Story

My Past. Sehemu Ya 2.

Thursday, April 13, 2017 naomimwakanyamale 0 Comments

“Kwa Mara ya Kwanza Mzee Masha Kujitokeza.”
S
iku moja ya Jumapili wakiwa wameamka, mhudumu alishawaletea kifungua kinywa, wakiwa wanakula huku wanaangalia tv, walisikia mlango unagongwa. Bella alisimama kwenda kufungua akijua muhudumu amerudi kuchukua vyombo, kumbe alikuwa Mzee Masha. “Shikamoo.” Bella akasalimia kwa heshima sana. “Marahaba. Hamjambo?” “Hatujambo. Karibu ndani.” Bella akampisha mlangoni. “Vipi hapa? Mnapaonaje?” “Tumepata wakati mtulivu, wametuhudumia vizuri. Asante sana.” Bella akashukuru. “Vizuri. Na mimi ndio nimerudi kutoka safari, niliwasindikiza familia yangu nchini Uholanzi.” “Pole na safari.” Bella akaongeza. “Asante. Poleni na nyinyi kwa matatizo.” Mzee Masha alikaa kwenye kochi.
Eric hakuwa hata na habari ya mgeni, kwani alikumbana na show yake ya   ‘Lab Rat’ aliyokuwa akiifuatilia tokea akiwa nyumbani kwa mama yake. Aliwapenda sana waigizaji hao. Walimfanya acheke na kutamani kama siku moja angekutana nao. Akili zake hazikuwepo pale kabisa, alikuwa akicheka na kuwasikiliza kwa makini sana, kwenye runinga iliyokuwa mbele ya kitanda chake.
Bella alikaa kitandani akimtizama Mzee Masha kwa hofu kidogo. “Sasa nimeamua kuwasaidia.” Mzee Masha alimwangalia Bella. “Asante.” Bella alijibu kwa kifupi tu huku amejawa maswali mengi. “Chochote unachotaka unaweza kuniambia.” Bella alibaki akiwaza huku ameinama. “Niambie tu Bella. Nataka kujua sasa hivi unashida gani?” “Natamani turudi shule. Hata kama hapatakuwa na pesa zakutosha kutupeleka shule sisi wote wawili, basi angalau Ric yeye ndiye arudi shuleni.” “Hilo halina shida kabisa. Wote mtasoma, lakini nashauri iwe kwa awamu. Aanze Ric, halafu ndio wewe.” Bella hakuamini anachosikia.
Akasimama na kumpa mkono Mzee Masha. “Asante sana. Alikuwa akisoma hii shule ya hapo Masaki DIS. Najua ni garama sana, lakini naweza kutoka kesho nikamtafutia shule nyingine.” Bella aliongea kwa heshima sana. “Kuna shule nyingine ipo Arusha, ndio nafikiria aende huko?” “Arusha!?” Bella akashtuka sana. “Ndiyo.”  Masha alijibu bila kusita, huku amemkazia macho Bella. “Kwa hiyo na mimi nahamia hukohuko? Siwezi kuishi mbali na Ric.” Bella aliongea kwa hofu kidogo. “Ni shule ya bweni. Nilifikiria unahitaji muda wakujipanga tena, wakati na yeye yupo kwenye mazingira mazuri huko shuleni! Unaweza kufanya huo ukawa mpango wa muda mfupi. Utakapoweka mambo sawa, unaweza kumchukua mkaendelea kuishi pamoja. Hata hivyo hiyo shule ni nzuri sana. Inakuza na vipaji. Walimu wapo karibu sana na wanafunzi. Eric atapata malezi mazuri, kana kwamba yupo bado na mama. Itakusaidia sana na wewe kujipanga ukiwa huna wasiwasi naye.” Bella aliona ni wazo zuri. “Ni kweli. Nafikiri hilo ni wazo zuri. Lini anatakiwa aanze?” “Nataka iwe haraka. Shule zilishafunguliwa. Nitaongea nao, ili muondoke na ndege ya kesho asubuhi kuelekea Arusha. Ukajaze fomu zote za huko shuleni, ili aanze shule mara moja.” Bella alishindwa kujizuia, alisogea mpaka pale alipokaa Mzee Masha nakupiga magoti. “Asante sana baba yangu. Asante.” Akampa mkono. “Karibu sana Bella. Kuanzia leo, nitakuwa na wewe bega kwa bega kukusaidia. Usiwe na wasiwasi.” Bella alihisi yupo ndotoni.
*************************************
Tangia mama yake alipoanza kuugua mpaka amefariki, hakuna mtu aliyewahi kuwasaidia kwa kiasi hicho. Ndugu waliwakana, marafiki waliwakimbia, wakabaki na Mat tu ambaye hawakuwahi kujua kama anaweza kuwa msaada wa namna ile. “Asante sana.” Bella akarudia. Kitendo cha mdogo wake kurudi shule, kwake ulikuwa muujiza. Mzee Masha alitoka na kumuacha Bella akiwa amejawa furaha sana.
Bella alitafuta njia nzuri sana yakuongea na Ric, ili akubali aende kusoma mbali na yeye. Kwa kuwa Eric na yeye alikuwa na hamu yakurudi shuleni, akakubali. “Lakini umeniambia ni kwa muda mfupi tu?” “Ndiyo Ric. Nikishaweka mambo sawa, nitakuhamishia kwenye shule za hapa mjini tuwe tunaishi wote.” “Asante Bella. Nitakuwa nakusubiri uje unifuate.” “Nitakufuata Ric, usiwe na wasiwasi. Lakini nataka ujitahidi shule. Umesikia Ric. Huyu baba anatusaidia tu, lazima tumuonyeshe na sisi tunathamini pesa anayotumia kwa ajili yetu.” “Nitajitahidi Bella.” Waliongelea mambo ya shule tu siku ile, Bella akijitahidi kumuhusia mdogo wake, na Eric naye alionyesha kutambua umuhimu huo, lakini alirudia rudia, kumkumbusha Bella, kuhakikisha anakwenda kumtoa huko Arusha ili arudi kuishi naye Dar. “Nitakufuata Ric. Usiwe na wasiwasi.”
*************************************
Asubuhi Kasimu au K, kama walivyozoea kumwita, alirudi kuwachukua ili awapeleke uwanja wa ndege, ili waelekee jijini Arusha. Bella alipewa pesa yakumtosha kutumia akiwa huko, na ya kununulia vitu ambavyo angeona Eric angehitaji akiwa shuleni. Alikwenda moja kwa moja kwenye hiyo shule mara tu walipotua kwenye uwanja wa ndege.
Hiyo shule ilikuwa nzuri sana. Wote wawili, Bella na Eric walifurahia mazingira yake. Baada ya kukamilisha taratibu zote hapo shuleni, yeye Bella kama mzazi wa Eric, alitoka na mdogo wake tena kurudi mjini kumnunulia vitu vyote alivyohitaji. Alipojiridhisha amemuacha mdogo wake kwenye mikono salama na mazingira mazuri , Bella aliamua kuwahi uwanja wa ndege ili arudi Dar. Njia nzima alikuwa akimuwaza Eric. Ukweli hakutaka kumuacha popote ambako ni mbali na yeye. Alitamani sana amlee mdogo wake yeye mwenyewe, lakini hakuwa na uwezo. Kwa wakati ule alifanya kile alichoweza, na kama Masha ndiye anayeonekana kuanza kutoa dira ya maisha yao kwa wakati huo, akaona afuate tu ushauri wake. Lakini ni kwa muda mfupi tu. Nitarudi kumchukua ili niishi naye.’ Bella aliendelea kuwaza.

 “Bella aanza maisha mapya, mikononi mwa Masha.”
Ndege hiyo ilitua jijini Dar, giza lilishakuwa limeingia. Alimkuta dereva akimsubiri nje ya uwanja huo wa Mwalimu Nyerere. Alimrudisha hotelini, Bella akaingia bafuni moja kwa moja na kujiloweka kwenye sinki lakuogea, Jacuzzi. Alikaa huko akiwaza, mpaka aliposikia hodi mlangoni. Kwa kuwa ilishafika jioni, Bella alijua ni muhudumu ameleta chakula.
Akatoka ndani ya maji, akajifunga taulo kubwa kifuani na kukimbilia mlangoni. Macho yalimtoka, baada ya kukutana na Mzee Masha. Alirudia kufunga taulo lake tena na tena huku mikono ikitetemeka. “Unatokaje na taulo tu?” Masha aliuliza kwa ukali. “Nilikuwa bafuni naoga, nikajua ni muhudumu analeta…” “Akiwa ni muhudumu ndio unatoka uchi!?” Mzee Masha aliendelea kuuliza kwa ukali zaidi kitu kilichozidi kumuogopesha Bella. “Sitarudia tena.” Mzee Masha alisukuma mlango na kuingia ndani, akakaa.
“Umenichanganya hata sikumbuki nikitu gani nilitaka kukwambia!” Mzee Masha aliendelea kulalamika. Bella alifunga mlango na kubaki amesimama. “Ulijua wazi kama ni muhudumu, tena wakiume, halafu ukatoka uchi! Unashida gani?” Aliendelea kugomba. “Ni kweli sikufikiria, nilikimbilia tu mlangoni bila kufikiria. Lakini sitarudia tena.” Bella aliendelea kuomba msamaha kwa unyenyekevu sana. “Hebu vaa nguo.” Bella alichukua nguo zake na kurudi bafuni kuvaa. Baada ya muda alitoka na kurudi kukaa kwenye kitanda.
“Samahani sana. Sitarudia tena.” Bella aliamua kuvunja ukimya mara baada yakuona Mzee Masha amekaa kwenye kochi akiwa bado na hasira. “Kuna safari ya Dubai, kesho kutwa. Nataka twende wote.” Mzee Masha aliongea kwa kuamrisha kidogo. “Dubai!?” Bella aliuliza kwa mshangao kidogo, kwani alitegemea wazungumzie maswala ya shule yake, sio safari nyingine. “Ndiyo, Dubai. Au ulitaka safari yakurudishwa Kigogo?” Mzee Masha aliuliza kwa kejeli. “Sema kama ndiko unakotaka kwenda, nikurudishe wewe na mdogo wako sasa hivi, mkaendelee kulala njaa.” Bella alijisikia vibaya sana moyoni. Akainama chini. “Jiandae, kesho utakuja kuchukuliwa na Kasimu, upelekwe kutengeneza hati yakusafiria. Umesikia Bella?” “Sawa.” Mzee Masha alisimama na kuondoka. Bella alibaki amekaa pale kitandani akiwaza. Alijikunja taratibu na kulala. Alishawapigia simu watu wamapokezi, wasilete chakula tena, kwani tumbo lilijaa gafla mara baada ya maongezi yake na Mzee Masha.
************************************* 
Aliamka asubuhi na mapeka, akaoga na kubaki amekaa kwenye kochi akisubiria kuja kuchukuliwa. Ilipofika saa nne, alikuja kuchukuliwa na Kasimu, akampeleka ofisi za uhamiaji. Kwa kuwa yule dereva alikuwa akifahamiana na watu kadhaa pale ndani, haikuchukua muda mrefu, Bella alipata hati yake yakusafiria. Akarudishwa hotelini, akabaki amejilaza kitandani akiwaza. Bado hakuwa na hamu ya chakula.
Baada ya muda akiwa amesinzia hapo kitandani, alisikia mlango unafunguliwa bila ya kubishwa hodi. Bella aliogopa sana akajiweka sawa ili kumuona huyo anayeingia bila hodi, au kufunguliwa, akadhani ni mwizi. Akashangaa kumuona Mzee Masha anaingia. “Shikamoo.” Bella akasimama. “Nimeamua kutafuta funguo yangu, ili niwe huru kuingia hapa muda na wakati wowote ninaotaka.” Mzee Masha alikaa chini baada yakuweka mifuko ya chakula mezani.
Chumba kizima kilikuwa kikinukia kuku wakuchoma. “Nimekuletea chakula, maana nimeambiwa tokea jana hujala kitu. Nilikuogopesha sana nini?” Bella alibaki akimwangalia huku amesimama. “Kaa chini ule. Lakini nataka ujue kuwa tokea mwanzo wa mahusiano haya, uwe unajiheshimu. Sitaki uwe unajiacha uchi uchi au kuwa na mahusiano na wanaume wengine.” Bella alishtuka sana. Maswali mengi yalipita kichwani mwake, lakini aliogopa kuuliza kwani Mzee Masha hakuonyesha utayari wakumsikiliza hata kidogo.
“Umenielewa Bella?” “Ndiyo.” “Nisiwahi kukusikia au hata kukukuta na mwanaume yeyote yule. Nataka utulie kabisa. Umalaya, mwiko. Unaelewa?” “Ndiyo.” Bella aliitikia. “Na ujue sikutanii Bella. Ukianza ujinga tu, nitaenda kumtoa mdogo wako kule shuleni na wewe nitakufukuza hapa, na nitahakikisha maisha yako yanakuwa magumu hapa mjini, kuliko nilivyokukuta. Na hakuna utakachofanya nisijue. Popote utakapokuwa, au chochote utakachofanya ujue nitajua tu. Narudia tena, NATAKA UTULIE. Sasa kaa chini ule, nataka uwahi kulala, kesho safari.” Taratibu sana, Bella akakaa.
Mzee Masha alisimama na kuwasha tv kisha akapiga simu mapokezi aletewe sahani mbili, kisu na uma. Baada ya muda mfupi sana muhudumu aliingia na sahani hizo, akaweka vyakula kwenye sahani, Mzee Masha alichukua ya kwake, akaanza kula. Bella na yeye alivuta chakula chake nakuanza kula kimya kimya. Mzee Masha alionekana kufurahia mpira uliokuwa ukiendelea kwenye luninga. Alikula huku akiangalia mpira huo mpaka ulipoisha. “Sasa ulale, kesho safari.” Bella alinyanyuka kuondoa ile sahani aliyokuwa akitumia Mzee Masha, kwenye meza ndogo pembeni ya kochi alilokuwa amekaa. “Mimi naongea halafu haujibu kitu?” Mzee Masha alifoka. Bella alisimama akimtizama bila kujibu kitu chochote. Mzee Masha akasimama, akaondoka bila hata kumuaga. Mwili wa Bella ulianza kutetemeka asijue kama ni hasira au hofu. Baada ya kusafisha pale, aliingia kuoga, na kurudi kulala.
************************************* 
Hakuna usiku uliokuwa mrefu maishani mwake kama ule. Hakuweza kufananisha na usiku wowote ambao alishawahi kulala maishani mwake. Hata kwenye chumba cha Mat, kilichokuwa na mbu, joto na harufu mbaya hakikumpa usiku mgumu kama ule aliokuwa amejilaza pale kwenye kile kitanda cha kifahari na AC ikimpuliza. Alijigeuza kulia na kushoto mpaka palipo  pambazuka ndipo usingizi ulipompitia.
“Ndege inaondoka muda mfupi sana kuanzia sasa.” Bella alishtushwa na Mzee Masha akiwa amemsimamia pembeni ya kitanda chake. Aliruka mpaka akaanguka pembeni ya kitanda. “Nimekushtua sana?” Bella hakujibu. “Pole. Lakini tunatakiwa kuondoka muda huu.” “Nitajitahidi kujitayarisha kwa haraka. Shikamoo.” Mzee Masha akatoa tabasamu bila ya kujibu ile salamu. Kidogo asubuhi hiyo alikuwa amebeba uso wenye tabasamu.
Bella alisimama na kuvuta taulo, akaelekea bafuni. Alioga harakaharaka na kutoka akiwa ameshavaa. “Sipendi hizo nguo zako. Haziniwakilishi vizuri.” Bella alianza kujiangalia juu mpaka chini. “Hatuwezi kusafiri ukiwa hivyo. Itabidi tupitie sehemu, angalau upate nguo moja ya kusafiria, na viatu ndipo tuondoke. Tukifika Dubai nitakuzungusha kwenye maduka ya nguo nzuri, uchague.” Bella hakujibu kitu alikaa pembeni ya kitanda akiwa kimya kabisa. “Upo tayari?” “Ndiyo.” “Twende.”
Walikuta dereva akiwa anawasubiri nje ya hoteli hiyo, sehemu ya kuegesha magari. Mzee Masha alimfungulia mlango wa nyuma, Bella akaingia, akafunga mlango. Na yeye akaingia upande mwingine. Wote walikaa nyuma. Bella aligeukia dirishani na kupotelea mawazoni.
************************************* 
“Ingia humo ndani, ukachague nguo nzuri.” Alimshtua Bella ambaye hata hakujua kama walishaondoka pale hotelini. Bella aliangaza vizuri macho. Akagundua wapo mbele ya Botique za Kinondoni. “Na ninakuomba usichelewe. Tusije tukakosa ndege.” “Sawa.” Bella aliitikia kwa upole. Akashuka na kuingia ndani ya duka hilo la nguo. Wakati anachagua akashangaa kumuona Mzee Masha amemsimamia nyuma yake. “Umepata unachoona kinakufaa au hata hujui nini cha kununua?” Bella alinyamaza na kendelea kutafuta. “Bella!” Aliita kwa nguvu kiasi ya kwamba kila mtu aliwageukia wao. “Ndio natafuta.” Bella akajibu taratibu na kubaki akimwangalia.
“Unajua nini? Utanichelewesha wewe. Nimesahahu kuwa umetoka uswahilini, hujui hata nguo za maana ni nini?” Bella alibaki akimwangalia. “Samahani dada, naomba msaidie huyu nguo moja nzuri, yamaana, ambayo atasafiria.” Mzee Masha alimgeukia muuzaji. “Bila shaka.” Alijibu na kusogea upande mwingine kulikokuwa kumetundikwa nguo. Baada ya muda mfupi akatoa nguo tatu. “Karibu hapa ndani ujaribishe.” Yule muhudumu alimgeukia Bella huku akimuashiria mlango wa chumba hicho chakujaribishia nguo. Bella akamfuata nyuma bila yakusema chochote.
Kila nguo ilimkaa vizuri. “Umependeza na una umbile zuri sana.” Yule muuzaji alimsifia Bella kila mara alipokuwa akitoka nje ya chumba cha kujaribishia, kumuonyesha zile nguo alizokuwa amevaa nakumtaka ushauri, ipi achukue. “Asante. Unafikiri nichukue ipi?” “Hiyo jumpsuit yenye nyeusi na nyekundu imekukaa vizuri zaidi. Chukua hiyo.” “Asante.” Bella alitoka akiwa amependeza sana.
“Hiyo siitaki. Kila mtu atakuwa akikuangalia wewe! Imekubana sana kwa chini.” Mzee Masha aliongea kwa sauti iliyojaa wivu na hasira kidogo, kila mtu akamgeukia Bella. “Huyo mtoto, hata umvalishe gunia, atakaa hivyohivyo. Chini mpana sana.” Mama mmoja mtu mzima kidogo, ambaye Bella alihisi ndio mwenye duka aliingilia maongezi yao. “Mtachelewa bure huko muendako. Wewe nenda tu baba yangu, hilo umbile halifichiki.” Kwa aibu Mzee Masha alilipia ile nguo, akatoka na Bella akiwa amevaa ile nguo mpya na kiatu cha juu kidogo. “Asante kwa nguo.” Bella alishukuru mara alipopanda kwenye gari. “Asante kushukuru.” Mzee Masha aliitikia kwa ustaarabu sana kama sio yeye!
************************************* 
Safari yakuelekea uwanja wa ndege ikaanza. Kimya, hakuna aliyemuongelesha mwenzake. Walifika uwanja wa ndege wakiwa hawajachelewa. Waliingia kwenye ndege, mara baada ya muhudumu kusoma tiketi alizokuwa amepewa na Mzee Masha. Kisha wakaelekea upande wa ‘first class’. Bella alifurahia ule utulivu wa aina ya watu waliokuwepo huo upande waliokuwepo. Wote walionekana ni watu wenye pesa zao, na hawakuwa watu wengi sana. Palikuwa patulivu na Wahudumu waliwahudumia kwa heshima sana.
Alionyeshwa pakukaa, akasogea moja kwa moja mpaka dirishani wakati Masha akitafuta sehemu ya kuweka mzigo mdogo aliokuwa ameshika mkononi. Alivuta pumzi mara kadhaa huku akizishusha taratibu, kisha akafunga macho. “Vipi? Una usingizi?” Mzee Masha aliingia na yeye kwenye vile viti na kukaa pembeni yake.   Bella alitoa tabasamu lakinafiki na kunyamaza bila kujibu lile swali. Alijirudisha nyuma kidogo, akajiegemeza vizuri, akageuzia macho yake dirishani.
“Ulishawahi kupanda ndege zakutoka nje ya nchi?”  Lile swali lilimkera sana Bella, lakini ilimbidi ajibu tu. “Hapana.” Alijibu kwa sauti ya chini sana. “Kwa hiyo hii ndiyo mara yako ya kwanza kupanda ndege za kimataifa!?” Alimuuliza tena kwa mshangao. “Ndiyo.” Bella alijibu tena kwa upole kisha akageukia dirishani kuonyesha hayupo tayari kwa swali jingine.
Nchini Dubai!
 Walifika Dubai, Bella akiwa amechoka sana, haswa mawazo. Akili ilikuwa imemvurugika kupita kiasi. Alishadhalilishwa na kunyanyaswa kihisia, kupita kiasi.  Waliingia kwenye taksii mpaka hotelini. Mzee Masha alisogea mapokezi, akaandika vitu fulani mbele ya muhudumu akapewa funguo za chumba. Maswali mengi yalikuwa yakiendelea kichwani mwa Bella, lakini aliogopa sana kuuliza.
“Twende juu. Chumba chetu kipo gorofa ya 10.” Bella alimgeukia kama aliyeuliza swali. Akijua kabisa anachofanya, Mzee Masha alijitahidi kuonyesha uso wa ukorofi ili kumuogopesha zaidi Bella, asiulize lile swali kwa sauti. Walipofika gorofa ya kumi, Masha akaanza kutafuta chumba chao, kwani ilikuwa hoteli kubwa sana, na kila gorofa ilikuwa na pande nyingi zilizokuwa na vyumba vingi pia. Bella akaamua kukaa kwenye moja ya makochi waliyoyakuta katikati ya vyumba hivyo hukohuko gorofa ya 10, wakati Masha akiendelea kutafuta chumba hicho mpaka alipokipata ndipo alipomwita Bella. Walisogea mpaka mlangoni mwa chumba hicho, akachomeka kadi mlangoni, na mlango ukafunguka. “Karibu ndani?” Bella aliingia na kukaa kwenye kochi.
“Chumba changu ni kipi?” Bella alijikaza, akauliza. “Si hiki! Au ulikuwa ukitegemea nini?” “Sitegemei chochote, kwa sababu pia sijui kwa nini tupo hapa?” Bella alijibu kwa ujasiri kidogo. “Huna shukurani kabisa wewe. Nakuleta Dubai kupumzisha mawazo, badala yakushukuru, unasema nini!?” Mzee Masha alianza kugomba, nakumuogopesha Bella. Alibadilika akawa mwekundu kwa hasira. Bella akabaki akitetemeka pale kwenye kochi.
Alikuwa akisikia kutoka kwa wanae vile yule Mzee alivyo mkorofi. Sasa leo ameangukia mikononi mwake, hakuwa na ujanja.  “Samahani, sikujua kama tupo hapa kwa ajili yangu. Naomba niingie bafuni nioge, halafu nilale. Kichwa kinaniuma sana.” Bella alisimama na kuingia bafuni.
Akiwa anaoga alishangaa kumuona Mzee Masha na yeye anaingia mle bafuni akiwa uchi kabisa.  Bella alishtuka sana. “Nataka unisugue mgongoni. Sijaoga vizuri muda mrefu sana. Mke wangu amekuwa na mambo mengi, amekosa muda na mimi. Naamini mambo madogo madogo kama haya, hutashindwa kumsaidia.” Bella alibaki ameshikilia matiti yake huku ameacha sehemu nyingine zote wazi. “Au unaona shida kunisaidia kusugua tu mgongo!? Maana kuna wanadamu wengine wameumbwa bila shukurani. Unaweza kumsaidia jambo kubwa sana, yeye akashindwa kukufanyia kitu kidogo tu!” Mzee Masha aliingia ndani ya maji, akajilowesha vizuri na kujipaka sabuni. Bella alibaki anatetemeka pembeni ya bomba, akitamani afunge macho.
Bella alilingana umri kabisa na mtoto wa pili au wamwisho wa Mzee Masha, Zera. Yaani alikuwa kama baba yake wakumzaa. “Chukua hicho kitaulo hapo pembeni ukipake sabuni unisugue mgongo.” Taratibu sana Bella alinyoosha mkono huku akitetemeka sana. Akavuta moja ya taulo dogo kabisa yaliyokuwa yamepambwa vizuri bafuni hapo. Maalumu kwa kujisugulia. Mzee Masha alikuwa ametulia kimya na kumpa mgongo Bella. Alikilowesha, akanyunyuzia sabuni ile yakuogea, na kuanza kumsugua taratibu mgongoni huku akitetemeka.
Alijifariji kumuona yule Mzee amegeukia upande mwingine, kwa hiyo alijua hatageuka na kumwangalia. Lakini baada yakumsugua kwa muda mrefu, Mzee Masha akamgeukia Bella. Bella alirudi nyuma kwa haraka na kubaki wakiangaliana na Mzee Masha. “Unataka nikusugue na wewe?” “Hapana, asante.” Mzee Masha akacheka. “Ona anavyojidai kutetemeka. Unataka kuniaminisha kuwa eti unaogopa? Wenzako wanalilia hata kunishika tu. Leo nimekupa bahati yakupanda ndege, nimekuvalisha nguo za thamani, nakupa bahati ya kugusa mwili wangu, halafu unajidai unaogopa! Acha unafiki wewe.” Bella alivuta taulo akajifunga nakutoka pale bafuni bila yakuongeza neno. Alijikausha harakaharaka, akavaa nguo zake za kulalia alizokuwa amenunua siku ya kwanza alipoenda kununua nguo na dereva wa Zera, Kasimu. Akapanda kitandani huku akitetemeka.
Masha Amtoa Enabella Utotoni!
Baada ya muda, Mzee Masha akaingia pale chumbani. Bella akafunga macho. “Unataka kula nini?” Mzee Masha akauliza lakini Bella akanyamaza, akijidai amelala. Alipanda na yeye kitandani, akafunua shuka alilokuwa amejifunika Bella, na yeye akaingia humo humo ndani. Wakawa wamejifunika shuka moja. Akaanza kumpapasa taratibu, Bella akizidi kutetemeka mwili mzima kama aliyekuwa akishikwa na mikono yenye baridi kali au kama aliyekuwa akitembewa na barafu mwilini. Alionyesha wazi, lakini Mzee Masha hakujali. Aliendelea kumpapasa mpaka alipofikia matiti yake. Akamgeuza taratibu nakuanza kumpandisha gauni yake ya kulalia mpaka alipofika kifuani, mikono ikagoma kutoka hapo. Ikaanza kuhama titi moja kwenda jingine, akiyapapasa matiti ya Bella taratibu kwa hisia zote. Bella alibaki kimya kabisa. Alishindwa hata kujisogeza. Taratibu machozi yakaanza kumtoka.
Kadiri alivyoendelea kumpapasa ndivyo Bella alivyozidi kutoa machozi. Sauti ya shoga ya mama yake ilianza kujirudia wakati akimsema mama yake kule kijijini walipoenda kumzika. Kama aliyezidiwa na kitu wakati akichezea matiti hayo, akaamua kumtoa nguo yote iliyokuwa juu kabisa ya matiti, karibu kabisa na shingoni. Wakati anamalizia kumvua, Bella akakaa. “Naomba utumie kondom.” Bella alijifuta machozi nakujifunika vizuri. Alibakiwa na chupi tu, akavuta shuka na kujifunika. “Tafadhali tumia kondom.” Bella aliongea huku akishindwa kujizuia nakujikuta akilia kwa kwikwi.
Alikunja miguu yake na kujiegemeza magotini mwake nakuendelea kulia. “Please!” Akarudia huku ameinama. Alishindwa kumtizama Masha kwani alikuwa kama alivyozaliwa na yeye akionekana yupo tayari kwa tendo. Bila kupoteza muda zaidi, Mzee Masha akatoka pale kitandani, akavuta droo na kutoa kondomu. Alivaa harakaharaka na kurudi kitandani. Alivuta shuka alililokuwa amejifunika Bella, akamvuta miguu kama kumnyoosha, yeye akiwa amepiga magoti.
Alipofanikiwa kumlaza chali ndipo akarudi kiunoni. Akampapasa kidogo tu nakuanza kumtoa chupi yake taratibu. Aliishusha huku akimbusu kuanzia kiunoni, mapajani huku akishuka taratibu akimbusu kadiri anavyovua ile chupi. Alipofanikiwa kuitoa yote, moja kwa moja akarudi kifuani kwa Bella nakuanza kunyonya matiti yake. Napo alionekana ni kama amelemewa hawezi kuendelea kwa muda mrefu, Bella akiwa amelala chali bila hata kujitingisha au kujisogeza, ila kulia tu, Masha akajitahidi yeye mwenyewe bila hata kuomba msaada, akamwingilia mtoto huyo ambaye bado alikuwa bikra kabisa.
Bella alimsikia akigugumia kwa hisia za ajabu, huku yeye akiendelea kulia. Akaendelea hivyo kwa muda, akamuona anaongeza mwendo, huku akigugumia zaidi. Baada ya muda mfupi sana, akamuona anaanza kupunguza mwendo, akatulia nakujilaza juu yake, kichwa pembeni ya shingo yake kama anayetafuta pumzi. Akiwa ameweka uso wake shingoni kwa Bella, pumzi zake zikitua kabisa kwenye shingo ya Bella, mkono wake wa kushoto ulitulia juu ya hips la kulia la Bella. Alilipapasa taratibu huku akihema kama kujiweka sawa baada ya shuguli nzito au kama aliyekuwa akikimbia. Mikono yake iliendelea kutembea juu ya mwili huo kwa chini tu. Alifika kiunoni na kurudi kwenye hips hilo, mpaka akatulia. Alijisogeza pembeni yake, akajilaza na kupitiwa na usingizi mzito bila kuongea tena au kumgusa tena Bella, aliyekuwa bado akilia kwa uchungu sana.

************************************* 
Japokuwa Bella alikuwa mzuri sana kwa kila kitu, lakini swala la wanaume au mahusiano ya kimapenzi hayakuwahi kupita mawazoni mwake hata mara moja. Ukweli ule haukuwa wakati alioona unafaa kufanya mapenzi. Tena kwa mtu ambaye siye mpenzi wake! Mbaya zaidi ni kama alimbaka tu. Alifanya naye mapenzi bila hata kumuomba au kumbembeleza. Zaidi ya yote alimuonyesha wazi anamdharau. Ilimuuma zaidi Bella.
Ni kweli alilelewa na mama ambaye aliishi kwa kuhongwa sana na wanaume wa kila namna, lakini Tunu alilinda sana watoto wake na kuwaambia kila wakati hasa Enabella kuwa yeye bado ni mtoto mdogo sana, asifikirie swala la mapenzi hata kidogo. Kwa hiyo wakati wote Bella alijiona bado ni mtoto, na mama yake ndiye aliyekuwa msiri wake mkubwa. Aliongea na kuishi kile anachoambiwa na mama yake. Hakuwahi kuwaza juu ya maisha au jambo lolote lile, mama yake ndiye aliyekuwa akiwaza na kufikiria kwa niaba yake na kumpa yeye maelekezo ya kitu gani chakufanya. Kila mwanaume aliyemtongoza, mtu wa kwanza kumwambia alikuwa ni mama yake.
Kwa hiyo Bella hakujua mambo ya mapenzi, na kila mwanaume aliyekaa na Bella hata nusu saa tu, alikiri Bella ana akili za kitoto. Kasoro darasani tu, ndipo Bella alipoweka heshima shuleni hapo, nakumfanya hata Tunu ambaye hakuwa msomi, kuheshimiwa kwenye shule hiyo iliyojaa watoto wa vigogo. Bella aliburuza madarasa yote, wakati wote alikuwa akifaulu kwa alama za juu sana. Mwanzoni walihisi ni mtoto wa mtu mmoja msomi sana, au wamezaliwa na mtu mmoja aliyevumbua kitu fulani, kwani hata Eric alijulikana kwa utaalamu wa Kompyuta.
Tunu alihakikisha watoto wake wanaishi maisha mazuri sana jijini. Sababu ya kuwalipia ada kubwa, na kupanga nyumba maeneo ya gharama, na yeye hakuwa na kipato cha kueleweka isipokuwa wanaume aliokuwa akitembea nao,   Tunu hakuwa ameacha urithi wowote kwa watoto wake zaidi ya hiyo elimu kichwani mwao.  Hakuwa amejiandaa kabisa na kifo chake. Kama mtu angemwambia Tunu angeugua na asipone, asingeamini hata kidogo.
Alianza kuugua gafla, na ni kweli aligua kwa muda mrefu sana kabla yakufariki kwake. Wakati mama yake ni mgonjwa, hapo ndipo Bella alipoanza kuelewa maisha ni nini. Pesa alizokuwa akizitapanya mama yake katika maisha yake na mdogo wake, zilianza kuisha, wakabaki wakihangaika. Mama yake aliyekuwa akimpa maelekezo kipi cha kuuza ili kuongeza kipato chao, alianza kupoteza kumbukumbu na kuwa kama amechanganyikiwa kwa muda mrefu sana kabla ya kifo chake.
Alibakia Bella peke yake akimuuguza mama yake, kwani hata msichana wa kazi aliyekuwa akiwasaidia kazi za nyumbani aliondoka baada ya kukaa miezi miwili bila malipo na kugundua hakuna dalili za kuja kulipwa tena. Pia aliingiwa na hofu baada ya kujua kwa hakika gonjwa linalomsumbua tajiri wake au mama mwenye nyumba wake. Aliogopa asijefanya makosa, akamuambukiza. Ndipo akaamua aondoke mapema akiwa mzima bila gonjwa, kunusuru afya yake. Alimuacha Bella akimlilia abaki nao.
 Ni Mat pekee,  dereva wa gari hiyo ndogo aliyokuwa amekabidhiwa na Tunu, ndiye aliyebaki kumsaidia Bella. Ndiye aliyekuwa akimpigia simu hata usiku sana endapo akiona hali ya mama yake imebadilika. Naye Mat hakuwahi kulalamika. Wakati wote alikuwa akifika hapo kwa haraka na kumsaidia Bella kumpeleka mama yake hospitalini na kumrudisha baada ya kupewa huduma ndogo ndogo. Kwani hata hospitalini kwenyewe walishindwa kumuweka kwa muda mrefu, hapakuwa na matibabu yakumsaidia kabisa Tunu ila kumtuliza. Kwa hiyo muda mwingi Tunu aliugulia nyumbani.
Akabakia Mat pekee kuwa msaada wao. Ndiye aliyekuwa akiwaletea pesa kidogo, kila apatapo wateja, na kumsaidia Bella kununua chakula na dawa za mama yake alizokuwa akitumia kwa kila ugonjwa uliokuwa ukijitokeza zaidi kwa wakati huo. Viliibuka viugonjwa vya hapa na pale mwilini mwa mama yake, na hivyo ndivyo Bella alivyokuwa akivitibu mpaka kifo chake.
************************************* 
Bella aliendelea kulia kwa maumivu makali, huku damu nyingi zikimtoka. Alijinyanyua kwa shida sana kutoka pale kitandani mpaka bafuni huku akiacha damu kitandani hapo na sakafuni alikokuwa amepita. Hofu ilimuingia alipoona anazidi kuvuja damu asijue nini chakufanya na nani wakumwambia. Hakujua kama damu ile inatokana na Masha kumchana wakati wakufanya naye mapenzi au ndio kutolewa bikra yake! Mtoto huyo aliyezoeshwa kubembelezwa na mama yake hata akijikata na wembe, usiku huo ulikuwa usiku wa hofu kubwa zaidi. Damu zilikuwa zikitoka, maumivu yakimsumbua akiwa peke yake bafuni. Aliendelea kulia kwa hofu, mwishowe alipoona anazidi kumwagika damu na kuchafua kila taulo pale bafuni huku Masha akiwa amelala bila hata habari, akaamua kuingia ndani ya sinki ya kuogea kusubiri hatima yake. Kama ni kifo au kukatika kwa ile damu. Akabaki amekaa pale akilia peke yake.
Mawazo mengi ya hofu yakaanza kupita kichwani mwake kwa mara moja huku akiona vile anavyokufa hapo nchini Dubai na kumuacha Eric mdogo wake akiteseka peke yake. Akajua Masha atamtoa kule shuleni na kuanza kuhangaika mtaani bila msaada wowote. Akamuona mdogo wake akiwa mtaani akiomba omba huku usiku wahuni wakimwingilia kwa kumlawiti bila huruma kama yeye alivyofanyiwa hapo na Masha. Tena aliwaona wanaume wengi wakimng’ang’ania Eric sababu ya uzuri wa kike aliobeba mdogo wake. Alimuona akilala usiku mtaani tu, tena kwa masaa machache sababu ya kuingiliwa na wanaume wengi kila usiku bila yakumuhurumia. Hofu ilizidi kumjaa. Aliwaza hili na like huku amejawa hofu mpaka akapata ‘Panic attach’. Akapoteza fahamu pale pale kwenye sinki.
************************************* 
 Bella alishtuka nakujikuta kitandani. “Pole Bella.” Bella alijaribu kujigeuza kichwa chake taratibu kutafuta anaye msemesha, akamuona Mzee Masha amekaa pembeni ya kitanda chake. Aliweza kujua kuwa hakuwa amelala kwenye kitanda cha pale hotelini, kile chumba kilifanana na nyumbani kwa mtu. Tena kidogo tu. Alitamani kuuliza, lakini alibaki akimwangalia Mzee Masha aliyekuwa akimtazama kwa uso wa wasiwasi. “Unajisikiaje?” Mzee Masha akamuuliza tena. Wakati ananyanyua mkono wake ili kujifuta machozi, akagundua amewekewa damu, akahisi yupo hospitalini. Akarudisha mkono wake taratibu, nakufunga macho bila kutaka kujua nini kilitokea, na alifikaje pale.
 “Unataka nikulishe?” Akamsikia Mzee Masha akimuuliza tena. Akiwa amefunga macho yake vile vile, Bella akatingisha kichwa kuashiria kukataa huku machozi yakimtoka. “Hujakula kitu chochote tokea jana Bella. Lazima ule chakula.” Bella alishangazwa na ukarimu wa gafla wa Masha. Alikuwa akiongea kwa upole na upendo sana kama sio yeye. Lakini Bella aliendelea kulia taratibu. Aligeukia ukutani akalala.
Alishtuliwa tena na daktari aliyekuwa ameingia hapo akimwita kama kutaka atoke usingizini. “Enabella!” Akafungua macho kwani haikuwa sauti ya Masha. “Unajisikiaje?” Akamuuliza kwa Kiswahili kizuri na fasaha kitu kilichomshangaza Bella. Akajiuliza daktari wa Kitanzania nchini Dubai! “Nipo wapi?” Bella akauliza taratibu. “Nyumbani kwangu.” Yule daktari akamjibu. Alizungusha macho kumtafuta Mzee Masha, lakini yule daktari akamuwahi, “Ametoka, amesema atarudi baadaye kidogo. Amekwenda kwenye kikao. Unajisikiaje?”  “Nini kilitokea?” Bella akauliza. “Ulikutwa na Mzee Masha chumbani kwako, asubuhi ya leo ukiwa umepoteza fahamu kwenye sinki. Amepoteza damu nyingi sana. Lakini usiwe na wasiwasi, tumebahatika kupata damu, nimekuwekea, utakuwa sawa tu.  Nimekuwekea chupa moja, utaendelea kutumia vidonge baada ya hapo.” Bella alifunga macho bila yakuongeza kitu. “Hapa tunavyakula vya nyumbani pia. Kama utataka tukuletee chakula chochote kile niambie, tutakutengenezea.” Bella alitingisha kichwa kukataa na kulala tena.
Ilipofika usiku, aliamshwa na kijana mwingine tena, aliyekuwa na bakuli la supu. “Nimekutengenezea hii supu. Naomba ukae unywe.” Bella alibaki akijiuliza yule ni nani tena! Alibaki akimtizama kwa muda bila kupata jibu, kisha akafunga macho. “Lazima ule Bella. Nikusaidie ukae ili ule?” Bella hakujibu. Taratibu aliona machozi yanatoka pembeni ya macho ya Bella. Palizuka ukimya wa muda, gafla mlango ukafunguliwa. “Vipi bwana mdogo Elvin, Kaka yako yuko wapi?” Bella alisikia sauti ya Mzee Masha, lakini hakutaka kufungua macho. “Shikamoo. Umetoka kwenda kazini kwake, amepigiwa simu kuwa kuna dharula, ‘emergency’. Lakini amesema atarudi pindi atakapomaliza. Nimeleta hii supu kwa mgonjwa.” “Asante sana. Weka tu hapo mezani, atakunywa akiamka.” Bella alikuwa akisikiliza kila kitu, lakini aliamua kujifanya amelala. Elvin alivuta meza pembeni ya kitanda alicholalia Bella, nakuiweka ile supu.
“Vipi lakini shule?” Masha alimuuliza yule kijana, aliyemtaja kama Elvin. “Ndio nipo likizo.” “Mwaka wa ngapi sasa?” Mzee Masha aliendelea kuhoji. “Nipo wapili.” “Naona mama amekung’ang’ania kweli!” Elvin alicheka. “Hata kuja huku kwenyewe kwa kaka, ilikuwa shuguli kweli! Hataki nitoke pale nyumbani.” “Anakuwa mpweke. Anaona watoto wote wameshakuwa wakubwa wanamkimbia pale nyumbani, inabidi akung’ang’anie wewe.”  Elvin alicheka. “Utarudi lini sasa?” “Nimetoka kuongea naye muda si mrefu, anataka nirudi nyumbani kwa kisingizio eti nikamsaidie Mzee kazi ofini kwake, lakini najua yeye ndio anataka nirudi.” Mzee Masha akacheka kidogo. “Lakini nitarudi tu, sitakaa sana hapa.” “Safi sana. Naona na Mzee wako anakusifia sana.” “Hahahaha!” Elvin alicheka tena.
“Wewe si unamjua baba? Anafurahia ninavyomsaidia kazi zake pale ofisini kwake, halafu hanilipi mshahara, anaita posho, ili nisilalamike.” Wote wakacheka. “Kuna chakula kidogo. Utapenda kula kitu chochote?” Elvin alimuuliza Mzee Masha. “Hapana, asante sana. Nataka nikawahi kulala, naona huyu nitamuacha hapahapa, nitarudi kumchukua kesho asubuhi nikishatoka kwenye kikao.” “Ndivyo mlivyokubaliana na Eno?” “Aliniambia anatakiwa kupumzika angalau siku moja zaidi ili apate muda wakumwangalia, kesho tunaweza kuondoka.” “Okay.” Elvin alitoka nakumuacha Mzee Masha ndani ya kile chumba.
“We Bella! Bella! Amka ule.” Mzee Masha alimuamsha Bella. “Nitakula baadaye.” “Itabidi niondoke, nikuache hapa kwa ajili ya matibabu. Kesho nina kikao cha asubuhi sana, lazima niwahi kulala, nikitoka huko nitarudi kukuchukua.”  “Sawa.” Bella alijibu nakufunga macho. Palizuka ukimya wa gafla, mwishowe Bella akasikia mlango ukifunguliwa na kufungwa. Akajigeuza ukutani na kupotelea usingizini.
************************************* 
 “Ni leo tu, kesho ataondoka.”  Kwa mbali akiwa anatoka usingizini, Bella alisikia watu wakiongea nje ya chumba alichokuwa amelala. Lakini haikuwa sauti ya Mzee Masha. “Usiwe na wasiwasi Eno. Mimi nipo sawa tu. Nikisikia usingizi nitalala hata hapo kwenye makochi.” “Unauhakika?” “Mbona unawasiwasi?” “Namjua mama yako. Akipiga simu, halafu akajua kama nimegawa chumba chako, huna pakulala, anaweza kuja kukufuata mwenyewe.” Wote wakacheka.
“Ameshanipigia simu anataka nirudi nyumbani.” “Hata mimi amenipigia, ananiomba nisikuweke sana huku. Umeamuaje?” “Itabidi nirudi tu. Kuna kitu namalizia hizi siku mbili tatu, nitarudi nyumbani. Sitaki kuendelea kumtesa. Najua huko halali vizuri.” Bella aliendelea kuwasikiliza. “Amekula kitu chochote?” “Hapana. Naona amekataa kabisa. Hata supu niliyompelekea amekataa kuinywa.” Elvin alimjibu kaka yake, Eno. “Ngoja nikamwangalie.” Bella alisikia hatua za miguu zikisogelea mlango wake, kisha ukafunguliwa.
“Vipi Enabella?” Bella akafungua macho na kukutana na Eno, ambaye alijua ndiye atakuwa daktari. “Nataka kwenda chooni.” “Utaweza kwenda mwenyewe? Nasikia hujala kitu chochote. Lazima ule, lasivyo kizunguzngu kitakusumbua sana.” “Nitaweza kwenda chooni mwenyewe.” Eno alisogea, akafunga ile damu na kutenganisha ule mrija uliokuwa ukipitishia damu ili aweze kwenda chooni bila chupa ya damu. Akampisha ilia toke pale kitandani.
Bella alijikaza mpaka chooni. Yalikuwa nimateso makubwa sana wakati akijisaidia haja ndogo. Alisimama akiwa analia peke yake pale chooni. Wakati alipokuwa akifanya naye mapenzi, Mzee Masha alimsababishia madonda. Hakumtayarisha kabisa. Alimparamia huku akijua wazi Bella anahofu. Alifanya naye mapenzi kwa pupa, tena bila huruma. Alimuumiza sana, hasa kwa kuwa ilikuwa mara yake ya kwanza. Alilia pale chooni, akaamua arudi tu chumbani akalale.
Alirudi chumbani akiwa amejawa machozi mengi sana usoni. “Pole sana Bella.” Eno alijaribu kuongea kwa upendo, lakini Bella hakujibu kitu. Akapanda kitandani na kufunga macho huku akifuta machozi yaliyokuwa yakiendelea kumtoka. Eno alirudisha ule mrija wakupitisha damu mkononi kwa Bella, akafungulia damu tena, nakuondoka pale chumbani.
Eno alitoka na kusimama nje ya mlango, akabaki akifikiria. “Vipi?” Alimsikia Elvin akimuuliza. “Sijui bwana! Ngoja mimi nikalale. Nitarudi usiku kuangalia hiyo dripu kama itaisha ili nimtoe.” “Usiwe na wasiwasi, mimi bado nipo hapa naandika, nitakuwa nikimwangalia. Kama kuna tatizo nitakugongea, au dripu ikiisha pia nitakuja kukuamsha. Wewe kapumzike tu.” “Hapo utakuwa umenisaidia. Nimechoka sana na kesho nipo ‘on call’ sijui nitaitwa saa ngapi! Kuna upungufu wa madajtari huko. Najua nitaitwa tu. Acha nikapumzike kidogo. Usiku mwema.” “Na wewe.” Bella alisikia wakiagana.

“Elvin kwa Bella.”
Baada ya muda kidogo kupita Bella akasikia mlango unafunguliwa, lakini hakutaka kufungua macho.  “Nitakuwa hapa kwenye meza nikifanya kazi zangu kwenye kompyuta. Ukitaka kitu chochote unaweza kuniambia.” Elvin alivuta kiti akakaa, lakini Bella hakujibu kitu. “Nikuzimie taa?” Bella hakujibu kitu. Elvin aliendelea na shuguli zake kwenye kompyuta yake  kimyakimya tu mpaka baada ya lisaa, akamsogelea Bella. “Nikusindikize kwenda kupiga mswaki kabla ya kula?” Bella akaanza kulia tena. “Upo mswaki mpya pale chooni, twende nikuonyeshe ili usugue meno wakati nakupashia moto supu yako.” Sio kwamba njaa haikuwa ikimuuma Bella, lakini alijawa na hasira na uchungu mwingi sana moyoni, kiasi cha kushindwa kula.
 “Twende!” Elvin alirudia tena. Bella alikaa kidogo kama akifikiria, mwishowe akasimama. Elvin alimbebea ile dripu ya damu, mpaka chooni akaitundika mlangoni. Alimuacha akiwa anaosha uso na kupiga mswaki, yeye akaingia jikoni. Baada ya muda alimfuata bafuni nakubaki akimsubiria, kwani Bella alikuwa akipiga mswaki huku akilia sana. Elvin alibaki kimya, asijue aseme nini. Alimaliza, wakarudi chumbani. “Usilale sasa. Kula kwanza.” Bella alishusha miguu kutoka kitandani na kuanza kula taratibu.
Alikunywa ile supu mpaka akamaliza yote. “Asante.” “Karibu. Ungependa nikuongezee kitu chochote? Juisi, maji au maziwa?” “Maji, tafadhali.” Bella alijibu, Elvin akatoka na kurudi na maji. Alipomaliza kunywa yale maji, Bella alirudi kulala, mpaka aliposikia mtu akimvuta mkono. Alishtuka sana, akakaa kwa haraka, akajivuta mbali kabisa, ukutani, huku akitetemeka. “Pole na samahani. Sikutaka kukuamsha. Nataka nikutoe hiyo dripu. Imeisha.” Alikuwa Eno. Bella alimtizama kwa muda, akafuta machozi, kisha akanyoosha ule mkono uliokuwa na sindano. “Samahani sana.” Eno alirudia baada yakuona vile Bella alivyoshtuka. Bella aliendelea kujifuta machozi.
“Kesho utajisikia vizuri.” Eno aliongeza huku akitoa plasta zilizokuwa zimezunguka ile sindano, mkononi mwake. “Itauma kidogo, wakati nazitoa hizi plasta, lakini haitachukua muda mrefu.” Eno aliongeza, huku akipiga miayo, akiashiria wazi ana usingizi. Alimtoa na kurudishia plasta moja pale alipochomoa sindano kuzuia damu isitoke. “Pole sana Anabella. Unaweza kurudi kulala.” Bella alibaki amejikunyata kwenye kona yakitanda, huku ameangalia chini. Eno akasimama kwa muda akimtizama Bella, mwishowe akaamua kuondoka. “Usiku mwema Elvin.” “Asante na wewe.” Elvin bado alikuwa mezani akiandika.
Baada yakumuona Bella ameshindwa kurudi kulala, akaamua kuvunja ukimya. “Nikuwekee nini kwenye luninga?” Elvin alisimama na kuwasha tv. “Kuna sinema nyingi tu hapa, mpaka za wanyama.” Alijua wazi asingejibiwa, lakini Elvin aliamua kuuliza tu. Alitafuta DVD akaweka. “Jilaze vizuri, uangalie mpaka utakapopitiwa tena na usingizi.” Bella alijinyoosha vizuri na kujifunika shuka. “Nyanyua kichwa nikuwekee mto ili uweze kuangalia luninga vizuri.” Bella alikaa vizuri, Elvin akamwekea mto vizuri. “Unaweza kulala sasa.” Bila kusema chochote, Bella alirudi kulala na kugeukia luninga. Aliangalia kwa muda, mwishowe alisinzia. Elvin alisimama na kumfunika vizuri, akazima taa, akarudi kukaa kwenye kiti chake, akitumia taa ya mezani bila ya kuwasha taa kubwa ili asimsumbue mgeni huyo ambaye ni mgonjwa. Sababu ya kushiba vizuri, Bella alipitiwa na usingizi mzito sana mpaka alipoamshwa na Mzee Masha tena.
“Twende. Utaenda kuoga hukohuko hotelini.” Bella alikaa kwa shida sana. Hakutaka hata kumwangalia Mzee Masha usoni. “Asanteni sana kwa msaada wenu.” Mzee Masha alimshukuru Eno huku akimkabidhi hundi. “Hapana Mzee Masha. Hatuwezi kulipana bwana. Sisi ni ndugu.” “Acha uswahili Eno. Unafikiri kazi ya pesa ni nini? Lazima izunguke ili inirudie. Sasa kama tusipojua kuenzi vya kwetu, unafikiri wageni watatuthamini kweli? Wewe ndio umeanza maisha, upo ugenini huku, unahitaji pesa. Chukua hii pesa.” Eno alicheka kidogo huku akipokea. “Asante sana.” “Mimi ndio nawashukuru nyinyi zaidi. Asante sana” Masha aliongea kwa tabasamu kubwa usoni. “Sasa Elvin?” Alimgeukia Elvin. “Ndio Mzee!” “Najua sisi tutaonana mjini. Usije ukazamia huku.” Elvin akacheka. “Siwezi. Nitarudi kusaidia wazee.” “Haya bwana.” Mzee Masha alimgeukia Bella. “Upo tayari?” “Ndiyo.” Bella alijibu kwa sauti ya chini, wazi alionyesha anamuogopa Mzee Masha. “Simama sasa twende! Unasema upo tayari wakati umekaa?” Bella alisimama na kutoka mle chumbani. Aliwaacha wote wakiwa chumbani, wakimsindikiza kwa macho.
Masha na Bella.
Walipofika tu hotelini chumbani kwao, Bella aliingia bafuni moja kwa moja. “Nikusaidie kuoga?” Mzee Masha aliingia bafuni. “Asante, lakini nitakuwa sawa tu.” Bella alitamani yule Mzee aondoke pale bafuni na kumuacha peke yake, lakini alibaki akimkodolea macho mpaka alipomaliza kuoga. Akatoka nakurudi kitandani. “Kabla hujalala, nataka nikupongeze kwa kujitunza. Nimefurahi sana mimi kuwa mpenzi wako wa kwanza. Nimeamua kukutafutia zawadi nzuri.” Alisimama na kusogelea meza. “Dhahabu za Dubai ni nzuri sana, na ni za viwango vya hali ya juu.” Bella alibaki ameinama. “Na huna haja yakuogopa, yaliyokupata ni mambo yakawaida kabisa, kadiri tutakavyoendelea ndivyo utakavyozoea, kwa hiyo usiogope. Na nina kuahidi, wakati mwingine nitakuwa mwangalifu sana ili nisikuumize. Juzi ilitokea bahati mbaya sababu yakuchoka na sikuwa najua kama hujawahi kulala na mwanaume mwingine. Nitakutafutia mtu mzima kidogo, mwenye uelewa na mambo hayo atakufundisha kila kitu, usiwe na wasiwasi.” Mzee Masha alirudi kitandani akiwa na kimkoba kikubwa mkononi. “Umenisikia lakini?” Aliuliza kwa ukali kidogo. “Ndiyo.” Bella alijibu. “Hizi ni moja ya zawadi nyingi na za thamani, zinazokujia.” Alimpa cheni ya shingoni, mkononi na mguuni, kulikuwa na hereni pia. Na kweli vilionekana ni vitu vya thamani sana.  Kila kimoja wapo kilikuwa na uzito wa kutosha.
“Kwa uzuri ulio nao, na heshima uliyonipa, lazima nitakutunza vizuri sana Bella. Nitakufanya uwe mrembo katika jiji zima lile la Dar. Nitahakikisha unaishi kwenye nyumba nzuri sana na kutembelea gari la kifahari. Nakuapia Bella utafaidi kuliko wanawake wote hapa duniani, ilimradi tu ufuate masharti yangu. Ukikiuka au ukinizunguka, au hata nikihisi kuna mwanaume mwingine katikati yetu, utajuta kuzaliwa Bella. Nitaanza na wewe, kisha nitamaliza kwa mdogo wako. Dunia itasahau hata kama mlishawahi kuwepo hapa duniani.” Bella alistuka sana. Akamtazama machoni.
“Mbona unashtuka? Ulipanga unikimbie nini?” Bella alikaa kimya. “Mimi ni wako Bella. Tena wakufa na kuzikana, hakuna wakututenganisha tena.” Mzee Masha alijivuta karibu na alipokuwa amejiegemeza Bella, akamkumbatia. “Nakupenda sana Bella.” “Naomba nilale kidogo.” Bella alijitoa mikononi mwa Masha. “Kweli unatakiwa kupumzika. Usiwe na wasiwasi Bella. Lala ukijua mimi nipo hapa pembeni yako. Ukiamka tunakwenda kuzunguka madukani kutafuta vitu vyako.” Bella alijivuta pembeni, akajilaza akiwa amekunja miguu yake. Mzee Masha alimsogelea, akalala pembeni yake huku amemkumbatia. Bella alikuwa akitetemeka huku ameshikilia dhahabu alizo zawadiwa. “Usiku wa jana umekuwa mrefu sana Bella. Umelala mbali na mimi. Nimefurahi umerudi.” Mzee Masha alijaribu kumtupia neno Bella, wakiwa wamelala. Lakini Bella alibaki kimya akiwa amefunga macho yake, amegeukia upande mwingine akilia taratibu. Baada ya muda kidogo alimsikia Mzee Masha, akihema kama aliyepitiwa na usingizi.
************************************* 
Mambo ndio kwanzaaa yanaanza.  Masha ameahidi ni ‘mpaka kifo ndio kiwatenganishe’. Amemuonya asiwaze hata kumtoroka.
Usikose Sehemu ya 3.


0 comments: