Story
likuwa bado ni mapema sana wakati Nanaa alipokuwa
akiuacha mji wa Kilimanjaro. Kila mtu
is mine - ni Wangu! Part 1, Sehemu ya 16
I
|
bado alikuwa amelala. James na yeye
akarudi chumbani kwake. Alikuwa amelala chumba kimoja na Zinda. Akakuta bado
anakoroma. Akapanda kitandani kwake na yeye akalala. Alikuja kushtuka tena saa
sita mchana. Watu wakiwa wameshaamka wapo tu, wamekaa nje wakizungumza. Baada
ya kujisafi, akatoka kuungana nao. Hata Zinda alikuwa ameshaamka.
Alifika pale akaangaza macho, akamuona Geb amekaa
na Liz, ila Danny na familia yake hawapo. Akawasogelea na kuwasalimia. “Tunaweza kuzungumza
hapo pembeni?” James akiwa anamwangalia Geb. “Ni nini hicho
ambacho hamtaki mimi nikisikie?” Liz akadakia. Kama kitu kikampanda James.
Hasira ikawaka moyoni. Alimwangalia Liz, Geb akasimama. “Hee! Yaani wewe
umetukuta tumekaa hapa na Geb, unamchukua mpenzi wangu unataka kwenda
kuzungumza naye bila mimi! Kivipi?” “Ni nini Liz!?” Geb alimuuliza kwa
kushangaa. “Unashangaa nini na wewe? Tupo hapa mapumzikoni. Tulikubaliana
tuje hapa kama couple ili kupumzika. Mambo yenu ya siri na biashara, yasubiri
mkirudi Dar. Acha kuharibu mapumziko yetu James. Kama huwezi kuzungumza hapa,
basi naomba uondoke usitake kubugudhi watu. Huo ni ustaarabu tu ambao kila mtu
anatakiwa awe nao.” Kidogo James alianza kuelewa kile Nanaa alichokuwa
akikipitia akiwa na Liz. Alimtizama kidogo tu, akaondoka.
*********************************************************
Sababu ya hasira, akaamua kutoka kabisa pale.
Zinda aliona akiondoka, akamuwahi. Akamwita kwa sauti. “Wapi
tena James?” “Nafika
mara moja Moshi mjini. Naenda kumuona baba.” “Acha na mimi niunge msafara.” “Na
mimi.” “Hata sisi tunataka tukazurule mjini leo.” Kila mtu alitaka
kuongozana na James. “Ndio
vizuri chakula cha mchana, tukakile mjini. Kuna mahali nitawapeleka, wanapika
kitimoto hiyo! Dar nzima hamna kitu nzuri kama hiyo.” “Acha hizo James.”
Baada ya ubishi wa muda, wakitajiana sehemu ambazo walishakula kitimoto ya
nguvu jijini Dar, huku wengine wakikataa na kutoleana kasoro ya hizo sehemu,
James akabakia mshindi kuwa, anako wapeleka ni bora zaidi. “Mtu
kwao bwana.” Wakakubaliana watoke kwa pamoja, kasoro Geb na Liz walibaki
kimya wamekaa tu.
Wakati wanasubiriana sehemu ya kuegeshea magari,
wakaona Danny na familia yake wanaingia. James akawasogelea mpaka pale kwenye
gari. Akamsalimia mama yao bado wakiwa mle mle ndani ya gari. James alikuwa
upande wa dereva ambaye alikuwa Danny kwa wakati huo, ila gari la Geb. Geb naye
aliyekuwa akizungumza na simu na mama yake, walipofika pale, akakata simu na
kusogelea gari. Liz akabaki amekaa pale pale.
James awajia
juu kina Magesa
“Afadhali wote mpo hapa.
Nataka kuzungumza na nyinyi.” James alianza. Walio kwenye gari wakashuka
ili kumsikiliza James. “Kwema James? Halafu
mbona naona watu wengi halafu mwanangu Nanaa simuoni?” “Hilo ndilo nililotaka
tulizungumze.” “Vipi tena?” Danny akauliza. “Nimemsafirisha Nanaa
leo asubuhi kurudi Dar. Nimeamua hivyo. Ameondoka na basi la saa 11 asubuhi.
Mungu akipenda kwenye mida ya saa 5 hivi atakuwa amefika Dar. Funguo zenu za
chumba hizi hapa.” Kama waliomwagiwa maji, wakabaki wametoa macho.
“Kwa nini umefanya
hivyo James? Tena bila kutuambia!” Aliuliza Geb, huku akilaumu. “Unafikiri hapa
nafanya nini?” James alijibu kwa hasira, na wote wakajua. Ule muonekano wa
jana aliorudi nao baada ya kuzungumza na dada yake, wakajua ulibeba hasira. “Hapa ndio nawaambia.
Ulitaka nifanye nini wakati kila nikitaka kuzungumza na wewe, mwanamke wako
amekukaba huwezi kufanya chochote?” “Sio kweli James. Nim..” Geb alitaka
kujitetea lakini James akamuwahi. “Nisikilize Geb.” James
akajiweka sawa, uso ukiwa mwekundu. Wakajua tayari za kichaga zimepanda.
Masikio na macho yalishakuwa mekundu.
“Mimi na wewe
tumetoka mbali sana. Tokea tupo tunakunywa uji wa shule na kusubiria ugali na
maharage. Tokea hujaanza kushika pesa, mimi nilikuwepo. Tokea hata hujaanza
kuendesha hayo magari ya thamani. Mimi na wewe tumekuwa marafiki. Marafiki wa
katika shida na raha. Tatizo lako ni langu, langu ni lako. Tokea tunakuwa, sisi
ni marafiki tuliogeuka tukawa kama ndugu. Na tunaheshimiana sana. Hatujawahi
kupishana hata mara moja. Hujui ninakuwa vipi linapokuja swala la Nanaa.
Umenielewa Geb?” James alikuwa mkali. Alibadilika kama sio yeye.
“Huwa ninamlinda
Nanaa na yeyote yule anayetaka kumuumiza. Hata ikibidi kumlinda na mikono ya
mama yangu mimi mzazi, huwa nafanya hivyo. Hakuna mwanadamu anaweza kumnyanyasa
Nanaa mbele yangu, nikatulia. Jana mnamuacha Nanaa anadhalilishwa pale mbele za
watu sababu ya sweta!? Nyinyi wote watatu! Danny, Grace na Geb mmenyamaza kimya
mnaacha dada yangu anadhalilika sababu ya sweta!? Sasa hivi kila mtu anajua
kuwa Nanaa amefukuzwa kwangu, mnamsaidia nyinyi! Ameenda kulala. Baada ya
manyanyaso yote yale na kumtangaza kuwa anashida, wewe Grace ulijisumbua hata
kidogo kwenda kumtizama amelalaje?” Kimya.
Akamgeukia Geb. “Na wewe Geb umekaa
umemkumbatia mwanamke wako pale, umejali hisia za Nanaa baada ya maneno yako na
mwanamke wako? Leo asubuhi nakuita kiustarabu tu, nataka tuzungumze. Mwanamke
wako anakukataza na wewe umekaa pale kimya! Sasa hivi ni saa saba mchana. Ukiwa
umetangaza kuwa Nanaa ni jukumu lenu au lako, sijui. Umehangaika hata kujua
Nanaa alipo? Umemuona akiwa anapata hata kifungua kinywa? Eti sasa hivi
nawaambia Nanaa amerudi Dar, ndio unajidai kuniambia kuwa sikufanya vizuri!
Mlitaka abaki hapa ili iweje? Muendelee kumnyanyasa dada yangu kwa sweta!?
Sijaona hata anayemjali Nanaa hapa kati yenu. Na kwa majibu aliyonijibu mimi
Liz sasa hivi, na wewe Geb kubaki kimya kama fala, inawezekana unafanya hivyo
hivyo kwa dada yangu.” Watu walishakusanyika kusikiliza.
“Acha kutukana
James.” Geb alijaribu kumuonya. “Nimekutukana Geb.
Fanya unachotaka.” James akamsogelea karibu kishari. “Huwezi kuendeshwa na Liz, mwanamke
aliyetukuta sisi tokea wadogo, na atakuacha tu wewe kama hujui.
Anakung’ang’ania sasa hivi kwa ajili ya hayo magari yakifahari unayobadilisha
sasa hivi. Akiona hapati anachotaka atakuacha kama hakujui. Unashindwa kutumia
akili kwenye mambo ya msingi ya maisha kama haya!? Umekuwa kama mjinga!”
James akaendelea.
“Wewe ndio
wakuamuliwa na Liz uzungumze na mimi niliyekuwepo kwenye maisha yako wakati
hata yeye pia alikuwepo lakini alikuwa kama hakuoni! Kama kweli anakupenda, kwa
nini asingekutongoza wakati ule tupo wote pale chuo kikuu cha Mlimani
wakati sisi tunakula kwa mama ntilie, yeye anaendesha gari kwenda kula kwenye
mahoteli ya nje? Liz si alikuwepo kipindi hicho!? Kwa nini sasa hivi ndio
anakutongoza na kukung’ang’ania kama anakupenda kweli? Sisi wote tumekuwa na
wewe Geb, hatujawahi kutengana. Hata ulipokuwa nje ya nchi, bado tulibaki kama
familia moja. Leo Liz ndio anakuamulia uzungumze na mimi au la! Kama sio
amekugeuza kuwa fala ni nini?” James alikuwa amekasirika anatamani kurusha
ngumi.
“Naomba usiniingize
kwenye mazungumzo yenu James. Niache. Mahusiano yangu mimi na Geb hayakuhusu.” “Nitakupasua
huo mdomo Liz wewe! Usithubutu kunijibu hata kidogo. Kaa mbali na mimi kabisa.
Maskini wa nafsi wewe.” “Maskini mimi au wewe James? Sijawahi kuwa na
shida na wala sina shida. Wewe ndio unahangaika. Na kwa taarifa yako kama
mlikuwa mkisubiri Geb aniache, mtasubiri sana.” “Nani akusubiri wewe? Huwezi
wala hutakaa kuwa kwenye maisha ya mtanzania yeyote hapa Tanzania. Labda
ubadilike.” James akamgeukia vizuri Liz.
“Umekuja unabinua
midomo kama unaingia chooni! Kila kitu unakilalamikia. Kila mtu anashangaa kwa
nini umekuja kama hukuwa unataka kuja. Unamkera kila mtu Liz. Na usifikiri
ulimdhalilisha dada yangu kwa sweta. Ulijidhalilisha wewe mwenyewe na hii
familia yako ya kina Magesa. Mpumbavu tu wewe. Wivu tu.” “Sina wivu na wala sio
mpumbavu.” James aliruka akataka kumkamata Liz, Liz akakimbia kwa haraka.
Danny akamshika James alipotaka kumkimbiza.
“Nitampasua mdomo
mimi!” Zinda akasogea. “Naomba tuondoke
James. Tafadhali.” James alikuwa anawaka kama moto. “Sitaki mtu anishike.
Niache Danny tafadhali. Nyinyi si mmekuwa mamilionea? Wengine wote tunashida
tu. Tunategemea rehema zenu? Usiniguse Danny. Watu wanawasema pembeni kwa kuwa
wanawaogopa kuwaambia kwa sababu ya vijisenti mlivyopata juzi wakati sisi
tunawaona hapa! Mimi siangalii pesa Geb na Danny. Mnanijua. Utu kwanza.”
Akajitoa mikononi kwa Danny kwa nguvu.
“Mmepata pesa,
mkaanza kujifanya mmekuwa wazungu nyinyi! Mmesahau tulikuwa tunalala chini
pamoja, tunasubiri mama G, atupikie chai ya rangi tuwahi mitihani chuoni?
Mmesahau tulipotoka nyinyi!? Mnamnyanyasa Nanaa, mtoto yatima? Kama nyinyi
mmetoka kimaisha, atashindwa vipi kutoka Nanaa? Acheni dharau na manyanyaso ya
waziwazi jamani! Mnacheza na Mungu nyinyi. Mungu ni baba wa yatima. Aliyewapa
nyinyi, ndio aliyetunyima sisi. Lakini hatujui kesho ya Nanaa. Acheni .”
“James! James!
Niangalie mimi.” Malii akamwita. James akageuka. “Kilichotuleta sio
hiki bwana. Tumekuja kuchukua mke, turudi zetu mjini. Naomba yaishe. Twende
zetu tukapige maji ya mjini. Tuwanyweshe washikaji mbege halisi ya JIJI letu.
Tukirudi, tunalala mpaka kesho tuchukue mke, jumapili tunarudi mjini. Tutapata
muda wa kuzungumza na Nanaa, tutamuomba radhi. Wote tuliona alivyodhalilishwa
jana. Lakini Nanaa ni familia, kaka. Wakati wote mambo ya familia ni magumu,
ila hatujawahi kushindwa kuyamaliza. Tupo wote miaka na miaka. Tumefanya mengi
pamoja. Naamini hatutashindwa kumchukua Mmarangu wangu kesho, tumuhamishie
mjini kwenye makochi masafi na kumbi nzuri kama alivyosema Liz. Tuvumiliane tu.
Mapenzi hayachagui. Unaweza kupenda mjini na kijijini.” Malii aliongeza.
“Ila naomba ombi moja
Geb.” Malii akamgeukia Geb, baada yakuona James ametulia. “Kama Liz hapafurahii
hapa atusaidie hivi, aondoke. Au ajitahidi kuficha hisia zake. Kila mtu ana
macho na kila mtu anahisia zake. Tafadhali sana,
tunaomba kwa heshima zote, asikanyage hisia za wengine. Naona kila mtu yupo
nafuraha hapa. Hata hawa wake zetu tulio oa pwani na kule bara ndani ndani,
wamepafurahia hapa Marangu. Basi, ni hilo tu kaka. Amani na tujali hisia za
kila mmoja wetu. Safari bado ndefu sana hii. Wengi wenu hapa bado hamjaoa. Leo
ni mimi tupo hapa Marangu, kesho ni mwingine. Weza kuta itakuja kutulazimu kwa
wengine kwenda hata na mtumbwi huko ukweni. Lakini kwa kuwa sisi ni ndugu, mama
yetu mmoja. Huyo hapo Mama G, amehangaika kutukusanya tokea watoto. Basi naomba
amani idumu.” “Samahani sana Malii. Samahani kaka.” James alishatulia. “Naelewa kaka. Ila
naomba kikao kihamie mjini basi. Kwenye kiti moto ya dunia.” Kidogo
pakatulia.
“Mama pole na safari.
Nimefurahi sana kukuona huku milimani.” Malii akamsogelea na kumkumbatia
mama G. Kila mtu akampa mkono Mama G, aliyekuwa amenyamaza kimya muda wote
akisikiliza. “Sasa
wewe nenda kapumzike. Jioni tukirudi, utupe neno la busara.” “Msilewe sasa.
Hasa wewe Malii. Kesho ni siku muhimu sana kwako.” “Na umuhimu huo ni wewe
kuwepo hapa. Ukishuhudia na mimi mwanao napata mke. Unakumbuka ulivyokuwa
unatutengenezea kahawa usiku ili tusome kipindi cha mitihani? Sasa shule
imeisha, shuhudia nachukua jiko.” Mama G, akacheka kidogo.
“Haya. Njooni wote
tushikane mikono tuombe. Hili jambo ni la baraka sana. Tusikubali shetani
aliharibu.” Wakakusanyika wote, wakatengeneza duara kubwa, wakashikana
mikono. Mama G akaanza kuomba. Aliomba toba kwa watoto wake hao wote.
Akawatakasa kila mmoja, huku akimsihi Mungu awasamehe. Akamshukuru Mungu kwa
ulinzi wake juu ya vijana wake hao na mke mtarajiwa wa Malii, kijana wake.
Akaomba amani na ulinzi kati yao, huku akisihi Mungu amlinde Nanaa popote alipo
na amfanikishe. Akamaliza.
Mpaka anasema amina, kila mtu akawa ametulia.
Wakaanza kupiga makofi. “Afadhali umekuja
mama.” Kila mtu alirudi kumpa mkono mama G. “Haya. Na mimi
nimefurahi kuwaona. Ila nataka muwahi kurudi na muwe waangalifu huko
mabarabarani. Madereva wote msinywe. Mtakuja kunywa hapa mkirudi. Umenisikia
James? Wewe unayewapeleka wenzako usiweke pombe mdomoni.” “Nimeelewa mama. Saa
12 jioni nawarudisha. Ngoja nikamsalie Mzee.” “Haya. Fikisha salamu zetu.
Tafadhali macho yako yote yawe kwa Malii. Arudi akiwa na meno yake yote.”
Wote wakacheka. Wakaingia kwenye gari, wakaondoka.
*********************************************************
Alibaki Mama G na wanae. Akamwangalia Geb. “Mbona midomo
imekukauka? Umekula wewe?” Akamuuliza Geb kisha akamgeukia Grace. “We Grace?” “Hajala
tokea jana njiani alipopewa vitu vya kula na Nanaa. Korosho na soda tu.”
Grace alijibu huku anarudi kwenye gari kuchukua mizigo ya mama yake. “Hata macho hayo
yanaonekana hujalala vizuri. Twende ukale halafu ulale kidogo.” “Sisikii njaa
mama. Kwanza pole na safari.” “Asante.” “Vipi magoti?” Geb akamuuliza mama
yake, huku akimuangalia magotini. “Aaah, hivyo hivyo.
Lakini usiwe na wasiwasi. Safari ilikuwa nzuri. Fupi. Hata lisaa halikuisha
huko angani. Twendeni ndani nikainyooshe kidogo.” Wakaongozana mpaka kwenye
chumba ambacho alitakiwa alale na Nanaa.
Wakalikuta lile sweta kitandani. “Sweta lenyewe ndilo
hili lililozua kizaizai!?” Mama G akalinyanyua akalitazama na kulitupa tena
pale pale kitandani. Kila mtu akanyamaza. “Kilichowashinda
kumjulia hali Nanaa, nyinyi ni nini?” Mama G akauliza huku akikaa. “Usiku sisi tulikuwa
tumechoka mama, na asubuhi tuliamka mapema ili tukuwahi wewe uwanja wa ndege.”
Mama yao akamgeukia Geb aliyekuwa amenyamaza kimya. Akajua hataongea. “Njoo ujilaze hapa.”
Bila aibu wala kubisha, Geb akapanda kwenye kile kile kitanda alichokuwa amekaa
mama yake. Akajilaza vizuri pembeni yake na kugeukia ukutani.
“Naomba hilo blangeti
hapo.” Mama G alimtuma Danny. Danny akavuta blangeti kutoka kwenye kitanda
kingine, akamkabidhi mama yao. Akamfunika vizuri Geb. “Hajala huyo mama.
Tokea jana hajaweka kitu mdomoni.” Grace alimuwahi mama yake kabla hajamfunika
vizuri Geb. “Wewe
unamjua Geb. Hawezi kula akiwa kwenye hali hiyo. Mwache alale kidogo. Akiamka
ndio atakula.” Alimjibu Grace huku akiendelea kumfunika Geb.
*********************************************************
“Nitolee
simu yangu kwenye pochi nimpigie Nanaa.” Grace akatoa simu. Akamkabidhi
mama yake baada ya kupiga simu ya Nanaa. “Mama!” Nanaa akapokea. “Umefika salama?” “Ndiyo. Nashukuru Mungu
nimefika salama. Pole na safari.” Nanaa
akajibu. “Asante.
Mbona nakusikia kama upo kwenye basi tena?” Mama G, aliuliza. “Nipo kwenye daladala mama
yangu. Dalali ameniita nikaangalie chumba maeneo ya Mwananyamala. Ndio nipo
njiani. Na simu inaishiwa chaji. Naomba mwambie kaka James nilifika salama,
asiwe na wasiwasi. Nikirudi nyumbani nitaichaji kisha niwapigie tena, tuzungumze
vizuri.” “Sasa utalala wapi na mimi nyumba nilifunga. Sikujua kama utarudi.”
“Usiwe na wasiwasi mama yangu. Nitapata tu mahali pakulala. Naomba nikuage kwa
sasa ili simu isiishe chaji kabisa nikashindwa kuwasiliana na dalali.” “Naomba
usisahau kunipigia Nanaa. Sitalala mpaka nikusikie.” “Usiwe na wasiwasi mama.”
“Hapana Nanaa. Nitataka kujua upo wapi, na unalala wapi. Kama ulikula na kama
ulifanikiwa.” Wakamsikia Nanaa
anacheka. “Haya mama yangu. Basi
nitajitahidi tuwasiliane. Uwe na wakati mzuri. Nyoosha miguu upumzike kesho
ukacheze kwenye harusi.” Mama G akacheka kidogo. “Asante mwanangu. Nasubiria simu yako.” “Usijali.” Nanaa akakata simu.
*********************************************************
“Nanaa anamoyo mwepesi huyu mtoto!”
Mama G, aliwaza kwa sauti. “Nimemsikia anacheka
mwenyewe.” Grace akaongeza. “Anapenda kucheka
kama nini sijui! Namtania namwambia ndio maana mashavu yake yamebonyea. Kila
kitu yeye kucheka.” Kidogo walifarijika baada ya kuzungumza na Nanaa.
“Ila niwaambie ukweli
kabisa wanangu. Kama tukishindwa kumtunza Nanaa, mjue wazi tumeshindwa kutunza
baraka za Mungu. Na hatutabaki kama hivi tulivyo. Wote mlikosea jana. Mlikosea
sana. Lazima tukubali kosa na mjue James alikuwa sahihi japo aliongea kwa
hasira. Baraka mlizonazo leo, hamjui mlizitoa wapi. Danny, uliweza kukusanya
wale vijana wote wale, ukatuletea nyumbani. Yatima na walio na makwao pale pale
jijini, walipaita kwetu ni kwao. Ni nyinyi mliwafanya wanipende na kunithamini.
Ni nyinyi ndio mliwageuza kutoka kuwa marafiki mpaka wakawa ndugu. Kundi lote lile
ni sisi tumelikusanya na kuwaunganisha. Wamekuwa kama kondoo wetu. Wewe Danny
ndio wamekuchagua kama mwenyekiti wao. Umekuwa ni mchungaji wao, halafu gafla
mnawaacha! Mnajitenga nyinyi wenyewe! Lazima kutatokea vurugu sana. Kuweni
makini kwa kila jambo. Wanawaangalia kwa karibu sana. Na si kwa mabaya, ni kwa
kuwa wanawapenda. Hakuna hata mmoja wao pale anayetaka kuwapoteza nyinyi. Ndio
maana popote mlipo. Au popote mnapoishi, wanawafuata. Na hawajihesabu niwageni
kwenu. Ndio maana wanaingia na kutoka pale nyumbani, watakavyo. Naombeni
msijisahau sasa hivi.” Wote walikuwa wamenyamaza.
“Mmesikia?” Mama
G akawauliza. “Binafsi
nimeelewa mama. Na ninakiri ni hasira tu ndizo zilinifanya ninyamaze. Kama
ningeendelea kuongea jana, au ningefungua mdomo wangu, ingekuwa mbaya zaidi
mama yangu. Wewe unanijua. Usingekuta hii hali ya leo. Au haya yaliyotokea leo,
ingekuwa mbaya zaidi yake. Kumbuka na mimi ni yatima kama Nanaa. Nilikuwa
nikitangatanga kwenye majumba ya watu kama Nanaa. Mpaka mliponifungulia mlango
kama hivi Nanaa. Kwa hiyo naelewa, na ninajua ugumu anaopambana nao Nanaa.”
Danny aliongea kwa hisia zote.
“Mimi unanijua mama.
Nikiongea sana kichwa kinauma au maneno yanakwama na ninaishia kulia kama
mjinga. Nilifanya kwa sehemu niliyoweza mpaka tukafika hapa. Japo nahisi sijui
sikusaidia sana au nilichelewa? Sijui. Lakini namuelewa Nanaa. Ni kweli alikuwa
na wakati mgumu. Na niliumia sana jana usiku. Ni kweli alidhalilika. Nakiri
tulikosea.” Grace aliongea upande wake.
“Na kwa upande wa Geb,
mimi namfahamu Geb. Heri mimi nikiwa na hasira huwa naweza hata kuongea kidogo.
Geb alikuwa kwenye nafasi ambayo kunyamaza pekee ndio ilikuwa suluhisho sahihi.
Sio kwamba namtetea. Jana angeongea zaidi, ingekuwa mbaya zaidi. Nilimsifu
jinsi alivyoweza kunyamaza. Japo nilijua alikuwa anaumia sana moyoni. Hata kule
kuongea pale mbele za watu na kutoa yale maelezo yote yale, ilimlazimu. Na
nashukuru alijibu. Ingekuwa mbaya zaidi kama angenyamaza. Kwa kujibu kwake
jana, Geb alituliza ugomvi mkubwa sana ambao Liz alikusudia kuzua chuki kubwa
sana katikati ya hawa marafiki. Geb hakuwa amekusudia kumdhalilisha Nanaa. Wote
tunajua jinsi anavyompenda Nanaa. Lakini mama, walimbana kwenye kona, ilikuwa
hamna jinsi lazima ajieleze vile tu. Lasivyo wangemuona msaliti.” Kama
kawaida ya Grace kumtetea kaka yake.
“Tukirudi nyumbani,
tutapata muda na Nanaa. Tutazungumza naye. Ninamfahamu Nanaa. Ataelewa tu. Huwa
hawezi kuweka kinyongo yule mtoto. Atasamehe tu.” Mama G, akamalizia.
Wakatulia kidogo kila mtu akiwaza lake.
*********************************************************
“Basi kwa kuwa
bibi amekuja. Wewe kaa hapa na bibi. Sisi tunakuja sasa hivi.” “Namtaka mama.”
“Kwani Fili vipi bwana!? Unataka kuharibu safari yangu nzima!” Mama yao
alianza kucheka. “Kamganda
mke wangu tokea jana! Sina raha!” “Muache mtoto Danny. Mimi namwambia labda
sababu yupo kwenye mazingira mageni, halafu hakuna watoto wengine. Anaogopa.”
“Sasa anachoogopa hapa ni nini wakati bibi yake huyu hapa? Yaani amepooza
kabisa. Haongei, anamtaka mama yake amkumbatie wakati wote bwana! Sina raha na
mke wangu!” “Mmemwangalia homa lakini?” Bibi yake akauliza.
“Danny
amempima, hana homa.” “Eti Fili. Unaumwa?” Bibi yake akamuuliza kwa upole. “Namtaka mama.”
“Yaani hiyo sentensi inazidi kuniudhi. Ameikazania tokea jana! Kama ananikomoa
vile!” Grace na mama yake wakaanza kucheka. “Si ukae hapo kidogo
tu, tunakuja sasa hivi. Umesikia Fili mwanangu?” Danny aliendelea
kubembeleza, lakini Fili akanyamaza. “Usiwe na wasiwasi
Fili mwanangu. Ongea na bibi kidogo tu, tutakuja. Sawa? Mfundishe ule wimbo
wako wa shule.” Fili alianza kutoa machozi.
“Hii safari kweli
imeingiwa mkosi.” “Usiseme hivyo bwana Danny. Hii sio kawaida ya Fili. Lazima
kuna jambo tu. Ngoja nilale naye hapo kitanda cha pembeni. Akilala
nitakufuata.” “Nasubiria hapa hapa. Hukawii na wewe kulala kama jana usiku.
Jana nimejikuta nimelala peke yangu usiku kucha!
Fili kalala na mke wangu. Leo umuache hapo sisi twende.” Grace alianza tena
kucheka. “Hata
mimi nilikuwa nimechoka na safari, wala sio Fili peke yake.” Mama G alikuwa
akicheka huku ameinamia simu yake. Danny akakaa. Grace na yeye akapanda
kitandani akamkumbatia mwanae wakalala.
Nanaa huko
Jijini.
Nanaa alikutana na dalali. Bei ikamshinda.
Ilikuwa vyumba viwili na sebule. Inajitegemea jiko na kila kitu. Alimwambia
yule dalali asingeweza. Bei nikubwa sana kwake. Na anatarajia kurudi chuoni
baada ya muda mfupi. Asingependa sehemu itakayomlazimu kuchukua daladala mbili
hasa kodi ikiwa juu kiasi kile. Nyumba ilikuwa nzuri ya kisasa. Isingeendana
kabisa na hadhi ya Nanaa kwa wakati ule.
Akakumbuka ofa ya Zinda. Kupewa gari na nyumba.
Ndoa ya haraka. Au wawe wote kwa wakati huo. “Nikimkubali Zinda,
sitahangaika tena.” Umaskini ukaanza kumsumbua Nanaa. “Nimejizubaisha kwa
Jeff, mpaka akapata mwingine. Nina tatizo gani mimi!?” Nanaa akaanza
kujichukia. “Lakini hapana.
Acha nijikane, mpaka nione huo mwisho wangu.” Wakaagana na dalali kwa
makubaliano ya kumtafutana tena pindi atakapo pata sehemu nyingine inayoendana
na yeye.
Nanaa
nyumbani kwa Antii.
Wapi pa kwenda baada ya hapo ndio ukawa mtihani.
Kama kawaida ya wachaga kusaidiana popote walipo. Nanaa akamkumbuka matroni wao
wa pale chuoni. Alikuwa mama wa kichaga, aliyetokea kumpenda sana Nanaa.
Japokuwa hakuwa akimjua baba yake, lakini alijua mama yake ni mchaga kwa
hakika. Akajenga mazoea na yule mama akimtambua kama mchaga mwenzake. Kwa hiyo
Nanaa hakuacha kuwa akipita hapo kila anapoelekea chumbani kwake na kumpa
salamu. Jina la Antii likawa la kawaida kwao. Wakawa wanaitana Antii yeye na
matroni.
Nanaa akaona ndiye mtu wakumpigia. Japokuwa simu
yake ilishaonyesha dalili zote za kuzimika, lakini hakupata shida wala kutumia
muda mrefu wa kujieleza kuwa anatafuta mahali pa kulala usiku huo. Akakaribishwa.
Alifika nyumbani hapo. Antii alikuwa mzungumzaji, Nanaa mchekaji. Stori
zikaanza, Nanaa kucheka tu wakati wote. Mpaka wanaagana kwenda kulala, hakuwa
ameulizwa kulikoni japo alikwenda na begi lake. Mama huyu wa kichaga hakuwa
ameolewa. Japo alikuwa na watoto wakiume wawili na wakike mmoja, ambaye alikuwa
anasoma hapo hapo chuoni, lakini alikuwa likizo na kaka zake, huko migombani
kwa bibi na babu yao. Nanaa akajikuta na yule mama tu mle ndani.
Antii alikuwa ni matroni wa hosteli za wasichana
pale pale chuo kikuu cha Mlimani, lakini pia anabiashara zake zinazomwingizia
pesa. Anasomesha watoto wake yeye mwenyewe na mkubwa alishaoa. Maisha yake
yalikuwa yakuhangaika kuanzia saa 11 asubuhi yupo macho mpaka usiku
anakimbizana na pesa ya jiji la Dar. Alishamwambia Nanaa asubuhi anawahi
mahali, akiamka yeye ajitengenezee chakula na maisha yaendelee kama kawaida,
asimsubiri.
*********************************************************
Usiku alijisahau kuchaji simu yake, sababu ya
stori. Akalala akiwa hoi. Hata mama G, hakumtafuta tena. Asubuhi akiwa peke
yake pale ndani ndipo akakumbuka anatakiwa kumtafuta kaka yake James na Mama G,
kuwaambia alipo. Akawasha simu mara ilipojaa. Tayari ilikuwa saa tano.
Wa kwanza kumpigia simu akawa kaka yake. “Mbona
unanitia wasiwasi?” “Pole kaka. Nipo kwa Antii. Si unakumbuka nilikwambia
alivyo muongeaji? Tulilala saa sita kwa stori.” “Na unavyopenda stori wewe!”
“Kama ulikuwepo. Nilikuwa nina kazi ya kucheka tu.” “Lakini nimefurahi kama
umepata wakati mzuri. Sasa umemwambia nini?” Nanaa
akamuelezea kaka yake habari za chumba kwa ufupi. “Lakini Antii hata hajauliza. Yeye kafurahi kuniona tu. Akaanza stori
zake. Lakini kaka, itabidi nizungumze naye atakaporudi. Ili aniweke mpaka
nitakapopata chumba changu. Ni mama mzuri. Mtu wa nyumbani. Kama nilivyokwambia, ananipenda tokea
zamani. Haachi kunitafuta na kunijulia hali na maendeleo yangu. Sidhani kama
atajali nikijishikiza hapa kwa muda mpaka nitakapo pata chumba changu.” “Sawa
kama atakubali kuishi na wewe. Itakua jambo zuri. Utanijulisha basi atakavyo
kwambia.” “Haya kaka. Asante.” “Unasalimiwa na Mama G.” James akamuwahi kabla hajakata simu. “Mwambie nitampigia kwenye simu yake.” Nanaa akakata simu.
Akampigia mama G. “Pole mama yangu.” “Mmmh! Umeniweka roho juu wala sijalala.” “Mbona
sauti yako nzuri kama uliyelala usingizi mzuri?” “Si ndio sauti yangu ilivyo!?”
Nanaa akacheka sana. “Unavyojisifia!”
“Kumbe. Hebu niambie kama ulifanikiwa.” “Vyumba ni ghali, mama! Sio kama
nilivyojipanga. Nimepelekwa sehemu jana, pazuri, lakini pesa nyingi. Hata hivyo
ni pakubwa sana. Mimi na mabegi yangu tu, mmh! Tutapwaya.” Wakacheka.
“Sasa,
sasa hivi uko wapi?” Mama G akauliza tena. “Nipo
kwa mama mmoja amenihifadhi. Ni mama mzuri sana. Nimelala nacheka tu.” “Na
unavyopenda stori wewe!” “Kama ulikuwepo. Nilikuwa na kazi yakucheka tu hapa.
Ametoka muda si mrefu, tulikuwa tukicheka hapa. Haishiwi vituko.” “Nimefurahi
kusikia una furaha Nanaa.” “Mimi mzimaa. Wewe furahia harusi. Nitakupigia
ukirudi.” “Unanipigia au unarudi nyumbani?” “Naona nitaendelea kuishi na huyu
mama tu. Ila mkirudi, naomba unijulishe ili nije kuchukua mizigo yangu.” Kimya.
Nanaa akaangalia simu kujua kama ilikatwa. “Mama!” Akaita.
“Nakusikiliza.”
“Basi tutawasiliana. Nikuache ujumuike na wanao. Angalia tu Zinda asije kukupa
pombe.” “Hapa nimeshaanza kulewa.” “Mama wewe!” Nanaa
akashtuka sana “Nakutania bwana.” “Haya mama yangu. Have fun. Baadaye.” “Sawa.” Mama G, alikata simu lakini kila mtu
alimuona alivyobadilika sura.
“Nanaa hajambo?”
Grace aliyekaribu naye akauliza. “Mzima. Anacheka tu
kama kawaida yake. Atakuja kuchukua mizigo yake tukirudi sisi nyumbani. Amepata
sehemu nyingine yakuishi wakati anatafuta chumba chake. Analalamika vyumba ni
garama. Nimeumia sana. Najiona kama sipo tayari kuachana na yule mtoto! Sijui
nikumzoea sana!?” Grace akanyamaza, Danny hakuongeza neno. Geb naye alikuwa
akisikia kila kitu kwani hakuwa mbali nao. Akanyamaza tu.
*********************************************************
Kuanzia asikie Nanaa anahama nyumbani kwake, Geb
hakutia hata maji mdomoni. Hata kwenye sherehe alikuwa kimya. Bila kula wala
kunywa. Watu walisherehekea, lakini Geb alikuwa kimya. Grace akajaribu kumpa
hata soda, lakini hakuinywa. Mama G alikuwa upande wa wazazi wa Malii wakiongea
na kucheka mpaka sherehe ilipoisha.
Baada ya sherehe kuisha Grace akamwita mama yake
pembeni, kabla hawajaingia kwenye gari kurudi hotelini. “Ujue tokea mtori
uliomlazimisha Geb kula mchana, akala vijiko sijui vinne sijui vitano, ujue
hajatia kitu kingine mdomoni?” “Haiwezekani! Hata kwenye sherehe!?” “Nimempa
soda, akaipokea na kuiweka chini ya kiti. Mpaka tunatoka pale, hakuiweka hata
tone mdomoni.” Mama G, akanyamaza.
“Sasa na wewe kwa
nini uliongea pale mbele yake kama Nanaa anahama nyumbani, mama jamani!? Si
ungesubiri mpaka turudi nyumbani?” “Nahisi nikujisahau bwana. Nitazungumza naye
tukifika hotelini.” “Sidhani kama
kunasafari ya Arusha tena!” Grace akaongeza. “Atafia njiani kama
asiporudi na kumuona Nanaa. Heri kesho alfajiri tugeuze.” Wakaingia kwenye
gari. Geb alikuwa amembeba Fili muda wote wa sherehe, akawa ameshatangulia naye
kwenye gari. Alikuwa amesinzia muda wote wakati amempakata.
Walifika wote ndani ya gari, Geb akawasha gari na
kuondoka bila ya kuongea chochote. Danny na mama G wakaendeleza stori za kwenye
sherehe. Walisimuliana vituko vilivyotokea kwenye shuguli nzima, wakawa
wanacheka wao wawili tu. Geb na Grace wakiwa kimya. Walipofika hotelini kabla
ya kushuka kwenye gari mama G, akaanza. “Nashauri Danny
uwaage wenzenu usiku huu huu, ili kesho alfajiri sisi tuondoke hapa turudi
nyumbani.” “Wazo zuri mama.” Danny akaafiki. Akamchukua mtoto wake na
mkewe, wakaondoka na kumuacha Geb na mama yake kwenye gari.
*********************************************************
“Nitazungumza na Nanaa, ili asihame.
Tuendelee kuishi naye.” Mama G akavunja ukimya wakiwa wamebaki wao wawili
kwenye gari. Geb akamgeukia mama yake. “Unafikiri baada ya
yote haya atakubali na wakati nimemsikia akisema amepata sehemu nyingine ya
kuishi, na kaka yake ameshamkubalia?” Geb aliuliza akionyesha kukata tamaa.
“Wewe ushawahi kuona nimekuahidi kitu halafu nikashindwa kukutekelezea?”
“Nahisi nimeingiwa
na hofu mama. Hali haikuwa nzuri. Halafu siku..” Geb akakwama. “Grace na Danny
wamenieleza kila kitu. Wewe usiwe na wasiwasi. Nataka utulize mawazo. Upate
mapumziko mazuri. Kama hakuna jingine litakalozuka, ikawa ni haya tu
yaliyotokea njiani na hapa hotelini. Nakuhakikishia Nanaa atarudi nyumbani.”
Geb akavuta pumzi kwa nguvu, akazishusha taratibu kama kujituliza “Asante mama.” Geb
akashukuru.
“Twende chumbani
kwangu ukanywe soda na karanga.” “Sijisikii kula mama. Naomba nilale tu.” “Basi
kama ndio hivyo, mimi sitazungumza na Nanaa.” “Mama!!” Geb akamshangaa mama
yake. “Sasa kwa
nini huridhiki moyoni wakati nimekwambia kesho Nanaa atalala nyumbani?” “Sasa
si mpaka akubali?” “Kwa hiyo huniamini?” Mama G akamuuliza. “Basi mama. Twende
nikanywe hiyo soda.” “Nimesema na karanga.” “Tumbo limejaa mama yangu. Lipo
kama lina gesi, acha nikanywe tu soda.” “Usinichezee akili Geb. Nimesema hilo
ndilo sharti langu. Hutaki kula, basi.” Geb akacheka kidogo na kutingisha
kichwa. “Unavyoninyanyasa
mama wewe!” “Kumbe!” “Haya twende mama yangu.” Mama G aliwapenda wanae.
Alitaka kuwapa chochote wanachotaka. Akishindwa, basi anakimbilia kufunga na
kuomba. Atamlalamikia Mungu kwa machozi mpaka afanikishie wanae. Na watoto wake
walimjua hivyo.
*********************************************************
Kwa shutuma
zote zile, Nanaa atakubali kurudi kuishi nyumbani kwa Geb tena akiwa amepata
sehemu nzuri na tulivu ya kuishi?
Usikose Sehemu ya 17.
0 comments: