Story

is mine - ni Wangu! Part 1 {Sehemu ya 23}.

Friday, August 24, 2018 naomimwakanyamale 3 Comments


L
iz akasimama pale kwa muda kama anashangaa ule mkao. Nanaa akaingiwa na hofu mpaka Geb akajua. Kabla hajatoa neno kinywani mwake na kumuumiza Nanaa, Geb akamuwahi. “Karibu.” “Nakaa wapi hapo?” Akauliza kishari na dharau, nakutaka kupitiliza chumbani kwa Geb kuonyesha hawezi kukaa sehemu moja na Nanaa au wale aliowakuta pale, labda na Geb tu. Tena chumbani kwake.

“Nashauri huko usiingie!” Geb akamuwahi kabla hajapotelea upande wa vyumbani, Liz akasimama. “Unasemaje!?” “Nimesema, sishauri uingie huko chumbani kwangu.” Geb akarudia. “Kwa nini?” “Kwa sababu mimi nimesema hivyo.” Palizuka ukimya mkubwa. Ni tv tu ambayo Danny alikuwa akiangalia na kufuatilia kwa sauti ya chini ndiyo ilisikika. Kana kwamba hapakuwa na mtu hapo sebleni. Kimyaa. Hata Liz alipigwa na butwaa kwa muda.
Kisha akajikaza, akaendelea. “Maana yake nini?” Liz akauliza tena. “Hamna maana nyingine isipokuwa hiyo tu. Sidhani kama huko nisehemu salama kwako na vitu vyako vya thamani. Vinaweza kupotea wakati wowote ule. Hii nyumba haiishi wageni, na Fili naye ndio naona anazidi utundu. Anaingia kila chumba siku hizi. Sitaki uingie huko, upoteze vitu vyako, uanzishe kelele nyingine zitakazo haribu amani ya humu ndani.” Kila mtu alimshangaa Geb, aliyezoeleka kuwa ni mkimya na mvumilivu anaongea siku hiyo. 
Liz akabaki amesimama. “Karibu hapa kwenye makochi.” Geb akaendelea kwa sauti iliyotulia tu kana kwamba hamna baya linaloendelea. Kumbe anatoa maamuzi mazito ambayo hata mama yake alitamani kumuona akiyafanya kwa muda mrefu sana. Liz akamwangalia mmoja baada ya mwingine, akajiweka sawa. “Naomba twende chumbani tukazungumze.” Liz akarudia. “Sio chumbani kwangu. Kama unataka kuzungumza na mimi karibu ukae hapa kwenye makochi, tuongee.” “Ni mazungumzo yanayotuhusu mimi na wewe, sitaki watu wengine wasikie.” Liz akaongeza. “Basi tutoke nje.” Geb akasimama.
“Kwa nini tusizungumzie chumbani?” Msichana huyo aliyezoea kuzungumza na watu kutekeleza popote tena kwa haraka, akaendelea kusisitiza. “Liz! Najua you are very smart. Huhitaji mimi nirudie jambo mara mbili. Kama kweli unataka kuzungumza na mimi, tutoke nje. Lakini si vinginevyo.” “Kwa maana nyingine ni kwamba hutaki kuniona tena chumbani kwako?” Geb akabaki akimwangalia. “Geb?” Liz akamwita akitaka ajibu swali lake. “Tunaweza kuzungumza hapo nje?” Geb akamuomba kistaarabu. “Kuna mbu.” “Nyumba yangu haina mbu. Na imetoka kupulizwa dawa hata siku tano hazijaisha. Hata hivyo, hatutatoka nje kabisa. Tunakaa hapo barazani kulipozungushiwa vioo na wavu. Hamna mbu. Ukiona kuna mbu, tutahamia kwenye gari.” “Yote hayo ni kunifukuza chumbani kwako?” Geb hakujibu tena, akatoka nje, Liz akamfuata.

*************************************************
“Mbona sikuelewi wewe Geb!?” Walimsikia Liz akiuliza kwa ukali. “Uliza jambo lolote nitakusaidia kukuelewesha.” Geb akasikika akiwa ametulia. “Kwa nini hutaki niingie chumbani kwako?” “Nimekupa sababu, Liz. Kama hujaridhika nayo, basi hiyo ni kitu kingine. Lakini nilisha kujibu.” “Unamaanisha nini?” “Hata hilo swali pia nilishakujibu.” “Naulizia juu ya mahusiano yetu ndio yanakuwaje?” “Unakumbuka masharti uliyokuwa umenipa mara ya mwisho tulipokuwa wote Marangu? Na ukasema bila hivyo, wewe huwezi kuendelea na mimi. Unakumbuka?” Liz akanyamaza.
*************************************************
Nanaa akanyanyuka kimya kimya akaenda chumbani kwake. “Jamani usiku mwema. Na mimi naenda kupumzika.” Mama G, naye akaaga. Akasimama. “Usiku mwema mama.”  “Na wewe Danny mwanangu.” “Nakuja chumbani kwako mama. Ngoja nikamlaze mtoto kwanza.” Grace naye akasimama. “Ukitoka chumbani kwa mama, uniambie basi nije tulale.” Danny akamuwahi mkewe. “Sawa.” Grace akaingia chumbani kwake, wakamuacha pale Danny peke yake akiwasikiliza Geb na Liz wakiongea hapo nje.
“Nanaa mikononi kwa Geb.”
Nanaa alipanda kitandani, akashangaa kitu kimemshika kooni. Machozi yakaanza kumtoka. Aliendelea kulia taratibu huku ameficha uso kwenye mto, wala asijue ni nini kinachomliza. Baada ya muda mfupi tu akasikia mlango unafunguliwa bila hodi. Geb akaenda kukaa kitandani kwake. “Hivi yameshapita masaa mangapi tokea uniahidi utakuwa mlinzi wangu, tena!?” Akamgeuza vizuri, Nanaa. Akaweka kichwa cha Nanaa kwenye mapaja yake. “Eti Nanaa?” Nanaa akajifunika uso na kuendelea kulia huku amemlalia Geb. “Sasa kama mlinzi wangu unakimbia, nani ananilinda tena?” Geb akauliza kwa utulivu, huku akimtoa mikono usoni na kumpangusa machozi. 
“Eti Nanaa? Yaani mlinzi unakimbia! Unafungua mlango, unaacha mali yako nje, wewe unakuja kujificha ndani!” Akaendelea kumpangusa machozi. “Itabidi mlinzi wangu nimpeleke chuoni kwanza. Ukafundishwe ujasiri, kujiamini, na upandiwe roho ya umiliki. Lazivyo nimeshaona sipo salama kabisa.” “Sijui mipaka yangu Geb.” Nanaa akajibu kwa upole huku akilia. 
“Unapolinda mali yako, kunakuwa na mipaka kweli?” Geb akainama na kumbusu midomo yake. Mwili mzima wa Nanaa ulipatwa na msisimko. Geb alikuwa akifikisha ujumbe au jibu ambalo Nanaa alilisubiri kwa muda mrefu sana. Kwa wivu:- kila anapomuona Liz anaingia pale ndani na kulala na Geb usiku kucha au labda mchana tu. Au anapoweza kumtawala Geb. Au Geb anapomuweka yeye Liz mbele, na yeye kumlazimu kusubiri. Kwa uvumilivu :- bila kujali hisia zake. Akimuhudumia Geb bila kuchoka, hata kama Liz yupo amelala kitandani kwa Geb hapo hapo. Bado Nanaa aliweza kuvumilia maumivu, akamuhudumia Geb. Akitaka asirudi kulala bila kula kwenye kitanda anachojua yupo Liz kwa wakati huo, anamsubiria Geb. Bado Nanaa alivumilia huku akiumizwa na wivu.
Akamtoa pale kwenye mapaja yake, akamkumbati vizuri kiwili wili chake, akamnyanyua juu kidogo, na kundelea kumbusu taratibu. Nanaa alikunja miguu vizuri, kama kujiweka sawa asiharibu au kukatisha lile busu. Alinyonya midomo ya Nanaa taratibu bila haraka, huku amemkumbatia. Machozi ya furaha yalikuwa yakimtoka Nanaa, akatamani Geb asimuachie. Zilikuwa hisia za namna yake. Furaha aliyokuwa akijisikia, hakuna jinsi angeeleza mtu akamuelewa. Geb alimrudisha mapajani kwake, akabaki akimwangalia kwa macho yake mazuri na matulivu. Nanaa akabaki aking’ata midomo yake huku akijaribu kukwepesha macho. 
Geb akamfuta machozi tena. “Niliogopa, Geb.” “Hutakiwi kuogopa. Jipe muda, kila kitu kitakuwa sawa.” “Unafikiri hivyo?” Nanaa akauliza kwa upole huku akikubali kuyaangalia macho ya Geb yaliyoweza kuyeyusha chochote kinachomkera rohoni, nakumfanya aseme ‘ndiyo’ hata sehemu aliyokusudia na kupanga kusema ‘hapana’. “Nina uhakika.” Geb akajibu, akainama na kuendelea kumbusu. Alimbusu kwa muda mrefu sana bila kuchoka.
 Alinyonya midomo yake ya nje kwa zamu na taratibu, huku akitaka Nanaa amwachie anyonye ulimi. Mwanzoni Nanaa hakuwa ameelewa. Geb aliendelea kutafuta huo ulimi mpaka akaupata. Alitoa pumzi ya kufurahia na kuupokea. Akaanza kunyonya ulimi wa Nanaa taratibu huku amemkumbatia. Alifanya utundu usioendana na muonekano wake wa nje hata kidogo. Nanaa hakuwahi kupata mabusu ya namna ile. Geb hakuonyesha haraka kwa kile anachokifanya. Alionekana ametulia na akifurahia anachokifanya. Mara kadhaa alimuachia na kumtizama kidogo, kisha akarudia kumbusu. Kama asiyeamini kama amemshika yeye Nanaa.
Baada ya muda akamrudisha kwenye mto. “Asante.” Nanaa akashukuru huku amejawa tabasamu la aibu na furaha machoni, akitamani aendelee. Alishalitamani hilo busu mpaka akalikatia tamaa. Akajua hatawahi kulipata kamwe maishani. Aandike maumivu. Geb akabaki akimwangalia kwa utulivu. Kama aliyeamkwa na hamu mpya. Akainama tena pale kwenye mto, akabusu midomo yake mara kadhaa. Kisha akamuachia.
“Naenda kumuangalia mama, halafu nakuja kukuchukua tukale. Usilale bila kula.” “Bado nimeshiba.” “Basi nitakuletea kitu kidogo ule, wakati mimi namalizia uji wangu.” “Na mimi nitamalizia kukutoa mwiba.” Geb akatabasamu, akainama na kumpa busu moja la mdomoni, akanyanyuka nakutoka. 
***************************************
Baada ya muda, akarudi tena. Walikaa kitandani kwa Nanaa, wakiwa wamekumbatiana na kuendelea kupeana mabusu bila kuridhika. Walimaliza na kuanza upya. Kila alipomuachia Nanaa, alihisi kama bado kidogo, au kuna kitu amesahau, alimsogeza na kuanza tena kumbusu. Alirudia tena na tena, bila kuchoka kama mtu aliyekuwa na kiu naye, kitu kilichomshangaza Nanaa. Aliona vile ilivyokuwa ngumu kwake kumuachia. Naye Nanaa akatulia kabisa. Hakuruhusu hata akili zake zimuwaze Liz. Akajiambia atajua baada ya hapo. “Acha nifurahie kidogo. Sina chakupoteza kwa mwanaume ninayempenda. Sasa hivi ni zamu yangu. Mengine yatajijibu baadaye.” Nanaa akazidi kupotelea mikononi mwa Geb huku akitoa mihemo laini yakumuashiria Geb kufurahia.
***************************************
Nanaa akakumbuka anatakiwa kazini kesho yake siku ya jumamosi. Alipoweka tu kituo na kutoka midomoni mwake na kumwangalia. Akarusha swali kwa haraka kabla hawajaendelea. “Kesho tunaenda kazini saa ngapi?” Nanaa akauliza. Geb akafikiria kidogo. Akaangalia saa yake ya mkononi. “Nitategesha alarm yakuniamsha saa tatu na nusu asubuhi.” Geb akajibu na kuendelea. “Naomba kesho na wewe ulale. Tutakuwa na siku ndefu sana. Usihangaike kuamka asubuhi kwa ajili ya kupika.” Nanaa akatabasamu. “Huwa usingizi unaniishia mapema. Lakini kama nitachoka katikati ya siku, nikirudi nyumbani kutoka kazini basi nitakuja kulala. Kama leo. Nimeweza kulala mchana.” “Kesho usiku nataka tutoke.” Nanaa akatoa macho akahisi hajaelewa au hajasikia vizuri.
“Unamaanisha tutoke mimi na wewe au na watu wote?” Nanaa akauliza na wasiwasi usoni. “Kuna mahali nataka nikutoe usiku. Ni hoteli nzuri. Na wanakuwa na vyakula vizuri sana. Nataka uvae upendeze.” Nanaa akainama na kujifunika macho asiamini. Geb alijua analia kwa furaha. Akamkumbatia. “Naamini tutakuwa na wakati mzuri.” “Asante sana Geb. Nakushukuru.” “Hata mimi nakushukuru Nanaa. Najua umenivumilia sana. Asante kwa kuendelea kunisubiria.” Wakatulia kwa muda kila mmoja akiwaza lake. Nanaa mikononi mwa Geb akichezea mkono wake taratibu. Aliupapasa huku akiwaza.  Mara kadhaa Geb aliinama na kumbusu huku akimpapasa bila kuvuka mipaka, nakurudi kufikiria na yeye.
“Ngoja nikuache upumzike.” Geb akamuaga. “Usiku mwema.” Nanaa akajibu kwa sauti ya chini iliyotulia na tabasamu huku akimwangalia Geb. Geb akamgeuza vizuri. Akaweka mto sawa na kumrudisha kwenye ule mto. Kama aliyetamani kumuachia lakini bado kuna kitu akahisi hajamaliza sawa sawa. Geb akainama tena. Akamtengeneza vizuri nywele zake huku akimtizama kwa uchu. Akainama na kuanza kumbusu tena. Safari hii hakuchukua muda mrefu. Kama aliyejionya kuwa na kiasi. Akajizuia asifike asikoweza kurudi kwani Nanaa alishatoa mihemo iliyoamsha hisia zote za mapenzi. Geb akamuachia na kumbusu mara kadhaa juu ya midomo yake, kisha akaondoka huku na yeye akiwa na hali mbaya Zaidi.
 Nanaa alibaki pale kitandani asiamini kama amepata mabusu mazito vile. Akabaki akijishika midomo yake huku akicheka. “Oooh Myyyy!” Nanaa alichekelea. “Geb Magesa amenibusu Nanaa mimi!” Nanaa alibaki akichekelea pale kitandani asiamini. “Anajua kubusu, si mchezo! Hii mpya na ngeni.” Nanaa akaendelea kufurahia. Kila akikumbuka ametoka kukumbatiwa na kupata mabusu mazito vile, alicheka na kutamani Geb arudi tena, waanze. Akachukia kutengana na Geb kwa usiku ule.
Kidogo heshima iliongezeka kwa Geb, kwa kumuacha usiku ule. Hata Nanaa alijua anaumbile ambalo wanaume wengi walitamani kumuweka kitandani akiwa mtupu. Na waliofanikiwa kumuweka kitandani, wote alikuwa akiwaona wanavyochanganyikiwa baada yakumuona kitandani wakiwa faraghani. Hakuna aliyewahi kumbusu tu, tena wakiwa kitandani, akaacha kufanya naye mapenzi. Wengine walikuwa wakikesha mwilini mwake na kumuacha na madonda wakitaka kukata kiu zao bila mafanikio. Walioanza na kumaliza, walitamani kuanza tena na tena kwenye mwili huo wa Nanaa. 

Nanaa akamshangaa Geb. “Kweli hana papara kwenye mambo yake.” Nanaa akawaza. “Sasa sijui ndio anamaanisha mimi ndio wake moja kwa moja!?” Nanaa akendelea kukumbuka maneno ya Geb. “Yaani Nanaa ammiliki Geb Magesa!” Akajicheka. “Ndio awe wangu kabisaaaa! Mimi Nanaa mtoto wa Win! Kweli!?” Maswali mengi na hofu vikaanza kuibuka kwa Nanaa. “Kesho ananitoa 'outing'!  'As a date!?'.”  Bado Nanaa hakuwa anaamini.
********************************************

Geb kasimama kiume. Nanaa ameanza kufutwa machozi kwa staili yake. Haamini kama amepata busu kutoka kwa Geb. Liz alitoa masharti gani? Utakubali Nanaa kumpokonya penzi? Endelea kufuatilia.

3 comments: