Story

is mine - ni Wangu! Part 1, Sehemu ya 15.

Wednesday, July 25, 2018 naomimwakanyamale 0 Comments


B
aada ya simu ya Liz, hakuna aliyechangia neno. Ukimya ukaendelea. Fili naye “Naona safari inamlevya mwanangu. Analala tu. Eti Fili? Unausingizi?” Akatingisha kichwa kukubali. “Muone anavyorembua macho kama ya anko wake.” Grace akambusu mwanae. “Lala.” “Sasa huyo usiku tutakesha naye. Mwache aamke bwana.” Baba yake aliwageukia. “Mwache tu alale.” “Sasa na wewe mbona macho yapo kwenye simu muda wote?” “Danny!” “Nauliza mke wangu.” “Kuna watu nawasiliana nao.” Grace akajibu. Mumewe akatulia kidogo, akaanza kusinzia. 

“Kwa ujumbe?” Danny akageuka tena na kuuliza. “Nilijua tu hayajaisha. Ukoje Danny lakini?” “Si unijibu roho yangu itulie?” “Wala haiwezi kukutulia Danny. Mimi nakujua.” “Sasa kama unajua si heri unisaidie tu.” “Siwezi kuweka hii simu chini kwa kuwa ni mambo ya kikazi.” “Basi wapigie.” “Kelele Danny. Ni nini lakini?” “Unataka kunichanganya tu Grace mke wangu.” “Wewe usichanganyikiwe. Tulia tu, endelea kupiga stori na Geb.” Danny akatulia kama dakika tano. Kisha akageuka tena.

“Bado tu!?” Danny akauliza. Grace akanyamaza huku ameinamia simu yake. Danny akamuona kama anatabasamu huku anaandika kitu. “Grace?” Danny akaita. “Subiri kidogo Danny.” Grace akamjibu mumewe huku macho yapo kwenye simu na tabasamu usoni. Nanaa na Geb walikuwa wakiwasikiliza maongezi yao. Lakini wakawa kimya bila kuingilia.

“Mambo gani hayo ya kikazi mnazungumza mpaka unacheka!? Anakwambia nini?” Danny akauliza akisikika tayari amepaniki. “Grace?” Danny aliita tena. “Namalizia sasa hivi. Subiri kidogo nitakujibu.”  “Hapana. Naomba mimi nihamie nyuma. Simamisha gari Geb.” “Bwana wewe kaa huko huko mbele.”  Grace aliongea kwa upole huku macho yapo kwenye simu. “Hataa! Simamisha gari Geb. Sasa hivi. Hapa hapa. Nataka nikakae na mke wangu hapo nyuma, tutume wote hizo jumbe za kikazi.” Nanaa alikuwa anasikiliza.

Akasikia gari linawekwa pembeni ya barabara, akajifunua. “Nanaa, samahani sana. Naomba uje ukae hapa mbele. Mimi nataka nikae na mke wangu hapo nyuma.” “Hamna shida.” Nanaa akashuka. Akakaa mbele, Danny akamsogeza mtoto dirishani, Grace akakaa katikati kisha Danny dirishani. Safari ikaanza tena.

“Sasa mbona hutumi tena hizo jumbe?” Danny akamuuliza mkewe. “Simu hii hapa kaa nayo. Nilikuwa situmi ujumbe wowote. Nilitaka kukurusha tu roho ili uhamie tu hapa.” Nanaa alitamani kucheka lakini alikuwa na mshangao. Lakini Grace alikuwa anacheka. “Acha bwana Grace!” “Ukiwa mbali siwezi kulala Danny.” “Sasa si ungesema tu?” “Usingekuja kwa haraka kama hivi. Halafu Geb asingesimamisha gari kwa haraka. Ukiwa na hasira huwa anakusikiliza kwa haraka.” Bado Grace alikuwa anamcheka mumewe.

“Lala basi.” “Lakini ujue nimefurahi umekuja hapa.” “Aaah!” “Aaah nini sasa Danny mme wangu? Hapo ulipo ndio nitalala haraka sio vile ulivyokuwa mbali.” “Unapenda kunichanganya kweli Grace!” Danny alisikika ametulia kidogo. “Yaishe basi. Ngoja nilale kidogo. Nahisi kichwa kimejaa usingizi.” “Lala basi hapa.” Grace akamlalia mumewe mapajani, akalala. Danny hakuongea tena. Akanyamaza.

**************************************************

 “Mbona kama unatetemeka baridi?” Geb alimgeukia Nanaa akaona amejikunja na amekalia mikono yake. “Hapa mbele ni baridi zaidi.” Nanaa akajibu. “Basi funga hapo na pale ili upepo usitoke upande wako.” “Haitakusumbua wewe?” “Hapana. Upande wangu upo wazi. Napata upepo kama kawaida. Umekumbuka sweta?” Geb akauliza. “Nafikiri nimeweka kwenye begi.” “Tutaingia hapo Korogwe muda sio mrefu. Tutasimama tuangalie.” “Lakini nipo sawa. Hamna haja ya kusimama sababu hiyo.” Geb akamwangalia kidogo, akarudisha macho barabarani.

“Huchoki kuendesha?” Nanaa akauliza. “Sio kwa safari fupi kama hizi. Huwa tunaendesha na kina Danny, James na Zinda safari ndefu sana. Wakati mwingine mpaka Mwanza au Tabora nyumbani kwa kina Zinda. Na huwa napenda kuendesha mimi. Kidogo huwa wananisaidia. Lakini hapo Moshi ni karibu sana. Sihitaji msaada.” Nanaa akatulia.

Baada ya muda mfupi akaona kibao cha Korogwe, akajua wamefika Korogwe. Geb akaingiza gari karibu kabisa na stendi ya mabasi ya Korogwe. “Twende kule nyuma, tuangalie kwenye begi lako, tuone kama ulibeba sweta.” Geb alishuka Nanaa akafuata. Akavuta begi la Nanaa. Lilikuwa limewekwa yale maua kwa juu. Geb akayaangalia. Nanaa akamuona akiyatizama. Geb alijua wazi amemuona. Akamwangalia kidogo yeye na yale maua. Kisha akayaweka pembeni kwa uangalifu, na kumsogezea begi lake karibu. Akaangalia kwa haraka, hakulikuta. “Nitakuwa nimelisahau pale nilipokuwa nakunywa chai. Nitamwambia mama anijie nalo kesho.” “Basi kwa sasa hivi, ngoja nikupe langu.” “Hamna haja. Mimi nipo sawa tu.” Danny alikuwa ametulia kimya, akiwasikiliza. Geb akatoa sweta kwenye begi lake alipokuwa ameweka nguo zake, akamkabidhi. “Nimekuona unavyotetemeka baridi. Vaa hili sweta.” “Asante.” Nanaa akalipokea. 

“Rudi kwenye gari ukakae. Nitarudi baada ya muda mfupi tu.” Geb akaondoka. Alikwenda kwenye moja ya duka lililokuwepo ndani ya stendi. Akanunua kama viblangeti vitatu vidogo. Akarudi kwenye gari. Moja akamkabidhi Nanaa na Danny. “Mfunike huyo.” Akimaanisha dada yake. Jingine akatoa kwenye lailoni akamfunika Fili. Fili na mama yake walikuwa wamelala hawana habari. “Muone alivyolala kama mama yake. Hapo alipo hana hata habari ya tulipo. Usiku kucha alikuwa akituelezea jinsi atakavyopendeza kwenye harusi ya Malii. Kama yeye ndio bwana harusi!” Danny aliongea huku anamtizama mwanae. Geb akacheka. 

Akamuweka sawa pale kwenye kiti chake. “Na hicho kiti ulichomnunulia kitamfaa sana. Naona atakalia mpaka anunue gari yake.” Danny akaongeza. Wote wakacheka. “Na anakipenda kweli! Akikaa hapo anajiita King Fili.”  Geb na yeye akaongeza. Wote wakacheka mpaka Nanaa. “Fili kwa kujikubali mwanangu huyu! Sijui ni hivyo anavyodanganywa na mama yake kila mara?” Geb alimuweka sawa na kurudi upande wa dereva. Safari ikaanza tena.

Sababu ya kijijoto alichoanza kupata kutoka kwenye sweta na blangeti, akaanza kusinzia. Ni kama alivaa furaha ya ajabu. “Sweta la Geb!” Nanaa aliwaza huku akijishika. “Unataka kulala?” Geb akamuuliza. Nanaa akatingisha kichwa kukubali na tabasamu usoni. “Bonyeza hapo pembeni ili kiti kirudi nyuma. Ndio utalala vizuri.” Akafanya kama alivyoelekezwa. Hakuwa tena mbishi. Akafuata maelekezo. Kwa urahisi sana kile kiti kikajilaza. Akajiweka sawa. Alipitiwa na usingizi kama yupo kitandani. Na kwa kuwa kulikuwa kimya, akalala usingizi mzito sana. Geb aliwasha radio akawa anasikiliza miziki ya taratibu. Waliendesha kwa muda, Danny naye akisinzia huku amepakata kichwa cha mkewe.

**************************************************

Simu ya Geb ndio iliyowatoa usingizini. Japokuwa hakuna aliyezungumza chochote, lakini wote waliamka, wakabaki kimya. Geb akapokea simu yake. Nimefika.” Sauti ya Liz ilisikika. Pole na safari.” “Asante. Nakusubiri.” “Nashauri ushukue taksii ikulete Liz. Sisi ndio tunaingia Himo. Hoteli aliyopata Danny, au tuliyokubaliana wote tulale ni Marangu hoteli kama nilivyokwisha kukwambia. Sasa mpaka niwafikishe hawa huko Marangu, ndio nije mpaka huko KIA, utasubiri sana.” “Mbona kama unaonekana hutaki kuja?” “Unatafuta sababu ya kukasirika Liz. Nimejieleza vizuri tu, tena kifasaha. Muda wa mimi mpaka nije huko halafu turudi tena Marangu, utajichosha zaidi.” “Sio lazima turudi leo Marangu. Tunaweza kuchukua hoteli huku huku.” Liz akaongeza wazo la kibinafsi kama kawaida yake.

“Sidhani kama ni sawa Liz. Nafikiri nivizuri tuwe na wenzetu.” “Si tutawafuata kesho!? Tatizo liko wapi? Au kuna kingine hutaki kuniambia.” “Liz!” “Nini? Maana sikuelewi naona kama unanikwepa, Geb.” “Kwa nini nikukwepe? Kama ungetaka, ningewaomba hawa watu nilio nao hapa, tukufuate wewe ndio tuelekee Marangu.” “Tangia lini unataka kuomba ruhusa kwa watu? Gari yako na pesa ni zako. Huhitaji kuomba ruhusa kwa mtu.” Geb akanyamaza. Alijua kwa maongezi yale, hata walio lala watakuwa wameamka.

**************************************************

Nanaa hakutoka ndani ya lile blangeti alilokuwa amepewa na Geb. Akatulia kimya. Grace akakaa. “Nataka kukojoa, mama.” Fili alimgeukia mama yake. “Subiri anko asimamishe gari, nitakupeleka. Njaa inauma?” Fili alitingisha kichwa kukataa. “Nina hamu na wewe Fili. Mbona umelala sana mwanangu?” Grace aliongea na mwanae kwa upendo. “Unaumwa?” Fili akakataa. “Umechoka tu?” Fili akakubali. “Basi anko atasimamisha gari, dad atakupeleka chooni. Au unanitaka mimi?” “Nakutaka wewe mama.” “Haya. Basi tutaenda wote. Mbusu mama.” Fili akambusu mama yake. “Umefurahi?” Fili akamuuliza mama yake. Grace akacheka. “Sana. Nimefurahi mpaka moyoni.” “Basi baadaye nitakubusu tena.” “Asante mwanangu.” Wote walikuwa wakiwasikiliza.

**************************************************

 “We Geb!?” Wakasikia tena upande wa pili Liz anaita. “Naomba nikushauri Geb. Tushushe sisi hapa. Tutachukua taksii mpaka Marangu. Wewe kamfuate Liz huko KIA. Tutakutana huko na itakupunguzia shuguli. Halafu pia utawahi kurudi, wote mpumzike.” Grace alimaliza. Kimya. “Au unasemaje Danny?” Mkewe akamuuliza. “Naona ni wazo zuri na rahisi. Itakurahisishia Geb.” Kimya, wakaona Geb anatafuta mahali pakuegesha gari.

“Geb!” Liz akaita tena. “Chukua taksii. Mwambie dereva akulete mpaka Marangu hoteli. Nitalipa.” “Kwa hiyo hutaki kuja kunichukua?” “Nikija sasa hivi ujue nitakuwa na watu wengine kwenye gari. Ni sawa?” “Nitafanyaje sasa? Sitaki kupanda taksii. Kwanza sijui kama nitapata nzuri yenye hadhi na sijui kama nitapata dereva mwaminifu. Akiamua kunibaka je?” “Basi tunakuja.” Geb akakata simu.

**************************************************

 “Twende nikupeleke chooni.” Geb alimgeukia Fili baada ya kuegesha pembeni ya kimgahawa kidogo. “Namtaka mama.” “Mwanangu anahamu na mama yake. Twende baba.” Grace akamfungua mkanda. “Naombeni mnivumilie kidogo, nikamchukue Liz uwanja wa ndege.” Geb aliongea huku akimwangalia Danny na dada yake. “Hamna shida.” Wote walijibu kwa pamoja. Grace akashuka na mwanae, baada ya muda wakarudi. Safari ya KIA ikaanza.

**************************************************

Ukimya mkubwa ulizuka ndani ya gari. Ni Fili tu ndiye aliyekuwa anaimba nyimbo alizokuwa ameweka anko wake kwenye gari, mpaka wakafika KIA. Geb alishakuwa ameangalia kwenye simu yake umbali aliokuwepo hapo Himo mpaka uwanja wa ndege wa Kilimanjaro, akaona itamchukua lisaa limoja na dakika karibia 30. Akajua wazi anawachosha wasafiri wenzake, lakini hakuwa na jinsi.

Akasogeza gari mpaka sehemu alipoelekezwa na Liz. Akamuona amesimama na sanduku moja kubwa, linalofanana na mabegi madogo mawili. Geb akashuka kwenda kumpokea sanduku ili amsaidie kupakiza kwenye gari. Akachukua lile kubwa na begi jingine mkono wa kushoto, Liz akabeba lililobakia. Wakazunguka nyuma ya gari kupakia hiyo mizigo. “Mbona naona nafasi yangu imerithiwa?” Alihoji Liz wakati wanapandisha mizigo yake huko nyuma ya gari. “Nitanyanyua hivi viti vya nyuma nilivyolaza, tutapata tu nafasi.” “Ili nani ake nyuma!?” Liz akauliza kishari na kuongeza kibabe. “Kama ni mimi ujue sitakaa nyuma.” Geb akanyamaza.

Sweta la Geb, lazua hekaheka.

Kwa kuwa kila mtu alikuwa akiwasikiliza, Nanaa akavuta kiti alichokuwa amekilaza. Akakaa vizuri. Akaanza kukunja vitu vyote alivyokuwa amejifunikia navyo, akafungua mlango akakuta Liz ameshafika mlangoni anamsubiria atoke pale mbele. “Hee! Mbona kama hilo sweta nalifahamu!” Liz akahoji kwa mshtuko.  Nanaa akajiangalia. “Ameniazima Geb.” “Mmeanza lini kuvaliana nguo na Geb?” Akauliza tena. “Nimesahau sweta langu nyumbani, ndio akaniazima hili. Lakini naweza kulirudisha tu.” Nanaa akajibu kiustarabu.

“Nanaa! Hebu ingia ndani ya gari.” Grace aliingilia. “Pitia huu upande aliokuwepo Danny. Atakupisha, uruke nyuma. Geb amenyanyua kiti cha upande huo aliokaa Danny. Njoo.” Nanaa akampita Liz kwa tahadhari, akazunguka gari akapanda ndani.

Liz kabla ya kukaa pale alipokuwa amekaa Nanaa kiti cha mbele, akaanza kusafisha. Alikung’uta kwa muda. Kisha akachukua kitambaa cha jasho alichokuwa nacho. Kilikuwa kisafi kabisa. Cheupee. Akakilowesha maji kidogo aliyokuwa akinywa. Kutoka kwenye chupa ya maji ya Kilimanjaro, akaanza kupangusa kiti kizima. Wote walikuwa wametulia kwenye gari wakimsubiria asafishe hicho kiti alichokuwa amekalia Nanaa.

“Itabidi tukutolee taulo kabisa. Maana kabla yakukaa Nanaa hapo, nilikuwa nimekaa mimi.” Danny akarusha neno. “Hata hivyo nimemaliza. Naona inatosha tu.” Liz alijibu baada ya kutoa mtandio ambao ulikuwa kwenye kibegi kidogo alichokuwa ameshika mkononi pamoja na pochi yake, na kuendelea kufuta kile kiti. Geb alikuwa kimya kabisa akiangalia simu yake. Hakuongeza neno. Aliporidhika na ule usafi, ndipo akapanda na yeye. Safari yakuelekea Marangu ikaanza.  Na hapo tena waliongeza kama lisaa. Kutoka KIA mpaka Marangu hoteli. Yote hayo Geb alikuwa akiangalia kwenye simu yake. Akajua adhabu anayowapa wasafiri wenzake. Ukimya ukatanda.

**************************************************

Wakaendesha kama dakika 10 tu, Liz akaanza. “Sasa kama na mimi nikipatwa baridi, utafanyaje?” Liz akamuuliza Geb. “Na wewe umesahau sweta lako?” Geb akamuuliza taratibu tu. “Mbona swali juu ya swali?” Geb akamtizama Liz kidogo, akarudisha macho barabarani. “Kwamba unanipuuza au?” Liz akauliza tena. “Endapo ukisikia baridi, na sweta lako halitatosha, tutajua kitu chakufanya wakati huo. Ila kwa kuwa sasa hivi upo sawa, naomba tutulie tu.” “Umejuaje kama sasa hivi sisikii baridi? Kwani Nanaa alikwambia anasikia baridi ndio ukampa sweta au uliona anasikia baridi ndio ukampa sweta? Eti Nanaa?” Liz alimgeukia Nanaa aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma ya Danny.

“Kwa nini unafanya hivyo Liz?” “Nini Grace? Kwa nini asivae sweta la Danny, avae la Geb?” Kimya. “Umeona eeh! Nina haki ya kuhoji mimi kama mpenzi wa Geb. Sijawahi kuja pale nyumbani nikamkuta Nanaa amevaa hata t-shert ya Danny. Iweje leo avae nguo za Geb!? Au basi angalau angevaa sweta lako wewe sio Geb.” “Unanijua mimi huwa siwezi kuongea sana kama wewe Liz. Ila naomba kuwe na amani. Kwanza sweta lenyewe Nanaa alishalivua. Kwa nini unaendeleza maneno unayojua yataondoa amani? Naomba yaishe. Kama ni kosa, basi samehe. Kuwe na amani. Wote tumeshaelewa kuwa hupendi nguo za Geb zivaliwe na mtu mwingine, basi, hakuna atakaye rudia tena.” Grace akaongeza kwa upole kabisa.

“Kama huwezi kuongea mbona umeongea maneno yote hayo? Kilichokushinda kujibu swali langu ni nini?” “Mimi sioni shida yeyote Liz. Hata sasa hivi Danny akitaka kumpa sweta au Nanaa akisema anasikia baridi, na sweta la Danny lipo karibu, tutampa tu. Sioni sababu ya mtu kuteseka na baridi wakati nguo zipo.” “Unaongea tu.” Liz akapinga. “Ni sweta tu Liz. Tafadhali tunaomba yaishe, kuwe na amani. Tunachotaka ni amani. Basi.” “Hata mimi nataka amani na kuwe na mipaka. Kila mtu ajue nafasi yake. Tusiingiliane.” “Sawa Liz, tumeelewa.” Grace alijibu kwa ustaarabu.


**************************************************

Hapakuwa na maongezi yeyote. Liz akaanza kubadili miziki humo ndani ya gari. Mara aweke huu, atoe. Mara azime redio ya gari, awashe miziki iliyokuwepo kwenye simu yake. Ilimradi wote walijua mmiliki wa Geb yuko pale. Akafanya hivyo bila kuongeleshwa na mtu, mpaka walipofika Marangu hoteli. Walikuta wenzao walishafika wamekaa kama kundi wakipiga stori. Vicheko vilikuwa vimetawala.

Walisalimiana, wakaelekea mapokezi. Danny alikuwa amechukua vyumba vitatu. Viwili double, na single kimoja. Nanaa na bibi Fili chumba chao. Danny na familia yake chumba chao na hicho single cha Geb na Liz. Wakapewa funguo kila mmoja akaelekea chumbani kwake kwa makubaliano wasikae sana vyumbani, watoke ili waungane na wenzao kwa chakula cha mchana.


Marangu Hotel.

Mwili mzima wa Nanaa ulikuwa ukitetemeka. Akaingia chumbani kwake, akajitupa kitandani. “Hivi ni kwa nini nilikubali kuja na kuvaa sweta la watu!?”  Nanaa akaanza kujutia. “Nimedhalilikaje!? Aibu gani hii niliyoingia!” Nanaa aliendelea kujisikitikia. 

Baada ya muda Grace akagonga. “Twende tukale.” “Naomba mimi nilale tu. Nitakula chakula cha usiku. Tafadhali Grace.” “Unauhakika? Naweza kukuletea huku huku ndani?” “Hapana. Hata kaka James nimemjibu hivyo hivyo. Ametoka kunipigia simu sasa hivi. Nataka kulala tu. Labda usiku ndio nitaweza kuungana na nyinyi. Tafadhali Grace, naomba uniache tu.” Grace alimpa tabasamu la upole kama kuelewa anachoongea. “Sawa. Lakini usiku lazima utoke. Usijifungie humu ndani peke yako.” “Sawa.” Grace akatoka.

**************************************************

Baada ya muda tena kidogo, akasikia tena mlango unagongwa. Akasimama na kwenda kufungua. Alipofungua tu na kumuona Geb, akafunga kwa haraka sana. “Nanaa!” Geb alianza kuita kwa upole huku akigonga taratibu, lakini Nanaa hakufungua. Akagonga kama mara mbili, Nanaa hakufungua. “Nanaa!” Kimya. Nanaa alibaki amesimama pale pale nyuma ya ule mlango akimsikia Geb akiita lakini hakutaka kufungua mlango. Nikitendo alichokifanya kwa haraka bila hata kufikiria.

 Walisimama pale mlangoni kwa muda. Geb akiwa kimya nje ya mlango, Nanaa ndani, nyuma ya mlango mapigo ya moyo yakienda kasi huku akilia taratibu. Geb alimsikia anavyolia kwa sauti ya chini. Akajaribu kufungua mlango, lakini Nanaa akawa amefunga kwa ndani. Walisimama pale kwa muda mwishowe akamsikia Geb anaondoka, ndipo na yeye akarudi kujilaza kitandani huku machozi yakiendelea kumtoka. Alilia asijue kinachomliza. Kitu kilimkaba kooni akabaki akilia pale kitandani mpaka alipopitiwa na usingizi.

Usiku wa Kwanza walipofika Marangu.

Aliamka ilishakuwa giza kabisa nje. Akaangalia saa ya kwenye simu yake, akakuta missed call mbili kutoka kwa kaka yake. Akampigia. “Nilikuwa nimelala kaka.” “Uje kula.” “Sisikii njaa kabisa, kaka.” “Basi njoo tu tukae wote.” “Nilikuwa nafikiria labda leo nipumzike tu.” “Hapana. Njoo tuwe wote. Hatujaonana zaidi ya week sasa! Huna hamu na mimi?” Nanaa akacheka. “Nakusubiri. Njoo nikupe habari zilizojiri mjini.” “Haya. Nakuja kaka yangu.” Nanaa akaogoa haraka haraka, akatoka.


******************************************************

Hakupata shida kujua walipo, kwani walikuwa na kelele kupita kiasi. Hoteli nzima zilisikika kelele za kina kaka hao wakicheka na kutaniana. Nanaa akasogea mpaka walipokuwepo. Akaangaza macho akamuona alipokuwa amekaa kaka yake, akamsogelea. “Nitakaa wapi sasa?” Nanaa akamuuliza kaka yake James kwa sauti ya chini kidogo, kumbe akasikika. “Kaa hapa kwenye kiti changu. Mimi nitaenda kuchukua kingine.” Zinda akiwa amelewa sana akajibu yeye. “Tafadhali sana Nanaa, mama watoto wangu. Kalia kiti hiki roho yangu itulie.” Watu wakaanza kucheka.

“Zinda! Zindaa!” Mmoja wa rafiki zao alimwita. “Mwimbie basi Nanaa ule wimbo uliokuwa ukituimbia.” “Nimeutunga maalumu kwa ajili yako mama watoto wangu.” Nanaa akakaa kwenye kiti alicholetewa na Zinda. Pembeni ya kaka yake. “Kila neno ndani ya huu wimbo ni lako mpenzi Nanaa. Nimetunga kwa ajili yako. Ni wewe mpenzi nikupendae. Sinywi wala kula….” “Mimi hapo ndipo anaponichosha Zinda. Maneno mengiiii. Mpaka unaharibu. Sasa kama hunywi wala kula, umelewaje na una mfupa wa nyama hapo mkononi? Wewe ungeimba tu, yakaisha. Umeharibu kila kitu. Na hakuna kuimba tena. Ukiimba tu tunakubeba na kwenda kukufungia chumbani kwako. Hatutaki umdanganye Nanaa.” Danny alimkata Zinda na kufanya watu wazidi kucheka.

“Sikudanganyi Nanaa.” “Sasa umelewaje? Na mfupa huo wa nyama ya mbuzi umefikaje mkononi mwako?” “Kwanza sijalewa. Pili huu mfupa sio wangu. Wa Malii.” Akaurusha kwa Malii. Watu walizidi kucheka.  Nanaa alibaki ameinama. “Nanaa! Nanaa!” Nanaa akamwangalia Zinda. “Nakupenda sana Nanaa.” “Asante Zinda.” “Sauti mimi jamani! Sauti ya Nanaa!” Zinda alilalamika kilevi nakufanya watu wazidi kucheka.

“Zinda! Ulisema unataka kufanya nini na sauti ya Nanaa?” Gozi alimuuliza kishabiki. “Nataka kuimiliki mpaka kifo changu. Nishaongea na James. Katika mahari watakayonitajia nilipe, nitaongeza nusu yake kwa ajili ya sauti ya Nanaa. Hiyo sauti nilazima nitalipia. Halafu nitamrikodi wakati ananiita jina langu. Niweke kama ringtone yangu.” Watu walizidi kucheka. “Yaani nyinyi mnanipigia mimi simu, basi mwenzenu naitwa jina langu na Nanaa. Zinda! Zindaa!” Nanaa aliinama huku anacheka kwa aibu. Pombe zilikuwa zikimsaidia sana Zinda. Alikuwa akiongea bila shida.

**************************************************

 Muhudumu akamsogelea Nanaa. “Nimeambiwa nikuulize unataka kula nini?” Nanaa akajua ni Geb tu. Alishindwa kukataa. Njaa ilishaanza kumuuma. “Kwani kuna chakula gani?” Kulikuwa na kelele, Nanaa akashindwa kumsikia. Yule muhudumu akarudia tena na tena lakini Nanaa alipata shida kumsikia na kufikiria ili kutoa maamuzi. “Naomba tuongozane mpaka jikoni. Nione mlichonacho labda nitaweza kuchagua.” Akasimama na kuongozana na yule muhudumu. Akafika jikoni, akapata kitu ambacho aliona anaweza kula wakati ule. Akaweka oda.

Wakati anarudi akiwa mbali kidogo na lilipokuwepo lile kundi la watu wengine, akamuona Geb akimjia. Akasimama na kuinama. Geb akamsogelea mpaka karibu yake, akamfunika tena na lile lile sweta. Lilikuwa la vifungo mbele. “Sihitaji tena sweta. Asante.” Nanaa akalitoa mwilini mwake. “Sasa hivi unaweza usione umuhimu wake, lakini unaweza kupatwa vichomi. Nimekuona vile ulivyokuwa umekaa pale, umejikunyata. Unasikia baridi Nanaa. Vaa hili sweta.” Geb akalirudisha tena mwilini kwa Nanaa. Akalizungusha juu ya mabega yake. “Mimi sitaki tena sweta lako Geb. Nikizidiwa na baridi nitajifunika mtandio wangu.” Machozi yalianza kumtoka Nanaa. Akalitoa lile sweta mabegani akalishika mkononi huku anajifuta machozi. 

“Naomba uvae hili sweta, halafu ndio ujifunike mtandio na kile kiblangeti nilichokununulia ili usiingiwe na baridi.” Geb akalichukua tena kutoka mkononi mwake. “Naomba mkono wako wa kushoto.” Nanaa akabaki ameinama akifikiria. “Nanaa!” Nanaa akaona avae yaishe, kwani Geb alishazunguka nyuma yake. Akaingiza mkono wake wa kushoto kwenye lile sweta alilokuwa ameshikilia Geb, akamvalisha na mkono wa kulia, akazunguka mbele akaanza kumfunga kifungo cha kwanza mpaka cha mwisho huku Nanaa akifuta machozi. Akalitengeneza kidogo mabegani kwake. Akaridhika.

“Afadhali hivyo. Hapo sasa hata ukiongezea na mtandio juu itakuwa afadhali.” Geb aliongea huku macho yakiwa kwenye sweta alilovaa Nanaa. Nanaa akajifuta tena machozi. “Asante.” Nanaa akashukuru kwa upole. “Karibu. Umepata chakula?” Geb akamuuliza, Nanaa akatingisha kichwa kukubali. “Umekipenda?” Nanaa akabaki kimya huku ameinama kama anayefikiria. “Kama haujakipenda, tunaweza kutafuta chakula kingine nje ya hapa.” “Nimekipenda. Umepata muda wa kupumzika?” Nanaa akauliza kwa upole huku akimwangalia. “Nitalala baadaye.” Geb akajibu.

Alionekana amechoka. “Umeshakula?” Nanaa akamuuliza tena. “Bado.” Geb alijibu huku akimwangalia. “Naomba uenda ukale.” Geb alibaki akimwangalia. “Vipo vyakula vingi. Mama alikutayarishia leo asubuhi. Hutakosa kitu cha kula. Naomba usilale bila kula.” Nanaa aliongea kwa sauti ya kubembeleza.

Wakagundua lile eneo zima lipo kimya. Zile kelele za wale marafiki zimeisha. Nanaa akageuka kuwaangalia ili kujua kulikoni. Akagundua macho ya watu wote yanawatizama wao. Geb alikuwa ametulia tu. Akawaangalia na yeye, akarudisha macho kwa Nanaa. Nanaa alikuwa ameinama. “Mimi nitakula. Nenda kakae watakuletea chakula chako.” “Naogopa Geb. Nimeingiwa na hofu. Najuta kwa nini nimekuja.” Nanaa alijikuta akiongea huku machozi yakimtoka. “Pole. Lakina huna haja yakuogopa, Nanaa. Leo ni alhamisi, tuna siku 3 mbele. Jumamosi ndio sendoff yenyewe. Jumapili tutaenda kuzunguka kidogo Arusha. Tutatafuta hoteli nzuri yakupumzika. Naamini utafurahia. Halafu jumatatu baada ya kifungua kinywa ndio tutarudi Dar. Naomba utulie, na ujiwekee akili yakutarajia wakati mzuri. Nina uhakika utafurahia tu. Sawa?” Nanaa alivuta pumzi kwa nguvu.

**************************************************

Akatamani asirudi tena pale, arudi chumbani kwake tu, kwani macho ya watu wote bado yalikuwa yakiwatizama wao. Lakini akakumbuka kaka yake alimwita. Anarudije tena pale? Anamwangaliaje tena Liz aliyelalamikia sweta lake halafu ameshuhudia Geb akimvalisha!? “Sasa kwa nini anivalishe tena wakati mpenzi wake alimkataza?” Nanaa akajiuliza, akamwangalia Geb, bado alikuwa akimtizama. 

**************************************************

 “Nanaa!” “Abee.”  Nanaa akaitika. “Naomba nikuombe kitu kabla hujarudi kukaa.” Nanaa alibaki akimtizama. “Ni sawa?” “Nakusikiliza Geb!” “Naomba siku nyingine usinifungie mlango nje.” Nanaa alijisikia vibaya sana. Geb aliongea kiustarabu akiwa ametulia. “Samahani.” Geb alibaki akimtizama na macho yaliyokuwa yakimchanganya Nanaa. “Sitakufungia tena mlango nje.” “Asante.” Maongezi hayo Geb aliyaendeleza wakiwa wamesimama karibu sana na Nanaa, na bado watu wengine waliwatizama na wengine waliinama. Hapakuwa na mazingira ya kaka na mdogo wake pale. Geb alisimama na Nanaa wakiongeleshana kwa upendo wa namna yake. 

**************************************************

Hisia zilizokuwepo ndani mwao ni wao wenyewe walizijua. Mazingira yote hayakuwa yakiwaruhusu, lakini kila mmoja wao alishindwa kujizuia. Bado Nanaa alitaka kumuona Geb amepumzika na kula vizuri. Na Geb bado aliweza kumuweka Nanaa mbele hata pale alipojua atazua maswali mengi. Anachojisikia Nanaa kwa Geb, hakuwahi kusikia maishani kwake kabla. Asijue kama ni mapenzi au upendo kwa baba mwenye nyumba wake. Au anamsaidia shoga yake mama G kumlea kiziwanda wake. Lakini alishindwa kujizuia. Akajikuta anafanya kile roho yake inamsukuma. Hata pale wengine walipokuwa haelewi, anawezaje!

**************************************************

Muhudumu alipita na chakula akielekea kule lilipokundi la marafiki. “Twende ukale.” Hakuwa hata anajua alipokuwa amekaa Geb. Hakuwa amemuona hata Grace na mumewe ila sauti ya Danny tu. “Twende.” Nanaa alibaki ameinama kama anawaza. “Nanaa!” “Labda nikale chakula changu chumbani.” “Hapana Nanaa. Twende. James alikuita. Unakumbuka?” Nanaa alitingisha kichwa kukubali. “Basi twende.” Geb alitangulia, Nanaa akamfuata nyuma mpaka pale mezani. Geb akavuta kiti pembeni ya James. “Njoo ukae hapa.” Nanaa akaenda kukaa, akainama. Watu wote walikuwa bado kimya. Geb hakuonekana kuwa na wasiwasi wowote usoni.

Geb akaondoka na kurudi kukaa pembeni ya Liz. “Kula chakula chako kisipoe.” James akavunja ukimya. Akamsogezea dada yake kile chakula. “Wewe umeshakula?” Nanaa akamuuliza kaka yake. “Tokea tunafika hapa, tulikuwa tunakula nyama choma. Hapa tumbo limejaa. Kula.” Bado watu walikuwa kimya. Hakuna aliyekuwa akiongea. Ilimlazimu Nanaa kula, kwa kuwa ndicho alichoambiwa na Geb na kaka yake. Lakini chakula kilishakosa ladha kabisa. Ni kama alikuwa akitafuna makapi.

Liz azua ugomvi mwingine.

“Unajua uliponiambia Nanaa anaishi pale kwako. Nikashtuka sana. Nikakuuliza iweje atoke kwa kaka yake, aje aishi pale nyumbani kwako? Ukanijibu James amemuombea aishi na nyinyi pale kwa muda tu, wakati anamtafutia kwake. Hilo nikalinyamazia japo naona siku zinazidi kwenda tu, na yeye yupo pale pale kwako hana hata dalili yakuondoka.” Liz akaendelea. Kila mtu alikuwa akimsikiliza. Kwani alijitahidi kuzungumza kwa sauti ya kusikika. Na ule ukimya uliokwisha kuwepo, kila neno lake lilisikika vizuri tu.

“Zinda akaja siku ile nyumbani kwako, akamuomba Nanaa aje huku kwenye sendoff kama mtu wake, Nanaa akakataa. Nashangaa jana nakuuliza watu tutakao kuwa nao safarini, ukanitajia na Nanaa atakuwepo. Nikashangaa zaidi. Nikajiuliza mara mbili mbili. Nanaa alishakataa kuja huku. Na Grace aliniambia Nanaa amekataa kuja huku kwa kuwa hata Malii mwenyewe hanamahusiano naye au hawafahamiani. Sijui. But something like that. Lakini ameamua kubaki tu. Nikaona ina make sense. Lakini leo yuko hapa. Sasa alikataa nini na amekubali nini? Kwa nani na kwa nini?” Liz akaendelea. 

“Maana naona wewe ndiye unahangaika naye kupita kiasi. Kila mtu anajua mimi ni mtu wako. Zinda ametangaza kumtaka Nanaa, tena kwa ndoa. Leo wewe unaniacha mimi hapa nikiwa nimekaa, unaenda kumvalisha sweta Nanaa!! Tena nikiwa nimeshakukataza njiani wakati tunatokea uwanja wa ndege. Tena Grace akaongeza kwa sauti kuwa ameelewa kuwa sitaki mtu avae nguo zako. Na akasema Nanaa alishalivua sweta lako. Sasa nisikilize Geb. Tusipotezeane muda wala kunyimana raha. Tuambie kama Nanaa ndiye mwanamke wako, mimi na Zinda tuwaache.” Geb alitabasamu akamwangalia Liz. Alishakasirika kupita kiasi.

“Usiniangalie kwa dharau Geb. Nimeuliza swali. Tena vizuri tu. Kwa niaba yangu na Zinda, naomba ujibu.” Liz akaona aongeze nguvu kwa kumtaja Zinda. “Umeshatangaza hapa kama tunaishi na Nanaa. Ni kweli James ametukabidhi dada yake. Tayari Nanaa amefanyika mmoja wa familia yetu. Na nyinyi wote mnajua jinsi tunavyoishi. Kila kitu tunafanya pamoja, kitu kilichokushinda wewe Liz. Kawaida yetu sisi ni kufungua mlango kwa kila anayetusogelea. Ilikuwa lazima kuja huku na Nanaa. Siwezi kuwa na amani eti sisi tupo huku tunastarehe, halafu tumemfungia Nanaa nyumbani na walinzi! Ilikuwa ni heri hata niahirishe safari nisije, kuliko kumuacha Nanaa pale nyumbani peke yake. Kwa hiyo ilinilazimu kumsihi yeye aje na sisi ili na mimi niweze kuwepo hapa na Malii. Hilo ni moja.” “Ulazima wa yeye kuwepo hapa ni upi?” Liz akauliza tena. 

“Naomba nimalize kuzungumza Liz. Umeuliza maswali ya kiuchonganishi mbele za watu ukitaka kuendeleza ugomvi. Sasa naomba nikujibu bila kuniingilia. Kwa kuwa unanijua siwezi kubishana, na siwezi kupigishana kelele. Sikiliza majibu yangu mpaka mwisho. Si lazima majibu yangu yalete maana kwako na wengineo, lakini najibu kutokana na kile ulichouliza.” Watu wote walikuwa kimya.

Grace akajua Geb alishakasirika. “Swala la sweta. Nanaa amesahau sweta lake nyumbani. Tumegundua hilo tukiwa njiani tena wote wakiwa wamelala, kasoro mimi niliyekuwa dereva na Nanaa ambaye ilimbidi kumpisha Danny, aende nyuma, Nanaa aje kukaa mbele. Kwa kuwa Grace alitaka kulala kwenye miguu ya mumewe. Ikabidi kubadilishana. Nanaa alipokuja mbele, baridi ilimshinda. Ikabidi kusimamisha gari ili akaangalie sweta lake kwenye begi lake. Ndipo akagundua amelisahau nyumbani. Ikabidi nimpe sweta langu, kwa kuwa kwanza sikuwa nikilitumia.” Geb akaendelea.

“Pili sikuona sababu yakuanza kumuamsha Grace kumuomba sweta ambalo hata sikujua kama na yeye alibeba au la. Tumekuja kukufuata wewe kule KIA, ukaanza maneno mengi yaliyomuogopesha Nanaa. Kuepusha ugomvi, akaamua kulivua na kuniachia pale kwenye gari. Kwa sasa James haishi na Nanaa. Mimi, Grace, Danny na Mama, tunahusika na Nanaa kwa asilimia zote. Sweta la Nanaa anakuja nalo mama kesho. Siwezi kumuacha Nanaa anateseka na baridi hapa, eti kwa sababu anakuogopa wewe! Hata kidogo Liz. Nitafanya kile ninachojua na kuelewa ni sahihi. Bila hila wala kificho.” Geb alijibu kifasaha, taratibu tu.

“Kwa hiyo sio kwamba ni mapenzi ndiyo yamekupelekea hivyo?” “Unataka kusikia nini kutoka kwangu, Liz?” “Hilo ni swali la jibu la ndiyo au hapana.” “Nimeongea kwa muda mrefu sana, Liz. Na wote mnajua sio kawaida yangu. Nimejieleza kupita kawaida yangu. Kwa heshima yako na Zinda. Kama mpaka hapo haujaelewa, hata nikirudia, hutanielewa tena. Naomba niishie hapo.” Geb akanyamaza.

“Na mimi nasikia baridi.” Liz akaendelea. “Ngoja nikakuletee sweta na kitu chakujifunika.” Geb akasimama na kuondoka kurudi chumbani kwao. Baada ya muda akarejea na sweta la Liz na mtandio wake. Akamvalisha taratibu, roho ikamtulia Liz. “Unacheka nini sasa?” Wakamsikia Geb anamuuliza Liz. “Nimefurahi.” Geb akamfunga vizuri, akamfunika na ule mtandio, akampitishia mkono juu yake kama kumkumbatia kwa mkono mmoja. Akaanza kumsugua viganja vyake kwa mkono wake mwingine. “Asante.” Liz alisikika akishukuru kwa sauti tulivu. Kidogo pakapoa.

**************************************************

Ukaanza utani wa muda. Angalau watu wakasahau. “Mimi naenda kulala, kaka.” Nanaa alimnong’oneza kaka yake. “Mbona mapema?” “Najisikia kuchoka. Nataka kupumzika. Labda kesho nitajisikia vizuri.” “Haya. Usiku mwema.” “Asante kaka, na wewe pia.” Nanaa akasimama. “Unaenda kulala, mama watoto?” Zinda alimuwahi Nanaa kabla ya kuondoka. “Ndiyo Zinda.” “Mbona mapema, mamaa?” “Nimechoka. Nataka nikapumzike.” “Basi naomba nikusindikize.” Zinda aliongeza. Nanaa akacheka kidogo. “Nitashukuru.” Watu wakaanza kushangilia.

“Siamini mwenzenu. Naweza nisirudi kabisa.” Watu walizidi kucheka. “Utaenda wapi?” “Nanaa anaweza kunihurumia akaamua anibembeleze nilale kabisaa.” “Ukichelewa hata dakika moja, nakufuata Zinda.” “Nakutania James na wewe. Mbona mkali hivyo kwa dada yako? Namsindikiza tu narudi.” “Hata ndani usiingie.” “James naye! Nikikaribishwa ndani je?” “Basi baki hapa.” “Siingii bwana James. Acha roho ya kwa nini!” “Na urudi Zinda. Sio uende kumng’ang’ania Nanaa. Akiniambia ulimfanyia fujo tu, au hata ulimuomba uingie ndani, nakutoa meno ya mbele na sitanii.” “James kwa mdogo wake! Ubinadamu unamwisha kabisa! Sasa mimi si nitakuwa shemeji yako?” “Wewe msindikize, urudi.” “Sawa mkuu.” Zinda na Nanaa wakaondoka.


Nanaa kwa Zinda.

“Zindaa!” Nanaa akamwita wakati wakitembea. “Niambie Nanaa.” “Najua umelewa sana. Unafikiri nikikwambia kitu leo, kesho utakikumbuka?” “Kabisa. Sijalewa kiasi chakushindwa kukuelewa.” Nanaa akamwangalia. “Kweli Nanaa. Sijanywa sana.” “Basi naomba tukae kidogo tuzungumze.” Wakatafuta mahali wakakaa.

“Naomba nikushukuru kwa heshima unayotaka kunipa. Kwangu sio kitu kidogo. Najua unafahamu kuwa mimi ni kama yatima. Ndugu niliyenaye ni kaka James tu. Nisipokuwa kwenye maisha ya kaka James, mimi sina tofauti na mtoto wa mtaani. Kama ulivyosikia nikitangazwa pale mbele za watu, kaka amekosa pa kuniweka kwa sasa, ameniombea niishi kwa muda nyumbani kwa Geb. Sifurahii hata kidogo haya maisha Zinda. Naumia kuona nakuwa mzigo kwenye maisha ya watu. Zaidi mvunja amani. Sijui kesho yangu ikoje au inafananaje? Sijui kesho nitakuwa wapi. Sijui kaka ataamua kunihamishia wapi na kwa nani.” Nanaa akaendelea.

“Ni maisha ambayo hayana utulivu hata kidogo. Si akilini tu, hata moyoni. Sijui ni nini nataka. Nimefanya makosa mengi sana kwa kukubali wanaume wengi sana ili wanitoe kwenye hii hali. Ungekuja miezi michache nyuma, ningekukubalia kwa haraka sana. Kwa kuwa nilikuwa natafuta mtu wakuninusuru kwenye hii hali. Bila kujali hisia zangu kabisa. Nimegundua sijitendei haki na wala sitakutendea wewe haki endapo nitakukubali sasa hivi. Akili, mawazo na hali yangu ya maisha, vyote vinataka kusema ndiyo kwako. Tena nikung’ang’anie hata kesho unioe. Lakini nimekusudia kutofanya tena, ‘permanent decision, for temporary situation’. Najua ipo siku nitatulia. Nitaweza kuruhusu hisia zangu kupenda kwa dhati.” Nanaa akatulia kidogo.

Kisha akaendelea. “Nitaumia sana kukukubali sasa hivi wakati ninashida. Sijafikiria. Unipe magauni na viatu. Nyumba na gari, halafu mwili ukishapata hivyo vyote, nafsi ije igundue haikupendi. Haitakuwa sawa kwako, Zinda. Naomba nikupe jibu la bila kukupotezea muda, mimi siye mke wako. Siye mwanamke unayetaka kuniweka ndani sasa hivi. Nitakuumiza Zinda na wewe unaonekana ni mtu mzuri sana. Sijui umenielewa?” “Nimekuelewa Nanaa. Naweza kukusuburi? Sio lazima tuoane kesho. Ila naomba tuwe hata kwenye mahusiano.” Zinda huyu siye yule aliyekuwa akifanya mizaa. Alitulia kabisa.

“Nikwambie ukweli Zinda? Ukweli usio na kificho. Kichwa changu chenyewe hakina mahusiano hata na mwili wake. Siwezi kukupa kitu ambacho sina Zinda. Hapana. Naomba wala usinisubiri. Sipo kwenye nafasi ya kuongeza mtu mwingine au kitu kingine kwenye maisha yangu kwa sasa. Akili zimevurugika. Tafadhali naomba unielewe.” “Daah! Sawa Nanaa. Lakini afadhali nimejaribu. Nakushukuru kwa kuwa muwazi kwangu.” “Asante Zinda. Basi naomba mimi nikapumzike.” “Usiku mwema. Tutaonana kesho.” “Asante na wewe.” Zinda akaondoka.

******************************************************

Nanaa akavuta pumzi kwa nguvu, akatoa simu yake akamtumia ujumbe kaka yake. Akamuomba afike chumbani kwake. James alipopata tu ule ujumbe, akasimama. Akamuona Zinda amerudi amenywea kama sio yeye. “Mzima kaka?” “Mzima kabisa. Wapi tena?” Zinda alimuuliza James. “Naenda kuzungumza na Nanaa.” Wote walimuona Zinda vile alivyorudi kwa upole. Alivuta kiti akakaa, bila kuongeza neno. Watu wakabaki wakimtizama. Zinda yule aliyekuwa na maneno mengi ya kilevi sie huyu. Kumbe walevi huwa wanaelewa! Nawaza kwa sauti tu.

“Mbona umekaa gizani peke yako?” “Nakusubiri tuingie ndani tuzungumze.” Nanaa akafungua mlango wakaingia na kaka yake. “Vipi mbona kama unalia?” “Nachukia maisha yangu kaka. Nachukia hivi nilivyo.” “Usilie basi. Acha tuongee. Pole.” “Sifurahii hivi ninavyozungumziwa mbele za watu. Nakuwa mtu wakutangazwa naishi wapi, nasaidiwa na nani! Hapa pameshaleta shida kaka. Hapatakuwa na amani tena. Nataka kuondoka nirudi Dar, nikaangalie vyumba. Nianze kujitegemea. Inatosha kaka yangu.” “Uondoke kabla ya shuguli iliyotuleta hapa!?” James akauliza.

“Liz yupo sahihi. Uwepo wangu hapa hauongezi chochote. Kwa nini niwepo hapa? Tayari Liz amekuwa na wasiwasi na mimi kaka. Siwezi kusema mengi juu yake kwangu, kwa kuwa akili yangu haijatulia. Lakini kwa maneno aliyokuwa akiongea hata jana nyumbani na leo njiani, naonekana nimeshakuwa tatizo tena hapa. Sitaki kuishi kwa kusumbua watu. Hawa watu nimewakuta wana amani na utulivu. Naomba mimi nisiwe sababu.” Huwa akili ya James inaacha kufanya kazi pale anapomuona dada yake huyo analia.

“Utarudije Dar peke yako?” “Kumbuka haya maeneo mimi ni mwenyeji kaka. Napafahamu vizuri. Nimesoma hapo Ashira Sekondary. Nitafika tu Dar. Nitaondoka mapema ili nimuwahi dalali, nizunguke kabla giza halijaingia.” James alibaki kimya kwa muda. 

“Kaka!” Nanaa alimshtua kaka yake. James alishapotelea mawazoni. “Sawa Nanaa. Lakini sipendi hivi unavyohangaika.” “Ipo siku nitatulia kaka yangu. Naamini hivyo. Acha nihangaike nipate kwangu. Sitaki tena kuishi kwenye majumba ya watu. Najiumiza tu.” “Nakuelewa. Unayo nauli sasa?” “Nina pesa kaka yangu. Wala usiwe na wasiwasi.” “Basi nitazungumza na kina Geb. Nitawaambia mimi ndio nimeamua urudi Dar. Lakini sasa hivi naomba usilie kabisa. Tumeshafikiria chakufanya. Tutafute sehemu yako. Huna haja yakulia. Tulia ili uweze kulala vizuri.” Nanaa akatulia. Akajifuta machozi kabisa. 

“Asante sana kaka yangu. Nakushukuru. Lakini ujue nitaondoka alfajiri sana. Nitaondoka na mabasi ya saa 11, ili nifike Dar mapema.” “Nitakuja kukusindikiza.” “Sitaki kukusumbua itakuwa mapema sana.” “Siwezi kukuacha utembee hapa mpaka kituoni halafu usubiri pale peke yako. Hapana. Lala mapema, nitakuja kukugongea saa 10:45asubuhi.” “Asante kaka.” James akaondoka.

******************************************************

James naye akarudi akiwa amepoa. “Kwani nyinyi vipi?” James akacheka. “Tunarudi kwa mafungu?” Akauliza James kwa utani. “Tena bila Nanaa, halafu wote mmepoaa. Zinda ameshindwa hata kuongea!” Mmoja wao akadakia. “Nanaa analala. Yupo sawa tu. Kila kitu kipo sawa.” James akajibu na kujituliza kitini. Vicheko na stori vikachanganya tena, James akaangalia saa yake, akagundua anatakiwa kulala na yeye mapema ili asimcheleweshe Nanaa kituoni. Akawaaga kuwa anakwenda kupumzika. Na wengine wenye wake zao wakatoka mmoja mmoja kuingia vyumbani mwao. Grace na Danny nao kwa kuwa walikuwa si wakataji maji, soda zilishawachosha. Wakaenda kulala na mtoto wao.

Nanaa maji yawa marefu. Aamua kujitoa.
Nanaa aliamka alfajiri na mapema. Akaoga haraka haraka, akavaa suruali yake ya jinsi, akachomekea blauzi yake ya mikono mirefu, akajitengeneza nywele zake vizuri. Akabaki akimsubiria kaka yake huku amejifunika blangeti dogo alilonunuliwa mjini Korogwe na Geb. Akakunja vizuri sweta la Geb, akaliweka hapo kitandani kwani alijua lazima Geb ataliona tu. Ndicho chumba bibi Fili alitarajiwa kulala pindi atakapo wasili. Yeye alikuwa akiingia na ndege ya asubuhi hiyo. Grace na Danny ndio waliokuwa wakienda kumpokea uwanja wa ndege wa KIA.

James hakuchelewa. Alimchukua Nanaa kwenye gari mpaka kituoni. Walipofika tu na basi la kwenda Dar nalo likawasili. Kaka yake akamsaidia kuingiza begi kwenye basi. “Naomba uniagie wenye nyumba wangu.” “Nitafanya hivyo. Usafiri salama, nitakupigia baadaye kidogo.” “Simu imezima kaka. Niliiweka kwenye umeme usiku kucha, kumbe switch ilikuwa mbovu. Hata iliyokuwepo imeisha kabisa. Nikifika nitaiweka tena kwenye umeme, halafu nikupigie.” “Usisahau.” “Siwezi kaka.” James akashuka baada ya konda wa basi hilo kuingia nakusema wanaondoka. Akasubiri mpaka basi lilipoondoka, na yeye akarudi hotelini.

**************************************************

Maji yamemfika Nanaa shingoni. Historia imejirudia. Aamua kuondoka. 

* Je, amani aliyotaka iwepo akiondoka itakuwepo?

* Geb bila Nanaa mjini Marangu!

* Nini kitatokea huko aendako Nanaa kutafuta kwake? Na huku nyuma alikokuacha Marangu?


Usikose Sehemu ya 16.

0 comments: