NILIPOTEA! PART 5 - SEHEMU YA ‘B’.
Kwa Net.
Siku ya tano, Net aliweza kuanza kupata
nafuu hata kufungua macho. Daktari aliyekuwa akimuhudumia swali lake la kwanza
alimuuliza jina lake. “Net.” Akajibu akijaribu kuangalia alipo. “Unajua upo
wapi?” Net akajaribu kuvuta kumbukumbu. Akabaki kimya kwa muda. Akili
ikamrudia. “Tunda!” Akahamaki. “Hapana. Upo hospitalini.” Yule dakttari
mwanamke akajaribu kumsahihisha akidhani anaweweseka.
“Hapana. Naitwa Nathaniel Cote.” Kila
mtu akashtuka sasa na kujaribu kumtizama vizuri. Hawakutegemea kama Nathaniel
Cote wanaomjua wao, awepo hospitalini kwa muda wote huo bila ndugu au hata kama
amepotea, basi isiwepo ni habari inayojulikana kila mahali!
“Oooh my God! Ni Nathaniel Cote!” Nesi
aliyekuwa kwenye chumba hicho pamoja na wauguzi wengine akaongea kwa sauti wote
wakamgeukia yeye. Kilikuwa kikundi cha madaktari waliofudhu na ambao wapo
mafunzoni, wote walikuwa hapo chumbani kwa Net, wanazungukia wagonjwa mida hiyo
ya asubuhi kwa mafunzo pia kwa madaktari waliopo mafunzoni pia.
“Ni nani!?” Mmoja akamuuliza yule nesi
aliyehamaki. Kama anayetaka kuuliza kuwa inatakiwa kumfahamu! Na yule nesi naye
akawa kama anawashangaa ni kwa jinsi gani wanashindwa kumfahamu Nathaniel Cote.
“Cote, Nathaniel Cote!?” Yule nesi naye akawauliza huku akiwatolea macho
kushangaa. “Ooooh! Cote.” Mwingine naye akawa kama amekumbuka. Ukaanza
mnong’ono pale wao kwa wao wakielezeana juu ya familia hiyo ya Cote, nakumsahau
hata mgonjwa mwenyewe.
Cote walikuwa maarufu sana kwenye huo
mji. Kampuni ya Cote hapo nchini Canada, ilikuwa ni kampuni kubwa sana ya
usafirishaji. Ilikuwa ikisambaza mizigo ndani na nje ya nchi ya Canada. Walikuwa
wakiingiza mamilioni ya pesa kwa mwaka. Bado umaarufu wa bibi yake ambao
ulijulikana kimataifa. Kwa hiyo walifahamika sana.
Net akawa anahangaika kuongea, wao
wanaelezana juu ya Cote. Akatoa kile kitu alichokuwa amefunikwa nacho mdomoni
na puani kwa ajili ya kupata oxygen zaidi. Akavuta na mipira iliyokuwa
imebandikwa kifuani na kidoleni vyote akang’oa. Kelele zilizoanza kusikika
kwenye mashine, zikawarudisha mawazo kwa mgonjwa. Wote wakamgeukia kwa mshtuko
wakidhani mashine zinawajulisha amezidiwa au kuna tatizo, kumbe Net alichomoa.
Alipoona wanamwangalia ndipo Net
akawauliza, “Sasa hivi ni saa ngapi?” Akitaka
kujua kwa muda ule bibi yake yuko wapi! Nyumbani au kazini. Alipotajiwa muda,
akaomba apigiwe simu bibi yake ofisini. Hapo hapo simu ikapigwa. Akapokea
sekretari wa bibi yake akawaambia bibi huyo alisafiri safari ya kikazi lakini
anarudi nchini hapo siku hiyo jioni. Ndipo akapewa taarifa za kuwepo Net
hospitalini hapo.
Akapewa azungumze naye Net mwenyewe.
Kwa mshtuko asitarajie kumsikia Net hospitalini, akapokea. “Nana yuko wapi?” Net akamuuliza hivyo ndipo akaamini ni
Net. Akamweleza kuwa bibi yao ni kweli yupo safarini ila anarudi siku hiyo na
dereva anajiandaa kwenda kuwapokea yeye na Maya uwanja wa ndege. Net akamuomba
yule sekretari amwambie dereva anapomtoa bibi yake uwanja wa ndege, ampeleke
pale hospitalini. “Do you need anything, Net?”
Mdada huyo wa kiCanada, akiwa kwenye mshtuko akamuuliza Net, ambaye alishawahi
kufanya naye kazi pia kama anahitaji kitu chochote kwa wakati ule. “No thanks, Claire.” Net akakata simu na kumrudishia simu
yule muuguzi.
Mambo yakabadilika sasa. Hata aina ya
matibabu yakabadilika. Habari zikaenea pale hospitalini kote, kuwa yule mgonjwa
aliyekuwa amepoteza fahamu, yupo kama kwenye koma, aliyeokotwa kwenye baridi ni
Nathaniel
Cote.
Uangalifu ukaongezeka. Akaanza kuangaliwa kwa jicho la pili wakijua ni habari
kubwa. Lolote likitokea kwa kijana huyo itajulikana kila mahali ni uzembe wa
hospitali hiyo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akiwa amepotelea usingizini kabisa.
Akasikia mtu akimbusu kwa kurudia rudia. Harufu ya bibi yake ikaanza kuenea
pale. Bila kufungua macho Net akaanza kulia. Alilia kwa muda. Maya akamnyanyua
mkono na kubusu kiganja chake. “Dokta amesema unaendelea vizuri. Pole baby
boy.” “Nipo kwenye matatizo makubwa sana Nana,
kuliko hivi unavyoniona hapa.” Bibi yake alikua kwenye mshangao. Net
alitakiwa awe kwenye fungate na Tunda, nchini Tanzania. Anashangaa kumkuta Net,
aliyemuacha nchini Tanzania, yupo nchini Canada tena hospitalini!
“Nini kinaendelea!?” Wakajikuta Maya na
bibi yake wakiuliza kwa pamoja. “Mama!” Net aliwaeleza kuanzia mwanzo, mpaka
kufika hapo. “She went too far this time. I will never forgive her for this.”
Alisikika bibi Cote akiwa amekasirishwa na umbali aliokwenda Ritha safari hiyo
kwenye hilo.
“Angefanya chochote kile, au
angenifanyia mimi kitu chochote kile, lakini asingekuingilia kwenye maamuzi
yako yakuoa! Hata babu yako alikupa baraka zake kwa Tunda!” “Mimi niliwaambia
yule mwanamke ni shetani mkasem…” “Usiseme hivyo Maya.” Akamkatisha kwa
kumkataza mjukuu wake.
“Sasa wewe bibi unamtetea nini?
Hujasikia alichokifanya?” “Haijalishi amefanya nini, lakini huruhusiwi kumsema
vibaya mama yako.” “Kwa nini wewe unaruhusiwa kumse…” “Mimi sio mama yangu.
Alikuwa mkwe wangu. Na nilimuheshimu kwa kuwa amenipa nyinyi lakini katika
hili, atapambana na hasira zangu. Lakini kwa sasa hivi, naomba wote tutulie,
mpaka Net apone. Ndipo tuanze kufikiria kitu chakufanya bila kujibu chochote
kwenye vyombo vya habari. Nimeweka ulinzi hapo nje, haruhusiwi mtu yeyote
kuingia kama sio muuguzi wa hapa. Na nimeomba muuguzi yeyote wa hapa, asiingie
humu ndani na simu. Sitaki picha za Net akiwa hospitalini zizagae mitandaoni na
wewe Maya usipost chochote mtandaoni. Tulia tu Net.” Bibi Cote alitoa muongozo.
“Amemfunga mke wangu,
Nana! Nawezaje kutulia?” “Unakumbuka ni nini alikwambia babu
yako kwa kurudia rudia mpaka akiwa hospitalini?” Akamuuliza Net. “Nikiingia kwenye matatizo, kabla sijachukua hatua, au
kupanic, natakiwa kufikiria.” “Okay. So, relax. Huu ndio uwe muda
wakujipanga. Ametengeneza kesi yake vizuri sana. Lazima na sisi tujue jinsi
yakufanya.” Bibi yake akaendelea kumtuliza huku akimbusu.
“Lakini namuhurumia sana
Tunda, Nana! Mimi ndiye nimemuingiza katika shida yote hii. Mimi ndiye nilimtia
moyo na kumwambia ni sawa kuongea chochote pale kanisani. Kitu ambacho
nikifikiria sasa hivi, sioni kama kulikuwa na ulazima huo, Nana!”
Net akaanza kujutia.
“Nisikilize Net. Wakati Tunda anatubu
pale kanisani mbele ya wachungaji na wale wote, alikuwa akitubu kwa Mungu. Wote
mlisimama pale kama wawakilishi wa Mungu. Balozi wa nchi ya Canada, anapokuwa
Tanzania, hakuna anayemtambua yeye kwa jina lake, ila kama Canada. Yupo pale
akiwakilisha Canada. Na ndio maana unapoingia kwenye ubalozi wowote ule, hata
kama ipo nchi ya ugenini, unakuwa umekanyaga ile nchi. Inamaana, kama ni
ubalozi wa Canada nchini Tanzania, ukiingia ndani ya geti la ubalozi wa Canada
haupo tena nchini Tanzania, unakuwa upo nchini Canada. Wanapokosea wafanyakazi
wa ubalozi wa Canada wakiwa nchini Tanzania, wanahukumiwa kwa sheria ya Canada,
sio Tanzania. Unanielewa?” Bibi Cote akamuuliza Net aliyekuwa akilia kwa kuugua.
Net akatingisha kichwa. “Kwa hiyo
ndivyo ilivyo kwa Kanisa. Wanawakilisha ufamle wa mbingu na wale ni watenda kazi
wa ufalme wa Mungu. Ndio maana wanaitwa, watumishi wa Mungu. Tunda alikiri kwa
Mungu kupitia wao. Hakukosea hata kidogo. Na ndio maana Mungu alimsamehe Tunda.
Waliyoyakosea wale watumishi wa Mungu, Mungu atashugulika nao. Waache kabisa.
Watahukumiwa kwa sheria za Mungu.” Yule bibi akaendelea taratibu tu.
“Ila ni kweli namuhurumia mama yako, na
wale wote wanao mzunguka na kumsaidia kumuangamiza Tunda. Tunda ni jukumu la
Mungu kwa asilimia 100, kuliko hata unavyoweza kufikiria wewe Net. Tufanye kwa
upande wetu, lakini nakuhakikishia, Mungu atampigania Tunda. Usiogope, na
tusiache kumuombea kokote alipo, Mungu akumbuke msamaha aliompa, na
akajidhihirishe.” Net alivuta pumzi kwa nguvu. Akafunga macho nakupitiwa na
usingizi asijue Tunda anahukumiwa na makosa mengine zaidi ambayo ni yeye
ameyasababisha.
Mama yake alimwambia hatamshitaki kwa
yale mawili ila la ngono lipo nje ya uwezo wake, anaachia sheria ya Tanzania,
kwa sababu amesaini karatasi za talaka na amekubali kuachana na Net, kumbe
uongo. Net alipoondoka, Tunda akafikishwa kituoni na kushitakiwa kwa makosa
yote, vilevile. Hapo alipolala Net, anajua kosa linalomkabili Tunda ni moja tu,
kumbe amemuacha kwenye matatizo makubwa sana.
Hiyo ilikuwa siku yake ya tano tokea
atoke nchini Tanzania, na Tunda akiwa jela. Alilazwa hapo akiwa kwenye matibabu
makali huku akimfikiria Tunda. Mengi yalikuwa yakiendelea kichwani. Kumuhurumia
Tunda ambaye ni kama alipokonywa tonge mdomoni. Katikati ya penzi zito la
fungate. Wakiwa ndio wanaamka siku ya pili tu! Hawakuwa hata nusu ya hayo
mapumziko yao waliyokuwa wakiyasubiri wote kwa hamu. Ni kama aliyeazimwa tu
huyo Tunda, kabla hajamfaidi, akapokonywa!
Mbaya zaidi, Tunda analiliwa na Gabriel
wanayefahamiana na kushibana vilivyo. Hata kama Tunda alikuwa kwenye biashara,
lazima kulikuwa na hisia. Ziwe za mapenzi au za urafiki tu, hawa watu wawili
wote wakiwa kwenye shida, wakakutananishwa, Net alihofia hapatachukua muda
mrefu kuweka penzi la uhakika si kama lake lenye vipingamizi vingi na vigumu.
Ilikuwa lazima atoke pale hospitalini
na kuhakikisha yeye ndio anayemtoa Tunda jela wala si Gabriel. Alijawa hofu na
wasiwasi uliokuwa hauwezi kuvumilika. Alishaonja penzi la Tunda, akataka
kujenga mzinga kabisa. Na hivi ndoa yenyewe aliambiwa haipo tena, basi
anatofauti gani na Gabriel ambaye alishakuwa na mahusino ya muda mrefu na
mazuri yasiyo na kipingamizi na Tunda?
Akiwa pale kitandani hospitalini, Net
aliendelea kukumbuka mazungumzo yake na Tunda juu ya Gabriel. Hayakuwa
mahusiano ya kawaida. Kwa hakika walishibana vilivyo na walikuwa na wakati
mzuri. Gabriel alijifunua kwa uwazi kwa Tunda si kama yeye ambaye hata Tunda
hakuwa akimfahamu kwa undani. “Ni kweli
siwezi kujilinganisha na Gabriel hata kidogo. Mwenzangu amenipita mbali sana.”
Akazidi kujikatisha tamaa.
“Gabriel
akifanikiwa tu kumtoa Tunda jela, mimi ndio basi tena. Nitabaki kuandika
historia yakuwa na ndoa ya masaa tu.” Net alizidi kukosa raha nakutamani
kutoka pale hospitalini kwa haraka.
Lakini alisisitizwa kuwa mvumilivu
mpaka amalize matibabu ili asije kupata matatizo yakudumu na bibi yake
aliendelea kumsisitiza awe mtulivu, ajipange vizuri ili kusiwe na kushindwa
tena. Net alikuwa akipewa matibabu ya hali ya juu, na uangalizi wa namna yake,
mpaka akapona. Bibi yao ndiye aliyekuwa akimuhudumia bila kuchoka akiwa na
Maya.
Alilazwa hapo kwa siku 9. Bibi yake
akihakikisha hapotezi mwanaume mwingine kwenye hiyo familia. Akifuatilia kwa
karibu, hatua kwa hatu, ili Cote huyo aliyebaki hapa duniani apone. Net ndiye
kijana wa pekee aliyebaki. Hakutaka kosa litokee. Abaki yeye na Maya tu!
Hapana. Net alishika hatima ya ukoo huo wa kitajiri wa Cote. Bila Net, ukoo huo
inamaana utakufa na kupotea. Ni kosa ambalo hakutaka mtu yeyote alisababishe.
Iwe kwa uzembe au bahati mbaya. Alihakikisha mjukuu wake anahudumiwa na
wataalamu tu. Na alihakikisha anamkumbusha Mungu kila siku kuwa, ahakikishe Net
anatoka pale kitandani.
Na kweli Mungu alimsaidia, Net
alimaliza matibabu yake yote aliyopangiwa. Na akapona kabisa. Ndipo akaruhusiwa
kurudi nyumbani. Bibi Cote hakutaka Net atoke akiwa na matibabu yeyote endelevu
nyumbani. Aliongea na madaktari wote waliokuwa wakimtibu hapo kuwa, lazima Net
atoke pale mzima kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku inayofuata baada ya kutolewa
hospitalini, Net alimka akiwa amechelewa kidogo. Akaambiwa bibi yake
alishakwenda kazini. Bila kuchelewa na yeye akajitayarisha na kumfuata bibi
yake kazini. Lengo ilikuwa ni kwenda kuzungumza na mwanasheria wa kampuni yao.
Bibi yake akashangaa kumuona Net pale.
Hakutegemea. Aliingia moja kwa moja ofisini kwa bibi yake. “Nilifikiri leo
utapumzika!” Aliongea bibi yake wakati anatoka kwenye kiti chake na kwenda
kumkumbatia Net. “Siwezi kutulia Nana, wakati mke wangu yupo jela!” “Naelewa.
Acha tumwite Logan tuzungumze naye, tuone atatushauri nini.” Net akakaa mbele
ya meza ya bibi yake.
Bibi yake akarudi kukaa kisha
akabonyeza simu kwa sekretari. “I need to see Logan, right
away.”
Akaamuru bibi huyo akimtaka huyo sekretari amwitie huyo mwanasheria ambaye na
yeye yupo hapo hapo kwenye hilo hilo jengo lao.
Yule kijana alifika bila kuchelewa.
Kikao kikaanza. Alikuwa Net, bibi Cote na yule mwanasheria, Logan. Walikaa
ofisini kwa bibi Cote. Net akamuelezea kila kitu yule mwanasheria bila kuficha
huku yule mwanasheria akiandika anachozungumzia Net. Aliuliza baadhi ya
maswali, mpaka akajiridhisha na habari nzima. Kuanzia ya ajira ya Net kwa mama
yake mpaka hiyo ndoa.
“Tunafanyaje?” Bibi Cote akamuuliza
Logan. “Cha kwanza.” Alianza Logan. “Net anaonekana bado anamaslahi makubwa
sana nchini Tanzania.” “My wife/mke wangu!” Akadakia Net. “Sawa kabisa. Ili
kuweza kuwa huru kuingia na kutoka hapo nchini, nilazima kutengeneza nyuma.
Kule alipoharibu Ms. Ritha.” Akaendelea Logan. “Kwa kufanyaje?” Akauliza tena bibi Cote.
“Kuhakikisha, kila kitu kipo kwa
maandishi. Nikimaanisha hivi, kuanzia mkataba wa kazi. Lini aliajiriwa na lini
alifukuzwa kazi. Tokea anaanza kazi, ni jinsi gani alikuwa akilipwa mshahara.
Majukumu yake na mipaka yake. Ananafasi ipi kwenye ile kampuni. Yote hayo
yalitakiwa yawe kwa maandishi tokea mwanzo, lakini kwa sasa ni kama itakuwa
ngumu.” Kila mmoja akabaki akifikiria.
“Sidhani kama ni ngumu.” Alivunja
ukimya bibi Cote. “Wakati Ritha anaanzisha ile kampuni kule Tanzania, aliisajili
kama ni tawi la Cote la huku, na babu yako ni kama mdhamini wake. Nikimaanisha
ni kama alimfungulia yeye ile kampuni. Kwenye memorandum ya ile kampuni ya
Cote, Tanzania, babu yako alionekana ni mmiliki mwenza kwenye ile kampuni. Sasa
kwa kuwa babu yako ameniacha mimi kama mrithi, na wewe of course, unazo haki
nyingi sana kwenye ile kampuni ya Tanzania, na hata mimi naweza nikatengeneza
ushahidi.” Net akatia wasiwasi. Alijua janja ya mama yake.
“Unafikiri babu yako angeruhusu
ukapoteze maisha yako kule kama anajua hajaweka mambo sawa? Asingekubali!
Pengine alifikiria mbali na kuhofia kitu kama hiki kutokea.” “Labda
alibadilisha Nana! Huwezi jua!” Net alitia mashaka.
“Kwa idhini ya nani!? Hawezi kubadili
mambo kiholela.” “Nana!” Bado Net
hakusadiki. Alijua janja ya mama yake kwa kuishi naye na kumbadilikia waziwazi
akigeuza maneno na nyaraka za muhimu waziwazi ili kujinufaisha na yake.
“Najua umeingiwa hofu Net, lakini mimi
ninauhakika na ninachozungumza. Mpe muda Logan. Atayarishe na kutafuta kila
kitu anachojua kitahitajika nchini Tanzania, halafu mimi mwenyewe na Logan
tutarudi nchini Tanzania kuzungumza na Ritha.” Logan yule mwanasheria akashtuka
kidogo. “Na mimi nakwenda!” “Ndiyo. Au kuna tatizo?” Bibi Cote akauliza kibabe kidogo.
“No ma’am.” Akajibu kinyenyekevu.
“Good! Go back to work.” Akimtaka arudi
kuanza kazi hiyo. “Tayarisha kila kitu unachofikiria tutakihitaji tukiwa kule.
Tafuta na file la kampuni ya Cote Tanzania. Soma kwa makini ujue nini chakujibu
na kukusaidia. Ukiwa tayari, nijulishe tupange safari. Tunakwenda Tanzania.
Nenda kaanze kazi.” Logan akasimama ili atoke. “And Logan!” Kabla hajatoka
mlangoni, bibi Cote akamwita. “Yes Ma’am!” Akageuka Logan. “God’s speed!” Logan
akaelewa kwa haraka sana. Bibi huyo anataka akamilishe kila kitu kwa haraka. “Yes
ma’am.” Akaitika kwa heshima, Logan akatoka nakufunga mlango.
“Nana!” Net akaita kwa upole akionekana
anamawazo. Bibi yake akamwangalia. “Samahani nakusumbua. Lakini nahitaji msaada
wako. Sina jinsi.” “Hata kidogo Net. Mimi nakufahamu.” “Nachukia kukurudisha
safarini tena. Zaidi Tanzania ambako umetoka hivi karibuni na inakugharimu
sana. Pia najua unamajukumu mengi. Lakini nampenda Tunda. Natamani nikae hapa,
nisahau kila kitu. Lakini siwezi. Nilimuahidi ni mpaka kifo.” Bibi yake
akacheka.
Akasimama na kurudi pale alipokuwa
amekaa Net, akambusu kichwani na kumkumbatia. “Usiwe na wasiwasi. Kila kitu
kitakuwa sawa. Lakini nafikiri na wewe unahitaji kwenda kutafuta Certificate of No Impediment. Nitataka kuondoka nayo.” Bado alikuwa
amemkumbatia mjukuu wake.“Nakwenda sasa hivi.”
Na yeye akambusu bibi yake, akamkumbatia kwa nguvu akiwa amekaa, bibi
yake amemuinamia pale kitini. Akamsikia akivuta pumzi mara kadhaa, akasima na
kutoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya kukamilisha kila kitu
anachohitaji Logan, nakujua kitamsaidia kwenye kesi ya Net, bila kupoteza muda,
wakapanga safari ya kurudi nchini Tanzania zikiwa zimeshapita siku 16 tokea Net
aondoke nchini.
Bibi Cote nchini Tanzania TENA.
Bibi Cote alifika nchini Tanzania akiwa
amejiandaa vilivyo akizungukwa na walinzi wake wawili ambao anazunguka nao kila
mahali hapa ulimwenguni na huyo Logan mwanasheria anayejua kazi yake. Alikuja
kibabe, aliyejawa na mamlaka, akikusudia kumkabili Ritha vilivyo. Alikusudia hakuna
atakayesimama mbele ya Net tena, ila yeye mwenyewe Net. Alivaa sura yake ya
uongozi, utajiri wala si kibibi tena. Alikuwa amevaa ule wajihi wake
uliozoeleka kuonekana kwenye majukwaa ya kimataifa, akitetea kile
anachokiamini. Sasa ndiye huyu aliyetua hapo nchini. Akitetea hatima ya ukoo
huo wa Cote. Hakika alijipanga.
Ilikuwa ni safari ya pesa nyingi,
lakini alikusudia kutengeneza jina la mjukuu wake, na akakusudia mpaka
anaondoka nchini Tanzania, awe amesafisha jina la mjukuu wake. Na Net awe huru kuingia
na kutoka nchini Tanzania kwa utajiri wao, bila kuficha uzaliwa wake wa nchini
Canada, na iwe bila msaada wa Ritha tena.
Walifika usiku, asubuhi ya siku
inayofuata, mwanasheria wa bibi Cote, Logan, akapiga simu ofisini kwa mama
Cote. Akaambiwa mama Cote hayupo na wala hana nafasi yakumuona mtu yeyote kwa
wakati huo. Hilo halikumtisha bibi Cote.
Akajitayarisha, akamwambia Logan waende
ofisini kwake bila miahadi. Ni kweli walifika pale, hawakumkuta. Akamuuliza
yule sekretari wake alipo Ritha na anatarajia kuwepo hapo siku gani, akasita.
Baada ya bibi Cote kujitambulisha, ndipo akapewa sasa habari zakushtua.
Aliambiwa mama Cote aliondoka hapo
ofisini, hajulikani alipo. “Kuna tatizo lolote?” Akauliza bibi Cote. “Alikuwa
akimkimbia Gabriel. Nilimsikia akiwa anazungumza naye hapa. Kuna mipango
aliifanya dhidi ya msichana fulani hivi ili..” “Unamaanisha Tunda?” Yule bibi
akauliza na kumshangaza kidogo yule dada ambaye hakuwa hata na taarifa kama Net
alifunga ndoa na Tunda. Ritha alihakikisha ni kosa ambalo hatafanya hata kwa
kuropoka kama hiyo ndoa ilifungwa.
“Endelea.” “Basi Gabriel alionekana
kukasirishwa na kitendo cha mama Cote na Bethy mkewe Gabriel kumfunga Tunda.
Ndio mama Cote akakimbia maana Gabriel alimwambia anakuja kumfuata hapa. Tokea
siku hiyo hajarudi tena, na sidhani kama atarudi. Maana anatafutwa na polisi.
Hivi hapa nimefurahi mmekuja ili mniambie chakufanya na hii ofisi, endapo
hatarudi tena.”
“Kwa nini anatafutwa na polisi?” Bibi
Cote akaendelea kuuliza. “Gabriel alipoondoka hapa majuzi na kumkosa mama Cote,
akamfuata mkewe ambaye alishirikiana na mama Cote kumuweka Tunda ndani. Hayo
yote niliyaona kwenye video iliyokuwa inasambazwa kwenye mitandao.” “Eehe, nini
kilitokea.” “Tena kama ungekuwa unajua Kiswahili, ningekuonyesha hiyo video.
Imeenea sana!” “Mtumie Logan, Logan atamtumia Net. Net atatuambia.”
“Net anaendeleaje? Aliondoka bila
kutuaga wakati..” “Anaendelea vizuri. Unaweza kutuma hiyo video sasa hivi?”
Bibi Cote alimkatisha kwa ukali kidogo. Yule sekretari akajua hakuna utani wala
kupoteza muda hapo. Logan akampa business card yake nakumuomba amtumie kwenye
email, kwani hawakuwa na simu yakutumia pale nchini.
Bibi Cote na Logan wakaaga nakutoka
baada yakuandika namba ya simu ya hoteli waliyofikia na chumba cha bibi Cote.
Walimwambia Ritha akirudi tu, ampigie simu. Akamwambia anaelekea polisi,
akipiga hotelini na kuwakosa, aache ujumbe.
Bila kupoteza muda yule msichana
sekretari wa mama Cote akamtumia Logan ile video, na Logan naye bila kuiangalia
akamtumia Net. Kwani walikuwa na hekaheka wakikimbizana na muda hapo nchini na
bibi Cote alionekana hataki kupoteza hata dakika moja. Alikuwa akitoa maelekezo
mfululizo na Logan akiandika bila kukosea ili asiwe anauliza uliza kama mjinga.
Alikuwa na walinzi wake na Logan hapo
kwenye gari wakati akizunguka hapo mjini. Walitoka hapo kwenye ofisi za Ritha,
wakielekea polisi. Walipofika kituo cha polisi ndipo walipoelezwa kwa mapana
kitu kinachoendelea. Waliambiwa ni tukio la siku mbili zilizopita. Bado watu wapo
kwenye mshtuko, hata Tunda waliyetaka kumtolea dhamana, waliambiwa kwa usalama
wake, hawezi kutolewa. Waliambia kwa wakati huo kila mtu anataka kumuona Tunda.
Kumtoa, ni kuhatarisha maisha yake. Na mama Cote ameanza kutafutwa kuanzia siku
hiyo. Bibi Cote akauliza ni jinsi gani anaweza kusaidia, akaambiwa aachie
vyombo vya usalama.
Yule bibi hakuridhika. Akaomba
kuzungumza na mkuu wa kituo. Kwa ulinzi unaomzunguka pale, vijana wakakamavu
waliovaa suti nyeusi, weupe, wanaoonekana wapo kazini, moja kwa moja akapelekwa
ofisi ya mkuu wa hicho kituo. Yule bibi hakutaka kupoteza muda. Akajitambulisha
na kuuliza kama hapo nchini anaweza kupata wapelelezi, atakao walipa. Ili
wamtafutie mama Cote kwa haraka na garama zake.
Baada ya mazungumzo ya hapa na pale, yule
mkuu wa polisi aliwapa namba za simu za watu ambao wanaweza kuwasaidia japo sio
chini yake ila ni watu wa usalama. Bibi Cote akashukuru na kuondoka ofisini
kwake.
Walitoka hapo nakurudi hotelini akiwa
kwenye mshituko wa kifo cha Gabriel na mama yake. Akajua jambo hilo ni zito
zaidi. Alifahamu hiyo familia kwa karibu sana. Mama yake Gabriel alikuwa kama
Ritha tu nyumbani kwao. Walifika na kuhudumiwa nyumbani kwa bibi Cote kama watu
wa hiyo familia.
Alishaishi na Gabriel kwa miezi kadhaa
nyumbani kwake kipindi wazazi wake waliporudi kuanza maisha tena, nchini
Tanzania. Walimuacha hapo nyumbani kwake, ndipo wakarudi kumchukua. Na kila
Gabriel anapokuwa nchini Canada, lazima afike kwake kumsalimia na kulala hapo
kwa siku kadhaa. Aliumia sana.
Kitu cha kwanza alipofika tu hotelini
akampigia simu Net. Bibi huyo alikuwa na simu ambayo aliitumia nchi au mahali
popote ulimwenguni. Walizungumza zaidi ya lisaa. Net aliumia sana kwa kifo cha
Gabriel na mama yake, zaidi alihuzunika kwa bibi yake kushindwa kumtoa Tunda
kwa dhamana. Ndilo lilikuwa ombi la Net, akamtoe Tunda polisi.
“Wamesema kwa ajili ya usalama
wake, Net. Na ukifikiria ni sawa. Wapo sahihi. Nimezungumza na mkuu wa kituo
kwa muda mrefu sana. Ni kama kwa sasa na yeye anahusika na hicho kifo, mpaka
upelelezi ukamilike. Tayari kwa namna moja au nyingine, anakabiliwa na kosa la
jinai. Japo hakuhusika moja kwa moja, lakini jina lake limetajwa.”
Net alibaki kimya. “Son!” Bibi yake akaita.
“Sijui nifanye nini Nana! Natamani kurudi mwenyewe.” “Niambie kile ungefanya hapa ili mimi nikufanyie Net.” “Sijui! Sasa utafanyaje juu ya mama?”
Net akauliza akisikika sauti ya kulia. “Ndio kitu nilitaka kukwambia.
Nimepata namba za private investigator. Nimeambiwa hao watanisaidia kumtafuta
na kumpata. Nataka wewe ndio uwapigie uzungumze nao, sababu ya hawa
niliozungumza nao, tumetumia muda mrefu sana kuelewa, sababu ya lugha.” “Pole
Nana. Na asante.” “Utanishukuru tukishaweka sawa
haya mambo.” Akamtajia ile namba.
Bila kupoteza muda, Net akawapigia simu
wale watu. Akawaambia wanamtafuta mama Cote. Na wapo tayari kulipia. Wakaomba
picha. Lakini Net akawasihi sana wasisambaze picha za mama yake mtandaoni.
Akawatumia picha moja tu. Akawaelekeza alipo bibi yake, nakuomba anayezungumza
kingereza fasaha ndio aende, ili waelewana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kesho yake vijana watatu walimfuata
bibi Cote pale hotelini kwa mazungumzo. Lakini Net alikuwa ndiye anayezungumza
nao kwenye simu huku akimweleza bibi yake. Bibi Cote alitoa maagizo kuwa
atafutwe, akishapatikana, wasitaarifu
vyombo vya usalama, wampeleke pale hotelini kwa siri bila kuonekana na yeyote,
na wasimwambie wapi anakwenda mpaka yeye mwenyewe aje akutane nao. Aliwalipa pesa
kiasi, wakakubaliana siku watakayomleta mama Cote, watamalizana. Wakaagana na
kutoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alitamani kwenda nyumbani kwa kina
Gabriel, yaani kwa wazazi wake kwa ajili ya kuwapa pole, lakini Net alimkataza
kabisa. Alijua familia nzima itakuwa imewachukia wao. Kitendo cha Gabriel
kumchukia yeye na kumuona adui au msaliti wake, alijua wazi mama yake alilijua
hilo, kwa hiyo hata baba yake alijua kinachoendelea kati yao.
Hakuna kilichoendelea kwenye maisha ya
Gabriel, mama yake asijue. Hata akiumwa kichwa, mama yake alijua. Na kama mama
yake alijua, basi na baba yake pia. Na kwa mkasa ule, lazima baba aeleze ndugu
wote tokea mwanzo mpaka kumfika mauti kijana wao. Kwa hiyo Net alijua kwenda
kwa bibi yake huko msibani, wakati Gabriel alikufa akiwa anamtaja mama Cote
kuwa ni adui yake, na akajua habari zake za kumpokonya mwanamke zitakuwa
zikijulikana huko. Akamsisitiza bibi yake akae mbali kabisa. Atulie hapo
hotelini akisubiria kupatikanika kwa mkwewe basi.
Ritha mbele ya Bibi Cote.
Watu husema pesa huongea popote. Kwa
pesa aliyolipa kwa haraka bila maswali na ahadi ya kulipwa nyingine, siku ya
tatu usiku wakati Net na Maya wakizungumza na bibi yao kwa kutumia skype,
walisikia mlango ukigongwa. Logan alikuwa amekaa kwenye makochi akiendelea
kujibu email na kuwasiliana na ofisi za Cote zilizoko nchini Canada na ndogo
iliyopo nchini Marekani, akamtizama bibi Cote. “Are you gonna open the door?”
Bibi Cote ni kama alimtuma afungue mlango.
Logan akaweka laptop aliyokuwa
akiitumia, akasimama. Net na Maya wakawa kimya upande wa pili. Logan aliuliza
ni kina nani kabla ya kufungua mlango. Mtu wa nje akajibu, lakini Logan
hakuelewa. Ikabidi Net awapigie simu wale wapelelezi waliowalipa. Ndipo
wakajitambulisha kwa Net kuwa ni wao wapo mlangoni ndipo Net akamwambia Logan
afungue. Na wakati huo huo Logan akawa amewapigia simu walinzi wa bibi Cote
chumba cha pili, wote wakafika hapo.
Wakashangaa wanaingia wakiwa wamemfunga
pingu mama Cote. Kimya. Alionekana ameingiwa na hofu ya kupita kiasi. Bibi Cote
akakaa sawa. Ritha alishtuka karibu kuanguka baada yakumuona mkwewe pale.
Wakaangaliana kwa sekunde kadhaa, kisha akawageukia wajukuu zake na kuwaaga. “Nataka kusikiliza Nana!” Maya akasikika. “No Maya.” Net akamkataza mdogo wake. “Fine.”
Maya akaondoka, Net akazima ile komputa hata yeye hakutaka kusikiliza.
“Sikuwa nimekusudia mabaya. Nilitaka
kumuokoa Net.” Ritha alianza kujitete huku akitetemeka midomo. “Save it Ritha!
Just STOP.” Bibi Cote akafoka. Alishakuwa mwekundu na mama Cote alijua
amekasirika. “Logan, mwambie ni nini tunachotaka kutoka kwake.” Wakiwa
wamesimama mbele ya bibi Cote, wale vijana na Ritha mwenyewe, Logan akafungua laptop
yake akaanza kusoma.
“Tuanze kikazi. Nahitaji barua yenye
tarehe ya kweli ya kuajiriwa kwa Net. Na barua au karatasi zinazoonyesha
majukumu yake Net aliyokuwa akifanya, na mshahara aliokuwa akilipwa, na ielezwe
njia sahihi alizokuwa akitumia kupokea mshahara wake. Nitahitaji pia vibali
vyote vya uhamiaji vinavyoonyesha tarehe alizoruhusiwa kuwepo nchini. Mwisho
kwa upande wa ajira yake, nitahitaji barua yakuachishwa kwake kazi. Vyote hivyo
viwe na muhuri wa kampuni na saini yako.” Logan akamaliza na kumtizama Ritha na
bibi Cote.
“Umemuelewa Logan au ungependa arudie?”
Bibi Cote akamuuliza Ritha kibabe. “Ninavyo vyote ofisini kwangu, nimefungia
kwenye safe.” Akajibu Ritha. “Good. Kwa hiyo tukienda sasa hivi, Logan atapata
kila kitu anacho kihitaji?” “Ndiyo.” Ritha alikuwa mnyenyekevu kama sio yeye.
“Okay. Hilo tumemaliza. Kinachofuata,
Logan muonyeshe makubaliano aliyokuwa ameingia na Mr. Cote wakati anafungua hii
kampuni ya huku.” Logan akatoa karatasi kadhaa, nakuanza kumsomea. Yalikuwa
makubaliano ya kuwa, anapokea pesa zote kutoka kwa Mzee huyo kwa makubaliano
kuwa, asilimia 75 ya hisa za kampuni hiyo ni za huyo Mzee na mkewe.
Watakapokufa, Nethaniel Cote ndiye mwenye hizo hisa, na ikitokea chochote kile,
kama Ritha anakufa yeye, au anashindwa kuendesha hiyo kampuni, na wakajikuta
wanaingia hasara, mali zote za kampuni ziuzwe, na kukabidhiwa yeye huyo Mzee
Cote na mkewe, na kama wao hawapo, apewe Net. Logan alisoma kisomi na kifasaha
mpaka akamaliza.
“Umeelewa Ritha?” Bibi Cote akamuuliza.
“Ndiyo.” Akajibu Ritha. “Je, unakumbuka kusaini hayo makubaliano wakati
unachukua pesa kwetu?” Bibi Cote akauliza tena. “Ndiyo lakini hiyo ni miaka
mingi sana iliyopita.” “Kwa hiyo!?” Bibi Cote akauliza. “Mambo mengi
yamebadilika.” “Nini?” Kimya.
“Ritha?” Bibi Cote akamwita kwa ukali
kama asiyetaka kupotezewa muda. “Huwezi kunipokonya mali nilizozihangaikia muda
wote huo! Hata kama ni pesa yenu, nimeifanyia kazi, na nimeizalisha zaidi.” “Sijakudai
chochote mpaka sasa. Na bado
sijakuhesabia pesa tulizokuwa tukikuongezea kila mwaka na jasho au juhudi ya
Net kwenye hii kampuni ya huku.” Kimya.
Ritha akakumbuka pesa aliyokuwa
akipokea kila mwisho wa mwaka kutoka kwa wakwe zake ili kumsaidia kwenye
biashara. Akaona atulie. “Sasa nataka unisikilize vizuri Ritha. Na ninataka
unisikilize kwa makini, kwa kuwa usipokubaliana katika hata moja katika haya,
utaona upande wangu mwingine, ambao nina uhakika hutaufurahia. Umekwenda mbali
sana, na sitakuruhusu. Hasa inapofika upande wa Net, ambaye amejitoa sana
kwako! Ameacha maisha mazuri, ili aje awe na wewe huku! Umewezaje hata
kuthubutu kumfanyia uliyomfanyia!?” “Nilikuwa namlinda mtoto wangu.” Ritha
akajibu kibabe na kuendelea.
“Wewe unawapa kila kitu wanachohitaji
au wanachokutamkia bila kufikiria madhara yake baadaye. Ilimradi wakulilie tu,
hufikirii, unatekeleza. Unawalea watoto wangu vibaya, na hufikirii madhara yao
ya baadaye. Mimi ni mama yao. Naijua Tanzania na watu wake. Najua ni nini
watoto wangu wanastahili na nini hawastahili. Sasa hivi Net anaumia kwa ajili
ya Tunda, lakini najua baadaye atanishukuru tu.” Hapo Ritha akajikaza na
kuongea.
“Niambie ni nini unachomuepusha Net kwa
Tunda? Niambie tu Ritha. Na usinitajie juu ya maisha aliyoishi zamani. Kwa
sababu mimi na wewe tunajua tatizo hapa si Tunda na maisha aliyoishi zamani.”
Bibi Cote akamuuliza huku amemkazia macho.
“Tunda anampendea Net pesa tu.” “Sasa
tatizo liko wapi!?” Yule bibi akamuuliza kwa mshangao. “Watu wote tunapenda
watu kwa sababu tofauti tofauti. Kama inatokea Tunda anampendea Net pesa, na
anamfanya anakuwa na furaha, tatizo liko wapi Ritha? Kwa nini umeshindwa kumpa
nafasi Net na Tunda? Ni nini inakuwa ngumu kwako? Kama Tunda atatapanya pesa ya
Net, wewe inakuhusu nini?” Bibi Cote aliongea bila wasiwasi akimshangaa Ritha.
“Net amejitenga na mali zako. Na wote
sisi anatutangazia kuwa yeye ni mfanyakazi kwako na ndivyo anavyoishi. Akiwa
hapa au kule nyumbani. Hakuna pesa ambayo Net anaipata kwa kupewa tu, kila pesa
inayoingia mfukoni kwake, ameifanyia kazi. Na wote sisi tunajua Net sio mjinga.
Angeweza kuoa msichana yeyote yule, lakini amemchagua Tunda.”
“Hata mimi ningependa au hata babu yake
alipenda kama angemuoa Chloe, lakini Net alishindwa kabisa. Babu yake alitamani
kumuona Net anaoa kabla ya kifo chake, lakini Net alishindwa. Wakati wote na
sisi wote alituambia anampenda Tunda. Ningekuwa na sababu zote zakumlazimisha
ili aoe na babu yake amuone, lakini mimi na babu yake tuliheshimu maamuzi yake
kama tulivyoheshimu maamuzi ya baba yake kukuleta wewe mgeni kabisa kwenye
maisha yetu. Sikuwahi hata kufikiria kama naweza kuwa na mtu mweusi kwenye
familia yangu! Lakini mbona tulikupokea Ritha?” Bibi Cote alikuwa mwekundu na
kuongea kwa hasira.
“Kulikuwa na mabinti wazuri tu.
Waliotokea kwenye familia zakitajiri kule kule Canada. Lakini ulipoletwa wewe,
japokuwa tulishtuka sana, ilitubidi kukupokea tu. Hatukuwa na jinsi, kwa kuwa
ulikuwa chaguo la CJ. Niambie ni wapi tulipokutendea ubaya wowote au
kukuonyesha hustahili kuwa na baba yake Net, CJ?” Kimya.
“Ritha? Sema ukweli. Ni wapi
tulipokuonyesha kuwa wewe hukustahili kuwa mkwe wetu?” Kimya. “Au wewe
ulifikiri ulikuwa wa maana sana kuliko Tunda!?” Yule bibi akamjia juu zaidi. “Tulikupokea
na kukuendelea kukuvumilia mpaka kifo cha Cote bado tulikuvumilia. Kwa mabaya
yako yote. Tena ya ajabu kupita kiasi, hatukuwahi hata kuropoka mbele ya watoto
wako kwa chochote! Ulifikiri mimi ni mjinga?” Kimya.
“Nakushangaa sana Ritha! Narudia tena.
Uliwezaje kumfanyia hivyo Net? Ni uchungu upi huo ulionao kwa Net, mtoto
uliyemtelekeza mikononi mwangu tokea unaishi nchini Canada!? Nani anayejua
uthamani wa Net kati yangu mimi na wewe? Ulitelekeza watoto wako, ulifikiri
mimi ni mjinga kutowaambia ukweli wakabaki upande wako?” Yule bibi alipata
jukwaa. Hakumbakiza Ritha.
“Uliuza kila kitu cha mtoto wetu, bila
hata kufikiria watoto aliowaacha, ukarudi huku na pesa yote. Ulipoharibikiwa
ndipo, ukarudi tena kuomba msaada bila hofu wala aibu ukijua wazi watoto
uliowatelekeza tena tangia wapo wadogo sana, nawalea mimi! Niambie ni lini
tulikaa chini tukakuhoji ni kwa nini uliuza mali zote za mumeo na kubaki na
pesa yote wewe mwenyewe bila kujali watoto wenu au ni kwa nini unatuomba tena
msaada wakati uliondoka bila kushauriana na sisi! Tulijifunza kuheshimu maamuzi
yako.” Bibi Cote akaendelea.
“Tukiwa tunakuletea watoto waje
kukusalimia kwa upendo tu. Ili msipoteze mahusiano, ulipoona Net atakufaa,
ukaanza kumgeuza moyo kwa maneno yako ya ujanja ujanja.” Ritha akashtuka
kidogo. “Ulifikiri nilikuwa sijui hila zako Ritha? Kumbuka mimi ndiye
niliyemlea Net. Akiongea jambo, najua ni yeye au ni mtu mwingine anayeongea
kichwani mwake.” Ritha akatulia.
“Ulipoona tumekuza kijana mzuri ambaye
atakufaa kwa maendeleo yako ndipo ukaanza kumchota akili taratibu huku
ukimdanganya kwa upendo wa kimama ambao haujawahi hata kuwa nao kwa watoto wako
Ritha! Ukafanya hivyo mpaka ukafanikiwa kumbadili malengo Net, akaamua kuja
kuishi na wewe huku wakati ulijua wazi tulijitahidi kuwekeza kwake ili aje awe
mtawala wa Cote. Lakini ukatuzunguka!”
“Ulifikiri hatukujua hila yako!?
Ilituumiza sana. Tulijua unakuwa mbinafsi, unashindwa kufikiria maisha yake ya
baadaye. Lakini tulinyamaza tu, nakumpa baraka zetu. Ulifikiri sisi ni
wajinga?” “Kwani na huku si alikuwa akifanya kazi?” Ritha akajibu kwa kiburi.
“Unaongea nini Ritha wewe? Umelewa?
Wamekutoa baa hawa vijana!?” Yule bibi akasimama akitetemeka hasira. Ritha
akarudi nyuma kidogo, wale waliomleta wakamsukumia mbele kwa bibi Cote. “Umemfukuza
Net hapa nchini ukimpa makosa kama mtu baki tu! Unamuondoa hapa kama mfanyakazi
wa kawaida! Unamtupia hati yake yakusafiria na tiketi bila hata sweta! Unajua
alizimia uwanja wa ndege, polisi ndio walimpeleka hospitalini?”
“Alilazwa Net kwa siku 9, kwa kumtoa
hapa kama mwizi wakati ni mtoto wako, aliyekuwa ameacha kila kitu kwa ajili
yako! Unamtoa katikati ya mapumziko akiwa na mkewe, humuogopi Mungu, Ritha?”
“Uliwezaje kumtoa kwenye mapumziko
aliyokuwa akiyasubiria miaka yote hiyo na wote tunamjua jinsi Net
alivyomwaminifu mbele za Mungu hata kwetu! Ulitaka Mungu akupe kijana wa namna
gani?” Ritha kimya.
“Sasa, nataka unisikilize na ujue
nataka utekeleze kwa haraka ili niweze kuondoka hapa nchini. Wewe unajua kuwepo
kwangu hapa ni kiasi gani napoteza wala sio kuongeza. Na kinachoniudhi zaidi ni
wewe Ritha ndiye unayesabisha haya yote ukiwa unajua ukweli wa kila kitu! Huna
tofauti na Tunda ulipokuja kwenye maisha yetu. Hukuwa bikra wala tajiri.”
“Hukuwa mkamilifu, na wala hukuwahi
kuwa mke mwema kwa CJ, mimi na baba yake tulijua uchafu wako wote, lakini
tulinyamaza kwanza kwa kuwa CJ alikuwa mgonjwa pili kwa ajili ya Net na mdogo
wake.” Hapo Ritha alipooza sana. Hakujua kama mkwewe alikuwa akijua kwa undani
kile kilichokuwa kikiendelea na mumewe.
“Sasa nataka umuache Net, na uheshimu
maamuzi yake. Hiyo ni moja. Unanisikia Ritha?” Kimya. “Sikutanii Ritha na
sitarudia kuwa na mazungumzo ya namna hii na wewe. Hii ni mara ya kwanza, na
hesabu ni onyo. Na ndio maana upo hapa
na wala sio kituo cha polisi ambako waliniambia unatafutwa kwa kusababisha kifo
cha Gabriel.”
“Sijamuua Gabriel.” “Hiyo ni juu yako
na vyombo vya usalama. Hainihusu, ila mambo ya Net ndiyo yananihusu. Ukishindwa
kufanya ninayotaka ufanye sasa hivi, hawa vijana wanakutoa hapa na kukupeleka
kituo cha polisi.” “Huwezi kufanya hivyo. Mimi ni mama yake Net na Maya.”
“Lini umelikumbuka hilo?” “Mimi najua
hivyo siku zote na ndio maana ...…” “STOP! Just stop. Sisi wote tunajua ukweli
juu ya malezi ya hawa watoto. Nimekuachia Net kwa miaka michache tu,
umemrudisha kwangu nusu mfu. Kwa hiyo nyamaza na unisikilize.” Ritha akatuli.
“Nataka ufanye yafuatayo, moja, kaa
mbali na Net, na usijihusishe na maamuzi yake. Usimtafute mpaka yeye atakapo kutafuta.
Mbili, ninataka nyumba ya Net, irudi kuwa ya Tunda.” Ritha alishtuka sana.
Akatoa macho. “Haiwezekani!” Akakataa. “Niamini mimi Ritha, utafanya tena kwa
maandishi. Na iwe leo. Uandike na kumkabidhi Logan kuwa nyumba ya Net au kama
ulivyomwambia Net ni ya kampuni ya Cote, inakuwa ya Tunda kuanzia tarehe
aliyoamua Net. Nitataka saini yako na muhuri wa kampuni kwenye hiyo barua. Na
uende kwenye ofisi husika za aridhi ukatoe mkono wako kule, uache waendelee
kushugulikia kubadilishwa kwa hati.”
“Huna nafasi ya kukataa katika hilo kwa
kuwa wote tunajua ile nyumba ni jasho la Net. Alikataa mtu yeyote kumsaidia
kuijenga ile nyumba. Hukuweka pesa yeyote ile kwenye ile nyumba. Anavyoamua juu
ya ile nyumba, mimi na wewe haituhusu. Unanielewa?” Kimya.
“Tatu, nataka umkabidhi Logan, karatasi
zote za talaka ulizomsainisha Tunda na za ndoa ulizochukua. Nne, nataka picha
na video zote za harusi ya Tunda na Net. Tano, nataka pete zao za harusi na
usithubutu tena kushika pete yangu ya uchumba. Nilimkabidhi Net, amvalishe
Tunda. Nina maana yangu. Usiwahi wala kuthubutu tena, kujaribu kunisahihisha. Iwe mwisho.” Ritha kimya.
“Sita na mwisho kabisa, achana na Tunda
kabisa. Umenielewa Ritha?” Kimya. “Namaanisha hivi, ushahidi wote ulionao dhidi
ya Tunda, nataka umkabidhi Logan na umpigie simu huyo aliyekusaidia kuprint
mawasiliano yote ya zamani ya Tunda, umwambie unampa tena kazi ya kufuta kabisa
mawasiliano yote yazamani ya Tunda na yasiwahi kuonekana tena hapa duniani.”
“Kama vile dhambi zake zilivyofutwa
huko mbinguni, ndivyo utakavyohusika wewe kuhakikisha unanipa hayo mawasiliano
uliyokwisha printiwa na kufutwa ili yasiwahi kuja kuonekana tena. Kisha
utakwenda kufuta kesi yake polisi.” “Huwezi kuniamrisha kitu chakufanya.”
Akajibu Ritha kijeuri.
“Wote tunajua kuwa NINAWEZA. Na ndicho
ninachofanya sasa hivi. Na ninataka hayo yote uyafanye usiku huu. Tunatoka wote
sasa hivi, ukakamilishe hayo yote. Leo kabla ya kesho. Na ukimaliza hapo,
hutaniona tena kwako, na upo huru kubadilisha jina la kampuni kuwa lako. Andaa
karatasi unazotaka nisaini, mtumie Logan, akiridhika zipo sawa, nitaidhinisha
na kukiri kuwa nimekuruhusu mali zote za Cote, kuhamishwa kwenye kampuni yako.
Lasivyo nitahitaji kila dola ya Cote iliyowahi kuingia kwenye mfuko wako.
Inamaana nitakufilisi vibaya sana, na utaishia jela. Logan anayo orodha ya kila
pesa tuliyowahi kuwekeza kwako. Sasa nataka kujua, ni nini uamuzi wako? Hao
vijana wanakupeleka polisi au ofisini kwako utukabidhi vitu vyote nilivyo
kutajia?” Kimya.
“Kwa usemi mwingine ninaotaka
kukwambia, kwa namna moja au nyingine, nitapata vyote ninavyovitaka kutoka
kwako. Iwe kutoka kwako kwa hiari au kwa kutumia vyombo vya sheria. Ila nataka
ujue tu, nitakapokushitaki mimi, nakutoa madai yangu, nitaidhinisha mali zako
zote mpaka kijiko chako, apewe Tunda. Kitu ambacho hutaki na ndicho
kimekufikisha hapo ulipo.” “Twendeni nikawape.” Baada yakusikia hivyo Ritha
akakubali kwa haraka sana. “That’s what I thought!” Bibi Cote alisikika kibabe,
akimkejeli Ritha.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Walifika ofisini kwa Ritha usiku huo
huo. Walikuwa wale wapelelezi wa kitanzania waliolipwa kumkamata Ritha, walinzi
wa bibi Cote, bibi Cote, Logan na Ritha mwenyewe. Moja kwa moja mpaka ofisini
kwake, akafungua Safe yake. Akaanza kutoa mikanda ya video na picha. Ikiwa hata
hazijakuwa print. “Mkabidhi Logan. Yeye atakwambia ni nini umpe.” Akamgeukia
Logan na kumwita. “Logan!” “Yes ma’am!” “Hakikisha una kila kitu kabla
yakuondoka hapa.” “Yes maam.” Akajibu Logan kwa heshima. Kisha akamgeukia mama
Cote.
“Kwa kuwa tumeanzia kwenye maswala ya
ndoa, nataka uhakika kama hizi ndizo picha zote na video?” Logan akamuuliza
Ritha. “Ndiyo. Kwani wewe unafikiri nini?” Ritha akamjibu Logan kwa hasira.
“Okay. Naomba na nyaraka zote za ndoa
yao.” Logan akaendelea akiwa ametulia bila jazba. Ritha akatoa, na kuzitupa
mezani. Logan akaziokota na kuanza kuzisoma huku akiangalia kwenye laptop yake
kama anayehakikisha kitu, kisha akamtizama mama Cote. “Hujanipa za Net’s wife.” “Tunda sio mke wa Net, hawakuwa
wamekamilisha mambo mengi sana na ndoa yao sio halali. Usi..” “Ritha! Ritha!”
Akaita bibi Cote. Ritha akamgeukia.
“Hayakuhusu kabisa. Mpe kile
anachokitaka Logan. Now Ritha.”
Akaamuru bibi Cote. Ritha akarudi kwenye safe tena. Kumbe alifanya makusudi
kutompa, akidhani Logan ni mbambaishaji, hatajua. Akatoa hizo nyaraka
zilizokuwa na picha za Tunda, safari hii akazitupa sakafuni kabisa. Logan
akaziokota bila kinyongo. Akasoma huku akihakiki kwenye laptop yake. Kisha
akaziweka pamoja na kuweka kwenye faili lililokuwepo kwenye mkoba wake.
“Umeridhika?” Bibi Cote akamuuliza
Logan. Logan akaendelea kusoma. “Naomba mawasiliano yazamani ya Tunda.” Logan
akamtizama Ritha. “Nimelipia pesa nyingi sana kupata haya mawasiliano. Kwa
hiyo…” “Acha kumzungusha Logan. Wewe mpe kila anachokihitaji.” Mama Cote
akafikiria kidogo, akarudi kwenye safe yake, akatoa bahasha iliyokuwa na
karatasi. Akaanza kuchana pale pale mbele yao. “Hizi ni pesa zangu.” Aliendelea
kuongea huku akichana kwa hasira, kisha akatupa pale sakafuni wote wakimtizama.
“Umemaliza?” Akamuuliza bibi Cote kwa
kumkejeli. Ritha akapiga tena teke vile vipande vya karatasi alivyokuwa
amevichana. “Sasa hivi ndio nimemaliza.” Akamjibu bibi Cote huku akimtizama kwa
jeuri. “Logan! Okota hivyo vipande na uhakiki kama kweli ni yenyewe, halafu
kama ni yenyewe, weka kwenye bahasha.” Logan akaanza kuokota vile vipande vya
karatasi vilivyokuwa vimezagaa pale sakafuni. Alizunguka pale ofisini akiokota
mpaka akamaliza. Nakurudi kukaa.
“Ili kumaliza kabisa upande huo wa
Net’s wife…” “Kwani huwezi kutamka Tunda!?” Bibi Cote akamuuliza Logan kwa
ukali kidogo. Logan akakohoa kidogo. “Okay. Ili kumaliza kabisa upande wa
Tu-n-da, naomba kwanza namba ya simu ya huyo aliyekusaidia kupata mawasiliano
yake, halafu kabla hujapiga, naomba Net ambaye anaelewa lugha ya Kiswahili
awepo hewani akisikiliza mazungumzo yenu unapomuomba kufuta mawasiliano yote ya
mke wake ya zamani ili anisaidie kuhakiki kuwa unachozungumza na hao wahusika
ni sawa na ili Net anisaidie kuwafuatilia baada ya mazungumzo yako ili
kuhakikisha ni kweli walifuta kila kitu.” “Hiyo ipo sahihi kabisa Logan. Good
job!” Hapo Logan akamfurahisha bibi Cote. Akakubaliana na lile wazo.
Akampongeza na kumgeukia Ritha
“Now
Ritha!” Akamuamuru. Ritha akabaki amesimama. “Unanipa au
umegoma?”“Sikumbuki namba zao.” “Usinichezee Ritha!” “Nimekwambia sikumbuki.”
“Basi twende kwa Bethy ambaye mmesaidiana naye kutengeneza huo ushahidi.”
“Bethy yupo polisi!” Ritha akajibu. “Kumbe unafikiri nitakupeleka wapi kama
sitapata kile ninachokihitaji!?” Bibi Cote akamshangaa kwa wazi.
“Najua unajua wazi unatafutwa na
polisi. Upo hapa, sijakufikisha polisi kwa kuwa najua utanisaidia kumuweka huru
Net. Sitakubali visa vyako, viharibu maisha ya Net. Atakuwa huru kuishi
atakapo, kwa msaada wako wewe uliyemuharibia. Sasa kwa kuwa wewe umeshindwa
kumsaidia kuwepo hapa nchini, Tunda atamsaidia. Kwa garama yeyote ile. Net
atapata anachokitaka. Kwa hiyo Ritha, nakuonywa, USINIJARIBU.” “Kama ndio
hivyo, mimi nitazungumza na Net mwenyewe.” Ritha akataka kujirudi.
“Nilikupa hiyo nafasi, ukashindwa
vibaya sana. Ulikuja kumtisha Net mbele yangu. Nikanyamaza nikijua ni hasira
tu, utajirudi. Lakini unaonekana huna hasira, umekusudia kumuharibia maisha
yake. Na kwa kuwa mimi nipo, sitakuruhusu tena Ritha. Kuanzia sasa kila kitu
kwa wale watoto utakifanya kupitia mimi na ninakuonya, USINIJARIBU.”
“Sasa kwa mara ya mwisho, mkabidhi
Logan mawasalino ya watu wanaohusika na mambo ya mtandao na uwapigie baada ya
Net kuwa hewani.” Akachukua kikaratasi
na kuandika ile namba. Akaacha pale pale mezani. Logan akasimama na kwenda
kukichukua.
Akampigia simu Net, akamueleza kitu
anachotaka afanye, Net akakubali lakini akaomba azungumze na bibi yake kwanza. “Namfahamu mama. Anaweza kutuzunguka wote tukiwa tunamtizama na
kumsikiliza. Naomba umwambie amwambie huyo muhusika, apokee simu yangu kwanza
kabla hajazungumza naye chochote, atuweke kwenye conference call wote ili
niweze kusikiliza mazungumzo yote. Na umwambie mama baada ya kukata tu simu
sasa hivi, amwambie huyo mtu, mimi ndiye nitaendelea naye, sio yeye mama tena.”
Nalo hilo wazo likawa jema.
“Lakini pia nana?”
Net akaita. “Hakikisha pia wakati anampigia sasa hivi ili
kumwambia apokee simu yangu, aweke kwenye sauti ili na mimi huku nisikie
kuanzia mwanzo akimwambia apokee simu yangu kabla sijakata na kumpigia yeye
huyo muhusika ili asije akaongeza neno lolote lile la kiswahi la kutuzunguka
kwa huyo muhusika ambalo nyinyi hamtafahamu.” Net akaongeza akijua
janja ya mama yake, anaweza katika kufikisha tu huo ujumbe mfupi wakati Net
hayupo kewani, akamkonyeza yule mtu kwa neno la kiswahili, ikawa kuzungumza na
Net tena akiwepo ikawa kazi bure.
Bibi Cote akamgeukia Ritha. Akamwambia
afanye kama alivyosema Net. Akataka kubisha, lakini ikabidi tu afanye. Ritha
akatoa simu yake, akapiga namba, akasubiria. Ikiwa inaita kwa sauti tu na Net
akisikia. “Mimi ni mama Cote.” Akajitambulisha. “Bado ninayo namba yako mama. Unataka kutupa deal nyingine? Wewe
mama yetu, safari hii tutakufanyia kwa bei nzuri.”
Net alimsikia yule kijana akizungumza na mama yake kwa utani kidogo. “Safari hii nataka kitu cha tofauti. Na..” Ritha akasita kidogo. Akawatizama bibi Cote, Logan, walinzi
wa bibi Cote. Mmoja alikuwa pale ndani, mwingine nje akilinda. Akawatizama na
wale walioenda kumtoa mafichoni. Akatulia kidogo.
“Nana?”
Akasikika Net akiita. “Why is she quet!?” Akauliza Net na kumwambia
bibi yake bado hajampa maelekezo yule mtu upande wa pili yakupokea simu yake,
asimruhusu kuongea chochote tena. Bibi Cote akamkazia macho. “Usinitanie
Ritha!” Bibi Cote akamuonya. “Kabla hatujaendelea, kuna namba inakupigia sasa hivi, naomba upokee na
utuweke kwenye conferenze call ndipo tuzungumze pamoja nikwambie chakufanya.
Kisha kuanzia hapo utaendelea na yeye. Mimi sihusiki tena.” Ritha
akaona aendelee tu.
“Mbona unanitisha tena?”
“Usiogope. Hakuna tatizo, ni ulaji mwingine. Tena safari hii watajie pesa
kubwa. Hawa wanapesa.” Ritha akataka kumkomoa bibi Cote. “Haya.
Mwambieni huyo Net ampigie sasa hivi, anawasubiri.” Ritha akaongea kishari.
Bibi Cote akamuuliza Net, ni nini ameongea kwanza. Net akamwambia vile
alivyomshauri yule mtu awatoze pesa nyingi zaidi. Bibi Cote akacheka kwa
kusikitika. Akamwambia Net apige, awepo kwenye hayo mazungumzo. Net akakata
huku kwa bibi yake, akampigia yule mtu aliyetoa mawasiliano ya zamani ya Tunda.
Walipokuwa wote watatu na bibi Cote
kusikia sauti ya Net upande wa pili ndipo alipomruhusu Ritha kuendelea
kuzungumza na yule kijana. Simu alikuwa ameweka mezani. Bibi Cote alimkatalia
hata kuigusa tena simu yake mpaka baada ya hayo mazungumzo yao watatu na Net
akiwepo.
Walimsikia Net akijitambulisha kwa yule
muhusika. Ndipo mama yake akaendelea. “Unakumbuka yale mawasiliano ya
yule mala..” “Nilikuonya usimtukane mke wangu.” Net alisikika tena. “Jina lake ni Tunda. Huwezi kutamka, niache mimi niendelee mwenyewe
katika hili. Kata simu.” Net akasikika akiwa amekasirika sio
kubembeleza tena. Bibi yake akasimama. Akamuuliza Net kama kila kitu kipo sawa.
“Sitaki amtukane mke wangu,
Nana. Amwite jina lake. Akishindwa kuzungumza aache.”
Akajibu Net kuonekana amekasirika. “Safari hii nataka ufute kabisa
yale mawasiliano uliyotupritia mimi na Bethy. Isiwahi kuja kuonekana tena,
popote.” Akaendelea Ritha bila kumjibu mwanae upande wa pili au yule
bibi aliyekuwa amemsimamia pale kwa hasira.
“Kwa nini tena mama yangu? Au…”
“Wewe usiulize maswali mengi, watajie garama yake, basi.”
Akamtajia garama yote. “Ukipewa hiyo pesa, ni lini utakamilisha hiyo kazi?” Wakamsikia Net akiuliza. “Haitachukua muda mrefu.” Yule mtu akajibu tena, safari hii Net
akaweza kuitambua ile sauti. Akashtuka sana. “Fred!”
Net akaita kwa mshangao. Kimya.
Fred ni rafiki wa Net na Gabriel pia.
Ndiye aliyemsaidia kumwambia Net, alipokuwa amekimbilia Tunda, Kigamboni baada
ya kufuatwa na Ritha ofisini kwake akamtukana sana. Tunda akakimbia asijulikane
alipo, Fred ndiye aliyemsaidia Net kumwambia Tunda yupo Kigamboni. Akashangaa
ndiye anayetumiwa na mama yake.
“Fred!?”
Net akaita tena. “Unazungumza na Net. Mimi sitaki kesi na wewe.
Nitakulipa pesa yako ila naomba unihakikishie utafuta kweli hayo mawasiliano ya
zamani ya Tunda.” “Kwanza naomba uniamini Net, sikufanya kwa nia mbaya. Hii ni
kazi yangu ya pembeni. Kama kuna jambo baya lolote lililotokea kwa hili, naomba
tusameheane.”
“Shida yangu ni hayo mawasiliano
yasije kuonekana tena. Unafikiri unaweza kunisaidia?” “Bila shaka. Tena nipo
kwenye kompyuta sasa hivi. Ukinipa dakika 10 tu, nitakuwa nimekamilisha.”
“Nashukuru. Basi nitakupigia baada ya dakika 10.” Wakaagana.
Net akampigia simu tena bibi yake. Akamweleza walipofikia na Fred. Bibi yake na
Logan wakaridhika. Wakaagana na Net ili wao wamalizane na Ritha.
Net alipokata tu, bibi Cote akamgeukia
Logan. “Umemaliza kila kitu kuhusu Tunda?” “Bado kufuta tu kesi.”“Hiyo
sitaweza. Ni kama mnataka kunifunga mimi ili yeye atolewe! Hapana. Hata kama
mmenichukia kiasi gani, hamuwezi kunifanyia hivyo. Mimi bado ni mama yake Net
na Maya. Hata ufanye nini, huwezi kubadili hilo. Huwezi kunifanya niende
polisi, wakati unajua wazi wananitafuta!” Hapo Ritha akawajia juu na yeye.
“Sasa
utajificha mpaka lini? Kwa nini usiende ili kusafisha jina lako?” “Sio sasa
hivi. Lazima niweke mambo yangu sawa ndipo nitaenda, lakini sio sasa hivi.
Nikienda sasa hivi sijui kama watanikamata au wataamini maneno yangu. Na
wakinikamata ujue ndio mali zangu zote zitapotea. Hapana. Nahitaji muda.
Niambieni nifanye chochote, lakini sio kurudi polisi.”
Bibi Cote
akamgeukia Logan. Logan akajua ndio anaulizwa. Akaendela. “Anaweza asifike
polisi kufuta kesi, lakini pia asitokee siku ya kesi ya Tunda kutajwa, au
asijihusishe tena na kesi ya Tunda ili endapo kunafanyika uchunguzi, au kama
kunafanyika utetezi wowote, namaanisha kama tukiamua kumtafutia Tunda wakili
wakumwakilisha, asipate shida. Kusiwe na ushahidi wowote wakupinga. Na kusiwe
na shahidi wakupinga.” “Hapo ndipo tunarudi kwenye swala la kukaa mbali kabisa
na Tunda. Umeelewa Ritha?” Kimya.
“Ritha?” Bibi Cote akaita kwa ukali. “Hata hivyo sina
muda huo tena. Na sijali tena. Nimejaribu kuwasaidia naona hamtaki.
Kitakachowapata na huyo Tunda, itakuwa juu yenu.” Ritha akaongeza. “Kuthibitisha
hilo na kuhakikisha husahau. Karatasi zako za kubadili jina la kampuni na
kuonyesha wewe ndio mmiliki wa hii kampuni peke yako, sitazisaini mpaka
nihakikishe huweki pingamizi kwenye kesi ya Tunda.” “Hiyo sio sawa. Kama hiyo
kesi ikichukua miaka 10?” Akauliza
Ritha.
“Kwenye ile
video ya Gabriel na Bethy, alisikika Bethy akisema ulihonga ili Tunda ahukumiwe
haraka. Sasa nashauri uongeze hongo ili kesi yake itajwe, kisha ijifute, ndipo
nikusainie karatasi ya umiliki. Lasivyo ujue kwa kadiri Tunda anavyosubiria
jela, ndivyo na wewe utakavyosubiri na ninaweza kuchoka nikaamua kubadili
mawazo.” “Utafanyaje!?” Akauliza Ritha kwa mshangao.
“Utajua pale
nitakapokuwa nimebadili mawazo.” Kisha akamgeukia Logan. “Logan!” Akimaanisha
Logan aendelee. Logan akaendelea. “Tumemaliza upande wa Tunda. Turudi kwa
upande wa barua za kikazi za Net, nitakazohitaji kutoka kwako.” Akarudia
kumtajia zile barua zote. “If I may!” Logan akamgeukia bibi Cote kumuomba atoe
ushauri. Bibi Cote akamruhusu.
“Kwa kuwa
mengi yanaendelea. Naomba atumie barua ambazo mimi nimeandaa mwenyewe. Asome
vizuri tu, na kama akiridhika, aweke saini yake na muhuri kwenye hizi
nilizoandaa mimi.” “Kwa nini!?” Akauliza Ritha kwa mshangao. Logan akamgeukia
bibi Cote. “Naomba iwe hivyo kwa sababu za kiusalama. Hizi nilizoandaa mimi
nimeandaa kiutaalamu, haziwezi kuja kubadilika baadaye.” Logan mwenyewe alikuwa ameshaziandika, ni
mama Cote tu kujaza tarehe na kusaini.
“Nafikiri
umemuelewa Logan. Mtolee asome, kisha akurudishie. Uzipitie tena Logan.
Ukiridhika, akupe wewe mwenyewe muhuri, uweke unapotaka.” Akaongeza bibi Cote.
Ritha akakaa
na kuanza kusoma zote ili asije kuwa na yeye ametegwa. Aliporidhika, bila shida
akaweka saini. Akatoa muhuri na kumkabidhi zile karatasi zote na muhuri. Logan
akazipitia huku akiweka muhuri kwenye sehemu alizotaka yeye. Aliporidhika na
kila kitu. Wakamuona anakusanya karatasi zote na kuzipanga vizuri kwenye mkoba
wake.
Kisha akatoa
bahasha iliyokuwa na pesa, akamkabidhi mmoja wa wale vijana waliokuwa
wamemkamata Ritha. Wakapokea. Bibi Cote akawashukuru, na kuondoka zao.
Wakawaacha walinzi waliokuja na bibi Cote nchini. Mmoja ndani na Logan na bibi
huyo, mwingine nje.
“Inaonekana
umefanya kwa sehemu.” Bibi Cote akaongea hivyo wakati anasimama kuashiria
amemaliza pale. “Kwa sehemu wakati nimekamilisha kila kitu!” Akashangaa Ritha. “Umebakisha
pakubwa ambapo panakushinda. Kaa mbali na Tunda. Nisisikie umetokea mahakamani
siku kesi yake ikitajwa. Nisiwahi kusikia umejihusisha na chochote kinachomuhusu
Tunda. Hakikisha hati ya nyumba ya Tunda..” “Ni ya Net.” Akakanusha Ritha
akionekana ameumia sana.
“Usirudie
kunikatisha ninapoongea Ritha.” Kimya. “Kama nilivyosema. Hakikisha unatoa
mkono wako kwenye hati ya nyumba ya Tunda huko wizara ya aridhi. Namaanisha,
wewe Ritha, uhakikishe hiyo hati inakamilika na
inamfikia Logan kwa haraka ikiwa na jina kamili la Tunda, wala si
kampuni ya Cote.” Kimya.
“Na siku
nyingine ninaporudi hapa nchini kwa ajili ya upuuzi mwingine wowote utakao
fanya, mazungumzo yetu yatakuwa tofauti na haitakuwa hapa. Na ujue wazi, safari
hii ni nyumba imeenda kwa Tunda. Safari nyingine kila kitu ambacho unadhani ni
chako kwa jasho letu, vitakuwa vya Tunda. Usinijaribu.” Akatoka yule bibi,
akafuata Logan, akaja yule mlinzi. Wakamuacha Ritha pale ofisini kwake.
Net arudi nchini Tanzania kwa
ajili ya Tunda.
Baada ya kushugulikia na yeye vitu ambavyo alijua vingehitajika nchini
Tanzania, Net alirudi nchini ukiwa umeshapita mwezi na siku kadhaa tokea
aondoke nchini katikati ya fungate. Alirudi akiwa amejiandaa na kila kitu
ambacho alijua kitahitajika kumtoa Tunda matatizoni. Logan alimkabidhi yeye
kila kitu alichokuwa amekipata kutoka kwa mama yake. Net alitua nchini akapewa
Visa kama mgeni tu anayekuja kutembea nchini Tanzania. Aligongewa Visa ya siku
90. Akajua kwa muda huo kabla hajaaribu Visa yake, atakuwa amemsaidia Tunda.
Alichofanya, nikumtafuta wakili yuleyule
aliyekuwa akifahamiana na Tunda, aliyekuwa akishugulikia kesi ya baba yake.
Alimweleza kisa kizima, akamshauri vizuri tu. Net akarudi kwenye ofisi za
usajili wa ndoa, akakutana na kijana muungwana tu mapokezi. Net hakuonyesha uso
wa tahadhari au wasiwasi. Alimweleza alifunga ndoa na Tunda, lakini hakuwa na
uhakika sana na nyaraka walizosaidiwa kuzikusanya na mwanasheria wao.
Yule muhusika bila hila akalitafuta
faili lao, akaliona. Na kweli halikuwa na baadhi ya nyaraka muhimu. Bila shida,
akapokea nyaraka alizokuwa nazo Net. Yeye mwenyewe akaanza kumpa pongezi Net
kukamilisha faili lake na madhara ya kutokuwa na nyaraka zote. Akamwambia kwa
kufanya vile, amekamilisha faili lake na Tunda, na ndoa yao inafahamika kimataifa.
Wakapeana mikono, Net akatoka pale asiamini kuwa ndio amefanikisha kirahisi
vile bila hongo wala shida yeyote.
Alikwenda tena ofisi za aridhi
kufuatilia hati ya nyumba. Alikuta inashugulikiwa. Akajua mama yake alitoa
mkono wake hapo. Akaambiwa baada ya majuma mawili itakuwa tayari. Hilo nalo
likawa limekaa sawa. Likabakia swala la kosa la uchangudoa tu ambalo yule wakili
alimwambia kama Bethy na mama yake hawakuwa wameficha ushahidi mwingine, ni
kesi ambayo watashinda bila shida.
Net kwa kina mama Penny Tena.
Net akaamua kwenda kuwaona kina mama
Penny na mchungaji ili kuwaeleza kinachoendelea na pengine watakuwa na
chakuzungumza. Alikwenda nyumbani kwao ilikuwa mida ya jioni. Na mchungaji
alikuwepo. Hakuna aliyemchangamkia. Net aliliona hilo, lakini akajikaza.
“Mlifanikiwa kwenda kumtembelea
gerezani?” Akauliza Net. “Tunda hataki kuonana na yeyote yule, Net. Tutakupa
barua alizotuandikia siku ya pili tulipokwenda kumuona. Kwa maana siku ya
kwanza alikubali kutoka. Alilia tu, mwishowe akaondoka. Siku ya pili
tulipokwenda na kuomba aitwe, yule askari magereza akatoka na hiyo barua.
Tuliporudi baada ya siku mbili, hakutoka na wala hakutuma ujumbe.” Akaongea
mama Penny.
“Mimi binafsi nimerudi pale zaidi ya
mara 10. Baba Penny ametoka huko jumamosi hii iliyopita, lakini hakumuona
Tunda. Hataki kuonana na mtu yeyote.” Mama penny akamalizia hapo na kusimama
kwenda kufuata barua alizokuwa amewaandikia Tunda.
Alirudi akamkuta Net amejiinamia kwenye
kochi. Akamkabidhi. Net akaanza kuzisoma. Muda ukazidi kwenda hamalizi na wala
habadili kurasa, yupo kwenye ukurasa ule ule wa kwanza wakati zipo kurasa kama
tano! Mpaka akamtia wasiwasi mama Penny. “Vipi?” “Inabidi kutumia akili ili
kusoma na kuelewa. Naunganisha maneno. Sijui kusoma kiswahili vizuri.” “Oooh!
Lete nikusomee.”
Mama Penny akachukua zile barua na
kuanza kumsomea kuanzia mwanzo kwa sauti ili asikie vizuri na kuelewa. Mpaka
anafika mwisho, Net alikuwa mwekundu kama nyanya. Na kuna sehemu mama Penny
alisoma kilawama kabisa. Kama anaye msisitizia Net kuwa yeye ndiye amesababisha
kila kitu.
“Nitakwenda kujaribu kumuona kesho.”
“Sawa. Kama itasaidia.” Akaitikia mama Penny. Kimya. Kwa hakika Net alijutia.
Akajua kwa asilimia zote yeye ndio amemuingiza Tunda kwenye matatizo na hata
mchungaji na mkewe wanamlaumu. Mapokezi aliyopewa hayakuwa kama zamani.
“Nimejitahidi kurekebisha mambo
kadhaa.” Net akavunja ukimya. Kimya. “Bibi yangu alirudi, akahakikisha anaweka
mambo sawa.” Kimya. “Maswala ya nyumba na ndoa yapo sawa kwa sasa. Kwa hiyo
kisheria Tunda ni mke wangu.” “Inasaidia nini yeye sasa hivi yupo jela?”
Mchungaji aliyekuwa kimya muda wote kwa mara ya kwanza akamuuliza.
“Eti Net?” Net akabaki kimya. “Unakumbuka
siku ya harusi nilikwambia rekebisha mambo ya familia yako kwanza ndipo umuoe
Tunda? Unaona ulipomfikisha Tunda lakini?” “Sikukusudia baba Penny.” Net
akajaribu kujitetea.
“Wewe ulijua kabisa hatari iliyopo
mbele. Ukaamua kumtoa muhanga mwenzio! Umemuingiza kwenye matatizo makubwa,
hata hatujui jinsi yakumtoa! Wewe sasa hivi unalala pazuri, mwenzio yupo
mahabusu! Halafu unarudi na stori ya nyumba na ndoa!? Itamsaidia nini Tunda?”
“Angalau kupunguza hayo makosa mawili.” “Hivi unajua kuwa sasa hivi hawezi
kutolewa dhamana sababu ya kifo cha Gabriel?” Kimya.
“Mimi najiuliza kulikuwa na haraka gani
Net!? Ni nini ulikuwa ukikimbilia nakushindwa kusubiri?” Kwa kuwa Net alijua
wamekasirika. Akaamua asijibu kitu akae tu kimya. Mama Penny akampokea mumewe
kulaumu. “Tunda alifika pazuri sana. Lakini wewe na familia yako mmemuharibia
kila kitu! Unafikiri kwa kashfa hiyo aliyonayo, hata akija kutolewa jela, nani
atampa yeye kazi?”
“Ndugu wa Bethy ndio wamechachamaa,
wanataka Tunda ahukumiwe wala si Bethy. Wanasema Tunda ndiye amesababisha kifo
cha Gabriel wala sio mtoto wao. Wanasema Tunda ameingilia ndoa yao, yeye ndio
amesababisha kutoelewana kati ya Bethy na marehemu Gabriel. Wanasema ndoa yao
ilikuwa na amani kabla ya Tunda. Sasa kwa namna hiyo Tunda hawezi kutolewa kwa
usalama wake.” Net alibaki kimya.
“Mbaya zaidi, alichotumia akili mama
yako. Amekwenda polisi kujisalimisha. Tena akishangaa ni kwa nini Bethy
anamtaja yeye. Akajitoa kwenye vyombo vya habari! Tena akitumia akili sana.
Hakumtaja kwa ubaya Tunda wala maswala ya Bethy na Gabriel. Alichojieleza ni
kuwa Gabriel na Bethy ni kama watoto wake. Walikuwa karibu sana. Alipoulizwa
maswala ya mahusiano kati ya Gabriel na Tunda, akatumia maneno ya ujanja
ujanja, akajitoa na hakutaka kabisa kuzungumzii maswala hayo. Ila akajiweka
katikati kwa kusema kuwa kwenye mahusiano ya ndoa, huwa kuna matatizo.
Akajieleza hapo ili asiharibu kwa yeyote yule.” Mama Penny akaendelea kwa
jazba.
“Alipoulizwa ni kwa nini hakuwa
akionekana wakati anatafutwa. Akajitetea kuwa yeye ni mfanya biashara, alikuwa
kwenye safari za kikazi. Hakuwa akijua anatafutwa na wala hana sababu
yakujificha. Na amejitetea kuwa hata safari zake za nje ya nchi ataahirisha ili
kama atahitajika kwa kusaidia polisi, awepo. Akaji.. ” “Na mimi nilitumiwa hiyo
video yake ya utetezi, mama Penny.” Net akamkatisha, maana aliona anamuumiza
tu.
“Ninachotaka kukwambia Net, nyinyi
maisha yenu yanaendelea kama kawaida. Wakati ya Tunda yamesimama na mmeyaharibu
kabisa. Tunda alikuamini wewe tokea mwanzo. Akijua utamuongoza vizuri. Matokeo
yake ukijua kabisa maisha machafu aliyoishi, eti unampeleka akakiri mbele za
watu ambao hamuwajui uwezo wao wa kiroho!” “Wale walikuwa wazee wakanisa.” Net
akajaribu kutetea tena.
“Sasa mbona walikuwa ni wateja wa
Tunda? Tena ukishajua kabisa hao wazee wenu wa hilo kanisa lenu sio waaminifu
hata kidogo, bado ukamtaka Tunda akiri mambo yake mbele ya watu! Kulikuwa na
umuhimu gani wakufanya hivyo? Ilikuwa ili iweje!? Ayaseme mabaya ya zamani
mbele ya watu ili iweje Net!?” Kimya.
“Kwanza ni utaratibu gani nyinyi
mnautumia kwenye hilo kanisa lenu? Eti watu wanasimama mbele ya watu na kuanza
kutaja dhambi zao!” Akashangaa mama Penny. “Halafu watu wenyewe ndio hao kina
Gabriel, Bethy, mama yako na hao wazee wakanisa wanaokwenda kwa machangu? Kweli
Net!?” Baba Penny akaongeza kwa mshangao.
“Wakati huo nilikuwa sijui kama…”
“Subiri kwanza Net. Usiniudhi zaidi. Wewe kabla ya kumpeleka Tunda kutubu mbele
ya hao wazee wenu, hukujua kama Gabriel alitembea na Tunda?” “Nilijua mama
Penny. Lakini..” “Lakini nini Net? Gabriel ambaye ndiye alikuwa na mfano wa
ndoa yakuigwa hapo kanisani kwenu. Na yeye alikuwa kiongozi wenu, ukajua
alikuwa akizini. Kwenye kanisa hilo hilo ambalo lilifunika dhambi yake, watu
wasijue, ndipo hapo hapo ukampeleka Tunda! Ulijuaje kama mchungaji huyo huyo
aliyeweza kuficha dhambi ya Gabriel ili asiumize washirika, hajaficha dhambi ya
viongozi wengine uliowapelekea Tunda?” Net akainama.
“Umeharibu maisha ya Tunda, Net. Iwe
kwa kutokujua au….” “Alijua baba Penny. Wala usimfiche. Mwambie tu ukweli.
Ameharibu maisha ya Tunda kwa haraka zake na kutokufikiria. Mimi ni mkweli Net.
Na sijui kumficha mtu. Hapo ulipo huna jinsi yakumsaidia tena Tunda. Umepunguza
makosa mawili tu. Je, na la ukahaba? Dhambi aliyokuwa amesamehewa, mmeiweka
mwangani!”
“Ushahidi wa hiyo pia bibi alihakikisha
unafutwa.” “Unajuaje kwa upande wa Bethy?” “Sijui mama Penny. Sijui. Ila nakiri
nilikosea. Naomba na nyinyi mnisamehe.” Net akasimama nakutoka.
Net kwa Tunda.
Siku inayofuata, Net akaenda kujaribu
bahati yake. Alifika mahabusu akajiandikisha kuwa yeye ni mume wa Tunda,
akaomba kabisa aambiwe kuwa mumewe amefika kumuona. Akaingia sehemu ya
kusubiria, akakaa hapo. Alikaa mpaka muda wakuona mahabusu ukawa unakaribia
kuisha.
Akamsogelea mmoja wa askari magereza
aliyekuwa akizunguka zunguka pale. “Mimi ni mume wake Tunda. Nimeomba kumuona.”
Yule askari akamtizama kwa mshangao kidogo. “Mimi ninachojua ni kuwa Tunda
hataki kuonana na yeyote yule. Nina uhakika ujumbe ameupata ila hataki kuonana
na wewe. Hajataka kuonana na yeyote yule tokea afike hapa. Wala wewe si
wakwanza.” Net akarudi kukaa mpaka muda ukaisha kabisa. Akaondoka.
Kesho yake akarudi tena. Safari hii
akarudi na barua. Akajiandikisha, akaomba aitiwe Tunda na apewe hiyo barua.
Akaenda sehemu ya kusubiri. Akakaa hapo mpaka muda ukaisha tena. Tunda
hakutokea. Siku inayofuata akarudi na kadi. Akafanya kama jana yake. Akakaa
hapo mpaka muda ukaisha tena, Tunda hakutokea. Akamuomba mmoja wa askari
ampelekee Tunda ile kadi. Akaondoka.
Alifanya hivyo zaidi ya mara 7. Anafika
hapo gereza la Keko, anajindikisha jina, nakusubiri bila mafanikio yeyote.
Alikuwa akirudia rudia kuomba wale askari warudi kumwita Tunda, lakini hakuwa
akipata majibu. Angalau mama Penny na mumewe walipata barua, lakini Net ilikuwa
kimya. Hakupata ujumbe wowote ule. Akapumzika siku mbili, akarudia mchezo uleule
bila mafanikio.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tunda bado hajahukumiwa. Japokuwa makosa mengine yamefutwa, lakini
bado yupo na kosa hilo la biashara ya ukahaba. Bado yupo rumande, na amekusudia
kuangamia peke yake. Amekataa kumuhusisha yeyote yule. Nini kitatokea? Usikose muendelezo...
0 comments: