NILIPOTEA! - SEHEMU YA 9.
S |
adiki
akamtaka Tunda akae chini. “Njoo hapa,
ukae sasa nianze kukueleza kuanzia
mwanzo mpaka mwisho. Ndio utaamini mimi na wewe tumekusudiwa kuwa pamoja.” Tunda akaguna na kucheka kama asiyesadiki. Kwa kuwa kulikuwa na pesa, akakaa. “Haya niambie Sadiki, baba Amini!” Sadiki akacheka. Tunda aliiona furaha ya ajabu kwake. Sadiki aliyekutana naye jana siye huyu wa leo. Leo anaonekana anamtaka Tunda hata kwa magoti!
“Kulikoni!” Tunda
akajiuliza. “Jana nilipotoka tu hapa.” Sadiki akaanza. “Nikapata simu ya mdeni wangu. Si unajua pesa ilivyongumu?” Tunda akabaki kimya akimtizama. Sadiki akacheka. “Basi. Nikikwambia ni mdeni, ni mdeni msumbufu kweli kweli. Nimemdai mpaka kwa mganga.” “Mganga!!” Tunda akashangaa. “Ni pesa nyingi kwelikweli. Si
umeona hilo begi? Nimehangaika kupita
kiasi. Ndio babu Chonde akaniambia
anaona ipo nyota yangu itanijia. Na ikinijia,
mambo yatafunguka. Madeni
yangu yatalipwa, na biashara
zangu zitafunguka.” Tunda akabaki akimsikiliza kwa kumshangaa.
“Sasa
nishahangaika na watu wengi tu. Wala
wewe sio msichana wa kwanza kukukubalia.
Maana babu Chonde alisema nyota
yangu na mke wangu imefifia,
tunahitaji nyota mpya..”
“Mimi unanichanganya wewe
Sadiki! Unaongea mambo mengi na mageni kwangu, sikuelewi!”
“Tatizo una haraka Ani.” “Kwa
maneno hayo mengiii, kwa hiyo kwa
kifupi unaamini mimi ndio hiyo Nyota?”
“Kabisa. Jana Nimetoka tu hapa kwako,
mdeni wangu. Ambaye hata
sikumtafuta. Na shida yote hii ya
pesa, kaniletea pesa yangu yote
kwenye ile baa yangu ya Sinza. Kwanza nilikuwa
hata siamini wakati anataka tukutane.
Nilishakaribia kukata tamaa. Na mimi
nilikuwa na haraka yakuwahi nyumbani nipeleke ile zawadi uliyonipa, lakini nikajipa moyo kumsubiri tu.”
“Nimesubiria
pale baa mpaka 7 usiku, ndio akanijia na
hizi pesa. Haya, asubuhi hii
mfanyakazi wangu ambaye
nilikuwa namwamini sana, anachapa
kazi, alichukuliwa kwenye baa ya jirani, lakini ameniomba, tena kwa magoti akitaka arudi kazini. Tena kwa
mshahara uleule niliokuwa nikimlipa
mwanzoni, wakati kule
walimuongezea! Sasa kama wewe sio
hiyo Nyota ni nini?” Tunda akasimama na
kuondoka pale.
“Njoo Ani
wangu.” “Unanichanganya tu mimi!”
“Na kwambia mambo
yetu yamebadilika.” Tunda
akasimama na kugeuka kabla hajaingia bafuni. “Mambo hayo, yamekubadilikia wewe na mkeo.” “Nimekwambia na wewe upo. Si ndio maana nimekuletea wewe kwanza pesa yote? Nusu zako na mimi na..” “Nyingine zako na mkeo?” Tunda akauliza kwa kejeli. Sadiki akacheka. Tunda akaingia bafuni na kufunga mlango.
“Njoo tupange mipango yetu sasa!”
Tunda akaoga na kutoka akiwa amejifunga
taulo. Alimkuta Sadiki amesimama nje ya
mlango wa bafuni akimsubiria akampita.
“Sasa nisikilize
Sadiki.” Sadiki akamsogelea kwa haraka. “Si ungenikaribisha tu bafuni kama jana, tukaoga wote?” “Ulivyokuwa
ukiniharakisha nirudi hapa!”
“Mambo hayaishi Ani?” “Sasa nisikilize
Sadiki. Hutazaa na mimi, hilo
moja.” “Hata katoto
kamoja kakuunganisha undugu,
Ani wangu?” Sadiki
akabembeleza. “Hapana. Na unisikilize
vizuri kwa makini.” “Mashariti bado yanaendelea!?” “Hakuna mapenzi ya mabusu ya mdomoni au bila kondom.” “Hee! Kondom si jana tu sababu tulikuwa hatufahamini? Lakini sasa hivi tunaingia kwenye maagano yakudum..” “Na nani!?” Tunda
akamuuliza kwa kumshangaa kabisa.
Mimi sio mkeo. Wala sitakaa kuwa mke wa pili. Kondom ni kwa ajili ya usalama wangu.” “Mimi nimetulia Ani?” Tunda akakunja uso.
“Umepafahamuje hapa wewe mume wa
mtu!? Halafu hata sijatumia nguvu nyingi kukutongoza, ukanileta hapa moja kwa moja na kulala na mimi!” “Ngoja nikurekebishe Ani. Wewe kukuruhusu kulala na mimi sio kwa ajili yako.” Tunda akapandisha nyusi juu na kukunja mikono kifuani. “Kuniruhusu!?” Tunda akauliza kwa kushangaa.
“Sawa nilivutiwa na wewe, lakini ukumbuke na mimi nilikuwa nipo kwenye mawindo yangu. Nilikuja hapa makusudi ili kutafuta na mimi bahati yangu. Na ndio maana nilianza kwa kushauri Kondom. Kumbuka Kondom ilikuwa wazo langu. Sasa, sasa hivi nishajua wewe ni mtu wangu wa kudumu, nakubali tukapime, tuendelee na maisha yetu.” “Na wakati wewe unajaribu hiyo bahati yako yakutafuta hiyo ‘nyota’ yako na mkeo, kwa kila mwanamke unayekutana naye barabarani, unajuaje kama na mkeo alikuwa hatafuti hiyo ‘nyota’?” Sadiki kimya kwa muda kama anayefikiria.
“Hawezi.” Akamkania mkewe. “Kitakacho mshinda na yeye
ni nini? Kwani mliambiwa kati yenu nyinyi wawili na mkewe, wewe peke yako ndio
mleta hiyo ‘Nyota’ yenu ya ajabu!?”
“Mama Amini hawezi.” Sadiki akasikika mwenye
wivu kabisa. “Acha habari za ajabu!
Kinachomshinda na yeye ni nini?
Mbona wewe umeweza? Wewe unalala
huku na hao wanawake zako na yeye
analala na vijana huko. Tatizo
liko wapi?” Akamuona anakasirika na kumshangaza kabisa
Tnda.
“Kwa hiyo
wewe ndio unajiona unayo haki ya kulala
na watoto wadogo, mkeo hana!? Nimeona
vijana wanao mfanyia kazi pale
Mwenge, na wewe umesema ile ni
sehemu moja tu. Wapo vijana wengine anaoshinda nao kuanzia asubuhi mpaka
mnakutana huo usiku mwingi. Sasa unajua kinachoendelea siku nzima kwenye hiyo
hangaika yake?” “Naomba tuyaache hayo.” Akamuona amebadilika kabisa.
“Sasa sikiliza masharti yangu, ukishindwa, mlango ule pale, ondoka. Huwezi kuja kuniua wewe na mkeo kwa imani zenu ambazo kwanza hata sizielewi! Wewe kama unataka kunufaika na mimi, na mimi ninufaike kwa masharti yangu.” Sadiki akashtuka kidogo. “Nakwambia mapema ili tusianze kusumbuana baadaye. Mama Amini sijui Sadiki ndio mkeo mpaka kifo. Mimi tumekutana jana, na ninajua ipo siku utaniacha tu.” “Kwa kuwa wewe mwenyewe hutaki kutulia na mimi.”
“Tungehalalisha ukawa mke wangu kihalali hata mama Amini akakufahamu!” “Hapana, na wala usifikiri itakuja kutokea. Na kwa kuwa nakuona umeanza kukasirika, ondoka. Akili
zikikutulia urudi usikilize masharti
mengine. Ukishindwa, huna haja
yakurudi. Nitakuelewa kabisa.”
Tunda akasimama hapohapo na kutoa
lile taulo na kuanza kujikausha mbele
yake, akijua wazi anamwangalia.
“Jaribu kupunguza mashariti ili kuwe na amani, Ani!” “Amani itakuwepo ukiyakubali mashariti yangu.
Mimi sikulazimishi. Dogo dogo wako wengi tu, na umetoka kuniambia mimi sio wa
kwanza kupita hapa. Ushapitisha wengi
tu. Endelea, utapata mwingine asiye
na mashariti.” “Nimekuchagua
wewe.” “Ndio utulie, usikilize
sasa.” “Kwa nini tusiendelee na
mashariti baadaye?” Akasimama ili
amguse. “Hapana. Acha bwana Sadiki. Nisikilize kwanza.” Akasogea pembeni. “Haya, nasikiliza.” Akakubali akiwa anavua nguo na kujitupa kitandani.
“Nitajitafutia
kwangu. Nitajinunulia vitu
vyangu. Ukinihitaji tunakutana
mahali.” “Haiwezekani Ani! Ni
jana tu tulipanga tutafute kwetu.”
“Naendelea. Hunimiliki kama mkeo.
Huniiti kama mtoto wako. Unaheshimu ratiba zangu kama mimi ninavyoheshimu za kwako. Sikufuati kwa mkeo na watoto wako, na mimi hivyo hivyo.” Hapo Sadiki akanywea. “Wewe
unako pakukimbilia, nyumbani kwa
mkeo na watoto. Na mimi nataka kwa
kukimbilia. Nyumbani kwangu. Na
nikisema kwangu namaanisha pazuri,
sio kwenye nyumba za vichochoroni na wapangaji wengi.” “Mimi nina wivu Ani. Kitendo chakutojua huko uliko ni wapi na upo na nani, utanitesa
sana. Angalau nipafahamu unapoishi
tu.” “Unaonekana utanisumbua sana Sadiki,
wewe!”
“Nakuahidi sitakusumbua. Nikitaka kuja, nitakuomba.” “Hapo mpaka nijiridhishe na tabia zako. Lakini mwanzoni,
hapana.” Sadiki akabaki kama anafikiria. “Nakuona unahitaji muda
wakufikiria. Nenda. Ukiafikiana
na mimi ndio urudi, ukiona
hutaweza, na huwezi mashariti
yangu, wala huna haja ya kurudi.
Nisipokuona tena, mimi nitaondoka hapa, wala hutakaa ukaniona tena.” Tunda akazidi kumuwekea ngumu. Akawa mkali. Gafla akajikuta yeye ndio ameshika
kwenye mpini. Hakutaka kurudia kosa la kufukuzwa kwenye nyumba kama alivyokwisha
fanyiwa tokea mtoto. Alikusudia
awe na kwake mwenyewe.
“Sawa Ani. Ila naomba na wewe unifikirie na unihurumie. Ujue mimi nitatulia na wewe tu.” “Na mkeo!?” “Sawa. Ila sitahangaika na mwengine. Mashariti mengine zaidi ya kimapenzi, legeza kidogo.” “Naona hujanielewa au umekataa. Acha mimi niondoke.” Tunda akajidai anakusanya vitu vyake.
“Hujaelewa Ani. Namaanisha
hapo baadaye utakaponisoma na kuridhika. Ninachoomba hapa ni unipe nafasi ya kunisoma. Sasa hivi tuendelee
hivyo unavyotaka wewe.” “Nakusoma wewe sawa, na mkeo huko? Wewe utaamua kutulia na mimi, sawa. Je, wewe unajua mkeo amefika umbali gani huko na hao vijana wake? Wewe utatulia na mimi. Na yeye anatulia na kijana wake. Haya, na huyo kijana wake unajua na yeye anatulia na nani huko mbali na mkeo?” Akamuona anazidi kuumia.
“Hii ni kwa
faida yako na yangu. Ila ukiona
ngumu, basi. Huwezi kuja kuniua
mimi kizembe hivi!” “Basi mama.
Tutafuata masharti yako.” Tunda
akaweka vitu vyake chini. “Kwa
hiyo mapenzi wakati wote na
kondom, hakuna mabusu ya mdomoni,
na kwangu ni kwangu.” “Sawa. Ila
sitajali kama utanikaribisha hapo baadaye.” Tunda hakumjibu.
Maisha Mapya ya Tunda.
Tunda akaanza kujitafutia nyumba. Sio chumba tena. Pesa ikawa inaingia nyingi mpaka akawa
haelewi. Mara kwa mara Sadiki alikuja na
pesa na kumuachia. Simu za kubadili maeneo kwa madalali zikawa haziishi.
Kila nyumba anayoonyeshwa, ikawa haiendani na uwezo wake. Maisha yakaendelea palepale hotelini, yeye na Sadiki. Lakini Sadiki akiondoka, Tunda anaendelea na maisha zake. Sadiki alikuwa akifika hapo asubuhi na jioni. Wanapata muda wa pamoja, anaondoka kwenda kwenye shuguli zake, Tunda anaendelea na ratiba zake. Kujinunulia vitu vya thamani na
kutafuta nyumba nzuri.
Mida ambayo
anajua Sadiki anakwenda pale
hotelini, basi na yeye anarudi
hapo. Kula, kulala
na kujitengeneza ikawa kazi
ya Tunda. Mapenzi ya haja kwa Sadiki, naye akawa anamwaga tu pesa.
Tunda hata haulizi
zinapotoka anapokea tu na
kutapanya. Baada ya kama mwezi
akapata nyumba nzuri sana. Ndogo tu ya vyumba viwili. Kila kitu kilikuwa humohumo ndani. Kazi ikawa ya kujaza hiyo nyumba. Wakati wengine wanalia njaa, pesa ngumu, Tunda alikuwa anatafuta matumizi. Akiwa anaishi hotelini, akaanza kujaza nyumba yake huku analipia kodi.
Akaanza jikoni.
Tunda aliyekwisha ishi kwenye
majumba mazuri na ya maana,
hakuwa akinunua takataka au vitu
vyakijinga. Vyombo vyake vya
chakula vyenyewe vilikuwa ni vya
maana. Sahani ya
Tunda ilikuwa ikianguka chini mpaka ivunjike, sio rahisi. Vijiko sio vya bati. Chuma
nzuri yakueleweka. Alianza kujaza jikoni taratibu. Akaanza kupata shida na thamani za kisasa. Alizunguka kila mahali hakuna kochi wala, meza aliyoona inafaa kwa hiyo nyumba yake. Ilipofika swala la kitanda, ndio kabisa. Alizunguka kwenye maduka ya matajiri na masikini, hakupata kilichomvutia
na kuona kinastahili kuwekwa ndani kwake.
Siku hiyo akiwa na Sadiki hapo hotelini
akilalamika huku anaangalia simu yake, akaona picha ya jumba la mfalme wa Arabuni. “Babe!” Akamwita Sadiki. “Hii nyumba inavifaa vyote ninavyotaka mimi.” “Huko ni Arabuni, Ani!” “Kwa hiyo? Kwani hapafikiki? Sio lazima viwe kama hivi, lakini hawa waarabu wanaonekana
wana vitu ninavyovitaka.” “Wewe hijabu hutaki. Hata juzi nilikwambia ujaribu kufunga, umekataa.” “Wewe tafuta tiketi na hiyo hijabu uone kama sitafunga, tukaenda.” Wakacheka hapoo, Sadiki akaona ndio wakati
wakuweka ombi lake na yeye.
“Kwa kuwa mimi nitakusindikiza kwenye safari yako, huoni na wewe unatakiwa kunisindikiza kwenye safari yangu?” Tunda akamtizama. “Nasafiri peke yangu tu, Ani! Nakuwa kama sina mtu wangu?” “Tatizo la hizo safari zako hazieleweki! Nikikuuliza unaenda wapi na kufanya nini, hunipi majibu ya maana. Ila ukirudi unarudi na pesa.” “Kwa nini sasa tusiende wote safari hii ili ukajionee mwenyewe?” Tunda akacheka.
“Kwa babu Cha, nani tena!?” “Babu Chonde. Au mwite tu Babu. Na sio mbali. Ni hapo Tanga tu, Handeni. Tena amekuwa akikuulizia sana. Anatamani kukuona.”
“Kwani ananijua mimi!?” “Si
ndiye aliyekutabiria na
imekuwa kweli?” Tunda akazidi
kucheka kama mazuri asielewe upana wake. “Kweli Ani. Huoni pesa inayoingia? Unafikiri ni bure?” “Unaipata
wapi sasa?” “Wewe unachangia. Sasa kabla ya safari ya Arabuni, twende tukachukue baraka
zake. Nipe muda
wakutengeneza pesa, twende
Arabuni tukiwa tumejiandaa
vizuri. Tafadhali Ani. usinikatalie.” Tunda akamtizama. Akataka kumkatalia tena, lakini akajirudi.
Sadiki amekuwa akijitoa sana kwake. Akajigeuza kuwa kama mtumwa
kwa Tunda. Mnyenyekevu. Anamtumikia bila kuchoka. Mchana na usiku. Kwa miezi hiyo 7 waliyoishi wote hapo hotelini, alikuwa akilipia na kumletea pesa bila kumuuliza matumizi.
Lakini kila mahali, alipotaka amsindikize, Tunda alimkatalia. Ni kama hakutaka wawe wanaongozana naye popote. Sadiki alishasafiri zaidi ya mara 5. Akimwambia anakwenda Tanga, anaomba amsindikize, Tunda alikuwa akimkatalia.
Kuna siku
alimfuata na kumuomba kama
atakubali sadaka ya shukurani kwa
pesa wanazopata nakutumia bila kuuliza zinatoka
wapi wala kuulizwa matumizi yake, akimtaka
amsindikize kutoa hiyo sadaka,
Tunda akamkatalia kwa jeuri kabisa, ila
siku hiyo akaona ajirudi.
“Nakupenda Ani. Mimi ni wako. Nimekuonyesha na kwa vitendo mpenzi. Sina haya na wewe. Sikutengi na
chochote kilicho changu. Bado kwa muda
wote huu tumeishi pamoja umeshindwa
kunipokea tu mama?” Tunda akamuhurumia.
“Sawa tutakwenda wote.” Tunda akajibu
kwa upole. Tunda huyu hata ukimuona mahali hutamtambua. Tunda wa viwango zaidi ya alivyokuwa kwa baba Tom. Kwanza sasa hivi amekua binti mkubwa. Pesa ipo, anapendwa na kudekezwa
vilivyo na Sadiki.
“Nakushukuru mama. Asante sana Ani. Na utaona tutakavyofanikiwa zaidi. Tena babu Chonde alikuwa akiniambia siku tukifanikiwa kusimama pamoja, tutakuwa watofauti. Baraka zitaongezeka.” Tunda akacheka kama asiyesadiki. “Tatizo huniamini Ani!” “Nishakukubalia
Sadiki. Wewe twende popote utakapo.”
“Na mimi nakuhakikishia hutajuta.
Si unafikiri hizi ni pesa nyingi? Basi nyingi zaidi zinakuja.” Tunda akacheka tu. Maana hapo alipo alikuwa na pesa, sasa akiambiwa nyingi zinakuja zaidi! Tunda akabaki na maswali mengi akivutiwa
moyoni. “Kwamba ndio nimeaga umasikini kabisa!” Tunda hakuwa akiamini. Ikabaki
fumbo ambalo aliona aache mwanya wakuja kujibiwa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Sadiki
akapanga safari. Akaandaa mazingira yote. Ndipo akamfuata sasa Tunda. “Naomba usibadili
mawazo Ani. Ulinihidi tutakwenda.”
“Sasa kesho nina miahadi mahali.
Kwa nini tusifanye week ijayo?”
“Babu Chonde anatusibiri! Na
ameandaa kila kitu. Kwanza hatutakaa
sana. Tunaondoka kesho
alfajiri, tukimalizana naye tu,
tunarudi. Tafadhali ahirisha hiyo
miahadi ya kesho, sogeza mbele kidogo tu. Nakuomba Ani wangu.” Sadiki akaongea kwa
upole akijinyenyekeza, ikabidi
Tunda akubali akiwa na maswali mengi
kuliko majibu. Lakini kwa jinsi Sadiki alivyo kwake, akaweka imani kwake.
“Na leo tutalala wote, siondoki.” Tunda
akacheka. “Karibu.” “Nashukuru.” Usiku huo aliokuja Sadiki,
hakuondoka kurudi nyumbani kwa mkewe. Walipata muda mzuri sana na Tunda. Tunda naye akawa kama analipa fadhila kwa wema wake wakupitiliza. Alimuhudumia na kumuenzi, mpaka
Sadiki akafurahia. Kulikuwa na utulivu wa aina yake usiku huo. Tunda akapunguza kiburi akamuhudumia vilivyo bila kelele. Na Sadiki
naye akamtendea haki kimapenzi. Tunda mwenyewe alifurahia wakati wao wapamoja.
Asubuhi ya saa 11 alfajiri, Tunda na Sadiki wakaondoka jijini Dar, wakielekea Handeni, Tanga. Alichojua ni wanakwenda kwa babu Chonde.
Kutambulishwa, na kukutana na huyo
babu aliyemtabiria. Kwa kuwa walikuwa na
usiku mzuri, njiani walikuwa na wakati
mzuri sana. Wakiongea na kucheka. Gari
ya Sadiki ilikuwa nzuri sana. Ilitangaza
uwezo wa kifedha wa Sadiki vilivyo. Safi na nzuri hata ndani imetulia. Kubwa na ipo juu. Japokuwa walikuwa wakiingia ndanindani sana. Vijiji vya ndanindani huko Handeni ambako hapakuwa hata na barabara yakueleweka, lakini Tunda
hakuwa akilalamika. Mitingishiko ilikuwa midogo tu. Vicheko
vikatawala na Tunda kupata muda wa kumuonyesha Sadiki umaana wake kwake.
Akamwaga sifa nzuri jinsi alivyo dume haswa hata kitandani, akampamba kwa
mengi, ilimradi tu kumfurahisha Sadiki,
mpaka walipofika na Sadiki akawa
amelewa sifa vilivyo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mengi yatajibiwa mbeleni, Endelea kusoma.
0 comments: