NILIPOTEA! PART 6 - SEHEMU YA ‘A’.
Bila kuongeza neno, Tunda akanyanyuka pale alipokuwa amekaa akatoka kurudi chumbani kwao. Net naye hakuongeza, akamfuata nyuma. Walimuacha baba yake Tunda, ameinama tu. Baada ya muda akampigia simu mama Penny. Alimweleza kila kitu. “Nakuja.” Ndilo lilikuwa jibu la mama Penny.
Mama Penny!
Haukupita
muda mrefu sana, saa tatu kamili usiku huo huo, mama Penny alikuwa mlangoni kwa
Tunda hapo hotelini. Akagonga, Net akafungua mlango. “Tunda yuko wapi?”
“Kitandani.” “Haya naomba mvae twendeni.” “Wapi tena!?” “Kwa mama yake.
Asinichezee akili.” “Usiku huu!” Net akashangaa.
“Nakwambia
sasa hivi. Najua anapoishi. Asijifanye amechanganyikiwa!” Akaingia ndani mpaka
alipokuwa amelala Tunda. “Haya, toka hapo kitandani, kausha machozi, twende.” “Amenitukana.” Tunda
aliongea huku akilia. “Ndio nataka nikayasikie matusi yake. Nataka nikamsikie
akikutukana wewe na baba yako, mimi nikiwepo. Yeye si mwehu? Sasa twende.” Net
alibaki ametoa macho.
“Na
wewe unakuja au unabaki?” Mama Penny akamuuliza Net. “Huna lazima ya kwenda.”
Akamwambia tu hivyo alipomuona Net anababaika. Kisha akamgeukia Tunda. “Baba
yako nimemwambia ajiandae, sasa hivi anakuja, twende.” Tunda akaingia bafuni, akatoka
ametulia.
Alimkuta
baba yake amekaa hapo kwenye kochi. “Mimi nipo tayari.” Tunda aliongea kwa
upole. “Haya beba chupa yako ya uji, twende.” Mama Penny alikuwa amesimama.
Tunda
akaanza kucheka. “Hivi sasa hivi unajua inakwenda saa tatu na nusu usiku!”
Tunda alimwambia mama Penny huku akichukua chupa ya uji. “Ndio vizuri, tumkute
nyumbani kwake.” Net akapokea ile chupa, akachukua na kikombe.
“Sasa
naomba mchukue gari yenu. Tukimalizana na mama Tom, mimi huku sirudi.” Tunda
akaendelea kucheka. “Muone na huyu naye! Utajifunza lini kujitetea wewe!?
Watakuja kukufunga tena kama unaishia kulia!” Tunda akaendelea kucheka
taratibu.
“Sasa
twendeni.” “Akikataa kutusikiliza?” Tunda akauliza. “Subutu! Atakusikiliza tu.
Wewe twende.” Wakatoka hapo wakiendesha magari mawili. Mama Penny na Tunda
kwenye gari ya mama Penny, Net na baba yake Tunda kwenye gari ya Tunda. Net
alisharudisha gari aliyokuwa amekodisha. Wakaendelea kutumia gari ya Tunda.
Kwa mama
Tom!
Mama
Penny alimuendesha Tunda, huku Net na baba yake mkwe wakiwafuata kwa nyuma
mpaka Kurasini nyumbani kwa mama Tom. “Nisubiri hapa kwenye gari, nitakupigia
mje. Sitaki kuwaingiza kwenye matatizo. Tukishindwana naye iwe juu yangu.
Nyinyi muondoke kabisa hapa. Kama ni polisi, atakuja kunitoa baba Penny.”
Alimtaka Tunda ahamie kwenye gari alilokuwa amekaa Net na baba yake.
“Naomba
uwe mwangalifu mama Penny bwana. Mimi sina wakunipikia uji.” Mama Penny
akacheka nakuondoka. Hawakuwa wameegesha mbali. Mbele tu ya nyumba.
Aligonga
mara kadhaa, mlango ukafunguliwa. Walimuona akizungumza na mama Tom, kisha
akapiga simu kuwaita. Wote watatu wakashuka, na kumfuata. Wakakaribishwa ndani.
Uzuri Tunda walipokuwa njiani alimsimulia mama Penny kila kitu. Na mama Penny
akampanga Tunda vizuri, mpaka wakafika pale. Wakaingia ndani.
Tunda
aliweza kutambua vitu vyake vyote mle ndani. Makochi, tv, kapeti, kabati la
vyombo. Asilimia 99 ya vile vitu mle ndani vilikuwa vya Tunda. Hata Net aliweza
kuvitambua
“Sasa
sisi hatutakaa sana. Tunajua umechoka, hatutachukua muda wako mrefu, ili
tukuache upumzike.” Alianza mama Penny. Wazi mama Tom alionekana ameshtuliwa na
ule ugeni wa ghafla. “Karibuni.” Alijibu kiuungwana mama Tom, kama sio yeye.
Lakini
Tunda alijua huwa anamuogopa sana mama Penny. Yeye huwa anamuweza. Hata baba
yake akashangaa uungwana huo wa gafla unatoka wapi!
“Sasa
Net na Tunda wanaondoka kesho kutwa. Kabla yakuondoka, nataka, umsikilize Tunda
upande wake wa stori. Hatujali kama utaamini au hutaamini. Hiyo ni juu yako
wewe, ila binafsi nisingependa kujua. Na ili kuwe na usalama hapa, ficha kile
unachokifikiria. Sijui kama unanielewa mama Tom?” Kimya.
“Maana
hili zoezi limekuwa likiahirishwa sana. Alianza nalo Net. Akakubaliana na Tunda
kuja kukueleza na kukuomba msamaha, japo sikuona sababu ya wewe kuombwa
msamaha.” “Alitakiwa..” Mama Tom akataka kumkatisha, lakini mama Penny
akamuwahi. “Nikiongea huwa sipendi kuingiliwa mama Tom. Na nilikwambia ficha
hisia zako.” Kimya.
“Isingekuwa
Tunda, mimi binafsi ningekushitaki. Nakumbuka hili nilishakwambia tokea tupo
pale mahabusu ya Keko. Tukatolewa. Na usifikiri iliishia pale! Kuna mtu
alinifuata baada ya wewe kuondoka, akasema nikushitaki, lakini nikawahurumia
hao wanao wengine. Wewe ni mama mzembe ambaye sijawahi ona. Nyamaza tu
umsikilize Tunda, maana ukianza na mimi, utaishia polisi usiku wa leo.” Kimya.
Mama Penny akaendelea.
“Net
alipokuja na Tunda nyumbani kwako ili kuzungumza na wewe, ndio akakukuta na
matatizo. Tunda akakuchukua wewe na wanao. Tena Aneti akiwa mgonjwa.
Akawahudumia, na kuwalisha.”
“Hapa
ulipo bado unatumia kodi aliyolipa Tunda. Kila ninachokiangalia hapa, ni cha
Tunda ambacho nilikupa mimi mwenyewe na vijana wangu ndio walikuhamisha hapa.”
Mama Penny akaendelea kibabe.
“Kazi
inayokuingizia pesa, inatokana na kampuni ya Tunda. Na mimi na Tunda ndio
tumekufundisha hii kazi, na wateja wengine mimi ndio nakupa. Ni jumamosi hii tu
iliyopita, umetoka kupamba ukumbi wa mtu niliyekutambulisha kwake. Kwa kifupi
tu, upo hapo ulipo sababu ya Tunda.”
“Nikiita
vijana wangu nikiwaambia wapakie vitu vya Tunda hapa, wewe na wanao mtalala
chini. Na nikienda umbali wakudai hii sehemu, utalala nje na wanao. Maana hata
hapa ni mimi na Tunda ndio tuliingia mkataba.” Watu wote kimya.
“Hayo
yote nimekukumbusha tu ili kukurudisha ulipotakiwa uwepo kabla ya Tunda hajaja
kukuokoa kule kwa ndugu wa mume wako. Kwa hiyo basi, nakusihi sana,
unapozungumza naye Tunda, kumbuka nafasi yako na uwe na shukurani. Sijui kama
unanielewa mama Tom?” Kimya.
“Unanisikia
au unataka nirudie kukukumbusha vile Tunda anavyokusitiri hapa mjini?” “Mimi
sio mtoto mdogo mama Penny. Nakusikiliza.” “Basi anza kuishi kama mtu mzima.
Acha kujidai umechanganyikiwa!” Mama Tom akamkazia macho mama Penny kama amjibu
lakini akashindwa.
“Naamini
umenielewa.” Mama Penny akaongeza kwa ukali, kisha akamgeukia Tunda. “Haya
Tunda, ongea kile ulichotaka kumwambia mama yako. Leo wote wapo hapa. Wazazi
wako wote wawili. Nina uhakika hata baba yako hajui ukweli. Ongea kwa utulivu
bila hofu, maana hapa ni kwako hakuna atakayekufanya chochote. Atakayeshindwa
kukusikiliza hapa, achukue mabegi yake aondoke. Hii nyumba nitaitafutia mteja,
turudishe pesa yetu. Kesho asubuhi, nauza kila kitu mpaka kijiko, uondoke na
pesa yako. Tena kwa dola.” Mama Penny akajiweka sawa, huku akimtizama Tunda.
Hatimaye Tunda
apata fulsa yakueleza upande wake mchungu kwa wazazi wake.
Net akamuwekea mkono mgongoni, akampapasa
taratibu. Tunda akamwangalia, nakujiweka sawa. “Kwanza mimi nilijua yule bibi
aliyenifukuza na kunionya nisiwahi kurudi tena kwao yeye na babu ndio wazazi
wangu. Yaani wazazi wa mama Tom ndio nilijua ni wazazi wangu. Na mama Tom ni
dada yangu. Shida yangu ilianza pale ndugu wa mama Tom walipotaka mimi
niondolewe pale kijijini.” Tunda akaanza kuelezea.
“Mama
Tom alinichukua kutoka pale kwa wazazi wake kunipeleka kwa baba, kwa hasira
sana. Njia nzima akinipiga kwa makosa haya na yale. Kwa kuwa nilikuwa simulewi.
Sikuwa nikijua kiswahili vizuri. Kijijini tulikuwa tukizungumza kilugwa, mpaka
darasani. Sasa mama Tom alipokuwa akinipa maelekezo kwenye gari, nikiwa
sijawahi hata kupanda gari, alikuwa akinipiga sana.” Tunda akaendelea.
“Alinifikisha
kwa baba, akiwa ametoka kunipiga sana nje ya ile nyumba. Kwa kuwa sikuwa najua
kufungua mlango. Nikiwa kwenye hofu vilevile, alinivuta mpaka sebuleni kwa mama
Chale na baba. Akaniacha hapo, akiniambia baba, ndio baba yangu.”
“Niliamini
kwa kuwa ni kweli tulifanana. Hata weusi aliokuwa akinitukana nao, ni kweli
nilifanana na baba hivyo hivyo. Maisha yangu yakaanza pale kwa baba.” Tunda akaeleza
mateso yote aliyokuwa akifanyiwa pale kwa baba yake, bila utetezi.
“Basi,
bibi alipokuja kunichukua kutoka hospitalini Dar, akanirudisha tena kijijini.
Ndio akaamua kumpigia simu baba Tom, aje. Ndipo akaja na mama Tom, baada ya
mazungumzo ya muda mrefu, wakakubali kuondoka na mimi pale kijijini.” Tunda
akatulia kidogo.
“Ukweli
mama Tom alikuwa akinichukia nakushindwa hata kujizuia. Mpaka yule msichana wa
kazi alikuwa akishangaa. Baba Tom alipoona udhaifu huo, mama hanipendi na
kunitukana kila mara, yeye ndio akapata mwanya. Weusi aliokuwa akiutukana mama
yangu kila wakati na macho haya akisema kama ya paka, akawa anasifia baba Tom.
Wakati mwingine mama alikuwa akinipiga mpaka ananiingiza chini ya meza, baba
Tom ndio akawa anakuja kunitetea.”
“Ukawa
sasa ndio mchezo. Mama akitaka kunipiga, mtetezi wangu ni baba Tom. Nikilia,
yeye ndio ananibembeleza kwa kunipakata.” Tunda akatulia kidogo. Akaelezea
mengi yaliyokuwa yakiendelea pale ndani bila mama yake kujua au kujali. “Ile
tabia yakunibembeleza ikawa mazoea. Wakati wote alinipakata hata mbele ya mama.
Lakini tulipokuwa wenyewe, ubembelezwaji ukaanza kubadilika.”
“Akaanza
tabia yakunichezea huku akinisifia mwili wangu. Alipoanza kuvuka mipaka,
nilimkatalia. Ndipo akanikumbusha nipo pale kwa sababu yeye anataka. Mara
nyingi mama alikuwa akinitishia kuwa atanirudisha kwa baba yangu, mkewe aniue
kabisa. Lakini baba Tom akawa akinitetea. Kwa hiyo akaniambia nikimkatalia,
hatanitetea tena. Atanirudisha kwa baba yangu.” Tunda akaendelea.
“Ile
tabia ikaendelea. Akawa ananichukua mpaka chumbani kwake. Siku ambazo mama Tom
analala kazini, na mimi ndio zilikuwa siku zangu zakuchezewa usiku kucha mpaka
yeye aridhike.”
“Ikitokea
mama Tom haingii kazini usiku, na baba Tom anajua, basi ujue mchana huo
nikitoka shule, ndio itakuwa nafasi yake. Ataniambia nikaoge, nipande kitandani
kwake. Wakati mwingine na nguo, wakati mwingine bila nguo. Atanifanyia hivyo
mpaka mida anayojua mkewe anarudi.”
“Siku
ambazo namkatalia, anaweza kuzua jambo lolote. Basi atanipiga wee, mpaka achoke
na mkewe ataniongezea. Akinilaumu namtia aibu kwa mumewe. Basi. Alipozoea
kunichezea, hapo bado nilikuwa mdogo, akaanza kunifundisha jinsi yakumchezea na
yeye. Hapo ndipo ilikuwa mateso kwangu.
Hatosheki wala haridhiki. Unalala umechoka na asubuhi anakuja kukuamsha umchezee
tena kabla hajakwenda kazini.”
“Nilipojua
kumfanyia anachotaka, akaanza mtindo hata wakunifuata shuleni. Anadanganya
labda ananipeleka kwa daktari, au sababu alizojua yeye. Atanichukua kwenye gari
au hata hotelini kama atajua mama atakuwepo nyumbani usiku au yupo likizo kwa
hiyo usiku hawezi kunichezea.”
“Kama
ni hotelini, ujue ndio nitakaa naye mpaka muda wakutoka shule, ndipo tunarudi
shuleni kumchukua mtoto wao Tom, tunarudi nyumbani.” Baba yake alibaki ameinama
akifuta machozi.
“Mama
Tom alipokwenda kupumzika kwa bibi kipindi alipojifungua Aneti, ndipo mumewe
sasa akaanza kuniingilia. Tulibaki nyumbani mimi, yeye baba Tom, Tom na kijana
wa kazi aliyekuwa akilala nje. Jamani baba alikuwa akinitesa yule!” Tunda
akaanza kulia. Alikumbuka maumivu aliyokuwa akisababishiwa na yule baba.
“Diclophenac, zile dawa za maumivu makali ilikuwa kama pipi
kwangu. Na alipoanza, hakuweza kusubiri hata nipone. Asubuhi na jioni ikawa
ndio kazi. Na hapo nilikuwa nikilala chumbani kwake kama mkewe!” Tunda alimfanya mpaka mama Penny aliyejua
hiyo historia aanze kulia tena.
“Alipoona navimba, na yeye hawezi kusubiri, akatafuta kama
mafuta hivi. Ananipaka, panakufa ganzi, basi ndio ujue utakesha naye mpaka
ganzi iishe. Anakupa dawa ya maumivu, ulale, mpaka alfajiri tena. Anaanza. Alifanya
vile mpaka nikazoea. Akaacha kunipaka hayo mafuta akawa ananitumia hivi hivi.
Nilipokuwa nikimuomba yale mafuta, akawa akinipiga, ananikatalia.” Kila mtu kimya.
Net
alikuwa mwekundu kana kwamba ndio anasikia kwa mara ya kwanza wakati
alishasimuliwa. Bado alikuwa amemshika mkewe.
“Basi. Aliendelea hivyo mpaka nikazoea kabisa. Akanifundisha
mambo mengi yakufanya. Aliporidhika kuwa nimejua, akaanza yeye kunipangia wapi
niwepo na kwa wakati wake. Hiyo inategemea na mkewe alipo.”
“Siku nyingine tunatoka kama nakwenda shule, kumbe nakuwa nipo
naye hotelini. Kuanzia hiyo asubuhi, mpaka muda wa shule kuisha.” Tunda akajifuta machozi. “Wakati mwingine siku za jumamosi alianzisha tuition hewa.
Kwa hiyo nilikuwa naaga nakwenda tuition, kumbe alikuwa akinitanguliza
hotelini. Baada ya kama lisaa hivi, anakuja. Hapo utashinda naye hapo hotelini
ukimuhudumia mpaka atosheke yeye. Ndipo ananiruhusu nirudi nyumbani, namuacha
yeye akilala.” Net aliendelea kumpapasa mgongoni.
“Ukweli nilikuwa nikichoka. Maisha yangu ilikuwa ni yeye tu.
Asubuhi, mchana ananifuata mpaka shule, na usiku kama mkewe hayupo au kama
mkewe akiwepo, ujue humo njiani nilazima nimridhishe ndipo turudi nyumbani.” “Tom anakuwa wapi?” Mama yake
akauliza.
“Unakumbuka
nilivyokuwa nikifeli akakwambia ananianzishia tuition za jioni?” Mama yake
kimya. “Basi hapakuwa na tuition wala kusoma. Ananitoa shule, ananipeleka hata
baharini. Anaegesha gari, naanza kazi yakumuhudumia yeye. Na ukitaka urudi
nyumbani salama, ni yeye aseme basi. Usiseme umechoka. Wakati mwingine anaweza
kukupiga huko huko halafu anakwambia muanze upya.”
“Siku moja nilikuwa nimechoka. Ilikuwa siku ya jumamosi, akataka
twende hotelini kama kawaida. Nikamwambia nimechoka. Aniache siku hiyo
nipumzike lasivyo namsemea kwa mama, namwambia ukweli. Akaniwahi, akaenda
kunisemea yeye kuwa nimeanza mambo ya wanaume, ndio maana nafeli darasani.
Jamani mama Tom alinipiga! Akaja sasa yule baba mwenyewe. Alinitandika na
mikanda ya suruali, mpaka leo nina alama.”
“Walipomaliza hapo, sijui kama mama Tom unakumbuka?
Ulinifungashia nguo chache, ukanirudisha kwa shangazi yako. Ukasema heri
nikaishi huko, kuliko kupoteza pesa yenu na kukutia aibu.” Baba yake Tunda alishindwa hata
kunyanyua uso.
“Basi.
Nilikaa kule kwa shangazi yake mama Tom, sijui ni kwa majuma mangapi, lakini
hata mwezi haukuisha, baba Tom akaja yeye mwenyewe kunichukua. Akamwambia huyo
shangazi kuwa amenisamehe, anaona nirudi tu nikaendelee na shule.”
“Nakumbuka
siku ile alikuja asubuhi tu, akanitoa milimani kule, akatafuta hoteli palepale
Morogoro mjini, tukaenda.” Tunda akaanza kulia tena.
“Akaniambia kuanzia siku hiyo, nisiwahi kumbishia tena. Nimeona
kilichonipata. Mama alinipiga, na kule kwa shangazi ni kama walianza
kunikasirikia. Walitaka kunifukuza. Akaniambia yeye ndio amebaki kuwa mkombozi
wangu. Ili niishi kwake vizuri, basi, lazima na yeye aishi vizuri. Na ili aishi
vizuri, ni mimi nimfanyie anayoyataka yeye, mpaka aridhike. Basi, hapo ndio
ikawa sina tena usemi juu ya mwili wangu. Alinifanyia kile atakacho yeye, muda
na wakati atakao yeye.”
“Mpaka nikavunja ungo. Ndio ikawa afadhali yangu. Nikiwa kwenye
siku zangu ndio pumziko, lakini napo ikawa anakuwa kama mbogo. Mkali pale
nyumbani, hapakaliki. Jambo kidogo tu, anagomba.” Net akafungua chupa ya maji aliyokuwa
amekuja nayo, akampa. “Asante.” Tunda akamshukuru, na kunywa kidogo ndipo
akaendelea.
“Akawa
akinipa mahela, na kuninunulia nguo. Anapanga wapi niwe na wakati gani ili
nimtumikie. Hata kama ni mchana, nimebaki nyumbani, anaweza kuniambia nihakikishe
nambembeleza mtoto alale, yeye anakuja, anataka anikute labda uchi, chumbani
kwake. Kipindi hicho namlea huyu Aneti.”
“Basi
ndio unahangaika kumbembeleza mtoto. Akija akikuta mtoto amelala, ndio
ananitumia. Akiridhika ndipo anarudi kazini. Anakuacha
hapo na mauchafu yake na maumivu. Akirudi mkewe jioni, hajaridhika na kile
alichokwambia umfanyie mwanae, basi unapigwa vibao vya usoni kama paka mwizi
huku akikutukana matusi mabaya.”
“Ikawa
hivyo hivyo. Nikagundua njia ya kusema nipo kwenye siku zangu, ili niwe
napumzika. Najikata mahali, napaka damu kwenye pedi, akihakikisha pedi ina damu
ujue utaachwa.”
“Hakuwa
akijua siku za hatari wala salama. Yeye ilimradi amepata anachotaka. Hakuwa
akitaka kondomu kabisa. Mwanzoni akawa anakumbuka kunipa dawa kwenye siku zangu
za hatari. Akishamaliza haja zake, akijua ni siku za hatari, basi anakupa dawa
ili usishike mimba, au anatoa nje. Mimi sikujua kama nimeshika mimba kwa kuwa
alikuwa makini sana.”
“Siku
aliponiambia nimfuate Arusha nikiwa nimetoka kwa bibi. Nilikuwa wala sijui kama
bibi alinigundua ni mjamzito. Kumbe alikuwa ameshamwambia mama. Nikatoka
Morogoro, nikamfuata Arusha, tulikaa nafikiri siku 4 au zaidi, nikimuhudumia tu
yeye, wakati yeye yupo kwenye semina iliyokuwa imempeleka kule Arusha.”
“Nikakaa
naye mpaka semina ikaisha maana nilikuta inakaribia kuisha. Alipomaliza semina,
tukaongeza siku zakukaa kule huku akimdanganya mkewe kuwa muda uliongezwa.
Baada ya siku 4 hivi nafikiri, akaniruhusu nirudi. Akanikatia tiketi ya ndege
ya asubuhi, yeye akaja na ya mchana.”
“Ndio
kwa mara ya kwanza nikashangaa eti mama Tom ananiuliza maswali yanayonihusu
mimi! Kumbe mwenzangu alishaambiwa na bibi kuwa mimi ni mjamzito, ndio maana
ananiuliza.”
“Japokuwa
tulikuwa tukiishi nyumba moja, hakuwa akinisemesha. Akinisemesha ujue ananipa
maagizo ya nini nimfanyie mtoto wake Aneti ambaye nilimlea, au kunitukana. Kila
mtu alikuwa anajua pale ndani mahusiano yangu na mama Tom. Basi ndio
akanichukua siku inayofuata, akanipeleka shule. Akashangaa matokeo yangu. Ni
kweli nilikuwa nakuwa mtoto wa mwisho darasani.”
“Akashtuka
sana mpaka akamshangaza mwalimu. Akamuuliza kwani alikuwa amesafiri? Nani
alikuwa akiishi na mimi asijue kilichokuwa kikiendelea kwa muda wote ule! Aliambiwa
nilishapewa barua nyingi tu niwe napeleka nyumbani juu ya maendeleao yangu
shuleni na vile ninavyolala darasani, lakini zote zilikuwa zikiishia mikononi
kwa baba Tom.”
“Akihitajika
mzazi shuleni, yeye alikwenda na kuzungumza na walimu. Walimu karibia wote
walikuwa wakimlalamikia baba Tom vile ninavyolala darasani. Yeye alijua sababu
ya ukweli, akazua ugonjwa.”
“Sijui
aliwaambia nilikuwa nikisumbuliwa na ugonjwa gani sijui, yeye baba Tom aliujua
na wale walimu wakauelewa. Basi ikawa ni sawa mimi kulala darasani na yeye kuja
kunitoa darasani muda na wakati anaotaka, na kunipeleka hotelini na si
hospitalini au kumuona daktari wa huo ugonjwa kama alivyokuwa akiaga walimu
shuleni.”
“Mama
Tom alinitoa hapo shuleni na kunipeleka kwa wafanyakazi wenzake. Wakanichoma
sindano ya usingizi, wakanitoa mimba.” Tunda akaanza kulia. “Nilikuja kuzinduka wodini nikiwa na maumivu, na baba
pembeni yangu na barua yakufukuzwa kwa mama na ndugu zake rasmi.”
“Baba aliniuguza bila hata maswali. Akawa ndiye wakuniletea uji
asubuhi na jioni. Mpaka nilipopona, na yeye akaenda kuniacha nyumbani kwa dada
yake. Ambako huko tena ni habari nyingine,
ila ndiko Mungu aliponikutanisha na Net.” Tunda akatulia kidogo.
“Kwa
hiyo hayo ndiyo niliyotaka uyasikie kwa upande wangu. Sijui utaamini kwa
asilimia ngapi, lakini namshukuru Mungu kwa kunipa mama Penny, aliniwezesha
kupata hii nafasi angalau na mimi unisikilize na nikuombe msamaha kwa pale nilipokosea kama mtoto.”
“Sijui nilitakiwa kufanya nini, ili isiwe kama ilivyokuwa.
Nyinyi wawili wote mlikuwepo kwenye maisha yangu, na mkaacha wenza wenu
wakinitesa.” Tunda akazidi kulia
zaidi.
“Baba ulijua jinsi mama Chale alivyokuwa akinitesa. Tena kwa
kuambiwa na majirani na yule msichana wenu wa kazi. Lakini ulishindwa
kunisaidia. Mama wewe ndio sijui hata niseme nini! Nashindwa hata nianzie wapi.
Tokea nilipokuwa kwa bibi, ulikuwa ukija kule hutaki hata kunitizama. Umebeba
chuki dhidi yangu, natafuta sababu siioni! Huoni shida kunitukana, au kuniumiza
kwa wazi kabisa, ukitaka onione ninavyoumia! Chuki imekujaa ndani yako kila
kitu ninachokufanyia huoni thamani yake!”
“Nilikulelea mtoto wako Aneti, lakini ulishindwa hata kupokea
salamu yangu! Hata kuniuliza tu hujambo, ulishindwa. Japokuwa nilikuwa nikimlea
mtoto wako na kutumiwa na mume wako, lakini umeua mtoto wangu bila idhini
yangu! Uliniacha hospitalini navuja damu, akaenda kuzunguka kila nyumba
kutangaza nimezaa na mume wako.”
“Haya, nilikuja kukusaidia wewe na watoto wako. Dunia ikiwa
imekugeuka kabisa. Nimewaweka hotelini kwa pesa yangu! Muulize mama Penny.
Nilikuwa nikichukua kazi nakuzifanya kama punda, bila msaada hata shilingi ya
Net, ili kukusaidia wewe na watoto wako. Bado hukuridhika.”
“Nimefungwa jela, hukuja hata kunisalimia, umechukua kampuni
yangu na mali zangu karibia zote. Sijalalamika wala sikukutafuta kukudai. Nakutafuta,
unakataa kupokea simu zangu mpaka nakwambia naondoka, ndipo ukaridhia
kunisikiliza! Hata usiulize afya yangu na ulijua nilikuwa nimefungwa, unadai
mali zangu zaidi!”
“Unakasirika mimi kumpa baba vitu nilivyotafuta kwa jasho langu!
Unanitukana mimi na baba ambaye alikuja kujirudi kwangu bila kutaka kujua
ukweli huu niliowaambia wote!” Net
akampa tena maji ya kunywa. Kama aliyekuwa akimkumbusha atulie. Akatulia.
“Mpaka
kochi ulikokalia sasa hivi hapo ni langu. Bado unakasirika kujua nampa baba
simu! Kweli!? Hakuna mtu yeyote mwenye haki yakuniambia nitumie vipi mali
zangu. Kwa kuwa nyinyi wote mliniacha nikiteseka mbele ya macho yenu.”
“Narudia,
ni afadhali baba, alinihudumia hospitalini na kunisaidia vile alivyoweza yeye,
lakini sio wewe. Huna haki kabisa mama Tom. Nimekuja kukwambia haya na kukuaga
kwa amani kama baba alivyonishauri. Mungu akikupa neema yakunisamehe pale
nilipokukosea, basi, naomba unisamehe.”
“Ila
mimi nawatangazia nyinyi wote wawili, nimesamehe yote mabaya mliyonitendea.
Nashukuru Mungu kunirudishia japo mzazi mmoja.”
“Ila
mama Tom, kuwa makini. Sasa hivi alipo Aneti, hakumbuki diaper za thamani
ulizokuwa ukimwaga pesa ukimnunulie nimvalishe. Sijui makopo ya maziwa ya
thamini au nyumba aliyokuwa akiishi yenye AC na sisi tukimtumikia.”
“Kumbukumbu
atakayokufa nayo huyo Aneti hata akifa akiwa mzee sana, ni kuwa mama yake
alimuacha akitendwa vibaya na baba yake. Mimi nilipita alipopita Aneti, sema
mwenzangu yeye ulimuuguza gonorea, mimi ulinitoa mimba na kunitelekeza
hospitalini.”
“Ila
madonda aliyoyaacha baba Tom, mumeo, wewe ukiwepo, ndani ya nyumba hiyohiyo,
hayaponi hata kidogo. Si kwa muda wala dawa. Hakuna pole au faraja yakuponya
hayo madonda.”
“Mwisho
kabisa, nashauri urudi kwa Mungu. Hata kama si kwa ajili yako, basi kwa ajili
ya Aneti. Mimi Net alinitafutia mchungaji akaniombea. Nilitokwa na mapepo mengi
tu. Lakini baadhi yalisema yalitokana na agano nililokuwa nimeingia na baba Tom
au mumeo. Kwa njia gani, mimi sijui. Unakumbuka Net?” Net akatingisha kichwa
kukubali.
“Basi
ni hayo tu. Mpeleke huyo mtoto akaombewe. Pengine itamsaidia na yeye kwa namna
moja au nyingine. Mungu hashindwi. Twendeni.” Tunda akasimama.
Baba yake Tunda naye..
“Naomba kabla yakuondoka, niweke jambo moja sawa. Mbele ya
Manda, ili kusitokee kubisha baadaye.” Baba yake Tunda alimuwahi Tunda kabla
yakutoka. “Naomba ukae kidogo Tunda. Maadamu
tumepata muda huu, naomba na mimi nikuweke sawa.” Baba yake akajifuta
machozi.
“Nakumbuka
kukwambia kwa sehemu Tunda, lakini wakati ule wote hatukuwa kwenye mazingira
mazuri yakuelezana jambo, ukaliweka akilini. Wewe kwangu sio mtoto wa bahati
mbaya, ila ni mtoto niliyekujua na kukabidhiwa kwa gafla nikiwa kwenye matatizo
makubwa sana ya ndoa yangu.” Yule baba akajiweka sawa.
“Manda
hakutaka kabisa nifahamu kama ana mtoto wangu. Kwa sababu zake binafsi. Ila
namjua tabia yake yakupenda kutumia watu. Huwa hajali unaonekana vipi au ukoje
linapokuja kwenye swala la pesa, na ndio maana nafikiri, ukampitisha Tunda huko
alipopita mpaka leo.”
“Hee!
Kwa nini gafla mimi ndiye naonekana mbaya?” “Subiri kwanza Manda? Wewe
kilichokushinda kuniambia una mimba yangu, si kwa kuwa ulitaka kumbambikizia
Mosi mimba ili akuoe? Si kweli?” Kimya.
“Mimi
nakujua sana Manda. Na ninahisi chuki yako na kisa cha kumtukana mwanangu ni
kule kuzaliwa mweusi na hayo macho, akazaliwa anafanana na mimi asilimia 100, ukaishia
kuachwa na Mosi.” Akaendelea.
“Wakati
unamalizia masomo yako pale chuo cha Muhimbili, kwa maswala ya uuguzi, rafiki
yako aliniambia mahusiano uliyokuwa nayo na rafiki yangu Mosi, na ukawatangazia
pale chuoni, mimi hunipendi, unachukua pesa yangu tu, lakini Mosi atakuja kukuoa.
Ulisema unanionea kinyaa mimi, isipokuwa pesa yangu.” Kimya.
“Baada
ya kusikia hayo, tena kutoka kwa rafiki yako, nikaamua kukaa mbali na wewe
kabisa. Wewe mwenyewe ukanitafuta. Ukaja mpaka nyumbani kwangu. Kwa kuwa
nilijua nia yako ilikuwa pesa tu, nikakukaribisha siku ile sebuleni, sikutaka
hata uingie chumbani kwangu.”
“Unakumbuka
ukaomba mpaka kulala kwangu na tulikuwa hatujaonana zaidi ya mwezi? Nikakwambia
ukweli wote niliojua juu yako, ukapinga.” Baba yake Tunda akaendelea.
“Ulimpigia
simu rafiki yako palepale kwangu mkaanza kusutana. Nilikwambia kama ni kweli
haupo na Mosi, umpigie simu mimi nikiwepo, na ajue upo kwangu. Ukanizungusha
wee, mpaka nilipokwambia kama hutazungumza na Mosi, uondoke usiku uleule. Ndipo
ukampigia simu Mosi, ukamwambia umeamua kurudi kwangu.”
“Siku
ile ukalala kwangu, ukaamka na shida ya pesa. Ukasema kama hutamaliza ada,
hutafanya mtihani wako wa mwisho. Nilikupa ada yote, ukaondoka kwangu.
Sikukuona tena.”
“Baada
ya miezi mitatu mkiwa mmeshamaliza chuo, nikamtafuta rafiki yako tena
kukuulizia. Nikamwambia uliondoka kwangu ukisema utakuwa busy sana na mitihani,
utanitafuta ukimaliza mitihani. Lakini sikukusikia tena. Ndipo nikaambiwa
unaishi kwa Mosi.” Baba yake Tunda akajicheka kidogo.
“Nilivyokuwa
nakuamini, nikambishia. Nikamwambia haiwezekani kwani wewe ulimkataa Mosi mbele
yangu. Yule dada akanicheka sana. Akasema siku ile usiku ulinitafuta sababu ya
pesa. Hukuwa na nia hata yakulala na mimi, ila nilipokufukuza, ndipo ukatafuta
njia yakunirudisha kwenye mitego yako, ili nikupe pesa.”
“Na
uliyempigia simu siku ile usiku hakuwa Mosi, ila rafiki yenu daktari alikuwa
mwaka wa kwanza pale Muhimbili. Yeye ndiye uliyempigia simu, kwa kuwa hakuwa
akikuelewa unachozungumza usiku ule ukimwita Mosi na kujidai unarudiana na
Yohana, ulipokata tu simu, na yeye ndio akampigia Agi, kumuuliza Mosi ni nani
na Yohana ni nani?”
“Ndipo
wakaunganisha habari, wakagundua usiku huo upo kwangu kunichomoa tena pesa. Agi
akanihakikishia upo kwa Mosi na ni mjamzito. Sikutaka mambo mengi. Nikakuacha
kabisa.” Akaendelea.
“Sijui
ulizaa mtoto aliyemfungua macho Mosi, sikuuliza kwa kuwa mimi na Mosi tuliacha
mawasiliano kabisa baada yakujua anaishi na wewe, msichana aliyekufahamu
kupitia mimi, tena kwa kumtambulisha kuwa ni mwanamke wangu. Mosi alihamishwa
mkoani, wewe sikukuona wala kukusikia tena mpaka siku mbili kabla hujaniletea
mwanangu.”
“Ukaniambia
kama hivi Tunda alivyosema unamtukania weusi wake. Ukasema kwa kifupi tu,
nijiandae, unaniletea Jaluo mwenzangu. Nikiwa sijakuelewa wala hukutaka
nikuulize jambo, ulinikatia simu, ndipo ukaja kunitupia mwanangu ndani ya
nyumba yangu, katikati ya ndoa iliyokuwa na matatizo makubwa sana.”
“Ukaondoka
na kuacha moto ukiwaka, si kwangu tu, na kwa Tunda pia. Naomba ukanushe
chochote nilichokusingizia Manda.” Kimya. Baba yake Tunda mtaratibu, ongea yake
kama anayejihami kwa ugomvi.
“Chuki
yako kwa Tunda haikuanzia kwa Tunda, ni kwangu. Sasa Tunda akaharibu zaidi
alipozaliwa anafanana na mimi. Alikuwa ni kama amekupokonya tonge mdomoni, kwa
kuwa ulitaka sana kuolewa na Mosi.”
“Nilisikia
mpaka nyumbani kwenu ulimtambulisha, na alishalipa mahari ilikuwa bado harusi
tu. Tunda akawa kosa ambalo ulishindwa kulisamehe wala kuliona, ukaamua kwenda
kumtupa kwa mama yako.” Baba yake Tunda akanyamaza kidogo kama anayefikiria.
Wote wakamtizama.
“Mungu
anisamehe sana, lakini nakuhisi vibaya sana Manda.” “Juu ya nini?” Mama Tom
akauliza kwa jeuri. “Kwa kuwa wewe ni mshenzi, mpenda pesa sana. Ulikuwa
ukinufaika kwa yule baba watoto wako, NAHISI, ulijua unyama anaomfanyia
mwanangu, lakini ukaamua unyamaze ili uendelee kujijenga, lakini Mungu
amekupiga kofi, akavunja pale ulipojenga kwa kumwaga damu ya mwanangu.” “Wala
mimi sikujua. Mbona nilimtoa mimba?” Manda alijitetea bila hofu.
“Ulivyo
mbinafsi wewe! Nina uhakika, ulihakikisha yule baba hana mtoto mwingine wa nje,
isipokuwa wako tu, ili mtu mwingine yeyote asinufaike na mali zake.” “Huo ni
uzushi Yohana, na usitafute kujisafisha hapa. Hata wewe ulishindwa kumlea mtoto
wako nilipokupa nafasi hiyo.”
“Mimi nilishindwa. Wala sikatai na
nilishamuomba msamaha Tunda. Lakini je,
mbona baba Tom alipotaka kumtafuta Tunda ili amsaidie baada yakumtoa mtoto
wake, ulimtisha?” Mama Tom akashtuka sana, na Tunda pia. Akamwangalia mama yake
na baba yake.
“Unafikiri
sifahamu hilo? Hivi unajua mumeo nilifungwa naye gereza moja? Unajua kama
nilitaka kumlipiza kisasi jela, ndio kuna afande akanionya kuwa nisikubali kosa
la mumeo likanifanya nifie jela! Unajua hilo?” Kimya.
“Huwezi
kujua kwa kuwa wewe ni mnyama, huwezi kutamfuta mtu asiye na manufaa kwako.” “Amenibakia
mtoto wangu, bado nikamtembelee jela!?” “Mbona alipomfanyia ubaya Tunda, na
yeye alikiri kuwa alikwambia kuwa alimbaka Tunda, mbona ulikubali kuendelea
kuishi naye huku ukimtisha kuwa akimtafuta tu tena Tunda, utamshitaki?” Akamuuliza
kwa kumsuta. Kimya.
“Swala
la kubakwa kwa Tunda na mumeo wala leo sio mara yako ya kwanza kulisikia. Mumeo
alishakiri. Kana kwamba haitoshi ndani ya nyumba hiyo hiyo mliyokuwa mkiishi alimbaka
msichana wako wa kazi, mbona ukalifumbua macho na hilo? Ukawalipa wazazi wa
yule msichana, mkaendelea na maisha yenu wala usimfukuze mumeo au kumfunga! Ukaendelea
kula pesa yake bila shida.”
“Ilikuja
kukuuma alipobakwa Aneti! Napo hapo pia anasema anahisi ni kwa kuwa alikuzunguka.”
“Ni muongo yule mwanaume. Shetani mkubwa. Amekwambia nini na uongo wake?” Manda
akawa na yeye amekasirika.
“Naombeni
mnivumilie jamani. Mnipe muda kidogo, nimwambie ukweli Manda, labda kwa mara ya
kwanza maishani atakuja kufunguka macho na kuwa mwanadamu wa kawaida. Tunda
mama, nivumilie kidogo. Tutaondoka sasa hivi.” Tunda akatingisha kichwa
kukubali.
“Asante.
Jiegemeze kidogo hapo kwenye kochi.” “Mimi nipo sawa baba. Wewe endelea tu.”
Tunda akajibu kwa utulivu akitaka kusikia yaliyojiri baada ya kutolewa mimba na
kufikiri ametelekezwa hata na baba Tom.
“Habari
za mume wako za tabia zake za kubaka zilienea pale gerezani. Mungu alivyomwema,
nikaja kujua ni mume wako wewe, na ndiye aliyempa mimba Tunda. Nikawasimulia
watu wangu wa karibu, maana nilishakuwa mwenyeji pale, wakasema tumfanyizie
vibaya sana. Kwa kuwa nilikuwa na machungu, nikakubali bila kujua Tunda yupo
wapi kwa wakati huo. Nilimuacha amepigwa, amevimba, yupo hospitalini hana
msaada.” Akaendelea kila mtu akimsikiliza.
“Tukamkamata
lijamaa lako likiwa bafuni linaoga. Yule baba alilia kama mtoto mdogo maana
jamaa walishaanza kumkata na wembe. Akieleza kila kitu juu ya Tunda. Na akasema
alikulaumu sana kuua kiumbe kisicho na hatia. Yule mtoto hakuchagua atungwe
mimba wapi. Anasema ukawa ugomvi mkubwa sana, ndipo akaamua kumtafuta Tunda.”
“Mumeo
alipoonekana hospitali ya Muhimbili, wafanyakazi wenzako wakakupigia simu,
ukamfuata, maana muda wakuona wagonjwa ulikuwa bado na yeye alikuwa anapita
mawodini kumuulizia Tunda.”
“Ukamtishia
kumfungulia kesi ya kumbaka mtoto wake, na ukamuhakikishia utashinda kesi na
yeye atafungwa kifungo cha maisha, akae mbali na Tunda. Yule baba akasema Tunda
amefikisha miaka 18, anaweza kabisa kuolewa, na yeye anataka kumuoa Tunda.”
Tunda akashangaa sana.
“Hapo
ndipo ukamwitia askari. Akachukuliwa mpaka kituo cha polisi, akasema yeye
hakuwa amembaka Tunda, Tunda anamiaka 18, aitwe yeye mwenyewe Tunda, aeleze. Ndipo
ukamwambia utatengeneza kesi kuwa alikuwa ukimbaka Tunda kabla ya miaka 18.
Yule baba akiwa hajui kama ilikuwa kitisho au la, akakubali kukaa mbali na
Tunda, ndipo ukafuta kesi.”
“Anasema
lakini akashanga japokuwa alikubali, na akarudi nyumbani ukawa kama mwehu,
ukapita kila nyumba, kuchafua jina la Tunda! Hapakutokea tena maelewano kati
yenu, ndipo akambaka yule mtoto wenu wa kazi. Ukamwambia utamsamehe kama ile
nyumba ya pale na Goba, ataiandika jina lako, na awe anakupa pesa kila mwezi
zakutuma kwa wale wazazi wa yule binti ili kuwanyamazisha.” Kila mtu akamgeukia
mama Tom kwa kumshangaa.
“Yule
jamaa alikiri mbele yetu kuwa anatatizo kubwa sana linapokuja swala la ngono.
Anasema akili inakuwa kama inamruka, anakuwa kama amepagawa halafu baadaye ndio
kama anarudia hali yake ya kawaida. Na akakiri kabisa, akiwa kwenye ile hali,
hawezi kuwaza wala kufikiria. Anakuwa kama amepagawa, mpaka aridhike. Ndio
akili inarudi.”
“Ni
kweli kabisa baba. Mimi mpaka nilimwambia labda anakuwa anapagawa mapepo. Maana
anakuwa kama mwehu. Hatulii, anakuwa kama mtu anayetaka kufa kwa njaa wakati unakuta labda hapo ulikesha naye usiku uliopita. Na
hawezi kusubiri! Na akikushika anakuwa kama mnyama, hana huruma.” Tunda
akamkatiza baba yake, akakumbuka ile hali ya baba Tom mpaka machozi yalianza
kumtoka tena. “Pole sana mama.” Baba yake akamuhurumia.
“Lakini
aliongeza jambo jingine, kwa upande wa pesa na akili za kazini, walimtegemea.
Anasema alijua wazi, akikupa mali zake utamshitaki tu. Akakukubalia masharti
yako yote uliyompa. Lakini akakupa hati za nyumba zote, feki.” Manda akashtuka
sana.
“Alisema
mali zake zoote, aliandika majina ya ndugu zake. Tena kwa taarifa yako tu, mumeo
alitumia akili ya haraka ili usije kushinda mahakamani kama mke wake uliyeishi
naye kwa muda mrefu na mtu uliye zaa naye.”
“Akaamua
kuandika kwa mkono wake kuwa amewauzia hao ndugu zake mali zake
alizozitengenezea makaratasi mazuri tu, tena ya kihalali. Akaonyesha
alishawauzia miaka 4 iliyopita, hata kabla ya wewe kumfunga jela baada ya
kugundua alichokuwa akimfanyia Aneti.” Wote walimuona jinsi Manda alivyoshtuka.
“Anasema
kwa maandishi, aliandika pale mlipokuwa mkiishi, Kitunda, mlipewa hifadhi na ndugu
yake baada ya kuishiwa na kumuuzia pale ili apate pesa. Upo Manda?” Akamuuliza
kwa kumkejeli.
“Eneo
na mali zote za Goba ulikokuwa ukifanya miradi yako, pia ameandika ni mali za
dada yake alizokuwa amemuuzia. Tena anasema alishaandaa karatasi zenye saini yake,
ya kupokea malipo yote ya mauzo ya mali zake zote.”
“Amekiri,
na alisema alikukomoa makusudi kwa kuua mtoto wake akijua nia yako ni mali.
Alisema inawezekana yeye ana pepo la ngono, ila wewe unapepo la chuma ulete. Linapofika
swala la pesa, na wewe huwezi kujisaidia. Unatoa yeyote kafara.” Baba Chale akamtizama
kwa kumsuta.
“Kwa
hiyo habari ndio hiyo. Poteza pesa, fanya lolote kwa huyo mwanasheria wako,
ujue hutakaa ukashinda kesi. Huna mali. Wewe ni mshenzi Manda, na Mungu
anakulipiza hapahapa duniani. Kalia makochi haya ya mwanangu. Na lalia kitanda
chake, ili iwe hukumu yako. Kila kitu utakachokiona humu ndani, ukumbuke damu
uliyomwaga ya mtoto wa Tunda, na Tunda mwenyewe.”
“Kila
pesa utakayoingiza kwa kutumia kampuni ya Tunda, ikawe chungu kama uchungu
aliokuwa akiupata mwanangu wakati akibakwa na mumeo.” Akamgeukia mama Penny.
“Mama
Penny, wala huna haja yakumpokonya hivi vitu. Mwache atumie machozi na jasho la
mwanangu. Vitampalia mpaka vimtokee puani. Wewe si ni mshenzi Manda? Basi
utakumbuka ubaya wako wote uliofanya na kuufurahia hapa duniani. Labda Mungu
aingilie kati, akusaidie. Hata hapa utapaona pachungu. Si unaishi kwa kodi ya
Tunda wewe, jasho litakutoka wakati feni la Tunda linakupuliza.”
“Dua
za kuku hizo Yohana! Hazinipati ng’o! Kwa taarifa yako napata tenda mpaka
nazikataa. Napamba vizuri, kila mtu anasifia. Nina pesa. Hamnibabaishi kwa
lolote.” “Sio wewe umetoka kuomba simu na gari kwa Tunda, ulipokataliwa ukaanza
kumtusi mwanangu?” “Sina shida.” “Sawa. Twendeni.” Akasimama baba Chale au baba
yake Tunda, akafungua mlango akatoka. Wengine wakamfuata nyuma.
Mama Penny aliingia
kwenye gari yake, akarudi kwake, Net ambaye alikuwa dereva, akaondoa gari
kurudi hotelini akiwa na Tunda na baba yake Tunda.
Tunda ahama
nchi.
Mama
Penny na familia yake walikuwepo uwanja wa ndege kumuaga Tunda na mumewe. Baba
yake pia alikuwepo. Ulikuwa ni utengano ambao kila mmoja alikuwa na hisia
tofauti tofauti juu ya Tunda kuondoka. Wakati mwingine walimfurahia, wakati
mwingine waliingiwa hofu wasijue kinachomkabili ng’ambo ya pili ya dunia.
Walikatiwa
tiketi first class. Tunda alikaa dirishani. Net alihakikisha anavaa nguo ambazo
hazitamsumbua baridi, akamuombea na blangeti hapo kwenye ndege, akamfunika.
“Nashukuru
kurudi na mimi Tunda. Angalau akili zitatulia, nitaweza kufanya kazi nikiwa
nimetulia. Nikijua upo nyumbani unanisubiri.” Tunda alitoa tabasamu lililojaa maswali
mengi, akijiambia muda ndio utajibu maswali yote.
Ndege
ilianza kuviacha viwanja vya ndege vya Mwalimu nyerere, Net akaushika mkono
wake, na kuubusu. Tunda alivuta pumzi kwa nguvu akajiweka sawa.
“Asante
Net. Nakushukuru mpenzi wangu.” “Karibu. Naamini tutakuwa sawa.” “Hata mimi
naomba Mungu iwe hivyo.” Wakatulia, safari ikaanza wakiwa wametulia. Hofu
kidogo kwa Tunda.
Ndege
ilipotulia angani, akaweza kulala Net akiwa amekilaza kiti chake mbavu
zisimuume. Aliamka baada ya masaa matatu, Net akiwa amelala. Akatoa mkoba wake,
akaanza kusoma barua alizokuwa akiandikiwa na Net kipindi yupo jela.
Zilikuwa
barua na kadi tofauti tofauti nzuri. Nyingine za kuomba msamaha na nyingine
zakumwambia ni kiasi gani anampenda na kumuomba atoke angalau amuone.
Tunda
akaanza kutokwa na machozi na kujutia kutosoma faraja kubwa aliyokuwa amefumbia
macho. Habari za kufutiwa kesi mbili alizosababisha Net mwenyewe zilikuwemo
kwenye moja za barua hizo. Kuwa alirudi kuishi nchini Canada na anafika hapo
nchini kwa ajili yake, pia alimwandikia.
Net
alifungua macho akabaki akimtizama anavyosoma. Mara nyingine alimuona akitulia
kama akifikiria. Analia na kugeukia dirishani, kisha anaendelea kusoma. Net
alipomuona anamgeukia akafunga macho haraka, akajidai amelala.
Akahisi
anamnyanyua mkono na kuubusu. Akamcheka moyoni. Akajigeuza kumgeukia vizuri,
huku akijidai amelala. Akajua anamwangalia. Aliposikia mlio mdogo wa karatasi,
akajua anaendelea kusoma. Akatulia kabisa kama kumpa nafasi mpaka amalize.
Safari
ilikuwa tulivu, Net alijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kumsaidia ili asichoke
au kuumwa mbavu. Kumgeuza na kumuwekea mto huku na kule, ilimradi tu asichoke. Alitaka
walale Dubai, lakini Tunda alimwambia yupo sawa tu, waendelee. Hilo pia
alilifurahia Net, ili tu awahi kazini.
Tunda atua nchini Canada.
Walifika
nchini Canada, ilikuwa baridi ndio inaanza.
Sio kali kwa wenyeji lakini si kwa Tunda. Mwezi huo wa 9, kwa Tunda
alihisi baridi kali sana. “Pole na safari.” Tunda akacheka. “Na wewe Net.
Hujachoka?” “Nimeanza kuzoea. Nimefanya hizo safari miezi sita mfululizo kama
rubani!” “Pole mpenzi wangu.” Net akacheka tu akijua amepata ukweli wote kwenye
zile barua. Akajua kilichokuwa kikiendelea wakati yupo jela, mwenzake akienda
kumtembelea na kukataa kumuona. Akajua ile pole ni ya mengi.
Tunda
alishangaa hayo mapokezi. Ni kama Net aliandaa kila kitu. Maya na bibi yake
walikuwepo uwanjani hapo na nguo nzito zaidi kwa Tunda ambaye alikuwa mgeni kwa
baridi. Maya akamsadia kumvalisha zile nguo. Kuanzia usoni mpaka buti nyepesi za
manyoya. Walimfurahia sana Tunda, mpaka Tunda aliweza kuona usoni mwao,
akafarijika na hofu ikaanza kupungua.
Gari
kubwa ilikuwa ikiwasubiria nje, na yenyewe ilikuwa imewashwa upande wa joto na
dereva alikuwa ndani akiwasubiri. Ilikuwa gari ya thamani sana iliyomtoa macho
Tunda. Kulikuwa na dereva mwingine na gari ambayo ilikuwa ikichukua mizigo ya
kina Tunda.
Alichokifanya
Net alipofika pale uwanjani alitoa maagizo juu ya mizigo yao kwa yule dereva
wakati yeye akikumbatiana na bibi yake na Maya. Akamuachia jukumu yule dereva.
Alipopata mabegi, akamuonyesha Net, akakubali kama niyenyewe. Yalikuwa na
majina ya Cote.
Aliyachukua
yale mabegi bila hata kuambiwa, akaondoka nayo wakati Maya akimvalisha Tunda
koti zito la baridi, skafu, buti hizo za baridi, kofia, gloves, ilimradi
kumsitiri na baridi.
Hakujua
kilichoendelea kwenye mizigo yao, ila akaona anaelekezwa kwenye gari ingine.
Alifurahia ile hali ya joto aliyoikuta mle ndani ya gari. Akajikuta anaanza
kusinzia wakati Net akiongea na kucheka na bibi yake pamoja na Maya viti vya
nyuma.
Aliweza
kumsikia mumewe akitoa habari za safari. Alitaka Tunda ndio akae kiti cha mbele
ili aweze kumlazia kiti kidogo. Mbavu zilikuwa zikimuuma.
“Hakupata shida sana.
Ila mbavu ndio zilikuwa zikumuuma.” “Anakula vizuri? Mwili wake umeisha sana!” Alimsikia
bibi Cote akiongeza hilo swali. “Anavitu ambavyo anapenda. Akivipata hivyo,
anakula bila shida.” “Natumaini na huku atapata vitu anavyopenda ili ale. Hivyo
alivyo hawezi kubeba mtoto wa miezi 9. Amedhoofu sana.” Yule bibi alimuona
wakati anamkumbatia pale uwanja wa ndege na wakati Maya akimvalisha.
“Atakuwa
sawa. Naamini akipumzika kwa mwezi mmoja mbele, asiugue, atarudisha nguvu.” Net
akaongeza. “Tutumaini hivyo. Akipumzika leo na kesho, kesho kutwa tutampeleka
kwa dakatri. Aanze kliniki lakini nilimwambia amfanyie vipimo yeye na mtoto.
Ili tuwe na uhakika kuwa wapo salama.”
“Asante
Nana. Ndio maana nakupenda.” Akamsikia mlio wa busu. Wakacheka. Yeye kimya.
Alikuwa amejilaza huku macho yapo nje ya dirisha yakifunga na kufungua kwa usingizi.
Ni kweli alisikia vichomi. Ilikuwa safari ya masaa 18. Alikuwa amechoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Macho
yalimtoka alipooona wanaingia ndani ya geti. Ikabidi afungue macho vizuri. “Utafikiri
jumba la kifalme!” Tunda akashangaa sana. Bustani iliyokuwa imetokea getini
ilikwenda mpaka kwenye hilo jumba. Ilionekana ni kama ya miaka mingi, kama
jumba la maonyesho au kihistoria.
Wasiwasi
ukamwingia Tunda. Dereva akasimamisha mbele kabisa ya hilo jumba. Net akaenda
kumfungulia mlango. “Vipi?” “Natamani tu kulala.” “Basi ndio itakuwa kitu cha
pili.” “Cha kwanza ni nini!?” Tunda akauliza huku akishuka garini. Baridi kali
ikaanza kumpiga.
“Kula,
ndio ukalale. Karibu nyumbani.” Tunda akanyanyua macho kutizama. Ilikuwa usiku.
“Pazuri!” Akasifia. “Hii ni nyumba ya zamani sana. Hata baba yangu alizaliwa
hapa.” Tunda akamtizama Net, Net akacheka.
“Kwa
hiyo na wewe umezaliwa hapa?” “Na Maya pia.” Tunda akacheka huku akitingisha
kichwa. “Kazi ipo!” Alikuwa amemshika mkono wakipandisha ngazi zilizojengwa
hapo kwa mtindo wake, wakielekea ndani.
“Karibu
sana Tunda.” Aliongea Maya kwa lugha ya Kiswahili nakumfanya Tunda acheke na
kugeuka kidogo. “Hujasahau tu kiswahili!?” “Nakumbuka vitu vyamuhimu.” Bibi
Cote naye alikuwa ameshashuka kwenye gari, akamkaribisha Tunda.
Alipofika
katikati ya hizo ngazi na kugeuka nyuma kumtizama bibi Cote na Maya waliokuwa
wakimuongelesha kwa kumkaribisha, Tunda akabaki ameduaa vile ule uwanja na
mataa yake vilivyo. Akazungusha macho kidogo kule macho yake yalipoweza kuona
kwenye mwanga wa taa zilizozunguka bustani mpaka getini. Akaona aingie tu ndani
asitie aibu hapo nje.
Alipoingia
ndani ndipo alipostaajabu zaidi. Jumba lilikuwa kubwa, na vitu vilivyojaza humo
ndani vilionekana ni vya thamani sana, lakini vyote vilionekana ni vya zamani.
Kulikuwa
na picha mbalimbali kubwa kwenye ukuta. Kusafi na wafanyakazi aliowakuta hapo,
wawili. Mfungua mlango alikuwa babu mtu mzima zaidi ya bibi Cote. Alikuwa
kwenye sare. Suti na gloves nyeupe. Mwanamke aliyemtambua kama maid, naye
alikuwa kwenye sare. “Hapa kazi itakuwepo!” Akajiambia Tunda, kisha
akamtizama Net.
Akamuona
anamcheka. “Sasa unacheka nini na wewe Net!?” “Kesho nitakuonyesha video
niliyokuchukua. Ni umeshangaa, mpaka raha.” Net akazidi kucheka. “Naomba uifute
Net, bwana!” “Lazima tuiweke ukumbusho.” Tunda akacheka. “Sasa kwa nini
hukuniambia kama tunakuja kwenye jumba la kifalme?” Mpaka Net akacheka kwa
sauti.
Bibi
Cote akawageukia. “Kuna nini?” Akamuuliza Net. “Naona amechoka tu. Atakuwa
sawa.” Net alijibu huku akimcheka Tunda. “Sasa hapa ili nisiendelee kutia aibu
zaidi, nipeleke chumbani kwanza. Nataka nijisaidie halafu nijilaze kidogo.
Mbavu zote zinauma!” Wakaongozana.
Tunda
aliendelea kushangaa korido nzima wakiwa wanaelekea huko chumbani kwa Net. Kila
kitu kilipangiliwa kwa ustadi wa hali ya juu. Upande mmoja wa hizo kuta, aliweza
kuona picha kubwa sana zilizopangwa kwa mpangilio. Baba ya babu yake Net, akaja
babu yake, baba yake kisha picha kubwa ya Net. Na zote ni nusu, wakiwa wamekaa
na mavazi nadhifu sana. Picha kubwa na fremu za chuma kizito cha dhahabu.
Akaendelea
kumfuata Net kwa nyuma. Akamuona anafungua lango kubwa. Tunda akavuta pumzi. “Hiki
chumba nilikilalia tokea siku ya kwanza naingia humu ndani.” Net aliongea
wakati anampisha mlangoni aingie. Mlango wenyewe ulionekana wa zamani halafu
wathamani.
Kuingia
humo ndani upande mmoja wa ukuta ulikuwa na picha za Net tokea ana siku ya
kwanza mpaka ya harusi yake na Tunda. Zilipangiliwa vizuri. Tunda akaduaa.
Hakuwa hata akijua kama kulikuwa na picha za harusi! Kilikuwa ni chumba kikubwa
sana, kizuri. Jinsi kilivyokuwa kikubwa hicho chumba ni kama nyumba ya mtu.
Akabaki ameduaa, asielewe ni nini Net amempendea yeye!
Akarudisha
macho nyuma. Alipita picha iliyomshangaza. Net alikuwa ameinama akimvalisha ile
cheni ya mguuni. Akamgeukia Net. “Kwani siku ile pale hotelini, kulikuwa na
mpiga picha!?” “Nilimwambia asisumbue, ndio maana hukumuona. Ila nilimleta
kutoka huku sio mtu wa kule.” Tunda akakunja uso, na kurudisha macho ukutani.
Ilitengenezwa vizuri sana. Kuanzia picha yenyewe mpaka ilivyoundwa pale
ukutani.
Akagundua
Net yule wa Tanzania, siye huyu wa nchini Canada hata kidogo. Taratibu akaanza
kuelewa ni nini Mama Cote alikuwa akimaanisha. Huo utajiri aliokuwa akiongelea.
Akameza mate. “Utajikojolea Tunda! Twende chooni.” Tunda akacheka na kumfuata
Net nyuma. Kuingia tu chooni, akasimama katikati ya kile chumba, akaanza
kuangaza macho.
“Usingizi
wote umeisha! Kesho nitakuwa na kazi yakupiga picha nimtumie mama Penny, dada
yangu. Tushangae wote.” Net alicheka sana. “Unafikiri Net?” “Naelewa Tunda.
Hata mimi najua kama ni pazuri. Bibi anatumia pesa nyingi sana kupatunza hapa.
Kila kitu hapa kina historia yake. Hakuna aliyewahi kufika hapa, akatosheka.
Kwa hiyo hata mimi naelewa. Sikushangai.” “Afadhali.” Tunda alielekea chooni,
akatoka. Alimkuta Net akimsubiria nje.
“Naomba
ukajaribu kula ndio ulale.” “Nimechoka Net, kuja kuanza kula vyakula ambavyo
sivielewi naweza kuanza kutapika, nikaishia kushindwa kulala. Acha nisijitibue
kwa usiku huu, nilale.” “Kabla hujakaa, naomba twende ukaangalie. Nana na Maya
wanatusubiria. Twende.” Akiwa amechoka, akajivuta taratibu akimfuata Net nyuma
huku akitupia tena macho kulia na kushoto.
Kwanza
alisimama alipofika sehemu ya kulia chakula. Akabaki amepigwa na butwaa. Bibi
Cote na Maya walikuwa wamekaa mezani wakiwasubiria. “Wametupa recipe ya hiki
chakula, wamesema huwa unapenda kukila. Na aina ya uji. Chef amejaribu kupika,
naamini utapenda.” Bibi Cote akavunja ukimya.
Meza
ilikuwa imeandaliwa, kama hotelini! Hicho chumba chenyewe tu na aina ya viti
pamoja na meza yenyewe, vilimtoa macho Tunda. Aliyekuwa akihudumia pale alikuwa
kijana wa kizungu, mrefu, mzuri na amevaa sare maalumu, akionyesha kweli yupo
kazini.
Net
akamvutia kiti. Tunda akakaa. “Asanteni sana.” Tunda alishukuru kwa lugha yao.
Na wote mle ndani walikuwa weupe kasoro Tunda tu.
Alicheka
alipoona ndizi za kupikwa Canada. Akamwangalia Net. “Nilimuomba mama Penny
aniandikie kila kitu na vipimo vyake, nikamtumia Maya, Maya akampa chef, sasa
onja kama amepatia.” “Asante Maya.” Maya akacheka na kubaki wakisubiria aonje
ili wajue kama atapenda.
“Tunatamani
ule vizuri Tunda. Umekonda sana!” “Nitakuwa sawa. Niliugua sana. Karibu kipindi
cha miezi mitano nyuma, sikuwa nakula vizuri. Magonjwa yalikuwa yakipokezana.
UTI haikuwa ikiisha. Hata first trimister ya mimba, haikuwa rahisi. Naamini
nitakuwa sawa tu.”
“Tutakwenda
kwa daktari kuangalia afya yako na ya mtoto. Wakupe na kinga zakukufanya
usiugue tena ili urudishe nguvu na mwili. Uweze kubeba mtoto vizuri.” Aliongeza
bibi Cote. “Nitashukuru.”
Net
alimuwekea chakula kwenye sahani. “Jaribu.” Tunda akajisogezea karibu. Akaweka
mdomoni. Wakamuona anacheka. “Nikizuri.” Tunda akasifia. “Asanteni.” Akashukuru
akiwatizama wote, maana ni kama wote walitulia wakimsubiria wajue kama atapenda
kile chakula.
Alimsikia
Net akivuta pumzi kwa nguvu. “Hey Gino! Thanks Man. She likes it.” Net aliongea
kwa sauti, akasikia mtu upande wa pili akicheka. “You’re the best, Gino.” Maya
akaongeza kutoa sifa wakimshukuru huyo Gino. Tunda hakuwa ameelewa Gino ni nani,
lakini akahisi ndiye mpishi. Alicheka tu taratibu akaendelea kula.
Bibi
Cote alikuwa kimya akitabasamu na bakuli dogo tu, Tunda alijua ni supu. Kwa
aina ya kijiko alichokuwa akitumia na bakuli kama kikombe. Akaamua atulie na
sahani yake ya ndizi.
Mara
yule kijana aliyekuwa akipanga chakula pale mezani akarudi pale kutoka chumba
cha pili, ambapo alijua ndio itakuwa jikoni. “You are welcome guys.” Akajua
ndio Gino.
“Ni
nini nilitakiwa kuongeza au kupunguza?” Akamuuliza Tunda kwa heshima sana. Wote
wakamtizama Tunda. “Mwambie ili kesho akupikie vizuri zaidi.” Akaongeza Maya. “Nakiona
kipo sahihi kabisa. Nimependa, asante Gino.” “Karibu sana.” Hapo Gino alijibu
kwa Kiswahili sio kingereza tena, nakufanya meza nzima wacheke.
Hata
hivyo alisikika na lafudhi tofauti na bibi Cote au hata Maya. Tunda akajua sio
mtu wa pale. Aliongea kingereza chenye lafudhi nzito kidogo.
“You
did your homework good, Gino!” “With Maya’s help too.” Gino akamjibu Net huku
akicheka baada yakusifiwa na Net. Wakacheka. “Nakushukuru sana. Utayafanya
maisha ya Tunda kuwa rahisi. Na samahani kukufanya kukaa kazini mpaka muda
huu.” “Chochote kwa ajili yako, Net.” Gino akajibu kwa heshima sana. Net
akatabasamu.
“Nafikiri
unaweza kwenda tu kupumzika. Tutamalizia sisi wenyewe hapa mezani, kesho
utakuja kuendelea pale tulipobakisha.” Net aliendelea kuzungumza na Gino kwa
lugha ya Kingereza. “Una uhakika?” “Kabisa. Sasa hivi ni usiku sana, najua na
wewe ungependa kwenda kupumzika. Lakini kabla yakuondoka, naomba nikutambulishe
kwa mke wangu. Najua yeye ndio mtakuwa naye hapa kwa muda mrefu.” Tunda
akanyanyua uso kumtizama Net, natabasamu usoni.
“Kwa
hiyo huyu ndiye mama Cote mwenyewe?” “Haswaa!” Net alijibu kwa kujivuna kidogo.
“Kweli ni unique kama ulivyokuwa ukituambia. Na ni mzuri.” “Asante Gino.”
Wakati wote Gino alizungumza huku mikono ameikutanisha mbele kwa heshima zote.
“Karibu
sana Tunda.” Gino akaongea tena kwa Kiswahili chakuunganisha kidogo. Tunda akacheka,
“Asante Gino. Nitakufundisha mapishi mengi ya Kitanzania.” Akajibu kwa
kingereza ila ‘Asante’ kwa kiswahili. “Na lugha pia.” Gino akaongeza, wakacheka
tena kidogo. “Bila shaka.” Akajibu Tunda. Gino akaondoka baada yakuwaletea
baadhi ya vitu pale mezani. Kama matunda, juisi na maziwa kwa bibi Cote. Akaaga
na kuondoka.
Tunda
alikula vizuri, lakini akakataa kunywa juisi. Akamwambia Net atashindwa kulala
kama atakunywa juisi au maji. Atakuwa akiamka kwenda chooni usiku wote.
“Kesho
tutakwenda kazini. Kama tutaondoka mkiwa bado mmelala, basi mjue atakuja
msaidizi wa Tunda, ambaye atakuwa akikusaidia mambo ya mtoto pia. Nilimwambia
aanze kazi mapema kidogo, ili mzoeane kabla ya mtoto kuja. Na mtu wa kukufanyia
masaji.” Tunda akatoa macho vizuri na kumgeukia Net. Net akacheka.
“Asante
Nana. Ndio maana nakupenda! Nitakuja kazini mchana, baada yakumuonyesha
mazingira Tunda.” “Hakuna shida. Wewe pumzika tu.” “Sawa, lakini nitakuja
ofisini mchana.” “Sawa.” Bibi Cote akajibu. Net akaenda kumbusu pale alipokuwa
amekaa, akambusu na Maya. Wakaondoka kurudi chumbani.
Net & Tunda!
Tunda
akamvuta Net kwenye kochi mara baada yakuingia chumbani kwao. “Kwanza hembu
njoo ukae hapa mimi niulize maswali.” Net akaanza kucheka. “Ujue wewe Net ni
mbaya sana?” “Nini tena?” “Kwa nini hukuniambia kama haya ndio maisha ya huku
kwenu!?” Net alizidi kucheka.
“Unaishi
kwenye jumba la maonyesho! Mnampishi anayewapikia, tena maalumu! Mnakaa mezani
kama wafalme, mnahudumiwa! Vyakula vinasindikizwa sijui na nini! Mnaanza na
supu, sijui mnakula nini na nini, mlo mmoja!” “Ni full course dinner, Tunda.” Net alimsaidia huku akicheka sana.
“Ewaah!
Hiyo hiyo. Sasa hiyo ni leo tu kwa kuwa mimi nilikuwepo au siku zote?” Net
alitingisha kichwa kukataa huku akicheka sana. “Basi kazi ipo! Haya,
mnajifunika vitambaa vinayoendana na…” “Ni napkins.” Net akaongeza.
“Bwana
mimi leo jasho limenitoka! Sasa ulaji ule na utaratibu wake itakuwa kila siku!?”
Net alicheka mpaka akainama. “Net hujanitendea haki bwana! Ungeniambia
mapema.” “Nisikilize Tunda. Acha
nikwambie ukweli. Hapa nchini, au haya maeneo, ukiuliza matajiri wa hapa, hutakosa
kusikia jina la Cote. Tunafahamika sana. Bibi na babu, wametafuta mali na
wakafanikiwa sana. Wamewekeza kwenye hii aridhi, kwa kiwango kikubwa sana.”
“Kwa
kifupi tu, yale yote aliyokwambia mama kwa sehemu, japo kwa wakati ule sikutaka
kwenda kwa undani, ni kweli. Pesa ipo. Nilikuja kuishi Tanzania moja ya lengo
kubwa ni kutafuta mwanamke atakayenipenda kwa vile nilivyo mimi, wala si jina
au mali.” Tunda akaanza kuishiwa utani.
“Wengi
wa wanawake hapa, nikisema wengi, namaanisha wapo wengi sana. Wanampenda
Nathaniel Cote kwa sababu ya mali. Na mbaya zaidi, hakuna mapenzi ya kweli.
Wakiingia kwenye ndoa kwa muda mfupi tu watataka talaka ili muachane, wanufaike
na mali ambazo wananufaika kwa ndoa waliyoingia kwa muda mfupi sana.”
“Walihangaika
sana kwa babu. Kwa kuwa babu alibahatika mwanamke mzuri, yaani Nana, hawakuwahi
kutengana. Upendo ukawa siri ya mafanikio yao. Hakuna sehemu ungewatengenisha,
kuanzia nyumbani mpaka kazini. Nana alimkuta papa akifanya kazi na baba yake
kwenye ile kampuni, akatulia, akafanya nao kazi, mpaka wote wamefariki
wakamuacha Nana.”
“Unakumbuka
nilikwambia habari za Chloe?” Tunda akatingisha kichwa. “Chloe alinikubali kwa
haraka sana. Nikataka kujua kwa hakika kama kweli anampenda Net au utajiri.
Nilimpa maisha mazuri sana hapa nchini. Sasa nilipomuomba kama anaweza
kuongozana na mimi Tanzania. Nilipata jibu langu pale aliposema yupo radhi
anisubirie hapa nchini, kuliko kuhama naye nakumpeleka nchi masikini kama
Tanzania.”
“Aliniomba
nimuoe, halafu nimuache hapa nyumbani, yeye atanisubiri tu. Nikajua moja kwa
moja anachotaka nikuishi humu ndani. Ndipo nikamwambia babu, Chloe sio Tunda.” “Sasa
wewe ulijuaje kama mimi ndio mkeo wakati ulinikuta kwenye mazingira ya ajabu
tokea mwanzo!?” Ikabidi Tunda kuuliza.
“Kwanza wewe nilikupenda tu. Yaani nilikuta
moyo wangu umefungamanisha na wewe, siwezi kujisaidia.” Tunda akacheka kidogo. “Ombi
kubwa na hata bibi nilimuomba azungumze na mama, tena kwa kumtisha, ni
asikwambie ukweli wote juu yangu. Lakini akawa ni kama anashindwa akihisi ni
kama unajua kwa kupitia mimi mwenyewe au Gabriel.”
“Ndio
maana akawa anahangaika akihisi unanipendea pesa. Lakini nilimuhakikishia kuwa
hunifahamu kwa undani na nikiwa na wewe huwa hatuzungumzii mali kabisa.
Nikamuhakikishia mama kuwa wewe hunipendei pesa, na wala hutaki pesa yangu.
Nikamwambia nilishajaribu mara kadhaa kutaka kukusaidia, lakini ulikuwa
ukikataa.” Tunda akazidi kushangaa kila alipofikiria kumbe alikuwa akisomwa na
Net.
“Hukufanya
vizuri Net!” “Hapana Tunda. Ninahaki yakupendwa mimi kama Net. Sikuchagua
kuzaliwa na kina Cote. Sikutaka hili jina, lininyime furaha maishani. Ndoa ni
ngumu Tunda, hasa hapa nchini kwetu na watu wa asili ya huku. Wengi
wanaendeshwa na hisia. Wanandoa wengi wanaoana sababu ya mali. Nyumba hazina
amani sababu ya mali.”
“Hilo
babu amekuwa nalo makini kuanzia kwa baba yangu mpaka kwangu. Alitufundisha
hivyo kwa makini, ndio maana hawabagui rangi. Ilimradi ukisema anafaa, hawana
neno. Watakuheshimu kwa heshima ileile wangemuheshimu mwanamke mweupe ambaye
angeolewa hapa.” “Unajuaje? Kwani wewe ulishawahi kuoa kabla?” Tunda akauliza.
“Baba
amemuoa mwanamke wa Tanzania. Mama alipendwa na kutumikiwa humu ndani, mpaka
alipoamua kuondoka yeye mwenyewe. Sikuwahi hata kumsikia akilalamika kuwa
anafanyiwa ubaguzi. Katika yote hilo hajawahi kulisema hata mara moja.”
“Ila
mimi namuogopa bibi yenu bwana! Anaonekana yupo serious sana akizungumza na
watu wengine mbali na wewe na Maya, sura inakuwa ya kazi tu!” Net akacheka. “Akiwa
na wewe na Maya, utafikiri sio yeye! Mtu wa tofauti kabisa! Sura na sauti
inakuwa ya tofauti kama mama anayelea watoto wadogo wakati ni nyinyi wakubwa
wazima!” “Utamzoea tu. Na yeye atakuzoea. Mpe muda.” Tunda akajivuta nyuma
akiwaza huku akiangaza macho kwenye hicho chumba kimoja tu, cha Net. Akawa kama
kuna habari imepita kichwani mwake kwa gafla.
Akamwangalia
Net, na kukunja uso. “Sasa ingekuaje kama ningekataa kuja huku?” “Kwanza siku
ile pale hotelini uliniogopesha sana Tunda! Kwa sababu nilishampigia simu Nana
nikamwambia umekubali kuja na mimi. Swala la kuwa unanipenda, hilo halikuwa na
swali tena. Ulishanionyesha unanipenda na umenichagua mimi. Ndio maana
sikukukatia tamaa hata ulipokuwa jela. Nilishamwambia Nana, wewe ndiye mwanamke
utakayeishi na mimi humu ndani na kunizika.” Hilo likamgusa Tunda, akatabasamu.
Net
akaendelea. “Wasiwasi ukamwingia kama utaweza kusamehe ubaya uliofanyiwa na
mama yangu! Maana alijua kuwa mama Penny na mumewe walinilaumu sana na wao ndio
wako karibu sana na wewe.” Tunda akakunja uso akiwa hajaelewa.
“Mama
Penny alikulaumu!?” “Oooh vibaya sana! Walinibana kwa shutuma za kweli tupu. Ni
kama walinifukuza nyumbani kwao kwa hasira siku ile. Maana kabla ya harusi, yaani
siku ile ya harusi, mama alipokuja na kuondoka kwa hasira, unajua baba Penny
alinisihi niahirishe harusi mpaka nikaweke mambo ya familia yangu sawa?”
“Sikujua!” Tunda hakuwa akijua lolote hata kama mama Cote alishamfuata mwanae
pale kwake siku ile ya harusi.
“Basi
siku ile ilikuwa mbaya, nusu harusi isifungwe. Anyways, nikakataa ushauri wa baba
Penny wa kuahirisha harusi. Ndoa ikafungwa ndipo sasa ukaishia jela! Mama Penny
na mumewe walinichukia sana. Mpaka nikashindwa kumtafuta baba yako, nikajua na
yeye itakuwa hivyo hivyo.” “Pole sana Net. Mimi sikuwa najua yote hayo!” Tunda
akajikuta akimuhurumia.
“Sasa
huo moyo wako wakunihurumia nakujali ninachokisikia, ndio kitu kilikuwa
kikifanya nione siku haziendi nirudi Tanzania kuja kukuona jela, na kukaa pale
bila kukata tamaa, nikijua labda unaweza kuja kutoka, ukaniangalia. Lakini
wapi.!” Tunda akacheka.
“Usicheke
Tunda. Was not Funny!” “Si ulishasamehe lakini na ukasema umejilipiza?” Net
akacheka, akakumbuka usiku aliofanya naye mapenzi, yeye akaridhika bila
kumridhisha Tunda, akamwambia amejilipiza.
“Sasa
nikaja kukutana na baba yako pale gerezani, hana hata lawama, amejawa tu
shukurani. Wewe ndio ukawa hata hujui ni kwa nini najilaumu. Nikasema asante
Mungu wangu kwa mke. Halafu ukatoka mjamzito! Nilijiambia kufa na kupona, damu
ya Cote haipotei bure. Ukanipotea kama week mbili. Nikakaribia kuchanganyikiwa.
Na ile hali yako ilivyokuwa baada yakutoka jela, nikawa namwambia mama Penny
labda utakuwa umezidiwa ukafia sehemu.” Tunda akazidi kucheka.
“Lakini
niliwatumia ujumbe wewe na mama Penny kuwa naumwa, nimepewa dawa. Tena wewe nilifanya
vile makusudi ili nisije kunywa zile dawa kali, mwanao akatoka, ukasema
nimemuua. Nikajiambia nikwambie mapema!” “Ulituma ujumbe na kuzima simu! Acha
nizidi kuchanganyikiwa nikawa kama mwehu namsumbua mama Penny kila wakati. Mara
baada ya majuma mawili, mama Penny akanipigia, akaniambia umempigia, unataka
akupe kazi. Lakini umeahidi utanitafuta. Nilikesha nasubiri simu yako, Tunda.”
“Pole!”
“Usiku
sana kama saa 7 hivi, uvumilivu ukanishinda. Nikampigia tena mama Penny. Ndio
akaniambia huwa ukiahidi kitu lazima utafanya. Akaniambia pengine unaweza ukawa
umeishiwa muda wa maongezi kwenye simu. Lakini akanifariji na kuniambia lazima
utatokezea pale ukumbini, nikufuate pale. Usipotokea, hapo hata yeye atapatwa
na wasiwasi.”
“Ndio
nikakupata pale, nikaja kukugundua sio kwamba ulikuwa umenikasirikia, ila ulihitaji
muda wakupumzika. Mbali na mimi na mama yangu.” Tunda akacheka sana.
“Maana
nilijiambia hata kama tutarudiana, na mama Cote akaamua kunisingizia kitu
kingine, anirudishe jela, basi angalau niwe nimelala kitanda kizuri,
nimepumzika. Kuliko anikamate tena kwa haraka, nikiwa nimechoka vile! Nikajiambia
ningefia jela siku ya kwanza naingizwa huko. Ehee, Endelea.” Tunda alitaka Net
aendelee.
“Basi,
ndio nikakupanga, nikaona kumbe hukuwa hata na chuki na mimi, ukakubali kila
nilichokwambia. Ndio nikampigia simu Nana nikamwambia narudi na Tunda.
Akafurahi, sasa nikashangaa baadaye unanigeuka!” “Mama Penny na mumewe
waliniogopesha bwana!”
“Ndio
utake kunikimbia!?” “Si hapa nipo na wewe?” “Mmh! Lakini ulinikataa kwanza!”
“Ni hofu tu Net. Siwezi kupata mtu anayenithamani kama wewe. Mimi mwenyewe
nilikuwa kama wewe. Natafuta mtu atakayenipenda mimi kama Tunda na matatizo
yangu yote.” “Basi umempata.” Net akaanza kumbusu.
“Uishie
hapo hapo Net. Mwenzio nimechoka, mbavu zinauma, nataka nioge, nilale.” “Hivyo
hivyo ukiwa umejilaza, mimi napata starehe yangu. Sikusumbui. Nipe ‘Kijiko’.” “Lakini ujue utanisafisha na kunifunika. Mimi
sijigusi.” Tunda akatoa sharti akijua atashindwa.
“Na
hivi nililala kwenye ndege, hata hapa nitakubeba mpaka bafuni. Nikuogeshe na
kukuweka kitandani.” “Kwani mimi sikujui janja yako? Ukifika bafuni utataka
nikupoze kwa kunibeba!” Net akaanza kucheka. “Tunda kwa kuhesabu mambo ya nyuma!” “Wewe
twende tukaoge, halafu upate kijiko, moja tu yakunikaribisha nyumbani. Uchovu
ukiisha, kazi itakuwa moja.” Net akamnyanyua kutoka pale kwenye kochi,
akakimbia naye bafuni. Mapenzi yalianzia bafuni, wala hawakuweza kusubiri mpaka
kitandani.
Tunda
akapata penzi la kwanza ndani ya jumba hilo, kwenye chumba hicho cha thamani.
Kwa yale tu mandhari, kila alipoguswa kwa penzi, haraka sana aliridhika na
kumaliza kwa kufurahia. Akachangamkia mchezo kwa raha zote.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Je, Tunda ndio ameyapatia maisha huko nchi ya ugenini tena uzunguni,
kwenye utajiri? Kweli wenyeji wamempokea vizuri sana.
Je, vita yake ndio imeisha? Ritha atakubali kusikia Tunda yupo
mjengoni akitumikiwa halafu yeye ameuza kila kitu anaishi kwenye apartment
ndogo tu? Usiache kufuatilia kujua mvujisha siri kwenye vyombo vya udaku huko
nchini Canada. Endelea kufuatilia.
0 comments: