Story
is mine - ni Wangu! Part 1, Sehemu ya 11
B
|
ado ilikuwa mapema tu, Nanaa akamtafuta Zena kwa simu. “Naweza
kuwaona kabla ya saa 12 jioni.” Zena akafurahi sana, akabaki anashangilia. “Wewe Zena, sasa nitawakuta wapi?” “Njoo
pale Sinza pub. Tutakusubiri.” “Kwani wewe unaishi na Yasini?” “Ukija,
nitakusimulia. Lakini hapa baba na mama, wanajua nimesafiri kikazi. Field.”
“Wewe sikuwezi.” “Nakusubiri shoga yangu. Hapa nikimalizana na wewe tu,
nampigia na Jeff, tukutane.” “Sawa. Mimi najiandaa nitoke.” Wakaagana.
Nanaa akajiandaa, nakutoka. Alimkuta bibi Fili anamsubiria
Geb sehemu ya kulia chakula. Geb alikuwa akioga chumbani kwake. “Mbona
umependeza hivyo?” “Naenda kukutana na rafiki zangu mara moja. Nimekuwa
nikiwaahirisha kila wakati.” Danny akakohoa. Alikuwa sebleni na mkewe,
wanaangalia tv. Nanaa akacheka na kuinama.
“Umependeza kweli Nanaa. Au ndio na
safari ya kwa Jeff?” Bibi
Fili akaendelea kuhoji kichokozi. “Na yeye pia atakuwepo mama.” Nanaa alijibu kwa aibu kidogo. “Sitakawia
kurudi. Nataka na wao nikawashirikishe swala la uhitaji wangu wa chumba.
Pengine wanaweza kunisaidia kwa haraka.” “Sawa.” Nanaa akasogea pale
sebleni.
“Umependeza sana Nanaa.”
Grace akamsifia. “Asante.”
Alijibu kwa aibu. “Nitarudi baadaye.” “Unataka usindikizwe?” Grace
akauliza. “Hamna haja. Nitachukua daladala hapo barabarani.” “Sawa. Uwe na
wakati mzuri.” Danny akaanza kucheka. Nanaa akatoka bila hata kugeuka huku
anacheka. “Anaonekana ni binti mtulivu sana.” Alimsikia bibi Fili
akisifia. “Na ni mzuri pia.” Akamsikia Grace anaongeza.
*****************************************************
“Naona Jeff amekaza kweli. Mpaka amekubaliwa!” Danny aliendeleza maongezi. “Nani?”
Geb alitoka akakuta wanaongea huku wanacheka. “Nanaa katoka.” “Sio katoka
bwana Grace. Wewe vipi? Sema katoka na amependeza kweli kweli. Halafu kamuaga
mama anaenda kumshirikisha Jeff, hana sehemu ya kuishi. Kama namuona Jeff
atakavyofurahi.” “Danny wewe! Nanaa anaenda kwa rafiki yake. Tena walikuwa
wakizungumza kwenye gari wakati namleta hapa.” Grace akatetea.
“Eti mama, Nanaa hajajibu kuwa na Jeff atakuwepo?” Danny alitaka uungwaji mkono na mama mkwe wake. “Kasema
hapa. Na alivyopendeza vile! Lazima huyo Jeff ampishe kwenye nyumba yake. Kwa
uzuri na utulivu ule! Lazima maombi ya Jeff yatakuwa yamejibiwa.”
Waliendelea kutania, lakini wasijue wanazidi kumchanganya Geb.
Huku kwa
Geb!
Hakwenda kulala kama alivyomwambia mama yake. Akaanza
kusafisha chumba kingine maalumu kwa ajili ya Nanaa. Grace alivyosikia kukuru
kakara nyingi, akaamua kwenda kusaidia. Geb alikuwa kimya kupita kawaida yake.
Swali moja, alichukua zaidi ya dakika tano kujibu. Kwa kuwa Grace anamfahamu
pacha wake, akaamua amuache tu. Wafanye kazi kimya kimya.
Alihangaika Geb, mpaka Grace alimuonea huruma. Akasafisha
kila mahali tena kwa mikono yake mwenyewe. Akahakikisha anafuta vumbi kila
mahali na kusafisha choo cha humo ndani. Chumba kikadekiwa vizuri. Ikaja kazi
ya kupanga sasa. Akatoa mashuka masafi na kumtandikia Nanaa. Akaenda chumbani
kwa bibi Fili, akahamisha mizigo yote ya Nanaa. Akampangia kwenye hicho chumba.
Mama yake akahamia kukaa kwenye makochi baada ya kuona
shuguli zimekuwa nyingi, hasira kwa mwanae zimeanza. Akajua hakuna kulala tena.
Wakabaki wanaangaliana na Grace. Aliingia na kutoka. Mara abebe hiki arudishe
kile. Ilimradi tu kukamilisha hicho chumba cha Nanaa.
Huko kwa
Nanaa!
Baada ya purukushani za panda shuka kwenye daladala hii
kuingia ile, Nanaa akawa amewasili Sinza Pub. Akakuta wote wanamsubiria. Jeff
akamvutia kiti, akakaa. “Mbona sasa unanishangaa?” “Ndio kupendeza gani hivyo?” Zena alimnong’oneza. “Si umesema tupendeze!?” Wakacheka. “Umependeza sana
Nanaa.” “Asante.” Akashukuru na ndipo akasalimia wengine. Jeff na Yasini.
“Unisamehe Jeff. Mambo yamekuwa yanaingiliana.” “Nini tena?” Jeff akauliza. “Nahangaika sehemu ya kuishi. Bado
sijatulia.” “Pole. Ungependa nikusaidie?” Jeff akauliza. Nanaa akacheka. “Msaada
mkubwa ninaotaka kwa sasa ni niwe na kwangu. Kama ukisikia kuna chumba
kinakodishwa, tafadhali nijulishe.” “Mimi ninayo sehemu kubwa tu yakuishi.
Nakukaribisha.” “Asante.” “Mbona unacheka kama huamini?” “Nimekushukuru jamani
Jeff! Natakiwa nifanyeje?” “Sasa shukurani hiyo utahamia au vipi?” “Kwa sasa
ninapo pakujishikiza. Natafuta kwangu.” “Hata kwangu panaweza kuwa kwako.”
Jeff aliendelea. Muhudumu akawasogelea.
“Nasikia njaa. Sijala tokea jana mchana nilivyokula kazini.
Nilipika tu kwa kaka, lakini sikula.” “Pole. Basi tuagize mbuzi wa kuchoma. Si
utapenda?” Jeff akauliza. “Mimi ni kama
fisi kwa nyama.” Nanaa akajibu, wakacheka. “Naomba usichelewe dada
yangu. Natakiwa kuondoka hapa kabla ya saa 12.” “Usijali. Nitahakikisha oda
yenu inakuwa mbele.” “Nitakushukuru.” Wakaendelea kuongea na kucheka. Ni
kweli Yasini alionekana kumjali Zena. Nanaa akabakia akiwatizama kwa
kuwatamania.
“Hongereni. Naona mpo vizuri. Na mmependezeana.” Nanaa akasifia. “Namshukuru Mungu kwa kweli. Nafurahia
kampani ya Zena. Hana makuu.” Yasini akasifia. Zena akacheka kwa aibu na
deko kidogo.
*****************************************************
Nanaa akaanza kuwaza maisha yake. Alipotoka, alipo ambapo
maisha yanaendelea kumchanganya na kujichanganya. Anapoelekea ndio ukawa
mtihani. Karata chache alizonazo mkononi alitakiwa azicheze kwa makini mno.
Lasivyo ataharibu kabisa. Akabaki anawaza.
*****************************************************
“Mbona upo mbali?”
Jeff akamshtua kwa swali. “Nipo hapa hapa jijini.” Nanaa alijibu huku
akitoa tabasamu. Wazi alionyesha ametingwa na mambo. Hajui afanye nini. Ni kama
jibu amelipata. Lakini moyo wake ulisita. Akabaki njia panda.
Vinywaji vilishaletwa, wakabakia kusubiria chakula. Wakawa
wanaendelea na vinywaji, huku stori za hapa na pale zikiendelea. Walipokuwepo
jana yake. Walifurahia nini. Wapi watakwenda baada ya pale. Nanaa alikuwa kimya
tu akisikiliza na kucheka. “Nilifikiri tutakaa mpaka usiku. Ili tuwe wote.”
“Ningependa kufanya hivyo. Niongozane na nyinyi kila mahali, lakini naishi kwa
watu. Au ndio nimehamia kwa watu. Lazima niweke heshima. Siwezi kuanza kurudi
usiku nyumbani kwa watu.” “Upo sahihi.” Jeff akakubaliana naye.
Chakula kikaletwa, wakaanza kula. Nanaa akaangalia saa yake,
akamalizia soda, akaamua aondoke. “Jamani nawashukuru.” “Unaondoka sasa hivi
Nanaa!?” “Nawahi daladala.” Nanaa alishasimama, na pochi yake akaiweka begani.
“Naomba nikusindikize.” “Kweli Jeff? Naona bado unakula.” “Usiwe na
wasiwasi. Twende.” Wakatoka wao wawili tu.
Jeff atupia ndoano kwa Nanaa wakiwa
garini.
“Naomba uniahidi utafikiria ombi langu.” Jeff aliongea mara baada ya kuondoa gari. “Ombi gani
tena? Maana kama kutoka kwa ajili ya chakula cha mchana, nimeshatimiza.”
Jeff akacheka. “Kweli hunitaki kwenye maisha yako Nanaa! Hivi ndio
umeshatoka na mimi?” “Jamani Jeff!” “Kweli Nanaa hii ndio picha uliyonayo ya
kutoka na mimi?” Nanaa akanyamaza. “Huwa wanasema, usikatae wito. Kataa
maneno. Lakini naona mwenzangu unanikatalia vyote.” “Akili yangu haijatulia
Jeff. Bado sijapata maisha ya kueleweka.” “Kwa nini usije kutulia kwangu kwa
muda mpaka utakapo jipanga?” “Sikufahamu Jeff.” “Na unampango gani juu ya
hilo?” “Sijui. Sitaki kuongezea kitu kingine kitakachonifanya nishindwe hata
kumaliza yanayonitinga.” “Kwa nini umeanza kunifikiria vibaya, wakati hata
hujanipa nafasi?” Kimya.
“Unajuaje labda chanzo cha kunifahamu ndio ukawa mwanzo wa
ufumbuzi wa maswala yako? Huwa wanasema, ‘Two are
better than one.’
Hujasikia hilo?” Nanaa akacheka. “Wawe wamepatana
na kuelewana. Unaweza kukuta ndio wanaongezeana matatizo zaidi maishani.”
Jeff akamtizama na kuendelea kuendesha. “Mbona sasa kimya?” “Nimeishiwa hoja
Nanaa. Kila ninachoongea unapinga. Nimekubali kushindwa.” “Usinielewe vibaya.”
“Sawa Nanaa.” Wakaendelea kuendesha, Nanaa akimuelekeza.
“Nakushukuru kwa kunirudisha.” “Anytime.” Jeff alijibu kwa kifupi sana. Nanaa akajua ameshakasirika.
Akacheka kidogo na kugeukia pembeni huku akifikiria. “Nini sasa?” Jeff
akamuuliza huku akiendelea kuendesha kwa makini. “Nikitulia nitakutafuta
Jeff. I promise.” “Unajuaje kama wakati huo bado nitakuwa nataka kukwambia
hichi ninachotaka kukwambia wakati huu?” Nanaa akapooza.
*****************************************************
“Nisije kuwa napiga teke bahati!” Nanaa akawaza akiwa anafikiria. “Geb!” Wazo
likamjia, akajicheka. “Mimi na yule kiumbe! Haitakaa ikatokea. Tena heri
nijiachie. Ana Liz, kwenye maisha yake. Tena asiyetaka wegazi. Heri
nimchangamkie Jeff.” Nanaa akaanza kushawishika.
*****************************************************
“Kama nilikusikiliza kwa makini, basi huu ndio mtaa
wenyewe.” Jeff alimtoa kwenye mawazo. “Ndio
hapa hapa. Lakini nyumba ipo kwa nyuma ya hiyo barabara inayongia kulia. Sio
mbali. Naweza kutembea hata ukinishusha hapa.” “Usijali. Naweza kukupeleka tu. Labda
iwe unaogopa.” “Hapana. Nyumba yenyewe ina ukuta na geti, hakuna atakayejua
hata kama nililetwa na gari. Twende tu. Ni nyumba ile pale.” “Kumbe
unaishi kwenye geti kali?” Nanaa akacheka. “Unaishi na nani tena?”
Jeff akauliza. “Yule dada, ambaye ni bosi wangu. Alisoma na kaka. Ndio kama
ameniombea kwao.” Geb hakutajwa. “Oooh!” Jeff akaitika.
Ilishakuwa saa 12:20 jioni wakati Jeff anaegesha gari nje ya
geti la Geb. “Nakushukuru sana Jeff.” “Anytime!” Jeff akanyamaza. Nanaa
akabaki akifikiria pale pale kwenye kiti kabla ya kushuka. Jeff naye akabaki
akimtizama. Nanaa alikuwa kwenye wakati mgumu sana. Hajui chakufanya.
“Nitakupigia.”
Nanaa alivunja ukimya. Jeff akacheka. “Kweli nitakupigia.” “Sawa.” Jeff
akajibu na tabasamu. “Mbona kama huniamini tena?” “Kwa nini tena? Mbona mimi
nimekubali yote? Au nilitakiwa kufanya nini?” Nanaa akanyamaza kwa muda. “Najua
nimekuwa kama… kam.. Ila naamini umenielewa.” Nanaa alianza kujing’ata
ng’ata. Jeff akabaki akimtizama tu. Wazi alionekana alishakata tamaa. “Usiku
mwema.” Nanaa akaamua kuaga. “Na wewe Nanaa.” Akashuka.
*****************************************************
Alimkuta Grace anaandaa chakula jikoni. “Pole na kazi.”
“Asante. Vipi huko?” “Kwema tu. Mama ameshakwenda kulala?” “Nimemuomba akae na
Fili huko chumbani ili nipike. Fili akiwa na mimi anadeka kweli! Siwezi kufanya
kitu chochote. Anataka niwe na yeye tu.” Nanaa akacheka. “Niachie basi
mimi nimalizie kukupikia wali. Naona umeshaivisha mboga zote.” “Hapa nilikuwa
nawaza kama nipike wali au nimtume Danny akanunue chapatti kule kwenye mgahawa
wa mwarabu. Wanakuwa na chapati nzuri.” “Basi wakati unafikiria hivyo, ngoja
nipike wali wa maua hata kidogo tu. Mtachanganya na chapati.” “Hayo ndiyo
mambo.” “Lakini nataka nikamsalimie mama kwanza. Najisikia vibaya nimechelewa!”
“Wala usijali na wala hujachelewa. Bado mapema kabisa.” Wakatoka wote
wakaongozana mpaka chumbani kwa bibi Fili.
*****************************************************
Alimkuta Geb na Fili wote wapo kitandani kwa bibi Fili. Fili
anaongea, wao wanamsikiliza. “Samahani nimechelewa.” “Mbona mapema tu.
Umepata muda wakutosha na wenzako kweli? Ni kama umekimbia kimbia tu.” Bibi
Fili aliitika yeye. “Nimeona kwa leo inatosha.” “Naona mambo sio mabaya
Nanaa mwanangu.” Nanaa akacheka na kuuliza. “Kwa nini mama?” “Umesema
kwa leo inatosha.” Nanaa akajisikia aibu. “Namaanisha jumamosi ijayo
nitawahi kutoka hapa na kuwahi kurudi.” “Jeff huyo!?” Nanaa akacheka mpaka
akatoka pale chumbani.
“Nanaa! Njoo nikwambie kitu.” Nanaa akarudi. “Abee mama!” Nanaa aliitika.
Bado Geb alikuwa amelala chali. Kimya, hata hakumsemesha Nanaa tokea aingie
pale. “Geb amekutayarishia chumba chako. Twende nikakuonyeshe.” Nanaa
akabaki kama haamini. “Mimi!?” Bibi Fili akacheka kidogo. “Samahani
mama. Sijak..” Akashindwa kuendelea, akanyamaza na kuinama.
“Ndio ujue tunataka ubaki. Twende nikakuonyeshe.” Bibi Fili akatoka pale kitandani, wakaongozana mpaka kwenye
hicho chumba. Kilikuwa kikubwa, kisafi, kitanda kimetandikwa vizuri, na vitu
vyake vyote vilikuwa humo. “Naona mmenitandikia mpaka na kitanda!” “Grace na
Geb ndio walikuwa wanasaidiana.” Nanaa alisimama pale, akashangaa machozi
yanamtoka. “Asanteni mama. Nashukuru kunipokea.
Nitajitahidi kutafuta chumba kwa haraka ili niwapishe hapa.” “Wewe
usijali. Tulia hapa mpaka
utakapo jiweka sawa.” “Asante mama yangu.
Nashukuruni sana.” “Sasa nimesikia kuna wali maua.” Nanaa akacheka nakufuta machozi.
“Nausubiri kwa hamu.” “Sawa mama yangu. Ngoja nikapike.” Mama G akatoka. Nanaa akabadili nguo kwa haraka. Alivaa
gauni la kawaida tu. Akarudi jikoni.
*****************************************************
Bado Geb alikuwa amejilaza kwenye kitanda cha mama yake,
akiwa kimya vile vile. Tayari walishajua hasira zile ni za wivu, na hawezi
kujisaidia. Mama yake akamfuata tena. Hakuwa ameongea kwa muda mrefu na wala
hakuwa amefungua macho japo alijua wazi hajalala. “Vipi?” Mama yake akamchokoza. Geb hakufungua macho. “Geb
Magesa! Najua hujalala.” Mama yake akaendelea. “Nenda basi kanywe hata
maji huko jikoni.” Kimya. “We Geb!” Mama yake akaita kwa
ukali. Akafungua macho. “Lazima utoke hapo kitandani. Kulala hapo haitakaa
ikasaidia. Haya nyanyuka.” Geb akatoka pale kitandani. Akiwa ameelewa mama
yake alichomwambia.
*****************************************************
Nanaa alishaanza kutayarisha vitu vya kupika. Alitaka kupika
wali wa kukaanga na kitunguu maji, na kitunguu swaumu. Ili baadaye aje aweke
njegere na karoti. Kulikuwa na tui la nazi limebaki kwenye friji, akajua
atalitumia hilo hilo. Akalitoa na kuweka jikoni ili lipate moto, huku akianza
kukaanga kitunguu. Moto aliweka mdogo, ili aweze kuendelea kutayarisha vitu
vingine kama kumenya vitunguu swaumu, njegere na karoti huku akipika.
Aliendelea kufanya mambo yake kwa haraka ili asiunguze na asicheleweshe
chakula.
Geb akaingia. Nanaa alishindwa hata kugeuka sababu ya ubusy
wa pale jikoni. Akaendelea kushika hiki, koroga pale, kata hiki, punguza moto
upande huu wa jiko hilo refu la gesi lenye sehemu 4 za kupikia. Akili zote
zikawepo pale jikoni asiunguze chakula cha kwanza kupika ugenini. Wala asijue
ni nani ameingia na nani ametoka.
Geb akasimama pale kwa muda. Akahisi kupuuzwa. Akatoka kwa
hasira za wivu na kurudi kwa mama yake. Akajitupa kitandani. “Nimeshakunywa
maji.” “Geb Magesa!” Mama yake akajua mambo hayakwenda kama alivyotaka. “Kwani
wewe huwezi hata kukata kitunguu jamani!?” Geb akacheka kama aliyepata wazo,
na kutoka pale kitandani. Alimsikia mama yake akimcheka nyuma. Akarudi na
kumbusu. “Muone!” Mama yake alimtizama kwa macho ya kumsuta. Geb
akacheka na kurudi tena jikoni.
Geb kwa Nanaa.
“Naona upo busy. Nikusaidie nini?” Nanaa akageuka, akamuona Geb. “Pole na safari.”
“Asante.” “Umepata muda wakutosha wa kupumzika?” Nanaa akauliza na
kumfanya Geb ajisogeze karibu ya jiko. “Nitalala baadaye.” Nanaa bado
alikuwa anachanganya viungo. “Kunanukia vizuri.” Geb akasifia. “Utakula
kidogo?” Nanaa akauliza huku akicheka. Akijua wazi Geb hawezi kula. Geb
alitabasamu nakushindwa kujibu. “Kwanza ulikula chakula mama alichokupikia?”
“Nilikula. Naona inatosha. Baadaye naweza kuongezea uji kidogo, naona itatosha
tu.” Nanaa akamwangalia.
“Ulisafiri lini?” “Niliondoka alhamisi.” Geb akajibu. “Niliona kimya.” Nanaa aliongea kwa
kulalamika kidogo. “Kwa nini hukuuliza?” “Sina namba yako Geb.” Geb akamwangalia.
“Nilikuomba msamaha. Unakumbuka?” Geb akacheka kidogo. “Hukuona
umuhimu wa kuwa na namba yangu Nanaa. Kama ujumbe haukuleta maana, ungefuta
ujumbe na kutunza namba.” “Nikikwambia najutia, utaamini?” Geb akatabasamu
kama asiyeamini.
“Kweli. Hata siku ile uliponishusha nyumbani, nikataka
kukuuliza kama mlifika nyumbani na mtoto
salama, lakini nikashindwa. Jumapili siku nzima nilikuwa nataka kukujulia hali
lakini nilishindwa. Sikuwa na namba yako. Nikajua labda hata ungenitumia ujumbe
mwingine. Lakini nikaona kimya.”
“Ningejuaje kama wa safari hii ungejibiwa?” Nanaa akanyamaza kidogo kama
anafikiria. “Ni kweli. Lakini nimefurahi umerudi salama.” Nanaa akarudi
kupika.
Geb akabaki amesimama pembeni yake akimwangalia.
Alipochanganya kila kitu kwenye sufuria, akafunika na kupunguza moto. Alikwenda
kwenye friji akamimina juisi kwenye glasi akamkabidhi Geb. “Asante.” Geb
alipokea na tabasamu la furaha ya kujaliwa na Nanaa. “Ametengeneza Grace.” Nanaa
aliongeza. Wakakaa pale pale jikoni.
*****************************************************
“Mbona sasa wewe haunywi?” “Nimeshiba. Nimekula muda sio
mrefu.” “Ulienda kukutana na Jeff?”
Geb akauliza swali la moja kwa moja. Nanaa akababaika kidogo. Akanyamaza. “Nilifikiri
nilisikia ukisema moyoni hujisikii. Mambo yalibadilika?” Geb akaendelea
kudadisi. “Jeff ni rafiki wa mpenzi wa Zena rafiki yangu. Na walikuwa
pamoja.” “Kwa hiyo ulienda kwa Zena, ndio ukakutana na Jeff bila kujua?”
Nanaa alijua anategwa. “Nilijua na Jeff angekuwepo, Geb. Nikaona ni wakati
muafaka wa kuwashirikisha uhitaji wangu wa chumba. Endapo watasikia sehemu kuna
chumba kinapangishwa, basi waniambie.” “Kwa hiyo?” Geb akaendelea kudadisi.
“Wameniambia kuna nafasi mahali.” “Kwa Jeff?” Geb akarusha swali jingine, Nanaa akanyamaza. “Nanaa? Ni
Jeff ndiye amekwambia ananafasi ya kukuweka?” Geb akarudia tena. “Ndiyo.
Alisema anasehemu kubwa tu yakuishi. Naweza kwenda kuishi naye kwa muda wakati
najipanga.” Geb alibaki akimtizama. Walikuwa wamekaa karibu, pale pale
kwenye meza ya jikoni.
“Nanaa?” Geb
akaendelea. “Nilimkatalia Geb.” “Kwa nini ulikataa?” Geb aliendelea
kuhoji. “Simfahamu na yeye pia hanifahamu.” “Kwa hiyo mmepeana muda wa
kufahamiana?” Nanaa akanyamaza kwa muda huku ameinama akichezea ganda la
kitunguu swamu. Akanyanyua macho, akakuta bado Geb akimtizama. “Nilimkatalia
msaada wa kuhamia nyumbani kwake. Nilimwambia kwa sasa ninapo sehemu
yakujishikiza. Ila msaada ninaohitaji ni kusaidiwa kutafuta kwangu. Kwa hiyo
kama akisikia kuna chumba kinakodishwa mahali, anifahamishe.” “Unafikiri
itakuwa na tofauti kama yeye akikusaidia kutafuta hiyo sehemu? Si yatakuwa ni
yale yale tu. Atakuwa anafahamu unapoishi, au kule kujua yeye ndiye
amekutafutia sehemu unayoishi! Kwanza utajuje kama atakapokutafutia sio
nyumbani kwake? Yaani ukajikuta unaishia kuishi naye yeye nyumbani kwake?”“Sikuwa
nimefikiria hivyo.” Wakanyamaza kidogo, Nanaa akanyanyuka kwenda kugeuza
wali.
*****************************************************
Akasafisha ile sehemu aliyokuwa akitumia. Huku Geb ametulia
kimya kwenye kiti akiendelea kutafakari. Nanaa akaanza kusuunza vyombo
alivyokuwa akitumia huku akivipanga vizuri kwenye dishwasher. “Naona wali
unakaribia kuiva.” Akamgeukia Geb aliyekuwa amekaa tu pale kwenye kiti
akinywa juisi yake taratibu.
“Onja hata kidogo.” “Umeweka vitu vingi sana Nanaa. Mimi
nikishaona karoti hivyo. Au njegere zinaniangalia kwenye wali, nachanganyikiwa
kabisa nakushiba hapo hapo.”
Nanaa akacheka. “Kidogo tu. Funga macho, halafu fungua mdomo, mimi
nitakuwekea. Tafuna, halafu uniambie.” “Nanaa!” “Kweli tena.” “Basi toa karoti,
njegere. Hakikisha kitunguu hakiingii kwenye kicho kijiko kimoja utakachokiweka
mdomoni kwangu.” “Sasa hapo si utakuwa unakula wali mweupe, wakati mimi
nimepika wali maua?” “Mimi hata wali mweupe huwa sipendi.” “Basi.” Nanaa
akageuka.
“Lakini sio kwamba sitaonja huo unaopika.” Akamsikia Geb akiongea kwa haraka na kusimama. “Sio
lazima. It’s ok.” Nanaa alijibu kwa upole. “Nataka kuonja.” “Kwa nini,
wakati umeshasema hupendi? Acha tu.” “Nanaa!” Geb alimsogelea. “Naomba
kuonja.” Nanaa akamgeukia. “Hamna haja. Kweli tena. Ni sawa tu.” “Nanaa!
Labda kama unaninyima.” “Unajua siwezi kukunyima Geb. Lakini nimejua sio
kitu ambacho ungependa hata kujaribu. Yaani umeshakataa kwa kukiangalia tu. Na
kitu chochote ukishakikatia tamaa mawazoni, huwezi kukikosea kasoro. Ukila tu
huo wali, hutakosa sababu. Acha tu.” Geb alijiona amekataa bahati ya
kulishwa. Tayari alishaanza kujutia kukataa bila kufikiria. Akajua hasira za
wivu ndizo zilizokuwa zikimsumbua wakati akijibu. Hofu ya kuwa Jeff anamzidi
mahesabu ilimwingia. Anaonekana anataka kumtoa Nanaa pale ndani.
“Samahani Nanaa. Nimekukatalia bila kufikiria.” Nanaa akatabasamu. “It’s ok.” Alijibu kwa upole.
Wakabaki kimya hapo hapo karibu wakiwa wamesimama. Nanaa ameangalia chini, Geb
akimtizama. “Ngoja nianze kupakua, niweke mezani. Njaa zitakuwa zinawauma.”
Akageukia kwengine nakuanza kutoa vyombo kwenye makabati, akatoka navyo nje na
kumuacha Geb amesimama pale pale. Akaanza kupanga kwenye meza ambayo huwa
wanakula kwa pamoja. Akaandaa kila kitu hapo mezani mpaka akaridhika.
Ndipo akaenda kumwita bibi Fili au Mama G kama wengi
walivyozoea kumwita, wote wakakaa mezani. “Naona kinavutia kwa macho.”
Nanaa akacheka. “Asante mama. Lakini mimi bado nimeshiba. Nitakula kiporo
kesho kama kitabaki. Naenda chumbani kuoga. Nitoe harufu ya vitunguu.” “Sidhani
kama utabaki.” Mama G akajibu na kufanya Nanaa acheke. “Asante Nanaa.
Naona wali unavutia.” Grace naye akashukuru wakati anampakulia mumewe. “Asante
kushukuru. Nitakuwepo hapo chumbani. Nitatoka kusafisha meza na vyombo.” “Wala
usijali. Tutamalizia tu.” Nanaa akaondoka.
Nanaa
ajikuta aangukia mikononi mwa Mama yake Mkubwa tena!
Siku inayofuata ilikuwa jumapili. Nanaa akaamua kurudi
nyumbani kwa kaka yake ili kusalimia wageni. Hakumkuta kaka yake, akajikuta
ameishia mikononi mwa Mama yake mkubwa na Viola. Alijuta hata kwa nini
alikwenda bila taarifa. Walimpa wakati mgumu sana. Mama yake mkubwa alimsema
kwa maneno ya kumnyanyasa mpaka alipomaliza roho yake ikatulia. Akamfukuza
rasmi hapo nyumbani kwa mwanae James.
Nanaa akatoka akatafuta sehemu karibu kidogo na kituo cha
daladala, akakaa hapo akiwaza. “Jeff anaweza kuwa suluhisho la kudumu.
Nikimkubali, naweza nikapata mkombozi wangu. Nikaepuka maneno.” Nanaa akawaza akiwa
amekereka sana rohoni. “Lakini nikiwa na Jeff, sijisikii vizuri kama
ninapokuwa na Geb, mchumba wa mtu!” Nanaa akajirudi na kuanza
kujichanganya tena mawazoni. “Alikuwa wapi huyo Jeff siku zote jamani!?”
Nanaa alilalamika. Alikaa pale akiwaza bila kufikia muafaka, mwishowe akaamua
kurudi nyumbani kwa Geb akajifikirie zaidi.
*****************************************************
Aliingia ndani mida ya saa 11 jioni, akawakuta wote wamekaa
sebleni. Mpaka Liz alikuwepo. Tena alikaa pembeni ya Geb. Fili alikuwa
amepakatwa na baba yake. Aliingia hapo akionekana kabisa hana furaha. “Kwema?”
Grace akamuwahi. “Kwema. Nimchukue Fili nikamuogeshe?” “Geb alishamuogesha,
amekula, hapo baba yake anambembeleza alale, kesho shule.” “Ooh! Nimemchelewa
Fili wangu!” “Nenda kachukue chakula, nimekubakishia.” “Labda nisafishe tu,
sitakula.” Nanaa alimjibu Grace huku akielekea jikoni. Alikuta jiko
limeshasafishwa, akatoka. “Naona kupo kusafi. Basi na mimi naenda kulala.”
“Mbona mapema? Njoo tukae kidogo.” Nanaa alisimama pale kimya, kama
anayewaza kitu. “Naomba mimi nitangulie tu. Naona nimechoka.” Nanaa
akajibu kwa upole, akaelekea chumbani.
*****************************************************
Picha ya Liz akiwa amekaa pembeni ya Geb ilipita kwa haraka
mawazoni. Akatulia. Kisha maneno ya mama yake mkubwa yakaanza kumrudia na
kukubali kuwa kweli yeye ni tatizo sugu. Aliona hastahili kuwepo pale. “Naona
nimeanza hata hisia zisizo sahihi kwa mchumba wa mtu. Wenyewe wanapendana. Mimi
nimejaa humu ndani. Geb anahangaika kutengeneza chumba, akashindwa hata
kupumzika!” Aliona vile anavyosumbua watu, akazidi kujisikia vibaya.
Lazima kutafuta suluhu ya kudumu.
Akaingia kuoga, akatoka na kubaki amejilaza kitandani. Baada
ya kuwaza hili na kushindwa kupata majibu, huku Jeff akionekana ndio suluhisho
la kudumu akaamua alale tu. “Sijui nimpigie Jeff? Nitamwambia nini?
Nirudie maisha yale yale ya zamani? Kukimbilia wanaume sababu ya sehemu ya
kuishi?” Nanaa akaanza kulia gizani. Wivu wa kumkuta Liz pembeni ya
Geb, na maneno ya mama yake mkubwa yalizidi kumliza. Asijue atafanyaje. Alilia
huku akiangalia simu yake akitamani ampigie simu Jeff, lakini moyo ulizidi
kusita. Alilia taratibu pale gizani, asijue chakufanya.
*****************************************************
Akasikia hodi mlangoni, akakaa na kujiweka sawa. “Karibu.” Mama
G akafungua mlango. “Mama!” Nanaa akafuta machozi. “Niwashe taa?” Mama
G akauliza. “Washa tu.” Akawasha akamsogelea kitanda alipokuwa amelala
Nanaa. Akaweka juisi kwenye mezani ndogo iliyokuwepo pembeni mwa kitanda. “Mbona
unalia?” Akamuuliza. “Sijui nifanyaje mama?
Sijui.” Mama G, akakaa. “Nini
kinakusumbua?” Mama G akauliza kwa utulivu.
“Nachukia haya maisha yangu mama. Nitakuwa
hivi mpaka lini? Nitazunguka kwenye majumba ya watu mpaka lini? Natamani
kutulia. Natamani na mimi kuwa na kwangu. Jeff….” Akakwama. “Nakusikiliza Nanaa.
Ongea tu usiogope.” “Jeff anaonekana ni muugwana na
anauwezo mzuri tu. Anaonekana angeweza kunioa. Nikaanza maisha yangu nakuacha
kusumbua watu wengine.”
Nanaa alijieleza huku machozi
yakimtoka.
“Umeshafikiria
baada ya ndoa? Yaani ameshakuoa, amekupa sehemu ya kuishi. Maisha yako
yatakuaje?” Mama G akauliza swali la
msingi akionekana ametulia kabisa. “Hilo ndilo
tatizo mama yangu. Nimekuwa nikifanya kosa hilo hilo. Kukubali wanaume sababu
ya kupata kimbilio. Nimechoka mama yangu. Nikaamua kupumzika. Nitulie pale kwa
kaka. Lakini sasa hivi tena ndio mambo yametibuka. Mama mkubwa amenifukuza
rasmi pale kwa kaka. Hataki hata nirudi kusalimia. Nitafanyaje? Na Jeff naye
ndio anaonekana mkombozi wangu. Lakini mama, moyo wangu umemkataa kabisa yule
kijana. Sijui nitafanyaje?” Nanaa alikuwa akiongea na Mama G,
kama anamfahamu.
“Samahani mama. Najua nakwambia mambo yasiyo
kuhusu. Lakini sina mtu wa kuzungumza naye?” “Nisikilize Nanaa. Kwanza nimefurahi kuwa umeweza kuniamini
na kunishirikisha. Pili, kuna usemi huwa wanasema, ‘Don’t make permanent
decision for temporary problem’. Unanisikia Nanaa?” “Nakusikiliza mama.” “Ehee! Tulia kabisa. Mungu amekuleta hapa
kwa makusudi. Nakuomba hapa uwe huru. Usijisikie kuwa unaharaka yakuondoka.
Utakapokuwa tayari ndio uondoke. Kwanza wewe bado mwanafunzi. Fikiria shule na
hiyo kazi uliyopewa. Basi. Naamini Mungu atakupa maisha mazuri tu. Umesikia
mama?” Bibi Fili alijaribu kumtuliza.
“Nashukuru mama. Asante.” “Yatapita tu haya. Tena naona unamwanzo mzuri kuliko watu wengi
sana. Vumilia, na ujipe muda. Usikimbilie kufanya maamuzi utakayojutia
baadaye.” Nanaa
akatingisha kichwa. “Tumuombe Mungu pamoja. Tumruhusu yeye ndio awe msaada
wako. Kisha jiruhusu kuipokea siku ya kesho ukiwa na amani.” Nanaa
alitoa tabasamu. “Asante mama yangu.” “Haya
kaa vizuri tuombe.” Bibi Fili akamshika mkono Nanaa,
akamuombea. Ilikuwa sala fupi, lakini ilimfariji sana Nanaa.
“Asante sana mama. Umenitua mzigo mzito. Nilikuwa sijui
chakufanya.” Bibi Fili au mama G, kama wengi
walivyozoea kumwita, akatoa tabasamu la faraja. Kama mama kwa mtoto wake
wakumzaa. Hakika hakujua alichokifanya kwa Nanaa. Ndio mama wa kwanza aliyeweza
kukaa naye chini na kumfariji kwa kiasi kile. Yale maombi yalikuwa kama barafu
nzuri ndani ya moyo uliokuwa mzito wa Nanaa. “Basi kunywa hiyo juisi, ndipo
ulale.” Bibi Fili akatoka, na kumuacha Nanaa amefarijika. Kwanza ni kama
alimsaidia kumpa majibu ya maswali yake. Juu ya Jeff na hisia zake. “Sina
haraka tena. Nitamtafuta Jeff, nimpe nafasi ya kumsikiliza. Kisha nimkatalie
rasmi. Nijiruhusu kufikiria, na kujipanga bila mtu nyuma yangu.” Nanaa
aliwaza. Akalala akiwa na furaha.
*****************************************************
Aliamka siku ya jumatatu akiwa na furaha zote. Huku
akijiambia anahitaji tu muda. Aliandaa kifungua kinywa, wakati akimwangalia
Mama G akimwandalia Geb uji wake. Akamsaidia Grace kumwandaa Fili, wakaondoka
mapema yeye na Grace na mwanae. Alifika kazini akiwa ametulia. Akafanya shuguli
zake, akaamua kumpigia simu Jeff!
“Unacheka nini sasa?” “Sikutegemea.” “Kwa
nini?” “Basi tu. Mzima wewe?” “Mzima. Naomba tukutane jumamosi.” Kimya. “Jeff!” “Nakusikiliza mrembo.” “Ndio
nimemaliza. Kama bado utataka kuniambia ulichotaka kuniambia. Na kama bado
sijachelewa.” Jeff akacheka. “Nimegairi Nanaa. Naona niache tu.” Nanaa akatulia kidogo. Akasikia kupooza. “Nanaaa!” “Nipo Jeff. Samahani sana.
Lakini naamini utakuwa umepeta sikio jingine la kukusikiliza.” “Naamini hivyo.
Asante.” “Haya. Kila la kheri.” Nanaa akakata simu, asiamini.
*****************************************************
“Daah! Mlango umeshafungwa hivyo. Sijui niseme
nimechezea bahati!?” Siku
ikaanza kuwa ngumu. Kukataliwa kubaya! Jeff alimfungia vioo kwa haraka sana.
Hakutaka kuzungushana naye. Nanaa alitamani yeye ndio awe wakumkataa, kuliko
vile alivyokataliwa. Akamkumbuka Geb. Akakumbuka Liz amekaba. “Nijipumzikie
tu.” Nanaa akawaza.
*****************************************************
Jeff hakutaka kuzungushwa na Nanaa. Mapemaaa,
ameshamfungia mlango na nyumbani kwa kaka yake amefukuzwa ramsi na mama yake
mkubwa. Liz naye amekaba penzi la Geb. Mpaka Jumapili siku hizi yupo nyumbani
kwa Geb. Je, amechezea bahati?
Usikose Sehemu ya
12.
0 comments: