Story

My Past...Sehemu ya 1.

Saturday, April 08, 2017 naomimwakanyamale 0 Comments


Walirudi tena kaburi. Safari hii walijikuta wako peke yao. Ilikuwa ni miezi michache tu imekwisha
pita tangia walipomzika mama yao kwenye makaburi hayo yaliyokuwa yamefurika umati wa watu waliokuwa wamehudhuria mazishi ya mama yao. Upweke wa namna yake uliwaandama ndugu hao wawili mara baada ya mama yao kuondoka. Ukweli hakuwa ameacha jina zuri hata kidogo kwenye jamii. Siku ya msiba, Bella alisikia watu wakimsema vibaya mama yao, hasa ndugu zake.

Alibaki akiumia sana, kila alipokuwa akiwasikia dada za mama yake jinsi walivyokuwa wakimsema mdogo wao. “Umalaya umemponza. Muone alipoishia.” “Alikuwa akiringia uzuri wake huku akitudharau ndugu zake akidhani yeye ndio amebahatika sana. Ona yaliyompata?” “Tunu, kafa kwa aibu jamani! Aliugua mpaka nilimuhurumia. Unajua mwanae ndiye alikuwa akimuuguza?” Shoga ya mama yake kipenzi aliyewasindikiza kijijini kwao kwa mazishi naye aliendelea kutoa habari za mama yake mbele ya dada wa marehemu, mama yake. Bella aliendelea kuwasikiliza wakidhani amelala chumbani, na wao wakiwa nje ya chumba hicho. 

“Sasa hatima ya hao wanae aliowaacha ni nini?” Yule rafiki ya mama yake Bella aliwauliza dada zake Tunu. “Nani anawachukua?” Alizidi kudadisi. “Heee! Mbona wote mnanigeukia mimi!?” “Sasa wewe si ndio dada mkubwa?” “Kwa hiyo!?” “Si ndio mzigo wako huo?” Dada yake mwingine Tunu alitoa wazo kwa kejeli. “Naomba usinichurie. Sichukui mtoto wa mtu, mimi. Alivyokuwa akifanya umalaya wake, hakuwa anafikiria juu ya wanae? Mnakumbuka ni mara ngapi baba na mama walivyokuwa wakimuhusia Tunu atulie na aolewe kama shule imemshinda, lakini akakataa? Kazaa watoto wawili na wote hawajui baba zao! Mnataka nikazunguke na watoto wasiojulikana mwanzo wala mwisho, halafu iweje? Watakaa hapahapa kijijini kwenye nyumba ya familia.” Wote walicheka. 

 “Lakini Tunu alitingisha mjini, sio mchezo bwana. Na atakuwa amekwenda na wengi!” Shoga mtu aliongeza. “Hivi kwani alijenga?” Mmoja wa dada yake Tunu, yaani Mama Bella, aliuliza. “Ajenge wapi? Shoga yangu yule akili alikuwa hana. Yeye starehe na kumwaga mipesa kwa wanae. Kazi yake ilikuwa kuwanunulia wanae nguo mpya kila kukicha na kuwasomesha shule za gharama, ilimradi kushindana na matajiri. Nilikuwa namwambia ahamishe watoto wake kutoka kwenye ile shule ya gharama, awapeleke kwenye shule za kawaida, ili tukanunue viwanja tuanze kujenga, kwani alikuwa ananisikia?” “Hana aliyekuwa akimsikiliza yule. Sisi wenyewe tulikuwa tukimwambia marehemu mama kuwa alimzaa yule mtoto bila masikio. Lakini mama ndio alikuwa akimtetea.” Dada yake mkubwa Tunu, Betty aliongeza.  

“Si kwa kuwa alikuwa anawaletea mi pesa!” Dada yake mwingine alidakia kwa haraka. “Lakini marehemu baba alimkatalia asiwe analeta mihela yake ya umalaya.” “Kweli dada Bety!?” “Nakwambia tena. Tena kwa kumsikia baba akimwambia, mpaka amwambie anapofanya kazi, na kama kweli ameajiriwa, ndio atapokea pesa yake.” Wote waliendelea kucheka. “Lakini bwana Tunu alikuwa ana roho nzuri. Hataki kumuona mtu anapata shida. Mimi mwenyewe alinisaidia sana kujenga ile nyumba yangu.” Shoga aliongeza. “Sio roho nzuri, alikuwa na kajiunafiki na ujinga ndani yake.” Betty aliongea  kwa wivu kidogo. “Kweli dada Bety. Tunu alikuwa mjinga. Wewe utajengaje kwa mtu wakati mwenyewe unakaa kwenye nyumba ya kupanga!? Kama si ujinga huo nini?” “Basi ndio aandike maumivu huko alipo. Wanae tutawaacha hapahapa. Sibebi mitoto ya mtu.” “Unaogopa nini, Betty?” Shoga mtu aliuliza kwa uchokozi,  wote wakacheka.  “Mwenzangu we, asije nivunjia ndoa yangu. Ndoa yenyewe yakuunga unga, halafu uje umpeleke mtoto kama yule, si kumuingiza mume majaribuni!” Walizidi kucheka huku wakigonga mikono.  

“Na kweli dada Bety. Wanaume wenyewe hawa macho juu, leo unamsogezea dogodogo! Tena na umbile lile kama la Tunu, mama yake. Anawaka kama taa, hata kama ukimwambia mtoto wa mdogo wangu, hakuelewi.” “Aku! Sitaki shida mie.” Bety alijibu. “Mimi siwashangai. Maana huruma nyingine zinaponza. Tena huyo mtoto ndio alikuwa karibu sana na mama yake. Wanaume wote wa mama yake atakuwa anawajua. Kwa hiyo tabia zake zinaweza kuwa kama za mama yake.” “Sasa wewe si ndio alikuwa shoga yako kipenzi? Ndio usaidie wanae sasa.” “Usinitafutie balaa. Nyumba yenyewe ndio tumehamia, hata mwaka hatujamaliza. Nisije nikafukuzwa mimi akaolewa yeye.” Wote walicheka huku Bella akiendelea kuwasikiliza.  

Mwenzangu akili kichwani eeh! Wakae tu hapahapa kijijini, wafungue shule, waanze kufundisha watoto wa hapa kijijini kingereza, ili wapate hela yeye na mdogo wake.” “Haswaa. Si ndio urithi walioachiwa na mama yao? Ndio wautumie vizuri.” “Wataongea kingereza hapa kijijini?” “Kumbe? Si ndio urithi wao bwana. Watoto wamesomeshwa shule za kimataifa, watumie ujuzi wao. Na nyumba hii tunawaachia, wakae bureeee, bila kulipa.” Wote waliendelea kucheka bila aibu wala huruma. Mwishowe Enabella aliamua atoke tu pale chumbani kwani alizidi kuumia. 

************************************* 

Majani yalishaanza kuota kwenye kaburi la mama yao. Enabella aliinama na kuanza kuyang’oa taratibu huku akiwaza. Mdogo wake wa kiume alikaa pembeni ya kaburi hilo la mama yake akilia. Bella aliendelea kusafisha taratibu mpaka alipomaliza na kukaa pembeni ya mdogo wake akiwaza. Ni kweli waliachiwa nyumba ya wazazi wa mama yao, lakini bila pesa, wala chakula. Walikuwa wakiishi na mjomba wa mama yao, naye alikuwa mlevi sana. Wengi walisema alitakiwa awe baba yake Tunu kwani tabia zao zilikuwa zikifanana sana. Na yeye alizaa kila mahali alipowahi kuishi, na hakuwahi kuoa wala kulea mtoto wake hata mmoja. Aliposhindwa maisha ya mjini, akarudi kuishi kijijini kwa dada yake, ambaye ni bibi yake Enabella na Eric. Na Tunu ndiye alikuwa rafiki yake kipenzi. Kila Tunu alipofika hapo kijijini kusalimia wazazi wake, hakuacha kupata muda wa kutosha na mjomba wake. Watu walisema wanaelewana sababu wote walikuwa na tabia mbaya, zisizofaa kwenye jamiii. 

Enabella na Eric, watoto wa Tunu waliachwa pale kijijini na huyo babu yao aliyekuwa mlevi wakupindukia. Lakini katika ulevi wake, hakuacha kuwaletea chakula angalau cha kuwatosha kula mlo mmoja kila siku. “Mungu alinipa mtoto mmoja tu, anaitwa Tunu.” Ulikuwa ni usemi aliokuwa akiurudia rudia babu yao huyo kila mara. Hakuacha kupata nao muda angalau kila siku akiwachekesha kisha kupotelea kilabuni kunywa pombe. Na hakuacha kurudi kulala nyumbani, kuhakikisha Enabella na Eric wapo salama. “Mtu asiwadanganye, katika watoto wote wa nne ambao dada yangu alizaa, Tunu peke yake ndio alikuwa mtoto anayejali nyumbani kwao. Japokuwa hakusoma sana kama wenzake, lakini yeye ndiye aliyekuwa na moyo mzuri sana na ndiye aliyekuwa akinitunza mimi na bibi yenu baada ya kifo cha babu yenu. Alikuwa mtu mzuri sana na moyo wake ulikuwa wa tofauti.” Angalau Enabella alikuwa akifarijika. 

Kilichokuwa kikimuumiza Enabella au Bella kama wengi walivyozoea kumwita, ni mdogo wake tu. Angalau yeye alishamaliza kidato cha nne, lakini mdogo wake ndio alikuwa shule ya msingi. Bella alifikiria kumuacha pale kijijini ili yeye arudi mjini, angalau akatafute pesa, lakini alimuhurumia sana Eric mdogo wake. Yeye na mama yake walimpenda na kumdekeza sana Eric, hakuwa akijua shida wala maisha bila Mama yake au Bella yanakuaje. Japokuwa walizaliwa na baba tofauti tofauti, lakini Tunu aliwalea watoto wake kwa mapenzi makubwa sana. Mapenzi hayo na umoja kati yao, viliwafanya hata wao wenyewe kutoona tofauti kati yao, na hawakuwahi hata kuwaza swala la baba. 

*************************************

“Eric!” Bella alimwita mdogo wake wakiwa bado wamekaa palepale makaburini. “Naomba nikuache hapa kwa babu kwa siku chache niende nikaangalie pesa mjini, halafu nitarudi kukuchukua. Umesikia?” “Nibaki peke yangu!?” “Babu atakuwepo.” “Naogopa Bella. Twende wote tu.” “Hatuwezi kwenda wote Ric. Sitakuwa na pakukuweka.” “Turudi nyumbani, Bella.” “Ndio nataka nikaangalie kama bado ile nyumba ipo au mwenye nyumba alishatutupia vitu vyetu nje. Kama bado ipo, nitakuja kukuchukua.” “Kama haipo?” Eric akamuuliza dada yake swali lililomfanya Bella abaki kimya afikirie kwa muda. “Nitatafuta njia nyingine yakufanya. Lakini hatuwezi kuendelea kuishi hapa, lazima turudi Dar.” Eric akanyamaza kimya. 

Walikaa pale makaburini mpaka babu yao alipokuja. “Nimewatafuta kweli, nikahisi tu mtakuwa huku. Turudini nyumbani, giza limeshaanza kuingia.” “Lakini babu!” Bella akasimama. “Naomba nikuachie Eric kwa muda, mimi nikimbie mjini mara moja nikaangalie vitu vyetu. Unajua tulipokuja huku, tuliacha vitu vyetu vyote kwenye ile nyumba tuliyokuwa tumepanga. Halafu tulikuwa na gari ndogo, mama alikuwa akiifanyia taksii. Nataka nikaangalie kama kaka Mat anaweza kutupa pesa, ili Eric arudi shule. Hatuwezi kuendelea kuishi tu hivi, babu.” Babu yao akafikiria kidogo. “Wazo zuri Bella. Nilikuwa nikifikiria hivyohivyo, huku nikijiuliza, mtaishi hapa kwa hali hii mpaka lini? Mwisho wenu utakuwa nini? Bila yakupata jibu. Heri uende tu.” “Asante babu. Lakini sina nauli.” “Nitakuombea kwa dereva wa lile basi la alfajiri sana, ni rafiki yangu, ili akuchukue bure.” Bella alifurahia lile wazo . Wakarudi nyumbani, Eric akiwa na mawazo sana. 

Wakati wamepanda kitandani kila mmoja akijaribu kutafuta usingizi, Eric alimwita Bella. “Bella!” “Hujalala tu Eric!?” “Umesema utarudi lini kuja kunichukua?” “Nitajitahidi nisichelewe.” “Mama aliniambia hutaniacha, Bella.” Eric alianza kulia. Bella alikaa. “Sikuachi Eric, nakuahidi nitarudi. Umesikia? Lazima nikaangalie sehemu tutakapoishi mimi na wewe.” Eric aliendelea kulia. “Njoo hapa kitandani kwangu.” Eric akahamia kwenye kitanda cha dada yake. “Nikikuta kila kitu kipo sawa na Kaka Mat akatupa pesa anazokusanya kwenye taksii, nitarudi kukuchukua.” “Naogopa Bella. Twende wote tu. Utakapopata pa kulala huko mjini, ndio hapo hapo na mimi nitalala.”  “Nisipopata pa kulala je?” “Nitakuwa na wewe popote  Bella, lakini usiniache hapa peke yangu.” Bella alibaki kimya akifikiria mpaka wakapitiwa na usingizi kwenye kitanda hicho kidogo wakiwa wamelala pamoja. 

************************************* 

Palipambazuka, lakini Bella alibaki kitandani akiwaza maisha ya mjini wakiwa peke yao bila mama yao. Alikumbuka kipindi cha mwisho kabla ya kifo cha mama yake, akiwa anamuuguza, jinsi alivyokuwa akihangaika kutafuta pesa zakuwawezesha kuishi. Ilimbidi kuuza baadhi ya vitu vyao vya thamani, zikiwepo hereni na cheni za dhahabu za mama yake, ili kuweza kuishi mjini na kulipa kodi ya nyumba. Mama yake Bella alikuwa akimtuma kwa marafiki zake mbalimbali kuomba msaada wa kifedha, lakini wengi walikataa kuwasaidia. Tunu, ambaye ni mama yake Bella aliugua muda mrefu sana, tena akiwa yeye na wanae tu, huku kila rafiki aliyemsaidia wakati akiwa na pesa, akimkana na kushindwa kupokea simu zake kabisa. Bella alitaka arudi mjini akiwa peke yake, akamalizie kuuza baadhi ya vitu alivyobakisha kabla mama yake hajafariki, ili angalau apate pesa ya kukodi japo chumba kimoja atakachoishi yeye na mdogo wake, lakini Eric alionekana kutokukubaliana na wazo la kutengana na Bella kabisa. Hata hivyo mama yao alishamuapisha sana Bella, kutosubutu kumuamini mtu yeyote na mdogo wake. 

************************************* 

“Bella!” Ric alishtuka usingizini huku akiita jina la dada yake kwa nguvu huku machozi yakimtoka. Bella alijua alikuwa akiota. Alivuta pumzi kwa nguvu mara baada ya kumuona dada yake yupo naye pale kitandani, akiwaza. “Nimeota umeondoka, halafu ukaniacha hapa peke yangu.” Machozi ya wasiwasi yalianza kumtoka Eric. Uso wake ulishabadalika na kuwa mwekundu sana. “Siwezi kukukimbia Ric. Basi usiwe na wasiwasi, tutaenda mjini pamoja, usiogope.” Bella alicheka kidogo, akamfuta machozi kama kumfariji, huku akijitahidi kuficha hofu yake kubwa iliyopo ndani yake yeye mwenyewe. “Kweli Bella?” Eric aliuliza huku akionyesha tumaini jipya usoni. Bella akatabasamu. “Nitakusaidia Bella.” Eric aliongea kama mtu mzima, lakini alikuwa ni mtoto aliyetamani kumfariji tu dada yake na kuhakikisha hatamuacha pale kijijini. Bella alijisogeza karibu na mdogo wake, akamkumbatia kisha akambusu, akijua wazi mdogo wake hajui anachoongea. “Sitakuacha Ric. Tutaenda wote.” Eric alifurahi sana. “Asante Bella. Nilikuwa naogopa kulala usiku peke yangu halafu kuna giza. Hamna taa. Ningeendaje kuchota maji peke yangu?” Waliendelea kucheka kidogo, mpaka walipomsikia babu yao akipiga miluzi nje, na wao wakatoka. 

“Mbona kaka anafuraha hivyo?” Babu yao aliuliza. “Naondoka na Bella.” Eric alijibu kwa haraka. Babu yao alifikiria kidogo. “Unauhakika Bella? Utazunguka naye huyu huko mjini, utaweza kweli?” Babu yao alihoji kwa wasiwasi sana. Kila akimwangalia Eric, hakufanana na mtoto anayeweza hata kutembea umbali mrefu. Alikuwa mlegevu, na kwa kumwangalia tu, alionekana ni mtoto aliyekuzwa kwa kudekezwa sana. “Mama aliniambia nisimuache Ric, popote ninapokwenda lazima niwe naye.” “Uwamuzi wa kwanza naona ndio ulikuwa sahihi Enabella. Huwezi kwenda na mtoto mjini. Huwezi kujua utakutaje hali ya huko.” “Hapana babu, lazima niondoke na Ric. Sitamuacha popote. Mama alishaniapiza kabla hajaondoka. Alisema nisimuache Ric na mtu yeyote isipokuwa mimi mwenyewe.” Tunu alimlinda sana Ric, kwani alikuwa na uzuri kama mtoto wa kike. Tunu alifanana sana na watoto wake. Enabella ndio alichukua kila kitu cha mama yake mpaka ukucha, ila Eric ni kwa kuwa tu alikuwa mtoto wa kiume, lakini haikuhitaji kuuliza kama wao ni ndugu. Wote walikuwa wazuri sana. 

 Babu yao bado alibaki kimya akionyesha kutoridhika kabisa na maamuzi ya pili ya Bella. “Naondoka na Ric, babu. Sitamuacha popote. Nitakapo lala ndipo na yeye atakapolala, nitakachokula ndicho na yeye atakachokula. Sitamuacha. Naomba utusaidie jinsi ya kutuondoa hapa mpaka mjini. Mengine nitajua hukohuko nitakapofika.” “Sawa.” Baada ya kuona Bella amemaanisha anachoongea na hana dalili yakubadili mawazo, ilibidi babu yao akubaliane nao tu. Hata hivyo na yeye mwenyewe alishalemewa na kuwatunza. Hakuna ndugu hata mmoja aliyekuwa akiwakumbuka hata kwa kuleta sukari ya chai pale kijijini.


 “Bella arudi jijini akiwa na mdogo wake.”
Bella alitua jijini na mdogo wake, mida ya jioni. Walipanda kwenye daladala na kwa bahati yao ilivyokuwa nzuri, hawakuulizwa nauli mpaka walipofika kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi na marehemu mama yao, Mikocheni B. Walikuta nyumba ilishapata wapangaji wengine. Bella alisimama pale kwa muda akifikiria. “Sasa vitu vyetu vipo wapi?” Bella alimuhoji mwanamke waliyemkuta kwenye nyumba hiyo. “Labda mumpigie simu mwenye nyumba. Sisi tuliikuta hii nyumba tupu kabisa. Hapakuwa hata na kijiko.” “Sina simu. Naomba kama unaweza kuniazima simu yako.” Yule mama alimtizama Enabella na mdogo wake kwa muda, “Mmesema majina yenu ni kina nani tena?” “Naitwa Enabella na huyu ni mdogo wangu Eric.” “Hebu nisubirini kidogo.” Aliingia ndani na kuwaacha palepale nje. Bella alianza kuwaza pa kulala usiku ule na mdogo wake. Usiku ulishaingia na majibu waliyopewa hayakuwa yakiridhisha hata kidogo. 

“Njaa inakuuma?” Bella akamuuliza Eric mdogo wake, huku akijisuta mwenyewe moyoni. ‘Hata akisema njaa inauma, nitampa nini?’ Bella aliwaza. “Eti Eric?” “Hapana.” Bella alijua anamdanganya kwani tokea asubuhi walipoanza safari, hawakuweka kitu mdomoni. Watu walishuka kwenye basi kwenda kula, lakini wao walibaki kwenye basi, kwa kuwa hawakuwa na pesa yeyote. “Umechoka?” Bella aliendelea kumuhoji mdogo wake kwa upendo sana. “Kidogo.” “Pole.” Akiwa anafikiria pakumlaza mdogo wake kwa usiku huo, mlango ukafunguliwa tena. “Eric anaumwa na njaa sana. Hatujala tokea jana.” Bella alimuwahi yule mama kabla hajazungumza kitu chochote. Yule mama akakunja uso, kama kuwashangaa. “Kwanza nataka niwaambie, nimetoka kuongea na mwenye nyumba. Anasema hajui lolote juu ya vitu vyenu, yeye alimuachia dalali hii nyumba ili atafute mpangaji mwingine. Na anavyosema hii nyumba ilikaa kwa muda wamiezi miwili bila kupata mteja, mpaka yeye mwenyewe, mwenye nyumba alipoamua kuingilia kati, kutafuta wapangaji, ndio akatupata sisi. Hata hivyo anasema mliondoka hapa akiwa bado anawadai. Kwa hiyo maswala ya vitu vyenu, yeye hafahamu.” Bella alitulia kwa muda. Alikumbuka kweli kabla hajamrudisha tena mama yake hospitalini wakati amezidiwa sana, alikuja mtu aliyekuwa akidai kodi ya mwaka mzima, lakini mama yake aliomba avumilie, atakapopata nafuu atalipa pesa yote. Mbali ya taksii aliyoona ikiingiza pesa, Bella hakujua chanzo kingine kilichokuwa kikimuingizia mama yake pesa. 

Waliishi kwenye nyumba hiyo nzuri sana, walisoma shule ya gharama sana pale mjini, na walivalishwa mavazi ya gharama sana. Kwa ufupi walikuwa wakiishi maisha yakifahari, lakini Enabella hakuwa akijua kazi ya mama yake. Bela alibaki akiwaza.  

“Nataka nikapumzike.” Yule mama alimshtua Bella aliyekuwa bado amesimama nje ya mlango na mdogo wake, akimwashiria anataka kufunga mlango. “Naomba nisaidie simu ili nimpigie mtu.” “Siwafahamu na siwaamini. Siwezi kukupa tu simu yangu. Siku hizi matapeli ni wengi sana mjini. Wewe nipe hiyo namba nimpigie huyo mtu wenu.” Bella alimpa namba ya simu ya dereva wa taksii yao, Mat, yule mama akapiga. “Inaita.” Yule mama aliwaambia Bella na mdogo wake wakiwa bado wamesimama nje na yeye amesimama mlangoni.  

“Haloo.” Mat alisikika upande wa pili wa kwenye simu. “Kuna watoto hapa, wanataka kuongea na wewe. Mkubwa anaitwa Bella, sijui..” Alimpa Bella simu. “Mko wapi Bella?” “Tunashida kaka Mat, naomba utusaidie. Nipo na Ric, amechoka, njaa inauma, halafu nyumba ilishapata mpangaji mwingine. Tupo tu hapa nje, hatuna pakwenda.” “Poleni sana. Sasa, sasa hivi nina mteja kwenye gari. Nisubirini, nitakuja kuwachukua nikimshusha.” “Asante kaka Mat.” Bella alirudisha simu kwa yule mama. “Amesema tumsubiri.” Bella aliongea kinyonge huku akimwangalia yule mama kwa macho ya huruma, ili angalau awakaribishe ndani, asiwaache pale nje kwenye mbu. “Basi msubirini pale getini kwa mlinzi.” Yule mama alifunga mlango na kuwaacha pale pale nje. 

“Kaka Mat anakuja muda sio mrefu. Twende tukamsubiri pale nje.” Bella alisogea na mdogo wake mpaka pale getini. Akatafuta mahali akakaa na mdogo wake, huku akiwaza kama kweli Mat atakuja na kama atawasaidia. Mat pekee ndiye aliyekuwa tumaini lao kwa wakati ule. Walikaa pale zaidi ya masaa manne, bila Mat kutokea. Bella alinyoosha miguu ili mdogo wake amuegemee alale. Akamfunika na mtandio aliokuwa amepewa na mama yake, Ric akapitiwa na usingizi.  

Bella alikaa pale akiwaza maisha yao bila ya kupata jibu mpaka ilipofika saa sita na nusu usiku, ndipo Mat akawasili pale. Alichukia sana kuwakuta wameachwa pale nje. Mat alianza kutukana kwa nguvu akitaka kufanya fujo pale kwenye ile nyumba, lakini mlinzi alimzuia.  “Roho zenu mbaya, maskini wakubwa nyinyi.” Aliishia kupiga bati kwa mawe kadhaa, huku akitukana mpaka Bella alipomsihi waondoke tu.
“Wapata hifadhi kwa dereva taksi, Mat.”
Mat aliwachukua Bella na Eric mpaka kwenye chumba alichokuwa amepangisha huko mtaa wa Kigogo. Kilikuwa chumba kimoja tu, kilichojaa takataka na kilikuwa kikinuka harufu mbaya sana ya jasho. “Najua chumba nikidogo sana, lakini nyinyi ni wadogo zangu tutajibana hivyohivyo.” Mat aliwapikia chai ya rangi na mkate aliokuwa amebakisha kabatini, Bella na mdogo wake wakala, wakajitupa kitandani bila hata ya kuoga, mpaka asubuhi. 

Mat aliwaambia biashara ya taksii ni ngumu sana kwa wakati ule, haingizi pesa nyingi, lakini aliwafariji na kuwaambia wasiwe na wasiwasi, wataishi tu. Waliishi  na Mat pale uswahilini, zaidi ya mwezi wakiwa kwenye kile kile chumba kimoja. Lakini Mat alihakikisha kila anapopata mteja na akiingiza pesa kidogo, anarudi nyumbani na kumuachia pesa kidogo Bella, ili akanunue chakula apike ndipo na yeye arudi kazini. Mat aliweza kulipia chumba hicho, na kuwalisha watoto wa Tunu, kwa kupitia taksii hiyo ya marehemu Tunu.  

Kila mtu alimjua Bella na Eric kama ni wadogo zake Mat, kwa hiyo hakuna aliyewasumbua pale uswahilini. Mat alijulikana sana pale mtaani. Mateja{Watumiaji wa madawa ya kulevya} na wezi wote wa pale mtaani kwao, Kigogo, walimuheshimu sana Mat kwa tabia yake ya ustaarabu. Alipenda kusaidia kila mtu, hata walipokuwa na shida, walimkimbilia Mat. Kwa hiyo Bella na Eric walilindwa, yaani walinzi wao wakawa ni watu wa hatari watupu pale mtaani. Yale majambazi sugu ya pale mtaani, yaliwatambua kama wadogo zao. Hakuna aliyekuwa akiwasogelea kutaka kuwadhuru, kitu kilichomtia moyo Bella. Angalau hakuwa na wasiwasi na mdogo wake, aliyekuwa akishinda mtaani akicheza, asubuhi mpaka jioni. 

Siku zilizidi kwenda bila hali ya kipato kubadilika kati yao. Bella alizidi kuumia kuona mdogo wake anabaki akizagaa pale mtaani bila kwenda shule. Alikuwa akitoka kwenda kucheza mpira na watoto wengine wa mtaani, kuanzia asubuhi mpaka jioni Bella anapokwenda kumsaka arudi kuoga na kula, ili alale. 

************************************* 

Mwishowe Bella akaamua kwenda nyumbani kwa rafiki yake kipenzi, Zera Masha, ili akaombe msaada. Zera alizaliwa kwenye familia ya watu wenye pesa sana. Na walimpenda sana Enabella. Zipo siku ambazo Bella alikuwa akienda kulala nyumbani kwa kina Zera na Zera naye alikuwa akienda kwa kina Bella, kipindi hicho wakiwa shuleni. Hata wazazi wao walifahamiana. Japokuwa mama zao walishindwa kuwa marafiki, kwani mama yake Zera alikuwa msomi sana, na elimu ya marehemu Tunu haikuwa ikieleweka na yeyote yule, kitu kilichowafanya wakati wote wa kina mama hao kila wanapokuwa pamoja, kujikuta hawana cha kuongea. 

Bella aliamka siku hiyo mapema kidogo, kabla Mat hajaondoka kwenda kazini. “Naomba utupeleke kwa kina Zera.” Mat alikuwa akipafahamu vizuri sana nyumbani kwa kina Zera, kwani yeye ndiye alikuwa akimpeleka huko mara zote alizokuwa akienda kumtembelea rafiki yake. “Itabidi niwaache huko kwa kina Zera, halafu niwafuate baadaye. Kuna mtu nataka nimuwahi ofisini kwake, ameahidi kunipa kazi yakuwazungusha wafanyakazi   wake. Nikipata hiyo kazi, angalau tutaweza kuishi vizuri. Lakini sasa hivi mambo sio mazuri kabisa. Pesa zote ninazowaletea hapa nyumbani, nakopa kwa marafiki zangu. Siingizi kitu kabisa.” “Pole kaka Mat. Ndio maana nataka kwenda kwa kina Zera, nikawaombe wazazi wake msaada, labda watatusaidia.” “Basi ndio tuondoke sasa hivi.” Bella alimsaidia Eric kujitayarisha kwa haraka ili wasimcheleweshe kaka yao, kisha wakaondoka. 

Ennabella & Eric nyumbani kwa Masha!
Kama kawaida yake, Mat aliwashusha Bella na mdogo wake getini, yeye akaondoka bila hata kuingia ndani. Kwa kuwa walikuwa wenyeji pale, Bella alimsalimia mlinzi wa zamu aliyemkuta pale getini, wakakaribishwa ndani. Zera alifurahi sana kumuona rafiki yake kipenzi. Aliruka na kumkumbatia. “Wenzako tunahama hapa nchini.” Zera aliongea kwa furaha sana. “Mnahamia wapi?” Bella aliuliza kwa unyonge. “Mama amechaguliwa kuwa balozi nchini Uholanzi. Twende chumbani kwangu.” Zera alimvuta mkono Bella mpaka chumbani kwake wakamuacha Eric amekaa kwenye kochi, sebleni. “Kwani mnaondoka lini? Naona mpaka na mabegi yapo tayari!” “Kesho usiku.” Zera alijibu kwa uchangamfu. “Mnaondoka wote?” “Baba atarudi, hatakaa sana huko sababu ya biashara zake huku. Lakini ameahidi kuwa anakuja kututembelea mara kwa mara.” Bella akakaa kitandani akiwa ameishiwa nguvu. “Hongera Zera. Mwenzako nahangaika kweli! Tangia mama alipofariki maisha yamebadilika. Hatuna hata pakuishi.” “Pale nyumbani kwenu!?” Zera akauliza kwa mshangao kidogo. “Ile ilikuwa nyumba ya kupanga. Imeshapata wapangaji wengine.” “Kwa hiyo ulinidanganya!?” Zera alimbadilikia Bella. “Wewe siuliniambia pale ni kwenu!?” “Sikukudanganya Zera, ndivyo na mimi nilivyokuwa nikijua, mpaka mama alipoanza kuugua.” Bella alimuona jinsi Zera alivyombadilikia. “Kwa hiyo hamna nyumba!?” Zera aliuliza kwa dharau kidogo. “Hatuna Zera. Ndio maana nakwambia tunahangaika mimi na mdogo wangu, hatuna pakwenda.”  Zera alibadilika kabisa sura yake. Ile furaha ilipotea kabisa usoni, na Bella alijua. 

“Zera!” Walisikia sauti ya mama yake ikimwita. Wote walitoka chumbani kwa Zera, wakashuka ngazi kuelekea sebleni alipokuwepo mama yake Zera, yaani Mama Masha. “Hujambo Bella?” “Sijambo, shikamoo.” “Pole na msiba wa mama.” “Asante.” “Sasa hivi mnaishi wapi?” “Hatuna pakuishi mama yangu, tunajishikiza kwenye chumba cha Kaka Mat, yule dereva taksi wetu, mtaa wa Kigogo.” “Unaishi Kigogo?” Zera alishtuka sana. “Ndiyo.” “Heee!” Zera alizidi kushangaa, kisha akacheka. 

Baba yake Zera alitoka chumbani. “Shikamoo.” Bella alimuwahi. “Marahaba Bella, hujambo?” “Sijambo.” “Pole na msiba wa mama.” Baba yake Zera, Mzee Masha, naye hakuwa amekutana na Bella tokea wafiwe. “Asa..” “Eti dad, siku hizi hawa kina Bella wanaishi Kigogo! Tena kwa yule dereva taksi wao. Hawana pakuishi.” Zera alimkata kwa kejeli rafiki yake Enabella, kabla hajaitikia pole aliyokuwa amepewa na Mzee Masha, baba yake.   

“Imekuwaje pale mlipokuwa mkiishi na mama yenu?” Mzee Masha akahoji taratibu tu. “Alinidanganya kwamba ni nyumbani kwao, kumbe ni nyumba ya kupanga. Sipendi sana watu waongo.” Zera alimjibia Bella kwa kumshutumu. “Na mimi sina cha kuwasaidia. Tunaondoka kesho kuelekea nchini Uholanzi.” Mama Masha aliingilia yale mazungumzo na kujibu kwa haraka, akionyesha wazi hayupo tayari kufanya chochote juu yao. “Ningekuwepo hapa nchini labda, lakini tunasafiri.” Aliongeza. Bella alibaki amesimama, hajui aseme nini. 

“Zera, hebu kunywa chai haraka tuondoke.” Mama Masha alimgeukia mwanae Zera. “Twende tu mama, sisikii njaa kabisa. Hamu ya kula imeshaniisha.” Zera alijibu. “Tunataka kuondoka Bella.” Zera na mama yake walimgeukia Bella kama wanaetaka waondoke pale, yeye na mdogo wake. Bella alitaka kuomba pesa kidogo, angalau ziwasaidie nauli ya daladala kurudi Kigogo, lakini kama kitu kilikuwa kimemkaba kooni, alishindwa kabisa hata kuongea. Alimsogelea mdogo wake, aliyekuwa akisikiliza kila kitu pale sebleni alipokuwa amekaa, akamshika mkono. “Twende Ric.” Ric alisimama na kutoka na dada yake. 

*************************************

Wakati wakiwa njiani wakitembea, wasijue watafika vipi Kigogo kutokea hapo Masaki, ilisimama gari ambayo Bella aliitambua, kwani ndio gari aliyokuwa akitumia Zera. “Bella!” Dereva alishusha kioo na kumwita Bella. “Shikamoo kaka K.” Bella alisimama akiwa amemshika mdogo wake mkono, akamsalimia yule dereva kwa kuwa walikuwa wakifahamiana kwa muda mrefu. Kwani ndiye aliyekuwa dereva pekee wa Zera. “Pandeni.” Yule dereva aliongea kwa ufupi tu, Bella akafungua mlango kwa haraka, akaingia yeye na mdogo wake. Haikuwa mara ya kwanza kwa Bella kupanda gari hilo. Alishapanda mara kadhaa, na Kasimu au K kama walivyozoea kumwita huyo dereva walikuwa wakifahamiana naye vizuri tu tena mara nyingi alipenda kumtania Bella.  

“Asante Kaka K. Unaelekea wapi?” “Nimeambiwa niwafuate niwapeleke mahali, mkakae hapo kwa muda, mpaka atakapokuja kuongea na wewe?” “Nani?” “Mzee Masha mwenyewe.” Bella alifikiria kidogo. “Wapi?” “Mbona unaharaka Bella? Wewe siumetaka msaada? Ndio unasaidiwa sasa, acha wasiwasi.” Bella alibaki kimya akifikiria, kwani wakati Mzee Masha anauliza maswali akiwa pale nyumbani kwake, yote aliyajibu Zera, na wala hakuongeza neno lolote na wala Bella hakupata muda wakujibu swali hata moja, na K naye hakutoa hata salamu kwa Bella na mdogo wake, alibaki upande wa pili wa kulia chakula, akisoma gazeti wakati anasubiria kupewa kazi za siku ile nyumbani hapo kwa Masha. K alikuwa akifuata gari hilo na kurudisha kila siku nyumbani hapo kwa Mzee Masha. Alikuwa ni dereva wa Zera, lakini inapotokea Zera hamuhitaji, basi K alipangiwa kazi nyingine. 

Walipelekwa mpaka Kawe beach, kwenye kihoteli ambacho kilikuwa kimefichwa na miti mingi sana, patulivu na palionekana pakisasa. Dereva aliwaambia wasubiri hapo nje, akaingia ndani mapokezi, akarudi baada ya muda mfupi na funguo mkononi. “Twendeni.” K au Kasimu aliongea kwa kifupi, kisha akaongoza njia. Walimfuata nyuma mpaka kwenye chumba cha mwisho kabisa, ambacho kilikuwa na vitanda viwili vikubwa vilivyotandikwa vizuri, bafu zuri lenye jakuzi humo ndani. Kulikuwa na friji ndogo humo chumbani, pamoja na Microwave iliyokuwa imening’inizwa kwenye ukuta na pembeni sinki dogo lakuoshea mikono, tv kubwa ambayo ilionyesha channels nyingi sana.  

“Sasa mmeambiwa mkae humu ndani mpaka atakapokuja yeye mwenyewe. Kila kitu mnachohitaji mpige simu hapo mapokezi watawaletea. Msikae na njaa, agizeni chakula chochote mnachotaka, mle.”  Bado Bella alikuwa na maswali mengi, lakini sio Eric. Eric alijawa na furaha sana. Alipenda kila kitu mle kwenye kile chumba. Alizunguka huku akishika kimoja baada ya kingine huku akichekelea na kumwita dada yake aangalie. Kufunga na kufumbua ni kama maisha yamerudi kuwa mazuri  gafla. Alivua viatu vyake, akapanda kitandani nakuanza kurukaruka. Bella alibaki kimya akifikiria pale kwenye kochi. Dereva aliondoka, Bella akafunga mlango na kurudi kukaa. Akifikiria huku akizungusha macho ndani ya kile chumba kilichoonekana kimekamilisha shida zao zote. 

“Tuagize chai, Bella. Njaa inauma.” Eric alimtoa Bella kwenye mawazo. “Kwani hujasikia kaka alivyosema? Tukipiga tu simu, watatuletea chochote tutakachotaka.” Bella alitabasamu kidogo. “Ngoja nijaribishe.” Eric alisogea mpaka ilipo simu. “Haloo. Tunaomba utuletee, chai ya maziwa, mayai, bacon, sausage, juisi, …” “We Ric!” Bella alikuwa akicheka wakati mdogo wake akiendelea kuagiza. “Subiri Bella. Haloo!” “Ndiyo.”  Mapokezi waliitikia. “Na matunda.” Eric alimaliza nakurudi kurukaruka kitandani huku anacheka. “Tusubiri tuone kama watatuletea.” “Wasipoleta?” Bella aliuliza huku akicheka. “Wataleta Bella, usiwe na wasiwasi.” Eric alimtia moyo dada yake. Bella alibaki akimtizama alivyojawa na furaha. 

Wazi alionekana amepata tumaini jipya. Hata ile sura ya majonzi ilimtoka Eric, akawa mwingi wa matumaini. Baada ya muda mlango uligongwa, muhudumu na kigari cha chakula akaingia. Eric alifurahi sana. Walikaa na Bella, wakala chakula chote bila kupumzika, huku wakikumbushana enzi za uhai wa mama yao wakati akiwa na pesa. Walikuwa wakicheka sana. Mwishowe walilala. Ilikuwa ni muda mrefu sana tokea walale kwenye mazingira mazuri vile, bila mbu wala harufu mbaya, tena wakiwa wameshiba. 
*************************************

Hodi ya mlangoni ndio iliyomuamsha Enabella. Taratibu ili asimwamshe mdogo wake, Bella alifungua mlango. “Vipi Kaka K.” “Nimekuja kuwaangalia kama mpo salama.” “Tupo sawasawa kabisa, lakini hatuna nguo za kubadilisha.” “Nimepewa bahasha hii, bila shaka ndani kuna pesa. Kwa kuwa sasa hivi nina nafasi twendeni mkanunue baadhi ya nguo na vitu mnavyoona mtahitaji.” Bella aliona yupo ndotoni. 

Akaingia ndani ili kufungua ile bahasha, akakuta pesa nyingi sana, alibaki akifikiria huku amekunja uso wake, asielewe pesa zote zile alizokuwa amepewa ni kwa ajili ya nini! Alimwamsha mdogo wake ili wakanunue baadhi ya vitu wanavyohitaji. Dereva aliwapeleka mpaka madukani. Bella alimnunulia mdogo wake baadhi ya nguo, na vitu baadhi ambavyo na yeye alihitaji kisha wakarudi hotelini. Maisha yakifahari yakaendelea. 

************************************* 

Walikaa hotelini hapo kwa zaidi ya juma moja, wakila na kunywa, huku wakihudumiwa kama watoto wa mfalme. Chumba chao kilisafishwa na kubadilishwa mashuka kila siku. Wahudumu walichukua nguo zao na kwenda kuzifua, na kila walipozirudisha, zilikuwa zimeshanyooshwa kabisa. Furaha kwa Eric ilirejea usoni na moyoni, kasoro Bella aliyekuwa na maswali mengi sana. Hakuna mtu yeyote aliyewatembelea kwa kipindi chote hicho na hawakuwa na simu hata yakumjulisha kaka yao Mat, sehemu walipo. Walikaa peke yao, huku Bella akimtoa mdogo wake nje kwenda kuogelea kwenye ‘pool’. Huko alikutana na watoto wengi wakizungu. Kwa kuwa Eric na Bella walikuwa wakisoma shule za watoto wa mataifa mbalimbali, lugha haikuwasumbua hata kidogo. Waliongea lugha nyingi tena kiufasaha bila shida. Kwa hiyo Eric alianza kutengeneza marafiki kwa wageni waliokuwa wakifikia hotelini hapo.

************************************* 

Kufunga na kufumbua maisha yamewabadilikia. Yalikuwa mazuri wakati wa uhai wa mama yao, yakawa mabaya sana baada yakumzika mama yao huko kijijini. Ndugu waliwatelekeza. Kutoka kula milo mingi kwa siku, wakaishia kula mlo mmoja tena usio na uhakika. Maji yalipomfika shingoni, Bella akarudi mjini, ugumu ukaendelea. Wameangukia mikononi mwa Mzee Masha. Maisha yamerudi kuwa mazuri sana. Wakati Eric akifurahia maisha mapya, yaliyojaa mafanikio, Bella  anaonekana kuwa na mashaka. Nini kitawapata YATIMA HAWA?


Usikose sehemu ya 2 ya simulizi hili la kusisimua na kusikitisha......

0 comments: