NILIPOTEA! PART 5 - SEHEMU YA ‘D’.
Tunda amaliza kifungo chake.
Siku ya mwisho, alisikia jina lake
likitajwa. Wafungwa wengine walikuwa wakitangaziwa tarehe zao za kurudi
mahakamani, wengine kuambiwa ndio wamemaliza muda wao, ndipo na Tunda akawa
amesikia jina lake. Alifuata taratibu zote zakuruhusiwa kutoka hapo jela. Wakati
anataka kutoka, askari wa mapokezi akamwambia siku iliyopita ilikuwa jumapili.
Akamwambia alipata mgeni ambaye alimwachia mzigo wake mapokezi kwa afande
aliyekuwa zamu, akamwambia akiwa anatoka apewe. Tunda hakuamini.
Akakabidhiwa mkoba ambao ulifanana
kabisa na wake aliokuwa ameuacha pamoja na vitu vyake vingine nyumbani kwa mama
Penny. Akaupokea na kusogea pembeni. Alipoushika tu hata kabla hajafungua na
kujua kuna nini ndani, ile harufu yake akajua ni mkoba wake. Ulinukia pafyumu
yake. Akastaajabu! Ni mkoba aliopenda kusafiria safari za siku chache. Mkoba
mzuri sana. Akafungua ndani kujua ni nini amemletea. Akakuta amemletea nguo
yakuvaa wakati anatoka, chupi, sidiria na sendozi za chini kabisa. Akajikuta
machozi yakimtoka.
Gari lake na vitu vyake vyote
alimuachia mama Penny. Akajifuta machozi. Kwa kuwa alikuwa amebadilika umbile,
alijua wazi hata hilo gauni aliloletewa hapo, lisinge muenea. Askari
aliyehusika kumsainisha kabla yakutoka, ndiye aliyemtafutia gauni la mfungwa
mwingine, ndilo ilibidi kulivaa ili kuweza kutoka pale gerezani.
Hakutaka hata kurudi tena ndani. Hapo
hapo pembeni ya mapokezi, akatoa kandambili mbaya alizokuwa nazo mguuni, akavaa
zile alizokuwa ameletewa na mama Penny. Vitu vyake vingine kama kadi na barua
alizokuwa akiletewa na Net, na baba yake, akatumbukiza kwenye huo mkoba.
Akatoka kwa kujivuta taratibu mpaka
nje. Akaanza kuangalia kulia na kushoto. Akashangaa kumuona Net, Mama Penny na
mumewe, wanamsubiria pale nje. Tunda akabaki amesimama kama aliyeduwaa na mkoba
wake mkononi. Nywele alikuwa amekata zipo chini kama mwanafunzi wa shule ya
msingi.
Tunda huyu alitoka na mimba kubwa tu.
Iliyoweza kuonekanika kwa wazi kabisa, sababu ya kukonda sana. Net alibaki
amekodoa macho. Akawatizama kwa zamu, wote walikuwa wamepigwa na butwaa.
Ilikuwa mchana, jua ni kali.
Akavuta pumzi na kuwasogelea palepale
walipokuwa wakimtizama kama walioona kitu ambacho hawakukitegemea. Akafika
mpaka pale walipokuwa wamesimama. “Pole kwa matatizo Tunda. Pole sana.”
Mchungaji yeye akajikaza. Tunda alitoa tabasamu lakichovu. Akamgeukia mama
Penny. Akamuona anatokwa na machozi. Akamgeukia Net bado alikuwa ameduwaa.
“Nimechoka, nataka nikalale.” Tunda
aliongea hivyo huku akimtizama mama Penny. “Twende
nyumbani.” Mama Penny akajibu huku akifuta machozi. “Pole Tunda.”
Mchungaji akarudia tena kutoa pole kama asiyejua ni nini aongee tena. “Asante.”
Tunda akajibu na tabasamu. Hakika alionekana amechoka. Midomo ilimkauka,
amekonda kama kijiti kasoro hapo tumboni.
Akamsogelea Net. “Nashukuru kwa kuja.”
“Unaendeleaje?” Net akauliza. “Vizuri.
Ni uchovu tu. Nataka nikalale.” Net akabaki akimtizama. Tunda akainama kwa muda
kama wasiojua chakuongea tena. Amshike mkono au amkumbatie! Aombe msamaha
kwanza! Net akabaki ametulia tu.
Kwa kuwa alilijua gari la mchungaji,
akalisogelea na kuwaacha wao bado wamesimama. Akasikia likitoa mlio kama
limeshafunguliwa. Akafungua mlango wa nyuma, akapanda na kukaa hapo na mkoba
wake. Ndipo akaona mama Penny na mumewe nao wanapanda. Net anaingia kwenye gari
ingine ambayo hakuwa anaifahamu. Tunda alikuwa amechoka, hakuwa na uwezo hata
wakujiuliza maswali. Akajiegemeza kwenye kiti, akalala. Kwa kuwa na kina mama
Penny walikuwa wakiishi hapo hapo Tabata, hawakuchukua muda mrefu. Tunda
akaamshwa kuwa wamefika.
“Nguo zangu bado zipo kule kule stoo?”
Akamuuliza mama Penny wakati anashuka. Net naye akawa anaingia getini. “Ndiyo.
Unataka nikutolee nini?” “Acha tu nikachambue. Nione kama nitapata chakuvaa.
Nioge ndio nikalale.” Ilikuwa siku ya shule. Alimkuta msichana wa kazi.
Akamsalimia Tunda wakati anaingia. Tunda alimuona vile anavyomsalimia kwa
kumshangaa huku akimuhurumia. Tunda akacheka. “Sasa unashangaa nini na wewe?”
Akamuuliza yule msichana wa kazi. “Mwenzio nakuhurumia!” Tunda akacheka na
kupitiliza sehemu aliyojua kuna vitu vyake.
Wakati anachagua nguo zake, kutoka
kwenye masanduku yake, mama Penny akaingia kule stoo. “Naomba nisaidie sanduku
dogo kidogo.” Bila swali akaenda upande wa pili. Akahamisha vitu vilivyokuwepo
kwenye sandugu fulani, akampa. Tunda akaanza kuweka vitu humo. “Gari yangu ina
mafuta?” “Inayo. Tulikuwa tukiiwasha mara kwa mara. Kwa hiyo ipo sawa.” Akajibu
mama Penny. Tunda akaweka vitu anavyovitaka. Akamgeukia mama Penny aliyekuwa
ameduwaa akimshangaa.
“Nataka nioge.” “Ingia hapo chumbani
kwa kina Penny. Nakuletea taulo sasa hivi. Ukioga, ule kabla hujalala.” Tunda
akatoka bila kujibu. Alitoka akiburuza sanduku lake mpaka chumbani kwa kina
Penny. Aliona kila mtu amepigwa na bumbuwazi kama wasiojua chakufanya.
Akaoga kwa muda mrefu sana huko bafuni.
Alijisugua tena na tena akifurahia uhuru
aliolipia garama. “Sidaiwi tena
na mtu.” Tunda aliendelea kufikiria wakati akiendelea kujikausha. Machozi
ya hapa na pale yalikuwa yakimtoka. Lakini hakutaka kulia mbele za watu.
Akatoka pale bafuni, akavaa nguo zake.
Kigauni kilichokuwa kimechanua chini. Kikamkaa vizuri tu. Angalau akawa na
nafuu. Alichana nywele zake, akatoka. Moja kwa moja akaenda jikoni. “Umepika
nini?” Akamuuliza yule msichana wa kazi. “Mlo wako unaolambaga vidole. Si
unasikia harufu ya Pilau? Sasa nikakuongezea rosti la kuku, lazima utalamba
sufuria leo.” Tunda akampa tabasamu lakini akabaki amesimama pale kama anayefikiria.
u“Njoo ukae hapa sebleni, atakuletea.”
Mama Penny aliongea akiwa sebuleni. Tunda akawasogelea pale walipokuwa wamekaa.
Mchungaji, Net na mama Penny.
“Naomba niwashukuru sana kwa kuwa mkija
kunitembelea na kuja kunichukua leo. Asanteni.” Kimya. “Nimechoka sana.
Nimekuwa nikiugua ugua sana nilipokuwa huko. Hapa natamani kulala tu. Nilale
bila kuamshwa wala kelele. Angalau nimalize huu usingizi nilio nao. Natamani
utulivu wa aina yake.” Kimya. Mama Penny alijua nyumba yake haiishi wageni na
kuna kelele muda wote, na hilo Tunda anajua. Akajua ndio wanaagwa.
“Nashukuru kwa chakula, lakini
sijisikii kabisa kula pilau. Naomba nikatafute chakula kingine huko njiani
wakati naenda kupumzika. Huu usingizi utakapoisha, na akili ikirudi vizuri,
nitawatafuta. Lakini kwa sasa, akili naona hata haifanyi kazi. Nilikuwa navaa
huku nasinzia.” Kimya.
“Mama Penny naomba pochi yangu.”
Akimaanisha na kadi zake za benki. Mama Penny akasimama kuingia chumbani kwake,
akatoka. “Naamini kuna pesa humu.” “Zipo. Nilitumia mwanzoni tu, tena kidogo.
Lakini naona Net alimaliza madeni yote ya mwanasheria. Mengine tutazungumza
ukisha pumzika.” “Nakushukuru dada yangu. Asante.” Net alikuwa amebaki kimya
akiwa ameinamisha kichwa chake.
“Net! Naomba nikuage hapo nje.” Net
alinyanyua kichwa akageuka. Tunda alikuwa amemsimamia nyuma yake. Akasimama,
Tunda akaenda kuchukua mzigo wake. Vile vitu alivyokuwa amevaa wakati anatoka
jela, alikwenda kuvitupa. Akarudi jikoni. “Mimi sijisikii kula pilau.”
Akamwambia msichana wa kazi wa mama Penny. “Nashukuru lakini. Ila sitakula
pilau.” Wote walimuelewa kuwa ni ile hali ya ujauzito. Akatoka jikoni, akakuta
Net alishatoka na ule mzigo wake, amesimama nje ya gari yake Tunda.
Baada ya miezi 6, Net & Tunda Tena.
Tunda akamsogelea karibu. “Naomba
nikuage nikapumzike. Nitakutafuta uchovu ukiisha.” “Lini?” “Sijui Net.” “Naomba
basi nikusindikize.” “Nashukuru, lakini hapana. Nataka nikapumzike Net. Sitaki
chochote kitokee kwenye hizi siku nitakazopumzika. Nimechoka. Sina nguvu ya
kujitetea kwa yeyote yule. Acha nikakusanye tena nguvu yakupambana na haya
maisha. Sasa hivi likitokea jambo lolote litakalonihitaji kufikiria, sitaweza.”
“Mimi nitakuwa na wewe Tunda.” “Hapana Net. Mara ya mwisho tulikuwa wote, mimi
niliishia jela.” Net akaumia sana.
“Tafadhali naomba nikapumzike.
Nimechoka sana. Nikiendelea kusimama hapa, nitalemewa hata nitashindwa
kuendesha. Ila naomba nikushukuru kwa kuja kunitembelea jela na kumsaidia baba.
Asante sana.” “Asante kushukuru. Basi acha nikuendeshe mpaka huko unakotaka
kwenda.” “Hapana Net. Nataka kuwa peke yangu kwa muda. Sitaki mtu yeyote ajue
nilipo ili nisifuatwe na yeyote kwa lolote. Iwe jema au zuri. Naomba matatizo
yangu yanifuate baada ya haya mapumziko mafupi ninayotaka kujipa. Tafadhali
Net.” “Sawa. Basi naomba nikupe namba yangu ya simu ili uje unitafute.” “Sawa.”
Tunda akafungua pochi yake.
Wazi
alionekana anatetemeka. Net hakujua kama ni njaa, au ugonjwa. “Mara ya mwisho
kula ilikuwa lini?” “Asubuhi. Nilikunywa uji. Njaa ilikuwa ikiniuma sana.”
Akamtolea kalamu na kijitabu kidogo ndani ya pochi yake. “Naomba uandike hapa.”
Net akaandika.
“Unafikiri utakuja kunitafuta tena
Tunda?” Net akauliza kinyonge. Tunda alikuwa anajisugua Tumbo. “Nitakutafuta
Net. Najua inabidi tuzungumze. Nakuahidi nitakutafuta. Acha nikapumzike.” Net
alimuhurumia Tunda, akatamani ingekuwa tofauti.
“Ulikuwa ukisoma barua zangu na kadi?”
“Hapana.” Tunda akajibu bila kudanganya. “Lakini ninazo. Nimetunza. Nitakuja
kusoma.” Net akabaki akimtizama. “Sijatupa hata moja, Net. Ninazo zote. Lakini
sikuwa tayari kusoma.” “Pole sana Tunda.” Tunda akatoa tabasamu la uchovu. “Nikienda
kulala, nitapoa.” Net akaonekana anatamani kama aondoke naye, lakini Tunda
alishajieleza. Kulazimisha ni kutokuwa mstaarabu. Maana ni kweli chochote
chaweza tokea.
Alibisha mwanzoni, Tunda akaishia
kuwekwa jela. Akaona safari hii awe mpole tu, amsikilize. “Naomba usisahau
kula.” Akaongeza Net. “Nitafanya hivyo. Maana nikianza kuumwa na njaa, nasikia
mpaka kichwa kinauma. Lazima nile.” Tunda akampita, akafungua gari yake.
Ilikuwa safi. Akajua waliisafisha makusudi wakijua anatoka siku hiyo. Net
akamwingizia mzigo wake nyuma ya gari, akafunga.
“Nakusubiri Tunda.” “Naomba usisubiri
Net. Nikipata nafasi, nitakutafuta.” Net akakunja uso. “Mbona kama uliniambia
utanitafuta?” “Sijui ni lini Net. Hali yangu kama unavyoniona. Nina uchovu na
usingizi wa miezi. Nahitaji kuwa sawa kiafya na kiakili. Sijui hayo yote
yanakamilika lini!” “Tunda please! Nimekuomba msamaha. Ni vile hukusoma barua
zangu.” “Sina lawama na wewe Net. Naomba uniamini na wala usijilaumu. Nilikuwa
jela kwa makosa yangu.” “Lakini mimi nimesababisha?” Tunda akakunja uso.
“Kivipi tena!?” “Mimi ndiye
niliyekupeleka kanisani. Isingekuwa mimi usingekuwa jela.” Tunda akashangaa
sana. “Kumbe ndio maana ulikuwa ukija jela sababu yakujilaumu!?” “Hapana Tunda.
Sio sababu hiyo.” “Naomba uniamini hivyo ulivyoongea, wala mimi sijawahi
kufikiria huko Net. Na ndio maana sikutaka kuonana na yeyote wala kusoma ujumbe
wa yeyote ili kutumikia kifungo changu nikiwa na mtazamo wangu tu. Mimi nimeamini
Mungu ameruhusu yaliyonipata, yanipate. Kama angetaka kuzuia, hakuna ambaye
angenifunga Net. Sasa ni kwa nini, mimi sijui. Tafadhali acha kujilaumu kabisa.
Naomba nikalale, nitakutafuta wakati mwingine.”
“Naomba usinisahau Tunda. Jua
nakusubiri.” “Naomba usinisubiri Net. Tafadhali. Endelea tu na maisha yako.”
“Mimi huwa sijui kuahidi na kubadilika Tunda. Sijui ndio mnafanyaje! Unamuapia
mtu hiki, kesho unafuta kabisa kiapo chako! Mimi siwezi. Sikujaliwa huo moyo au
huo uwezo. Ninapokuahidi jambo, nakuwa nalisimamia.” Tunda akainama. Akajua
anakumbushia kiapo chao cha ndoa. “Lakini
si tulisha achana?!” Tunda akajiuliza. Net akaondoka pale dirishani kwenye
mlango wa dereva, Tunda akaondoa gari bila kuongeza neno.
Baada yakutoka jela.
Tunda alitafuta hoteli ambayo hata mama
Penny hakuwa akiifahamu. Alikwenda mikocheni B. Ilikuwa ni hoteli aliyolala na
mteja wake wa kwanza kabisa, Sadiki. Natangia Sadiki afariki, na kurudi
kuchukua mizigo yake pale, hakurudi tena. Ndio siku hiyo akarudi. Alipenda ule
utulivu wa pale.
Wakati akisubiria funguo zake za
chumba, akaomba kuongea na mtu wa jikoni. Akamuagiza chupa nzima ya chai ya
rangi na mkate mkavu. “Basi?!” Yule muhudumu akauliza kwa kushangaa. “Hivyo tu.
Niletee bila kuchelewa. Ila chai isiwe na kiungo chochote ila sukari tu. Iwe ya
moto. Na mkate usipake chochote. Usichelewe tafadhali.” Yule muhudumu akarudi
jikoni.
Wakati Tunda anafungua mlango wa
chumbani kwake, chakula nacho kikaja. Akashangaa. “Kweli umefanya haraka.”
“Tayari nilikuwa na maji ya moto. Nilichofanya nikuweka tu majani na sukari.
Mikate ipo.” Tunda akacheka. “Basi na asubuhi ufanye hivyo hivyo.” Akafungua
mlango. Yule muhudumu akamwingizia chakula chake ndani. Alikaa chini kabisa
sakafuni, akaanza kula. Alikula ule mkate karibia robo tatu na vikombe viwili
vya hiyo chai ya rangi. Kisha akatoa nguo zote, akajitupa kitandani.
Alishawapigia simu mapokezi kuwa
wasimpigie simu, wasiruhusu mtu chumbani kwake. Iwe usafi au kuna swali lolote.
Akataka wamuache kabisa, yeye ndio atakuwa akiwapigia. Alilala kuanzia muda
amejitupa hapo kitandani mpaka usiku. Akala tena ule mkate uliobakiza na chai
bado ilikuwa moto. Akarudi kulala.
Siku inayofuata akaamka na homa kali.
Akapuuza akijua ni uchovu tu. Akaenda kununua dawa zakupunguza maumivu akaanza
kuzinywa. Asubuhi mchana na jioni. Siku ya tatu homa ikazidi kuwa juu. Akaamua
kwenda hospitali ya karibu na pale Mikocheni, TMJ. Muda wake wakumuona daktari
ulipofika akaingia. Alimueleza hali anayojisikia. Akaandikiwa vipimo. Akapimwa
akakutwa na UTI. Akarudi chumba cha daktari, kutokana na ujauzito wake,
akaandikiwa dawa ambazo alitakiwa kutumia siku 7.
Akarudi hotelini akiwa na zile dawa.
Akamkumbuka Net. Akaamua kuwasha moja ya simu zake, akamtumia ujumbe. ‘Net! Nimetoka hospitalini. Afya imekorofisha tena kidogo. Lakini
sio tatizo kubwa sana. Nimepewa dawa zakutumia siku 7. Naweza kuwa nalala tu,
nikashindwa kuwasiliana, msiwe na wasiwasi mjue ni dawa. Asante.’
Akamtumia ujumbe huohuo mama Penny, akazima simu.
Alijiuguza hapo hotelini akinywa dawa,
kulala na kula. Na chakula chake ni kilekile. Chai ya rangi na mkate mkavu.
Akibadili ni kipande cha limao kidogo, kwenye chai. Basi. Akaendelea kumeza
dawa bila kukosa mpaka akamaliza. Ni kweli aliona kuna utofauti kwenye mwili
wake. Tayari zilikuwa zimeisha siku 10 tokea atoke jela.
Akapumzika tena siku mbili mbele, siku
ya tatu yake akaamka akiwa na nguvu. Akaamua kwenda kutengeneza nywele. Kama
kawaida ya Tunda, kujipenda. Alitumia siku nzima kutengeneza nywele na kucha.
Angalau alirudi hotelini akiwa Tunda wa zamani. Kasoro kukonda na ujauzito.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alipokuwa akitengenezwa huko saluni,
hamu ya mkate na chai ya rangi ikampata. Alikuwa anatamani atoke, akale kwanza
ndipo arudi wammalizie, lakini akaona avumilie tu. Kitu chakwanza alichofanya
baada ya kurudi hotelini ni kuelekea jikoni. Akaomba wampe chakula chake kwa
haraka.
Na kweli, bila kuchelewa wakampa.
Walishamzoea na walijua lazima ale hivyo hivyo asubuhi na jioni. Akarudi na
chakula chake chumbani. Akaanza kula kama mwenye njaa ya mwaka mzima.
Aliposhiba akaenda kujilaza kitandani. Akaamua kumpigia simu mama Penny. “Vipi wewe!? Mbona unanitia wasiwasi?” “Sasa hivi naendelea vizuri.
Nimekupigia kukuomba kazi. Kama una sehemu zakupamba kesho, naomba nikufuate,
nitengeneze pesa kidogo.” Mama Penny akatulia kidogo.
“Mama Penny?” “Sawa. Lakini
umejaribu kumtafuta Net? Mwenzio anawasiwasi Tunda. Yule kijana
atachanganyikiwa!” “Mbona nilimwambia naendelea vizuri asiwe na wasiwasi?”
“Hapana Tunda. Naomba uzungumze naye. Yupo kama mwehu!” “Basi nitampigia.”
Akamuelekeza ni wapi pakwenda kesho yake asubuhi kufanya kazi, wakaagana.
Akategesha alarm ya kumuamsha asubuhi
ili asichelewe. Ile amemaliza tu kutegesha alarm, Tunda alikuja kuamshwa na
kelele za alarm kuwa imeshakuwa asubuhi. Hakuamini akahisi alikosea kutegesha
saa. Akaangalia muda, akakuta pameshakuchwa. Alilala vile vile na nguo zake
alizokuwa ametoka nazo saluni. Pale pale alipokuwa amejiegemeza kitandani.
Alitamani kama asiende alipokuwa
amekubaliana na mama Penny, lakini akaona asiahirishe. Aliingia kuoga,
akabadili nguo. Akatoka kwenda mapokezi kuomba wambadilishie mashuka. Tunda kwa
asili alikuwa msafi sana kama mama yake. Kitendo cha kulala kwenye kitanda
alichokuwa amevaa nguo alizokaa nazo saluni, akawa ameshakichukia chumba chake.
Akatoka kwenda kufanya kazi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alifika ilikuwa imeshatimu saa mbili.
Ndio na mama Penny na vijana wake nao walikuwa wameingia. Hawakupishana sana.
Vijana wakashusha mizigo, kazi ikaanza. Alijua hata wale vijana wanamshangaa.
Lakini hakujali. “Umependeza Tunda.” Mama Penny akamsifia. Akatoa tu tabasamu
bila kujibu kitu. Akaendelea na kazi.
Hazikupita hata dakika 20, Net naye
akaingia hapo ukumbini. Alipomuona tu, akastuka sana. Akasimama wima. Akaweka
kila kitu chini, walikuwa wanapamba jukwaa yeye na mama Penny wakati wale
vijana wawili wakitengeneza nguzo. Akashuka pale jukwaani akamfuata.
“Za asubuhi?” Tunda akaanza. “Nzuri.
Vipi na nyinyi?” Akimaanisha yeye na mtoto. “Tunaendelea vizuri. Nilimaliza
dawa. Naona na homa imeshuka.” “Ilikuwa ni nini?” Net akauliza taratibu, kwa
kujali.
“Infection ya mkojo. UTI. Iliniletea
homa kali, ndipo nikaenda hospitalini.” Net akaonekana kuumia. Akatamani aongee
kitu, Tunda akamuona anasita. “Pole sana.” Mwishoe akaona atoe tu pole. “Asante.
Jana nilitaka kukupigia, lakini nikapitiwa na usingizi. Nimeamka asubuhi hii
nakuja kazini. Lakini nilipanga kukupigia leo.” “Hamna neno. Nimefurahi kama
unaendelea vizuri. Umeangalia na afya ya mtoto?” Tunda akavuta pumzi kwa nguvu.
Akajiangalia tumbo na kujishika. “Sijaanza
kliniki bado. Nilitoka nikiwa naumwa. Nikaona nitibiwe mimi kwanza.” “Pole sana
Tunda.” “Asante. Lakini sasa hivi nipo sawa. Hata mtoto mwenyewe yupo sawa.”
Akafikiria kidogo. “Nafikiri.” “Mbona umesita?” Tunda akatoa tabasamu kidogo. “Kwa
kuwa sina uhakika. Ila alikuwa akicheza muda sio mrefu. Nafikiri yupo sawa.”
“Naomba na mimi nimsalimie.” Tunda akawa hajaelewa. “Ni sawa?” Tunda
akatingisha kichwa kukubali akiwa hajui salamu hiyo kwa mtoto tumboni inakuaje!
Net akapiga goti akashika tumbo la
Tunda. “Hey baby! Ni mimi dad.” Akabusu tumbo la Tunda huku akilipapasa
taratibu. “I love you so much. Nasikitika tumechelewa kufahamiana, lakini amini
kuwa nakupenda sana. Wewe ni baraka iliyokuja kwenye maisha yetu tukiwa
tunakuhitaji sana.” Kadiri alivyokuwa akimpapasa, taratibu yule mtoto akaanza
kuzunguka na Tunda akaanza kupata faraja ya ajabu sana moyoni.
Akajikuta machozi yakimtoka. “Nimemsikia anageuka! Si ni
kweli?” Net akanyanyua kichwa na kumtizama Tunda akiwa amehamasika usoni na
cheko la furaha juu. Tunda akatingisha kichwa kukubali huku na yeye anacheka na
kufuta machozi. Net akambusu tumbo.
“Okay! Take it easy! Take it easy!” Net
akamuongelesha mtoto wake huku akimbusu nakufurahia vile yule mtoto anavyocheza
mpaka Tunda akamshangaa. Ametoka jela na mimba, hata hajamwambia kama ni yake,
Net akajimilikisha! Ilimgusa sana Tunda. Kwake ilikuwa na maana kubwa.
Net akawa anajaribu kumtuliza mtoto
wake tumboni huku akicheka na wengine wakijiiba kuangalia. “Usimsumbue mama.
Kwa sasa take it easy. Naamini tutapata tena muda wakati mwingine wakucheza.
Nakupenda sanaaaa. Tutaongea tena hivi karibuni. Promise.” Akambusu tena na
tena huyo mtoto aliyekuwepo ndani ya tumbo la Tunda kisha akasimama.
“Asante Tunda. Nilikuwa nasubiri huu
wakati kwa hamu sana. Nakushukuru sana.” Tunda alijisikia vibaya. Hakujua kama
hata yeye anajipunja. Tunda akatoa tabasamu tu huku akijikausha machozi. “Naona
umerudi kazini kwa kasi zote!” “Nataka hela!”
Tunda akajibu huku akicheka taratibu, na kuendelea kujifuta machozi.
“Twende na mimi nikasaidie, hata
kusogeza maua.” “Huendi kazini?” “Hapana. Nilichukua likizo. Nipo likizo kwa
jili yako Tunda.” Tunda akainama kama anayefikiria mbele ya Net. Akanyanyua
uso, akakuta Net ametulia akimtizama. “Nitakutafuta Net.” “Bado nakusubiri.”
Tunda akatoa tabasamu, akionekana hata yeye amefarijika. “Turudi kazini basi,
tutafute pesa.” Net alizungumza huku akimshika mkono kurudi alipo mama Penny.
“Za asubuhi
mama Penny?” “Nzuri tu. Naona umeamkia asubuhi asubuhi kwa mwanao?” Net akacheka.
“Naona na yeye alikuwa na hamu na baba yake. Amenisalimia bwana!” Net alikuwa
amebadilika gafla. Wazi alionekana amefurahi.
Mama Penny
akacheka. “Naona umefurahi!” “Sana. Siku yangu imeanza na baraka.” Tunda
alikuwa akiwasikiliza tu huku akicheka taratibu. Hata yeye alifurahia kupapaswa
kwa upendo kwa kiasi kile. “Na mimi naomba kusaidia. Ni sawa?” Mama Penny
akacheka. “Utajichosha Net. Wewe pumzika tu.” “Ndio nimeamka. Acha Tunda awe
ananituma nimsogezee vitu.” Wote walijua anataka tu kuwa karibu na Tunda. Mama
Penny akawaacha pale, yeye akasogea sehemu nyingine akaendelea kupamba.
“Niambie
nikusaidie nini. Vyote vyakunyanyua ni kazi yangu mimi. Wewe nitume tu.” Mama
Penny alimsikia Net akimwambia Tunda. “Asante.” Tunda akashukuru na tabasamu.
Wakaangaliana kidogo na Net, kazi ikaanza tena.
Walisaidiana
hapo. Ukumbi ulikuwa mkubwa sana na wa pesa nyingi. Kwa hiyo mama Penny
hakutaka kuharibu. Mida ya saa nne asubuhi, mmoja wa mwanakamati, alifika hapo.
Akaangalia na kutoa maelezo zaidi. Wakazungumza na mama Penny, Tunda na Net
wakiendelea na kazi. Walitaka maua fresh kwa ukumbi mzima. Watu wamaua walikuwa
wameshafika hapo mida ya saa tatu, wakazungumza na mama Penny, wakaendelea
kuyapamba. Na yule mwanakamati alifika hapo kuhakikisha kama hayo maua yamefika.
Hakuna kitu kinaharibika.
Ilipofika
saa saba mchana, Tunda alikuwa amechoka. Mgongo unamuuma. Net akamuona anaanza
kujinyoosha mara kwa mara huku akikunja uso. Akamsogelea. “Simama, halafu shika
hiyo nguzo na mikono miwili.” Tunda akamwangalia kidogo, kisha akafanya kama
alivyoambiwa. Net akaanza kumsugua mgongoni na kumminya kiuno. “Kwa hapo chini
kidogo ndio nasikia maumivu zaidi.” Net alikuwa amesimama nyuma yake. Akatumia
vidole vyake gumba viwili kuminya sehemu aliyoambiwa na Tunda. Ilikuwa katikati
ya kiuno. Alifanya hivyo kwa muda, Tunda akiwa ametulia tu.
“Asante.”
Tunda akasimama wima. “Unajisikia nafuu?” “Afadhali.” “Nashauri usiende kwenye
kazi ya pili, ili upumzike Tunda.” Tunda akabaki akifikiria. “Unahitaji
kupumzika, angalau mwili urudie hali yake. Umerudi kuwa mrembo lakini bado
unaonekana umechoka.” “Nahitaji hela Net. Nahitaji kufanya kazi. Nikijiendekeza
hivi, maisha yatanishinda nitabaki nikihangaika.” “Lakini afya yako ni muhimu
Tunda. Naomba urudishe kwanza nguvu, halafu utafanya kazi kwa kadiri ya uwezo
wako. Sasa hivi ukumbuke unaishi kwa ajili yako na mtoto.” Tunda akanyamaza.
Akageuka nakuendelea na kazi.
Walimaliza
saa 8 mchana. Mama Penny na vijana wake walishakuwa tayari kuhamia ukumbi
mwingine ambao walisema hauhitaji kazi kubwa. “Naomba Tunda akapumzike. Itoshe
kwa leo.” Net aliongea huku akimtizama Tunda na mama Penny. “Mimi naona ni wazo
zuri. Umetoka kifungoni, unaumwa, ukazidiwa, umejiuguza mwenyewe. Hatujui
ulikuwa unakula vitu vyakujenga mwili au la! Hata hujapata nguvu vizuri,
unaanza kazi! Na mtoto huyo, unahitaji kumpumzika Tunda. Mimba sio mchezo.”
“Siwezi kukaa hivi hivi. Lazima nitengeneze pesa. Nitaishije?” “Afya yako na
mtoto ni muhimu Tunda!” Tunda akanyamaza.
Mama Penny
akabaki akimtizama kama kuweka msisitizo. “Nimeelewa dada.” “Na uanze kliniki.
Lazima kujua mtoto anahali gani. Uzito wake na wako ambao hauridhishi kwa
kukuangalia tu! Bado unaonekana umechoka. Huko unapoelekea utalemewa! Usifanye
mchezo. Hakikisha wanakupima damu na uanze kunywa dawa za kuongeza damu na zile
za kina mama wajawazito. Umenielewa Tunda?” Mama Penny akaendelea kuweka
msisitizo.
“Nitafanya
hivyo jumatatu. Kesho jumapili nitapumzika tu.” “Sawa. Uje nyumbani kwa chakula
cha usiku kesho.” “Labda unipikie zile ndizi za mchuzi.” Mama Penny akacheka. “Haya.
Nitapika. Uje.” Mama Penny akaondoka na vijana wake, nakuwaacha Net na Tunda.
Net na Tunda Tena.
Net akamgeukia Tunda kama anayemtaka
muongozo. “Naomba nikapumzike. Nikutafute baadaye nikiamka.” “Naomba
usinifukuze Tunda. Tafadhali.” “Sikufukuzi. Nakwenda kulala, nikiamka,
nitakutafuta.” Net akabaki akimwangalia. “Nakuahidi nitakutafuta Net. Acha
nikalale kwanza, nimechoka.”
“Unaishi wapi?” “Hotelini.” “Wapi?”
“Mikocheni B. Nipatulivu, hakuna kelele kabisa.” “Naomba twende wote.
Sitakusumbua. Nataka kuwepo tu. Tafadhali Tunda. Naomba na mimi kupata muda na
mtoto.” “Sio kwamba sitaki usumbufu tu.” “Ni nini?” Net akamuuliza.
“Nilitaka muda wakufikiria.” “Nakuahidi
sitakusumbua. Naomba unifikirie na mimi Tunda!” “Basi twende.” “Na chakula?”
“Mimi huwa naagiza pale pale.” “Sasa leo unahamu ya kula nini?” Tunda akacheka
huku akifikiria. “Labda nijaribu kuku wa makange.” “Basi twende Back point.”
Wakaongozana.
Walifika, wakakaa. Net alikaa mbele
yake akabaki akimtizama. Tunda akainama huku akichora meza kama anayefikiria. “Pole
Tunda.” “Nimeshapoa. Asante.” Wakanyamaza mpaka muhudumu akafika kuwaulizia
kinywaji. Wakaomba mtu wa jikoni. Kila mmoja akaagiza chakula. Wakatulia.
“Bado unanipenda au nimekuudhi kabisa?”
Net akamuuliza taratibu tu. “Hujaniudhi Net. Kwa nini unafikiria hivyo?” “Sijui
Tunda. Nataka tu kujua.” Tunda akanyamaza.
Chakula kililetwa, wakala kimya kimya.
Tunda alikula kidogo tu, huku Net akimtizama anavyokula. Akawa ni kama hajapata
mdomoni kwake kitu ambacho alitarajia. Akavuta sahani mbele kidogo, akanywa
maji kidogo, akatulia huku akikitizama kile chakula.
“Ndio umeshashiba hivyo!?” “Nitaongeza
kitu kingine. Kwa chakula hiki inatosha. Nataka nikalale.” “Naweza kukuagizia
kitu chochote nikakuletea. Unaweza kutangulia ukaoge. Nitakufuata.” “Nashukuru.
Lakini kuhusu chakula, nitaagiza palepale. Usiniletee kitu. Acha niondoke sasa
hivi. Ni kweli nimechoka.” Akamuachia funguo ya pili ya chumba, akampa namba ya
chumba, akaondoka.
Kwa mara nyingine tena, Net&Tunda hotelini.
Kwa asili Tunda alithamini sana
usingizi, na alipenda kulala. Alishamwambia Net, ndio muda pekee anaweza kuwepo
duniani na asihisi taabu yeyote na wala asikumbuke machungu yake. Ni muda ambao
alihesabu Mungu huwa anampa pumziko la masaa machache. Kwa hiyo linapofika
swala la kulala huwa hajikosei. Iwe mchana au usiku, atavaa nguo ambayo anajua
haitamkera akilala na anapenda alale pasafi.
Aliingia hotelini, kwenye chumba chake.
Akapiga simu mapokezi na kuagiza chai ya rangi na mkate. Akamwambia akileta
aingize na kuweka mezani. Akaingia kuoga. Bado akili za kuwa gerezani alikokuwa
akibanwa zilikuwa zikimsumbua. Kila alipooga na kumaliza, alitaka arudie tena
kujihakikishia yupo sehemu safi. Alioga tena na tena, ndipo akatoka.
Alijikausha nakuanza kujipaka lotion.
Kwa kuwa Net alishajua aina ya vitu anavyopaka mwilini, hata alipokuwa jela
ndio vitu alikuwa akimpelekea. Aliiangalia ile lotion, akapotelea mawazoni
akiwa amekaa palepale kwenye kochi na taulo lake bichi.
Mawazo yalimrudisha jela. Akakumbuka
yale maisha. Akavuta pumzi kwa nguvu na kujirudisha nyuma. “Nimelipa deni yangu!” Alijisemea kwa sauti huku akiendelea kuwaza.
Mwishowe akaamua kula chakula chake. Chai yake na mkate vilivyokuwa vimeletwa.
Wakati Net anaingia na mtoto wake
alikuwa anacheza. “Vipi?” “Nimepumzika tu, nimeshashiba, namsikilizia mtoto
anavyocheza.” “Naomba kumshika.” Safari hii Tunda hakuwa amevaa nguo. Net
aliweka vitu mezani, akamsogelea. “Labda nivae kwanza.” Net akabaki
akimwangalia. “Ndio nimetoka kuoga Net!” “Sasa mpaka uvae, umalize si na yeye
atakuwa amemaliza kucheza?” “Basi nipande kitandani nijifunike shuka. Taulo
bichi!” Hakusubiri ajibiwe. Akatoa lile taulo, akapanda kitandani, akajifunika
shuka. Net akaenda kupiga magoti pembeni yake.
“Muone anavyozunguka!” Wote wakacheka. “Sijui
anafanya nini huko ndani!? Unaumia?” “Hapana.” Net akambusu na kuanza kumpapasa.
Alizungusha mikono kuzunguka tumbo lote. Juu mpaka chini, Tunda akiwa amejilaza
chali, ameegemea mto. Yeye mwenyewe Tunda alifurahia. Net alianza kuzungumza na
mtoto wake taratibu kama wapo ana kwa ana.
“Unavyoongea naye! Utafikiri anakusikia
au anaelewa!” Tunda akamshangaa. “Wataalamu wanasema anaelewa na kusikia.” Net
alijibu huku akicheka. “Unaonekana umefurahi Net! Ukimshika mpaka unabadilika!”
“Unakumbuka tulivyokuwa kwenye honeymoon yetu nilikwambia nataka mtoto?”
“Nakumbuka. Halafu mimi sikujua kama naweza kushika mimba!” Net akambusu tena
na tena.
“Naomba tumshukuru Mungu pamoja Tunda.
Sijui tunakokwenda, lakini ninachojua hata hapa tulipo sasa hivi ni Mungu ndio
ametusaidia.” “Lakini naomba na mimi nikushukuru Net. Unaweza usielewe, lakini
nilikuwa nikifurahia sana ulivyokuwa ukija kunitembelea.” “Sasa kwa nini
hukutaka kuniona Tunda!?” “Nisingeweza Net. Ingeniumiza zaidi na nisingeweza
kuendelea kuishi mle ndani. Nia yangu ilikuwa nimalizie kifungo changu nitoke,
mengine nije kuyajulia huku nje.” Mikono ya Net ilikuwa bado ikipita tumboni
kwa Tunda taratibu.
“Mwezi ule wa mwisho ambao hukuja,
niliumia Net, nikashindwa hata kulala!” “Kweli!?” Net akashangaa sana. “Kweli. Nikajua umenisahau.” “Nianzie wapi?
Nilijua ungetoka baada ya siku sita. Halafu sikujua itakuaje ukitoka. Kama ndio
utataka kuniona au ndio utanifukuza moja kwa moja. Kwa hiyo ikabidi nimwombe
nana nifanye kazi mpaka overtime, ili ukitoka niwe na wewe. Nikusubiri tuwekane
sawa. Nikishajua hatima yetu, ndio nirudi..” Tunda hakuwa ameelewa.
“Kwani siku hizi hufanyi tena kazi na
mama yako ni bibi yako!?” Tunda akauliza kwa mshangao. “Siishi hapa nchini
Tunda. Hata nilipokuwa nikija kukutembelea, nilikuwa nikitokea nyumbani,
Canada.” Tunda alikaa kwa mshtuko. “Net!!” “Kweli. Nilikuwa nafika siku ya
ijumaa. Nakufuata wewe siku ya jumamosi na jumapili. Jumatatu narudi Canada
kuwahi kazi.” Tunda alishangaa machozi yanamtoka. “Haiwezekani
Net!” Net akacheka tu na kukaa pembeni yake. Kitandani.
“Pole na samahani Net.
Sikujua kama ulikuwa ukitoka mbali hivyo kuja kuniona! Mimi nilijua
mlisameheana na mama yako, ukarudi kazini, maisha yakaendelea.”
“Inawezekanaje Tunda, wakati tuliambiwa sisi ni mwili mmoja!?” “Lakini ile ndoa iliisha Net!” “Uliniapia nini Tunda?” Kimya.
“Mimi nakumbuka uliniapia mbele za
Mungu, Nana, Maya na watu wengine kuwa ni mpaka
kifo kitakapo tutenganisha, sio mpaka usaini tena sehemu nyingine. Au
sikuwa nimekuelewa?” Net akauliza taratibu tu.
“Mimi bado nakithamini kile kiapo
changu. Binafsi bado najua mpaka kifo, ndio kinaweza kututenganisha. Huwezi
kuumia wewe, mimi nikawa salama. Au mama hawezi akakuumiza wewe, halafu mimi
nisiumie. Hata nana anaheshimu sana kiapo chako Tunda. Alirudi hapa nchini,
akachukua picha zetu za harusi, video na pete zako za ndoa na uchumba ambazo
mama alikupokonya.” Net akaendelea.
“Nana aliporudi kunisaidia kuweka mambo
sawa, akanichukulia kila kitu, akaniletea kule nyumbani.” Tunda hakuwa
ameelewa. “Mimi nilikuacha na mama yako Net!” Ndipo Net ikabidi amuelezee
kuanzia walipoachana mpaka walipokuwa wamekaa hapo.
Tunda alishangaa sana. “Sijamtafuta
tena. Nimeona nimpe nafasi. Najilaumu sana Tunda.” “Kwa nini!?” “Mama hakuwa
mnafiki juu ya mahusiano yetu. Tokea mwanzo kabisa, alikiri wazi hakutaki
kwenye maisha yetu kama mkwe. Lakini ni kama nilimlazimishia. Nakumbuka tokea
mwanzo nilimwambia nampa nafasi mpaka atakapokutafuta, lakini sikufanya hivyo.”
“Niliruhusu ajue maisha uliyoishi nyuma
kitu ambacho haikuwa lazima. Na mbaya zaidi, mambo yalivyokuwa mabaya, sikumshirikisha
nana. Najua kwa upande mwingine, nana analaumu, lakini hataki kuniambia kwa
kuwa anajua haitasaidia tena. Na pia najua anaelewa nilikuwa nikimlinda mama na
yeye ili wasifike hapa walipo. Mimi mwenyewe nilikosea sana.” Tunda hakujibu,
akajirudisha nyuma, akajilaza.
“Sasa, sasa hivi ukiwa hapa nchini
unaishi wapi?” Tunda akauliza. “Hotelini.” Tunda akazidi kushangaa. “Sasa kwa
nini usikae kwenye ile nyumba!?” “Sikutaka ije ikae hivi hivi tu wakati mimi
sipo hapa nchini, na sikujua hatima yetu. Yule mwanasheria ambaye alinisaidia
mambo yako na baba, anaonekana ni mwaminifu. Aliniunganisha na ndugu yake.
Wanafanya kazi ya kuuza, kukodisha na wananunua nyumba. Nafikiri ni kama
biashara ya familia. Kwa hiyo niliwaomba wawe wanakodisha. Lakini sio ile ya
mtu kuishi hapo kwa muda mrefu! Hapana. Labda watalii au watu wanao tafuta
sehemu ya kuishi kwa muda mfupi. Iwe chumba kimoja, au nyumba nzima. Inakuwa
kama sehemu ya mapumziko tu. Si unajua watu wengine wanasafiri kama familia,
wanaepuka gharama za hotelini?” Tunda kimya.
“Basi nilijisajili pia na Air bnb,
ndipo ninapopata wateja pia, na hao ndugu ndio wananisaidia. Kwa hiyo ukiingia
online, unatafuta sehemu ya kushukia Tanzania, utakutana na nyumba ya Tunda
Cote. Unalipia, unakutana na Emma yule kijana wangu pale nyumbani. Anasaidia
kuwasafishia kwa siku mtakazokuwa mkiishi pale. Basi.” Tunda akabaki
namshangao. Mambo mengi yalikuwa yakipita kichwani. Hajui aulize lipi, aache
lipi tena.
“Naomba nilale kwanza.” “Unajisikiaje
lakini?” Net akauliza kwa upendo huku akimpapasa. “Kuchoka tu.” “Jumatatu
itabidi twende hospitalini. Waangalie huo mwili kujua kama unauwezo wakubeba
huyo mtoto. Ili kilichopungua, kiongezwe kwa haraka. Kama ni damu, au madini
yeyote yale, uanze kutumia dawa na kula vyakula vizuri.”
“Nitatoka hapa hotelini nikaanze maisha
yakujipikia. Niwe napika vyakula vya maana. Haya maisha ya hapa ni gharama
sana, na nilifanya kwa muda tu ili nipumzike. Naamini nikianza kula vizuri,
nitarudisha mwili.” Net akanyamaza.
“Unataka na wewe kupumzika?” “Ni mpaka
na mimi nioge, ndio nitajisikia vizuri kulala. Pale ukumbini kulikuwa na joto
kali. Siwezi kulala vizuri.” “Kwa hiyo unaondoka kurudi hotelini kwako?” “Sio
sasa hivi. Mpaka ukiamka, na kula tena labda ndio nitaondoka. Sasa hivi
nitakuwa nikifanya kazi zangu pale kwenye kochi.” Tunda akanyamaza. Net
akambusu tena pale tumboni nakuanza kumpapasa taratibu.
“Lala tu. Mimi nitakuwepo ukiamka.”
“Wakati mwingine huwa napitiwa na usingizi na lala mpaka asubuhi. Kama jana
nilipanga nikupigie, nikapitiwa hapa na viatu miguuni.” Net akacheka kidogo na
kumbusu tena tumbo.
“Wewe muda wako wakuondoka ukifika,
funga tu mlango. Usiwe na wasiwasi. Nikiamka hata kama ni usiku sana,
nitamalizia mkate wangu na chai, nakurudi kulala.” “Ni sawa ikifika saa 3
nikuamshe ili ule? Kuna chakula kingine nimekuletea, ujaribu.” “Nitapata shida
kurudi kulala. Acha tu nilale.” “Sitaondoka mpaka uwe umepata usingizi tena.
Nitakubembeleza mimi mwenyewe mpaka ulale.” Tunda akacheka taratibu.
Net alimtizama kama amkumbatie na
kumbusu, akakwepesha macho, kisha akayafunga. Akamsikia Net akimpapasa na
kumbusu tena na tena. Hiyo furaha yake ilimchukua ikampa usingizi mzito.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Aliamka saa mbili usiku, bado Net
alikuwa akifanya kazi zake kwenye laptop.
“Vipi?” “Nahisi nilikunywa chai nyingi. Nasikia kwenda chooni.” Tunda
alitoka na shuka kuelekea chooni. Bado hakuwa amevaa nguo yeyote ndani. Baada
ya muda akatoka chooni, akamfuata Net pale kwenye kochi.
“Ndio unafanya nini?” “Kile nilichokuwa
nikimfanyia mama, ndio namfanyia nana. Namtafutia wateja. Lakini sio kama
zamani nilivyokwambia namfanyia kwa nchi kadhaa. Sasa hivi nimechukua kitengo
kizima. Ninaendesha mimi mwenyewe matawi yote, kwenye nchi zote.” “Hongera Net.
Ni vilevile usafirishaji?” “Yeah. Usafirishaji.” Tunda akajua kuwepo pale kwa
Net, anamkwamisha mambo mengi.
“Net!” Tunda akaita kwa sauti yake ya
chini kama anayefikiria kitu. Net akafunga laptop yake akajiweka sawa. “Kwa
kuwa sasa hivi nimetoka jela, unaweza kurudi tu ukaendelea na kazi.” “Nikuache
wewe na mtoto!” “Utakuwa ukija kututembelea unapopata nafasi.” Net akakunja
uso.
“Ndio yanakuwa ni maisha gani hayo?”
Tunda akabaki akifikiria. “Kama tunabaki hapa, tubaki wote. Kama nikuondoka,
tunaondoka wote watatu.” Tunda akabaki ameinama akifikiria.
“Unajua nimeanza kukuombea kibali
chakuweza kuishi Canada?” Tunda akashangaa sana. Akakunja uso. “Unakumbuka kile
cheti chetu cha ndoa, nilikwambia lazima kiwe kinatambulika kote? Sasa baada ya
kukamilisha kila kitu, na kikawa sawa. Nikaanza kutuma maombi. Unakumbuka
ninayo hata hati yako yakusafiria?” “Hata sikumbuki!” Tunda alijibu huku
akionekana akifikiria.
“Nilibakiwa nayo tokea wakati ule.
Niliifungia ofisini, nana alipoenda ofisini kwa mama, nilimtuma anijie nayo.
Naona imefika pazuri. Lakini Tunda, upo huru kuishi popote unapotaka wewe. Mimi
ndio nitabadilika na matakwa yako. Nitajua chakufanya baada ya kuamua wewe.”
Tunda kimya.
“Ukiamua kuishi Tanzania, ni sawa.
Ukiamua kuishi na mimi Canada, nitakushukuru sana, kwa kuwa nana ni kama
anatamani niwepo kule ili aniachie ile kazi apumzike. Anataka kustaafu.” Wakati
ule ilikuwa ngumu kufikiria kuondoka na Net sababu ya biashara yake ilikuwa
imechanganya. Wateja kila kona mpaka anakataa kazi. Sasa sasahivi Tunda ni
mjamzito. Alishapita mtandaoni kama mvunja ndoa ya marehemu Gabriel na Bethy.
Wengi walishamsema. Gabriel alimtetea na wengine, lakini tayari jina lake
lilishaingia doa. Alibaki ameinama akifikiria maisha yake hapo nchini.
“Nikuagizie chakula gani au nikupashie
nilichokuwa nimekuletea?” Net alimstua kutoka mawazoni. “Mimi chakula ninacho.
Nilibakiza. Na wewe?” Net akafikiria kidogo. “Naweza kwenda kula hotelini
kwangu au nikanunua kitu kidogo tu njiani. Bado najihisi kushiba.” “Unataka
kuondoka saa ngapi?” Tunda akamuuliza kama anayetamani abaki. “Utakaponiruhusu.”
Tunda akacheka na kuinama. Net akamsogelea, akambusu kichwani.
“Natamani kukukumbatia. Nikupe pole
ukiwa mikononi mwangu, Tunda. Unafikiri naweza kufanya hivyo?” Tunda akajifuta
machozi, akatingisha kichwa kukubali na tabasamu usoni.
Net akajiegemeza vizuri kwenye kochi. “Njoo
hapa.” Akimuonyeshea kifuani. “Nikavae nguo kwanza?” “Haina haja. Njoo.
Japokuwa nina hamu na wewe sana, lakini sitafanya kitu bila idhini yako.” Tunda
akajisogeza mpaka pale kifuani. Akajilaza upande ili kulipa tumbo lake nafasi.
Net akaingiza mikono ndani ya lile shuka, akamfunika ili asimwache uchi,
akamkumbatia vilevile uchi ndani ya shuka.
Tunda alivuta pumzi mara kadhaa,
akatulia. “Asante Net.” “Pole na matatizo, na samahani sana.” “Usiendelee
kuomba msamaha Net. Nimefurahi nimeweza kulipa deni langu. Mwenzio najiambia
kila wakati kuwa sidaiwi tena. Najisikia uhuru zaidi. Ilikuwa ngumu lakini
namshukuru Mungu ameniwezesha kupita.” Net alikuwa akimpapasa ubavuni. Juu
mpaka chini. Taratibu huku akimsikiliza. Kichwa ameegemeza kichwani kwake.
“Umebadili perfyumu?” “Inakukera?”
Tunda akatingisha kichwa kukubali. Net akacheka. “Haya mama. Lakini sijabadili.
Ni ileile.” “Mbona sasa hivi harufu yake mbaya!?” “Huyo anayesikia hiyo harufu
sasa hivi sio wewe, ni mtoto. Wewe ulikuwa ukiipenda mpaka unavaa mashati
yangu.” Tunda akaanza kucheka, akakaa. “Kama ndio inaninyima kukumbatia,
itabidi nikaitupe!” Tunda akazidi kucheka. Akavuta shuka nakusimama.
“Nilishaanza kunogewa.” Tunda akacheka
sana. “Njaa inauma, dad!” “Ngoja nikachukue chakula. Pengine nikirudi naweza
kupewa taulo nikaoge, ili niweze kukumbatia zaidi.” Tunda alizidi kucheka. “Net!”
“Ninahamu ya kufa mtu.” “Wewe uliniahidi ukiwa hapa, hutanisumbua.” “Na ahadi
yangu inabaki palepale. Sitakusumbua hata kidogo. Nitakuwa dad mzuri.
Nikihurumiwa, sawa. Nikifukuzwa, usiku naenda kulala peke yangu kule, namuacha
mtoto wangu na mke wangu wanalala peke yao huku. Asubuhi tena narudi, mpaka
nihurumiwe.” Tunda akazidi kucheka.
“Siamini Net!” “Hata mtoto atakuwa
anatushangaa wazazi sisi ni wanamna gani! Eti wazazi wanalala hotelini, tena
mbalimbali!” “Nilijua tumeachana Net.” “Hivi wewe ndoa unafikiri nikuandika tu?
Sio mchezo Tunda. Ni agano la kimungu. Halivunjiki kwa kuandika kwenye
makaratasi au haliingiwi kwa kuandika kwenye makaratasi. Ingekuwa ni hivyo
mbona ingekuwa rahisi sana! Au labda ni mimi tu na vile nilivyolelewa kwetu!
Mimi nimekuwa kwenye mazingira ya kutokuwa na talaka. Nana amekaa kwenye ndoa
ya zaidi ya miaka 50 mpaka papa akafariki. Nimefunzwa kuheshimu ndoa.” Tunda
akacheka taratibu huku akifikiria.
Net alitoka kwenda kupasha chakula
alichokuwa amemletea Tunda tokea mchana, akidhani angependa. Tunda akashangaa
anarudi na sanduku. “Kwani ulikwenda wapi?” “Kupasha moto chakula, na kuchukua moja
ya mzigo wangu kwenye gari. Sitaki kukosa bahati kwa kisingizio cha kutokuwa na
nguo, sijui taulo, hapana!” Tunda akaanza kucheka tena.
“Net wewe ni mtundu bwana! Sasa gari
umepata wapi? Mbona hili silijui!” “Nimekodi. Ujue ulipotoka jela ukapotelea
hapa, nilikuwa nampigia mama Penny simu kila baada ya masaa matatu kumuuliza
kama mwenzangu umemtafuta! Sasa ulipozungumza naye jana ukamuomba kazi,
akanipigia na kuniambia pia uliahidi kunipigia. Acha nikeshe nikisubiri. Kimya.
Asubuhi nikaona nifanye marefu kuwa mafupi. Nikakusanya vitu vyangu vyote pale
hotelini, nikaweka kwenye gari. Nikajiambia nitakufuata hapo kazini.
Nikubembeleze mpaka ukubali nikufuate unapoishi. Nikajiambia nikishafunguliwa
tu mlango!” Tunda alikuwa akicheka sana.
“Basi nitafute sababu za kulala.
Nikishindwa kabisa, niondoke tena na mizigo yangu, nikatafute tena hoteli.
Kesho tena asubuhi, nianze upyaa.” Tunda akazidi kucheka. “Kwa hiyo hapa
unavyoniona, nipo kamili.” “Net!” “Niruhusu tu nitumie bafu lako, nitoe hii
pafyumu wakati wewe unakula.” “Haya nenda.” Tunda akamruhusu huku akicheka.
“Mvumilivu hula mbivu. Unaweza kuta
nikitoka kuoga, nikakubaliwa kukumbatia tena. Huwezi jua!” Tunda alizidi
kucheka. “Tena ngoja nioge kwa kutumia sabuni yako kabisa. Na vile hali yangu
ilivyo mbaya, napaka na lotion yako kabisa. Vitu vyangu vyote naenda kuvitupa,
ili nisiharibu.” Tunda akazidi kucheka. Net akaelekea bafuni huku akipiga
mluzi.
Tunda alijawa furaha na faraja ya
ajabu. Akajua usiku huo atalala akiwa amekumbatiwa na kupewa penzi la nguvu.
Hakutumia muda mrefu huko bafuni akatoka. “Net! Mbona kama umekimbia tu huko
bafuni?” “Ninuse kama utasikia harufu ya ile pafyumu. Sasa hivi nanukia kama
wewe. Labda uwe unanitafutia sababu tu.” Tunda akacheka sana, Net akamsogelea
pale. Alitoa taulo mbele yake, akabaki amesimama. Tunda akavuta pumzi kwa nguvu
huku ameng’ata midomo ya chini, akacheka.
“Nina hamu na wewe Net!” Net akainama,
nakuanza kumbusu tumboni juu ya shuka. Akazidi kumbusu huku akimtoa lile shuka
palepale kwenye kochi. Taratibu huku akimbusu na kumpapasa, akambeba kutoka
pale kwenye kochi akamuweka kitandani. Wote wakiwa kama walivyozaliwa. Net
akapanda kitandani na kuendeleza mabusu ya mwilini kabla hajafika midomoni.
“Maziwa yanauma?” Akamuuliza taratibu. “Sio
sana.” “Basi nitakuwa mwangalifu. Ninahamu na wewe Tunda! Mama alitukatili.” “Nakupenda
na ninakushukuru kwa kuwa mwaminifu, kunisubiri na kutonikatia tamaa. Ungeweza
kuondoka bila kugeuka nyuma.” “Halafu nikose haya yote!?” Tunda alianza kucheka
tena taratibu.
Net akamwinamia, kilichokuwa kikisikika
ni kunung’unika kwa Tunda. Net alishindwa romance ya muda mrefu. Hata yeye hali
ilikuwa mbaya, taratibu kwa hisia zote, alimnyanyua miguu, akiwa amelala vilevile
chali, Net akaanza mapenzi huku na yeye akigugumia. Tunda alimsikia akisugua
meno huku amefunga macho kama anayesikilizia. Alikuwa amemshikilia hips zake
kwa nguvu, huku akijaribu kumwinua taratibu.
“Naomba niangalie Tunda, ili niridhike
kuwa upo hapa na mimi.” Net alimuongelesha taratibu alipofungua macho yake
akakuta na Tunda amefunga ya kwake. Akamuomba huku akiendelea kuingia na kutoka
kwa hisia zote bila kuacha. Tunda akatoa tabasamu na kufungua macho. Net
aliendeleza mchezo huku wakiangaliana kwa penzi zito, hakuchukua muda mrefu Net
akafanikiwa.
Tunda akacheka. “Nilikuwa najilipa
safari zakuja huku, halafu hutaki kuniona.” “Net!” Tunda akamsukuma kidogo.
Akajilaza pembeni yake, akalala hapohapo wakati Tunda akimwangalia. Akacheka,
akajua alikuwa amechoshwa na mawazo pia. Akambusu, na kumfunika. Akarudi mezani
kula mkate wake na chai. Wala hakugusa chakula alichokuwa ameletewa na Net.
Alipomaliza akarudi kujilaza pembeni ya Net.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Aliamshwa na mikono ya Net ikitembea
tumboni. Akacheka. “Umeamka saa ngapi!?” “Muda mrefu, unajua sasa hivi ni saa
ngapi?” Tunda akafikiria kidogo. “Lakini leo si jumapili?” “Ndiyo.” “Nataka
kupumzika.” “Unasali?” Net akamuona amenyamaza. “Tunda?” “Nitaanza kwenda
kanisani week ijayo.” “Hapana Tunda. Unajua sivyo ninavyomaanisha.” Tunda
akanyamaza. “Nasali lakini sio kama zamani.” “Kwa nini?” “Sijui Net. Ni kama
nimechanganyikiwa, sielewi tena. Naona mambo mengi niliyoyaelewa na yanayoendelea kwangu ni kama…” Tunda akajifuta
machozi.
“Nafikiri nahitaji muda
tena. Kile nilichoelewa tokea mwanzo kuhusu Kanisa, wokovu na Mungu imekuwa
tofauti Net. Watu wenyewe wa kanisani wamenitenda au wananitenda kama watu
niliowaacha tu huko duniani. Simaanishi kanisani kwa mama yako tu, lakini hata
pale kwa kina mama Penny. Wamenitendea vibaya tofauti na ulivyoniambia mwanzo,
Net.” “Pole
Tunda.”
“Nimefika sehemu sijui
bora vipi! Kule nilikokuwa mwanzo, peke yangu na maisha yakiendelea, au kuwa
kanisani ambako watu wananihukumu!” Net alibaki akimsikiliza, akamfuta
machozi na kumbusu.
“Nahitaji muda. Nahitaji
kufikiria. Nahitaji kujijenga upya. Kwa jinsi gani, hata mimi sijui.” “Pole.”
Tunda akacheka. “Bwana acha kusema pole kila
wakati.” “Namaanisha. Mimi nilijua haya yatakupata lakini si kwa umbali
wa kuwekwa gerezani.” “Halafu mbaya zaidi ni watu wa kanisani Net! Naona watu wa nje wanaelewa na wana utu kuliko hata
walioko kanisani! Ipo tofauti kubwa sana ya watu niliowakuta kule jela na wale
niliowaacha kanisani.” Tunda akajifuta machozi.
“Nikuulize kitu Tunda?” Tunda
akatingisha kichwa kukubali. “Kwa sasa hivi, mtu akikuuliza mimi ni nani kwako,
utanitambulishaje?” Tunda akanyamaza kidogo, akamwangalia, kisha akabaki kimya
akifikiria. Akamsikia mtoto anacheza. “Naona ameamka, anataka chakula.”
Akajishika tumbo, Net akamtizama machoni, akarudi tumboni akaanza kumpapasa
Tunda taratibu huku akizungumza na yule mtoto tumboni.
Akambusu mara kadhaa akaendelea
kumpapasa. Tunda mwenye alisikia raha. Akabaki amejiegemeza kitandani huku
akimtizama vile Net anavyochezea tumbo lake. “Siku chache zilizopita.” Net
akaanza huku akionekana bado anaongea na mtoto wake tumboni. “Tena kabla ya
Mungu hajatuonyesha vile anavyotuthamini kwa kutupa wewe. Dady wako nilipewa
ahadi ya mpaka kifo. Niliambiwa nitapendwa, nitalindwa. Katika uzima na
maradhi. Shida na raha, mpaka kifo kitutenganishe.” Tunda akaanza kucheka. “Net
wewe! Ndio unanisemea sasa kwa mtoto!?” Net akambusu tena.
“Naomba unisikilize Net.” Net akarudi
kwenye mto huku mikono ipo tumboni. “Nakupenda sana Net. Sijapata mtu
akanithamini hivi. Kwa kashfa zote nilizonazo, nimetoka jela nikiwa mjamzito,
umeamini kabla na baada ya kwenda jela, nimekuwa mwaminifu kwako. Bila hata
kuuliza, umeamini mtoto ni wako wakati tulitengana miezi 6. Kwa hilo
limeniongezea imani kubwa sana kwako.”
“Kingine, hukunitelekeza japo uwezo
ulikuwa nao na sababu pia. Lakini ulimtuma bibi yako kuja kukusaidia
kukutengenezea njia pia ili uweze kurudi kwangu. Umekuja kunitembelea jela bila
kuchoka, na sasa hivi upo hapa na mimi. Kwa hilo, nitakuenzi daima. Umehangaika
kunitetea na kunitafutia mwanasheria. Akafuta makosa yote uliyonisababishia.”
Net akacheka.
“Samahani sana Tunda. Mimi sikujua kama
mama anaweza kufika umbali huo bwana!” “Subiri kwanza. Wakili uliyenitafutia
akahangaika kutaka nisiwekwe jela hata kwa kosa ambalo nilifanya. Mimi mwenyewe
nilikataa, kwa kuwa niliona nimepewa muda mfupi, sikutaka kuanza tena kufufua
kesi nikaendelea kuwepo jela.”
“Tena hata wale askari waliniambia nitulie
kwanza ndani kwa kuwa sijui ni nani bado anahasira na mimi. Naweza kutoka,
wakanidhuru. Halafu kitendo cha kesi yangu kutajwa mara ya kwanza na siku hiyo
hiyo kupewa hukumu bila kusogezwa mbele, mimi binafsi nikajua ni Mungu
amenitetea kwa namna yake. Sikutaka kufanya mambo yakawa marefu wakati
nilishajijua mimi ni mjamzito.” “Sasa kwa nini hukuniambia?” Net akauliza.
“Kama ni swala la ujauzito, nilijua
ungepaniki Net. Tena ungezidi kuchanganyikiwa kama ungejua nipo na mwanao jela!
Usingeweza hata kufanya kazi.” “Ulijuaje!?” Tunda akacheka. “Nilikuona siku
natoka jela vile ulivyokufa ganzi na hivi ninavyokuona ukimshika huyu mtoto
jinsi unavyobadilika! Sasa niambie hiyo hali ungeipata wakati unajua
nimehukumiwa kifungo cha mwaka, halafu nipo mjamzito na huwezi hata kumgusa
mwanao!” “Nahisi ningechanganyikiwa wala si uongo.” Tunda akacheka.
“Ndio maana sikutaka kukuona wala
kukudanganya juu ya afya yangu. Miezi ile mitatu ya mwanzo, nilikuwa natapika
kupita nitakavyokueleza. Kila harufu kule jela ilikuwa mbaya. Nilikonda kama
kijiti. Hakuna chakula kilichokuwa kinapita.” “Hata sasa hivi umekonda sana.”
Tunda akacheka.
“Baada ya kipindi chakutapika kuisha,
nikaanza kula kidogo kidogo ndio nikaugua tena. Mara nipone hiki, nije kile.
Ngozi yenyewe ikawa imeharibika mpaka ulipoanza kuniletea sabuni na lotion
nilizokuwa nikitumia. Ndio ngozi ikaanza kurudia hali yake. Kwa hiyo nikajua
ukiniona wakati ule, au baba angeniona, angeumia na kukwambia wewe.
Isingekusaidia Net. Ungeumia wakati hukuwa na uwezo wa kunisaidia tena.”
“Ulifanya kwa nafasi yako ndio maana
nipo hapa leo. Yale makosa yasingefutwa, nina uhakika ningekuwa jela mpaka
sasa. Kwa hiyo umenielewa na hasira zimeisha?” “Nimeelewa Tunda. Na pole sana.”
“Kwa hiyo sasa hivi utafanya mapenzi na mimi mpaka niridhike?” Net akacheka
sana.
“Jana uliniacha hivi hivi wakati sio
kawaida yako!” “Uliniudhi Tunda. Mimi nakufuata, halafu hutaki kuniona!?”
“Lakini sasa hivi umenielewa?” “Inabidi kukuelewa tu Tunda. Wewe ndiye uliyekuwepo
ndani. Ulifanya kile ambacho ulijua kitasaidia. Japo najua ungeniona,
tukazungumza kama hivi, tungepanga kitu chakufanya pamoja. Tafadhali matatizo
yasitutenge, bali yatusogeze pamoja.” “Sasa mbona hata sijajibu swali lako?”
“La kuwa kama mimi ni nani kwako?” “Ndiyo.” Net akacheka tena.
“Sifa zote hizo ulizonimwagia! Utapata wapi mwanaume kama mimi? Eti
mwanangu? Nani atampenda mama yako kama mimi!?” Tunda alikuwa akicheka tu na
kumfurahisha Net kumuona angalau anaweza kumfanya acheke. “Unavyojiamini!”
“Sana. Mimi mwenyewe huwa mpaka nakuonea wivu jinsi ninavyokupenda.” Tunda
aliendelea kucheka.
“Kingine Net. Sasa hivi nakusikiliza
wewe katika kila kitu. Mwenzio ni kama nimepoteza ramani kabisa. Ni kama
natakiwa nianze moja na mimi ndio kama unavyoniona. Bado sina nguvu, halafu
hata nikija kurudisha nguvu, labda ndio nitatakiwa kujifungua, itabidi kuwa na
muda na mtoto. Sijui Net.” “Basi kama wewe umepoteza ramani, naomba ufuate ya
kwangu Tunda. Tutakuwa salama, na ninauhakika hutajuta.” “Nakusikiliza.” Net
akajiweka vizuri.
“Nitakwambia kwa kifupi tu bila ahadi
nyingi, halafu mengine iwe ni kwa kadiri Mungu atakavyo tubariki.” Tunda
akajiweka sawa. “Naomba tukaishi Canada. Ili tuwe msaada kwa nana. Anatamani
kupumzika, lakini hawezi. Ukishajifungua, na mtoto akawa yupo sawa kuwa
nyumbani, tutafanya kazi pamoja.” Tunda akashtuka kidogo.
“Acha uoga. Unakumbuka tulivyokuwa
Arusha jinsi tulivyofanya kazi vizuri?” Tunda akatabasamu. “Sasa ni kama vile
vile tu, lakini safari hii utafanya zaidi, ukijua ni urithi wa watoto wetu pia.
Ni kampuni ya muda mrefu sana. Tokea baba yake babu. Akamrithisha babu, babu
alitaka baba aiendeleze, ndio akafariki, na mama akasema anataka kurudi huku.
Ikabidi na mimi nimfuate, kitu kilichomuumiza sana babu. Ndio bibi ameniambia
majuzi. Kuwa walitaka kustaafu ili niiendeleze, lakini nilipochagua kurudi
kuishi huku Tanzania, na kukataa kumuoa Chloe msichana wa kule, wakajua bibi
akifa, na ndio ile kampuni imekufa.” Net akaendelea.
“Kwa hiyo ukikubali tukaishi kule,
utakuwa umenifanyia kitu kikubwa sana na..” “Tutaenda Net. Wala huna haja
yakunibembeleza.” “Kweli!?” “Si unakumbuka hata kabla ya kwenda jela huo ndio
ulikuwa mpango wetu?” “Nilijua umebadili mawazo.” “Hapana Net. Nataka kuwa na
wewe tu, nipendwe kizungu.” Net alicheka mpaka machozi.
“Tunda wewe ni mtundu!” “Sikutanii
mwenzio. Mambo kama haya ningeyapata wapi! Kushikwa shikwa hivi, unaongea na
mtoto ambaye mimi hata sikujua kama watu wanaongeaga na watoto! Acha kunitania
na wala sijivungi.” Net alizidi kucheka.
“Sasa nirekebishie basi kama mimi
nilivyokurekebishia jana usiku. Huwezi jua, naweza kupata nguvu yakwenda
kanisani.” “Si umesema unataka muda?” “Najua utanisaidia Net. Nimeumizwa sana.”
“Na mimi najua ni maumivu tu. Unachohitaji ni muda tu Tunda. Ila amini nguvu za
Mungu na uwezo wake. Nilikwambia, haya yote utapitia. Sasa wewe umetoka salama,
unatakiwa kuwa msaada kwa wengine. Si unakumbuka?” “Nakumbuka.” “Basi. Naomba
ujipe muda, samehe, na kuwa msaada kwa wengine. Ila ujue unaye mtu ambaye atakupenda
daima.” “Yesu?” Tunda akuliza, Net akaanza kumbusu. “Yesu kupitia mimi.” Tunda
akaendelea kucheka.
“Bado unanidai fungate Tunda.” “Nilijua
ndio basi.” “Hapana. Mama alinikatili. Unakumbuka siku kabla ya kukamatwa
uliniomba na mimi unihudumie?” “Usahau!?” “Nilijuta mpaka jana nilipopata bao
na kulala.” Tunda alicheka sana.
“Nilikuwa natamani siku zirudi, angalau
hata kwa lisaa tu. Nikufurahie zaidi.” “Mungu ametupa nafasi nyingine.” “Lakini
sio hapa. Leo tukitoka kanisani na kwenda kwa mama Penny kula ndizi, nakutoa
hapa nchini haraka sana. Safari hii sitaki kuingiliwa.” Tunda alizidi kucheka.
“Tunaenda wapi?” Tunda akauliza akiwa
amejawa furaha ya namna yake. “Yaani hata wewe sitakwambia. Nachukua passport
yako, naanza kushugulikia safari.” “Lakini lazima kumuona dokta kwa ajili ya
kuangalia afya ya mtoto.” “Ni kweli, na pia tujue jinsia, sio naongea na mtoto
ambaye hata sijui ni nani!” Tunda alibaki akimtizama, haamini.
“Tukiwa huko, wakati tunasubiria visa
yako ya Canada, nitarudi Canada kidogo, sikumbili au tatu halafu…” “Sasa si ni
heri mimi nirudi kuishi hata kwa mama Penny wakati nakusubiria?” “Hapa
sikuachi. Wanavyokuwinda hivyo! Hapana. Kama hutataka, ni afadhali tubaki wote.
Na pia inategemea, kama nana akisema sio lazima kwenda, tutabaki wote mpaka
tuondoke wote kabisa.” Tunda akahema kwa nguvu kama aliyepata nafuu.
“Ningekuwa sio kuwa mjamzito, ningeenda
kuona anapoishi baba kabla yakuondoka.” “Kwani mnawasiliana?” “Tunawasiliana.
Anaonekana ana amani na utulivu, japo biashara hazimuendei vizuri.” “Watoto
wake?” “Alipotoka jela, moja kwa moja alikwenda kwa mkewe. Kwenye nyumba yao.
Anasema yule mama alimfukuza na kumwambia aondoke kabla hajamwitia mwizi. Sasa
baba akasema ilibidi aondoke tu, asije akajiingiza kwenye matatizo mengine,
akarudishwa jela.”
“Anasema mama yangu alinitenga naye,
lakini kwa kuwa hakuwa na kosa, Mungu amemrudishia mimi. Kwa hiyo hata kina
Chale, hatawapoteza.” “Mzee wako mpole sana Tunda. Hana makuu.” “Mpaka nahisi
ndio maana wanamuonea. Amezidi jamani! Ungemuona jinsi alivyokuwa akiishi na
yule mke wake, mama Chale, mpaka aibu. Utafikiri mjinga!” Tunda aliongea kwa
upole.
“Mungu atamsaidia. Yeye aliyemuumba
hivyo, anajua ni kwa nini alimpa haiba ya namna hiyo, na atamsaidia. Amejawa
shukurani huyo, hana lawama kama hivyo wewe ulivyo. Watu wengi walinilaumu kuwa
mimi ndio nimekusababisha ufungwe. Nikaogopa hata kuonana na baba yako. Yule
wakili ndio akawa mtu ninayemtumia kunifikishia ujumbe kwake. Siku moja
tukakutana pale gerezani. Yaani yeye alijawa shukurani tu mpaka akanishangaza.
Tulizungumza kidogo tu, akaniaga kuwa ameamua kurudi kwao, Mara. Basi.” Tunda
akanyamaza.
“Mama yako
je?” Tunda akavuta pumzi kwa nguvu akakunja uso. “Hatukuwahi kuwa na mahusiano
na mama, Net. Unakumbuka mama yupo sasa hvi ni kwa sababu tulimfuata? Hajawahi
hata kuja kunitembelea jela. Juzi uliponikuta na mama Penny napamba, aliniambia
alimfukuza, lakini baadaye akawahurumia
sababu ya watoto wake. Kina Tom. Ikabidi ampe vile vitu vyangu vyote.
Kwa hiyo akawa akipata tenda nyingi, nyingine anampa na yeye. Anasema
hakutegemea, lakini anafanya vizuri tu. Hajawahi kulalamikiwa. Ameniambia
anaonekana kwa muda mfupi alioanza hiyo biashara, yupo vizuri tu.” “Kwa hiyo
anavyo vitu vyako vyote vya biashara?” Net akauliza.
“Mama Penny
alimpa. Alisema yeye hakujua kama nitatoka mjamzito. Na pia alimuona ni msafi
sana na mtunzaji. Kwamba ningetoka, ningeendeleza biashara yangu. Hata kama
nikununua vitu baadhi, nisingehangaika. Lakini huwezi amini Net!” Tunda alikuwa kiongea kwa unyonge. “Nini?”
Net akauliza.
Tunda
akacheka kwa kuguna. “Mama Penny anasema week iliyopita nilipokuwa nimejifungia
hapa hotelini baada ya kutoka jela, akaamua kupitia website yangu. Akakuta
imefungwa. Akampigia simu mama. Akamuuliza kulikoni
mbona haoni website yangu tena! Mama akamwambia aliamua kubadili au kufunga
kabisa jina la kampuni yangu. Sasa hivi kampuni ipo kwa jina lake. Kwa kuitwa
Tunda, wateja wanamkimbia sababu ya kashifa zinazonikabili.” Net aliumia sana. Hakutaka hata kuweka neno.
Akamtoa
Tunda pale kwenye mto, akamuweka kifuani. “Nataka tukabariki ndoa yetu kanisani
Tunda.” Net akabadili kabisa yale mazungumzo. “Wapi?”
Tunda akauliza, Net akiendelea kumfuta machozi. “Tukifika nyumbani. Kwenye
kanisa tutakalowakuzia watoto wetu.” Tunda akaanza kujisikia faraja baada ya
kukumbuka ubaya wa mama yake. Akamkumbatia Net vizuri na kujiweka kichwa chake
kifuani huku akijaribu kutulia.
“Nakupenda
Tunda.” “Sasa mbona hatu..…” Wakasikia hodi mlangoni kabla Tunda hajamalizia
swali lake. Lakini Net alikuwa ameshaelewa analalamikia nini na ni kweli
alikuwa akimzungusha pale kitandani. Kila Tunda alipotaka mapenzi, Net
alimzungusha kwa hili na lile.
“Hiyo ndio
sababu.” Alitoka kitandani huku akicheka. Tunda hakuwa akielewa. “Ni nani
huyo?” “Vaa nguo, mama Penny huyo.” Tunda akakurupuka. Alilala uchi. “Mbona
hukuniambia bwana!? Kafungue mlango sasa.” Tunda alikuwa akicheka huku
akikimbilia bafuni.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Net alivaa
sweat pants harakaharaka na t-shert nyeupe aliyotoa kwenye sanduku lake,
akarudisha nywele vizuri, akafungua mlango. “Karibu.” “Nimewaamsha nini?”
“Hapana. Tulishaamka. Nilikuwa namuongelesha ili asiagize tena mikate.”
Wakacheka, mama Penny akaingia na chupa ya uji, na hotpot kubwa, akaweka
mezani.
“Yupo
bafuni, atatoka sasa hivi.” “Mimi mwenyewe sitakaa sana, nawahi kwenye ibada.
Mtakuja?” “Sijui.” Net alijibu kwa sauti ya chini kama kunong’ona huku
akipandisha mabega. Mama Penny akavuta pumzi kama anayefikiria kidogo kisha
akauliza.
“Anaendeleaje?”
Mama Penny akauliza na yeye kwa sauti ya chini. “Anahitaji tu muda. Atakuwa
sawa.” “Na kula vizuri. Amechoka sana. Sio sawa kwake na kwa mtoto. Anahitaji
kumuona na dokta, tena kwa haraka.” Mama Penny alisisitiza. “Lazima kesho
tutaenda.” Tunda akatoka.
“Karibu dada
yangu.” “Nimekuletea chakula kinachoeleweka. Hiyo afya yako haiendani na mikate
mikavu unayokula siku nzima.” Tunda akamgeukia Net kama anayemsuta. “Sio mimi.
Ni mama Penny mwenyewe ndiye aliyenituma kuulizia wana vitafunio gani hapa.
Wakaniambia huwa unakula mikate mikavu na chai nyingi ya rangi.” Tunda akaanza
kucheka, akaenda kukaa kwenye kochi.
“Kwa hiyo
umeniletea nini dada yangu?” “Usifanye mchezo Tunda. Mwili huo ni dhaifu kubeba
mtoto. Huo sio mwili wako, umekonda kwa maradhi. Mkifanya mchezo mtapoteza huyo
mtoto!” “Usiniogopeshe bwana!” “Nakwambia ukweli. Acha kula mikate mikavu na
chai ya rangi! Haviwezi kukujenga huo mwili na mtoto wenu. Lazima kubadilika
jinsi unavyojitunza. Makazi magumu sio kwako wewe ambaye umepitia shoruba.
Umebakiza miezi mitatu ujifungue, tulia.” Tunda akainama akifikiria.
“Unanisikia
Tunda?” “Net amesema atatutunza mimi na mtoto, nipumzike kwanza mpaka nitakapo
jifungua. Na kesho tutaenda kufanya vipimo vyetu wote. Mimi na mtoto kabla
yakusafiri.” “Mnakwenda wapi!?” “Kumalizia fungate, na mambo mengine tutakuja
kuzungumza na nyinyi nyumbani.” “Sawa. Basi mimi natangulia kanisani. Si
mnakuja?” Swali hili aliuliza huku akimtizama Tunda. Tunda akamgeukia Net, wote
wakabaki wakimwangalia yeye.
“Mimi bado
nahitaji muda.” Tunda akajibu taratibu. “Wa nini?” Mama Penny akamuuliza. “Eti
Tunda? Muda mbali na Mungu?” Kimya. Tunda akainama. “Hapo ndipo utapotea kabisa
Tunda. Unanisikia?” Tunda akabaki ameinama. “Ni heri uangukie msalabani kuliko
nje. Unayoyaona ndani ya Kanisa sasa hivi, ni afadhali hivyo kuliko utoke.
Usifikiri jaribu lako limepita. Kushindwa kwako ni kukimbia baada ya yote
yaliyokupata.” Mama Penny akaendelea.
“Wengi
wanabaki hivyo hivyo kwa kuwa wakijaribiwa, hawasimami. Wanataka kukimbia kama
wewe. Umefanya sehemu ya kwanza kwa uaminifu na juhudi zote. Usirudi nyuma. Huo
mtihani lazima kumaliza. La sivyo utajaribiwa tena na tena na utakuwa wewe ni
mtu wakuanza upya kila siku. Unanisikia Tunda?” Tunda akajifuta machozi huku
ameinama.
“Na Mungu
hatakuacha mpaka umefaulu mitihani yake. Sasa ni wewe mwenyewe na juhudi zako.
Unaamua kuahirisha leo, au la. Na ujue utarudia tu hiyo mitihani unayokimbia
leo. Sasa nijuu yako wewe. Upo tayari kuanza upya au kuendelea?” Tunda
akapandisha mabega kukataa. “Basi ndio nikuone kanisani baadaye, na kwenye
bible study jumatano na maombi alhamisi.” Mama Penny akaweka kila kitu chini.
“Na hizo ni
nguo nimekununulia jana. Acha kuvaa nguo za ajabu. Uje kanisani ukiwa umependeza.”
Tunda akaanza kucheka huku anafuta machozi. “Yaani
mama Penny, jamani!” “Wewe unataka kujiliza hapo mpaka lini? Umeanguka,
umesimama, tena umesimama vizuri sana. Kung’uta vumbi, endelea na safari.”
Akamaliza hivyo na kutoka.
“Mama
Penny!” Tunda akabaki akimtafakari dada yake wa hiari. “Lakini
amekwambia ukweli.” “Nahitaji muda, Net.” “Mpaka
lini!? Kujifungia hapa na kuwa mbali na watu ndio kujipa sababu yakuzidi
kujitenga na watu na kuona mabaya zaidi. Kula tutoke humu ndani. Na uzuri
unatoka na mumeo akiwa pembeni yako! Huoni huo ni ushindi?” Tunda akacheka
taratibu.
“Kwa hiyo
ulijua kama atakuja?” “Aliniambia atakupitishia chakula asubuhi ndio maana
sikutaka kuanza mapenzi, halafu aje atukatishe katikati.” Tunda akacheka.
“Kula.”
“Nawaza ingekuwaje bila wewe na mama Penny! Unajua maisha yangu yote nimekuwa
peke yangu! Nikikutana na changamoto ni mimi mwenyewe nachukua hatua na kile
ninachofikiria kinafaa kwenye akili zangu zilizojaa kusalitiwa, manyanyaso,
kutumiwa bila kujaliwa, kutothaminiwa na mengi mabaya. Sasa unaweza kufikiria maamuzi
yote yatakayotoka kwenye fikra kama hizo!”
“Afadhali
sasa hivi na mimi nipo.” “Hilo linanifanya nimshukuru Mungu, Net. Asante.” Net
akainama pale alipokua amekaa. Akaanza kumbusu. Tunda alikuwa na robe tu,
aliyojifunga baada kukimbilia bafuni. Ndani hakuwa amevaa kitu.
Net aliivua,
nakumtoa pale kwenye kochi akiwa mtupu nakumuweka kitandani. Alihakikisha
anamkata kiu yote ya tokea wanaachana. Anampa pole ya namna yake, na
kumridhisha. Tunda alikuwa akifurahia kila alichokuwa akifanyiwa na mumewe pale
kitandani. Hakutaka amalize. “Tutashindwa kwenda kanisani Tunda. Njoo ule
twende.” “Natamani kulala tu.” “Najua. Twende, tukirudi nitakufanya ulale,
sitakusumbua.” “Nataka unisumbue.” Net akacheka na kumbusu.
Kwa mara nyingine tena, Tunda
na mumewe Kanisani.
Walipofika
kanisani wakaegesha gari na kubaki wakizungumza ndani ya gari. Mara wakawaona
Penny na mdogo wake wanachungulia dirishani. “Anti! Anti!” Penny alisikika
akiwa na furaha sana. Tunda akashuka garini. “Nilikuwa na hamu na wewe anti!”
Penny akaanza. “Hata mimi Penny. Hujambo?” “Mwenzio mama amemwambia Penny
akikuuliza yale maswali yake tu, anamkata ulimi wake wote.” Mdogo wake
akaingilia. Tunda akaanza kucheka.
“Maswali gani?” Tunda akamuuliza Penny
mwenyewe. “Si ndio ameniambia atanikata ulimi sasa! Huu hapa wote.” Penny
akatoa ulimi wake wote. “Amemwambia atamkata kuanzia kwenye koo.” Pendo, akaweka msisitizo.
Tunda akazidi kucheka. “Kweli. Ila
ameniambia utakuwa na mtoto. Nikamuuliza kwa hiyo mtoto wako atakuwa wakizungu
kama dad wake?” “Maana Penny yeye ananywele za kipilipili kama za dad.” Pendo
akaingilia nakumfanya Tunda na Net wacheke.
“Nywele za Penny hazichaniki.” “Zinachanika
ila dada ndio hajui kuchana.” Penny akabisha. “Anajua sana, mbona zangu
zinachanika?” Pendo na yeye akambishia dada yake.
“Hajui.” “Anajua.” Wakabishana Tunda na
Net wakiwasikiliza. “Kwa hiyo mtoto wako atakuwa mzungu?” Penny akaendelea. “Dad
wake mzungu na yeye atakuwa mtoto wakizungu. Mama amesema atakuwa hasumbui
kuchana nywele kama wewe.” “Mama anachana kwa nguvu ndio maana!” Penny akakunja
uso akilalamika.
“Anti, kwa hiyo kweli atakuwa mzungu?”
“Sijui, Pendo.” Tunda akamjibu huku akicheka. “Ningekuwa mimi ningetaka mtoto
wakizungu na macho ya rangi ya bahari kama ya dad wake.” Net akazidi kucheka. “Yaani
watoto hawa! Mama yenu yuko wapi?” “Yupo kanisani. Amemwambia Penny aje
asalimie tu. Asiulize yale maswali yake mengine, ila kuhusu mtoto amemruhusu.”
Tunda akacheka tena.
“Kwani ulitaka kuuliza maswali gani?”
Tunda akamgeukia tena Penny na kumuuliza. “Mwenzio nitakatwa ulimi na mama. Ila
nitakwambia kitu.” “Nakusemea Penny. Mama amesema nikusikilize kila neno.
Ukisema tu, nikamwambie.” “Sijasema bado. Nimemwambia nitamwambia kile kitu
kingine.” “Hata kile mama amesema usiseme.” Wakaendelea kubishana ndugu hao
wawili, Tunda na Net wakiwaangalia huku wakicheka. Penny akakunja uso na
mikono.
“Wala sio raha tena!” Penny
akanung’unika. “Kwani ni nini?” “Pendo mmbea. Nikikwambia tu kama niliwasikia
kina mama Vero wanakusema kuwa umefungwa jela hutakaa utoke tena, atamwambia
mama, halafu nitakatwa ulimi.” “Hee! Pennyy! Pennyyyy! Umesema! Naenda
kumwambia mama.” “Sijasema hata nusu yake. Niliwasikia kila kitu. Kwani anti
nimekwambia?” Tayari Penny akawa ameingiwa hofu. Kama aliyeropoka.
“Hujaniambia Penny! Usiogope.”
“Umesikia na umbea wako? Sasa mimi anti amenitetea. Shauri yako!” “Naenda
kumwambia mama.” Pendo akaondoka akikimbia. Penny akaanza kulia huku akimfuata
mdogo wake akisema hajasema. Net na Tunda wakabaki wakicheka.
“Mama yake ndio kiboko yake. Sasa ngoja
Pendo akamsemee. Atapooza leo, mpaka walimu wake wamshangae huko Sunday school.
Ujanja wote utamwisha kwa hofu yakuchapwa huko nyumbani.” Tunda na Net walizidi
kucheka. Wakaamua kuingia kanisani.
Kuanzia nje mpaka ndani, kila mtu
alikuwa akimshangaa Tunda na Net. Walijua, lakini hawakujali. Penny alishawapa
kwa kifupi kilichokuwa kikiendelea. Mama Penny akawasogelea huku amemshika
Penny mkono. “Hajasema bwana. Muache.” Tunda akajaribu kumtetea. “Huyu leo
nakaa naye pale mbele kama shemasi. Hasikii Penny.” Mama yake aliongea huku
akimwangalia Penny.
“Sio mimi ni kina mama
Vero ndio wanadhambi ya kusengenya.” Penny aliwafanya wacheke mpaka mama
yake. Kila mtu akawageukia pale kanisani wakimsikiliza Penny akiongea huku akilia.
Mbaya zaidi na mama Vero na mumewe
walikuwepo. “Yeye ndio wakumkata ulimi mama, sio
mimi.” “Penny wewe mtoto utalia Penny! Nyamaza.” “Mimi sijamwambia kitu anti. Pendo muongo.”
“Amemwambia vile alivyowasikia kina
mama Vero wakimsema anti Tunda, mama. Muulize anti mwenyewe.” “Lakini
sijamwambia kila kitu. Si ndio anti, eeh? Yale mambo waliyokuwa wakionyeshana
kwenye simu kwani nimekwambia?” “Penny! Penny! Mdomo huo wewe utakuponza
mwanangu!”
“Pendo ananisingizia
mama. Muulize anti. Sijasema. Hata vile walivyosema mzungu wake amemkimbia
sijamwambia anti. Muulize.” Penny alitaka utetezi wa Tunda huku akilia
kwa hofu na kuzidi kuharibu zaidi.
“Sasa wewe mama Penny ndio utamfanya
ayaseme yote hapa. Unamjua Penny. Hawezi kunyamaza mwenzio. Bora umuache kabla
hajayasema yote hapahapa.” Tunda alikuwa akicheka mpaka machozi.
“Mbona yeye amemwambia anti
achague mtoto awe wakizungu na macho ya rangi ya bahari kama dad wake, na
nywele za kizungu kama dad wake zisiwe kama zangu za kipilipili hazichaniki
kama za dad wangu. Mimi sijamsemea?” Kila mtu alikuwa akicheka.
“Si nimekwambia mama Penny wewe? Mimi
naona umuachie tu, kesi tukamalize nyumbani.” “Hata mimi naona.” Mama Penny
akakubaliana na Tunda tu. Maana Penny alizidi kutoa maneno. Mpaka Net alikuwa akicheka.
“Mama Vero ndio
ananiponza mama. Sio mimi. Mimi nilimtetea anti. Hata walivyosema hataolewa na
Mzungu, mimi nikasema...” “Penny wewe mtoto!” “Sikusema vibaya mama. Mungu wangu shahidi. Mimi sisemi
uongo kama shetani. Nilimwambia mbona alishamuoa!?”
“Penny nakuonya wewe mtoto nyamaza!” Net alikuwa akimwangalia Penny, nakuzidi
kucheka. Alimsikiliza vile anavyojitetea na kuzidi kuharibu.
“Basi mama. Mimi siongei
tena. Sisemi yote aliyoyasema mama Vero, tena alikuwa na..”
“Penny!” Mama yake akamwita kwa
ukali, akanyamaza.
“Haya poteeni haraka. Na niwakute
mmekaa kimya darasani kwenu.” “Yaani hata maswali
tusijibu!?” Penny akauliza huku akifuta machozi. “Penny utalia zaidi
wewe mtoto!” “Mimi sitajibu mama. Hata mwalimu akinichagua, sijibu. Mimi mtoto
mzuri.” Pendo akajitetea kwa haraka huku akiondoka taratibu kwa tahadhari.
“Tena na wewe unyamaze Pendo.
Aliyekwambia ukaulizie maswala ya watoto wa kizungu ni nani?” “Na Penny pia
amemwambia anti achague mtoto wa kizungu, mama. Sio mimi peke yangu.” Kila mtu
alizidi kucheka.
“Haya poteeni haraka.” “Mimi siongei
tena mama. Kwa hiyo hata nyumbani usiniulize tena. Yaishie tu hapahapa
kanisani.” “Penny utalia wewe!” “Basi mama Penny!” Penny alimfanya mpaka mama
yake acheke. Akaondoka.
Mchungaji aliingia nakukuta kanisa zima
wakicheka. “Kuna nini?” Akauliza. “Wala hutaki kujua. Jiachie tu.” Mama Penny
akajibu, nakufanya kila mtu azidi kucheka.
“Huyu Penny ni wakutoa sadaka kabisa.
Awe anaishi hapahapa kanisani na mlinzi.” “Kafanyaje tena mwanangu!?” Mchungaji
akauliza.
“Ningekuwa naye zile enzi za Mtume Eli akimlea
Samweli kule hekaluni, na Penny ningempeleka akasaidie hata kusogeza kuni za
kuteteteza sadaka. Angalau aishi huko huko asirudi tena nyumbani. Labda na yeye
Mungu angemwita jamani kama Samweli!” Watu wakazidi kucheka. “Mtoto huyu!”
Mchungaji akaanza kucheka. Alimjua Penny, akajua ameacha jambo hapo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ibada ikaanza, muda wakutoa ushuhuda
mchungaji alikaribisha watu. Net akanyoosha mkono. Akaenda. “Napenda kumshukuru
Mungu kwa ajili ya mema yake kwangu na familia yangu. Haikuwa rahisi si kwa
Tunda mke wangu tu, hata kwangu na mtoto wetu. Haikuwa rahisi hata kidogo.
Mengi yamesikika, lakini ni mimi na Tunda ndio tunaojua ukweli. Sipo hapa
kusafisha jina la Tunda, mke wangu kwa kuwa nimejua ni ngumu kubadili fikra za
binadamu ila nipo hapa kumshukuru Mungu.” Net akaendelea.
“Katika kipindi hicho kigumu cha miezi
sita, Mungu amemuwezesha mke wangu kubeba mtoto wetu kwenye mazingira magumu
mno. Kusimangwa na maneno yakusingiziwa ambayo watu walimshutumu nayo bila
huruma. Amelipa deni ambayo Mungu alimfutia msalabani. Lakini bado yupo hapa na
sisi akiamini kanisani ni sehemu sahihi anayotakiwa kuwepo na nyinyi watakatifu
wa Mungu. Ni kwa Neema na Rehema za Mungu kwa Tunda kuwa hapa.”
“Huwa nafikiria na kutafakari kule
Tunda alikotoka, anakopitishwa sasa hivi, nashindwa kujiweka kwenye viatu
vyake. Ni yeye tu mke wangu ndiye anayeweza kuvivaa viatu hivyo. Na mimi pia
nimechangia kupita alikopitishwa. Lakini Tunda yupo kama baba yake. Hajui
kulaumu. Hajui kunyoshea watu vidole. Amekubali mapito yake, namuombea Mungu
azidi kumtia nguvu. Namshukuru Mungu kwa kunipa Tunda. Na sasa ametuamini na
maisha ya mtoto ambaye tunamtarajia miezi michache ijayo.”
“Kwa niaba
yangu na familia yangu, naomba pia niwashukuru mama Penny na mume wake. Kwa
Tunda wamefanyika zaidi ya wachungaji. Wamembeba mke wangu bila aibu wala
kuchoka. Kwa asilimia kubwa sana, wamechangia yeye kuwa hapa leo. Sina
chakusema zaidi, ila nawaombea Mungu awabariki sana.”
“Kabla
sijaendelea na shukurani za mwisho, tumekubaliana na mke wangu, kutoa sadaka ya
shukurani. Naomba mtuvumilie.” Net akaendelea. “Tungeweza kusubiri wakati
mwingine, lakini tumeona hapana. Mkono wa Mungu umekuwa juu yetu kwa namna ya
tofauti na ya ajabu. Ametulinda. Amepigana vita kwa niaba yetu. Ametenda mambo
makubwa zaidi ya tulivyoomba na kufikiri. Acha leo tutoe sadaka yakutambua
uwepo wake kwenye maisha yetu.” Watu
wakapiga makofi.
“Mwisho
katika yote, nakipekee, namshukuru mke wangu. Am so proud of you babe! ‘Binti za watu
wengi wamefanya vizuri, lakini wewe Tunda, mke wangu, umewapita wote’.” Net akampongeza mkewe kwa kupitia andiko la
kutoka kwenye bibilia. {Mithal 31:29}. Tunda alikuwa ameinama. Akanyanyua uso akamtizama.
“Thanks Net.” Alijibu kwa kunong’ona, na
tabasamu lenye chozi juu. Hata kina mama Penny walijisikia vizuri. Tunda
akasimama na kwenda kumsindikiza Net kwenye kutoa sadaka ya shukurani. Waliweka
pesa kwenye bahasha. Wakamaliza, watu wakapiga makofi wakati Net na mkewe
wanaenda kukaa.
Waliosutwa wakasutwa. Waliofungwa mdomo
wakafungwa na Net. Maana neno mke wangu alihakikisha analitamka bayana kama
anayesisitizia ndoa yake kwa Tunda, na ni kama kusema hakukosea kumuoa Tunda.
Alijawa na shukurani kwa mkewe na Mungu wao.
Net&Tunda Kwa Mchungaji
Tena.
Baada ya ibada, Net na Tunda walielekea
nyumbani kwa mama Penny lakini baada ya kupitia dukani kama kawaida ya Net.
Akanunua vinywaji na dessert ya keki ndipo akaelekea nyumbani kwa mchungaji.
Njia nzima walikuwa wakicheka kila wakimkumbuka Penny.
Walifika wakamkuta Penny amekaa kwenye
kochi kimya ametulia wala hatingishiki. Tunda akaanza kucheka. “Subirini
chakula kitakuwa tayari sasa hivi. Njaa inauma?” Walimsikia mama Penny jikoni. “Net
aliniwekea ule uji wakati tupo njiani. Ndio nimemalizia hapo nje na kuingia
ndani.” Akajibu Tunda na kwenda kukaa pembeni yake Penny.
“Penny!” Tunda akamwita taratibu huku akimgusa lakini
Penny hakuitika. Akabaki amefunga mdomo kwa nguvu huku akimtizama. “Mbona
huongei bwana!?” Tunda akamuuliza Penny. Pendo akawahi yeye kujibu. “Mwenzio
ameambiwa na mama, akifungua tu huo mdomo wake, iwe kunywa maji au chakula. Lasivyo
anaenda kumtoa sadaka kwenye kanisa la watu wanaokunywa damu za watu ili
wainywe damu yake yote.” Tunda alicheka na kucheka bila kunyamaza mpaka
mchungaji na yeye akaingia kutoka kanisani.
“Mbona Tunda anakufa kucheka? Wewe
Penny umemwambia nini?” Penny akatingisha kichwa kukataa, Tunda akazidi
kucheka. “Mbona huongei wewe!? Umeng’oa jino?” Mpaka Net akacheka.
“Mwanao ameambiwa na mama, akifungua tu
huo mdomo wake, anaenda kumtoa sadaka kwenye yale makanisa ya wanao kunywa damu
za watu.” Pendo akajibu kishabiki.
“Wanakula na nyama za watu pia. Tena za
watoto ndio wanazipenda sana. Si niliwasomea kwenye bibilia kuna wakati watu
walipoasi, walikuwa wakitoa sadaka za watu kwa miungu yao na kuwateketeza kwa
kuwachoma moto kama sadaka?” Mchungaji akaongeza. Pendo akazidi kucheka, Penny
akaanza kulia huku amefunga mdomo.
“Leo lazima wakamchome Penny. Hawezi
kunyamaza huyo.” Pendo akazidi kumcheka dada yake. “Mwache bwana Penny wangu!
Si umenyamaza?” Tunda akamuuliza. Penny akatingisha kichwa kukubali huku
akilia. “Na akifungua tu mdomo wake huyo, anaondoka hapa leo. Halali humu
ndani.” Mama Penny alitoka jikoni na sahani. Penny akazidi kujivuta mwisho
kabisa wa kochi. Akakunja miguu, akainamisha mdomo kwenye magoti huku
akimwangalia mama yake. Tunda akazidi kucheka.
Mama yake akapanga chakula huku
wakicheka hili na lile, wakamuona Penny ananyoosha kidole. “Penny! Penny wewe
mtoto wewe! Kuna linalokutafuta.” Wakaanza kucheka tena. “Mwanao huyo hawezi kunyamaza.
Na mazungumzo yote haya yanayoendelea, asiongee chochote! Sijui!” Baba yake
akaongeza. “Basi dada aende akamfungashie mizigo yake. Maana akifungua tu mdomo
wake, anaondoka humu ndani.” Penny akashusha mkono taratibu huku akilia. Pendo
akazidi kucheka. Wakampelekea chakula palepale alipokuwa amekaa. Wao wakahamia
mezani.
Walikaa hapo mezani wote wakila na
kucheka. Net ndiye aliyempakulia Tunda chakula kama kawaida yeke. Tunda alikula
sahani mbili za ndizi za mchuzi, bila shida. Kwa mara ya kwanza akaonekana
amekula chakula chakueleweka. Net akalifurahia hilo. “Nashukuru mama Penny.
Naomba nimuwekee kingine hapa kwenye hii sahani. Ili ale tena usiku.” “Wala
usijali. Nitamuwekea kwenye bakuli zuri, mtaenda kupasha moto.” “Asante. Naona
hizo ndizi zimekubaliwa.” Net akashukuru. Wote wakacheka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Naomba niwashukuru Mchungaji na mama
Penny.” Wote wakamgeukia Tunda. “Asanteni kwa kuja kuniona nilipokuwa jela bila
kunikatia tamaa japo niliwafukuza.” “Sasa mbona hukuwa ukitoka kutuona Tunda?”
“Nisingeweza kumaliza muda wangu baba Penny. Ingeniwia ngumu sana. Halafu muda
mfupi tu nilipoingia mle, nikajigundua ni mjamzito. Nilijua mama Penny akiniona
tu, angejua, halafu ingemuumiza zaidi na pengine angemwambia Net, angezidi
kuchanganyikiwa.”
“Halafu nikaanza kuugua mfululizo.
Kilianza kichefuchefu na kutapika sababu ya mimba. Miezi mitatu ya mwanzo
ilipoisha tu, wakiniambia labda nitapata nafuu, zikaanza UTI. Nikadhoofu! Kuna
kipindi nilikuwa siwezi hata kusimama. Sikutaka kuhurumiwa. Ingenikatisha
tamaa, nikaogopa pengine ningeshindwa hata kutoka.” Kila mtu kimya.
“Ila nilikuwa nikifurahi sana
nilipokuwa nikisikia mmekuja kuniona. Nilikuwa nasubiria siku za kutembelewa
kwa hamu kweli. Ile kusikia baba Penny, au mama
Penny amekuja kuniona, nilikuwa nafajirika nakupata nguvu. Net ndio kabisa.”
Tunda akacheka kidogo, nakujifuta machozi.
“Nilikuwa naangalia saa, nasubiri kuja
kuitwa kuwa Net amekuja. Wakichelewa kuja kuniambia, nilikuwa nasikia kama
kuchanganyikiwa. Uzuri kila mtu alikuwa akimfahamu
pale. Basi nikiambiwa yupo pale ananisubiri, nilikuwa nasikia uwepo wake kule
nilipo. Ilikuwa ikinifariji sana.” Kimya. Tunda akaendelea.
“Siku moja moja nilikuwa naumwa. Ndio
kipindi hicho siwezi hata kusimama. Hakuna kinachopita mdomoni.” “Walikupeleka
hospitali?” Net akauliza.
“Hapana! Waliniambia ni hali ya ujauzito
tu, nitakuwa sawa. Basi, nilikaa nikilia, namsubiria Net. Halafu kama Mungu,
siku hiyo Net akawa mtu wa kwanza kujiandikisha. Askari akanifuata kule
infumary, kijihospitali cha jela, nilipokuwa nimelazwa, akaniambia, ‘Mzungu wako kaamkia gerezani. Amekuwa wa
kwanza leo na kabeba maua kibao!’” Wakacheka wote.
“Nilifurahi
mpaka basi. Ndio nikamwambia asimwambie kama ni mgonjwa. Net akaondoka baada ya
muda kuisha, akarudi tena mchana. Akakaa hapo mpaka jioni, akarudi tena kesho
yake. Najua mnaweza msielewe, lakini kwangu ilikuwa faraja sana. Nawashukuru.”
Kimya kikazuka kwa muda. Kila mmoja akiwaza lake.
“Pole sana Tunda. Pole mama.” Akavunja
ukimya mchungaji. “Sasa hivi nimepoa.” Akacheka huku akijiweka sawa. “Lakini
lazima kuangalia afya yako Tunda. Bado umedhoofu mama.” “Kesho tutaenda kumuona
daktari.” “Na ujitahidi kula. Umesikia Net?” Mama Penny akaingilia. “Nakusikia.”
“Huo mwili hauna nguvu yakubeba mtoto mkubwa. Msizembee hata kidogo. Ale
virutubisho vingi na kwa haraka ili kushindana na muda uliobaki kujifungua.”
Mama Penny akasisitiza.
“Sawa. Na pia nafikiria kuwachukua wote
wawili. Pengine kabla hata bado hajajifungua.” “Mnakwenda wapi?” Mchungaji
akauliza. “Kwanza mapumzikoni. Kumalizia mapumziko yetu, pili tunarudi nyumbani
kwetu sasa. Akatulie kabisa mpaka amalize swala la uzazi ndipo afikirie swala
la kazi.” “Inamaana unakwenda naye Canada!?” Mama Penny akashtuka sana.
“Kule ndio nyumbani mama Penny.
Nilikuwa hapa kwa kuwa nilikuwa nikimsaidia mama na maswala yangu na Tunda.
Sasa mama haitaji tena msaada wangu. Halafu hata hivyo naona niwakati muafaka
na mimi nijenge familia yangu.” “Mama yako yuko wapi?” “Hata sifahamu.” Net
akajibu kwa kifupi tu.
“Sasa hufahamu alipo, halafu unamchukua
Tunda hapa! Kama yuko huko huko Canada!?” “Naomba uniambie ni nchi gani Tunda
atakuwa salama, ili mimi nimpeleke nikaishi naye huko!” Kimya. “Hapa nyumbani
kwao, walitufuata hotelini wakamchukua. Sasa..” “Si kwa kuwa mama yako ndiye
aliyesababisha hayo!” Mama Penny akaongea kwa hasira.
“Isingekuwa mama yako yote hayo
yasingempata Tunda.” “Nishauri natakiwa kufanya nini mama Penny. Nifanye nini!?
Mama Cote ni mama yangu. Nipende nisipende yupo kwenye maisha yangu hilo siwezi
kukwepa. Wapi anaishi na nini anafanya, siwezi kuzuia. Tunda ni mke wangu.
Siwezi kuishi popote bila Tunda. Sasa natakiwa kufanya nini?” Net
alishabadilika rangi. Tunda kimya.
“Kuongeza umakini juu ya mama yako kwa
Tunda. Na hilo sitalinyamazia Net. Nakuambia ukweli kabisa. Usije kuwa mnaruka
moto, mnaenda kukanyaga tanuru. Tumeona nguvu ya mama yako na kile anachoweza
kufanya akiamua. Amewasha moto, ameishia kuteketea Gabriel na mkewe ambaye
hatakaa akatoka jela. Yeye yupo sehemu ametulia. Sasa kinachonitia hofu ni
kuona ile juhudi yake mpaka kufikia kumwaga damu halafu haijatoa matunda
aliyotarajia!” Tunda kimya. Akabaki ameinama.
“Sijui kama unanielewa Net? Mimi ni
mkweli, na sitawaficha kwa lolote. Gabriel amekufa akiongea machache juu ya
mipango yake ya kumuokoa Tunda dhidi ya mama yako na mkewe. Sasa na wewe upo
tayari kupambana na adui wa Tunda kama Gabriel?” “Ukinilinganisha na Gabriel
unakosea mama Penny.”
“Kivipi? Maana na yeye alikuwa
akimpenda Tunda na kumpigania. Niambie tu, ni juhudi gani unafanya au utafanya
kumlinda Tunda dhidi ya mama yako? Maana mama ni mama.” “Sina majibu ya
kukutosheleza mama Penny. Tokea Tunda yupo jela nilikwambia kile nilichofanya
kumsaidia Tunda.”
“Kwa kumtumia bibi yako! Net?” Mama
Penny akamshangaa sana. “Hatuombei mabaya, lakini endapo bibi yako akifa leo,
ukabakia wewe na mama yako. Akamkabili Tunda kwa staili ileile na uongo
atakaochanganya na ukweli fulani kwa vile anavyomfahamu Tunda, utafanyaje? Wewe
mkeo anasainishwa talaka mbele yako, umetulia tu!” “Alisema angemuweka jela
kama hatasaini.” Net akajaribu kujitetea.
“Sasa ulizuia nini na ni nini kilimpata
Tunda na mtoto wenu? Uliishia palepale, Net. Ulishindwa kumlinda Tunda na mtoto
wako. Leo tupo hapa, tukizungumzia haya kwa ajili ya maamuzi mabaya
uliyochukua, au kushindwa kumlinda Tunda.” Mama Penny alikuwa mkali kwa Net.
Alizungumza naye bila kumficha.
“Leo unataka kumtoa tena hapa, unampeleka
Canada sijui! Nakuuliza mama yako alipo, hujui! Mipango gani uliyonayo dhidi
yake, huna! Kuna mambo yakuombea, na mambo yakusimama wewe kama mume na baba.
Ukifanya mchezo, Tunda ataishia jela maisha yake yote. Hakuna mwanadamu ambaye
anaweza kutafutwa kasoro, ikakosekana.” Net kimya. Akabadilika, akawa mwekundu.
Alishindwa hata kuzungumza tena.
“Labda mimi nikuulize Net. Huko
unakotaka kumpeleka Tunda, ni kwako au kwa bibi yako? Na ni kama ni kwa bibi
yako, anazo taarifa za ujio wa Tunda? Na je, ameridhia? Nikimaanisha, yeye
mwenyewe anafurahia kumpokea Tunda? Kabla hujajibu, naomba kukumbusha Net.”
Mchungaji aliingilia, nakuanza kuongea yeye.
“Unakumbuka siku ya harusi yenu? Siku
yenyewe kabisa ambapo alikuja mama yako wakati maharusi wapo nje kwenye gari,
wanasubiri kuingia? Unakumbuka?” Net kimya. “Mama yako alikuja, akakutisha sana
tu. Alilolifanya kwa Tunda, halikuwa geni kwako ila kwa Tunda.” Tunda
akamwangalia Net kwa mshangao kisha mchungaji.
“Sina nia yakuwagombanisha, ila nataka
kukukumbusha ule ushauri wangu. Nilikwambia, Tunda ni muelewa sana. Ahirisha
harusi, nenda kawekane sawa na mama yako, ndipo ujipange upya. Nafikiri
unakumbuka majibu yako kwangu. Lakini mlitulia siku mbili tu, Tunda akaishia
jela, wewe ukarudishwa Canada na mama yako.” Mchungaji akaendelea.
“Fununu zinasema. Sasa sijui ni kweli
au la. Maana zinatoka kwa ndugu wa Bethy. Kuwa mama yako aliwachezea akili
Bethy na Gabriel. Ni kama alikuwa akiwazunguka. Akikutana na Gabriel, anapanga
hili, na akikutana na Bethy anapanga jingine tofauti na alilolizungumza na
mumewe. Amefanya huo mchezo, akijua kote atafanikiwa kufikia lengo moja tu,
kumtoa Tunda kwenye maisha yake. Kwa
Gabriel alimwambia atakutoa wewe nchini, akutenge na Tunda, ili warudiane. Kwa
mkewe, wamfunge Tunda, amtenge na mumewe. Wanandoa wale wote wamekosa, yeye
alishinda kwa muda. Lakini katika mipango yake yote, hakutaka kukuumiza wewe
hata kidogo, fununu ndio zinasema hivyo.” Mchungaji akaendelea.
“Kinachoendelea sasa hivi, si Tunda
tena kusakwa na ndugu wa Bethy na Gabriel, ni mama yako ndiye anayesakwa. Na
ninasikia, alichofanya. Tena kwa akili sana. Ameuza mali zake karibia zote hapa
nchini, akatoroka.” Tunda na Net wakashtuka sana.
“Lakini kila alichouza, au kila mpango
aliofanya hapa nchini, alihakikisha hachafui jina lake. Inasemekana kisheria,
ameacha mambo yake vizuri sana. Tena kwa kuaga kwenye vyombo vya usalama kuwa
anasafiri kikazi au kibishara. Alikaa hapa akiuza mali zake huku akienda polisi
akijidai anatoa msaada wowote watakao uhitaji.” Mchungaji akaendelea.
“Kisheria, mama yako ni mtu mzuri sana.
Na alihakikisha anaondoka bila lawama, wala deni. Alipokwenda, ndio
hapajulikani. Sasa ndio wasiwasi alionao mama Penny.”
Alipitiwa na usingizi palepale kwenye
kochi alipokuwa amekaa. Na mdogo wake alilala pembeni yake. “Kinachomtia
wasiwasi mama Penny, au kinachomuumiza ni vile Tunda alivyotupwa. Hata akiwa
jela huyo au akapotea, hakuna atakayemdai Tunda wala kumgombania akitaka
atolewe.” Tunda akafuta machozi.
“Amefungwa jela, mama yake akachukua
kampuni yake, akaigeuza yake. Tena na yeye anafanya vizuri tu! Muulize mama
Penny. Anatumia vifaa vya Tunda huyo huyo. Mwanzoni mama Penny alitaka
kumpokonya, lakini akawahurumia watoto wake. Akamfundisha kazi kidogo tu.
Akaamuachia aendelee kivyake. Alimpa kazi mbili tatu alizokuwa akizipokea mama
Penny, hakuchukua hata mwezi, yule mama anakipaji kizuri sana. Tunafikiri ndiko
Tunda alikorithi. Mama Penny alikuwa akiniambia jinsi watu wanavyomsifia kama
Tunda.”
“Hakuonekana jela, wala hajarudi hapa
kutoa shukurani au kujua la kheri wala la shari! Hatujamsikia akimuulizia
Tunda, ila akisema anafuta jina la Tunda kwenye kampuni yake, ili isimuharibie
kazi. Baba yake naye ndio hivyo. Yule mzee ni muungwana, mpole wa kupitiliza.
Hataki maneno kama Tunda. Mkewe kamfukuza, alikuja hapa akaaga, anarudi kwao
kufanya biashara. Wewe unamchukua Tunda, unampeleka Canada, wakimfunga huko, ni
nani atamtetea?”
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Bado mambo hayajamkalia sawa Tunda. Atafanyaje na bado Ritha hajapata anachotaka? usikose muendelezo. Mazito na ya Kusimisimua bado yapo mbeleni.
0 comments: