SIMULIZI

NILIPOTEA! PART 6 - SEHEMU YA ‘B’.

Monday, July 12, 2021 naomimwakanyamale 0 Comments

Asubuhi ya kwanza nchini Canada.

Asubuhi ya siku inayofuata, Net alimzungusha Tunda kwenye ile nyumba. Akafahamu kila sehemu. Akamtambulisha kwa wafanyakazi wote waliokuwa wakihudumia ndani ya hiyo nyumba. Ilipofika saa nne na nusu, akaja mtu wakumfanyia masaji, na mfanyakazi atakayekuwa akimsaidia yeye na kazi zake mpaka atakapojifungua. Pale pale akamgeukia Net, akazungumza naye kwa kiswahili. Alikuwa ni dada wa makamu, wakizungu.

“We Net! Mimi nafanya nini na huyu mama?” “Chochote unachotaka, mtume.” “Kwani Gino na yule mama mwingine kazi zao ni nini!?” “Gino ni mpishi. Akitayarisha kifungua kinywa asubuhi, anaondoka mpaka jioni anapokuja kuandaa chakula cha usiku au cha jioni. Maana sisi wote tunakuwa kazini. Milo inayoliwa hapa ndani ni asubuhi na jioni. Ms Emily yeye ni usafi wa hapa na pale kwa sababu wapo watu wanaohusika maalumu na usafi wa ndani na nje ya hii nyumba. Yeye anaweka sawa mambo ya humu ndani. Amekuwa akimsaidia bibi tokea Maya ni mtoto mdogo.” Net akaendelea.

“Haya na yule mzee uliyemuona pale mlangoni, ni Carter. Mimi mwenyewe nimezaliwa, nimemkuta na kazi hiyohiyo. Ni watu waaminifu sana. Anapokea wageni, simu na kuwasiliana na Nana, endapo chochote cha humu ndani kinahitajika. Ndio kama kiongozi wa Gino, Ms Emily na watu wanaokuwa wanafika humu ndani kusafisha au kufanya matengenezo. Lazima wapitie kwa Carter au waitwe na Carter.” Net akendelea.

          “Kwa hiyo huyu uliyeletewa sasa hivi, atakuwa ni wako tu na mambo yako binafsi.” Tunda akavuta pumzi akifikiria. “Mkubali tu.” “Hapana Net. Sitaki unigeuze kiwete humu ndani. Nakuwa kama mgonjwa! Sihitaji mimi mtu wakunifuata nyuma bwana!” “Hatakufuata ni mpaka umwite.” “Hapana. Umeshanionyesha sehemu yakufua nguo na kupiga pasi. Sitashindwa kutandika kitanda chetu nakufua nguo zetu. Niki...” “Yupo mtu maalumu wakufua, kupiga pasi na kupanga nguo sehemu husika.” Net akamkatiza. Tunda akabaki amemkodolea macho. Net akaanza kucheka.

“Sasa na huyu naye atakuwa akifanya nini kama si kufuatana nyuma tu?” “Utakuwa ukimtuma vitu vidogo vidogo na ndio utamfundisha kukupikia vitu unavyotaka.” “Hapana Net. Mimi hayo maisha sitayaweza! Sihitaji mtu wangu tena baada ya kazi zote kufanywa! Hapana.” Tunda akaonyesha kama anataka kuadhibiwa!

“Niache hivi hivi. Nitajifanyia vitu vilivyobaki mimi mwenyewe. Nikichoka kupika, Gino atanisaidia. Umeniahidi nikikaribia kujifungua, utamleta mama Penny. Sihitaji mtu Net. Tafadhali.” Tunda alikataa kabisa.

“Wewe unanijua mimi nisivyopenda usimbufu na kuingiliwa. Nataka nikiwa chumbani niwe peke yangu, nitulie. Sio hodi za kuulizwa maswali kila wakati!” “Nitamwambia asifanye hivyo.” “Hapana Net.” “Utamuhitaji Tunda. Kumbuka mimi nitakuwa kazidi kuanzia asubuhi mpaka jioni. Utakuwa peke yako hapa ndani.” Bado Net aliona umuhimu wa yule mfanyakazi aliyeletwa kwa ajili ya Tunda.

“Sihitaji mtu Net. Tafadhali. Nikitaka mtu wakuzungumza naye nitamfuata babu Carter au Ms. Emily. Nitapiga nao stori. Gino akipika vitu ambavyo havinikeri, nitaenda niwe naye jikoni ili anifundishe na nitakuwa naweka chakula mimi kesho yake mchana wakati nyinyi mpo kazini.” “Ule viporo!?” Net akashangaa sana.

“Ujue wewe Net unazungumza na mimi Tunda? Naomba mruhusu tu huya mama aende. Mwambie mpaka mtoto akizaliwa, mimi ndio nitamtafuta. Nikiwa na maana, nitakapoona uhitaji.” “Sawa Tunda.” Ikabidi Net akubali tu.

Akamruhusu yule mfanyakazi aliyekuwa ameletwa kwa ajili ya Tunda. Akamwambia atampigia wakati mwingine. Aliondoka akionekana kunyongea kabisa. Ni kama Tunda alimnyima ulaji.

“Haya twende kwenye masaji. Ila mimi nitakuacha wakati wakikufanyia, naenda kazini. Nitarudi baada ya muda mfupi.” “Wewe nenda kafanye kazi dad!” Net akacheka na kumbusu.

“Ndio maana nakupenda. Nilijua utataka tukae wote.” “Mimi na Cote tutakufa njaa kama mama na dad wakiendekeza kupendana.” Net akacheka sana, na hilo likamfariji. “Nashukuru kama unaelewa. Ila sitachelewa. Nitarudi mapema.” “Nakuombea uwe na wakati mzuri.” Net akambusu tena.

“Sasa wakati wanakufanyia masaji, wewe lala kabisa, usiwe na wasiwasi. Wakimaliza, wataondoka.” “Sawa. Lakini Net, naomba uwaambie wote, sitaki kufuatwa chumbani tafadhali. Nikiwa chumbani waniache kabisa na wasiingie mpaka mimi mwenyewe niwapigie kama nitawahitaji.” Net akaanza kucheka. Alimjua Tunda.

“Wakati mwingine watataka kujua kama una njaa!” “Hayo ndio nisiyoyataka mimi. Nikitaka kitu nitawapigia au nitafuata chakula mimi mwenyewe. Ratiba ya usafi hapa, Ms Emily anayo. Asubuhi wakati nakwenda kupata kifungua kinywa, nitakuwa napanga naye. Wakitaka kusafisha, nitajipanga niwaachie chumba.  Lakini sio hodi yakuulizwa kama nataka maji, matunda sijui chakula! Hapana kwa kweli! Wataninyima raha Net. Wewe unajua jinsi ninavyothamini chumba ninacholala. Ndio sehemu pekee napata utulivu nakuweza kufikiria.” “Sawa. Nimeelewa. Nitawaambia hakuna mtu yeyote anaruhusiwa kuingia chumbani kwetu mpaka awe ameitwa.” Tunda akacheka akionekana kuridhika. Muda wote huo walikuwa wakizungumza kwa lugha ya Kiswahili tu. Kwa hiyo ilikuwa rahisi kuteta.

Tunda alielekezwa kwenye chumba maalumu, akapewa kitu cha kujifunga. Wakaanza kumfanyia masaji. Ile hali ya utulivu ndani ya kile chumba na mziki uliokuwa umewekwa kwa sauti ya chini, ikamfanya alale, wala asijue walimaliza saa ngapi.

Masaa yakaenda, muda wakula chakula cha mchana ukafika na kupita, Tunda akawa bado amelala. Maagizo ilikuwa aachwe apumzike.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Asubuhi yake Gino alikuwa ametengeneza kifungua kinywa kikubwa, Tunda alifika pale mezani nakubaki ametoa macho. Akamuona bibi Cote amepakua matunda. Alipomaliza, akala na yogurt. Akawa amemaliza mlo wa asubuhi. Maya yeye alianza juisi ya nanasi, baada ya muda akapakua mayai, akamtuma Gino amfungashie kahawa, wakaondoka na bibi yao, ndipo Tunda akahema.

“Haya nisogezee mimi hivyo vyakula, nianze kula kwa raha yote. Mnakula kwa kudonoa!” Net akaanza kucheka. Akamsogezea. Akapakua becon, mayai, sausages na muffin nzima. Akaanza kula. “Mimi nataka kunenepa. Acha nile.” Net alikuwa akimwangalia tu na kumsogezea hiki na kile, Tunda anaendelea kula. Akamaliza na kuongeza tena na tena, mpaka akaridhika.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Sasa ukichanganya na hayo masaji na Gino alimwambia amempikia uji wa ulezi upo kwenye chupa, Tunda alilala mpaka akapata na ndoto. Butler wao, mzee Carter akampigia simu Net kuwa mkewe amelala tokea ile asubuhi. Net akacheka. “Muache tu. Amechoka na safari.” “Vipi kuhusu chakula? Muda unazidi kwenda!” “Akisikia njaa ataamka yeye mwenyewe. Ila na mimi nitakuja baada ya muda sio mrefu. Thanks Carter.” “Any time Son!” Net akakata simu huku akicheka.

Akakumbuka usiku yeye mwenyewe Tunda aliyesema amechoka waoge tu walale, lakini baada ya kumchokoza kidogo tu wakati wapo bafuni Tunda mwenyewe akaanza kumng’ang’ania. Kila Net alipotaka kukatisha, Tunda alimvuta tena. Walipofika kitandani pia wakaendeleza mapenzi. Walilala kwa kuchelewa kwa sababu yakuzungumza na mapenzi.

Net alirudi akamkuta mkewe bado amelala. Akaanza kucheka. “Sasa unacheka nini bwana Net!?” Tunda aliamshwa na kicheko cha mumewe. “Umelala kihasara!” “Bwana yale masaji si mchezo! Nahisi ni mtaalamu haswa. Sijawahi pata masaji ya namna hii. Ndio inakua kila siku?” Net akaanza kucheka tena.

“Wewe ukitaka tu, mwambie Carter. Atawapigia. Na wakija, uwaambie lini tena unataka warudi.” “Mimi naona kwa sasa, iwe kila siku mpaka uchovu uishe.” Net akazidi kucheka. “Haya, twende ukale. Nitamwambia Carter awapigie, kesho waje tena.” “Hayo ndiyo maneno.” Akamsaidia kuvaa, wakatoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Siku inayofuata Net aliondoka asubuhi kuelekea kazini, lakini akarudi kwenye saa nane mchana. Akapumzika na Tunda. Wakazunguka humo ndani wakiongea hili na lile, Tunda akamlalamikia hajazungumza na baba yake na mama Penny kuwataarifu alifika kwao salama. Ndipo wazo likamjia kuagiza simu yenye line yake.

“Hebu subiri kwanza Net. Yaani unaagiza mtu anakuletea hapahapa?!” “Ni mfanyakazi wa ofisini anayehusika na manunuzi. Usiwe na wasiwasi, atakuletea simu nzuri tu.” “Sasa kwa nini tusiende wenyewe?” “Na yeye atakuwa akifanya kazi gani sasa?” Tunda akatoa macho. Hakika Net huyu siye aliyemjua tokea mwanzo.

Na kweli, baada ya masaa mawili tu, alikuja kijana mtanashati. Alikuwa mweupe na lafudhi ya pale. Akafunguliwa mlango na Carter, akaelekezwa alipokuwepo Net na mkewe. Akasalimia kwa heshima zote, akamkabidhi Net ile simu.

“Ipo kwa jina la Mrs Cote kama ulivyoniambia. Imeshafunguliwa, anaweza kutumia.” “Asante.” Aliongea tu hivyo, na Net akajibu kwa kifupi tu, akaondoka. Tunda akabaki ametoa macho. Ilikuwa simu nzuri sana. Mpyaa.

Akamkabidhi Tunda. “Asante mpenzi wangu.” “Unaweza kuwapigia kesho, maana sasa hivi watakuwa wamelala.” Tunda akakumbuka walipo na Tanzania ni tofauti ya masaa 9 kwa wakati ule. Akajua kweli itakuwa kule ni usiku.

 

Kwa mara ya kwanza Tunda Awasiliana na Nyumbani Tanzania.

Kesho yake Net alipokwenda tu kazini, Tunda akampigia wa kwanza simu mama Penny. “Nimeona namba ya majuu, nikajikonyeza.” Tunda akaanza kucheka. “Nimekumiss dada yangu!” “Wala mimi sitaki kuongea. Niambie, ulipokelewa huko vizuri?” “Mimi naomba utafute mahali, ukae dada yangu. Nina mengi, nilijua wewe utanifaa.” “Mbona unanitisha?” “Mambo mazuri, usigope. Nataka kukupigia kwa video, nikuonyeshe. Tafuta mahali pazuri ukae.” Mama Penny akaenda sebuleni, akijua anataka kuonyeshwa mtoto huko tumboni.

Tunda akapiga tena kwa video. “Naona mpaka uso umebadilika mdogo wangu!” Tunda akacheka, “Ninavyopendwa!” “Eeh Tunda!” “Sana dada. Napendwa mno!” Tunda akajisifia, mama Penny akacheka simu ikasogea akamuona na mchungaji pembeni. Akaona aibu.

Akamsalimia huku anacheka. “Hujambo Tunda?” “Nilikuwa nataka kumtoa ushamba dada yangu ndio maana nimempigia kwa video.” Tunda aliongea kwa aibu huku akicheka. “Mimi mwenyewe nataka kushangaa. Wewe tuonyeshe tu.”  Tunda akacheka kidogo kama anayejishauri. Alishaishiwa mori baada ya kumuona mchungaji.

“We Tunda!” Mama Penny akamshtua. “Nilichokuwa nataka kusema ni hivi, yule Net tuliyekuwa tukimfahamu huko nyumbani, siye huyu wa huku, dada yangu.” “Kwa nini?” “Kwanza wanatoka kwenye ukoo wa kitajiri sana huku. Yaani ni zaidi ya matajiri hao mnaowasikia huko nyumbani. Yaani..” “Ndio maana mama yake alikuwa akihangaika!” Mama Penny akamkatisha.

“Sawa sawa mama Penny. Yaani humu ndani tu hapa chumbani kwetu, sijamaliza kushangaa. Hiki chumba chetu tu, ni ukubwa kama wa kile kinyumba chote nilichokuwa nikiishi kule Kimara!” “Haiwezekani Tunda!” Mama Penny akashangaa.

“Nakwambia mimi mwenyewe sijamaliza kushangaa. Hicho chumba cha nguo cha Net, kama duka. Na pembeni kuna chumba cha viatu. Kumepangwa, mimi mwenyewe mpenda vitu vya thamani, hapa nimepakubali. Hujawahi ona vitu vizuri na vya thamani kama hivi, dada yangu!” “Mimi naona utuonyeshe tu.” Tunda akaanza kucheka.

“Naomba nianzie kwenye madirisha tu yakuzunguka hichi chumba na mapazia yake na muundo.” Akageuza kamera akaanza kuwaonyesha. “Oooooh! Tunda?” Mama Penny akaanza kushangaa.

“Mbona unakimbia Tunda, bwana!? Rudi nyuma kidogo. Kuna kitu kama nimeona hapo!” Tunda akarudisha. “Wewe Tunda, hicho ndio kitanda chenu!?” “Hapo nilitaka kukuonyesha mwishoni mama Penny. Hilo ndio eneo la kitanda!” “Mungu wangu!”  Wakajikuta yeye na mumewe wanashangaa kwa pamoja.

“Hapo mimi nisingeamka.” Tunda akacheka sana. “Wanatumikiwa kama nini sijui! Kuna wafanyakazi wa kila kitu. Mkija naona ndio mtashangaa vizuri.” “Hapo ni wapi?” “Bado ni humu humu ndani baba Penny. Chumba kilichokuwa cha Net, tokea mdogo. Ngoja niwaonyeshe na picha za mpaka harusi yetu.” Akawageuzia ukutani kuonyesha hizo picha jinsi zilivyopangwa.

Angalau Tunda aliongea na kucheka akapata wanoweza kumuelewa vizuri sio Net aliyekuwa akicheka jinsi anavyoshangaa.

Waliongea zaidi ya lisaa. “Tunda mama, huyo kijana anakupenda. Kwa hayo mazingira hapo, na vile ulivyokuwa ukimfanyia, nikijana anayekupenda sana. Mshukuru Mungu wako kwa hizo baraka, na umuombe asiache kukusaidia kukufundisha jinsi ya kuzitunza hizo baraka. Na sisi tunakuombea.” “Amina baba Penny. Naamini tutaonana siku za karibuni sana.” Wakazungumza mpaka akaridhika na kuagana.

Kisha akampigia simu baba yake. Alimtoa wasiwasi. Yeye hakumuonyesha chochote zaidi yakumwambia amekuta mazingira mazuri, wamempokea vizuri na wanaonekana kumfurahia. Hilo baba yake akaridhika nalo. Wakazungumza kidogo tu, wakaagana.

 Kwa Mara ya Kwanza, Tunda kwa daktari nchini Canada.

Baada ya siku tatu mbele, Net aliondoka asubuhi lakini alimwambia angerudi mchana kumchukua waende kwa daktari. Na kweli, mchana Net alirudi wakaelekea hospitalini. Akashangaa kumkuta bibi Cote na Maya, wakiwasubiri.

“Na nyinyi ni wagonjwa!?” Akauliza Tunda akimsogelea Maya. “Hapana. Nana anataka kumuona mtoto, na mimi ndio nikaona nije naye.” Maya aliongea akionekana amehamasika. “Ni sawa kumshika?” Maya akauliza. Tunda akacheka. Akakumbuka ushikwaji wa huyo mtoto kutoka kwa Net.

“Ni sawa. Tena alikuwa akicheza tokea tunatoka nyumbani, Net alikuwa akizungumza naye. Ametulia sasa hivi tulipokuwa tukitembea kuingia humu ndani.” Wakaonekana kufurahia. “Unaonekana unatetemeka baridi!” “Nasikia bariki kila wakati!” “Jana usiku ilibidi kumuongezea blangeti la umeme. Alikuwa akitetemeka baridi kama tupo msimu wa winter!” Net akaongeza.

“Daktari atatuambia ni kwa nini. Lakini nahisi ni upungufu wa madini ya chuma, damu. Lakini pia msimu wa baridi unakaribia kuanza tena. Msimu huu wa Fall hali ya hewa inabadilika. Inabidi kununua nguo za kuendana na hali yako na msimu huu.” Bibi Cote akaongeza.

“Tukitoka hapa, mimi nitaenda naye kumsaidia kununua nguo. Ni sawa Tunda?” Akauliza Maya. “Nitashukuru.” Tunda alijibu kwa sauti ya heshima. Maya akaonekana kufurahia hilo.

 “Kwa hiyo ni sawa, nimshike?” Maya akarudia na tabasamu usoni. “Kabisa.” Tunda akakubali.  “Come on Nana! She said it’s okay!” Maya alimtaka na bibi yake asogelee hilo tumbo la Tunda, yeye mwenyewe akiwa amehamasika hasa. Bibi Cote akacheka.

Maya akabusu tumbo la Tunda. “Hey Cote!” Akamsalimia. “Ni mimi aunt yako Maya. Nipo na Nana pamoja na dad wako. Ila dad yako ameondoka sasa hivi kwenda kuandikisha jina ili tukakuone kwenye mashine. Tunakupenda na kukusubiri kwa hamu sana.” Maya akampapasa kidogo, kisha akambusu. Tunda alibaki akijishangalia na kutoa tabasamu.

Bibi Cote naye akasogea. “Hey Son! Its Nana here. Can’t wait to hold you and kiss your precious chins.” Akampapasa kidogo tu, na kumbusu. “Anacheza!” Bibi Cote akashtuka na kushangilia mpaka akamshangaza Tunda. “That’s not fare Nana!  Sio sawa kabisa. Kwa nini kwangu hakucheza?” Mshtuko wa kufurahia yule bibi ukamfanya Net ageuke kuangalia. “Come on Net, he is talking back to me!” Net akaja kwa haraka huku akicheka. Akapiga magoti mbele ya Tunda.

Hata hawakumkaribisha akae. Alikuwa amesimama, wanachezea tumbo lake. Tunda akabaki akicheka tu. “Hapa kazi itakuwepo.” Tunda akajisemea moyoni.

Net, Maya na bibi yao walikuwa wakiongea na huyo mtoto, kila mmoja akisema lake kwa wakati wake. Hata waliokuwa wamekaa pembeni yao wakisubiri huduma za hapo hospitalini wakaanza kucheka. Huyo bibi alikuwa na majukumu mengi. Kuwepo hapo kwa wakati ule, ni kweli alijitoa na alithamini uzao wake.

“Tunda Cote!” Akaitwa na nesi aliyefungua mlango wakuingia ndani. Wote wakanyanyuka wakiongozana na Tunda. Akapimwa uzito na pressure. Akaacha mkojo na damu sehemu ya vipimo. Ndipo akaingia kwenye chumba ambacho waliambiwa daktari atawafuata huko. 

Wakati wakicheka na stori zimekolea, akaingia mama mtu mzima kama mwenye miaka 60 na uchache. Akasalimiana na bibi Cote akionekana wanafahamiana vizuri tu. Akamtania Maya, akampa pongezi Net na Tunda, ndipo akarudi kwenye tablet aliyokuwa ameshika mkononi.

“Uzito wa Tunda sio mzuri kwa ujauzito alio nao sasa hivi.” Alianza yule daktari akiwa anasoma ile tablet. “Pressure ipo chini kidogo. Lakini siyo mbaya. Majibu ya mkojo tuliyokuwa tukiyasubiria naona wamesha ya tuma kwenye system.” Akasoma kidogo kisha akendelea.

“Safi kabisa. Kuanzia juma lijalo, nitataka kumuona mara moja kwa juma, ili kuendelea kufuatilia huo uzito. Na kwa kumuangalia, anaonekana yupo dhaifu!” Akamtizama viganja vyake, akamwambia atoe ulimi nje, akamtizama na macho.

“Ni kweli huna damu yakutosha kama vipimo vinavyoonyesha. Nitakuandikia dawa zakuongeza damu. Hizi nilazima kuzinywa kila siku.” Akamgeukia na Net kama kuweka msisitizo. “Nitahakikisha anameza kila siku. Hamna shida.” Akajibu Net kwa kuwa yule daktari alibaki akimtizama yeye. Alipojibu Net na kumuelezea kidogo umuhimu wa hiyo damu kurudi kwa haraka, akarudisha macho kwenye ile tablet.

Akasoma tena kidogo. “Naamini atakuwa sawa tu. Damu yake ni safi. Hakuna ugonjwa wowote zaidi ya upungufu wa uzito, damu na hiyo pressure kuwa chini. Mnaswali lolote?”  Daktari akawatizama kwa zamu. Bibi Cote akauliza maswali ya msingi, akajibiwa. Akaonekana ameridhika.

Wakaambiwa wampishe Tunda avue nguo waangalie mtoto. Wakatoka. Wazi walionekana wamehamasika kupita maelezo. Net alibaki naye mle ndani, akamsaidia kutoa nguo. Akavaa vazi alilopewa. Akapanda kitandani, akajilaza. Taa ilizimwa, ndipo akaingia bibi Cote na Maya.

Baada ya muda akaingia muhusika wa ultrasound. Ilikuwa ni mashine nzuri sana na ya kisasa. Maya alikuwa akimchukua video yule mtoto. Wakaona kichwa, na kiwiliwili kwa wazi kabisa. Akaanza kucheza mle ndani. Kwa wazi kabisa. Machozi yalianza kumtoka Net.

Tunda akaona anambusu kichwani mara kadhaa. Akamshika mkono. Net akaunyanyua na kuubusu mkono wake, akaukumbatia, macho kwenye ile mashine inayoonyesha mtoto wake. Kulikuwa kuna kelele kwenye hicho chumba. Bibi Cote na Maya walikuwa wakishindana kuongea kwa shangwe. Kila kitu alichofanya yule mtoto kule tumboni na kukiona kwenye ile screen, walishangilia na kuonyeshana kana kwamba wengine hawapo hapo wapo nje hawaoni. Tunda hakuwa akiamini. Walitaka kuona tena na tena.

“Kick again!” Net aliyekuwa amesimama pembeni ya Tunda huku amemshika mkono alikuwa akimwambia mwanae. Arudie hiki na kile huku bibi yake na Maya wakifurahia. Tunda akamuona yule bibi anafuta machozi huku akicheka. Net akaendelea kumwambia mwanae azunguke huko tumboni kwa mama yake, wote wanacheka.

Hapo Tunda akajisikia wamaana! Akajiona ni kama amebeba lulu, asiamini kama ni yeye Tunda aliyesota kimaisha vile Bongo nchini Tanzania. Akajikuta machozi yakimtoka pale alipokuwa amelala wakimshangilia yule mtoto. Net mwenyewe alikuwa akifuta machozi yafuraha kila wakati.

Waliambiwa uzito wa yule mtoto, urefu wake. Bibi Cote akasema atakuwa mrefu kama mumewe. “Yaani sio kama mimi, Nana!? Am standing right here!” Net akashangaa sana vile bibi yake anavyomfananisha mtoto wake na babu yao na sio yeye baba mtu! Wote wakaanza kucheka tena. Waliambiwa yule mtoto ni mzima kabisa na ana afya njema tu. Bibi Cote aliomba picha zote za yule mtoto nakutaka awekewe video kwenye flash drive. Wakaondoka.


Maya kwa Tunda.

Bibi Cote na Net walirudi ofisini, Tunda na Maya wakaenda madukani, kuanza kufanya shopping. Maya alipenda shopping sana. Alimwambia Tunda huo ndio udhaifu wake. “Mshahara wangu wote huwa unaishia kununu vitu.” Tunda akacheka. “Kwanza hongera kwa kumaliza chuo.” “Wewe ndio nikushukuru. Wakati ule nilikuwa na akili za kitoto, sikujua kama naweza kutulia na kuwa msaada. Sasa hivi nafanya kazi na Net pamoja na bibi. Wanafurahia sana utendaji kazi wangu.”

          “Unafanya nini?” Tunda akauliza. “Masoko. Ndicho kitu nilisomea, nikajua nitamsaidia Net upande huo. Na kweli. Nimekuwa msaada kubwa! Hata mimi mwenyewe najua.” Tunda aliendelea kucheka huku akimwangalia Maya.

Maya alimpenda sana Tunda tokea mara ya kwanza wanaonana. “Unajisikia mpweke?” Akamuuliza. Tunda akacheka. “Kidogo. Nakumbuka nyumbani.” “Nani unamkumbuka zaidi?” “Baba yangu na mama Penny.” “Ndio nani?” “Ni dada niliyempata baada ya kutoka Arusha?” “Mama alipokufukuza?” Maya akauliza swali la moja kwa moja na kumshangaza Tunda.

“Umejuaje?” “Nilimuona Net akilia kwa Nana. Nana akanifukuza. Lakini nilijificha, nikamsikia akimsimulia Nana kuwa alikuacha ofisini, lakini mama amemwambia umeondoka. Ndio Nana akamshauri arudi haraka akutafute. Aliporudi Tanzania, akapiga simu huku siku hiyo akiwa hana raha. Ndio Nana akamuuliza ni nini, akamwambia alikutafuta sana, hakukupata.” Tunda akashangaa ile ya kuduaa.

“Wanampenda sana Net kwa kuwa amekuwa bila kuwasumbua sio kama mimi. Akisema kitu chochote, tokea Papa yupo hai, walihakikisha anapata. Kwa hiyo Nana akamwambia asiumie, kama ni mpango wa Mungu, atakupata tena. Atulie, na kumuomba Mungu. Ndio Net akatulia.” Maya akaendelea.

“Baadaye sana kama baada ya mwaka karibia miwili, ndio akasema amekupata tena, kumbe sio kwamba uliondoka, ni mama alikufukuza.” Tunda akabaki akifikiria akiunganisha hili na asikubaliane na lile.

“Mama yangu hakupendi.” Maya akaanza tena. Tunda akacheka. “Najua.” “Nikwambie kitu, lakini usimwambie Net? Nana amesema nisiwaambie, lakini mimi siwezi kunyamaza.” Tunda akaanza kucheka tena. “Niahidi hutamwambia Nana.” “Juu ya nini?” “Mama.” “Ila nitamwambia Net.” “Tunda!” “Kweli Maya. Najua na yeye angependa kujua.” Maya akang’ata meno kwa nguvu kama anayejitahidi asizungumze jambo, lakini anashindwa.

“Kwani ni nini?” “Hapana. Nikikwambia wewe, halafu na wewe ukamwambia Net, Net hajui kumficha Nana jambo lolote, atamwambia, halafu bibi atakasirika. Amesema tusubiri mpaka ujifungue ndio atawaambia.” Tunda akakunja uso. Akanyamaza.

“Basi sahau hata kama nilikwambia. Twende tukanunue nguo zako. Net amenipa kadi yake, na mimi nitajinunulia pochi. Naomba umwambie umeninunulia zawadi.” “Maya! Mimi siwezi kumdanganya Net.” “Basi nitamwambia kuwa nilikuomba wewe, ukanikubalia.” Tunda akacheka asiamini kama Maya anataka kumzidi mahesabu.

“Basi ngoja nianze upya. Naomba uninunulie pochi, Tunda!” Tunda akazidi kucheka. “Sina hela Maya.”  Alijibu huku akicheka.  “Come on Tunda! You are Net’s wife! You DO have money!” akamshangaa wifi yake akisema hana pesa wakati yeye ni mke wa Net! Tunda akaendelea kucheka. “kweli mimi sina hela hapa.” “Ninayo hii kadi yake. Ameniambia nikusaidie kununua vitu, halafu nikupe umrudishie.”

“Niambie ukweli Maya. Umekupa kadi unipe au amekupa uninunulie.” Tunda akambana, akajidai kufikiria kidogo. “Labda atakuwa amenipa nikupe.” Tunda akacheka huku akitingisha kichwa.

“Hujabadilika tu Maya!?” “Net anapesa nyingi sana, ila hajui matumizi ya pesa. Sasa huwa namchukulia kadi yake, nanunua vitu, na zawadi ya Nana, halafu namwambia nimemnunulia Nana nyingi, na mimi nikajinunulia kidogo.” Tunda akamtizama kwa kumfikiria.

Kuanzia juu mpaka chini alikuwa amependeza sana. Kwa kuwa Tunda alipenda sana kuvaa, alijua kila kitu pale mwilini mwake ni cha gharama. Gari yenyewe anayoendesha Maya, ni ya mapesa yakutosha. Alijipenda sana.

“Ngoja nikusimulie mkasa moja. Ndio maana Net haniamini tena na kadi yake.” Tunda alianza kucheka upya, alijua tu alikuwa akimdanganya. “Kuna siku alinituma nikamnunulie Nana zawadi ya birthday. Yeye alikuwa na kazi nyingi kama kawaida yake. Anafanya sana kazi Net. Utamuona!” Tunda akashangazwa na kitu.

Akamgeukia Maya. “Maya, njoo hapa karibu nikuulize kitu!” Maya akasogea. “Kwa nini watu wanatupiga picha na kutuchukua video, tokea tunashuka kwenye gari!?” “Kwani Net hajakwambia?” “Juu ya nini?” Maya akacheka kwa kumsikitikia Tunda. “Usinitaje kwa Net, pengine hakukwambia kwa makusudi au amepuuza. Lakini ujue wazi kuja kwako huku na Net, ni kama umepoteza uhuru wako kwa namna fulani.” “Kwa nini!?” Maya akafikiria kidogo.

“Sijui nianzie wapi! Lakini ujue kila kitu utakachokifanya kuanzia sasa hivi, ni tukio la kwenye magazeti au mitandaoni. Kwa kifupi, ule uhuru uliokuwa nao wa kufanya kila kitu kila mahali, haupo tena. Zaidi wewe.” Tunda akakunja uso kama ambaye hajaelewa.

“Yaani ni hivi, kila kitu utakachoshika, utakachofanya hadharani ujue kesho kipo mtandaoni. Popote na yeyote utakayekuwa naye, ujue kesho upo mtandaoni. Hata hapo, wanasubiri kukuona unanunua nini, kesho utakuta kwenye magazeti zaidi ya mitindo.” Tunda akashangaa sana.

“Hata hivyo ulivyo hapo sasa hivi, kesho wataanza kukuchambua kwenye mitandao kuanzia hizo nywele, hereni ulizovaa, pochi uliyoshika, nguo zako zote, mpaka viatu.” “Maya!” “Nitakuletea gazeti la kesho uone. Watathaminisha. Watapanga bei, na kukupigia mahesabu mke wa Net leo umetoka kwa kiasi gani.” Tunda akaishiwa nguvu. Akaelewa ni kwa nini Maya anamsisitiza apendeze.

“Wanauza mitandao yao na magazeti kwa kutumia maisha ya kina Cote. Wengine wana followers wengi mitandaoni kwa kupata habari zetu wakisema ni za kweli na fresh. Watu wanawafuatilia ili kujua kinachoendelea kwenye maisha yetu. Wanapata umaarufu kwa jina la Cote. Utazoea tu.” Tunda akabaki akifikiria.

“Basi turudi kwenye stori yangu. Achana nao, wala usiwaangalie. Wengine wanajidai wananunua humu ndani kumbe waongo, hawana hata hela. Wanataka tu kuwa karibu na sisi ili wapate habari. Tuendelee na yetu.” Maya akataka kumtoa kwenye mawazo. “Juu ya kadi ya Net?” Maya akacheka. “Kumbe unanisikiliza!” Akamuona amefurahi. Akaendelea.

“Basi, Net aliponipa tu kadi yake, nikampigia simu boyfriend wangu wa wakati ule, nikamwambia twende mapumzikoni kisiwa cha Vancouver. Nikatoroka na kadi ya Net. Acha nianze kuitumia mimi na huyo boyfriend wangu! Sikuwasha simu mpaka papa alipotuma watu waje wanitoe huko.” Tunda akakunja uso.

“Walinitoa usiku wa siku ya saba nafikiri, saa nane usiku, kunirudisha nyumbani. Muda wote huo na starehe zote hizo, nilikuwa natumia kadi ya Net.” “Maya!” Tunda akashangaa. “I was young and stupid, Tunda!” Tunda akatingisha kichwa kwa utetezi wa Maya akisema alikuwa bado na akili za kitoto. “Nilimkuta Net ni mwekundu kama hiyo sweta hapo. Kumbe alishaangalia kadi yake, akaona mahela niliyotumia. Nikahamia kulala chumbani kwa papa na Nana.” “Kwa nini!?” Tunda akauliza kwa mshanago.

“Nilikuwa naogopa Net ataniua!” Tunda akamtizama. “Ulitumia kiasi gani?” “Kama mimi nikikwambia ni pesa nyingi, ujue ni pesa nyingi haswa. Nilikuwa namfuata Papa mpaka chooni kwa kumuogopa Net. Nikikwambia nililala na Papa na Nana, namaanisha katikati yao. Ubavuni kwa Papa. Shuka moja. Akigeuka na mimi nageuka.” Tunda alicheka mpaka machozi.

“Usicheke Tunda! Niliingiwa na hofu sana. Papa na mama wakashauriana adhabu yangu ni nihamie kuishi kule Tanzania. Mama akaja kunichukua. Nilikaribia kuchanganyikiwa. Unajua mimi na mama hatupatani kabisa?” Tunda alikuwa akimwangalia Maya bila kummaliza. “Nilikaa na mama kama nipo jela! Hakuna kutoka, nikitoka natakiwa nitoke naye. Wafanyakazi wote walikuwa hawajui kuzungumza kingereza, natakiwa kujifunza Kiswahili. Hakuna simu wala kompyuta. Alifanya maisha yangu yakawa magumu kuliko nitakavyokwambia kama kuniadhibu.”

“Sasa umebadilika?” “Sana. Huoni nilirudi shule? Nikaachana na wanaume woooooote. Nikawa mtoto mzuri. Ila Net haniamini tena.” Tunda akamtizama, akarudisha macho kwenye nguo.

“Kwa hiyo utaninunulia pochi?” “Umenikumbusha nimpigie Net.” “Mimi najua jibu lake. Wewe anakupenda, atakwambia tumia zozote unazotaka.” Akaendelea kuongea wakati wifi yake anachagua nguo.

Akaanza tena. “Ujue Net amechukua nafasi ya Papa pale ofisini? Hakuna kinachofanyika kwenye kampuni nzima. Namaanisha ofisi zote za Cote, nchi zote bila idhini ya Net! Hajakwambia?” “Mimi ameniambia ni Nana.” Tunda akajibu taratibu tu huku akiendelea kuangalia nguo.

“Nana anataka kustaafu. Kila kitu sasa hivi kipo chini ya Net. Hata mshahara wake sasa hivi, wanamlipa kama Papa. Halafu analipiwa karibia kila kitu kwenye maisha yake. Gharama zake zote za maisha. Yeye na mke wake pamoja na watoto wenu wote, mnaingia kwenye gharama za kampuni. Mpaka gari yako imeagizwa na pesa ya kampuni.” Tunda akashtuka kidogo, akamgeukia. Alikuwa amesimama nyuma yake akiendelea kuongea nyuma ya wifi yake kama kasuku.

Tunda hakuwa hata akijua kama anaagiziwa gari. “Kwani ulikuwa hujui? Gari yako Net ametoa special order kiwandani. Amewaambia vile anavyotaka iwe kwako na kwa Cote akiwa mchanga mpaka anakuwa na umri wa miaka 3. Ni gari ya pesa nyingi sana, Tunda. Lakini zote hizo ni gharama za kampuni. Pesa yake Net haina kazi. Tununue tu.” Akaendelea kumshawishi wifi yake.

“Hapana Maya. Net anafanya kazi sana. Lazima tuheshimu juhudi zake.” “Fine! Mpigie lakini usimwambie niliyokwambia juu ya gari. Anataka akufanyie surprise kabla hujajifungua. Lakini hataki sasa hivi uanze kuendesha. Anasema mpaka ujifungue ndio atakutafutia leseni ya huku. Sasa hivi amesema atakuwa anakuendesha yeye mwenyewe.” Tunda akamtizama, akatoa simu yake kwenye pochi bila yakujibu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akampigia Net. Akapokea kwa haraka. “Maya amekupa kadi?” Ndio lilikuwa swali lake la kwanza. “Amenipa.” “Basi usimwache karibu na hiyo kadi hata kwa sekunde. Anaugonjwa wa kushop.” “Am standing right here Net, na ninakusikia.” “Then don’t touch my card.” Akamtaka asiguse kadi yake.

“Fine! Lakini kuna kitu Tunda anataka kukuuliza.” “Unataka aniulize nini?” Net akamuuliza swali Maya, nakumfanya Tunda aanze kucheka. Akaamini anamjua mdogo wake vizuri sana. “Sasa ni nini kinakupelekea kufikiri ni mimi ndio namtuma mke wako?” “Nakufahamu sana Maya. Unataka kumuomba nini Tunda? Pochi?” Tunda akazidi kucheka. “Ahaa!” Maya akajidai kuhamaki.

“Usimnunulie kitu chochote kipya huyo. Leo ni siku yako tu. Maya ananunua vitu kila siku.” “Nitumie kiasi gani?” Tunda akauliza kiustarabu. “Chochote.” “Si nilikwambia?” Maya akaingilia. Alikuwa karibu sana na Tunda alisikia kila kitu.

“Hakikisha unapata vitu vizuri, na ambavyo ungependa. Maya anafahamu huu msimu na vitu ambavyo utahitaji. Tumia tu hiyo kadi, usiwe na wasiwasi.” “Asante.” “Maya asitumie kadi yangu hata kwa kujinunulia soksi.” Net akaweka msisitizo. “Brother of the year!” Maya aliongea hivyo kwa kejeli akaondoka pale.

“Au nimnunulie pochi moja, mimi nipunguze vitu? Hata hivyo sihitaji vitu vingi sana, nitakuwa ndani tu.”  Tunda akaingiwa na huruma. “Hivi unajua aina ya pochi anazobeba huyo Maya? Pochi moja ya Maya ni zaidi ya dola elfu mbili.” Hapo Tunda akawa mpole.

“Na anazo zimejaa kwenye closet yake kama duka. Anaugonjwa, ndio tupo kumsaidia. Hajui kutunza pesa. Kila akiingiza pesa, ananunua viatu au pochi na ni vya pesa nyingi sana. Ana ukurasa mtandaoni wa mavazi huyo. Yaani kuna watu wanalipwa au wanatajirika kwa ajili ya kuvaa kwake Maya.”

“Hata Nana siku hizi anamkatalia. Tumemwambia mpaka abadilike, au afanye kazi kwa bidii, aweze kujiingizia pesa za kujinunulia mwenyewe. Kwa hiyo usimuhurumie. Msaidie.” Tunda akageuka. Akamkuta amekaa kwenye kochi la hapo hapo pembeni ya sehemu ya kujaribishia ngua, ameinama anaangalia simu yake, ametulia kimya.

“Anatia huruma!” “Ndivyo hivyo alivyo. Tena anaweza hata kulia. Ndio fimbo yake kwetu, na zaidi aliitumia sana kwa Papa. Papa alikuwa akimwaga pesa kwa Maya bila kufikiria. Akiona tu hiyo sura yake na machozi, ndio kabisaa. Alikuwa hawezi kusema hapana kwa Maya. Tunasema yeye ndio amemuharibu zaidi Maya.” Net akaendelea.

“Yaani sisi sasa hivi, ndio tumemgundua. Imebidi kuwa naye makini sana. Ni kwa faida yake Tunda. Naomba na wewe umsaidie. Maisha yake hayatakuwa mazuri kama ataendelea hivyo. Usimuendekeze.”  Net akaweka msisitizo.

“Hatanichukia?” “Hajui kukasirika huyo. Atakuwa sawa tu. Mpigishe stori. Anapenda sana kuongea! Mwambie akupe stori. Atachangamka tu.” Tunda akacheka huku akimwangalia Maya. “Nitakuona nyumbani.” Net akaaga. “Asante kwa pesa.” Akamsikia Net anacheka. “Karibu. Ngoja nimalizie kazi hapa, ili unikute nyumbani.” “Sawa.” Tunda akajibu, Net akakata.

Tunda akamgeukia, akamuona bado ameinama. “Njoo Maya wifi yangu.” Tunda akamwita kwa upole na kumbembeleza. Maya akapandisha mabega kukataa huku amemuwekea sura ya majonzi. “Kwanza unajua maana ya wifi?” Tunda akaendelea kumchokoza taratibu huku akichagua nguo. Maya akatingisha kichwa kukubali.

“Unajua kweli maana ya wifi au umetumia tu akili wewe Maya!?” Akamuona anacheka. Akajua ni kweli hawezi kukasirika muda mrefu. “Nimetumia tu akili.” Akajisogeza karibu na Tunda. Akaendelea kumtajia maneno ya kiswahili anayoyajua. Kwa jinsi alivyokuwa akiyatamka, Tunda alizidi kucheka. “Na yote hayo nimejifunza kwa lazima nilipopelekwa kwa mama. Mimi sio kama Net anayejua lugha nyingi. Sina mpango wa kuishi popote ulimwenguni isipokuwa hapa.” “Sasa wewe meneja masoko gani wa kampuni kubwa hivyo, hujui lugha?” Maya akatulia kidogo. Tunda akamgeukia. Akamuona anafikiria, akacheka.

“Yaani Maya wewe!” “Ujue mwenzio nikipata wateja ambao hawajui kuzungumza kingereza, nawaunganisha na Net?” Tunda akamtizama. “Sasa nifanyaje?” “Wewe sasa hivi unafanya nini kinachokushinda kujifunza lugha kama yeye Net?” “Tunda!” “Wewe niambie tu. Shule umesema hutaendelea tena. Huna majukumu yoyote yale kwa sasa, uwezo unao. Jifunze hata lugha nyingine mbili tu.” Tunda akamuona anacheka.

“Net atafurahi huyo!” Maya akajiongelesha. “Kwa nini?” “Ananiona huwa siwezi kufikiria wala kujituma. Sasa watashangaa safari hii nitakavyowajia na kitu kingine kipya.” Tunda akamwangalia na kuendelea na shuguli zake.

“Lakini sasa usimwambie kwa haraka kama wewe ndio umenishauri Tunda. Ili wanisifie mimi. Ni sawa?” “Hamna shida.” “Nitawaambia kwa kuwa kazi yangu inahitaji niwe najua lugha tofauti tofauti nimeamua kujifunza...” Tunda akaendea kumsikia akijiwekea mikakati.

Akamuona kama amekumbuka kitu. “Tunda!” Akamwita kwa kumgusa. Tunda akamgeukia. “Net amekwambia habari za Vic?” “Vic!?” Tunda akauliza taratibu. “Utamuona. Alikuwa na Net, akadhani Net atamuoa.” Maya akaanza kucheka. “Kwani walikuwa na mahusiano?” “Oooh yeah. Tokea zamani, yaani tokea wadogo. Vic akamsaliti kwa kutembea na mmoja wa rafiki wa wale rafiki zake Net waliokuja Tanzania kipindi anakuchumbia. Unawakumbuka?” Tunda akafikiria kidogo.

“Namkumbuka Troy. Yeye anaonekana ni mcheshi zaidi kuliko yule mwenzake.” “Basi Vic alilala na rafiki yake huyo huyo Troy. Sasa Troy yeye mwaminifu sana na ni rafiki wa Net tokea watoto. Akaja kumwambia Net. Net akamuuliza Vic, Vic akamuomba msamaha. Akamsamehe. Wakaendelea kidogo, lakini ni kama mambo hayakurudi kama zamani. Net akaja kushindwa baadaye.” Tunda kimya akisikiliza.

“Ila yeye Vic anatangaza anasema hakuna mwanamke atakayemfaa Net ila yeye. Mpaka majuzi hapa wakati wewe ulipokuwa jela alikuwa anajitangazia kwa watu wote eti yeye ndio atakuwa mke wa Net. Na yeye ndio anastahili kiti cha bibi Cote.” Tunda akashtuka kidogo. Akakumbuka hiko kitu kusikia kwenye siku ya tafrija ya kuchumbiwa kwake na malalamiko ya Ritha.

Kumbukumbu ikamjia ile shamra shamra na upigwaji picha baada ya yule bibi kutangaza kitu kama hicho. Akamgeukia Maya. “Kiti cha bibi Cote!?” Tunda akauliza. “Umesahau bibi alikutangaza kuwa wewe ndio utamrithi?” Tunda akatulia.

“Basi kesho yake, ulitoka kwenye magazeti karibu yote huku kuwa wewe utakuwa ndio mrithi wa Nana. Unafahamika sana huku na nivile watu hawakujua kama umefika. Net ameomba hata wafanyakazi wanaojua kama upo hapa nchini, wasiseme mpaka upumzike. Sasa labda hii leo ndio inaweza kuharibu ulivyoonekana hapa na mimi.” “Kwa nini?” “Mapaparazi watakusumbua sana! Si wewe mwenyewe umeanza kuona?” Tunda kimya.  

“Sasa nikwambie huwa inakera zaidi. Utakuja kuona. Wanakufuata hata sehemu ndogo tu pengine utakayokuwa umesimama ukaamua hata kununua kitu kidogo au labda unahamu ya kula kitu fulani. Nayo ni habari, watataka kukuhoji hiki au kile. Unapigwa picha hovyo! Hakuna tena faragha.” Tunda akanyamaza. Akawa hajui tena aulize nini aache nini maana Maya aliendelea kuzungumza mengi kwa wakati mmoja.

“Kwani Net hakukwambia kuwa kina Nana, wana taasisi yao? Wapo wanawake ambao walikuwa pamoja tokea zamani sana. Sasa kwa kuwa Nana alikuwa mwanzilishi na bado yupo hai, na ni kama yeye ndiye anapesa kuliko wote, yeye ndio amebaki kuwa mwenyekiti wao.” Maya akaendelea.

“Wanachama wa huo umoja, wakifa au wakitaka kustaafu, sheria ni unamuachia mtoto wako mkubwa wa kike, au mkwe utakaye mchagua. Sasa kwa Cote, alitegemewa mke wa Net, ndio apokee hicho cheo. Ni chama kikubwa sana, cha matajiri watupu. Kila mtu hapo anapesa nyingi na amesoma. Nana amekuwa kiongozi wao tokea msichana mpaka sasa. Sasa alitangaza anataka kustaafu. Sasa fumbo kubwa likawa nani atakuwa mrithi wa hicho chama! Magazeti yaliuliza, wakubwa wa nchi walishawahi kumuuliza Nana. Lakini hakuwahi kusema. Ndio Vic akajua atakuwa yeye tu.” Tunda alitamani kukaa chini.

“Kwa mara ya kwanza, Nana ndio alitangaza pale kwenye ile tafrija yako. Ilikuwa habari inayozungumzwa na magazeti na vyombo vya habari vyote hapa nchini. Tuliporudi, wakamtaka Nana azungumze ramsi sasa. Ila Nana akawaambia atakapokuwa tayari, ataongea na vyombo vya habari. Nana anapanga mambo yake kwa akili sana. Sio mkurupukaji.” Tunda akabaki akitetemeka kwa hofu.

 

“Kwa hiyo wewe ndio utakuwa mpokea cheo cha Nana.” Maya aliongea kana kwamba ni habari njema, kumbe ndio anamuogopesha Tunda. Alizidi kulaumu ni kwa nini Net hakumwambia hadhi yake tokea mwanzo!

Majukumu yanayomkabili Net mwenyewe na mkewe, ni makubwa kuliko uwezo wake Tunda. “Hivi huyu Net wakati ananioa, alikumbuka elimu yangu kweli!?” Tunda akawaza wakati ameingia kujaribisha nguo walizochagua na Maya. Kila nguo pale ilikuwa ya gharama haswa.

“Na Vic anafikiri yeye ndio msichana mzuri, ulimwenguni kote.” Maya aliendelea kuongea nje ya chumba alichokuwa akijaribishia nguo Tunda.

“Sasa ninahamu yakuona sura yake atakapokuona na kujua umebeba mtoto wa Net! Nitamcheka waziwazi.” “Maya!” “Wewe humjui Vic. Anakera hata kwa kumuangalia tu. Siwezi kuacha kumkera, na nita mtag picha za Cote huko Facebook?” Tunda akashtuka mpaka akatoa kichwa nje.

“We Maya! Unamaanisha Cote huyu tumboni?” “Huyo ndio Cote pekee aliyebakia hapa duniani.” Tunda akashtuka sana. “Naomba umuulize kwanza Net.” “Come on Tunda! Kwa nini unakuwa hivyo?” Maya akalalamika. “Tafadhali kabla hujapost, muulize Net.” “Fine. Nitamuuliza kabla sijapost.” Tunda akahema.

Baada ya shopping.

Tunda na Maya walirudi nyumbani, Tunda akiwa amejazwa maneno na Maya, kichwa kinakaribia kupasuka. Wakamkuta Net na bibi yao wapo sebuleni. Net akasimama. Akamsogelea Tunda. Akambusu midomoni na kumkumbatia kisha mikono ikatua tumboni.

“Ni sawa nikipost picha za Cote, Facebook? Maana Tunda ameniambia nikuulize kwanza wewe!” “Mimi sioni tatizo.” Akajibu Net huku akipapasa tumbo la Tunda. “Yay!” Akashangilia Maya. “Tena namtag Vic.” Net alishtuka, mpaka Tunda akamuona.  Akajishtukia. Akamtizama Tunda na bibi yake. Akarudisha macho kwa Tunda. Tunda alikuwa ametulia tu.

Alibabaika Net, mpaka Maya mwenyewe akabaki amekodoa macho. “Net! Kuna tatizo?”  Maya akauliza huku ameshika simu yake. “No. Not at all!”  Akajibu Net akionekana anababaika. “Tumezunguka sana. Naomba nikapumzike kabla muda wa chakula.” Tunda akaamua kubadili ile hali ya hewa pale. Akawaaga. “Carter atakuletea mizigo yako ndani.” Aliongeza bibi Cote. “Asante.” Akashukuru Tunda, nakuondoka pale sebuleni. Akawaacha pale.

Alipoingia tu chumbani, Net naye akafuata. “Umepata vitu ulivyopenda?” “Ndiyo.” Tunda akajibu hivyo, akaelekea chooni. Net akamfuata huko huko chooni. “Unafikiri vitafaa?” Lilikuwa swali la kijinga, ambalo hata Net mwenyewe alijua. Lakini hakuwa na jinsi, ilikuwa lazima azungumze chochote na Tunda. “Nafikiri hivyo.” Akajibu Tunda taratibu tu.

“Umechoka sana?” Akauliza tena na kumkera sasa Tunda. “Net?” Tunda akamgeukia. “Please stop. Please!”  Tunda akamsihi taratibu. “Okay.” Akatulia. “Nakupenda wewe Tunda.” Akiwa ameingia chooni akamsikia tena Net nje ya mlango wa chooni. “Nafahamu Net.” Tunda akatoka chooni, akarudi chumbani. Net yupo nyuma yake.

“Kwani Maya amekwambia nini juu ya Vic?” “Wewe ulitaka aniambie nini?”

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Vic naye ni nani? Visa vyake vya kusisimua vinafuata. Usikose maisha, visa na mikasa ya Tunda huko ugenini....

0 comments: