Story
is mine - ni Wangu! Part 1, Sehemu ya 8
Nanaa alitoka pale mida ya
saa 8:30 mchana. Akatembea kidogo tu, akajikuta amefika kituoni. Ndipo
akagundua pale ni Tabata Barakuda. Akasubiri daladala ya kumpeleka Kariakoo
kutafuta zawadi ya Fili. Hakukaa sana kituoni, daladala ikapita. Akapanda mpaka
Kariakoo. Jasho lilikuwa likimtoka kila alipokuwa akifikiria kitu cha
kumnunulia Fili kama zawadi. Kila kitu alichokiona cha Fili pale kwao, kilikuwa
cha thamani. “Nitanunua nini angalau kifanane na hali yao?” Nanaa aliwaza.
Baada ya kuhangaika akizunguka madukani, akaona mpira wenye picha ya Spider Man,
unauzwa. Kwa kuwa alisikia akijiita Spider Man,
akanunua na kuondoka zake.
Wakati yupo njiani
kuelekea kwao, Zena akampigia tena simu kumsisitiza asichelewe na kumwambia
wakutane Mlimani city, asiende nyumbani kwao. Nanaa akakubali. Akafika nyumbani
kwao, akaoga kwa haraka. Kutoa jasho na vumbi la Kariakoo, akatoka kuelekea
Mlimani City.
Walikubaliana wakutane
nje ya duka la nguo la Maikos. Nanaa alisimama pale, akampigia simu Zena. “Nimefika.”
“Subiri dakika moja tu.” Nanaa
akakata simu. Akamuona Zena anakuja na vijana wawili. Nanaa akacheka na
kutingisha kichwa. “Sasa
unacheka nini?” Zena
aliuliza. Nanaa akamvuta pembeni kwa nguvu. “Maneno yote yale kumbe nia yako nikuja
kuniuza mimi na wala huna ishu unayotaka nikusaidie.” “Sio kwa mtu mbaya Nanaa
shoga yangu. Njoo nikutambulishe. Utampenda.” “Wewe ni muongo Zena. Sijui kwa
nini nilikuamini.” “Chonde shoga yangu. Naomba usiniabishe hapa.” Nanaa hakuwa akiamini aliweza vipi
kumuamini Zena, tena kwa uongo wa kijinga kama ule.
Zena na yeye akamvuta
kumrudisha kwa wale vijana. “Huyu
anaitwa Yasini, ndie rafiki yangu. Na huyu ni rafiki yake anaitwa Jeff.”
Akawageukia wale vijana wawili. “Huyu ndiye Nanaa. Shoga yangu yangu
kipenzi. Tupo sisi watatu. Tia tu ndio amekosekana hapa.”
Nanaa hakuwa anaamini. Alibaki akimtizama Zena. “Tumefurahi kukufahamu Nanaa.” Jeff akaitika. “Asante.” Nanaa alishindwa hata kujibu na mimi.
Kwani hakukusudia kuangukia kwa mwanaume wakati huo. Hasa wanaume aliokuwa
akiunganishwa na Zena.
**************************************************
Na Zena huo ndio ulikuwa
mchezo wake. Mwanaume wa mwisho alimfanyia hivyo hivyo. Alimwita Nanaa mahali
akimwambia amekwama mahali. Wamekula yeye na Tia, lakini wakagundua hawana pesa
ya kulipa. Wanaomba awafuate kwenye huo mgahawa. Nanaa akaacha shuguli zake
zote, akapanda daladala mpaka Sirender Bridge pub, ili kunusuru mashoga zake.
Alipofika pale akapiga simu kuwaambia hawaoni. Zena kwa ujasiri wote,
akamwambia atafute meza akae, wameenda chooni mara moja watatoka. Tena hapo ni
baada ya kumuuliza aina ya nguo alizokuwa amevaa.
Babaada ya Nanaa kukaa
kwenye hiyo meza, akashtukia anafuatwa na kijana, aliyemsalimia kwa kumtaja
jina kana kwamba wanafahamiana. Akiwa kwenye mshangao, yule kijana ndipo
akamwambia ameunganisha na Zena. Anatafuta mchumba aliyetulia aoe. Nanaa hakuwa
anaamini mchezo aliomchezea Zena. Akajua wazi alishakula pesa ya yule kijana.
Tena ndio walikuwa wamemaliza mitihani, Nanaa ametulia kwao.
**************************************************
“Tunaweza kwenda kula sehemu?” Yasini akauliza kiungwana. Nanaa
akacheka kwa kuguna. “Samahani.
Mimi nimetoka kula muda si mrefu. Na baada ya muda mfupi sana kuanzia sasa,
natakiwa kwenda mahali.” “Una miahadi ya saa ngapi?”
Jeff alimuuliza Nanaa. “Baada
ya dakika 45 kuanzia sasa.” Nanaa akajibu. “Basi haina shida.
Kama ni sawa. Na tunakuomba. Twende hapo ‘Saad restarant’. Muda ukifika,
nitakupeleka.” Nanaa
alicheka, ikabidi akubali.
Waliingia hapo kwenye
hiyo restaurant, wakatafuta meza wakakaa. Walionekana ni vijana waungwana na
watu wazima walio tulia. Wao waliagiza chakula na vinywaji, Nanaa akaagiza maji
ya kunywa ya baridi. Akaletewa kwenye glasi. Wakaanza kula. Hapakuwa na maneno
mengi sana. Yalikuwa mazungumzo ya maana tu. Jeff akamuuliza Nanaa ni wapi
anafanya field yake. Kama anapafurahia. Wanamlipa kutokana na kazi wanazompa.
Anampango wa kufanya hapo kwa muda gani. Hayo yote yalikuwa maswali waliyouliza
Jeff na Yasini kwa kupokezana.
Jeff mwenyewe ndiye
aliyemkumbusha Nanaa juu ya miahadi yake. Nanaa akashangaa. “Sitaki sisi ndio tuwe
sababu ya kutokufanikisha miahadi yako.” Nanaa alitabasamu. “Nashukuru.” “Tunaweza
kukupeleke tu mpaka huko, kama ni sawa. Vinginevyo tutakuchukulia taksii.”
Jeff aliongea na tabasamu usoni. “Sio sehemu ya siri. Nimealikwa kwenye
birthday ya mtoto wa bosi wangu. Anatimiza miaka 5. Kwa hiyo mnaweza
kunisindikiza tu, kama mtapenda. Lakini nina uzoefu mzuri sana na daladala.” Nanaa
aliongea kwa tabasamu. “Basi kwa kuwa tuna usafiri, nafikiri tukusindikize tu.”
Wakasimama wote kwa pamoja. Wakatoka.
**************************************************
Jeff na Yasini
walitangulia mbele, Nanaa na Zena wakabaki kimya. “Hebu niambie shoga
yangu. Hapo vipi?” “Ukoje wewe Zena?” “Acha hasira, niambie ukweli. Huyu wa
safari hii muugwana.” “Sasa wewe huyu Yasini
si mkristo? Mzee Mgiza utamwambia nini?” “Hapo ndipo atakapojua penzi halina
dini. Nilivyompenda huyu kaka! Hamna mtu ataniambia kitu nikaelewa. Labda na yeye
ajekugeuka tapeli kama Dula.” Nanaa alimwangalia Zena mtoto wa
ustadhi, asiamini. Baba yake alijulikana mtaani kwa kushika dini. Alikuwa Mzee
mstaarabu na mwenye maadili. Swala 5, zisizopungua kila siku.
**************************************************
Jeff na Yasini walikaa
mbele, Nanaa na Zena wakakaa nyuma. Sehemu yenyewe waliyokuwa wakifanyia
shuguli nzima ya Fili ilikuwa Masaki. Wakaondoa gari kuelekea Masaki. “Umefurahia chakula,
Zena?”
Yasini alikuwa ndiye dereva, alirusha
swali. “Ndiyo.
Nashukuru.” Zena
alijibu huku akimkonyeza Nanaa. Akionyesha wazi amefurahia lile swali la
kuonyeshwa kujaliwa. Nanaa akatabasamu. “Hongera.” Alinong’ona. “Asante shoga yangu.
Mungu kanipumzisha.” Wote
wakacheka kwa pamoja. Nanaa akaanza kujifikiria maisha yake. Akapotelea
mawazoni.
“Si ndio hapa?” Jeff alimshtua Nanaa. “Sijawahi hata kufika.
Kama nyinyi ndio mnasema ni hapa, basi itakuwa hapa. Nawashukuru sana na
nawatakia wakati mzuri.” Nanaa
akashuka. Kabla hajafunga mlango, Jeff alimwita. “Abee!”
Nanaa
akarudisha kichwa ndani. “Naomba
tuzungumze kidogo.” Nanaa akamtizama Zena, akarudisha macho
kwa Jeff. Akakuta anamtizama. “Sawa.” Akakubali.
**************************************************
Nanaa na Jeff.
Wakatoka na kusimama
pembeni kidogo ya gari. Mbele ya uzio wa michongoma. “Naomba kesho
tuonane.” Jeff alivunja ukimya mara baada ya kuridhika wako
peke yao. “Mimi
sijui Zena amekwambia nini juu yangu. Lakini sina mpango wa kuolewa hivi
karibuni.” Nanaa
alikataa haraka sana. Jeff akacheka kidogo. “Sijasema nataka kukuoa Nanaa. Nimeomba
tukutane kesho.” Nanaa
akaingia aibu tena, akacheka kidogo. “Samahani. Nahisi kwa sababu namfahamu
Zena, ndio maana nimekuwahi mapema. Sitaki kukupotezea muda.” “Hata mimi
nisingependa kupotezewa muda.” Nanaa akainama na kufikiria.
“Nanaa?” “Nafikiria Jeff!” “Nini?” Jeff akauliza tena. “Najiona sipo tayari
na hizo heka heka. Na wewe unaonekana ni mtu mstaarabu, pengine ungenielewa tu.
Sipo tayari kwa mahusiano aina yeyote ile.” “Mbona vipingamizi vingi Nanaa?
Nimeomba tutoke. Kwa nini usikubali, ukasikia ni kwa nini nataka tutoke kabla
hujaanza kuweka vipingamizi?” Nanaa
akacheka tena kidogo. Lakini wazi alionekana hafurahii.
“Ulitaka twende wapi?” “Tutoke kwa
chakula cha usiku.” Nanaa alivuta pumzi. “Naishi na kaka yangu
Jeff! Siwezi kutoka usiku. Nitamwambia nakwenda wapi na wewe sikufahamu?” “Basi
tufanye iwe mapema.” “Labda hujanielewa. Ninaposema naishi na kaka yangu.
Namaanisha ndiye kama Mungu wangu wa pili hapa duniani. Ndiye mama yangu.
Nikisema mama, namaanisha ndiye aliyenilea tokea siku nimezaliwa natolewa
hospitalini mpaka hivi sasa. Kuninyonyesha, kuniogesha nakunivalisha mpaka
nepi. Ni kama baba kwangu, kwa kuwa ndiye anayehangaika kula. Kulala kwangu.
Ndiye anayehangaika na kuvaa kwangu tokea mtoto mpaka hivi sasa. Ni kama baba
anayesumbukia na soma yangu pia. Amechukua nafasi ya dada pia kwa kuwa ndiye
anayenishauri kwa karibu. Na ndiye mtu wa pekee katika maisha yangu ambaye yupo
karibu yangu tokea nazaliwa mpaka sasa. Siwezi kufanya lolote hasa nikiwa
nyumbani bila kumshirikisha yeye kwanza. Sasa hata nikikubalia tutoke mapema,
namwambia nini juu yako, Jeff wakati wala sikufahamu?” Nanaa alizidi kumsisitiza Jeff, ili
tu amuache.
Lakini bado Jeff
alipambana. “Unaweza
kumuaga tu na kumwambia kuna mtu nakwenda kuonana naye. Mwambie utamwambia zaidi
juu yangu baada ya mazungumzo yetu ya kesho tukitoka. Tukishakutana.
Tukazungumza. Ukajua unipe nafasi gani kwenye maisha yako, utakaporudi nyumbani
unaweza kumwambia chochote kile juu yangu. Lakini baada ya mazungumzo yetu.
Ninachoomba ni unipe tu nafasi Nanaa. Tafadhali.” “Mmmh!” Nanaa akaguna. Wazi alionyesha
hajaridhika
“Vipi?”
“Sijui kwa nini Jeff, moyo wangu unakataa. Naomba nipe muda wa kufikiria
tafadhali.” “Unafikiria nini wakati hata hujui ni nini nataka kuzungumza na
wewe? Si ungenisikiliza kwanza ndipo uniambie kama utataka kufikiria?”
Nanaa alitulia. “Nanaa
please!” “I don’t know Jeff. Naomba nifikirie hata huko kutoka. Sijajiandaa.
Naomba nikutafute nikiwa nipo tayari. Tafadhali Jeff. Najua ni nini
nazungumzia. Nahitaji muda.” “Unaniahidi kunipigia?” “Nafikiri.” “Nanaa!?” Jeff akamwita kwa masikitiko. “Sijui Jeff. Labda.
Sitaki kukupa ahadi za uongo. Mimi sio muongo Jeff.” Kwa
hakika Nanaa hakuwa na uhakika.
“Nanaa please.” “Kwa nini unanisihi
wakati hata hunifahamu? Umetajiwa tu na Zena. Unajuaje kama mimi ndio mtu
sahihi unayetaka kumwambia hicho unachotaka kuongea tukikutana?” “Hilo swali
naomba nilijibu tukitoka wote.” Nanaa
akacheka akionyesha wazi cheko lile sio la furaha. Hata uso wake ulionyesha
kutokukubaliana.
Wakasikia mtu anakohoa
upande wa pili wa ule uzio. Wote wakageuka. “Pole Danny mwanangu. Upepo huo.”
“Asante mama yangu. Upepo mkali kweli.” Danny akajibu. Wakasikia
watu wengi wanacheka. Ndipo wakajua kuna watu walikuwa wakiwasikiliza. Nanaa
akainama. Jeff akacheka. “Nitasubiri
simu yako Nanaa.” Jeff
akaaga. “Asante
kwa lifti. Nitakutafuta.” Jeff
akaondoka. Nanaa alibaki akiwaza.
Birthday ya Fili.
“Uwiii! Danny si mume wa
Grace? Sasa si watakuwa wamesikia kila kitu?”
Nanaa aliwaza akiwa amesimama pale pale. “Njoo tu Nanaa. Hatujawasikia kabisa.
Kwanza hatukuwa tukiwasikiliza.” Nanaa alitamani
kuanguka. Akasikia sauti za watu wakicheka zaidi. Nanaa akajua wapo kundi la
watu. “Nyamaza
Danny! Utamfanya ashindwe kuja.”
Alisikia
sauti ya Grace. “Uwiii!
Kwani na kaka James yupo hapo?” Nanaa aliuliza. “Yupo. Lakini
hajasikia kama utatoka kesho usiku.” Danny alijibu na kufanya
wazidi kucheka. “Uwiii!”
Nanaa alizidi kulalamika. “Njoo
Nanaa. Achana na Danny!” Alisikia
sauti ya kaka yake akimwita huku akicheka sana.
“Njoo mara moja kaka!” Nanaa akamwita kaka yake, lakini
akasikia wanazidi kucheka. “Nenda
kamlete mkwe wangu, James.” Alimsikia
Grace akiongea.
James akazunguka uzio,
akatoka kwenye kigeti kidogo. Alitoka anacheka. “Usicheke kaka.” “Usiwe na wasiwasi.
Twende.” “Naona aibu kweli. Natamani niondoke tu.”
Nanaa alijaribu kunong’ona zaidi, lakini bado akasikika. “Wala usione aibu
Nanaa. Nimekwambia hakuna aliyesikia.”
Danny
alidakia tena, vicheko vikazidi kuongezeka. Nanaa akajifunika uso. “Danny nyamaza bwana.
Ujue Nanaa akiondoka hapa, mwanao hatakata keki? Wewe fanya mchezo.” Hata James mwenyewe alikuwa anacheka
sana. Akamshika mkono Nanaa, akaongoza njia mpaka ndani.
Alikuwa akitembea nyuma
ya James. Aliishiwa nguvu baada ya kukuta hilo kundi la watu waliokaa hapo.
Alishindwa kujua akifika hapo aanze vipi. Mungu bariki Fili akawa amemuona
kabla hajawafikia. Akaanza kupiga kelele huku anamkimbilia Nanaa. Nanaa
akasimama. “Nanaa!
Nanaaa!”
Nanaa akafungua mikono kama kumlaki. Maana Fili alikuwa akija kwa mwendo kasi.
“Usimchafue bwana.” Grace alimuwahi kabla Fili
hajamkumbatia Nanaa. “Hamna
neno. Mwache tu.” Fili alikuwa amejaa michanga mpaka
kichwani. “Umechelewa.
Lakini bado sijakata keki. Leo Mama ameniruhusu kunywa soda wakati nakusubiri.” Fili alianza. “Kumbe ulikuwa
unanisubiri mimi?” “Ndiyo. Kwani ulikuwa hujui? Nilimwambia anko Geb akupigie,
akasema unakuja sasa hivi.” Fili aliendelea. “Mwache hata akae basi.
Unamdaka na maneno mengii. Ataondoka sasa hivi.” Alimsikia Danny
akiongea. “Eti
utaondoka, Nanaa?” Fili
aliuliza kwa upole.
“Njoo ukae hapa mwaya. Huyo atakuchosha
tu.” Grace alisimama huku
akimuonyeshea pakukaa. “Eti
utaondoka? Maana nimewaambia rafiki zangu wote kuwa unakuja. Wakataka kukuona.
Sasa utaondoka kabla hawajakuona?”
Fili
alirudia tena kuuliza. “Hapana.
Siwezi kuondoka, mpaka niwaone rafiki zako, tucheze wote ndio nitaondoka. Na
hii ndio zawadi yako.” Fili
akacheka kufurahia zawadi aliyopewa na Nanaa. “Asante
sana Nanaa.” “Karibu na samahani kwa kuchelewa.” “Mimi nimeshakusamehe Nanaa.” Fili
akajibu huku macho yapo kwenye zawadi. Wakacheka wote.
Nanaa akasogelea lile
kundi la watu wazima waliokuwa wamekaa, wakiangalia watoto wanavyocheza. Bado
alikuwa amembeba Fili wakati akifungua mfuko uliokuwa na zawadi yake.“Nanaa ameniletea
mpira wa Spider man!” Fili alifurahia sana. “Nilikwambia nini juu
yakufungua zawadi hapa? Nitakufinya masikio mimi. Kwa nini husikii?”
Danny alimbadilikia mwanae. “Si
ni ya Nanaa tu, ndio nimefungua?”
Wote
walicheka.
“Fili! Fili!” Liz akamwita. “Eeeh!” Fili aliitika. “Unaitikaje kama mtoto wa kike wewe?
Sema naam!” Danny
alimgombesha tena. “Naam!” Fili
akarekebisha haraka haraka. “Sasa
lini unamuoa Nanaa?” Liz alimuuliza kumchokoza. “Dad amesema mpaka
nipate hela nyingi, nimlipe kwanza anko James, halafu nimchukue Nanaa, niende
naye kwangu, nisirudi naye nyumbani.”
Kila
mtu alianza kucheka.
“Wewe Fili! Ndio nilivyokwambia hivyo?” Danny alimuuliza nakumfanya Fili
afikirie kidogo. “Umeruka
kitu kimoja.” Danny
alimkumbusha. “Ehe,
nimekumbuka. Dad amesema, nisome sana, nipate pesa nyingi, nimlipe
anko James, akinipa Nanaa, niende naye nyumbani kwangu, nisirudi naye nyumbani
kule kwa dad.” Kila mtu alikuwa anacheka sana.
“Itabidi ukazane sana. Bado una safari
ndefu sana.” Rafiki
mmoja aliongeza. “Shule
yenyewe bado hujaanza.” Mwingine alichangia. “Sio mbali sana. Dad
wangu amesema naanza jumatatu. Ameshanitafutia.” Kila mtu alikuwa
anacheka. Ni kweli Fili alikuwa mzungumzaji. Tena anaongea kwa ufasaha, bila
woga. Mama yake alikuwa akitingisha kichwa.
“Bibi Fili amesema atanisindikiza
kumlipa anko James pesa. Mimi sijui kuendesha gari, sioni mbele.”
Watu walizidi kucheka. “Kumbe
mama wewe ndio dereva?” Danny
aliuliza. “Nimepewa
hiyo kazi. Amesema yeye hafikii sehemu ya kukanyaga mafuta na kuweka breki. Kwa
hiyo mimi nimsindikize kwa anko James.”
Mama
Grace na Geb, au Mama G kama wengi walivyozoea kumwita, alijibu nakufanya watu
wazidi kucheka. “Bwana
mwanangu amejipanga. Lazima atamuoa Nanaa.” Grace aliongeza. “Tena Jeff akae mbali kabisa.” Danny
alifanya Nanaa afunike uso kwa aibu. “Bora
umemkatalia.” Danny aliongeza nakufanya watu wazidi kucheka. Mama G ndio kabisa mpaka
machozi.
“Nina
mpango wakuacha kazi, nasubiri mahari yangu kutoka kwa Fili.”
James alidakia. “Ujipange mwanangu. Huyo
anko James anapenda pesa kuliko benki.” Danny aliongeza. “Nitampa. Nitakuwa nazo nyingi sana.”
Fili alijibu kwa kujiamini na kufanya watu wazidi kucheka. “Mmemsikia Dume langu? Nipe namba ya simu ya Jeff nizungumze naye.”“Bwana
Danny muache Nanaa.” Grace alimwambia mumewe anyamaze huku yeye mwenyewe
anacheka. “Lazima taarifa zimfikie Jeff
King’ang’anizi. Jamaa kakaba kweli! Kila akikataliwa hivi, anang’ang’ania tu.
Haelewi!” “Ndio ikabidi uokoe jahazi Danny mwanangu?” “Kabisa mama. Mtu gani
hataki kuelewa?” Wakazidi kucheka huku Nanaa amejificha nyuma ya Fili na
yeye anacheka taratibu kwa aibu.
“Twende
Nana tukacheze.” Fili alimuokoa.
“Bwana wewe nenda kacheze na wenzako, mwache Nanaa apumzike.” Danny
alimkoromea mwanae. “Acha tu niende naye.
Leo ni siku yake, mwache afurahi.” Nanaa akamshusha, akamshika mkono.
Wakaanza kuondoka huku wengine wakicheka. “Najua
kuogelea, dad alinitafutia mwalimu akanifundisha kuogelea. Halafu pia najua kucheza
mpira wa kikapu na miguu. Nachezea kwenye timu ya mpira wa kikapu ya kina anko Geb. Mimi ndio mfungaji wao. Kila
jumamosi jioni huwa naenda naye mpirani. Wananitegemea mimi hapa.” Geb
alitingisha kichwa huku anacheka na wengine. Fili akaendelea. “Halafu huwa nacheza mpira wa miguu na dad
wangu pale pale nyumbani. Najua pia kukimbia. Mama yangu ananisifia najua sana
kuruka Kamba. Pia…” Fili aliendelea kujisifia kwa Nanaa.
“Daah!
Mwaangu kachanganyikiwa kabisa. Msikieni anavyojinadi kwa Nanaa. Vitu vyote leo
anajua kuvifanya yeye, wakati muoga kweli wa maji.”
Danny alifanya watu wazidi kucheka. “Bwana
mwanangu ameweza kuogelea. Mwalimu wake anayemfundisha kuogelea anamsifia
kweli.” Grace alimtetea. “Mmmh! Mbona
mimi nilivyompeleka mazoezini alikuwa analia mpaka ulipongea naye kwa simu,
ndio akakubali kuingia kwenye maji? Kioga kweli, utafikiri kitoto cha kike!”
Danny alimjibu mkewe. “Sasa wakati ule si
alikuwa bado hajazoea? Siku hizi mjuzi kweli. Muulize Geb ambaye pia huwa
anampelekaga kwenye mazoezi ya kuogelea.” “Hana lolote huyo mwanao. Maneno
mengii, muoga kama mama yake.” Danny alizidi kuchekesha watu.
**************************************************
Nanaa alianza kumsukuma
Fili na rafiki zake kwenye bembea. Walipeana zamu, Nanaa akawa anawasukuma. Mara
akamuona tena Jeff amerudi na kuingia mpaka ndani. Akamuangalia Jeff, kisha
akawaangalia wale waliokuwa wamekaa pale. Kina Danny. Akaona wote wameinamia
simu zao. Kama hawajamuona Jeff. Nanaa akamsogelea akiwa amembeba Fili. Lakini
wazi alijua kwa unamaji ule, wote wamemuona Jeff. “Vipi?” “Nimekumbuka
sijachukua namba yako ya simu, na Zena amesema hawezi kunipa. Nikuombe
mwenyewe.” Nanaa
akacheka kwa aibu. Akijua wazi kina Danny wanasikiliza. “Au basi chukua namba yangu
mimi ya simu. Kama unaona shida kunipa yako.” Jeff aliongeza.
Na yeye alijitahidi kuzungumza kwa sauti ya chini. “Hamna shida. Hapa nilipo sina simu.
Nimeiacha pale mezani. Nacheza na watoto. Chukua tu ya kwangu. Utanitumia
ujumbe ili niwe na ya kwako pia.” Nanaa alijibu taratibu. “Asante. Nitafanya
hivyo.” Jeff
alionekana kufurahia hilo wazo.
Jeff akatoa simu yake. “Sasa sio na wengine
muanze kukariri namba ya simu ya Nanaa. Mwenyewe ameamua kumpa Jeff tu.” Danny
aliongea kwa sauti. Mpaka Jeff akacheka. “Kwani huwezi kunyamaza Danny jamani!?”
Grace alimfinya. “Mimi nawajua binadamu mke wangu. Bahati ya Jeff wanaweza
kuikalia mlango wazi. Kabla hajafanikisha dinner ya kesho, wakamuwahi kwa
lunch.” Watu
walizidi kucheka mpaka machozi wengine yalikuwa yakiwatoka.
“Ningekuwa mimi Jeff, ningempa Nanaa
simu aandike tu. Asiitaje. Wote waliokaa hapa watu wa namba tupu. Tokea
wanaanza kuongea mpaka leo wanacheza na namba tu. Yaani wapo hapa mjini
wanalipwa kwa kuchezea namba kwenye maofisi ya watu. Nakuhakikishia Jeff, hawatashindwa kukariri
hizo tarakimu 10 tu za namba ya simu ya Nanaa. Ni ushauri tu kaka. Unaweza
kuuchukua au kuuacha. Na ujue wengi wao hapa bado hawajaoa na hawana hata
wachumba. Sasa juu yako Jeff.” Danny
aliongeza. Nanaa na Jeff walishindwa hata kuongea, wakabaki wanacheka. Nanaa
akiangalia chini, Jeff akiwatizama.
“Au kuondoa mzizi wa fitina. Chukua hii
kalamu na karatasi Jeff. Mimi nawajua binadamu. Hapo wote wasikio wazi. Wewe
unaandika kwenye simu, wenzio kichwani. Halafu ulogwe ukosee namba hata moja hapo,
utaandika maumivu. Maana hivi vichwa hapa, mimi navijua. Vinahistoria
yakutokusahau. Heri kuandika tu kimya kimya. Hata Nanaa akikosea kuandika hata
tarakimu moja tu, potelea mbali. Wote mkose. Kuliko wewe uliyehangaika hivyo vyote,
eti ukose. Halafu majamaa hapa yapate.”
Danny
akasimama na kumpelekea Jeff kalamu na karatasi.
“Mimi nakukabidhi wewe mwenyewe. Uamuzi
ni wako.” “Nakushukuru.” Jeff
alishukuru huku akicheka. “Tupo pamoja kaka.
Wema ndio asili yangu.” Danny
alijibu kiungwana sana huku akijisifia. Mama G, alikuwa akicheka mpaka machozi.
Jeff akamkabidhi Nanaa ile kalamu na karatasi. Nanaa akapokea, akaandika ile
namba akamrudishia Jeff ile kalamu na karatasi, yeye akarudi upande
walipokuwepo watoto na kuwaacha wazazi wao wakizidi kucheka. Jeff akamrudishia
Danny kalamu yake. “Asante.”
“Karibu Mkuu. Kila la kheri. Naamini hujapewa namba za gari.” Danny
akapokea kalamu na kumpa mkono. Mpaka Jeff akacheka. Akaondoka na kaucha huku
nyuma wanazidi kucheka.
**************************************************
Nanaa akamrudisha Fili
kwenye bembea. Akaendelea kumsukuma. Fili alisikika akicheka kwa furaha. “Hivi nimekwambia kama
umependeza sana?” Fili alisikika akimuuliza Nanaa nakufanya
mpaka Nanaa mwenyewe acheke. “Asante
Fili.” “Umependeza sana. Gauni yako nzuri. Nitamwambia mama yangu atupige
picha. Halafu dad akaitoe tuiweke ukutani. Nikihama na wewe, nahama na picha
yangu.”
Mpaka Danny alicheka safari hii. “Bwana mwanangu amekazana!” Walitoka kwenye mchezo huu, na
kuhamia kwenye mchezo mwingine huku Fili akiendelea kumsifia Nanaa, akionekana kufurahia
uwepo wa Nanaa kwenye party yake.
**************************************************
Wala Nanaa hakuwa amevaa
nguo ya ajabu sana. Alivaa gauni lake alilokuwa amelipata mtumbani. Lenye
viboksi vyeusi na vyeupe kote. Kata mikono lakini linakiungio kiunoni. Kwahiyo
kiuno chake kilibanwa vizuri na kuachia chini mpaka chini ya magoti. Halikuwa
limechanua sana. Liliendana na umbile lake zuri. Chini kote lilizunguka muundo
wa kashata kashata. Kama lililochanwa makusudi. Alivaa na sendozi zake za
kimasai zilizojazwa shanga nyingi nyeupe. Alishazivua pembeni ya kiti
alichokuwa amekalia kaka yake ili aweze kutembea mchangani kwa uhuru.
Kama kawaida, alikuwa
amesukwa rasta ndogo ndogo. Lengo kubana matumizi. Wakati wote alisuka rasta
ndogo ndogo ili zikae muda mrefu. Zisimgarimu kwenda saluni mara kwa mara. Na
pili zilimrahisishia kila asubuhi anapokwenda kazini. kwa hiyo usingemkuta
Nanaa na kipilipili chake kikavu. Wakati wote alisuka nywele zake. Hapo napo
alibana mtindo wa butterfly. Pande mbili ambayo moja ilikuwa ndogo, mstari wa
pembeni na kuzivuta mpaka katikati huku nyuma zimeanguka mpaka mgongoni.
Hereni zake za duara
kubwa kiasi, alizokuwa amenunua kwenye urembo zilimkaa vizuri sana na ule
mtindo wa nywele ambao hata upepo uwe mkali vipi, bado kichwani alibaki msafi
na gauni halikumfanya awe uchi. Japokuwa alionekana amevaa vitu vya hali ya
chini sana, cheap, lakini bado alipendeza. Ungetaka kumwangalia tu.
**************************************************
Walikuwa watoto 15,
kutoka familia tofauti tofauti, na wazazi wao walionekana kufahamiana vizuri. Danny
ndiye alikuwa akiwachekesha wazazi wao. Geb naye alikuwepo. Alikuwa amekaa
pembeni ya Liz, ametulia kama kawaida yake. Akajikuta macho yake yakihama na
kwenda kila anaposogea Nanaa. Alitulia akabaki akimtizama kwa utulivu, kama
anayetafakari kitu.
“Mwenzetu
umepotelea wapi?” Liz alimshtua Geb. “Nipo tu, nasikiliza.” Geb alijibu. “Mama Fili anakuuliza.” Geb hakujua hata kama aliongeleshwa.
Akashtuka kidogo akamwangalia dada yake. “Keki
vipi?” Grace alirudia. “Unataka sasa hivi?”
“Ndiyo. Naona njaa zitaanza kuwauma sasa hivi, wadai chakula kabla ya keki.
Nataka wakate keki kwanza ndio wale.” “Basi ngoja nikamuombe yule muhudumu
anipe. Nilimuomba anihifadhie kwenye friji.” Geb alisimama. “Usisahau kuja na
juisi yake huyu. Akili zikitulia, ataikumbushia. Ni heri uilete tu moja kwa
moja ili usifanye safari nyingi za kwenda na kurudi.” “Hamna shida.” Geb aliondoka kwenda kufuata keki.
“James!”
Mmoja wa kijana aliyekuwepo pale aliita. “Vipi Zinda?” “Sasa si unajua mimi pesa
ipo? Sihitaji kukusanya kama Fili. Au kuomba namba kama Jeff. Mimi mtoto wa
nyumbani. Tumetoka mbali sana mimi na wewe. Tumalizane kabisa.”
Watu walianza kucheka. “Wewe tu.
Changamka. Si umemuona mwenzio Jeff karudi?” James alijibu, Geb akarudi na
keki akaiweka mezani.
“Tena
Jeff mwenzio kakazana kweli. Si ulisikia mama?”
Danny alimuuliza Mama G nakumfanya acheke. “Kila
alivyokuwa anakataliwa, jamaa amekazana.” Danny aliongeza. “Yaani nina uhakika Nanaa ni mke wangu mimi.
Wengine wanahangaika tu” “Sasa si umfuate pale? Maneno mengii. Au unaogopa?”
Danny alimuuliza. “Kukataliwa kubaya!”
Wote walicheka.
“Jikaze
kiume, Zinda.” “Ngoja nivute pumzi.” Zinda alijisogeza kwenye
kiti. “Vipi Mkuu? Mbona unatoa jasho
wakati upepo mkali?” Geb aliuliza na kuamsha kicheko kingine. “Anataka kumzidi mahesabu mwanangu na Jeff.
Sasa anapanga maneno ya kumwambia Nanaa. Maana amesikia ya mwenzake Jeff, hana
hali. Akirudi kwa Fili, yeye ndio anamikakati mpaka ya mahari. Halafu mke
anacheza naye.” Danny alijibu. Wote wakacheka.
“Nawaambieni
kweli, Nanaa mke wangu mimi.” “Kwani kuna aliyekukatalia Zinda? Wewe si uende!”
Danny alifanya wote wazidi kucheka. “Eti
bibi Fili?” Zinda akamgeukia mama G. “Nenda
tu baba. Mwenye kisu kikali ndio mlanyama.” Mama G, alijibu, wote
wakacheka.
**************************************************
Mara wakamuona Nanaa na
Fili wanarudi pale walipokuwa wamekaa. “Ehee! Huyo anakuja.” Zinda akajiweka sawa, wengine
wakakwepesha macho wakijidai hawakuwa wanamwangalia. “Anataka nini huyo?” Danny akauliza. “Anataka kutumia choo. Sijui ni wapi?” Nanaa aliuliza. “Ngoja nikusindikize Nanaa.” Zinga
alidakia. “Sio mimi, ni mtoto.” Nanaa
alijibu kwa upole nakufanya kila mtu acheke. “Sasa Zinda unachanganyikiwa nini? Nanaa kasema wazi kabisa, ni Fili.”
“Si ndio na mimi nimesema niwasindikize, au nyinyi mmesikiaje?” Kila mtu
alicheka. “Wewe mmpeleke mtoto chooni,
acha kujitetea. Umesema umsindikize Nanaa.” Danny hakuwa anajua kunyamaza,
watu walizidi kucheka.
“Muone
na huyu anavyoruka ruka. Nilikwambia nini hukusu kubana mkojo?”
Danny alimuuliza mwanae kwa ukali. “Ulisema
nisibane mkojo. Nikisikia tu mkojo, niache michezo niende chooni kwanza.” “Sasa
kwa nini unaruka ruka?” “Si ruki ruki.” Fili alijitetea. “Nilikwambia nini juu ya kusema uongo?”
Aliendelea kumuhoji mwanae. “Nisiseme
uongo hata kidogo. Ni heri niingie matatizoni kuliko kusema uongo, hata mdogo.”
Fili alimjibu baba yake kwa upole na kuacha kuruka ruka. Alionekana huwa
anammudu Fili cha utundu. “Mmpelekeni
mwanangu chooni jamani. Atajikojolea.” Grace alilalamika.
“Anko
Geb, nipeleke chooni.” Fili alimgeukia anko wake. “Nipeleke au naomba unipeleke?” Danny
alimkoromea tena. “Anko Geb naomba
nipeleke chooni.” Fili alirudia tena kwa upole. “Kwa nini mimi nisimpeleke mara moja chooni?” Nanaa alitaka kupunguza shuguli nyingi. “Hapana. Wewe
utanipeleka choo cha kike.” Watu
walianza kucheka, na wote walikuwa wakiwasikiliza. Nanaa bado hakuwa
akimuelewa. Tokea anamtoa kwenye mabembea alitaka apelekwe kwa Geb, au baba
yake ndio wampeleke chooni.
“Kwani choo cha kike kina nini? Mimi
nitakuwa na wewe. Sitakuacha Fili.” Nanaa alimuongelesha kwa
upole. “Hapana.
Dad alisema hakuna kuvaa tena diaper, wala kukojoa nikiwa nimechuchumaa.
Nikojoe choo cha kiume, tena nikiwa nimesimama.” Watu wote
walicheka mpaka Nanaa alishindwa kujizuia akacheka mpaka machozi, lakini Fili
alikuwa ametulia akionekana anajikaza tu lakini amebanwa na mkojo.
“Bwana Geb mpeleke mtoto chooni.
Atajikojolea.” Grace alilalamika tena, Geb akasimama huku anacheka. “Twende. Na hakuna
kubana tena mkojo.” Geb
alimshika mkono na kuondoka naye. Kila mtu alibaki anacheka.
**************************************************
“Twende
tukacheze Nanaa.” Zinda
alianza tena, nakufanya watu wazidi kucheka kasoro Nanaa alikunja uso na
tabasamu la mshangao. “Zinda vipi leo?”
Danny aliuliza huku akicheka sana. “Namaanisha twende tukacheze na watoto,
bwana. Kwani nyinyi mmesikia nini?” “Mimi nashauri leo uache tu.
Ishashindikana. Utaishia kumtukana Nanaa mwenyewe bure! Maana mara umwambie
umpeleke chooni, mara mkacheze, hujielewi hata kidogo.” “Nafwata ushauri wako
Danny. Naona kweli leo bahati sio yangu. Upepo unavuma pabaya.”
Walizidi kucheka, lakini Nanaa hakuwa ameelewa.
“Naomba
James unikaribishe nyumbani kwako.” Zinda alimgeukia James. “Ushindwe hapa,
nyumbani utaweza? Sitaki wageni nyumbani kwetu. Wewe malizana na Nanaa hapa
hapa. Ukija nyumbani ni kulipana tu kama Fili.” James alijibu. “Mimi bado naona
mwanangu ndio Dume. Kwanza kashatongoza mapemaa. Kajinadi mpaka Nanaa mwenyewe
amemkubali. Hang’ati maneno. Na ameshaweka utaratibu wa kulipa mpaka mahari. Msimzibie
mwanangu bahati yake. Katafute kwengine.”
Danny
alifanya watu wacheke zaidi.
Geb alirudi na Fili. “Njaa imeanza kumuuma
huyu. Anataka juisi yake.” Danny
akataka kumpa chupa yake ya juisi. “Usimpe bwana Danny. Hatakula wala
hataweza kukata keki, ataishia kulala na chupa ya juisi mdomoni. Njoo kwanza
hapa mwanangu.” Fili
alimsogelea mama yake kinyonge, akionekana ameshachoka. “Njaa inauma?” Fili akatingisha kichwa . “Wee!” Danny alikuwa kama anamkumbusha mwanae kitu, haraka Fili
akakumbuka na kujirudi. “Ndiyo mama, njaa
inauma.” “Mwache bwana Danny. Amechoka.” “Hakuna tabia za kuitikia na kichwa. Kwani
yeye mtoto wa kike?” “Amechoka.” Grace alimtetea. “Ndio akae hapo apumzike, asubirie chakula.” Danny aliongeza. “Huo utakuwa mtihani. Akae chini huyo!
Hawezi. Kateni tu hiyo keki, ale, akacheze. Akitoka hapo, nikulala.” Liz
aliongeza.
**************************************************
Wakawaita watoto wote,
wakamwimbia Fili, akakata keki. Alimlisha Nanaa wa kwanza, mama yake, dad, Bibi
Fili na anko Geb. Wakaagiza chakula, Nanaa akaona ni heri aenda kukaa kwenye
meza ya watoto kuliko kukaa pale na kina Danny. Akajua watazidi kumchokoza. Akamuaga
kaka yake. “Kaka!
Naenda kuwalisha watoto.” Nanaa alimwita kwa sauti
ya chini ili asisumbue wengine. “Poa poa.” James akiwa amenogewa na porojo za
Danny, akakubali bila kupinga. Nanaa akamchukua Fili wakaondoka.
**************************************************
Kilipoletwa chakula cha watoto
Nanaa akaanza kuwagawia wote. Na kuanza kumlisha Fili huku akisimamia na watoto
wengine wale wapunguze michezo. Wengi wao walikuwa na njaa. Kwa hiyo wakala
bila shida. Wakamaliza kwa haraka bila Nanaa kutegemea. Akabaki akibembelezana
na Fili pale mezani.
“Na wewe utakula nini?” Alishtukia Geb amemsimamia nyuma yake.
Akageuka, macho yao yakagongana, haraka sana Nanaa akarudisha uso pale mezani. “Nimemwambia muhudumu
asubiri kwanza, asiniletee chakwangu mpaka watoto wamalize kula.” Nanaa alijibu huku amekaa, na kumpa
mgongo Geb. “Ungekula
sasa hivi. Tunakaribia kuondoka.” “Basi nitaenda kufuata ndani.” “Unataka kula
nini? Mimi naweza kwenda kukuchukulia.”
Geb
aliendelea. “Usihangaike.
Nitakwenda tu.” “Sio usumbufu hata kidogo.”
Nanaa
alifikiria kitu gani chakula, akajikuta
hajui achague nini, akabaki kimya akifikiria nini ale.
Grace na mama yake
wakasogea pale. “Bibi
Fili! Njoo tule wote.” Fili
alimuwahi bibi yake. “Mwenzio
nimemaliza chakula changu. Na wewe maliza cha kwako.” Bibi yake alisogea mpaka pale mezani.
“Sidhani kama atakula vizuri. Danny
amempa keki kubwa sana.” Grace na yeye akasogea. “Lakini anakula. Anakaribia kumaliza.” Nanaa alimtetea. “Basi atakuwa alikuwa na njaa sana.”
Grace alivuta kiti akakaa.
“Unataka
kula nini ili nimwite muhudumu akuletee?” Grace naye
aliuliza. “Nahisi kushiba.” Nanaa
alijibu. “Basi agiza, mwambie akufungie
ubebe. Ukale nyumbani ukisikia njaa.” Grace akavuta sahani ya Fili akaanza kumlisha
yeye. “Labda hivyo. Ngoja niende hukohuko
ndani ili niangalie wanavyakula gani.” Nanaa akasimama. “Usije kulipia lakini. Geb ndio atalipia
vyakula na vinywaji vyote.” Grace aliongeza wakati anamnyanyua Fili ili
ampakate. “Ameshaanza kusinzia huyu.
Inabidi tuondoke.” Grace alimbusu mwanae kichwani, Fili akajilaza kifuani
kwa mama yake. “Hivyo unavyomkumbatia,
ujue ndio hatakula tena.” Bibi yake aliongea huku akikaa kwenye kiti
alichokuwa amekaa Fili.
**************************************************
Nanaa aliingia ndani ili
kuchagua chakula, akamuona Geb naye anamfuata. Alisimama sehemu wanayo agiza
chakula akabaki akisoma Menu, ili aagize. Geb naye akasimama pembeni yake.
Nanaa alisoma mpaka mwisho bado hakuona kitu chakuagiza. “Unaweza kulipia tu. Sidhani kama nitakula.” “Hujapenda kitu hata kimoja
wapo hapo?” Geb aliuliza. “Nahisi
bado nimeshiba.” “Ungechukua chakula
chochote tu, watakufungia vizuri utakula baadaye.” “Ili nisikucheleweshe
kulipia, ungelipia tu vyakula vya watu wengine, halafu nikiamua baadaye
kuchukua kitu chochote, nitalipia mwenyewe.” Alimsikia Geb akicheka kwa
kuguna kidogo, akageuka kumwangalia.
“Sina haraka yakulipia Nanaa. Ila sitaki
uondoke bila kula kitu chochote.” “Mbona wewe sijakuona ukila? Umekula kweli?” Nanaa alimuuliza kwa kujali. Hata
huwezi kujua alionaje kama Geb hakula wakati alikuwa kwenye meza ya watoto na
Geb alikuwa katikati ya meza iliyojaa marafiki zao. “Mama alinipikia uji,
nikanywa kabla hatujaja hapa. Bado nimeshiba.” “Bado unakunywa uji mpaka leo?” Nanaa alijikuta anaropoka kwa
kushangaa sana, nakumfanya Geb acheke kidogo. “Naomba hilo swali umuulize Bibi Fili.
Na mimi huwa nashangaa hivyo hivyo.” “Sasa kwa nini na wewe usibebe chakula?
Baada ya muda utasikia njaa. Uji huwa haukai muda mrefu tumboni.” “Hapa naona
wanavyakula vya kukaanga tu. Na mimi huwa sipendi vyakula vyakukaangwa na
mafuta mengi, kama chips. Nakinahiwa haraka sana. Nikifika nyumbani naweza kula
chakula alichopika Grace mchana. Kwa hiyo mimi nipo sawa tu.” Yalikuwa
ni maongezi ya mara ya kwanza waliyozungumza kwa muda mrefu kwa kuangaliana.
Nanaa alikuwa
akimsikiliza huku akitizama macho yake. “Haya macho si mchezo!” Nanaa
aliendelea kuwaza moyoni wakati bado akimsikiliza. “Kwa hiyo utachukua
nini?” Geb
aliendelea kuuliza. “Nitarudi
baadaye wakati tunaondoka. Nahisi nitachukua tu Icecream, nikale nyumbani.” Nanaa
akageuka tena kama kusoma tena ile Menu kujiridhisha. “Huwa
unapenda Ice cream gani?” Geb alihoji kiustarabu. “Vanilla ndio napenda zaidi.” Nanaa
alijibu na kumgeukia tena. “Kwa nini
umeuliza?” Nanaa akamuuliza na tabasamu lenye mshangao kidogo. “Nataka tu kujua.” Nanaa alitabasamu
tena akageukia tena ule ubao mkubwa uliokuwa umening’inizwa juu kabisa. Ulikuwa
umebeba Menu zote. Akageukia upande ulipo Ice cream na bei zake. Akaangalia kwa
muda kisha akageuka na kuondoka.
**************************************************
Alitoka na kukuta baadhi
ya wazazi walishaondoka na watoto wao, lakini James na kina Danny bado walikuwa
wakiongea na kucheka kama ndio wamefika hapo. Danny alikuwa amempakata mtoto
wake, Fili, amelala. “Naomba nikupokee.”
Nanaa alimsogelea Danny. “Mzito
huyu. Wewe muache tu hapahapa. Pumzika.” Danny alimjibu Nanaa
huku akimwangalia Mtoto wake aliyekuwa amelala. “Maneno yote yamemuisha kwa kuchoka.” Liz aliongeza huku akisimama.
“Geb yuko wapi? Nataka kuondoka.” Liz
aliuliza huku akiangaza macho kumtafuta Geb. “Grace! Umemuona wapi Geb?” Grace alikuwa ndio anarudi kutoka
kusindikiza wageni wengine waliokuwa wamekuja kwenye sherehe ya mtoto wake. “Unataka muondoke?” Grace aliuliza. “Nataka kumuaga. Kunamahali nataka kupita
kwanza.” Liz alijibu. “Mwangalie
ndani, atakuwa analipia.” Grace alijibu na kwenda upande walipokuwa
wakicheza watoto ili kujaribu kusafisha kabla yakuondoka. Nanaa akamfuata ili
kumsaidia. Waliendelea kuokota huku wakihifadhi baadhi ya vitu walivyosahau
watoto.
“Najua
utakuwa umechoka, lakini nakushukuru. Umenisaidia kucheza na watoto.
Wamefurahi.” Grace alimshukuru Nanaa wakati wakiendelea
kusafisha. “Na mimi nimefurahi. Napenda
sana watoto.” “Mimi napenda watoto, lakini wasiwe watundu kama Fili. Jamani
mtoto ananichosha akili huyo! Nafikiria kama mimi mama yake ananichosha hivi,
sijui inakuaje kwa wasichana wa kazi.” Nanaa alicheka. “Unafikiri
nakudanganya? Mimi napenda akiwa ameanza kuchoka, hapo sina neno. Na anapenda
kulala kama mgonjwa. Hajiwezi kwa usingizi.” “Labda anakuwa anachoka sana.”
Nanaa alijibu huku akicheka. “Kwa
shuguli zile, lazima achoke. Ukimuona amekaa chini ametulia, ujue Danny yupo,
au ananjaa au usingizi umemlemea. Basi.”
Nanaa
alizidi kucheka.
“Hakuna urefu asioweza kupanda. Hakuna neno
asiloweza kuongea. Hakuna jambo asilolielewa. Na hasahau. Anarudia neno kwa neno.
Sasa akianza kusimulia habari zake, namtuma kwa Geb, yeye huwa hachoki
kumsikiliza. Halafu anamjulia. Sasa mimi siwezi. Nakuwa na mambo mengi
yakufanya na kuwaza. Sasa ubaya wake ni kila akizungumza kidogo, anakuuliza
maswali kutaka kujua kama unamsikiliza au umempuuza. Na anajua.”
Nanaa alizidi kucheka.
“Niwasaidie nini?” Geb aliwasogelea. “Afadhali umekuja.
Msaidie hapa Nanaa, mimi nikakae. Nimechoka. Liz ameshaondoka?” “Ameondoka,
kuna mahali amesema anataka kwenda.” “Ana mambo mengi shoga yangu yule! Sasa
usiku huu anaenda wapi?” “Sijamuuliza.”
Geb
alijibu kwa upole na kwa ufupi, na kuendelea kukusanya takataka. “Mmh!” Grace aliguna na kuondoka. Akawaacha
Nanaa na Geb. Kimya kikazuka. Wakaendelea kukusanya mpaka wakamaliza. “Hivi ni baadhi ya
vitu walivyoacha watoto.” Nanaa
alimkabidhi. “Asante,
na tunashukuru kwa kuja.” Nanaa
alitabasamu.
**************************************************
“Naona kikao ndio kimeanza rasmi.” Geb aliongea huku akiangalia meza
waliyokaa kina Danny na rafiki zake waliobaki pale bila watoto. Walikuwa
wakicheka huku wakiongea kwa sauti kubwa. “Unamaana hawataondoka pale sasa hivi?” Nanaa aliuliza. “Sio leo. Huwa wanakaa muda mrefu sana. Unaharaka yakutaka kuondoka?
Naweza kukurudisha nyumbani.” Geb aliuliza. “Hapana. Naweza kumsubiri tu kaka. Sina pakwenda.” “Basi tukazunguke
kidogo, ndio turudi kukaa.” Nanaa alimwangalia vizuri.
“Unamaanisha
na mimi?” Aliuliza kutaka uhakika. Maana alijua huwa
anajichanganya sana kila anapokuwa na Geb. Hakutaka kufurahia safari isiyo
muhusu. Geb akatabasamu. “Ndiyo.” “Wapi?”
Nanaa aliuliza tena. “Hapo nje ya uzio,
kumepakana na bahari. Au umechoka?” “Hapana. Tunaweza kwenda tu. Labda kama
wewe ndio umechoka.” Tayari alishaanza kujichanganya. Akasahau kama Geb
ndiye alimwambia watembee kidogo. “Mimi
nipo sawa kabisa. Nililala muda mrefu mchana.” Geb alijibu huku akitoa
tabasamu. “Nisubiri nikaweke hivi vitu
kwenye gari. Grace atawarudishia wazazi wao akipata nafasi.” “Sawa.” Geb
aliondoka, akamuacha Nanaa amesimama akiwaza.
**************************************************
“Atakuwa alilala na Liz, pale nilipowaacha
nyumbani kwa dada yake.” Nanaa aliwaza huku wivu ukimtesa. “Wanaonekana
wanapendana. Alimuomba aje pale huku akisisitiza ana hamu naye.”
Aliendelea kukumbuka. “Wote wanaonekana wanajielewa. Liz
anaonekana ni msichana msomi, anapesa, na mzuri. Ni haki yake kumuhitaji.”
Wivu ulishamjaa kwa mwanaume asiye wake. “Liz anakaumbile kazuri. Hana nyama uzembe.
Kila kitu chake ni cha kiasi mwilini wake. Mpaka rangi ya mwili wake inavutia.”
Nanaa aliendelea kuwaza akiwa amesiamama pale peke yake akimsubiria Geb. Hamu
ya kuzunguka naye ikaanza kumwisha. “Nitakuwa najiumiza tu.” Nanaa
aliendelea kusononeka.
**************************************************
Namzungusha Nanaa baharini kidogo.” Alimsikia Geb akiwaaga lile kundi la
vijana waliokuwa wakiongea na dada yake. “Afadhali,
ili asichoke.” Grace alijibu. “Unataka
twende wote, mama?” Geb alimuuliza mama yake. “Nimechoka bwana. Acha niendelee kusikiliza stori, nicheke.” Mama
yao alijibu huku akionekana anafurahia sana kinachoendelea pale.
Geb alimsogelea Nanaa,
aliyekuwa amepooza. “Upo tayari?” Geb
alimuuliza huku akimwangalia, Nanaa alitingisha kichwa kukubali, wakaondoka.
Ukimya mwingine ukazuka wakati wakiendelea kutembea nje ya uzio, mchangani.
Mawimbi ya bahari yalipigwa kwa nguvu na upepo, lakini giza lilishaingia,
ilikuwa ngumu kuyaona.
Walitembea kwa muda
kidogo, hakuna aliyemuongelesha mwenzake.
“Tusiende mbali sana. Kunakuwa na wahuni wengi mida hii.” Geb alivunja
ukimya. “Unasikia baridi? Naona upepo
mkali kweli.” Aliuliza tena. “Hapana,
nipo sawa tu.” Nanaa alijibu kwa kifupi, akanyamaza. “Unataka tukae kidogo au umechoka unataka kurudi?” Geb aliuliza. “Vyovyote tu, nipo sawa.” Geb
alimwangalia kwa utulivu. “Upo sawa?
Mbona kama umekosa raha gafla?” “Nipo tu sawa.” Nanaa alijitahidi kutoa
tabasamu, Geb akabaki akimwangalia akionyesha wazi amelikataa tabasamu feki.
****************************************************************
Kwa mara ya
Kwanza Nanaa anapata nafasi ya kuwa na Geb. Maongezi yao ya kwanza ambayo
angalau yalichukua muda mrefu kidogo, yalijawa kujaliana. Kila mmoja akitaka
mwenzie asilale njaa. Sasa wapo peke yao ufukweni. Nanaa aliyejawa na wivu kwa
mwanaume asiye wake. Huku akikataa wanaume wanao mbembeleza, atatumiaje nafasi
hiyo hapo ufukweni.
Usikose Sehemu ya 9.
0 comments: