, asijue ni nini kinachomsababishia ile hali. Kama ni maneno ya kashfa aliyokumbuka kuambiwa na mama yake mkubwa, au ujio wa Liz, au aibu ya ndugu zake hapo kwa kina Geb, hakujua ni lipi, lakini moyoni alikuwa ameshafuka kabisa. Alibaki kimya mpaka walipomaliza. Grace alikuwa akiongea na mama yake huku Danny akiangalia mpira.

“Naona tumemaliza mapema na bado tuna muda mwingi uliobaki wa sherehe ianze. Naomba niondoke, kuna mahali nataka nipitie kabla ya kuja huko kwenye birthday.” Nanaa aliaga baada yakumaliza. “Basi ngoja nimwite Geb akupeleke.” Grace alitaka kusimama. “Hapana. Mwache tu apumzike. Ningependa kwenda peke yangu.” Grace akacheka. Haya Mkwe wangu. Lakini usimsaliti tu mwanangu.” Grace alirudi kukaa, akamfanya Nanaa acheke kidogo. “Wala usijali. Nitakuja kwenye sherehe, nicheze naye.” Nanaa alichukua pochi yake akamuaga mama yao na Danny aliyekuwa akishangilia mpira kwenye tv, akatoka.

*****************************************************

Nanaa alitoka pale mida ya saa 8:30 mchana. Akatembea kidogo tu, akajikuta amefika kituoni. Ndipo akagundua pale ni Tabata Barakuda. Akasubiri daladala ya kumpeleka Kariakoo kutafuta zawadi ya Fili. Hakukaa sana kituoni, daladala ikapita. Akapanda mpaka Kariakoo. Jasho lilikuwa likimtoka kila alipokuwa akifikiria kitu cha kumnunulia Fili kama zawadi. Kila kitu alichokiona cha Fili pale kwao, kilikuwa cha thamani. “Nitanunua nini angalau kifanane na hali yao?” Nanaa alibaki akijiuliza. Baada ya kuhangaika akizunguka madukani, akaona mpira wenye picha ya Spider Man, unauzwa. Kwa kuwa alisikia akijiita Spider Man, akaamua kununua na kuondoka zake.



Wakati yupo njiani kuelekea kwao, Zena akampigia tena simu kumsisitiza asichelewe na kumwambia wakutane Mlimani city, asiende nyumbani kwao. Nanaa akakubali. Akafika nyumbani kwao, akaoga kwa haraka. Kutoa jasho na vumbi la Kariakoo, akatoka kuelekea Mlimani City.



Walikubaliana wakutane nje ya duka la nguo la Maikos. Nanaa alisimama pale, akampigia simu Zena. “Nimefika.” “Subiri dakika moja tu.” Nanaa akakata simu. Akamuona Zena anakuja na vijana wawili. Nanaa akacheka na kutingisha kichwa. “Sasa unacheka nini?” Zena aliuliza. Nanaa akamvuta pembeni kwa nguvu. “Maneno yote yale kumbe nia yako nikuja kuniuza mimi na wala huna ishu unayotaka nikusaidie!” “Sio kwa mtu mbaya Nanaa shoga yangu. Njoo nikutambulishe. Utampenda.” “Wewe ni muongo Zena. Sijui kwa nini nilikuamini.” “Chonde shoga yangu. Naomba usiniabishe hapa.” Nanaa hakuwa akiamini aliweza vipi kumuamini Zena, tena kwa uongo wa kijinga kama ule.



Zena na yeye akamvuta kumrudisha kwa wale vijana. “Huyu anaitwa Yasini, ndie rafiki yangu. Na huyu ni rafiki yake anaitwa Jeff.” Akawageukia wale vijana wawili. “Huyu ndiye Nanaa. Shoga yangu yangu kipenzi. Tupo sisi watatu. Tia tu ndio amekosekana hapa.” Nanaa hakuwa anaamini. Alibaki akimtizama Zena. “Tumefurahi kukufahamu Nanaa.” Jeff akaitika. “Asante.” Nanaa alishindwa hata kujibu na mimi nimefurahi kuwafahamu, akaishia kusema asante tu. Kwani hakukusudia kuangukia kwa mwanaume mwingine kwa wakati huo. Hasa wanaume aliokuwa akiunganishwa na Zena.



*****************************************************

Na Zena huo ndio ulikuwa mchezo wake. Mwanaume wa mwisho alimfanyia hivyo hivyo. Alimwita Nanaa mahali akimwambia amekwama mahali. Wamekula yeye na Tia, lakini wakagundua hawana pesa ya kulipa. Wanaomba awafuate kwenye huo mgahawa. Nanaa akaacha shuguli zake zote, akapanda daladala mpaka Sirender Bridge pub, ili kunusuru mashoga zake. Alipofika pale akapiga simu kuwaambia hawaoni. Zena kwa ujasiri wote, akamwambia atafute meza akae, wameenda chooni mara moja watatoka. Tena hapo ni baada ya kumuuliza aina ya nguo alizokuwa amevaa.



Babaada ya Nanaa kukaa kwenye hiyo meza, akashtukia anafuatwa na kijana, aliyemsalimia kwa kumtaja jina kana kwamba wanafahamiana. Akiwa kwenye mshangao, yule kijana ndipo akamwambia ameunganishwa na Zena. Anatafuta mchumba aliyetulia aoe. Nanaa hakuwa anaamini mchezo aliomchezea Zena. Akajua wazi alishakula pesa ya yule kijana. Tena ndio walikuwa wamemaliza tu mitihani, Nanaa ametulia kwao.



Zena amuunganisha tena Nanaa kwa Jeff.

“Tunaweza kwenda kula sehemu?” Yasini akauliza kiungwana. Nanaa akacheka kwa kuguna. “Samahani. Mimi nimetoka kula muda si mrefu. Na baada ya muda mfupi sana kuanzia sasa, natakiwa kwenda mahali.” “Una miahadi ya saa ngapi?” Jeff alimuuliza Nanaa. “Baada ya dakika 45 kuanzia sasa.” Nanaa akajibu. “Basi haina shida. Kama ni sawa, tunakuomba twende hapo ‘Saad restarant’. Muda ukifika, nitakupeleka.” Nanaa alicheka, ikabidi akubali.



Waliingia hapo kwenye huo mgahawa, wakatafuta meza wakakaa. Walionekana ni vijana waungwana na watu wazima walio tulia. Wao waliagiza chakula na vinywaji, Nanaa akaagiza maji ya kunywa ya baridi. Akaletewa kwenye glasi. Wakaanza kula. Hapakuwa na maneno mengi sana. Yalikuwa mazungumzo ya maana tu. Jeff akamuuliza Nanaa ni wapi anafanya field yake. Kama anapafurahia. Wanamlipa kutokana na kazi wanazompa. Anampango wa kufanya hapo kwa muda gani. Hayo yote yalikuwa maswali waliyouliza Jeff na Yasini kwa kupokezana.



Jeff mwenyewe ndiye aliyemkumbusha Nanaa juu ya miahadi yake. Nanaa akashangaa. Sitaki sisi ndio tuwe sababu ya kutokufanikisha miahadi yako.” Nanaa alitabasamu. “Nashukuru.” “Tunaweza kukupeleke tu mpaka huko, kama ni sawa. Vinginevyo tutakuchukulia taksii.” Jeff aliongea na tabasamu usoni. “Sio sehemu ya siri. Nimealikwa kwenye birthday ya mtoto wa bosi wangu. Anatimiza miaka 5. Kwa hiyo mnaweza kunisindikiza tu, kama mtapenda. Lakini nina uzoefu mzuri sana na daladala.”  Nanaa aliongea kwa tabasamu. “Basi kwa kuwa tuna usafiri, nafikiri tukusindikize tu.” Wakasimama wote kwa pamoja. Wakatoka.



*****************************************************

Jeff na Yasini walitangulia mbele, Nanaa na Zena wakabaki kimya. “Hebu niambie shoga yangu. Hapo vipi?” “Ukoje wewe Zena!?” “Acha hasira, niambie ukweli. Huyu wa safari hii muugwana.” “Sasa wewe huyu Yasini si mkristo? Mzee Mgiza utamwambia nini?” “Hapo ndipo atakapojua penzi halina dini. Nilivyompenda huyu kaka! Hamna mtu ataniambia kitu nikaelewa. Labda na yeye ajekugeuka tapeli kama Dula.” Nanaa alimwangalia Zena mtoto wa ustadhi, asiamini. Baba yake alijulikana mtaani kwa kushika dini. Alikuwa Mzee mstaarabu na mwenye maadili. Swala 5, zisizopungua kila siku.



*****************************************************

Jeff na Yasini walikaa mbele, Nanaa na Zena wakakaa nyuma. Sehemu yenyewe waliyokuwa wakifanyia shuguli nzima ya Fili ilikuwa Masaki. Wakaondoa gari kuelekea Masaki. “Umefurahia chakula, Zena?”  Yasini alikuwa ndiye dereva, alirusha swali. “Ndiyo. Nashukuru.” Zena alijibu huku akimkonyeza Nanaa. Akionyesha wazi amefurahia lile swali la kuonyeshwa kujaliwa. Nanaa akatabasamu. “Hongera.” Alinong’ona. “Asante shoga yangu. Mungu kanipumzisha.” Wote wakacheka kwa pamoja. Nanaa akaanza kujifikiria maisha yake. Akapotelea mawazoni.



“Si ndio hapa?” Jeff alimshtua Nanaa. “Sijawahi hata kufika. Kama nyinyi ndio mnasema ni hapa, basi itakuwa hapa. Nawashukuru sana na nawatakia wakati mzuri.” Nanaa akashuka. Kabla hajafunga mlango, Jeff akamwita. “Abee!” Nanaa akarudisha kichwa ndani. “Naomba tuzungumze kidogo.” Nanaa akamtizama Zena, akarudisha macho kwa Jeff. Akakuta anamtizama. “Sawa.” Akakubali.



Nanaa na Jeff.



Wakatoka na kusimama pembeni kidogo ya gari. Mbele ya uzio wa michongoma. “Naomba kesho tuonane.” Jeff alivunja ukimya mara baada ya kuridhika wako peke yao. “Mimi sijui Zena amekwambia nini juu yangu. Lakini sina mpango wa kuolewa hivi karibuni.” Nanaa alikataa haraka sana. Jeff akacheka kidogo. “Sijasema nataka kukuoa Nanaa. Nimeomba tukutane kesho.” Nanaa akaingia aibu tena, akacheka kidogo. “Samahani. Nahisi kwa sababu namfahamu Zena, ndio maana nimekuwahi mapema. Sitaki kukupotezea muda.” “Hata mimi nisingependa kupotezewa muda.” Nanaa akainama na kufikiria.



“Nanaa?” “Nafikiria Jeff!” “Nini?” Jeff akauliza tena. “Najiona sipo tayari na hizo heka heka. Na wewe unaonekana ni mtu mstaarabu, pengine ungenielewa tu. Sipo tayari kwa mahusiano aina yeyote ile.” “Mbona vipingamizi vingi Nanaa? Nimeomba tutoke. Kwa nini usikubali, ukasikia ni kwa nini nataka tutoke kabla hujaanza kuweka vipingamizi?” Nanaa akacheka tena kidogo. Lakini wazi alionekana hafurahii.



“Ulitaka twende wapi?” “Tutoke kwa chakula cha usiku.” Nanaa alivuta pumzi. “Naishi na kaka yangu, Jeff! Siwezi kutoka usiku. Nitamwambia nakwenda wapi na wewe sikufahamu?” “Basi tufanye iwe mapema.” “Labda hujanielewa. Ninaposema naishi na kaka yangu. Namaanisha ndiye kama Mungu wangu wa pili hapa duniani. Ndiye mama yangu. Nikisema mama, namaanisha ndiye aliyenilea tokea siku nimezaliwa natolewa hospitalini mpaka hivi sasa. Kuninyonyesha, kuniogesha nakunivalisha mpaka nepi. Ni kama baba kwangu, kwa kuwa ndiye anayehangaika na kula yangu na kulala kwangu. Ndiye anayehangaika na kuvaa kwangu tokea mtoto mpaka hivi sasa. Ni kama baba anayesumbukia na soma yangu pia. Amechukua nafasi ya dada pia kwa kuwa ndiye anayenishauri kwa Karibu sana. Na ndiye mtu wa pekee katika maisha yangu ambaye yupo karibu yangu tokea nazaliwa mpaka sasa. Siwezi kufanya lolote hasa nikiwa nyumbani bila kumshirikisha yeye kwanza. Sasa hata nikikubalia tutoke mapema, namwambia nini juu yako Jeff wakati wala sikufahamu?” Nanaa alizidi kumsisitiza Jeff, ili tu amuache.



Lakini bado Jeff alipambana. “Unaweza kumuaga tu na kumwambia kuna mtu nakwenda kuonana naye. Mwambie utamwambia zaidi juu yangu baada ya mazungumzo yetu ya kesho tukitoka. Tukishakutana. Tukazungumza. Ukajua unipe nafasi gani kwenye maisha yako, utakaporudi nyumbani unaweza kumwambia chochote kile juu yangu. Lakini baada ya mazungumzo yetu. Ninachoomba ni unipe tu nafasi Nanaa. Tafadhali.” “Mmmh!” Nanaa akaguna. Wazi alionyesha kutokuwa tayari.



“Vipi?”  “Sijui kwa nini Jeff, moyo wangu unakataa. Naomba nipe muda wa kufikiria tafadhali.” “Unafikiria nini wakati hata hujui ni nini nataka kuzungumza na wewe? Si ungenisikiliza kwanza ndipo uniambie kama utataka kufikiria?” Nanaa alitulia. “Nanaa please!” “I don’t know Jeff. Naomba nifikirie hata huko kutoka. Sijajiandaa. Naomba nikutafute nikiwa nipo tayari. Tafadhali Jeff. Najua ni nini nazungumzia. Nahitaji muda.” “Unaniahidi kunipigia?” “Nafikiri.” “Nanaa!?” Jeff akamwita kwa masikitiko. “Sijui Jeff. Labda. Sitaki kukupa ahadi za uongo. Mimi sio muongo Jeff.” Kwa hakika Nanaa hakuwa na uhakika.



“Nanaa please!” “Kwa nini unanisihi wakati hata hunifahamu? Umetajiwa tu na Zena. Unajuaje kama mimi ndio mtu sahihi unayetaka kumwambia hicho unachotaka kuongea tukikutana?” “Hilo swali naomba nilijibu tukitoka wote.” Nanaa akacheka akionyesha wazi cheko lile sio la furaha. Hata uso wake ulionyesha kutokukubaliana.



Wakasikia mtu anakohoa upande wa pili wa ule uzio. Wote wakageuka. “Pole Danny mwanangu. Upepo huo!” “Asante mama yangu. Upepo mkali kweli!” Danny akajibu. Wakasikia watu wengi wanacheka. Ndipo wakajua kuna watu walikuwa wakiwasikiliza. Nanaa akainama. Jeff akacheka. “Nitasubiri simu yako Nanaa.” Jeff akaaga. “Asante kwa lifti. Nitakutafuta.” Jeff akaondoka. Nanaa alibaki akiwaza.



Birthday ya Fili.

“Uwiii! Danny si mume wa Grace? Sasa si watakuwa wamesikia kila kitu?” Nanaa aliwaza akiwa amesimama pale pale. “Njoo tu Nanaa. Hatujawasikia kabisa. Kwanza hatukuwa tukiwasikiliza.” Nanaa alitamani kuanguka. Akasikia sauti za watu wakicheka zaidi. Nanaa akajua wapo kundi la watu. “Nyamaza Danny! Utamfanya ashindwe kuja.” Alisikia sauti ya Grace. “Uwiii! Kwani na kaka James yupo hapo?” Nanaa akauliza. “Yupo. Lakini hajasikia kama utatoka kesho usiku.” Danny alijibu na kufanya wazidi kucheka. “Uwiii!” Nanaa alizidi kulalamika. “Njoo Nanaa. Achana na Danny!” Alisikia sauti ya kaka yake akimwita huku akicheka sana. “Njoo mara moja kaka!” Nanaa akamwita kaka yake, lakini akasikia wanazidi kucheka. “Nenda kamlete mkwe wangu, James.” Alimsikia Grace akiongea.



James akazunguka uzio, akatoka kwenye kigeti kidogo. Alitoka anacheka. “Usicheke kaka.” “Usiwe na wasiwasi. Twende.” “Siwezi hata kusogea hapa. Naona aibu kweli! Naona niondoke tu, kaka yangu.” Nanaa alijaribu kunong’ona zaidi, lakini bado akasikika. “Wala usione aibu Nanaa. Nimekwambia hakuna aliyesikia.” Danny alidakia tena, vicheko vikazidi kuongezeka. Nanaa akajifunika uso. “Danny nyamaza bwana. Ujue Nanaa akiondoka hapa, mwanao hatakata keki? Wewe fanya mchezo.” Hata James mwenyewe alikuwa anacheka sana. Akamshika mkono Nanaa, akaongoza njia mpaka ndani.



Alikuwa akitembea nyuma ya James. Aliishiwa nguvu baada ya kukuta hilo kundi la watu waliokaa hapo. Alishindwa kujua akifika hapo aanze vipi. Mungu bariki Fili akawa amemuona kabla hajawafikia. Akaanza kupiga kelele huku anamkimbilia Nanaa. Nanaa akasimama. “Nanaa! Nanaaa!” Nanaa akafungua mikono kama kumlaki. Maana Fili alikuwa akija kwa mwendo kasi.



“Usimchafue bwana.” Grace alimuwahi kabla Fili hajamkumbatia Nanaa. “Hamna neno. Mwache tu.” Fili alikuwa amejaa michanga mpaka kichwani. “Umechelewa. Lakini bado sijakata keki. Leo Mama ameniruhusu kunywa soda wakati nakusubiri wewe.” Fili alianza. “Kumbe ulikuwa unanisubiri mimi?” “Ndiyo. Kwani ulikuwa hujui? Nilimwambia anko Geb akupigie, akasema unakuja sasa hivi.” Fili aliendelea. “Mwache hata akae basi! Unamdaka na maneno mengii. Ataondoka sasa hivi.” Alimsikia Danny akiongea. “Eti utaondoka, Nanaa?” Fili akauliza kwa upole.



“Njoo ukae hapa mwaya. Huyo atakuchosha tu.” Grace alisimama huku akimuonyeshea pakukaa. “Eti utaondoka? Maana nimewaambia rafiki zangu wote kuwa unakuja. Wakataka kukuona. Sasa utaondoka kabla hawajakuona?” Fili alirudia tena kuuliza. “Hapana. Siwezi kuondoka, mpaka niwaone rafiki zako, tucheze wote ndio nitaondoka. Na hii ndio zawadi yako.” Fili akacheka kufurahia zawadi aliyopewa na Nanaa. Asante sana Nanaa.” “Karibu na samahani kwa kuchelewa.” “Mimi nimeshakusamehe Nanaa.” Fili akajibu huku macho yapo kwenye zawadi. Wakacheka wote.



Nanaa akasogelea lile kundi la watu wazima waliokuwa wamekaa, wakiangalia watoto wanavyocheza. Bado alikuwa amembeba Fili wakati akifungua mfuko uliokuwa na zawadi yake. “Nanaa ameniletea mpira wa Spider man!” Fili alifurahia sana. “Nilikwambia nini juu yakufungua zawadi hapa? Nitakufinya masikio mimi! Kwa nini husikii?” Danny alimbadilikia mwanae. “Si ni ya Nanaa tu, ndio nimefungua?” Wote wakacheka tena.



“Fili! Fili!” Liz akamwita. “Eeeh!” Fili aliitika. “Unaitikaje kama mtoto wa kike wewe? Sema naam!” Danny alimgombesha tena. “Naam!” Fili akarekebisha haraka haraka. “Sasa lini unamuoa Nanaa?” Liz alimuuliza kumchokoza tu. “Dad amesema mpaka nipate hela nyingi, nimlipe kwanza anko James, halafu nimchukue Nanaa, niende naye kwangu, nisirudi naye nyumbani.” Kila mtu alianza kucheka.



“Wewe Fili! Ndio nilivyokwambia hivyo?” Danny akamuuliza nakumfanya Fili afikirie kidogo. “Umeruka kitu kimoja.” Danny akamkumbusha. “Ehe, nimekumbuka. Dad  amesema, nisome sana, nipate pesa nyingi, nimlipe anko James, akinipa Nanaa, niende naye nyumbani kwangu, nisirudi naye nyumbani kule kwa dad.” Kila mtu alikuwa anacheka sana.



“Itabidi ukazane sana. Bado una safari ndefu sana.” Rafiki mmoja aliongeza. “Shule yenyewe bado hujaanza!” Mwingine alichangia. “Sio mbali sana. Dad wangu amesema naanza jumatatu. Ameshanitafutia shule.” Kila mtu alikuwa akicheka. Ni kweli Fili alikuwa mzungumzaji. Tena anaongea kwa ufasaha, bila woga. Mama yake alikuwa akitingisha tu kichwa.



“Bibi Fili amesema atanisindikiza kumlipa anko James pesa. Mimi sijui kuendesha gari, sioni mbele.” Watu walizidi kucheka. “Kumbe mama wewe ndio dereva?” Danny akauliza. “Nimepewa hiyo kazi. Amesema yeye hafikii sehemu ya kukanyaga mafuta na kuweka breki. Kwa hiyo mimi nimsindikize kwa anko James.” Mama Grace na Geb, au Mama G kama wengi walivyozoea kumwita, alijibu nakufanya watu wazidi kucheka. “Bwana mwanangu amejipanga. Lazima atamuoa Nanaa.” Grace aliongeza. “Tena Jeff akae mbali kabisa.” Danny alifanya Nanaa afunike uso kwa aibu. “Bora umemkatalia.” Danny aliongeza nakufanya watu wazidi kucheka. Mama G ndio kabisa mpaka machozi.



“Nina mpango wakuacha kazi, nasubiri mahari yangu kutoka kwa Fili.” James alidakia. “Ujipange mwanangu. Huyo anko James anapenda pesa kuliko benki.” Danny aliongeza. “Nitampa. Nitakuwa nazo nyingi sana.” Fili alijibu kwa kujiamini na kufanya watu wazidi kucheka. “Mmemsikia Dume langu? Nipe namba ya simu ya Jeff nizungumze naye.”“Bwana Danny muache Nanaa.” Grace alimwambia mumewe anyamaze huku yeye mwenyewe anacheka. “Lazima taarifa zimfikie Jeff, King’ang’anizi. Jamaa kakaba kweli! Kila akikataliwa hivi, anang’ang’ania tu. Haelewi!” “Ndio ikabidi uokoe jahazi Danny mwanangu?” “Kabisa mama. Mtu gani hataki kuelewa?” Wakazidi kucheka huku Nanaa amejificha nyuma ya Fili na yeye anacheka taratibu kwa aibu.



 “Twende Nana tukacheze.” Fili alimuokoa. “Bwana wewe nenda kacheze na wenzako, mwache Nanaa apumzike.” Danny alimkoromea mwanae. “Acha tu niende naye. Leo ni siku yake, mwache afurahi.” Nanaa akamshusha, akamshika mkono. Wakaanza kuondoka huku wengine wakicheka. “Najua kuogelea, dad alinitafutia mwalimu akanifundisha kuogelea. Halafu pia najua kucheza mpira wa kikapu na miguu. Nachezea kwenye timu ya mpira wa kikapu ya kina anko Geb. Mimi ndio mfungaji wao. Kila jumamosi jioni huwa naenda naye mpirani. Wananitegemea mimi hapa.” Geb alitingisha kichwa huku anacheka na wengine. Fili akaendelea. “Halafu huwa nacheza mpira wa miguu na dad wangu pale pale nyumbani. Najua pia kukimbia. Mama yangu ananisifia najua sana kuruka kamba. Pia…” Fili aliendelea kujisifia kwa Nanaa.



“Daah! Mwanangu kachanganyikiwa kabisa! Msikieni anavyojinadi kwa Nanaa. Vitu vyote leo anajua kuvifanya yeye, wakati muoga kweli wa maji.” Danny alifanya watu wazidi kucheka. “Bwana mwanangu ameweza kuogelea. Mwalimu wake anayemfundisha kuogelea anamsifia kweli.” Grace akamtetea. “Mmmh! Mbona mimi nilivyompeleka mazoezini alikuwa analia mpaka ulipongea naye kwa simu, ndio akakubali kuingia kwenye maji? Kioga kweli, utafikiri kitoto cha kike!” Danny alimjibu mkewe. “Sasa wakati ule si alikuwa bado hajazoea? Siku hizi mjuzi kweli. Muulize Geb ambaye pia huwa anampelekaga kwenye mazoezi ya kuogelea.” “Hana lolote huyo mwanao. Maneno mengii, muoga kama mama yake.” Danny alizidi kuchekesha watu.



*****************************************************

Nanaa alianza kumsukuma Fili na rafiki zake kwenye bembea. Walipeana zamu, Nanaa akawa anawasukuma. Mara akamuona tena Jeff amerudi na kuingia mpaka ndani. Akamuangalia Jeff, kisha akawaangalia wale waliokuwa wamekaa pale. Kina Danny. Akaona wote wameinamia simu zao. Kama hawajamuona Jeff. Nanaa akamsogelea akiwa amembeba Fili. Lakini wazi alijua kwa uinamaji ule, wote wamemuona Jeff. Vipi?” “Nimekumbuka sijachukua namba yako ya simu, na Zena amesema hawezi kunipa. Nikuombe wewe mwenyewe.” Nanaa akacheka kwa aibu. Akijua wazi kina Danny wanasikiliza. “Au basi chukua namba yangu mimi ya simu. Kama unaona shida kunipa yako.” Jeff aliongeza. Na yeye alijitahidi kuzungumza kwa sauti ya chini.  “Hamna shida. Hapa nilipo sina simu. Nimeiacha pale mezani. Nacheza na watoto. Chukua tu ya kwangu. Utanitumia ujumbe ili niwe na ya kwako pia.” Nanaa akajibu taratibu, kwa sauti ya chini. “Asante. Nitafanya hivyo.” Jeff alionekana kufurahia hilo wazo.



Jeff akatoa simu yake. “Sasa sio na wengine muanze kukariri namba ya simu ya Nanaa. Mwenyewe ameamua kumpa Jeff tu.” Danny aliongea kwa sauti. Mpaka Jeff akacheka. “Kwani huwezi kunyamaza Danny jamani!?” Grace alimfinya. “Mimi nawajua binadamu mke wangu. Bahati ya Jeff wanaweza kuikalia mlango wazi. Kabla hajafanikisha dinner ya kesho, wakamuwahi kwa lunch.” Watu walizidi kucheka mpaka wengine walikuwa wakitokwa na machozi.



“Ningekuwa mimi Jeff, ningempa Nanaa simu aandike tu. Asiitaje. Wote waliokaa hapa watu wa namba tupu. Tokea wanaanza kuongea mpaka leo wanacheza na namba tu. Yaani wapo hapa mjini wanalipwa kwa kuchezea namba kwenye maofisi ya watu.  Nakuhakikishia Jeff, hawatashindwa kukariri hizo tarakimu 10 tu za namba ya simu ya Nanaa. Ni ushauri tu kaka. Unaweza kuuchukua au kuuacha. Na ujue wengi wao hapa bado hawajaoa na hawana hata wachumba. Sasa juu yako Jeff.” Danny aliongeza. Nanaa na Jeff walishindwa hata kuongea, wakabaki wanacheka. Nanaa akiangalia chini, Jeff akiwatizama.



“Au kuondoa mzizi wa fitina. Chukua hii kalamu na karatasi Jeff. Mimi nawajua binadamu. Hapo wote masikio wazi. Wewe unaandika kwenye simu, wenzio kichwani. Halafu ulogwe ukosee namba hata moja hapo, utaandika maumivu. Maana hivi vichwa hapa, mimi navijua. Vina historia yakutokusahau. Heri kuandika tu kimya kimya. Hata Nanaa akikosea kuandika hata tarakimu moja tu, potelea mbali. Wote mkose. Kuliko wewe uliyehangaika hivyo vyote, eti ukose. Halafu majamaa hapa yapate!” Danny akasimama na kumpelekea Jeff kalamu na karatasi.



“Mimi nakukabidhi wewe mwenyewe. Uamuzi ni wako.” “Nakushukuru.” Jeff alishukuru huku akicheka.  “Tupo pamoja kaka. Wema ndio asili yangu.” Danny alijibu kiungwana sana huku akijisifia. Mama G, alikuwa akicheka mpaka machozi. Jeff akamkabidhi Nanaa ile kalamu na karatasi. Nanaa akapokea, akaandika ile namba akamrudishia Jeff ile kalamu na karatasi, yeye akarudi upande walipokuwepo watoto na kuwaacha wazazi wao wakizidi kucheka. Jeff akamrudishia Danny kalamu yake. “Asante.” “Karibu Mkuu. Kila la kheri. Naamini hujapewa namba za gari.” Danny akapokea kalamu na kumpa mkono. Mpaka Jeff mwenye akacheka. Akaondoka na kaucha huku nyuma wanazidi kucheka.



**************************************************



Nanaa akamrudisha Fili kwenye bembea. Akaendelea kumsukuma. Fili alisikika akicheka kwa furaha. “Hivi nimekwambia kama umependeza sana?” Fili alisikika akimuuliza Nanaa nakufanya mpaka Nanaa mwenyewe acheke. “Asante Fili.” “Umependeza sana. Gauni yako nzuri. Nitamwambia mama yangu atupige picha. Halafu dad akaitoe tuiweke ukutani. Nikihama na wewe, nahama na picha yangu.” Mpaka safari hii Danny alicheka kwa sauti. “Bwana mwanangu amekazana!” Walizidi kucheka huku wakiwatizama Nanaa na watoto wote. Walitoka kwenye mchezo huu, na kuhamia kwenye mchezo mwingine huku Fili akiendelea kumsifia Nanaa, akionekana kufurahia uwepo wa Nanaa kwenye party yake.



**************************************************



Wala Nanaa hakuwa amevaa nguo ya ajabu sana. Alivaa gauni lake alilokuwa amelipata mtumbani. Lenye viboksi vyeusi na vyeupe kote. Kata mikono lakini linakiungio kiunoni. Kwahiyo kiuno chake kilibanwa vizuri na kuachia chini mpaka chini ya magoti. Halikuwa limechanua sana. Liliendana na umbile lake zuri. Chini kote lilizunguka muundo wa kashata kashata. Kama lililochanwa makusudi. Alivaa na sendozi zake za kimasai zilizojazwa shanga nyingi nyeupe. Alishazivua pembeni ya kiti alichokuwa amekalia kaka yake ili aweze kutembea mchangani kwa uhuru.



Kama kawaida, alikuwa amesukwa rasta ndogo ndogo. Lengo kubana matumizi. Wakati wote alisuka rasta ndogo ndogo ili zikae muda mrefu. Zisimgarimu kwenda saluni mara kwa mara. Na pili zilimrahisishia kila asubuhi anapokwenda kazini. Kwa hiyo usingemkuta Nanaa na kipilipili chake kikavu. Wakati wote alisuka nywele zake. Hapo napo alibana mtindo wa butterfly. Pande mbili ambayo moja ilikuwa ndogo, mstari wa pembeni na kuzivuta mpaka katikati huku nyuma zimeanguka mpaka mgongoni.



Hereni zake za duara kubwa kiasi, alizokuwa amenunua kwenye urembo zilimkaa vizuri sana na ule mtindo wa nywele ambao hata upepo uwe mkali vipi, bado kichwani alibaki msafi na gauni halikumfanya awe uchi. Japokuwa alionekana amevaa vitu vya hali ya chini sana, cheap, lakini bado alipendeza. Ungetaka kumwangalia tu.



**************************************************



Walikuwa watoto 15, kutoka familia tofauti tofauti, na wazazi wao walionekana kufahamiana vizuri. Danny ndiye alikuwa akiwachekesha wazazi wao. Geb naye alikuwepo. Alikuwa amekaa pembeni ya Liz, ametulia kama kawaida yake. Akajikuta macho yake yakihama na kwenda kila anaposogea Nanaa. Alitulia akabaki akimtizama kwa utulivu, kama anayetafakari kitu.



“Mwenzetu umepotelea wapi?” Liz alimshtua Geb. “Nipo tu, nasikiliza.” Geb alijibu. “Mama Fili anakuuliza.” Geb hakujua hata kama aliongeleshwa. Akashtuka kidogo akamwangalia dada yake. “Keki vipi?” Grace akarudia. Unataka sasa hivi?” “Ndiyo. Naona njaa zitaanza kuwauma sasa hivi, wadai chakula kabla ya keki. Nataka wakate keki kwanza ndio wale.” “Basi ngoja nikamuombe yule muhudumu anipe. Nilimuomba anihifadhie kwenye friji.” Geb akasimama. “Usisahau kuja na juisi yake huyu. Akili zikitulia, ataikumbushia. Ni heri uilete tu moja kwa moja ili usifanye safari nyingi za kwenda na kurudi.” “Hamna shida.” Geb akaondoka kwenda kufuata keki.



“James!” Mmoja wa kijana aliyekuwepo pale aliita. “Vipi Zinda?” “Sasa si unajua mimi pesa ipo? Sihitaji kukusanya kama Fili. Au kuomba namba kama Jeff. Mimi mtoto wa nyumbani. Tumetoka mbali sana mimi na wewe. Tumalizane kabisa.” Watu walianza kucheka. “Wewe tu. Changamka. Si umemuona mwenzio Jeff karudi?” James alijibu, Geb akarudi na keki akaiweka mezani.



“Tena Jeff mwenzio kakazana kweli. Si ulisikia mama?” Danny alimuuliza Mama G nakumfanya acheke. “Kila alivyokuwa anakataliwa, jamaa amekazana.” Danny aliongeza. “Yaani nina uhakika Nanaa ni mke wangu mimi. Wengine wanahangaika tu” “Sasa si umfuate pale? Maneno mengii. Au unaogopa?” Danny akamuuliza Zinda. “Kukataliwa kubaya!” Wote wakacheka.



“Jikaze kiume, Zinda.” “Ngoja nivute pumzi.” Zinda alijisogeza kwenye kiti. “Vipi Mkuu? Mbona unatoa jasho wakati upepo mkali?” Geb aliuliza na kuamsha kicheko kingine. “Anataka kumzidi mahesabu mwanangu na Jeff. Sasa anapanga maneno ya kumwambia Nanaa. Maana amesikia ya mwenzake Jeff, hana hali. Akirudi kwa Fili, yeye ndio anamikakati mpaka ya mahari. Halafu mke anacheza naye.” Danny alijibu. Wote wakacheka.



“Nawaambieni kweli, Nanaa mke wangu mimi.” “Kwani kuna aliyekukatalia Zinda? Wewe si uende tu!” Danny alifanya wote wazidi kucheka. “Eti bibi Fili?” Zinda akamgeukia mama G. “Nenda tu baba. Mwenye kisu kikali ndio mla nyama.” Mama G, alijibu, wote wakacheka.



**************************************************



Mara wakamuona Nanaa na Fili wanarudi pale walipokuwa wamekaa. “Ehee! Huyo anakuja.” Zinda akajiweka sawa, wengine wakakwepesha macho wakijidai hawakuwa wanamwangalia. “Anataka nini huyo?” Danny akauliza. “Anataka kutumia choo. Sijui ni wapi?” Nanaa akauliza. “Ngoja nikusindikize Nanaa.” Zinga akadakia. “Sio mimi, ni mtoto.” Nanaa alijibu kwa upole nakufanya kila mtu acheke. “Sasa Zinda unachanganyikiwa nini? Nanaa kasema wazi kabisa, ni Fili.” “Si ndio na mimi nimesema niwasindikize, au nyinyi mmesikiaje?” Kila mtu alicheka. “Wewe mmpeleke mtoto chooni, acha kujitetea. Umesema umsindikize Nanaa.” Danny hakuwa anajua kunyamaza, watu walizidi kucheka.



“Muone na huyu anavyoruka ruka. Nilikwambia nini hukusu kubana mkojo?” Danny alimuuliza mwanae kwa ukali. “Ulisema nisibane mkojo. Nikisikia tu mkojo, niache michezo niende chooni kwanza.” “Sasa kwa nini unaruka ruka?” “Si ruki ruki.” Fili akajitetea. “Nilikwambia nini juu ya kusema uongo?” Aliendelea kumuhoji mwanae. “Nisiseme uongo hata kidogo. Ni heri niingie matatizoni kuliko kusema uongo, hata mdogo.” Fili alimjibu baba yake kwa upole na kuacha kuruka ruka. Alionekana huwa anammudu Fili cha utundu. Watu walizidi kucheka. “Mmpelekeni mwanangu chooni jamani! Atajikojolea.” Grace alilalamika.



“Anko Geb, nipeleke chooni.” Fili alimgeukia anko wake. “Nipeleke au naomba unipeleke?” Danny alimkoromea tena. “Anko Geb naomba nipeleke chooni.” Fili alirudia tena kwa upole. “Kwa nini mimi nisimpeleke mara moja chooni?”   Nanaa alitaka kupunguza shuguli nyingi. “Hapana. Wewe utanipeleka choo cha kike.” Watu walianza kucheka tena, na wote walikuwa wakiwasikiliza. Nanaa bado hakuwa akimuelewa. Tokea anamtoa kwenye mabembea alitaka apelekwe kwa Geb, au baba yake ndio wampeleke chooni.



“Kwani choo cha kike kina nini? Mimi nitakuwa na wewe. Sitakuacha Fili.” Nanaa alimuongelesha kwa upole. “Hapana. Dad alisema hakuna kuvaa tena diaper, wala kukojoa nikiwa nimechuchumaa. Nikojoe choo cha kiume, tena nikiwa nimesimama.” Watu wote walicheka mpaka Nanaa alishindwa kujizuia akacheka mpaka machozi, lakini Fili alikuwa ametulia akionekana anajikaza tu lakini amebanwa na mkojo.



“Bwana Geb mpeleke mtoto chooni. Atajikojolea.” Grace alilalamika tena, Geb akasimama huku anacheka. “Twende. Na hakuna kubana tena mkojo.” Geb alimshika mkono na kuondoka naye. Kila mtu alibaki anacheka.



**************************************************



 “Twende tukacheze Nanaa. Zinda alianza tena, nakufanya watu wazidi kucheka kasoro Nanaa alikunja uso na tabasamu la mshangao. “Zinda vipi leo?” Danny aliuliza huku akicheka sana. “Namaanisha twende tukacheze na watoto, bwana. Kwani nyinyi mmesikia nini?” “Mimi nashauri leo uache tu. Ishashindikana. Utaishia kumtukana Nanaa mwenyewe bure! Maana mara umwambie umpeleke chooni, mara mkacheze, hujielewi hata kidogo.” “Nafwata ushauri wako Danny. Naona kweli leo bahati sio yangu. Upepo unavuma pabaya.” Walizidi kucheka, lakini Nanaa hakuwa ameelewa.



“Naomba James unikaribishe nyumbani kwako.” Zinda alimgeukia James. “Ushindwe hapa, nyumbani utaweza? Sitaki wageni nyumbani kwetu. Wewe malizana na Nanaa hapa hapa. Ukija nyumbani ni kulipana tu kama Fili.” James alijibu. “Mimi bado naona mwanangu ndio Dume. Kwanza kashatongoza mapemaa. Kajinadi mpaka Nanaa mwenyewe amemkubali. Hang’ati maneno. Na ameshaweka utaratibu wa kulipa mpaka mahari. Msimzibie mwanangu bahati yake. Katafute kwengine.” Danny alifanya watu wacheke zaidi.



Geb akarudi na Fili. “Njaa imeanza kumuuma huyu. Anataka juisi yake.” Danny akataka kumpa chupa yake ya juisi. “Usimpe bwana Danny. Hatakula wala hataweza kukata keki, ataishia kulala na chupa ya juisi mdomoni. Njoo kwanza hapa mwanangu.” Fili alimsogelea mama yake kinyonge, akionekana ameshachoka. “Njaa inauma?” Fili akatingisha kichwa . “Wee!” Danny alikuwa kama anamkumbusha mwanae kitu, haraka Fili akakumbuka na kujirudi. “Ndiyo mama, njaa inauma.” “Mwache bwana Danny. Amechoka.” “Hakuna tabia za kuitikia na kichwa. Kwani yeye mtoto wa kike?” “Amechoka.” Grace alimtetea. “Ndio akae hapo apumzike, asubirie chakula.” Danny aliongeza. “Huo utakuwa mtihani. Akae chini huyo! Hawezi. Kateni tu hiyo keki, ale, akacheze. Akitoka hapo, nikulala.” Liz akaongeza.



**************************************************



Wakawaita watoto wote, wakamwimbia Fili, akakata keki. Alimlisha Nanaa wa kwanza, mama yake, dad, Bibi Fili na anko Geb. Wakaagiza chakula, Nanaa akaona ni heri aenda kukaa kwenye meza ya watoto kuliko kukaa pale na kina Danny. Akajua watazidi kumchokoza. Akamuaga kaka yake. “Kaka! Naenda meza ile ya kule, kuwalisha watoto.”  Nanaa alimwita kwa sauti ya chini ili asisumbue wengine. “Poa poa.” James akiwa amenogewa na porojo za Danny, akakubali bila kupinga. Nanaa akamchukua Fili wakaondoka.



**************************************************



Kilipoletwa chakula cha watoto Nanaa akaanza kuwagawia wote. Na kuanza kumlisha Fili huku akisimamia na watoto wengine wale wapunguze michezo. Wengi wao walikuwa na njaa. Kwa hiyo wakala bila shida. Wakamaliza kwa haraka bila Nanaa kutegemea. Akabaki akibembelezana na Fili pale mezani.



“Na wewe utakula nini?” Alishtukia Geb amemsimamia nyuma yake. Akageuka, macho yao yakagongana, haraka sana Nanaa akarudisha uso pale mezani. “Nimemwambia muhudumu asubiri kwanza, asiniletee chakwangu mpaka watoto wamalize kula.” Nanaa alijibu huku amekaa, na kumpa mgongo Geb. “Ungekula sasa hivi. Tunakaribia kuondoka.” “Basi nitaenda kufuata ndani.” “Unataka kula nini? Mimi naweza kwenda kukuchukulia.” Geb aliendelea. “Usihangaike. Nitakwenda tu.” “Sio usumbufu hata kidogo.” Nanaa alifikiria kitu  gani chakula, akajikuta hajui achague nini, akabaki kimya akifikiria nini ale.



Grace na mama yake wakasogea pale. “Bibi Fili! Njoo tule wote.” Fili alimuwahi bibi yake. “Mwenzio nimemaliza chakula changu. Na wewe maliza cha kwako.” Bibi yake alisogea mpaka pale mezani. “Sidhani kama atakula vizuri. Danny amempa keki kubwa sana.” Grace akasogea Karibu zaidi. “Lakini anakula. Anakaribia kumaliza.” Nanaa alimtetea. “Basi atakuwa alikuwa na njaa sana.” Grace alivuta kiti akakaa.



“Unataka kula nini ili nimwite muhudumu akuletee?” Grace naye akauliza. “Nahisi kushiba.” Nanaa akajibu. “Basi agiza, mwambie akufungie ubebe. Ukale nyumbani ukisikia njaa.”  Grace akavuta sahani ya Fili ili amlishe yeye. “Labda hivyo. Ngoja niende hukohuko ndani ili niangalie wana vyakula vya aina gani.” Nanaa akasimama. “Usije kulipia lakini. Geb ndio atalipia vyakula na vinywaji vyote.” Grace aliongeza wakati anamnyanyua Fili ili ampakate. “Ameshaanza kusinzia huyu! Inabidi tuondoke.” Grace alimbusu mwanae kichwani, Fili akajilaza kifuani kwa mama yake. “Hivyo unavyomkumbatia, ujue ndio hatakula tena.” Bibi yake aliongea huku akikaa kwenye kiti alichokuwa amekaa Fili.



**************************************************



Nanaa aliingia ndani ili kuchagua chakula, akamuona Geb naye anamfuata. Alisimama sehemu wanayo agiza chakula akabaki akisoma Menu, ili aagize. Geb naye akasimama pembeni yake. Nanaa alisoma mpaka mwisho bado hakuona kitu chakuagiza. “Unaweza kulipia tu. Sidhani kama nitakula.” “Hujapenda kitu hata kimoja wapo hapo?” Geb akauliza. “Nahisi bado nimeshiba.” “Ungechukua chakula chochote tu, watakufungia vizuri, utakula baadaye.” “Ili nisikucheleweshe kulipia, ungelipia tu vyakula vya watu wengine, halafu nikiamua baadaye kuchukua kitu chochote, nitalipia mwenyewe.” Alimsikia Geb akicheka kwa kuguna kidogo, akageuka kumwangalia.



 “Sina haraka yakulipia Nanaa. Ila sitaki uondoke bila kula kitu chochote.” “Mbona wewe sijakuona ukila? Umekula kweli?” Nanaa akamuuliza kwa kujali. Hata huwezi kujua alionaje kama Geb hakula wakati alikuwa kwenye meza ya watoto na Geb alikuwa katikati ya meza iliyojaa marafiki zao. “Mama alinipikia uji, nikanywa kabla hatujaja hapa. Bado nimeshiba.” “Bado unakunywa uji mpaka leo!?” Nanaa alijikuta anaropoka kwa kushangaa sana, nakumfanya Geb acheke kidogo. “Naomba hilo swali umuulize Bibi Fili. Na mimi huwa nashangaa hivyo hivyo.” “Sasa kwa nini na wewe usibebe chakula? Baada ya muda utasikia njaa. Uji huwa haukai muda mrefu tumboni.” “Hapa naona wanavyakula vya kukaanga tu. Na mimi huwa sipendi vyakula vyakukaangwa na mafuta mengi, kama chips. Nakinahiwa haraka sana. Nikifika nyumbani naweza kula chakula alichopika Grace mchana. Kwa hiyo mimi nipo sawa tu.” Yalikuwa ni maongezi ya mara ya kwanza waliyozungumza kwa muda mrefu kwa kuangaliana.



Nanaa alikuwa akimsikiliza huku akitizama macho yake. “Haya macho si mchezo!” Nanaa aliendelea kuwaza moyoni wakati bado akimsikiliza. “Kwa hiyo utachukua nini?” Geb aliendelea kuuliza. “Nitarudi baadaye wakati tunaondoka. Nahisi nitachukua tu Icecream, nikale nyumbani.” Nanaa akageuka tena kama kusoma tena ile Menu kujiridhisha. “Huwa unapenda Ice cream gani?” Geb alihoji kiustarabu. “Vanilla ndio napenda zaidi.” Nanaa akajibu na kumgeukia tena. “Kwa nini umeuliza?” Nanaa akamuuliza na tabasamu lenye mshangao kidogo. “Nataka tu kujua.” Nanaa akatabasamu na kugeukia tena ule ubao mkubwa uliokuwa umening’inizwa juu kabisa. Ulikuwa umebeba Menu zote. Akageukia upande ulipo Ice cream na bei zake. Akaangalia kwa muda kisha akageuka na kuondoka.



**************************************************



Alitoka na kukuta baadhi ya wazazi walishaondoka na watoto wao, lakini James na kina Danny bado walikuwa wakiongea na kucheka kama ndio wamefika hapo. Danny alikuwa amempakata mtoto wake, Fili, amelala. “Naomba nikupokee.” Nanaa alimsogelea Danny. “Mzito huyu! Wewe muache tu hapahapa. Pumzika.” Danny alimjibu Nanaa huku akimwangalia mtoto wake aliyekuwa amelala. “Maneno yote yamemuisha kwa kuchoka.” Liz aliongeza huku akisimama. “Geb yuko wapi? Nataka kuondoka.” Liz aliuliza huku akiangaza macho kumtafuta Geb. “Grace! Umemuona wapi Geb?” Grace alikuwa ndio anarudi kutoka kusindikiza wageni wengine waliokuwa wamekuja kwenye sherehe ya mtoto wake. “Unataka muondoke?” Grace akauliza. “Nataka kumuaga. Kuna mahali nataka kupita kwanza.” Liz akajibu. “Mwangalie ndani, atakuwa analipia.” Grace alijibu na kwenda upande walipokuwa wakicheza watoto ili kujaribu kusafisha kabla yakuondoka. Nanaa akamfuata ili kumsaidia. Waliendelea kuokota huku wakihifadhi baadhi ya vitu walivyosahau watoto.



“Najua utakuwa umechoka, lakini nakushukuru. Umenisaidia kucheza na watoto. Wamefurahi.” Grace alimshukuru Nanaa wakati wakiendelea kusafisha. “Na mimi nimefurahi. Napenda sana watoto.” “Mimi napenda watoto, lakini wasiwe watundu kama Fili. Jamani mtoto ananichosha akili huyo! Nafikiria kama mimi mama yake ananichosha hivi, sijui inakuaje kwa wasichana wa kazi.” Nanaa alicheka. “Unafikiri nakudanganya? Mimi napenda akiwa ameanza kuchoka, hapo sina neno. Na anapenda kulala kama mgonjwa. Hajiwezi kwa usingizi.” “Labda anakuwa anachoka sana.” Nanaa alijibu huku akicheka. “Kwa shuguli zile, lazima achoke. Ukimuona amekaa chini ametulia, ujue Danny yupo, au ananjaa au usingizi umemlemea. Basi.” Nanaa alizidi kucheka.



“Hakuna urefu asioweza kupanda. Hakuna neno asiloweza kuongea. Hakuna jambo asilolielewa. Na hasahau. Anarudia neno kwa neno. Sasa akianza kusimulia habari zake, namtuma kwa Geb, yeye huwa hachoki kumsikiliza. Halafu anamjulia. Sasa mimi siwezi. Nakuwa na mambo mengi yakufanya na kuwaza. Sasa ubaya wake ni kila akizungumza kidogo, anakuuliza maswali kutaka kujua kama unamsikiliza au umempuuza. Na anajua.” Nanaa alizidi kucheka.



“Niwasaidie nini?” Geb akawasogelea. “Afadhali umekuja. Msaidie hapa Nanaa, mimi nikakae. Nimechoka. Liz ameshaondoka?” “Ameondoka, kuna mahali amesema anataka kwenda.” “Ana mambo mengi shoga yangu yule! Sasa usiku huu anaenda wapi?” “Sijamuuliza.” Geb alijibu kwa upole na kwa ufupi, na kuendelea kukusanya takataka. “Mmh!” Grace aliguna na kuondoka. Akawaacha Nanaa na Geb. Kimya kikazuka. Wakaendelea kukusanya mpaka wakamaliza. “Hivi ni baadhi ya vitu walivyoacha watoto.” Nanaa akamkabidhi. “Asante, na tunashukuru kwa kuja.” Nanaa alitabasamu tu.



**************************************************



“Naona kikao ndio kimeanza rasmi.” Geb aliongea huku akiangalia meza waliyokaa kina Danny na rafiki zake waliobaki pale bila watoto. Walikuwa wakicheka huku wakiongea kwa sauti kubwa. “Unamaana hawataondoka pale sasa hivi!?” Nanaa akauliza. “Sio leo. Huwa wanakaa muda mrefu sana. Unaharaka yakutaka kuondoka? Naweza kukurudisha nyumbani.” Geb akauliza. “Hapana. Naweza kumsubiri tu kaka. Sina pakwenda.” “Basi tukazunguke kidogo, ndio turudi kukaa.” Nanaa akamwangalia vizuri kwa mshangao kidogo.



“Unamaanisha na mimi?” Aliuliza kutaka uhakika. Maana alijua huwa anajichanganya sana kila anapokuwa na Geb. Hakutaka kufurahia safari isiyo muhusu. Geb akatabasamu. “Ndiyo.” “Wapi?” Nanaa akauliza tena. “Hapo nje ya uzio, kumepakana na bahari. Au umechoka?” “Hapana. Tunaweza kwenda tu. Labda kama wewe ndio umechoka.” Tayari alishaanza kujichanganya. Akasahau kama Geb ndiye aliyemwambia watembee kidogo. “Mimi nipo sawa kabisa. Nililala muda mrefu mchana.” Geb alijibu huku akitoa tabasamu. “Nisubiri nikaweke hivi vitu kwenye gari. Grace atawarudishia wazazi wao akipata nafasi.” “Sawa.” Geb akaondoka, akamuacha Nanaa amesimama akiwaza.



**************************************************



 “Atakuwa alilala na Liz, pale nilipowaacha nyumbani kwa dada yake.” Nanaa aliwaza huku wivu ukimtesa. “Wanaonekana wanapendana. Alimuomba aje pale huku akisisitiza ana hamu naye.” Aliendelea kukumbuka. “Wote wanaonekana wanajielewa. Liz anaonekana ni msichana msomi, anapesa, na mzuri. Ni haki yake kumuhitaji.” Wivu ulishamjaa kwa mwanaume asiye wake. “Liz anakaumbile kazuri. Hana nyama uzembe. Kila kitu chake ni cha kiasi mwilini wake. Mpaka rangi ya mwili wake inavutia.” Nanaa aliendelea kuwaza akiwa amesimama pale peke yake akimsubiria Geb. Hamu ya kuzunguka naye ikaanza kumwisha. “Nitakuwa najiumiza tu.” Nanaa akaendelea kusononeka.



**************************************************



 “Namzungusha Nanaa baharini kidogo.” Alimsikia Geb akiwaaga lile kundi la vijana waliokuwa wakiongea na dada yake. “Afadhali, ili asichoke.” Grace alijibu. “Unataka twende wote, mama?” Geb alimuuliza mama yake. “Nimechoka bwana. Acha niendelee kusikiliza stori, nicheke.” Mama yao alijibu huku akionekana anafurahia sana kinachoendelea pale.



Geb akamsogelea Nanaa, aliyekuwa amepooza. “Upo tayari?” Geb akamuuliza huku akimwangalia, Nanaa alitingisha kichwa kukubali, wakaondoka. Ukimya mwingine ukazuka wakati wakiendelea kutembea nje ya uzio, mchangani. Mawimbi ya bahari yalipigwa kwa nguvu na upepo, lakini giza lilishaingia, ilikuwa ngumu kuyaona. Walitembea kwa muda kidogo, hakuna aliyemuongelesha mwenzake. “Tusiende mbali sana. Kunakuwa na wahuni wengi mida hii.” Geb alivunja ukimya. “Unasikia baridi? Naona upepo mkali kweli.” Aliuliza tena. “Hapana, nipo sawa tu.” Nanaa alijibu kwa kifupi, akanyamaza. “Unataka tukae kidogo au umechoka unataka kurudi?” Geb akauliza tena. “Vyovyote tu, nipo sawa.” Geb akamwangalia kwa utulivu. “Upo sawa? Mbona kama umekosa raha gafla?” “Nipo tu sawa.” Nanaa alijitahidi kutoa tabasamu, Geb akabaki akimwangalia akionyesha wazi amelikataa tabasamu feki.



Nanaa & Geb.



G

eb akatafuta mahali akakaa, “Tukae hapa.” Nanaa naye akaenda kukaa pembeni yake, wakatulia kidogo. “Vipi shule lakini?” Geb akauliza. “Tupo field, kwa sasa. Tukirudi ndio mwaka wa tatu na wa mwisho, tunamaliza.” Nanaa akajibu. “Unampango wa kuendelea kusoma?” Geb akauliza tena. “Mimi sio mpenda shule.” Geb akacheka. “Kweli tena. Hata hapa nilipofika ni kwa sababu ya kaka James. Sasa kuja kurudi tena kusoma shahada ya pili! Hapana kwa kweli.” “Utataka kufanya nini ukimaliza?” “Hata sijui. Nilikuwa na mipango mingii, lakini yote imevurugika. Nahisi nitajua mbele ya safari.” Geb akamwangalia.



“Nini kimevurugika?” “Kila kitu. Naomba Mungu asaidie tu, nikimaliza shule, nipate kazi, maisha yaanze.” “Unampango wakuishi wapi? Namaanisha utatafuta kazi maeneo gani?” Geb aliendelea kudadisi. Nanaa alitulia kidogo kama anafikiria. Akajibu kwa upole. “Popote pale nitakwenda kufanya kazi au nitatafuta kazi, isipokuwa Moshi na Arusha.” Geb aliweka uso wa kuuliza kidogo kisha akatupia swali jingine. “Kwa nini hupataki Moshi na Arusha?” Nanaa akanyamaza, akabaki anafikiria.



“Eti Nanaa?” Geb akauliza tena. Alikuwa na sauti nzuri iliyotulia na kumfanya mtu yeyote apende kumsikiliza. Labda ni Nanaa tu. Lakini alijisikia vizuri kuwa karibu na Geb. “Hiyo mikoa sitamani kuja kurudi tena. Imebeba historia mbaya tupu ya maisha yangu” “Ikitokea unapata kazi huko, je? Tena kwa ahadi ya pesa nyingi.” “Mmmh! Sitakwenda.” Nanaa akajibu kwa hisia za majonzi akiwa ameinama kama amekumbushwa mbali. “Kweli umepachukia.” Kwa muonekano ule, Geb mwenyewe akaamini kuwa Nanaa amekusudia kutorudi.



 “Lakini si unajua ukishindwa hiki unapanga tena mipango mingine? Usiache kujiwekea malengo, kwa kuvunjika kwa malengo uliyokuwa umejiwekea zamani.” Geb alishauri. “Wakati mwingine unakata tamaa au unajishuku labda unaweka malengo yasiyowezekanika maishani. Unaamua kuacha tu. Usubiri litokee lakutokea, upambane nalo mbele ya safari. Kuliko kuumia kila wakati.” “Pole. Lakini ipo siku nitataka uniambie hiyo mipango iliyogoma kutimia.” Nanaa alicheka kidogo, akainama kama anayefikiria.



“Wewe mipango yako yote inatimia?” Safari hii Nanaa naye akauliza swali nakumfanya Geb acheke huku akifikiria kidogo. “Daah! Swali zuri sana. Japokuwa sikuwahi kuulizwa kabla na na..” Geb akababaika kidogo. “Lakini labda niwe muwazi.” Akaendelea. Siwezi kulalamika. Ni mambo madogo madogo tu ambayo naweza kurekebisha. Yapo ndani ya uwezo wangu. Siwezi kulaumu. Namshukuru Mungu kwa hilo.” “Hongera.” Geb alicheka akamwangalia. “Natakiwa hongera eeh?” “Kabisa. Niwachache sana wanaoweza kufikia ndoto zao.” Geb alitabasamu. “Asante. Namshukuru Mungu kwakweli.” Alijibu na kunyamaza. Ukimya wa muda ukapita tena.



“Unafurahia kufanya kazi na Grace?” Geb akauliza tena. “Ukweli hana shida. Ilimradi ufanye tu majukumu yako. Kwanza anachoka kuongea na kusikiliza maneno mengi. Mpole kama wewe.” Nanaa alijibu na kumfanya Geb acheke. “Umejuaje kama mimi mpole? Au kwa kuwa sijalalamika kwa kutojibu ujumbe wangu?” Nanaa akacheka kwa aibu nakujificha uso. “Eti Nanaa?” “Samahani.” “Kabla yakuomba msamaha, niambie kwa nini hukunijibu.” Nanaa alinyamaza kama anafikiria.



“Eti Nanaa?” “Ni habari ndefu. Lakini unisamehe tu.” Walijikuta wakiangaliana. Nanaa alijaribu kukwepesha macho lakini akakuta bado Geb akimwangalia kwa utulivu. “Ni mambo mengi, Geb.” Nanaa alijilalamisha kwa upole. Yanayohusiana na ule ujumbe niliokutumia au ni kitu kingine? Maana nilitaka kujua unaendeleaje na kama ulifika nyumbani salama. Basi. Nikaona umesoma ujumbe wangu, halafu kimya. Hukurudisha majibu Nanaa.” Nanaa akainama.



“Ukweli niliiingiwa na wasiwasi. Ikabidi kukufuata nyumbani kujua unaendeleaje. Tena wala hukunisalimia mimi. Au kuna kitu nilikuudhi tulipokuwa wote pale ofisini?” Nanaa akajisikia vibaya sana moyoni. Japokuwa siku ile usiku walipoenda kumtizama nyumbani baada yakuondoka ofisini bila kuaga na kumuacha Geb haelewi, aliyezungumza ni Grace na Danny tu. Geb alikuwa kimya. Kumbe yeye ndio aliyekuwa na safari ya kwenda kumuona. Grace na mumewe walikuwa wasindikizaji tu!



“Nilikuudhi nini?” Geb aliuliza kwa kubembeleza. “Hapana. Hakuna ulipokuwa umekosea. Ni mimi mwenyewe tu. Naomba unisamehe.” Nanaa alimwangalia tena. Angemuudhi mtu yeyote, lakini sio Geb. Kijana mgeni kwake, lakini akajikuta ameshateka moyo na fahamu zake.



“Siweze kusamehe kama sifahamu kosa, Nanaa. Kama nikitu cha kurekebisha, si niafadhali tujue turekebishe ili isitokee tena?” Nanaa akanyamaza. “Eti mchumba wa Fili? Au Jeff ameshamzidi mahesabu?” Nanaa alijikuta akicheka kwa sauti. “Kumbe na wewe mchokozi hivyo?” Geb alicheka. “Mimi sio mchokozi. Najiandaa kwa harusi.” “Kwani na wewe ulisikia mazungumzo yangu na Jeff?” Nanaa aliuliza kwa aibu sana huku akicheka. Geb alibaki akitabasamu tu. Nanaa akapata jibu lake moja kwa moja.



“Usiniambie kama na wewe ulisikia!” “Mlikuja kuongea nyuma yetu. Tena Danny alikuwa akionyesha kitu alichokuwa akifanya Fili. Wakawa wamepingiana pesa na Zinda. Kuna mtoto mmoja hivi, bonge kidogo.” “Ni Tyrii?” Nanaa akauliza. “Ehee! Umeshawajua!?” “Kumbuka nilicheza nao muda wote.” Wakacheka.



“Sasa Tyrii alimsukuma kwa makusudi Fili. Wote tukaona. Fili akakasirika sana. Zinda akasema nilazima Fili atampiga ngumi. Danny akasema mwanae sio mgomvi kabisa. Zinda akambishia. Ndio Danny akasema tunyamaze kimya tuone kama mwanae atamrudishia au la. Wakapingiana dau. Tukakubaliana tunyamaze kimya tuangalie tuone. Kwa hiyo wote tulikuwa kimya tukifuatilia tukio zima. Na wakamwambia mama yake asiende kuwaingilia. Sasa wakati tunawaangalia watoto, na nyinyi mkaja nyuma ya ule uzio mkaanza kuongea. Basi tukawa tunaangalia watoto, huku tunawasikiliza.” Nanaa akaziba uso huku anacheka kwa aibu.



“Mungu wangu! Kwa hiyo mkasikia kila kitu?” Nanaa akauliza tena huku ameficha uso.Naona jamaa amekazana na Fili naye yupo na mipango iliyokamilika. Mahari mpaka sehemu ya kukuweka. Sasa sijui nani ataibuka na mke!?” Nanaa akacheka tena. “Naona  safari hii nimebahatika. Nimempata mchumba Fili anayenipenda, na kujivunia mbele za watu.” Geb akamtizama, na kuuliza, “Kwani safari zingine hukubahatika?” Nanaa alipooza usoni, akatingisha kichwa kukataa. Cheko likaisha. Huzuni ikamjaa kadiri alipokumbuka wanaume aliokwisha kuwa nao kwenye mahusiano ndivyo furaha iliendelea kupotea mpaka usoni akaonyesha.



Taratibu Geb aliona machozi yanachirizika pembeni ya mashavu ya Nanaa. Akayafuta kwa haraka na kurudisha tabasamu lake la kumtuliza tu. Lakini wazi alionekana kuna huzuni nyuma ya hilo tabasamu. “Pole Nanaa. Basi safari hii, tutahakikisha Fili anakufikisha kanisani.” Nanaa akacheka tena. “Geb wewe ni mchokozi bwana, kama Danny!” “Mimi nakwambia ukweli, sikuchokozi.” “Haya bwana.” Geb alimtizama kidogo, nakuangalia pembeni huku akitabasamu.



“Unacheka nini sasa?” Nanaa akamuuliza pale alipomuona anatabasamu. “Ukicheka unapendeza. Una dimpozi nzuri sana, Nanaa.” Geb alimgeukia na kumtizama wakati anamsifia. Nanaa alibabaika kidogo, akajishika machavuni. “Zipo hapa bwana. Unajishika wapi huko?” Geb aliweka kidole chake kwenye kishimo kilichopo kwenye shavu la kulia la Nanaa, Nanaa akacheka. “Ewaa! Hapo ndio zimetokea vizuri.” Geb akasifia tena. Kule kushikwa tu na Geb, Nanaa alijisikia vizuri sana.



*********************************************************



 “Sijui hata nafanana na nani?” Nanaa alijiongelesha. “Najua mama yako alifariki, lakini hukuwahi hata kuona picha zake?” Geb alimfanya Nanaa amwangalie kwa mshangao. “Umejuaje!?” Nanaa akauliza kwa mshangao. “Kaka yako anakupenda sana, Nanaa. Huwa akizungumzia habari za ndugu zake, haachi kukutaja na wewe. Kwa hiyo nakufahamu kwa kiasi.” Nanaa alibaki hajui aseme nini. Kwa kuwa hakujua Geb anamfahamu kwa lipi.



“Ninazo picha za zamani za mama yangu.  Lakini sifanani naye hata kidogo. Sasa sijui kwa kuwa alifariki akiwa bado mtoto mdogo!? Lakini hatufanani kabisa hata sifanani na ndugu zake. Labda hii rangi kama ya kaka. Lakini nipo watofauti kabisa. Nimejaribu kujifananisha hata na bibi, lakini sijioni kabisa kwake. Isipokuwa rangi tu. Bibi mzaa mama anarangi kali sana. Ndio maana wote mpaka kina Viola, mtoto wake, kaka, mimi, kina mama zetu. Wote tumechukua rangi ya bibi. Lakini sioni kingine. Nahisi nitakuwa nafanana na upande wa baba yangu.” “Ulifanikiwa kumuona baba yako?” Geb akauliza.



“Kuna kipindi nilitamani kumtafuta, lakini mama mkubwa aliniambia sio jambo sahihi, kwa kuwa alikana mimba yangu, na hata wazazi wake walimfukuza mama yangu na kumuonya asiwahi kurudi tena. Na hapo mama alikuwa amefukuzwa nyumbani kwao. Mama mkubwa anasema mama alipofukuzwa kule nyumbani kwao, na kwa huyo mwanaume, akawa hajui pa kwenda. Ndio akamchukua yeye. Lakini alipomuuliza zaidi juu ya baba yangu, mama alishindwa kueleza zaidi alikuwa akilia tu. Akasubiri labda akijifungua ndipo anaweza kumuuliza tena, lakini wala hakutoka kwenye chumba cha kujifungulia. Akafa bila kueleza zaidi juu ya baba yangu. Sasa kwa kuwa bado mama hakuwa namawasiliano mazuri na wazazi wake, au niseme zaidi bibi ambaye ndiye aliyekuwa mzazi wa pekee aliyekuwa akiwalea kina mama. Bado alikuwa na hasira na mama, hata baada ya mazishi, bibi alinikataa kabisaa. Hakutaka hata nirudishwe kule kijijini, nyumbani kwake. Akamwambia mama mkubwa kwa kuwa yeye alifanya kosa lakumpokea mama, yeye ndio anipeleke kwa baba yangu, sio pale.” Nanaa akaendelea.



“Anasema aliponirudisha kule kwa upande wa aliodhania ndio baba yangu, na wao walinikataa kabisa. Wakamfukuza mama mkubwa akiwa na mimi. Hata hivyo mtoto wao, yaani yule baba ambaye ni mwanaume aliyekuwa ametajwa na marehemu mama, mwanzoni wakati mama mkubwa alipoenda na mama akiwa mjamzito, alisema mama alikuwa na wanaume zaidi yake. Sasa kwa nini achaguliwe yeye kupewa huo mzigo, ambao ni mimi? Ndio mama mkubwa akakosa nguvu ya kuniacha pale, anasema akahangaika sana kutafuta mtu anayetaka mtoto wakati ule, akakosa. Akatafuta hata kunipeleka kwenye vituo vya watoto yatima, akashindwa. Walimwambia kwa wakati ule kituo hicho kilikuwa kimejaa, na hawana fedha, na mimi sio kwamba ni yatima nisiye na ndugu. Nipelekwe kwa ndugu zangu.” Geb akashangaa.



“Kwa nini yeye hakuta kukulea mwenyewe!?” Geb akauliza kwa kumuhurumia.  Nanaa akanyamaza kidogo, akainama kama kuzuia machozi. “Tokea nazaliwa mpaka leo, mume wake hakuwahi kunipenda. Alihesabu mimi ni mzigo mzito ambao hakutaka kujihusisha nao, na wakati huo na wao walikuwa na mtoto mdogo Viola. Kwa hiyo baada yakushindwa pakunipeleka, ndio nikaishia kwao. Kwa kifupi mpaka hivi leo, hatukuwahi kujua baba yangu ni nani.” Nanaa alitoa tabasamu lililoonyesha limejaa maumivu.



“Pole sana. Sikuwa nikijua kwa undani hivyo.” “Ndio hivyo. Sasa imekuwa kama ni roho chafu nilizaliwa nayo. Nakuwa nakataliwa na kila mtu. Kila ninaposhika, hapashikiki. Nimebakiwa na kaka tu. Inaniingizia hofu ya kuendelea kukaribisha watu karibu yangu. Nimeona hata nikiwakaribisha kwenye maisha yangu, nawachefua kwa haraka sana.” Geb alimuhurumia asisadiki anayosema Nanaa. Yeye asingechefukwa kama angebahatika kuwa karibu yake. Aliwaza Geb.



Kabla hajaongea kitu, wakasikia Geb akiitwa. “Geb!” Wakashtukia Grace anakuja huku anaita. “Vipi?” “Mpeleke mwanangu akalale bwana. Danny anazidi kuongea hataki turudi nyumbani. Mbu watamng’ata.” Wakasimama. “Mnisamehe kama nimewakatisha.” “Hamna shida. Hata mimi naona niombe lifti tu kwa Geb. Nataka nikapumzike.” Nanaa alijibu kiustarabu tu. Alikuwa kwenye wakati mzuri sana. Geb alionyesha yupo tayari kumsikiliza. Pole za hapa na pale zilikuwa zikimliwaza Nanaa. Na kufurahia kuwa karibu yake, asitamani watoke pale.



“Sasa Geb?” Ilibidi Grace amuulize Geb aliyekuwa ni kama yupo njia panda. Amepokonywa tonge mdomoni, hakujua ajibu nini kwa haraka. Ni kama alitaka kuendelea kuwepo pale.  “Tafadhali Geb!” Grace akajaribu kubembeleza. “Hamna neno. Ngoja nikamchukue. Vipi mama?” “Naona ana kazi yakucheka tu. Si unamjua anavyopenda porojo za Danny? Sasa wamekutana na James. Zinda ameshalewa! Na wengine ndio wanazidi kuagiza, naona tutakesha leo.” “Basi namuacha. Nitamshusha Nanaa nyumbani kwao, ndipo niende nikamlaze Fili. Nimuogeshe kwanza kabla yakumbadilisha nguo?” Walianza kuondoka kurudi ndani hotelini. “Fanya chochote utakachoweza. Maana amejaa michanga mpaka kichwani.” “Uzuri akilala huwa haamki, nitamuosha kidogo.” Walikuwa wametangulia Grace na Geb, Nanaa akiwafuata nyuma taratibu. Ukweli Grace alivutia kumwangalia. Nanaa alikubaliana na kaka yake, James.



*********************************************************



Alimpokea mtoto kutoka kwa shemeji yake, Nanaa akaaga kwa kaka yake, wakaondoka. Njiani kulikuwa na utulivu kidogo. Lakini ukimya huu haukuwa kama ule wa mwanzoni. Grace aliwakatisha mazungumzo yaliyoibua hisia za huzuni katikati yao. Nanaa alijiegemeza vizuri kwenye kiti, akabaki akiangalia nje ya dirisha. Geb alimtupia macho mara kadhaa kama anayetaka kuongea kitu, akajikuta anakwama, hajui aongee nini.



Simu ya kwanza ya Jeff kwa Nanaa.



Akiwa amepotelea mawazoni kwenye gari hilo ambalo Geb ni dereva, simu yake ikaanza kuita. Nanaa akaingalia kwa muda, akaipokea. “Ni mimi Jeff!” “Nilihisi tu.” Nanaa akacheka kidogo. “Vipi? Ulishatoka kwenye sherehe au nikufuate?” “Asante kwa kujali Jeff. Lakini nimepata lift. Hapa nipo njiani narudishwa nyumbani.” “Ulikuwa na wakati mzuri huko?” Jeff aliendelea kudadisi taratibu. “Siyo mbaya. Nimefurahia.” “Ulikula?” Nanaa akacheka. “Ulikataa kula mchana. Ndio maana nauliza.” “Hapana Jeff. Sikula. Bado nilihisi tumbo limejaa. Mchana nilikula chakula kingi. Na mbaya zaidi ilikuwa ugenini. Kila nikifikiria hivi nilivyoshiba mpaka sasa, nahisi nilitia aibu huko ugenini. Sijui kama wenyeji wangu walishiba.” Akamsikia Jeff anacheka na yeye. “Inawezekana una tumbo lenye shukurani tu.” “Haya bwana. Nipe moyo tu.” Wakatulia kidogo.



“Jeff!” Nanaa akaita. “Nipo Nanaa.” “Nilifikiri umekata.” “Bila kukuaga?” Nanaa akacheka. “Siwezi kufanya hivyo.” Geb alikuwa akiwasikiliza maongezi yao. Lakini alikuwa kimya kabisa. Wala hakuonyesha kama yuko pale. “Asante kwa kupiga.” Nanaa akashukuru. “Mbona kama unaniaga?” “Hapana.” Nanaa alijibu kiungwana. Lakini alijua wazi mazungumzo ya muda mrefu akiwa na Geb pale kwenye geri, sio ustaarabu. “Unaweza kuendelea kuzungumza?” “Naomba nikupigie kesho.” “Upo sehemu ambayo huwezi kuongea?”  Nanaa akatulia kidogo.



“Unakumbuka nilikwambia nimepewa lift? Sasa tupo njiani ndio narudishwa nyumbani.” “Oooh! Sawa. Basi nitasubiri simu yako kwa hamu.” “Lakini unakumbuka nilisema kesho?” Jeff akacheka. Sawa Nanaa.” “Muda gani ni mzuri?” Nanaa akauliza tena. “Iwe tu kabla ya lunch. Ili usije ukashiba sana, ukashindwa kula na mimi dinner.” Nanaa akacheka. “Sawa. Nitafanya hivyo. Usiku mwema.” “Asante. Na wewe Nanaa.” “Asante.” Akakata simu.



*********************************************************



Hakuna aliyemuongelesha mwenzake tena pale ndani ya gari. Hata hivyo walikuwa wamekaribia kufika nyumbani kwa James. Geb alisogeza gari karibu kabisa na nyumba. “Nashukuru kwa lifti na kunisikiliza. Samahani kama nilikwambia mambo yasiyokuhusu.” “Hata kidogo. Na mimi nimefurahia wakati mfupi, tuliokuwa nao.” Nanaa akacheka. “Sio mfupi hivyo. Nimeongea vyote hivyo! Mpaka nimeishiwa maneno.” “Mmmh!” Geb alijifanya kama anafikiria. Nini?” “Sikumbuki kusikia maelezo ya kutojibiwa ujumbe wangu.” Nanaa alicheka tena.



“Hivyo hatukuongea.”  “Basi huwezi kuwa umeishiwa maneno. Bado nasubiri maelezo.” “Lakini si umeshasamehe?” “Mpaka nijue sababu.” “Haya bwana. Muwe na usiku mwema.”  Geb alikuwa akimtizama na tabasamu lililomfanya Nanaa azidi kufurahia na kusahau hata kama dunia inazunguka. Kwamba masaa yanasogea. Alitamani kuendelea kuwepo na Geb. Kitu ambacho hakuwahi kusikia kabla, na wala hakuwa tayari. Lakini akajikuta inamtokea “Na wewe pia. Usiku mwema.”  Nanaa akashuka akiwa na furaha moyoni. Akasubiri afungue mlango, akaingia ndani bila ya kugeuka nyuma tena, ndipo Geb alipoondoka.



*********************************************************



Hakutaka kuharibu ile furaha na chochote. Akaoga haraka haraka akakimbilia kitandani huku anacheka. “Sasa nacheka nini?” Nanaa akajiuliza kwa sauti. “Furaha hii ni ya Geb!? Mmmh! Acha kabisa Nanaa. Mchumba wa mtu huyo! Labda Jeff. Lakini Jeff anaonekana muungwana. Mmmh! Ni wale wale. Kuona pipi kwenye karatasi, wanataka kufungua waonje ladha. Sidhani. Nimpe nafasi nione? Lakini mbona nilipokuwa naye sijajisikia hali niliyojisikia wakati nipo na Geb? Labda Jeff ndio amenifanya nianze kujisikia vizuri hata nilipokuwa na Geb nikafurahia kwa sababu tayari Jeff aliku…” Nanaa aliendelea kuwaza.



*********************************************************

Geb aliondoka pale akielekea kwao njiani akikumbuka dimpozi za Nanaa. Akacheka. “She is nice!” Akasifia moyoni na kucheka. Akakumbuka kicheko kizuri cha Nanaa. Kuna wakati alicheka huku machozi yakimtoka. Pia Geb akavutiwa zaidi.  “Well, not only nice but also beu…” Geb akatulia kwanza. 



Akakumbuka mazungumzo kati ya Nanaa na Jeff. Akavuta pumzi kwa nguvu. “Lakini hamna kitu. Sina haja yakutilia shaka.” Akajiliwaza. Lakini akakumbuka vile Jeff alivyong’ang’ania na kurudi kuomba namba ya simu. Isitoshe akapiga. Geb akakumbuka ni kama kwenye mazungumzo aliyosikia yakiendelea ndani ya gari, Nanaa aliahidi kupiga kesho yake. “Tena ni kama Jeff amesema kabla ya lunch ili asishindwe kula naye dinner. Sikumsikia Nanaa akikataa. Infact…” Geb aliendelea kuwaza.



Siku ya Jumapili baada ya birthday ya Fili.



Walimuona Geb anaingiza simu yake mfukoni na kuitoa kila mara. Mama yake akaona, akanyamaza. Grace naye akaona, mwanzoni akanyamaza. Alipoona na hasira zinaanza. Hata muda wa kula ukaanza kusogezwa mbele, Grace akamfuata mama yake chumbani kwake. “Kwani leo vipi?” “Mimi mwenyewe nimejibiwa majibu mafupi. Nimeona ninyamaze tu, nije kujituliza kitandani kwangu. Kwani Liz anakuja saa ngapi?” Mama yao akauliza. “Leo jumapili mama. Unajua Liz anatumia siku ya leo na familia yake. Labda kuwe na dharula.” “Naona inakaribia kuwa dharula.” Grace akacheka na kuondoka.



*********************************************************



 “Mbona ni kama alifurahia kuwa na mimi?” Geb alijiuliza. “Au ni mawazo yangu tu? Nini kilichonipelekea kudhani alifurahia mazungumzo yetu!?” Geb alianza kujisuta. Lakini akakumbuka vile Nanaa anavyomtizama na kucheka kila alipokuwa naye. “Mmh! Labda nimewaza kwa haraka. Nilimsikia akicheka hata na Jeff. Kwa asili, Nanaa anapenda kucheka.” Geb alizidi kunyong’onyea kila alipokuwa akiitazama simu yake na kukosa jumbe za Nanaa. Alitoa sauti kwenye simu yake ili kama Nanaa akituma ujumbe mtu asijue. Lakini tena akaona aweke tu sauti ili Nanaa akimtafuta hata kwa kuomba radhi na kutoa maelezo ya kwa nini hakujibu ujumbe wakujuliwa hali siku ile, asichelewe kujibu. Akabaki anahangaika na simu yake.



“Tokea enzi za Frida, tena nikiwa mtoto,  mpaka sasa, Nanaa ndio msichana pekee amenipuuza kwa kiasi hichi! Angejua msafara wa wanawake wanaotaka hata kupata namba yangu ya simu, hakika angeshukuru hata kupata ujumbe kutoka kwangu.” Geb aliendelea kuwaza.



Hamna haja yakujiumiza kichwa. Sina sababu yakusubiria simu yake. Naachana naye kabisa. Siwezi kujikosesha raha bure. Kwanza ilikuwa nafanya kiuungwana tu. Kwa kuwa aliondoka akisema hajisikii vizuri nikiwa naye. Kama anaona hamna umuhimu wakuwasiliana na mimi, basi. Ulazima unaletwa na nini?” Geb aliendelea kujiuliza, kujifariji, kujitia moyo na kujiwekea mikakati ya kupuuza majibu kutoka kwa Nanaa. Lakini hakuacha kutupia jicho kwenye simu yake kila mara.



 Alikumbuka wakati mfupi aliopata na Nanaa. Cheka na dimpozi zilizokuwa zikitokea mashavuni kwake. Akakumbuka vile alivyokuwa akimtizama wakati anacheza na watoto. Akajikuta anacheka peke yake na kutoa tena simu na kuangalia kama alimtafuta hata kwa salamu. Shauku yakutaka kumuona tena ikaongezeka.



*********************************************************



Nanaa akaamka na kuandaa kifungua kinywa chake na kaka yake. Kwa kuwa aliona kaka yake bado amelala, akaona aue ndege wawili kwa jiwe moja. Akatengeneza chapati za kusukuma. Akapasha moto mchuzi wa nyama ya kuku na njegere vilivyokuwa kwenye friji. Akaweka kwenye hotpots. Alitengeneza chai nzuri ya tangawizi, hiliki na mdalasini. Akaweka kwenye chupa ya chai, akampangia kaka yake mezani.



Alirudi kuoga, akabaki amekaa kitandani anajipaka mafuta huku anawaza na kucheka. “Geb!” Wazo likamjia. “Natamani ningempigia. Lakini naanzia wapi!? Heri ningekuwa nimemjibu ujumbe wa kwanza. Au jana ningemalizana naye juu ya kwa nini sikumjibu ujumbe wake. Pengine leo ningekuwa huru hata kumuulizia hali. Ningejidai kumuuliza kama walifika nyumbani salama na mtoto.” Nanaa akaendelea kuwaza. “Ni kama nimeshakuwa na hamu naye tayari!” Nanaa akajicheka na kujisuta.



*********************************************************



Ujumbe kutoka kwa Jeff ukaingia. “Oooh Jeff!” Nanaa akakumbuka wakati ameshika simu yake akitaka kusoma. Nimemsahau kaka wa watu wakati nilimuahidi kumpigia. Ngoja nisome.” Nanaa akafungua ule ujumbe. ‘Uliamka salama?’ Nanaa akasoma na kubaki hajui kama amjibu au apige tu. “Sipo tayari.” Akajiambia.



Jeff akapiga, akapokea. “Nimeona umesoma ujumbe wangu.” Nanaa akacheka. “Ndio nilikua nafikiria nijibu nini?” “Umeshajua?” “Najiona sipo tayari kutoka, Jeff. Moyo wangu umesita kabisa.” “Kwa nini usije kunisikiliza tu? Nipe nafasi ya kunisikiliza. Ndipo ukatae.” “Basi naomba isiwe leo.” “Lini?” “Weekend ijayo. Jumamosi.” “Kweli?” Nanaa akanyamaza huku akiuma meno.



“Nanaa?” “Kweli.” “Usinidanganye.” “Nitakutafuta Jeff.” “Sio kunitafuta kwa kunipigia simu tu, tunatoka.” “Basi nitakupigia kwa uhakika kama itawezekana au la.” “Nanaa! Mbona tunaenda mbele na kurudi nyuma!?” “Kwa kuwa sipo tayari Jeff. Kweli sipo tayari hata kidogo. Sitaki.” “Basi. Naomba nisikulazimishe.” Alisikika akiongea kwa sauti ya kukata tamaa. “Utakapokuwa tayari, naomba unikumbuke.” “Sawa, asante.” Nanaa akakata kwa haraka bila kupoteza muda.



Alimuhurumia, lakini akaamua ajipe nafasi. Anachojisikia kwa Geb, hakijawahi kutokea kabla maishani mwake. “Sitaki kujichanganya. Nikaanza huku, kumbe moyo wangu haupo. Hata hivyo sina haraka. Akitaka kusubiri, anisubiri. Kama hawezi basi.” Nanaa akakubaliana na wazo lake. Akatupa simu pembeni. Akaendelea na shuguli zake.



*********************************************************



Ilipofika mchana Grace akamuhurumia mdogo wake. Akaamua kumpigia simu Liz ili kumfanya aje hapo nyumbani, amtulize Geb. Asijue yanayomsibu pacha wake. “Vipi?” “Nipo na familia Grace. Tumetoka kanisani, tumekuja hapa Sea Cliff, kupata chakula cha mchana.” Liz aliongea sauti yakutotaka kusumbuliwa. “Ninahamu na Samaki wa kuchomwa!” Grace alipata sababu ya haraka. “Basi nitakununulia. Nikuletee. Lakini naweza kuchelewa.” “Hamna shida.” Grace akashukuru mtego wake umefanikiwa.



Kitu kisicho cha kawaida, Geb alirudi chumbani kulala. “Umekunywa hata uji?” Grace akamuuliza mama yake. “Kanywa kidogo. Anaonekana kuna kitu kinamsumbua. Vipi huko kazini?” “Kila kitu kipo sawa.” Grace akajibu. “Sasa ni nini?” Mama yake akahoji tena. “Labda ni vile Liz alivyomuacha jana pale kwenye sherehe ya Fili. Nimezungumza naye, amesema anakuja.” “Afadhali aje, watu tucheke. Khaa!” Grace akatoka chumbani kwa mama yake.



*********************************************************



Ilipofika mida ya saa 9 mchana, Liz akaingia na samaki wa kuchoma. Danny akampokea na kuanza kula na mkewe pale pale sebleni. “Geb yuko wapi?” Liz akauliza. “Kamwangalie chumbani kwake, amelala.” Grace alishukuru Mungu. “Naona nimuache tu, nisimsumbue.” “Kwa nini?” Grace aliuliza kwa mshtuko kwani lengo ni Liz aje pale, amtulize mdogo wake. Liz akafikiria kidogo. Akamwomba Grace watoke nae nje.



“Kwani vipi?” “Kwani huko kazini mambo yakoje?” Liz akauliza swali kama la mama yake. “Kwema tu. Kwani vipi?” Grace akauliza kutaka kujua zaidi. Mmmh! Geb amebadilika kidogo. Week hii nzima nimekuwa nikimbembelezea mapenzi. Ananipa sababu. Sasa jumamosi jana, akanipigia simu nije. Nikakataa kwa kuwa nimechoka. Lakini akasisitiza nije tu. Nikaja nikiwa natumaini angalau nitaambulia kitu. Nimeingia kuoga, natoka, Geb amelala kitu ambacho si kawaida yake. Tumeamka, kabla hata muda wa shuguli kuanza. Nimemshika, unajua alinikatalia. Akasema hajisikii. Nikambembeleza, akasema labda kwa kuwa hajala vizuri. Tujaribu baadaye. Tumekuja pale kwenye shuguli pia ameshindwa kula. Namuuliza mbona hali? Kama unavyomjua Geb, kujibu anapojisikia. Hakunijibu Grace. Namuaga kuwa nakwenda sehemu usiku ule, hata kuonyesha kujali wakati mchana wake au week nzima nimekuwa nikimbembelezea mapenzi. Mtu anayejali si angekuwa na wasiwasi labda nakwenda kwa mwanaume mwingine? Naona nimuache kidogo.” Grace akatulia.



“Au unashaurije?” Liz alimtaka shoga yake ushauri. Grace akabaki akiwaza kidogo. Wewe Grace?” “Si ndio nawaza?” “Sasa unawaza nini wakati ni mdogo wako, unamjua vizuri?” Hilo ndilo lilikuwa tatizo. Grace alimjua vizuri sana Geb. Akaogopa kumpa ushauri kwa vile anavyomfahamu mdogo wake. “Naona kweli umpe muda. Labda mgonjwa au uchovu. Au kuna kitu anapanga kichwani, kinashindana na pesa yake. Na Geb akianza mipango yake mikubwa, kichwa chake huwa akiwi sawa.” “Afadhali kunituliza. Nilianza kuhisi ananikwepa.” Grace na yeye alijua hivyo hivyo. Lakini hakutaka yeye ndio amuumize Liz.  Akaona amtulize tu, watajua mbele ya safari.



*********************************************************



Uzalendo ukamshinda mtoto wa kike. Akaonelea aingie tu chumbani kwa Geb. Akamkuta ndio anatoka. Wala hakuonyesha dalili yakumtaka arudi naye ndani. Umependeza sana Liz.” Geb akamsifia. “Asante. Jumapili yako ikoje?” “Nimeshinda kitandani tu.” “Kwema?” Liz akauliza. “Yeah! Kwema tu. Twende.” “Wapi?” “Sebleni. Nataka nikale. Sijala.” Liz akapooza sana. Hakutegemea kuitiwa sebleni na si kitandani. “Leo ni jumapili Geb. Nipo hapa. Chumbani kwako. Unafikiri nimekuja kuzungumza na kina Grace kweli? Niambie ni nini kinaendelea Geb.” “Mbona kila kitu kipo sawa tu! Kwa nini unafikiri hivyo?” “Unanikwepa kimapenzi.” Geb aliinama na kuanza kumbusu. Alimvutia kitandani akaandelea kumbusu.



Alimbusu kwa muda kisha akamuweka sawa, na kumuuliza. “Umefurahi sasa?” “Nakutaka zaidi Geb. Please.” Liz alibembeleza. “Please Geb.” Isivyo ya kawaida, alimuona akivuta pumzi kwa nguvu kama anayejishauri. Akamvua nguo na kufanya naye mapenzi. Haikuwa kama alivyozoea Liz, lakini angalau alishukuru. Geb alimfanikishia yeye tu, akaacha.



“Mbona unatoka kitandani wakati haujamaliza?” “Unakumbuka nilikwambia sijala? Nataka kwenda kula.” “Kuna kitu nimekuudhi?” Liz akauliza kinyonge. “Hapana Liz. Acha kuwaza hivyo. Ni njaa tu. Wewe umefurahia?” Liz alitoa tabasamu la kuridhika. “Nashukuru kwa kidogo ulichonipa.” “Utaniua Liz.” Kidogo wakacheka. Walizungumza kidogo, angalau ile hali ya wasiwasi kupita kiasi ikampungua Liz hata na Geb. Wakatoka wote wametulia.



Siku ya Jumatatu yake.

Asubuhi kama kawaida yake, akawahi ofisini. Kwenye saa mbili na nusu, Grace akaingia na habari za kuwa Fili ameanza shule rasmi. Akamuonyesha Nanaa picha alizompiga mwanae. Akiwa anatoka nyumbani mpaka yupo darasani. “Mchumba amependeza.” Nanaa akasifia, Grace akacheka. Alikuwa akiimba njia nzima. Amefurahi kweli.” Wakaongea kidogo. Grace akarudi ofisini kwake.



Ilipofika mchana, wakati kazi zimechanganya, Grace akapigiwa simu shuleni kwa kina Fili. Nanaa  akashtukia Grace amemsimamia ofisini kwake, akiwa hana raha. “Vipi?” Nanaa akauliza. “Fili huyo! Yaani leo ndio ameanza shule, siku ya kwanza, hata masaa saba hayajaisha tangia awepo hapo shuleni, tayari nimepigiwa simu natakiwa niende.” Nanaa akacheka. “Amefanyaje?” “Sikutaka hata kujua. Naona niende tu, nitajua huko huko.” “Pole.” “Sitakawia kurudi.” Grace akatoka kwa haraka ili akajue kinachoendelea huko shuleni kwa mwanae.



Baada ya muda wakarudi. Yeye anacheka, mwanae analia. “Wamemfanyaje tena?” Nanaa akauliza kwa wasiwasi. Lakini Grace alishindwa hata kuongea kwa kucheka. “Nyamaza mwanangu, eeh!” Kila Grace alipokuwa akimwangalia Fili alizidi kucheka. “Njoo Fili mtoto mzuri.” Nanaa alisimama akenda kumchukua akampakata. Akasikia mlango unafunguliwa bila hodi.



Alikuwa Geb, aliingia huku nayeye anacheka kama dada yake. “Muone alivyopooza. Kama sio yeye.” Geb aliongea huku cheko limemjaa. Walizidi kucheka yeye na dada yake wakati Fili analia. “Nimekuletea ice cream yako na ya Nanaa. Njoo uchukue.” Geb alimwita Fili. Lakini Fili akakataa.



*********************************************************



 “Kwani analia nini?” Nanaa akauliza tena. Hakuwa amepewa jibu tokea wanaingia. Grace na Geb walikuwa wakimcheka Fili. “Si Danny huyo. Kamwambia mtoto ataende shule, atasoma sana, atapata pesa nyingii, halafu atamlipa anko James, amchukue Nanaa, aende naye kwake. Sasa mwalimu wake anasema tangia amefika shule, hataki kucheza wala kuimba, anataka afundishwe kusoma tu. Mwalimu anamwambia sio muda wakusoma, atoke nje acheze na wenzake, hataki. Kakataa mpaka kula. Sasa mwalimu anasema tangia afike, hajafanya kitu chochote yeye anasoma tu vitabu. Imefika mchana wanatakiwa kulala, amekataa anasema apewe hela yake.” Nanaa nayeye akaanza kucheka akawa ameshaelewa.



Wote wakajikuta wanacheka bila kujizuia, lakini sio Fili. “Sasa mwalimu anamuuliza pesa gani? Fili amekazana, dad amemwambia akisoma sana, atapata pesa nyingi sana, kwa hiyo yeye ameshasoma, anataka apewe pesa nyingi sana, hataki kulala. Yeye mchana analala na Bibi Fili na usiku analala na Mama Fili. Hajaenda pale kulala wala kucheza au kula. Yeye ameenda kusoma na kupata pesa, basi. Kama ni chakula amemwambia yule mwalimu kuwa Bibi Fili anampikia uji mzuri na dad amemkataza kula kwa watu. Na kama ni michezo yeye anamichezo mingi sana nyumbani kwao na anachezea timu ya mpira wa kikapu ya anko Geb. Yeye amekwenda pale kusoma na kupata pesa. Sasa ashasoma, apewe pesa yake nyingi, aondoke.” Geb na Nanaa walikuwa wakicheka mpaka machozi.



“Hataki kunipa pesa yangu.” Fili alizidi kulia. Geb akaenda kumbemba. “Nyamaza mtoto mzuri.” Geb akaendelea kumbembeleza. “Hivi baba yake yuko njiani. Nimemwambia aje, amuelezee mwanae vizuri, aelewe. Maana yeye ndio ameyataka yote haya.” Grace aliendelea, kidogo wakamsikia Danny ameingia anaongea. “Yuko wapi Dume langu?” “Njoo huku ofisini kwa muhasibu.” Grace alimwita mumewe.



Danny aliingia tu na kuanza kucheka. “Pole mwanangu. Njoo.” Danny alimpokea kutoka kwa Geb, huku anacheka. “Usilie sasa na wewe. Wanaume huwa hatulii.” Danny akamkoromea mwanae. “Amekataa kunipa pesa nyingi, wakati mimi nilishasoma sana.” Walizidi kucheka. “Sasa anko Geb ameniambia amekuletea ice cream yako. Chukua ice cream kutoka kwa anko, halafu twende tukazungumze ofisini kwangu. Anko James anakusubiri. Anataka tukakueleweshe vizuri kwa vitendo. Una akili sana Fili, najua utazidi kuelewa. Sawa?” Fili alitingisha kichwa kukubali.



“Kwa hiyo unaondoka naye?” Grace akamuuliza mumewe. “Anavyosubiriwa huko, kama shujaa. Kila mtu anataka kumuona Fili, Dume langu.” “Hapo atakuwa amesimulia kila mtu. Danny jamani!” “Dume langu hili. Kwanza anamsikiliza dad wake, pili akiweka malengo anahakikisha yanatimia, haruhusu vitu vya kijinga viingilie malengo yake. Wanataka kumdanganya mwanangu kwa uji na michezo wakati kwao vyote vipo!? Sasa leo lazima upate zawadi. Sawa?” Danny alitoka akiwa amembeba mtoto wake, huku akijaribu kumtuliza.



Akawaacha wote wanacheka. “Huko ofisini wataenda kukoma. Wakutane nao hao wawili! Itakuwa ni stori tupu leo, hawatafanya kazi mpaka muda wakufunga ofisi ufike. Ngoja na mimi nikamalizie nilichokuwa nafanya.” Grace alinyanyuka akatoka pale, akamuacha Nanaa na Geb.



****************************************************



Furaha ilimjaa Nanaa, asijue ni nini. “Nimekuletea Ice cream yako. Uliisahau siku ile ya birthday ya Fili.” Nanaa akacheka. “Nilisahau hata kama niliagiza Ice cream. Asante. Lakini usingesumbuka kuleta.” “Grace alinipigia simu akanielezea kisa cha Fili. Akasema wapo njiani na bado analia. Nikaona nimtulize kwa ice cream, ndio nikaamua nikuchukulie na wewe pamoja na chakula. Najua hujala.” “Na chakula!?” “Mbona huamini?” “Sikutegemea. Asante kwa kunifikiria. Nashukuru sana.” Nanaa alifurahi mpaka akatamani kuruka ruka.



*************************************************



Labda hujaelewa. Chakula kimeletwa na Geb! Wakajikuta hawajui waseme nini tena. Nanaa alijawa na furaha akabaki na tabasamu usoni huku akiangalia vile vitu alivyoletewa. Kiliwekwa kwenye boksi zuri, lunch box, na kubebwa kwenye mfuko wa maana. Kwa hiyo akajua ni chakula kilichotolewa kwenye mgahawa wamaana. Sio kibandani. Inamaana imefanyika juhudi za makusudi, kununuliwa na kuletwa pale kwake.



*************************************************



 “Vipi kazi lakini? Mambo yanaenda?” Akabadili mazungumzo. “Hivyo hivyo nakazana.” “Taratibu utaelewe tu.” “Naogopa kuharibu nikamuuzi Grace, akashindwa kunipa kazi nikimaliza shule.” Geb akacheka kidogo. “Basi ndio ukazane ili usiharibu soko.” “Samahani. Nimefurahi mpaka nimeshindwa kukupokea!” Geb akacheka.



“Karibu ukae hata kidogo. Ule ndio urudi kazini.” Nanaa akampokea kile chakula na ice cream. Akaweka mezani. “Nina haraka natakiwa niwahi sehemu. Tutawasiliana.” “Nakushukuru sana. Asante.” Nanaa alishindwa kujizuia. Alihisi asante pekee haitoshi. Alibaki akichekacheka nakushukuru. “Nimefurahi. Asante.” Akarudia tena. Geb akacheka na yeye. “Karibu.” Hakika Geb aliona furaha ya Nanaa usoni. Hakujua kama furaha ile ni ya chakula tu, au alikuwa na furaha yake tokea mwanzo. Akatabasamu. “Kazi njema.” Geb akamuaga. “Na wewe pia.” Geb akatoka na kuacha Nanaa anafuraha sana moyoni, asiamini kama bado Geb alikuwa akifikiria anachokipenda. Alileta aina ya Ice cream ile ile ya ‘Vanilla’ aliyomwambia anaipenda. Halafu akamletea na chakula! Nanaa alitamani kupiga mayowe kwa furaha. Alibaki akicheka cheka tu.



*************************************************



Si kwamba Grace hakuona chakula alicholetewa Nanaa. Aliona na harufu ya kuku wa kuchoma ilienea ofisi nzima. Watu wakaanza kulalamika kuumizwa pua. Grace mwenyewe akabaki na mshangao. “Geb!” Grace alikaa ofisini kwake akawaza. “Geb Magesa, anakwenda kununua chakula na kumletea Nanaa! Mmmmh!” Grace alifikiria kidogo. Akataka kumpigia simu mama yake ampe umbea. Akaona anyamaze kwanza mpaka aelewe vizuri. Maana hata yeye mwenyewe hakuwa ameletewa kitu chochote chakula. “Halafu na mabadiliko Liz aliyoyaona je!? Inawezekana Nanaa ndio sababu!?” Grace akajiuliza. Akapiga mahesabu ya siku alizokutana Nanaa na Geb, akagundua ndio muda ambao Liz alimwambia Geb amembadilikia. “Mmmmhhh!” Grace akaguna huku akimfikiria pacha wake.



*************************************************



Nanaa hakumsikia tena Geb. Siku hiyo ikaisha. Jumanne mpaka ijumaa zikawa siku ndefu kupitiliza. Geb hakuonekana pale ofisini wala hakusikia lolote linalomuhusu Geb. Ijumaa wakati anafunga mahesabu ya siku, akaona Zena anampigia simu. Akacheka kwanza. Akajua ni mambo tu ya Jeff. Akapokea. “Vipi shoga yangu?” Zena akaanza kwa upendo “Kama mtu vile. Ukitaka kuniunganishia kwa mwanaume, unakuwa unanipenda kweli.” Zena akacheka. Tutoke kesho basi.” “Nimemkatalia Jeff.” “Kwa nini Nanaa? Hawa vijana ni watofauti.” Zena akamwaga sifa nyingi weee, akimuuza Jeff.

Lakini Nanaa akakataa. “Basi naomba tutoke kwa ajili yangu tu. Nisaidie shoga yangu. Safari hii umenikatalia pabaya kweli. Ni best wake Yasini. Tutoke tu tumsikilize.” “Zena akitaka jambo lake!” “Nihurumie shoga yangu. Ndio kwa mara ya kwanza napata mwanaume wa maana na yeye ana rafiki wa maana anakutaka wewe!” Zena akajihuzunisha mpaka Nanaa akamuhurumia. “Sawa. Kesho. Lakini isiwe usiku.” “Usiwe na wasiwasi. Mimi mwenyewe nitazungumza na kaka James kukuombea ruhusa, wala usijali.” Nanaa akacheka. “Atakuchoka kaka yangu na maombi yako yasiyoisha.” Zena akacheka. “Tukitoka jioni ndio vizuri. Sio mchana jua kali bwana.” “Basi nitazungumza na kaka.” “Lakini tupendeze kama kawaida yetu.” “Wala usijali.” “Nakuaminia Nanaa.” Nanaa akacheka na kukata simu.



“Nanaa atakiwa kuondoka kwa kaka yake.”

Alimaliza shuguli zake, akatoka ofisini ikiwa mapema tu. Akapanda daladala mpaka nyumbani. Akashangaa kumkuta kaka yake yupo  nyumbani, kitu ambacho sio kawaida sana. “Leo mbona mapema? Shikamoo.” “Marahaba. Kuna kitu nilitaka kuzungumza na wewe kabla hujakwenda kulala.” Nanaa akakaa. “Mama anakuja kesho na Viola. Amenipigia simu kuniambia mtoto wa Viola ni mgonjwa na ameambiwa huku ndiko kwenye daktari mzuri wa watoto. Nimejua ni uongo tu, kwa kuwa najua wapo madaktari wazuri tu KCMC. Lakini sikutaka niwape sababu. Sasa najua hapa pataanza kuwa padogo sana kwako. Naona nikutafutie chumba karibu na maeneo ya chuo au karibu na hapa.” “Mmmh!” Nanaa aliishiwa nguvu kabisa.

“Pole.” “Sasa kipindi hicho tunatafuta chumba, nitaishije nao hapa?” Nanaa alishakosa raha. “Nimezungumza na Grace na Danny. Nimewaomba wakuhifadhi kwa muda wakati nahangaikia sehemu yako yakuishi.” Nanaa alivuta pumzi kwa nguvu, akabaki ameinama akiwaza. “Ni mambo ya muda tu Nanaa. Namuamini Mungu ipo siku utapumzika.” Nanaa akanyamaza.

“Kina Grace ni watu wazuri sana. Hutapata shida.” “Unafikiri niondoke lini?” “Mapema kesho asubuhi, ili msikutane humu ndani hiyo jioni wakifika hapa. Unaweza kuja kuwasalimia tu, lakini sio kuja kukaa nao hapa. Watakuvuruga sana.”Nakushukuru kaka yangu. Asante kunifikiria.” Nanaa alisimama akaingia chumbani kwake. Alijikuta machozi yakimtoka.

Alianza kukusanya vitu vyake vyote bila kusahau hata kimoja. Akaweka kitandani. James aligonga akaingia. “Nimekuletea haya mabegi mengine. Najua utahitaji.” “Asante.” Nana aliendelea kukusanya na kuweka kwenye mabegi huku akifuta machozi, mpaka alipomaliza. James alikuwa amekaa kitandani akimwangalia. “Usiwe na wasiwasi. Kila kitu kitakuwa sawa.” “Naamini hivyo kaka yangu.” “Ukiwa kwa kina Grace nitakuwa sina wasiwasi. Najua utapata utulivu, ila mimi ndio unatakiwa unihurumie.” Nanaa alicheka huku akifuta machozi. Alikumbuka uvivu na uchafu wa Viola. Vile mtoto wake alivyo mtundu, maneno mengi ya mama yake. “Nitakuwa nakuja kukusaidia usafi siku za jumamosi.” James akacheka, akatoka pale chumbani bila kuongeza neno. Alijua wazi haitasaidia.

*********************************************************



Asubuhi ya saa nne, Grace alikuja na mtoto wake. “Yaani mapema hii tayari umeshaivisha!?” Alimshangaa Nanaa. “Namuonea huruma kaka. Yaani atoke kazini halafu asikute chakula! Hapa nimeshamfulia kabisa na kumwandalia chumba cha wageni.” “Ndio maana James anakupenda. Unamfikiria sana kaka yako.” “Sio kama yeye anavyonifikiria mimi. Kaka ananipenda sana. Bila yeye nina uhakika nisingekuwa hapa.” Nanaa aliongeza na kumgeukia Fili aliyekuwa kimya.

“Mbona Fili wangu leo hana raha?” “Danny amemchapa mwanangu. Yaani alikuwa analia njia nzima. Amenyamaza tu hapo nje kwenu. Ilibidi nikae naye atulie kwanza ndio tuingie ndani. Nimemwambia wanaume huwa hawalii mbele ya wachumba, akanyamaza.” Nanaa akacheka.  “Jamani Fili wangu! Pole. Kwani alifanyaje?” Fili bado alikuwa na hasira. Alikuwa akihema kwa hasira. “Eti Fili? Tumwambie Nanaa?” Fili alitingisha kichwa kukataa huku anataka kuanza kulia tena. “Basi Fili. Nyamaza mtoto mzuri.” Nanaa alimbeba.

“Twende tuwahi. Nimemuacha Danny nyumbani. Leo hakwenda kazini. Nikusaidie kubeba nini?” “Wewe rudi na Fili tu kwenye gari. Nitaleta tu.” “Unauhakika?” “Sio vitu vingi. Nenda tu umfanye Fili wangu atulie.” Grace alitaka kutoka na mtoto wake lakini Nanaa akamuwahi. “Grace!” Nanaa akamwita. “Nashukuru kwa kukubali kunihifadhi. Nitajitahidi kutafuta sehemu ya kuishi kwa haraka.” “Wala usijali. Sisi wenyewe pale tunahifadhiwa na Geb.” “Geb! Geb mdogo wako!?” Nanaa alishtuka mpaka usoni akaonyesha. Hakujua kama pale ni nyumbani kwa Geb. 

Historia ya Grace, Geb na Danny.

Grace akacheka baada yakuona ule mshtuko usoni kwa Nanaa. Ikabidi arudi kukaa kwenye kochi, akampakata na kumkumbatia mtoto wake. “Unajua Nanaa, maisha ni kitu cha ajabu sana. Lakini unatakiwa usikate tamaa.” Nanaa alirudi kukaa na yeye. “Wapo wenye wazazi wote na bado wanataabika maishani. Sisi tulizaliwa kama watoto wa nje ya ndoa tu. Mama alizaa na mume wa mtu. Lakini yule baba hakukataa kututunza. Kwanza tunafanana naye mno. Haya macho unayaona kwangu mimi na Geb, ndivyo alivyokuwa baba yetu. Vile unavyomuona Geb, kila kitu anafanana na baba. Mama anasema mpaka anavyokaa, anavyofikiria. Jinsi alivyo, ni baba mtupu mpaka anavyotembea. Ni kama baba. Kwa hiyo hapakuwa na jinsi yakutukataa. Alitutunza mpaka tulipofika kidato cha kwanza, akafariki.” Nanaa alikuwa ametulia kabisa akisikiliza.

“Alimjengea mama nyumba huko maeneo ya Kibamba. Tukawa tukiishi hapo mpaka kifo chake. Hata baada ya kufariki, watu walitaka kutunyang’anya lakini baba akawa ameacha barua kwa watu wamuhimu, akisihi vitu vile aachiwe mama. Baada ya purukushani nyingi, huku mama akilaumiwa kuwa kwenye mahusiano na mume wa mtu, akashinda kesi, maisha yakaendelea.” Grace akatulia kidogo kama anayetafuta pumzi. Kwa asili alikuwa mvivu wa kuongea. Nanaa akahisi kama amemaliza. “Lakini mbona ndio kama ameanza?” Nanaa akajiuliza.

“Nikuletee maji ya kunywa?” “Nipo sawa tu. Asante.” Akaendelea. “Kwa asili Geb anaakili sana ya mahesabu au akili za mambo ya sayansi tofauti na mimi. Mimi nilisomea mambo ya lugha, mwenzangu akachukua sayansi. Tukafaulu kwenda kidato cha kwanza. Yeye akaenda shule ya bweni Iliboru, mimi mama akataka nibaki naye nyumbani nikasomea Jagwani sekondari. Tulipomaliza kidato cha nne, mwenzangu akachaguliwa kusomea PCM, mimi HGL. Geb akapata msichana tuliyekuwa tukisoma naye sisi shule moja. Alikuwa akiitwa Frida.” Grace akaendelea.

“Geb ni mpole sana na anajua kupenda kupita nitakavyokwambia. Mama akamkataza yale mahusiano, na kumwambia itamuathiri masomo yake, lakini Geb hakusikia. Wakaendelea, Geb akamaliza kidato cha 6, akachaguliwa chuo kikuu cha Mlimani kusomea mambo ya Eletronics. Akajikuta tena yupo na kina Danny na James, au tuseme lile kundi ulilolikuta pale siku ya birthday ya Fili.” Nanaa akacheka kwa aibu. Akakumbuka mkasa wake na Jeff mbele yao.

“Utawazoea tu. Wachokozi sana. Mimi mwenyewe huwa wananichokoza mpaka leo.” Nanaa akacheka. “Vituko vyao haviishi kwa kuwa ni kama wamekua pamoja. Kuanzia wapo kidato cha kwanza walipokuwa Iliboru mpaka leo. Sasa mimi na yule msichana wa Geb, Frida, pia tukapangiwa chuo kikuu cha Mlimani. Tulipoingia tu pale chuoni, tukiwa wote mwaka wa kwanza yule msichana akaanza kumsumbua sana Geb. Kalikuwa kadada karembo kwa kweli. Akaanza fujo. Mara awe na mwanaume huyu, mara afumaniwe, ikawa fujo tupu. Geb naye akawa amempenda yule msichana kupita maelezo. Akimuomba tu msamaha, Geb anasamehe, wanaendelea. Shule ikaanza kumuia ngumu, Geb. Akawa kama amechanganyikiwa na yule binti. Mitihani ya kuingia mwaka wa pili, Geb alifeli mitihani yote kabisa. Nikikwambia yote, namaanisha yote na wakati aliingia pale chuoni na Division 1, ya “A” tupu.” Nanaa alikaa vizuri.

“Mama akaanza kuzungumza naye, kumfanya atulie. Mungu akabariki, akatulia, akamkubalia mama kurudi tena shule. Akaanza kutafuta tena chuo kingine kwa kutumia tena matokeo yake ya kidato cha 6. Mungu akasaidia, akapata chuo mwaka huohuo nchini India. Akaamua kwenda kusomea mambo hayo hayo ya Electronics. Sasa hapo baba hatuna, mama ndio tunayemtegemea kwa kila kitu. Na yeye mwenyewe mama kipato chake hakikuwa kikubwa chakuweza kumsomesha Geb nje ya nchi. Alikuwa na duka anauza yogurt na maziwa kidogo. Halafu akaendeleza biashara ya kufuga kuku aliyokuwa akifanya tangia baba yupo hai. Alikuwa akiuza, lakini sio kwa kiwango cha juu. Kwa hiyo hata pesa tuliyokuwa nayo, ilikuwa ya kawaida tu.” Grace akaendelea.

 “Lakini Mama akawa amekusudia Geb lazima asome. Kufupisha habari, ilimlazimu mama kuuza lile shamba, ng’ombe wote aliokuwa ameachiwa urithi na baba. Akauza  na ile nyumba ya urithi pia, ili kupata pesa yakumfanya Geb amalize hiyo shule. Ukweli mambo yakatubadilikia. Maisha yakawa magumu. Ilitulazimu kuhamia kwenye chumba kimoja na sebule, ili mama aweze kubana matumizi ili Geb amalize shule yake. Mimi nilikuwa nalipiwa na serikali. Kwa hiyo ikawa ni kazi ya kumsaidia Geb tu.” Grace akacheka kidogo.

“Vipi?” Nanaa akahoji. “Nakumbuka yale maisha. Yaani ilikuwa Geb akiwa likizo akirudi hapa nchini, anakuja hapo tunaishi naye. Tukawa tunaishi humo kwenye hicho chumba kimoja na mama. Mama yetu ni muhangaikaji sana, akikwambia kitu hakiwezekani, ujue ni kweli amefika mwisho. Akawa anamtumia pesa Geb. Kila pesa anayotaka Geb, bila kuuliza, mama akawa anamtumia. Sasa hatujui Geb alikuwa anafanyaje huko chuoni, lakini alirudi baada ya mika 4, ana shahada mbili tena zote ni nzuri zakueleweka. Maisha yakaendelea hapo kwenye hicho chumba kimoja na sebule, tena uswahilini tu. Mimi nikawa nimepata kijikazi cha kawaida sana, kinachotusaidia wote pale nyumbani, huku Geb akitafuta kazi, na mama anahangaika kivyake. Hatukuhama pale tunapoishi. Tukaendelea kuishi hapo mpaka Mungu alipomsaidia Geb akapata kazi BOT.” Nanaa alizidi kushangaa.

“Nikikwambia ni Mungu, ujue na amini kuwa ni Mungu tu. Hatukuwa tunamfahamu mtu yeyote huko BOT. Aliona tu tangazo, akatuma maombi kama kujaribu. Wakampigia simu kumwita kwenye usahili. Nakumbuka siku anakwenda, mama akamshika mkono, akamuombea. Basi akaenda. Kwenda kufanyiwa usahili, wakampenda. Mwaka wa kwanza tu wa Geb kuanza kazi hapo, ndipo maisha yakaanza kubadilika. Turudi kwa Danny.” Grace akacheka.

 Nanaa naye akaelewa. Mumewe alikuwa mtundu sana. “Katikati ya hizo shida zote hizo, Danny naye akawa ananisumbua kweli anataka kunioa. Kazi hana, na hataki kutafuta kazi, anataka arudi shule. Nikawa namkwepa. Lakini kama unavyomjua Danny, hakwepeki. Yaani pale kwenye ile nyumba ya kupanga, kila mtu alikuwa anatufahamu mimi na Danny. Alikuwa anakuja pale, ananibembeleza na maneno yake hayaishi.” Nana alianza kucheka.

“Mama akawa anamwambia kwa nini asimalize shule ndio arudi tena? Hataki. Anasema yeye anawajua vijana wa mjini, watamzidi mahesabu. Anataka vyote viende pamoja. Anioe na andelee na shule. Yaani Danny nyie! Hapo anafanya fujo zote hizo, hana hata mahari.” Nanaa alikuwa anacheka mpaka basi.

“Sasa wale wapangaji wakawa wanamuuliza, anataka kumuoa Grace wakati mahari hana wala hana pakuniweka? Akawa anawaambia yeye atanioa tu, halafu mama aendelee kunitunza.” Nanaa alizidi kucheka. “Yaani wewe muone Danny vile vile. Watu wakawa wanamwambia huo sio utaratibu. Ukioa unatakiwa umchukue mke wako. Ujue Danny hana aibu nyie jamani!” Grace alianza kucheka kila akimkumbuka Danny. “Ikawaje sasa?” Nanaa akauliza.

“Mmh! Kwanza namshangaa anavyomwambia mwanae akioa asimlete mkewe hapo nyumbani. Ujue Danny alining’ang’ania mpaka ikabidi nikubali tu. Yaani alikuwa anatoka shule, anakuja kunisubiri nyumbani. Sasa na mimi nilikuwa nikijua yupo nyumbani nilikuwa najificha. Alikuwa haondoki mpaka anione. Na hapo fujo hizo alizianzia tokea tupo chuo. Kila mtu alikuwa anatufahamu mimi na Danny. Nikimwambia simtaki, anaweza kupiga magoti eti hata cafteria mbele za watu, eti ananibembeleza.” Nanaa alizidi kucheka.

“Wewe muulize James vituko vya Danny na mimi. Tuliacha historia pale chuoni. Kila ninavyomkataa ndivyo alivyokuwa akijitangazia mimi ni mke wake. Basi kwa kifupi ndani ya shida zote za kuishi chumba kimoja, pesa zote zikienda kwa Geb, Danny naye akahamia hapo hapo nyumbani akawa analala kwenye makochi na Geb. Geb akiwa shuleni, yeye ndio anarithi yale makochi. Hapo wala hajakaribishwa wala hatuna mahusiano. Anajikaribisha mwenyewe. Mimi na mama tulikuwa tunamshangaa yupo ndani, maisha yake yanaendelea kama kawaida yaani yupo kama kwao. Upande mwingine alikuwa rafiki wa Geb, upande mwingine alikuwa anasema haondoki hapo mpaka anioe. Mama anamuuliza akinioa ataniweka wapi? Akawa anamwambia mama bila aibu wala hofu, eti akinioa tutaendelea kuishi hapo hapo.” “Haiwezekani!?” Nanaa alikuwa anacheka haamini.

 “Wewe muone Danny vile vile. Akili zake anazijua yeye mwenyewe. Na si unakumbuka ile timu ya wale wanaume pale?” Nanaa akaitikia. “Basi wote walishawahi kuishi hapo kwenye kile chumba.” “Haiwezekani!? Mliishije?” “Wala sijui Nanaa. Na Danny ndiye alikuwa akiwakaribisha hapo wasome. Eti hawezi kusoma mbali na mimi.” Nanaa alizidi kucheka.

“Basi, baada ya purukushani nyingi, tukaoana na Danny bila hata kulipa mahari wala sehemu ya kuishi. Tena hapo ukumbuke mimi nilikuwa ndio nimemaliza shahada yangu ya kwanza ya  miaka mitatu, yeye anajiandaa kwenda kusomea shahada yake ya pili mlimani. Yaani ni kama mwanafunzi tu. Maana ukumbuke pia nilimuacha anamalizia mwaka wake wa 4. Yaani mwanafunzi asiye na mbele wala nyuma, wakati hapo nilikuwa natongozwa na watu wenye magari yao na maisha yakueleweka. Halafu alichokuwa akinikera zaidi ni vile ambavyo shule yake haiishi, ni shida tupu. Mipango mingii kama mwanae Fili.” Wote walicheka.

“Haya, turudi kwa Geb. Si nilikwambia alipata kazi BOT?”  “Ndiyo” Nanaa aliitikia. “Basi, baada ya muda akaanza kuingiza pesa nzuri. Mimi nikashindwa kazi kwa kuwa nilishika mimba ya Fili nikawa mgonjwa kweli kweli, nikafukuzwa kazi. Tukarudi sifuri mimi na Danny wangu. Danny anasoma, mimi nipo nyumbani. Geb anaakili sana. Akaanza kufanya biashara na kazi. Hata ile kampuni ninayoiendesha sasa hivi ni yake.” Nanaa alizidi kushangaa.

“Alikuwa anakusanya mazao mikoani, anakuja kuyauza kwa Baressa. Alinunua lori lake, akawa anaenda vijijini anapata mazao kwa bei nafuu, anakuja kuuza huku mjini. Sasa faida ikawa kubwa kwa haraka. Kwa kuwa yeye halimi wala haangaiki. Kazi yake ni kwenda kununua tu. Akafungua tena sehemu kubwa yakuuza mchele. Akamuweka mama asimamie. Anachukua mchele Morogoro na Kyela, anasambaza hapa jijini. Akaongeza lori jingine lililokuwa linaenda kufuata matunda Lushoto, analeta Dar. Anauza pia  kwa Baressa na masokoni kwa jumla. Pesa ikawa inaingia kila kona huku anaendelea kuwekeza kwenye mazao, lakini bado anafanya kazi yake kule kule BOT.” “Kwa hiyo mpaka sasa hivi unasema Geb anafanya kazi BOT!?” Nanaa akauliza akionekana ni kama amechanganyikiwa kabisa.

“Anapenda sana kazi yake anayoifanya. Kwa hiyo anafanya vyote, ndio maana namsaidia kusimamia biashara. Hivi tunavyozungumza yupo safarini kibiashara. Akipata mwanya tu kazini kwake, anahamisha akili kwenye biashara. Na yupo makini sana kwenye mambo yake. Anauwezo mkubwa sana wa kupanga mambo yake na kufanikisha.” Nanaa alizidi kushangaa.

“Mambo yalipoanza kuwa mazuri, yeye na mama wakahahama. Wakapata nyumba ya kupanga. Mimi na Danny tukabakia pale kwenye kile chumba chakupanga. Hapo mimi namlea Fili nipo tu nyumbani sina kazi, Danny yupo bado shule. Sasa Geb alipoona mtoto amekuwa mkubwa kidogo, ndio akaniambia nisitafute tena kazi, nimsadie ile biashara. Tunachukua mazao mikoani, na kusambaza hapa jiji. Mambo yalipokuwa mazuri, akanogewa na kuanza kuuza na nchi za jirani. Alijaribu kidogo, akapata masoko, akaanza kuuza sukari kutoka Mtibwa kwa bei nafuu, anauza nje ya nchi wakati watu wa hapa wanaingiza sukari kutoka nje. Maajabu! Lakini anyway, ikawa faida kwetu.” Bado Nanaa alikuwa kwenye mshtuko.

“Akaanza kujenga pale pale Tabata. Ndani ya mwaka mmoja jirani yake akamwambia ameshindwa kumalizia nyumba yake, anunue. Nyumba yenyewe ni ile nyumba tunayoishi sasa hivi. Ilikuwa imefika kwenye bati. Geb akainunua, akamalizia haraka, akahamia hapo na mama, wakati akimalizia nyumba yake taratibu. Ile nyumba ipo kwa pembeni ya nyumba tunayoishi sasa hivi, ni ya Geb pia. Sema alijenga ukuta mrefu sana huwezi kupaona. Walipakana na huyu mzee aliyemuuzia hii nyumba, ndio maana alijenga ukuta mkubwa ili wasiingiliane, akaishia kupamiliki kote.” Nanaa alipooza sura. Hakutegemea kama Geb, ndio anapesa vile. Hasa baada ya kumdhania anatunzwa na dada yake. Tayari akajua si saizi yake tena.

“Sasa turudi kwangu. Geb akawa ananifundisha ile biashara huku anaendelea na kazi yake. Mimi ikawa inaniwia vigumu kazi na mtoto. Wasichana wananisumbua mchana na usiku, na bado Danny yupo shuleni siwezi kumtegemea. Ikawa ni kazi yakupokezana kumlea Fili. Mara tusikie msichana anamtesa mtoto, Geb anaenda kumchukua anakaa naye kidogo, mara anampeleka kazini kwa mama, mara mimi. Ikawa fujo isiyoeleweka, ndio Geb akasema kwa kuwa tunalipia pale walipotuacha. Halafu chumba chenyewe ni kimoja tu ndio tunatumia, ni heri tuhamie kuishi naye pale iwe rahisi kumlea yule mtoto kwa pamoja. Ndio tena tukahamia pale wote, na Danny wangu nyuma.” Nanaa akacheka.

“Anafujo nyie Danny! Usimuone vile. Lakini mama anampenda Danny, kama nini sijui. Akikaa kidogo tu anamuulizia Danny. Anampenda kupita kiasi, sijui anampendeaga nini! Sijui ni kule kumdanganya danganya? Haishiwi maneno ya kuongea na watu.” Nanaa alizidi kucheka.

“Haya, Geb akatupa gari moja, ndio tukawa tunatumia. Mungu bariki wametuvumilia, mpaka Danny amemaliza shule yake, amesaidiwa na James kupata hiyo kazi. Tunamshukuru Mungu analipwa pesa nzuri sana. Tumechanganya pesa ninayolipwa na Geb, na yeye mshahara wake, ndio na sisi tunajenga sasa hivi. Tumefika mbali, Mungu akisaidia mwakani tunahamia kwetu. Kwa hiyo unaona? Imechukua muda mrefu, lakini kwa kuwa bado tuna malengo, hatukati tamaa. Isingekuwa Geb, naona wote tungeaibika hapa mjini. Kwa hiyo na sisi tunawekwa pale na Geb kama wewe tu. Fanya yako, Mungu akikufungulia mlango, unatoka.” “Sasa mmemwambia Geb mwenyewe kama na mimi nakuja pale? Tusijekuwa tunamlemea.” Grace akacheka.

“Cha kwanza, vile unavyomuona Geb alivyo, ndivyo hivyo hivyo alivyo mpaka moyoni. Mkarimu sana na hana neno. Yeye ilimradi msimtoe mama kwenye ile nyumba, basi. Hawezi kuishi popote bila mama. Na urefu wote ule, mara nyingi analalaga kitandani kwa mama wala hatumii chumba chake. Labda mpaka Liz aje pale.” Nanaa alicheka kidogo kwa hofu. “Amesafiri, atarudi leo usiku. Tutamwambia tu wala usijali.” “Au labda nisubiri mpaka mumwambie?” Nanaa alishaingiwa na hofu.

“Hana neno kabisa, usiogope. Mwenye neno ni Liz. Liz huwa hapendi watu wengi pale ndani. Hajalalamika moja kwa moja, lakini kwenye mazungumzo yake utamsikia akigusia jinsi anavyopenda nyumba yenye utulivu. Nafikiri ndio kitu kinachowafanya washindwe kuendelea na Geb. Alivyolelewa Liz, ni tofauti sana na sisi. Liz tulisoma naye mimi, kwao anauwezo mkubwa wa kifedha. Hata alipomaliza tu chuo, alitafutiwa kazi haraka na wazazi wake. Hajuagi shida hata kidogo. Halafu wamezaliwa wawili tu kama sisi. Halafu wakaishi  yale maisha ya kizungu, hakuna wegazi. Kwa hiyo inamsumbua kiasi fulani kuona Geb anajaza watu nyumbani kwake, nafikiri ndio maana hataki kujiingiza zaidi kwa Geb. Hataki mzigo. Lakini sio Geb. Geb anaelewa maisha na anapenda sana kusaidia. Furaha yake nikuona kila mtu anafanikiwa, na ndio maana anaweza kuishi na kila mtu. Wala usiogope. Kwanza mama mwenyewe anakusubiri nyumbani. Anakusifia, anasema unaonekana ni  mtoto mzuri.” Nana akacheka kidogo. “Twende. Utakuwa na Bibi Fili, usiogope.” Wakasaidiana kuingiza mizigo kwenye gari, wakaondoka.

****************************************************

Wakati wapo njiani Nanaa akiwaza maisha yake, simu ya Zena ikaingia. “Haya ndio majaribu. Wakati nina shida, ndio Jeff anatokea. Nikimkubali naweza kuolewa, nikapumzika na shida za kuzunguka kwenye majumba ya watu. Nikapata kwangu.” Nanaa akawaza. Akapokea ile simu. “Zena!” “Naamini bado hujabadili mawazo. Jeff amefurahi sana kusikia umekubali.” “Lakini Zena, leo sio siku nzuri.” “Nanaa! Naomba usianze.” “Kweli Zena. Nipo kwenye wakati mgumu sana.” “Basi nakuja kwa kaka James tuongee.” “Huwezi amini Zena, ndio ninahama pale.” “Kwa nini tena?” “Ni habari ndefu. Naomba kukusimulia wakati mwingine. Hapa ndio nipo njiani.” “Unahamia wapi?” “Tabata Barakuda.” “Duuu! Shoga pole.” “Kwa kuwa bado mapema, nikiweka mambo sawa nitakutafuta. Sitaki kukuharibia kwa Yasini. Ila nikishindwa, nakuahidi kesho lazima tutaonana.” “Sawa kipenzi. Nashukuru kwa hilo. Maana ni kweli nimempenda Yasini. Naomba Mungu atujalie. Ananipenda.” Nanaa akacheka. “Nimemuona. Hongera Zena. Nawaombea kila la kheri. Na mimi nitajitahidi nisikuangushe.” “Asante.” Wakakata simu. Nanaa akanyamaza kwani Grace na yeye alikuwa kimya kama kawaida yake.

Nanaa ahamia nyumbani kwa Geb.

Alifika nyumbani kwa Geb, akakuta anasubiriwa kwa hamu. “Karibu tukuonyeshe chumba chetu.” Bibi Fili aliongoza njia wakati Danny akisaidia mizigo. “Kitanda chako kitakuwa kile pale, hiki kikubwa ni changu. Maana napataga wageni hapa, wanaojua kujikaribisha wenyewe. Unaweza ukalala peke yako, usiku mnajikuta mko wawili, tena wakati mwingine hata watatu.” Nanaa akacheka, akakumbuka Grace alimwambia Geb huwa analala na mama yeke.

“Wengine wakigombeshwa usiku, pia wanakuja hapahapa.” Bibi Fili aliongeza, wakacheka.  “Huyu bwana huwa hatulii. Akianza fujo zake, lazima kumfukuzia huku huku kwa bibi yake.” Danny aliongeza huku akimuangalia Fili.

“Nitakuwa nalala naye.” Nanaa aliongeza. “Wala hutaweza. Anaanza kulala kichwani, mkiamka yuko miguuni. Usiku kucha Danny anakazi ya kumpanga hapo kitandani. Akichoka ndio anamwamishia huku kwa bibi yake.” Grace aliongeza. Waliendelea kuongea hapo hapo chumbani huku wakicheka na kutaniana kidogo. Kilikuwa chumba kikubwa na kizuri sana. Kisafi na kitanda cha bibi Fili kilionekana cha tofauti. Kizuri na mashuka yake pia yalikuwa mazuri. Kilionekana cha gharama sana.

*************************************************

“Ngoja nikampikie. Akija hapa atakuwa na njaa kweli.” Bibi Fili akasimama. “Si alisema anakuja usiku?” Grace akauliza. “Mimi kanipigia muda sio mrefu, kasema yupo Chalinze na njaa inamuuma.” “Mpaka Geb alalamike njaa!” “Ujue hapo ana siku mbili hajaweka kitu mdomoni.” Mama yake alimalizia na kusimama. Nanaa akamfuata nyuma.

“Unataka kupika nini?” Nanaa akauliza. “Wala hutaweza kunisaidia. Geb anasumbua sana kula. Anachagua chagua kweli! Na akiweka kitu mdomoni tu, akisikia kina ladha sio yake, hali.” Nanaa akacheka idogo. “Nachemsha chemsha tu, lakini hataki kuona nyanya wala karoti kwenye chakula chake. Kwa hiyo lazima nisage kila kitu. Na hataki mafuta mengi.” Mama yake aliongeza.

“Nitampikia na uji wa ulezi. Nitaweka kwenye chupa. Halafu namchemshia ndizi na kipande cha kuku. Basi.” “Basi ngoja niangalie ili siku nyingine nikusaidie.” Nanaa akaongeza. “Hayo ndio maneno.” Wakaingia jikoni. Mwanzoni Nanaa alikuwa akimuogopa sana yule mama. Alionekana mkimya kama Geb. Wakaishia kuwa kimya hapo jikoni mpaka walipo maliza. Nanaa akasaidia kusafisha, wakatoka.

*************************************************

Ilipofika saa nane mchana, Geb akaingia. “Mama yuko wapi?” Ndio ilikuwa salamu yake mara alipoingia tu ndani. “Nipo huku chumbani, njoo.” Nanaa alikuwa na bibi Fili hapo chumbani. Akajiweka sawa. Akajivuta nyuma kabisa, akatulia akiwa amejiegemeza ukutani. Geb akaingia na kujirusha kitandani. “Njaa inauma, mama.” Geb alilalamika huku amejilaza kifudi fudi, pembeni ya mama yake amefunika uso kwenye mto. “Pole na safari.” “Sijalala vizuri. Nimechoka. Tangia nimeondoka hapa nilikuwa nazunguka tu. Nina usingizi.” Geb aliendelea kulalamika kama mtoto mdogo. “Sasa ndio uamke ukale kabla hujapitiwa na usingizi hapo!” Geb akanyamaza.

Mama yake akajua atalala kama asipomsisitiza kuamka. “Umemuana Nanaa lakini?” Geb akaruka na kukaa kama mshale. Nanaa akacheka. “Pole na safari.” “Asante. Sikuwa nimekuona.” Wote wakacheka, Geb akasimama na kutoka bila kuaga. Mama yake akaanza kumcheka. “Kaingia aibu leo. Ngoja nikamsimamie ale. Anaweza kwenda kulala bila ya kula.” “Mama!” Walimsikia Geb akiita. “Nakuja.” Mama yake akaitika na kutoka.

*************************************************

 “Tutakuwa tukiishi na Nanaa.” Alimsikia mama yake akizungumza na Geb wakati anakula. “Kwema?” Geb akauliza. “Mama yake mkubwa anakuja leo na Viola. James hakutaka wamsumbue pale.” Kimya. Geb hakujibu. Nanaa akapatwa na wasiwasi.  “Lakini James ameomba tumuhifadhi kwa muda mfupi tu wakati anamtafutia chumba chake kabla chuo hakijafungua. Anatafuta chumba karibu na maeneo ya chuo. Amesema akipata tu chumba, hata kesho atamuondoa hapa. Ilikuwa gafla ndio maana hatukukwambia. Nikaona nikusubiri mpaka urudi.” Mama yake aliendelea kujieleza kwa mwanae.

 “Haina shida kabisa. Mlifanya vizuri kuwasaidia. Hii nyumba ni kubwa, hawezi kuongeza chochote akiwepo hapa.” “Na mimi nilifikiria hivyo hivyo. Maana tunakuwa na wasichana wakazi mpaka wawili, na bado tunatoshea.” “Sasa kwa nini hukumpa chumba chake?” “Tumeona mpaka uje mwenyewe.” “Mama jamani!” “Hata hivyo kile chumba kingine ambacho nilidhani kingemfaa yeye, bado kina vitu vingi. Hapakuwa na muda wakukisafisha. Hamna shida nikilala naye kule chumbani kwangu.” “Kesho nitamtengenezea kile chumba, ili awe huru.” Alivyoongea vile Geb, angalau Nanaa akatulia.

“Vipi lakini safari yako?” “Mambo yameenda vizuri. Nimepata mtu aliyeniunganisha na mkulima mwingine. Lakini ilibidi tumfuate mbali kweli. Ndio maana sikulala vizuri. Jana niliamka asubuhi sana na tukarudi usiku. Lakini nimefanikiwa, asante kwa kuniombea.” “Afadhali. Utukufu ni kwa Mungu.” Mama yake akasikika na sauti ya furaha iliyojaa shukurani.

“Utakuja chumbani kwangu?” Geb akamuuliza. “Kwani si uje tu ulale pale pale?” “Mbele ya mgeni! Njoo bwana mama. Nataka nikusimulie kitu.” “Muongo Geb. Unahabari gani kama sio unataka niwepo tu pale ili ulale?” Geb akacheka. “Shauri yako, utapitwa.” “Huna lolote.” “Sawa mama. Lakini sio baadaye uanze kulalamika mbona sijakwambia!” “Haya. Nenda kaoge ukimaliza, uje uniite.” Nanaa alibaki pale pale chumbani akiwasikiliza huku anacheka kimya kimya.

  **************************************************

Bado ilikuwa mapema tu, Nanaa akamtafuta Zena kwa simu. Naweza kuwaona kabla ya saa 12 jioni.” Zena akafurahi sana, akabaki anashangilia. “Wewe Zena, sasa nitawakuta wapi?” “Njoo pale Sinza pub. Tutakusubiri.” “Kwani wewe unaishi na Yasini?” “Ukija, nitakusimulia. Lakini hapa baba na mama, wanajua nimesafiri kikazi. Field.” “Wewe sikuwezi.” “Nakusubiri shoga yangu. Hapa nikimalizana na wewe tu, nampigia na Jeff, tukutane.” “Sawa. Mimi najiandaa nitoke.” Wakaagana.

Nanaa akajiandaa, nakutoka. Alimkuta bibi Fili anamsubiria Geb sehemu ya kulia chakula. Geb alikuwa akioga chumbani kwake. “Mbona umependeza hivyo?” “Naenda kukutana na rafiki zangu mara moja. Nimekuwa nikiwaahirisha kila wakati.” Danny akakohoa. Alikuwa sebleni na mkewe, wanaangalia tv. Nanaa akacheka na kuinama. “Umependeza kweli Nanaa. Au ndio na safari ya kwa Jeff?” Bibi Fili akaendelea kuhoji kichokozi. “Na yeye pia atakuwepo mama.” Nanaa alijibu kwa aibu kidogo. “Sitakawia kurudi. Nataka na wao nikawashirikishe swala la uhitaji wangu wa chumba. Pengine wanaweza kunisaidia kwa haraka.” “Sawa.” Nanaa akasogea pale sebleni.

“Umependeza sana Nanaa.” Grace akamsifia. “Asante.” Alijibu kwa aibu. “Nitarudi baadaye.” “Unataka usindikizwe?” Grace akauliza. “Hamna haja. Nitachukua daladala hapo barabarani.” “Sawa. Uwe na wakati mzuri.” Danny akaanza kucheka. Nanaa akatoka bila hata kugeuka huku anacheka. “Anaonekana ni binti mtulivu sana.” Alimsikia bibi Fili akisifia. “Na ni mzuri pia.” Akamsikia Grace anaongeza.

*****************************************************

“Naona Jeff amekaza kweli. Mpaka amekubaliwa!” Danny aliendeleza maongezi. “Nani?” Geb alitoka akakuta wanaongea huku wanacheka. “Nanaa katoka.” “Sio katoka bwana Grace. Wewe vipi? Sema katoka na amependeza kweli kweli. Halafu kamuaga mama anaenda kumshirikisha Jeff, hana sehemu ya kuishi. Kama namuona Jeff atakavyofurahi.” “Danny wewe! Nanaa anaenda kwa rafiki yake. Tena walikuwa wakizungumza kwenye gari wakati namleta hapa.” Grace akatetea.

“Eti mama, Nanaa hajajibu kuwa na Jeff atakuwepo?” Danny alitaka uungwaji mkono na mama mkwe wake.  “Kasema hapa. Na alivyopendeza vile! Lazima huyo Jeff ampishe kwenye nyumba yake. Kwa uzuri na utulivu ule! Lazima maombi ya Jeff yatakuwa yamejibiwa.” Waliendelea kutania, lakini wasijue wanazidi kumchanganya Geb.

Huku kwa Geb!

Hakwenda kulala kama alivyomwambia mama yake. Akaanza kusafisha chumba kingine maalumu kwa ajili ya Nanaa. Grace alivyosikia kukuru kakara nyingi, akaamua kwenda kusaidia. Geb alikuwa kimya kupita kawaida yake. Swali moja, alichukua zaidi ya dakika tano kujibu. Kwa kuwa Grace anamfahamu pacha wake, akaamua amuache tu. Wafanye kazi kimya kimya.

Alihangaika Geb, mpaka Grace alimuonea huruma. Akasafisha kila mahali tena kwa mikono yake mwenyewe. Akahakikisha anafuta vumbi kila mahali na kusafisha choo cha humo ndani. Chumba kikadekiwa vizuri. Ikaja kazi ya kupanga sasa. Akatoa mashuka masafi na kumtandikia Nanaa. Akaenda chumbani kwa bibi Fili, akahamisha mizigo yote ya Nanaa. Akampangia kwenye hicho chumba.

Mama yake akahamia kukaa kwenye makochi baada ya kuona shuguli zimekuwa nyingi, hasira kwa mwanae zimeanza. Akajua hakuna kulala tena. Wakabaki wanaangaliana na Grace. Aliingia na kutoka. Mara abebe hiki arudishe kile. Ilimradi tu kukamilisha hicho chumba cha Nanaa.

Huko kwa Nanaa!

Baada ya purukushani za panda shuka kwenye daladala hii kuingia ile, Nanaa akawa amewasili Sinza Pub. Akakuta wote wanamsubiria. Jeff akamvutia kiti, akakaa. Mbona sasa unanishangaa?” “Ndio kupendeza gani hivyo?” Zena alimnong’oneza. “Si umesema tupendeze!?” Wakacheka. “Umependeza sana Nanaa.” “Asante.” Akashukuru na ndipo akasalimia wengine. Jeff na Yasini.

“Unisamehe Jeff. Mambo yamekuwa yanaingiliana.” “Nini tena?” Jeff akauliza. “Nahangaika sehemu ya kuishi. Bado sijatulia.” “Pole. Ungependa nikusaidie?” Jeff akauliza. Nanaa akacheka. “Msaada mkubwa ninaotaka kwa sasa ni niwe na kwangu. Kama ukisikia kuna chumba kinakodishwa, tafadhali nijulishe.” “Mimi ninayo sehemu kubwa tu yakuishi. Nakukaribisha.” “Asante.” “Mbona unacheka kama huamini?” “Nimekushukuru jamani Jeff! Natakiwa nifanyeje?” “Sasa shukurani hiyo utahamia au vipi?” “Kwa sasa ninapo pakujishikiza. Natafuta kwangu.” “Hata kwangu panaweza kuwa kwako.” Jeff aliendelea. Muhudumu akawasogelea.

“Nasikia njaa. Sijala tokea jana mchana nilivyokula kazini. Nilipika tu kwa kaka, lakini sikula.” “Pole. Basi tuagize mbuzi wa kuchoma. Si utapenda?” Jeff akauliza. “Mimi ni kama fisi kwa nyama.” Nanaa akajibu, wakacheka. “Naomba usichelewe dada yangu. Natakiwa kuondoka hapa kabla ya saa 12.” “Usijali. Nitahakikisha oda yenu inakuwa mbele.” “Nitakushukuru.” Wakaendelea kuongea na kucheka. Ni kweli Yasini alionekana kumjali Zena. Nanaa akabakia akiwatizama kwa kuwatamania.

“Hongereni. Naona mpo vizuri. Na mmependezeana.” Nanaa akasifia. “Namshukuru Mungu kwa kweli. Nafurahia kampani ya Zena. Hana makuu.” Yasini akasifia. Zena akacheka kwa aibu na deko kidogo.

*****************************************************

Nanaa akaanza kuwaza maisha yake. Alipotoka, alipo ambapo maisha yanaendelea kumchanganya na kujichanganya. Anapoelekea ndio ukawa mtihani. Karata chache alizonazo mkononi alitakiwa azicheze kwa makini mno. Lasivyo ataharibu kabisa. Akabaki anawaza.

*****************************************************

“Mbona upo mbali?” Jeff akamshtua kwa swali. “Nipo hapa hapa jijini.” Nanaa alijibu huku akitoa tabasamu. Wazi alionyesha ametingwa na mambo. Hajui afanye nini. Ni kama jibu amelipata. Lakini moyo wake ulisita. Akabaki njia panda.

Vinywaji vilishaletwa, wakabakia kusubiria chakula. Wakawa wanaendelea na vinywaji, huku stori za hapa na pale zikiendelea. Walipokuwepo jana yake. Walifurahia nini. Wapi watakwenda baada ya pale. Nanaa alikuwa kimya tu akisikiliza na kucheka. “Nilifikiri tutakaa mpaka usiku. Ili tuwe wote.” “Ningependa kufanya hivyo. Niongozane na nyinyi kila mahali, lakini naishi kwa watu. Au ndio nimehamia kwa watu. Lazima niweke heshima. Siwezi kuanza kurudi usiku nyumbani kwa watu.” “Upo sahihi.” Jeff akakubaliana naye.

Chakula kikaletwa, wakaanza kula. Nanaa akaangalia saa yake, akamalizia soda, akaamua aondoke. “Jamani nawashukuru.” “Unaondoka sasa hivi Nanaa!?” “Nawahi daladala.” Nanaa alishasimama, na pochi yake akaiweka begani. “Naomba nikusindikize.” “Kweli Jeff? Naona bado unakula.” “Usiwe na wasiwasi. Twende.” Wakatoka wao wawili tu.

Jeff atupia ndoano kwa Nanaa wakiwa garini.

“Naomba uniahidi utafikiria ombi langu.” Jeff aliongea mara baada ya kuondoa gari. “Ombi gani tena? Maana kama kutoka kwa ajili ya chakula cha mchana, nimeshatimiza.” Jeff akacheka. “Kweli hunitaki kwenye maisha yako Nanaa! Hivi ndio umeshatoka na mimi?” “Jamani Jeff!” “Kweli Nanaa hii ndio picha uliyonayo ya kutoka na mimi?” Nanaa akanyamaza. “Huwa wanasema, usikatae wito. Kataa maneno. Lakini naona mwenzangu unanikatalia vyote.” “Akili yangu haijatulia Jeff. Bado sijapata maisha ya kueleweka.” “Kwa nini usije kutulia kwangu kwa muda mpaka utakapo jipanga?” “Sikufahamu Jeff.” “Na unampango gani juu ya hilo?” “Sijui. Sitaki kuongezea kitu kingine kitakachonifanya nishindwe hata kumaliza yanayonitinga.” “Kwa nini umeanza kunifikiria vibaya, wakati hata hujanipa nafasi?” Kimya.

“Unajuaje labda chanzo cha kunifahamu ndio ukawa mwanzo wa ufumbuzi wa maswala yako? Huwa wanasema, ‘Two are better than one.’ Hujasikia hilo?” Nanaa akacheka. “Wawe wamepatana na kuelewana. Unaweza kukuta ndio wanaongezeana matatizo zaidi maishani.” Jeff akamtizama na kuendelea kuendesha. “Mbona sasa kimya?” “Nimeishiwa hoja Nanaa. Kila ninachoongea unapinga. Nimekubali kushindwa.” “Usinielewe vibaya.” “Sawa Nanaa.” Wakaendelea kuendesha, Nanaa akimuelekeza.

“Nakushukuru kwa kunirudisha.” “Anytime.” Jeff alijibu kwa kifupi sana. Nanaa akajua ameshakasirika. Akacheka kidogo na kugeukia pembeni huku akifikiria. “Nini sasa?” Jeff akamuuliza huku akiendelea kuendesha kwa makini. “Nikitulia nitakutafuta Jeff. I promise.” “Unajuaje kama wakati huo bado nitakuwa nataka kukwambia hichi ninachotaka kukwambia wakati huu?” Nanaa akapooza.

*****************************************************

“Nisije kuwa napiga teke bahati!” Nanaa akawaza akiwa anafikiria. “Geb!” Wazo likamjia, akajicheka. “Mimi na yule kiumbe! Haitakaa ikatokea. Tena heri nijiachie. Ana Liz, kwenye maisha yake. Tena asiyetaka wegazi. Heri nimchangamkie Jeff.” Nanaa akaanza kushawishika.

*****************************************************

“Kama nilikusikiliza kwa makini, basi huu ndio mtaa wenyewe.” Jeff alimtoa kwenye mawazo. “Ndio hapa hapa. Lakini nyumba ipo kwa nyuma ya hiyo barabara inayongia kulia. Sio mbali. Naweza kutembea hata ukinishusha hapa.” “Usijali. Naweza kukupeleka tu. Labda iwe unaogopa.” “Hapana. Nyumba yenyewe ina ukuta na geti, hakuna atakayejua hata kama nililetwa na gari. Twende tu. Ni nyumba ile pale.” “Kumbe unaishi kwenye geti kali?” Nanaa akacheka. “Unaishi na nani tena?” Jeff akauliza. “Yule dada, ambaye ni bosi wangu. Alisoma na kaka. Ndio kama ameniombea kwao.” Geb hakutajwa. “Oooh!” Jeff akaitika.

Ilishakuwa saa 12:20 jioni wakati Jeff anaegesha gari nje ya geti la Geb. “Nakushukuru sana Jeff.” “Anytime!” Jeff akanyamaza. Nanaa akabaki akifikiria pale pale kwenye kiti kabla ya kushuka. Jeff naye akabaki akimtizama. Nanaa alikuwa kwenye wakati mgumu sana. Hajui chakufanya.

“Nitakupigia.” Nanaa alivunja ukimya. Jeff akacheka. “Kweli nitakupigia.” “Sawa.” Jeff akajibu na tabasamu. “Mbona kama huniamini tena?” “Kwa nini tena? Mbona mimi nimekubali yote? Au nilitakiwa kufanya nini?” Nanaa akanyamaza kwa muda. “Najua nimekuwa kama… kam.. Ila naamini umenielewa.” Nanaa alianza kujing’ata ng’ata. Jeff akabaki akimtizama tu. Wazi alionekana alishakata tamaa. “Usiku mwema.”  Nanaa akaamua kuaga. “Na wewe Nanaa.” Akashuka.

*****************************************************

Alimkuta Grace anaandaa chakula jikoni. “Pole na kazi.” “Asante. Vipi huko?” “Kwema tu. Mama ameshakwenda kulala?” “Nimemuomba akae na Fili huko chumbani ili nipike. Fili akiwa na mimi anadeka kweli! Siwezi kufanya kitu chochote. Anataka niwe na yeye tu.” Nanaa akacheka. “Niachie basi mimi nimalizie kukupikia wali. Naona umeshaivisha mboga zote.” “Hapa nilikuwa nawaza kama nipike wali au nimtume Danny akanunue chapatti kule kwenye mgahawa wa mwarabu. Wanakuwa na chapati nzuri.” “Basi wakati unafikiria hivyo, ngoja nipike wali wa maua hata kidogo tu. Mtachanganya na chapati.” “Hayo ndiyo mambo.” “Lakini nataka nikamsalimie mama kwanza. Najisikia vibaya nimechelewa!” “Wala usijali na wala hujachelewa. Bado mapema kabisa.” Wakatoka wote wakaongozana mpaka chumbani kwa bibi Fili.

*****************************************************

Alimkuta Geb na Fili wote wapo kitandani kwa bibi Fili. Fili anaongea, wao wanamsikiliza. “Samahani nimechelewa.” “Mbona mapema tu. Umepata muda wakutosha na wenzako kweli? Ni kama umekimbia kimbia tu.” Bibi Fili aliitika yeye. “Nimeona kwa leo inatosha.” “Naona mambo sio mabaya Nanaa mwanangu.” Nanaa akacheka na kuuliza. “Kwa nini mama?” “Umesema kwa leo inatosha.” Nanaa akajisikia aibu. “Namaanisha jumamosi ijayo nitawahi kutoka hapa na kuwahi kurudi.” “Jeff huyo!?” Nanaa akacheka mpaka akatoka pale chumbani.

“Nanaa! Njoo nikwambie kitu.” Nanaa akarudi.  “Abee mama!” Nanaa aliitika. Bado Geb alikuwa amelala chali. Kimya, hata hakumsemesha Nanaa tokea aingie pale. “Geb amekutayarishia chumba chako. Twende nikakuonyeshe.” Nanaa akabaki kama haamini. “Mimi!?” Bibi Fili akacheka kidogo. “Samahani mama. Sijak..” Akashindwa kuendelea, akanyamaza na kuinama.

“Ndio ujue tunataka ubaki. Twende nikakuonyeshe.” Bibi Fili akatoka pale kitandani, wakaongozana mpaka kwenye hicho chumba. Kilikuwa kikubwa, kisafi, kitanda kimetandikwa vizuri, na vitu vyake vyote vilikuwa humo. “Naona mmenitandikia mpaka na kitanda!” “Grace na Geb ndio walikuwa wanasaidiana.” Nanaa alisimama pale, akashangaa machozi yanamtoka. “Asanteni mama. Nashukuru kunipokea. Nitajitahidi kutafuta chumba kwa haraka ili niwapishe hapa.” “Wewe usijali. Tulia hapa mpaka utakapo jiweka sawa.” “Asante mama yangu. Nashukuruni sana.” “Sasa nimesikia kuna wali maua.” Nanaa akacheka nakufuta machozi. “Nausubiri kwa hamu.” “Sawa mama yangu. Ngoja nikapike.” Mama G akatoka. Nanaa akabadili nguo kwa haraka. Alivaa gauni la kawaida tu. Akarudi jikoni.

*****************************************************

Bado Geb alikuwa amejilaza kwenye kitanda cha mama yake, akiwa kimya vile vile. Tayari walishajua hasira zile ni za wivu, na hawezi kujisaidia. Mama yake akamfuata tena. Hakuwa ameongea kwa muda mrefu na wala hakuwa amefungua macho japo alijua wazi hajalala. “Vipi?”  Mama yake akamchokoza. Geb hakufungua macho. “Geb Magesa! Najua hujalala.” Mama yake akaendelea. “Nenda basi kanywe hata maji huko jikoni.” Kimya. “We Geb!”  Mama yake akaita kwa ukali. Akafungua macho. “Lazima utoke hapo kitandani. Kulala hapo haitakaa ikasaidia. Haya nyanyuka.” Geb akatoka pale kitandani. Akiwa ameelewa mama yake alichomwambia.

*****************************************************

Nanaa alishaanza kutayarisha vitu vya kupika. Alitaka kupika wali wa kukaanga na kitunguu maji, na kitunguu swaumu. Ili baadaye aje aweke njegere na karoti. Kulikuwa na tui la nazi limebaki kwenye friji, akajua atalitumia hilo hilo. Akalitoa na kuweka jikoni ili lipate moto, huku akianza kukaanga kitunguu. Moto aliweka mdogo, ili aweze kuendelea kutayarisha vitu vingine kama kumenya vitunguu swaumu, njegere na karoti huku akipika. Aliendelea kufanya mambo yake kwa haraka ili asiunguze na asicheleweshe chakula.

Geb akaingia. Nanaa alishindwa hata kugeuka sababu ya ubusy wa pale jikoni. Akaendelea kushika hiki, koroga pale, kata hiki, punguza moto upande huu wa jiko hilo refu la gesi lenye sehemu 4 za kupikia. Akili zote zikawepo pale jikoni asiunguze chakula cha kwanza kupika ugenini. Wala asijue ni nani ameingia na nani ametoka.

Geb akasimama pale kwa muda. Akahisi kupuuzwa. Akatoka kwa hasira za wivu na kurudi kwa mama yake. Akajitupa kitandani. “Nimeshakunywa maji.” “Geb Magesa!” Mama yake akajua mambo hayakwenda kama alivyotaka. “Kwani wewe huwezi hata kukata kitunguu jamani!?” Geb akacheka kama aliyepata wazo, na kutoka pale kitandani. Alimsikia mama yake akimcheka nyuma. Akarudi na kumbusu. “Muone!” Mama yake alimtizama kwa macho ya kumsuta. Geb akacheka na kurudi tena jikoni.

Geb kwa Nanaa.

 “Naona upo busy. Nikusaidie nini?” Nanaa akageuka, akamuona Geb. “Pole na safari.”  “Asante.” “Umepata muda wakutosha wa kupumzika?” Nanaa akauliza na kumfanya Geb ajisogeze karibu ya jiko. “Nitalala baadaye.” Nanaa bado alikuwa anachanganya viungo. “Kunanukia vizuri.” Geb akasifia. “Utakula kidogo?” Nanaa akauliza huku akicheka. Akijua wazi Geb hawezi kula. Geb alitabasamu nakushindwa kujibu. “Kwanza ulikula chakula mama alichokupikia?” “Nilikula. Naona inatosha. Baadaye naweza kuongezea uji kidogo, naona itatosha tu.” Nanaa akamwangalia.

“Ulisafiri lini?” “Niliondoka alhamisi.” Geb akajibu. “Niliona kimya.” Nanaa aliongea kwa kulalamika kidogo. “Kwa nini hukuuliza?” “Sina namba yako Geb.” Geb akamwangalia. “Nilikuomba msamaha. Unakumbuka?” Geb akacheka kidogo. “Hukuona umuhimu wa kuwa na namba yangu Nanaa. Kama ujumbe haukuleta maana, ungefuta ujumbe na kutunza namba.” “Nikikwambia najutia, utaamini?” Geb akatabasamu kama asiyeamini.

“Kweli. Hata siku ile uliponishusha nyumbani, nikataka kukuuliza kama mlifika nyumbani  na mtoto salama, lakini nikashindwa. Jumapili siku nzima nilikuwa nataka kukujulia hali lakini nilishindwa. Sikuwa na namba yako. Nikajua labda hata ungenitumia ujumbe mwingine. Lakini nikaona kimya.” “Ningejuaje kama wa safari hii ungejibiwa?” Nanaa akanyamaza kidogo kama anafikiria. “Ni kweli. Lakini nimefurahi umerudi salama.” Nanaa akarudi kupika.

Geb akabaki amesimama pembeni yake akimwangalia. Alipochanganya kila kitu kwenye sufuria, akafunika na kupunguza moto. Alikwenda kwenye friji akamimina juisi kwenye glasi akamkabidhi Geb. “Asante.” Geb alipokea na tabasamu la furaha ya kujaliwa na Nanaa. “Ametengeneza Grace.” Nanaa aliongeza. Wakakaa pale pale jikoni.

*****************************************************

“Mbona sasa wewe haunywi?” “Nimeshiba. Nimekula muda sio mrefu.” “Ulienda kukutana na Jeff?” Geb akauliza swali la moja kwa moja. Nanaa akababaika kidogo. Akanyamaza. “Nilifikiri nilisikia ukisema moyoni hujisikii. Mambo yalibadilika?” Geb akaendelea kudadisi. “Jeff ni rafiki wa mpenzi wa Zena rafiki yangu. Na walikuwa pamoja.” “Kwa hiyo ulienda kwa Zena, ndio ukakutana na Jeff bila kujua?” Nanaa alijua anategwa. “Nilijua na Jeff angekuwepo, Geb. Nikaona ni wakati muafaka wa kuwashirikisha uhitaji wangu wa chumba. Endapo watasikia sehemu kuna chumba kinapangishwa, basi waniambie.” “Kwa hiyo?” Geb akaendelea kudadisi.

“Wameniambia kuna nafasi mahali.” “Kwa Jeff?” Geb akarusha swali jingine, Nanaa akanyamaza. “Nanaa? Ni Jeff ndiye amekwambia ananafasi  ya kukuweka?” Geb akarudia tena. “Ndiyo. Alisema anasehemu kubwa tu yakuishi. Naweza kwenda kuishi naye kwa muda wakati najipanga.” Geb alibaki akimtizama. Walikuwa wamekaa karibu, pale pale kwenye meza ya jikoni.

“Nanaa?” Geb akaendelea. “Nilimkatalia Geb.” “Kwa nini ulikataa?” Geb aliendelea kuhoji. “Simfahamu na yeye pia hanifahamu.” “Kwa hiyo mmepeana muda wa kufahamiana?” Nanaa akanyamaza kwa muda huku ameinama akichezea ganda la kitunguu swamu. Akanyanyua macho, akakuta bado Geb akimtizama. “Nilimkatalia msaada wa kuhamia nyumbani kwake. Nilimwambia kwa sasa ninapo sehemu yakujishikiza. Ila msaada ninaohitaji ni kusaidiwa kutafuta kwangu. Kwa hiyo kama akisikia kuna chumba kinakodishwa mahali, anifahamishe.” “Unafikiri itakuwa na tofauti kama yeye akikusaidia kutafuta hiyo sehemu? Si yatakuwa ni yale yale tu. Atakuwa anafahamu unapoishi, au kule kujua yeye ndiye amekutafutia sehemu unayoishi! Kwanza utajuje kama atakapokutafutia sio nyumbani kwake? Yaani ukajikuta unaishia kuishi naye yeye nyumbani kwake?”“Sikuwa nimefikiria hivyo.” Wakanyamaza kidogo, Nanaa akanyanyuka kwenda kugeuza wali.

*****************************************************

Akasafisha ile sehemu aliyokuwa akitumia. Huku Geb ametulia kimya kwenye kiti akiendelea kutafakari. Nanaa akaanza kusuunza vyombo alivyokuwa akitumia huku akivipanga vizuri kwenye dishwasher. “Naona wali unakaribia kuiva.” Akamgeukia Geb aliyekuwa amekaa tu pale kwenye kiti akinywa juisi yake taratibu.

“Onja hata kidogo.” “Umeweka vitu vingi sana Nanaa. Mimi nikishaona karoti hivyo. Au njegere zinaniangalia kwenye wali, nachanganyikiwa kabisa nakushiba hapo hapo.” Nanaa akacheka. “Kidogo tu. Funga macho, halafu fungua mdomo, mimi nitakuwekea. Tafuna, halafu uniambie.” “Nanaa!” “Kweli tena.” “Basi toa karoti, njegere. Hakikisha kitunguu hakiingii kwenye kicho kijiko kimoja utakachokiweka mdomoni kwangu.” “Sasa hapo si utakuwa unakula wali mweupe, wakati mimi nimepika wali maua?” “Mimi hata wali mweupe huwa sipendi.” “Basi.” Nanaa akageuka.

“Lakini sio kwamba sitaonja huo unaopika.” Akamsikia Geb akiongea kwa haraka na kusimama. “Sio lazima. It’s ok.” Nanaa alijibu kwa upole. “Nataka kuonja.” “Kwa nini, wakati umeshasema hupendi? Acha tu.” “Nanaa!” Geb alimsogelea. “Naomba kuonja.” Nanaa akamgeukia. “Hamna haja. Kweli tena. Ni sawa tu.” “Nanaa! Labda kama unaninyima.” “Unajua siwezi kukunyima Geb. Lakini nimejua sio kitu ambacho ungependa hata kujaribu. Yaani umeshakataa kwa kukiangalia tu. Na kitu chochote ukishakikatia tamaa mawazoni, huwezi kukikosea kasoro. Ukila tu huo wali, hutakosa sababu. Acha tu.” Geb alijiona amekataa bahati ya kulishwa. Tayari alishaanza kujutia kukataa bila kufikiria. Akajua hasira za wivu ndizo zilizokuwa zikimsumbua wakati akijibu. Hofu ya kuwa Jeff anamzidi mahesabu ilimwingia. Anaonekana anataka kumtoa Nanaa pale ndani.

“Samahani Nanaa. Nimekukatalia bila kufikiria.” Nanaa akatabasamu. “It’s ok.” Alijibu kwa upole. Wakabaki kimya hapo hapo karibu wakiwa wamesimama. Nanaa ameangalia chini, Geb akimtizama. “Ngoja nianze kupakua, niweke mezani. Njaa zitakuwa zinawauma.” Akageukia kwengine nakuanza kutoa vyombo kwenye makabati, akatoka navyo nje na kumuacha Geb amesimama pale pale. Akaanza kupanga kwenye meza ambayo huwa wanakula kwa pamoja. Akaandaa kila kitu hapo mezani mpaka akaridhika.

Ndipo akaenda kumwita bibi Fili au Mama G kama wengi walivyozoea kumwita, wote wakakaa mezani. “Naona kinavutia kwa macho.” Nanaa akacheka. “Asante mama. Lakini mimi bado nimeshiba. Nitakula kiporo kesho kama kitabaki. Naenda chumbani kuoga. Nitoe harufu ya vitunguu.” “Sidhani kama utabaki.” Mama G akajibu na kufanya Nanaa acheke. “Asante Nanaa. Naona wali unavutia.” Grace naye akashukuru wakati anampakulia mumewe. “Asante kushukuru. Nitakuwepo hapo chumbani. Nitatoka kusafisha meza na vyombo.” “Wala usijali. Tutamalizia tu.” Nanaa akaondoka.

Nanaa ajikuta aangukia mikononi mwa Mama yake Mkubwa tena!

Siku inayofuata ilikuwa jumapili. Nanaa akaamua kurudi nyumbani kwa kaka yake ili kusalimia wageni. Hakumkuta kaka yake, akajikuta ameishia mikononi mwa Mama yake mkubwa na Viola. Alijuta hata kwa nini alikwenda bila taarifa. Walimpa wakati mgumu sana. Mama yake mkubwa alimsema kwa maneno ya kumnyanyasa mpaka alipomaliza roho yake ikatulia. Akamfukuza rasmi hapo nyumbani kwa mwanae James.

Nanaa akatoka akatafuta sehemu karibu kidogo na kituo cha daladala, akakaa hapo akiwaza. “Jeff anaweza kuwa suluhisho la kudumu. Nikimkubali, naweza nikapata mkombozi wangu. Nikaepuka maneno.” Nanaa akawaza akiwa amekereka sana rohoni. “Lakini nikiwa na Jeff, sijisikii vizuri kama ninapokuwa na Geb, mchumba wa mtu!” Nanaa akajirudi na kuanza kujichanganya tena mawazoni. “Alikuwa wapi huyo Jeff siku zote jamani!?” Nanaa alilalamika. Alikaa pale akiwaza bila kufikia muafaka, mwishowe akaamua kurudi nyumbani kwa Geb akajifikirie zaidi.

*****************************************************

Aliingia ndani mida ya saa 11 jioni, akawakuta wote wamekaa sebleni. Mpaka Liz alikuwepo. Tena alikaa pembeni ya Geb. Fili alikuwa amepakatwa na baba yake. Aliingia hapo akionekana kabisa hana furaha. “Kwema?” Grace akamuwahi. “Kwema. Nimchukue Fili nikamuogeshe?” “Geb alishamuogesha, amekula, hapo baba yake anambembeleza alale, kesho shule.” “Ooh! Nimemchelewa Fili wangu!” “Nenda kachukue chakula, nimekubakishia.” “Labda nisafishe tu, sitakula.” Nanaa alimjibu Grace huku akielekea jikoni. Alikuta jiko limeshasafishwa, akatoka. “Naona kupo kusafi. Basi na mimi naenda kulala.” “Mbona mapema? Njoo tukae kidogo.” Nanaa alisimama pale kimya, kama anayewaza kitu. “Naomba mimi nitangulie tu. Naona nimechoka.” Nanaa akajibu kwa upole, akaelekea chumbani.

*****************************************************

Picha ya Liz akiwa amekaa pembeni ya Geb ilipita kwa haraka mawazoni. Akatulia. Kisha maneno ya mama yake mkubwa yakaanza kumrudia na kukubali kuwa kweli yeye ni tatizo sugu. Aliona hastahili kuwepo pale. “Naona nimeanza hata hisia zisizo sahihi kwa mchumba wa mtu. Wenyewe wanapendana. Mimi nimejaa humu ndani. Geb anahangaika kutengeneza chumba, akashindwa hata kupumzika!” Aliona vile anavyosumbua watu, akazidi kujisikia vibaya. Lazima kutafuta suluhu ya kudumu.

Akaingia kuoga, akatoka na kubaki amejilaza kitandani. Baada ya kuwaza hili na kushindwa kupata majibu, huku Jeff akionekana ndio suluhisho la kudumu akaamua alale tu. “Sijui nimpigie Jeff? Nitamwambia nini? Nirudie maisha yale yale ya zamani? Kukimbilia wanaume sababu ya sehemu ya kuishi?” Nanaa akaanza kulia gizani. Wivu wa kumkuta Liz pembeni ya Geb, na maneno ya mama yake mkubwa yalizidi kumliza. Asijue atafanyaje. Alilia huku akiangalia simu yake akitamani ampigie simu Jeff, lakini moyo ulizidi kusita. Alilia taratibu pale gizani, asijue chakufanya.

*****************************************************

Akasikia hodi mlangoni, akakaa na kujiweka sawa. “Karibu.” Mama G akafungua mlango. “Mama!” Nanaa akafuta machozi. “Niwashe taa?” Mama G akauliza. “Washa tu.” Akawasha akamsogelea kitanda alipokuwa amelala Nanaa. Akaweka juisi kwenye mezani ndogo iliyokuwepo pembeni mwa kitanda. “Mbona unalia?” Akamuuliza. “Sijui nifanyaje mama? Sijui.” Mama G, akakaa. “Nini kinakusumbua?” Mama G akauliza kwa utulivu.

“Nachukia haya maisha yangu mama. Nitakuwa hivi mpaka lini? Nitazunguka kwenye majumba ya watu mpaka lini? Natamani kutulia. Natamani na mimi kuwa na kwangu. Jeff….” Akakwama. “Nakusikiliza Nanaa. Ongea tu usiogope.” “Jeff anaonekana ni muugwana na anauwezo mzuri tu. Anaonekana angeweza kunioa. Nikaanza maisha yangu nakuacha kusumbua watu wengine.” Nanaa alijieleza huku machozi yakimtoka.

“Umeshafikiria baada ya ndoa? Yaani ameshakuoa, amekupa sehemu ya kuishi. Maisha yako yatakuaje?”  Mama G akauliza swali la msingi akionekana ametulia kabisa. “Hilo ndilo tatizo mama yangu. Nimekuwa nikifanya kosa hilo hilo. Kukubali wanaume sababu ya kupata kimbilio. Nimechoka mama yangu. Nikaamua kupumzika. Nitulie pale kwa kaka. Lakini sasa hivi tena ndio mambo yametibuka. Mama mkubwa amenifukuza rasmi pale kwa kaka. Hataki hata nirudi kusalimia. Nitafanyaje? Na Jeff naye ndio anaonekana mkombozi wangu. Lakini mama, moyo wangu umemkataa kabisa yule kijana. Sijui nitafanyaje?” Nanaa alikuwa akiongea na Mama G, kama anamfahamu.

“Samahani mama. Najua nakwambia mambo yasiyo kuhusu. Lakini sina mtu wa kuzungumza naye?” “Nisikilize Nanaa. Kwanza nimefurahi kuwa umeweza kuniamini na kunishirikisha. Pili, kuna usemi huwa wanasema, ‘Don’t make permanent decision for temporary problem’. Unanisikia Nanaa?” “Nakusikiliza mama.” “Ehee! Tulia kabisa. Mungu amekuleta hapa kwa makusudi. Nakuomba hapa uwe huru. Usijisikie kuwa unaharaka yakuondoka. Utakapokuwa tayari ndio uondoke. Kwanza wewe bado mwanafunzi. Fikiria shule na hiyo kazi uliyopewa. Basi. Naamini Mungu atakupa maisha mazuri tu. Umesikia mama?” Bibi Fili alijaribu kumtuliza.

“Nashukuru mama. Asante.” “Yatapita tu haya. Tena naona unamwanzo mzuri kuliko watu wengi sana. Vumilia, na ujipe muda. Usikimbilie kufanya maamuzi utakayojutia baadaye.” Nanaa akatingisha kichwa. “Tumuombe Mungu pamoja. Tumruhusu yeye ndio awe msaada wako. Kisha  jiruhusu kuipokea siku ya kesho ukiwa na amani.” Nanaa alitoa tabasamu. “Asante mama yangu.” “Haya kaa vizuri tuombe.” Bibi Fili akamshika mkono Nanaa, akamuombea. Ilikuwa sala fupi, lakini ilimfariji sana Nanaa.

“Asante sana mama. Umenitua mzigo mzito. Nilikuwa sijui chakufanya.” Bibi Fili au mama G, kama wengi walivyozoea kumwita, akatoa tabasamu la faraja. Kama mama kwa mtoto wake wakumzaa. Hakika hakujua alichokifanya kwa Nanaa. Ndio mama wa kwanza aliyeweza kukaa naye chini na kumfariji kwa kiasi kile. Yale maombi yalikuwa kama barafu nzuri ndani ya moyo uliokuwa mzito wa Nanaa. “Basi kunywa hiyo juisi, ndipo ulale.” Bibi Fili akatoka, na kumuacha Nanaa amefarijika. Kwanza ni kama alimsaidia kumpa majibu ya maswali yake. Juu ya Jeff na hisia zake. “Sina haraka tena. Nitamtafuta Jeff, nimpe nafasi ya kumsikiliza. Kisha nimkatalie rasmi. Nijiruhusu kufikiria, na kujipanga bila mtu nyuma yangu.” Nanaa aliwaza. Akalala akiwa na furaha.

*****************************************************

Aliamka siku ya jumatatu akiwa na furaha zote. Huku akijiambia anahitaji tu muda. Aliandaa kifungua kinywa, wakati akimwangalia Mama G akimwandalia Geb uji wake. Akamsaidia Grace kumwandaa Fili, wakaondoka mapema yeye na Grace na mwanae. Alifika kazini akiwa ametulia. Akafanya shuguli zake, akaamua kumpigia simu Jeff!

“Unacheka nini sasa?” “Sikutegemea.” “Kwa nini?” “Basi tu. Mzima wewe?” “Mzima. Naomba tukutane jumamosi.” Kimya. “Jeff!” “Nakusikiliza mrembo.” “Ndio nimemaliza. Kama bado utataka kuniambia ulichotaka kuniambia. Na kama bado sijachelewa.” Jeff akacheka. Nimegairi Nanaa. Naona niache tu.” Nanaa akatulia kidogo. Akasikia kupooza. “Nanaaa!” “Nipo Jeff. Samahani sana. Lakini naamini utakuwa umepeta sikio jingine la kukusikiliza.” “Naamini hivyo. Asante.” “Haya. Kila la kheri.” Nanaa akakata simu, asiamini.

*****************************************************

 “Daah! Mlango umeshafungwa hivyo. Sijui niseme nimechezea bahati!?” Siku ikaanza kuwa ngumu. Kukataliwa kubaya! Jeff alimfungia vioo kwa haraka sana. Hakutaka kuzungushana naye. Nanaa alitamani yeye ndio awe wakumkataa, kuliko vile alivyokataliwa. Akamkumbuka Geb. Akakumbuka Liz amekaba. “Nijipumzikie tu.” Nanaa akawaza.



*****************************************************

Maisha yakaanza ndani ya nyumba ile. Kulikuwa na amani na utulivu wa aina yake. Kama Danny asipokuwepo nyumbani, basi ni Fili ndio alikuwa akichangamsha nyumba, lakini wengine wote walikuwa wakimya. Akaanza kujiwinda na Geb. Hakutaka kuwa karibu naye kabisa ili asijiumize nafsi yake. Geb alikuwa akiibua hisia ambazo zilimfanya kumtaka zaidi. Nanaa akaona hatendei haki hisia hizo mpya na ngeni. Kwani Geb alikuwa ni wa Liz. Na Liz mwenyewe alikuwa akikaba kweli kweli.

Siku hiyo ya jumatatu jioni waliporudi nyumbani baada ya kazi. Nanaa akiwa anatayarisha chakula cha usiku, Bibi Fili naye anaoga baada yakutoka kwenye shuguli zake, wakamsikia Liz na yeye ameingia. “Naona umetoka dry clener!” Alimsikia Grace akimuongelesha. “Hapana. Nilipitia nyumbani kuchukua baadhi ya nguo zangu za kuvaa kazini week hii nzima. Nikilalaga hapa, halafu kuamka kwenda kuvaa nyumbani, nachelewa kazini. Nimeona heri niwe natokea hapa hapa kwenda kazini. Halafu weekend hii Geb amesema hatasafiri. Tutakuwepo wote nyumbani.” Moyo wa Nanaa ulipasuka. “Liz anahamia hapa!!!”  Akajiuliza.  “Lakini ni kwake. Sasa si nilisikia hapendi watu wajazane hapa ndani?” Nanaa akajiuliza. Gafla amani ikatoweka moyoni mwake, asijue chakufanya. Pakwenda hana, analazimika kuwepo pale kwa wakati ule. Akabaki akiwaza pale jikoni yeye mwenyewe.

 Akatayarisha chakula. Akala huko huko jikoni. Kingine akakipanga vizuri mezani. “Chakula tayari.” Akamsogelea Grace akamwambia kwa sauti ya chini. “Una mkono mwepesi! Hapa ndio nilikuwa najipanga kuja kukusaidia.” Nanaa akacheka. “Usicheke Nanaa. Nilikuwa nakuja.” “Wala usijali. Ilikuwa ni kuunga tu njegere. Nyama zile tulizokaanga jana bado zilikuwa nyingi. Nimepasha tu. Na nimeona chapati alizoleta Danny bado za moto. Kwa hiyo wala sijachukua muda mrefu.” “Pia nashukuru. Nimejikalia kizembe, utafikiri nimetoka shamba!” Nanaa akacheka. “Basi usiku mwema. Kuna kitu nataka kufanya huko chumbani kabla sijalala.” “Haya mwaya. Usiku mwema.” “Na nyinyi pia.” Nanaa akaenda kumuaga Mama G, akaingia chumbani kwake.

Jumanne alifanya hivyo hivyo kuingia chumbani kabla hata Geb hajatoka kazini. Jumatano akafanya hivyo hivyo.

*************************************************

Alhamisi usiku Zena akamtafuta kumwambia akaribie kwenye birthday party ya Yasini. “Ni wapi tena Zena? Mwenzio nimeamua kutulia.” “Mbona nimeelewa. Hata Jeff ametusimulia kila kitu wote tumeelewa. Nataka tu uje uniunge mkono. Sitaki nijikute peke yangu nikiwa nimezungukwa na marafiki wa Yasini tu.” “Kwa hiyo mtafanyia wapi hiyo sherehe?” Nanaa akahoji akionyesha wazi hataki kwenda. Tutaelekea Kigamboni. Tutaondoka saa nne, na kurudi jioni. Nakuomba usinitupe Nanaa.” Baada ya kubembelezwa sana na kupewa mipango yote, Nanaa akakubali. Hata hivyo alijua itamsaidia kuwa mbali na ile hali pale. Geblizim.

*************************************************

Ijumaa kabla hajaingia kulala, akamfuata Mama G, chumbani kwake. “Niambie mwanangu Nanaa.” Nanaa akatabasamu, akasogea. “Unakumbuka habari za yule rafiki yangu Zena?” Nanaa akauliza. “Yule ambaye mchumba wake ni Yasini, rafiki wa Jeff?” Nanaa akacheka kwa sauti. “Mama! Husahau?” “Nasahauje wakwe? Haya, kuna nini tena?” Nanaa akavuta pumzi. “Kesho ni birthday ya Yasini. Wanaenda kufanyia Kigamboni. Wamenialika. Wamekubaliana kukutana pale kivukoni saa 3:30 asubuhi, ili saa 4 waanze kuelekea huko. Kwa hiyo nilitaka kukutaarifu hivyo.” Mama G, akajua kazi itakuwepo kesho yake Nanaa akiondoka pale.

“Sawa. Utataka kusindikizwa, au watakuja kukufuata hapa?” “Nimemwambia Zena asisumbuke. Nitakutana nao huko huko kivukoni. Kwa hiyo naweza kutoka mapema kabla hamjaamka. Ila nitahakikisha nimeacha kila kitu tayari.” “Wewe nenda kapumzike na wenzako. Mambo mengine tutafanya tukiamka.” “Haya mama yangu. Usiku mwema.” “Mbona mapema?” “Nimeanza kuandika ripoti. Ndio inanichukulia muda mwingi huko chumbani.” “Haya mama. Usiku mwema. Na uwe na wakati mzuri na wenzako kesho.” “Asante mama yangu.” Nanaa akaelekea chumbani kwake.

Jumamosi ya heka heka baada ya Nanaa kutoka.

Kesho yake asubuhi Nanaa akaamka mapema. Akaandaa kifungua kinywa cha kila mtu. Akapika mpaka uji wa Geb, ndipo akarudi chumbani kwake. Akaoga vizuri na kuanza kujitengeneza. Kama kawaida yake ya kupenda kuvaa vigauni. Akavaa kigauni kizuri sana. Refu mpaka chini. Lilimkaa Nanaa vizuri mpaka mwenyewe alijua akabaki akicheka. Alilichagua hilo makusudi kwakuwa lilikuwa kata mikono juu. Ilishikiliwa na kamba nzito zilizokuwa zimepita juu ya shingo. Sehemu kubwa ya mgongo ilikuwa wazi. Kwahiyo rasta zake akazibana kiasi zile za mbele, za nyuma akaziachia kufunika ule uwazi wa mgongoni. Akafurahia na rangi ya hilo gauni sababu ya jua kali. Akajua litamfaa na joto la jiji hilo.

 Hereni zake za bati tu. Kubwa na duara zilizokuwa zimechomvya kwenye maji ya dhahabu, nakuzifanya uhisi ni dhababu tupu kama ukiangalia kwa haraka, zilimkaa vizuri sana. Alichukua kofia maalumu ya beach, akaining’iniza kwenye kimkoba chake kama cha mkeka. Miwani ya jua akaining’iniza mbele ya gauni yake kwenye ile ‘V’ iliyotengenezwa kutokana na ile mikanda iliyopita shingoni. Akavaa zile zile sendozi zake zilizokuwa na shanga nyingi nyeupe. Akajua zitaendana na gauni hilo lililokuwa na rangi nzuri iliyokolea bluu kama maji ya bahari.

 Usiku kucha alikuwa akipaka rangi kucha zake. Kwa hiyo kucha za miguu zikawa zinavutia kwenye zile sendozi zake. “Hapa ningekuwa na gari!” Nanaa akawaza. “Nitajichafua tu, kwa kutembea hapa mpaka kituoni.” Nanaa alijiongelesha. Akataka kusahau rangi ya midomo anayopenda kupaka. Nyekundu. Akaweka huku akifurahia jinsi alivyozidi kuwaka.

*************************************************

 Alipojikubali kuwa amependeza na hana chakuongeza mwilini mwake. Akaamua kutoka. Wakati anatoka chumbani akakumbana na Danny koridoni. “We Nanaa? Unaenda wapi asubuhi yote hii wakati bosi wako kalala ndani!?” Nanaa akacheka kidogo. “Naelekea Kigamboni kwenye birthday.” “Mmmh! Birthday ya asubuhi hiii!?” “Tutashinda huko siku nzima. Hata hivyo tunatakiwa kuondoka pale kivukoni saa 4 asubuhi. Lakini sababu ya daladala, imenibidi kuwahi kidogo.” “Khaaa! Naona kweli umekamia hiyo birthday! Sio kwa kupendeza hivyo bwana!” Nanaa akataka kuondoka huku anacheka.

“Nanaa!” Nanaa akageuka. “Nisubiri nikusogeze. Mimi mwenyewe naenda kazini leo.” “Asante. Utakuwa umenisaidia.” “Basi nifungie vitafunio vyangu. Harufu nzuri imeenea mpaka chumbani!” “Nimepika sambusa.” “Acha masihara Nanaa! Sambusa!?” Nanaa akacheka. “Mimi naona nile tu hapa hapa. Nikienda nazo, James atanimalizia.” “Nimepika nyingi. Naomba mbebee na yeye.” “Kama ndio hivyo sawa. Tena tenganisha kabisa, na weka majina yetu juu. Ili akimaliza zake, akatulie ofisini kwake.” Nanaa akacheka na kuingia jikoni.

“Umeamsha nyumba zima Danny. Kwani huwezi kuongea sauti ya chini?” “Wewe umeamshwa na Sambusa bwana. Acha kunisingizia Grace.” Mkewe akacheka na kuelekea jikoni. “Kwa mwendo huu tutanenepa humu ndani mpaka tupasuke.” Grace akabaki akimtizama Nanaa. “Mbona unanishangaa? Nimetisha? Niambie ukweli.” “Sidhani kama utarudi leo. Ndio umependeza hivyo!” Nanaa akacheka sana. “Ukichelewa tu, sisi tunakufuata.” “Nitajitahidi nisichelewe sana.” “Wala usijali. Wewe nenda kafurahie na wenzako.” Akajua tayari bibi Fili amemwambia.

Huko kwa Nanaa!

Danny alimpeleka mpaka Kigamboni. Akamshusha. Alikuwa amewahi kidogo. Mara akaja Yasini na Zena. Wakasalimiana. Baada ya muda akaja Jeff na msichana mwingine. Nanaa akabaki amepigwa butwaa. Wakawasogelea wakasalimiana. Jeff akamtambulisha yule msichana kama ‘girlfriend’ wake. Wakasalimiana na Nanaa. Wakaja tena marafi zao wengine wawili. Baada ya muda, wakajikuta wameshakuwa kundi kubwa. Nanaa akapanda kwenye gari la Yasini na Zena. Jeff na msichana wake wakaingia kwenye gari yao. Na wengine hivyo hivyo, wakavuka.

Kwa haraka sana, Nanaa alikosa raha asijue ni kwa nini. Alijuta hata kufika pale. Na walipofika kule, ni kama Jeff alikuwa akimfanyia makusudi. Mabusu ya hapa na pale kwa huyo msichana hayakuisha. Alimlisha mbele za watu. Alitaka kukaa naye kiti kimoja huku amemkumbatia. Kila mtu aliona vituko vya Jeff na msichana huyo mpya. Ni kama alimfanyia makusudi Nanaa.





Huku kwa Geb!

Maongezi, sifa na shamra shamra za Danny kwa Nanaa, ni kweli ziliamsha kila mtu pale ndani. Geb alibaki amelala pale kitandani kama amemwagiwa maji. Akili ilishavurugika. Alilala pale kwa muda, kisha akaamua kutoka nje kabisa. Akaanza usafi wa nje ya nyumba yake. Ilifika saa nne asubuhi watu wote wakawa wameamka wanakunywa chai, lakini Geb alikuwa anazunguka nje. “Nenda kamwite anywe uji.”“Mie mama? Akuu. Wewe unamjulia mwanao. Nenda mwenyewe.” Grace akajitoa mapema. Walikuwa wakinong’ona kwa kuwa Liz alikuwepo.

Akatoka mama G. Akamkuta jasho linamtoka kama maji. Anasafisha sehemu ambazo ni safi. Akasimama pale akimwangalia. Akamuona anaenda stoo, akatoka na jembe mkononi. “Unachimba shimo?” Mama yake akatupia neno kuchokoza. “Nataka kupanda miti.” “Wazo zuri ili tupate vivuli.” Akaanza kuchimba mashimo kama makaburi.

“Kwani miti hiyo unayotaka kupanda hapo, ni mirefu ya kiasi gani?” Kimya. “Naona kama mashimo hayo ni marefu sana Geb, mwanangu.” “Sitaki mizizi ije kuungua na jua.” “Wazo zuri.” Akatulia. Akaona anaendelea kuchimba.

“Nikuletee uji wako hapa nje?” “Mpaka nimalize.” “Nashauri ule kwanza. Hayo mashimo ni marefu sana.” Kimya. “Kwani unapanda miti mingapi?” Kimya. Geb akaendelea kuchimba. Jasho lilikuwa likimwagika kama maji. “Hivi ulisema ni miti gani tena?” Kimya. “Utapanda mbegu au miti ile mikubwa kama mibuyu? Maana hayo mashimo!” “Mama!” Geb akagomba. “Basi baba nanyamaza.” Akatulia kidogo. “Ngoja nikakuletee uji unywe ili upate nguvu.” “Sitakula sasa hivi. Natoka kwenda kufuata hiyo miti.” “Kumbe hiyo miti yenyewe pia huna!?” Geb akatupa jembe kwa hasira akarudi ndani.

Mama yake akamfuata nyuma. “Uji huu hapa mezani.” Mama yake akarudia. “Nimekwambia sinywi.” “Oooh! Nimekumbuka umeniambia ndio unaenda kufuata miti.” Liz akatoka chumbani akiwa ndio ameamka. Alionekana ameoga vizuri na amependeza. Nyumba nzima ilikuwa ikinukia manukato yake. “Unakwenda wapi Geb?” Liz akauliza kwa upendo. “Nitarudi sasa hivi.” “Nilifikiri leo tunapumzika kama ulivyosema.” Geb hakujibu. Akatoka akiwa ameshika funguo zake za gari. Wakasikia akiondoka. “Sasa ananuna nini?” Liz akauliza kishari. “Mimi mambo ya visirani asubuhi asubuhi siyawezi.” Liz akaendelea. Grace alikuwa amenyamaza kimya mezani akimlisha mwanae, kama hayupo pale. “Siku ndio imeanza.” Mama G, akaongea na kurudi  chumbani kwake.

Baada ya lisaa, wakasikia gari ya Geb inaingia. Wote wakajua amerudi. Wakatulia. Wakasubiri labda ataingia ndani, lakini muda ukazidi kwenda kimya. Fili akataka mama yake atoke naye nje amwangalie anavyoendesha baiskeli. Grace na mwanae wakatoka. Wakakuta mashimo mengi urefu wa Geb. Grace akabaki ametoa macho. Liz akatoka. Grace akaona akamtoe mama yake. Akamkuta chumbani. “Wewe mama! Hivi umeyaona hayo mahandaki hapo nje?” “Nimeyaona. Amesema anapanda miti. Nahisi mibuyu!” Wakacheka. “Nenda kazungumze naye mama. Ataanguka azimie.” “Wewe kwa nini usiongee naye? Si kaka yako!” “Si unamjua Geb. Hatakaa anijibu kitu. Nenda kampelekee hata maji.” Wakatoka.

Grace akampelekea mama yake jagi la maji na glasi. Wakacheka pale sebleni. Wakati wanataka kutoka nje, wakasikia Liz anagomba. Grace akamvuta mama yake. “Subiri kwanza wamalize.” Grace akanong’ona. Liz aliongea kama dakika 10 bila kujibiwa kitu. Wakamsikia anarudi ndani huku anaongea kwa hasira. Na yeye akachukua funguo zake za gari, akatoka. Baada ya kama dakika 3, akarudi tena ndani. Akakusanya nguo zake, akaanza kuweka kwenye gari yake. “Huwezi kunibabaisha mimi!” Liz alikuwa akiongea kwa hasira na jazba. Aliingia mara mbili na kutoka, wakasikia milango ya gari inafungwa kwa nguvu, akaondoa gari karibu agonge geti.

 Waliposikia kimya, ndipo na wao wakatoka. Akasogea mpaka kwenye shimo alilokuwa ameingia Geb. “Maji ya kunywa haya.” Mama G alikuwa anamchungulia kule ndani ya shimo alipokuwepo. Kweli mashimo yalikuwa marefu. “Sina kiu mama. Naomba niache.” “Najua huna kiu. Lakini naomba kunywa haya maji Geb. Jua kali na wewe unashinda juani. Utaanguka kwa kizunguzungu.” “Nimegundua nimeyashimba marefu sana, nataka kuyafukia ndio nipande.” “Miti yenyewe iko wapi?” “Si hiyo hapo pembeni!” Mama G alipoiangalia, ilikuwa ni miche. Hata haijafikia urefu wa mkono wake.

Akajua kazi ya kufukia tena inaanza. Alikuwa amechimba mashimo matatu, marefu sana. “Naomba kabla hujafukia hayo mashimo, kunywa maji.” “Nimesema sina kiu.” “Geb Magesa!” Mama G, akaita kwa ukali. Geb akajua ameshambadilikia. Akatoka. “Kwani ni lazima mama jamani!?” “Ndiyo.” Mama G akajibu kwa ukali na kibabe. Geb akanywa maji glasi moja, akarudi kuendelea na kazi yake ya kufukia yale mashimo. Grace akamtizama mama yake. Wakaangaliana, akaendelea kucheza na mwanae.

Akafukia yale mashimo yote. Jua lilikuwa kali sana. Alikuwa amelowa chapachapa kwa kuwa udongo ulikuwa mkavu sana. Alipomaliza kuyafukia. Akaenda upande mwingine, akachimba mashimo mengine. Lakini ya safari hii aliyafanya mafupi. Akapanda ile miti. Wakajua amemaliza.

Wakaona ametoka tena na gari. “Sasa sijui anakwenda wapi!?” Grace akauliza kwa kumuhurumia kaka yake. “Siku mbona ndio imeanza. Baba yake alikuwa hivyo hivyo. Akianza mambo yake ya wivu, basi hatakuuliza. Anaanza kazi kwenye hiyo nyumba. Asubuhi mpaka usiku.” “Sasa ulikuwa unafanyaje?” “Inategemea. Kama amenikera au ananisingizia mahusiano, namuacha ahangaike mpaka atulie mwenyewe. Wakati mwingine nikimuhurumia, naenda kuzungumza naye. Anatulia. Sasa huyu Geb, anasumbuliwa na mengi. Mwache ahangaike mpaka akili yake ikae sawa. Hajui anataka nini.” Grace akaguna.

*************************************************

Danny akarudi. “Mbona ukoka umechimbuliwa tena wakati uligarimu pesa nyingi sana kupandwa na kutunzwa mpaka kufikia hivyo?” “Kuna shuguli hapa. Hujawahi kuona.” Mama G, akajibu. “Kwema?” Danny akaendelea kuhoji. “Geb kaamka na matengenezo ya nyumba, hapa!” Danny akaanza kucheka. “Huyo ni Nanaa tu.” “Kumbe umejua?” “Mimi nilijua. Na nilifanya kusudi kongea kwa sauti asubuhi, ili ajue Nanaa anaondoka.” Grace akampiga ngumi mumewe. “Hivi wewe ukoje Danny jamani!? Unaona raha hivyo anavyohangaika?” Danny akacheka na kuruka pembeni.

“Sasa, sasa hivi kaenda wapi?” “Ndio tumekaa hapa barazani, tunasubiri tuone. Hajala kuanzia kifungua kinywa wala hajataka kula chakula cha mchana. Maji yenyewe kanywa glasi moja, tena baada ya kuwa mkali.” “Ngoja na mimi nikae, nishuhudie.” Akaenda kuchukua chakula ndani, akatoka kula pale barazani kulikokuwa kumezungushiwa vioo, kwenye ukuta ulikuwa umejengwa vizuri sana nakupendezesha hilo baraza. Kwa hiyo AC ya baridi ilikuwa ikipuliza. Fili akapitiwa na usingizi pale pale.



Kwa Nanaa!

Nanaa alipoona vitimbwi haviishi, akamwita Zena pembeni. “Samahani Nanaa!” Zena akamuwahi kabla hata Nanaa ahajasema kitu. Nanaa akacheka. “Sasa mpenzi, acha mimi niondoke.” “Hata mimi nilitaka kukwambia hivyo hivyo. Haya mambo ya ajabu kweli! Mpaka nimejisikia vibaya. Lakini usije ukafikiri nimehusika.” “Wala usijali. Mimi naelewa. Hata yeye nimemuelewa tu. Naomba niagie Yasini. Mwambie zawadi yake inamngoja ng’ambo ya bahari.” Wakacheka, Nanaa akaondoka bila kuaga mtu.

Kwa Geb!

Mara Geb akarudi na makopo ya rangi. Danny na Mama G, wakaanza kucheka kimya kimya. “Leo patamu leo!” Danny aliongea kishabiki. “Mama wewe! Muwahi bwana.” Mama G akaendelea kucheka taratibu. “Nenda bwana mama. Usimfuatilishe Danny.” Mama G, akatoka pale. Akamfuata. “Unabadili rangi ya geti au ukuta?” “Vyote?” Akajibu Geb kwa kifupi.

“Unapaka nyeusi!?” Mama yake akaendelea kuhoji taratibu lakini kwa mshangao baada ya kugundua ni rangi nyeusi. “Ndiyo. Nataka ukuta mweusi, na geti jeusi.” “Mmmh!” Ilikuwa saa tisa mchana. “Si ungepumzika mpaka jua litue?” “Sijachoka mama. Naomba niache.” Grace na Danny walikuwa wakiangalia. “Naona kuna brashi mbili, ngoja nikusaidie kupaka.” “Hapana mama. Naomba niache.” “Nikuletee maji ya kunywa tena?” “Sitaki mama. Naomba niache. Nataka kuwa peke yangu.” “Haya baba.” Mama G akaondoka taratibu.

Nanaa arudi na kuokoa jahazi.

Mara Nanaa akaingia. Akamkuta Geb amelowa jasho yupo karibu na getini. Amechoka mpaka usoni. Anajifuta jasho kwa mikono yake. Akamsogelea. “Pole na kazi.” “Asante.” Nana akabaki anamtizama. Alikuwa ameinamia yale makopo ya rangi anahangaika nayo. Kina Grace walikuwa bado wakimwangalia kwa mbali wakiulizana, kama anataka kuchanganya au kumwagia kwenye geti.

Mama yao akasema hawezi kumwagia. “Nyinyi hamjajua. Pale anapiga mahesabu jinsi gani yakufanya ile kazi kuwa ngumu zaidi ya vile.”  Danny alizidi kufurahia. Grace akamfinya. “Sasa unafurahia nini?” “Nyinyi si mnanionaga mimi chizi kupenda? Sasa leo muone mwalimu wa machizi.” “Usiseme hivyo Danny bwana! Mimi namuhurumia Geb. Najua anashindwa chakufanya. Anaona yupo huku, na kule anapoteza.” “Ndio atie akili. Sasa tusubirie tuone. Nanaa kawasili.” Grace alimwangalia mumewe asimmalize. Mama G, na yeye akajiweka sawa.

*********************************************************

 “Geb!” Nanaa akamwita. Geb akamtizama. “Are you okay?” Nanaa akamuuliza kwa upole. “Umeweza hata kula?” Nanaa akauliza tena kwa upole. “Nimekuwa na kazi nyingi.” “Pole.” Nanaa akabaki akimwangalia. “Umekuwa na wakati mzuri huko?” Geb na yeye akauliza. “Hapana.” Nanaa akajibu bila kufikiria. “Vipi?” Geb akauliza tena. “Aaah! Mambo ya kitoto tu. Nimeamua kurudi.” “Pole. Umekula sasa?” “Hapana. Nilikuwa nimekasirika, nikashindwa hata kunywa soda. Haya maji nimenunua njiani sababu ya jua kali.” Nanaa akaanza kutokwa na machozi.

Geb akakaa vizuri. “Pole. Usilie sasa. Ni nini?” “Mambo ya kitoto. Hayana hata maana.” “Mbona yamekuumiza sasa?” Nanaa akaanza kujifikiria ni nini cha kusimulia na nini cha kuacha. Kwanza ni Jeff. Halafu amsimulie Geb! Atamwambia nini? Kwa haraka sana atasema ni wivu. Akaamua abadili mazungumzo. Akajifuta machozi.

“Kama unataka kupaka rangi, naweza kukusaidia.” Nanaa akaona atoe msaada. “Jua kali sana. Labda baadaye. Kwanza umeipenda hii rangi?” Geb akamuuliza Nanaa huku akimuonyesha ile rangi ya maji, nyeusi. “Unataka kupaka wapi?” Nanaa akamuuliza huku akimsogelea karibu zaidi. “Ukuta na geti.”  “Kwa nini unataka kubadili hii iliyokuwepo? Inaonekana bado mpya tu na imependezea. Sidhani kama hiyo nyeusi itapendezea ukuta. Labda geti.” “Basi heri niache tu. Mpaka hii ichakae ndio nifikirie tena.” Hata Nanaa alikuwa akitokwa jasho.

Nanaa akaona malengelenge kwenye mikono ya Geb. “Tuone.” Akamvuta mkono wake akawa ameushika anaangalia. “Mbona vidonda vikubwa hivi!?” Nanaa akamuuliza huku akiviangalia vile vidonda. Wala asijue mama yake Geb na kina Danny wapo barazani wanawaangalia. “Vinauma?” Nanaa akamuuliza kwa upendo? “Vikiingia jasho ndio vinauma.” Geb alijibu huku akifikiria. Ndio hisia za maumivu zilianza kumjia. Kabla ya kuja Nanaa, hakuwa akisikia chochote kile. Si njaa, si kiu, si maumivu wala kuchoka. Bado alikuwa na nguvu nyingi tu ya kuendelea.

“Pole.” Nanaa akatoa mtandio wake kutoka kwenye mkoba aliokuwa nao, akampa. “Futia jasho.” Geb akacheka. “Mbona mtandio wenyewe ni msafi hivi?” “Nitafua tu. Ni heri kutumia huu mtandio kuliko hivyo unavyojifuta kwa mkono. Jasho linaingia kwenye vidonda. Utazidi kujiumiza.” Geb akaupokea akaanza kujifutia jasho.

Akafungua chupa ya maji ya baridi aliyokuwa nayo. “Nipe huo mkono wako wa kulia kwanza. Naona ndio una kidonda kikubwa.” Geb akaunyosha mkono na kufungua kiganja chake. Nanaa akammiminia yale maji ya baridi kwenye lile lengelenge kubwa lililogeuka kidonda. Mikono hiyo ya BOT, iliyozoea kucheza na kompyuta muda mwingi, leo ilipitishwa kwenye shuruba, ikasalimu amri. Akaona Geb anacheka. “Umeona  eeh?” “Napata nafuu kubwa. Huu ubaridi wa maji unapoozesha maumivu.” Geb alisifia anachokifanya Nanaa. Wakacheka.

“Umetembea sana?” Geb akauliza huku akiendelea kujipangusa jasho kwa kutumia mkono wake wa kushoto. Aligeuza ule mtandio upande mwingine, uliokuwa mkavu, akaendelea kujipangusa.  “Sio sana, ila jua kali. Leo nimetamani kama ningekuwa na gari langu.” Nanaa aliongea na kujicheka. “Eti hata pakulala sina, nataka gari!” “Ungenipigia simu nikufuate.” “Kwanza niliacha bado mmelala, pili nilikwambia sina namba yako Geb. Tatu hata kama ningekuwa na namba yako ya simu, nisingethubutu kukupigia na kukuvurugia mapumziko yako na Liz. Najua leo ni weekend. Mngehitaji muda usio na mwingiliano wa mambo yasiyo maana.” “Kuomba lifti sio kitu cha maana!?” Geb akauliza. “Inategemea na muombaji Geb. Kumbuka ni mimi Nanaa.” Nanaa alijionyeshea kidole kinyonge.

“Ningekufuata Nanaa.” Nanaa akajicheka.“Huniamini?” Geb akauliza, Nanaa hakujibu. Akachukua mkono wake wa kushoto, akaanza kumwagia maji kama alivyofanya kwenye mkono wa kulia. “Nanaa?” Geb aliita kama kumkumbushia swali lake. Akayamalizia yale maji yote kwenye ule mkono. “Twende tukale Geb.” “Huniamini?” Nanaa akamwangalia, akaona amekusudia kupata jibu. “Nakuamini lakini mimi mwenyewe nisingeruhusu ufanye hivyo.” Geb alibaki akimtizama. Nanaa akatoa tabasamu lake la upole huku akiachia mkono wa Geb taratibu.  

“Twende Geb.” “Maji uliyokuwa unanimwagia yamenifanya nitamani kuoga mwili mzima na maji ya baridiii.” Nanaa akacheka. “Asante kwa kujali.” “Anytime.” Nanaa akajibu na cheko lililofanya dimpozi zake machavuni zikae vizuri. Geb alikuwa akimwangalia kwa kumu admire sana. Kama kitu kizuri cha thamani anachokitamani. Nanaa akainama.

“Hata mimi nataka nikaoge kwanza. Lakini tuyatoe haya makopo hapa katikati ya barabara. Mtu akitaka kutoka au kuingia, atashindwa.” Nanaa alitoa wazo. Akainama na kunyanyua makopo mawili ya rangi, kuepuka kuangaliana pale juani. “Tukayaweke stoo.” Geb akatoa wazo. Wakawaona wanaanza kuyabeba yale makopo kuyapeleka stoo. Geb alinunua makopo 10 ya rangi.

******************************************************

Kila mtu akahema. “Duuh! Nanaa angechelewa kidogo tu, tungejishindia geti jeusi na ukuta mweusi.” Mama G, akaanza kucheka. “Danny huwa ananiudhi mimi jamani! Ukoje huna huruma?” “Unafikiri pale anakuwa anachoka? Yaani wivu mzuri sana. Pale alikuwa anajiona ndio anaanza.” “Na angemaliza mapema, angeanza kazi nyingine.” Mama yao akaongeza. “Natamani siku nyingine akumbuke kuchimba shimo la taka, refu.”  Grace alimrushia mumewe kiatu cha mwanae kilichokuwa karibu. Danny akakwepa. Mama G, na Danny walikuwa wanacheka taratibu ili Geb asisikie maana walikuwa wanapita mbali kidogo, kuelekea stoo kubwa ya nje. Kuyapanga yale makopo ya rangi.

******************************************************

Uchokozi ukawazidi yeye na mama G, kupokezana maneno. Wasijue wenzao walishamaliza. Mara wakaona wanaingia. Wakanyamaza kwa haraka. Danny akatoa simu yake akajidai anasoma ujumbe. “Hiyo ni kalenda Danny!” Geb akajua wala hasomi kitu kwani macho yake yalitua kwenye kalenda ya simu akashindwa hata kuhamisha macho. Geb akamkamata. Akang’ata meno kwa nguvu. “Mmmhhh! Lazima kujua tarehe Geb. Mambo ya majira. Kiangazi, masika na… ” Geb akatingisha kichwa, akaingia ndani. “Uchokozi mpaka umekamatwa. Muone. Ujanja wote umekuisha.” Mkewe alimcheka.

Mama G ndio alikuwa hana mbavu kwa kucheka. Nanaa akamsogelea. “Kumbe mlikuwa mmekaa hapa?” Nanaa akauliza huku akimwangalia mama G.  “Sio muda mrefu sana. Ila tumeona kila kitu.” Danny akajibu yeye kwa haraka. Nanaa akacheka. “Shikamoo Mama!” “Mbona umewahi?” “Mambo hayakwenda kama nilivyodhani. Nikaona nirudi tu nyumbani.” “Afadhali. Kuna chakula ndani. Nenda ukale.” “Asante mama.” Na yeye akaingia ndani.

******************************************************

Alikuta Geb amesimama nje ya mlango wa jikoni akisoma ujumbe. Nanaa akampita, akatangulia jikoni. Haraka sana Geb akamfuata. Wakasahau swala la kuoga kwanza. “Nini kinaanza? Uji au chakula?”  Nanaa akamuuliza mara alipoingia. “Uji kwanza, halafu ndio chakula.” Nanaa akaanza kumtayarishia. Kwa kuwa alikuwa mvivu wa kula, mama yake alihakikisha kila kitu anachokula, lazima kisindikizwe na bakuli la matunda. Kwa hiyo na Nanaa, akamuwekea kwenye sinia yake hiyo maalumu aliyomuona mama yake akimpangia mwanae chakula. Akamimina uji kutoka kwenye thermos na kuweka kwenye bakuli lake maalumu la kunywea uji. Akafungua friji, akakuta mama yake alishamwandalia matunda. Akayaweka kwenye hilo sinia. Akaongeza glasi ya maji na napkins tatu, juu yake akaweka uma, kijiko na kisu. Akamsogezea pale. “Karibu.” “Nashukuru Nanaa. Asante.” “Karibu.” Na yeye akajiwekea chakula kwenye sahani, akaenda kukaa pembeni yake pale pale jikoni. Wakaanza kula.



 “Wamekuudhi nini huko?” Geb alimgeukia akamuuliza. “Hata sio mambo ya maana.” “Nataka kujua Nanaa.” Nanaa akafikiria ni nini chakumwambia. “Sijui niseme nini? Lakini ni juu ya Jeff.” “Na yeye alikuwepo!?” “Ndiyo. Lakini kwa kuwa nilimkataa, akaja na msichana mwingine. Akawa anafanya vitimbwi kama kunikera tu.”“Uliona wivu?” “Hapana Geb. Najua alifanya kusudi kuniumiza, kwa kuwa na mimi nilimuumiza kwa kumkataa. Tena baada ya kufanya juhudi na kunisisitizia yeye sio tapeli kwangu. Anania ya dhati. Naelewa kwa nini amenikasirikia. Au kuja na msichana mwingine pale. Ni kama kunionyesha aliyokuwa akiyataka kwangu sio uongo. Maana alianza hata kusema pale mbele ya watu kuwa anafikiria kufunga ndoa haraka. Hayo yote alikuwa akinithibitishia mimi kuwa hakuwa akidanganya au akitaka kunidanganya. Lakini..” Nanaa akasita.

“Lakini nini?”Geb akataka aendelee. “Najiuliza sijui nimepiga teke bahati au la!” “Kwamba unajutia?” Likarushwa swali jingine. “Kwa sasa sijutii Geb. Kwa kuwa najiona sipo tayari kabisa kwenye swala la mahusiano. Ila najua siku moja nitahitaji kuwa na mtu. Sasa iweje kama Jeff ndio alikuwa mtu sahihi kwangu, halafu nilishamfukuza?” Geb akanyamaza.

“Lakini moyoni nilishindwa kumpokea kabisa.” “Basi ujue siye Nanaa. Jipe muda kila kitu kitakuwa sawa.” “Naona nifanye tu hivyo. Hata hivyo naona nimeshachelewa.” “Ikitokea anakupigia simu na kutaka mrekebishe?” “Hilo ndilo tatizo Geb. Moyoni nimeshindwa kumpokea kabisa. Japo naona ni kama ameshika majibu ya maswali mengi au ni kama atakuwa ni msuluhishi wa matatizo yangu.” “Ki vipi?” “Sijui Geb! Hata sijui niseme nini?” Geb alibaki akimtizama kwa muda.

Geb akamaliza uji wake wote. “Tunaweza kutoka kidogo?” Nanaa alimtizama kwa makini, kama asiyeelewa. “Na Liz?” Nanaa alijikuta akiuliza bila kufikiria. “Liz anahusikaje na kutoka kwetu?” Nanaa akanyamaza baada ya kuropoka. “Nanaa?” “Nilimsikia akisema weekend hii ulimwambia mtakuwa pamoja. Alisema ulimuahidi mtakuwa naye kwa kuwa hutasafiri. Ndio maana nauliza.” Nanaa akajitetea, Geb akasimama. Akaweka sinia alilokuwa akitumia lililokuwa na bakuli la uji na matunda akaweka kwenye sinki. Akabaki amesimama kama anafikiria kitu cha kuongea huku akiangalia vile vyombo pale kwenye sinki. Akashindwa chakuongea, akaamua kutoka.

******************************************************

Nanaa akahisi amekosea. Akaingia kuoga. Akabadili nguo. Safari hii alivaa kigauni kifupi mpaka katikati ya magoti. Kilichanua kuanzia juu mpaka chini. Akajitengeneza kidogo, akavaa na hereni zake zile zile za duara zilizofanya uso wake uzidi kuvutia. Aliporidhika, akaenda kugonga mlangoni kwa Geb. Geb akafungua. Akabaki amesimama mlangoni akimwangalia. “Naomba lifti.” Geb akacheka na kujiweka vizuri pale mlangoni. Nanaa alijua wazi amefurahi kumuona pale. Na anafurahia anachokiona mbele yake. Yeye.

Akakumbuka alimwambia akimuomba lifti atampeleka popote pale. “Sawa. Nisubiri nimalizie kuvaa.” Geb alikuwa ndio ametoka kuoga. Alikuwa amevaa jinsi na singlendi tu. “Utanikuta jikoni nakupashia moto chakula chako. Ukila ndio tutatoka.” “Sawa.” Geb alishafurahia mpaka uso wake ulionyesha kuna furaha moyoni mwake. “Nanaa!” Geb akamwita. Akageuka kabla hajapotelea jikoni. “Umependeza.” Nanaa akacheka na kujitazama gauni lake hilo. Kwa hakika alikuwa akivaa vitu vya rahisi sana. “Kila kitu huwa kinakupendeza.” Geb akaweka msisitizo kumuhakikishia huwa anaangalia kila anachoweka mwilini mwake.  “Asante.” Nanaa akashukuru na cheko ya aibu kisha akageuka na kupotelea jikoni.

**********************************************

Geb alitoka akiwa na furaha, sio kama yule aliyeamka asubuhi. Akaingia jikoni, akamkuta Nanaa anamsubiria. “Sasa kwa kupendeza huko, unataka nikupeleke wapi?”  Nanaa akacheka. “Kaa chini kwanza ule wakati nakusimulia habari ya tunapokwenda.” Geb akakaa. “Ehee!” Geb akataka Nanaa amuelekeze. “Kuna mahali mpenzi wake Tia, anaitwa Evan alitupeleka. Wakati wao wanakula na kunywa na kuzungumza mambo yao, nikawaomba nitembee mimi mwenyewe kuosha macho. Nikatoka na kutembea kama umbali wa dakika 10 mbeleni. Nikagundua kijiwe changu.” Nanaa akacheka kidogo.

“Pazuri, patulivu. Nilijikuta peke yangu. Nikajisifu kuwa labda mimi ndio wakwanza kupagundua hapo au hamna watu wengi wanaofika hapo. Nikaamua siku nyingine nije kurudi peke yangu. Nikatafuta siku nyingine, nikaenda peke yangu. Nilikaa zaidi ya masaa 4, bila kukutana na mtu yeyote hapo. Basi nikajua ndio sehemu yangu.” “Wapi?” Geb aliendelea kudadisi huku anacheka.

“Sitakwambia mpaka twende ukajionee mwenyewe. Unaweza usipapende sababu tu ya jina la mtaa au hoteli, wakati hilo eneo langu, nililoligundua ni zuri.” Geb akacheka huku akimwangalia Nanaa, msichana aliyeshindwa kushibisha macho yake. “Pazuri. Wewe kula nikupeleke, halafu utakuja kuniambia kama hutakuwa ukiwa unaenda peke yako kila unapotaka muda mtulivu.” “Sawa.” Geb akakubali. Hakujali eneo. Popote kule, ilimradi awe na Nanaa. Vilisikika vicheko huko jikoni. Angalau mama G na Grace wakatulia mioyo.

******************************************************

Wakati Geb anamalizia kula, wakasikia Liz ameingia. Danny akafuata nyuma. “Ngoja niangalie kama kuna mpira. Njoo mama.” Grace alijua ni umbea tu wa mumewe. Na lazima mama yake awepo, ili wakonyezane. Grace yeye akabakia pale pale nje amempakata mwanae. Mama G akaingia, akaenda kukaa kwenye kochi karibu na Danny. Wakawasha tv kwa sauti ya chini ili wasikie kinachoendelea.

“Geb!” Walimsikia Liz akipita kuelekea chumbani kwa Geb huku akimwita. Geb akamwangalia Nanaa, akamuona vile alivyonyong’onyea. Tabasamu lote lilimwisha. Zile dimpozi alizokuwa akifurahia kuzitizamana wakati anaongea hapo jikoni hazikuwepo tena. Alibaki akichora mezani, gafla akamuona ananyanyuka na kutoka pale jikoni. Akarudi chumbani kwake.

“Geb!” Liz akaita tena. “Nipo huku jikoni, nakula?” “Hee! Kwa nini ule jikoni kama msichana wa kazi!?” Liz akaingia. “Ulimaliza kazi?” Akamuuliza Geb. “Ndiyo. Vipi?” “Kuna kitu nataka nikakuonyeshe.” “Nimechoka sana Liz. Nataka kupumzika.” “Mimi nitakuendesha. Wewe utakaa tu wala hutafanya kitu.” Geb alitulia kwa muda kama anafikiria. “Hutachoka Geb! Nakuahidi. Na ukirudi huko, utanishukuru. Ni kitu sahihi kwa kazi ngumu uliyofanya leo.”  Kimya. Wadada wawili wote wanataka kumfurahisha weekend hiyo. Wote wanamuhakikishia furaha mara yakufika huko. “Nani mwenye kisu kikali?”

“Uliniahidi leo utakuwa na mimi Geb. Nimeahirisha mambo yangu yote leo, ili tuwe wote. Naomba usinigeuke tafadhali. Wewe sio mtu wakutoa ahadi ukashindwa kuzitimiza.” Geb akawa amebanwa, akashindwa cha kujitetea. Asubuhi alimwambia ana kazi. Lakini sasa hivi amemkuta msafi na hana kisingizio chochote. “Basi subiri nimalize kula.” “Utanikuta basi hapo sebleni. Si unanijua mimi na jiko? Hatuna urafiki ki hivyoo.” Liz akatoka na kwenda kukaa sebleni wakati Geb anamalizia kula pale jikoni.



*********************************************************

Liz akajiweka kwenye kochi na miguu kakunja 4. Miwani yake nzuri sana ya jua, aliweka kichwani ikashilia nywele zake ambazo kwa asili alijaliwa nywele nzuri. Japo ziliongezwa umaridadi na aina ya dawa aliyokuwa anaweka kichwani. Nakuzifanya nywele hiyo nzito, ianguke mabegani kama sufu. Inang’aa hata gizani. Kuonyeshwa huwa inashugulikiwa kitaalamu.

Alivaa pensi yake nyeupe na blauzi ya kata mikono, nyepesi. Ilifanana na sendozi ndefu za wazi alizokuwa amevaa. Huwezi ukamkuta Liz mahali ukachoka kumtizama. Ungeweza kusema ni mwanamitindo huko Hollywood. Hajikosei. Kila kitu kizuri na garama. Aliupenda huo mwili wake, wenye rangi nyeusi kamili iliyong’aa kama alikuwa akipiga msasa ngozi yake kila mara. Msafi kuanzia nywele, mpaka ukucha wa mguu. Ni ngumu kujua kama huwa anakutana na vumbi. Kimwili chake kizuri. Alipo Liz, utajua kuna neema ya uchumi, elimu na afya njema.



*********************************************************

Akatoa simu yake akaanza kuitumia bila kumsemesha Danny wala mama G. Akainamia simu yake akaendelea na shuguli zake kwenye hiyo simu, wakati mama G na Danny macho yapo kwenye luninga. Harufu na uwepo wa Liz ukatawala pale ndani akimsubiria mpenzi wake.

Geb alimaliza kula, akatoka. Akaagalia ile hali pale sebleni. Mama yake, Danny na Liz. Akabaki akifikiria. Liz akanyanyua macho na kumtizama mpenzi wake. Hakumnyima tabasamu. “Utafurahia na utanishukuru. Twende.” Liz alionekana amechangamka kweli tofauti na alivyoondoka. Wakatoka.

Nanaa akajicheka. Akaamua alale tu ili asianze kuwaza jinsi siku yake ilivyozidi kumsisitizia kuwa yupo mpweke na kila mwanaume ana mwanamke wake. Mungu bariki, akalala hapo hapo. Bila shida.

*********************************************************

Wakati amepotelea usingizini, akasikia mtu anagonga mlango. Akahisi ni ndoto, lakini akaendelea kusikia mlango unagongwa taratibu. Akajua ni chumbani kwake. Akafungua macho, giza lilishaingia nje. Akajua amelala na kupitiliza. Akasimama kwa haraka, akajiweka sawa, akaenda kufungua mlango. Akakuta Geb amesimama mlangoni. “Ulikuwa umelala?” Nanaa akatingisha kichwa kukubali na tabasamu la kinyonge. Bado alikuwa amevaa vile vile kama alivyokuwa amejiandaa kutoka naye masaa machache yaliyopita.

“Nimekuletea Icecream.” Nanaa akatoa tena tabasamu la kinyonge akainama kama anayefikiria. Geb alibaki amenyosha mkono kumkabidhi kopo lake dogo la Icecream. “Nanaa!” Geb aliita kwa upole. “Abee!” Nanaa alinyanyua uso akamwangalia. “Hii ni ice cream yako nimekuletea.” Geb akarudia kana kwamba hakuwa amesikiwa tokea mwanzoni. “Nakushukuru, lakini hapana.” Nanaa alijibu kwa upole huku machozi yakiwa yamejaa ndani ya macho yake. Yakafanikiwa kujaa mpaka kuchirizika nje ya macho yake yaliyokuwa yamejaa huzuni. Akajifuta. “Usiku mwema Geb!”  Akamuaga kwa sauti ya chini kabisa, kama kunong’ona huku akiangalia chini. Akafunga mlango. Akarudi kulala, alimuacha Geb amesimama pale pale nje ya mlango wake na icecream mkononi. 

*********************************************************





Mapenzi yamtatiza Geb. Yu njiapanda. Liz au Nanaa?



Usikose kuendelea kufuatilia Sehemu ya 13 mpaka 25 ya Part 1 ya simulizi hili la  

Is Mine – ni Wangu!

Nani wa Nani? Itakuaje maisha ya Nanaa? Ziko mpaka Part 3, zilizosheni visa vingi vya kusisimua. Endelea kufuatilia.








0 comments: