Nilipotea! -PART 3 - Sehemu ya B.
Tunda
alichoka kabisa. Akidhani ile bibilia ingemtia hofu yule mzee, lakini ndio
ikawa njia moja wapo ya kumtongozea. Akageukia dirishani. Moyoni akaanza
kumwambia Mungu, ‘Nilikuomba
unisaidie nisirudi huko tena, lakini mtu wa kwanza unanikutanisha naye baada ya
maombi, ni huyu! Ni njia gani hii unatumia kunisaidia? Unanikutanisha na mtu kama
huyu ambaye anauwezo wa kunipa msaada wa vitu unavyojua wazi ndio ninahitaji
kwa sasa! Kwa nini hunihurumii? Nimeteseka miaka yote, ndio kwanza nafurahia
utulivu nilio nao. Umenipa furaha na amani, kisha unachukua kila kitu kwa
wakati mmoja! Umechukua kazi yangu, umenifukuza pale kwenye ofisi, halafu
unaniletea mtu wakunisaidia kurudi kwenye yale yale maisha niliyokwambia
siyataki!’ Tunda aliendelea kumlaumu Mungu kwa kunung’unika moyoni.
Akapitiwa
na usingizi, mpaka aliposhtuliwa na yule
Mzee kumwambia ashuke wakale. Tunda akakataa. “Asante, lakini sitakula.” “Kwa
nini?” “Nataka nipate muda wa kuongea na Mungu. Wewe nenda tu.” Yule Mzee
alimtizama Tunda kwa muda mrefu kidogo, kisha yeye akashuka.
Alibaki
peke yake kwenye basi, akafunga dirisha ili kupunguza fujo za watu wanaotaka
kumuuzia vitu. Akainama nakuanza kuomba upya huku akijiuliza yeye mwenyewe
maswali na huyo Mungu aliyetambulishwa na Net. Tunda aliomba huku akilia kwa
hofu ya itakuaje. Akaendelea kumsihi Mungu asimjaribu zaidi. Alijua wazi mshahara
aliolipwa na pesa nyingine alizonazo, haziwezi kudumu kwa muda mrefu.
Alifikiria
wapi pakwenda mara baada ya kushuka kwenye hilo basi! Nini chakufanya mara
baada ya kujua pakwenda! Yule mama alikuwa sahihi kabisa, hakuwa na cheti. Kama
pale kwenye ile ofisi aliweza kufanya kazi vizuri, wakaona utendaji kazi wake
na bado wakataka vyeti, nani atampa kazi bila vyeti wakati hawamfahamu? Maombi
ya Tunda yalichanganyikana na maswali mengi sana. Alibaki ameinama ili aombe,
akajikuta haombi tena anawaza tu.
Tunda na fundisho la
watoto njiani.
Aliamua
kukaa vizuri na kugeukia dirishani aendelee tu kuwaza. Aliona watoto wadogo
wawili wakicheza wakati mama zao wakiuza matunda. Mtoto mmoja alikuwa mkubwa
kidogo kwa mwenzake. Yule mtoto mkubwa alikuwa na gari alilokuwa ametengeneza
vizuri sana kwa vijiti, alivyovipangilia kwa ustadi, mpaka akatengeneza muundo
wa gari. Akaweka matairi ya mifuniko ya soda{Visoda}. Tunda alimuona jinsi
alivyokuwa akiendesha lile gari pembeni ya mama yake, akienda mbali kidogo na kurudi,
lakini si mbali na macho ya mama yake.
Mtoto wa
pili, yule mdogo, alikuwa akichezea vumbi tu, mwishowe yule mdogo akamuomba
yule mtoto mwenye gari ampe achezee na yeye. Bila tatizo, akampa.
Yule
mtoto mdogo, alionekana kufurahia zaidi lile gari kuliko mtoto mkubwa ambaye ni
mmiliki. Alitoa milio mbalimbali kwenye mdomo wake kuonyesha akiigiza mlio wa
magari ya kweli, kitu kilichomvutia Tunda na kuanza kucheka na kujikuta
akifungua dirisha na kuendelea kumtizama yule mtoto aliyeazimwa gari. Alitoa
mlio wa honi, kuweka breki kwa nguvu, huku akiendelea kucheza na gari ya
mwenzake.
Mwenye
lile gari alipoona yule mwenzake anafaidi na gari yake zaidi yake, akaamua
ampokonye, tena kikatili, kwa jeuri kwa kuwa lilikuwa lake. Tunda akashtuka kwa
kumuhurumia. Ulizuka ugomvi kati yao, lakini mwishowe mwenye nacho alishinda
baada ya wazazi kuingilia kati.
Yule
mdogo alianza kulia sana, akitaka lile gari ambalo halikuwa lake. Na yule
mwenye nalo akaanza kuchezea kama yule mdogo alivyokuwa akifanya. Alitoa milio
ileile, na alifanya zile zile mbwembwe kama mwenzake alivyofanya lakini
haikupendeza hata kidogo. Mwishowe akaigiza kuweka breki kama yule mtoto, lile
gari liligonga jiwe na kuharibika kabisa.
Lakini
kabla ya lile gari kuharibika. Wakati yule mkubwa akiendelea kuchezea gari
lake, yule mdogo aliacha kulia, akaokota boksi la biskuti, akatumia meno yake
kutengeneza madirisha na mlango. Kisha akaokota pale pale vijiti vile vya
kutolea uchafu kwenye meno ambavyo watu walisha tumia na kutupa tu.
Akaunganisha kadhaa ili viwe virefu na vigumu. Akatoboa sehemu ya kuchomeka
matairi, akaweka vile vijiti. Tunda bado akiwaangalia tu. Yeye ndani ya basi,
wale watoto nje pembeni kwa mama zao, na wao wakiongea yao na kubembeleza
wateja.
Kwa kuwa
yule mtoto mdogo hakuwa na visoda, au mifuniko ya chupa za soda, yeye aliweka
makaratasi magumu kidogo ndio yakawa matairi yake. Akaokota tena kijiti au mti
mdogo, lakini mrefu na mwembamba akachomeka nyuma ya lile boksi, iwe kama
usukani wake wakuongoza lile gari. Tayari akawa ametengeneza gari zuri tu, tena
kwa muda mfupi, akaanza kuliendesha.
Wakati
ndio analifurahia gari yake hiyo, ndio mwenzake akapata ajali na yakwake,
ikaharibika. Kwa hiyo akabaki yule mdogo ambaye alinyang’anywa gari, akiwa na
lake. Tunda alimuona yule mdogo akicheka sana. Akimcheka mwenzake, yule mkubwa
aliyekuwa amekaa chini hana tena gari. Lilikuwa ni tukio la muda mfupi tu,
lakini lilichukua akili za Tunda zote na kumfanya atulie na kutafakari.
Basi lilianza kuondoka huku bado
Tunda akiwawaza wale watoto. Alijiambia ni ujinga kuwaza jambo la kitoto kama
lile, lakini bado akili ilimrudisha pale kwenye wale watoto. Akasikia swali
mayoni mwake, ‘Kama
yule mtoto asingepokwanywa lile gari, je angepata wazo la kutengeneza gari
lake?’ Tunda alifikiria kidogo akaamua kujijibu. ‘Lakini kweli! Afadhali alivyopokwanywa akapata akili ya kutengeneza
gari lake.’ Tunda akajijibu. ‘Lakini alilia sana!’ Tunda akawaza kwa
kumuhurumia yule mtoto.
Likapita swali jingine. ‘Kama angeendelea kulia pale alipokuwa amekaa pembeni ya mama
yake, bila kusimama na kuchukua hatua ya kutengeneza gari lake, angepata gari
jingine?’ Tunda akafikiria na kukumbuka lile tukio tena. Alikumbuka
jinsi mama yake alivyokuwa akimbembeleza kwa kumpa matunda ili atulie lakini
yule mtoto alikataa kata kata, aliendelea kulia akitaka gari ya mwenzake mpaka
alipoamua kunyanyuka na kutengeneza gari lake.
‘Afadhali alitumia akili. Angekubali tu kubembelezwa na mama yake akala
yale matunda, angesahau kabisa kitu anachokita, gari. Akabaki hana gari mpaka
sasa.’ Tunda akajijibu na swali jingine
likamjia tena. ‘Kwani angekubali faraja ya mama yake,
akaacha kutengeneza gari yake, ingeondoa ujuzi alionao wakutengeneza gari?’ ‘Hata
kidogo. Si angekuwa ni mjinga tu, amekataa kutumia ujuzi wake na kubaki
akililia gari la mwenzake!’ Tunda akajibu haraka haraka tena kwa hasira.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya
hapo Tunda akapitiwa na usingizi, kisha akashtuka sana. Ikawa kama kitu
kimemuamsha huko usingizini “Mimi ni mjinga sana, hata yule mtoto anaakili
kunizidi mimi!” Tunda akamwambia yule Mzee na kumuacha akimshangaa. “Sipo hata
nusu ya yule mtoto!” Tunda akarudia kumsisitizia yule Mzee, lakini yule mzee
aliyekuwa amekaa pembeni yake akamtongoza, alijua Tunda anaota kwa kuwa alikuwa
amelala. “Binti, punguza sauti. Ulikuwa umelala, na hapa tupo kwenye gari.”
“Hapana sioti.” Watu wapembeni yao waliwageukia na wa mbele pia waligeuka kwani
Tunda alikuwa akiongea kwa sauti iliyojaa kufunguka kimawazo.
“Ni
kweli yule mtoto ana akili sana. Sikiliza nikwambie hiki kisa, kimetokea sasa
hivi mliposhuka kwenda kula.” Tunda akasimulia kile kisa chote cha wale watoto
na kuvuta masikio ya abiria wengi sana ndani ya lile basi. “Nisikilize vizuri.
Mimi nimetoka Arusha sasa hivi sababu ya kufukuzwa kazi ambayo niliifanya
vizuri sana. Sikuwahi kuiba, wala kukosea hata siku moja. Niliifanya kwa makini
na juhudi zangu zote. Niliifanya ile kazi mpaka usiku bila kuomba malipo ya
ziada.”
“Lakini
leo asubuhi mwenye ofisi amemleta mtu mwingine, na kunifukuza mimi kazi
kikatili, kwa kuwa tu sikuwa na vyeti.” “Kwa nini na wewe huna vyeti?” Yule
Mzee aliuliza swali lililomfanya Tunda aliyekuwa akisimulia kwa kuchangamka
apooze ghafla. Abiria wengine wakaongezeka kusikiliza. Maana wengi walikuwa
wakisinzia mara baada ya kula chakula basi liliposimama. Ila kwa sauti ya
kuchangamka ya Tunda, hata waliokuwa wamelala, wakaamka na kuendelea kumsikiliza
Tunda aliyegutuka baada yakubaini ule mfano unamuhusu. Kwanza kwa sauti hiyo ya
Tunda, lazima utataka kuisikiliza hata ukiwa mbali, utageuka tu ili kutaka
kuiweka kwenye sura husika. Kuiona sura ya hiyo sauti.
“Sikusoma
baba yangu. Nilipata hiyo bahati ya shule lakini ilichanganyikana na majanga
mengi yaliyonifanya nishindwe kusoma kabisa. Sikubahatika kulelewa na wazazi
wote wawili. Nimekuwa nikihama hama huku na kule.” Tunda akaelezea kisa chake
kilichowavuta watu wote sasa kwenye lile basi huku wakimuomba aongeze sauti.
Akapiga magoti kabisa kwenye kiti chake, nakusimulia. Wazazi wengine walianza
kumtukana mama yake Tunda, wengine bibi, wengine mama wa kambo wengine shangazi
ilimradi basi zima pakageuka kukawa gumzo juu ya Tunda.
“Lakini baadaye niliishi maisha machafu sana,
mpaka nikakutana na mtoto wa huyu mama aliyenifukuza kazi.” Napo hapo Tunda
aliwaacha midomo wazi. “Mmmh! Pole sana mwanangu. Dunia mzunguko! Inaweza
kukufanya ukafanya jambo ambalo hata hukutegemea.” Mama mmoja mtumzima pembeni yake
aliongea.
“Ndio
muache kuwasema machangudoa. Hamjui kwa nini wanafanya wanayofanya.” Dada
mwingine kiti cha mbele alidakia. “Ndio maana yake. Maana kuna watu wanapenda
kweli kuhukumu watu.” Mwingine akadakia. Abiria wengine wakawageuzia na wao
macho kuwasikiliza na wao wakizungumza kwa jazba.
“Lakini
mimi Mungu amenipa nafasi nyingine. Mtoto wa huyo mama alinirudisha kanisani,
nikatubu, Mungu amenisamehe. Nilitolewa majini kwa mapepo kwenye huu huu mwili
watu waliokuwa wakiutamani na kutumia. Wasijue walikuwa wakilala na majini pia.
Anyways, baada ya yote, huyo kijana akanipa na hiyo kazi niliyopokonywa.” Tunda
aliwakata maneno.
“Bahati
yako wewe ulimpata huyo kijana. Sasa unakuta ndio kama hivyo mtu hana maisha,
leo unamwambia aache uchangudoa, unataka aishije? Wewe umepata kazi, ndio maana
umeacha.” Huyo dada aliongeza, kila mtu alihisi yule dada na yeye ni changu.
“Lakini nisikilize dada,
nakwambia leo nimefukuzwa kazi. Hapa nilipo naelekea Dar, sina pakwenda, sijui
chakufanya na wala simfahamu mtu yeyote huko Dar japo nimeishi kwa miaka mingi
na nilikuwa na kwangu tena pazuri, kama nilivyowasimulia. Nipo kama hivi
mnavyoniona.” Tunda akaendelea akiwa amejawa nguvu hata asijue amewezaje
kuzungumza vile bila woga.
“Mlipokuwa
mmeenda kula nilibaki humu ndani nikilia, ndipo nikaona kisa cha hawa watoto.
Nikikwambia kulia, nilianzia kulia kule hotelini. Lakini huu mfano wa huyu
mtoto mdogo, umenifundisha au unanihusu. Huku kulia kutanichelewesha na mimi
kupata changu. Kurudi kuwa Changu ni kama nakubali faraja ya matunda ya muda
mfupi, itakayonifariji kwa muda mfupi tu, nakusahau nini nataka katika maisha.”
Tunda akaendelea.
“Lazima nisimame na mimi nitengeneze chakwangu.
Hata kama sijasoma, na mimi nitaanza kwa kuokota maboksi, vijiti vyakutolea
uchafu kwenye meno ambavyo watu wanatupa, nitatengeneza gari yangu kama yule
mtoto.” Kisha akauliza swali. “Kwani huyu aliyetengeneza hili basi tulilopanda
sasa hivi, si binadamu kama sisi tu? Alikubali kuacha vishawishi vyote,
akajikana na kukaa chini, akaunganisha vyuma na mipira mpaka tukaliita basi.”
“Basi na mimi nitatafuta cha kwangu. Sitaki kulia
tena wala kumchukia mtu. Nitajichelewesha kupata vyangu.” Tunda alishangaa
kuona watu wote kwenye basi wakimpigia makofi. Alishtuka sana, kwani bado
alikuwa amepiga magoti kwenye kiti chake akiongea kwa sauti na yule dada kwenye
kiti cha mbele kabisa aliyekuwa akitetea
uchangu. Akawa kama ameshtuliwa, akarudi kukaa vizuri na aibu ya ghafla usoni.
“Unaakili binti. Nakupongeza.” Yule mzee
aliyemtongoza na kumpa wazo hata lakumtafutia hoteli akajikuta akimpongeza tena
Tunda. Lakini kwa sauti ya chini iliyojaa aibu kidogo na kujirudi. “Asante.”
Tunda akacheka taratibu. “Na naomba nikuombe radhi.” “Wala usijali baba yangu.
Ulikuwa mtihani wangu huo. Mungu alitaka kunipima, ajue nimeamua vipi kutorudi
nyuma. Pale uliponiambia vile, ukaniona nimegeuka dirishani, nilikuwa
nikimlilia Mungu aniepushe na watu kama wewe. Kwa kuwa ndivyo nilivyoanza kazi
ya uchagudoa hivyohivyo.”
“Nilitoka hospitalini nikiwa sijui pakwenda. Wakati
nimeenda kula mahali, nikakutana na mmiliki wa hilo eneo. Ndiye niliyeanza naye
hiyo biashara. Akaniweka hotelini kama vile ulivyonishawishi mwanzo. Sasa na
wewe ulivyonitongoza, na ahadi ya pakuishi, niliumia sana. Nikakumbuka
niliingia kwenye ule uchafu mwanzoni kabisa sababu sikuwa na pakwenda. Sasa
nikaona historia inataka kujirudia tena. Inakuwa vile vile na sababu ile ile.
Ila nimekusudia baba yangu, sitarudi nyuma. Hata kama nitalala stendi ya
mabasi, acha nihangaike tu mpaka nione mwisho ni nini.” Yule mzee alijisikia
vibaya sana, na dhamira ikamsuta.
“Binti naomba unisamehe sana. Nimepitiwa na shetani
tu.” Tunda akacheka. “Yameisha baba yangu.” “Ila kile chumba nilichokwambia ni
kweli kilikuwepo, ila sijui kama dalali alishapata mteja! Kama upo tayari
kuishi maeneo ya Temeke, naweza kumpigia simu yule dalali ili asikikodishe tena
ili wewe ukaishi huko.” “Kodi ni kiasi gani?” “Yule mzee akamtajia.” Tunda
akafikiria kidogo.
“Naomba nikulipe ya miezi mitatu wakati najipanga
upya.” “Nitaongea na mke wangu tuone, maana ndio nyumba anategemea sana yeye.”
“Unaweza kuwasiliana nao hao watu wawili ili mpaka tukifika Ubungo kituo cha
mabasi, niwe najua kama nimepata au nihangaike kwingineko?” “Sawa.” Yule Mzee
akakubali.
Alimpigia simu dalali, dalali akamwambia ndio
ametoka kumpeleka mtu na mkewe hapo kwenye hicho chumba, wamepapenda na
wamekubaliana kesho awapeleke kwa mke wa yule Mzee wakaandikishiane mkataba. “Basi hebu usubiri kidogo, usikikodishe kwanza niongee na mke
wangu.” “Wanalipa kodi ya mwaka Mzee.” “Naelewa. Lakini hebu subiri.”
Akakata simu.
“Vipi? Amesemaje?” Tunda akauliza kwa wasiwasi
kidogo. “Anasema amepata mteja, tena mwenye kodi ya mwaka. Ngoja nimpigie simu
mke wangu kwanza kabla hajawakodisha.” Tunda akakosa raha. Akabaki kimya.
“Mimi nitalipia hiyo kodi ya huyu binti.” Tunda akashtuka
sana. Akamgeukia huyo aliyesema. Alikuwa ni kijana tu. Alikuwa amependeza,
akaonekana nadhifu, kijana aliyefanikiwa. Shingoni alikuwa amevaa cheni
aliyofanya juhudi za makusudi kuonekana. Ilikuwa dhahabu. Tunda muelewa vitu
vya thamani, aliweza kutambua uhalisia wa ile cheni shingoni kwa yule kaka. Na
saa nzuri sana tena ya thamani. Alikuwa amekaa kiti cha nyuma kabisa. Watu wote
wakamgeukia.
“Kwamba?” Yule Mzee akauliza kutaka uhakika kabla
hajazungumza na mkewe. “Nimesema mimi nitalipa hiyo kodi ya mwaka mzima ya huyo
binti. Kama kumtia moyo kwa maamuzi magumu anayofanya.” Tunda aliogopa sana.
Hakutaka kuja kudaiwa mapenzi baadaye. “Na wala hizo pesa hutazipata kwangu,
utazikuta kanisani kwetu. Nitamkabidhi mama Mchungaji wetu. Utakapokuwa tayari,
ukiipenda hiyo nyumba, wewe njoo kanisani kwetu utachukua pesa yako. Hata kama
hutaipenda hiyo nyumba, tafuta nyingine, ila ujue pesa ya kodi ya mwaka mzima
unayo tayari.” Tunda alianza kulia kwa furaha.
“Sikilizeni jamani.” Yule kaka akasimama. Akaanza
kuongea mambo ya Mungu. Watu walikuwa wakimwangalia bila kupepesa macho. “Huyu
Mungu yupo na wakovu ni halisi. Ukubali ukatae.” Yule kaka alianza kwa kusema
hivyo.
“Wengine tumeua, tukauza madawa ya kulevya,
tukavunja majumba ya watu, tumepita humo magerezani kama watu wanavyokwenda
dukani kununua sukari, mpaka Mungu alipoingilia kati. Huyu dada anachoongea
mimi namwelewa kabisa. Kuna mahali unapitishwa na maisha, msaada uliobaki pekee
nikusalimisha maisha kwa Yesu. Ni uamuzi mgumu, lakini unalipa sana baadaye
unapoamua kukubali nakubadilika.” Yule kijana akaendelea.
“Mimi nilipokubali kuokoka, nilipoteza kila kitu
mpaka mke alinikimbia jinsi nilivyofilisika. Tena akaolewa na mwenzangu
tuliyekuwa tukifanya naye biashara zetu za magendo. Nilirudishwa chini kabisa,
nikawa masikini, omba omba. Nilikuwa na sababu zote zakurudi kufanya niliyokuwa
nikifanya kwa kuwa nikweli nilikuwa nikitengeneza pesa ya haraka, lakini sikuwa
na amani niliyokuwa nayo kama baada yakumpa Yesu maisha.”
“Wengi walinicheka na kuniambia nimepotea njia,
lakini nilijua hawajui vile ninavyojisikia moyoni. Nilirudi kuosha magari
Ubungo, mpaka nilipopata wazo lakurudi migodini kutafuta madini. Sikuwa na
maandiko mengi kutoka kwenye bibilia, na nilikuwa mchanga sana Kiroho, lakini
nilikuwa nikimkumbusha Mungu kuwa ‘fedha
na dhahabu ni mali yake.’ Na mimi ni mali yake, nikawa nikimuomba Mungu
anikutanishe navyo. Basi kila nilipokuwa nikizama kule machimboni nilikuwa
nikimkumbusha Mungu hayo maneno. Ilinichukua miaka miwili migumu ya shida,
nikiwa kule kwenye machimbo ya dhahabu, mpaka nikafanikiwa. Na mimi sasa hivi
namiliki sehemu yangu huko.”
“Nilipochelewa ndege leo asubuhi, na kukosa gari ya
kukodi kunipeleka Dar, nilipata amani sana yakupanda hili basi, kwani imekuwa
muda mrefu, tokea nipande basi. Nimefurahi sana kukutana na huyu dada. Na
inawezekana lilikuwa kusudi la Mungu ili nikutane na Tunda. Mungu akubariki
sana dada yangu.” Akamtizama sasa Tunda, maana alikuwa ni kama anazungumza na
basi zima.
“Hakuna sababu yeyote itakayokufanya kuishi kwenye
dhambi na ikawa sawa. Hakuna. Hata ukijitetea vipi, hakuna. Dada Tunda
nakuombea Mungu akutie nguvu, umeanza hii safari si rahisi, lakini Mungu
hatakuacha, na kwa kuwa umefunguliwa ufahamu wako mapema, naona hutapata shida
kama wengine.” Yule kaka akaendelea.
“Tatizo la wana wa Mungu wengi ni pale tunapoonywa
na kukataa kubadilika. Au pale tunapoonyeshwa njia, tunakataa kufuata njia ya
Mungu, na kutengeneza njia zetu. Tunachelewa na wakati mwingine hatufiki
kabisa. Tunakubali faraja kama wewe ulivyosema. Faraja ya matunda, nakusahau
vitu vikubwa tunavyotaka. Kama Mungu amekwambia akota boksi la biskuti
utengeneze gari, okota na tengeneza. Acha ubishi, huwezi kujua katika kuinama
huko, utaokota nini kingine!”
“Wengi wanapenda kuletewa wakiwa wanaomba Mungu.
Haiwi hivyo kabisa. Muujiza wako uko pale unaponyanyuka na kuchukua hatua.
Pengine yule mtoto asingekubali kutengeneza gari yake, ungekuta bado analia
mpaka sasa, na asingegundua mbali ya vijiti, hata boksi pia linaweza
kutengeneza gari. Tusibaki kung’ang’ania vya watu. Tutafute vya kwetu.” Yule
kaka aliongea kwa mifano huku akisema maandiko kwa kichwa kitu kilichomshangaza
sana Tunda.
‘Mwenzangu
anaonekana amekaa kwenye wokovu muda mrefu! Anauwezo mkubwa wakusema maandiko
ya bibilia bila kusoma!’ Tunda aliwaza.
Alishangaa uweza wa kuchanganya kila analoongea na neno la Mungu. Ilimtia moyo
sana Tunda. ‘Kweli huyu Mungu ana watu
wengi! Wengine wanampenda na kuishi kwa dhati, wengine wanacheza. Ni uamuzi wako
wa kuamua uishije naye.’ Tunda aliendelea kuwaza wakati yule kaka
akizungumza mpaka akamaliza na kurudi kukaa nakuacha watu wote kimya kila mtu
akitafakari lake.
Walipofika Ubungo, yule kijana akamsogelea Tunda,
akampa kadi yenye mawasiliano ya Mchungaji wake. “Kuanzia kesho ukimpigia simu
atakuwa na pesa yako. Mungu akubariki sana, na kamwe usirudi nyuma.” “Asante
sana kaka yangu.” Yule kaka alikuja kufuatwa na gari nzuri ya kisasa,
akaondoka. Tunda alibaki ametoa macho. Alipokea muujiza wake bila kutarajia.
Maisha yamrudisha Tunda Jijini Dar, Na bila kutarajia, katikati ya
Jaribu kali, pakatokea mlango wake wakutokea.
Tunda
hakutoka hata hapo kituoni Ubungo. Akaenda kwenye ile hoteli pale pale ndani ya
Ubungo. Alishalala hapo na baba Tom, kwa hiyo alipafahamu. Akachukua chumba
hapo. Kulikuwa kumejaa kumbukumbu ya mambo mengi aliyoyafanya humo ndani ya
hiyo hoteli na baba Tom, lakini ikawa siku hiyo nayo amemuona Mungu. Akatulia
kwa muda akiwa amekaa kitandani tu. Asiamini yupo hapo na hata siku hiyo,
katikati ya jaribu gumu, lakini hana mtu anayetakiwa kumuhudumia kimapenzi ili
kupata pesa.
Akajisiki
machozi yakianza kumtoka. Akaamua kupiga magoti na kumshukuru Mungu huku akilia.
Alikaa kwa muda mrefu magotini akilia mbele za Mungu wake, akaishia kujiambia
hataweka kitu mdomoni mpaka mambo yake yakae sawa. Mpaka aushuhudie muujiza
wake kwa macho. Ni kama aliamua kufunga.
Siku
inayofuata, aliamua kutafuta sehemu ya kulipia ya kupiga simu. Akampigia simu
huyo Mchungaji ili kujua kama kweli kuna pesa au la. Mchungaji akamwambia ni
kweli mkewe alipewa pesa na kupewa maelekezo amkabidhi yeye. Tunda alifurahi
sana. Kilichofuata ni kwenda kuona hicho chumba. Yule mzee wa kwenye basi
mwenye nyumba alimpa namba yake ya simu na ya dalali. Alishazungumza na dalali,
akamwambia atamsubiri Temeke hospitali ndio kituo atakachokitumia kufika kwenye
hiyo nyumba.
Bila
kupoteza muda, Tunda akiwa ameacha mizigo yake hapo hotelini, akapanda daladala
mpaka Temeke kuona hicho chumba. Na kweli, aliweza kumtambua huyo dalali kwa
nguo alizomwambia atamkuta nazo, kwa kuwa Tunda alimwambia hana simu,
amwelekeze alivyo ili asimpotee. Akamchukua kutoka hapo kituoni mpaka kwenye
hicho chumba. Tunda akaridhika nacho.
Akapapenda,
akamuomba yule dalali atumie simu yake. Tunda akaongeza muda wa maongezi,
akampigia tena simu yule Mchungaji, akampa namba ya simu ya mkewe. Tunda
akampigia simu mke wa Mchungaji, yule mama akaamua amfuate.
Baada ya
muda kama wa lisaa, alishangaa gari nzuri sana, SUV nyeupe, kubwa, imevimba
vizuri, ikasimama mbele kidogo kituoni, pale pale Temeke hospitalini kama
walivyokubaliana. Tunda na yule dalali wakamuona mwanamke akishuka kwenye hiyo
gari. Alikuwa mtanashati, wakisasa. Akajitambulisha na kumwambia yeye ndiye
waliyekuwa wakiongea naye kwenye simu, akamwambia wengi wamezoea kumwita mama
Penny. Tunda akamsalimia na kujitambulisha na yeye.
Yule
dalali akawapeleka kwa mwenye nyumba. Hakuwa akiishi mbali na hapo. Mama
mchungaji akalipa ile kodi yote, Tunda akakabidhiwa funguo.
“Una kitanda?” Mama Penny akamuuliza wakati
akimrudisha Tunda hotelini. “Ndiyo. Nina kila kitu, lakini nimefungia mahali.
Itabidi kesho nitafute gari nihamie kwangu.” “Usiwe na wasiwasi, nitawatuma
vijana wa pale kanisani na gari ya kanisa ikusaidie kuhama.” Tunda hakuwa
akielewa kinachomtokea.
Akamgeukia mama Penny. “Nakushukuru sana dada
yangu. Mungu akubariki. Asante kwa kila kitu.” “Karibu.” Alijibu kwa ufupi tu. Akamshusha
hapo hotelini Ubungo, akaondoka na kumuacha Tunda na funguo za chumba chake na
sebule.
Ile furaha ikageuka kilio kwa Tunda. Alilia Tunda,
asiamini kama Mungu amemrudishia kwake. Kwa Tunda huo ulikuwa ni muujiza wa
kama kumfufua maiti. Ilikuwa ni zaidi ya kuponywa. Historia yakufukuzwa kwenye
majumba ya watu, kwa Tunda, haikuacha kujirudia.
Ametoka kufukuzwa kwenye nyumba ya watu Arusha.
Mama Cote alimtoa nyumbani kwake usiku. Akampokonya chumba alichopewa na Net,
funguo za gari na kazi. Anampa nini huyo Mungu kumfungulia mlango mkubwa kama
huo! Tunda alilia, asijue nini chakusema mbele ya huyo Mungu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kesho yake asubuhi alipigiwa simu na mtu wamapokezi
kuwa anamgeni pale mapokezi. Alipotoka alishangaa kukutana na mama Penny na
vijana. “Uliamka salama?” “Ndiyo. Japo sijala.” “Sasa itabidi ujikaze.
Nimewakamata hawa vijana wakusaidie kuhama kabla siku haijaanza, wakakimbilia
kwenye majukumu yao. Wakishakuhamisha ndipo tutatafuta sehemu ya kula.” “Sawa.
Nashukuru sana.” Tunda akachukua mizigo yake yote aliyokuwa nayo pale hotelini,
wakaweka kwenye gari ya mama Penny. Akalipia kile chumba, wakaondoka pale.
Tunda alikuwa kwenye gari ya mama Penny, na wale
vijana walikuwa wakiwafuata nyuma kwenye gari kubwa kidogo, aina ya Kenta.
Walitoka hapo Ubungo kuelekea Salasala nyumbani kwa Net alipokuwa ameacha vitu
vyake.
Walipofika pale, akawaambia wasubiri nje akagonge
kwanza. Aliwaambia hiyo nyumba inalindwa na mbwa mwenye mafunzo ya kijeshi.
Ndiye Max. Tunda alishapewa habari za Max. Net alikuwa akimsifia sana huyo
mbwa. Alikuwa akisema kwa huyo mbwa mmoja tu kulinda hiyo nyumba yake, ni sawa
na kulindwa na askari watatu wa kimarekani, tena waliokwisha kwenda kupigana
vita huko Iraq. Huyo Max alikuwa akihudumiwa nakutunzwa kwa hali ya juu.
Tunda aligonga kengele nje ya geti, baada ya muda
Emma akatoka. Wakasalimiana, akamwambia bado Net hajarudi nchini. Akamweleza
kuwa amefika hapo na wale watu kuchukua baadhi ya vitu vyake. Emma alikwenda
kumfungia Max, ndipo akarudi kufungua geti na ile sehemu alipohifadhiwa vitu
vyake.
Kutokana na ile sehemu kuwa ndogo sana, ilimbidi
Tunda kuchukua vitu baadhi, vingine akaacha pale pale. Emma alivifunika vile
vilivyobaki kama mwanzoni ili visiingie vumbi, wao wakaondoka. Huku Tunda
akiviambia vitu vyake vilivyobaki pale kwenye stoo ya Net, ‘ipo siku
tutarudi kuwa pamoja. Nipeni tu muda.’ Roho ilikuwa ikimuuma sana Tunda. Ni
kweli alikuwa na vitu vizuri. Hata wale vijana waliokuwa wakimsaidia kubeba,
walisifia na kuongeza umakini kwenye kubeba.
Walimrudisha mpaka Temeke kwenye chumba chake,
wakamsaidia kupanga vile vitu, kisha wale vijana wakaondoka. Tunda alikuwa
akicheka sana jinsi wale vijana walivyokuwa wakitaniana na mama Penny.
Walionekana wamezoeana vizuri. Yule mama alipohakikisha Tunda ameweka kila kitu
chake vizuri, alimchukua mpaka nyumbani kwake Tabata.
Walimkuta dada wa kazi, akiwa anaandaa chakula cha
mchana. Na yeye yule mama akaingia jikoni nakuanza kumsaidia yule dada huku
akimuuliza maswali Tunda. Baada ya muda mfupi sana, Tunda akajisikia yupo
nyumbani. Mama Penny alikuwa mcheshi wakupitiliza.
Mchungaji naye akaingia. “Wewe siulikuwa ukicheka
kila ninaloongea? Sasa kaja mwenyewe, utapasuka mbavu.” Tunda alikuwa akicheka
sana. Mchungaji na mkewe walikuwa kama ni mtu na rafiki yake. Walitaniana kwa
kila kitu.
“Hivi kuna wakati huwa wanakuwa serious hawa?”
Tunda alimuuliza msichana wa kazi. “Mmh!
Sikumbuki. Labda wakiwa kanisani kidogo, lakini watu wameshawazoea. Mtakaa
mkicheka hapa, mpaka mnaenda kulala. Hawaishiwi maneno hao na vituko.” Tunda
alikaa hapo mpaka usiku akarudishwa kwake na yule mama.
“Kesho unaratiba gani?” Yule mama akamuuliza Tunda
kabla hajashuka. “Bado natafuta kitu chakufanya.” “Sasa mimi ninafanya kazi ya
kupamba kumbi za sherehe. Kesho nina kwenda kupamba ukumbi mahali. Kuliko ukae
tu nyumbani, ni heri twende wote. Mimi sipendi watu wanaokaa kaa kihasa hasara,
mwishowe shetani anapata nafasi ya kukupa kazi zake.” Tunda akacheka.
“Unafikiri nakudanganya? Shetani anapenda mijitu
isiyo na kazi. Iliyokaa kaa tu haina kazi zakufanya, ndiyo anaanza kuipa kazi
zakijinga.” “Basi tutaenda wote dada yangu.” Yule mama akacheka kidogo kama
aliyefurahia utayari wa Tunda.
“Sasa mimi mambo yangu ni asubuhi ili jioni niwe na
familia yangu. Kwa hiyo asubuhi nakuja kukufuata. Au unasemaje?” “Sawa kabisa.”
Yule mama akacheka, akafungua loki ya mlango pembeni ya mlango wake, ndipo
Tunda akaweza kufungua mlango wake,
wakaagana na kushuka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alianza kulia tena mara baada yakufika chumbani
kwake, akapiga magoti pembeni ya kitanda chake. Alishindwa hata kumwambia Mungu
asante. Alibaki amepiga magoti akilia. Moyo wake ulijaa shukurani sana mbele za
Mungu. Nyumba ilikuwa nawapamgaji wengine wanne, wote walikuwa na familia
kasoro Tunda. Ilikuwa uswahilini tu, tena wala si uzunguni kama alikokuwa
akiishi karibu na baharini.
Uswahilini hapo ni kelele mida yote tena kitanda chake
kiliwekwa pembeni ya dirisha alilokuwa akisikia kila kitu wapita njia
wakizungumza nje. Choo anatumia na watu zaidi ya 15. Alishaambiwa kuna zamu za
kusafisha sijui choo, uwanja na mambo mengi. Ni maisha ambayo hakuwahi kuishi
binti huyo. Lakini alijawa na furaha ya aina yake. Alikubali yote bila shida. Furaha
aliyokuwa nayo moyoni, ni kama alipewa jumba la thamani sana.
Alipanda kitandani kwake, asiamini kama amerudi kukilalia
kitanda hicho alichokipenda na kukithamini sana. Aligaragara kwenye hicho
kitanda akinusa hayo mashuka yake kwa furaha sana. Akaanza kuongea na vitu
vyake kama binadamu. Akakumbuka kazi aliyoambiwa atafuatwa asubuhi asubuhi.
Ikabidi alale haraka ili aamke akiwa na nguvu.
Tunda aanza Safari ya Kupata chake. Bila kujijua, kwa kutii agundua
kipaji chake.
Aliamka asubuhi na mapema kuwahi
kuoga kabla wengine hawajaamka na watoto wao, akachelewa. Akaoga na kuvaa
akabaki kwenye kiti akimsubiria mama Penny. Akasikia mlango wa bati, mdogo tu wakuingilia
ndani ukigongwa, akajua ni mama Penny. Akatoka akiwa amebeba na pochi yake, ni kweli
alikuwa mama Mchungaji. Wakasalimiana, wakarudi kwenye gari na kuondoka. Na
hilo likamfurahisha mama Penny, hakutegemea kumkuta akiwa tayari kwa kiasi
hicho.
Waliongea
mambo mawili matatu mpaka walipofika kwenye ukumbi wenyewe. Ulikuwa ukumbi wa
kawada sana huko Mbezi ya kimara. “Si unaona hili liukumbi lilivyo baya? Sasa
utaona nitakavyo pabadilisha mpaka wenyewe watashangaa.” Akajisifia yule mama.
Wale wale vijana waliomuhamisha Tunda jana yake, waliingia na ile ile gari
iliyomuhamisha Tunda siku iliyopita, ila safari hii ilibeba viti vya maharusi
na mapambo. Walianza kushusha huku wakiendelea kutaniana.
“Leo
mama wametupa godauni.” “Hilihili leo, mpaka paeleweke hapa! Masaa matatu tu,
tunaondoka humu ndani. Nataka nikampikie mume wangu ugali wa bada. Mnaujua
lakini bada au mnanitolea mimacho tu?” “Umeanza mama Penny.” “Kumbe! Ndio muoe
muache kula magengeni! Wakati wenzenu wanaoa nyinyi mmekazana mnaomba. Mtaomba
mpaka Yesu anarudi anawakuta bado mnaomba. Hebu njooni tuombeni kwanza ndio
tuanze kazi.” Wote walikuwa wakicheka.
Tunda
alikuwa akiwashangaa furaha waliyonayo na yule mama. Wakashikana mikono,
wakaanza kuomba kwa pamoja ndipo wakaanza kazi. Walianza kazi kwa nguvu zote.
Wale vijana wakijua chakufanya. Na kweli baada ya masaa matatu na nusu ule
ukumbi ulibadilika kabisa. Walianza kupongezana. Mama Penny akawalipa pesa yao
pale pale wakaagana.
“Na wewe
hii ndiyo pesa yako.” “Wala sijafanya kazi kubwa sana!” Tunda alitaka kukataa.
Yule mama akambadilikia. “Huwa sipendi watu wajinga. Unanisikia Tunda? Kila
mtenda kazi anastahili ujira wake. Au husomi bibilia wewe?” “Nasoma.” “Sasa!?
Au maandiko ya bibilia yalisema kila mtenda kazi sana ndiye anastahili ujira? Acha kuzubaa! Mjini hapa. Kusanya
pesa, jenga nyumba, nunu magari ya maana, uache kuishi uswahilini. Unafikiri
nitakuwa nakuja kukuchukua kila siku?” “Hapana.”
“Ndio
unatakiwa uchangamke, unasikia? Umelipiwa kodi mara moja tu, ujue inayofuata ni
juu yako. Huwezi jua. Mara nyingine Mungu anatokea mara moja tu, na akitokea
usiachie hiyo bahati. Sasa hivi unakusanya kila kinachoingia. Hata kama kidogo.
Halafu huwezi jua hii ndiyo inaweza kuwa ajira yako. Au unaonaje?” Yule mama
akamuuliza.
“Nimeifurahia
sana.” “Basi jipe muda. Omba Mungu hizi tenda ziwe nyingi, ujifunze kwa haraka,
na wewe uwe na yako kama hii.” “Kama hii tena, sio uniajiri?” “Wewe mtoto wa
wapi lakini!?” Tunda alitulia kidogo. “Mbona neno ‘changamka hapa mjini’ ni kama hulielewi!? Wewe Dar yote hii
unafikiri harusi leo zinafungwa ngapi, au kuna sherehe ngapi zinazotaka
wapambaji?” Tunda akacheka baada ya kufikiria kidogo.
“Muone
kwanza! Ushapata jibu eeh? Sasa ndio uchangamke haraka, jifunze, pata ujuzi
halafu unachanganya miguu. Sio ukae hapa unasubiri ajira. Nikikufukuza kama
yule mama wa Arusha? Unahama tena kuajiriwa kwengine? Hapo Mungu alikuwa
anakufungua macho anakwambia uwe na chako! Shule sio kila kitu. Mwenzio
nimesoma, lakini napamba maukumbi. Naingiza pesa nyingi tena kwa muda mfupi.
Umeona kuna sayansi niliyotumia hapa? Ujuzi tu na utundu.” Akawa ni kama
anamfungua akili zaidi Tunda.
“Asante
sana.” “Asante kavukavu tu?” Mama Penny akamuuliza Tunda, akaanza kucheka tena.
“Sasa nifanyaje?” “Ukipata tenda ya kwanza unaninunulia pafyumu nzuri. Sio zile
zakuita nyuki au kuleta mafua.” Tunda aliangua kicheko zaidi, wakaondoka pale.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Yule mama alikuwa akifahamika
sana. Kwa juma moja hakuacha kupamba kumbi si chini ya tatu. Kuanzia kichen
party, send off, harusi, na kila shughuli zilizokuwa zikihitaji wapambaji,
aliweza kupata yeye hizo tenda, mpaka alikuwa akikataa. Alikuwa akiingiza pesa
nyingi kwa juma.
Kwa kuwa
alikuwa na watoto wadogo na huduma ya kanisani, mara nyingi alimtuma Tunda
kwenye vikao vya harusi kwenda kuonyesha picha za kumbi walizokwisha kupamba na
kuongelea gharama. Baada ya muda mfupi kweli Tunda akaanza kuwa mwenyeji na
mjuzi wa ile biashara.
Akajiongeza.
Akatengeneza albamu nyingine. Akapangilia picha na bei vizuri. Ikawa rahisi
kila akitumwa na mama Penny, anaonyesha picha na bei. Kwa muda mfupi Tunda
akaonekana amefikishwa kwenye uwanja wake anaomudu. Yeye ndio mtoa ushauri kwa
mama Penny, kitu kilichomfurahisha sana mama Penny. Lugha nzuri ya biashara
akawa anayo. Hakuna alikotumwa kwenye vikao viwe vya harusi au kiofisi, akarudi
bila hiyo kazi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Sasa tunaanza kugawana. Wewe unapamba huku na
mimi napamba kule.” Tunda akaingiwa hofu. “Yaani bila wewe? Sitaweza peke
yangu.” “Wewe mtoto vipi!? Hata watoto wachanga huwa wanaacha kunyonya.
Ulipokuwa ukikubali kupokea kazi za watu, tena nyingi kwa tamaa, ulifikiria
nini? Unataka tuongozane kama makondoo mpaka lini!? Kwanza mimi huwa sipendi
kufuatwa fuatwa nyuma.” “Nikiharibu sasa?” Tunda alijawa na wasiwasi.
“Shauri
yako! Mimi hainihusu. Itakuwa ni juu yako wewe na hao waliokupa kazi. Mimi
nachukua ukumbi mmoja tena wakaribia na kwangu, nikimaliza kazi yangu
nitakupigia simu bosi wangu uje ukague, ukiridhika nataka pesa yangu
uliyolipwa.” Tunda akazidi kuchanganyikiwa.
“Sasa na
ule ukumbi wa tatu nani atapamba?” “Kwani wewe ulivyochukua kumbi tatu, kwa
siku moja, ulitegemea nini? Mwenzio nina mume na watoto. Kazi yangu moja tu kwa
siku na wewe unajua. Ulivyochukua kazi zote hizo, ulifikiri nini?” “Jamani mama
Penny!? Basi tufanye wote hizi zote halafu siku nyingine nitajipanga vizuri.” Tunda
akabembeleza akiwa na hofu.
“Akuu
wewe mtoto usinivunjie ndoa yangu. Baba paroko unamsikia Tunda.” Yule mama
alimwita mumewe. “Atalijua jiji! Na akikutana na walevi lazima wamshushie
kipondo kama ukumbi haujaisha kwa wakati.” Mchungaji na mkewe wakaanza kumcheka
Tunda, huku wakikumbushiana visa vya kazi hiyo ya upambaji kama wahusika
wanakuwa hawajaridhika na kazi.
“Sasa
nitafanyaje?” Tunda akauliza akilalamika. “Omba funguo za ukumbini ukalale nazo
kwako. Amka hata saa kumi za usiku, nenda kaanze kupamba. Tena nakupa Josh na
Julius wakusaidie. Wote wale wachapa kazi. Ukiamka mapema kwenye saa kumi
jioni, utakuwa ushamaliza kupamba kumbi zote mbili.” Hilo likamfurahisha Tunda.
“Sasa
mapambo?” Tunda akauliza tena. “Mapambo!?” Mama Penny naye akauliza kama
anayemshangaa. “Nauliza mapambo nitapata wapi?” “Piga magoti uanze kuyaomba kwa
Mungu. Utakuta Mungu kakushushia huko huko ukumbini yanakusubiri. Kila ukumbi
atakuwekea mapambo yake. Anza kuomba.” “Jamani mama Penny!” Kila mtu akaanza
kucheka mpaka msichana wa kazi jikoni.
“Kumbe!
Wewe hujui hii ni nyumba ya Mchungaji? Hapauzwi mapambo hapa. Ushauri
utakaopewa ni kuomba. Ukiona hapa unabanwa, rudi kwako kule uswahilini, kwenye
kelele, kajifungie anza kuomba kwa kulia.” “Au piga magoti nikuwekee mkono
Tunda.” Mchungaji akaongeza. “Jamanii!” Tunda akazidi kulalamika.
“Changamka
Tunda. Mjini hapa!” “Basi naenda kununua vitu vyangu.” “Kumbe unaakili?”
“Usafiri sasa?” Tunda akauliza tena. “Piga magoti Mchungaji akuwekee mikono ili
mkimaliza kuomba, ulikute gari hapo nje linakusubiri.” “Jamani mama Penny
wewe!” “Kwani wewe huamini nguvu ya maombi? Au hujasikia kama kuna miujiza?”
“Naamini lakini si kihivyo!” “Basi changamka. Una siku tatu za kukamilisha kila
kitu uingie kazini.” Tunda akaondoka.
Tunda
aanza biashara yake ya kupamba.
Usiku
huo hakulala. Akaanza kuandika kila kitu alichokiona kwa yule mama, ambacho
alijua atakihitaji na yeye. Kesho yake asubuhi akaanza kuzunguka madukani akiwa
na Julius ambaye ni mpambaji wa mama Penny na ni dereva wa ile Kenta.
Akaanza
kununua vitu kama vile alivyoviona kwa mama Penny. Anamwita Julius, anasogeza
gari, wenye duka wanamsaidia kupandisha vitu kwenye gari, Julius anamsubiri,
yeye anazunguka madukani peke yake.
Viti vya
kukalia maharusi ndivyo vilimtoa jasho. Alitaka kama vya mama Penny, ila bei
ilikuwa kubwa. Akaanza kujishauri akikumbuka akiba ya pesa aliyokuwa nayo.
Inamaana kazi yote tangia aanze kazi kwa mama Penny na ile aliyolipwa Arusha,
itaishia hapo kwenye manunuzi! Akajishauri Tunda. Lakini alitaka awe anafanya
kazi nzuri kama mama Penny. Ikabidi ajikaze tu, anunue kila kitu vile vile na
vizuri zaidi, mpaka akaishiwa kabisa.
Walirudi
nyumbani kwa mama Penny na mchungaji Tabata akiwa na mizigo yote aliyokuwa amenunua
Tunda. Tunda mwenyewe alikuwa hoi. Amechoka na ule weusi ukaongezeka kwa kupigwa
na jua pamoja na vumbi.
“Naomba unikopeshe pesa nikaongeze kwenye
mapambo.” Mama Penny akaanza kucheka. “Umeshaanza kupata akili eeh? Safi sana.
Sasa hapa kwetu kukopa ni mara moja tu,
na unalipa ndani ya juma moja. Ukizidisha siku saba unaanza kulipa na riba.”
“Mama Penny jamani!?” “Haya nenda kakope kwenye mabenki.”
“Haya basi nitakulipa nikilipwa baada ya kupamba.”
“Hiyo ndio akili. Sasa uchangamke na siku za alhamisi na ijumaa hapa mjini pia
kunakuwa na sendoff na Kitchen party. Zote hizo siku hakikisha unapata kazi.”
“Si nitachoka sana!” Tunda akashangaa. “Sawa. Nenda kalale. Kwanza hivi
umepaona nyumbani kwake?” Mama Penny akamuuliza mumewe.
“Hapana.” “Kama chumba cha mbwa! Hapafai.” “Jamani
mbona pazuri tu.” “Kama pazuri mbona mizigo yako ipo hapa? Si ungetoka Kariakoo
na kuipeleka kwako?” “Mama Penny wewe? Pale padogo halafu nahofia wezi.” “Sasa
unakataa nini na unaongea nini hapa? Dari lenyewe limeshuka mpaka mlangoni!
Yaani kuingia inabidi uiname na unakuwa kama unatumbukia ndani hivi. Tena kama
wewe baba Paroko na miguu mirefu hiyo! Lazima uiname ndio uweze kuingia
mlangoni, na ukifika ndani itakulazimu kukaa tu. Lasivyo utagonga dari.” Tunda
alianza kucheka huku anatingisha kichwa.
“Nitahama bwana.” “Utahama bila pesa? Nakwambia
fanya kazi kwa bidii. Unasema utachoka! Tena kesho kuna kazi nimepewa ni
kupamba ukumbi wa tamasha, pale Mlimani City, sitaweza kwenda namsindikiza mume
wangu kwenye huduma Morogorooo. Sasa itabidi uwahi ukapambe na hao vijana.” Tunda
akachoka kabisa.
“Utaniua mama Penny! Mlimani City? Nikiharibu?”
“Ndio utakuwa umeniharibia biashara. Na tunakuomba ule uondoke Tunda. Nina mazungumzo
ya faragha na mume wangu.” Msichana wa kazi alikuwa akicheka muda wote.
“Sawa bwana.” “Na tunakupa miezi miwili tu, hakuna
tena kutumia gari yetu kubebea vifaa vyako vya kupambia. Tafuta gari yako,
mrembo. Mjini hapa, watu tunaishi kwa mahesabu. Hakuna kuomba chumvi kwa
jirani.” “Gari!?” “Na hivyo vifaa vyako hapo stoo, kuanzia mwezi wa kumi na
mbili utaanza kulipia hicho chumba.” “Jamani mama Penny wewe!?”
“Sitaki hodi za asubuhi asubuhi wakati unakuja
kuchukua vifaa vyako ukapambe. Ni usumbufu Tunda.” “Si kwa muda tu!” “Muda
wenyewe ndio nakwambia mwisho ni mwezi wa kumi na mbili. Kwa hiyo wakati
unapumzika huko kwako hutaki kufanya kazi kwa bidii, ujue unatakiwa gari na
nyumba kubwa.”
“Patamu hapo. Na vyote hivyo si chini ya mamilioni
ya pesa. Ukiiba tu, sisi tunakutenga. Ukihongwa tu, mimi Mchungaji nakupandisha
madhabahuni nakutangaza kuwa wewe ni mzinzi, kisha nakutenga mbele ya watu.”
Mchungaji akaongeza. Yule mama alisaidiana na mumewe kumshambulia Tunda.
“Hivi nyinyi mlikutana wapi?” Iliibidi Tunda
kuuliza jinsi wanavyopokezana maneno kwa kupatana, kama wamepanga. “Maana
mnafanana kila kitu!” Wote wakacheka. “Kanisani. Mimi nilikuwa kiongozi wa
vijana, na bibie hapa alikuwa ndani ya kundi. Akanipenda ndio nikamuhurumia
nikamuoa.” “Uringe. Alihangaika huyu, muone maneno mengi hivyo hivyo. Nilimtoa
jasho!” Tunda alikuwa akicheka sana.
“Kwa
hiyo mlianzana tokea wadogo?” “Nimemfundisha hesabu za sekondari huyo, usimuone
hivyo. Nilivyomuona anapenda pesa, nikaona nioe kabisa ili yeye awe anatafuta
pesa mimi nahubiri injili. Ukimfatilisha huyu, ndani ya miaka miwili utakuwa
mbali sana Tunda. Kazana, jiamini, utaweza tu.” “Umesahau kumwambia na awe
anatoa fungu la kumi kanisani.” Mama Mchungaji, yaani mama Penny, akaongeza,
nakumfanya Tunda aangue kicheko zaidi.
“Na sadaka kubwa kubwa. Umesikia Tunda? Sio zile
sadaka unatumbukiza kwenye kapu la sadaka umekunja ngumi. Na baraka za Mungu
zitakuwa ndogo ndogo hivyo hivyo”
“Nitatoa.” Tunda akakubali akicheka
Tunda
aanza kupambana jijini.
Mwanzo
wa Tunda haukuwa rahisi hata kidogo. Ilikuwa kazi tu. Hakuna masaji wala
kutengeneza kucha na kubadili nywele kila week. Alianza kufanya kazi kwa
bididii zote, akili ikiwa imetulia kazini asiharibu. Ndani ya juma moja alikuwa
akipata kazi si chini ya nne. Zote hizo anasukumiwa na mama Penny. Kuna siku
nyingine alikuwa akipamba kumbi mbili mpaka tatu.
Tunda
akawa busy. Mchana na usiku yupo na kazi. Hakuna waxing tena kwenye huo mwili kutoa
vinyweleo. Kazi tu. Anasaka pesa kwa juhudi zote. Na Mungu akawa akimfungulia milango
kwa namna ya ajabu. Akawa ni kweli anapata kazi. Kila akijisikia kuchoka na
kutaka kukataa kazi, alikuwa akijisuta na kukumbuka maisha yake. Basi anatoka
kitandani bila hata alam.
Alianza
kuingiza pesa na kufahamika mjini kwa kazi nzuri ya upambaji. Na akaongeza
uaminifu kama mama Penny. Mkikubaliana aina fulani ya mapambo, basi ujue
atakuwekea hayo hayo mapambo. Kama ni maua Rose, ujue hatachanganya wala
kukuibia. Uwe na pesa usiwe, basi atakupambia kutokana na pesa yako na vile
mlivyokubaliana.
Alipata
familia kubwa pale kanisani kwa kina mama Penny. Tunda alijawa furaha, upweke
wote ukaisha. Akawa mtu wa furaha wakati wote, na nyumbani kwa mama Penny ikawa
ndio kituo chake kikubwa. Na mama Penny akafanyika dada kweli kweli. Ukimkosa
Tunda kwenye simu, muulize mama Penny. Mchana na usiku wawili hao walikuwa
wakiwasiliana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya
mahangaiko mengi akichapa kazi mchana na usiku, akafanikiwa kuhama Temeke,
akapata nyumba. Haikuwa nzuri kama ile aliyoishi La dolce Vita, lakini ilikuwa
na ukubwa unaolingana na ile. Vyumba viwili kama ile, inajitegemea, maeneo ya
Kimara, karibu sana na Ubungo. Akaenda kuchukua vitu vyake vyote kwa Net,
akahamia kwake. Akaongeza bidii ili kupata usafiri pia. Kazi akafanya mchana na
usiku bila kuchoka wala kulalamika. Hakuna tenda yeyote alipata akaacha.
Alipopata
pesa, mama Penny akamsindikiza Tunda kununua gari. Kwa kuwa alikuwa na mambo
mengi, alinunua gari nzuri lakini sio kama ile ya Mama Mchungaji iliyokuwa ya
aghali sana. Tunda akapata usafiri wake wakumzungusha mjini.
Kila
mama Penny alipopata kazi nyingi alimpa na yeye. Watu wakaanza kumfahamu yeye
kama Tunda sasa. Akaanza kutafutwa yeye kama Tunda sio kwa kupitia tena mama
Penny. Na kazi zake zilikuwa nzuri sana. Akaanza kuuzika kama Tunda, na watu
wakaweza kutambua kazi zake.
Hakuwa
amesoma, lakini kwa hakika kile kilikuwa kipaji chake bila kuuliza.
Kilijionyesha kwenye kila kumbi aliyokuwa akipamba. Alijiongeza na ungeweza
kutofautishi ukumbi aliopamba yeye au mama Penny, japo walitumia karibu kila
kitu kinachofanana. Kipaji chake cha upambaji kilimkutanisha na watu waina
mbali mbali. Wasomi na wenye pesa. Wake za mawaziri na mabalozi.
Alipoona
kazi inakuwa kubwa, hana haja yakusaka kazi, zinamfuata tu, akatafuta ofisi na
kuajiri watu wawili waliokuwa wakipokea kazi kutoka kwa watu. Alifungua website
ambayo ilijaa picha zakuonyesha kazi zake. Kwa muda mfupi sana Tunda akawa
mashuhuri pale jijini. Lakini katika yote hakuacha kuwa karibu na Mungu wake.
Msingi wa kusoma bibilia na kuomba aliokuwa amefundishwa na Net, hakuacha hata
kidogo. Kila akirudi nyumbani kwake, atapiga magoti na kuomba Mungu japo kwa
ufupi.
Kwa
Mara ya Kwanza, Tunda amsaka baba yake
jela.
Alianza
kuulizia kwenye magereza ya pale mjini, kutaka kujua alipofungwa baba yake,
mpaka akajua kule baba yake alipokuwa amefungwa na siku ambazo wanaruhusiwa
kutembelewa. Akaamua kwenda kumtembelea baba yake huko gerezani Segerea. Baba
yake alifurahi sana kumuona Tunda. Lakini alikuwa amedhoofu na hakuwa na furaha
hata kidogo.
“Wamenisingizia mwanangu. Kwa kuwa sina hela,
nashindwa kutafuta mwanasheria mzuri wakunitetea.” “Mimi nitakutafutia baba.”
Hilo likamfariji sana baba yake. Mtoto ambaye hakuwa hata anamtegemea, ndio
anaahidi kuwa mkombozi! Akashukuru. “Unafanya
nini sasa hivi? Umependeza mama.” Ilibidi baba yake kuuliza. Maana ni kweli
Tunda alionekana ametulia na pesa ipo.
Swali alilokuwa akilikwepa wakati ule akizunguka na
wanaume, ndilo hilo baba yake anamuuliza. Lakini safari hii akamjibu baba yake
kwa ujasiri wote. “Mungu ananilinda na kunitunza kwa namna ya ajabu baba! Mimi
mwenyewe bado nipo kwenye mshangao baba yangu. Napamba kwenye kumbi za shuguli
mbali mbali! Na wala sikurudi shule. Nilifundishwa tu.” Tunda akamuelezea juu
ya wakovu aliopokea, familia ya mama Penny na mafanikio yake. Baba yake akafurahi
sana, wakawa wanaongea mpaka muda ulipoisha, Tunda akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alianza kuzunguka kwenye ofisi za wanasheria pale
mjini. Akiongea nao, kuona kama wataweza kumsaidia baba yake. Akiwa anajaribu
kwenye ofisi nyingine, sekretari wake alimpigia simu kumwambia yupo mtu amesema
anataka kuongea na yeye mwenyewe. Tunda alichukua ile namba akapiga.
Walimuomba huduma yake ya upambaji na kumtaka afike
kwenye moja ya kikao chao cha ijumaa ili kuongea na wanakamati. “Mlishaona kazi zangu
lakini? Maana mnaweza kupitia kwenye website yangu, mkachagua muundo
mnaoupenda, kisha unapiga simu ofisini onatoa oda yako. Sio lazima mimi nikawepo
kwenye kikao.” “Tungependa kukuuliza maswali
kabla ya kuchagua.” Tunda akakubaliana nao muda na eneo atakalokwenda
siku hiyo ya ijumaa kukutana na wanakamati wengine.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilikuwa siku hiyo ya ijumaa jioni, Tunda akiwa
amejitayarisha vizuri kwenda kuonana na wanakamati hao. Alikuwa na kazi moja tu
siku hiyo. Alishakamilisha tokea asubuhi. Akarudi nyumbani, akapumzika na
kujiandaa tayari kwa kikao cha jioni. Kama kawaida yake, hakuwa akifanya makosa
kwenye mwili wake. Alipendeza sana, akachukua picha zote alizojua angehitaji
kuvutia wateja wake, akaelekea kwenye kikao.
Eneo tu walilokuwa wakikutania hao wanakamati,
Tunda alijua watakuwa na pesa. Aliingia kwenye hoteli hiyo iliyokuwa Masaki,
akasalimia pale mapokezi, kisha akampigia simu mtu aliyekuwa ameongea naye
kwenye simu, akafika pale mapokezi kumchukua.
Tunda alimuona yule kaka jinsi alivyobabaika baada
yakumuona. Akaongeza ujasiri. Wakaongozana mpaka upande wa chakula walipokuwepo
wale wanakamati wenzake. Walikaa ndani, kwenye eneo kubwa kidogo.
Waliunganishiwa meza mbili ili waweze kuonana. Tunda aliwasalimia bila
kuwaangalia huku akijaribu kuvuta kiti alichoonyeshwa na mwenyeji wake.
Ana kwa Ana na Net tena!
“Tunda!” Tunda alishtuka kidogo baada yakusikia
jina lake likitajwa pale mezani. Akanyanyua uso kutafuta aliyemwita na kukutana
na Net. Tunda akatoa tabasamu kubwa sana la mshtuko. “Net! Habari za siku!?”
Net alikuwa kwenye mshangao mkubwa sana, uliowafanya wanakamati wote wabaki
wakiwakodolea wao macho. Tunda alikaa chini, na kumwangalia tena Net, pembeni
ya Net, alikuwepo Gabriel. Tunda akashtuka sana, akaamua kutokuwaangalia tena.
Akabaki akimtizama mwenyeji wake tu.
“Naona tumeshatambulishwa jina, tumeshajua unaitwa
Tunda.” Yule mwenyeji akavunja ukimya. “Ndiyo. Ninaitwa Tunda, ndiye
ninayehusika na mambo ya upambaji. Uliniambia mlishapitia kwenye website yangu.
Si ndiyo?” Tunda akauliza huku akimtizama yule mwenyeji. “Ndiyo.” “Sio wote
bwana.” Mwingine akakanusha. “Basi haina shida. Nimewaletea baadhi ya picha,
ili muone baadhi ya kazi zangu kisha mchague.” Tunda akatoa zile picha
alizokuwa amezipanga vizuri kwenye albamu.
“Bei
zako zikoje?” Mmoja wao akauliza wakati akiendelea kuangalia. “Inategemea na
nini unataka ukumbini. Ukichagua moja ya picha hapo naweza kukutajia bei. Na
pia kama hakuna muundo hata mmoja mtakao kuwa mmependa hapo, naweza kuwapambia
kutokana na mtakavyo nyinyi. Mnaniambia nini mnataka, ukubwa wa ukumbi, meza na
idadi ya wageni mnao tarajia, nitaandika na kwenda kuwapigia mahesabu kisha
nitawajulisha. Mara nyingi najitahidi kwenda kutokana na bajeti ya mteja.”
Tunda akajieleza vizuri sana na sauti yake tulivu bila pupa, nakubaki
akiwasikiliza, ila macho yake yakiwa kwa mwenyeji wake tu.
Zile picha zilizunguka pale mezani watu wote
wakiangalia kwa kurudia rudia. “Kazi yako nzuri dada Tunda.” Mmoja wa
wanakamati akasifia. Tunda akatabasamu na kufanya azidi kuvutia kumtizama. “Asante.”
“Umeolewa?” Mwanakamati mwingine akauliza. “Acha
hizo Tino, bwana! Wewe mtafute kwa wakati wako. Acha sisi tuongee mambo ya
maana.” Wote walianza kucheka mpaka Tunda akatabasamu na kuinamia kwenye picha
alizokuwa ameshika mkononi mwake. “Tatizo lako wewe Mgeekwa, unapenda kupania
mambo sana. Si watu bado wanaangalia picha? Sasa kuna tatizo gani mimi
nikaendelea kuongea na Tunda?”
“Utamchanganya bwana.” “Tunda mwenyewe haonekani kama ni mtu wakuchanganyikiwa
hovyo. Halafu jibu lilikuwa fupi tu, ‘ndiyo au hapana’ ili nipate nguvu ya
kuendelea kumtafuta baada ya hapa. Au hamtaki kikao kingine?” “Wewe si muoaji Tino. Acha fujo.” “Sasa ningemuoa nani
wakati Tunda ndio amekuja leo? Eti jamani?” “Mgeekwa anakubania tu.”
“Mmeona eeh? Tuendelee Tunda. Sasa vipi?” Tino
akaendelea kumchokoza Tunda. “Kwa kuwa wengi wenu hamkuwa mmeona kazi zangu,
nashauri mtembelee website yangu ili muweze kuona kazi zangu nyingine ili
mmfanye maamuzi sahihi. Kisha mnaweza kupiga simu ofisini ili kutoa maamuzi
yenu na kujua gharama zinakuaje.” “Bwana Tunda yupo kikazi! Na mimi nimesoma
Tunda. Nimeelewa kuwa hunitaki.” Kila mtu akacheka.
“Achana naye huyo Tunda. Tuendelee na kazi.”
Mgeekwa ambaye alionekana ndio muongoza kikao, aliingilia.
“Jamani
nyinyi mnamjua bibi harusi mwenyewe. Mimi naomba nikubaliane na Tunda.
Nikamuonyeshe, achague. Kisha tutakuja kuongea na Tunda.” “Au kwa nini
msitukutanishe naye, yeye mwenyewe huyo bibiharusi? Tuone kitu gani anataka. Na
kama atataka ushauri pia tunaweza kumshauri.
Anaweza kufika ofisini kwetu, ninao wataalamu pale watamshauri vizuri au
watamsikiliza anachotaka.” “Sisi tunakutaka wewe Tunda. Usitutupie kwa watu
wengine.” Yule mwenyeji wake akamkatisha.
“Msiwe na wasiwasi kabisa. Hakuna
kitakachoharibika. Naomba niwaache, tuwasiliane mtakapo kuwa tayari.” Tunda
akasimama. Net hakuwa ameongea kitu chochote alibaki akimtizama tu Tunda. “Naomba
nikusalimie pembeni kidogo, Net.” Tunda aliongea kwa sauti tulivu huku akimtizama
Net. “Mimi hutaki kunisalimia pembeni kidogo?” “Acha Tino, nini lakini?”
“Tatizo lako Mgeekwa, hutaki nioe kaka!” Tunda akacheka akiwa bado amesimama. “Tundaaa!”
Tino akarudia. Net akavuta kiti na kuondoka pale. Tunda akamfuata nyuma. Net
alikuwa akiongoza njia huku Tunda akimfuata nyuma.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Mbona huonekani kama una furaha, Net? Mzima?”
Tunda akauliza mara baada ya Net kusimama nje ya ile hoteli na kumgeukia Tunda.
“Kila kitu kipo sawa?” Tunda akarudia kwa upole akionyesha kujali. “Kwa nini
hukunitafuta tena Tunda?” “Mama alichukua simu kwa ghafla, Net! Sikuweza
kuchukua namba zako za simu. Nilishindwa jinsi ya kukupata. Hata nilipokwenda
nyumbani kwako kufuata baadhi ya vitu vyangu, Emma hakuwa anajua lini unarudi
nchini na hakuwa akijua njia ya kuwasiliana na wewe. Babu anaendeleaje?”
“Alifariki. Unasema mama alikupokonya simu!?” Tunda akatulia kidogo.
“Tunda?” “Kwani yeye amekwambia nini?” Tunda
akauliza. “Kwa nini unauliza swali juu ya swali Tunda? Nani anamjibu mwenzake?”
“Samahani Net. Hakunipokonya, bali alichukua.” “Ilikuaje?” “Net please!” Tunda
akamsihi kwa upole. Akimtaka ayaache tu. “What?” “Naomba tusiongelee mambo ya
nyuma.” “Kwa kuwa wewe ushapita huko?” “Hapana Net. Kwa nini tusiongelee mambo
ya sasa?” “Ya sasa yapi?” Tunda akanyamaza.
“Kama unashindwa kunijibu basi naona nikuache tu.”
“Sishindwi Net. Lakini sijui ni nini mama alichokwambia juu yangu?” “Kwa kuwa
wewe huna haja yakujua alichoniambia, mimi ninataka kujua nini kilitokea. Maana
tuliagana vizuri siku ile ya jumamosi, ukaniambia tutawasiliana kesho yake.
Ndio nakuona leo! Nakuuliza kulikoni, naona unashidwa kunijibu.” Tunda akaona
ajieleze tu. Net alikuwa amekasirika.
“Siku ile tulipoagana, mimi niliendelea kukaa pale
ofisini nikimalizia oda ya Nchawa. Si unakumbuka nilikwambia alipiga simu
akitaka tumpelekee mzigo wake wote kwa pamoja siku ya jumanne?” “Ndiyo.” Net
akajibu. “Sasa kumbuka nilikuwa sina lori kubwa. Yote mawili yalikuwa
yamepeleka mizigo mikoani. Wazo lilinijia kuazima kwa kina Masai, ili
nihakikishe napeleka mzigo wote siku ya jumanne ili kuhakikisha simpotezi
Nchawa. Maana alisema nikimfanikishia, atakuwa anatupa kazi kila week hata kama
mara mbili kwa week itategemea na sisi wenyewe na uwezo wetu. Sasa ikabidi
kupambana ili nisiharibu, nimfurahishe.” Tunda akaendelea.
“Niliongea na Masai mwenyewe akasema lori analo
lakini hana dereva anayemuamini. Dereva wake ambaye anatumia hilo lori amepatwa
na matatizo, hayupo kazini. Akawa amenipa namba za simu za watu kadhaa,
akaniambia huwa anawatumia mara moja moja. Nilikaa pale mpaka usiku nikijaribu
kutafuta dereva wakupeleka mzigo wa Nchawa Moshi, siku hiyo ya jumanne asubuhi.
Nilitaka kufikia jumatatu niwe nina uhakika na kila kitu. Dereva na usafiri
wenyewe. Nilikuja kukamilisha kila kitu usiku kama kwenye saa mbili.” Net
alikuwa akisikiliza tu.
“Niliporudi nyumbani baada ya kukamilisha kila
kitu, nikamkuta mama na Safia.” Tunda akatulia kidogo. “Nini kilitokea?” Kama kawaida ya Net, akataka amalizie. “Mama
alionekana amenikasirikia sana na zaidi hakupenda kabisa kitendo cha mimi kuwa
nikiishi pale bila yeye kuwa na taarifa. Alilaumu ni kwa nini uliweza kuruhusu
mtu mwenye tabia kama zangu kuishi mle ndani na Maya, na mambo mengine mengi
ambayo siwezi kurudia, itakuwa ni kama najitusi tena mwenyewe.”
“Lakini aliniambia Safia ndiye atakuwa bosi wangu,
anahitaji nimkabidhi kila kitu ikiwemo simu ile ya mkononi na usiku uleule
nimpishe Safia kwenye chumba kile nilichokuwa nikilala pale nyumbani kwake. Na
usiku uleule niondoe mizigo yangu pale. Nilimkabidhi kila kitu, tena nilimuomba
kwa kuwa ilikuwa usiku, na nilikuwa na mizigo, aniruhusu kuondoka na gari yako
kisha niirudishe kesho yake, lakini mama alikataa. Nilijaribu kumuuliza
kulikuwa na shida gani kwa nini amekuwa vile! Lakini mama alikuwa mkali sana,
Net. Alinitaka niondoke pale usiku uleule. Ikabidi niondoke na mizigo yangu
mpaka barabarani ndipo nikapata taksii.”
“Siku ya jumatatu asubuhi niliwakuta walishafika
ofisini, Safia alikuwa kwenye meza yangu. Nikaamua kwenda kumsalimia mama
ofisini kwako.” Tunda akanyamaza akageukia pembeni. Net akamuona Tunda akianza
kufuta machozi. Alilia sana Tunda. Net akamshika mkono akamvuta nyuma ya gari.
“Nini kilitokea Tunda?” Tunda alishindwa kuongea
kwa muda. Akajaribu kutulia ndipo akaendelea huku akilia. “Mama Cote alitumia maisha yangu ya nyuma kunidhalilisha
Net. Alinitukana mbele ya Safia na yule kijana. Akinitaka nirudi kwanza shule niache
umalaya, nikipata vyeti ndio nirudi pale kazini. Akanilipa na kunitaka
niondoke.”
“Kweli sijui ni baya gani
niliwatendea! Nilijitahidi kufanya ile kazi kwa kadiri ya uwezo wangu, na
nilikusudia kuacha yale maisha machafu Net. Niliacha umalaya. Niliumia sana
kuona mama Cote anatumia maneno niliyoongea kanisani tena mbele ya wazee,
Mchungaji akinisihi niseme tu, pale ni sehemu salama, na wewe ukasema nisiwe na
wasiwasi, lakini baadaye tena baada ya kutubu, na Mungu kunisamehe, bado
nakumbushwa tena kwa kutukanwa! Bila kosa! Niliumia sana Net. Sana.” Tunda akajifuta machozi.
“Historia yangu yakufukuzwa
ikajirudia, Net. Alinifukuza mama yako usiku nikiwa na mizigo, na pale
ofisini akinitukana. Lakini nimesamehe. Sikutaka kurudia kuzungumzia na
wewe yaliyotokea kwa kuwa yananikumbusha mambo ambayo hayanijengi bali
kunibomoa. Isingekuwa Mungu, nisingeweza kurudi tena kanisani Net. Nisingeamini
watu wa kanisani, na nisingekuwa kanisani mpaka sasa.”
“Lakini Mungu ameniponya Net. Amenipa familia ya
kanisani. Nzuri sana. Nina mama na baba wa Kiroho wanao nifuatilia vizuri sana.
Tena wao ndio wamenisaidia kufikia hapa. Na wala sikurudi tena shule. Kwa elimu
ileile ndogo niliyonayo ninaweza kuishi.” Net alibaki kama amemwagiwa maji. “Pole
Tunda na samahani sana.” “Yameshakwisha Net. Mungu amenisaidi ninaishi vizuri
na nina amani.”
Simu ya Tunda ikaanza kuita. Akasogea pembeni
kidogo na kuanza kuongea. Alisikiliza kwa muda, akiwa kimya “Naomba subiri kidogo.” Net akamsikia Tunda akiongea kwenye simu,
akimwambia anayezungumza naye asubiri, kisha akamgeukia tena Net. “Net! Naomba
nikuage, Mungu akipenda tutaonana tena.”
Tunda alikuwa bado ameshikilia simu yake kama kuna mtu anayemsubiri
upande wa pili. Net alibaki akimwangalia. “Bye!” Tunda akamuaga, kisha akaondoka
pale akilifuata gari lake. “Samahani kuna mtu nilikuwa
nikizungumza naye hapa. Ehe! Kwa hiyo umesema inawezekana?” Net akamsikia
Tunda akiongea huku akiishia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku
inayofuata, Tunda akiwa ukumbini anapamba, mida ya saa mbili asubuhi, mmoja wa
wafanyakazi wake, Jazi, alimpigia simu kumwambia ametoka kuzungumza na simu ya
wateja wake wa siku iliyopita, wakina Mgeekwa, wanamuomba wakutane tena jioni
yake, walishafikia uamuzi. Jazi alikuwa ameandika kila kitu chini, muda na mahali.
Tunda akamtaka huyo huyo Jazi ndio aende kumuwakilisha muda huo utakapofika.
Siku za jumamosi usingeweza kumuweka Tunda kwenye kikao chochote. Anakuwa busy kupita
kiasi.
Ilipofika
jioni Jazi alitoka kwenda kumuwakilisha Tunda kule kwa wale wanakamati alipokuwepo
Net na Gabriel. Jazi alitoka pale akiwa amejiandaa kwenda kukamilisha oda,
lakini alipofika pale walimkataa kabisa. “Tunda yupo na majukumu mengine.
Chochote mtakachoniambia mimi, kitamfikia na yeye.” “Hapana. Kamwambie Tunda
aje yeye mwenyewe. Na sisi pia ni wateja. Tunataka huduma yake. Kwani ni bure?
Na sisi tutamlipa.” “Siku za jumamosi inakuwa ngumu sana kumpata Tunda jamani!
Naomba mniamini kuwa, mkiniona mimi, ndio mmemuona Tunda.” “Bwana wee! Sisi
tunamtaka Tunda. Wewe nenda zako.” Wote wakamshambulia Jazi kwa maneno
wakimtaka Tunda, mwishowe Jazi akaondoka.
Alimpigia
simu Tunda akiwa analia kuwa amedhalilika sana. “Usichukie Jazi, ndio
changamoto za kazi hizo.” “Wamenifukuza, kama..” “Kwanza
ujue wengi wao pale ni walevi. Wala usiumie. Umenielewa Jazi? Nitawapigia simu
baadaye kuzungumza nao. Wewe rudi nyumbani ukapumzike. Pole sana.” Siku ya
jumamosi ilikuwa siku ambayo Tunda anakuwa na kazi mbili au tatu. Sasa jumamosi
hiyo alikuwa akipamba kumbi tatu, tena zote kubwa. Tangia saa 9 usiku au
alfajiri, Tunda alishafika kazini kwenye ukumbi wa kwanza.
Alichokuwa
akifanya ili kumaliza kwa wakati, kila ukumbi alitanguliza vijana wake waanze
kupamba kisha yeye alipita kumalizia. Hakuwa akipokea simu ya mtu yeyote
isipokuwa wafanyakazi wake na mama Penny, basi. Ile simu ambayo namba alikuwa
akiwapa wateja, alikuwa hata hagusi siku hizo za jumamosi. Kwanza hakuwa akitoa
kwenye pochi mpaka akimaliza kazi, ndipo ataitoa tena kwa ajili ya kumpigia
simu muhusika, afike hapo, amkabidhi huo ukumbi, basi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku
hiyo alishinda kwenye kazi mpaka ilipofika usiku ndipo aliporudi nyumbani
kwake. Siku hiyo hakuwa hata na hamu ya chakula. Aliingia kuoga akatoka na
kujitupia kitandani kwake. Ni kweli alikuwa akitengeneza pesa, lakini
alihitajika nidhamu ya hali ya juu kwenye kazi hiyo. Kwa kuwa alikuwa akichukua
kazi nyingi, ilibidi kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha hakuna anapokosea,
na hakuna anayemuudhi. Iwe wanaolipia pesa nyingi au wale wenye kutaka
kupambiwa kwa kawaida tu, kote alihakikisha anaridhisha wateja wake. Na mara
nyingi siku za jumamosi ndio alikuwa na kazi nyingi sana kuliko siku nyingine
zote.
Akiwa
anakaribia kupitiwa na usingizi, akasikia mlio wa sauti wa simu yake kuashiria
ujumbe umeingia. Alijichukia kwa kutokuzima ile simu kabisa. Bila kutaka
kuwasha taa, alinyoosha mkono kwenye meza ndogo pembeni ya kitanda chake, ili
kuivuta simu yake na kuizima kabisa, ili apumzike.
Wakati
anataka kuizima kabisa ile simu, akaonelea aone ule ujumbe ambao kwanza
umeingia muda ule, ukawa umemtoa kwenye usingizi. Alitaka kusoma kesho yake
lakini akaona amjue huyo msumbufu wake. “Anataka nini usiku huu jamani!”
Tunda akajiuliza kwa hasira. Akasoma. ‘Najua una mambo
mengi Tunda, lakini naomba utafute muda tuzungumze. Net.’ Tunda aliruka
pale kitandani, akakaa. Akaamua kujibu. ‘Tunaweza
kuongea wakati wowote.’ ‘Lakini leo hukupokea simu zangu kabisa, Tunda!’
‘Samahani Net, sikujua kama ni wewe. Siku za jumamosi nakuwa na kazi nyingi
sana. Kama simu siifahamu huwa sipokei. Sasa hivi ndio narudi nyumbani.
Nimechoka kweli, hapa nipo kitandani.’ ‘Pole.’ ‘Asante.’ Tunda akajibu,
kisha akatulia.
‘Lini sasa unaweza kuwa na nafasi?’ Net akatuma ujumbe
mwingine. ‘Naweza kukupigia sasa hivi?’ Tunda
akauliza. Mara akaona simu yake ikiita. “Net!” “Vipi?”
“Safi tu. Nimeona ni heri tuongee tu kwa simu.” “Hutaki kuniona tena!?”
“Hapana. Sio hivyo Net.” “Hivi unakumbuka uliniacha sehemu ya kuegesha magari?”
Tunda akafunga macho na kuvuta kumbukumbu.
“Lakini nilikuaga Net.” “Unakumbuka mimi kukuaga?” “Hapana. Naomba
unisamehe. Nimekuwa na mambo mengi kweli! Yananivuruga akili.” “Nini tena?”
“Nahangaika kumtoa baba jela, anaumwa. Natamani atoke mapema ili akatibiwe.”
“Umepata wakili mzuri?” Net akauliza kuonyesha kujali.
“Nafikiri hivyo. Sijui. Ndiyo yupo anahangaikia kufufa hiyo kesi.
Ila baba amedhoofu sana, Net. Anatakiwa kutoka jela mapema ili awahi matibabu.
Kesho nataka niende nikamuone tena.” “Pole sana. Tunaweza kwenda wote
kumtizama?” “Twende wote jela!?” Tunda akauliza kwa mshangao.
“Si ndipo alipo?” Net akauliza kiustarabu tu. “Ndiyo. Bado yupo jela.” Akajibu kwa upole. “Basi tutaenda wote.” “Asante Net.” “Unaabudu kanisa gani?”
Tunda akamuelekeza na kumwambia ni muda gani wanaanza ibada. “Basi nitakuja kanisani kwenu kukutembelea.” “Nitafurahi
kukuona Net. Karibu.” “Asante. Basi ngoja nikuache upumzike, nitakuona kesho.”
“Asante, usiku mwema.” “Na wewe pia.” Waliagana, Tunda akabaki akijiuliza maswali
mawili matatu, mwishowe akaonelea alale tu.
Jumapili.
Net Kanisani kwa Kina Tunda.
Siku
hiyo ya jumapili, alimkuta Net ameshafika kanisani akimsubiri nje ya gari yake.
Tunda akaegesha gari yake pembeni ya alipokuwa amegesha Net gari yake. Kama
kawaida yake hakujikosea. Alikuwa amependeza haswa. Alishuka akiwa ameshikilia
pochi yake na bibilia yake mkononi. Akamsalimia Net huku akijaribu kuweka vitu
vingine kama simu yake ya mkononi na funguo za gari ndani ya pochi yake.
“Karibu sana, hapa ndipo Mungu alinipa familia
nyingine. Ni watu wazuri sana. Utamfurahia Mchungaji wetu na mkewe. Wamefanya
hapa kanisani kukawa kimbilio la wengi. Wanahimiza sana vijana kufanya kazi kwa
bidii. Mkewe ndiye mwenye kipaji cha kugundua vipaji vya watu na kuviendeleza.
Yeye ndiye amenisukuma kwenye hii kazi ninayofanya, tena nikiwa na hofu nyingi
kweli.” “Auntie Tunda!” Watoto wa Mchungaji walimkimbilia Tunda. Penny na mdogo
wake Pendo.
“Dady ametufukuza ofisini kwake.” Tunda akacheka. “Huu
ni muda wenu wa Sunday School. Muwahi msichelewe.” “Huyo ni mzungu?” Mmoja wao
ambaye Tunda alimlaumu sana mama yake kuwa alimuharibu mwanae kwa vituko, Penny
alimnong’oneza hilo swali Tunda lakini aliweza kusikika. “Na anasikia
Kiswahili.” Tunda akamjibu, wote wakacheka.
“Umekamatwa leo na maswali yako yasiyoisha we
Penny!” Mdogo wake alimwambia ndugu yake huku akimcheka. “Shikamoo. Naitwa
Penny, kipenzi cha dady.” Penny akamwambia Net. Net alikuwa akicheka tu. “Muongo,
mimi ndiye kipenzi cha dad and by the way, dady yetu ndiye bosi hapa.” Net akazidi
kucheka.
“Nilikwambia hili kanisa lina vituko! Sasa bado
hujakutana na wazazi wao. Ndio utachoka zaidi. Haya naomba muende Sunday
school.” Tunda aliwashika vichwa na kuwageuza, kama kuwaelekezea upande
lilipokuwepo darasa lao kwa kuwasukuma kidogo.
“Hata hatujamjua mgeni wakizungu sababu yako!”
Walimsikia mdogo wake Penny akimlaumu Penny. “Ni mchumba wa auntie Tunda?” Pendo
akamuuliza Penny, “Wewe! Akikusikia anko Juli, atakupiga makwenzi. Anko Juli
ndio mchumba wa auntie Tunda.” “Muongo.” “Kweli.” “Muongo.” “Kweli tena.
Nilimsikia mama akimwambia dady.” Waliwasikia wale watoto wakibishana huku
wakielekea darasani kwao. Walijawa fujo na kelele kupita kiasi. Tunda alibaki
akitingisha kichwa huku akicheka.
“Shalom!” Tunda na Net walishtuliwa na sauti
iliyokuwa ikiwasalimia, maana akili zao zilikuwa zimezama kwenye mazungumzo ya
wale watoto. Wote wakageuka. “Amina Juli. Shalom!” Tunda akajibu. Juli
akamsogelea na kumkumbatia Tunda huku akimtizama kwa tabasamu. “Umependeza sana
Tunda.” Tunda akacheka kidogo. “Usingenisifia ningeshangaa!” Wote wawili
wakacheka.
“Ni kweli bwana. Au hutaki nikupe sifa zako?”
“Hapana, nashukuru. Juli! Huyu anaitwa Net, Net huyu anaitwa Julius au Juli
kama wengi tulivyozoea kumwita.” Walipeana mikono. “Net ndiye mtu aliyenitoa
duniani nakunileta kanisani.” Tunda akaongeza huo utambulisho mfupi tu. “Tunashukuru
bwana kwa kutuletea kondoo. Maana kuna vifaa vingine muhimu sana kanisani, ndio
kina Tunda.” Juli aliongeza huku akicheka. Juli na Tunda walitaniana kidogo
mbele ya Net, waliposikia nyimbo zimeanza kusikika kanisani, Tunda akamwambia
Net waingie kanisani, ibada imeanza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tunda
alikaa na Net mpaka mwisho wa ibada, ndipo walipotoka na kwenda kusalimiana na
Mchungaji na mkewe ofisini. “Wote nilisha waambia juu ya Net. Nafikiri
mnakumbuka.” Tunda akaongea kwa hakika akijua lazima Mchungaji na mkewe
watakuwa wakimkumbuka tu Net. Wakabaki wametoa macho. “Jamani nyinyi! Net!?
Pale kanisani alijitambulisha kama Nathaniel Cote, lakini kwa kifupi ni Net.
Net yule niliyewaambia habari zake!” Tunda akashangaa wanawezaje kumsahau Net!
“Tunakumbuka
sana. Lakini sikumbuki kama ulituambia kama ni mzungu!” Mama Penny akajibu na
kumgeukia mumewe. “Au wewe baba Paroko unataarifa hizo?” “Hata kidogo.” Tunda
na Net wakaanza kucheka.
“Unaposimulia
jambo, usiwe unaondoa mambo ya muhimu.” “Sasa swala la uzungu wa Net ungeongeza
nini kwenye ushuhuda wangu?” “Usitutanie kabisa wewe Tunda! Kuna uzito wake
mkubwa sana. Wewe kutolewa jalalani na Mzungu na kuketishwa na wakubwa kama
sisi, sio kitu kidogo!” “Mama Penny wewe! ” Tunda alibaki akimshangaa.
“Kabisa!”
Kama kawaida ya mumewe kuunga mkono kila kitu anachoongea mkewe. Net alikuwa
akicheka tu. “Kwanza ujue Net anasikia na kuongea Kiswahili fasaha kama mtu
aliyezaliwa Tanzania. Yaani hata hapa anawasikia kila kitu.” Wakatulia kidogo.
“Eti ni kweli?” Mama Penny akauliza huku akimwangalia Net ambaye yeye alikuwa
akicheka muda wote. “Sasa unafikiri ile salamu ya pale kanisani alikariri?” Mama
Penny akamtizama Net na mumewe. “Tunajua sana kama anajua kiswahili.” Mumewe
akasaidia, wote wakacheka.
“Jamani nimefurahi
kuona Tunda yupo na watu wanao mjali.” Ikabidi Net azungumze tu. “Sisi
tumefurahi kukufahamu na kuja kututembelea Net. Hatujawahi kupata rafiki wa
kizungu tangia tuanze hii huduma.” “Jamani Mama Penny wewe!” Tunda akazidi
kushangaa. “Naongea moyo wangu. Kwa nini nisiseme ukweli?” “Mimi ndio kabisaaa,
sijawahi kuwa na rafiki mzungu tokea nizaliwe.” Mchungaji akaongeza. Wote
wakacheka.
“Net,
tuondoke zetu.” Tunda akasimama. “Lazima twende naye nyumbani akale.” “Nina
haraka mama Penny!” Tunda alitaka kukataa. “Haituhusu sisi. Ulimleta mwenyewe.
Kama unaharaka ndio mtangulie nyumbani, sisi tutawakuta huko huko. Huwezi
kumleta mgeni halafu ukaishia naye ofisini.” Mama Mchungaji akajibu.
“Atakuja
nyumbani siku nyingine.” “Mbona hilo tunalifahamu? Na tutahakikisha lazima aje
nyumbani siku nyingine. Leo haiwezi ikawa mwisho wake wakufika nyumbani kwetu”
Tunda akatingisha kichwa, huku akiguna. Alijua jinsi mama Penny alivyo
king’ang’anizi. “Twende Net mwaya.” “Ukajisikie nyumbani Net. Sisi tuko nyuma
yenu tunakuja. Ngoja nikusanye vifaranga vyangu vyote. Tunakuja sasa hivi.”
“Asante sana.” Net akashukuru wakatoka.
Tunda
na Net kwenye gari.
Wote wakajikuta
wakianza kucheka tena mara ya kutoka hapo ofisini. “Huwa wanakuwa serious hawa?”
Net akauliza. “Heri Mchungaji kidogo huwa anajitahidi, lakini huyo mkewe! Sijawahi kumuona. Lakini anaupendo sana. Hana
roho ya wivu hata kidogo, anapenda kila mtu afanikiwe.” Waliongozana mpaka
kwenye magari yao.
“Unataka
tuendeshe magari mawili kama tupo kwenye msafara bwana! Njoo upande kwenye gari
yangu, tutakuja kuchukua gari yako baadaye.” Tunda akacheka, akaona ni wazo
zuri. Akaingia kwenye gari ya Net. Alipokaa tu, Net akamvuta mkono wake
wakushoto akaangalia vidole vyake. “Mbona Juli hajaweka pete bado!?” Tunda akatulia
kidogo kama anayefikiria.
“Hatujafika
huko.” Tunda akajibu baada yakumuona Net akimtizama. “Mmefikia wapi? Maana
naona mpaka mnakumbatiana.” “Nisalamu tu, Net jamani!” “Salamu yenu nyinyi
wawili tu!? Mnasalimiana kwa kukumbatiana?” Tunda akatulia tena kama
anayefikiria kwa kuvuta kumbukumbu. “Eti Tunda?” Net akauliza tena na kuwasha
gari kisha akaondoa gari pale kanisani.
“Watu
wengi huwa wanasalimiana pale kanisani kwa kukumbatiana.” “Oooh! Basi inabidi
nirudi tena. Maana leo sikubahatika kukumbatiwa kabisa, na wala sikubahatika
kuona watu wengine walio kumbatiana. Hata Juli mwenyewe hakunikumbatia na mimi
ila wewe tu wakati tulikuwa tumesimama wote.” Tunda akanyamaza.
“Kwa
hiyo sasa hivi mpo kwenye hatua gani ya mahusiano?” “Hatujafika popote.”
“Anatambulika mpaka kwa viongozi wako kama ni mchumba wako, bado hamjafika
popote!?” “Alinigusia tu nia yake yakutaka kunioa.” Tunda akaongea tu hivyo na kunyamaza,
Net akamgeukia kama kumwambia aendelee, anamsikiliza.
“Ndio na
mimi nikamwambia mama Mchungaji, au tuseme mama Penny. Yeye ndio kama rafiki
yangu au mshauri wangu, nafikiri watoto walimsikia wakati akimwambia mumewe.
Lakini hamna mwendelezo wowote.” “Unamaanisha nini?” “Tuliishia hapo hapo tu,
Net!” “Mbona sikuelewi Tunda? Mtu alikufuata kukueleza nia ya kutaka kukuoa.
Halafu unaniambia mliishia hapo hapo! Inamaana mmeishia hapo hapo kama
wachumba, au kama mke na mume au?” “Net
jamani! Nilishindwa kitu chakumjibu.” Net akamgeukia huku amekunja uso.
“Huyu
kaka anamtaka Tunda asiyemfahamu hata kidogo. Nilijua anataka kujiingiza kwa
mtu asiyemfahamu kabisa. Anamuona Tunda aliyesimama pale, lakini hamjui Tunda
wa kweli na maisha niliyoishi nyuma. Najua wazi Mungu amenisamehe, lakini hapa
duniani mambo yote niliyofanya bado yapo kwenye akili na miayo ya watu, Net.”
“Mama
yangu mpaka leo sina mahusiano naye kwa kosa la kutembea na mumewe na wanawake
wengine wengi ambao nimevunja ndoa zao au nimeathiri ndoa zao kwa namna moja au
nyingine. Ndugu zangu wenyewe hawaniamini hata na marafiki zao wakiume! Hebu
niambie Net, huyu Julius siku moja akitaka kuja kukutana na familia yangu
nampeleka wapi?” Tunda akauliza kwa upole.
“Wewe
ulikaa na ndugu zangu kwa muda mfupi sana, lakini waliweza kukwambia mabaya
yangu yote. Japo mengine ni ya uongo, lakini yanasababishwa na chuki waliyonayo
juu yangu kwa yale niliyo watendea. Naogopa hata kufikiria swala la mahusiano
na mtu yeyote yule, kuhofia kuja kunilazimu kueleza historia yangu ya aibu au
chafu kama vile! Sitaki nije nianze kupenda, halafu nikaumizwa kwa maisha
niliyoishi zamani.”
“Ni
ngumu kuja kuishi na mwanaume halafu akaja kukuamini kwa asilimia zote kama
ambavyo angemuheshimu mwanamke aliyeanza naye mahusiano ya kimapenzi.
Namaanisha labda msichana aliyemkuta bikra. Kwangu itakuwa ngumu Net.
Nilishaharibu sana maisha yangu.”
“Nikichelewa
kurudi nyumbani, atahisi nimetoka kwa mwanaume mwingine. Nikichelewa kupokea
simu yake, au niongea na simu na mwanaume yeyote asiye mfahamu yeye, au hata
nikiwa na mahusiano ya kawaida tu na mwanaume mwingine, huyo mume au mchumba
wangu atahisi vinginevyo. Kuja kuwa na mahusiano kwa upande wangu ni kukubali
kuingia kwenye maisha yatakayoninyima uhuru, furaha, na naona nitakuwa
najiingiza kwenye matatizo tu.”
“Nimeamua
niishi hivihivi, hata hivyo nimeshakinahiwa, halafu ninahofu yakuja kuingia
kwenye ndoa nikashindwa kuzaa. Nitateseka sana.” “Kwa nini?” Net akauliza.
“Mama
aliponitoa ile mimba, sijui walinitoaje! Sijui kama haikuathiri kizazi changu
au la. Sitaki kuingia kwenye ndoa, nikiwa na wasiwasi huu.” “Kwani hukuwahi
kushika mimba tena?” Net akauliza huku akimtizama Tunda. Tunda akainama.
“Ni Baba
Tom tu, ndiye mwanaume pekee niliye lala naye bila kondom. Alikuwa hataki hata
kusikia neno kondom. Ila baada yakutoka pale, au baada ya pale kila mwanaume niliyewahi kulala naye, hata Sadiki
nilihakikisha natumia kondom kila wakati. Sikuwahi au sikurudi tena kutotumia
kondom. Hata hivyo wengi nilihakikisha nawamaliza nguvu zakutoweza kuniingilia.
Niliishia kuwa..” Tunda akanyamaza. Akageukia dirishani, nakuanza kufuta
machozi.
“Nisikilize
Tunda. Hayo nimaisha uliyoishi zamani. Ulishakiri, Mungu amekusamehe. Hutakiwi
kuendelea kuumia kwa ajili ya hayo. Huko umeshatoka, na umeamua kutokurudi
tena. Naomba utafute jinsi yakutumia hayo maisha kuwa msaada kwa wengine.
Nilazima ubadilishe kutoka kuwa aibu na kuwa msaada kwa mtu mwingine. Ukikubali
kuwa ni kwa ajili yako tu, na ukakubali ikutese, kweli itakuwa shida ulizopitia
ni bure kabisa. Umenisikia?” Tunda
alikuwa akiendelea kulia.
Net akamvuta
mkono wake aliokuwa akijifuta machozi akaubusu kiganjani. Ilikuwa ni mara ya kwanza
Net kumbusu Tunda. Mwili mzima wa Tunda ulisisimka. Hakuwahi kujisikia vile
tokea anazaliwa. Eti mtu kumbembeleza akiwa mkosaji! Kwanza huo mwili wengi
waliugusa ili kujinufaisha nao. Wakike kwa wakiume. Sasa leo anapokea busu la
faraja! Ilikuwa faraja ya pekee kwake. Tunda hakuamini kupata busu kutoka kwa
Net anayemfahamu akiwa mchafu vile! Hata hivyo ni Net jamani!
“Huna
haja yakulia kabisa Tunda. Lazima tugeuze yale maisha yako kuwa msaada kwa
wengine.” “Nitafanyaje?” Tunda akauliza huku
akifuta machozi, hata yeye hakuwa anaelewa alipitaje kule kote. Aliwezaje!?
Hapo alipotulia ndipo picha ya kila kitu alichofanya nyuma ikaanza kumjia.
Wakati mwingine aliweza kuhudumia wanaume hata watatu kwa siku moja!
Kinyaa,
shida na mateso yote aliweza kuyapuuza akawa akifanya kama mchezo mwepesi sana.
‘Niliwezaje!?’ Ni swali alilokuwa akijiuliza kila wakati Tunda bila
kupata jibu. Achilia mbali kujidhalilisha alikopitia bila kufanikiwa. Ilikuwa
ni kama chombo cha thamani sana, kinachostahili kutumiwa kuwekea chakula hata
cha wafalme, halafu chombo hicho hicho umpe mtoto mdogo, asiyejua thamani yake,
achee nje kwenye matope.
“Kwa kuwa habari mbaya zinazagaa kwa haraka,” Net
akaendelea. “lazima wewe mwenyewe uwe msemaji wa habari zako. Geuza kuwa msaada
kwa mabinti na vijana. Huwezi kujua hata wazazi wengine wanaweza kupona.” “Kweli Net!?” “Kabisa. Acha watu wakufahamu kwa
yale maisha ya zamani, na waone kazi kubwa Mungu aliyofanya ndani yako. Hakuna
mwanadamu ambaye angeweza kukutoa ulipokuwa Tunda, isipokuwa Yesu mwenyewe.
Ulikuwa umefungwa na nguvu za giza tokea mtoto unaishi na baba Tom. Ufahamu
wako ulitekwa, ulikuwa ukitumikia falme nyingine kabisa. Kwa nini usitumie kile
ulichofanyiwa na Mungu kufungua wengine?” Net akaendelea taratibu.
“Wapo wengi wanapitia ulipopita wewe, lakini
wanakosa msaada. Ona jinsi ulivyofanikiwa kwenye maisha kwa kukubali kutumia
kipaji Mungu alichokupa tena bila shule ya maana. Lazima kutumia maisha yako
yaliyopita kwa ushindi. Yale shetani aliyokuwa amekusudia kuwa mabaya kwako, Mungu
amekugeuzia kuwa mema. Sasa kwa nini unalia tena? Lazima ufurahie kama mshindi
na si uliyeshindwa. Eti Tunda?” Machozi ya Tunda yalikauka gafla, akajawa
tabasamu kubwa usoni mwake.
“Nilimiss hayo macho na hilo tabasamu!” Tunda akajifunika
uso wake na kucheka kwa sauti. Net akaendelea kumfariji, huku akiendesha mpaka
Tunda akafunguka kabisa. “Unajua Net, Mungu anakutumia sana katika maisha
yangu? Kila wakati huwa unanitoa sehemu moja na kunipeleka sehemu ya juu!
Isingekuwa wewe unajua sasa hivi nisingekuwa hapa?” “Ndio nakushangaa sasa
unavyokuwa unanikimbia kila wakati!” Tunda akacheka.
“Sijakukimbia bwana!” “Unanipuuza sana Tunda!
Hunichukulii maanani hata kidogo.” “Jamani Net!” “Kweli Tunda. Hebu niambie ni
juhudi gani umefanya kunitafuta tokea ulipoondoka Arusha?” Tunda akabaki kimya.
“Inawezekana Arusha ni mbali sana. Lakini
tulikutana majuzi pale hotelini, ukaniacha sehemu yakuegesha magari! Niambie
ukweli Tunda, hivi ulikuwa hata na mpango wakuja kunitafuta tena?” Tunda
alijisikia vibaya sana. “Nilijua tungeonana tu.” “Kwa njia gani, Tunda? Maana
hata simu yangu hukuomba na kikao kilichofuata ulimtuma mfanyakazi wako aje
kwenye kikao sio wewe mwenyewe. Mimi ndio nahangaika kulazimisha mahusiano
ambayo hata sijui niite mahusiano au sijui niitaje.” “Ni mahusiano Net.” “Ni
mahusiano gani haya Tunda!? Mimi ndiye wakukutafuta kila wakati, lakini
mwenzangu ni kama nakusumbua tu.”
“Hunisumbui hata kidogo Net.” “Unauhakika Tunda?” Tunda
akatulia kidogo. “Nikwambie ukweli Net?” “Niambie tu.” “Naomba nielewe kabisa.
Nakosa ujasiri kwako.” “Kwangu tena!?” “Kabisa Net. Sijui nikujishtukia au
vipi? Najiona nakuchosha na kukugharimu sana. Kwa hiyo wakati mwingine
najiambia kukaa mbali na mimi ni kama unapumzika. Naona kama kazi yako
uliyoifanya kwenye maisha yangu ni kama imetosha, sasa hivi nalazimika mimi
mwenyewe kusimama, sio kukuchosha zaidi. Sijui umenielewa?” Walifika nyumbani
kwa Mchungaji.
“Tutazungumza vizuri baadaye.” Net aliongea hivyo wakati anaegesha gari. “Lakini
naomba uniamini kuwa hunichoshi Net. Nisamehe pale unapoona ni kama nakupuuza.
Sasa hivi nipo kwenye wakati wa hekaheka. Siwezi kusema mgumu, ila ni kama
mtoto ambaye yupo kwenye kutambaa, lakini mazingira yanamtaka akimbie. Nina
majukumu ambayo yote yananiangalia mimi na lazima niyatimize.”
“Siku kama ya leo ndio huwa napumzika. Ila siku
nyingine, akili inabidi kufanya kazi kwa haraka ili kuweza kuchukua hatua na
nisiharibu.” “Am so proud of you Tunda. Najivunia sana. Nilifurahi sana kukuona
juzi ukiongea kwa kujiamini. Tena ukijinadi kipaji chako!” “Yote hiyo ni wewe
Net.” Net akacheka.
“Na wewe Tunda. Ulikubali na kuchukua hatua.
Nilijua jinsi wanaume walivyokuwa wakikusumbua tulivyokuwa pamoja kule Arusha.
Wenye pesa na wafanyabiashara wakubwa. Lakini ulitulia. Umenifurahisha.”
“Asante.” Tunda akacheka taratibu na kumwangalia Net. “Umenisamehe sasa?” Tunda
akauliza kwa kujali akibembeleza. “Tutaongea zaidi baadaye. Twende ili
tusichelewe kila mahali. Si uliniambia kule jela wana muda maalum?” “Ndiyo.”
“Basi tusalimie hapa, halafu tuwahi.” Wakachuka garini.
Kwa Mara ya Kwanza Net Nyumbani, kwa Mchungaji.
Wakamkuta
Mama Penny alishafika. “Mlipitia wapi!?” “Net alitaka tupitie dukani angalau
tusije mikono mitupu.” “Ndio faida
yakuwa na mahusiano na wazungu! Maana wageni wengine wakija humu ndani, utasikia
naomba nikanunuliwe Fanta, mimi sipendi Coca, au sijui Sprite! Lakini watu
walio staarabika wanakuja na zawadi mkononi.” Mama Penny aliongea akimsuta
Tunda. Net akacheka tu.
“Yaani
mama Penny! Mwenzio nakuwa nimechoka, na Fanta pekee ndiyo inaniburudisha.”
Tunda akajibu. “Sasa uwe unanunua kreti nzima unaliacha hapa ndani, sio
kusumbua watu.” “Huwa naacha, ila wanao wanamaliza.” “Ni Penny huyo, anti.”
Pendo akadakia. “Hata dady anapenda Fanta.” Penny naye akaongeza na kufanya
watu wote wacheke.
“Watoto
hawana siri hawa! Kwanza mpenzi wangu huwa hanywi soda nyingi kwa siku, tatu
mwisho.” “Sasa kama anakunywa tatu, na wanao mbilimbili, hiyo kreti inakaa siku
ngapi?” “Na dada naye anapenda Fanta.” Penny akaongeza tena. “Haya umesikia
wanao?” Tunda akadakia. “Naombeni
muondoke nyinyi watoto!” Mama yao akawafukuza. Wote walikuwa wakicheka.
“Karibu
Net. Hapa ndipo nyumbani kwetu wote. Tukupokee mzigo, ila huna haja ya kuja
hapa na vitu bwana. Uwepo wako ni zawadi tosha.” “Asante Mama Penny.” Ulikuwa ni
wakati Net alioufurahia sana. Alikula na kucheka tokea anaingia mpaka wanatoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Sijawahi
kuona Mchungaji na Mama Mchungaji wa namna hiyo!” “Nilikwambia mimi. Yaani mimi
nilikuja na uchungu moyoni, hata sijui viliishia wapi, na lini! Wana jinsi ya
kukuonyesha maisha sio magumu ki vileee!!” “Si umemsikia hata huyo mama
mwenyewe anavyosema?” “Basi ndio usemi wake kila wakati. Eti, ‘acha kuwa serious wewe, maisha sio magumu
hivyo!’ au utamsikia, ‘Usituharibie
hali ya hewa hapa kwa kuwaza kama unataka kuumba dunia wakati Mungu mwenyewe
alishasema imekwisha, kazi yetu sisi tutawale.’ Wakati wote husema watu
tunashindwa hutawala sababu ya ujinga tu.”
“Usimuone
maneno mengi vile, anapesa sana yule mama. Karibu kila siku anayo kazi
inayomuingizia sio chini ya milioni. Kama sio kupamba, basi anabiashara zake
nyingine. Jina lake linafahamika sana hapa mjini, ndiye aliyenisaidia kuniuza
kwa watu mpaka sasa na mimi nafahamika au napata kazi kwa jina langu. Mkarimu
na hana tamaa. Ukifanikiwa ndiyo furaha yake.” Tunda na Net waliendelea kuongea
wakiwa wanaelekea kumuona baba yake Tunda jela.
“Nimefurahi
Tunda. Nimepata wakati mzuri sana. Nilihitaji mapumziko ya akili baada ya
mawazo mengi.” “Unawaza nini tena Net!?” “Nitakwambia tukitoka kumuona baba,
kama bado utakuwa na muda wakunisikiliza.” “Hata kama ni saa sita usiku,
nitakusikiliza Net. Unajua ni wewe pekee ambaye sina haja yakujificha kwako?
Sina sababu ya kujifanya Tunda huyu wasasa tu. Nakuwa huru, najua nipo na mtu
anayenifahamu vizuri, na bado amenikubali.” Net akamtizama Tunda na kutabasamu.
“Nini
sasa? Si kweli?” “Ni kweli Tunda. Na sio kukukubali tu, najipendekeza pia.”
“Jamani Net! Hujipendekezi bwana.” “Unauhakika Tunda?” “Kweli Net. Nakuwa
nakosa tu ujasiri. Nilikwambia. Lakini nafurahia tukiwa wote. Unaniheshimu japo
unanijua kuliko yeyote yule hapa duniani.” Walifika gerezani, hapakuwa mbali na
nyumbani kwa mchungaji. Ni eneo hilohilo la Tabata. “Twende kwanza tukamuone
baba, kisha tutaongea.” Wakashuka.
Net akiwa
na Tunda gerezani.
Waliingia
ndani japo muda ulikuwa unakaribia kuisha wa kuwaona wafungwa, lakini baba yake
Tunda alifurahi sana kumuona Tunda. Waliongea kidogo, Tunda akamuahidi, kufanya
kila awezalo kumtoa humo. “Tunda aliniambia jinsi ulivyomsaidia kumtoa kwenye
matatizo. Nakushukuru sana. Nilimuacha mwanangu hospitalini bila msaada, tena
nikijua kila mtu hamtaki!” Baba yake akaendelea.
“Nilipo
hukumiwa pale mahakamani nililia kama mtoto wa kike nikimfikiria mwanangu pale
kitandani hospitalini. Nilimlaani Mungu kwa kukubali mimba ya huyu mtoto
itungwe siku nilipolala na mama yake. Na pesa yenyewe niliyompa ilikuwa ndogo
kweli, sikujua kama nitakuja kumuona tena Tunda!” Tunda alikuwa ameinama tu
kama anayefikiria wakati baba yake akisimulia. Akili zilimrudisha mbali,
akabaki akimsikiliza Net na baba yake huku akifikiria hili na kukumbuka lile.
“Nakushukuru
sana.” “Hata mimi namshukuru Mungu kunikutanisha na Tunda. Nampenda sana
Tunda.” Tunda akashtuka sana. Hakutegemea kusikia Net anasema vile, tena akiwa
na baba yake! ‘Upendo huu ni wa namna
gani!?’ Tunda akajiuliza kwa mshangao akanyanyua kichwa na kumgeukia Net
palepale walipokuwa wamekaa upande mmoja wakimwangalia baba yake. “Nisije kujichanganya. Nisifurahie mengine.
Net ni mzungu. Neno upendo ni kitu cha kawaida kutamka kwa wenzetu.”
Akajirudi Tunda, akiogopa kufurahia zaidi.
“Ni
kweli ni upendo pekee, ndio uliokuwa ukihitajika kumpokea Tunda. Nakushukuru
sana.” “Asante baba. Tunaweza kuomba pamoja?” Net akauliza kiuungwana. “Mimi
sijui kuomba Net, wewe omba tu kama utataka.” Baba yake Tunda akajibu. Na hapo
ndipo Net alipomfundisha yule mzee kuomba, na kumuhubiria. “Hata Tunda amekuwa
akinihubiria, lakini…” Yule Mzee akasita.
“Haina
haraka baba. Pata muda wakufikiria, kisha utaamua.” “Nina dini yangu nzuri tu.
Sitaki kubadili dini.” “Kuokoka si kubadili dini baba. Nikupatanishwa na Mungu.
Bibilia inasema watu wote tumekosa na kupungukiwa na utukufu wa Mungu. Kwa
kutubu na kumkaribisha Yesu maishani mwako, nikukubali yale Mungu aliyokusudia
kwa maisha yako. Kama ukiokoka, na ukaona dini uliyonayo inakusaidia kukusogeza
karibu na Mungu, ujue upo katika njia sahihi.”
“Lengo
la dini nikukupatanisha na Mungu, au iwe msaada kwa roho yako, basi. Lakini kama itakuzuia kuwa na mahusiano na
Mungu, basi itabidi ufikirie mara mbili, juu ya hiyo dini. Maana itakufaa nini
kuwa na dini halafu ikakukosesha mbingu? Au itakusaidia nini kuiacha dini yako
ukahamia kwenye kanisa, na pia ukakosa mbingu?” Net akaendelea.
“Lengo
si kuhama kanisa moja kwenda jingine, lengo ni kuhama kutoka falme ya giza na
kuhamia kwenye ufalme wa Mungu, na kukaa huko. Sio unahamia kwenye kanisa
jingine, wenye jina fulani, ukajulikana na wewe upo kwenye kanisa hilo kumbe
maisha yako ni chukizo mbele za Mungu. Ukibaki wewe peke yako na Mungu, hamna
mahusiano yeyote, huo sio mpango wa Mungu.”
“Mungu
anataka mahusiano na mtu mmoja mmoja si kanisa, wala dini. Ukifa leo mzee,
hutaulizwa dini yako. Mungu atataka mahesabu ya jinsi ulivyotumia maisha yako
hapa duniani.” “Maisha yenyewe yameisha haya kijana wangu. Nishatupwa huku.”
“Nilikwambia usikate tamaa baba. Nahangaika kukutoa.” Tunda akaingilia.
“Hata
hivyo, hata hapa ulipo pia utakuja kuulizwa na Mungu ulifanya nini?”
“Ananiuliza nini huyo Mungu wakati yeye ndiye amenileta hapa, tena bila kosa!?”
“Ewaa! Umezungumza sahihi kabisa. Kuwa Mungu alikuleta hapa kwa kusudi. Basi
ujue lipo kusudi. Kwa nini iwe wewe na sio mwingine? Inawezekana kuna kazi
anakupa humu gerezani uifanye au umeletwa humu kwa ajili yako mwenyewe. Unasema
unayo dini. Huwa unasoma bibilia?” “Hapana, lakini nafahamu vihabari vyake.” Akajibu
baba yake Tunda akiwa kama anavuta kumbukumbu.
“Unakumbuka
historia ya Yusuph?” Yule mzee akatulia. “Kwa utizamaji huo, naamini unaijua
habari nzima. Unakumbuka mwisho wake? Unakumbuka jinsi alivyotoka gerezani kitu
Mungu alimfanyia?” “Si ndiye alikuja kusaidia ndugu zake?” Net akatabasamu kwa
kuridhika.
“Si
ndugu zake tu, watu wengi walipata msaada kupitia kukaa kwa Yusuph gerezani.
Kama angelia na kubaki kulalamika, inamaana kuonewa kwake kule gerezani
ingekuwa bure kabisa. Tunda amekupa ushuhuda wake?” “Upi tena?” Net akamtizama
Tunda kama anayemuomba ruhusa, yakusema. Kwa vile Tunda anavyomfahamu Net,
akajua hawezi kumdhalilisha kwa baba yake. Akamruhusu asimulie chochote na yeye
akiwa na hamu yakusikia jinsi Net anavyoanza kutumia maisha yake kuwa msaada
kwa wengine.
“Nilimwajiri
Tunda kwenye kampuni ya mama yangu. Nikasafiri nikamwacha Tunda pale ofisini.
Huku nyuma mama yangu alimfukuza Tunda vibaya sana. Aliondoka Arusha akiwa
hajui chakufanya, akilia njiani akimlaumu Mungu. Lakini Mungu alimfundisha kwa
mfano wa kupitia watoto, huku akimuonya kulia hakutamsaidia, mpaka
atakapoangalia mazingira yanayomzunguka, akasimama na kuchukua hatua.”
“Tunda
alitii, ndio maana yupo leo kama alivyo. Kama Tunda angeendelea kulalamika
mpaka leo asingekuwa hapo. Na yale ambayo shetani ameyakusudia kuwa mabaya
kwake, yangeendelea kumkandamiza na kumwangamiza kabisa.”
“Usikubali
maisha yako yakawa hayana maana. Kila kinachotokea katika maisha yako baba
yangu, kitumie kutengeneza hesabu ya kumpa Mungu siku ukisimama mbele zake.
Maana ni kweli wote atatudai tu siku moja. Lakini uzuri, kila utakapochukua
hatua, yeye anakuwa na wewe, anakuinua, atakutia nguvu na kukubariki.” Tunda
alikuwa akimwangalia Net bila kummaliza. Kijana mzuri wakuvutia kwenye kila
jicho la mtu anayemtizama, mpaka watoto! Aliyesoma vizuri, anayejua maisha
vizuri, na pesa nzuri yakueleweka na bado anasimama na Mungu wake!
“Kwa
mfano mwingine tu. Najua unajua maisha ya Tunda kwa sehemu. Tena ni maisha
yasiyofaa kutamkika mbele za watu. Lakini tutahakikisha, maisha hayo hayo
aliyoishi Tunda, yanasikika, tena vizuri, mpaka watu wakombolewe. Tutafundisha
vijana kwa wazee, wakina baba na mama, tutamfikia kila mtu kwa maisha aliyoishi
Tunda mpaka watu wapate msaada. Nje na ndani ya nchi. Wazi wazi bila kificho
mpaka shetani ataogopa kushika ndoa za watu, maisha ya vijana, watoto wa watu,
kila baya lililotendeka kwa Tunda, tena sirini, tutatumia mwangani kufikia
jamii nzima, mwenye sikio atasikia na kubadilika.” Tunda hakuwa akiamini. “Inamaana na yeye anajiweka!” Bado
Tunda hakuwa ameelewa.
Ilimgusa
sana baba yake Tunda. Hata yeye hakuwahi kuona mtu aliyempokea Tunda kwa kiasi
hicho. “Asante sana kijana wangu. Asante baba. Na mimi Mungu akinipa uzima, na
akanitoa humu ndani, nitaungana na nyinyi.” Net akacheka. “Si umeona Tunda?
Tunazidi kuwa wengi? Sasa wewe Mzee tunaomba uanzie humo ndani. Kwa kuwa mimi
na Tunda hatuwezi kufikia wafungwa wenzako, wewe ndio uwe nao.”
“Naanzaje
wakati hata kuomba siwezi!?” “Tutakuwa na wewe kwa maombi. Na wewe kazana
kusoma bibilia ili uwe unaongea habari unazozifahamu. Tutakuombea ili ujazwe na
nguvu za Mungu, halafu mruhusu Mungu akutumie kwa jinsi apendavyo na
alivyokusudia. Kama alikuleta huku, lazima ujue lipo kusudi, na yeye
atakusaidia kufikia lengo.” Yule mzee alifurahi sana. Net alimuongoza sala ya
toba, akamuombea na kumuachia bibilia yake.
Baada yakutoka gerezani kumuona baba yake Tunda, Tunda & Net.
Tunda hakuwa akiamini.
Alishindwa hata kuongea kwa muda. Net aliongea mambo kadhaa, yaliyomgusa na
kumuogopesha Tunda. Hakuwa akiamini na aliogopa asije akafurahia kama
alivyofurahia kwa Waziri Mbawala, ikawa tofauti. Ikaja kuwa ni Net aliongea
yale yote sababu yakufikia roho ya baba yake. “Net anapenda watu watubu na
wamrudie Mungu. Ingekuwa kunipenda mimi, angeniambia mwenyewe.”
Tunda akaona ajitulize.
Net akaendelea
kuendesha na yeye kimya, wakirudi kanisani kufuata gari ya Tunda. Alikaa kimya,
baadaye ndipo akaweza kushukuru. “Nashukuru sana kwa kumsadia baba yangu.
Umemuona jinsi alivyobadilika? Hata uso wake umechangamka. Asante sana. Mimi
nimekuwa nikimuhubiria kwa muda mrefu sana bila Mafanikio.” “Ndio maana bibilia
inasema katika kitabu cha {muhubiri 4:9 Two people are better off than one, for they can help
each other succeed.} Au kwa Tafsiri ya Kiswahili ni {Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja, maana wapata ijara njema
katika kazi au unaweza sema wanasaidiana kufanikiwa katika kazi}. Si umeona jinsi mimi na wewe
tunavyoweza kufanya jambo likafanikiwa?”
“Mbona
mimi pale sikusema kitu?” “Si kweli. Ulishapanda mbegu kwenye moyo wake, ukawa ukimwagilizia
mimi nilienda kumalizia tu kuvuna.” Tunda akatabasamu kama anayefikiria. Wakawa
wameshafika kanisani.
“Karibu
nyumbani kwangu.” “Nilivyokuwa nasubiri kwa hamu huo ukaribisho!” “Bwana Net!
Kwangu usisubiri kukaribishwa.” “Lazima nisubiri, na hivi kuna kina Julius tena!”
Tunda akacheka na kushuka kwenye gari. “Unifuate nyuma, ndio itakuwa rahisi
kufika nyumbani.” Tunda akafunga mlango na kuingia kwenye gari yake, kisha
akaondoa gari yake, Net akawa akimfuata nyuma.
Net apasua jipu kwa Tunda.
Bado
Tunda alikuwa akiishi pale pale maeneo ya Kimara, karibu sana na Ubungo.
Alimkaribisha Net ndani, wakakaa kwenye makochi. “Hapa kwangu hakuna soda, nina
maji tu. Ila naweza kwenda kukununulia kama utapenda. Mimi sio mpenzi sana wa
Soda. Labda niwe nimechoka sana na kazi, ndio nitakunywa soda. Lakini sio hapa
kwangu. Najitahidi zisiwepo.” “Hapana. Mimi nipo sawa tu. Bado nimeshiba.”
Tunda akaweka vitu vyake ndani, akarudi kukaa hapo hapo kwenye kochi kubwa
alilokuwa amekaa Net.
“Hongera.
Naona nyumba imekamilika.” “Asante Net. Ndio moja ya vitu vilivyokuwa
vikiniliza mwenzio! Sina ndugu wala ukoo wakusema nakwenda kutembea. Sasa hata
nishindwe kuwa na kwangu! Ilikuwa ikiniuma sana. Nilianza kutafuta pakuishi
hata kabla ya gari. Nilijiambia lazima nipate kwanza kwangu. Angalau nipate
kimbilio.” “Hongera sana Tunda. Hakika umenifurahisha.” “Asante Net. Napambana
kweli!” “Na juhudi zako zinakulipa. Nimepitia kwenye website yako, upo vizuri
sana.” Hilo lilimfurahisha sana Tunda, kujua Net alimfuatilia zaidi.
“Nikuulize
kitu Net? Nahofia nisiwe nimekuelewa vibaya.” “Karibu.” Net akajiweka sawa na
kumgeukia. “Ulisema ‘utakuwa’ na
mimi kunisaidia kutumia maisha yangu kufikia jamii?” Net akacheka pale Tunda
alipoweka msisitizo kwenye ‘utakuwa’.
“Unajua
umenipa hamasa sana? Ni kama umenitoa kwenye kona na kunivuta mwangani! Sasa
hivi sioni haya tena. Lakini sijui ndio ninafanyaje! Umesema utanisaidia?” “Sio
kukusaidia Tunda. Tutakuwa wote.” Tunda akawa bado kama hajampata vizuri. Net
akaendelea.
“Nahisi
ndio kazi Mungu anataka niifanye, labda mpaka kufa kwangu. Nimejaribu kukwepa,
nikimpa Mungu sababu za msingi ili niweze kukwepa, lakini Mungu ananirudisha
tu. Hata nifanye nini, bado najikuta nimerudi hapa hapa.” Hapo ndio akawa
amempoteza kabisa Tunda. Akapandisha miguu yake kwenye kochi akaikunja vizuri
nakumgeukia Net.
“Sikuelewi
Net.” “Wewe kwa nini hushangai kila unavyozidi kunikwepa, ndivyo tunavyozidi
kukutana?” “Net Jamani! Mimi mbona sikukwepi?” Net akacheka.
“Siku ya
kwanza nafika nyumbani kwa shangazi yako, unakumbuka ulinifungulia mlango?”
Tunda akatingisha kichwa kukubali. “Huwezi amini, naweza kukwambia mpaka aina
ya gauni ulilokuwa umevaa siku ile, jinsi ile picha ilivyo niganda mawazoni.
Hayo macho yako ya kusinzia, siku ile ndio yalikuwa yamezubaa yakinitizama.”
Tunda alicheka na kufunika uso wake.
“Nikaanza
kujifariji ili niepukane na mawazo yako. Nikasema kule kupigwa na butwaa na
kunishangaa ni kitu ambacho nishazoea kwa watu wengi hasa wadada. Huwa
wananiangalia kwa namna yao, ambayo huwa hainisumbui hata kidogo, lakini wewe
ikawa tofauti.” “Mimi nilikuwa nakushangaa ulivyo mzuri zaidi ya nilivyosikia
sifa zako! Mzungu unayeongea kiswahili chenye heshima.” Net akacheka.
“Sasa
nikaanza kupuuza. Lakini bado nikawa nasumbuka. Ndio maana nikawa nahangaika
kuja pale nikuone ili nijue ulichonacho wewe cha tofauti na kinadada wengine ni
kipi! Nikawa nakuja mchana na usiku, ili nikuone, lakini sikufanikiwa. Nikawa
namuomba Mungu angalau uje basi hata kufungua mlango tena, lakini wapi.”
“Baadaye
nikajiambia niachane na wewe, usinisumbue. Tena hapo ndipo nilipokuwa nikipata
na habari zako mbaya kabisa. Nikawa nikijiambia nina sababu zote za kuwa mbali
na wewe. Lakini nikawa najikuta nataka kukuona tu. Mwishowe nikajiambia siwezi
kujitesa kwa namna hii ni afadhali nitafute hata sababu nikae na wewe, ili hata
nitafute sababu moja utakayonikera, nikuchukie, niondoke zangu nirudi shuleni
kwa amani niwe nimekutoa mawazoni.” Tunda alikuwa haamini.
“Unakumbuka
niliwakaribisha kwenye maombi nyumbani? Hukufanikiwa kuja, na nia ya
kuwakaribisha nyinyi wote mpaka Nyangeta ilikuwa nikupata muda na wewe,
nyumbani kwetu. Maana pale kwa shangazi yako ilishindikana kabisa kwa kuwa kila
nilipokuwa nikijaribu kukusogelea ndivyo Sera na mdogo wake walivyozidi kunifuata,
na kuishia kukutukana mbele yangu kitu kilichokuwa kikiniumiza sana.”
“Uliposhindwa
kuja nyumbani siku ile, na mimi nikaona muda wangu wakurudi chuoni umefika,
lazima niondoke, na mimi ni mtu ambaye nikianza jambo lazima nimalize, ndipo
nikajitosa kumuomba shangazi yako nirudi kesho yake nije kuongea na wewe kabla
sijaondoka. Kumbe ndio naharibu zaidi.”
“Nilirudi
Canada chuoni, lakini sikuwa na furaha, nikafikiria kitu chakufanya, nikaamua
kutafuta msichana wa kanisani ili tuwe na mahusiano kuepuka msongamano wa
mawazo. Nilipata binti mzuri tu wa kanisa ambalo nilikuwa nikiabudu na bibi na
babu. Wazazi wake walikuwa wakifahamiana na kina babu. Kwa kipindi hicho wakati
mimi nipo chuoni na yeye pia alikuwepo chuoni, lakini ndio alikuwa akianza,
mambo yalienda vizuri sana.”
“Hapakuwa
na shaka kuwa siye mwanamke Mungu aliyenipa. Tulielewana kwa mambo mengi tu,
mengine yalikuwa madogo madogo yakurekebishana kama wanadamu au tuseme
yakuchukuliana.”
“Siku
moja nikiwa na yule dada nikajikuta nikijiambia afadhali nimeweza kuachana na
mawazo ya Tunda. Hapo ndipo ikawa ni kama nimerudisha kumbukumbu zote. Na ndio
ilikuwa nakaribia kumaliza chuo, na kwa muda wote huo hata sikuwa
nimekufikiria, tulikuwa na amani na furaha na Chloe. Nilijuta sana kuleta zile
kumbukumbu zilizokuwa zikinitesa bila sababu. Sikuwa nakufahamu, halafu
nilikuwa na sifa mbaya tu za kwako. Nikawa nikimwambia Mungu na kumkumbusha
mabaya yako niliyokuwa nimesikia.” Tunda akainama nakujifuta machozi.
“Shule
yangu ilipoisha, mama akaniomba nirudi nimsaidie kazi zake kwa muda. Kama
nitavutiwa kuishi naye sawa, nikitaka kurudi kuishi Canada pia ni sawa.
Nikakumbuka wosia aliokuwa ameniachia baba, juu ya mkewe. Baba alimpenda sana
mama. Wakati wote alikuwa akiniambia hata kama akiondoka kesho, I should watch
over Maya na mama, yaani nimtunze mkewe na Maya. Ukumbuke aliniacha bado
nikiwa mdogo tu, lakini sikuwahi kusahau hilo. Alinilea kuwa mwanaume wa
familia tokea mtoto na babu hivyo hivyo. Japokuwa mambo yangu yalikuwa yakienda
vizuri kule, ilinibidi nirudi Tanzania kumsaidia kazi mama.”
“Nilimuomba
Chloe aihirishe angalau mwaka mmoja ili tuje naye huku, nikishaweka sawa mambo
ya mama, tungerudi. Lakini Chloe alikataa. Nikamwambia hata kama itatulazimu
kufunga ndoa kwanza, naweza kumuoa kisha tukaja naye Tanzania, na babu
alimwambia endapo ataacha chuo kwa ajili yangu, akapoteza udhamini, babu
alimuahidi angemsomesha kwa gharama zozote zile mpaka amalize. Lakini alisema,
anaweza kunisubiri kwa huo muda wa mwaka mmoja, lakini hakuwahi kufikiria
kuishi maisha mengine nje ya nchini kwao na amejiwekea malengo ya kumaliza
shule ndani ya huo muda, hawezi kusogeza. Nikamkubalia, nikaja huku.”
“Baada
ya mwaka, nikarudi na kumwambia inabidi niongeze muda, maana mama alianza
kupata tenda za ujenzi wa barabara zilizokuwa zikimuingiza pesa nyingi sana
lakini zilihitaji mtu kama mimi kuwepo na kusimamia. Nikamuomba tuondoke naye,
bado akakataa. Akasema atanisubiri tu. Nikaamua kumvalisha kabisa pete ya
uchumba ili asije kubadili mawazo. Nikarudi huku nikawa nikifanya kazi kwa
bidii sana ili nimwache mama kwenye mazingira mazuri, na wafanyakazi wazuri ili
nirudi kwenye maisha yangu. Safari za Canada zikawa nyingi kumfuata Chloe kwa
kuwa alianza kulalamika anachoshwa na mahusiano ya mbali.” Net akatabasamu.
“Mambo
yalianza kunichanganya pale nilipokuona tena. Katikati ya kazi nyingi, na
mahusiano ya lawama, kati yangu na Chloe, kwa nini sipigi simu, kwa nini siendi
kumuona, na mambo kama hayo. Unakumbuka mazingira tuliyokutana tena? Ulikuwa na
mwanaume na wazi alionekana ni mume wa mtu. Niliumia mpaka nilijichukia.
Nilijaribu kujiliwaza kwa kukuunganishia na maneno ya kina Sera, na kusema sina
haja yakuumiza akili zangu, kwa msichana ambaye hukuwa na maadili, mimi ni
mchumba wa mtu. Unajua tena, ili kujipa aghueni moyoni. Lakini nilishindwa
Tunda. Nilikuwa nikiumia sana. Na Mungu naye alikuwa akinikutanisha na wewe
kwenye mazingira yaliyokuwa yakizidi kunitesa sana.”
“Nilikuwa
nikiumia nakujiuliza chakufanya, sikuwa najua pakukupata wala sikujua
chakufanya. Ukweli niliteseka Tunda. Kila nilipokuwa najaribu kukupuuza, ndivyo
nilivyozidi kukufumania. Hasira juu ya kila mwanaume niliyekukuta naye
ilinifanyanya nichukie hata kazi ya mama. Kwa kuwa wanaume wote niliokuwa
nikikukuta nao, ni watu muhimu sana kwenye biashara za mama.”
“Nilishindwa
kabisa kuendelea na ile kazi, nilijawa hasira, nikashindwa kuwa mvumilivu
kwenye kila kitu. Mama alidhani nimechoka kuwepo hapa Tanzania, akanishauri
nirudi tu kwa bibi na babu, lakini nikajikuta siwezi tena kuondoka kukuacha
kwenye mikono ya wanaume wanaotaka kukuchezea.” Net alicheka kidogo kama
anayefikiria.
“Huwezi
kuamini kutoka kwenye kukuchukia sana kwa kunisababishia maumivu ya uchafu
unaofanya, nikageuza hisia nikaanza kuona uthamani ulio nao. Na kuzidi kuchukia
kila mwanaume anayekuchezea. Nilikuwa nikijiambia wanakuchezea kwa kuwa hawajui
thamani yako. Unakumbuka yule Mzee tulikutana wote Mwanza pale baa akiwa
amelewa, akikuelezea jinsi ulivyo mzuri, na kueleza mambo kwa undani kabisa?”
Tunda alishinda hata kumtizama Net, akabaki ameinama.
Net
akaendelea. “Ukweli nilikuwa nikiteseka sana. Mwishowe nikaamua kujisalimisha
kwa Mungu. Nilikuwa sijui chakufanya Tunda. Kila ninapoenda nakutana na wewe
ukiwa na wanaume tofauti tofauti, huku Chloe naye ananitaka nirudi tufunge
ndoa, huku najiambia siwezi kukuacha. Nikamwambia Mungu akinisaidia nikakupata,
ukakubali kubadilika, nitaondoka haraka sana kurudi kwa mchumba wangu.”
“Siku
iliyoniuma zaidi ni pale nilipokukuta na Gabriel. Niliumia sana. Gabriel
alikuwa rafiki yangu tokea Canada. Baba yake alikuja kusoma kule, akawa chuo
kimoja na mama, kwa hiyo Gab alikuja Canada akiwa mtoto sana, nilizaliwa yeye
akiwa na miaka kama mitatu hivi. Tuliishi nao Canada, wao wakarudi huku nchini,
Gabriel akiwa na miaka 18. Na ndio watanzania pekee tuliokuwa nao karibu kule.
Hatukuacha kuwasiliana na Gab mpaka sasa. Na hata anapokuwa akija Canada, yeye
na mkewe au wazazi wake, wanafikia nyumbani kwetu. Kwa hiyo ni kama ndugu.”
“Kuja
kujua ulikuwa na mahusiano naye, nikaamua kuondoka kabisa nchini. Lakini Gab
aliniomba sana radhi, nikamwambia akuache kabisa na asirudie kukutafuta tena.
Maana alikuwa yupo tayari kumuacha mkewe kwa ajili yako. Nilimwambia endapo
atamuacha mkewe, kwa ajili yako ndio itakuwa hata mwisho wangu na yeye pamoja
na familia yake yote. Yaani mpaka wazazi. Ndio Gab akakubali kukuacha kabisa.
Na kuniahidi hatakutafuta tena.”
“Lakini
aliniudhi sana siku ile ulipomfuata hotelini unamlilia shida halafu anakwambia
atakupiga! Iliniuma toka moyoni. Unakumbuka nilikukuta umejificha kwenye kona ukilia?”
Tunda alitingisha kichwa kukubali akiwa anafuta machozi.
“Pale
nilikuwa nimeshazunguka sana. Na gari na kwa miguu huku nikikimbia kukutafuta.
Nilijua ndio wakati pekee Mungu alionipa kukupata. Kwa upande mwingine
nilifurahi kuona umefika mwisho, watu wote wamekukimbia. Nikajiambia nakaribia
kumaliza kazi yangu. Nikupatanishe na Mungu, kisha niondoke niende kwa mchumba
wangu.”
“Kule kuishi na wewe Arusha ikawa msaada kwangu
mimi mwenyewe. Hukuwa umefikia hata maamuzi ya kubadili maisha, lakini nilikuwa
nikifurahia sana tukiwa pamoja. Nikaona jinsi ile ofisi inavyokuwa, nikajiambia
wewe ni mtu utakayenifaa kwenye mambo mengi. Kwamba ukikubali kumpa Yesu
maisha, nitakuwa nimeua ndege wawili kwa jiwe moja. Nitakuwa nimemalizana na
wewe kwa amani, na ofisi nitaiacha kwenye mikono salama. Sasa unakumbuka siku
tumeenda kwa mama akakwambia nitasafiri?” Tunda akatingisha kichwa kukubali.
“Alikuwa akijua muda wangu wakuondoka moja kwa moja
kwenda kwa mchumba wangu umeshakaribia. Maana nilishakuwa nimekupa muda, nikasema
ninakuachia muda fulani, uje ufikie maamuzi ya kubadilika bila mimi
kukulazimisha. Nikajiambia muda huo ukifika hujafikia maamuzi, nitaongea na
wewe, ukubali au ukatae, nikajiambia nitaondoka. Ndio nikawa nimemwambia mama
kuwa ikifika mwezi wa kumi na moja nitaondoka moja kwa moja. Kumbe ule muda
niliokuwa nimekupa wewe kukuangalia, ndio kipindi hicho na mimi nilianza
kukuzoea. Huwezi amini jinsi ilivyokuwa ngumu kukuacha usiku. Nilikuwa nikitamani
niwe na wewe wakati wote.” Tunda akamtizama huku amekunja uso, haamini.
“Siku zikazidi kwenda, wewe ukaokoka, lakini nikawa
nashindwa kabisa kuondoka. Chloe naye akawa amenipa muda, kuwa ikifika mwezi wa
kumi na moja sijarudi kule, hataweza kuendelea kunisubiri tena. Nilikuwa tayari
kwa hilo. Kila mama alipokuwa akiniuliza naondoka lini, sikuwa na jibu tena.”
“Ndipo babu akaugua sana, ikabidi niende tu lakini
hapo nilishakuwa nimeahirisha sana. Kila Nana alipokuwa akinipigia simu
akiniambia hali ya Papa, nilikuwa nikimwambia nitakwenda, lakini nashindwa
kukuacha. Huo mchezo ukaendelea, ndipo nikaambiwa majibu ya hospitalini
yameonyesha Papa hawezi kupona. Nana akaniambia Papa anataka kuzungumza na
mimi. Lazima niende haraka.”
“Ndio nikaondoka ule mwezi wa 11 mwanzoni. Kwa hiyo
ikawa nimefika kabla ya kipindi alichokuwa amenipa Chloe kuisha. Tukaanzisha
mahusiano kwa uhakika, huku nikimuahidi kutokuondoka tena Canada. Hapo
nikajihesabia nimemaliza kazi yangu. Umeokoka, na ofisi ipo kwenye mikono
salama.”
“Ila sasa mahusiano yakawa mazito sana kwangu,
kwani Chloe hakuwa Tunda. Sikuwa nikiona maisha yangu na yule binti hata
kidogo. Babu alinishauri labda nimchukue nimpeleke sehemu mbali mbali ili
kupata naye muda, labda zile hisia za mwanzoni zingerudi. Aliniambia ni kwa
kuwa tuliishi mbali mbali kwa muda mrefu sana. Nikamuacha babu akiwa bado
anaumwa nikaanza kuzunguka na Chloe.”
“Hata
Papa alijua angekufa, kwa hiyo alitaka kuniona nimeoa kabla hajafariki.
Madaktari walitupa muda uliobaki wa papa au babu uliobaki kuishi. Nikakusudia
babu awepo kwenye harusi yangu, angalau anione tu nikioa kwa kuwa ni kitu
alichokuwa akikitamani kuondoka akiwa ameniacha nimeanzisha familia yangu.
Nilizunguka na yule dada, lakini hakuwahi kuwa Tunda. Alikuwa na sifa zote za
kuwa mke wa mtu, lakini sio mke wa Net.”
“Nakumbuka tulitoka safari tulitua uwanja wa ndege
na Chloe nikaenda moja kwa moja hospitalini kwa babu. Nilimkuta na bibi yuko
pale, nikajikuta machozi yakinitoka, nikimuhurumia babu yangu, kuwa yale
aliyotamani nimeshindwa kumpa.”
“Nakumbuka babu alinitazama kwa huruma, nikajikuta
namwambia, ‘She is not Tunda.’ Alitabasamu
na kuniambia kwa kifupi tu, ‘then go and
tell her, NOW’. Nikachukua ushauri wa babu pale pale, sikutaka hata
kusubiri. Nilitoka pale hospitalini nikamfuata Chloe nyumbani kwao. Nikamwambia
sitaweza kumuoa tena, nampenda mtu mwingine. Ilikuwa ngumu sana, lakini niliona
ni heri yale maumivu ya wakati ule kuliko aje aumie akiwa mke wangu.” Mwili
mzima wa Tunda ulikuwa ukitetemeka.
“Basi, nilirudi hospitalini nikamwambia babu, babu
alitabasamu na kuniambia hata baba yangu angekuwepo angenisifu kwa kufanya
maamuzi magumu na muhimu kama yale. Kwa hukumu yakuona nimemshindwa kumpa babu
yangu kile alichokitamani, kwa kutokuoa akiwepo, nilimuuguza bila kuondoka
pembeni yake mpaka alipofariki. Zilikuwa zimebaki siku chache afariki, kwa hiyo
mimi ndiye niliyekuwa naye pale hospitalini muda wote.” Tunda alikuwa ameinama
huku ameficha uso wake akilia. Net akacheka tena.
“Ungenihurumia pale mama alipokuja kwa mazishi,
halafu ananiambia uliondoka Arusha, hajui ulipo. Nilitamani wawe wamenizika
mimi sio babu yangu. Nilikasirika sana. Nikahisi Mungu anataka kunichanganya
akili tu. Nilikaa Canada sijui nirudi tena huku au niendelee na maisha yangu tu
moja kwa moja hukohuko. Mama alipopata matatizo kwenye ile ofisi ya Arusha
ilinibidi nirudi kuja kumsaidia.” Tunda akashtuka.
“Alipata matatizo gani tena!?” Tunda akajifuta machozi na kuuliza. “Safia
alimtapeli. Kwa kifupi aliiba wateja wote wa mama, kwa kuwaambia hatuna uwezo
wa kuwasafirishia tena mizigo yao. Kwa sababu tofauti tofauti. Mara awaambie
malori yameharibika, au yote yamesafirisha mzigo sehemu nyingine, kumbe akawa
ameingia ubia na mtu mwingine. Anamlipa kwa asilimia 40, kwa kila mteja
anayempelekea. Kwa hiyo tukawa tunatumia pesa nyingi kujitangaza, wakipiga
kuomba huduma, Safia anawapeleka kwenye kampuni ingine.”
“Safia alipoona amenogewa, akaja
kufungua kampuni kama ileile. Akawa anatumia magari yaleyale ya mama, lakini
aliajiri madereva wake. Wale niliokuwa nimeajiri mimi aliwatafutia sababu, mama
mwenyewe akawafukuza. Tena aliwafukuza vibaya tu. Basi, Safia akajinufaisha kwa
gharama ya mama. Mama kuja kushtuka, akakuta alishafilisiwa kabisa na anadaiwa
sana. Alimtia hasara kubwa tu.”
“Tuliuza ile nyumba ya Arusha na yale malori yakiwa
kwenye hali mbaya sana, tukalipa madeni yote tukabakia na biashara za huku Dar
tu.” “Pole Net.” “Mama amejifunza sana. Aliogopa kuniambia ukweli kama
alikufukuza, alijua ningemlaumu sana. Lakini juzi tulipokutana pale hotelini,
ulipokuja kwenye kikao, ukanisimulia
kila kitu, nikatamani kujua kwa nini alikubadilikia.” “Ulijua ni kwa nini?”
Tunda akauliza kwa upole, lakini Net alionekana kusita kidogo.
“Nimbie tu Net. Nataka kujua nini nilifanya kiasi
chakubadilisha moyo wa mama Cote. Alinipokea vizuri sana nilipofika Dar, na
alinipenda hata kabla hajaniona akawa haishi kunisifia na kunishukuru kwa kazi
nzuri niliyokuwa nikimfanyia. Lakini akaja kubadilika ghafla!” Net akavuta
pumzi kwa nguvu huku amefunga macho kama anayejishauri.
“Net?” Tunda akaita tena taratibu akijua kuna kitu
Net anataka kumficha. “Unawakumbuka wale wazee wa pale kanisani, ambao
uliwahudumia?” Tunda alianza kuogopa. Alihisi kitu. “Mmoja wao alikuwa kwenye
mahusiano na mama, walitaka kuja kuniambia, kisha wafunge ndoa.” “Mungu wangu
Net!” Tunda aliweka mikono kichwani nakuanza kulia.
“Kwa hiyo aliumia sana, ndio maana alikuchukia.” “Naomba uniombee msamaha kwa mama, Net. Uwii jamani!
Balaa gani hili!?” “Tunda! Nimekwambia lazima ukubali kubadilisha
historia ya maisha yako.” “Siwezi tena Net.”
“Unaweza. Mama ni mmoja ya watu wengi walioumizwa na shetani kupitia wewe.
Hujapata fulsa ya kusikia wengine wanasemaje. Huwezi jua ulivunja ndoa za
wangapi. Inawezekana ni wengi sana, ndio maana unajukumu la kusimama sasa na
kusaidia ndoa nyingine.” Net aliendelea taratibu. Hakuonekana na hasira hata
kidogo.
“Ukikubali kushindwa, ujue wapo wengine wanaotumiwa
na shetani kama vile ilivyokuwa kwako. Na ujue ndoa au mahusiano mengi yapo
hatarini. Wewe sio wa kwanza Tunda, na wala hutakuwa wa mwisho. Wapo
waliokubali na kutubu, na wapo wanaokataa na kuendeleza huo uchafu mpaka sasa.
Wewe umechagua jambo jema, lazima usaidie wengine. Hata hivyo binafsi
nakushukuru, maana bila wewe mama yangu angeolewa na mwanaume anayejua ni mcha
Mungu, kumbe ni tapeli tu.” Tunda aliendelea kulia.
“Nakupenda sana Tunda.” “Naomba
unisamehe Net. Nisamehe. Nimekuumiza sana. Naomba unisamehe.” Tunda
akapiga magoti. “Yamepita hayo Tunda. Nitafurahi kama utaishi na mimi bila
hukumu. Mungu amekusamehe, na ni kweli anakupenda. Aliniweka kwenye maisha yako
makusudi kunifundisha upendo wake kwa watu tunao wahukumu. Tokea unaishi
dhambini, wanadamu wakiwa wanakuchukia na kukuhukumu, Mungu alikuwa
akinionyesha mimi upendo wake kwako wewe Tunda.”
“Alinitoa kwenye nafasi ya kukuchukia na kukupenda
kupita ninavyoweza kukwambia. Aliuweka uthamani wako bayana kwangu. Na
amekuonyesha hata wewe kwa vile alivyo kufanikisha. Amekusamehe, amekupokea na
elimu uliyo nayo, na ameonyesha wasomi kuwa anaweza kubariki yeyote ampendaye.
Unamaisha mazuri kuliko wasomi wengi hapa nchini! Zaidi amekupa furaha na
amani.” “Amenipa na wewe.” Net akacheka. “Ndiyo,
na mimi ambaye nitakuwa na wewe kwenye maisha yangu yote.” Tunda hakuwa
akiamini.
Alifunga
macho yake tena na kuendelea kulia. Alianza kufikiria maisha yake kama mke wa
Net, aliyekuwa anamezewa mate na warembo wengi, wasomi wa kila namna.
Waliojitunza na kulelewa kwenye familia nzuri, lakini alishangaa vile Mungu
alivyomtunza Net, kwa ajili yake yeye aliyekuwa akihangaika na wanaume wa watu!
Tunda alishindwa kunyamaza. Net akamnyanyua pale chini, akakaa naye pale kwenye
kochi na kubaki amemkumbatia.
“Nakupenda sana Tunda. Sana.” “Asante Net. Nashindwa niseme nini!” Net akacheka.
“Kweli. Mpaka naogopa.” “Unaogopa nini
sasa?” Tunda akanyanyua uso wake, akamwangalia. “Nagopa
isije kuwa nipo usingizini halafu nikaamka nikakuta kila kitu ni ndoto tu.”
“Nini unachohofia zaidi?” “Kukupoteza tena.” “Hata
nikiamua kukutoroka, ujue Mungu wako atanirudisha tu.” Wote wakacheka.
Net akambusu Tunda kwenye kipanda uso. Hiyo ni mara
ya pili Tunda kupata busu la Net. Kwanza ilikuwa kwenye mkono na hapo ni mara
ya pili, na mara zote zilimsisimua. Hata kule kukumbatiwa ilikuwa ni mara yake
ya kwanza. Tunda alijivuta karibu sana na Net na kumkumbatia huku akilia tena.
Kwa mara ya kwanza alihisi ulinzi mkubwa sana. Alimkumbatia Net kwa kumng’ania
huku akilia na kushukuru Mungu kwa kumthamini.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tunda aliyepitia kwa wanaume wengi, hakuwahi
kukumbatiwa maishani mwake kwa namna ile ya upendo. Hata tu mtu kutoa muda wake
na kumtaka atulie mikononi mwake. Si mama yake mzazi hata wanaume aliokuwa
akiwahudumia ilikuwa ni yeye kuwahudumia kwa juhudi zote waridhike, basi, labda
kidogo waziri Mbawala tena yeye mwenyewe Tunda alikuwa akiomba kukumbatiwa.
Hakuwahi kupendwa na kuthaminiwa vile.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akiwa amejificha hapo kwa Net, wazo la kumtia hofu
likamji. “Lakini Net! Umeshafikiria tutakuwa na mahusiano ya namna gani? Kila
ninapopita yupo mtu anayenifahamu. Nimemuumiza mpaka mama yako mzazi, Gab naye
ndio hivyo, itakuaje? Si itakuwa kama nakudhalilisha tu kila wakati?” “Wao
walikuwa wezi tu, mimi ndio nimekabidhiwa na Mungu. Wanatakiwa waniogope mimi
sio mimi kuwaogopa. Halafu Tunda, kila mtu anamapito yake, tumetofautiana tu matukio.
Unakumbuka ule mfano wa Yesu walipomletea yule mwanamke kahaba?” Tunda
akatingisha kichwa kukubali.
“Walikuwa na sababu zote za kumpiga mawe yule
mwanamke. Lakini unakumbuka jibu la Yesu?” “Nakumbuka.” “Basi huna haja yakuwa
na wasiwasi, na kama nilivyokwambia, hatutasubiri watu watumie maisha uliyoishi
zamani kukunyanyasa. Sisi wenyewe tutayatumia kusaidia watu. Itasaidia kama
utakuwa jasiri, hata kama watakushtukiza kwa nia ya kukudhalilisha, unatakiwa
ujue jinsi ya kutulia wala usikubali hata mara moja mtu akakuumiza.”
“Itakuwaje kuhusu sisi wenyewe Net? Unaweza
ukaniamini kama ambavyo ungemuamini mwanamke ambaye hakupita mapito kama yangu?
Sitaki kuja kuumia tena. Sitaki uje unionyeshe upande wa
pili wa maisha ambao sijawahi ishi, halafu ukanikimbia.” Tunda alianza
kutokwa na machozi tena.
“Sijawahi kupendwa na kuthaminiwa
tokea mtoto. Wala sijawahi kuishi kwenye familia na mimi nikahusishwa na
kuthaminiwa mawazo yangu. Naogopa usije kunionjesha hayo maisha halafu baadaye
ukaja kuniacha, Net au tukashindwa kuishi kwa amani sababu yakutokuniamini kila
ninapokuwa na mtu mwingine au nimechelewa kurudi nyumbani.”
“Naomba Mungu anisaidie Tunda. Sitakuumiza hata
kidogo. Nimeamua kuwa na wewe nikiwa nakufahamu vizuri sana. Sijakurupuka. Ni
kitu ambacho nishajiuliza maswali yote ambayo wewe unaniuliza sasa hivi na
Mungu amenisaidia kupata majibu yake. Hakuna kipya kitakachobadilika.”
“Nakupenda, na nimekusudia uwe mke wangu. Nakuahidi
kukupenda Tunda. Nitakupenda kwa dhati na kukuheshimu, kama Tunda huyu
niliyenaye sasa hivi hapa mkononi. Tunda aliyeoshwa na kutakaswa na damu ya
Yesu. Sitaishi na Tunda yule wazamani.” “Asante
Net. Nakushukuru kunipokea.” Tunda alijirudisha kujiegemeza kwa Net na
kukunja miguu juu ya kochi. Wakatulia kila mtu akiwaza lake kama wasio amini.
Tunda
alijituliza pale akiogopa hata kusogea. Kichwa pembeni ya shingo ya Net
aliyekuwa amepitisha mikono yote miwili juu yake, akimpapasa taratibu kwa mkono
mmoja mgongoni. Wakatulia. Kama ambaye haamini, akanyanyua uso kumtizama Net
kuhakikisha kama ni yeye. Macho yakagongana. “Nimefurahi sana Net. Siamini!” “Hata mimi nimefurahi.” Tunda akajiweka
sawa.
“Sasa ndio tunafanyaje?” “Hatuna sababu yakusubiri
tena. Nataka kukuoa Tunda. Nataka uwe mke wangu. Nitaenda kuongea na mama, na
wewe kamwambie Mchungaji wako. Taratibu za harusi zianze.” Tunda akacheka. “Siamini kama na mimi
nimepata mtu wa kunioa! Nilijikatia tamaa.”
“Naomba salamu za kukumbatiana na Julius ziwe
mwisho.” Tunda alicheka kwa mshangao. “Husahau!?” “Nisahau wakati pale nilikuwa
nammezea mate jamaa? Yeye amekumbatiwa wakati mimi sijawahi kukumbatiwa hata
mara moja!” Tunda alizidi kucheka. “Eti na mimi nitaanza kuvaa pete za ndoa!”
Net akacheka lakini Tunda alipooza ghafla na kujitoa mikononi mwa Net.
“Nini tena?” “Nisipo zaa je? Kama waliharibu kizazi
changu wakati wananitoa ile mimba, nikapoteza uwezo wa kuzaa?” “Sijui Tunda.
Ila nakuomba usiniingizie hofu nyingii. Naomba unipe nafasi nifurahie hii hatua
niliyofikia leo. Hujui nilivyoteseka.” “Samahani Net. Nataka tusiharakishe,
tupate muda wakutafakari kwanza tusije tukakosa raha baadaye na kulaumiana.”
Hofu ilishamwingia Tunda, akamkumbuka Tunda halisia.
“Naomba unielewe Tunda. Haya mahusino yetu kwako
nimageni, lakini si mimi. Mwenzio nimekuwa nayo kwa muda mrefu sana. Nakwambia hayo
maswali yote nimeshajiuliza na Mungu amenipa jibu. Nikwambie swali jingine
ambalo nimeshajiuliza?” “Swali gani tena!?” Tunda akauliza, akisikika kuishiwa
nguvu.
“Itakuwaje kama tukienda kupima, nikakukuta
umeathirika? Umeshafikiria hivyo?” Tunda alibaki kama amemwagiwa maji yabaridi.
Akajivuta pembeni kabisa. “Sasa hata kabla hatujafika hospitalini mimi na wewe
tukapewa majibu yako, mimi nilishachanganyikiwa, nilishakuuguza, tena
nilishajiona jinsi nitakavyo kuuguza peke yangu kwa kuwa watu wamekususa,
nimeshalia na kuomboleza na Mungu wangu, mwishoni nikaamua kumuachia Mungu,
nitembee kwa hatua. Sitaki kuleta matatizo ya siku ya kesho, leo, Tunda. Ndio
maana nakuomba uache angalau nifurahie hii hatua ya leo. Naomba tutembee hatua
kwa hatua, ili tusije pitwa na chochote.” Tunda alijirudisha vizuri pembeni ya
Net, akanyamaza asiamini kama Net ni mtu wa kubaki naye maishani. Sio
muondokaji! Amekusudia kuwa naye.
“Sasa hivi kinachofuata nitaenda kumwambia mama.
Halafu nianze maisha ya kuwa mchumba wa Tunda. Niwe namtoa mchumba wangu sehemu
tofauti tofauti za starehe, nifanye yote ninayotakiwa kufanya kwa mchumba
wangu, kabla sijawa mume. Sitaki kupitwa na hatua hata moja kwenye maisha yako
Tunda. Hata kama tutaoana mwezi ujao, nataka hizo siku zilizobaki kabla
sijakuoa, nikutunze kama mchumba wangu.”
“Nataka nifurahie hatua yangu ya uchumba na wewe,
bila kuazima matatizo ya kesho. Leo nataka nikufurahie, msichana
niliyekusubiri, na kukutamani kwa muda mrefu sana.” Tunda alikuwa akilia
asiamini. Alijutia mapenzi aliyokuwa akiyagawa kwa kujidhalilisha. Hakujua kama
yupo mtu mahali fulani anampenda nakumsubiri kwa kiasi kile.
“Nilikuwa nikimuuliza Mungu kwa nini anachelewa
kukukabidhisha kwangu! Nilimuhakikishia kila kitu. Nilimwapia nitakupenda mpaka
kifo. Nikamwapia sitakusaliti wala kukunyanyasa. Yote hayo niliyafanya kama
mwehu ili tu anipunguzie siku za kunikutanisha na wewe.” Akajiegemeza kwenye
kichwa cha Tunda, aliyekuwa amemkumbatia, na Tunda alikuwa bado amekaa ubavuni
kwa Net, huku amekilaza kichwa chake hapo shingoni.
“Sina cha kusema Net. Sikuwahi hata kuwaza kama
unamawazo na mimi! Nilijua utakuwa ukinichukia kwa kunifumania zaidi ya mara
nne, tena na wanaume tofauti tofauti! Yaani hata sikuwahi kukuwazia hata
sekunde moja. Ila nilikuwa nikikuogopa sana. Kila ulipokuwa ukinifumania
nilikuwa nashindwa kulala kwa hofu.” Tunda akakaa vizuri.
“Nilijaribu kujipa moyo kuwa hunihusu, sikujui wala
hunijui kwa hiyo haijalishi lakini nilishindwa hujiliwaza. Nikaanza kupunguza
wanaume, nikabakia na wachache watakaonisaidia kuniweka mjini, lakini pia bado
niliteseka. Haya, mama Cote aliponifukuza Arusha, sikujua hata kama utajali.
Nikajua utashukuru Mungu kutuliwa mzigo. Sikuwahi hata kukuwazia kama unaweza
kuja kunitafuta tena, Net!”
“Nilipokuona pale juzi, nilifurahi
kukuona kama mtu muhimu ambaye umehusika kwenye maisha yangu. Lakini sikujua
hata kama nina maana yeyote kwako. Sikuwa hata nikijua kama uwepo wangu kama
una maana yeyote ile au unafanya kutimiza tu wajibu kama mkristo tu wakawaida.
Hakika wala sikudhani kama unaweza kuniwazia hivi. Nakushukuru kwa
kutokunikatia tamaa.” Net alikuwa akimsikiliza huku akitabasamu. Alimvuta mkono
mmoja, akambusu na kubaki wakiangaliana.
“Sasa inabidi nirudi nyumbani tu. Nikiendelea kukaa
hapa, naweza kushindwa kuondoka kabisa.” Tunda akatabasamu. “Nitakuona tena
lini?” Tunda akauliza, Net akacheka. “Kila siku nitajitahidi tuwe tunaonana.
Ila kesho itakuwa mchana, kuna tenda naifuatilia. Nikipata hiyo, najua
itamsaidia sana mama. Mambo yake yameenda pabaya sana. Biashara zake haziendi
vizuri.” “Mungu atakusaidia Net. Nitakuombea.” Net akatabasamu. “Afadhali
nimepata na mke muombaji.” “Umesahau wewe ndio ulikuwa ukinifundisha?” “Siwezi
kusahau. Lala. Kesho tutapata muda mzuri wakuongea zaidi.” Net akaaga na
kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Usingizi haukuja kwa Tunda. Alivaa haraka haraka
akapanda kwenye gari yake mpaka, Tabata, nyumbani kwa Mchungaji wake. Mlinzi
alipoona gari ya Tunda akafungua geti. Shida ikawa kufunguliwa mlango kuingia
ndani. “Bwana Mama Penny fungua!” “Hatukusikii, tumelala.” “Sasa mbona
unajibu?” “Unataka nini Tunda kwenye dirisha la chumbani kwangu?” “Kuna kitu
nataka kukwambia. Siwezi kulala mpaka tuongee.” “Kuna msiba?” “Hapana.” Tunda
akajibu.
“Umefukuzwa kwenye nyumba?” “Hapana.” “Basi naomba
utuache mimi na mume wangu, tumelala. Washirika wote tumewafundisha kuomba.
Hakuna haja yakutugongea milango usiku au simu za usiku usiku hatutaki. Kama
mtu anashida, unapiga magoti unaomba, halafu Mchungaji unaonana naye asubuhi.”
Tunda akaanza kucheka.
“Sasa muda wote huo unaongea hapo kitandani, mama
Penny, dada yangu, si ungeshakuwa umenifungulia mlango, tumeonge, na mimi
nimeondoka?” “Sitaki kutoka kitandani bwana! Wengine nyumba zetu zina AC. Usiku
tunawasha baridi. Nishajifunika, sitaki kutoka kitandani. Wewe niambie ukiwa
hapo hapo dirishani.” Tunda akatulia kwa muda.
“We Tunda?” Mama Penny akamwita. “Nimepata
mchumba.” Akaruka kitandani nakuanza kupiga vigelegele. Akawasha taa ya
chumbani kwake huku akipiga vigelegele. “Acha kelele mama Penny bwana! Watoto
wamelala.” Tunda aliongea kwa sauti ya chini kidogo, kama kumtuliza. “Siamini
kama nimepata harusi yakusimamia!” Tunda na Mchungaji wote walicheka kwa sauti.
“Hebu amka baba Penny, tukapange mipango ya
harusi.” “Hata mchumba mwenyewe hujaonyeshwa, unataka kuanza mipango!?” “Hebu
amka bwana na wewe! Yeyote tutakayeletewa huyohuyo tutampokea ilimradi na mimi
nisimamie harusi.” Alimsha watoto wote kwa vigelegele.
“Ingia ndani bibi harusi wangu.” Tunda alifunguliwa
mlango. “Kuna nini mama?” Penny akauliza akiwa na usingizi. “Anti Tunda
anaolewa?” Pendo naye akauliza baada yakusikia vigelegele vikiendelea bila jibu
kutoka kwa mama yao. “Na yule Mzungu?” Penny akauliza tena. Tunda akacheka
sana. “Penny wewe! Upo kama mama yako!”
“Hebu niambie Tunda. Mchumba ni nani?” Mchungaji
alitoka na yeye akakaa kwenye kochi, mkewe alikuwa akiendelea kushangilia hata
mchumba hajauliza. “Acha kelele bwana na wewe mama Penny. Mchumba mwenyewe hata
hujamjua!” “Atakuwa ni yule mzungu tu. Wewe hukuwaona hapa walivyokuwa
wakiangaliana? Yule mzungu alimpakulia chakula Tunda. Wewe hukuona? Atakuwa ni
yeye tu. Eti Tunda mdogo wangu?” “Ni yeye.” Yule mama akaendelea kushangilia.
“Afadhali tutapakata vitoto vya kizungu.” Tunda
akacheka sana. “Sasa wewe Penny mwanangu utakuwa msimamizi wa nyuma. Kazi yako
kuangalia shela ikae vizuri.” “Sasa nikikaa nyuma, kwenye picha si sitatokea!?”
“Utatokea kwenye harusi yako.” Mama yake akamjibu na kufanya wote wacheke.
“Mama Penny naomba ukae chini bwana tuongee.”
“Tunaongea nini? Hapa ni mipango ya harusi tu.” “Si ndio hivyo sasa! Mimi
nilijua wewe ndiye utakuwa mpambaji wa ukumbi na Mchungaji ndiye atatufungisha
harusi.” “Aka! He! Wewe Tunda ukoje? Mimi na mume wangu ndio wasimamizi.
Akitaka mwenyewe atafungisha hiyo ndoa, halafu atachukua nafasi yake ya
kumsimamia bwana harusi tukitoka kanisani. Lakini mimi nasimamia kila mahali.”
Tunda alitingisha kichwa huku akicheka.
“Sasa nani atapamba ukumbi!?” “Mimi na wewe
haituhusu, kwani sisi wanakamati bwana? Hebu tuongee mambo ya msingi.” “Haya
Penny na mdogo wako, mkalale.” Baba yao akaingilia. “Lakini mimi sitaki
kusimamia nyuma, dady!” Penny akalalamika. “Mama yako ameshakwambia, utulie
mpaka utakapokuwa mkubwa, ukileta mchumba wako, siku yako ya harusi utasimama
mbele. Sasa hivi unakwenda kulala, kesho shule. Haya simama haraka kabla
sijakubadilikia.” Tunda akabaki akicheka, Penny na mdogo wake wakasimama
kuelekea chumbani kwao kulala huku Penny akilalamika “Na mimi nataka kutokea
kwenye picha! Sitaki kusimama nyuma.” Akapotelea chumbani kwao huku
akilalamika.
“Kweli hawa watoto wamepata wazazi!” Tunda
aliendelea kucheka. Waliongea kwa muda mrefu sana, Tunda akitoa historia yake
na Net, tena na tena huku machozi yakimtoka. “Ulikuwa unamzungusha Julius wa
watu, kumbe unaye mwanaume wako!” “Mungu wangu nishahidi mama Penny. Sikuwahi
kumfikiria Net kuja kuwa naye kwenye mahusiano hata kidogo! Hata dunia yote tungebaki mimi na yeye tu,
pia nisingefikiria kama yule kaka angekuja hata kutamani niwe mpenzi wake!
Sikuwahi hata kumuhisi. Net anamaadili na msimamo wakupita kiasi. Kwanza
nilikuwa nikimuogopa ile yakutetemeka.” Waliongea mpaka usiku sana, ndipo Tunda
aliporudi kwake.
Kwa
Net!
Huku kwa
Net nako, alirudi mpaka nyumbani kwao. Alimkuta mama yake sebuleni akisoma
kitabu. Alipomuona tu Net akaweka kitabu chini. “Sijawahi kukuona ukiwa na
furaha hivyo! Kuna nini?” “Tunda amenikubali mama.” “Hebu tulia kwanza. Tunda
amekukubali!?” “Yaani ni hivi, Tunda amekubali nije kuwa mume wake.” Yule mama
alishtuka sana, akavua miwani. Net alimuona jinsi mama yake alivyobadilika.
“Tunda,
Tunda!?” “Ndiyo mama. Tunda.” “Sijaelewa. Tunda huyu unayemzungumzia ndiye
Tunda huyu Malaya! Aliyekwisha shika mimba ya baba yake. Aliyevunja uchumba
wangu na kuvunja ndoa ya Mzee Mati baada ya mkewe kujua alikuwa akihudumiwa na
huyo Tunda na kumpeleka na mwenzie Meto! Aliyetembea mpaka na Gabriel, ambaye
ni kama kaka yako!? Achilia mbali msururu wa wanaume za watu ambao alishakuwa
na mahusiano nao kimapenzi!?”
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Itakuaje? Tunda akiwa na furaha yakupitiliza, maisha ya nyuma yanapambana
kumtoa Tonge mdomoni
0 comments: