Story
is mine - ni Wangu! Part 1, Sehemu ya 6 & 7.
"...ni Wangu!"
Sehemu ya 6 & 7.
Nanaa akajituliza mpaka mwaka
huo wa pili ulipoisha. Hapakuwa na mapenzi tena. Alishakinahiwa. Jamal ndio
alimchefua kabisaa. Mawazo yakawa shuleni, na Mungu akamfanikisha hapo.
Hakukamatwa somo hata moja. Na yeye akawa amefaulu vizuri sana. Tena kwa alama
za “A” tupu. Kwa hakika hata James
akafurahi na kujisifu kwa wenzake. Lakini Nanaa akatakiwa kwenda field kabla yakurudi
chuo kumalizia mwaka wake wa mwisho.
Wapi akafanye field hiyo?
Akaanza kuhangaika kutafuta maofisi ambayo angefanya field hiyo lakini angalau wamlipe
pesa kidogo ya kumsaidia hata nauli na hata wakiweza kumuajiri mpaka chuo
kifungue, lakini akakosa. Hapo ndipo ikambidi azungumze na kaka yake. Ili
amsaidie kumtafutia sehemu yakufanya
field. James akamwambia ampe muda kidogo wa kutafuta.
Baaada ya kama siku mbili
akamwambia amefanikiwa kumpatia kazi mahali. Amepata ahadi ya kazi kwa muda
ambao muhasibu wa hiyo ofisi atakapokuwa likizo ya uzazi. Nanaa alifurahi sana
na kumshukuru Mungu wake.
*******************************************
Siku ya jumamosi asubuhi
Nanaa alisikia watu wakicheka na James sebleni kwao. Ndio na yeye alikuwa
ameingia tu chumbani kwake baada ya kumaliza shuguli zake. Akaona atoke
aangalie ni kina nani wanaomfanya kaka yake acheke hivyo. Alikuta ni mtu na
mkewe. Wakitaniana sana na James. Akajua lazima watakuwa marafiki wa James. “Njoo Nanaa usalimie
na uongee vizuri na Grace. Ndiye atakuwa bosi wako. Hakikisha unamuelewa
usibaki unayashangaa hayo macho yake, akamaliza kuongea hujaelewa kitu.” Nanaa akamtizama
Grace vizuri. Kweli alikuwa na macho yakuvutia. Akacheka.
“Usicheke mtoto wa kichaga. Tumekuja
mjini kuzisaka pesa. Changamka na usipumbazwe na hayo macho na sauti hiyo, ukashindwa
kuomba pesa kubwa. Maana wakati tupo pale chuo kikuu cha mlimani, huyo Grace alizungusha
vichwa vya wasomi wenye shahada zao, wafanyakazi, maprofesa, na wafanyabiashara wa jiji. Watu wazima
tukabaki kama wehu. Muulize Danny. Mimi mwenyewe nilitaka kuoa, lakini
nikashindwa. Kila alipokuwa akiniangalia, maneno yalikuwa hayatoki. Mwenzangu
Danny akaamua kufa kiume, lakini karibia tumkimbize Mirembe kwa kuchanganywa na
Grace.” Wote
walianza kucheka tena. Lakini Nanaa akawa ameshapata utambulisho
wakujitosheleza. Danny ni mume wa Grace bosi wake. Marafiki wa kaka zake
waliosoma pamoja.
“Achana nao hao. Wanapenda kunichokoza
tu. Tutaelewana Nanaa, usiogope.” Grace alijibu huku
akicheka. “Ashindwe
kuelewa Danny mpaka leo, ataelewa mdogo wangu huyo? Kwanza hayo macho kwa mara
ya kwanza yakikuangalia unakuwa kama unapumbaa hivi. Sasa Danny ndio alikuwa
anatuchosha. Pesa hana, anamtaka Grace. Ukiangalia mgongo wa Grace, Danny
alikuwa anazidi kuchanganyikiwa. Basi tukajua pakumpatia Danny. Tukitaka
kumchanganya, tunamtisha, tunamwambia tumemuona Grace amepakizwa kwenye gari
zuri sana, halafu huoni ndani, vioo vyeusi. Basi weee, Danny anapagawa!” James aliongeza nakuwafanya wazidi
kucheka.
“Nakwambia nilipambana mpaka
nikafanikiwa.” Danny
aliongeza. “Na usifikiri
akikwambia alipambana anadanganya? Nilikuwa sina raha. Alikuwa ananisumbua kupita
maelezo. Yaani namgombesha mbele za watu, labda asubuhi, lakini mchana utamuona
huyo amerudi. Angekuwa hasomei Eletronics huyu, watu wangesema hana akili
vizuri.” Grace
alijibu kwa sauti yake ya upole. “Mimi nakwambia vile ulivyokuwa
ukinigombesha huku unanifukuza, nilikuwa nasikia raha. Nilikuwa narudi kwa kina
James nawaambia Grace ameniongelesha.” Walizidi kucheka.
“Yaani anagombeshwa, lakini yeye
anasikia raha. Danny mjinga sana huyu. Yaani mpaka tulikuwa tunamuhurumia.”
“Halafu sasa suruali yake ni moja tu ya jinsi. Tisheti tu ndio alikuwa
anabadili. Marafiki zangu walikuwa wananicheka. Halafu alivyo sasa Danny,
anakufuata mpaka kwenye lecture, mbele za watu. Eti ananijulia hali! Nilikuwa
nakasirika mpaka basi.” Grace
aliwafanya wazidi kucheka. “Mvumilivu hula mbivu. Huoni
niliibuka mimi mshindi? Namiliki chombo mwenyewe. Nimewapiga bao watu na pesa
zao.”
Mumewe alijibu.
“Hawa wawili hawa, na wenzao wenye
akili kama zao, walisoma sekondari pamoja. Wakachaguliwa hapo chuo kikuu cha
Mlimani. Wakawa chuo kimoja, mwaka
mmoja, darasa moja, na sasa hawa wawili katika kundi lao, wanafanya kazi sehemu
moja. Hawana jipya. Wananikera na macho yangu, sina raha. Huyo James kaka yako,
na wenzake, walikuwa wanamsindikiza Danny kunitongaza. Basi James na wenzake
walikuwa wanasimama mbali kidogo, wanatuangalia mimi na Danny tunavyoongea.
Walikuwa wananiudhi kundi lao hawa! Sina hamu. Twende mwaya Nanaa tukazungumze
hapo nje. Maana yule muhasibu wangu amepitisha siku za kujifungua, muda wowote
ule anaweza akajifungua, nikabaki nahangaika. Ofisi yenyewe sio kubwa, lakini
yeye ndiye anamajukumu mengi.” Wakatoka
nje. Kuzungumza.
*******************************************
Grace alizungumza naye
taratibu. Kwa kumsikiliza tu, Nanaa akavutiwa na bosi Grace. “Sasa upo tayari
kuanza kazi lini?” Grace aliuliza. “Hata kesho. Sina kitu
chakufanya sasa hivi.” “Mbona wewe utanifaa. Ndio vizuri uanze mapema
akuelekeze kila kitu, ili ikitokea anajifungua, tusikwame.” Nanaa akafurahi sana. Wakakubaliana
mshahara, Grace na mumewe wakaondoka.
*******************************************
“Naona ulivyofurahi.” James alimchokoza dada yake. “Kasema atanilipa.” Nanaa
alijibu huku akicheka. “Ni watu wazuri sana,
hawana shida. Ninauhakika utafurahia kufanya kazi na Grace. Ni dada muungwana
sana.” “Ni kweli ulitaka kumuoa? Mzuri kweli.”
James
akacheka. “Hapana.
Huwa tunapenda kumchokoza tu. Danny, mumewe ni mtundu sana. Halafu Grace ni
mpole. Wakati mwingine tunamchokoza tu ili aongee. Tokea shule huwa tunapenda
vile anavyoongea kwa upole. Usipomchokoza Grace, hazungumzi hata. Atabaki kimya
tu.” “Kwa hiyo Danny ni rafiki yako tokea zamani?” “Danny ni mtu wa watu sana.
Alikuwa au tuseme ni rafiki wa kila mtu.
Alituunganisha marafiki tuliokuwa tukisoma pamoja tokea sekondari. Tukajikuta
tunakundi letu. Utakuja kuwaona wengine. Danny hawezi kupoteza mtu. Mmoja wetu
akipotea tu, atamtafuta mpaka tujue alipo. Mwishowe tumejikuta lazima kukutana
mara kwa mara. Tulipotezana kwa muda, yeye alipoamua kurudi chuoni kufanya
shahada ya pili. Akawa kimyaa. Alipomaliza akatukusanya tena. Ameajiriwa pale ofisini
kwetu. Hata mwaka hajamaliza pale kazini, lakini kila mtu anamfahamu. Mpaka
wafagizi wanamjua Danny. Kila anapopita anatengeneza marafiki anaowafanya wawe
karibu yake. Mtundu sana na haishiwi maneno.” Waliendelea
kuzungumza wakicheka vituko vya Danny alivyokuwa akisimulia James.
Nanaa aanza field
Nanaa akaanza kazi
kipindi huyo muhasibu anafunga mahesabu na kutengeneza ripoti ya mwezi.
Walifanya kama siku mbili tu, Nanaa akiweka juhudi na kuuliza maswali mengi
kadiri awezavyo. Akijua ile si field tu, sasa ni kama kazi. Na kama akiongeza
juhudi, ni sehemu anayoweza kurudi kuomba ajira pindi atakapomaliza chuo. Mshahara wa mwanzoni tu ulimvutia. Akajua
akirudi na vyeti, basi mambo yake yatakuwa safi.
Kabla huyo muhasibu hajakamilisha
ripoti, na Nanaa kuona inakuaje mpaka mwisho, chupa ya uchungu ikavunjika
wakiwa ofisini. Wote walifurahi kwa kuwa huyo mtoto alikuwa akisubiriwa na watu
wote pale ofisini lakini sio Nanaa. Nanaa alitaka waendelee kuwa naye ili
amfundishe mpaka mwisho ili asije haribu, lakini ndio katikati ya mafundisho,
chupa ikavunjika. Grace alimkimbiza hospitalini huku akiwa amempigia simu
mumewe awafuate hospitalini. Nanaa alibaki pale hajui chakufanya.
*******************************************
Alikaa hapo mpaka jioni
wakati anakaribia kufunga, akasikia sauti ya mtu akiongea nje ya ofisi yao,
akiwa mapokezi. “Sasa hivi
siwezi kufanya kitu cha maana G. Nimechoka na nina mambo mengi. Akili
haijatulia. Kwa nini nisije siku ya jumamosi?” Alimsikia mtu
akiongea taratibu kama Grace. Lakini huyu sauti yake ilikuwa nzito, nzuri ya kiume.
Akasikia kimya kama mtu anayesikiliza upande wa pili. “Bwana wewe
ni muoga tu, G. Unaweza.” “Siwezi. Wewe msaidie.” Nanaa
alishtukia yule mtu amefungua mlango amemsimamia mbele ya meza yake na sauti ya
Grace ikasikika kutoka kwenye sauti. Moyo wa Nanaa ukapasuka. Akabaki kimya
asijue kwa nini.
“Labda jumamosi. Leo nitakuharibia
kazi. Jumamosi akili itakuwa imetulia, au usubiri baada ya week ijayo.” Yule
kaka aliendelea kuongea kwenye simu huku akivuta kitabu cha invoice mbele ya
meza ya yule muhasibu, akaanza kuangalia taratibu. “Kwanza wala
huna transanctions nyingi! Acha uvivu G. Fanya mwenyewe.” Waliendelea
kuzungumza, Grace akisikika akimsisitiza yeye ndio afanye. “Basi
nitakuja hiyo siku ya jumamosi, wewe zungumza naye muelewane. Nikifanya leo,
nitamchanganya tu.” Grace
aliendelea kuzungumza upande wapili. “Sawa. Hamna shida.” Akaitikia na kukata simu,
na kumuangalia Nanaa.
*******************************************
Nanaa hakuhitaji
utambulisho, alijua wazi ni kaka yake Grace bosi wake. Walifanana sana na
Grace. Macho yao yalikuwa yakifanana sana. Makubwa kiasi na yakusinzia.
Aliongea kwa utulivu kama Grace, yaani haiba ya utulivu kama Grace. Mweusi na
nywele nyingi zilizoonekana alifanya juhudi za makusudi kuzitengenezea mustachi
mzuri kuzunguka midomo yake na usoni. Nanaa alibaki akimtizama.
“Naitwa Geb, kaka yake Grace.” Akampa Nanaa mkono na kuendelea. “Alitaka nimalizie
kazi ya muhasibu wake, lakini leo nimechoka sana. Nikisema nikae hapa,
nitashindwa kukuelekeza vizuri. Ingekuwa nafanya peke yangu, hapo sawa. Lakini
inaonekana G, anataka nikufundishe na wewe.” “Kwani ni ngumu sana? Naweza
kukuangalia wakati wewe unafanya. Huna haja yakuongea sana.”
Nanaa aliuliza, yule kaka akakaa kwenye kompyuta ya yule muhasibu na kuanza
kuangalia bila kujibu kwa muda.
“Huyu mwenzako
nilitumia karibia mwaka mzima kumuelekeza kutengeneza hii ripoti tu. Mpaka
kipindi fulani nikawa natengeneza tu mwenyewe. Nafikiri kama nikuweza vizuri,
amefanikisha kama ripoti mbili za mwisho, nyingine zote ilikuwa lazima
nizirekebishe sana. Ni kama nilikuwa nafanya mwenyewe tu.” Aliendelea kuperuzi kwenye kompyuta
ya huyo muhasibu huku Nanaa amekaa meza ya pembeni isiyokuwa na kompyuta.
“Yaani mpaka hapa tu, naona nitahitaji
siku nzima. Vitu vingi sana havijakamilika.” Aliendelea
kuperuzi huku Nanaa akiwa kimya. “Daah! Kuko hovyo sana.” Aliendelea kuzungumza mwenyewe
akiendelea kuperuzi.
Akaingia dereva wa hiyo
kampuni. “Mzima bosi?” Geb alisalimia. “Kumbe mkuu mwenyewe
upo hapa?” “Nipo.” Geb alijibu akarudisha macho kwenye
kompyuta. “Kama
upo basi ipo neema. Maana nina mzigo hapa, natakiwa kumkabidhi muhasibu kisha
anikatie kiasi.” “Usinitie matatizoni bwana. Mimi sina pesa. Na sitaki kukaa na
pesa ya mtu.” Geb
alijibu huku akiendelea kuangalia kompyuta kwa makini.
“Unanikatalia bure bosi wangu. Najua
wewe huna shida na pesa ndogo ndogo hizi.” “Unamuongelea Geb wa jana, leo hali
mbaya. Mpigie simu bosi wenu umuulize chakufanya.” Yule dereva aliendelea kuzungumza na
Geb wakionekana kufahamiana. Kwani walitaniana kidogo, mwishowe Grace alimpigia
simu Nanaa. “Pokea pesa kutoka kwa huyo dereva, kisha uumpe elfu 10. Hakikisha
mnaandikishiana na anaweka saini sehemu kuthibitisha amepokea hiyo pesa na amekupa
hiyo pesa.” “Sawa nitafanya hivyo. Kwani hutarudi tena?” Nanaa
akauliza. “Nitakuwepo
hapo kesho. Geb bado yupo?” “Yupo.” “Sawa. Analalamika amechoka, hawezi
kukusaidia kufunga mahesabu. Anataka kuja kufanya jumamosi. Utaweza?” “Saa
ngapi?” “Atakwambia mwenyewe. Hapendi kufanya kazi siku za jumamosi asubuhi asubuhi,
kwa hiyo haitakuwa asubuhi sana, usiogope.” Nanaa akacheka kidogo. “Sawa.” Alimuelekeza kidogo
Nanaa, wakaagana.
*******************************************
Yule dereva aliondoka na
kumuacha Nanaa na Geb pale ofisini. Geb alipiga simu kitengo cha stoo kuomba
transction zote. “Mbona nilishatuma?” Dada
aliyekuwepo kwenye kitengo hicho alijibu. “Ni sawa kama nikikuomba
utume tena?” Geb aliomba kiustarabu
sana. Nanaa akabaki akimwangalia kwa kujiiba. “Sawa. Nitafanya hivyo.”
“Asante sana na samahani kwa usumbufu.” “Hamna shida.”
Akakata simu na kusimama.
*******************************************
“Nilikwambia
naitwa Geb?” “Ndiyo.” “Samahani. Akili zimechoka. Sasa bosi wako ameniambia
huwa hufanyi kazi siku za jumamosi. Mimi nitakuwepo hapa asubuhi ya saa nne.
Ukiweza kuja kutizama ninachofanya ni sawa. Ukishindwa, nitakuelekeza wakati
mwingine. Haina haraka.” “Sawa.”
Geb
alimtizama kwa macho yaliyomfanya Nanaa abaki ameduwaa, asijue kama aliulizwa
swali na kama alijibu sahihi. Akakumbuka kaka yake alimwambia asili ya macho
yale yakikuangalia kwa mara ya kwanza, hupumbaza.
Nanaa akajiweka sawa
baada ya kuona bado anamtizama. “Si umesema jumamosi utakuwa hapa, saa
nne ya asubuhi?” Nanaa aliuliza kama kupata uhakika. “Ndiyo. Na wewe
umesema sawa. Sasa sawa hiyo nitegemee utakuja au utataka kujifunza wakati
mwingine?” “Nitajitahidi kuwepo.” Nanaa aliongeza. “Basi
usiku mwema. Tutaonana Mungu akipenda.”
Geb
akatoka. Ndipo Nanaa akapumua kwa nguvu kama aliyepata aghueni. Alihisi tokea
Geb amtazame ni kama alishindwa kupumua. Akabaki anababaika. “Si
kwa macho yale. Daah!” Nanaa alijiambia huku akijicheka.
*******************************************
Isivyo kawaida yake,
Nanaa ambaye hakuwahi hata kumfikiria mwanaume kwa umbile, akajikuta anabaki na
taswira ya Geb. Kutoka kwenye kuapa hataki tena mwanaume, lakini akajisikia
shauku ya kutamani jumamosi ifike haraka akamuone tena Geb. Hiyo ilikuwa siku
ya jumatano Geb alipowatembelea ofisini. “Hivi hata jina nilimtajia kweli? Sijui
ameoa au anampenzi? Daah! Yule akikutamkia ndoa, unasamehe hata mahari.”
Nanaa aliwaza wakati amejilaza kitandani kwake. Alitamani Geb arudi tena pale
ofisini au ajue habari zake zaidi, lakini hakujua amuulize nani.
*******************************************
Siku ya jumamosi
ilipofika, Nanaa alimka asubuhi na mapema nakuanza kujiandaa. Kila nguo siku
hiyo haikumpendeza. Alivaa yakumbana, “Mmh! Ataona najirahisisha sana.”
Akavua na kuvaa kubwa kidogo. “Hii hapana. Hata kiuno changu
hakionekaniki! Wakati hiki ndicho kinawachanganya wengi!” Akacheka na
kuvua. Alihangaika kuvua na kuvaa, mpaka akaishia kuvaa gauni la kawaida tu kwa
kuwa muda ulikuwa umeisha, akaona atachelewa na kuonekanika sio msomi.
Alitoka akiwa na haraka, akabahatisha daladala
mpaka ofisini. Akakuta walinzi tu, na watu wa stoo waliokuwa wakipokea na kutoa
mizigo. Aliingia ofisini kwa muhasibu akakaa akisubiri mpaka saa nne na nusu
ndipo akamsikia Grace na Geb wanaingia.Walipita moja kwa moja ofisini hapo
alipo Nanaa, wakiwa na mtoto mzuri sana wakiume, mwenye macho yanayo fanana na
wao. Rangi yake pia alikuwa mweusi kama wao. Nanaa akabaki akijiuliza kama ni
mtoto wa Geb au Grace.
Alimsalimia Nanaa kwa
heshima akabaki anamwangalia. Nana akacheka. “Wewe vipi Fili?” Grace alimuona akimkodolea macho
Nanaa. Akampa ishara ya ainame ili amnong’oneze. Grace akacheka na kuinama
kumpa sikio. Yule mtoto alimnong’oneza kitu Grace nakumfanya acheke sana. Akatoa
simu na kupiga, kisha akaweka sauti kubwa.
Alipopokea tu, Grace
akaanza . “James! Umepata shemeji.” “Nani?” Upande
wa pili aliuliza ambaye ni James, kaka yake Nanaa. “Fili amesema Nanaa ni mchumba wake.”
Wote
walicheka mpaka Geb. “Kwa kuwa naonana na Danny jioni, mwambie Fili nimemkabidhi. Nitamalizana
na dad hukohuko.” Ndipo
Nanaa akajua kuwa yule ni mtoto wa Grace wala si Geb. Roho ikatulia. “Labda
bado hajaoa.” Nanaa akawaza kwa haraka huku akicheka.
Nanaa alikuwa akicheka
kwa aibu kwani bado Grace alikuwa akicheka huku akimwangalia mwanae. Akampigia
simu Danny mumewe na kumsimulia. “Mwanao anataka kumuoa
Nanaa.” “Sasa huko ndiko kuingizana umaskini. Mwambie kabla hajafikiria kuoa
atafute kwanza kazi, ili apate pesa ya kumlipa James ya mahari. James atataka
nyumba yangu bure.” Grace aliendelea kucheka
na mumewe akilalamika.
Baada ya muda Danny
akamuunganisha James kwenye simu wakawa wote watatu. “Hapa
nishaanza kutafuta mteja wa nyumba yangu ile mbavu za mbwa. Mahari ya Nanaa ni
mjengo wako Danny.” James
aliongea mara baada ya kupokea simu. “Si nilikwambia Grace? Mtoto
anataka kuniingiza umaskini huyo. Mahari yenyewe si umesikia?” “Acha
kumuogopesha mwanangu bwana James. Hata kwa mkopo sisi tutaoa tu.” Grace
alimtetea mwanae.
“Tena Grace uishie hapo hapo. Mwambie Fili kama anamtaka Nanaa, awe
na pesa yake. Mtoto anataka vitu vizuri huyo! Hajui vizuri garama?” Wote walicheka. “Mpango wangu ilikuwa
nimepeleke huyo Fili kijijiniii. Nikamchukulie mke kwa joo mbili, basi.” Danny
aliongeza. Waliendelea kutaniana, huku vicheko vikiendelea. Ikabidi Grace
awaage.
*******************************************
Akamgeukia Nanaa. “Huyu anaitwa Geb.
Mdogo wangu.” “Kaka yako bwana.”
Geb
alimkatisha. “Kwa
kupenda ukubwa huyu! Mimi ndio mkubwa, nimempita kwa lisaa lizima.”
Ndipo Nanaa alipojua kuwa ni mapacha. “Kwani ukiniita kaka unapungua wapi,
G?” “Haya. Na hivi unanisaidia, acha niwe mpole. Huyu ni Geb, anko wa Fili.
Ndiye anayenisaidia mambo ya mahesabu kwenye maisha yangu yote. Usifikiri ni
hapa ofisini tu.”
Nanaa
akacheka kidogo kama asiyesadiki. “Usifikiri nakutania. Nachukia
sana hesabu, lakini yeye ni mtaalamu sana wa mambo ya mahesabu tokea watoto
yeye ndio alikuwa mwalimu wangu. Halafu huwa achoki kufundisha. Atakuelekeza
mpaka wewe mwenyewe ndio utachoka. Nitakuacha naye hapa. Ukichoka wewe uondoke
tu, maana yeye anaweza kulala hapahapa.” “Siwezi kulala bwana. Saa kumi jioni
mwisho. Naenda mazoezini.” Geb
alidakia tena huku macho yakiwa kwenye makabrasha yaliyokuwepo hapo juu ya
meza.
“Haya Nanaa, kazi kwako. Mtumie vizuri
kumuuliza maswali yote, ili jumatatu ukiachiwa ofisi, usipate shida.” “Sawa,
asante.” Nanaa
alishukuru.
“Nitakuja baadaye kumchukua Fili twende
wote mazoezini. Au unasemaje?” Geb
alimtizama Fili, akampa 5. “Ewaa.
Ujiandae na uvae kabisa ile jezi yako na viatu. Nikija tu, tunaondoka.” Wakaona
Fili anababaika wala hafurahii tena kwenda mpirani na anko. “Nini?” Geb
alimuuliza. “Unabaki naye?” Fili
aliuliza nakuwafanya wote wacheke. “Yaani huyu mtoto kama Danny!” Geb
alicheka huku anatingisha kichwa. “Nanaa yupo kazini. Anatoka jioni.
Ukimtaka umtafute kesho, hafanyi kazi. Sawa?”
Geb
alimjibu Fili. “Sawa.” Fili alijibu kwa kuridhika kwa ahadi
ya kuonana na Nanaa kesho yake.
“Tutamtafuta kesho?” Wakati
wanatoka walimsikia Fili akimuuliza mama yake na kumfanya Nanaa na Grace
wacheke. “Wewe
Nanaa umemchanganya mwanangu. Wala hakuwa hivi.”
Grace
aliongea huku akifungua mlango wakutoka nje ya ofisi, wakasikia wakifunga
nakutoka.
*******************************************
Palipita hali ya ukimya
kidogo, Geb akiendelea na shuguli zake, na Nanaa akifikiria chakufanya. “Nimeshajisahau.
Naendelea bila kukuonyesha. Sogeza kiti uone jinsi ninavyokusanya kila kitu, na
kupangilia mpaka kupata ripoti nzima.”
Nanaa
alisogeza kiti na kukaa naye meza moja, kazi ikaanza. Kulikuwa na utulivu wa
namna yake pale ofisini. Mara kadhaa Geb alitaka kujua kama bado wapo pamoja au
alimuacha mbali, na mara zote Nanaa alisema anaelewa.
“Kama una swali lolote, usisite
kuniuliza.” Geb
alimgeukia kuona kama bado Nanaa yupo au alishahama pale. Yale macho alitamani
yaendelee kumuangalia kwa muda. “Naelewa.” Nanaa
alijibu kwa utulivu. “Na
ujue mwezi ujao hii ndio kazi utatakiwa kufanya. Kwa hiyo uelewe kweli kweli.
Ukiwa na swali uliza. Usisite. Na hakuna swali dogo au kubwa. Yote ni ya
msingi.” “Sawa.” Nanaa
alijibu.
*******************************************
Waliendelea na kazi, ilipofika
saa 7:30 mchana, Grace akampigia kaka yake. “Nikuletee chakula?” “Nataka
nimalize kabisa. Nikila sasa hivi nitapata uvivu.” “Ndio maana hunenepi.”
“Niwekee chakula changu, nikirudi nitakuja kula.” “Mama anasisitiza uwahi
kurudi. Usikae huko ukajisahau kula.” “Sasa unataka nikumalizie kazi yako au
unataka nije kula?” Grace alisikika
akicheka.
“Liz amesema atakuja
baadaye.” “Mfanye anisubiri, asiondoke mpaka nije.” “Changamsha mikono sasa.”
“Sitachelewa.” “Vipi Nanaa?” “Yupo. Anaonekana kuelewa.” “Mruhusu akale.”
“Sawa. Nitakuona baadaye, lakini usisahau kumfanya Liz anisubiri.” “Nitampa
hiyo kazi Danny. Amuongeleshe mpaka umkute.”
Geb
alicheka kidogo, akakata simu.
*******************************************
Hapo hapo baada ya Nanaa
kusikia kuna Liz, alichafukwa na roho yake. Hasira za kusalitiwa zikampanda.
Kumbukumbu za juhudi zake kujitoa kwa wanaume nakuishia kujidhalilisha zikamjia.
Akaamua atoke pale. “Vipi!?” Geb aliuliza baada ya kuona Nanaa
anavuta kiti chake kwa nguvu na kusimama bila taarifa. “Ni muda wa kula, si
ndio?” Nanaa
aliuliza kishari kidogo. Geb akabaki akimtizama. “Nakwenda kula.” Nanaa akaaga nakutoka bila kuongeza
wala kujibiwa.
Hakuna chakula
kilichopita kooni, akajikuta akitokwa na machozi asijue ni kwa nini. Aliingia
chooni akakaa humo kwa muda, akarudi tena jikoni akatengeneza chai, lakini
akaishia kuimwaga kwenye sinki. Alishikwa na hasira za ajabu, akashindwa
kujizuia. Chuki kwa wanaume ikamwingia, akaamua kurudi ofisini.
Alifungua mlango
akapokelewa na macho matulivu ya Geb. “Kwema?”
Geb
aliuliza kwa utulivu. “Najisikia
vibaya, naondoka naenda kupumzika.”
Alijibu
kwa kifupi. Akachukua kipochi chake, nakutoka. Geb alibaki ameshangaa. Lakini
lilikuwa jukumu lake kumaliza kazi aliyokuwa amepewa na dada yake. Akabaki
akifanya ile kazi, asielewe kilichompata mwanafunzi wake. Kilikuwa kitendo cha
muda mfupi. Hakujua kama ni maumivu ya gafla au alikuwa nayo kwa muda mrefu!
Anamuuliza nani na Nanaa alishaondoka?
****************************************
Nanaa alitoka pale
akarudi nyumbani. Akashukuru kutomkuta James nyumbani, akaingia chumbani kwake
nakuanza kulia. Alilia kana kwamba Geb alikuwa mpenzi wake akamfumania. Na wala
hakuwahi kulia vile hata alivyowafumania wapenzi wake wote. Alilia kwa
kusononeka kutoka moyoni, huku akikubali kushindwa.
Alilia kukosa ambacho
wala hakuwahi kumiliki na wala hakuwa akimfahamu Geb. Labda ni juhudi alizoweka
kwenye kuvaa akitaka kumfurahisha? Ni kweli Nanaa kwa mara ya kwanza amependa? Amependaje
mtu kwa kumuona tu? Hamfahamu Geb. “Sasa kwa nini nilie wakati hanifahamu na
mimi simfahamu? Anamaisha yake na mimi ninayo yangu. Huu ni ujinga.”
Nanaa aliwaza na kujikashifu. Akaamua kulala.
****************************************
Sababu ya kulia muda
mrefu, alipitiwa na usingizi mzito mpaka akaamshwa na simu ya James. “Pole.
Nasikia uliondoka kazini ukiwa unaumwa. Vipi?”
James
aliuliza. “Sasa hivi najisikia vizuri. Nilipatwa na kizunguzungu cha gafla,
tumbo lilikuwa linauma.” “Unataka nije nikupeleke hospitalini?” “Hapana kaka
yangu. Nimepumzika angalau sasa hivi najisikia vizuri.” “Pole sana.” “Asante.” Ukimya ulizuka kidogo.
“Unauhakika utakuwa sawa bila
kwenda hospitalini?” Bado
James alionyesha wasiwasi. “Usiwe na wasiwasi. Nikijisikia vibaya nitakupigia. Lakini sasa hivi
najisikia vizuri.” “Basi nitamjulisha na Grace. Amenipigia simu akiwa na
wasiwasi.” Nanaa
alijisikia vibaya sana kwa jinsi alivyoondoka, hata yeye hakujua kilichompata. “Naomba
uniombee msamaha. Niliondoka gafla.” “Afadhali uliwahi kuondoka kuliko kuzidiwa
ofisini. Basi pumzika, usihangaike na kupika. Mimi nitakula hukuhuku,
nitakuletea na wewe.” “Asante. Lakini usiwe na wasiwasi, nipo sawa tu.” “Sawa.
Basi pumzika.” Nana
alivuta pumzi akajirudisha kulala vizuri.
****************************************
Wakati amejilaza ujumbe
ukaingia. ‘Vipi, unaendeleaje? Geb.’ Nanaa
aliusoma ule ujumbe na kuufuta pale pale bila hata kutaka kujibu. “Hayamuhusu.”
Nanaa alijisemea na kuiweka simu yake pembeni kwa hasira. Akarudi kulala mpaka
James alipokuja kumgongea kuwa amerudi na chakula. Aliamka kula na kurudi
kulala. Siku inayofuata alilala karibia siku nzima. Aliamka jioni na kujikuta
peke yake, James hayupo. Akapika na kuosha vyombo, akarudi chumbani kwake.
Ilipofika usiku akasikia
sauti ya Grace, Danny na James wakiingia huku wakicheka sana. “Nenda kamuamshe tujue
anaendeleaje?” Alimsikia Grace akimtuma James. “Unawasiwasi
wakupoteza mfanyakazi nini?” Danny
aliuliza huku akimcheka mkewe. “Ninavyomuhitaji huyo
Nanaa. Sitaki yule dereva awe analala na pesa. Ataanza kuzitumia. Nenda bwana
James.” Alimsikia
James akisogelea chumba chake huku anacheka. “Nanaa! Bosi wako amekufuata.” Nanaa akafungua mlango. “Nilikwambia uwaambie
najisikia vizuri, kaka. Wasiwe na wasiwasi.” “Wewe njoo uwasalimie, labda
wataridhika.” Nanaa
akatoka kuelekea sebleni.
“Tumekuletea na mchumba wako. Labda
utapona.” Grace
alimuwahi Nanaa mara alipotokea, akacheka. Fili alikuwa amepakatwa na Geb
kwenye kochi dogo, wametulia kimya. Halafu Grace na Danny wamekaa kwenye kochi
kubwa.
“Nimepona. Nilimwambia kaka James
akwambie, ili usiwe na wasiwasi.” “Afadhali. Pole sana. Tulikuwa tunamwambia
James, tunaanza kupunguza mahari, tumekuletea icecream.” Nanaa alicheka, akaenda kupokea kopo
dogo la Vanilla Ice cream. “Sijui
kama utapenda. Tumechukua tu.” “Asanteni sana kwa kujali, na poleni kwa
usumbufu.” “Hamna shida. Kwanza ndio tumepata sababu ya kuja hapa.”
Danny alidakia nakumfanya James acheke.
“Sasa unataka nini hapa kwetu?” James
akauliza huku akicheka. “Si
basi tu. Kwani hujawahi kuona wale watu wasiopenda kwao?”
Danny aliongeza nakufanya wote wacheke kasoro Geb, alibaki akimbembeleza Fili
aliyekuwa amelala kifuani kwake. Aliendelea kupitisha mkono wake mgongoni kwa Fili
taratibu. Nanaa alijifanya kama hajamuona na wala na yeye hakuzungumza
chochote, alibaki kimya tu akibembeleza mtoto.
****************************************
Alifika ofisini siku ya
jumatatu akaendelea na shuguli zake kama kawaida. Ilipofika mchana, alisikia
sauti ya Geb akiwa ameingia hapo ofisini akiongea na dada yake wakiwa mapokezi.
“Utakuwa
hunidai.” Alimsikia
Geb akimwambia Grace. “Mbona nakushukuru.
Nimeipitia ripoti nzima, naona mambo sio mabaya.” “Lakini bado nikiangalia
nafikiri unaweza kutengeneza faida kubwa zaidi, G.” “Umeniambia. Tupate basi
muda tuzungumze zaidi ili unishauri chakufanya.”
Geb
aliaga, akaondoka bila hata kusogelea ofisi ya Nanaa, akamsikia Grace anakuja
ofisini kwake. “Geb
ametuletea bank statement ya mwezi uliopita. Naomba uitunze, atakuja kudai
wakati wakutengeneza ripoti.” “Sawa.”
Nanaa
aliipokea na kuiweka kwenye faili lake.
****************************************
Yalipita majuma mawili
mfululizo bila kumuona Geb pale ofisini wala hakutuma tena ujumbe. Alitamani
kumfahamu zaidi kama anakofanya kazi, na mambo mengine mengi lakini akaishia
kujiambia haina sababu. Siku ya ijumaa wakati anakaribia kutoka, akiwa
anarudisha mafaili mengine pale mapokezi, akamuona Grace anaongea na simu
kwenye mlango wakutokea nje ya ofisi. “Nanaa!”
Grace
akamwita. Nanaa akamsogelea. “Kesho ni birthday ya
mchumba wako. Tutamfanyia sherehe ndogo tu. Unaweza kuja na James kama huna
kitu kinachokufunga.” “Saa ngapi?” “Saa kumi na nusu jioni. James anafahamu
hoteli ambayo huwa tunafanyia. Nitamwambia mje naye.” “Anapenda zawadi gani?” Nanaa aliuliza. “Mmh! Wala
usihangaike. Anamichezo mingi sana, naona hata mingine hachezei. Wewe njoo tu.”
“Nije mikono mitupu!?” Grace
alicheka. “Basi
njoo nyumbani uje unisaidie kuandaa zawadi zakuwapa watoto watakao hudhuria hiyo party, halafu
tutaondoka wote kuelekea huko kwenye sherehe na hizo zawadi.” “Hapo sawa.”
Wote wakacheka. “Mnakaa
wapi?” “Nitamtuma Danny au James wakulete nyumbani. Usiwe na wasiwasi.
Utafikishwa tu.” Nanaa alifurahia kuona amepata kitu
chakufanya siku inayofuata.
****************************************
Siku inayofuata, siku ya
jumamosi ambayo amealikwa kwenye shuguli ya Fili, aliamka asubuhi na mapema
akiwa amejawa furaha. Akafua nguo zake na kaka yake. Akasafisha nyumba, baada ya
kuandaa kifungua kinywa, akabaki amekaa chumbani kwake akimsubiria James aamke
ili ajue ni saa ngapi atampeleka nyumbani kwa Grace. Alimsikia James ameamka,
anamwita. Akatoka. “Nahisi
Grace atakutaka mapema. Danny amenipigia kuniambia msichana wao wa kazi
ameondoka leo asubuhi.” “Utanipeleka?” “Ngoja nile kwanza. Nimeamka na njaa. Nitakupeleka
kwenye saa tano hivi.” Nanaa alirudi chumbani kwenda
kujitayarisha, akamuacha James anapata kifungua kinywa huku akiongea na kucheka
kwenye simu.
****************************************
Ilipofika saa tano na
nusu, Geb alifika. “Niambie
Muhashamu wa jimbo!” James
alimchokoza. “Nipo
kaka. Nimetumwa kumfuata Nanaa.” “Pole kwa usumbufu. Kuna mahali natakiwa
kwenda sasa hivi. Nikaona mpaka nimalize huko, nije nimchukue hapa na kumleta huko
kwenu, nitachelewa.” “Hamna shida.” Geb alijibu.
James alienda kumwita
Nanaa ambaye tayari mapigo ya moyo yalikuwa yakimwenda mbio baada yakusikia
sauti ya Geb ndani ya nyumba yao. “Nilimuomba Grace amtume mtu akufuate. Kunamahali
natakiwa kwenda. Geb ndio amekuja kukuchukua. Tutaonana jioni kwenye shuguli.” “Hamna shida.” Nanaa alitoka akamkuta Geb amekaa
kwenye kochi akimsubiri.
Hakuwa amemuongelesha
tokea siku alipomuacha ofisini, tena kwa hasira na hata alipofika siku ile
akiwa na familia ya dada yake, Nanaa hakumsalimia. “Habari yako?” Nanaa alisalimia. “Nzuri.” Geb alijibu kwa ufupi tu. “Mimi nipo tayari.” Nanaa aliongeza, Geb akasimama. “Sasa kaka?” Geb alimgeukia James. “Tutaonana jioni. Ngoja nikasake pesa.”
James alijibu. “Sawa.
Baadaye basi.” Geb
aliaga nakutoka, Nanaa akamfuata nyuma baada ya kuagana na kaka yake.
****************************************
Alikutana na gari ya
rangi ya silver, aina ya ‘Cadillac Escalade, SUV’ ikisubiri nje. Nanaa alibaki ametoa macho.
Hakuwahi kuona gari nzuri vile. Akabaki anashangaa. Alisikia Terry na Evan
pamoja na marafiki zake wakishindana kutajiana aina ya magari ambayo ndio ndoto
zao. Na kama endapo watafanikiwa kimaisha watanunua magari hayo. Nanaa hakuwa
hata anaelewa hayo majina. Hakuwa kwenye ulimwengu huo wakuwaza aina ya magari
wakati hata pa kulala ilikuwa shida. Hakujua aina ya magari, na hakuona umuhimu
wa mtu kupoteza pesa nyingi eti kwa ajili ya kununua tu gari, mpaka alipokutana
na ile gari pale nje. Ndipo akaelewa kwa nini kuna aina ya magari, na watu
wanapenda aina fulani.
Wazo la kwanza alifikiria
kama angepiga picha kwenye lile gari. “Hata nikipiga picha itasaidia nini? Niache
ushamba.” Nanaa alijisuta. “Khaaa! Sio kwa uzuri huu wa gari jamani!”
Alibaki akikodoa macho. Geb alipoona amezubaa pale nje, akarudi upande wa
abiria. Mlango wa mbele, akamfungulia mlango. “Karibu.”
Akamkaribisha
kama kumshtua na kumtaka waondoke. “Asante.”
Akasogea.
Tayari miguu ilikuwa ikicheza. “Ndani litakuaje? Hizi nguo haziendani na
hili gari hata kidogo.” Nanaa aliendelea kuwaza wakati anasogelea
mlango. Akaingia, Geb akafunga mlango.
Geb alijua wazi Nanaa
amebabaika na lile gari. Alitegemea. Akamcheka moyoni kwani alishindwa kuzuia
mshangao wake. Alishangaa mpaka mdomo aliacha wazi. Geb hakujua kama Nanaa
alijijua jinsi alivyoachama mdomo na kutoa macho baada ya kuona lile gari.
Alicheka tena moyoni, akatulia tu usoni.
Alimsubiri ajifunge
mkanda ndipo aondoe gari. Nanaa hakujua hata kama anatakiwa kujifunga mkanda.
Akabaki ametulia kwenye kitu huku akishangaa ile dashboard. Akagundua safari
haijaanza. Wapo pale pale. Akamgeukia dereva wake. “Nasubiri ufunge
mkanda.” Haraka
sana, Nanaa akajiangalia gauni alilokuwa amevaa. Lilikuwa la lastiki kiunoni.
Ni kweli lilikuwa na vijinyuzi vyembamba pembeni. Vyakupitishia mkanda wa gauni.
Lakini Nanaa hakuwa amevaa mkanda. Alivaa bila mkanda. Lilikuwa la kuchanua
chini. Kigauni cheusi. Polka dots za gold. Kilikuwa kina mikono mifupi
iliyoshuka chini kidogo ya mabega. Kilimwagika vizuri sana chini ya kiuno.
“Sikupataga mkanda unaofanana na hili
gauni.” Nanaa
alijitetea. Bado Geb alikuwa akimtizama wakati anajiangalia na kuendelea kuvuta
lile gauni na kulikusanya chini ya mapaja kama kulikalia. “Kwa hiyo hapa sina
mkanda.”
Aliendelea kujieleza, akionekana kupaniki tayari. “Namaanisha mkanda wa
gari. Kwa ajili ya usalama wako.” Geb aliongea kiungwana. “Oooh! Mkanda wa gari.
Nil..nil …nilifikiri..” Akaanza kupambana kuvuta mkanda wa hilo
gari pembeni ya hicho kiti alichokuwa amekalia. “Nikusaidie?” Geb aliuliza baada yakuona anatumia
nguvu nyingi kwa kuvuta mkanda ambao hata Fili huwa anavuta bila shida.
****************************************
Nanaa alijisikia aibu
mara mbili. Sio kosa lake. Amepanda wapi gari zuri hivyo? Kaka yake James ana gari
nzuri. Lakini ni y akawaida tu, na huwa Nanaa mwenyewe hapandi mara kwa mara
kwa kuwa James anatumia gari ya ofisini siku za kazi, na hawaongozani na Nanaa.
Wanafanya kazi pande mbili tofauti za Dar. Ofisi za kina James zipo njia
yakuelekea Kawe kutokea Morocco. Na ofisi ya kina Nanaa, ipo Kariakoo Karibu na
Fire. Siku za weekend James anakuwa na mishuguliko yake na gari yake, Nanaa
anabaki nyumbani. Akiwa na safari basi daladala itahusika.
Mwanaume mwingine
aliyekuwa naye na mwenye gari alikuwa Jamal. Jamal alikuwa na gari aina ya Mark
2. Nayo ilikuwa ya kawaida sana. Tena
ilionekana ni ya zamani. Jamal aliinunua kwa mfanyakazi mwenzake akiwa
ameshaitumia kwa miaka mingi tu. Na huyo mfanyakazi mwenzake alinunua used ya
Japan. Vioo vilishaharibika. Hakumbuki hata kama lilikuwa na mkanda. Milango ya
hilo gari ya Jamal ilikuwa lazima ufunge kwa nguvu. Tena wakati mwingine mara
mbili au tatu.
****************************************
Nanaa aliendelea
kupambana na mkanda wa kiti chake mpaka alipochoka. Akakubali kushindwa. Geb
alikuwa ametulia kimya, akimsubiria achoke ndipo amsaidie. Kwa kuwa alijua kwa
uvutaji ule, lazima mikanda iji lock. Kwa hiyo alimuacha apambane mpaka ache
ndipo arudie tena kuuliza kama angetaka msaada. “Naona mikanda mibovu.” Nanaa aliongea kwa upole, baada ya
kupambana na ule mkanda na kushindwa.
Geb alimsogelea. Mapigo
ya Nanaa yalianza kwenda kasi. “Ananipa pole kwa kunibusu!?” Aliwaza
harakaharaka huku mapigo ya moyo yakienda kasi wakati Geb akijivuta upande
wake. Akanyoosha mkono kwa tahadhari kama asiyetaka kumgusa. Akavuta ule mkanda
kwa urahisi sana, akamfunga. Nanaa alivuta pumzi kwa nguvu. Akajiweka sawa pale
kitini huku aibu imemlemea.
****************************************
Kwenye nyumba
aliyopangisha kaka yake, hapakuwa na geti. Kwa hiyo ilikuwa rahisi kuingia na
kutoka bila shida. Hakujua aseme nini tena. Alishajidhalilisha vyakutosha. “Sio
kosa langu. Sijazaliwa kwenye magari. Hata yeye kuna mambo hajui. Kwani yeye ni
Mungu kuwa anajua kila kitu? Wala sio jambo la ajabu nililolifanya.” Nanaa
alijitetea kwenye nafsi yake. “Lakini nisingesingizia kuwa mikanda ni mibovu.
Gari yenyewe inaonekana mpya. Lazima nibadili mazungumzo. Kuondoa hii aibu.”
Akawaza kama ajieleze juu ya ujumbe ambao hakujibu au vile alivyomuacha pale
ofisini bila maelezo ya kutosha, na pia akamfuata nyumbani kwao, akashindwa
hata kumsalimia. “Labda nitulie tu.” Nanaa aliwaza.
****************************************
Akajifunga mkanda wake na
yeye, kisha akaondoa gari. Geb hakuongeza neno wala kuuliza swali, aliendelea
kuendesha akiwa ametulia kimya kana kwamba yupo peke yake kwenye lile gari. “Itakuwa
gari ya dada yake hii. Grace anapesa sana.” Nanaa alianza kuwaza wakati
Geb akiendelea kuendesha. Akakumbuka ripoti ya mwezi uliopita ilivyoonyesha
faida kubwa waliyoingiza. “Hakika Mungu amembariki yule dada.”
Nanaa akaendelea kuwaza.
Alishangaa kuona wanapita
Ubungo, wakielekea njia ya Mabibo hosteli. Akamkumbuka Zac, mpenzi wake
wazamani. Kidogo akaanza kukosa raha. Akajiweka sawa na kugeukia dirishani.
Akaegemeza kichwa vizuri hapo dirishani, akabaki akiangalia nje ya dirisha.
Mawazo yalimpeleka moja kwa moja mpaka siku alipomfumania Zac. “Mmmh!”
Alipumua kwa nguvu huku ameshika shavu. Geb alimtizama, lakini akagundua Nanaa
hakuwepo pale kimawazo hata kidogo. Macho yake yalikuwa nje ya lile gari.
****************************************
Mawazo yakampeleka siku
ya kwanza akitolewa bikra na Alex. Akakumbuka yale maumivu. Akakusanya miguu
yake pamoja. Akakumbuka ule utayari baada ya kujishauri kwa muda mrefu kama
amkubalie Alex au la. Alex alikuwa mkubwa kwake. Lakini wakati wote
alimbembeleza wafanye mapenzi. Ili asimpoteze au akaenda kuridhishwa na
mwingine, Nanaa aliyekuwa na shauku ya kutoka kwa mama yake mkubwa. Akaamua
kumpa Alex bikra yake. Akamruhusu yeye ndio awe mwanaume wake wa kwanza.
Akiwa anavuja damu pale
kitandani wakati Alex amekimbilia dukani kununua pedi, Nanaa aliendelea
kugugumia maumivu. Kwani ni kama Alex hakuwa amemuelewa Nanaa, pale alipokuwa
akimsihi afanye taratibu. “Naomba
uwe mwangalifu Alex. Mwenzio sijawahi kufanya mapenzi.”
Akiwa amejawa hofu, binti huyo wa sekondari alimsihi Alex aliyekuwa chuoni.
Akiwa na tumaini la kuja kuolewa. Lakini Alex alimwingilia kama aliyekuwa
anapambana. Na bado Nanaa alivumilia mpaka mwisho wa Alex akapiga bao. “Nilijua
kwa hakika Alex anganioa! Nilijua ni wangu! Lakini aliamua kuzaa na Viola! Nina
kasoro gani mbaya hivyo inayowafanya wanaume kunikimbia?” Hakukumbuka
kufurahishwa kimapenzi na Alex hata mara moja. Na wakati wote Alex hakuonyesha
kama anajali furaha ya Nanaa kwenye tendo hilo. Ilimradi yeye amefanikiwa,
aliishia kumshukuru kwa juhudi zake.
Akarudishwa kwa Jamal. “Jamal
ndio alinionyesha ni kama alikuwa akipunguza haja zake tu mwilini mwangu.
Hapakuwa na penzi lolote pale. Hata nilipomwambia ninafahamu kuwa ana mke,
hakuonyesha kujali hisia zangu. Mbona sina bahati? Ni nini wanakutana nacho
huko kwenye mwili wangu kinachowachefua na kushindwa kunithamini?”
Nanaa aliendelea kuwaza moyoni.
****************************************
Walikutana na foleni
kubwa kwenye njia yakuingilia Tabata. Wakasimama. Ndipo Nanaa akajua wanaelekea
Tabata. Alishindwa kuuliza wanaelekea Tabata ipi, kwani hakuwa amemuongelesha
chochote dereva wake, tokea amfunge mkanda. “Hivi nilisema hata asante
kweli?” Nanaa alijiuliza na kujichukia. “Ustarabu ni kitu kidogo Nanaa
jamani! Hata asante hukusema!” Akajisuta kidogo. “Nitakuwa nimesema bwana.” Akajitetea
nafsini mwake. “Hata kama sikusema, nani alimwambia anifuate na mgari wa ajabu?
Kwanza abiria huwa hawatakiwi kufunga mkanda. Ajali ikitokea? Au kwa nini basi
mikanda iliwekwa?” Nanaa aliendelea kupambana na mawazo yake.
****************************************
Simu ya Geb ilianza
kuita. Nanaa akagutuka, na kujiweka sawa. Alishangaa mlio unalilia kwenye spika
za gari. Akatulia kidogo. “Huo sio mziki bwana! Hata kama ni ushamba
sio kwa kiasi hiki. Niache kujifanya mjinga wakupita kiasi.” Akaona Geb
anabonyeza kwenye kitufe kilichopo kwenye usukani wa hilo gari. “Kuna foleni
kweli. Lakini tupo njiani tunakuja.” Geb aliongea. “Amejuaje
aliyempigia?” Nanaa akajiuliza huku akitafuta kusoma kama kuna sehemu
iliandikwa jina la mpigaji. “Mbona anazungumza naye bila mwenzie
kujitambulisha? Au namba imetokea mahali ndio akajua? Lakini wapi sasa!?”
Nanaa aliendelea kujiuliza.
“Kama
hutajali naomba upitie matunda sokoni. Nilimtuma Danny, amesahau.” Alikuwa ni Grace. Nanaa akatambua
sauti ya bosi wake. “Lakini amemjuaje mpigaji? Maana ameanza kuongea moja kwa moja baada ya
kupokea tu!” Akaanza kuchungulia kwa makini kwenye dashboard kuona kama
kuna mahali kunaonyesha namba au jina. “Hamna shida. Tunaweza
kupitia sokoni. Lakini ujue tutazidi kuchelewa. Kuna foleni kubwa kweli.” Geb
alijibu. “Ni afadhali
mchelewe lakini mje na hayo matunda. Fili ameshaanza kuulizia juisi yake.
Nimemzungusha lakini naona anaanza kunibadilikia.” “Sawa.” Geb alijibu na kukata simu. Walikuwa wakizungumza kwa
kutumia spika ya gari, kwa hiyo hata Nanaa alikuwa akiwasikiliza. Grace
aliongea kwa utulivu kama Geb. “Watakuwa wanaishi wote na dada yake.”
Nanaa aliwaza.
“Naona twende hapo Buguruni sokoni,
itakuwa karibu zaidi.” Geb
alimgeukia Nanaa, macho yao yakagongana. “Sawa.”
Nanaa
alijibu na kukwepesha macho kwa haraka. “Lakini alijuaje aliyempigia?” Bado
Nanaa aliendelea kujiuliza lakini hakutaka kujiabisha zaidi. Aliona Geb anahama
upande mwingine kurudi barabarani ili kuelekea Buguruni sokoni. “Kwani
huko kwao hakuna magenge wanayouza matunda!?” Nanaa alijiuliza.
Zena kwa
Nanaa tena.
Simu yake ikaanza kuita. Yake
haikutolea mlio kwenye spika za gari, bali kwenye kipochi chake kidogo
alichokuwa amekipakata. Akaitoa ikiwa imeshakatika. Aliposoma jina la
aliyempigia. Akaguna kwa sauti. “Mmmh!” Geb akamtizama. Ikaanza
kuita tena. “We Zena? Umekosea namba au ulitaka kunipigia mimi?”
Nanaa aliuliza mara baada ya kupokea. “Nanaa naye!?” “Nini?”
“Nakupigia wewe bwana. Za siku?” “Nzuri.” Nanaa alijibu, wazi
alionekana yupo kwenye mshangao.
“Sasa mbona hata huniulizi na
mimi?” “Nipo bado kwenye mshangao Zena. Siamini kama umenipigia mimi simu.”
“Hamna bwana. Nimekuwa na hamu na wewe. Ulishaanza field?” “Wewe Zena? Hebu
acha kunidanganya bwana. Niambie una shida gani?” “Nakujulia hali tu shoga
yangu.” “Yameanza lini? Kwani Tia ameenda wapi?” “Nanaa naye?” “Zena?
Usinifanye mimi mtoto mdogo. Najua unashida. Wewe niambie tu.” “Mpaka naona
aibu.” Nanaa
akacheka. “Aibu ya nini sasa? Wewe niambie. Mimi nilielewa. Wala usijali.”
“Mmmh Nanaa wewe! Kweli?” “Kabisa Zena. Wala usijali. Niliwaelewa kabisa wewe
na Tia.” Walifika
sokoni.
Geb aliegesha gari. Akabaki ametulia. Nanaa
hakuwa ameelewa ule ukimya. “Naomba usubiri kwanza Zena.” Akamgeukia Geb baada ya
kubonyeza sehemu ya MUTE ili Zena upande wa pili asisikie. “Tumefika sokoni. Unaweza
kunisubiri tu kwenye gari. Nitajitahidi kuwahi kurudi.”, “Hutataka msaada?”
Nanaa aliuliza. Geb akafikiria kidogo. “Hapana. Nitarudi baada ya muda mfupi
sana. Nisubiri tu.” Akashuka na kumuacha Nanaa ndani ya gari.
Akaendelea na Zena. “We Zena?” “Kwani uko
wapi?” “Buguruni sokoni. Kwani vipi?”
Nanaa
aliuliza. “Kwanza nikuombe radhi shoga yangu. Nilikukosea.”
Nanaa akacheka. “Mbona kama huamini?” “Nakusikiliza.” “Umenisamehe?” “Wewe Zena?
Nimekwambia nilielewa. Mbona kama nahisi shida yako ni kubwa sana? Unanianzia
mbalii!” “Wala sio uongo shoga yangu. Nimepata mwanaume.”
Nanaa akaanza kucheka.
“Usicheke bwana. Sasa Tia
yupo mbali. Jamaa mwenyewe anaonekana yupo vizuri. Natamani anioe.” “Hongera
Zena.”
Nanaa alimpongeza mwenzie bila hila. “Lakini nataka uje leo tutoke
wote. Na yeye akiwepo. Kisha kwenye mazungumzo yetu, nitagusia maswala ya ndoa
kwa ujumla, halafu wewe naomba uulize maswali kwa makini. Kama swala la kumpima
na mengineyo. Sitaki kupoteza naye muda.” “Ujue una kichaa wewe Zena?”
“Nisaidie shoga yangu. Mimi kama namuogopa.” “Sasa utaolewaje na mwanaume
unayemuogopa? Mtazungumzaje mkisha oana? Au utataka nihamie kwenu?” Zena
aliendelea kumbembeleza Nanaa, huku akimsikiliza hoja zake. Baada ya muda Geb akarudi
na mifuko mingi sana ya matunda.
****************************************
Akafungua mlango wa
nyuma. “Subiri kwanza Zena.” Nanaa akamuweka tena kwenye Mute na kumgeukia Geb. “Naweza kukusaidia?
Naweza hata kuyapakata hapa mbele.”
Nanaa
aliuliza. “Haina
haja. Nitayaweka tu hapa kwenye boksi kubwa, yasikuchafue wala kuchafua gari.” Geb alijibu. Akaanza kuyapanga huko
nyuma ya gari kwa uangalifu huku Nanaa akimtizama akiwa amegeuka nyuma, akabaki
akimtizama vile anavyoyapanga kwa makini. “Anaogopa kuchafua gari ya dada yake. Wala
sio mimi.” Nanaa alijisemea moyoni.
“Labda atakuwa hana kazi
ya maana, ndio maana dada yake anamtumatuma.”
Nanaa aliendelea kuwaza. “Wakati mwenzake anasoma na kujiendeleza
sijui yeye alikuwa wapi!? Kweli duniani watu hawafanani. Yaani hawa ni mapacha,
mmoja kafanikiwa, mwingine mzurulaji. Atakuwa na kazi ya kujitengeneza kama
mtoto wa kike, na kulala na kila mwanamke anayempitia. Mwanaume gani kucha
zimelingana kama anafanya kazi saluni ya kutengeneza kucha! Ananukia
kama mtoto wa kike! Mimi mwenyewe mwanamke lakini sinukii hivyo. Nywele
utafikiri anafanya kazi kwenye saluni ya kinyozi! Ndevu zimejipanga mstari,
utafikiri askari wa Uingereza! Basi kazi yake itakuwa ndio hiyo tu.
Kujitengeneza na kuzunguka na gari ya dada yake. Na macho hayo, wanawake
watakuwa wanapangwa mstari mpaka wanachoka.” Nanaa aliendelea kuwaza
huku akimwangalia Geb aliyekuwa ameinama nyuma ya gari akiendelea kupanga
matunda.
****************************************
“We Nanaa!? Akamsikia Zena anaita.
Akakumbuka kama amemsahau shoga yake kwenye simu. “Zena?” “Uko
wapi wewe? Mbona sikuelewi?” “Nimekwambia nipo Buguruni sokoni.” “Mbona
patulivu hivyo? Soko hilo soko gani?” “Nipo ndani ya gari na wewe.” Zena akaanza kucheka. “Siku hizi
shoga yangu umepata bwana mwenye gari lenye AC?” “Leta dharau zako, uone kama
nitakusaidia.” Geb
akafungua sehemu nyingine kwenye boksi, pale pale nyuma ya gari alipokuwepo akatoka
na chupa mbili za maji. Akarudi ndani ya gari, akafungua ile chupa ya maji,
akamkabidhi Nanaa. “Naona
jua kali sana. Karibu maji.” “Asante.” Nanaa alishukuru akapokea
yale maji yaliyokuwa baridi. “Karibu.” Geb naye akajibu.
“Asante ya nini na wewe Nanaa?” Zena aliuliza. “Siongei na
wewe?” Geb
akakunja uso. “Sio
wewe. Samahani ni...” Nanaa aliongea huku akinyoosha kidole
kwenye simu. Geb akaelewa. “Nani? Uko na nani wewe Nanaa?” Zena aliendelea kudadisi upande wa pili wa simu. “Nimesahau kuikausha
hiyo chupa. Chukua hii napkins itakusaidia kuikausha hiyo chupa, usilowe.”
“Asante.” Baadhi ya matone kutoka kwenye chupa aliyopewa ya maji
ya kunywa, yalishaanza kumdondekea Nanaa. Akapokea zile napkins. Geb akafunga
mkanda, akaondoa gari.
****************************************
“Mbona unasena asante kila
mara? Umepata bwana mwanajeshi nini? Naona nidhamu imeongezeaka.” “Zena! Naomba
nikupigie simu baadaye.” “Nanaa wewe! Tafadhali shoga yangu.” “Si umtafute
Tia?” “Tia yuko mbali na ameshaanza field. Hawezi kuja.” “Nitakufikiria.” “Acha
kunifanyia hivyo Nanaa. Kwanza Terry anakutafuta.” “Mmmh! Mimi ndio wakula
makombo?” Nanaa
aliuliza. “Sio makombo. Terry alinikataa kabisa. Anakutaka wewe.” “Naona
umesahau shida yako wewe.” “Basi. Naacha habari za Terry. Njoo basi leo
nyumbani tuzungumze.” “Kuna mahali nakwenda jioni.” “Mbona sasa hivi mapema tu.
Njoo kabla hujakwenda huko. Tupange mambo yetu vizuri. Tena anabest yake na yeye
hajaoa. Ukikubali tutoke wote, nitamwambia aje naye. Mambo yao safi. Siwezi
kukuunganisha kwa wanafunzi kama kina Terry.” Nanaa akacheka.
“Akikusikia Tia.” Zena na yeye akacheka. “Hawana hela
bwana. Kutwa chips mayai! Mtoko huu ni wa uhakika shoga yangu. Tutaenda kwenye
mahoteli makubwa ya maana. Usijivunge. Au ushapata bwana?” “Wapi? Nipo tu.” “Basi
njoo nyumbani tuzungumze vizuri. Lazima kieleweke.” “Ntakuja baadaye.” “Ndio
maana nakupenda.” “Acha kunidanganya. Nitakuwa siji.” “Nanaa naye!?”
Nanaa akacheka kidogo. “Haya Zena. Nashukuru kunikumbuka. Nitakuona baadaye.” alimsikia Zena akipiga
kelele za kushangilia. Nanaa akacheka na kukata simu.
Alibaki na tabasamu
usoni. Gafla akakumbuka mazungumzo yake na Zena. Tabia yake yakumuunganisha na
wanaume. “Mungu wangu! Sijui amenielewa huyu?” Nanaa akawaza. Akaamua kumtumia
ujumbe Zena baada ya kufikiria tena kidogo. “Sina uhakika kama umenielewa
vizuri Zena. Naomba
usiniunganishe na yeyote, yule. Hata aweje. Bado nipo mapumzikoni. Naomba
nikusaidie ishu yako tu, basi. Sitaki mwanaume kwa sasa.” “Nanaa naye!” “Kweli
tena Zena. Tafadhali sana. Nimeamua hivyo na naomba ibaki hivyo. Nitakuja kwa
ajili yako, basi.” “Lakini…” Wakaendelea kujibizana mpaka
wakawekana sawa. Baada ya majibizano hayo ya jumbe na kuridhika kuwa Zena
ameelewa, hatamtafutia mwanaume, akarudisha simu yake kwenye pochi. Alishangaa
kuona wamesimama mbele ya geti kubwa tu. Akajua wamefika. Akajua ameongea na
Zena kwa muda mrefu, au hawakuwa wakikaa mbali sana. Labda maeneo ya Tabata ya
mwanzoni. Pia hakuuliza. Geti likafunguliwa, wakaingia ndani. Nyumba ilionekana
bado mpya. Kulimwagwa vitofali vizuri. Kuanzia getini mpaka mlangoni. Baiskeli
ndogo ilikuwa pembeni, akajua itakuwa ya Fili.
Kwa mara ya
kwanza, Nanaa nyumbani kwa Bosi wake.
“Karibu.” Nanaa alifungua mkanda. “Asante. Nikusaidie
nini?” “Nisubiri tu twende wote ndani. Nitabeba tu mwenyewe, sio vitu
vingingi.” Geb alitoa boksi zima. Lilikuwa ni boksi la plastiki,
lenye mishikio miwili. Lilionekana ni maalumu kwa kubebea vitu kama hivyo. Akafunga
mlango akamkaribisha ndani. Wakaongozana mpaka ndani sebleni.
“Karibu Nanaa, nipo huku jikoni.
Msichana wa kazi ameondoka leo asubuhi, amefiwa. Natayarisha chakula cha
mchana, tukishakula ndio tuanze kufunga zawadi.” Nanaa alimfuata
Geb kule jikoni kulikosikika sauti ya Grace. “Asante na pole na shuguli.” Nanaa akaingia. “Asante mwaya.” Grace alijibu na tabasamu.
“Mama yuko wapi?” Geb
aliuliza mara baada yakutua mzigo. “Alikuwa anasinzia
hapa, Fili amempa nyanya, kala nusu, nusu amekufunikia hapo kwenye meza.
Ameniambia ukija uile.” Grace
aljibu, Geb alinawa mkono akasogelea ile sahani. “Halafu nimempatia maparachichi.” “Atafurahi
kweli. Alikuwa ananiambia anahamu nayo.” “Tena nimepata yale mazuri
anayopenda.” Geb aliendelea kukila kile kipande cha nyanya huku
akiongea na dada yake.
“Fili yuko wapi?” Nanaa
aliuliza. “Yupo na bibi yake
huko chumbani. Na anavyopenda kuongea mwanangu yule, sijui kama mama atakuwa
ameweza kulala!” Nanaa
akacheka. “Ngoja
nikamwangalie mama. Nitakuja kukusaidia kutengeneza juisi.”
Geb alitaka kutoka. “Ungenielekeza
tu mimi, nitatengeneza.” Nanaa
alimuwahi. “Anza
basi kuosha matunda mawili mawili kutoka kwenye hilo boksi. Nikirudi
nitakutolea tangawizi na Blenda, nikuonyeshe tunavyosaga. Ni rahisi tu.” Geb
alitoka akamuacha Nanaa anaanza kuosha matunda.
“Pole.” “Nimeshazoea. Wasichana huwa
hawakai hapa kwangu, sijui kwa nini! Mwanzoni nilifikiria wanalemewa na kazi,
tukawa tunawasaidia, lakini wapi. Nikafikiri ni sababu ya Fili.” “Kwa nini
Fili?” “Mtoto ni mtundu huyo, hujawahi kuona. Yupo kama baba yake. Akianza
kuongea mpaka kichwa kinauma na anataka umsikilize. Nahisi ndio maana
wanatukimbia, wanachoka. Nikataka kumuanzisha shule mapema ili niwe natoka naye
asubuhi na kurudi naye jioni, ili kuwafanya wasichana wa kazi wasitukimbie,
lakini Danny hataki aanze shule kabla yakufikisha miaka 5. Kwa hiyo wasichana
wa kazi wakitukimbia, inabidi wote tupeane zamu ya kubaki naye hapa. Lakini
bibi yake ndio huwa anakuwa naye zaidi, kwa kuwa hachoki.” Nanaa akacheka.
“Kweli tena. Bibi yake
anatabia kama za Geb. Huwa hawachoshwi na kelele nyingi, wanawezana naye. Kwa hiyo
muda mwingi hata tukiwa na mfanyakazi, bibi yake huwa anachelewa kwenda kwenye
shuguli zake. Anamuhudumia Fili. Anahakikisha amemuogesha, anamuacha amekula
ndio anaondoka, ili Msichana wa kazi asiwe anahusiki na mtoto, nayo pia
haikusaidia.” “Poleni.” Nanaa
akaona ampe pole.
“Haya na anko wake pia akaanza kazi ya
kufua nguo zote. Mara mbili kwa week. Tena wakati mwingine akiona nguo nyingi
anafua mpaka usiku na kukunja nguo zote, anampangia Fili kabatini kwake, na
mimi nakuwa napika chakula cha usiku mara nyingi, ili tu kumpunguzia msichana
wa kazi majukumu, lakini pia naona hawakai. Sasa sijui itakuaje, lakini kwa
kuwa ametimiza miaka mitano, ni heri aanze tu shule, nitachanganyikiwa bure.”
“Pole. Na Danny?” Nanaa
aliuliza baada yakuona dad mtoto hayupo kwenye ratiba ya ulezi.
“Huyo sitaki akae na mwanangu siku
nzima. Mwanangu anakuwa hana raha. Mkali sana kwa Fili. Anamlea kama mtu mzima
bwana! Hapana. Yaani nikimuacha mwanangu na Danny hata masaa mawili tu, tumbo
linauma. Kila saa nampigia simu au naomba Geb arudi aje awaangalie. Najikuta
kazi zenyewe zilizonipeleka ofisini sifanyi, nina kazi yakumpigia simu Danny,
kumkumbusha umri wa Fili. Ndio tumeona tuache kumpa yeye hiyo kazi ya ulezi
tubaki nayo sisi tu.” Nanaa
alikuwa akicheka sana.
****************************************
Geb alirudi akiwa amembeba Fili mabegani. “Usimuweke hapo juu
bwana. Ataanguka. Si unamjua hawezi kutulia?” “Nimemtoa kule kwa mama ili
apumzike kidogo. Anaruka ruka tu kitandani mama hawezi kulala.” “Tulia basi
kidogo Fili mwanangu. Huchoki? Au nimpigie simu dad arudi aje akuchukue?”
“Hapana mama. Natulia” “Basi tulia. Tumalize kazi haraka ili tuwahi kwenye
birthday yako.” Tayari Grace alionekana kulemewa.
Alishika hiki na kuacha nusu.
“Mwache bwana. Mimi si nipo? Hawezi
kuanguka. Haya nenda kamsalimie Nanaa, halafu uje ukae hapa kwenye meza.” Alienda kusimama mbele ya Nanaa
akabaki akimtizama huku anacheka.
“Anajua kuchanganyikiwa vibaya huyu!
Sasa unacheka nini badala usalimie.”
Mama
yake alidakia huku akiendelea na shuguli zake. “Hapo anataka uiname, akubusu.” Geb aliongeza, wakacheka. Fili
alienda kuvuta kiti mpaka karibu ya Nanaa, akapanda na kumfikia Nanaa. “Ningeinama tu.” Nanaa akacheka. “Uiname umpunguzie
shuguli? Anapenda shuguli huyo!”
Grace
aliongeza. Fili alimbusu shavuni kisha akamkumbatia. “Asante Fili.” Nanaa alishukuru na tabasamu la aibu
usoni. Hakuzoea.
“Karibu. Umekuja kuishi na mimi?” Fili aliuliza. “Nitakuchukua twende
tukaishi wote kwangu.” “Afadhali. Umchukue moja kwa moja. Lakini James anaweza
kumrudisha usiku huyo.” Grace
aliongeza na kufanya Nanaa acheke. “Wewe ndio uje uishi hapa kwetu.” Fili aliongeza. “Kwa
nini?” “Dad amesema nisubiri mpaka nisome, nipate mahela mengiiiii.”
Fili alionyesha ukubwa wa pesa anazotakiwa awe nazo kwa kupanua vimikono vyake.
“Halafu
ndio amesema nikishapata pesa niende kwa anko James, tumlipe hela, nikuchukue.
Lakini amesema nikikuchukua nisirudi hapa, nikupeleke kwangu.”
Walicheka sana.
“Yaani Danny jamani!” Grace alilalamika. “Lakini wewe ukija
hapa sasa hivi, usimwambie kama mimi ndio nimekwambia uje tuishi wote hapa.
Wewe umwambie umeamua kuja kuishi hapa na mimi, wala sijakuita. Halafu hawezi
kukufukuza.” Fili
aliongeza na kuwafanya wote wazidi kucheka, Geb alikuwa akitingisha kichwa. “Hapa kazi ipo. Akili ya ujanja ujanja
kama baba yake. Wewe! Tulikwambia nini juu ya kusema uongo?” “Hapo anko
nitakuwa mimi sijadanganya. Nanaa atakuwa ndio amekuja hapa.”
Fili alijitetea.
“Kwa hiyo unamfundisha Nanaa kusema
uongo?” “Hapana anko.” “Na hapo pia unasema uongo. Si umemfundisha aje hapa
asikutaje kwa dad wako kama wewe ndio umemkaribisha?” Fili alinyamaza kidogo kisha
akauliza. “Kwani
huo ni uongo?” “Sasa je? Hakuna kusema uongo.” “Basi Nanaa. Usiseme tena.
Samahani anko.” “Haya, nenda kacheze, usubiri mpaka upate hela kama alivyokwambia
dad, ndio utaenda kumlipa anko James, umchukue Nanaa, umpeleke kwako sio hapa.
Sawa?”
Fili alipooza. “Sawa
anko. Kwani utamwambia dad?” Aliuliza
kwa upole. “Ukirudia
tena kumfundisha Nanaa kusema uongo, ndio nitamwambia.” “Mimi sirudii tena. Usimwambie
dad wangu.” “Ujue nitakuwa nakusikiliza kila neno unaloongea. Usirudie tena.
Haya nenda.” Alishuka
kwenye kiti, akatoka.
****************************************
“Afadhali umemuweza. Fili anaongea
jamani! Halafu hasahau jambo kama baba yake. Hapo ataenda kumsimulia kila mtu
kuwa anataka kuoa lakini dad amemwambia atafute kwanza pesa.” Wote waliendelea kucheka wakati Grace
anasimulia vituko vya mwanae, Geb anatengeneza juisi. “Sasa si atarudi tena
kwa bibi yake?” Nanaa
aliwakumbusha, Geb akatoka kwa haraka kwenda kumtafuta, akarudi amemshika. “Alishafika chumbani
kwa bibi yake nakuanza kumsimulia habari zake zisizo isha. Nimekwambia kaa
hapa.”
Geb
alimpandisha tena juu ya meza. “Msimulie
Nanaa badala ya bibi.” Fili
akaanza kusimulia huku akiruka ruka hapo juu ya meza.
“Utaumia Fili mwanangu. Tulia basi.”
“Naweza kuruka hapa, mama. Juu mpaka chini. Muulize anko.” Fili
alimchonganisha anko wake. “Wewe
Fili?” Geb
alimshtua huku akimkonyeza anyamaze lakini hakunyamaza. “Namwambia ukweli mama
yangu. Mwenzio anko sio muoga. Ananiruhusu nipande halafu niruke.” Nanaa alicheka sana. “Geb jamani!” Grace alilalamika. “Hawezi kuumia bwana. Huyu
ni spider man. Acha hofu.” “Usikubali awe anaruka.” “Hana neno bwana. Kwanza
hapo pafupi.” Geb alitetea. Alikuwa akimruhusu kuruka kwa siri,
akiona mama yake hayupo. Alikuwa akivaa nguo zake za spieder man na kumuomba
anko wake aruke kama spider man.
“Kwani ni lazima aruke? Tafuta mchezo
mwingine. Umesikia Fili?” “Spider man lazima aruke mama.” “Hapana Fili
mwanangu. Mwambie dad au anko wakutafutie kazi nyingine za spider man, ufanye.
Kuliko kuruka. Ukivunjika, mama ataumia sana.” “Basi mama yangu. Nitaruka
kidogo tu.” Geb na Nanaa wakacheka. “Kwani lazima kuruka
Fili? Acha tu mwanangu. Utaumia.”
Mama
yake alisisitiza huku akimpa juisi aliyokuwa ametengeneza Nanaa. Alimuwekea
kwenye chupa yake maalumu yenye picha za spider man, akaanza kunywa, ndio
akanyamaza. Geb alimbeba na kutoka naye pale jikoni akabaki Nanaa na Grace
wakimalizia usafi.
****************************************
Grace alipanga chakula
mezani, akamwita kila mtu aje kula. Wakati wamekaa mezani ili wale, mama yao
naye akatoka chumbani. Umbile alifanana sana na Grace kama alijizaa huyo
mwanamke, hata rangi alifanana na watoto wake lakini sio yale macho. Nanaa akasimama.
“Nilikuwa
naaambiwa mchumba umefika.” Yule
mama alitoa mkono na kumpa Nanaa, wote wakacheka. “Naona sasa hivi kila
mtu anamfahamu Nanaa. Kila anayepiga simu, anakaribishwa kwenye birthday na
kuambiwa Nanaa atakuwepo. Mwanangu amependa jamani.” Grace alidakia.
Wote wakacheka. “Shikamoo mama.” Nanaa alisalimia huku akicheka. “Marahaba. Karibu
sana.” Yule
mama alikaa.
****************************************
“Mbona sahani yako haina nyama?” Mama yao alimuuliza Geb. “Nimeshakula zote.” Geb alijibu. “Chukua na hizi
zangu.” “Kula bwana mama. Nikitaka nitaongeza. Mbona bado zipo tu nyingi.”
“Basi chukua hii moja.” Walibishana
kwa muda, mwishowe Geb akachukua nyama kutoka kwenye sahani ya mama yake. “Hajawahi kukua huyo
kwa mama. Utawazoea tu. Mama akila kitu, anataka na mwanae ale. Hata kama
hayupo nyumbani, anakula nusu, nusu anamuwekea.”
Grace
alimwambia Nanaa, Nanaa akacheka kidogo na kuinama. “Mvivu sana wakula
huyu. Usipomsisitiza kula, ndio basi tena. Hizo nyama zilizofanikiwa kuingia
huko tumboni ndio kashamaliza hapo. Huo mdomo hautapitisha tena kitu kingine.”
Mama yao alimtetea Geb, Nanaa alicheka tena kidogo na kuinamia sahani yake tena,
akaendelea kula bila yakuongeza neno.
“Watakuwa wanamdekeza ndio maana hataki
kutoka nyumbani kwa dada yake, akaishi peke yake ajitegemee. Amenikalia
kudeka!” Nanaa aliwaza. Wakala lakini hawakuwa wakizungumza sana, mpaka
Danny alipoingia ndio akaanza kuongea nakuwafanya wote waanze kucheka. Kitu
kidogo, Danny alikikuza, akakisimulia kwa mbwembwe nyingii na kuwafanya wote
wacheke. Fili alianza kusinzia, Grace akambeba kwenda kumuogesha ili amlaze
angalau apate usingizi wa mchana. Nanaa alitoa vyombo pale mezani wakisaidiana
na Geb.
“Acha niwasaidie tu kusafisha. Sio
vingi.” Nanaa
alitaka Geb ampishe pale kwenye sinki. “Ni vyakupanga tu hapo kwenye mashine.
Huwa mashine inatusaidia kuosha. Labda sufuria ndio zakuziosha. Ngoja
nikuonyeshe.” Geb alisuuza kidogo, akavipanga vyote kwenye mashine
iliyomtoa macho Nanaa, hakuwahi kuona mashine yakuoshea vyombo. Ili kuepuka
mshangao usoni, akaamua aanze kuosha sufuria. “Sasa kwa nini wasichana wa kazi
hawakai kama kuna mpaka mashine za kuoshea vyombo?” Nanaa aliwaza.
****************************************
Simu ya Geb iliita.
Akatoa mfukoni na kupokea. “Vipi?” Aliuliza. “Nimetoka kazini, nimechoka.” Akasikia sauti ya kike
upande wa pili. “Njoo upumzike hapa kwetu.” “Fili anakelele bwana.” Yule msichana alilalamika, Geb
akacheka. “Ameenda kulala, hatakusumbua.” “Acha tu niende kwangu. Nipumzike,
nikiamka ndio nijiandae kuja kwenye birthday yake.” “Njoo basi, angalau
nikuone, Liz.” Geb alimbembeleza. “Kwani una
hamu na mimi?” Liz
aliuliza. “Si ndio maana nataka uje?” Liz alisikika akicheka. “Niache nikalale kidogo, Geb.
Nimechoka. Tukitoka kwenye sherehe tutakuwa wote, mpaka utanifukuza.” “Sawa
mama. Baadaye basi. Ulale unono.” Liz alisikika akicheka tena. “Asante.” Wakakata
simu.
****************************************
Mara Grace akaingia. “Usingehangaika kuosha hayo masufuria,
Geb angeosha tu.” “Hamna shida. Kwanza namalizia.” “Basi ukimaliza uje tukae
hapo sebleni, tupumzike kidogo. Fili amelala.” “Mbona Fili mwenyewe sio mtundu
wa hivyo?” Geb
na Grace waliangaliana wakacheka. “Kweli. Nipeni mimi siku za jumamosi
niwe nakaa naye.” “Kama ulikuwa unatania ujue ndio imekula kwako. Na hivi sina
msichana wa kazi, jumamosi ijayo asubuhi na mapema, nakuletea kwako.” Nanaa alicheka. “Kweli tena, wewe
mlete tu. Ndugu yangu ana mtoto wa kiume, yule mtoto ndio mtundu. Huwa tukienda
nyumbani na kaka kusalimia, huwa kaka anachoka. Anasemaga ameshaona watoto
watundu, lakini pale mwisho.” “Mtoto wa Viola?”
Grace
aliuliza na kumfanya Nanaa kushangaa kidogo.
“Kumbe unawafahamu dada zake James?” Wakacheka. “Alishawahi kufika
hapa. Zamani kabla ya kupata mtoto. Alimpenda sana Geb, lakini tatizo la Geb
kazubaa. Sasa hivi angekuwa na mtoto mkubwa tu na Viola.”
Nanaa alitulia kidogo kama anawaza. “Tena hata Vai pia alishafika hapa.
Walikuja kumtembelea kaka yao hapa Dar, James akawaleta waje watusalimie.”
“Kumbe! Sikuwa nafahamu kama mnafahamiana vizuri hivyo.” “Sana tu.” Grace
akaitika bila shaka. Nanaa alikosa raha asijue ni kwa nini. Alikausha mikono,
akabaki amesimama kama aliyeduwaa.
****************************************
Kumbukumbu za mateso pale
nyumbani kwa Mama yake mkubwa zilimjia. Vile Viola alivyompokonya mwanaume
wake, akazaa naye, huku akipongezwa na mama yake bila kujali machungu
aliyomsababishia. Alimkumbuka Alex, ahadi walizokuwa wamewekeana, majina ya
watoto waliokuwa wameamua kuwapa pindi watakapo jaliwa watoto hao. Lakini akaishia
kuzaa na Viola.
Alex alifanikiwa kulipa
mahari kama alivyoahidi, Viola akabaki akimsubiri amalize chuo ili wafunge
ndoa, lakini walikuja kusikia Alex alioa mwanamke mwingine, kwa haraka sana,
mara tu baada yakumaliza chuo chake. Ilimchukua zaidi ya miaka miwili kwa Nanaa
kuja kurudi nyumbani kwa mama yake mkubwa, Moshi. Kila James alipokuwa akienda
kusalimia, Nanaa alikataa kurudi. Alimuomba ampe kwanza muda wakupona. James
alikuwa akimletea habari zote ya kinachoendelea nyumbani kwao, lakini Nanaa hakuwa
akienda kusalimia na alikata mawasiliano kabisa.
Yalikuwa ni majuma machache
sana yaliyopita kabla yakuanza kazi kwa Grace ndipo alipoona ni vyema kuungana
na James, kwenda kusalimia nyumbani kwao. Siku alipokwenda kusalimia, alijuta. Asubuhi
ya siku inayofuata baada ya kutua tu Moshi, Mama yake mkubwa aliimwita kutoka
chumbani alipokuwa amelala na kumtaka aende hapo sebleni kwa mazungumzo. Nanaa
alivaa, akaosha uso, na kwenda kukaa alipokuwa amekaa yeye na watoto wake. Bila
hata kujua linaloendelea kwenye maisha ya Nanaa ambaye hawakuwa wameonana kwa
zaidi ya miezi 24, tena waliachana katika hali ya machungu, yule mama alianza
kumsema sana Nanaa.
James na baba yake walikuwa wametoka, kwa hiyo
alimsema vile atakavyo. Alimsema Nanaa bila kupumzika tena akitumia maneno
machafu ambayo asingethubutu kumsema mtoto wake aliyemzaa. Alimsema vile
alivyonyimwa shukurani. Amefanikiwa kidogo tu na kusahau alipotoka. “Usifikiri hapo ulipo
umefika mwenyewe. Hata hapo unapoishi sasa hivi ni kwa James, mtoto wangu. Tulimsomesha
na kumtunza kwa jasho letu. Sasa hivi wewe usiye na shukurani ndio unafaidi
jasho la mtoto wangu. Umekuwa mzigo kwenye maisha yake mpaka anashindwa
kumsomesha mdogo wake, anakusomesha tu wewe mtu baki. Hunashukurani kabisa.
Umeondoka hapa, unashindwa hata kunijulia hali! Mwenzio anashindwa kusaidia
nyumbani kwao, kwa kuwa wewe umekuwa mzigo kwake! Unajidai msomi kwa kuwa
umefika chuo kikuu! Tutakuona utafika wapi.” Alimsema Nanaa mpaka
aliposikia gari ya mumewe wakirudi nyumbani na James, ndipo akanyamaza na
kubadilika kuwa mwema kwake kana kwamba sio yeye na kubadili mazungumzo mara
James alipoingia tu ndani.
****************************************
“Nanaa amemshauri Vai mrudi naye Dar na
yeye akatafute shule asome.” Alimuwahi James kabla hajakaa, na
tabasamu usoni. James alipoona sura ya Nanaa alijua kilichokuwa kikiendelea na
kujua ule ulikuwa uongo. “Mbona
baba ameniambia kuwa Vai anataka kuolewa? Sasa anasoma lini na kuolewa lini?” James
aliuliza huku akikaa. “Kwani
mtu akiolewa hawezi kurudi shule?” “Nini kinaanza sasa?” James
aliuliza tena. “Vyote
vinaweza kwenda kwa wakati mmoja.”
Mama
yake alimjibu. “Basi
kama ndio hivyo akasomee kwake na mumewe amsomeshe.” James alijibu.
“Mwanaume mwenyewe hana pesa. Sijui tutaishije?” Vai aliongeza. “Nanaa twende
nikakuonyeshe kitu.” James hakutaka kuingilia kabisa.
Alishawazira wadogo zake. Alichukia vile mama yao anavyowakingia kifua, hata
walipokuwa wakikosea, hakutaka waonywe. “Sasa utaondoka na Vai, ili aanze
kujiandaa na safari?” Mama
yake alirudia tena. “Hapana.” James alijibu bila hata kufikiria.
Kama aliyekuwa ameshaandaa jibu tayari.
“Kwa nini!?” Mama yao aliuliza kwa mshangao na
hasira. “Yaani
upo radhi kumsaidia huyu mtu baki na sio mdogo wako, ambaye ni damu yako?! Tumeshamsaidia huyo Nanaa vyakutosha.
Ni wakati sasa atafute maisha yake, apishe nafasi ya wenzie wapate msaada.
Kwanza bibi yako anashida.” “Nimeshazungumza na bibi na nimeshamtumia pesa za
matumizi.” “Sasa nini kinachokushinda kumchukua Vai?” James alirudi kukaa kwenye kochi.
“Unakumbuka Viola na Vai walishakuja
Dar ili waishi na mimi? Unakumbuka kuwa mimi ndiye niliwarudisha? Nilikueleza
sababu zote za kwa nini nawarudisha nyumbani. Nilishindwa kuishi nao. Nafasi
niliyotaka kuwapa wao, sasa hivi nimempa Nanaa na anaitumia vizuri. Nanaa
amekuwa msaada kwangu. Tunaheshimiana. Hawa watoto wako walinitia aibu kwa
marafiki zangu, mpaka ikabidi niwafukuze. Kila mwanaume walikuwa wanamtongoza
wao. Mpaka waume za marafiki zangu wanawatongoza. Kama rafiki zangu wangekuwa
watu wasio na ndoa za kueleweka si wangevunja ndoa zao? Na pia hawana uwezo
wakufanya kazi za nyumbani kama Nanaa. Wakati naishi nao, Viola na Vai,
ilinilazimu kuwatafutia msichana wa kazi wakuwahudumia wao, wakati wao wamekaa
tu, wanaangalia tv, mchana na usiku. Shule walikataa, wakaishia kuniingiza
hasara zakulipa ada bila wao kuhudhuria darasa hata moja. Nanaa amekubali
kusoma. Anahangaika na shule, amebakiza kidogo tu amalize.” James alijieleza
kwa kituo bila jazba, ili mama yake aelewe.
“Watu wanabadilika James. Dada zako
wamebadilika sana.” “Basi watafute chuo hapahapa Moshi waanze kusoma. Kama baba
ameshindwa kuwasomesha, mimi nitatuma hiyo pesa itakayohitajika ya ada.”
“Sijashindwa kumsomesha hata mmoja wao hapo. Muulize Viola kama sijambembeleza
ajikaze arudi shule. Tena nilimwambia nitamsaidia kumtafuta mtu wakumlelea
mtoto wake, wakati anasoma, lakini amekataa. Ni week iliyopita tu nilimkumbusha
tena, akakataa. Jana pia nilizungumza nao wote wawili kutaka warudi shule,
lakini wamekataa. Sijashindwa kuwasomesha hata kidogo.” Baba yao aliingilia. “Nanaa twende.” James akasimama na kutoka nje
kumsubiria Nanaa.
****************************************
Alikumbuka yale maneno
yote. Akakumbuka vile Grace naye alivyosema anawafahamu vizuri sana. Aibu na
hofu ikaanza kumwingia. “Sasa sijui walimtaka mume wa Grace, Danny
au wote wawili? Aibu gani hii! Kumbe muda wote nipo hapa wananiangalia tu,
kumbe wanazijua habari zetu! Sijui niage niondoke?” Nanaa alibaki
ameduwaa, huku Grace na Geb wakizungumza pale pale jikoni, akasikia wanacheka.
Akashtuka.
“Twende
basi.” Grace alitoka pale jikoni, akamfuata nyuma, wakaenda kukaa pale
sebleni, Nanaa akiwa amepotelea kwenye mawazo. Zile kumbukumbu za maneno ya
mama yake mkubwa zilishamuharibia utulivu wa moyoni. Akabaki kimya nakushindwa
kuchangia lolote. Geb naye alitoka akaenda kukaa pale akisaidia kufunga zawadi.
****************************************
Mara waliona mlango
unafunguliwa. “Liz!” Geb alishangaa. “Si ulisema una
usingizi?” “Nimekubali ile ofa ya kuja kulala hapa hapa. Shikamoo bibi wa Fili.” Liz alimgeukia mama yao nakusalimia. “Marahaba. Karibu.” Alijibu kwa ufupi tu mama huyo
akanyamaza. “Njaa
inauma, nina usingizi, sijui nifanye lipi niache lipi?” “Nilikwambia napika.
Chakula tumekirudisha sasa hivi kwenye friji. Wewe nenda kale ndio ukalale.” Grace
alijibu, Geb akasimama, Liz akambusu midomoni. “Twende nikusindikize ukale, ndio ulale.”
Wakaondoka na Geb kuelekea jikoni, akamsikia Liz akiongea na kucheka akiwa na Geb
huko huko jikoni. Akajua ni wapenzi.
“Liz! Liz!” Grace aliita. “Nimesahau
kukutambulisha kwa Nanaa. Njoo.” Liz alitoka. “Huyo ndio Nanaa.” “Mchumba wa Fili?”
Liz aliuliza na kuamsha kicheko. “Amemng’ang’ania! Kabla hajalala
alikuwa anamfundisha Nanaa uongo wakumwambia baba yake ili ahamie hapa.” “Aje
amlee?” Liz akauliza. “Naona. Maana
wasichana wa kazi wote wanamkimbia. Lakini Geb akamgombesha aache uongo, naona
akapooza mpaka akapata usingizi.”
Wakacheka
tena.
“Sasa Nanaa ujiandae. Mume yule hamna
kulala sababu ya maneno mengi. Sura ya upole kama mama yake. Akikuangalia hivi
na macho yake yale, utafikiri ni malaika ambaye hajaanza kuongea. Lakini ngoja
afungue mdomo, ndio utajua ni mtoto wa Danny. Jana amenipigia simu ananieleza
habari zako, mpaka nikapitiwa na usingizi. Mtoto hachoki! Kila nikimuaga
ananiita, ‘Anti Liz, nimekwambia Nanaa ni mzuri?’ Namwambia
ulishaniambia zaidi ya mara hamsini, anasema ‘Ndio unatakiwa usisahau sasa’.”
Kila
mtu alikuwa anacheka. “Sasa Nanaa ujiandae.
Hajuagi kuongea kwa kifupi huyo mumeo, na hachoki.”
Liz
alirudi jikoni, baada ya kula wakaongozana na Geb chumbani.
**************************************************
Japokuwa alikuwa
akicheka, lakini moyoni alishakosa amani, asijue ni nini kinachomsababishia ile
hali. Kama ni maneno ya kashfa aliyokumbuka kuambiwa na mama yake mkubwa, au
ujio wa Liz, au aibu ya ndugu zake hapo kwa kina Geb, hakujua ni lipi, lakini
moyoni alikuwa ameshafuka kabisa. Alibaki kimya mpaka walipomaliza. Grace
alikuwa akiongea na mama yake huku Danny akiangalia mpira.
“Naona tumemaliza mapema na bado tuna muda
mwingi uliobaki wa sherehe ianze. Naomba niondoke, kuna mahali nataka nipitie
kabla ya kuja huko kwenye birthday.”
Nanaa
aliaga baada yakumaliza. “Basi
ngoja nimwite Geb akupeleke.” Grace
alitaka kusimama. “Hapana.
Mwache tu apumzike. Ningependa kwenda peke yangu.”
Grace akacheka. “Haya Mkwe wangu.
Lakini usimsaliti tu mwanangu.” Grace
alirudi kukaa, akamfanya Nanaa acheke kidogo. “Wala usijali. Nitakuja kwenye sherehe,
nicheze naye.” Nanaa alichukua pochi yake akamuaga mama yao na Danny
aliyekuwa akishangilia mpira kwenye tv, akatoka.
**************************************************
Kwa mara ya
kwanza Nanaa akiwa amekusudia kuachana na mapenzi. Akiwa ameumizwa vyakutosha,
anapatwa na hisia za tofauti kwa Geb ambaye anamvutia kwa ajabu asijue ni nini. Hamfahamu Geb hata kidogo, ila kwa hakika anajua anampenzi wake, Liz. Liz si msichana
wa vichochoroni. Anafahamika mpaka kwa mama yake Geb. Anaonekana kufahamiana na
Grace vizuri tu. Na ni Anti wa Fili
Nini
atafanya? Je, atatupia mbali hisia hizo ngeni zinazomliza na kumuumiza moyo?
Nini kitatokea
kwenye sherehe ya Fili?
Je, Zena
ataheshimu ombi la Nanaa?
Usikose Sehemu ya 8.
0 comments: