Lifestyles

*WAZO LA LEO*

Tuesday, August 16, 2016 naomimwakanyamale 1 Comments


Umeshafika mahali, iwe ofisi mpya au makazi mapya, ukahamia pale kisha ukakuta kila mtu analalamikia mazingira ya pale? Awe anaye lalamikiwa ni mwajiri wao, au hali ya uchumi ya mahali pale? Umeshakutana na usemi huu kuwa 'Hapa ni pagumu sana.' Au 'Wenzako wote wamejaribu hiyo wameshindwa. Hata fulani ameshindwa.' Au 'Maisha hayawezekaniki hapa, biashara haziendi.' Au 'Mwajiri huyu ni mkorofi, analipa mshahara mdogo sana.' Wakati wote kabla ya kuanza kazi mnakuwa mmekubaliana mshahara na mwajiri, ndipo unaanza kazi. Au watu hao hao wanao kwambia hapa hapafai unawakuta bado wapo eneo hilo hilo wakiendelea kuishi au kuhangaika kutafuta ridhiki zao, na wala kamwe hawana mpango wakuondoka. 

Yapo madhara makubwa sana, endapo utanyamazia malalamishi hayo. Mojawapo ni kujikuta taratibu sana unaanza kujikuta unakuwa kama wao, au ukajikuta unakuwa na hali mbaya zaidi ya wao. Utaongea kama wao na kujikuta ukilalamika kama wao na baadaye utageuka wewe ndiye mvunja moyo wageni wengine wanao kuja eneo hilo. Kumbuka kila mtu anauwezo au uelewa watofauti. Kushindwa kwa fulani, haimaanishi wote tutashindwa. Au kushindwa kuelewana kwa fulani na fulani, hakumaanishi kuwa watu wote watashindwa kuelewana na mtu huyo.

Jihadhari na mawazo hasi, iwe kazini au kwenye makazi. Jitahidi kutumia akili zako kung'amua mambo. Si vibaya kusikiliza wasemavyo watu, lakini si sahihi kukubali watu wengine kufikia hitimisho la maamuzi yako, hasa yanayochangia maendeleo yako binafsi. Tumeumbwa na uwezo tofauti. Unawezekana ukawa mahali sahihi lakini usiwe na taarifa sahihi. Au ukawa na mawazo sahihi lakini usizungukwe na watu sahihi. Epuka kutaka kukubaliana na kila mtu katika maamuzi yako, hasa unapotaka kujaribu kufanya jambo unalosukumwa mayoni litakuletea mafanikio. Wakati mwingine, wengine watakubaliana na wewe baadaye sana, wakishaona umefanya kitu sahihi, tena zaidi kama umefanikiwa. Epuka kuvuta watu wote kwenye uyafanyayo. Utashindwa kufanikiwa au utachelewa sana.

*KUWA MLINZI WA MAWAZO YAKO MWENYEWE.*

1 comment:

  1. Uko sahihi kabisa wako watu wana PHd ya kukatisha watu Tamaa nasijajuwa huwa wanalipwa na nani kama wewe yanekushinda kaa kando sio kila
    Dereva anajuwa kubadilisha tairi likipata pancha.King Msuya

    ReplyDelete