Nilipotea! Part 9 - Sehemu ya B
Maya kituo cha Polisi.
M |
aya alifika kituo cha polisi akakimbia mpaka
mapokezi, “Naitwa Maya Cote, nataka kumuona Malcom Marshall. Mlimkamata jana
usiku.” Akaanza Maya. Kabla hajajibiwa,
akamuona Roy. Akamsogelea. “Malcom yuko wapi?” “Ya safari hii ni mbaya
Maya. Zoe amamzushia uongo ambao hata dhamana hawezi kutolewa.” “Kwani ameua!?”
Akauliza Maya kwa hasira na sauti ya juu huku akirudi pale mapokezi ambapo wapo
polisi. “Maya Cote!” Akasikia sauti ya
bibi yake ikiita nyuma yake. Akageuka. “Neno jingine lisitoke kinywani mwako.”
Akamuona bibi yake na Logan, alifurahi Maya akamkimbilia na kumkumbatia. “Asante Nana. Asante kwa kuja.” Bibi yake
akambusu.
Logan akawapita na kusogelea mapokezi. Tayari
ikajulikana bibi Cote yupo pale. Mlinzi wake hakuwa mbali. Alisimama nyuma
kabisa. Kimya. Logan akasalimia. “Naitwa Logan, mwanasheria wa Malcom Marshall.”
Mkuu wa kituo akatoka. Bibi Cote kimya. Ila ule uwepo wake tu pale, ulishajaa
kila mahali. Yule mkuu wa kituo akamsogelea bibi Cote aliyekuwa amesimama na
Maya. Mlinzi nyuma. Bibi Cote akampa mkono kiustarabu tu. Kimya.
“Malcom yupo chini ya ulinzi kwa tuhuma za
ubakaji.” Wakamsikia polisi wa mapokezi akimwambia Logan. “Mmeshathibitisha
hilo?” Akauliza Logan taratibu. “Ndio tupo kwenye uchunguzi.” “Basi, mpaka
mtakapothibitisha, naomba niondoke naye.” Logan akaweka msisitizo akijua bibi
Cote anasikiliza. Mkuu wa kituo akasogelea pale mapokezi. “Tupo kwenye
uchunguzi kwa kuwa simu ilipigwa na Zoe, mama watoto wake. Mpaka polisi kufika
eneo la tukio, Malcom alikuwa ameshaondoka. Amekamatwa njiani tu. Kumtoa sasa
hivi bila kukamilisha uchunguzi, itakuwa...” “Naomba usubiri kwanza.” Logan
akamwingilia.
“Unataka kumshikilia mpaka mmalize uchunguzi!?”
Logan akauliza kwa kushangaa. “Hivi mnajua Malcom ni mfanyakazi ambaye jumatatu
anatakiwa awepo ofisini? Ana mtoto ambaye anamlipia pesa za matunzo.
Atakapofukuzwa kazi kwa mashitaka ambayo bado hamjathibitisha kama ni kweli,
halafu ikajulikana kuwa ni uongo, mnajua nitarudi tena hapa ya madai ya kiasi
gani?” Logan akamuuliza. Kimya. “Wakati mnatafakari hayo, naomba kuzungumza na
mteja wangu kwanza.” Akaomba Logan akijiamini. Akaruhusiwa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati Logan anazungumza na Malcom kwenye chumba
alichoelekezwa, Maya akiwa anasubiri na bibi yake, Net naye akaingia hapo kituo
cha polisi. “Samahani Maya, nilichukua muda mrefu kidogo.” “Sio kwamba
ulichelewa, mimi ndio niliondoka muda mfupi tu uliposhuka.” Net hakuwa
ameelewa. “Pale ulipoondoka tu na nikakwambia nitasubiri, nikaona kwenye
Facebook ya Zoe, emeandika mkasa mzima wake na Malcom kuwa alimbaka kwa nguvu
na kutoroka, ndio polisi wamemkamata na kumfunga. Nilipaniki Net. Nikashindwa
kusubiri.” Net akamsogelea na kumkumbatia.
Akamgeukia bibi yake. “Asante kwa kuwa hapa na
samahani.” “It’s okay.” Bibi yake akarudisha tabasamu la kumtuliza. “Vipi,
Logan anasemaje?” “Nimapema sana. Tumpe muda.” Bibi Cote akajibu. Net akambusu
Maya kichwani. Wakatulia wakimsubiria Logan. Baada ya mazungumzo ya muda kidogo
kati ya Logan na Malcom, Logan akaomba vipimo kadhaa afanyiwe Malcom siku hiyohiyo
kabla hata yakwenda nyumbani. Akaomba afanyiwe pale kwenye maabara ya palepale
polisi, kabla hata ya kutoka pale. Akiwaambia itawasaidia hata wao kwenye
kukusanya ushahidi wao.
Yaani kupimwa Malcom ili kuona kama watakuta DNA ya
Zoe mwilini kwa Malcom. Kwa kuwa bado hakuwa ameoga wala kunawa, na Zoe alikuwa
na mikwaruzo aliyosema amepatiwa na Malcom kabla na wakati wakumbaka. Logan
akaomba Malcom apimwe chini ya kucha zake kama zitakuwa na ngozi ya Zoe.
Akapimwa na sehemu zake za siri kama kweli alimwiingilia Zoe.
Akafanyiwa vipimo hapo, kisha bibi Cote akaomba
askari mwingine aongozane nao kama shahidi kuwa wanatoka hapo na kuelekea
kwenye hospitali ya kulipia moja kwa moja kwa vipimo zaidi. Alitaka huyo askari
awe kama shahidi kuwa Malcom hakupitia popote. Tokea walipomkamata hakuoga na
wala hakujisafisha. Yote hiyo ni kwa ajili yakupata ushahidi zaidi na
wakutosha. Bibi Cote alitaka ushahidi wa kila pande ili safari hii wamkamate Zoe
kama amedanganya, na kumdhibiti kabisa.
Alipofanyiwa vipimo alivyoshauri Logan palepale
kwenye maabara ya polisi, ndipo akaruhusiwa kwa dhamana ya pesa nyingi sana.
Roy akashangaa bila swali au kupepesa macho, Logan akatoa hundi na kuandika
kile kiwango chote cha pesa, na kuwakabidhi ile hundi askari husika. Akaambiwa
Malcom anatakiwa asisafiri mpaka uchunguzi na kesi iishe.
Baada yakukamilisha taratibu zote za pale kituo cha
polisi, Malcom akasindikizwa na askari polisi kwenye gari ya polisi mpaka
kwenye hospitali aliyowaambia Logan. Familia hiyo ya Cote na mwanasheria wao nao
walifuata nyuma pamoja na Roy aliyekuwa akifuata nyuma nyuma tena kimya kimya
naye alikuwa akiendesha gari yake mpaka kwenye hospitali hiyo ya kulipia.
Walifika hapo, Logan akaongozana na yule askari na
Malcom mpaka kwa daktari. Baada ya kushauriana na daktari, Malcom akaandikiwa
tena vipimo vingine. Ni kama alianza upya kabisa kutokana na ushauri wa huyo daktari.
Wakaongozana tena na yule askari mpaka maabara ili Malcom afanyiwe vipimo kwa
upya ambavyo sasa vingekuwa ni vya Logan atakavyovitumia mahakamani siku ya
kesi pamoja na ushahidi wa huyo daktari
mwenyewe afike na aeleze kile alichoona kwenye vipimo hivyo. Daktari mwenyewe
alifahamiana vizuri tu na bibi Cote. Alishakubali kutoa ushirikiano wote na
hiyo sio mara ya kwanza kumtumia daktari huyo. Wakati Malcom akifanyiwa vipimo hivyo,
wasindikizaji wake walikuwepo hapo wakimsubiri, na safari hii kesi ya Malcom
ilishachukua sura mpya, Zoe asijue amecheza na moto.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Zoe alishazoea kuwazungusha Roy na Malcom. Na wala
kufungwa kwa Malcom haikuwa mara ya kwanza. Roy ndiye aliyekuwa akimtoa huko
mahabusu kila mara kwa kusingiziwa hili au lile. Kadiri alivyojisikia Zoe. Kuna
kipindi pesa za matunzo ya mtoto alibadilisha njia ya kupokea kwa Malcom. Yeye
mwenyewe akasema akaunti yake imesumbua, kwa hiyo awe anampa pesa taslimu. Kwa
miezi minne mfululizo wakawa wanapeana tu mkononi.
Baada ya hiyo miezi minne, Malcom na Roy wakiwa
ofisini wakashangaa wanafuatwa na barua kuwa Malcom anatakiwa mahakamani kwa
kutolipa matunzo ya mtoto kwa muda wa miezi minne. Kesi ilipotajwa, Zoe alikana
kabisa kuwa hajapokea pesa kwa miezi minne mfululizo. Malcom aliwekwa jela.
Akawa anatoka asubuhi kwenda kazini, nakurudi kulala jela mpaka muda wake
aliopangiwa ulipoisha.
Ilimuma sana kila aliyemzunguka Malcom, lakini
hawakuwa na jinsi ya kumfanya Zoe. Kwanza ni mama watoto wa Malcom na bado
alikuwa na dhamana yakuishi na Ethan. Lazima kunyenyekea.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Sasa safari hii kesi ya Malcom imeshikwa na kina
Cote. Wapo hapo bibi Cote akiwa ameshapewa historia nzima ya Malcom na Zoe.
Hapo Logan anafanya kazi yake akijua kesi zote alizokuwa ameshashitakiwa nazo
Malcom na huyo mzazi mwenzake. Walijua ujanja wa Zoe, na bibi Cote alimwambia
Logan aweke kikomo ili kama inatokea Malcom atamuoa Maya, asihamishe hizo kashfa
na skendo kwenye familia yake.
Familia hiyo ya Cote ilibaki hapo sehemu ya
kusubiria wagonjwa, kimya kila mtu akiwaza lake. Maya hata hakutaka kuuliza
habari za mama yake. Net naye akabaki akimtafakari mama yake. Bibi Cote kama
kawaida yake, alishajua hilo limeisha, mawazo akahamisha kwengine. Net akamuona
anavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu, akajivuta nyuma kabisa ya kiti,
akaegemea na kutulia kabisa.
Net alikuwa amekaa kati kati ya Maya na bibi yake.
Maya amejiegemeza ubavuni kwa Net, Net akamzungushia mkono mabegani kwake.
Akajisogeza kichwa mpaka akafikia shavu la bibi yake, akambusu. “Nakupenda
Nana.” Bibi yake akacheka kidogo. “I know Son. Najua.” Net akajiegemeza kichwa
kwa bibi yake kidogo kama anayefikiria kitu, akarudi kutulia. Net huyo
alitakiwa jana yake awe amefunga ndoa takatifu, kanisani kabisa wala si
bustanini au sehemu nyingine, kanisani kama ilivyo desturi ya familia yao. Bado
walishikilia mila na desturi za zamani.
Ilikuwa ifanyike harusi kubwa sana iliyokuwa
ikisubiriwa na maelfu ya watu na muda huo alitakiwa awe fungate na mkewe. Na muda huo pia kwa bibi huyo alitakiwa awepo
kanisani kwa ibada ya jumapili kama mkristo wa kawaida, lakini waliishia kituo
cha polisi na kuhamia hospitali moja hadi nyingine. Bibi Cote alikuwa akitoa
ushirikiano wa ajabu na wa mara ya kwanza kwa Maya. Uwepo wake huyo bibi kwa
siku hiyo ya jumapili katika sehemu hizo ulishangaza kila mtu na kuogopesha,
lakini kila alipofika, aliwaambia yupo pale kama bibi ya Maya tu na si
vinginevyo. Maya alikuwa akilifurahia hilo na kujivunia kuona bibi yake yupo
naye kwa wakati huo.
Kila mmoja alikuwa ametulia pale,
wakiendelea kuwaza yao na watu kuwashangaa kwa kujiiba familia hiyo iliyojaa
skendo zilizofululiza, na jana yake naye Maya akaongeza yake tena
iliyosindikizwa na kejeli ya huyo aliyembusu hadharani kuishia kumbaka mama
watoto wake, Zoe. Wengine walisema Malcom alitaka tu pesa ya Maya lakini
mapenzi yapo kwa mama watoto wake, Zoe. Wengine walimsema Maya kutokana na
kashfa zake za nyuma, kuwa ni mtoto anayesumbua familia. Katikati ya matatizo
makubwa ya familia yao, yeye hajali. Anafanya kama zamani alivyokuwa mlevi,
akifanya mapenzi bila haya, tena hadharani tu!
Kwa hakika familia hiyo, walipamba mitandao, redio,
television na magazeti ya udaku. Kila
mtu akiongea lake kwa zamu. Zaidi wakithaminisha pesa atakayoondoka nayo Tunda
mara atakapomtaliki Net kwa kashfa ya ngono iliyozizima na kushangaza kila mtu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakaona yule askari, Logan na Malcom wanatoka na
kuwasogelea. Wote wakasimama. “Naruhusiwa kumshika sasa hivi?” Maya akamuuliza
bibi yake baada ya Malcom kuwa anawakaribia. “Kila kitu kimeenda sawa?” Bibi
Cote naye akamgeukia Logan. “Kila kitu kimeenda sawa. Nafikiri nina kila kitu
ninachokihitaji. Nimemruhusu hata huyu askari aondoke tu. Lakini nimemshauri
Malcom kwa kipindi hiki, akae mbali kabisa na Zoe. Naona ameelewa na ameahidi
atakaa naye mbali.” Logan akajibu kifasaha.
Bibi Cote akaonekana ameridhika na hayo maelezo.
Hakuongeza neno, akamgeukia Maya na tabasamu. Maya akajua ndio ameruhusiwa. Akamsogelea
Malcom aliyekuwa amesimama nyuma kidogo pembeni ya yule skari. Akamkumbatia. “Nanuka
Maya!” “Sijali. Unaendeleaje?” “Nilikuwa nipo kwenye hofu kubwa sana. Sijafanya
chochote anachosema Zoe. Tafadhali naomba uniamini.” Maya akambusu. “Nakuamini Malcom na ndio maana
nipo hapa.” Malcom akamkumbatia tena kwa nguvu, akavuta pumzi kama aliyepata
aghueni.
Maya alibaki ametulia hapo mikononi kwa Malcom hata
asijali bibi yake na Net wanasubiri hapo nyuma yao. “That means a lot to me,
Maya. Nilijua unaweza kunitilia mashaka.” “Hata kidogo.” Maya akaongea huku
akitingisha kichwa kwa kumuhakikishia. Wakacheka kidogo. “Asante kwa kuja.”
Akambusu Maya kama mara mbili hivi mfululizo ndipo wakageuka, maana Malcom
aliwapa mgongo alipomkumbatia Maya, na alijitahidi kuzungumza naye kwa sauti ya
chini.
Akiwa amemshika Maya, hapohapo akamsogelea bibi
Cote akiwa na Logan. “Nashukuruni kwa kila kitu. Zaidi kuwa hapa na Maya. Najua
sio rahisi. Ni aibu na fedheha.” Malcom akaanza mbele ya bibi Cote, Net, Logan
na Roy aliyekuwa pembeni kidogo akimtizama Malcom bila kummaliza.
“Mungu wangu ni shahidi, sijambaka Zoe. Kama
hawatabadilisha matokeo, vipimo vitaonyesha. Sijambaka. Mimi mwenyewe
nilishtuka waliponisimamisha polisi njiani na kuniambia nipo chini ya ulinzi
kwa kosa la ubakaji na kumjeruhi Zoe.” Malcom akaendelea taratibu. “Nilishangaa
kwa kuwa mbali ya kumshika mkono wakati wa kuingia ukumbini, tena kwa
kunilazimisha, na kucheza naye mziki, sikumgusa tena Zoe. Nilipotoka pale
ukumbini na Maya na nikahakikisha amepanda gari, Zoe alitoka na kutaka
nimrudishe nyumbani akiwa amekasirika sana. Sikutaka kuzungumza naye chochote
njiani wakati namrudisha kwa wakati ule, kwa kuwa ninamjua Zoe.” Bibi Cote
akakunja uso kidogo.
“Zoe anahasira na anapenda kupigana. Kwa hiyo
nilijua nikiongea chochote na mimi ndiye niliyekuwa nikiendesha, nilijua
anaweza kuanzisha ugomvi tukiwa njiani, tukaishia kupata ajali mbaya kama sio
kifo.” Malcom akaendelea. “Na yeye akanyamaza mpaka nilipomfikisha kwake, kabla
hajashuka aliniambia hivi, ‘utalipa kwa yote uliyonitendea. Na safari hii
nitahakikisha hutatoka jela hata kwa dhamana.’ Sikumjibu. Akashuka.”
“Wakati nataka kuondoka, akapiga jiwe gari kwa
nguvu. Ikabidi nisimame. Niliposimamisha tu gari, akaja upande wangu akaanza
kugonga kioo kwa nguvu, nikashusha kioo nikifikiria pengine aliniambia kitu halafu
sikusikia. Nikashangaa anaanza kunipiga makofi. Nilichofanya nilikwepa na
kuondoa gari nikijua anataka ugomvi tu. Na hata hapo naapa hata sikumrudishia.
Kwanza huwa simrudishii.” “Kwani huwa anapenda kupigana!?” Akauliza Maya kwa mshangao.
“Zoe?”
Akauliza Roy kwa mshangao, wote wakamgeukia. “Yaani hata siku ile pale
mgahawani, ilinibidi kuwahi kuja, nikijua angewafanyia fujo.” “Na pia nivile na
wewe ulikuwa umetulia na ukaonekana mstaarabu zaidi yake, ndio maana alikosa
sababu ya kuanzisha fujo.” Malcom akamkata Roy.
“Kwani Malcom hakukwambia kama Vic alishampiga
Zoe?” Bibi Cote na Net wakamgeukia tena Roy na kutoa macho. “Vic yupi?” Akauliza bibi Cote. “Vic huyuhuyu Vic
aliyekuwa akimdhuru Maya. Zoe alitaka kumfanyia fujo, Vic akampiga sana tu.”
Roy akaendelea. “Walichofanya wazazi wa Vic na mwanasheria wao, baada ya Vic
kumpiga sana Zoe, wao ndio wakawahi polisi. Yaani wao wakawa kama ndio
wamemshitaki Zoe. Zoe akaomba msamaha, wakafuta kesi. Kwa hiyo Zoe anapenda sana
kesi na ugomvi.” Kimya.
“Nenda ukapumzike Malcom. Tutawasiliana.” Maya
akamuongelesha kwa upendo. Malcom akambusu kichwani kwa upendo na kumvuta
karibu. Safari hii karibu kabisa ya ubavu wake, mbele ya Net na bibi Cote huku
akimwangalia. “Malcom!” Roy akamshtua kwa kumwita kidogo. Malcom akamwangalia
Roy, akamkonyeza. “Nashukuruni sana kwa kuja.” Akarudia Malcom kuwashukuru kina
Cote kama aliyekosa chakusema.
“Nitawapa muendelezo.” Akaaga Logan baada yakuona
hakuna chamaana tena. “Unisalimie Maria na watoto.” “Asante sana.” Logan akamjibu bibi Cote kwa heshima na
kuondoka. Maya akajua bibi yake na Net wapo pale kwa ajili yake, na hawawezi
kuondoka bila yeye ikabidi na yeye aagae. “Tutawasiliana Malcom. Nenda
ukapumzike.” “Nikiamka nitakupigia.” Maya akambusu Malcom. “Asanteni sana.”
Ikabidi na Roy naye aage kwa kushukuru. Net na bibi Cote wakageuka kidogo. “Asanteni.”
Akarudia. “Anytime. Naamini safari hii Logan atalimaliza hili.” Net akaongea
kwa kujiamini, akiwahakikishia.
“Ethan yuko wapi?” Akauliza bibi Cote. Malcom
akamgeukia Roy. “Alikuja kumchukua usiku uleule.” Hapo hapo Malcom akabadilika
sura, mpaka macho yakawa mekundu. “Kama alivyosema Net. Naamini safari hii
Logan atamaliza kila kitu. Jitahidi kufuata kile alichokushauri. Ukiwa na
swali, mpigie Logan, atakushauri vizuri.” Malcom akajifuta machozi. “Pole
Malcom.” Maya akamsugua mgongoni kama kujaribu kumfariji.
“Sasa kuhusu mtoto?” Maya akamuuliza bibi yake kama
ndio hakimu au mfanyakazi wa ustawi wa jamii. “Jumatatu Logan atafuatilia.
Naamini mpaka jioni atakuwa na jibu lakueleweka.” Angalau Malcom akaridhika na wengine.
Ni bibi Cote ameongea. Wakaagana, Maya akaondoka na bibi yake pamoja na Net.
Roy akaondoka na Malcom.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Waliporudi nyumbani wakaambiwa Tunda amelala, Bibi
Cote akamwita Net ofisini kwake. Maya akaenda moja kwa moja chumbani kwake. Net
alimweleza bibi yake yote yaliyoendelea kati yake na mama yake. Lakini akamuona
ametulia kama amekosa raha. “Asikuogopeshe. Ritha ni mjanja na anaakili, lakini
safari hii amekamatwa na hatakaa akatoka. Naomba fikiria juu ya familia yako
sio aliyokwambia Ritha.” Net akafikiria kidogo.
“Lakini Nana, sidhani kama huyu mtu yupo sawa na sidhani
hata kama anadhamira! Kwa upande fulani nimejuta kwenda, Nana. Nimepata majibu
ambayo ni heri nisingeyajua. Natamani kama ningefanya kama Maya.” Bibi Cote
kimya. “Hana majuto na chochote kile!” Net akaendelea kama anayevuta
kumbukumbu. “Hajutii kutotulea! Hajutii kuharibu mahusiano na sisi! Hajutii
kutaka kumuangamiza Tunda! Ni kama hana dhamira kabisa!” Net alilalamika.
“Kitu kilichomshtua tu, ni pale
nilipomwambia nitamfilisi. Basi! Ni kama..” “Niangalie
Net.” Net akajifuta machozi. “Mungu amekupa dhamana ya mambo mengi. Amekuamini
na mke mzuri, mdogo ambaye unajua ni wapi amepita na wapi ameathirika. Pesa. Na
sasa ni baba.” Bibi Cote akasimama na kumsogelea. “Sasa hivi ni wakati wa wewe
kusimama kwa nafasi yako kufanya kwa juhudi zako zote, huku ukiangalia nyuma na
kurekebisha kule ambako sisi wote. Kuanzia baba yako, mama yako, Papa, hata
mimi, kule kote tulikokosea. Rekebisha na msaidie Tunda kuwa mke mzuri na mama
anayetamani kuwa. Msaidie Maya aishie kwenye mikono ya mwanaume mzuri. Kama
hivi leo ambavyo umefanya. Najua ni ngumu, lakini kile kiasi cha kujishusha.
Kuacha mke wako akiwa mgonjwa na mtoto mdogo kuwepo pale na yeye. That’s a lot,
Son!” Akambusu.
“Am so proud of you.” “Asante Nana.” “Hakikisha
huishii hapo. Ni ngumu, kunagarama yakulipa, lakini nakujua utaweza tu.” Net
akamtizama bibi yake.
“Mbona kama unakitu hujui ukiweke vipi? Ni juu ya
Malcom?” Bibi yake akamuuliza huku akimcheka. “Nahitaji muda Nana!” “Nimekuona
jinsi unavyomtizama. Tafadhali mpe nafasi.” Net akasimama. “Sijui Nana!”
“Niambie ni nini kinachokufanya umfungie moyo?” Net akafikiria. “Amejawa
matatizo mazito kila kona ya maisha yake! Tunaanza mahusiano na kurekebisha
matatizo yake wakati na sisi tuna mambo mengi sana! Maya mwenyewe hana muda
mrefu tokea atoke rehab. Anajiingiza tena kwenye matatizo mengine! Anakuwa ni
mtu ambaye anamikasa mizito kila wakati!” Net akaendelea kulalamika.
“Huyu mtu alishakuwa na ndoa ya kanisani. Kwa nini
alioa na kwa nini aliacha?” “Watu wanakosea Net.” Bibi yake akajaribu kutetea. “Na
huo ndio wasiwasi wangu Nana. Ndoa sio kitu cha kukurupuka. Msichana kama Zoe
ni kama Vic tu. Hawana tofauti na hawajifichi. Alifanyaje maamuzi ya kumuoa na
kupata naye mtoto? Ananitia mashaka kwenye maamuzi yake na uchukuaji wake hatua
pia kwenye mambo, haonekani kama ni kijana anayeelewa ni nini anataka kwenye
maisha! Sijui kama unanielewa?” Net alikuwa akiongea huku amesimama.
“Maya amepitia kwenye ukuaji uliomuathiri. Sitaki
aje aishie kwenye ndoa itakayo muathiri pia. Sijui kama unanielewa Nana?” “Njoo
hapa.” Akanyoosha mkono, Net akamsogelea. Akamshika mikono yote miwili. “Sipo
kipofu katika hili. Nilishaulizia tabia zake. Na uzuri wote ule, hana mwanamke
yeyote na wala hakuanzisha mahusiano yeyote yale baada ya kuachana na Zoe. Ni
kijana ambaye anajitunza na ni mtu wa familia. Katika ugumu wote huo, hajatelekeza
mtoto wake. Nimeambiwa walitaka kumuhamisha hapa Norfolk apelekwe Toronto kwa
ahadi ya mshahara mkubwa tu, lakini alikataa sababu ya mtoto wake.” Bibi yake
akaendelea.
“Ungedhani ndio angekubali ili awe mbali na Zoe,
awe anatuma tu pesa za matumizi, lakini alishangaza viongozi wake pale alipokataa
kwa sababu yakuwa karibu na mtoto wake. Tukio la jana limezidi kidogo tu,
lakini nimeambiwa hayo ndiyo yamekuwa maisha ya Malcom. Jela na mahamani. Zoe
anamwendesha vile atakavyo. Lakini amebaki. Kwa sehemu kubwa sana, kwa sasa
hana sifa za kuwa mtumishi wa CSIS. Alishapoteza vigezo hivyo tokea amuoe Zoe,
lakini nimeambiwa hao vijana wawili wanawashikilia kwa karibu sana. Na inabidi
kufumbia macho matatizo ya Malcom, sababu ya utendaji kazi wao yeye na Roy.”
“Walichokifanya kwa Maya. Kuanzia kupeleleza mpaka
kumuokoa, wanasema sio tukio geni kwenye chombo cha CSIS. Wanawatumia sana, na
ni wazuri. Ninachotaka kusema ni hivi. Ni kweli Malcom hana kitu upande wa sifa
na pesa, sababu ya kashfa zake na Zoe. Anakatwa pesa kubwa sana kwa ajili ya talaka
ambayo aliiomba yeye mwenyewe Malcom.” “Kwamba pale alipo anamtunza Zoe pia!?”
Net akashangaa kidogo. “Yeap! Ameambiwa mpaka Zoe atakapoweza kujitegemea, na
yeye Zoe nasikia anafanya makusudi. Hatafuti kazi kwa kuwa anajua mshahara wa
Malcom upo. Na hilo Logan atashugulikia.” Bibi Cote akaongeza.
“Ila ni kweli Malcom anampenda Maya, ile
yakutojifanya.” “Hilo halina ubishi.” “Basi msaidie kufikia viwango unavyotamani
kuona mume wa Maya yupo.” Net akaweka mikono kichwani, akageuka. “Sina muda wa
kufix au kurekebisha maisha ya watu Nana! Nina mambo mengi. Nina...” Akanyamaza
kama aliyekumbuka kitu. Akamgeukia bibi yake na uso uliojaa cheko la kujisuta. “Nitafurahi
‘kujikana na kumsaidia. Najua itakuwa ngumu, lakini najua nitaweza’.”
Akarudia maneno aliyoambiwa mwanzoni na bibi yake kwa kejeli. Bibi Cote akaanza
kucheka.
“Ukitulia, na akili zako zinatulia. Usiruhusu Ritha
akakuchanganya wewe Net! Wewe umekuwa Cote kwa sababu.” “Nimekubali Nana. Ni
hasira tu za mama. Lakini najua Malcom anampenda Maya. Na hilo ndilo
ninalotamani kuliona kwa Maya. Anapendwa kwa dhati ili atulie. Maya ana moyo
mzuri sana. Anastahili mtu ambaye atamuenzi.” “Sasa hivi umeanza kuongea.”
Wakacheka.
“Na sasa hivi lazima uwe naye makini sana.” Bibi
Cote akamtahadharisha. “Nimemuona. Ameweza mpaka kunigombesha!” Wakacheka kwa
sauti ya chini na kuendelea kuteta. Angalau hasira za Net alizopandisha
alipokwenda kukutana na mama yake zikaisha. Wakapanga mipango mingi tu, safari
hii wakiwa na amani kuwa Ritha na Jeff wamekamatwa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Juma hilo likaanza na hekaheka. Logan na kesi ya
Malcom akifuatilia kila kona. Juu ya mtoto wa Malcom ambaye Zoe anamtumia kama
fimbo huku mahakama kumpa yeye dhamana kubwa kuliko baba yake. Akaendelea
kufuatilia malipo makubwa anayokatwa Malcom kwa ajili ya Zoe ambaye anakataa
kutafuta kazi. Na uthibitisho kuwa Zoe amedanganya hakubakwa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Net naye akaanza kuhangaika ubalozini tena kuondoa
vile vikwazo alivyowawekea kina mama Penny ili wafike Canada week hiyo. Jumatatu
alipothibitishiwa tu kuwa Ritha alipelekwa jela siku ile ya jumapili, ndipo
alipowasiliana na ubalozi na kuwapigia simu kina mama Penny. Akimsihi zaidi
mama Penny afike yeye kwa haraka, hata kama mchungaji na wengine watachelewa,
lakini yeye awahi kwani Tunda anamuhitaji sana.
BadoTunda hakuwa akitaka mtu yeyote amsaidie yeye
wala mtoto. Maya ndio akawa msaada wakati bibi Cote na Net wakienda kazini. Na
Ms Emily naye akawa msaada kwa sehemu tena Tunda akimwita, mara chache sana.
Napo akimsikia tu mtoto wake analia, hata kama anausingizi kiasi gani, anaamka
nakutaka apewe mtoto wake. Tunda akawa hapati muda wakutosha kupumzika.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Bibi Cote yeye alikuwa akihangaikia kifungo cha
Ritha kuhakikisha safari hii hashindi kesi na anafungiwa sehemu yenye ‘maximum
security’. Ulinzi mkali sana ambao hawasiliani na yeyote. Na kweli alitolewa
hospitalini na maumivu yake vile vile na kupelekwa kifungoni.
Familia ya Mchungaji na baba yake Tunda,
nchini Canada.
I |
likuwa siku ya jumatano Tunda alikuwa amelala kulekule
chumbani kwa mtoto wake mida hiyo ya mchana, akiwa usingizini akasikia mtu
anamwita sauti yataratibu kama mama Penny. Akajua anaota. Maana hata kumpigia
simu, Net alimwambia asubiri. Kwa hiyo hawakuwa wamewasiliana kwa muda mrefu
kidogo. Tunda akaendelea kulala. “We Tunda!” Tunda akafungua macho. Akabaki akimtizama
mama Penny. Akatulia kwa muda akidhani anaota. Wakabaki wakiangaliana kwa muda.
“Mama Penny!?” Akaita taratibu. “Vipi? Nimeambiwa unaumwa.” “Kwa hiyo sio
ndoto?” Mama Penny akaanza kucheka.
“Nimekuja na timu yangu yote.” Tunda akakaa. “Wako
wapi!?” “Sebuleni. Wako na Maya pamoja na Net. Nimeingia hapa nimekukuta
umelala sana. Nikakuacha, hapa nimerudi kukuangalia tena kujua kama umeamka.”
Tunda alishaanza kulia. “Naumwa mwenzio.”
Mama Penny akakaa pale kitandani, Tunda akamsogelea na kumkumbatia. Akaendelea
kulia. “Nini?” “Sijui hofu! Kidonda cha operation
kinaendelea vizuri. Ila nimejawa hofu, sina raha dada.” “Pole mama. Pole
sana. Net ametusimulia kila kitu tulipofika tu hapa. Lakini Tunda, tumekuombea
sana mdogo wangu. Mungu yupo na wewe. Usigope kabisa. Sasa hivi lea mwanao kwa
furaha.” Akajaribu kumtuliza, maneno mengi ya mama Penny, nyumba hiyo isiyozoea
kelele, kwa mara ya kwanza wakamsikia Tunda anacheka kwa sauti. Mpaka Carter
akashangaa.
Tunda alikuwa akicheka kama sio yeye aliyekuwa
anamuhofu kila mtu! Tokea arudi hapo ndani na mtoto wake, hata uchangamfu mdogo
aliokuwa nao, ulimwisha kabisaa. Siku hiyo akatokea Tunda mwingine tena.
Kicheko kikajaa hapo chumbani kwa mwanae. “Ninavyocheka kwa sauti! Mpaka Cote ataamka!”
“Mbona nishaanza kazi ya ulezi! Mwanao hayupo hapo kitandani kwake.
Nilivyoambiwa tu ukimsikia akilia unaamka,
nikaomba aende akakae na babu yake hapo sebuleni na kina Penny wamshangae mtoto
wa kizungu, ili ulale kidogo.” Tunda akacheka sana.
“Na nimzungu haswa dada! Hafanani hata na Net!
Hajachanganya hata!” “Maya ametuambia amefanana na babu yao.” “Hata Nana
amesema hivyohivyo.” Mara kina Penny wakaingia. “Sasa sio mumvamie. Mwenzenu
anamshono wa upasuaji.” Mama yao akawazuia. “Tumemuona mtoto wa kizungu! Alikuwa
amelazwa kwenye kitanda cha kizungu, sasa hivi dady yupo naye!” Penny akaanza
bila hata salamu. Tunda akazidi kucheka.
“Anti Tunda unaishi kwenye jumba la kifalme!” Pendo
naye akadakia. Tunda akazidi kucheka. “Yaani nyinyi viumbe nilikuwa na hamu na
nyinyi! Halafu Net hakuniambia kama mtakuja!” Net akaingia na tabasamu la
ushindi. Tunda akatoka pale kitandani na kumfuata pale mlangoni na kumbusu. “You
are the best husband in the entire wide world.” Tunda akambusu tena. “I know.”
Net akajibu kwa kujigamba kuwa yeye anajua kama yeye ni mume bora. Tunda
akampiga ngumi ya bega.
“Kweli sitanii. Hii ni suprise ambayo sikuwa hata
naifikiria. Asante Net.” “Nilijua tu utafurahi.” “Umemuona Penny lakini?” Net
akamtizama Penny na kuanza kucheka. “Tumekutana tu pale uwanja wa ndege, akaniuliza
kama bado nakumbuka kiswahili.” Wote wakacheka. “Halafu akauliza kama mtoto ni
wa kizungu.” Tunda akazidi kucheka. “Yaani Penny nyinyi! Sasa umemuona?”
“Nimemuona na mama ameniosha mikono nikamshika nywele. Ni za kizungu!” Tunda akazidi
kucheka na kushangaa.
“Basi nimelala sana! Hata sikuwasikia wakati
mnafanya yote hayo.” “Maya alituambia ndio umelala tu. Tukaona tukuache
tuondoke na mtoto. Maana maswali yalianza hapahapa! Pendo naye akataka kujua
kama macho ni ya rangi ya bahari!” Wakazidi kucheka. “Nikaona tutoke naye tu
huyo mtoto, akaamkie hukohuko mbele ya safari, tuyaone na hayo macho.” Tunda akabadilika
kabisa. Furaha ilimjaa, utafikiri ndio anaingia kwenye hilo jumba lenye kila
kitu, kumbe amepata watu anaofahamiana nao, na anauhakika kuwa wanampenda kwa
dhati. Hata wazo la mtoto kama yupo salama au la, halikupita tena kichwani
mwake. Yeye kicheko tu. Akatoka kwenda kumsalimia baba yake na mchungaji.
Ilikuwa ni furaha iliyojaa kilio kwa Tunda.
Hakuamini kama kwa mara nyingine tena, yupo nyumba moja na baba yake. Baada ya
salamu mchungaji akataka waombe wote kwa pamoja. Wakamuombea Tunda na mtoto, na
kukemea roho ya hofu ili Tunda ajawe amani yakulea mtoto wake. Angalau nyumba
hiyo siku hiyo watu waliomba, wakaongezewa na vicheko.
Kina Cote na mahakamani.
K |
ina Cote wakawa na kesi mbili kwa wakati mmoja. Ya Malcom
na ya Ritha ambayo ilinguruma haswa, na kupamba vyombo vya habari. Mama anayedhuru
watoto wakuwazaa mwenyewe na watoto wanaomshitaki mama yao! Halafu ni kina Cote
sasa! Jeff alitoa ushahidi wake wote bila kuficha jambo hata moja. Akaeleza
sehemu ya kwanza ambayo walikutana Malinda na Ritha kumkabidhi pesa ya kwanza.
Net akamsikia bibi yake amesema “Yess!”
Maana Ritha alitumia hoja ileile kuwa siku ile
alikiri kwa kuwa Jeff alimshikia risasi na alishampiga. Kwa hiyo alikana kuwa
hamfahamu Jeff wala Malinda, ila alikiri kwa kuwa alikuwa anatishwa na Jeff. Pale
pale mahakamani, wakati kesi inaendelea. Jeff akitoa ushahidi wake kuwa
walitumwa na Ritha, bibi Cote akaandika kiujumbe kwenye kikaratasi kumwambia
Logan aombe kwa hakimu apewe muda wakuleta ushahidi mwingine.
Logan aliposoma tu ule ujumbe, akafanya kama
alivyoambiwa na bibi Cote. Akamuomba hakimu. Kesi yao ikaairishwa. Wakapewa
tarehe ya kurudi mahakamani wakiwa na huo ushahidi mwingine.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati kina Cote wanahangaika kutafuta ushahidi wa
kumfunga Ritha, Logan naye akahamia kwenye kesi ya Malcom. Hiyo haikusumbua.
Malcom alikuwa afisa usalama pia. Wenzake walimbemba vizuri sana. Na kwa kuwa
Logan alishaanza vizuri, haikusumbua hata kidogo kumshinda Zoe.
Siku walipoitwa mahakamani. Kesi ikawa nyepesi
sana. Polisi waliomkamata Malcom siku ile usiku na kumsindikiza kwenye vipimo
pia wakawa mashahidi wa Malcom. Logan akawakilisha ushahidi wake wote, Zoe
akaishia kuwa mkosaji. Malcom hakutaka kumshitaki. Yeye akasema anataka haki
yake na ya mtoto wake, tu. Akapewa siku sawa za kuwa na mtoto wake. Matumizi
kwa Zoe yakafutwa kwa kuwa mahakama ilimwamuru kwa kipindi hicho ambacho wanagawana
au ku share custody ya mtoto, siku ambazo mtoto yupo na Malcom, yeye aende
kazini.
Na palepale mahakamani, Malcom akaomba kuongea.
Akasema mtoto wake anaakili sana. Haoni kama ni sawa awe anakaa tu nyumbani,
anataka kumuanzisha shule na yeye mwenyewe ndio atalipia. Mahakama ikakubali.
Hatimaye Maya naye!
W |
akati wanatoka mahakamani siku hiyo ya mwisho ya hukumu
kati ya Malcom na Zoe, Malcom akiwa amesindikizwa na familia yote ya Roy na baadhi ya
wafanyakazi wenzake. Maya naye akiwa amesindikizwa na bibi yake pamoja na Net
na mkewe, Tunda. Na ndivyo walivyokuwa wakifanya kila siku, siku ya kesi ya
Malcom. Wote watatu yaani mpaka Tunda, kumsindikiza Maya, ili Maya asiwe peke
yake mahakamani. Na kweli ilimsaidia sana Maya. Akachukua sura mpya mitandaoni.
Hakuwa kituko tena. Kwani safari hii familia yake, mpaka bibi Cote, alisimama
naye kila mahali. Badala ya kashfa kwa Malcom na Maya, ikawa sifa sasa.
Sasa wakiwa nje ya mahakama siku hiyo wakipongezana
na kufurahia ushindi wa Malcom, familia ya Roy kama ndugu wa karibu wa Malcom
na Ethan, ikishukuru familia ya Cote, Malcom akapiga goti mbele ya Maya. Pakazuka
ukimya mkubwa sana kwani kila mtu alijua ni nini Malcom anakaribia kufanya.
Hata vyombo vya habari, wapiga picha na watangazaji waliokuwa wamewapa kina
Cote kipaumbele wakiwapiga wao picha, nakutaka bibi Cote au hata Net, azungumze
chochote, wakawageuzia kamera, macho na masikio yao Malcom na Maya.
“Umesimama na mimi, na kuniamini kipindi ambacho
nilihitaji sana. Hapakuwa na mazingira yakuaminika tokea siku ya kwanza
tunakutana Maya. Lakini nimeona mapenzi ya kweli kutoka kwako. Nimeona vile
unavyokuwa na mimi na Ethan. Umejawa upendo na heshima kwangu, Maya. Unawapenda
na kuwaheshimu wazazi wangu.” Akimaanisha wazazi wa Roy. Grandma Pauline naye alikuwa
hapo na mumewe, akakubali kwa kutingisha kichwa huku akifuta machozi. “Kweli wewe ni mwema Maya. Tunakupenda.” Akaongeza
Grandma Pauline, watu wakacheka kidogo. Bado Malcom alikuwa amepiga magoti
mbele ya Maya, amemshika mikono yake yote miwili.
“Nataka uishi na mimi pamoja na Ethan. Tutengeneze
familia ambayo hata mimi sikubahatika kuwa nayo. Itakayojengwa na mapenzi tu.”
Maya alibaki anacheka kwa furaha akijifuta machozi. “Marry him already!” Akasikika
Roy, watu wote waliokuwa wamewazunguka wakacheka. “Marry me, Maya!” Akasisitiza
tena Malcom akiomba ndoa kwa mrembo huyo. “With one condition.” Akajibu Maya. Kila
mtu akatulia wakitaka kujua hilo sharti la Maya. Ni picha tu ndizo zilizokuwa
zikisikika mlio wake. Wakavuta watu pale nje ya mahakama. Wakasogea kushuhudia.
“Anything.” Malcom akawa tayari kwa lolote. Maya
akacheka huku aking’ata meno akimfikiria. “Ni nini?” Akauliza Malcom kwa shauku
akiwa bado amepiga magoti, akitaka kujua hicho kitu anachotaka Maya. “Kama
tutaishi na Nana!” Watu wote wakacheka tena, mpaka bibi Cote. Malcom akatoa kimkoba
cha pete mfukoni bila kujibu, Maya akashangaa. “Ndio umekubali!?” “Oooh yeah!
Popote nitaishi na wewe Maya, hata kama ni chini ya mti ilimradi tu niwe na
wewe.” Watu wakapiga makofi nakufurahia jibu la Malcom ambalo lilijaa hekima si
lakilimbukeni. Malcom akamvalisha ile pete, akasimama kupata busu sasa. Malcom
alilitendea haki hilo busu, ungependa kuona jinsi alivyomshikilia kimwana huyo.
Picha zilipigwa kila kona. Ni kweli kwa kuwaangalia tu, ungejua wanapendana.
Malcom akaomba msamaha kwa kina Cote. “Samahanini
sana. Najua huu sio wakati mwafaka wa kumchumbia Maya, lakini nisingeweza
kusubiri. Najua nimefanya makosa mengi kwenye maamuzi yangu, lakini si katika
hili na kumpenda Maya.” “Hakuna muda mwafaka kwenye mapenzi Malcom. Na wakati
wote mapenzi hayatakiwi kusubiri. Nawapongeza sana, na karibu kwenye familia.”
Net akajibu yeye wa kwanza na kumpa mkono, wakakumbatiana. Ilimfurahisha sana bibi
Cote, na kumgusa Maya. Ilikuwa na maana kubwa sana kwao. Ni Net amemkaribisha
Malcom kwenye familia! Tena kwa kumkumbatia! Hata Malcom alijisikia vizuri.
Bibi Cote naye akapata nafasi ya kuwapongeza palepale.
Naye akamkaribisha Malcom na Ethan kwenye familia. Kila mtu akajua jinsi Ethan
alivyogusa moyo wa huyo bibi. Alimsifia na kumwambia ni jinsi gani anasubiri
kwa hamu kupata naye muda wa pamoja. “Mimi sijui kupika kama grandma Pauline,
ila naamini tutakuwa na wakati mzuri tu.” Bibi Cote alimwambia Ethan nakufanya watu wacheke. Tunda naye
akawapongeza kwa kuwakumbatia ndipo kila mtu akapata nafasi yakuwapongeza.
Kwa heshima kubwa sana, familia ya Roy, yaani
wazazi wake wakawakaribisha kina Cote nyumbani kwao kwa sherehe ya kuwapongeza Malcom
na Maya. “Tunajua huu sio wakati mwafaka kwenu kufanya sherehe, lakini
tunawakaribisha kwa chakula cha usiku ili kumshukuru Mungu pamoja.” Akaongea
grandma Pauline akimtizama kwa heshima zote bibi Cote. Bibi Cote naye akamtizama
Net na Tunda. “Na mimi nataka nikale cookies za grandma Pauline.” Tunda akajibu
huku akicheka. Wote wakacheka. “Nafikiri kila mtu anataka kula cookies za
grandma Pauline. Ethan amekuwa akizisifia sana.” Net akaongeza kwa mkewe.
Inamaana wamekubali huo mwaliko. Maya akashukuru sana familia yake. Angalau
kina Cote wakawa wameshinda kesi moja ya Malcom na angalau safari za mahakamani
zikapungua ikabaki kazi ya kukusanya ushahidi kumaliza kesi ya Ritha.
Hatima ya Ritha yawa
Mbaya zaidi na alivyo fikiri.
N |
dani ya muda huo waliopewa na mahakama, bibi Cote
akaomba mtu avute picha kutoka kwenye satelite siku na muda aliosema Jeff kuwa
Malinda na Ritha walikutana kwa makabidhiano ya pesa. Bahati nzuri Malinda na
Ritha walikutana Park. Sehemu ya wazi kabisa. Yule mtu wa bibi Cote, alitoa
picha za Malinda na Ritha, kama waliokwenda kupiga picha studio. Akamkabidhi
Logan. Wakatafuta ni wapi Ritha alipata kiwango chote cha pesa bila kuonekana
amekitoa kwenye akaunti zake za hapo nchini. Ndipo sasa Net kama mmiliki wa
Cote, akawasiliana na benki za Tanzania kuomba benki statement zote za kampuni
aliyokuwa amefunga mama yake, lakini akaunti za benki hakuwa amefunga.
Ritha alijua hakuna mtu ambaye angeweza kufikiria
hilo. Kuwa akaunti za kampuni aliyofunga bado zinafanya kazi! Akasahau mwembe
hauzai pera. Net akafikiria na kuomba kupewa benk statement. Ndipo wakajua
alichukua hiyo pesa kutoka nchini Tanzania. Wakawa wamemkamata Ritha vizuri
sana. Wakawa na ushahidi ambao Ritha hawezi kupinga tena. Kiwango kilekile cha
pesa Ritha alichokitoa kwenye dola akaunti ya akaunti ya Cote ya nchini
Tanzania ndicho hicho hicho Jeff alisema alimlipa Malinda kama malipo ya awali.
Na ushahidi mwingine ukawa sasa wa hizo picha
ambazo zilionekana Ritha na Malinda wamekaa kwenye benchi la Park, kama
waliokuwa kwenye mazungumzo kabisa. Na siku ya kesi mtaalamu wa mahakama alipopewa
hizo picha kuzitazama, akathibitisha si zakutengenezwa ni picha za ukweli. Siku
hiyo ndipo hukumu ya Ritha ikatolewa. Kifungo cha maisha tena kwenye jela yenye
maximum security,
kama muuaji hatari sana. Kwani hata njama zake za Tanzania, wakati Net
alipokuwa akihojiwa mahakamani hapo, alizieleza kwa undani kabisa, mbele ya hakimu
na waandishi wa habari.
Alimshitaki mama yake bila kumbakisha huku akisema
hana sababu yakumsingizia mama yake ambaye aliacha maisha yake huko nchini
Canada na kwenda kumtumikia bila kujua anatumika kwenye mali zake mwenyewe. Na
hilo Net alilishitaki kuwa mama yake alijua, lakini alimficha ili kumdhulumu
tu. Akimpa mshahara kama mfanyakazi wa kawaida, na baadaye kumsingizia kuwa
alikuwa akimwibia.
Bibi Cote alikuwa akishangaa vile Net alivyokuwa
amejipanga kwenye kumshitaki mama yake bila hata kuzungumza naye. Net
hakumbakisha mama yake. Aliongea mengi huku akiomba vyombo vya usalama
vimsaidie yeye na mke wake Tunda, kumfungia Ritha, ili waweze kukuza familia
ambayo yeye na Maya waliikosa na ili pia Ritha asiendelee kumwaga damu ya watu
wasio na hatia.
Aliposikia mama yake anakwenda kufungiwa kwenye
aina ya jela aliyomuahidi siku alipoenda kumtembelea hospitalini akiwa na pingu,
Net akafurahia sana moyoni, akamgeukia bibi yake akijua hiyo ni kazi ya bibi
yake. Bibi Cote akamkonyeza, wakacheka. Wakati Ritha anataka kutolewa pale
mahakamani bibi Cote akamwita taratibu. Ritha akageuka. “Gotcha!” Akamnongoneza
kwa sauti ya chini iliyojaa ushindi kuwa amemkamata. Ritha akageuka bila
ya kujibu.
Si Maya wala Tunda waliotaka kufika mahakamani siku
za kesi ya Ritha. Maya alisema yeye hataki hata kuiona sura yake. Ila anataka
kujua kama yeye yupo huru. Akimaanisha uhuru wake unategemea na kufungwa kwa
mama yake. Kwa muujiza na kufahamika kwa bibi Cote, kesi ya Ritha ilichukua
miezi mitatu na nusu tu mpaka hukumu yake. Hilo likawa jambo lililowaridhisha
wote.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Bibi Cote akaona wao kama familia, wanawajibika kwa
vyombo vya habari na raia ambao walikuwa wakiwafuatilia kwa karibu sana.
Angalau kuzungumza nao na kuwaambia kilichokuwa kikiendelea na kujibu maswali
yao. Waandishi wa habari wakakusanyika kwa wingi sana sehemu yakutoa habari
katikati ya mji. Bibi Cote, Net, Tunda, Maya na Malcom waliwasili hapo. Mdahalo
ukaanza. Bibi Cote akaeleza kwa kifupi kilichokuwa kikiendelea kwenye familia
hiyo. Akakiri makosa yake yeye kama mlezi wa Maya na Net. Akatoa nafasi ya
maswali matano tu.
Moja wapo likawa kwa Tunda ambaye hakutegemea
kabisa. “Watu wengi wamekisia kiasi cha pesa ambayo utapata baada ya kumtaliki mumeo.
Kwa hakika ni pesa nyingi sana. Unalichukuliaje hilo?” Mpaka Net akabadilika
rangi, lakini wakashangaa Tunda anacheka taratibu. “Pesa bila Net! Labda nipewe
pesa na Net wangu.” Akajibu Tunda huku akicheka taratibu. “Huyu atabaki na mimi
tu, hana pakwenda.” “Na juu ya kosa lake la kuzini baada ya ndoa?” Wakamuongezea
Tunda swali la haraka haraka. “Nani ambaye angepata nafasi yakumlevya mtu kama
Nathaniel Cote na asitumie bahati hiyo ipasavyo! Na by the way, ndoa takatifu
bado. Namdai ndoa ya kanisani kwa hiyo msiseme baada ya ndoa, mnanifupishia
safari. Nahesabu ndoa baada ya kiapo cha kanisani.” Tunda akampiga kidogo Net
begani, angalau akabadilisha ile hali ya kashfa pale, wakacheka.
“Ahadi ipo pale pale.” Net akajibu na kumbusu. “Na
usichelewe hivyo!” Watu wakacheka tena. Angalau wakasafisha ile hali ya hewa,
ujasiri ukarudi kwa Net na kuweza kuongea machache. Yakaongezwa maswali
machache kwa Maya na Malcom, wakatangaza tarehe yao ya harusi kina Cote wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kwa heshima ya kaka yake, Maya akasubiri mpaka kaka
yake aoe ndipo na yeye aolewe. Maandalizi ya harusi kati ya Net na Tunda
yakaanza upya. Tena safari hii na Tunda ambaye amejifungua. Hana kichefu chefu,
hana uchovu wala ugonjwa. Jasiri akijiamini na kujua yeye ndio mama Cote haswa!
Amri yote ipo kwake! Na Net naye akawa amejifunza kutokana na makosa. Adabu na
heshima kwa kila anachofanya Tunda ikaongezeka.
Muda wote huo mama Penny na familia yake bado
walikuwepo pale. Mama Penny akisaidia kumlea Cote na kulipwa pesa nzuri tu.
Shida ya kurudi Tanzania ambako kanisa lilishakufa na biashara ya upambaji
ilishaanza kusumbua ikaanza kuingia akilini. Wanaishi kwenye jumba la kifahari,
wamepewa malazi upande wao. Wapo huru. Watoto wakaingizwa kwenye shule za hapohapo
wakipelekwa na kurudishwa! Wanakula chakula chakupikiwa na mtaalamu wa mapishi
kabisa! Hamu yakurudi Tanzania ikaisha.
Mchungaji akachangamkia maisha. Akamuomba kazi Net.
Akamwambia anaweza hata kumpa lori moja akaanza kuendesha. Net akafurahia
utayari wake. Akampa kazi upande wa boti zinazozungusha watalii kwenye mto. Wakaanza
kujiingizia dola. Mama Penny kwa kumlea Cote, mchungaji kwenye kazi hiyo kwenye
boti akizungusha watalii. Wanaishi na kula buree. Watoto wanasomeshwa shule
nzuri. Yote hayo Net alifanya kwa ajili ya mkewe, kumfanya ajisikie vizuri. Na
mtoto akawa analelewa vizuri. Tunda akawa huru hata kutoka na kufanya vitu
vingine sababu ya mama Penny kuweza kummudu mtoto wake.
Kipindi hicho Tunda alimwambia baba yake apumzike
tu. Alimpeleka hospitalini na kufanyiwa
vipimo kama yeye. Kisha akamtafutia mtu maalumu wa kumfanyia mazoezi na chakula
maalumu chakumjenga mwili. Mzee huyo akawa anafurahia uzazi, huku akisubiri
siku ya harusi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
M |
aandalizi
yao yalipokamilika, ndani ya mwezi tu, Net na Tunda nao hatimaye wakafunga ndoa
takatifu kanisani, wakiwa wamezungukwa na watu wanao wapenda. Baba yake Tunda
ndiye aliyemshika mkono kumkabidhisha Tunda kwa Net pale kanisani. Kama shauku ya Tunda. Tunda alipendeza sana.
Akakata kiu yake. Alivaa gauni ambalo lilisimuliwa mitandaoni bila kikomo.
Alikuwa amesimama mbele ya mchungaji mbele kabisa kanisani, lakini shela ilikuwa
katikati ya kanisa hilo. Na ilikuwa imejaa vizuri sana.
Bibi
Cote alimvalisha taji ya alumasi tupu kichwani. Na ule weusi wa Tunda, alijawa
alumasi, usingejua kama ni yule Tunda aliyezaliwa na kutupwa milima ya Ulugulu,
mjini Morogoro. Ambaye hata hakuwa akizungumza si kingereza tu, hata
kutengeneza sentensi ya kiswahili ilikuwa ni shida!
Siku
hiyo ndipo watu waliposhuhudia utajiri wa Cote. Kuanzia muonekano wa Tunda
mpaka sherehe yenyewe. Habari zake na picha zake na Net, zilipamba magazeti ya
uzunguni, akabakia gumzo.
Mrembo
huyo kutoka Africa, tena Tanzania, alikataa talaka yenye pesa nyingi, akisema
anamtaka Net. “Kama nitalipwa pesa yote hiyo halafu
wakanipa na Net, sitafikiria hata mara mbili. Lakini si pesa bila Net wangu.” Usemi huo wa Tunda ulifunga wengi
midomo, na ukawa wa kusemwa kila mahali.
Maya
naye akafunga ndoa nzuri sana na Malcom. Iligaramiwa na kina Cote kama
ilivyodesturi yao, mwanamke kugaramia harusi. Maya akamtaka Tunda ndio awe
msimamizi wake wa harusi. Na Malcom naye akamtaka Roy ndio awe msimamizi wake. Harusi
nzuri, tulivu ikafungwa. Wasimamizi Tunda na Roy.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Maisha
ya kina Cote yakaendelea bila hata kutamkwa tena mama mzazi wa Maya na Net.
Nana akawa ndio Mama. Ila wito wa utumishi ukazidi kumsumbua baba Penny. Kila kitu
alikuwa nacho, lakini si utumishi kama alivyokuwa mchungaji. Akakosa raha ya
kila kitu. Kila akimtizama Tunda, pale alipo na yale aliyofanikiwa kuyapata
sababu ya msaada wao yeye na mkewe, akaona wanajifunga kwenye madogo sana.
“Wapo
kina Tunda wangapi huko nyumbani ambao tunaweza kuwasaidia na kuwafikisha kama
hapa tulipomfikisha Tunda?” Baba Penny akazungumza na mkewe walipokuwa wenyewe,
chumbani kwao, kwenye jumba hilo la kifahari! Alijua wazi ni kama kujipokonya
tonge mdomoni kwa aina ya kipato wanachojiingizia, na maisha wanayoishi kwa wakati
huo lakini wakakubaliana na mkewe warudi tu kuishi nyumbani.
Ilimuumiza
sana Tunda lakini na yeye akakubaliana nao. Asiwe mchoyo na kufungia wengine
bahati zao kama yeye alivyonufaika na utumishi wa baba na mama Penny. Wakawaruhusu
kwa upendo kurudi Tanzania kwa utumishi. Familia hiyo waliosimama pamoja kwa
utumishi wakarudi nchini Tanzania. Mama Penny wakakubaliana na familia ya Cote.
Yaani Tunda na Net, kusimamia nyumba za Tunda nchini Tanzania kwa biashara huku
wakiwekeza yeye na Tunda kwa kila wazo wanaloshauriana. Mama Penny kichwa
inayofanya kazi, akawa mtu wakubuni na kushauriana na Tunda, kisha wanawekeza
kwa pamoja. Maisha yakaendelea kuleta maana kwao. Mchungaji alianzidha tena
kanisa na kituo kama kinachofanana na cha bibi Cote kusaidia wanawake, Tunda
akiwa msimamizi mkuu. Wakiita tawi dogo la Canada. Angalau mchungaji akaweza kutumika
katika wito wake vizuri wakisaidia sana wanawake.
*************MWISHO**************
0 comments: