NILIPOTEA PART 8 – SEHEMU YA A
Kwa Vic, Maya na
Jake.
V |
ic alishamlazimisha Maya kusafisha damu za Jake
pale sakafuni na risasi ikimfuata nyuma
mpaka akamaliza kusafisha na Vic akaridhika kwamba panafaa kwa Net. Akafanya
kama alivyoshauriwa na Malcon. Akamfunga Maya aliyekuwa bado akilia, mdomo,
mikono na miguu kwa kutumia tape. Akamfungia chumbani kwa Jake. Yeye akaanza
kujitengeneza vizuri ili Net akija
amkute msafi. Akaosha uso palepale jikoni na bastola yake mkononi. Akaachia
nywele zake vizuri huku akizitengeneza na vidole. Akatoa lile koti la juu
jeusi. Akabakiwa na kiblauzi cha ndani. Akafungua vifungo kadhaa juu. Na
kupandisha matiti yake juu kidogo ili kumvutia Net.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kule alipotolewa Jake, hakukimbizwa hospitalini.
Uzuri risasi ilipita kwenye nyama. Akaambiwa hatakufa. Akafungwa kile kidonda
ili kisitoe damu zaidi. Akahamishiwa kwenye gari ya CSIS na kukabidhiwa laptop
palepale kwenye gari. “Usipompata Mrs Cote sasa hivi. Tunafungua kicho kidonda
na tunakupeleka jela.” Wakajaribu kumtisha. Jake akacheka.
“Haunitishi. Na siogopi. Nitafanya kwa sababu
nilimuahidi Maya. Maya ni mpenzi wangu. Nitafanya chochote kwa ajili ya..”
Malcom akampiga Jake ngumi ya nguvu na ya kushtukiza mpaka akaanguka. Maafisa
waliokuwa karibu naye wakamshika Malcom. Roy akamtoa pale ndani ya gari.
“Tafadhali tulia Malcom. Usitake baada ya hii kesi,
tukaanza ya kwako.” “Amefanya mapenzi na Maya!” Malcom akapiga ngumi gari. “Najua,
na ninaomba utulie.” “Mshenzi kabisa.” “Naomba utulie na tukajaribu kumtoa Maya
kwa nyuma.” “Hapo sawa. Ngoja nikamuulize Jake jinsi...” “Hapana Malcom.
Nisubiri mimi ndio nitazungumza na Jake. Sio wewe. Wewe utaharibu. Jake
anatakiwa kutulia ili amtafute Mrs Cote. Na kama akipatikanika ujue sifa zote
zitakwenda kwako.” “Sifa za kusababisha Maya afanywe mapenzi!?” Malcom akauliza
kwa hasira.
“Naomba nisubiri hapa nje. Na usiingie ndani ya hii
gari. Hata kama nitachelewa. Nisubiri hapa nje. Sawa Malcom?” “Fine.” “Fine?”
Roy akataka uhakika. “Nimesema fine! Unataka kusikia nini tena?” Malcom
akagomba. “Sawa Malcom. Lakini nataka kukukumbusha kuwa, ulianza vizuri sana,
unataka kuharibu mwishoni, hii ni promotion kubwa sana kwako.” “At her cost?
Wote mmemwangalia wakati akilia huku akifanywa mapenzi! Hivi sivyo nilivyotaka
kupanda cheo. Na wewe unajua. Itanisaidi nini kukalia kiti ambacho najua
nilimtoa mtu kafara!? Nina tofauti gani na wanaume wengine waliokuwa
wakimchezea na kumdanganya?” Malcom akamuuliza kwa machungu.
“Maya amefanya kila kitu kwa hiyari yake. Alituma
ujumbe kwa wazi kabisa. Akisema kama aliweza kutumiwa mwili wake kwa ujinga, si
zaidi sasa hivi ili kumuokoa Mrs Cote! Ule ujumbe ulikuwa ni wako Malcom.
Alikwambia wewe. Tafadhali tulia na uache kujihukumu.” Malcom akaondoka pale
bila ya kumjibu tena.
Roy akarudi ndani ya lile gari akamkuta Jake
akishugulika haswa. Wakamkonyeza Roy kuwa asimsumbue. “Lazima nimuulize njia
yakumtoa Maya pale ndani. Lazivyo Malcom ataingia mle ndani kwa kupitia mlango
wa mbele, na ninajua nyinyi wote hamtaki kumuona Malcom anaingia matatizoni.”
Akamsogelea bosi wao.
“Wote tunajua jinsi Malcom alivyohangaika na hii
kesi. Tafadhali mfikirie.” Roy akambembelezea kwa bosi wake. “Mnataka nini?”
“Ajue chumba alichofungiwa Maya kama kina madirisha mangapi na lipi linaweza
kufunguka kwa urahisi, ili akamtoe. Nitakuwa naye, nakuahidi tutakuwa makini.
Na tutafanya hivyo wakati helicopter inashuka. Kukiwa na kelele ndipo na sisi
tutavunja dirisha. Kwa haraka na kwa umakinifu.” “Tafadhali kusitokee makosa
kama yale ya Toronto, Roy! Msichanganye mapenzi na kazi.” Akaonya bosi wao. “Mimi
nimekwambia nitakuwa naye. Usiwe na wasiwasi.” Bosi wake akamtizama.
Akamkumbuka Roy na Malcom. Akasita.
“Hapana Roy. Nyinyi nawafahamu vizuri sana.
Muongezeni na Dan.” “Mbona kama hutuamini?” “Ukitaka ruhusa yangu, kamchukueni
na Dan nje. Lasivyo hapana. Nyinyi akili zenu
wote wawili zinafanana. Mtanifanya niitwe tena kujieleza kama ile safari
niliyowatuma Toronto. Hapana.” “Sawa.” Roy akakubali. Akamsogelea Jake. Na kweli Jake alionekana ametulia.
Alimjibu maswali yote Roy huku akiendelea na kazi kwenye ile laptop.
“Sogeeni niwaonyeshe kitu.” Wote wakamsogelea Jake.
“Unaona hili gari?” Akawaonyesha gari lililokuwa likiingia chini ya daraja. “Angalia
uzito wake hapa kwenye kompyuta kabla halijaingia chini ya daraja kwenye muda
huu. Kisha angalia hapa wakati linatoka.” Wote wakaangaliana na kustaajabu.
“Wakati haya mengine, kabla na baada ya kupita
chini ya hii tunel, yote yaliingia kwa uzito huu na kutoka kwa uzito huohuo.”
Mpaka yule bosi wa CSIS akacheka nakumpongeza. “Man you are Genius!” “Sasa subiri tulifuatilie. Lakini..” Jake
akaacha kila kitu na kumgeukia Roy. “Unakwenda kumuokoa mpenzi wangu au niende mwenyewe?” Jake akamuuliza Roy.
Kama anayemwambia Roy kuwa aende haraka lasivyo
ataacha hiyo kazi ili akamuokoe Maya, yeye mwenyewe. “Wewe ni mwenda wazimu
J..” Bosi wake akamvuta Roy nje kwa haraka kabla hajamtibua Jake. “Usirudi humu
ndani Roy. Wewe na Malcom. Nisiwaone tena.” “Fine.” Akajibu kwa jeuri Roy
nakupiga ngumi gari, kisha akaondoka pale kwenda kumtafuta Malcom.
Hawakumwita afisa Dan kama walivyoagizwa na bosi
wao, wakaenda wao wawili kujaribu kumuokoa Maya. Walizunguka mpaka nyuma ya
hiyo nyumba. Wakamuona Vic akizunguka ndani huku akipiga piga ile bastola
taratibu kichwani mwake.
“Unafikiri na huyu naye ni mzima?” Roy akamuuliza
Malcom kwa kunong’ona. “Wote wawili yeye na Jake ni ma Psycho. Vichaa waliotakiwa wawe hospitali ya vichaa
hatarishi kwa muda mrefu sana, ila pesa ndio imewaacha mtaani wakiangamiza raia
wema.” Akajibu Malcom kwa kuumia akisikika kulalamika pia. Mara wakasikia mlio
wa helicopter, wakajua ndio iliyombeba Nathaniel Cote. Bosi wao akawaacha
maafisa wawili pale ndani ya ile gari na mtu wa CSIS upande wa Kompyuta kusaidiana
na Jake, yeye akatoka kwenda kumpokea Net.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Anakwenda wapi?” Jake akauliza. “Wewe tuliza akili
kwenye kazi.” “Kwani na wewe unatatizo gani!? Si nataka kujua tu.” “Amekwenda
kumpokea Nathaniel Cote.” Ikabidi tu amjibu. Jake akashtuka sana. “Unamaanisha
The Nathaniel Cote!?” Akauliza Jake kwa mshangao. “Ndiyo! Kwani wewe
unawafahamu kina Nathiel Cote wangapi?” Yule mtu wa Kompyuta wa CSIS akamuuliza
kama asiyetaka azidi kupoteza muda.
“Ooooh! Vic anampenda sana. Anakuwa kama anamwabudu
kuliko hata Mungu. Unajua wakati mwingine ananilipa niwe kama Nathaniel Cote?”
Wote wakamwangalia kwa mshangao. “Sidanganyi. Anapokuwa ananiita labda kwenye
hoteli nifanye naye mapenzi, anakuwa
anakuja na pafyume kama anayojipulizia Nathaniel Cote na lotion zake.
Ananiambia nioge kabisa, halafu ananipaka lotion na pafyume kama zake Mr Cote.
Halafu ananifundisha jinsi ya kuwa kama Nathaniel Cote hapo kitandani.
Namfanyia kama yeye. Hapo Vic anaweza kucome zaidi
hata ya mara 4 kwa muda mfupi sana.” Wakabaki wametoa macho. Jake akafikiria tena.
“Hawa watu wanatumia pafyume za gharama zaidi ya
mshahara aliokuwa akipokea mama yangu kwa mwezi! Saa zao na...” “Tafadhali
rudisha mawazo kwenye kazi tumpate Mrs Cote.” Afisa mmoja akamrudisha kazini. “Kweli.
Kila dakika moja inayokwenda bila kumpata, ujue yupo hatarini.” Akaongea Jake
na kuendelea kufuatilia gari ya pili aliyodhani itakuwa imemtoa Tunda pale
kwenye tunel.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Malcom na Roy walishamuomba bosi wao kuwa ile
helicopter iendelee kuwepo pale kwa dakika tano zaidi. Zikiisha tu ndipo
inaweza kuondoka au kuzima ili wavunje dirisha. Kwa hiyo ilipotua tu, Malcome
na Roy wakajua wanadakika tano kwa hiyo lazima kufanya kazi kwa haraka. Malcom
akachungulia dirishani, akamuona Maya amefungwa akilia sana. Wakaanza kazi
yakufungua hilo dirisha kwa kulivunja kwa tahadhari ili wasimshtue Vic huko
ndani.
Bosi wa kina Malcom alitoka hapo akikimbilia
ilipokuwa imetua ile helicopter ili kumpokea Net na kumpa chakuzungumza
atakapokutana na Vic. Maafisa wengine wakawa wanaongozana na huyo kiongozi wa
CSIS, wakashtuka sana kumuona na bibi
Cote. Magari ya polisi na CSIS yalikuwa yakimiminika hapo kama nyuki. Hali
ikawa imechafuka na kubadilika kuwa ni ‘hostage situation’. Tena hostage
mwenyewe ni binti wa Cote! Vyombo vya habari vilishaanza kujaa hapo kuwa Miss Cote ameshiliwa na risasi ndani na Vic.
Wazazi wa Vic nao walishapigiwa simu kuelezwa hiyo hali,
na wenyewe wakawa wapo njiani kuletwa kama Net, ikitokea kama Net akishindwa
kumtuliza ili wazazi wake wamtulize na kumtoa pale bila kumdhuru mtu.
Net na Vic .
N |
et alivuta pumzi mara kadhaa akajiweka sawa, kisha
akaenda kugonga mlango. “Ni Net?” “Fungua mlango Vic.” Vic akafungua mlango kwa
haraka. “Kwa nini unabastola mkononi?” Net akamuuliza huku akimpita pale
mlangoni. “Sio mimi Net.” “Unaongea nini?” Net akamuuliza taratibu tu. “Najua
umenikasirikia Net. Lakini wazo la kusambaza ile video linatoka kwa mama yako.
Mimi nakupenda Net, nisingeweza kukufanyia hivyo.” “Kama unanipenda ni kwa nini
ulinilevya ili kufanya mapenzi na mimi?” Vic akaanza kulia.
“Naomba utulie Vic.” Vic akaendelea kulia. Ikabidi
Net ajirudi. “Niangalie Vic na uzungumze na mimi. Kwanza unafanya nini huku
mbali na nyumbani?” “Nilimfuata Jake. Gina alisema
Maya amekuja huku.” “Sasa Maya yuko wapi?” “Nimemfungia
ndani Net. Maya ndiye anayetutenganisha.”“Tulia tuzungumze.” Vic
akajifuta machozi kwa haraa. “Si unajua jinsi Maya asivyonipenda?” “Kwa nini
unadhani Maya anakuchukia?” “Anataka kuchukua nafasi yangu kwako Net. Tokea
yupo mtoto, hataki mimi na wewe tuwe pamoja.” “Ndio maana ulimtafutia Jake?”
Hapo Vic akaanza kulia tena.
“Kwa nini mahusiano yetu unataka yaendeshwe na mama
yangu?” “Mama yako alisema Tunda ndiye
anatutenganisha mimi ndio mke wako sahihi. Natakiwa tu kukukumbusha.” “Kwa
kumchukua Tunda!?” “Hapana Net. Mimi sihusiki
kabisa. Huko sihusiki. Na mama yako nilimkatalia kabisa. Naomba niamini Net.”
Akazidi kulia akimbembeleza Net. “Mpaka sasa hujaniambia chochote Vic, unataka
niamini nini?” “Kuwa sio mimi. Ni mama yako ndiye
anayefanya kila kitu.” “Amefanya nini?” Net akaendelea kumuuliza huku
amesimama akimtizama kwa utulivu tu.
“Nakupenda Net. Lakini unanipuuza!” “Vic! Tulia, acha kuhama hama kwenye mazungumzo.
Focus.” “Kwani hunipendi tena, Net? Hata mama yako
anajua kama mimi nakustahili. Nini kimekosekana kwangu? Niambie nijitengeneze
niwe mke unayemtaka.” “Vic, huna tatizo lolote. Naomba utulie.” “Sasa kwa nini unanipuuza? Siku unamkaribisha Tunda,
hukunitaja mimi. Ulimtaja Troy na Lean tu. Mimi ukanisahau! Ndio maana
nilichukia Net. Uliniumiza. Lakini nisingerusha ile video. Nilitaka
kukukumbusha na mimi nipo. Niambie kama unanipenda Net.” Vic alikuwa akilia
sana.
“Nisikilize Vic. Kwanza unajua huwa siwezi kutuliza
akili ukiwa unaongea mambo mengi kwa wakati mmoja tena ukiwa unalia. Wewe
unataka nikusikilize au niondoke?” “Usiondoke Net.”
“Basi tulia tuzungumze vizuri. Nataka utulie kabisa uniambie kila kitu.” Vic
akamsogelea. “Nikumbatie kidogo, angalau nitulie,
Net. Au umenikasirikia?” “Sikuelewi Vic. Huwa tunazungumza mambo na
tunayamaliza. Kwa nini unarusha mambo mtandaoni nikiwa sijui hata ni nini
kinaendelea! Na kwa nini umemchukua Tunda?” Bado Net hakuwa hata amemgusa.
Amesimama mbele yake, mikono mfukoni. Mrembo huyo analia mbele yake akiwa
amejishusha hasa, anabembeleza.
“Sio mimi
Net. Naomba uniamini.” “Futa machozi. Utulie. Uniambie ni nani?” Net
akaonekana yeye anamuweza. Alifanya kila alichomuamuru, tena kwa haraka sana.
Akatulia kabisa. Ndipo akaanza. “Unakumbuka mwanamke aliyeletwa kumsaidia kazi
Tunda akamkataa?” Net akavuta kumbukumbu akamkumbuka yule mwanamke, Tunda akiwa
mgeni kabisa. Akamkataa akisema hataki kufuatwa nyuma.
“Nimemkumbuka sura lakini si jina.” “Anaitwa
Malinda. Yule alikuwa mtu wa mama yako. Aliwekwa na mdogo wake, ambaye ni
mtaalamu sana wa kompyuta. Anajua jinsi ya kuingia kwenye mitandao na kufanya
mambo. Hakuwa hata kwenye ile kampuni ya kupata wafanyakazi. Ila alichomekwa
pale makusudi na kwa haraka akiwa ametengenezewa CV nzuri na mdogo wake ili afisa
mwajiri wenu, akiingia kule kutafuta mfanyakazi wa Tunda wa kumwajiri, amchague
yeye kwa haraka kwa kuwa alikuwa na sifa zote alizokuwa ameandikiwa na mdogo
wake. Alizoambiwa na mama yako. Ritha alisema kwa sifa hizo, nilazima
akipelekwa kwa bibi yako na afisa mwajiri wenu, atamkubali yeye Malinda na
kumpa kazi awe karibu na Tunda.” Net alitamani isiwe hivyo, lakini ni mama yake
tena! Aliumia sana.
“Naomba uniamini Net mimi sihusiki.
Hata aliponipigia simu kuniambia Tunda alimkataa Malinda. Tu..” “Vic, stay focus. Unaruka mambo na unachanganya
habari nyingi kwa wakati mmoja rudi nyuma. Na uache kulia, tafadhali.” Vic
akajaribu kutulia. “Nimeshakwambia Net. Yule mwanamke ni mtu aliyekuwa ametumwa
na mama yako. Alikuja pale makusudi ili awe karibu na Tunda.” “Ili iweje?”
“Ndio ilikuwa akishapata kazi, akafanikiwa kuwa karibu na Tunda, ndio ammpe
muongozo.” “Ikawaje?” Net akauliza tena.
“Si ndio Tunda akamkataa wakati yule dada alikuwa
na shida sana ya pesa kwa wakati ule! Alifukuzwa kazi katikati ya matibabu,
akapoteza insurance na akawa haajiriki tena. Ritha alijua yeye angefaa kwa kuwa
kwanza alikuwa nesi, pili alikuwa na shida sana na pesa.” Vic akaendelea. “Ritha
aliniambia amempata yeye Malinda ni mtu mzuri, atafanya kila tutakachomwambia,
kwa kuwa alikuwa na shida sana na mtoto aliyekuwa akimtafuta kwa miaka mingi.
Akashindwa kwa njia ya kawaida ya yeye na boyfriend wake, ndipo wakapata
tumaini ya Malinda kupata mimba kwa njia yakupandikiziwa mbegu kwenye hiyo
kliniki ambayo inataka pesa nyingi na ni kama Malinda amechelewa. Mbegu zake
yeye mwenyewe zinaisha sababu ya umri wake. Yupo desparate, anaweza kufanya
chochote ili tumlipe, akafanyiwe matibabu. Sasa si ndio Tunda akamkataa mbele
yake. Akaumia sana na ni kama Tunda akawa amempokonya mtoto na mwanaume wake
alishachoka kusubiri. Alimwambia hiyo ndio mara ya mwisho. Wasipofanikiwa,
anamuacha. Ndio wakapanga. Wakapanga..” Akaanza kujipiga piga kichwani kama
aliyesahau anatafuta kukumbuka.
“Vic, Vic. Niangalie.”
“Nakupenda Net.” “Najua. Walipanga nini?”
“Mbona sasa huniambii tena kama zamani?” “Kwa kuwa mambo yamebadilika
Vic. Mimi sasa hivi nimeoa na ni baba. Unataka nikudanganye?” Vic alilia mpaka
akakaa chini. Sivyo Net alivyoambiwa na wale maafisa usalama. Aliambiwa
amwambie kitu chakumtuliza ili azungumze wajue anachojua. “Ni bora nijiue nife!”
Akajiwekea risasi mdomoni. Hapo ndipo akili zikamrudia Net akakumbuka
alichoambia.
“Njoo kwanza Vic. Njoo.” Huku akilia Vic akaanza kumsogelea.
“Najua unanichukia sasa hivi.” “Sikuchuii
Vic. Kwa nini ufikiri hivyo? Sisi bado ni watu wakaribu sana. Unakumbuka siku
yetu ya prom?”
Vic akacheka. “Ulipendeza sana Net.
Kila mtu alikuwa akinisifia kuwa nimebahatika.” “Hata wewe ulipendeza na
ndio maana tulichaguliwa King na queen.” “Unajua
ndio nilijua itakuwa hivyohivyo kwenye maisha yetu yote?” Vic akauliza
huku akilia.
“Unafikiri tutakuwa tumechelewa?” Net akamuuliza
kwa kumbembeleza. “Sijui Net. Mambo
yamechanganyika. Nimeingiwa hofu. Jake naye anaonekana anaweza kutoa siri na
kunifanya nifungwe.” “Hawana ushahidi, usiogope. Rudisha mawazo hapa
kwangu. Acha kufikiria watu wengine.” “Sijawahi
kuacha kukufikiri Net.” Vic akajisogeza kwa Net.
“Nakupenda sana Net. Kuliko nafsi
yangu. Kuliko wanaume wote duniani.” “Sasa kwa
nini hukuniambia mipango yao juu ya Tunda?” “Kwa
sababu mimi nilijitoa mapema kidogo. Yule mwanamke Malinda alitaka amteke Tunda
siku atakapokwenda kujifungua kama hivi.
Halafu amfungie, ampandikizie mbegu. Tunda ambembee mtoto wake mpaka miezi 9
ndipo amzalishe yeye mwenyewe. Kisha amwachie Tunda, mama yako. Lakini nafikiri
hawakujua kama atazaa kwa operation. Kwa hiyo hii ya kuzaa kwa operation
imeharibu.” Net alishtuka sana kusikia hiyo mipango ya kinyama dhidi ya
mkewe iliyokuwepo kwa muda mrefu tu!
“Jana usiku alinipigia simu kunilaumu
ni kwa nini nimeharibu mpaka Tunda kufanyiwa operation! Inamaana itabidi
kuongeza gharama yakumuweka ndani Tunda. Kumtibu kwanza mpaka kidonda cha
operation kipone ndipo wampandikizie mbegu, abebe mtoto mwingine. Akakataa
kusubiri mpaka atibiwe pale apone. Akasema eti Ritha amemwambia kina Cote hawawezi
kumuacha aendelee kuwa pale, mtamuhamishia sehemu yenye ulinzi mkali. Kwa hiyo
bora awahi kumtoa pale. Ndio akasema yeye atamchukua hospitalini akiwa vilivile
mgonjwa na kumtibu mwenyewe mpaka apone. Sasa kwa kuwa mimi ndiye
niliyesababisha aanguke na kufanyiwa upasuaji, eti mimi ndio nilipie matibabu
yake Tunda akiwa nyumbani kwake yeye Malinda, mpaka apone, na ndipo
wampandikizie mbegu.” “Tulia kabisa
unielezee vizuri. Futa machozi kwanza.” Vic akatulia. Akawa kama amekumbuka
kitu.
“Nimekumbuka Net.” “Nini?” “Anavimbe tumboni ambazo
ameambiwa zinakuwa kwa kasi. Kwa hiyo kwa kadiri anavyochelewa kushika mimba
ndivyo kadiri ambavyo hatakuja kushika tena mimba. Halafu akaambiwa pia hata
akishika mimba, kuna hatari ya akija kushika mimba, mtoto anaweza kutoka mapema
sababu ya zile vimbe.”
“ Sasa kuja kufanya kazi kwenu ingemsaidia mambo
mengi. Mshahara ambao bibi yako alisema atamlipa ulikuwa ni mkubwa na
alimuahidi angemlipia pesa ya matibabu pia kama mnavyowalipia wafanyakazi
wengine na Ritha naye alisema atakuwa anamlipa kwa kila kazi atakayokuwa
akimtuma afanye kwa Tunda. Kwa hiyo alikuwa na uhakika wakupata mtoto na
kumtunza pia bila shida. Kitendo cha Tunda kumkataa, inamaana amemkosesha
mengi.”
“Sasa eti Ritha na Malinda walitaka
mimi nisubiri mpaka Tunda ajifungue! Mimi nikawaambia siwezi kusubiri mpaka
ajifungue kwa sababu itaanza kwanza harusi. Si unakumbuka ilikuwa muone kwanza
ndipo muende honeymoon, aje ajifungue? Inamaana
Ungemuoa Tunda kanisani wakati ndio ulikuwa mpango wetu mimi na wewe Net, tokea
watoto.” Vic akaanza kulia upyaa.
“Ilikuwa ni harusi na honeymoon yetu
Net. Lakini umeamua kumpa mwanamke mwingine! Unawezaje Net? Tena kwa honeymoon
tuliyokuwa tukiisubiria tokea watoto!?” “Hukuniambia
kama bado ulikuwa ukisubiria honeymoon Vic!” “Nilikuwa
nasubiria kwa hamu Net. Nataka unioe mimi sio mtu mwingine. Na ndio maana
ikabidi kumuwahi Tunda na kumwambia ukweli kuwa sisi tunapendana. Asije kuolewa
na wewe. Sisi hatukuwahi kuacha kuwa na mahusiano.” Vic akaendelea
kulia.
“Ilibidi kuzungumza naye, Net. Japo
mama yako yeye ananilaumu kuwa nimeharibu kila kitu. Tunda hakutakiwa
kuzungumza naye, ila kummaliza tu.” “Yeye anataka
mumuue!?” “Hapana Net. Sio mimi. Ni yeye mama yako
peke yake ndiye anayetaka Tunda afe. Na ndio maana wamepingana hata na
Malinda.” “Wamepingana nini?” Hasira zilikuwa zimempanda Net,
anatetemeka kabisa.
“Malinda anataka mtoto kutoka kwa
Tunda. Unajua Malinda anaamini Tunda ana bahati kuliko hata mimi! Eti anasema
hata tumbo lake linabahati ndio maana limeweza kubeba mtoto wako wewe Net,
anataka na yeye mtoto wake apitie kwa Tunda, lakini mama yako, Ritha anataka
Tunda auwawe.” Net akasikia kuishiwa nguvu kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Huku kwa kina Malcom, muda huo wanazungumza,
walishafanikiwa kufungua lile dirisha. Roy akambemba Malcom, ndiye akapenya na
kuingia ndani ya chumba alichokuwa amefungiwa Maya. Alimkuta Maya amefunga
macho akilia sana. Mengi yalikuwa yakiendelea kwa Maya. Amefanywa mapenzi ya
muda mrefu tu. Tena sio na Andy mpenzi wa zamani. Na Jake, kichaa kabisa! Na
hakufanya kwa kifupi. Kwa kirefu haswa akiwa na uhakika wale afisa hata kama
hawakuangalia, basi walijua alichokuwa akifanyiwa muda walipozima kamera.
Maya aliendelea kulia taratibu huku amefungwa mdomo
na mikoni. Malcom aliingia kwa kunyata, hata Maya hakuwa amejua kama kuna mtu
ameingia hapo chumbani. Akamgusa taratibu huku akimfanyia ishara ya kidole
kwenye mdomo kuwa asitoe mlio wowote. Maya akatingisha kichwa kukubali huku
akilia. Akamfungua mikono na miguu, akamtoa kwa dirishani. Maya alikuwa akilia
sana.
Roy akampokea nje ya dirisha na kumuweka chini.
Malcom naye akatoka dirishani. Maya alikuwa akitetemeka huku akilia pembeni.
Alijivuta mbali kidogo na Roy. Malcom akamsogelea na kumkumbatia. “Pole sana
Maya. Pole na samahani.” Maya aliendelea kulia huku akitetemeka. Malcom
akamvuta mpaka kifuani kwake akamkumbatia kwa nguvu huku akimbembeleza. “Lazima
tuondoke hapa Malcom. Sio salama. Anaweza akachungulia akatukuta bado tumesimama
hapahapa. Naomba tuondoke.” Roy akatoa ushauri. Malcom akaafikiana naye.
Wakatoka hapo taratibu huku amemkumbatia Maya.
Walipotokeza tu mbele, polisi wakawakimbilia na
kumchukua Maya. Wakamfuata bibi yake
kule ndani walipokuwa wakimsikiliza na kumwangalia Net na Vic. Wakamwambia bibi
Cote wamefanikiwa kumtoa Maya. Yule bibi aliruka na kutoka pale kwenye gari
kumfuata kule walipompeleka Maya kwenye gari ya wagonjwa ili wamwangalie kama
amedhuriwa. “Maya! Baby!” Aliita bibi Cote.
Wazazi wa Vic na wenyewe walishafika eneo la tukio.
Walikuwa hapo nje wakisubiri kujua kitakachotokea humo ndani kwa mtoto wao.
Alipotolewa Maya, yule kiongozi wa afisa usalama
ambaye alikuwa pale akiendesha mambo kwenye eneo la tukio na viongozi wake
wengine wakiwa kwenye simu na kompyuta wakifuatilia kila kitu kinachoendelea,
akaamuru waizunguke ile nyumba sasa ili kama kuna lolote litakalotokea wamuokoe
Net na kumkamata Vic. Mama yake Vic alikuwa akilia sana huku akiwasihi
wasimdhuru mtoto wake. “Vic ni mgonjwa jamani! Amesahau
tu kunywa dawa na amekuwa na stress nyingi mfululizo. Tafadhali msimdhuru.” Mama
yake akasikika akilia.
J |
ake naye alishafuatilia ile gari mpaka kwenye
nyumba ambayo ilikuwa porini kabisa. Peke yake. Afisa wakawa wameshatumwa huko
na helicopter ya usalama ikaelekea kwenye ile nyumba hiyo gari ilipoonekana
imekwenda hapo. Na pale tu Vic aliposema Malinda ndio anahusika, na ilikuwa
akamfungie Tunda kwake, palepale mtaalamu wa kompyuta huko ofisini kwao ili
wasimchanganye pale Jake, akaanza kutafuta anapoishi Malinda. Akaonekana
aliishi kwenye apartment moja katikati ya mji, lakini alifukuzwa sababu
yakushindwa kulipa kodi.
Wakatafuta walipo wazazi wake. Wakaona walifariki
na waliacha nyumba. Kuifuatilia hiyo nyumba, ikaonyesha ni palepale alipopaona
Jake gari ile aliyokuwa akiifuatilia kuwa imembeba Tunda, imekwenda. Hapo ndipo
wakaamini ndipo alipo Tunda. Ila swali likawa je, bado yupo hai! Wakajua
watapata jibu tu maana hapakuonyesha kama ile gari iliondoka pale.
Kwa Net & Vic
N |
et ilimlazimu kujikaza ili kuendelea kutafuta
chochote kutoka kwa Vic, kitakachosaidia kumpata mkewe. Alijua anasikilizwa na
wanaona kila kitu. “Sasa nani yupo na Tunda sasa hivi?” Net akamuuliza taratibu
tu huku Vic akiendelea kulia. “Weka hiyo bastola chini nikukumbatie Vic.
Usilie.” Kwa haraka sana, akatupa ile bastola na kumkimbilia Net. Net
akamkumbatia. “Nyamaza.” “Nimefurahi umenishika
Net. Hujui ni kiasi gani nilikuwa na hamu na wewe!”
“Tulia uniambie wapi walipompeleka Tunda.” “Sijui Net. Lakini jana tuligombana sana. Mimi nikakataa
kumlipa Malinda pesa, nikakata simu. Ila ninauhakika hawapo kwenye maelewano
hata na Ritha. Ila nahisi Malinda na kaka yake pamoja na huyo mwanaume wake,
ndio wamemchukua Tunda. Wao wanataka kumtumia Tunda sio kumuua kama Ritha. Ila
sipajui kwa kina Malinda na wala sikuuliza ni wapi watampeleka wakishamkamata.”
Mpaka hapo Vic hakuwa na matumizi tena na watu wa usalama.
Alishaongea yote, hata ambayo hawakutarajia
kuyasikia. Alishakiri maovu yake yote mpaka kuua usiku huo. Akataja wahusika
wote, na bahati nzuri vikawa vimeendana na uchunguzi wa Jake. Gari lililotoka
chini ya daraja aliloona Jake, likafuatiliwa likawa kweli lipo kwenye nyumba ya
wazazi wa Malinda. Kwa hiyo wakachukulia aliyosema Vic yote ni kweli.
Akabaki amemkumbatia Net huku amejificha shingoni.
Net akaona afisa usalama wale wa CSIS mlangoni wakitaka kuingia. Akawapa ishara
kuwa waingie tu, wakaingia kwa nguvu na haraka, wakamkamata Vic. Vic alilia
kama amechinjwa akimtaka Net amsaidie. Bila hata kugeuka nyuma, Net akatoka na
kupokelewa na kiongozi wa CSIS.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Vipi, upo salama?” “Mmefikia wapi juu ya mke
wangu?” Net akauliza bila kujibu swali. “Njoo.” Akampeleka alipokuwa Jake,
wakawa wanaangalia kwenye kompyuta. Wale maafisa walikuwa wameshazunguka hiyo
nyumba, Net akawaona ni kama wanasubiri amri waingine. “Wanasubiri nini!?” Net
akauliza kwa kuona wanachelewa kuingia na kumuokoa mke wake. “Wanasubiri amri
kutoka makao makuu. Huo uokoaji mzima unaendesha na mtaalamu wa uokoji huko
makao makuu.” Ikabidi Net awe mpole.
“Nimefurahi sana kukuona uso kwa uso Mr Cote.
Naitwa Jake.” Jake akataka kumpa mkono lakini Net akakunja uso, akamtizama tu
kwa sekunde kadhaa, akarudisha macho kwenye kompyuta bila hata kumpa mkono au
kumjibu kitu Jake. Wale maafisa waliona, wakajibaraguza tu.
Kule kwenye nyumba kunakosadikiwa amefichwa Tunda,
maaskari walikuwa wamejipanga kila mahali, tayari kwa kuvamia hiyo nyumba bila
ya aliyendani kutoroka wasimuone. Nyumba hiyo ilikuwa imezungukwa na usalama!
Kuanzia polisi mpaka watu wa CSIS. Helicopter ya CSIS ilikuwa inazunguka juu ya
hiyo nyumba, huku magari ya polisi na wagonjwa yakiendelea kumiminika hapo.
Bibi Cote naye akarudi pale ndani ya ile gari
aliyokuwepo Net kufuatilia uokolewaji wa Tunda. Kama yupo na kama watamkuta
yupo hai. Kila mtu alikuwa na wasiwasi na hilo. Walipopewa tu amri, walivamia
ile nyumba kama nyuki. Wangine walikuwa juu ya dari, wengine walivunja
madirisha. Kulikuwa na hekaheka ya namna yake. Net na bibi yake wakitizama.
Kwa kuwa ilikuwa usiku walivaa kofia zilizokuwa na
tochi. Zinazowasaidia kuona ndani. Ilikuwa giza. Lakini kiongozi wa kile kikoso
kilichovamia pale alikuwa amevaa kitu ambacho makao makuu na pale walipokuwa
kina Net, wanauwezo wakuona kinachoendelea. Walikata tamaa walipoonyesha juu ni
giza kabisa kama hakuna hata mtu anayeishi humo.
“Hakuna dalili ya kuwa kulikuwa na mtu
hapa!” Muongoza kile kikosi cha uokoaji pale kwenye ile
nyumba, akaongea kwa sauti baada yakuzunguka kila chumba pale juu. Akawa
anawaambia viongozi wake huko makao makuu. Jake na yeye akasikia. “Hapana. Angalieni kwa makini. Hilo gari lilionekana
limeishia maeneo hayo. Na nimetafuta, hakuna nyumba nyingine kwenye hilo eneo,
ila hapo. Lazima kuna basemant.” Jake akabisha akionekana anauhakika.
Kile kikosi na kiongozi wao wakaambiwa watafute
kama kuna mlango wakushuka au kuingilia chini. Wakaanza kusaka mlango. “Hakuna.” Yule muongoza kikosi cha uokoaji akajibu. “Dammit!”
Jake akagomba kwa sauti na kugonga meza karibu kupasua zile mashine pale. Wote
wakashtuka mpaka afisa mmoja akamshika Jake kwa nguvu. “Nimesema Mrs Cote yupo
hapo. Najua ninachozungumza. Najua kazi yangu. Mimi sio kichaa.” Jake akaanza
kulia. “Mtafuteni hapo. Vuteni hata makochi.
Angalieni hata chini ya kapeti. Lazima kuna njia ya kwenda chini.”
Akaendelea kuongea kwa sauti huku akilia. Net na bibi Cote wakashangaa sana wakimwangalia
yeye Jake. Hata hawakuwa wakimfahamu!
Ndipo bibi Cote akaomba wafanye tu kama
anavyoshauri Jake, wasikate tamaa. Wakaanza kutoa hayo makochi na kapeti kama
alivyoshauri Jake, kutafuta kama hata kuna tundu dogo tu, lakini hapakuwa na kitu
chini. Hawakukuta kitu chochote hata alama kuwa kulikuwa na mlango ukajengewa,
ila vumbi tu kuashiria hakuna hata aliyegusa kusafisha hapo kwa muda mrefu
sana. “Hakuna.” Kiongozi akarudisha ripoti ila
na wenyewe walikuwa wakiangalia pia. Kila mtu akawa amekata tamaa.
Jake akawa kama amefikiria na kukumbuka kitu. Akajitoa kwa yule askari
aliyekuwa amemshikilia. “Nipe mimi hizo headphone. Nimeshajua jinsi yakufika
chini.” Wakampa. Akamwambia yule kiongozi kule kwenye nyumba ya kina Malinda,
mlango utakuwa kwenye kabati fulani alilokuwa ameliona mwanzoni Jake wakati
wanapita humo ndani. “Sukuma kulia au kushoto. Nyuma ya hilo kabati la vitabu
ndio utakuwa mlango wakuelekea chini. Ninauhakika.” Wakawa kama wameshampuuza
tena. Jake akajua. “Jamani, ninauhakika. Ukiangalia jinsi lilivyowekwa,
utagundua linasogea, na limetoka kusogezwa muda sio mrefu.” Jake akashangaza
kila mtu pale. Uzuri, walikuwa akisikilizwa na wakubwa wa CSIS pia ambaye ni
rafiki wa bibi Cote. Wakaamuriwa wafanye tena.
Wakasogeza tu kulia na kushoto lile kabati halikusogea. “Hamna
kitu.” Akarudisha jibu tena. “Nilimuahidi Maya nitampata Mrs Cote.
Siwezi kumuangusha. Tafadhali niaminini. Hapo ndipo ilipo njia.” Kimya. “Dammit! Tumieni akili.” Akagomba Jake. “Sogezeni hilo kabati. Msipofanya, nakuja mimi mwenyewe
kufanya. Siwezi kumuangusha Maya. Tafadhalini nisaidieni. Kama sio kwa ajili
yangu basi fanyeni kwa ajili ya Maya.” Bibi Cote na Net wakabaki
wanamshangaa, Jake alikuwa akilia sana.
“Hakuna kitu hapa.” Akabisha yule muongoza kikosi cha uokoaji kule
huku akitingisha tingisha lile kabati. “Upo mlango
hapo. Angalieni chini. Wazi panaonyesha hapo ni pasafi kuliko kwengine. Kwa
nini nyinyi hamshangai nyumba nzima ni vumbi kasoro hapo! Inamaana pametoka
kusafishwa muda si mrefu kufuta alama za mikwaruzo wa hilo kabati.” Jake
akasisitiza huku akilia. Alikuwa akitoa mambo ya kina. Kama mtu anayeangalia
vitu kwa makini sana. Hakusikika kama kichaa. Mtu asiye na akili. Akamgusa bibi
Cote
“Mike!” Bibi Cote akaita kwenye headphone. Alijua
director huyo, kiongozi wa CSIS atakuwa anaona hicho anachoona yeye na kumsikia
Jake hukohuko alipo na viongozi wengine. Mike akaitika. “Tafadhali, naomba wafanye tu kama anavyoshauri Jake. Hakuna chakupoteza.
Tafadhali.” Bibi Cote akamsihi kiongozi wao. “Naombeni
msogeze hilo kabati. Ninauhakika hapo ndipo upo mlango wa kwenda chini na huko
ndipo alipo Mrs Cote. Angalieni hata lilipowekwa hilo kabati. Katikati ya
sebule na sehemu yakulia chakula! Na nyinyi fikirieni hata kidogo tu! Hakuna
nyumba inaweka kabati la vitabu kwenye sehemu kama hiyo. Inamaana wameliegesha
mahusudi. Wanaficha mlango.” Akaendelea kuwaaminisha Jake huku akilia.
Ikabidi director wao awaamuru wafanye kama
alivyosema Jake. Ndipo ikabidi
walisogeze hilo kabati kabisa. Wakasaidiana kulisukuma kwa nguvu, wakafanikiwa
kulitoa kabisa. Kweli wakaona mlango
mdogo sana upo juu ya sakafu, chini ya lilipokuwa limesimama lile kabati, wakajua
ndio wakuelekea chini. Jake akasikika akishukuru
mfululizo kwa sauti ya chini. Wakamtizama, kila mmoja akarudisha macho kwenye
kompyuta. Alikuwa amefunga macho. Kazi ya kufungua ikaanza maana ni kama
ulifungwa sana. Haikuchukua muda. Walitumia vifaa maalumu, wakafanikiwa kuvunja
na kufungua. Kila mtu roho mkononi. Kiongozi wao akatangulia kushuka. Ilikuwa
ngazi ndefu sana kufika chini. Wakaendelea kushuka na risasi mkononi mpaka
chini kabisa.
Karibu na ngazi za mwisho, walikuta mwili wa kijana
tu, wakizungu. Alionekana amepigwa risasi. Damu nyingi chini. Wakamshika, wakataarifu
kuwa ameshakufa. Kila mtu akaingiwa hofu. Zaidi Net. Wakaendelea kushuka kwa
tahadhari huku wakitangaza kwa sauti kuwa ni watu wa usalama wanashuka. Kama
kuna mtu huko chini, atulie asirushe risasi. Lakini ikawa kimya.
Pembeni tena wakakuta mwili wa Malinda. Naye
alikuwa amelala chini damu kifuani na tumboni. Ikazidi kuwaingia hofu.
Wakamgusa. Akataarifu yule kiongozi kuwa yupo hai lakini hana fahamu. Pakawa
hakuna tena kitu hapo. Chumba walichofikia kikawa kitupu. Machozi yakaanza
kumtoka Net.
Katika kukata tamaa huko, wote kimya, mara
akasikika mmoja wa wale maafisa kule akiongea kwa sauti.“Kipo chumba hapa nyuma ya ngazi.” Kingozi wao ambaye amevaa kamera akageuka kwa
haraka na wao kweli wakaona kimlango kidogo tu nyuma ya ngazi zakushukia chini.
Wote wakaelekea huko. Wakafungua mlango
kwa tahadhari, wakamkuta Tunda amelala, hana hata habari na dripu ya maji
mkononi. Wakamgusa. Wakatangaza kuwa yupo hai.
Net akaanza kulia tena. Safari hii kwa kupaniki
kama mtoto mdogo. Wakajaribu kumuamsha, hakuamka. Hapohapo bibi Cote akaita. “Mike?” “Nipo.” “Unaona kinachoendelea?” “Ndiyo.” “Naomba
akimbizwe hospitalini sasa hivi kwa kutumia helicopter yenu ili tujue ni nini
wameweka mwilini kwake.” “Nipo mbele yako.” Akajibu yule director wa
CSIS.
Tunda alichomolewa yale maji. Hapo hapo akawekewa
maji yakusafisha sumu mwilini, akapandishwa kwenye helicopter akakimbizwa
hospitalini. Umbali wa waliokuwepo hapo kina Cote mpaka alipopelekwa Tunda ni
masaa mawili na nusu kwa kuendesha gari ya kawaida. Hakuna jinsi bibi Cote
angeondoka hapo kwa gari. Ikabidi waite helicopter yao.
Wakati wakisubiri huo usafiri, wote wakaenda kwa
Maya, wakamkuta na Malcom akijaribu kumtuliza. “Yupo kwenye mshtuko tu.
Tunafikiria kumpeleka hospitalini ili akaangaliwe vizuri zaidi.” Mtu wa huduma
ya kwanza alitoa hiyo taarifa kwa kina Cote. “Haitakuwa hapa. Nitataka sehemu ambayo
ninauhakika anakuwa na ulinzi wakueleweka na ambapo mimi mwenyewe nipo.”
Akajibu bibi Cote. “Usafiri utafika hapa baada ya dakika 15 tu, tutaondoka.
Yupo daktari tayari anayemsubiria. Kwa hiyo nashukuru, ila tutandoka.
Hatatibiwa hapa.” Bibi Cote akaweka msisitizo.
Maya alikuwa amekaa nyuma kwenye gari ya wagonjwa,
amefunikwa na blangeti, ameinama akilia. “Come little sis.” Net akamvuta na
kumkumbatia. “Asante sana Maya. Niangalie nikwambie.” Maya akaendelea kulia.
Net akambusu kichwani mara kadhaa. “Leo usiku umemrudishia Cote mama yake.
Umenirudishia mke wangu na kusafisha jina langu. Naomba katika hayo tu
ujifariji kuwa kujitoa kwako kumetoa matunda mazuri.” Net akaongea naye akiwa
amemkumbatia, asijue alichofanywa dada yake kupata hayo matokeo mazuri.
“Mbali na hapo sweetheart, umefungua mambo makubwa
na mazito yaliyokuwa yakiendelea bila sisi kujua. Umesaidia vyombo vya usalama
kwa asilimia kubwa sana.” “Na umesafisha jina lako pia.” Akaongeza Malcom pale
alipokuwa akizungumza bibi Cote. Malcom alijua wazi alitakiwa apishe muda huo
wa familia, lakini ni kama aliyegongewa misumari hapo. Mtu wa huduma ya kwanza
alishapisha. Malcom akabaki hapo katikati yao. Roy alimkonyeza kuwa apishe,
lakini alikuwa amesimama hapo na Net na bibi Cote mbele ya Maya kama yeye ni
ndugu wa familia.
Roy akamgusa begani. Akasogea pembeni kidogo kama
asiyetaka kusumbuliwa. Roy alimjua jinsi alivyo mbishi. Akasubiri kidogo. “Malcom!”
Akamwita tena kwa sauti ya chini kama asiyetaka kusumbua. Hata hakugeuka. “Hey
Malcom?” “Leave me alone, Man!” Akagomba Malcom mpaka akafanya Net na bibi Cote
wawageukie wao wawili. “Nataka kuzungumza na wewe kidogo.” “Hapana.” “Basi
labda nikwambie kuwa unaitwa.” “Come on Roy!” Malcom akalalamika. “Sikutanii.
Unaitwa.” Net na bibi yake wakabaki wakiwatizama.
“Come on Malcom!” Roy akaweka msisitizo. “Nitarudi
Maya.” Malcom akaaga na kuzidi kuwashangaza. “Wewe ni nani?” Akauliza bibi
Cote. “Malcom.” “No Man! Wewe sio Malcom, wewe ni afisa wa CSIS.” Akakanusha
Roy na kujisogeza karibu. “Sisi, ndio tumekuwa na Maya kuanzia mwanzo na ndio
tumemtoa ndani alipokuwa amefungiwa na Vic.” Akaongeza Roy na kuendelea tena. “Sisi
ni CSIS.” Akaongeza Roy.
“Hayo ni maelezo marefu sana kwa wakati huu.”
Akabisha Malcom. “Hapana si marefu. Kwa jina tu, haisaidii chochote kama
hawajajua ni kwa nini tupo hapa!” Akamgeukia bibi Cote. “Hatukutaka kumuacha
Maya hapa peke yake. Tukaona..” “Roy na Malcom, ondokeni hapo haraka.” Akawa
anawasogelea kiongozi wao. “Yes Sir.” Wakaitika kwa pamoja na kuondoka kwa
haraka bila kubisha. “Hawa ni kina Cote, Malcom! Unapozungumza nao lazima
uhakikishe unatoa utambulisho wakueleweka ili wa..” “Mimi sijali. Ninachotaka
kuona Maya..” Wakawasikia wakiongea kwa kubishana huku wakiondoka.
Bosi wao akatingisha kichwa. “Samahanini sana kwa
hilo.” Kiongozi wao akaomba radhi na kumsogelea Maya. “Unajua Miss Cote leo
umefanya kazi kubwa sana ya CSIS? Itabidi kukuajiri ili utusaidie zaidi.” “Jake ndiye aliyempata Tunda?” Maya akauliza huku
akilia. “Ndiyo. Bila Jake pengine wote tungekuwa tumekwama mpaka sasa na bila
heshima yake kwako, angekata tamaa yakufikiria zaidi. Pengine mpaka sasa Mrs
Cote angekuwa amefungiwa chini ya basement. Lakini kwa ajili yako, amefikiria
zaidi na zaidi mpaka akafanikiwa ku..”
Akamueleza kwa kifupi. Angalau Maya akajisikia vizuri.
“Ila nasikitika kuwa kwa sasa yupo chini ya ulinzi.
Jake anatatizo la akili lakini anauwezo mkubwa sana kwenye mtandao na
kufikiria. Lazima apewe matibabu na awe chini ya uangalizi ili asitumie akili
yake kudhuru.” Maya akanyamaza na kujirudisha kwa kaka yake. “Hapa
tunapozungumza wamekwenda kumkamata mtu anayehusika na kumuuzia Vic aina hizo
za madawa. Na Vic mwenyewe yupo chini ya ulinzi. Haya, ile nyumba aliyokuwa
amefichwa Mrs Cote bado inafanyiwa uchunguzi ili kujulikana na kukamatwa
wahusika wote. Hayo yote ni wewe Miss Cote! Naomba ujipe faraja katika hayo.”
Yule afisa akaendelea kumfariji. Net naye akaendelea kumbembeleza dada yake na
kumbusu.
“Na mama?” Akauliza Net. “Naye amekwenda
kuchukuliwa. Lakini mpaka kupatikane ushahidi wa kutosha ili kumuhusishanisha
na tuhuma zote hizo. Hawezi kutuhumiwa kwa maneno tu. Na tokea asubuhi amekuwa
akichunguzwa upande wa fedha, simu zake na nyumbani. Hawakumkuta na kitu
chochote chakutilia mashaka.” “Ritha anaakili sana. Anatakiwa mtu mwenye uwezo
wakufikiri kumzidi yeye. Hivi hivi ataendelea kutusumbua tu.” Akaongeza bibi
Cote.
“Yupo kwenye uangalizi wetu wa masaa 24. Msiogope.
Na nina uhakika ulinzi kwenu wote utaongezwa mpaka watuhumiwa wote wakamatwe na
kesi ifungwe.” Wakasikia mlio wa helicopter. Wakajua usafiri wao umewasili. Kina
Cote na maafisa wawili wa CSIS wakaondoka hapo kuelekea hospitalini. Maya
alimuegemea bibi yake wakiwa njiani. “Am so proud of you, baby girl.” Bibi Cote
alimwambia na kumbusu pale kichwani alipokuwa amemuegemea. Maya akajivuta
karibu zaidi na kutulia akijifikiria jinsi anavyojisikia mchafu kuanzia akilini
mpaka mwilini.
Uzuri ile helicopter iliwashusha juu kabisa ya gorofa
la hapo hospitalini. Ilikuwa hospitali nyingine sio ile ya kwanza. Kwa hiyo
hawakusumbuliwa na waandishi wa habari. Bibi Cote hakutaka Tunda arudishwe tena
kwenye ile hospitali. Kwanza alishawachukia na kuwaona ni wazembe kupita kiasi.
Daktari kiongozi wa pale alikuwepo hapo juu
kuwapokea kina Cote na watu wa usalama. “Vipi Tunda?” Akauliza Net na bibi Cote
kwa pamoja mara tu walipoingia kwenye lift yakuwashusha chini. “Aliweza kuamka
walipokuwa wakimshusha hapa. Alikuwa akilalamikia kichwa kuwa kizito hawezi
hata kusogea.” “Unafikiri watakuwa wamempa dawa ya kumdhuru?” Net akauliza. “Ameshatolewa
damu, imepelekwa maabara ili kuchunguzwa. Ila tokea kule, daktari wa CSIS,
alishamuwekea maji ya kusafisha damu kama kuna sumu yeyote. Hiyo ilikuwa baada
ya kutoa hiyo damu ambayo imekimbizwa maabara. Baada ya muda mfupi sana
tutakuwa na majibu yote.” Akajieleza daktari.
Lift ilipofunguka tu, wakakuta na director wa CSIS,
Mr Mike Underson akiwasubiria pamoja na viongozi wengine. Bibi Cote
akamsogelea. “Asante haiwezi kutosha kufikisha shukurani zangu kwako Mike. Lakini
jua nakushukuru sana.” Akampa mkono. Akageukia na wale maafisa wengine. Akawapa
mkono kwa kuwashukuru kila mmoja wao.
Hiyo ilikuwa ni saa sita za usiku. Inamaana hao
watu tokea Tunda anaibiwa asubuhi mpaka hapo ni kweli hakuna aliyekuwa
amepumzika. Net naye akiwa amemkumbatia dada yake, akawasogelea. “Asanteni sana
kwa kunisaidia kumrudisha mke wangu na kuweza kumpa Cote mama.” Akawapa mkono
kila mmoja. Bado Maya alikuwa amemkumbatia kaka yake kwa mikono yote miwili na
kujilaza ubavuni kwake, amejificha nusu uso kama anayechungulia kidogo, kimya. Huku Net amempitishia mkono mmoja wa kushoto
begani akimpapasa taratibu.
Mr Underson au Mike kama alivyozoea kumwita bibi
Cote, akamsogelea bibi Cote. “Ulinzi utaongezeka hata kwenu. Kwa kuwa bado
hatujawakamata watu wote wahusika, na
Malinda bado yupo chumba cha upasuaji. Hawajui kama atatoka chumba cha upasuaji
akiwa hai, na hata akitoka hawajui itachukua muda gani kuja kuzungumza na
kutaja wahusika wote.” Mr Mike akaendelea.
“Ile nyumba waliyokuwa wamemficha Mrs Cote ipo
kwenye uchunguzi wa kina kuona kama tunaweza hata kupata alama za vidole ili
tujue mbali na Malinda na mdogo wake, nani mwengine alikuwepo ili ataje wahusika
wote. Ritha amegoma kabisa kukiri chochote.” Bibi Cote akatingisha kichwa kwa
masikitiko. “Kwa hiyo mpaka sasa hatujui wahusika wako wapi, wangapi, na kama
watafanya jaribio jingine lolote au ndio watakimbia kabisa! Hatujui. Sasa mpaka
hapo ni lazima kuongeza umakini kwenu wote. Nitaomba mtoe ushirikiano wenu kwa
maafisa watakao pangiwa kwenu.” Akasisitiza Mike kwa bibi Cote.
“Hilo halina shida kabisa.” Akajibu bibi Cote. “Lakini
Maya lazima aangaliwe na daktari.” Wote wakamgeukia yule afisa wa CSIS
waliyekuwa wamekuja naye kwa helicopter, aliyesema hivyo. “Mimi nipo sawa.”
Maya akakataa. “Ni utaratibu ambao lazima daktari aidhinishe kwa karatasi.
Ndipo tutajiridhisha kuwa upo sawa. Naamini haitachukua muda mrefu.” Yule afisa
akajieleza kwa heshima, maana alikuwa mbele ya kina Cote, na bosi wa mabosi
wake wote alikuwepo hapo.
“Yupo sahihi.” Mike kiongozi wao akamtetea. “Ni
utaratibu ambao lazima ukamilike. Miss Cote alikuwa kwenye mazingira hatarishi.
Alipigwa na kutishiwa. Lazima kujiridhisha kama yeye mwenyewe yupo sawa, ndani
na nje ya mwili. Hakuna kilichodhuriwa. Na kutaka kuzungumza naye kujua hata
hisia zake kama zipo sawa.” Maya akaanza kulia tena. “Nataka
na mimi kumuona Tunda kwanza.” Akaongea huku akilia akimwangalia bibi
yake. “Please Mike. Amemuhangaikia sana Tunda. Mwache akamuone kwanza, mimi
mwenyewe nitampeleka kuonana na daktari.” “Yeah, nafikiri anaweza kusubiri
kidogo.” Akimfikishia ujumbe yule afisa ambaye anahusika na Maya.
Daktari akawaongoza alipokuwa amelazwa Tunda. “Kabla
hatujaingia ndani kumuona Mrs Cote.” Daktari akawageukia wote. Wakasimama. “Mrs
Cote hana taarifa na chochote kilichotokea. Anaonekana muda wote alikuwa
amelala. Naomba tusimpe taarifa nyingi za kushtua kwa wakati mmoja.” “Inamaana
hajui kama alitekwa nyara!?” Akauliza bibi Cote kwa mshangao.
“Hana taarifa hata kama yupo hospitali nyingine.
Ametaka aletewe mtoto wake ili amnyonyeshe. Hilo tu. Na anaonekana katika hilo
hawezi kusubiri. Naomba mjaribu kumtuliza mpaka tujue kwa hakika majibu ya damu
yake.” Akasisitiza yule daktari. “Hiyo imeeleweka. Nitawaambia hata maswali
isiwe leo. Wampe muda kabisa.” Akaongeza Mike, director wa CSIS. “Ila kesho
kwenye saa nne asubuhi, tafadhali naomba atoe ushirikiano ili kusaidia vyombo
vya usalama kwa chochote kile.” “Lakini umesikia kuwa hakuwa na taarifa ya
kutekwa kwake nyara?” Net akakanusha.
“Mr Cote!” Mike akamgeukia Net vizuri. “Nimuhimu
sana yeye mwenyewe kujua na kutuambia kile ambacho anafahamu. Hata kama
nikidogo sana. Huwezi kujua kitasaidia vipi usalama wake na wenu. Bado kesi
yake haijafungwa. Watuhumiwa hawajakamatwa. Lazima kuweka kikomo katika hili
ili kujiridhisha.” Net akamwangalia bibi yake. “Ni sawa mpate kwanza ruhusa
kutoka kwa daktari atakaye kuwa akimtibu? Yeye ajiridhishe kwanza kama Tunda
yupo tayari kwa kupokea taarifa kama hizo. Tafadhali Mike. Mmefanya pakubwa
sana. Tusije tukawa tumemuokoa kutoka kwenye mikono ya watu wabaya, tukampoteza
kwa pressure kwenye mikono yenu.” Bibi Cote akaingilia. “Hiyo inaeleweka.
Tutawasiliana na uongozi wa hospitali kwanza kabla ya mahojiano.” “Nashukuru.”
Hapo wakakubaliana na kuingia.
Walimkuta Tunda amelala. “Mmempa tena dawa za
usingizi?” Bibi Cote akauliza. “Hapana. Hizo..” Tunda akafungua macho. “Nana!”
Akaita taratibu, wote wakamsogelea. Bibi Cote akamkumbatia. Net na Maya
wakabaki hawajui kama bado amewakasirikia au la. “Namtaka
mtoto wangu ili nimnyonyeshe. Hakuna anayenisikiliza!” Tunda akalalamika
na machozi yakitoka. Net akamsogelea. “Unajisikiaje?” “Nasikia
kichwa kizito. Cote yuko wapi?” Tunda akauliza huku akionekana anapata
shida kugeuka.
“Nisikilize kwa makini Tunda.” Bibi Cote akamshika
mkono na kuubusu. “Cote yupo salama kabisa. Aliruhusiwa kurudi nyumbani.” “Kwa nini walimruhusu bila mimi? Anakula nini huko?”
Tunda akaanza kulia tena. “Nitapiga simu, umuone akiwa amelala. Anaendelea
vizuri kabisa. Asubuhi sana nitamleta.” “Kwa nini
mimi nisiende nyumbani kumfuata? Sitaki kumuona kwa video, Net. Nataka
kumnyonyesha na nimshike mwanangu.” “Daktari ameomba usiku wa leo
upumzike kabisa. Kesho utakuwa naye. Na atarudi hapa mpaka siku utakayoruhusiwa.”
Tunda akafunga macho wakamuona analia.
“Yamebaki masaa machache sana papambazuke. Vumilia
kidogo tu.” Bibi Cote akambusu kichwani huku akimsihi. “Namtaka
mtoto wangu, Nana. Siwezi kulala bila mtoto wangu.” Tunda akaendelea
kunung’unika huku akilia taratibu. “Subiri nikuthibitishie kuwa mtoto yupo sawa
Tunda, ili na wewe utulie.” Chumba kilikuwa na watu zaidi ya watano, wakiwepo
hao viongozi wa CSIS. Wote walinyamaza. Tunda akaendelea kulia taratibu.
Net akapiga simu kwa Carter na kuambiwa
ampelekee simu huyo nesi aliyeachiwa mtoto nyumbani. Kwa bahati mbaya akamkuta
mtoto analia, na Carter alikuwa ameshaweka video. “Kwa
nini analia!?” Net akauliza. Bibi yake na Maya wakasogelea ile simu. “Ameamka muda sio mrefu. Nilikuwa nikimbadilisha diaper sasa
hivi, kisha nimpe maziwa.” Akajibu yule nesi. “Mnyanyue
hapo, mshike kidogo.” Net akaongeza. “Namtaka
mtoto wangu Net. Kamlete tu.” Tunda aliendelea kulia taratibu. “Au mimi mwenyewe niende tu.” Tunda akajaribu
kukaa ndipo yule daktari ikabidi amsogelee.
“Mrs Cote! Mrs Cote.” Akamwita taratibu. “Unakumbuka
umetoka kwenye operation masaa machache tu yamepita? Na unakumbuka ulilalamika
kichwa kinauma sana huwezi hata kukinyanyua?” “Sasa
hivi naweza.” Tunda akataka kukaa. Akamshika. “Japokuwa mimi si daktari,
ila nashauri akachukuliwe huyo mtoto, aletwe hapa karibu na mama yake, ili
kuweza kumtibu. Sidhani kama kunakuelewana tena bila huyo mtoto kuwepo hapa.
Huo ni ushauri wangu tu, kama mzazi.” Akaongea Mike kwa kujihami.
“Namtaka mtoto wangu, Nana.” Tunda akasisitiza. “Sisi
wote tupo hapa halafu mnamuacha na mtu mgeni kabisa hata hajawahi kumsikia! Sio
sawa kwa Cote. Atakuwa akitulilia sisi.” Tunda akalalamika. Asijue
hekaheka waliyopitia kina Cote mpaka muda huo. “Basi nakwenda kumchukua Tunda.
Naomba utulie ili nikirudi na mtoto, kichwa kiwe kimetulia. Sawa?” “Asante Net.” Akashukuru na kurudi kujilaza
vizuri. Bibi Cote akambusu tena. Net akaondoka. Maya alikuwa akifuta tu
machozi.
“Samahani Nana. Lakini namtaka mtoto wangu.
Umemsikia alivyokuwa akilia.” “Naelewa. Baada ya muda mfupi sana atakuwa hapa.
Naomba jaribu kufunga macho ulale kidogo.” Tunda akafunga macho. Maya akaanza
kumfuta machozi. Tunda akafungua macho wakabaki wakiangaliana. Maya akaanza
kulia. “Nisamehe Tunda. Usinikasirikie.”
Maya akaongea kwa uchungu. “Unajua ninavyokupenda.
Siwezi kukuumiza hata kidogo.” Tunda akafunga macho wakamuona machozi
yakimtoka. “Sikukusudia kukuumiza. Najua na wewe
unajua.” Maya akaendelea kumbembeleza. Akahisi anamshika mkono. Maya
akajilaza hapo kwa Tunda na kuzidi kulia. “Nisamehe.”
Maya akaendelea kulia huku amemugemea.
Tunda akapitisha ule mkono ambao hauna dripu
akamkumbatia. Asijue umbali aliokwenda huyo Maya, kumfanya awepo hapo. Chumba
kizima kimya. Wakatulia kidogo huku Maya amemkumbatia na yeye. Wakatulia kwa
muda.
“Niliingiwa na wasiwasi. Unajisikiaje?” Maya akamuongelesha
taratibu. “Kichwa tu ndio kipo kama nimebeba kitu. Sijui kwa nini!” Tunda
akajibu taratibu. “Kidonda je?” Maya akamuuliza tena. Tunda akafikiria kidogo. “Hakina
maumivu sana, mpaka nikohoe. Umemuona Cote?”
Wakacheka. “Ni mzuri kama wewe Maya! Nilikwambia lazima mnafanana.” Maya
akacheka tena. “Ana macho yangu.” Akajisifia Maya. “Sio ya Net?” Tunda
akamuuliza huku wakicheka. “Hapana. Hafanani na wewe wala Net.” “Maya!” “Kweli
Tunda. Muulize Nana.” Kidogo pakatulia hapo ndani ndipo wakaanza kumsalimia na
kumpa pole na hongera ndipo Tunda akajua kumbe pale ndani kulikuwa na watu
wengi! Hakuwa na wasiwasi wa kwa nini wamjalie vile, akaelewa kwa kuwa ni kina
Cote, lazima ni watu wakubwa wamefika hapo kumuona, asijue janga linaloendelea.
Baada ya
muda kidogo wakaaga wale maafisa, bibi Cote akasema anatoka kuwasindikiza.
Akamgeukia daktari. Akamkonyeza watoke naye nje. “Kwa nini kichwa chake kinakuwa
kizito!?” Akaumuuliza dokta mara tu walipotoka. “Inaonekana aina hizo za dawa
walizompa, ni kali sana kwake. Alikuwa akitumia kileo chochote?” “Sidhani hata
kama alishawahi kunywa pombe. Ni kama aliniambia hakuwahi kunywa pombe. Sina
uhakika sana.” Bibi Cote akamjibu yule dokta.
“Inaweza ikachangia. Na pia majibu ya damu yake,
yatatupa jibu ni aina gani ya madawa waliyokuwa wakimpa kumfanya alale kiasi
cha kupoteza fahamu kabisa.” “Hakuna jinsi yakuharakisha hayo majibu?” Akauliza
bibi Cote. “Tafadhali fuatilia. Sitaki mtoto aje, aanze kilio cha kutaka
kumnyonyesha mtoto wake, halafu mimi ndio niwe mtu wakumzuia! Hapana. Nisaidie
tujue kama ni sawa kunyonyesha.” Bibi Cote akasisitiza. Yule daktari akaondoka
kwenda kuweka msisitizo huko maabara.
Alipoagana na Mike pamoja na maafisa wengine bibi
Cote akarudi ndani. Ni kweli safari hii kulikuwa na ulinzi mkali. “Jaribu
kulala kidogo Tunda, ili kichwa kitulie.” Bibi Cote alishamsogelea na kumbusu.
Tunda akafunga macho. “Tutatoka kidogo, baada ya muda tutarudi.” “Sawa.” Tunda
akajibu bila kufungua macho. Hapo hapo akalala, Maya na bibi yake wakatoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilikuwa lazima Maya akapimwe ili kujiridhisha kuwa
yupo sawa. Bibi yake akamsindikiza. “Tunda amenisamehe.” Bibi yake akamwangalia
tu na kunyamaza. Hata yeye katika hilo walimtenda vibaya. “Usinikasirikie Nana! Vic alitutega.” Maya akaanza
kulia. “Hapana Maya. Mlipaswa kuniambia. Hata ingekuaje, mlipaswa kuniambia,
pengine hiki kilichotokea leo, kisingetokea. Tungejua hila ya Vic mapema sana.
Kuwa huwa anatumia dawa kuwalevya na kuwasahaulisha.” Bibi Cote akaendelea kwa
ukali kidogo.
“Leo umejiingiza hatarini kwa sababu ya kunyamazia
jambo lililoonekana ni kama lakupuuza, kumbe limebeba hila kumbwa sana!” “Nisamehe
Nana. Hata wewe ungemuona vile Net alivyoingiwa na hofu siku ile, usingethubutu
kusema.” Maya akawa kama anakumbuka. “Aliingiwa na hofu sana. Alishindwa kula
siku nzima, akawa kama mgonjwa.” “Ila itamgharimu sana. Atajieleza vipi kwa
Tunda akamuelewa?” “Kuwa alilevywa!” Maya akaongea kirahisi tu.
“Kwa nini asimwambie na Tunda amekuwa pale nyumbani
kwa miezi miwili sasa? Atamuamini vipi na yeye hakuwepo wakati Vic akikiri kama
alimlevya? Vic amemwambia maneno mazito sana ambayo hayaondoki kwa neno ‘Nisamehe’.”
Maya akanyamaza akifikiria.
“Utamfanya nini mama?” Baada ya muda Maya akauliza. “Nitahakikisha
anapata kinacho mstahili. Kwa kuwa nilimfuata Tanzania na kumuonya. Kuja
kumfuata huku Tunda, na kupanga mauaji yake kwa siri, hilo ni kosa ambalo
sitamsamehe. Hata akitumia akili vipi, safari hii nitahakikisha anapata kinacho
mstahili. Acha wewe utibiwe na Tunda atoke hapa.” “Utafanyaje?” Maya akauliza.
“Nguvu ile ile niliyotumia kumtafuta Tunda na
kufanya wakubwa wote wa nchi waweke akili zao kwenye kumsaka Tunda, ndivyo
nitakavyo hakikisha ninatumia nguvu hiyohiyo mpaka kumtia Ritha nguvuni. Yeye
na wote wanaohusika.” Akaapa bibi Cote. Maya akafurahia sana. Alimjua bibi yake
huwa haropoki. Kwa hiyo mama yake lazima akamatwe.
Kwa Mara ya kwanza Net na familia yake
yote.
N |
et aliingia na mtoto wao, Tunda akiwa amelala
kabisa. Kwa kuwa walimwambia wametoka kumpa dawa za maumivu ya kichwa, hakutaka
kumuamsha. Mtoto akatengenezewa kitanda palepale ndani ya kile chumba. Akalazwa
akiwa alishapewa maziwa ya kopo tu. Ameshiba. Net alisimama pale akiwaangalia
Tunda na Cote jinsi walivyolala, baada ya kuachwa peke yao, asiamini vile hata
mipango iliyopangwa kwa umakini sana na pesa nyingi jinsi inavyoweza kubadilika
na kuvurugika kabisa. Kufumba na kufumbua kutoka kwenye maisha yaliyojaa
heshima sana na kusifiwa, Net anajikuta yu uchi mitandaoni akifanya mapenzi nje
ya ndoa ya mwanamke waliyetoka kuvishana sifa mbele ya umati!
Net akamwangalia vile Tunda alivyolala. “Sidhani
kama Tunda atakuja kunielewa?” Akawaza Net. Akamgeukia mtoto wake. Cote
alikuwa amelala na yeye. Akakumbuka jinsi walivyokuwa wakimsubiria huyo mtoto
kwa hamu. Alivyokuwa akitangazwa mitandaoni na kwenye vyombo vya habari
akitabiriwa makubwa na mazito kama ujio wa Mkombozi kutoka mbinguni. Leo
amefika hakuna hata anayemzungumzia ila kashfa yake yeye baba mtu, akifanya
ngono na mwanamke ambaye si mama yake!
Net aliweka mikono kichwani na kuvuta pumzi.
Yalikuwa masaa machache hata hayakuzidi 50, lakini yalibadilisha na kutingisha
maisha yake vilivyo. Mpaka hapo hakuwa akijua kama ndoa ipo au la! Tunda
ataamua nini juu ya ndoa yao. Hakujua kama usiku ule alichukuliwa video ndio
maana akaamua kunyamazia swala la kulala na Vic. Alijua wale walioona Vic
akiamka pale kwao. Carter na Maya, ambao alishawaaminisha hakuna lililotokea
huko chumbani, watanyamaza wasiseme kwa mtu. Kwa hiyo hakutaka mtu mwingine
ajue, asijue kama Vic aliondoka na ushahidi mzito. Anakanusha vipi aliyosema
Vic, kama alishindwa kueleza kisa chenyewe kabla!
Net akaenda kukaa kwenye kochi pembeni ya kitanda
cha Tunda na kilipowekwa kitanda cha mtoto wao. Lile kochi lilikuwa na uwezo wa
kugeuka kitanda, na alijua wazi mashuka na mto wa ziada vipo hapohapo kwenye
kabati la pembeni, lakini alishindwa hata kulala. Akakumbuka maelezo ya Vic
kuhusu ushiriki wa mama yake. Akainama huku ameshika kichwa, Net hakujua kama
hatari ilikuja mpaka ndani ya nyumba yake wakati anamzungushia mkewe ulinzi
anaolipia kwa pesa nyingi sana nje. Hasira juu ya mama yake ikawaka tena ndani
yake. Akajiambia nilazima kuweka kikomo kati yake, familia yake na mama yake.
Wakaingia Maya na bibi yake kwa kunyata. “Vipi
Maya?” Net akauliza. “Kila kitu kipo sawa.” Akajibu Maya na kumsogelea. “Pole
Net. Naamini kila kitu kitakuwa sawa.” “Sijui Maya. Sidhani.” Maya akaenda
kukaa pembeni ya kaka yake. Bibi Cote akamsogelea Tunda. Akambusu kichwani. Kisha
akamsogelea Cote. Akamfunika vizuri. Akabaki amesimama na kumtizama yule mtoto
bila kuongeza neno. Wakakaa kimya kwa muda. Maya akambusu kaka yake shavuni. “Nakupenda
Net.” “Na mimi nakupenda na ninakushukuru kwa kunipigania mimi na Tunda.
Sitasahau hilo.” Maya akambusu na kumkumbatia.
Walikuwa wakinong’ona. “Nikwambie kitu?” Maya
akamuuliza huku akimnong’oneza. Net akamgeukia mdogo wake. “Sasa hivi unaweza
ukaona ulimwengu mzima umekugeukia wewe. Umeingiwa hofu. Kila mtu hakuelewi
umewezaje kufanya hivyo. Hata watu wako wa karibu watakuwa hawakuelewi. Kila
kitu kinakuwa kimegeuka. Zaidi maisha na mipango. Lakini unajua nini?” Net
akajifuta machozi huku akimsikiliza Maya.
“Kumbuka. It always gets better. Be strong, because
things will get better. It may be stormy now, but it never rains forever. Haitanyesha daima. Yoote yatapita na kukupa sura mpya ya
maisha. Hutakuwa sawa, lakini nakuhakikishia haya yote yamekupata ili kukufanya
uwe bora zaidi.” Net akamuegemea Maya. “Lini
umekuwa na hekima hivi!?” Net akamuuliza na kumbusu Maya. Wakacheka huku
wakilia. Bibi yao kimya. Macho kwa Cote. “Asante
Maya.” “Karibu. Sasa acha mimi nimrudishe Nana akapumzike. Kama kwetu imekuwa
ngumu hivi, najua Nana zaidi.” Maya akambusu na kusimama.
Net akabaki amekaa ameinama. Aliogopa hata
kumtizama bibi yake. Wawili hao hawakuzungumza tokea Net akiri ni kweli alilala
na Vic pale nyumbani kwao, tena akiwa ameoa! Bibi Cote akatoka bila hata
kumsemesha Net. Na Net naye hakutaka hata kumsemesha. Akaona anyamaze na
kumuacha kwanza. Pengine akienda kulala, kesho yake atakuwa sawa. Maya akambusu
tena kichwani vilevile alivyokuwa ameinama pale kwenye kochi. Akatoka na yeye.
Akaanza kusinzia. Akaona ajiegemeze kwenye kochi.
Baada ya kama masaa mawili mbele akiwa amepotelea usingizini akasikia Cote
akilalamika kwenye kitanda. Akaamka kwa haraka ili Tunda asiamke. Akamtoa
kitandani. Cote akazidi kulia, Tunda akaamka. “Mlete nimnyonyeshe.” “Nisubiri
nakuja sasa hivi.” Net akatoka kwa haraka na yule mtoto akilia. Akaenda kutafuta
wauguzi. Akamuacha Tunda haelewi.
Akakimbilia mapokezi. “Majibu ya mke wangu yakoje?
Anataka kunyonyesha.” “Daktari alikuja kuzungumza na wewe akakuta mmelala.
Lakini kila kitu kipo sawa. Amesema anaweza tu kunyonyesh..” Kabla hajamaliza,
Net akarudi haraka chumbani kwa mkewe.
“Kuna nini, kwa nini unakimbia na mwanangu?”
“Nilienda kuzungumza na daktari kama unaweza kunyonyesha.” Tunda akakunja uso
akampokea mtoto wake. Akamuona anatabasamu mara alipoona sura ya mtoto wake. Akambusu
mtoto wake zaidi ya mara moja. Nesi akaingia na kitu cha kumsafishia. “Lazima
kukusafisha kabla hujanyonyesha.” Tunda akakubali.
Net akamchukua mtoto tena. Akaanza kumbembeleza
wakati mama yake akishugulikiwa. Yule nesi akamsafisha Tunda vizuri kifuani.
Akambadilisha na nguo. Akanyanyua kitanda vizuri, akarudishiwa mtoto wake.
Akamuweka kwenye ziwa, Cote akaanza kuvuta. Yule nesi akacheka jinsi Cote
alivyonyamaza gafla na kudaka nyonyo ya mama yake. “Labda alikuwa na njaa.”
“Labda.” Tunda akajibu taratibu huku akimtizama. Nesi aliondoka na kuwaacha.
Net bado alikuwa amesimama. Tunda macho na yeye kwa
mtoto akimpapasa taratibu huku akimwangalia. “Unajisikiaje?” Net akauliza,
lakini Tunda hakujibu wala kumtizama. “Nakupenda Tunda. Nakupenda sana mke
wangu.” Net akasikika kwa sauti iliyojaa hofu. “Hata kama sasa hivi haileti
maana tena, lakini nataka ujue. Na sitaacha kukwambia hivyo.” Tunda akajifuta
machozi. “Ukiwa na Cote, usipokuwa na Cote, nakupenda wewe Tunda. Na
nilikuchagua wewe kabla hata Cote hajaja kwenye maisha yetu. Naomba usije
kulisahau hilo.” Tunda kimya. Net akaenda kukaa kwenye kochi.
Tunda akanyonyesha mpaka akasikia tena maziwa
yanasisimka, akajua yanaanza kutoka. “Naona
yanaanza kutoka!” Akaongea Tunda taratibu akisikika kuhamasika.
Akajiangalia ziwa jingine akaona yanaanza kuchuruzika. Akaanza kucheka huku
akilia. Net akasimama. “Kwani yalikuwa hayatoki!?” Net akauliza. Tunda
akatingisha kichwa kukataa huku anamwangalia mtoto wake wala sio Net.
Akaendelea kujifuta machozi.
Cote alianza kusinzia, Tunda akajitahidi kumwamsha
ili anyonye asilale na njaa. Akamuhamishia kwenye ziwa jingine. “Unafikiri
hajashiba?” Net akauliza. “Naona nyonyo linamliwaza tu ndio maana analala.
Lakini maziwa sio mengi. Nahisi kesho yataanza kutoka mengi.” Tunda akajibu
taratibu macho kwa mtoto wake. “Siamini kama na
mimi nimeshika mtoto wangu mwenyewe!” “Hongera Tunda.” Tunda akanyamaza
hakuitia pongezi ya Net. Net akabaki amesimama akimtizama na kutamani aongeze
neno jingine, ila akaona atulie.
Baada ya nusu saa nesi akarudi. “Bado ananyonya
tu!” “Angekuwa amemaliza, ila mimi ndio namwamsha kila wakati nataka aendelee
kuvuta, ashibe vizuri.” Wakacheka taratibu. “Nahisi atakuwa hajashiba! Maziwa
hayakuwa yakitoka mengi.” “Hata hivyo na yeye tumbo lake bado ni dogo. Kile
kinachotoka, kinamtosha kabisa. Usiwe na wasiwasi.” “Unafikiri hivyo?” Tunda
akauliza taratibu akiwa na wasiwasi. “Najua hivyo. Kwa sasa tumbo lake ni dogo
sana. Linapanuka kutokana na anavyokua. Kwa hiyo hata akipata kidogo tu,
inatosha.” “Ataweza kulala muda mrefu kwa chakula kidogo hivyo!?” Yule nesi
akatabasamu.
“Lazima ujue kila akijisaidia atataka abadilishwe.
Atalia. Amezaliwa bado hajui mchana na usiku. Bado anaji adjust na hali ya hewa
na mazingira, atalia. Ndio maana atakuwa akiamka kila baada yamuda mfupi.
Lakini si kwa kuwa anatatizo kubwa. Hapana. Anajizoeza mazingira mapya.”
“Oooh!” Tunda akaitika na kumwangalia mtoto wake.
“Ila hivyo unavyopenda kunyonyesha imetugusa
wauguzi wote hapa. Kila mtu anakusifia. Kina mama wengi siku hizi au huku
hawapendi kunyonyesha. Ukiendelea hivyo itamsaidia sana yeye. Maziwa hayo ya
mwanzo yanavirutubisho muhimu kwa mtoto. Nakupongeza.” Tunda akacheka wala
asielewe inakuaje usitake kumnyonyesha mtoto uliyemzaa mwenyewe! Jinsi yeye
alivyokuwa na hamu yakunyonyesha, kwanza alihisi Cote ni mvivu, hamtendei haki.
Akampima pressure. “Vipi, ikoje?” Akauliza Net. “Sio
mbaya. Kesho watamtoa catheter ili ajaribu kutembea.” “Nakuoga. Natamani kuoga
maji mengi. Nahisi nitajisikia vizuri zaidi.” Tunda akaongeza. “Basi
nitamwambia dokta. Akija kukuona mtazungumza.” “Asante sana.” Yule nesi akatoka
na kuwaacha wote macho kwa mtoto.
“Nilitamani Cote aje akute kuna amani kati yetu!”
Net akajiongelesha. Tunda hata hakujibu. “Naomba nikupokee.” Tunda kimya. “Unatakiwa
kupumzika Tunda. Mweke chini upumzike.” Kimya. Akamuona anaweka mto vizuri,
akamuweka mtoto wake kifuani, akajilaza akiwa amemkumbatia mtoto wake. Akafunga
macho. Net akaenda kumbusu kwenye kipanda uso. Akabaki anamwangalia. Tunda
hakufungua macho, lakini machozi yakaanza kutoka. Net akaweka uso wake pembeni
ya shavu lake. Akabaki amesimama lakini amejificha uso hapo kwenye shavu la
Tunda. Alipolala, akamtoa mtoto taratibu na kwenda kumlaza. Angalau na Net naye
akarudi kulala mpaka pakapambazuka.
Asubuhi baada ya kutekwa.
Saa moja
asubuhi nesi tena akaja na daktari. Wakampima Tunda. Kila kitu kikaonekana kipo
sawa. Wakamtoa catheter na kumruhusu kwenda kuoga.Alitoka kuoga, Maya na bibi
yake walikuwa pale wameleta supu. Baada ya salamu, Tunda akiwa amepoa, sio kama
zamani. Kila bibi Cote alipomuuliza kama anamaumivu mahali, alimwambia yupo
sawa. “Mbona kama kuna kitu unataka kuniambia lakini unasita?” Bibi Cote
akamuuliza. Tunda akafikiria kidogo. Akamwambia ni kweli kuna kitu anataka
kuwaambia.
“Ni nini?” Bibi Cote akamuuliza tu taratibu. “Daktari
alipita alfajiri. Amenipima na majibu ya maabara yote yanaonekana nipo mzima
kabisa.” Akatulia kidogo. Akainama. Na kujifuta machozi. Wote kimya. Maya, Net
na bibi yao walikuwa hapo. Wote wasiwasi wakitaka kujua nini kinafuata. “Ni
nini Tunda?” Bibi Cote akauliza tena. “Nilitaka kurudi nyumbani Tanzania.” Tunda
akaongea huku akilia. Kimya kilizuka cha gafla. Kama waliopigwa na ganzi.
“Naomba nirudi nyumbani tu.” Net akainama na
kushika magoti kama aliyepatwa na kizunguzungu cha gafla. Maya akaanza kulia
taratibu. “Nikuulize kitu Tunda?” Bibi Cote akamuuliza taratibu. “Unafikiri
kama isingekuwa Vic, au kabla ya kisa cha Vic, ungeondoka?” Tunda akanyamaza. “Niambie
ukweli Tunda.” “Naomba nikujibu hilo wakati
mwingine nikisharudi nyumbani na kupumzika. Ila naomba niwatoe wasiwasi.
Sihitaji chochote kutoka kwenu, zaidi ya nauli tu. Sitadai chochote na wala
sihitaji chochote.” “Unamaanisha unaachana na Net!?” Bibi Cote akauliza
kwa mshangao sana.
“Nilikuja huku kwa ajili ya Net,
Nana. Nahitaji muda wakujijenga upya. Kisha nitawatafuta. Nahitaji kusafisha
akili zangu pengine kujipanga upya na kumpa nafasi Net yakufikiria. Ni kweli
nilitoka jela nikiwa mjamzito. Asingeweza kuondoka bila kujua hatima ya mtoto
wake. Lakini nafikiri Net anahaki ya kuwa na furaha Nana! Tunda akaendelea taratibu tu huku akijifuta
machozi.
“Naomba niwahakikishie kwangu
hamtampoteza Cote. Mpo huru kuja kumuona muda na wakati wowote, na kama mkitaka
niwe namleta, nitamleta muda na wakati wowote ule.” “Na mimi Tunda?” Maya akauliza huku akilia. “Na taasisi
niliyokuachia? Unafikiri mimi nina akili kama za Vic? Unafikiri mimi
nilikurupuka? Wale wanawake na watoto wao wanakuhitaji Tunda. Ile taasisi ni
yako. Ukirudi Tanzania utaendeshaje ikiwa huku?” Tunda akazidi kulia sana. “Nilipokuchagua
si kwa sababu yakuambiwa na Net. Ni kwa kuwa najua unastahili. Usikubali Vic
akakukimbiza!” Bibi Cote akasogea karibu.
“Nilikwambia nini? Kila maamuzi unayofanya usifanye
kwa hisia. Kwa sasa hisia zako zimeumizwa. Utafanya maamuzi kutokana na hisia zilizoumia.
Wakati wote, unaposema nakwenda nyumbani iwe ni pale nilipo mimi. Unanielewa
Tunda?” Bibi Cote akaweka msisitizo. “Ile nyumba ni kubwa sana. Tutarudi wote
nyumbani. Utapata sehemu yako nzuri na yakutosha kupumzika na kulea mtoto wako
vizuri na kwa utulivu. Mwachie uhuru wake Net. Akafanye kile anachokitaka na
yeyote. Hata mimi sijali tena. Mwache achague yeyote anayemtaka. Hata mimi
nimejiapia sitahangaika naye tena.” Net akajua ule ujumbe alikuwa akipewa yeye
si Tunda.
“Usiwahi kufikiria kuondoka Tunda. Unamajukumu
mengi sana mbali na kuwa mke wa Net. Na nilikwambia, kuanzia sasa, kila maamuzi
unayochukua, fanya ukimfikiria mjukuu na watoto wa Cote. Unanielewa?” Tunda
akatingisha kichwa kukubali huku akifuta machozi. Akafurahi kuona bibi Cote yupo
upande wake. “Niambie tu. Nitawaambia wakuhamishie kila kitu chako kutoka
kwenye kile chumba cha Net, uwe na kwako palepale ndani. Lakini si kurudi
Tanzania. Sawa?” Tunda akatingisha tena kichwa kukubali.
“Naomba usimwamini Vic, Tunda. Kwanza ni mgonjwa wa
akili.” Tunda hakuwa ameelewa akajua ni msemo tu. Maya akajua. “No Tunda.
Namaanisha ni mgonjwa kabisa wa akili. Unakumbuka habari za Andy?” Tunda
akatingisha kichwa kukubali. “Sasa kumbe Andy ni Jake. Jana ndio nimegundua
kila kitu.” “Jana!?” Tunda akawa hajaelewa. “Kuna kitu tunataka kukwambia
lakini naomba usishtuke.” Bibi Cote akaingilia.
Net akamuwekea supu akiwa mwekundu usoni kama
aliyekuwa akikaribia kulia. Akamvutia kijimeza cha wagonjwa kirefu cha
kitandani. “Asante.” Akashukuru na kuanza kunywa. “Umependa?” Net akauliza. “Ni
nzuri.” “Gino amekutengenezea.” Tunda akanywa tena.
“Nana ulitaka kuniambia nini chakunitahadharisha
nisiogope?” “Labda nikuulize wewe unajua umejifungua lini?” Tunda akakunja uso
kama anayefikiria. “Jana jioni au usiku nilipoanguka nyumbani na kupoteza
fahamu! Daktari ndivyo alivyoniambia alipopita janaaa...” Akatulia kidogo.
“Hapana. Jana usiku ndio mlikuwepo hapa, nikaomba
mkaniletee mtoto wangu.” Akasita na kuweka bakuli chini. “Nahisi kama
nimechanganyikiwa. Kwani mbona kama nina usiku miwili ila asubuhi moja ambayo
ndio hii! Maana..” Akatulia. “Alfajiri
ile ingine waliniletea mtoto wangu nikamnyonyesha. Alikuwa hospitalin... Halafu
hii ya leo..” Akatulia. “Mbona nahisi kuchanganyikiwa! Au nilipoteza fahamu?” Akawaangalia kwa zamu. Net akamtizama bibi
yake, akajua ndio anamwachia yeye.
“Nataka unisikilize kwa makini sana na usiogope.”
Tunda akaanza kuingiwa na wasiwasi. “Unakumbuka nilikuahidi nini uliponiambia
juu ya Ritha na watu kama Vic?” “Uliniambia nisiogope kwa kuwa wewe umesema
nitakuwa salama na hawawezi kunigusa, na wakinigusa watapambana na wewe. Kitu
kama hicho.” Tunda akajaribu kukumbuka huku akiwa na wasiwasi kidogo. “Sasa
walijaribu.” Tunda akakunja uso.
“Jana asubuhi tulipokuja sisi. Mimi na Maya, tulimkuta
Net akikusubiri.” Wakamuelezea mwanzo mpaka hapo walipokuwa. Tunda alibaki
ametoa macho na machozi. “Nitafanyaje na Ritha,
Nana? Hawezi kutulia mpaka ahakikishe ameniangamiza. Sina ninapoweza kumkwepa!”
“Huhitaji kufanya chochote. Nakuahidi mwisho wake umefika Tunda. Naomba
usiogope.” “Naachaje kuogopa Net? Kila ninapokwenda
anajitahidi kutengeneza au kugeuza na kutafuta watu wa karibu yangu ili
waniangamize. Mwisho wa hii ni nini?”
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
v
Ritha
bado amebaki amesimama. Na huko tena nchini Canada ametengeneza jeshi la
kizungu. Wote wamempisha mtaani, maisha yake yakiendelea. Aliopanga nao mipango
wao wamegonga mwamba, lakini si Ritha mwenyewe.
- Vic mtoto wa milionea wa nchi amemudu
kumfikisha jela, kama mke wa Gabriel.
- Malinda yu mahututi huku mdogo wake
fundi mitambo/kompyuta amekwenda kulazwa chumba cha maiti kama Gabriel na mama
yake.
v
Tunda
naye anataka kukimbia nchi ampishe tena kama alivyofanikiwa kumpisha nchini
Tanzania na kumuweka jela.
Nini hatima ya kichwa nzuri kwa
mipngo, Ritha?
Endelea kufuatilia.....
0 comments: