Story

is mine - ni Wangu! Part 1, Sehemu ya 13.

Monday, July 16, 2018 naomimwakanyamale 0 Comments


K

ila mtu alijua Geb anakwepwa. Na kila alipofanikiwa kumkuta Nanaa mahali akiwa peke yake kama jikoni, Nanaa alimuonyesha heshima kubwa. Kama anayeongea na baba mkwe wake. Salamu aliziitikia kwa heshima sana. Mtoto huyo aliyelelewa uchagani aliweza kutoa mpaka goti la Kinyakyusa kwa Geb. Heshima asilimia 100 alizitoa, endapo atamsalimia. Hakutaka kumtizama, wala kuwa naye karibu. Akiingia huku, anatoka na kwenda sehemu nyingie. Liz anapokuja hapo ndani, ndio ilikuwa kabisaa, Nanaa hatoki chumbani kwake mpaka asikie anaaga.

Ila akaona upendo kwa mama G, unaongezeka kwake. Alitaka kuwa naye karibu na kuzungumza naye wakati wote. Udhaifu wa Nanaa ni kupenda stori. Akajikuta yeye na bibi Fili ndio wapo peke yao mle ndani hawana wapenzi, ushoga ukaanza. Alianza kuzoeana na bibi Fili wakawa wakipata muda mwingi wakucheka na kupeana stori za hapa na pale.

Alisaidia kazi za mle ndani, akawa msaada mkubwa sana. Alifundishwa kupika chakula cha Geb, na chakula cha watu wengine. Kwa hiyo alipokuwa akitoka kazini tu, alipitiliza jikoni kuandaa chakula. Na asubuhi hivyo hivyo. Alikuwa wa kwanza kuamka kufanya usafi na kuandaa kifungua kinywa. Akajitahidi kutoa mawazo yake kwenye kila kitu alichojua kitamtibua, na kumnyima raha, ila kazi za mle ndani na ofisini tu. 

Hakumtafuta tena Zena, wala hakujihangaisha tena na Geb. Kazi za ofisini akaanza kuzimudu vizuri bila shida kubwa. Akawa msaada sana kwa Grace ofisini. Na kwa kuwa hakuwa na safari yeyote. Si kwa James ambako alishapigwa marufuku, wala kwa rafiki. Nanaa akajikuta ana muda mwingi tu wa kutosha kuwa mbunifu wa mambo mbali mbali hasa ya pale nyumbani kufurahisha wenye nyumba wake. Akawafaa sana katika kila eneo.

**************************************

 “Bwana nyumba hii siku hizi tunakunywa chai asubuhi kabla ya kwenda kazini! Tena sio chai na mkate. Tunapata chai ya kueleweka kama tupo kwa mama lishe. Wakati wale wasichana wa kazi wapo hapa, ilikuwa fujo tupu! Chakula hamna, sijui walikuwa wanafanya kazi gani humu ndani!?” Danny alikuwa akiongea wakati anakunywa chai ili awahi kazini. 

“Basi sio utumalizie Danny! Maana nasikia sifa zako zinasindikizwa na kutafuna.” Danny akacheka sana. “Mikate ipo mama.” “Mmmh! Na sisi pia tunataka bajia. Wewe kuwa na kiasi bwana!” Danny alizidi kucheka “Usiwe na wasi wasi mama yangu. Siwezi kukumalizia.” Nanaa alikuwa akicheka peke yake chumbani.

**************************************

Juma la kwanza likapita tokea Nanaa akatae Ice cream aliyoletewa chumbani na Geb, na kuacha kuwa karibu naye kabisa. Pakawa patulivu. Ijumaa Liz akaja kulala, akaondoka jumamosi usiku. Tena aliondokea huko huko walipokuwa wametoka na Geb. Walishinda hapo nyumbani siku nzima. Ilipofika jioni wakamsikia Liz akimuaga Grace wanatoka na Geb kwa ajili ya chakula cha usiku. Liz alikuwa amependeza sana. Alivaa suruali ya jinsi nyeupe iliyokuwa imemshika juu mpaka chini, na top nzuri sana ya wazi juu ya rangi ya kijani kibichi. Ilionekana ya thamani sio ya mtumbani anakonunua Nanaa nguo zake. Kiatu cha juu kilichofanana na blauzi yake. Aliacha harufu ya pafyumu nzuri, imeenea nyumba nzima.

**************************************

Siku ya jumapili ambayo Liz anakuwa na familia yake hafiki hapo nyumbani, Geb alikuwepo tu. Walikwenda kanisani ibada ya asubuhi sana, Nanaa na yeye akaenda kanisani Mwenge. Kanisa la Mtakatifu Joseph, kwenye misa ya saa 4:30 asubuhi. Mama G na familia yake waliondoka asubuhi, wakamuacha Nanaa ndio na yeye anajiandaa. Walirudi mara baada ya ibada kuisha mchana wakitegemea kumkuta Nanaa nyumbani lakini hawakumkuta hapo. Wakaona wasimsumbue kwa kumpigia simu. Mama G akashauri aachwe tu asipigiwe hata simu. Kwa kuwa anapokuwa hapo nyumbani anakuwa na kazi nyingi sana. Akasema angalau hiyo jumapili aitumie kwa mambo yake binafsi. 

Kadiri muda ulivyozidi kwenda, ndivyo  hali ya Geb ilivyokuwa inazidi kuwa mbaya. Mama yake akamuona anazunguka mle ndani kama pia. Lakini akiwa ametulia. Anaingia chumbani kwake, anatoka. Anakaa sebleni kidogo, anatoka nje. Grace akamtizama mama yake. “Amekula?” Grace akauliza kwa kunong’ona. Mama yake akaitikia kwa kutingisha kichwa. “Afadhali.” Grace akajibu akisikika amepata aghueni.

Mpaka inafika saa 11 jioni, Nanaa hakuwa amerudi nyumbani. Hakuna aliyemuulizia. Wote wakajikuta wapo hapo sebleni wanaangalia tv kimya kimya. Geb alikuwa ametulia kwenye kochi amejiegemeza. Hakuwa amezungumza na mtu kitu chochote tokea watoke kanisani. Danny alitoka kwenda kuleta chakula. Alinunua nyama ya mbuzi ya kuchoma, chips kidogo, ndizi za kuchoma kiasi. Grace akaingia jikoni kutengeneza kachumbari. Tayari michale ya saa ilikuwa ikigonga saa 12 kamili jioni hiyo wakati Nanaa anaingia.

“Shikamoo mama.” Nanaa akasalimia na kwenda kukaa pembeni yake. “Marahaba mwanangu. Za huko?” “Nzuri. Nashukuru nimepata wakati mzuri. Na nyinyi za kushinda?” “Nzuri tu. Tumekuwa hapa siku nzima. Baada ya ibada tu, tukarudi nyumbani.” Bado alikuwa akiongea Nanaa na Mama G. Geb na Danny macho walisharudishwa kwenye tv baada ya kuhamishia mlangoni wakati Nanaa anaingia. 

“Ngoja nikaoge nipumzike, mama yangu. Nimekuwa na siku ndefu kweli leo.” Nanaa aliendelea kuongea na mama G kwa sauti ya chini kama asisumbue wanao angalia tv. “Haya mwanangu Nanaa. Grace akimaliza kutengeneza kachumbari nitakuita uje ule kabla hujalala.” “Nimeshakula mama. Asante. Kesho.” Nanaa akasimama. “Haya, usiku mwema.” “Na wewe mama yangu.” Nanaa akaondoka. Siku hiyo nayo ikaisha bila Nanaa na Geb kuzungumza lolote hata salamu japo walionana. 

**************************************

Siku ya 8 tokea Nanaa aweke mgomo wa Ice cream ikawa jumatatu. Kila mtu anaenda kazini. Utaratibu wa Nanaa ukawa ule ule. Kuamka asubuhi na mapema, anapika ndipo anarudi kuoga. Kama amewahi kujitayarisha, akimsikia Grace ameamka, anaenda kumgongea amchukue Fili amwandae yeye. Ili Grace apate muda wa kujiandaa na kupata kifungua kinywa kabla hawajaenda kazini.

Hiyo week ikaanza kuwa nzito. Kila kitu kikaanza kuwa na kasoro kwa Geb. Matatizo yakaanza kwa wafanyakazi wake. Akigundua unakosa kidogo, anataka wafukuzwe kazi wala sio kupewa onyo. Chakula kikawa hakiliwi vizuri. Akiondoka na chupa ya uji asubuhi kama kawaida yake, atarudisha bado imejaa uji vile vile. Inamaana siku hiyo nzima anakuwa hajala kitu. Jumatatu na jumanne ikawa hivyo hivyo. Jumatatu alirudisha uji, lakini saa mbili akawepo nyumbani, kwa hiyo mama yake akambembeleza akala chakula cha usiku. Jumanne mpaka mama yake anaenda kulala, hakuwa amerudi nyumbani.

Ikawa kisirani mpaka kwenye biashara yake. Ikabidi Grace amwambie mama yao. Siku ya jumatano akampigia simu mama yao, na yeye akiwa kwenye biashara zake. “Hivi Geb anakula vizuri?” “Kwani vipi?” Mama yake akauliza. “Zile hasira zake akiwa na njaa naona zimeanza, mama.” “Anafanyaje?” “Anataka nimfukuze huyu dereva kazi. Anasema si mwaminifu. Wakati huyu dereva amekuwa naye kwa muda mrefu, mama. Na wote tunamjua sio mwaminifu. Kuna kipindi nikataka kumfukuza kazi, Geb mwenyewe akamtetea. Akatafuta njia ya kumfanya asiibe. Ndio tunaitumia wakati wote. Yaani kwa kifupi hamna jipya. Lakini hamtaki tena. Anasema nimfukuze kazi, wakati huyu dereva anatufaa sana. Anafanya kazi hata siku za weekend. Ukimpigia simu apeleke mzigo mahali popote pale, hawezi kukubishia. Anakwenda. Amekuja jana usiku amekuta mlinzi mmoja ameenda kujisaidia, amekasirika. Anataka nibadilishe kampuni nzima ya ulinzi.” Mama yake akamtuliza Grace. “Usiwe na wasi wasi, nitazungumza naye.” Wakakata simu. Siku hiyo nayo ikaisha.

Siku ya alhamisi wakati Grace na Nanaa wametoka tu kazini wapo njiani, Geb akampigia simu dada yake, kumwambia ametoka kazini kwake, BOT amepitia hapo ofisini kwa Grace. Yaani kwenye biashara yake. Anaona kuna uzembe mkubwa sana kwa mtu wa stoo. Ndio maana wanapata hasara. Anataka Grace amfukuze kazi kesho yake. “Nimekuwa na siku ndefu sana Geb. Naomba tutazungumza vizuri jumamosi, tukiwa tunapitia kazi yake pamoja.” Akamkatia simu dada yake bila kuaga. Grace akajua ni hasira tu.

Grace na yeye akawa ameshakasirika na walikuwa wamekaribia nyumbani. Waliposogelea tu geti la nyumbani kwao, mlinzi akawafungulia geti kwa haraka, bila hata kuwachelewesha. Grace akaingiza gari bila ya kusalimia walinzi pale getini kitu ambacho si kawaida yake. Akaenda kuegesha gari. Nanaa akamuona ameshuka kwenye gari bila hata kuchukua vitu vyake mle ndani ya gari. Mpaka funguo za gari aliacha zinaning’inia pale pale baada ya kuzima gari. Akamuona anashuka kwa hasira.

“Mama! Mama!” Grace alisikika akiita kwa hasira kidogo. “Nipo jikoni wewe mtoto. Kwani kuna nini?” Grace akaongoza njia mpaka jikoni alipo mama yake. Mama yake akamuona anaingia kwa hasira. “Nilikwambia uongee na Geb, naona hujazungumza naye.” “Kuna nini tena?” “Ananiingilia kazi yangu mama, na si kawaida yake.” “Nitazungumza naye bwana, tulia.” “Sasa kwa nini hujaongea naye mpaka sasa hivi?” Mama G akacheka.

“Usicheke bwana mama!” “Kwani amefanya nini tena?” “Anataka nimfukuze kazi mtu wa stoo.” Mama G akacheka kama mazuri. “Bwna mama!” “Nilitaka kuongea naye leo. Nikamwambia aje pale kazini kwangu tule naye chakula cha mchana. Kwa kuwa nimeona hata chupa ya uji ameacha. Nikajua ameacha kula. Akasema leo yupo busy. Tupange wakati mwingine.” “Hana ubusy wowote ule. Sasa hivi yuko kazini kwangu. Ametoka kuzungumza na mimi sasa hivi.” “Basi ujue hapo ananikwepa. Anajua akija hapa nitamkera na maswala ya chakula. Nikimuacha hivyo, hatarudi hapa mpaka usiku wa saa sita. Ngoja nimpe lisaa limoja. Nitampigia, nimlazimishe arudi nyumbani, ale halafu alale.” Grace akatoka akiwa na hasira zake vile vile. Nanaa akajisikilizia. Akanyamaza. Akaingia chumbani kwake baada ya kula. Akalala. Wala asijue kinachoendelea. 

**************************************

Asubuhi wakati yupo jikoni, siku ya ijumaa akiandaa kifungua kinywa. Akashangaa Mama G, naye anaingia. “Mbona mapema mama?” “Geb hayupo sawa. Hali chakula. Halali vizuri. Jana kachelewa kurudi, na ameshaondoka bila hata kula.” Nanaa akanyamaza. Asijue aongee nini. Maana alijua hata mama G, anajua kuwa amemnunia Geb. Hawaongeleshani. Mama G akalalamika hapo jikoni bila kupata uungwaji mkono na Nanaa, mpaka Nanaa akamaliza kazi zake, akamuacha hapo jikoni.

Hakuna aliyemsikia siku hiyo. Usiku wa saa mbili wakamuona anaingia. Akasalimia vizuri akaingia chumbani kwake. Mama yake akampa kama lisaa, akijua anaoga labda atatoka. Lakini kukawa kimya. Akaamua kumfuata chumbani kwake. Akamkuta amelala. “Pole na kazi?” Akamuanza. “Asante.” Mama G hakuwasha taa, akamsogelea mpaka pale kitandani. “Nimekutengenezea mchemsho wa mboga mboga na samaki.” “Leo nilikuwa na semina kazini. Karibia siku nzima. Wametupa chakula. Kwa hiyo nimeshiba. Nataka kulala.” “Utakuja tulale wote?” Kimya. “Geb?” “Unalala saa ngapi?” Akamuuliza mama yake. Muda sio mrefu.” “Basi nitakuja.” Mama G akatoka.

Ni kweli alikwenda kulala na mama yake. Lakini alikwenda usiku karibia panapambazuka. Mama yake alimsikia akipanda kitandani, akajua hakuwa amelala kwa muda wote alipokuwa kitandani. Akamuhurumia, asijue amwambie nini muda huo na yeye alikuwa na usingizi. 

**************************************

Asubuhi siku ya jumamosi, akatoka baada ya kunywa uji. Akamwambia mama yake anakwenda Bagamoyo, atarudi jioni. Akaondoka. Kila Mama G alipokuwa akimuona Nanaa, alijiongelesha juu ya Geb. Nanaa alijua ni kama anataka kumfikishia ujumbe fulani lakini alishindwa asaidiaje. Mama huyo alilalamika jinsi mwanae alivyo na wakati mgumu. Hali vizuri. Halali vizuri. Lakini hataki kuzungumza naye. Akaendelea kuongea kwa kurudia rudia kama Mungu angemfanyia muujiza wa kumtumia mtu akaweza kuzungumza na Geb, angeshukuru sana. Nanaa alijua anatumwa yeye tu. Kwani mama G, anajua wazi hawazungumzi. Lakini hakujua kama chanzo cha heka heka zote zile za Geb, ni yeye Nanaa.

**************************************
Jioni ilipofika Geb akaingia bila salamu, akaanza. “Nataka kusitisha mkataba na hii kampuni ya ulinzi ya hapa nyumbani. Wanachukua muda mrefu sana kufungua geti.” Grace na mama yake wakaangaliana. Akapita kwenda chumbani kwake kwenda kuoga. Nanaa naye alikuwa jikoni, akasikia. “Hivi mama umesikia lakini?” “Nimesikia. Sasa leo ndio tutalala hapa bila walinzi. Akitoka huko ndani, wanafukuzwa leo leo wala si kesho. Subirini muone.” Mama yao akajibu huku cheko limemjaa. Nanaa akatoka jikoni akaenda kukaa pembeni ya mama G. 

“Bwana mama! Acha kufanya utani. Ujue atawafukuza kweli?” “Tupo wanaume wawili humu ndani. Tutapeana zamu ya kulinda. Acha Geb awafukuze tu. Waache utani na bosi wao! Kwa nini wamuweke getini muda mrefu?” Danny kama kawaida yake ya uchochezi. Naomba nyamaza Danny.” Mama G na Danny wakawa wanacheka. Nanaa alikuwa amekaa pembeni ya mama G, akawa anasikiliza tu bila hata kuongeza neno. Geb alitoka chumbani kwake akasogea pale sebleni. Alipoonyesha dalili za kutaka kukaa tu, hapo hapo Nanaa akanyanyuka, akaenda zake chumbani kwake.

Mara Zinda akaingia akiwa na maneno mengii, ikabidi Geb akae tu amsikilize. Stori zikaanza. Vicheko. Mara Liz naye akaingia. Wakakaa kwenye makochi. Stori zikaendelea. Watu wakasahau hekaheka za Geb. Kila akikutana Zinda, James, Danny, Malii, Gozi na marafiki zao wengine, hutaacha kucheka. Sasa hapo alikuwa Zinda na Danny tu, lakini nyumba nzima ilijaa vicheko. Mama G ndio alikuwa akisikika akicheka kila wakati.

**************************************

Nanaa alibaki pale chumbani akijisomea kitabu chake cha hadithi ya mapenzi cha Endless Love. Alikuwa amejilaza kwenye kochi la pale pale chumbani kwake. Kwenye simu yake aliweka miziki iliyokuwa ikimtumbuiza taratibu huku akiendelea kusoma. Alifikia sehemu nzuri sana ambapo msichana Mercy wa kwenye kitabu hicho ameondoka kwa siri nyumbani kwa kina Ben, baada ya mchumba wa Ben kumdhalilisha vibaya sana wakiwa mezani. Mara nyingi Nanaa alijifananisha na Mercy. Jinsi wanavyohangaika kwenye mapenzi na wote ni kama walikuwa yatima

Uzuri wa Mercy uliosemwa kwenye stori hiyo ya Endless Love, alijifananisha nao sana. ‘Kasoro mimi sio mchanganyiko wa damu ya kizungu. Nywele ndio sitaki hata kujifanisha naye. Zangu kipilipili kisichoweza kuchanika.’ Nanaa alijisemea na kujicheka. ‘Lakini weupe upo bwana. Hata maumbile yetu! Japo huyu Mercy mwenzangu anaonekana amezidi.’ Nanaa alijiangalia kidogo akacheka. ‘Ila na mimi aahaa! Najikubali, hata kama wanaume wananizingua. Lakini najijua umbile na sura Mungu hakufanya haraka. Alitoa ujuzi wake japo kwa sehemu.’ Nanaa akajisifia wakati akijilinganisha na Mrembo Mercy wa kwenye stori huku akicheka. 

Wakati amezama kwenye kitabu akiendelea kumfuatilia Mercy aliyekwisha fika Mlimani city, Nanaa akimuonea huruma Mercy kuwa peke yake usiku ule. Tena kwenye jiji asilolifahamu. Uzuri ulio bayana hata gizani! Nanaa alikuwa akiogopa asije akakamatwa na vibaka wakamtendea ubaya. Hofu ilimjaa Nanaa pale kwenye kochi kana kwamba yupo kwenye tukio la kweli. Aliendelea kusoma kitabu hicho cha ‘Endeless Love’ huku akiomba Mungu kuwa Ben apite maeneo hayo ili akutane na Mercy usiku huo, wazungumze wayamalize. Wapenzi hao warudi wote nyumbani, mambo yaishe. Alishamchukia Bety. Akamlaumu. Akamfananisha na kina Viola. Nanaa aliendelea kusoma, akili zikawa zimezama kitabuni. Akasahau alipo na matatizo yake yote.

**************************************

Mara akasikia mlango unafunguliwa. “Nimegonga naona kimya, nimeamua kuingia tu.” Alikuwa mama G. “Samahani sikukusikia wakati unagonga. Karibu mama.” Nanaa akashusha miguu kwenye kochi, kumpisha akakaa. “Una mgeni.” Nanaa akakunja uso. “Mimi!?” Mama G akacheka. “Ndiyo Nanaa. Una mgeni.” Hakuna aliyejua anaishi hapo. Nanaa hakuwa na marafiki wakufuatana nyumbani. Na kama ni kaka yake, mama G angesema James anakuita sio mgeni. James hakuwa mgeni kwenye hiyo nyumba na wala kwenye maisha yake. Mama G akabaki amekaa kama anawaza.

Ni nini mama?” “Bado hali ya Geb sio nzuri. Tokea arudi hajala. Natamani kuzungumza naye lakini nimeshindwa kabisa.” “Kwa kuwa Liz nimemsikia amekuja, labda atamuweka sawa. Usiwe na wasiwasi mama yangu.” Nanaa akajaribu kumtuliza, akikwepa huo mpira. “Ngoja tuone kama Liz atafanikiwa. Lakini Liz huwa hana mtindo wa kumlazimisha chakula. Anasema kutokula sana ndio vizuri kwa afya yake. Wakati mwenzie sio kwamba yupo kwenye diet, ni hapendi kula.” Nanaa akabaki kimya. “Lakini labda leo atanisaidia na kumfanya ale.” Mama G, akatoka akamuacha Nanaa anajiuliza. Alijua ndio amemtuma hivyo. “Lakini Geb anaye Liz  jamani! Kunihusisha na mimi kwenye maisha yake, It’s not fair.” Nanaa akajilalamisha, akanyanyuka na kutoka.

****************************************************

Alifika hapo sebleni akakuta ni Zinda na Liz ndio wameongezeka. Hapakuwa na mgeni. Si Zinda wala Liz waliokuwa wageni nyumbani hapo. Zinda ni kama kaka yake James kwenye familia hiyo. Aliingia hapo na kutoka bila taarifa. Alipokuwa akija na njaa, alipitiliza kwenye friji bila kusubiri kukaribishwa. Wakati mwingine aliwasikia wakimlalamikia bibi Fili wakiwa huko huko jikoni kwamba wao wananjaa na hakuna chakula. Tena wakiwa wameshafika mpaka kwenye friji. Hapo ndipo bibi Fili huenda jikoni na kuwatengenezea kitu cha kula kwa haraka, wanakaa naye wanakula huku wakizungumza hili au lile. 

Liz alijichukulia kama mama mwenye nyumba hiyo. Mpenzi wa mwenye nyumba. Aliingia hapo na kutoka atakavyo. Tena alipokuja wakati mwingine alisalimia tu na kupitiliza chumbani au wakati mwingine alipowakuta sebleni, hakutoa hata salamu. Alipitiliza chumbani kwa Geb, moja kwa moja. Kama Geb alikuwepo, alisimama na kumfuata chumbani. Na kama alikuja Geb akiwa hayupo, basi ujue Geb anakuwa na yeye anakaribia kurudi hapo nyumbani. Basi watapishana dakika chache sana. Hata dakika 5 hazitaisha, Geb naye atakuwa anaingia hapo ndani. Baada ya salamu tu bila hata kuambiwa kama mpenzi wake yupo chumbani anamsubiri, Geb atapitiliza chumbani moja kwa moja kuashiria waliwasiliana kabla ya Liz kufika hapo. Kwa hiyo mpaka hapo, Nanaa hakuona mgeni aliyeitiwa. 

 **************************************

“Habari zenu?” Nanaa akasalimia. Salama kabisa.” Zinda akajibu kwa haraka, Liz kama kawaida yake huwa hujibu pale anapojisikia. Ni kawaida. Wote walishamzoea. Kwa hiyo yeye hakuitikia salamu ya Nanaa. Alinyamaza tu. Kimya kikapita. “Huyo mgeni wangu yuko wapi?” Nanaa akauliza huku akimwangalia mama G aliyemwita. “Ni mimi, Nanaa.” Zinda akajibu kwa upole sana, akasimama. Alikuwa amekaa karibu sana na Danny. 

Nanaa akakunja uso. “Wewe ndio mgeni wangu mimi!?” Nanaa akauliza huku anajionyeshea kidole. Watu wote walikuwa wakiwaangalia. Nanaa alikuwa na haki ya kushangaa. Siku zote alizomuona Zinda akifika hapo nyumbani, hakuwahi hata kumuona akitafuta hata kuwa na maongezi naye zaidi ya salamu. Alifika akiwa na habari nyingi za mtaani. Bila salamu alikuwa akiingia na stori huku akitaniana na kila mtu kasoro yeye. Leo iweje awe mgeni wake yeye!? 

“Ndiyo Nanaa. Nataka kuzungumza na wewe.” Nanaa akaingiwa na wasiwasi kidogo. “Kaka James ni mzima?” “Mzima kabisa. Ni mazungumzo yangu mimi mwenyewe binafsi.” Kidogo akavuta pumzi kama kupata aghueni. “Sawa. Karibu.” Kimya. Nanaa akabaki akimtizama. Bado walikuwa wamesimama pale pale sebleni watu wote wakiwepo kimya wamekaa. “Wewe Zinda vipi bwana!? Mbona kimya? Nanaa anakusikiliza.” Danny alimpiga ngumi ya mguuni. “Kumbe unanisikiliza? Basi tutoke hapo nje tukakae kabisa.” Nanaa akakubali. Wakatoka nje.

Zinda kwa Nanaa.

Kimya kidogo kikapita pale walipokuwa wamekaa nje barazani. Palitenganishwa na vioo na nyavu kuzuia mbu na wadudu wengine kutoka nje. Baraza lilifunikwa na nondo za urembo wa maua. Kuanzia kwenye dari mpaka kati kati kufikia nusu ya ukuta uliojengwa kwa muundo nadhifu sana. Ndani ya nondo hizo kulikuwa na vioo pia, ambavyo vilizuia hewa ya AC isitoke nje. Paliweka sakafu yenye marumaru za kuvutia. Kulipangwa makochi mazuri sana ya rangi nyeusi na meza za vioo ndogo tu kama stuli. Baraza lenyewe lilikuwa na thamani ya sebule ya mtu.

Nanaa alishangaa Zinda hazungumzi kitu. “Umetumwa na kaka!?” Nanaa akavunja ukimya kwa kuuliza swali. “Hapana.” Kimya. Zinda huyu wa leo siye Zinda aliyezoea kumuona Nanaa. Kwa asili Zinda alikuwa mtundu sana. Kimya. “Kuna nini, mbona unaniogopesha?” “Usiwe na wasiwasi kabisa. Ni mazungumzo tu.” Kimya. Nanaa akakunja uso akaona na yeye anyamaze. Akajirudisha nyuma kwenye kochi, akanyamaza.

“Umesikia Malii anaoa?” Nanaa akamgeukia Zinda. “Ndiyo.” Nanaa akajibu. Zinda akaendelea. “Tena Fili anasimamia harusi. Sendoff itakuwa Marangu. Anaoa msichana wa Marangu. Lakini si unajua Malii na yeye ni mchaga? Wachaga wanapenda kuona wenyewe kwa wenyewe. Sasa naona mwenzangu ameamua kuaga ukapela, ametuacha sisi, anaoa. Ni hatua kubwa sana ya maisha. Na mkewe ana kazi. Na mdada mwenyewe sio mbaya, ila hana rangi kama yako. Ila ni Mmarangu wa nguvu. Kwa hiyo sendoff itakuwa Marangu, huko Kilimanjaro. Sijui umewahi kupasikia?” Nanaa alikuwa haelewi. Zinda alianza kuongea kama mashine.

“Nimezaliwa Moshi mjini. Nikasoma miaka 2, katika shule ya wasichana Ashira sekondari. Ipo Marangu.” Nanaa akajibu kwa utulivu. “Kumbe wewe ni mwenyeji sana huko? Basi utakuwa mwenyeji wangu.” “Wapi!?” Nanaa hakuwa ameelewa. “Huko Marangu. Tutaondoka hapa siku mbili kabla ya sendoff. Tunamsindikiza Malii, kuchukua jiko. Wote tunakwenda. Au hujasikia?” “Mama na Grace wameniambia, lakini mimi sitakwenda.” Nanaa akajibu.

“Tungeenda tu ili tuwe pamoja. Umoja ni nguvu. Nitakununulia gauni na viatu. Nitakununulia cheni na bangili. Lakini vitakuwa vya dhahabu. Dhahabu itakupendeza sana. Halafu nitakununulia gari. Nyumba yangu ile niliyokuwa najenga, inakaribia kukamilika. Sasa hivi..” Mara wakasikia Danny anakohoa sana. Zinda akatulia kidogo.

Nanaa akabaki ametoa macho akimshangaa Zinda. Alipotulia Danny, Zinda akaendelea. “Kwa hiyo kama nilivyokuwa nikikwambia. Tukioana tutahamia kwenye nyumba yetu hiyo mpya. Nitaenda kuleta wadogo zangu kutoka nyumbani. Kwetu ni Tabora. Usifikiri ni kijijini. Hata wao ni watu tu wa mjini. Kwa hiyo wakija huku mjini, itabidi waanze kusoma hapa hapa mjini. Usiwe na wasiwasi, nyumba yenyewe ni kubwa sana. Najua utawapenda tu. James anakusifia una roho nzuri na…” “Aibu gani hii jamani!?” Walimsikia Danny akigomba kwa sauti. Gafla kila mtu akaanza kucheka.


“Wewe Zinda, hebu njoo kwanza.” Danny alitoka pale barazani. “Hebu njoo. Njoo.” Danny alisisitiza huku akimwita kwa ishara ya mkono. Zinda akasimama, akamfuata. Wakaingia ndani. Kila mtu alikuwa anacheka. “Kamleteeni maji ya kunywa.” Nanaa alimsikia bibi Fili akiongea huku anacheka sana. “Grace, nenda kamleteeni mwenzenu maji.” Wote waliendelea kucheka. “Kaa hapa Zinda mwanangu. Kaa hapa baba.” Alimsikia bibi Fili akipiga piga kiti huku anaendelea kucheka.

“Vipi? Kwani nimeharibu?” Zinda aliuliza. “Kumbe wewe ujanja wote huo hujui kutongoza bwana!? Kelele nyingi kumbe hujui kutongoza!” Danny alikuwa kwenye mshangao na hasira juu. Lakini wengine walikuwa wakicheka sana. “Sasa wewe magauni na cheni za dhahabu za nini Zinda ndugu yangu!?” Danny alimuuliza kwa mshangao sana. “Nitamnunulia.” Zinda alijitetea akiwa amepoa kama sio yeye. Walizidi kucheka.

“Daah! Ahadi hizo unamwambia mama yako Zinda. Sio watoto wa mjini. Hayo mambo yamepitwa na wakati. Watu wanataka surprise. Sasa wewe unaanza kutoa ahadi nyingiii. Tena nyingine zinaogopesha! Hujamuoa unaanza kumpa na majukumu ya wadogo zako!? Mara unampa ahadi ya gauni, mara gari, mara bangili. Bangili? Wewe vipi Zinda bwana!?” “Huyu mtoto ananichanganya bwana.” “Wewe hujui kutongoza bwana. Acha kumsingizia Nanaa. Hujui uanzie wapi wala uishie wapi. Unaanza kumsifia mchumba wa Malii kwa Nanaa! Wapi na wapi?” “Si ndio nilikuwa naanza sasa ili nipate pakutokea?” Zinda alijitetea nakufanya watu wazidi kucheka kasoro Danny aliyekuwa anamuhoji kwa mshangao.

“Ushafika kwenye ndoa bila kumtongoza, sasa kitakachofuata ni nini kama sio kifo?” Danny aliuliza nakufanya watu wazidi kucheka. “Zindaaaa!!” Grace alikuwa akicheka mpaka machozi. “Huyu hatakaa aoe. Unafikiri mama?” “Taratibu Zinda mwanangu.” “Eti mama, eeh?” Zinda alitaka kutiwa moyo baada ya shutuma nyingi za Danny. “Kabisa mwanangu. Lakini nahisi umemuogopesha Nanaa. Ungefanya kama ulivyosema mwanzo au vile mlivyokuwa mmekubaliana na Danny, kabla ya Nanaa hajaja. Kuwa leo unamuomba tu muende naye Marangu. Basi. Umetoa ahadi nyingi mno Zinda mwanangu. Halafu..” Bibi Fili alishindwa kuendelea akaanza kucheka upya. Zinda alikuwa mpole kama sio yeye.

“Yaani wewe unapitwa hata na Fili bwana? Yaani huwa nikimsikia mwanangu Fili akiongea na Nanaa, mwenyewe naona nimezaa. Mtoto anajua kupanga maneno. Hachanganyikiwi kama wewe! Kwanza akijinadi kwa Nanaa, Nanaa mwenyewe anamkubali mwanangu. Pointi zake zinaeleweka. Wewe unachanganya mambo kama nini sijui! Hujulikani kama ni mtabiri wa hali ya hewa, au mchimba madini. Mara uwe kama pedeshee la mjini, mara mshamba wa kijijini kabisaa. Fujo tupu. Hebu nenda kamwangalieni Nanaa. Weza kuta mtoto wa watu amezimia hapo nje.” Zinda akatoka kwa haraka.

Akamkuta Nanaa ameinama. “Hajazimia bwana. Ameinama tu.” “Kachoka! Umemchosha mtoto wa watu.” Watu walizidi kucheka. “Na nitamwambia James.” “Acha hizo Danny. Ngoja mimi nikazungumze tena na Nanaa.” “Hakuna. Toka kwetu. Nenda Zinda. Hatutaki tena. Toka.” Danny akasimama, kila mtu alikuwa anacheka. “Nini bwana Danny! Sasa hivi nishajua makosa yangu nitarekebisha.” “Hamna. Toka Zinda. Ushamchosha Nanaa kwa maneno mengi.” “Sasa kwa nini unamjibia Nanaa? Mwache mwenyewe aongee.” Zinda na Danny wakaendelea kubishana.

“Njoo Nanaa mwanangu.” Nanaa alisimama kwa haraka aliposikia bibi Fili akimwita. Alishukuru Mungu. Kila mtu alianza kucheka upya pale Nanaa alipoingia ndani. Zinda naye akarudi ndani kwani bado alikuwa amesimama mlangoni pale alipoenda kumwangalia Nanaa akamkuta ameinama. 

Danny akamuwahi Nanaa. “Eti Nanaa, unataka mkufu na bangili?” “Vya dhahabu bwana!” Zinda aliongezea kwenye swali la Danny, nakufanya watu wazidi kucheka. “Yaani ndio unaharibu zaidi. Eti Nanaa, unataka dhahabu wewe?” Danny akauliza tena. “Hapana. Sitaki.” Nanaa alijibu huku akicheka kwa aibu. Alitamani aondoke pale. “Unataka gauni?” “Na viatu Danny. Wewe vipi bwana? Atavaaje gauni bila viatu?” “Sawa Zinda. Eti Nanaa?” Watu walikuwa wakicheka mpaka machozi. Geb pia aliyekuwa amekasirika, ilibidi acheke tu. Liz ndio kabisa. Mpaka alikuwa akinyanyua miguu juu kwa kucheka.

“Mimi sitaki kitu chochote. Sitaki hata gari na nyumba. Na sipo tayari kuolewa sasa hivi, bado nasoma. Na sitakwenda Marangu.” Nanaa alimaliza akaondoka kurudi chumbani kwake huku akicheka na wengine wakicheka sana.

“Haya. Toka kwetu. Lione. Janaume zima linashindwa na mtoto mdogo! Nimekufundisha maneno yakuongea, unakuja kusema mambo ya ajabu, tena yazamani! Nani kakwambia Nanaa anataka magauni kama sio kutiana tu aibu hapa? Wote atatuona tupo hivyo hivyo kama wewe. Atajua kaka yake haoi mpaka leo kwa kuwa hajui kutongoza kama wewe. Toka bwana. Ushatudhalilisha vyakutosha. Toka Zinda.” “Daah! Naona kweli niondoke tu.” “Mwache anywe hata maji, Danny. Mwanangu Zinda amekuwa na wakati mgumu sana.” “Mwache aende mama. Akanywe maji huko mbele ya safari, sio hapa. Kaniudhi sana. Nimekohoa mara ngapi hapa ili kumshtua, lakini hasikii. Wewe habari za Fili mwanangu kusimamia harusi zinahusikaje na kutongoza kwako? Eti mkewe anakazi! Aibu tupu hii. Hebu nenda kwenu bwana. Toka.” Zinda akatoka akawaacha wanacheka sana. 

****************************************************

Kila walipokuwa wakikumbuka waliendelea kucheka. Hakuna aliyeweza kuangalia Filamu tena. Walikumbushana habari za Zinda na Nanaa, nakuzidi kucheka. “Naona Nanaa hatakaa akasahau.” Grace aliongeza huku anacheka. “Maneno mengi vile, kumbe hajui kutongoza!? Atanikoma Zinda. Amezoea sana kunichokoza. Nishajua pakumpatia.” Grace aliendelea kucheka. “Halafu mimi nimemfundisha kweli hapa.” Danny alimkata mkewe. “Basi uulizaji ule wa maswali, nikajua kaelewa. Maana alimtuma mama kwa ujasiri wote. Eti ‘nenda kaniitie mkweo, nimpange.’ Kumbe hana lolote!” Liz aliongeza huku akicheka. 

“Tena alikuwa akimuuliza mwenzie Danny maswali ya msingi kweli! Danny naye akarudia rudia kumwambia hilo ongea mwanzo, na hili mwisho.” “Tena akanijibu ameelewa, bwana! Akaenda kututia aibu!” Danny alimkatiza bibi Fili. “Ila mimi niliona dalili tokea Nanaa anauliza hapa mgeni wake yuko wapi. Kama mlimwangalia Zinda, alianza kubabaika tokea mwanzo. Akawa kama amepata ganzi mpaka Danny alipompiga ngumi.” Grace alichangia nakufanya waendelee kucheka.

Liz akanyanyuka huku anacheka. “Ngoja niondoke zangu. Lakini njiani lazima nimpigie Zinda nicheke zaidi.” “Sasa hivi atakuwa baa. Kwa aibu hii, lazima akanywe ndio aweze kulala.” Danny alijibu na kuwafanya wazidi kucheka. Liz akatoka, wakasikia gari imewasha, akafunguliwa geti akaondoka bila hata kuulizia swala la chakula kwa Geb wala hata kujua alishindaje. Wakashangaa hata hakulala siku hiyo. 

Geb akanyanyuka. “Chakula baba!” Mama G akauliza kwa upole. “Nitakula kesho. Sasa hivi nimechoka naenda kulala.” Geb akajibu huku anaelekea chumbani kwake. Bibi Fili akawaza kidogo, na yeye akasimama kuelekea chumbani kwa Nanaa. “Na mimi naenda kulala. Lakini lazima nipitie chumbani kwa Nanaa mwanangu niangalie hali yake.” Bibi Fili akaondoka. Akabaki Grace akicheka na mumewe.

****************************************************

Akagonga chumbani kwa Nanaa. “Karibu.” Nanaa aliitika. Mama G akaingia. “Nimekuja kukuangalia wewe unayekataa bahati ya dhahabu na gari.” Nanaa akacheka sana. “Mama wewe! Balaa gani hilo!?” “Tumepata kituko cha mwaka.” Wakacheka kidogo, mama G akaenda moja kwa moja kwa kile kilichompeleka huko chumbani kwa Nanaa. 

“Geb ameenda kulala bila kula!” Akajilalamisha. “Na sijui ataendelea hivyo mpaka lini? Zinda ametoa vichekesho pale, naona akajisahau kwa muda. Zinda ameondoka na yeye akanyanyuka kwenda kulala, na huzuni zake. Nikumuombea tu.” Nanaa akanyamaza. Usiku mwema Nanaa mwanangu.” “Asante na wewe mama.” Mama G akataka kutoka. “Mama!” Nanaa akamuhurumia. “Unajua sina namba ya simu ya Geb?” “Ni rahisi sana. Unaweza kuishika hata kwa kichwa tu.” Nanaa akaona mama G amechangamka gafla. Akamtajia ile namba, akatoka akiwa anacheka.

****************************************************

Nanaa alibaki akifikiria chakufanya. Akaamua kumtumia ujumbe. Hey! Ni mimi Nanaa.’ Baada ya muda mfupi sana, akaona Geb amerudisha ujumbe. ‘Mimi bado ninayo namba yako Nanaa.’ Nanaa akamuhurumia. ‘Pole na kazi.’ ‘Asante.’ Kimya. Nanaa akafikiria amwambie nini tena. ‘Umeshalala?’ Nanaa akauliza. Bado. Na wewe ndio unalala?’ Geb akauliza. Bado nipo nipo. Nasoma kitabu cha hadithi.’ ‘Kinahusu nini?” Geb akauliza. ‘Mikasa ya mapenzi. Bado sijamaliza. Ndio nipo katikati. Unaweza kuja kukiona.’ Hata dakika haikuisha Geb akawa ameshafika mlangoni kwa Nanaa.

“Karibu.”  Geb akaenda kukaa pembeni yake. “Kina jina gani?” “Kinaitwa Endless Love.” Geb akakichukua. “Ni kizuri sana.” Nanaa akasifia. “Kumbe ndio maana unajifungia mwenyewe huku chumbani ukifaidi!” Nanaa akacheka kidogo. “Unakipendea nini?” “Namfananisha huyo msichana na mimi. Maisha yetu naona kama yanafanana!” “Kivipi?” Geb alidadisi tena huku akijaribu kuperuzi kurasa za kile kitabu. Alimuona vile alivyochoka usoni.

Eti Nanaa?” “Naona mapito yake yanafanana na mimi katika kila eneo la maisha. Lakini naona yeye mwenzangu Mungu alimpa Ben, mimi Mungu amenipa kaka James.” “Na yeye Ben ni kaka yake?” Geb aliendelea kudadisi taratibu huku macho yakiwa kitabuni.  “Hapana. Ni kijana tu waliyekutana kwenye hangaika za Mercy. Lakini Ben anaonekana kumpenda sana Mercy. Mpaka hapo nilipofika, bado hajamwambia chochote juu ya mapenzi. Japo anampenda na kumuhangaikia sana. Mercy naye hana wazazi kama mimi, anahangaika pakuishi kama hivi mimi ninavyohangaika pakuishi.” Geb akamtizama. Nanaa akainama.

“Wewe upo hapa na sisi.” “Hata yeye alikuwa akipata sehemu anahifadhiwa kwa muda kama mimi. Namaanisha sehemu ya kudumu na ndugu wanao kuhitaji.” Geb akamtizama tena nakurudisha macho kwenye kitabu. “Namaanisha nyumbani.” Nanaa akajaribu kutetea hoja yake zaidi. “Unaweza kupafanya hapa ni nyumbani Nanaa.” Nanaa akacheka kidogo akainama kama anayefikiria. 

Akafikiria maneno ya mama yake mkubwa, akaguna. “Nyumbani ni pale moyo wako ulipo, Nanaa. Ukiamua kuwa na sisi, utapafurahia tu hapa na kupafanya ni nyumbani kwenu.” Nanaa akanyamaza. Ukapita ukimya wa muda. Geb akiwa ameshika tu kitabu, hakuwa akisoma tena. 

“Geb!” Nanaa akamwita kwa upole, akamgeukia. “Are you okay?” Akamuuliza kwa upole huku akimwangalia. “Sijui Nanaa.” “Pole. Naamini Mungu atakusaidia. Kila kitu kitakuwa sawa. Usiwe na wasiwasi.” Nanaa aliongea kwa upendo, akimfariji. “Nakushukuru. Na samahani.” Nanaa alielewa msamaha ule ni wa nini. Machozi yakaanza kujaa machoni. “It’s okay.” Nanaa akajibu kwa upole akitaka kumtoa hukumu moyoni. Geb akabaki akimtizama, Nanaa akainama. Wakabaki kimya kwa muda.

Nanaa akajifuta machozi. “Vidonda vya mikononi vilipona?” Nanaa akauliza. Geb akajiangalia viganja vyake. “Tuone.” Nanaa akamsogelea karibu zaidi. Akamshika mkono wa kushoto uliokuwa upande wake. Akakiweka kiganja chake mkoni mwake akawa amemshikilia. “Mkono huu unaonekana kidonda kimekauka. Tuone mkono mwingine.” Geb akampa. “Huu bado kidogo. Pole.” Alimpa pole huku akiangalia vile vidonda mkononi. “Asante.” Geb akashukuru kwa sauti iliyosikika kutulia. 

Nanaa akawa anapitisha kidole chake kimoja juu ya vile vidonda kama anachora pembeni yake kuzunguka mduara mzima wa kile kidonda. Taratibu sana huku akikipuliza. “Kinauma?” Akauliza kwa upendo kama kwa mtoto. “Kikiingia sabuni au kitu cha chumvi chumvi ndio kinauma zaidi.” Geb akajibu huku na yeye akiangalia vile Nanaa alivyomshika. “Pole. Utapona tu.” Nanaa akaendelea taratibu. Hata na yeye alishakuwa na hamu na Geb. Alifurahia kuwa naye pale.

“Naomba nikuletee chakula ule.” Nanaa akamwangalia tena, macho yakagongana. Mwili mzima wa Nanaa ulisisimka, yale macho yalipotua kwenye macho yake. “Wewe ulishakula?” Geb akauliza. “Tulikula na mama.” “Nitashukuru. Nimekuwa na kazi nyingi sana. Naona nikila, ndio nitaweza kulala vizuri.” Nanaa akafurahia moyoni. “Pole. Na kweli unaonekana umechoka.” “Asante.” Geb akajibu akiwa ametulia na mnyenyekevu kama sio yeye aliyekuwa akimsumbua Grace karibia juma zima. “Basi nisubiri nikakupashie moto chakula. Nitakuletea hapa hapa, pumzika tu.” “Asante.” Nanaa akatoka.

****************************************************

Bado Danny na mkewe walikuwa hapo sebleni. Kwa kutokumuuliza kitu, Nanaa akajua wanajua Geb yupo chumbani kwake. Akapasha chakula moto kwa haraka, kwa kutumia microwave. Akaweka kwenye trei. Wakati anataka kuweka na maji, mama yake akaja jikoni haraka. “Naomba muwekee na juisi.” Nanaa akacheka na kutingisha kichwa. “Unanicheka Nanaa? Sawa. Utazaa na wewe. Utaona tu.” “Kwani mimi nimesemaje mama?” Mama G alionyesha wazi amefurahi. Akachangamka kuongeza kwenye hilo sinia bakuli dogo la matunda. Kwa hiyo kukawa na mchemcho wa kuku na viazi, bakuli la matunda, glasi ya maji na juisi. “Asante Nanaa mwanangu.” Nanaa akacheka na kutoka.

****************************************************

Alimkuta Geb amejiegemeza kwenye kochi. “Unasinzia?” Nanaa akamuuliza. “Nahisi kuchoka. Sijapata muda mzuri wakupumzika. Nimekuwa na mambo mengi.” “Basi kula haraka, ukalale.” Geb mwenyewe alishavuta stuli karibu yake. Nanaa akaweka ile sinia. Akaanza kunywa juisi, akaja matunda, ndipo akala chakula huku Nanaa akimwangalia kwa kujiiba. Alionekana kweli ananjaa. Alikuwa akila kwa bidi zote utafikiri sio yeye aliyekuwa akimkatalia mama yake chakula.

****************************************************

“Tunaondoka alhamisi kwenda Marangu kama alivyokwambia Zinda. Wote tutaondoka. Kwa nini umekataa kuwa na sisi?” Geb alivunja ukimya wakati anamalizia chakula chake. Nanaa akanyamaza. “Mama ameniambia umekataa kwenda. Kwa nini?” Geb akarudia swali. “Nakumbuka nilikwambia Moshi na Arusha sio sehemu natamani kurudi Geb. Nakuwa ni kama najitonesha vidonda. Kumebeba historia ngumu sana ya maisha yangu.” “Pole Nanaa. Japo sifahamu ni kwa nini, lakini hudhani labda ni wakati wa kuandika historia mpya?” “Sidhani Geb. Kwa sasa sina historia mpya na nzuri ya kuandika kwenye ule mji.” “Utakuwa na sisi. Na tunakwenda kwenye sherehe. Hiyo pekee iwe sababu. Tutalala hotelini. Sio nyumbani kwa mtu. Tutakuwa na muda mtulivu wa kupumzika. Mbali na kazi na kelele za huu mji. Hufikirii chochote mbali na wewe tu. Nashauri twende wote. Utafurahia tu.” Kwa sauti ile ya utulivu. Na macho mazuri na laini ya Geb, hata kama ulitaka kusema hapana, mdomo utatamka ndiyo. Nanaa akanyamaza.

Akamaliza kula. Nanaa akatoa vyombo nje. Akavirudisha jikoni. Alibakisha maji ya kunywa akasema atayanywa baadaye. Nanaa alirudi kukaa pale pale, pembeni yake. “Twende wote bwana! Naamini tutakuwa na wakati mzuri sana.” Moyo wa Nanaa ulishalainika tokea zamani, ni vile tu alizuia jibu lake. “Eti Nanaa? Au basi niseme nakuomba twende pamoja.” Geb alikuwa akimtizama. “Tutakuwa na wakati mzuri.” Geb aliendelea kubembeleza. “Naomba usikatae kwanza. Angalau niambie utafikiria. Bado una siku kama tatu zakufikia maamuzi. Usinikatalie tafadhali.” Nanaa akacheka kidogo.  “Okay.” Geb akaweka kidole chake tena kwenye dimpo ya shavu la Nanaa, lile lililokuwa karibu yake kama akichezea kidogo tu. “Okay, unafikiria au umenikubalia?”  “Nitakwenda na nyinyi.” “Asante.” Geb alitabasamu akabaki akimwangalia.

“Nakuona umechoka Geb. Nenda kapumzike.” “Kweli nimechoka.” “Usiku mwema.” Sio kwa sauti ile kwa Geb. Nanaa aliongea naye vizuri, tayari akili zake zikawa zimeshatulia. Hasira zikaisha. Akajua kila kitu kinawezekana hapa duniani. “Asante na wewe, Nanaa.” Geb akasimama. “Unisalimie Mercy na Ben.” Nanaa akacheka. Akavuta kitabu chake cha Endless love, akarudisha macho kwenye kitabu huku amejawa furaha moyoni. 

Alifurahia uwepo wa Geb. Hata yeye alikuwa na hamu naye. Japokuwa hawakuwa wanapata muda mwingi wa pamoja, lakini alifurahia kila anapozungumza naye na kila anapomtizama yeye. Alicheka na kujishika shavu ambalo Geb aliweka kidole chake. Hiyo ni mara ya pili kufanya hivyo. ‘Anaonekana anapenda kuchezea dimpozi zangu.’ Nanaa alijiambia akiwa bado ameshika shavu lake. Akasimama na kuhamia kitandani. Akabaki akimuwaza Geb huku anatabasamu. ‘Liz amebahatika!’ Kidogo wivu ulimwingia. Akawaza kidogo, akapitiwa na usingizi.

****************************************************

v Kasoro Liz na Nanaa pekee ndio hawajua tatizo la Geb ni nini. Hasira, kujizira na kuamua kujiadhibu kwa kiasi kile. Mama yake ameshajua tulizo pekee analohitaji na kumuweka sawa mwanae latoka kwa Nanaa. Aamua kumuweka Karibu yake yeye ili asimpoteze katikati ya uwepo wa Liz kwa Geb. Mpaka lini? Je Nanaa ataendelea kuumizwa hivyo mpaka lini?

v ‘Hapana’ kwa kila mwanadamu, lakini si kwa Geb. Muda mfupi tu ulikuwa umepita tokea Nanaa aseme HAPANA kwa Zinda, lakini NDIYO ya haraka kwa Geb ambaye hakutoa ahadi nyingi kama Zinda. Japo hapakuwa na maongezi yeyote juu ya mapenzi kati yao, lakini faraja wanayojisikia kila wakiwa pamoja, ni Nanaa na Geb wenyewe ndio wanajua. Watafanyaje?

v Safari ya Marangu kule alikokataa kurudi Nanaa, sababu historia mbaya. Geb anaomba safari hii yeye awepo, pengine wataandika historia mpya. Watafanikiwa? Na Liz naye? Zinda je?



Usikose Muendelezo wa hadithi hii ya kila mtu anayetaka kumiliki…

0 comments: