Story
is mine - ni Wangu! Part 1, Sehemu ya 21.
A
|
liamka jioni, akatoka pale chumbani. Alikuta kila
mtu amekaa pale sebleni. Akaenda kukaa “Vipi uchovu umeisha?” Nanaa akatingisha kichwa kukubali
huku akitabasamu. “Njoo ukae hapa.” Alimuonyeshea pembeni yake. Nanaa
akasita kidogo. Akaangalia watu wote waliokuwa wamekaa pale, akaogopa. “Hapa
panatosha.” “Basi ngoja mimi nikufuate.” Nanaa akasimama kwa haraka akaenda
kukaa naye kabla yeye Geb hajasimama kumfuata. Geb akatabasamu.
sehemu yakulia chakula. Geb
akamwangalia.
“Mbona unajisugua kidole?” Nanaa
akamuuliza kwa sauti ya chini. “Nahisi nilichomwa na mwiba muda mrefu.
Pameanza kuwasha.” “Tuone.” Nanaa akamvuta mkono taratibu. Akaangalia. “Naona
kuna kitu cheusi kwa ndani. Itakuwa mwiba. Upo ndani kidogo. Utavumilia
nikutoe?” “Nitashukuru. Unanikera kweli!” Nanaa akaenda kuchukua pini
chumbani kwake, akarudi kukaa pembeni yake. Akaanza kumtoa ule mwiba taratibu. “Nikikuumiza
uniambie.” Geb akacheka. “Unavyoshika kwa woga! Sijui kama huo mwimba
utatoka.” “Naogopa kukuumiza.” Nanaa akaendelea kumtoa huku wengine
wakiendelea kuangalia tv pale pale sebleni. Alijua wazi wanawasikiliza.
******************************************************
“Nasikia Nanaa leo umepelekwa Bagamoyo?”
Grace alitupia swali, Nanaa akacheka. “Lakini wala hatukukaa sana. Tulikuta
ndio wanamalizia kupakia.” Nanaa akajibu. “Na mimi nilijaribu kuwa na
kwenda kuangalia upakizwaji wa mazao, lakini nikashindwa.” Nanaa akashangaa
kuona wote wanaanza kucheka. “Kwa nini?” Nanaa akauliza. “Yaani
Nanaa, si unaaga hapa. Unasema unapokwenda na pengine muda utakao rudi kama watamaliza
mapema. Unakubaliwa vizuri. Unasindikizwa mpaka kwenye gari, hata mkanda
unaweza kufungwa, na maneno mazuri ya kutakiwa safari njema, ‘Mungu
akurudishe salama mke wangu. Tukumbuke mimi na Fili, tunakupenda na
tunakuhitaji. ’ Na maneno mengi mazuri, mengi tu. Haya, unafungiwa
mlango wa gari vizuri, unawasha gari unaondoka.” Grace akacheka yeye
mwenyewe.
“Nini?” Nanaa akauliza huku na yeye
ameanza kucheka. “Danny nyie! Acheni tu. Yaani wakati unatoka tu hapo
getini, unamuona kwa kutumia vioo vya gari, simu zinaanza. ‘Unarudi saa
ngapi?’ Unarudia tena maelezo yote uliyoyatoa jana yake na muda mfupi
wakati mnaagana. Haya. Ukifika tu kwenye hayo mataa ya kwanza hapo barabarani,
simu nyingine. ‘Umefikia wapi?’ Swali la kwanza na la pili huwa halina
shida, ila hayo yanayofuata lazima ukereke tu. Utasikia, ‘mbona kama hapo
ulipo pako kimya?’ Unajibu labda nimesimama kwenye mataa. Utasikia tena, ‘mbona
hata sisikii mlio wa gari?’ Ujue hapo kazi ndio imeanza.” Watu walizidi
kucheka.
“Yaani hapo nimeondoka nyumbani hata dakika
kumi hazijaisha, tayari kelele zimeanza. Mpaka uje ufike huko, njia nzima ni
maneno. Unafika umenuna, huwezi kuongea na wafanyakazi. Na ukikaa hapo shamba,
nusu saa nyingi, na yeye anakuwa amefika.” Nanaa alikuwa anacheka sana,
akashangaa kidogo.
“Haiwezekani Grace! Sasa anatumia njia gani
kufika mpaka Bagamoyo? Kulivyo mbali hivyo!” “Wewe humjui Danny na kichwa
chake. Yaani ile simu ya 3 kuwa mbona hasikii mlio hata wa gari, ujue hapo na
yeye anavaa nguo, ananifuata.” Wote walikuwa wanacheka. “Sasa na yeye
kazini inakuwaje?” Nanaa akauliza. “Kazi gani tena? Wewe unafanya kazi
wakati unaibiwa mkeo? Kazi itasubiri kwanza.” Danny akajibu. “Huna
utakalomwambia Danny kwa mkewe mkaelewana.” Mama yao akaongeza. “Mimi na
Geb tulishajua. Grace akitoka tu, ujue Danny atafuata nyuma. Yaani umtume mkewe
Bagamoyo! Humtakii mema Danny.” Nanaa alizidi kucheka huku anashangaa.
“Alivumilia mara ya kwanza na ya pili. Ya
tatu, akamfuata Geb. Eti aache kumvunjia ndoa yake.” Walikuwa wakicheka
sana. “Na usifikiri anatania? Yaani hapo kanifuata amenikasirikia kweli
kweli. Eti kama shida yangu aachwe, yeye ahangaike na mtoto hapa mjini, basi
niendelee kumtuma mkewe mashambani. Nakuwa kama namuuza mkewe kwa watu. Eti
nashindwa kufikiria swala la usalama wa mkewe, namtuma kwa wanaume. Kama ni
pesa, eti basi. Hapo Danny kawaka kweli kweli. Unajua alinitoa kazini akanituma
nikamfuate mkewe nimrudishe nyumbani?” “Haiwezekani! Sasa ulienda?” Nanaa
hakuwa akiamini, akamuuliza Geb kwa mshangao.
“Unacheza na Danny wewe? Hivyo hapo ni kwa
kuwa hakuwa akipafahamu alipo mkewe, lasivyo angeenda mwenyewe. Ikabidi niage
ofisini nimfuate Grace. Kwanza alinipa dakika kumi ya kuondoka pale nikamfuate
mkewe, lasivyo angewasha moto majengo yote yale ya BOT.” “Haiwezekani!” “Humjui
Danny wewe. Hapo kaja na kiberiti, kakishika mkononi.” Danny alikuwa kimya
kama sio yeye.
“Kwanza nilikuwa kwenye kikao, simu nimeacha
ofisini. Nilipokuja kuitwa kwenye kikao kuwa Danny anataka kuniona. Nikaanza
kujipapasa mifukoni kuangalia simu yangu. Nikajua atakuwa amenipigia amenikosa
ndio maana yupo pale. Haraka sana nikaanza kujiuliza alipo Grace, nikakumbuka
alisema angeenda Bagamoyo. Basi nikatoka pale nikiwa nimeshajiandaa. Nimefika
tu pale, akanitupia swali, eti ‘hivi wewe Geb, tatizo lako ni kwamba
hujui kutangaza biashara yako au simfikirii yeye na mwanae, Fili?’ Nikatulia
kwanza sikujibu kwa haraka, kwa kuwa alikuwa amekasirika sana. Nikabaki kimya.”
Geb akaendelea.
“Eti akaniambia kuwa najua wazi kuwa mkewe
anavutia. Hakuna mwanaume atakayemuona Grace asimtamani. Eti akiwa amekaa tu
huyo mkewe anavutia usoni, akisimama ndio kabisaa. Hakuna mwanaume atakayeacha
kumtamani mkewe, hata kipofu akisikia sauti ya mkewe atataka kumshika mkewe.”
Wote walikuwa wanacheka.
“Usifikiri maneno hayo Danny anaongea akiwa
amekaa, ni amesimama, anawaka kama moto. Sasa hapo najiuliza moyoni, sijui
Danny kama hapo alipo wakati huo anaponigombesha najiuliza hakuna kweli wazo
hata moja linalopita na kumkumbusha kuwa Grace ni dada yangu, tena pacha!? Sasa
zile sifa anazozisema za mkewe, hajui kuwa anamwambia kaka yake? Huku natamani
kumjibu kuwa labda huo uzuri wa mkewe anauona yeye tu, wanaume wengine
hawauoni, lakini sikuthubutu, nikajua utakuwa ugomvi mkubwa zaidi.” Geb akaendelea.
“Hapo ananitukana na kunigombesha eti kwa kuwa
nimeshindwa kufanya biashara zangu, ndio nimeona nitumie uzuri wa mkewe
kujipatia wateja. Sasa hapo ni kelele, na amenitoa katikati ya kikao.
Nikamuomba kiustarabu, nikamwambia, naomba tukazungumze nyumbani. Wewewewe,
ndio niliharibu zaidi. Akaniambia, ananipa dakika kumi, niwe nimetoka pale
nikamfuate mkewe popote nilipomtuma. Nimletee mkewe ndipo tutazungumza. Lasivyo
hata ikizidi sekunde, anawasha moto lile jengo lote. Hapo katoa kiberiti. Na
ananiambia nimebakiza dakika 9, niwe nimetoka pale. Haraka sana anamtaka
mkewe.” Walikuwa wanacheka sana. Nanaa ndio alikuwa anafuta machozi.
“Sasa kwa nini usimpigie simu Grace mwenyewe
umwambie arudi?” “Hapo Grace mwenyewe kakasirika kweli kweli. Danny
kashamchemsha kwa maswali kuanzia anaondoka mpaka anafika huko. Mara amesikia
sauti ya mwanaume pembeni yake. Mara kama amesikia sauti kama yupo kwenye
chumba kitulivu, ilimradi tu. Sasa Grace hapo na yeye kashakasirika anawazimia
simu wote au hapokei simu ya mtu. Hataki kurudi mpaka akamilishe kazi yake, na
Danny naye anamtaka mkewe. Basi hapo ni shuguli. Simu zinapigwa kila mahali
mpaka kwa mama.”
“Sasa na mimi huko kazini kwangu shuguli sio
ndogo. Grace anapiga simu analia, Geb naye anakwambia Danny amemwambia
akamfuate mkewe, na alikuwa kwenye mkutano, sasa bado simu ya mwenye mke. Hapo
ndio utachoka. Utasikia ‘mama, si unayajua maumbile ya mke wangu
yanavyotamanisha?’” Watu walizidi kucheka.
“Basi mimi namjibu taratibu maana hapo anawaka
kweli kweli, namwambia ‘Sijui mwanangu.’ Kidogo ndio anashtuka kuwa
anaongea na mama yake Grace, anatulia. Lawama zinahamia kwa Geb. Geb anamuuza
mkewe kwa wanaume. Geb sio muungwana. Geb anashindwa kumfikiria yeye na Fili.
Mkewe akiwaacha yeye ataleaje mtoto peke yake. Yeye ni yatima, hataki maisha
aliyoishi yeye ndio Fili ayaishi. Geb anaweka pesa mbele kuliko utu. Hapo
atalalamika mpaka wafike Bagamoyo amuone mkewe ndio anakata simu.” “Bagamoyo
tena!?” Nanaa akauliza.
“Kwani wewe unafikiri aliponituma
kumfuata mkewe Bagamoyo yeye alibaki? Tuliongozana naye mpaka Bagamoyo
akamuone mkewe.” “Haiwezekani!” Nanaa hakuwa akiamini. “Hujamjua Danny.
Hapo tena wewe adui. Unamuuza mkewe, hawezi kukuamini tena. Kwanza haamini mtu
na mkewe. Hataki umsifie mkewe hata kidogo. Mbona kina James wanajua. Ukitaka
ugomvi na Danny, anza kumsifia mkewe. Hapo utamjua yeye ni nani.Wewe utakuja
kumuona tu. Si Upo hapa? Utamuona, na hana aibu yeyote linapofika swala la
mkewe.”
"Basi huyo Grace anakuwa anarudishwa
nyumbani kutoka Bagamoyo na msafara. Yeye Grace mbele, mumewe anafuata, halafu
mimi nafuata nyuma nikishamalizana na watu huko shamba. Hapo kashanitukana
mbele ya mkewe, kama ni mshahara ninao mlipa mkewe, nisimbambaishe nao. Na yeye
pesa anayo, anauwezo wa kumlipa mkewe, tena kwa dola. Niache dharau. Magari
matatu au watu watatu tumeenda kufanya kazi ya mtu mmoja. Na sio kwamba wengine
hatuna kazi, tumeacha kazi maofisini kwetu, tumemfuata Grace. Ndio mama
akasema niwe naenda mwenyewe, nisimtume tena Grace. Ndio pakatulia.”
Walizidi kucheka.
“Lakini niliona hata tulipokuwa safarini
kuelekea Marangu. Sikuwa nimeelewa. Grace alijidai kama anatuma ujumbe. Kumbe
anataka mumewe ahamie pale alipokaa.” “Ehee! Unakumbuka alivyotaka nisimamishe
gari katikati ya barabara?” Geb
akauliza. “Mimi mwenyewe niliogopa mama. Ilikuwa kati kati ya barabara
kubwa. Magari makubwa na madogo yanapita kwa kasi kweli!” Nanaa
akaongeza
“Basi pale nisingesimama hata dakika moja
mbele, ungeshuhudia varangati yake. Ikifika swala la mkewe, Danny ubinadamu
unamuisha.” “Yaani huyu, raha yake anione nimekaa hapa kama mjinga. Sijui
yukoje Danny?” “Mimi nawafahamu wanaume wa mjini bwana. Hawakawii kunipora
halafu maisha yote yakakosa ladha. Mwanangu akakua hana mama.” “Kwa nini uporwe
bwana? Kwani mimi sina akili?” “Shetani yupo kama simba angurumae. Hachoki.”
“Mimi nilijua akishanioa labda tutapumzika. Lakini naona ndio vinazidi.”
Walizidi kucheka.
******************************************************
“Danny!” Grace akamuita mumewe na
kuanza kucheka. “Danny! Unakumbuka yule mwanaume wangu wakati tupo chuoni?”
“Yupi?” Grace akazidi kucheka. “Yaani huwa nakaaga mwenyewe,
nikimkumbuka Danny nacheka mwenyewe mpaka machozi. Yaani sijui huwa
anafikiriaga nini huko kichwani mwake.” “Ilikuwaje?” Nanaa akauliza.
“Geb alipoondoka pale chuoni mwaka wa pili,
akaniachia kina James na Danny kama kaka zangu. Danny akaanza taratibu
kunifuata na kuniuliza naendeleaje na mambo mengine. Basi hapo na mimi nikawa
nimepata mwanaume wangu. Alikuwa na kazi nzuri, na usafiri. Anakuja kunichukua
jioni ananipeleka kula, halafu ananirudisha chuoni. Ananinunulia vinguo, na
kunipa vihela vya matumizi, nikawa napendeza kweli. Sijui bwana Danny akatokea
wapi? Sijui akaambiwa na nani!? Akaanza kuniambia niachane na yule mwanaume.
Sasa nikamwambia, ni mpenzi wangu, hata mama anamfahamu.”
“Hapo ndipo nilipo haribu kabisa. Akaanza
fujo. Sina raha. Kila mahali Danny ananifuata, mpaka darasani. Yaani upo kwenye
kipindi, unashangaa Danny huyo. Basi wenzangu walikuwa wakimuona tu
wanaanza kucheka, nikiona wanacheka tu, najua Danny yupo nje. Usipotoka kwenda
kumsikiliza, anaingia yeye. Mbele ya Profeser na mbele ya wanafunzi wote.
Nilikuwa nachukia jamani, natamani kulia. Na yeye hakomi Danny. Akikukosa
kwenye kipindi, anakusaka kila mahali. Unamfukuza asubuhi, jioni amerudi.”
Nanaa alikuwa anacheka mpaka machozi.
“Sasa siku hiyo natoka chumbani, yule mwanaume
kaja kunichukua tunaenda kula. Nimependeza kweli kweli. Kila mtu ananisifia.
Ile nafika kwenye gari tu, Danny naye akaja. Eti anamuuliza yule mwanaume, ‘unampeleka wapi mke wangu?’ Jamani
nilitamani kukaa chini.” Kila mtu alianza kucheka upya.
“Yaani eti mimi ni mke wake sio hata mchumba,
mkewe! Bwana Danny alifanya fujo hapo. Kina James, Zinda, Malii, Gozi na wale
wenzake wote uliowaona tukiwa safarini kule Marangu, eti wako hapo
wanamsubiria. Mimi nikamwambia yule mwanaume tuingie kwenye gari tuondoke.
Tukaondoka. Njia nzima nina kazi yakujitetea kwa yule mwanaume. Namwambia
simjui Danny, wala sina mahusiano naye. Tukafika hotelini. Tukaagiza chakula
na vinywaji, hatujaanza hata kula, Danny tena huyu hapa.” Walizidi kucheka,
bila kunyamaza.
“Sasa ulifanyaje?” “Nilitamani kuingia chini
ya meza. Hapo amekasirika kweli kweli. Eti anamwambia alishamuonya akae mbali
na mkewe lakini hasikii. Sijakaa sawa, sijui yule kaka alimtukana au alimwambia
nini, Danny akarusha ngumi. Wakaanza kupigana. Danny akafanya fujo zakutosha
huku anamtukana yule jamaa anamwambia yeye sio mwanaume, kama angekuwa ni
mwanaume kweli angekuwa na uwezo wakutafuta mwanamke wake kuliko kung’ang’ania
wake za watu.” “Jamani!” Nanaa akazidi kushangaa huku amejawa cheko.
“We acha tu. Basi, Danny akafanya fujo pale,
tukafukuzwa sisi wote watatu, tukatolewa nje. Sasa mwenzetu akapanda kwenye
gari lake akaondoka, katuacha mimi na Danny. Hapo mimi ninalia kweli kweli.”
“Sasa yeye anasemaje?” “Ananibembeleza. Eti pole, lakini wanaume ndivyo walivyo
ni wadanganyifu. Jamani Danny nyie! Nilikuwa natamani kummeza. Tubebaki
tumesimama nje ya ile hoteli. Pesa hana hata yakunichukulia taksii kunirudisha
chuoni. Ananiambia twende tukapande daladala. Yaani Danny!” Nanaa alizidi
kucheka huku anashangaa.
“Yaani amekutoa kwenye gari, halafu
anakupandisha kwenye daladala!?” Nanaa akauliza. “Tena bila aibu.
Huku ananiambia vumilia mpenzi wangu, Mungu atatujalia magari yetu.”
“Haiwezekani!?” “Mimi nakwambia kichwa chake anakijua mwenyewe Danny. Hapo tupo
kwenye daladala ananirudisha sasa chuoni. Mimi nalia na yeye ananibembeleza
mpaka tunafika. Mchezo ukaendelea hivyo hivyo. Akisikia tu nasoma na
mwanaume popote pale, na yeye anakuja kusoma hapo hapo na kina James. Hata kama
nichumbani kwa huyo mwanaume na wao wanakuja kusoma humo humo ndani. Akikataa
kuwafungulia mlango, anaanza kufanya fujo. Ikifika siku za ijumaa narudi kwa
mama, na yeye ananifuata.””Haiwezekani! anakufuata mpaka tena kwa mama?” Nanaa
hakuwa anaelewa.
“Hakuna asikofika Danny kama mkewe yupo.” Mama
G akajibu yeye maana Grace aliishia kucheka. “Hivi unajua atakaa hapo kwa
siku zile ambazo na mimi nakaa nyumbani?” “Kweli?” “Muulize mama. Yaani yeye
ndio akawa kama Geb pale ndani. Haitaji kukaribishwa wala nini, analala kwenye
makochi anaamka. Anasaidia usafi, nakuomba kupewa kazi za kutumwa na mama. Sasa
arudi hapo nyumbani asinikute, hapatakalika. Mtaa mzima walikuwa
wanatujua mimi na Danny. Wapangaji wote walikuwa wamemzoea, wanamwita mtoto wa Mama
G.” Grace akaendelea.
“Basi mama ananiambia wewe si umkubali tu
yaishe. Namwambia hana sifa hata moja yakuwa mume wangu. Namwambia namtaka
mwanaume mrefu kama Geb, sijui awe na gari, nyumba, basi sifa zote ambazo Danny
hana ndizo namtajia mama ndio aina ya mwanaume ninayemtaka mimi. Akipata
hela siku hiyo, mtamjua. Anaenda kuninunulia chips, kuku,mayai na soda. Anakuja
navyo pale nyumbani ananiletea, kama ni chuoni, atakutafuta huku ameshika
mifuko yake. Anaweza akakununulia losheni, dawa ya mswaki na mswaki mpya. Hebu
niambie mtu ndio anavyohonga hivyo jamani! Yaani nilikuwa namwambia mama,
sitaki kumsikia hata kidogo.” Walizidi kucheka.
“Sasa Geb akarudi likizo. Akanikuta nipo
kwenye heka heka ya Danny. Sina raha. Nikamuelezea matatizo yangu yote na
Danny, nikamuomba azungumze naye.” Watu wote walianza kucheka mpaka Danny
mwenyewe. “Bwana, nilimjia juu Geb, hatakaa asahau.” Danny alifanya kila
mtu acheke upya. “Yaani nilishindwa hata kujieleza, nikaishia kumwambia ‘lakini Grace anaomba umpe nafasi, Danny’.
Danny alitaka kunipiga. Nikaamua kumuacha. Huwezi kumwingilia Danny, kwa Grace.
Hana undugu wala urafiki. Hajali kama wewe ni kaka yake au mama yake Grace.
Yeye anachotaka Grace tu. Na hataki ushauri.” Nanaa alihisi ni stori tu.
“Sasa ikawaje mkaona?” “Hiyo fujo
ikaendelea mpaka namaliza chuo. Sina mwanaume yeyote, ni yeye tu yupo mgongoni
kwangu. Mchana na usiku.” “Sasa ulipomaliza chuo si alichanganyikiwa?”
Nanaa akauliza. “Achanganyikiwe kwani nyumbani hapafahamu? Yaani ndio
akafurahi. Na yeye akahamia nyumbani rasmi. Anatoka asubuhi anakwenda chuo,
jioni anarudi na kina James. Wanasomea hapo hapo nyumbani. Hajakaribishwa na
mtu yeyote. Yaani kundi la marafiki wa Geb, likahamia hapo nyumbani. Chumba
chenyewe ni kimoja, na sebule. Mwaka wake ule wa mwisho, alikuwa anaishi hapo
hapo nyumbani. Siku za mwisho za mitihani, wote wakahamia kabisa hapo hapo
nyumbani wanasoma.”
“Kila nikijaribu kumshauri Danny, kuwa arudi
chuoni mpaka mitihani iishe, hataki. Anasema yeye anamjua shetani vizuri
sana. Na usemi wake ni huo huo, shetani ni simba angurumaye, anazunguka
kutafuta mtu amrarue. Mama naye akawa na kazi ya kuwapikia. Wamejaa humo ndani,
sina raha.” Kila mtu alikuwa akicheka na kutingisha kichwa.
“Nikapata kijikazi, nako huko ilikuwa shida.
Akaenda kujitambulisha kuwa yeye ndio mume wangu, na tunaishi pamoja.”
“Jamani!” Nanaa akashangaa. “Hapo wala sijamkubalia. Kwa hiyo ofisini
wote wakajua nimeolewa, naishi na mume wangu, Danny. Kukanusha tena huwezi, kwa
kuwa ikifika jioni, giza limeingia hajaniona nyumbani, utamuona mwenyewe huyo
amekuja kunichukua kazini. Utasikia mlinzi getini anatangaza kwenye kipaza
sauti, Grace umekuja kufuatwa. Unaweza kudhani nimefuatwa na gari.” “Kumbe!?”
Nanaa akauliza kwa mshangao.
“Alitoe wapi gari huyo Danny!? Mnatembea kutafuta daladala. Siku
za mvua ndio alikuwa anakuja mapema mwenyewe, ananisubiri mpaka nitoke naye.
Eti nisitembee peke yangu kwenye mvua.” “Kumbe alikuwa anakujali!” “Sana. Wewe
subiri usikie.” Grace alitaka kuendelea.
“Basi, kuna dada mmoja alikuwa sekretari wa
kampuni, akawa ananiunganishia na wanaume. Ananiambi mdogo wangu, kiuno hicho,
na tako hilo, ukichanganya na macho hayo, huyu ameahidi kukupa gari,
yule nyumba. Kila siku anakuja na majina mapya ya wanaume na ahadi mpya.” “Sasa
uliwakubalia?” “Hivi wewe Nanaa hujaelewa. Naanzia wapi? Danny alikuwa
ananikaba mpaka kooni, sina pakuhemea. Si nyumbani, si kazini. Akiona
mwanaume amekusogelea, anamuonya kwa maneno kwanza, kinachofuata ngumi. Mkali
kwa mama, mkali kwa Geb. Anawaambia Grace ni jukumu lake, Mungu amempa.”
Mama G, alikuwa anacheka tu.
“Danny! Mimi sijawahi kuona jamani. Na hana
aibu hata. Utamuona anaamka asubuhi, anakuomba nauli ya kwenda chuoni.
Namwambia sasa Danny mwanangu, labda ungekaa tu chuoni kwa muda. Utamuona
anavyobadilika. Hapo hapo anakasirika. Tena nilichompendea Danny, hakuwahi
kuniona mimi ni mama mkwe wake au sijui mama yake Geb. Nakwambia alinimiliki
kuliko hata Geb mwenyewe. Akipata tu pesa, zote anamnunulia Grace vitu.
Namkumbusha, namwambia labda angehifadhi pesa baadhi zimsaidie nauli ya kwenda
chuoni. Basi mwenyewe anakutolea kidaftari chake alichokuwa akiandika vitu vya
kuja kumnunulia Grace.” Mama G akaendelea.
“Akimsikia tu analalamika anataka kitu fulani,
anaandika chini, kila kitu anaandika. Hata kama akimsikia anahamu ya kula kitu
fulani, hutamsikia akiongea kitu, anaandika chini. Sasa akilipwa huko chuoni,
pesa yote itaisha siku hiyo hiyo. Utamuona anaingia humu ndani na mifuko.
Atanunua chakula kidogo tu cha kula watu wote humo ndani, lakini pesa nyingine
zote zinaishia kwa Grace. Yeye anasuruali zake mbili tu za jinsi, na t-sheti 3.
Namwambia labda ujiongezee t-sheti, hapo tena ugomvi, Grace kwanza.” “Jamani!
Kumbe alikuwa anampenda hivyo?” Nanaa akavutiwa. “Mpaka leo Danny yupo
hivyo hivyo. Ni heri akose yeye, mimi nipate kwanza. Hakuna nitakachotaka kwa
Danny asinipe. Mpaka wakati mwingine sipendi kulalamika mbele yake.” Grace
akaongeza.
“Kwa hiyo ndio mkaoana?” “Hapana. Yaani yote
hayo alikuwa ananifanyia nilikuwa wala sijamkubali. Wewe hujakutana na Grace wawakati
huo. Nilikuwa gumzo kila mahali, halafu nije kuolewa na mtu kama Danny!
Hana gari, nguo zake kila mtu anazifahamu! Sithubutu. Kila anayeniona anataka
kunioa. Wanawake wananithaminisha, basi wananiambia yaani wewe Grace, hongo ya
mwanaume anayekutaka wewe ni gari, huyo ni masikini, au Jumba. Ukiwa makini
utapata vyote. Basi hapo kichwa kinazidi kuwa kikubwa, wala sioni anayonifanyia
Danny. Yaani naona anajipotezea muda tu.”Grace akaendelea.
“Sasa yule dada wa ofisini kwetu, sekretari,
alikuwa dada mtu mzima tu, akaniunganishia kwa kijana mmoja mfanyabiashara.
Alikuwa anakujaga pale ofisini. Alikuwa na pesa kweli kweli. Nikaamua kuolewa
naye bila hata kipingamizi, hapo yule dada ananishawishi kila akiniona,
anamsifia huyo kaka. Ananiambia kama ni kuyapatia maisha, basi hapo
nimeyapatia. Basi tukakubaliana na yule kaka, nikaamua kumuwahi kabisa.
Nikamuelezea tabia zote za Danny. Nikamwandaa nakumwambia mambo yote ambayo
Danny anaweza kumfanyia. Akaelewa kwa haraka sana. Maana na yeye alikuwa kama
kachangayikiwa. Kila ninachomwambia anakubali, ilimradi tu anioe.”
“Basi wakati huo mama ananiambia nizunguke
kila ninakotaka, lakini kulala na mwanaume mwiko. Hapo mama akawa mkali kweli
kweli, hanichekei. Kila wakati swali ni hilo hilo, sina raha. Hata ukipata
mwanaume, huwezi kulala naye! Sasa yule mwanaume akawa anataka sana tulale
naye. Kila akiniona ananibembelezea mapenzi. Mimi nikamwambia mama yangu
ameniambia ni marufuku kulala na mwanaume asiye mme wangu. Bila kufikiria,
akatangaza ndoa. Akasema nakuoa. Akanipeleka kwao, wakanipokea. Ndugu zake wote
wakamsifia kapata mke mzuri. Sasa na yeye akawa anataka aje amuone mama,
wapange siku ya kulipa mahari.” Grace akatulia kidogo.
“Nakumbuka siku niliyompeleka kwa mama,
Danny alikuwepo. Nikamtambulisha. Alikuwa kijana mtanashati, pesa ipo,
anajielewa, sio kama Danny. Sitasahu sura ya Danny aliyoniangalia siku ile
wakati nimemleta yule kijana. Danny aliumia mpaka mama alimuhurumia. Sasa hapo
mama mapenzi yashakuwa kwa Danny. Anampenda Danny kama mwanae Geb. Huna
utakachomwambia mama tena juu ya Danny akakuelewa. Kamaliza chuo, eti mama
anamwambia aendelee kusoma. Nikaona hapa nikucheleweshana. Mtu hana pesa,
amemaliza chuo, badala atafute kazi, apate pesa kama wenzake kina James, eti
anarudi tena chuo! Nikaamua niolewe, niendelee na maisha yangu.” “Ehe!”
Nanaa alitaka aendelee.
“Basi, mama akamkarimu huyo mchumba mtu. Baada
ya chakula mimi na yule kijana tukaondoka. Nikashangaa siku ile Danny
hakuzungumza neno hata moja wala hakufanya fujo kama nilivyotarajia. Alinyamaza
kimya akisikiliza mipango mizito ya yule kijana ya kulipa mahari. Kijana
alijigamba pale siku ile, si mchezo. Basi kama unavyomuona mama pale,
ndio alikuwa vile vile siku ile katulia kimya anamsikiliza kijana akitoa
mikakati yake. Sasa najiuliza mbona mama mwenyewe hafurahii. Maana tulipewa
ahadi chungu mzima, ikiwemo yakuhamishwa pale kwenye chumba cha kupanga,
kupelekwa kwenye nyumba. Tena akasema kwa haraka kabla ya hiyo siku ya mahari,
kwa kuwa siku hiyo atakuja na marafiki zake wengi sana, magari yatakuwa mengi,
hapatakuwa na sehemu ya kuegesha magari pale uswahilini tulipokuwa tukiishi.”
“Nakwambia kijana ametoa mikakati kibao. Mama,
mtoto wa mjini katulia kimya yeye na Danny wake wanamsikiliza. Basi mimi cheko
imenijaa. Furaha tele. Napewa nyumba na gari! Basi hapo huna utakaloniambia
nikaelewa juu ya kuyapatia maisha. Basi, baada ya kujigamba pale tukaondoka na
yule kijana, hapo alikuwa ameleta vyakula kibao, akamuachia mama pesa za
matumizi.” Grace akatulia.
Alipo ondoka Danny
“Sasa akanirudisha usiku mwenyewe nimejawa
furaha, nimehongwa pesa, nina ahadi ya kuolewa na kwenda kuishi kwenye jumba la
kifahari, akasema ataninunulia gari ili nisipate shida ya usafiri. Nimeingia
pale ndani, Danny hayupo sehemu aliyokuwa analala. Alikuwa analala kwenye
makochi sebleni, mimi na mama chumbani. Mama akasema aliondoka mara tu
tulivyotoka. Usiku ukapita, Danny hajarudi. Usiku wa pili tena, Danny hajarudi.
Nikaanza kukosa raha.”
******************************************************
Usikose
kufuatilia mkasa wa Grace na Danny. Nini kilitokea mara baada ya Danny
kuondoka? Ilikuaje mpaka kijana huyo asiye na kitu, akaishia kummiliki Grace,
msichana aliyesumbua wengi wenye pesa zao?
Endelea Sehemu ya 22.
0 comments: