SIMULIZI

Nilipotea! - PART 3 - Sehemu ya A

Wednesday, June 30, 2021 naomimwakanyamale 0 Comments

 

    Gabriel alimuona vile Net alivyobadilika. “What Net? Nini?” Gabriel aliuliza kwa kujihami baada ya kumuona jinsi Net anavyomuangalia. “No man! Hamna neno.” Net alijibu na uso ulionekana kusikitishwa sana na rafiki yake. “No. Say it. Just say it Net. Kumbuka mimi nakufahamu wewe vizuri sana Net. Wewe ongea tu kile kilichopo mooni mwako. Maana ni wewe mwenyewe ndiye uliyeniambia niachane na huyu msichana. Tena kwa mikwara mingi sana! Nilikwambia jinsi ninavyompenda Nancy.” “Hujawahi kumpenda. Ulikuwa ukitumia tu mwili wake, lakini si kumpenda.” Net akamkatalia Gabriel na kumshangaza.

    “Unajuaje!? Nilimpenda na….” “Please don’t. Just Don’t. Nyamaza  tu.” “What’s wrong with you Net? Unatatizo gani Net!? Mbona mimi sikuelewi?” Net aligeuka akataka kuondoka, kisha akamgeukia rafiki yake tena. “Na kwa taarifa yako tu Gabriel, jina lake ni Tunda, sio Nancy.” Gabriel alibaki ametoa macho asielewe, huku manyunyu ya mvua yakiongeza kasi kuashiria mvua kubwa inakaribia kumwagika. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

    Tunda alienda kuchukua mizigo yake aliyokuwa ameiacha pale mapokezi asijue anarudije Dar, na hata usiku huo anakwenda wapi. Alitoka pale hotelini taratibu huku akilia kwa uchungu sana. Mvua kubwa na radi iliyoanza gafla ilimfanya akimbilie kwenye moja ya jengo la hoteli hiyo. Alikimbia mwisho kabisa kwenye kona akajibanza huku akilia kwa hofu.

    Kwa asili Tunda alikuwa muoga sana wa radi. Alianza kutetemeka baridi, kwani pale alipojificha pia mvua ilikuwa ikimfikia na hali ya hewa jijini Arusha ilikuwa baridi haswa. Tunda hakuwa hata amevaa sweta. Baridi na hofu vilimjaa, na kila aliposikia ngurumo za radi alizidi kutetemeka na kuzidi kulia. Pesa ya kuchukua taksii hakuwa nayo. Halafu akajiuliza, hata akichukua taksii, inampeleka wapi usiku ule! Akaendelea kulia. Mambo yamembadilikia gafla.

    Aliona gari ikizunguka pale, ikienda na kurudi mara kadhaa. Tunda aliendelea kulia. Baada ya muda akamuona mtu akikimbia, kwenda na kurudi. Mvua kubwa bado ilikuwa ikinyesha. Kwa mbalii akasikia mtu akiita jina lake. “Tundaa! Tundaaaaaa!” Alihisi ni mawazo. Lakini kila alipojaribu kupuuzia ile sauti ndivyo alivyoisikia kwa karibu zaidi.

    Akasimama kutaka kuthibitisha kama ni mawazo yake au la. Akajitokeza pale alipokuwa amejificha na kuchungulia nje huku radi ikipiga sana. “Tundaaa!” Ana kwa ana na Net, aliyekuwa amelowa chapachapa. Net alikuwa akimwita kama mwehu. Alipomtambua kuwa ni Net, Tunda alifunika uso wake nakuzidi kulia kwa aibu na uchungu. 

    Net alimsogelea karibu kabisa, akasimama mbele yake asijue aseme nini tena. Alibaki akihema kama mbwa aliyekimbia mwendo mrefu sana. Akabaki akimtizama Tunda. Tunda akajua ni yeye ndiye aliyemuona akikimbia. Wakabaki wamesimama pale. Tunda akilia huku amejificha uso, akiwa amebeba mizigo yake, Net akihema.

    “Twende kwenye gari.” Net alimpokea mabegi yake, akayabeba kwa mkono mmoja, kisha akamshika mkono Tunda kwa mkono wake mwingine, akamuongoza lilipokuwepo gari yake. Wote wawili walikuwa wamelowa haswa. Akamfungulia mlango wa gari, kiti cha mbele, Tunda akapanda na kujikunja kwenye kile kiti huku akitetemeka baridi. Net aliwasha heater ili kuleta joto mle ndani ya gari. Tunda aliendelea kulia mpaka alipopitiwa na usingizi. Hakujali anapopelekwa na Net, akalala.

    Net aliendesha mpaka hoteli nyingine mbali kidogo na ile hoteli aliyokuwepo Gabriel na mkewe pamoja na mama yake Net, akaingia yeye mwenyewe kwanza akachukua chumba ndipo alipoenda kumuamsha Tunda. “Twende ukalale ndani.” Net alimbebea vitu vyake akaongoza mpaka chumbani. Kilikuwa ni chumba chenye kitanda kimoja tu, kochi na choo humo humo ndani.

    Akamuwekea mizigo yake mle ndani nayo ilikuwa inachuruzika maji. “Pumzika nitakuona kesho.” Tunda alishindwa hata kumtizama Net usoni. Alibaki akilia sana, huku amefunika uso wake. Net alibaki kimya huku bado amesimama pale asijue aseme nini.

    “Nenda kabadili nguo utaanza kukohoa. Nitawaambia hapo mapokezi wakuletee chakula. Utataka kula nini?” Tunda akatingisha kichwa kukataa bila hata kumtizama. “Basi nitakuoana kesho. Usiku mwema.” Net alisimama tena mlangoni kwa muda bila kusema kitu. Lakini ni kama maneno mengine yaligoma kutoka, gafla akajikuta hajui aseme nini tena. Akaona ni heri aondoke tu. Alipomuona Tunda anaelekea bafuni, akatoka na kufunga mlango.

    Kesho yake asubuhi aliletewa kifungua kinywa na muhudumu wa ile hoteli, bila hata yakupiga simu kuagiza. Mchana akaletewa tena chakula cha mchana. Lakini ilipofika jioni aliamua kupiga simu mapokezi kuwaomba wasilete tena chakula kingine usiku.

    Ilipofika saa mbili, akasikia mlango ukigongwa. Alisimama kwenda kufungua. Alikuwa Net. Mwili mzima wa Tunda ulikuwa ukitetemeka baada yakumuona Net. Alimpisha mlangoni, Net akaingia.

    “Mbona wameniambia umekataa chakula cha usiku?” “Bado nimebakiza kile cha mchana. Sikula, nilikuwa bado nimeshiba” “Sasa sikitakuwa kimeharibika?” “Hapana. Bado kizuri tu.” Net alikaa kwenye kochi nakujiegemeza. Tunda akabaki amesimama pale pale mlangoni, Net akamgeukia. “Vipi! Mbona hukai?” Tunda alikwenda kukaa pembeni ya kitanda akainama.

    “Tumefungua ofisi nyingine huku Arusha, nimekuwa huku kwa muda mrefu kidogo. Nipo kwenye kutafuta watu wakunisaidia kazi. Kama unataka kazi, unaweza kupata.” Tunda akatulia tu kama hakuwa akiongeleshwa yeye. Akabaki ameinama. “Tunda?” “Sijasoma Net. Sina kitu kichwani. Elimu niliyonayo ni kama ya darasa la pili tu.” Net alitulia akimwangalia mrembo mwenye elimu ya darasa la pili. Bado Tunda alikuwa ameinama nakushindwa kumwangalia kabisa Net.

    “Kila kitu ni kujifunza Tunda. Ukiwa na nia hakuna kinachoshindikana. Hata hivyo sio kazi zote zinahitaji elimu.” “Nitaishi wapi huku Arusha?” “Sio lazima ukaendelea kuishi huku. Nahitaji msaada kwa sasa mpaka nitakapopata watu wa kudumu. Ukipenda kubaki sawa, ukitaka kuondoka baadaye pia siyo mbaya.” “Asante.” “Huwa unafanya kazi siku za jumamosi?” “Sina kitu chakufanya kwa sasa, naweza kufanya tu kazi.” “Basi nitakuja kukuchukua kesho twende wote kazini.” “Asante Net. Asante sana.” “Karibu. Nitakuona kesho.” Net akaondoka.

                           ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

     Net alirudi pale hotelini asubuhi hiyo ya jumamosi akamkuta Tunda alishajiandaa. Alimtizama mara mbili mbili, Tunda alikuwa amependeza sana, lakini uso ulijaa majonzi. Net alimchukua mpaka ofisini. Ofisi ilikuwa nzuri na yenye vitu vya kisasa tupu, lakini havijapangiliwa. Tunda akaanza kubabaishwa na aina ile ya ofisi nakujiona hafai kuwepo kwenye meza nzuri za kiofisi, viti vyakuzunguka kama vile na makabati ya kioo! Ilikuwa rahisi kuigiza ni msomi na anakazi sehemu fulani. Lakini akakumbana na uhalisia, anatakiwa aishi kile alichokuwa akikiigiza kwa muda mrefu, hofu yakuishi vile ikamwingia.

    “Ninae dada mmoja tu anayenisaidia. Naona kama analemewa kuwa peke yake. Jumatatu utakutana naye, atakuelekeza baadhi ya mambo ya kufanya.” “Sidhani kama nitaweza. Naona kama…..” Tunda akasita. “Sijui Net! Sina uwezo huo.” Net alibaki akimwangalia anavyojitetea kwa kubabaika. “Siwezi kukaa kwenye ofisi kama hii! Nitakuwa nikifanya nini?” “Mbona unashindwa kitu ambacho hata hujajaribu Tunda? Umeshajua kazi yenyewe? Au hutaki kuwa hapa? Kama hutaki upo huru kuondoka Tunda. Sitaki niwe nakulazimisha.” Tunda alianza kulia.

    “Sina pakwenda Net. Ila nahofia kuharibu.” “Usigope. Utafundishwa taratibu mpaka utaweza. Kwani ulikuwa ukiishi wapi?” “Nilikodi nyumba. Lakini nimeshindwa kulipa kodi. Mwenye kampuni ya Ulinzi amenitumia ujumbe jana usiku kuwa, mlinzi aliyekuwepo pale nyumbani akinilindia vitu vyangu, amempigia simu usiku huo kumwambia mwenye nyumba ameenda pale na kuanza kunitolea vitu vyangu nje.” “Pole sana. Unataka kwenda kuvichukua?” “Nitaviweka wapi? Nipo kama nilivyo hivi.” “Hatuwezi kukosa pakuviweka. Tunaweza kuondoka kesho siku ya jumapili na ndege ya asubuhi nakurudi jioni.” Kwa kulia, Tunda hata hakusikia kauli sahihi ya ‘tuna’. Yaani Net akijiunganisha. Akaendelea kulia.

    “Sina hata nauli ya basi, nitaweza wapi ya ndege!?” “Kwanza umekubaliana na wazo langu?” “Wazo ni zuri, lakini utekelezaji wake ndio mgumu. Nikifikiria pakuweka hivyo vitu ndio nachanganyikiwa kabisa. Sina ndugu wala rafiki kwenye ule mji.” “Kwanza naomba unyamaze. Acha kulia. Halafu nashauri twende wote kwanza tukaviangalie ndio tutajua pakuviweka.” “Asante Net.” “Basi usilie. Tufanye kile kinachowezekana sasa hivi kwanza. Hatua moja hadi nyingine. Sawa?” Hapo Tunda akawa ameelewa kuwa na yeye atasaidia. “Sawa?” Tunda akatingisha kichwa kukubali. Net akaingia ofisini kwake, akamwambia Tunda akae pale kwenye meza ya mapokezi amsubirie kidogo.

    Walishinda siku nzima pale kazini. Net akionekana ana kazi nyingi zakufanya. Alibaki ofisini kwake bila kutoka. Tunda akahisi amemsahau. Akaangaza macho akijiuliza kitu chakufanya. Maana muda ulizidi kwenda, yeye amekaa tu. Mwishoe akaamua kusafisha na kupanga ile  ofisi iliyokuwa imejaa vitu vizuri, lakini hakuna mpangilio.

    Akazunguka hapo ndani akakuta jiko na choo. Akapata vifaa vya usafi. Akaanza kusafisha. Net bado alikuwa ofisini kwake. Tunda hakujua kinachoendelea huko ndani. Ofisi yake ilikuwa ndani na mlango umerudishiwa. Pako kimyaa. Tunda akaanza kusafisha na kupanga ofisi nzima bila kusababisha kelele. Aliendelea kusafisha kwa haraka huku akimsubiria bosi wake atoke ampe kazi.

    Baada ya muda ndipo Net akatoka nakubaki akishangaa. “Nimesafisha na kupanga. Sijui ni sawa?” Tunda alimuwahi huku akimalizia kuweka mafaili yaliyokuwa sakafuni, na kuyapanga kwenye kabati ambalo bado lilionekana jipya tu, zuri sana lenye milango ya kioo mbele, lakini lilikuwa tupu kabisa. “Ona kulivyopendeza! Angalau panaeleweka sasa hivi. Halafu unasema huwezi kufanya kitu chochote! Hapo si umefanya kitu kizuri kabisa? Pamependeza sana. Mama akija kurudi tena atashangaa sana.” Tunda alifurahi kuona amepongezwa.

    “Nimewasiliana na watu wa ndege, tumepata tiketi ya asubuhi sana. Utaweza kusafiri asubuhi hiyo?” “Nitaweza. Asante.” “Twende basi tukale, uwahi kulala. Kesho nitakuja kukuchukua mapema sana.” Net alimpeleka sehemu ambayo alidhani Tunda hapafahamu kumbe vilikuwa ndio viwanja vyao yeye na Gabriel. Net alimwambia waende wenyewe jikoni wakachague nyama.

     Wakaongozana mpaka kwenye dirisha la jikoni. Walikuta watu wengine wakisubiri. Na wao wakajiweka kwenye foleni yakusubiria. Mchoma nyama ndani alipomuona tu Tunda, akaanza kumchangamkia, kwani alimfahamu yeye na Gabriel jinsi walivyokuwa wakiwapa tip/pesa pale kila walipokuwa wakienda kula nyama choma.

    “Mzee yuko wapi?” Yule kijana alimuuliza akiwa ameonyesha kumchangamkia kweli Tunda huku akiendelea kuchoma nyama. Tunda akaanza kubabaika, Net alibaki kimya pembeni. “Au leo uko peke yako?” “Sikuja naye.” Tunda akajibu kwa shida kidogo huku akijikanyaga kanyaga.

    Walirudi mezani Tunda alishindwa kuongea kabisa. Wahudumu wote walimuulizia Gabriel, mwishowe Tunda akaamua kuondoka pale. “Naomba nikakusubirie kwenye gari, Net.” “Basi ngoja niwaambie watuletee chakula hukohuko kwenye gari, tutaenda kula hotelini.” Tunda alijisikia vibaya sana. Akatoka pale bila hata kusubiria zaidi.

     Baada ya muda akamuona Net anarudi garini na chakula. “Naona tumefanyiwa upendeleo. Nilienda kuaga, naona wamenikabidhi chakula.” Tunda akakumbuka walikuwa wakifanyiwa hivyo hivyo kila walipokuwa wakienda pale na Gabriel kwa kuwa Gabriel alikuwa akiwapa tip nzuri.

    Walirudi hotelini Tunda akiwa kimya kabisa na Net hakutaka kuuliza. Net aliwasha tv mara tu alipoingia chumbani kwa Tunda na kujitupa kwenye kochi. Alikula chakula chake huku akiangalia tv. Alibadilisha tv huku na kule ili kupata taarifa ya habari wakati akiendelea kula. Alipomaliza kula na kuangalia taarifa ya habari, akataka kuondoka. Tunda na yeye alikuwa ameshamaliza kula.

    “Nitarudi kesho asubuhi na mapema, Tunda. Usichelewe kulala.” “Lakini Net.” Tunda alimuwahi Net akiwa anataka kutoka, akiwa amesimama, na yeye akasimama huku akibabaika sana. Alimuogopa sana Net, hata hakuwa akiweza kumwangalia vizuri. Net alibaki akimwangalia vile anavyotetemeka mbele yake. “Kuna nini?” Net akamuuliza taratibu. “Au usiku mwema.” Tunda alishindwa kuongea kwa hofu, akaamua kumuaga tu.

    Net akarudi kukaa. Taratibu machozi yalianza kumtoka tena Tunda. “Vipi Tunda?” “Naona tuache tu.” “Nini?” Net akauliza. “Hiyo safari ya Dar. Nitakuja kwenda wakati mwingine.” “Kwa nini? Unajua nimeshakata tiketi?” “Samahani, lakini nadaiwa. Siwezi kurudi mikono mitupu, bila pesa za watu.” Net akatulia kidogo.

    “Nani anakudai?” Net akauliza. Tunda akajifuta machozi na kujaribu kutulia. “Kodi ya miezi 3, kampuni ya ulinzi na kijana niliyemwajiri wa kazi.” “Kwa hiyo unataka kukimbia deni?” Net akamuuliza taratibu tu. “Sijui chakufanya Net. Sielewi nitafanya nini. Kwa mfano yule kijana wa kazi alikuwa akinipigia simu siku nzima ya leo akitaka nimpe pesa yake. Ndio jioni hii nimemtumia ujumbe, wakumtaarifu kuwa bado sijapata pesa, ila anaweza kwenda kuchukua kitu chochote kwenye vitu vyangu kama kujilipa. Hajanijibu. Haya, yule mmiliki wa kampuni ya ulinzi alinipigia simu siku ya jana akinitishia kunipeleka polisi kama sitampa pesa yake. Ameniambia jumatatu ndio mwisho. Nataka na yeye nimuombe kama anaweza kuchukua baadhi ya vitu vyangu, akae navyo mpaka nitakapo mlipa. Ila kodi ndio inanichanganya zaidi, sijui nitafanyaje!”

    “Usiwe na wasiwasi, wewe twende tu. Watumie ujumbe sasa hivi, waambie ukutane nao wote hapo nyumbani kwako, siku ya kesho asubuhi ya saa nne. Na uwaambie wasichelewe, kwa kuwa tunarudi kesho hiyo hiyo huku Arusha. Hatutakuwa na muda wa kumsubiri mtu.” Tunda alifuta machozi kwa mikono yake, akafuata simu yake, akatuma ujumbe kwa wote kama alivyoambiwa na Net.

    “Nimeshawatumia.” “Naomba uniambie kila mmoja anakudai kiasi gani. Nitawalipa kwa hundi. Unafikiri ni sawa? Maana sina pesa hapa mfukoni.” “Hawatakuwa na shida. Wanachotaka ni kulipwa.” Tunda akajibu na kumtajia kwa woga sana kiwango anachodaiwa na kila mmoja wao. “Lakini Net, naweza kuwaomba niwalipe kidogo kidogo. Sio lazima kuwalipa zote kwa pamoja.” Net akasimama. “Usiwe na wasiwasi. Wewe lala. Nitakufuata kesho.” “Asante sana Net. Nakushukuru.” “Karibu. Usiku mwema.” “Na wewe.” Net akatoka.

    Alipofunga mlango tu, Tunda akaanza kulia kwa uchungu sana. Net alibaki nje ya mlango akimsikiliza jinsi anavyolia kwa kuugua. Alitamani arudi ndani, lakini aliona aache tu. Tunda aliendelea kulia kwa muda mrefu sana huku akigugumia kama mtu asimsikie. Alifika mwisho kabisa. Kama ni kuzama kisimani, basi alishazama na kunywa maji mengi sana, akabaki akielea kama mzoga.

    Aibu ilikuwa imemuandama, hofu ndiyo ilizidi kumtesa. Net ndiye mtu wa mwisho kabisa kwenye Maisha yake angetamani kuwa naye karibu, kwa vile anavyomfahamu kwa uchafu wake. Alijua Net anamjua jinsi alivyo mchafu, yeye mwenyewe alijionea kinyaa. Net je? Alijiuliza huku akitamani asiwe Net anayemsaidia. Lakini hakuwa na namna nyingine. Alibanwa vyakutosha. Net aliposikia kimya, akajua amepitiwa na usingizi, ndipo alipoondoka.  

 

Net arudi Dar akiwa na Tunda, Kumlipia madeni.


    Net alifika hotelini hapo asubuhi hiyo na mapema akamkuta Tunda alishajiandaa, anamsubiria akiwa mnyonge na macho mekundu. Alionekana aliamka na kuanza kulia tena. Net aliogopa kuuliza asije akaanzisha kilio kingine na kushindwa kuwahi ndege. Waliondoka mpaka uwanja wa ndege, akaacha gari lake uwanjani hapo, wakaenda kupanda ndege kuelekea Dar. Tunda alipofika tu kwenye ndege, alilala mpaka Net alipomuamsha kuwa wamefika. Alikuwa amechoka, zaidi akili.

    Ndege ilitua jijini Dar, Net akamkuta Wanja, mtu anayemtumia kwa maswala ya usafiri hapo Dar. Alikuwa akimiliki magari makubwa na madogo anayofanyia biashara. Ndiye aliyemuomba afike hapo awasaidie usafiri wa kuwapeleka kwa Tunda akijua hata huko atakuwa msaada wakupata usafiri mwingine. “Nakushukuru sana Mkuu, na samahani kwa kukusumbua najua leo jumapili ni siku ya familia.” “Hamna shida kabisa. Nilipomwambia tu wife kuwa ni wewe, akaniambia nikimbie haraka sana.”  Wote wakacheka. Tunda alikuwa ameingia chooni mara tu walipotoka kwenye ndege. Kwa hiyo Net alikuwa na mwenyeji wake tu wamesimama wakiongea wakati wakimsubiria Tunda.

    Alitoka chooni, na kuwasogelea pale walipokuwa wamesimama. Jicho kwa jicho na mteja wake huyo Wanja. “Judy!” Tunda aliinama. Net akabaki akiwatizama, kama aliyeshtuka. Hakutegemea hata Wanja! Alionekana mtu wa familia na mwadilifu. Wanja akajaribu kupotezea, lakini asijue Net anaelewa kila kitu. “Nafahamiana na huyu dada alinisaidia lifti kipindi gari langu lilipoharibika. Hata jina lake simfahamu vizuri.” Akajichanganya. Gafla akasahau kuwa alitoka kumwita Tunda, jina la Judy na wala Tunda hakuwahi kumiliki gari. Akajitetea kwa kubabaika sana huku akiongopa. “Ooh! Kumbe hamna haja ya utambulisho? Basi twendeni.” Net akajibu na kuwaacha wakitizamana nyuma yake. Kisha wakamfuata.

    Tunda alipanda garini akabaki ameinama bila hata kuongea. Tunakutegemea wewe Tunda ili utuambie ni wapi unaishi na utuongoze njia. Nataka tuone vitu vyenyewe kwanza ndipo nijue ni aina gani ya gari itahitajika kuvibeba.” Tunda akanyanyua uso. Hakuwahi kutaja jina la mtaa anaoishi hata mara moja. Ni kama alilifuta hilo jina kichwani mwake kwa makusudi ili asije wahi hata kuropoka kwa mtu. Akabakia kujua njia tu.

    “Nielekee wapi?” Wanja ambaye ni dereva akauliza wakati anatoa gari pale uwanja wa ndege. “La Dolce Vita.” Tunda akajibu taratibu. Mpaka Net akamgeukia. “Unamaanisha unaishi mitaa ya karibu ya ile hoteli ya La Dolce Vita ya Oyster bay!?” Net akauliza kwa mshangao. “Ndiyo. Twendeni mpaka kule baharini kabisa. Nyumba haipo mbali na ilipo hoteli.” Tunda alijibu kwa upole, Net akaelewa ni kwa nini anadaiwa kodi kubwa vile. Dereva akakanyaga mafuta, Tunda akarudisha uso wake kuangalia chini         .

Dereva alipofika mpaka baharini akataka kuelekea Coco Beach, Tunda akamwambia akate kona kulia. Akamuelekeza mpaka kwenye nyumba aliyokuwa akiishi. 

“Hapa ndio kwako Tunda!?” Net akauliza kwa mshangao. “Ndiyo.” Nyumba ndogo lakini nzuri sana. Ilikuwa ya kisasa. Kuanzia getini mpaka ndani, ungependa. AC ilikuwa nyumba nzima. Pasafi. Kuja kuona hivyo vitu vyenyewe vya Tunda, ambavyo baadhi vilishaanza kutolewa nje, Net akamwangalia Tunda.

Vilikuwa vitu vizuri, vilivyotangaza utajiri mtupu kwa kuviangalia tu kwa macho. Marembo ya dhahabu nzuri iliyokatwa kwa ustadi yalizungushiwa kwenye kila kifaa cha Tunda. Kitanda, meza zake, makabati, vioo vyakujiangalia, meza yakujitengenezea na viti vyake, kila kitu kilikuwa na marembo mazuri sana na manyoya mazito meupe.

    “Ulipata wapi haya makochi, meza…!? Kila kitu!” Wanja aliuliza kwa kushangaa sana. “Nilienda kununua Arabuni.” Tunda alijibu kiunyonge bila ujasiri.

    “Daah! Ni vizuri sana. Sijawahi on ahata kwenye picha! Na vinaonekana ni vya thamani sana. Kwa ile lori yangu, Mkuu, itabidi kubeba hata mara tatu. Hivi vyombo ni vingi sana na vyote vinaonekana ni vya thamani sana. Tukivibebanisha, tutaharibu.” Net alibaki kimya akiwaza huku akiangalia vile vitu vyote, akifikiria pakuviweka. “Unapakuviweka lakini?”  Wanja akamuuliza Net. “Maadamu tupo hapa, lazima tutatafutia ufumbuzi. Hatutashindwa. ” Net akajibu na kuendelea. “Ili kuokoa muda, naomba ukatutafutie usafiri unaweza kubeba hivi vitu.” Wanja akaondoka na kuwaacha Tunda na Net.

    Baada ya muda kidogo, akaingia mwenye nyumba na mwenye kampuni ya ulinzi. Ni kama waliongozana. Tunda akasalimia. “Ulituambia tuje leo.” Mwenye nyumba akavunja ukimya. Net akawasogelea. “Nashukuru kwa kuwa hapa. Niombe kama mtaridhia, mpokee hundi.” “Bila shida. Ilimradi tumalizane kwa amani.” Mwenye kampuni ya ulinzi akajibu.

    Net alikuwa ameshawaandikia hundi zao kutokea Arusha. Alichofanya ni kumkabidhi Tunda anayewafahamu, ili awakabidhi bila kuchanganya. Tunda akazipokea huku akitetemeka. Hata mikono yake ilikuwa ikionyesha jinsi anavyo tetemeka. Akasoma kiasi kwenye kila hundi, akawakabidhi kila mmoja wao.

    Net hakuwa ameandika majina yao, ila pembeni ya sahihi aliandika sababu. Ya kwanza, ‘Kodi ya Tunda.’ Hundi ya pili, ‘Ulinzi wa Tunda.’ Hundi ya tatu, ‘Mfanyakazi.’ Tunda mwenyewe akashangaa vile alivyoandika. Alimtajia tu walipokuwa hotelini, aliondoka pale Tunda akiwa hana uhakika kama atakumbuka. Lakini alikumbuka na akaandika kiasi kwa usahihi.

    Aliwakabidhi hao wawili. Wakashukuru.  Wakamsikia mwenye nyumba akimwambia mwenye kampuni ya ulinzi angependa waendelee kulinda hapo mpaka mpangaji mpya atakapohamia hapo week inayokuja. Wakakubaliana, wakaondoka. “Nashukuru Net.” Net akamgeukia Tunda, akamuona anafuta machozi. “Karibu.” Net akajibu.

    Baada ya muda wakati Tunda akikusanya vitu vyake vizuri, Net akifungua vitu kama kitanda, nakumsaidia Tunda kuweka vitu vyake pamoja na kirahisi ili viweze kuhamishika, kijana wake Tunda, wa usafi na yeye akafika hapo akiwa na usafiri wa baiskeli akiwa na maboksi mengii. Tunda akamtambulisha kwa Net. “Wewe naomba tumalizane ukishatusaidia kuhamisha hivi vitu hapa. Nitakulipa. Ni sawa, au kuna mahali unataka kuwahi?” Net akamuuliza. “Hamna shida Mkuu.” Akakubali kwa haraka bila shida.

     Wakaungana kufungasha pale pale nje. Ni kweli vitu vyake karibu vyote vilikuwa nje. Nguo na viatu bado vilikuwa ndani, na vyombo vya jikoni. Wakasaidia kwa juhudi zote ili gari litakapofika iwe ni kupandisha tu.

    Walifanya kazi kubwa. Mpaka lori linafika hapo, walikuwa wameshakusanya karibu kila kitu. Net alimwambia Tunda yeye asibebe vitu vizito. Wao watasaidiana kubeba. Kazi yakupandisha ikaanza, huku Tunda akipandisha nguo zake na viatu. Alikuwa ameweka kwenye masanduku na maboksi aliyoletewa na yule kijana wake wa usafi. Alimuagizia usiku uliopita. Alimwambia afike hapo kuchukua pesa zake, aje na maboksi makubwa na magumu. Na kweli yule kijana alifanya hivyo. Yakamsaidia sana Tunda.

    Net na yule rafiki yake, Wanja pamoja na kijana wa Tunda na dereva wa lile lori walisaidiana kupandisha vitu vyote kwa tahadhari. Net akihakikisha hakiharibiki kitu hata kimoja. Akasimamia upangwaji wake, vitu vingine vikawekwa kwenye hiyo gari kubwa iliyokuwa imekuja kuwapokea uwanja wa ndege. Hasa viatu na nguo za Tunda. Walipohakikisha kila kitu kipo ndani ya magari, ndipo Net akamwambia rafiki yake apande kwenye lori, yeye ataendesha gari lake na Tunda. Wawafuate nyuma. Tunda akamuona akizungumza nao yeye akiwa anasubiri ndani ya hiyo gari ya Wanja, akamuona Net anarudi. “Tuondoke sasa.” Akawasha gari na kuondoka, Tunda hata hakuwa akijua wanaelekea wapi. Akaamua kunyamaza tu.

    Akaona Net akiongoza njia mpaka Salasala. Tunda alikuwa ametulia kimya akimtizama na kumtafakari bila jibu. Kijana mtulivu. Alionekana kila kitu anakipigia mahesabu na kukifanya kwa makini sana kama asiyetaka kufanya kosa. Yupo makini, na kila walipopita na Tunda, alikuwa ameshaandaa mazingira. Kuanzia wanatoka Arusha, mpaka hapo walipo wanahamisha vitu vyake. Watu waliokutana nao pia aliwaandaa siku moja kabla. Anakwenda kwa muda na mpangilio. “Huyu kweli mzungu.” Alijisemea Tunda.

    Waliendesha kimya kimya. Hakuna aliyemuongelesha mwenzake. Kutoka hapo Oysterbay mpaka Salasala. Tunda alikuwa amejiegemeza kimya, haamini kama Net anamtua mzigo mkubwa vile! Akaona wamefika. Net alipiga honi mara moja tu, geti likafunguliwa. “Hapa ni wapi?” Ikabidi Tunda aulize sasa. “Ni kwangu, lakini siishi hapa kwa sasa. Naishi na mama na mdogo wangu akiwa likizo. Kwa hiyo vinaweza kukaa tu hapa.” Tunda akajiweka sawa pale kitini ili kuangalia.

    Na yenyewe ilikuwa nyumba nzuri sana. Ilijengwa peke yake ndani ndani kidogo kwenye huo mtaa wa Salasala. Juu ya mlima. Ukisimama kwa nyuma, unaona bahari kwa kwa mbali na nyumba nyingine. Madhari yake na ramani, Tunda akabaki akishangaa. Ni kama kulipitishwa gari kubwa la greda ili kuchonga sehemu fulani fulani za bustanini. Kulizungushwa rembo za namna yake. Mbele ya hiyo nyumba kulikuwa na sanamu ya kipekee, inayotoa maji mdomoni, yaliyotengeneza bwawa la rangi ya bluu, humzunguka huyo sanamu. Na lile bwawa lilijengewa kisanifu. Tunda akabaki anakodoa macho.

    Net akavuta gari mpaka pembeni ili kupisha lori iliyokuwa imebeba vitu vya Tunda. Akawaonyeshea ishara wapite kama wazunguke nyuma kidogo. “Twende tukawaelekeze, halafu ndipo tutakuja kuchukua vitu vya humu ndani ya hili gari.” Net akashuka, Tunda naye akafuata. Net akamuelekeza dereva wa lori mpaka kwenye kinyumba cha nyuma. Tunda na yeye anafuata nyuma. Kumbe ilikuwa stoo. Walipoingia, palikuwa pakubwa. Humo ndani ni pasafi na kumepangiliwa pia.

    Akaingia kijana aliyemsalimia kwa heshima sana Net. Tunda akajua ni mfanyakazi wake. “Vipi Max?” Akamsikia akimuulizia yule kijana. “Nimetoka kumuogesha sasa hivi na kumpulizia dawa. Yupo sawa.” “Chakula chake bado kipo?” Net aliendelea kuuliza. “Bado kipo kingi tu. Week hii ndio ya chanjo. Nakumbuka. Nitampeleka.” Akajibu yule kijana. “Sawa sawa.” Net akajibu na kumgeukia Tunda.

    “Huyu anaitwa Emma. Ndiye anayeishi hapa.” Akamtambulisha kwa Tunda. “Emma, huyu ni Tunda, ndiye mwenye hivi vitu vyote.” Wakasalimiana, Tunda akawa anajiuliza sasa Max ni nani!? Ila kama kawaida yake, akajua hayamuhusu. “Karibu dada.” Akampa mkono Tunda. “Asante.” Tunda akashukuru na kumgeukia Net. Macho yakagongana. “Asante Net.” “Karibu. Njaa inauma sana?” “Hapana. Sijisikii kula kabisa.” Tunda akaanza kutokwa na machozi. Dereva na rafiki wa Net wakaingia na wao.

    Net akamshika mkono Tunda na kumsogeza pembeni mpaka sehemu iliyokuwepo makochi. “Naomba utulie. Tumeshapata hii sehemu. Tunaweza kuhifadhi hivi vitu kwa muda wote mpaka utakapokuwa tayari kuvichukua. Kaa hapa kwenye makochi, ni pasafi tu. Nisubiri tusaidiane kushusha vitu, tuondoke. Unataka soda?” “Hapana.” Tunda akakataa. “Basi nitamtuma Emma akuletee maji ya kunywa.” “Asante.” Ndilo neno ambalo Tunda lilikuwa likimtoka kila mara. “Naomba utulie. Naamini kila kitu kitakuwa sawa. Sawa?” Tunda akajifuta machozi, na kuvuta pumzi. “Nakushukuru Net.” “Karibu. Basi ngoja tuanze kazi.” Akamuacha amekaa hapo, akawasogelea wengine.

    Akamuona anawaonyesha sehemu ya kuviweka vile vitu vya Tunda. Ukweli palikuwa pakubwa na pazuri. Ilikuwa ni bohari ndio, lakini sakafu yake ilionekana nzuri sana. Upande yaliopo hayo makochi, kulikuwa na kinanda cha kawaida tu. Tv kubwa imening’inizwa na meza yakuchezea tenesi. Kuliwekwa kapeti chini. Zuri sana.

    Upande kulikuwa na vifaa vilivyofunikwa na mashuka makubwa. Tunda hakujua ni nini kilichofunikwa humo ndani ya hayo mashuka. Ila nakwenyewe kulikuwa kusafi. Kona ingine kulikuwa na chumba alichohisi ni choo. Ndio upande mwingine ulikuwa wazi kabisa. Ndipo alipoona akielekeza watu waweke vitu vya vyake.

     Alimuona Net akivipangilia vizuri. Walisaidiana wote wanne. Net, Emma, rafiki wa Net, Wanja, ambaye alishakuwa mteja wa Tunda na dereva wa lile lori. Walifanya kwa haraka mpaka wakamaliza. Net akamlipa yule kijana wa lori, akatoa lori yake pale.

    Net alilisogeza ile gari ndogo karibu kabisa na mlango. Tunda alipomuona anashusha, akamsogelea. “Usibebe vitu vizito. Emma atatusaidia.” Net na Emma wakashusha mpaka wakamaliza. Vitu vyote vya Tunda viliweza kutoshea kwenye huo upande tena bila kubebanisha. Tunda alibaki na maswali lakini aliogopa kuuliza zaidi kwani alijua Net ndiye ana maswali mengi zaidi yake. “Asante sana Net. Nakushukuru.” “Karibu.” Akabaki amesimama kama anataka kuuliza swali, Net akaelewa. Akaomba Emma na rafiki yake wasubiri nje.

    Wakabaki wao wawili. Akamgeukia Tunda. “Sijui nibebe nini kwa kuwa sijui nitakuwa kule kwa muda gani!” Tunda akaonge kinyenyekevu. “Inategemea na wewe. Unataka kuwepo Arusha?” “Sina uchaguzi Net. Kama unafikiri naweza kufundishika, nikaelewa, nitashukuru.” “Naamini utaweza tu. Ondoa hofu.” Tunda akajifuta machozi tena. “Basi naomba muda mfupi wa kuchukua baadhi ya nguo na vitu nitakavyovihitaji.” “Sawa.” Net akatoka nje kama kumpa nafasi.

    Tunda alichukua begi kubwa. Akaanza kufungasha. Kila kitu alitamani kubeba. Kila kitu aliona kina umuhimu. Akaanza kulia kuacha vitu vyake. Alilia Tunda, asiamini kuwa ndio ni kama anaanza tena maisha. Alipenda kwake. Alifurahia kila kitu chake kwani alinunua si kwa bahati mbaya. Kila kitu alinunua kwa kusudi. Leo anaviacha stoo! Mpaka lini! Hilo ndilo lilimuogopesha Tunda.

    Net akarudi. “Nikusaidie nini?” Akasimama kwa haraka kama aliyefumaniwa tena. “Unaweza kuchukua mabegi hata mawili au matatu. Beba vile utakavyo. Tutalipia kwenye ndege.” Net akaongeza. “Asante.” Tunda akainama kuendelea kufungasha mpaka akamaliza na kujifuta machozi vizuri. “Naona hivi vitatosha. Asante.” “Basi acha nikusaidie kubeba. Wewe beba huo mkoba mdogo. Tuondoke sasa hivi, tuwahi.” Net akachukua yale mabegi wakaondoka.

 

Tunda Arudi Arusha Kuanza Maisha Mengine Akiwa na Net.


    Walirudishwa uwanja wa ndege, na Wanja tayari kwa safari ya kurudi jijini Arusha. Wakiwa kwenye ndege Tunda akiwa amekaa dirishani, Net alimuona akivuta pumzi mara kadhaa na kuzishusha huku akifuta machozi. Baadaye alimuona akijivuta karibu naye, akajiegemeza pembeni yake, akalala. Net alimuhurumia sana Tunda. Alionekana amechoka, zaidi mawazo. Akabaki akimtizama akiwa usingizini, akamfunika vizuri na mtandio wake, akabaki akimtizama huku akimtafakari. 

Walifika Arusha, Net akachukua gari yake sehemu alipokuwa ameegesha asubuhi, akamrudisha hotelini kwake. Wakaingia ndani, kama kawaida yake, alikaa kwenye kochi, kwa mara ya kwanza Tunda akakaa pembeni yake, kama anayetaka kuzungumza kitu lakini anasita. Net aliligundua hilo kwa hiyo hakutaka kuaga kwa haraka, akataka kumsikiliza. Akaamua kuagiza chakula kiwafuate palepale chumbani.

Baada ya muda kikaletwa. Net akiwa anaangalia luninga kama kawaida yake, huku amejiegemeza kwenye kochi, akimsubiri aongee. Kimya. Alimuona vile anavyotetemeka mpaka mikono iliyokuwa imeshikilia ile sahani ya chakula. Mwishoe akamuona amekiweka mapajani, napo sahani ikawa inacheza. Kwamba anatetemeka mpaka miguu. Net akaendelea kula na kubadili channels kama kumtoa kwenye mawazo.

Walimaliza kula bado Tunda alishindwa kuongea. Net naye akawa kama hana haraka. Akaendelea kuangalia tu luninga. Akibadili hiki na kile. “Huwa unapenda kuangalia nini kwenye tv?” Akamuuliza Tunda. Tunda akaanza kufikiria. Hakuwa hata akiangalia tv. Ilikuwepo kwake kama haipo. “Sio mpenzi sana wa tv.” Akajibu taratibu. Net akamwangalia. “Lakini huwa nawasha na kuangalia chochote kilichomo.” Akaendelea Tunda kama anayejitetea.

“Na movie?” Akamuuliza tena. “Napenda ila isiwe za vita au watu wasipigane.” Net akacheka. Nia yake ilikuwa kumtuliza tu ili aongee. Wakatulia kidogo. “Net!” “Vipi?” “Asante.” Net akatabasamu. Maana alishapokea hizo asante, kama nikuziweka kwenye gunia, zingekuwa zikifurika. “Asante kwa kila kitu. Namaanisha kila kitu. Angalau sasa hivi naweza kulala vizuri. Sidaiwi tena. Hiyo kodi ilikuwa inanifanya sipati usingizi. Nilijiingiza kwenye gharama ambazo sikuwa najua nitajitoaje.” “Pole.” Tunda akatulia kidogo.

Kisha akaendelea. “Sitaki kurudia yale maisha tena Net. Hapa hotelini ni gharama sana na kwa kuwa nitakuwa hapa Arusha kwa muda, labda nitafute chumba cha kupanga kwa muda.” “Wazo zuri. Lakini naomba tufikirie kazi kwanza. Tuna mambo mengi sana pale ofisini, hizi gharama za hapa hotelini unapoishi, ofisi italipa.” “Je nikishindwa hiyo kazi Net? Huoni mtakuwa mmepoteza pesa bure? Kwa nini usione kwanza utendaji kazi wangu, ukiridhika ndipo angalau utajua hata kama mnanilipa kiasi gani?” “Acha wasiwasi Tunda! Kila kitu kitakuwa sawa.” Akajibu hivyo tu, tena kirahisi tu. Akakaa tena kidogo, akamuaga kwa makubaliano yakumfuata hapo kesho yake kwenda kazini.

 

                                           Tunda aanza kazi jijini Arusha.

    Ilipofika saa mbili kamili, Net alikuwa akigonga mlangoni. Hakuingia hata ndani. “Kama upo tayari, twende.” Tunda akachukua pochi yake kwa haraka na kutoka. Walifika kazini siku hiyo ya jumatatu asubuhi, Net akapokea simu kutoka kwa dada aliyekuwa amemuajiri pale ofisini na kumwambia anauguliwa na mumewe hataweza kufika kazini mpaka atakapopona. Tunda aliingiwa na hofu sana. “Usiogope, nitakuelekeza utaelewa tu. Hata yeye mwenyewe mimi ndiye niliyemfundisha. Halafu mimi mwenyewe nitakuwepo, nitakusaidia.” Tunda akakubali lakini bado alikuwa na hofu sana.

Na hivi Net alionekana makini, hakurupuki! Ni kama hana mlango wa makosa kwenye maisha yake, wasiwasi ulizidi kumwingia Tunda. Hata wateja aliokuwa akiwahudumia kwa ngono, wote waliokuwa wakikutana na Net, au aliofumaniwa nao na Net, walianza kutoa sifa za Net hata kabla hawajakutana naye. Hata Tunda alipokuwa akiwaambia wamwambie Net wakutane club au baa, walikuwa wakisita na wengine kukataa kabisa. Kwamba yupo makini, anakwenda na muda, muadilifu, hataki hata kugusa pombe na kadhalika. Sasa leo umkutanishe na Tunda aliyekwisha kumfumania mara kadhaa, na kila wanayekutana naye, ameshamuhudumia!

Hofu iliyokuwa imemjaa Tunda, alitamani yeye ndio akakae na huyo mgonjwa, muhusika arudi pale kazini. Lakini akajikumbusha hayupo kwenye kuchagua. Amewekwa hotelini ili afanye kazi. Vitu vyake vipo kwenye stoo ya Net, juhudi zake ndio zitakazomfanya avirudishe chini ya himaya yake. Hana pakwenda, hapo alipo ndipo mwisho. Lazima atulize akili, aelewe.

Tunda akatulia kuelewa kwa makini. Na Net naye alimuelekeza taratibu bila haraka, kuhakikisha hapaniki na anaelewa ni nini wanafanya bila shida. Ilikuwa ni Kampuni mpya ya usafirishaji. Walihusika na watalii pamoja na kusafirisha bidhaa ndani na nje ya nchi. Net alimwambia ndio wanaanza tu. Kwa upande wawatalii wao walikuwa ni wakala tu. Wanafanya kazi na mahoteli mengi makubwa ya hapo nchini, walioingia nao ubia.

Wakipokea wao wateja, watatumia usafiri wao kina Net. Lakini watalala kwenye hoteli zao. Kisha hoteli kuwalipa wao asilimia fulani kwa kuwaletea watalii au wateja. Iwe mbugani au mijini na vijijini. Kina Net wao ndio walitumika kama wasafirishaji. Unahama kutoka sehemu moja kwenda nyingine, basi wanakuwa na malori makubwa na madogo, inategemea na ukubwa wa nyumba au ofisi unayotaka kuhamisha. Unayo bidhaa kubwa au ndogo, unataka usafirishe ndani ya nchi au nje, wao kina Net, watakusafirishia.

Kampuni yao ilikuwa ikiitwa African Cote transit. Jina la Net alikuja kugundua kuwa ni Nathaniel Cote. Kwa hiyo akahisi labda ile kampuni ni yake. Ila kama kawaida ya Tunda, haulizi kisichomuhusu, ila kufuata yake. Akaweka akili na kuendelea kumsikiliza Net. Kazi yake ikawa kupokea kazi zote kutoka kwa wateja. Kujua aina ya mzigo au watalii. Anaandika kwenye kompyuta kutokana na aina. Kwa urahisi tu, kompyuta yenyewe inamletea aina ya magari ambayo yapo.

Kama ni wateja wa kuzungushwa mjini, basi itampasa kumsomea mteja aina ya  magari ambayo yapo kwa wakati huo. Kama ni mbugani hivyohivyo. Kama mtu anayehama kutoka sehemu moja kwenda nyingine, Tunda alifundishwa aina ya maswali ya kuuliza. Ukumbwa wa vifaa vya hiyo nyumba anayohamisha. Umbali, na kadhalika.

Kama ni bidhaa, alimfundisha maswali yakuuliza pia. Ukubwa wa hiyo bidhaa, aina yake, umbali wakupelekwa na kadhalika. Kwa hiyo kazi kubwa ilikuwa ni kuelewa vizuri wateja, kuandika na kutoa lugha nzuri kwa kila mteja.

Hilo kwa Tunda likawa halina shida. Kwanza hana tatizo kubwa la lugha. Angalau lugha mbili muhimu alikuwa akizifahamu bila shida. Kingereza na Kiswahili. Pili, Tunda alijaliwa ulimi laini. Mtulivu na anayo lugha ya ushawishi. Akizungumza na wewe hata ukitaka kugairi, atakupanga mpaka ukubali.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kazi ikaanza. Tunda na Net wakisaidiana bega kwa bega. Kwa kuwa ilikuwa siku ya kwanza, Net alikuwepo kumsaidia. Walikuwa naye hapo mezani wakifanya pamoja. Alimsikia Net jinsi anavozungumza na wateja. Maswali gani anayajibu. Akawa anaandika yale maswali aliyoona wateja wengi wanauliza.

Tunda alijua ni kweli wanatengeneza pesa. Walikuwa busy kupita kiasi mpaka ile hali ya hofu kwa Net ikaanza kupungua kwa kuwa walikuwa wamekaa naye hapo mezani siku nzima. Wakizungumza wao wawili, wateja na Tunda ilimlazimu kuuliza maswali ili akija kuachiwa pale, asiharibu.

Hakuna aliyekumbuka kula. Mpaka inafika jioni ya saa kumi na mbili, ndio pakatulia. Simu zikaacha kupigwa. “Mambo yatabadilika Tunda. Utakuja kupata muda wakupumzika. Mwanzo mgumu.” “Hamna shida kabisa. Nimefurahi kuweza kuwa busy hivi. Imenisaidia sana.” Net akacheka kidogo.

“Hujuti kukubali?” “Hata kidogo. Angalau akili yangu imetulia kwa muda nakuacha kujifikiria. Lakini najua wewe njaa itakuwa ikikuuma.” “Na wewe?” “Mimi sio mlaji sana. Umeona kile kichupa nilichokunywa mchana?” Net akakumbuka kumuona akinywa kitu. “Ni meal replacement. Inachukua nafasi ya mlo mmoja. Imebeba virutubisho vingi tu. Kwa hiyo wakati mwingine ni kinywa ile, nikapata na matunda, inakuwa inanitosha.” Net akatabasamu. Maana kwa kumwangalia tu, utajua huo mwili unatunzwa vizuri.

“Mbona na mimi hukunipa sasa?” Tunda akababaika kidogo. Akataka kujitetea, Net akimtizama. “Unisamehe tu. Sikujua kama ungependa. Nimebakiza vingine hotelini. Nilikuja navyo kutoka Dar. Naweza kwenda kukupa.” “Nashukuru. Ila sasa hivi njaa inaniuma sana. Nataka kula chakula chakueleweka. Twende tukale chakula kabisa.” Wakaanza kufunga kazi kwa siku ile, na kutoka pale.

Walirudi hotelini na kuagiza chakula. Kililetwa chumbani. Wakaanza kula. “Nikuulize Net?” “Uliza tu.” Net akajibu huku wakila. “Nimeona ofisi ndio mpya. Lakini mnao wateja wengi. Mnafanyaje?” Net akameza chakula kilichokuwepo mdomoni ili aweze kuzungumza.

    “Chakwanza, kujitangaza. Nimejitahidi kutangaza na nimehakikisha watu wengi wametusikia na kufahamu huduma yetu. Nilitangaza kwenye maredio, televisheni, na kugawa vipeperushi kwa wingi. Mjini, mitaani na maofisini. Ukiangalia hapa nchini, wengi wanatumia kupanga. Kama sio nyumba anayoishi, basi ofisi. Sasa ili kuwapata hao watu, basi, nimeweka uwanja mkubwa kwa watumiaji wote. Wenye pesa na wasio na pesa nyingi wanaweza kutumia huduma zetu. Ndio maana utakuta kuna aina tofauti tofauti za magari. Hiyo inategemeana na uwezo wa mtu. Sijui nimejibu?” Net akauliza.

“Hapo nimeelewa.” “Lakini umeonaje? Si ni kazi inayowezekana?” “Nafikiri. Si bado tutakuwa wote ili kuhakikisha siharibu?” Net akacheka. “Tunda wewe ni muoga sana. Acha kufikiria kuharibu kwanza. Naomba ufikirie ni jinsi gani utaboresha. Ni vipi pale patanufaika kwa Tunda tu kuwepo pale. Tunda huyohuyo unayemfahamu wewe, mfikirie ni kwa jinsi gani pale pamebahatika kupata uwepo wako. Ukifikiria kwa namna hiyo, utaona mambo yatakavyokuwa rahisi.” Tunda akatoa tabasamu kama anayefikiria.

“Niamini Tunda, kila mtu anahaiba yake na kitu kinachomfanya awe yeye. Wewe unajijua. Sasa jifikirie hivyo ulivyo unawezaje kupanufaisha pale! Jiweke kwenye nafasi ya kama ile kampuni ndiyo imebahatika kumpata Tunda. Jiambie kwanza hivyo. Hivyo tu. Weka mbali maswala yakukaa darasani na elimu. Wewe tu kama ulivyo. Jiambie kampuni ya Cote, imebahatika kumpata Tunda. Sasa utainufaisha vipi! Utaona jinsi itakavyokusaidia kukubadilisha mtazamo wako. Kwanza hofu itaondoka, na utashangaa utapata ujasiri wa umiliki.” Tunda akacheka kidogo.

“Kesho tutaanza kwa kukupa nafasi upokee simu.” Tunda akastuka. “Net!” “Si umenisikia leo jinsi nilivyokuwa nikipokea simu?” Tunda akakubali. “Basi fanya hivyohivyo na usiogope kuuliza mteja maswali kuhakikisha unamuelewa. Ukiona anaomba huduma ngumu kwako, au humuelewi, mwambie ili kumuhudumia vizuri, unamuunganisha na mtu atakayeweza kumsaidia vizuri zaidi. Basi, niunganishe naye kwenye simu yangu. Ila kwa kesho, pia tutakuwa wote. Usiogope.” Tunda akacheka kwa hofu.

“Sawa. Nitajitahidi Net.” “Hayo ndio maneno. Na ninakuhakikishia utaweza tu. Sio ngumu kabisa. Kwanza ile kompyuta ipo pale kukusaidia kukupa kila jibu. Si umeona?” “Nilikuona jinsi unavyofanya.” “Sawa sawa.” Wakazungumza kidogo, Net akaondoka.

 

Siku ya Pili, Tunda kazini.

    Tunda alitegesha alamu ili imuamshe mapema kidogo. Akaoga na kujitayarisha. Kwa kuwa alirudi na baadhi ya vitu vyake kutoka Dar, Tunda alijitengeneza kawaida, kiofisi kama vile alivyokuwa akiwatengeneza kina Fina mwilini mwake anapokwenda kulaghai wanaume. Alivaa vizuri. Kiofisi. Kama msomi mwenye majukumu mazito. Ila kiheshima kwa kuwa alikuwa na Net.

Akaagiza kifungua kinywa. Chake akala. Cha Net, akaomba wamfungie maalumu kwa ajili ya kula ofisini. Alimuona akinywa kahawa, na walikuwa na microwave ofisini. Akaomba waweke kila kitu tayari na kuwaambia atapitia hapo mgahawani.

Net alifika hapo. Hakupanda juu kwenye chumba cha Tunda. Akampigia simu kuwa ashuke. Kwa haraka bila kuchelewa, akapitia mgahawani akachukua kifungua kinywa cha Net, akatoka nje. Alitoka kwenye mlango wa hoteli, Net akiwa kwenye gari akimtizama. Hakika Tunda alikuwa amependeza. Kigauni chakuchanua chini kama mwamvuli, juu kilimshika na kilikuwa kata mikono. Kilimfika chini kidogo tu ya magoti. Kiatu cha kufunika, cha juu. Hereni ndefu bila cheni shingoni ila hakuacha kuvaa ile  ya mguuni na mkononi. Pochi inayoendana na kiatu alibeba mkono wa kushoto, mkono wa kulia chakula cha Net.

“Waw!”  Akajisemea Net mwenyewe wakati akimwangalia akimsogelea. Mwishoe akaamua kwenda kumpokea. “Hii ni kwa ajili yako.” Tunda aliwahi wakati Net amemsogelea na yeye akawa ameshafika karibu ya gari. “Asante. Sasa mbona ya kwako sioni?” “Uliniambia leo ni zamu yangu kupokea simu. Sasa wakati mimi nazungumza na wateja, wewe unakula.” Net akacheka. “Naona mudi wa kazi ameanza kukuingia.” Wakacheka. Net alikuwa ameshapokea kile chakula. Akamfungulia mlango, Tunda akapanda. Na yeye akaingia garini nakuanza kunywa kahawa yake. Kimya mpaka kazini.

Walipoingia tu, simu zikaanza. Net akakimbilia na kupokea. Tunda akaanza kuwasha kompyuta akijua wazi Net atahitaji. “Naomba nikupe mtu ambaye atakusaidia.” Tunda akashtuka na kumgeukia Net. Net akamkabidhi simu. Tunda akavuta pumzi. “Halow!” Tunda akaipokea. Net akavuta kiti nakuanza kula pale pale kwenye meza bila hata kumtizama Tunda.

Mteja alikuwa akisafirisha mzigo kutoka Arusha mpaka Moshi. “Ni mzigo wa aina gani na unaukubwa gani?” Alimsikia Tunda akiuliza taratibu tu. Akamuona anaandika huku akisikiliza kwa makini tu. “Kwa aina hiyo ya mzigo, tunaweza kusafirisha. Lakini naomba nishauri.” Mpaka Net mwenyewe ikabidi atulie asikilize huo ushauri. “Asante.” Akamsikia Tunda akishukuru na cheko kidogo. Akahisi amesifiwa huko kwenye simu. Sauti ya Tunda ni kweli ilikuwa nzuri.

“Nimesikia aina ya gari unayotaka. Na ukisisitiza unakwepa garama. Lakini naona mzigo wako unathamani kubwa. Isingekuwa vizuri kwanza tukufikishie pale ukiwa haupo kwenye hali nzuri. Lengo letu kama kampuni sio kukusafirishia tu. Tungependa kuhakikisha tunafikisha mzigo wako ukiwa salama pia.” Net mwenyewe akashangaa. Tunda akaendelea kusikiliza, akamuona anacheka.

“Hapana. Nitakupa kwa bei nzuri tu. Naomba nipe kama dakika moja au mbili, nikutajie aina ya magari yatakayofaa kwa bidhaa yako.” Tunda akabonyeza spika, akaweka simu chini, akaanza kuperuzi kwenye kompyuta. Net kimya. “Lakini hujanitajia jina lako.” Wakamsikia yule mteja. Tunda akaanza kuogopa. “Mrembo? Maana nataka kila nikipiga, niwe nasikia hiyo sauti nzuri. Au siruhusiwi?” Tunda na Net wote walikuwa wakisikiliza.

Tunda akanyanyua simu. “Naitwa Tunda na nimepata aina mbili ya magari ambayo nafikiri yatafaa kwa mzigo wako.” Tunda hakutaka kuendeleza maongezi juu yake. Akamtajia hayo magari na bei yake. Akampa nafasi achague. Akachagua moja na kutaka namba ya simu ya Tunda. “Naomba utumie hii ya ofisi kwa kikazi.” Net akajua anatongozwa na ameombwa namba yake binfsi ya simu. Yule mteja akaendelea kuongea, Net akamuona Tunda anakosa raha, akamuomba yeye hiyo simu.

Tunda akamkabidhi Net simu. “Malipo ni kama alivyokwisha kukwambia. Tutajitahidi kufika sehemu ya kuchukua mzigo kwa wakati na wewe tunaomba uwataarifu kuwa dereva wa kampuni ya Cote, atafika hapo akiwa na kitambulisho chetu. Asante.” Net alizungumza hivyo tu, na kukata simu. Tunda akasimama na kutaka kuondoka.

“Njoo kwanza Tunda.” Tunda akarudi. “Nisikilize. Kwanza umefanya vizuri sana. Hata mimi sikutegemea.” Tunda akatabasamu na kufuta machozi. “Kweli kabisa. Na ninataka uelewe hivi, kazi kubwa hapa au utakayofanya ni kuhudumia wateja wa aina tofauti tofauti. Usiogope kwangu au kwao. Fanya kazi vizuri, wakifika kwenye mambo yao binafsi, wajibu vile unavyotaka wewe. Usiogope. Sijui kama unanielewa?” Tunda akavuta pumzi.

“Lazima ufikie hatua uweze kutofautisha kazi na mambo binafsi. Na ile kauli ya ‘sina uwezo wa kuchagua’, ufike mahali ijifute. Wewe ndio ubakiwe kiongozi wa maisha yako. Yaani wewe ndio unajukumu lakuongeza nafasi kwenye maisha yako. Uchague chakufanya ukiwa unafikiria ili kuepuka majuto ya baadaye. Sijui kama umenielewa?” “Nimeelewa.” “Haya. Tuendelee na kazi.” Tunda akacheka na kurudi kukaa.

Kufika mchana, hofu ikawa imemuisha kabisa Tunda. Anapokea simu kwa ujasiri wote. Net alishangaa vile Tunda anavyozungumza kingereza kizuri. Akahisi Tunda alimdanganya. Alimwambia hajasoma. Na ni mtanzania! “Kingereza amekijulia wapi?” Akajiuliza Net kwa kadiri alivyokuwa akimsikiliza akikizungumza na wateja kwa ufasaha bila hofu na ujasiri usoni.

Hakuna aliyekumbuka chakula cha mchana. Kukawa busy mpaka jioni tena kama jana yake, ila siku hiyo walikaa hapo mpaka usiku wa saa moja. “Naona utajuta.” “Kwa nini?” “Si hivi unavyotumia muda mwingi hapa ofisini!” “Kwanza ndio nafurahia. Kwa mara ya kwanza maishani naona nafanya kitu cha kueleweka na mtu anakifurahia. Nashukuru kwa hii nafasi Net.” Tunda aliongea kwa upole. “Karibu. Na ninaona umeshakuwa mtaalamu.” Tunda akacheka taratibu wakati wanatoka.

“Ni hivyo hivyo tu, tena naona na umejaliwa lugha ya ushawishi. Hiyo pia itakusaidia zaidi.” Tunda akatabasamu. Walikuwa kwenye gari. “Hata nikiwa mbali na pale. Ukipata mteja ambaye unataka nizungumze naye, kama nilivyokufundisha jinsi ya kuunganisha. Kwa simu ya mezani na ya mkononi. Rahisi tu. Niunganishe na yule unayetaka nizungumze naye.” “Sawa.” Tunda akaitika          `.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Tunda na Net wakaendelea kufanya kazi kwa bidii zote. Wakisaidiana bega kwa bega. Wateja wao wengi walikuwa wafanyabiashara wakubwa hapo nchini na watalii. Walisafirisha bidhaa kubwa na za thamani huku wakipokea watalii nje na ndani ya nchi. Walikuwa wakipokea watalii kutoka nchi mbali mbali. Net alijitangaza kwenye website iliyokuwa ikivutia watalii kutoka nchi mbali mbali.

Tunda alimshangaa uwezo wake wakuzungumza lugha. Alikuwa akiongea lugha tano tena kifasaha. Kama sio kingereza au Kiswahili, Tunda alimuhamishia simu Net popote alipo azungumze na aina hiyo ya wateja. Na Net aliacha kusafiri. Akawepo Arusha kwa muda huo aliokuwa na Tunda hapo. Kwa hiyo, hiyo miezi ya mwanzoni ikawa rahisi kwa Tunda.

Wafanyabiashara wengine waliomsikia Tunda kwenye simu walipatwa tamaa. Baada yakushindwa kupata namba zake za simu, walikuwa wakiamua kufika kabisa hapo ofisini, ilimradi tu kumuona nakujaribu kumtongoza. Tunda akashangaa sana. “Kipindi nilipokuwa na shida nao, wote walijificha, sasa hivi ndio wanajitokeza!” Tunda akajiuliza. Net alikuwa akimtizama kwa karibu na alijua nia ya wengi wao.

Kila walipofika pale, Tunda alipowasukumia kwa Net, bado walitaka kuzungumza naye Tunda zaidi. Ghafla yeye akawa wamuhimu kuliko mwenye kampuni! Tunda akajua ni janja yakumpata tu         . Akawa akiwakwepa kiustarabu lakini akimaanisha kabisa. Alishatendwa na kuwatumikia hao wanaume, hakuwa na hamu tena. Alikinahiwa na swala la mapenzi, Gabriel akawa amegongelea msumari wa mwisho.

Hakuwa akijua kama anaweza kufanya kazi kama wasomi wengine kwenye ofisi kama ile. Tena alifanya vizuri sana, mpaka mama yake Net aliyekuwa akizungumza naye kwenye simu alikuwa akimfurahia sana. Tunda alifanya kazi kwa bidii sana bila kuchoka wala kulalamika na Net alimwambia atamlipa. Akajiambia hana sababu yakuuza mwili wake tena. Kwa mara ya kwanza akawa amepata nafasi ya kuchagua nini afanye kwenye maisha yake. Kuuza mwili au kufanya kazi ili kujipatia kipato. Sasa kwa kuwa wanaume walishamtenda na kutumia huo mwili vibaya, kwenye swala la biashara ya ngono, akaona aweke kikomo. Hakuna aliyemkubalia.

Hakuwa na jumamosi wala jumapili, pale alipokuwa na mambo yake yakufanya ofisini, hakuangalia muda hata kidogo. Aliongeza juhudi kazini. Hakujiangalia yeye tena. Akataka kumfurahisha Net na kulipa fadhila. Tunda alijua pesa inayomtoka Net kwa kuwekwa pale hotelini. Sasa ili kulipa fadhila, ni kuweka juhudi. Net mwenyewe alikuwa mchapa kazi. Wakaendelea kuchapa kazi kwa pamoja

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Siku moja ilikuwa jumamosi. Walifanya kazi hiyo week, kuanzia asubuhi mpaka usiku. Jumatatu mpaka siku hiyo jumamosi usiku. Net akamwambia Tunda wanastahili kwenda kula chakula kizuri sehemu kama kujipongeza. Tunda akacheka akijua wazi amefurahia. Waliingiza pesa hiyo week. Kuanzia dola mpaka pesa ya madafu.

“Unahamu ya kula nini?” Akamuuliza Tunda. “Mimi ikishafika usiku kama hivi, nilishakwambia, siwezi kula kitu kigumu. Sitaweza kulala.” Tunda akajibu na kumalizia kufunga kompyuta aliyokuwa akitumia.

“Lazima tujipongeze.” Tunda akacheka. Siku za jumapili ilikuwa wakionana jioni. Tena kwa muda mfupi. Net alikuwa akimpitia hapo hotelini kama kumsalimia tu. Wakati mwingine alikaa kidogo, wakati mwingine aliondoka. Tunda hakujua anaishi wapi. Kama ameoa au la. Anaye mwanamke hapo Arusha au la. Katika watu aliowaogopa hapa duniani ni Net. Alimuogopa huyo kaka kupita kiasi. Mbali na mambo ya kazi, hakuwa na ujasiri wakumuuliza chochote.

“Nishushe mimi hotelini. Wewe nenda tu Net.” “Hapana bwana. Hii ni tunajipongeza wafanyakazi wa Cote. Wewe vipi Tunda?” Tunda akacheka. “Twende basi ukale hata matunda wakati mimi nakula nyama choma. Njaa inaniuma.” Wakakubaliana.

Walitafuta hoteli nzuri. Ni kweli Net hakupenda sana kwenda baa, labda awe anakutana na rafiki zake au mambo ya biashara, ndipo itamlazimu kwenda. Waliingia sehemu ya chakula. Tunda akaagiza maji na fruits salad. Akiwa hana hata habari kama atamwingiza Net matatizoni siku hiyo. Alikuwa amependeza japo alikuwa ameshinda kazini siku nzima tena siku ya jumamosi.

 

Aibu ya Mwaka kwa Tunda  Mbele ya Net. Ya Nyuma Bado Kumfuata Tunda.

Net aliagiza chakula chake na juisi ya embe. Hiyo hoteli juu ilikuwa na vyumba na kumbi ya mkutano. Hali ya Tunda ikabadilika ghafla hata kabla chakula hakijaletwa, Net asielewe ni kwa nini. Meza ya pembeni, mbele kidogo, akaona wamekaa wanaume wakila na kunywa huku wakiongea na kucheka. Watatu wa hao waliokuwa wamekaa hapo kwenye hiyo meza, Tunda alishawahudumia. Tena wakiwa kwenye baa.

Wote waliokuwa wamekaa pale walikuwa marafiki, walikuja mjini Arusha kwenye mkutano. Na wote walikuwa wakifanya kazi ofisi moja. Kwenye NGO ya kigeni. Vijana wenye pesa na wasomi tu. Sasa watatu wao pale ndio hao Tunda alishawahudumia zaidi ya mara moja. Mmoja alimpata kwa kuiba namba ya simu kwenye simu ya mteja mwingine.

Wawili aliwatongoza baada ya kukutana nao baa. Akafanya ule mtindo wake wakumchomoa mmoja baada ya mwingine. Siku ya kwanza akampata mmoja wao wakiwa wamekaa wote mezani wakinywa. Akatoka naye nje, akamalizana naye kwenye gari. Akamuomba namba yake Tunda. Wakaja kukutana tena kwenye nyumba za kulala wageni. Akampa kwa mapana na urefu. Wakati akiwa anaoga aondoke pale hotelini, kabla Tunda hajamfuata huko bafuni, akaiba ya watatu. Kwa kuwa aligundua hao wawili walikuwa karibu akajua lazima atakuwa na namba yake ya simu. Na kweli akafanikiwa.

Siku inayofuata, akampigia simu huyo wa tatu, akijidai anamuulizia yule wa kwanza kabisa ambaye alienda naye baa ndipo akakutana nao wote. Akamzungusha kwa maneno mazuri kwenye simu, mpaka akajikuta na  yeye anaomba penzi. Tunda akajidai kumkatalia kwa kumwambia wenzake watajua kwani alishaonekana na wote akiwa na yule rafiki yao. Akambembeleza akimwambia yeye ni mtu mzima, sio mropokaji. Basi, akachukua chumba mahali, Tunda akaenda kumpa kwa mapana na marefu. Na yeye huyu wa tatu akajua kuwa anamuibia rafiki yake. Ikawa siri yao wawili, ila nafuu zaidi kwa Tunda anayewazunguka wote. Marafiki hao watatu wasijue wanapewa uroda na mwanamke mmoja.    

Siku ingine aligonganisha magari wakiwa baa. Alijikuta na wote watatu meza moja, akiwa ameenda na yule yule wa kwanza, yule wa pili aliyemsaidia kumpata wa tatu akapewa penzi kwenye gari mpaka akatafuta chumba, akamtumia ujumbe wakiwa pale pale mezani kuwa watoke nje. Tunda alipopata ujumbe akiwa anacheza game yake pale kwenye meza ya wale marafiki walevi, akarudisha ujumbe akamwambia anatoka, ila asubiri baada ya dakika mbili kamili ndipo amfuate.

Basi wakafanya hivyo. Alipotoka tu, yule watatu naye akatuma ujumbe kuwa anamuhitaji. Akiwa anamsubiria yule wa pili, ndani ya zile dakika mbili akachat na watatu. ‘Ushawahi kuonja vya garini?’ Akamtumia ule ujumbe. Watatu akajibu kwa haraka. ‘Hapana mama. Ila nipo tayari kujifunza.’ ‘Basi nisubiri. Nikija kuomba funguo za gari hapo mezani. Unifuate baada ya dakika tatu tu.’ ‘Asante mama.’ Usiku huo akawapa dozi marafiki wote watatu bila wao kujijua.

Kwani alipomalizana na wa pili, akamwambia arudi ndani haraka na asiseme kitu. Baada ya muda, akarudi na kumwambia yule wa kwanza tumbo limejaa gesi. Anaomba funguo za gari yake aende akatafute dawa za gesi kwenye duka la madawa. Katikati ya pombe na vile anavyohudumiwa na Tunda, akatoa funguo za gari. Tunda akatoka, yule rafiki wa tatu akafuata nyuma. Alichofanya Tunda nikuhamisha upande lililokuwepo hilo gari. Akaenda kulificha mbali kidogo, hapo hapo baa. Dakika tano zikawa nyingi. Akamalizana na rafiki watatu. Akamshukuru sana na kufurahia ule wepesi. Akampa mahela, akamwambia arudi ndani kwa haraka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Sasa wote watatu wakawa wanajua uwezo wa Tunda wa mapenzi, na wale wawili walishapewa penzi la garini tena kwa muda mfupi sana na wote wakijua wanamwibia mwenzao. Na hawakuwahi kukamatwa hata mara moja. Yule mwizi wa halali, wa kwanza akawa amemuona Tunda pale kwenye meza. Akaamua kwenda kumsalimia Tunda pale pale mezani alipokuwa amekaa na Net.

“Habari Lina?” Akanyoosha mkono kwa Tunda. Net akamgeukia yule kijana na kumtizama Tunda. Tunda akakwepa ule mkono kwa kunyanyua glasi ya maji. “Nzuri tu.” Akajibu Tunda na kunywa maji. “Nikuombe msamaha. Majuzi ulipokuwa ukinitafuta, nilikuwa nimebanwa kweli ndio maana nikashindwa kabisa kupokea simu yako.” Yule kijana alijieleza kwa Tunda. “Hamna neno. Nilielewa.” Akajibu Tunda taratibu, Net akisikiliza.

“Vipi, umehamia Arusha nini?” Akamuuliza Tunda. “Nipo kikazi. Huyu ni bosi wangu.” “Oooh! Nimefurahi kukufahamu Kiongozi.” Akampa mkono Net, yeye Net akaupokea mkono na kujibu salamu. “Nipo hapa Arusha na wenzangu. Tumekuja kikazi. Nipo gorofa hii ya pili tu. Hapa hapa hotelini. Nakukaribisha.” Akamgeukia Tunda. “Asante, lakini hapana. Nipo busy na kazi.” Tunda alimjibu kwa msisitizo tena akimtizama machoni.

 “Kesho ni jumapili Lina. Najua hufanyi kazi. Na mimi kuanzia asubuhi nitakuwepo tu hapa hotelini. Kwa nini usije? Sitakuweka sana.” Tunda alitamani kama aondoke lakini ikamlazimu kujibu tu. “Nina mipango mingine. Tafadhali naomba uondoke ili nile. Unanisimamia hapa, tunashindwa kula. Nimeshakwambia hapana, inatosha.” Chakula kilikuwa kimeshaletwa.

“Au umekasirika sababu sikupokea simu yako?” Akaendelea kusisitiza. Mpaka Net akaweka kisu na uma chini. “Hapana sijakasirika ila sitaki kuonana na wewe tena. Naomba utupishe.” “Daah! Sawa Lina. Lakini…” Tunda akavuta kiti kwa nguvu na kusimama. Akamtizama machoni. “Samahani Lina, sikutaka kuwakwanza.” Tunda akaondoka kuelekea chooni, yule kijana naye akaondoka. Harufu ya pombe ndiyo ilikuwa ikitoka mdomoni kwake na kuenea pale kwenye meza ya Net na Tunda.

Wakati anarudi, ndio anatoka choo cha kike anaingia pale mgahawani alipomuacha Net, akakumbana na wale wengine wawili. “Samahani Lina, tunaweza kuzungumza kidogo hapo nje?” Mmoja wao akaanza na yule mwingine akabaki ameduaa. Kumbe wote waliaga pale mezani kwa rafiki zao kuwa wanakwenda msalani, kumbe walikuwa wakimfuata Tunda. Mmoja akawa amewahi.

Kabla Tunda hajajibu, mwenzie akadakia. “Mimi ndio nataka kuzungumza naye mara moja hapo nje. Hatutachukua muda mrefu, si ndio Lina?” Watatu akadakia, akijua Lina mwenyewe anaelewa. Huwa wanamalizana kwa muda mfupi sana, asijue na rafiki yake naye anachomtakia huyo Lina sio mazungumzo. Ni huduma kama anayoitaka yeye.

Wakiwa wote wamelewa, wakaanza kubishana. “Mimi sitachukua naye muda mrefu. Dakika tano tu.” “Aliyekwambia mimi ninamchukua kwa muda mrefu ni nani? Natoka naye mara moja tu, tunarudi.” Wakajibishana wale marafiki wawili, mmoja akiwa amemshika mkono Tunda. Tunda alitamani kukimbia lakini akajikuta wote wamemshika mkono. Mmoja huku mwingine kule. Ndipo ulipozuka ugomvi, wote wakimng’angania huyo Lina, hakuna anayetaka asubiri kwanza.

“Nakwambia mimi ni mara moja tu! Mbona unafanya mambo ya kitoto, Zimbe?” “Wewe ndio nakuona huelewi. Nimekwambia hata mimi sitamkawisha. Anarudi sasa hivi.” Watu wote mle ndani macho ya kawa kwao wote watatu. Tunda anatetemeka, anataka kubebwa juu juu ili watoke naye pale ndani. Uzuri wakaanza kurushiana wao ngumi, na kumuachia Tunda. Hakujua Net alipotokea, akamsogelea pale akiwa ameshika funguo za gari na pochi yake. Akamshika mkono kwa nguvu, akamvuta kumtoa pale.

Waliingia kwenye gari, Net akaondoa gari kwa haraka Tunda akitetemeka kama aliyetoka kwenye friza. Hata asante alishindwa kusema kwa aibu. Alipofika hotelini, alichukua pochi yake na kushuka kwa haraka kama anayekimbia. Net akaona amuache tu usiku huo. Hata yeye hakumfuta nyuma. Akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kuanzia siku hiyo Tunda alijiapia kutotembelea tena sehemu za starehe au kwenye mabaa. Na kwa kuwa Net alikuwa mstaarabu, hakuwahi kumuuliza tena juu ya ule mkasa. Ila alimuona ile hofu ya mwanzoni kabisa imerudi vile vile. Tunda aliacha hata kumuangalia machoni. Mara nyingi ilipomlazimu kumuongelesha alimuongelesha akiwa anaangalia pembeni. Kama yupo ofisini basi macho kwenye kompyuta au mafaili. Labda Net afanye juhudi za makusudi kumwita jina lake. Hapo atageuka na kukwepesha macho kwa haraka. Alikosa ujasiri kabisa, akapooza hata tabasamu likamwisha.

Wakajikuta muda mwingi wanakuwa pamoja ofisini, wakitoka hapo, anamrudisha hotelini. Week ya tatu Net alipata kijana wa usafi. Akamwambia Tunda atakuwa akifika hapo kusafisha na kutoka mchana. Na huyo ndio mara nyingi Net alianza kumtuma kwenda kuwanunulia chakula na kuwaletea hapo ofisini au wanapitia sehemu. Net anaingia ndani. Ananunua chakula, wanaenda kula hotelini huku Net akiangalia taarifa ya habari. Aliondoka muda alioona Tunda anataka kulala. Hakuna maongezi. Kimya kimya.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Karibu ya mwezi kuisha tangia aanze kazi, Net alimwambia inamlazimu kwenda Dar kwenye ofisi nyingine ambapo yupo mama yake. “Kuna mambo kadhaa yakuweka sawa. Ungependa tuongozane?” Akamuuliza Tunda. “Hapana. Wewe nenda tu. Niache mimi hapa. Nikikwama nitakujulisha.” “Hutaki kuona ofisi ya Dar?” “Halafu hapa tufunge!?” Tunda akauliza kwa mshangao kidogo.

“Hapana. Si unajua hiyo kazi unaweza kufanya popote tu?” Akamuuliza na kumuelekeza kuwa nikupokea simu ambazo wanaweza kuzihamishia hata kwenye simu ya Net au yake. Na kompyuta wanaweza kutumia laptop tu ambayo wanaweza kwenda nayo popote. Tunda akaelewa ila akanyamaza. “Hatutakaa muda mrefu.” “Kama sio lazima, naomba uniache hapa Net. Tafadhali.” Tunda akaongea kwa upole.

“Sio lazima Tunda. Ila sikutaka ubakie hapa peke yako kazi zikakulemea.” “Nitakuwa sawa. Nikishindwa jambo, nitakutafuta unisaidie. Ila nakuahidi kila kitu kitakuwa sawa.” Akasisitiza, Net akamwangalia. “Samahani lakini. Naomba usifikiri nakukaidi au nakataa kazi. Ndio maana nimeuliza kama kunakitu chakikazi natakiwa kufanya mimi huko. Uliponiambia hapana, ndio maana nimeomba nibaki tu.” Tunda aliongea kwa utaratibu na kujihami.

“Sasa hivi natamani maisha haya niliyonayo Net. Napenda hivi ninavyoweza kukufanyia kazi. Au kujiona nafanya kitu chamaana. Acha akili zangu zitulie kazini kwa muda. Nimepoteza muda mwingi sana kwenye lile jiji. Mbaya zaidi nimepoteza ‘kwangu’! Inaniuma sana kujiona nimegeuka kuwa mgeni kwenye nchi yangu mimi mwenyewe! Nyumbani kwangu ndio ilikuwa kimbilio langu. Nikishahangaika huko, nilikuwa nikijifariji ninalo kimbilio. Sasa hivi sina. Hii kazi ndio imegeuka kuwa kimbilio. Nikiamka asubuhi, najiambia ninakitu chakufanya. Inanipunguzia mawazo. Kuja kurudi Dar kama mgeni, nikijua sio kwangu tena, itaniumiza zaidi. Ndio maana nakuomba kama sio lazima, kwa sasa naomba nibaki tu hapa.”

“Nimeelewa. Hamna shida. Tutawasiliana basi. Ukikwama usisite kunipigia. Na bado zile simu unazotaka mimi nijibu, endelea kuwahamishia kwangu.” “Asante Net. Ungependa nikusindikize uwanja wa ndege?” Tunda akauliza kwa upole akionyesha kujali. “Ningeshukuru. Tena itakuwa vizuri nikuachie gari. Nitaondoka na ndege ya mchana. Utanipeleka na wakati wakurudi ningeomba uje kunipokea.” “Sawa. Lakini naomba usinielewe vibaya.” Bembeleza hiyo ya Tunda. Net mwenyewe alikuwa akilainika.

“Nimeelewa kabisa. Usiwe na wasiwasi.” Wakatulia kidogo. “Basi nitakuona kesho. Nitakuja kukuchukua asubuhi twende kazini, mchana ndio utanisindikiza.” “Sawa. Usiku mwema.” “Na wewe.” Net akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Net na Tunda walifika uwanja wa ndege, wakabaki kwenye gari upande wa kuegeshea magari. Hawakushuka. Kila mtu kimya kwa muda. Net macho kwenye simu yake, Tunda ametulia tu pale kwenye kiti kama hayupo garini. Hana simu mkononi. Ametulia kimya.

Baada ya muda akaita. “Net!” Akaita kwa upole. Net akamgeukia. “Unarudi lini?” “Nitajitahidi nisikae sana. Kuna kitu ulitaka kuniagiza? Hata kwenye vitu vyako. Nitakwenda kule Salasala kumuona Max.” “Max ni nani?” Ikabidi kwa mara ya kwanza Tunda kuuliza kitu mbali na kazi.

“Kumbe siku ile sikukuonyesha?” Tunda akatingisha kichwa kukataa. “Ni mbwa. Nilimnunua na akapatiwa mafunzo ya kiulinzi. Mzuri sana. Ananisaidia sana pale kwa ajili ya ulinzi. Yeye tu na Emma wanatosha.” Tunda akatabasamu. Net akacheka. “Ni mzuri sana. Nampenda.” “Mimi muoga wa mbwa.” “Max utampenda. Tutakuja kwenda wote siku moja, nikutambulishe. Kwa sasa ananijua mimi, Emma na daktari wake. Ni mkali au hatari kama akijua sio mtu salama.” Tunda akacheka na kutulia.

Wakatulia hapo kwa muda. Net alianza kuona uzito wa ile safari. Walishakuwa kwa karibu sana na Tunda karibia mwezi sasa. Kula na kuwa pamoja kila siku, tena kwa ukaribu! Tunda anautulivu fulani hivi, huchoki kuwa naye. Akaona uzito kumuacha. Akamwangalia, akamuona amegeukia dirishani kama anayewaza. Na yeye akatulia tu akimwangalia na kupotelea mawazoni.

Tunda akageuka, akamuona amejiegemeza kwenye kiti chake akimwangalia. “Huna haja yakunisindikiza mpaka kule.” Ikabidi amuwahi. “Sawa.” Tunda akakubali. “Kama hutataka lakini.” Akajihami Tunda asijefikiri anamkwepa. “Hamna neno.” Akajibu taratibu. “Au ungependa kufika mpaka kule ninapoingia kupanda ndege?” Akababaika tena kwani aliongea bila kufikiria baada ya Tunda kugeuka na kugundua anamwangalia. Akapaniki. “Ni sawa tu. Wakati wakuja kukupokea pia nikusubirie hapa hapa?” Tunda akauliza taratibu bila kuonyesha tatizo lolote. “Utakavyopenda. Ila tutawasiliana.” “Sawa. Uwe na safari njema.” “Asante na wewe ubaki salama. Unipigie ukikwama.” “Naamini kila kitu kitaenda sawa.” Tunda akajibu.

Inamaana hatutawasiliana mpaka nirudi?” Akajiuliza Net. Akaona amejifunga kwa maneno yake mwenyewe. “Unarudi hotelini au kazini?” “Sasa hivi nimapema sana. Acha nirudi ofisini tu. Nifanye fanye kazi upaka usiku, ndio nirudi kulala.” “Basi nikifika tu nitakujulisha.” Akachomekea Net na kujishtukia. “Na kujua umefikia wapi huko kazini.” “Sawa.” Tunda akajibu. Net akaona asije kuongea mengi na kuharibu zaidi, akashuka garini japo muda haukuwa umefika. Tunda akarudi kazini akitumia hiyo gari ya Net.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Net alitua jijini Dar, akili zikiwa Arusha. Mama Cote alikuwepo uwanja wa ndege kumpokea mwanae. Hawakuwa wameonana karibia mwezi. Kila weekend alipokuwa akimpigia simu nakumtaka arudi nyumbani, Net alisema yupo busy labda weekend ijayo. Siku zikazidi kwenda akahisi lipo jambo tu huko Arusha. Net sio mtu wa kung’angania Arusha na kushindwa kumuona mama yake zaidi ya majuma matatu tena akiwa hapo hapo nchini! Akajua lipo jambo kwa kijana wake. Na kwa kuwa alishazungumza na Tunda kwenye simu, akamsikia sauti yake, vile anavyoongea, akajua huyo Tunda pengine ndiye anayembakisha huko Arusha.

“Vipi Tunda?” Mama yake akauliza kiuchokozi tu na Net akajua. “Naona anaendelea vizuri. Kazi nyingi ameshazijua. Wateja wengi amewamudu.” “Lazima. Ana lugha nzuri. Namaanisha sauti.” Net akacheka. “Umeanza mama Cote.” “Jamani!”  Wote wakacheka. “Sasa kwa nini hukuja naye?” “Si yupo kazini mama jamani!” “Sawa, namaanisha weekend zile nyingine? Mkaribishe nyumbani. Hizo kazi mnaweza kufanyia hata huku Dar kama ulivyokuwa ukifanya.” Net akatingisha kichwa. “Sawa mama.” Wakacheka.

Net alikaa Dar siku mbili tu, tayari akawa anataka kurudi Arusha. Ghafla chakula cha Dar kikaanza kuwa hakiliki vizuri, masaa hayaendi. Ofisi ya Arusha ikawa inamuhitaji sana, basi ikawa vurugu. Akamuaga mama yake. “Nilijua week hii utamalizia huku urudi jumatatu! Maana leo ni ijumaa. Jumapili twende wote kanisani. Hata mchungaji amekuwa akikuulizia.” “Nitarudi weekend ijayo.” Mama yake akajichekea moyoni.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jioni hiyo akampigia Tunda simu. “Nimepata tiketi ya asubuhi.” “Basi nitakuja kukupokea.” “Sawa. Ila kama utakuwa na mambo mengine naweza kuchukua taksii.” “Hamna neno. Nitatokea ofisini. Nitakuja kukupokea, halafu unirudishe ofisini kama umechoka unaweza kuniacha tu wewe ukapumzike.” “Sawa. Lakini nafikiri na mimi nitarudi ofisini.” “Sawa.” Tunda akajibu taratibu kama kawaida yake.

     “Kuna kitu chochote unataka nikujie nacho kutoka huku?” Net akauliza. Tunda akafikiria kidogo. “Sidhani Net. Nipo tu sawa. Asante sana.” “Basi nitakuona kesho asubuhi.” “Uwe na safari njema.” Ikabidi kuagana tu. Hapakuwa na nyongeza.

                            Jumamosi Siku Isiyo ya Kazi, Net Arudi Arusha.

    Kesho yake Net alitua uwanja wa ndege wa Arusha, Tunda akiwa anamsubiria hapo nje, wala si kule kwenye gari. Net akafurahi sana kumuona pale. “Pole na safari.” “Asante. Na asante kwa kuja kunipokea.” Tunda akatabasamu. “Nimefurahi umerudi.” Tunda akaongea kwa upendo kama aliyekuwa ameachwa hapo kwa muda mrefu. Net kijana wa kizungu akacheka. Na macho yake yale ya rangi ya bahari, Tunda akakwepesha huku akinyoosha mkono ampokee.

“Sio mzito!” Net akajihami kama asiyetaka kupokelewa, anaweza kubeba kila kitu yeye mwenyewe. “Lakini angalau nikupokee. Usibebe kila kitu peke yako.” Akampa mkoba wa laptop. “Nimekuletea movie za stori kama unazopenda.” Tunda akacheka. “Asante. Nitaangalia kesho jioni. Asubuhi nataka niende kazini kidogo.” Net akanyamaza. Ni siku ya jumapili. Yeye alikuwa lazima kwenda kanisani. Wakarudi ofisini mpaka jioni.

Jumamosi huwa kijana wa usafi hafiki hapo ofisini. Walikuwa wao tu wawili. Net alifikia kwenye meza ya Tunda. Tunda akashangaa haingii ofisini kwake. Yupo tu hapo mezani kwake akifanya kazi zake hapo hapo. Japokuwa alikuwa akimuogopa, lakini alifurahia uwepo wake hapo. Hawakuwa wameonana kwa ‘Siku mbili! Nzima’. Wakashinda wote hapo wakifanya kazi pamoja. Hapakuwa na maongezi mengi. Tunda anamuogopa Net. Zaidi ya kumjibu endapo atauliza, basi hatazungumza chochote. Net naye kimya akifanya kazi zake kwenye laptop yake, Tunda asijue ni nini kinachomfanya kijana huyo kuwa busy kwenye hiyo laptop kila wakati. Kazi zikaendelea kwa utulivu siku hiyo ya jumamosi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakaendelea kufuatana. Kazini, hotelini kwa Tunda mpaka wakiagana kwenda kulala. Mwishowe Net akaonelea kutafuta vitu ambavyo angefanya pamoja na Tunda kila wawapo pamoja, baada ya kazi angalau wazoeane au kupata kitu chakuzungumza mbali ya kazi. Akaanzisha siku na muda wao wakuangalia movie pamoja.

Wakitoka kazini, badala ya kukimbilia rimoti na kuanza kuangalia taarifa ya habari peke yake, alimtaka Tunda wakae wote hapo waangalie movie pamoja, au wacheze karata. Basi watacheza hapo kisha anaondoka na kumuacha Tunda. Lakini hakuwahi kumuuliza Tunda swali hata mara moja juu ya mara zote alizowahi kumkuta na wanaume au hata kisa kile alichotaka kubembwa juu juu. Tunda alishindwa kumuelewa kabisa Net. Walicheza na kuzungumzia kile kilichopo mbele yao tu kana kwamba hakuwa akimfahamu.

Kitu alichokigundua kwa Tunda kila walipokuwa wakiangalia tv hapo kwenye kochi, chumbani kwa Tunda, Tunda alijivuta pembeni yake, alikunja miguu yake vizuri na kuweka mikono yake juu ya kochi kama mto na kulala usingizi mzito sana. Net alijaribu kubadili aina ya movie. Alileta za visa vya kusisimu, wakati mwingine historia za kusisimua lakini mara zote Tunda aliishia kulala kabla hata hazijafika hata nusu! Na ulalaji wake ulikuwa wa usingizi mzito sana, na mara nyingi Net aliishia kumfunika pale pale kwenye kochi na Tunda aliishia kulala hapo mpaka asubuhi, kwani alishamuomba wakati akiwa anaondoka asiwe  anamuamsha ili ahamie kitandani, alitaka aondoke kimya kimya amwache tu vile vile alivyolala.

Yeye Net alikuwa akifurahia sana kuwa na Tunda, lakini wawe wanazungumza. Macho na sauti ya Tunda ni kweli vilimsumbua Net. Alikuwa akipenda awe anamtizama sio vile anavyokwepesha macho au basi angalau azungumze ili tu asikie ile sauti yake akizungumza naye yeye. Na iwe kwa muda mrefu. Kila alivyojitahidi Net, Tunda hakuwahi kubadilika. Wakati mwingine anaweza akanyamaza hapo chumbani kana kwamba hayupo. Atatulia kimya, akijitahidi ni kutoa tabasamu.

Net alijua kwa hakika anamuogopa sana. Swala la afanye nini kuondoa ile hofu ndio ukawa mtihani mkubwa. Tunda kimya. Kila alipoanza maongezi alianza kwa kumwita jina lake, kumfanya angalau Tunda  amtizame ayaone hayo macho.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Uliniambia unapenda sana kuangalia movie za stori, Tunda. Kwa nini kila nikiweka movie unalala? Nataka tuwe tunaongea bwana! Tunakuwa ofisini busy week nzima, angalau jumamosi jioni au jumapili tuseme ndio tunapata muda wakupumzika na wewe unalala! Au hufurahii hizi movies ninazochagua mimi?” “Ni nzuri sana tu. Mbona mwenzako huwa naangalia tena kwa kuzirudia rudia? Kila nikitoka kazini, ukiondoka au nikishtuka usiku nakujikuta nimebaki peke yangu, naziangalia.” Net hakuelewa.

“Sasa kwa nini hutaki kuangalia na mimi?!” “Hata nikikwambia hutaelewa Net.” “Bila kunijaribu!?” Tunda akanyamaza. “Au nakukera nikiwepo hapa?” “Nisingelala Net.” Net akakunja uso kidogo kama ambaye hajaelewa.

 

Kwa Mara ya Kwanza, Tunda aamua kufunguka kwa Net

Tunda akajiweka sawa. Net akajua anataka kuongea jambo. “Tokea siku ile nitolewe au niseme nifukuzwe kwa bibi yangu nikiwa darasa la pili, sikuwahi kupata utulivu wa akili. Nakumbuka kwa mara ya kwanza siku ile jioni nikisikia ndugu zake mama wakitaka nitolewe pale kwa mtu niliyedhani ndiye mama yangu au nikidhani nyumbani kwetu, na ndio nikajua mwanamke aliyekuwa akinichukia sana hata alipokuwa akija pale kijijini mara zote hakutaka nimwangalie, ndiye alikuwa mama yangu wa kunizaa.” Tunda akaanza taratibu.

“Nilimsikia jinsi anavyobisha kunichukua akitaka niendelee kuishi pale pale kwa bibi na babu, yaani kwa wazazi wake. Walipomlazimisha sana, wakitaka lazima niondoke pale ili kupunguza matumizi ya pale kwa bibi, pale nilipodhani ni nyumbani kwetu, na mimi ni mdogo wao wa mwisho, ndipo nilipoona jinsi mwanadamu anavyoweza kubadilika na kuwa mnyama mkali kuliko hata simba.”

“Alinichukua kwa hasira sana kwa kuwa walimlazimisha lazima anitoe pale. Njia nzima yule mwanamke ambaye nilisikia wakisema ni mama yangu, alikuwa akinifinya na kunipiga sana. Kama sio makonzi ya kichwani, basi ngumi nzito sana kwa kutofanya alichoniagiza kwa mtoto wake. Ni kweli sikuwa nikimuelewa. Kwanza alinitajia majina ya vitu ambavyo sikuwahi kusikia mimi mtoto mdogo, niliyekuzwa kijijini, tena wakati huo hata Kiswahili chenyewe sikuwa nikielewa sawa sawa. Wakati wote tulikuwa tukizungumza kilugha pale kijijini. Pili, nilikuwa kwenye mshtuko wa kutolewa kwa kufukuzwa kwenye nyumba niliyokulia, kwa watu niliojua ni wazazi wangu.” Tunda akaendelea taratibu.

“Nakumbuka ile hali ya kuchanganyikiwa, hofu na wasiwasi nisijue huyo mwanamke anayenichukia waziwazi, alikuwa akinipeleka wapi! Yeye ndiye alikuwa dereva, nilikaa kiti cha nyuma na mtoto wake. Mbali na usafiri wa vibasi vya pale kijijini kututoa kijiji kimoja kwenda kijiji kingine, sikuwahi kupanda gari aina yeyote ile. Sikujua jinsi ya kushusha kioo cha gari au kupandisha. Na wala sikuwa nikijua wanafunga na kufungua vipi mlango wa gari! Hilo ni kosa pia lililonifanya nipigwe njia nzima. Kila aliporudisha mkono wake nyuma tukiwa njiani ilikuwa ni kunifinya sana au kunipiga kofi.” Net alikuwa akisikiliza kwa makini huku akishangaa.

“Alijawa na hasira juu yangu, hata uso wake alionyesha. Nilishindwa kujua ni kwanini, lakini matusi aliyokuwa akinitukana ndiyo yalinifanya baadaye nihisi labda baba yangu alimtendea kitu kibaya sana ndio maana alinichukia kwa kiasi kile.”

“Tokea siku ile, ndipo maisha yangu yalipobadilika kabisa, Net. Na ndio ukawa mwisho wa kila kitu ambacho wanadamu wengine walibahatika kuwa navyo hapa duniani, wakichezea na kudharau. Mimi ndio ukawa mwisho wangu.”

“Jina la Tunda liliisha kabisa.  Kila aliyeniona aliniita vile anavyotaka yeye. Mama yangu mzazi aliniita majina mengi lakini ambalo lilibaki masikioni mwangu ni ‘Paka’. Alichukia rangi yangu, macho yangu na sauti yangu ndio ilikuwa kero kabisa, kwani ilikuwa ikinichukua muda mrefu kidogo kutengeneza sentensi moja ya Kiswahili, mtu akanielewa. Aliishia kuniwasha vibao vya usoni kila wakati na kunigeuza bubu.”

“Mambo hayakuwahi kugeuka tena, mpaka sasa wewe ndiye mtu wakwanza kupongeza kazi ninayofanya na kunipokea jinsi nilivyo ukijua jinsi nilivyooza, lakini bado unaniheshimu Net. Ndio maana kila ninapokuwa na wewe, najikuta sina hofu Net. Sina sababu ya kujificha, au kujibaraguza au hata kubadili jina langu. Napata amani ya ajabu, najua nipo na mtu anayeweza kunitazama kama binadamu mbali na maovu yangu yote.” Machozi yakaanza kumtoka Tunda.

“Huu usingizi ninaopata nikiwa na wewe sio ninaopata nikiwa peke yangu. Tena afadhali sasa hivi naweza kulala hata masaa machache nikijua kesho nitaenda kazini, kitu ambacho sikuwahi kufikiria kama naweza kufanya maishani. Wanadamu nilioishi nao wote, walihakikisha wananikandamiza na kunihubiria jinsi nilivyo kiumbe dhaifu na siwezi kufanya chochote hapa duniani, mpaka kweli na mimi nikaamini hivyo.” Net alikuwa akimsikiliza kwa kumuhurumia. Akajifuta machozi.

“Ushawahi kukaa kwenye jua kali sana mpaka ukachoka, halafu gafla ukahamishwa kwenye kivuli tena chenye upepo mzuri?  Kitu cha kwanza utakachotamani ni maji ya kunywa ya baridi. Sio kwamba hata ukipewa soda hutakunywa, utakunywa tu. Lakini kitakachoburudisha moyo wako ni maji pekee. Ndivyo ilivyo kwangu. Utulivu wa akili ninaopata ukiwepo hapa na mimi, unanifanya nilale. Ndio maana sitaki hata uniguse wakati ukiondoka, ili angalau pakuche nikiwa katika ile hali ya utulivu akilini mwangu.” Net alianza kuelewa.

“Mama alikupeleka wapi siku hiyo alipokutoa kwa bibi na babu kijijini?” Net akauliza taratibu. “Ilikuwa siku ya maajabu sana kwangu siku hiyo. Alinipeleka kwa baba yangu. Tena hata sikutambulishwa. Baada ya kushindwa kufungua mlango aliponiambia tumefika, ilimbidi ashuke aje kunifungulia yeye. Lilikuwa nikosa ambalo alishindwa kunisamehe. Alifungua mlango kwa hasira. Akanipiga sana, kisha akanitupia nje ya gari huku akinifinya mdomo nisilie hata kidogo. Alinivuta mpaka ndani ya hiyo nyumba ambayo alipofunguliwa mlango tuliingia huku ananivuta kama mwizi, na kuniacha hapo kati kati ya sebule nikiwa nimesimama na wenyeji wakiangalia tv. Sikuambiwa kuwa yule ndiye baba yangu ila nilimsikia akimwambia baba, ‘nimekuletea jaluo mwenzako, sijui kabila gani! Mtajijua wenyewe’. Kisha akaondoka na kuniacha pale.” Tunda akajifuta machozi.

“Pale pale pakaibuka tena ugomvi kuwa sitakiwi na pale tena. Baba alikuwa na yeye ameoa, mkewe alianzisha zogo jingine pale pale akitaka niondolewe usiku uleule, lakini nikafanikiwa kuishi pale kwa muda wa miaka miwili iliyokuwa migumu na iliyosaidia kuharibu akili yangu kabisa, mpaka nilipotolewa pale nusu mfu na jirani kama nilivyotolewa nusu mfu nyumbani kwa mpenzi wako.” Net akakunja uso.

“Mpenzi wangu mimi?!” “Ndiyo.” “Nani mpenzi wangu!?” “Si Sera? Au mliachana?” “Sera hakuwahi kuwa mpenzi wangu bwana.” Tunda akakunja uso kidogo. “Sisemi Samatha yule mdogo, nasemea Sera yule mkubwa.” “Namfahamu Sera na Samatha vizuri sana.” “Sasa mbona unakataa kama sio mpenzi wako wakati ulikuwa ukija kumuona pale hata mara mbili kwa siku?” “Nani alikwambia nilikuwa nikimfuata Sera?” Tunda akawa kama ameshachanganywa kidogo.

“Net jamani!? Au umesahau?” “Nakumbuka kila kitu. Lakini sikuwa nikimfuata Sera.” Tunda akatulia kidogo kama anayefikiria. “Kwanza wewe umejuaje kama nilikuwa nikifika pale? Maana kila nilipokuwa nikija sikuwa nikikuona?” Net akauliza. “Mle ndani ya ile nyumba, ulikuwa kama lulu! Zilikuwa zikianza kutajwa sifa zako, hamtahema. Mimi mwenyewe nilikufahamu hata kabla sijakuona.” Tunda akacheka kidogo.

“Siku ya kwanza unakumbuka nani alikufungulia mlango?” Net akatabasamu kama anayefikiria kidogo. “Siwezi kusahau.” “Basi ulipoingia tu na Joe, nilipokuona tu nikajua ndio Net aliyekuwa akisifiwa mle ndani.” Net akacheka.

“Sera alikupenda sana. Mliishia wapi?” “Kwani tulianzia wapi?” “Net!?” “Nini?” “Safari zote zile ulizokuwa ukija pale, ukamfanya Sera achanganyikiwe! Mpaka wazazi wake walijua mtaoana!” “Walijichanganya wenyewe tu.” “Mmmh! Siamini kama hapakuwa na mwendelezo wa yale mahusiano. Uliwaalika mpaka nyumbani kwenu?” “Tunda! Hebu achana na hayo. Naona wote hamkuwa mmeelewa. Kwanza nijibu kwa nini ulikuwa unanikimbia?” “Weee! Nilipigwa marufuku mwenzio, tena kwa kumwagiwa ndoo ya maji nikiwa nimelala.” Net akashangaa.

“Kwa nini!?” “Wewe unacheza na wale watoto nini? Halafu walivyo washenzi, eti siku inayofuata wewe ulinikuta naingiza godoro ndani baada ya kutoka kuanika baada ya wao kunimwangia maji wakati nimelala, tena nakumbuka ukauliza, ‘vipi mbona kama kuna wanao hama?’. Eti wakakwambia huwa nakojoa kitandani. Hivi uliamini?” “Mimi sio mjinga Tunda. Nilishawasoma watu wote pale ndani, kwa muda mfupi niliwafahamu kwa asilimia kubwa sana. Kila nilichokuwa nikiambiwa nilikuwa nikijua ni kweli ama sivyo.” Tunda akatulia kama anayefikiria.

“Unajua siku uliyoondoka, nilikuja pale kutaka kuongea na wewe?” Tunda alishtuka kidogo. Akageuka nyuma na pembeni kisha akajishika kifuani. “Mimi?” “Ndiyo.” “Unamaanisha mimi Tunda?” “Acha utundu Tunda, tupo wawili tu hapa ndani. Kwani hawakukwambia kama nilimuomba shangazi yako kuja kesho yake, usiku ili kuzungumza na wewe?” Tunda afikiria harakaharaka.

“Basi wewe ndiye uliyenisababishia matatizo Net!” “Nilifanya nini?” “Kama uliwaambia wale, ujue wewe ndio sababu kubwa yakutoka pale nusu mfu.” “Nusu mfu tena? Wakati mimi nilipofika siku hiyo kuja kuzungumza na wewe kama nilivyowaomba, waliniambia ulitoroka tena baada ya kuiba!” Tunda akaumia sana, Net akamuona anaguna.

“Kwani ilikuwaje?” “Aiii! Haina hata haja yakusimulia, haisaidii chochote.” “Mimi nataka kujua.” “Tuache tu.” “Kwa hiyo unataka mimi nibaki na sifa yako ya wizi?” “Nina madhambi mengi sana unayoyajua Net. Kutokuwa mwizi pekee, hakutasafisha uozo wangu. Tuache tu.” “Siwezi kuacha kama mimi ndiye niliyekusababishia matatizo Tunda. Nieleze kilichotokea.” Tunda akatulia kidogo, usoni alibadilika kabisa.

          “Tunda?” Net akaita akitaka Tunda amueleze tu. Tunda akaona amuelezee tu. “Tuliamka siku ile, shangazi akilalamika amepoteza mkufu wake wa dhahabu. Yeye na watoto wake wote walisema mara ya mwisho waliona huo mkufu usiku uliopita wakati wanakuja kwenu. Kwa hiyo tukabaki wezi ni mimi na Nyangeta. Haa!” Tunda akashtuka. “Nini?” “Jamani Nyange! Hivi bado yupo?” “Sijui. Mimi mwenyewe sikurudi tena pale.” “Kwa nini!?” Tunda akauliza kwa mshangao.

“Aaah!” Net alitaka asitoe sababu ya msingi iliyomfanya asirudi tena nyumbani kwa kina Sera. “Lakini hata hivyo muda wangu wa kurudi chuo ulikuwa umeshafika. Niliondoka nchini.” “Shule iliisha sasa?” “Nashukuru Mungu iliisha. Niambie nini kilitokea.” “Kuhusu nini tena?” “Sababu ya kukutoa pale nusu mfu.” “Husahau!?” “Hilo ndilo tatizo langu Tunda. Sisahu na nikikusudia kufanya jambo fulani, ni lazima nifanikishe. Hata kama lina gharama kubwa kiasi gani, lazima nilitimize. Mpaka bibi yangu huwa ananihurumia.” “Lakini ndio maana umefanikiwa Net” “Nimefanikiwa kwenye nini?” “Ona bishara ulizo nazo.” Net akatabasamu.

“Chakwanza nataka uelewe zile ni biashara za mama yangu. Mimi ni mwajiriwa kama wewe tu. Nampa tu mawazo kama hivi unavyonishauri mimi, na yeye anachagua kipi chakutendea kazi, basi.” “Lakini kwa hapo ulipo Net, ni kama huna kitu unataka maishani.” Net akatabasamu akabaki akifikiria kidogo.

“Nikikwambia pesa hainunui kila kitu hapa duniani, huwezi kuniamini.” “Mimi tena? Naamini sana tu Net. Nimezihangaikia hizo pesa jamani! Sitakaa nikasahau maishani. Nilidhani nikiwa na maisha fulani ndio itanisaidia kurudisha ile hali ya kabla sijatolewa kwa bibi yangu kwa mara ya kwanza, lakini wapi Net! Nimetafuta kurudisha ile hali kwa mateso sana, lakini sijafanikiwa. Nimeishia kudhalilika tu.” Tunda aliongea kinyonge.

“Sijui nilipatwa na nini!? Nilikuwa kama mbwa, tena mbwa wa uswahilini. Mchafu kuliko, sijui nini!” Tunda akatulia kidogo. Net naye kimya. Hapo hakuongeza.

“Turudi kwenye swali lako Net.” “Ehe!” Tunda akajifuta machozi. “Kweli wewe king’ang’anizi.” “Sitaondoka leo mpaka nijue.” “Haya bwana. Basi yule Mzee akaanza kutukaba mimi na Nyange, tutoe huo mkufu wa mkewe.” Tunda akatulia kidogo.

“Sikukuzwa au kulelewa kwenye mazingira ya kusikilizwa Net, kwa hiyo sijui kabisa kujitetea. Vile mtu anavyosema juu yangu, huwa mara nyingi inabaki vile vile. Kwa kuwa siwezi kukanusha, hasa pale ninaposhutumiwa moja kwa moja. Nakuwa kama ninapatwa na ganzi mwili mzima. Mwenzangu Nyangeta alijitetea haraka haraka akapona. Mimi nikabaki kama bubu. Basi pale mimi ndio nikaonekana mwizi moja kwa moja.”

“Yule Mzee akaamuru iletwe mifuko yangu ya nguo. Maana nilikuwa na mifuko miwili ya plastiki, ndio nilikuwa nikiwekea vitu vyangu vyote. Hatukuruhusiwa kutumia makabati ya mle ndani chumbani.” “Kwa nini!?” Tunda akacheka kidogo. “Mimi waliniambia wanaogopa naweza kusababisha wadudu kwenye hayo makabati ya ukutani. Yalikuwa yamejengewa kwenye ukuta. Mazuri kweli. Lakini yalikuwa yakifungwa kabisa na funguo ambazo alikuwa akitunza shangazi. Kwa hiyo tukawa tunaweka vitu vyetu kwenye mifuko tu ya plastiki.” Net alibaki na mshangao.

“Basi mifuko yangu ikaletwa. Walipomwaga chini vitu vyangu ili kukagua, ule mkufu wa shangazi si ukaanguka kutoka kwenye huo mfuko wangu! Tena mfuko wa kwanza tu, hata hawakwenda wa pili. Net! Nilipigwa mimi. Nafikiri Mungu alinihurumia. Maana alinipiga sehemu iliyonisaidia kupoteza fahamu, sikujua kinachoendelea mpaka nilipopata fahamu nikiwa hospitalini.”

“Nilijua nilipigwa sana kutokana na maumivu niliyokuwa nayo, na jinsi nilivyokuwa nimepasuka. Nilipasuka hapa juu ya macho, midomo, mbavu zilivunjika. Mkono huu ulivunjika, mpaka mifupa ilikuwa ikionekana kwa nje kuwa imetengana. Bega lilitenguka.”

Nilikaa hospitalini zaidi ya mwezi sababu ya kuvuja damu kwenye mbavu, na kutobolewa kuwekwa vyuma, kama mshikaki. Halafu sikuwa na pakwenda. Kila mahali nimefukuzwa. Ikabidi kuomba kuendelea kukaa pale pale hospitalini mpaka nipone. Mtu aliyekuwepo hapo kuniuguza ni baba, naye alifungwa nikiwa bado hospitalini.” Tunda alinyamaza na kufuta machozi.

“Na yeye ni mtu mwingine aliyenikubali vile nilivyo. Mpaka nilikuwa namshangaa. Alikuwa akipewa habari zangu mbaya tupu, lakini wakati wote alinithamini. Nililia sana baada ya kumkuta tena kwa mara ya pili pembeni ya kitanda changu hospitalini.” “Mara ya pili?” Net akauliza.

“Mara ya kwanza ni pale mama aliponiacha hospitalini baada ya kunitoa mimba. Nilikuwa peke yangu na barua aliyokuwa ameniachia niisome mara baada ya kuzinduka usingizini, akinitaarifu yeye na ndugu zake wote hawataki kuniona tena, kwa kosa la kuwa na mahusiano na mumewe. Lakini hata baba alipoambiwa hilo kosa langu, alikuja kuniuguza mpaka nikatoka.”  Tunda alitulia akainama kwa muda.

Kisha akaendelea. “Na mara ya pili nilizinduka hospitalini nikamkuta baba tu, tena hata hapo nikiwa ninatuhumiwa za wizi wa huo mkufu wa shangazi. Lakini mara zote hizo baba amekuwa akinihudumia bila shida. Siku aliyokuwa ananiaga kuwa anaweza asirudi tena, aliniambia nisiwahi kufikiri kama mimi ni mtoto wa bahati mbaya. Alinieleza kuanzia mwanzo wa kuzaliwa kwangu mpaka nilipoishia kijijini.”

“Ilikuwaje?” Tunda alimsimulia Net kila kitu juu ya baba yake na mama yake, mpaka alipoenda kutelekezwa kijijini. “Daah! Unahistoria ngumu Tunda!” “Lakini wewe pia ulichangia Net!” Net akaanza kucheka. “Jamani mimi nilifanyaje?” “Nikifikiria juu ya kile kisa cha mkufu wa shangazi, sasa hivi ndio naelewa kuwa ni mpango shangazi alifanya na wanae. Walimtumia yule baba kuniadhibu bila yule baba mwenyewe kujua kinachoendelea.” Net hakuwa ameelewa vizuri.

“Ukweli kile kitendo cha kuwa na mahusiano na mume wa mama yangu kilinipotezea uaminifu kwa watu wengi sana. Hakuna aliyeniamini na mumewe au hata marafiki zao wa kiume. Shangazi mwenyewe alinipiga marufuku hata kupita pale sebuleni mumewe akiwepo. Sasa na wewe walijua kabisa ungemuoa Sera, kwa hiyo hawakutaka mimi niwe hata nakuona. Waliniambia kila unapokuja niwe natoka nje kabisa, nisirudi mpaka wewe utakapokuwa umeondoka.” Hapo Net akawa ameelewa.

“Samahani sana Tunda. Sikukusudia kukusababishia matatizo.” “Wala usijisikie vibaya Net. Nilikuwa navuna nilichopanda. Nilikuwa nalipa uovu wangu.” “Sio kwa njia hiyo Tunda.” Tunda akacheka tena taratibu, huku akifikiria.

Akawa kama amekumbuka. “Ulitaka kuniambia nini Net?” Tunda alinyanyua uso, nakumuuliza. “Tuache tu. Sasa hivi haina maana tena.” “Kwa nini unasema hivyo!?” “Tunda wa wakati ule niliyetaka kuzungumza naye sio Tunda huyu wa sasa. Umebadilika sana Tunda. Hata nikikwambia sasa hivi, haitaleta maana tena.” Tunda aliumia sana moyoni.

“Naelewa Net. Naelewa kabisa, wala sikatai. Mimi mwenyewe wakati mwingine sijitambui kabisa. Nahisi ni kama mtu ninayeangalia watu wengi tofauti tofauti ndani ya mwili mmoja wakiishi kwa kupeana zamu. Mimi mwenyewe sijitambui. Nimepotea kabisa. Hata sasa hivi hapa sijui anayeishi kwa kutumia huu mwili wangu ni nani! Kuna umbali mkubwa sana kati yangu mimi binafsi na watu wote unaowafahamu kupitia huu mwili wangu. Kuna mambo nilikuwa nikifanya mpaka mimi mwenyewe nilikuwa naogopa Net! Nilikuwa nikirudi nyumbani kwangu nashindwa hata kulala kwa mshtuko.” Tunda akaendelea kuongea huku akivuta kumbukumbu taratibu.

“Ni kweli mwanadamu ana uwezo mkubwa sana. Siku chache zilizopita kama mtu angeniambia wale kina Anna, Judy, Irini, sijui Pamela, Nancy,  Mwajuma, Latifa, Fina, Lina wanaweza kuja kuwa mimi nikakaa ofisini nikafanya kitu kinachoweza kuonekana, nisingekubali. Nilishapotea kabisa katika ulimwengu mingi tofauti, tofauti.” Tunda aliongea taratibu huku ameinama akichezea vidole vyake.

“Sikuwahi kujua kama kuna siku naweza kula chakula kwa pesa ninayoweza kutengeneza kupitia kuajiriwa kihalali na si kwa kutumia kulala na watu, tena wengine walevi, wavuta bangi, wengine wachafu huwezi hata kuvumilia harufu zao, nisingeamini. Nashindwa kujielewa kama huyu tena sasa hivi kwenye huu mwili wangu kama ni mtu mwingine kati ya wale watu wengi ambao wanaishi kwenye huu mwili wangu au la!”

“Nikiwa peke yangu naogopa nasema itakuwaje wale watu wengine kina Nancy wakaamua kurudi tena, wakaishi? Nina hofu ya kurudia yale maisha Net. Pesa mnayonilipa wewe na mama yako kwa kuwafanyia kazi mwezi mzima, nilikuwa na uwezo wakuitengeneza hata ndani ya siku mbili, au moja. Inategemea na mtu niliye naye. Lakini siyo maisha ninayotamani kuja kurudia Net. Yanatisha.” “Unao uwezo wakutorudia tena Tunda.” “Sidhani kama ni uamuzi wangu Net. Sijui.” “Kwa nini unasema hivyo?” Tunda alifikiria kidogo kisha akacheka na kuguna.

“Unajua watu wote wananilaumu kwa nini nililala na mume wa mama yangu. Najua hata wewe utakuwa huelewi. Lakini hakuna mtu hata mmoja aliyewahi kuniuliza ilikuwaje! Hata baba mwenyewe hakuniuliza. Kila mtu ananilaumu na kunishangaa.” “Ilikuwaje Tunda?” “Kwa nini unaniuliza leo Net, wakati ulinifahamu muda mrefu tu?” Tunda akauliza kwa upole huku akijifuta machozi.

“Kumbuka hatufahamiani Tunda. Nimekufahamu kwa kutambulishwa na watu. Na kote nimekuwa nikitambulishwa majina tofauti tofauti, nimeamua kubaki na la Tunda, kwa kuwa ndilo nililotambulishwa na ndugu zako. Na kila nilipokutana na wewe nilikuta upo kwenye matatizo makubwa sana, au tuseme mazingira ambayo hayakuniruhusu hata kukusalimia kwa kukushika mkono. Nina habari zako nyingi na nasikitika zote ni mbaya na ni za kuogopesha.” Net akaendelea.

 “Sijui nauliza nini naacha nini? Nashindwa naanzia salamu kwa kukushika mkono kwanza ndipo nikuulize jina lako, au nijipe muda labda ipo siku nitajua wewe ni nani! Nina hofu sijui mwisho wa yote hayo naishia kumfahamu Tunda, au Judy! Yeyote yule sasa hivi aliyepo ndani yako sikuwa na ujasiri wa kukimbilia kukuuliza  ilikuwaje ukawa na mahusiano na baba yako wa kambo, wakati nina maswali makubwa sana na ya msingi nilitaka kujibiwa kabla ya swali kama hili ambalo nilijua nikipata majibu ya maswali ya msingi, mengine yangejijibu yenyewe.” Net akaendelea.

“Huwa sipendi na ninahofia sana kufikia mwisho wa maamuzi ya jambo lolote lile maishani mwangu, kwa kuwa ninatatizo la kutosahau na huwa ni mgumu sana kurudi nyuma. Siwezi na sijawahi. Nikifika mwisho wa jambo, nikakubali kuwa hapo ni mwisho ujue hakuna mwanadamu mwingine anayeweza isipokuwa Mungu ameingilia kati. Kwa kuwa huwa natumia kila kitu Mungu alichonipa katika kukabiliana na mambo yangu, na huwa ni mvumilivu sana.”

“Mpaka mimi nikikwambia nimefika mwisho, ujue hakuna mwanadamu angeweza kuvumilia. Ndio maana naogopa sana kufika kwenye kumuhukumu mtu. Kama ni mwanadamu, nataka kumjua si kwa maneno yake tu bali nataka nimfahamu vile alivyo kwa kuishi naye. Nione na kujua jinsi alipopita mpaka akafika hapo, na kujaribu kuangalia anatumia vipi nafasi ya pili ambayo Mungu amempa? Hapo ndipo nachora mstari, si vinginevyo.” Tunda alikuwa ametulia akimsikiliza Net.

“Leo nimepata ujasiri wa kukuliza kwa kuwa kwanza nimeona umekuwa tayari wewe mwenyewe kuongea. Nimehisi umeniamini, kitu kilichonifurahisha. Sikutaka mimi nigeuke kuwa hakimu wako, kukuhoji. Nilijua ipo siku kama utataka, basi utazungumza na mimi. Lakini sikutaka mimi ndio niwe naanza kukukera na maswali, nilijua utakosa raha. Ndio maana nilikuwa nikinyamaza kabisa.” “Asante Net. Asante sana.” Tunda akajifuta machozi, nakujiona mdogo zaidi. Aliona vile Net alivyokuwa akimfikiria bila majibu. Akatamani kujua mawazo yake juu yake, lakini Net alionekana ni mtu makini sana. Hakuwa mropokaji hata kidogo na alikuwa makini sana kwa kila anachoongea.

“Tunda!” “Abee!” “Nakusikiliza.” Ilikuwa ni mtu wa kwanza maishani mwake kutaka kumsikiliza Tunda, bila hukumu. Tena mtu wa maana, msomi, pesa ipo na tena mwenye heshima kwenye jamii! Japokuwa alijua uozo wake tena kwa kushuhudia, lakini bado alimuonyesha kutaka kumsikiliza. Tunda aliinama kwa muda akaficha uso wake nakuanza kulia kwa uchungu sana.

Alilia sana hapo mbele ya Net nakushindwa kujisaidia. Kimya kimya ila kwa kwikwi. Aliruhusu maumivu yote aliyokuwa ameyaficha moyoni mwake akivumilia akijua kesho itakuwa nafuu, aliyatoa siku hiyo. Alilia bila kunyamaza. Picha ya mapito yake yote tokea utoto mpaka siku  Net anamtoa kwenye mvua na radi ilimjia, na kuendelea kulia. Alipoona anashindwa kunyamaza akaamua kuingia bafuni kuoga.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alitoka akiwa amevaa nguo zake za kulalia nzuri na huku amejifunika shuka. “Nasikia baridi sana. Naomba nilale tutaongea wakati mwingine.” Tunda akapanda kitandani na kujifunika blangeti. Ulikuwa msimu wa baridi kali sana jijini Arusha. “Naweza kukusubiri mpaka utakapo lala.” Net akasogea pale kitandani akakaa pembeni yake. Akabaki akimwangalia Tunda kwa utulivu na macho yake yaliyokuwa yakimpeleka kasi Sera, binamu wa Tunda. Tunda alikuwa ndani ya mablangeti akitetemeka baridi.

Net akavuta blangeti vizuri na kumfunika zaidi. Tunda aliendelea kujikunja ndani ya lile blangeti huku akificha kila kiongo chake ndani, akabakiza uso tu. “Asante.” Net alitoa tabasamu. “Ninayo machine ndogo ya joto, {Space Heater} pale nyumbani, kesho nitakuletea.” “Na wewe utatumia nini?” “Mimi sio muoga wa baridi kama wewe. Jione unavyo tetemeka.” Tunda akatabasamu.

“Unawasiliana na mama?” Net akauliza. “Nilikwambia jinsi alivyoniambia Net. Mama alisema nisikanyage tena nyumbani kwake. Hata hivyo hatukuwahi kuwa na mahusiano yeyote na mama hata tulivyokuwa tukiishi pamoja. Nilimsaidia sana kumlelea yule mtoto wake wa pili, kwa hiyo hapo ilimbidi awe akizungumza na mimi, kunipa maelekezo ya mtoto wake na si vinginevyo. Na hiyo ndiyo sababu kubwa iliyonifanya niwe karibu na mumewe.” Tunda akatulia kidogo.

“Yeye alikuwa akifanya nini?” “Ni nesi. Nilimuacha akifanya kazi katika hospitali ya Muhimbili lakini pia alikuwa na miradi iliyokuwa ikimfanya hatulii nyumbani. Alikuwa akiingia kazini mida tofauti tofauti. Na kama hatakuwepo kazini, basi yupo kwenye biashara au miradi yake. Halafu walikuwa pia na msichana wa kazi naye alikuwa akiishi humo humo ndani. Ila alikuwa muhuni sana. Hatulii ndani.  Mama alipokuwa akiondoka na yeye alikuwa akiondoka, anaaga labda anaenda kusuka au dukani. Na akitoka hapo kurudi ni majaliwa.”

“Sasa huyo baba hakuwa akimuuliza?” Net akaendelea kudodosa japo alishaambiwa wataendelea wakati mwingine. Ila alikusudia kujibiwa usiku huo. Akaendeleza taratibu. “Hapana. Ndio muda na yeye alikuwa akiusubiri kwa hamu sana. Kwani ndio tulikuwa tukibaki naye. Mimi na yeye tu.” Tunda akatulia kidogo.

“Hatukuanzia kwenye kufanya mapenzi moja kwa moja! Alihakikisha anajenga mazoea ambayo hakuna mtu alimtilia mashaka. Alimuonyesha mama kuwa ananipenda kama mtoto wake. Kutoka katika mateso makali ya mama wa kambo, nikaangukia kwenye mikono ya baba wa kambo aliyekuwa akinipakata na kunitekenya wakati wote.”

“Nilikwambia nilitolewa kwa baba nikiwa nusu mfu kwa kupigwa. Baba alikuwa na mtoto mwingine aliyekuwa akiitwa Chale. Yule mtoto alikuwa mwizi Net, hawezi kujisaidia. Alikuwa akiiba kila pesa anayoona mbele yake. Sasa mara ya mwisho aliiba pesa kwenye pochi ya mama yake, akanisingizia mimi. Na yule mama alikuwa akijua kupiga, na ana mkono mwepesi sana. Basi. Alinipiga siku hiyo zaidi ya siku zote, wakaenda kunitupa nje, majirani wakanipeleka hospitalini. Bibi akaja kunichukua, nakunirudisha kijijini.” Tunda akatulia kidogo.

“Kosa alilolifanya bibi, akiwa na nia nzuri, akampigia simu huyo mume wa mama ambaye hata hakuwa akijua kama mama ana mtoto mwingine.” “Kwani hamkuwahi kuonana?” Net akauliza.

“Alishawahi kufika kijijini wakati anamlipia mahari mama, akanitambulisha kama mimi ni mdogo wake.” Net akashangaa sana. “Basi. Bibi akanitambulisha kwa yule baba mbele ya mama, akitaka wawe wanatuma pesa za matumizi angalau kila mwezi. Chakushangaza kila mtu mpaka mama, yule baba akanipokea kwa upendo. Akataka nirudi nao mjini ili wanisomeshe.” Tunda akajifuta machozi.

“Huwezi amini hayo mapokezi yake! Alikuwa akinipenda sana. Akiona mama ananigombesha, basi yeye ananibembeleza na kunitetea hata kwa mama, akimuelewesha kuwa mimi bado ni mdogo. Natakiwa nifundishwe. Yale mateso ya kwa mama wa kambo, huku ikawa faraja ya baba wa kambo. Nilikuwa nikivalishwa vizuri. Vyakula vya kila namna ananinunulia. Akiona kama kuna chakula ambacho yeye hajakipenda mle ndani, basi alikuwa akitutoa na Tom, mtoto wao mkubwa, kwenda kula nje. Chips yai na kuku.”

“Wakati mwingine alikuwa akitupeleka sehemu tofauti tofauti zakucheza. Mara nyingi mida ya jioni alikuwa akitupeleka kwenye sehemu zinazo uzwa Icecream. Hata kama ni siku za shule. Anatoka kutuchukua shuleni, anatupitishia mahali kula au kupata icecream. Na ilikuwa hivi, kama dereva hakuwa akitufuata kuturudisha nyumbani, basi ni yeye mwenyewe anatufuata. Tulikuwa tukisoma shule yakulipia, kwa hiyo kama mzazi alitaka watoto wakae zaidi, unaongeza pesa, mnakaa mpaka saa 12 jioni. Hapo mtasaidiwa kusoma na kunakuwa na michezo tofauti tofauti.” Tunda akaendelea.

“Sasa kwa kuwa Tom yeye alikuwa mtundu sana, na alikuwa akicheza mpira wakati mwingi, basi kila alipokuwa akiingia kwenye gari, alikuwa akiishia kulala njia nzima wakati tunarudishwa nyumbani. Na hapo yule baba ndipo alipokuwa akipata nafasi nyingine nzuri ya kunichezea ipasavyo. Kumbuka nilikuwa darasa la nne, sio mkubwa sana, lakini nilikuwa nikielewa kiasi. Mwanzoni nilikuwa nikifikiri ni mchezo aliokuwa akicheza akitutekenya mimi na Tom hata mbele ya mama, lakini niliona mimi inaanza kuwa tofauti.”

“Akijua jioni hiyo mama haingii kazini, atalala nyumbani, basi lazima atakuja kutufuata yeye shuleni. Akijiridhisha Tom amelala kabisa kwenye gari, alikuwa akisimamisha gari pembeni ya barabara na kuniambia nifungue mkanda niruke kiti cha mbele, kisha anaanza kunichezea. Alianza kwa kunisifia nimeanza kuwa mkubwa nimuonyeshe matiti yangu huku akinitekenya na kujifanya anashika juu ya gauni na kucheka cheka.”

“Siku ambazo tupo nyumbani mama hayupo, akawa anataka niwe nakwenda kuangalia tv chumbani kwake. Na kwa kuwa nilikuwa nikifeli sana shuleni, basi alitaka niwe nafanya kazi za shule pembeni yake. Kumbuka nilitoka kijijini sijui kuzungumza hata Kiswahili. Nikapelekwa kwa baba, nikaishi huko miaka miwili ya mateso. Darasani wanafundisha Kiswahili kitupu na kingereza. Nimetolewa hapo darasa la nne, sijajifunza chochote kwa hiyo miaka miwili. Nikahamishiwa kwa mama, nikapelekwa shule ya kingereza kitupu. Hakuna hata wakumuomba maji ya kunywa kwa kilugha au kiswahili. Nikajua kuongea kingereza kwa mawasiliano tu, lakini hakuna ninachoeleweka darasani. Kumbuka hapo nipo darasa la 4 ambalo ilibidi nirudie, sababu kwanza sikufanya mitihani ya kitaifa ya darasa la nne  kuingia la tano kule kwa baba. Mkewe alinipiga na kunivunja mkono huu wa kulia.” “Tunda!” Net akazidi kushangaa.

“Kweli Net. Mama Chale au mke wa baba, alikuwa mama wa nyumbani, halafu baba yeye anakwenda kazini asubuhi mpaka usiku, hapo bado safari za kikazi za baba. Kwa hiyo nikaishia kulelewa na mama wa kambo, huyo mama Chale. Alikuwa akinitesa yule mama, siwezi kusoma wala kufikiria. Kwenda shule ni siku ambazo anaamua yeye. Mateso, akili ikawa haitulii kabisa. Nilikuwa kama mwehu kwa hofu. Akinikuta nimekaa sehemu, kosa. Atanipiga wee na kunipa kazi. Nikifanya asivyopenda yeye, pia kosa. Atanipiga tena. Wenzangu walifanya mitihani ya darasa la nne, mimi mkono umefugwa POP kwa kipigo.” “Pole sana Tunda.”

“Asante. Haya, sasa huku kwa mama nako sina nilichokuwa nikielewa. Nafeli kwenye hiyo shule ya kingereza kitupu. Ndio yule baba naona akapata mwanya huo. Akamwambia mama yeye atakuwa akinisimamia masomo. Yaani ni kama alikuwa akijitengenezea njia yakutoshtukiwa. Basi ikawa inajulikana kwamba kila nikitoka shule, lazima baba anisimamie kufanya homework zangu.”

“Hapo sasa ikawa inategemea na ratiba ya mama au alipo yule msichana wa kazi. Inaweza kuwa sebuleni kama tupo mimi na yeye tu au chumbani kwake. Kama nilivyokwambia. Tom alipenda sana mpira. Kila alipokuwa akitoka shule, alikuwa akiingia mtaani kucheza. Yeye hakuhimizwa kufanya homework. Alikuwa anataka awe anatoka hapo ili atupishe. Na yule msichana ni kama nilivyokwambia kuwepo kwake nyumbani ni mpaka ajue mama yupo au anakaribia kurudi nyumbani.”

“Na ikitokea msichana wa kazi yupo hapo nyumbani, basi hiyo homework tunaenda kufanya chumbani kwao. Eti nikiwa na elimu ya darasa la pili ya kijijini, unipe homework niliyofundishwa kwa lugha ya kingereza darasani! Mimi niliyekuwa nikizungumza kipogolo tu! Hata Kiswahili sikuwa naongea vizuri. Kwanza niseme sikuwa nikikijua. Nilikwenda kukijua kule nilipopelekwa kwa baba. Nilijifunza Kiswahili kwa kupigwa. Alidhani ni kiburi, kumbe sikuwa na muelewa. Ndio msichana wa kazi akamwambia simuelewi. Ndio kipigo kikageuka kuwa mimi ni mjinga, mzito kuelewa.” “Jamani!” Net akashangaa.

“Sasa eti kwa hali hiyo nikaanza hiyo shule ya kingereza, bila msaada wa mtu. Mama ni mkali, baba anamalengo yake. Usifikiri hata hiyo homework basi alikuwa anania nifanye?” “Hakuwa akikusaidia?” “Hata kidogo Net. Ukitukuta chumbani, ujue mikono yake kama haipo kwenye maziwa yangu, basi ataniambia nilale kama naandika. Yaani nilale kifudifudi. Niweke daftari mbele. Yeye atakaa huko nyuma yangu. Atanifunua gauni mpaka kiunoni, ataanza kunichezea. Anakwambia usihangaike tulia tu. Atakuchezea hapo, wakati mwingine anaweza akanitoa hata chupi kabisa ananichezea tu.”

“Mwanzoni hakuwa akiniingilia. Ananichezea tu. Ila alikuwa anapenda sana sauti yangu na nimwangalie. Kwa hiyo alipokuwa akifika juu sana, ananiambia nimwite dad, dad, mpaka amalize. Hapo sasa anakuwa amenitoa kitandani, amenipakata. Mikono kwenye sehemu za chupi nyuma. Ananiminya minya.” Tunda aliogopa kusema makalio. Lakini Net akaelewa.

“Halafu huku ananinyonya tumaziwa twangu. Basi hapo utamwita dad taratibu huku anakuchezea mpaka anamaliza. Na usifikiri anamaliza ndio inakuwa basi. Anaweza kwenda kuoga. Anakwambia endelea na kazi za shule wakati akioga. Niambie Net, hapo utasoma tena?” “Huwezi. Pole Tunda.” “Nilikuwa nashindwa. Hasira. Na akitoka kuoga anapumzika kidogo, na mikono yake anapopumzika inakuwa mwilini mwako. Akikuvua nguo ya ndani, ujue hutaivaa tena mpaka akuruhusu utoke hapo chumbani kwake. Na ujue hapo sio kitu cha muda mfupi. Ni mpaka aridhike kweli kweli.” Tunda akajifuta machozi.

“Akaanza kuzoea ile tabia. Baadaye akaanza kuniita usiku chumbani kwake wakati watu wote wamelala, mama yupo kazini, kisha anavua nguo na kunifundisha vitu vya kumfanyia. Nilipomwambia naogopa, aliniambia vile mama yangu asivyonipenda, hataki niwepo pale, yeye ndiye aliyenitoa kijijini na anauwezo wakunirudisha kwa baba yangu kama sitamfurahisha.”

“Akawa ananiambi kukaa kwangu pale, kunategemea na kumfurahisha kwangu. Mama alikuwa akijua kunitukana Net! Bila aibu wala huruma, hata mbele za watu alikuwa akinitukana. Ndio ikawa silaha ya yule baba Tom. Akawa ananikumbusha vile ambavyo mama yangu hanipendi. Na vile nilivyoteswa kule kwa baba yangu. Akawa ananiambia yeye ananipenda. Hata hayo macho mama anayoyaita ni ya paka na kuyachukia pamoja na weusi wangu, yeye anavipenda ndio maana anapenda nimwangalie na nimwite dad.”

“Aliniahidi kunipa vitu vingi, kama nikimfanyia kile anachotaka na kweli alikuwa akininunulia vitu. Basi. Nikaanza kujifunza jinsi ya kumfanyia anachotaka. Sina mtu wa kuniuliza hata ninaendeleaje! Hakuna anayenitizama usoni kama nina furaha au la. Maisha yangu yakawa ni huyo baba tu. Ndiye anayejua kula yangu, soma, na vaa. Furaha yangu ikawa inategemeana na kumridhisha. Na kweli, akilala ukiwa umemridhisha, utafurahia jinsi anavyokuwa mstaarabu.”

“Kazi yangu ikawa ni yeye tu. Nimejawa hofu na wasiwasi wakati wote. Alianza kunizoeza kumzoea kumtizama akiwa uchi. Akanifundisha mwili wake na viungo vyake ili kuweza kuvichezea, na kumfurahisha. Na mbaya zaidi hakuwa akitosheka. Ukidhani umemaliza, anakwambia unamwamsha zaidi. Labda macho au sauti yangu ndivyo vinamsababisha asitosheke. Hapo inabidi kuanza upya.”

“Maisha yangu kielimu yakawekwa pembeni kabisa. Nikageuka faraja yake. Nikiingia chumbani kufanya homework, anafunga mlango, ananitoa nguo, na yeye anatoa nguo, tv inawashwa kwa sauti ya juu, kazi inaanza mpaka dada aje agonge kuwa chakula kipo tayari. Hapo ndio anatumwa kwenda kumfuata Tom huko anakocheza mtaani, ili aje aoge, ale, alale.”

“Na usifikiri atakuacha usiku ulale kama mama hayupo?” “Anataka mlale naye!?” Net akauliza kwa mshangao. “Alikuwa anaanza hivi. Nakwenda kulala kama kawaida. Tulikuwa tunatumia chumba kimoja na Tom. Tom akisha lala, anakuja kuniamsha. Tena wakati mwingine ananibeba nikiwa nimelala. Akishanifikisha kitandani kwake, naweza kushtuka kiwa ananivua nguo au anakunyonya sehemu ambayo lazima uamke tu.”

“Ukishaamka tu, anataka uanze kumchezea yeye mpaka aridhike. Na usifikiri ni mchezo wa masaa mawili au ataridhika kwa safari moja! Hapana. Kwa hiyo alikuwa akinimbia niendelee mpaka nikimuona amelala, nimsafishe, ndipo na mimi nirudi chumbani kwangu. Haya, akiwa amekwenda muda mfupi usiku, ujue lazima asubuhi atakuja kuniamsha tena, nimfanyie kabla hajakwenda kazini na mimi hajanipeleka shule.”

“Ikawa ndio mtindo huo. Mama akiwepo nyumbani week mbili tatu mfululizo, alikuwa akitutoa mimi na Tom kwenda kutembea na njiani nilimfanyia hivyo. Au siku za jumamosi ambazo mama yupo nyumbani, alianzisha tuition ambayo hata sikuwa nikienda. Alimwambia mama amenianzishia ili niwe nafundishwa inisaidie kuelewa zaidi. Basi, jumamosi yeye hakuwa akienda kazini. Alikuwa ananichukua, kama hatutaenda ofisini kwake, anaweza hata kunitafutia nyumba za kulala wageni niende nikamchezee huko mpaka jioni, ndio ananirudisha nyumbani.” Tunda akaanza kulia.

“Nilikuwa nachoka Net, sina jinsi nikakwambia ukaelewa.” “Pole Tunda.” “Unachoka mwili mzima. Hulali vizuri. Sehemu pekee yakupumzika ni shuleni. Na ukifika hapo darasani kwa kuwa sielewi hata wanachozungumza, basi nikulala tu. Ukumbuke hapo labda niliamshwa kwenye alfajiri sana ili kumchezea kabla hatujatoka nyumbani. Haya, unaingia darasani umechoka, na hapo unajua jioni akija kukuchukua kazi inaanza upya. Kwa hiyo darasani ikawa ndio kama kitanda. Sikuwa nikielewa chochote kwa usingizi na hofu.” Tunda alitulia kidogo.

“Nilipofika darasa la saba wakati mama amejifungua, alikwenda kwa bibi kama likizo ya uzazi. Mbaya zaidi kwangu, alikwenda na yule msichana wa kazi. Kwa hiyo tukabakia mimi, Tom, yeye na kijana wa kazi ambaye alikuwa akilala kwenye vyumba vya nje. Hapo ndipo niligeuka kuwa mke wa yule baba kihalali. Kila Tom alipopitiwa na usingizi, alikuja kunitoa chumbani na kunihamishia chumbani kwake, na ndipo kipindi hicho alipofanya majaribio ya kuniingilia mpaka alipofanikiwa.”

“Haikuwa kazi ya siku moja Net. Ilinichukua miezi kuja kuweza, na kumudu bila maumivu. Kwa kuwa alikuwa baba mkubwa kimaumbile, usitake kujua maumivu yake.” “Mama yako hakuwahi hata kuhisi!?” Net aliuliza akiwa anamaumivu, mpaka uso ulikuwa mwekundu.

“Nilikwambia mama yangu hakuwa na muda na mimi, Net. Hata hivyo alikuwa busy sana na kazi na biashara zake nyingine. Na yule mzee alikuwa akiniuguza kwa makini sana. Yeye ndiye alikuwa akitupeleka shule kwa hiyo kabla hajanishusha alihakikisha ananipa dawa kali sana zakuzuia maumivu. Kwa hiyo sikuwa nikiishi kwa maumivu, ni pale tu wakati ananifanyia, na labda nikiwa najisaidia. Napo mwanzoni alikuwa akinipaka mafuta. Na akawa ananiambia kila nikioga, nikakikishe napaka mafuta huko chini ili pasikauke, au nisiumie wakati najisaidia. Basi. Mchezo huo ukaendelea.”

“Nilipozoea na yeye akanogewa, akazua ugonjwa ambao ukawa unajulikana pale shuleni. Basi anaweza kuja hata katikati ya muda wa shule, ananiombea ruhusa kuwa ananipeleka kwa daktari wangu. Na ndio akaeleza huo ugonjwa ndio unaosababisha niwe nalala sana darasani na kuwa nikifeli vile. Basi walimu wote wakanichukulia kama nina matatizo.” “Haiwezekani Tunda!” Net akashangaa sana.

“Kweli Net. Basi, akawa anakuja kunichukua. Nakwenda naye alipopaandaa yeye. Atanitumia mpaka achoke au muda wa kwenda kumchukua na Tom. Ndio tunamchukua Tom, na kurudi nyumbani. Alinifundisha kumfanyia hapo hapo kwenye gari. Kwa hiyo anaweza kuja mida ya mchana. Wakati wa chakula. Anakuita nje, unaenda kumfanyia kwenye gari. Alikuwa na gari kubwa. Vioo vya nyuma alivifanya vikawa kama silver kwa nje. Inawakaa. Huwezi kuona ndani. Basi. Mnahamia kiti cha nyuma. Unamuhudumia, akiridhika, narudi darasani na yeye anarudi zake kazini mpaka tena jioni. Hayo yakawa maisha yangu. Sasa hebu fikiria utoke kufanya uchafu kama huo, unarudi darasani, hapo utaelewa nini?” “Huwezi. Pole sana Tunda.”

“Mchezo wake ukaendelea hivyohivyo mpaka nikaja kuvunja ungo. Na yule baba alikuwa hawezi kusubiri Net. Hajui siku za hatari zakushika mimba au siku salama. Yeye anataka kila wakati na ndipo nikapata na hiyo mimba. Kila nilipokuwa nikimwambia naogopa, au nikimsihi tuache huo mchezo tutakuja kukamatwa, alikuwa akiniambia hataweza kuacha tena, na nisiwe na wasiwasi hata mama akitukamata, atanitafutia pakuishi nitakuwa na maisha mazuri.”

“Siku za jumamosi ndio tution ikawa kisingizio chakututoa pale nyumbani, tunahamia nyumba za kulala wageni. Ujue hiyo siku nzima ni kufanya naye mapenzi tu. Atakuchezea siku nzima mpaka aridhike, ndio anakwambia rudi nyumbani. Ananipa pesa, nachukua taksii. Ukifika nyumbani kama baada ya masaa mawili au matatu, na yeye ndipo anaingia. Na akiingia hapo anakuwa mkali kweli kweli. Ataniita mbele ya mama kuniuliza habari za tuition siku hiyo. Kama nimeelewa au nahitaji msaada zaidi. Yaani yeye ndio akawa wakunifuatilia zaidi. Na alikuwa mkorofi kweli. Mama mwenyewe alikuwa akimuogopa. Akianza kufoka hapo, nyumba nzima inatetemeka.”

Tunda akatoka ndani ya blangeti akakaa. Akavua ile nguo nzito ya juu ya kulalia huku amempa mgongo Net. Net akashtuka sana. “Ona huko mgongoni.” Tunda alikuwa na alama nyingi sana mgongoni mwake. “Hata yeye alikuwa akinipiga sana. Siku zile nilizokuwa nikimwambia nimechoka sitaweza kutoka kwenda kufanya naye mapenzi, hapo nilikuwa nikivizia mama yupo. Basi alikuwa akitafuta sababu yeyote ile ilimradi anichape sana, tena mbele ya mama huku akitutishia mimi na mama atanifukuza mle ndani. Mama naye alikuwa akiniongezea kwa kosa hilo atakalokuwa amechagua baba Tom siku hiyo.”

“Kama ni kuvunja kioo cha dirisha au glasi, basi ilimradi tu. Lakini sikuwa na jinsi Net. Kunakipindi mwili ulikuwa ukichoka. Nilikuwa mtoto na yeye alitaka niwe nikimuhudumia kila siku. Kumbuka mimi sikuwa nikipata ladha yeyote, kwa hiyo nilikuwa siishiwi vidonda. Kwa kuwa nilijua hatanifukuza, nilikuwa nikiwageuzia mgongo wanipige mpaka wachoke ilimradi angalau nijiuguze, vile vidonda vipone, ili tukianza tena nisiwe naumia.”

“Na nilipovunja ungo kila nilipokuwa nikijaribu kumdanganya nipo kwenye siku zangu haamini mpaka ahakikishe. Kwa hiyo pia nikawa najikata hata kidole napaka kwenye pedi kumdanganya nipo kwenye siku zangu, ilimradi nipumzike kuingiliwa. Labda nimchezee tu aridhike au aniache kabisa.”

“Nilipofika kidato cha kwanza nikaamua kuachana na huo mchezo na nimwambie mama, nilikosea sana nilipomwambia nia yangu. Akaniwahi kunisemea kwa mama kuwa usiku uliopita wakati mama yupo kazini, nilitoraka nyumbani sikurudi mpaka asubuhi hiyo.”

“Jamani sitakaa nikasahu kipigo alichonipa yule mwanamke nakunifungasha mpaka kwa shangazi yake. Sio bibi. Shangazi yake ambaye hata sikuwa namfahamu. Kijijini huko, hamna hata umeme. Nilikaa huko karibia mwezi. Hamna chakula, hali mbaya hata maji ni shida. Nikajua mama alinipeleka kule makusudi. Halafu huyo shangazi yake mwenyewe alikuwa mzee, hajiwezi. Lakini ikabidi kukaa hivyohivyo.”

“Nikaishia kuja kuchukuliwa tena na yule yule baba na hapo ndipo hapo aliponihakikishia sina haki juu ya huu mwili wangu, isipokuwa yeye. Net! Yule baba alinifanya vile atakavyo. Yeye alipanga ni muda gani na wakati gani atumie huu mwili wangu. Huku akinihakikishia kuwa yeye ndio aliyebaki kuwa mkombozi wangu. Na ndipo nikashika na hiyo mimba.” Net alivuta pumzi kwa nguvu na kufikicha macho yake. Alinyoosha mkono na kushika yale makovu ya majeraha ya Tunda mgongoni kwake, taratibu sana kama anayefikiria kitu. Tunda alisikia faraja ya ajabu. Machozi yalikuwa yakimtoka kama mvua.

          Japokuwa kulikuwa na baridi sana, lakini alitamani Net asitoe mkono wake mgongoni mwake. Net aliendelea kupitisha vidole vyake taratibu mgongoni kwa Tunda, akishika kila kovu taratibu. “Pole sana Tunda.” Alijibiwa maswali yaliyokuwa yakimsumbua kwa asilimia 90. Alimrudishia lile shati  bila Tunda kugeuka, kisha Tunda akavaa vizuri ndipo alipogeuka na kujilaza tena. Net akamfunika tena kila mahali, kisha akajinyoosha pembeni yake akalala pembeni yake, huku akimwangalia.

“Tunda!” Akamwita taratibu. Tunda akanyanyua uso  kidogo kutoka kwenye blangeti na kumtizama Net, kwa macho yake yaliyokuwa yakimchanganya sana Net tokea siku ya kwanza alipomuona. “Ulishaenda kumuona baba gerezani?” “Sijamuona tena tokea siku ya mwisho aliponiacha pale hospitalini. Hata sijui yupo gereza gani!” “Kwa nini hukutafuta kujua?” “Wazo lilinijia Net. Nilitamani sana kumtafuta, japo kumwambia nilitoka hospitalini, na kumuonyesha ninaendelea vizuri. Lakini niliogopa.”

          “Kwa nini uliogopa tena?” Net hakuwa anaelewa.  “Kwa kuwa aliniachia pesa ndogo sana Net. Nilijua angeniona tu na hali ile angekuwa na maswali mengi ambayo nisingekuwa tayari kuyajibu. Mojawapo najua angetaka kujua nafanya kazi gani, na mimi sikutaka kumdanganya mwanadamu mmoja tu aliyenipokea maishani mwake vile nilivyo. Tena wakati wote tumekutanishwa kwenye mazingira ambayo yote nimekamatwa na uhalifu, na pia sikutaka kumwambia ukweli wa maisha machafu niliyokuwa nikiishi kuhofia kumuongezea machungu akiwa gerezani. Niliona ni heri niache tu.” Net akatulia kidogo kama aliyeridhika na ile sababu.

Kisha akauliza tena. “Ulikwenda wapi baada ya kutoka hospitalini?” “Naomba nisikwambie Net. Tafadhali.” “Kwa nini?” “Inatosha.” Net akabaki akimwangalia Tunda, Tunda akajifunika vizuri na kuficha uso wake, akabakiza sehemu ndogo sana ya macho ambayo hakutaka kumtizama tena Net, akaangalia chini.

          “Nikwambie siri yangu?” Tunda alishtuka sana. “Uniambie mimi siri yako?!” “Ndiyo wewe Tunda.” Tunda akiwa na wasiwasi asijue ajibu nini, akaamua anyamaze. “Ushajiuliza ni kwa nini tunapokuwa ofisini mara kwa mara napenda usiwe unanipa ujumbe kwa simu, bali uje ofisini kwangu wakati kuna simu ya mezani unaweza kunipigia tu tukaongea?” Swali lilikuwa gumu sana kwa Tunda ambaye hakuwahi kufanya kazi kwenye ofisi yeyote. Yeye mwenyewe Net ndiye aliyemfundisha kazi kwa mara ya kwanza.

“Sijui Net! Mimi nilijua ndivyo inavyokuwa. Sijawahi kufanya kazi ofisini.” “Basi huwa wanatumia simu kuwasiliana watu wakiwa ofisini, labda iwe kuna kukabidhiana kitu ndipo watu hutembeleana kwenye maofisi yao.” Tunda akajivuta kidogo nje ya blangeti kwa mshangao.

“Wewe unafikiri kama bosi ni mmoja na anawatu kumi au ishirini chini yake, halafu wote wakitaka kuuliza swali, au kumpa taarifa wanamwendea ofisini kwake, si hiyo ofisi ya bosi ingekuwa imejaa watu kila wakati na angeshindwa kufanya kazi? Ndio maana pia kuna email,{barua pepe}. Kwa hiyo kila mwenye swali lisilo na haraka au ripoti zote hutumwa huko ili bosi ajibu anapopata nafasi.” Tunda akatabasamu kama aliyepata wazo.

“Basi na sisi tuanze hivyo!” Net akacheka. “Mimi sikukufundisha hivyo Tunda. Nilikwambia kila ukiwa na swali uwe unanifuata ofisini kwangu.” “Kwa nini sasa!?” “Ndio swali na mimi nimekuuliza muda mfupi uliopita. Kwa nini unafikiri ninataka uwe unakuja ofisini kwangu na sio kunipigia simu au kuniandikia ujumbe?” Tunda akafikiria kidogo huku akitabasamu kama anayetaka kucheka. Net aliweza kuona meno yake mazuri, yaliyokuwa yanang’arishwa zaidi na rangi yake nyeusi.

Akamgeukia Net. “Sijui.” “Unataka kujua?” Tunda akatingisha kichwa kukubali huku akicheka. Tunda alikuwa na uzuri wa aina yake, hasa anapotulia, akiwa na furaha hakuchosha kumtizama.

“Kwa kuwa huwa napenda nikiongea na wewe uwe unanitizama, Tunda. Napenda kukuangalia.” Tunda alishtuka sana, akajificha tena uso kwa mikono yake nakuanza kurudi ndani ya blangeti. Katika watu ambao hakuwafikiria hata kuwatega ni Net. Alimuogopa sana tokea mwanzo kitu kilichomshangaza hata asijue ni kwa nini amuogope Net, wakati hakuwa akimfahamu hata kidogo.

          “Napenda sana macho yako Tunda. Napenda kukuona mara kwa mara, lakini usifiche macho yako. Napenda kuona macho yako yakinitizama mimi. Sipendi ninapozungumza na wewe uangalie pembeni. Nataka unitizame mimi. Kwa hiyo nimekupa siri. Ukitaka kuniadhibu ufanye kama hivyo ulivyofanya sasa. Nataka uwe ukinitizama kila tunapoongea ndio nafurahia maongezi yetu.” Tunda aliogopa sana. Hakujua baada ya kutoka pale alipojificha, atamtizamaje tena Net. Wakatulia kidogo.

Net akaendelea. “Nimekuuliza swali Tunda. Ulipotoka hospitalini ulikwenda wapi?” “Net jamani!? Bado tu unataka kujua? Nilimekuomba nisikwambie. Naomba nisizungumzie hilo. Tafadhali.” Tunda alikuwa ameinama. “Kwa nini?” Tunda alibaki kimya. “Tunda!?” “Abee.” Tunda akamtizama.

“Ujue unaongea na mimi, sio mtu mwingine? Huna cha kuficha kwangu.” “Itasaidia nini, Net?” Tunda akauliza kwa upole huku akimtizama. “Bila ya kuniambia, siwezi kujua jinsi yakusaidia. Nataka kufahamu kila kitu. Tafadhali usinifiche au usibakize kitu. Nataka kusikia kutoka kwako wewe mwenyewe.” Tunda alivuta pumzi huku akionekana kujishauri. Mwishowe akaamua kumaliza tu, kwani ni kama alishaongea kila kitu. Na kweli hakuwa na chakuficha kwa Net, aliyefanikiwa kumfahamu kwa majina yote, wakati wengine walimfahau kwa jina moja moja tena ya uongo. Hata hivyo Net ndio ameshika mpini wa maisha yake kwa wakati huo. Aliona amalize tu, aone mwisho wake.

“Sikujua pakwenda Net. Baba aliniachia pesa chache sana. Ilinitosha nauli na kula siku chache. Nilipotoka pale hospitalini nilikwenda kula kwenye kibanda kimoja cha chips pale pale kituo cha Mwenge, ndipo nilipokutana na mmiliki wa pale au mkewe ndiye aliyekuwa mmiliki. Nilipojua anapesa na anasehemu nyingi za biashara, nikajua atanifaa.” Tunda akanyamaza.

“Nakusikiliza Tunda.” “Nimemaliza.” “Sijaelewa chochote. Nimeishia upo kwenye kibanda cha chips.” “Kumbuka historia yangu Net. Maisha yangu yote sikuwa na elimu bali ujuzi niliokuwa nimepata kutoka kwa baba Tom. Mapenzi. Ndipo nikaamua kutumia huo uzoefu wangu kuishi mjini.” Tunda akaanza kulia.

“Nilikuwa silali Net. Kazi yangu ilikuwa kutongoza wanaume mchana na usiku! Nilikuwa nikilala na wanume hata watatu kwa siku, na wengine ilikuwa sio lazima kufanya nao mapenzi, nilikuwa nikitumia utundu wangu tu kuwaridhisha ilimradi kupata pesa ambazo sijui hata zilikuwa zikiishia wapi! Nilikuwa nikinunua mavazi ya gharama ili kupata wateja wa maana.”

“Nilitaka kulipa machungu kwa kuishi nyumba nzuri na kununua vitu vya kisasa ili kulipiza kisasi kwa manyanyaso yote niliyopitia, lakini haikusaidia hata kidogo. Ukweli nilikuwa nikipata pesa ndiyo, lakini nilikuwa nikiteseka sana. SANA.” Tunda akatulia kidogo. Akafuta machozi.

“Nimefanya mambo ya ajabu hapa duniani! Wakati mwingine silali kwa hofu na ndoto mbaya. Huyo mwanaume wa kwanza niliyemtongoza baada ya kutoka hospitalini, nikakwambia nimfanyabiashara mkubwa lakini Net, kuna maajabu huku duniani, hujawahi ona. Watu wanahangaika kupata pesa, mpaka unaweza usiamini.” “Vipi?” Net akauliza.

“Yule baba alinitoa pale akanipa maisha. Lakini nililipia Net. Na sijui nilikuaje. Ni kama akili yangu ilibadilika! Nakwambia sasa hivi silali sababu ya hofu, utafikiri siye mimi nilifanya.” “Ulifanya nini?” “Ushirikina.” “Ushirikina!?” Hilo mzungu Net akawa hajalielewa

“Uchawi ule wa hali ya juu! Usiku badala yakulala, tulikuwa tunakwenda makaburini kufanya ibada za kichawi.” Mpaka mwili wa Net ukasisimka. “Na usifikiri mnaenda tu? Hapana. Mnafanya mambo ya ajabu Net. Mnaita majini mpaka majoka yanatokea. Mnafanya hiyo ibada mpaka yaondoke. Haya, wakati mwingine mnakwenda kwa huyo mganga mwenyewe. Usiku Net. Giza. Mtakaa huko mpaka pakaribie kupambazuka. Tena mpo ndani ya mto huko, chini ya miamba. Giza, mnafanya ushirikina. Mpaka alipokufa.” “Kufa tena!?” Net akashtuka. Tunda akamuelezea mkasa mzima wa Sadiki na kumuacha Net hoi.

“Ilikuwa ni shida Net! Nimeishi kwa kuhangaika sana, mpaka wewe uliponitoa mvuani nikijificha kwa hofu ya radi.” “Daah! Pole sana Tunda.” Net alitulia kama anawaza.

Akamfuta machozi. Akamgeukia vizuri. “Hivi Tunda, unajua unaweza kubadilisha hayo maisha ukaamua kuishi wewe kama wewe na ukaweza kuwa mtawala mzuri wa maisha yako?” “Sidhani Net. Mimi mwenyewe sijijui mimi ni nani!” “Ukitaka kujitambua unaweza Tunda. Na ukawa kiongozi mzuri sana wa maisha yako. Unaweza ukajiamuru kuwa na maisha mazuri na matulivu. Najua au tuseme nimeelewa mazingira uliyopitia tokea unazaliwa, yamekupelekea kuishi maisha uliyoishi. Lakini Mungu amekupa nafasi ya pili. Nafasi ambayo hukustahili, lakini Mungu amekupa. Kubali kubadilika ili uitumie vizuri.”

“Mbona nimeshaanza kubadilika?” “Kweli Tunda?” “Sijalala na mwanaume tokea…” Tunda akafikiria. “Hujalala na mwanaume kwa kuwa yeye alikukataa Tunda, sio wewe ndiye uliyekataa. Hebu fikiria kama siku ile Gabriel angekukubali akakupokea, sasa hivi ungekuwa wapi?” Tunda akajifunika na kuanza kulia.

“Usinifikirie vibaya wala sina nia ya kukuumiza ila nataka kukuelimisha kwa kukufungua macho. Upo hapa ulipo kwa kuwa mimi nilikutoa pale. Je, kama na mimi ningetaka kulala na wewe sio kukusaidia, au tuseme kama ningekutoa pale nikakuweka hapa hotelini nikaanza kukutumia kama wanaume wengine, ungekataa?” Ulikuwa ukweli mtupu ambao Tunda aliogopa hata kumtizama Net.

“Inamaana mpaka sasa, ningekuwa na wewe nikiutumia mwili wako kwa furaha zangu, na wewe ukiteseka moyoni na mwilini, ilimradi tu utengeneze pesa! Kwa hali niliyokukuta nayo siku ile, maisha hayakukupa uhuru wa kuchagua kitu gani ufanye ni wewe kupokea kitakacho kujia. Au niambie ukweli Tunda, ikitokea nakufukuza kazi sasa hivi, utaenda wapi? Huna cheti hata cha kidato cha nne. Unafikiri akitokea mtu kama Gabriel akakupokea tena mtaani baada ya mimi kukufukuza kazi hapa, je utamkataa?” Tunda hakujibu, akaendelea kulia.

Net anampa nafasi nyingine Tunda.

Net akaendelea. “Ndio maana nakuambia hii ni nafasi ya pili Mungu amekupa Tunda, anataka uanze upya. Usikubali kuiachia.” “Mungu mwenyewe hata simjui, Net!” “Ukikubali, mimi nitakufundisha. Lakini lazima ukubali wewe mwenyewe kwanza. Na usikubali kwa kuwa mimi ndiye ninayekwambia, hapana. Pata muda wakufikiria kwanza. Na hata ukisema hapana, siwezi kukuchukia na sitaacha kukuombea. Lakini nakuhakikishia ni maamuzi ambayo hutakaa ujute.” Kidogo akamchanganya. “Ulikuwa ukiniombea Net?” Tunda akauliza kwa upole sana huku akimtizama Net na uso uliojaa machozi, nakumfanya atabasamu.

“Wewe ni mzuri sana Tunda, hutakiwi kuchezewa na watu. Thamani yako haipo kwenye nyumba unayoishi au kiasi cha pesa unachomiliki au elimu uliyonayo. Usikubali mtu akakwambia vinginevyo.” Tunda hakuwa akiamini. “Hata wakikutupa jangwani bila kitu chochote, thamani yako inabaki palepale.” “Unaongea na mimi, Net! Au umesahau?” “Nimekwambia huwa sisahau kitu. Na hilo ndilo tatizo langu.”

“Sasa hiyo thamani naitoa wapi? Sina thamani yeyote ile Net. Sipo huru kwenda popote tena. Sina mtu anayeweza kunisaidia hivi au hata kunisikiliza zaidi yako. Tena hata wewe sikuelewi, Net! Jinsi ninavyo kudhalilisha, aibu ninayokutia! Kweli sikuelewi! Mimi mwenyewe nimechoka, nimeamua kujifungia humu ndani. Maana kila ninapoenda naishia kudhalilika tu. Kama sitakutana na watu niliokwisha lala nao, basi nilishawahudumia kimapenzi kwa namna moja au nyingine.”

“Kwa kuwa najua kuwa, kila mtu ananafasi ya pili, hapa duniani. Unayo nafasi ya kuanza upya Tunda. Upya kabisa wewe mwenyewe. Haijalishi nini umefanya kwenye maisha yako, unaweza kuanza upya na Mungu asikumbuke kabisa ulichofanya. Hata kama wanadamu tutakumbuka, lakini si kwa Mungu ambaye ndiye wa muhimu sana. Atakusamehe, atakutakasa, atakupa furaha ya ajabu moyoni kwako. Atafanya upya nafsi yako na roho yako pia.” “Kwani na mimi nina nafsi kweli!?” Net akacheka.

“Sitanii. Nahisi hivyo vyote vitakuwa vilishakufa au mwenye navyo, huyo Mungu alishavichukua.” “Unanafasi ya pili Tunda. Yakupatanishwa na Mungu. Fanya maamuzi sahihi. Atakurejeshea vyote ambavyo shetani alivichukua.” “Umesema utanisaidia?” “Kwa asilimia mia moja. Sitakuacha hata kwa hatua moja.” Tunda alifurahi sana.

“Asante sana Net. Sasa ndio natakiwa nifanyaje?” “Swali zuri sana. Kwanza nataka kujua kama upo tayari.” “Umeniambia nijaribu. Nataka nijaribu na mimi nione.” “Najua sasa hivi umechoka. Naomba nikuache upate muda wa kupumzika, kisha kesho nikupeleke kwa mtu atakayekuambia nini chakufanya.” “Kesho huendi nyumbani?” “Tutaenda wote Dar, na huko ndiko nitakupeleka kwa mtu atakayekwambia chakufanya.” “Net!” Net alikuwa akivaa viatu ili atoke. Tunda akakaa.

“Asante kwa kila kitu. Asante sana.” Net akatabasamu. “Asante kushukuru, na mimi asante kwa kuniamini na kuniambia kila kitu tena kwa uwazi.” Tunda akafikiria kidogo. “Nikuulize kitu Net?” “Uliza tu.” “Baada ya kujua uchafu wangu wote niliofanya, unanifikiriaje?” “Ninafikiria hiki unachotaka kufanya sasa hivi Tunda, sio maisha uliyoishi zamani. Wewe hukupata nafasi ya kulelewa kama wengi wetu. Hukubahatika. Ila sasa hivi umekubali kupokea nafasi mpya kwenye maisha yako, tena ukiwa na mimi niliyekuahidi kuwa na wewe katika kila hatua ya maisha yako, hilo tu ndilo linanipa nafasi ya kuweza kuongea kitu juu ya maisha yako, si vinginevyo.” Tunda hakuamini, akabaki ametulia tu akimwangalia kama asiyemsadiki.

“Nina kusifu Tunda. Ikifika kesho kama sasa hivi, utakuwa kiumbe kipya kabisa. Pata muda wakupumzika kesho tutaongea vizuri tukiwa njiani.” Net akaondoka akamwacha Tunda akiwa amelala, kwani alikumbuka Tunda alivyomwambia kuwa, huwa anapata usingizi pale anapokuwa naye. Alirudi kukaa pembeni yake, akawasha tv akiwa bado amevaa viatu. Tunda alibaki akishangazwa na Net alijua. “Pumzika, ulale. Nataka nikuache ukiwa umelala.” Tunda alitoa tabasamu zuri, lililofanya azidi kuvutia. “Asante Net.” Alijirudisha ndani ya yale  mablangeti na shuka, huku Net akimsaidia kumfunika vizuri. “Usiku mwema.” “Na wewe Net.” Tunda akalala na ndipo Net naye alipoondoka.

 

Tunda akiwa safarini kuanza maisha mapya.

Wakiwa kwenye ndege kuelekea Dar, Net alimueleza Tunda umuhimu wakuanza upya na faida nyingi atakazopata katika hayo maisha aliyoyachagua. “Naona kama ndege inachelewa, natamani kufika haraka!” Net akacheka. “Lakini kwanza tunapitia nyumbani.” “Kwa mama yako!?” “Tena atakuwa akitusubiri uwanja wa ndege. Amefurahi uamuzi uliofikia, akaomba tupate muda wa pamoja mfahamiane kwanza kabla ya kwenda kwa Mchungaji. Ni sawa?” “Hamna shida, ndio vizuri na mimi nimfahamu bosi wangu. Tumekuwa tukizungumza kwenye simu tu. Na mimi nitafurahi kumuona. Yeye ni mzungu?” Swali la Tunda lilimfanya Net acheke sana.

“Nini sasa?” “Hapana bwana. Mama yangu ni Mtanzania. Baba ndiye alikuwa mtu wakutokea Canada.” “Sera alikuwa akiringa kuwa anaolewa na Mzungu.” “Mzungu gani?” “Si wewe?” Net akazidi kucheka. Alikuwa kijana mstaarabu sana na muungwana. Alijaliwa utulivu ambao mtu yeyote angetamani kuzungumza naye.

“Hakuwa amenielewa vizuri. Nilijitahidi sana kuwa muwazi kwake na sikuwahi kumuonyesha hisia zozote za kimapenzi. Sijui kwa nini alifikiria ndoa!” “Atakuwa alikupenda sana.” Net akamtizama Tunda. “Nini sasa? Kweli! Sera alikupenda.” Net akatabasamu kisha akapotelea mawazoni.

“Net! Nikuulize swali?” “Mmh!” “Kwani unamchumba?” “Sijui!” Tunda alikunja uso, kama ambaye hakuwa amemuelewa Net. “Vipi? Umenipatia mchumba nini?” “Hapana, lakini nashangaa kwa nini hukumpenda Sera wakati naona alikuwa msichana ambaye mlikuwa mkiendana sana!” “Unamaanisha nini?” “Wote mmelelewa kwenye mazingira mazuri, mmesoma, wazazi wenu wanauwezo mzuri, yaani mnapesa. Ni msichana mzuri, na yeye ni mweupe, halafu Sera hakuwa muhuni kabisa. Hakuwa na mambo ya wanaume. Alijiheshimu sana.” “Daah! Kama ungekuwa mshauri wangu wa ndoa, ningekufukuza kazi sasa hivi.” “Kwa nini tena!?” Tunda akaanza kucheka.

“Vigezo vyako viko dhaifu sana, havimsaidiii mtu kupata mke hata kidogo!” “Jamani Net!” Tunda akazidi kucheka. “Hebu niambie, weupe, usomi, pesa na nini tena?” Net akauliza huku Tunda akicheka. “Kulelewa na wazazi wenye uwezo, yaani wote mmetoka kwenye malezi yanayoeleweka.” “Ehe! Sasa hivyo ndio vinasaidia kuwa na mke bora?” “Ndiyo. Na mwanamke aliyetulia. Sasa ukioa mwanamke ambaye hajatulia ndio inakuaje sasa?” Net alicheka kwa kuguna kisha akageuka pembeni. Tunda naye akaanza kuwaza maisha yake mapya aliyoamua kuanza.

Kwa Mara ya Kwanza Tunda na Mama Cote.

    Ndege ilitua viwanja vya ndege vya Mwalimu Nyerere, Dar. Kweli walimkuta Mama yake Net na msichana mwengine aliyeonekana mzungu kwa asilimia kubwa sana kuliko hata Net. Alikuwa mzuri sana na nywele za rangi ya thahabu, tofauti na Net,  zilianguka mpaka chini ya mabega. Macho ya rangi ya blue kama Net. Tunda alimsalimia mama yake Net baada ya Net kumsalimia mama yake kwa kumkumbatia na kumbusu.

“Kuna nini tena?” Net akauliza baada yakumuona yule dada hajawasalimia. “Am leaving with you.” Alijibu yule dada kwa lugha ya kingereza huku akionyesha uso wakutaka kulia. “I just got here, Maya! What’s going on?” Net akamuuliza kwa upendo huku akimwangalia mama yake. “Siwezi tena Net. I got enough of her. I want to go.” Yule dada aliendelea kumlalamikia Net, huku machozi yakimtoka. “Can at list have a hug first?” Net akamuuliza kwa upendo kama kumbembeleza.

Yule dada akamsogelea Net na kumkumbatia kisha akaanza kulia. “She doesn’t take me out of her sight! She took everything away from me.  She is ruining my life, Net.” Aliendelea kumlalamikia Net. “Can we talk about it later?” Yule dada akanyamaza kwa muda.

“Mwambie anirudishie funguo zangu za gari kwanza. She listen to you Net. Tell her, NOW.” “You know we have to talk first, Maya. Naomba utulie kwanza kisha tutaongea tukifika nyumbani.” “I don’t want to talk, I want my life back.” “I understand, but let’s go back home first.” Walikuwa wamewapa mgongo Tunda na yule mama, wakati wao wawili wakizungumza.

“Naomba umsalimie Tunda.” “Tunda? Is that a name or fruit!?” Yule dada akauliza kama kwa kejeli akitaka kujua kama Tunda kweli linaweza kuwa ni jina la mtu! “I know you are upset Maya, but can you try to be nice?”  Net akamwambia anaelewa kuwa amekasirika, ila ajaribu kuwa mwema kwa mgeni. “Am sorry.” Maya akaomba msamaha na kumgeukia Tunda.

“Hey! Am Maya.” “Kiswahili Maya!” Mama yake Net akaingilia akitaka azungumze kiswahili na Tunda si lugha ya kingereza. “See! Everything am doing to her it’s a problem.” “She speaks Swahili, Maya. Just use Swahili, please.” Net aliweka msisitizo akiungana na mama yake kuwa Maya atumie kiswahili. “Fine!”  Akakubali Maya  nakufuta machozi.

“Habari yako. Naitwa Maya Cote.” Tunda akajua lazima ni mdogo wake Net kwani ndiyo jina alilokuwa akitumia hata Net, Nethaniel Cote. Tunda akanyosha mkono. “Naitwa Tunda, kama vile fruit.” Maya akacheka kwa aibu kidogo. “Samahani. Mama ananiudhi sana.” “Usijali. Hata shule walikuwa wakinitania hivyo hivyo.” Tunda alijibu huku akitabasamu, wakacheka.

“You have a pretty face. I love your sleeping eyes. The way you talk and smil..” “Swahili, Maya.” Mama yake alimkata Maya akitaka azungumze kiswahili. “See Net! I told you she…” “Maya!” Net akamwita kama kuweka msisitizo. “Fine!” Maya akamjibu kaka yake. “Wewe ni mzuri sana. Napenda macho yako na, anyways everything. You pretty.” Tunda akacheka akiona aibu. “Asante Maya.” Akamgeukia kaka yake na kumwambia, “I like her.” Akisema amempenda Tunda. Wote wakacheka.

“Ukiondoka unichukue na mimi, sitaki kubaki hapa na Mama Cote.” Alimnong’oneza Tunda masikioni, lakini kwa sauti iliyoweza kusikika na kila mtu pale. Tunda akacheka. “Mama akiruhusu, tutaenda wote.” Tunda akajibu huku akicheka. “Trust me, she wont. Labda Net ndio amwambie. Anafanya chochote anachoambiwa na Net, lakini siyo mimi.” “That’s enough Maya.” Mama yake akamkatisha. “See! That’s why I want to go away.” Maya akalalamika na kurudi nyuma akiwa amenuna. Walionekana wawili hao hawapatani.

“Karibu sana Tunda. Samahani umetukuta katika wakati mbaya, lakini nimefurahi kukufahamu. Mimi ndiye Mama Cote. Mama yake Maya.” Maya akamwangalia na kujisogeza kwa kaka yake. Alikuwa mama wakawaida tu. Hakuwa mweupe wala mweusi. Mswahili kabisa mwenye rangi ya kawaida. Maji ya kunde. Lakini alizaa watoto wote weupe sana, yaani wazungu. Maya alikuwa ndio anamwili wa kizungu, nimpaka aongee hicho Kiswahili chake na akuonyeshe mama yake ndipo utajua amechanganya. Wote walikuwa na nywele nyeusi lakini Maya alizibadili rangi nywele zake.

“Net aliniambia mnataka kwenda kumuona Mchungaji.” “Ndiyo.” “Umefanya vizuri. Lakini twende kwanza nyumbani mkale ndio twendeni kwa Mchungaji.” Walikwenda mpaka nyumbani kwa huyo mama. Alijenga sio mbali sana na alipokuwa amejenga Net. Maeneo hayo hayo lakini lazima utumie usafiri kufika kutoka kwa Net kwenda kwa mama yake. Palikuwa na umbali kidogo.

Tunda akabaki ametoa macho. Lilikuwa ni jumba la kisasa. Kumbwa picha za familia zilijaza hiyo nyumba kwa wingi. Kuanzia unaingia mlangoni mpaka sebuleni. Kubwa na nzuri. Na hapo ndipo alipoiona picha ya baba yake Net. Kweli alikuwa mzungu kabisa. Na alifanana sana na Net. Tunda alipita akiangalia.

Heshima ikaongezeka kwa hiyo familia. Kwa vile alivyoona pale, na biashara huyo mama anafanya, Tunda akakubali kuwa huyo mama kichwa yake inafanya kazi. Alimshukuru Tunda kwa kazi nzuri aliyokuwa akifanya kwenye ofisi yao huko Arusha. Akamsifia kuwa anampunguzia majukumu makubwa yeye na Net kwa utendaji wake mzuri.

“Net anakusifia sana. Hata wateja wetu wanakusifia. Asante sana na ninakuomba uvumilie tu, baada ya muda nitaongeza mtu mwingine wakukusaidia.” “Hamna shida mama. Kwa sasa naona nimeweza kumudu kazi zote, hata hivyo Net ananisaidia sana.” “Utalemewa pindi Net atakaposafiri.” Tunda alishtuka sana akamgeukia Net.

“Sisafiri sasa hivi Tunda. Acha kuogopa.” Tunda akacheka taratibu lakini wazi alionekana ameingiwa hofu. Walikaa pale wakizungumza mambo mbali mbali. Zaidi Net na mama yake ndio waliokuwa wakiongea zaidi. Walikuwa wakizungumzia mambo yao ya biashara. Tenda alizoshinda huyo mama. Tunda alibaki kusikiliza huyo mama, nakumtamania. Alionekana ni mama aliyefanikiwa sana.

Walikaa hapo mpaka mida ya jioni ndipo walipoamua kwenda kanisani. Tunda alikuwa amepewa chumba pale pale, akaacha baadhi ya vitu vyake kwenye hicho chumba, kwani Net alimwambia wangelala hapo siku hiyo mpaka kesho yake.

Tunda na Mkasa wa Kanisani.

Walipofika kanisani wakakuta ndio wanamalizia kikao cha wazee wakanisa, ofisini kwa Mchungaji. Ilibidi wasubiri kwenye viti vya nje. Alikuwa Tunda, Net na Mama Cote. Waliendelea kuongea mambo mawili matatu wakiwa pale nje, mpaka walipoona wazee wengine wakitoka kwenye ofisi ya Mchungaji. Mama Cote akasimama akatangulia humo ndani, baada ya muda, Tunda na Net walianza kusikia vicheko mle ndani ofisini wakahisi wamesha sahauliwa. “Ngoja nikawashtue.” Net akasimama na kuingia ndani.

“Shikamooni.” Tunda akamsikia Net akisalimia huko ndani. Mchungaji akaongea na Net maneno mawili matatu huku akimtania na kumuuliza habari za Arusha kisha Net akaamua amkumbushe baada ya kukuta bado kuna wazee wengine watatu mle ndani. “Bado utakuwa na nafasi yakuongea na Tunda?” Net akauliza. “Kabisa. Umekuja naye?” “Yupo hapo nje.” “Mkaribishe awasalimie na hawa wazee wa kanisa.” Mchungaji akajibu. “Ni kweli. Yaani Tunda ni binti mzuri sana.” Mama Cote naye akaanza kumwaga sifa za Tunda, akimsifia utendaji kazi wake. Net akatoka kwenda kumwita Tunda.

Net alimtanguliza Tunda aingie kwanza, yeye akafuata nyuma. Tunda aliingia na kusalimia “Shikamooni.” Huku akinyoosha mkono akitaka kuwapa mkono wale wazee na wachungaji kwa heshima zaidi. Wakati anasogea mbele kidogo ili aanze kuwashika mikono huku akiwaangalia vizuri, Net akamuona Tunda ameshtuka sana, akainama na kurudi nyuma huku akishusha mkono wake. Mama yake na Mchungaji hawakuelewa, lakini Net alishaelewa kwani alishakaa na Tunda kwa muda mfupi lakini alishamuelewa vizuri sana. Net alikasirika sana.

Wakiwa wengine hawajaelewa kilichompata Tunda, akamgeukia Net na kumsogelea kwa karibu. “Naomba kuondoka Net.” Tunda akataka ampishe sehemu ya mlangoni. “Vipi tena!?” Mchungaji akauliza kwa mshangao, huku akisimama. “Eti Tunda?” Tunda alishaanza kulia. “Naomba niondoke tu.” Hakuna aliyeelewa, Net aliwageukia wale wazee, akashangaa kuona wawili wameinama. “No way!” Net alisikika akilalamika huku ameshika kichwa. “Seriously!?” Net akawauliza kwa mshangao huku akiwatizama wale wazee wawili. Tunda akamsogeza kidogo Net kwa mkono wake, akatoka nje.

“Tunda! Tunda! Naomba nisubiri.” “Umenidanganya Net. Umeniambia nakuja kuanza upya, halafu unakuja kunikutanisha na waliokuwa wateja wangu, tena mbele ya mama yako! Nilikuamini Net, umenigeuka!” Tunda alikuwa akilia. “Tunda please. Naomba usiondoke.” Tunda alikuwa ameshatoka nje ya geti la kanisa, alikuwa akitembea kwa mwendo wa kasi, Net akimkimbilia kwa nyuma.

“Naomba usimame Tunda, Please.” Tunda akasimama huku akilia. “Naomba unisikilize. Unafikiri mimi ningejuaje kama wale walikuwa wateja wako? Sikuwa nafahamu hilo! Wale wazee wanaheshimika sana hapa kanisani, sikuwahi hata kuwaza kama wanaweza ku..” Net akasita. “Sasa unataka nifanye nini na wale watu tena? Ni maisha gani mapya unataka nianze na watu kama wale? Si yatakuwa ni yale yale tu?” Tunda alikuwa akiongea ukweli kabisa. Net akapooza, alishindwa chakujitetea kabisa.

Mahali ambapo alimwahidi Tunda angepata msaada na kubadili maisha yake, anakutana na wazee aliokuwa akiwaamini sana na wao walikuwa wakiishi yale maisha machafu. Alibadilika sura akawa mwekundu, nakushindwa kushusha mikono yake. Alibaki ameweka mikono kichwani akizunguka zunguka pale mbele ya Tunda.

“Naomba niondoke Net.” “Kumbuka tumekuja na mama! Naomba nikamchukue mama ili tuondoke pamoja. Sawa?” Tunda akatingisha kichwa kukubali. “Asante sana Tunda.” Net alikuwa amesha changanyikiwa. “Twende basi ukasubiri kwenye gari.” Akarudi naye mpaka kwenye gari, akawasha gari, akamuacha Tunda amekaa humo ndani ya gari.

          Alikuta Mchungaji akimsubiri, bado haelewi kilichotokea. “Kuna nini, Net?” “Naomba tuwaulize hawa wazee, kwa nini Tunda amekimbia mara baada ya kuwaona.” Mmoja wao akasema sijui. “Wewe hujui lakini Mzee Meto namwenzie wao wanafahamu.” Net alikuwa amekasirika sana.

 “Hivi unajua ni kwa muda gani nimekuwa nikitaka huyu binti afikie haya maamuzi? Hivi mnajua ni jinsi gani nilivyomuhubiria? Nimemwambia huku kanisani lipo tumaini. Ameteswa na shetani kwa muda mrefu sana, nimemuahidi atapata pumziko. Halafu anakuja kukutana na nyinyi watu wa kanisani mliokuwa wateja wake!” “Wateja?” Mama Cote alishtuka sana. “Ndiyo. Tunda alikuwa akifanya biashara ya kikahaba.” Net alikuwa amekasirika sana, hata hakuwa akifikiria alichokuwa akiongea. Aliendelea kuropoka. Wote walikuwa kimya wakimsikiliza.

“Hivi mnajua mlichofanya nyinyi? Mmechukua tumaini la pekee lililokuwa limebaki kwa yule binti! Mtamfanya asiamini tena.” “Tulia Net. Kwa kuharibu kwa hawa wawili, hakuchukui nafasi ya Mungu hata kidogo. Kama wao wameshindwa, bado tunayo mifano mizuri ya watu wengi wanaoweza kuishi maisha maadilifu. Naomba ukamwite Tunda.” Mchungaji akapiga simu kwa baadhi ya wazee aliojua wanaweza kufika pale kwa haraka, wakaanzisha kikao.

Tunda akarudi ndani, wakamuomba aelezee mahusiano aliyokuwa nayo na wale wazee. Tunda akakiri kila kitu huku akilia na kusema ni kweli amechoka anatafuta njia ya kupumzika nakuondoa ile hukumu moyoni mwake lakini si pale. “Hamuwezi nyinyi kunisaidia. Hamtaweza hata kidogo.” Tunda akatoka. Net alimkabidhi funguo mama yake na kumfuata Tunda.

Ilikuwa ni aibu ya miaka kwa kanisa. Hakuna aliyeamini uchafu Tunda aliosema alikuwa akiwafanyia wale wazee. Net ndiye aliyeishiwa maneno kabisa. Alishindwa aongee nini na Tunda. Tunda alikataa kabisa kurudi kwa mama yake Net, akaishia kulala hotelini. Aliomba Net akamchukulie mizigo yake nyumbani kwao, usiku uleule.

 

Tunda Arudi Arusha bila Msaada wa kiroho.

Kesho yake asubuhi na mapema, bila hata kumuaga Net, Tunda aliondoka jijini Dar kurudi Arusha kwa kutumia usafiri wa basi. Usiku ule ulikuwa mrefu sana kwa wale viongozi wa kanisa lile. Wale wazee walikiri uchafu waliokuwa wakifanyiwa na Tunda, na kesho siku ya jumapili kwenye ibada, walisimamishwa mbele ya kanisa na Mchungaji akawatenga.

Ilikuwa ni hali ya kusikitisha, kushtua na aibu kubwa. Kwani ni wazee walioheshimika sana pale kanisani na wao ndio walikuwa wakitoa michango mikubwa ya kifedha pale kanisani, wakisaidiana na Mama Cote. Mmoja alikuwa ana mke wake pale pale kanisani. Watoto wao walishakuwa wakubwa tu. Na Meto yeye alifiwa na mkewe, japo naye alikuwa Mzee wakuweza kumzaa hata Net. Alitambulishwa Tunda na huyo Mzee mwenzake. Tunda akamridhisha kwenye gari kitu alichopenda. Hakuhitaji kwenda naye popote. Kwa hiyo walimpenda Tunda, wakijua hawataweza kukamatwa. Waliegesha magari yao sehemu tulivu mida ya usiku giza limeshaingia. Tunda anafika hapo kwenye magari yao, anawahudumia, wanamlipa, maisha yanaendelea.

Mchungaji Amfuata Tunda.

Baada ya ibada yule Mchungaji alipanda ndege kuelekea Arusha na Net, kumfuata Tunda. Walimkuta amelala chumbani kwake. Mchungaji alimuomba waongee. Tunda alishtuka sana. Hakutegemea kuja kufuatwa tena baada ya kugundulika uchafu wake. Yule Mchungaji aliongea kwa muda mrefu na Tunda. Akimpa mifano hata ya watu waliokuwepo kwenye bibilia walioaminiwa na Mungu, lakini walikuja kumkosea Mungu, lakini baadaye walipotubu tena Mungu aliwasamehe. Alimpa mfano wa Petro aliyemsaliti Yesu mara tatu, lakini baada ya kutubu alisamehewa, na akamueleza jinsi Petro alivyokuja kuwa msaada mkubwa kwa kanisa mpaka sasa.

          “Kama sio Petro kukubali kosa, kazi kubwa ya kanisa iliyoifanya baada ya kutubu isingekuwepo leo. Kikubwa ni kukubali kuwa umekosa na kuhitaji msaada wa Mungu. Halafu Tunda, wale wazee hawatakuwa mfano wako wakuiga pindi utakapoamua kumpa Yesu maisha yako. Wote tunamwangalia mmoja tu, ambaye aliishi hapa duniani bila kutenda dhambi, Yesu.”

“Wote tunamtizama yeye peke yake. Hata mimi huwa najikwaa kwa namna nyingine, na ndio maana tupo kanisani. Kanisani ni kama hospitalini, Tunda mwanangu. Wote tuliogundua tunahitaji msaada wa Mungu, ndio tumekimbilia pale kama wagonjwa wanavyokimbilia hospitalini. Kanisani ndio mahali pekee utakapopata msaada. Sisemi kama utakuwepo kanisani na uendelee kutenda dhambi, hapana. Lakini ujue kuna madhaifu mengine yanachukua muda kuondoka, lakini utakapotulia kwa Mungu, ukanyenyekea, ipo nguvu na uwezo wa kushinda dhambi endapo utakusudia.” Yule mchungaji aliendelea.

“Mungu halazimishi mwanadamu kuacha kufanya dhambi. Mimi na wewe ndio tunachagua. Kwa hiyo unaweza ukawepo kanisani, na ukachagua kuendelea kutenda dhambi kama mtu wa nje kabisa, lakini haiondoi uweza na nguvu za Mungu. Utende dhambi, usitende, bado Mungu atabaki kuwa Mungu ila wewe ndiye utakayeteseka.” Net aliendelea kusikiliza na yeye kwa makini tu akiomba Mungu huo ukweli umuingie Tunda.

“Hakuna pumziko kwa mwenye dhambi, si sasa au baadaye. Bali ipo faraja, amani na utulivu kwa wale walioamua kweli kuishi maisha yakumpendeza Mungu. Mpe Yesu nafasi kwenye maisha yako uone. Mruhusu Net awe mwalimu wako, utajifunza mengi sana kupitia yeye. Nikijana aliyetulia sana na anamjua Mungu. Anaishi maisha ya kikristo kweli kweli, najua wewe ni shahidi.” Tunda akatingisha kichwa kukubali. Kidogo Mchungaji akapumua.

“Basi, na wewe unaweza kuwa kama yeye, kama utakubali, ukatii na kutubu. Je upo tayari?” Tunda alishatulia kabisa. Alimuelewa vizuri sana yule Mchungaji. Akakubali kuombewa. Aliongozwa sala ya toba na Mchungaji akamuombea. Tunda alikuwa na mapepo mengi sana.

Alikuwa amefungwa na nguvu za giza, nyingine tokea alipokuwa mtoto mdogo kwa baba Tom. Mashetani na majini mengine aliyapata akiwa na Sadiki. Tunda akiwa amepagawa hayo mapepo, aliongea mengi sana. Basi ikawa vurugu tupu hapo chumbani. Mchungaji na Net walimuombea, wakikemea yale mapepo yamtoke. Kuna yaliyokuwa mabishi. Yakidai hiki na kile. Lakini yule mchungaji alikazana akisaidiana na Net. Haikuwa kazi rahisi wala ya masaa machache.

Lilitoka pepo hili, na kuibuka jingine ndani yake. Wakidhani wamemaliza, linaibuka jingine. Mara liseme ni jini lililomuoa Tunda. Jingine lilisema ndilo linalomfanya awe na bahati na kuvutia wanaume kwake. Ikawa fujo. Tunda alijawa nguvu za giza. Lakini Net hakushangaa. Tunda alishamsimulia ibada za kipepo alizokuwa akifanya makaburini na huko Handeni alipokuwa na Sadiki.

Maombi hayo yaliendelea, mpaka yote yakamtoka Tunda. Akawekwa huru. Kuja kuangalia saa ni saa saba usiku. Ikabidi Mchungaji achukuliwe chumba hapo hapo hotelini. Kesho yake asubuhi akaondoka kurudi Dar, akiwa amefanikiwa kumpatia Mungu roho ya Tunda.

Maisha ya Tunda baada yakumpokea Yesu.

Net ndiye alikuwa na furaha kuliko hata Tunda mwenyewe mpaka Tunda akashangaa. Alikabidhiwa rasmi kazi ya kumtunza Tunda kiroho. Kitu cha kwanza alichomnunulia Tunda ni bibilia. Akaanza kumfundisha Tunda jinsi ya kusoma bibilia. Kitu alichogundua Tunda kwa Net, ni muombaji. Net alikuwa ni muombaji sana, kitu kilichokuwa kikimshangaza Tunda. Kwa jinsi alivyo Net, na maisha anayoishi, ingekuwa ngumu kumdhania kama ni mcha Mungu wa kiasi kile. Lakini Tunda alijua ndiyo siri yake kubwa ya hekima na utulivu alio nao.

Kwa harakaharaka wasichana wengi walikuwa wakichanganywa na Net, pindi wamuonapo. Lakini baada ya kukaa naye kwa muda mfupi, wengi walimkimbia. Mara nyingi Net alikuwa akimshukuru Mungu kwa kumuwahi. “Unamaanisha nini?” “Najijua hivi nilivyo Tunda. Si watoto au watu wazima wanao nijaribu kunitongoza. Isingekuwa Yesu kunificha, pengine sasa hivi ningeshakuwa nimekufa. Nashukuru Mungu kwa kunipa baba na babu wenye msingi imara wa dini, zaidi babu. Walinikuza kwenye maadili mazuri.”

“Yuko wapi sasa hivi baba?” “Alishafariki.” “Pole sana.” “Asante, lakini ilimuathiri zaidi Maya. Unajua yeye ndiye alilelewa sana na baba wakati mama yupo shuleni. Kwa hiyo baba alipofariki, ndipo mama alipoamua kurudi huku Tanzania.” “Kwani hamkuzaliwa hapa?” “Hapana. Tulizaliwa Canada. Mama alienda huko kimasomo, ndipo akakutana huko na baba. Hata msingi wa shule niliyokuwa nayo ilikuwa ni hukohuko, ndio maana ilinilazimu kurudi hukohuko kumaliza shahada yangu ya pili.”

“Alitangulia kurudi huku mama peke yake. Akatuacha kule mimi na Maya tukilelewa na bibi na babu. Mama alipoweka mambo sawa, nikaanza kuja huku mimi ndipo tukamchukua Maya. Maya hana muda mrefu sana hapa nchini. Na hapapendi kabisa. Anataka sana kurudi kwa bibi na babu. Lakini mama hataki, anaona kule hana uangalizi mzuri. Pale alipo hataki kufanya kitu chochote hapa nchini, anataka kurudi kwa bibi na babu.” “Labda mngemruhusu ili akasome.” Tunda akajaribu kushauri. 

“Mama hawezi. Ni mtundu sana Maya. Na amedekezwa sana na kina bibi. Hana maadili mazuri hata kidogo. Hata huko pia shule yenyewe hataki kwenda. Amemaliza high school tu, anatapanya pesa ya bibi na babu. Ndio maana mama ameamua kumchukua.” “Natamani kama mimi ndio ningepewa hiyo nafasi Net.” “Mungu amekupa nafasi nyingine Tunda. Unaweza kuwa chochote utakacho.” Tunda akainama kama anayefikiria kidogo.

“Lakini sikurudi tena shule. Naanzia wapi?” “Sio lazima ukasomea elimu ya msingi au sekondari. Kwa sasa unaweza kutafuta ujuzi wa kitu fulani unachopenda, kisha ukaanza kukifanyia kazi.” “Ni kweli. Labda nianze kufikiria na mimi nikitu gani napenda. Maisha hayakuwahi kunipa nafasi kama hii. Sasa hivi ninafuraha na amani. Siamini kama na mimi Tunda, nipo kwenye nafasi yakuchagua.” Net akacheka.

“Nikwambie ukweli Net, zile ndoto mbaya zimeisha. Halafu nilikuwa nina hofu fulani hivi. Kama wasiwasi moyoni. Umeshawahi kulala usiku au hata kuwa umekaa tu hivi, ukasikia moyo unashtuka?” Net akawa anafikiria. “Unaweza usijue, lakini nilikuwa na hiyo hali. Hofu kila wakati kama moyo unashtuka kila wakati.” “Kwa hiyo sasa hivi imeisha?” “Imeisha. Namshukuru Mungu. Najisikia huru.” “Afadhali.”

Cheni ya Mguuni ya Tunda!

Ilikuwa jioni wametoka kazini. “Nikuulize kitu Tunda?” “Niulize tu.” “Hiyo cheni ya mguuni ulipata wapi?” Tunda akakunja mguu akaitizama na kuizungusha kidogo. “Alinivalisha Sadiki. Nimeshindwa kuitoa Net.” “Kwa nini?” Tunda akafikiria. “Kuna jinsi Sadiki alikuwa akinifanyia, sijui niseme kunidekeza au nini! Lakini kuna jinsi alikuwa na mimi, alikuwa akinifanya kama yai! Alikuwa hapendi niwe na shida. Kabla sijalia shida, ananipa pesa. Manguo haya yote, ni ya pesa nyingi sana Net.” “Nakuona.” Net akaongeza.

“Basi ni Sadiki. Nilikuwa nikiwa naye, japo nilimdanganya jina, lakini sikuwa nikijitahidi kujifanya kuwa sivyo. Alinipenda yule kaka, karibu kuchanganyikiwa. Wakati mwingine nilikuwa nikimgombesha sana, lakini anavyojishusha, mpaka utamuhurumia. Sikuwa na shida na pesa nilipokuwa naye. Sikuwa nikihangaika kwa yeyote na chochote. Alinilipia kila garama, tena bila kuchoka au kulalamika.”

“Alikuwa akiniona nimetulia tu hivi nawaza kitu, basi hata kama alikuwa anafanya kitu, ataacha, anakuja japo aniguse. Nitakuwa mawazoni, naweza kushtuka kwa sababu ananisugua mahali kwa upendo. Kiganja, bega, ilimradi tu kunionyesha yupo na mimi.”

“Japokuwa alikuwa anasema ananufaika na mimi, lakini Net, Sadiki alihakikisha nina furaha wakati wote. Alinipenda sana. Nilipata miaka miwili ya aina yake na yule kaka. Hii cheni nimeshindwa kuitoa kabisa. Wakati mwingine najiona ni kama nipo na ule upendo wake. Sijui kama unanielewa?” Tunda akauliza na kuendelea bila kusubiri jibu.

“Sijapata mwanaume anayenipenda vile Net. Labda nikija kubahatika upendo kama ule tena. Huyo mwanaume ndiye atakayekuja kuitoa hapa mguuni kwangu. Lakini mimi nimeshindwa.” Tunda aliongea taratibu huku akiiangalia ile cheni na kuizungusha pale mguuni mwake. Net akavuta pumzi kwa nguvu maana alikuwa akimsikiliza kwa makini sana.

“Lakini sasa hivi hauhitaji upendo wa Sadiki, Tunda. Unaye Mungu aliye hai. Upendo wake unatosha. Usijifunge na upendo ambao haukuwa halisi. Nilivyokusikia juu yako na Sadiki, mlifanya mengi na ya kutisha huku akikutumia wewe kama chambo yakuvuta utajiri. Hudhani kama hiyo kitu inaweza ikawa imebeba mambo mengine?” Tunda akashtuka kidogo.

“Nikuombe kitu?” Tunda akamwangalia. “Naomba mimi niitoe, halafu nije niweke hapo nyingine.” Tunda akajifuta machozi. “Hamna sababu yakufanya hivyo Net. Acha tu. Lakini naomba nipe muda wakuja kuitoa. Isiwe sasa hivi. Najiona sipo tayari Net. Mmeniombea, naamini hii cheni haiwezi kuwa na madhara yeyote. Alininunulia cheni tatu. Shingoni, mkononi na mguuni. Akaniletea na kuniambia ni ishara ya upendo wake kwangu. Najiona sipo tayari kuviachia.” Net alibaki akimtizama.

“Ni sawa?” Tunda akauliza kwa upole. “Sio sawa Tunda.” Tunda akaumia sana. “Tena kwa maelezo hayo, ndio sio sawa kabisa. Kwa nini unataka kukumbatia upendo wa mtu aliyepita vibaya kwenye maisha yako?” Tunda akanyamaza.

“Unakuwa unang’ang’ania agano la mapenzi yaliyowekwa kwenye msingi mbaya na hatari sana kwako! Tumekuombea, na tunaendelea kuomba. Lakini unakuwa uko kwa Mungu huku umekumbatia maagano ya mtu mwingine kwenye ufamle mwingine! Hujui nia ya kukuvalisha hiyo ki ukweli.” “Aliniambia ni ishara ya mapenzi yake kwangu.” Tunda akatetea.

“Ndivyo yeye alivyokwambia. Unajuaje kama ni kweli? Halafu Sadiki alikuwa mume wa mtu. Unajifunga kwenye maagano ya ndoa ya mtu! Si sawa Tunda. Unatakiwa ubadilike hata kifikira. Kuwa upande wa Mungu huku ukitetea mapenzi ya wizi, unajifungulia milango mingine mibaya. Naomba ufikirie zaidi.” “Nimeelewa Net. Nitatoa.” Tunda akaongea taratibu.

“Lini?” Net akauliza bila kutaka kumpa nafasi Tunda. Tunda akanyamaza. “Tunda?” Net akamwita. “Unataka kuishi kama Tunda au Ani wa Sadiki?” Tunda akashtuka kidogo akamwangalia. “Ani alikufa na Sadiki, Net.” Tunda akajibu. “Haionyeshi hivyo. Bado yupo na maagano yake yapo hai!” Akamuona anaizungusha ili aitoe.

Net akasogea pale mguuni. Akapiga magoti. “Naomba mimi niitoe.” Tunda akamwangalia kama ambaye hamuelewi vizuri. “Ni sawa?” Tunda akatingisha kichwa kukubali. Net akaitoa. Nakubaki ameishika. “Utaifanyia nini?” Tunda akauliza. “Sijui. Tumuombe Mungu. Kwanza akutoe kwenye haya maagano na akupe amani. Mengine Roho wa Mungu atatusaidia.” “Basi acha nikupe vyote. Na cheni ya mkononi na shingoni.” Tunda akaenda juu ya meza hapo hapo hotelini alipokuwa amening’iniza mikufu yake.

Akarudi na hizo cheni zote, akamuwekea Net mkononi. Ni kweli zilikuwa nzito. Net akamwangalia. “Nipo sawa Net. Nimeridhia kutoa.” “Hilo ndilo la muhimu. Wewe mwenyewe ukubali kutengana navyo kwanza. Ndio hata tukiomba na kuvunja hayo maagano, itawezekana.” “Basi tuombe wote.” Tunda akapiga magoti pale alipokuwa amepiga magoti Net akimvua. Net akacheka kwa furaha.

“Mungu atakupa mtu anayekupenda kwa dhati.” Tunda akacheka kidogo huku akifikiria. “Mmmh! Sidhani Net. Acha tu tuombe, niachane na Sadiki nitulie kwanza. Nishahangaika na wanaume mpaka nimekinahiwa nafsi. Umenipa mapumziko ambayo, hujui tu! Mungu atakuja kukulipa Net. Hujui kile umekifanya kwangu. Mungu akuonekanie na wewe siku utakapomuhitaji. Kwa lolote lile. Akumbuke kile ulichonifanyia mimi.” “Amina.” Wakatulia.

Net akaweka vile vitu pale kwenye kochi akaanza kuomba. Ameanza tu, akashangaa Tunda anaanguka tena na mapepo. Akajua ndio maana alikosa amani na ile cheni pale mguuni. Yale mapepo yakasema yalikuwa hapo kutunza agano. Na lile agano ilikuwa ni kama ndoa kati ya Tunda na Sadiki. Net alijua tu.

Kijana huyo wa kizungu, alitumia mamlaka yote aliyopewa na Mungu. Akiwa peke yake pale chumbani na Tunda akigaragara chini. Akaanza kutambaa kama nyoka na kutema mate kama nyoka. Safari hii Net hakutumia muda mrefu, akayaamuru yale mapepo yamtoke na yasirudi tena kwa kuwa Tunda ameshavunja yale maagano na amekiri kifo cha Ani.

Akajinyonga pale chini, yakatoka. Ndipo Tunda akazinduka sasa pale sakafuni. Net akamsaidia kusimama. Alijawa mate. Akawa amejichafua sana. “Nini kimenipata Net!?” “Ulikuwa na mapepo Tunda.” “Tena!?” Tunda hakuamini. Siku anaokoka alitolewa mapepo kwa majini.

“Yalikuwa yakilinda maagano yako na Sadiki. Mlikuwa mpo kwenye maagano yaliyoshikiliwa kwa nguvu za giza Tunda. Hizi cheni zilikuwa ni ishara za hilo agano.” “Mungu wangu!” “Usiogope. Umewekwa huru.” “Basi yeye Sadiki alijua anachokifanya. Mimi nikijua ni zawadi tu, kumbe ni mambo yake. Tena aliniletea akiwa ametoka safari. Ukute alizinunua ndio akaenda nazo kwa babu, wakazifanyia dawa. Sadiki alitamani sana anioe nijulikane mimi ni mke wake kihalali. Nilipokataa akaniomba angalau nimzalie hata mtoto mmoja! Napo nilikataa.” “Basi mshukuru Mungu upo huru. Anza upya ukitumia uhuru wako vizuri. Nenda kaoge. Nakusubiri.” “Acha nifute hapo chini sakafuni kwanza.” “Nenda ukaoge. Mimi nitaita mtu wa hoteli apige deki.” Tunda akaingia bafuni akamuacha Net akiita muhudumu kwa ajili ya kusafisha.

Tunda alitoka bafuni na kumuomba Net waombe tena. “Acha woga Tunda.” “Tuombe tena ili kuwa na uhakika yametoka yote.” Net akacheka. “Usinicheke bwana! Tena tupige magoti. Ujue mwenzio nilijua nimewekwa huru kabisa na hayo mapepo!” “Yapo maagano mtu unaingia. Kama si ya kimungu ni mpaka ukubali kuyavunja. Shetani anakuwa na haki nayo, Mungu hawezi kuingilia. Ukikubali kuyavunja, hapo Mungu anakuwa na uwezo wakukudai kwa shetani. Anakuwa na haki zote.” “Sasa hivi sitaki tena Net.” “Na Mungu ameliheshimu hilo, sasa hivi wewe ni wake.”

“Kwani wewe ulionyeshwa na Mungu juu ya hii sheni?” “Sio moja kwa moja. Ni kweli inakupendeza sana. Huwa siachi kuitazama hapo mguuni. Lakini kila nilipokuwa nikitazama sipati amani kama jinsi ilivyokukaa. Unajua kuna kitu kinavutia. Ukikitazama kwa karibu, kinatakiwa kifurahishe sio kukukosesha amani! Ndivyo sasa ilivyokuwa hiyo cheni kila nikiitazama kwa karibu, nilikuwa sipati amani.” Tunda akatulia.

“Tutakuja kurudisha nyingine hapo mguuni.” Tunda akacheka. “Sio lazima Net. Nakushukuru kwa kusimama na mimi. Hujanikatia tamaa.” Net akacheka akijiambia ‘hujui hata nusu yake!’ Wakapiga magoti, wakaomba, ndipo Net akaondoka pale na kumuacha Tunda amelala.

Maajabu ya zile Cheni!

Asubuhi Net alifika na kumpigia simu ashuke chini waende kazini. Tunda akamwambia aende chumbani kwake. Net akajua kuna jambo. Akatafuta sehemu ya kuegesha, akapandisha juu kwa haraka. “Vipi?” “Nimeamka asubuhi, zile cheni hazipo. Au ulizitupa?” “Hapana. Niliweka hapo juu ya meza. Zote tatu. Na niliziacha hapa wakati umelala.” “Basi zimetoweka.” “Mwache shetani achukue mali zake.” “Nimeshtuka Net! Yaani nilikuwa nimevaa na kujifunga mapepo!” “Lakini unachotakiwa kuwa nacho ni kuwa, umebakiwa na uhuru.” Wakaomba tena na kwenda kazini.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Net alitafuta kanisa pale pale jijini Arusha, wakawa wakienda na Tunda.  Alipata naye muda mwingi wakumfundisha kila baada ya kazi. Tunda alibadilika sana kimaisha hasa kimtazamo. Ile hukumu aliyokuwa nayo zamani iliisha kabisa. Tunda alisahau shida zote akawa akiishi kwa furaha. Net alijitahidi sana kumuelekeza kwenye neno la Mungu. Alimjengea msingi wa kusoma bibilia. Kila alipomuuliza swali Net, Net alijitahidi kumuelekeza kwakupitia bibilia.

Maya jijini Arusha, amtaka Tunda aishi nao.

Babu yao aliugua huko nchini Canada, ikamlazimu mama yao aende kumtizama, ndipo ikabidi Maya aende akaishi na Net jijini Arusha. Kwa kuwa Net ni kama alihamia Arusha, na kushindwa kurudi tena Dar kwa kila sababu. Kazi anazofanya Net haikumlazimu awepo Arusha na kushindwa kusafiri kwenda popote, lakini hakuacha kutoa sababu zilizoonyesha ugumu wakuliacha hilo jiji.

Ofisi ya Dar ambayo ilimuhitaji zaidi, kazi zake nzito ndio akawa akizifanya sasa kwa simu na kompyuta, tena kwa juhudi ili kumnyima mama yake sababu. Tunda hakujua anayopitia Net, ili kuwepo naye hapo Arusha. Alikuwepo hapo kwenye ofisi za usafirishaji, lakini alifanya na kazi za mama yake pia huko Dar.

Tunda alishangaa siku hiyo asubuhi Net anampigia simu kumtaka ashuke waelekee kazini, akiwa na Maya. Alifika garini akamkuta Maya anamsubiria kwa hamu. Walikwenda naye ofisini akiwa na Tunda wakati wote. Maya alionyesha kuvutiwa na Tunda kitu kilichomshangaza hata Net.

Alikuwa muongeaji sana tofauti na Net. Lakini binti mdogo tu na nadhifu. Baada ya kazi, waliamua kwenda kula wote watatu kwenye mgahawa wa pale pale hotelini anapoishi Tunda. Wakati wanakula wao watatu, akumuomba Tunda akaribie kuishi nao nyumbani kwao. Tunda akashangaa kujua kuwa Net ananyumba kule Arusha. “Nilifikiri unaishi hotelini Net!” “Hapana. Tulinunua nyumba.” Hata Maya akashangaa.

“Hujawahi kufika!?” Akamuuliza Tunda kwa mshangao. Tunda akacheka. Maya akamgeukia kaka yake. “You must be kidding me!” Akamwambia kaka yake. “Acha fujo Maya.” “Tatizo la Net, yupo sooooo..” Akawa anafikiria Maya jinsi ya kumsimulia Tunda jinsi alivyo Net. “Aaah! Sijui hata nikwambie nini! Lakini umenishangaza kushindwa hata kumkaribisha sehemu unayo ishi!” “Ningemkaribisha bwana. Sema tumekuwa na mambo mengi.” Tunda alishamjua Net ni mwadilifu sana na hana haraka.

 Maya aliaga kuwa anakwenda kutumia choo. Net akamgeukia Tunda. “Upo huru kuja kuishi naye kama unataka. Labda itamsaidia. Hana rafiki hapa nchini na kila kitu mama anachomwambia anaona anaonewa. Labda wewe unaweza kuwa karibu naye, ukamsaidia.”  Tunda akashangaa Net anazungumza nini!

“Net! Namwambia nini mimi Maya!? Mwenzangu amezaliwa uzunguni, mimi mtoto wa mtaani.” Wakacheka. “Inawezekana historia yako, ikawa msaada mkubwa sana kwake. Usidharau.” “Mmmh!” Tunda akaguna na Maya akawa amerudi akawakuta wanacheka. “Sasa Tunda umeamua nini? Nakuja kuishi hapa na wewe au wewe unakuja tuishi kule?” “Upo kama kaka yako!” Wote wakacheka.

          “Kweli. Wote hamsahau jambo, na mking’ang’ania kitu, kinakuwa hichohicho na mpaka mpate.” “Hiyo ipo kwenye damu. Sasa hujakutana na Nana. Nana ndio mbaya zaidi. Hajui jibu la ‘hapana’ anapotaka jambo lake. Na hapendi mtu aombe kitu ambacho hajakifikiria, au hana umuhimu nacho. Na anashangaa ukiwa unataka kitu halafu ukakikosa, ukatulia. Anasema inamaana unataka kitu ambacho kwanza kinakuwa hakina umuhimu. Na inamaana hujafikiria ndio maana ukikikosa inakuwa rahisi kuridhika.” Tunda akapata hapo somo.

“Nana ni nani?” Tunda akamgeukia Net. “Bibi ndio tunamwita Nana.” Net akajibu. “Oooh! Anaonekana ni smart.” Tunda akasifia. “Hujawahi kuona mwanamke kama huyo hapa duniani.” Tunda na Net wakacheka. “Lakini ni kweli. Nana yupo very smart. Wakati wote huwa anajua anachokitaka. Na kama alivyosema Maya, huwa hajui jibu la hapana, linapofika swala la kukamilisha jambo lake. Anaweza kuhamisha milima, ili kukamilisha swala dogo ambalo kwako linaweza hata lisilete maana.” Net akaweka msisitizo.

“Kwa hiyo tunakwenda au tunabaki?” Maya akarudia swali. Wakacheka. “Eti Net? Haitakuwa usumbufu?” “Hata kidogo. Ni sehemu kubwa. Utapata chumba chako na utanisaidia kusikiliza kelele za Maya, ili niweze kufanya kazi.” “Heeee!” Maya akalalamika nakukunja mikono kifuani kwake kama mtoto, akimtazama kaka yake. Wakacheka. “Basi nitahamia kesho. Acha nifungashe usiku wa leo.” Tunda akubali kwenda kuishi nao nyumba moja.

Tunda afanyika Msaada kwa Maya.

Nikweli alibadili maisha ya Maya. Kwa kuwa na yeye alikuwa akiongea kingereza kizuri, ilimrahisishia sana Maya kwenye mawasiliano, kwani mama yake ndiye aliyekuwa akimlazimisha kujifunza kiswahili. Tunda alimweleza maisha ya shida aliyopitia, bila kwenda kiundani zaidi, na kumwambia kama angepata nafasi kama yake, angeitumia vizuri sana.

Ilikuwa ni muujiza hata kwa Net. Maya alikuwa akimsikiliza sana Tunda kuliko mwanadamu yeyote yule aliyekwisha kuwa naye karibu. Kwa asili Maya alikuwa mbishi sana. Haambiliki na alilelewa maisha ya kudekezwa sana na bibi na babu yao. Hakuwa akijua shida hata kidogo. Tunda aliongea na Maya mpaka akakubali kurudi shule. Net alifurahi sana, akamshukuru Tunda. Alimpigia simu mama yake akiwa kule kule nchini Canada, Maya akarudishwa Canada kwa ajili ya kuanza chuo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hali ya babu yao ilizidi kuwa mbaya huko nchini Canada, ikamlazimu Net aende. Hawakuwa ni babu tu na bibi. Waliwalea Net na Maya tokea wadogo sana tokea  baba yao alipoanza kuugua mpaka akafariki. Na hata mama yao alipoondoka nyumbani kwa wakwe na kurudi nchini Tanzania, wao walibakia kwa bibi na babu yao. Walitunzwa wakachukua nafasi ya watoto kwa hao wazee waliokuwa wamepata mtoto mmoja tu ambaye ndiye baba yake Net na Maya.

Net alichukuwa jina la babu yake. Natheniel Cote. Ilibidi kuwa wakiandika sehemu muhimu wawe wanaandika Jr au Seniour ili kujua ni yupi. Shule zote za mahela yote hayo alizosoma Net, alikuwa akilipiwa na babu yao. Alipendwa sana, na alimkuza Net kwenye maadili ya msingi. Ndio maana Net alikomaa mapema japo alitoka kwenye familia ya kitajiri sana. Kila mtu alijua Net ndiye mrithi wa mali nyingi za huyo mzee Cote.

Kwa kuwa Maya alishaondoka nchini, wawili hawa walibaki wakiishi pamoja, kazini pamoja, kwenye gari pamoja. Japo haikuwa kwa muda mrefu, lakini palishajengeka ukaribu kati yao.

Net Arudi nchini Canada, Nakumlazimu kutengana na Tunda.

Tunda ndiye aliyemsindikiza Net uwanja wa ndege. Alikuwa amepooza. “Utakuwa sawa Tunda. Na nitakuwa nikikupigia simu kila siku. Kama ukiwa na maswali yeyote kazini, nikipiga simu nitakuwa nakusaidia.” “Lakini haitakuwa sawa kama tulivyokuwa wote! Najiona kama bado nakuhitaji sio tu ofisini, hata kwenye maisha ya kawaida. Naomba uniahidi kuwa utarudi Net.” Net alimuhurumia Tunda akajua aliingiwa na hofu na ndio maana hakumuaga mapema.

Tunda hakujua huyo Net alikuwa akisubiriwa kwa muda mrefu sana, lakini akawa akiahirisha safari kwa ajili yake. Kila alipojiambia ataondoka, alikuwa anaona bado hili na lile. Akawa akimwambia bibi yake nitakuja hivi karibuni. Lakini hakwenda mpaka alipoambiwa hali mbaya, anaweza asimkute babu yake, ndipo ikamlazimu kuondoka.

Akamgeukia vizuri. “Niangalie Tunda.” Tunda akamwangalia vizuri. “Nikikwambia hata mimi natamani nisiondoke, utaamini?” Tunda akatingisha kichwa kukubali. “Basi ujue nitarudi haraka. Niombee mambo yaende vizuri.” Walitafuta sehemu wakakaa, wakati wakisubiria muda wa Net wakuondoka. Tunda alikuwa amejisogeza karibu yake, ameinama. Hakuondoka mpaka Net alipoingia kwenye ndege.

 

Maisha bila Net.

Tunda alitulia, akashika usukani. Ni kweli aliiendesha ile ofisi bila shida, huku akitumia gari ya Net na kuishi kwenye nyumba yao. Tunda hakuacha kuwasiliana na Net kumpa taarifa kwa kila kinachoendelea na kumtaka ushauri. Na kwakuwa na yeye alifanywa kuwa muweka saini benki, hata malipo mengine alifanya yeye mwenyewe, tena kwa uaminifu sana. Kila mwishoni mwa juma, alimtumia Net benki statement na ripoti ya matumizi yote. Walishauriana kwenye simu, na Net aliweza kuendesha mambo ya pale ofisini, akiwa mbali, kirahisi sana kwa msaada wa Tunda.

 

Tunda apambana na Mama Cote.

Tokea aachane na Mama Cote pale kanisani hakuwa amemsikia tena huyo mama. Hata kupokea simu yake ya salamu hakupokea tena. Haikumsumbua Tunda kabisa, alijua ni hali ya ubusy kwani yule mama alikuwa muhangaikaji sana kisha akawa amekwenda nchini Canada kumuona huyo mgonjwa ambaye ni mkwewe.

Ilikuwa siku ya jumamosi ambapo Tunda alishazoea kufanya nusu siku alipokuwa na Net, lakini sababu ya kuwa peke yake aliitumia hiyo siku kukaa ofisini mpaka usiku. Alifanya mambo mengi, na akatayarisha ofisi ile kwa siku ya jumatatu. Kijana wa usafi hakuwa akija siku za jumamosi, kwa hiyo kila alipotumia ofisi siku za jumamosi, alijitahidi kuacha safi ili asimsumbue kijana wa usafi anapokuja siku ya jumtatu.

Alishaongea na Net wakati Canada ilipokuwa usiku wakapeana maelekezo na miahadi yakupigiana tena simu siku inayofuata, pale Tunda atakapo amka. Tunda akarudi nyumbani akiwa amechoka sana. Mlinzi akamfungulia geti, akamsalimia kwa kumpungia mkono akaingia ndani.

Alipoingia ndani, akakuta Mama Cote amekaa na msichana mwingine pale sebuleni. “Net hakuniambia kama mnaishi naye hapa!” “Sikuwa nikiishi na Net peke yake, mama. Maya ndiye alinikaribisha hapa.” “Maya!?” “Ndiyo mama. Shikamoo.” “Mwanzoni ulikuwa ukiishi wapi?” “Hotelini, mama.” “Kweli Net alikubali kukutoa kwenye nyumba za kulala wageni akakuweka hapa na mtoto mdogo kama Maya!?” Tunda akanyamaza. Hakuwa ameelewa kabisa, kwani Mama Cote aliyemfahamu yeye alijawa na hekima na mwingi wa shukurani. Na alimkarimu sana nyumbani kwake, akampa hata chumba chakuweka mizigo yake na kukitumia kama angelala.

“Kuna nini mama!?” “Nimeshtuka sana kukukuta nyumbani kwangu!” “Samahani mama, itakuwa Net amesahau kukwambia. Hata hivyo naweza kuondoka tu hata sasa hivi.” “Kabla hujaondoka nataka kukutambulisha kwa bosi wako mpya, huyu hapa. Anaitwa Safia. Safia amesoma na anauzoefu wa kazi, kwa hiyo atakusaidia sana.” “Karibu sana Safia. Basi jumatatu nitakuonyesha pale ofisini.” “Sio kumuonyesha tu! Nataka umkabidhi kila kitu, yeye ndiye atakuwa akikwambia kitu gani chakufanya.” Tunda alishtuka kidogo, lakini hakujali. “Sawa mama.” Tunda akaitika.

“Na atakuwa akitumia hicho chumba ulichoweka mizigo yako.” “Hakuna shida mama yangu. Nitaondoka na kila kitu.” Tunda akaingia ndani, akakusanya vitu vyake vyote, akaweka kwenye begi lake akaanza kulivuta kulitoa nje pamoja na mizigo yake mingine iliyokuwa na nguo, viatu pamoja pochi zake nyingi tu ambazo alipenda kubadili kama viatu. Akakumbuka amesahau funguo za gari ndani.

Akarudi wakati ameacha mizigo yake yote nje. Alipoingi tu, “Halafu binti!” Tunda hakujua kama anaitwa yeye, aliendelea kuelekea kule alipokuwa ameacha pochi yake aliyotumia siku hiyo. “Wewe Tunda, umeanza lini kiburi?” “Kwa nini mama?” “Nakuita kwa nini unanyamaza!?” “Sikujua kama unaniita mimi. Samahani.” Tunda aliendelea kujibu kwa heshima sana. 

“Naomba na funguo za gari. Atakuwa akitumia yeye hilo gari, kabla hatujamnunulia la kwake.” Tunda alifikiria kidogo. “Sasa hivi ni usiku mama. Naomba niondoke na gari, kisha nitarudisha gari asubuhi ili nisipate shida ya usafiri na mizigo yangu.” “Naweza kukuitia taksii.” Tunda akatulia kidogo, kisha akamsogelea Mama Cote.

“Kwani kuna tatizo lolote mama yangu? Mbona kama..” “Hakuna tatizo lolote. Mimi ndiye mmiliki wa kila kitu, au Net hakukwambia hilo?” “Nafahamu.” “Sasa unauliza nini endapo mwenye mali anadai mali zake!?” Tunda akabaki ameduaa.

“Na ninaomba funguo za ofisini kabisa, pamoja nafunguo za safe. Kwa kifupi naomba funguo zote za ofisi na simu ya ofisi pia naomba.” “Unamaanisha simu yangu ya mkononi!?” “Si ulinunuliwa kwa matumizi ya ofisini? Sasa unapunguziwa majukumu, huhitaji tena simu ya mkononi.” Tunda alibaki ametoa macho kwa muda.

“Vipi? Au uliahidiwa nini na Net? Isijekuwa navunja makubaliano fulani.” Tunda alivuta pumzi kwa nguvu, kisha akanyanyua pochi yake, akatoa simu na funguo zote za ofisi na gari kisha akamkabidhi. “Asante mama, usiku mwema.” Tunda akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ulikuwa ni mshtuko mkubwa sana kwa Tunda. Alijiuliza maswali mengi bila kupata jibu. Alifikiri hili na lile bila kuhisi kosa lake. Alikuwa na wakati mgumu sana akisubiria hiyo siku ya jumatatu, hata kanisani alishindwa kwenda.

Hakuwa na simu ya kuwasiliana na Net, kwa kuwa simu alinyang’anywa. Simu yake ilipotea kwenye mazingira ya kutatanisha. Hakujua kama aliiacha sehemu au aliibiwa kwenye pochi. Alijikuta hana simu ndipo Net akampa iliyokuwepo tu pale ofisini na kumtaka aitumie akisema ni muhimu kwa kazi kwa kuwa yeye alimwambia hana shida tena na simu. Hana mtu wakuwasiliana naye. Lakini yule mama alimpokonya. Ilikuwa simu nzuri sana.

Jumatatu ya machungu na mapinduzi!

Siku hiyo ya jumatatu aliamka mapema, na kuwahi ofisini. Alifika ofisini na kumkuta Mama Cote yupo ofisini kwa Net, na Safia yupo kwenye meza yake. Tunda aliweka pochi yake pembeni ya meza, akaingia kumsalimia Mama Cote. “Shikamoo mama.” “Naona hapa mambo yamekuwa yakiendeshwa kienyeji enyeji kweli! Sioni faili lako la kuajiriwa. Sioni vyeti vyako wala barua zako zakuomba kazi.” Tunda akabaki kimya, lakini mwili mzima ukitetemeka.

“Naomba ukaniletee vyeti vyako vyote vya shule,  ili tujue kama ni kazi ninakuajiri upande upi.” Tunda alibaki kama amepigwa na butwa. Kimya. “Umenisikia?” “Sina vyeti mama.” “Kwa nini huna vyeti?” “Sina vyeti kabisa.” “Kwani hukusoma!?” Yule mama akamuuliza kwa namna yakumdhalilisha mbele ya Safia na yule kijana wa usafi, waliokuwa wakisikiliza pale nje. Tunda akanyamaza.

“Hata cheti cha kidato cha nne huna!?” “Sina mama.” Tunda alishaanza kupaniki. Hofu yakufukuzwa kazi ikamjaa. “Wewe ulilemea upande mmoja tu, kutembea na wanaume za watu! Ukapata ujuzi wa kuvutia wanaume, ukakosa ujuzi wa ofisini! Sasa hapa Net wa kumrembulia macho ili aendelee kukuweka hapa ofisini, hayupo. Hii ni ofisi yangu. Nimehangaika sana kufika hapa nilipo. Sikutafuta pesa kwa kuvulia nguo waume za watu, nimehangaika mimi mwenyewe. Uzembe mdogomdogo sitaki. Hamkawii kunirudisha chini kimaendeleo!” Yule mama alianza kupiga mahesabu, kisha akanyanyuka.

Akafungua safe akatoa pesa. “Huu ndio mshahara wako wa mpaka siku ya leo. Rudi shule binti, acha kuruka ruka na wanaume. Ukishapata vyeti ndipo urudi tuzungumze.” Bila kuongeza neno, Tunda akapokea pesa yake, na kuondoka pale.

Historia Yajirudia! Maisha mengine tena kwa Tunda mara baada ya kufukuzwa ‘Tena’ kwa kina Cote.

Tunda alirudi hotelini, akakaa chini asiamini kinachomtokea. Aliumia sana kusikia anatukanwa na Mama Cote, kwa kupitia maneno aliyosema kanisani, tena akiwa ameambiwa ni sehemu pekee ambapo atakuwa salama! Tunda akalia sana, lakini alikumbuka jinsi alivyofundishwa na Net kuomba.

Akapiga magoti akamuomba Mungu kwa kulia sana. Tunda akamlilia Mungu kwa uchungu akirudia rudia kumweleza maumivu aliyonayo. Hakuwa mjuaji sana wakuomba, lakini alijua kumueleza Mungu kile alichokuwa akijisikia. “Naogopa sana Mungu wangu. Nimeumia, nina maumivu makali sana. Sijasoma, sina kimbilio, sijui naanzia wapi tena maisha. Katika yote naomba nisaidie nilinde mwili wangu usiteswe tena. Sitaki kurudia yale maisha tena. Nisaidie kwa njia yeyote ile ili niweze kuishi kwa uwezo au karama yeyote uliyoniumba nayo, ukaweka ndani yangu kama alivyoniambia Net, kuwa kuna kipaji lazima umekiweka ndani yangu ambacho kitanisaidia. Usiniache tena. Milango yote naiona imefungwa, lakini najua Mungu wewe unaona kwa tofauti. Nisaidie.” Tunda akamaliza kuomba, akapata faraja ya ajabu.

          Wazo la kurudi Dar likamjia. Hakutaka kupoteza muda tena pale hotelini, akabeba mizigo yake yote, asubuhi hiyo hiyo akaenda kituo cha mabasi pale jijini Arusha, akakata tiketi yake akapanda basi kurudi Dar. Alionelea ni heri kurudi Dar, mji alioufahamu vizuri kuliko kuendelea kuishi Arusha. Hata hivyo vitu vyake vyote aliviacha huko.

Tunda arudi jijini Dar na kupambana Njiani na Jaribu akumrudisha kule Yesu alikomtoa kupitia Net.

Tunda alipata siti ya upande wa watu wawili. Pembeni yake alikaa baba mmoja mtu mzima kidogo. Walisha salimiana, lakini yule Mzee hakutosheka kumtizama Tunda. Na Tunda alijua. Akaamua kutoa bibilia yake asome ili kumfanya yule baba amuogope. “Soma kwa sauti basi na mimi nisikie neno.” Yule mzee alimtupia neno Tunda.

“Naweza nikakupa tu, usome mwenyewe.” Tunda akataka kumkabidhi. “Unakwenda kanisa gani?” Tunda hakuwa hata na kanisa analolifahamu huko Dar. “Ndio nahamia Dar, bado sijajua nitapata wapi kanisa.” “Ooh! Karibu sana jijini. Kwa hiyo hata sehemu yakuishi bado hujapata?” “Ndio naelekea huko. Naamini nikifika huko nitapata.” “Basi mimi niwe mwenyeji wako. Nina nyumba yangu napangisha vyumba huko Temeke. Naweza kukupangisha. Tena kuna mpangaji mmoja ametoka juma lililopita tu, nilikuwa nakikarabati hicho chumba. Ni chumba kimoja na sebule yake. Kwa kuwa ndio unahamia hata huna haja yakunilipa kodi kwa sasa, tutakatana juu kwa juu.” Tunda alitabasamu kisha akageukia dirishani.

“Vipi?” Akaendelea kutaka Tunda amsikilize. “Na kanisani nitakupeleka usiwe na wasiwasi.” Tunda akamgeukia yule Mzee akamtizama kwa muda, asiamini kama historia inajirudia kwa haraka kiasi hicho! “Au hutaki kuishi Temeke? Tunaweza tukashukia hotelini wakati tunatafuta nyumba nzuri ya wewe kuishi.” Tunda alifunga bibilia yake akairudisha kwenye pochi yake....

      ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alianza uchangudoa, akiuza mwili wake akitokea hospitalini akiwa hajui chakufanya kwa namna hiyohiyo huyo Mzee anayotaka kumpa hapo.

 Je, historia yajirudia tena?

 Safari hii Tunda anaponea wapi? Endelea kusoma.

0 comments: