Story

is mine - ni Wangu! Part 1 {Sehemu ya 25}.

Friday, August 31, 2018 naomimwakanyamale 0 Comments


Usiku wa Kwanza wa Nanaa & Geb!

 Geb alimpeleka Sea Cliff hotel. Nanaa hakuwahi kufika huko hata mara moja. Alifurahia yale madhari. Alishapasikia. Lakini hakuna aliyewahi kumpeleka huko. “Unataka tukae nje?” “Na hii nguo! Nitasikia baridi.” “Kama utataka kukaa nje, nitakupa koti langu.” Nanaa akacheka. “Kama ni hivyo sawa.” Wakatafuta meza ambayo ipo mwisho kabisa inayoangalia baharini, akamvutia kiti, Nanaa akakaa. Na yeye akakaa.

Akamuona anacheka. “Nanaa kwa kupenda kucheka! Sasa unacheka nini?” “Mwenzio sijawahi kuishi haya maisha. Ila nimeona kwenye movie.” Geb alianza kucheka huku anatingisha kichwa. “Kweli tena. Sasa wewe unavyofikiria nani angenileta huku? Au nani aninunulie magauni ya bei hii. Hata mimi mwenyewe najua nimependeza.” Geb alizidi kucheka. “Kwa mara ya kwanza na mimi nimevaa vitu vya dukani.” “Acha bwana Nanaa.” “Kweli tena. Hata nilivyojaribu kulala, usingizi ulikuwa hauji.” “Sababu ya vitu vipya?” “Sasa je? Yaani mimi mwenyewe ndio nimekuwa wakwanza kutoa lebo zake! Tena vilebo vyenye bei! Acha utani Geb. Sijui kama usiku nitalala.” Geb alikuwa akicheka huku akimwangalia Nanaa, haamini.

Walipata wakati mzuri sana wa pamoja. Ilikuwa siku ya kufahamiana zaidi. Waliambiana siku za birthday zao. Wakaagiza vinywaji. Wakaanza kunywa huku wakicheka na kuongea mambo yao. Siku hiyo hata Geb aliagiza chakula. Akala. Nanaa alishaanza kuchoka. Wakaamua waondoke tu.

Yaliyojiri!
Kwa kuwa walikaa meza ya mwisho kabisa iliwalazimu kupita meza kadhaa ili kutoka hapo. Wakati wanatoka Geb akiwa ametangulia kidogo, Nanaa akasikia dada mmoja akiita jina la Geb kwa mshangao na furaha. Akasimama, akamkumbatia Geb na kumbusu mdomoni huku akionekana amejaa furaha zote. Alimtambulisha kwa marafiki zake wengine wawili waliokuwa wamekaa nao. Wote wakasimama. “We heard so much about you.” Mmoja alisema na kumpa mkono Geb. “Finally. Nice to meet you.” Mwingine akaongeza kwa lugha hiyo ya kingereza. Na yeye akampa mkono.

Japokuwa Nanaa hakuwa akijua kuongea kingereza, hakuwa na tatizo la kuelewa hata kidogo. Na aliliona lile busu la mdomoni na vile yule msichana alivyomkumbatia Geb kwa nguvu. Hakuwa rafiki wa kawaida kwa hakika, alikuwa mpenzi. Nanaa akabaki amesimama pale nyuma ya Geb akiangalia wale warembo waliokuwa wamesimama wakiongea na Geb.

“Umerudi lini?” Geb akauliza. “Sina muda mrefu hapa nchini. Nilikufuata kule mlikokuwa mkiishi zamani na mama. Nikaambiwa mlishahama muda mrefu. Sikujua nitakupata vipi!” Yule msichana aliyemkumbatia Geb akaongeza akionyesha bado yupo na shauku kubwa. “Naomba namba yako ili kesho nikutafute.” Geb akamtajia bila shida. “Basi nitakupigia kesho.” “Sawa. Usiku mwema.” “Na wewe pia Geb. Nimefurahi sana.” Akatoa busu jingine la mdomoni. Wakaagana tena. Wale wasichana wakarudi kukaa. “OMG! Nimemuona Geb! Yiiiiiii!” Walimsikia yule dada akishangilia wakati wanaondoka.

Kulikuwa na ukimya mkubwa sana kati yao. Nanaa alianza kusikia baridi mpaka ndani ya mifupa. Alijawa hofu, wala si wivu. Geb alimfungulia mlango, akaingia. Na yeye akaingia. Pakawa kimya kabisa ndani ya gari. Walitoka pale wakiitafuta Morogoro road. Hapakuwa na maongezi mpaka walipokuwa wakikaribia maeneo ya fire, simu ya Nanaa ikaanza kuita kutoka kwenye pochi. Ilikuwa inaelekea saa 4 usiku. Akatoa simu yake, jina lilionyesha ni Zena. Kwa hali aliyokuwa nayo, ikabidi apokee tu.

************************************************

 Haloo!” Sauti ya kiume. “Zena!?” “Hapana. Mimi Yasini. Zena mgonjwa.” “Nini tena?” Nanaa akauliza. “Ni habari ndefu. Lakini mpaka nakupigia wewe, ujue nimekwama.” “Yeye yuko wapi?” “Yupo hapa nyumbani. Ameniomba nikupigie. Ukiweza uje.” “Saa hizi!?” Nanaa akajikuta anashangaa kwa sauti huku akiangalia muda kwenye simu yake. “Ingekuwa si muhimu hivyo nisingekusumbua Nanaa. Nimekwama. Naomba msaada.” “Labda niulize, ni msaada wa namna gani?” “Zena ni mgonjwa Nanaa. Tupo peke yetu. Sina msaada. Nahisi kuchanganyikiwa.” “Kwa nini msiende hospitalini?” Akaendelea kuhoji.

“Labda ukija utaelewa zaidi.” “Sasa hivi ni saa 4, Yasini. Hata kama nataka kuja leo, nakujaje?” “Nitakufuata.” “Mmh! Mbona unaniogopesha?” “Naomba msaada wako.” “Lakini sasa hivi mimi naelekea Tabata Barakuda. Sipo kwa kaka. Jeff anapafahamu.” “Basi Jeff atakuja kukuchukua.” “Naomba mwambia basi aje kama baada ya dakika 45 kuanzia sasa.” “Sawa. Nakushukuru sana Nanaa.” Nanaa hakujua ajibu nini. Akakata simu.  

************************************************

 “Zena ni mgonjwa. Anahitaji msaada wangu. Inabidi niende.” Nanaa akavunja ukimywa. “Nimesikia mazungumzo yenu. Kwani wazazi wake wako wapi?” “Hapa hapa Dar. Lakini Zena huwa anawadanganya anasafiri kikazi, kisha anaishia nyumbani kwa Yasini. Nafikiri ndio huko alipoanza kuugua. Sijui.” “Kuwa mwangalifu. Chochote kisije kikatokea, ukaja kujulikana na wazazi wake kuwa na wewe unahusika.” Nanaa akanyamaza. 

“Ningeweza kukupeleka.” “Ni usiku sana sasa hivi. Acha tu waje wanichukue wao wenyewe. Nisikusumbue zaidi. Leo inatosha kwa ajili yangu. Kapumzike tu.” Wakanyamaza. Hapakuwa na mazungumzo mengine mpaka wanafika nyumbani.

************************************************

Hawakukuta mtu pale sebleni. Lakini wakasikia Danny na mkewe wakiongea na Fili chumbani kwao. Wakajua na wao ndio wamerudi nyumbani. Akawahi chumbani kwa mama G. “Mbona upo hivyo?” Mama G akamuuliza Nanaa. Nanaa akatabasamu kidogo. “We Nanaa? Mbona umenyongea hivyo?” “Unamfahamu yule rafiki yangu Zena?” “Zena wa Yasini, Yasini rafiki yake Jeff?” Mama G akajibu nakumfanya Nanaa acheke kidogo.



“Sasa Zena ni mgonjwa sana. Yasini kanipigia simu wakati tupo njiani.” Nanaa akamuelezea kwa kifupi. “Kwa hiyo wanakuja kukuchukua sasa hivi!?” “Yasini anaonekana amekwama.” “Lakini kuwa makini.” “Hata Geb ameniambia hivyo hivyo. Ngoja nifike huko ndio nitajua chakufanya. Nitakujulisha.” “Sasa utarudi lini?” “Nikifika huko ndipo nitajua mama. Nitakupigia kesho. Najua sasa hivi ni usiku. Mpaka nifike kwao, tuzungumze na kama ni wakumpeleka hospitalini tuende, sio leo. Mpaka kesho. Ngoja nikajiandae.” Nanaa akatoka.

Akarudi chumbani kwake. Akabadili nguo. Akavaa suruali yake ya jinsi na top ya kawaida tu. Akachukua vitu muhimu alivyojua angehitaji. Akatoka pale chumbani akaenda kumuaga mama G. “Nanaa! Kuna nini?” Mama G akauliza tena. “Sijui mama.” Nanaa akajibu kwa unyonge. Mama G akabaki akimwangalia. “Naomba niagie na wengine. Ngoja mimi nitoke ili asije fika, halafu mlinzi akaja kuanza kusumbua. Usiku mwema mama.” Nanaa akatoka bila kusubiri jibu.

****************************************************

Alipotoka tu, mama G akamwita Geb. Geb akaja, na yeye akiwa ametulia kabisa. “Kaa hapo.” Geb akakaa. “Kuna nini?” Mama yake akahoji. “Nimekutana na Rita, mama.” “Rita! Rita yule alikuwa mpenzi wako akaenda masomoni?” Mama G akashtuka sana. “Ndiyo. Amerudi. Anasema alikwenda kunitafuta mpaka pale tulipokuwa tukiishi mimi na wewe.” “Pale alipotuacha?” “Ndiyo. Anasema akaambiwa tulihama.” “Sasa?” “Sijui mama yangu. Nahisi akili ilisimama kwa muda. Unajua nilishindwa hata kumtambulisha Nanaa! Tumeachana pale na Rita, nimeshindwa hata kujua namwambia nini Nanaa.” Mama G akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha.

“Alikuwa wapi na yeye siku zote hizo!?” “Hata sijui, mama yangu. Amechukua namba yangu. Najua atanitafuta.” Wakatulia kidogo, wote wakiwa wamepigwa na butwaa. “Lakini uzuri hujafika mbali na Nanaa. Ni kumwambia ukweli tu, ataelewa.” Geb akabaki kimya. “Naomba nikapumzike mama yangu.” “Pole. Mimi naelewa kabisa. Lakini kuwa sana makini na maamuzi yako. Ujue wazi, utakachoamua sasa hivi, hakuna kurudi tena nyuma.” “Nanaa ameshaondoka?” Geb akauliza akionekana wazi ameishiwa nguvu. “Ndiyo. Amesema watakuja kumfuata. Hataki waje halafu mlinzi aje asumbue ndani. Pengine yupo hapo nje ya geti.” Geb alifikiria kwa muda akatoka.

Alisimama pale sebleni kwa muda akifikiria. Mwishowe akaamua kutoka kumfuata Nanaa, angalau ahakikishe yupo salama pale nje. Akamkuta amekaa nje kabisa, kwenye kipande cha tofali amejiinamia akichora chini. Geb akamuhurumia. Akamsogelea. Alipomuona akasimama kwa haraka. “Vipi?” “Bado hajafika. Nafikiri yupo karibu kufika.” Nanaa akajibu. Akabaki akimwangalia asijue aseme nini. “Utarudi leo?” “Sijui.” Nanaa akajibu. “Basi nitakaa na wewe hapa mpaka aje. Ili usiwe peke yako.” “Naona mlinzi anakuja kunichungulia kila wakati. Hamna neno. Nenda kapumzike tu.” Geb akajivuta mpaka ukutani, akaegemea. Nanaa akarudi kukaa. Kimya.

Baada ya muda Jeff akafika. “Uwe na usiku mwema.” Nanaa akamgeukia Geb. “Asante na wewe.” Hapakuwa na kupeana mkono wala busu. Nanaa akapanda ndani ya gari ya Jeff akaondoka. Geb akasimama pale kwa muda kama aliyepigwa na bumbuazi. Asijue chakufanya, mwishoe akaingia ndani.
************************************************

Nanaa alipelekwa mpaka Sinza anapoishi Yasini. Mbali na salamu, hawakuzungumza chochote na Jeff. Alimkuta Zena ni mgonjwa sana. Anatokwa damu nyingi, mpaka ameishiwa nguvu. “Kuna nini?” Akamuuliza Yasini mara alipoingia chumba alichoelekezwa na Jeff. “Zena alishika mimba. Imetoka.” “Mlienda hospitalini?” “Tulimpeleka hapo kwenye hicho kihospitali hapo kama zahanati. Tukamkuta daktari wa hapo, akampa dawa. Alimwambia kwa kuwa mimba ilikuwa ni changa, atapona tu. Jioni hii akazidiwa. Nimemrudisha hapo, kamchoma sindano akasema turudi nyumbani. Lakini analalamika sana tumbo.” Nanaa akavuta pumzi kama na yeye yupo kwenye mshtuko.

“Alimchoma sindano ya nini?” “Kupunguza maumivu, na kushusha homa.” “Kama ameanza kupatwa na homa ujue amepata infection. Lazima tumpeleke hospitali kubwa na ya maana. Sio hizi hospitali za mtaani.” “Zena hataki. Anasema anaweza kukutana na mtu anayewafahamu wazazi wake.” “Naomba utupishe Yasini.” Yasini akatoka, akamuacha Zena na Nanaa.

“Pole Zena.” “Nahisi nitakufa Nanaa.” Zena aliongea kwa sauti ndogo. “Kwa nini hutaki kwenda ukatibiwe? Nashauri ukatibiwe kwa garama yeyote ile ili uishi kuliko ufie hapa? Hata kama wazazi wakijua si basi!” “Watamchukia Yasini. Na kunitenga naye maisha.” “Sasa bora lipi. Ufe umtie Yasini matatizoni, afungwe kwa kukufungia wewe humu ndani mpaka kifo, au uende hospitalini ukatibiwe? Hata kama sasa hivi wazazi watakasirika, ukipona si utarudiana  na mpenzi wako?” Zena akafikiria, akaona Nanaa yupo sahihi.

Wakaamua kwenda hospitalini. Yasini akaendesha mpaka hospitali ya Agakhani. Zena akapokelewa, akaonana na daktari. Yasini alieleza kila kitu. Daktari akauliza kama Zena alisafishwa baada ya mimba kutoka. Ikawa hapana. Akasema ni infection na ni lazima asafishwe kwa kuwa mimba haikuwa ndogo kama walivyoambiwa. Zena akaingizwa chumba cha upasuaji kusafishwa kwa haraka. 

Alitolewa huko akiwa analia maumivu. Mpaka saa 8 usiku, ndipo Zena anatulia, akiwa ameshapewa kitanda chake. Hapakuwa na jinsi Nanaa angemuacha Zena akiwa kwenye hali hiyo. Akakubaliana na Yasini yeye abakie na Zena pale hospitalini amuuguze mpaka atakapo ruhusiwa. Yasini awe anakuja na kuondoka. Matibabu ya Zena yakaendelea, Nanaa akiwa muuguzaji.

Ilibidi kuanzishiwa antibaiotic kali sana ili kutoa ile infection. Zena alikuwa ameshapoteza damu nyingi sana. Yasini na Jeff ilibidi kutoa damu ili aongezewe. Nanaa alikuwa akihangaika na Zena, mchana na usiku. “Kwa nini nisimpigie hata mama simu?” “Ni afadhali uondoke uniache peke yangu kama umechoka, kuliko kuwaambia wazazi wangu. Wataniua nikiwa hapa hapa hospitalini.” Zena alikataa kabisa.


Geb na Rita.
Siku inayofuata, Geb aliamshwa na ujumbe mzuri sana kutoka kwa Rita. ‘I choose you. And I will choose you, over and over and OVER. Without pause, without a doubt, in a heartbeat. I will keep choosing you’. Geb alifikicha macho, akarudia ule ujumbe tena. Haukuwa na jina lakini alijua aliyetuma ni Rita. Msichana waliyekuwa kwenye mahusiano ya muda mfupi, lakini yalikuwa mapenzi ya moto kweli kweli.

************************************************

Geb alikutana na Rita wakati akitafuta kazi, mara aliporudi nchini Tanzania. Alielekezwa ofisini kwa baba yake Rita, akaangukia mikononi kwa Rita. Alipojitambulisha kwake kuwa anamtafuta Mzee Simba na anashida ya kazi, akidhani Rita ni secretary wake. Akamkarimu sana Geb. Alimpa kinywaji wakati akimsubiria baba yake. Alipofanikiwa kuonana na Mzee Simba, alimwambia ni kweli anatafuta mtu, lakini yeye Geb ame ‘over qualify’. Vyeti vyake vilikuwa vikubwa sana kwa kazi yake. Kwa kuwa Geb alikuwa na shida sana ya pesa, akamuomba ajishikize kwa siku chache, kwa mshahara huo huo mdogo mpaka atakapopata kazi yakueleweka.

Mzee Simba akamkubalia, akampa majukumu yanayofanana na yeye. Akawa kama msaidizi wake. Ni kweli ofisi ilikuwa ndogo. Wakawa wao watatu tu wakisaidiana pale ndani. Rita kama muhasimu, na Geb akifanya kazi zozote atakazopewa kwa siku hiyo. Muda mwingi wakajikuta peke yao pale ofisini. Geb na Rita.

Rita alikuwa amebakisha kama miezi mitatu tu arudi chuoni alipokuwa akisoma nchini Canada. Alirudi nchini kwa mapumziko baada ya chuo kufungwa. Na ndipo alipokuwa akisaidia kazi kwenye biashara za baba yake aliyekuwa aki supply vitu mashuleni. Mzee huyo alitafuta tender kwenye mashule mengi ya hapo jijini, akawa akipeleka vitu huko. Kuanzia vitu vya maofisini mpaka vyakula. Kwa shule za kutwa na bweni. Na Geb akawa ndio mnunuaji na msambazaji. Hakuwa akilipwa pesa nyingi sana. Lakini ilimtoshea nauli ya kumtoa na kumrudisha nyumbani. Ikampunguzia yale mawazo yakukaa tu nyumbani. Na angalau aliweza kuchangia chakula cha nyumbani kwa wakati ule kabla hajapata kazi BOT.

Mzee Simba alishajua Geb ni kijana mwenye ndoto kali. Kwa hiyo tangia mwanzoni alionyesha kumuheshimu sana Geb. Alijua siku Mungu atakapomfungulia milango, hatakuwa mtu wa kawaida. Akamfanya kuwa ni kijana wake wa karibu sana. Huku akimuuza kwa Rita. Asijue hata Rita alishaanza kumpigia mahesabu Geb. Mzee Simba akazungumza na mkewe kufanya juhudi za makusudi kumkaribisha Geb na familia yake nyumbani.

Mahusiano ya karibu yakaanza. Hata mama G akawafahamu wazazi wa Rita. Wakaheshimiana sana. Ndani ya muda mfupi, Rita na Geb wakaanza mahusiano. Mzee Simba alipokuwa akitoka na kuwaacha wao wawili, mapenzi yaliendelea pale ofisini. Penzi likakolea kati yao. Iwe asubuhi iwe jioni, walitaka kuwa pamoja. Tena si tu kuongea, Rita alitaka penzi la Geb.


Rita Simba

Rita akiwa ameshaishi nchini Canada kwa miaka takribani 2, akisomea shahada yake ya kwanza, na akiwa na malengo ya kusoma mpaka shahada ya 3, nchini humo humo. Aliona ni vyema kutafuta uraia nchini humo ili kwanza kupunguza ada. Asome kama raia wa hapo, na sio ‘International student’ ambapo ilimgarimu sana baba yake. Na yeye ilimbidi kufanya kazi nyingi ili kuweza kujikimu.

Njia moja wapo aliamua kutafuta raia wa nchini hapo ili amuoe. Alijua akiolewa na raia wa hapo nchini Canada, ataweza kubadili uraia kwa haraka. Atapata ‘permanent Resident’, itakayompunguzia garama kubwa sana. Kwa hiyo Rita alitafuta kijana wa hapo hapo nchini Canada. Japokuwa hakuwa akimpenda sana, lakini akaamua aolewe ili afanikishe mipango yake. Alifanya harusi ya kimya kimya hata wazazi hawakuhudhuria. Japo alishawashirikisha na kuwaeleza mipango yake. Kwa hiyo wazazi wake walijua anaolewa ndoa ya kupata uraia nchini Canada, lakini si huyo kijana aliyemuoa wala wazazi wake huyo kijana wa Canada waliojua ndoa hiyo ina hila.

Ili kuaminisha serikali hiyo ya Canada kuwa ndoa yao ni ya kweli na si yakutaka uraia tu, Ilimlazimu Rita kupiga picha kadhaa za harusi hiyo na mumewe huyo mzawa wa nchi hiyo. Wakatafuta sehemu ya kuishi pamoja. Maisha yakaanza wakiwa wote wanatumia anuani moja. Kama mke na mume. Akapata uthibitisho wakutosha kuwa anahaki ya kupata vibali vya kuishi nchini humo kwani ameolewa na raia wa nchini hapo. 

Mungu akawa upande wa Rita, vibali vya kusafiria na kufanya kazi kavikukawia. Ndio kwa mara ya kwanza tokea afike nchini humo kwa miaka miwili, akawa amerudi nyumbani. Na ndipo akaangukia mikononi mwa Geb. Akiwa na mume nchini Canada na amekolezwa kimapenzi na Geb ambaye ndio alikuwa hana kitu, anawafanyia kazi hapo ofisini kwao. Akaadhimia kuficha siri ya huko nchini Canada. Akajua kwa hakika, baada ya miaka mitatu ya kumiliki hiyo Permanent Resident Card, ataweza kuachana na mumewe huko nchini Canada, na kuja kuolewa na Geb.

Hakutaka kufanya kosa kote kote. Rita akahakikisha hashiki mimba ya Geb wala ya mumewe. Kwa hiyo alilala na Geb kwa kutumia kondom wakati wote. Mapenzi yakanoga kati yao. Wazazi wakafahamiana. Hata siku za sikukuu, walialikwa nyumbani kwa Mzee Simba. Kwa hiyo picha za kina Grace, Danny, Fili akiwa mdogo kabisa, mama G na Geb, zilijaa nyumbani kwa kina Rita. Kwani kwa muda mfupi sana, wakawa ni familia moja yenye umoja, wakijua vijana wao siku moja wataoana.

Ugumu ulianza pale Rita alipotakiwa kurudi chuoni au kwa mumewe. Akaihirisha muhula mmoja. Akaendeleza penzi jijini na Geb. Lakini siku hazigandi, lazima Rita arudi kwa mumewe. Ilikuwa ngumu sana. Geb alimuaga kama mchumba wake, kwa makubaliano ya kuwasiliana na Rita  na kurudi kumtembelea hapa nchini mara kwa mara. Kumbe Rita anarudi kwa mumewe asiyejua kuwa anatumiwa tu.

Hapakuwahi kutokea ugomvi wala tatizo kati ya Rita na mumewe. Japokuwa aliolewa kwa hila, lakini Rita hakuwa na mahusiano yeyote nchini Canada. Kwa hiyo alijituliza kwa mumewe. Na alikuwa mtiifu sana akihakikisha lolote halitokei kabla hajakamilisha mipango yake yakuwa raia. Alimpa mapenzi mumewe. Yule kaka alijisifia kuoa mwanamke wa kitanzania anayempenda. 

Rita alimpa yale yote aliyojua wanawake wa kizungu hawawezi kumpa mumewe. Si kitandani tu, hata kwenye mambo ya chakula. Ukweli ndoa ya Rita ilikuwa nzuri huko nchini Canada. Na uzuri yule mwanaume alikuwa mfanyakazi. Kwa hiyo kulikuwa na unafuu mkubwa sana kimaisha. Ada ilipungua. Tena mlipaji akawa mumewe. Rita aliacha kazi kabisa, akatulia na shule tu. Matatizo ya ndoa yake yalianza baada ya Rita kurudi kwa mumewe akiwa ameshachanganywa na penzi la Geb.

**********************************************

Wakati Geb anasoma ule ujumbe, Rita akampigia. “Nina hamu na wewe Geb. Mpaka nasikia kuchanganyikiwa.” Geb akacheka kidogo. “Tunaweza kuonana leo?” Rita akauliza. “Ndiyo. Naomba tukutane pale pale Sea Cliff.” Geb akakubali nakutoa wazo. “Saa ngapi?” “Wewe tu. Utakapokuwa tayari unijulishe nije.” Rita akafurahi sana. Basi tukutane kwa chakula cha mchana.” “Hamna shida.” Geb akakubali.

Geb alikwenda kumwambia mama yake kuwa hatakwenda kanisani siku hiyo, anakwenda kukutana na Rita. Mama yake kama kawaida hakuchangia neno. Akanyamaza. Grace alikuwa akisikiliza wakati anamalizia kifungua kinywa chake pale pale jikoni. Akasimama ili kuweka vyombo alivyokuwa akitumia kwenye sinki. 

“Naomba nikwambie kitu Geb.” Geb akamgeukia akitaka kumsikiliza dada yake kwani alikuwa amesimama na mama yao pale pale jikoni. “Mimi nakufahamu Geb. Naomba uwe makini.” Kama kawaida yake. Grace akawa amemaliza. Na wao wakajua amemaliza, akaondoka. Mama G akageuka pale alipokuwa jikoni, akendelea na shuguli zake bila hata kuongeza neno. Geb akatoka.


Rita na Geb wakutana tena Sea Cliff.

Alimkuta Rita akimsubiria sehemu ya kuegesha magari. Geb alijua wazi amechanganywa na gari yake. Alibaki amekodolea macho ile gari. “Unaonekana mambo yako safi Geb!” Geb akatabasamu. Rita akamsogelea na kumbusu tena. “Si tutachukua chumba, tukalie chakula chumbani?” Rita akauliza. “Naomba tukae kule nje kwanza, halafu baada ya hapo ndio tutajua.” Rita akashangaa kidogo. Geb alikuwa mtu wakuchangamkia penzi lake. Iweje leo asite? “Au kwa kuwa hatujaonana muda mrefu anataka kujua nilikuwa wapi, au ananikwepa kwa ajili ya yule msichana aliyekuwa naye jana usiku?” Rita akawaza.

Wakaongozana mpaka sehemu yakulia chakula. “Vipi mama, Grace, Danny na Fili? Wanaendeleaje?” Rita akauliza wakati tu wanakaa. “Hawajambo. Waliniacha tokea asubuhi wakati wao wanaenda kanisani.” “Nina hamu nao. Itabidi nije kuwaona.” Geb akatabasamu. Muhudumu akasogea. Rita akaagiza red wine, Geb akaomba aletewe chupa ya maji ya Kilimanjaro.

“Umerudi lini?” Geb akamuuliza. “Sio muda mrefu sana.” Akakwepesha lile swali, Geb akajua. “Shule imeisha?” “Bado. Nilipunguza madarasa. Nilikuwa na mambo mengi. Nikaona nipunguze mzigo wa shule. Si unakumbuka nilikwambia nilikuwa nachukua madarasa mengi?” “Nakumbuka uliniambia ilikuwa ni moja ya requirement kama international student.” “Husahau!” Rita ni kama alisifia. Geb akacheka.

“Sasa nilipobahatisha kupata ile permanent resident, nikaona nisijiue!” “Okay.” Geb akajibu huku akimwangalia. Rita akacheka. “Kwa hiyo unampango wa kurudi lini tena Canada?”Geb akarusha swali jingine. “Sasa hapo inategemeana na wewe Geb. Tukiamua nibaki, na kama utaweza kunipa support yako, naweza kubaki nikasomea hapa. Kwanza naona mambo yako safi. Hebu nipe siri ya mafanikio.” Muhudumu alileta vinywaji. Rita akaanza kunywa wine yake.

“Niambie Geb, unafanya nini?” “Nilipata kazi BOT.” “OMG!” Rita akashangaa sana. Akasimama na kwenda kumpa busu Geb. “Hongera sana. Nilikwambia utafanikiwa tu. Ndio maana umebadilika Geb! Unaonekana mambo sio mabaya. Nipe tano.” Wakagonga. Muhuhumu wa chakula akawasogelea na Menu.

“Yaani mimi leo nina hamu ya vyakula vya baharini tu. Sina haja hata yakusoma menu. Niletee chips, shirmps wa kukaanga na samaki wakuchoma.” Rita akamuwahi muhudumu. Akamgeukia na Geb. Geb kama kawaida yake akasema akiwa tayari ataagiza. Alishakunywa uji aliotengenezewa na mama yake, akawa yupo tu sawa. Muhudumu akaondoka.

“Kwa hiyo sasa hivi mnaishi wapi?” Rita akatupia swali mara baada ya muhudumu kuondoka huku akinywa wine yake. “Tunaishi Tabata.” “Usiniambie kama ulijenga!” Geb akatabasamu. “Hongera sana Geb. Am so happy for you! Sasa kina Grace bado wanaishi kule kule kwenye nyumba ya chumba kimoja na mumewe?” “Hapana. Tunaishi wote.” “Waw! Kumbe! Safi sana kama uliamua kuwasaidia. Kile chumba kilikuwa kidogo, na mtoto! Bado mumewe anasoma tu?” Rita akauliza tena. “Alimaliza shule yake.” Geb akajibu taratibu.

“Afadhali atafute na yeye kazi asaidie familia yake. Umeona sasa? Karibia unatua mzigo mmoja. Shemeji yako akipata kazi, anatafuta hata nyumba ya kupanga wakati anajenga kwake. Na mama naye?” Rita akaongeza swali jingine. “Mama yupo mzima kabisa.” “Jamani mama yangu! Nina hamu naye kweli. Mama ana roho nzuri yule! Ndio maana Mungu alimjalia hata umbile zuri. Tena akamrithisha na dada yako.” Rita akacheka. “Nimefurahi sana kukuona Geb. Jana nilimwambia mama. Akaomba kama leo tutawahi kutoka hapa, upitie kumsalimia. Maana nilimwambia sijui nitakuachia saa ngapi! Nina hamu na wewe kweli Geb. Kwa nini tusiende kula chakula chumbani tu. Najua hutashindwa kuchukua chumba hapa, wewe mfanyakazi wa BOT!” Rita akagonga.

Chakula nacho hakikukawia. Baada ya dakika 20 tu, kikaletwa. “Kinaonekana kizuri!” Rita akasifia. “Unauhakika wewe huna njaa Geb? Mwenzio hata chai sikunywa.” Rita akaanza kula. “Tena chamotoo. Onja hata kidogo.” Rita aliendelea wakati anasogelea glasi yake ya wine. “Onja.” Rita akamsogezea sahani. “Asante. Mimi naona nipo sawa tu.” “Waw! Yaani! Sikujua kama nitakuona tena Geb. Nimefurahi sana. Kwanza nimefurahi Mungu amekukumbuka na wewe jamani! Lakini baba alikuwa anakusifia sana. Alijua utatoka tu.” Rita aliendelea kula huku akiongea bila kujali kama anajibiwa. Ni kweli alionekana anafurahia kile chakula.

Geb alitoa simu yake mfukoni akaangalia muda. “Unategemea simu?” Rita akauliza. “Kwanza kabla hatujaendelea. Yule msichana uliyekuwa naye jana ni nani? Maana hata hatukupata muda wa kutambulishana. Nilikuwa kama nimechanganyikiwa baada ya kukuona. Nilikuwa siamini! Hata wale rafiki zangu walijua kama nimefurahi. Nilikufuata mpaka kule ulipokuwa ukiishi na mama. Sijui nilikwmbia?” Geb akabaki hajui ajibu swali la kwanza au la pili. “Bwana chips zao tamuu. Halafu hawa shrimps wamewaweka kilimao kwa mbalii. Basi wee. Mpaka moyoni.” Rita alisharudisha macho yake kwenye sahani yake.

“Kwa hiyo yule msichana ndio nani?” “Anaitwa Nanaa!” Ile kutaja tu jina lake, Geb mwenyewe moyo ukampasuka. “Woowwww! Simu yako nzuri. Hebu tuione.” Rita alihamaki sana baada ya kuona simu ya Geb. Akiwa na mikono yenye mafuta ya samaki, akanyoosha ili aipokee ile simu. “Kweli Geb nimekukubali. Mambo yako sio mchezo. Kwani huko BOT wanawalipa mshahara kiasi gani? Hebu nipe niione kwa karibu.” Ilimbidi Geb ampe tu. Akaipokea na kuanza kuiangalia mbele na nyuma.
**********************************************

 “Nanaa!” Geb akakumbuka. Mpaka usoni akabadilika. Akakumbuka alichomfanyia Nanaa. Akakumbuka mabusu aliyokuwa akiyapata kutoka kwa Rita usiku ule. Tena ya mdomoni. Vile Rita alivyokuwa amemkumbatia mbele yake. Kutoka kwenye kumkumbatia na kumuahidi ahadi ya kumfuta machozi, Geb akajikuta anashindwa hata kumtambulisha mbele ya Rita. Ikawa kama ufahamu ndio unamrudia.

Akakumbuka vile Nanaa alivyomwambia anaogopa, lakini akamuahidi asiogope. Tena kwa mabusu mengi. Mazuri. Huku amemkumbatia. Akakumbuka furaha aliyoiweka moyoni kwa Nanaa, mara baada ya kumbusu mbele ya walinzi wake. Na hayo wala hayakuwa ni ya muda mrefu. Aliyafanya siku iliyopita tu. Na aliyaanzisha yeye mwenyewe siku ya ijumaa. Tena kwa Nanaa aliyekuwa muwazi sana kwake. Akimsimulia vile wanaume walivyomtenda. Na yeye akarudia yale yale muda mfupi tu wa kuanza naye.

 “Lakini sikujua kama Rita huyu ndiye yule wa wakati ule! Rita amebadilika. Hakuwa hivi. Halafu na mimi nilikuwa kwenye mshtuko. Sikujua niseme nini kwa Nanaa. Wakati mwingine ni heri kunyamaza.” Geb akajitetea nafsini kwake. “Lakini hata kutoa maelezo baada ya pale!?” Sauti nyingine ikamsuta. Akakumbushwa jinsi alivyomuona Nanaa amekaa pale nje kwenye tofali. Tena peke yake. Halafu usiku. Nanaa alipanda kwenye gari akionekana ana huzuni. Alishindwa hata kumpa mkono wa kwa heri.

 **********************************************

Ni kama kitu kilimtoa kwenye mawazo, akamuona Rita anasoma kitu kwenye simu yake. Akashtuka alipomuona Geb anamwangalia. “Huna hata game!? Wenzio kwenye simu kama hizi, hazikosagi game.” Akamrudishia simu yake. Na yeye akatoa simu yake. Akaanza kuandika kitu, Geb asijue anaandika nini. “Sio mchezo Geb. Nimekukubali. Iphone 9!? Wewe wa ukweli. Natamani simu kama hiyo yako.” Akaita muhudumu amuongezee wine nyingine. “Utakunywa hayo maji? Nahisi mwiba wa samaki umenikwama.” Geb akamsogezea ile chupa. Hakuwa hata ameifungua. Akamfungulia, akamkabidhi. Rita akayanywa kama nusu ya chupa. Akabeuka kwa nguvu. “Excuse me!” Kaongea huku akijipiga piga kifuani.

“Oooh! Afadhali.” Akaonekana amepata nafuu. “Sasa Geb?” Rita akauliza huku akipokea glasi nyingine ya wine. “Kuna mahali nataka kwenda.” “Haiwezekani Geb! Leo ni siku yetu.” “Tunaweza kupanga kukutana wakati mwingine?” “Kabisa. Leo hauwezi ukawa mwisho wetu wa kukutana. Kwanza namalizia hapa, halafu twende chumbani tukakate kiu. Huwezi kuniacha hivi nilivyo Geb. Kumbuka mapenzi yetu. Mpaka juu ya meza tulikuwa tukiridhishana. Sasa Mungu amekujalia pesa. Lazima tukafaidi kitandani.” Rita akamaliza ile wine ya pili kwa haraka sana, kisha akamwita muhudumu alete nyingine. Akarudi kwenye sahani yake kuendelea kula.

 Bila kuchelewa, muhudumu akaleta wine nyingine. Akainywa nusu ya glasi. Akamwangalia Geb. “Geb!” Akamwita. “Unakumbuka penzi letu lakini?” Rita akamuuliza kwa upendo. “Nini kimetokea au ni huyo Nanaa? Maana sikuelewi mpenzi. Nakuomba penzi, unanikatalia! Nakuomba simu, pia unanikatalia. Unakumbuka enzi tuko wote? Pesa ndogo niliyokuwa nayo tulikuwa tukigawana mpenzi. Nilijinyima kwa ajili yako. Nilikukaribisha penzi wakati nikijua wewe si kitu. Au leo unanionea kinyaa kwa kuwa nimeishiwa?” Rita akaanza kulia. Geb asijue amelewa au ni janja yake. Aliendelea kulia kwa kulalamika, huku watu wa meza za pembeni yao wakiwaangalia kujua kinachomliza mrembo huyo ni nini.

***********************************************

Rita alikuwa amependeza kweli kweli. Alivaa wig ya lace front, yenye mawimbi. Aliachia ikawa imeanguka kila mahali. Ilifunika mabega yake yaliyokuwa yameachwa wazi. Alivaa kigauni kifupi mpaka kati kati ya mapaja. Kilimbana vizuri. Kilikuwa cheusi. Akavaa na kiatu chekundu kirefu. Mapaja yake ya rangi ya maji ya kunde na miguu mizuri vilikuwa wazi na kung’arishwa na ule weusi wa gauni. Aliweka kucha nzuri za bandia za rangi nyekundu. Geb aliweza kuona kwani mara kadhaa alijaribu kurudisha nywele zake kwa ustadi ili zisiingie machoni au kwenye chakula. Akapaka na lipstiki nyekundu kabisa, kama rangi ya viatu. Alijaliwa macho mazuri na midomo iliyoweza kuwakilisha hiyo lipstic ipasavyo. Hakika alikuwa amependeza. Kama mwanamitindo mashuhuri wakutokea Hollywood.

**********************************************

 “Naomba niambie ukweli Geb!” Rita akaendelea kulia. Wakati Geb akijaribu kumtuliza, mmoja wa wafanyakazi mwenzake akiwa amekuja na familia yake eneo hilo akawasogelea. Alikuwa mkubwa kidogo kwa Geb. Na waliheshimiana kazini japo walikuwa vitengo tofauti. “Vipi kaka?” Geb akasimama. “Kwema tu. Nipo na familia.” “Safi sana.” Geb alijibu akionyesha kutotulia kwani bado Rita alikuwa akilia. “Nakupenda Geb. Na sitabadilika mpenzi. Nimekuchagua wewe. Kwamwe sibadiliki hata iweje. Nanaa ametukuta na atatuacha.” Yule mfanyakazi mwenzake aliposikia hivyo, akaamua kuaga kwa haraka sana.

 “Naomba utulie Rita.” “Hapana Geb. Wewe sio wakunitolea nje.” “Lakini mbona sijakataa kitu hata kimoja hapa? Umezungumzia swala la simu, kabla sijajib...” “Unafikiri nimelewa? Nakumbuka kila kitu.” “Naomba punguza sauti Rita.” “Unanionea kinyaa kwa kuwa wewe unapesa sasa hivi. Unashindwa kunisaidia wakati mimi nilikuwa nawewe wakati unashida! Huna kitu.” “Rita! Sijakukatalia kukununulia simu.” “Kwa hiyo unanipa pesa?” “Hapa nilipo sina pesa. Mpaka labda kesho.” “Nashukuru Geb. Basi ngoja nikachukue chumba.” Rita akasimama akiwa halii tena.

“Rita! Rita!” Geb akamkimbilia. Rita akasimama. Muhudumu naye akamuwahi Geb na bili. Akatoa wallet yake ili amtolee pesa ya chakula na vinywaji. Rita akaondoka. Geb akaangalia tena ile bili yao. Akaanza kuhesabu pesa. Akalipia chakula, na kumpa tip yake. “Nashukuru sana.” yule muhudumu akashukuru. Geb akarudisha ile wallet kwa haraka, akamkimbilia Rita ambaye alishatokomea ndani upande wa vyumba. Nia ya Geb ilikuwa ni kumuwahi kabla hajachukua chumba.

Akakimbia mpaka ndani. Alimkuta mapokezi ndio anakabidhiwa kadi za chumba. “Rita, naomba tuzungumze kwanza.” Wakati anamvuta pembeni, muhudumu naye akamsogelea Rita na chupa nzima ya whisky. “Afadhali kama mna HIBIKI. Yaani hii nilikuwa naipenda sana wakati nipo Canada. Tena 17 years Old! Waw…” Rita akaipokea kwa furaha. “Ingiza kwenye bili ya chumba.” Akamwambia yule muhudumu. 

“Twende tukapumzike Geb. Nimefurahi sana. Hii whisky nilikuwa na hamu nayo, sema bei ndio ilikuwa inanishinda. Leo nataka nikate kiu zote. Mzinga mzima niumalize peke yangu wakati na wewe ukinifaidi utakavyo.” Rita akaanza kuondoka kuelekea  vyumbani huku amejawa furaha sana. Geb akabaki haelewi chakufanya. Rita aliondoka huku anacheka kwa sauti. Ilikuwa hata shida kuongozana naye. Kila mtu alikuwa akiwatizama wao.

Rita akafungua ile chupa ya whisky  na kuanza kuinywa huku akitafuta chumba chao. Alikunywa kama maji, wakati ni whisky. Ikabidi Geb amfuate. “Rita! Rita!” Geb akazidi kumwita huku akijaribu kumsimamisha. “Yaani hii whiskey, Canada huwezi pata kama huna dolla 270 na kuendelea. Inategemea unainywea wapi.” Rita aliendelea kuongea huku akiitwa. “Nimechukua Presidential suite. Najua hutashindwa kuilipia mpenzi. Nataka leo tuandike historia. Nakupa huu mwili, uchezee tani yako!” Rita aliongea huku akiendelea kutafuta chumba.

“Rita. Naomba tuzungumze kwanza.” “Mpaka tuingie ndani.” Akachomeka kadi kwenye chumba chao. Ile kuingia ndani tu, moyo ukampasuka. Kwa hakika chumba kilikuwa ni kizuri sana. Akakumbuka na bei aliyotajiwa  ya ile whiskey huko nchini Canada, Geb alijua lazima awe na si chini ya milioni moja ndipo ataweza kutoka pale. Kwa haraka sana Rita alivua nguo zote akabaki kama alivyozaliwa. Akamrukia Geb na kumvuta kwa nguvu mpaka akachana shati lake. 

“Acha kwanza Rita. Subiri.” “Nina uchu na wewe Geb. Siwezi kusubiri.” Akamvuta tena kwa nguvu. Akafanikiwa kulirarua kabisa lile shati likachanika kabisa. Geb alikuwa kwenye mshtuko asijue ni nini kinamtokea. Wakaanza kukimbizana humo chumbani. Rita anataka kumtoa suruali kwa nguvu, Geb hataki. Ilimbidi Geb kumkwepa pale pale chumbani huku akimtuliza, akijua hatakuwa na jinsi yakutoka pale. Kwanza alishamchania shati. Akajua akimkamata suruali, basi tena. Atatoka uchi na pesa hana. Geb akaruka kushoto na kulia huku akijaribu kumtuliza. Lakini Rita ni kama alikuwa amepagawa. Anamtaka Geb kwa hali na mali. Alikuwa akimlilia kwa sauti ya kujilalamisha akimtaka kimapenzi. 

Kila waliposimama, Rita alimpiga picha na kujipiga na yeye. Geb akahisi anatuma ujumbe mahali. Akaogopa isije kuwa anatuma na zile picha anazompiga yeye Geb na kujipiga yeye mwenyewe tena akiwa uchi. “Unafanya nini Rita? Nani unamtumia hizo picha?” Rita akawa anacheka sana. Zoezi la kumkimbiza Geb ili amkamate kwa nguvu afanye naye mapenzi akalisitisha, likawa zaoezi la picha. Geb akaamua kumpokonya ile simu ili kujua anachofanya. Rita akakimbia.

 Ikawa sasa Geb ndiye anamkimbiza Rita mle mle chumbani. Kutoka upande kilichopo kitanda mpaka sehemu ya makochi. Rita yupo uchi, Geb shati limeraruliwa. Kwa kuwa alikuwa amelewa sana, Geb akaamua amrukie ili amkamate kwa rahisi kuliko vile wanavyokimbizana. Kwanza Rita alikuwa akipiga kelele. “Niachie! Niache Geb!” Geb akajua kwa mtu yeyote atakayekuwa akisikiliza nje, ataelewa yeye ndio anataka kumbaka Rita. Akaona apunguze ule mchezo wa kukimbizana, amrukie na kumkamata ili ampokonye simu, ajue anachofanya.

********************************************

Geb ni kijana mdogo aliyekuwa amefanikiwa sana kimaisha. Alishawakuta wazee wa mjini wakihangaika kwenye ulimwengu wa biashara, akawapita. Hakika mkono wa Mungu ulikuwa juu ya Geb. Alitoka kwa namna yake na kushangaza watu wengi sana. Waliojaribu kuiga wakaiga lakini hapakuwa na mafanikio kama yake. Walimtafuta katika kila eneo ili kujua udhaifu wake, wautumie ili kumwangusha lakini wakakuta ni kijana wa kawaida tu. Maisha yake ni kazini, nyumbani. Tena mtoto wa mama. Ambaye anaweza kulala na mama yake. Kisha kanisani. Tena hata huko kanisani utamkuta pembeni ya mama yake. 

Huwezi kumkuta baa akinywa, wala kumbi za starehe akijichanganya na vijana wenzake au na matajiri wenzake kubadilishana mawazo. Akisafiri ni mashambani kutafuta mzigo. Ila alijulikana kwa aina ya magari mazuri aliyokuwa akiendesha. Akipita, watu walijua Geb Magesa amepita. Alijulikana kwa magari ya kifahari aliyokuwa akiendesha. Wengine walisema ndiko anakomalizia pesa zake. Wengine walisema ni utajiri wa kichawi, una masharti ndio maana anashindwa kutapanya pesa yake. Ilimradi walioweza kuongea waliongea.

 Ukimya wake ndio uliwanyima watu maneno. Hawakujua anawaza nini juu ya yeyote wala usingeweza kutoa siri kifuani mwake Geb. Labda kwa kupitia mama yake. Ambaye na yeye ajira yake ya kwanza na kubwa ni wanae kwanza. Aliyatoa maisha yake yote kwa ajili ya Grace na Geb. Aliwalinda hao watoto kama mboni ya jicho lake. Hata kuna kipindi wakati anahangaika na ada ya Geb, alipata mwanaume aliyechanganywa na umbile lake mama G, alitaka kumuoa, lakini alikataa. Alijua hataweza kuwafikiria wanae kama akiolewa na mtu mwingine. Ni heri abakie kuwa Magesa kama Geb na Grace.

********************************************

“Rita! Unafanya nini? Unataka nini wewe?” Geb akaamua asimame kwanza. “Nakutaka wewe Geb. Wewe ni wangu. Hilo halina ubishi. Huwezi kuninyima mapenzi sasa hivi kwa kuwa umefanikiwa, wakati ulikuwa ukitumia mwili wangu kipindi kile unatembea na jua kali. Ulikuwa ukiugusa mwili wangu bila shida tena popote na muda wowote, hatukujali. Nilikuruhusu uniguse hata ukiwa unanuka jasho, wakati umetoka Kariakoo kununua vitu. Sikujali jasho lako. Nikakuachia mwili wangu uufanye utakavyo. Leo tupo kwenye mazingira mazuri. Mungu ametukumbuka, unanikataa!”  Geb akataka kumrukia ili amkamate kirahisi kwa kuwa alikuwa amesimama, ametulia anazungumza naye, Rita naye akashtuka kuruka upande wa pili akajikwaa na kujigonga kwenye meza akachanika kwenye kipanda uso. Damu zikaanza kumwagika kama maji.

********************************************

Geb alishtuka sana. Akaogopa asije akamfia pale ikawa kesi kwake. Bila kufikiria, akapiga simu mapokezi kwa haraka kuomba huduma ya kwanza. Baada ya nusu saa, chumba kikawa kimejaa wahudumu na polisi. Alipoona hali mbaya anahojiwa na kuonekana alifanya makusudi, ilibidi kumpigia Danny simu. “Uko wapi wewe? Mbona nasikia mtu analia?” Danny akauliza. Rita alikuwa akilia sana kuwa Geb amemuumiza kikatili.Naomba msaada Danny. Nimejiingiza kwenye matatizo bila kujua ndugu yangu.” Geb alikuwa akitetemeka mpaka kwenye simu alikuwa akisikika. Geb! Ni nini?” “Nahisi ninapelekwa polisi Danny. Naomba uje unisaidie.” “Polisi!?” Danny alikuwa nyumbani, akashtua kila mtu.

Mama G akaruka akampokonya simu Danny. Kuna nini Geb?” Geb akaanza kulia. “Geb!” Mama yake aliita kwa sauti ya juu akionekana ameshapaniki. “Itabidi twende Osterbay polisi kuandikisha kesi.” Mama G alisikia mtu anazungumza na Geb upande wa pili wa simu. Akashtuka sana. “Geb! Geb!” “Napelekwa polisi mama.” “Wapi?” “Osterbay.” “Nisikilize Geb. Naomba utulie kabisa. Tulia. Mimi nitakukuta huko.” “Watanifunga mama! Maisha yangu ndio yameshaharibika.” Kimya. “Mama! Naogopa sana.” “Usiogope Geb. Nakuja.” Mama G akakata simu. Geb akatolewa pale akiwa na pingu mkononi. Akaingizwa kwenye gari la polisi, mpaka Osterbay polisi.

Mama G alitoka anakimbia. Grace akamkimbilia mpaka nje akamshika. “Nisikilize mama. Sasa hivi kuchanganyikiwa hakuta saidia kitu. Geb anakuhitaji sana sasa hivi. Tena ukiwa na akili iliyotulia sio hivyo ulivyo sasa hivi. Naomba utulie, Danny atatupeleka.” Danny akatoka akiwa amembeba mwanae na funguo za gari. Wakaingia kwenye gari, kuelekea Osterbay polisi.

********************************************

Njia nzima akiwa kwenye gari ya polisi kama mtuhumiwa akipelekwa polisi, Geb alikuwa akimuwaza Nanaa. Shutuma ambazo ataaminishwa na watu na vyombo vya habari. Akakumbuka jinsi anavyowindwa na matajiri wa mjini na hata rafiki zake. Akajua ni wengi watalipia habari zake zianikwe mitandaoni. Akajua wengi watamfuata Rita kumuhonga pesa nyingi ili tu aongee uongo wakumtoa yeye mtaani afungwe, ili awapishe kwenye ulimwengu wa biashara.

Lakini hilo halikumsumbua Geb kama vile Nanaa atakavyoweza kusadiki kirahisi kwani hata jana yake alishindwa kumtambulisha kwa Rita wakaagana bila maelezo yeyote. Na hapo ilikuwa jumapili jioni, hata hakuwa amemtafuta Nanaa kumjulia hali. Kujua kama alifika salama huko alikokwenda kumuona mgonjwa? Kwanza alikuja kuchukuliwa na Jeff, mwanaume aliyekuwa akimuonea wivu wakati wote. Lakini alikuja kumchukua Nanaa, Geb hakuonyesha hata kujali. Kama aliyeshukuru kuondoka kwake. Hakutaka hata kujua kama alimfikisha salama. Kama je, alimka salama na anaendeleaje. Yeye aliamshwa na jumbe za Rita, mpenzi wa ujanani. Waliyejuana kwenye shida. Wakapendana na kukubaliana kuja kuoana. Bila kufikiria wala kujipanga, akamkimbilia hotelini.

Yote hayo Geb aliyakumbuka akiwa na pingu zake mkononi, akipelekwa kituoni kama muhalifu. Alikumbuka mabusu aliyoyapokea kutoka kwa Rita, tena mbele ya Nanaa, bila hata kubisha au kuyatolea maelezo. “Nanaa wangu jamani!” Geb akawaza akiwa ndani ya hiyo gari ya polisi, machozi yakimtoka asiamini kuwa juhudi zake zote zinaishia jela. Mali, majumba na mapesa yake yote aliyoweka benki hatakaa afaidi tena kwa kusa la jinahi ambalo amebambikiziwa na Rita aliyekuwa akilia kuwa Geb alitaka kumuua. Rita alitolewa pale akapelekwa hospitalini.

********************************************

 “Kwani mama wewe amekwambia nini?” Grace akahoji wakiwa njiani. “Hajaniambia kitu chochote zaidi analia tu.” “Na wewe Danny?” “Mimi ameniambia anaomba msaada. Anahisi watampeleka polisi. Basi.” “Mmh! Sijui nini kimempata. Tutajua huko huko.” Grace ndiye aliyekuwa akiwahoji.

********************************************

Walipofika polisi, Geb alifunguliwa kesi ya ‘jaribio la kutaka kuua’. Kwani Rita alikuwa akilia na kuwaambia polisi kuwa Geb alimsukuma kwa makusudi wakati walipokuwa chumbani humo. Rita aliwaambia kulitokea kutoelewana kidogo, Geb akataka kumpiga. Akafanikiwa kukimbia mara ya kwanza, lakini mara ya pili akamkamata. Ndio purukushani hizo za kumchania mpaka shati wakati akijitetea. Rita aliendelea kuelezea polisi akiwa tayari amefunikwa shuka walilolitoa kitandani hapo, pale pale chumbani. Polisi aliyekuwa akimuhoji alijaribu kumtuliza ili kupata maelezo yakutosha kwani Rita alikuwa akilia kwa uchungu sana. “Geb alipoona namzidi nguvu, ndio akanirukia kwa nguvu na kunisukuma kikatili.” Rita alihitimisha maelezo yake kabla yakuwahishwa hospitalini kwani bado alikuwa akivuja damu.

Geb aliwekwa lupango, asiamini kama ndio maisha yake yanaishia jela. “Sijui nani atamuoa Nanaa wangu!” Geb aliwaza wakati amekaa chini kwenye chumba hicho kichafu kinachonuka. Asiamini ni masaa machache tu alikuwa akipuliziwa na Ac ya nyumbani kwake, kwenye gari na upepo mwanana wa Sea cliff.

****************************************************

Kufumba na kufumbua, Historia imembadilikia Geb. Kutoka kuwa kijana wakuheshimiwa na kutamaniwa mtaani, mambo yamembadilikia kabisa. Rita amembadili jina. Kutoka kuitwa milionea, gafla ni mfungwa. Tena kwa kosa la jaribio la kutaka kuuwa.

Kwa shutuma au kesi inayomkabili Geb, adhabu yake ni kifungo cha maisha tu. Hakuna mjadala. Rita yu hospitalini, akilia kutaka kuuawa. Hakuna shahidi, ila Mungu mwenyewe ndiye aliyekuwepo nao tokea mwanzo na Nanaa aliyewashuhudia wakikumbatiana na kupeana mabusu bila hofu mbele yake.

Hakuitwa na mtu, amejiingiza na kujipeleka yeye mwenyewe kwenye matatizo. Hana wakumlaumu. Hukumu ndio inamtesa kwa yale aliyomfanyia Nanaa.

Kipi kitaendelea kwa Geb?


USIKOSE SEHEMU YA PILI/ PART 2 YA HADITHI HII YA
* Is mine - ...ni Wangu!*

ITAKAYO KUWA IKIUZWA Tsh. 300, 6 kr, 6 $, 1 Euro

 

HAYO NDIO MAELEZO ZAIDI YA JINSI YA KUPATA HADITHI HII KWA BEI NAFUU MNO. USIKOSE KUJUA YATAKAYO ENDELEA KWA FAMILIA HIYO YA MAGESA NA NANAA....

0 comments: