Story

is mine - ni Wangu! Part 1, Sehemu ya 20.

Monday, August 13, 2018 naomimwakanyamale 0 Comments


G

eb na Nanaa walifika Mwenge, bado ilikuwa mapema tu. “Naomba nishushe hapo kituoni. Wewe nenda kapumzike,Geb. Nikimalizana na huyo dalali, nitakuja nyumbani.” “Ulishawahi kuonana naye?” Geb akauliza. “Hapana. Huyu ni mwingine. Kaka ndiye amenipa simu yake.” “Mpigie simu, aje hapa kituoni tuzungumze naye kwanza. Asijekuwa tapeli, akakuchukua hapa akakupeleka sehemu siyo.” “Halafu kweli. Nilikuwa hata sijafikiria hivyo.” Nanaa akatoa simu akazungumza naye na kumuelekeza afike sehemu watakayoegesha gari. 
Yule dalali akafika. Alikuwa na maneno mengii. Alisimama upande aliokaa Geb. Aliongea kama dakika kumi, Geb na Nanaa wakimsikiliza. “Kwa hiyo chumba kipo au hakipo?” Nanaa alimkatisha. “Kipo. Lakini si unajua inabidi unilipe ya kukupeleka?” “Hata kabla sijaona chumba chenyewe?” “Hiyo ndio garama ya kukupeleka kwanza.” Akajibu. “Naomba unisubiri hapo pembeni kwanza.” Nanaa alimwambia na kumuomba Geb apandishe vioo vya gari wazungumze. 
“Nakushukuru sana kwa moyo wakutaka kunisindikiza. Lakini hivyo wewe ulivyo, na gari lako hili, tukiongozana wote, sitaweza kulipia chumba hata mwezi mmoja.” Geb akaanza kucheka. “Jamani Nanaa! Mimi nimefanyaje?” “Kuanzia wewe na gari lako, mnaonekana ni pesa tupu. Ndio maana ameanza kunidai hapa pesa zisizokuwa kwenye makubaliano. Anajua wewe ni mtu wangu, unataka kunipangishia chumba. Na kwa kuwa amekuona una pesa, anajua hata akikutajia pesa kubwa vipi, utalipa tu. Wakati mimi mwenzio pesa yangu ndogo. Naomba nishuke hapa. Wewe ondoka.” Geb alizidi kucheka.
Usinifukuze Nanaa.” “Mimi nawafahamu vijana wa mjini. Wanapenda pesa wasiyoitolea jasho. Watadai pesa nyingi, Geb. Wewe niache tu, nitakufuata nyumbani.” “Sasa kama nitapeli, akikuchukua halafu akaenda kukufanyizia na wenzake?” “Acha kuniogopesha bwana Geb! Mbona yule mwingine hakunitapeli?” “Mimi nakwambia ukweli. Sikuogopeshi. Watu hawafanani. Ni heri twende wote. Kila pesa atakayokuongezea, mimi nitailipia.” “Hapana bwana Geb. Hata kodi wanaweza kunitajia kubwa mara mbili ya hapo.” “Nitalipa ile itakayoongezeka.” “Hapana Geb, bwana! Na ya mwakani nani atalipa?” “Mimi.” Nanaa akamwangalia.

“Nimekuomba usinidanganye Geb. Nishadanganywa sana maishani. Usiweke tumaini la uongo moyoni mwangu.” “Kwa nini unafikiri nakudanganya?” “Sasa mwakani utanionea wapi mimi!?” “Kwa hiyo inamaana wewe ukiondoka leo, ndio basi!? Mbona ni kama ulisema ukiondoka utanitafuta? Uliniahidi ukikwama utaniambia, au na wewe ndio unanidanganya?” “Sikudanganyi Geb.” Nanaa akaishiwa nguvu.
“Sasa mbona unanigeuka!? Naomba kuwa makini na kila unachoniahidi, Nanaa. Huwa naumia sana nikidanganywa. Ni heri uniambie ukweli, hata kama unajua utaniuma, kuliko kuniwekea ahadi ambayo unajua huna hata mpango wa kuja kiitimiza.” “Sikuwa na maana mbaya, Geb. Samahani. Ila sitaki..” Nanaa alikwama akanyamaza. Geb akabaki akimwangalia.
“Nakuahidi sitakudanganya, na wewe nakuomba usinidanganye. Kitu unachojua hutakitimiza kwangu, naomba usiniahidi. Tafadhali Nanaa. Huwa naumia vibaya sana.” “Lakini sijakudanganya, Geb.” “Uliponiambia utakuwa mlinzi wangu. Ulimaanisha ni hapa barabarani tu, tukifika nyumbani unakuwa unaendelea na maisha yako? Yaani unakuwa umemaliza kazi yako, au ulimaanisha nini?” Nanaa alianza kutokwa na machozi asijue kama ni hofu ya kuamini mtu tena au ni hofu hata ya kufikiria kujaribu kurudi kwenye hiyo njia yakuahidiana na mtu kwenye mapenzi. Kumbukumbu za kutendwa na wanaume gafla zikamrudia zikiwa ‘so fresh’. Mpaka mwili ukaanza kutetemeka baridi.
Lakini huyu ni Geb Magesa. Mwanaume ambaye hisia zake zote zimekubali kuwa anampenda, tatizo ni Liz tu. Swali la je na yeye akimuumiza, ndilo lililokuwa likikubaliana na wazo la kuhama nyumbani kwake angalau waachane wakiwa na kumbukumbu nzuri.  “Naomba uniambie ukweli Nanaa. Na naomba usinidanganye.” Geb akasisitiza. “Naogopa Geb. Naogopa sana.” Geb aliondoa gari pale kituo cha Mwenge, akaendesha mpaka Mlimani city, akaenda sehemu ya kuegesha magari.
Akashuka na kwenda upande alipokuwa amekaa Nanaa, akafungua mlango, akamfungua mkanda, akamgeuza na kumkumbatia. Alimkumbatia kwa nguvu huku akimpapasa mgongoni kama kumtuliza. Nanaa aliweka uso wake mwilini mwa Geb aliyekuwa amesimama. Alipata faraja ambayo aliihitaji kwa wakati ule. Alipata utulivu wa nafsi, akajikuta anatulia. Alikuwa ameficha uso wake na viganja vyake huku amemuegemea Geb, akatoa mikono taratibu akapitisha mikono yake nyuma ya Geb na yeye akamkumbatia. 
***************************************
 “Oooooh! Siamini kama nimemkumbatia Geb Magesa!” Nanaa akawaza. Akashindwa hata kujisogeza jinsi mwili ulivyokuwa umekufa ganzi. “Uwiii Nanaa! Au ni ndoto?” Hakuwa akiaamini. Ni vidole vya Geb mgongoni mwake vilivyomsisitizia kuwa ile haikuwa ndoto. Alitamani dunia isimame, kwa muda. Imuachie ule wakati ambao alitamani uje utokee, lakini alijua haitakaa ikatokea. Alivuta pumzi taratibu kama akichukua hisia nzuri ndani yake.
***************************************
Walikaa vile kwa muda mpaka simu ya dalali ilipoingia tena. Nanaa akajitoa kwa Geb, akachukua simu yake. “Ni dalali.” Nanaa alibaki akiingalia ile simu. “Sijui nifanyaje Geb?” “Naomba tubaki wote Nanaa.” “Mpaka lini?” Mahusiano ya Geb na Liz hayakuwa ya siri. Nanaa aliogopa kujidanganya. “Unakumbuka nilikwambia tutafute chumba hosteli, utakachokitumia pale itakapo lazimu?” Nanaa akanyamaza. “Naomba tuishi wote, Nanaa. Nitakuwa nikikupeleka chuoni, nakuja kukuchukua mimi mwenyewe.” “Sasa ni lini na mimi nitaanza kujitegemea?” “Ndio unaanza kujitegemea sasa hivi.” “Najitegemeaje nyumbani kwako, Geb!?” “Kwani ulitaka kufanya nini ukiwa kwako?” Nanaa akanyamaza. 
“Yale uliyotaka kuyafanya nyumbani kwako, naomba uyafanye pale kwangu. Kuwa huru. Hesabu kama Mungu amekupa familia nyingine, tunayokupenda. Acha kukimbilia chumbani. Kaa na sisi pale sebleni. Zungumza na kila mtu, sio unaenda kujificha kwa bibi Fili kila wakati.” Nanaa alicheka, akainama. 
“Naomba tuishi wote. Sio kwa sababu nataka kukusaidia, ni kwa kuwa nataka uwepo kwenye maisha yangu.” Nanaa akamwangalia kidogo kama kumuuliza kitu kilichoshindwa kutamkika mdomoni, akainama. “Naomba jipe nafasi nyingine yakumuamini mtu fulani Nanaa. Najua unaogopa, hutaki kuumizwa tena, lakini ujue ndio unajiumiza zaidi. Kadiri unavyojifungia milango, ndivyo unavyokaribisha simanzi moyoni. Lazima uje umuamini mtu fulani na upende tena. Kwanza katika mazungumzo yote tuliyozungumza, sijakusikia kama ulipenda Nanaa.” Nanaa akacheka kidogo.
“Hicho kipengele ni cha muhimu kwa kila mwanadamu.” “Nikija kuumizwa?” Nanaa alijiuta akiuliza. “Hayo ni matokeo. Lakini umeshajiuliza kama usipoumizwa? Ikatokea unapata mtu anayekupenda kwa dhati. Umeshafikiria hiyo furaha yake?” “Itakuaje nije kupenda nisipopendwa,Geb? Yaani ikatokea ninayempenda hanipendi mimi anampenda mtu mwingine?” Nanaa aliuliza huku akilia. “Naogopa hata kuwaza. Naogopa kufika umbali ambao nitashindwa kurudi. Nimebakisha muda mfupi sana nimalize chuo. Naogopa kuja kuchanganyikiwa nikiwa nahitajika kutuliza akili chuoni.” “Unakumbuka niliomba kazi ya kufuta machozi?” Nanaa akainama. “Pia nitahakikisha hayatoki. Na kama yatatoka, mimi nitakuwepo.” Nanaa akabaki akifikiria huku akikausha machozi. “Naomba usiwaze mbali sana Nanaa. Mimi nipo hapa na wewe.” Geb alikuwa akiongea kwa utulivu sana. Nanaa akavuta pumzi. 
“Anamaanisha nini?” Nanaa akawaza. “Bahati kama hii inaweza isirudie tena! Ni Geb ndio ananiambia hivi!” Nanaa alikuwa akijikumbusha. “Kwa hiyo umekubali kubaki tuishi wote?” Geb akamuuliza kwani Nanaa alibaki akiangalia simu yake iliyokuwa inaonyesha namba ya yule dalali. Alikuwa kwenye wakati mgumu sana. Njia panda haswa. Achague nini? Geb ameongeza kitu kingine. Amemtupia swali lililozidi kumfanya afikirie. Alimwambia, ‘Lakini umeshajiuliza kama usipoumizwa? Ikatokea unapata mtu anayekupenda kwa dhati? Umeshafikiria hiyo furaha yake?’ Huo ukawa mtego mkubwa kwake.
“Kama utakataa. Nitakuruhusu ushuke hapa, urudi kwa huyo dalali, ukatafutie chumba. Lakini ukikubali kubaki, nakuahidi hutalala ukilia tena. Na ikitokea unalia, nitakuwepo kukufuta machozi.” Nanaa akamwangalia kama haamini huku machozi yakimtoka. Ni kama na yeye Geb  alijiweka kwenye nafasi yakutaka kuchaguliwa. Alitaka mtu anayemchagua yeye zaidi ya kitu kingine. Lakini zipo siku Geb anakuwa amelala na Liz chumbani kwake. Atajuaje kama Nanaa analia? Hata kama akijua. Kweli ataweza kumuacha Liz kitandani na kwenda kumbembeleza yeye Nanaa? Hayo ni maswali ambayo yalikuwa yakiendelea hata kwa Nanaa.
“Najua huamini na una maswali mengi. Lakini chukua hatua ya imani tu. Jaribisha. Ila sitakulazimisha Nanaa, upo huru kuchagua na kufanya kile unachotaka.” Geb akampisha mlangoni, akarudi upande wake, akaingia ndani ya gari, akakaa akabaki akimwangalia. Hata yeye mwenyewe asiamini nafsini mwake.
******************************************************
Ni msichana wa pekee anayekutana naye katika kipindi hiki cha mafanikio yake, eti anashindwa kumkubali moja kwa moja! Anachukua kuda kufikiria ombi zito kama lile! Hata Geb alishangaa. Hata kabla hajafanikiwa sana kimaisha, umbile na macho yake vilimuuza sana kwa wasichana. Alitongozwa kila aendapo. Alijua wazi ni wengi wanamtamani. Na kumuota awe wao. Hata hakuwa mtongozaji sana. Walijileta wenyewe na pesa yake iliongea. Lakini ni Nanaa aliyempenda na ndiye anayemringia. Yupo tayari kuacha nyumba yake, na kwenda kuanza maisha yake kwengine, hata baada ya ahadi ambazo hakumbuki kumpa mwanamke mwingine, ila yeye Nanaa.
******************************************************
Nanaa bado alikuwa akifuta machozi, huku haelewi ile ofa ya Geb inaishia wapi. Inamipaka gani? “Na Liz?” Nanaa alizidi kusita moyoni na mawazoni. Alikuwa akikimbilia kitandani kwa haraka sana kutoa penzi. Bila kuangalia umbile wala utajiri. Alitumia mwili wake kama silaha ya kuvutia wanaume. Lakini leo hofu na maumivu ya kusalitiwa na wanaume wengine, vinamzuia kumpokea mwanaume ambaye moyo wake umempenda. Anasifa ambazo hata hakuwahi kuzihitaji kutoka kwa mwanaume. Ni zaidi ya matarajio yake. Akabaki amechanganyikiwa. Hajui afanye nini na Geb asiyeweza kumkatalia kitu, ameng’ang’aniza ombi lake.
******************************************************
“Naomba usilie Nanaa. Nitakuunga mkono kwa kila utakachoamua.” “Nimechoka kulia peke yangu, Geb.” “Basi mwambie huyo dalali tutamtafuta wakati mwingine. Turudi nyumbani.” Nanaa akafuta machozi, akamtumia ujumbe yule dalali na kumwambia atamtafuta wakati mwingine.
“Nimeshamtumia ujumbe.” Geb akavuta pumzi kwa nguvu. “Asante Nanaa. Naomba twende tukapumzike nyumbani.” Geb akaondoa gari mpaka kwake. Hapakuwa na maongezi mengine yeyote mpaka walipofika nyumbani kwa Geb. Kila mtu alikuwa akiwaza lake pale ndani ya gari. Ulikuwa umbali wa kutokea Mlimani City mpaka Tabata Barakuda. Lakini uliwapa nafasi nzuri na tulivu kila mmoja kutafakari maneno aliyomwambia mwenzake.

Baada ya safari ya Bagamoyo.
Walifika nyumbani. Wakakuta gari ya Mama G tu. Wakajua Grace na Danny bado hawajarudi kutoka kazini. Bado ilikuwa mapema tu kama saa kumi jioni wakati mlinzi akiwafungulia geti. Nanaa akamsaidia kushusha yale matunda, wakaingiza jikoni, moja kwa moja wakajikuta wanaelekea chumbani kwa Bibi Fili. “Mmeniletea matunda?” Akawauliza. “Yapo jikoni.” Geb akajibu na kujirusha kitandani kwa mama yake. “Amekula?” Akamuuliza Nanaa, Nanaa akacheka.
“Leo Nanaa amenibadilikia bwana! Amehakikisha nimekula chakula cha kwanza nilichoagiza.” Mama yake akacheka. “Kwani na yeye ashaujua ule mchezo wako wakujidai kama unataka kula, halafu unaagiza vyakula vya kila aina, ili kupoteza muda halafu huli?” Mama yake akauliza, wote wakacheka. “Kumbe ndio mtindo wake!?” Nanaa akashangaa.
 “Kumbe ulikuwa hujui!? Basi akiona utamkera kwa kumlazimisha kula, ukiagiza cha kwako, na yeye anaagiza chakwake. Anaanza na ugali na nyama choma. Kachumbari inakuwa na masharti mengii. Vikiletwa hapo, anaanza kutoa kasoro kimoja baada ya kingine. Halafu ili usimjue kama hataki kula, anaagiza kitu kingine, wakati wewe unaendelea kula. Kikiletwa hicho cha pili, basi kimoja wapo lazima kitakuwa na kasoro kubwa na ya msingi sana, itakayosababisha chakula chote kisiliwe. Basi. Anaendelea kuagiza kingine tena. Lakini cha tatu, lazima kiwe kigumu na kichukue muda mrefu sana kutengenezwa huko jikoni. Tena anaweza akaagiza ambacho anajua wazi pale hakipo. Lakini mwenyewe anaita special order.” Nanaa alikuwa anacheka sana.
“Bahati yake ikiwa nzuri, yule mpeleka oda jikoni akikataliwa na mpishi. Basi mwanangu huyu anakuwa amepata sababu ya kuondoka pale bila kula. Wakimletea kwa haraka kabla wewe uliyenaye hujamaliza, ule mchezo wake utaendelea vile vile. Anaagiza na kutoa kasoro, mpaka uliyenaye uwe umechoka kusubiri. Kama ni Grace basi huwa anaharaka zake. Si unamjua Grace? Kama hana haraka ya kuwahi kazini, basi anamuwahi mumewe au mtoto. Basi Grace anaomba afungiwe vyakula vyote, anaondoka naye huyu bila kula. Ujue hapo kapona kupika usiku. Atakuja kuvipanga hapo mezani, ndio chakula chenu cha usiku huo. Grace kamaliza.” Geb alikuwa anacheka kama sio yeye.
“Haya, kama ni mimi, basi tena nakua nimechoka kelele za baa, nataka anirudishe nyumbani au kazini kwangu. Akiwa nawenzake kina Malii, Danny, Zinda, Gozi na James, wao huwa wanakula chakula chote bila shida. Na ndio furaha yake, kwa kuwa wao hawamuulizi. Akikataa hiki, wakati anaagiza kile, wao wanagawana na kula kile alichokataa mwanzo. Kikija cha pili akikikataa, wakati anaagiza cha tatu, wenzie wanakula kile cha pili. Basi mchezo unaendelea mpaka waondoke pale. Tena huo mchezo wa kuendelea kuagiza akiwa na wenzake anaufanya kama na wao wakimkera kwa swali la kwa nini yeye hali kitu wakati wao wanakula? Sasa ili asieleweke vibaya, kama labda amepadharau pale au la, basi anaendelea kuagiza tu. Mpaka waagane na wenzake.” Geb na Nanaa wote walikuwa wanacheka.
“Sasa leo Nanaa amenitolea uvivu. Hakutaka hata niagize sahani ya pili. Ile ile ya kwanza, akaniambia nile. Sasa na mimi ikabidi niwe mstaarabu huku nikitamani pale pale angegeuka akawa wewe.” “Ili unikaripie, nikuache usile?” “Sikukaripii bwana mama. Sema wewe huwa nakuweza.” Nanaa alizidi kucheka. “Basi mimi ndio mnyonge wake. Nikijaribu kumlazimisha kula. Anakuwa mkali kweli kweli. Mpaka naona heri nimuache tu, nije kumpikia huku nyumbani, yaishe.” Geb aliendelea kucheka. 
“Haya, mlifanikiwa huko?” “Sanaaa.” Geb alijibu harakaharaka huku akimwangalia Nanaa. Mama yake akaguna. “Labda niulize. Mafanikio haya tunayozungumzia hapa ni ya matunda au kuna jingine?” “Yote.” Geb akajibu tena, wakacheka. “Haya, nenda kaoge, uje unisimulie kila kitu.” “Acha kupenda stori, Mama G. Hamna nyongeza.” “Umeanza kunificha?” “Sasa kama hamna nyongeza, nikwambie nini mama?” Geb alikuwa kicheka huku akitoka. “Na usirudi hapa. Kalale huko huko chumbani kwako.” “Acha hizo mama bwana!” “Wewe si unajidai msiri wewe? Sasa hapa kitandani kwangu nisikuone. Nenda na siri zako.” “Basi nakuja kukusimulia. Mama naye!” Geb akatoka, wote wakacheka. 
“Ukimuona anachekacheka hivyo, ujue kuna kilichomfurahisha. Mlalamishi kama nini huyo.” Nanaa akacheka. “Na mimi naenda kuoga, nilale kidogo.” Nanaa akasimama. “Nanaa!” Akamwita kabla yakufungua mlango. “Nashukuru kwa kumsindikiza. Naona amerudi na furaha.” Nanaa akacheka asijue ajibu nini.
******************************************************
 “Anakuwa mpweke kweli. Anazunguka huko maporini peke yake, hali kitu na wala hana mtu wakuzungumza naye. Hana mtu anayeweza kumfikia hisia zake binafsi na kumtuliza, yeye kama Geb. Kule kuwepo tu pembeni yake, kunamsaidia sana. Huwa nakuwa naye kwenye simu wakati wote, angalau kumfanya asijisikie yuko peke yake, lakini kama unavyojua mimi ni mama. Siwezi kumliwaza kabisa. Halafu na magoti yangu yananisumbua mara kwa mara. Siwezi kuwa naye kila mahali.”
“Grace naye kama unavyoona. Hao wanaume wawili, Fili na Danny, wanamganda hana hata pakuhemea. Kila wakati Danny anamtaka awepo alipo yeye. Tena afadhali yeye asiwepo nyumbani kuliko Grace. Danny anakuwa kama mtoto anayenyonya. Anataka Grace awepo kazini na hapa nyumbani, basi. Akijua yupo nyumbani halafu aje hapa asimkute, hapatakalika hapa. Atafanya fujo mpaka Grace arudi. Anawivu Danny,  wakupitiliza. Kila saa anahisi ataporwa huyo Grace. Akianza kumtafuta hapa, utafikiri mtoto mchanga analilia nyonyo.” Nanaa akacheka. 
“Nilimuona juzi.” “Ile juzi mbona alijikaza, kwa kuwa alijua yupo na Fili. Nakwambia inakuwa kelele hapa, mpaka Grace arudi. Tena wakati mwingine anamfuata huko huko.” Nanaa akacheka sana. “Sasa wewe huwa unamwambiaje?” “Kimyaa. Nawaangalia tu. Huna utakachomwambia Danny juu ya Grace, mkaelewana. Tokea anamchumbia mpaka leo. Yupo hivyo hivyo kama amechanganyikiwa. Kila saa anataka amsikie mkewe. Ajue yupo sehemu anayotaka yeye, na watu anaowajua. Sio mwanaume asiyemtaka yeye. Akisikia yupo mahali na mwanaume asiyemjua yeye, anaacha kazi zote anamfuata mkewe.” Nanaa akashangaa. 
“Haiwezekani Mama! Sasa Grace anasemaje?” “Nakwambia huna utakachomwambia Danny, kwa mkewe. Atakuja kukusimulia yeye mwenyewe stori za Danny wakati wanachumbiana. Utacheka mpaka ulie. Ngoja siku wakiwa wamekaa hapo sebleni, nitawachokoza umsikie Grace mwenyewe. Haishiwi vituko. Kutwa yupo na mkewe huko chumbani. Akiwa hapo sebleni, basi Grace awepo jikoni. Tena asikae sana huko jikoni, atamfuata. Hataki mkewe eti akae jikoni muda mrefu anampikia yeye! Haiwezekani. Yupo radhi akanunue chakula sehemu yeyote. Tuje kula, kuliko kumwambia mkewe akae jikoni apike, wakati yeye yuko sebleni. Ni heri na yeye ahamie hapo jikoni au mtu mwingine apike. Na uzuri wake, hachagui chakula. Chochote atakachowekewa na yeyote yule, atakula tu. Utamuhurumia huyo Danny. Nenda mwaya kapumzike, lakini asante sana.” Nanaa akatoka akiwa anacheka.
******************************************************
 Nanaa alikuwa akiwaza na kujiuliza nafasi yake kwenye maisha ya Geb itakuwa ipi, lakini mama yake Geb, alimsaidia kumjibu swali hilo gumu sana lilokuwa limemsumbua sana Nanaa, asijue kwa nini Geb alimtaka asihame, aishi nae pale. Alienda kujilaza kitandani kwake baada ya kuoga, akabaki akiwaza. “Labda kweli Geb ananihitaji. Amekuwa akinifuata kazini siku nne mfululizo. Ametaka niende naye Bagamoyo. Anaonekana anafurahia nikiwa naye karibu. Anajitahidi kuniongelesha. Marangu alinivalisha sweta mbele za watu, huku akinituliza. Labda kweli lipo pengo maishani mwake ambalo naweza kuziba. Liz anaonekana mbinafsi sana. Labda hamjali.” Nanaa aliendelea kuwaza. “Lakini ngoja nisiharakishe nisije kuwa nimeelewa vibaya, nikajiingiza kichwa kichwa nikaishia kuumia.” Nanaa alipitiwa na usingizi. 
******************************************************

Nanaa amesitisha ramsi swala la kujitafutia mahali pa kuishi ili awe na Geb. Hajui kwa wazi na wala hajatamkiwa kwa hakika nafasi yake kwenye maisha ya Geb ni ipi. Japo ipo ahadi yakufutwa machozi na kuhakikisha halii tena. Ni nini Geb atafanya kuhakikisha anatunza furaha ya Nanaa na Liz akiwa pichani?

Usikose Sehemu ya 21.

0 comments: