Story

My Past - Sehemu ya 7.

Tuesday, May 16, 2017 naomimwakanyamale 0 Comments

A
lijaribu kufikiria anavyojisikia akiwa na Irene na Bella, akaona tofauti kubwa sana. Usiku Bella aliolala kifuani mwake, alipata hisia ambazo hakuwahi kusikia kabla, tokea azaliwe. Alikuwa ni kama amelala amekumbatia alumasi. Kila alipofikiria, ilimjia sura ya Bella akimtizama na macho yake mazuri na matulivu. Elvin aliendelea kumfikiria Bella, wakati mama yake akisubiria jibu. Alikumbuka jinsi Bella alivyoonekana na furaha wakati wakicheza mpira ziwani, meno yake mazuri na dimpozi zake zilizoongeza uzuri wa sura yake. Elvin aliendelea kufikiria. Mpaka wanarudi nyumbani, Elvin hakuwa ametoa jibu.
Walimkuta Mzee Mwasha amesharudi nyumbani. “Kumbe bwana mdogo umerudi!?” “Shikamoo baba.” “Marahaba, likizo imeisha?” “Hapana, nitaondoka tena kesho kutwa, alfajiri, lakini nitarudi usiku sana.” “Wapi tena?” Mzee Mwasha akauliza. “Namsindikiza Bella na Ric, kwenye kaburi la mama yao.” Mzee Mwasha na mkewe wakaangaliana, Elvin aliwaona. “Mbona mnaangaliana?” “Hebu kaa chini kwanza Elvin.” Elvin akakaa.
“Mazungumzo ya mwisho na Irene nilikusikia ukimwambia unahitaji muda wa kufikiria. Umefikia wapi?” “Hata week haijaisha baba, unataka nitoe jibu leo! Bado nafikiria.” “Kweli Elvin?” “Tangia lini umeanza kunitilia mashaka, baba!?” “Mimi sidhani kama hiyo ni njia sahihi yakufikiria Elvin. Huwezi ukawa kwenye matatizo na msichana huyu, ukasema unataka upate muda wakufikiria, halafu unakuwa na msichana mwingine, ambaye ni msichana kama Enabella! Huwezi kufikiria vizuri.” “Bella ana nini?” “Anakila kitu ambacho kinaweza kukufanya ushindwe kufikiria vizuri. Huwezi kumfikiria Irene kama ukiendelea kujiingiza kwenye maisha ya Bella. Utafikia mahali hutaweza kutoka tena.” Elvin alinyamaza.
“Unanielewa Elvin?” Elvin alikaa kimya. “Utajichanganya sana Elvin. Hujafikia mwafaka na Irene, unaanza tena na Bella!” “Hamna kitu chochote kinachoendelea kati yangu mimi na Bella, baba.” “Elvin!” Mama yake alimuita kwa kushangaa. “Kweli mama, nipo nao kwa kuwa mdogo wake aliniomba niwasindikize. Hawana ndugu, wako tu wenyewe. Ni kama nawasaidia tu.” “Sikiliza Elvin, ukubali au ukatae, kuna namna huyu msichana ameshaanza kukuingia kwenye akili yako. Mimi nakufahamu mwanangu. Tokea anaugua hospitalini, mpaka umeenda naye huko, umerudi umebadilika kabisa.” “Nimekuaje mama?” “Kuna kitu kimebadilika Elvin. Nimekuuliza kama unampenda Irene wakati umenipeleka kutembea, unajua hujajibu mpaka sasa?” “Ni kwa kuwa Irene amenisaliti mama. Unafikiri hisia zinaweza kuwa vilevile?” “Ni lini umejua kama Irene amekusaliti?” Baba yake akamuuliza swali lililomfanya Elvin kuishiwa nguvu kidogo.
 “Ni muda kidogo, baba.” Elvin akajibu bila ujasiri. “Sasa kwa nini unafikiri sasa hivi ndio unahitaji muda?” “Kwa kuwa na mimi nilijua Irene ni binadamu, anaweza kukosea baba. Nikaamua kumpa muda, nimefungua moyo wangu wote kwake. Nimefanya kila kitu ili aamini nampenda na kumuhitaji ili tu aniamini, angalau akiri kosa lake. Lakini ameshindwa. Wewe ulikuwepo kwenye mazungumzo yetu, baba. Umemuona jinsi alivyojibu hata baada ya kumwambia kama nimejua amenisaliti. Je unafikiri ni mtu kweli anayeweza kuja kubadilika baadaye? Nyinyi wenyewe mmeona kitendo alichofanya cha kudanganya kuwa amekunywa sumu wakati ni muongo, shida yake ni watu wamuonee huruma, na kunilazimisha mimi niwe naye, bila kutaka kubadilika. Naombeni mnisaidie wazazi wangu, kweli huyu ndio mwanamke mnataka niwe naye kwenye maisha yangu yote hapa duniani? Leo amedanganya hili, na amefanikiwa kuniwekea picha mbaya kwa watu, nikiwa sijamfanyia kosa lolote lile. Kila mtu sasa hivi ananisema vibaya. Haya, nikija kumuoa je? Akinisingizia kitu kikubwa zaidi? Najua watu wanabadilika, na ndio maana nataka nimpe muda Irene, nione kama atabadilika. Siwezi kukimbilia kwa  Bella. Hata hivyo Bella anafahamu kuwa Irene anakaribia kuwa mchumba wangu, na ameonyesha kuheshimu hilo.” Mzee Mwasha na mkewe waliishiwa maneno kabisa. Elvin alikuwa kijana mtulivu sana, hakuwa akipenda makuu, na hakuwahi kuwasumbu.
“Mimi nimeelewa Elvin. Nakuombea Mungu akupe busara katika maamuzi yako.” “Asante baba.” “Mimi ninachotaka uwe na furaha tu. Lakini sitaki uje kuwa njia panda. Maamuzi utakayofanya mapema yatasaidia sana. Kwanza wewe mwenyewe, pili Irene na tatu jamii inayotuzunguka. Maneno yanaenea Elvin. Sitaki ukageuka ukawa gumzo kwa marafiki zetu. Umekuwa kijana mzuri sana. Usikubali ukaharibu sifa yako kwa kuchelewa kutoa maamuzi. Na pia nataka ufahamu hili, hautalazimishwa na mtu yeyote kuoa. Sisi tupo nyuma yako tunakuombea Mungu akupe mwanamke atakaye kufaa. Umesikia?” “Asante mama.” Elvin akasimama na kumbusu mama yake. “Naomba nikaoge ili nilale.” “Huli chakula?” Mama yake akauliza. “Nilikula na kina Bella kabla hatujaanza safari. Kwa hiyo sina njaa. Nitawaona kesho.” Elvin alienda chumbani kwake akaacha wazazi wake wakitizamana.
**********************************

Ni kweli alioga na kupanda kitandani kwake, lakini usingizi ulikuwa hauji. Kila akifunga macho alimuona Bella. Alitamani usiku ule uwe ni kama ule usiku aliokuwa amelala naye akamuweka kifuani mwake. Alihangaika pale kitandani mpaka alipopitiwa na usingizi. Alianza kuota amelala na Bella, huku amemkumbatia na kumfariji. Elvin alishtuka akakaa kitandani. ‘Mungu wangu! Inawezekana mama yupo sahihi. Bella ameshaniingia akilini mwangu!’ Elvin aliendelea kuwaza. ‘Lakini hapana. Nikawaida tu, kwa kuwa nililala naye na kwa kuwa sikuwahi kulala na mwanamke kwanza. Yeye ndio msichana wa kwanza kulala naye. Lakini Bella ni mzuri sana.’ Elvin aliendelea kuwaza huku akicheka.
Alikumbuka utani waliokuwa wakitaniana, jinsi Bella alivyokuwa akicheka mpaka machozi yalikuwa yakimtoka kwa kucheka. Elvin alibaki akicheka peke yake pale kitandani. Alivuta laptop yake kuangalia kama Bella alimwandikia kama alivyoahidi, moyo wake ulijawa na furaha sana, kukuta email kutoka kwa Bella.
‘Elvin, hakuna neno linaloweza kuwakilisha shukurani zangu kwako. Asante kwa kukubali kuwa na sisi, inamaana kubwa sana kwetu, hasa Eric. Amefurahi sana. Najua unamaswali mengi ungependa kupata majibu kutoka kwangu, lakini nakuomba Elvin, unipe muda. Ipo siku nitayajibu yote, bila kukuacha na swali hata moja. Kama hakuna lolote litakalotokea hapa katikati, nategemea kukuona kesho kutwa saa 11 asubuhi kama tulivyopanga. Asante kwa kila kitu Elvin. Nakushukuru.’
Bella.
Ilimchukua muda mrefu sana Elvin kumaliza kusoma huo ujumbe na kufunga hiyo laptop yake. Alikuwa akirudia rudia na kujiuliza maswali. ‘Amesema Eric amefurahia sana, kwani yeye hajafurahia? Lakini atakuwa amefurahia, mbona kila alipokua akiniegemea alikuwa analala hapo hapo.’ Elvin alitabasamu lakini taratibu tabasamu lilianza kupotea. ‘Kwa nini Bella hataki nimpigie simu? Nani alimpiga Bella? Nini anaficha na ni kitu gani kinamnyima raha? Ni kama anatamani kuniambia lakini anaonekana anaogopa sana. Nini anaficha? Na lini ataniambia?’ Ulikuwa ni usiku mrefu sana kwa Elvin, alitamani pakuche masaa yaende haraka, ili akiamka tena akaonane na Bella.
Huko kwa Bella baada ya kurudi kutoka Safari.
Wakati anakaribia kulala, aliona ujumbe unaingia kwenye simu yake, Bella akajua ni Mzee Masha. Akavuta simu na kuanza kusoma. ‘Naona mmesharudi!’ Zikaanza kuingia picha zake akiwa uwanja wa ndege na Elvin nje ya gari wakizungumza. ‘Nimechoka nataka kulala, T. Naomba tuongee kesho.’ Bella alijibu kwa kifupi, akamtumia huo ujumbe. Baada ya muda mchache tu kupita simu ikaanza kuita. “Ni nini tena T? Nimekwambia nimechoka nataka kulala.” “Kesho nasafiri na nitakaa huko muda mrefu, nataka tuagane.” “Nitakuja kesho T, nimechoka na nimeshalala.” “Amka uje chumba hicho kinachoangaliana na chako. Sasa hivi, nakusubiri Bella.” Bella alibaki kimya akitaka kulia. “Unakuja au unataka mimi ndio nije huko?” Mzee Masha aliuliza kwa jeuri.
Bella alibaki akimwangalia mdogo wake huku akijutia kujibu ujumbe wa Masha. Bella!” “Nakuja T.” Bella alitoka kwa kunyata mpaka chumba alichokuwepo Mzee Masha. Alimkuta anamsubiria kwa hamu. “Njoo kwanza hapa. Nilikuwa na hamu na wewe kupita kiasi.” Bella hakutaka kujibu. Akapanda kitandani. “Mbona umenuna?” “Nimekwambia nimechoka T.” “Kwani ulikuwa unalala na Elvin huko?” Bella alishtuka sana. “Unawezaje kufikiria uchafu kama huo? Unafikiri watu wote wana mawazo kama yako? Maisha sio kufanya mapenzi tu, T. Kuna mambo mengine yakufanya.” “Hata mimi sifanyi mapenzi tu, nafanya kazi na mapenzi. Tena nafanya mapenzi na wewe tu.” Bella aliguna.
“Wewe si umesema unanichunguza? Sasa umeshaona kama nina mwanamke mwingine?” “Mkeo?” Bella akamuuliza. “Kama ningekuwa nalala na mke wangu, ningekuwa hapa sasa hivi? Siku hizi muda mwingi sana natumia na wewe Bella, kuliko hata mke wangu. Naweza nikaenda kule nisimguse hata mara moja mpaka narudi kwako. Huoni nilikuwa nakusubiri tuagane ndio niondoke?” Bella alikuwa amechoka sana. “Naomba tumalize nikalale T.” “Ukalale wapi wakati nakwambia nipo hapa kwa ajili yako?” “Siwezi kulala hapa T, wakati Ric yupo chumba kinachofuata.” “Leo utaweza. Anza kufikiria kitu cha kumwambia. Lakini leo hutatoka humu ndani mpaka asubuhi. Unataka kuanza kunichezea akili. Nimekuruhusu kwenda na Elvin, unarudi unaanza kuleta jeuri! Mara ngapi tumekuwa tukisafiri na Ric, halafu mimi nalala na wewe, yeye analala peke yake?” “Kwa kuwa tunakuwa safarini T. Hapa ni kama nyumbani kwetu. Nitamwambia nini asubuhi?” Bella alitamani kulia.
“Hainihusu mimi, hiyo ni kazi yako. Hata hivyo unamasaa mengi sana yakufikiria chakumwambia hiyo asubuhi, maana ndege yangu itaondoka kesho saa sita ya usiku. Na hatutakuwa wote kwa muda mrefu sana. Nitakuwa na wewe mpaka nitakapokuja kuchukuliwa kupelekwa uwanja wa ndege.” “Haiwezekani T. Unataka na siku nzima ya kesho niwe na wewe humu ndani.” “Mbona unashindwa kuelewa Bella? Nakwambia naondoka na ndege ya KLM, saa sita usiku. Wakati mimi naondoka, na wewe ndio utaendelea na mdogo wako. Usitake kunifanya mimi mjinga. Nina mizigo yangu yote hapa. Nitaondokea hapa hapa. Wewe mwenyewe hutaki mdogo wako anifahamu. Angekuwa ananifahamu angalau mchana tungekula naye chakula pamoja.” “Mbona na mimi hutaki mkeo na watoto wako wanifahamu? Tuondoke wote kesho ukanitambulishe kwa wanao.” “Bella umekuwa mkorofi sana. Haukua hivi.” “Naomba kulala T. Wewe mwenyewe ndio umenifundisha kuwa mkorofi. Unawezaje kunifungia humu ndani kama mfungwa, halafu unajua mdogo wangu yupo chumba cha jirani!” “Kwa kuwa wewe mwenyewe umechagua kuyaona haya maisha kama ni jela. Angalia wenzako wanavyohangaika mtaani hawana pesa. Wewe unacheze pesa yangu utakavyo! Umesahau ulipotoka wewe Bella? Huna shukurani kabisa. Nimewaokota wewe na mdogo wako mnatangatanga mtaani, hamna hata chakula! Namsomesha mdogo wako kwenye shule yakimataifa. Ada ninayomlipia hata watoto wangu sikuwahi kuwalipia hivyo. Unaendesha gari ambayo hata mke wangu haendeshi gari kama hiyo na wala hakuna mwanangu hata mmoja ameshawahi kuwa na gari kama yako! Unaishi kwenye nyumba ya kifahari hapa mjini, umezungukwa na wafanyakazi, tena ninao walipa mimi. Mdogo wako akiwa likizo mnaishi hapa, kila kitu mnafanyiwa. Unataka nikufanyaje Bella? Ulitaka nikupe nini? Leo nakuomba tuwe wote kwa masaa machache tu, unalalamika!”
“Hunithamini mimi kama Enabella. Unaniweka hivi kwa manufaa yako, kwa kuwa hutaki watu wachafu, una kinyaa. Halafu subiri kwanza T. Unanipa vitu vya thamani au unaniazima? Ukikasirishwa tu kidogo, mimi ndio sehemu yako yakutolea hasira zako. Utanipiga karibu ya kuniua, halafu unaniacha hapo sakafuni navuja damu bila ya kujali. Ukitoka hapo, wakati umeniacha nusu mfu hapo sakafuni unaanza kunipokonya kila kitu chako, halafu ukirudi hutaomba msamaha, wala kunipa pole kwa mabaya uliyonitendea, tena wala huniulizi kama nimepona au vipi, utatumia mwili wangu hata kama ni siku mbili bila kujali maumivu unayonisababishia.” “Huna shukurani wewe Bella. Hakuna kitu nitakufanyia ukaridhika.”   Waliendelea kubishana kwa muda Bella akijua baada ya hapo watalala. Lakini alimshangaa Mzee Masha, na ugomvi wote ule waliokuwa wakibishana, alimgeuza kwa nguvu na kuendelea kufanya naye mapenzi mpaka alipochoka ndipo alipomuachia, akalala hapo hapo. Bella aliingia bafuni nakuanza kulia sana.
**********************************
Alitamani kama Elvin angekuwepo chumba cha jirani akamkimbilia, amshike japo kidogo tu labda ule uchungu alionao moyoni ungepotea, akalala tena. Alikumbuka kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu wa machungu na kutokulala vizuri, jinsi alivyolala kifuani kwa Elvin. Ilikuwa kama mtu aliondoa moyo wake wa uchungu na kuweka moyo mwingine wakati amelala na Elvin. Hakuwahi kusikia hivyo kabla. Mzee Masha ndiye mwanaume wa kwanza kumshika kimapenzi, lakini kila alipomshika alikuwa akisikia kupiga kelele. Aliona ni mateso makubwa sana hata kulala naye wakiwa wamegusana.
Kwa kuwa alikuwa hapati usingizi kwa haraka, alikuwa akisubiri kila Mzee Masha anapolala, na yeye alijivuta mbali naye sana ndipo alipoweza kulala japo kidogo. Mara nyingi kila alipokuwa akimalizana na Mzee Masha, alinyanyuka na kuhamia sebleni kufanya mambo yake kwenye laptop yake ili kusafisha mawazo. Wakati mwingine alikuwa akishindwa kulala kabisa kila baada ya kufanya mapenzi na Mzee Masha. Alijikuta inamlazimu kuangalia movie nyingi sana ndipo aweze kulala.
**********************************
Alikaa ndani ya sinki la kuogea, akiwa amejaza maji humo akiwaza hili na kupanga lile. Mwishowe alipoona panakaribia kupambazuka alimwamsha Mzee Masha. “Nitarudi baadaye. Nawahi kabla Ric hajaamka.” “Uwahi kurudi Bella, lasivyo nitakufuata huko huko.” Bella hakumjibu kitu. Alivaa harakahaka nakurudi chumbani kwake. Alimkuta Ric bado amelala. Kama katoto kadogo, Bella alipanda kwenye kitanda chake, akajikunja kama paka baada ya kulia kwa muda mrefu akapitiwa na usingizi. Alishtuka ilishakuwa saa nne. Eric alikuwa bafuni akioga. Alianza kuwaza jinsi ya kumuaga mdogo wake, maana alijua muda atakao rudi mdogo wake atakuwa ameshalala.
Eric akatoka bafuni. “Uchovu umeisha?” “Najisikia vizuri.” Eric akajibu. “Naomba leo uwahi kulala Ric, ili kesho tupate muda mzuri kule kwa mama.” “Nitawahi kulala Bella. Kwani wewe hutakuwepo?” “Kuna mtu anashida, anataka nikamsaidie. Anakaa mbali kidogo, itabidi niende sasa hivi, nitarudi baadaye. Lakini hata nikichelewa nataka ulale. Umesikia Ric?” “Naomba basi nicheze game wakati haupo.” “Usiache kula. Hakikisha unaagiza chakula cha mchana na usiku, na ule.” Eric alifurahi sana kuachwa peke yake ili acheze mpaka achoke. “Unanielewa lakini?” “Nimeelewa.” “Nini?” “Nile chakula cha mchana na usiku.” “Nikirudi hujala halafu bado unacheza game tu, nakupokonya game zote hamna kucheza tena.” “Nitakula Bella.” Bella alijitayarisha harakaharaka kwani simu yake ilishaanza kuita zaidi ya mara tatu. “Nakuja.” Bella alijibu kwa kifupi na kukata.
**********************************
Alitoka mle ndani, akaenda alipokuwa ameegesha gari yake, akatafuta sehemu akalificha hilo gari, ili ikitokea mdogo wake anatoka mle ndani, asilione gari la dada yake. Kisha akarudi kwa Mzee Masha. Kweli, Bella alikaa huko ndani mpaka usiku wakati Mzee Masha alipokuwa anataka kuondoka.
“Kesho tunaenda kwa mama.” Bella alikuwa akimtaarifu Mzee Masha wakati anavaa ili aondoke. “Sawa. Au kuna kitu unataka?” “Hapana. Lakini Ric alimuomba tena Elvin twende naye.” Mzee Masha aliweka kila kitu  chini na kumgeukia Bella. “Eti nini!?” “Hujanisikia au ndio unataka kuanza ukorofi, T?” “Usinichezee akili Bella. Ni wewe unamtaka Elvin au ni Ric?” “Namtaka Elvin wa nini mimi wakati nipo nae kazini kila siku?” Bella alijibu huku na yeye amekasirika. “Unawivu T, mpaka unashindwa kufikiria. Elvin nipo nae kuanzia jumatatu mpaka Ijumaa. Tena wakati mwingine mpaka jumamosi na jumapili kazi zikiwa nyingi nakuwa naye ofisini. Sasa ni kwa nini tena nimtoe hapa nimpeleke huko kijijini? Hujawahi kuniamini na hutakaa ukaniamini, hata nifanyaje. Ningekuwa Malaya, ungenikuta bado bikra? Zera mwenyewe hana tabia kama zangu. Ana wanaume kila kona.” Mzee Masha alimpiga Bella kibao cha nguvu tena cha kushtukiza. Bella alikuwa amesimama, kile kibao kilimfanya apepesuke mpaka akaanguka na kujigonga kwenye kona ya kitanda. Alijigonga karibu sana na jicho, alianza kulia kwa uchungu sana. “Usiwahi kumleta mtoto wangu kati yetu.”  Bella alibaki akilia pale chini kwa muda.
Kichwa kilianza kumuuma sana. “Inauma ukifikira wapo wanaume wanaomfanyia mwanao kama unavyonifanyia mimi?” “Nitakupiga tena nikuumize Bella, naomba unyamaze.” Bella aliendelea kulia. “Uliniahidi hutanipiga tena. Mbona umenipiga?” Bella alikuwa akilia sana. “Umenikorofisha wewe mwenyewe. Mimi sikuwa hata na nia yakukupiga.” “Mkeo akikorofisha pia huwa unampiga hivi, au ni mimi tu unanionea?” “Naomba uondoke Bella. Unataka kuniudhi bure nikuumize.” Bella alikusanya vitu vyake akataka kuondoka.
“Nikirudi nikuletee nini?” “Sitaki.” Mzee Masha alianza kucheka. “Njoo Bella wangu.” “Naomba nikapumzike T. Umeniumiza sana, mpaka kichwa kinaniuma. Halafu sasa hivi ni saa tano usiku, sijapata muda wakupumzika hata kidogo. Siku nzima tuko wote hapo kitandani. Na kesho mimi ndio dereva, nataka tuondoke asubuhi sana ili turudi usiku.” “Hamta lala?” “Hapana, natakiwa kazini kesho kutwa.” “Usiendeshe. Mwambie Elvin aendeshe ili upumzike.” “Nani atamuonyesha njia?” “Kweli nenda basi kalale. Lakini kabla hujaondoka njoo kwanza karibu yangu.” “Umetoka kunipiga T. Ona ulivyoniumiza, halafu  sasa hivi unataka nini tena?” “Acha maneno mengi Bella. Njoo.” “Utachelewa ndege T na umeshavaa, kwa nini usiniache nikapumzike?” “Nimekwambia njoo.” Mzee Masha aligomba kwa nguvu sana mpaka Bella akatetemeka. Aliweka vitu vyake chini na kumsogelea.
“Kila ukinitizama na kuongea ndivyo unazidi kunifanya nikutamani Bella. Nakupenda sana.” Kama sio yeye aliyempiga Bella na kumgombesha. Bila ya kumpa pole au kuomba msamaha, Mzee Masha alimuweka Bella kitandani, hakumuachia mpaka dereva alivyokuja kumgongea. “Ric akiondoka tu, urudi nyumbani. Umenielewa Bella?” “Nimeelewa.” Bella alivaa harakaharaka nakutoka pale.
 “Mkasa mwingine wa kutisha kwa Bella lakini Safari hii aiangukia mikononi kwa Elvin.”
Alifika chumbani kwao akamkuta Eric ameshalala. Bella alipanda kitandani na kuanza kulia tena. Alilia mpaka ilipofika saa kumi alfajiri. Kila alivyojitahidi kunyamaza alishindwa. Kichwa kilikuwa kikimuuma sana, na pale alipojigonga palizidi kuuma. Hakuwa na dawa yeyote yakupunguza maumivu. Aliendelea kuhangaika, mpaka alipoamua kwenda kuoga. Alishtuka sana alipojiangalia kwenye kioo. ‘Nitamwambia nini Ric na Elvin? Itabidi kuvaa miwani ya jua.’ Jicho lake lilikuwa jekundu sana, na pembeni lilivilia damu pakawa peusi kabisa. Na kwa kuwa alikuwa na rangi nyeupe, hata gizani alionyesha. Bella alianza kulia tena huku amejishika kichwani. Kichwa kilikuwa kikimuuma sana.
Alioga na kurudi chumbani. Alimwamsha mdogo wake, ili ajitayarishe, lakini alikataa kuoga, akasema alioga kabla yakulala. Kwa kuwa Bella alikuwa akisikia maumivu makali, hakutaka kubishana naye. Alitamani kama Elvin angekuwa haendi nao ili aahirishe safari, aende siku nyingine, kwanza ili apumzishe mwili uliokuwa ukitumiwa zaidi ya masaa 24, huku akiwa na michubuko mingi sana na pili labda jicho lake lingekuwa limepungua. Alimfikiria babu yake jinsi atakavyoshtuka baada ya kumuona. Alitamani asiende, lakini aliangalia saa, akajua Elvin atakuwa yupo njiani kuelekea walipokubaliana wakutane. Alianza kuweka vitu kwenye gari na michezo ya mdogo wake, aliyodhani angehitaji njiani. Akamuwekea mdogo wake mto na shuka la kujifunika, kama akitaka kulala akiwa njiani. Alipohakikisha kila kitu kipo tayari, ndipo alipomuamsha tena Eric. Alikuwa na usingizi sana, alipanda kwenye gari, akajilaza viti vya nyuma, akapotelea usingizini.
Bella aliondoa gari kwa kasi ili asimchelewe Elvin, kwani ilishakuwa saa kumi na moja kasoro. Aliendesha kwa shida kutoka Kawe akapitia njia ya Coca cola, iliyomfikisha Mwenge. Kwa kuwa ilikuwa bado mapema, na hapakuwa na foleni yeyote, haikuchukua muda mrefu sana kutoka Mwenge mpaka Ubungo. Alipomuona tu Elvin, alichukua miwani yake ya jua akavaa, kisha akajifunika mtandio aliouvuta mpaka usoni. Alifanikiwa kuficha lile jeraha.
“Za asuhubi?” Bella alisalimia huku akiangalia mbele. “Nzuri. Mliamka salama?” Elvin alijibu na kuuliza swali kabla hajafunga mkanda. “Naona Ric bado amelala.” Akaongeza tena. “Atakuwa amechelewa sana kulala.” Bella alijibu bila ya kumtizama. “Kwani mlilala saa ngapi?” Bella alinyamaza, kama kawaida Elvin alikuwa akishamuona Bella amekaa kimya alijua hataki kujibu hilo swali. “Bella! Hata swali dogo kama hilo pia huwezi kujibu!? Au na lenyewe utakuja kunipa jibu siku nyingine!?” Elvin alikuwa akishangaa, asijue lile swali, jibu lake limebeba uchungu mzito sana kwa Bella.
“Hapana. Sijui yeye alilala saa ngapi?” “Haukuwa naye nyumbani?” “Hapana.” Elvin alitulia kidogo. “Mbona leo unaongea na mimi hutaki kuniangali? Kuna nini?” “Hamna kitu Elvin. Labda usingizi.” “Unataka nikusaidie kuendesha?” “Nitashukuru, ili nilale kidogo.” Bella alishuka wakabadilishana viti, Elvin akaanza kuendeshea baada ya kuelekezwa kidogo. “Lakini kabla yakufika Chalinze nitakuwa nimeamka.” “Hamna shida, nikiona napotea, nitakuamsha.” “Asante sana Elvin.” “Karibu.” Bella alipandisha miguu kwenye kiti, akavua miwani, akahakikisha amejifunika vizuri mpaka usoni akapotelea, usingizini.
Elvin aliendesha huku abiria wote wakiwa wamelala. Bella alilala, lakini maumivu ya kichwa yalikuwa yakimsumbua sana. Alikuwa akigugumia usingizini, sababu ya maumivu makali. Mwanzoni Elvin alijua ni ndoto, lakini kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda, Bella alizidi kulalamika usingizini. Elvin akaamua atafute sehemu asimamishe gari. Alikuwa wameshafika maeneo ya Kibaha. Alitafuta sehemu wanayouza mafuta ya gari{gas station}, akaingia hapo.
Akaegesha gari vizuri, kisha akashuka na kuhamia upande alipokuwepo Bella. Alifungua mlango taratibu, akamtoa ule mtandio usoni ili amwamshe kujua kulikoni. Baada ya kuutoa, Elvin alishtuka sana mpaka akarudi nyuma. Upande mmoja wa uso wa Bella ulikuwa unatisha sana. Ulikuwa umevimba na pakawa pamevilia damu. Ilikuwa ngumu kumtizama mara mbili. Palikuwa peusi sana. Machozi yalijaa machoni kwa Elvin.
Alimgusa taratibu, bado alikuwa akilalamika. “Bella! Bella!” Bella alifungua macho, jicho lile moja lilikuwa jekundu sana. “Kichwa kinaniuma sana Elvin. Siwezi hata kunyanyua kichwa.” “Ngoja niulizie hospitali hapa karibu.” Elvin alimuulizia mtu aliyekuwepo karibu yake, na yeye alikuwa akijaza mafuta kwenye gari yake, akaelekezwa hospitali ilipo. Aliendesha kwa haraka mpaka pale hospitalini. Alimwamsha Eric akamwambia afunge gari amfuate. Akaenda upande aliokuwepo Bella, akafungua mlango, akambemba mpaka mapokezi.

“Safari ya kwenda kijijini kuona kaburi la mama yao, yaishia hospitalini.”
Kila mtu alishtuka sana walipomuona Bella. Alikuwa akilia huku anatetemeka. Walimpisha ili ahudumiwe yeye kwanza. Elvin alimuweka kwenye kitanda kilichokuwepo kwenye chumba kidogo pale pale mapokezi. “Kwa nini unapiga wanawake, we kijana?” Daktari aliyekuwepo pale aliuliza. “Sijampiga.” “Ona alama ya vidole hii hapa imevilia kabisa. Acha kusema uongo. Hasira hizo zitawasababisha kuua, mje kufia jela bure!” Elvin alinyamaza asijue ni jinsi gani atajitetea tena na kueleweka. Aliamua kurudi kumuangalia Eric wakati wakimshugulikia Bella.
Baada yafunga gari, Eric aliingia ndani kwa haraka, akakutana na Elvin naye akimfuata. “Kwa nini tupo hapa hospitalini?” Eric akamuuliza Elvin. “Bella anaumwa.” “Bella!” Eric alishtuka sana. “Anaumwa nini?” “Sijui.” “Is she going to be okay.” “Usiogope Ric. Atapona. Kwani jana mlienda wapi?” Ilibidi Elvin aulize. “Mimi sikwenda mahali, ila yeye aliniaga asubuhi kuwa anatoka kwenda kwa rafiki yake anashida sana, anakwenda kumsaidia. Mpaka saa nne na nusu usiku mimi nina lala, yeye alikuwa hajarudi. Hata sijui nimefikaje kwenye gari. Atakuwa aliniamsha asubuhi akanisaidia kupanda kwenye gari. Sijamuona tokea jana asubuhi.” Elvin alibaki kimya.
“Nataka nikamwone Bella.” Ric alianza kulia. “Ngoja kwanza wamtibu, halafu tutaenda kumuona. Njoo tukae hapa chini.” Walipokaa tu, alitoka nesi, akamwita Elvin. Daktari anataka kuzungumza na wewe. Elvin aliongozana na yule muuguzi mpaka ofisini kwa daktari.  “Mgonjwa wako analalamika sana kichwa, nashauri afanyiwe kipimo cha kichwa. Kina bei kidogo lakini naona ni muhimu. Je upo tayari akapimwe?” “Kabisa. Itachukua muda gani mpaka kupata majibu?” “Leo leo. Ngoja nesi aende akaangalie kama kuna watu wengi wanasubiri hicho kipimo. Kama hamna, nitawaomba wampime sasa hivi, ili tupate majibu haraka.” “Nitashukuru sana kama mtaharakisha. Naweza kuingia kwenda kumuona?” “Ingia tu. Na mimi nitakuja baada ya muda mfupi kumchoma sindano” Yule nesi aliyemwita na kuwa naye kwenye chumba cha daktari alijibu nakuondoka. Elvin alitoka pale kwenye ofisi ya daktari kuelekea kwenye kile chumba alichokuwepo Bella.
 “Elvin, Elvin! Nisaidie.” Akiwa nje ya mlango, Elvin alisikia Bella akiita jina lake huku akilia kwa uchungu mkubwa sana. Aliharakisha kuingia ndani, akamkuta Bella amefunga macho huku analia sana. Elvin alimsogelea mpaka pale kitandani. “Bella! Bella! Niangalie.” Bella alifungua macho. “Si ni kichwa kinauma?” “Sana, nahisi kuchanganyikiwa.” “Pole sana. Nimeongea na dakatri wanakuja kukuchoma sindano ya kutuliza maumivu, lakini kwa sasa, naomba usilie kabisa jaribu kutulia, ili kichwa na chenyewe kitulie. Sawa?” Bella alitingisha kichwa. “Ric yuko wapi?” “Nimemwambia asuburi nje kidogo. Ataogopa sana kukuona kwenye hiyo hali. Acha kwanza kichwa kitulie kabisa, ndipo atakuja kukuona. Sawa?” “Asante.” “Basi usilie kabisa, vumilia. Sasa hivi watakuja kukuchoma sindano, halafu wakuchukue kwenda kwenye kipimo cha kichwa. Waangalie kuna nini kinachoendelea huko kichwani.” Bella alitulia. Muuguzi aliingia, akamchoma sindano, baada ya muda walimuona ametulia, wakajua maumivu yameisha. Elvin alimshika kichwani pembeni ya ule uvimbe, kichwa kilikuwa cha moto sana. Alikaa naye mpaka alipokuja kuchukuliwa kwenda kufanyiwa vipimo.
Elvin alirudi kukaa na Eric. “Anaendeleaje?” “Wamemchukua kwenda kumfanyia vipimo, akirudi utaenda kumuona.” Eric alikaa kimya kwa muda. “Elvin!” Eric akamwita, Elvin akamgeukia. “Vipi?” “Asante kwa kutusaidia.” Elvin alimuhurumia sana Eric. “Usiwe na wasiwasi Ric, Bella atapona.” Eric alifuta machozi. “Asipopona Bella nitafanyaje? Mama alisema nisiwe na wasiwasi nitakuwa na Bella.” “Usilie Ric. Bella lazima apone.” “Bella aliniambia hivyohivyo wakati mama mgonjwa. Lakini hakupona alizidi kuugua kila siku, wakamrudisha nyumbani. Bella alihangaika naye sana, alikuwa peke yake akimuuguza. Unajua dada aliyekuwa akitusaidia kazi na yeye alitukimbia?” “Sikuwa najua hilo.” Elvin alijibu. “Basi alitukimbia. Akatuacha peke yetu na mama mgonjwa. Bella alikuwa akiniambia kila siku nisiwe na wasiwasi mama atapona, lakini ujue nini?” “Eehee!” Ric alikuwa akitia huruma sana.
“Mama alikufa akiwa amekonda sana, halafu akawa hatukumbuki kabisa. Hata mimi hakuwa akinikumbuka tena. Wakati mimi ndio alikuwa akinipenda sana. Nitaenda wapi Bella akifa?” “Bella hawezi kufa. Usiogope Ric. Ni kichwa tu kinamuuma, amepewa dawa ametulia, na anafanyiwa vipimo ili tukiondoka hapa tuwe na uhakika yupo salama. Usiogope.” “Naogopa sana Elvin.” Elvin aliweza kuhisi hali anayopitia Eric. Alimuona mama yake akiugua mpaka kufa. Hapendi mtu aumwe kabisa, kila akiona mtu anaumwa, anajua atakufa tu.
“Elvin!” Eric alikuwa akiwaza, kama aliyekumbuka akamwita tena. “Vipi Eric?” “Tulikuwa na kaka yetu anaitwa Mat. Mama alisema Kaka Mat pia atakuwa na sisi. Lakini nilimsikia mke wake akimwambia….” Eric alitulia kidogo. “Alimwambia nini?” Elvin alimuuliza aliposhindwa kusema. “Lakini usimwambie Bella.” “Sitamwambia.” “Naomba usimwambie. Bella ataumia sana.” “Niambie tu.” “Nilimsikia akimwambia Kaka Mat, hapendi kumuona Bella pale nyumbani kwao, na hataki Bella awe anakwenda hata kule dukani kwao. Na ili Kaka Mat asionane na Bella, alimwambia lazima wanifukuze mimi pale nyumbani kwao. Sasa unajua kilichoniuma ni nini?” “Nini kilikuumiza Ric?” “Kaka Mat hakututetea kabisa. Alinyamaza, wakati sisi ni wadogo zake. Mkewe alikuwa ananinyima chakula, halafu ananiambia nifue. Unajua mimi sijui kufua?” “Sifahamu kama hujui kufua.” “Sijui kufua, halafu sipendi kabisa hiyo kazi. Nikiwa nyumbani Bella ndio ananifulia nguo zangu zote mpaka soksii au anawalipa watu watufulie. Sasa yule mke wa kaka Mat akawa ananipa nguo nyingi sana nifue, halafu ngumu sana. Akawa hanipi chakula mpaka zitakate. Na mara nyingi nilikuwa nashindwa kuzitakatisha, sababu ya vidonda. Nilikuwa natokwa na vidonda sana mikononi sababu yakufua. Sasa nikawa namwambia Kaka Mat, amwambie mke wake asinipe nguo za kufua, unajua kaka Mat aliniambiaje?” “Alikwambiaje?” Elvin alikuwa akimsikiliza kwa makini Eric aliyejawa hofu. Alikuwa akiongea kwa kutetemeka. Elvin aliona amsikilize tu, pengine angetulia. Na pia ilikuwa ni njia mojawapo yakuwafahamu zaidi.
“Usimwambie Bella lakini, atalia sana.” “Sitamwambia.” “Alikuwa ananiambia nijikaze mimi mtoto wa kiume, hata vile vidonda nisiviwekee dawa, vitageuka kuwa sugu nitazoea. Unafikiri vilipona?” “Havikupona?” Elvin akamuuliza kama kumuonyesha bado yupo na yeye. “Havikupona kabisa. Tena ndio vilikuwa vikizidi kuuma akiniambia nioshe vyombo. Si unajua ukiosha vyombo nilazima utumie sabuni?” “Nafahamu Ric.” “Basi ile sabuni ikiingia kwenye vidonda ilikuwa inauma sana. Usije kumwambia Bella kabisa. Atalia sana.” “Siwezi.” “Unajua siku alipokuja kunichukua kwa kaka Mat akakuta naosha vyombo juani, Bella alilia sana mpaka akashindwa kuendesha gari kwa kulia?” “Sikuwa nafahamu hilo.” “Alilia sana. Hata tulipofika hotelini aliendelea kulia. Unajua Bella hapendi mtu anitese kabisa?” Eric akauliza tena. “Nimemuona.” “Basi yupo hivyo tokea tupo shuleni. Bella ananipenda sana mimi. Na ukitaka kumuona amekasirika, unifanyie mimi kitu kibaya. Huwa hapendi kabisa, anakasirika sana. Unajua pia huwa anafanyaje?” “Sifahamu Ric.” “Huwa pia analia sana. Huwa anawaambiaga watu ni heri umfanyie  yeye kitu chochote kibaya, lakini sio mimi mdogo wake. Bella ananipenda sana kama mama alivyokuwa ananipenda. Usimuone vile. Ananipenda sana, ni heri akose yeye ila mimi nipate.” Ric alitulia kidogo kama anayefikiria kitu.
“Nataka kumuona Bella.” “Subiri, wakimrudisha tutaenda.” “Huko walipompeleka si atakuwa peke yake? Labda mimi niende nikakae naye. Sipendi awe peke yake sasa hivi akiwa mgonjwa.” Eric alitoa wazo. “Au mimi ndio niende, wewe unisubiri?” Elvin alimuuliza swali lakumfanya yeye mwenyewe amkubalie. “Sawa. Lakini akiniulizia tu uje unite, ujue ananitaka mimi.” “Nitafanya hivyo, Eric.” Elvin akasimama na kumuacha Eric amekaa kwenye benchi akiwaza.
Bella alifanyiwa vipimo, lakini kila kitu kilikuwa sawa. Hakuonekana na tatizo lolote kubwa ndani ya kichwa chake. Waliruhusiwa na kupewa dawa ya kutuliza maumivu. “Nina usingizi sana Elvin.” “Naona turudi tu nyumbani ukapumzike. Unaonekana umechoka sana. Ric alikuwa anakuulizia, anawasiwasi sana na wewe.” “Najua atakuwa na wasiwasi. Muoga sana. Yeye akimuona mtu anaumwa ndio anachanganyikiwa kabisaa. Naomba mtandio wangu nijifunike ili asilione hili jeraha. Atalia sana akiniona hivi, anaweza asilale.” Elvin alimsogezea mtandio wake, kichwa kilikuwa kimeshatulia, maumivu makali aliyokuwa nayo yalikuwa yameisha. Alijifunga vizuri, akavaa miwani yake kubwa, mweusi kabisa iliyoweza kuficha macho yake, akajaribu kuvuta pumzi mara mbili tatu, ili kujiweka sawa anapokukutana na mdogo wake. Elvin alikuwa akimwangalia.
 “Nikushike mkono.” “Asante, lakini hapana Elvin. Nitamuogopesha sana Ric. Hata hivyo nipo sawa sasa hivi. Ni kuchoka tu.” Bella alitoka akiwa anatembea. Eric alipomuona, alimkimbilia akamkumbatia. “Nilikuwa naogopa Bella. Unaumwa nini?” “Kichwa ndio kilikuwa kikiuma sana. Lakini wamenichoma sindano, kimepona kabisa.” “Afadhali. Tutaenda kwa mama?” “Wamenishauri nikapumzike kabisa. Inabidi turudi nyumbani nikapumzike. Najua unatakiwa shuleni siku tatu zijazo, usiwe na wasiwasi, nitakuja kukufuata shule ili twende kwa mama. Sawa?” “Sawa. Upone Bella. Sipendi kukuona unaumwa.” Eric alianza kulia. “Usiogope bwana. Mbona nimeshapona. Natakiwa kupumzika tu kwa kuwa wamenichoma sindano ya usingizi ili nilale kabisa nipumzishe kichwa, lakini nimeshapona.” “Nakupenda Bella.” “Hata mimi nakupenda Ric.” Eric alifuta machozi akambusu dada yake shavuni, lakini hakuona jeraha. “Asante Ric. Twendeni sasa.” Walirudi tena kwenye gari, ikabidi Elvin ndio awe dereva tena.
Alitamani kama waagane njiani ili asifike pale hotelini wanapoishi, lakini Bella alikuwa amechoka sana, asingeweza kuendesha tena. Alipomtajia wapi wanaenda, alijilaza kwenye kiti cha gari na kupotelea usingizini.
Walifika hotelini, Eric akamuelekeza sehemu ya kuegesha gari, ambapo anamuona dada yake kila wakati akiliweka hapo. Alimwambia ni karibu na chumbani kwao. Bella alikuwa amelala kabisa. “Unaweza kumbeba?” Eric alimuuliza Elvin. “Naweza, unafikiri nimbebe?” “Ingekuwa vizuri, ili tusimuamshe.” Eric alinong’ona, Elvin akacheka. “Haya. Lakini itabidi wewe ufunge gari.” “Nitabeba na pochi yake.” Eric aliendelea kunong’ona. Elvin alienda upande alipokuwepo Bella, akamfungua mkanda, akamtoa pale kwenye kiti taratibu akambeba. Eric alifunga gari harakaharaka akakimbia mbele ya Elvin kuonyesha chumba chao na kufungua mlango. Elvin alimuweka kitandani taratibu, akamfunika shuka vizuri, mpaka upande wajeraha, akauficha ili Eric asimuone, kisha akakaa pembeni yake akimwangalia.
“Njaa inaniuma Elvin.” “Unataka nikakuletee chakula gani?” “Hapana, nikupiga tu simu hapo mapokezi, halafu watatuletea. Wewe unataka kula nini?” “Nitakula baadaye. Wewe agizia tu.” Elvin alikuwa haelewi maisha anayoishi Bella na mdogo wake. Yalionekana ni ya gharama sana, mtu wakawaida hawezi kuishi vile. Gari yenyewe ya Bella, ilimbabaisha sana. Ilikuwa gari ya kisasa, ilibidi kutumia akili kuiendesha bila kuuliza uliza, kwani haikuwa na sehemu ya kuingiza funguo kama gari nyingine, ilitumia rimoti tu na iliwashwa kwa kubonyeza ile sehemu ya kuingizia funguo.
Eric alipiga simu mapokezi. Akaagiza chakula chake. Baada ya muda Elvin akaona muhudumu anaingia na chakula. Vile kilivyoletwa tu, jinsi kilivyobebwa na kigari maalumu, Elvin alibaki na mshangao.  Kilipambwa maridadi. Juisi ilivutia kwenye glasi. Matunda yalipangiliwa vizuri. Visu na uma. Vyote viliashiria pesa yakutosha, inamwagwa pale. Eric alikula, muhudumu akarudi kutoa vyombo, akageukia tv na kuanza kucheza game.
**********************************

Ujumbe akaingia kwenye simu ya Elvin. Elvin aliitoa simu yake mfukoni na kuanza kusoma. Ulikuwa ujumbe kutoka kwa Irene. ‘Naomba leo usiku tuonane Elvin. Ninahamu sana na wewe. Nahisi sijakwambia hivyo vyakutosha. Nakuahidi kubadilika Babe. Umekuwa kimya kwa muda mrefu sana mpenzi wangu. Tafadhali mpenzi, naomba leo tuonane. Hata kama ni kwa dakika chache tu, lakini nataka kukuona.’  Elvin alibaki akiangalia simu yake kwa muda, kisha akarudisha mfukoni kwake, hakujua kama yupo tayari kuonana na Irene au bado anahitaji muda. Alikaa pale zaidi ya msaa matatu akimsubiria Bella aamke.
Simu yake ilianza kuita mfululizo ndani ya mfuko wake, alihangaika kuitoa, kwa haraka ili asimuamshe Bella, lakini alishachelewa. Bella alijigeuza, giza lilishaanza kuingia. Elvin aliikata ile simu. “Pole, nimekuamsha.” “Hamna shida, hata hivyo nimelala vyakutosha.” “Vipi unajisikiaje sasa hivi?” “Kichwa kimetulia kabisa na nimelala nimepunguza uchovu. Jana sikulala kabisa.” “Pole.” Simu ya Elvin ilianza kuita tena, Bella alibaki akimwangalia, mwishowe aliamua kupokea. “Vipi Irene?” “Ulipata ujumbe wangu?” “Ndiyo.” “Mbona hujajibu sasa, na nimeona umekata simu yangu! Kwani uko wapi?” Elvin alitabasamu huku akitingisha kichwa kama kusikitika. “Elvin?” Irene aliita kwa ukali. “Umepiga kutaka kujua nilipo au umepiga kwa kuwa umesema unahamu na mimi unataka kuniona?” Irene akanyamaza. “Naomba nikupigie baadaye.” Elvin akamuaga. “Irene? Unanisikia? Naomba tuongee baadaye. Nitakupigia.” “Sawa.” Elvin alikata simu na kuirudisha mfukoni.
“Elvin!” Bella akaita kwa utulivu sana. “Unaweza kwenda tu hata sasa hivi, mimi najisikia vizuri. Tutakuwa sawa tu, nakushukuru.” Elvin hakujibu kitu alikaa kimya kwa muda kama anayefikiria kitu. “Unataka kula nini?” Akamuuliza Bella. “Nasikia njaa, lakini sina hamu yakula kabisa.” “Ngoja nikatafuate chakula, tuje kula wote.” “Asante Elvin. Nakushukuru.” Elvin alimtizama Bella akatabasamu. “Karibu. Nitarudi baada ya muda mfupi.” “Kwa nini tusiagize chakula hapahapa? Wana vyakula vizuri sana.” Elvin alisita kidogo. “Sitakawia, nitarudi baada ya muda mfupi sana. Kwani kuna chakula maalumu unachokitaka?” “Hapana. Sijisikii kula kabisa. Natamani kulala tu. Mwili umechoka. Hata nikilala bila kula ni sawa tu.” “Lazima ule kidogo, ndio ulale. Sitachelewa, nitarudi baada ya muda mfupi.” Elvin alitoka, Eric alikuwa kwenye michezo yake, hakuwa hata na habari na mtu. Kila anapokuwepo kwenye games zake, aliweka akili zake zote huko. Na aliweza kukaa siku nzima bila kula wala kunywa, akiwa anacheza tu. Mara nyingi Bella alikuwa akimpokonya remote, na kutoa headphones masikioni mwake ili angalau waongee, au ale na kuoga, lasivyo hakuwa akikumbuka kabisa.
**********************************
Bella hakutaka kumsumbua. Alijivuta ndani ya shuka akabaki anawaza. Alikumbuka vitendo vyote vibaya, Mzee Masha anavyomtendea, jinsi anavyompiga na bado akimlazimisha mapenzi hapo hapo, Bella alianza kulia. Hofu ya kifo cha gafla ilimjia. ‘Ningeanguka vibaya jana, ningeweza kufa. Au jinsi anavyojua kunipiga mateke anaweza kupasua kitu cha hatari ndani yangu, akaniua. Ric atabaki na nani? Nitaendelea kuishi hivi mpaka lini?’ Bella aliendelea kuwaza huku akilia mpaka Elvin aliporudi. “Kaa tule Bella. Nimeleta chakula, naamini utakipenda.” Kimya. “Bella?” Elvin alimsogelea. “Mbona unalia?” Bella alijitahidi kunyamaza lakini alishindwa, kilio cha kwikwi kilimkamata, alishindwa kuongea kabisa.
Alisimama kwenda chooni na simu yake. Akaanza kujipiga picha uso mzima, akajaribu kuosha uso wake ili kutulia, kisha akatoka akiwa ametulia kidogo. “Tunaweza kwenda kula hapo nje?” Bella akauliza. “Sawa.” Elvin alibeba chakula wakatoka kwenda kukaa sehemu inayoangalia bahari.
“Hofu ya kifo, yamfanya Bella kumkabidhi Eric kwa Elvin.”
Kitendo cha Elvin kuendelea kuwepo pale pamoja nao, bila kuonyesha kuchoka, kilimgusa sana Enabella. Akaona ndiye mtu pekee anayeweza kumkabidhisha Eric, mdogo wake. “Elvin!” Bella aliita baada ya kukaa kimya muda mrefu kidogo. “Maisha yangu hayatabiriki, sijui hata kesho kama nitakuwa hai. Nakuomba nikukabidhi hii kadi ya benki, inapesa nyingi kidogo, ndipo hata mshahara wangu unapoingia. Sijawahi kutoa humo hata shilingi. Nahifadhi kwa ajili ya Ric tu. Zinaweza kumtosha Ric kumaliza shule yake, mpaka atakapofika chuo. Mungu akiendelea kunipa uzima, nitakuwa naweka mara kwa mara. Nakuomba sana Elvin, ukisikia nimekufa, au usiponiona kwa siku hata tano mfululiza, na usione hata email yeyote kutoka kwangu, ujue kuna kitu kibaya kimenitokea. Cha kwanza naomba ukamchukue Ric shuleni, ukae naye mpaka utakapojua nilipo au kama nimekufa iwe mpaka umeona nimezikwa kabisa. Hakikisha mtu yeyote hamfikii mpaka utakapoona nimezikwa ndipo unaweza kumuacha awe huru. Unafikiri utaweza kunisaidia?” Elvin alikuwa kwenye mshtuko mkubwa sana.
“Sitaweza Bella, mpaka uwe umeniambia nini kinaendelea.” “Nitakwambia Elvin, lakini sio leo. Kama Mungu akinipa uhai, nitakwambia kila kitu. Lakini naomba isiwe leo?” “Kwa nini Bella? Au huniamini.” “Nakuamini sana Elvin, lakini wewe ukijua tu kinachoendelea, nitakuweka matatizoni. Halafu tutamuacha Ric peke yake, tena kwenye matatizo makubwa sana. Sina mtu mwingine ninayeweza kumwamini na Ric, ila wewe. Kaka Mat angekuwa yupo na sisi, ningekuwa nina tumaini jingine. Lakini sasa hivi naogopa Elvin, naona nimebakiwa na wewe tu. Jana nilianguka vibaya sana, nafikiria kama sikuwa nimeangukia uso, nikaangukia upande mwingine wa kichwa labda sasa hivi ningekuwa nimekufa halafu Ric angeteseka sana. Ndio maana nakushirikisha ili ujue. Tena hizo siku tano nilizokwambia nikama yuko shuleni. Lakini kama yuko nyumbani, unajua yuko likizo na mimi, halafu ikafika hata jioni hujanisikia, naomba mtafute Ric tafadhali. Nitajitahidi niwe nawasiliana na wewe angalau mara moja ndani ya masaa 24. Japo salamu tu ili kukujulisha kama nipo. Tafadhali Elvin.” “Nitafanya hivyo Bella.” Elvin alifikiria kidogo.
“Nikuulize kitu Bella?” Bella alifikiria. “Kama nitaweza kujibu nitajibu Elvin, uliza tu.” “Mtakuwa mnaishi hapa maisha yenu yote?” “Nitatafuta nyumba haraka sana. Yaani nikipona tu, nitatafuta nyumba ninunue. Sidhani hata kama nitajenga, na nikiipata tu wewe ndio utakuwa mtu wa kwanza kukuonyesha ili upafahamu. Na nitaomba ukae na hiyo hati ya nyumba kwa ajili ya Ric, ili asiishi maisha ya kutangatanga. Sifurahii hivi tunavyoishi Elvin, lakini kwa sasa sina jinsi nyingine.” Elvin alibaki kimya akifikiria.
“Labda naweza kukusaidia Bella. Kwa nini usinishirikishe.” Bella alianza kulia. “Siwezi Elvin. Naomba tuyaache kabisa, ila ujue nakushukuru, na ninaomba unisamehe. Najua nakupa majukumu mazito, tena ukiwa hutufahamu hata kidogo, lakini sina jinsi. Sina mtu mwingine. Nahisi Mungu amekuleta kwenye maisha yetu kwa wakati sahihi, sitaki kuchelewa kukuomba msaada, nikisubiri tuzoeane sana, kwa kuwa sijui hata kesho itakuaje.” “Hamna shida Bella, naomba uache kulia kichwa kitauma. Kula kidogo, kisha twende ukalale.” Bella alijitahidi kutulia.
Akala, wakarudi chumbani wakamkuta bado Eric amevaa ‘Headphones’ zake huku anacheza.  “Hivi huyu alikula kweli?” Bella akauliza. Eric hakuwa hata na habari na kinachoendelea. Akili zake zote zilikuwa kwenye mchezo anaocheza. “Aliagiza chakula, akala.”  “Hapo ni mpaka nimpokonye hiyo michezo yake ndio akili yake inamrudia. Hapo alipo hajui hata kama kuna watu ndani ya hiki chumba.” Elvin alicheka huku akimtizama Eric.
“Nataka nioge kwanza ndipo nilale. Sitaki kukuchelewesha. Unaweza kwenda tu.” “Nitakwenda Bella, usiwe na wasiwasi.” “Usije ukafikiri nakufukuza, sitaki uwe matatizoni.” “Nenda ukaoge.” Bella alitabasamu na yeye, akaingia kuoga, akatoka akiwa ameshavaa nguo zakulalia. “Njoo hapa ulale vizuri.” Bella alicheka kidogo. Akapanda kitandani, akajivuta karibu na Elvin. “Nisikilize Bella. Naomba niangalie.” Bella alikaa vizuri akamgeukia Elvin. “Ninatisha sana?” Bella aliuliza. “Usijali, utapona. Nimeshakuona ukiwa kwenye hali mbaya kuliko hiyo, na ukapona, najua utapona tu.” Elvin alitoa ule mtandio na kuacha sura ya Bella wazi. Alimshika taratibu na kwa upendo pale penye jeraha. “Pole sana.” Machozi yalianza kumtoka Bella. “Asante.”
Elvin alimfuta machozi nakumshika mikono yake yote miwili. “Nisikilize Bella. Naweza nisiwe msaada mkubwa sana kwako, lakini amini Mungu yupo na anauwezo wa kukusaidia. Wazazi wangu walinifundisha kitu kimoja kikubwa sana, ambacho huwa nakitumia tokea mtoto na kinanisaidia.” “Kitu gani?” Bella akauliza. “Waliniambia hivi, kila ninapokuwa kwenye matatizo, nakuona nimekwama kabisa, sina msaada wa aina yeyote ule, na hakuna mwanadamu anayeweza kunisaidia, waliniambia huo ndio wakati pekee wa kumuachia Mungu. Mama yangu huwa anamwita Mungu wa ‘imposibilities’, yaani Mungu wa yasiyowezekana. Anasema yale ambayo ndio magumu sana kwetu au kwenye akili za binadamu, yeye Mungu ndio anapenda kuyafanya ili apate sifa au atukuzwe. Sasa cha msingi ni kufanya hivi, unamuomba yeye Mungu, halafu unamuachia yeye afanye.” Bella aliguna.
“Mbona unaguna?” “Unajua kuna wakati Kaka Mat alikuwa akitupeleka kanisani. Nilisikia Mungu hapendi watu wenye dhambi, Elvin. Na mimi naishi kwenye dhambi, na sijui lini ninatoka kwenye hayo maisha. Sasa namuombaje huyo Mungu?” “Japokuwa sijui unaishije kwenye dhambi, au sijui unatenda dhambi gani ambayo huwezi kuacha, lakini lazima ujue Mungu hachukii wenye dhambi, ila anachukia dhambi. Kama hivi unavyoongea na mimi, ndivyo hivyohivyo mwambie yeye atajua jinsi gani anaweza kukusaidia. Umesikia Bella? Usiache kabisa kuongea na Mungu. Hata iweje, pata muda wa kuongea na Mungu, mwambie kila kitu unachotamani, utashangaa mambo yanavyokubadilikia.” “Kweli Elvin?” Bella alianza kulia. “Kabisa Bella. Jaribu uone.” Bella alifikiria.
“Nipo katika wakati mgumu sana Elvin, ni kweli nahitaji msaada.” “Basi usilie, tuombe wote.” “Sijui kuomba.” “Hakuna maneno sahihi yakuomba. Ila ujue wewe unaongea na baba yako. Ongea nae chochote unachotaka. Hata ukiongea naye mawazoni, ukaomba bila yakutoa sauti, yeye anasikia. Tuombe wote, ili usikie mimi ninavyoongea naye, halafu na wewe unaweza kuomba kimya kimya.” “Sawa.” Elvin alishika tena mikono ya Bella akaanza kumuomba Mungu taratibu. Akamuombea Bella na Eric, akawaombea ulinzi, amani na furaha, kisha akamaliza.
Machozi yalikuwa yakimtoka Bella. “Nimefurahi sana Elvin, asante.” Elvin akacheka. “Umeona ilivyorahisi?” “Sana. Umeanza kwa kumuomba Mungu msamaha kwa yote uliyotenda, kwa kuwaza, kutenda au hata kutotimiza wajibu, kisha, ukaanza kumshukuru, ndio ukaanza kuomba.” Elvin akacheka. “Kumbe ulikuwa ukisikiliza?” “Sana tu.” Wote walicheka. Elvin aliongea naye maneno yakumfariji Bella, mpaka akaona sura ya huzuni ya Bella imebadilika, ikawa ya furaha. “Nitakuwa nikikuombea Bella. Kila siku.” “Kwa kuwa sasa hivi na mimi najua kuomba, nitakuwa nikikuombea wewe na Ric kila siku.” “Asante. Basi naomba ulale, naamini mpaka kesho uvimbe utakuwa umepungua.” “Nikipitiwa na usingizi, kabla hujaondoka, naomba umwambie Ric azime tv, aache kucheza alale.” “Hatanikasirikia?” “Hapana. Ric ni mtoto rahisi sana kuishi naye. Nimsikivu sana. Hata hivyo amechoka, akizima tu hapo atalala.” “Basi usiwe na wasiwasi, nitaongea naye.”  Bella alijisogeza kwenye mto vizuri ili alale. Elvin naye akajivuta karibu kabisa na Bella, akaegemea kwenye kitanda, akamfunika vizuri, kabla hata Elvin hajakaa sawa, tayari alimsikia Bella akihema vizuri, akiashiria ameshalala. Alicheka kidogo na kubaki akimtizama kwa muda.  Alihakikisha Ric ameoga, akawazimia taa, nakuwaacha wamelala.
**********************************
Wakati anatoka tu, Irene akapiga tena simu. “Nimeona nikupigie, naona masaa yanazidi kwenda, halafu hupigi simu kama ulivyoniahidi.” Elvin alinyamaza. “Sasa unakuja?” “Ulitaka tuonane wapi?” Elvin akamuuliza. “Popote tu.” “Kwa kuwa nimechoka, naomba uje nyumbani kama baada ya saa moja kuanzia sasa, nitakuwa nimeshafika nyumbani na nitakuwa nimetulia.” “Kwani ulikuwa wapi? Maana nilikufuata leo mpaka ofisini kwako, baada ya kutokujibu ujumbe wangu, baba yako ameniambia upo likizo. Nyumbani haukuwepo na ofisini hukuwepo pia, na mama yako alishaniambia ulirudi tayari kutoka safari yako na Bella. Sasa leo ulikuwa wapi? Maana hata Bella mwenye hakuwepo ofisini mpaka jioni hii wanafunga ofisi, au ulikuwa naye?” Irene aliendelea kumkaba Elvin. “Nitakuona baadaye Irene, kwaheri.” Elvin alikata simu.
Alipofika tu nyumbani kwao, alimkuta Irene alishafika. Alisimama mlangoni akabaki akimwangalia. “Unaweza kuingia tu ukaoge, mimi nitakusubiria.” Elvin aliinamisha kichwa, akabaki akifikiria pale pale mlangoni.
*Tumaini jipya kwenye maisha ya Bella. Je itasaidia?
*Maji yameanza kuzidi unga kwenye maisha ya Elvin. Wanawake wawili, wote wakionyesha  kumuhitaji sana. Irene king’ang’anizi  wa Penzi la Elvin, na Bella kiumbe anayeanza kumfanya achukie kuwa naye mbali japo anazidi kumchanganya
Nini kitatokea? Usikose
Sehemu ya 8.

0 comments: