Story
is mine - ni Wangu! Part 1, Sehemu ya 4.
"...ni Wangu!"
Sehemu ya 4.
Kilichokuwa kikimuumiza
Nanaa ni vile alivyokuwa amejitoa kwa Zac. Alikuwa muaminifu sana kwake. Hata
rafiki wa Evan, Terry aliyekuwa akisoma IFM alipokuwa akimtongaza Nanaa,
alikataa kata kata, huku akijigamba anaye mpenzi. Alimwambia Terry kuwa si
kwamba anaye tu mpenzi, bali mume. Nanaa alijisifia siku hiyo mbele ya kundi
hilo walipokuwa wamekwenda beach ya Kigamboni, kupumzika. “Nampenda Zac. Na yeye ananipenda kwa dhati. Sijaona wala hakuna
mwanaume kama Zac.” Nanaa alijisifu mbele ya marafiki hao wakiume wa Evan.
Wote walimsikiliza na kufunga kinywa wakijua ule ujumbe ulitoka kwa Nanaa ukiwa
hauna hila, ila ulimuumiza sana Terry.
****************************************
Terry mtoto wa mama.
Rafiki wa karibu sana na Evan. Watoto wa jiji. Lakini walicheza kwa tahadhari.
Wakilindana wasije wakapitiliza starehe, wakawaumiza wazazi wao. Wote walitoka
kwenye familia zenye hali nzuri inayoenda kwenye nzuri sana. Wazazi wasomi.
Baba yake Evan alikuwa daktari katika hospitali kubwa ya Muhimbili, wakati baba
yake Terry alikuwa daktari katika hospitali binafsi waliyokuwa wameanzisha yeye
na marafiki zake. Wote walitoka kwenye familia ambazo hazikuwa zikilia shida.
Wazazi wanaoamini katika professinals, na wao walikuwa wasomi. Kwa hiyo hata
watoto wao walijua elimu ndio kila kitu. Hawakuzidisha starehe na kusahau shule
hata kidogo.
****************************************
Tokea mara ya kwanza Tia
anamtambulisha Nanaa kwenye kundi hilo. Yeye akiwa mgeni. Kwani Zena na Tia
walishawahi kutoka nao mara kadhaa kabla ya Nanaa. Walisha alikwa kwenye
shuguli mbali mbali za wadogo zao huko majumbani kwao. Iwe ni communion ya
kwanza au kipaimara cha mmoja wa wadogo zao kwenye kundi hilo la kina Evan, Tia
na Zena pia walialikwa. Kwa hiyo walijikuta wanafahamiana na wote kwenye kundi
hilo kabla ya Nanaa kujiunga nao, lakini Terry hakuonyesha hata uhitaji wa
mwanamke mpaka alipokuja Nanaa.
Ilikuwa ni birthday ya
mmpenzi wake Tia, Evan ndipo Nanaa alipokwenda na yeye. Walianzia nyumbani kwa
kina Evan. Walikuwa ndugu, jamaa na marafiki wakaribu wa wasomi hao, wazazi wa
wakina Tery na Evan. Walikula na kunywa. Lakini Nanaa akaona jambo la pekee na
ndipo akaja kuelewa baadaye, ni kwa nini kina Evan na Terry, japokuwa ni watoto
wenye uwezo wa kujitosheleza majumbani kwao, lakini bado wamebaki kuwa ni
vijana wenye kiasi. Kabla ya kukata keki, wazee hao na wake zao, pamoja na
ndugu. Walimtaka Evan aelezee alipo, anapofikiria kwenda. Changamoto
anazokabiliana nazo kwa wakati huo. Ni hatua gani amechukua mpaka hapo. Na nini
anampango wa kufanyia kazi. Basi hapo ndipo ataulizwa maswali na kuomba ashauri
wenzake. Na kuelezea makosa aliyoyafanya, na kushauri wasipite alikopita yeye
au wasifanye kosa kama alilofanya yeye.
Nanaa aliona ni kitu cha
ajabu jinsi wazee hao wanavyofanya kwa vijana wao, lakini akavutiwa sana. Walikuwa
ni wakina baba wa makamu, na walionekana wasomi tu. Wake zao hivyo hivyo. Lugha
ya kingereza ndiyo iliyokuwa ikitumika kati yao. Hata watoto wadogo kabisa
walikuwa wakitumia lugha hiyo kuashiria wote wanasoma kwenye shule za maana na
kingereza kwao sio lugha ya kujidaia. Ndio lugha ya mawasiliano kati yao.
Terry alimganda sana
Nanaa jioni hiyo. Alimfuata kila mahali na kutaka azungumze naye. Nanaa aliamua
amuwahi mapema kabla hawajaagana. “Ninaye
mpenzi wangu. Anaitwa Zac. Anamaliza chuo mwaka huu. Tunampango wa kuoana.”
Terry alitabasamu. “Nilitaka
kukukaribisha kwenye birthday yangu na mimi jumamosi ijayo.” “Mmmh! Ningependa
kuja, lakini kuanzia ijumaa nitakuwa na Zac. Weekend hii nimeshindwa kwenda,
kwahiyo weekend ijayo lazima tuwe wote.” Nanaa alikataa kwa kujitetea. “Haitakuwa siku nzima. Ni jumamosi jioni.
Ukiweza kufika, nitafurahi kukuona Nanaa.” “Naomba nisikuahidi Terry. Huwa
nikiwa na Zac, hapendi niende mahali. Nakuwa naye mpaka jumapili jioni.
Nashukuru kwa mwaliko lakini.” Nanaa alitoa tabasamu na kuondoka.
****************************************
Terry alikuwa mwaka wa
pili kwenye chuo cha IFM. Ulishapita mwaka, tokea asalitiwe na mpenzi wake.
Akaapa hatapenda tena. Lakini hata wenzake waliona tofauti pale alipotokea
Nanaa. Alikuwa akihangaika kupita walivyomzoea. Evan alimshauri awe muwazi kwa
Nanaa, kuliko vile anavyojifanya kuwa katuni mbele za marafiki zake kila
anapomuona Nanaa.
****************************************
Siku ya birthday yake
ilikuwa mbaya zaidi, kwani Nanaa mpaka sherehe inaisha, Nanaa hakuwa ametokea.
Alitoka na kwenda kukaa nje, nyuma ya nyumba yao. Wakati wenzake wakifurahia
ndani, wakila na kucheza Terry alikuwa nje mpaka watu wote wakatawanyika pale
ndani nyumbani kwao. Hawakuwa wamemuona Terry. Alijichukia kumpenda msichana
ambaye kwanza alikuwa mgeni kwake. Hamfahamu. Pili tayari anajua yupo na mpenzi
wake. Tena mwanaume anayetarajia kumuoa. Hicho ndicho kilimuuma zaidi. Lakini
alishindwa kujisaidia. Anampenda Nanaa.
****************************************
Kidogo wivu ukaanza kwa
Zena ambaye aliona anamstahili Terry. Kwanza yeye kama ndiye wakwanza aliyemfahamu
Terry kabla yake. Kila walipokuwa wakikutana kwenye kundi hilo ambalo Tia ndiye
alimkaribisha na kukutana na kina kaka hao. Palikuwepo na mazungumzo ya pamoja.
Ukweli hapakuwepo na mazungumzo binafsi kati ya Zena na Terry. Japo Zena
alishaonyesha kumpenda sana Terry. Kwanza alijua ni yeye peke yake kwenye kundi
lile ambaye hana msichana. Halafu ni Terry jamani! Nani asimpende?
Analishwa na kutuzwa vizuri na mama yake. Hana
mawazo ya kufikiria pesa, kama watu wengi. Mtoto wa mama. Hawezi kutoka
nyumbani mpaka mama yake ahakikishe amekula na ananguo safi. Akitoka mama akiwa
kazini, basi atapigiwa simu kuulizwa. Na pengine kuambiwa apitie ofisini kwa
mama, akachukue pesa za matumizi. Gari anayotembelea ni ya nyumbani. Hajui hata
kama huwa inafanyiwa matengenezo. Hilo lilikuwa jukumu la dad au mama.
Kwa nini usimpende Terry?
Ngozi nzuri. Anaongea lugha ya kingereza na tabasamu zuri usoni. Akionyesha ametulia.
Hana shida ya kumnunulia mtu yeyote zawadi kutoka kwenye pesa ya ziada
anayopewa nyumbani. Hawazi kutaliwa nini, wala kulipa garama yeyote. Ni yeye
tu. Kila ijumaa anarudi nyumbani na nguo chafu za juma nzima. Zinafuliwa na
kupigwa pasi ndipo zirudi tena hosteli. Shida hamna. Ila sasa ni mapenzi. Alisalitiwa,
akampenda Nanaa mchumba wa mtu, ambaye anamuumiza moyo wake.
Zena alia wivu.
Wivu ulimsumbua Zena
kwani alishamwambia Tia na Nanaa juu ya hisia zake kwa Terry. Hasira ilimpanda zaidi pale alipowakuta
Nanaa na Terry wakizungumza na kucheka upande wa baa wakati wote wamekaa
baharini walipokuwa Kigamboni juma moja baada ya birthday ya Terry. Nanaa
alitoka upande wa baharini akiwaaga anakwenda maliwatoni. Baada ya muda kidogo,
Zena akamuona Terry na yeye amesimama
anaondoka kuelekea upande aliokwenda Nanaa. Akajua wazi anayemfuata ni Nanaa.
Kwani Terry alionyesha wazi kuvutiwa na Nanaa. Hakuacha kumuuliza maswali mbele
yao na kuchangia chochote Nanaa anachozungumza.
Wakati Nanaa anatoka
chooni, akamuona Terry. Alimfanyia ishara ya kumwita, Nanaa akamfuata pale
alipomkuta amekaa upande wa baa kama anaagiza vinywaji. Kwa kuwa Terry
alimwalika kwenye birthday yake na hakwenda, Nanaa akaona huo ndio wakati
mwafaka wakuomba radhi na kuuliza mambo yalikwendaje siku hiyo. Akiwa hajui
jinsi alivyomuumiza Terry, Nanaa aliongea kama jambo la kawaida huku akitaka
michapo ya siku hiyo.
Wakiwa kwenye mazungumzo,
hata hawajafika mbali, Zena naye akawasogelea.
Akiwa hajui hili wala kile kinachoendelea si kwa Zena tu ambaye ni
rafiki kipenzi, hata Terry pia. Nanaa akatoa ahadi isiyo na hatia. “Basi
kwa malipizi, itabidi nikutoe kwa chakula cha mchana. Tusherehekee birthday
yako. Nitakuletea zawadi. Ili ujue sikuwa nimekusudia kukosa birthday yako.”
Nanaa aliongea huku akicheka. “Nilishamwambia ilikuwa ni weekend ya Zac.
Ulikuwa kwa mpenzi wako.” Zena aliongeza. “Afadhali
unitetee Zena shoga yangu. Terry anajua nilikimbia.”
Nanaa aliongeza.
“Tusirudi
nyuma, tukaharibu ahadi ya kunitoa.” Terry aliongeza. Nanaa
akacheka. “Hilo tu? Usijali. Nakutafutia
siku yako maalumu.” Nanaa akaongeza akijua ni utani kabisa, akacheka na
kuondoka. Aliwaacha pale Zena na Terry. Wala asijue walirudi baada ya muda gani
pale kwenye kundi. Asijue kama Zena alirudi akiwa na furaha au la. Kwa kuwa
muda ulikuwa umeshakwenda, hata Zena alipowaambia Tia na Nanaa waondoke, Nanaa
hakuona kuna jambo la ajabu. Walishakula. Wakaongea na kucheka. Ilishakuwa
jioni. Akaona sawa waondoke. Asijue kinachoendelea.
****************************************
Halikuwa kosa la Nanaa. Kwani
wakati Zena anawaambia jinsi anavyompenda Terry, wakiwa chumbani kwao. Kila
mmoja kitandani kwake, yeye Nanaa alikuwa aki chat na Zac. Ukweli alikuwepo
pale, lakini mawazo hayakuwepo pale hata kidogo. Alikuwa akipata jumbe za
mapenzi kutoka kwa Zac. Akisifia penzi alilompa kabla hawajaagana siku hiyo ya
jumapili. Zac alimwambia alifurahishwa na hiki na kile, ilimradi tu
kumfurahisha Nanaa. Kwa hiyo akili ya Nanaa ikawa imezama kwenye simu yake
akifurahia zile jumbe, huku akifikiria na yeye maneno mazuri ya mapenzi ya
kurudisha kwa Zac wakati Zena akiendelea na yeye kueleza hisia zake kwa Terry.
Hata hakuwa akiwasikiliza Tia na Zena. Kwanza alijua ni mazungumzo yao binafsi
marafiki hao aliowakuta. Na yeye alikuwa amechoshwa na mapenzi ya kuanzia
ijumaa usiku mpaka jumapili hiyo anarudi hosteli.
****************************************
Siku hiyo walipotoka Kigamboni,
Terry na Evan ndio waliokuwa wakiwarudisha hosteli kwa gari. Nanaa aliomba
ashushwe kwa kaka yake, mtaa wa Kijitonyama. Karibu sana na Usalama wa Taifa, badala ya hosteli. Yeye Zena alipelekwa mpaka
kwenye kituo cha daladala karibia na kwao. Asingethubutu kuonekana kwao
anarudishwa na wanaume. Wakati wote wakijua Tia atabaki na Evan kama kawaida
yao mpaka siku inayofuata ya jumapili. Evan akirudi chuoni SUA, mjini Morogoro
ndipo Tia anarudi hosteli.
Wakati Nanaa anashuka, aliwaaga
kwa kicheko asijue kinachoendelea. Aliwaacha Zena, Tia, Terry na Evan kwenye
gari. Mazungumzo yote ndani ya gari baada ya kushuka Nanaa, ilikuwa Terry
akifurahia ahadi yakutolewa na Nanaa. Hata Tia aliumia sana. Asiamini Nanaa anawezaje
kumfanyia hivyo Zena. Tena baada ya kuwaambia wazi vile anavyojisikia kwa
Terry. Halafu tayari Nanaa alikuwa na mpenzi wake Zac!
Tia akaona vile Zena
alivyoumia, akamwambia Evan waonane kesho ili yeye awe na Zena usiku huo. Akaamua
akalale na shoga yake nyumbani kwao, ili amfariji. Evan hakuwa na tatizo. Akawashusha
kituoni, na hapo ndipo wakapata nafasi ya kumsema vizuri Nanaa. “Tabia
yake mbaya.” Zena
alianza kutupa shutuma. “Hatosheki na wanaume!” Tia
akamuunga mkono shoga yake Zena. “Amesahau sisi ndio tumemtambulisha kwao?
Ametawala kundi zima sasa hivi, utafikiri yeye ndio mwenyeji wetu jamani!”
Zena alilalama. “Hukumuona vile alivyokuwa akijishaua
kwa Terry. Niliwakuta peke yao kule upande wa baa. Nanaa akijinadi.”
Mashoga hao waliongea mapungufu yote ya Nanaa, wakakubaliana kumtema tu.
Mkakati wa jumatatu kumtoa kwenye urafiki
rasmi ukapangwa wakiwa hapo hapo kwenye kituo cha daladala cha Tangibovu karibu
sana na kwa kina Zena. Wakaadhimia kufuta kabisa urafiki na wala wasiongozane
naye popote ili inapofika siku ya kukutana na kundi la kina Evan, Nanaa asiwepo.
Baada ya kuafikiana na mikakati yao juu ya Nanaa ambaye gafla amekuwa adui,
ndipo wakaelekea nyumbani kwa kina Zena ambako ni kama kwa kina Tia pia. Kwa
kuwa wazazi wa Tia walishakuja kumkabidhi Tia rasmi hapo kwa wazazi wa Zena,
basi Tia hakumuhitaji Zena kufika kwa mama Hiza. Akawa ameshazoeleka pale
nyumbani. Urafiki wa wazazi uliokuwa unaelekea kwenye undugu kati ya familia
hizo mbili ukawa umeshakomaa.
****************************************
Akiwa hajui lolote Nanaa alirudi
hosteli siku inayofuata ya jumapili akiwa na tabasamu lake lote. Akawakuta Tia
na Zena chumbani kwao. Akaona wote wamenuna. Nanaa akaanza kuwatizama kwa zamu
na kucheka. “Mbona kama mmeninunia? Nimefanyaje
tena!?” Nanaa aliwauliza huku akiwatizama kwa zamu. Ndipo
Zena alipomjibu kwa jazba vile walivyokerwa na tabia yake yakutaka kumpora
Terry wake. Wakashangaa Nanaa anacheka sana. Wakatulia kidogo.
“Unacheka nini sasa? Unafikiri mazuri?”
Zena aliuliza akiwa amepunguza jazba. “Kumbe unamtaka Terry?”
Nanaa aliuliza huku anacheka. “Kumbe?”
Zena alijibu. “Aiii! Mimi sina hata shida
naye. Wewe tafuta neno baya lolote la kunichafua kwa huyo Terry, halafu mwambie
unampenda.” Wakaangaliana. “Kweli?” “Sasa mimi wa nini huyo Terry?
Zac mwenyewe ananishinda. Terry nitamuweka wapi mimi na ratiba ngumu ya Zac?
Ijumaa mpaka jumapili ananitaka kitandani mpaka nimkimbie weekend nyingine
sababu ya kaka.” Tia na Zena wakajiweka sawa.
“Tena kukusaidia tu Zena, mimi niache
kuja kwenye mikusanyiko yenu kwa muda. Akishajiona mpo naye tu, lazima
atakuchangamkia. Kwanza unalipa shoga yangu.” Roho ilisuuzika.
Zena akaanza kucheka. “Sasa kwa nini hukuniambia
tokea mwanzo? Mimi hata sikuwa na wazo. Kwanza mbona nilishamwambia Terry kuwa
ninaye Zac?” “Niliwaambia.” “Basi mimi hata sikuwa na wazo. Labda akili yangu
haikuwepo. Sasa mlipanga kuninunia mpaka lini!?” Nanaa aliuliza kwa
kuwasuta. “Wala hatukuwa tumekununia.” “Mmmh! Aibu zenu wanawake.” Vicheko
na mikakati yakumpata Terry ikaendelea jioni hiyo mpaka wakaamua kutoka na
kwenda kujisomea.
Nanaa baada ya kusalitiwa kwa
mara ya Pili.
Alitoka pale Mabibo
hosteli moyo na mwili ukiwa kama umekufa ganzi. Asielewe anatatizo gani. Kama uzuri,
alisifiwa mpaka na wanawake wenzake. Kwa hakika Ndina haoni ndani. “Nilijua Zac ni wangu!” Nanaa
aliendelea kuwaza. Mapenzi aliyokuwa akionyeshwa na Zac, kwa hakika Nanaa
alijua amefika. Sifa zilizokuwa zikimwagiwa kwake, kuanzia umbile na mambo wanayofanya
pamoja, hakuwahi hata kuhisi kama Zac anaweza kugusa mwanamke mwingine. Faraja
aliyokuwa akimpa! Mbele za watu alimkumbatia na kumbusu. Ni kama alikuwa
akitangazia uma wote, kuwa Nanaa ni wake.Anarudishaje sura yake kwa watu
waliokuwa wakiyajua mapenzi yale? Anaishije tena bila penzi zito la Zac?
Zikiwa zimebaki siku
chache za mitihani, Nanaa akijaribu kujifikiria hatima yake kimapenzi, alishindwa
kusoma kabisa. Kila akiinamia vitabu, badala yakuona maandishi, macho yalimuona
Zac na Ndina pale kitandani. Akaamua awekeze muda mwingi wakujisomea kwenye
makundi ya wenzake wanao soma pamoja. Lakini pia haikusaidia. Mawazo yaligoma
kuwepo pale. Yalisambaa kwenye jumbe za mapenzi alizokuwa akitumiwa na Zac.
Simu za kutakiwa usiku mwema kila siku na maneno matamu kutoka kwa Zac. Si
asubuhi si mchana, Zac aliwasiliana naye. Hata akiwa kwenye vipindi, aliweza
kumtumia ujumbe Nanaa kuwa anamfikiria yeye. Leo anaishije bila hayo maisha
matamu yaliyokuwa yamejaa faraja?Mitihani yakumaliza mwaka wa kwanza
ilimalizika kwa shida mno. Matokeo yalitoka lakini yalikuwa mabaya sana kwa
Nanaa. Alifeli masomo mawili nakutakiwa kuyarudia. Na yale masomo aliyokuwa
amefaulu ni kama alikuwa kwenye mstari wa kufeli kabisa. Yote alipata alama ya “C”.
****************************************
Shule ambayo aliapa kuwa mkombozi wake ipo matatizoni. Ndoa
a
nazolilia kumtoa kwenye wegazi, hazionekani kutoa matokeo
mazuri kwa Nanaa.
Nini kitaendelea?
Usikose Sehemu ya 5.
0 comments: