NILIPOTEA! PART 8 – SEHEMU YA D
Usiku Kwa Ritha.
Usiku huo
wakati kina Cote wamelala wakiwa wanazungukwa na ulinzi mkali, ikawa na kwa
Ritha pia hivyohivyo. Polisi na CSIS walikuwa mbele ya nyumba aliyokuwa akiishi
Ritha wakiwa wamevaa kama raia wa kawaida tu. Lengo ilikuwa ni ili kujua kama
atatoka kwenda kukutana na Jeff, mwanaume wa Malinda, aliyehusika kumteka nyara
Tunda. Na kusadikika kuhusika na mauaji ya Malinda pamoja na mdogo wake, ili kujipatia pesa zote watakazolipwa
na Ritha, yeye mwenyewe
Na kule mbele ya Motel aliyokuwa amejificha Jeff pia
kulikuwa na polisi wanamwangalia kuona ni nini atafanya. Nia ni kumkamata akiwa
na Ritha, kwa ushahidi. Kwa kuwa Ritha yeye alikuwa makini sana. Hawakuwa na
ushahidi mkamilifu kuwa anahusika ila ukiri tu wa Vic. Ila kwa Jeff, yeye walishapata ushahidi kuwa ni
yeye muuaji kwani aliacha alama za vidole sehemu moja tu, ambayo
inaonekana alijisahau kuifuta. Kwenye
dripu waliyokuwa wamemuwekea Tunda. Walikuta alama zake yeye za vidole, na Malinda. Ni kama alimsaidia kunyanyua hiyo
chupa ambayo ilichukuliwa na kwenda kupimwa, ndipo ikakutwa na alama zao wao
wawili. Kuwa wao wiwili waliishika ile chupa ya maji waliyokuwa wamemuwekea
Tunda.
Mpaka hapo hawakuwa wamekuta risasi iliyohusika
kumuua Malinda na mdogo wake ila miili yao tu. Na Jeff alionekana alifanya
juhudi za makusudi kusafisha kwa kutoa alama zake za vidole kila mahali kwenye
ile nyumba.
Huku kwa Ritha alilala akiwa hajui hata
kinachoendelea. Habari za kukamatwa kwa Vic zilifichwa kabisa na kuhakikisha
hazivuji. Mbali na wazazi wa Vic ambao walifurahia kutotangazwa hizo habari,
hakuna hata aliyejua kama usiku huo Vic na Jake wapo chini ya ulinzi wa CSIS,
na wamelala ndani kama wafungwa.
Jeff alisubiria simu ya Ritha akiwa na simu yao
waliyokuwa akitumia Ritha na Malinda, bila kuona mafanikio. Akasubiri na
kusubiri, akaanza kukosa uvumilivu. Siku nzima hakumsikia Ritha, na huo usiku
pia. Akajua Ritha anataka kuwachezea mchezo mchafu. Walishafanya hatua ya
kwanza waliyokuwa wamekubaliana kumteka nyara Tunda. Hayo malipo alifanya kiasi
tu, bado hakumaliza. Alisema mpaka amuone Tunda yupo chini yao, na kama Malinda
akikubali wamuue, anampa pesa yote.
Yeye Jeff hakuona sababu ya mtoto, alitaka
wammalize Tunda, walipwe, maisha yaendelee. Lakini Malinda alitaka mtoto.
Alitaka wamfungie Tunda mpaka awazalie mtoto ndipo amwache kwa Ritha. Ndio
maana alimgeukia Vic kumdai pesa ya matunzo. Vic alipokataa, na Malinda bado
akang’ang’ania kumtunza Tunda hivyohivyo mpaka apone ndipo wampandikizie mtoto,
hapo ndipo pakatokea kutokuelewana kati yake na mpenzi wake Jeff.
Jeff akaona Malinda anataka kupoteza muda na Tunda
ambaye atakuwa mzigo na kuzidi kuwagharimu wakati pesa kutoka kwa Ritha
inawasubiri! Na Ritha aliwaambia ni afadhali wamalizane mapema na Tunda,
wakamtupe au kumfukia mahali, lasivyo watakamatwa tu.
Jeff aliposhindwa kumshawishi Malinda,
na mdogo wake akawa upande wa dada yake akitaka dada yake apate anachokita.
Yaani mtoto, ndipo Jeff alipowaua wote wawili ili akutane na Ritha, arudi
kumuonyesha Tunda kama ushahidi, wamuue, alipwe pesa yote yeye mwenyewe.
Alipotoka baada yakufanya mauaji hayo, na
kusafisha. Akaamua kumpigia sasa Ritha simu na kumwambia kwa wakati huo yeye
ndio kiongozi. Akapiga simu ya Ritha ikawa haipatikaniki tena. Kumbe
alichofanya Ritha, baada tu ya kutembelewa na afisa wa CSIS wakamuulizia Tunda
kwake, akachukua ile simu aliyokuwa akiwasiliana na kina Malinda, ilikuwa ni ‘Burner
phone’ tu. Simu ambayo haijasajiliwa popote, sio rahisi hata wataalamu wa simu
kuifuatilia na kumpata. Akaichukua hiyo simu na kuitumbikiza kabisa chooni ili
kuua ushahidi.
Baada yakujaribu kupiga simu ya Ritha mara kadhaa
na kukomkosa, Jeff alitoka pale akiwa na njaa usiku ule kwenda kununua chakula,
kurudi kwa mbali ndipo akaona helicopter na taa za polisi kwa mbali kwenye lile
eneo walilokuwa wamemficha Tunda. Akajua tayari watu wa usalama wameshajua eneo
alilofichwa Tunda na wamefika.
Hakutaka kukamatwa. Hapohapo akageuza na kukimbilia
kujificha kwenye hiyo motel. Napo akajisahau akanunua sigara mchana baada
yakujifungia kwenye hiyo motel kuanzia usiku ule. Ndipo maafisa wa CSIS wakachunguza
kutoka ilipotumika kadi yake Jeff kama kuna nyumba za wageni karibu na hapo
alipoonekana amenunua sigara, ndipo wakampata hapo amejificha kwenye hiyo
motel.
Wakati director wa CSIS anazungumza na bibi Cote
kumpa maendeleo walipofikia, bibi Cote akamsihi wasimkamate kabisa mpaka waweze
kumuunganisha na Ritha. “Tafadhali Mike, naomba
unielewe. Najua Ritha ni mjanja sana na ana akili kwenye mipango yake. Hamuwezi
mkamkamata kwa ujumbe, au kwa kufuatilia kadi zake za benki au hata mazungumzo
ya zamani aliyozungumza na hao wahusika.” Bibi Cote akasisitiza.
“Ni heri tuchukue muda mrefu, lakini
tuhakikishe safari hii tunamkamata. Naomba Jeff aendelee kuachwa ili tuone
anahusika vipi na Ritha. Pesa anazitoa wapi! Atajifungia hapo lakini tunajua
ataishiwa tu, au atakosa uvumilivu na kufanya kosa, na hapo ndipo tutajua ni
wapi atakapokwenda kupata hizo pesa au mahusiano yake na Ritha.” Hilo wazo la
bibi Cote likawa zuri.
Maafisa wawili wa CSIS, wakike na wakiume,
wakachukua chumba pembeni ya chumba alichochukua Jeff, kama wapenzi tu ili wasimshtue
Jeff. Salamu za kawaida kila wakikutana naye nje ya mlango na kujaribu
kumzungumzisha mambo ya kawaida tu kama hali ya hewa na kadhalika. Walipomuona akitoka kwenda kununua chakula na
sigara tena, wakaingia chumbani kwake na kutegesha kamera. Ili kuweza kumuona
na kumsikia kwa kila atakachozungumza na kila ambaye angezungumza naye.
Hapakuwa na kulala kwa hao maafisa wawili.
Walipeana zamu kulala, kwenda chooni mpaka hata kutoka kwenda kununua chakula.
Macho yalikuwa kwenye screen wakimwangalia Jeff kwa kila anachofanya. Mvuta
bangi huyo Jeff alishakata tamaa yakumsubiria Ritha kwa muda wote huo. Akaona
amfuate tu anapoishi. Jeff alikuwa na number ya simu ambayo haikuwa hewani.
Ikawa kazi kujua nyumba yenyewe anayoishi.
Wale maafisa wakaona na kujua shida ni sehemu
anayoishi Ritha. Wakacheza na mtandao mpaka wakamdokeza jina kamili analotumia
Ritha kwenye kazi mpya. Akaweza kujua ni wapi Ritha anafanya kazi.
Kutoka alipokuwa amejificha Jeff mpaka alipo Ritha, ilikuwa mbali. Lakini Jeff
akaamua kuendesha tu ilimradi kumfikia Ritha apate haki yake.
Malcon kwa Maya.
A |
subuhi ya saa 12 Maya akapokea ujumbe kutoka kwa
Malcom. ‘Naomba tupate kifungua kinywa pamoja.’
Bibi yake akamuona anacheka. Akamuonyesha ule ujumbe bibi yake. “Utamjibu nini
sasa?” “Nataka kwenda, Nana.” “Basi mjibu.” Maya akambusu bibi yake kwa furaha
akijua amempa ruhusa. ‘Ningefurahia. Unataka tukutane
wapi na saa ngapi?’ Maya akajibu. ‘Mimi ndio
nakutoa. Nitakuja kumuomba Ms Cote au kaka yako. Wakiniruhusu tunakwenda kwa
kifungua kinywa. Itakuwa saa mbili na nusu. Itakuwa sawa?’ Maya
hakuamini.
“Angalia heshima anayonipa Nana!” Bibi Cote akasoma
na kucheka. “Labda huyu atakuwa ndiye Nana!” “Naomba mpe muda Maya. Najua moyo
wako. Naomba mpe muda wakumfahamu ndipo mfungulie moyo wako kabisa. Sitaki kuja
kukuona unaumia tena.” Bibi Cote akamtahadharisha. “Ila kwa mwanzoni tu,
anaonyesha dalili nzuri. Ananiheshimu huku akinijua ni mimi Maya ambaye
nimepoteza heshima kwenye jamii!” “Hiyo ni kweli.” Bibi yake akakubaliana naye.
‘I would love that.’ Maya akamjibu Malcom kuwa angelipenda hilo wazo
lake. ‘Okay. Nitakuona baada ya muda mfupi.’ ‘Okay.’ Wakamaliza
hapo, Maya akatoka kitandani kwa bibi yake akikimbilia chumbani kwake kwenda
kujitayarisha.
Saa mbili na dakika 20 Malcom alikuwa kwenye geti
akigonga kengele akiomba afunguliwe. Baada yakujitambulisha, Carter
akamfungulia. Maya, Tunda na bibi Cote walikuwa dirishani wakimchungulia.
Alishuka nakuanza kujitengeneza. Akajitengeneza cola ya shati. Akasimama kwenye
kioo cha dirisha cha gari, akaanza kuchomekea shati tena na tena. Tunda akaanza
kucheka. “Atakuwa anaoogopa!” Wakamuona anachomoa shati. Akajiangalia tena
kwenye kioo cha dirisha cha gari, akachomekea tena. Akarudi ndani ya gari.
Wakamchungulia wakamuona anachana tena twele. Wote wakacheka.
“Anaonekana anahali mbaya sana.” “Sidhani kama
ataingia.” Wakacheka. Akatoka tena. Wakamuona anaangalia saa yake ya mkononi.
Akazunguka kwenye mlango wa abiria. Akajaribu kufungua na kufunga akiwa
anajidai kama anamfungulia mtu. Akasimama mbele na nyuma ya mlango mpaka
akaridhika. Akajiangalia tena, akajiweka sawa, kisha wakamuona anatoa maua
mawili. Wakashangaa. “He is a gentleman!” Bibi Cote akasifia.
Akajipanga tena. Wakamuona anajiweka sawa, akaanza
kusogea kwenye ngazi. Wakati yupo ngazi ya tatu tu, akajikwaa na kuanguka
vibaya sana, wakamuona yupo ngazi ya chini kabisa, amelalia maua yote. Kila mtu
akashika mdomo. Wakamuona ananyanyuka haraka haraka. Akaangalia kushoto na
kulia. Akaokota yale maua. “No No No nooo!” Maua yakawa yameharibika kabisa.
Shati la rangi ya bahari alilokuwa amevaa na jinsi nzuri sana ya blue iliyoiva,
na vyote vilionekana kama vipya, vikawa vimeshafuka, zaidi shati. “Nooooo!” Malcom
akazidi kusikitika kila alipojiangalia.
Wakamuona anakusanya yale maua na kuyatupia nyuma
kabisa kwenye gari yake. Ndani ya buti. Wakamuona anatoa t-shert nyingine nyeupe.
Akavua ile shati aliyokuwa amevaa nzuri imempendeza lakini ikachafuka sababu ya
kuanguka, akavaa hiyo tshirt aliyoitoa garini huku akiangalia kulia na kushoto
kama kuna mtu anamuona. Kisha akaanza kujifuta ile suruali. Akaangalia muda,
akakuta amechelewa kwa dakika mbili. Akafunga gari kwa haraka, akaanza
kukimbilia ndani. Alipofika katikati ya ngazi akatulia. Wakamuona anajaribu
kuvuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu kama anayetafuta kujituliza.
Wakaanza kucheka wote. Mara wakasikia kengele.
Carter akaenda kufungua. Ile anaingia tu, akakutana na Net alikuwa akipita
karibu na hapo mlangoni alipoingia yeye. Net akakunja uso. Akamsalimia. “Vipi,
mbona asubuhi asubuhi! Kila kitu kipo sawa!?” “Kipo sawa kabisa. Nilitaka kuomba
kumtoa Maya kwa kifungua kinywa.” “Hivyo ulivyo hata nywele hujachana!” Net
akamuuliza kwa kumshangaa.
“Nilichana. Sema zimevurugika muda si mrefu hapo
nje, wakati navaa.” “Ulikuja hapa uchi!?” Net akaendelea kumchemsha. “No no
noooo, Sir. Not at all. Nilikuja nikiwa nimevaa kabisa, ila ikabidi
kubadilisha.” Malcom alisikika akibabaika haswa. Kule walikokuwepo Maya, bibi
Cote na Tunda walizidi kucheka taratibu wakisikiliza.
“Hukuamini ulichovaa kutoka nyumbani kwako!?
Unakuwa mtu usiye amini mawazo yako na uamuzi wako wa kwanza! Itakuaje utoke
hapa na Maya, ufike huko ugundue ulifanya kosa?” “Hapana, kuhusu..” “Nisikilize
nani tena?” Net akamsogelea. “Malcom, Sir.” Malcom akajitambulisha huku akimeza
mate kwa wasiwasi. Alishakuwa mwekundu. “Yes, Malcom. Maya sio binti wa
kuchezea na wamajaribio kama ulivyokuwa ukimuona kwenye mitandao. Sasa hivi
macho yangu yapo wazi nikiangalia kila mtu anayemsogelea Maya. Unanisikia?”
“Yes Sir.” Malcom akaitika.
“Kama upo hapa kujaribisha, uondoke.” “Hapana. Mimi
sijaribishi. Mimi namfahamu Maya kwa miaka mingi sana na sijawahi kumdharau
hata mara moja. Wakati wote namuheshimu na ninamtetea. Hata Roy anajua. Sipo
hapa kujaribu.” Malcom akajikaza na kujieleza kwa ujasiri. “Nampenda sana
Maya.” Akajikuta akiropoka. Net akamkazia macho. “Umesema?” “Nampenda Maya.”
Akaongea kwa utulivu, safari hii akaweka na hisia. “Na sipo hapa kujaribu. Na
wala sitaki kumuona anaumizwa tena. Ndio maana nipo hapa. Kama ukinipa nafasi
hiyo Sir, mimi nitahakikisha Maya anakuwa na furaha. Na ule moyo wake wa
ukarimu na kuamini watu, nitauenzi. Sitamchezea kama watu wengine walilolijua
hilo na kumtumia vibaya.” Malcom akaendelea kutetea hoja yake.
“Sipo hapa kujaribu au kuchunguza. Nipo hapa kwa
mtu ninayemfahamu kwa muda mrefu, tena nina uhakika au ujasiri wakusema
ninamfahamu zaidi ya kila mtu au yeye mwenyewe. Kwa kuwa nimemfuatilia kwa muda
mrefu sana. Nampenda Maya.” Kule alipo Maya akaanza kutokwa na machozi ya
furaha. Ilimgusa kila mtu. Hapo hata Net akafungwa mdomo katika hilo.
“Unatokwa jasho na hujachana nywele. Huwezi kutoka
na msichana kwa mara ya kwanza wewe mwenyewe ukiwa hujatulia. Carter
atakuonyesha kilipo choo. Ujisafishe kidogo, ndipo uitiwe Maya.” “Asante sana.
Nashukuru sana.” Karibia Malcom apige magoti. Net akaondoka. Akamsikia akihema
kwa nguvu na kuinama ameshika magoti kama asianguke. Net akacheka moyoni, hakugeuka.
Akaondoka asijue bibi yake na kina Maya walikuwa wakiwasikiliza wakati
akimchemsha Malcom.
Malcom alipelekwa kwenye choo cha wageni hapo
karibu na sebuleni. Akaanza kuchanganyikiwa humo ndani. Kulikuwa na kila kitu.
Akaanza kujisafisha akatamani kama aoge kabisa. Ila akajua atachelewa zaidi.
Akatumia taulo dogo kujisafisha. Aliporidhika ndipo akavaa tena ile t-shert
yake. Akaamua kuchomekea. Akajiweka sawa. Nakutoka.
“Upo tayari?” Ilibidi Carter amuulize maana alitoka
nakuanza kushangaa hapo. “Yes. Naomba uniitie Maya. Au unafikiri nizungumze na
bibi yake kwanza?” “Una maua?” Carter naye akaanza kumchanganya. “Nilikuwa nayo
kabisa na Mungu wangu ni shahidi. Lakini..”
Akasita Malcom. “Sina.” Akaongea kwa upole Malcom. “Lakini nampenda sana
Maya. Sitaki kuharibu mwanzoni.” Carter akampa tabasamu.
“Nina uhakika atafurahia moyo ulio muwazi kuliko
maua.” “Unafikiri hivyo?” Malcom akauliza kwa wasiwasi huku akimsogelea Carter.
“Najua hivyo. Upo tayari.” Malcom akatingisha kichwa kukubali. Carter
akashangaa. “Come on Son! Man up!” Akajiweka sawa. Akasimama kwa kujiamini. “Upo
tayari?” Carter akamuuliza tena. “Yes Sir.” Akajibu kwa kujiamini. Carter
akamtengeneza vizuri kola ya ile t-shirt.
“Halafu usiongee sana kwa Ms Cote, labda iwe lazima
sana. Maneno machache tu, tena yamuhimu.” Akamshauri huku akimpiga piga
mabegani. “Nitakumbuka hilo.” Akakubali kwa haraka sana. Akameza mate, Carter
akaondoka. Baada ya muda akaona bibi Cote na Maya wanakuja. Malcom akabaki
ameduaa kwa Maya. Maya alivaa vizuri na akapendeza sana. Maya akacheka, ndipo
Malcom akagutuka.
Akasalimia mikono ameweka kwa heshima huku
akimtizama bibi Cote na Maya. “Umependeza sana.” Akanong’ona huku akimwangalia
Maya. Maya akacheka. “Asante.” Maya akajibu na cheko la taratibu. Malcom
alibaki akimtizama.
Akakumbuka bibi Cote anamtizama. “Maam!” Akaanza Malcom. Bibi Cote akabaki akimtizama
na yeye. “Naomba nitoke na Maya kwa kifungua kinywa. Nitamrudisha salama.”
“Salama na mwenye furaha kama hivi alivyo hapa.” Bibi Cote akajibu kwa
msisitizo. “Nitahakikisha hivyo, Maam!” Malcom akakubali kwa haraka sana. “Okay.
Mimi sitawachelewesha zaidi.” Malcom akakumbuka amechelewa. “Samahani sana kwa
kuchelewa. Nilifika kwa wakati lakini...” Carter akasafisha koo kidogo kama
kumkumbusha. Akatulia. Akakumbuka asiongee sana. “Samahani kwa kuchelewa.”
Akajirudi. Lakini wote walijua hajachelewa. Kwani walimuona muda wote tangia
anaingia hapo kwenye ua wao.
“It’s okay, Mal.” Maya akamtuliza. Akajisogeza
taratibu kwa Maya. “Nilikuletea maua lakini niliyaharibu.” Akaongea kwa upole
na sauti ya chini. “It’s okay. Nimefurahi kukuona.” Maya akajaribu kumtuliza.
Akanyoosha mkono, Maya akamshika, wakatoka. “Umependeza sana Maya!” Wakamsikia
akimsifia tena wakati wanatoka. Maya akacheka. Akamfungulia mlango kama vile
walivyomuona akijaribisha kabla ya kuingia ndani. Maya alipokaa, akafunga
mlango. Akaenda upande wa dereva akawasha gari.
{Atafuataye, Hachoki}.
Kwa Mara ya Kwanza Malcom Afanikiwa Kumtoa Maya.
“Kabla hatujaondoka hapa, naomba nikutahadharishe
kitu.” Maya akaanza. “Unatoka na mimi.” Malcom akawa hajaelewa. Akabaki
akimsikiliza. “Inamaana haitakuwa siri, Malcom. Kila mahali utakapotokea na
mimi, watakuandika mitandaoni na magazetini. Haiwezi ikawa siri, labda tupate kifungua
kinywa hapahapa nyumbani.” Malcom akatulia kidogo.
“Najua ni nini nafanya Maya.” “Nina uhakika
hujafikiria kwa upande huu. Watakuchunguza kuanzia siku ya kwanza
utakayoonekana na mimi. Yale yako ya sirini ambayo hukutaka watu wasijue,
watayajua kwa undani, hadharani. Watakudhihaki kwa
kuwa upo na Maya Cote.” Maya akaanza kutokwa na machozi.
“Utakuwa gumzo kwa mabaya. Watu
watakukumbusha upo na mimi. Watakwambia nitakuharibia maisha yako. Mimi ni bomu
ambalo hulipuka wakati wowote. Naa..” “Please stop.”
Malcom akamtaka atulie. “Mimi sijui ulikuwa unakuwa na kina nani kwenye maisha
yako. Sijui wamekuwa wakikwambia nini! Lakini nipo hapa nikiwa nakufahamu Maya.
Nimechagua kuwa hapa kwa kuwa ni nafasi niliyoitamani muda mrefu sana, lakini
sikuwahi hata kufikiria kama naweza kubahatika kuwa hapa na wewe.” Malcom
aliongea taratibu tu.
“Na kama kuchambuliwa hadharani ndio garama yangu
yakulipa ili kuwa na wewe, nipo tayari.” “Wata..” “Naomba
niangalie mimi, Maya.” Akamkatisha. Maya akajifuta machozi na kumwangalia. “Tafadhali,
naomba kwa mara ya kwanza kwenye maisha yako, angalia karibu. Hapa. Halafu
funga masikio, macho na muda wako kwa watu wasiojalisha kwenye maisha yako.
Anza taratibu, utajikuta unazoea hayo maisha. Acha waandike watakacho. Acha
wakufuatilie. Acha wakuhesabie siku zilizobaki kurudi kwenye madawa.” “Kumbe unajua!?” Maya akashangaa, hakutegemea.
Malcom akamgeukia vizuri. “Naomba uamini nipo hapa
nikiwa nakufahamu Maya. Sitaki pesa yako wala umaarufu. Nataka kuwa na wewe
kama Maya, basi.” Ilimgusa sana Maya. “Asante Mal.
Kwa hiyo wakiniuliza juu yako, nisijibu?” Maya akauliza taratibu tu. “Mpaka
iwe muhimu na ukiwa na uhakika. Usikimbilie kujibu mtandaoni. Jipe muda
kujiridhisha na kila kitu. Ndipo ujipe muda wa kujibu na unaweza pia usiwajibu.
Huwajibiki kwao. Wakati mwingine ukimya au kunyamaza ni jibu kubwa na la
hekima.” Maya akavuta pumzi kwa nguvu, akajiegemeza nyuma.
Malcom akabaki akimwangalia vile alivyofunga macho.
“Njaa inauma!” Maya akasikika ametulia, akafungua macho na kumtizama Malcom,
macho yakagongana, akacheka. “Najua sehemu wanayouza kifungua kinywa kizuri
sana. Twende.” Malcom akaondoa gari. Maya akawa kimya akimtafakari Malcom na
maneno yake.
Malcom hakuwa tajiri kama wao, lakini alikuwa
kijana aliyesoma vizuri na mwenye kazi yakuheshimika kwenye jamii. Japokuwa
hakuwa akipata mshahara kama Maya, wala hana hata gari inayoendana na Maya,
lakini alijawa hekima na utulivu wa aina yake.
Huyu Maya ashachezewa sana. Akipita popote au
akionekana popote, huna haja yakujiuliza mwili wake ndani ukoje, ni kwenda tu
mtandaoni na kuangalia kama ni matiti au sehemu yeyote ya ndani ya Maya, utaona
tu. Alianikwa vilivyo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alipotoka tu, Tunda akamsikia bibi Cote akiongea
kwenye simu. “Maya ametoka hapa sasa hivi. Hakikisha
anarudi nyumbani leo, tena in one peace. I don’t want any surprises.”
Akakata simu. Tunda akajua ndio unatumwa ulinzi kumfuatilia Maya na Malcom.
Malcom&Maya
Hadharani Pamoja.
M |
alcom alimpeleka mpaka kwenye mgahawa wakawaida sana.
Lakini waliuza ‘Butter tarts’ nzuri sana. “Najua hapaendani na hadhi yako,
lakini hakuna sehemu utapata butter tarts nzuri hapa Norfolks, kama hapa.” Maya
akacheka taratibu. “It’s okay.” Malcom akamtizama kama anayejua anajikaza tu
kuwepo pale. “Kweli mimi nipo sawa, Mal. Tuingie na kuagiza chochote ulichokuwa
unakifikiria.” “Kama ndio hivyo sawa. Nakuahidi hutajuta.” “Okay.” Wakatafuta
sehemu ya kuegesha, kitu ambacho Maya hakuzoea. Alishazoea kufika kwenye mlango
wa mahoteli makubwa, watu wanakwenda kuchukua gari yake na kutafuta wao sehemu
ya kuiweka. Akitoka hapo, gari yake inaletwa palepale mlangoni.
Sasa siku hiyo walikwenda kuegesha gari wenyewe.
Gari ya kawaida sana. Maya hakuwahi kupanda gari ya hadhi ya chini kama ile.
Malcom akabaki kuwa muungwana. Akamfungulia mlango. Wakaanza kutembea kurudi
sehemu ulipo huo mgahawa. Akamfungulia na mlango, Maya akapita akimshukuru.
Maya akaanza kuangaza ili kutafuta meza ili akae. “Hapa wanapanga mstari
unachukua kahawa yako kama unataka kahawa na kitafunwa. Lakini naweza
kukuchukulia.” Malcom akamnong’oneza. “Sikujua!” Wakacheka kidogo.
“Niambie ni nini unataka, nitakuletea.” Maya
alizoea chakula kuletwa mpaka mezani. “No. It’s okay. Twende wote.”
“Unauhakika? Mimi naweza kwenda kuchukua na kukuletea.” “Nashukuru. Lakini
twende wote.” Wakasogea walipokuwa watu na wengine wakishangaa kumuona Maya
hapo, tena wakiongozana na Malcom! Ulikuwa mgahawa mdogo tu, lakini ulijaza
watu wanaoonekana wanawahi makazini.
“Watu wengi wanapapenda hapa. Lakini kwa kununua
vitafunio na kahawa, na kuondoka. Sio kukaa.” “Lakini sisi tutakaa. Si ndiyo?”
“Labda kama unataka tuondoke, naweza kubeba.” Malcom akajua pengine yale
mazingira yamemshinda. “Hapana. Mimi nipo sawa tu. Tunaweza kukaa, tukala.”
“Unauhakika?” “Tafadhali usiwe na wasiwasi na mimi. Nipo sawa kabisa.
Unakumbuka maisha niliyoishi ya club?” “Unaongelea zile club zenu za mapesa
mengi?” Maya akacheka taratibu.
“Naomba usiwe na wasiwasi. Nimefurahia kuwa hapa na
wewe.” “Kweli?” Malcom akauliza na kumshika mkono. Maya akacheka kwa deko huku
akitingisha kichwa. “Nimefurahi sana. Sijali tulipo, ilimradi tupo wote.
Unaniheshimu Malcom. Kwa hilo linaniongezea ujasiri.” Malcom akatoa tabasamu la
kuridhika na kumvuta mkono karibu akauweka kwapani. Maya akajiegemeza kidogo
begani. Wakaendelea kusogea na mstari wote kimya. Kama hawajui kama kuna watu
hapo wanawatizama.
Walifika mbele ya muhudumu, hata muhudumu
akashangaa. “Nimekufananisha au kweli ni wewe!?” Maya akacheka kidogo. “Umenifananisha
na nani?” “Maya Cote!” Maya akacheka kidogo. “Ni mimi.” “Wao. Ni mzuri zaidi in
personal kuliko kwenye picha.” Akacheka zaidi. “Asante. Mimi nitakula kile
atakachokula Malcom.” Akaongea huku akimtizama Malcom. Malcom akamtizama Maya
na kurudisha macho kwa yule dada ambaye bado alikuwa akimshangaa Maya.
Malcom akakohoa kidogo kama kumshtua. “Yuko wapi
Roy?” Yule mrembo akamuuliza Malcom. “Leo nimeamua kupunguza kelele humu
ndani.” Wakacheka na kutaniana kidogo ndipo wakaagiza vyakula vya wote wawili,
wakasogea pembeni wakisubiria namba yao itajwe wachukue chakula chao.
“Inamaana wewe hapa unafahamiana na watu wote na
umeshakula kila kitu?” “Yule msichana ni mtoto wa huyu mwenye mgahawa. Mimi na
Roy nilazima tupite hapa karibu kila siku kununu vitafunio kama si kukaa na
kuanza kula hapahapa.” “Lakini huyu msichana ni mzuri!” Malcom akacheka. “Hatuji
hapa sababu yake, Maya! Baba yake ni mcheshi zaidi. Na Roy anawapenda sana
wazazi wake. Akija ni lazima awachokoze.” Maya akatabasamu na kunyamaza.
Akamvuta tena mkono na kuushika. “Na ndiyo.
Nimeshakula hapa karibu kila kitu. Ila napenda ‘butter tarts’ zao zaidi.
Nzuri.” Maya akamwangalia na kumtolea tabasamu. Kisha akarudisha macho kwenye
ubao mkubwa wa menu uliokuwa umetundikwa mbele yao.
Baada ya muda ikatajwa namba yao, Malcom akaenda
kuchukua chakula chao ndipo wakaenda kutafuta meza iliyokuwa pembeni kabisa
kwenye ukuta wa kioo. Kwa hiyo walikuwa wakiona wapita njia, nje. Maya akaonja
hizo butter tarts zilizokuwa zikisifiwa. Malcom akabaki akimwangalia ili asome
sura yake aone kama atapenda. Akamuona anatafuna huku akisikilizia utamu wake,
akameza na kucheka. “Ni kweli ni nzuri.” “Nilijua tu utapenda.” Wakacheka na
kuendelea kula.
“Unafikiri siku nyingine unaweza kurudi hapa?” Maya akacheka kama anayefikiria huku
akiangaza kulia na kushoto. “Labda niwe na wewe. Lakini si peke yangu.” “Kwa
nini? Nilifikiri umependa hizi butter!” Maya akacheka kidogo. “Yule
aliyetuhudumia jana kwa chakula cha usiku pale nyumbani, anaitwa Gino. Anakipaji
cha ajabu sana. Unaona hii butter tarts?” “Ehe!” “Nikiichukua hii na
kumpelekea Gino, nikamwambia naitaka hii kwa kifungua kinywa kesho asubuhi,
atatengeneza kitu kama hiki au kinachofanana na hiki, ila kizuri zaidi.” Malcom
akashangaa.
“Haiwezekani Maya!” “Kabisa. Ndio maana sisi
tukitoka kwenda kula, sio sababu ya chakula, ni kwa sababu ya matembezi tu. Ila
tunaye mpishi mzuri sana. Lakini hiyo sio sababu yakutorudi hapa.” Maya akanywa
kahawa kidogo. “Ni nini?” “Kwa wakati huu, zaidi sifa yangu. Baada ya kutulia
sasa hivi na kusikia watu wazima na vijana waliotulia kama wewe wanazungumza
vipi juu yangu. Au wananitazamaje, imenitoa ujasiri kabisa Malcom.” Malcom
akatulia kidogo akimtizama.
“Unajua zamani nilizungukwa na watoto au vijana
wadogo au tuseme watu ambao wote hatukuwa tukiitizama jamii kwa macho haya
niliyonayo sasa hivi. Nilikuwa nikiishi katika ulimwengu tofauti na huu
ulimwengu ninao ishi sasa hivi.” “Ulimwengu wa sasa ukoje?” Akauliza taratibu
Malcom. “Ulimwengu wa kuwajibika katika kila eneo la maisha yangu. Kwa maneno
na vitendo. Nililelewa na Papa akiwa ananipa kila kitu. Kazi yangu ilikuwa ni
matumizi tu. Sikujali ni nani anayehusika au kuumia kwa kuwepo kwenye maisha
yangu.”
“Sasa, sasa hivi nimetulia ndipo
naangalia madhara niliyoacha kwenye familia za watu!” Maya akajifuta machozi. “Wapo
wakina mama wanao nilaumu kwa vijana wao. Wanasema mimi nilikuwa nikiwapa
watoto wao unga.” “Kivipi?” “Sijui Malcom!
Lakini ndivyo wanavyoniambia. Sasa sijui nilipokuwa nikinunua na wao walikuwa
wakitumia ya kwangu! Mimi sijui.” Maya akajifuta machozi.
“Haya, wapo vijana kama wewe.” “Ndio wakoje hao?”
“Wanao jiheshimu. Walio tulia. Waliokwenda shule na kutulia na kazi zao.
Wananikimbia Malcom. Hawataki niwe karibu nao kabisa.” Malcom akakunja uso. “Subiri
kwanza Maya. Hilo la vijana wanao kukwepa, umejua kutokana na watu wangapi
uliozungumza nao?” Malcom akauliza taratibu tu. “Kwa sababu usije kuchukua
mawazo ya watu wawili au mmoja, ukayaweka moyoni kuwa ni mawazo ya watu wote.”
Maya akabaki kama anafikiria.
“Maya?” “Unakumbuka nilikwambia kuna kitu nilitaka
kumwambia Tunda kabla hajatekwa? Ulipokuja nyumbani wakati unaondoka,
ukaniuliza kama nilimwambia. Nikakwambia bado. Unakumbuka?” “Nakumbuka.” Malcom
akaitika. “Basi jana niliporudi ndani baada ya kukusindikiza, nilipata muda na
Nana, Tunda pamoja na Net. Nikazungumza nao. Unataka na wewe nikwambie?” Maya
akauliza kwa upendo.
“Ningependa kujua na mimi.” Malcom naye akajibu kwa
kujali. “Kuna mtu. Nilimuomba tukutane sehemu kwa chakula cha mchana.” “Kama
date?” Malcom akauliza kwa wivu kidogo. “Hapana. Nilitaka tuzungumzie maswala
ya harusi. Ni kipindi namsaidia Tunda na maandalizi yake ya harusi. Sasa yeye anautaalamu
na mambo fulani. Nikataka tupange naye, tukishakubaliana ndipo nimshirikishe
Tunda.” Maya akanyamaza kidogo.
“Nini kilitokea?” Malcom akauliza baada ya kumuona
Maya amenyamaza kama anayeshindana na machozi. “Pale ndipo alipowakilisha
mawazo ya wengi na watu wanavyonifikiria.” Malcom akakunja uso kidogo. “Aliniambia
maneno mabaya sana. Kwa kifupi hakutaka hata kuwa karibu na mimi au hata
kuonekana na mimi hadharani ili kwanza nisimuharibie sifa na baadaye nisije
nikamuharibu.” “Kivipi!?” Malcom akauliza tena.
“Alisema huwa nina mtindo wa kuanza na vijana vizuri,
wakiwa vijana wazuri tu na malengo makubwa ya maisha. Kisha nawaharibia maisha
na kuwageuza mateja. Wanashindwa kuendelea na shule
au hata kazi.” “Ouch!” Malcom akafanya kama aliyeumia. Maya akacheka
huku akifuta machozi.
“Alitumia maneno mabaya sana akiwakilisha kile
ninafanya na vile nilivyo. Kuwa ni kama bomu. Ukilishika ni dogo na halionekani
kama halina madhara, lakini mwishoe nalipuka vibaya sana na kuathiri wengi. Kwa
kifupi alikataa kukutana na mimi.” “Unajua Maya, kuna watu wanauwezo mkubwa
sana wakuumiza watu, zaidi kwa maneno. Simjui ni nani na hao vijana anao
walalamikia ni kina nani lakini hata mimi kuna kipindi nilitoka chini ya
uangalizi wa wazazi nikatupwa kwenye ulimwengu huuhuu wanaoishi wengine na
kuishia kufanya maamuzi mabaya.” Malcom akaendelea.
“Yapo makosa nilifanya kama mwanadamu, na sina mtu
wakumlaumu kwayo. Siwezi nikageuka nyuma na kumnyooshea mtu kidole kwamba
amenisababisha kutenda niliyotenda. Sijui kama unanielewa?” Malcom akaendelea. “Nimelelewa
na mama kiasi na sehemu kubwa ni bibi. Wakati nikiishi nao au wakati nikiishi
na bibi, hatukuwa matajiri, lakini alijitahidi kuwekeza kwangu kiasi ya kwamba
nilitoka nyumbani nikijua mema na mabaya. Niliyoyafanya, nilijua ni nini
nafanya. Sina mtu wakumlaumu.”
“Mzazi unayemsikia anamlaumu mtoto wa mwengine kwa
ajili ya mtoto wake, huyo anatatizo tu.” Maya akatabasamu. “Kweli. Unawezaje
kumlaumu mtoto mwingine kwa ajili ya kuharibika kwa mtoto wako? Inamaana
hukumwandaa mtoto wako kukutana na watu wa namna hiyo.” Malcom akajiweka sawa.
“Wote tunatupwa kwenye ulimwengu uliojaa wema na
ubaya. Ni jukumu langu mimi kama baba, kumuandaa kijana wangu kukabiliana na
kila hali ndipo niwe huru kumruhusu kutoka nyumbani.” Malcom akaendelea.
Taratibu tu. “Huwezi kumruhusu mtoto asiye na maadili hata madogo tu nyumbani,
kwenda kukutana na marafiki ambao hata huwafahamu! Nyumbani tu anashindwa
kufanya maamuzi sahihi, unamwamini vipi akiwa club? Ataweza vipi kushinda
vishawishi vya huko!” Maya akainama.
“Huko ni kujifariji katika kushindwa kwao. Kila mtu
anatakiwa kuwajibika kwa maamuzi yake mabaya. Wewe unagarama ya kulipa kwa
maisha uliyoishi zamani, lakini sio kwa vijana waliokuwa wakitaka kutumia na
wewe madawa! Huo ni uongo na wanatafuta kukubebesha mzigo kwa kushindwa kwao.”
“Sasa wewe ungefanyaje?” Maya akauliza. “Kama hivyo wewe. Kukubali kuwa ulikosa
na kufanya maamuzi mabaya yaliyokupelekea kuishi kama vile. Nilisoma post yako
moja, na nilisikia mahojiano yako wakati ulipotoka rehab. Ukaomba msamaha hata
kwa mabinti wadogo waliokua na ambao bado wanakuangalia wewe kama msichana
kwenye jamii. Unakumbuka?” Malcom akamuuliza Maya, akatingisha kichwa.
“Ulisihi mabinti vizuri sana. Ukawafundisha na
kuwaambia yale sio maisha mazuri kwa mtu yeyote kuyaishi na wanatakiwa kutumia
kila fulsa Mungu anayowapa, hata ikiwa ndogo ya namna gani, kufanya kwa bidii,
na kusaidia wengine. Na mengine mengi. Basi. Endelea na maisha kama mtu
mwingine ila safari hii ukiwa makini zaidi, ili usirudi ulipoanguka.” Maya
akanyamaza.
“Huwezi kuruhusu watu wenye roho mbaya wakuumize
Maya. Lini na wewe utaishi kile ulichowaambia mabinti wengine waishi kama
utajifungia ndani?” “Sijui Malcom!” “Hapana. Sasa hivi ndio unatakiwa uishi na
kugusa maisha ya watu bila woga. Tena sasa hivi ni rahisi ukiwa unajua kuwa
ulikuwa ukifanyiwa makusudi na watu ili kukuweka kwenye hiyo hali. Basi, chagua
watu sahihi wa kukuzunguka na hakikisha unakuwa mahali sahihi. Fanya kile
unachoweza. Huna haja yakujibu kila shutuma. Acha muda ujibu shutuma, zaidi za
kijinga.” Maya akaanza kujisikia vizuri.
Jingine Tena kwa Maya!
W |
akati wapo katikati ya mazungumzo na ndio wanaanza
tu vicheko hata hawajui ni nani yupo pale akiwaangalia. Ni kama walikuwa kwenye
ulimwengu wao peke yao. Hawajali watu wengine. Maya akashangaa kitoto cha kiume
kimesogea pale mezani. “Hey!” Maya akamsalimia kwa upendo na tabasamu. Mara
akasogea mdada mwingine, mrembo tu. “Nilikwambia usiwe unakimbia!” “Acha
kumgombeza mtoto!” Maya akashangaa Malcom anamjibu huyo mrembo kwa hasira. Akahisi
ndiye mama watoto wake. “Ulitaka nimwambieje!? Kama kila kitu ninachozungumza
naye ni kosa, mbona sijaona leo sura yako wewe unayejidai ni baba mzuri? Leo
ilikuwa siku yako ya kuja kumchukua, mbona hukuja?” “Nilimtuma Roy aje
amchukue!” Malcom akajibu.
“Kwani Malcom ndiye baba yake?” “Tokea lini imekuwa
tatizo kwa Roy kumchukua Ethan?” Yule dada akavuta kiti palepale kwenye meza
yao akakaa. “Utalala na wasichana matajiri wangapi ili kuweza kufanya kazi
yako?” “Tafadhali usianze Zoe. Tafadhali sana.” “Hapana. Mimi nataka tu kujua.
Utalala nao wangapi?” Maya akaona awapishe.
“Ni sawa kusogea na Ethan pale pembeni ili kuwapa
nafasi? Sitakwenda naye mbali. Tutakuwa hapo nje tu.” “Unafikiri wewe ni
tofauti na kina Vic, Gina, Renee, Emily na wengineo alio lala nao huyu?” Zoe
mama mtoto wa Malcom akamuuliza Maya kwa kumkejeli. Maya akamwangalia Malcom. “Tafadhali
acha kumchanganya Maya, kwa shutuma zako ambazo huna hata..” “Kama unafikiri
mimi natupa shutuma tu, nenda kazungumze na warembo wenzako wakitajiri, uone
kama wote hawajamuona huyu akiwa uchi, kwa kisingizio cha kazi.”
“Ni sawa nikitoka na mtoto?” Maya akasisitiza swali
lake. “Sikuamini, na wala sikujui zaidi ya kukuona kwenye mitandao ukiwa uchi
na umelewa.” Zoe akammkatalia mtoto wake
kwa kumkashifu. “Tatizo lako ni nini Zoe!?” Maya akatoa tabasamu akainama
kidogo. Akachukua pochi yake. Akaifungua palepale mbele ya Zoe. Akamwaga kila
kitu pale mezani. “Hamna madawa humo ndani. Kwa hiyo kuwa na amani kuwa
ninachotaka ni kutoka tu na Ethan hapa, wakati mkizungumza. Sio kumpa madawa.
Na sitakuwa mbali na hapa. Ni hapo nje sehemu ambayo mtakuwa mkizungumza huku
mkimuona Ethan. Unafikiri ni sawa?” Maya akawa ametulia hata Malcom
hakutegemea.
“Hapana.” Akajibu Zoe kibabe. “Hata hivyo leo ni
siku yangu na Ethan. Na kwa kuwa naona umeamua kuja kunitukana hapa mbele za
watu, basi naomba Maya atoke na mtoto wangu, asisikie jinsi unavyozidi
kunitukana na kunidhalilisha.” Malcom na yeye akaongea kwa msisitizo. “Asante
Maya. Nitawafuata hapo nje baada ya muda mfupi sana.” Maya akamwangalia Ethan. “Unataka
twende nje nikufundishe kitu?” Ethan kimya. “Nina uhakika hukijui. Twende, dad
atakuja sasa hivi.” “Nenda na Maya, Ethan. Nitakuja sasa hivi.” “Okay.” Yule
mtoto akakubali kutoka na Maya baada yakupata ruhusa kutoka kwa baba yake.
Maya akaanza kuokota vitu vyake pale mezani
akirudisha kwenye pochi ili atoke na mtoto. “Na kwa taarifa yako tu, usifikiri
wewe ni bora kuliko wanawake wengine wote ambao anawapitia huyu Malcom. Kazi
yake ni kulala na warembo wenye majina kwenye jamii, ili kuwapeleleza.
Usifikiri ni mapenzi.” Zoe akamwambia Maya, lakini wazi alionekana ameishiwa
nguvu. Maya akacheka tu. Akamaliza kuweka kila kitu kwenye pochi akamgeukia
Ethan aliyekuwa amesimama kimya akisikiliza wazazi wake. “Twende Ethan.”
Akamshika mkono, wakatoka.
“Una miaka mingapi Ethan?” Akamuanza kwa kuwa
alimuona Ethan ameinama. “Minne.” Akajibu Ethan akionekana amenyong’onyea,
akajua pengine alikuja na mama yake akiwa anamgombeza huko njiani au kuna
lililotokea huko ndio maana akapooza hivyo. “Wao! Kumbe wewe ni kaka mkubwa
hivyo!” Ethan kimya. “Umekula?” Akatingisha kichwa kukubali. “Niangalie halafu
nikuonyeshe kitu.” Ethan akamwangalia. “Umeniona sasa hivi?” Akatingisha kichwa
kukubali. “Niangalie sasa hivi uniambie tofauti ni nini?” Ethan akamwangalia
kwa makini.
Maya akainama ili amfikie. “Nini?” “Nyusi hii ipo
chini hii juu.” Maya akacheka. “Na hivi?” Ethan akamwangalia. “Unafanyaje
hivyo!?” Ethan akamuuliza huku akianza kucheka. “Mimi nina super power ya
sikio. Naweza kutingisha masikio.” “Umepata wapi huo uwezo?” Ethan akauliza. “Nimezaliwa
nao. Jaribu na wewe.” Ethan akajaribu na kuishia kujicheka. “Unatingisha kichwa
bwana, unatakiwa kuchezesha sikio tu.” Ethana akazidi kucheka akitingisha
kichwa huku akimwambia Maya ameweza. “God, you are so Cute!” “Hata dad
ananiambia hivyohivyo na anasema am too smart for my age.” Maya alicheka sana.
“Unafikiri ni nini kilimpelekea kusema hivyo?”
“Naweza kumsoma mtu kwa kumwangalia tu.” “Haiwezekani Ethan!” “Na mimi ndio
super power yangu.” Maya akacheka sana. Ethan alionekana mtoto mdogo lakini
kweli anaakili. “Haya, nisome mimi uniambie.” Ethan akacheka sana. “You are so nice
na sweet.” Ethan aliongea hivyo kuwa Maya ni mzuri na mwema sana huku akicheka
na kumshangaza sana Maya. “Ethan!” “Kweli. Wewe ndivyo ulivyo.” Maya akabaki
ameduaa. Akaanza kumfikiria yule mtoto na wazazi wake. Mama yake anaongea kila
kitu mbele ya yule mtoto mwenye akili vile!
“Nafikiri umeshakutanishwa na Ethan.” “Anko Roy!”
Ethan akamkimbilia, Maya akageuka. Roy akambeba na kumkumbatia kwa upendo na
kumbusu. “Samahani kwa alichokwambia mama. Lakini ujue mimi nakupenda.” Ethan
akamwambia Roy. “It’s okay Ethan. Unafikiri nimekasirika?” Roy akamuuliza huku
amembeba. “Sijui!” Akajibu Ethan. “Hata kidogo. Leo ni lazima tukacheze
hockey.” “Halafu tunaenda kwa grandma Pauline kula cookies na hot coco?” Ethan akauliza. “Kabisa!” Akamjibu. “Yesss!” Akashangilia
Ethan. Maya akacheka.
Roy akamsogelea. “Upo sawa?” “Ethan alikuwa
akinishangaza vile alivyo smart kwa umri wake!” Alijibu Maya, akijua kabisa Roy
anachouliza. “Na ninaondoka na Ethan.” Wote wakageuka. Malcom na Zoe wakawa
wanatoka ndani. Wakawasikia tena. “Sisi tuna mipango na Ethan leo. Huwezi
kumchukua.” Akajibu Malcom. “Unataka ukamzungushe mtoto na mwanamke wako ambaye
hata jamii haimkubali!” “Niliposema sisi, namaanisha mimi na Roy. Huyo mtoto anasubiriwa
nyumbani kwa kina Roy. Jioni mimi, Roy, mdogo wake Roy na baba yake Roy
tunakwenda kucheza hockey. Baba yake Roy ameshaweka reservation kwenye huo
uwanja. Na ndio maana Roy alikuja kumchukua ili ampeleke kwa grandma Pauline
kwanza, amekuwa akimuulizia sana Ethan.” Akaongea Malcom kwa utaratibu kama
anayeepusha shari.
“Kwa hiyo unaenda kumtupa kwa mama yake Roy!?”
Akashangaa kwa ukali sana Zoe. “Tafadhali punguza sauti Zoe. Unamuogopesha Ethan
bila sababu! Kwa nini unashindwa kuzungumza kawaida tu. Hatugombani.” “Nani
amekwambia tunagombana?” Zoe akamjia juu. “Namuomba mtoto wangu Roy.”
Akamsogelea Roy. “Come on Zoe! Ni siku ya leo tu! Mama anataka kumuona Ethan
halafu jioni ndipo twende naye hockey. Kwa nini leo unakataa wakati jana usiku
ulikuwa ukipiga kelele aje achukuliwe leo asubuhi na mapema kwa kuwa unamambo
yako yakufanya?” “Ratiba imebadilika. Leo na mimi nataka muda na Ethan.” “Upo
naye jumatatu mpaka ijumaa. Leo tu!?” Roy akauliza kwa kumshangaa sana Zoe huku
amembeba Ethan.
“Nilikwambia acha kumng’ang’ania Ethan. Ni mtoto wa
Malcom sio wako. Kinachokushinda na wewe kuzaa mtoto wako ni nini? Zaa na wewe
mtoto wako umpelekee mama yako!” Akamnyang’anganya Ethan kwa nguvu. “Hiyo ni
roho mbaya sana Zoe! Usifikiri unayemuumiza hapo ni Roy, unamwadhibu mtoto bila
sababu! Kwa nini unafanya hivyo?” Malcom akamsogelea akiongea kwa kuumia na kwa
tahadhari kama wanao mugopa. Maya akashangaa.
Ethan akaanza kulia. “Nataka
kwenda kwa grandma Pauline. Nataka kuwa na dad na anko Roy, mami!”
Akamuweka chini na kuanza kumvuta. Akashangaa Roy na Malcom wamenyamaza
wanamwangalia tu. “Usilie Ethan, tutapanga wakati mwingine. Sawa Ethan?” Roy
akajaribu kumtuliza, Malcom akabaki kama bubu. “Come on buddy!” Roy akaendelea
kuwafuata kwa nyuma akimbembeleza Ethan. Huku Ethan akivutwa mkono na mama yake
wakielekea sehemu yakuegesha magari. “Nipe tano?” Ethan aliendelea kulia tu.
Roy akakimbilia mbele ya Zoe. “Naomba nisikilize Zoe. Niambie chochote
unachotaka nitakupa. Ilimradi leo utuachie Ethan.” Zoe akasimama.
“Chochote?” Zoe akauliza kama anayefikiria. “Chochote.”
Roy akamwakikishia. “Mmmh! Akafikiria.” Akamgeukia Malcom aliyekuwa amesimama
kimya nyuma yao palepale walipomuacha amesimama kama aliyeonywa asisogee hata
hatua moja. Malcom alikuwa mwekundu kama anayetamani kulia.
“Nataka jioni ya leo Malcom anisindikize kwenye
harusi ya binamu yangu, kama..” “No way Zoe! Hapana.” Hapo Malcom
akakataa. Zoe akamgeukia Roy. “Kuwa mtu unayefikiria Zoe! Nimekwambia usiku wa
leo ndio tunakwenda kucheza hockey sisi wanaume. Sasa..” “Nawezaje kumuacha
tena Ethan acheze na watu wengine halafu mimi mwenyewe nisiwepo?! Maana lengo
ni na mimi niwe na mtoto wangu!” Akaingilia Malcom na kumkata Roy.
“Nitamuhitaji aje anichukue na ile gari yako wewe
Roy, sio ule uchafu wake. Hakikisha yupo kwenye suti nyeusi. Saa kumi na moja
kamili, awe amefika mlangoni kwangu ili saa 11:30 jioni tuwe kwenye harusi.
Hatutakwenda kanisani. Ila kwenye sherehe tu.” Akaendelea kuongea Zoe kama
hajamsikia Roy wala Malcom. “Hapana Roy.” Malcom akakataa. Ethan akazidi kulia.
Roy akamtizama Ethan, akarudisha macho kwa Zoe. “Unataka avae suti nyeusi, na
viatu gani?” Roy akamuuliza Zoe.
“Come on Roy!” Malcom akamlalamikia Roy. “Hakikisha
unamuweka kwenye tabia yake njema. Na mwambie sihitaji mlinzi, ila mpenzi. Kwa
hiyo unaelewa ninachomaanisha.” Akamkonyeza Roy na tabasamu usoni. “Mabusu na
kukumbatiwa kila ninapohitaji.” “No way Zoe and Roy! Siwezi kumbusu na kum..”
“Deal.” Roy akamkubalia Zoe kwa haraka kama asiyemsikia Malcom.
“Na usinitanie Roy. Ukimchukua Ethan sasa hivi,
Malcom aje kwangu jioni. Akija Malcom kama yule!” Zoe akamnyooshea kidole
Malcom pale aliposimama. “Ujue jumatatu yupo mbele ya hakimu. Na ujue ndio
utakuwa mwisho..” “Acha kututisha Zoe. Nimekwambia Malcom atakuja kukuchukua
jioni. Nipe Ethan.” Akamuachia mkono Ethan. Ethan akaenda kumbusu mkono Roy,
kisha akamkimbilia baba yake. Malcom akambeba mtoto wake huku akifuta
machozi. “Na...” “No Zoe. Inatosha.
Huwezi kuendelea kutoa vitisho wala matakwa mengine. Wewe ondoka.” “Fine.” Akataka kuondoka Zoe, akamgeuka Malcom na
tabasamu la ushindi.
“Sina pesa ya kwenda saluni kutengeneza nywele na
kucha.” “Kwa hiyo?” Akamuuliza Malcom kwa hasira huku amembeba kwa kumkumbatia
mtoto wake. “Ndio unipe! Tunatokaje nikiwa sijapendeza!?” “Unafikiri mimi
naitoa wapi?” “Unamlala mtoto wa Cote, unakosaje pesa? Kwani wewe hakuhongi
kama wenzako?” Maya alikuwa ni kama mwili umeishiwa nguvu, umepigwa na ganzi
kama kilichompata Tunda mbele ya Vic na Renee.
“Unataka kiasi gani?” Akadakia Roy. “Ngoja
nifikirie. Mmmh! Kucha dola 85, nywele dola 120 naaa..” “Nakupa dola 200, Zoe.
Uondoke na usiongeze kitu kingine. Tafadhali.” Zoe akaanza kucheka. “Shida sana
kuwa karibu na wanaume maskini kama nyinyi wawili! Dola 200 tu! Labda Miss Cote
atabadilisha maisha yenu.” Zoe akavuta zile pesa kutoka mkononi kwa Roy,
akaondoka huku akicheka. Wakabakishwa pale wote kimya. Wameduaa Maya akikumbuka
maonyo ya bibi yake juu ya kutofungua moyo kwa haraka kwa Malcom. Akajicheka taratibu.
Hali ya Malcom ilikuwa imebadilika kabisa. Akabaki
amemuinamia mtoto wake aliyekuwa bado amembeba, akaendelea kumsugua mgongoni. “Mimi
naweza kuita dereva akaja kunichukua kunirudisha nyumbani.” Maya akavunja
ukimya. Kimya. Akamsogelea Ethan pale alipokuwa amebebwa na baba yake, akamgusa
taratibu mgongoni. Akageuka huku amejawa machozi. “Uwe na wakati mzuri kwa
grandma Pauline, na kwenye hockey.” Akatingisha kichwa kukubali. Maya akampa
tabasamu na kumfuta machozi.
“Bye Malcom.” Maya akamuaga kwa upole. Malcom
alikuwa mwekundu mpaka masikio. Alibaki akimwangalia Maya. “Asante kwa kifungua
kinywa.” Akaongeza Maya na tabasamu la kiuungwana lakini akisikika ndio anaaga
moja kwa moja. Kimya. Maya akamgusa begani, na kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mambo yanazidi kuchanganya. Ni kweli Maya
analipa gharama ya maisha machafu aliyoishi zamani na kusubutu kumtoa tonge
mdomoni. Malcom aliyekuwa na vigezo vyote, akamgusa moyo wake vilivyo! Naye
ndio huyoooo!
Jeff yupo njiani kumfuata Ritha kudai
haki yake. Kama amemudu kumuua mpenzi wake kwa ajili ya pesa, kwa Ritha je? Usipitwe
na muendelezo...
0 comments: