Story

*My Past* Sehemu ya 14.

Wednesday, July 05, 2017 naomimwakanyamale 1 Comments

*My Past*
Sehemu ya 14.

Bella na yeye alibaki amesimama mbele ya ile picha ya harusi ya Elvin, kama sanamu
na mtoto aliyelala mgongoni mwake. Mwishowe walimuona akifikicha macho, na kuhangaika kama anayetafuta pumzi. JJ alisimama kwa haraka ili kumshika, lakini Bella alianguka na kupotelewa na fahamu, ndipo watu walipoanza kushtuka. Walimtoa yule mtoto mgongoni, Mama Mwasha akambeba, lakini alikuwa na joto kali sana, kuashiria ana homa. Walijaribu kumpepea Bella lakini hakuzinduka. Wakaamua kumkimbiza hospitali. Mtoto alikuwa wakiume, lakini anasura ya Bella, wala haikuhitaji kuuliza kama ni mtoto wake au la. Bella na mtoto wake walipokelewa hospitalini hapo, na kwa kuwa ilikuwa ya kulipia, walianza kufanyiwa huduma ya harakaharaka.

Midomo ya Bella ilionekana imekauka sana mpaka imetoa vidonda, mwili wake ulirudi ukawa kama mtoto mdogo, alikwisha, hakuwa wala na nyama, wazi alionekana huko alipokuwa hakuwa na chakula. Aliwekewa maji akabaki amelala pale kitandani wakisubiri azinduke. Sura yake nzuri ilibaki vilevile, ilikuwa kama uwa la rozi lililoanguka kwenye matope, na kubaki sehemu chake za ua hilo kufunikwa kwa tope. Hakuna Daktari au nesi aliyefanikiwa kumtoa Elvin pembeni ya kitanda hicho cha Bella. Mama Mwasha alikuwa akimuhangaikia mtoto wa Bella, ambaye naye alionekana amedhoofu sana na wazi alionyesha hajapata chakula kwa siku nyingi.

Bella alizinduka, lakini baada ya muda mfupi sana, alirudi kulala. Hakuwa hata akiweza kuongea. Mzee Mwasha aliamua kumpigia simu Mzee Masha kumueleza ujio wa Bella na mtoto wanayehisi ni wake. “Umefanya vizuri Mwasha, asije akatufia huyu mtoto halafu Masha akatuletea fujo. Mkewe alimpongeza.

Haukupita muda mrefu Mzee Masha akawa amefika hospitalini hapo. Alimtizama yule mtoto kwa muda mrefu sana. “Amenichanga huyu mtoto. Ni wakiume au wa kike?” Masha aliuliza. “Wakiume.” Mama Mwasha alimjibu. Mzee Masha akaanza kucheka. Uso wake ulibadilika, hakuna mtu aliyewahi kumuona Mzee Masha akiwa na uso wa furaha hivyo. “Naomba nimshike.” Alipewa mtoto wake akambeba. Cha kwanza alimbusu shavuni. “Mbona ana joto kali hivi?” “Ndio tunasubiri vipimo.” “Lazima atibiwe sasa hivi.” Mzee Masha akaanza kugomba. “Hii hospitali ina daktari wa watoto?” Masha alisimama. “Daktari wa watoto yuko wapi? Kama hakuna anayeweza kumtibu huyu mtoto, naomba niondoke naye akatibiwe kwengine.” Mzee Masha aliendelea kuongea kwa sauti ya juu. “Bella yuko wapi? Amesema alikuwa wapi?” “Anahali mbaya sana. Alikuwa amezimia, sijui kama ameshazinduka.” Mama Mwasha alijibu kwa sauti ya chini. “Kama haijajulikana alipokuwa, ni lazima ulinzi uongezeke hapa. Inawezekana alitekwa nyara, ndio amefanikiwa kutoroka. Wakimfuata tena? Nani atamtibu mtoto wangu, sasa hivi?” Mzee Masha alikuwa kama amechanganyikiwa. Walikuja wauguzi wawili. “Tunasubiri vipimo Mzee ili tujue anapewa dawa gani.” “Mmeshampa dawa yakushusha homa?” “Bado.” “Pumbavu zenu kabisa. Akifa huyu mtoto hapa, nitashitaki hospitali nzima.” Mzee Masha aliendelea kugomba kama kawaida yake na alifanya fujo za kutosha pale mpaka mtoto wake alipoanzishiwa matibabu.

Alitoka kwenda kuongea na simu, akarudi kwenda alipolazwa Bella. Alimkuta akiwa amelala. “Huyo aliyemteka nyara Bella akiwa na mtoto wangu, nitampa adhabu ambayo hatakaa akasahau maishani. Na ninaapa nitamkamata tu.” Masha aliendelea kugomba kwa sauti bila kujali kama yupo hospitalini. Baada ya muda mfupi tayari hospitali ilishafurika maaskari. Hapo ndipo ilipojulikana na watu wote waliokuwepo wakati ule hospitalini hapo kuwa yule ndiye Mzee Masha anayefahamika mjini na anaye mgonjwa wake pale. Watu walikumbushana kisa cha Bella na mdogo wake, kila mtu akataka kumuona na waandishi wa habari walianza kufika usiku huo.

Masha alihakikisha anaweka ulinzi wakutosha mpaka nje ya mlango aliolazwa Bella na mtoto wake, na hakuna mtu yeyote, awe nesi au daktari aliyekuwa anaingia humo vyumbani bila kukaguliwa. Mzee Mwasha na familia yake walibaki wakimshangaa Mzee Masha alivyojaa pale hospitalini bila hofu wala aibu akitangaza yeye ndiye baba wa yule mtoto. Aliweza kufanya kila kitu yeye mwenyewe akisaidiana na pesa yake. Alitoa amri ya hiki kifanyike au kile, ilimradi yeye ndio aliyeonekana anaongoza mambo mahali pale na Bella anapatiwa matibabu ya haraka.

 ***********************************************************

“Elvin! Elvin! Nisaidie.” Bella alisikika akiongea akiwa usingizini. Alikuwa akihangaika sana huku akilia kwa hofu kubwa. “Bella! Bella! Amka unaota.” Elvin alimshtua. Bella alishtuka. Alimwagalia kwa muda kidogo, kisha akafunga macho na kulala tena. Alikuwa kwenye chumba chake peke yake. Baada ya majibu kutoka, mtoto wa Bella alikuwa na typhoid kali sana. Alianzishiwa matibabu na yeye alikuwa kwenye chumba chake kilichokuwa na ulinzi mkali sana, upande wa wodi ya watoto. Mzee Masha alipohakikisha mtoto wake yupo salama, alirudi alipolazwa Bella, akamkuta Elvin amekaa. “Utaondoka hapa?” Mzee Masha alimuuliza Elvin. “Hapana. Nitakuwa naye.” “Tafadhali, chochote kitakachotokea unipigie simu.” “Sawa.” Walipoona Bella na mwanae wameshaanzishiwa matibabu na wametulia, kila mtu aliondoka, wakamuacha Elvin. Bella alilala mpaka asubuhi.

JJ ndio alifika hospitalini hapo asubuhi sana akiwa na kapu la chakula kama alivyozoea kumuona mama yake akifanya. Kwanza alikwenda kule alipolazwa mama yake na mtoto wa Bella, alipohakikisha mama yake amekula vizuri ndipo akaamua kwenda alipokuwepo Elvin na Bella, lakini waliongozana na mama yake, na yeye alitaka akamuone Bella. “Pole Elvin. Umepata muda hata wakulala?” Aliuliza Mama Mwasha mara alipoingia yeye na JJ, walimkuta Elvin amekaa kwenye kiti akimtizama Bella aliyekuwa amelala. “Nimeshindwa hata kusinzia, mama. Hajaamka usiku kuchwa.” “Madaktari walirudi tena?” “Walirudi. Wakamchukua akiwa usingizini wameenda kumfanyia vipimo, wanasema wamekuta utumbo umeanza kufungana, anaonekana hajala chakula siku nyingi.” “Mungu wangu, Bella wangu. Sijui nani alimchukua mwanangu.” Mama Mwasha alianza kutokwa na machozi. Alimsogelea akamfunika vizuri. “Pole Bella. Pole sana mama.” Mama Mwasha aliongea kwa upole sana. Akambusu kwenye kipanda uso. “Ule sasa.” “Siwezi kula mama.” “Kwa nini?” “Sijui ni mshtuko au nini! Tumbo limejaa tokea jana. Hata soda aliyoniletea Eli nimeshindwa kuinywa.” “Pole.” Elvin alibaki akimwangalia Bella. “Mwili wake umebadilika sana, lakini kasura kake kako vile vile.” Elvin aliongea huku akitafakari. “Basi jilaze hata hapo kwenye kochi kidogo.” “Siwezi mama. Naogopa hata kufumba macho, naona naweza kuamka nisimkute tena. Nililala hivyohivyo kule Bagamoyo, wakamwiba.” “Sasa si JJ atakuwepo hapa Elvin mwanangu? Lala kidogo.” “Usingizi umepaa mama. Siwezi kulala. Acha tu nimwangalie.”

Walimuona Bella anaanza kuhangaika sana pale kitandani, kila walipojaribu kumwita, Bella alishindwa kufumbua mambo alianza kulia sana huku jasho likimtoka. Alikuwa kama mtu anayepambana. “Vinnn! Elvinnn! Vin! Nisaidie Vin! Pleeease…., Help me. Vin!” Bella aliendelea kulia sana huku amefunga macho akiendelea kupambana. Ilibidi aitwe nesi, akagundua na yeye ana homa kali sana. Daktari aliitwa, akasema achomwe sindano, baada ya muda akatulia. Elvin alikuwa akilia sana. “Usilie Elvin!” “Bella anaonekana aliteseka sana mama, tena bila msaada wowote ule. Najuta kumuacha peke yake.” “Acha kujilaumu Elvin. Hukujua kama kuna watu walikuwa na nia naye mbaya.” “Daah!” Elvin aliendelea kulalamika, akimuonea huruma Bella. Alirudi kulala, lakini alichukuliwa vipimo vingine zaidi. JJ bado alikuwa kimya kama asiyejua nini aseme. Alikuwa kwenye mshtuko mkubwa sana.

Familia nzima ya Mwasha ilirudi hospitalini hapo asubuhi hiyo. “Basi nyinyi mbakie hapa na Elvin na Bella, mimi nirudi kwa mtoto. Nilimuacha na manesi mara moja ili nije kumuona Bella.” “Vipi Bella?” Mzee Mwasha aliuliza. “Homa ipo juu sana, wamechukua vipimo, lakini Mwasha!” “Eeeh!” “Huyu mtoto anaonekana alikuwa kwenye mateso makali sana. Analia akiwa usingizini akiomba Elvin amsaidie.” “Sijui ni nani amemfanyia huyu mtoto ubaya huu jamani!”  “Labda ndio maana Elvin ameshindwa kupata amani kabisa tokea aondoke, kumbe alikuwa akimwita sana.” Mama Mwasha aliongea kwa masikitiko sana. Alitoka na kuwaacha wanae na baba yao hapo chumbani kwa Bella.

********************************************************

Mtoto wa Bella alianza kupata nafuu kabla ya mama yake. Alianza kula kidogo kidogo, na homa ikaisha, kitu kilicho waridhisha madaktari wakaamua kumruhusu arudi nyumbani na dawa zakuendelea kutumia. Mzee Masha alimuomba Mama Mwasha watoke nje waongee. “Naona kama unamlea huyu mtoto vizuri na amekuzoea. Nakuomba ukaishi naye, nimepata nesi nitakaye muajiri awe anakuja hapo nyumbani kuanzia asubuhi akifanya kazi zake huyu na kuondoka jioni au mpaka utakapo mruhusu.” “Kwa kipindi hichi akiwa mgonjwa?”  Mama Mwasha aliuliza. “Hapana ndio atakuwa dada yake wa kazi. Sikutaka kuanza kuleta watu wasio na uelewa waanze kujifunzia kazi kwa mwanangu. Huyo nesi atakuwa akiangalia afya yake kwa ujumla, na kufanya kazi zote utakazompa.” Mama Mwasha alibaki akifikiria. “Tafadhali Mama Mwasha.” “Wala huna haja yakunibembeleza Masha. Bella ni kama binti yangu. Kwa hiyo huyu mtoto ni mjukuu wangu kabisa. Ninachofikiria umuhimu wa huyo nesi.” “Usimkatae. Wewe mpokee kwa siku za mwanzoni akusaidie mpaka huyu mtoto atakapokuwa sawa. Ukiona humuhitaji, basi tutamuondoa.” “Sawa.” “Asante sana. Mambo mengine nitaongea na Mwasha mwenyewe.” “Sawa.” Mama Mwasha alikubali. Walikuja kugundua yule mtoto hajui kuongea Kiswahili kabisa, anaongea kilugha. Swali likawa ni lugha gani hiyo anayoongea yule mtoto?

Mama Mwasha alimchukua yule mtoto mpaka nyumbani kwake. Alikuwa mtoto mzuri sana. Alijitahidi kumlisha kila wakati ili kujenga afya yake, maana alikuwa mifupa mitupu, japo alionekana ni mtoto aliyekomaa. Hakuonekana na tabia za mtoto wa umri wake, miaka 3, wazi alionyesha kweli alikulia kijijini. Alikula vyakula vya watu wazima bila shida, lakini alikuwa mkimya kama mtoto aliyepitia magumu sana. Alishtuka kila wakati hata mlango ulipokuwa ukifunguliwa alimkumbatia Mama Mwasha huku akitetemeka. Hakutaka watu wamshike kabisa isipokuwa Mama Mwasha peke yake. Hakumwangalia mtu yeyote machoni, wakati wote alijificha uso.

*********************************************************

Bella alianza kupata nguvu, aliweza kukaa, lakini hakuwa akiongea. Alikuwa endapo ataamua kukaa, anajivuta mwisho kabisa kwenye kona ya kitanda, anakunja miguu yake, nakubaki ameinamisha kichwa chake, kama anayeficha sura yake. Daktari alishauri aachwe kabisa kwa muda hata wapunguze kumtembelea. Lakini baada ya siku moja kuisha, ya pili yake Mzee Mwasha aliomba kuongea na daktari. “Sidhani kama ni sawa kumuacha tena bila watu. Bella anapenda watu. Inawezekana huko alikokuwa alikuwa amefungiwa peke yake na mtoto wake, maana jinsi anavyoficha uso wake na kutetemeka kila mtu anapofungua mlango, ndivyo na mtoto wake anavyofanya hivyohivyo kule nyumbani. Lazima tuhakikishe anajua sasa hivi yupo na watu wanaompenda. Naomba uniruhusu leo nikaongee naye.” “Naona ni wazo zuri. Tujaribu” Alipopata ruhusa ya daktari, Mzee Mwasha akaondoka.

Aliingia chumbani kwa Bella, alikuwa amelala amegeukia ukutani. Watoto wake wote walikuwa wamekaa na Elvin hapo kwenye hicho chumba. Alisogea mpaka pale kitandani. “Bella! Bella mama! Baba huyu amekuja. Ninahamu na wewe mwanangu.” Bella alifungua macho akabaki akimsikiliza kwa muda. “Ni mimi baba.” Mzee Mwasha alirudia. Bella akageuka, akamtizama kwa muda. “Baba?” Bella aliuliza kama anayetaka uhakika. “Ni mimi Bella.” Bella alikaa akamkumbatia Mzee Mwasha. “Umepona baba?” Bella alimuuliza huku amemkumbatia kwa nguvu Mzee Mwasha. “Nilipona kabisa. Unajisikiaje?” Bella alinyamaza kwa muda kisha akamuachia Mzee Mwasha akamtizama machoni. “Ni kweli kuwa Elvin ameoa au ni ndoto tu?” Bella alimuuliza tena bila kujibu swali. “Ndiyo.” Mzee Mwasha alijibu. Bella alirudi kumkumbatia kwa nguvu na kuanza kulia sana kwa uchungu kama anayegugumia maumivu, kisha akarudi kumwangalia tena Mzee Mwasha.  “Is he happy?” Bella aliuliza tena kwa upole huku akilia. Mzee Mwasha alibaki akimfuta machozi Bella. “Kila kitu kitakuwa sawa Bella. Umesikia mama?” Bella alitingisha kichwa huku akilia. “Tulikuwa na hamu na wewe Bella.” Bella alitabasamu, akarudi kumkumbatia tena Mzee Mwasha. Elvin na kaka zake walikuwa nyuma kabisa wamekaa wakisikiliza mazungumzo yao. “Mama yuko wapi?” Bella aliuliza tena. “Yupo na mtoto nyumbani.” “Mtoto?” “Ndiyo. Mtoto wako?” “Mimi nina mtoto?” “Yule mtoto uliyekuja naye pale nyumbani siku nne zilizopita.” “Sio mtoto wangu yule. Na mimi nilimuokota.” “Wapi?” Bella alifikiria kidogo. “Kwani leo ni tarehe ngapi?”  Akatajiwa. “Mmmh!” Bella aliguna baada ya kufikiria tena kwa muda mrefu sana.

“Nina hamu yakula chakula baba.” Mzee Mwasha alifurahi sana. “Unataka kula nini?” “Sijui. Lakini ninataka kula.” “Ngoja nimpigie simu mama akupikie chakula haraka uletewe. Sawa?” “Hii dripu ni ya nini?”  Bella aliuliza taratibu huku akiangalia mkono wake wenye dripu. “Kwa kuwa ulikuwa hauli chakula kabisa, ndio maana wamekuwekea hiyo. Na wakati mwingine wanakuwekea na dawa humo humo.” “Ninaumwa?” Bella aliuliza tena. “Kidogo tu.” “Sipendi sindano baba. Waambie watoe.” “Utakula? Maana ukitolewa hiyo inamaana inabidi ule chakula vizuri na ukubali kumeza dawa za vidonge.” “Nitakula. Naomba waambie watoe.” “Basi ngoja nikazungumze nao.” “Nataka kulala.” “Kaka zako wapo hapo pembeni wanataka kukusalimia.” Bella alijitoa kwa Mzee Mwasha akageuka kuanza kuwatafuta.

Wote walimsogelea. “Pole sana Bella.” “Pole.” Akasogea Eli. “Mimi bila kunikumbatia siondoki hapa.” Bella alicheka kidogo. “Eliii!” “Kumbe unanikumbuka?” Bella alicheka huku akitokwa na machozi. “Kuja hapa.” Eli alimvuta karibu akamkumbatia. “Utapona eeh.” Eli alimwambia Bella wakati amemkumbatia. Bella alitingisha kichwa. “Unajisikiaje sasa hivi?” JJ aliuliza. “Nina hamu ya kula.” Bella alijibu huku akitabasamu. “Muone! Anapenda msosi huyu! Wagonjwa huwa hawali wewe Bella.” Eli alimchokoza Bella. “Usimsikilize Eli. Ngoja nikafuate chakula. Nitarudi baada ya muda mfupi.” “Asante mwaya kaka JJ.” Bella alishukuru. Wote walimsubiria Elvin na yeye asogee amasalimie Bella. Alikuwa amebaki amekaa ameinamisha kichwa chini, kama aliyetingwa na mawazo. Bella alimgeukia akabaki akimwangalia. Chumba kizima kilitulia, wakimwangalia Elvin. Kama aliyeshtuliwa, alinyanyua kichwa akamuona Bella na kaka zake wakimwangalia. Akasimama na kumsogelea Bella.

“Kwa mara nyingine tena, Bella mikononi mwa Elvin.”
“Mbona umekonda hivyo? Unakula Vin?” Bella alimuuliza kwa shida sana sababu yakuanza kulia tena kwa uchungu baada ya kumuona Elvin. Elvin alishindwa kujibu kabisa, alijitahidi kuzuia machozi lakini akashindwa. Alimsogelea na kumnyanyua pale kitandani na kumkumbatia na dripu yake ya maji mkononi. Bella alimzungushia mikono yote mabegani kwake, Elvin akabaki amemkumbatia kwa mkono mmoja kiunoni na mwingine ameweka mgongoni mwake. Waliendelea kulia kwa muda mrefu mpaka baba yao aliporudi na nesi. “Naona mgonjwa wangu amepata nafuu, nasikia hataki tena dripu.” Nesi aliyekuwa akimuuguza Bella alivunja ukimywa. Bella alijitoa kwa Elvin, akakausha machozi. “Najisikia vizuri. Nafikiri naweza kula.” Bella alijibu. “Kweli naona unanafuu kubwa. Hata usoni umechangamka.” Bella alitabasamu.

“Mama yenu amesema mmoja wenu akafuate chakula.” Mzee Mwasha aliwageukia watoto wake. “Mimi nitaenda baba. Baadaye kidogo jamani. Bella, nikirudi nilikute hilo tabasamu.” Bella alicheka. JJ akatoka. Walimtoa ile dripu, Bella akabaki akiangalia mkono wake. “Nimekonda sana, eeh?” Bella aliuliza. “Lakini chakushangaza bado unavutia vilevile.” Eli alijibu na kumfanya Bella acheke, akamgeukia Elvin. “Midomo imekukauka sana Elvin. Kunywa maji kidogo.” Bella alitaka Elvin anywe maji. Elvin alicheka. Kwa mara ya kwanza walimuona Elvin ametoa kicheko cha kutoka moyoni. Hata uso wake ulionekana umefunguka. “We Eli, mpe maji bwana.” “Bella kwa kunionea! Mbona na mimi midomo imenikauka lakini huniambii ninywe maji?” Bella alicheka. “Nenda bwana Eli ukalete maji. Kwanza nilikupa kazi ya kuhakikisha Elvin anakula, umezembea mpaka amekonda!” “Bwana kichwa changu kimerudi. Na matatizo yote hayo husahau!? Kumbe umekonda mwili tu akili zipo vile vile?” Kila mtu alicheka. “Nenda bwana kalete maji, soda na keki ya Vin. Ale sasa hivi.” “Chakula kinaletwa Bella. Mbona unapenda kunitesa bure?” “Basi kamletee maji anywe wakati tunasubiri chakula.” “Kweli mama umerudi!” Eli alitoka na kuacha angalau watu wanacheka. Bella alitulia kidogo, akajilaza akionekana kweli amechoka. “Naomba nilale kidogo, bado najihisi nimechoka sana.” “Lala tu. Wakileta chakula tutakuamsha.” “Msiniamshe baba. Acha nilale kidogo.” “Watakurudishia dripu wakikuona hutaki kula.” “Basi mniamshe.” Bella aligeuka ukutani akapitiwa na usingizi palepale.

Baada ya muda akaanza kuhangaika tena. “Vin! Elvin! Nisaidie… Vin please!” Bella alikuwa akihangaika sana. Elvin alikuwa amekaa na baba yake, Eno na Eli, akasimama kwa haraka sana. “Bella! Bella! Amka.” Bella alikaa haraka sana akajivuta kwenye kona na kukunja miguu yake na kubaki akitetemeka. “Bella! Bella! Niangalie. Ni mimi Elvin.” Taratibu kama anayejiiba, Bella alinyanyua uso wake kuchungulia. “Elvin!” “Ni mimi Bella. Upo salama. Sasa hivi tupo wote. Njoo hapa karibu yangu.” Bella alijivuta karibu na Elvin. “Upo salama Bella. Usiogope tena.” Elvin alimlaza kwenye mto vizuri, akabaki amemshikilia mkono, kuku akimbembeleza kwa kumpapasa mgongoni, Bella akarudi kulala.

Aliamshwa chakula kilipoletwa. “Nataka kula na Vin!” “Mbona na mimi sijala?” Eli alichokoza. “Kama tukibakisha ndio tutakupa na wewe.” Bella alijibu nakufanya kila mtu acheke. “Yaani huyu Bella! Akiwa mgonjwa au mzima, ulaji wake upo vile vile. Sasa vyakula vyote hivi utamaliza wewe na Elvin tu?” Bella alicheka. “Unacheka nini sasa?” Eli alimuuliza. “Unakumbuka nilichukua busu langu?” “Mama wavisasi! Husahau?” “Sasa wewe endelea kunisimangia chakula, nitakuwa sikupi hata hug.” Kila mtu alicheka tena. “Njoo mwaya Vin tule.”  Walikula pamoja, Bella akala vizuri sana na kunywa dawa, akarudi kulala huku akimcheka Eli akila chakula cha mgonjwa. “Akija mgonjwa hapa ndani, nitampa chakula chake. Lakini mpaka sasa hivi, sijaona mgonjwa humu ndani.” Eli aliendelea kula.

Japokuwa alionekana dhaifu, lakini kila alipoamka na kumkuta Eli, alifurahi sana na kuanza kutaniana naye maneno mawili, matatu na kurudi kulala. Familia hiyo ilihamia hapo hospitalini wakimuuguza Bella. Eli na yeye alikuwa akishinda hapo kuanzia asubuhi akimka mpaka usiku Bella anaenda kulala. Aliacha pombe kwa siku zote Bella alizokuwa amelazwa hospitalini hapo. Walimuacha kwa siku mbili mbele, walipoona anakula vizuri, na anameza dawa bila shida, ndipo aliporuhusiwa kurudi nyumbani akiwa ameandikiwa dawa zakuendelea kutumia nyumbani kwani alikuwa na mchafuko wa mkojo, UTI na Typhoid kama mtoto wake. Kwa hiyo alikuwa akitumia madawa makali sana.

*************************************************************

Alipofika nyumbani kwa Mwasha akakutana na yule mtoto tena. Akabaki akimtizama kwa muda mrefu sana. “Huyu mtoto anafana sana na…..” Bella akashtuka sana. “Ric! Eric mdogo wangu!” Bella akasimama. “Eric yuko wapi?” Alimgeukia Elvin. “Nilikuacha umelala na Ric, na yeye walimchukua?” “Hapana Bella. Hawakumchukua.” Bella alivuta pumzi kwa nguvu akarudi kukaa kuonyesha ametulia. Kila mtu alianza kupatwa na wasiwasi hawakujua jibu la kumpa Bella atakapouliza tena juu ya Eric.

“Mama!” Yule mtoto alimsogelea Bella, mara baada yakumaliza kulishwa na Mama Mwasha na kushushwa kutoka kwenye kiti chake. “Mama?” Bella aliuliza. “Huyu mtoto amekazana kweli kuniita mama.” Bella alitabasamu huku akinyoosha mikono kumpokea. “Njoo.” Bella alimwita. “Kwani ulimtoa wapi huyu mtoto?” “Mimi niliamka kwenye nyumba moja porini sana, nikawa najiuliza pale ni wapi na nimefikaje! Sikuwa na mtu wakumuuliza. Nyumba yenyewe ndani ilikuwa giza sana. Nikaamua kutoka nje, kumbe nilikuwa ndani ya chumba. Nilipofungua mlango mwanga ukaingia ndani ndio nikamuona huyu mtoto kumbe muda wote alikuwa amekaa pembeni yangu, kamenyamaza kimya kabisa. Sijui kalikuwa kamesinzia? Basi nikatoka nje kuangalia kama kuna mtu, lakini sikuona mtu. Nikarudi ndani kwa huyu mtoto, nikajaribu kumuongelesha akawa ananijibu vitu nisivyoelewa ila ananiita mama. Nikamtoa mle ndani, nikakaa naye nje ya hiyo nyumba kwa muda lakini sikuona nyumba hata moja na wala sikumuona mtu yeyote. Ndio kumbukumbu ikanijia ya siku wale vijana walivyokuja kunivuta kule baharini, Bagamoyo, nilipokuwa nikiogela. Nikajua ndio walinitoa kule na kuja kunifungia hapo na huyo mtoto nikahisi kabisa ni wao wamemfungia hapo. Ndio nikajua labda wameniacha hapo kwa muda kuna mahali wameenda. Kwanza nikaamua kutoroka mwenyewe. Lakini ikawa kila nikifikiria kumuacha huyu mtoto pale nitoroke peke yagu, nikawa nikimuhurumia sana. Japokuwa sikuwa nikimjua ni mtoto wa nani, nikaona nisimwache peke yake kwenye yale mazingira. Ikabidi nirudi ndani nichukue kitenge nimfunge mgongoni nianze kukimbia naye. Nimetembea usiku na mchana kama siku tatu bila hata chakula ndipo nilipoiona barabara. Nikakuta basi limesimama, watu wanajisaidia, na mimi nikapanda bila kuongea na mtu, mpaka kituo kikubwa cha mabasi yanayotoka mikoani, Ubungo. Nimefika Ubungo nilikuwa nimechoka sana, nikashindwa hata kutembea. Nikakaa pale ubungo nje, nikalala na huyu mtoto mgongoni. Nilishtuka imeshakuwa usiku ndio nikapanda kwenye daladala mpaka kule kituoni nikatembea mpaka hapa. Sasa nashangaa tarehe aliyonitajia baba.” “Ni miaka 3, miaezi 7 na siku 20 tokea upotee Bella.” Elvin alijibu, kila mtu alimgeukia kwa mshangao. “Muda wote huo! Kwa hiyo mimi nilikuwa hapohapo kwenye hiyo nyumba?” Bella aliwaza kidogo.

“Bella apewa taarifa ya mtoto ambaye hakuwa hata akijua kama ni mjamzito”
“Sasa na huyu mtoto ni wa nani?” “Ni wako Bella.” Mama Mwasha alijibu na kumshtua sana Bella. “Wangu!?” “Ulipotea ukiwa mjamzito.” Elvin alidakia. Bella alikunja uso. “Mama ndiye alikugundua kama ni mjamzito tokea mpo India. Akaniambia nikwambie wakati tumeenda Bagamoyo. Siku niliyotaka kukwambia ndiyo siku uliyopotea.” Bella alitulia. “Kwa hiyo huyu ni mtoto wa Masha?” Bella aliuliza tena. “Ndiyo.” “Mungu wangu!” Bella alishtuka sana, akamuweka yule mtoto pembeni akasimama kwa haraka sana, akabaki akimwangalia. “Njoo ukae Bella. Bado unahitaji kupumzika. Usiwe na wasiwasi Masha amempokea vizuri sana, ndiye anayemtunza.” Mama Mwasha alijibu. “Mmh! Amemkubalije, wakati aliniambia hataki kuzaa na mimi? Kuna siku nilisahau kunywa dawa za kuzuia mimba, alinipiga karibu aniue. Sasa kwa nini leo amemkubali huyo mtoto?” Bella alitaka kuanza kulia. “Unataka ukapumzike?” Mama Mwasha aliuliza. “Sasa huyu mtoto…” Bella alisita. “Kwanza anaitwa nani?” “Mzee Masha amesema tumwite Tito.” Mama Mwasha alijibu.

Bella alianza kulia. “Simtaki huyo baba kwenye maisha yangu tena, mama. Nitafanyaje? Sitaki hata kuiona sura yake tena.” “Usiwe na wasiwasi Bella. Mimi nipo.” “Naomba mama wewe uwepo katikati ya Masha na huyo mwanae. Usinihusishe na chochote kile.” Bella aliendelea kulia. “Sawa Bellla. Usiwe na wasiwasi.” “Simtaki Masha, mama. Sitaki hata kumuona. Kama atamtaka mtoto wake, mumpelekee hukohuko asije hapa. Asikajage hapa.” “Sawa Bella.” “Na umwambie sitaki hilo jina alilompa mwanangu jina lake baya, akae nalo mwenyewe hilo lijina lake. Nitamtafutia jina jingine. Simtaki kabisa Masha. Mahusiano yake yabaki na mtoto wake tu. Tena asiwahi hata kunitafuta. Nyinyi mmalizane hukohuko. Simtaki Masha, mama.” Bella aliendelea kulia kwa hasira.

“Usilie Bella. Kila kitu kitakuwa sawa. Mama amekubali kukaa na huyu mtoto. Usiwe na wasiwasi.” Elvin alijaribu kumtuliza. “Asante mama na naomba unisamehe. Nimeshtuka sana, sikutaka Masha arudi kwenye maisha yangu tena. Niliondoka kwake nikijua ndio nimeachana naye moja kwa moja. Siku….” Yule mtoto alibaki akimwangalia mama yake kwa muda akaanza kulia na kuongea maneno ambayo hakuna aliyeelewa, huku akimwangalia Bella. Bella alitulia kidogo, kisha akamwita yule mtoto. “Njoo. Huyu mtoto anaongea kilugha! Tukijua ni lugha gani anaongea, tunaweza kufahamu tulipokuwa kwa muda wote huo.”

Yule mtoto alisogea karibu na Bella, akamkumbatia Bella huku akiongea kitu. “Jamani! Inaonekana tulikuwa na mahusiano ya karibu huko tulipokuwa. Ona anavyo nibembeleza. Sijui walikuwa wakinitesa na yeye akiona. Ana upendo kama Ric. Na amefanana naye sana.” Alimshika shika huku akifikiria. “Ric yuko wapi? Atakuwa amekuwa mkubwa sasa hivi. Na alivyo mrefu!” Bella alitabasamu huku akimwangalia yule mtoto.

“Si atakuwa alipata sana shida kipindi chote hicho wakati mimi sipo? Najua Eric hawezi kuishi bila mimi. Alifanyaje mlipogundua nimepotea?” Bella alimgeukia Elvin. “Alikuwa kwenye wakati mgumu sana.” “Maskini Ric. Nilijua tu angeteseka. Aliona mimi na mama wote tumemuacha peke yake.” Bella alibaki akifikiria tena. “Unaweza kukumbuka wapi mlikuwepo Bella?” “Sikumbuki baba. Na wala sikuuliza abiria wengine kwa hofu yakugunduliwa halafu wakatushusha, kwa kuwa sikuwa na nauli. Na wakati natoroka pale, nilijua ndio nazinduka, kwa kuwa walipokuwa wakinivuta kutoka kwenye maji, tulikuwa tukishindana nguvu. Nikamuona Elvin kwa mbali kama anataka kuja baharini, nikaanza kumwita, ili aje aniokoe, mmoja wao akatoa kitambaa mfukoni akanifunika nacho puani, hapo hapo nikapoteza fahamu. Kwa hiyo hata sijui walinipeleka wapi baada ya hapo.” Wote walinyamaza.

“Nimechoka, nataka nikalale.” Wote walishukuru sana baada ya Bella kuaga, wakajua wamekwepa kwa muda swali la Eric. “Twende nikusindikize chumbani kwako Bella.” “Asante mama.” Bella alisimama, kabla hajafika mbali alimgeukia Elvin. “Hujanijibu mahali alipo Ric. Sitaki anione nikiwa na hali mbaya hivi, lakini nataka angalau niongee naye kwenye simu ili nimtoe wasiwasi.” Wote walinyamaza. Bella alipatwa na wasiwasi akakunja uso. Alitaka kugeuka vizuri ili amwangalie Elvin, kidogo akapepesuka, Mama Mwasha akamuwahi kumdaka ili asianguke. “Asante mama. Naona mwili bado haujapata nguvu.” “Kwa kuwa umekula vizuri, twende ukapumzike tutaongea baadaye.” “Ni kweli. Lakini kabla sijalala naomba niwashukuru kwa kumlea Eric kwa kipindi chote hiki wakati sipo. Asanteni sana.” “Karibu Bella! Tangia umlete humu ndani Eric alichukua nafasi ya Elvin, akawa yeye ndio mziwanda wetu.” Mzee Mwasha alijibu, Bella akacheka. “Na anavyopenda kupendwa yule! Si atakuwa aliwadekeeni na kuwasumbua sana?” “Eric ni mtoto mzuri sana. Rahisi kuishi naye. Hakusumbua hata kidogo.” Bella alitabasamu wakaingia chumbani. Alipanda kitandani, Mama Mwasha akamfunika. “Asante mama. Naona nikiamka nioge, nanuka.” “Kweli unanuka.” Bella alicheka. “Lakini sasa hivi sitaki kuoga mpaka nikiamka.” “Wewe lala tu, utaoga ukiamka.” Bella alipitiwa na usingizi. Kwa muda wa siku tatu mfululizo Bella alikuwa akilala tu, bila yakutoka hata kitandani. Aliletewa chakula hapo hapo kitandani, alikula  na kumeza dawa zake na kurudi kulala.

*******************************************************

Alimaliza dawa zote, akaamka siku hiyo ya asubuhi akiwa na nguvu, akaamua kutoka pale chumbani. Akaenda mpaka jikoni, akamkuta Mama Mwasha. “Unajisikiaje?” “Najisikia nina nguvu, hata ukinipa shamba nitalima.” Wote walicheka. “Elvin yuko wapi?” Bella aliuliza. “Nyumbani kwake.” “Alimaliza nyumba yake?” “Alimaliza.” Bella alifikiria kidogo. “Unajua aliniambia akimaliza kujenga nyumba yake, atanichukua nikaishi naye?” “Sikuwa najua.” Mama Mwasha alijibu. “Aliniambia siku ile tumerudi kutoka India. Tena mimi na Eric. Alisema pale ndio patakuwa nyumbani kwetu mimi, yeye na Ric. Hata kama Eric akija kuoa, tulikubaliana tungebaki mimi na yeye tu.” Bella aliongea kwa huruma sana. “Kwa hiyo ndiko anakoishi sasa hivi na mke wake?” Bella aliendelea kuhoji. “Ndiyo.” Bella alikaa kimya. “Unataka kunywa uji wa mtoto au utasubiri chai?” “Mtoto mwenyewe yuko wapi?” “Bado amelala.” “Analala wapi?” “Nalala naye. Una mtoto mzuri sana Bella.” Bella alicheka kinyonge. “Amefanana sana na Ric. Elvin amempeleka wapi Eric au amemchukua anaishi naye huko kwake?” Bella aliuliza lakini Mama Mwasha alinyamaza. “Eti mama?” Safari hii Bella alionekana anataka kupata jibu la uhakika.

“Bella apata taarifa za kifo cha mdogo wake.”
Mama Mwasha alizima jiko, na kumgeukia Bella. “Twende tukaongee vizuri hapo sebleni.” Bella aliongoza njia bila wasiwasi, akafika sebuleni akakaa kwenye kochi. “Vipi mama? Au aliwasumbua sana mkamgawa?” “Hapana Bella. Eric alikuwa mtoto mzuri sana.” Bella alikunja uso. “Alikuwa? Kwani amebadilika?” “Ulipopotea, hatukujua kama ulitekwa, tulihisi umepotelea baharini. Masha alitafuta kikosi cha waokoaji wakakutafuta sana baharini zaidi ya  siku tatu, mchana na usiku, kwa maboti na waogeleaji, juu na chini ya bahari, bila mafanikio. Ndio Masha akasema upo uwezekano mkubwa kuwa ametekwa nyara, lakini Elvin hakuamini kabisa. Alikaa Bagamoyo siku nane akikutafuta baharini mchana na usiku bila kukata tamaa, mpaka alipougua akarudishwa nyumbani. Ric alipoona Elvin amerudishwa akiwa mgonjwa, bila kukupata, akaamua kurudi yeye mwenyewe Bagamoyo kukutafuta. Akawa anatoroka hapa anakwenda huko.” Bella alianza kulia. “Maskini mdogo wangu!” “Sasa alipokukosa huko, akatuambia labda maji yatakuwa yamekupeleka sehemu nyingine, inabidi tukutafute sehemu zote za baharini. Ikabidi kuongea naye kwa muda mrefu sana kwani alijilaumu sana kwa kupotea kwako. Alisema isingekuwa yeye kukuomba mkaogelee baharini, usinge potea.” Bella alizidi kulia.

“Jamani Eric! Asingejilaumu. Sasa mkafanyaje?” “Tukampeleka kwa wataalamu ili wajaribu kumuelewesha akubaliane na swala kwamba wewe umeondoka hutarudi tena na hapa ni nyumbani kwao. Mwanzoni ni kama tulifanikiwa, akakubali. Lakini kadiri siku zilivyozidi kwenda ndivyo alivyozidi kubadilika. Akawa hana raha kabisa, shuleni anafeli, mwishowe tukaambiwa hafiki shuleni. Elvin alijaribu kuongea naye, kujua anapoenda kwani yeye alikuwa akimshusha kwenye geti la shule na jioni Mwasha alikuwa akimfuata au Elvin mwenyewe kama hajazidiwa kazi, alikuwa akirudi kumchukua hapo hapo. Alipoongea naye, akagundua kuwa aliacha kwenda shule kwa muda mrefu, alikuwa kila akishushwa na Elvin pale kwenye geti la shule, alikuwa haingii ndani, alikuwa anakwenda baharini kukutafuta mpaka ukifika muda wa kutoka shule ndio alikuwa akirudi tena pale pale getini, anachukuliwa na kurudishwa nyumbani, kila siku. Elvin aliongea naye sana siku hiyo, lakini hakujibu kitu chochote, akawa analia sana. Tukamchukua siku hiyo tukalala naye huku tukiongea naye sana. Asubuhi aliamka akaonekana yupo sawa, akasema anataka apelekwe shule. Elvin alimchukua kama kawaida akamshusha kwenye geti la shule. Mida ya kwenda kumchukua ilipofika, Mwasha alikwenda shuleni, akasimama getini kwa muda mrefu sana, hakutokea. Ndipo alipoamua kuingia ndani kuuliza, akaambiwa siku hiyo hakuwa amefika shuleni. Alitupigia simu, tukatoa taarifa kila kituo cha polisi, akasakwa, huku tukizunguka ufukweni kumuangalia, bila mafanikio.” Bella alikuwa na hali mbaya sana.

“Kwa hiyo hamjampata mpaka leo?” Bella aliuliza huku akilia. “Tulimpata Bella.” Bella alipumua kwa nguvu. “Nilishaanza kuogopa, nilija kitu kibaya kilimpata. Asante Mungu wangu. Nahisi ningechanganyikiwa. Unajua ndio ndugu pekee niliyebaki naye hapa duniani? Nataka nikipata nguvu, turudi kwetu maisha yaendelee.” “Hutuishi wote Bella?” “Nitakaa hapa mpaka lini mama? Elvin amesh…” Bella alisita kidogo, kisha akaendelea kinyonge sana. “Lazima niendelee na maisha, mama yangu. Na hivi nimeshakuwa mama, nitafute mahali pakuishi nianze majukumu ya umama na nimlee tu mdogo wangu maisha yaendelee.” Bella aliongea kwa uchungu sana. Alibaki ameinama akiwaza.

Kama aliyekumbuka kitu, akakaa vizuri. “Samahani mama nimekukata. Kwa hiyo sasa Ric mkampeleka wapi?” Mama Mwasha alijiweka sawa, huku amejawa hofu. “Mwili wake uliokotwa baharini baada ya siku tatu.” “Sijaelewa. Unaposema mwili unamaanisha nini?” “Anaonekana aliogelea mbali sana, akaishiwa nguvu akiwa mbali na ufukweni…” “Hapana mama.” Bella alijivuta mbali ya Mama Mwasha akiwa kama ndio amefunguliwa macho. “Nooo. No, no no no no noooo. Naomba usiniambie, tafadhali sana mama. Please.” “Pole Bella.” “Hapana mama. Hapana.” Bella alianza kulia kwa uchungu sana. Alitaka kusimama, akashindwa akaanguka sakafuni, akaendelea kulia.  “Ricccc! Ric jamani! Mungu nisaidie nina kufa.” Bella aliendelea kulia akiwa pale sakafuni hakutaka kushikwa. “Tumbo lina niuma mama, nisadie jamani! Ninakufa mama yangu. Ricccc!” Watu wote waliamka, nakubaki wakilia wakimuhurumia Bella. “Tumbo langu mama. Linauma sana.” Mama Mwasha alichukua khanga akaiviringisha kama kamba na kumfunga nayo tumboni.

Bella alisimama. “Hapana mama. Unanidanganya jamani! Naomba unipeleke mlipomuweka.” Bella alipelekwa nyuma ya hiyo nyumba, alipozikwa Ric. Walilijengea vizuri sana. Bado Bella alikuwa haamini, aliinama kusoma jina na kuangalia kwa muda mrefu sana picha ya mdogo wake huku akimwita. Alikaa hapo chini pembeni ya lile kaburi akiendelea kulia. Bella alilia mpaka akakaukiwa. Alibaki akifuta machozi huku akigaragara pembeni ya lile kaburi. Alimliza kila mtu aliyekuwepo pale. Alikataa kusimama wala kuguswa na mtu.

“Bella aomboleza kifo cha mdogo wake na machungu ya Elvin kuoa.”

Eno alitoka kwenda kwenye duka la madawa kununua sindano na dawa ya usingizi. Wakati anarudi na Elvin naye ndio anaingia. “Hali yake ni mbaya sana, hashikiki.” “Tutafanyaje?” Elvin aliuliza. “Itabidi kumshika kwa nguvu, tumchome hii sindano ya usingizi apumzike. Amelia muda mrefu sana na anajipigiza mpaka anatoka damu. Atajiumiza zaidi tusipomuwahi.” Elvin alikimbilia nyuma ya nyumba yao. Alimkuta Bella yupo mavumbini analia sana. JJ naye alishafika. Eno akaomba wamkamate wamchome sindano. Walipofanikiwa kumchoma sindano, Bella alipotelea usingizini. Walimbeba kumrudisha kitandani kwake. Mama Mwasha akaanza kazi yakumsafisha huku Eno akimpima pressure yake. Alipoona ile sindano aliyomchoma haitamdhuru, Eno alitoka na kumuacha mama yake aendelee kumsafisha vizuri. Mama Mwasha alimsafisha mwili mzima na kumbadili nguo. Alimfunika shuka vizuri, akabaki amekaa pembeni yake akimtizama.

Elvin aliingia. “Asante mama.” “Jamani huyu mtoto amepitishwa katika wakati mgumu hapa duniani! Sijui maisha yake yatakuaje!” Mama Mwasha alianza kulia. “Namfahamu Bella, mama. Atapita tu. Atashinda. Ana roho ya ajabu sana Bella, najua atashinda tu.” “Sijui Elvin. Tulikuwa tukiongea naye hapo kabla sijamwambia habari za Eric, inaonekana habari za kuoa kwako pia zinamuumiza sana. Sana. Alianza kukuulizia alipoamka tu, nilipomwambia uko kwako, alipooza sana. Na kuuliza kama ulimaliza ile nyumba, na kama ndiko huko unakoishi na mkeo. Nilipomjibu ndiyo, aliinama chini na kubaki kimya. Anasema ulimuahidi mtaishi wote watatu. Elvin alishindwa kujibu kitu chochote alibaki kimya.

Bella alilala kwa muda mrefu sana, na Elvin hakutaka hata kusogea mbali naye. Alikaa naye humo humo chumbani. Alitumiwa ujumbe na mkewe  akimtaka awahi kurudi nyumbani na baadhi ya vitu vya mtoto vilivyokuwa vimeisha. Kila wakati alikuwa akiangalia saa yake, huku akimtizama Bella. “Mbona una wasiwasi?” Mama yake alimuuliza. “Natakiwa kupeleka vitu vya mtoto nyumbani.” “Unataka kuondoka sasa hivi?” “Amesema anavihitaji tangia muda aliotuma ujumbe wa kwanza.” “Kwani hivyo vitu huko maeneo ya nyumbani kwenu hamna?” “Vipo.” “Sasa kwa nini usiwe unamwachia mkeo pesa za matumizi, ili akiishiwa vitu awe ananunua mwenyewe kuliko awe anakuomba kila kitu? Mwishowe atajisikia mzigo kama humuachii pesa, anakuwa anakuomba mpaka pesa ya chumvi! Hata mwenyewe itakuchosha.” “Naacha mama. Na huwa nampa pesa kila wakati, lakini sijui anazifanyia nini. Hajawahi kuacha kuomba pesa za matumizi ya pale ndani wakati huwa nampa pesa na wakati mwingine nanunua kila kitu mimi mwenyewe.” “Labda hajaelewa kama hizo pesa unazompa ni za matumizi ya mle ndani.” “Anafahamu sana, mama. Nampa za kwake yeye binafsi na zamatumizi ya pale ndani. Lakini kila siku anakupa matatizo ya kwao. Mara akwambie alimpa kaka yake za biashara, mara alimpa tena, zile za mwanzoni hazikutosha, mara alimpa baba yake, mara alimtumia bibi yake kijijini kulikuwa na matatizo. Ukitoka hapo linakuja swala la ada za ndugu zake, nayo hiyo ni pesa ndefu mama, usitake kujua. Kila siku kuna jambo linalohitaji pesa.” “Umejaribu kumshauri atafute kazi? Maana mama yake yupo wakumsaidia mtoto, na yule dada mwingine nilimkuta pale siku ile.”Ni ndugu yake, alimleta asaidie kazi.” “Umeona sasa? Wote wale wanaweza kumsaidia mtoto, yeye akarudi kazini.” “Hataki. Anasema mbona wewe haujaajiriwa mahali popote unakaa tu hapa nyumbani?” “Happiness jamani! Anafikiri ile kampuni ya Mzee Mwasha, nani ameanzisha? Tangia nyinyi mpo wadogo nilikuwa nikihangaika na baba yenu mambo ya biashara, sikuwahi kuacha kufanya kazi. Tena kote kote. Kazini na nyumbani nikimsaidia Mwasha kutafuta pesa na kuwalea nyinyi. Sijui kulala mchana kukoje mimi katika maisha yangu yote tokea naolewa na Mwasha, labda nilipougua. Lakini Elvin, mwache tu. Hatutashindwa pesa yakufanya nyinyi muishi vizuri. Wewe fanya utakachoweza, mengine umuachie Mungu.” “Najitahidi mama, lakini nyumba haina amani. Analalamikia kila kitu. Nyumba imejaa vurugu kama vile ulivyoona. Hamna utaratibu wa chakula. Unaweza ukarudi nyumbani unakuta umeachiwa chakula kwenye sufuria, kimejaa nzi, hujui kama ni cha  mchana, au kimepikwa usiku. Sebleni hapakaliki kwa uchafu, ukisema ukakae chumbani atakufuata na maneno, analalamikia hili au lile. Kila kitu kwa Happiness ni kibaya kwake.” “Labda mtoke nyinyi watatu. Wewe, yeye na mtoto wenu muende mkapumzike mahali, ili akili yake itulie.” “Hataki. Anataka tukienda mapumzikoni twende na mama yake akatusaidie mtoto. Nikimwambia mimi na yeye tutakuwepo na mtoto, hatutashindwa kumtunza mtoto wetu kwa hizo siku mbili au tatu. Mama! Hilo nalo likazua ugomvi usiku kucha analia na kulalamika.” “Analia nini sasa?” Elvin kwa mara ya kwanza ilimbidi amuelezee mama yake maisha anayoishi na mkewe. “Anasema namuona yeye mvivu, hawezi kulea mtoto wake mwenyewe, simthamini, ni maneno mengi siwezi kuyamaliza. Ukiamua unyamaze ulale, anasema unamdharau, ukimwambia natakiwa nilale ili kesho niwahi kazini, nalo hilo linazua mjadala mwingine. Hamna jema mama. Yale maisha ya uombaji, akinibariki na kuniombea, hakuna tena. Sijamuona hata akishika bibilia. Kutwa yupo anaangalia Tv chumbani. Sidhani hata kama kweli yule msichana aliwahi kunipenda mama. Sidhani. Ni mvivu hujawahi ona. Analetewa mtoto hapo hapo chumbani alipo lala akiangalia tv, akimaliza kunyonyesha, anaita mtu aje amchukue mtoto, anasema mgongo unamuuma. Hata kusafisha mwili wake mwenyewe ni kazi. Uchafu ulioona pale nje, ndivyo kulivyo hata chumbani kwetu.” Elvin ni kama alipata pakutolea dukuduku, alimuacha mama yake akitokwa na machozi. “Mmmh!” Mama Mwasha aliguna tu. Walikuwa wakijitahidi kuongea sauti ya chini sana chumbani hapo ili wasimuamshe Bella.

“Itabidi niende mama. Nitarudi kesho asubuhi sana, lasivyo huu usiku utakuwa mbaya zaidi ya siku zote.” “Sawa.” Elvin alisimama akamsogelea Bella. Alimtizama kwa muda mrefu kidogo, akatoka. Bella alilala siku nzima. Aliamka ilishakuwa jioni. Aliangaza macho mle chumbani akajikuta peke yake. Alijivuta mwisho wa kitanda kabisa, akakaa nakuanza kulia tena taratibu. Bella hakumlilia mama yake kama alivyomlilia Eric. Alilia kwa muda mrefu sana, mpaka Mama Mwasha alipoingia. “Bella! Nilijua bado umelala mwanangu. Vipi?” Bella aliendelea kulia taratibu huku akigugumia maumivu. “Nyamaza Bella, mwanangu. Nyamaza mama.” Bella aliendelea kulia bila kunyamaza huku amejiegemeza kitandani. Alikuwa akikumbuka jinsi alivyokuwa akivumilia mateso ya Mzee Masha, ili Eric aishi vizuri. Alikumbuka ndoto za Eric, za kwenda kuchezea kombe la dunia. Bella alilia sana. Vipaji vingi alivyokwenda navyo Eric, upendo wa kweli aliokuwa nao juu yake, vyote vilipotea. ‘Amekufa kwa ajili yakunitafuta mimi.’ Bella aliwaza kwa sauti huku akilia.

Alishuka kitandani akakaa, chini sakafuni akaendelea kulia. Mama Mwasha alienda kukaa naye pale. “Njoo Bella.” Mama Mwasha alitaka kumkumbatia, lakini Bella alikataa. “Nina maumivu makali sana mama.” “Najua Bella. Pole mwanangu.” Mwili mzima wa Bella ulianza kuuma. Ni kama yale maumivu yakupigwa na Mzee Masha yalirudi kwa upya, lakini ya safari hii yalikuwa makali zaidi, na kushindwa kuyavumilia. Alikaa pale sakafuni akilia kwa muda mrefu sana. “Naumwa mama.” “Pole Bella.” “Naumwa sana mama yangu, sijui nitafanyaje!” “Pole sana mwanangu. Panda kitandani ujaribu kulala kidogo.” Bella alirudi kitandani. Alihangaika mwishowe akaanza kulia kichwa kinamuuma sana.

“Kinakaribia kupasuka mama.” “Ngoja nikamwite Eno.” Eno aliingia na kukaa kitandani. Bella alikuwa amejifunika na mto kichwani akiendelea kulia. “Bella! Bella!” Bella aliendelea kulia. “Kichwa kinauma?” Eno aliuliza. “Sana, kinakaribia kupasuka.” “Nautoa huo mto kichwani kwako ili tuongee.” Eno aliuvuta ule mto taratibu, akanyanyua kichwa chake taratibu, akaweka ule mto chini ya kichwa chake. “Dawa ya kwanza kabisa ya hicho kichwa ni kuacha kulia kabisa. Na ya pili nitakupa dawa ya kutuliza maumivu na dawa nyingine ya usingizi unywe, ili ulale. Lakini huwezi kuendelea kunywa dawa za usingizi Bella. Afya yako imedhoofu sana. Unatakiwa ule milo yote vizuri, kurudisha mwili. Sukari ya mwilini mwako ipo chini sana, hata pressure yako ipo chini sana. Madawa ya usingizi, yatazidisha kushusha pressure yako, kitu ambacho sio kizuri. Umenielewa Bella?” Bella alitingisha kichwa. “Labda ale kidogo, kabla hajalala tena.” Mama Mwasha aliyekuwa amesimama pembeni alitoa wazo. “Eti Bella?” “Elvin yuko wapi?” Bella aliuliza. “Alikuwa hapa siku nzima akikusubiri uamke, lakini ameondoka.” Mama Mwasha alijibu, Bella akanyamaza. “Nilete chakula?” Mama Mwasha aliuliza tena. Bella alitingisha kichwa kukataa, akageuka kulala kifudifudi, akaficha uso wake kwenye mto akaanza kulia tena kwa kwikwi. “Ngoja nimpe tu dawa mama. Bella yupo katika wakati mgumu sana. Atakula akiamka. Sitampa dawa kali kama zile za asubuhi.” Eno alisimama, Mama Mwasha akakaa karibu sana na Bella. Alimvuta kwa nguvu na kumlaza mapajani mwake huku akimsuga mgongoni taratibu. Mwishowe Bella alitulia akapitiwa na usingizi bila ya kunywa dawa. Eno aliporudi na dawa, mama yake alimkataza asimpe. “Sipendi aendelee kuishi kwa dawa Eno, tumuache tu hivi. Kama ameweza kutulia bila dawa, ndio vizuri.” “Sawa mama.” Eno alikaa pale na mama yake mpaka walipohakikisha Bella amelala kabisa. Walimrudisha kwenye mto na kumfunika vizuri wakamuacha.

Bella alilala kama masaa mawili tena akaamka. Alitoka na kuelekea sebleni. Alikuta kila mtu amekaa pale sebleni, kasoro Elvin tu ndio hakuwepo. Alijisogeza mpaka miguuni mwa Mzee Mwasha, akakaa chini kabisa kuelekea ilipokuwa tv, huku ameegemea kidogo miguu ya Mzee Mwasha. Alikuwa amekunja miguu yake akaegemea magoti yake, akabaki ameinama. “Vipi kichwa?” Mzee Mwasha aliuliza. “Kinauma.” Alijibu kwa upole sana. “Ngoja nikalete dawa.” Eno alisimama. Bella aliendelea kufuta machozi. “Nikuletee chakula hapohapo?” Mama Mwasha aliuliza. “Sisikii njaa mama.” “Lazima kula Bella. Huwezi kunywa dawa bila chakula. Utaanza kuumwa tena tumbo. Umesikia mama.” Mzee Mwasha alimshika Bella mgongoni. “Mleteeni chakula  kidogo tu ale kabla ya kunywa dawa.” Eli alienda kuleta chakula. Bella alikula akamaliza chote, akanywa dawa akarudi kujiegemeza bila kuongea kitu. Waliendelea kuangalia tv, kimya kimya.

“Naona kichwa kimetulia kabisa.” Baada ya muda Bella alivunja ukimya. “Afadhali.” Mzee Mwasha alijibu. “Ukazane kunywa maji Bella. Yatakusaidia sana.” Eno alishauri. “Basi Eli nenda kaniletee maji.” “Mimi ndio mnyonge wako Bella.” Bella alitabasamu. “Nenda bwana.” “Kilichokushinda kumtuma Eno mtoa ushauri ni nini, Bella?” Kidogo watu walicheka. “Nakutaka wewe.” “Haya mama.” Eli alinyanyuka akaenda kumletea maji.

 “Tulikuwa tukikumbuka kweli Bella mwanangu.” Mzee Mwasha aliongea huku amemshika Bella mgongoni. “Sijui nini kilinitokea baba. Sina kumbukumbu za hiyo miaka yote kabisa. Nahisi kama niliondoka juzi tu. Inakuwa ngumu kuamini kama ni miaka yote hiyo imepita.” “Lakini ndio vizuri Bella. Mimi namshukuru Mungu kwa kuficha ufahamu wako. Ungeteseka sana.” Mama Mwasha aliongeza. “Ni kweli. Ningekuwa ninawahurumia kwa kunitafuta, hasa Elvin na Ric ambao niliwaacha kule Bagamoyo.” “Elvin alichanganyikiwa sana. Alikuwa akiogelea huko baharini kama mwehu. Alikataa kurudi nyumbani kabisa. Alikaa huko usiku na mchana anakutafuta baharini mpaka alipougua. Miaka miwili ya mwanzoni alichanganyikiwa kabisa. Alikuwa kama mgonjwa. Mpaka akapelekwa Dubai kwa Eno. Alikaa huko karibia mwaka mzima akifanyiwa counseling, ndio akapata nafuu. Hata kifo cha Eric kilimchanganya sana. Hatukujua kama atakuja kuwa vile.” Eli aliongeza. “Maskini Elvin!” Bella alimuhurumia sana. “Hata hivyo hayupo sawa kabisa. Ni hivyo tu kwa kuwa ni mtoto wa kiume inabidi kujikaza. Elvin hajarudia hali yake.” Eno aliongeza. Bella aliinama nakuanza kulia tena, taratibu.

“Kwa hizo siku tatu wakati natembea na huyu mtoto, Elvin pekee ndiye alikuwa akinitia nguvu yakurudi nyumbani. Kila nilipokuwa nimechoka nataka kukata tamaa, nilikuwa nikisikia akiniita. Kuna siku nilishindwa kutembea kabisa, jua lilikuwa kali, nikaamua kupumzika kwenye kivuli nikapitiwa na usingizi. Kila nilipokuwa nikijaribu kuamka nilishindwa. Nikarudi kulala, na huyu mtoto mgongoni. Nikamsikia Elvin ananiambia, ‘Amka Bella. Wewe ni jasiri kama simba. Nimekuona ukishinda kifo, hutashindwa kurudi nyumbani, amka twende.’ Nilishtuka kutoka usingizini, nikaanza kutembea ilikuwa imeshafika jioni. Nakumbuka nilitembea usiku kucha, na mchana bila kupumzika, mpaka nilipofika barabarani. Nikama nilipata nguvu mpya. Elvin ndiye aliyenifanya nirudi.”  Bella alimalizia kwa sauti ya chini sana.

“Tumefurahi umerudi Bella. Uliondoka na furaha yetu.” Bella alicheka akafikiria kidogo. “Lakini nani aliniteka, na kwa nini?” Wote walibaki kimya. “Ameyabadili maisha yangu kabisa. Ameondoa ladha nzima yakuishi kwangu hapa duniani. Noana nimepoteza kila kitu. Natafuta sababu ya kuishi tena siioni.” Bella alilalamika huku akilia. “Sisi tupo Bella, na una mtoto anayekuhitaji.” “Huyo mtoto wala simjui mama. Ni kama ulale uamke uambiwe ulipokuwa usingizini ulizaa mtoto. Sikujua hata kama ni mjamzito, sijui amekuaje mpaka kufikia hapo. Nani alikuwa akitulea, tuliishije, sijui. Yaani nashindwa kumuunganisha na mimi, labda hiyo sura ya Eric.” “Mungu amekurudishia Eric, Bella. Alijua ni kiasi gani utaumia kumpoteza Eric, akaamua akuletee Eric aliyetoka kwenye tumbo lako.” Kama aliyefunguliwa macho. “Kweli mama! Mungu amenirudishia Eric kwa njia nyingine, tena nilikuwa nikiishi naye. Mungu amsaidie asiwe kama Masha.” Wote walicheka. “Ndio vizuri akukomeshe, uchokozi wote ukuishe.” Eli alimfanya Bella acheke. “Tena mama, akija Mzee Masha usisahau kumwambia sitaki hilo jina lake alilompa mtoto. Abaki na jina lake mwenyewe. Kwanza limekaa la kizee sana, huyu mtoto ataitwa Ric.” “Eric?” “No. tumwite tu Ric. Angalau nimempata Ric.” “Hata Elvin hujampoteza Bella.” “Haitakuwa kama zamani mama. Elvin sasa hivi ni mume wa mtu, ana majukumu ya familia yake.” Bella aliongea kinyonge, akabaki ameinama kwa muda wakamuona analia tena kwa uchungu sana. “Gosh! I miss Elvin sooooo much.” Bella alilalamika mbele yao, nakushindwa kuficha hisia zake. “Pole Bella. Mungu atakusaidia. Jipe muda mama.” Mwasha alimtuliza mpaka akatulia.

“Eti naweza kuendelea kuishi hapa? Sitaki kuondoka tena na kumuacha Eric.” “Hapa ni kwenu Bella. Ulitaka kuondoka uende wapi?” Mzee Mwasha alijibu. Bella alinyamaza. “Wewe ulishakuwa mdogo wetu Bella. Ni dada ambaye Mungu aliyetupa bila kutarajia.” JJ aliyekuwa kimya muda wote alijibu. “Karibu kwenye familia Bella.” Wote walimkaribisha. Bella alibaki akifuta machozi. “Nimefurahi mmenipokea. Ndio mjue nimefika. Naona Eli ataondoka humu ndani aniache.” “Aliyekwambia nina mpango wa kuondoka humu ndani nani? Tutabanana humuhumu ndani. Labda Mungu amlete mwanamke anayefanana na Mama Mwasha, ndio nitaondoka. Vinginevyo, nitazeekea hapahapa.” Kila mtu alicheka. “Wewe sio muoaji Eli.” “Wala hujakosea kaka. Ni heri nikae humu ndani kama Mzee Mwasha. Hamumuoni jinsi baba alivyotulia? Haongei kwa kuwa kapata mke mzuri.” “Ukimya wa baba ni wa asili bwana!” JJ alijibu. “Kwa taarifa yenu, nyinyi wote watatu mpo kama baba. Kasoro mimi tu, sijui mama alibadilishiwa hospitalini?” Wote waliendelea kucheka. “Kaka JJ wewe kuongea ni mpaka uchokozwe sanaaaa, kama Elvin tu na Eno.  Sasa mimi najijua nilivyo mkali. Nitapiga mtoto wa watu niue bure, nifungwe jela. Heri nisisubutu kuoa.” “Na pombe uache Eli.” “Umeanza baba. Pombe zangu mbona hazina shida? Tena siku hizi saa mbili nipo nyumbani, na mama. Nakunywa mbili au tatu narudi nyumbani.” “Sasa si uache kabisa? Zinakusaidia nini?” “Baba bwana! Haya Mzee wangu nimekusikia.” Bella alianza kucheka. “Nini sasa na wewe.” “Acha pombe Eli.” “Kwani nimekataa. Tatizo lenu mnataka niache starehe pekee niliyonayo hapa duniani. Halafu nifanyaje?” “Mimi nitakupa cha kufanya.” “Nini?” Eli alimuuliza Bella. “Wewe acha kwanza pombe ndio nitakwambia.” “Mmh! Unanifanya mimi mtoto?” “Na nikipata tu nguvu tunaanza kwenda wote kanisani Eli. Nakugongea asubuhi na mapema, ujiandae utakavyo, ili usitucheleweshe.” “Kila Jumapili!?” “Ndiyo.” Bella alimjibu. “Mbona hiyo itakuwa ngumu Bella bwana. Ndio siku yangu ya kulala.” “Utalala tukirudi kutoka kanisani. Lakini lazima tuanze kwenda wote kanisai Eli.” “Daah!” Eli alilalamika. “Afadhali Bella mwanangu. Tushaongea swala la kanisani mpaka tumechoka.” Mama yake alidakia. “Tutakuwa tukienda naye kanisani mama. Usiwe na wasiwasi. Nitahakikisha Jumapili gari haliondoki humu ndani bila Eli.” Kila mtu alikuwa akicheka huku akimtizama Eli. “Karudi mama king’ang’anizi. Akitaka jambo lake huyu!” Eli aliongeza. Waliendelea kuongea. Mpaka walipoagana kwenda kulala.

**********************************************************

Wote waliamka asubuhi hiyo wakakaa mezani wakaanza kunywa chai, Elvin akaingia. “Bella yuko wapi?” “Amelala.” Elvin aliingia chumbani kwa Bella moja kwa moja bila hata kukaa chini,  lakini hakuwepo chumbani kwake. “Bella hayupo mama. Unaamkaje bila kumuangalia jamani!?” Elvin alianza kulalamika. “Sasa atakuwa ameenda wapi?” “Jana amelia sana Elvin. Sikutaka kuingia chumbani kwake kuhofia kumuamsha. Nilitaka apumzike.” Elvin alitoka kwa haraka nakuanza kuita huku amepaniki. “Bella! Bellaaaaa!” “Atakuwa hajaenda mbali Elvin. Hebu tulia.” Eli alijaribu kumtuliza mdogo wake lakini haikusaidia. Elvin alikuwa kama ameweka pamba maskioni, aliendelea kuita huku akizunguka kila mahali. “No No nooo, Bella hawezi kupotea tena mama. Nitakufa.” Kila mtu alitoka kumsaidia kumtafuta.

Bella arudi na kupewa taarifa zote zakumuumiza sana. Kifo cha mdogo wake, Elvin kuhama ndani ya ile nyumba, si wake tena ni wa Happiness, na mtoto wa Masha akiwa anamsubiria amlee kama mama. Yeye hamfahamu lakini mwanae  anaonekana kumfahamu vizuri sana. Swali gumu linalomchanganya ni…
*Je nani alimteka nyara?
*Je maisha yatakuaje bila Eric, wala Elvin?
*Masha tena anarudi ndani ya maisha yake!

AMEKWENDA WAPI TENA ASUBUHI HIYO!?


Usikose Sehemu ya 14.

1 comment:

  1. I like it!, I like it,I like it!indeed cool waiting next chapter

    ReplyDelete