Nilipotea! Part 4 - Sehemu ya A
T |
ayari juma zima na siku kadhaa
ilishakatika tokea apatwe na huo mkasa. Kanisani hapaendeki, nyumbani
hapakaliki. Kula yake ilishakuwa ya shida, hakuwa akilala vizuri. Ilipofika
jumamosi alikuwa amedhoofu kwa njaa na hofu, alitamani asiende kazini, lakini
ilimbidi. Alikuwa na kazi kubwa inayomsubiri siku hiyo. Kupamba ukumbi wa
harusi ya mtoto wa balozi wa Tanzania nchini Uholanzi. Na alishalipwa nusu ya
pesa. Hata hivyo alihitaji sana pesa, ilikuwa lazima akafanye kazi. Alikumbuka
jinsi alivyohangaika kuianzisha ile biashara, hakutaka kurudi kwenye ule
umasikini wa zamani.
Alishtuka
saa kumi asubuhi akaamua kwenda tu ukumbini kuanza kupamba mara baada yakukosa
ujumbe kutoka kwa Net. Alishinda akipamba siku nzima, akitoka ukumbi mmoja
kwenda mwingine mpaka usiku sana ndipo aliporudi nyumbani.
Akaamua
kutuma ujumbe mwingine kwa Net. ‘Nimekosa Net, nimekosa
kukuficha kuwa niliwasiliana na Gabriel. Nisamehe. Lakini sikuwa na nia mbaya
mpenzi wangu. Sikutaka kuwachonganisha na Gab. Lakini nilimwambia kabisa kuwa
nimebadilika, nimemkataa, na nilimwambia kabisa nakupenda wewe. Nakupenda Net,
na nimejifunza kutokana na makosa, sitarudia kukuficha kitu tena. Naomba
nisamehe.’ Tunda alikaa pale akisubiri mwishowe akaona simu ya Mama
Penny inaingia.
“Mbona unalia na kanisani huji tena?” “Nimechanganyikiwa
dada yangu! Ghafla maisha yamenibadilikia. Net ameniacha na kanisani wananisema
vibaya sana. Nashindwa kurudisha sura yangu pale.” Tunda alikuwa akilia
sana. Tokea jumatano ya juma lililopita alipotoka katikati ya ‘bible study’
wale kina mama wakimsema kwa kujidai wanamuuliza maswali mchungaji, hakurudi
tena. Jumapili yake alimtumia ujumbe mama Penny kumwambia kuna kitu muhimu kule
gerezani kwa baba yake, lazima aende kumuona. Ni kweli alikwenda na mwanasheria
ili kuangalia hiyo afya ya baba yake atengenezee kesi. Jumatano kwenye kipindi
cha ‘bible study’ kanisani pia hakwenda. Akamtumia ujumbe kuwa ana kazi,
hatamaliza kwa wakati.
Sasa
jumamosi hiyo usiku ndipo mama Penny akampigia. “Wale
kina mama wa kanisani, Mchungaji aliniambia nimeshazungumza nao wote, wala
usiwe na wasiwasi. Umesikia?” Tunda aliendelea kulia tu. “Net amekuacha kivipi!?” “Nilikosea
dada. Net akajua kitu nilichofanya bila kumshirikisha. Amenikasirikia kuanzia
siku hiyo, hajanitafuta wala hajibu jumbe zangu. Na nilishamwambia sikuwa na
nia mbaya.” “Labda amesafiri ndio maana
anashindwa kupata na kujibu jumbe zako.” Mama Penny akajaribu kumtuliza.
“Simu ya Net
inapokea ujumbe wa yeyote, kutoka popote hapa ulimwenguni na yeye akiwa popote
hapa ulimwenguni. Muda na wakati wowote, dada. Ni ameamua kuniacha tu.” “Usilie bwana. Naamini anayo sababu tu. Unataka nije?” “Nimechoka sana dada yangu, siwezi hata kusogea.” “Lala basi, kesho nitakuja asubuhi kabla sijaenda kanisani.”
“Sawa.” Tunda akajivuta na kujilaza hapohapo
kitandani bila hata ya kuoga.
Jumapili.
Asubuhi na mapema, mama Penny alifika nyumbani kwa Tunda
kumuona kabla ya kwenda kanisani. Ikabidi Tunda amuelezee kila kitu bila
kumficha. “Nilikosea dada.” “Najua Tunda,
lakini huwezi kufa hapa na ukashindwa kuendelea na maisha. Tulia kabisa, mpe
muda kama alivyoomba. Kama ni wako, atarudi, kama sio wako basi. Naomba
ujiandae twende kanisani.” Alihakikisha Tunda amevaa vizuri, akampa kifungua
kinywa akamwambia aache gari yake yeye
atamuendesha. Kidogo Tunda akatulia.
Maneno mengi ya Mama Penny yalianza kumfanya Tunda aanze
kucheka njiani. Alimpa vituko vya wanae na mikasa mbali mbali ya siku iliyopita
wakati ameenda kupamba. Tunda alikuwa akicheka, japo kinyonge.
Walifika kanisani, kwa kuwa Tunda alikuwa amechoka sana
aliingia moja kwa moja ndani kanisani akatafuta kona ambayo alijua watu
hawatamsogelea akaenda kukaa na kuinama ili alale kidogo. Mama Penny kama
kawaida yake ya kuwahi na kuhakikisha kanisa limekaa vizuri. Kuanzia usafi wa
mazingira, chooni, ndani na nje ya kanisa, na kumalizia kupamba kabla mumewe
hajaja na watoto, aliendelea na pilika pilika zake wakati Tunda amelala
kanisani.
Ibada ilianza, watu waliingia na kwa kuwa Tunda alijua kila
mtu anamkwepa, hata Julius mwenyewe hakuonyesha kutaka kuwa karibu naye tena,
kwa hiyo hakutaka kusumbua nafsi yake, alibaki ameinama bila kusimama wala
kumsalimia mtu. Ibada iliendelea, nyimbo mbalimbali ziliimbwa, lakini
hakuinuka.
Alisikia watu wa viti vya mbele wakihamishiwa viti vya nyuma
kabisa kule alipokuwa amekaa yeye, huku akisikia minong’ono kuwa kuna wageni
ambao watakaa viti hivyo vya mbele. Tunda aliwaza kidogo. ‘Kina nani hao!? Mbona Mama Penny hajaniambia kitu chochote?’
Lakini kwa kuwa alikuwa amechoka sana, hakutaka kuendelea kufikiria juu ya
mambo ya wageni wakanisani wakati ya kwake yanamshinda! Akabaki ameinama vilevile.
Watu waliendelea kuimba na kucheza wakati bado Tunda amekaa
chini huku ameegemeza kichwa chake kwenye kiti cha mbele yake, anasinzia.
Mara akasikia Mchungaji akiongea na watu wote wakakaa, ndipo
Mchungaji alipokaribisha watu watoe ushuhuda. Walisimama watu wachache
wakashuhudia yale mambo Mungu ametenda, kisha akasikia Mchungaji akisema,
naomba mtulie kimya, msikilize. Kwani waumini wengine walikuwa wakishangilia
yale waliyokuwa wakishuhudia wengine.
“Naomba msikilize kwa makini sana yale Mungu amefanya kwenye
maisha ya huyu binti.” Kanisa zima likatulia.
“Nimepata msaada
Gabriel. Nimesamehewa dhambi. Huko kwenye hayo maisha sitakaa nikarudi tena.
Nilitumikishwa na ibilisi mchana na usiku. Mungu amenifungua, nipo huru.
Nimeanza biashara yangu kwa jasho langu bila kuhongwa, na sasa hivi ninafurahia
maisha.”
Tunda alisikika akilia kisha akaendelea.
“Sasa hivi anayeishi hapa ni Tunda, aliyesamehewa dhambi na kuishi
maisha ya nidhamu mbele za Mungu. Na mabaya yote niliyofanya zamani, Net
amenipokea na ananipenda kwa dhati. Naridhika na pesa ninayoingiza kwa jasho
langu na mapenzi ya Net, basi.”
Akaona kabla hajaharibu zaidi pale kanisani anyanyuke,
akatafute taksii, arudi nyumbani akalale. ‘Isije kuwa naanza
kuchanganyikiwa!’ Akajisemea Tunda
akilini.
Suprise!
Tunda akahisi ukimya mkubwa sana pale kanisani, akaamua
kunyanyua kichwa. Hakuamini baada yakumuona Net amepiga goti pembeni yake. “Net!?” Tunda akashtuka sana kumuona Net pale. “Ni nini, kina...” Tunda akasita. Mambo mengi
yakaanza kupita akilini. Akatulia kidogo. “Naomba
nisamehe Net. Nia ilikuwa nzuri, sikutaka kuwachonganisha na Gab. Lakini
nakuahidi siku nyingine sitakuficha kitu. Nisamehe.” “Kama utakubali
nikuoe.” Net akazidi kumchanganya Tunda. Usingizi, kutokulala kwa muda mrefu
kwa wasiwasi na uchovu kwa ujumla, vilimfanya ashindwe kuelewa kwa haraka.
“Nini!?” Alijaribu kukausha machozi kwenye macho
yake ili amtizame Net vizuri, lakini machozi yalikuwa yakichirizika kama maji. “Nataka
uwe mke wangu Tunda.” Ilibidi tu ainame. Alishindwa kujibu, wala kuelewa kwa sekunde
kadhaa. Net aliacha kupokea simu zake na kujibu jumbe zake, leo anatokea
kanisani, anasema nini! Alishindwa kuinuka wala kuongea.
“Kiss her already!” Sauti ya kizungu ya kike, ilisikika
ikipaza sauti ikimtaka Net ambusu Tunda. Baadhi ya watu wakaanza kucheka. “Nathaniel
Cote!” Ilirudia tena kumwita kwa msisitizo. “We are at the Church, Nana!” Net
akababaika akijua maadili ya kiafrica na hapo walipo, kanisani! Anaanzia wapi
kumbusu Tunda! “So what?” Bibi yake akamshangaa kinachomshinda ni nini kutoa
busu kwa mpenzi wake. “Nooo!” Net
akakataa kwa mshangao.
“I thought we raise you well!” Aliendelea kumchokoza Net. “Yes
you did.” “Then man up and kiss her.” “No Nana! We are here.., you know?” Net
akajaribu kumuonyesha mazingira na watu waliokuwepo pale, wanao wazunguka. Kama
kumkumbusha ni Africa!
“See what you have done to him? He can not even kiss his own
fiancé.” Yule bibi alimgeukia Mama yake Net nakumlaumu. Lakini Ritha alibaki kimya, akacheka kidogo
tu kwa kujibaragusa. Maya yeye alikuwa akicheka sana mpaka machozi pamoja na
watu wengine waliokuwa wakiwaelewa.
“I told you Nana! Look at him. She can not even kiss Tunda!”
Maya akaongeza. Net na Maya walikuwa wakimwita bibi yao Nana na babu yao papa. “I
bet your papa is very embarrassed by you, right now! Can’t imagine your dady!”
Yule bibi aliendelea kumchochea Net akimwambia anawaaibisha babu yake na baba
yake huko walipo.
“What am I suppose to do? She can not even look at me.” Net
akasikika akijitetea kwa bibi yake kuwa hajui chakufanya kwani hata Tunda
mwenyewe hamwangalii. “Mam up! Lift her up, hold her in your arms and then kiss
her. That’s all!” Bibi yake akajibu kwa msisitizo akimwelekeza kitu chakufanya
mjukuu wake kama asiyejua.
“You mean now?” Net
akauliza akionyesha wasiwasi huku akimwangalia mama yake. “Right NOW Son. Do
it.” Akajibu yule bibi kwa msisitizo kwamba huo ndio wakati wa kumnyanyua
Tunda, kumuweka mikononi vizuri na kumbusu. Kisha yeye na Maya wakaanza
kushabikia kwa kuimba, “Do it! Do it! Do it! Do it!” Waliendelea kuimba kama
kumtia morali Net, Ritha kimya.
Net alibadilika rangi akawa mwekundu mpaka jasho, kwa hofu.
Maya na bibi yake hawakunyamaza mpaka Net aliposimama na kumnyanyua Tunda.
Akamkumbatia huku akimsugua mgongoni. “I said kiss her not petting her back!
What’s wrong with you!?” Bibi yake alipaza tena sauti kwa mshangao kuwa
alimwambia amnyanyue na kumbusu, sio kuishia kumbembeleza tu! Bado watu walikuwa
wakiwatizama na walioelewa kucheka.
Net akajikaza. Akamvuta Tunda nyuma kidogo, akashika shingo
yake kwa mikono yake yote miwili huku akimtizama, kisha akaanza kumbusu. Yule
bibi na Maya wakaanza kushangilia kishabiki, ndipo watu wakaanza kupiga
vigelegele. “You are a man now.” Bibi yake akamsifia kwa sauti ya juu kuwa
ameshakuwa mwanaume.
Net alipiga tena magoti na kuuliza swali huku ameshikilia
pete yake. “Will you mary me, Tunda!” Tunda aliendelea kufuta machozi huku
akitingisha kichwa kukubali. Mambo aliyokuwa akiyaona kwenye luninga, aliona
yanamtokea siku ile. Net alimvuta mkono na kumvalisha ile pete. Tunda
hakunyamaza. Busu hilo alilokuwa amelitunza muda wote, ameishia kulipata
Nathaniel Cote, kijana wakichotara, aliyebeba damu nyingi ya weupe.
Net akamshika mkono wakataka kutoka nje. “No no no nooo. Hold
up son!” Net akasimamishwa na bibi yake. “What!?” Net akamuuliza huku
akimtizama bibi yake kwa mshangao. “She is not your wife yet!” Akamuonya mjukuu
wake asije nogewa, si mkewe. “I know Nana! I just want her to calm down and
then we will be right back.” Net akajitetea kuwa anakwenda tu kumbembeleza ili
atulie, kisha warudi. Maana ni kweli Tunda alishindwa kunyamaza. Kitu kilimkaba
kooni, akawa haelewi tena. “You better!” Bibi yake akaweka msisitizo. Wote
wakacheka, Net akatoka na Tunda nje.
“Nilijua umeniacha Net. Nilijua hunitaki tena.
Kwa nini ulinifanyia hivyo?” “Samahani sana Tunda.
Sikukusudia kukutesa kwa muda mrefu mpenzi wangu. Nilitaka kukufanyia surprise
kwa jinsi ulivyonifurahisha.” “Nimekufurahisha na
nini tena!?” “Nyamaza kwanza.” “Hapa nina
usingizi na njaa, Net. Sijalala vizuri tangia siku ile ya mwisho
tulipowasiliana. Nilichanganyikiwa, nilijua umeniacha!” “Naanzia wapi
Tunda!? Siku ile mnawasiliana na Gab, ule ulikuwa mtego tu.” Tunda akashtuka
sana.
“Sitaki kukutia hofu, lakini nakutahadharisha tu. Unafuatiliwa
sana. Wapo watu hawaamini kama kweli unanipenda kwa dhati, wanafikiri upo na
hila.” “Kina nani!?” “Hilo sio la msingi ila ujue wanakufuatilia. Kuanzia siku
ya kwanza Gabriel anakutumia ujumbe, halafu ukashindwa kuniambia, walianza
kunicheka sana. Siku ulipoenda kukutana naye alikuwa amevaa spika, unasikika
live, na kuna mtu walimuweka kuwapiga
picha. Niliumia sana nilipopigiwa simu kuambiwa umeshafika eneo la kukutania na
Gab. Mwili wote ulikuwa ukitetemeka, nikiwaza itakuwaje kama utamkubalia Gab.
Nilikuwa nashindwa hata kupumua. Nilitamani kuja pale nishuhudie, lakini
nikajikaza.”
“Ikabidi kuja kuwapigia tena simu kuuliza mambo yalikwendaje,
ndipo nikaambiwa kwa sasa umemkataa. Ndipo ikabidi kufuatilia mazungumzo yote
waliyokuwa wamekurikodi. Nilifurahi sana, na kumshukuru Mungu wangu.” Hofu ilimwingia Tunda mwili mzima ukaanza kutetemeka.
“Sasa
baada ya hapo, nikawa kama nimewasuta, lakini bado hawaamini. Wanahisi kwa kuwa
ni Gabriel. Umemkataa kwa kuwa alikuumiza na umejua kuwa tunafahamiana.
Wakasema kama ingekuwa mwanaume mwingine mwenye pesa ungemkubali tu. Lakini
kwangu nilikuwa nafuraha yakupitiliza. Nikawa nina kazi yakurudia rudia yale
mazungumzo kati yako na Gab.” Tunda alibaki anashangaa nakushindwa hata
kujisogeza akifikiria kwa upya ni nini alizungumza na Gab siku ile.
“Nilifurahi
nakushindwa hata kusubiri tena. Nikampigia simu Nana kumwambia kuwa nataka
kuoa. Ndipo aliposema nilazima awepo kwenye kila hatua mpaka ndoa. Ikabidi
nikate tiketi ili nikamfuate, aje ashuhudie ninavyokuvalisha pete ya uchumba.
Sikujua kama naweza kuchukua muda mrefu kiasi hiki Tunda. Nilijua naenda Canada
mara moja kumfuata Maya na bibi, kisha nirudi nao baada ya siku mbili, kisha
nikuvishe pete ya uchumba wao wakiwepo. Lakini kufika kule kuna mambo
yakajitokeza, ikabidi nimsubirie Nana kidogo. Tumeingia jana. Nimepata ule
ujumbe wako wa jana, nikajua hali yako ni mbaya, ikabidi kumuomba mama Penny
akupigie ili akutulize.” Tunda akashtuka
kidogo.
“Mama Penny!?” Tunda akauliza kwa mshangao. Net akacheka
kidogo. “Ndiyo, mama Penny. Anafahamu kila kitu. Na hata nilipokuwa kule
niliongea na Mama Penny nikamuomba aniandalie mazingira yote, ili nikija iwe ni
kukuvalisha hii pete tu. Lakini aliniambia nifanye haraka una hali mbaya. Pole
sana mpenzi wangu. Sikukusudia kukutesa.” Bado Tunda alikuwa kwenye mshtuko na
hofu.
“Twende
ukalale sasa hivi, ili baadaye uweze kuhudhuria tafrija. Mama Penny amenisaidia
kukuandalia tafrija nyumbani kwa mama ambako bibi na Maya ndiko walikoshukia
hapo. Wale wageni wote niliokuja nao hapa kanisani kwenu ni wakutoka kanisani
kwetu, na wengine nimarafiki zangu wa hapa na wachache tumekuja nao kutoka
Canada. Wapo na marafiki niliokua nao tokea watoto. Wapo wawili, sijui kama
umewaona?” “Mimi nimekuona wewe tu pale ndani.” Net akacheka kidogo.
“Basi na wao wamechangia kuchelewa
kwangu. Nilipowaambia naoa, wakataka tuongozane nao waje huku nchini.
Wanaondoka kesho asubuhi kurudi kuwahi majukumu yao. Jana nilipofika tu,
nilienda kuongea na baba yako. Ilibidi kuomba kuwa ni dharula ili waniruhusu
kumuona maana ilikuwa sio siku ya kuwatembelea. Nikaruhusiwa. Amefurahi sana.
Amesema kesho tumpelekee picha.” Tunda alihisi yupo usingizini.
“Ungeniua Net!” “Sitarudia tena kufanya hivyo.
Kwanza nilitaka kukupa onyo. Usiwahi kunificha jambo, na pia nilitaka
kukufurahisha.” “Samahani Net. Naahidi sitarudia tena.
Umenipa somo ambalo nimejifunza kwa mateso sana. Nilijua umeniacha!” Machozi
yakaanza kumtoka tena Tunda.
“Lakini pia imekusaidia kufikiria
Tunda. Angalau umejua kama unataka kuwa mke wangu au la. Unajua nilikuja
kujilaumu? Ni kama nilikuja kukuvamia tu! Tokea mwanzo kila kitu kikawa
kinaenda kwa vile nilivyokuwa nikitaka mimi. Angalau umepata muda mtulivu
wakuwaza.” “Sikuhitaji muda wa kujua kama nakupenda
au la Net. Nakupenda.” “Sasa hivi nimehakikisha.” Net alimvuta tena na
kuanza kumbusu midomoni. Hiyo furaha aliyojisikia Tunda, hakuna jinsi angeweza
kueleza. Alikuwa akikwepesha hiyo midomo akitaka kuja kupata busu la uhakika.
Na kweli Mungu akamsaidia na kupata busu la Net. Alikuwa akifurahia sana.
Japokuwa Tunda alishakuwa na
wanaume wengi hakuwahi kupata busu kama lile. Net alimshika vizuri na kwa
heshima wakati akimbusu kama anashika mwili wa thamani sana kumbe ni mwili wa
Tunda uliopitiwa na wanaume kibao, na yeye akilijua hilo. Tunda alilihisi lile
busu katika kila kiungo cha mwili wake. Machozi ya furaha yalikuwa yakimtoka si
huzuni tena, asiamini.
“Asante sana Net. Asante.”
“Umeipenda pete?” Tunda akanyoosha mkono wake na kuanza kuiangalia ile pete. “Nzuri
sana. Nimeipenda. Asante.” “Hiyo ni pete ya bibi. Alivalishwa na babu,
alinitunzia kwa muda mrefu akasema nikipata mwanamke ninayempenda, nimvalishe.”
Tunda akacheka.
“Anaonekana mcheshi!” “Anavituko
huyo! Akiamua kukufungulia moyo, wala huhitaji siku nyingi zakumzoea. Ila
anatupenda sana mimi na Maya.” “Nikwambie kitu Net?” Net alikuwa bado
amemkumbatia Tunda, hapohapo nje ya kanisa huku akimwangalia kwa upendo kama
aliyeokota lulu kumbe ni Tunda kituko kwa wengine.
“Mmhh!” “Umenipa heshima ambayo
sikuwahi kufikiria hata siku moja kama naweza kuja kupata. Sikujua hata kama
nastahili! Hapa nahisi nipo ndotoni. Asante sana.” “Wewe ni wathamani sana
Tunda. Sio kwangu tu, hata machoni pa Mungu, ndivyo anavyokuona. Sijafika hata
nusu ya punje ya mchele, vile Mungu anavyokupenda na kukuheshimu.” Kabla
hajambusu tena, “Mnaitwa na Mchungaji mkaombewe.” Mama Penny alitoka na
kuwakuta bado wamekumbatiana wakitaka kupeana mabusu tena.
“Asante sana mama Penny, kwa kila
kitu. Naamini mpaka sasa tupo sawa.” “Karibu Net. Kila kitu kipo sawa kabisa.” “Tunashukuru
sana, lakini naomba baada ya maombi tu, nimrudishe Tunda nyumbani akapumzike
kidogo, halafu tutakuja kwenye tafrija baadaye akishatulia.” “Mnaacha wageni
wenu hapa!?” “Wewe si upo?” Net alimshangaza mama Penny.
“Leo ni siku yangu na Tunda. Nataka
aifurahie. Kwa jinsi alivyochoka hivi, sidhani kama atafurahia chochote kwenye
tafrija.” “Utamuaga mama yako?” Akauliza mama Penny. “Nitaongea naye. Kwa kuwa
tafrija itakuwa saa moja usiku, nyinyi mkitoka hapa mnaweza kwenda nyumbani kwa
mama moja kwa moja, au mkaja hiyo jioni. Sisi tutakuja huko jioni.” “Sawa.”
Akakubali mama Penny.
Tunda akamsogelea Mama Penny. “Kumbe
ulikuwa unajua kila kitu, halafu ukaniacha mwenzako nalia mchana na usiku!”
Mama Penny akaanza kucheka. “Net aliniomba sana nisikwambie, nivumilie. Mimi
mwenyewe nilikuwa nikiumia, lakini nilijua mwisho wa yote utacheka tu. Haya
hebu jione jinsi ulivyopendeza na hiyo alumasi hapo kidoleni, mdogo wangu!
Mvumilivu hula mbivu.” “Lakini mmenitesa sana!” Wakacheka huku wakimuomba
msamaha, mwishowe wakaingia ndani.
Net na Tunda walipiga magoti mbele
ya kanisa, wakaombewa. Net alitoa neno la shukurani, nakurudia historia yake
fupi yeye na Tunda, kisha akaomba aondoke kabla ya ibada haijaisha. “She is not
your wife.” Bibi yake akarudia kwa sauti. “I know Nana.” “Just saying!” Kila mtu alicheka, Net akaenda kumbusu mama
yake, na bibi yake akataka kutoka. “Heyyy! What about me!?” Maya alishangaa
kuona kaka yake anampita. “Tunda amechoka.” “It doesn’t take even a minute to
give sugar to your baby sister!” “Fine!” Net akarudi akabusu mdogo wake. “Happy?”
Net akamuuliza mdogo wake. “Oooh yeah!” Net akacheka na kumrudia Tunda
aliyekuwa amemuacha amesimama, akamshika mkono. “She is not your wife.”
Alisikia bibi yake akirudia tena kumkumbusha kuwa bado si mkewe, wasije
wakapitiliza huko waendako. “I said, I know.” Net akamjubu bibi yake kuwa analijua
hilo, huku akiondoka na Tunda akiwa amemshika mkono.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Walifika nyumbani kwa Tunda, akiwa anasinzia. Aliingia
bafuni, akaoga tena hasa kusafisha uso uliokuwa umechanganyikana machozi na
vipodozi. Akavaa nguo za kulalia kabisa,
akatoka pale sebuleni alipokuwa amemuacha Net. “Mbona nguo za kulalia tena!?
Tutawaweka sana watu kule kwenye tafrija Tunda! Nilitaka upumzike kidogo tu.”
“Utaniamsha muda unaotaka tuondoke. Nimechoka sana Net, nataka nilale vizuri.”
“Pole.” Net akamsogelea, akambusu tena bila kumkumbatia ila kumshika tu
kichwani ili kuweza kumbusu. Akamuachia.
“Twende nikusindikize.” Akamshika mkono na kuingia naye
chumbani kwake, Tunda akiwa na wasiwasi. Alimuogopa sana Net. “Njoo hapa.” Net akajilaza kitandani, kisha
akavuta mto akaweka chini ya kichwa
chake. “Njoo ulale hapa.” Tunda alibaki amesimama, akakunja uso akionyesha
wasiwasi na hofu. “Njoo usiogope, Tunda.” “Kifuani kwako!?” Akauliza kwa hofu
kidogo. “Hutaki?” “Sio..” Tunda akasita. “Usiogope, njoo. Nataka ulale vizuri.
Ni leo tu, hutazoea.” Tunda akacheka. “Nitagoma kuamka mimi!” Tunda akamfanya
Net acheke.
“Ndio nabembelezea msamaha, kwa kukutesa kwa siku zote hizo.”
Tunda akatabasamu, akapanda kitandani na kujivuta mpaka kifuani kwa Net. “I
miss you so much Net.” “Miss you too, babe. Nitaongea na Mchungaji wako,
atusaidie tufunge harusi mapema. Nataka tuanze kuishi pamoja.” Tunda akapitisha
mikono yake kifuani kwa Net, akamkumbatia kwa nguvu na kupitiwa na usingizi
bila ya kujibu kitu. Net aliendelea kumpapasa taratibu maeneo ya mgongoni na
begani, huku akimbusu kichwani mpaka na yeye akapotelea usingizini.
Tafrija ya kuvalishwa pete ya uchumba Tunda.
Ilikuwa
ni kwa mara ya pili Tunda kufika nyumbani kwa mama Cote. Mara ya kwanza
alipopelekwa kutubu akiwa mwenye dhambi haswa. Baada ya kukiri alishajihusisha
kimapenzi na mchumba wa mama Cote, uadui ukaanza. Sasa anarudi kwenye jumba
hilo kama mchumba wa Net. Ilikuwa nyumba yenye thamani za kisasa, tena za aina
yake. Nyumba nzuri, iliyojengwa kwa namna yake. Magari yaliyokuwepo hapo nje
sehemu yakuegeshea tu magari, Tunda akajua ni watu wenye uwezo watupu
watakaokuwepo huko ndani.
“Umependeza
sana Tunda.” Tunda akatulia kidogo. “Nini?” “Itakuaje nikifika huko ndani
nikakutana na..” Tunda akanyamaza. Net akamuona akifuta machozi huku akiangalia
nje ya dirisha. “Naomba uniangalie Tunda.” Tunda akamgeukia. “Naona kama nakuingiza aibu tu Net!” “Naomba
usipeleke mawazo yako huko kabisa. Kila mmoja utakayemkuta humo ndani
anahistoria yake. Sema ya kwako umeigeuza imekuwa yamsaada.” Net aliendelea
kumtuliza akisikika ametulia kabisa, bila hata wazo la pili la wasiwasi.
“Nilifurahi
sana jinsi ulivyoweza kuongea na Gab. Umethibitishia kila mtu umeshakomaa
Kiroho. Tumia ujasiri huo huo kwa kila atakayekusogelea. Na hakikisha
unajitambua acha hofu kabisa. Nipo na wewe nikikujua vizuri, na nimeridhika na
wewe. Kwa hiyo tembea mbele ya watu ukiwa huna hofu. Umenisikia?” Tunda
akatingisha kichwa kukubali.
“Haya
naomba tabasamu. Maana hii yote nimeandaa kwa ajili yako. Nataka ufurahie.
Sawa?” Tunda akacheka taratibu. Walikuwa wameegesha gari nje ya hiyo nyumba ya
mama yake, sehemu ya kuegesha magari. Net akamvuta karibu na kumbusu tena na
tena bila kumuachia kama mwenye kiu naye mpaka simu yake ilipoanza kuita. “Mama
huyo!” Net akasema wakati anaiangalia simu yake akaamua kupokea. Alisikiliza
kidogo mama Cote akiongea, kisha Net akajibu. “Tupo
hapa nje, tunaingia ndani sasa hivi.” Akakata na kumbusu tena Tunda. “Twende,
Nana ameanza kusinzia.” Wote wakacheka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Bibi yake Net alimuomba
Net, amvalishe tena ile pete Tunda huku
akichukuliwa vizuri video kama kumbukumbu ya familia, akidai kuwa siku hiyo
ndipo anapomkabidhi Tunda cheo cha Bi. Cote rasmi kama mrithi wake. Kwanza
alivaa pete aliyochumbiwa nayo yeye na pili anaolewa na mjukuu wake mwenye jina
kama la mume wake. Alisema anakikundi cha marafiki zake kanisani huko nchini
Canada, anafanya nao bible study, walimuomba arikodi kila kitu ili akifika
awaonyeshe. Zile zilikuwa habari zilizomtibua mama yake Net, na kumnyima raha
kwenye ile shuguli nzima.
Mama
Penny alikuwa ameandaa sehemu si ya nje, lakini si sebuleni. Kulikuwa na eneo
la ndani lakini kama baraza kubwa tu lililokuwa limezungushiwa kuta nzuri mpaka
juu ambako ndiko vyumbani. Chini kwenye hilo eneo la katikati kulikuwa kama na
bustani tena ambayo ilishamtoa macho Tunda tangia mara ya kwanza anaingia
kwenye hiyo nyumba.
Haikuwa
bustani kubwa lakini duara kubwa iliyozungushiwa majani mazuri, yaliyokatwa
chini yakawa kama mkeka. Vyungu vya thamani vyenye maua mazuri yaliyokuwa
yamezunguka kwenye hayo maua na pembeni ya kona kwenye hilo baraza zima na
nguzo, mama Penny alitendea haki. Kuzunguka hilo eneo zima kulikuwa na fremu za
picha nzuri sana na aina mbali mbali ya maua. Ndipo mama Penny akapaandaa
vizuri na kupendeza.
Yote
hiyo alifanya Net kwa ajili ya Tunda. Sasa mpambaji akawa ni mama Penny,
nyumbani kwa Ritha, mama yake Net, asiyempenda Tunda. Leo Tunda anavalishwa
pete nyumbani kwake akiwa ameonya asikanyage pale tena. Mbaya zaidi,
anavalishwa pete ya thamani sana, urithi ambao yule bibi aliuwekea maana kubwa
mbele ya watu! Mambo hayo yote wanayafanya nyumbani kwake! Hakuna jinsi mtu
angeangalia moyo wa huyo mama ulivyochafuka, akaweza kueleza wengine.
Alikuwepo
kanisani na pale kwenye ile tafrija japo ni nyumbani kwake, lakini sababu ya
uwepo wa huyo bibi milionea ambaye hata Tunda hakujua uzito wa huyo bibi kuwepo
pale. Alisikia akipiga kelele kanisani, akitaniana na Maya na Net. Asijue uwepo
wa huyo bibi hapo nchini hata usalama wa taifa nchini Tanzania na Canada,
unajua kama yule bibi yupo nchini Tanzania.
Waalikwa
ambao Net alimwambia wengine ni wakutoka kanisani kwao na marafiki, wengi pale
ni askari kanzu na usalama wa taifa walikuwa wamejaa hapo, kuhakikisha huyo
bibi, raia muhimu sana wa huko nchini Canada yupo salama, na hakuna
linalotokea, mpaka anarudi nchini kwake salama.
Na hao
wazungu wachache aliowaona Tunda pale, hawakuwa ni rafiki wa karibu tu wa Net ,
ni askari waliopitia mafunzo makubwa sana ya kiaskari ya kimataifa, walifika
nchini na huyo bibi kwa ajili ya usalama wake tu. Kwanza alitua nchini na ndege
yake ambayo ndio ilibidi kufanyiwa taratibu ya eneo la kutua hapo nchini
Tanzania. Kimya kimya bila gazeti lolote kuripoti ujio wa bibi huyo nchini
Tanzania.
Mama
Cote, au Ritha, alijua ni mapesa ya kiasi gani yamemwaga kwa huyo bibi
anayefanya mchezo na kuonekana wa kawaida sana kuwepo hapo. Ritha alipigia
mahesabu ya huyo bibi kuwepo tu hapo! Tena kwa ajili ya Tunda, ambaye amempokonya
ndoa na mapenzi ya mtoto wake! Anamwita Malaya. Anajua wazi, amemchagua Net
badala ya Gab kwa kuwa anamfahamu Net, anataka kunufaika naye. Ritha akajiambia
hiyo pesa angefanyia kitu kikubwa sana badala yakupoteza kwa malaya, Tunda.
Kila
neno alilotamka bibi Cote, halikuwa bure. Hakuwa mropokoji. Ni mwanamke
aliyekuwa akiongea na maraisi na watu wakubwa sana ulimwenguni. Pesa yake na
kile anachokifanya nchini Canada, kama mwanaharakati wa mambo ya wanawake si
nchini kwao tu, bali ulimwenguni, kilimketisha na wakuu wa ulimwengu huu na
kumwingiza sehemu kubwa mbalimbali hapa ulimwenguni. Alishahutubia mara kadhaa
kwenye vikao vikubwa vya UNO. Kila aliloongea, watu walilinukuu na kulisikiliza
kwa makini sana hata kugeuza ni habari ya kuuza gazeti lolote lile haswa nchini
kwao anakofahamika na familia hiyo kufuatiliwa kwa karibu sana.
Ritha
alijua na kuzidi kuumia kwa kila neno analozungumza huyo bibi Cote usiku huo
kwenye tafrija hiyo. Alijua si mropokaji. Kwa hiyo hata usiku huo hakuna
aliloropoka hata moja juu ya Tunda na Net. Inamaana ni maneno au hotuba maalumu
aliyokuwa ameiandaa kwa muda mrefu kuja kuzungumza kwenye tafrija ya Net
akichumbia. Na lazima hiyo hotuba au hayo maneno anayoongea hapo yamesomwa na
kurudiwa na msaidizi wake wakaafikiana na ndipo anatamka mbele ya huo umati
kirafiki tu kama akizungumza na familia yake, lakini wazi anajua ni habari
nzito nchini kwao siku inayofuata, japo amezungumzia nchini Tanzania. Na
akitamka yeye, ndio mwisho.
Ni
ukweli ambao hakuna ambaye angesema, Tunda angeamini. Kwa hakika Tunda hakuwa
akijua lolote lile juu ya Net mwenyewe wala huyo bibi. Net alikuwa makini sana
anapozungumza na Tunda. Na alifanya makusudi akijua umuhimu wa mwanamke
atakayemuoa. Sio tu kuitwa mke wa Nathaniel Cote, alijua atabeba majukumu
mazito sana. Tunda asijue.
Net
hakuwahi kujifungua kwa Tunda zaidi ya idadi ya waliozaliwa nyumbani kwao. Kile
anachofanya pale nchini. Kazi za mama yake. Hakuwahi hata kuropoka utajiri
mkubwa unaomsubiri nchini Canada. Au anavyosubiriwa kwa hamu huyo mke wa Net,
huko nchini Canada. Hata kujulikana jina tu, ingekuwa habari ya kuuza magazeti.
Picha yake ndio kabisa. Tunda hana hili wala lile. Anajionea ni bibi amekuja
kwenye shuguli ya mjukuu akichumbia. Basi. Kumbe ameingia kwenye historia kubwa
sana.
Vyombo
vya habari vya nchini kwao na watu wengi walio ijua hiyo familia, na
kuifuatilia walitaka angalau kupata fununu kujua hata kwa fununu tu,
atakayekuwa mke wa Net. Anaposema video nzuri ichukuliwe Net anapochumbia kwa
ajili ya marafiki zake wa kanisani, sio kwa sura hiyo aliyoelewa Tunda hata
kidogo. Ni kumbukumbu ya vizazi hadi vizazi na ni habari nzito sana ambayo mtu
anaweza hata kuuza kwa pesa nzuri tu za kicanada. Nathaniele Cote amechumbia
siku hiyo! Ilikuwa ni habari kubwa yakuuza magazeti nchini kwao.
Lakini
Tunda yeye kila kitu aliona kawaida tu, na Net alikusudia iwe hivyo. Hakutaka
askari yeyote avae sare na wala pale pasionekane risasi yeyote ile hata ya
kiunoni mwao. Kwa hiyo kila mgeni akaonekana wa kawaida. Nadhifu na wengi
wamevaa suti. Kumbe suti hizo zimeficha mengi. Tunda na kina mama Penny pamoja
na wageni wengine wakawa hawaelewi kinachoendelea. Kumbe hiyo nyumba ilikuwa
chini ya ulinzi mkubwa sana tokea huyo bibi anafika pale.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Yakawekwa
mazingira mazuri pale. Katikati ya kula na kunywa, watu wakicheka, Net akapiga
tena goti akimuuliza Tunda aliyekuwa amesimama, kama atamkubali amuoe, “Will you mary me?”. Tunda akakubali, kwa kusema, “Yes.” Net akamvalisha tena ile pete akiwa amepiga
magoti vilevile. Kisha akasimama, akamkumbatia vizuri na kumbusu Tunda.
Haikuwa
mara ya kwanza kwa Tunda kupata busu au kukumbatiwa na mwanaume. Baba Tom
alishambusu akiwa bado mdogo na mwili huo ulishashikwa na wengi tu. Kimapenzi
na kupigwa kama mwizi. Lakini busu la Net na jinsi alivyomgusa huo mwili!
Ilikuwa tofauti kabisa. Hakuna aliyeona asitamani. Wenye wivu ndio walizidi
kuumia.
Net
alijua wapi amshike kabla ya kumbusu, na hata jinsi alivyomwangalia baada ya
kumshika kabla ya kumbusu, akili na mawazo ya Tunda alijua wazi anapendwa na
kuthaminiwa sana. Ile hofu na aibu mbele ya wateja wake ilimuisha kwani ni
kweli walikuwepo wanaume wakutosha tu ambao walikuwa wateja wake, lakini kwa
jinsi Net alivyo mtizama na kumshika, hakuna jinsi Tunda ungemkumbusha kuwa
alishakuwa changu, ukamuumiza.
Mama Cote na Tunda tena.
Wakati watu
wakiwa wanaongea na kucheka, huku wakila na kunywa, Mama Penny na mumewe
wakaamua kuaga. Muda ulishakwenda. Watoto wanatakiwa shuleni kesho yake.
Wakamuaga Net na Tunda. Wao wakaondoka. Kwa kuwa walikuwa wamekaa meza moja na
Tunda, walipoondoka, Net naye akasimama, akamwambia Tunda atarudi baada ya muda
mfupi. Tunda naye akaamua kuingia ndani kutafuta choo kilipo ili angalau
ajitengeneze vizuri na kujirudishia vipodozi na nywele. Kujitengeneza.
Wakati
anatoka chooni, mama Cote au Ritha alikuwa akimsubiria mlangoni akiwa amejawa
wivu baada ya kuona jinsi mkwewe alivyomthamini Tunda. Na ni kama alitangaza
kumpa Tunda cheo kikubwa sana ambacho hakuwahi kupata mtu sahihi wakumpa ila
Tunda. Lakini alitangaza kwa kujihami huku akisema, atatangaza rasmi au
atamkabidhi rasmi cheo hicho baada ya kupata muda wakutosha wamazungumzo na
Tunda.
Tunda
alicheka tu kwa kuwa yule bibi aliongea kama kitu cha utani, kumbe ni jambo
zito lililokuwa likisubiriwa kwa muda mrefu sana. Wengi walitamani kujua cheo
hicho angalau yule bibi anamfikiria kuja kumkabidhi nani! Nani angekuwa mrithi
wake! Nani anakalia kiti hicho! Angalau kwa fununu tu. Leo kwa mara ya kwanza,
anatangaza, tena nchini Tanzania! Hata Net na Maya walibaki mdomo wazi.
Hawakuamini.
Lakini
si Tunda ambaye hakujua chochote. Alimuona jinsi Maya na wale wageni wote
kutoka Canada wakishtuka mpaka kusimama na kushangilia sana, na Net kubadilika
mpaka rangi ya sura akiwa ametoa macho asiamini kile bibi yake anafanya kwa
Tunda. Tunda mwenyewe hata asielewe ni nini bibi huyo anaongea. Akajiambia ni
mambo tu ya kizungu.
Tunda
akawa ndio ametamkwa kwa mara ya kwanza na bibi huyo kuwa ndiye atakalia kitu
hicho baada yake. Ritha alijua ni habari itakayoenea sana nchini Canada na
picha za Tunda kuanza kuonekana huko na habari zake kufika kwenye nchi mbali
mbali za wawakilishi wa umoja wa bibi huyo. Tunda hana habari.
Picha
nyingi zilipigwa asijue umuhimu wake. Aliona mpaka rafiki wa Net wakimuomba
akae vizuri wampige picha akiwa peke yake tena kwa kupokezana. Akiwa anacheka
tu, akakubali kufuata maelekezo. Marafiki hao wakampiga picha akiwa peke yake,
kisha wakamuomba mmoja mmoja wapige naye picha. Kwa zamu. Nyingine wakapiga
wakiwa na Net. Ikawa shamra shamra imeongezeka gafla baada ya tangazo la bibi
huyo, Tunda hana habari.
‘Tunda!’ Ritha aliumia sana. Bibi
Cote alitamka kumkabidhi Tunda kiti ambacho inamaana yeye hakustahili! Tena
anatamka hayo mbele za watu bila hata kuzungumza na wao kwanza kama familia,
wakajua kama amekusudia kuwa ni Tunda! Hata wao watu wa karibu ndio wanasikia
pale kama watu tu wa nje! Yule bibi hakumshirikisha yeyote. Yaani pale ndio
anatoa hiyo habari kwa mara ya kwanza.
Alihisi
ni kama yule mama mkwe wake ametangaza kumtoa kwenye familia kwa wazi tena kwa
kumdhalilisha vibaya sana. Ni kama anasema Tunda ni bora kuliko yeye! Alichukia
sana kuona anadhalilishwa pale mbele za watu tena nyumbani kwake! Ni Tunda,
binti anayejihesabu amempita kwa kila kitu! Leo anapewa heshima yote aliyokuwa
amebeba yeye, na kudhani anastahili yeye Ritha! Hasira zilizidi kumpanda na
kumchukia Tunda zaidi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Naomba
tusogee hapa pembeni tuzungumze.” Tunda akamfuata nyuma. Akashangaa anamtoa
kabisa pale mpaka sehemu ya nje karibu na mlango wa kutokea. Akaangalia kulia
na kushoto, wakajikuta wawili tu. Kulikuwa na askari kanzu wawili nje ya huo
mlango walionekana kwa kupitia kioo cha mlango. Yule mama akaonekana kuridhika
na hiyo faragha.
Akamgeukia
Tunda. “Upo hapa leo sababu ya huyu bibi, tu.” Mama Cote akaanza huku amemkazia
macho. “Umenielewa Tunda? Unaweza kumdanganya kila mtu hapa, lakini sio mimi.
Mimi sio mtoto mdogo au mjinga kama hao wanaume zako uliokuwa ukiwavulia nguo
na kuwaloga. Najua janja yako. Upo hapa na kumkataa Gabriel kwa kuwa umejua Net
anapesa kuliko Gab. Anamapesa ya urithi wa babu yake na bibi yake akifa ndio
kabisa. Yeye ndio anakuwa mrithi au mtawala wa mali zote za Cote.” Tunda
akakunja uso. Hayo yote hakuwa hata akiyajua. Na wala hajui kama hiyo familia
ya Cote ina mali za hivyo!
“Sijui
unamlogea wapi mtoto wangu! Sijui kama na yeye unamfanyia sadaka za makaburini
au la! Lakini mimi na wewe tunajua wazi, kwa akili za Net hawezi kukupenda mtu
kama wewe hata kidogo. Nina uhakika kuna ulichofanya kwa Net. Wewe ni mzoefu wa
ushirikina, hushindwi kuzika akili zake. Na ninajua wazi, yale majini
yanayosadikika kukutoka, hayajatoka. Bado yanaharibu akili za wanaume, ndio
maana na Net amechanganyikiwa.” Ritha akataka kuendelea.
“Subiri
kwanza mama Cote.” Tunda akamkata. “Wewe si upo safi mbele za Mungu? Unaamini
kwenye wokovu na nguvu ya damu ya Yesu? Sasa kwa nini humkomboi mwanao kwa
maombi ili atoke kwangu? Kwa nini humtoi kwangu kwa maombi? Unahangaika tu na
mimi kwa maneno mengiii! Au huamini kama Mungu wako ananguvu kuliko nguvu ya
shetani?” Tunda alimshtua sana Ritha.
Akababaika sana akiongea hili na kujibu lile, Tunda akimtizama kwa kumsuta.
“Subiri
kwanza Ritha. Acha maneno mengi. Wewe si mama yake Net? Inamaana unazo haki
zote za kumkomboa mwanao kwa njia takatifu kama wewe ulivyo mtakatifu. Mbingu
inajua unayo haki, hata kuzimu kule unakosema mimi ninaenda, wanajua kuwa wewe
kama mama yake Net, unayo haki na Net. Sasa kwa nini unahangaika na mimi ambaye
hata sijaunganishwa na Net kwenye agano lolote!?” Tunda akamuuliza taratibu tu
bila jazba kama yeye alivyokuwa akiongea kwa jazba.
“Usifikiri
ndio umeshinda Tunda. Namuombea mwanangu. Ila ujue maombi ni kotekote. Ni mimi,
na Net mwenyewe aamini.” Tunda akamtizama kwa kumsuta. “Na usifikiri
nimeshindwa. Nipo kwenye maombi yakumfungua akili zake mpaka afunguke. Net ni
kama amechanganyikiwa kwa kuwa anataka kuwa mtumishi wa Mungu kama babu yake,
ila hajui ni jinsi gani atumike. Kwa kuwa wewe ulikuwa malaya, na bibi yake
anapambana na haki za wanawake na kutoa wanawake wenye hali kama yako na
kuwawezesha kimaisha ili waweze kujitegemea, ndio anaona wewe utafaa.” Akaanza
kuropoka, Tunda akimtizama kwa mshangao.
“Kwanza
atakutumia wewe kama kielelezo cha kufikia roho za watu waliopotea na pili
anaona anamfurahisha bibi yake kwa kumuunga mkono kwa kile anachokifanya kwako
wala si mapenzi. Ndio maana anadhani wewe utamfaa.” Hilo likamwingia Tunda na
kumuumiza sana. Ila akajikaza mbele ya Ritha.
“Upo
wewe kama daraja kutimiza ndoto zake, na ndio maana hata bibi yake pia yupo
hapa leo kuhakikisha Net anafikia ndoto zake na yule bibi anajipatia sifa
kimataifa. Kuwa ni mkweli kwa kile anachokipigania. Kwani ameweza kuruhusu hata
changudoa kama wewe kuolewa na mjukuu wake. Usifurahie jinsi unavyoitwa Mama
Cote leo, ukadhani kuna kitu cha maana walichokiona kwako au uchawi wako pekee
ndio umeshinda. Hamna kitu.” Tunda alibaki kimya ametoa macho. Habari zilikuwa
mpya, ngeni lakini kweli zilianza kumuumiza.
“Wewe
loga utakavyo. Lala makaburini utakavyo. Lakini jua mimi nipo. Na uelewe kabisa
nawajua wazungu kuliko wewe. Wanajua kutumia watu. Umeruhusiwa na yule bibi
kuwepo na Net kwa ajili ya kumnufaisha yeye mwenyewe yule bibi. Kimataifa na
kiuchumi. Na kwa upande wa Net, kama nilivyokwambia. Ila sasa, ujue wazi, MIMI
nipo. Sitakubali kwa nia yao yeyote ile, wewe unufaike kwa kile ninachostahili
mimi.”
“Nimehangaika
sana kufika hapa. Mchana na usiku kujenga hili jina huku Tanzania. Nani alijua
Cote huku Tanzania kama sio mimi? Hapa uliposimama, ni kwangu nimejenga kwa
jasho langu. Hata kama Net alikwambia babu yake ndiye alijenga hapa, lakini
ujue mimi ndiye niliyekuwepo hapa kuhakikisha jengo linasimama.” Na hapo napo
Ritha akajikuta anaropoka mengiii kwa hasira huku Tunda akimshangaa. Hakuwa
anaelewa chochote anachozungumza pale.
“Kwa
hiyo ujue sitakubali. Wakati wewe unahangaika na suruali za wanaume, mimi
nilijua kufunga miguu yangu, nikatumia akili, mpaka kumfikisha hapo alipo hata
huyu Net ambaye sasa hivi unafurahia mali zake hapa nchini Tanzania. Yupo hapa
nchini kwa sababu ya juhudi zangu wala sio pesa. Hawezi kuishi Tanzania bila
idhini yangu mimi ambaye ni raia wa Tanzania.” Hapo napo Tunda hakuwa hata akielewa.
“Sasa,
sitakubali hata iweje uvune usipopanda. Labda usubiri niwe nimekufa ndio
utakuja kuitwa mama Cote. Vinginevyo ujue utapambana na mimi na utajuta, malaya
mkubwa wewe.” Tunda akatabasamu. “Umemaliza?” Tunda akamuuliza mama Cote swali
lililomshangaza, tena akiwa ametulia tu. Kimya.
“Acha
kuniogopesha Ritha. Wala sitakuita Mama Cote maana umejishusha sana. Mimi huwa
sitishwi. Na wewe wala usifikiri ndio wa kwanza kunijia na vitisho. Tokea
napata akili zangu, nimeishi na watu wa aina yako. Vitisho imekuwa sehemu ya
maisha yangu. Yaani wewe hapo ulipo hivyo, hunitishi hata kidogo.” Tunda
akaendelea taratibu tu.
“Unanisikia
Ritha? Sikuogopi. Halafu na uache kujipa kazi zitakazo kuchosha bure! Ngoja
nikusaidie tu kwa kuwa umenizalia Net. Huko unakonitafuta mimi simo tena.
Nimetoka na nimeamua kupumzika. Mungu alishanitoa makaburi na kwa waganga wa
kienyeji, muda mrefu sana. Nimeacha kuvua suruali za wanaume muda mrefu sana na
wala sijivunii kwa hilo. Najua nimesamehewa, lakini bado nipo na majuto tu.
Nasikitika kuwa na wewe umekuwa muhanga na maisha niliyoishi zama...” “Acha
kunipa maneno unayomdanganya nayo Net. Mimi ni Ritha Cote. Najielewa. Na
nimekwambia hata Net anakutimia tu.” Ritha akamkata. Tunda akacheka kwa
kumuhurumia.
“Hata
kama Net ananitumia tu. Au bibi yake ananitumia. Sijali. Nataka ujue na mimi
msaada ndio nilio kuwa nikiutaka siku zote za maisha yangu. Net amepata
alichokuwa anakitaka maishani mwake, na mimi nimempata mwanaume ambaye hata
sikuwahi kumuota na heshima kubwa ambayo hata sikuwahi kufikiria nina stahili.
Wewe ni shahidi kwa kile tu kilichonitokea leo. Ulikuwepo tokea asubuhi
ukishuhudia kile kinachonitokea mpaka sasa hivi uliposhindwa kuvumilia. Umeona
heshima iliyowekwa kwa Tunda tu!” Tunda akacheka taratibu.
“Kwa
hiyo kwa upande wangu mimi, kwa ufupi, sina chakupoteza hata kidogo. Kama Net
na bibi yake wataendelea hivi, aisee ujue mimi ndio nilichokuwa nikikihangaikia
tokea zamani mpaka kulala makaburini nakushindwa kukipata kwa shetani ila kwa
huyu Mungu ninayemtumikia sasa hivi. Sasa kama na yeye unamwita shetani, hakuna
injili itakayowahi kuja kunitoa kwa huyu Mungu ninayemtumikia sasa hivi.
Nakushauri na wewe umfuate. Analipa. Na itakupunguzia kupambana na watu au
kuzunguka kwenye maofisi ya watu ukijidhalilisha bila wewe mwenyewe kujijua.”
Ritha alishtuka sana asiamini.
Tunda
akataka kufungua mlango ili aondoke lakini akageuka. “Na wala usipate shida na
uwepo wangu. Nitajitahidi tusionane kabisa mpaka utakapo kuwa tayari kuniona
tena. Naomba uniagie Net.” Tunda akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya
muda kupita bila kumuona Tunda, Net akaanza kumtafuta. Aliingia ndani na kutoka
mara kadhaa, mwishowe akakumbuka kumuona mama yake akiingia ndani wakati Tunda
yupo ndani. Akamsogelea, “Umemuona wapi Tunda?” “Aaah! Nilisahau kukwambia.
Aliniambia nikuage yeye ameondoka.” Net akakunja uso na kujiweka sawa.
“Umemwambia nini tena, Tunda?” “Kwa nini unafikiria
maneno yangu ndio yamemuondoa hapa?” “Mama?” Net akaita kwa ukali kidogo. “Umemwambia
nini Tunda?” “Labda atakuwa hajanielewa.” “Juu ya nini?” Net akauliza. “Acha
kunihoji maswali mengi. Hapa ni nyumbani kwangu.” Ritha akambadilikia mwanae.
“Ni nini kinaendelea mama!? Shida yako ni nini? Kwa nini
umeshindwa kumpokea Tunda kama mwanamke ninayempenda?” “Kwa kuwa umekataa kukaa
chini na kumfikiria vizuri.” “Unataka nifanye nini kukuthibitishia kuwa Tunda
amebadilika? Umempa mtego wa Gab, ameshinda. Nini unataka kutoka kwake!?
Ulitaka afanye nini!?” Net alikuwa anamshangaa mama yake nakushindwa hata
kuelewa.
“Nishakujibu kuhusu Gab. Ule sio mtihani wakumpima mtu kama
Tunda, nakusema ameshinda. Gab angekuwa mwanaume mwingine, hakika asingemkataa.
Mbali na sababu nyingine nyingi za mwanamke kama Tunda, kwanza lazima ujue bado
ana uchungu na Gabriel ndio maana alimkataa. Na yeye si binadamu bwana! Anaweza
kuumizwa. Huwezi kumpima mtu kama Tunda na Gab wakati amekukamata wewe. Nini
atanufaishwa na Gab ambacho hatapata kwako? Anajua hilo ndio maana anajifanya
mtakatifu kwako.” Yule mama akaendelea.
“Siwezi kuwa mjinga au kudanganywa na Tunda kama alivyofanya
kwa Gab na wewe sasa hivi. Eti nimekaa hapa, namwangalia tu anavyojidai kuwa
amebadilika, ameokoka, eti sasa hivi ni malaika na wewe unataka kumuoa! Hata
kidogo. Sikubali.”
“Wageni wote hapa wakiume, karibia asilimia 90, kasoro ya aliokuja nao bibi yako tu, amelala nao. Kwa nini unataka kunidhalilisha hapa mjini? Wasichana wote waliojaa humo makanisani, leo unakuja kumuoa yeye!? Kwa nini Net? Naomba pata muda ufikirie. Tunda hawezi kuwa mke wako. Naomba mwanangu punguza mwendo. Umefanya haraka sana juu ya huyu Tunda.” Net akazidi kuumia.
“Nafikiri nimefanya sana haraka kwako mama. Hata hii shuguli
sikutakiwa kuifanyia hapa. Nana angeshukia nyumbani kwangu, na mambo mengine
yangeendelea kama kawaida, nyumbani kwangu. Lakini sikutaka haya mambo yaende
mbali. Sikutaka tumuingize Nana katika hili ndio maana nikamleta hapa na
kumrudisha Tunda kwako japo ulimuumiza sana.”
“Nakupa muda zaidi. Utakapokuwa tayari utanitafuta. Lakini
ukae ukijua nitamuoa Tunda, tena haraka iwezekanavyo. Unajua pakunipata pindi
utakapo kuwa tayari. Na kwa kuwa Tunda ni kero kwako, nitajitahidi kumuweka
mbali sana na wewe, ili asikukere na usimuumize.” Mama Cote alishtuka sana.
Akajua Net akihama pale ndani tena, akarudi nyumbani kwake, bibi Cote atafahamu
na kuibua maswali zaidi.
“Kwa hiyo na wewe unaondoka!?” “Humtaki Tunda, na Tunda
atakuwa mke wangu hivi karibuni, unafikiri nitafanya nini?” “Na kazi unaacha?”
“Kwa nini niache kazi!?” “Sijui. Labda unataka
kuniadhibu.” Mama Cote alitumia silaha yake kwa haraka, aliyojua kumvuta
nayo Net. Machozi. Net akamsogelea. “Nakupenda sana mama yangu. Na nilimuahidi
baba nitakuwa na wewe wakati wote. Hakuna mtu wala kitu kitaingilia katikati
yetu. Siwezi kuacha kazi. Nilikuahidi maisha yangu ya familia hayataingilia
kazi yangu, na bado itabaki hivyo.”
“Siwezi kukuadhibu kwa kutokumkubali mwanamke ninayempenda
mimi, lakini naona haitakuwa sawa kuendelea kukuletea Tunda, halafu unaiishia
kumuumiza. Sio sawa kwako wala kwake. Nilikubali kuja naye hapa leo, kwa kuwa
ulisema huna neno. Lakini sasa hivi nimejua kuwa ulikubali sababu ya Nana.
Ulijua Nana asingefurahia kuona Tunda hakaribishwi nyumbani. Lakini usiwe na
wasiwasi, Tunda hatakubugudhi tena na wala haya mambo hayatafika kwa Nana.
Usiwe na wasiwasi juu ya hilo. Usiku mwema mama.” Net akambusu mama yake,
akaenda kumsindikiza bibi yake kitandani huku wakitaniana. Waliomba naye, kisha
akondoka kwenda kumfuata Tunda.
Net kwa Tunda.
Net alimkuta Tunda, ameshaogo na kuvaa nguo zake za kulalia,
amejilaza kwenye kochi anaangalia tv. “Nilikuomba usiwe unanikimbia Tunda.”
“Nilimuomba mama yako aniagie.” “Tangia lini mimi na wewe tunawasiliana kwa
kupitia mama yangu? Ingechukua dakika ngapi kuniaga pale wakati unaondoka?”
“Sikutaka kukusumbua katikati ya wageni. Halafu nilikuwa nimekasirika Net,
sikutaka kuongea kabisa. Kuhofia kuongea neno ambalo lingekuudhi bure, wakati
nilikuona unafurahia na wenzako.” Net akakaa, Tunda akasogeza miguu vizuri kama
kumpisha apate nafasi vizuri.
“Net!” Tunda akaita na kukaa vizuri. Net akabaki
akimwangalia. “Naomba uniambie ukweli. Na kumbuka maisha ambayo nimeishi. Tokea
nazaliwa nimekuwa mtu wa kukataliwa na watu, nimeishi kwenye majumba ya watu
kwa kubembeleza. Nataka kujua ukweli ni kwa nini unataka kunioa wakati…” Tunda
akaanza kulia. “Mimi naona..” Tunda
akakwama.
“Unaona nini Tunda? Niambie unachotaka.” “Sijui Net. Naona kama najiingiza kwenye matatizo.
Nilitegemea kupata faraja kwenye ndoa, lakini inaanza na vipingamizi vikali!
Tena kutoka kwa mtu wa muhimu sana kwako, anayenitangazia vita mpaka kifo
chake. Niambie itakuaje? Tutakuwa na ndoa ya namna gani?” Net akavuta
pumzi kwa nguvu, akakaa vizuri na kujiegemeza kwenye kochi.
“Hata mimi sijui Tunda. Sikuwahi kupenda kabla, na wala
sijawahi kuoa. Sitakuwa na majibu yote ya maswali yako.” Net akanyamaza kwa
muda. Kisha akaendelea. “Unajua umenifanya nijiulize Tunda. Hivi kweli
unanipenda wewe au ni kwa kuwa nimetokea tu unanifahamu? Hivi mtu akikuuliza
kwa nini unakubali kuolewa na Net, utasemaje?” “Nakupenda Net.” Net akakaa
sawa.
“Kweli? Naomba usichanganye upendo, na wewe kujikuta
umeangukia mikononi mwangu. Mtu unayempenda huwezi ukawa ukimfanyia hivi. Hii
ni mara ya pili kunikimbia Tunda. Tena leo umeniacha katikati ya tafrija yetu,
mbele ya wageni niliowaalika kuja kuona nikimvisha pete ya uchumba mwanamke
niliyewatangazia nina mpenda. Mimi ndiye nimekuwa mtu wakukukimbilia kila
wakati na kukuomba urudi. Mimi ndiye nimekuwa mtu wakupigania haya mahusiano
yetu kila wakati!” Net alikuwa amekasirika na yeye.
“Unamuacha Nana, Maya na marafiki zangu waliosafiri safari
ndefu kuja maalumu kwa ajili ya hili tukio. Bila kuaga, tena katikati yao! Huonekani kama mwenzangu unahaja na haya
mahusiano hata kidogo. Unanifanya nitilie mashaka viwango vyangu vya uanaume.
Labda sijafikia viwango vya mwanaume unayemtaka maishani mwako.” “Hapana Net.”
Tunda alijua angebembelezwa, kumbe ameharibu uzunguni.
“Naomba nikuombe kitu kimoja Tunda, tena kabla hatujafika
mbali. Pata muda wakufikiria. Nataka ufikirie kama kweli mimi nafaa kuwa mume
wako au la. Usiogope kuniambia, nitakuelewa tu.” “Net na..” “Usiharakishe
Tunda.” Tunda alitaka kujibu, Net akamkatisha. “Naomba pata muda. Tutaongea
zaidi baada ya hapo.” Net akasimama.
“Ukiondoka humu ndani, ujue unaondoka na mimi Net. Hutaniacha
nikilia tena. Nimeamua kuwa mke wako, wala sihitaji kufikiria. Niliondoka
kuepusha vurugu pale mbele za wageni. Mama hataki kuniona na wewe. Naomba
usiondoke tafadhali. Nakupenda na nimeamua kuwa na wewe. Ila naomba nisiwe
naenda pale kwa mama yako kwa kipindi hiki. Naomba tumpe nafasi.” Tunda alikuwa
amesimama na yeye. Net akarudi kukaa.
“Kweli nakupenda Net,
wala sihitaji kufikiria juu ya hilo. Umekuja kwangu nikiwa sijajiandaa kama
naweza kuolewa na mtu kama wewe na mpaka sasa siamini kama utakuwa mume wangu.
Naona kama naota!” “Usicheke Tunda! Unanitia wasiwasi bwana! Kila wakati wewe
unanikimbia tu!” “Mimi mkeo, Net. Wala huna haja yakunikimbia.” “Wewe ndio
unakimbia.” “Napaniki vibaya sana, hasa nikivamiwa na watu kama mama Cote. Huo
ndio udhaifu wangu. Nitajirekebisha.”
“Kwani alikwambiaje?” “Haitasaidia hata nikikwambia. Ila
nimemuahidi sitamsumbua kwa kufika nyumbani kwake au sitafika mahali ninapojua
atakuwepo, mpaka atakapokuwa tayari kuniona.” Tunda akarudi kukaa pembeni ya
Net na kuanza kuangalia pete yake.
“Umeipenda?” Net akauliza. “Sanaaaaa! Imetoka kidoleni kwa
bibi Cote! Usinitanie kabisa. Nahisi nipo ndotoni. Sasa unajua kinachofuata
nini?” “Sijui.” Net akajibu huku akicheka. “Na wewe uende ukweni.” “Wapi tena?
Nishamuona baba na akanipa baraka zote.” “Ujue siamini! Baba atakuwa amefurahi
sana!” “Sana. Ila nimemuhurumia. Alitamani kuwepo. Na anaonekana mgonjwa.
Umefikia wapi maswala yake?”
“Naona nimepata wakili mzuri kweli. Anafanya mambo kwa
haraka! Ameshaanza kukusanya uthibitisho. Yaani hii ni siku kama ya 10 tokea
aanze, ameshakwenda kuzungumza na baba zaidi ya mara tatu, ashakata rufaa.
Ijumaa alinipigia simu kuwa anashugulikia jumanne apate ruhusa ya kwenda hospitalini.
Japokuwa kampuni yao inadai pesa nyingi, lakini naona wanafanya kazi kwa
ukweli.” Tunda akaendelea.
“Pesa ya kodi ya hapa nimemuomba mwenye nyumba anisubirie
kidogo. Ili kuwalipa wao wanasheria kwanza, ili wajue ninampa baba kipaumbele,
wafanye haraka. Na nimelipa kodi yote ya kule ofisini. Ili mwenye nyumba
asinitoe. Pale napapenda. Ni rahisi watu kufika, halafu pako wazi, barabarani.
Panajiuza penyewe. Sitaki kupapoteza kwa sasa. Kwa hiyo kuhusu baba, naona
jumanne, anaweza kupata ruhusa ya kwenda kutibiwa. ” Tunda akamalizia hivyo.
“Cha kwanza nakupongeza Tunda. Umekuwa na malengo
unayohakikisha unayafuatilia. Unanifanya nijisikie vizuri.” Tunda akacheka. “Najitahidi
hivyo hivyo.” “Unafanya vizuri sana. Halafu kuhusu hapa, kwani unampango wa
kupafanyia nini baada ya kufunga ndoa?” Tunda akacheka tena, nakuzungusha pete
yake ya uchumba.
“Bado siamini!” “Ndio tunatakiwa kufikiria hilo.” “Kwani
ulitaka tufunge ndoa lini?” “Haraka iwezekanavyo.” Tunda akatulia kidogo kama
anayemtaka afikirie zaidi. “Au wewe ulifikiriaje?” “Mimi tena! Sina kipingamizi
Net. Nasubiria kwa hamu kweli!” “Kwani kodi ya hapa inaisha lini?” “Mwisho wa
mwezi huu. Nilitakiwa kulipa kodi tokea tarehe moja.” “Basi mwambie mwenye
nyumba kuwa utahama. Unaomba umlipe ya mwezi mmoja mwingine, lakini unaweza
usikae mpaka huo muda ukaisha.” “Akipata
mmpangaji kabla hatujafunga ndoa?” Tunda akauliza.
“Cha kwanza nitajitahidi kuhakikisha tunafunga ndoa haraka.
Nitazungumza na mchungaji wako na wangu. Japo walishatangulia kuniambia, ni
lazima itangazwe mara tatu. Inamaana kama tukifanya kwa haraka, wataanza
jumapili ijayo. Zipite jumapili tatu, Mungu akisaidia pakawa hakuna
kipingamizi, basi, jumamosi ya nne yake, itakuwa harusi yetu.” Tunda akacheka
kama asiyeamini.
“Ikitokea kuna jambo hapo katikati, tukashindwa kuona kwa
muda huo, sitashindwa pakukuweka mpaka tufunge ndoa.” Tunda akajisikia vizuri
sana. “Asante Net. Ninafuraha yakupitiliza.” Net akacheka. “Karibu.” Akajibu
Net.
“Lakini Net, baba akitoka jela, nilitamani kuishi naye kwa
muda. Angalau arudie hali yake ndipo nimtafutie kitu chakufanya awe na maisha
yake.” “Na mkewe?” Net akauliza. “Kwa jinsi alivyonisimulia, ni kama yule
mwanamke alimwambia waachane siku tatu kabla ya hukumu. Akambembeleza
wasiachane, amsamehe kwa lolote linalomsababisha kumuomba talaka. Lakini
anasema siku moja kabla ya kwenda mahakamani, mama Chale, alimwambia
ameshafuatilia mipango ya talaka. Hamtaki tena. Hata kama atashinda kesi,
akitoka mahakamani asirudi tena nyumani. Aendelee na maisha yake. Na baba
anasema hajamona tena tokea afungwe.”
“Alishajaribu kumtafuta kwa simu?” “Hizi ni jela za Tanzania
Net. Anamtafutaje? Ila anasema alipokuwa mahakamani siku ile, alimwambia dada
yake, mama Sera, akamwambie Mama Chale kuwa amehukumiwa kifungo na atakuwa
Segerea. Hakumtafuta mpaka juzi ijumaa mimi nazungumza naye, baba hajamuona
wala kumsikia.” Net akanyamaza.
“Sitaki akitoka jela ajikute peke yake mtaani.” “Hata mimi
nisingetaka iwe hivyo. Tutajua chakufanya siku hiyo. Ila kwa sasa chamuhimu ni
kumkazania huyo wakili wake, ahakikishe anakwenda kutibiwa. Amedhoofu sana.
Halafu nilimshika ni kama anahoma.” Tunda aliinama na kunyamaza.
“Atakuwa sawa tu. Jumanne sio mbali. Nikuwatafuta tena kesho
na kuweka msisitizo.” “Nitampigia tena kesho kujua amefikia wapi. Na nitakwenda
kumuona baba kama nitaruhusiwa kumuona. Nijue anaendeleaje.” Net akamsogelea na
kumbusu kichwani pale alipokuwa amekaa na kuinama kama anayefikiria. “Asante.”
Tunda akamgeukia na kumshukuru. Akampa tabasamu.
“Unafikiria nini tena? Mbona hilo la baba ni kama limekaa
vizuri?” “Kuna sehemu mbili nataka kwenda.” “Wapi?” Net akauliza wakati
anamvuta mkono. Akaubusu. Tunda akacheka. “Kwa shangazi. Huko ni lazima twende
wote, kama kuwaringishia tu kina Sera, lakini nitajidai nimeenda kuwashukuru
kwa kunipa hifadhi wakati ule mpaka nikakutanishwa na wewe.” Net akacheka sana.
“Tunda!” “Oooh kabisa Net. Walijaribu kuzuia baraka zangu,
lakini ona Mungu alivyohakikisha mpaka nimepata, japo kwa kuchelewa!” Tunda
akamuonyeshea Net kidole chake chenye pete. Wakacheka.
“Usifanye mchezo na Mungu wangu! Hatatulia mpaka
aone napata aliyonikusudia.” “Sasa mbona unatingishwa na mama kama unalijua
hilo?” “Mama yako yule habari nyingine. Kwanza ujue ni kama kwake inabidi
kujirudi kidogo. Nimemuumiza yule mama. Anahaki. Tuendelee na sehemu nyingine
ninayotaka kwenda. Japo...” Akasita na kumwangalia Net, macho yakagongana,
ikawa kama ameamsha kitu kwa Net. Akashangaa Net anamvuta karibu nakuanza
kumbusu.
Tunda akaona alitendee haki lile busu. Akapandisha
miguu yote kwenye kochi, akamgeukia Net akawa kama amejilaza kwake. Walipeana
mabusu ya muda huku Net akimpapasa vizuri, mpaka akamuamsha Tunda, nakuanza
mihemo. Ile hali ikaendelea, Tunda akiendelea kupata busu huku akisikia mikono
ya Net mwilini mwake nakumfanya azidi kujisogeza. Kasi ikaongezeka, wakaanza
kung’ang’aniana kwa uchu na tamaa, kila mmoja anamtaka mwenzake zaidi. Net
alipoona na yeye anakaribia kupitiliza, akasimama kwa haraka, akaenda kwenye
friji ya Tunda.
“Kuna maji ya kunywa humu?” Tunda akaendelea kuvuta
pumzi taratibu huku ameinama kwa aibu akijaribu kutulia na Net mwenyewe
akijaribu kutulia huko alipokua. Tunda hakumjibu wala kumwangalia. Akamsikia
anafungua friji. Kimya kikazuka. Akamuona anaelekea chooni. Tunda kimya,
ameinama palepale sebuleni. Nyumba ikawa kimya kama hakuna mtu.
“Niambie
sehemu nyingine unayotaka kwenda.” Baada ya muda akamsikia akiongea akiwa
anatokea chooni. “Kwa mama.” Tunda akatulia kidogo. Net akarudi kukaa palepale
kwenye kochi. Akambusu tu kichwani. Tunda akacheka kwa aibu bila hata kumtizama
akaona aendelee. “Nataka nikamuombe msamaha, kwa chochote nilichokosea,
ilimradi tu yaishe. Nataka kuanza maisha mapya. Hata asiponisamehe, lakini
nataka niwe nimefanya upande wangu, hayo mengine namwachia Mungu kama
ulivyonishauri.” “Ni uamuzi mzuri.” Tunda akatulia kidogo.
“Nakuonea wivu Net! Unaye mama anayekupigania.
Hataki akuone unaingia matatizoni, kitu ambacho mimi sikuwahi kukipata
maishani. Hicho tu ndio kitu ninacho muheshimu mama yako. Anakupenda sana.” “Ila
natamani ajifunze kuheshimu maamuzi yangu. Naona anavuka mipaka.” “Hapana Net.
Yupo sahihi. Sio rahisi kwa mama mwenye upendo wa kiasi kile kwa wanae eti kuruhusu
tu, mwanae awe na mtu kama mimi! Haijalishi Net. Niwe nimebadilika au la, bado
ni ngumu. Ndio maana naona nimpishe kabisa. Anione pale itakapo lazimu tu, sio
vinginevyo. Lakini sijui nifanyaje upande wa mali.” Net akakunja uso.
“Mali tena?” Net akauliza akiwa hajaelewa. “Hata
sielewi Net. Ujue mama yako anapokuwa na mimi anapandwa sana na hasira sana.
Anazungumza mambo mengi, sijui lipi ni lipi.” “Niambie kuhusu mali. Alikwambia
nini?” “Naweza nisipatie sana, lakini ni kama alitamka kuwa sasa hivi
nakung’ang’ania wewe simtaki tena Gabriel kwa kuwa wewe una mali nyingi kuliko
Gabriel.” Moyo wa Net ulipasuka paa! Walimuonya mama Cote asije zungumza na
Tunda mambo ya utajiri unaozunguka hiyo familia ya Cote.
“Umesema nini juu ya mali!?” Net akataka kujua sasa
zaidi kile mama yake amesema. Kama ameharibu mpango mzima au bado. “Ni kama
alisema nimejua kuwa umeachiwa urithi mkubwa sana na babu yako, na ni kama bibi
yako pia akifa, wewe ndio mtawala wa mali zote huko nchini Canada. Kitu kama
hicho, sijui! Akasisitiza kuwa siwezi kuwa mtawala kwenye Cote. Yeye ndio
anastahili kwa kuwa amehangaika tokea mwanzo kujenga. Akasema hata kama babu
yako ndio amelipia kujenga ile nyumba pale anakoishi, au sijui alisema nini,
ila amesisitiza uwa yeye ndio amesimamia ujenzi wa ile nyumba kuanzia mwanzo
mpaka mwisho.”
“Amesisitiza hakuna Cote hapa nchini bila yeye.
Yaani hata wewe upo hapa nchini kwa sababu yake. Kitu kama hicho. Halafu
anasema nakudanganya wewe na bibi yako
kuwa nimebadilika. Lakini yeye sio mjinga na wala nisidhani kuwa nimeshinda.
Mnanitumia tu.” “Kivipi!?” Net akauliza akiwa hajaelewa.
“Ni mambo mengi magumu hayaelewiki Net.” “Lakini
yeye alisemaje? Niambie kile alichokwambia yeye.” “Amesema wewe na bibi yako mnanitumia
kila mmoja kwa sababu zenu tofauti tofauti. Vile bibi yako leo alivyonitangaza
mimi kama ndiye mama Cote au mrithi sijui wa kiti chake! Wale rafiki zako na
Maya wakachangamka sana pale?” Tunda akataka kumkumbusha Net, asijue Net
mwenyewe bado yupo kwenye mshtuko wa hilo tangazo.
“Nakumbuka. Ehe?” Net akataka aendelee. “Mimi
sikuelewa pale. Lakini yeye anasema ni kwa ajili ya mambo yake anayoyafanya.
Ametangaza vile kwa ajili sijui ya watu wa chama anachokiongoza na wakubwa
sijui wanaomfuatilia au watu wanaomfuatilia sijui sina uhakika! Lakini amesema
amenitangaza mimi malaya ili kuonyesha na kuaminisha ulimwengu kuwa anakubali malaya,
au machagudoa kwa kiasi cha kukubali malaya kama mimi kuolewa na mjukuu wake
ambaye alikuwa akisubiriwa na kila mtu kujua atamuoa nani!” Net akaumia sana.
“Haya.
Akasema na wewe umenichagua mimi sio sababu ya mapenzi, ila ni sababu kama za
bibi yako. Lakini zaidi kumfurahisha bibi yako kumuonyesha unamuunga mkono
kwenye hizo harakati za wanawake, sijui kitu kama hicho! Yaani kuoa kahaba, au
Changudoa kama mimi ni kumuunga mkono kwenye anachokifanya! Sijui bwana Net! Lakini
ni mambo yanayofanana na hayo lakini
sikuelewa vizuri kwa kuwa zilikuwa shutuma nzito, zinazoendana na kweli.” Tunda
akaendelea.
“Haya, ukimsikiliza tena zaidi ni kama hata mimi
mwenyewe haniamini! Anasema nimekuloga. Nimekuzika makaburini ili nirithi
mapesa yenu ambayo mnayo mengi, sijui! Kwa hiyo hatakubali huo utajiri au
urithi ukaja kwangu wakati yeye amehangaika sana na kina Cote. Hapo napo
aliongea sana Net. Mambo mengi. Sikuelewa na wala sijui katika hilo
namsaidiaje.” Tunda ndiye hakuwa ameelewa. Lakini Net akafunguka macho na akili
ikapata mwanga, juu ya chuki kubwa ya mama yake kwa Tunda.
Aliumia sana Net, akabaki akijiuliza hili na
kujumlisha lile. Akajua mengi yanatokana na mali tu! Yeye akidhani ni mapenzi
kutoka kwa mama yake, kumbe analinda mali! Ilimuumiza sana Net. Mama yake
alimwambia Tunda mambo mengi ambayo alishaomba familia nzima, wasimuhusishe
nayo Tunda, ili yeye Tunda aweze kumtenga Net na mali kama wasichana wengi
nchini Canada. Wanaompenda yeye Net kwa kuwa ni Cote.
Net alimtaka Tunda amtizame yeye kama Net kwanza.
Kabla ya Nathaniel Cote anayetangazwa na kuabudiwa huko alikozaliwa, aliko bibi
yake. Kitu kinachomkera na kuona ni bora kuwepo nchini Tanzania ambapo yupo
huru, hakuna anayemfahamu isipokuwa huyo mama yake na kina Gabriel. Alikotoka
Net, chochote watakachofanya familia hiyo, ni tukio la kuuza magazeti kitu
kinachowanyima uhuru wakuishi maisha yao.
Leo mama yake amemkosea sana, na kumuumiza sababu
ya pesa! Tena akiwa amejitoa akimtumikia kwa kiwango cha chini sana akizunguka
kumtafutia tenda zilizokuwa zikimuingizia yeye pesa wala si Net. Hakumdai zaidi
ya mshahara wake tu. Net aliumia sana.
“Lini sasa tunaenda ukweni?” Tunda akauliza na
kujisogeza kwa Net aliyekuwa amepotelea mawazoni akiwa amefunga macho. “Au
umebadili mawazo, ndoa hutaki tena?” “Kukuoa wewe, sijambo nililokurupuka
Tunda. Mungu alisha niandaa kwa muda mrefu sana. Nakupenda na lazima nitakuoa
tu. Lakini siku kama ya kesho, jumatatu nakuwa na kazi nyingi sana, labda
twende jioni.” “Sawa kwa kuwa itakuwa jioni, tuanze kwanza kwa mama. Kesho iwe
mama tu.”
“Nataka nimalize hili la mama kwanza. Ikiwezekana
tuwekane sawa ndipo niende kwa kina Sera. Lakini kwa kina Sera lazima.” “Sawa.”
Waliendelea kuongea wakiweka mipango, mwishowe Net akaaga na kuondoka akiwa
ameumia sana, Tunda sijue.
Jumatatu!
Siku hiyo ilianza na hekaheka kweli hasa kwa Tunda. Alianzia
ofisini kwa wakili wa baba yake. Wakazungumza na kumuhimiza ni lazima baba yake
kesho apelekwe hospitalini. Baada yakumsikia mikakati yake na pale alipofikia,
akaridhika na kuondoka kurudi ofisini kwake. Siku za jumatatu hawakuwa
wakiwasiliana sana na Net zaidi ya salamu ya asubuhi kabla hawajatoka
kitandani. Watapeana mipango ya siku nzima, siku inaanza.
Hakuwa amemsikia Net siku hiyo, na yeye akaendelea na kazi
zake akiwa na Betty tu, wakiongea hapa na pale. Betty alikuwepo kanisani siku
iliyopita. Akataka kuiona kwa karibu pete hiyo ya Tunda. Basi, akaitizama na
kuishika. “Umeuchinja dada Tunda!” Pesa huleta heshima. Japokuwa Betty alikuwa
mkubwa kwa Tunda bosi wake, aliweka heshima. Tunda alicheka tu.
Kazi ziliendelea, ilipofika mchana Jaz, msichana aliyemkimbia
Tunda pale kazini, akarudi kuomba kazi tena. Week ilishapita, hakuwepo kazini,
na siku ya jumatano alipokwenda kwenye bible study, hakumsalimia Tunda bosi
wake. “Kwa nini unataka kurudi na kwa nini uliondoka Jaz?” Kimya. “Umesambaza
maneno mengi machafu kanisani juu yangu.” “Nisamehe.” “Nimekusamehe lakini hapa
sitahitaji tena mtu wa pili. Tumeshauriana na mama Penny, tumeona Betty peke
yake atatosha. Kwanza ameweza kufanya kazi zote bila shida. Ni kweli hata
ukirudi humu, hutakuwa na kazi ya kufanya. Halafu sitaweza tena kukulipa na
wewe kwa kuwa nimeamua kumuongezea mshahara Betty, kwa kuwa nimemuona ameweza
kufanya kazi zako vizuri bila shida wala kulalamika kama wewe Jaz. Nashauri
urudi kwa mama Penny, anafahamiana na watu wengi. Atakusaidia kupata kazi
kwengine.” Tunda akamuaga, ikabidi Jaz aondoke. Hata Betty hakuamini kama Tunda
amefanya hivyo. Na yeye nidhamu ikaongezeka.
Baada ya miaka mingi, Net mrudisha Tunda kwa
mama yake mzazi, Akiwa mchumba.
Ilipofika
kwenye mida ya saa 10 jioni, Tunda alirudi nyumbani kwake kwenda kujitayarisha
kwa kwenda kumuona mama yake. Wasiwasi ulizidi kumsumbua. Hofu ya kuja kuiona
tena sura ya baba Tom, ikazidi kumkandamiza nakutamani kama asiende tena. Baba
Tom alikuwa msaliti mkubwa sana kwake. Alimtelekeza akiwa na mimba yake!
Net
alifika nyumbani kwa Tunda. Alimkuta ameshajiandaa lakini anawasiwasi sana. “Umependeza
sana. Lakini usoni unaonekana una hofu yakupitiliza!” “Nimeshindwa kula siku
nzima, namuwaza yule baba. Nafikiria kwenda kuomba msamaha ambao nilikuwa
nikisubiri miaka yote kuja kuombwa mimi!” Tunda akaanza kulia.
“Hujui jinsi alivyonitesa, tena bila msaada wa mama, Net.” “Nisikilize
Tunda. Unafanya kitu sahihi. Unasamehe kwa ajili ya nafsi yako si kwa ajili
yao. Utaona amani utakayopata baada ya hapo. Muachie Mungu atapambana naye.
Wewe twende ukafanye kwa nafasi yako.” “Mama
akinifukuza?” “Tutaondoka. Wala usiwaze upande wao, twende ukafanye
upande wako.” Tunda na Net wakaondoka mpaka nyumbani kwa mama yake Tunda huko
mitaa ya Kitunda alipowaacha wakiishi.
Kitunda kwa Mama Tunda!
Tunda
alishangaa kukuta familia ngeni kabisa kwake. Akamsalimia mama aliyemfungulia
mlango, kisha akaeleza shida yake. “Tunaweza kumuona Mama Tom?” Akaguna yule
mama akiwa amesimama palepale mlangoni. “Sipendi usumbufu wa usiku usiku!”
“Samahani. Tumechelewa kwenye foleni.” Tunda akajibu kiustarabu. “Sijui kama
huyo Mama Tom Yupo! Labda mpite huko nyuma.” Alijibu mwanamke aliyewafungulia
mlango, huku akionyesha kidole kuwaashiria wapite. “Asante sana.” Tunda akashukuru
na kumvuta Net mkono.
Nyumba
ilikuwa imejaa watu asiowafahamu kabisa. Ule usafi aliouacha kwenye ile nyumba
haukuwepo kabisa. Kwa kuwa alikuwa akiifahamu ile nyumba, Tunda hakupata shida
kutokea vyumba vya nyuma, ambavyo havikuwa vikitumiwa kipindi anaishi kwenye
nyumba hiyo isipokuwa chumba kimoja kilikuwa kama stoo na kingine alikuwa
akilala mfanyakazi wa kiume.
Na huko
uwani nako Tunda alikuta watu wengine.
Alisita kidogo. “Habari zenu?” Wote walibaki wakimtizama. Mara ukagongwa
mlango wa nyuma, mtoto akitaka auziwe icecream. Alisimama binti ambaye alikuwa
na umri unaokaribiana na Tunda, akaingia ndani na kutoka na icecream. Tunda
akabaki ameshangaa.
“Tunda!”
Net akamshtua kidogo. “Samahanini jamani. Tunataka kumuona Mama Tom.”
Wakatizamana na kucheka. “Na nyinyi pia mnamdai?” Walimuuliza Tunda na Net. “Kama
mnamdai muandike maumivu tu. Wenzenu wanapishana hapa! Hivi ni jana tu walikuja
kumbeba wanawake wenzake wakampeleka polisi. Kala pesa ya kikoba!” Wakacheka
wote kwa kupokezana. Tunda aliumia sana.
“Sisi
hatumdai. Mimi ni mwanae na huyu ni mchumba wangu.” Wote wakabaki wametoa
macho. “Wewe ndio Tunda!?” Mmoja wao akauliza. “Ndiyo.” Tunda akajibu. “Mama
Shangazi! Mama Shangazi!” Mmoja aliita. “Njoo umuone Tunda!” Tunda akabaki
ametulia. Alishangaa kuona watu wengine wanatoka nyumba kubwa na wengine
vyumbani kuja kumshangaa yeye kama mnyama wa mbuga za wanyama.
“Jamani,
kwani Mama Tom yuko wapi?” Ikabidi Tunda kuuliza tu. “Wanae wapo chumba hicho
hapo. Anawafungia kama kuku!” Tunda akasogea mpaka kwenye hicho chumba
alichoonyeshwa, huku Net akimfuata nyuma.
Akaanza
kugonga. “Nani?” Sauti kutoka ndani ikauliza. “We Tom! Ni mimi Tunda. Fungua
mlango.” Waliona taa ya ndani imewashwa kisha mtu akachungulia dirishani. “Umesema
Tunda, dada Tunda?” “Ndiyo. Ni mimi, fungua usiogope.” “Wewe Tom, mama amesema
tusimfungulie mtu yeyote. Shauri yako.” Walisikia sauti ya mtoto wa kike
ikimuonya Tom.
“Ni
Tunda. Tunda yule dada yetu. Wewe humjui ulikuwa mdogo sana. Tena alikulea.
Nimfungulie?” “Sijui.” Walikaa kimya kwa muda. “Kwani mama yuko wapi?” Tunda
akauliza. “Ametoka muda kweli! Amesema tusitoke wala kufungua mlango mpaka yeye
mwenyewe awepo.” Tom akajibu. “Basi sisi tunaenda kumsubiria nje kwenye gari.
Akirudi mama, mje kutuita.” Tunda akashangaa mlango unafunguliwa, kisha Tom
akatoka.
“Mbona
uliondoka bila kuniaga?” Ndio swali la kwanza Tom akamuuliza Tunda. “Sikujua
kama sitarudi tena. Mnaendeleaje?” “Njooni ndani.” Tom aliwataka waingie ndani.
Tunda na Net wakaingia kisha akafunga mlango tena. “Aneti amekuwa mkubwa! Njoo
unisalimie. Sijui unanikumbuka?” Tunda alimuongelesha yule mtoto wa kike kwa
upendo.
“Mimi
ndiye nilikuwa nikikulea.” Tunda aliongeza, lakini Aneti hakujibu. “Umekuwa
mkubwa Tom! Mnaendeleaje?” “Umependeza sana Tunda, dada yangu!” Tom akajibu. “Asante.”
“Huyo ni nani?” Tom akauliza. “Ni mchumba wangu, anaitwa Net.” “Umepata mchumba
wa kizungu!? Ndio maana umebadilika Tunda. Anaonekana ni mzungu mwenye hela. Anasikia
Kiswahili?” Tunda akacheka. Akakumbuka utundu wa Tom.
“Anaelewa
kila kitu. Hapo alipo anakusikiliza na anaelewa kila kitu unachoongea.” “Acha
masihara bwana Tunda! Usiniogopeshe. Mbona haongei sasa?” Tunda akazidi
kucheka. “We Tom hujaacha utundu tu?” “Mambo yamebadilika dada! Mama amekuwa
kama kichaa.” “Baba yako yuko wapi?” “Amefungwa.” Tunda akashtuka sana. “Nini
tena!?” Tom akanyamaza, akaonekana kusita.
“Kuna
nini Tom?” “Alikuwa akimfanyia mambo mabaya Aneti, halafu alimbaka dada wa
kazi.” “Yule niliyemuacha?” “Yule alizaa naye, mama akamfukuza na kuletewa na
bibi mtoto mdogo kutoka kijijini. Ndiye aliyekuwa akitusaidia kazi.” Tunda
alimwangalia Aneti kwa kumuhurumia sana. “Pole Aneti.” “Hapo bado yupo kwenye
matibabu. Tulikuwa hatujui kitu anachomfanyia Aneti, mpaka akaanza kunuka
sana.” Tom akaendelea.
“Kumbe
alimuambukiza mtoto ugonjwa wa zinaa, mama kuja kumpeleka hospitalini akaambiwa
Aneti ameharibika sana na anaugonjwa wa gonorea. Ikabidi asafishwe sana.
Alikuwa ameoza. Wakati mama yupo hospitalini amelazwa na Aneti, baba akambaka
yule msichana wa kazi. Sasa mimi wakati najiandaa kwenda shule asubuhi,
nikashangaa yule mtoto haamki kunisaidia kuandaa chai. Kwenda kugonga,
nikamkuta amepoteza fahamu.”
“Ndio
ikabidi nimpigie simu mama, baba alikuwa ameshatoroka. Nahisi alimziba mdomo na
pua ili asipige kelele wakati anambaka, ndio akapoteza fahamu. Mama akatuma
majirani waje wamchukue na kumkimbiza hospitalini. Mambo yakafika polisi, baba
akatafutwa na kukamatwa.”
“Hivi
hao wote unaowaona hapo ni ndugu zake baba, wametuchukia sana. Wanatulaumu eti
kwa nini tulimshitaki baba ambaye anategemewa sana huko kwao. Wanatuambia ni
mambo ambayo tungepaswa kuyamaliza kindugu tu. Tangia waje baada ya baba
kukamatwa, hawajaondoka tena. Wametufukuza kwenye hiyo nyumba kubwa, lakini
mama amekataa kuondoka, ndio ameomba tupewe angalau hiki chumba kimoja wakati
anatafuta pakwenda kuishi. Mama amechanganyikiwa kabisa, Tunda. Kazi
imemshinda, anakazi ya kukopa mpaka aibu! Kila siku anakuja kudaiwa hapa, tena
anadhalilishwa kweli!” Tunda alizidi kuumia.
“Amekwenda
wapi sasa?” “Anasema kuna mahali anadai pesa zake. Ni mwezi sasa, anazifuatilia
hizo pesa. Nikimshauri aachane nazo tuanze kuhangaika kutafuta pesa kwa njia
nyingine, anakuwa mkali kweli. Anatufungia mchana na usiku. Hataki tutoke.
Akitukuta nje, utamuonea huruma. Anakuwa kama mwehu. Biashara zote zimemshinda.
Anazurula tu mtaani.”
“Sasa na
wewe shule?” “Na kwambia siruhusiwi kumuacha Aneti hata sekunde. Nampeleka
mpaka chooni. Hataki nisogee hata hatua moja mbali na Aneti. Nikimwambia
maswala ya shule, ni kama haelewi naongea nini. Nikikwambia hali ni mbaya, si
utani.” Tunda akabaki amepigwa na butwaa. Net alikuwa kimya akisikiliza tu.
Akavuta mkono wa Tunda na kuubusu. Tunda akavuta pumzi kwa nguvu nakubaki kimya
akiwatizama wale watoto.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Usikose muendelezo
kujua kitakachojiri mbeleni...
0 comments: