Story
alipoanza kupambazuka tu, usingizi ulimwisha Nanaa. Bado ilikuwa mapema sana. Asijue kama ni furaha au la. Ni kweli alishazoea kuamka mapema, lakini akashangaa asubuhi hii akawahi zaidi. Akafikiria kidogo pale kitandani. Akakumbuka mabusu aliyoyapata usiku uliopita. Akacheka huku akishika midomo yake. “Kama ndoto vile!” Nanaa akacheka akiwa peke yake pale kitandani. Akawaza hili na lile mwishoe akakumbuka inabidi aende kazini kufidia siku aliyokosa ya jana yake ijumaa.
is mine - ni Wangu! Part 1 {Sehemu ya 24}.
P
|
alipoanza kupambazuka tu, usingizi ulimwisha Nanaa. Bado ilikuwa mapema sana. Asijue kama ni furaha au la. Ni kweli alishazoea kuamka mapema, lakini akashangaa asubuhi hii akawahi zaidi. Akafikiria kidogo pale kitandani. Akakumbuka mabusu aliyoyapata usiku uliopita. Akacheka huku akishika midomo yake. “Kama ndoto vile!” Nanaa akacheka akiwa peke yake pale kitandani. Akawaza hili na lile mwishoe akakumbuka inabidi aende kazini kufidia siku aliyokosa ya jana yake ijumaa.
Akaelekea jikoni kuanza kutengeneza kifungua kinywa. Siku ya
jumamosi huwa wanachelewa kuamka. Kwa hiyo Nanaa akaamua awatengenezee ‘brunch’
ya nguvu. Kulikuwa na maini kwenye friji ambayo hayakuwa yamepikwa. Akayatoa.
Baada ya kuyakatia kitunguu swaumu na kitunguu maji, akayabandika jikoni na
kuacha yakijipika. Akaanza kutengeneza chapati haraka haraka huku akifikiria
kitu gani kingine chakupika. Akatengeneza na njegere. Alikuwa na mchanganyiko
wa nyama ya kusaga aliokuwa amebakisha siku chache wakati anapika sambusa.
Akafunga sambusa kama 20 tu kwa haraka. Kwa kuwa alijua Fili na baba yake
wanapenda sana sambusa. Akaziacha baada ya kufunga ili zikauke kwa nje kidogo.
Akatengeneza unga wa dengu. Kidogo tu kwenye kibakuli. Akajua atapata bajia
zakutosha, kwa kuwa bajia zina mtindo wa kutuna. Mpaka inafika saa tatu
asubuhi, Nanaa alikuwa amejaza meza kwa vyakula vidogo vidogo tena vya hamu.
Akarudi chumbani kwake kuoga. Akawa amekaa tu kitandani
akisubiria. Saa 4 asubuhi kila mtu akawa ameamka. Vilijaa vicheko pale mezani.
Danny akishangilia vitafunio. Akapiga picha kila kitu pale mezani, akatuma kwenye
kundi lao la Whatsapp. Watu wakaanza kutuma jumbe zao kwenye kundi hilo. ‘Mko hotel gani, kaka?’ ‘Mbona mapema
kaka?’ ‘Sherehe kama hizo huwa hatuachani Danny.’
Grace alikuwa anasoma zile jumbe huku wanacheka wote, kwani na yeye alikuwa
kwenye hilo kundi. ‘Tupo
nyumbani kwetu. Nanaa kapageuza hotel. Na hatutaki wageni.’ ‘Tumetoka mbali
sana bwana Danny.’ Danny akawajibu. ‘Kuleni makwenu jamani! Leo jumamosi nataka kupumzika na mke wangu.
Msitujalie huku kwetu. Tulieni.’ ‘Lazima mama atatoa exception kwa bwana
harusi. Kwanza nina shida naye.’ Malii aliendelea. ‘Mama hayupo. Nipo mimi na Grace tu.’ Simu zikaanza kwa mama G. Aliposema tu yupo nyumbani. Kila
mtu alitaka kufika hapo nyumbani. Mama G akawakaribisha.
Geb na yeye alikuwa mmoja kwenye hilo kundi. Alipoona wote
wanakaribishana nyumbani kwake. Akamwambia Nanaa waondoke haraka kabla
hawajawakuta pale. Lasivyo hawataweza tena kutoka. Nanaa akachukua pochi yake.
Geb akachukua uji wake wakatoka. Baada ya lisaa limoja, tayari nyumba ya Geb
ikawa imejaa. Kila mmoja ananjaa. Anataka chakula kwa mama G.
***********************************************
“Naomba nikupe kazi moja. Lakini kuna masharti.” Geb alianzisha hayo mazungumzo wakati wanaelekea kazini siku
hiyo ya jumamosi. Nanaa akacheka kidogo akamwangalia. “Mmh!” “Nataka
ufikirie na uandike chini, kitu chochote. Namaanisha kitu chochote, ambacho
unatamani kuwa nacho. Nikimaanisha mahitaji yako binafsi. Kuanzia asubuhi
unapotoka kitandani mpaka unapoenda kulala. Kila kitu. Nataka ufikirie sasa
hivi. Halafu tukifika kazini uandike wakati mimi nafanya kazi za jana. Andika
kila kitu. Iwe mswaki, nguo za ndani, nguo za kuvaa kazini, nguo za kulalia,
pochi, hereni, chochote. Sio lazima ukanionyesha. Labda utake mwenyewe. Lakini
naomba andika kila kitu. Usiache kitu chochote. Mimi nitakuwa dereva wako leo.
Unaweza kuvigawa kwenye mafungu. Ukasema kama leo ni nguo za ndani tu.
Nitakupeleka kwenye hayo maduka. Ukanunue vile utakavyo, mimi nitalipia. Kama
muda hautatosha, kesho tutaenda kwengine. Hivyo hivyo mpaka tumalize.”
Nanaa akainama akifikiria.
Geb akamuona amekosa raha badala yakufurahia. “Umenielewa
lakini?” “Sina kitu ninachotaka uninunulie Geb.” “Unanidanganya Nanaa. Mimi
mwenyewe nina vitu nataka kununua. Sema naona uvivu kuzunguka madukani au
sijipi muda. Na ninakumbuka uliniambia James anakuwa na majukumu mengi. Wakati
mwingine unakuwa na shida, unashindwa hata kumwambia matatizo yako. Sasa nataka
uniambie mimi.” Nanaa akakumbuka ni kweli alimwambia wakati wa safari ya
Bagamoyo.
“Kwa hiyo naomba usinidanganye Nanaa. Labda uniambie
hutaki.” “Sio kuwa sitaki Geb. Sitaki tena nigeuke kuwa mzigo kwako. Yaani uone
ni kama una mradi fulani wa kuufanyia kazi. Nakushukuru kwa hilo, lakini
nimechoka kusaidiwa. Acha nitajinunulia tu mwenyewe.” “Kwa hiyo unayo mahitaji?” Nanaa akanyamaza.
“Labda niulize hivi. Ni lini unampango wa kuyatimiza hayo
mahitaji yako?” “Sijui Geb. Nikipata pesa. Sasa
hivi kipaumbele ni kukusanya pesa kwa kadiri ya uwezo wangu. Ili niweze
kujikimu baadaye. Najua navaa nguo za kawaida sana. Tena nanunua kwenye ile
mitumba ya bei ya chini sana. Sinaga nguo za kulalia. Sio kwamba sijui kama
kuna nguo maalumu za kulalia. Najua zipo. Naweza kuvaa nguo za ndani miaka na
miaka. Sio kwamba sijui natakiwa kubadilisha kila baada ya muda mfupi. Nafahamu
Geb. Najua kama kuna aina nzuri za nguo za ndani. Najua watu wanavaa za ma
‘designer’. Na ninawafahamu. Lakini mimi sijafika huko. Naogopa hata kuwaza
huko kwa sasa. Sitaki kujiwekea mahitaji yakuja kuniumiza mimi mwenyewe
baadaye. Nina mahitaji ya msingi kuliko kufikiria kununua nguo za kulalia
wakati naweza kununua tshet ninayoweza kuvaa darasani na pia nikalalia usiku.
Sijui umenielewa? Naomba huko tusiende Geb. Ni papana, na parefu mno. Naogopa
hata mimi mwenyewe kupaangalia.” Geb akamtizama na kunyamaza.
Walifika kazini. Geb akaegesha gari yake. Wakashuka. Walinzi
walikuja kumsalimia. Nanaa akataka kuondoka kama kuwapisha, Geb akamuwahi kwa
kumshika mkono. “Nisubiri twende wote.” Kisha akamvuta karibu yake na
kuanza kumbusu, mbele ya wale walinzi. Nanaa alifurahia sana japo aliogopa. Geb
ni mmiliki wa lile eneo. Na nikijana anayeheshimika sana pale. Inakuaje leo
kumbusu hadharani mbele ya wafanyakazi wake? Hakuwahi hata kumuona akimbusu Liz
kwa muda mrefu vile mbele za watu. Kwanza hakuwahi kumuona akimfanyia Liz vile
mbele ya wafanyakazi wake. Alimuona akipewa busu na Liz, tena juu ya mdomo tu. Lakini
yeye alimshika kiuno na kumvutia karibu yake na kumbusu bila haraka. Akamuachia,
na kumwangalia kidogo. Akaendelea kuzungumza na wale walinzi. Akaagana nao.
“Twende nikaangalie huko stoo. Nataka kuzungumza na yule
kiongozi wa mambo ya stoo.” “Leo jumamosi Geb.” Nanaa akamkumbusha. “Nilimwambia aje leo. Kuna uzembe
mwingi unafanyika na yeye akionekana yupo kwenye payroll ya wafanyakazi. Sasa
nataka kujua kama huwa anakuwepo kwenye majukumu yake? Na ni mlalamishi sana.
Grace huwa hamuwezi.” Wakaongozana mpaka stoo ndogo tu waliyokuwa nayo ya
hapo hapo ofisini, akiwa amemshika mkono Nanaa.
Walimkuta akiwasubiri. Alikuwa mtu mzima kidogo. Mkubwa hata
kwa Geb mwenyewe. Alikuwa na kijana mwengine anayefanya kazi hizo hizo za stoo,
wote wawili walikuwa wakimsubiria Geb. Wakakaa naye chini. Yule kiongozi
alikuwa na maneno mengi sana. Wote pale kazini walimjua ni mbishi na jeuri.
Lakini Nanaa alishangaa vile Geb alivyokuwa akizungumza naye kwa kumuuliza
maswali ya papo hapo mpaka akaishiwa maneno. Akakubali kosa.
Kulikuwa na uwizi unaendelea kati yao. Na yeye ndiye aliyekuwa
akituma madereva kudanganya. Anakuwa akikubaliana na madereva pindi
wanaposhusha mzigo kuandikisha hata robo ya lori kuwa mazao hasa matunda
yalifika yameharibika, yeye anayapakia kwenye gari yake aina ya pickup ndogo na
kwenda kuwauzia wateja hao hao wa Geb, lakini sehemu nyingine.
Geb aliambiwa na wateja wake kuwa meneja wake anawauzia
mzigo kwa siri. Ndipo akazungumza naye. Baada ya kuzungumza naye kwa muda mrefu
akibisha. Geb alimpigia simu mmoja wa wateja wake, akakiri kuuziwa naye
matikiti jana yake usiku. Nanaa akashangaa sana. “Ni yale ya jana
tuliyoyapakia Bagamoyo!?” Nanaa akauliza kwa mshangao. Geb akacheka. “Ona
hasara mliyoandika tuliyoingia kwenye yale matikiti. Lakini huyu dereva mpya
alinipigia simu jana jioni kuniambia mnaniibia sana. Yeye hawezi kukubali kosa
la kuharibu mzigo njiani wakati anasema alifikisha mzigo wote salama. Tena
aliwaonya na kuwaambia msidanganye kwa kuwa mimi mwenyewe nilihusika katika
upakiaji. Na tukahakikisha yamekaa vizuri hakuna yatakayoharibika. Mkamwambia
yeye anakazi ya kuyafikisha tu hapa. Basi. Mambo mengine awaachie
nyinyi.” Wakanyamaza.
Nanaa aliumia sana. Akamuhurumia Geb. Alimuona vile
alivyoteseka jana yake kule mjini Bagamoyo. Kwanza alimka alfajiri. Akajinyima
usingizi wake. Akaenda kufanya kazi, si kusimamia. Alifanya kazi kwa makini
mpaka mwisho. “Wanawezaje kuiba kirahisi hivyo?” Nanaa
akajiuliza.
“Naomba tusifikishane mbali ndugu yangu. Mimi nitakwenda
kukusanya pesa yote huko nilikouza hayo matunda. Nitakurudishia. Tamaa ndiyo
iliniingia. Haitatokea tena.”
Yule kiongozi wa stoo akakiri mwishoni. “Basi, pesa yote naomba mumkabidhi
muhasibu.” Geb akasimama. “Twende Nanaa.” Wakaondoka.
***********************************************
Geb alikuwa na godown kubwa tu alilokuwa akikodisha kutoka
kwa tajiri mmoja wa kihindi, maeneo ya Temeke, Kurasini. Hapo hapo
jijini. Ndipo alipokuwa akihifadhia bidhaa zake zote. Lakini ofisi ambazo
zilikuwa zikiendesha biashara hizo ambazo Grace ndio alikuwa akisimamia,
zilikuwa maeneo ya Fire kama ukielekea Kariakoo. Walipata na stoo kubwa tu,
iliyokuwa kama na cold room ili kufanya mazao yasiharibike. Hasa matunda.
Waliweka baadhi ya mazao waliyokuwa wakiuza kwa wateja wao wadogo wadogo pale
pale mjini. Kwa kuangalia uwekezaji wake tu, utajua ni kweli ni kijana mwenye
kufikiria. Hakurupuki.
***************************************************
Nanaa hakuamini. Akabaki akimtizama Geb. “Ndio basi?”
Geb akacheka. “Yaani huwafukuzi kazi! Unawasamehe!?” “Watu waaminifu ni
wachache sana Nanaa. Wengi wakiwa kwenye hizo nafasi, ni rahisi kushawishika.
Ataingia mwaminifu, baada ya muda huwa wanabadilika. Heri huyu nimeshajua
ni mwizi. Nimeshajua jinsi ya kumdhibiti. Kuliko kuanza na mwingine mpya.
Nitampunguzia majukumu. Na kuweka kamera hapo wanaposhusha mizigo. Screen yake
itakuwa ofisini kwa Grace tu. Kila mzigo utakapokuwa ukishishwa, Grace atapata
rikodi yake hata kesho yake. Kuanzia mazungumzo mpaka picha zenyewe. Nitaweka
hapa na kule kwenye godown ya kurasini. Basi.” Nanaa akamshangaa sana Geb.
“Una akili wewe! Hongera Geb.” Geb akafungua mlango wa ofisini ya
muhasibu.
Akamvutia Nanaa ndani. Akamkumbatia kwa nguvu kabisa. Karibu
naye, kisha akaanza kumbusu tena. Alimbusu taratibu kisha akaacha kumbusu,
akamwangalia akiwa bado mikononi mwake, tena karibu yake. Nanaa akacheka kwa
aibu. “Nimefurahi umenibusu pale nje. Mbele ya walinzi! Nimeona raha.”
Geb akacheka.
“Naomba usijifikirie kama wewe ni mzigo kwangu Nanaa. Najua
unahistoria ngumu sana ya maisha. Naomba fungua moyo wako kupokea vitu vipya.
Nilikwambia lazima ufungue moyo wako na ukubali kutambua na kupokea upendo
mpya. Usifananishe watu na matukio ya nyuma. Sikuchukulii na ninakuahidi,
sitakuchukulia wewe kama mradi wangu. Na mimi nitakuwa muwazi kwako.
Nitakapochoka, au nitakapoona jambo litakuwa gumu kwangu, naahidi kukwambia.” Geb aligusa hisia za Nanaa.
“Kweli?” Nanaa aliuliza huku akilia baada ya
kukumbuka masimango kwenye maisha yake. Ni James tu ndiye aliyembeba bila
kuchoka. Lakini sasa hivi mama yake ameanza kumsimangia misaada anayopewa na
James. “Nakuahidi hivyo, Nanaa. Chochote nitakachofanya kwako, ujue kipo
ndani ya uwezo wangu. Kwa hiyo usiogope. Sawa?” “Sawa.
Nakushukuru Geb.” Geb akambusu
tena.
“Basi naomba tuangalie pamoja kule ‘kurefu na kupana sana’. Kule unakoogopa kuangalia ukiwa peke
yako.” Nanaa akaanza kutokwa tena na
machozi, akiwa pale pale mikononi mwa Geb. “Naomba uandike kila kitu. Hata
kile unachoona ni cha kijinga sana. Hata kile unachoona ni cha garama sana.
Naomba uandike tafadhali.” “Ni vingi Geb.” “Basi
naomba uanze sasa hivi.” “Okay.” Geb akambusu tena kwa muda huku amemkumbatia kwa
kumvutia kwenye mwili wake. Kisha akamwachia. “Asante.” Nanaa akashukuru
akiwa ameshatulia na tabasamu usoni. “Karibu” Akamvutia kiti pembeni ya
kompyuta ya muhasibu alipojua atakuwa akifanya kazi. Wakakaa. Nanaa akaanza
kuandika.
***********************************************
Akamuona ameinama anaandika huku anacheka. “Unacheka
nini?” “Leo naenda kutupa vitu vingi sana vilivyokuwa vinanikera.” Geb
akacheka. Akakumbuka ni muda mrefu umepita hakuwa amebadilisha nguo zake za
ndani. Sidiria alizokuwa amenunua mtumbani alikuwa nazo zaidi ya miaka miwili.
Tena tatu tu. Na zote zilikuwa nyeusi. Alijitahidi kuzitunza kwa kadiri ya
uwezo wake. Chupi zilikuwa nyingi kidogo. Alizotenga kwa ajili ya kuvaa kipindi
cha hedhi, na siku za kawaida. Alikuwa nazo tatu alizotenga za kutokea. Nazo
zilikuwa ni za muda mrefu sana.
********************************************
Kwa asili yake hakuwa akichagua wanaume wenye pesa sana. Na
alikuwa muoga kuonyesha anatanguliza pesa. Alijitahidi kuwaonyesha wanaume wote
kuwa yeye ni mwanamke anayejua kubana matumizi. Na anafaa kuolewa na kuwekwa
ndani. Kwa hiyo hata wao walipata aghueni wakawa hawajisumbui hata kumpa pesa
za kujikimu. Zaidi ni pesa ndogo ndogo kama zakupandia daladala baada ya kulala
nae. Hakuna aliyekuwa akimfikiria yeye kama Nanaa. Walitumia mwili huo mzuri,
na kumuacha aende zake. Leo Geb anataka kubadili historia! Ilikuwa ngeni na
mpya kabisa kwa Nanaa.
********************************************
Akainua macho akamwangalia Geb. “Vipi?” Geb
akamgeukia. “Hata kama nataka kubadili mswaki niliokaa nao kwa muda mrefu,
pia niandike?” Nanaa akauliza akiwa hana uhakika. “Andika kila kitu
unachotaka.” Nanaa akacheka, akaendelea kuandika. Geb alimtizama kwa
kumuhurumia. Akamuona ametulia kama amesita. Anang’ata kalamu. “Hata hicho
unachosita kuandika, pia kiandike.” “Naona kama nimeandika vitu vingi sana,
inatosha Geb.” Nanaa akaonyesha wasiwasi. “Naomba andika Nanaa. Andika
tu.” Nanaa akavuta pumzi kwa nguvu. Akabaki akifikiria.
“Unajua body spay?”
Akamuuliza Geb. Geb akacheka. “Lakini haina ulazima.” Nanaa akainama. “Naomba uandike Nanaa.”
“Nahisi ni tamaa tu. Nilimuona rafiki yangu Tia, aliletewa na Evan mpenzi wake.
Nikapenda. Ila nitamaa tu. Nimeshaandika deodorant, inatosha. ” Geb
akavuta kile kijitabu alichokuwa akiandikia Nanaa, akaanza kuandika na yeye.
“Body spry, perfume, nguo za kutokea usiku, pochi
zake na viatu, Accessories, pochi ya kazini, pochi ya kanisani, pochi ya
kawaida, sandals, viatu vya kanisani, nguo za kanisani, nguo za kushindia,
na..” Geb akamkabidhi tena kile kijitabu kidogo na karatasi. “Vyote
hivi!?” Nanaa akashangaa. “Sasa kwani wewe ulikuwa ukiandika nini hapo?”
Nanaa akacheka. “Unataka nikusomee?” “Nisomee.” “Haya. Mswaki, dawa ya mswaki, sabuni ya kuogea, malapa,..”
Akamuona Geb anaanza kucheka. “Bwana usinicheke Geb!” “Nimekwambia andika
Nanaa. Kwa nini unanipa mahitaji ya vitu unavyoweza kupata dukani kwa Mangi?”
“Naona itakuwa garama sana.” Geb akamgeuza kwenye kile kiti chakuzunguka.
“Niangalie mimi Nanaa na unisikilize kwa makini. Ninafanya
kazi na nina biashara. Kwa sasa sina ndugu wala mtu anayenitegemea isipokuwa
wewe tu. Mama anabiashara zake, zinamwingizia pesa nzuri tu yakumtosha
mwenyewe. Grace na mume wake hivyo hivyo. Mimi sio kama James. Sina majukumu
mazito. Nataka wewe uwe na kila kitu unachokitaka. Kila kitu. Kwa mfano kuna
kipindi nilisoma kwenye kundi letu, James alituma ujumbe akiuliza kama kuna mtu
anayo laptop anayotaka kuuza. Nikasoma majibu na maswali ya watu wengine na
vile James alivyokuwa akijibu kuwa anatafuta laptop kwa bei nafuu, kwa ajili
yako.” Nanaa akainama.
“Aliweza kukupatia laptop?” “Nilimwambia aache, nikawa
natumia ya Zena. Majuzi akaniazima ya kwake ili nianze kuandikia ripoti.” “Sasa
mbona hapo kwenye kidaftari chako sioni?” “Laptop!?” Nanaa akashangaa kwa sauti. “Ndiyo. Si unahitaji?
Unafikiri utapataje sasa?” “Naona itaku..” Akanyamaza. Akainama na kuandika
huku anang’ata meno. “Nimeandika.” “Naomba uandike kila kitu Nanaa. Acha
woga.” Nanaa akainama nakuendelea kuandika tena mpaka akamaliza.
“Mimi nimeandika kila kitu. Haina maana nilazima uninunulie
au..” “Nanaa! Mimi ndio nimetaka mahitaji yako. Acha mimi ndio niamue. Sasa
unataka kunionyesha au unajua wapi pakuvipata nikusindikize?” “Naomba
nikuonyeshe ili unishauri.” Geb akavuta
kile kitabu. Akasoma mwanzo mpaka mwisho. Akamuona Geb anavigawa kwa makundi
mpaka akamaliza.
“Sasa hapa na mimi nimeshamaliza. Nilikuwa napitia pitia tu
kuona kazi za watu wengine. Kuna maduka maalumu unataka ukanunue hivi vitu?”
“Mwezio nguo zangu mpaka sidiria huwa nanunua mtumbani. Nikitaka nguo nzuri
yakutokea ndio naenda pale Magomeni kuna kaka mmoja namfahamu ndio ananiuzia
magauni mazuri ya mtumba, kwa bei nafuuu.” “Naomba leo tusiende huko.” Geb aliongea kiustarabu kidogo.
“Wanauza vitu kwa bei ya chini sana.” “Naelewa.
Lakini nitakupeleka sehemu nyingine. Tuanzie kwenye hili duka, nalifahamu. Linauza
nguo za ndani nzuri. Hata kama hufahamu saize yako, watakusaidia. Nina uhakika
mpaka utoke hapo, utakuwa umepata chupi, sidiria na nguo za kulalia za kutosha.
Lakini naomba nikuombe kitu kimoja Nanaa.” “Nini?” “Tafadhali usiangalie bei.
Halafu ukachukua kitu kimoja kimoja sababu ya uoga wa bei. Wewe chagua vitu
vya kutosha na utakavyopenda, halafu muachie yule muhudumu. Toka nje, mimi
nitaingia kulipia. Tafadhali sana. Sitaki tena tuje turudi huko kila baada ya
siku tatu. Mimi ni mvivu sana wa shopping. Nikinunua vitu huwa nanunua hata vya
miezi, ili nisirudi tena madukani. Ukifanya hivyo itanisaidia sana. Sawa?”
“Sawa.” Wakakubaliana na kutoka.
Mpaka inafika jioni wanarudi nyumbani, Nanaa alikuwa na robo
tatu ya mahitaji yake. Wote walirudi wakiwa wamechoka. Lakini Nanaa anafuraha
yakupitiliza. Alinunuliwa vitu vya thamani vitupu ambavyo hata hakuwa
amevifikiria.
********************************************
Akaingia chumbani kwake akaviweka vile vitu kitandani kwake
kisha akaenda kumwita mama G akiwa amefurahi sana. “Njoo nikuonyeshe vitu.”
“Ulivyofurahi!” “Njoo haraka.” “Geb yuko wapi?” “Nimemuacha kwenye gari
anaongea na simu. Njoo.” Akakuta amemwaga kila kitu kitandani. “Ona
mavitu yote hayo nimenunuliwa mwenzio.” Mama G akaanza kucheka huku
anasogelea kitanda cha Nanaa.
“Nimepelekwa kwenye maduka ya maana matupu mama. Ona.” Nanaa akaanza kunyanyua kimoja baada ya kingine.“Ujue mwenzio sijawahi kuvaa vitu kama hivi!”
Nanaa akaanza kulia. “Sijategemea mama.” “Usilie sasa. Wewe ukoje? Mwenzio amekununulia
ufurahi, halafu aje akute unalia!?” “Sijawahi pata
mtu ananijali hivi mama yangu.” “Kwa kuwa na wewe unamjali ndio maana.
Sasa mbona hizi chupi sizielewi!? Au sio chupi?” Nanaa akaanza kucheka. “Bwana mama!” “Aaah! Naona vimikanda tu. Unavaaje?”
Nanaa akazidi kucheka.
“Huku ndiko kutembea uchi huku! Sasa kwa nini usinunue chupi
nzuri, zinazokusitiri vizuri!?” “Angalia huo mfuko mwingine.” Mama G, akafungua. “Sasa hizi ndio chupi. Nguo za
kulalia nzuri. Kila kitu kizuri.” “Sasa fungua mfuko huo mwingine. Ni wako.”
“Wewe Nanaa vipi? Umepelekwa wewe, unaanza kununua vitu vya watu wengine!”
“Ukiona zawadi yenyewe utaacha kulalamika.” Alimnunulia Mama G nguo nzuri
mbili za kulalia. “Njoo kwanza nikukumbatie mwanangu. Nimependa kweli. Kwanza
nilikuwa nikiona uvivu tu kwenda madukani. Kila siku Grace ananizungusha. Mara
tutaenda kesho, mara leo jioni. Na mimi kuzunguka mwenyewe sipendi. Nakushukuru
sana.” Nanaa akacheka. “Umeona sasa? Kama nilijua.” Geb akaingia
akakuta Nanaa amekumbatiana na mama yake.
Waliongea watatu hao wakicheka chumbani hapo kwa Nanaa. “Kina
Grace wako wapi?” Geb akauliza. “Wameenda kuangalia nyumba yao.” “Sasa
kwa nini na wewe hukwenda!?” “Danny anataka kututoa kwenda kuangalia sinema
usiku. Kwa hiyo nikamwambia wao waende huko waniache mimi nipumzike mpaka
baadaye wakirudi, ndio nitaongozana nao huko sinema.” Mama G akamjibu
mwanae. “Lakini mimi na Nanaa tuna ratiba nyingine.” Geb akaongeza.
“Mnaenda wapi?” “Namtoa kwa chakula cha usiku.” Nanaa akacheka. “Muone
anavyofurahi.” Mama G akamgeukia Nanaa.
Usiku wa Nanaa na Geb.
Ilikuwa mida ya saa moja usiku wakati Nanaa na Geb wanatoka.
Mpaka Grace akataka kumpiga picha Nanaa. Alipendeza sana. Alikuwa amenunuliwa
na Geb, kigauni cha rangi ya damu ya mzee. Kigauni hicho kilikuwa kinafika juu
ya magoti kisha kimechanua vyakutosha tu kuanzia chini ya kiuno kilichokuwa
kimeshikiliwa na kiungio kama mkanda mweusi kwenye kiuno chembamba cha Nanaa.
Juu kilikuwa hakina mikono, ila kilipita kitambaa kimoja kama kola. Kikazunguka
shingoni na kuja kufunika matiti yake kwa mbele. Alinunuliwa kiatu cha sandals
cha juu kidogo. Rangi nyeusi.
Alivuta nywele zake zote juu kabisa akazizungusha katikati.
Alivaa hereni kubwa kidogo kwa kuwa hakuwa amevaa mkufu wowote. Akaweka lipstic
nzuri nyekundu aliyokuwa amenunuliwa mchana huo. Mkono wake wa kushoto
alivaa bango kubwa sana la dhahabu iliyofanana na hereni. Nanaa aliwaka. Kila
mtu alikuwa akimshangilia pale ndani.
“Kumbe mwanangu na wewe wamo!?” Nanaa akajificha uso. “Utajitoa sasa urembo. Acha
kujishika usoni. Muone!” Mama G akamuwahi. Geb alimpitisha sehemu akanunu
foundation waliyomjaribisha kwanza. Ikaendana na uso wake. Hakika Nanaa alikuwa
amependeza.
Geb akatoka amevaa jinsi nzuri nyeusi na t-shert ya maruni
kama Nanaa. Akavaa na blazer nyeusi. Nzuri sana. Akavaa sneakers za rangi ya kijivu,
zilizoendana na mkanda aliovaa wa hiyo jinsi. Hakuna aliyemuona Geb huyu.
Alikuwa ametulia, lakini usoni alionekana kuna tofauti. Alijawa furaha ya namna
yake. Kitu kidogo alicheka mpaka akatoa sauti. Alikuwa akinukia pafyum nzuri
sana ya kiume aina ya Creed. Ile harufu tu, ilisikika ni harufu ya pesa nyingi
iliyomwagwa pale.
“Yaani mmependeza mpaka raha. Zaidi amani nafuraha usoni
mwenu. Hivyo ndio vimeongeza mvuto.”
Grace akasifia. “Asante.” Nanaa akaitikia. “Lakini Nanaa
unapungukiwa kitu.” Geb akamtizama akaona yupo vizuri. “Nini tena?”
Geb akauliza. “Nyumba zima imejaa harufu nzuri ya Geb, lakini sio wewe.”
“Mwenzio sijuagi pafyumu.” Nanaa akanong’ona. Wote wakacheka.
“Geb amenipeleka leo kwenye maduka ya pafyumu. Nikasikia
kutapika.” “Walimpulizia harufu nyingi sana mpaka akashindwa kuchagua.” Geb alimtetea. “Basi njoo upulizie ya kwangu. Huwezi
kutoka hivi hivi.” Grace akanyanyuka kuelekea chumbani kwao. Nanaa
akamfuata. Geb akabaki akimsindikiza kwa macho. Kile kigauni kilichanua, lakini
hakikuacha kuonyesha umbile la Nanaa. Baaada ya muda wakatoka chumbani. “Nitakuletea
zawadi mama.” “Hapana Nanaa. Naomba ukatulize mawazo. Usiku wa leo ukajifikirie
wewe tu. Usianze kuwaza huku tutakula nini, au itakuaje. Katulie ufurahie. Na
sisi tutatoka sasa hivi. Tunamsubiria Fili aamke, tuondoke. Tutakula, na
tutakuwa na wakati mzuri tu.” Nanaa akacheka. “Asante mama yangu.”
Mama G, amrithisha mkoba Nanaa, bila
kujijua.
“Na mimi kuna kitu nataka kukupa. Ulikataa cha
Zinda, mimi mama yako huwezi kunikatalia.” Nanaa akacheka na kuuliza kwa
utani. “Unataka kunipa nyumba?” Wote wakacheka sana. “Nanaa wewe
mtundu sana.” Grace akadakia. “Nina sheni yangu nzuri sana ya dhahabu.
Dhahabu nzuri sana. Nimekaa nayo kwa muda mrefu sana nikiitunza. Inaweza kuwa
ina umri wa huyo Geb au zaidi kidogo. Nilikoitoa, nitakuja kukwambia siku
nyingine. Ila nataka uitunze sana.” Wakaona Nanaa analia.
“Yaani huyu bwana!”
Mama G akadakia. “Usilie sasa Nanaa. Furahia.” Grace akaongeza. “Basi
hapo ataondoa urembo wote. Ushamba tu!” Mama G akamfanya Nanaa acheke huku
analia. “Ona ulivyotoa wanja machoni! Ukoje bwana Nanaa!?” Mama G
aliendelea kuzungumza naye lakini Nanaa akaendelea kulia. Geb akamsogelea na
kumkumbatia pale pale mbele ya watu. “Nipe nimvalishe mimi au haiendani na
nguo aliyovaa?” Geb akauliza. “Mimi nataka
kuvaa sasa hivi. Sijawahi kuvaa dhahabu mwenzio.” Mpaka Danny
akacheka. “Basi itabidi tutafute na hereni zake. Usilie sasa.” Geb
akajaribu kumtuliza.
Mama G akaingia ndani na kwenda kumtolea hiyo cheni. Ilikuwa
imewekwa kwenye kiboksi kizuri sana na cha thamani. Nanaa akaipokea na
kuifungua huku Geb amemsimamia nyuma yake, amemkumbatia kiunoni. Ilikuwa nzuri
na nzito. Pana na imekerezwa maua mazuri yaliyochanganywa na maua yenye staili
ya moyo. Hakika ilikuwa nzuri. Nanaa akainama tena nakulia. “Ningejua wala
nisingekupa sasa hivi.” Mama G akaongeza.
Geb akaichukua na kuiweka shingoni mwa Nanaa. “Umependeza
sana.” Geb akamsifia. “Asante mama.” Geb akashukuru mama yake. “Karibu.”
Mama yake akajibu. Nanaa akenda kumkumbatia. “Nanaa wa dhahabu!” Mama G
akamchokoza. “Mbona nitalala nayo! Siivui mpaka
mwili wangu uzoee dhahabu.” Nanaa
akafanya wote wacheke. Akabaki anajiangalia.
“Haya nendeni sasa. Mungu awajalie muwe na wakati mzuri.” Wakatoka. “Umependeza sana Nanaa.” Walimsikia Geb
akimsifia. “Asante. Nakushukuru. Halafu na wewe umependeza. Unaonekana
ulipata muda mzuri wa kupumzika.” “Wewe hukulala?” Geb akamuuliza. “Nilikuwa
nahangaika kujipamba na kujaribisha vitu vyangu. Sijalala kwa furaha.” Wote
wakacheka.
************************************************
Mambo ya Nanaa yanazidi kunoga. Mama G,
ameonekana kutoa baraka zake zote kwake. Hakuna asiyempenda Nanaa pale ndani.
Yale aliyoyakataa kwa Zinda, anaanza kuyapata maradufu. Amani hiyo na furaha
vinadumu milele?
Usikose kuwa naye kujua anakopelekwa na
nini kitaendelea huko kwenye chakula cha usiku.
0 comments: