Nilipotea! Part 9 - Sehemu ya A
Usiku wa Ritha.
U |
siku huo
wakati kina Cote wamelala wakionekana kushindwa kwa hali ya juu. Harusi kubwa
ambayo ilikuwa imetangazwa na watu wa maana walikuwa wameshaalikwa, kushindwa
kufanyika na kubakiwa na hofu tupu, wakijiwinda kwa hali na mali, maisha ya
Ritha yaliendelea kwa furaha zote. Kwa mara nyingine tena, akaibuka mshindi.
Hana hatia. Hana alipoguswa na sheria. Aliowahusisha kwenye njama zake wapo
chumba cha maiti na wengine kifungoni. Hapo ni mpaka kina Cote waliokuwa
wakizungukwa na askari masaa 24 na kushindwa kwenda kila watakapo, waligeuka wafungwa
wa Ritha. Kilikuwa ni kama kifungo tu cha nje, ila kiukweli hawakuwa na tofauti
na Vic na Bethy waliokuwepo jela bila kuhukumiwa. Hata wao kina Cote walilijua
hilo, kuwa Ritha amefanikiwa kuwapa kifungo cha nje.
Wakati kina Cote wakiwa wanazungukwa na ulinzi
mkali na wa waziwazi, ikawa hivyo hivyo na kwa Ritha ila asijue. Kwake ilikuwa
tofauti. Bado polisi na askari wa CSIS walikuwa mbele ya jengo hilo kubwa
alilokuwa amepangisha apartment ila usingeweza kuwatambua kama ni askari.
Walionekana kama raia tu. Lakini wakimfuatilia Ritha kwa karibu sana. Kila
alipotoka, alifuatwa nyuma bila yeye kujua.
Gari yake yenyewe ilishachomekwa kitu ambacho
kilionyesha kwenye mitandao ya CSIS, kila alipo na anapokwenda. Lengo kubwa ni
kujua kama atatoka kwenda kukutana na Jeff, ili wawakamate wakiwa pamoja. Askari
wa hao walishamuona Jeff amefika kwenye mji anaoishi Ritha mapema tu siku hiyo
ya jumamosi. Wakaendelea kumfuatilia na kujua ni nini anafanya mjini hapo bila
kumpoteza hata dakika moja.
Alikwenda mpaka kwenye jengo hilo analoishi Ritha.
Akagundua kuna ugumu wakuingia humo. Huwezi kuingia tu mpaka mtu wa ndani
unayekwenda kwake, akufungulie. Akaona wengine wanafika hapo, wanabonyeza namba
ya apartment ya mwenyeji, wanazungumza kwa spika, kisha mtu wa ndani kama
anamkubali ndipo anamfungulia akiwa hukohuko kwenye apartment yake.
Na kulikuwa na askari pia. Kwa hiyo usingeweza tu
kupita na mgeni yeyote, kwani askari alikuwepo hapo kuhakikisha umekaribishwa
na mtu wa ndani. Jeff akajaribu kuingia hapo na wengine, karibu siku nzima,
akashindwa. Namba ya apartment anapoishi Ritha alishaijua, lakini shida ikawa
kufunguliwa na kuingia ndani.
Siku ya Ritha ilianza na kuendelea kama kawaida.
Kwa upande wake akiwa na furaha kuwa jumamosi hiyo ilikuwa harusi ya mwanae na
Tunda, amefanikiwa kuivunja tena kwa kishindo kikubwa tu. Akawatikisa kina Cote
na afisa usalama hapo nchini vyakutosha tu. Na yeye alikuwa miongoni mwa
mamilioni ya watu waliokuwa wakifuatilia kwenye vyombo vya habari tokea Tunda
anaanguka mbele ya Vic mpaka kutekwa.
Walimuona Ritha akielekea kufanyiwa manicure na
pedicure, kisha akafanyiwa masaji ya lisaa. Baada ya hapo akarudi nyumbani. Baada ya muda wakutosha tu, wakamuona anatoka
tena akiwa amependeza sana. Wakaendelea
kumfuatilia wakaona amekwenda kupata chakula cha jioni sehemu nzuri sana tena
ya pesa nyingi, kama anaye sheherekea jambo. Kwa muonekano wake, usingejua ni
Ritha, mtanzania. Alijawa ujasiri, akajibeba kishujaa, hata tembea yake ungejua
ni mshindi.
Baada ya chakula hicho alichokula kwenye hoteli hiyo
ya kifahari sana hapo mjini, wakamuona anarudi nyumbani kwake. Ritha alipishana
na kuhudumiwa na watu tofauti tofauti asijue kama ni askari waliovaa nguo za
kiraia. Hata askari wa jengo lao aliyeingia mida ya jioni hiyo na kusalimiana
naye wakati anarudi kwa chakula cha jioni, pia alikuwa ni afisa wa CSIS aliwekwa
hapo makusudi kwa muda kama mlinzi wa hilo jengo kwa kumfuatilia yeye Ritha.
Mfagizi aliyekuwa akisafisha gorofa yao ya juu
kabisa na kwenda kumgongea kumuomba takataka mchana aliporudi tu kutoka kutengeneza
mwili wake, pia alikuwa ni afisa wa CSIS. Jengo zima lilizungukwa na afisa wa
CSIS kuanzia ndani mpaka nje, wakifanya kazi tofauti tofauti, wengine kama ombaomba
tu wa mtaani, ilimradi kuhakikisha hakuna linaloharibika na wote wanakamatwa
wakiwa hai.
Baada ya juhudi za kuingia kwa Ritha kugonga
mwamba, Jeff aliondoka, wakamuona amerudi tena, safari hii akiwa amevalia nguo
za kiaskari kabisa, kama polisi. Ilishakuwa imetimu saa tatu usiku. Askari wa kawaida tu wa hilo jengo, aliyekuwepo
hapo ambaye alikuwa ni afisa wa CSIS, akamsalimia kawaida tu, Jeff akaitika na
kumdanganya yeye ni polisi wa mji wa karibu na pale. Bila shida yule afisa wa
CSIS aliyejidai ni askari au mlinzi pale, akamtania kidogo, Jeff akabonyeza
namba ya Ritha, Ritha akasikika kwenye spika.
“Nikusaidie nini?” Ritha akamuuliza. Jeff akajitambulisha kama yeye
ni polisi, anataka kumuhoji maswali machache kutokana na tukio la kina Cote.
Ritha kwa kujiamini sana, akamkatalia na kumwambia azungumze palepale,
anamsikia ameshachoshwa na maswali ya kijinga.
Aliposhindwa kuingia, yule askari wa CSIS akamtania
kidogo, kuwa watu huwa wanakimbia polisi bila sababu. Jeff akamuomba kama
anaweza kumruhusu aingie. “Lakini usije kunitaja.” Yule afisa akajidai kama
anamuonya Jeff. “Kwanza hata sikufahamu wala sijakuona.” Wakacheka kidogo,
akamfungulia mlango mkubwa wakumwingiza ndani. Akamfungulia tena mpaka lift
yakumpandisha anakoishi Ritha, Jeff akamshukuru sana, na kuingia ndani ya lift.
Jeff alipoingia tu kwenye lift, afisa wa CSIS
wakaanza kumiminika hapo ndani ya jengo kama nyuki. “Show
time! Show time!” Kila mmoja akahamasika, wakijua muda waliokuwa
wakiusubiria kwa hamu umefika.
Jeff alipanda mpaka gorofa la mwisho kabisa ambako
alikuwa akiishi Ritha kwa kutumia lift huku askari wengine wakipanda kwa
kukimbia, wakitumia ngazi. Alipotoka tu
kwenye lift, Jeff akakutana na yule mfagizi wa jengo akiwa na vifaa vyake vya
usafi, akijidai kufuta vumbi na kupangusa vioo. Akamsalimia asijue na yeye ni
afisa wa CSIS pia.
Akafika mlangoni kwa Ritha, akagonga na kujificha
pembeni ili akichungulie kwenye tundu la mlango, asimuone. “Ni nani?” Ritha akauliza.
“Housekeeping!” Jeff akadanganya kuwa ni mtu wa usafi. “Sina takataka
walisha...” Ritha akawa anamjibu huku anafungua mlango. Hapo hapo Jeff
akamsukumia ndani na kufunga mlango.
Alimvuta mpaka sebuleni na kumuweka kwenye kochi. “Kaa
vizuri, tuzungumze. Sipo hapa kukudhuru.” Akaanza Jeff na kuendelea. “Labda
nianze kwa kujitambulisha kwa kuwa ulikuwa ukikutana na Malinda tu. Naitwa
Jeff. Ndiye niliyekuwa mtekelezaji wa kile ulichokuwa ukipanga na Malinda.”
“Mimi sijui unazungumza nini?” Ritha akakataa. Jeff akatoa kofia.
“Labda nianze upya.” Jeff akatoa kofia, nakukaa
mbele yake. “Mimi naitwa Jeff. Sio polisi kama unavyoniona. Hii ni sare tu ili
kuweza kuingia humu. Na hii ni risasi niliyotumia kwa Malinda na mdogo wake.
Nasisitiza, sio lazima nikaitumia kwako labda unilazimishe. Sijui kama
unanielewa?” Jeff akauliza. Hofu ikamwingia Ritha. Maafisa wa usalama walikuwa
wakiwasikiliza tu.
“Nipo hapa kupata haki yangu. Sipo kukudhuru.” Jeff
akaweka msisitizo. “Kwa hiyo wewe ndiye uliyewaua kina Malinda?” Ritha
akauliza. “Narudia. Sipo hapa kukudhuru wewe. Wao ilinilazimu kuwaua ili kufupisha
malumbano na safari yakupata pesa yangu. Kwa hiyo, kama ulivyokubaliana na
Malinda. Ulimlipa pesa kiasi kama kianzio cha kazi uliyompa kumtorosha Mrs
Cote, halafu zingine uliahidi kulipa tutakapo kamilisha kazi nzima.” Jeff
aliongea taratibu tu.
“Sasa kama wewe unajua malipo yote ni mpaka kazi
itakapo kamilika, yuko wapi huyo Mrs Cote?” Akajikaza kuuliza Ritha. Alikuwa
akitetemeka kwa hofu. “Kazi ilikuwa nikumteka nyara Mrs Cote. Tulimtoa pale
bila shida. Kazi yetu ilikamilika, ila wewe hukutokea. Ninachotaka ni pesa yote
ya kazi kama tulivyokubaliana.” Akaendelea Jeff taratibu tu.
“Mimi sikujui. Ndio nakuona hapa leo. Sijawahi
kupanga chochote na wewe. Naomba uondoke.” Ritha akasimama. Jeff alimrukia,
akamshika kwa haraka kabla hajafika mlangoni. Akampiga kichwa cha nguvu
kichwani, Ritha akaanguka sakafuni. Akampiga mateke ya mfululizo mbavuni. Kisha
akamvuta kutoka pale sakafuni alipokuwa akivuja damu, mpaka kwenye kiti cha
sehemu yakulia chakula. Ritha alikuwa akilia, damu za puani na kwenye kipanda
uso alipochanwa baada ya kupigwa kichwa, zikaendelea kuchirizika usoni, Ritha
asiamini kama ni damu na si machozi na kamasi. Hofu ikazidi kumwingia akijua
kilichompata Malinda na mdogo wake, ndicho kimemfikia na yeye.
Jeff akampiga tena begani na kitako cha bastola. “Tafadhali
usitoe sauti. Nitakuumiza zaidi.” CSIS wa mpaka ofisini walikuwa wakifuatilia
mazungumzo yao yote. Walimsikia Ritha akilia kwa maumivu makali, na baadhi ya
maafisa walikuwa hapo nje ya mlango tayari, lakini amri kutoka makao makuu
ilikuwa wasiingie mpaka wapate ukiri wa uhakika kutoka kwa Ritha, ndipo
wataruhusiwa kuingia.
Mpaka hapo Ritha hakuwa bado amekiri chochote. Kwa
hiyo hawakuwa wamepata amri yakuingia, hata kwa kilio na kitisho cha namna gani,
wale maafisa wasingeweza kuingia mpaka kwa amri. Ritha akawa anajitahidi
kupunguza sauti kwa hofu ya kipigo kingine, lakini aliendelea kugugumia
maumivu, akabaki akifuta machozi na damu.
“Nimekwambia sipo hapa kukudhuru. Ninarudia tena, nimekuja
kwa amani kudai haki yangu. Tafadhali usitake nikuumize zaidi. Kama nimemuua
Malinda mpenzi wangu na mdogo wake, watu ninaowafahamu unafikiri nitakufanya
nini wewe?” Akampiga tena kwa nguvu begani. “Ni kweli hukuzungumza na mimi. Lakini
kama utakumbuka Malinda alikwambia tupo watatu anataka malipo ya watu watatu.
Kazi yakumteka nyara Mrs Cote haikuwa ya mtu mmoja! Na wewe unajua. Nimewatoa
kina Malinda, ili kufupisha mambo. Nipe pesa yangu niondoke na ninakuahidi
hutakaa unione tena.” Akaendelea Jeff huku Ritha akilia taratibu kwa kugugumia.
“Ritha? Naomba pesa yangu. Na kama huna hiyo dola
elfu 85 yote iliyobaki kwa taslimu, nihamishie kwenye akaunti ambayo hakuna mtu
atajua, kama alivyokuahidi Malinda. Tulishaiandaa hiyo akaunti. Mdogo wake
aliitengeneza kwa umakaninifu sana, hata watu wa usalama hawatajua. Naomba pesa
yangu.” Akasisitiza Jeff akimpiga piga mgongoni.
“Kwanza hiyo pesa uliyoitaja siyo
niliyokubaliana na Malinda. Tulikubaliana elfu 20 tu kwa kazi nzima. Ndio maana
nilimpa elfu 5, nikamwambia akinipa Tunda, namalizia 15.” Jeff akaanza kucheka. “Kama unafikiri utanizidi
ujanja katika hili, fikiria mara mbili. Mimi si mjinga wakuweza kumuua Malinda
kwa sababu ya elfu 15 tu! Nataka pesa yangu na ninaitaka sasa hivi. Unaweka
wapi kompyuta yako unihamishie pesa yangu au lete simu yako unihamishie pesa
yangu sasa hivi.” Ritha akasimama.
“Unakwenda wapi?” “Kufuata
simu ili nikuhamishie hiyo pesa yako! Unafikiri nitahamishaje sasa?” “Nakuonya
Ritha, usifanye chochote kile, nitakuumiza. Chukua simu kwa ajili
yakunihamishia pesa tu.” Ritha akaondoka pale sehemu yakulia chakula, akichechemea
na kutema damu akielekea sebuleni alipoacha simu yake.
Jeff alibaki palepale akimtizama kwa makini sana.
Aliiacha kwenye kochi. Wakati anaichukua, akabonyeza kwa makini 911, kuita
polisi. Kama wasiwasi ukamwingia Jeff akasogea pale kwa haraka. Wakati Ritha
anabonyeza tu sehemu yakupiga, Jeff akawa ameshafika. Jeff akaona. Akaiwahi kabla
hata haijapokelewa na watu wa 911. Akaizima kwa haraka, wakati amezama kwenye
simu, Ritha akawahi urembo wa meza ndogo ya hapohapo mezani, akaunyakua na kumpiga
nao Jeff, akakwepesha kichwa chake kwa haraka, akakinga kwa mkono nakumpiga
teke Ritha. Alipoanguka akampiga risasi ikampata ya mkono. Hapo hapo askari wa wa
CSIS wakavamia ule mlango, ukaanguka pembeni ya Ritha.
Maana amri ilikuwa ni kuwakamata wote wawili wakiwa
hai. Zaidi Ritha akiwa ameshakiri. Na kwa kuwa alishakubali mpaka na kiasi
alichokuwa amekubaliana na Malinda, ikabaki uokoaji tu. Waliingia wengine wakamuwahi
Jeff. Wakamfunga pingu na kuichukua ile risasi kama ushahidi. Maana ndiyo
aliyokiri kuwa ndiyo aliyotumia kumuulia nayo Malinda na mdogo wake,
ikachukuliwa kwenda kupimwa.
Ritha aliokotwa
pale sakafuni akilia kama mtoto huku akivuja damu. Watu wa huduma ya kwanza nao
walikuwa tayari. Wakamchukua na kumkimbiza hospitalini baada yakumpa huduma ya
kwanza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati bibi Cote anapitiwa na usingizi, simu ya
Mike ikaingia. Akawasha taa ndogo ya mezani, akapokea. “Unahabari
njema?” “Ritha amekamatwa. Yupo chumba cha upasuaji.” “Hapana Mike, nilikwambia
namtaka akiwa hai!” Akalalamika bibi Cote. “Hawezi
kufa. Ni risasi ya mkononi tu. Usiwe na wasiwasi.” Hapo kidogo roho
ikamtulia bibi Cote. “Na akitoka tu chumba cha
upasuaji, nimewaambia wamuhamishe huku, usiku huuhuu.” Bibi Cote
akafunga macho, akasikia machozi yanamtoka.
“Asante sana Mike. Najua unajua
namaanisha.” “Najua.”
Mike akajibu huku akicheka. “Tafadhali watakapomfikisha
tu huku, niwe wa kwanza kujua ili nimuone mimi kwanza.” “Sawa kabisa. Hamna
tatizo.” Wakaagana, bibi Cote akainamisha kichwa chini asiamini kama amefanikiwa
kumtia nguvuni Ritha, mwanamke aliyemwendesha kichwa na kumuumiza roho yake kwa
miaka mingi sana, tokea yupo na CJ mtoto wake wa pekee, akitamani amlipize
kisasi, lakini akafanikiwa kumzidi mahesabu kila wakati na kushindwa. Ritha
alikuwa kama samaki aliye hai baharini, mikononi kwa bibi Cote. Alimteleza kila
alipodhani amemkamata.
Usingizi ulishindwa kurudi kwa bibi Cote, akabaki
akimfikiria Ritha huku akisubiria simu yakutaarifiwa kuwa Ritha amerudishwa
Norfolks, kwenye himaya yake. Mji anaotawala kwa pesa yake na mamlaka. Uwanja
wa nyumbani. Bibi Cote akabaki akimpigia mahesabu.
Ushindi
wa Bibi Cote.
I |
likuwa saa 12 asubuhi bibi Cote alipopokelewa na
Mike, kiongozi mkubwa sana, ngazi ya juu kabisa ya CSIS nchini Canada. Moja kwa
moja wakaelekea chumba alicholazwa Ritha. Alimkuta na pingu mkononi, amelala. Wakamuona bibi Cote amefunga macho na kuvuta
pumzi kwa nguvu kama aliyetua mzigo mzito sana, uliokuwa umemlemea kwa muda
mrefu. Akatulia kwa muda akiwa amefunga macho, na wao pia wakanyamaza kama
kumpa nafasi.
Baada ya muda bibi huyo akafungua macho. “Naomba
muda naye.” Mike akakunja uso. “Unauhakika?” “Unafikiri atanifanya nini huyu?”
Bibi Cote akauliza kwa kejeli na kumgeukia Ritha, akamuona amefungua macho
anamwangalia. Mike akatoka na walinzi wote. Mpaka mlinzi wa bibi Cote naye alimtaka
asubiri nje. Aliporidhika kuwa wamebaki wao wawili pale chumbani, akacheka kwa
kejeli huku akimtizama Ritha alivyoumizwa kichwani. Akashusha macho mpaka
kwenye mikono alipokuwa amefungwa pingu kote. Hata mkono uliokuwa umepigwa
risasi pia ulikuwa na pingu, ukaegeshwa kwenye chuma ya kitanda. Na huo ulinzi
hapo nje, bibi Cote akacheka na kurudi kumtizama usoni.
“Hivi ulivyo sasa hivi, ndivyo nilitamani sana
kukuona ukiwa hivi kwa muda mrefu sana.” Akaanza bibi Cote. “Ni kwa muda tu.
Unajua mimi nina akili ya kukuzidi wewe. Hapa nitatoka tu.” Akajibu Ritha kwa
jeuri. “Nashauri utoe hilo tumaini Ritha. Anza kuzoea hayo maisha.” Akaendelea
bibi Cote akiwa ameshaanza kubadilika kwa hasira.
“Unakumbuka mara ya mwisho kuzungumza na wewe,
Ritha?” “Ulipokuwa ukijaribu kunitisha, kama wafanyakazi wako?” Ritha
akamuuliza na yeye kwa kumkejeli akionekana wazi yupo kwenye maumivu makali. “Kama
ulifikiri nilikuwa nikikutisha tu, jua safari hii nitakupitisha kwa vitendo. Nitahakikisha
hutakaa ukaonja uhuru wako tena. Pingu zitakuwa sehemu ya maisha yako mpaka
kifo chako. Nitahakikisha kila siku kuanzia jana, unajisikia uchungu aliopitia
CJ, mtoto wangu wa pekee uliyemchagua kumtapeli ili ujinufaishe hapa duniani.”
“Hakika utalipa Ritha. Utalipa kwa uchungu kama
unazaa. Na nitahakikisha ni kila siku, unakumbushwa kwa uchungu. Nitahakikisha
unaumia sana ili na wewe kwa sehemu uonje kule ulikompitisha Maya ambaye
amekuwa bila wewe kuwa mama kwake ila tapeli, ukijinufaisha kwa mali za Cote
kwa kuwatumia wao kama kitega uchumi. Utakaa matesoni, ukikumbuka Tunda ndiye
mama Cote, wewe hutambuliki popote.” “Hata ufanye nini, mimi ndiye niliyewazaa
Net na Maya.” Ritha akamjibu tena akitaka kumuumiza zaidi.
“Na tafadhali sana, hilo usiwahi kulisahau mpaka
unapoingia kaburini. Ulibeba miezi 9, ili mimi na Tunda tunufaike kila mmoja
kwa namna yake. Wewe utabakia ni njia tu ambayo ulituletea hao watu wawili,
kazi na safari yako imeisha. Nitahakikisha hilo unakumbushwa huko kifungoni kwa
uchungu sana.”
“Nitahakikisha wanakufungia jela ya wale wauwaji
makatili sana tena wazoefu. Serial killer. Utaishi na wafungwa wale
ambao nivichaa wakubwa, tena wanao ogopewa hata na askari wenyewe. Utakwenda
kula na kunywa nao kila siku. Kila
utakapofungua macho, nitahakikisha ni wao tu ndio unao waona, ili wakakutese
sana.” Bibi Cote akaendelea.
“Na nitahakikisha macho ya askari wote yanakuwa
kwako ili hao wafungwa wenzako wasije kukua kabisa, ila mateso tu. Na ili usije
kujiua kwa haraka ili uonje hayo mateso kwa muda mrefu sana. Ukakae huko ukijua
ninakulipa Ritha. Na kamwe hukuwahi kunishinda Ritha, ila nilikuwa nikitaka
kukuweka mwangani ili kila mtu akubaliane na mimi kuwa huko utakapokuwa baada
ya hapa, panakustahili. Na nimefanikiwa vizuri tu. Kila muhusika anafikiri huko
ndiko kutakapokustahili kwa kuwa wewe ni mtu wa ajabu sana na hatarishi.” Kidogo
akamuona hofu imemuingia. Ritha akanyamaza. Akamtemea mate usoni. Akatoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alirudi nyumbani mida ya saa moja na robo, karibia
na muda wa kifungua kinywa. Akaelekea mezani moja kwa moja. Hakumkuta mtu hata
mmoja hapo. Akalifurahia hilo ili ajaribu kutulia baada ya kumuona Ritha.
Alikuwa amekasirika sana. Baada ya kama dakika 5 hivi, akamuona Maya. “Mbona
uso una wasiwasi?” “Malcom hapokei simu yangu Nana!” “Labda bado amelala Maya.
Sasa hivi ni asubuhi sana.” Mara Net na mkewe nao wakasogea hapo sehemu yakulia
chakula.
Wakasalimiana, Maya macho kwenye simu. “Ni nini
tena?” Net akamuuliza. “Nina wasiwasi na Malcom. Tokea tulipoachana naye jana,
sijamsikia tena na wakati aliniahidi angenipigia simu ili kujua kama nilifika
salama. Malcom sio muongo.” Akaanza kutokwa
na machozi. “Kabla yakuanza kulia, nashauri mpe muda zaidi. Lolote linaweza
kuwa linaendelea.” “Na huo ndio wasiwasi wangu. Iweje sasa kama Zoe amemfunga?”
Wote wakawa kama wamegutuka.
“Mimi naenda kumtafuta kila kituo cha
polisi.” “Tafadhali naomba utulie kwanza Maya. Inaweza pia
ikawa sio hivyo. Huyu mtu anajukumu la mtoto pia. Inawezekana kabisa,
amejifikiria na kuona anafanya maamuzi ya haraka, yatakayo muathiri mtoto wake.”
Net akaendelea kumsihi taratibu tu. “Basi ndio nimpate,
aniambie mimi mwenyewe. Siwezi nikabaki nikidhani tu!” “Kwa nini usimpe
muda? Mwache kwanza. Mwache akutafute yeye kama alivyokwambia.” Hapo Maya
akazidi kulia.
“Uliniahidi utakuwa na mimi Net.” “Na ahadi yangu ipo palepale.” “Hivyo si kuwa na mimi Net. Hivyo ni mimi kuwa na wewe!”
Net akashangaa. Bibi Cote na Tunda kimya wakiwasikiliza. “Ulitaka nifanye nini
sasa!?” “Uwe na mimi katika maamuzi yangu.”
Maya akajibu huku akiendelea kulia. “Hata nisikushauri!?” “Sio ushauri wa kukaa mbali na Malcom!” Hapo Net
akaishiwa nguvu.
“Sijakwambia ukae mbali naye, ila kumpa muda Maya.
Please! Huyu mtu anamajukumu.” “Malcom alinichagua
mimi jana, Net. Mbele za watu. Malcom sio mtu kigeugeu. Mbona inakuwa ngumu
kuamini hilo!” Net kimya. “Kama inakuwa
ngumu kwako, basi Net. Ila mimi sitasubiri. Nitakwenda kumtafuta mwenyewe. Hayo
unayoniambia, nataka nikayasikie kutoka kwake yeye mwenyewe.” “Sawa
Maya. Mimi nitakwenda na wewe popote utakapo. Naomba unyamaze. Tupate kwanza kifungua
kinywa ndipo tutoke tukamtafute Malcom mpaka tumpate.” Hapo Maya akatulia.
“Ni sawa?” Net akamuuliza. Maya akatingisha kichwa
kukubali huku akijifuta machozi. “Unayo namba ya Roy?” Tunda akamuuliza. “Hapana. Sina.” “Basi tulia Maya. Tuliza akili ili
uweze kufikiria vizuri. Kama kweli yupo matatizoni, hivyo unavyoanza, ukiwa na
hali hiyo, hutaweza kumsaidia.” Tunda akamtuliza, mpaka akanyamaza. Wakatulia
kidogo, bibi yao kimya.
“Ulikwenda wapi Nana?” Net akamuuliza. Bibi yake
akashangaa kidogo. “Ulijuaje kama nilitoka?” “Nana! Am the man of the house.”
Net akaongea kwa kujivuna kidogo huku akijisogezea sahani ili ajiwekee chakula.
Bibi yao akacheka kidogo. Kimya. Wote wakamwangalia. “What?” Bibi yao akauliza
alipoona wote wanamshangaa. “Ulikuwa wapi Nana? Mbona kama unasita!” Net akauliza
kwa msisitizo. “Nilikwenda kumuona Ritha.” Pakazuka ukimya. Hata sauti ya
kijiko haikusikika.
“Wamemkamata jana usiku...” Akawasimulia kila kitu.
Kimya. “Kuna anayetaka kumuona kabla hajapeleka mahabusu?” “Binafsi yangu
hapana kwakweli. Sina huo muda wakupoteza.” Maya akajitoa mapema kabisa. “Mimi nataka
kwenda.” Wote wakamwangalia Net. “Nina swali nataka nikamuulize. Huwa linanisumbua
sana.” Maya akamcheka kaka yake kwa kejeli na kumwambia, “Goodluck with that!” “Kwa
nini?” Net akamuuliza.
“Kweli Net unauliza swali kama hilo kwa mtu kama
yule!? Unategemea jibu gani kutoka kwa mtu kama yeye ambaye kweli haijawahi
kutoka kinywani kwake?” “Labda kujiridhisha tu. Acha mimi niende.” Maya
akaaanza kulia tena. “Hakuna mtu ananijali mimi! Mnanipuuza.
Ona sasa hivi amekuja yeye, unaamua kuniacha mimi na kumfuata yeye! Mimi
naondoka, hata sisubiri tena. Nakwenda kumtafuta Malcom binadamu anayenijali
mimi, Maya.” Maya akasimama.
“Tunakwenda Maya. Naomba utulie tafadhali. Nakwenda
kuzungumza naye kidogo tu, kisha
tunakwenda popote unapotaka wewe. Tafadhali nifikirie na mimi hata kidogo. Huyu
mtu amenitenda ubaya mkubwa sana bila sababu. Kumbuka niliacha maisha hapa
nikaenda kumtumikia. Ameniadhibu mimi bila kosa, kama haitoshi amehamia kwa
mtoto wangu! Kweli Maya unafikiri sina haki yakumuona mtu kama huyo?” Maya
akatulia kidogo.
“Hata kwa dakika moja tu, nataka niione sura yake
ajue kile ninachojisikia.” “Unafikiri ameshawahi
kujali kile tunachojisikia?” Maya akamuuliza kwa kuumia sana. “Safari
hii nitahakikisha anajali Maya. Acha nikamuone na kuzungumza naye kwa mara ya
mwisho, kwa kuwa sitakaa nikazungumza naye tena. Tafadhali nivumilie.” “Sawa, lakini mimi sitaingia ndani. Sitaki hata kuiona
sura yake tena maishani mwangu kote.” “Sawa. Basi usilie. Hilo halina
shida. Utanisubiria kwenye gari. Nenda kaoshe uso.” Wakakubaliana ndugu hao
wawili. Maya akaondoka kurudi chumbani kwake kuosha uso na kuchukua pochi.
Net akambusu mkewe na kusimama. “Sasa mbona huli
tena na wakati ulikuwa unalalamika umeamka na njaa!?” Tunda akamuuliza. “Hamu
ya chakula imeisha yote! Acha tu niende. Nitakuja kula nikirudi.” Akamgeukia
bibi yake. Akaenda kumbusu. “Asante kwa kwenda na Maya. Nitajitahidi kuulizia
alipo Malcom, nikijua mapema, nitawapigia kuwataarifu alipo ili msisumbuke sana.”
“Utakuwa umeturahisishia sana.” Net akaondoka.
Tunda & Bibi
Cote.
T |
unda akajikuta amebaki kimya yeye na bibi Cote. “Hiyo
hasira na kilio cha Maya sio cha Malcom peke yake. Maya ana mengi yanayoendelea
kichwani kwake. Ameumizwa sana na mama yake. Acha Net akamsaidie labda
atatulia. Ningekwenda mimi mwenyewe lakini najua itawaogopesha watu zaidi.”
Tunda akafikiria kidogo. “Mungu atamsaidia hata haya yatapita tu.” Akaongea
Tunda taratibu kama anayefikiria. “Unajua kabla ya haya yote kutokea, alikuwa
akiniambia kuwa kuna kitu kimoja tu, ambacho anacho Vic na ndio maana wakati
wote alikuwa akimshinda, japo yeye Maya anaakili kumzidi yeye!” Bibi Cote
akakunja uso kidogo.
“Kitu gani!?” Akauliza bibi Cote huku na yeye
akikitafuta kama asikione. Wao walikuwa matajiri sana kuliko kina Vic, baadhi
ya biashara ni wao wamewafundisha wazazi wa mama yake Vic. “Alisema wazazi wa
Vic wakati wote wamekuwa upande wa Vic hata katika ujinga wake. Hawakuwahi
kumuacha tokea mtoto mpaka sasa na ndio maana katika maovu yake yote, Vic
hakuwahi kukamatwa kwa kuwa wazazi wake wamemzunguka na kumfuatilia kwenye kila
hatua ya maisha yake.” Bibi Cote aliumia mpaka Tunda akamuona usoni. Akainama
kwa muda, akanywa juisi aliyokuwa amewekewa na Gino.
“Ulitaka kwenda kumuona Ritha na wewe?” Akabadili
yale mazungumzo. Tunda akashtuka sana. “Hapana Nana. Nahisi sitaweza hata
kulala usiku. Acha tu Net aende.” Bibi Cote akafikiria kidogo, akamuona anatoa
simu. “Nataka kujua alipo Malcom sasa hivi.” Akakata
simu na kupiga tena simu kwengine. “Net na Maya
wametoka, nataka macho kwao wakati wote mpaka wanarudi hapa in one piece.”
Akakata.
“Pole Nana.” Tunda akamuhurumia. Bibi Cote
akacheka. “Hivi unapata muda wakulala kweli?” Akacheka. “Sina tofauti na wewe
Tunda. Si umeona mwenyewe tokea upewe mtoto wako!” “Kweli Nana! Silali tena
usingizi kama zamani!” Wakacheka kidogo. “Basi ndio hivyohivyo. Huwa hawakui,
na hata wakionekana nje wamekua na kuondoka nyumbani, bado mawazo yanawafuata
huko huko. Hupumziki.” Tunda akafikiria kidogo.
“Sasa ulifanyaje Net alipokuwa Tanzania?” “Mwanzoni
alikuwa akilindwa masaa 24. Alipoanza mambo ya kuchumbia, akitaka kupendwa kama
yeye.” Tunda akacheka. “Net! Yupo kama babu yake! Akakataa kabisa ulinzi.
Nikamwambia hutawaona hao walinzi, akasema hawezi akawa anazunguka au kuonekana
na wazungu kila mahali halafu isikushtue. Nikamwambia nimbadilishie waje weusi,
pia akakataa. Akasema huko Tanzania kuna amani, hakuna anayemfahamu, hakuna
atakaye mdhuru. Yeye anataka Tunda ampende kama yeye.” Tunda akacheka sana.
“Lakini alijuta mlipokuja kukamatwa na Ritha! Wewe
ukaishia jela, yeye akafika huku nusu mfu! Alijuta sana. Alikuwa akilizwa na
mengi, mimi nilijua nikaona nimwache tu, ajifunze aache ubishi kama babu yake.”
Tunda akanyamaza kidogo.
“Mbona kama kuna kitu ambacho unasita kuniambia?”
Tunda akacheka na kuhamia pale karibu yake. “Sasa hivi Net anajua maisha yote
na kwa undani vile walivyoishi wazazi wake, Nana. Ndio maana unamuona ameumia
sana.” Bibi Cote akashtuka sana na kushangaa. “Amejuaje!?” “Kumbe kuna sehemu
Papa alikuwa akiandika. Sasa hizi siku ambazo hakuwa anakwenda kazini. Tokea
mimi nipatwe matatizo, amepata muda wakupitia mafaili yote ya Papa, kule
ofisini kwake. Amekutana na hayo mambo kwenye kitabu cha kumbukumbu Papa alichokuwa
akimwandikia yeye Net binafsi. Alikuta jina lake limeandikwa nje, kwa mwandiko
wa Papa, Nathaniel Cote. Ndipo alipofungua.”
Bibi Cote akabadilika kabisa.
“Hivi unajua kuwa mali zote za Ritha ambazo
alizipokea kutoka kwenu, Papa aliandika ni za Net yeye ni kama mwajiriwa au
msimamizi tu?” Bibi Cote kimya. “Hata Net hakuwa akijua. Ila inavyoonekana,
Ritha anajua, ila akakusudia kunyamazia tu. Zipo karatasi zote alizosaini Ritha
na kukubali. Mlizoziona wewe na Logan, hazikuwa na maelezo yakutosha na ilikuwa
kwa baadhi ya pesa.” Bibi Cote akakunja uso.
“Alisaini kwa makubaliano kuwa pesa zote, mali zote
mpaka nyumba aliyouza Ritha ambayo mlimnunulia CJ, ilikuwa ni yako na Papa,
mrithi ni Net. Wala haikuwa ya CJ kama
ulivyodhani. Nafikiri Papa alishajua ujanja wa Ritha, akaamua kuwa naye makini.
Na hakutumia mwanasheria huyo wenu Logan, ameandika copies zote sahihi zipo kwa
mwanasheria wenu mwingine wa mambo ya mirathi. Net amemtaja kwa jina moja tu la
Leon.” Bibi Cote akajiweka sawa.
“Papa ameandika kuwa siku akifa tu yeye, kila
kwenye jina lake yeye Papa, watu wasome Nathaniel Cote au kila anapotakiwa
kusimama yeye Papa, asimame Nathaniel Cote. Kusiwahi hata kuwepo na kuhisiwa na
utofauti, popote. Kasoro tu sura yake ndio iwe haipo. Ila Papa amemwambia Net,
anajua ataishi kwa kupitia yeye, kwa kuwa anauhakika na alichokifanya akiwa
hai.” “Hiyo najua na nina uhakika. Alijihamisha kwa
Net, kwa asilimia 100.” Bibi Cote akathibitisha na kufuta machozi.
“Basi ndio hivyo. Kwa kifupi, mali zote
alizouza Ritha ni za Net. Sasa Net ameamua kuchukua kila centi iliyoingia
kwenye mfuko wa Ritha.” “Tunda!” Bibi Cote akashtuka sana.
“Hivi moja ya sababu ambayo anaenda kumuona Ritha leo, ni
kumuonyesha aliposaini baada ya makubaliano na Papa. Na kumwambia atamfilisi
mpaka centi ya mwisho ili hiyo pesa yake yeye Nathaniel Cote, ambayo aliishika
kwa dhamana tu, asiendelee kuitumia kudhuru watu.” “Nyumba ya Tanzania?” Bibi
Cote akauliza.
“Amesema atafanya kama alivyofanya ile yake kule
Tanzania. Atahamishia kwa jina langu. Na vyote ameniambia anaenda kumwambia
siku atakayoiona sura yake. Ndio maana mimi nimeona leo nisiende.” Bibi Cote
akavuta pumzi. “Usiku hajalala, Nana! Kuna muda niliamka usiku nikamkuta akilia
bafuni. Nikasema nimuache. Kwenye saa 9 usiku tena, nikamkuta bado yupo macho.
Ndio nikambembeleza, akalala.”
“Pengine anahofia utamuacha!” “Hapana Nana. Hilo
tulishalimaliza.” “Mbona bado umehama chumba?” Tunda akacheka. “Siwezi kulala
chumba mbali na mwanangu Nana! Sitalala. Nahisi kama wanaweza kuja kumuiba
nikiwa usingizini!” Wakacheka. “Hawawezi. Unaulinzi mkali sana hapa.” Tunda
akabaki kama anayefikiria. “Anyway. Hilo tulishalimaliza. Yameisha na
nimemwambia tutafunga ndoa kama alivyotaka tokea mwanzoni.” “Kweli Tunda!?”
Bibi Cote hakuamini.
“Nana! Nitapata wapi mimi mwanaume atakayenipenda
kama Net?” Bibi Cote akafikiria kidogo. “Mimi nilipoona wanaanza kutangaza
kiwango cha mali utakachopata baada ya kuachana na Net, na kuwa hata mtoto
atakuwa wako sababu Net amezini, nikajua watakuchanganya.” “We Nana! Nipate
mali nimkose Net!? Halafu hizo mali zitanisaidia nini mimi? Sijawahi kupata
utulivu wa akili na moyo maishani mpaka alipokuja Net kama Net kwenye maisha
yangu.”
“Labda aje anikatae mwenyewe. Lakini hivihivi,
nitatafuta sababu yakusamehe tu ili niwe naye mpaka kufa.” Bibi Cote alicheka
sana. “Bila kuombwa msamaha?” “We Nana, asiponiomba je?” Tunda akamfanya bibi
Cote azidi kucheka. “Nimekwambia nitatafuta sababu yakusamehe tu Nana, ili
nikae na Net wangu. Hapa nimemwambia kwa kunikosea, nataka watoto mapacha, tena
haraka.” Bibi Cote akatoa macho.
“Tunda! Hujachoka?” “Hata kidogo. Ndio tiketi yangu
hiyo mwenzio yakuweka ugumu wakutoachana.” Angalau bibi Cote alicheka asubuhi
hiyo baada ya juma hilo lililokuwa limejaa hekaheka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Simu ya bibi Cote ikaita. Akamuona amepokea kwa
haraka. Akasikiliza kwa muda bila kujibu akamuona bibi Cote amefunga macho kwa
sekunde kadhaa. “Mtaarifu Logan, mwambie anipigie na
majibu ya nini chakufanya. Isichukue muda mrefu.” Akakata simu. “Ni nini
Nana?” Akavuta pumzi kwa nguvu. “Maya atachanganyikiwa.” “Kwa nini tena?”
Akavuta tena pumzi kwa nguvu. “Malcom alikamatwa na polisi jana usiku akiwa
njiani kuelekea kwake, ameshikiliwa na polisi.” Tunda akashtuka sana.
“Kwa nini?” “Zoe alipiga simu polisi na kuwaambia
Malcom ametoka kwake akiwa amembaka. Ameonyesha majeraha aliyomjeruhi wakati akimbaka.”
“Nana! Unafikiri ni kweli?” “Tutajua.
Lakini...” Akasita. Akaonekana kama anafikiria. “Nikuulize Nana?” Bibi Cote
akamwangalia. “Katika vipindi kama hivi vya matatizo makubwa mfululizo. Tena
ambayo yote yanakuhitaji, unafanyaje?” Akamuona
amecheka kidogo na kubaki akifikiria.
“Maana mimi
kwa tukio moja tu, nilitaka kukimbia kabisa.” Tunda akamfanya bibi Cote
acheke tena kidogo. “Muonekano wa nje usikudanganye Tunda.” “Hapana Nana. Nimekutizama tokea Tanzania na nilipokuja
hapa! Unawezaje?” Akajiweka sawa. “Unakumbuka
nilikwambia wakati wote katika kila maamuzi unayochukua chukua ukiwafikiria mpaka watoto wa huyo
Cote. Unakumbuka?” Tunda akavuta pumzi kwa nguvu, nakunyamaza.
“Umetoka kusema utafanya kila njia kubaki na Net.
Hiyo ni hatua ya kwanza na ya msingi. Unachotakiwa kufanya sasa, kila jambo
zito na gumu linapokuja mbele yenu, ukumbuke hilo, ndipo hisia zifuate. Kingine,
najua mimi nikichanganyikiwa hata kidogo tu sasa hivi, si hasara kwa Net na
Maya peke yao, hata Cote ataathirika. Kwa hiyo tunarudi palepale. Lazima
kuwafikiria mpaka watoto wa Cote. Na lazima kufikiria kwa haraka na kuchukua
hatua ya haraka bila kupoteza hata sekunde. Na wakati wote huwa nahakikisha
nipo hatua moja mbele ya kila kitu.”
“Kwa mfano katika hili la Malcom, kabla sijafanya
chochote na kuharibu au kuaibika, nimemtaka Logan anipe ushauri wa kisheria juu
ya hili. Sitatoa mguu wangu hapa. Wala sitampigia simu yeyote, bila kujua
nataka kuongea nini na nani. Sijui kama unanielewa?” Tunda akabaki kimya. “Kupaniki
kwangu ni jambo la mwisho sana na huwa siruhusu kupaniki katika maisha yangu.
Kwa kuwa sijajaliwa hiyo nafasi kama wengine. Nafasi yangu kwenye jamii na
familia, hainiruhusu kupaniki, ila kutafuta suluhu katika kila jambo. Na ndio
maana huwa sishindwi.”
“Imenisaidia kufanya akili yangu kuwa na uwezo wa
kufikiria kwa haraka sana. Mfano. Nilipokuja hospitalini siku uliyotekwa nyara,
nilimkuta Net anakusubiri, wewe haupo. Akaniambia umekwenda kufanyiwa vipimo
hata yeye hakukukuta. Hapohapo nikajua kuna kitu hakipo sawa.” “Nana!” Tunda
akashangaa kidogo.
“Hata wao hawakuwa wakiamini na kuelewa. Walishangaa ninachukua hatua kama kuna moto mkali sana
unaowaka nakutaka kuteketeza jengo wakati mazingira yalikuwa matulivu, hakuna
chakushtua, kwa kuwa Tunda yupo kwenye vipimo! Lakini tangia naingia pale
hospitalini, mpaka kujua haupo kwenye vipimo. Umetoroshwa na watu wawili,
wamekutoa pale kwenye mazingira ya hospitalini na gari fulani. Kuifuatilia hiyo
gari mpaka ilipoishia chini ya tunel,
haikuchukua hata dakika 20. Sijui kama umenielewa?”
“Mpaka wale polisi walishangaa. Nilijua nini
chakufanya na wakati gani. Nani nimpigie kwa haraka ili anipe majibu ya haraka.
Na ni hapohapo mbele ya polisi, mpaka wao wenyewe wakabaki wamepigwa na butwaa.
Lakini sio kwa sababu ya akili kuwazidi
wao au pesa yangu tu, lakini ni kwa sababu yakujizoesha kufikiria kwa
haraka bila kutoa nafasi ya kupaniki. Lakini sio kwamba huwa siingiwi hofu? Hapan..” Simu ya bibi Cote ikaita.
Akapokea akamuona ameshtuka sana. “No No nooo! Usingemuacha akashuka kwenye gari.”
Akakata simu. Akamuona anapiga simu nyingine. “Maya
yuko wapi?” Tunda akabaki akimtizama. “Nashukuru
sana. Hata iweje, asiwe mbali na wewe hata kwa hatua tano. Unanielewa? Nakuja
sasa hivi, tutakutana huko huko.” Akakata. “Nahitaji gari yangu iwe
tayari sasa hivi.” “Yes ma’am.” Carter akajibu.
“Ni nini tena Nana?” “Nafikiri Maya amepata taarifa
za Malcom kutoka vyombo vya habari au
kwenye mitandao yao hiyo! Dereva aliyekuwa nao anasema walikuwa wakimsubiria
Net nje ya hospitali, akamsikia Maya anapiga simu kuulizia alipofungwa Malcom,
inaonekana alipojua, akatoka ndani ya gari na kuanza kukimbia. Bahati nzuri
mlinzi niliyemtuma kuwafuatilia alimuwahi akamwambia apande kwenye gari yake.
Hapa walipo wanaelekea kituo cha polisi. Inabidi niende Tunda. Hali aliyonayo
Maya, kama mimi mwenyewe nisipoenda pale, watamfunga na yeye. Anahasira na mama
yake, ataenda kumalizia polisi huko kituoni. Acha niwahi.” Hapo hapo akanyanyuka.
Tunda akamsikia akipiga simu nyingine. “Nikukute na majibu
yote kituo cha polisi cha Norfolk sasa hivi.” Tunda akajua huyo ni Logan
tu. Akamsikia kama anayekimbia, baada ya dakika 2, kimya. Akajua ameachwa peke
yake humo ndani na wafanyakazi. Tunda akavuta pumzi na kujivuta nyuma ya kiti.
Akabaki kimya ameduaa.
Net kwa mama yake.
N |
et alifika pale
akamkuta mama yake amelala vizuri, kama aliye kwenye usingizi mzito. Nesi
aliyekuwepo pale akataka kuwapisha. “Hapana. Moja ya sifa zake huyu, ni mzuri
sana wakubadilisha maneno. Tafadhali kama huna kazi nyingi, naomba uwepo hapa
ili nizungumze naye. Haitachukua muda mrefu. Na acha mlango wazi. Tafadhali
sana.” “Sawa.” Yule nesi akakubali kwa heshima. Alipogeuka akamkuta mama yake
amefungua macho.
“Unakumbuka mara ya mwisho nilipozungumza na wewe
tulipokuwa nchini Tanzania?” Net akamuuliza mama yake, akiwa ametulia tu tena
kwa lugha ya kingereza. “Nilikwambia angalia usifike umbali ambao ukashindwa
kurudi. Usiruhusu hiyo roho iliyokuingia ikakufikisha mbali, lakini nisijue
kuwa ndivyo ulivyo tokea kabla hujakutana na baba.” Ritha akacheka kwa kejeli.
“Naona bibi yako amekazana kweli! Safari hii
ameamua aniangamize mimi na watoto wangu. Amekusudia kukuharibu kichwa chako
ili tu kuniumiza. Haya, endelea kuongea ili nijue amekwambia nini?” Net akazidi
kuumia. “Wala Nana hajaniambia baya lolote kuhusu wewe! Na ni kama amejionya juu
ya hilo. Hajawahi hata kuropoka kukutaja kwa ubaya mbele yetu. Nafikiri ni kwa
kuwa anatupenda sana, hataki kuona tunaendelea kuumizwa na wewe. Na wala
hafahamu ni nini nataka kuzungumza na wewe.” Net akaendelea.
“Ni mimi mwenyewe nimechunguza mpaka nimejua ukweli
wote. Nikisema wote namaanisha nimegundua ambayo hata Nana hakuwa akiyajua. Au
ambayo hata wewe hukuwa ukijua kama Papa anayajua.” Ritha akakunja uso. “Sipo
hapa kurudia maovu yako. Kwa kuwa najua unayajua maovu yako yote. Ila najua
kwako sio maovu ni maisha uliyoyachagua kuyaishi zamani sana hata kabla mimi na
Maya hatujazaliwa na wala hata kabla hujakutana na baba.” Bado Ritha alikuwa
anamtizama mwanae kwa makini tu, kutaka kujua ni nini amejua!
“Wewe kwa asili ni muovu na wala huwezi
kutenganishwa na uovu kwa kuwa wewe ni MUOVU.” “Acha kunipotezea muda Net.
Nenda kwenye pointi, maana sina muda mrefu wa kijinga wakukusikiliza. Kama bibi
yako amekudanganya kuwa wamenikamata safari hii, nitakaa hapa muda mrefu, ujue
amekudanganya. Hapa kwenye hizi pingu sina muda mrefu. Tumia huu wakati vizuri.”
Ritha akaongea kwa kugomba na kujiamini.
“Anachotaka bibi yako nikunilipiza kisasi. Na
ninakuhakikishia, hajanipata. Mimi nina akili, usifikiri ni mjinga. Huwezi
kunishitaki kwa ukiri nilioongea nikiwa nimeshikiwa risasi. Au nimepigwa
risasi!” Akaongea Ritha bila wasiwasi. “Mtu anaongea chochote anapokuwa akitishwa
ili kujiokoa. Confession under duress!
Jua sheria wewe mtoto, acha kukurupuka nakuja hapa kuongea ujinga! Kwanza
ondoka ili nilale. Sidhani hata kama una kitu chakuzungumza na mimi isipokuwa
uzushi tu.” Net alishtuka sana maana mama yake aliongea ukweli. Lakini
akajikaza.
Ritha alishageuza kichwa upande mwingine. “Jiandae
kutafuta mwanasheria atakayetetea huo ujinga unaoendelea kichwani mwako tena
atakayekufanyia bure. Maana mimi kwa kutumia kila cent ambayo unadhani ni yako nitahakikisha unakaa sehemu ambayo hutaweza
kumdhuru mtu mwingine yeyote hapa duniani, hiyo ni hata na wewe mwenyewe, mpaka
Mungu mwenyewe atakapoamua kukutoa hapa duniani.” Ritha akashtuka sana.
Akageuka.
Net akacheka. “Ninapokwambia nimefanya uchunguzi wa
kina na ninajua mambo zaidi ya unayodhani
wewe na anayojua Nana, ulifikiri nakutania?” Net akacheka akionekana anahasira
yakupitiliza. “Wewe unasainishana na Nana, bila mimi? Mimi ndio mrithi wa CJ na
Cote. Mimi ndio mwenye mali. Papa amekufa mwili, lakini anaishi hapa.” Net
akajionyeshea kidole yeye.
“Hilo ameandika kwa maandishi, kwa mkono wake yeye
mwenyewe Papa. Na ameacha nakala tatu. Kwa wanasheria wawili tofauti tofauti,
siwezi kukutajia wewe, na nakala moja ameniachia mimi. Kila mkataba alioingia
yeye akiwa hai, amesema yeye ndio atakufa, lakini mikataba yoote aliyoingia
yeye, haitawahi kufa kama Nathaniel Cote, ninaishi.” Net akaongea kwa jeuri.
“Sasa ni hivi, mkataba uliongia na Nana, kupitia Logan, SIUTAMBUI. Hapa ninapozungumza mimi kama Nathaniel Cote,
nimeshatuma Tanzania makaratasi ya kumuuzia Tunda ile nyumba uliyodhani ni
yako, kwa shilingi 100 tu.” Akamuona mama yake amebadilika. Net akacheka.
“Umesikia?” Net akamuuliza kwa kejeli. “Sio
milioni. Shilingi 100 tu. Ambayo hivi karibuni itakosa thamani. Itakuwa ni kama
nimempa bure kabisa. Nimesema kila kitu kilichopo ndani mpaka kijiko ulichotumia
muda kwenda kununua kwa pesa yangu, ni cha Tunda. By the way, yupo hai.
Nimemuacha anakaribia muda wa kwenda kumnyonyesha mtoto wetu.” Net akamtizama
usoni.
“Usiku wa jana, nimeandaa madai yangu yote kwako.
Na uthibitisho wote mliokubaliana na Papa. Nitamlipa mwanasheria mkubwa sana,
ili kuhakikisha kabla hujafikishwa mahakamani, uwe na uhakika kuwa umefilisika
kabisa. Huna hata chumvi unayomiliki kwa jina lako.” Net akamkazia macho.
“Nitahakisha safari hii hutakimbia hukumu yako
Ritha. Najua umeshajipanga kwa utetezi, lakini
ujue safari hii utalipa kwa kifo cha
Gabriel. Alikufa akiwa anakutafuta, nimekuja kukutangazia, NIMEKUPATA. Na
nitahakikisha unalipa.”
“Hii ni Canada. Hakuna ujanja ujanja wa meneno
kugeuzwa geuzwa. Utahukumiwa kwa maneno ya kinywa chako mwenyewe. Na ujue hapo
unapolala ni dakika za mwisho. Unakaribia kupelekwa kunapokustahili.” Ritha
akakunja uso. “Mimi bado mgonjwa!” “Wapo wauguzi watakaoendelea kukuhudumia
ukiwa jela. Usiwe na wasiwasi. Baada ya muda mfupi sana gari ya kukupeleka
unakostahili itakuja kukuchukua. Utapata muda wakujifikiria na kujipanga vizuri
huko jela. Wewe si umesema unayo akili? Nenda sasa ukajipange ukijua huna pesa
na upo na pingu mkononi. Na kingine, kuwa na uhakika kuwa, pesa yangu uliyokuwa
ukiihangaikia kuizalisha miaka yote, ndiyo itakayosaidia kuhakikisha unakaa
ndani mpaka kifo, ili mke wangu alee vizuri na kwa amani akijua hutaweza
kumdhuru tena.” Net akaongeza.
“Na nitahakikisha, Cote na wadogo zake, wanapata
kutoka kwa mama yao, ambaye ni Tunda kile ulichoshindwa wewe kutupa mimi na Maya, kwa kuhakikisha unaishi jela
maisha yako yote, bila kutoka au hata kuwa na uwezo wa kutumia watu kufanya
maovu yako tena, kwa kuwa hutakuwa hata na
cent moja kwa jina lako, kuweza kuwalipa watu kama kina Jeff.” Akamtizama
na kutaka kuondoka. Akasimama.
“Nilitaka kukuuliza kitu, lakini naona Maya yupo
sahihi. Nitapoteza muda tu. Wewe ni muongo, na wala kweli haijawahi kukaa ndani
yako. Huna majibu ya maswali yangu.” “Nijaribishe.” Net akageuka akamtizama kwa
muda. Akakunja uso, huku akicheka kwa kumkejeli mama yake. “Naaaah! Nina mambo ya muhimu ya kufanya na mke wakumuwahi.” “Malaya yule!” “Yeap! Yale yooote aliyokuwa akiwapa wengine,
sasa hivi mimi ndio nayafaidi peke yangu! Nalala nikiwa tajiri. Nina uhakika wa
utajiri wa mpaka kifo changu na watoto wangu, halafu napata na penzi safi
kutoka kwa Tunda. Na ninakuhakikishia, ni mzuri kitandani.” Akamtusi mama yake
huku akicheka. “Deal with it!” Akamuwekea mama yake msisitizo wakati
anatoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Je
ni kweli safari hii wamemkamata Ritha? Amashatengeneza hoja ya kweli kisheria. Huwezi
kuchukua ukiri wa mtu aliyekuwa akitishwa kama ushahidi. Mtu akiwa anatishwa
anaweza kuzungumza chochote ili kujitetea nafsi yake. Ritha ndio umesimamia huo
utetezi wake. Watafanyaje kushinda hilo?
Maya
na Malcom nao je?
Usikose
sehemu ya mwisho ya Simulizi hii.