SIMULIZI

Nilipotea! Part 4 - Sehemu ya A.

Wednesday, July 07, 2021 naomimwakanyamale 0 Comments

 

T

ayari juma zima na siku kadhaa ilishakatika tokea apatwe na huo mkasa. Kanisani hapaendeki, nyumbani hapakaliki. Kula yake ilishakuwa ya shida, hakuwa akilala vizuri. Ilipofika jumamosi alikuwa amedhoofu kwa njaa na hofu, alitamani asiende kazini, lakini ilimbidi. Alikuwa na kazi kubwa inayomsubiri siku hiyo. Kupamba ukumbi wa harusi ya mtoto wa balozi wa Tanzania nchini Uholanzi. Na alishalipwa nusu ya pesa. Hata hivyo alihitaji sana pesa, ilikuwa lazima akafanye kazi. Alikumbuka jinsi alivyohangaika kuianzisha ile biashara, hakutaka kurudi kwenye ule umasikini wa zamani.

Alishtuka saa kumi asubuhi akaamua kwenda tu ukumbini kuanza kupamba mara baada yakukosa ujumbe kutoka kwa Net. Alishinda akipamba siku nzima, akitoka ukumbi mmoja kwenda mwingine mpaka usiku sana ndipo aliporudi nyumbani.

Akaamua kutuma ujumbe mwingine kwa Net. ‘Nimekosa Net, nimekosa kukuficha kuwa niliwasiliana na Gabriel. Nisamehe. Lakini sikuwa na nia mbaya mpenzi wangu. Sikutaka kuwachonganisha na Gab. Lakini nilimwambia kabisa kuwa nimebadilika, nimemkataa, na nilimwambia kabisa nakupenda wewe. Nakupenda Net, na nimejifunza kutokana na makosa, sitarudia kukuficha kitu tena. Naomba nisamehe.’ Tunda alikaa pale akisubiri mwishowe akaona simu ya Mama Penny inaingia.

“Mbona unalia na kanisani huji tena?” “Nimechanganyikiwa dada yangu! Ghafla maisha yamenibadilikia. Net ameniacha na kanisani wananisema vibaya sana. Nashindwa kurudisha sura yangu pale.” Tunda alikuwa akilia sana. Tokea jumatano ya juma lililopita alipotoka katikati ya ‘bible study’ wale kina mama wakimsema kwa kujidai wanamuuliza maswali mchungaji, hakurudi tena. Jumapili yake alimtumia ujumbe mama Penny kumwambia kuna kitu muhimu kule gerezani kwa baba yake, lazima aende kumuona. Ni kweli alikwenda na mwanasheria ili kuangalia hiyo afya ya baba yake atengenezee kesi. Jumatano kwenye kipindi cha ‘bible study’ kanisani pia hakwenda. Akamtumia ujumbe kuwa ana kazi, hatamaliza kwa wakati.

Sasa jumamosi hiyo usiku ndipo mama Penny akampigia. “Wale kina mama wa kanisani, Mchungaji aliniambia nimeshazungumza nao wote, wala usiwe na wasiwasi. Umesikia?” Tunda aliendelea kulia tu. “Net amekuacha kivipi!?” “Nilikosea dada. Net akajua kitu nilichofanya bila kumshirikisha. Amenikasirikia kuanzia siku hiyo, hajanitafuta wala hajibu jumbe zangu. Na nilishamwambia sikuwa na nia mbaya.” “Labda amesafiri ndio maana anashindwa kupata na kujibu jumbe zako.” Mama Penny akajaribu kumtuliza.

“Simu ya Net inapokea ujumbe wa yeyote, kutoka popote hapa ulimwenguni na yeye akiwa popote hapa ulimwenguni. Muda na wakati wowote, dada. Ni ameamua kuniacha tu.” “Usilie bwana. Naamini anayo sababu tu. Unataka nije?” “Nimechoka sana dada yangu, siwezi hata kusogea.” “Lala basi, kesho nitakuja asubuhi kabla sijaenda kanisani.” “Sawa.” Tunda akajivuta na kujilaza hapohapo kitandani bila hata ya kuoga.

Jumapili.

Asubuhi na mapema, mama Penny alifika nyumbani kwa Tunda kumuona kabla ya kwenda kanisani. Ikabidi Tunda amuelezee kila kitu bila kumficha. “Nilikosea dada.” “Najua Tunda, lakini huwezi kufa hapa na ukashindwa kuendelea na maisha. Tulia kabisa, mpe muda kama alivyoomba. Kama ni wako, atarudi, kama sio wako basi. Naomba ujiandae twende kanisani.” Alihakikisha Tunda amevaa vizuri, akampa kifungua kinywa akamwambia aache  gari yake yeye atamuendesha. Kidogo Tunda akatulia.

Maneno mengi ya Mama Penny yalianza kumfanya Tunda aanze kucheka njiani. Alimpa vituko vya wanae na mikasa mbali mbali ya siku iliyopita wakati ameenda kupamba. Tunda alikuwa akicheka, japo kinyonge.

Walifika kanisani, kwa kuwa Tunda alikuwa amechoka sana aliingia moja kwa moja ndani kanisani akatafuta kona ambayo alijua watu hawatamsogelea akaenda kukaa na kuinama ili alale kidogo. Mama Penny kama kawaida yake ya kuwahi na kuhakikisha kanisa limekaa vizuri. Kuanzia usafi wa mazingira, chooni, ndani na nje ya kanisa, na kumalizia kupamba kabla mumewe hajaja na watoto, aliendelea na pilika pilika zake wakati Tunda amelala kanisani.

Ibada ilianza, watu waliingia na kwa kuwa Tunda alijua kila mtu anamkwepa, hata Julius mwenyewe hakuonyesha kutaka kuwa karibu naye tena, kwa hiyo hakutaka kusumbua nafsi yake, alibaki ameinama bila kusimama wala kumsalimia mtu. Ibada iliendelea, nyimbo mbalimbali ziliimbwa, lakini hakuinuka.

Alisikia watu wa viti vya mbele wakihamishiwa viti vya nyuma kabisa kule alipokuwa amekaa yeye, huku akisikia minong’ono kuwa kuna wageni ambao watakaa viti hivyo vya mbele. Tunda aliwaza kidogo. ‘Kina nani hao!? Mbona Mama Penny hajaniambia kitu chochote?’ Lakini kwa kuwa alikuwa amechoka sana, hakutaka kuendelea kufikiria juu ya mambo ya wageni wakanisani wakati ya kwake yanamshinda! Akabaki ameinama vilevile.

Watu waliendelea kuimba na kucheza wakati bado Tunda amekaa chini huku ameegemeza kichwa chake kwenye kiti cha mbele yake, anasinzia.

Mara akasikia Mchungaji akiongea na watu wote wakakaa, ndipo Mchungaji alipokaribisha watu watoe ushuhuda. Walisimama watu wachache wakashuhudia yale mambo Mungu ametenda, kisha akasikia Mchungaji akisema, naomba mtulie kimya, msikilize. Kwani waumini wengine walikuwa wakishangilia yale waliyokuwa wakishuhudia wengine.

“Naomba msikilize kwa makini sana yale Mungu amefanya kwenye maisha ya huyu binti.” Kanisa zima likatulia.

“Nimepata msaada Gabriel. Nimesamehewa dhambi. Huko kwenye hayo maisha sitakaa nikarudi tena. Nilitumikishwa na ibilisi mchana na usiku. Mungu amenifungua, nipo huru. Nimeanza biashara yangu kwa jasho langu bila kuhongwa, na sasa hivi ninafurahia maisha.”

Tunda alisikika akilia kisha akaendelea.

 

“Sasa hivi anayeishi hapa ni Tunda, aliyesamehewa dhambi na kuishi maisha ya nidhamu mbele za Mungu. Na mabaya yote niliyofanya zamani, Net amenipokea na ananipenda kwa dhati. Naridhika na pesa ninayoingiza kwa jasho langu na mapenzi ya Net, basi.”

 

Ile sauti ikapotea. Tunda akahisi yupo usingizini anaota. Alianza kutetemeka palepale alipokuwa amekaa, akashindwa hata kusogea. Alijiambia ni ndoto kwani alikumbuka ni maneno aliyokuwa amemwambia Gab. ‘Lazima hii ni ndoto! Hii ni ndoto tu.’ Tunda aliwaza huku akifuta machozi. Alihisi ni uchovu wakuto kulala vizuri kwa muda mrefu.

Akaona kabla hajaharibu zaidi pale kanisani anyanyuke, akatafute taksii, arudi nyumbani akalale. ‘Isije kuwa naanza kuchanganyikiwa!’ Akajisemea Tunda akilini.

Suprise!

Tunda akahisi ukimya mkubwa sana pale kanisani, akaamua kunyanyua kichwa. Hakuamini baada yakumuona Net amepiga goti pembeni yake. “Net!?” Tunda akashtuka sana kumuona Net pale. “Ni nini, kina...” Tunda akasita. Mambo mengi yakaanza kupita akilini. Akatulia kidogo. “Naomba nisamehe Net. Nia ilikuwa nzuri, sikutaka kuwachonganisha na Gab. Lakini nakuahidi siku nyingine sitakuficha kitu. Nisamehe.” “Kama utakubali nikuoe.” Net akazidi kumchanganya Tunda. Usingizi, kutokulala kwa muda mrefu kwa wasiwasi na uchovu kwa ujumla, vilimfanya ashindwe kuelewa kwa haraka.

 “Nini!?” Alijaribu kukausha machozi kwenye macho yake ili amtizame Net vizuri, lakini machozi yalikuwa yakichirizika kama maji. “Nataka uwe mke wangu Tunda.” Ilibidi tu ainame. Alishindwa kujibu, wala kuelewa kwa sekunde kadhaa. Net aliacha kupokea simu zake na kujibu jumbe zake, leo anatokea kanisani, anasema nini! Alishindwa kuinuka wala kuongea.

“Kiss her already!” Sauti ya kizungu ya kike, ilisikika ikipaza sauti ikimtaka Net ambusu Tunda. Baadhi ya watu wakaanza kucheka. “Nathaniel Cote!” Ilirudia tena kumwita kwa msisitizo. “We are at the Church, Nana!” Net akababaika akijua maadili ya kiafrica na hapo walipo, kanisani! Anaanzia wapi kumbusu Tunda! “So what?” Bibi yake akamshangaa kinachomshinda ni nini kutoa busu kwa mpenzi wake. “Nooo!”  Net akakataa kwa mshangao.

“I thought we raise you well!” Aliendelea kumchokoza Net. “Yes you did.” “Then man up and kiss her.” “No Nana! We are here.., you know?” Net akajaribu kumuonyesha mazingira na watu waliokuwepo pale, wanao wazunguka. Kama kumkumbusha ni Africa!

“See what you have done to him? He can not even kiss his own fiancé.” Yule bibi alimgeukia Mama yake Net nakumlaumu.  Lakini Ritha alibaki kimya, akacheka kidogo tu kwa kujibaragusa. Maya yeye alikuwa akicheka sana mpaka machozi pamoja na watu wengine waliokuwa wakiwaelewa.

“I told you Nana! Look at him. She can not even kiss Tunda!” Maya akaongeza. Net na Maya walikuwa wakimwita bibi yao Nana na babu yao papa. “I bet your papa is very embarrassed by you, right now! Can’t imagine your dady!” Yule bibi aliendelea kumchochea Net akimwambia anawaaibisha babu yake na baba yake huko walipo.

“What am I suppose to do? She can not even look at me.” Net akasikika akijitetea kwa bibi yake kuwa hajui chakufanya kwani hata Tunda mwenyewe hamwangalii. “Mam up! Lift her up, hold her in your arms and then kiss her. That’s all!” Bibi yake akajibu kwa msisitizo akimwelekeza kitu chakufanya mjukuu wake kama asiyejua.

“You mean now?”  Net akauliza akionyesha wasiwasi huku akimwangalia mama yake. “Right NOW Son. Do it.” Akajibu yule bibi kwa msisitizo kwamba huo ndio wakati wa kumnyanyua Tunda, kumuweka mikononi vizuri na kumbusu. Kisha yeye na Maya wakaanza kushabikia kwa kuimba, “Do it! Do it! Do it! Do it!” Waliendelea kuimba kama kumtia morali Net, Ritha kimya.

Net alibadilika rangi akawa mwekundu mpaka jasho, kwa hofu. Maya na bibi yake hawakunyamaza mpaka Net aliposimama na kumnyanyua Tunda. Akamkumbatia huku akimsugua mgongoni. “I said kiss her not petting her back! What’s wrong with you!?” Bibi yake alipaza tena sauti kwa mshangao kuwa alimwambia amnyanyue na kumbusu, sio kuishia kumbembeleza tu! Bado watu walikuwa wakiwatizama na walioelewa kucheka.

Net akajikaza. Akamvuta Tunda nyuma kidogo, akashika shingo yake kwa mikono yake yote miwili huku akimtizama, kisha akaanza kumbusu. Yule bibi na Maya wakaanza kushangilia kishabiki, ndipo watu wakaanza kupiga vigelegele. “You are a man now.” Bibi yake akamsifia kwa sauti ya juu kuwa ameshakuwa mwanaume.

Net alipiga tena magoti na kuuliza swali huku ameshikilia pete yake. “Will you mary me, Tunda!” Tunda aliendelea kufuta machozi huku akitingisha kichwa kukubali. Mambo aliyokuwa akiyaona kwenye luninga, aliona yanamtokea siku ile. Net alimvuta mkono na kumvalisha ile pete. Tunda hakunyamaza. Busu hilo alilokuwa amelitunza muda wote, ameishia kulipata Nathaniel Cote, kijana wakichotara, aliyebeba damu nyingi ya weupe.

Net akamshika mkono wakataka kutoka nje. “No no no nooo. Hold up son!” Net akasimamishwa na bibi yake. “What!?” Net akamuuliza huku akimtizama bibi yake kwa mshangao. “She is not your wife yet!” Akamuonya mjukuu wake asije nogewa, si mkewe. “I know Nana! I just want her to calm down and then we will be right back.” Net akajitetea kuwa anakwenda tu kumbembeleza ili atulie, kisha warudi. Maana ni kweli Tunda alishindwa kunyamaza. Kitu kilimkaba kooni, akawa haelewi tena. “You better!” Bibi yake akaweka msisitizo. Wote wakacheka, Net akatoka na Tunda nje.

“Nilijua umeniacha Net. Nilijua hunitaki tena. Kwa nini ulinifanyia hivyo?” “Samahani sana Tunda. Sikukusudia kukutesa kwa muda mrefu mpenzi wangu. Nilitaka kukufanyia surprise kwa jinsi ulivyonifurahisha.” “Nimekufurahisha na nini tena!?” “Nyamaza kwanza.” “Hapa nina usingizi na njaa, Net. Sijalala vizuri tangia siku ile ya mwisho tulipowasiliana. Nilichanganyikiwa, nilijua umeniacha!” “Naanzia wapi Tunda!? Siku ile mnawasiliana na Gab, ule ulikuwa mtego tu.” Tunda akashtuka sana.

“Sitaki kukutia hofu, lakini nakutahadharisha tu. Unafuatiliwa sana. Wapo watu hawaamini kama kweli unanipenda kwa dhati, wanafikiri upo na hila.” “Kina nani!?” “Hilo sio la msingi ila ujue wanakufuatilia. Kuanzia siku ya kwanza Gabriel anakutumia ujumbe, halafu ukashindwa kuniambia, walianza kunicheka sana. Siku ulipoenda kukutana naye alikuwa amevaa spika, unasikika live, na kuna mtu walimuweka  kuwapiga picha. Niliumia sana nilipopigiwa simu kuambiwa umeshafika eneo la kukutania na Gab. Mwili wote ulikuwa ukitetemeka, nikiwaza itakuwaje kama utamkubalia Gab. Nilikuwa nashindwa hata kupumua. Nilitamani kuja pale nishuhudie, lakini nikajikaza.”

“Ikabidi kuja kuwapigia tena simu kuuliza mambo yalikwendaje, ndipo nikaambiwa kwa sasa umemkataa. Ndipo ikabidi kufuatilia mazungumzo yote waliyokuwa wamekurikodi. Nilifurahi sana, na kumshukuru Mungu wangu.”  Hofu ilimwingia Tunda  mwili mzima ukaanza kutetemeka.

“Sasa baada ya hapo, nikawa kama nimewasuta, lakini bado hawaamini. Wanahisi kwa kuwa ni Gabriel. Umemkataa kwa kuwa alikuumiza na umejua kuwa tunafahamiana. Wakasema kama ingekuwa mwanaume mwingine mwenye pesa ungemkubali tu. Lakini kwangu nilikuwa nafuraha yakupitiliza. Nikawa nina kazi yakurudia rudia yale mazungumzo kati yako na Gab.” Tunda alibaki anashangaa nakushindwa hata kujisogeza akifikiria kwa upya ni nini alizungumza na Gab siku ile.

“Nilifurahi nakushindwa hata kusubiri tena. Nikampigia simu Nana kumwambia kuwa nataka kuoa. Ndipo aliposema nilazima awepo kwenye kila hatua mpaka ndoa. Ikabidi nikate tiketi ili nikamfuate, aje ashuhudie ninavyokuvalisha pete ya uchumba. Sikujua kama naweza kuchukua muda mrefu kiasi hiki Tunda. Nilijua naenda Canada mara moja kumfuata Maya na bibi, kisha nirudi nao baada ya siku mbili, kisha nikuvishe pete ya uchumba wao wakiwepo. Lakini kufika kule kuna mambo yakajitokeza, ikabidi nimsubirie Nana kidogo. Tumeingia jana. Nimepata ule ujumbe wako wa jana, nikajua hali yako ni mbaya, ikabidi kumuomba mama Penny akupigie ili akutulize.”  Tunda akashtuka kidogo.

          “Mama Penny!?” Tunda akauliza kwa mshangao. Net akacheka kidogo. “Ndiyo, mama Penny. Anafahamu kila kitu. Na hata nilipokuwa kule niliongea na Mama Penny nikamuomba aniandalie mazingira yote, ili nikija iwe ni kukuvalisha hii pete tu. Lakini aliniambia nifanye haraka una hali mbaya. Pole sana mpenzi wangu. Sikukusudia kukutesa.” Bado Tunda alikuwa kwenye mshtuko na hofu.

“Twende ukalale sasa hivi, ili baadaye uweze kuhudhuria tafrija. Mama Penny amenisaidia kukuandalia tafrija nyumbani kwa mama ambako bibi na Maya ndiko walikoshukia hapo. Wale wageni wote niliokuja nao hapa kanisani kwenu ni wakutoka kanisani kwetu, na wengine nimarafiki zangu wa hapa na wachache tumekuja nao kutoka Canada. Wapo na marafiki niliokua nao tokea watoto. Wapo wawili, sijui kama umewaona?” “Mimi nimekuona wewe tu pale ndani.” Net akacheka kidogo.

“Basi na wao wamechangia kuchelewa kwangu. Nilipowaambia naoa, wakataka tuongozane nao waje huku nchini. Wanaondoka kesho asubuhi kurudi kuwahi majukumu yao. Jana nilipofika tu, nilienda kuongea na baba yako. Ilibidi kuomba kuwa ni dharula ili waniruhusu kumuona maana ilikuwa sio siku ya kuwatembelea. Nikaruhusiwa. Amefurahi sana. Amesema kesho tumpelekee picha.” Tunda alihisi yupo usingizini.

“Ungeniua Net!” “Sitarudia tena kufanya hivyo. Kwanza nilitaka kukupa onyo. Usiwahi kunificha jambo, na pia nilitaka kukufurahisha.” “Samahani Net. Naahidi sitarudia tena. Umenipa somo ambalo nimejifunza kwa mateso sana. Nilijua umeniacha!” Machozi yakaanza kumtoka tena Tunda.

“Lakini pia imekusaidia kufikiria Tunda. Angalau umejua kama unataka kuwa mke wangu au la. Unajua nilikuja kujilaumu? Ni kama nilikuja kukuvamia tu! Tokea mwanzo kila kitu kikawa kinaenda kwa vile nilivyokuwa nikitaka mimi. Angalau umepata muda mtulivu wakuwaza.” “Sikuhitaji muda wa kujua kama nakupenda au la Net. Nakupenda.” “Sasa hivi nimehakikisha.” Net alimvuta tena na kuanza kumbusu midomoni. Hiyo furaha aliyojisikia Tunda, hakuna jinsi angeweza kueleza. Alikuwa akikwepesha hiyo midomo akitaka kuja kupata busu la uhakika. Na kweli Mungu akamsaidia na kupata busu la Net. Alikuwa akifurahia sana.

Japokuwa Tunda alishakuwa na wanaume wengi hakuwahi kupata busu kama lile. Net alimshika vizuri na kwa heshima wakati akimbusu kama anashika mwili wa thamani sana kumbe ni mwili wa Tunda uliopitiwa na wanaume kibao, na yeye akilijua hilo. Tunda alilihisi lile busu katika kila kiungo cha mwili wake. Machozi ya furaha yalikuwa yakimtoka si huzuni tena, asiamini.

“Asante sana Net. Asante.” “Umeipenda pete?” Tunda akanyoosha mkono wake na kuanza kuiangalia ile pete. “Nzuri sana. Nimeipenda. Asante.” “Hiyo ni pete ya bibi. Alivalishwa na babu, alinitunzia kwa muda mrefu akasema nikipata mwanamke ninayempenda, nimvalishe.” Tunda akacheka.

“Anaonekana mcheshi!” “Anavituko huyo! Akiamua kukufungulia moyo, wala huhitaji siku nyingi zakumzoea. Ila anatupenda sana mimi na Maya.” “Nikwambie kitu Net?” Net alikuwa bado amemkumbatia Tunda, hapohapo nje ya kanisa huku akimwangalia kwa upendo kama aliyeokota lulu kumbe ni Tunda kituko kwa wengine.

“Mmhh!” “Umenipa heshima ambayo sikuwahi kufikiria hata siku moja kama naweza kuja kupata. Sikujua hata kama nastahili! Hapa nahisi nipo ndotoni. Asante sana.” “Wewe ni wathamani sana Tunda. Sio kwangu tu, hata machoni pa Mungu, ndivyo anavyokuona. Sijafika hata nusu ya punje ya mchele, vile Mungu anavyokupenda na kukuheshimu.” Kabla hajambusu tena, “Mnaitwa na Mchungaji mkaombewe.” Mama Penny alitoka na kuwakuta bado wamekumbatiana wakitaka kupeana mabusu tena.

“Asante sana mama Penny, kwa kila kitu. Naamini mpaka sasa tupo sawa.” “Karibu Net. Kila kitu kipo sawa kabisa.” “Tunashukuru sana, lakini naomba baada ya maombi tu, nimrudishe Tunda nyumbani akapumzike kidogo, halafu tutakuja kwenye tafrija baadaye akishatulia.” “Mnaacha wageni wenu hapa!?” “Wewe si upo?” Net alimshangaza mama Penny.

“Leo ni siku yangu na Tunda. Nataka aifurahie. Kwa jinsi alivyochoka hivi, sidhani kama atafurahia chochote kwenye tafrija.” “Utamuaga mama yako?” Akauliza mama Penny. “Nitaongea naye. Kwa kuwa tafrija itakuwa saa moja usiku, nyinyi mkitoka hapa mnaweza kwenda nyumbani kwa mama moja kwa moja, au mkaja hiyo jioni. Sisi tutakuja huko jioni.” “Sawa.” Akakubali mama Penny.

Tunda akamsogelea Mama Penny. “Kumbe ulikuwa unajua kila kitu, halafu ukaniacha mwenzako nalia mchana na usiku!” Mama Penny akaanza kucheka. “Net aliniomba sana nisikwambie, nivumilie. Mimi mwenyewe nilikuwa nikiumia, lakini nilijua mwisho wa yote utacheka tu. Haya hebu jione jinsi ulivyopendeza na hiyo alumasi hapo kidoleni, mdogo wangu! Mvumilivu hula mbivu.” “Lakini mmenitesa sana!” Wakacheka huku wakimuomba msamaha, mwishowe wakaingia ndani.

Net na Tunda walipiga magoti mbele ya kanisa, wakaombewa. Net alitoa neno la shukurani, nakurudia historia yake fupi yeye na Tunda, kisha akaomba aondoke kabla ya ibada haijaisha. “She is not your wife.” Bibi yake akarudia kwa sauti. “I know Nana.” “Just saying!”  Kila mtu alicheka, Net akaenda kumbusu mama yake, na bibi yake akataka kutoka. “Heyyy! What about me!?” Maya alishangaa kuona kaka yake anampita. “Tunda amechoka.” “It doesn’t take even a minute to give sugar to your baby sister!” “Fine!” Net akarudi akabusu mdogo wake. “Happy?” Net akamuuliza mdogo wake. “Oooh yeah!” Net akacheka na kumrudia Tunda aliyekuwa amemuacha amesimama, akamshika mkono. “She is not your wife.” Alisikia bibi yake akirudia tena kumkumbusha kuwa bado si mkewe, wasije wakapitiliza huko waendako. “I said, I know.” Net akamjubu bibi yake kuwa analijua hilo, huku akiondoka na Tunda akiwa amemshika mkono.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Walifika nyumbani kwa Tunda, akiwa anasinzia. Aliingia bafuni, akaoga tena hasa kusafisha uso uliokuwa umechanganyikana machozi na vipodozi.  Akavaa nguo za kulalia kabisa, akatoka pale sebuleni alipokuwa amemuacha Net. “Mbona nguo za kulalia tena!? Tutawaweka sana watu kule kwenye tafrija Tunda! Nilitaka upumzike kidogo tu.” “Utaniamsha muda unaotaka tuondoke. Nimechoka sana Net, nataka nilale vizuri.” “Pole.” Net akamsogelea, akambusu tena bila kumkumbatia ila kumshika tu kichwani ili kuweza kumbusu. Akamuachia.

“Twende nikusindikize.” Akamshika mkono na kuingia naye chumbani kwake, Tunda akiwa na wasiwasi. Alimuogopa sana Net.  “Njoo hapa.” Net akajilaza kitandani, kisha akavuta mto  akaweka chini ya kichwa chake. “Njoo ulale hapa.” Tunda alibaki amesimama, akakunja uso akionyesha wasiwasi na hofu. “Njoo usiogope, Tunda.” “Kifuani kwako!?” Akauliza kwa hofu kidogo. “Hutaki?” “Sio..” Tunda akasita. “Usiogope, njoo. Nataka ulale vizuri. Ni leo tu, hutazoea.” Tunda akacheka. “Nitagoma kuamka mimi!” Tunda akamfanya Net acheke.

“Ndio nabembelezea msamaha, kwa kukutesa kwa siku zote hizo.” Tunda akatabasamu, akapanda kitandani na kujivuta mpaka kifuani kwa Net. “I miss you so much Net.” “Miss you too, babe. Nitaongea na Mchungaji wako, atusaidie tufunge harusi mapema. Nataka tuanze kuishi pamoja.” Tunda akapitisha mikono yake kifuani kwa Net, akamkumbatia kwa nguvu na kupitiwa na usingizi bila ya kujibu kitu. Net aliendelea kumpapasa taratibu maeneo ya mgongoni na begani, huku akimbusu kichwani mpaka na yeye akapotelea usingizini.

 

Tafrija ya kuvalishwa pete ya uchumba Tunda.

Ilikuwa ni kwa mara ya pili Tunda kufika nyumbani kwa mama Cote. Mara ya kwanza alipopelekwa kutubu akiwa mwenye dhambi haswa. Baada ya kukiri alishajihusisha kimapenzi na mchumba wa mama Cote, uadui ukaanza. Sasa anarudi kwenye jumba hilo kama mchumba wa Net. Ilikuwa nyumba yenye thamani za kisasa, tena za aina yake. Nyumba nzuri, iliyojengwa kwa namna yake. Magari yaliyokuwepo hapo nje sehemu yakuegeshea tu magari, Tunda akajua ni watu wenye uwezo watupu watakaokuwepo huko ndani.

“Umependeza sana Tunda.” Tunda akatulia kidogo. “Nini?” “Itakuaje nikifika huko ndani nikakutana na..” Tunda akanyamaza. Net akamuona akifuta machozi huku akiangalia nje ya dirisha. “Naomba uniangalie Tunda.” Tunda akamgeukia. “Naona kama nakuingiza aibu tu Net!” “Naomba usipeleke mawazo yako huko kabisa. Kila mmoja utakayemkuta humo ndani anahistoria yake. Sema ya kwako umeigeuza imekuwa yamsaada.” Net aliendelea kumtuliza akisikika ametulia kabisa, bila hata wazo la pili la wasiwasi.

“Nilifurahi sana jinsi ulivyoweza kuongea na Gab. Umethibitishia kila mtu umeshakomaa Kiroho. Tumia ujasiri huo huo kwa kila atakayekusogelea. Na hakikisha unajitambua acha hofu kabisa. Nipo na wewe nikikujua vizuri, na nimeridhika na wewe. Kwa hiyo tembea mbele ya watu ukiwa huna hofu. Umenisikia?” Tunda akatingisha kichwa kukubali.

“Haya naomba tabasamu. Maana hii yote nimeandaa kwa ajili yako. Nataka ufurahie. Sawa?” Tunda akacheka taratibu. Walikuwa wameegesha gari nje ya hiyo nyumba ya mama yake, sehemu ya kuegesha magari. Net akamvuta karibu na kumbusu tena na tena bila kumuachia kama mwenye kiu naye mpaka simu yake ilipoanza kuita. “Mama huyo!” Net akasema wakati anaiangalia simu yake akaamua kupokea. Alisikiliza kidogo mama Cote akiongea, kisha Net akajibu. “Tupo hapa nje, tunaingia ndani sasa hivi.” Akakata na kumbusu tena Tunda. “Twende, Nana ameanza kusinzia.” Wote wakacheka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Bibi yake Net alimuomba Net,  amvalishe tena ile pete Tunda huku akichukuliwa vizuri video kama kumbukumbu ya familia, akidai kuwa siku hiyo ndipo anapomkabidhi Tunda cheo cha Bi. Cote rasmi kama mrithi wake. Kwanza alivaa pete aliyochumbiwa nayo yeye na pili anaolewa na mjukuu wake mwenye jina kama la mume wake. Alisema anakikundi cha marafiki zake kanisani huko nchini Canada, anafanya nao bible study, walimuomba arikodi kila kitu ili akifika awaonyeshe. Zile zilikuwa habari zilizomtibua mama yake Net, na kumnyima raha kwenye ile shuguli nzima.

Mama Penny alikuwa ameandaa sehemu si ya nje, lakini si sebuleni. Kulikuwa na eneo la ndani lakini kama baraza kubwa tu lililokuwa limezungushiwa kuta nzuri mpaka juu ambako ndiko vyumbani. Chini kwenye hilo eneo la katikati kulikuwa kama na bustani tena ambayo ilishamtoa macho Tunda tangia mara ya kwanza anaingia kwenye hiyo nyumba.

Haikuwa bustani kubwa lakini duara kubwa iliyozungushiwa majani mazuri, yaliyokatwa chini yakawa kama mkeka. Vyungu vya thamani vyenye maua mazuri yaliyokuwa yamezunguka kwenye hayo maua na pembeni ya kona kwenye hilo baraza zima na nguzo, mama Penny alitendea haki. Kuzunguka hilo eneo zima kulikuwa na fremu za picha nzuri sana na aina mbali mbali ya maua. Ndipo mama Penny akapaandaa vizuri na kupendeza.

Yote hiyo alifanya Net kwa ajili ya Tunda. Sasa mpambaji akawa ni mama Penny, nyumbani kwa Ritha, mama yake Net, asiyempenda Tunda. Leo Tunda anavalishwa pete nyumbani kwake akiwa ameonya asikanyage pale tena. Mbaya zaidi, anavalishwa pete ya thamani sana, urithi ambao yule bibi aliuwekea maana kubwa mbele ya watu! Mambo hayo yote wanayafanya nyumbani kwake! Hakuna jinsi mtu angeangalia moyo wa huyo mama ulivyochafuka, akaweza kueleza wengine.

Alikuwepo kanisani na pale kwenye ile tafrija japo ni nyumbani kwake, lakini sababu ya uwepo wa huyo bibi milionea ambaye hata Tunda hakujua uzito wa huyo bibi kuwepo pale. Alisikia akipiga kelele kanisani, akitaniana na Maya na Net. Asijue uwepo wa huyo bibi hapo nchini hata usalama wa taifa nchini Tanzania na Canada, unajua kama yule bibi yupo nchini Tanzania.

Waalikwa ambao Net alimwambia wengine ni wakutoka kanisani kwao na marafiki, wengi pale ni askari kanzu na usalama wa taifa walikuwa wamejaa hapo, kuhakikisha huyo bibi, raia muhimu sana wa huko nchini Canada yupo salama, na hakuna linalotokea, mpaka anarudi nchini kwake salama.

Na hao wazungu wachache aliowaona Tunda pale, hawakuwa ni rafiki wa karibu tu wa Net , ni askari waliopitia mafunzo makubwa sana ya kiaskari ya kimataifa, walifika nchini na huyo bibi kwa ajili ya usalama wake tu. Kwanza alitua nchini na ndege yake ambayo ndio ilibidi kufanyiwa taratibu ya eneo la kutua hapo nchini Tanzania. Kimya kimya bila gazeti lolote kuripoti ujio wa bibi huyo nchini Tanzania.

Mama Cote, au Ritha, alijua ni mapesa ya kiasi gani yamemwaga kwa huyo bibi anayefanya mchezo na kuonekana wa kawaida sana kuwepo hapo. Ritha alipigia mahesabu ya huyo bibi kuwepo tu hapo! Tena kwa ajili ya Tunda, ambaye amempokonya ndoa na mapenzi ya mtoto wake! Anamwita Malaya. Anajua wazi, amemchagua Net badala ya Gab kwa kuwa anamfahamu Net, anataka kunufaika naye. Ritha akajiambia hiyo pesa angefanyia kitu kikubwa sana badala yakupoteza kwa malaya, Tunda.

Kila neno alilotamka bibi Cote, halikuwa bure. Hakuwa mropokoji. Ni mwanamke aliyekuwa akiongea na maraisi na watu wakubwa sana ulimwenguni. Pesa yake na kile anachokifanya nchini Canada, kama mwanaharakati wa mambo ya wanawake si nchini kwao tu, bali ulimwenguni, kilimketisha na wakuu wa ulimwengu huu na kumwingiza sehemu kubwa mbalimbali hapa ulimwenguni. Alishahutubia mara kadhaa kwenye vikao vikubwa vya UNO. Kila aliloongea, watu walilinukuu na kulisikiliza kwa makini sana hata kugeuza ni habari ya kuuza gazeti lolote lile haswa nchini kwao anakofahamika na familia hiyo kufuatiliwa kwa karibu sana.

Ritha alijua na kuzidi kuumia kwa kila neno analozungumza huyo bibi Cote usiku huo kwenye tafrija hiyo. Alijua si mropokaji. Kwa hiyo hata usiku huo hakuna aliloropoka hata moja juu ya Tunda na Net. Inamaana ni maneno au hotuba maalumu aliyokuwa ameiandaa kwa muda mrefu kuja kuzungumza kwenye tafrija ya Net akichumbia. Na lazima hiyo hotuba au hayo maneno anayoongea hapo yamesomwa na kurudiwa na msaidizi wake wakaafikiana na ndipo anatamka mbele ya huo umati kirafiki tu kama akizungumza na familia yake, lakini wazi anajua ni habari nzito nchini kwao siku inayofuata, japo amezungumzia nchini Tanzania. Na akitamka yeye, ndio mwisho.

Ni ukweli ambao hakuna ambaye angesema, Tunda angeamini. Kwa hakika Tunda hakuwa akijua lolote lile juu ya Net mwenyewe wala huyo bibi. Net alikuwa makini sana anapozungumza na Tunda. Na alifanya makusudi akijua umuhimu wa mwanamke atakayemuoa. Sio tu kuitwa mke wa Nathaniel Cote, alijua atabeba majukumu mazito sana. Tunda asijue.

Net hakuwahi kujifungua kwa Tunda zaidi ya idadi ya waliozaliwa nyumbani kwao. Kile anachofanya pale nchini. Kazi za mama yake. Hakuwahi hata kuropoka utajiri mkubwa unaomsubiri nchini Canada. Au anavyosubiriwa kwa hamu huyo mke wa Net, huko nchini Canada. Hata kujulikana jina tu, ingekuwa habari ya kuuza magazeti. Picha yake ndio kabisa. Tunda hana hili wala lile. Anajionea ni bibi amekuja kwenye shuguli ya mjukuu akichumbia. Basi. Kumbe ameingia kwenye historia kubwa sana.

Vyombo vya habari vya nchini kwao na watu wengi walio ijua hiyo familia, na kuifuatilia walitaka angalau kupata fununu kujua hata kwa fununu tu, atakayekuwa mke wa Net. Anaposema video nzuri ichukuliwe Net anapochumbia kwa ajili ya marafiki zake wa kanisani, sio kwa sura hiyo aliyoelewa Tunda hata kidogo. Ni kumbukumbu ya vizazi hadi vizazi na ni habari nzito sana ambayo mtu anaweza hata kuuza kwa pesa nzuri tu za kicanada. Nathaniele Cote amechumbia siku hiyo! Ilikuwa ni habari kubwa yakuuza magazeti nchini kwao.

Lakini Tunda yeye kila kitu aliona kawaida tu, na Net alikusudia iwe hivyo. Hakutaka askari yeyote avae sare na wala pale pasionekane risasi yeyote ile hata ya kiunoni mwao. Kwa hiyo kila mgeni akaonekana wa kawaida. Nadhifu na wengi wamevaa suti. Kumbe suti hizo zimeficha mengi. Tunda na kina mama Penny pamoja na wageni wengine wakawa hawaelewi kinachoendelea. Kumbe hiyo nyumba ilikuwa chini ya ulinzi mkubwa sana tokea huyo bibi anafika pale.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Yakawekwa mazingira mazuri pale. Katikati ya kula na kunywa, watu wakicheka, Net akapiga tena goti akimuuliza Tunda aliyekuwa amesimama, kama atamkubali amuoe, “Will you mary me?”. Tunda akakubali, kwa kusema, “Yes.” Net akamvalisha tena ile pete akiwa amepiga magoti vilevile. Kisha akasimama, akamkumbatia vizuri na kumbusu Tunda.

Haikuwa mara ya kwanza kwa Tunda kupata busu au kukumbatiwa na mwanaume. Baba Tom alishambusu akiwa bado mdogo na mwili huo ulishashikwa na wengi tu. Kimapenzi na kupigwa kama mwizi. Lakini busu la Net na jinsi alivyomgusa huo mwili! Ilikuwa tofauti kabisa. Hakuna aliyeona asitamani. Wenye wivu ndio walizidi kuumia.

Net alijua wapi amshike kabla ya kumbusu, na hata jinsi alivyomwangalia baada ya kumshika kabla ya kumbusu, akili na mawazo ya Tunda alijua wazi anapendwa na kuthaminiwa sana. Ile hofu na aibu mbele ya wateja wake ilimuisha kwani ni kweli walikuwepo wanaume wakutosha tu ambao walikuwa wateja wake, lakini kwa jinsi Net alivyo mtizama na kumshika, hakuna jinsi Tunda ungemkumbusha kuwa alishakuwa changu, ukamuumiza.

 

Mama Cote na Tunda tena.

Wakati watu wakiwa wanaongea na kucheka, huku wakila na kunywa, Mama Penny na mumewe wakaamua kuaga. Muda ulishakwenda. Watoto wanatakiwa shuleni kesho yake. Wakamuaga Net na Tunda. Wao wakaondoka. Kwa kuwa walikuwa wamekaa meza moja na Tunda, walipoondoka, Net naye akasimama, akamwambia Tunda atarudi baada ya muda mfupi. Tunda naye akaamua kuingia ndani kutafuta choo kilipo ili angalau ajitengeneze vizuri na kujirudishia vipodozi na nywele. Kujitengeneza.

Wakati anatoka chooni, mama Cote au Ritha alikuwa akimsubiria mlangoni akiwa amejawa wivu baada ya kuona jinsi mkwewe alivyomthamini Tunda. Na ni kama alitangaza kumpa Tunda cheo kikubwa sana ambacho hakuwahi kupata mtu sahihi wakumpa ila Tunda. Lakini alitangaza kwa kujihami huku akisema, atatangaza rasmi au atamkabidhi rasmi cheo hicho baada ya kupata muda wakutosha wamazungumzo na Tunda.

Tunda alicheka tu kwa kuwa yule bibi aliongea kama kitu cha utani, kumbe ni jambo zito lililokuwa likisubiriwa kwa muda mrefu sana. Wengi walitamani kujua cheo hicho angalau yule bibi anamfikiria kuja kumkabidhi nani! Nani angekuwa mrithi wake! Nani anakalia kiti hicho! Angalau kwa fununu tu. Leo kwa mara ya kwanza, anatangaza, tena nchini Tanzania! Hata Net na Maya walibaki mdomo wazi. Hawakuamini.

Lakini si Tunda ambaye hakujua chochote. Alimuona jinsi Maya na wale wageni wote kutoka Canada wakishtuka mpaka kusimama na kushangilia sana, na Net kubadilika mpaka rangi ya sura akiwa ametoa macho asiamini kile bibi yake anafanya kwa Tunda. Tunda mwenyewe hata asielewe ni nini bibi huyo anaongea. Akajiambia ni mambo tu ya kizungu.

Tunda akawa ndio ametamkwa kwa mara ya kwanza na bibi huyo kuwa ndiye atakalia kitu hicho baada yake. Ritha alijua ni habari itakayoenea sana nchini Canada na picha za Tunda kuanza kuonekana huko na habari zake kufika kwenye nchi mbali mbali za wawakilishi wa umoja wa bibi huyo. Tunda hana habari.

Picha nyingi zilipigwa asijue umuhimu wake. Aliona mpaka rafiki wa Net wakimuomba akae vizuri wampige picha akiwa peke yake tena kwa kupokezana. Akiwa anacheka tu, akakubali kufuata maelekezo. Marafiki hao wakampiga picha akiwa peke yake, kisha wakamuomba mmoja mmoja wapige naye picha. Kwa zamu. Nyingine wakapiga wakiwa na Net. Ikawa shamra shamra imeongezeka gafla baada ya tangazo la bibi huyo, Tunda hana habari.

‘Tunda!’ Ritha aliumia sana. Bibi Cote alitamka kumkabidhi Tunda kiti ambacho inamaana yeye hakustahili! Tena anatamka hayo mbele za watu bila hata kuzungumza na wao kwanza kama familia, wakajua kama amekusudia kuwa ni Tunda! Hata wao watu wa karibu ndio wanasikia pale kama watu tu wa nje! Yule bibi hakumshirikisha yeyote. Yaani pale ndio anatoa hiyo habari kwa mara ya kwanza.

Alihisi ni kama yule mama mkwe wake ametangaza kumtoa kwenye familia kwa wazi tena kwa kumdhalilisha vibaya sana. Ni kama anasema Tunda ni bora kuliko yeye! Alichukia sana kuona anadhalilishwa pale mbele za watu tena nyumbani kwake! Ni Tunda, binti anayejihesabu amempita kwa kila kitu! Leo anapewa heshima yote aliyokuwa amebeba yeye, na kudhani anastahili yeye Ritha! Hasira zilizidi kumpanda na kumchukia Tunda zaidi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Naomba tusogee hapa pembeni tuzungumze.” Tunda akamfuata nyuma. Akashangaa anamtoa kabisa pale mpaka sehemu ya nje karibu na mlango wa kutokea. Akaangalia kulia na kushoto, wakajikuta wawili tu. Kulikuwa na askari kanzu wawili nje ya huo mlango walionekana kwa kupitia kioo cha mlango. Yule mama akaonekana kuridhika na hiyo faragha.

Akamgeukia Tunda. “Upo hapa leo sababu ya huyu bibi, tu.” Mama Cote akaanza huku amemkazia macho. “Umenielewa Tunda? Unaweza kumdanganya kila mtu hapa, lakini sio mimi. Mimi sio mtoto mdogo au mjinga kama hao wanaume zako uliokuwa ukiwavulia nguo na kuwaloga. Najua janja yako. Upo hapa na kumkataa Gabriel kwa kuwa umejua Net anapesa kuliko Gab. Anamapesa ya urithi wa babu yake na bibi yake akifa ndio kabisa. Yeye ndio anakuwa mrithi au mtawala wa mali zote za Cote.” Tunda akakunja uso. Hayo yote hakuwa hata akiyajua. Na wala hajui kama hiyo familia ya Cote ina mali za hivyo!

“Sijui unamlogea wapi mtoto wangu! Sijui kama na yeye unamfanyia sadaka za makaburini au la! Lakini mimi na wewe tunajua wazi, kwa akili za Net hawezi kukupenda mtu kama wewe hata kidogo. Nina uhakika kuna ulichofanya kwa Net. Wewe ni mzoefu wa ushirikina, hushindwi kuzika akili zake. Na ninajua wazi, yale majini yanayosadikika kukutoka, hayajatoka. Bado yanaharibu akili za wanaume, ndio maana na Net amechanganyikiwa.” Ritha akataka kuendelea.

“Subiri kwanza mama Cote.” Tunda akamkata. “Wewe si upo safi mbele za Mungu? Unaamini kwenye wokovu na nguvu ya damu ya Yesu? Sasa kwa nini humkomboi mwanao kwa maombi ili atoke kwangu? Kwa nini humtoi kwangu kwa maombi? Unahangaika tu na mimi kwa maneno mengiii! Au huamini kama Mungu wako ananguvu kuliko nguvu ya shetani?”  Tunda alimshtua sana Ritha. Akababaika sana akiongea hili na kujibu lile, Tunda akimtizama kwa kumsuta.

“Subiri kwanza Ritha. Acha maneno mengi. Wewe si mama yake Net? Inamaana unazo haki zote za kumkomboa mwanao kwa njia takatifu kama wewe ulivyo mtakatifu. Mbingu inajua unayo haki, hata kuzimu kule unakosema mimi ninaenda, wanajua kuwa wewe kama mama yake Net, unayo haki na Net. Sasa kwa nini unahangaika na mimi ambaye hata sijaunganishwa na Net kwenye agano lolote!?” Tunda akamuuliza taratibu tu bila jazba kama yeye alivyokuwa akiongea kwa jazba.

“Usifikiri ndio umeshinda Tunda. Namuombea mwanangu. Ila ujue maombi ni kotekote. Ni mimi, na Net mwenyewe aamini.” Tunda akamtizama kwa kumsuta. “Na usifikiri nimeshindwa. Nipo kwenye maombi yakumfungua akili zake mpaka afunguke. Net ni kama amechanganyikiwa kwa kuwa anataka kuwa mtumishi wa Mungu kama babu yake, ila hajui ni jinsi gani atumike. Kwa kuwa wewe ulikuwa malaya, na bibi yake anapambana na haki za wanawake na kutoa wanawake wenye hali kama yako na kuwawezesha kimaisha ili waweze kujitegemea, ndio anaona wewe utafaa.” Akaanza kuropoka, Tunda akimtizama kwa mshangao.

“Kwanza atakutumia wewe kama kielelezo cha kufikia roho za watu waliopotea na pili anaona anamfurahisha bibi yake kwa kumuunga mkono kwa kile anachokifanya kwako wala si mapenzi. Ndio maana anadhani wewe utamfaa.” Hilo likamwingia Tunda na kumuumiza sana. Ila akajikaza mbele ya Ritha.

“Upo wewe kama daraja kutimiza ndoto zake, na ndio maana hata bibi yake pia yupo hapa leo kuhakikisha Net anafikia ndoto zake na yule bibi anajipatia sifa kimataifa. Kuwa ni mkweli kwa kile anachokipigania. Kwani ameweza kuruhusu hata changudoa kama wewe kuolewa na mjukuu wake. Usifurahie jinsi unavyoitwa Mama Cote leo, ukadhani kuna kitu cha maana walichokiona kwako au uchawi wako pekee ndio umeshinda. Hamna kitu.” Tunda alibaki kimya ametoa macho. Habari zilikuwa mpya, ngeni lakini kweli zilianza kumuumiza.

“Wewe loga utakavyo. Lala makaburini utakavyo. Lakini jua mimi nipo. Na uelewe kabisa nawajua wazungu kuliko wewe. Wanajua kutumia watu. Umeruhusiwa na yule bibi kuwepo na Net kwa ajili ya kumnufaisha yeye mwenyewe yule bibi. Kimataifa na kiuchumi. Na kwa upande wa Net, kama nilivyokwambia. Ila sasa, ujue wazi, MIMI nipo. Sitakubali kwa nia yao yeyote ile, wewe unufaike kwa kile ninachostahili mimi.”

“Nimehangaika sana kufika hapa. Mchana na usiku kujenga hili jina huku Tanzania. Nani alijua Cote huku Tanzania kama sio mimi? Hapa uliposimama, ni kwangu nimejenga kwa jasho langu. Hata kama Net alikwambia babu yake ndiye alijenga hapa, lakini ujue mimi ndiye niliyekuwepo hapa kuhakikisha jengo linasimama.” Na hapo napo Ritha akajikuta anaropoka mengiii kwa hasira huku Tunda akimshangaa. Hakuwa anaelewa chochote anachozungumza pale.

“Kwa hiyo ujue sitakubali. Wakati wewe unahangaika na suruali za wanaume, mimi nilijua kufunga miguu yangu, nikatumia akili, mpaka kumfikisha hapo alipo hata huyu Net ambaye sasa hivi unafurahia mali zake hapa nchini Tanzania. Yupo hapa nchini kwa sababu ya juhudi zangu wala sio pesa. Hawezi kuishi Tanzania bila idhini yangu mimi ambaye ni raia wa Tanzania.” Hapo napo Tunda hakuwa hata akielewa.

“Sasa, sitakubali hata iweje uvune usipopanda. Labda usubiri niwe nimekufa ndio utakuja kuitwa mama Cote. Vinginevyo ujue utapambana na mimi na utajuta, malaya mkubwa wewe.” Tunda akatabasamu. “Umemaliza?” Tunda akamuuliza mama Cote swali lililomshangaza, tena akiwa ametulia tu. Kimya.

“Acha kuniogopesha Ritha. Wala sitakuita Mama Cote maana umejishusha sana. Mimi huwa sitishwi. Na wewe wala usifikiri ndio wa kwanza kunijia na vitisho. Tokea napata akili zangu, nimeishi na watu wa aina yako. Vitisho imekuwa sehemu ya maisha yangu. Yaani wewe hapo ulipo hivyo, hunitishi hata kidogo.” Tunda akaendelea taratibu tu.

“Unanisikia Ritha? Sikuogopi. Halafu na uache kujipa kazi zitakazo kuchosha bure! Ngoja nikusaidie tu kwa kuwa umenizalia Net. Huko unakonitafuta mimi simo tena. Nimetoka na nimeamua kupumzika. Mungu alishanitoa makaburi na kwa waganga wa kienyeji, muda mrefu sana. Nimeacha kuvua suruali za wanaume muda mrefu sana na wala sijivunii kwa hilo. Najua nimesamehewa, lakini bado nipo na majuto tu. Nasikitika kuwa na wewe umekuwa muhanga na maisha niliyoishi zama...” “Acha kunipa maneno unayomdanganya nayo Net. Mimi ni Ritha Cote. Najielewa. Na nimekwambia hata Net anakutimia tu.” Ritha akamkata. Tunda akacheka kwa kumuhurumia.

“Hata kama Net ananitumia tu. Au bibi yake ananitumia. Sijali. Nataka ujue na mimi msaada ndio nilio kuwa nikiutaka siku zote za maisha yangu. Net amepata alichokuwa anakitaka maishani mwake, na mimi nimempata mwanaume ambaye hata sikuwahi kumuota na heshima kubwa ambayo hata sikuwahi kufikiria nina stahili. Wewe ni shahidi kwa kile tu kilichonitokea leo. Ulikuwepo tokea asubuhi ukishuhudia kile kinachonitokea mpaka sasa hivi uliposhindwa kuvumilia. Umeona heshima iliyowekwa kwa Tunda tu!” Tunda akacheka taratibu.

“Kwa hiyo kwa upande wangu mimi, kwa ufupi, sina chakupoteza hata kidogo. Kama Net na bibi yake wataendelea hivi, aisee ujue mimi ndio nilichokuwa nikikihangaikia tokea zamani mpaka kulala makaburini nakushindwa kukipata kwa shetani ila kwa huyu Mungu ninayemtumikia sasa hivi. Sasa kama na yeye unamwita shetani, hakuna injili itakayowahi kuja kunitoa kwa huyu Mungu ninayemtumikia sasa hivi. Nakushauri na wewe umfuate. Analipa. Na itakupunguzia kupambana na watu au kuzunguka kwenye maofisi ya watu ukijidhalilisha bila wewe mwenyewe kujijua.” Ritha alishtuka sana asiamini.

Tunda akataka kufungua mlango ili aondoke lakini akageuka. “Na wala usipate shida na uwepo wangu. Nitajitahidi tusionane kabisa mpaka utakapo kuwa tayari kuniona tena. Naomba uniagie Net.” Tunda akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya muda kupita bila kumuona Tunda, Net akaanza kumtafuta. Aliingia ndani na kutoka mara kadhaa, mwishowe akakumbuka kumuona mama yake akiingia ndani wakati Tunda yupo ndani. Akamsogelea, “Umemuona wapi Tunda?” “Aaah! Nilisahau kukwambia. Aliniambia nikuage yeye ameondoka.” Net akakunja uso na kujiweka sawa.

“Umemwambia nini tena, Tunda?” “Kwa nini unafikiria maneno yangu ndio yamemuondoa hapa?” “Mama?” Net akaita kwa ukali kidogo. “Umemwambia nini Tunda?” “Labda atakuwa hajanielewa.” “Juu ya nini?” Net akauliza. “Acha kunihoji maswali mengi. Hapa ni nyumbani kwangu.” Ritha akambadilikia mwanae.

“Ni nini kinaendelea mama!? Shida yako ni nini? Kwa nini umeshindwa kumpokea Tunda kama mwanamke ninayempenda?” “Kwa kuwa umekataa kukaa chini na kumfikiria vizuri.” “Unataka nifanye nini kukuthibitishia kuwa Tunda amebadilika? Umempa mtego wa Gab, ameshinda. Nini unataka kutoka kwake!? Ulitaka afanye nini!?” Net alikuwa anamshangaa mama yake nakushindwa hata kuelewa.

 

“Nishakujibu kuhusu Gab. Ule sio mtihani wakumpima mtu kama Tunda, nakusema ameshinda. Gab angekuwa mwanaume mwingine, hakika asingemkataa. Mbali na sababu nyingine nyingi za mwanamke kama Tunda, kwanza lazima ujue bado ana uchungu na Gabriel ndio maana alimkataa. Na yeye si binadamu bwana! Anaweza kuumizwa. Huwezi kumpima mtu kama Tunda na Gab wakati amekukamata wewe. Nini atanufaishwa na Gab ambacho hatapata kwako? Anajua hilo ndio maana anajifanya mtakatifu kwako.” Yule mama akaendelea.

“Siwezi kuwa mjinga au kudanganywa na Tunda kama alivyofanya kwa Gab na wewe sasa hivi. Eti nimekaa hapa, namwangalia tu anavyojidai kuwa amebadilika, ameokoka, eti sasa hivi ni malaika na wewe unataka kumuoa! Hata kidogo. Sikubali.”

“Wageni wote hapa wakiume, karibia asilimia 90, kasoro ya aliokuja nao bibi yako tu, amelala nao. Kwa nini unataka kunidhalilisha hapa mjini? Wasichana wote waliojaa humo makanisani, leo unakuja kumuoa yeye!? Kwa nini Net? Naomba pata muda ufikirie. Tunda hawezi kuwa mke wako. Naomba mwanangu punguza mwendo. Umefanya haraka sana juu ya huyu Tunda.” Net akazidi kuumia.

 

“Nafikiri nimefanya sana haraka kwako mama. Hata hii shuguli sikutakiwa kuifanyia hapa. Nana angeshukia nyumbani kwangu, na mambo mengine yangeendelea kama kawaida, nyumbani kwangu. Lakini sikutaka haya mambo yaende mbali. Sikutaka tumuingize Nana katika hili ndio maana nikamleta hapa na kumrudisha Tunda kwako japo ulimuumiza sana.”

“Nakupa muda zaidi. Utakapokuwa tayari utanitafuta. Lakini ukae ukijua nitamuoa Tunda, tena haraka iwezekanavyo. Unajua pakunipata pindi utakapo kuwa tayari. Na kwa kuwa Tunda ni kero kwako, nitajitahidi kumuweka mbali sana na wewe, ili asikukere na usimuumize.” Mama Cote alishtuka sana. Akajua Net akihama pale ndani tena, akarudi nyumbani kwake, bibi Cote atafahamu na kuibua maswali zaidi.

“Kwa hiyo na wewe unaondoka!?” “Humtaki Tunda, na Tunda atakuwa mke wangu hivi karibuni, unafikiri nitafanya nini?” “Na kazi unaacha?” “Kwa nini niache kazi!?” “Sijui. Labda unataka kuniadhibu.” Mama Cote alitumia silaha yake kwa haraka, aliyojua kumvuta nayo Net. Machozi. Net akamsogelea. “Nakupenda sana mama yangu. Na nilimuahidi baba nitakuwa na wewe wakati wote. Hakuna mtu wala kitu kitaingilia katikati yetu. Siwezi kuacha kazi. Nilikuahidi maisha yangu ya familia hayataingilia kazi yangu, na bado itabaki hivyo.”

“Siwezi kukuadhibu kwa kutokumkubali mwanamke ninayempenda mimi, lakini naona haitakuwa sawa kuendelea kukuletea Tunda, halafu unaiishia kumuumiza. Sio sawa kwako wala kwake. Nilikubali kuja naye hapa leo, kwa kuwa ulisema huna neno. Lakini sasa hivi nimejua kuwa ulikubali sababu ya Nana. Ulijua Nana asingefurahia kuona Tunda hakaribishwi nyumbani. Lakini usiwe na wasiwasi, Tunda hatakubugudhi tena na wala haya mambo hayatafika kwa Nana. Usiwe na wasiwasi juu ya hilo. Usiku mwema mama.” Net akambusu mama yake, akaenda kumsindikiza bibi yake kitandani huku wakitaniana. Waliomba naye, kisha akondoka kwenda kumfuata Tunda.

Net kwa Tunda.

Net alimkuta Tunda, ameshaogo na kuvaa nguo zake za kulalia, amejilaza kwenye kochi anaangalia tv. “Nilikuomba usiwe unanikimbia Tunda.” “Nilimuomba mama yako aniagie.” “Tangia lini mimi na wewe tunawasiliana kwa kupitia mama yangu? Ingechukua dakika ngapi kuniaga pale wakati unaondoka?” “Sikutaka kukusumbua katikati ya wageni. Halafu nilikuwa nimekasirika Net, sikutaka kuongea kabisa. Kuhofia kuongea neno ambalo lingekuudhi bure, wakati nilikuona unafurahia na wenzako.” Net akakaa, Tunda akasogeza miguu vizuri kama kumpisha apate nafasi vizuri.

“Net!” Tunda akaita na kukaa vizuri. Net akabaki akimwangalia. “Naomba uniambie ukweli. Na kumbuka maisha ambayo nimeishi. Tokea nazaliwa nimekuwa mtu wa kukataliwa na watu, nimeishi kwenye majumba ya watu kwa kubembeleza. Nataka kujua ukweli ni kwa nini unataka kunioa wakati…” Tunda akaanza kulia. “Mimi naona..” Tunda akakwama.

“Unaona nini Tunda? Niambie unachotaka.” “Sijui Net. Naona kama najiingiza kwenye matatizo. Nilitegemea kupata faraja kwenye ndoa, lakini inaanza na vipingamizi vikali! Tena kutoka kwa mtu wa muhimu sana kwako, anayenitangazia vita mpaka kifo chake. Niambie itakuaje? Tutakuwa na ndoa ya namna gani?” Net akavuta pumzi kwa nguvu, akakaa vizuri na kujiegemeza kwenye kochi.

“Hata mimi sijui Tunda. Sikuwahi kupenda kabla, na wala sijawahi kuoa. Sitakuwa na majibu yote ya maswali yako.” Net akanyamaza kwa muda. Kisha akaendelea. “Unajua umenifanya nijiulize Tunda. Hivi kweli unanipenda wewe au ni kwa kuwa nimetokea tu unanifahamu? Hivi mtu akikuuliza kwa nini unakubali kuolewa na Net, utasemaje?” “Nakupenda Net.” Net akakaa sawa.

“Kweli? Naomba usichanganye upendo, na wewe kujikuta umeangukia mikononi mwangu. Mtu unayempenda huwezi ukawa ukimfanyia hivi. Hii ni mara ya pili kunikimbia Tunda. Tena leo umeniacha katikati ya tafrija yetu, mbele ya wageni niliowaalika kuja kuona nikimvisha pete ya uchumba mwanamke niliyewatangazia nina mpenda. Mimi ndiye nimekuwa mtu wakukukimbilia kila wakati na kukuomba urudi. Mimi ndiye nimekuwa mtu wakupigania haya mahusiano yetu kila wakati!” Net alikuwa amekasirika na yeye.

“Unamuacha Nana, Maya na marafiki zangu waliosafiri safari ndefu kuja maalumu kwa ajili ya hili tukio. Bila kuaga, tena katikati yao!  Huonekani kama mwenzangu unahaja na haya mahusiano hata kidogo. Unanifanya nitilie mashaka viwango vyangu vya uanaume. Labda sijafikia viwango vya mwanaume unayemtaka maishani mwako.” “Hapana Net.” Tunda alijua angebembelezwa, kumbe ameharibu uzunguni.

“Naomba nikuombe kitu kimoja Tunda, tena kabla hatujafika mbali. Pata muda wakufikiria. Nataka ufikirie kama kweli mimi nafaa kuwa mume wako au la. Usiogope kuniambia, nitakuelewa tu.” “Net na..” “Usiharakishe Tunda.” Tunda alitaka kujibu, Net akamkatisha. “Naomba pata muda. Tutaongea zaidi baada ya hapo.” Net akasimama.

“Ukiondoka humu ndani, ujue unaondoka na mimi Net. Hutaniacha nikilia tena. Nimeamua kuwa mke wako, wala sihitaji kufikiria. Niliondoka kuepusha vurugu pale mbele za wageni. Mama hataki kuniona na wewe. Naomba usiondoke tafadhali. Nakupenda na nimeamua kuwa na wewe. Ila naomba nisiwe naenda pale kwa mama yako kwa kipindi hiki. Naomba tumpe nafasi.” Tunda alikuwa amesimama na yeye. Net akarudi kukaa.

 “Kweli nakupenda Net, wala sihitaji kufikiria juu ya hilo. Umekuja kwangu nikiwa sijajiandaa kama naweza kuolewa na mtu kama wewe na mpaka sasa siamini kama utakuwa mume wangu. Naona kama naota!” “Usicheke Tunda! Unanitia wasiwasi bwana! Kila wakati wewe unanikimbia tu!” “Mimi mkeo, Net. Wala huna haja yakunikimbia.” “Wewe ndio unakimbia.” “Napaniki vibaya sana, hasa nikivamiwa na watu kama mama Cote. Huo ndio udhaifu wangu. Nitajirekebisha.”

“Kwani alikwambiaje?” “Haitasaidia hata nikikwambia. Ila nimemuahidi sitamsumbua kwa kufika nyumbani kwake au sitafika mahali ninapojua atakuwepo, mpaka atakapokuwa tayari kuniona.” Tunda akarudi kukaa pembeni ya Net na kuanza kuangalia pete yake.

“Umeipenda?” Net akauliza. “Sanaaaaa! Imetoka kidoleni kwa bibi Cote! Usinitanie kabisa. Nahisi nipo ndotoni. Sasa unajua kinachofuata nini?” “Sijui.” Net akajibu huku akicheka. “Na wewe uende ukweni.” “Wapi tena? Nishamuona baba na akanipa baraka zote.” “Ujue siamini! Baba atakuwa amefurahi sana!” “Sana. Ila nimemuhurumia. Alitamani kuwepo. Na anaonekana mgonjwa. Umefikia wapi maswala yake?”

“Naona nimepata wakili mzuri kweli. Anafanya mambo kwa haraka! Ameshaanza kukusanya uthibitisho. Yaani hii ni siku kama ya 10 tokea aanze, ameshakwenda kuzungumza na baba zaidi ya mara tatu, ashakata rufaa. Ijumaa alinipigia simu kuwa anashugulikia jumanne apate ruhusa ya kwenda hospitalini. Japokuwa kampuni yao inadai pesa nyingi, lakini naona wanafanya kazi kwa ukweli.” Tunda akaendelea.

“Pesa ya kodi ya hapa nimemuomba mwenye nyumba anisubirie kidogo. Ili kuwalipa wao wanasheria kwanza, ili wajue ninampa baba kipaumbele, wafanye haraka. Na nimelipa kodi yote ya kule ofisini. Ili mwenye nyumba asinitoe. Pale napapenda. Ni rahisi watu kufika, halafu pako wazi, barabarani. Panajiuza penyewe. Sitaki kupapoteza kwa sasa. Kwa hiyo kuhusu baba, naona jumanne, anaweza kupata ruhusa ya kwenda kutibiwa. ” Tunda akamalizia hivyo.

“Cha kwanza nakupongeza Tunda. Umekuwa na malengo unayohakikisha unayafuatilia. Unanifanya nijisikie vizuri.” Tunda akacheka. “Najitahidi hivyo hivyo.” “Unafanya vizuri sana. Halafu kuhusu hapa, kwani unampango wa kupafanyia nini baada ya kufunga ndoa?” Tunda akacheka tena, nakuzungusha pete yake ya uchumba.

“Bado siamini!” “Ndio tunatakiwa kufikiria hilo.” “Kwani ulitaka tufunge ndoa lini?” “Haraka iwezekanavyo.” Tunda akatulia kidogo kama anayemtaka afikirie zaidi. “Au wewe ulifikiriaje?” “Mimi tena! Sina kipingamizi Net. Nasubiria kwa hamu kweli!” “Kwani kodi ya hapa inaisha lini?” “Mwisho wa mwezi huu. Nilitakiwa kulipa kodi tokea tarehe moja.” “Basi mwambie mwenye nyumba kuwa utahama. Unaomba umlipe ya mwezi mmoja mwingine, lakini unaweza usikae mpaka huo muda ukaisha.”  “Akipata mmpangaji kabla hatujafunga ndoa?” Tunda akauliza.

“Cha kwanza nitajitahidi kuhakikisha tunafunga ndoa haraka. Nitazungumza na mchungaji wako na wangu. Japo walishatangulia kuniambia, ni lazima itangazwe mara tatu. Inamaana kama tukifanya kwa haraka, wataanza jumapili ijayo. Zipite jumapili tatu, Mungu akisaidia pakawa hakuna kipingamizi, basi, jumamosi ya nne yake, itakuwa harusi yetu.” Tunda akacheka kama asiyeamini.

“Ikitokea kuna jambo hapo katikati, tukashindwa kuona kwa muda huo, sitashindwa pakukuweka mpaka tufunge ndoa.” Tunda akajisikia vizuri sana. “Asante Net. Ninafuraha yakupitiliza.” Net akacheka. “Karibu.” Akajibu Net.

“Lakini Net, baba akitoka jela, nilitamani kuishi naye kwa muda. Angalau arudie hali yake ndipo nimtafutie kitu chakufanya awe na maisha yake.” “Na mkewe?” Net akauliza. “Kwa jinsi alivyonisimulia, ni kama yule mwanamke alimwambia waachane siku tatu kabla ya hukumu. Akambembeleza wasiachane, amsamehe kwa lolote linalomsababisha kumuomba talaka. Lakini anasema siku moja kabla ya kwenda mahakamani, mama Chale, alimwambia ameshafuatilia mipango ya talaka. Hamtaki tena. Hata kama atashinda kesi, akitoka mahakamani asirudi tena nyumani. Aendelee na maisha yake. Na baba anasema hajamona tena tokea afungwe.”

“Alishajaribu kumtafuta kwa simu?” “Hizi ni jela za Tanzania Net. Anamtafutaje? Ila anasema alipokuwa mahakamani siku ile, alimwambia dada yake, mama Sera, akamwambie Mama Chale kuwa amehukumiwa kifungo na atakuwa Segerea. Hakumtafuta mpaka juzi ijumaa mimi nazungumza naye, baba hajamuona wala kumsikia.” Net akanyamaza.

“Sitaki akitoka jela ajikute peke yake mtaani.” “Hata mimi nisingetaka iwe hivyo. Tutajua chakufanya siku hiyo. Ila kwa sasa chamuhimu ni kumkazania huyo wakili wake, ahakikishe anakwenda kutibiwa. Amedhoofu sana. Halafu nilimshika ni kama anahoma.” Tunda aliinama na kunyamaza.

“Atakuwa sawa tu. Jumanne sio mbali. Nikuwatafuta tena kesho na kuweka msisitizo.” “Nitampigia tena kesho kujua amefikia wapi. Na nitakwenda kumuona baba kama nitaruhusiwa kumuona. Nijue anaendeleaje.” Net akamsogelea na kumbusu kichwani pale alipokuwa amekaa na kuinama kama anayefikiria. “Asante.” Tunda akamgeukia na kumshukuru. Akampa tabasamu.

“Unafikiria nini tena? Mbona hilo la baba ni kama limekaa vizuri?” “Kuna sehemu mbili nataka kwenda.” “Wapi?” Net akauliza wakati anamvuta mkono. Akaubusu. Tunda akacheka. “Kwa shangazi. Huko ni lazima twende wote, kama kuwaringishia tu kina Sera, lakini nitajidai nimeenda kuwashukuru kwa kunipa hifadhi wakati ule mpaka nikakutanishwa na wewe.” Net akacheka sana.

“Tunda!” “Oooh kabisa Net. Walijaribu kuzuia baraka zangu, lakini ona Mungu alivyohakikisha mpaka nimepata, japo kwa kuchelewa!” Tunda akamuonyeshea Net kidole chake chenye pete. Wakacheka.

“Usifanye mchezo na Mungu wangu! Hatatulia mpaka aone napata aliyonikusudia.” “Sasa mbona unatingishwa na mama kama unalijua hilo?” “Mama yako yule habari nyingine. Kwanza ujue ni kama kwake inabidi kujirudi kidogo. Nimemuumiza yule mama. Anahaki. Tuendelee na sehemu nyingine ninayotaka kwenda. Japo...” Akasita na kumwangalia Net, macho yakagongana, ikawa kama ameamsha kitu kwa Net. Akashangaa Net anamvuta karibu nakuanza kumbusu.

Tunda akaona alitendee haki lile busu. Akapandisha miguu yote kwenye kochi, akamgeukia Net akawa kama amejilaza kwake. Walipeana mabusu ya muda huku Net akimpapasa vizuri, mpaka akamuamsha Tunda, nakuanza mihemo. Ile hali ikaendelea, Tunda akiendelea kupata busu huku akisikia mikono ya Net mwilini mwake nakumfanya azidi kujisogeza. Kasi ikaongezeka, wakaanza kung’ang’aniana kwa uchu na tamaa, kila mmoja anamtaka mwenzake zaidi. Net alipoona na yeye anakaribia kupitiliza, akasimama kwa haraka, akaenda kwenye friji ya Tunda.

“Kuna maji ya kunywa humu?” Tunda akaendelea kuvuta pumzi taratibu huku ameinama kwa aibu akijaribu kutulia na Net mwenyewe akijaribu kutulia huko alipokua. Tunda hakumjibu wala kumwangalia. Akamsikia anafungua friji. Kimya kikazuka. Akamuona anaelekea chooni. Tunda kimya, ameinama palepale sebuleni. Nyumba ikawa kimya kama hakuna mtu.

          “Niambie sehemu nyingine unayotaka kwenda.” Baada ya muda akamsikia akiongea akiwa anatokea chooni. “Kwa mama.” Tunda akatulia kidogo. Net akarudi kukaa palepale kwenye kochi. Akambusu tu kichwani. Tunda akacheka kwa aibu bila hata kumtizama akaona aendelee. “Nataka nikamuombe msamaha, kwa chochote nilichokosea, ilimradi tu yaishe. Nataka kuanza maisha mapya. Hata asiponisamehe, lakini nataka niwe nimefanya upande wangu, hayo mengine namwachia Mungu kama ulivyonishauri.” “Ni uamuzi mzuri.” Tunda akatulia kidogo.

“Nakuonea wivu Net! Unaye mama anayekupigania. Hataki akuone unaingia matatizoni, kitu ambacho mimi sikuwahi kukipata maishani. Hicho tu ndio kitu ninacho muheshimu mama yako. Anakupenda sana.” “Ila natamani ajifunze kuheshimu maamuzi yangu. Naona anavuka mipaka.” “Hapana Net. Yupo sahihi. Sio rahisi kwa mama mwenye upendo wa kiasi kile kwa wanae eti kuruhusu tu, mwanae awe na mtu kama mimi! Haijalishi Net. Niwe nimebadilika au la, bado ni ngumu. Ndio maana naona nimpishe kabisa. Anione pale itakapo lazimu tu, sio vinginevyo. Lakini sijui nifanyaje upande wa mali.” Net akakunja uso.

“Mali tena?” Net akauliza akiwa hajaelewa. “Hata sielewi Net. Ujue mama yako anapokuwa na mimi anapandwa sana na hasira sana. Anazungumza mambo mengi, sijui lipi ni lipi.” “Niambie kuhusu mali. Alikwambia nini?” “Naweza nisipatie sana, lakini ni kama alitamka kuwa sasa hivi nakung’ang’ania wewe simtaki tena Gabriel kwa kuwa wewe una mali nyingi kuliko Gabriel.” Moyo wa Net ulipasuka paa! Walimuonya mama Cote asije zungumza na Tunda mambo ya utajiri unaozunguka hiyo familia ya Cote.

“Umesema nini juu ya mali!?” Net akataka kujua sasa zaidi kile mama yake amesema. Kama ameharibu mpango mzima au bado. “Ni kama alisema nimejua kuwa umeachiwa urithi mkubwa sana na babu yako, na ni kama bibi yako pia akifa, wewe ndio mtawala wa mali zote huko nchini Canada. Kitu kama hicho, sijui! Akasisitiza kuwa siwezi kuwa mtawala kwenye Cote. Yeye ndio anastahili kwa kuwa amehangaika tokea mwanzo kujenga. Akasema hata kama babu yako ndio amelipia kujenga ile nyumba pale anakoishi, au sijui alisema nini, ila amesisitiza uwa yeye ndio amesimamia ujenzi wa ile nyumba kuanzia mwanzo mpaka mwisho.”

“Amesisitiza hakuna Cote hapa nchini bila yeye. Yaani hata wewe upo hapa nchini kwa sababu yake. Kitu kama hicho. Halafu anasema  nakudanganya wewe na bibi yako kuwa nimebadilika. Lakini yeye sio mjinga na wala nisidhani kuwa nimeshinda. Mnanitumia tu.” “Kivipi!?” Net akauliza akiwa hajaelewa.

“Ni mambo mengi magumu hayaelewiki Net.” “Lakini yeye alisemaje? Niambie kile alichokwambia yeye.” “Amesema wewe na bibi yako mnanitumia kila mmoja kwa sababu zenu tofauti tofauti. Vile bibi yako leo alivyonitangaza mimi kama ndiye mama Cote au mrithi sijui wa kiti chake! Wale rafiki zako na Maya wakachangamka sana pale?” Tunda akataka kumkumbusha Net, asijue Net mwenyewe bado yupo kwenye mshtuko wa hilo tangazo.

“Nakumbuka. Ehe?” Net akataka aendelee. “Mimi sikuelewa pale. Lakini yeye anasema ni kwa ajili ya mambo yake anayoyafanya. Ametangaza vile kwa ajili sijui ya watu wa chama anachokiongoza na wakubwa sijui wanaomfuatilia au watu wanaomfuatilia sijui sina uhakika! Lakini amesema amenitangaza mimi malaya ili kuonyesha na kuaminisha ulimwengu kuwa anakubali malaya, au machagudoa kwa kiasi cha kukubali malaya kama mimi kuolewa na mjukuu wake ambaye alikuwa akisubiriwa na kila mtu kujua atamuoa nani!” Net akaumia sana.

          “Haya. Akasema na wewe umenichagua mimi sio sababu ya mapenzi, ila ni sababu kama za bibi yako. Lakini zaidi kumfurahisha bibi yako kumuonyesha unamuunga mkono kwenye hizo harakati za wanawake, sijui kitu kama hicho! Yaani kuoa kahaba, au Changudoa kama mimi ni kumuunga mkono kwenye anachokifanya! Sijui bwana Net! Lakini ni  mambo yanayofanana na hayo lakini sikuelewa vizuri kwa kuwa zilikuwa shutuma nzito, zinazoendana na kweli.” Tunda akaendelea.

“Haya, ukimsikiliza tena zaidi ni kama hata mimi mwenyewe haniamini! Anasema nimekuloga. Nimekuzika makaburini ili nirithi mapesa yenu ambayo mnayo mengi, sijui! Kwa hiyo hatakubali huo utajiri au urithi ukaja kwangu wakati yeye amehangaika sana na kina Cote. Hapo napo aliongea sana Net. Mambo mengi. Sikuelewa na wala sijui katika hilo namsaidiaje.” Tunda ndiye hakuwa ameelewa. Lakini Net akafunguka macho na akili ikapata mwanga, juu ya chuki kubwa ya mama yake kwa Tunda.

Aliumia sana Net, akabaki akijiuliza hili na kujumlisha lile. Akajua mengi yanatokana na mali tu! Yeye akidhani ni mapenzi kutoka kwa mama yake, kumbe analinda mali! Ilimuumiza sana Net. Mama yake alimwambia Tunda mambo mengi ambayo alishaomba familia nzima, wasimuhusishe nayo Tunda, ili yeye Tunda aweze kumtenga Net na mali kama wasichana wengi nchini Canada. Wanaompenda yeye Net kwa kuwa ni Cote.

Net alimtaka Tunda amtizame yeye kama Net kwanza. Kabla ya Nathaniel Cote anayetangazwa na kuabudiwa huko alikozaliwa, aliko bibi yake. Kitu kinachomkera na kuona ni bora kuwepo nchini Tanzania ambapo yupo huru, hakuna anayemfahamu isipokuwa huyo mama yake na kina Gabriel. Alikotoka Net, chochote watakachofanya familia hiyo, ni tukio la kuuza magazeti kitu kinachowanyima uhuru wakuishi maisha yao.

Leo mama yake amemkosea sana, na kumuumiza sababu ya pesa! Tena akiwa amejitoa akimtumikia kwa kiwango cha chini sana akizunguka kumtafutia tenda zilizokuwa zikimuingizia yeye pesa wala si Net. Hakumdai zaidi ya mshahara wake tu. Net aliumia sana.

“Lini sasa tunaenda ukweni?” Tunda akauliza na kujisogeza kwa Net aliyekuwa amepotelea mawazoni akiwa amefunga macho. “Au umebadili mawazo, ndoa hutaki tena?” “Kukuoa wewe, sijambo nililokurupuka Tunda. Mungu alisha niandaa kwa muda mrefu sana. Nakupenda na lazima nitakuoa tu. Lakini siku kama ya kesho, jumatatu nakuwa na kazi nyingi sana, labda twende jioni.” “Sawa kwa kuwa itakuwa jioni, tuanze kwanza kwa mama. Kesho iwe mama tu.”

“Nataka nimalize hili la mama kwanza. Ikiwezekana tuwekane sawa ndipo niende kwa kina Sera. Lakini kwa kina Sera lazima.” “Sawa.” Waliendelea kuongea wakiweka mipango, mwishowe Net akaaga na kuondoka akiwa ameumia sana, Tunda sijue.

Jumatatu!

Siku hiyo ilianza na hekaheka kweli hasa kwa Tunda. Alianzia ofisini kwa wakili wa baba yake. Wakazungumza na kumuhimiza ni lazima baba yake kesho apelekwe hospitalini. Baada yakumsikia mikakati yake na pale alipofikia, akaridhika na kuondoka kurudi ofisini kwake. Siku za jumatatu hawakuwa wakiwasiliana sana na Net zaidi ya salamu ya asubuhi kabla hawajatoka kitandani. Watapeana mipango ya siku nzima, siku inaanza.

Hakuwa amemsikia Net siku hiyo, na yeye akaendelea na kazi zake akiwa na Betty tu, wakiongea hapa na pale. Betty alikuwepo kanisani siku iliyopita. Akataka kuiona kwa karibu pete hiyo ya Tunda. Basi, akaitizama na kuishika. “Umeuchinja dada Tunda!” Pesa huleta heshima. Japokuwa Betty alikuwa mkubwa kwa Tunda bosi wake, aliweka heshima. Tunda alicheka tu.

Kazi ziliendelea, ilipofika mchana Jaz, msichana aliyemkimbia Tunda pale kazini, akarudi kuomba kazi tena. Week ilishapita, hakuwepo kazini, na siku ya jumatano alipokwenda kwenye bible study, hakumsalimia Tunda bosi wake. “Kwa nini unataka kurudi na kwa nini uliondoka Jaz?” Kimya. “Umesambaza maneno mengi machafu kanisani juu yangu.” “Nisamehe.” “Nimekusamehe lakini hapa sitahitaji tena mtu wa pili. Tumeshauriana na mama Penny, tumeona Betty peke yake atatosha. Kwanza ameweza kufanya kazi zote bila shida. Ni kweli hata ukirudi humu, hutakuwa na kazi ya kufanya. Halafu sitaweza tena kukulipa na wewe kwa kuwa nimeamua kumuongezea mshahara Betty, kwa kuwa nimemuona ameweza kufanya kazi zako vizuri bila shida wala kulalamika kama wewe Jaz. Nashauri urudi kwa mama Penny, anafahamiana na watu wengi. Atakusaidia kupata kazi kwengine.” Tunda akamuaga, ikabidi Jaz aondoke. Hata Betty hakuamini kama Tunda amefanya hivyo. Na yeye nidhamu ikaongezeka.

Baada ya miaka mingi, Net mrudisha Tunda kwa mama yake mzazi, Akiwa mchumba.

Ilipofika kwenye mida ya saa 10 jioni, Tunda alirudi nyumbani kwake kwenda kujitayarisha kwa kwenda kumuona mama yake. Wasiwasi ulizidi kumsumbua. Hofu ya kuja kuiona tena sura ya baba Tom, ikazidi kumkandamiza nakutamani kama asiende tena. Baba Tom alikuwa msaliti mkubwa sana kwake. Alimtelekeza akiwa na mimba yake!

Net alifika nyumbani kwa Tunda. Alimkuta ameshajiandaa lakini anawasiwasi sana. “Umependeza sana. Lakini usoni unaonekana una hofu yakupitiliza!” “Nimeshindwa kula siku nzima, namuwaza yule baba. Nafikiria kwenda kuomba msamaha ambao nilikuwa nikisubiri miaka yote kuja kuombwa mimi!” Tunda akaanza kulia.

“Hujui jinsi alivyonitesa, tena bila msaada wa mama, Net.” “Nisikilize Tunda. Unafanya kitu sahihi. Unasamehe kwa ajili ya nafsi yako si kwa ajili yao. Utaona amani utakayopata baada ya hapo. Muachie Mungu atapambana naye. Wewe twende ukafanye kwa nafasi yako.” “Mama akinifukuza?” “Tutaondoka. Wala usiwaze upande wao, twende ukafanye upande wako.” Tunda na Net wakaondoka mpaka nyumbani kwa mama yake Tunda huko mitaa ya Kitunda alipowaacha wakiishi.

Kitunda kwa Mama Tunda!

Tunda alishangaa kukuta familia ngeni kabisa kwake. Akamsalimia mama aliyemfungulia mlango, kisha akaeleza shida yake. “Tunaweza kumuona Mama Tom?” Akaguna yule mama akiwa amesimama palepale mlangoni. “Sipendi usumbufu wa usiku usiku!” “Samahani. Tumechelewa kwenye foleni.” Tunda akajibu kiustarabu. “Sijui kama huyo Mama Tom Yupo! Labda mpite huko nyuma.” Alijibu mwanamke aliyewafungulia mlango, huku akionyesha kidole kuwaashiria wapite. “Asante sana.” Tunda akashukuru na kumvuta Net mkono.

Nyumba ilikuwa imejaa watu asiowafahamu kabisa. Ule usafi aliouacha kwenye ile nyumba haukuwepo kabisa. Kwa kuwa alikuwa akiifahamu ile nyumba, Tunda hakupata shida kutokea vyumba vya nyuma, ambavyo havikuwa vikitumiwa kipindi anaishi kwenye nyumba hiyo isipokuwa chumba kimoja kilikuwa kama stoo na kingine alikuwa akilala mfanyakazi wa kiume.

Na huko uwani nako Tunda alikuta watu wengine.  Alisita kidogo. “Habari zenu?” Wote walibaki wakimtizama. Mara ukagongwa mlango wa nyuma, mtoto akitaka auziwe icecream. Alisimama binti ambaye alikuwa na umri unaokaribiana na Tunda, akaingia ndani na kutoka na icecream. Tunda akabaki ameshangaa.

“Tunda!” Net akamshtua kidogo. “Samahanini jamani. Tunataka kumuona Mama Tom.” Wakatizamana na kucheka. “Na nyinyi pia mnamdai?” Walimuuliza Tunda na Net. “Kama mnamdai muandike maumivu tu. Wenzenu wanapishana hapa! Hivi ni jana tu walikuja kumbeba wanawake wenzake wakampeleka polisi. Kala pesa ya kikoba!” Wakacheka wote kwa kupokezana. Tunda aliumia sana.

“Sisi hatumdai. Mimi ni mwanae na huyu ni mchumba wangu.” Wote wakabaki wametoa macho. “Wewe ndio Tunda!?” Mmoja wao akauliza. “Ndiyo.” Tunda akajibu. “Mama Shangazi! Mama Shangazi!” Mmoja aliita. “Njoo umuone Tunda!” Tunda akabaki ametulia. Alishangaa kuona watu wengine wanatoka nyumba kubwa na wengine vyumbani kuja kumshangaa yeye kama mnyama wa mbuga za wanyama.

“Jamani, kwani Mama Tom yuko wapi?” Ikabidi Tunda kuuliza tu. “Wanae wapo chumba hicho hapo. Anawafungia kama kuku!” Tunda akasogea mpaka kwenye hicho chumba alichoonyeshwa, huku Net akimfuata nyuma.

Akaanza kugonga. “Nani?” Sauti kutoka ndani ikauliza. “We Tom! Ni mimi Tunda. Fungua mlango.” Waliona taa ya ndani imewashwa kisha mtu akachungulia dirishani. “Umesema Tunda, dada Tunda?” “Ndiyo. Ni mimi, fungua usiogope.” “Wewe Tom, mama amesema tusimfungulie mtu yeyote. Shauri yako.” Walisikia sauti ya mtoto wa kike ikimuonya Tom.

“Ni Tunda. Tunda yule dada yetu. Wewe humjui ulikuwa mdogo sana. Tena alikulea. Nimfungulie?” “Sijui.” Walikaa kimya kwa muda. “Kwani mama yuko wapi?” Tunda akauliza. “Ametoka muda kweli! Amesema tusitoke wala kufungua mlango mpaka yeye mwenyewe awepo.” Tom akajibu. “Basi sisi tunaenda kumsubiria nje kwenye gari. Akirudi mama, mje kutuita.” Tunda akashangaa mlango unafunguliwa, kisha Tom akatoka.

“Mbona uliondoka bila kuniaga?” Ndio swali la kwanza Tom akamuuliza Tunda. “Sikujua kama sitarudi tena. Mnaendeleaje?” “Njooni ndani.” Tom aliwataka waingie ndani. Tunda na Net wakaingia kisha akafunga mlango tena. “Aneti amekuwa mkubwa! Njoo unisalimie. Sijui unanikumbuka?” Tunda alimuongelesha yule mtoto wa kike kwa upendo.

“Mimi ndiye nilikuwa nikikulea.” Tunda aliongeza, lakini Aneti hakujibu. “Umekuwa mkubwa Tom! Mnaendeleaje?” “Umependeza sana Tunda, dada yangu!” Tom akajibu. “Asante.” “Huyo ni nani?” Tom akauliza. “Ni mchumba wangu, anaitwa Net.” “Umepata mchumba wa kizungu!? Ndio maana umebadilika Tunda. Anaonekana ni mzungu mwenye hela. Anasikia Kiswahili?” Tunda akacheka. Akakumbuka utundu wa Tom.

“Anaelewa kila kitu. Hapo alipo anakusikiliza na anaelewa kila kitu unachoongea.” “Acha masihara bwana Tunda! Usiniogopeshe. Mbona haongei sasa?” Tunda akazidi kucheka. “We Tom hujaacha utundu tu?” “Mambo yamebadilika dada! Mama amekuwa kama kichaa.” “Baba yako yuko wapi?” “Amefungwa.” Tunda akashtuka sana. “Nini tena!?” Tom akanyamaza, akaonekana kusita.

“Kuna nini Tom?” “Alikuwa akimfanyia mambo mabaya Aneti, halafu alimbaka dada wa kazi.” “Yule niliyemuacha?” “Yule alizaa naye, mama akamfukuza na kuletewa na bibi mtoto mdogo kutoka kijijini. Ndiye aliyekuwa akitusaidia kazi.” Tunda alimwangalia Aneti kwa kumuhurumia sana. “Pole Aneti.” “Hapo bado yupo kwenye matibabu. Tulikuwa hatujui kitu anachomfanyia Aneti, mpaka akaanza kunuka sana.” Tom akaendelea.

“Kumbe alimuambukiza mtoto ugonjwa wa zinaa, mama kuja kumpeleka hospitalini akaambiwa Aneti ameharibika sana na anaugonjwa wa gonorea. Ikabidi asafishwe sana. Alikuwa ameoza. Wakati mama yupo hospitalini amelazwa na Aneti, baba akambaka yule msichana wa kazi. Sasa mimi wakati najiandaa kwenda shule asubuhi, nikashangaa yule mtoto haamki kunisaidia kuandaa chai. Kwenda kugonga, nikamkuta amepoteza fahamu.”

“Ndio ikabidi nimpigie simu mama, baba alikuwa ameshatoroka. Nahisi alimziba mdomo na pua ili asipige kelele wakati anambaka, ndio akapoteza fahamu. Mama akatuma majirani waje wamchukue na kumkimbiza hospitalini. Mambo yakafika polisi, baba akatafutwa na kukamatwa.”

“Hivi hao wote unaowaona hapo ni ndugu zake baba, wametuchukia sana. Wanatulaumu eti kwa nini tulimshitaki baba ambaye anategemewa sana huko kwao. Wanatuambia ni mambo ambayo tungepaswa kuyamaliza kindugu tu. Tangia waje baada ya baba kukamatwa, hawajaondoka tena. Wametufukuza kwenye hiyo nyumba kubwa, lakini mama amekataa kuondoka, ndio ameomba tupewe angalau hiki chumba kimoja wakati anatafuta pakwenda kuishi. Mama amechanganyikiwa kabisa, Tunda. Kazi imemshinda, anakazi ya kukopa mpaka aibu! Kila siku anakuja kudaiwa hapa, tena anadhalilishwa kweli!” Tunda alizidi kuumia.

“Amekwenda wapi sasa?” “Anasema kuna mahali anadai pesa zake. Ni mwezi sasa, anazifuatilia hizo pesa. Nikimshauri aachane nazo tuanze kuhangaika kutafuta pesa kwa njia nyingine, anakuwa mkali kweli. Anatufungia mchana na usiku. Hataki tutoke. Akitukuta nje, utamuonea huruma. Anakuwa kama mwehu. Biashara zote zimemshinda. Anazurula tu mtaani.”

“Sasa na wewe shule?” “Na kwambia siruhusiwi kumuacha Aneti hata sekunde. Nampeleka mpaka chooni. Hataki nisogee hata hatua moja mbali na Aneti. Nikimwambia maswala ya shule, ni kama haelewi naongea nini. Nikikwambia hali ni mbaya, si utani.” Tunda akabaki amepigwa na butwaa. Net alikuwa kimya akisikiliza tu. Akavuta mkono wa Tunda na kuubusu. Tunda akavuta pumzi kwa nguvu nakubaki kimya akiwatizama wale watoto.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Usikose muendelezo kujua kitakachojiri mbeleni...

0 comments: