NILIPOTEA! SEHEMU YA 7.
Wakiwa kitandani mama na baba yao kina Sera, mama akaanza njama zake kwa kuanza kumdanganya mumewe. Akaanza kumwambia juu ya mipango mizuri anayofikiria juu ya Tunda mpaka akamshangaza na mumewe. “Mbona umebadilika gafla!?” “Hata nifanye nini Tunda ni damu yangu. Nimeona heri tumsaidie tu. Nitamsomesha, hata kama ni mafunzo ya muda mfupi kisha nimtafutie kazi.” Baba yake Sera akacheka. “Ingekuwa hatujatoka kwa walokole, ningesema umelewa!” Mama Sera akacheka sana.
“Au yale maji mwenzangu uliyokuwa ukinywa ilikuwa konyagi?” Mama yake Sera akaendelea kucheka. “Pale napo kazi ipo! Nyumba imepooza, haina hata wine! Khaa! Balaa gani hili?” “Hawamalizi kuomba! Mimi niliamua kufunga macho kukubali yaishe.” Walizidi kucheka kwa sauti. “Lakini yule mama ni mtanzania kabisaa, imekuaje awe na mtoto mzungu!?” “Huwajui walokole wewe! Wanahangaika hukooo, wakishindwa maisha, ndio wanarudi kwa Mungu wanajidai wameokoka. Wanafiki tu.” Mama Sera na mumewe waliendelea kukashifu na kucheka sana, mpaka walipolala.
Jumapili ambayo Net aliomba kufika jioni ili
azungumze na Tunda.
Waliamka siku inayofuata ilikuwa siku ya jumapili. Familia hiyo hawakuwa wakiacha kwenda kanisani. Kwa hiyo Tunda na Nyange walikuwa wakiamka alfajiri kama kawaida yao kuwaandalia kifungua kinywa, na kunyoosha nguo zao ili wawahi misa ya kwanza ya lugha ya kingereza. Tunda alijitahidi kuandaa meza vizuri sana, ili kuepuka ugomvi wa asubuhi asubuhi.
Lakini ghafla
hali ya hewa ikatibuka. Shangazi yake alianza
kwa kuulizia mkufu wake wa dhahabu aliokuwa amenunuliwa na watoto wake siku
ya mother’s day. Ikaanza kazi ya kusakwa huo mkufu. “Kwani uliweka wapi?” Mumewe akahoji huku akiendelea kusaidia
kutafuta. “Jana wakati naenda kwenye shuguli
ya Net nyumbani kwao, niliuacha hapa mezani! Tena nilitaka kuvaa
dhahabu, lakini nikaona nivae tu silver. Yaani nilinyanyua kabisa
nikitaka kuuvaa, tena niliweka mpaka shingoni,
nikarudisha hapa mezani na kuamua
kuvaa silver. Tena moyo ulisita kabisa! Najuta kupuuzia hisia
zangu!” Shangazi akalalamika kwa majuto.
“Basi muulize
Tunda na mwenzie tuliowaacha hapa ndani.” Ndicho alichokuwa akisubiria. Mumewe
alipoweka tu kituo, akatoka na kuwaita wote.
Watoto wake wote walisema waliuona huo mkufu mara ya mwisho
mezani kwa mama yao. Ndipo baba mwenye nyumba na yeye
akapandwa na hasira . “Sasa sikilizeni mabinti. Nautaka huo
mkufu wa mke wangu sasa hivi kabla
sijawang’oa meno. Sitaki mchezo.” Tunda na Nyange walibaki wametoa
macho.
“Mmesikia?” “Mimi sijaingia tena chumbani kwenu baba. Ni vile asubuhi tu
wakati nasafisha. Sijarudi huko tena.” Nyangeta
akajitetea, lakini Tunda alibaki
kimya kama hakuwepo pale kimawazo. “Na
wewe Tunda?” Kama aliyeshtuliwa
kutoka usingizini. “Abee!” “Mkufu wa shangazi
yako uko wapi?” Kabla hajajibu shangazi
yake akamnasa kofi kubwa sana la usoni. Tunda alipepesuka akarudi
nyuma. “Aaaaahh!” Tunda alisikika akigugumia maumivu huku ameshikilia uso kama unaotaka
kuanguka!
“Jizi hili mama! Ndiye atakuwa amekuchukulia mkufu
wako. Maana Nyange tumeishi naye
miaka yote hapa, mbona kusiibiwe kitu iwe sasa hivi yeye akiwepo?” Samatha akadakia.
“Nyange kalete mifuko yake tuangalie ndani.” Shangazi akatoa amri.
Nyange alikwenda na kuleta mifuko ya
Tunda. Mfuko wa kwanza ulipomiminwa tu, ule mkufu ukaanguka chini
mbele ya macho yao wote. “Haaa!” Kila mtu akashtuka mpaka
Tunda mwenyewe.
Yule
Mzee hakupoteza muda. Alichomoa mkanda
kiunoni mwake, nakuanza kumpiga
Tunda kila mahali huku akimpiga mateke kama mbwa na kumtukana sana.
Alimpiga mpaka jasho lilikuwa likimtoka huku akimwambia
jinsi alivyolaaniwa na hana
bahati kwenye maisha. Kwa kuwa ndio
shangazi yake alikuwa anataka kumpeleka shule lakini ameharibu kwa
kumwibia.
Tunda
alikuwa kigaragazwa pale chini kama tambara bovu mpaka Nyange alipoanza kupiga
yoe akikimbia nje kama mwehu akiomba msaada
kwa majirani, ndipo yule mzee alipomuachia na kuanza kumkimbiza sasa Nyange, kumrudisha ndani. Nyange alimnyanyua pale chini na kumpeleka
chumbani kwao. “Na asitoke huko ndani
mpaka baba yake atakapokuja kumchukua.
Hatuwezi kukaa na jizi humu ndani.” Shangazi akaweka msisitizo.
Baba yake alipigiwa simu palepale, huku akitishiwa kuwa
akichelewa kidogo tu, atamkuta mwanae kituo cha polisi. Baada ya muda
mfupi sana baba yake Tunda alifika pale. Alielezwa mabaya mengi ya
Tunda, na jinsi walivyomvumilia kwa muda mrefu,
lakini wamefika mwisho. Yule baba hakusema chochote katika hizo shutuma ila
kumuulizia mwanae. “Yuko wapi Tunda mwenyewe?” “Huko chumbani, amejifungia kwa aibu.” “Nimewasikia
na ninaomba radhi
kwa yote aliyofanya. Naomba mniitie, tuondoke.” Aliitwa
Nyange, nakuambiwa akamwite Tunda.
Baada ya muda Nyange alirudi huku akilia kwa hofu. “Hawezi
hata kunyanyuka kitandani.” Baba yake akasimama kwa haraka na wasiwasi. “Kwani nimgonjwa?”
Baba
yake akauliza huku akimtizama Nyange. Nyange
alishindwa kujibu akakimbilia
jikoni. “Kuna nini dada? Tunda ni
mgonjwa?” “Kwani huwa wezi wanafanywaje?” Mama Sera akamuuliza mdogo wake kwa jeuri sana.
Baba yake Tunda akaonelea aende akajionee yeye mwenyewe. Alishtuka na kurudi nyuma mara baada yakuingia mle
ndani na kumkuta Tunda hatizamiki. Alikuwa amepasuka sehemu ya juu ya jicho iliyosababisha kuvuja kwa
damu na kulowesha uso mzima mpaka mto aliokuwa amelalia. Midomo
yake ilikuwa imepasuka juu na chini, kila alipotoa pumzi nje, damu
zilitoka puani.
“Mungu wangu dada! Unauwa mtoto wangu
sababu ya mkufu!? Mmekosa utu kiasi cha kuweka mali mbele kuliko
binadamu?!” “Unatetea
tabia chafu kama hiyo kwa kuwa na wewe
ni mwizi.” Shemeji
yake akadakia. “Naomba muondoke sasa hivi ndani kwangu, na sitaki kukuona
wewe wala mtoto wako tena mkikanyaga hapa nyumbani kwangu. Nikiiona sura
yako hapa, baada ya dakika tano zijazo, nakupiga risasi ya mguu.
Toa mzoga wako uondoke.” “Mungu atakulipa shemeji. Ipo siku mtajutia
unyama mliofanya kwa mwanangu.” Yohana akambeba mwanae, Tunda na kuondoka naye.
Hakuna Msiba Usiekuwa na
Mwenzie.
Alikuwa
amevunjwa mbavu na damu ilikuwa
ikivuja kwa ndani. Mkono wake
wakushoto pia ulikuwa umevunjika kabisa mpaka ulitengana
na kuonekana mfupa kwa nje kuwa imetengana.
Na bega hilohilo la kushoto, lilitenguliwa. Matibabu yakaanza baada
yakufanyiwa x-ray. Akatobolewa na kuwekewa vyuma vilivyotokeza nje kama mshikaki.
Waliambiwa sio wakutoka pale siku za karibuni. Hilo likawa sio jambo baya.
Zikawa habari njema zaidi kwa baba yake ambaye hakujua atampeleka
wapi binti huyo aliyekuwa anakaribia miaka 20. Akaanza matibabu. Baba yake peke yake ndiye
aliyekuwa akimuuguza bila kuchoka asubuhi na jioni alirudi pale hospitalini kumuona
mwanae. Alimletea vyakula
vyakawaida. Wakati mwingine uji, wakati mwingine Tunda alijua kabisa amemletea chakula alichonunua kwa mama Lishe. Lakini
hakuacha kufika hapo. Alileta juice za kuongeza damu na kumsisitiza awe anakunywa.
Na kabla hajaondoka jioni, alihakikisha angalau anamnywesha hiyo juisi,
ndipo anamuacha mpaka kesho yake anapomletea
uji. Napo pia alikuwa akiwahi sana. Anahakikisha anamsaidia
kumpigisha mswaki, anamsaidia kunywa uji. Akiona ameshiba vizuri,
anamuongezea tena juisi ya kuongeza damu, ndipo anamuachia nyingine pembeni na kumsihi awe anakunywa kila wakati. “Itakusaidia
kuongeza damu.” Alisisitiza baba yake.
Wakati mwingine alimletea juisi za majani ambayo
alisema ameambiwa na watu inaongeza damu
kwa haraka. Rosella. Au matembele. Ikawa basi tu, anamuona vile baba yake
anavyohangaika kumuuguza na hakuwahi
kuzungumzia habari za ujauzito aliokuwa amepata wakati anaishi na mama yake,
ila tu kumuuguza kwa juhudi zake zote.
Siku zilikwenda,
madaktari
akiridhishwa na upataji wake nafuu. Swali la akitoka hapo atakwenda
wapi, sio kuwa lilimsumbua Tunda peke yake, hata baba yake pia. Anampeleka wapi
binti huyo! Elimu yake ni ya darasa la pili. Ndugu aliyebaki ni yeye tu. Hata Tunda
mwenyewe alizidi kukosa raha kila alipoambiwa anaendelea vizuri.
Akakumbuka kuwa kwa ndugu wote amezuiliwa kwenda kuishi. Hana ujuzi wowote ule, na baba yake
hakuonekana kama anazo pesa zakumtafutia chumba kama alivyokuwa ameahidiwa na
baba Tom.
Ilimbidi
baba yake azungumze na uongozi wa
hospitali kuomba Tunda aendelee kuwepo hapo mpaka atakapopona kabisa.
Alieleza hali yake na maisha ya Tunda
kwa ujumla, ndipo akaruhusiwa kuendelea kuugulia pale akiwa anapewa chakula cha bure bila kutakiwa kuondoka, kwa
sababu kwa taratibu za kihospitali alitakiwa akishawekewa vile vyuma, baada ya juma moja, arudi nyumbani.
Ila kurudi hospitalini hapo kwa siku maalumu atakazokuwa amepangiwa na daktari kuwa akifika kuonana na wataalamu na baadaye kufanyiwa lazoezi. Lakini
ndipo uongozi ukamruhusu kubakia hospitalini hapo.
Ndipo
maisha ya Tunda yakaendelea hapo hospitalini
akiuguzwa kwa utulivu, huku akifikiria
pakwenda baada yakutoka hapo. Hakuwahi kumsahau baba Tom na ahadi zake nzuri alizokuwa akimpa kila
akimtumia. Ni kweli hakutegemea kama angemtelekeza na kutomtafuta hata kujua anaendeleaje! Akazidi kuumia kujikuta
yeye ndiye aliyebaki akilaumiwa wala si baba
Tom. “Mama ameweza kumsamehe mumewe, lakini sio mimi!” Tunda alizidi kuumia.
Lakini hakumshangaa sana mama yake. Alijulikana hata na ndugu zake pamoja na wazazi wake kuwa ana roho mbaya na ni mbinafsi wakupitiliza. Tokea anakuwa pale kijijini kwa bibi yake, alikuwa akisikia aliyedhani wakimsema ni dada yake anayemfuata, kumbe mama! Baba yake akaendelea kumuuguza bila kuchoka. Hakukosa kila siku asubuhi na jioni pia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Hata kama hutakaa ukaniona tena maishani, nataka
ujue wewe sio mtoto wa bahati mbaya. Mama yako
alinikimbia akiwa na ujauzito wako, kwa sababu zake mwenyewe. Akaenda
kumdanganya mwanaume mwingine
kuwa ile mimba ni yake. Ulipozaliwa na rangi hiyo na yule
jamaa yake alikuwa akijua wazi
mahusiano yangu na mama yako, ila walikuwa wakiiba tu, ndipo akamuacha
mama yako na mama yako akaamua kwenda kukuacha kwa wazazi
wake. Siku ya kwanza kuniona ndio na mimi ilikuwa mara yangu ya kwanza hata kujua kama mimba
yako ilitungwa.” Hofu iliyokuwa imemuingia Tunda, hakuweza hata kuongea ila kulia tu.
“Na wakati ule tunaishi wote, unakumbuka
uliondoka nikiwa safarini? Nilimpigia
simu mama yako maana niliambiwa na mke wangu ulitoroka
nyumbani. Mama yako
akasema nisiwahi kumpigia simu kamwe
kukuulizia kwa unyama niliokufanyia mimi na mke wangu. Tena
alinitishia na kuniambia alikupiga picha zote wakati unamajeraha
tuliyokusababishia wakati tukiishi wote. Kwa hiyo ikitokea tu nakutafuta tena, hatasita
kuniripoti polisi. Nikaamua kunyamaza,
mpaka tena siku ile alipokuja nyumbani kwangu tena na kuanza
kuongea kama mwehu kuwa hakutaki tena kwa kuwa
unamahusiano na mumewe, na ulitaka
kuzaa naye pia. Aliniambia upo hospitalini amekutoa ile mimba
hataki nikupokee tena.” Baba yake aliendelea kuongea kinyonge.
“Nilitamani
urudi nyumbani, lakini ndoa yangu
ilishaanza kuwa kwenye misukosuko sana. Nilisimamishwa kazi,
nikawekwa kwenye uchunguzi. Yule mama
ndiye anatunza familia kwa sasa. Niseme ndiye anayenilisha.
Nilijua wazi asingekubali atulishe
mimi na wewe. Nilimomba dada akae na wewe nikijua kibiashara
ambacho nilikuwa nimekianza kukifanya, kingenilipa kidogo,
ili nikutafutie angalau chumba uanze
maisha, lakini nimesumbuka mpaka hivi leo sijafanikiwa. Kwa
hiyo Tunda, sijawahi kukuona wewe ni
mzigo, mwanangu. Ni hivyo maisha yangu yamekuwa kama nina laana,
lakini ningekutunza mama.” Tunda alikuwa akilia
sana.
“Lazima niondoke sasa hivi, lasivyo nisipotokea mahakamani nitaonekana nimekimbia kesi, au nimetoroka. Kila la kheri mwanangu. Chukua hii bahasha ina pesa kidogo, angalau utapata pakuanzia ukitoka hapa.” Baba yake aliondoka na kumuacha Tunda akiwa amechanganyikiwa kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku zilizidi kwenda akiwa pale hospitalini bila
baba yake kutokea, akazidi kuamini ni kweli baba yake amefungwa.
Kosa alilojiapia kutofanya nikukubali
kuondoka pale kwa haraka, mpaka atakapopona
kabisa. Na kwa kuwa hakuna mtu mwingine aliyetokea hapo hata kumjulia
hali, uongozi wa hospitali ukamkubalia kuendelea
kukaa pale. Akaanza kula chakula cha pale hospitalini, na kwa kuwa alikaa pale
muda mrefu kidogo, manesi wengine walianza kumfahamu. Walimletea vitu vidogo vidogo vyakula.
Kwake
yale yalikuwa mapumziko makubwa sana. Alipata
muda mtulivu wakula na kushiba, huku akiwaza kitu cha kufanya akitoka pale.
Mbali na lugha ya kingereza aliyoweza kuiongea kifasaha, hakuwa na elimu yeyote
ile. Kifaransa hakuwa mzuri sana, lakini
aliweza kuongea japo chakuombea maji. Alijaliwa mwandiko mzuri sana. Ndio hatua ya mwisho aliyofanya
kwa makini alipokuwa shuleni wakati akili zake zimetulia akiwa kwa
bibi yake. Darasa la kwanza na la Pili. Aliishia kwenye kujifunza
kuumba herufi na kusoma, ndipo
akapelekwa mjini na mikasa yake ya
maisha ikafuata.
“Nani ataniajiri sababu ya mwandiko?” Tunda aliendelea kuwaza akiwa pale hospitalini akiendelea kupona na madaktari wakimpa habari walizodhani ni njema kwake. Kuwa karibuni sana, watamruhusu. “Lazima kujua kitu chakufanya mara baada ya kutoka hapa.” Tunda aliendelea kuwaza wakati wanamtoa vyuma vya mkono baada ya mifupa yote kuunga vizuri.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mwenge nako hapakuwa mbali kwa mida hiyo ambayo hapakuwa na foleni, alisikia konda akitangaza wamefika mwisho, na hakuwa hata amepata jibu la wapi pakwenda. Ikabidi tu kushuka na kuamua kutafuta sehemu ya kula. Alikuwa na pesa kidogo aliyokuwa ameachiwa na baba yake. Akasogea mpaka kwenye vibanda vya chips. Akaagiza chips yai. Alikuwa hajala hicho chakula kwa muda mrefu sana. Tokea akiishi kwa mama yake. Akajicheka akiwa amekaa anasubiria. Kumbukumbu ya vile baba Tom alivyokuwa akimuhonga aina hiyo ya chakula ikamjia. Alichokuwa akimfanyia ni kubadili tu. Kama sio chips yai na firigisi, basi alimnunulia kuku wakukaanga. Atamfungia kwenye mifuko na kumpelekea nyumbani. Mpaka na yeye akajenga mazoea. Akibakia nyumbani peke yake, basi ataagiza chips yai. Chuki ikazidi kujengeka kila alipokuwa akimfikiria baba Tom kituoni hapo, peke yake hajui pakwenda.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tunda anatakiwa aanze maisha mapya yakujitegemea akiwa
anahesabika ni tatizo la jamii. Ndugu
hawamtaki, shule hana, ujuzi aliyonayo ni wa mapenzi tu. Endelea kuwa na Tunda
kujua ni nini atafanya huko mtaani baada yakutoka hospitalini!?
Usikose Sehemu ya 8
0 comments: