Story

My Past - Sehemu ya 6

Wednesday, May 10, 2017 naomimwakanyamale 0 Comments



B
ella alijua wazi Mzee Masha ndiye aliyetuma watu shuleni kwa kina Ric akachukuliwe ili Bella arudi nyumbani. Alikwenda kwenye hoteli ambayo huwa wanaishi na Eric kila anapokuwa yupo likizo ili kuthibitisha hisia zake lakini hakumkuta. Alirudi nyumbani akamkuta Mzee Masha. Bella alikuwa akitembea kwa hasira na maumivu. “Nitakuuwa kama hutaniambia alipo Eric, T.” Mzee Masha alibaki akimwangalia Bella. Bella aliingia jikoni akarudi na kisu mkononi. “Ric yuko wapi?” “Utajiumiza bure Bella. Wewe huna roho ya kikatili. Rudisha kisu, halafu njoo hapa.” Akiwa jikoni Bella alishindwa hata kusogea, akaanguka.

Mzee Masha alikwenda kutaka kumbeba. “Usiniguse.” “Utafikaje kitandani?” Mzee Masha alibaki akimwangalia. “Ric yuko wapi?” “Wewe ulikuwa wapi?” “Hospitali. Nimetoroka baada yakusikia Ric haonekaniki. Umemuweka wapi mdogo wangu?” “Ukiacha ukorofi nitakwambia alipo.” Mzee Masha alikuwa akicheka. “Twende ukalale.” “Nitengenezee uji kwanza. Sijaweka kitu mdomoni tokea siku umenipiga, nilikuwa naishi kwa dripu.” Mzee Masha alibaki akimwangalia. “Nipikie uji T. haraka.” Bella alirudi kulala pale pale sakafuni.

Mzee Masha alipika uji harakaharaka, akamwekea kwenye bakuli. “Nikulishe?” “Swali gani hilo? Si unaona kabisa sina nguvu?” “Nimeona umerudi na mkakati mpya, hutaki nikuguse.” Bella alijaribu kukaa mwenyewe kwa shida huku akigugumia maumivu. “Ric yuko wapi?” “Nimekwambia yupo. Nilienda kumchukua, ili wewe urudi nyumbani.” “Unataka nirudi hapa kufanya nini?” “Wewe ni wangu Bella. Hakuna kitu wala mwanadamu atakaye kutoa mikononi mwangu. Nilikwambia kifo pekee ndicho kitatutenganisha. Ukiwa hai, wewe ni wangu daima.” “Nisogezee huo uji hapa. Halafu niwekee simu yangu kwenye umeme.” Bella alijaribu kunywa uji, lakini akashindwa. “Acha ukorofi usio na maana Bella. Unahitaji msaada ambao ni mimi peke yangu ndio naweza kukusaidia sasa hivi. Ngoja nikunyweshe.” Mzee Masha alimnywesha Bella uji wote. Alimaliza kisha akaomba kuongezwa. ‘Lazima nipone.’ Bella aliendelea kuwaza huku Masha akiendelea kumlisha mpaka alipomaliza.

“Nipeleke kitandani.”
 Mzee Masha alijaribu kumshika lakini alimtonesha. “Niache T. Unazidi kuniumiza.” “Wapi?” “Umenivunja mbavu mbili za upande wakushoto na kupasua mirija ya damu. Imebidi kufanyiwa upasuaji japo sio mkubwa lakini nina mshono upande huo huo.” “Basi ngoja nikushike upande wa kulia.” Bella alizidi kumchukia Mzee Masha. ‘Anashindwa hata kusema pole.’ Bella alianza kulia.

Alimbeba mpaka kitandani. “Niambie Ric alipo.” Mzee Masha alikuwa amemficha Ric mahali. “Waambie hao watu wako wamwachie mdogo wangu. Tena wampeleke kwa kaka Mat.” “Sasa hivi?” Masha akauliza. “Ndiyo, sasa hivi. Mimi si niko hapa. Makubaliano yangu mimi nikiwa jela, mdogo wangu anakuwa huru. Kwa hiyo nimerudi jela, mdogo wangu anakuwa huru. Piga simu sasa hivi.” Mzee Masha alianza kucheka. “Unakufuru mbaya wewe! Unaiita hii jela? Nitakupeleka jela ukalale huko hata siku moja, ili ukirudi kutoka huko uwe na shukurani.” “Ni heri wanaotesa mwili tu, kuliko wewe unayenitesa mwili na nafsi yangu. Hakuna mateso ninayoweza kupata duniani, yakafikia ukatili na unyama unao nifanyia weweHakuna na kwa kuwa nilikubali mimi mwenyewe, acha nilipe gharama yangu. Piga simu, T. Tafadhali nataka kulala.” Mzee Masha alikuwa anacheka sana. “Umeanza kunifurahisha Bella. Nyumba ilikuwa inapowa kweli, nagomba peke yangu! Lakini sasa hivi naona tutakuwa wawili.”  “Piga simu T.” Mzee Masha alitoka kwenda kuongea na simu.

Baada ya muda akarudi. “Umemsumbua mdogo wako bure! Alikuwa amelala hana hata shida, imebidi aamshwe sababu hutaki kusikiliza kila ninacho kushauri.” “Naomba dawa ya maumivu.” Mzee Masha alimpa Bella dawa ya maumivu. Akapanda kitandani na yeye akalala pembeni ya Bella.  “Unajua nilirudi hapa Tanzani kwa ajili yako Bella?” Bella akanyamaza. “Nimeahirisha mambo mengi sana, yanayohusu familia ili nije kuwa na wewe, halafu nafika hapa na wewe haupo ulikuwa unazurula, mpaka saa tano za usiku! Ndio maana nilikasirika sana.” Bella hakujibu kitu alibaki kimya. 

“Nilipoondoka hapa siku ile ya ugomvi, nikajilaumu sana kukupiga. Nikarudi kuja kukuangalia kesho yake sikukukuta. Sikujua kama nilikuumiza kiasi cha kwenda hospitalini.” Bella alifungua macho kumwangalia kama anamshangaa. “Kweli Bella. Sikujua kama nimekuumiza kwa kiasi hiki, nikajua umeamua kunikimbia, ikabidi nikamuwahi mdogo wako ili urudi. Nilipotuma watu shuleni kwao, wakaniambia amesafiri kwa michezo halafu wakirudi wanafunga shule. Ndipo iliponibidi kumsubiria. Siwezi kuishi bila wewe Bella. Hata nifanyaje, siwezi tena. Najua nimeshakutendea mambo mengi sana, nimejaribu kukuchukia lakini najikuta wewe ndio mtu pekee ninayekuhitaji.” “Naomba nifunike shuka vizuri, nilale.” Bella hakutaka kuendelea kusikiliza. Yalikuwa ni maneno machungu sana kwake. Kwa namna nyingine, ni kama alikuwa akitangaziwa kifungo cha maisha. Alipitiwa na usingizi akalala.

Mzee Masha alimuuguza mpaka akapona kabisa wakati huo Eric yuko likizo nyumbani kwa Mat. Bella alikuwa akimuhurumia sana Ric, alijua atakuwa na wasiwasi kuona yupo likizo halafu Bella hayupo. Lakini Bella asingethubutu kwenda kwa Ric akiwa na hali ile. Alijua atazidi kumuumiza mdogo wake, alitaka apone kabisa ndipo aende kumchukua .

************************************************

Mat alioa na kuhamia kwenye nyumba ndogo mitaa ya Mwenge, ambapo aliweza kufungua na duka la vitu mbalimbali, kutokana na pesa alizokuwa akipewa na Bella. Maisha ya Mat yalibadilika. Bella alishakwenda nyumbani kwa Mat, kwa hiyo alikuwa akipafahamu. Hakuwa akifahamiana vizuri na mke wa Mat, kwani mara zote aliwasiliana kwa simu na kaka yao, sio yeye. Hata Eric, ile ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kufika nyumbani hapo. Alipooa Bella aliamua kumuacha kwa muda ili kumpa nafasi na mkewe. Waliwasiliana pale ilipokuwa ni muhimu sana, tena kama alitaka kumtuma kwa mdogo wake huko Arusha au kwa babu yake kule kijijini.

Hakuacha kumtunza babu yake. Alihakikisha anapata maendeleo yake mara kwa mara kupitia Mat. Sasa kwa kuwa Mat alijua pesa anatoa wapi, au nani ameyabadili maisha yake, na mahusiano yao tokea zamani, aliongeza heshima kubwa sana kwa Bella. Muda na wakati wowote Bella aliomuhitaji, Mat hakusita kutoa ushirikiano, hata kama yupo katikati ya shuguli nyingine, akipiga simu Bella, atapokea tu. Hiyo tabia ikaanza kumkera mkewe ambaye hakuwa akijua na wala kumuelewa mumewe pale alipojaribu kumuelewesha umuhimu wake yeye kwenye maisha ya yatima hao.

************************************************

Alipoona anatizamika, ndipo alipoamua kwenda kumfuata Eric. Aliamka asubuhi hiyo, akakusanya baadhi ya vitu vyake ambavyo alijua atavihitaji kwa muda huo atakaokuwa akiishi hotelini na mdogo wake, akachukua na vitu vya Eric alivyokuwa akimnunulia wakati alipokuwa shuleni. Nguo na viatu vya thamani, akaenda kwenye ile hoteli akapanga kila kitu kumuonyesha mdogo wake kuwa pale ndipo anapoishi wakati  yeye anapokuwa shuleni. Alipojiridhisha kuwa pako sawa, ndipo akaenda nyumbani kwa Mat. Alijipaka foundation zile za hali ya juu kama kawaida yake, yakuficha makovu yake ili mtu yeyote asijue kama anamakovu. Kwa hiyo ilikuwa ni ngumu kujua kama Bella anaalama yeyote usoni mwake.

Ilishakuwa mchana na jua lilikuwa kali wakati anafika nyumbani kwa Mat. Alimkuta Eric anaosha vyombo nje kwenye jua kali. Bella alitamani kuchanganyikiwa. Alikuwa amekaukwa mdomo alionekana wazi hajala. Alifurahi sana kumuona Bella. Alimkimbilia dada yake na kumkumbatia. “Bella!” Eric aliita taratibu huku amemkumbatia dada yake. Hasira zilimpanda Bella. Alikumbuka mateso anayopata kwa ajili ya Eric. Pesa nyingi anazokuwa anampa Mat, tena akimwambia kabisa atafute mahali ambapo na wao itakuwa kimbilio. Hata kodi ya hiyo nyumba anayoishi sasa hivi na mkewe, ni Bella alilipia, tena alilipa kodi ya mwaka mzima!

“Mbona unaosha vyombo hapa nje? Tena kwenye jua kali hivi!? Umekula?” Bella akamuliza mdogo wake kwa upendo. “Mpaka nimalize kazi.” Bella alianza kutetemeka kwa hasira. Alijua ndivyo alivyokuwa amembiwa na mke wa Mat. “Kaka Mat, yuko wapi?” “Ameenda kazini. Lakini mke wake yupo ndani.” Bella aliingia ndani na kumkuta yule mwanamke anaangalia tv, amekaa kwenye kochi na kunyoosha miguu kwenye meza. 

“Kwa nini Ric, anaosha vyombo kabla ya kula na  yupo juani?” Bella aliuliza bila ya salamu. “Ulitaka aishi hapa bila kufanya kazi?” “Mbona wewe unaishi hapa bila kufanya kazi?” “Wewe umechanganyikiwa nini? Hapa ni kwangu.” Kama simba, Bella aliinyakuwa ile tv na kuitupa chini, akaipasua vipande vipande. Akageukia kabati la vyombo lililokuwepo karibu na sebleni, akaanza kuvipasua vyombo vyote huku akigonga vioo vya ile kabati. “Hii yote ni pesa yangu. Muulize mumeo.” Bella alikuwa akilia kwa uchungu sana. “Nahangaika, nateseka kwa ajili ya Ric, halafu wewe unamtesa!? Muulize mumeo pesa anapata wapi.” Bella aliingia jikoni akachukua kisu. Akaanza kuchana makochi yote kuanzia juu mpaka chini. Akageukia meza za kioo zilizokwepo pale sebleni na kuanza kuvunja moja hadi nyingine huku akilia. 

Mke wa Mat aliogopa sana, huku analia, akampigia simu Mat. Eric aliingia mle ndani baada yakusikia dada yake analia huku anafanya fujo mle ndani. Alimkuta dada yake kama amechanganyikiwa. “Bella! Hey Enabella! That’s enough. Stop it! Eric alimshtua dada yake. Bella akasimama huku anahema nakulia kwa uchungu sana. Watu walishajaa. Alitoka nje, akakusanya vyombo alivyokuwa akiosha mdogo wake, akatafuta jiwe akaanza kuvivunja, huku akitupa vijiko, visu na vyombo vyote vya plastiki. 

“Bella, please!” Eric alitoka tena huku akilia. Alipoona mdogo wake ameanza kulia, akamsogelea, akamshika mkono. “Twende Ric.” Akamgeukia mke wa Mat. “Na mwambie mumeo, kwa kuwa amekuchagua wewe, na akaacha umtese mdogo wangu, leo undugu umekufa rasmi. Asiwahi kusogelea shule ya Eric, wala asitutafute tena. Na siku nitakayo rudi tena hapa, nakuja kuchoma moto duka analouza, maana pia ni pesa yangu yote ile.” Majirani walianza kucheka. “Kazidi huyu dada, na leo kapata kiboko yake.” “Jeuri kama anamiliki ndege!” “Sura yenyewe mbaya, utafikiri kalamba ndimu.” “Na angemkung’uta huyu, mpaka jeuri imwishe.” Kila mtu alisema lake huku wakicheka. Bella alimfungulia mlango mdogo wake, wakaondoka. Alikuwa akilia njia nzima. Mwishowe aliegesha gari pembeni ya barabara, akainamia usukani na kuendelea kulia kwa uchungu sana, mkapa Eric alipomtuliza.

Bella alimlaani sana Mzee Masha. Alijua isingekuwa yeye kumpiga, asingeshindwa kwenda kumchukua mdogo wake kama kawaida, na kuishi naye. Bella aliendelea kulia. “Is gonna be okay Bella. Don’t cry, please.” Eric alikuwa mwema sana na hakupenda ugomvi na wala hakutaka kumuona mtu yeyote anashida, hasa Bella. Walifika hotelini wakaingia kwenye chumba chao. Bella alipanda kitandani na kuendelea kulia. Ric alipanda kwenye kitanda cha Bella, akatoa mto aliokuwa amelalia dada yake, akaweka kichwa chake miguuni mwake na kuanza kumbembeleza bila kujua dada yake analizwa na mengi.

Walikaa pale kwa muda mpaka Bella alipotulia. “Samahani Ric, nilikuwa na hasira sana. Nilichukia kukuacha peke yako unateseka.” “Usijali Bella. Nimefurahi umekuja kunichukua.” “Alikuwa akikutesa sana.” “Kidogo, wakati kaka Mat hayupo.” “Alikuwa anakufanyaje?”  Eric alinyamaza kidogo. “Alikuwa ananimbia nifue nguo zote. Nikamwambia sijui kufua, akasema lazima nijifunze na nifue nguo mpaka zitakate, lasivyo hakuna kula. Sasa wakati mwingine mikoni ilikuwa inavidonda. Nikimwambia mikono inavidonda siwezi kufua, anagomba sana.” “Ulimwambia kaka Mat?” “Nilimuonyesha vidonda, nikamwambia anitafutie dawa, akasema sawa. Lakini hakunipa dawa.” Bella alizidi kuumia, alimuhurumia sana mdogo wake.

“Bella?” Eric aliita kwa upole, Bella akamgeukia akiwa bado amemlalia. “Unafikiri tutakuja kuwa na sisi na nyumbani kwetu kama zamani?” Bella alijaribu kuzuia machozi yake lakini alishindwa. Alikaa vizuri akamkumbatia mdogo wake. “Usiwe na wasiwasi Ric. Sasa hivi tukazane na shule kwanza. Ada ninayokulipia ni kubwa sana. Sitaweza kujenga kwa sasa. Lakini nakusanya pesa, baadaye tutajenga, na sisi tutakuwa na kwetu. Kwani hupapendi hapa?” “Napapenda sana, lakini sio kwetu Bella. Natamani tuwe na nyumbani kwetu, ili nikiwa natoka shule, niwe najua naenda nyumbani kwetu, hata kama wewe haupo.” “Wazo zuri Ric. Basi tuanze kutafuta hata nyumba ya kupanga kwa muda. Ukimaliza shule, tutajenga nyumba yetu.” Eric alifurahi sana. “Njaa inauma Bella.” “Na mimi njaa inauma. Ngoja nipige simu watuletee chakula, sasa hivi. Halafu tukaogelee.”

Baada ya kula, Bella na mdogo wake walitoka kwenda kuogelea hapo hapo hotelini. Wote wakiwa wametulia. Eric alianza kumsimulia dada yake mafanikio makubwa anayoyapata huko shuleni. “Asante Bella. Najua unalipia pesa nyingi, lakini nikija kushinda kwenye Olympic, tutakuwa na mahela mengi sana.” Bella alianza kucheka. Angalau aliliwazika. Akaona mateso yake sio bure. “Bado ndoto zako za kwenda Olympic kwenye mashindano hazijafa tu?” “Nilimuahidi mama kuwa nitafika. Lazima nifike Bella. Nitaenda kushindana kwenye kombe la Dunia, na ninajua nitashinda tu.” Eric alikuwa mzuri sana kwenye michezo. Bella alifikiria. “Mwenzio ndoto zangu zote zimekufa Ric.” “Najua Bella. Lakini tusikate tamaa, mimi nitaenda kukuwakilisha. Wakati wananipa zawadi, nitakuita tupokee wote.” Bella alianza kulia. “Unajua kwa nini ninakazana?” Bella alicheka huku anafuta machozi. “Nakazana kwa kuwa najua nacheza kwa ajili yangu mimi na wewe.” Bella alicheka. “Itabidi siku nyingine ukienda kwenye mashindano na mimi nije kukutizama.” “Nitafurahi Bella. Mashindano mengine tutaenda South Africa. Unajua kuna wanafunzi wengine wazazi wao huwa wanakuja? Tunasafiri nao.” “Mbona hukuniambia sasa?” “Sikutaka kukusumbua, si uliniambia ulianza kazi?” “Tena nina ofisi yangu.” Eric alianza kucheka. “Unakumbuka yale mambo ya kompyuta tulikuwa tunafanya nyumbani wakati mama yupo?” “Nakumbuka.” “Nilienda kuyasomea tena, ndio sasa hivi nafanyia kazi.” “Wanakulipa vizuri?” “Sanaa.” Bella na Eric walikuwa wakiongea na kucheka karibu usiku kucha. Bella alikuwa amepona kabisa. “Tulale Ric, kesho mwenzio natakiwa kazini. Tutaenda wote ukanisaidie kazi?” “Nitafurahi Bella.” Wakalala.

Kwa Mara ya Kwanza, Eric kazini kwa Bella.

Bella na Eric waliamka asubuhi kuelekea ofisini kwa Bella. Njia nzima walikuwa wakiimba kama kawaida yao tokea utoto wao waliimba pamoja. Vilitawala vicheko kati yao, na Bella alijawa na furaha sana. Elvin alibaki hamuelewi Bella. Bella aliyeachana naye hospitalini au waliyezoea kumuona pale kazini sio huyu wasasa. Alijawa tabasamu wakati wote. Eric alikuwa kila kitu kwa Bella. “Kumbe una dimpozi?” Elvin alimtania Bella. Bella akacheka. Hakuacha kumwangalia mdogo wake kila wakati. Ric naye alikuwa kama Bella. Anajiamini na alipenda kujua mambo. Kwa haraka sana, akamzoea Elvin, na kuhamia ofisini kwake. Alishinda ofisini kwa Elvin akiomba amsaidie kazi ndogo ndogo. Elvin alimzungusha ofisi nzima, akimuelezea kazi anazofanya pale.

“Mbona kama wewe una kazi nyingi kuliko wote?”
 Eric alimuuliza Elvin wakati wanazunguka. Elvin akacheka. “Nafanya kazi mbili kwa wakati mmoja. Namsaidia na baba yangu. Yeye ndio mwenye hii kampuni, na mimi nimeajiriwa kama Bella.” “Unaingia kazini saa ngapi?” “Mimi ndio mtu wa kwanza kufika hapa ofisini. Lazima saa kumi na mbili niwahi kufungua mlango.” “Ni sawa na mimi nikifika kesho muda huo, nione kazi unazofanya, tangia asubuhi?” “Hamna shida.” Walirudi ofisini kwa Elvin, Eric akiwa amejawa furaha sana.

Bella alimfuata. “Mbona umenikimbia?” “Namsaidia kazi Elvin. Tumekuwa marafiki.” Bella alicheka. “Kweli. Muulize Elvin. Na kesho nitakuja saa 12 asubuhi, nimsaidie kazi.” “Eric!?” Bella akamshangaa mdogo wake. “Kesho unatakiwa kupumzika.” “Nimezoea kumka mapema nikiwa shuleni. Naomba unilete Bella.” “Kama Elvin akisema ni sawa, nitakuleta.” “Au mimi mwenyewe naweza kumfuata ili usisumbuke kuamka asubuhi asubuhi.” Elvin alitoa wazo. “HAPANA!” Bella alisema kwa nguvu na kwa kushtuka sana. Elvin na Eric walibaki wakimwangalia. “Namaanisha itakuwa usumbufu kwako Elvin. Nitamleta tu mimi mwenyewe hapa kazini.” Wote walibaki kimya, wakishangaa ule mshtuko wake. Haukuendana na ile kelele.

“Twende tukale Eric.”
 Bella aliona aondoke tu, kwani ni kweli alikataa kwa nguvu sana na kumshtua kila mtu. “Twende wote Elvin.” Eric naye akamgeukia Elvin. “Sijawahi kumuona Bella anatoka kwenda kula mchana. Sijui hata kama anajua panapouzwa vyakula.” Bella alitabasamu. “Ningemkimbiza City Garden mara moja, napafahamu.” Elvin alibaki akimshangaa. “Kwa nini ukalipe mapesa yote hayo!? Twendeni niwapeleke mkale chips vumbi.” Wote walicheka na kuondoka.

Ulitawala utani kati yao, Eric akimtania Elvin. Alijiona ni kama amepata kaka. Walifika sehemu, wakakuta watu wengi wamejaa wanasubiria chips, kila mtu alikuwa akimshangaa Bella. Bella alikuwa na mvuto wa aina yake. Umbile lake, lilimfanya kila mtu kumwangalia bila kujiiba. Alijaliwa uso mzuri sana na macho mazuri. Ilikuwa ngumu kuelewa msichana kama yule, na mavazi ya thamani aliyovaa, na kiatu cha juu vile, anafanya nini sehemu kama ile. Bella alifanana sana sura na rangi ya mwili na mdogo wake. Na kwa kuwa Eric alikuwa mrefu, ungeweza sema ni mapacha. Walikuwa wakicheka, bila kujali mtu. 

“Mtaweza kula hapa au mnataka tukale ofisini?”
 Elvin akauliza. “Umesema leo tunakula chips vumbi, tule hapahapa kwenye vumbi.” Bella alijibu nakumfanya Elvin amwangalie huku akicheka. “Naona Bella huyu wa sasa ni bora zaidi.” “Jamani Elvin! Bella yupi sio mzuri?” “Yule anayevaa sura ya kazi kila wakati. Sijawahi kukuona ukicheka hivi Bella!” Bella alicheka tena na kuendelea kula. Waliendelea kula huku wakicheka, Eric ndiye alikuwa na furaha sana. Elvin alimuona vile Bella alivyokuwa akimtizama mdogo wake kwa makini huku akimuuliza maswali kila wakati. Kama anataka amuongeze hiki au kama amependa hicho chakula, au kama chakula kitamu. Alimuona vile akili zake zote zilivyokuwa kwa mdogo wake, akajua ndipo furaha yake ilipo.

“Mimi na Bella, tutasafiri kwenda kutembea. Unataka twende wote?” Eric alimuuliza Elvin wakati wanaendelea kula.  Bella alitamani amfunge mdomo Eric. “Hapana Ric. Elvin anatakiwa sana kazini. Hawezi kusafiri na sisi.” “Kwani mnataka kwenda lini?” “Bella amesema ile week ya sabasaba, ndio itakuwa weekend ndefu. Ndio tutasafiri kipindi hicho.” Bella alikuwa kimya kabisa, akiomba Mungu Elvin amkatalie Eric. “Nafikiri tunaweza kwenda wote, hatutafungua ofisi.” “Asante Elvin. Umeona Bella? Safari hii tutakuwa na wakati mzuri zaidi, Elvin atakuwa na sisi. Wakati wote tumekuwa mimi na Bella tu.” Eric alikuwa na furaha sana, lakini sio Bella. Angemwambia nini Mzee Masha akaelewa? Lakini katika vitu ambavyo hawezi kufanya ni kumkatili Eric, mdogo wake kipenzi. Walikuwa wakitembea kurudi ofisini, Eric na Elvin wakicheka sana, lakini sio Bella. 

Walipokuwa wakiingia tu ofisini huku wamejawa vicheko, walikutana na Irene pale mapokezi. Sura yake haikuwa na furaha hata kidogo. “Nimekupigia simu zaidi ya mara tano hujapokea.” “Niliacha simu ofisini, pole. Vipi lakini?” “Unaachaje simu ofisini sasa!?” Irene alionekana kukasirika. “Tuliongea muda sio mrefu Irene, na tukakubaliana nikitoka kazini nije nyumbani kwenu. Sikujua kama utapiga tena. Pole.” Bella alipoona hali sio shwari alimshika mkono Eric. “Twende ofisini kwangu.” Bella na Eric waliondoka na kuwaacha Elvin na Irene pale mapokezi wakiendelea kuongea.

“Ulikuwa wapi?”
 Bella alisikia Irene akimuhoji Elvin. “Nilienda nao kula. Yule ni mdogo wake Bella, amekuwa akinisaidia kazi siku nzima leo. Nikaona nimpeleke kula. Vipi Irene? Mbona kama umekasirika?” “Nashangaa nakupigia simu hupokei, kumbe umetoka kwenda kula na Bella. Kwanza tokea lini mmeanza kwenda kula pamoja?” “Naomba twende tukaongelee ofisini, Irene.” “Kwani unaficha nini?” “Tunasumbua watu maofisini kwao, Irene. Tuliposimama hapa, kila mtu anatusikiliza sisi. Naomba tuingie ofisini kwangu.” Irene alibaki amesimama. “Tafadhali Irene.”  Waliingia ofisini kwa Elvin, pakawa kimya.

Eric alipooza sana. “Usiwe na wasiwasi Ric, kila kitu kitakuwa sawa.” “Unafikiri nilikosea, Bella?” “Nimekwambia usiwe na wasiwasi Ric, ulikuwa na nia nzuri.” “Unafikiri nimekuharibia kazi?” Bella alicheka kumfariji mdogo wake. “Itabidi uwe unakuja hapa kazini mara kwa mara, ili ujue mambo ya kazi. Huwezi kuharibu kazi kwa kuwa mkarimu. Ulifanya vizuri, kumkaribisha Elvin kwenda kula na sisi. Naamini kila kitu kitaenda sawa. Usiogope.” Eric hakuwa akipenda kumuudhi mtu, alibaki kimya ofisini kwa Bella mpaka jioni wanakaribia kuondoka. 
“Ric! Wewe muoga bwana. Nimekwambia usiogope.” “Ni sawa kwenda kuongea naye?” Bella alifikiria kidogo. “Kwa nini usiongee naye kesho? Twende ukapumzike, halafu kesho ndio utaongea naye?” “Sawa.” Bella aliweka vitu sawa, akabeba pochi yake akamwambia mdogo wake muda wa kazi umeisha, waondoke.

Wakati Bella anafunga ofisi yake, naye Elvin alitoka ofisini kwake akiwa na Irene. Eric aliwasogelea. “Samahani, mimi ndio nilimkaribisha Elvin kula naye chakula cha mchana. Naomba usimlaumu Bella.” Bella alishtuka sana. “Bella alitaka niende naye mimi tu, lakini kwa kuwa mimi nilikuwa na Elvin tokea asubuhi tukifanya wote kazi, nikaona nimkaribishe chakula. Sio Bella. Usimlaumu Bella. Bella hana kosa.” “Usiwe na wasiwasi Eric, kila kitu kipo sawa. Hukukosea. Na mimi nilifurahia tumepata muda wa pamoja. Usisahau kesho umeniahidi utakuja asubuhi ya saa 12 tuanze kazi pamoja.” Ilibidi Elvin amjibu kwa utani kidogo, kwani Irene alibaki kimya akimwangalia wakati Eric anamtetea dada yake. Eric alicheka kidogo. “Bella amesema atanileta.” “Sawa. Muwe na usiku mwema.” Elvin aliaga huku akimtizama Bella aliyekuwa amesimama kimya akimwangalia mdogo wake. “Asante.” Bella alijibu kwa hofu kidogo. “Twende Eric.” Bella alitangulia mlangoni, Eric akafuata.

************************************************

Eric aliendelea kumganda Elvin kila siku, kila alipokuja kazini na Bella, alishinda ofisini kwa Elvin. Waliacha kwenda kula nje wakawa wakiletewa chakula pale pale ofisini na kula jikoni wote watatu. Taratibu Elvin na Bella wakaanza kuzoeana. Minong’ona ikaanza pale ofisini juu ya Bella na Elvin.

Muda wa safari yao waliyopanga ukawadia. “Naomba siku ya Ijumaa niwahi kutoka Elvin, tunasafiri na Eric.” Bella alimfuata Elvin ofisini kwake. “Mmeamua kuniacha? Hutaki twende wote?” “Hapana Elvin, nilijua baada ya ile siku, tusingeweza kwenda pamoja.” “Nilimuahidi Eric, tutakwenda wote. Siwezi kubadilisha sasa hivi.” “Sitaki ije ilete matatizo Elvin. Naweza kuongea na Ric, naamini ataelewa tu.” “Mbona kama hutaki niende? Eti Bella?” “Hapana Elvin, ningependa twende wote. Najua Ric atafurahi zaidi, lakini nisingependa tukusababishie matatizo.” “Usiwe na wasiwasi. Itakuwa sawa tu.” Kwa upande mwingine Bella alifurahi lakini alimuhofia  sana Mzee Masha.

************************************************

Eric alipolala, Bella alitoka nje na kumpigia simu Masha. “Umenikumbuka leo?”  Bella akaanza kulia. “Nini Bella?” “Umesababisha mdogo wangu ateseke sana. Nimemkuta ananjaa, tena yupo juani.” “Si ulisema Mat atamtunza vizuri?”  “Hakuna mtu anaweza kuishi vizuri na Eric isipokuwa mimi mwenyewe. Mke wa Mat alikuwa anamtesa sana mdogo wangu. Na yote hayo wewe ndio umesababisha, T. Ulinipiga bila kosa, ukasababisha niugue, nikashindwa kukaa na mdogo wangu. Wewe unajua nafanya kila kitu kwa ajili ya Eric. Naumia sana kuona wote tunaishia kuteseka. Inakuwa haina maana yeyote. Kama nashindwa kumsaidia Eric basi hata wewe huna maana yeyote kwenye maisha yangu.” Bella alikuwa amekasirika sana, alikuwa akiongea huku analia. “Unanisikia?” “Nakusikiliza Bella.” “Mbona hujibu sasa?” “Unataka nijibu nini wakati umenipigia simu usiku, tena nikiwa nimelala, halafu unagomba?” “Wewe ndio umesababisha yote haya TTunakuwa watu wakutangatanga mchana kutwa. Hatuna nyumba, tunabaki kukaa hotelini tu.” “Kwa nini usimlete hapa nyumbani?” “Tunataka nyumba yetu. Sio yako ambayo ukiamua siku hiyo kunipiga unanipiga karibu ya kuniua. Halafu nakujua T, unamtindo wakunipokonya vitu vyako ukikasirika. Siku ukikasirika halafu ukatufukuza mimi na Eric? Heri niteseke nae hivi hivi huku mahotelini kuliko siku moja aje kushuhudia unavyonipiga halafu ukatufukuza nyumbani kwako. Itaniumiza zaidi ya unavyonipiga.”  “Ninakuwa na hasira tu Bella, sina maana yakukuumiza au kukunyanyasa. Nimekwambia sitakupiga tena.” “Sasa hivi ndio unaongea hivyo kwa kuwa unajua nipo na Ric siwezi kuwa na mwanaume mwingine. Akiondoka tu utaanza kunipiga kama zamani.” “Nimeshawahi kukuahidi kitu na nikashindwa kutimiza?” Bella alinyamaza.

“Yote haya nafanya kwa kuwa nakupenda Bella. Ninamatatizo yakifamilia yamenipanda kichwani, lakini nimekubali kuwa hapa na wewe. Nakupenda na sitaki mwanaume mwingine akuguse.” Bella alibaki kimya akilia. “Bella?” “Nataka tuwe na kwetu T. Tumechoka maisha ya hotelini.” “Basi chukueni hii nyumba.” “Hapana T. Hapo utatusumbua tu. Wewe nipe pesa, nikatafute nyumba sehemu nyingine, ambayo hutakuwa unapafahamu na wala hutakaa ukafika huko. Najua hiyo nyumba ni yako na familia yako, haitakaa ikawa yangu hata siku moja.” “Kwa nini unasema hivyo?” “Nimeona hati ya nyumba T. Umeandika jina la Junior, wala sio langu.” “Yaani unaingia mpaka kwenye Safe yangu ile ndogo!?” “Ndiyo, huwa naingia.” Mzee Masha akanyamaza.

“Tunasafiri kwa siku nne, nataka Ric akapumzike. Lakini Ric amemuomba Elvin, yule mtoto wa Mzee Mwasha, tuende naye safari.” Mzee Mwasha alinyamaza. “Umenisikia?” “Na mimi?” “Huwezi kuja T. Elvin akikuona?” “Basi na yeye asiende.” “Wewe unajua siwezi kumkatalia Ric, kitu chochote.” “Katika hili itabidi uweze tu, Bella.” “Labda hujanielewa. Nimekwambia SITAMWAMBIA Ric hapana.” Bella aligomba tena kidogo. “Huyu mtoto hana baba, wala mama, halafu leo amepata rafiki anataka kwenda nae mapumzikoni, nimwambie hapana. Nitampa sababu gani?” “Tafuta sababu yeyote Bella.” “Sitafanya hivyo T. Mimi nipo na wewe wakati wote. Nina mwezi mmoja tu wakupumzika na mdogo wangu, nao huo pia unataka kuumiliki!? Katika hilo hapana. Nisubiri mpaka nitakapo rudi.” “Hivi unajua nimeacha familia yangu ili nije kuwa na wewe Bella?” “Basi rudi huko kwa familia yako, likizo ya Ric ikiisha ndipo na wewe urudi kwangu. Nimekwambia nimemkuta mtoto kwenye mateso, halafu unataka na mimi niendelee kumnyima raha? Kama wewe unavyowawazia familia yako mambo mema, ndivyo hivyohivyo na mimi ninavyomuwazia mdogo wangu mambo mema. Ulitaka nimpeleke kwenye shule ya bweni, ili uweze kunimiliki utakavyo, nikakubali na nikafanikiwa kumshawishi na yeye akakubali. Sasa hivi yupo likizo, pia hutaki niwe na mdogo wangu!? Nyumba uninyime,  unitenganishe na mdogo wangu karibu mwaka mzima, halafu  hata huu mwezi mmoja nao unataka pia uninyime raha na mdogo wangu! Haitakaa itokee T. Kama unampango wa kuniua, naona huu ndio utakuwa wakati wako mwafaka. Umesikia?” Mzee Masha alicheka kidogo. 

“Nani amekwambia nimekunyima nyumba, Bella?” “Mbona umeandika jina la mtoto wako na sio langu?” “Kwani tatizo liko wapi?” “Usinifanye mimi mtoto T. Naomba nikalale. Ila ujue nitasafiri.” “Nimeelewa mama.”  “Na ninakuomba T, usianze fujo zako. Naomba uniache nitulie na mdogo wangu, akiondoka nitarudi nyumbani. Tafadhali sana. Unanielewa?” “Si nimekwambia nimekuelewa Bella? Na nimekuruhusu kwa kuwa nina mwamini sana Elvin, nikijana mwenye maadili, vinginevyo nisingekuruhusu. Usije ukaja siku nyingine na mwanaume mwingine ukafikiri nitakuruhusu Bella. Ni Elvin tu.” “Mimi nakwenda kulala.” “Mtakwenda wapi?” “Sitakwambia T. Nakujua wewe huwezi kujizuia, lazima utanifuata. Sitakaa siku nyingi, nitarudi. Naomba unisubiri. Na usianze kunitumia watu wanifuatilie. Tafadhali T.” “Daah! Kweli umebadilika Bella.” “Naenda kulala T, usiku mwema.” Bella akakata simu.

***************************************************

Kesho yake wakati wa chakula cha mchana, alimuacha Eric na Elvin akaenda kukata tiketi ya ndege. Bella alikuwa na furaha sana, kuona ameweza kummudu Mzee Masha na amefanikiwa kumpa mdogo wake kitu anachokitaka, Elvin. Alijitahidi kuwahi kurudi ofisini, kabla muda wa kazi haujaisha. Alimkuta Eric na Elvin wapo pamoja. “Ric! Naomba ukanisubiri ofisini kwangu mara moja, nataka kuongea na Elvin.” Eric akatoka bila yakuuliza swali. 

“Vipi?” Elvin aliuliza mara baada ya Ric kutoka. “Nilitaka kuhakikisha kama bado unampango wa kusafiri na sisi, au ulibadili mawazo.” Elvin aimwangalia Bella vizuri. “Naomba uwe mkweli Bella, ni kweli unataka niende au hutaki?” “Nataka twende wote Elvin.” “Sasa mbona una wasiwasi?” “Sina wasiwasi, nilitaka uhakika tu.” “Ni juzi tu umeniuliza swali hilo hilo, na leo tena! Vipi?” Bella alinyamaza kidogo akatoa zile tiketi. “Nimeshakata tiketi zetu wote, hizi hapa. Nilitaka tu uhakika Elvin, sikutaka kumwambia Ric, akafurahia, kumbe ukawa umebadili mawazo.” Elvin alibasamu kidogo. “Nitakwenda Bella, na nilipanga mimi ndio nilipie tiketi.” “Basi wakati mwingine utafanya hivyo. Asante Elvin.” Bella ni kama aliwaza kidogo. Kisha akakaa.

“Ni kweli nakushukuru, Elvin. Unaweza usijue kitu unachofanya sasa hivi, lakini kina maana kubwa sana kwangu na Ric. Baada ya mama kufariki, nimekuwa nikimlea Eric mimi mwenyewe, nikisaidiana na kaka Mat tu. Kaka Mat, alikuwa dereva wetu wakutokea zamani. Lakini kwa Ric ni zaidi ya dereva, amezaliwa akamkuta Mat. Amekuzwa na kaka Mat. Ndiye aliyekuwa anampeleka shule tokea mtoto. Hata alipokuwa akiumwa au akilazwa hospitalini, kaka Mat ndiye aliyekuwepo kusaidia kumuuguza. Ndiye aliyemfundisha kucheza mpira, kuendesha baiskeli na mambo mengine mengi hata kupiga kinanda na gitaa, yeye ndiye alimfundisha. Alikuwa akienda naye kanisani kwao siku za mafundisho ya kwaya. Alifanya mpaka mama akatununulia kinanda hapo nyumbani. Yeye Kaka Mat, akawa anatufundisha. Ric hajui kama ni dereva, anajua ni kama ndugu kwa vile alivyokuwa akiishi na mama. Na walikuwa marafiki sana na Ric. Tulimuhesabu kama ndugu kabisa, lakini na yeye ameoa, nafikiri mkewe ameshindwa kutupokea. Wakati ule naumwa, nilishindwa kwenda kumchukua Ric. Sikutaka anione nikiwa nimeharibika mwili vile, nikamuomba Kaka Mat akae naye kwa muda mpaka nipone kabisa. Lakini Kaka Mat, amebadilika sana, na mkewe amekuwa mkali sana kwake. Sasa haya mabadiliko ya kaka Mat ya gafla yanazidi kumuogopesha. Ric ana upendo sana, na hapendi kumuudhi mtu.” “Nimemuona. Ni mtoto wa tofauti.” Elvin aliongeza. Bella alitabasamu. 

“Sasa akisikia au kumuona mtu anamchukia au kumfanyia ubaya wowote, anaumia sana. Anazidi kuamini kuwa watu hawatupendi, wanatuchukia. Maana alishawasikia hata ndugu zake mama kipindi cha msiba wakitusema vibaya sana na zaidi walitukana mbele za watu. Hawakutaka kutuchukua wakatuacha pale pale kijijini tulipokwenda kumzika mama. Baada ya mateso ya pale tulipokuwa tumeachwa peke yetu kijijini kuwa makali sana, tukaamua kurudi huku mjini kwenye nyumba tuliyokuwa tukiishi na mama, kabla hajafariki. IIikuwa ni nyumba ya kupanga. Tulifika hapo usiku sana, tukiwa na njaa na hatujui pakulala. Tulikuta hiyo nyumba ilishapata mpangaji mwingine na vitu vyetu vyote vimeuzwaNilimuomba huyo mama tuliyemkuta, angalau atupe chakula cha Ric tu
, lakini alikataa na kutufukuza pale, tukaenda kukaa nje ya geti, mbu walikuwa wakitung’ata, na Ric alikuwa akisikia wakati namuombea chakula. Anamaumivu mengi sana moyoni, amekuwa akishuhudia mambo ambayo yeye hawezi kumfanyia mtu, tukifanyiwa sisi. Na…” Bella alifuta machozi.
“Sasa kwa wewe kumkubali hivi, ndio maana anakuganda kila mahali. Anaogopa anaona tutaishia kuwa peke yetu tu, na anajua ni kama tumempoteza Kaka Mat, kwa hiyo anakutaka wewe. Lakini nakuomba kitu kimoja Elvin.” Elvin aliwahurumia sana. “Naomba wakati mwingine Ric atakapokuomba ufanye kitu, sio lazima ukakubali. Usijilazimishe kabisa kufanya kitu usichotaka, lakini naomba kama haupo tayari, uwe unamwambia hivinitafikiria, halafu nitakupa jibu baadaye’halafu mimi mwenyewe nitajua jinsi yakumueleweshakuliko kumkatalia moja kwa moja au wewe kujiona unawajibika kumkubalia kila kitu. Bado ana akili za kitoto. Haelewi majukumu ya kazi, au hajui kama wewe una mchumba wako, na ni lazima wakati mwingine mkubaliane na mwenzako kwanza. Mimi ninaelewa, kwa hiyo nitamsaidia taratibu mpaka ataelewa maisha yakoje. Lakini naomba usimkubalie halafu ukashindwa kumtimizia, anaumia sana na nisingependa aendelee kuumizwa.” Elvin alikuwa kimya kabisa akitafakari. “Nimeelewa Bella. Lakini nina maswali mengi sana, natamani unipe majibu yake.” Bella alitabasamu kinyonge. “Nafahamu hilo, Elvin. Nakuahidi ipo siku nitayajibu yote, lakini isiwe leo tafadhali. Leo naomba nikuachie tiketi yako tu.” Bella aliiweka pale mezani na kutoka pale ofisini kwa Elvin akimuacha na maswali yake.

************************************************

Ilikuwa siku ya alhamis na walipanga kusafiri siku ya Ijumaa. Ndege yao ilikuwa ikiondoka saa tano na nusu asubuhi. Kwa kuwa siku ya saba saba ilikuwa jumatatu, walipanga kukaa huko kwa siku tatu ya nne ndipo warudi. Ric alikuwa anafuraha sana. Alikuwa akimsimulia Elvin vitu wanavyofanya na Bella wakiwa mapumzikoni. “Huwa tunaenda kucheza volleyball baharini na Bella. Usimuone Bella hivyo, anajua sana kucheza mpira wa Volleyball, sijawahi kumfunga. Ila hajui basketball.” “We Ric! Si kwa kuwa nakuhurumia, nakuacha ufunge tu? Angalau upate sifa kwenye mchezo mmoja?” Elvin alikuwa akicheka.  Eric aliinama kumnong’oneza kitu Elvin. Muongo, hajui kucheza basketball. Tukifika huko wakati wa kucheza Volleyball unichague mimi uwe upande wangu ili tumfunge.”  “Haaa!” Bella alishangaa. “Told you! You’re a bad whisperer. Muone hujui kunong’ona.” “Kwani umesikia Bella?” “Kumbe!? Nimesikia njama zako zote. Na hiyo ni rushwa Ric.” Wote walikuwa wakicheka sana. “Na ujue mimi nipo vizuri sana, hata ukimkodisha ‘Ivan Zaytsev’ awe kwenye timu yako, nitawafunga tu.” Bella aliongeza kwa kujigamba kidogo.

Bella alikuwa mchezaji mzuri sana wa volleyball. Hata wakati yupo shuleni walimtegemea kwenye timu yao. Na wakati wote alitamani kumfikia Ivan Zaytsev, kijana mashuhuri sana kutoka Russia, aliyenunuliwa kwenye timu ya Itali kwa pesa nyingi sana. Bella alikuwa akijifananisha naye, na alisema siku moja na yeye atakwenda kushindana kwenye mashindano ya Dunia, na atakuwa na jina kubwa kama Ivan. Wote walikuwa kwenye wakati mzuri sana.

************************************************

Walikuwa wakila jikoni, pale pale ofisini siku hiyo ya alhamis. Vilitawala vicheko kati yao. Wafanyakazi wengine waliingia kuchukua vitu vyao kwenye friji na kutoka, na kuwaacha wao wakiongea. Kila mtu alishangaa kumuona Bella amekaa  akiongea na kucheka kwa sauti kiasi kile. Walishamzoea akifika kazini, akishaingia ofisini kwake hatoki mpaka jioni anapoondoka, au labda awe ameitwa kwenye kitengo fulani kufanya kazi. Alikuwa mtundu sana wa kompyuta, kwa hiyo kazi zote za vitengo vyote alikuwa na uwezo wa kuziona kwenye kompyuta yake, ofisini kwake.

Mlango wa jikoni ulifunguliwa na Irene aliingia akiwa na tiketi ya ndege mkononi. “Nimekuta hii tiketi mezani kwako, inaonyesha unasafiri kesho. Mbona mimi sina taarifa?” “Ndio maana nilikutumia ujumbe jana nikakuomba tuonane, ukasema kunamahali unaenda hatutaweza kuonana ile jana. Na leo nimekupigia simu, ukasema upo mahali huwezi kuongea. Nikakwambia ni lazima leo tuonane. Nilitaka tuzungumzie juu ya hii safari.” Elvin alijibu akionyesha ametulia kabisa usoni. “Unaenda wapi?” Irene akauliza tena. “Tunaweza kwenda kuongea ofisini kwangu?” “Kwani ni siri?” Irene aliuliza kwa ujeuri kidogo. “Sio siri, lakini naomba tukazungumzie ofisini kwangu.” Irene alibaki amesimama kwa muda, mwishowe akavuta kiti akakaa. “Mimi sioni tofauti ya ofisini na hapa. Wewe nielezee tu.” Bella aliamua kusimama. “Twende Ric.” Ric na Bella walitoka ili kuwapa nafasi.

Bella na Eric waliingia ofisini kwa Bella. “Usiogope Ric, kila kitu kitakuwa sawa. Umesikia?” Ric aliinama kwenye kompyuta yake na yeye akiwa kimya kabisa. Baada ya muda walisikia Irene akigomba huku anapiga meza. Gafla akatoka nakuingia ofisini kwa Bella. “Nilishakwambia Elvin ni mchumba wangu. Unawezaje kwenda na mchumba wa mtu mapumzikoni? Huoni aibu? Hujafundwa kwenu?” Wakati Irene anagomba, Elvin akaingia. “Tafadhali Irene, naomba usifanye hivyo. Please.” Irene alitoa simu. “Ngoja tuwaulize wazazi wetu kama ni sawa. Huwezi kunichezea akili Elvin. Wewe ukisikia mimi nimesafiri na mwanaume mwengine ungefurahi?” “Irene please. Naomba acha kufanya fujo zisizo na maana. Mbona wewe ulikuwa ukisafiri na kina Junior mimi sikuwa nikikasirika? Kwa kuwa nakuamini.” “Huwezi kumfananisha Junior na huyu msichana. Junior ni mmoja wetu, huyu hatumfahamu kabisa. Hata wazazi wake hutuwajui na wala hujui maadili yake. Kama ni msichana mwenye tabia ya kuiba wanaume za watu, je?” Moyo wa Bella ulishtuka sana, alibaki kimya. 

“Ukute yeye ndio anamtuma mdogo wake.” Irene alikuwa akiongea kwa sauti, mpaka wafanyakazi wengine walianza kutoka maofisini kwao nakuja kuangalia kulikoni. Irene alitoa simu palepale na kuanza kumpigia simu mama yake Elvin, akamueleza kwa kifupi, kisha akampigia na baba yake. Baada ya muda mfupi alishapigia simu watu zaidi ya wanne. Elvin alibaki akimtizama. Bella na Eric walikuwa wameinamia kompyuta zao.

Bella alipoona mambo yanakuwa mabaya, akaamua kumuandikia pale pale barua pepe, {email}, Elvin bosi wake, kuomba siku ya kesho asije kazini kabisa. Walikuwa wamekubaliana siku ya kesho, Ijumaa, wafike hapo kazini wakiwa na mabegi yao tayari kwa safari. Yaani wafanye kazi mpaka muda wakwenda uwanja wa ndege, ndipo waondoke pamoja. Alipomaliza kuiandika, na kuituma,  Bella alifunga kompyuta yake, akaweka vitu sawa pale mezani, akamgeukia Eric. “Twende Ric.” Ric akasimama, akakusanya vitu vyake vyote, na laptop yake, wakatoka na Bella na kuwaacha Elvin na Irene ofisini kwake, Bella. Kila mtu alikuwa akiwashangaa.

************************************************

Bella alishindwa aongee nini na Ric. Walirudi nyumbani/hotelini kwao wote wakiwa kimya kabisa. Bella alishachukua vyumba viwili huko waendako, cha Elvin na chake yeye na Ric. “Unataka twende tukaogelee?” Bella akamuuliza Ric, aliyekuwa kimya kabisa akicheza game yake kwenye kompyuta yake. “Naona huu ndio muda mzuri kama unataka kuogelea. Jua litaisha, halafu kutakuwa baridi, haitakuwa raha tena kuogelea. Twende sasa hivi.” “Na leo tunashindana kama jana?” Bella alicheka. “Hujachoka kushindwa?” “Bella wewe!” Eric alianza kucheka. “Wakati mimi ndio nilishinda!” “Mimi naona unaanza kupoteza kumbukumbu Ric. Jana nilikushinda. Twende leo nikakuonyeshe jinsi nilivyokuwa hodari. Utaingia aibu.” “Twende Bella. Tukaone nani anaingia aibu.” Hawakutaka kuzungumzia ule mkasa wa ofisini kabisa. Walikaa kwenye maji wakikumbushana mambo yao yaliyowafanya wacheke sana. Walikula huko huko kwenye Pool mpaka ilipofika usiku sana wakarudi kulala.

Wakati wanalala, Eric alimwita dada yake. “Hey Bella?” “Yes.” “Are we gonna have fun there?” “Like always. Usiwe na wasiwasi Ric. Tutakuwa na wakati mzuri sana. Cha muhimu ni mimi na wewe tuwe pamoja. Maadamu wewe upo, nina uhakika mimi nitakuwa na wakati mzuri sana. Sijui wewe?” “Nakupenda Bella.” “I know, Ric.” Walikaa kimya kwa muda. “Unafikiri Elvin atakuja?” Eric akauliza tena. “Sijui Ric. Lakini ujue Elvin ana majukumu mengi sana. Wakati mwingine inakuwa ngumu hata yeye mwenyewe kupata muda wake binafsi. Lakini naamini ingewezekana, angeweza kuja.” Ric akatulia kidogo. 

“Unafikiri Elvin anatupenda?” Bella alibaki akifikiria, alijua Ric ameumia. Alihamia kitandani kwake na kujisogeza karibu yake. “Sikiliza Ric, ninachojua Elvin ni mtu mzuri sana. Anapenda kusaidia kila mtu, na asingependa kukuumiza. Lakini wakati mwingine katika maisha, inakulazimu kuweka familia mbele. Kwa mfano mimi, inapokuja katika swala la kuchagua, hata iweje, hata kama mtu mwingine ataumia, au hata kama itanilazimu mimi kuumia, ni lazima nitakuchagua wewe kwanza. Kila kitu kinakuja kwenye maisha yangu baada ya wewe, Ric. Ndivyo ilivyo hata kwake Elvin. Lazima amchague mchumba wake kwanza, kwa kuwa ndiye mtu wa muhimu sana katika maisha yake, lakini haimaanishi anachukia watu wengine. Ila ni kwa kuwa lazima kuweka familia kwanza. Sijui umeelewa?” “Nimeelewa Bella. Na mimi ninakuweka wewe kwanza. Wewe kwanza halafu wengine baadaye.” Bella alianza kucheka. “Sasa hapo inamaanisha unachukia watu wengine?” “Hapana Bella. Familia kwanza.” Waliendelea kucheka. “Sina usingizi Bella. Unataka tucheze ‘game’ kwenye kompyuta yangu?” “Sawa.” Walichukua kompyuta ya Ric wakaanza kushindana kucheza, karibu usiku kucha mpaka panakaribia kupambazuka ndipo walipo lala.

“Mkasa wa Irene.”
Huku nyuma Irene alifanya fujo zakutosha, mpaka Mzee Mwasha akaja pale ofisini. Alimkuta Irene akigomba sana, na Elvin yupo kimya akimsikiliza. “Naombeni tuzungumze ofisini kwangu.” Mzee Mwasha aliingia nao ofisini. “Haiwezekani Mzee Mwasha. Elvin anakitu na yule Bella. Nimeambiwa siku hizi wanakula wote chakula hapa ofisini, na leo anataka kwenda nao mapumzikoni! Maana yake nini? Elvin ni mchumba wangu mimi, au tuseme anakaribia kunichumbia. Inakuaje anatoka na wasichana wengine?” Bado Irene alikuwa akigomba sana. Alikuwa akiongea bila kunyamaza, Elvin na baba yake walikuwa kimya kabisa wakimsikiliza. Alielezea mambo mengi sana juu ya uhusiano wao, jinsi Elvin anavyoonekana kutokumthamini. Simu ambazo hakuwa hajibu kwa wakati, mpaka baba yake alipokuja pale ofisini. Irene alianza kulia kwa baba yake, huku akiongea kwa kulalamika sana. Elvin alikuwa kimya kabisa akisikiliza tuhuma zote.

************************************************

Irene alikuwa mtoto wa Mzee Banda, mmoja wa wazee kwenye kundi lakina Mzee Mwasha. Ni watoto waliokuwa wamekuzwa pamoja. Malezi yao yakifahari, huku wakiigiza uzungu mwingi na kupewa kila wanachotaka. Tokea watoto Irene na Elvin walikuwa ni marafiki wakawaida tu, mpaka baadaye walipokuwa wameshakuwa wakubwa tena Elvin akiwa anakaribia kumaliza chuo, ndipo walipoanza mahusiano ya kimapenzi. Wazazi walijua, na hakikuwa kitu cha ajabu kwani wazee hao walishazoea na kufurahia jinsi watoto wao walivyokuwa wakioana. Tabia za Irene za kudeka na kutaka kumiliki kila mtu, Elvin alizijua lakini alijiambia atakuja kubadilika. Irene alipenda atambuliwe na kuheshimiwa kila alipo. 

************************************************

“Hukufanya vizuri Elvin. Unawezaje kusafiri bila kumtaarifu mwenzako?” Mzee Mwasha alimgeuki kijana wake. “Hapana Mzee Mwasha, hapo unakosea. Ukisema bila kumtaarifu Irene tu, inamaanisha unaidhinisha Elvin asafiri na msichana mwingine na sio Irene! Kama ni mapumziko, kwa nini asisafiri na Irene?” Mzee Banda aliingilia. “Kweli daddy. Kama anataka kupumzika kwa nini asiende kupumzika na mimi?” Aliendelea kuongea Irene na baba yake akimuunga mkono, huku Elvin mtuhumiwa akiwa hajapewa nafasi yakujitetea hata mara moja. Mzee Mwasha naye alikuwa kimya kabisa akiwasikiliza mpaka walipomaliza na kuanza kumpa Elvin masharti huku wakimtaka Bella afukuzwe pale kazini. Elvin alicheka kidogo.

“Umenielewa Elvin? Huyu dada lazima afukuzwe kazi.” “Siwezi kumfukuza kazi Bella. Anahitajika sana hapa kazini.” Elvin alijibu taratibu tu. “Anahitajika au wewe ndio unamuhitaji?” Irene akauliza kwa jazba. “Ni kweli Bella anahitajika sana hapa kazini. Hakuna jinsi tukamfukuza labda aamue kuacha kazi yeye mwenyewe.” Mzee Mwasha aliongeza. Umeona daddy? Hata baba yake anamtetea?” Irene alianza kulia.

Unajua Irene unanishangaza sana wewe! Unajua msimamo wangu jinsi ulivyo. Mimi siwezi kwenda mapumzikoni na wewe, kwa kuwa najua mwisho wake utakuaje.” Elvin alijibu. “Kama unahofia mapenzi, kwa nini sasa unakwenda na Bella?” “Siendi na Bella, kama Bella. Nimekwambia mdogo wake ndiye aliyeomba niende nao.” “Muongo Elvin. Kuna kitu anaficha.” Irene alijibu tena. “Kati yangu mimi na wewe nani nimuongo, Irene? Unafikiri sijui uliyofanya na Phil wakati mmesafiri na kina Junior Masha?” Irene alitulia. “Mimi nilikuamini, ukasafiri nao, lakini ulifanya uchafu ambao hukutaka nije niambiwe. Lakini nilikuja kuambiwa. Tena Phil alikuja kuomba msamaha yeye mwenyewe, akijitetea ni kwa kuwa alikuwa amelewa sana siku ile, akawa hajitambui. Nilikuacha makusudi bila kukuuliza. Nikijua labda siku moja ungeona uliyofanya ni mabaya na kuja kukiri kwangu, lakini naona hujali, na unaendelea kunidhalilisha mbele za watu na wafanyakazi wetu. Umenitia aibu mbele za watu, wakati unanijua kabisa, au kila mtu anajua msimamo wangu. Nilikuapia Irene, hata wewe sitakugusa mpaka ndoa. Inakuaje leo unafanya fujo kwa Bella, msichana mgeni kabisa hapa, simfahamu, humfahamu! Umeishi na mimi muda wote huo, umeshawahi kusikia nimekuwa na mahusiano ya kimapenzi na msichana mwingine yeyote?” Elvin akamuuliza.

“Umeshafikiria maisha yetu ya ndoa yatakuaje kama tukiishi kwa kutokuaminiana kwa kiasi hiki!? Mimi nilikuamini nikakuruhusu usafiri na wavulana, nikijua utajiheshimu na kuishi ulichoniahidi. Lakini umefanya tofauti, na bado hukuja kuniambia. Halafu bila hofu leo unaona nipo nakula na watu, tena hadharani, unaleta fujo za namna hii! Umepiga simu kila mahali kwa tuhuma zisizo za maana. Huogopi? Hivi unajua mimi ni kiongozi wao hapa ofisini? Unanidhalilisha kwa tuhuma za uongo, mbele ya watu ninaowaongoza tena na mfanyakazi wa humu humu ndani wanaemtegemea awasaidie kikazi! Unategemea kesho akirudi hapa ofisini anafanyaje kazi na wenzake?” Elvin alifunga mdomo kila mtu.

Sasa na mimi nakupa sharti moja. Usinitafute kwanza mpaka nitakapo kutafuta. Naomba upate muda wa kufikiria, kabla hatujaingia kwenye hatua nyingine ya mahusiano yetu. Inawezekana unampenda Phil kuliko mimi.” “Nakupenda Elvin.” “Naomba usiniambie sasa hivi. Nenda, pata muda wakutosha, fikiria, nitakapokutafuta, tutaongea.” “Nimeshafikiria. Nimekuchagua wewe.” “Sio kweli Irene. Ungekuwa unanipenda kwa dhati, ungeniambia uchafu uliofanya na Phil, lakini umeficha, ishara ya kwamba utakuja kurudia tena.” “Hapana Elvin.” “Basi kama wewe ulipata muda wakufikiria, basi mimi nahitaji muda. Nipe muda, nitakutafuta. Nipo katika wakati mgumu sana hapa kazini, nahitaji msaada ambao ni Bella peke yake ameonekana anaweza kuutoa, tena kwa gharama ya chini. Tukiendelea hivi mimi na wewe, tutazidi kuwachanganya wafanyakazi hapa kazini, mwishowe na hii biashara itanishinda. Nahitaji muda Irene.” “Nitabadilika Elvin.” Irene aliendelea kung’ang’ania.

“Mimi naona kitu alichoongea Elvin ni cha msingi sana. Unahitaji muda wakufikiria Irene. Ndoa sio kitu cha kuchezea. Mnaweza kuja kujuta sana baadaye.” Mzee Mwasha aliingilia. “Kama hatanioa Elvin, ni afadhali kufa.” “Hayo ndio mambo nilikuwa nikizungumzia Irene. Wakati wote unataka mambo yaende unavyotaka wewe, hutaki namimi nishauri kitu katika mahusiano yetu. Sijakwambia tunaachana, nimekwambia tupate muda wakufikiria.” Irene alinyanyuka. “Najua yote hayo amesababisha Bella. Ulikuwa tayari kusamehe yote, mpaka alipokuja Bella.” Elvin alitingisha kichwa kwa kusikitika. “Sidhani kama utabadilika Irene. Wakati wote unatafuta mtu wa kulaumu na hutaki kuwajibika kwa makosa yako mwenyewe.” Irene alitoka na baba yake akamfuata nyuma.

“Samahani sana baba. Najua nimeharibu leo.” “Hapana, lakini nataka uniambie ukweli Elvin. Unampenda Bella?” Elvin alikunja uso. “Hapana baba, sio kimapenzi.” “Nimekuona jinsi ulivyohangaika wakati alipolazwa.” “Bella ni mfanyakazi wetu baba, sikujua natakiwa nifanyaje wakati alikuwa na matatizo. Hana ndugu, na alihitaji msaada. Umesahahu jinsi alivyojitolea kwenye hii kampuni? Nafikiri haikuwa vibaya kumuonyesha na sisi tunamjali. Na nimekubali kusafiri nao, kwa sababu ya mdogo wake. Alikuwa karibu sana na mimi hizi siku mbili tatu alizokuwa hapa kazini. Aliponiomba nisafiri nao, sikuona tatizo, kwa kuwa ni kweli nahitaji mapumziko baba. Nimekuwa na kazi nyingi mfululizo na Irene yupo kila mahali. Sipumui baba. Sina raha, kila kitu anataka iwe yeye. Na leo sio mara ya kwanza, hataki niongee na mtu wala niwe na mtu yeyote ila yeye tu. Lakini yeye anataka awe huru na kila mtu, na mimi nisiingilieNa kila ninapomuhusisha kwenye mambo yangu au kumkaribisha kwa marafiki zangu, nashindwa hata kuongea na wenzangu. Anataka niwe naongea na yeye tu, au atataka watu wote wamsikilize yeye, wakati wewe unajua aina ya marafiki zangu baba. Ni watu na heshima zao. Nahitaji kupumzika. Na wala hutahitaji kuja kazini, nitaondoka hizi siku za sikukuu, jumanne nitakuwepo kazini.” “Ni kweli tumekusahau Elvin, na wewe unahitaji mapumziko. Akili zangu zote zimekuwa kwa mama yako, tukakusahau wewe. Kwa kuwa sasa hivi anaendelea vizuri, unaweza kuchukua hata siku kumi, mimi nitakuwepo hapa kazini.” “Asante.” Kila mtu aliondoka pale ofisini, lakini Elvin alibaki ofisini kwake akifikiria.

************************************************

Maneno machafu aliyokuwa akitupiwa Bella na Irene, yalianza kujirudia kichwani kwa Elvin. Alizidi kuumia, alizunguka ofisi nzima akikumbuka hili na kutamani Irene asingesema lile mbele ya Eric. Aliingia jikoni, akatoka. Akaingia ofisi za masoko asijue ni nini kilimpeleka huko. Alizunguka huku sura ya Eric ikimjia jinsi alivyoonekana kuumia mpaka usoni. Aliamua kurudi ofisini kwake angalau awapigie simu Bella na mdogo wake angalau aombe radhi, lakini wakati yupo mlangoni alisikia simu yake ikiita. Aliingia na kuichukua simu, kutoka mezani. Alikuwa dada yake Irene. Elvin aliiangalia kwa muda kisha akapokea. “Irene amekimbizwa hospitali amekunywa sumu.” Elvin alibaki kimya. “We Elvin, umesikia?” “Amepelekwa hospitali gani?” Alipoambiwa, alijibu kwa kifupi. “Nakuja.” Kisha akakata simu. Elvin alifikiria, akaamua kukaa. Alijua michezo ya Irene, alijua tu anataka ‘attention’. 

Akaamua kuwapigia simu wazazi wake kuwataarifu. 
“Hivi na sisi tupo njiani tunaelekea huko hospitalini. Mama yake ametupigia simu alikuwa analia sana. Nahisi hali yake ni mbaya sana.” Mama yake Elvin alimjibu, akisikika anawasiwasi sana“Na mimi nitakuja huko muda si mrefu, ngoja nifunge ofisi.” Elvin alifunga ofisi, akaelekea hospitalini.

Elvin alifika hospitalini akakuta wazazi wa familia zote wapo hapo na baadhi ya watoto wa familia zote wako hapo. Kila mtu alikuwa akimtizama Elvin wakati anaingia, akajua tayari maneno yameshaanza kuenea. Alisogea mpaka alipokuwa amesimama baba yake Irene, Mzee Banda. Alionekana na wasiwasi sana. “Vipi anaendeleaje?” “Ndio yupo humo ndani na madaktari, wanajaribu kuokoa maisha yake.” Mama yake Irene alikuwa akilia sana. “Poleni sana. Naamini atapona.” Kila mtu alibaki akimwangalia yeye. Alikumbuka simu alizokuwa akipiga Irene wakati amekasirika akiwa pale ofisini kwake, akajua kila mtu anataarifa za yeye kutaka kwenda mapumzikoni na Enabella. Akaamua anyamaze tu, kwani alijua hata angeeleza ukweli isinge saidia kitu. 

Mama yake akamsogelea. “Pole na kazi.” Elvin alishukuru Mungu, maana alikuwa ni kama ametegwa. “Asante mama. Vipi na wewe? Unajisikiaje?” “Leo nimeshinda nimelala tu. Najisikia vizuri.” Wakati wanaongea, kaka yake Elvin naye akaingia. “Vipi Dogo?” “Shikamoo.” “Marahaba. Poleni bwana. Mimi ndio nimepata taarifa sasa hivi, wife yupo njiani na yeye anakuja. Vipi anaendeleaje?” “Ndio madaktari wanahangaika humo ndani, naamini kila kitu kitaenda sawa.” Alimgeukia mama yake. “Shikamoo mama.” “Mbona midomo imekukauka hivyo!? Umekula kweli wewe?” Mama Mwasha alimuuliza mwanae mkubwa. “Mambo yalikuwa mengi, sijala. Nitakula baadaye nikifika nyumbani.” Mama Mwasha aliendelea kuongea na wanae mpaka daktari alipotoka kuongea nao.

“Anaendeleaje?” Baba yake alisimama kwa haraka nakuuliza. “Anaonekana hakuna sumu iliyokuwa imeingia tumboni. Mlimtapisha kabla yakuja hapa?” Daktari akauliza. “Hapana.” “Basi nafikiri ni wasiwasi tu, vipimo vyote vinaonyesha hakuna sumu yeyote mwilini mwake.” Watu walibaki wakiangaliana, lakini Elvin alijua kabisa jinsi Irene anavyojipenda, asingethubutu kujiua. Alichotaka nikushtua tu watu. Mama yake aliomba wakamuone. 

“Kwani nyinyi, ni nani aliwaambia amekunywa sumu?” 
Mama Mwasha aliuliza. “Mimi nilikuta kikaratasi alichokuwa amekiandika, ni bora afe kuliko kumkosa Elvin, na yeye alikuwa amelala na kujifunika shuka mpaka kichwani.” Msichana wa kazi alijibu, kwa kuwa wazazi wa Irene na ndugu zake walikuwa wameingia ndani kumuona Irene. Wengine walianza kucheka kimya kimya.

“Mama! Mimi naomba utaniagia kwa Mzee Banda, nimechoka nataka nikalale.” Kaka yake Elvin akaondoka, na watu wengine nao wakaanza kuondoka bila hata kuingia ndani na kumtizama huyo mgonjwa aliyewashutua sana. Wote wakaondoka mpaka Elvin akajikuta amebaki peke yake pale nje, akimfikiria Irene. Kwa vipimo vyote alivyokuwa amefanyiwa Irene, mpaka kulipia matibabu, na daktari kupata muda wa kuongea kidogo na wazizi wa Irene na Irene mwenyewe kwa ushauri, walijikuta wanaondoka hospitalini hapo asubuhi. Na Elvin naye kama mchumba mtarajiwa ilibidi abaki nao pale mpaka walipo ruhusiwa. 

************************************************

Bella na mdogo wake walifika uwanja wa ndege mapema kabisa. Walikaa pale wakisubiri muda wao wakuondoka ufike, huku Eric akiamini Elvin atakuja tu. Bella alikuwa akimwangalia vile anavyozunguka pale nje akifikiria labda angemuona Elvin, akamuhurumia sana mdogo wake, asijue chakufanya. “Unafikiri Elvin atakuja?” “Naomba uje ukae hapa, Ric.” Eric alikwenda kukaa pembeni ya dada yake. “Unakumbuka nilikwambia Elvin anakuwa na mambo mengi?” Eric alinyamaza. “Najua angeweza, angekuja.” “Lakini alituahidi kuwa atakuja.” “Lakini si umeona jinsi familia yake wanavyomuhitaji? Kumbuka Ric, familia kwanza.” “Kwa hiyo sisi hatuna familia? Mbona hakuna mtu anayetuweka sisi kwanza?” “Mimi nakuweka  wewe kwanza, Ric. Wewe ni familia yangu.” “Hapana Bella. Unajua ni nini namaanisha. Unakumbuka ndugu zake mama? Kumbuka kaka Mat. Hakuna mtu anayetuweka sisi kwanza.” Bella aliishiwa maneno. Muda wa kupanda ndege ulifika, ndege ikaondoka, Ric asiamini kama kweli wanaondoka jijini Dar bila Elvin.

Bella alikodisha vyumba viwili vizuri sana kwenye hoteli hiyo ya Malaika Beach Resort, iliyojengwa ndani kidogo ya Ziwa Victoria. Ilikuwa ni hoteli nzuri na ya kitalii. Hata muonekano wake tu, ungejua binti huyo alimwaga mapesa yakutosha ili kumfurahisha tu mdogo wake, ambaye tayari alishaonekana kupoteza ladha ya kuwepo kwenye madhari ile.

Walifika mapokezi Bella akijitambulisha ili kupata funguo za chumba kimoja na kurudisha cha pili ambacho alikikodi maalumu kwa ajili ya Elvin huku mdogo wake akiwa amegeukia mlangoni bado akiamini Elvin anaweza kuingia wakati wowote ule. Bella alimalizana na muhudumu, akapewa funguo za chumbani kwao, huku akisaidiwa na muhudumu mwingine kubeba mizigo yao kuingiza ndani. Eric bado hakuwa na taarifa na kinachoendelea, kwani macho na akili zake zilikuwa zikisubiri mtu yeyote anaeingia hapo huenda akawa ni Elvin.

Bella alisimama akimtizam kwa muda, akamuhurumia sana. "Ric! We Ric!" "Namsubiri Elvin." Bella alivuta pumzi kwa nguvu akazishusha. "Naomba twende kwenye chumba chetu, kama Elvin atakuja, watu wa mapokezi watatupigia simu. Twende angalau tukapumzike." "Mbona unamkatia tamaa mapema, Bella? Tungemsubiri. Elvin atakuja." "Sijamkatia tamaa, ila sioni sababu yakuendelea kukaa hapa mapokezi tukimsubiri. Naomba tuendelee na maisha yetu Ric. Kama atakuja sawa, asipokuja pia ni sawa. Au hutaki kuwa na mimi?" "Hapana Bella. Nafurahi kuwa na wewe." "Basi twende chumbani kwetu." Eric aliondoka pale huku akigeuka nyuma kila wakati.

Waliingia chumbani hapo akajitupa kwenye kochi bila hata kuzunguka na kuangalia madhari ya mle ndani chumbani kama kawaida yake ya kupenda kuchunguza kila sehemu mpya anayofika. Bella alimuomba yule muhudumu amsaidie kuingiza vitu vyote upande wa chumbani akarudi kukaa pembeni ya mdogo wake. “Tutakuwa na wakati mzuri Ric, naamini hivyo. Wakati wote tumekuwa na furaha tukiwa pamoja.” “Naamini hivyo Bella. Nataka nioge kwanza kabla yakulala.” “Nimebeba movie nzuri, tuangalie kabla ya kulala.” Ric akakubali. Wakaoga kisha wakapanda kitandani, na kuanza kuangalia movie yao. 

Movie ikiwa katikati walisikia mtu akigonga. “Umeagiza kitu mapokezi?” Bella alimuuliza mdogo wake. “Hapana.” Mlango uliendelea kugongwa. Bella akajua atakuwa Mzee Masha tu. Akasimama haraka ili yeye ndio awe wakwanza kufungua na kumkabili kabla Eric hajamuona.

Alipofungua mlango alibaki ametoa macho. Taratibu machozi yalianza kumtoka Bella huku ameziba mdomo wake kwa mikono yote miwili. “Are you okay Bella? Ni nani?” Eric alimuuliza dada yake baada ya kuona mlango umefunguliwa kisha pakawa kimya. “Bella?” Eric alirudia tena, lakini Bella alikuwa kwenye mshtuko ulimfanya ashindwe kuongea. Alijisogeza karibu kabisa na Elvin akiwa bado nje ya mlango akamkumbatia huku akilia. Eric alipoona kimya, akaamua kwenda kutizama, kwa kuwa Bella alichukua 'suit room'. chumba kilichokuwa na sebule kabisa kwa hiyo ilikuwa ngumu ukiwa chumbani kuona sebleni kwa urahisi. 

“Elvin!?” Eric alishtuka sana na yeye akasogea na kumkumbatia Elvin. Wote waliendelea kulia huku wamemkumbatia Elvin. Hawakutegemea kumuona Elvin pale, tena kwa wakati ule. Hata Eric mwenyewe alishakata tamaa, akajua Elvin hawezi kuja tena. Elvin alizidi kuwahurumia, na kuona alifanya vizuri kuja. Aliona ni kama watoto ambao wako wapweke. Walisimama pale nje kwa muda huku Bella akirudia rudia “Asante, Asante Elvin!” wakiwa wote bado wamemkumbatia Elvin pale pale nje. Mwishowe Bella alimpokea mizigo na kumkaribisha ndani. Walichukua muda kidogo, Bella na mdogo wake kutulia. Wote waliingia ndani, wakakaa kwenye makochi wakaendelea kulia, wasiamini kama kweli Elvin aliwafuata.

“Nilikusubiri sana uwanja wa ndege, mpaka ndege ilitaka kuniacha.” Eric alikuwa akifuta machozi huku akiongea. “Sikujua kama utakuja. Bella aliniambia familia yako inakuhitaji, na wakati wote katika maisha unaweka familia kwanza.” Eric aliendelea kuongea akiwa bado analia. “Nilikuahidi nitakuja Ric, nisingeacha kuja. Nilifika uwanja wa ndege nilikuwa nimechelewa sana, nikakuta ndege imeshaondoka, ikabidi nichukue ndege ndogo tu niliyokuwa nimeikuta pale uwanjani. Na kwa kuwa Bella alishaniambia hoteli tutakayofikia, haikuwa shida kuwapata. Nilipotua tu uwanja wa ndege wa hapa, nikachukua taksii, ikanileta mpaka hapa.” Bella bado alikuwa ameinama analia asiamini kitu Elvin alichofanya. Eric alimsogelea karibu dada yake na kumkumbatia. “Asante Elvin kwa kuja. Nimefurahi sana.” Eric aliendelea kushukuru.

“Mmekula? Mimi njaa inauma, sijala tokea kile chakula cha jana mchana tulichokula pale ofisini.” Elvin aliwaangalia Eric na Bella. “Na mimi njaa inauma.” “Ric! Wewe si nimekuuliza kama unataka kula, ukakataa!?” Bella alimshangaa mdogo wake. “Nilikuwa sina njaa, sasa hivi nataka kula na Elvin.” “Na mimi nataka kula.” Bella aliongeza. “Sasa mbona mmeshavaa nguo za kulalia?” Elvin akauliza. “Tulikuwa tunaangalia movie, kisha tulale.” Bella alijibu kinyonge kidogo. “Haiwezekani. Mapema hivi! Kavaeni nguo tukazunguke kutafuta chakula.” “Bella anaweza kuwapigia simu watuletee humuhumu chumbani.” Eric alijibu. “Hapana bwana. Itakuwa hamna maana ya kuja huku kwenye jiji kubwa hivi halafu tukaishia kujifungia humu ndani. Lazima tuzunguke na tupafahamu vizuri, ili tupate chakusimulia.“Yey…” Eric alianza kushangilia. 

Walirudi chumbani haraka, kila mmoja akabadili nguo, Bella alivaa gauni harakaharaka akatoka. “Hujachana nywele Bella!”  Eric alimuwahi dada yake wakati anatafuta viatu vyake avae. “Who cares?” Bella alijibu huku anacheka. “Bella!!” Eric alimshangaa dada yake huku akicheka. “Yupo sawa tu, twendeni.” Bella alifurahi kuona Elvin hana shida kutoka naye vile alivyo. Hata hivyo hakuna jinsi Bella akaonekana asivutie kumwangalia. Alikuwa na kila kitu kizuri, kinachofanya urudie kumwangalia tena na tena. Lakini angekuwa na Masha, asingeruhusu atoke vile hata kidogo. Wakati wote Masha alimtaka awe msafi na kila kitu mwilini mwake kimuwakilishe vizuri. Wakati wote Bella alikuwa na kucha zilizotengenezwa vizuri, nywele safi tena zilizotengenezwa kwa ufasaha, na mavazi nadhifu, yaani kila kitu chake kilitakiwa kiwe kizuri. Na alienda kutengeneza kwenye saluni zamaana, sio uswahilini.

Walitoka pale ndani, wote wakiwa na furaha sana. Walikodi gari ya hoteli ili iwapeleke mjini wakazurule, kwa kuwa ile hoteli ilikuwa imejitenga, mbali kabisa na makazi ya watu. Walishushwa katikati ya mji. Elvin aliwazungusha pale kwenye ule mji. “Unajua unapokuwa mbali na nyumbani, unatakiwa kuweka kumbukumbu. Na kufanya vitu vya ajabu, lakini vizuri kwa kuwa mpo ugenini hakuna anayewafahamu.” Elvin aliwaambia. “Kama mimi nimetoka bila kuchana nywele.” Wote walicheka. “Sasa leo tunaenda kula gengeni.” “Kweli Elvin!?” “Ndiyo.” “Ric hataumwa tumbo?”  Bella alianza kuwa na wasiwasi na mdogo wake. “Hakuna kuumwa. Mbona watu wanaenda kula kwa Mama Lishe na hawaumwi? Tena wanapika chakula kitamu sana. Twendeni tukakae pale pale tule. Hakuna anayetufahamu huku.” Elvin aliongeza. Wote wakakubaliana na wazo lake. Na kweli walizunguka wakitembea kwa miguu huku wakicheka na kutaniana, huku wakitafuta Mama Lishe mwenye nafasi ya kukaa wote watatu.

Wakakuta mmoja hajajaza watu wengi. “Kunanukia?” Eric alinong’ona, wote wakacheka. “Sharti la kwanza.” Elvin aliwaambia kabla hawajakaa. “Msiangalie wapi wanapohifadhi sahani zao. La pili, usingalie jikoni. Mnasubiri kupewa chakula chenu, unaangalia chakula chako tu, unaanza kula. Sawa?” Elvin alinong’ona, wote wakacheka na kuitikia, “Sawa.” “Haya twendeni tukakae tusubiri chakula.” Walikaa na kuanza kuongea bila hata kukumbuka wapi walipo. Walikula wakamaliza na kubaki wamekaa pale pale wakiongea na kucheka kwa muda mrefu sana, mpaka watu wote walipomaliza kula na wakataka kufunga biashara yao. Bella alipiga picha nyingi sana pale walipokuwa wamekaa. Walikodi tena taksii ikawarudisha tena hotelini.

Waliingia chumbani kwao wote wakiwa wamejawa vicheko. Walicheka hata vitu visivyo na maana. Walikuwa wakicheka mpaka machozi ya furaha yalikuwa yakiwatoka. “Nilijua hautakuja Elvin, nikarudisha chumba chako.” Bella alimgeukia Elvin mara walipokaa kwenye makochi. “Hamna shida. Kwa usiku huu naweza kulala kwenye kochi, kesho tutaenda kuchukua chumba kingine. Nitataka kuoga tu, ili nibadilishe hizi nguo. Kwa hiyo naomba ruhusa kutumia chumba chenu na bafu.” “Nilikuwa nina wazo. Kwa kuwa nyinyi mpo wawili, mlale hapo chumbani, mimi nilale kwenye kochi.” Bella alitoa hilo wazo. Kuwa Elvin na Eric wao ndio walale chumbani. “Naomba nikaoge kwanza halafu tutakuja kupanga vizuri.”

Elvin aliingiza mizigo yake chumbani, akaingia kuoga na kurudi akiwa amevaa tayari nguo za kulalia. “Ric zamu yako.” “Nilishaoga, Bella!” “Hapana, nenda ukaoge tena. Ulioga kabla hatujatoka. Sasa hivi utakuwa umechafuka. Tumetembea na kukimbia. Nenda kaoge.” “FINE.” Eric aliitikia kwa kutoridhika, akasimama kuelekea bafuni kuoga kama dada yake alivyomwambia. “Elvin!” Elvin alikuwa akiwaangalia wanavyoongea Bella na mdogo wake. Alitabasamu na kumgeukia Bella vizuri. “Asante sana kwa kuja. Ric alikuwa...” Bella alisita. “Nakushukuru sana, umeweza kufika.” Elvin alitabasamu tena. “Wenzetu huwa wanasema ‘Thanks for having ME’. Na mimi nimefurahi kuja Enabella. Nilihitaji kutoa mawazo yangu kutoka katika lile jiji la purukushani nyingi, angalau hapa tutapumzika kidogo.” Bella alicheka kidogo.

Walikaa kwenye kochi moja, kwa mara ya kwanza Bella alimuona Elvin akimwangalia kwa kutulia. Alimtizama Bella huku akifikiria. “Umeacha kila kitu sawa nyumbani?” Bella alijaribu kuvunja ukimya. “Sijui Bella. Ninachojua ni sasa hivi nipo hapa na nyinyi, na ninataka kuutumia huu muda vizuri, sitaki hata kusoma ujumbe kutoka sehemu yeyote ile.” “Na kazini!?” “Baba amenipa siku 10 zamapumziko. Yeye ndio atakuwa pale ofisini. Tukitoka hapa, nitarudi nyumbani, nilale tu na kumlea mama yangu kwa hizo siku zilizobaki ndipo nitarudi kazini. Sitaki kusikia kitu kingine chochote. Nataka kupumzika kabisa.” “Ni jambo zuri.” Eric alitoka.

We Ric! Umepaka sabuni kweli wewe!?” Bella alishangaa Eric ameshavaa nguo za kulalia na hakumaliza hata dakika tano. “Hukuniambia nipake sabuni, umeniambia nikaoge, Bella.” “Kila siku nakwambia kuoga ndio nakupaka sabuni, ukoje wewe!?” “Hapana, kuoga nikutoa uchafuUnaweza kutoa uchafu na maji bila sabuni, kwanza ndio afya. Sabuni zina makemikali mengi.” Eric alirukia kochi kwa nyuma na kukaa katikati ya Bella na Elvin akambusu dada yake. Bella alimvuta sikio kwa nguvu. “Auuuu! What did I do.” “Hiyo ni yakuoga bila kupaka sabuni.” Bella akaondoka. Wote walikuwa wanacheka. Bella aliingia kuoga na yeye akarudi kukaa palepale kwenye kochi lakini pembeni ya Elvin, wakajikuta wamemuweka yeye kati. Waliendelea kuongea huku  wakiangalia movie yao, wishowe Elvin akajikuta amebaki peke yake, wote wawili walikuwa wamemuegemea wamelala.

Hapo ndipo Elvin alipopata muda wakumwangalia Bella vizuri bila kupepesa macho. Walikuwa watoto wadogo, na wote walikuwa wamemuegemea kama vitoto vilivyohitaji mapenzi. Walifanana sana, karibu kila kitu, isingekuwa rahisi kujua kama ni watoto wa baba tofauti. Elvin alimuweka Bella vizuri nakubaki akimwangalia. Alilala kama mtoto mdogo, sura yake ni kweli alionekana ni mtoto. Lakini alikuwa na maisha ya hali ya juu sana. Kila kitu alichoshika yeye na mdogo wake, kilikuwa cha gharama sana. Hata hiyo hoteli ilionekana ni ya gharama sana. Maswali mengi sana yalimsumbua Elvin.
Alikumbuka ni kama Bella alizungumzia wapo peke yao katika maisha. Ndugu waliwakana na walikuwa wakilelewa na mama yao, ambaye alishafariki. Na walipoteza kila kitu. Bella alionekana ni msichana anayejitambua, na akili zake zinafanya kazi vizuri. Elvin alipingana na wazo kuwa anaweza kuwa anachuna mabuzi. ‘Lakini ni nani anampiga? Au anamwanaume ambaye alimfumania, akampiga sana? Lakini bado ni mtoto mdogo, hawezi kuwa ameanza mambo ya wanaume. Au watakuwa wanautumia uzuri wake kuwauzia madawa ya kulevya? Elvin alikuwa akiwaza, na mwishowe akakubaliana na wazo hilo la mwisho. ‘Atakuwa anauza madawa yakulevya. Maskini Bella, shida zimemsukumia kwenye biashara hatari.’ Elvin alibaki akimwangalia huku akimuhurumia. Alimtengeneza nywele zake vizuri, akamshika kwa upendo kama anayemuhurumia.

Alimnyanyua kwa nguvu Eric, akamsimamisha na kumvuta kumrudisha kitandani. Alionekana kuchoka sana, hata hakuwa na habari wakati Elvin amemshika mkono mpaka kitandani. Alimfunika vizuri, akarudi kwa Bella. Akampandisha miguu yake vizuri kwenye kochi, akaweka mto chini ya kichwa chake ili asiumie shingo, kisha akachukua moja ya shuka kwenye kitanda cha pili kilichokuwa kimebaki, akamfunika mpaka shingoni akabaki amekaa pembeni ya kochi akimwangalia kama mtu anayetaka kushibisha macho yake. Muonekano wake alikuwa mtoto mdogo, lakini akifungua mdomo wake, alijawa hekima tupu. ‘Unaweza kulipa gharama yeyote ile, ili kila siku uamke pembeni ya hii sura.’ Elvin aliwaza kisha akatabasamu. Alikaa pale kwa muda akimtizama mpaka alipolemewa na usingizi, akaamua kwenda kulala. Alizima tv, nakuzima taa, akarudi chumbani.

Sura ya Bella ilibaki machoni mwake, akabaki akikumbuka anavyocheka na kutabasamu huku dimpozi zake kubwa zikipamba mashavu yake yakitoto. ‘Inaonekana Ric, ndiyo furaha pekee ya Bella. Amekuwa watofauti sana, baada ya Ric kuja. Furaha yake itadumu pindi Ric atakapo ondoka? Ataendelea kuwa karibu na mimi au mimi nimekuwa ni njia yakumfurahisha mdogo wake tu?’ Elvin alianza kuona anamuhitaji sana Bella. ‘Lakini hapana, Bella ni mfanyakazi wangu na itabaki hivyo. Sitaki kujichanganya. Nina misingi yangu ya maisha nimejiwekea, lazima niishi hivyo kwa kufuata kanuni hizo.’ Elvin aliendelea kujikumbusha misimamo yake, huku mawazo mengine yakimfikiria Bella. Akapitiwa na usingizi.

************************************************

Walikuwa na wakati mzuri sana wapamoja. Wote walikiri hawakuwahi kuwa na mapumziko ya namna hiyo. Kila siku walifanya kitu kipya na Elvin akiwa kiongozi wao. Walishinda wakicheza ufukweni mwa Ziwa Victoria, walirudi kulala mchana, jioni walizunguka kuangalia mji au waliota moto nje ufukweni mida hiyo ya jioni wakati baridi imeingia, huku wakisimuliana hili au  lile ambalo wote litafanya wacheke. Bella na mdogo wake waliimba wakati wote kipindi hicho wakiwa wanaota moto, au walikaa tu pembeni ya pool wakiongea huku wakila na kunywa bila ya kujali muda wala watu waliokuwepo pembeni yao mida hiyo ya jioni. Walikuwa kwenye ulimwengu wao peke yao, wao watatu tu. Walipiga picha nyingi sana, ambazo Elvin alikuwa akiziangalia kila anapokuwa peke yake usiku kitandani, kwani wakati wote yeye ndio alikuwa wamwisho kulala, na akajikuta kila wakati macho yake yanagotea kwenye picha za Bella.

Alihakikisha simu yake inachaji kila wakati ili kuweza kuchukua picha zakutosha na ibaki ya kuziangalia awapo peke yake kitandani. Bella naye alikuwa mwenye furaha kupita kiasi. Alisahau kabisa maisha anayoishi jiji Dar akiwa na Mzee Masha. Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, alisafiri bila Mzee Masha, na aliweza kuwa mtoto tena, bila kuguswa au kulazimishiwa kufanya mapenzi. Alijiambia yupo kwenye mapumziko ya akili na mwili. Eric ndiye aliyekuwa na wakati mzuri kuliko wote. Alikuwa akiongea na kujisifia juu ya michezo anayocheza akiwa shuleni bila kuchoka. Alijiona ni kama yuko katikati ya wazazi wake, gafla maisha yakaleta maana. Wazo la Elvin kuchukua chumba kingine, walisha litupilia mbali, wakaishia kutumia chumba hichohicho kimoja.

Kila siku walipokuwa wakirudi hotelini Eric na Bella hawakuacha pia kuimba pamoja kabla ya kulala. Eric alikuwa mtunzi mzuri sana wa nyimbo, lakini mama yake alimshauri atulie kwenye michezo, kwani aliona atafanikiwa sana kwenye michezo kuliko uimbaji. Lakini Mat hakuacha kumpeleka kanisani wakati wa mazoezi yake ya kwaya, kwa hiyo Eric alijifunza kutumia vyombo vya mziki, kanisani. Bella naye alikuwa na uwezo mzuri sana wakupiga kinanda. Tunu alipoona hivyo, akaamua kuwanunulia vyombo hivyo na kuwawekea nyumbani kwao wawe wanatumia wawapo nyumbani. Alimwaga pesa nyingi sana kwa watoto wake, na waliishi kama watoto wa milionea pale jijini. Tokea wakiwa watoto Tunu aliwasogeza watoto wake kwenye vitu alivyoona vitawasaidia baadaye. Eric alikuwa na uwezo wa kutunga nyimbo katika kila tukio, mpaka alikuwa akimshangaza Bella na kila aliyekaribu naye. Hata kitu cha utani tu, aliweza kutungia wimbo na kuimba vizuri sana.

“I miss my gutar, Bella.” Ric alikumbuka gitaa lake wakati akiimba. “I miss my piano.” Bella naye alikumbuka kinanda chake. Elvin alikuwa akiwasikiliza wakati wanaongea. “Kwani viko wapi?” Elvin aliuliza. “Tulipoteza kila kitu tulipoenda kumzika mama. Tulirudi tukakuta wapangaji wapya, wakasema hawajui vitu vyetu vilipo.” “Nakumbuka uliniambia, poleni sana.” “Asante.” Bella alijibu. “Hey Bella! I made a knew song. You wanna hear it?” Eric alitunga wimbo mpya, alitaka dada yake asikilize, usiku huo waliporudi hotelini wakiwa kwenye nguo zao zakulali baada ya kutoka mjini kuzurula. “Mmmh!” Bella aliitikia huku akijiweka sawa. “Wewe utakuwa kinanda na gitaa langu. Sio mrefu sana, wala sio mgumu, nitaimba mara moja tu halafu tutaimba wote.”  “Sawa.” Elvin alikaa vizuri kuwasikiliza. Ulikuwa wimbo mzuri sana, lakini uliwaliza Bella na mdogo wake, kiitikio kilikuwa hivi.

So soon you have gone,
So soon you left us,
See how soon the world have forgotten us,
Like a drop of tear  in a sea, see how soon the world covered us.
It was so soon, still so soon.

Bella alilia mpaka akasimama na kwenda bafuni. Alishindwa kujizuia kabisa. Eric alitibua machungu moyoni mwake, alikumbuka vile ilivyomlazimu kukua kwa haraka baada ya kifo cha mama yake. Alikumbuka maumivu makali anayopata kila anapofanya mapenzi na Mzee Masha, lakini ilimlazimu kucheka na kumuonyesha anafurahia kila kitu anachomfanyia au anachofanyiwa kwenye mapenzi ili yeye na mdogo wake waendelee kuishi. Bella alilia sana. Mwili mzima ulikuwa ukitetemeka kila akifikiria jinsi Mzee Masha anavyompapasa na kumbusu mwili wake. Bella aliendelea kulia. Vipigo anavyovipata tena bila kosa kutoka kwa Mzee huyo anayetumia mwili wake bila shukurani, Bella alizidi kulia na kumkumbuka mama yake. 

Eric aliingia bafuni na kutoka naye. Walipanda kwenye kitanda chake akamfunika dada yake, akabaki amelala pembeni yake. “Is gonna be fine Bella. Soon we are gonna be fine.” Bella alimsikiliza mdogo wake akijua hajui analoliongea, tayari alikuwa na ndoa ambayo alihakikishiwa haitakaa ikavunjika labda kifo. Alikumbuka anasubiriwa kwa hamu pindi atakaporudi nyumbani. Bella alijikunyata ndani ya lile shuka na kuficha uso wake huku akitetemeka kwa hofu na machungu. Alitamani mama yake arudi aje ampokee huo mzigo japo kwa siku chache apumzike kuwaza kesho itakuwaje kwake na hasa kwa mdogo wake.

Elvin alikaa pale sebleni kwa muda asijue afanyaje. Alisogea karibu na chumbani akabaki amesimama  akiwatizama ndugu hao wawili ambao ni kama mapacha, wakibembelezana. Alipoona wote wanaendelea kulia na hamna dalili ya kunyamaza, Elvin alimwambia Eric ahamie kitandani kwake, alale. Na yeye akakaa pembi ya Bella aliyekuwa amejifunika mpaka kichwani. Aliweza kuhisi jinsi Bella anavyotetemeka. Akaamua kupanda na yeye kitandani, akamtoa ndani ya mashuka, akamvuta mpaka karibu yake, alimuegemeza kichwa chake kifuni kwake, akamzungushia mikono yake, baada ya muda Bella alitulia na kupitiwa na usingizi pale pale alipokuwa amekumbatiwa na Elvin. Walikaa vile kwa muda, mwishowe Elvin akaamua asimtoe pale, amwache alale tu mpaka atakapo amka, kwani Bella alikuwa amelala vizuri sana. Elvin alivuta mto, akauweka nyuma ya mgongo wake, akajiegemeza vizuri, na yeye akapitiwa na usingizi.

Bella alifungua macho ilishakuwa asubuhi, tena yupo kifuani kwa Elvin, akiwa anamtizama. Alishtuka sana, akajisogeza pembeni. “Ulilala salama?” Elvin aliuliza kwa sauti ya chini ili wasimuamshe Eric. Bella alijisogeza pembeni zaidi, mbali kidogo ya Elvin akatingisha kichwa kuashiria kukubali huku akikwepesha macho yake. Elvin alibaki akimtizama. Bella alivuta shuka, Elvin akamsaidia kumfunika. “Asante.” Bella aliongea kwa sauti ya chini sana lakini Elvin alisikia. “Unataka kurudi kulala?” Elvin aliuliza, Bella alitingisha kichwa kukubali. Elvin alinyoosha mkono kama aliyetaka Bella amshike. Alikuwa amejisogeza mbali sana na yeye. Mwishoni kabisa ya kitanda hicho kikubwa. Bella alibaki akiangalia mkono wa Elvin bila kumtizama machoni, mwishowe alitoa mkono wake kwenye shuka taratibu akaushika mkono wa Elvin, Elvin akamvuta karibu sana na yeye, akamgeuza kama ampe mgongo, akamfunika tena vizuri. “Lala mimi nipo hapa na wewe.” Elvin aliongea kichwani kwa Bella, akambusu kwenye kichwa chake, hapohapo akamsikia Bella akihema akiashiria amepotelea usingizini. Hakutaka kumkumbatia tena, lakini walikuwa wamelala karibu. Elvin alibaki akimwangalia huku akiwaza, mpaka na yeye akapitiwa na usingizi mida hiyo ya asubuhi ya siku yao ya mwisho pale hotelini. Walijikuta wote wanaamka saa sita mchana. Walikaa wakiongea palepale kitandani, Bella na Ric wakitaniana, mpaka Bella alipoamua kuwaacha aende kuoga.

************************************************

Walikuwa na mtindo kila wanapokuwa wanakuwa mapumzikoni, usiku wa mwisho kabla ya kuondoka, wanaandika vikaratasi na kila mtu anaandika kitu anachokitamani kitokee. Waliita ‘Wishing list game.’  Kila mmoja anaandika kwenye kikaratasi, kisha wanabadilishana na kusoma kwa sauti ili wote wasikie. Eric alimuelezea Elvin huo utaratibu wao na kutaka aungane nao. “Lakini sio lazima Elvin. Kama unaona haupo tayari, unaweza kucheza wakati mwingine.” Bella aliingilia. “Hamna shida, hata mimi ningependa kuandika kitu ninachotamani.” Bella alitengeneza vikaratasi vitatu akawagawia kila mmoja. “Natakiwa kuandika vitu vingapi?” Elvin akauliza. “Kimoja au viwili. Visizidi viwili.” Kila mmoja alitulia akaandika, kisha Eric akampa Bella, Bella akampa kikaratasi chake Elvin, Elvin akampa Eric. 

“Nani anataka kuanza kusoma?”
 Bella aliuliza. “Mimi nitaanza.”  Eric aliwahi akafungua cha kwake akaanza kusoma. “Hii inatoka kwa ElvinNatamani kupata mapumziko kama haya wakati mwingine.” Wote walipiga makofi. “Kwa hiyo umefurahia, Elvin?” Bella akauliza huku akitabasamu na kumwangalia Elvin kwa upole. “Sana. Naamini wakati mwingine tutapata nafasi kama hii.” Walibaki wakiangaliana kwa muda, mwishowe Bella aliinama kama kukwepesha macho huku akitabasamu, akafungua kikaratasi cha Eric. “Mimi nitasoma wa pili, kinatoka kwa Ric‘Natamani kuwa na familia watakayo niweka mimi na Bella mbele.’ Walitulia kidogo kama wanaotafakari ule ujumbe. “Namimi nitasoma wish ya Bella.” Elvin alivunja ukimya. “Mko tayari kusikia wish ya Bella?” Elvin alitaka warudishe mawazo pale. “Soma Elvin, mimi nasikiliza.” “Sawa. Bella anasema, ‘Natamani kurudi kuwa mtoto tena. Hata kwa dakika moja tu, kupata mtu anayeweza kuwaza kwa niaba yangu. Kama wakati wa uhai wa mama. I want to be her little girl again. I want to get the place where I can hide my sorrow and fear again. I wish to be a little girl again.’ Machozi yalikuwa yakimtoka Bella. Na hiyo ndiyo ilikuwa shauku yake. Alikuwa akipigwa na kuonewa na Mzee Masha, lakini hakuwa na rafiki au mtu wakumwambia maisha anayoishi. Kila aliyemuona na Mzee Masha, alimuhukumu kama mwizi wa mume wa mtu, wasijue mateso anayopitia. Hakuruhusiwa kuwa na rafiki awe wakiume au wakike. Na simu yake ilikuwa ikifuatiliwa, kwa hiyo asingethubutu hata kumpigia mtu yeyote simu.

Baada ya kimya kirefu kupita. Bella aliamua kumshukuru tena Elvin. “Tunashukuru kwa kuja na kuwa pamoja na sisi. Asante sana.” “Na mimi nimefurahi kupata muda wakuwa pamoja na nyinyi. Nimekuwa na wakati mzuri zaidi ya nilivyotarajia. Mimi ndio natakiwa niwashukuru nyinyi. Asanteni.” Elvin alimwangalia Bella kidogo, kisha akahamisha macho yake kwa Eric. “Asante Elvin. Utakwenda na sisi kuangalia kaburi la mama kabla sijarudi shule?” “Eric!” Bella alishtuka sana. “Hataweza. Elvin ana kazi nyingi sana. Hawezi akaendelea kuwa anazunguka na sisi kila mahali. Hata hivi alivyofanya tunatakiwa kushukuru.” Eric akanyamaza. Alishajua dada yake akimuita jina lake lote kama lilivyo Eric, anakuwa hayupo kwenye utani na amekasirika.

“Kwani mnataka kwenda lini?” “Hamna haja Elvin. Hamna sababu kabisa yakutusindikiza. Huwa tunaenda kila wakati Ric anapokuwa likizo, sio kitu kigeni, huhitaji kwenda. Najua una mambo mengi…”
 “Bella!” Elvin alimwita kama kutaka atulie. “Mnataka kwenda lini?” Bella alitulia kidogo. “Sijajua, naona siku za Ric kurudi shule zimekaribia, anatakiwa mpaka ifikapo Jumapili awe yupo shuleni. Kwa hiyo nilitaka kuomba kama naweza kupata siku zangu chache nyingine za likizo kabla hajarudi shule, ndio twende kwa mama.” “Na mimi si nimewaambia nipo likizo ya siku 10? Bado nimebakiza siku nyingi tu za kutosha. Mtakapokuwa tayari naweza kuwasindikiza.” “Huna sababu yakufanya hivyo Elvin, najua…” “Bella! Mimi ndio nataka kwenda. Labda kama una sababu nyingine.” “Hapana Elvin.” “Basi tupangeni safari.” “Nilifikiria labda turudi nyumbani, tupumzike hata siku moja, ndipo twende.” Bella alijibu.

“Mnaishi wapi?” Bella alishindwa kujibu kabisa. Alibaki akibabaika. “Namaanisha nyumbani ni wapi mnapoishi kwa sasa?” Elvin alirudia tena akidhani Bella hajaelewa. “Tunaishi Villa in Hotel. Ipo Kawe.” Eric alijibu, na kumfanya Elvin ashtuke kidogo na kumgeukia Bella. Bella aliinama. “Okay.” Elvin aliamua asiongeze kitu katika hilo. “Kwa hiyo ni lini unafikiria tusafiri?” Elvin aliendeleza maongezi akijitahidi kuficha hisia zake. Bella alibaki ameinama akiwaza. “Bella?” Elvin aliita. “Nilikuwa nafikiria labda twendeni Jumatano asubuhi na mapema, tugeuze jioni ili alhamis niwepo kazini.” Bella alijibu kwa shida sana, akionyesha wazi ameishiwa nguvu. “Ni sawa kabisa, wazo zuri.” Wote wakanyamza.

“Nataka niwahi kulala leo.”
 Bella alivunja ukimya. Elvin akamwangalia, kisha akauliza. “Hatuangalii movie leo?” “Mimi nitatangulia niwahi kulala.” Bella alijibu kinyonge sana. “Sawa.” Bella alisimama akaingia bafuni kuoga ili alale. “Nimefurahi tunaenda wote kwa mama, Elvin.” “Hata mimi nimefurahi Ric. Unataka tuangalie wote movie kabla hujaenda kulala?” “Leo naomba tucheze game. Bella ameninunulia game mpya nataka nicheze sana kabla sijarudi shule.” Walikubaliana wakaanza kucheza. Elvin aliposikia Bella anapanda kitandani, akamwambia Eric amsubiri kidogo anakuja.

Alimkuta Bella ameshapanda kitandani kwake na amejifunika shuka. “Umeshalala?” Bella alitoa kichwa nje. “Bado ndio nataka kulala.” Bella alikuwa amepooza sana. “Upo sawa?” “Ndiyo.” “Mbona leo mapema wakati ulituahidi leo hatuta lala?” “Naona nimechoka mapema.” “Njoo tuangalie hata movie moja bwana. Usilale mapema. Tutumie huu muda vizuri.” Bella alitabasamu. “Twende.” Bella alitoka ndani ya shuka na kuongozana na Elvin kurudi alipokuwa Eric. Eric alikuwa na michezo yake aliyokuwa ameunganisha kwenye tv hakutaka mtu aguse tv. “Huyo hapo hatatoka. Hata ukimsemesha hatakujibu.” Bella alikuwa akimwambia Elvin. “Nimeona. Maana aliniambia tucheze wote, naona mwenzangu amenogewa hanikumbuki tena.” Wote wakacheka. “Ni sawa tukiangalia kwenye kompyuta yangu?” Bella aliuliza kwa heshima kidogo akionyesha hofu kama ni sawa au la. “Wazo zuri, ili tusimsumbue. Tumuache afaidi kwa mara ya mwisho kabla hajarudi shuleni.” Walicheka wakarudi chumbani ili wakaangalie huko.

Bella alianza kubabaika ukaaji. “Tutaangalizia hapa kitandani au tukae chini tu?” Bella akauliza. “Sakafuni tena? Baridi bwana. Tukae tu hapo kitandani.” Bella alipanda kitandani akaingiza miguu ndani ya shuka, akapaka laptop yake. “Nilikuja nazo nyingi, sijui hii itakuwa nzuri?”  “Hata mimi sijawahi kuiona. Tuangalie tu kupoteza muda. Unapenda sana movie?” Elvin aliuliza. “Inanibidi kuangalia tu. Ric akiwa shuleni najikuta sina kitu chakufanya.” “Mnaishi peke yenu?” Bella alinyamaza kwa muda mrefu sana, mpaka Elvin alijua hatajibiwa.

“Eric akiwa likizo, huwa napenda kuwa na yeye tu.” Hilo jibu lilikuwa la jumla sana. Elvin alitamani kuuliza tena, lakini kutokana na muda Bella aliochukua kujibu swali lililopita, alijua ni kiashirio kwamba hayupo tayari kuzungumzia maisha yao. Movie ilianza, wakaanza kuangalia, wote wakiwa kimya. “Unataka kujiegemeza hapa?” Bella hakujibu akabaki amekaa wima kwa muda mwishowe akamuona anajivuta mpaka karibu yake na kumuegemea. Elvin alihisi Bella anapitia wakati mgumu sana wamaisha. Ule muonekano wa utajiri, alihisi unafunika machungu makubwa sana ndani yake. Alitamani kujua zaidi, lakini aliona awe mvumilivu. Bella aliendelea kujivuta mpaka alipojiegemeza vizuri kwa Elvin. Movie ilipoisha, Bella alikuwa ameshalala kabisa. Elvin alimtizama kama mtoto anayetafuta sehemu ya kujificha, na anapoipata ni kama akili zake zinatulia kabisa na kuweza kulala usingizi mzito sana. Kila alipokuwa karibu na Elvin, Bella alilala muda huohuo, bila kupoteza muda. Alimuweka vizuri kwenye mto, akamfunika na kurudi kumwangalia Eric, ambaye ndio ilikuwa kama kuna kucha.

************************************************

Walitua jijini Dar, mida ya jioni. “Niliacha gari hapahapa uwanjani. Unataka tukusindikize mpaka nyumbani?” Bella aliuliza wakati wanashuka kwenye ndege. “Kama hamjachoka sana. Vinginevyo naweza kuchukua taksii tu.” “Sawa.” Bella alijibu. “Sawa nini sasa?” Elvin akauliza. “Sawa kama ulivyosema, kuchukua taksii.” Elvin alimtizama Bella. “Nataka uwe huru Elvin, sitaki tukupeleke halafu iibue matatizo mengine.” “Twendeni mlipoegesha gari kwanza. Tutaongelea huko sio hapa.” Walifika kwenye gari Eric akaingia na kulala kwenye kiti cha nyuma. Alikesha akicheza ‘games’ zake kwenye tv, mpaka palipo pambazuka. Bella aliamka na kumkuta bado anacheza, ndipo alipompokonya ‘remote’ alizokuwa akichezea, na kumlazimisha alale japo kwa lisaa kabla hawajaondoka, kwa hiyo bado alikuwa na usingizi.

 Elvin aliwasaidia kupandisha mizigo yao kwenye gari hilo la kifahari sana, akabaki akijiuliza bila majibu. Alipiga mahesabu ya kuacha hilo gari hapo uwanjani kwa siku zote nne, walizokuwa wamesafiri, alijua itamlazimu Bella kulipia pesa nyingi, lakini Bella hakuonekana na tatizo lolote juu ya pesa. Aliingia akakaa kwenye kiti chake cha dereva, Elvin akaenda kusimama dirishani kwake.

Naomba nichukue taksii, ili wewe umuwahishe Ric akalale. Kuna foleni sana sasa hivi, mpaka unifikishe mimi nyumbani halafu mje mrudi kwenu, itakuwa usiku sana.” “Sawa.” Bella aliitikia. Elvin alimuangalia Bella kutaka kujua kama kweli ameridhika, lakini Bella alikwepa sana kumuangalia machoni. “Nitakupigia simu basi baadaye kujua kama mlifika salama.” “HAPANA.” Bella alishtuka, kama aliyetaka kuruka kutoka kwenye kile kiti cha gari, nakutokea dirishani. Bado Elvin alikuwa amesimama dirishani kwake akimtizama. “Namaanisha hamna sababu ya kupiga, tutafika salama tu.” Elvin alibaki akimtizama wakati anajitetea. “Sawa. Basi utanijulisha mkifika salama.” Bella alinyamaza. “Bella?” Elvin alikuwa amekunja uso kama haelewi tena. 

“Kwa hiyo hatutawasiliana tena? Yaani hapa ndio mwisho wa maongezi yetu!!?” “Ulisema tutaenda wote kule kwa mama.” Bella alionyesha wasiwasi sana usoni. “Tunaendaje bila mawasiliano, Bella? Sijui mnaishi wapi, wala hutujapanga mpango wowote ule. Haya kwenu sipafahamu labla nije kuwachukua au niwafuate tuondoke pamoja, sijui tunakutana wapi, sijui tunaondoka saa ngapi! Mpaka sasa sina uhakika kama kweli unataka twende wote!” “Nataka twende wote Elvin, lakini..” Bella alinyamaza nakuanza kufuta machozi. “Hata nikikwambia hutaelewa Elvin. Nitakutumia email.” “Unajuaje kama sitaelewa wakati hujajaribu kuniambia kitu hata kimoja, nikashindwa kukuelewa?” Bella alibaki kimya. “Eti Bella?” “Naomba nikutumie email nikifika tu nyumbani. Nitakuwa nimetulia na nitakuwa nimejua muda na mahali pa kukutania hiyo kesho kutwa.” “Naweza nikaenda na basi pia, ili kupunguza usumbufu. Halafu nitawatafuta tukifika huko. Muwe na usiku mwema.” Elvin aliaga akaanza kuondoka, Bella alijua kabisa Elvin amekasirika. Bella alishuka na kumkimbilia.

“Elvin! Elvin! Naomba usiondoke.” Elvin alisimama na kumgeukia Bella akiwa kimya kama anayetaka kumsikiliza anachoongea. “Unakumbuka nilikwambia ipo siku tutaongea, na nitajibu maswali yote?” Bella alikuwa akiongea huku akifuta machozi. Alionekana anazidiwa na uchungu uliopo ndani, machozi yalikuwa yakichirizika kama mvua. Naomba univumilie, ipo siku nitaweza kujibu maswali yako, lakini sio leo. Tafadhali Elvin. Naomba usikasirike na naomba twende wote kwa mama. Nitakupitia mahali ambapo naomba uniambie sehemu itakayokuwa rahisi kwako, na ninaomba iwe asubuhi sana. Tukiondoka hapa Dar hata saa kumi na moja asubuhi itakuwa vizuri, ili tuweze kugeuza siku hiyohiyo, ili kesho yake niwe kazini. Please!” Elvin alivuta pumzi akatulia kidogo. “Mtanikuta nje ya kituo cha mabasi ya Ubungo, hiyo saa kumi na moja kamili ya asubuhi.” “Asante sana.” Bella akashukuru. “Muwe waangalifu huko njiani. Tutaonana kesho kutwa.” “Usiku mwema Elvin.” Bella aliaga na kurudi kwenye gari yake. Asingethubutu kumwambia ukweli Elvin hata iweje, si kwa ajili ya aibu tu, hata usalama wa Elvin mwenyewe.

 “Historia ya familia ya Mwasha.”
Elvin ni mtoto wa mwisho katika familia ya Mzee Mwasha. Walizaliwa wanne, wote watoto wa kiume. Walilelewa kwenye maadili yaki Mungu sana. Katika kundi la wazee la kina Mzee Masha, Mzee Mwasha hakuwa miongoni mwa matajiri sana kama kina Mzee Masha. Mara nyingi biashara yake ilikuwa inafilisika lakini kwa msaada wa kifedha wa Masha na watoto wake Mwasha mwenyewe, alikuwa akifufua biashara hiyo na kuendelea. Katika maisha yake, Mzee Mwasha alichoangalia ni kusomesha watoto wake na kusaidia watu. Utajiri au kuwa na mapesa mengi haikuwa furaha yake au lengo la kuhangaika kwake.

Furaha yake na mkewe nikuona wana uwezo wa kusaidia watu. Kwa hiyo hata watoto wao waliwalea hivyo. Katika watoto wa kundi lao, ni vijana wa Mzee Mwasha tu ndio walikuwa na tofauti kubwa na hata wenzao waliwajua. Walikuwa na maadili mazuri sana, isipokuwa anayemfuata Elvin. Wanasema katika kila familia hakosekani angalau mwana mpotevu mmoja, basi ndivyo alivyokuwa Eli. Wengi walimjua kama ‘cha pombe’. Alisomeshwa kama wenzake mpaka shahada ya kwanza, na kubaki kuwa mlevi. Yeye na Elvin ndio walikuwa wakiishi nyumbani kwao. Japokuwa alikuwa ni mlevi sana, lakini Eli alikuwa akimpendwa sana na mama yake.  Alishasema ni msalaba atakao beba mpaka kifo chake.

Na Eli alimpenda mama yake sana, kila mtu alijua, hata kwenye baa alizokuwa akienda kunywa walijua Eli anampenda mama yake. Alizunguka na picha ya mama yake kwenye walert yake. Nakumuonyesha kila mtu. Chumbani kwake kulikuwa na picha moja tu ya mama yake. Hapakuwa na siku Eli alirudi nyumbani bila kuwa amelewa na kila siku hata kama alikuwa mbali vipi, alihakikisha lazima kila usiku akutane na mama yake kwanza kabla mama yake hajalala, ndipo yeye arudi bar kwenda kunywa na hakuacha kumletea zawadi, hata pipi alinunua na kumjia nayo mama yake, ndipo alipotoka kwenda kunywa. Hata kama mama yake akisafiri, alihakikisha kila usiku anampigia simu kabla hajalewa. Mzee Mwasha alishaongea naye sana, mpaka akashindwa. Ilikuwa ngumu sana kumkuta Mzee Mwasha anaongea na Eli. Mbali na salamu, hawakuwa na maongezi yeyote yale ya ziada.

Mtoto wa kwanza wa Mzee Mwasha, alishaoa na alijaliwa kazi nzuri. Alimuoa mtoto wa kwanza wa Danny Mwanja, mmoja wa Wazee wenzake Mzee Mwasha. Mtoto wa pili ndio alikuwa Daktari nchini Dubai, ndiye aliyemtibu Bella, halafu Eli ambaye alikuwa akiishi kwa pombe tu. Hakutaka kuoa wala hakuna aliyejua kama ana msichana. Alikuwa akinywa karibia usiku kucha. Wakati mwingine alirudi nyumbani kubadili tu nguo na kuwahi kazini. Alikuwa ni Muhandisi katika kampuni ya simu akisaidia mitambo ya simu. Kila mtu alijua analipwa vizuri. Na hata kazini alikuwa akijituma sana. Alishaombewa kwenye makanisa mbali mbali, akapelekwa kwa washauri, lakini haikusaidia, alibaki kuwa mlevi wakupindukia.  Hapakuwa na jinsi Eli alikubali kuishi mbali na mama yake. Alipewa chumba cha nje kwenye nyumba hiyohiyo ya Mzee Mwasha. Mbali na kitanda cha kifahari alichonunua ambacho alilalia yeye, na gari zuri sana alilokuwa akiendesha, hakuwahi kununua hata kiwanja. Alijua kuvaa, na alikuwa mcheshi sana. Hata wakikusanyika nyumbani kwao, bila kuwepo Eli, wanakuwa wamepooza sana. Watoto wa kaka yake mkubwa, yaani JJ, walimpenda sana Eli.

Elvin alisomea mambo ya uongozi. Na ndugu zake walimuomba yeye ndiye abaki nyumbani kusaidia wazazi. Kuanzia mambo ya biashara zao, na pale nyumbani, kwani Mama yao alikuwa akiugua mara kwa mara na baba yao alikuja kuanza kusumbuliwa na pressure pia. Kwa hiyo mambo ya kampuni yao yakabaki yakilegalega, kwa kuwa muda mwingi Mwasha aidha alikuwa mgonjwa yeye mwenyewe au alibaki nyumbani akimuuguza mkewe. Kwa kuwa Elvin alikuwa mtu sikivu sana, Mzee Mwasha alimpenda na kumtumia katika kila kitu. Yeye ndiye alifuata njia zote za wazazi wake, ikiwemo kumcha Mungu. Alikwenda kanisa moja na wazazi wake, na hakuwahi kusumbua kabisa tokea utoto wake. Alipomaliza chuo, baba yake akamwajiri, na kuanza kumlipa mshahara mzuri tu. Na kwa kuwa hakuwa na makuu, na msichana wake Irene alitoka kwenye familia inayojiweza, hakuhitaji pesa yeyote kutoka kwa Elvin, kwa hiyo Elvin akajikuta anauwezo wakutunza pesa yake. Alinunua kiwanja, akaanza kujenga taratibu kutokana na mshahara anaolipwa na baba yake.

************************************************

Elvin alirudi nyumbani kwao, moja kwa moja aliingia chumbani kwa mama yake. “Vipi, umekuwa na wakati mzuri huko?” “Nimepata muda wakupumzika. Shikamoo mama.” “Marahaba.” Mama yake alibaki akimwangalia kama anayemsoma. Elvin alijua, akataka kumtoa kwenye mawazo. “Mbona upo peke yako?” “Eli ameondoka hapa muda sio mrefu, na baba yako yupo njiani anarudi.” “Unajisikiaje?” “Kuchoka tu.” “Twende ukatembee kidogo.” “Nimechoka Elvin.” “Sitakuzungusha sana. Tutoke ufanye mazoezi kidogo tu. Ukirudi ndio utalala vizuri.” Mama Mwasha alitoka na Elvin wakaanza kutembea mtaani kwao.

 Alikuwa akimwangalia Elvin kwa makini sana. “Vipi Elvin?” “Safi tu. Kwa nini?” “Nauliza tu.” Waliendelea kutembea, lakini safari hii Elvin alionekana tofauti. Japokuwa hakuwa mcheshi kama Eli, lakini angalau alikuwa akiongea na mama yake mambo mengi sana yanayoendelea kwenye maisha yake. Hakuwa akimficha kitu. Lakini safari hii hata yeye hakujua ni nini amwambie mama yake. Mengi yalikuwa yakiendelea kichwani mwake.

“Mmewasiliana na Irene?” Mama yake alimtupia swali, Elvin akashtuka kidogo, alishasahau kabisa habari za Irene. Akili yake ilijaa Bella tu. “Nilimuomba anipe nafasi ya kufikiria. Nataka muda mama. Sitaki tuje tuoane na Irene halafu wote tukaja kujuta.” “Ni kweli. Baba yako aliniambia juu yake na Phil. Kwa nini hukuniambia?” “Nilikuwa nampa muda nione kama atajirudi. Phil alisema sio kwamba walikuwa na mahusiano, ni kitu kilitokea akiwa amelewa na alisema ni bahati mbaya.” “Na Irene?” Mama yake akauliza. “Sijui mama. Wewe unamjua Irene. Hajaniambia chochote. Kitu kinachonichanganya zaidi ninajua Irene hanywi pombe. Sasa najiuliza ni kwa nini alifanya hivyo? Je Phil ndio mwanaume pekee anayefanya nae huo uchafu au wapo wengine nje ya kundi letu ambao hatuwafahamu? Na mbaya zaidi Irene hawezi kukubali kosa lake hata iweje. Wakati wote anatafuta kulaumu mtu ndio atoke kwenye kosa lake.” Mama Mwasha alibaki kimya. 

“Nitafanyaje mama?” “Bado unampenda?” Mama yake akamuuliza swali dogo tu, lakini Elvin alishachanganywa na Bella, mpaka akawa hajui tena kumpenda mtu kimapenzi kukoje. Hakuweza kulinganisha hisia anazojisikia akiwa na Irene na kile anachojisikia akiwa na Bella. Mtoto huyo mcha Mungu tokea kuzaliwa, alianza kupatwa na hisia ambazo hakuwahi kusikia hata alipokuwa chuoni alipokuwa akizungukwa na warembo wa kila namna. Bella aliibua hisia mpya, ngeni tena za tofauti ndani yake na kuachwa hajielewi hata kidogo.

************************************************

Mambo yanambadilikia Elvin. Taratibu Bella anaanza kumchanganya. Wana miahadi ya kwenda kutembelea kaburi la mama yao huko kijijini.
* Je, Masha atakubali waongozane tena?
* Nini kitatokea kwa Elvin na Bella anayechungwa kama roho ya Masha?
* Nini kitaendelea kati ya Bella na Masha?

Usikose kuendelea kufuatilia kwenye Sehemu ya 7.

0 comments: