NILIPOTEA! PART 8 – SEHEMU YA B
Bibi Cote asingeruhusu kuondoka Tunda na mtoto
wake, alijua ni kweli familia itasambaratika na kinachozungumzwa mitandaoni
kitatimia. Kuwa ukoo wa Cote ndio umekufa na Mzee Cote mwenyewe. Na asingethubutu
kumpa ushindi Ritha. Safari hii alitaka kumrudi Ritha vilivyo. “Nisikilize
Tunda. Mwisho wa Ritha upo karibu sana. Usiogope.” Bibi Cote akajaribu
kumtuliza. Tunda akabakia akiwaza.
“Kwani
hukumbuki chochote?” Maya akamuuliza. “Hapan..” Tunda akanyamaza kidogo. “Umekumbuka
nini?” Maya akaendelea kumuhoji. “Sina uhakika sasa kama ni ndoto, au kama ni
hospitali ile nyingine au la. Lakini nakumbuka kuamka na kumuomba nesi
aliyekuwepo karibu na kijana mmoja hivi, waniletee mtoto nimnyonyeshe. Yule
kijana, alikuwa mdogo kwa yule nesi, akamwambia watakuwa wamenipunguzia dozi,
waniongeze. Nikaendelea kuwadai mtoto, nikiwa bado nina usingizi mzito hata
siwezi kuamka vizuri. Ni kama yule nesi akaongeza kitu kwenye ile dripu,
nikapotelea usingizini.” Tunda akazidi kuingiwa hofu.
“Labda nirudi kwanza nyumbani
Tanzania mpaka watakapo kamatwa wote.” Tunda
akamwangalia bibi Cote. “Kukimbia ni kuwatangazia kushindwa na watakufuata
popote uendako. Lazima kusimama imara. Huwezi kumkimbia adui Tunda. Lazima
umtizame usoni na kupambana naye.” “Lakini hii ni
mara ya pili Nana! Ritha anafanikiwa kunikamata hata katikati ya ulinzi mkali!
Anaakili sana. Naomba tusimpe nafasi ya tatu. Naombeni mniruhusu niondoke kwa
muda.” Tunda aliendelea kuwasihi.
“Nilikuahidi na nimetimiza Tunda. Naomba unipe
nafasi yakuweka kikomo kwenye hili. Ukiondoka tu utakuwa umenivunja nguvu
kabisa. Nitashindwa kupambana naye.” Bibi Cote akamsihi kwa kumbembeleza. Hata
yeye alijua anahaki yakuogopa. “Sio ndio utakuwa huru kwa kuwa nitakuwa mbali?”
Tunda akauliza huku akilia. “Siwezi kuwa na amani ukiwa mbali na mimi. Nitakuwa
sijui nani anakuzunguka wewe na Cote huko! Wala nitakuwa sijui wewe na mtoto
mnaendeleaje! Siwezi kufikiria tukiwa tumetawanyika. Nahitaji kuwaona wote
sehemu moja ili tuweze kufanya kitu kimoja kwa pamoja ndipo tutaweza.” Bibi
Cote akasisitiza.
“Halafu nikwambie ukweli tu Tunda. Akili na mipango
ya hata Vic ndivyo ilivyo. Alikuwa akitumia marafiki zangu wa karibu sana ili
kuniangamiza na ndio maana wakati wote amekuwa akifanikiwa. Na amefanya kwako
hivyohivyo. Amekuja kwako kwa makusudi na kuhakikisha anakutenga na watu wote
ambao wameonyesha wapo upande wako.” Maya akaona na yeye aongee.
“Upendo na mapokezi uliyoyapata kutoka kwenye
familia yetu, hakuna mtu aliyewahi kupokea kwa kiwango chako. Sisi wote
tumefuatilia mazungumzo yako na Vic.” Tunda akashangaa. “Mlifuatilia wapi?”
“Yule msichana aliyekuwa naye, Renee. Alichukua video kuanzia mwanzo wanaingia
mpaka mwisho. Kama ukifikiria kwa makini, na ukakumbuka kila neno, alianza kwa
kukugombanisha na kila mtu ambaye ulimsifia siku ya tafrija ya kukaribishwa kwako
hapa nchini au kwenye familia yetu.” Tunda akawa kama anavuta kumbukumbu.
“Wewe kumbuka tu. Alianza kwa Nana, akaja kwangu,
na wafanyakazi wote wa pale ndani ambao uliwataja siku ile kuwa walikupokea na
wanaishi vizuri na wewe.” Tunda akatulia. “Usifikiri alifanya kwa bahati mbaya
kukwambia kama alilala pale nyumbani na mimi
pamoja na Carter tulijua! Anajua ukaribu wangu na wewe, pamoja na Carter
au wafanyakazi wote wa pale ndani. Na anajua wewe utafikiria kama Carter
anajua, inamaana na Ms Emily anajua pengine hata Gino. Kwa hiyo utatuchukia
wote. Utajiona upo peke yako na wale watu wote pale wanaokuonyesha upendo, ni
wanafiki. Akakusudia uwachukie kabisa.” Maya akaendelea kwa makini.
Hakuna aliyemuona Maya huyu. Alijawa hekima na
mtulivu. Alishamiri kwenye hiyo dhoruba bila shida. Yeye ndio akaonekana jasiri
kuliko wote. Alijawa hekima, kama sio yeye Maya waliyekuwa wakimdharau tu. “Hotuba
ya siku ukikaribishwa nyumbani na yote tuliyoongea kwa upendo, yanazungumziwa
mpaka leo kwenye mitandao.” Maya akaendelea. “Na ili kuhakikisha kama yeye
alivyoshindwa kufikishwa kanisani na Net, alihakikisha anamchafua kabisa Net,
kama alivyokuwa akinifanyia mimi. Kwa kusambaza video na picha za ngono
mtandaoni ili watu wote wawe kinyume na Net, hata wewe ushindwe kabisa hata
kumtizama Net. Na mshindwe kufunga ndoa.” “Hata mimi alikiri kwangu.” Net
akaongeza.
“Vic ni kichaa anayesaidiwa mipango yake na watu
wenye akili. Anajua anachokifanya.” “Ukisema ni kichaa unamaanisha ni kichaa
kweli?” Tunda akauliza. “Namaanisha ni kichaa kweli. Anatatizo la akili kabisa.
Wazazi wake walificha. Akawa anatibiwa mbali na Norfolk. Ndio huko huko kwenye
matibabu akakutana na kichaa mwenzie Jake ambaye akampa jina la Andy. Akamlipa
ili aje kwangu aniangamize.”
“Ni kweli Vic anampenda sana Net, na hawezi
kuruhusu mtu yeyote kusimama kati yake na Net. Amekiri ndio maana alikuwa
akihangaika kuniangamiza hata mimi kwa kuwa tokea tupo wadogo, nilikuwa namtaka
Net, wakati na yeye alitaka muda naye. Unakumbuka Net?” Maya akamuuliza. “Ndivyo
alivyoniambia na mimi jana.” Net akathibitisha kwa unyonge. “Mimi nilikuwa
nikiwasikiliza kila kitu wakati amenifungia chumbani.” “Vic ni mwendawazimu.” “Hapana
Tunda. Nikichaa kabisa. Nafikiri ndio maana hata wazazi wake wameshindwa kumwajiri
hata kwenye kampuni yao. Sisi tunasema hataki kufanya kazi, kumbe hana uwezo.”
Akaongeza bibi Cote.
“Kabisa Nana. Mama yake alikiri yeye mwenyewe
wakati polisi walipotuvamia ndani. Kuwa siku hiyo alikuwa na mambo mengi,
akasahau kunywa dawa, lakini hana uwezo wa kudhuru mtu.” “Lakini Net, nao ni
waongo. Akiwa amekunywa dawa na akiwa hajanywa dawa, Vic ni hatarishi.
Kumbukeni mabaya yote aliyokuwa akinitendea! Halafu usiku uleule alikiri kwangu
mimi na Jake kuwa ametoka kuua na alimpiga Jake risasi mbele yangu!” Maya
akaongeza na kuzidi kumshangaza na kumuogopesha Tunda.
“Kwa hakika, Vic hawezi kuwasumbua tena. Labda mtu
amwite mwenyewe na ajifungie naye mwenyewe.” Bibi Cote akaongeza. Net akajua
anaambiwa yeye tu maana Vic yupo jela na hawezi kuachiliwa siku za karibuni. “Aliniwekea
madawa kwenye juisi Nana! Sikujua hata nini kilitokea usiku ule. Yaani na mimi
ndio nilisikia kama wewe Nana.” Bibi Cote hata hakumjibu wala kumwangalia Net.
“Na kwa vile alivyochukuliwa na CSIS, watampa
kifungo cha hukohuko hospitalini. Hatatoka leo wala kesho.” Akaongeza bibi Cote
bila hata kumjibu Net. Net akajua bado amemkasirikia. Akanyamaza na kurudi
kukaa kwenye kochi akainama. “Kwa hiyo Tunda, tafadhali usifikirie kwenda
popote, ila kurudi nyumbani na kulea mtoto wako bila wasiwasi.” “Tena wakikuona
umetulia ndio utazidi kuwatoa nguvu.” Maya akaongeza kwa bibi yake. Tunda
akabaki kimya.
Malcom na Roy tena!
Wakasikia watu wanabishana nje ya dirisha kwa sauti
ya chini. “Subiri kwanza Roy. Tufikirie kwa upya.” “Acha woga Malcom! Sisi
tuingie hapo kama maafisa wa CSIS. Tunafuatilia hali ya tuliyemuokoa. Na
usianze kumtaja jina. Sema Miss Cote.” “Au turudi baadaye? Bibi yake
anafahamiana na wakubwa wote pale. Akipiga simu kuulizia kama tupo hapa kiofisi
au?” “Sasa wewe usiongee sana. Tukifika hapo tuonyeshe vitambulisho vya kazi na
tuwe kikazi.” “Wewe ndio unaongea sana Roy. Jitahidi kuwa mchache wa maneno.”
“Sawa twende.” Wakatulia.
“Subiri kwanza Roy. Nahisi kama safari hii
tukikamatwa hapa, habari zikafika ofisini, ndio tutarudishwa kwenye benchi
kabisa au tukapewa kazi za stoo! Hatutapata kazi za nje tena.” “Kwa muda tu.
Hawawezi kutotuona kwenye field.” Wakacheka kidogo. “Twende?” Wakasikia mmoja anamuuliza mwenzake. “Sasa
kama kina nani? Hawa watu hawadanganyiki.” Wakasikia ukimya kidogo.
“Kumbuka. Maneno machache. Halafu tuwakumbushe kuwa
sisi ndio tuliomuokoa Maya kwenye..” “Sasa hapo unaharibu Malcom. Nimekwambia
Miss Cote.” Roy akamrekebisha. “Yeah.
Miss Cote.” “Usisahau Malcom! Tuwaambie sisi ndio tulimuokoa ili asiuawe na
Vic.” “No way. Unataka kumuua kwa mshtuko! Usiseme hivyo. Leo iwe smooth.” Wote
kule ndani walikuwa wakiwasikiliza. Maya akainama huku akicheka
“Come on Malcom! Lazima tuonyeshe umuhimu wetu!
Hata hivyo haitakuwa tunadanganya. Ni kweli bila sisi angeuawa.” “Njoo kwanza
Roy.” Wakasogea tena. “Kumbuka lengo ni kumuona Maya, sio kumkumbushia
machungu.” “Miss Cote.” Wakamsikia Roy akimsahihisha tena. “Yeah Miss Cote.”
Malcom akakubali. “Au tuwaambie tunamtaka atoke nje kwa mahojiano?” “Oooh NOO
Malcom! Watampigia director hapohapo. Kumbuka Mr Underson ni best ya bibi yake.
Hapo ndipo tutafukuzwa kazi bila onyo jingine.” Wakawasikia wakicheka taratibu.
“Au kwa nini tusiseme kwa kuwa sisi ndio tulikuwa
tukifanya kazi na Maya jana yakumtafuta Mrs Cote,” “Miss Cote Malcom. Please
usijisahau!” “Nikiingia pale nitasema Miss Cote sio Maya. Ni kwako tu.” “Okay.”
Roy akakubali. “Sasa tuseme sisi ni maafisa waungwana. Tunataka kujua hali ya
Maya.” “Miss Cote.” Roy akamrekebisha tena. “Sawa, Miss Cote. Kwa kuwa jana
alipatwa na mshtuko.” “Ripoti ya daktari imesema hajapatwa na mshtuko.
Usianzishe kitu kingine Malcom. Tutajiingiza kwenye matatizo.”
“Mimi naona tuondoke tu. Hii kitu imeshakuwa
ngumu.” “Usikate tamaa Malcom. Tumehangaika kote huko mpaka kufika hapa! Lazima
tuingie.” “Sio kukata tamaa. Naona twende tukajipange tena kwa upya. Halafu
tukaanzie kwa bosi tuombe kazi ya kufuatilia chochote kinachohusiana na kina
Cote. Halafu ndio tumtafute Maya.” “Miss Cote.” Roy akamkumbusha tena. “Gosh
Roy!” Malcom akalalamika. “Fine. Mimi nakukumbusha kuwa kikazi.” “I am.” Roy
akaanza kumcheka.
“Huu ni muda wakufikiria Roy sio kubezana.” “Basi
nimepata wazo. Tuingie na kuonyesha vitambulisho, halafu tuombe kazi
yakujitolea ya kumlinda Miss Cote, mpaka watuhumiwa wote wakamatwe.” “Sasa hivi
umeanza kuongea.” Wakawasikia wakigonga. “Tuingie tuseme sisi ndio tulifanya
kazi na Maya.” “Miss Cote.” Roy akamsahihisha tena. “Yeah, nakuahidi nikifika
kule nitakumbuka. Sitasema Maya.” “Usisahau kuwatizama machoni ili wajue
unajiamini.” “Okay. Nitawaambia kutokana na mazingira hatarishi aliyokuwa nayo
Maya jana.” “Miss..” “Najua. Acha kuniingilia Roy!” Wakamsikia Malcom amemkatisha
kabla hajamsahihisha tena kusema Miss Cote.
Kule ndani walikuwa wanakaribia kucheka. “Tuingie.
Tujitambulishe majina na kazi zetu.” “Hudhani kama inabidi kuwaambia kuwa
katika darasa letu la CSIS sisi ndio tulikuwa bora?” “Hapo tutawaboa. Matajiri
hawana muda mrefu wakusikiliza ujinga Roy. Utaniharibia.” “Kwa nini hufikirii
kama tunaweza kupata sifa? Ms Cote akitupenda, akampigia simu director, sisi
tutakuwa watu wengine kabisa Malcom.” “Unaanza kupotea lengo Roy! Upo hapa
kunisindikiza kwa Maya.” “Kwani hatuwezi kupata vyote?” “Nilishakuonya Roy.
Naomba usihame kwenye lengo.” “Sawa.” Wakatulia.
“Kwahiyo tujitambulishe. Tuwaambie sisi ndio tulihakikisha
Maya yupo salama. Na kwa kuwa hatujakamata watu wote, sisi tunajitolea
kumlinda.” “Na kazini?” “Acha kuweka vipingamizi Roy bwana! Kila mtu sasa hivi
macho yapo kwa kina Cote. Kule kazini tutawaambia tunafuatilia ushahidi wa kina
Cote. Na kwa kuwa jana tulimsafishia bosi kwa director bado anakumbuka kutulipa
fadhila. Au unasemaje.” “Usisahau ni Miss Cote sio Maya.” Wote mle ndani
wakatamani sasa waingie ili wawaone na kuwasikiliza.
“Oooh no!” “Nini?” “Usigeuke. Lakini director
Underson anakuja! Ametoka kwenye lift, amepokelewa na daktari. Waanaongea pale.
Lazima yuko hapa kwa ajili ya kina Cote.Tuondoke, na usigeuke.” “Inama tuondoke
kimya kimya?” “Hamna hata haja yakukimbia. Wala hatufahamu. Wewe anza kuondoka
kwa kujiamini. Ukianza kujihami hapo ndio utaharibu.” Wakasikia kimya. Wakajua
wameondoka.
Bibi Cote akatingisha kichwa. Ikabidi Tunda tu
acheke na kumtizama Maya. Kaka yake naye akamwangalia Maya. “Unawafahamu?” Maya
akacheka. “Nilikuwa nao jana siku nzima. Wao ndio walinihoji na kweli ndio walioniokoa
pale kwa Jake.”
Mlango ukagongwa alikuwa kweli director wa CSIS
ambaye ni rafiki wa bibi Cote. Mike Underson. Baba mtumzima sana. Na kweli
alionekana ameshiba mamlaka na pesa. “Naona leo kuna matumaini!” Akawatania
kutokana na ile hali aliyoikuta pale. Wote walikuwa kwenye hali yakucheka kwa
mazungumzo ya Roy na Malcom. Japokuwa hawakuwaona, lakini walishapata habari
zao.
“Ninaendelea vizuri. Asanteni kwa kunisaidia jana
na kunirudisha kwa mtoto wangu.” Tunda akaongea kwa heshima. “Umeshaambiwa!?”
Akauliza kwa mshangao, kwani Tunda hakuonyesha hata kuchanganyikiwa au hali ya
hofu. Mazungumzo ya Malcom na Roy wote yaliwatoa kwenye ile hali ya tukio la
jana yake. “Nimesimuliwa, lakini sikuwa hata na taarifa kwa kile kilichokuwa
kikiendelea. Sikujua ni wakati gani nimetolewa hospitalini na wakati gani
nimerudishwa. Hata sikuwa na taarifa kama nipo hospitali nyingine. Ndio maana
jana nilikuwa nashangaa kwa nini hawataki kunipa mtoto wangu!” “Pole sana.”
Yule director akampa pole.
“Lakini mimi naona ni afadhali hivyo kuliko ungejua
kinachoendelea.” Akaongeza bibi Cote. “Unafikiri
hivyo Nana?” “Kabisa Tunda. Hebu fikiria ile hofu yakujua wamekuteka!” “Na
pengine ungeongea na kuibua kitu kingine, wakakudhuru! Au wakahofia kuwa
umewaona sura zao, wakahofia kuja kuwataja baadaye. Pia wasingekuacha hai.”
Yule director akaongeza. Tunda akabaki akifikiria.
“Anyway, nilikuja kuangalia mnaendeleaje na
kuwahakikishia kila jicho na sikio la maafisa wa usalama lipo kwenye kesi yenu.
Hakuna kitakacho endelea mpaka tumkamate yule aliyewaua kina Malinda na...”
“Malinda alikufa!?” Akashtuka sana bibi Cote. “Yeah! Kumbe sikukwambia?”
“Hapana. Lini?” “Hakutoka chumba cha upasuaji. Alishapoteza damu nyingi sana
kabla yakufikisha hospitalini na ile risasi alipigwa kusudi kuuwawa. Karibu
kabisa na moyo. Hakuna jinsi angepona.” Bibi Cote akaishiwa nguvu. Alitegemea
Malinda ndio aje awe msaada, kwa kuja kumtaja Ritha na kutoa ushahidi hata
kidogo, kama upo.
“Wala usiwe na wasiwasi. Kifo cha Malinda
hakijabadilisha chochote. Tupo pazuri tu.”
Mike akamtuliza bibi Cote. “Kwani mmeshamjua ni nani aliyewaua Malinda
na mdogo wake?” “Kabisa. Na tunajua tatizo ni pesa. Watakuwa walikuwa
wakisubiria pesa kutoka kwa mtu. Tunahisi ndio maana aliua wenzake, ili amtumie
Mrs Cote kama kitega uchumi kwa huyo anayewatuma kumteka. Ili pesa zote ziingie
kwake. Tunajua alipo na tunamtega ili kuona anakutana na nani ili tuwakamate
wote. Msiwe na wasiwasi kabisa.”
Akamgeukia Tunda.“Umesikia Mrs Cote? Usiogope hata
kidogo. Kesi yako inafuatiliwa na wataalamu. Na tunamshukuru Miss Cote kwa
kuturahisishia. Ndani ya masaa 24, tuliweza kukurudisha kwa familia yako. Ni
ushindi mkubwa na imewanyenyekeza wengi. Hata kama kuna aliyefikiria kuja
kurudia, nina uhakika hawatafanya hivyo tena.” Tunda akatingisha kichwa
kukubali.
Akamgeukia Maya. “Kibinafsi na kama
kiongozi wa CSIS naomba kukupongeza na kukushukuru. Umefanya kitendo cha
kijasiri sana. Na umekipa sifa chombo cha usalama, CSIS. Ndani ya masaa 24,
tumeweza kufanya mambo makubwa sana. Ikiwepo kukamata watu wa yale madawa
hatarishi. Tumeweza kumuhoji Vic mmpaka tumejua alikokuwa akiyatoa na aliyemua,
na wapi aliacha mwili wake.” “Wapi na ni nani?” Maya akauliza kwa haraka.
“Mmoja wa kijana aliyekuwa akimtumia kumtafutia
hayo madawa. Alimuua ili asije kumtaja. Alimwita kule eneo la bandarini,
akampiga risasi na kumficha huko kwenye moja ya boti ambazo ni mbovu.
Inaonekana ndiko walikokuwa wakikutania huko wakati wakipeana hayo madawa.”
“Mungu wangu!” Wote wakahamaki.
“Haya, tumemkamata Jake. Tumempata Mrs Cote,
tumeweza kupata maiti ya Malinda na mdogo wake ambazo zilikuwa zimeachwa kule
chini kwenye nyumba ya wazazi wao. Na kwa uchunguzi wa alama za vidole
tulizopata kwenye ile nyumba waliyokuwa wamemficha Mrs Cote. Ndio tumejua
muuaji ni nani, na ndio huyo anafuatiliwa ili kuweza kumkamata na aliyewaagiza.
Kwa hiyo hayo yooote, ni kwa sababu yako wewe Miss Cote na ujasiri wako.”
Akamsogelea na kumpa mkono.
“Na mimi naomba nikushukuru sana Mike.
Na uniombee msamaha kwa Nancy kwa kukutoa nyumbani kuanzia asubuhi ya jana
mkiwa mmelala mpaka kukurudisha usiku kama ule!” Bibi Cote akashukuru. Mike
akacheka. “Na yeye ametuma salamu. Atakuja kukuona nyumbani mkitulia.” “Ni
kweli nashukuru kutoka moyoni Mike. Mmekuwa msaada mkubwa sana kwa familia
yangu. Umeona yule mtoto pale?” Mike akacheka
na kumsogelea Cote kwenye kitanda chake. Alikuwa amelala.
“Usiku wa jana amerudi kunyonya kwa mama yake
sababu ya watu ambao hawajalala wala kupumzika siku nzima ya jana, kuhakikisha
Tunda anarudi nyumbani. Naomba uwashukuru kwa niaba ya familia yangu. Asante,
asante sanaaa.” Bibi Cote alisikika kama hajatosheka kutoa shukurani zake kwa
chombo hicho cha usalama. “Utatushukuru vizuri tutakapomaliza hili. Acha nirudi
ofisini nijue kinachoendelea. Ila naomba ushirikiano kwa maafisa watakaotumwa
kuzungumza na Mrs Cote.” “Bila shida.” Mike akawapa mkono na kutoka na bibi
Cote. Kukawa kimya.
“Nikupashie hiyo supu moto?” Akavunja ukimya Net.
Tunda akaangalia ile supu na kunyamaza kimya. Akabaki amejiinamia. Net
akasimama na kuchukua ile bakuli. Akagairi kupasha moto. Akamwaga na kuweka
supu nyingine. Tunda akaanza kunywa tena.
Bibi Cote akarudi. “Hao maafisa wapo nje. Upo
tayari kuzungumza nao?” “Naomba amalize kunywa hiyo supu kwanza. Tutawaruhusu.”
Akajibu Net. Kimya. Tunda akaendelea kula mpaka akamaliza ndipo wakaruhusiwa
wale maafisa wawili.
Mahojiano ya Tunda na Maafisa wa CSIS.
“Unaendeleaje?” “Vizuri tu.” Tunda akajibu. “Hatutachukua
muda mrefu. Tutakuuliza maswali machache tu. Na kama ukiona haupo tayari
kujibu, basi.” “Nitajitahidi.” Akajibu Tunda. “Tutaanzia siku ya kwanza kabla
hujaletwa hospitalini. Unakumbuka kitu chochote?” Tunda akavuta pumzi.
Akajaribu kukumbuka.
“Nilikwenda kwa matembezi, niliporudi ndipo Vic na
rafiki yake, walipoingia nakuomba kuzungumza na mimi. Katikati ya mazungumzo
ndipo nilipopoteza fahamu.” “Walikufanyia kitu chochote chakukufanyia vurugu?” Akamuhoji. “Hapana. Sikumbuki hata kama
walinigusa. Nakumbuka walikaa upande wa pili wa ile sebule. Na hapakuwa na
fujo. Alitumia tu maneno.” Mmoja alikuwa akiandika.
“Kuna kitu chochote unakumbuka kabla yakurudi
nyumbani ukiwa matembezini?” Mmoja akauliza. Tunda akabaki akivuta kumbukumbu. “Chochote
kile ambacho labda kilikufanya kufikiria. Mtu au tukio? Labda mtu aliyekuwa
akikufuata au kukuangalia kila wakati?” Mwenzake akaongeza kama kumsaidia
Tunda.
Tunda akafikiria. “Nilijua mlinzi yupo karibu
yangu, kwa hiyo hata sikuwa na wasiwasi wakuangalia nilipo na nani ananifuata.
Kwa kuwa wakati mwingine huwa nakuwa na walinzi hata wawili na mara nyingine
wapili huwa anabadilishwa badilishwa. Kwa hiyo ni ngumu kujua nani ni mlinzi
nani siye. Kwa kifupi huwa sinataarifa na nani yupo karibu yangu.” Akajibu
Tunda.
“Je, baada ya kufikishwa hospitalini, unakumbuka
chochote?” “Ilikuwa ni hali ya kupoteza fahamu na kurudi. Ila nilipofikishwa
chumba cha upasuaji, daktari wangu aliyekuwa akinihudumia tokea nipo mjamzito.
Aliniambia nipo hospitalini, kwenye chumba cha upasuaji. Wanataka kunisaidia
kumtoa mtoto. Watanichoma sindano ya usingizi. Hapo hapo nililala, wakaja
kuniamsha tena na kuniambia nilipata mtoto mzima, wakiume na wananirudisha
chumbani kwa mapumziko.” Tunda akanyamaza.
“Na baada ya hapo?” “Niliporudi chumbani nakumbuka
kuwaona Nana, Maya na Net. Waliondoka baada ya kutakiwa waniache nipumzike.
Niliamka katikati ya usiku. Nikaomba mtoto wangu. Wakaniletea. Nilimnyonyesha. Wakamchukua
na kumrudisha kwenye nursery.” “Unakumbuka muda?” Wakamuuliza. Akafikiria kama
anayevuta kumbukumbu. “Ile ilikuwa saa sita hivi. Nakumbuka yule nesi alisema
muda, wakati akinilazimisha kunipima pressure na kunipa dawa. Nilipomkatalia na
kumwambia mpaka aniletee mtoto wangu kwanza, aliniambia muda ule ilikuwa ni saa
sita, nilitakiwa kupewa dawa.” “Safi sana.” Wakaandika.
“Nini kilitokea baada ya hapo?” “Kwenye saa 10
alfajiri. Niliamka tena. Nikawaomba tena waniletee mtoto ajaribu kunyonya tena
kwa kuwa maziwa hayakuwa yakitoka mengi. Wakanisafisha na kidonda kabisa.
Wakanibadilisha, ndipo wakanipa mtoto. Nilimnyonyesha nafikiri kama dakika 15
hivi, nikaanza kusinzia mtoto naye akiwa amelala, ndipo wakamchukua mtoto, na
mimi nikarudi kulala ndio mpaka hapa.” “Kuna kumbukumbu nyingine?” Akauliza
taratibu tu.
“Mmmmh! Nilipoteza masaa kadhaa mpaka muda mfupi
uliopita ndipo nikaelezwa nilitekwa nyara. Lakini sikumbuki chochote. Ni kama
nilipolala wakati ule, nikaja kuamshwa kwa nguvu sana na madaktari hapa.
Wakinitaka nijitahidi hata nifungue macho. Kumbe ndio muda walikuwa
wananirudisha hapa. Sikuwa nikijua.” Wakaandika.
“Hukumbuki chochote hata kama inafanana na ndoto?”
“Ndio nilikuwa nikiwaambia hawa. Sina uhakika.” “Tuambie tu. Hata kama ni kitu kidogo.”
Tunda akavuta pumzi kwa nguvu, akajisogezea mto. Maya naye akamsaidia,
akajilaza vizuri. Maya akambusu. “Nakupenda Tunda.” “Asante Maya. Nashukuru.”
Akamshika mkono na kuwageukia wale polisi.
“Kuna muda ni kama nilitoka usingizini. Lakini bado
nilikuwa na usingizi. Nikafungua macho kwa shida. Nikamuona mwanamke aliyevaa
nguo za kinesi. Kama tu wale waliokuwa wakinihudumia na kuniletea mtoto. Nikamuomba
akaniletee mtoto. Sasa nakumbuka kusikia sauti ya kiume iliyonifanya nigeuke,
kwa kuwa hakuwa akisikika kama Net.” “Alisema nini?” Akamuhoji tena.
“Naweza nisipatie sana kwa kuwa nilikuwa na
usingizi, hata macho hayakuwa yakifunguka vizuri. Ila alimwambia yule nesi kwa
kumlaumu kwamba amenipa dawa kidogo. Sio dozi iliyokamilika ndio maana
nimeamka. Alitakiwa kuwa makini. Sasa kwa kuwa mawazo yangu yalikuwa kwa mtoto.
Nikimtaka akaniletee mtoto wangu, nikarudisha macho kwa yule nesi ili kumuomba
akaniletee mtoto. Nikamuona anachoma sindano kwenye ile sindano iliyokuwa
imeunganishiwa dripu. Hapo hapo nikalala. Sikuamka tena mpaka hapa.” “Tukikuonyesha
picha, unaweza kuwatambua?” Tunda akajifunika uso kwa mkono mmoja.
“Upo sawa, Tunda?” Net akauliza. Tunda akatoa
mkono. “Sikumbuki kuwaangalia usoni. Nilikuwa ninausingizi mzito sana. Hata
sijui kama ni kweli au ilikuwa ndoto!” “Ungependa kujaribu kama unaweza
kuwatambua?” Wakamuuliza kiuungwana. “Sidhani. Kwa sababu nina uhakika hata
wakirudi tena leo hapa, sitawafahamu. Sikumbuki chochote. Lakini kwa
kuwaridhisha, acha tu niangalie.” Wakamtolea picha za wanaume na wanawake wengi
kwenye tablet.
Tunda aliangalia kwa kutulia. Kuanzia mwanzo mpaka
mwisho. “Samahanini jamani. Sikumbuki kabisa!” “Na hizi?” Wakamfungulia sehemu
nyingine. Akaangalia tena mpaka mwisho. “Hakika sikumbuki kuona hizi sura zote
hapa. Samahanini sana.” “Usijali kabisa. Hata hapo umekuwa msaada.” Tunda
hakuwa ameelewa.
“Kivipi wakati hakuna nilichofanya?” “Kutokana na
damu uliyochukuliwa jana kabla ya matibabu, kuna aina fulani ya kemikali
zilikutwa humo ambazo zinatokana na madawa ambayo yanauzwa na mtu ambaye
amekiri kuwauzia baadhi ya watu. Kuwafanya walewe. Na kufanya mambo fulani
ambayo hufuta kabisa zile kumbukumbu siku inayofuata au pale hayo madawa
yanapoisha. Huyo mtu ameshakamatwa. Na baadhi ya madawa yamekamatwa nyumbani kwake.”
“Mmejua ni kina nani alikuwa akiwauzia?” Akauliza Maya.
“Wapo wateja wake ambao huwauzia, na bado
tunaendelea na uchunguzi mpaka utakapo kamilika.” “Ni Vic?” Maya akauliza tena
moja kwa moja akijua wanaficha. “Bado tupo kwenye uchunguzi. Utakapokamilika,
tutawajulisha.” Walishindwa kumtaja mtu hata mmoja. Wakamshukuru Tunda na kina
Cote, wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Rudi nyumbani ukaoge ulale kidogo.” Maya
alimsogelea kaka yake pale alipokuwa ameinama kwenye kochi. “Jana niliondoka,
huku nyuma wakamteka nyara mke wangu. Nataka nikitoka hapa, nitoke nao wote.”
Maya akambusu kichwani. “Pole Net.” Net akamwangalia tu. “Unaonekana umechoka
sana. Basi jilaze kidogo hapo kwenye kochi. Mimi nipo hapa kumsaidia Tunda.”
Maya akasimama. Akamtolea kaka yake mto na shuka. Akamfunika. Akazima taa ya
pembeni yake ya kwenye meza. Akambusu kaka yake shavuni. Hapo hapo Net
akapotelea usingizini. Tunda na bibi Cote kimya kama hawapo pale.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Net alilala pale kwenye kochi kama na yeye amepewa
dawa za usingizi. Akili ilikuwa imepitishwa kwenye mikasa mizito, kisha
akatengwa na watu wawili muhimu sana kwake. Kwa mara ya kwanza Net anakuwa
kwenye matatizo nakushindwa kusaidia na wala hakuna anayemtambua! Na kwa mara
ya kwanza kwenye maisha yake ndio anapatwa na kashfa mbaya sana na ikasababisha
madhara kwa mkewe. Vic alimchafua haswa hakuwa hata na hamu na simu yake wala
kushika kompyuta. Redio ndio kabisa, hakuta iwashwe popote alipo.
Video yake ya ngono ilisambazwa na watu walishare
kila mahali. Ilipata watizamaji kuliko hata habari nzito za nchi. Kila
alipopita na kuzungumza hata na manesi wa hapo, alijihisi yupo uchi. Ile
kufunga macho akijua angalau mkewe na mtoto wapo pale salama, ikamsaidia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Upade mzima alipokuwa amelazwa Tunda, ilikuwa haina
mgonjwa mwingine ila yeye tu. Hakuna aliyeruhusiwa kwenye huo upande wa gorofa
hilo bila kitambulisho. Manesi pia waliingia hapo wachache na walichunguzwa
kila walipokuwa wakiingia na kutoka. Hakuna aliyeruhusiwa kumpa dawa Tunda,
bila daktari na mlinzi wa Tunda kuwepo hapo. Tunda alishakataa dawa yakumfanya
kulala. Alikataa kabisa.
Na tokea aelezwe kuwa alitekwa akiwa usingizini,
hakuweza kulala tena. Alibaki amekaa hapo kitandani, hata hakufunga macho.
Wakati wote macho kwa mtoto wake. Alikuja nesi kutaka kumchukua mtoto wake
akamuogoshe, nusura Tunda avunje mguu. “Nooooo.” “Nakwenda kumuogesha.” Yule
nesi akajibu kwa upole na tabasamu ili kumfanya Tunda atulie. “Hapana. Hapana
na HAPANA.” Tunda akasimama. Ikabidi bibi Cote asimame na yeye.
“Wanaenda kumuogesha na kumbadilisha. Huyu ni nesi
wa hapa. Ni salama.” “Hapana Nana. Naomba usimguse.
Tafadhali mwache tu.” Tunda akawa ameshaingiwa hofu. Akasogea mpaka
kwenye kitanda cha mtoto wake. Machozi yakaendelea kumwagika. “Basi twende wote
Tunda. Twende naye.” Maya akamtuliza. “Naona sipo
tayari aogeshwe, Maya. Kwanza amelala. Kwa nini aogeshwe sasa hivi? Naomba
mumuache mwanangu apumzike.” Bibi Cote akamsogelea.
“Niangalie Tunda.” Tunda akageuka. “Hakuna
atakayefanya kitu kwa Cote bila wewe kutaka. Mwambie ni nini unataka. Basi.” “Sitaki mtoto wangu ashikwe na kila mtu! Diaper
anabadilishwa na huyu. Nguo anabadilishwa na yule! Siwafahamu na ..” “Aliyekuwepo
asubuhi ametoka.” Yule nesi akaongeza kwa tabasamu. “Mimi
nimepona. Nitamuhudumia mtoto wangu mwenyewe, Nana. Tafadhali. Najua kuogesha
watoto na kuwavalisha. Sihitaji msaada. Nimefanya hivyo..” Net akatoka
usingizini akamkuta Tunda akilia.
“Kuna nini?” Net akauliza taratibu. “Nataka kwenda nyumbani. Sehemu nitakayotulia na mtoto
wangu tu. Hapa watu wengi wanapishana kila wakati. Naogopa, situlii mawazo.
Kila mtu anamgusa mtoto wangu. Wanapishana hapa kila wakati kunigusa, wakati
vipimo vinaonyesha nipo sawa! Sitaki nesi yeyote aingie tena humu ndani, Net. Na
ninataka kurudi nyumbani.” “Okay. Tulia. Ngoja nikazungumze na daktari.
Turudi nyumbani.” Net akasimama pale.
“Njoo ukae hapa kitandani.”
“Mimi sio mgonjwa Net. Wakati umelala hapo wamekuja kuangalia kidonda wamesema
kipo sawa na pressure ipo nzuri. Lakini kila baada ya nusu saa wanarudi humu
ndani! Siwezi kutulia! Tafadhali nitoeni hapa. Nitachanganyikiwa. Sasa hivi
kila anayeingia humu ndani naingiwa hofu. Nataka kurudi nyumbani, Net.”
“Sawa. Tutaondoka.” Net akatoka.
Bibi Cote akamwambia yule nesi atoke. Kisha
akamwambia mlinzi, asiruhusu mtu mwingine yeyote aingie hapo ndani. Kisha
akamfuata Net kule alipokwenda kwa daktari. “Hajalala hata kusinzia tokea wale
maafisa waliomuhoji waondoke. Nafikiri ameingiwa hofu. Naomba uturuhusu tu, tuondoke.
Kukitokea chochote nitampigia simu daktari wake. Nashukuru sana. Lakini
nafikiri mturuhusu tu tuondoke. Itamsaidia kutulia.” Bibi Cote akaweka
msisitizo.
“Hiyo inaeleweka kabisa. Kwake sasa hivi hospitalini
hapatakuwa sehemu salama tena. Hata hivyo hakuonekani kama kuna tatizo
lakuendelea kumlaza hapa. Nafikiri anaweza kurudi nyumbani tu.” Wakaongozana mpaka chumbani kwa Tunda. Wakamkuta
amembeba mtoto wake. “Upo tayari kurudi nyumbani?” “Ndiyo.” Tunda akaitikia kwa
haraka. “Ungependa nesi aje kukuonyesha jinsi ya ...” “HAPANA.” Tunda akakataa
kwa haraka bila hata kumruhusu yule daktari amalizie.
“Sihitaji kufundishwa chochote kwa
mwanangu.” “Je, kwa nyumbani ungetaka nesi awe
anakuja kuku..” “Hapana. Sihitaji nesi karibu yangu
wala mtoto wangu. Please Nana!” “Hakuna nesi kwenye ile nyumba.” Bibi
Cote akatoa kama amri. Tunda akatulia. “Asante Nana. Si tunaweza kuondoka sasa
hivi?” Tunda akauliza huku akimbembeleza mtoto aliyekuwa amelala, hana hata
habari. “Hapa silali kabisa. Halafu..”
Akasita. “I just want to go home.” “Sawa. Twende ukatoe nguo za
hospitalini wakati usafiri wakututoa hapa ukiandaliwa.” Net akamtuliza.
“Mpe Maya mtoto.” Taratibu akamkabidhi Maya
mwanaye. “Naomba usimpe yeyote kwa chochote. Iwe wewe na Nana tu. Tafadhali
Maya. Au twende naye tu?” Akamgeukia Net akiwa amebadili tayari mawazo. “Sitamuweka
hata chini Tunda. Nitampakata. Kwanza na mimi nina hamu naye.” Maya akawahi
kabla hajapokonywa huyo mtoto. Akambusu mara kadhaa, hapo Tunda akaridhika. Net
akamsindikiza bafuni. “She will be fine.” Bibi Cote akanong’ona.
Tunda arudi nyumbani na mtoto wake.
T |
unda akashangaa anapanda gari ngeni kabisa kwake na
imefungwa kiti maalumu kwa umri wa mtoto wake. Nzuri, safi sana. Dereva alikuwa
yuleyule wa Tunda. Net ndiye alikuwa amembeba mtoto wao. Huo ulinzi uliokuwa
ukiwazunguka, mpaka Tunda akaingiwa hofu. Waliambiwa wasubiri dakika 20 ili
kuweza kusindikizwa. Na kweli walisindikizwa. Ilianza gari ya usalama. Akaja
bibi cote na ulinzi wake pamoja na Maya. Ikaja hiyo gari ya mtoto, Tunda na
Net. Polisi nyuma yao. Wakaondoka.
Hakuna waliposimama hata kwenye taa, polisi wa pikipiki
waliwasaidia kusimamisha magari wapite bila kusimama hata kwa sekunde chache.
Walifika nyumbani geti lilifunguliwa kama waliokuwa wakisubiri. Kulikuwa na
ulinzi, Tunda akashangaa sana. Net alimfungulia mlango, akakuta Maya bibi Cote,
Carter, Ms Emily wamesimama mwanzo kabisa wa
kwenye ngazi wakiwasubiria. Walizungukwa mpaka na askari wa bunduki.
Tunda alishuka na kuzungusha macho kote. Uzio mzima
ulikuwa na ulinzi. “Twende ndani ukapumzike.” Net akaongea kwa kujihami. Carter
akasogea kumkumbatia, kisha Ms Emily. “Nimefurahi umerudi nyumbani.” Ms Emily
alimnong’oneza wakati amemkumbatia. Tunda akatoa tu tabasamu. Net alikuwa
amebeba mtoto. Walisimama hapo kidogo kwa picha, kisha wakaingia ndani. Cote
alimka palepale nje wakati baba yake akimnyanyua ili apigwe picha na
kuchukuliwa video.
“Namuomba nikamnyonyeshe.” Net akamkabidhi, Tunda
akaelekea chumbani kwa mtoto, Maya na yeye akafuata nyuma kwa haraka bila hata
kusubiri aitwe. “Nikusaidie nini?” “Sitaki msaada Maya. Nataka muda na mtoto
wangu.” Tunda akajibu huku akiingia chumbani kwa Cote. Na Maya naye akaingia. “Kwani
bado umenikasirikia au umenisamehe? Maana ulipoondoka mwenzio nilikuwa
nakulilia!” Maya akaanza. “Unajua nilikuwa nakulilia nini?” “Kuwa umenificha
kitu kikubwa na kuniacha mimi nimedhalilika?” “Tunda!?” Maya akashangaa sana.
“Sio hicho. Wewe usimsikilize Vic. Vic anataka
kutugombanisha mimi na wewe.” “Kwani ni uongo? Wewe hukujua kama alilala hapa
baada ya kufunga ndoa na kaka yako?” “Nilijua Tunda. Lakini..” “Naomba undoke
uende kwa kaka yako.” “Come on Tunda! Hata wewe mwenyewe ungekuwepo siku ile
Net ameamka pembeni ya Vic ungemuhurumia. Alikuja ofisini kwangu, Net
anatetemeka mpaka midomo. Akaniomba msamaha akasema hata hakujua ilikuaje
ameamka pembeni ya Vic!” Maya akajaribu kujitetea.
“Yeye kwa nini alimwalika chumbani kwake, kama sio
alikuwa anataka?” “Sasa kwa nini wewe, mimi na Nana, tusiungane tukamkasirikia
Net? Na mimi mniingize kwenye kundi lako na Nana!” Tunda akamwangalia na
kuendelea kunyonyesha.
Maya akajilaza kwenye kapeti mbele ya Tunda. “Ujue
hata Nana hataki kuniongelesha kama wewe ambavyo humuongeleshi Net?” Maya
akaendelea. “Lakini turudi kwenye pointi yangu Tunda.” “Pointi gani? Ile ya
kunililia ukijuta?” “Ndio maana nilikuwa nakulilia Tunda. Wewe unanisikiliza.”
“Mbona sasa hukuniambia huyo ambaye hataki kukuamini tena?” Tunda akamuuliza
habari waliyozungumza hata kabla hajafuatwa na Vic.
“Si ndio maana nilikuwa nakulilia sasa? Nikasema
wasingekuiba kabla sijakwambia siri yangu!” “Kwa hiyo ungekuwa umeniambia, ndio
ingekuwa sawa mimi kutekwa?” “Hata kidogo. Nani sasa angenisikiliza sasa hivi?”
Akakaa. “Ndio ujue nyumba hii ilivyo. Sasa hivi kila mtu analake kichwani. Basi
ujue mimi nitasahauliwa kabisa. Net ndio atakuwa hata hajui ninaendeleaje tena.
Na ilimradi Nana anajua nipo humu ndani, hakuna hata atakayeniuliza kama
nimekunywa hata maji!” Tunda akamwangalia.
“Umeniudhi Maya!” “Usinichukie Tunda. Mimi
nitakusaidia kumnunia Net. Lakini mimi niwe na wewe. Au hata Net tumsamehe tu.
Kwa kuwa hakuwa akijua kama..” “Unaniudhi zaidi Maya!” “Basi. Net ni mbaya sana.
Tumchukie kabisa. Hamia chumbani kwangu. Tulale mimi na wewe tu. Tuwe tunaongea
usiku kucha!” Ikabidi Tunda acheke.
“Na mtoto?” “Usiku tunahamisha kitanda chake
chumbani kwetu.” Tunda akamwangalia na kurudisha macho kwa mwanae. “Kwa hiyo
hutataka mfanyakazi wa mtoto?” “Amshike mtoto wangu wakati mimi nafanya nini!?”
Maya akanyamaza. Tunda akamwangalia. “Nini sasa?” “Cote anabahati, sio kama
mimi na Net. Sidhani hata kama mama yangu alininyonyesha Tunda! Mimi sikulelewa
kama Vic. Sikukuzwa na wazazi wangu!” Maya akaongea kwa kunung’unika.
“Lakini Papa na Nana walikupenda sana.” “Lakini
hawakuwa wazazi wangu Tunda. Ni tofauti mtoto akilelewa na mama yake. Ona hivyo
ulivyomkumbatia mtoto wako! Mimi sidhani kama nilipata hayo mapenzi.” “Sasa
wewe hakikisha watoto wako wanapata hayo mapenzi. Hata mimi mama yangu
hakunitaka Maya. Alinizaa tu na kwenda kuniacha kwa wazazi wake. Tena afadhali
wewe alikuwa akija hata kukuangalia kujua unavyoendelea. Mimi mama yangu
hakunipenda kabisa. Kwanza nilizaliwa na hii rangi ambayo hakuwahi kuipenda.
Mpaka sasa hanipendi. Lakini..” “Mungu amekupa Net.” Maya akamalizia.
“Nilitaka kusema lakini hainizuii mimi kutompenda
mwanangu. Mungu amenipa nafasi ya kurekebisha kile nilichokosa.” “Nikuulize Tunda.”
“Uliza tu.” “Wasichana wengi hapa. Hata Vic alikuwa akisema kama ni kuzaa,
atazaa mtoto mmoja tu na hata akizaa hatamnyonyesha mtoto ili asiharibu matiti
yake, zaidi mwili. Maana wanasema ukinyonyesha unazidi kusikia njaa.” Tunda
akacheka sana.
“We Maya!” “Kweli. Sasa wewe huogopi?” “Akuu. Hata
kidogo. Kwanza nilishafundishwa jinsi yakunyonyesha ili matiti yasiharibike.
Halafu vipo vyakula unaweza kula na usinenepe. Hata hivyo sijali Maya. Zipo
faida nyingi kwa mtoto wangu kunyonya kuliko mimi kutilia mashaka huu mwili unaoweza
kuharibika hata kwa magonjwa tu.” “Ndio maana nakupenda Tunda.”
“Yaani nishindwe kumnyonyesha mtoto wangu sababu
yakuhofia matiti yataharibika! Hata kidogo. Nitamnyonyesha Cote bila kumpa kitu
kingine mpaka afikishe miezi 6, ndipo nitamchanganyia na kitu kingine.
Akifikisha mwaka, ndipo naweza kufikiria
kumuachisha.” “Mpaka mwaka!” Maya akashangaa sana. “Kabisa.” Wakaendelea
kuongea. Huwezi kumkasirikia Maya.
Net kwa bibi yake.
N |
et alijikuta ameachwa hapo sebuleni peke yake.
Akafikiria akaona ni lazima atengeneze. Akatoka hapo bila yakuaga. Alikwenda
kununua maua ya bibi yake na Tunda. Na zawadi kidogo. Akarudi nyumbani. Moja
kwa moja akaenda ilipo ofisi ya bibi yake. Akamkuta ameinamia kompyuta yake.
Kimya. Net akagonga na maua aliyojua bibi yake akiyapenda sana. Tulip. Akawa ameshika
tulip bouquet mkononi. Bibi yake akatoa miwani na kuiweka mezani. Akamtizama.
Kwa aina ile ya rangi za hayo maua ya Tulip, bibi
Cote akajua ameingia kuomba msamaha. “Nimekuja kuomba msamaha Nana. Samahani
sikukwambia kilichotokea siku ile na Vic. Samahani nilimkataza Carter na Maya
pia wasikwambie. Najua ningekwambia mapema, tungejua kitu chakufanya. Nilikosea
sana. Ninaomba unisamehe.” Bibi yake akavuta pumzi kwa nguvu. Akajiegemeza kwenye
kiti.
“Hayo ni maua yangu?” Net alikuwa bado
ameyashikilia. “Ni yako Nana.” Akampelekea. “Naweza kukukumbatia? I miss you so
much Nana.” “Umenifedhehesha vibaya sana Net.” Bibi yake akalalamika. “Najua
Nana. Lakini nakuhitaji sana sasa hivi. Sijui nitafanya nini na mama! Amefika
mbali sana. Anataka kumuua Tunda!” “Ritha ni mama yako. Mwache sheria
imshugulikie ili usije kujilaumu baadaye.” Net akanyamaza.
“Niangalie Net. Nimetoka kuzungumza na Mike, hawana
muda mrefu, watamkamata tu. Labda asiwe yeye anahusika. Naomba tuliza mawazo
kwenye familia yako. Hakikisha Tunda hahami chumba.” Net akaenda kumkumbatia na
kumbusu bibi yake. Akatulia hapo kwa muda. Akambusu tena na kutoka akiwa
ameelewa jukumu alilopewa na bibi yake.
Net kwa Tunda!
Aliingia na kukuta Tunda ameweka mtoto wake kifuani
anamsikiliza Maya akiongea akiwa amekaa hapohapo chini mbele ya Tunda. Maya
akasimama kwa haraka. “Mimi nilijua unasaidia mambo ya mtoto!” “Nimesaidia
kuongea na mama yake huku akinyonyesha. Ameshiba. Tunamuacha alale, akiamka
tunamuogesha. Sisi wenyewe sio mfanyakazi!” Maya akaanza. “Unajua kuwa huyu
mtoto atalelewa na sisi tu sio wafanya...” Akamwangalia Tunda, akamuona
amenyamaza wala hamwangalii Net. “Nimekumbuka, wote tumekununia.
Hatukuongeleshi. Bad bad dady!” Maya akamkunjia uso kaka yake kama
amemkasirikia. Net akatingisha kichwa na kumfanyia ishara atoke.
“Nitarudi baadaye Tunda. Nikusimulie stori yangu.
Mimi na wewe ni marafiki. Usisahau hilo. Nikirudi tunaanzia kwenye urafiki.
Tumeshasahau mambo ya.....” Tunda akasimama kwenda kumlaza mtoto. “Umemletea
mtoto maua?” Maya akanong’ona wakati anatoka. “Noo! Haya maua ni ya mke wangu.”
Maya akamcheka. “Mwenzio nimesamehewa.” Akamnong’oneza Net. “Lakini wewe
sidhani.” “Toka Maya.” Net akamsukumia
nje.
Tunda akabaki akimfunika mtoto wake pale kwenye
kitanda. “Unajisikiaje?” Akaanza Net.
Kimya. “Kila kitu unachohitaji cha mtoto kipo?” Kimya. “Yule nesi aliyekuwepo
hapa, aliandika orodha ya vitu vyote ambavyo vinahitajika kwa Cote, vikanunuliwa.
Nikuangalia tu humuhumu ndani na Ms Emily ata...” “Naenda kuoga na kubadili.
Unafikiri unaweza kukaa hapa na mtoto mpaka nirudi?” “Au nikusindikize kule
kuoga halafu..” “Net!” Tunda akaita kwa ukali. “Basi mimi naona nibaki
na mtoto hapa mpaka utakaporudi kutoka chumbani kwetu. Chumba changu mimi na
wewe.” “Na Vic.” Akaongeza Tunda na kutoka. Net akang’ata meno.
Tunda alioga. Na kubadili nguo zake. Akatoka na
kibegi kidogo chenye baadhi ya nguo zake. Wakati anaingia pale chumbani kwa
mtoto, Net akamuona anaingia na begi akilivuta. “Umetoka kufanyiwa upasuaji
Tunda. Naomba usibebe vitu vizito.” Akaenda kumpokea. “Ni sanduku la nini
tena?” Tunda hakujibu, akaenda kukaa kwenye kiti chake chakunyonyeshea.
Net akafungua lile sanduku alilokuja nalo Tunda.
Akakuta baadhi ya nguo zake. “Basi ngoja na mimi nikafungashe nguo zangu,
nije.” “Naomba wewe usihamie huku.” “Tunahamia wapi?” Net akauliza. “Naomba
uache kelele mtoto amelala na uondoke humu ndani nenda kwenye lichumba lako
ambalo unaingiza wanawake zako na kulala nao mpaka asubuhi.” “Tunda naomba
uniamini. Sikumkaribisha Vic mle chumbani. Alinifuata nyuma na kuingia na juisi
ambayo niliacha kule sebuleni nilipomwambia anisubiri nakwenda kumfuatia vitu
vyake chumbani. Nimeingia tu chumbani na yeye akanifuata. Aka..” “Naomba acha kelele
Net.” Tunda akamkatisha.
“Hayo maelezo ungetaka kunipa, ungenipa kabla na
mimi hujaniingiza kwenye kile chumba. Sasa hivi unaongea hivyo kwa kuwa unaona
siri yako imejulikana. Naomba uondoke, unipishe na mtoto wangu. Sitaki maneno
mengiii na sitaki uanze kuongea uchafu wako mbele ya mtoto wangu. Huoni aibu
kueleza mambo ya mwanamke wako mbele ya mtoto!” “Sio mwanamke wangu Tunda.
Mbona hunielewi?” “Ondoka Net. Lasivyo naenda kumwita Nana akutoe humu ndani.”
“Tunda!” “Tena toka na maua yako. Usirudi hapa na maelezo yako ya uzinzi.”
“Mimi sijazini Tunda. Alinilevya.”
“Kitendo cha kunificha mimi kuwa uliamka pembeni ya
mwanamke wako, tena baada ya kunidanganya mbele ya umati wa watu kuwa utakuwa
mwaminifu kwangu daima, huo ni uzinzi Net. Naomba uondoke.” Tunda akaendelea.
“Unanirudisha kwenye maisha machafu sana ya zamani
Net. Maisha ya kuishi ya kudanganywa! Nakuwa kwenye mahusiano ya watu watatu!
Bado na mwanamke wako naye alikuwa na wanaume wengine. Nakuwa kwenye mahusiano
ya watu zaidi ya wawili! Kunakuwa na tofauti gani vile nilivyoishi zamani na
hiki unachonifanyia sasa hivi?” Net akaishiwa nguvu kabisa.
“Ipo tofauti Tunda.” “Tofauti gani? Unatofauti gani
wewe na wanaume wengine wengi waliokuwa wakinitumia na kunidanganya? Kama kweli ungekuwa unanipenda na kunithamini, usingeacha
nadhalilishwa na mwanamke wako!” Tunda akaanza kutokwa na machozi. “Mimi namfukuza chumbani nikijua ni chumbani kwangu na
mimi kumbe ndio na yeye ni chumbani kwake! Tena ulipo mhalalishia! Unaniacha
natoa viapo hadharani, nikijua nipo mimi na wewe tu, kumbe unavyo viapo na
maagano uliyokuwa umewekeana na kuishi na mwanamke wako!” Tunda aliongea
kwa kuumia sana huku akilia na ongea yake ni ileile ya taratibu, akapunguza
sauti zaidi ili mtoto wake asiamke.
“Kwa ujasiri bila woga, anaingia hapa
si kama mgeni, kama mtawala humu ndani! Tena baada ya mimi kumfukuza!
Ananiongelesha kama anaongea na takataka, kumbe hiyo jeuri anaitoa kwako wewe
mwenyewe Net. Unafikiri nitakaa humu ndani kama kina Ms Emily mimi? Hapana Net.
Ulinikuta nikiheshimiwa na mimi nilikuwa na wafanyakazi waliokuwa wakiniheshimu
kama hivyo wewe unavyoheshimiwa. Umenitoa nyumbani, unakuja kunidhalilisha
huku! Unanitukana mbele ya watu na ndugu zako!” Net akakumbuka kugomba kwake siku yakuonja chakula alipochelewa Gino.
“Ninakusihi utulie. Mimi ndiye
nilipanga mambo yote. Kwa kuwa huniamini na kuniheshimu kama mwanamke wako
unayeweza kumtunzia siri na kumsitiri hadharani, unatokea tu nakuanza
kunitukana na kudhalilisha mbele za watu! Kama kweli wewe ni mtu mwadilifu kama
ulivyonifanyia mimi na kuwa na msimamo mkali kwangu na kama hukupenda kubakwa
na Vic, si ungechukua hatua siku ileile?”
“Mbona ulinyamaza na mkaendelea kama
kawaida? Unanidanganya mimi eti hukujua kama ulifanya mapenzi naye, kama si
kunifanya mimi mtoto mdogo, wewe ufanye mapenzi muda wote huo uamke asubuhi
usijue kama ulifanya mapenzi usiku!”
“Ulijua sana tu na kupenda mlichofanya kwa kuwa ni
mwanamke wako. Ukafurahia kufanya naye mapenzi. Wala usinidanganye kama
ulibakwa. Ni uongo wa kijinga sana. Nenda kadanganye mashabiki wako huko nje.
Kamtetee kuwa hana akili ndio maana alifanya aliyofanya. Pengine anatakiwa
kuongezewa dawa. Wampe dawa, wamtoe, muendelee. Lakini Net, sio na mimi.”
“Nilishaachana na watu kama wewe kwa
garama kubwa sana. Wewe hujui hilo kwa kuwa wakati mimi nahangaika kubadili
maisha yangu, ulikuwa ukifurahia na watu kama Ritha na Vic. Huko sitarudi Net.
Na kama nikiamua kurudi, nitarudi kwa heshima sio kwa kudhalilishwa.” Net akavuta pumzi kwa nguvu.
“Na ujue wakishakamatwa tu hao watu wako wanaotaka
kuniua, naondoka humu ndani. Nitaondoka kwa heshima yangu kabla
hujanidhalilisha zaidi. Na wala usiwe na wasiwasi na pesa yako. Sitakuchukulia
chochote. Kwa hiyo uwe na amani, utaendelea kuwa na mali zako kama kawaida.
Ondoka humu ndani ya hiki chumba Net.” Net akataka kuondoka. “Usisahau maua yako. Beba na uondoke nayo. Usirudi na
maua hapa. Nilikwambia tokea tupo Tanzania. Sikufuata maua mimi. Nilikufuata
wewe. Kama nimeshindwa kukupata wewe..” Tunda akasimama akilia kuelekea
upande wa chooni huko huko ndani bila hata kumalizia.
Gino akawa anagonga na kigari cha chakula. Net
akamfungulia. Gino akaingia ndani, akaacha chakula na kutoka. Net naye akatoka
na maua yake mkononi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Maya akabaki akimwangalia kwa kujiiba huku macho
yapo kwenye simu. Wakati anamaliza tu kula, mtoto akaamka. Akaweka kila kitu
chini. Akaenda kumchukua mtoto wake akaenda naye bafuni. Maya akamfuata nyuma.
Akamuona anaandaa maji ili amuogeshe mtoto. Akaendelea kumfuata kila
anaposogea. “Ulijifunza wapi mambo ya watoto? Jinsi unavyomshika Cote, ni kama
mzoefu kabisa!” “Nilimlea mtoto wa mama
tokea mdogo sana. Au tokea anazaliwa. Kwa hiyo najua.” Tunda akajibu.
Alipomaliza kumuogesha, akaenda kukaa naye kwenye
kiti. Tunda huyu alikuwa amefanyiwa upasuaji. Lakini hakuwa hata akijifikiria
kwa hofu na hasira. Akakaa na mtoto wake kwenye kiti nakuanza kumnyonyesha.
Maya akimwangalia. “Nikuulize Tunda?” Maya akamrushia swali. Tunda
akamwangalia. “Unafikiri mtoto kama huyo hapo ulipomshika, anahisi kama umebeba
uchungu?” Tunda akaanza kulia.
“Najua umeumia sana Tunda. Lakini nikwambie ukweli
Tunda, hilo ndilo lilikuwa kusudi la Vic. Kwamba kama yeye amekosa, basi
mwingine asimpate Net. Na pia ndio furaha ya mama yetu. Mimi najua kama mama
alitutelekeza Tunda. Najua mama hajali kile mimi na Net tunajisikia. Ndio maana
yupo radhi kukuangamiza wewe, bila kujali kile Net atajisikia.” Maya aliongea
taratibu tu.
“Unajua ni kwa nini nilihangaika mpaka nikakubali
kufanywa mapenzi mbele ya wale maafisa wa CSIS?” Tunda akashtuka sana. “Maya!” “Sijamwambia mtu yeyote. Lakini sharti la
Jake ilikuwa nilazima nifanye naye kwanza mapenzi ndipo akutafute wewe. Nikijua
kabisa wale maafisa wananisikiliza na kutuangalia, nilikubali Tunda.” Tunda
aliumia sana.
“Na haikuwa kitu kidogo cha muda mfupi! Jake
alihakikisha ananitumia haswa. Unafikiri ni kwa nini yule director wao
alinishukuru vile? Anajua kilichonipata, ila hawezi kumwambia Nana.” Tunda akaumia
sana. “Usingekubali Maya!” “Leo usingekuwepo
hapa Tunda. Huwezi kujua wangekufanya nini huko walipokuteka. Tena kama sasa
hivi ambavyo wamembana mama! Yule nesi, Malinda walimpiga risasi wakitaka kummaliza
kabisa kama walivyomuua kaka yake wakiwa hukohuko walipokuficha na wewe.
Unafikiri huyo mtu aliyebakii na kuwauwa wale angekufanya nini na wewe kama sio
kukuua kwa kuwa huna faida tena kwake? Ungegeuka kuwa mzigo ambao asingeweza
kukuhudumia tena.”
“Kumbuka aliwaua wale wenzake mpaka mwanamke wake,
polisi wanahisi ni kwa kuwa alitaka mama amlipe yeye pesa yote na kufuta
ushahidi. Kumbuka nia ya mama pia ilikuwa uuwawe. Sasa unafikiri mpaka sasa
ungekuwa hai?” Maya akamuuliza taratibu tu.
“Hakuna anayetupenda mimi na Net kama
sisi. Hata mama yetu mzazi amekuwa akitutumia tu ili kujinufaisha. Hakuna
anayejali furaha yetu kama sisi. Ndio maana mimi nikakimbilia madawa ya
kulevya, Net akakimbilia Afrika. Unafikiri ni kwa nini?” Maya akajifuta machozi.
“Wote tulikuwa tukihangaika kutafuta kujaza pengo
ambalo halikuwahi kujazwa tokea baba yetu afariki. Tulikuwa tukitafuta mapenzi
ambayo tunajua yapo, lakini sisi hatukubahatika tena baada ya baba kufariki,
Tunda. Baba alitupa mapenzi mazito sana, halafu akatuacha tukiwa bado
tunamuhitaji. Akatuacha tukitafuta kujaza hilo pengo. Pesa kwetu imekuwa kama
laana. Imetuweka mbali na uhalisia. Tumezungukwa na watu wanaotaka kunufaika na
pesa ya Cote tu.”
“Vic hakuwahi kumpenda Net kama Net. Ila marupurupu
yanayotokana na Net kama Cote. Nina
uhakika, Vic angekutana na Net uliyekutana naye wewe Afrika, asingemng’ang’ania
kama hivi.”
“Mimi nililelewa na dad, wakati mama alikuwepo! Dad
alipofariki, nililelewa na Papa na Nana, bila mama, wakati mama alikuwepo! Ninachokuomba
Tunda, usimuunge mkono mama katika kuendelea kutuumiza. Hujui nikiasi gani Net
alivyofurahi ulipokubali kuja kuishi huku na yeye, tena baada ya mama
kukufunga. Alipiga simu huku akilia kwa furaha. Kuwa umemchagua yeye, zaidi ya
majaribu yote shetani aliyowatupia!”
“Na ninakuomba usikubali Vic akuingie akilini mwako
kama alivyowaingia familia yangu kipindi akiniangamiza mimi. Ni ngumu sana
Tunda. Huwezi kuelewa mpaka uwe umepita hapo.” Maya akaendelea taratibu tu. “Mimi
najua anakopita Net, kwa kuwa Vic alinipitisha hapo. Na ni mjanja sana katika
mipango yake. Anaakili katika maovu yake. Haachi mwanya wa mtu kusimama na wewe
anapokutenda jambo.”
“Nilikuwa nikilia mimi Tunda, sina
msaada. Yaani hiki anachopitia Net, ndio nilikuwa nikipitia mimi, halafu sina
mtu wakumueleza au kunisikiliza akanielewa. Maana ni kweli
nakuwa nilienda club kunywa kama kawaida. Kesho unakuta video zimesambaa
mitandaoni. Unajitetea nini kwa watu? Unasema nini na wakati unakuwa ni kweli
ulienda baa! Kweli unatumia madawa ya kulevya. Lakini hata hukumbuki kumruhusu
mwanaume akuguse. Lakini video zinaonyesha unafanya mapenzi. Wakati mwingine
kwenye gari yangu mwenyewe nje club au hata kwenye mahoteli. Huonekaniki wakati
huo kama unabakwa! Inaonekana unatoa tu ushirikiano. Halafu sasa Tunda, sio
mara moja. Ni matukio yakujirudia. Kila mtu humu ndani alikuwa hanielewi.
Ananilaumu mimi. Lakini sikujua jinsi ya kufanya, kwa kuwa kumbe hata marafiki
zangu wale wakaribu sana, walikuwa wakitumiwa na Vic.” “Kivipi?” Tunda akauliza
kwa mshangao kidogo
“Alisema Vic mwenyewe, kuwa kina Gina. Wale
marafiki niliokuwa nikikwambia walikuwa wakinifukuza kama nisipokunywa au
kutumia madawa. Nikawa nawakimbilia, kumbe walikuwa wakitumwa na Vic.” “Jamani
Maya!” Tunda aliumia sana. “Kweli Tunda. Ndio maana ilikuwa rahisi sana kwangu
kuharibikiwa. Vic alikuwa na akili na anafanya mambo yake kwa makini sana. Tena
akitumia watu wa karibu yangu. Akiamua jambo lake Vic, anahakikisha
anafanikiwa. Na hakurupuki. Anapanga hata miezi 6
kabla.” Maya akaanza kulia tena.
“Tafadhali usimsikilize Vic.
Usituache sababu ya Vic. Net na mimi tunakuhitaji sana kuliko utakavyofikiria.
Hatujawahi kupendwa hivi Tunda. Tunatumikiwa sana na watu wanatuchekea, lakini
kwa sababu ya pesa.” Maya akajifuta
machozi. “Ulisema wewe hauna tofauti na sisi. Lakini nikwambie ukweli Tunda,
huyo Cote, hatakuwa na tofauti yeyote ile na mimi, wewe pamoja na Net. Mama
atampitisha huyo mtoto kule alikotupitisha sisi wote watatu. Atamnyima Cote mapenzi
ya kweli.”
“Cote naye atakuwa kama sisi akihangaika. Net
anakupenda sana Tunda, naomba usisahau hilo na kukubali watu wawaibie huu
wakati mliokuwa mkiusubiria kwa hamu sana. Wote wewe na Net mlikuwa mkimsubiria
huyu mtoto. Ona sasa hivi upo hapa peke yako, Net na yeye yupo kwengine akiendelea
kusononeka! Usikubali Tunda. Wewe umebeba hatima ya kina Cote. Wewe ndio
unaweza kuvunja upweke wa watoto wako na sisi. Mimi nakuacha, uamue mwenyewe.
Ila ujue popote utakapokwenda, mimi nitakufuata tu.” Tunda akacheka huku
akifuta machozi.
Maya akasimama. “Njoo
kwanza unikumbatie hapa.” Maya akacheka na kumsogelea Tunda pale
alipokuwa amekaa na mtoto wake. Akambusu na kumkumbatia kwa tahadhari yeye na
mtoto. “Nakupenda Tunda.” “Lini umekuwa mkubwa kiasi hicho na kuwa na hekima
hivyo!?” Maya akacheka wote machozi yalikuwa yakiwatoka. “Muweke mtoto kwenye kitanda chake na wewe ulale kidogo.
Bado hujapona Tunda!” “Acha nimshike tena kidogo ndipo nimuweke chini. Bado
ninahamu naye.” “Kesho zamu yangu.” Wakacheka Maya akatoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tunda akamuweka mtoto wake kifuani, akampapasa
kidogo, akapitiwa na yeye na usingizi palepale kwenye kiti akiwa amemuegemeza
mwanae kifuani. Tokea asubuhi mpaka jioni hiyo hakuwa amelala kwa hofu. Na
chumba hicho walizuia mtu yeyote asiingie ili kumfanya atulie.
Akiwa usingizini, Net alirudi hapo ndani akamkuta
Tunda na mwanae wote wamelala. Akajaribu kumtoa mtoto mkononi taratibu. Tunda
alishtuka mpaka akapiga kelele.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Bado Ritha yupo mtaani, amewasha moto mwingine
tena. Wengi wameteketea. Tunda ameharibiwa akili kwa hofu. Yu mgonjwa katikati
ya utajiri mkubwa, anahangaika kulea peke yake sababi ya utisho wa Ritha. Je na
ndoa ya Net nayo itapona? Maya aliyekuwa kidharaulika na watu wote ndiye
ameibuka mwenye hekima na mkombozi wa hiyo familia wala si Net mrithi wa
mamilioni ya pesa. Nini kitaendelea? Ritha atamudu kuwazidi akili hata hao
maafisa wa CSIS nchini Canada?
Endelea kufuatilia...
0 comments: