Story
is mine - ni Wangu! Part 1, Sehemu ya 12.
M
|
aisha yakaanza ndani ya nyumba ile. Kulikuwa na amani na
utulivu wa aina yake. Kama Danny asipokuwepo nyumbani, basi ni Fili ndio
alikuwa akichangamsha nyumba, lakini wengine wote walikuwa wakimya. Akaanza
kujiwinda na Geb. Hakutaka kuwa karibu naye kabisa ili asijiumize nafsi yake.
Geb alikuwa akiibua hisia ambazo zilimfanya kumtaka zaidi. Nanaa akaona
hatendei haki hisia hizo mpya na ngeni. Kwani Geb alikuwa ni wa Liz. Na Liz
mwenyewe alikuwa akikaba kweli kweli.
Siku hiyo ya jumatatu jioni waliporudi nyumbani baada ya
kazi. Nanaa akiwa anatayarisha chakula cha usiku, Bibi Fili naye anaoga baada
yakutoka kwenye shuguli zake, wakamsikia Liz na yeye ameingia. “Naona
umetoka dry clener!” Alimsikia Grace akimuongelesha. “Hapana. Nilipitia
nyumbani kuchukua baadhi ya nguo zangu za kuvaa kazini week hii nzima.
Nikilalaga hapa, halafu kuamka kwenda kuvaa nyumbani, nachelewa kazini. Nimeona
heri niwe natokea hapa hapa kwenda kazini. Halafu weekend hii Geb amesema
hatasafiri. Tutakuwepo wote nyumbani.” Moyo wa Nanaa ulipasuka. “Liz
anahamia hapa!!!” Akajiuliza. “Lakini ni kwake. Sasa
si nilisikia hapendi watu wajazane hapa ndani?” Nanaa akajiuliza. Gafla
amani ikatoweka moyoni mwake, asijue chakufanya. Pakwenda hana, analazimika
kuwepo pale kwa wakati ule. Akabaki akiwaza pale jikoni yeye mwenyewe.
Akatayarisha chakula. Akala huko huko jikoni. Kingine
akakipanga vizuri mezani. “Chakula tayari.” Akamsogelea Grace akamwambia
kwa sauti ya chini. “Una mkono mwepesi! Hapa ndio nilikuwa najipanga kuja
kukusaidia.” Nanaa akacheka. “Usicheke Nanaa. Nilikuwa nakuja.” “Wala
usijali. Ilikuwa ni kuunga tu njegere. Nyama zile tulizokaanga jana bado
zilikuwa nyingi. Nimepasha tu. Na nimeona chapati alizoleta Danny bado za moto.
Kwa hiyo wala sijachukua muda mrefu.” “Pia nashukuru. Nimejikalia kizembe,
utafikiri nimetoka shamba!” Nanaa akacheka. “Basi usiku mwema. Kuna kitu
nataka kufanya huko chumbani kabla sijalala.” “Haya mwaya. Usiku mwema.” “Na
nyinyi pia.” Nanaa akaenda kumuaga Mama G, akaingia chumbani kwake.
Jumanne alifanya hivyo hivyo kuingia chumbani kabla hata Geb
hajatoka kazini. Jumatano akafanya hivyo hivyo.
*************************************************
Alhamisi usiku Zena akamtafuta kumwambia akaribie kwenye
birthday party ya Yasini. “Ni
wapi tena Zena? Mwenzio nimeamua kutulia.” “Mbona nimeelewa. Hata Jeff
ametusimulia kila kitu wote tumeelewa. Nataka tu uje uniunge mkono. Sitaki
nijikute peke yangu nikiwa nimezungukwa na marafiki wa Yasini tu.” “Kwa hiyo
mtafanyia wapi hiyo sherehe?” Nanaa akahoji akionyesha wazi hataki kwenda. “Tutaelekea Kigamboni.
Tutaondoka saa nne, na kurudi jioni. Nakuomba usinitupe Nanaa.” Baada ya kubembelezwa sana na kupewa mipango yote, Nanaa
akakubali. Hata hivyo alijua itamsaidia kuwa mbali na ile hali pale. Geblizim.
*************************************************
Ijumaa kabla hajaingia kulala, akamfuata Mama G, chumbani
kwake. “Niambie mwanangu Nanaa.” Nanaa akatabasamu, akasogea. “Unakumbuka
habari za yule rafiki yangu Zena?” Nanaa akauliza. “Yule ambaye mchumba
wake ni Yasini, rafiki wa Jeff?” Nanaa akacheka kwa sauti. “Mama!
Husahau?” “Nasahauje wakwe? Haya, kuna nini tena?” Nanaa akavuta pumzi. “Kesho
ni birthday ya Yasini. Wanaenda kufanyia Kigamboni. Wamenialika. Wamekubaliana
kukutana pale kivukoni saa 3:30 asubuhi, ili saa 4 waanze kuelekea huko. Kwa
hiyo nilitaka kukutaarifu hivyo.” Mama G, akajua kazi itakuwepo kesho yake
Nanaa akiondoka pale.
“Sawa. Utataka kusindikizwa, au watakuja kukufuata hapa?”
“Nimemwambia Zena asisumbuke. Nitakutana nao huko huko kivukoni. Kwa hiyo
naweza kutoka mapema kabla hamjaamka. Ila nitahakikisha nimeacha kila kitu
tayari.” “Wewe nenda kapumzike na wenzako. Mambo mengine tutafanya tukiamka.”
“Haya mama yangu. Usiku mwema.” “Mbona mapema?” “Nimeanza kuandika ripoti. Ndio
inanichukulia muda mwingi huko chumbani.” “Haya mama. Usiku mwema. Na uwe na
wakati mzuri na wenzako kesho.” “Asante mama yangu.” Nanaa akaelekea chumbani kwake.
Jumamosi ya heka heka baada ya Nanaa
kutoka.
Kesho yake asubuhi Nanaa akaamka mapema. Akaandaa kifungua
kinywa cha kila mtu. Akapika mpaka uji wa Geb, ndipo akarudi chumbani kwake.
Akaoga vizuri na kuanza kujitengeneza. Kama kawaida yake ya kupenda kuvaa
vigauni. Akavaa kigauni kizuri sana. Refu mpaka chini. Lilimkaa Nanaa vizuri
mpaka mwenyewe alijua akabaki akicheka. Alilichagua hilo makusudi kwakuwa
lilikuwa kata mikono juu. Ilishikiliwa na kamba nzito zilizokuwa zimepita juu
ya shingo. Sehemu kubwa ya mgongo ilikuwa wazi. Kwahiyo rasta zake akazibana
kiasi zile za mbele, za nyuma akaziachia kufunika ule uwazi wa mgongoni.
Akafurahia na rangi ya hilo gauni sababu ya jua kali. Akajua litamfaa na joto
la jiji hilo.
Hereni zake za bati tu. Kubwa na duara zilizokuwa
zimechomvya kwenye maji ya dhahabu, nakuzifanya uhisi ni dhababu tupu kama
ukiangalia kwa haraka, zilimkaa vizuri sana. Alichukua kofia maalumu ya beach,
akaining’iniza kwenye kimkoba chake kama cha mkeka. Miwani ya jua akaining’iniza
mbele ya gauni yake kwenye ile ‘V’ iliyotengenezwa kutokana na ile
mikanda iliyopita shingoni. Akavaa zile zile sendozi zake zilizokuwa na shanga
nyingi nyeupe. Akajua zitaendana na gauni hilo lililokuwa na rangi nzuri
iliyokolea bluu kama maji ya bahari.
Usiku kucha alikuwa akipaka rangi kucha zake. Kwa hiyo
kucha za miguu zikawa zinavutia kwenye zile sendozi zake. “Hapa ningekuwa
na gari!” Nanaa akawaza. “Nitajichafua tu, kwa kutembea hapa
mpaka kituoni.” Nanaa alijiongelesha. Akataka kusahau rangi ya midomo
anayopenda kupaka. Nyekundu. Akaweka huku akifurahia jinsi alivyozidi kuwaka.
*************************************************
Alipojikubali kuwa amependeza na hana chakuongeza
mwilini mwake. Akaamua kutoka. Wakati anatoka chumbani akakumbana na Danny
koridoni. “We Nanaa? Unaenda wapi asubuhi yote hii wakati bosi wako kalala
ndani!?” Nanaa akacheka kidogo. “Naelekea Kigamboni kwenye birthday.”
“Mmmh! Birthday ya asubuhi hiii!?” “Tutashinda huko siku nzima. Hata hivyo
tunatakiwa kuondoka pale kivukoni saa 4 asubuhi. Lakini sababu ya daladala,
imenibidi kuwahi kidogo.” “Khaaa! Naona kweli umekamia hiyo birthday!
Sio kwa kupendeza hivyo bwana!” Nanaa akataka kuondoka huku anacheka.
“Nanaa!” Nanaa
akageuka. “Nisubiri nikusogeze. Mimi mwenyewe naenda kazini leo.” “Asante.
Utakuwa umenisaidia.” “Basi nifungie vitafunio vyangu. Harufu nzuri imeenea
mpaka chumbani!” “Nimepika sambusa.” “Acha masihara Nanaa! Sambusa!?” Nanaa
akacheka. “Mimi naona nile tu hapa hapa. Nikienda nazo, James atanimalizia.”
“Nimepika nyingi. Naomba mbebee na yeye.” “Kama ndio hivyo sawa. Tena
tenganisha kabisa, na weka majina yetu juu. Ili akimaliza zake, akatulie
ofisini kwake.” Nanaa akacheka na kuingia jikoni.
“Umeamsha nyumba zima Danny. Kwani huwezi kuongea sauti ya
chini?” “Wewe umeamshwa na Sambusa bwana. Acha kunisingizia Grace.” Mkewe akacheka na kuelekea jikoni. “Kwa mwendo huu
tutanenepa humu ndani mpaka tupasuke.” Grace akabaki akimtizama Nanaa. “Mbona
unanishangaa? Nimetisha? Niambie ukweli.” “Sidhani kama utarudi leo. Ndio
umependeza hivyo!” Nanaa akacheka sana. “Ukichelewa tu, sisi
tunakufuata.” “Nitajitahidi nisichelewe sana.” “Wala usijali. Wewe nenda
kafurahie na wenzako.” Akajua tayari bibi Fili amemwambia.
Huko kwa Nanaa!
Danny alimpeleka mpaka Kigamboni. Akamshusha. Alikuwa
amewahi kidogo. Mara akaja Yasini na Zena. Wakasalimiana. Baada ya muda akaja
Jeff na msichana mwingine. Nanaa akabaki amepigwa butwaa. Wakawasogelea
wakasalimiana. Jeff akamtambulisha yule msichana kama ‘girlfriend’ wake. Wakasalimiana na Nanaa. Wakaja tena marafi zao
wengine wawili. Baada ya muda, wakajikuta wameshakuwa kundi kubwa. Nanaa
akapanda kwenye gari la Yasini na Zena. Jeff na msichana wake wakaingia kwenye
gari yao. Na wengine hivyo hivyo, wakavuka.
Kwa haraka sana, Nanaa alikosa raha asijue ni kwa nini.
Alijuta hata kufika pale. Na walipofika kule, ni kama Jeff alikuwa akimfanyia
makusudi. Mabusu ya hapa na pale kwa huyo msichana hayakuisha. Alimlisha mbele
za watu. Alitaka kukaa naye kiti kimoja huku amemkumbatia. Kila mtu aliona
vituko vya Jeff na msichana huyo mpya. Ni kama alimfanyia makusudi Nanaa.
Huku kwa Geb!
Maongezi, sifa na shamra shamra za Danny kwa Nanaa, ni kweli
ziliamsha kila mtu pale ndani. Geb alibaki amelala pale kitandani kama
amemwagiwa maji. Akili ilishavurugika. Alilala pale kwa muda, kisha akaamua
kutoka nje kabisa. Akaanza usafi wa nje ya nyumba yake. Ilifika saa nne asubuhi
watu wote wakawa wameamka wanakunywa chai, lakini Geb alikuwa anazunguka nje. “Nenda
kamwite anywe uji.”“Mie mama? Akuu. Wewe unamjulia mwanao. Nenda mwenyewe.”
Grace akajitoa mapema. Walikuwa wakinong’ona kwa kuwa Liz alikuwepo.
Akatoka mama G. Akamkuta jasho linamtoka kama maji.
Anasafisha sehemu ambazo ni safi. Akasimama pale akimwangalia. Akamuona anaenda
stoo, akatoka na jembe mkononi. “Unachimba shimo?” Mama yake akatupia
neno kuchokoza. “Nataka kupanda miti.” “Wazo zuri ili tupate vivuli.”
Akaanza kuchimba mashimo kama makaburi.
“Kwani miti hiyo unayotaka kupanda hapo, ni mirefu ya kiasi
gani?” Kimya. “Naona kama mashimo hayo
ni marefu sana Geb, mwanangu.” “Sitaki mizizi ije kuungua na jua.” “Wazo zuri.”
Akatulia. Akaona anaendelea kuchimba.
“Nikuletee uji wako hapa nje?” “Mpaka nimalize.” “Nashauri
ule kwanza. Hayo mashimo ni marefu sana.”
Kimya. “Kwani unapanda miti mingapi?” Kimya. Geb akaendelea kuchimba.
Jasho lilikuwa likimwagika kama maji. “Hivi ulisema ni miti gani tena?”
Kimya. “Utapanda mbegu au miti ile mikubwa kama mibuyu? Maana hayo mashimo!”
“Mama!” Geb akagomba. “Basi baba nanyamaza.” Akatulia kidogo.
“Ngoja nikakuletee uji unywe ili upate nguvu.” “Sitakula sasa hivi. Natoka
kwenda kufuata hiyo miti.” “Kumbe hiyo miti yenyewe pia huna!?” Geb akatupa
jembe kwa hasira akarudi ndani.
Mama yake akamfuata nyuma. “Uji huu hapa mezani.”
Mama yake akarudia. “Nimekwambia sinywi.” “Oooh! Nimekumbuka umeniambia ndio
unaenda kufuata miti.” Liz akatoka chumbani akiwa ndio ameamka. Alionekana
ameoga vizuri na amependeza. Nyumba nzima ilikuwa ikinukia manukato yake. “Unakwenda
wapi Geb?” Liz akauliza kwa upendo. “Nitarudi sasa hivi.” “Nilifikiri
leo tunapumzika kama ulivyosema.” Geb hakujibu. Akatoka akiwa ameshika funguo
zake za gari. Wakasikia akiondoka. “Sasa ananuna nini?” Liz akauliza
kishari. “Mimi mambo ya visirani asubuhi asubuhi siyawezi.” Liz
akaendelea. Grace alikuwa amenyamaza kimya mezani akimlisha mwanae, kama hayupo
pale. “Siku ndio imeanza.” Mama G, akaongea na kurudi chumbani
kwake.
Baada ya lisaa, wakasikia gari ya Geb inaingia. Wote wakajua
amerudi. Wakatulia. Wakasubiri labda ataingia ndani, lakini muda ukazidi kwenda
kimya. Fili akataka mama yake atoke naye nje amwangalie anavyoendesha baiskeli.
Grace na mwanae wakatoka. Wakakuta mashimo mengi urefu wa Geb. Grace akabaki
ametoa macho. Liz akatoka. Grace akaona akamtoe mama yake. Akamkuta chumbani. “Wewe
mama! Hivi umeyaona hayo mahandaki hapo nje?” “Nimeyaona. Amesema anapanda
miti. Nahisi mibuyu!” Wakacheka. “Nenda kazungumze naye mama. Ataanguka
azimie.” “Wewe kwa nini usiongee naye? Si kaka yako!” “Si unamjua Geb. Hatakaa
anijibu kitu. Nenda kampelekee hata maji.” Wakatoka.
Grace akampelekea mama yake jagi la maji na glasi. Wakacheka
pale sebleni. Wakati wanataka kutoka nje, wakasikia Liz anagomba. Grace
akamvuta mama yake. “Subiri kwanza wamalize.” Grace akanong’ona. Liz
aliongea kama dakika 10 bila kujibiwa kitu. Wakamsikia anarudi ndani huku
anaongea kwa hasira. Na yeye akachukua funguo zake za gari, akatoka. Baada ya
kama dakika 3, akarudi tena ndani. Akakusanya nguo zake, akaanza kuweka kwenye
gari yake. “Huwezi kunibabaisha mimi!” Liz alikuwa akiongea kwa hasira
na jazba. Aliingia mara mbili na kutoka, wakasikia milango ya gari inafungwa
kwa nguvu, akaondoa gari karibu agonge geti.
Waliposikia kimya, ndipo na wao wakatoka. Akasogea
mpaka kwenye shimo alilokuwa ameingia Geb. “Maji ya kunywa haya.” Mama G
alikuwa anamchungulia kule ndani ya shimo alipokuwepo. Kweli mashimo yalikuwa
marefu. “Sina kiu mama. Naomba niache.” “Najua huna kiu. Lakini naomba
kunywa haya maji Geb. Jua kali na wewe unashinda juani. Utaanguka kwa
kizunguzungu.” “Nimegundua nimeyashimba marefu sana, nataka kuyafukia ndio
nipande.” “Miti yenyewe iko wapi?” “Si hiyo hapo pembeni!” Mama G
alipoiangalia, ilikuwa ni miche. Hata haijafikia urefu wa mkono wake.
Akajua kazi ya kufukia tena inaanza. Alikuwa amechimba
mashimo matatu, marefu sana. “Naomba kabla hujafukia hayo mashimo, kunywa
maji.” “Nimesema sina kiu.” “Geb Magesa!” Mama G, akaita kwa ukali.
Geb akajua ameshambadilikia. Akatoka. “Kwani ni lazima mama jamani!?” “Ndiyo.”
Mama G akajibu kwa ukali na kibabe. Geb akanywa maji glasi moja, akarudi
kuendelea na kazi yake ya kufukia yale mashimo. Grace akamtizama mama yake.
Wakaangaliana, akaendelea kucheza na mwanae.
Akafukia yale mashimo yote. Jua lilikuwa kali sana. Alikuwa
amelowa chapachapa kwa kuwa udongo ulikuwa mkavu sana. Alipomaliza kuyafukia.
Akaenda upande mwingine, akachimba mashimo mengine. Lakini ya safari hii
aliyafanya mafupi. Akapanda ile miti. Wakajua amemaliza.
Wakaona ametoka tena na gari. “Sasa sijui anakwenda wapi!?”
Grace akauliza kwa kumuhurumia kaka yake. “Siku mbona ndio imeanza. Baba
yake alikuwa hivyo hivyo. Akianza mambo yake ya wivu, basi hatakuuliza. Anaanza
kazi kwenye hiyo nyumba. Asubuhi mpaka usiku.” “Sasa ulikuwa unafanyaje?”
“Inategemea. Kama amenikera au ananisingizia mahusiano, namuacha ahangaike
mpaka atulie mwenyewe. Wakati mwingine nikimuhurumia, naenda kuzungumza naye.
Anatulia. Sasa huyu Geb, anasumbuliwa na mengi. Mwache ahangaike mpaka akili
yake ikae sawa. Hajui anataka nini.” Grace akaguna.
*************************************************
Danny akarudi. “Mbona ukoka umechimbuliwa tena wakati
uligarimu pesa nyingi sana kupandwa na kutunzwa mpaka kufikia hivyo?” “Kuna
shuguli hapa. Hujawahi kuona.” Mama G, akajibu. “Kwema?” Danny
akaendelea kuhoji. “Geb kaamka na matengenezo ya nyumba, hapa!” Danny
akaanza kucheka. “Huyo ni Nanaa tu.” “Kumbe umejua?” “Mimi nilijua.
Na nilifanya kusudi kongea kwa sauti asubuhi, ili ajue Nanaa anaondoka.”
Grace akampiga ngumi mumewe. “Hivi wewe ukoje Danny jamani!? Unaona raha
hivyo anavyohangaika?” Danny akacheka na kuruka pembeni.
“Sasa, sasa hivi kaenda wapi?” “Ndio tumekaa hapa barazani,
tunasubiri tuone. Hajala kuanzia kifungua kinywa wala hajataka kula chakula cha
mchana. Maji yenyewe kanywa glasi moja, tena baada ya kuwa mkali.” “Ngoja na
mimi nikae, nishuhudie.” Akaenda
kuchukua chakula ndani, akatoka kula pale barazani kulikokuwa kumezungushiwa
vioo, kwenye ukuta ulikuwa umejengwa vizuri sana nakupendezesha hilo baraza.
Kwa hiyo AC ya baridi ilikuwa ikipuliza. Fili akapitiwa na usingizi pale pale.
Kwa Nanaa!
Nanaa alipoona vitimbwi haviishi, akamwita Zena pembeni. “Samahani
Nanaa!” Zena akamuwahi kabla hata Nanaa ahajasema kitu. Nanaa akacheka. “Sasa
mpenzi, acha mimi niondoke.” “Hata mimi nilitaka kukwambia hivyo hivyo. Haya
mambo ya ajabu kweli! Mpaka nimejisikia vibaya. Lakini usije ukafikiri
nimehusika.” “Wala usijali. Mimi naelewa. Hata yeye nimemuelewa tu. Naomba
niagie Yasini. Mwambie zawadi yake inamngoja ng’ambo ya bahari.” Wakacheka,
Nanaa akaondoka bila kuaga mtu.
Kwa Geb!
Mara Geb akarudi na makopo ya rangi. Danny na Mama G,
wakaanza kucheka kimya kimya. “Leo patamu leo!” Danny aliongea
kishabiki. “Mama wewe! Muwahi bwana.” Mama G akaendelea kucheka
taratibu. “Nenda bwana mama. Usimfuatilishe Danny.” Mama G, akatoka
pale. Akamfuata. “Unabadili rangi ya geti au ukuta?” “Vyote?” Akajibu
Geb kwa kifupi.
“Unapaka nyeusi!?” Mama
yake akaendelea kuhoji taratibu lakini kwa mshangao baada ya kugundua ni rangi
nyeusi. “Ndiyo. Nataka ukuta mweusi, na geti jeusi.” “Mmmh!” Ilikuwa saa
tisa mchana. “Si ungepumzika mpaka jua litue?” “Sijachoka mama. Naomba
niache.” Grace na Danny walikuwa wakiangalia. “Naona kuna brashi mbili,
ngoja nikusaidie kupaka.” “Hapana mama. Naomba niache.” “Nikuletee maji ya
kunywa tena?” “Sitaki mama. Naomba niache. Nataka kuwa peke yangu.” “Haya
baba.” Mama G akaondoka taratibu.
Nanaa arudi na kuokoa jahazi.
Mara Nanaa akaingia. Akamkuta Geb amelowa jasho yupo karibu
na getini. Amechoka mpaka usoni. Anajifuta jasho kwa mikono yake. Akamsogelea. “Pole
na kazi.” “Asante.” Nana akabaki anamtizama. Alikuwa ameinamia yale makopo
ya rangi anahangaika nayo. Kina Grace walikuwa bado wakimwangalia kwa mbali
wakiulizana, kama anataka kuchanganya au kumwagia kwenye geti.
Mama yao akasema hawezi kumwagia. “Nyinyi hamjajua. Pale
anapiga mahesabu jinsi gani yakufanya ile kazi kuwa ngumu zaidi ya vile.”
Danny alizidi kufurahia. Grace akamfinya. “Sasa unafurahia nini?” “Nyinyi si
mnanionaga mimi chizi kupenda? Sasa leo muone mwalimu wa machizi.” “Usiseme
hivyo Danny bwana! Mimi namuhurumia Geb. Najua anashindwa chakufanya. Anaona
yupo huku, na kule anapoteza.” “Ndio atie akili. Sasa tusubirie tuone. Nanaa
kawasili.” Grace alimwangalia mumewe asimmalize. Mama G, na yeye akajiweka
sawa.
*************************************************
“Geb!” Nanaa akamwita. Geb akamtizama. “Are
you okay?” Nanaa akamuuliza kwa upole. “Umeweza hata kula?” Nanaa
akauliza tena kwa upole. “Nimekuwa na kazi nyingi.” “Pole.” Nanaa
akabaki akimwangalia. “Umekuwa na wakati mzuri huko?” Geb na yeye
akauliza. “Hapana.” Nanaa akajibu bila kufikiria. “Vipi?” Geb
akauliza tena. “Aaah! Mambo ya kitoto tu. Nimeamua kurudi.” “Pole.
Umekula sasa?” “Hapana. Nilikuwa nimekasirika, nikashindwa hata kunywa soda. Haya
maji nimenunua njiani sababu ya jua kali.” Nanaa akaanza kutokwa na
machozi.
Geb akakaa vizuri. “Pole. Usilie sasa. Ni nini?” “Mambo ya kitoto. Hayana hata maana.” “Mbona
yamekuumiza sasa?” Nanaa akaanza kujifikiria ni nini cha kusimulia na nini
cha kuacha. Kwanza ni Jeff. Halafu amsimulie Geb! Atamwambia nini? Kwa haraka
sana atasema ni wivu. Akaamua abadili mazungumzo. Akajifuta machozi.
“Kama unataka kupaka rangi, naweza kukusaidia.” Nanaa akaona atoe msaada. “Jua kali sana. Labda baadaye.
Kwanza umeipenda hii rangi?” Geb akamuuliza Nanaa huku akimuonyesha ile
rangi ya maji, nyeusi. “Unataka kupaka wapi?” Nanaa akamuuliza huku
akimsogelea karibu zaidi. “Ukuta na geti.” “Kwa nini unataka kubadili
hii iliyokuwepo? Inaonekana bado mpya tu na imependezea. Sidhani kama hiyo
nyeusi itapendezea ukuta. Labda geti.” “Basi heri niache tu. Mpaka hii ichakae
ndio nifikirie tena.” Hata Nanaa alikuwa akitokwa jasho.
Nanaa akaona malengelenge kwenye mikono ya Geb. “Tuone.”
Akamvuta mkono wake akawa ameushika anaangalia. “Mbona vidonda vikubwa hivi!?”
Nanaa akamuuliza huku akiviangalia vile vidonda. Wala asijue mama yake Geb na
kina Danny wapo barazani wanawaangalia. “Vinauma?” Nanaa akamuuliza kwa
upendo? “Vikiingia jasho ndio vinauma.” Geb alijibu huku akifikiria.
Ndio hisia za maumivu zilianza kumjia. Kabla ya kuja Nanaa, hakuwa akisikia
chochote kile. Si njaa, si kiu, si maumivu wala kuchoka. Bado alikuwa na nguvu
nyingi tu ya kuendelea.
“Pole.” Nanaa
akatoa mtandio wake kutoka kwenye mkoba aliokuwa nao, akampa. “Futia jasho.”
Geb akacheka. “Mbona mtandio wenyewe ni msafi hivi?” “Nitafua tu. Ni heri
kutumia huu mtandio kuliko hivyo unavyojifuta kwa mkono. Jasho linaingia kwenye
vidonda. Utazidi kujiumiza.” Geb akaupokea akaanza kujifutia jasho.
Akafungua chupa ya maji ya baridi aliyokuwa nayo. “Nipe
huo mkono wako wa kulia kwanza. Naona ndio una kidonda kikubwa.” Geb
akaunyosha mkono na kufungua kiganja chake. Nanaa akammiminia yale maji ya
baridi kwenye lile lengelenge kubwa lililogeuka kidonda. Mikono hiyo ya BOT,
iliyozoea kucheza na kompyuta muda mwingi, leo ilipitishwa kwenye shuruba,
ikasalimu amri. Akaona Geb anacheka. “Umeona eeh?” “Napata nafuu
kubwa. Huu ubaridi wa maji unapoozesha maumivu.” Geb alisifia anachokifanya
Nanaa. Wakacheka.
“Umetembea sana?”
Geb akauliza huku akiendelea kujipangusa jasho kwa kutumia mkono wake wa
kushoto. Aligeuza ule mtandio upande mwingine, uliokuwa mkavu, akaendelea
kujipangusa. “Sio sana, ila jua kali. Leo nimetamani kama ningekuwa na
gari langu.” Nanaa aliongea na kujicheka. “Eti hata pakulala sina,
nataka gari!” “Ungenipigia simu nikufuate.” “Kwanza niliacha bado mmelala, pili
nilikwambia sina namba yako Geb. Tatu hata kama ningekuwa na namba yako ya
simu, nisingethubutu kukupigia na kukuvurugia mapumziko yako na Liz. Najua leo
ni weekend. Mngehitaji muda usio na mwingiliano wa mambo yasiyo maana.” “Kuomba
lifti sio kitu cha maana!?” Geb akauliza. “Inategemea na muombaji Geb.
Kumbuka ni mimi Nanaa.” Nanaa alijionyeshea kidole kinyonge.
“Ningekufuata Nanaa.”
Nanaa akajicheka.“Huniamini?” Geb akauliza, Nanaa hakujibu. Akachukua
mkono wake wa kushoto, akaanza kumwagia maji kama alivyofanya kwenye mkono wa
kulia. “Nanaa?” Geb aliita kama kumkumbushia swali lake. Akayamalizia
yale maji yote kwenye ule mkono. “Twende tukale Geb.” “Huniamini?” Nanaa
akamwangalia, akaona amekusudia kupata jibu. “Nakuamini lakini mimi mwenyewe
nisingeruhusu ufanye hivyo.” Geb alibaki akimtizama. Nanaa akatoa tabasamu
lake la upole huku akiachia mkono wa Geb taratibu.
“Twende Geb.” “Maji uliyokuwa unanimwagia yamenifanya
nitamani kuoga mwili mzima na maji ya baridiii.” Nanaa akacheka. “Asante kwa kujali.” “Anytime.” Nanaa
akajibu na cheko lililofanya dimpozi zake machavuni zikae vizuri. Geb alikuwa
akimwangalia kwa kumu admire
sana. Kama kitu kizuri cha
thamani anachokitamani. Nanaa akainama.
“Hata mimi nataka nikaoge kwanza. Lakini tuyatoe haya makopo
hapa katikati ya barabara. Mtu akitaka kutoka au kuingia, atashindwa.” Nanaa alitoa wazo. Akainama na kunyanyua makopo mawili ya
rangi, kuepuka kuangaliana pale juani. “Tukayaweke stoo.” Geb akatoa
wazo. Wakawaona wanaanza kuyabeba yale makopo kuyapeleka stoo. Geb
alinunua makopo 10 ya rangi.
******************************************************
Kila mtu akahema. “Duuh! Nanaa angechelewa kidogo tu,
tungejishindia geti jeusi na ukuta mweusi.” Mama G, akaanza kucheka. “Danny
huwa ananiudhi mimi jamani! Ukoje huna huruma?” “Unafikiri pale anakuwa
anachoka? Yaani wivu mzuri sana. Pale alikuwa anajiona ndio anaanza.” “Na
angemaliza mapema, angeanza kazi nyingine.” Mama yao akaongeza. “Natamani
siku nyingine akumbuke kuchimba shimo la taka, refu.” Grace
alimrushia mumewe kiatu cha mwanae kilichokuwa karibu. Danny akakwepa. Mama G,
na Danny walikuwa wanacheka taratibu ili Geb asisikie maana walikuwa wanapita
mbali kidogo, kuelekea stoo kubwa ya nje. Kuyapanga yale makopo ya rangi.
******************************************************
Uchokozi ukawazidi yeye na mama G, kupokezana maneno.
Wasijue wenzao walishamaliza. Mara wakaona wanaingia. Wakanyamaza kwa haraka.
Danny akatoa simu yake akajidai anasoma ujumbe. “Hiyo ni kalenda Danny!”
Geb akajua wala hasomi kitu kwani macho yake yalitua kwenye kalenda ya simu
akashindwa hata kuhamisha macho. Geb akamkamata. Akang’ata meno kwa nguvu. “Mmmhhh!
Lazima kujua tarehe Geb. Mambo ya majira. Kiangazi, masika na… ” Geb
akatingisha kichwa, akaingia ndani. “Uchokozi mpaka umekamatwa. Muone.
Ujanja wote umekuisha.” Mkewe alimcheka.
Mama G ndio alikuwa hana mbavu kwa kucheka. Nanaa
akamsogelea. “Kumbe mlikuwa mmekaa hapa?” Nanaa akauliza huku
akimwangalia mama G. “Sio muda mrefu sana. Ila tumeona kila kitu.”
Danny akajibu yeye kwa haraka. Nanaa akacheka. “Shikamoo Mama!” “Mbona
umewahi?” “Mambo hayakwenda kama nilivyodhani. Nikaona nirudi tu nyumbani.”
“Afadhali. Kuna chakula ndani. Nenda ukale.” “Asante mama.” Na yeye
akaingia ndani.
******************************************************
Alikuta Geb amesimama nje ya mlango wa jikoni akisoma
ujumbe. Nanaa akampita, akatangulia jikoni. Haraka sana Geb akamfuata.
Wakasahau swala la kuoga kwanza. “Nini kinaanza? Uji au chakula?”
Nanaa akamuuliza mara alipoingia. “Uji kwanza, halafu ndio chakula.”
Nanaa akaanza kumtayarishia. Kwa kuwa alikuwa mvivu wa kula, mama yake
alihakikisha kila kitu anachokula, lazima kisindikizwe na bakuli la matunda.
Kwa hiyo na Nanaa, akamuwekea kwenye sinia yake hiyo maalumu aliyomuona mama
yake akimpangia mwanae chakula. Akamimina uji kutoka kwenye thermos na kuweka
kwenye bakuli lake maalumu la kunywea uji. Akafungua friji, akakuta mama yake
alishamwandalia matunda. Akayaweka kwenye hilo sinia. Akaongeza glasi ya maji
na napkins tatu, juu yake akaweka uma, kijiko na kisu. Akamsogezea pale. “Karibu.”
“Nashukuru Nanaa. Asante.” “Karibu.” Na yeye akajiwekea chakula kwenye
sahani, akaenda kukaa pembeni yake pale pale jikoni. Wakaanza kula.
“Wamekuudhi nini huko?” Geb alimgeukia akamuuliza. “Hata sio mambo ya maana.”
“Nataka kujua Nanaa.” Nanaa akafikiria ni nini chakumwambia. “Sijui
niseme nini? Lakini ni juu ya Jeff.” “Na yeye alikuwepo!?” “Ndiyo.
Lakini kwa kuwa nilimkataa, akaja na msichana mwingine. Akawa anafanya vitimbwi
kama kunikera tu.”“Uliona wivu?” “Hapana Geb. Najua alifanya kusudi kuniumiza,
kwa kuwa na mimi nilimuumiza kwa kumkataa. Tena baada ya kufanya juhudi na
kunisisitizia yeye sio tapeli kwangu. Anania ya dhati. Naelewa kwa nini
amenikasirikia. Au kuja na msichana mwingine pale. Ni kama kunionyesha
aliyokuwa akiyataka kwangu sio uongo. Maana alianza hata kusema pale mbele ya
watu kuwa anafikiria kufunga ndoa haraka. Hayo yote alikuwa akinithibitishia
mimi kuwa hakuwa akidanganya au akitaka kunidanganya. Lakini..” Nanaa
akasita.
“Lakini nini?”Geb
akataka aendelee. “Najiuliza sijui nimepiga teke bahati au la!” “Kwamba
unajutia?” Likarushwa swali jingine. “Kwa sasa sijutii Geb. Kwa kuwa
najiona sipo tayari kabisa kwenye swala la mahusiano. Ila najua siku moja
nitahitaji kuwa na mtu. Sasa iweje kama Jeff ndio alikuwa mtu sahihi kwangu,
halafu nilishamfukuza?” Geb akanyamaza.
“Lakini moyoni nilishindwa kumpokea kabisa.” “Basi ujue siye
Nanaa. Jipe muda kila kitu kitakuwa sawa.” “Naona nifanye tu hivyo. Hata hivyo
naona nimeshachelewa.” “Ikitokea anakupigia simu na kutaka mrekebishe?” “Hilo
ndilo tatizo Geb. Moyoni nimeshindwa kumpokea kabisa. Japo naona ni kama
ameshika majibu ya maswali mengi au ni kama atakuwa ni msuluhishi wa matatizo
yangu.” “Ki vipi?” “Sijui Geb! Hata sijui niseme nini?” Geb alibaki akimtizama kwa muda.
Geb akamaliza uji wake wote. “Tunaweza kutoka kidogo?”
Nanaa alimtizama kwa makini, kama asiyeelewa. “Na Liz?” Nanaa alijikuta
akiuliza bila kufikiria. “Liz anahusikaje na kutoka kwetu?” Nanaa
akanyamaza baada ya kuropoka. “Nanaa?” “Nilimsikia akisema weekend hii
ulimwambia mtakuwa pamoja. Alisema ulimuahidi mtakuwa naye kwa kuwa hutasafiri.
Ndio maana nauliza.” Nanaa akajitetea, Geb akasimama. Akaweka sinia
alilokuwa akitumia lililokuwa na bakuli la uji na matunda akaweka kwenye sinki.
Akabaki amesimama kama anafikiria kitu cha kuongea huku akiangalia vile vyombo
pale kwenye sinki. Akashindwa chakuongea, akaamua kutoka.
******************************************************
Nanaa akahisi amekosea. Akaingia kuoga. Akabadili nguo.
Safari hii alivaa kigauni kifupi mpaka katikati ya magoti. Kilichanua kuanzia
juu mpaka chini. Akajitengeneza kidogo, akavaa na hereni zake zile zile za
duara zilizofanya uso wake uzidi kuvutia. Aliporidhika, akaenda kugonga
mlangoni kwa Geb. Geb akafungua. Akabaki amesimama mlangoni akimwangalia. “Naomba
lifti.” Geb akacheka na kujiweka vizuri pale mlangoni. Nanaa alijua wazi
amefurahi kumuona pale. Na anafurahia anachokiona mbele yake. Yeye.
Akakumbuka alimwambia akimuomba lifti atampeleka popote
pale. “Sawa. Nisubiri nimalizie kuvaa.” Geb alikuwa ndio ametoka kuoga.
Alikuwa amevaa jinsi na singlendi tu. “Utanikuta jikoni nakupashia moto
chakula chako. Ukila ndio tutatoka.” “Sawa.” Geb alishafurahia mpaka uso
wake ulionyesha kuna furaha moyoni mwake. “Nanaa!” Geb akamwita.
Akageuka kabla hajapotelea jikoni. “Umependeza.” Nanaa akacheka na
kujitazama gauni lake hilo. Kwa hakika alikuwa akivaa vitu vya rahisi sana. “Kila
kitu huwa kinakupendeza.” Geb akaweka msisitizo kumuhakikishia huwa
anaangalia kila anachoweka mwilini mwake. “Asante.” Nanaa
akashukuru na cheko ya aibu kisha akageuka na kupotelea jikoni.
**********************************************
Geb alitoka akiwa na furaha, sio kama yule aliyeamka
asubuhi. Akaingia jikoni, akamkuta Nanaa anamsubiria. “Sasa kwa kupendeza
huko, unataka nikupeleke wapi?” Nanaa akacheka. “Kaa chini kwanza
ule wakati nakusimulia habari ya tunapokwenda.” Geb akakaa. “Ehee!”
Geb akataka Nanaa amuelekeze. “Kuna mahali mpenzi wake Tia, anaitwa Evan
alitupeleka. Wakati wao wanakula na kunywa na kuzungumza mambo yao, nikawaomba
nitembee mimi mwenyewe kuosha macho. Nikatoka na kutembea kama umbali wa dakika
10 mbeleni. Nikagundua kijiwe changu.” Nanaa akacheka kidogo.
“Pazuri, patulivu. Nilijikuta peke yangu. Nikajisifu kuwa
labda mimi ndio wakwanza kupagundua hapo au hamna watu wengi wanaofika hapo.
Nikaamua siku nyingine nije kurudi peke yangu. Nikatafuta siku nyingine,
nikaenda peke yangu. Nilikaa zaidi ya masaa 4, bila kukutana na mtu yeyote
hapo. Basi nikajua ndio sehemu yangu.” “Wapi?” Geb aliendelea kudadisi huku anacheka.
“Sitakwambia mpaka twende ukajionee mwenyewe. Unaweza
usipapende sababu tu ya jina la mtaa au hoteli, wakati hilo eneo langu,
nililoligundua ni zuri.” Geb
akacheka huku akimwangalia Nanaa, msichana aliyeshindwa kushibisha macho yake. “Pazuri.
Wewe kula nikupeleke, halafu utakuja kuniambia kama hutakuwa ukiwa unaenda peke
yako kila unapotaka muda mtulivu.” “Sawa.” Geb akakubali. Hakujali eneo.
Popote kule, ilimradi awe na Nanaa. Vilisikika vicheko huko jikoni. Angalau
mama G na Grace wakatulia mioyo.
******************************************************
Wakati Geb anamalizia kula, wakasikia Liz ameingia. Danny
akafuata nyuma. “Ngoja niangalie kama kuna mpira. Njoo mama.” Grace
alijua ni umbea tu wa mumewe. Na lazima mama yake awepo, ili wakonyezane. Grace
yeye akabakia pale pale nje amempakata mwanae. Mama G akaingia, akaenda kukaa
kwenye kochi karibu na Danny. Wakawasha tv kwa sauti ya chini ili wasikie
kinachoendelea.
“Geb!” Walimsikia
Liz akipita kuelekea chumbani kwa Geb huku akimwita. Geb akamwangalia Nanaa,
akamuona vile alivyonyong’onyea. Tabasamu lote lilimwisha. Zile dimpozi
alizokuwa akifurahia kuzitizamana wakati anaongea hapo jikoni hazikuwepo tena.
Alibaki akichora mezani, gafla akamuona ananyanyuka na kutoka pale jikoni.
Akarudi chumbani kwake.
“Geb!” Liz akaita
tena. “Nipo huku jikoni, nakula?” “Hee! Kwa nini ule jikoni kama msichana wa
kazi!?” Liz akaingia. “Ulimaliza kazi?” Akamuuliza Geb. “Ndiyo.
Vipi?” “Kuna kitu nataka nikakuonyeshe.” “Nimechoka sana Liz. Nataka
kupumzika.” “Mimi nitakuendesha. Wewe utakaa tu wala hutafanya kitu.” Geb
alitulia kwa muda kama anafikiria. “Hutachoka Geb! Nakuahidi. Na ukirudi
huko, utanishukuru. Ni kitu sahihi kwa kazi ngumu uliyofanya leo.”
Kimya. Wadada wawili wote wanataka kumfurahisha weekend hiyo. Wote
wanamuhakikishia furaha mara yakufika huko. “Nani mwenye kisu kikali?”
“Uliniahidi leo utakuwa na mimi Geb. Nimeahirisha mambo
yangu yote leo, ili tuwe wote. Naomba usinigeuke tafadhali. Wewe sio mtu
wakutoa ahadi ukashindwa kuzitimiza.”
Geb akawa amebanwa, akashindwa cha kujitetea. Asubuhi alimwambia ana kazi.
Lakini sasa hivi amemkuta msafi na hana kisingizio chochote. “Basi subiri
nimalize kula.” “Utanikuta basi hapo sebleni. Si unanijua mimi na jiko? Hatuna
urafiki ki hivyoo.” Liz akatoka na kwenda kukaa sebleni wakati Geb
anamalizia kula pale jikoni.
**********************************************
Liz akajiweka kwenye kochi na miguu kakunja 4. Miwani yake
nzuri sana ya jua, aliweka kichwani ikashilia nywele zake ambazo kwa asili alijaliwa
nywele nzuri. Japo ziliongezwa umaridadi na aina ya dawa aliyokuwa anaweka
kichwani. Nakuzifanya nywele hiyo nzito, ianguke mabegani kama sufu. Inang’aa
hata gizani. Kuonyeshwa huwa inashugulikiwa kitaalamu.
Alivaa pensi yake nyeupe na blauzi ya kata mikono, nyepesi.
Ilifanana na sendozi ndefu za wazi alizokuwa amevaa. Huwezi ukamkuta Liz mahali
ukachoka kumtizama. Ungeweza kusema ni mwanamitindo huko Hollywood. Hajikosei.
Kila kitu kizuri na garama. Aliupenda huo mwili wake, wenye rangi nyeusi kamili
iliyong’aa kama alikuwa akipiga msasa ngozi yake kila mara. Msafi kuanzia
nywele, mpaka ukucha wa mguu. Ni ngumu kujua kama huwa anakutana na vumbi.
Kimwili chake kizuri. Alipo Liz, utajua kuna neema ya uchumi, elimu na afya
njema.
******************************************************
Akatoa simu yake akaanza kuitumia bila kumsemesha Danny wala
mama G. Akainamia simu yake akaendelea na shuguli zake kwenye hiyo simu, wakati
mama G na Danny macho yapo kwenye luninga. Harufu na uwepo wa Liz ukatawala
pale ndani akimsubiria mpenzi wake.
Geb alimaliza kula, akatoka. Akaagalia ile hali pale
sebleni. Mama yake, Danny na Liz. Akabaki akifikiria. Liz akanyanyua macho na
kumtizama mpenzi wake. Hakumnyima tabasamu. “Utafurahia na utanishukuru.
Twende.” Liz alionekana amechangamka kweli tofauti na alivyoondoka.
Wakatoka.
Nanaa akajicheka. Akaamua alale tu ili asianze kuwaza jinsi
siku yake ilivyozidi kumsisitizia kuwa yupo mpweke na kila mwanaume ana
mwanamke wake. Mungu bariki, akalala hapo hapo. Bila shida.
******************************************************
Wakati amepotelea usingizini, akasikia mtu anagonga mlango.
Akahisi ni ndoto, lakini akaendelea kusikia mlango unagongwa taratibu. Akajua
ni chumbani kwake. Akafungua macho, giza lilishaingia nje. Akajua amelala na
kupitiliza. Akasimama kwa haraka, akajiweka sawa, akaenda kufungua mlango.
Akakuta Geb amesimama mlangoni. “Ulikuwa umelala?” Nanaa akatingisha
kichwa kukubali na tabasamu la kinyonge. Bado alikuwa amevaa vile vile kama
alivyokuwa amejiandaa kutoka naye masaa machache yaliyopita.
“Nimekuletea Icecream.”
Nanaa akatoa tena tabasamu la kinyonge akainama kama anayefikiria. Geb alibaki
amenyosha mkono kumkabidhi kopo lake dogo la Icecream. “Nanaa!” Geb
aliita kwa upole. “Abee!” Nanaa alinyanyua uso akamwangalia. “Hii ni
ice cream yako nimekuletea.” Geb akarudia kana kwamba hakuwa amesikiwa
tokea mwanzoni. “Nakushukuru, lakini hapana.” Nanaa alijibu kwa upole huku machozi yakiwa
yamejaa ndani ya macho yake. Yakafanikiwa kujaa mpaka kuchirizika nje ya macho
yake yaliyokuwa yamejaa huzuni. Akajifuta. “Usiku
mwema Geb!” Akamuaga kwa
sauti ya chini kabisa, kama kunong’ona huku akiangalia chini. Akafunga mlango.
Akarudi kulala, alimuacha Geb amesimama pale pale nje ya mlango wake na
icecream mkononi.
**********************************************
Mapenzi yamtatiza Geb. Yu njiapanda. Liz au Nanaa?
0 comments: