Story
is mine - ni Wangu! Part 1, Sehemu ya 22.
G
|
race akaendelea. “Nilikuwa nimeshazoea mwenyewe nikiamka
tu asubuhi na yeye Danny anaamka. Ananibebea maji mpaka bafuni, ananisubiria
nje ya mlango wa bafu, naoga, nikimaliza kuoga, nikitoka tu na ndoo,
ananipokea, tunarudi ndani. Naenda kuvaa, ananisindikiza kituoni, napanda
daladala naenda kazini, yeye anarudi kulala. Kila siku ndio ratiba yetu.”
Nanaa akashangaa machozi yanamtoka. “Jamani ni
upendo wa ajabu! Mimi sijawahi ona!” Sauti ya Grace ikaanza kupooza.
“Huyo ndio Danny. Pale kwenye ile nyumba, wapangaji wote walikuwa
wanatujua. Mpaka mtaani pale uswahilini mimi na Danny tulikuwa gumzo. Walikuwa
wanasema ukimuona Danny yupo nje ya mlango wa bafuni, ujue Grace anaoga ndani
na ukimuona Grace anapita, ujue Danny yupo nyuma au pembeni yake. Inategemea
siku hiyo tunarudije. Akiwa ameniudhi huko nilipotoka, tunarudi nyumbani kwa
Mama G, mimi nalia nipo mbele, yeye ananibembeleza yupo nyuma ananifuata. Hapo
amenitoa kwa mwanaume, kafanya fujo, au kapigana, ndio tunarudi sasa nyumbani
kushtakiana kwa mama.” Wakacheka.
“Basi, siku ya nne Danny hajarudi nyumbani, nikaanza
kuchanganyikiwa. Danny hayupo na hatujui yuko wapi. Yule kijana hata akija
kunisalimia, sitaki tena. Kila nikimfananisha na Danny, ni kama Mungu na
shetani. Hawafanani hata kidogo. Gafla pakawa hamna tena mwanaume kama Danny
hapa duniani. Nahangaika sasa. Si unajua tabia ya mama? Kimya mwenyewe
ananiangalia ninavyohangaika.” Wakacheka kidogo.
“Sijui pakumpata Danny, chuo kilishaisha, wenzake wote
walisharudi makwao. Najaribu sasa kuvuta kumbukumbu kujua kama Danny alishawahi
kuniambia kama ana ndugu hapa
Dar. Kumbukumbu hazinijii hata kama anawazazi au la, sijui. Kwa kuwa
nilikuwa nampuuza. Simchukulii maanani. Hata akiongea tukiwa wawili, mawazo
yalikuwa sio pale na yeye, nawaza mambo yangu. Kwa hiyo nikajikuta simfahamu
Danny, mwanaume aliyekuwa kwenye maisha yangu zaidi ya miaka miwili. Tena kwa
karibu.” Grace akatulia.
“Endelea!” “Nanaa kwa kupenda stori!” Danny aliingilia. “Ndio kazi yake hiyo. Basi anakazi ya
kudodosa tu. Wewe uongee, yeye acheke au alie. Na hataki umfupishie stori.” Mama
G akaongeza, wote wakacheka. “Basi, hali yangu ikazidi kuwa mbaya. Niliamka
siku hiyo siwezi hata kutoka kitandani, nalia kama ninaumwa. Sitaki tena kwenda
bafuni, Danny wakunibebea maji hayupo. Mama naye anajifanya hajui
kinachoniliza, eti ananiambia nikupeleke hospitali? Nashindwa kujibu, nalia
tu.” Wakacheka tena.
“Kazini siwezi kwenda tena, kitandani siwezi kutoka.
Nilishazoea nikiamka namkuta Danny kwenye makochi ananipeleka kuoga, halafu
ananisindikiza kituoni, anasubiri mpaka nipande daladala ndio anaondoka. Na
jioni siku za mvua, nilizoea nikimaliza kazi namkuta
ananisubiri nje na mwamvuli na koti la mvua, ananivalisha koti, ananishikia
mwamvuli nisilowe. Danny ndiye anajua kama sina dawa ya mswaki. Danny ndiye
anajua natakiwa kubadili mswaki, ananinunulia. Danny ndiye anajua sabuni yangu
ya kuogea kama imeisha anunue nyingine au la. Yaani nikajikuta Danny ndio
anajua kila kitu changu. Vile vitu vidogo vidogo mwanadamu yeyote anavyohitaji.
Vya msingi kabisa kwenye maisha, ndio Danny alikuwa ananifanyia.” Grace
akaendelea.
“Si unajua hata kama unamamilioni ya pesa, nyumba na gari,
lakini lazima utahitaji kuoga na maji, sabuni na lazima taulo. Kusafisha kinywa.
Kwa hiyo pia ni lazima utahitaji mswaki na dawa ya mswaki. Na lazima uwe na
malapa kwa sisi tuliokulia uswahilini. Bafu la watu wote. Lazima kuvaa malapa.”
“Usisahau mashuka.” Mama G akaongeza. “Ehee, mama. Na
mashuka. Vyote hivyo Danny ndio alikuwa mnunuaji. Akiona chochote kimekaa muda
mrefu, akipata pesa tu, anaenda kubadilisha. Tena kama ni shuka, akinunua
jipya, anakuja kututandikia kabisa. Hata kama mliamka mkatandika kitanda. Akinunua
shuka lake, mtakuta limetandikwa kitandani. Sasa mtu wa hivyo huwezi
kumlinganisha na mwenye ahadi ya gari hata siku moja. Danny hajui kuahidi kama
vile alivyokuwa akikwambia Zinda. Yeye huwa ananiletea tu. Tena hata sikumbuki
kama nilikuwa nikimwambia asante. Eti Danny?” Grace akauliza.
“Hivi nilikuwa hata nasema asante kweli?” “Mimi nilikuwa
naangalia upande wangu tu. Nilikuwa najiambia lazima nikufanyie hiki.
Nikikitimiza ndio ilikuwa furaha yangu, wala sikuwahi kuzingatia upande wako.”
“Jamani! Lazima ulichanganyikiwa Grace. Huwezi kumpoteza mtu kama huyo hata
iweje.” Nanaa akaongeza.
“Kwani nilichanganyikiwa kidogo? Nilikuwa nimechanganyikiwa
haswa. Kumbukumbu zilikuwa zikinijia kwa kila kitu alichokuwa ananifanyia.
Nikawa ninakazi ya kulia tu. Nakumbuka nilikuwa nimelala pale kitandani nalia.
Sijaoga, sijala, wala mswaki sijapiga. Ilipofika jioni hali yangu ikazidi
kuwa mbaya, ikabidi kumuuliza mama kama katika mazungumzo yake na Danny,
alimwambia kwao ni wapi. Mama akaharibu zaidi aliponiambia Danny ni yatima.
Sijui alilelewa na mapadri, na hakumbuki ni wapi. Nilikaribia kuchanganyikiwa.
Kumbe Danny ni yatima! Mimi nimemfukuza, basi nilizidi kulia.” Grace akaendelea.
“Siku inayofuata, nikaenda kuchukua likizo kazini.
Nikawaambia naumwa, sitaweza kufanya kazi. Nikarudi nyumbani. Nililala siku
tatu. Sitaki kula wala kunywa maji, nalia nalala, nalia nalala huku nikitegemea
labda Danny atarudi, lakini wapi. Mama alivyo na tabia mbaya, eti akawa
ananiacha kitandani, anaenda zake kwenye shuguli zake, akirudi anajinyamazia
zake kimyaa. Akijitahidi sana, atanishika kichwa, eti anaangalia homa. Halafu
utamsikia ananiambia, ‘lakini huna joto,
itakuwa ni kuchoka tu’.”
Wakajikuta wote wanacheka mpaka Mama G, mwenyewe.
“Sasa mama kwa nini hukuwa unamtuliza?” Nanaa akauliza. “Wewe hukumuona wakati ule namwambia
amkubali Danny, halafu ukayasikia majibu yake. Basi na macho hayo kama ya baba
yake, anasimama ananiambia, ‘niangalie
vizuri mama. Nitazame juu mpaka chini, nilinganishe na Danny. Mimi sio mtu
wakuolewa na mtu kama Danny bwana. Naliliwa na watu wamaana! Danny suruali
moja!’ Basi maneno yalikuwa hayamwishi.” Mama G akaendelea huku wengine
wanacheka.
“Nikawa namwambia, mimi nazijua pesa. Zikiwa mahali
hazihitaji zisemewe, zinaongea zenyewe. Tena huwa zinakelele kweli. Hazihitaji
mdomo wa mwanadamu. Haya nikawa namuona vile mwenzie anavyohangaika naye,
namwambia Grace mwanangu, mimi nayajua maisha, wanaume kama Danny hawapo. Danny
anakujali wewe. Basi majibu yake huyo Grace utasikia, ‘Wewe mama unayajua
maisha, lakini hujayaishi bwana. Acha mimi niyaishi maisha.’ Basi
ananitajia mahoteli anayopelekwa. Ahadi anazopewa. Nikasema basi ngoja nimwache
mwenzangu ayaishi hayo maisha. Eti leo Danny kaondoka, anataka anitie
matatizoni! Nikasema nimuache kwanza atie akili. Bwana Grace alikuwa analia
kama kafiwa na mama yake mzazi! Basi mimi nilikuwa najifanya sijui. Naenda,
namshika kichwa najidai nampima homa, huku moyoni namcheka na kumwambia akome.” Wote walicheka mpaka Danny.
“Lakini tokea mwanzoni, nilijua hatafika mbali. Nikajua hao
wanaume wote wanahangaika naye tu. Wala hatawaweza.” “Kwa nini mama?” Nanaa akauliza tena. “Grace ni mwanangu. Namjua sana.
Anapenda sana kupendwa na kufuatilizwa kwenye vitu vidogo vidogo. Hana tamaa ya
maisha, labda akutane na mtu, amtie wazimu. Lakini hasumbuliwi na magari au
nyumba. Ukimsikia anaongelea hayo mambo, ujue sio yeye anayeongea, kuna
anayeongea huko akilini mwake. Yeye anataka akumbatiwe, ashikwe shikwe,
abembelezwe basi.” Nanaa akacheka sana.
“Akiumwa na kichwa, asikwambie. Yaani unatakiwa wewe ujue tu
kama kichwa chake kinamuuma. Akikasirika, ujue kilichomuudhi bila yeye
kukwambia. Sasa kazi hiyo niliiona ni Danny peke yake ndiye anayeiweza kama sio
mimi. Maana mimi niliwalea hawa wawili kwa pamoja. Tena kwa karibu sana ni kama
sikusaidiwa hata na msichana wa kazi.” Mama
G, akaendelea.
“Geb yeye anataka akuone wakati wote. Anaweza akawa na shida
yake, asikwambie au hata asitake ujue, lakini atataka akitaka yeye kukuona
akuone tu. Huyu dada mtu yeye, umfuatilize. Tena Grace anadeka kuliko hata Geb.
Lakini watu wanasema Geb ndio mdekaji, lakini Grace ndio amezidi. Nilikuwa
namwambia baba yake, sifikirii hata kuongeza mtoto mwingine sababu ya Grace.
Nakuwa kama nina watoto wawili kwa wakati mmoja. Kuongea hawezi, basi wewe
unakuwa na kazi yakumfuatiliza nyuma. Ujue kila kitu kinachoendelea kwenye
maisha yake na umsaidie. Ukiona analia, ujue kuna ulipompuuza tu. Lakini si
Geb.”
“Sasa alipokuja Danny, nikasema asante Mungu wangu. Nikajua
huyu ndiye mume wa Grace. Maana kabla Grace hajalia shida, Danny ataitimiza.
Hata kama hana pesa. Kwa kadiri ya Mungu atakachomjalia, atamsaidia. Na anamjua
mkewe kwa kumwangalia tu. Tokea wapo chuoni. Sasa walipokuwa wanakuja wanaume
hapa wanataka kumuoa Grace, na ahadi za magari na nyumba, nilikuwa nawajua
kabisa hao sio. Nikawa nazidi kuthibitisha kuwa Danny ndio mumewe. Sasa uzuri
mwingine Danny akawa ananisaidia, yeye hajui. Kila analoliona kwa Grace,
anakuja kuniambia. Ikawa ni kama Mungu amenipunguzia mzigo, akampa hiyo kazi
Danny.” Walizidi kucheka.
“Endelea Grace.” Nanaa
alitaka Grace aendelee. Grace akacheka tena kidogo. “Yaani nyie mama ni
mchokozi! Eti mwenzie nalia, yeye ananiuliza, ‘Ni lini sasa tunahamishwa
kwenye hiyo nyumba ya mchumba wako?’ Basi ndio nazidi kulia, sitaki hata
mama amtaje. Kwanza yeye ndio kasababisha Danny wangu aondoke. Sitaki hata
kuiona sura yake.” Walizidi kucheka.
“Nilipoona yananifika shingoni nikamwambia mama nahisi
nisipomuona tena Danny, nitakufa. Eti mama anazidi kunichokoza ananikumbusha maneno
yangu. Ananiambia, ‘Mimi naona uachane na Danny tu. Kwanza Danny maskini.
Danny suruali moja! Achana naye. Twende hospitalini, ukaangaliwe afya yako,
upone tuanze kujiandaa na kuhama hapa. Tufikirie maisha mapya tukiwa na nyumba
na gari.’ Basi ndio ananikera zaidi nazidi kulia.” Watu wakazidi
kucheka.
“Mama wewe!” Nanaa
akashangaa huku anacheka. “Kumbe!” Mama G akajibu. “Na usifikiri
anaongea hayo kwa kifupi. Anaongea mwenyewe huku anafanya shuguli zake hapo
ndani wakati mwenzie nimelala, nalia. Eti ‘huu ndio wakati wa kuyaishi
maisha bwana!’ Anajiongelesha huku anaingia na kutoka. Akaenda kuoga,
akala, akapanda pale kitandani nilipolala. Akanishika tena kichwa, hapo
nimeanza kupandisha homa kwa kulia. Eti ananiambia nimpe namba ya simu ya yule
mchumba amuombe alete gari, anipeleke hospitalini.” Nanaa alizidi kucheka.
“Yaani mama wewe!” Nanaa
akaongeza. “Nilitaka nimwache mpaka akiri ujinga wake. Nikajidai kama sijui
kinacho mliza.” “Ndio nikamwambia mama, mimi siumwi. Namlilia Danny. Namtaka
Danny. Eti mama akajifanya kama gafla hamjui tena Danny. Eti ananiuliza Danny
yupi? Eti yeye anakumbuka jina la yule mchumba niliyemletea haitwi Danny. Tena
akaanza kunishauri, eti niwe makini sana na ninavyowataja majina yao. Nisije
kuwachanganya, nikaachwa. Eti kupata wanaume wanaohonga magari na nyumba ni
shida sana. Mimi nimebahatika, niwe makini, nisije kuishia kama yeye,
nikashindwa kuyaishi maisha.” Walizidi kucheka.
“Nikajua ananikejeli tu. Nikawambia namtaka Danny huyu
tuliyekuwa tunaishi naye. Akaniuliza sasa nyumba na gari? Hapo anazidi kuniliza.
Nalia kweli. Nikamwambia mimi sitaki nyumba wala gari, namtaka Danny wangu.
Mama akazidi kunikera sasa, si nilimwambia hajayaishi maisha? Sasa akaamua
kunikomoa. Eti ananiambia nafanya maamuzi mabaya sana kwa kumchagua Danny.
Sitayaishi maisha. Jamani nikaangua kilio zaidi. Namwambia hamna maisha bila
Danny mama. Namtaka Danny. Lasivyo nitakufa. Nikawa nalia kwa kwikwi sinyamazi.
Hapo ndio akanionea huruma, akashauri niwatafute marafiki zake. Namba za
simu sina. Mama akaongea na Geb, Geb akamtumia namba zote za marafiki zake
Danny.” “Kwani yeye mwenyewe hakuwa na simu?”
Nanaa akauliza.
“Hela ya simu atoe wapi wakati pesa yote anampa Grace?” Mama G akajibu nakufanya wote wacheke. “Hakuwa na simu.
Basi mama akaanza kazi yakumpigia mmoja baada ya mwingine. Ndio akaambiwa Danny
yupo kwa kina Zinda, Tabora. Anafanya biashara na baba yake Zinda. Anakusanya
pesa, ili aje arudi chuoni asome sasa shahada yake ya pili. Nikaanza kukusanya
mizigo yangu.” “Unaenda wapi sasa?” Nanaa akauliza.
“Tabora kumfuata Danny! Nilikuwa siwezi tena kusubiri, na
sikutaka aambiwe kuwa naenda, asije kunikimbia. Mama akamuomba Zinda, anisubiri
kituo cha mabasi, nakwenda kesho yake. Basi, nikaamka asubuhi, nikawahi mabasi
mpaka Tabora. Zinda akanipokea kituo cha mabasi. Ilishakuwa jioni, akaniambia
Danny huwa anarudi usiku kutoka kwenye biashara zake na baba yake. Mama yake
Zinda akanitayarishia chakula, sikuweza hata kula, nilikuwa nalia tu. Nikabaki
namsuburia Danny. Hapo nalia kama nimefiwa, hakuna aliyekuwa ananielewa.
Ikafika kama saa tatu usiku, ndio Danny akarudi.” Nanaa akamuhurumia.
“Nakumbuka alikuwa amechoka mwenyewe, halafu amekondaa
gafla. Hakuamini aliponiona pale. Akaniambia nimsubiri aoge, halafu tuzungumze.
Akaoga, akaniambia tuzungumze nje.
Nilishindwa hata kuongea kwa furaha. Nililia mpaka basi. Akanichukua akaenda
kunitafutia chumba, kwenye nyumba ya kulala wageni. Maana pale kwa kina Zinda
kulikuwa kumejaa, hakuna hata pakukanyaga. Zinda akikwambia anakwenda kufuata
wadogo zake kwao awalete mjini, usifikiri anakutania. Ni kweli anampango wakuwahamishia
ndugu zake mjini. Kwa hiyo Nanaa ujiandae.” Nanaa alicheka mpaka machozi.
“Unacheka nini? Ndio ujiandae.” Mama G, akamchokoza. “Zinda hawezi kuwa mume wangu.
Nilishamwambia, tokea tupo Marangu.” “Ndio maana alikuwa amepooza! Basi kila
nikimuuliza Zinda vipi mwanangu, ananiambia maisha tu mama.” “Alituambia usiku
ule ule mimi na James. Kuwa Nanaa amemkataa. Amesema hayupo tayari kuolewa.
Nikamuuliza kwa nini hakuomba hata wawe kwenye mahusiano? Akaniambia
alimuomba, lakini Nanaa amemkataa kata kata. Huku akisema mpaka amalize shule,
ajiweke sawa kwenye maisha. Wakati huo bado hajatulia. Ndio James akajaribu
kumuelezea wakati mgumu anaopitia Nanaa wakati huo, akaomba Nanaa aachwe
kabisa. Lakini Zinda akanifuata baadaye akasema anahisi James anamkatalia tu
kwa dada yake, kwani kama angetaka James, angeweza kuzungumza na Nanaa,
akamkubalia. Akaniambia hata siku tuliyokuwa tukimnunulia vitu Nanaa, James
hakuonekana kufurahia.” Danny aliongeza na kumshangaza Nanaa.
“Zinda alininunulia mimi vitu!?” Nanaa akauliza kwa mshangao sana. Geb akamtizama. Nanaa
akajishtukia. Akamtizama Geb. “Sio kwamba navitaka jamani! Nauliza tu.”
Nanaa akajitetea kwa sauti ya chini, akainama kuendelea kuangalia kidole cha
Geb. “Unafikiri alikuwa akikudanganya alivyosema atakununulia viatu na
magauni?” Danny akauliza, wote wakacheka kasoro Nanaa. “Mwenzio alikuwa
hatanii. Sema tu hajui kutongoza. Pale walikuwa wakiendesha gari yake, kwa
kusudi kwa kuwa ilibeba mizigo yako. Vyote alivyokutajia siku ile alinunua
kweli. Ila akaongeza na maua. Mpaka nguo yakuvaa kwenye ile Sendoff ya mke wa
Malii, alikununulia.” Danny akaongeza.
“Kukimbia kimbia kumekufanya ukose zawadi.” “Nisingepokea
mama. Nisingeweza kumfanyia hivyo wakati nilijua wazi nisingemkubalia. Na yeye
nilimwambia ukweli. Zinda ni mtu mzuri. Sikutaka kuja kumuumiza baadaye.”
“Hukumpenda?” “Mama na wewe! Hayo ni maswali yetu tukiwa mimi na wewe tu? Mpaka
watu wajue siri zetu?” Wakacheka
sana.
“Si utuambie tu Nanaa! Na sisi tunataka kujua bwana. Kwa
nini ulimkataa Zinda?” “Bwana Grace achana na mambo hayo. Tuendelee na stori ya
Danny na wewe. Ndio nzuri, kwanza inafundisha.” “Anapenda stori huyu! Hapo
mbona umemfikisha. Na hataki umalize. Ukimuendekeza Nanaa, mtalala hapa.”
“Bwana mama! Usimfanye Grace agairi. Endelea mwaya Grace. Uliishia
alikukodishia chumba.” Watu wote
walicheka kwa pamoja.
“Si niliwaambia? Huyo kwa stori hamtamuweza. Anakumbuka neno
kwa neno.” Mama G, akaongeza. “Mimi ndio
msikilizaji mzuri. Si eti Grace? Naonyesha nakusikiliza kwa makini. Mwenzio
najifunza. Endelea.” “Mmmh!” Mama G, akaguna. “Nini mama jamani? Endelea
Grace.” Grace akacheka.
“Basi. Nakumbuka Danny alitaka aondoke, aniache pale
kwenye nyumba za kulala wageni, akaniambia atarudi asubuhi yake, lakini
nilishindwa kumuachia. Nilikuwa nalia sana. Basi akapanda kitandani, tukalala
akawa ananimbembeleza. Ndio kwa mara ya kwanza tokea aondoke, usiku huo
nikalala.” “Si niliwaambia anapenda kubembelezwa? Basi hata umuudhi vipi Grace.
Wewe mbembeleze tu. Tena usichoke. Akikufukuza ukaondoka, ndio umeharibu kabisa.
Wewe hata akikufukuza, wewe endelea kubaki hapo mbembeleze kama Danny
anavyomfanyiaga. Ndio anajua unamjali.” Wote
wakacheka.
“Na Danny anajua kubembeleza. Anaweza kukuudhi mpaka ukasema
leo ndio mwisho wetu. Lakini akianza kukubembeleza, mwenyewe unasamehe.”
“Mmmh!” Mama yake akaguna. “Sasa nini
mama?” “Wewe endelea na stori, Nanaa asijekuniona mimi ndio mbaya. Maana
usipomaliza, mimi leo sitalala. Atanifuata mimi mpaka kitandani kwangu
nimalizie hiyo stori.” Wakacheka.
Grace akaendelea. “Basi, asubuhi nikaamka nikamuona
mwenyewe alishaamka kama kawaida yake, ameenda kuniombea maji ya moto ya kuoga.
Ananisubiria niamke nikaoge. Akanipeleka bafuni, nikaoga. Tukarudi chumbani.
Ndio nikamwambia nimemfuata. Nikamwambia sirudi Dar bila yeye. Kwa hiyo kama
hataki kurudi nyumbani, basi atafute sehemu yakuishi na mimi pale pale Tabora.
Danny hakuamini.”
“Basi tulikaa pale kama siku nne, akikusanya pesa yake na
kuanza kumfahamu sasa. Kujua yeye ni nani. Kwao ni wapi, kabila gani na mambo
yote, ndio tukarudi Dar. Hatukukaa sana, tukaamua kufunga ndoa kabla hata
hajarudi tena chuoni. Basi, tukafunga ndoa. Harusi ilikuwa ndogo tu, ya pilau
na soda, tena pale pale kanisani. Tukarudi zetu nyumbani. Ndio tupo mpaka leo
na Danny wangu tunazungushana.” “Daah! Hongereni sana. Kumbe mmetoka mbali!?
Basi mtu akiwaona, ni kama mmeoana jana. Pale kazini hawaishi kusimulia habari
zenu.” Wote wakacheka.
“Tena pale ndio wametuchoka. Akiamua Danny kuja
kuwasha moto hapo, utafikiri nini sijui! Wateja wote mbona wanatufahamu! Fujo
za Danny kila kukicha. Anaweza kuja pale kazini muda anaotaka yeye, hakwambii,
utasikia mlango umefunguliwa. Sasa akukute unaongea na mteja mwanaume, umekaa
naye peke yenu pale ofisini, mlango umefungwa. Weeee!” Wote walianza kucheka.
“Ataanza kufanya fujo hapo, utafikiri amekufumania. Na heri
mteja awe mstaarabu. Akifanya fujo, anaanza kurusha ngumi. Akiwa mstaarabu sio
kwamba atamuacha, simu inapigwa kwa Geb, anamuuliza kama anamfahamu huyo
mteja.” “Haiwezekani!” Nanaa
akazidi kushangaa. “Wewe muone Danny katulia hapo hivyo hivyo. Yaani
ukimuona Danny katulia kama hivyo, ujue macho yake yanamuona mkewe alipo.
Akinyanyuka tu pale alipokaa, na yeye akili imeshavurugika. Iwe anaenda chooni
au jikoni, anamuhesabia sekunde. Zikizidi tu sekunde alizomuwekea, na yeye
anasimama, anamfuata mkewe popote alipo.” Mama G, akaongeza.
“Tena anione nimekaa kweli. Sio nimekaa na simu mkononi,
hapana. Anataka nikae kabisa nitulie tukae tunaangaliana hapa. Ndio anaweza
hata kuangalia taarifa ya habari akaelewa au ukamuuliza swali akakujibu vizuri.
La sivyo hii nyumba inakuaga ndogo. Anamtaka mkewe. Na hana yale majina ya
sijui honey, sweet, sijui mpenzi, hana huo muda. Anachojua mkewe tu, tena tokea
zamani hata hatujaoana.” Grace
akaongeza.
“Na ikifika swala la mkewe, huyo Grace anakuwa hana
mama wala kaka. Anambadilikia kila mtu. Na anakuwa mkali kweli kweli. Basi
nikiona tu simu yake, hata kama nipo kwenye kikao nilazima niipokee lasivyo
utasikia nina mgeni. Na simu zake hazianzi na salamu, ni swali moja kwa
moja. Utasikia, ‘Unamfahamu mteja fulani?’ hapo najua yupo ofisini kwa
Grace, na mafaili yote ya huyo mteja yameshaagizwa aletewe. Kuanzia oda
alizowahi kuzitoa, ulipaji wake, yaani kila kitu anataka kiletwe.” “Sasa
aletewe wapi?” Nanaa akamuuliza Geb. “Hapo hapo ofisini kwa Grace, tena
mbele ya huyo mteja. Ili kuthibitisha kama kweli yeye ni mteja, na kweli
anashida na mzigo sio kwamba anamtaka mkewe.” “Sasa mteja anasemaje?” “Huna
utakachosema kwa Danny linapofika swala la mkewe. Hapo anawaka kama moto.
Kazi zote zinasimama hapo ofisini mpaka mafaili yote yaletwe, yeye mwenyewe
ajiridhishe na huyo mteja.” Mama G akajibu yeye.
“Na usifikiri akijiridhisha ndio inaisha. Anapiga tena simu
kwangu. Hapo ananibadilikia, utafikiri hatufahamiani, au hatuishi nyumba moja
au huyo mkewe sio pacha wangu. Anaanza sasa, ‘Nisikilize vizuri Geb. Kama
biashara imekushinda, acha. Tulia kazini. Acha kutumia uzuri wa mke wangu
kukuingizia pesa. Utaniona mbaya kabisa.’ Hapo ataniwakia kwenye simu, anakutukana, anakutisha, mpaka ajiridhishe ndio anakata
simu.” Nanaa alizidi kucheka wakati Geb anasimulia.
“Sasa Grace anasemaje?”
Nanaa akauliza. “Inategemea na mimi siku hiyo amenikutaje. Nikiwa vibaya,
nakusanya vitu vyangu pale ofisini wakati anafanya fujo zake, naenda kwa mama.
Kama yupo nyumbani narudi nyumbani. Kama yupo kazini kwake, nitaenda. Popote
alipo mama ndipo nitakapokwenda. Basi nitalia weee. Utafikiri ndio mwisho wetu.
Basi muda haupiti na yeye ananifuata. Hapo anakuwa ameniletea zawadi ya kitu
chochote kunituliza.” “Na akiingia hapo Danny, utafikiri wanamsingizia. Anakuwa
mpole kweli kwa mkewe. Atamtuliza wee kwa maneno mengi utafikiri kakosewa na
mtu mwingine. Yale aliyoyafanya kule hatayasema kabisa. Anaweza kumchagua
Geb kuwa ndio mbaya wao, anataka kuwavunjia penzi lao au yeyote yule.
Atambembeleza mkewe hapo, huku anamsema Geb. Utasikia, ‘Geb anataka kutuchonganisha
mke wangu. Anataka kukuuza kwa wanaume wengine sababu ya kujipatia pesa. Geb
anaroho ya wivu, hafurahii kutuona tunavyopendana. Nyamaza mke wangu’ Yaani
Grace anaishia kucheka tu.” Mama G akaongezea nakufanya wote wacheke.
“Lazima ucheke. Eti anakubembeleza hasemi ugomvi
aliouanzisha yeye kule kazini, au aibu aliyokutia mbele za watu, eti lawama
zote anamtupia mtu. Tokea tupo chuo, kazi yake ni hiyo hiyo. Anakutoa hotelini
kwa kupigana kama amekufumania, basi aibu kweli, nalia, hana pesa ya taksii,
mnaishia kupanda daladala tunarudi chuo au kwa mama kusemeana. Umeenda hotelini na gari, umependeza, unatolewa kwa
aibu, kama umefumaniwa! Na hapo anatangaza mimi ni mkewe, sio hata mchumba,
mkewe. Halafu heri akukodishie taksii kukurudisha nyumbani, mnapanda naye
daladala. Kwenye daladala si ninaendelea kulia, yeye ananiambia, ‘pole
mke wangu. Mungu yupo, ipo siku na sisi tutakuwa na gari yetu. Nitakupeleka
kwenye mahoteli makubwa, tutakuwa tunakula na kulala huko huko.’ Basi
nazidi kulia. Aibu mara mbili. Watu wote kwenye daladala wanajua unalilia
kupanda gari, kumbe katoka kunifanyia fujo.” Nanaa alikuwa anacheka mpaka
machozi.
“Basi wakifika hapo nyumbani, Grace akiingia analia, na
Danny anafuata nyuma, najua tayari. Kashamtoa mkewe mahali.” “Sasa mama ulikuwa
unawaambiaje?” “Ndio unaanza kusikiliza tena kesi, lakini Danny hathubutu
kukupa nafasi yakuingilia ugomvi wake. Utafikiri anayesemwa hapo na Grace ni mtu mwingine sio yeye. Yeye ndio yupo mstari
wa mbele kumtuliza Grace, tena hapo anamwita mkewe. Wataongea wawili hapo Grace
analia huku anagomba, Danny kajishusha kweli kweli. Mpole kama yeye hamna. Kila
anachoongea Grace anaitikia, huku anambembeleza, mpaka Grace anaishia kucheka.
Asubuhi wanaondoka tena kurudi chuoni. Naweza kutulia siku mbili au tatu,
utawasikia tena hao wamerudi, au utasikia mtoto anakuja mlangoni kwako huku
anakimbia, utasikia, ‘Mama G! Mama G! Grace na Danny wanakuja.’ Basi
tena hapo natafuta mahali pazuri, nakaa. Najua kesi inaanza.” “Kwa hiyo mpaka watoto
walikuwa wanawajua!?” Nanaa akauliza.
“Mpaka vitoto vidogo vilikuwa vinatujua. Wakimuona Danny
anapita, wanamuuliza dada Grace yuko wapi, au mimi nikipita, watamuulizia kaka
Danny! Kila mtu alikuwa akitujua pale mtaani. Maji yangu ya kuoga anayafuata
Danny bombani. Na wakati mwingine anafika amechelewa anakuta watu wapo bombani.
Utasikia naombeni mniruhusu nichote ndoo moja tu. Basi watu wanamuuliza, ‘ya
Grace?’” Nanaa akacheka. “Yaani
walishatujua. Kila siku mimi na Danny ni vituko tu.” Waliendelea kucheka.
“Yaani hata hii kazi kama Geb angekuwa sio ndugu yangu,
mbona angeshanifukuza muda mrefu sana! Fujo zikianza pale, kuna wateja
wanafukuzwa, kuna wanaojibiwa vibaya, yaani ni fujo mpaka mama akanishauri
nisiwe nafunga mlango wa ofisi. Kwa hiyo siku hizi mlango wa ofisi yangu
haufungwi. Nikiingia tu naacha mlango wazi kabisa, ili akija awe anaona
ninayezungumza naye huko ndani.”
Grace akaendelea.
“Na akifika tu, hana salamu. Anaenda moja kwa moja kwa
mteja, anajitambulisha kuwa yeye ni mume wangu na tumeshazaa mtoto mmoja. Basi
wakati mwingine ni aibu. Unakuta upo na mteja wa maana, na heshima zake, Danny
naye anaingia. Unatamani kumficha huyo mteja. Mara Geb anapigiwa anaanza
kugombeshwa na kuulizwa majukumu yangu.” “Hilo swali nishalizoea. Kila siku
naulizwa kwani kazi za Grace pale ni zipi. Naelezea. Mama akaniambia
nimwandikie Danny nimpe ili ajue majukumu ya mkewe. Lakini akikasirika
hakumbuki. Na usithubutu kumwambia nilikuandikia. Hapo utajuta. Ni heri akikuuliza
wewe umtajie tu. Mkewe anaingia nakutoka kazini siku na muda anaotaka yeye
Danny, na usimuulize. Ukimuuliza mbona Grace hajafika kazini mpaka sasa hivi,
upo naye? Utasikia, ‘kwani wewe wakati unamwajiri, hukujua kama Grace
ameolewa? Grace anamajukumu ya muhimu sana kuliko hiyo kazi yako’.” Nanaa akazidi kucheka.
“Basi hapo inabidi kumpigia simu mama, utasikia Grace yupo
chumbani analia, mumewe kamkataza kwenda kazini. Labda utaambiwa siku hiyo
alitoka na nguo yakumbana. Kwa hiyo amehisi siku hiyo Grace atakuwa kuna
anapokwenda au kuna mtu atakwenda pale ofisini kwake, kwa hiyo Grace ameambiwa
asitoke humu ndani. Hapo ukute kuna kitu cha muhimu ulitaka Grace afanye siku
hiyo, ila mumewe kasema asiende kazini. Na ukizidi kumuuliza anakwambia ukizidi
kumkera, mkewe anaacha kazi. Basi inabidi siku hiyo ufanye kazi mara mbili.
Nitoke ofisini kwangu, niende tena ofisini kwa Grace kufanya kazi zake. Ukija
hapa nyumbani Grace naye analia amemnunia mumewe, mumewe anakulaumu wewe,
halafu umechoka! Utajuta kumuajiri Grace. Unatamani kumfukuza kazi, lakini
huwezi. Mama anakwambia wavumilie tu.”
Waliendelea kuongea hapo huku wakicheka.
**************************************************
Nanaa akarudi kwenye kidole cha Geb. “Kinauma?” Nanaa
akauliza kwa upendo. “Wala sisikii kitu.” Nanaa akacheka. “Utanifanya
nilale hapa hapa kama Fili.” “Mbona natumia nguvu nyingi!” “Ona mikono yako
inavyotetemeka. Inatoa jasho kwa woga.” “Naona kama nitakuumiza.” “Huniumizi
Nanaa. Acha woga.” “Haya. Lakini nikikuumiza, naomba uniambie.” Geb
akacheka. “Usicheke bwana.” “Kila sasa unarudia kusema hivyo hivyo, lakini
hunitoi huo mwiba!” “Sasa hivi nakutoa.” Nanaa akajifuta jasho la kwenye
viganja vyake, Geb akaanza kucheka.
“Nakwambia huyo nesi wa Geb anavyohangaika! Yeye ndio
anamaumivu kuliko mgonjwa.” Wote
wakacheka na kuwageukia. “Naogopa mama.” “Basi hutautoa huo mwiba. Mtakesha
hapo.” “Sasa hivi nautoa.” Akasogea karibu akaendelea kumtoa mwiba huku Geb
akimwangalia.
Liz ndani ya nyumba.
Sababu yakucheka na stori nyingi pale, hawakusikia hata geti
likifunguliwa. Wakashtukia Liz ameingia. Watu wote wakanyamaza. Nanaa akaachia
mkono wa Geb taratibu, akajisogeza pembeni kwa tahadhari.
**************************************************
Akiwa na
ahadi ya kulindwa asilie, na kama atalia basi atafutwa machozi. Hata siku
haijaisha, historia inataka kujirudia. Mwenye mali amerudi. Liz aliyeanza
kumtilia mashaka Nanaa, amemkuta amekaa karibu na mpenzi wake. Ilikuwa sweta la
Geb, leo ni mkono wake. Kipi chakujitetea tena juu ya mkono wake mikononi mwa
Nanaa?
Amani na
furaha iliyokuwepo pale, gafla imepotea baada ya mwenye mmpenzi kuingia. Ni
kweli wengine wamemzoea na kumfahamu tabia zake. Lakini anamnyima raha Nanaa
kitu kinachomfanya Nanaa kutaka kuhama pale. Na amekwisha kumwambia Geb jinsi
asivyopenda kumnyima raha mpenzi wake. Ni heri yeye aondoke. Na Geb ameshindwa
kuishi mle ndani bila Nanaa. Ni nini Geb atafanya usiku huo katikati ya
wanawake hao wawili?
Nani wa Nani?
Usikose Sehemu ya
23.
0 comments: