Story
{...ni Wangu - Is mine} Part 1 - Sehemu ya 3.
"...ni Wangu!"
Sehemu ya 3
Nanaa alitua jijini Dar
akiwa na James, ambaye alikodisha nyumba ya vyumba viwili na alikuwaakitumia
gari ya kampuni akiwa jijini. Gari yake hiyo aliitumia siku za weekend tu
kwenye shuguli zake binafsi. Alibahatika kazi kwenye kampuni moja ya simu kama
muhandisi. Alisomea mambo ya “Eletronics Engineering”. Kwa hiyo alikuwa na
kazi nzuri, na maisha yakueleweka. Lakini kwa kuwa alikuwa na akili ya
maendeleo, bado alikuwa kwenye kuwekeza. Kwa hiyo hakuwa na pesa nyingi
mkononi. Lakini alijitahidi kuishi maisha ya kawaida tu kama mtu msomi mwenye
mshahara mzuri.
Alikuwa na kijana aliyekuwa
akifika kumsaidia usafi nyumbani hapo, lakini Nanaa akaanza kushika usukani.
Alimfulia, akampikia kaka yake na bado aliweza kufanya usafi ndani na nje ya
hiyo nyumba ndogo, bila shida. Kwa kuwa walikuwa wakielewana tokea zamani,
furaha na amani havikukosekana ndani ya hiyo nyumba yao.
James alitoka asubuhi na
mapema, na kurudi usiku. Wakati mwingine alichelewa kurudi na kumkuta Nanaa
alishalala, ila ameachiwa chakula mezani. Alimsaidia Nanaa kufanya maombi ya
kujiunga katika vyuo mbali mbali pale jijini, na kumsisitiza kuomba na chuo
kikuu cha Dodoma na Mzumbe. “Huwezi jua
utabahatika wapi. Tupia ndoano kila mahali.” James alimtia moyo. Na kweli
Nanaa alituma maombi kwenye vyuo vingi tofauti tofauti. Akafanikiwa kupata nafasi
katika chuo kikuu cha Mlimani. James alimsaidia kufuatilia mkopo, Nanaa akapata
mkopo wa asilimia 80, James akaahidi kumalizia.
Nanaa, Chuo Kikuu Cha Mlimani.
Shule ya Nanaa ikaanza. Akabadilika,
kama siye Nanaa aliyekuwa akiishi mkoani Kilimanjaro. Akanoga na kuiva kwa joto
la jijini Dar. Nanaa huyu ni Nanaa aliye huru. Anayejifikiria mwenyewe. Kutoka
kwenye manyanyaso mengi. Kazi nyingi mfululizo, leo yupo hosteli! Peke yake.
Anajiwazia yeye tu. Kuanzia akiamka asubuhi mpaka usiku anakwenda kulala,
jukumu lake likawa ni shule na yeye peke yake. Pesa ikaanza kuingia. Kutoka bodi ya mikopo na kwa kaka yake. Akaanza urembo
wa nywele na kucha. Akatafuta sehemu wanazouza mitumba, akaanza kuvaa vizuri.
Akawa anapendeza na kuvutia. Wakati wote
utakaomuona Nanaa, alikuwa msafi. Kuanzia kichwa ambacho alikisuka wakati wote.
Kama si rasta, basi alishonea weaving. Hakuacha nywele zake hivi hivi. Alizaliwa
na kipilipili kikavu sana. Kwa hiyo wakati wote alizisuka nywele zake. Miguuni
na mikononi, safi wakati wote.
Urembo, uzuri na unadhifu
wa Nanaa haukujificha kwenye macho ya wengi. Hata wenzake wakaanza kumsifia
kuanzia rangi ya mwili wake, umbile na kila kitu mwilini mwake kilipewa sifa. Wanaume
wakaanza kuvutiwa. Kila mmoja aliyebahatika kumuona, alitaka na kuota kumiliki
penzi la Nanaa. Kuanzia wenzake wa mwaka wa kwanza mpaka wa ngazi za juu. Kila
mmoja akajitosa kwa wakati wake. Wakimtaka Nanaa aliyeumizwa, kimapenzi. Huku
akiwa na hofu ya kuumizwa tena, lakini bado shauku ya kuja kuwa na kwake na
wake, haikumwisha moyoni. Ni kweli Alex alimuumiza, “lakini si wanaume wote ni wabaya
bwana!” Nanaa alijiambia.
Haiba yake ya kupenda
kucheka na kuwa msikilizaji mkubwa ikawavuta hata wa kina dada wa darasani
kwao. Akajikuta ameingizwa katikati ya marafiki wawili wa muda mrefu. Zena na
Tia. Waliokuwa wameanza urafiki wao tokea shule ya sekondari. Wakatengeneza
kundi dogo la marafiki watatu. Akawa Nanaa, Zena na Tia. Na wote wakajikuta wamepata
chumba kimoja ‘main campas’, Hall 3. Lakini siku za weekend mara
moja moja na likizo Nanaa alikuwa akirudi nyumbani kwa James. Kipindi cha
mitihani alikuwa akipotea kabisa hapo nyumbani. Lakini James alikuwa akielewa
na kufurahia juhudi za dada yake. Alimsisitiza kutulia na kuweka akili chuoni.
Nanaa na penzi la Zac chuoni.
Kadiri siku zilivyozidi
kwenda ndivyo alivyozidi kusitasita kwenye njia mbili katika kufungua moyo kwa
mwanaume mwingine. Lakini Zac akawazi wenzake. Yeye akawa king’ang’anizi kweli
kweli. Hodi na zawadi tofauti tofauti na za mara kwa mara kwa Nanaa, chumbani
kwao hazikukoma. Kama Zac hakumkuta
chumbani hapo, basi aliacha zawadi hizo chini ya mto anao lalia Nanaa,
kitandani kwake. Ilimradi tu kuonyesha kumjali na kuwa anamfikiria wakati wote.
Zac alikuwa mwaka wa
mwisho, wakati Nanaa ndio yupo mwaka wa kwanza. Hilo nalo likaongeza nafasi ya
kuanza kufikiriwa yeye na Nanaa zaidi ya wengine wote. Nanaa akaanza kumpigia
mahesabu. “Naona huyu atanifaa. Si kwa kujali huku!” Nanaa alijiambia
huku akicheka moyoni na tabasamu kubwa usoni, mara baada ya kurudi chumbani
kwao na kina Tia kumwambia anamzigo chini ya mto, kitandani mwake. Uliokuwa umeachwa
na Zac masaa machache yaliyopita.
Wenzake wote walikaa huku
wamemkodolea macho, kuona kile alichokuwa ameletewa safari hiyo. Nanaa akatoa
kwa madaha yote. Zilikuwa chocolate nzuri aina ya ‘Godiva’. Zilibeba umbo la moyo mkubwa na ndani yake
zilipangwa chocolate 32 zenye ladha tofauti tofauti ikiwemo caramels, dark
chocolate, milk chocolate na truffles. Kila mtu alitoa macho. Hata Nanaa
mwenyewe alishangaa. Ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kuletewa zawadi ya
chocolate. Kwake pia yalikuwa mageni. Akajisikia vizuri mbele za wenzake.
Akaanza kuwagawia ili nao waonje.
“Kweli huyu ndio
wakunioa. Kwanza atamaliza chuo mapema, kabla yangu. Atapata kazi, na kutafuta
sehemu yetu ya kuishi pamoja mara baada ya harusi yetu. Yaani hapa namaliza
chuo, naenda kwangu sio narudi tena kwa kaka.” Nanaa
akaendelea kumpigia mahesabu usiku huo huku akila chocolate zake.
Ujumbe wa shukurani kwa chocolate
nzuri alizofurahia yeye na wenzake kwa Zac, ndio ukawa mwanzo wa mawasiliano na
penzi zito kati yao. Shule na mapenzi vikaanza kwenda pamoja. Zac alionekana
kumpenda sana Nanaa. Kama kwa mara ya kwanza, Nanaa akapata mwanaume
anayemjulia. Hakutaka amuone Nanaa akiwa mnyonge. Wakati wote alipokuwa naye,
alimuweka mikononi mwake. Popote na mbele ya yeyote, alimkumbatia Nanaa na
kunyesha mvua ya mabusu.
Nanaa alipoona Zac ni
mwaname wakueleweka, akamsimulia kaka yake, James juu yake. “Mbona sasa humleti nyumbani?” James
aliuliza. “Tumepanga akimaliza chuo, ndio
tujitambulishe rasmi kwa pande zote.” Nanaa aliongea na tabasamu usoni. “Kumbe mpo serious?” James alishangaa
kidogo. “Huyu anaelekea kaka. Ameapa
kunioa, na ananipenda sana na kunijali kuliko nilivyowahi kufikiria. Naamini
safari hii Mungu amenifuta machozi.” James aliuona uso wa dada yake vile
ulivyojaa furaha ukionyesha kutulia, akajua ni kweli amepata kijana
wakueleweka.
************************************************
Lakini hakuachana na
rafiki zake hao wawili. Zena na Tia. Urafiki ukanoga. Alipokuwako Tia, ndipo
utampata Zena na Nanaa. Waliongozana kila mahali. Wakati Nanaa yupo na Zac,
Zena hakuwa amepata mwanaume bado, na Tia alikuwa na mpenzi wake, Evan
aliyekuwa akisoma SUA, mjini Morogoro. Wakati mwingine alikuwa akija jijini
kutembea nyumbani kwao na kuona rafiki zake pia hapo Chuo kikuu Mlimani na IFM.
Tia, Nanaa na Zena hawakuacha kujumuika na Evan na kundi la marafiki zake. Kama
ni siku za weekend, basi watatoka kwenda kumbi na sehemu za starehe pamoja, wao
kama kundi.
Ikitokea kama wanatoka
siku za weekend au kwenye vilikizo vifupi ambavyo kaka yake anajua angekuwepo
nyumbani kwake, na Nanaa akajua kuwa watachelewa kurudi, au watapanga kwenda
mahali watachelewa, basi alimtaarifu kaka yake, na kuishia kulala chuoni bila
kurudi nyumbani kwa kaka yake. Na mara nyingi Evan anapokuwa jijini, basi Tia
ambaye na yeye alifaulu kutokea shule ya wasichana Iringa, na wazazi wake
walikuwa wakiishi Iringa mjini, alitumia siku hizo bila shida, kulala popote
anapotaka Evan mpaka Evan atakaporudi chuoni.
Evan na Tia.
Evan mtoto wa jijini.
Alizaliwa hapo hapo Dar. Lakini shule ya secondary alisomea Tosamaganga, huko
huko Iringa. Enzi hizo shule hizo mbili, Iringa girls na Tosamaganga walikuwa
maswahiba. Ikitokea kuna mziki kwenye shule hiyo ya wasichana wa sekondari ya
Iringa, basi shule ya wanaume watakayo karibishwa ni Tosamaganga. Na hivyo
hivyo upande wa shule hiyo ya bweni ya wavulana, Tosamaganga. Wasichana wao
walijulikana kama ‘Iringa girls’.
Wakati Tia na Zena
wanakaribishwa kidato cha 5, kama ilivyo ada. Sherehe nzuri ya shule ilifanyika.
Shule ya wanaume Tosamaganga ikakaribishwa ili kuja kucheza mziki shuleni hapo.
Na hapo ndipo Evan na Tia walipokutana kwenye mziki. Yeye Evan akiwa kidato cha
6. Japokuwa wote wawili hawakuwa na watu wakucheza nao, washamba kabisa. Zena
mtoto aliyetoka kwenye nyumba ya wazazi walioshika dini, Tia mtoto hapo hapo
Iringa. Lakini hakuwahi hata kuingia Club. Wakakusudia siku hiyo wasipitwe.
Japo waingie kuosha macho. Kujua kinachofanyikaga humo ndani ya mziki.
Walipofika kwenye mziki ndipo
Evan akatokea na kumuomba Tia, pale pale ukumbini wacheze pamoja. Zena na Tia
waliangaliana na kucheka kwa aibu. Kisha Tia akamgeukia tena Evan na kuuliza
akiwa hana uhakika sana, kwani hata wao wenyewe walijua kati ya wasichana wote
waliokuwepo pale ndani, wao walikuwa wasichana wa kawaida sana kuliko wenzao. “Unamaanisha mimi?” Tia aliuliza huku
akijinyooshea kidole huku akijicheka. Evan alicheka kwa kujiamini. Mikono
mfukoni. “Ndiyo. Nimeomba tucheze wote.”
Tia alimgeukia Zena kwa mshangao. Akiwa haamini.
Evan hakuwa amekurupuka
hata kidogo. Yeye na marafiki zake, walishamuona Tia na Zena wakiwa wamekaa
peke yao wanacheka kitoto huku wakishangaa jinsi wengine wanavyocheza.
Walionekana ni wasichana wenye mambo ya kitoto. Evan aliwaambia wenzake
anakwenda kuzungumza na mmoja wao bila kuamua ni yupi kabla. Lakini kadiri
alipokuwa akiwasogelea, ndipo macho yake yakavutiwa na Tia.
Zena na Tia.
Tia na Zena walikutana
siku ya kwanza kabisa walipowasili shuleni hapo. Zena akiwa anatokea jijini
Dar, na Tia hapo hapo mjini Iringa. Wote waliletwa na baba zao. Wakati wazazi
wakilipia ada ya shule, wakajikuta wamebaki wao peke yao. Ikabidi wasalimiane.
Wakajikuta wote wanapenda kucheka hata pasipo sababu. Kule tu kujitambulisha
mimi naitwa Zena, natokea Dar, tayari cheko. Bila kujijua na Tia naye akaanza
kucheka wasijue wanacheka nini. Mvua ilikuwa ikitaka kunyesha. Wazazi
walipomaliza taratibu zote za kuwasajili watoto wao wakataka kuwaaga. Baba yake
Zena kuwahi usafiri ili akajipumzishe hotelini, na baba yake Tia kwenye gari
lake.
Walipotoka na kukuta
watoto wao wakicheka kama ndege, ikabidi wafahamiane. Mzee Hiza, ambaye ndiye
baba yake Zena aliposema anakimbilia hotelini kabla hajalowa, ndipo baba yake
Tia, Mzee Sonzigwa alipomwambia, kamwe mkewe hatamsamehe, kama akisikia aliacha
mgeni akalale hotelini na si nyumbani kwao. Hapo ndipo Zena alipojua wapi Tia
alipata utundu. Mzee huyo alikuwa mzungumzaji tofauti na baba yake, Mzee Hiza, swala
5. Alikuwa mtulivu sana. Kikubwa alichoweza kufanya ni kushukuru na kucheka tu.
Mzee Sonzigwa alimchukua
baba yake Zena, wakaondoka na kuwaacha Tia na Zena wakipelekwa bwenini na
kiranja aliyekuwepo zamu siku hiyo. “Baba
yako anaonekana mpole!” Tia alisifia. “Sasa
ngoja uje ukutane na mkewe. Ndio utauliza walikutana wapi.” Tia akacheka. “Kwani yukoje?” Tia alihoji huku
akijiandaa kucheka. “Unamjua kasuku?”
Tia aliangua kicheko bila kutoa jibu. “Basi
ndio Mama Hiza. Hakuna asiyemjua pale mtaani kwetu. Kwanza hakujaliwa aibu. Hana
cha mgeni wala mwenyeji. Akianza jambo, hamalizi. Mshari, hujawahi ona.
Usithubutu ukamuanza. Utajuta.” Tia alizidi kucheka. “Sasa baba yako anasemaje?” “Kama vile ulivyomuona. Yeye ilimradi
aswali. Basi. Anabaki akimsikiliza tu mkewe. Humuwezi mama Hiza. Watoto wote
wanao anza kuongea pale mtaani wanajua kutamka mama Hiza.” Urafiki ukanoga
kati yao. Wakajikuta darasa moja mpaka wakafaulu chuo kikuu. Hawakufanya kosa.
Wakahakikisha wapo chumba kimoja hapo Hall 3. Na kukusudia kumuongeza Nanaa kwenye
kundi lao.
************************************************
Kwa kuwa walikuwa watundu
sana na wachokozi, hawakuacha kumtania Nanaa. Walipenda umbile lake na
hawakuacha kumtupia neno kila Nanaa anapoingia darasani kana kwamba hawakuwa
wakitoka chumba kimoja. Mbaya zaidi, awe amechelewa na wao wawe wamewahi lecture. Wataanza, “Jamani mmemuona Nanaa ameingia?” “Nanaa wa
ukweli.” Tia atarusha neno jingine kumuunga mkono shoga yake Zena.
“Nanaa wakuvutia bwana!”
Zena ataongeza. “Hana atakachoweka
mwilini, Nanaa kikamchukiza.” “Nanaa Mashallah!” “Nanaa wa dimpozi.” “Nanaa wa
mitego!” “Nanaa wakuumiza mioyo!” “Nanaa ndoto ya wengi!” Zena na Tia watapokezana
maneno huku watu wakicheka, na Nanaa akicheka na kutingisha kichwa. “Hivi nyinyi mlifikaje hapa Mlimani?”
Mara zote Nanaa aliwauliza.
************************************************
Siku moja, kabla ukaribu
wao haujachanganya. Bali kulala chumba kimoja tu. Wakimuona Nanaa akiwasikiliza
na kucheka wakiwa chumbani, na darasani kuwa kama hayupo. Zena na Tia
walimwandikia Nanaa barua, na kuamua kuisoma mbele ya darasa zima wakati
profesa aliyetakiwa kuingia kwenye kipindi, kuahirisha kipindi hicho. “Jamani! Kuna barua rasmi kwa Nanaa. Sisi
kama wapenzi wa Nanaa, tutaisoma.” Zena aliongea kwa sauti kufanya wale
waliokuwa wanataka kutoka darasani wasubiri na kuwasikiliza. Nanaa alijiweka
sawa, akabaki akiwatizama. Tia na Zena walijulikana kwa vituko. Swali likawa,
wakiwa wao wawili peke yao, wanaweza kuzungumza kitu cha maana?
“Kwa Nanaa! Kutokana na tabia
ya wanaume wa hapa mjini, kupenda wasichana kama wewe. Na mimi ndugu yako Zena,
kushindwa kubahatika kumvutia hata mmoja wao. Kamati ya Tia na Zena,
imetafakari kwa kina. Imefikia maamuzi yafuatayo.”
Tia na Zena wakatizamana. Wote wakiwa wamesimama mbele ya ukumbi huo wa lecture.
Wakaweka sura za kazi. Tia akiwa msomaji, Zena akampa maji, kama kusafisha koo,
kisha Tia akaendelea. “Tumeazimia yafuatayo. Nanaa atakuwa rafiki wa Zena. Haraka
iwezekanavyo. Tia akiwa katikati yao. Kwa haraka sana, ni lazima Nanaa ahakikishe
kila anapokwenda kula, maktaba, au kutembea kokote kule, lazima Tia na Zena
wawepo.”
“Umesahau kuweka, endapo ataweza
kuniunganisha na kaka yake, basi afanye hivyo mara moja. Ili kunusuru hali ya
upweke, na kunitoa nyumbani kwa mama Hiza.” Zena aliingilia na kuongezea
huku akiwa uso usio na masihara hata kidogo. Watu walizidi kucheka.
Wakiwa mwaka huo huo wa
kwanza, tena wote wakiwa wageni hapo chuoni. Watu wakiwa bado wanaogopana hapo
darasani. Wakipeana heshima. Hawajuani vizuri. Zena na Tia, binti hao
waliokwishajulikana ni watundu wa kupindukia. Walinyimwa hofu kwa yeyote,
wakafanikiwa kumvuta Nanaa katikati yao na kumfanya rafiki. Maisha yakazidi
kuleta ladha kwa Nanaa. Marafiki waliomfanya acheke wakati wote na mpenzi Zac!
Hakuna jinsi ungemwambia Nanaa amekosea maisha au alizaliwa kwa bahati mbaya,
akakubali.
************************************************
Evan alipokuwa akija kwa
Tia hapo chuoni, alikutana na Zena na Nanaa. Utundu mwingi, maneno yasiyoisha
na stori nyingi vuliwavutia hata rafiki wa Evan pia. Wakikosekana kina dada hao
kati yao, lazima wauliziwe ndipo kikao kinanoga. Evan alikuwa akifika chuoni
hapo na gari la baba yake akiwa na rafiki zake. Basi kitawekwa kikao mahali.
Watacheka mpaka wanaagana au wakati mwingine aliwatoa wote watatu na kwenda
kukutana na marafiki zake huko club. Starehe zinaendelea.
Mwanzoni Nanaa
alijitahidi kutolemea upande mmoja. Lakini akajikuta upande wa Zac unaanza
kupendelewa zaidi kadiri siku zilivyozidi kwenda na penzi lilivyozidi kuwa
zito. Ikawa ikimlazimu wakati mwingi wa weekend, ambapo alizoea kuwepo na kina
Tia na Zena, kuwepo Mabibo hosteli ambako alikuwa akiishi Zac mpenzi huyo mpya.
Walipokuwa
wakimlalamikia, alijitahidi kutoka nao japo kwa masaa machache na kurudi kwa
Zac. Ikitokea wamechelewa kutoka kwenye starehe, Nanaa na Zena watarudishwa
hosteli. Siku inayofuata kama bado ni weeked, basi Zena atarudi kwa mama Hiza,
Nanaa kwa kaka yake au kwa Zac. Wakati Tia akitumia siku hizo, mchana na usiku
na Evan. Maisha yakaendelea.
Wakati mwingine watatu
hao walipochoka na kusoma, walikwenda kwa Mama Hiza kwenda kucheka. Wakazoeleka
nyumbani kwa kina Zena. Na kila walipokuwa wakiondoka mama Hiza, mjuzi wa
vitafunio hakuacha kuwatengenezea vitu kadhaa vya kurudi navyo chuoni.
Walimpenda mama huyo kwa stori nyingi na vichekesho. Wakati mwingine wa weekend
kabla hawajatawanyika, walimpigia simu kujua kama yupo nyumbani au la. Basi
akiwaambia yupo, wote wataingia kwenye gari mpaka Tankibovu, nyumbani kwa kina
Zena. Kwenda kumsalimia mama huyo, japo kwa dakika chache tu ndipo Nanaa aende
kwa kaka yake au Zac. Tia aende kwa Evan au alale hapo hapo na Zena mpaka
jumapili usiku.
Basi hapo mama Hiza
atawasimulia habari za mtaa mzima. Nani kaachika, nani kafumaniwa, nani
anamuhisi mchawi wake. Nani anayejidai anaswali sana lakini mmbeya. Habari zote
za mtaani hapo atawasimulia kina Zena mpaka watakapo ondoka. Na alikuwa na
uwezo mkubwa sana wakusimulia. Hata jambo likiwa dogo kwa namna gani, lakini
mama huyo atalikuza kwa kadiri ya muda wao. Atalisimulia jambo hilo kwa mbwembwe
zote, nakuwafanya wacheke mpaka watoe machozi. Na wakati wote mumewe hubaki
kimya akimsikiliza na kumtizama kama yuko karibu nao. Maisha yakawa mazuri na
yakupendeza.
************************************************
Wakati wanakaribia kumaliza mwaka, wakiwa
wanakaribia mitihani, Nanaa kumaliza mwaka wa kwanza, Zac kumalizia mwaka wake
wa tatu na wa mwisho chuoni hapo, Nanaa kama kawaida yake, alifika nyumbani kwa
James siku ya ijumaa baada ya mtihani wake uliokuwa umemlaza macho. Alimsaidia
kusafisha na kumpikia kama kawaida huku akimsubiri kaka yake arudi kutoka
kazini. James alirudi nyumbani kutokea kazini akidhani Nanaa atalala siku hiyo,
lakini kumbe alifika tu kuaga.
“Hivi nimekuja kukuona na kukuaga, kaka yangu. Mitihani imekaribia.
Baada ya siku 8 tu, tunaanza mitihani ya kufunga mwaka. Hutaniona kwa majuma
matatu na siku kadhaa. Nataka nikatulie kabisa chuoni. Ila nikimaliza tu
mitihani, nitarudi hapa nyumbani.” “Si leo ulale? Nitakupeleka kuona movie.”
“Acha nijikaze kaka yangu. Nikimaliza mitihani tutazurula wote mpaka uchoke
wewe.” James akacheka, Nanaa akachukua mkoba wake na kutoka.
************************************************
Nia ya Nanaa haikuwa
kurudi hostel kusoma kama alivyomuaga kaka yake. Ilikuwa kwenda kumsurprise
mpenzi wake Zac aliyekuwa akimtegemea siku inayofuata ya jumamosi. Walikubaliana
kutoka pale hostel na kwenda kujifungia mahali. Wakatumie siku ya jumamosi na
jumapili pamoja kabla hawajaingia kipindi hicho kigumu cha mitihani ambacho
alijua itakuwa ngumu kuonana mara kwa mara. Nanaa alikwenda mpaka hostel za Mabibo
ambako alikuwa akiishi Zac, bila hata kumtaarifu mpenzi wake kuwa anakwenda siku
hiyo si kesho yake kama walivyokuwa wamekubaliana.
Nia alitaka kumfurahisha
kwani siku iliyopita alimbembeleza sana Nanaa, waanze mapumziko yao siku hiyo
ya ijumaa, lakini Nanaa akakataa akimwambia ana mtihani mmoja siku hiyo ya
ijumaa mchana na angekuwa na vipindi mfululizo mpaka usiku, kwa hiyo atakuwa
amechoka sana. Akamuomba mpenzi wake aliyekuwa amemwambia anahamu naye sana,
amvumilie mpaka kesho yake ili apumzike usiku huo. Wakikutana awe na nguvu. Kwa
shingo upande Zac akakubali. Lakini baada ya mtihani huo wa mchana, maprofesa
wa vipindi vya jioni wakaahirisha vipindi. Ndipo Nanaa akaonelea aende kwa kaka
yake. Amsaidie kazi na kwenda kumsuprise mpenzi wake. Waanze mapumziko mapema.
************************************************
Zac alikuwa na rafiki
mfanyakazi. Bachela, aliyekuwa akiishi peke yake kwenye nyumba yake hiyo
Makongo juu. Mara nyingi aliwaachia chumba kimoja watumie hapo hapo nyumbani
kwake kila walipohitaji. Kwa hiyo weekend hiyo, Nanaa na Zac walipanga kuwepo
huko.
************************************************
Alishuka kwenye daladala
na lengo la kuelekea moja kwa moja chumbani kwa Zac na rafiki yake akiwa
amejawa furaha zote akimfikiria vile Zac atakavyofurahi kumuona usiku huo wala
si kesho yake. Wakati anakaribia jengo ambalo lina chumba chao akakutana na
rafiki yake Zac ambaye anaishi naye chumba kimoja, Felix. Wakasalimiana na
Felix na kutaniana kidogo, kisha wakaongozana moja kwa moja chumbani kwao huku
wakiongea na kucheka.
Walipofika mlango wa
chumbani kwao, wakasikia mziki mkubwa ndani. Kitu ambacho si kawaida yao. “Jamaa katoka nini? Maana namjua Zac,
hapendi kelele.” Felix aliongea huku akifungua mlango. “Labla aliacha radio wazi kukuashiria yupo maeneo ya karibu.” Nanaa
aliongeza huku akiwa na shauku ya mlango ufunguliwe waangalie ndani. Na
alijiambia yupo tayari kusubiri kama Zac hatakuwepo. “Atakuwa ameenda kufuata chakula hapo Cafe.” Felix Akaongeza baada
ya kufanikiwa kufungua mlango na funguo na kuchomoa funguo mlangoni ili waingie
ndani.
Alipomaliza kuchomoa
funguo, wakaingia ndani bila hata kugonga wakijua kwa kelele zile, Zac asiyependa
kelele, hawezi kuwepo ndani. Wote walibaki wameduwaa mara baada ya kuingia na
kumkuta Zac na msichana mwingine
aliyekuwa kwenye kundi moja la kujisomea na Zac wapo kitandani, uchi na wao
wakiwashangaa.
************************************************
Huyo msichana hakuwa
mgeni kwa Nanaa. Walifahamiana na Nanaa. Nanaa alimfahamu kwa jina moja tu la
Ndina. Mara nyingi Nanaa alimkuta na Zac na marafiki zao wengine wakijisomea
pamoja. Kama hawakuwa maktaba pamoja, basi chini ya mdigrii wakisoma. Hata mara
nyingine aliwakuta cafeteria wakila pamoja mara baada ya lectures au wakiwa wamemaliza kujisomea.
Zac hakuwahi kusita
kumbusu Nanaa mbele yake huyo dada na marafiki zake wengine. Walishawazoea na
kuwaelewa. Kwani mara nyingine Nanaa alipowakuta mahali wakisoma, Zac
alitengeneza nafasi pembeni yake, nakumtaka Nanaa akae hapo akimsubiria wakati
wao wanamalizia kusoma. Basi hapo Zac ataendelea kusoma na wenzake huku
amemkumbatia Nanaa. Mara nyingine alimtupia mabusu ya hapa na pale. Ilimradi
tu, kuonyesha mapenzi kwa Nanaa. Na kundi lao zima walimfahamu Nanaa kuwa ni wa
Zac rafiki yao. Kwa hiyo hata alipokuwa akimkuta Zac na Ndina peke yao,
haikumsumbua kwani waliheshimiana sana.
Ndina alikuwa msichana wa
kawaida sana ukimlinganisha na Nanaa. Hakuwa na vitu vya ajabu ambavyo mtu au
hasa wanaume wengi wa kiafrika wanaweza kuvitaja na kuvisifia kama jinsi Nanaa
alivyo. Mara nyingi Nanaa alipokutana naye mara baada ya salamu, hapakuwa na
maongezi mengi. Kwani Zac alimtawala Nanaa wakati wote.
************************************************
Nanaa alibaki ametoa
macho huku maswali mengi aliyotamani kuuliza yakibakia kupiga kelele ndani yake
bila mtu wa pembeni yake kusikia. Ndina alishavuta shuka pembeni yake akajifunika
nakubaki kimya. Felix yeye aliweza kusogelea radio iliyokuwa na mziki mkubwa,
kelele nyingi zaidi pale ndani, akaizima. Nanaa alimwangalia wakati akisogelea
radio. Chuki ikamwingia. “Inamaana hata Felix alikuwa akijua? Mbona
haonekani kushtuka ila kusikitika tu?” Nanaa akaanza kujisikia vibaya,
akijihisi ni mjinga mbele ya kundi zima lakina Zac. Swali la kuwa aliyeingilia
mapenzi ya mwenzake, likaanza kukosa jibu kwa Nanaa. Ni yeye au Ndina?
“Nilijua
wewe ni wangu Zac!” Ndilo neno pekee aliloweza kutoka mdomoni
mwa Nanaa. Aliongea kwa masikitiko makubwa kutoka moyoni. Zac alijua historia
ya Nanaa na Alex. Vile alivyomsaliti. Akamuahidi kumuenzi na kumpa mapenzi ya
kweli. Hakutaka kuendelea kujidhalilisha pale mbele yao, akaamua kutoka.
************************************************
Haikuwa mara ya kwanza
kwa Nanaa kumsaprizi Zac. Lakini lilikuwa ni jambo ambalo hata Zac alikuwa
akilitegemea hasa siku za ijumaa. Alijua wazi Nanaa huwa anakwenda kwenye
chumba hicho kumsubiria endapo atachelewa kurudi hapo Mabibo hostel. Naye Zac
hakuwa akichelewa. Kila ijumaa baada ya vipindi, aliwahi kurudi hostel akijua
aidha atamkuta Nanaa au atamsubiri. Mara nyingi walitumia usiku wa ijumaa
pamoja. Kisha siku ya jumamosi, Nanaa alikuwa akirudi kwa kaka yake kama
kawaida.
Kwa kuwa nyumbani kwa
kina Felix ilikuwa hapo hapo jijini, basi mara nyingi walijikuta wapo peke yao
hapo chumbani. Basi siku hizo za Ijumaa walikuwa wakizitumia chumbani hapo,
kitanda hicho hicho alichomkuta Ndina yupo uchi usiku huo aliomkatalia yeye Zac
na kumwambia atakuwa amechoka mpaka kesho yake ndipo wakajifungie Makongo juu
kwa rafiki yake mwingine Zac, ambapo walikuwa wakipata uhuru wote.
************************************************
Nanaa alitoka hapo asijue
ni kama alimfumania Zac na Ndina, au alibahatika kujua ukweli. Hakujua kama amekamatwa
na wivu au aibu. Chuki au amejidhalilisha. Kila alipojifananisha na Ndina, bado
alijiona ni bora kuliko yeye. Mawazo yakampeleka vile anavyojituma kitandani
kumridhisha Zac, “na bado analala na Ndina!? Kwa..” Nanaa akataka kujinyeshea mvua ya maswali,
lakini akasikia sauti ya Zac ikimwita kwa mbali kama anayemkimbiza.
Kwa haraka sana alijionya
hata asisimame. Akaongeza mwendo akielekea zilipo daladala, barabarani bila
hata kugeuka. Kumbe baada ya kutoka tu pale chumbani, ni kama akili ikamrudia
Zac waliokuwa kimya pale kitandani na Ndina. Felix aligeuka na kuendelea na
shuguli zake pale pale chumbani. Wala hakutoka kuwapa nafasi. Akavuta suruali
yake. Akavaa kwa haraka na kuanza kumkimbiza Nanaa bila shati. Kifua kikiwa
wazi kabisa.
Alimuona Nanaa akiongeza
mwendo kwa mbali kukiwa na giza tayari. Aliendelea kumkimbiza bila viatu mpaka
kituo cha daladala akiomba msamaha na kusema ni bahati mbaya. Lakini Nanaa
hakujibu kitu. Akapanda ndani ya
daladala huku akikumbuka vile alivyosalitiwa na Alex pia, daladala iliondoka, Zac
akiwa amepiga magoti nje ya daladala hiyo akiomba Nanaa ashuke ili wazungumze.
Hakumjibu kitu, alibaki ameinama nakushindwa hata kumwangalia Zac nje ya
dirisha. Wasafiri wengine walibaki wakichungulia dirishani wakishangazwa na Zac.
************************************************
Hazikuwa siku nyingi
zilizopita tokea Nanaa na Zac wawe na wakati mzuri wa pamoja. Ilikuwa weekend
iliyopita tu, pale James alipomwambia Nanaa amsindikize au warudi wote nyumbani,
mkoani Kilimanjaro, Moshi, kusalimia wazazi. Nanaa akamkatalia kaka yake na
kumsihi sana aende yeye mwenyewe, yeye atakuja kurudi kwa mama yake mkubwa
wakati mwingine.
Kwa kuwa ilikuwa katikati
ya muhula, James akaonelea ni sawa kumuacha. Asimlazimishe na kuishia kuchanganywa
na mama yake mara baada ya kufika huko kwao. Nanaa akashindwa shule. James
alisafiri yeye mwenyewe. Aliondoka siku hiyo ya Jumamosi alfajiri sana. Nanaa
akampigia simu Zac na kumuelezea kila kitu. Zac akamuomba wakutane Makongo juu
kwa rafiki yake, kwa kuwa Felix alikuwepo pale hosteli. Hakwenda kwao. Kwa kuwa
James alikuwa akirudi siku ya jumatatu, Nanaa aliondoka hapo nyumbani siku ya
jumamosi asubuhi na kwenda kujifungia na Zac mpaka siku ya jumatatu ndipo
alipotoka hapo na kwenda kwenye kipindi kilichokuwa kikianza saa nne asubuhi.
************************************************
Nanaa aliondoka, lakini
akiwa ameumia kupita alivyowahi kuumizwa kabla. Moyo ulikuwa unauma kama
umechomwa mkuki. “Mbona alionekana kuridhishwa na penzi langu. Wakati wote aliniambia
mimi ni mzuri kitandani. Anapenda jinsi ninavyomfanyia kitandani. Na umbo langu
linazidi kumsisimua kila nikiwa mtupu mbele zake.” Nanaa aliendelea
kuwaza hapo ndani ya hiyo daladala asijue ashuke wapi! Arudi kwa kaka yake au
hostel.
************************************************
Nini kitaendelea kwa Nanaa?
Usikose Sehemu ya 4.

0 comments: