NILIPOTEA! PART 8 – SEHEMU YA E
“Naomba usubiri Maya.” Akamsikia Malcom, akageuka. “Naomba nikurudishe mimi mwenyewe. Tafadhali.” “It’s okay, Malcom. Wewe kuwa na wakati mzuri na Ethan. Mimi nitapata usafiri tu bila shida.” “Nafahamu hilo. Lakini kwa kuwa mimi ndiye niliyekuchukua naomba nikurudishe. Tafadhali Maya.” “Ni sawa. Ila tu sikutaka kukusumbua.” Maya akajibu akionekana ametulia tu.
“Tunakwenda na Ethan?” Maya akauliza huku
akimchungulia Ethan kule alikojificha kwa baba yake. “Naweza kumchukua Ethan.”
Akadakia Roy. “Mmmh! Unafikirije Ethan? Bado unataka nikuonyeshe super power
nyingine?” Ethan akacheka kidogo huku akitingisha kichwa. “See! We still have
unfinished business.” Maya akafurahia kwa Ethan kukubali. “Wakati dad ananirudisha
nyumbani, njiani mimi na wewe tunaonyeshana super power nyingine. Nahisi kama
unazo nyingine nyingi!” Ethan
akatingisha kichwa kukubali. “Yess!” Maya akaonyesha kufurahia.
“Basi mimi naondoka. Tutawasiliana.” Roy akaaga. “Thanks
Man! Mwambie grandma Pauline, Ethan atakuwa amefika kabla ya chakula cha
mchana.” Malcom akamwambia Roy, akionyesha uchungu kwenye maneno yake. “Okay.”
Akajibu Roy. “You are the best uncle in the entire
wide world. And I love you so much.”
Ethan aliongea kwa upendo huku akijifuta machozi. Roy akamsogelea Ethan
akambusu. “Na kwa taarifa yako tu, mimi najua ila baba yako ndio halijui hilo.”
Roy akajibu huku akimtekenya, Ethan akaanza kucheka. “Kwa hiyo, unatakiwa uwe
unamwambia dad kila wakati. Kuwa anko Roy, is the best.” Roy akambusu tena na
tena. “Okay. Nitamwambia dad.” Ethan akajibu huku akicheka. Angalau Malcom
akaanza kutulia.
“Njoo
nikwambie kitu.” Roy akamchukua kutoka kwenye mikono ya baba yake. “Unajua kwa
nini nilikuja kukuchukua asubuhi na hapa?” “Kwa sababu mimi ni mtoto mzuri.”
Mpaka Maya akacheka. “Kabisa. Sijawahi ona, mtoto mzuri hapa duniani kama wewe Ethan.
Muulize dad wako. Tumezunguka nchi nyingi tu. Eti dad? Umeshaona mtu kama
Ethan?” “Nope.” Akakataa Malcom huku akitingisha kichwa kabisa.
“Umeona sasa? Ndio maana mimi, dad, grandma
Pauline, grandpa, uncle Neo, antie Kyle, tunakupenda sana na tunakung’ang’ania.
Wote wanataka kukuona leo nyumbani. Grandpa amesema leo hakuna mtu atacheza
hockey bila Ethan kuwepo. Eti amesema ni heri dad akose, ila wewe uwepo. Can
you imagine?” Ethan akatingisha kichwa kukataa akicheka sana. “Hata mimi
sikuamini hilo. Lakini unajua ni kwa sababu wewe ni mtoto mzuri sanaaaa!” Roy
akambusu kwa kumtekenya na mdomo. Ethan akazidi kucheka. “Hatuwezi kuishi bila
wewe Ethan. Si ndio dad?” “Kabisa.” Malcom akajibu akisikika angalau ametulia. “Now.
Kamuonyeshe Miss Cote super power zooote ulizo nazo.” “Okay uncle.” Ethan
akambusu Roy, akamshusha. Roy akaondoka.
Njiani vilisikika vicheko vya Ethan na Maya tu.
Ethan alikuwa akicheka sana kila Maya anavyotingisha sikio. Walikuwa wamekaa
naye kiti cha nyuma. Mpaka Malcom akaanza kucheka. “Nilijua tu unayo super
power nyingine.” “Ipi?” Ethan akauliza huku akicheka sana. “Yakucheka mpaka
kumfanya mtu mwenye huzuni afurahi.” “Kweli?” “Kabisa. Niangalie mimi.
Unakumbuka mwanzoni nilikuaje?” “Unashangaa!” “Haiwezekani Ethan! Ulinisoma?”
“Nimekwambia hiyo ndio super power yangu.” “No kidding!” Maya akashangaa sana.
“Lakini ona sasa hivi!” “Bado upo kama huelewi?”
Ethan akawa kama anamuuliza na kumshangaza zaidi Maya. “Kweli upo too smart for
your age.” Wakacheka. “Unataka nikwambie siri?” Ethan akamuuliza Maya. “Yeah.”
“Kwenye sikio silly! Dad asisikie.” Maya akampa sikio huku akicheka. “Mama
yangu huwa anakasirika zaidi akimuona dad na msichana mwingine, zaidi akiwa
mrembo kama wewe.” Moyo wa Maya ukapasuka. Maya akamwangalia usoni akabaki
ameduaa.
Ethan akatingisha kichwa kama anayemthibitishia
anachoongea. “Kweli?” Maya akamuuliza
kwa kunong’ona kwa mshangao. “Nilimsoma hivyo.” “Oooh!” Maya akawa hajui
chakusema tena. “Kwa hiyo?” Ethan akamuuliza Maya akiwa bado amepigwa na
butwaa, akimtafakari huyo mtoto mwenye akili na uelewa wa namna hiyo, ameyaona
hayo mangapi. “Kuhusu nini?” Maya akauliza akiwa hajui Ethan anauliza nini!
“Unafikiri nitakuja kukuona tena?” Akauliza Ethan,
safari hii sio sikioni. Maya akabaki kimya, hajui ajibu nini. “Au na wewe umekasirika
utakaa mbali na sisi? Anko Roy hajawahi kutukatia tamaa. Wakati wote amekuwa
akihakikisha nakuwa na dad.” Maya alijisikia vibaya sana. Yeye binafsi
alishaamua kujiachia. Alitaka akishuka hapo, ndio iwe ndio basi kabisa na
Malcom. Hakutaka hiyo fujo kwenye maisha yake. Aliumia kumuona Zoe akimtumia
Ethan kama mchezo tu. Akamkumbuka mama yake alivyokuwa akiwatumia na wao
kujipatia pesa za Cote, akapandwa na hasira. Akaona ni heri aachane nao kabisa,
ili asije ishi hayo maisha tena kwa kuyatizama kwa mtoto mwingine akifanyiwa
hivyo na mama mzazi.
Maya akabaki kimya, hajui amjibu nini huyo mtoto. “Nilijua
tu kuwa hunampango wa kuja kutuona tena. Lakini unajua nini?” “Nini?” Maya
akamuuliza akionyesha kuishiwa nguvu. Mtoto huyo hakuwa mdogo kama
anavyoonekana. “Mimi naelewa. Ni ngumu.” Maya akaishiwa maneno. Akabaki kimya.
Na Malcom naye kimya. Akaendesha mpaka getini, safari hii akashangaa geti
linafunguliwa bila kubonyeza kengele. Maya alijua ni kwa nini lakini sio
Malcom.
“Mbona geti linafunguka lenyewe?” “Kwa sababu yupo
mtu ameshawaambia ndani kuwa tunakaribia hapa.” Malcom akawa hajaelewa. “Waoooooo!”
Ethan akasikika akishangaa. “Naweza kusimama dad?” Malcom akamruhusu.
Akajifungua mkanda, akasimama. “Unaishi kwenye castle kama mtoto wa mfalme!?”
Ethan alimfanya Maya aanze kucheka. “Waoooo! Kwa hiyo mama hakukosea. Wewe ni
tajiri!” Ethan akamgeukia Maya kwa kushangaa sana. Maya akazidi kucheka.
“Unajua ndani ya hiyo castle kuna nini?” Maya
akamuuliza huku akicheka. “Naamini kuna kila kitu.” Ethan akamjibu Maya,
nakumfanya azidi kucheka. “Sio kila kitu ila kuna warm pool! Bwawa linalotoa
maji yenye vuguvugu.” “Watu wanaogelea!?” Akashangaa kwa kuhamasika. “Yeah. Na
ujajua hata wewe unaweza kuogelea?” “Utanikaribisha kwenu!?” “Kabisa. Siku
utakapokuwa tayari, umwambie dad, tutapanga. Halafu unakuja kuogelea.” “Yesss!
Na mimi nitaingia kwenye castle.” Akafurahia Ethan.
Malcom akasimamisha gari karibu kabisa ya
ngazi. Akaenda kumfungulia mlango, Maya
akashuka. Maya akamuona vile alivyoishiwa ujasiri. “Samahani sana Maya.” Maya akacheka.
“Sina jinsi yakukuahidi kwa kuwa ulichoona leo, ni sehemu kubwa ya maisha
yangu. Na ninauhakika itarudia tena na tena.” “Tatizo ni nini!?” “Hakuna
anayejua Maya.” Maya akanyamaza kama anayefikiria.
“Maya?” “Kwa hiyo huwa
mna..” Maya akasita. Lakini Malcom alishamuelewa. Maya akajifuta
machozi. Malcom akainama akijua ndio anaachwa. “Maisha
yangu yamekuwa magumu Malcom. Sijawahi kutulia na kuwa na mtu wangu mwenyewe,
kwenye maisha yangu. Na wewe unajua. Siwezi..” “Naelewa. Naelewa kabisa
Maya.” Malcom akajibu akisikika amekata tamaa kabisa.
“Natamani ingekuwa tofauti Maya. Natamani kama
ningejua hii hali itakuja kuisha lini, lakini sina jibu. Zoe anaishi na mtoto
wangu na kwa sasa ndiye amepewa dhamana na mahakama. Anafanya kile anachokitaka
kwangu na mtoto.” “Kwa nini usikae naye chini ukajua ni nini anataka?” Maya
akajaribu kushauri. “Huwa hatuwezi kufika popote na Zoe. Hata nijitahidi vipi,
huwa naishia kulala jela au Roy ndio anakuja kunitoa kabla sijalala huko jela.
Inategemea.” Maya akakunja uso.
“Mnaweza mkakubaliana mzungumze. Akakwambia umfuate
nyumbani. Akiniambia jambo nikikataa, anapiga simu polisi. Wakija, anawaambia
nimewafanyia fujo yeye na mtoto. Kuna wakati nilipewa restrain order. Nilikuwa
siwezi kumuona mtoto wangu. Karibia miezi sita.” “Malcom!” Maya akashangaa
sana. “Kweli tena. Ndio ikabidi baba yake Roy aende akazungumze naye, akanipa
masharti, ndio nikaanza tena kumuona mtoto wangu. Mshahara wote unaishia kwa
Zoe.” “Wazazi wako wako wapi?” Maya akauliza.
“Mwanzoni mimi na mama tulikuwa tukiishi kwa bibi.
Lakini baadaye mama alikuja kuolewa, anaishi Califonia. Nikabaki kwa bibi.
Akanilea vizuri tu mpaka chuo. Alikuja kufariki wakati nipo mwaka wa mwisho
chuoni.” “Unamaanisha mama yako yupo nchini Marekani!?” “Ndiyo. Anamaisha yake
mazuri tu na familia yake ya watoto wengine wawili. Aliolewa na mwanasheria
akampa maisha mazuri sana. Kwa kifupi mimi nilishatoka kwenye maisha yake muda
mrefu sana. Hata mawasiliano ni mara moja kwa mwaka, tena yanakuwa ni kama
tunalazimishia tu.” “Malcom!” Maya
akashangaa sana.
“Kawaida tu. Lakini ninachotaka kukwambia Zoe
hajaanza leo na usifikiri ameniharibia kwako tu. Nina rekodi mbaya sana.
Usishangae hata usiku wa leo nitakapotoka naye, nikaishia kulala jela nisirudi
nyumbani.” “Malcom, lazima kuna njia yakufanya.” Maya akaumia sana. “Njia ipi
na yeye anaye mtoto wangu, Maya? Nisipofanya anachotaka yeye, Ethan ndio
anaumia. Na mimi nipo tayari kulipa garama yeyote kwa ajili ya Ethan. Sitaki
aje aishie kama mimi, Maya. Nimekua bila wazazi na wote wapo wanaendelea na
maisha yao. Nimejiapia kwa garama yeyote ile, Ethan atakuwa akitambua nipo na
nina muhitaji. Sitamtelekeza. Japo inanigarimu sana, lakini sina jinsi. Hapa
nilipo siwezi kupandishwa cheo na siwezi kwenda popote kwenye maisha, sababu ya
kuharibiwa na Zoe. Ni kama amenishika miguu. Mpaka lini, sijui!” Maya akatulia
kidogo, kisha akamwangalia.
“Umeshakuwa na mahusiano na Vic?” Maya akauliza
taratibu na kwa wasiwasi akihofia jibu la ndio. “Naomba uniamini Maya, mimi sio
muhuni.” “Nataka kujua kama ulishawahi kuwa na mahusiano na Vic.” “Ya kimapenzi
hapana. Ila nilimfanya awe karibu yangu tu ili kupata habari fulani kutoka
kwake. Lakini hakuna chochote kilichotokea na ndipo nilipofahamiana na kina
Gina, na wengineo. Lakini sikulala hata na mmoja wao.” Maya akashangaa sana.
“Kumbe hao watu wote unawajua!?” “Tunafahamiana
vizuri tu. Hukumbuki Vic aliponiona siku ile alipokuwa amekushikia risasi pale
kwa Jake, alizungumza na mimi kwa kunitaja kabisa jina?” “Nilikuwa nimeingiwa
hofu hata sikuwa nikifikiria kitu zaidi ya kifo.” Maya akaongea huku akivuta
kumbukumbu.
“Alizungumza na mimi vizuri kwa kuwa tulikuwa
tukifahamiana kabisa. Lakini sivyo atakavyokwambia Zoe. Hawezi kuniona na
msichana yeyote yule. Na hata hilo aliniadhibu nalo. Nikajaribu kumueleza kuwa
ni kazi tu. Lakini bado ikawa shida. Akaenda kumtafuta Vic, akataka kumfanyia
fujo. Wewe unamjua Vic.” Maya akaanza kupata picha. “Vic akampiga akaenda
kunishitaki mimi mahakamani kuwa mwanamke wangu amempiga.” “Malcom!” “Muulize
Roy. Nina rikodi mbaya, ni hivyo nafanya kazi vizuri ndio maana mabosi wangu
wananivumilia. Lakini najua itakuja kufika mwisho, watachoka itabidi kufukuzwa
kazi.” Maya akanyamaza, huruma ikaanza kumwingia, asijue chakufanya.
“Ni sawa nikurudishe ndani au unafikiri itakuwa
mbaya wakimuona mtoto wangu?” “Hapana Malcom! Simuonei aibu Ethan wala simuoni
kama ni tatizo. Twendeni tu.” Akafungua mlango. “Unataka uingie kwenye castle?”
Akamuuliza Ethan. “Naweza kuingia dad? Please!” “Kama Miss Cote amekukaribisha,
ni sawa.” “Yesss!” Akaruka Ethan kutoka kwenye gari. Wakaanza kupandisha ngazi
kuelekea ndani.
Wakafunguliwa mlango. “Good morning Sir!” Ethan
akamsalimia Carter kwa heshima sana. “Well behave, Son! Well, good morning to
you too.” Ethan akampa mkono. Maya akacheka. “Huyo anaitwa Mr Carter. Ni mtu mzuri
sana anapenda watoto. Ni kama papa wangu wa pili. Amenilea tokea nazaliwa.
Alikuwa akinipa maziwa usiku.” “Na cookies!?” Akauliza Ethan. “Usiku alikuwa
anakataa. Ila asubuhi alikuwa akinipa.” Wakacheka. Carter akajisikia vizuri kwa
heshima aliyopewa na Maya yakutambulishwa kama babu. Maya akambusu shavuni.
Carter akacheka. “Well, nice to meet you Mr Carter.” “Like wise Ethan.” Carter
akajibu na tabasamu. Malcom alikuwa akimwangalia tu mwanae.
“Unataka kumuona Nana wangu?” “Na yeye ni mzuri
kama grandma Pauline.” “Nafikiri hivyo.” Akatoka bibi Cote. “Woooo!” Akashangaa
sana Ethan wakati anatokea Bibi Cote. Akainamisha kichwa kwa heshima mkono
mmoja nyuma ya mgongo, mwingine akakunja kwenye tumbo kama anaye msalimia
malkia. “Ma’am!” Kakasalimia ka Ethan kwa heshima sana. “Someone has all his
manners!” Akasifia bibi Cote akimshangaa yule mtoto. “How are you?” “Very well
ma’am!” Ethan akajibu kwa heshima sana. “And you are?” Bibi Cote akamuuliza
jina lake kistaarabu. “Ethan Malcom Marshal. Son of Malcom, ma’am!” Alijitambulisha kwa heshima sana akashangaza
kila mtu pale. Bibi Cote alitoa tabasamu la kuvutiwa. “Well, I am Ms Cote. Nice
to meet you Ethan.” “Pleasure is all mine!” Mpaka Maya akamgeukia Malcom huku
ameshangaa. Malcom akacheka.
“Ethan, huyo ndio Nana wangu.” “You didn’t tell me
you are Nana is a Queen!” Wote wakacheka. “You look magnificent, maam!” “Well,
thank you Ethan.” Akashukuru bibi Cote na tabasamu usoni. Na kweli Ethan hakuwa
amekosea. Bibi huyo hapo alikuwa kwenye kiatu cha juu na mavazi mazuri sana ya
thamani. Lipstick imetulia mdomoni. Nywele imetengenezwa vizuri na alumasi yakueleweka masikioni na shingoni,
mida hiyo mapema tu, kama malkia kwelikweli ndani ya jumba la kifamle.
“Unataka Mr Carter atuzungushe kidogo ndani ya
castle? Yeye anaijua hii castle vizuri kuliko hata mimi.” Maya akamuuliza. “Nitafurahi.
Nitaenda kumwambia grandma Pauline kuwa leo nimebahatika kuingia kwenye castle
na nimemuona Queen Cote and princess Maya!” Wakacheka, na kuondoka pale
wakimzungusha. Carter akiwa naye mbele akimuonyesha na kumueleza kila picha na
maana ya kila kitu.
Alionekana ni mtoto aliyefundishwa vizuri, mtulivu.
Na kweli hakuwa akiendana na umri wake. “Hongera sana Malcom! Sasa hivi nahisi
nakuelewa kwa lolote unalofanya kwa ajili yake. Anastahili huyu mtoto.” “Asante
Maya. Na samahani sana.” “Huhitaji kuendelea kuomba msamaha Malcom. Nimekuwa na
wakati mzuri kuliko nilivyotarajia.” “Kweli?” “Ooh yeah! Unafikiri ni nini
kitakuwa kimeniudhi? Tena baada ya kupata muda na Ethan! Mimi mwenyewe sijawahi
kuona mtoto kama Ethan!” Malcom akanyamaza huku akitoa tabasamu la kinyonge.
“Kwanza niambie, huyu mtoto unamleaje wewe Malcom!?
Anamaadili mazuri sana!” Waliendelea kuzungumza wao wakiwa nyuma, Ethan
akitembea mbele yao na mikono ameikutanisha nyuma akimsikiliza Carter kwa
makini sana. “Huyo mtoto anakuzwa na mimi, Roy ndio zaidi kwa kuwa anaweza kuwa
kati yangu na Zoe. Na ameshazoea matusi ya Zoe. Akikwambia Ethan kuwa Roy
hajatukatia tamaa, ujue ni kweli. Huwa anamtusi Roy, mimi mwenyewe huwa
najiweka kwenye nafasi ya Roy, najua wazi nisingeweza. Lakini Roy hakati tamaa.
Na kwa kuwa yeye hajawahi kumshitaki mahakamani, basi Roy huwa anakwenda
nyumbani kwa Zoe muda na wakati wowote kumtizama Ethan. Akimkuta ametulia, anaweza akaondoka
na Ethan hata kwa masaa mawili au matatu katikati ya juma, na kumrudisha.
Akimkuta siku hiyo akili haijatulia, basi ujue atamtukana na hatakubali hata
amuone Ethan.”
“Haya, na nyumbani kwao kina Roy, anapendwa sana
Ethan. Ndugu zake wote kina Roy, wanamuona Ethan kama mtoto wao kabisa. Halafu
baba yake Roy alikuwa mwanajeshi. Kwa hiyo naye anamlea kijeshi. Huwezi kumkuta
anazungumza naye au anamfanya ajione ni mtoto. Hizo heshima zote ni kazi ya baba
yake Roy. Ndiye anayemfundisha na kutumia muda mwingi na Ethan kwa kuwa
amestaafu. Yupo tu nyumbani. Wakati mwingine tunaweza kumchukua, tukaitwa
kazini kwa gafla, basi ujue atakuwa na grandma Paulina na mumewe mpaka tutoke
kazini. Kwa hiyo anatumia muda mwingi sana na hao wazee. Na ukirudi
kumwangalia, utakuta anafanya kazi na huyo mzee. Anamfundisha mambo mengi sana
ambayo hata mimi mwenyewe sikubahatika kwenye makuzi yangu.” “Kwa kweli
amezungukwa na watu sahihi.” Malcom akamwangalia na kunyamaza.
“Ni mtoto mzuri sana Malcom.” “Lakini hakutakiwa
kuishi maisha anayoishi, Maya! Zoe ni mkali kwake bila sababu. Anaweza
akakosana na mimi, akaamua kummalizia yeye. Ilimradi tu.” “Dad! umemuona Cote
the first and Second?” Ethan akamwita baba yake na kumuonyesha. Akaanza
kumuelezea. “Huyu ni Cote wa kwanza, huyu ni wa pili, huyu ni wa tatu, huyu ni
wa nne, huyu hapa mdogo kabisa, ndiye Cote the fifth. Nimeambiwa hawa wawili.
Cote the 4th na 5th, wapo humu humu ndani.” “Oooh yeah?”
Malcom akawa kama anashangaa. “Yeah dad! Hawa wawili wapo.” Yaani Net na mtoto
wake ndio wapo kwa wakati huo. Ethan akaongea kionekana amefurahia. Maya
akacheka.
Akamgeukia Carter. “Samahani Sir!” Carter
akasimama. Ikabidi na kina Maya wasimame. “Nina miahadi na grandma Pauline.
Ameniandalia chakula cha mchana. Unafikiri itakuwa sawa kama tukiishia hapa kwa
leo, halafu ikitokea ninarudi siku nyingine, tutaendelea kuanzia hapa?” Maya
akashangaa na kumgeukia Malcom.Yaani na kuhamasika kote huko, bado alikumbuka
miahadi! “Absolutely, Ethan. Nitafurahi kupata nafasi ya kukutembeza tena.” “Asante.”
Akampa mkono Carter na kumgeukia baba yake. Maya akacheka taratibu na kwa
makini akijua akili ya huyo mtoto si ya kuchezea.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Malcom na mtoto wake walipoondoka, Maya akaenda
kumtafuta Tunda, akaambiwa amerudi kulala. Ikabidi kwenda ofisini kwa bibi
yake. Hapo hapo nyumbani. Wote wawili, yeye na Net wana ofisi zao na hapo nyumbani
pia. Alimkuta bibi yake ameinamia meza, akionekana anakazi inayomfanya
afikirie. Alipoingia na kumuona hivyo, akaenda kujilaza kwenye kochi la wageni.
Kimya. Baada ya kama dakika 6 hivi, bibi Cote akavua miwani na kumwangalia.
Akamkuta akimwangalia lakini kama akiwaza. “Zoe alikufanyia vurugu yeyote?”
Maya akashangaa sana. “Nana! Umejuaje?” “Nimekwambia sasa hivi sitatoa macho
yangu kwako.” Maya akakaa.
Akamsimulia mwanzo mpaka mwisho. “Nitafanyaje
Nana?” “Wewe unataka nini?” Maya akainama. “Pata muda wakufikiria, halafu
uniambie. Tutajua chakufanya kuanzia hapo. Lakini ni kweli Malcom anamtoto
mzuri sana. Haendani na umri wake hata kidogo.” Bibi Cote akasifia. Maya
akanyamaza kama anayefikiria zaidi.
“Sijawahi kupata mtu wangu mwenyewe Nana! Natamani
kumpata mtu wangu, peke yangu, nianze naye mimi mwenyewe.” “Unaweza ukampata
ambaye hana Ethan wala Zoe, lakini asikutazame kama Malcom.” “Hicho ndicho kinachoniumiza
kichwa!” Maya akamsogelea. “Natamani kama Malcom angekuwa hana Ethan wala Zoe
au Ethan awe wangu.” “Lakini Ethan ni wa Zoe!” Bibi yake akaweka msisitizo.
Maya akainamia meza.
“Nafikiri nijipe muda Nana. Naweza kumpata Malcom mwingine.
Huyu naona...” “Hutakuwa center of his attention? Kwamba kabla hajakufikiria
wewe itabidi aanze kumfikiria kwanza Ethan?” “Sio hivyo Nana!” “Mimi nakujua
Maya. Na ninajua hilo ndilo tatizo kubwa.” Maya akajilaza kichwa kwenye meza. “Pata
muda wa kufikiria. Uamue vizuri ili usije kujuta baadaye. Na ujue kabisa, kila
utakaloamua, nipo nyuma yako.” Maya akabaki amefunga macho.
Kabla hapajapoa..!
B |
ibi yake akarudisha kichwa na mawazo kwenye
alichokuwa akifanya, Maya akabaki amejilaza. Simu yake ikaanza kuita. Bibi yake
akamwangalia na kurudisha macho kwenye kazi yake. “Menson!”
Akaanza Maya. Bibi yake akamuona anacheka kidogo huku akisikiliza. “Sijui Menson. Ningefurahi kuhudhuria, lakini...”
Akasita na kumwangalia bibi yake. “Subiri kwanza.
Nitakupigia.” Akakata na kumwangalia bibi yake. “Nana!” Akamwita kama
kutaka ahamishie mawazo kwake. Akamwangalia. “Kuna kijana anaitwa Menson,
anamdogo wake anaitwa Mat. Menson alikuwa kwenye madawa. Nilikutana naye wakati
tupo rehab, hii safari ya mwisho. Akawa rafiki yangu sana.” Maya akaendelea.
“Mimi nilitoka kabla yake, nikawa naendelea
kumfuatilia kuhakikisha anamaliza muda wake vizuri na anatoka. Baadaye
akaniambia alitoka, akakuta mdogo wake ameishiwa kabisa, sababu yakumlipia pale
rehab.” “Na ile rehab ni gharama sana.” Bibi Cote akaongeza. “Sana. Ila wanatoa
huduma nzuri. Ndio mdogo wake akahakikisha anamgaramia kaka yake mpaka akatoka.
Alitoka hapo maisha yakawa kwao magumu na mdogo wake akawa amepoteza kazi.”
“Kufupisha stori, niliwasaidia kuwalipia kodi ya
nyumba, ilikuwa wafukuzwe, na garama nyingine mpaka mdogo wake akapata kazi na
Menson naye nikamsaidia kazi ya kuosha vyombo kwenye mgahawa wa mtu ambaye
nilikuwa nikifahamiana naye mimi. Sasa baada ya Mat kufanya kazi huko,
wanaonekana walimpenda na ananidhamu ya kazi, wakampandisha cheo, kwa kifupi
maisha yake yakarudi kuwa mazuri akaamua kumuoa mchumba wake ambaye walikuwa
naye muda mrefu tu.”
“Sasa walinialika leo kwenye harusi yao, lakini
niliwaambia sitaweza kwa kuwa unakumbuka leo ndio ilikuwa iwe harusi ya Net?”
Bibi yake akanyamaza kama aliyekumbushwa kitu. “Amenipigia hapa kuniomba
niende, kwa kuwa harusi yetu haikufanikiwa. Unafikiri ni sawa?” “Ooh Year! Why
not? Maisha yetu yanatakiwa yaendelee kama kawaida.” Bibi yake akamkubalia bila
shida. Hakuona tatizo lolote.
“Kweli Nana?” “Kabisa. Usiogope, nenda kafurahie na
wenzako, nitahakikisha unarudi nyumbani salama.” Maya akaelewa. “Asante Nana.”
Akasimama kwenda kumbusu. “Lakini umenifurahisha Maya. Sikujua kama ulikuwa
ukisaidia watu!” “Sio pesa nyingi sana, ila wao walikuwa wakiona pesa nyingi
mpaka nilikuwa nikishangaa.” “Hakuna msaada mdogo kwa muhitaji. Ule moyo wa
kuwa nao tu wakati wa shida, nafikiri hilo ndilo la muhimu. Am so proud of you
baby girl.” Akambusu. Maya akacheka na kuondoka pale kutafuta chakuvaa kwenye
harusi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilikuwa mida ya 11:45 jioni wakati dereva
anamshusha Maya kwenye ukumbi waliofanyia hiyo harusi ya Mat. Alimkuta Menson
akimsubiria nje. Kwanza yeye ndiye aliyemfungulia mlango wa gari. Walipoonana
tu wakaanza kucheka. Maya hakuwa akijifanya Miss Cote mbele ya Menson. Aliishi
naye rehab akiwa teja. Akihangaika na matibabu. Kuugua kipindi anatolewa madawa
mwilini, Menson alikuwepo. Na ikawa hivyohivyo kwa Menson. Aliugua Maya
akimuona. Wakawa watu wakutiana moyo.
Maya alikuwa akitokea rehab na kwenda mahakamani,
Menson ndiye alikuwa mtu wa karibu yake akimfuatilia kutaka kujua
kilichoendelea kiundani huko mahakamani, mbali na taarifa za mitandaoni. Kwani
kesi ya Maya wengi waliirusha mitandaoni kutokana na hisia zao juu ya binti
huyo. Kwanza sababu ya utajiri wa kwao au umaarufu wa kwao na tabia zake mbaya
walizozoea. Wengi walimfuatilia mitandaoni. Kila alipokuwa akitoka mahakamani,
Menson alikuwa akimsubiria kujua kilichoendelea huko kwa hakika na kumtia moyo endapo
akirudi akiwa amenyongea. Wawili hao wakawa karibu sana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Mat amesema lazima tupate wimbo mmoja.” “Come on
Menson, look at me!” Akamuonyesha Menson vile alivyopendeza. Menson akacheka
sana. “Unatunza status?” “Ulijuaje!?” Wakacheka huku wakiingia. Menson
amekumbatia mkono wa Maya, akamvuta karibu ubavuni, Maya akajiegemeza kidogo
wakawa wanaingia huku wakicheka. Mat na mkewe walipowaona tu wakasimama pale
high table, Mat akaanza kucheza style yao ambayo huwa wanacheza wao watatu
wakamuingiza na aliyekuwa mchumba wa Mat, ambaye sasa ni mke, ndiye huyo bibi
harusi.
Mke wa Mat, Myla alipoona Mat anacheza, na yeye
akaanza kucheza. Maya akazidi kucheka. “Maya amesema leo anatunza status!”
Menson akamsemea kwa Mat na mkewe. “Come on Maya! Leo ni harusi yetu.” “Kwa
sababu sikuja kanisani, nalipiza kwa dance.” Wakaanza kushangilia watatu hao.
Menson akaomba Dj awapigie wimbo wao. Hakuna aliyeelewa na haikuwa kwenye
ratiba. Wote wanne wakaingia katikati.
Myla akakunja shela yake, wakajipanga nakuanza
kucheza. Walicheza huku wakicheka sana, kila mtu akiwatizama wao wanne. Kwanza
walifanya wakati tu Maya akiingia na Menson. Ni Maya Cote! Mtoto wa kitajiri,
mzuri sana, mwenye kashfa mitandaoni mchana kutwa. Anajulikana na kila mtu,
lakini wachache walibahatika kumuona uso kwa uso. Tajiri na mtu maarufu kama
Maya akiingia popote, kila mtu anajua. Sasa ameingia kwenye harusi ya watu hao
wa kawaida sana, akapokelewa na kucheza.
Wanne hao walicheza ni kama walikuwa wameandaa show
yao yakuonyesha watu kumbe hata hawakupanga! Walicheza kwa kupatana vizuri huku
wakicheka. Kuna kipindi walitengeneza mduara wa karibu sana na kugonga. Wengi
walijiuliza vijana hao wawili, walimfahamuje mtu kama Maya ambaye waliweza
kumfanyia utani na kucheza kama vile!
Wimbo wao ulipoisha, ndipo Maya alipowasalimia na
kuwapongeza Mat na Myla huku akiwabusu shavuni na kuwakumbatia kwa furaha. “Finally!”
Hatimaye! Wote wakajikuta wakiongea kwa pamoja na kucheka. Kwamba wawili wale
wameoana. Baaada ya kusubiriana kwa muda mrefu sana, hatimaye wameoana.
“Samahanini sana. Tumefurahia peke yetu.” Akaongea
Mat. “Huu wimbo na aina hii ya uchezaji ni wa Maya. Alipokuwa akija pale
tulipokuwa tukiishi akitukuta mimi na Menson tumekaa kizembe na mawazo. Wakati
nimepoteza kazi. Mimi na Menson hatujui chakufanya, tumekata tamaa.” Mat
akatulia kidogo. “By the way, they were realy broke.” Myla akafanya watu
wacheke pale aliposema Mat na shemeji yake kuwa ni kweli walikuwa
wameishiwa. Kidogo Mat akacheka na
kuendelea.
“Ni kweli tulikuwa tumeishiwa. Na wote hatukuwa na
kazi. Basi Maya alikuwa akija labda kutuletea chakula au kuja kutuona tu,
alikuwa anaweka huu wimbo. Mwanzoni alikuwa akicheza peke yake huku
tukimwangalia. Mnamjua Maya!” Menson na Myla wao walicheka, kwa kuwa
walimfahamu Maya kwa karibu. Si wengine. “Akaendelea kucheza yeye peke yake
sisi tukimwangalia tu. Ukweli hatukuwa na hamu yakucheza kwa kile kipindi
tulikuwa tukipitia. Na hatukuwa na sababu. Mwishoe akanishawishi mimi, mpaka
akanifundisha kucheza kama yeye. Tukaja kumfundisha na Myla ndipo akaja Menson.
Kwa hiyo kila alipokuwa akija, wote tulikuwa tukicheza ndipo anaondoka.
Ilitusaidia sana kupunguza ile hali ya wasiwasi kwetu. Ndio maana leo tuliona
tucheze tena.” Wakacheka.
“Nawapenda nyinyi watu!” Akaongea Maya akiwa
ameshikiliwa kiunoni na Menson. Ungejua tu hao watu ni marafiki. “Kitu kimoja
alituambia Maya.” Myla akataka na yeye kuzungumza. “Mnajua umaskini huwa
unakuja na kutokuelewana! Tulifika kipindi mimi na Mat tulitaka kuachana
kabisa. Maya alinifuata mimi kazini kwangu.” Wakamuona Myla anaanza kulia na
kushindwa kuzungumza kwa muda.
Mumewe akamsugua mgongoni kama kumtuliza. “Nilikuwa sijamuona Mat kama siku tano hivi, ni kama
tulijua ndio itakuwa mwisho wetu. Nikashangaa Maya anakuja kazini kwangu.
Akaniambia, pesa haiwezi kununua tulicho nacho mimi na Mat.” Myla
akajifuta machozi. “Akaniambia akijitolea mfano
kuwa, yeye anazo pesa, lakini hana tulicho nacho mimi na Mat, na hata angetaka,
hawezi kununua. Na akasema kama ingekuwa inauzwa popote, kwa garama yeyote ile,
yeye na wengine wengi wenye uwezo wangenunu.” Watu wakapiga makofi.
Wakajikuta wao watatu. Maya, Myla na Mat wakifuta
machozi. “Alinipa mifano mingi, akiniambia nyumba haijengwi na pesa tu, japo ni
muhimu, lakini hujengwa na kile tulichonacho mimi na Mat. Akanisihi sana nisikubali
kuua tulicho nacho hata kwa garama ya umaskini.” Watu wakapiga tena makofi. “Nakumbuka Maya alipoondoka tu, nikamtafuta Mat,
nakumuomba anioe.” Watu wakacheka sana.
“Hata Mat alishangaa.” Myla akaongeza huku akicheka na kufuta machozi. “Lakini
kufupisha stori, Maya ni rafiki tuliyeletewa na Menson, amekuwa rafiki wa
karibu sana na sisi wote watatu. Anavyosema Mat, ni kweli. Alikuwa akija,
lazima tucheze huo wimbo ndipo aondoke. Alikuwa karibu sana na kina Mat,
akiwasaidia kifedha na faraja, mpaka Mat na Manson wakapata kazi.” “Ndio maana
tumefurahi sana kumuona hapa. Ilikuwa asihudhurie harusi yetu kwa kuwa
iliingiliana na ratiba zake. Lakini Mungu amemfanikisha na ameweza kuja
kushuhudia kile tulichofanikisha.” Mat akaongezea kwa mkewe. “Karibu sana Maya
na tumefurahi umekuja.” Akamalizia Manson huku akimtizama Maya aliyekuwa
amemshikilia kwa karibu sana wakati Mat na mkewe wakizungumza baada ya kucheza.
Maya akawakumbatia tena na kuwabusu wote watatu.
Wakaenda kwenye meza aliyokuwa wamekaa wazazi wa
Myla na ndugu zake, wakamtambulisha tena Maya. Maya akawasalimia kwa heshima
akiwa karibu sana na Menson. Wote wanne walikuwa wakihama meza moja kwenda ya
pili kwa ndugu wa Myla wakisalimia. Menson na Mat hawakuwa na ndugu yeyote siku
hiyo. Ndipo Maya akaongezeka. Kwa hiyo Maya ndio akaenda kukaa na Menson kwenye
meza aliyokuwa amekaa Menson tokea
mwanzo. Wakaendelea kuzungumza huku wakicheka.
Wawili hao hawakuhitaji kutafuta mazungumzo maalumu
yakuongea. Waliongea chochote na kucheka sana. Haikuwa harusi ya watu wengi
wala si yakitajiri, lakini akili na mawazo ya Maya yalikuwa kwa Menson,
hakuhangaika kuangalia kulia wala kushoto, wakaendelea kunywa na kula. Na kwa kuwa wote walitoka kwenye ulevi, meza
yao ilikuwa ya soda, maji na juisi tu. Hawakuwa wakinywa hata wine.
Muda wa mziki wa taratibu ukafika ambapo maharusi
walianza wao kwanza. Akaja Myla na baba yake. Walicheza vizuri sana. Na kweli
Myla alipendeza. Wakati Maya anaangalia vile Myla anavyocheza na baba yake
katikati ya ukumbi, baba yake
akimzungusha binti yake kwenye ukumbi huo. Waalikwa wakiwafuata kwa macho, na
Maya vilevile, Maya akajikuta macho yamegongana na Malcom aliyekuwa amekaa
upande wa pili.
Kwanza akahisi ni kama amemfananisha. Akainama kwa
muda. Kisha akanyanyua macho na kumtizama tena. Alikuwa Malcom kweli.
Akamtizama na watu waliokuwa wamekaa naye meza moja, akamuona na Zoe yupo.
Akajua ni kweli ni yeye. Akarudisha macho kwa maharusi. Malcom alikuwa
akimwangalia Maya muda wote tokea anaingia. Lakini Maya hakuwa amemuona.
Akakumbuka Zoe alimwambia ili awape mtoto, nilazima Malcom atoke naye.
Akajua wapo pale pamoja.
Maya akawatizama tena. Akakuta bado Malcom
akimwangalia. Alikuwa amependeza sana. Msafi na suti aliyokuwa amevaa kama
alivyoamrishwa na Zoe, nyeusi. Ni kweli alipendeza. Maya akajua ndio maana Zoe
alimtaka baba watoto wake avae hivyo. “Umependeza sana.” Akasoma midomo ya
Malcom. Maya akarudisha tabasamu. “Asante.” Akashukuru nakuongeza. “Na wewe
umependeza.” Maya akamsifia na yeye. Wote wakacheka.
Akili na mawazo ya Malcom na Maya yakahama kabisa
pale harusini wakabaki wakiangaliana wao kwa kurudia rudia. Walikaa upande
ulitizamana. Kila walipokwepesha macho, wakajikuta wanaangaliana tena. Menson
akagundua hata uso wa Maya umebadilika. “Ni nini kinaendelea?” Menson
akamuuliza. “Hamna kitu.” Maya akakataa huku akicheka. “Haiwezekani Maya. Mimi
nakufahamu. Hukuwa hivyo muda mfupi uliopita. You are blushing!” “No am not!”
Akabisha Maya huku akicheka kwa aibu. Wakaanza kunong’ona wawili hao pale
mezani, Maya akicheka na kukataa kumwambia juu ya Malcom.
Menson akaona amtege. Akajifanya kama amemwamini na
mawazo hayapo tena kwake. Akamuona anarudisha macho upande wa pili walipokuwa
wamekaa wao. Akamuona mpaka uso wa Maya unabadilika na kuwa na furaha
zaidi. Menson akaanza kuchunguza anamwangalia nani upande ule! Akakuta Malcom
akimtizama na yeye Maya, wala macho hayapo kwa bibi harusi na baba yake.
“Oooh!” Maya akashtuka na kumgeukia Menson. “Nini?”
“Sasa hivi najua.” Maya akaanza kucheka. “Huwezi Maya.” “Kwani mimi nimesema
nini Menson!” “Nimeona sura yako Maya.” Maya akacheka tena na kuinama. “Huwezi
hata kuruhusu moyo wako kumfikiria Malcom.” “Kwa nini?” Maya akauliza taratibu.
“Alikuwa mume wa Zoe, Zoe ni mtoto wa mjomba wake Myla. Wana mtoto mmoja
anaitwa Ethan. Sitaki kukuona unaumia tena Maya. Achana na Malcom, Zoe
hawezi kuruhusu uwe karibu naye.” “Kwa
nini na wakati wameachana!?” Maya akauliza kwa kushangaa.
“Zoe hawezi kuona mwanamke mwingine anamsogelea
Malcom kimapenzi akakubali. Na anaamini ipo siku watarudiana tu. Anawaambia
hivyo kila mtu na kuwahakikishia lazima aje arudiane na Malcom. Kwanza Zoe ni
mwendawazimu. Humuwezi.” Maya akainama kama anayefikiria. “Maya?” “Nahisi
nampenda Malcom.” “Come on Maya!” “Kweli Menson. Leo asubuhi nilikuwa naye
kwenye kifungua kinywa. Zoe akaja akitaka kufanya fujo. Alikuwa na Ethan.” “Kwa
hiyo kumbe unawafahamu?!” Menson akashangaa. “Zoe na Ethan ndio nimekutana nao
leo. Ila Roy na Malcom walishakaribia mpaka nyumbani kwa chakula cha usiku.”
Menson akamgeukia Maya vizuri. Maya akacheka.
“Hayo yote yanaendelea mimi nikiwa wapi!?” “Hayana
muda mrefu Menson. Na sharti la Zoe
kumtoa Ethan awepo kwa kina Roy leo, ilikuwa nilazima Malcom awepo hapa na
yeye.” “Na kweli Zoe anamtumia mtoto wao kama fimbo kwa Malcom.” Maya
akanyamaza.
“Nikushauri kitu Maya? Japo nahisi nimechelewa.”
Maya akamwangalia. “Kama kunauwezekano na haujafika mbali, achana na Malcom.”
“Nahisi nimechelewa Menson. Hata mimi nilijiambia hivyohivyo kuwa sitaweza fujo
za Zoe na kashfa nyingine mtandaoni.” Maya akamwangalia tena Malcom. “Lakini..”
Maya akasita na kunyamaza. Wakasikia watu wanapiga makofi. Wakajua Myla
amemaliza kucheza na baba yake. Wao walizama kwenye mazungumzo.
Mc akaruhusu watu wengine waingie na kucheza.
Wakamuona Zoe na Malcom nao wanasimama kwenda kucheza. Ilikuwa karibu na
mwisho. Maya akamvuta Menson. Akainama. “Mimi naomba niondoke.” Menson
akamwangalia kidogo. Maya alikuwa amebadilika usoni. Ile furaha iliisha gafla,
akapooza. “Nina zawadi hii ya Mat, nataka kumkabidhi kabla sijaondoka.” Ilikuwa
bahasha. “Sikupata muda wa kuzunguka
madukani kuwanunulia zawadi. Kumekuwa na mambo mengi.” “Pole kwa matatizo
Maya.” Maya akatoa tu tabasamu, kwa sababu ni kweli bado walikuwa kwenye
mataatizo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Waliohusika kumteka wifi yake walitangazwa kuwa
wawili wameuwawa na hawajui walikuwa wahusika wangapi. Kwa hiyo inamaana bado walikuwa hatarini. Na harusi ya kaka
yake ndio ilikuwa imevuma, ilikuwa ifanyike siku hiyo, haikufanyika. Picha za
kaka yake akifanya ngono bado zilikuwa zimeenea mtandaoni. Kashfa ya Vic
kumvamia Tunda nyumbani bado ilikuwa habari moto kabisa maredioni. Mambo ya
juma hilohilo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakasimama kumsogelea Mat aliyekuwa akicheza na
mkewe. Maya akamuwekea ile bahasha kwenye mfuko wa suti. “Nilishindwa kwenda
madukani.” “Naelewa kabisa Maya. Hata hukutakiwa kuleta zawadi. Kufika kwako
hapa ni zawadi tosha.” Maya akambusu Mat. “You are sweet, Mat.” Wakacheka.
Lakini Maya huyu alishabadilika, sio kama alivyoingia. Wivu ulishamuingia
kumuona Malcom amemkumbatia Zoe.
Akambusu na Myla. “Muwe na wakati mzuri
mapumzikoni.” “Unaondoka?” “Tuna mtoto mchanga, nataka nimuwahi kabla hapajawa
usiku sana.” “Naelewa. Asante kwa kuja.”
Akambusu Myla shavuni. Akamgeukia Menson. Akamuona Malcom akiendelea kucheza
na Zoe mziki huo wa taratibu, mbali kidogo na pale walipokuwa wamesimama.
Akasikia kuumia. Walishikana kama wapenzi haswa.
Akiwa ameshangaa na Menson akimwangalia tu, macho
yakagongana na Malcom, Maya akakwepesha yake na kurudisha kwa Menson. Kweli Maya alibadilika. “Mimi nipo tayari
kuondoka. Naomba unisindikize mpaka nje.” Maya akaongea kwa kunyong’onyea,
Menson akajua kinachoendelea kwa Maya. “Huwezi kuondoka hivyo. Tucheze kidogo.”
Kabla Maya hajajibu, Menson akamvuta karibu. Akamshika vizuri, na wao wakaanza
kucheza mziki huo wa taratibu.
Wakati wanacheza mziki huo wa taratibu, Maya
amejiegemeza kwa Menson, akasikia mtu anamgusa begani. Akageuka. “Malcom!” Maya
akashtuka, hakutegemea. “Naomba tucheze wote.” “Na..?” Maya akasita. “Wewe
niangalie mimi tu.” Malcom akamwambia kwa utulivua. Maya akashangaa kidogo kama
anayejishauri mbele ya Menson na Malcom aliyekuwa amebaki amenyoosha mkono
akitaka Maya amshike.
Mwishoe Maya akajitoa kwa Menson, akanyoosha mkono
wake mpaka akaufikia ule mkono wa Malcom. Malcom akamvuta karibu haswa.
Akamkumbatia. Maya akajisahau, akapitisha mikono yote juu shingo ya Malcom, akamkumbatia kwa huba. Si
kama vile alivyokuwa na Menson. Aliweka mkono kwenye bega tu wakaendelea
kucheza. Hapa kwa Malcom alimkumbatia na kujilaza karibu kabisa ya shingo.
Malcom aliweza kuzipata sawia pumzi zake shingoni kwake na yeye akajilaza
kichwa chake juu yake.
Wakazunguka kidogo. Maya akatoa uso shingoni kwa
Malcom. “Itakuaje sasa juu ya Zoe? Si
atakasirika sana!” Maya akauliza taratibu wakati bado wanacheza na
wamekumbatiana. “Sio kwa hiki, ila kwa ambacho nakaribia kukifanya.” Maya akawa
hajaelewa. “Nini?” Maya akamuuliza huku wakiangaliana machoni na kuendelea
kucheza taratibu. “Nataka kukubusu Maya.” “Hapa hapa!?” Maya akaingiwa na
wasiwasi. “Sasa hivi.” “Na Ethan?” Maya akauliza akijua nilazima Zoe
atamuadhibu.
“Sijui Maya! Ila ninachojua nakupenda wewe na sasa
hivi nataka kukubusu wewe. Naruhusiwa?” “Ningefurahi Malcom.” Hapohapo Malcom
akamsogeza karibu kabisa, mkono wa kushoto akaupitisha chini ya kichwa cha
Maya, akawa ni kama amekilaza kichwa chake kwenye kona ya kiwiko cha mkono wake
huo wa kushoto, mkono wa kulia akamshika shingo chini kidogo ya sikio, na
kuanza kupata busu. Pale pale mbele ya umati.
Vile alivyoshikwa Maya, ungejua anapendwa. Alijaa
mikononi kwa Malcom akavutwa kwa karibu na kukumbatiwa kama mtoto mdogo
anayeepushwa na baridi au anayenyonyeshwa kwa mapenzi mazito na mama yake. Maya
alitulia hapo, akaendelea kusikilizia lile busu bila kujali kashfa
itakayomkabili baada ya kumaliza hapo. Na yeye Malcom hakujali anamtizamaje Zoe
baada ya hapo. Alijiambia atajua yote baada ya hapo. Alimbusu kwa hisia zote,
huku mziki wa taratibu ukiendelea kupigwa na wengine wakiendelea kucheza
taratibu huku wakishuhudia kimwana huyo akipewa busu na Malcom aliyekuja na
Zoe.
Halikuwa busu la sekunde chache. Malcom
alihakikisha busu lake la kwanza kwa Maya, linabeba historia na hata kama
ataadhibiwa baada ya hapo, iwe kwa haki. Akamtendea haki Maya, akamshika
vizuri, kwa heshima, akaendelea kupata busu la mrembo huyo. Malcom anamaliza
lile busu, wakakuta ukumbi mzima unawashangaa wao kwani mziki ulishaisha muda
tu. Maya akarudisha macho kwa Malcom. Bila kupoteza sekunde, akamshika mkono na
kutoka naye pale ukumbini.
Walikuta dereva wa Cote ameshasogeza gari mlangoni.
Akasogea mtu na kufungua mlango. Maya akajua ndio mlinzi aliyekuwa hapo
akimlinda. Hata hakuwa amemuona. Akaingia bila hata kumuaga Malcom, dereva
akaondoa gari.
Wakati yupo njiani akasikia simu inaita kwenye
spika ya gari, dereva akapokea. Akajibu kwa kifupi tu, “Nipo
naye hapa. Ndio tunarudi nyumbani.” Simu ikakatwa, Maya akajua ni bibi yake na habari
zilishamfikia. Hakujali. Akajiegemeza vizuri, akashika midomo yake, akailamba
na kucheka, kisha akaanza kupitisha kidole kwenye midomo yake taratibu huku
akikumbuka vile alivyoshikwa na Malcom. Jinsi alivyombusu. Harufu nzuri ya
midomo aliyokuwa akiipata wakati Malcom akimbusu. Maya akaendelea kuvuta
kumbukumbu za furaha.
Geti lilifunguka mara tu walipokaribia wala
hawakusimama getini. Akafunguliwa mlango walipofika akashuka. Ilikuwa ni mwendo
kama wa nusu saa huko alipokwenda kwenye harusi na nyumbani kwao.
Alifunguliwa mlango na Carter. Kwa mtazamo tu ule
wa Carter akajua anasubiriwa ndani. Maya akasimama pale mbele ya Carter kama
anayesita kuingia ndani. “Nampenda Malcom.” Akamwambia Carter kama anayetaka
kulia. Carter akambusu kichwani. Maya akaelekea sebuleni alijua kwa kutoongea
Carter, bibi yake anamsubiria sebuleni. Hakumkuta tu bibi yake. Alimkuta na Net
pamoja na Tunda. Akabaki amesimama.
“Kweli Maya!?” Net akamuuliza kwa ukali kidogo kama
anayemshangaa. “Yaani katika siku zote. Na yote yanayoendelea katika
familia, na wewe ndio umeamua kuongeza
jingine!” Net akaongea kwa kushangaa kidogo. “Nampenda Malcom, Net. Nimeamua kuwa naye. Mengine nitajua baadaye.” Maya akaanza kulia. “Nimekataa mama kuendelea kututesa Net. Maisha yetu
hayawezi kuendelea kusimama kwa ajili yake.” Maya akaendelea kulia.
“Hatuwezi kukosa kila kitu kwa ajili
yake. Ona wewe. Ulitakiwa uwe umeona leo. Lakini amekufanya hujao na hujui ni
lini utaoa tena. Kama isingekuwa Mungu, sasa hivi tusingekuwa na Tunda hapa.
Mama anataka kutupokonya kila kitu, Net. Mimi sikubali kuendelea kufanywa
mtumwa wake.” Maya akaendelea kujitetea.
“Nampenda Malcom. Sijakosea. Na
nimeamua kuwa naye leo kwa kuwa sijui kama kesho nitakuwa hapa au mama atatuma
mtu aje anichukue na mimi! Siwezi kuendelea kusubiri Net. Kama wewe na Tunda
mnaendelea kumsubiri yeye, hiyo ni juu yenu. Lakini mimi sisubiri.” Hasira zikazidi kumpanda Maya.
“Aliniacha hapa mdogo sana bila
kunilea au hata kujali nakuaje! Jana
Tunda anamlilia mtoto wake pale hospitalini mpaka mimi roho ikaniuma! Kwa nini
na sisi mama hakutulilia? Tunda amefanyiwa operation, hataki mtu amguse mtoto
wake, anahangaika naye yeye mwenyewe! Kwa nini sisi mama hakutaka hata kuwa
karibu na sisi, Net?” Maya akazidi
kulia kwa hasira. “Ametuacha tumelelewa na watu
baki bila kujali mimi nitakuwa vipi! Nimekua peke yangu kwenye hili jumba
wakati nyinyi wote mpo na yeye akiwepo! Nimecheza na Carter mpaka nimekuwa
mkubwa na kuweza kutoka kwenda kutafuta watu wa kuwa na mimi huko nje. Matokeo
yake wote mmeyajua!”
“Leo Malcom anaonyesha kunihitaji.
Ameonyesha hadharani amenichagua mimi mwenye sifa mbaya. Mbele ya Zoe
aliyenitusi vibaya sana asubuhi ya leo mbele yao. Amenichagua mbali na mtoto
wake! Hakufanya kwa bahati mbaya! Malcom ametangaza kunichagua mimi kwanza
akijua wazi anajiingiza matatizoni. Anajiabisha, lakini amenichagua mimi.
Halafu eti mimi leo niachie bahati kama hiyo, sababu yakutunza sifa ipi ambayo
bado tunataka kung’ang’ania hapa?” Maya alikuwa
akiongea na yeye kwa hasira na ukali.
“Sisi tunateseka na kujinyima wakati
mama yeye anafurahia lengo lake limetimia kwetu. Ameshajinufaisha na pesa za
Cote kutuuza sisi kama bidhaa. Haya, na kwako wewe Net sasa hivi amefanikisha
kutokuoa kwako. Ukute sasa hivi hata amefungua champagne anajipongeza kwa kazi
nzuri aliyofanya. Anakunywa na kufurahia kinachokutokea wewe na Cote. Hajali
furaha yetu Net. Ameanza na sisi, sasa hivi ameingia hata kwa CJ huyo mtoto
wako. Hajawahi kuacha na ataendelea tu. Tunasubiri mpaka lini?”
“Mimi nimekataa kuwa kama wewe.
Nataka kuwa nafuraha Net. Hata kama ni ya muda mfupi, sijali. Naombeni mniache
nifurahie kwa kuwa hatujui anampango gani na kesho. Wakati wote mwenzenu
nimekuwa nikitafuta kuhitajiwa na kupendwa, na ndio maana niliishia kwa watu
wabaya. Na Malcom anaonekana ananipenda mimi. Halafu mnataka nikatae!?” Maya aliwafunga wote mdomo wakabaki kimya. Akashangaa
Net anamsogelea na kumkumbatia. “Nampenda Malcom,
Net. Na yeye ananipenda sana. Leo amenichagua hadharani!” “Okay.” Maya
akashtuka sana. Akajitoa pale mikononi.
“Umesema okay!?” Akamuuliza kaka yake na uso uliojaa machozi. “Si
umesema unampenda?” “Nampenda sana. Siwezi kupata
mtu anayeniangalia kama Malcom, tena baada ya uchafu wote huo! Na mimi nimepata
mtu anayeniangalia kama hivyo wewe unavyomwangalia Tunda, Net.” “Okay.”
Net akaitika hivyo tena bila maneno mengi.
Maya akafurahi sana, akatoka pale kwa Net na
kumsogelea bibi yake akamuona anatabasamu. “He
kissed me!” Akamwambia bibi yake vile Malcom alivyombusu huku akifuta
machozi. “Hilo busu limeshaenea kila mahali.” “Sijali Nana. Nampenda Malcom.”
“Am happy for you sweetheart.” Tunda alikuwa akicheka taratibu. Akamkumbatia
bibi yake palepale alipokuwa amekaa kwenye kiti chake.
Wakatulia kwa muda. Maya akasimama. “Samahani Net.”
“Hapana. Upo sahihi Maya. Kama inawezekana, inatakiwa maisha yetu yaendelee tu.
Umeongea ukweli. Kama umebahatika ulichokuwa ukikitafuta. Usisubiri. Nitakuwa
na wewe na mimi nitakuunga mkono.” Maya akarudi kwa kaka yake akakumbatia. “Asante
Net. You are the best brother in the whole wide world.” Wakacheka.
Hapo ndipo Maya akapata jukwaa la kuwasimulia kwa
mbembwe kuanzia alipokuwa akicheza na Menson mpaka alipokuja Malcom. “Kwani
wewe ulijua kama atakuwepo?” Tunda akauliza. “Hata sikuwa na taarifa. Ila
asubuhi wakati tulipokuwa tunapata kifungua
kinywa,...” Maya akasimulia kila kitu juu ya Zoe, Ethan, Malcom na Roy.
Wakabaki wanashangaa.
“Sasa kwa nini?” “Menson ameniambia anamtumia mtoto
wao kama fimbo kwa Malcom na pia kama njia ya warudiane. Najua kesho lazima
Malcom atakuwa matatizoni tu.” Maya akaongea kwa kumuhurumia Malcom. “Na yeye anajua.
Nilimuuliza hata kabla hajanipa busu.” Wakamuona anacheka na kushika midomo. Wote
wakacheka. “Maya!” “Ni mzuri huyo, Tunda. Kwani wewe hukumwangalia vizuri?”
“Nimemuona.” Tunda akajibu huku akicheka. “Sasa je!” Maya akajisifia. “Basi
nilipomkumbusha juu ya Ethan na kile atakachofanyiwa na Zoe, kwa kuniomba
nicheze naye, unajua aliniambia nini?” Bibi yake akacheka.
“Nitamwambia Tunda baadaye, sasa hivi Net yupo.
Naona aibu.” “Video yako kuanzia unaanza
kucheza na Menson, unapewa mabusu na Malcom mpaka unatolewa ukumbini ukiwa
umeshikwa mkono na huyohuyo Malcom, huyo kaka yako ameiona. Ni vile maneno
yalikuwa hayasikiki, ila pia mlionekana mnaongea kabla ya busu.” Maya
akajifunika na mto usoni huku anacheka.
“Malcom ananipenda mimi.” Maya aliongea huku
amejifunika mto usoni. Wote wakacheka. “Ni kweli anaonekana anakupenda. Kitendo
cha kukubusu pale. Wakati ule ambao hata wazazi wa Zoe pia walikuwepo, aliamua
haswa.” Maya akashtuka mpaka akatupa mto. “Nana!” Maya akashangaa. “Kwani wewe
hukujua kama Mayla na Zoe ni ndugu?” “Hapana Nana. Nimekuja kujua leo pale
ukumbini. Na sikujua kama wazazi wa Zoe wapo. Mimi nilitambulishwa kwa wazazi
wa Mayla tu. Wewe habari zao umezijuaje?” “Nimekwambia macho na masikio yangu
vyote vipo kwako sasa hivi. Na nilikuahidi kwa kila uamuzi utakaochukua
nitakuwa na wewe.”
“Sasa mbona umeacha Net akanigombesha?” Maya
aliongea kwa kulalamika. “Yeye ananafasi yake kama kaka na mimi kama Nana.
Haviingiliani.” Maya akacheka huku akimsogelea bibi yake. “Sasa itakuaje?”
Akamuuliza bibi yake. “Kwa kuwa sasa hivi umeamua. Na naona umekubaliana na
kaka yako. Tunaanza juu ya Malcom na Ethan kwanza. Tutahakikisha Malcom anapata
mwanasheria mzuri ambaye atamtetea na kupata haki ya kuwa na mtoto wake.”
“Yes.” Maya akafurahi sana.
“Ili isijeonekana kama wewe umeua mahusiano kati
yake na mtoto wake. Tumsubiri kesho atakapoenda kumshitaki, ili sasa tuweke
utetezi mzuri. Safari hii Malcom atashauriwa asikimbilie kujitetea, ila
mwanasheria kudai haki ya Malcom kwa mtoto wake. Apangiwe siku za kuwa na mtoto
wake ambazo zitasimamiwa na mahakama.” Bibi Cote akaendelea.
“Akipewa masaa 24, lazima yawe 24 na Malcom
ayatumie atakavyo bila Zoe kuingilia.” Maya akaenda kumbusu bibi yake. “Asante
Nana. You are the best.” “I know.” Bibi Cote akajivunia akisema anajua kama
yeye ni bora, nakufanya wote wacheke.
Wakaweka mikakati ambayo mingi ilishindwa kufika mwisho,
kwa kuwa wote hawakujua hatima yao ipoje! Ritha anafikiri na kupanga nini! Huo
ukabaki mtihani uliomuumiza zaidi bibi Cote, kuona Ritha, mwanamke mweusi,
anaweza kuwazidi wazungu hao na heshima zao, ujuzi wao, amemudu kuwazidi mahesabu
kwa kiasi hicho! Amefanikiwa kusimamisha harusi ya Net. Vizuri na kirahisi tu.
Vic aliyemtumia kijanja, na yeye ameishia jela kama Bethy. Yeye hajaguswa!
Alimteka nyara Tunda, katikati ya ulinzi alioweka yeye
mwenyewe bibi Cote! Kwake ilikuwa ni kumfedhehesha kwa hali ya juu. Ni kama
alimuhakikishia, anaweza kufika popote anapotaka. Na yeye bibi Cote si kitu
kwake, amemzidi mahesabu. Napo hapo akaishia kufa Malinda na mdogo wake, kama
vile Gab. Yeye yu hai, maisha yake yanaendelea swafi mtaani akiwa na kazi nzuri
tu.
Mpaka siku hiyo ya jumamosi wanakwenda kulala, siku
ambayo ilitakiwa Net awe ameshaoa yupo fungate na mkewe, wameishia hapo na
majonzi, hawakuwa na ushahidi wa kumkamata yeye Ritha. Kwamba Ritha anayo akili
kumzidi yeye bibi Cote anayevuma mitandaoni na kusikika na mipango mizito,
lakini inamaana Ritha amemzidi mbali sana. Anajua kujipanga vizuri katika njama
zake kuliko yeye bibi Cote katika mipango yake ya kifahari.
Ilikuwa ikimuuma sana bibi Cote kila alipokuwa
akimfikiria Ritha ambaye maisha yake yalikuwa yakiendelea kama kawaida. Kwa
uhuru wote, wakati wao wamefungiwa ndani, hawawezi hata kwenda kazini kwa hofu.
Hawajui nani ni mbaya wao. Nani anatumiwa na Ritha! Wakabaki wao na pesa zao
ndio kuwa wafungwa ndani ya hekalu lao, na askari wakiwalinda nje.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Usikose Muendelezo wa
Simulizi hii ili kujua kilichoendelea kwa familia hiyo ya Cote inayozungukwa na
mikasa mizito kila kukicha na yote inabidi bibi Cote aitafutie ufumbuzi.
Ø Malcom naye
yuko ataponaje usiku huo baada ya alichokifanya kwa mama watoto wake?
Ø Je safari
hii Maya atafanikiwa kupata alichokuwa akikitafuta maishani?
Ø Hatima ya
Tunda & Net!
Ø Hatima ya
Ritha nayo ni ipi!?
USIPITWE vyooote vipo mbeleni.
0 comments: