Story

{...ni Wangu - Is mine} Part 1 - Sehemu ya 1.

Thursday, May 17, 2018 naomimwakanyamale 0 Comments


H
akujua kama ni laana au mkosi unaomwandama katika maisha yake. Kila akijiangalia hakuona tofauti kubwa aliyonayo na wasichana wengi wanao tamkwa ni warembo. Alijua“Sasa kasoro yangu mimi ni nini?” Niswali lililokuwa likimuumiza sana Nanaa, binti aliyekulia kwenye nyumba ya dada wa mama yake, tokea anazaliwa mpaka anakua.
Kwa hakika wakiitwa wasichana wazuri, na yeye akakisimama, hawezi akaambiwa akae. Hata umbile halikuwa na tofauti sana na maumbile ya wasichana wengine wanaofanya wanaume washindwe kujizuia kuwasindikiza kwa macho. Hata ngozi yake ya mwili, si wanaume tu walioisifia kuwa ana rangi nzuri, tena moja mwili mzima, bali hata wasichana wenzake walitaka kujua ni nini anatumia kinachomfanya kuwa na rangi nzuri kiasi hicho.

********************************************

Mama yake Nanaa, Wini, alishika mimba akiwa mwanafunzi wa sekondari ya shule ya wasichana Weru Weru. Wini akiwa binti mdogo wa kidato cha tatu tu, ndipo alipotimiza kusudi zima la kuletwa Nanaa duniani. Ugumu ulikuja kwa Wini, asijue tumbo hilo analipeleka wapi kwa kuwa alikuwa akilelewa na mama ambaye alishawapa msimamo wake tokea wanakuwa. Alishajiwekea misingi na kanuni ambazo aliwahakikishia hazitawahi kuvunjika. Mojawapo ni kutoleta nyumbani kwake mtoto nje ya ndoa, zaidi mtoto huyo akiwa hana majibu yakutosheleza. Kama baba yake.

Haikuwa bure. Mama yake Wini na Maria ambaye ndio dada mkubwa, alishakuwa gumzo pale kijijini. Hakutaka watoto hao watimize kile watu wanachosema juu ya uzazi wake. Baada ya kashfa nyingi akichekwa hapo kijijini, Kirua Vunjo, hapo hapo Moshi. Ilimbidi mama huyo kuangukia kanisani. Alishika dini bila kupenda. Kanisani ikawa ndio kimbilio pekee. Masista na mapadri, wakageuka kuwa rafiki zake hapo kijijini baada ya kuachwa na mumewe. 

Nyumbani kwa Ulimali, yaani baba yake Wini na Maria, na mkewe huyo mkubwa, ilikuwa huzuni kila mwaka. Kama sio mimba ya mama huyo kuharibika. Basi mtoto aliyebahatika kuzaliwa, atakaa siku chache tu, kabla ya kutimiza hata mwezi, tena mara zote wanakuwa watoto wakike, hufariki bila hata ugonjwa. Maria ambaye ni dada yake Wini, mama yake mkubwa Nanaa, ndiye alizaliwa wa kwanza. Hapakuwa na shida. Mara tu baada ya mama huyo kuolewa, akampata Maria. Mzee Ulimali akajipa moyo akijua mtoto atakayefuata, atakuwa wa kiume kama alivyotarajia. Miaka ikazidi kwenda. Vifo vya watoto wa kike vikaongozana, mpaka Mzee huyo akakata tamaa.

Alitafuta mke mwingine. Hakutaka kwenda mbali sana. Alioa hapo hapo kwenye kijiji cha Kirua Vunjo. Lakini safari hii alipata mke upande wa kaskazini, na kumuacha mkewe mkubwa upande wa kusini. Alibahatika kuoa binti mdogo tu. Mkewe huyo wa pili akaanza kwa kuzaa watoto wa kiume mapacha, jambo lililomfurahisha huyo mzee, nakuamua kuachana kabisa na mkewe wa kwanza, ambaye alikuwa na uzazi wa shida, tena wa watoto wakike watupu ambao Mzee Ulimali hakuwataka. Aliwaita hasara.

Wakati Mzee Ulimali anaondoka rasmi kwa mkewe, alimuacha akiwa mjamzito. Mkewe hakutaka kumwambia kwa kuhofia historia kujirudia. Asije akamwambia ni mjamzito, baada ya siku chache mimba ikaharibika, au akaja kuzaa mtoto mwingine wa kike, tena asikae muda mrefu, akafa. Akaamua anyamze na ujauzito wake. Akaachwa na mtoto mmoja tu wa kike, Maria. Ndipo baada ya miezi tisa kutimia, hatimaye ndipo akazaliwa mama Nanaa, yaani Wini, ambaye naye alibahatika kifo cha utotoni. Wini mwenyewe alipatikanika au alizaliwa wakati baba yake alishakimbia nyumba hiyo, aliyosema ina mkosi.

Mama huyo alizalia hospitali ya serikali ya hapo hapo Kirua Vunjo kusini. Akasaidiwa kulea watoto wake hao wawili wa kike na kanisa katoliki la Uchira, yeye kama mwajiriwa wa kanisani hapo. Kanisani kukawa ndio kimbilio pekee kwa mama huyo. Kusali na kwenda kwenye misa, kwao haikuwa ni swali. Ratiba za kanisani zilijulikana nyumbani humo kama wanavyojua majina yao. Kuanzia jumatatu mpaka jumatatu. Asubuhi mpaka jioni. Kipindi cha kwa resma, kufunga halikuwa ni jambo la mjadala. Kulipikwa chakula cha usiku tu wakati wakufungua. 

Dini na maadili yake ndio ulikuwa wimbo ndani ya ile nyumba. Mama huyo alisisitiza kufuatwa bila kukwepa au kukosea. Watoto wake wote walishapitia mafunzo ya komunyo ya kwanza na kipaimara na wakafuzu. Waliijua katekisimu ukurasa kwa kurasa. Walijua Sala za kuombea mambo mbali mbali na mtakatifu nani anasaidia nini ili wamuombe, halafu huyo mtakatifu awaombee kwa Mungu. Kama ni safari, basi walijua wazi, mtakatifu Christopher ndiye mtakatifu sahihi wa kuwa naye safarini. Ikija kwenye kusali rozari, hapo hawakuhitaji hata kufikiria. Walijua wapo kifungu gani, wamtaje nani au watamke nini, bila shida yeyote na bila kukosea. Kwa kuwa sala ilikuwa sehemu ya maisha yao.

Akitaka kusisitizia jamii kuwa yeye hatetereki kwa kuachwa na mumewe sababu ya kuzaa watoto wakike watupu, ambao ni Maria, na Mama yake Nanaa, ambaye ndio Wini, mama huyo wakichaga, alipapambana kufa na kupona kulea binti zake kimaadili na kusomesha. Alimpa mtoto huyo jina la Wini baada ya kufanikiwa kushinda kifo, na kuzaa akiwa na umri wa utu uzima. Sista aliyekuwa akimsaidia kipindi alipojifungua mtoto huyo, ambaye walikuwa marafiki, alimshauri ampe jina hilo la Wini. Kwani alishakaa muda mrefu sana bila kushika mimba baada ya kuzika watoto wengi, wakati Maria mtoto wake wa kwanza akiwa ameshakuwa binti mkubwa tu. Kumpata mama yake Nanaa, aliyefanikiwa mpaka kutoka naye hospitalini akiwa hai, ulikuwa ushindi mkubwa sana kwake. Hata aibu ya kuwa ni mtoto wa kike, iliisha. Baada ya kutoka naye, akarudi naye nyumbani. Mwezi ukapita mtoto huyo akiwa bado hai, ndipo alipombatiza jina la Wini. Lakini akiwa hana mume tena, na anajulikaana anamkosi. 

Watu walisubiri kifo cha Wini, lakini wakashangaa akikuwa mpaka akafaulu vizuri sana kwenda shule ya wasichana Weru Weru sekondari. Mtoto huyo alijulikana pale kijijini kama anaakili sana. Aliwaendesha wakaka aliokuwa nao darasani, kitu kilichofuta machozi ya mama yake.

Mama huyo alifanya kila aliwezalo kutunza binti hao waliokuwa na tofauti kubwa sana ki umri. Hakuwa masikini wala tajiri. Alifanikiwa kuwapa wanae maisha ya kawaida tu. Dada mkubwa alibahatika kupata mume akiwa binti mdogo baada ya kuhitimu chuo chake cha ualimu, akaolewa kwa heshima kubwa sana pale kijijini, wakati bado mama yake Nanaa, Wini yupo shuleni.

************************************************

Mara baada ya Wini kushika mimba, hapakuwa na mjadala. Mama yake alimfukuza nyumbani kimya kimya, kuepusha aibu. Hatimae yale yaliyokuwa yamezungumzwa na baba yao na watu wengine yakatimia. ‘watoto wa kike ni bure kabisa. Wanaishia kuzaa nyumbani tu!’ Ndio usemi huo aliokuwa akiusema baba yao mpaka kuondoka kwake. Akiwa anaficha aibu hiyo, mama yake alimtoa yule binti bila kutaka kujua anakwenda wapi na huku akimuonya asije wahi kurudi tena pale kijijini bila ya ndoa au na huyo aliyempa mimba. “Ukirudi hapa uwe na baba wa huyo mtoto, tena akiwa anakuja kulipa mahari. Akuoe.” Ndivyo alivyoagwa Wini nyumbani kwao.

Wini alitoka kijijini kwao na kuhamia mjini akiwa bado binti mdogo, asiyejua maisha. Akajitupa jijini Moshi akijaribu kupambana na maisha bila mafanikio. Alitoka kwao akidhania angeweza kuishi peke yake, lakini akagundua maisha si rahisi kama alivyodhani. Aliona vile mama yake akihangaika na kazi za shamba na hapo kanisani ambako aliajiriwa, akajua ingekuwa rahisi kwake. 

Wakati anakua, alimuona wakati mwingine mama yake akibeba parachichi na ndizi kwenda kuuza kwenye uzio wa kanisani na mashuleni. Kwa pesa chache alizokuwa ametoka nazo nyumbani, na yeye akaiga. Hakuhitaji mtaji mkubwa kununua sinia na parachichi. Akaanza huku akijiwekea mikakati kama alivyomuona mama yake akifanya wakati anamlea yeye na dada yake kabla ya kuolewa. Ndivyo alivyojua na yeye atapambana mpaka mtoto wake akue. 

Mambo hayakuwa marahisi hivyo. Alianza kutanga tanga jijini Moshi, akitafuta pakuishi bila mafanikio. Kufunga na kufungua akajikuta ni omba omba mkamilifu, asijue chakufanya mtaani. Jua mvua vyote vilikuwa vyake. Hakuna aliyekuwa akimuona yeye kama yeye. Cha kwanza walilitambua tumbo. Binti mdogo, mrembo, mjamzito. 

Kwake siku hazikuwa zikikimbia kama alivyokuwa akisikia kwa watu wengine wakilalamika. Aliweza kuhesabu sekunde, dakika, saa, siku, juma, mwezi akiwa hana tumaini. Maisha yale duni aliyokuwa akiona wanaishi nyumbani kwao na kutamani maisha ya wengine, gafla akageuka kuyatamani sana. Alikuwa akilia nakutamani arudishe siku nyuma ili awepo nyumbani kwao. Hata nyumba ya mama yao akaanza kuona ilikuwa jumba la kifahari, akatamani arudi, lakini alikumbuka jinsi alivyotolewa kwa siri pale kijijini. 

************************************************

Ilikuwa ni alfajiri sana. Mama yake alimpandisha kwenye gari ya kwanza iliyokuwa inapita pale kijijini kwao, ili hata mtu asimuone baada ya usiku uliopita kupata uhakika Wini ni mjamzito. Hakutaka kujua aliyempa mimba wala hakutaka mjadala. Baada ya kuona mabadiliko kwa mwanae huyo aliyekuwa yupo likizo, wakati anakaribia kurudi shuleni, ilibidi kumuuliza. Kwa kuwa alikuwa mkali sana, ilimbidi Wini akiri kuwa yeye ni mjamzito. Mama yule hakutaka kesi. Alimwambia aende kulala. Wini akijua yamekwisha, alishangaa anaamshwa kukiwa hata hapajapambazuka. Akaambiwa akaoge, ndipo alipopewa maneno yake ya mwisho, na kuagwa rasmi hapo nyumbani asiamini kama kweli yamemkuta.

************************************************

 Kitanda cha kawaida sana alichokuwa akilalia nyumbani kwao, akaanza kukiona kilikuwa cha thamani kubwa kila inapofika usiku na kutafuta pakujilaza. Hofu ya kubakwa kila siku usiku anapolala huko mtaani, ikamfanya anze kutanga tanga kila siku usiku akibadili sehemu za kulala ili wahuni wasijue usiku huo alipo. Alihangaika kila sehemu  mpaka dada yake mkubwa alipomchukua na kumuhifadhi nyumbani kwake. 

Tena alimuhifadhi kwa kuwa watu walikuwa wakimsema na kumtaka msaidie mdogo wake aliyekuwa akitangatanga mtaani na ujauzito. Hakujulikana anaishi wapi, lakini alionekana akizunguka mchana akitafuta kazi au msaada kwa ndugu jamaa na marafiki. 

Ndipo habari zikamfikia dada yake, yaani Maria. Alipotolewa nyumbani, mama yake alitangazia kila mtu kuwa Wini alikwenda kwa dada yake huko mjini. Akitoka huko atarudi shuleni moja kwa moja, hatarudi tena pale kijijini. “Dada yake amemwita huko mjini, kabla hajarudi shuleni.” Huo ndio ukawa usemi wa mama yao kwa kila aliyemuulizia Wini pale kijijini. Kwa hiyo kwa pale kijijini ikawa mama huyo ametoa balaa hilo, la aibu kwa muda. Hakuna aliyejua kama Wini alikuwa mjamzito.

Isipokuwa majiraji wa chache wa dada yake pale pale mjini. Walikuwa wakimuona Wini akimfuata dada yake kazini kuomba msaada hata wa pesa ya kwenda kula. Mwanzoni Maria alidanganya walimu wenzake kuwa hamfahamu ni nani. Lakini ikawa ngumu. Rangi zao za mwili zilifanana sana. Wakachukua umbile linalofanana na mama yao. Kuanzia urefu na muonekano mzima wa nje. Maria na Wini walifanana kwa asilimia kubwa, japo Wini alikuwa mdogo sana kwa Maria. 

Wini alikuwa akihangaika. Akiona amekwama kabisa, njaa imemlemea, alikuwa akikimbilia kazini kwa dada yake aliyekuwa akimsema sana ndipo anamsaidia vijisenti kidogo. Dada yake alipoacha kazi, akahamia kuomba msaada pale nyumbani kwake. Wakati mwingine alikuwa akifika hapo nyumbani kwa dada yake kwa kujiiba. Anajificha mpaka ahakikishe shemeji yake hayupo ndipo anamfuata msichana wa kazi, ataomba hata kiporo. Akishakula, anaondoka kwa haraka sana ili shemeji yake asimkute nyumbani kwake kwani alishampiga marufuku yeye na dada yake. Akikataa kabisa Wini kukimbilia pale. Alimtaka Wini arudi nyumbani kwao, akaombe msamaha, atulie kijijini baada ya kushindwa shule kuliko vile anavyotangatanga mjini. Na hapo ndipo majirani na wafanyakazi wenzake Maria, ndipo walipomuona Wini na kujua kama ni ndugu na Maria.

************************************************

Lakini huo haukuwa wakati wa dada yake, Maria, kumkaribisha mtu yeyote aende kuishi nyumbani kwake. Kwanza ndio na yeye alikuwa kwenye bed rest ya mimba aliyokuwa ameitafuta kwa takribani miaka 10, tena kwa shida sana.

Dada huyo ambaye alikuwa kwenye ndoa ya muda mrefu, alijaliwa mtoto wa kwanza wa kiume. Wakamwita James. James alikaa akiwa mtoto wa pekee kwa muda mrefu sana huku wazazi wakihangaika kutafuta watoto wengine lakini baba yake, au mumewe Maria akiwa hana pressure sana, kwani tayari analo dume lake, James. Shuguli ilikuwa kwa Maria akitaka watoto wengine. Alikumbuka shida alizokuwa akimuona mama yake akipata wakati akitafuta watoto, akazidi kuchanganyikiwa. Hakutaka apitie huko. Lakini angalau yeye alitanguliza mtoto wa kiume. Ikawa nafuu kwenye ndoa.

 James alipatikanika mwaka wa kwanza tu baada ya wazazi wake kufunga ndoa. Ilikuwa faraja kubwa sana. Baada tu ya kujifungua James, Mama yake na Wini akiwa bado mdogo, walifika hapo mjini kumsaidia kumlea Maria. Baada ya siku chache alimchukua Maria na mwane huyo mchanga James, na kurudi naye kumlea kipindi hicho cha uzazi pale kijijini. Wakaomba James abatizwe pale pale kijijini kwa bibi yake. Angalau tu kusuta watu na kuwaonyesha watu kuwa hakuwa na uzazi mbaya. Mume wa Maria alikuwa na kazi nzuri. Alijijenga mjini maeneo ya Majengo. Kwa hiyo muda Maria yupo pale kijijini analelewa uzazi, ndio Wini naye yupo binti mdogo tu. Baba yake James akaweka heshima pale kijijini. Kulikuwa kukimwagwa vyakula hapo. Na siku ya ubatizo wa James, kukachinjwa na ng’ombe, watu wakaalikwa. Wakala na kunywa mbege mpaka wakachoka. Bia zakueleweka zilikuwepo. 

Ukweli Maria alimpa heshima mama yake. Maria ukawa ndio mfano anaoimbiwa Wini tokea anakuwa mpaka anafukuzwa kwao. Ni kweli Maria alifanana zaidi na mama yao hasa, tabia. Wote walikuwa wazungumzaji sana. Na walipendana na mama yake kama marafiki. Ukiwakuta Maria anazungumza na mama yake, utafurahi. Ungejua ni marafiki walio shibana. Kwa mshahara wake wa ualimu, hakuacha kumsaidia mama yake kumtunza Wini. Tena alipoolewa na mume mwenye uwezo. Ndio kila mtu alijua. Maisha ya mama huyo yakaleta aghueni kubwa sana.

************************************************

Lakini baada ya kumzaa James. Kipenzi cha bibi yake. Maria alikaa miaka 10, akihangaika kila mahali kutafuta watoto. Huku akikumbuka kashfa na adha ya mama yake aliyomuona akipitia mpaka baba yao kuwakimbia, wakati anakuwa. Hofu ya kuolewa mke wa pili au kukimbiwa, ikaanza kumtesa. Mama yao alizunguka kila mahali na Maria, kuhakikisha anashika mimba ya pili. Hakuta kile alichopitia yeye, ndio Maria apitie. Alihakikisha kule kote alikoshindwa kupita yeye kusaka mtoto, ndiko anakompitisha Maria ili kumsaidia kupata mtoto. James akageuka kuwa mtoto wa bibi kipindi hicho mama yake anahangaika na uzazi.

************************************************

Mwaka huo mama yake Nanaa anafukuzwa nyumbani, ndio na dada yake naye alikuwa ameshika mimba. Akawa radhi kuacha kazi na kuchukua bed rest ya ujauzito wa mtoto aliyemtafuta kwa shida sana. Wakati Wini anahamia kwa dada yake akiwa na mimba ya miezi 6 anaelekea 7, dada yake ndio alikuwa amebakisha siku chache ajifungue. 

Wakati mtoto wake wakiume James alishatimiza miaka 10 anatafuta 11, ndipo akajifungua mtoto mwingine wa kike. Wakampa jina la Viola. Na ndipo baada ya miezi mitatu baadaye, binti huyo mdogo, yaani mama yake mdogo James na Viola, Wini, akiwa hajulikani mwenye mimba hiyo ni nani, akapatwa uchungu mida ya saa tatu usiku. 

Alihangaika mwenyewe chumbani akitaka asisumbue wenye nyumba wake. Hasa shemeji yake aliyetamka wazi wazi na yeye hamtaki mle ndani. Lakini muda wa mtoto kutoka au kuzaliwa ukifika, umefika tu. Hauchagui mazingira wala ulipo. Haujali hali ya mama aliyonayo wakati ule. Akitakiwa kutoka duniani, lazima atoke. Alihangaika mpaka usiku sana chupa ikapusuka akiwa peke yake chumbani. Alishtuka alipoona damu zinatoka, ndipo akaenda kumgongea dada yake. Akakimbizwa hospitalini. Akaingizwa chumba cha kujifungulia, lakini binti huyo mdogo, yaani mama yake Nanaa hakufanikiwa kutoka humo kwenye chumba cha kujifungulia, akiwa hai. Hata hakubahatika kumnyonyesha Nanaa. Alipata matatizo ya uzazi, akafariki wakati daktari wa zamu alipokuwa akimsaidia kumtoa mtoto. Damu chache aliyokuwa nayo Wini, iliendelea kumwagika mpaka mauti ilipomfika.

*****************************************************

Ndipo ilipobidi Maria, dada yake Wini arudi na huyo mtoto, nyumbani bila kutarajia. Jina hilo la Nanaa, Wini alimuachia James, mtoto wa dada yake. James alikuwa akijisogeza sana karibu na Wini wakati yupo nyumbani kwao. Siku moja alimfuata mama yake mdogo, akamuuliza mtoto akizaliwa ataitwa nani, akamwambia Nanaa. Baada ya mtoto kurudishwa nyumbani, Maria akiwa amechanganyikiwa. Hajui chakufanya na huyo mtoto asiye na mama wala baba, ndipo James akawaambia wasimwite tu mtoto, anaitwa Nanaa. Kila mtu alimshangaa James. Lakini alionekana anauhakika na huyo mtoto. Ndipo kuanzia hapo akaanza kuitwa Nanaa.

Alilelewa kwa shida sana kwani alikuwa ameingilia penzi la mtoto aliyetafutwa kwa shida na mume wa Maria alikuwa akimuhesabia Wini siku ili atoke nyumbani kwake. Alimruhusu Wini kujifungua tu, kisha akamwambia mkewe baada ya hapo anataka Wini aondoke na mtoto wake. Wakati Viola mtoto wao anatimiza miezi mitatu ndio Nanaa alizaliwa na kuachwa akiwa hajulikani baba, ila mama aliyefariki. Kwa hiyo ikabidi siku za mwanzoni na yeye kunyonyeshwa kama Viola na mama huyo ambaye aliona mtoto wake anapunjwa. Huku mumewe akimlaumu mkewe kumpokea Wini, mama yake Nanaa tokea mwanzoni. Kila Nanaa alipokuwa akilia wakati mdogo, mumewe alitoka nje kabisa akisema hataki kusikia sauti ya mtoto huyo. Alimlaumu mkewe kuleta matatizo ndani ya ile nyuma.

Nanaa alikataliwa hata kwa bibi yake. Mama yake Maria na Wini alikataa kata kata huyo mtoto kurudishwa pale kijijini. Alikataa hata kumtambua kama ni mjukuu wake. Baba yake James, ambaye ni mume wa Maria, alikuwa akimsimanga mkewe, mchana na usiku. “Kama hata mama yake mzazi alimfukuza, kwa nini wewe ulimpokea? Huyo binti ni tatizo mke wangu. Unajitafutia balaa.” Hayo ndiyo maneno aliyokuwa akiyapata kutoka kwa mumewe wakati wa uhai wa Wini. Tena mbele yake. Mbaya zaidi ni pale mdogo wake alipofariki. 

Ni kweli balaa likatokea. Akaachiwa mtoto ambaye hawakujua pakumpeleka. Mumewe alisema sana. Kwani hata mazishi ya Wini ni kama yalifanywa na rafiki za dada yake. Mumewe alikataza kabisa maswala ya msiba nyumbani kwake. Maiti ya Wini iliagwa katika hospitali ya taifa KCM na kupelekwa makaburini. Alizikwa kimya kimya, bila ibada wala mama yake kuwepo. Ni kama alitupwa tu, habari ikaisha.

Baada ya kuzunguka na huyo mtoto akitaka amtoe pale ndani na kushindwa, ndipo ikabidi amlee Nanaa mle mle ndani. Lakini kwa shida sana. Mumewe alikataa kumsaidia kabisa. Hakutaka hata shilingi yake kumtunza huyo mtoto aliyejua ni balaa ambalo mkewe amelileta ndani ya hiyo nyumba. Watu walisema mama yake Nanaa alikufa sababu ya kulaaniwa na mama yake. Kwa hiyo hata Nanaa, amebeba mkosi.

*****************************************************

Kwa shida, dhiki na mateso, Nanaa akakua. Alikula chakula kama watu wote mle ndani. Alinunuliwa nguo pale inapolazimu, hasa sare za shule. Lakini mara nyingi alivaa nguo za watoto wa mama yake mkubwa pale zinapokuwa ndogo kwao au mama huyo anapotaka kubadilisha nguo za mwanae Viola, ndipo alipopewa Nanaa. Kwa Nanaa hakuona shida, kwani alikuwa akikua akiona hivyo. Na tangia anapata uelewa wake, akiwa mtoto mdogo sana, mama huyo alihakikisha anamuelewesha Nanaa na kuelewa kuwa pale alipo anasaidiwa tu. Kwa hiyo Nanaa alikuwa akijua anasaidiwa tu. Na alisimuliwa vile alivyokuwa ikimlazimu mama huyo kukesha kumlea yeye, badala ya kupumzika na mumewe. Kwa hiyo kila alichokuwa akipewa Nanaa, alishukuru sana na kufurahia.

Alishajua hastahili chochote mle ndani. Yeye anasaidiwa tu. Tena aliaminishwa pale alipo ni sehemu ya thamani sana kwake, kwani alikataliwa kila mahali. Hata bibi yake alimkataa. Alimuona hata akifika pale hataki kumgusa wala hata kuzungumza naye. Alikaa naye mbali kabisa huku akimkaripia kila akimsogelea. Alimuona bibi yake vile anavyompenda Viola, mjukuu wake aliyemuhangaikia sana mpaka kushikwa mimba yake. James ndio alikuwa kipenzi kabisa cha bibi huyo. Na hata Nanaa alijua. Yale mazingira yote yakamfanya kuelwa na kujua ni kweli pale alipo ni sehemu sahihi, na yale ni maisha anayopaswa kuyatumikia vizuri. 

Usingemkuta akilalamika kama anateswa. Hakujua maisha mengine zaidi ya yale aliyokuwa akiishi pale kwa mama yake mkubwa. Kwa hiyo akajua inamlazimu kuishi vile. Tena alitakiwa kushukuru sana. Ila kadiri alivyozidi kukua na kuona mapenzi anayopewa Viola na wazazi wake, kitu kipya kikaanza kujengeka ndani yake. Ikaanza kuibua shauku ya kutaka kupendwa na kuthaminiwa na yeye kama Viola. Lakini hakuacha kukumbushwa bahati aliyoipata baada ya mama yake kumuacha na mama yake mkubwa kumpokea. Kwa upande mwingine, ikabidi awe mpole.

**********************************************************

Walipofikisha miaka miwili tu, Viola akiwa amemtangulia kwa miezi 3, mama mkubwa akapata mimba ambayo hakutegemea. Akazaa mtoto wa kike mwingine ambaye alimwita Vai. Hapo ndipo Nanaa alipokuwa mtu mzima gafla. Akaanza kutumwa hiki na kile kumsaidia mama mkubwa kulea mtoto huyo mchanga. Baada ya muda mfupi mtoto huyo mdogo, aliyekuwa akilingana kabisa na watoto wake akageuka kuwa mtumwa, akiwatumikia wanae wote mle ndani. Nanaa akageuka kuwa mkubwa kuliko hata James. Alibeba majukumu makubwa kuliko wenzake, na akalinganishwa na msichana wa kazi.

Nanaa alisoma shule za kawaida za serikali, lakini wenzake walisoma shule za kulipia. Walikuwa wakifuatwa na basi la shule pale nyumbani, yeye ilimlazimu kuamka mapema kama anavyoamka msichana wa kazi pale nyumbani, ambaye alikuwa akilala naye chumba kimoja. Anaandaa kifungua kinywa na kusaidia usafi, baada ya kula ndipo awahi shuleni akitembea kwa miguu. Na jioni anapotoka shule, ilimlazimu kusaidia kazi za pale ndani. Ikiwemo kupika, kunyoosha nguo za wazazi wa mle ndani, na ndugu zake kama alizilifua siku hiyo asubuhi, na kuwawekea vyumbani kwao, na kusaidia kazi nyingine za mle ndani. 

Kama ungelimuuliza Nanaa kuwa anateswa, asingesema anateswa. Aliambiwa anawajibika kufanya yote hayo ili baba yake mkubwa asije kutafuta msichana mwingine wa kazi, akachukua nafasi ya kuishi yeye mle ndani. Kwa hiyo alipambana kwa kadiri ya uwezo wake kuonyesha hamna kazi ya kuhitajika msichana wa kazi wa pili mle ndani. Yeye na msichana wa kazi, wanatosha kabisa, kumudu kazi zote za mle ndani. Mwanzoni majukumu ya kuwahudimia wenzake yalimlemea sababu ya umri mdogo na kazi nyingi. Lakini kadiri siku zilivyozidi kwenda na umri uliposegea, akaweza kumudu majukumu yake vizuri, hakuona shida tena. Alijipendekeza kwa kadiri ya uwezo wake ili kuwafurahisha walezi hao ambao baba mwenye nyumba hakuwa hata na muda naye.

************************************************

Mida ya jioni walikuwa na utaratibu wa kula pamoja, na kila mwenye habari zake huo ndio muda wakuziongea na kucheka kabla ya kwenda kulala. Kina Viola walikuwa wao ndio wenye habari za kuvutia kwani walisoma shule za kisasa na walikutana na watoto wa matajiri, lakini sio Nanaa. Kwanza anakuwa amechoka, na pili alikuwa akiomba wamalize mazungumzo hayo mapema ili wakamalizie kazi za siku hiyo na wao wapumzike. Yeye Nanaa na dada wa kazi ndio walikuwa wa mwisho kulala ili kuhakikisha sinki la jikoni halilali na vyombo vichafu na jikoni panaachwa pasafi kila siku.

Muda wa kuangalia tamthilia ukifika, watu wote walikusanyika sebleni wanaangalia tamthilia pamoja. Mama yake mkubwa alikuwa mcheshi sana, maneno mengi hayakuwa yakimwisha. Basi huo nao ukawa muda wake wa kuchekesha kila mtu mle ndani. Baada ya watoto wake kukua, alijitupia kwenye biashara. Hakuweza kurudi tena kwenye kazi yake ya mwanzoni, ya ualimu.

Alikuwa na maduka ya nguo na vipodozi anayomiliki hapo mjini. Kwa hiyo alikutana na watu wengi tofauti tofauti na vituko vingi alivyokuwa akisimulia arudipo nyumbani kila siku. Mumewe alikuwa meneja wa kampuni ya kahawa pale pale jijini Moshi. Aliweza kuongeza kipato hapo nyumbani, nakufanya maisha ya familia yake kuwa mazuri. Lakini alihakikisha pesa yake au jasho lake linakwenda kwa wanae aliowazaa yeye tu, na si vinginevyo. 

Alijulikana kama mwanaume mbahili, lakini si kwa watoto wake. Tokea Nanaa anazaliwa na kuletwa pale nyumbani, alishawekeana makubaliano na mkewe, huyo mtoto wa nyongeza sio jasho lake na yeye hatahusika kwa lolote. Kwa hiyo Nanaa aliishi pale, lakini akihudumiwa na mama yake mkubwa huku akikumbushwa mara kwa mara tokea mtoto anasaidiwa tu. Na kila pesa iliyotumika kwake kibinafsi, aliambiwa ni kiasi gani na ni jinsi gani ilivyomgarimu mama yake mkubwa. Iwe ni ada au michango midogo midogo aliyotakiwa kupeleka shuleni. Tena shule yenyewe ilikuwa ya bure ya serikali. 

Lakini ilikuwa lazima awekwe chini na kuelezwa ugumu wa pesa alionao huyo mama. Majukumu mazito yanayomkabili yeye kama mama mwenye watoto watatu wenye mahitaji kama yake Nanaa, lakini anawanyima wanae, au anajinyima yeye, au anashindwa kumsaidia mama yake mzazi kule kijijini, inabidi apewe pesa hiyo yeye ambaye baba yake hakujulikana na mama yake alishafariki bila hata kuacha usia wowote ule. Kwa hiyo Nanaa alikuwa akikuwa akijijua yeye ni mzigo kwa mama yake mkubwa, na inamgarimu sana kuwepo pale na kumsaidia.

************************************************

 Japokuwa hapakuwa na mateso ya moja kwa moja ambayo mtu anaweza kulalamika kuwa anateswa, lakini yale maisha yaliendelea kuibua shauku mbali mbali ndani ya Nanaa. Akitamani kuwa na chake au mtu anayemuhitaji, asiyemuona mzigo wala kumlalamikia kwa kila kitu. Ni kweli hakuwa akiteswa kwani alitakiwa kufanya kazi kama watoto wengi wanavyokuzwa, japo wenzake hawakuwa wakifanya kazi pale nyumbani. Alitakiwa kuamka asubuhi na mapema, kama mtoto mwingine yeyote anayepewa malezi mazuri ya kufundishwa maisha, japo ilimlazimu yeye kuamka kuwaandalia mazingira mazuri wenzake kina Viola na Vai, wenye umri mmoja au wakubwa kidogo, ili waende shule wakiwa hawajachoka. 

Alikwenda shule kwa kutembea tofauti na wenzake, lakini hilo pia aliambiwa ni baba yao ndio anawalipia usafiri wa kuwaleta na kuwarudisha shule, yeye Mama Mkubwa hana pesa ya kumsomesha huko wanakosoma wenzake, kwa kuwa inabidi kununua chakula cha kutosha na yeye ale vizuri na alale vizuri. Nanaa hakuwahi kulalamika. Akaelewa ni kweli anatakiwa kuwa mtu wa shukurani. Tena wakati mwingine alifanya kwa ziada ili kumfurahisha mama yake mkubwa. Alijitahidi sana kufanya kazi pale ndani ili kumfanya Mama Mkubwa akitoka kazini apate muda wa kupumzika tu. Kila alipokuwa akirudi nyumbani, Nanaa alimuwahi na kikombe cha chai, au maji na ikitokea kuna juisi, basi alimpa Mama Mkubwa hiyo juisi na tabasamu kubwa usoni lililojaa unyenyekevu huku akitoa pole na kupokea mkoba.

Alijitahidi sana asiwe tatizo mle ndani ya nyumba. Kila wakati alikumbushwa yaliyompata mama yake. Akajitahidi kutulia kabisa. Hasa katika mapenzi. Japo Mama Mkubwa alisharuhusu kama kuna mmoja wao amepata mwanaume, basi ahakikishe huyo mwanaume anafahamika hapo nyumbani. Alitoa ruhusa ya kuletwa pale nyumbani afahamike. Aliwaambia binti zake kuwa hiyo itasaidia kuongeza heshima kwa huyo mwanaume. Kwa hiyo hata kama alikuwa na wazo la kumchezea tu, kama mama yake Nanaa alivyochezewa, basi huyo mwanaume ataogopa. 

****************************************************

Japokuwa ni kama walilingana na Viola mtoto wa mama yake mkubwa, lakini mwenzake alimpita mbali sana kimakuzi. Alizungumza lugha ya kingereza kwa ufasaha. Alikuwa binti mwenye kujiamini. Alisoma shule nzuri. Alijua kuzungumza mbele za watu bila shida na alishaleta wanaume pale kwao kama marafiki, tena vijana wazuri tu na wanaonekana wasomi kama yeye mwenyewe Viola na Vai. Na Nanaa alihusika katika matayarisho ya pale ndani ikitokea Viola na mdogo wake wanataja siku ya wanaume zao kufika hapo nyumbani.

Nanaa alikuwa akiwatamania wenzake waliofanikiwa kupata wazazi wanaowapenda na kuwajali, na pia isitoshe, walibahatika kupata wanaume wazuri. “Na mimi nikija kumpata mwanaume wangu kama huyo kaka, nitampenda sana. Nitahakikisha tunaoana naye ili tukizaa watoto wetu tuwalee wenyewe wasihangaike au kusumbua watu kama mimi. Tutaishi kwenye nyumba yetu nzuri na watoto wetu wazuri, tuta..” Ni mikakati aliyokuwa akijiwekea Nanaa kila siku alipokuwa akikaribisha wanaume wa Viola na Vai. 

Alikuwa akimshangaa Viola vile anavyochezea bahati. Alipata bahati ya wanaume waliompenda lakini hakuwa kuridhika. Hawakukosa kasoro. Akaishia kuwabadilisha mchana na usiku huku akieleza vituko vyao na kuwafanya hata mama yake acheke, kama jambo la kawaida tu.

***************************************************

Mpaka Nanaa anamaliza kidato cha nne, katika shule za kutwa. Hakuwa akimjua mwanaume kimapenzi. Alipata vishawishi vingi. Zikiwemo lifti za kurudishwa nyumbani. Walimu na wanafunzi wa shuleni hapo Old Moshi sekondari. Wakimpa ahadi nyingi zakuvutia, lakini Nanaa akafunga moyo. Akakana nafsi yake, akamaliza kidato cha 4. Alifaulu kwenda kidato cha 5. Akachaguliwa katika shule ya wasichana Ashira. 

Ilikuwa furaha kubwa moyoni mwa Nanaa. Angalau anakwenda kuanza maisha sehemu nyingine, mbali na nyumbani hapo kwa mama yake mkubwa. Akaanza kuonja ladha ya maisha mapya. Akafurahia utulivu aliokuwa akipata mbali na kelele za pale ndani kwa kina Viola ambazo alikuja kujua upo uwezekano wa kuishi mahali pengine na ukafurahia maisha mengine mbali na maisha aliyoaminishwa ndio maisha pekee hapa duniani. Shule akawa mkombozi wa kwanza wa Nanaa. Ikampa ladha ambayo hakutarajia. Moyo wake ukapenda na kuthamini zaidi elimu. Akajiambia shule ndio mkombozi wake.

Akaanza kupendeza na kuvutia. Shule hiyo iliyokuwepo juu kabisa ya kimlima kikali cha Marangu, kwake ilikuwa ni mbingu ndogo. Hakuwa akitamani shule zifungwe. Hakuwa akielewa wanafunzi wengine waliokuwa wakilalamikia maisha ya pale shuleni. Alituliza akili zake zote shuleni. Baada ya muda mfupi tu, akapata na rafiki ambaye ndio aliongeza ladha nzuri zaidi ya maisha hapo shuleni. Aliitwa Anni. Wakaanza kuongozana kila mahali na Anni.



Nanaa na Alex.
Siku moja Anni alitembelewa na kaka yake Alex. Akamtambulisha Nanaa kwa kaka yake. Alex akampenda sana Nanaa. Akaanza kutafuta sababu za kuwepo Shuleni hapo kwa kisingizio anakwenda kwa dada yake. Kila wazazi walipotaka kumtumia kitu Anni shuleni, Alex akawa mtu mzuri sana wakujitolea kwenda Ashira kupeleka mahitaji ya dada yake. Hakujali mlima huo wa Marangu kufika shuleni hapo, nia ni kumuona na Nanaa. Ukaanza urafiki kati ya Nanaa na Alex pia.

Safari za Alex kumtembelea Anni dada yake Ashira zikawa nyingi. Nyumbani kwa kina Alex na Anni ilikuwa Arusha. Kwa hiyo Alex akapata sababu nzuri sana ya kila siku za jumamosi kuwepo kwenye shule hiyo ya wasichana Ashira, tena akigaramiwa na wazazi wao, wakijua anakwenda kumtembelea Anni, binti yao mdogo.

Hisia za kimapenzi zikaanza. Nanaa akavutiwa na ujio wa mara kwa mara wa Alex kwenda kuwatembelea. Lakini Alex alisisitiza huwa anakwenda pale maalumu kwa ajili yake yeye. Nanaa akaona ni upendo ulioje? Arusha mpaka Marangu! Tena kupandisha kilima kikali kile ili kumfikia yeye tu, hakika Alex akawa ni kijana mwenye mapenzi ya dhati.

Shauku kubwa ya Nanaa, ilikuwa kupata mtu atakayeonyesha anamuhitaji. Hakujali sura wala umbile. Yeyote yule atakayemuhitaji, basi alijiapia kujitoa kwake. Sasa kumpata Alex aliyeonyesha utayari wa kuvunja ratiba zake zote, ili awe naye. Ilimgusa sana. Akajua yeye ndio atakuwa mwanaume wakumtoa pale nyumbani kwa mama yake mkubwa. Amuoe, kisha wakaishi naye popote kule Mungu atakapowajalia. Ampunguzie mzigo mama yake mkubwa na kuepuka chuki ya baba yake mkubwa ambayo wala hakuhitaji kuificha. Alimuonyesha kila mtu waziwazi, kuwa hataki kujihusisha na huyo mtoto.

Mahusiano ya mapenzi yakaanza. Nanaa akamwaga moyo wake wote kwa Alex, akionyesha wazi yupo tayari kufanya lolote kwa kijana huyo. Kama ulishaona wanawake desparate hapa duniani, basi Nanaa aliwashikia bendera. Akawa kama aliyechanganyikiwa na Alex. Naye Alex akaonyesha kumuhitaji vilivyo. Kwa mara ya kwanza, Nanaa akapata mtu baki, mbali na kaka yake James, anayempenda na kumjali. Akapata faraja ya ajabu moyoni. Akapata mwanaume wa kwanza, mbali na James, anayeweza kukaa naye na kumsikiliza. Mwanadamu anayefunga safari, kupandisha mlima mkali wa Marangu, kwenda kumuona yeye! Kwake lilikuwa jambo la faraja sana.

Anni alipokuja kugundua, akaamua awe anawapa nafasi. Alex anapokuja shuleni, anafikia Ashira B, atajificha sehemu ambayo alikuwa akikutana na Anni na Nanaa. Anni  atamsalimia kaka yake na kuchukua mizigo yake, na kuwapisha. Yakaanza mabusu yakuagana. Akifika tu shuleni hapo, wa kwanza kuitwa ni Nanaa, ndipo ataitwa mdogo wake. Yakaja na mabusu ya kukaribishana. Moto wa mapenzi ukawaka ndani yao. Wakaona hawatosheki kwa mabusu. Tena mbaya zaidi mabusu yenyewe hayakuwa ya muda mrefu sababu ya mazingira. Wote waliona hamna sababu yakusubiri tena, wakakubaliana kipindi cha likizo fupi, kabla Nanaa hajarudi nyumbani, watafute chumba mahali, watumie siku hiyo kuridhishana, kisha jioni ndipo aende nyumbani akijidai ndio ametoka shuleni.

Na ikawa hivyo. Nanaa akiwa hamjui kabisa mwanaume kwa umri huo akiwa kidato cha 5, akaamua kugawa bikra yake kwa Alex. Haikumsumbua wala dhamira haikumuuma kwani walikubaliana kuona mara Alex atakapo maliza chuo. Alex alikuwa chuo cha uhasibu Arusha. Ndio alikuwa mwaka wa 1, wakati Nanaa yupo kidato cha 5. Kwa hiyo Nanaa alikuwa amejitoa kwa moyo mweupe kwa mwanaume atakayekuwa mumewe pindi atakapo maliza chuo hicho. “Hata hivyo sifanyi kosa kama mama. Mimi nafahamika na Anni dada yake. Halafu Alex sio muhuni kama mwanaume aliyemrubuni mama. Mimi nitakuwa mwangalifu, sio kama mama. Siwezi shika mimba.” Hayo ndio maneno aliyokuwa akijifariji nayo Nanaa anapokwenda kujifungia nyumba za wageni na Alex.

Kwa kuwa hakukamatwa mara ya kwanza, basi wakajenga mazoea ya kukutana mahali, nakutumia siku nzima kufanya mapenzi, ndipo Nanaa anarudi nyumbani. Mwaka wao wa kwanza wa mapenzi ukaisha vizuri. Nanaa anapokuwa likizo, basi mawasiliano hayakukauka. Alex akiwa jijini Arusha, Nanaa nyumbani kwao Majengo, hapo hapo jijini Moshi. Wakati mwingine akiwa likizo, Alex alikuja Moshi kumtembelea Nanaa. 

Siku za kufungua shule zinapofika, Alex alimsubiria Nanaa mjini, akiwa ameshachukua chumba mahali. Nanaa anakwenda hapo. Wanatumia siku hiyo wakiwa wawili, kisha jioni Nanaa anakwenda shuleni, au analala mpaka kesho yake ndipo anakwenda shuleni. Na siku za kufunga shule hivyo hivyo. Alex alimfuata mpaka shuleni. Anamchukua asubuhi hiyo, wanakwenda Moshi mjini. Wanachukua chumba kwenye nyumba za kulala wageni. Mpaka jioni ndipo Nanaa anarudi nyumbani na kuendelea kwenda kumtembelea Alex hapo hotelini. Atamtumikia mwanaume huyo bila kuchoka, mpaka anapoondoka kurudi kwao Arusha.

Penzi likakolea. Alex akawa anapata anachokitaka kwa Nanaa, japo kwa upande wa Nanaa, yeye mapenzi hayakuwa muhimu. Hakujali kama anafurahia yale mapenzi. Ilimradi alipata mtu atakayemtoa kwenye yale maisha. Ni kweli hapakuwa na shaka kama watakuja kuona pindi watakapomaliza shule. Alex alishamuhakikishia maisha mazuri mara baada ya kuona. Basi Nanaa alitoa mwili wake kwa Alex kama mumewe huku akiwa mwangalifu asishike mimba, asije zaa kabla ya kufunga ndoa. Wakachagua majina ya watoto wao. Wakapanga idadi na jinsia ya watoto watakao zaa. Penzi likaendelea mpaka Nanaa alipomaliza kidato cha 6. Akaona ndio muda muafaka na yeye kupeleka mwanaume nyumbani kwao.

***************************************************

Wakati Nanaa anapanga kumpeleka Alex nyumbani, alikuwa ndio anajiandaa kwenda kumaliza mwaka wa mwisho chuoni. Nanaa na Viola ndio walikuwa wamemaliza kidato cha sita, wapo nyumbani wanasubiria matokeo yao. Baada ya kumaliza tu shule yake ya kidato cha sita, Viola akaenda jijini Dar kumtembelea James, kaka yake. Alikaa kwa muda kidogo tu, ndipo Vai naye baada ya kufunga shule akamfuata Viola dada yake. Wote waliondoka huku wakimringishia Nanaa kuwa wanaenda jijini Dar, kwenye starehe. Yeye anatakiwa abaki asaidie kazi za mle ndani. 

Nanaa alitamani sana na yeye aongozane nao, angalau akapaone tu Dar, au atoke nje ya mkoa wa Kilimanjaro, lakini mama mkubwa alimkatalia. Kwanza alimwambia hana pesa ya kumpa ya nauli halafu anamajukumu pale nyumbani. Hawezi kumruhusu asafiri. Nanaa akaridhika. Akabaki mle ndani akifanya kazi. Siku Alex alizoweza kwenda kumtembelea, basi Nanaa ilimlazimu kutoroka nyumbani mida ya mchana ambayo mama yake mkubwa yuko kwenye majukumu yake ya kila siku, anakwenda kumuhudumia Alex huko hotelini. 

*****************************************************

Maisha yakaendelea. Nanaa akitafuta wakati mtulivu wakumtambulisha Alex kwa mama mkubwa. Kila mama mkubwa aliporudi nyumbani, hakuacha kueleza starehe wanazopata wanae huko jijini Dar kwa kaka yao James na vile kaka yao anavyowafurahia. Ikawa hamna nafasi ya mtu mwingine kuzungumzwa pale ndani, wala kusikilizwa. Ni matambo ya mama mkubwa tu, kwa wanae huko jijini Dar.

Siku wasiyotarajia, kabla hata shule ya Vai haijafungua, akaona Viola na Vai wanarudishwa pale nyumbani na kaka yao James. Alimuona James akizungumza na mama mkubwa, lakini hakujua kulikoni. Lakini akamuona kaka James akiondoka bila mmoja wao.

 Nanaa akafurahi kuona wamerudi, akajiambia ule ndio wakati wa kumtambulisha kwao Alex, ili wasiendelee kumdharau. Ilikuwa ndio kwa mara ya kwanza na yeye Nanaa ana habari njema kama wenzake ya kupeleka mwanaume anayempenda nyumbani kwao. Kwa muonekano Alex hakuwa mbaya. Aliweza kutambulishwa kokote bila shida. Swala la kuwa analafudhi ya kiarusha ikawa ni mojawapo ya kivutio kwa Nanaa. Wala hakujali. Na ukichanganya pesa ya wazazi wake, basi Nanaa alijua lazima ataweka heshima hapo nyumbani.

Tofauti na matarajio yake, alijua angesifiwa baada ya kutoa habari hizo. Lakini walimcheka sana. Wakijua kwa ushamba alionao kwa wanaume, ataleta kituko mle ndani. Wasijue Alex ni mtoto wa mjini na Nanaa sio mshamba kama wanavyodhani. Alishakuwa na huyo mwanaume kwa takribani miaka miwili sasa. Na Nanaa hakuwa bikra kama walivyodhani. Alex alikuwa akifaidi penzi lake kwa siri kwa muda mrefu tu.

*****************************************************
Endelea kufuatilia Sehemu ya 2

0 comments: