Story

is mine - ni Wangu! Part 1, Sehemu ya 18 & 19.

Monday, August 06, 2018 naomimwakanyamale 1 Comments


Geb na Nanaa.



U

siku huo haukua mzuri tu kwa Nanaa. Hata Geb alilala sana. Tokea walipotua Marangu‘Usiku mwema Geb. Mungu akusaidie upate usiku mtulivu na upumzike. Kesho uamke ukiwa na nguvu mpya.’ ‘Asante na wewe Nanaa. Nitakuona kesho.’ Sio kuwa Nanaa alikuwa mbali. Ni chumba kinachofuata tu. Ndani ya nyumba yake. Lakini ile kujua Nanaa yupo hapo nyumbani kwake, akili yake ilitulia. Geb alisoma ule ujumbe kwa kurudia rudia, mpaka akapitiwa na usingizi. Kwa sababu alikuwa ameshiba, hata hakugeuka usiku.
mpaka siku ya jumapili asubuhi wanaondoka Marangu mtoni, Geb hakuwa akila wala kulala vizuri. Usiku huo wa jumapili kuamkia jumatatu, ulisindikizwa na ujumbe kutoka kwa Nanaa,

****************************************************

Kila mtu aliamka akajitayarisha kwenda kazini, lakini isivyo kawaida ya Geb hakuwa ameamka. Grace alitoka chumbani akiwa yupo tayari yeye na Fili. Akamkuta Nanaa ameshajiandaa. “Nisubiri nimlishe huyu mara moja ndio tuondoke. Mwalimu wake anasema hataki kula akiwa shuleni. Nahisi anakuwa na michezo mingi.” Grace aliongea huku akijaribu kumuweka mwanae kitini ili amlishe kwanza kabla hajampeleka shule. Nanaa akanyamaza.

Mama G naye akaamka akajitayarisha. Akatoka chumbani muda mmoja na Danny. Nanaa akasikia wakisalimiana koridoni wakija pale sehemu ya kupata kifungua kinywa. “Wewe! Mbona umesimama hapo na wasiwasi?” Mama G akamuuliza Nanaa. “Njoo nikwambie kitu.” Nanaa akamshika mkono na kumvutia jikoni. “Unamfahamu Geb?” Nanaa akaanza kumuuliza mama G, akabaki akimwangalia. “Nijibu bwana mama!” “Simfahamu.” “Mimi sijui nianzie wapi bwana!” Nanaa alionekana ameshachanganyikiwa. “We Nanaa? Hebu niangalia kwanza.” Nanaa akamwangalia. “Haya ongea.” “Sijui nianzie wapi sasa!” “Ujue Grace atakuacha wewe, shauri yako! Endelea kujizubaisha.” “Ndio shida yangu hiyo. Lakini sijui nimwambie nini? Sasa kwa nini umechelewa kuamka bwana mama?” Mama G akaanza kucheka.

“Usicheke kwa sauti sasa!” “Kwa hiyo leo hutaki kwenda na Grace?” “Shhhhhhh! Punguza sauti mama! Grace bosi wangu. Na natakiwa kazini saa 2. Lakini mimi sitaki kwenda naye.” “Unataka kwenda na Geb?” Mama G akauliza. “Unaona unavyoelewa haraka?” Nanaa akaendelea. “Mwenzio Geb amaeniambia kuanzia leo tutakuwa tunaenda kazini na kurudi nae hapa. Ila akichelewa kutoka, ndio niwe narudi na Grace. Lakini nisilale mpaka yeye awe amerudi. Nikakubali. Sasa unakumbuka uliniambia ukimuahidi kitu Geb lazima utimize?” “Nanaa wewe! Acha kuniingiza kwenye mipango yako! Mbona wakati ulipokuwa ukikubali hukunishirikisha?” Nanaa akacheka.

“Sasa hapo ndipo unapotakiwa kucheza karata zako vizuri. Usiniharibie kazi kwa bosi wangu, halafu tumpe kiziwanda anachotaka. Yaani akiamka hapo, anikute namsubiria hapa. Kumbuka leo ni jumatatu. Natakiwa niwepo kazini muda mfupi sana kuanzia sasa. Sasa wewe nenda kanirekebishe mambo hapo kwa bosi wangu. Nashauri ‘play mama card’. Lazima atakusikiliza tu. Haya nenda.” Nanaa alikuwa akinong’ona. Mama G akaanza kucheka mbavu hana.

“Nanaa wewe ni mtundu sana!” “Sasa wewe unafikiri nitafanyaje kwa hali hii? Nianze kuomba ruhusa mapema hivi!? Si nitafukuzwa kazi? Halafu namwambiaje Grace?” “Mbona mke wangu muelewa sana?” Danny akadakia akiwa yupo sehemu ya kulia chakula. Grace akaanza kucheka. Nanaa akabaki ameshika mdomo. Mama G alikuwa anacheka mpaka anatoa machozi. “Uwiii mimi! Sitakaa nikatoka chini ya hii meza mama.” Nanaa akanong’ona. “Hapo ndipo utakapo fukuzwa kazi sasa. Na huyo Geb unayetaka kumsubiria akiamka hatakuona huko chini ya meza. Utakosa vyote, kote.” Danny akajibu tena, nakufanya kila mtu azidi kucheka.

“Haya Danny ondoka zako. Nenda kazini.” Grace alimfukuza huku akicheka. “Kwani na wewe Grace umesikia kila kitu?” Nanaa akauliza kwa aibu akiwa jikoni. “Kuwa unataka kumsubiria Geb?” Danny akauliza huku anatoka. Kila mtu alikuwa anacheka. “Sio mimi, ni Geb mwenyewe.” Nanaa akajitetea. “Wewe msubirie tu. Mimi nitaanzia ofisini kwako kupokea pesa zote za tokea tuondoke mpaka jana jumapili. Wala usijali.” “Mwaya mama hajui kunong’ona!? Siku nyingine nakutoa nje ya nyumba kabisa.” Mama G alikuwa akicheka na kushindwa kuongea.

Mara Geb akatoka chumbani kwake akiwa bado na nguo za kulalia. “Asante kwa kumruhusu Nanaa.” Geb alimshukuru dada yake huku akielekea jikoni. Nanaa aliposikia hivyo, akakimbilia nyuma ya mlango akaufungua mpaka mwisho akajificha. Mama G akazidi kucheka. “Shhhhh!” Geb akaingia jikoni. Kwa kuwa mlango ulikuwa umefunguliwa mpaka mwisho na mama yake alikuwa amesimama hapo akicheka peke yake,  Geb alikwenda moja kwa moja nyuma ya mlango akamchungulia Nanaa. “Uliamka salama?” Akamuuliza pale pale alipokuwa amejificha. Nanaa akatingisha kichwa kukubali. “Tunaondoka sasa hivi. Sitakuchelewesha sana kazini. Usiwe na wasiwasi.” “Kwani na wewe umesikia?” Nanaa akamuuliza, Geb akabaki akicheka. “Bwana hujasikia. Eti Geb?” Geb na mama yake walibaki wakicheka.

“Toka sasa uje unywe chai. Kila mtu kashasikia.” Mama G akavuta kiti akakaa. “Ni mama ndio hajui kunong’ona!” Geb alibaki kucheka. Grace akaondoka mapema na mwanae. Kwa kuwa alikuwa akimshusha kwanza shule ndio aende kazini. Ilikuwa bado ni saa 12 asubuhi, bado hata saa moja haijafika. Wakati wote walikuwa wakitoka mapema sana ili kuwahi foleni.

******************************************

Maisha yakaanza kati ya Geb na Nanaa. Geb ndiye alikuwa dereva wa Nanaa. Kumpeleka na kumrudisha jioni. Siku hiyo ya jumatatu alimfuata kazini muda wa mchana. Akamtoa kwa chakula cha mchana. Alimtafutia mgahawa mzuri. Wakaenda kukaa na kula chakula kizuri cha mchana, akamrudisha ofisini kwake na yeye akarudi kazini kwake. Jioni alirudi tena kumchukua. Lakini kabla yakuondoka, alihakikisha anapata muda pale ofisini kwake. Akapitia kazi zake zote alizozifanya kwa siku ile. Akamshauri hili na kumtengenezea lile, ndipo wakaondoka kurudi nyumbani.

Alifanya hivyo jumatatu, jumanne na jumatano pia. Alihakikisha kila anapofika hapo, anaingia ndani, ofisini kwa Nanaa na kupitia kazi zake. Ilimradi kuhakikisha kazi yake haina lawama kwa yeyote. Nanaa alikuwa akifurahia na kuuliza maswali mengi ili kuwa bora zaidi ya muhasibu wao aliyeuwa likizo.

******************************************

 “Nikuombe kitu Nanaa?” Geb alianza siku hiyo ya jumatano asubuhi wakiwa wanakwenda kazini yeye na Nanaa. “Unataka nini?” Nanaa aliuliza kwa upole. “Naomba unisindikize Bagamoyo siku ya Ijumaa.” Nanaa akafurahia akataka kukubali kwa haraka, lakini akakumbuka kitu. “Ningependa twende wote Geb. Lakini ijumaa ni siku ya kazi. Tena ndio nakuwa nafunga mahesabu ya juma zima. Na unajua ijumaa Grace huwa anawahi kutoka kazini. Labda ingekuwa siku ya jumamosi, ningekusindikiza. Unaenda kikazi?” “Nimepata dereva mgeni. Nimeambiwa mzigo upo tayari. Ukiendelea kukaa hapo muda mrefu, utaharibika.” “Ni nini?” Nanaa akauliza tena. “Matikiti maji. Yasipoenda kuchukuliwa ijumaa, mwenye shamba anasema itabidi ayauze kwa hasara, ili yasimuharibikie. Na huwa tunapenda matikiti yake. Yana maji mengi na matamu. Lazima mimi niyapate. Nataka kumtuma huyohuyo dereva mgeni. Lakini lazima mimi mwenyewe niwepo ili nikaangalie upakizwaji wake. Sitaki ayafikishe hapa yakiwa yameharibika.” Nanaa akanyamaza.

Ningefurahi tungeenda wote.” Akamtupia tena jicho. “Hata mimi Geb.” “Kama tatizo ni Grace tu, usiwe na wasiwasi.” “Hapana. Sio Grace tu, lakini ni majukumu yangu. Sipendi niwe naomba ruhusa mara kwa mara halafu anaishia yeye kufanya kazi zangu na zake!” “Usiwe na wasiwasi. Nitazungumza na Grace, apokee pesa yote. Halafu jumamosi tutaenda kuweka mahesabu yote sawa. Yeye hatafanya kitu zaidi ya kupokea pesa tu.” Nanaa akafurahia hilo wazo. “Asante. Na ninakuahidi jumamosi nikiamka tu, nitakimbilia kazini nikakamilishe. Sitaharibu kazi.” “Utaniacha tena!?” Geb akauliza na kumtupia tena macho wakiwa bado barabarani. Nanaa akacheka kwa aibu kidogo. Huwezi kutofurahia kuangaliwa na Geb. Akarudisha macho chini kwa haraka kama kukwepesha.

“Najua siku ya jumamosi ndio siku yako yakupumzika. Nikiwahi kutoka kwenda kazini, nitarudi mapema hata kabla hujaamka.” “Nisubiri tutakwenda wote.” Nanaa akatoa tabasamu lakuridhika. “Basi sawa. Nitakusubiri mpaka uamke ndio twende wote.” Wakajikuta macho yamegongana na tabasamu usoni.

******************************************

Hakuna ambae hakuona furaha ya Geb. Alibadilika akawa mtu mwenye furaha kila wakati. Akili ilikuwa imetulia. Chakula kinaliwa bila shida. Hakuna kununa wala kulalamika. Asubuhi alitoka na Nanaa, na hata jioni walirudi pamoja, japo wakati mwingine kwa kuchelewa. Kila Geb anapokuwa akipanga kukosa siku moja ya kazi ndani ya week, alikuwa akichelewa kurudi nyumbani. Ilimlazimu kufanya kazi zaidi ili kupunguza majukumu ya siku hiyo ambayo asingekuwepo kazini na asilemee wenzake.

******************************************

Siku hiyo ya jumatano baada yakutoka kazini Geb alimpitisha mahali kula ice cream. Walikaa hapo wakiongea na kucheka. Geb alikuwa akimwangalia kwa kumtamania sana. Vile alivyokuwa akicheka na mashavu kubonyea, ilimfanya Geb kucheka na yeye huku akimwangalia. Kitu kidogo tu, Nanaa alikuwa akicheka na kumfariji Geb. Kwa siku hizo chache tu tokea aanze kwenda na Nanaa kazini au kuwa naye karibu, tayari maisha yake yalibadilika. Utulivu wa akili na amani ya moyoni aliyokuwa nayo Geb, aliomba iwe hivyo daima. Asijue amempokonya mama yake Rafiki.

 ******************************************

Kwani muda mwingi Nanaa alikuwa akiongea na mama G ambaye alikuwa peke yake mle ndani. Geb alikuwa busy na Liz. Grace na familia yake. Na wote wawili, Danny na Fili walitaka kumuona Grace kila wakati. Walikuwa wakishindana kumwita. Nanaa na mama G walikuwa wakiwasikiliza na kucheka. Ikitokea Grace ananyanyuka tu na kuhamia sehemu nyingine, Danny na mtoto wake wataanza kumtafuta. Kwa hiyo muda aliokuwa akiupata Grace na mama yake ulikuwa mfupi sana. Mara zote ungemkuta Grace na hao watu wawili. Danny na Fili. Hata kama Danny atakuwa anacheza game na mwanae kwenye tv, lakini watataka Grace awepo hapo pembeni yao. Akinyanyuka tu, mchezo nao ujue umeisha.

******************************************

“Nataka nimpelekee mama ice cream. Kwa hiyo tuwahi kurudi nyumbani kabla hajalala.” Nanaa alimwambia Geb. Wakamalizia za kwao, wakanunua na ya mama G, wakaondoka kuelekea nyumbani. Geb alichelewa kutoka kazini, akamkuta Nanaa akimsubiria tu ofisini. Hakutaka kuondoka na Grace mapema. Akampeleka kwenye icecream, mpaka wanafika nyumbani, tayari ilikuwa saa 3 na robo usiku. Moja kwa moja chumbani kwa bibi Fili.

“Nimelala Nanaa. Wewe vipi bwana?” “Kama ndio hivyo sikupi zawadi niliyokuletea. Endelea kulala.” Nanaa akajidai anataka kutoka. “Njoo mwanangu Nanaa.” Geb akawasha taa. Wakacheka. “Unapenda zawadi mama wewe!” “Nipe basi hiyo zawadi, acha kuniweka roho juu.” Nanaa akampa ile ice cream. “Haya ndio majaribu haya. Sasa ice cream hii saa hizi!? Wakati nimekwambia kabisa nimeambiwa kama nataka haya magoti yapone, basi nipunguze huu mwili.” “Basi nirudishie nikakuwekee kwenye friji mpaka kesho.” “Aiii! Sitaweza kulala. Heri tu niile.” Wote wakazidi kucheka. Geb akajirusha kitandani kwa mama yake, Nanaa akakaa kitanda cha pembeni.


“Muone alivyojawa furaha.” Mama G alimchokoza Geb. “Ni kawaida yangu.” Geb akajibu huku anacheka. “Mmmh!” Mama yake akaguna. “Mmekula sasa?” “Bado.” Nanaa akajibu. “Mbona mmechelewa hivyo?” “Mimi ndio nimechelewa kutoka kazini.” “Sasa wewe Nanaa si ungerudi na Grace? Umekaa mwenyewe kazini mpaka saa hizi!?” “Nilimuomba anisubiri. Kwani umechoka?” Geb alijibu na kumuuliza Nanaa. Nanaa akatingisha kichwa kukataa. “Mmmh!” Mama G akaguna huku akiendelea kula ile icecream yake akiwatizama kwa zamu. “Sasa unaguna nini mama?” Geb akamuuliza huku anacheka. “Nasafisha koo. Niache.” Wakacheka.

“Inanisaidia kujua…” Nanaa akanyamaza na kuanza kucheka. Mama G akabaki amemkodolea macho. “Bwana mimi naenda jikoni kumchukulia Geb chakula.” Nanaa akasimama. “Umeanza mwenyewe. Kaa hapo chini uyamalize.” “Nini?” Nanaa akauliza huku akijua mama G anachouliza. Ila alitaka kumzungusha tu. “Huko kukaa kazini unamsubiria Geb. Inakusaidia nini wewe? Usiyerudi hapa nyumbani ukapumzika wakati unamsubiria hapa kama si kuchoshana tu?” “Mama wewe! Kuchoshana? Usiseme hivyo.” Geb na mama yake waliangua kicheko. Nanaa akatoka anakimbia kuelekea jikoni kuleta chakula.

Alikuta mama yake alishampikia Geb chakula chake na kipo chakula cha nyumba nzima. Akapakua chake na cha Geb akarudi chumbani wakawa wanakula huku wanaongea.

******************************************

 “Ijumaa naenda na Nanaa Bagamoyo.” Geb akamwambia mama yake. “Kazi ipo.” Mama G akaongea huku akiendelea kula ice cream yake. Wakacheka. “Tunaondoka saa ngapi?” Nanaa akauliza huku akicheka. “Nikishakunywa uji wa Bibi Fili ndio tunaondoka.” “Mbona hiyo biashara nilishamkabidhi Nanaa? Yeye ndio anakibarua cha kuupika huo uji kila siku asubuhi.” Mama yake akajibu. Geb akamwangalia mama yake. “Unaniangalia nini sasa? Siamki siku hizi asubuhi asubuhi. Nanaa ndio anaamka, anakupikia huo uji. Anakuwekea kwenye bakuli na mwingine kwenye chupa wa kunywa kazini.” Geb akainamisha kichwa kwenye mkono wake.

“Aibu zako. Baba mzima unakunywa uji mpaka leo!” “Ni wewe mama ndio umenianzishia kunywa uji.” “Si kwa kuwa huli! Yaani alikuwa anarudi hapa nyumbani hajala siku nzima. Alibaki mifupa tu huyu.” Nanaa alikuwa anacheka taratibu huku anakula. “Nakula bwana mama. Mbona nakula ugali?” “Lakini hutaki mchuzi utakao kuwa na kitunguu au karoti.” “Lakini nakula na mboga za majani.” Mama yake akaguna. “Nini sasa?” “Na hivyo vyakula vyenyewe vipikwe humu ndani na dada yake au mimi, lakini si vinginevyo.” “Nyamaza mama bwana. Nanaa atanikimbia bure.” “Kwani unafikiri hakujui kuwa unashida ya kula? Anakujua sana.” “Eti Nanaa?” Nanaa alibaki akicheka tu.

“Wewe ukitaka aendelee kuongea huko mtakapo kuwa, hakikisha anakula mara kwa mara.” “Mama! Nyamaza bwana.” “Ukimuona maneno hayatoki ujue ni njaa tu. Beba karanga zakutosha. Korosho zake. Halafu usisahu ile chupa ya uji, juice na maji ya kunywa. Hapo mtawezana. Halafu sio ubebe tu halafu usimpe, ujue hatakukumbusha mpaka mnarudi hapa. Utarudi navyo. Vitu vyake vyakula ni vitu vidogo vidogo, tena uwe unamkumbusha kula. Mshikishe mkononi. Yaani hakikisha vimefika kwenye mkono wake, hapo ndipo vitaingizwa mdomoni, lakini si vinginevyo.” “Mama! Usimfanye Nanaa akagairi kwenda na mimi bwana. Hali sio mbaya hivyo. Huwa nakula bwana.” Geb alijitetea. “Basi wewe usimpe, halafu utakuja kuniambia kama alikula.” “Nitakula bwana.” Geb alizidi kujitetea

“Huwa hali. Hata tukiwa kazini, atanifuata tukale, lakini yeye hali. Jumatatu tulipotoka hapa.” “Siku ile uliyokuwa hutaki kuondoka na bosi wako?” Wote wakacheka. “Wewe ndio uliharibu mama. Huwezi kunong’ona.” “Mmmh! Mbona sasa Danny alisikia maneno yako na si yangu?” “Mimi sijui. Lakini akanifuata mchana tukale. Mimi nikajua maana ya twende tukale, ni tunaenda kula wote. Yaani na yeye atakula. Nikashangaa anaagiza chupa ya maji baada ya kunisisitiza mimi niagize chakula kwanza. Nikadhani ataagiza chakula baadaye. Unajua tukaondoka hajala! Akasema anawahi ofisini, atakula chakula hukohuko ofisini.” “Ndio kawaida yake kama humjui.” Geb alikuwa anacheka tu.

“Sasa jana akaja tena. Nikamwambia kama yeye hali, ni afadhali tusiende. Akasema atakula. Ujue mama akaagiza matunda tu. Mbaya zaidi wakaleta hayo matunda yamekatwa. Yaani mama, yalikuwa yanavutia kama nini pale kwenye sahani. Mimi mwenyewe niliyatamania. Unajua Geb aliyatazama yale matunda kwa muda, kisha akaniangalia. Alipoona namtizama. Akamwita muhudumu. Akamwambia amletee matunda mazima na kisu. Hataki yaliyokwisha kukatwa.” “Siamini Nanaa kama na wewe unanigeuka!” “Ni kweli Geb, unashida ya kula.” Hapo alipokuwa, Geb alikuwa akila bila shida. Kitandani kwa mama yake. Alikaa vizuri akawa amepakata sinia lake la chakula.

“Sasa akayala hayo yaliyoletwa?” Mama G akauliza. “Sasa matunda yenyewe aliyoagiza sasa. Tango, karoti, parachichi na nyanya.” “Na usifikiri ameagiza hapo kwa bahati mbaya? Aliagiza hivyo makusudi ili wambambie kimoja wapo hakipo, aseme basi.” “Uzuri vyote aliletewa, tena baada ya muda mfupi sana. Ikaanza kazi ya kuviosha.” Mama G akaanza kucheka.  “Chupa ya kwanza ikaisha, akaagiza ya pili.” “Hapo ujue alikuwa anavuta muda ili umalize akwambie twende.” “Sasa na mimi nikawa nimeduaa namtizama.” Geb na mama yake walizidi kucheka.

“Kwa kuwa hujamjua. Kila mtu anamjua Geb. Ndio mtindo wake huo. Wala hakuwa akifanya usafi wa hayo matunda. Alikuwa anapoteza muda tu, umalize muondoke asiyale hata hayo matunda.” “Basi nitabadilika.” “Mmmh! Usimdanganye mwenzio. Tangia mtoto mdogo ndio yupo hivyo hivyo. Nishampa madawa ya kuongeza hamu ya kula mpaka nikachoka. Si madawa ya mahospitalini, si miti shamba. Amekunywa mpaka nikasalimu amri. Watu wakaniambia akikuwa atabadilika, lakini sioni dalili. Namwambia akiona anachoka, hawezi kuongea, ajue ni njaa. Ale. Wapi! Basi huwa nikiona yupo kazini, ananipigia simu mara kwa mara na kulalamikia mambo yake mengine, najua ni hasira za njaa tu. Maana akishiba huyo, hana shida na mtu. Hata umkanyage makusudi, hutamsikia akiongea. Kimyaa.” Geb alikuwa akicheka.   

 “Safari ya Bagamoyo.”
Geb alishazungumza na Grace juu ya kutokuwepo Nanaa kazini siku ya ijumaa. Kama kawaida ya Grace, hakuwa na neno akijua kazi za Nanaa, atazifanya tu Geb mwenyewe. Kwa kuwa ni biashara yake, hatakubali kitu kiharibike.

Siku ya ijumaa asubuhi, Nanaa aliamka asubuhi kama kawaida yake. Akapika uji na chapati kwa ajili ya watu wote watakapoamka. Akakusanya vitu alivyonunua Mama G kwa ajili ya kula Geb njiani. Akaweka kwenye kibegi kidogo cha chakula ambacho Geb huwa anasafiria, na mama yake ndipo anapoweka vyakula vyake, na yeye akavipanga kama alivyofundishwa na mama G. Alipohakikisha kila kitu ambacho angehitaji njiani kipo tayari akavichukua na kuweka kwenye meza iliyokuwepo karibu na mlango. Ili wakitoka wasisahau. Wakati anasafisha jikoni, Geb akatoka chumbani akiwa ameshajiandaa. Wakati Geb akinywa uji, yeye akarudi chumbani kujitayarisha. Wakatoka nyumbani saa 12 asubuhi. 

Nanaa aanza kufunguka kwa Geb na Geb kwa Nanaa..

“Si utakuwa na usingizi? Vuta kiti nyuma ulale kidogo.” “Maisha yangu yote nimeshazoea kuamka kabla ya saa 11 asubuhi. Sikumbuki kuamka kabla ya hapo. Kwa hiyo nipo sawa tu.” “Haiwezekani!” “Kweli tena, tokea nipo mtoto.” “Na mchana huwa unarudi kulala?” Nanaa akacheka sana. “Urudi kulala mchana halafu nani atafanya kazi?” Geb akamwangalia Nanaa akabaki anashangaa. 

“Sasa kwa nini ulikuwa unaamka mapema?” Geb akaendelea kuhoji. “Nilikuwa naamshwa kusaidia kazi, au kuwaandaa kina Viola kwenda shule. Labda kuhakikisha kabla hawajaamka nguo zao zimepigwa pasi, soksi zote zipo tayari, viatu visafi, na chai ipo tayari ndio unawaamsha. Kama watataka kuoga asubuhi, si unajua Moshi kuna baridi? Basi unakuwa ulisha wachemshia maji yakuoga, ili waoge. Wakishamaliza kunywa chai, unaosha vyombo, ndio na wewe ujiandae haraka uwahi shuleni.” Geb aliulimia sana, kwani kina Viola ni umri sawa na Nanaa. Lakini Nanaa alikuwa anacheka kama kawaida yake. 

“Sasa kwa nini usizifanye hizo kazi ukitoka shule?” “Ilikuwa inategemea. Wakati mwingine Viola na mdogo wake walikuwa wakitoka shule, wanaenda tuition. Mimi nawahi kurudi nyumbani kupika. Wakirudi wanakuwa wamechoka. Labda wanasema wanataka kula kwanza. Kwa hiyo inabidi kuwatayarishia chakula. Wakimaliza kula, unamsaidia dada kuosha vyombo. Maana kazi ya kupika mara nyingi ilikuwa hivi, mchana nikiwa shule ni dada ndio anapika. Jioni nikitoka shule napika mimi na kuosha vyombo vya usiku. Kutayarisha vitafunio vya asubuhi ilikuwa inategemea. Kama mimi na dada hatujachoka sana, tunapika usiku ili tukiamka inakuwa kupika tu chai. Mama Mkubwa hakuwa anataka chai iliyo lala. Tukichoka sana, ndio tunaamshana asubuhi asubuhi. Mimi napika kitafunio, yeye anafanya kazi nyingine.” Nanaa akaendelea.

 Haya, turudi ratiba ya usiku, kama nilivyokwambia mimi ndiye nilikuwa mpishi wa usiku. Napika, nawatayarishia mezani au sebleni walipokaa. Unawasubiria wale. Wakati wao wanakula labda na mimi nakula kama sijachoka sana au siumwi ndio nitakula. Lakini mara nyingine wakati wakila kama nimechoka, nasafisha jikoni kupunguza kazi huku unawachemshia maji ya kuoga na kuwawekea kwenye ndoo mpaka kiasi cha kuwatosha wote. Wakishakula hiyo usiku, unatoa vyombo na kuwapelekea hayo maji bafuni ili waoge. Wakati wanaoga ndio unakusanya nguo zao za shule kwenda kufua, na kuosha vyombo. Hapo inakuwa usiku tayari, na mimi nakuwa nimeshachoka, nataka kwenda kulala, tayari kwa asubuhi.” Geb alizidi kushangaa.

“Kwani walikuwa na sare ya shule moja tu?” “Mbili. Lakini Mama mkubwa hakuwa anataka kulaza ndani nguo chafu au vyombo vichafu. Lazima mkienda kulala, mnaacha nyumba yote safi. Hata na mimi ilikuwa inanisaidia kufua nguo chache kuliko nikizirundika zikawa nyingi.” “Ngoja kwanza Nanaa. Ulikuwa ukiwafulia wote?” “Ndiyo. Sasa unafikiri nani atafua?” “Wao wenyewe au msichana wa kazi!” Nanaa akacheka. 

“Pale ndani tulikuwa tunafuga kuku, ng’ombe na mbuzi. Kwa hiyo dada alikuwa akikamua kila siku asubuhi na jioni akisaidiana na baba mkubwa. Mama mkubwa alikuwa akinunua tu majani, hapakuwa na kijana wakufuga. Ila kusafisha banda walikuwa wanalipa kijana wa jirani anakuja kusafisha. Ila ikitokea huyo kijana hajaja labda amepata dharula, ndipo tutasaidia. Kwa hiyo dada alikuwa akimka asubuhi kama mimi. Anakwenda kwenye banda la kuku kuokota mayai. Kuosha vyombo vyao na kuwaekea chakula na maji. Pakianza kupambazuka, anahamia kwenye banda la ng’ombe kukamua. Wakati huo na mimi nafanya kazi za ndani.” 

“Kwa nini kina Viola walikuwa hawakusaidii lakini!?” Geb akamkatisha. “Walikuwa wakilalamikia baridi ya asubuhi na jioni. Hawawezi kukaa nje au kushika maji ya baridi. Na mara zote walikuwa wakitoka shule wanakuwa wamechoka.” Geb akamwangalia Nanaa akanyamaza akaendelea kuendesha.

“Lakini Geb, namshukuru sana Mungu. Katika yote hayo, niliweza kusoma. Japokuwa sikuwahi kufaulu sana darasani, lakini nilikuwa nikipita kwenye hayo madarasa kimiujiza ujiza tu. Sikuwahi kuwa na masomo ya ziada, tuition. Sikuwahi kuwa na makundi ya kujisomea, au muda wakukaa chini kurudia nilichofundishwa darasani. Kama sikuelewa darasani, ndio basi tena. Sikutani na hayo madaftari mpaka nikiwa darasani. Lakini Mungu alikuwa ananipitisha kwa namna yake.” Geb alimwangalia na kunyamaza.

“Hakuna kipindi ulikuwa ukichoka?” Baada ya muda Geb akauliza. “Kuchoka na kazi, hapana. Kwa kuwa sikuwa najua maisha mengine mbali na yale. Nimezaliwa hapo, na kukua hapo. Hata wakati wao walipokuwa wakisafiri labda wanaenda kwa bibi kijijini, kama nitachukuliwa mimi, basi ujue ni kwenda kuwasaidia kazi. Kwa hiyo hata tunapokuwa huko kijijini ratiba inaweza isibadilike sana. Au naweza nikaongezewa majukumu mengine kwa kuwa dada anakuwa amebaki yeye nyumbani. Na kama nitabakishwa mimi, ujue dada wa kazi atakwenda nao. Kwa hiyo majukumu yote ya pale ndani nabakiwa nayo mimi. Tokea ninakuwa nilikuwa nikifanya kazi hizo hizo. Masaa ya kulala ni yale yale. Na maisha hayakubadilika sana, mpaka tulipokuwa wakubwa ndipo mambo yalipobadilika.” Nanaa akatulia kidogo kama aliyekuwa akijaribu kujituliza.

“Yalibadilikaje tena?” Geb akauliza. “Tokea zamani, kulikuwa na hii shauku ya ‘sense of belonging’. Sujui kama utanielewa. Yaani ile shauku ya kutaka kuhisi ninahitajika mahali, au kwetu ni sehemu fulani. Yaani na mimi nihesabike kama ni mmoja wa familia hiyo sio mzigo. Yaani ni kama nilikuwa natamani itokee siku moja mtu ananiambia ananihitaji mimi.” Nanaa akaanza kutokwa na machozi.

******************************************

Geb akakumbuka mkasa aliomsimulia. Kuanzia yupo tumboni wazazi wa mama yake walimfukuza mama yake Nanaa, hata mwanaume ambaye alisadikika ni baba yake Nanaa, alimkana mama yake alipopelekwa mjamzito akiwa na mama yake mkubwa. Na hata baada ya Nanaa kuzaliwa akiwa mtoto mdogo kabisa ndio amezaliwa tu baada ya kifo cha mama yake, mama yake mkubwa aliporudishwa nyumbani kwa huyo mwanaume, wazazi wa huyo mwanaume walimfukuza mama mkubwa akiwa na Nanaa.

******************************************

 “Pole Nanaa.” Geb alijikuta akitoa pole baada ya kumbukumbu hiyo kujirudia akilini mwake. “Yaani habari au jambo la kwanza nahisi nililolielewa tokea napata akili zangu na mama mkubwa alihakikisha analiweka sawa, kuwa pale ninapoishi sio kwetu, nasaidiwa tu, na mimi ni mzigo. Yaani hilo ni jambo nilikuwa nikiambiwa nafikiri kila siku, mpaka majuzi nilipoenda kumsalimia kwa kaka James, aliniambia. Mama mkubwa alihakikisha ninaelewa hilo. Hakuacha kunilalamikia kuwa anahangaika sana kuniweka pale. Baba mkubwa alishakataa kunisaidia kwa lolote. Kwa hiyo niliishi hapo kwao, mama mkubwa ndiye alikuwa akinihudunia kwa kila kitu. Lakini Geb, hakika nilikuwa nikilipia ule msaada kwa machungu sana. Hata akikupa shilingi yake, atahakikisha atakuelezea jinsi alivyoipata kwa shida. Jinsi ambavyo anamahitaji mengi, lakini inamlazimu kunipa mimi. Na mara zote alikuwa akijiambia mbele yangu kuwa mimi ni mzigo ambao hajui atautua lini.” Nanaa aliongea huku akitokwa na machozi. “Pole sana Nanaa. Naomba usilie.” Geb akajaribu kumtuliza. Akatulia kidogo.

 “Unajua, nilizaliwa mwaka mmoja na Viola. Mama yangu akafa akiwa anajifungua kama nilivyokusimulia. Kwa hiyo anasema tokea nazaliwa mpaka leo, nimekuwa tatizo ambalo hajui Mungu atampumzisha lini. Anasema hakuwa akilala tokea mimi nazaliwa kwa kunibadilisha nepi na kuninyonyesha. Ilibidi kuninyonyesha kama Viola kwa kuwa anasema nilikuwa mlizi sana. Anasema nilikuwa nikilia usiku kucha. Kwa hiyo anasema hakuwa akilala kwa ajili ya kunibembeleza na kuninyonyesha.  Na anasema mpaka leo halali akifikiria jinsi ya kunilea. Anasema ni mzigo ambao hajui ni lini Mungu atampumzisha nao. Na ndio anasema sasa hivi ndio imekuwa mbaya zaidi.” “Daah! Pole sana. Pole Nanaa. Naomba usilie. Geb alizidi kuumia.

Nanaa alitulia kidogo.  “Kwa nini anasema sasa hivi imekuwa mbaya zaidi wakati hauishi naye tena?” Geb alikuwa na maumivu yaliyompelekea kutaka kujua zaidi. “Anasema alijua kaka ndio angekuwa msaada pale nyumbani, lakini anaumia kuona misaada ya kaka yote inahamia kwangu sio kwao. Nimechukua nafasi yake kwa kaka. Kaka hawezi kusaidia ndugu zake, wala hawezi kuoa, eti kwa ajili yangu. Anasema nimekuwa tatizo ambalo halijawahi kuisha na wala hadhani kama itakuja kuisha mpaka naona nije kuwa na kwangu, na maisha mbali na yeye na watoto wake. Hapendi kabisa hivi kaka James anavyonisaidia. Anaumia sana. Kadiri siku zinavyokwenda ndivyo nahisi nachoka moyoni. Sijui nifanyeje kujikwamua. Nimejitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu, lakini naona juhudi zangu zinagonga mwamba. Nikijitahidi hivi, najikuta kama siharibu kwa wengine basi ujue nitaumia vibaya sana.” Nanaa akatulia kidogo.

“Nimekuwa nikifanya kila niwezalo kuondoka pale nyumbani, au kutafuta mtu ambaye angalau atanipokea. Lakini wapi! Nimeishia kujidhalilisha tu. Wakati mwingine  nilikuwa nikifanya mambo ya ajabu, ili tu kuridhisha wanaume, wanichukue. Nakumbuka bado nilikuwa mdogo tu. Tena sekondari, wakati nikimkubali mwanaume ambaye alikuwa mkubwa kwangu. Tena alikuwa akisoma chuo kwa matumaini kuwa akimaliza chuo, akipata kazi, anichukue ili nitoke pale kwa mama mkubwa. Ndiye alikuwa mwanaume wangu wa kwanza kabisa.” “Alex?” Geb akadakia kwa kuuliza.  Nanaa akashtuka sana. 

Maana Geb aliuliza kana kwamba yeye ndio James. Yaani ni kama watu waliokuwa wakifahamiana tokea zamani. Akamgeukia vizuri. “Umemjuaje?” Geb akacheka. “Ukumbuke nimesoma na James, na ni rafiki wa karibu sana kwetu kama ndugu. Lile kundi lote pale, wengi tulikuwa pamoja tokea sekondari halafu wengine tukakutana tena chuoni. James anakupenda sana, huwa haachi kukuongelea.” Nanaa akashangaa. “Ananiongelea kwenu!?” “Kabisa. Na ukitaka kuona ubaya wa James, mtu akuguse wewe lakini si vinginevyo.” Nanaa akabaki na maswali kidogo. Asijue aendelee vipi. 

“Kwa hiyo alituambia vile Viola alivyozaa naye Alex na mama yao kuona ni sawa tu.” Geb alielezea historia nzima kwa kifupi na kumfanya Nanaa abaki anashangaa. “Kumbe unanifahamu hivyo!!?” Nanaa akazidi kushangaa. “Sio sana. Endelea.” Geb alijibu huku anacheka. 

“Lakini Geb, Viola hakuniumiza kama Alex. Yule kaka nilijitoa kwake kupita kiasi. Yaani ndiye mwanaume wangu wa kwanza kulala naye. Nilikuwa naenda umbali wa kudanganya nipo shule, kumbe nipo naye kwenye nyumba za kulala wageni, kumridhisha yeye ili anipende tu. Huku nikimuomba aje anioe. Shida yangu ilikuwa nitoke tu pale kwa mama mkubwa nimpunguzie mzigo. Na nilikuwa nikimwambia kila kitu. Yaani alikuwa akimjua Viola, tabia zake, kila kitu. Lakini alikuja kuzaa na Viola, na akawa anakuja pale pale nyumbani, ananiona vile ninavyomuhangaikia Viola aliyekuwa mjamzito wa mimba yake.” Nanaa akafikiria tena kidogo.

 “Haya, sikukata tamaa. Nilipofika chuoni tena nikakutana na kijana mwingine aliyekuwa mwaka wa pili. Tukaanza mahusiano. Jinsi alivyokuwa akionyesha kunipenda, nikajua atanioa kabisa. Yaani Geb, yule kaka alikuwa akinipenda na kunijali kupita matarajio yangu. Alikuwa akiishi Mabibo hosteli, na mimi nilipata chumba Main Campus. Lakini kila siku atataka kujua nimeamkaje na kunitakia usiku mwema. Uzuri wangu, niliujua kama upo mwilini mwangu kutoka kwake. Sikuwahi kujithamini mpaka nilipokuwa na yule kaka. Alikuwa akinisifia kila kitu changu. Tukiwa peke yetu hata mbele za watu. Angalau watu wakaanza kuniangalia kwa tofauti. Alinyanyua uthamani wangu. Kutoka mavumbini, na mimi nikajiona mtu. Nikajua kwa mara ya kwanza maishani, nimepona.” 

“Naye nikaja kumfumania na msichana aliyekuwa akijua kabisa tunamahusiano. Walikuwa darasa moja na kwenye kundi moja la kujisomea. Lakini nikawafumania. Sasa nikawa najiuliza, kama alikuwa na mahusiano na yule dada waliyekuwa wameanza naye tokea mwaka wa kwanza, kwa nini alinifuata tena mimi? Yaani ni kama alikuwa akinichezea tu! Si mwili wangu tu, mpaka hisia zangu. Tena bila huruma. Huku akijua ni kiasi gani nilikuwa nikimuhitaji.” “Huyo alikuwa Zac?” Geb aliuliza, Nanaa akamgeukia na kubaki akimtizama. Geb akacheka.

“Kwa hiyo wewe unafahamu kila kitu changu!?” Geb akazidi kuckeka. “Nilikwambia huwa sisahau kitu, Nanaa. Sasa wakati upo kwenye mahusiano na Zac, James alituambia kuwa amefurahi angalau ulipata mwanaume mwingine anayeonekana kukupenda na kukuthamini. Alikuwa amekuahidi akimaliza chuo atakuoa.” Nanaa akanyamaza kwa muda, akabaki akiwaza. 

“Nakusikiliza, Nanaa. Shauku yako ndio ikaishia hapo?” “Hapana, Geb. Sikutaka kukata tamaa, nikaja kuangukia tena kwa mwanaume mwingine.” Nanaa akacheka. “Unacheka nini?” “Najicheka mwenyewe! Yaani sijui nikuchanganyikiwa au vipi? Nilijitupa kwa Jamal kama mwendawazimu.” “Jamal si ni mwislamu?” “Kumbe! Yaani nilikuwa hata tayari kubadilisha dini ili tu aje anioe.” Geb akamwangalia. 

“Najua utaniona nimechanganyikiwa, lakini ndivyo ilivyokuwa. I was that desparate. Kutaka kutoka kwenye maisha ya zamani, kuingia kwenye maisha mapya. Nikajitupia kwa Jamal, akili zote na mwili, tena bila kufikiria. Hatukukaa hata muda mrefu sana na Jamal, tena hata sikumtambulisha kwa kaka, ndipo nilipokuta ujumbe kutoka kwa mkewe. Alikuwa mtu wa Tanga, ana mke na mtoto. Mkewe anamtafuta kule, kumbe yupo huku na mimi. Niliumia sana, nikimuhurumia mkewe. Alikuwa akimsubiria nyumbani, mtoto mgonjwa, kumbe yeye yuko na mimi huku anastarehe. Aliniudhi, sikutaka hata kumuangalia mara mbili, nikaondoka.” 

“Sasa si ndio kitu ulikuwa unataka? Mtu anayekuhitaji wewe kuliko mtu mwingine?” “Geb! Sio kihivyo. Yaani amuache mwanamke wake, aliyemuoa na kumpatia mpaka watoto, aje kwangu! Nitampa nini ambacho amekosa kwa mkewe? Halafu nilijua wazi ipo siku ambayo angenifanyia kama alivyomfanyia mkewe, endapo angepata mwanamke mwingine wakunizidi mimi au atakayeweza kumpa kile nitakachoshindwa kumpa. Nilitamani kuwa na mtu wangu. Mimi mwenyewe. Sio wakumpokonya mtu.” “Ulitamani?” Geb akauliza lakini Nanaa akanyamaza kwa muda.

“Eti Nanaa? Shauku imeisha?” Geb akaendelea kudadisi taratibu. “Niliachana kabisa na hayo mambo, Geb. Nilikuwa natafuta kwa juhudi zote, nimeishia kuumizwa tu, bila mapenzi ya kweli. Nimetumiwa kwa faida za watu wasiojali hisia zangu. Nimeamua kupumzika labda shule yangu ndio itakuwa mkombozi. Kabla yakufunga chuo hapa majuzi, alikuja kaka mwingine, akitaka mahusiano. Achilia mbali kina Jeff na wengineo. Yule kaka alikuja na ahadi nyingi zinazosikika vizuri. Akawa akiwahonga rafiki zangu ili kunifikia, lakini kila nilipojitahidi kufungua moyo wangu kumpokea, nilishindwa kama ninavyoshindwa kwa wengine sasa hivi. Nafikiri nimekinahiwa. Sitaki tena.  Nimegundua sina nilichobakiza kumpa mtu akaridhika na mimi. Sitaki kuchezewa tena na wala sitaki kumtumia mtu.” Nanaa akafikiria.

“Nimeamua kusitisha zoezi la ukolewaji.” Nanaa aliongeza huku akitoa tabasamu lake la huzuni. “Na imenibidi niwe hata muwazi kwa Zinda.” “Zinda ameumia sana.” “Nafahamu Geb. Lakini nilimwambia ni heri aumie sasa hivi ili aje apate mwanamke atakayempenda na kumliwaza, kuliko sasa hivi nimkubalie kwa kuwa nataka nyumba na gari! Hapana Geb. Ninashida ambayo najua Zinda angeweza kunisaidia. Tena aliniambia yupo tayari hata kama sio ndoa, basi tuwe kwenye mahusiano naye ili tuwe pamoja. Ni kitu kizuri sana kwangu kwa sasa hivi. Lakini sikutaka kumfanyia hivyo Zinda.” Nanaa akaendelea.

“Sitaki awe msaada sasa hivi, halafu nikaja kufanikiwa baadaye, nikagundua nilikuwa naye kwa ajili ya pesa au msaada aliokuwa akinipa tu. Nikajikuta hana tena matumizi kwenye maisha yangu. Nikaamua kumuacha. Ingemuuma zaidi. Ni heri nivumilie shida za sasa, natumaini muda sio mrefu nitapumzika tu. Kitu cha kwanza nipate kwangu, shule iishe, kisha nipate kazi. Naamini kutakuwa na utulivu kwangu na kwa wanao nizunguka pia. Nitapumzisha wengi.” Nanaa akamalizia hivyo, akanyamaza.

*************************************************

“Wakati mwingine mahusiano ya muda mrefu, huleta mapenzi ya kweli.” “Na mimi nilijua hivyo. Lakini si umesikia historia yangu na wanaume niliokuwa nao? Wakati mwingine haitokei hivyo. Halafu pia nimechoka Geb. Huo mchezo nimecheza sana na sijaona matokeo yake. Nimeona ni heri nipumzishe hisia zangu. Sijitendei haki. Ndio maana hata uliponitumia ujumbe, kuuliza ninaendeleaje, sikutaka hata kuweka ule ujumbe, nikafuta palepale. Najua ulifanya kiuungwana tu.” “Ki vipi?” Geb akauliza. 

“Unajua kama vile unavyokutana na mtu barabarani, unamuuliza tu ‘Mambo!’ Sio kwa kuwa unataka kujua yanayoendelea kwenye maisha yake, bali ni kama salamu tu. Na unakuwa hutegemei aanze kukuelezea matatizo yake au furaha yake, unampita tu baada ya kusema ‘mambo’, ukitegemea atakujibu tu ‘safi’ hata kama ni mgonjwa au anamatatizo. Sijui kama unanielewa?” “Kwa hiyo ndivyo ujumbe wangu ndivyo ulivyomaanisha kwako?” Geb akauliza.

“Kwa kusema ukweli ndivyo hivyo. Hapakuwa na cha ziada nilichofikiria. Kwa kuwa hukuonyesha kunijali mimi kama Nanaa. Niliondoka na kukuacha ofisini nikikwambia sijisikii vizuri. Hukuonyesha hata kujali kama ninaumwa nini, au nitafikaje nyumbani wakati nilikuaga nikikwambia sijisikii vizuri. Halafu eti  nafika nyumbani ndio unanitumia ujumbe! Kweli Geb? Nimeshapita huko. Nimejifunza mambo mengi, tena kwa machozi, ambayo hakuna aliyewahi kuyafuta. Moyo wangu umejaa madonda ambayo nayauguza kwa shida sana. Naamini ipo siku yatapona. Kwa hiyo nipo makini sana na kila neno na kila mtu, ili nisizidi kuumia. Kwa kuwa sasa hivi najijua mimi ni nani na nini nataka. Kama nimeshindwa kupata kutoka kwa mtu mwingine, afadhali nijipe mimi mwenyewe. Matatizo mengine sikujitakia. Ningetamani na mimi ningekuwa na familia kama watu wengine, lakini sikujaliwa, na sijui kwa nini. Ila matatizo mengine nakubali kabisa nilijitakia, wala sina wakumlaumu. Sasa siwezi kuendelea kujiumiza.” Ukimya mkubwa ulipita, Geb hakujibu kitu, akaendelea kuendesha.

Baada ya muda, Geb akavunja ukimya. “Samahani kwa kushindwa  kuonyesha kujali siku ile ofisini.” Geb akaongea kwa upole, Nanaa hakutegemea, akabaki na kigugumizi. “Nanaa?” “Haina shida Geb. Nimeshazoea. Hata hivyo sikutegemea kitu cha tofauti kutoka kwako. Kwa hiyo ni sawa tu.” Nanaa akajibu, Geb akamwangalia. Akajishangaa machozi yanatoka. Akajifuta kwa haraka, akaamua kubadili mazungumzo.

*************************************************

“Huko Bagamoyo unakuwa na mashamba yako ya Matikiti maji, au wakati wote unaenda kununua kwa wakulima?” “Bado sijafikiria kuwa na mashamba. Sina muda wakutosha kuanza kulima au kuwa mkulima. Kwa hiyo huwa nategea kipindi cha mavuno ndio huwa nakwenda. Leo asubuhi nimetuma lori likafuate mzigo. Kwa hiyo huwa wakati mwingine napenda sisi wenyewe kwenda kusimamia. Hasa nikiwa na dereva mgeni kama nilivyokuwa nimekwambia juzi. Dereva huyu aliyekwenda huko ni mgeni kabisa. Ndio mara yake ya kwanza. Sijamfahamu anatabia zipi. Kwa hiyo lazima kuwepo.” Akatulia kidogo.

“Halafu najikuta mimi ndio nalazimika kwenda kwa kuwa Grace anahitajika sana na familia yake.” “Nimeona. Yaani hata akiwepo pale ndani, Danny na Fili wanamfuata nyuma kila mahali.” Nanaa akaongeza. Wakacheka. “Kwa hiyo hata mikoani huwa naenda mimi mwenyewe. Kama tunataka mzigo mkubwa zaidi ya ule tuliozoea kuchukua, nakwenda kutafuta wakulima wapya na kukubaliana nao kabisa. Ili tukituma dereva anakuwa na kazi ya kubeba tu, sio kuhangaikia tena kutafuta mzigo.” “Ooh! Kwa hiyo huwa unasafiri mara kwa mara?” Nanaa akauliza tena.

“Sio sana. Inategemea na wapi nachukua mzigo, na ni mzigo gani. Kwa mfano mchele huwa najua bei zake, na nina watu wengi nafahamiana nao kwa muda mrefu. Nikitaka zaidi, sina haja ya kwenda. Nawaomba wakulima ambao nimekuwa nao kwenye biashara kwa muda mrefu, waninunulie kwa wakulima wengine wanitumie, kisha ninawalipa. Kwa hiyo kuna mikoa mingine nimeshatengeneza mahusiano ambayo yananirahisishia. Halafu kama unavyojua, katika maisha lazima ukubali kuamini mtu fulani. Lasivyo utateseka sana.” Nanaa akanyamaza akijua anajaribu kumfikishia na yeye ujumbe.

*************************************************

Akamtolea karanga akampa. “Asante.” “Nikupe na maji au juisi?” Nanaa akauliza. “Maji tafadhali.” Akatoa na kumkabidhi. “Asante.” “Karibu.” Geb akaendelea kula huku akiendesha. “Nikuulize kitu, Nanaa?” “Niulize tu” “Unapoamka asubuhi na kunitayarishia kifungua kinywa, unaona unalazimika kwa kuwa unaishi pale au?” Nanaa alishtuka sana, hakutegemea hilo swali. “Naomba uwe tu mkweli, haitabadilisha chochote.” “Sijawahi hata kufikiria. Labda sasa hivi nianze kutafakari. Lakini..” Nanaa akasita. 

“Lakini nini?” “Pale kwako ni tofauti Geb. Mama yako na Grace wamenionyesha upande mwingine kabisa wa maisha. Naogopa kusema zaidi ili nisijiwekee tumaini ambalo halipo. Lakini kuna jinsi wananichukulia, sijisikii kama ni mzigo nikiwa pale kwako.” “Lakini si unajua lazima ufungue tena moyo wako? Huwezi kuishi hivyo Nanaa. Watu wakikuonyesha upendo, lazima kuutambua huu ni upendo na kuupokea. Lasivyo utazidi kujiumiza.” “Naogopa Geb.” “Lakini hivyo hujisaidii, na itakuchukua muda mrefu sana kupona. Huwezi kutoka hapo. Kuna watu wengine Mungu anawaleta kwenye maisha yako, kukufariji. Lakini usipokuwa mwangalifu, unaweza kuwafungia watu wote mlango.” Nanaa akanyamaza.

Sitaki uishi pale, na kufanya kitu chochote kwa ajili ya kulipa fadhila. Hata usipofanya jambo lolote, ukaamka na kujishugulikia wewe mwenyewe na kuondoka pale, nakuhakikishia kabisa, hakuna atakaye kulaumu Nanaa. Mama na Grace watakupenda kwa upendo uleule wanao kupenda sasa hivi.” “Unajuaje?” “Nanaa! Lazima ukubali sio watu wote watakao kuja kwenye maisha yako, watataka kukutumia tu. Wengine watakuja kwa nia nzuri na watakupenda wewe kama Nanaa. Labda nikupe mfano utakao kusaidia. Najua kwa sehemu umeanza kumfahamu Liz ni mtu wa namna gani.” “Unamaanisha Liz mpenzi wako?” Nanaa akauliza ki uchokozi tu, na Geb akajua. Akamtazama kidogo na kurudisha macho barabarani.

Akaendelea. “Sasa Liz alisoma na Grace darasa moja. Wakajikuta wanakuwa marafiki. Alishamfanyia Grace mambo mengi sana yakumuumiza, lakini bado wakabaki kuwa marafiki na kumkubali Liz kwa tabia zake kama alivyo. Kipindi mimi nipo chuoni nje ya nchi, wakati Grace na mama wapo kwenye shida sana, bado Liz alikuwa rafiki wa Grace. Liz amezaliwa kwenye familia yenye uwezo sana, na wapo watoto wakike wawili tu. Nikikwambia wana uwezo, ni watu wenye uwezo. Liz hajui shida hapa duniani. Anaendesha magari tokea hata hajafikisha miaka 18. Namaanisha magari ya nyumbani kwao, sio yakuhongwa. Anapesa yakutosha. Walikuwa marafiki na Grace tokea zamani kama nilivyokwambia, lakini hata Grace alipokuwa na shida, Liz hakuwahi kumsaidia hata mara moja.” Nanaa alikunja uso akiwa haamini.

“Anasema wakati wapo chuoni, wakati mwingine walikuwa wakienda kula pamoja, kundi la marafiki, Grace anashindwa kujinunulia chakula, wenzake wanampunguzia chakula sehemu ili ale, lakini sio Liz. Liz haelewi kwa nini mtu anakosa pesa. Inakuaje mtu analipwa na chuo, halafu akose pesa ya kujinunulia chakula. Anaposema kwa nini watu wanazaliwa milimani au wanaishi milimani, sio kuwa anatania au anakejeli, ni kweli haelewi. Na kingine Liz ni muwazi sana. Hawezi kuficha hisia zake. Anaongea kile anachofikiria akidhani ni jambo la kawaida tu au na wengine walitakiwa waelewe hivyo. Anashangaa pale wengine wasivyofikiria kama yeye. Haelewi.” Nanaa akainama huku akimfikiria Liz.

“Amesoma bila shida na kupata kazi bila tatizo lolote. Sio kama mimi nilivyokwambia ilibidi mama kuniombea mpaka vyeti na mimi kuzunguka karibia mji mzima kutafuta kazi. Sio Liz. Alikuwa anamalizia chuo, akiwa na ahadi ya kazi tayari. Ana ndugu na marafiki wanaoshika nyadhifa kubwa sana hapa nchini. Amezaliwa kwenye pesa, na yeye sasa hivi anaingiza pesa nzuri tu bila shida. Huwezi kumueleza mtu anakosaje pesa akaelewa. Anaishi kwenye jumba la thamani. Kubwa na wapo wao tu. Familia ya watu wanne. Hawajawahi hata kuona ndugu analala nyumbani kwao. Amekuwa akiona wageni wakija kutembea kwao wametokea nchi za nje, si kijijini na wanalala hotelini. Na kama watakaa kwa muda mrefu, watawakodishia nyumba mahali. Zile nyumba ambazo zipo full furnished. Kwa hiyo haelewi inakuaje watu wengi wanaishi nyumba moja.” Nanaa akacheka taratibu kama na yeye asiyeelewa asichoelewa Liz.

“Kweli tena. Haelewi kwa nini mtu atake kupumzika aende sehemu kama Marangu! Au useme unakwenda likizo kijijini. Haelewi kwa kuwa hana marafiki wa namna hiyo na wala hajawahi kukaribisha mazungumzo ya matatizo kwenye maisha yake. Yaani kwa Grace ilimbidi tu kwa kuwa mwaka wa kwanza walijikuta wamepewa chumba kimoja. Japokuwa hakuwahi kulala chuoni hata siku moja sababu ya mazingira yale ya hosteli yalimshinda, lakini alikuwa akiacha madaftari yake chuoni na kusoma na kina Grace darasa moja na kundi moja. Alikuwa akiendesha gari ambalo hata maprofesa pale chuo wakati ule walikuwa wakishangaa. Tena jipyaa. Sio lililotumiwa huko Japan. Anaingia chuoni asubuhi, na kurudi kwao usiku. Anaweza kukufanyia kitu, ukabaki huelewi. Lakini sio yeye. Yeye anaona ni kawaida tu. Kila mtu anamfahamu hivyo Liz.” “Kwa hiyo unachojaribu kuniambia na mimi ni kujaribu kumuelewa mpenzi wako na kumpokea kama wengine?” Tayari wivu ulishakuwa ukimtesa Nanaa.

 Geb akamtizama kidogo, kisha akaendelea. “Katika yote hayo, bado Grace anamtamka Liz kama rafiki yake na akaja kumtambulisha kwangu, na kuniambia ananipenda. Yaani akaniunganisha naye. Tumeanza mahusiano, ndio baadaye anakuja kuniambia tabia za Liz na kuniambia nisimshangae, ndivyo alivyo. Na nikikwambia ni rafiki yake, ni marafiki. Hata kitendo cha Liz kunilalamikia mimi kwa nini ninaishi nao, Grace na mumewe, Grace anakijua, alishamsikia akinilalamikia tukiwa jikoni, anataka Danny na familia yake waondoke pale ndani. Grace akaingia nakucheka tu. Baadaye nikajaribu kuongea na Grace kama kumtuliza kwa yale mazungumzo aliyotusikia tukizungumza na Liz, chakushangaza yeye ndio akanituliza. Aliniambia nisiwe na wasiwasi, yeye anamuelewa Liz vizuri kuliko mimi ninavyomuelewa. Alishaishi naye chuoni kwa miaka 3. Hamsumbui. Nilishangaa kidogo, ndipo na mimi nikajifunza kuwa kuna watu kwenye maisha, wanapendwa vile walivyo. Sijui unanielewa?” “Nimeelewa.” Geb akamwangalia.

“Umenielewa kweli?” “Nimeelewa Geb.” “Basi naomba uanze kuishi pale nyumbani ukiwa unajisikia uhuru wote. Usifanye kitu ambacho hujisikii kufanya. Nakuhakikishia hakuna atakaye kulaumu.” “Lakini sijafanya kitu chochote ambacho nimelazimisha Geb. Yote ninayofanya sasa hivi ni aidha ni kwa kuwa nipo hivyo, yaani sijui jinsi ya kufanya vinginevyo, au nafurahia kufanya.” “Kama nini unafurahia kufanya?” Geb alitaka kujua zaidi, ili ahakikishe ayasemayo Nanaa.

“Kukupikia chakula au kukufanyia wewe kitu ambacho kinamsaada. Yaani kuona nafanya kitu, halafu naona mtu mwingine anafurahia, najisikia vizuri. Hata kama sitashukuriwa, lakini najiona sio mtu wa hasara. Geb akamwangalia na kutabasamu.

“Kweli tena. Kwa mfano, mwanzoni hukuwa ukijua kama mimi ndio nakupikia chakula, au uji. Lakini kule kukuona unakula, nakufurahia kama amekufanyia mama yako, kwangu ni furaha tosha. Siku ya kwanza kumuomba mama yako nikupikie, aliniambia nijaribu, tusikwambie, kama utaona tofauti na hautakula, ataendelea kupika yeye mwenyewe. Lakini kama utakula bila kulalamika, ataniachia. Akaanza kuniachia kukupikia uji kwanza kabla ya chakula. Siku ya kwanza nilipopika mimi uji, ukauchukua kwenda nao kazini, hukunywa ule wa kwenye bakuli kwa kuwa ulichelewa kuamka. Ukasema utakula ukifika kazini. Ukaondoka na ule wa kwenye chupa. Uliporudi jioni mama akakupokea chupa, kisha akaniita jikoni akaniambia umeupenda ule uji ndio maana uliumaliza wote.” Nanaa akatabasamu kisha akaendelea.

“Siku nyingine akaniachia nikupikie mchemsho wa samaki na ndizi. Lakini alikuwa ameshanifundisha jinsi ya kukupikia. Nakumbuka ilikuwa siku ya jumamosi mchana. Ukala, ukatoka na Fili kwenda kucheza mpira na wenzako. Ilipofika jioni ukampigia simu mama yako ukamwambia njaa inauma, lakini unataka ukirudi, ukute chakula kama alichokupa mchana. Mama yako akaniita na kuniambia utakuwa umekipenda sana, kwa kuwa huna tabia yakurudia chakula, labda uji. Ndio akaniachia hiyo kazi mimi.” Geb alikuwa akimsikiliza kwa makini tu.

“Lakini Geb, nasema kweli, kwa mara ya kwanza maishani nilijiona ninamanufaa. Kaka James anakuwa ananishukuru sana, mpaka wakati mwingine nilikuwa najisikia vibaya. Tokea tupo nyumbani kwao, kila kitu nilichokuwa nikiwafanyia ndugu zake, hata mama yake, walikuwa wakikosoa. Tena kwa kunigombesha sana au kupigwa, lakini sio kaka. Tena wakati mwingine alikuwa akinipa mpaka pesa kunipongeza kwa kazi nzuri ninayofanya, na kuniambia ninunue chochote ninachotaka. Sawa, nilikuwa napata pesa yakujinunulia vitu vyangu binafsi, lakini kwa upande mwingine nilikuwa nikijiambia labda nakuwa nakosea, yeye ananitia moyo tu. Sasa kuona nafanya kitu pale nyumbani kwako, na wewe unakikubali, halafu hujui kama ni mimi ninafanya, nafurahia sana Geb. Sijali kama unajua kama ni mimi au la, kwa kuwa najua mimi ni mpita njia tu, nitaondoka hivi karibuni na mnaweza msinikumbuke tena, lakini huwa natamani muda wa kukupikia ufike, nipike  ili nimpokee hiyo kazi mama yako anayeonekana kuridhika na ninachofanya halafu na wewe ule bila shida. Inanifariji kwa upande fulani.” Nanaa akacheka kidogo. 

“Haya, kingine najiona nafanya kitu cha maana vile Danny anavyoshukuru kwa kupata kifungua kinywa tofauti tofauti kila siku asubuhi. Alimwambia mpaka kaka, kaka akanipongeza. Na wakati mwingine Danny huwa anambebea na yeye kaka. Kwa hiyo kaka naye anapata kitu cha kula kazini.” Nanaa akaendelea.

“Kingine ni vile Grace anavyoniomba nimsaidie kumuogesha au kumlisha mtoto wake. Naona ameniamini, au amefurahia ninavyomfanyia mwanae, na mengine mengi tu. Pale kwako kunanisaidia kwa upande fulani. Najua hata nikiondoka pale, kutakuwa na kitu kingine kimejengeka kwenye nafsi yangu tofauti nilivyojengwa na maisha tokea nakua.” Geb akamtupia jicho kidogo akaendelea kuendesha. 

*************************************************

Baada ya ukimya kidogo, Nanaa akatupia swali. “Kwa hiyo umeelewa kwa nini sikujibu ujumbe wako?” Geb akatulia kidogo. “Nafikiri nimeelewa. Lakini imeniumiza.” “Kwa nini tena!?” Geb akanyamaza kidogo kama anayefikiria kitu. Kisha akaongeza, “Unajua nakumbuka maongezi yote yaliyokuwa yakiendelea siku ile? Kila neno nililokwambia na vile ulivyonijibu, Nanaa.” Nanaa akamwangalia. 

“Sijui kama wewe unakumbuka? Lakini mimi nakumbuka vizuri tu. Ulinyanyuka gafla, nikakuuliza, ‘vipi?’  Unakumbuka jinsi ulivyonijibu?” Nanaa akanyamaza. “Ulinijibu kwa ukali, Nanaa. Uliniambia ni muda wa kula, unaenda kula, kisha ukaondoka hapo hapo. Baada ya muda ulirudi, nilikuona kabisa haupo sawa, nikakuuliza tena, ‘kwema?’, ukanijibu kwa kifupi sana, ‘najisikia vibaya, naenda kupumzika’. Hapo hapo ukachukua pochi yako na kuondoka. Ningefanyaje?” “Angekuwa Grace au Liz, ungefanyaje?” Nanaa alitupia swali la harakaharaka, nakumfanya Geb ashindwe kujibu. Waliendelea kuendesha kimya kimya mpaka walipofika. 


Wakiwa Bagamoyo!

“Naomba kabla hujashuka, umalizie hizo karanga, Geb. Zimebaki kidogo tu hapo.” “Asante. Nilishazisahau. Nisaidie chupa nyingine ya maji ili nisafishe meno baada ya hapa, ili nisishuke na meno yaliyojaa karanga.” Nanaa akacheka. “Naona huyu dereva mpya amejitahidi. Sijui amefika saa ngapi! Anamalizia kupakia. Naona hatutakaa sana.” “Namimi naomba nishuke.” Geb akacheka. “Mbona unanicheka?” Nanaa akauliza. “Utachafuka.” Nanaa akajiangalia. “Haina shida. Nikirudi nitaoga. Sitaki kukaa humu ndani kama mtalii.” Geb alitabasamu huku akimwangalia na kumalizia kunywa maji yake. “Basi twende.” Wakashuka pamoja.

Geb alisalimiana na wenyeji wake na kurudi kwenye lori kusaidia kupakia. Nanaa na yeye akaanza kusaidia. Alikuwa akikusanya matikiti maji yaliyosambaa, na kuwasogezea karibu. Baada ya masaa mawili wakawa wamemaliza kabisa. “Pole.” Nanaa alimsogelea Geb. “Asante. Pole na wewe.” “Kumbe ukija huku na wewe huwa unafanya kazi! Nilijua huwa unasimamia tu.” Geb akatabasamu. “Wakikuona na wewe unafanya kazi na wao wanapata moyo, wanaongeza juhudi.” “Lakini umelowa!” “Nimekuja na nguo zakubadilisha.” “Kumbe unakuwa unajua!?” Geb akatoa tabasamu jingine kama kawaida yake.

“Lazima. Huwa sipendi kufika sehemu nisimame tu. Napenda kufanya nao kazi.” Akajibu na kumuuliza Nanaa swali. “Umechoka?” “Bado nina nguvu tu. Kuna sehemu nyingine ya kwenda kupakia?” “Hapana. Hapa ndio mwisho, na naona lori lenyewe limejaa.” “Kwa hiyo hapo unakuwa umeshapata wateja?” “Kwa huo mzigo, ndiyo.” “Hongera.” “Asante. Lakini sio mara zote inakuaga hivyo. Si unaona hata kwenye ripoti ile niliyokusaidia kutengeneza tukampa Grace, nilionyesha kuna hasara?” “Nakumbuka.” “Basi ujue kuna mzigo uliokuwa umeharibika. Wakati mwingine dereva anaweza kuharibikiwa na Lori porini, matunda yote yakaharibika. Au ukatokea uzembe pale ofisini kama nilivyokuwa nikimwambia Grace. Mtu wa masoko asifuatilie wateja kwa wakati, mzigo ukafika, ukawa hakuna pakwenda kwa haraka, ukaishia kuharibika tu.Tunaongeza hasara. Kwa hiyo ndio biashara.” Nanaa alibaki akiangalia lile lori.

“Unaratiba gani baada ya hapa?” Geb akauliza. “Yule dalali amenitumia ujumbe. Ameniambia kuna chumba amepata kule mitaa ya Savei karibu na chuo. Amesema kama naweza kwenda leo, ingekuwa vizuri, ili nikakiangalie. Lakini nimemwambia nipo mbali kidogo, sijui ni muda gani nitarudi. Ameniambia muda wowote nitakapofika mjini, nimtafute anaweza kunipeleka.” Geb alibaki akimwangalia. “Lakini haina haraka, amesema hata kama ni usiku atanipeleka tu. Kwa hiyo haina haraka.” Geb alivuta pumzi kwa nguvu. Akazishusha kwa wakati mmoja.

“Naomba nisubiri kidogo. Nataka niagane na huyu dereva, nitarudi sasa hivi.” “Sawa.” Geb akaenda kuzungumza na yule dereva huku Nanaa akimwangalia. Alitoa pesa akamkabidhi. Wakazungumza kidogo, Geb akarudi na matunda. “Nimembembea Fili matunda ya juisi. Twende.” Wakaingia kwenye gari.

 “Asante.” Geb akashukuru. “Kwa nini?” “Kusaidia kazi.” Nanaa akacheka. “Karibu. Na mimi nimefurahia kuja huku.” “Sasa hivi bado mapema sana. Tunaweza kwenda mahali tukakae kwa muda mfupi, ndio turudi nyumbani?” “Sawa.” Geb akaondoa gari. Wakaendesha umbali kama wa dakika 20, ndipo wakaanza kuona mahoteli. Aliingia kwenye hoteli moja nzuri, akaegesha gari. “Tuingie humu, lakini mimi nitaanzia chooni kwanza. Nijisafishe kidogo, halafu nitabadili t-sheti. Nimejichafua. Naona mwenzangu ulikuwa mwangalifu.” Nanaa akacheka kidogo. “Nikusubiri hapa hapa ndani ya gari?” “Kama hutajali. Sitachelewa sana.” “Sawa.” Geb alichukua kibegi kidogo nyuma ya gari, akaondoka.

Na kweli baada ya muda mfupi, Geb akarudi akiwa anaonekana msafi, akiwa amevaa t-shet nyingine, na alionekana alinawa kidogo, maana hata uso ulionekana umetulia. “Twende ndani.” “Nishuke na uji?” Geb akafikiria kidogo. “Nikikosa kitu cha kula humo ndani, ndio tutarudi kuja kuuchukua. Nataka kunywa baadaye.” Nanaa akashuka, wakaongozana mpaka ndani. Alitafuta sehemu wakakaa. “Pazuri sana. Sijawahi kufika sehemu nzuri kama hii.” Nanaa akasifia, Geb akacheka kidogo. “Usinicheke bwana! Unafikiri maeneo kama haya huwa nafikaje sasa?” “Nakuelewa. Napapenda hapa, huwa pametulia.” Muhudumu akawasogelea kutaka kujua wanataka kula nini. “Mimi bado nimeshiba, Geb. Nimekula sana korosho na ile soda yote nilimaliza, njiani.” “Unauhakika?” Geb akauliza. “Kabisa. Nikisikia njaa nitaagiza.” Nanaa akajibu. “Basi. Asante. Tukihitaji kitu tutafuata tu. Asante sana.” Geb akamshukuru yule muhudumu, akaondoka na kuwaacha wawili.

*************************************************

Kila mtu alikuwa kimya akiangalia sehemu yake. “Nanaa!” Geb akaita, Nanaa akageuka. “Naomba unisamehe, kwa kutokujali uliponiambia hujisikii vizuri siku ile ofisini. Nisamehe kwa kukuacha ukaondoka bila kujali. Samahani.” Nanaa aliona machozi yanatoka. Akajifuta mara kadhaa. “Samahani. Sikufanya vizuri. Na najua angekuwa Grace au Liz kama ulivyosema, ningefanya tofauti, lakini nilikosea. Samahani. Haitakaa itokee tena. Wakati mwingine nitakuwa makini.” Ilimgusa sana Nanaa. “Kwa hiyo naomba unisamehe.” Nanaa alitingisha kichwa kukubali huku akikausha machozi. “Asante.” Geb akashukuru, wakatulia tena.

“Nikuombe kitu kingine?” Geb akauliza. Nanaa akatingisha kichwa kukubali. “Naomba usiondoke nyumbani.” Nanaa aliinama na kukunja uso. “Naomba tuishi wote, mpaka chuo kikifungua ndio unaweza kuchukua chumba pale ‘Main campus’, tukakiweka kwa ajili ya siku za mitihani au siku unazotaka kuwepo chuoni kwa ajili ya kujisomea na wenzako. Lakini kwa sasa naomba tuishi wote.” “Sidhani kama ni sawa, Geb. Acha tu niondoke, nitakuwa nikirudi kuwasalimia.” “Kwa nini?” Nanaa akabaki kimya.

“Eti Nanaa?” “Sijui niseme nini Geb. Lakini naomba uwe na amani. Umeshanisaidia, au nimeshasaidiwa vyakutosha. Ngoja na mimi nianze maisha yangu. Naomba usijisikie kama unajukumu lakutimiza kwenye maisha yangu. Huku kukufahamu  kwa muda huu mfupi tu, umeacha somo kwenye maisha yangu. Na ninakushukuru. Naona na mimi nikatumie yale niliyojifunza kwenu. Naamini na mimi nitakuja kuwa msaada siku moja kwa mtu mwingine.” 

“Mbona hata sasa wewe ni msaada kwetu. Huwezi jua faraja unayoileta pale nyumbani. Mama anakupenda Nanaa. Amepata rafiki wakuzungumza naye. Grace anakuwa busy sana na mtoto wake  na mumewe. Muda mwingi anajikuta anakazi, au hao watu wawili wanamuhitaji, hana muda na mama kama ulivyoona. Halafu hata hivyo karibuni sana wanaondoka. Nyumba yao imebakia padogo sana kukamilika, watahama. Tutabakia wapweke kweli.” Nanaa akacheka kidogo. “Liz si atakuwepo?” Nanaa akatupia swali na kumfanya Geb atulie kidogo. “Naona kama mama amekuzoea wewe zaidi.” Nanaa akamwangalia, nakunyamaza. “Eti, Nanaa?” “Kwa hiyo unataka nibaki kwa ajili ya mama yako?” Nanaa akauliza, lakini Geb hakujibu. Akanyamaza.

Walizungumza mambo mengine. Baada ya muda, Nanaa akasema njaa imeanza kumuuma. Walimuita muhudumu, wakaagiza chakula. Geb alitaka ugali, nyama choma, na kachumbari. “Lakini usiweke kitunguu wala karoti. Iwe nyanya, tango na limao tu.” Nanaa akacheka. “Usinicheke bwana Nanaa. Huoni nimeagiza chakula?” “Kuagiza ni hatua ya kwanza, na nzuri sana, tena huwa unapenda kweli kuagiza. Kikija na kukiweka mdomoni ndipo kazi ilipo.” “Basi leo nitahakikisha kinaingia mdomoni.” “Tutaona.” Geb akacheka. “Na wewe utakula nini?” “Nyama ya kuchoma na ndizi za kukaanga. Naomba na kachumbari kama ya Geb lakini mimi weka karoti.” Muhudumu akaandika, na kuondoka.

Chakula kikaletwa. Nanaa akamuona vile Geb anavyokiangalia, akajua hatakula. “Geb! Naomba kabla hujakikataa hicho chakula kwenye akili zako, jaribu kukiweka kidogo tu mdomoni. Naomba usishibe kwa macho.” Geb akacheka. “Ulijuaje? Nishaangalia hii kachumbari ilivyowekwa hapo, ikanikinahi kwa haraka sana. Nyama yenyewe ni kama imekaushwa sana, ugali kama umepoa!” “Naomba jaribu kuchukua hatua nyingine. Naomba jaribu kuweka mdomoni. Jaribu tu. Halafu uniambie na mdomoni kinakuaje.” Geb akacheka huku akikiangalia kile chakula. 

“Kwani nikikuagiza kuku wa kuchoma itachukua muda gani?” Geb akamgeukia muhudumu. “Nakuomba ujaribu kidogo tu. Nakuomba Geb. Najua utaagiza tena huyo kuku, itakuwa tena kama hiyo nyama ya ng’ombe, hutakosea sababu. Unakumbuka majuzi mchana? Uliponifuata kazini, tukaenda kula chakula cha mchana?” Geb akacheka. “Wale waliacha nyama ina damu bwana.” “Unakumbuka uliagiza nyama ya ng’ombe tena? Ukashindwa. Ukaomba kuku wa kuchoma. Pia ukashindwa. Ukataka tena samaki. Akaletwa. Vyote ukaishia kuviangalia kwa macho bila kuweka mdomoni. Tukaishia kuondoka hujala, lakini umelipia vyakula vya watu karibia watano.” Geb alibaki akicheka.

“Kumbe siku ile ulikuwa ukiniangalia tu. Leo umeamua kunitolea uvivu?” “Leo umefanya kazi ngumu sana, unahitajika kula. Naomba ujikaze kula hata kidogo. Utaenda kuongezea na uji kwenye gari.” Geb alivuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha huku akiangalia kile chakula chake. “Sawa. Nitakula hiki hiki.” “Kwa hiyo nisilete tena kuku?” Muhudumu akamuuliza Geb, Nanaa akabaki akimwangalia, akacheka. “Hapana. Nitakula hikihiki chakula. Asante.” Muhudumu akaondoka. 

“Chakula ni kizuri Geb. Jaribu.” Geb alianza kula taratibu. Nanaa alikuwa akimwangalia. “Vipi nyama?” “Sio mbaya. Ni laini kwa ndani, tofauti inavyoonekana.” “Na ugali ni baridi sana? Kama nibaridi naweza kuwapelekea, niwaombe watupashie.” “Naona inatosha. Asante.” Geb alijibu kwa tabasamu. Alionekana anafanya kazi asiyoipenda kabisa. Heri ile kazi yakupandisha matunda kwenye Lori alionekana amechangamka sio kama kula kile chakula pale. Lakini alijitahidi, akala zaidi ya nusu. “Naomba nikamalizie na uji. Hiki chakula kilikuwa kingi sana.” Nanaa akacheka. “Hata hivyo umejitahidi.” Geb akacheka.

Nanaa akamaliza chakula chake chote. “Umeshiba?” Geb akauliza. “Sana. Nahisi nikipanda tu kwenye gari, nitalala.” Geb akacheka. “Unaniacha niendeshe mwenyewe?” “Nakutania bwana. Mimi si ndio nakulinda?” “Kama unanilinda mbona unafikiria kunikimbia sasa?” Nanaa akainama. “Usiondoke bwana Nanaa. Naomba tubaki wote. Wewe huoni ukiwa na mimi unavyonihimiza kula? Unanipikia vizuri, unanisindikiza huku. Nakuwa sipo mpweke. Usiondoke bwana.” “Kwani huwa hujagi huku na Liz?” Geb alicheka kwa sauti mpaka akapaliwa na maji.

“Liz!?” Akazidi kucheka. “Ndiyo.” “Kwanza umeona mwili wake? Hathubutu kuja shamba. Anajipenda na kujithamini sana Liz. Sehemu kama zile hawezi kukanyaga. Kwanza kumwambia aje huku ni kumtusi. Kila kitu kinachoingia mwilini kwake lazima kiwe ni cha thamani. Kila anapoenda ujue nisehemu ambayo ni mazingira yanayoendana na mwili wake. Kila week, lazima mwili wake auweke kwenye sauna, na kufanyiwa masaji. Na akikosa hata mara moja tu, anajua kuwa week hiyo amekosa, na ni mara chache sana. Sasa mwili kama huo, huwezi kuupeleka shamba au kuuweka karibu na moto. Yaani aanze kumpikia mtu! Yeye mwenyewe hawezi kujipikia, anaogopa moto, halafu umwambie ampikie mtu mwingine! Hathubutu, na atahisi umeamua kumtukana vibaya sana. Hata kitendo cha kuja kule Marangu, nilimsifu sana. Kwake yale ni mazingira hatarishi. Na sio kwamba anajidai, ndivyo alivyo.” Nanaa akacheka kidogo na kuzidi kumtafakari Liz. 

*************************************************

Alikuwa ni binti mweusi. Mweusi mwili mzima. Rangi moja tu. Laini hata kwa kumtizama kwa macho, alionekana laini. Alikuwa na umbile namba 6 isiyo kubwa hata kidogo. Alikuwa na kamwili kazuri sana. Hakuna muda wala wakati ungemkuta Liz ni mchafu. Na wakati wote alikuwa kwenye kiatu cha juu. Hata kama ni sandals tu. Ilikuwa lazima iwe ya juu. Tena kucha safi wakati wote. Nanaa hakukumbuka kumuona amekaa mahali bila kupishanisha miguu yake. Popote alipokaa, alikunja 4. Tena alikaa vizuri, si kihasara. Wakati wote, mabega yake yalikuwa yamenyoka. Usingemkuta amepindisha mgongo hata akiwa amekaa kwenye kochi alinyooka vizuri. Ni kweli kila kitu chake kilikuwa kisafi na cha thamani. Lazima ungependa kumtizama tu. 

Jinsi alivyotembea na kujiweka, utajua anajielewa. Mikono yake ilikuwa mizuri na laini. Rangi yake ya weusi ilimkaa vizuri na alihakikisha kila anachokivaa, kinaendana na rangi yake hiyo. Hakukumbuka kuona hata kipele mwilini mwa Liz. Kila alipomkumbuka Liz, Nanaa akacheka. Hakukumbuka kumuona akifanya kitu chochote hata alipokuwepo pale ukweni. Na hakuwa mnafiki. Kila kitu aliuliza kilipo. Si kwamba hakujua vinapowekwa, bali alitaka aletewe alipo. Na akagundua ni kweli pale ndani kwa kina Geb wanamjua. Kwani kila alipoulizia kitu, aliona kama sio Geb anasimama kumletea, basi shoga yake Grace atakwenda kukifuata hicho kitu na kumpelekea alipo yeye. Nanaa akacheka tena.

*************************************************

 “Unacheka nini?”“Namfananisha Liz na watoto wa mama mkubwa. Wanafanana hivyo hivyo. Kama sasa hivi namfikiria kaka jinsi anavyoishi nao pale nyumbani kwake, nashindwa jinsi yakumsaidia kwa kuwa mama mkubwa amenikataza kwenda. Atakuwa anachoka sana. Kuwapikia, awasafishie, na bado awapeleke kila wanapotaka kwenda! Nahisi ataisha mwili wote.” Nanaa aliongea akionekana kumfikiria kaka yake.

“Unajua nilipohamia kwake, alikuwa anaishia kulala kwenye makochi? Anasema chumbani kwake pia alikuwa anapaona mbali kwa kuchoka.” “Na James anajua kujituma sana. Si kazini, si kwenye biashara zake. Anajua kujituma bila kuchoka.” “Namuombea Mungu aje kumpata mwanamke mzuri, atakayempenda na kumthamini. Anastahili.” “Kwa hiyo mimi sistahili?” Geb akauliza akisikika kumuonea wivu James.

“Unamfikiria James tu! Mimi nakuomba ubaki na mimi, unanikatalia!” Geb aliongea kwa kulalamika kidogo. “Wewe unaye Liz,  Bibi Fili na Grace. Wote hao wanakulea kama yai. Huhitaji mtu waziada kwenye maisha yako Geb. Lakini sio kaka. Kaka yupo peke yake.” Geb alicheka sana

“Umesema wananilea kama yai?” “Kabisa. Wakiwa wanamzungumzia Geb, unaweza kufikiri wanamzungumzia mtoto wa chini ya miaka 10. Kila mtu anawasiwasi wa ulipo, umekula nini, au ulisikikaje mara ya mwisho kwenye simu. Kama uliongea kwa huzuni au furaha. Mara ya mwisho wa kusikika ni saa ngapi. Hayo yote ndio mazungumzo ya Grace na mama yako.” Geb alicheka sana.

“Yaani wewe huna haja ya mtu mwingine kwenye maisha yako, Geb. Na ndio maana unauwezo wa kuishi na Liz bila shida na wala usione kama umepungukiwa. Kwa kuwa umezungukwa na watu wanaokufikiria wewe wakati wote. Lakini sio kaka. Hamna anayemjali yeye kama James. Wakati wote nyumbani kwao wanamuomba pesa. Hawajali kama anazo au hana. Hawajali kama yeye mwenyewe ni mzima au la. Akipigiwa simu mpaka utamuhurumia. Wakati wote ni simu za matatizo. Na lazima asaidie. Asiposaidia kosa la kwanza na kubwa ni kuendelea kumsaidia Nanaa.” Nanaa alikuwa akiongea kwa upole na masikitiko.

“Ataambiwa Nanaa anamkosi, hakuna mahali anapoishi mtu akafanikiwa, au Nanaa ana roho ya chuma ulete. Ndio maana eti anafanya sana kazi lakini haoni matokeo mazuri. Maneno mengii, mpaka utamuhurumia kaka. Na hapo anakuwa ametoka kuwatumia pesa hata week haijaisha. Na mama mkubwa bado anabiashara zake, na zote zinamwingizia pesa. Japokuwa baba mkubwa alistaafu, lakini pia anabiashara zinazomwingizia pesa. Ila baba mkubwa yeye ni afadhali. Huwa hamuombi kaka pesa. Akipiga ni kutaka kumjulia hali mtoto wake, ni mara chache sana kuomba pesa. Tena huwa anakopa, na kurudisha. Sasa unakuwa unamfikiria, mpaka unakuwa na shida unashindwa kumwambia jinsi tulivyo wengi tunaohitaji msaada kutoka kwake. Huwa naamua kunyamaza tu na shida zangu.” Nanaa aliongea kwa kumuhurumia kaka yake.  “Naomba Mungu anisaidie nimalize shule, labda na mimi naweza kupata kazi yakumsaidia kaka yangu, na yeye siku moja akapumzika.” Geb alikuwa akimsikiliza tu.

*************************************************

Walirudi kwenye gari, walipokaa tu, kabla Geb hajawasha gari alimgeukia Nanaa. “Naomba usitafute chumba sasa hivi. Naomba tubaki wote.” “Hapana Geb. Acha tu nianze maisha yangu. Pesa ninayo yakujilipia na kuanza maisha. Nikikwama nitawaomba msaada. Nishasadiwa sana, tena kwa manyanyaso makubwa sana. Sikunyimwa chakula wala sehemu ya kulala. Hivyo havikuwahi kuwa tatizo kwenye maisha yangu. Lakini nilivipata kwa garama kubwa sana. Huwezi kujua ni mara ngapi nilikuwa nikilala bila kula na mimi ndio nilikuwa mpishi. Si kwa kuwa nilikuwa nanyimwa chakula, lakini kile chakula kinakuwa kwenye sahani na maneno mengi sana Geb. Mbali na kuchoka mwili, nafsi pia ilikuwa inachoka, naishia kwenda kulala tu bila kula.” Nanaa akaanza kulia.

“Unalia usiku kucha. Hakuna wakukubembeleza, hakuna wakukupa pole. Tena hata hapo kitandani kwenyewe unafuatwa na maneno mengi tena ya kweli tupu. Uchovu pekee ndio unakufanya ulale. Hujui unaumwa lini, hujui unapona lini. Ukisema unaumwa, unaambiwa unadanganya ili usifanye kazi. Hamna dawa, hamna pole. Sina shida ya kuendelea kusaidiwa, Geb. Sina sababu yakuniweka nyumbani kwako. Naomba usijisikie ni kama nakimbia msaada, au unalazimika kunisaidia. Nakuahidi nikikwama nitakutafuta nikuombe msaada, lakini sasa hivi nipo sawa tu. Acha watu wote wapumzike na mimi niwe na kwangu.” Nanaa alikuwa akiongea kwa uchungu huku akitokwa na machozi. “Nashukuru kwa moyo wako wa ukarimu, Geb. Lakini nimeamua kuanza kujitegemea, acha na mimi niwe na kwangu. Nianze maisha yangu. Inatosha.” Geb alijivuta kwenye kiti chake akabaki amefunga macho. 

“Unataka kuondoka lini?” Geb akafungua macho baada ya muda na kutupa hilo swali. “Nikipata tu chumba, nitaondoka. Ninazo pesa kiasi za kodi na kujinunulia vitu vya kunisogeza mpaka nimalize chuo.” “Kwa hiyo unanikimbia, Nanaa?” “Hunihitaji Geb. Mengi ninayokufanyia hata hukuwa ukijua kama ni mimi nilikuwa nikikufanyia. Ulijua ni mama yako ndiye anayekufanyia. Na mama yako hajashindwa kukufanyia kitu hata kimoja wapo. Ni mimi tu ndiye nilimuomba nifanye kwa kuwa nilijiona naamka asubuhi sana, halafu sina kitu cha kufanya. Wakati yeye analalamika magoti yanamuuma. Inamlazimu kuamka, akupikie halafu arudi tena kulala. Lakini bado kuna vitu vingine huwa anataka akufanyie yeye mwenyewe. Haridhiki hata Grace akikufanyia. Ni lazima akufanyie yeye mwenyewe. Kwa hiyo sina sababu yakuwa pale. Naongeza idadi ya watu tu mle ndani, tena bila sababu. Kitu kinachomuumiza Liz mpenzi wako.” Geb akamgeukia akamwangalia.

“Kama unataka kunisaidia, na kama utakuwa kwenye nafasi ya kunisaidia, nikimaliza chuo, nitawaomba tena kazi. Si mtaniajiri?” Nanaa akauliza, Geb kimya. “Kama nafasi ipo lakini. Na mimi nilikwambia nitakwenda mkoa wowote ukinipa kazi, kasoro Moshi na Arusha tu. Hata ukitaka kuniajiri kijijini nikukusanyie mazao, mimi sina neno. Ilimradi pesa iingie.” Geb aliwasha gari wakaondoka bila ya kujibu kitu.

 *************************************************

Wakati wanarudi, hapakuwa na maongezi mengi. Nanaa alimmiminia uji kwenye kikombe kirefu kinachokaa vizuri kwenye gari yake, Geb akaendelea kunywa huku anaendesha. Safari hii Dalali akapiga simu. “Kuna chumba kingine nimekipata mitaa ya Sinza.” “Sinza itakuwa garama sana na itanilazimu kuchukua daladala mbili kufika chuoni. Kwani kile cha Savei imekuaje tena?” “Mwenzangu amempeleka mtu huko, na ninaona wamekubaliana pesa.” “Usifanye hivyo bwana! Mbona na mimi nilikwambia ninayo pesa? Ninayo kodi hata ya mwaka mzima.” “Lakini haupo dada yangu. Fimbo ya mbali haiuwi nyoka.” “Hapa nipo njiani nakuja. Baada ya muda mfupi sana nitakuwa hapo Mwenge, unipeleke. Hata ukitaka niwalipe pesa yenu leo, nitafanya hivyo. Ila naomba usikiuze hicho chumba mpaka na mimi nikione.” “Basi nakusubiri hapa Mwenge. Ukifika unipigie.” “Nitafanya hivyo, asante. Lakini zungumza na mwenzako sasa hivi, mwambie asikiuze kwanza.” “Sawa.” Nanaa akakata simu. 

*************************************************

 “Nimekuponza?” Geb akauliza. “Kwa nini?” Nanaa akauliza na yeye. “Umenisindikiza huku, umekosa chumba.” Nanaa akacheka. “Wewe huwajui madalali. Hiyo ni lugha yakunionyesha ananihangaikia sana ili nimuongezee pesa. Anaweza akawa yupo sahihi, au ni lugha tu. Naomba unishushe Mwenge, nikamalizane naye kabisa. Nitarudi nyumbani baadaye. Nitajitahidi kuwahi kabla baba mwenye nyumba wangu, hajalala.” Nanaa aliongea kwa utani lakini Geb hakucheka, alimwangalia tu akaendelea kuendesha. 

“Sasa mbona umekasirika badala ya kufurahi pamoja na mimi!?” “Natakiwa kufurahia nini? Kwamba unaondoka nyumbani kwangu?” “Ufurahie kuwa nimepata chumba, naanza kujitegemea. Hakuna usiku wa machozi tena. Nitakuwa kwangu.” “Naomba mimi hiyo kazi ya kukufuta machozi.” Geb alimfanya Nanaa acheke sana. Alicheka mpaka akainama. 

*************************************************

“Kama kweli vile!” “Kwa hiyo huniamini?” Geb akauliza, Nanaa akamwangalia akamuona anamaanisha. “Naomba usifanye hivyo Geb. Please.” “Kwa nini?” “Hapana. Nimeshaumizwa sana hisia zangu. Naomba na wewe usiwe miongoni mwao. Usinipe tumaini ambalo halipo.” “Unajua Nanaa, ni lazima ufike mahali ufungue moyo wako tena? Ili kuamini mtu fulani, na kupenda. Nilishakuwa hapo ulipo. Tena mwenzio nilikaribia kuchanganyikiwa.” “Hata mimi nilikaribia kuchanganyikiwa Geb.” “Hapana Nanaa. Mimi namaanisha kukaribia kurukwa na akili kabisa. Nilikwambia habari ya kufeli chuo. Basi amini nilifeli. Nikikwambia nilifeli, nilifeli masomo yote. Nilikuwa sielewi tena sababu ya mapenzi.” Nanaa alimtizama.

“Sijisifii kwako, lakini mimi Mungu alinijalia akili ya ajabu. Sijawahi kupata alama chini ya 100, tokea naanza shule mpaka namaliza. Kwa kuwa huwa sisahau kitu na nilijaliwa uwezo mkubwa sana wakufikiri. Ukiniambia jambo, linaenda kukaa kichwani, halitoki. Inanisaidia kwa upande mwingine, lakini inanitesa sana. Na ndio sababu yakutaka kujiua niliposalitiwa na mpenzi wangu wa kwanza. Yale maneno aliyokuwa akiniambia, ahadi tulizokuwa tumewekeana, zilikuwa zikijirudia kana kwamba ndio alikuwa akiongea na mimi wakati huo. Nilikuwa silali, wala kula. Halafu yeye anaendelea na maisha yake kana kwamba hakuna kilichotokea. Geb akaendelea.

“Mimi ndiye nilikuwa mwanaume wake wa kwanza. Tokea sekondari nilikuwa naye. Tulipofika chuo, akapata mwanaume aliyekuwa akisomea mastares, shahada ya pili. Hivi unajua yule binti aliniacha bila hofu wala kujiuliza! Si unajua pale Mabibo hosteli watu wa Mastars walikuwa wakipewa vyumba vyao? Sasa yule binti alihamia kwa yule jamaa, akawa anaishi naye. Jamaa alikuwa na gari, yaani alikuwa anamaisha fulani hivi. Watu wakawa wananiambia vile wanavyomuona anatoka na jamaa na kuingia bila aibu na tulikuwa tukifuatana naye kila mahali pale chuoni. Yaani watu walikuwa wanatujua sisi ni wapenzi. Hapakuwa na mahali utamuona Geb bila yule binti. Si asubuhi si usiku kasoro darasani tu. Tulikuwa kama kumbikumbi. Pale Mabibo hosteli walikuwa wakitujua. Wenzangu walinipa jina la chizi kupenda. Nilimpenda yule msichana kama mwehu.” Geb akajicheka.

“Nilikuwa namfuata chumbani kwa yule jamaa, nampigia magoti. Namuomba anirudie. Yule jamaa alinipiga marufuku kuingia kwenye lile jengo lao, kwa hiyo nilikuwa nakaa pale nje, hata masaa manne, nikijiambia labda atatoka nijaribu kuzungumza naye, anirudie. Sijui niliingiwa na nini!? Nilikuwa kama nimerukwa na akili. Kina James, Zinda, Malii na Danny, walikuwa wakija kunitoa pale, nakunirudisha chumbani kwangu. Wakiondoka tu, na mimi narudi kukaa pale nje. Nilijidhalilisha vyakutosha tena bila kuchoka wala kujali. Ndio kina James na Danny ikabidi kwenda kumwambia mama. Maana tulikuwa tumemaliza mitihani, lakini mimi sitaki kuondoka chuo. Tena yote hayo yalitokea kipindi cha karibia na mitihani.”

“Kuna somo yule jamaa alikuwa anawafundisha kundi la huyo binti. Kwa hiyo wakati mwingine yule binti alikuwa akienda na marafiki zake kusoma, na mimi nakuwa na kina Danny. Muda ukifika, naenda kumfuata, tunarudi chumbani kwangu. Sasa akaanza vituko, hataki nimfuate tena, au anakwenda yeye mwenyewe kwa huyo jamaa bila marafiki zake, mpaka akahamia kabisaa.” “Pole Geb. Kwa hiyo ikawaje?” Geb akajicheka tena.

“Ndio mama ikabidi aje pale chuo, anichukue. Grace yeye alipata chumba Main Campus, kwa hiyo alikuwa akiishi huko na wenzake. Mama akanirudisha nyumbani. Nilikuwa ninahali mbaya sana Nanaa. Ndio kipindi hicho hicho mama na yeye akaokoka kwa ajili yangu. Mama alikuwa akiniombea bila kuchoka. Matokeo yakatoka, mimi nikawa nimefeli kabisaa, yeye yule binti amefaulu. Lakini usifikiri sikuwa namfuatilia nyumbani kwao? Nilikuwa naenda mpaka kwao, kumbembeleza. Maana nyumbani kwao wote walikuwa wananifahamu.” Nanaa alibaki anashangaa

“Baada ya muda akahamia kwa huyo jamaa, tena alikuwa mfanyakazi, ameajiriwa. Kipindi cha likizo au tuseme chuo kikifungwa, jamaa alikuwa akirudi kazini. Haya, nikapeleleza mpaka nikaja kupajua nyumbani kwa huyo jamaa. Nikaenda. Lakini nikamkuta yule binti, ana mimba kubwa tu. Ndio nikasalimu amri, nikamuaga rasmi na kumuacha. Lakini niliumia sana. Kwa kuwa aliniacha bila kosa. Labda kwa kuwa sikuwa na pesa. Sijui. Ndio maana nachukia sana umaskini. Napenda kulala, sana.” “Grace aliniambia.” Wakacheka.

“Napenda na nina furahia kulala. Na ndio maana nimetumia pesa nyingi sana kwenye kitanda na mashuka ya kitanda changu, kwa vile ninavyothamini usingizi. Najua mama amekwambia huwa nalala naye.” Nanaa akacheka huku akikubali. “Mama hana siri! Ananidhalilisha sana. Lakini ngoja niendelee, ndio maana hata yeye nimehakikisha anakitanda kizuri, ili nikienda kulala kwake, nilale sehemu nzuri. Napenda sana usingizi. Lakini kila nikifikiria pesa, yaani nikiona kuna jinsi yakuingiza pesa, huwa najilazimisha kuamka. Starehe yangu ya kwanza ni kulala. Lakini ikifika kwenye pesa, huwa usingizi inabidi kusubiri.” Nanaa akacheka.

“Kwa hiyo Nanaa, usifikiri sielewi unachoongea. Naelewa sana. Mimi nilitoka hapo kwa maombi ya mama yangu. Alikuwa akinishika mkono hata nikiwa usingizini, ananiombea. Lakini ni lazima ifike mahali, uchore mstari na uruhusu watu kwenye maisha yako.” Nanaa alifikiria kidogo. “Nitajitahidi Geb. Lakini naogopa sana. Nimekuwa makini kupita kiasi. Mimi nakiri kuwa sijawahi kupenda hivyo. Yaani ilikuwa ni kama natafuta mkombozi tu kwenye maisha yangu. Mtu wakunitoa pale kwa mama mkubwa, na kuishi na mimi. Sikuwa na vigezo vingii. Sijui mrefu, mwenye pesa, mweupe, au mweusi. Sikujali hayo. Ilikuwa yeyote atakaye nijia.” Nanaa akafikiria kidogo.

“Lakini sasa hivi nimeamua kuchunga moyo wangu, naogopa hata kufikiria kumwingiza mwanaume moyoni. Yaani hata wazo likinijia tu, najionya kwa haraka sana. Nahisi nitakufa, Geb. Sitaweza. Hawa wanaume wote walionitenda niliumia hivyo, sasa ije itokee nipende kama wewe ulivyompenda huyo binti, si ndio nitakufa?” “Sasa hivi utafanikiwa Nanaa. Kwa kuwa utaanza mahusiano mengine ukiwa umetulia, huna haraka au haupo desparate. Toa nafasi yakupendwa tu.” Nanaa akacheka sana.

“Unavyoongea kama rahisi vile!” “Ni rahisi.” “Mmmh! Haya bwana. Naanza kutoa hiyo nafasi. Sasa sijui nitoe tangazo kwenye vyombo vya habari na social media, ili waanze kuja!? Au nimtafute Zinda kwanza?” Geb akamtizama.  “Anza kuwa makini na watu wanokuzunguka kwanza. Usikimbie, tulia. Unaweza kuweka mawazo na macho yako mbali, ukawapita walipo karibu.” Nanaa akanyamaza.

*************************************************



Nanaa na Geb.

Nanaa agundua Geb anamfahamu zaidi ya alivyofikiria. Geb anataka Nanaa aendelee kuishi naye wakati Liz bado yupo ndani ya picha. Hatoi maelezo yakumtosheleza Nanaa kumfanya akubali kubaki nao pale nyumbani kwake. Hofu ya kuumizwa tena inazidi kumtesa. Ni kama kwa mara ya kwanza maishani, vitu vyote alivyokuwa akivitamani sana vinafunguka kwa wakati moja. Anapata matarajio ya kupata nyumbani kwake na mwanaume ambaye hana uhakika naye, Geb yupo pembeni yake akimsihi tu abaki. Aende wapi? Achague kuhama akaanze maisha yake, au aendelee kubaki na Geb ambaye anafunguka nusu nusu. Kwa nini?



Usikose mwendelezo Sehemu ya 20.

1 comment:

  1. Asante Naomi wangu ndo nimemaliza Kisoma saiv jaman leo imekuwa tamu hatari mnoo asante sana my dear mm nazid kujifunza Mungu akibariki

    ReplyDelete