NILIPOTEA! PART 6 - SEHEMU YA ‘C’.
“Nilipanga nije kukutambulisha rasmi kwa Vic. Anajua kama nilikuoa, na ninakupenda sana. Nilimwambia nimekuchagua wewe, wala sina mpango wa kuja kumuoa yeye tena. Sikumficha kabisa.” “Njoo hapa Net.” Tunda akapiga piga pale kwenye kochi alipokuwa amekaa.
Net
akasogea kwa kujihami. “Naomba utulie. Tafadhali. Sijali mambo ya Vic mimi.
Kwanza hata simjui!” “Sasa mbona umebadilika?” “Nimechoka Net! Unajua tulikuwa
shopping zaidi ya masaa 4! Nimechoka tu wala si sababu ya huyo Vic. Ila hivyo
ulivyopanic, ndio umenitia wasiwasi, itabidi tukae tuzungumze vizuri.” “Ham..”
“Hapana Net. Sio sasa hivi. Mimi nimechoka. Halafu natamani kusikia habari za
mtoto wangu tu, sio habari zako na Vic.” Net akatulia. Akajisogeza vizuri.
“Usiseme
habari zangu na Vic! Hatuna habari zetu. Mimi nina habari zangu na Tunda wangu tu.”
Tunda akamwangalia kama kumsuta. Net akacheka kwa aibu. Maana alikuwa
ameshapaniki mpaka akabadilika na rangi. Akajichekesha hapo, Tunda
akimwangalia, akaanza kumuonyesha picha za mtoto walizoona hospitalini kana
kwamba Tunda hakuwepo. Pakatulia.
Maisha ya Tunda kwenye hilo
hekalu, Nchini Canada.
Maisha
yake yakaanza hapo nchini Canada kwenye hilo jumba kama la maonyesho au
kihistoria. Kila picha, kila ukuta au sehemu ilikuwa na maelezo yakutosha ya
kihistoria. Akawa na kazi ya kuzunguka na kuangalia picha na sehemu husika.
Ndani tu, kabla hajaanza kuzunguka nje.
Akaanza
kutumia madawa aliyokuwa ameandikiwa hospitalini, na virutubisho. Walishauriwa
wasisafiri kwenda popote au kutokatoka hovyo kwenda popote ili kuhakikisha hapati
maambukizi yoyote yale ya ugonjwa wowote hata mafua. Ili arudishe kinga mwilini
kwa haraka kabla ya muda wa kujifungua.
Walishauriwa
kwa mwezi mmoja mzima, apate mapumziko kama mgonjwa mahututi. Kula na kulala tu.
Ili kuhakikisha anaongezeka uzito wake uliokuwa ukishandana na ukuaji wa mtoto
wake. Wapo watu wembamba kama Tunda wa safari hii aliyetoka jela, lakini wao
huwa wakakamavu, shupavu na afya njema. Yaani ndio miili yao ilivyo, lakini Tunda
alikuwa amedhoofu. Kwa kumwangalia na Tumbo kubwa alilokuwa amebeba ni kama
alikuwa amelemewa.
Akapewa
na dawa za kuzuia kutapika, na kujenga huo mwili wake na watoto. Hivyo
virutubisho alivyokuwa amenunuliwa na bibi Cote, vilikuwa vya asili vilivyokuwa
vimetengenezwa nchini hapo. Net alihakikisha anavitumia bila kuzembea.
Na
bibi Cote pia akahakikisha hawapati wageni ndani ya ile nyumba ili kwanza Tunda
apumzike kabisa, na kusiletwe magonjwa yeyote kwa huyo Tunda. Na kweli kazi ya
Tunda ikawa kula na kulala.
Kwa muda wa siku 15 tu
tokea aanze hivyo virutubisho na dawa, hata Tunda mwenyewe alihisi tofauti
kwenye mwili wake. Ile hali yakuchoka sana ikaisha. Baridi ikapungua mwilini. Maumivu
ya viungo pia yakapungua.
Angalau
ile hali ya usingizi mwingi ikaanza kupungua. Akawa mtu wakupata mapumziko ya
masaa mawili tu mchana, tena wakati mwingine alijilazimisha kulala mchana ili
kuchelewa kulala usiku apate muda na Net. Lakini hakuwa akisikia usingizi
hovyo. Ni kama usingizi wa usiku ulimtosha.
Ndipo
akaweza sasa kuzunguka vizuri kwenye hilo jumba akiangalia kila kitu kwa
kutulia na kuanza kuzoea mazingira ya mle ndani. Net ndiye aliyekuwa akirudi
yeye mwenyewe nyumbani siku anazotakiwa kwenda kliniki. Hakutaka mtu amsogelee
mkewe, kwa kuhofia magonjwa.
Anamchukua
mkewe, anampeleka kliniki. Tena huko kliniki akifika, wala hatakaa nje na watu
wengine kusubiri. Alichukua masaa ambayo akifika na mkewe, wanahudumiwa wao
bila kusubiri. Tena alihakikisha anafanya kliniki kwa huyo mama wa kizungu,
ambaye ni daktari wa muda mrefu sana wa wakina mama kwenye kliniki yake ambayo
ni ya kulipia. Sio ya wenye uwezo wa kawaida.
Tunda
akimalizana na huyo daktari, anamrudisha nyumbani moja kwa moja bila kumpitisha
kwenye maeneo ya watu wengi, kuepusha magonjwa, kisha Net anarudi tena kazini. Tunda
alikuja kugundua ni kweli Net anahitajika kazini. Kule kuwepo Tanzania na yeye,
nakuacha kazi huku, ni mapenzi tu.
Kampuni ya Cote!
Siku
moja walipotoka kliniki, Net alimuuliza kama angependa kwenda kutembea ofisini
kwao akapaone. Tunda akafurahia hilo wazo. Wakaenda. Ilikuwa ofisi kubwa sana.
Ofisini kwa Maya.
Akaanzia
ofisini kwa Maya. Alimkuta Maya cha utundu ametulia kama sio yeye! Tunda akaingia
nakuanza kucheka. “Kumbe ukiwa kazini unakuwa mtoto mzuri hivi?” “Hivi wewe
unawajua mabosi zangu?” Tunda akacheka. Maya akasimama na kumkumbatia.
“Mabosi
wenyewe hata chakula cha mchana hawali, wala hawatoki mchana kwenda shopping!
Kila saa simu ile pale ya mezani inapigwa, kuhakikisha nimetulia hapo mezani.
Na Nana anataka kazi zangu azipitie yeye mwenyewe kwanza, kabla hazijafika
ofisi kubwa!” Akamkonyeza akimuonyeshea Net.
“Lazima
nitulie.” Tunda akaendelea kucheka, Net alikuwa akimsikiliza tu huku macho yapo
kwenye file, alilokuwa amelikuta hapo juu mezani kwa Maya. Kimya akiperuzi kama
hamsikii mdogo wake.
Wakazungumzia
mambo ya mtoto. Tunda akampa habari kuwa mtoto yupo vizuri na yeye yupo salama.
“Na ofisi yako nzuri sana. Safi kama wewe mwenyewe.” Maya akacheka kwa furaha. “Asante
Tunda.” “Ngoja mimi nikuache uendelee na kazi.” Net na Tunda wakatoka.
“Kabla
hatujaenda kwa Nana, acha nikuonyeshe upande wa pili ambapo kuna ofisi za wafanyakazi
wengine. Huku juu ni ofisi za utawala. Kwa chini ndipo wafanyakazi wengine.”
Tunda akafuata nyuma. Akaonyeshwa upande wa chini ambapo kulikuwa na ofisi
ndogo ndogo tu zilizotengenezwa kwa kugawiwa vizuri sana ndani ya ukumbi mkubwa
sana, ndani ya hilo hilo jengo lao.
Ofisi
hizi za wafanyakazi wa kawaida zilitengenezwa kama vyumba au vioksi ambavyo juu
vilikuwa wazi kabisa bila milango. Ila walitenganishwa na viukuta vifupi kupita
vichwa vyao. Na kuweza kumpa kila mmoja faragha ya kile anachofanya.
Tunda akawaangalia akiwa
amesimama juu. Aliweza kuwaona wote vizuri tu. Yeye na Net walikuwa wamesimama
sehemu ya juu kidogo ya huo ukumbi mkubwa uliogawiwa hizo ofisi ndogo ndogo za
wafanyakazi wote. Kila mmoja wao alionekana yupo kazini ameinamia kompyuta yake.
Ni kweli palivutia kwa macho. Tunda akavuta pumzi.
Kwa Bibi Cote.
Ndipo
sasa akarudishwa juu, ndani zilipo hizo ofisi za utawala. Wakaelekea ofisini kwa
huyo bibi. Hapo ndipo Tunda akaelewa kweli yule bibi ni mtu wa maana. Hiyo
ofisi yake tu, ilijaa vitu vya maana vitupu. Kulipoa na kulipendeza kuanzia
kiti alichokalia yeye mwenyewe mpaka meza na kapeti.
Watu
aliokuwa akiwaongoza, au waliokuwa chini yake, ungejua anafanya kazi za maana.
Alionyeshwa wasichana wawili ambao aliambiwa ni sekretari wake huyo bibi tu kutokana
na majukumu mengine yanayomkabili mbali na ile kazi pale.
Wakati
wote bibi huyo alikuwa kwenye kiatu cha juu. Kwa ule umri wake, usingemtegemea
kama anaweza kukitembelea. Nadhifu sana na alijua kujitengeneza vizuri. Akili
yake ilionekana ipo makini wakati wote. Na alijibeba kitawala.
Akasimama
pale Tunda na Net walipoingia. Akavua miwani yake, na kuiweka juu ya meza.
Ofisi yake ilinukia pafyumu anayotumia yeye mwenyewe. Kusafi. “Huku sio salama
kwa Tunda, bwana! Kwa nini umemleta?” “Daktari amesema ni sawa. Kwa sasa
anaweza kutoka kidogo.” “Ila sio kupeana mikono! Umekumbuka hand sanitizer?” Akauliza bibi Cote akionyesha wasiwasi kidogo
na kujali. “Ninayo kwenye pochi.” “Afadhali.” Akaonekana kuridhika.
“Cote
anaendeleaje?” Akauliza tena. “Uzito umeongezeka na urefu zaidi. Kweli dokta
anasema atakuwa mrefu kama Papa.” Bibi yake akacheka. “Na Tunda?” Akamgeukia
Tunda. “Kila kitu kipo sawa kabisa. Amefurahia kuongezeka kwangu. Anasema
japokuwa sijafikia uzito ninaotakiwa, lakini ameridhishwa na mabadiliko
aliyoyaona. Amesema naweza kuanza kutembea kidogo.” “Hizo ni habari njema.
Kazana kula, na usisahau dawa.” Tunda akamuona ameridhika.
“Nakwenda
naye ofisini kwangu. Nitakaa naye mpaka tukiwa tunatoka.” Net akamwambia bibi
yake wakati anamsogelea. Akambusu. “Okay. Akichoka umrudishe nyumbani.”
“Atakuwa sawa tu. Si ndio Tunda?” Tunda akacheka na kutingisha kichwa kukubali.
Net akamshika mkono, akambusu, wakatoka pale.
Alipita
akimtambulisha kwa wafanyakazi waliokuwa wakikutana nao hapo njiani, ndipo
akaenda ofisini kwake. Nje alikuwa na sekretari mwanamke mtu mzima kama wa
miaka 60 hivi. Alionekana kumfahamu
vizuri sana Net. “Alikuwa na meza yake hapo ndani kwenye ofisi ya babu yake,
akifanya kazi zake za shule pembeni ya babu yake. Ngumu kuamini kama na yeye
anakaribia kupata mtoto!” Akamwambia maneno machache Tunda kumuonyesha
anamfahamu huyo Net tangia anazaliwa mpaka hapo alipo. Akamuonyesha na picha
zake na Net alipokuwa mtoto mdogo tu, wakacheka kidogo, ndipo wakaingia ofisini
kwa Net.
Alikuta
picha yake na yeye mwenyewe Net, walipigwa na Maya. Net alikuwa amepiga magoti
akibusu tumbo lake. Tunda akacheka wakati anaiangalia. Ilitoka vizuri sana. Hakujua
kama aliitengeneza. “Nzuri!” Akasifia. “Thanks.” Net akajibu huku akikaa. “Mbona
wewe ofisi yako kubwa kuliko wote!?” “Na majukumu ni makubwa. Ofisi yangu
ilikuwa ni pale alipo Maya. Hii ilikuwa ofisi ya babu kama ulivyomsikia
akikusimulia Ms Linda. Nimechukua majukumu yake yote.”
“Natakiwa
kukupa hongera. Si ndiyo?” “Siwezi kulalamika. Bibi kukupa jukumu lolote, ujue
amekuamini. Kwa hiyo nilifurahi. Japo imenibidi kuongeza nidhamu na umakini.
Nana amefanya kwenye hii kampuni akiwa mdogo kidogo kwa Maya, akisaidiana na Papa.
Anasema umakini na kutozembea ndio kitu pekee kilichoweza kuwaweka sokoni mpaka
sasa.” Akaendelea.
“Usimuone
vile, haondoki pale ofisini kwake kila siku, mpaka amepitia kazi za kila mtu
humu ndani. Hakuna kinachoendelea humu ndani, kwa yeyote, asijue.” Tunda akaendelea
kuzunguka mle ndani ofisini kwa Net.
Alishika
hiki, akaangalia kile. Picha tofauti tofauti. Akaona picha za Net na babu yake.
Kisha picha nyingine alikuwa baba yao, Net mwenyewe, Maya akiwa mdogo sana kama
anayejifunza kukaa, mama yao, babu na bibi yao. Ilionekana ni ya zamani sana
kama kipindi cha Chrismas kutoka na yale mapambo kwenye ile picha na nguo
walizokuwa wamevaa. Akaangalia hiyo picha kwa muda. Wote walikuwa pamoja.
Kisha
akaiweka chini na kuendelea kuangalia hiki na kufungua kile. Akazunguka mle
ofisini, kisha akarudi kukaa. Kimya. Kwa kuwa Net alishapotelea kwenye kazi
zake. Akatulia bila hata kuuliza swali. Baada ya kama nusu saa ndipo Net
akanyanyua uso kumtizama. Tunda akacheka.
“Nipe
kazi yeyote.” Net akafikiria kidogo. Akanyanyua simu. “Hey
Nana!” Moyo wa Tunda ukapasuka. “Ni sawa Tunda
akija hapo kwako ukamuonyesha kitu unachokifanya sasa hivi?” Akamuona
Net anacheka na kukata simu. “Haya nenda kwa Nana.
Amesema anakazi anataka umsaidie.” “Net! Mimi nilitaka wewe bwana!” Net
akasimama, akaenda pale alipokuwa amekaa akaanza kumbusu. Akambusu taratibu tu.
Kisha akamtengeneza vizuri.
“Hapa
nina mambo ninafanya, yanahitaji umakini kidogo.” “Ni nini?” “Wewe nenda kwa
Nana, atakwambia ninachokifanya, maana kila nikimaliza, lazima apitie
kujiridhisha. Nenda na uache kumuogopa. Itakusaidia kuanza kuzoeana. Kazi zote
anazozifanya yeye, ujue siku moja zitakuwa zako. Kwa hiyo nenda kaige na uzoefu
wa miaka ya karibia 70 sasa.” Hapo Tunda akaridhika. Akamsaidia kusimama,
akatoka bila kusindikizwa, Net akarudi kuendelea na kazi zake.
Mazungumzo ya kwanza ya Tunda & Bibi Cote
wakiwa peke yao.
Alimkuta bibi Cote akimsubiria.
“Ofisi yangu ni ofisi ya ukaguzi. Unaweza kusema nafanya auditing kitaalamu.
Ahitajiki msomi kuwepo hapa nilipokaa, ila mtu makini, na anayejua kazi kwa
kufanya. Sijui kama umenielewa?” Tunda akakaa.
“Nakusikiliza.”
“Wasomi tunao wahitaji humu ndani ni wachache sana, kama Logan, ambaye ni
mwanasheria wa kampuni, na watu wengine. Hata kazi anayofanya Maya ya masoko,
inahitajika mtu makini tu. Kujua wapi kuna uhitaji, na kufuatilia bila kukubali
jibu la hapana au subiri. Kwa kuwa ukikubali jibu la subiri la siku moja tu,
utaua kampuni.” Bibi Cote akaendelea.
“Kwa
hiyo ninapokaa hapa, nafuatilia kazi za Maya. Kujua kwa siku hiyo ametupatia
masoko mangapi. Yale tuliyo nayo anayatunzaje ili tusipoteze wateja. Napigia
simu wateja tulio nao kwa sasa ili kufuatilia kama madereva walifikisha mizigo
kwa wakati na salama.” Akaendelea.
“Napitia
kila matumizi ya humu ndani. Kuanzia mshahara mkubwa mpaka wa vibarua. Kupitia
majukumu ya kila mtu humu ndani. Kujua nani anabaki, nani ahamishwe na nani
haitajiki tena. Pesa zinakwenda wapi na kwa nini ziende huko. Mteja yupi ni wa
kumuacha na yupi wakumbana atupe kazi nyingi zaidi.” Tunda akakunja uso.
“Mbona
sasa wewe ni kama unakazi nyingi kuliko wote?” Bibi Cote akacheka. “Kwa mfano
Maya. Pale alipo amepewa mwezi mmoja wakutafuta angalau wateja wapya wawili
watakao taka huduma yetu. Bila hivyo Net amemwambia atamuhamisha kitengo, mbali
na hapa, kwa mshahara mdogo, kwa kuwa atakuwa haingizii kampuni faida. Anakuwa
anaendelea na wateja alio wakuta tu.” Tunda akaanza kucheka.
“Ndio
maana halali! Usiku anachelewa kulala, na asubuhi anawahi kuamka!” Tunda
akaanza kuelewa. “Na hatoki mchana muda wa kula, kwenda kununua vitu visivyo
vya maana. Bila hivyo tulijua hataweka akili kazini na atajua wote tunacheza tu
hapa.” Tunda akaendelea kucheka akimfikiria Maya.
“Hata
muda wachakula siku hizi haulizii tena. Isingekuwa hivyo, sasa hivi ungemkuta
amelala pale kwenye lile kochi pale mbele yangu, analalamikia hili au lile,
anataka tuwahi kutoka tukatengeneze kucha.” Tunda akaendelea kucheka.
“Jumamosi
hii ameniambia twende kwenye kucha.” “Mkubalie tu. Amefanya kazi sana mpaka
tunamuhurumia.” “Lakini si anajua hata asipopata wateja, Net hawezi kumfukuza?”
Bibi Cote akacheka sana. “Kumbe humjui mumeo hata kidogo!” Akacheka tena,
akakaa vizuri kwenye kiti chake kilichofanana na Net, lakini chake kilikuwa na
rangi za dhambarau kama vitu vingi vilivyojazwa ofisini kwake. Hata kapeti ya
juu ndogo ya manyoya kuzunguka meza yake na kiti alichokalia ilikuwa Zambarau
nzuri sana. Alionekana anapenda rangi hiyo yakitajiri.
“Net!?”
Tunda akauliza kwa kushangaa kidogo. “Wewe unafikiri ni kwa nini babu yake
alitaka akalie kile kiti pale?” Tunda akaangalia alipokuwa Net. Ofisi zao, bibi
yake na yeye, zilitenganisha na vioo tu. Lakini ni kama Net alimpa mgongo bibi
yake. Ni kama meza yake ilikaa pembeni kidogo. Akamuona ameinama akiandika kwa
makini vilevile.
“Vile
unavyomuona Net, ndivyo alivyokuwa babu yake. Baba yake Net, CJ, alikuwa kama
mimi. Soft kidogo. Huruma na anasikiliza hata matatizo ya wafanyakazi na
kusamehe. Lakini sio wao. Wao wanataka kazi ifanyike. Wafanyakazi wote wanamjua
Net. Akikupa jukumu, anataka ulifanye. Yaani aone matokeo.” Tunda akamgeukia
tena Net kama asiyeamini.
“Kutofanya,
kwa sababu yeyote ile. Namaanisha sababu yeyote ile, inamaana huwezi kufanya
kazi kwenye hii kampuni. Na hajui kutoa onyo la kwanza na la pili. Anakwambia
wafanyakazi wote humu ndani ni kama mwili mmoja. Hakuna wa muhimu na asiye na
muhimu. Ukishindwa kufanya jukumu lako hata moja, inamaana umekwamisha kazi za watu
wote, na hilo haliwezi kuvumiliwa. Hakika anakutoa. Ni Maya tu ndio anaahadi
yakupunguziwa mshahara na kuhamishwa kitengo.” Tunda akamgeukia tena Net.
Alikuwa vilevile ameinama.
“Vile
unavyomuona pale, hatanyanyuka mpaka akamilishe anachokifanya. Anamaadili
mazuri sana ya kazi aliyofundiswa na babu yake. Ile ofisi alikuwa akiikaa tokea
anatoka shule, mtoto, anaingia pale kufanya kazi zake za shule. Jumatatu mpaka
ijumaa. Na wakati mwingine siku za jumamosi alikuwa akija na babu yake hapa kazini.
Labda awe na kitu anachofundishwa jioni. Yaani masomo ya ziada. Ndipo akitoka
shule, atarudishwa nyumbani kufundishwa. Lakini wakati wote utamkuta na babu
yake.” Akamuona anafikiria kidogo, kisha akaendelea.
“Kitendo
cha kuamua kwenda kuishi Tanzania, tena babu yake akijua hatapona, kilimuuma
sana babu yake. Maana alimlea akijua atachukua majukumu yake. Lakini pia
aliamua kumuamini kwa kila uamuzi anayoamua Net.” “Nini kilimpelekea kuchagua
Tanzania?” Tunda akauliza taratibu.
Bibi
Cote akacheka kidogo. “Hakukwambia?” Tunda akatulia kidogo kama anayefikiria. “Alipokuwa
anamalizia chuo huku, hakuwa ameamua kama ataishi Tanzania akimsaidia mama yake
au la. Lakini kwa jinsi alivyokuzwa, wote tulijua atamaliza chuo na kuanza kazi
hapa.” Akaendelea bibi Cote.
“Alikwenda
likizo kwa mama yake, mama yake akaanza kumpanga ili akamfanyie yeye kazi.
Akawa yupo njia panda. Akawa mtu wa kwenda na kurudi tu bila uamuzi wa kuishi
Tanzania moja kwa moja mpaka akamuona Tunda.” Tunda akashtuka sana. Hakutegemea.
“Hapo
ndipo kila kitu kikabadilika kwenye maisha yake. Kila kitu akataka kisubiri,
atafute ‘true love’. Babu yake akamwambia hata
hapa anaweza kupata, lakini tayari akawa ameingia Tunda kwenye picha.” Bibi
Cote akacheka kidogo kama anayevuta kumbukumbu. “Kila tukimuuliza Tunda ni
nani? Yeye mwenyewe hamfahamu, lakini ikawa ni vurugu. Yupo huku, akili zipo
Tanzania.” Tunda hakuwa anaamini,
akamgeukia tena Net. Bado alikuwa ameinamia kompyuta yake, lakini safari hii
alinyanyua kichwa kidogo kama anayefikiria.
“Alipomaliza
tu chuo, akarudi tena Tanzania. Akamtafuta Tunda kama mwezi, akamkosa. Lakini
mwezi huo mmoja alikuwa akimsaidia kazi mama yake. Mama yake akautumia huo
mwezi vizuri sana kubadili akili ya Net, baada yakuona jinsi anavyochapa kazi
na akili aliyonayo kwenye kuwekeza.”
“Sijui
alimwambia nini, akafanikiwa kuingia kwenye akili yake, akageuza kabisa akili
ya Net, akajiona analo jukumu kubwa sana lakumtunza au kumsaidia mama yake.
Kuishi huku na mama yake kuwepo kule peke yake ni kama kumtelekeza.” Bibi Cote
akaendelea, Tunda akimsikiliza.
“Alirudi
huku siku moja tukijua ndio anaanza majukumu ya huku, akaomba kikao cha mimi
pamoja na babu yake. Akazungumza mambo mengi, akijitetea maamuzi yakuamua
kuishi akimsaidia mama yake nchini Tanzania huku akisema anamtafuta Tunda
aliyeambiwa alifukuzwa huko alikokuwa akiishi kwa ndugu. Ni kama Mungu anamtuma
kitu kwa Tunda.”
“Hapo
hakuwa amesema moja kwa moja anakutafuta sababu ya mapenzi. Hata yeye hakuwa
anajua ni kwa nini anataka kukuona. Babu yake aliumia sana na kumlaumu sana
Ritha. Lakini hakutaka kumwambia Ritha mwenyewe. Kwa kuwa Ritha ni kama
aliwatelekeza watoto wake hapo, tena wakiwa wadogo, sisi, au niseme mimi
niliwalea kama watoto wangu.” Tunda akakunja uso.
“Lakini
Net aliniambia kuwa mama yake alianzisha biashara iliyokuwa ikimuhitaji sana
huko Tanzania, nyinyi ndio mkamuomba muwalee wao. Net na Maya.” Bibi Cote
akatabasamu huku akifiria kidogo.
“Jumamosi
sitakuja kazini. Nimemwambia Net naanza kupunguza masaa ya kazi. Ikiwemo siku
ya jumamosi, nitakuwa nakuja ikilazimu. Lakini msimu huu hauna kazi nyingi
sana, hata nyumbani naweza kufanya kazi zangu hizo siku za jumamosi. Tena
ikilazimu. Nitakwambia kitu ambacho si Net tu, hata Maya mwenyewe hafahamu.”
Tunda akatulia kidogo kisha akajibu sawa.
Alimuonyesha
kazi anazofanya hapo. Akamzungusha kwenye kila ofisi kwa kutumia kompyuta yake
palepale ofisini kwake. Nani anafanya nini wakati huo. Siku hiyo kama ametimiza
jukumu lake, na kama hakutimiza, ni kwa nini na akamwambia inamaana Net anajua
kama huyo mtu hajatimiza, na ni kwa makubaliano.
Muda
wakutoka ukafika. Wafanyakazi wakaanza kutoka, Maya akafika ofisini kwa bibi
yake akajitupa kwenye kochi kama aliyelemewa haswa, bibi yake akamkonyeza Tunda,
Tunda akacheka na kumgeukia Maya pale alipolala.
“Hey
baby girl!” Bibi yake akamuanza wa upendo. “I just wanna go home.” Akalalamika
huku amefunga macho akimwambia anataka kwenda nyumbani. Mpaka hapo, wafanyakazi
wote walikuwa wameshaondoka, wamebaki wao tu wanafamilia.
“Umemaliza?”
“Hapana Nana. Naomba uzungumze na Net. Anafanya maisha yangu yanakuwa magumu.
Kila kitu ananikosoa. Hakuna kitu nafanya sahihi!” “Kwa hiyo unakuwa umefanya
sahihi lakini anakusingizia?” “Come on Nana!” Maya akakaa.
“Mimi
nauliza tu!” “Ni vitu vidogo vidogo havina
hata maana, Nana! Anavikuza. Anataka kila kitu kiwe vile anavyotaka yeye!”
“Sidhani ni kama anavyotaka yeye, nafikiri ni kama inavyotakiwa.” “Nilijua
hutakosa sababu yakumtetea. I just wanna go home.” Maya akaendelea kulalamika.
Siku hiyo walikwenda kazini na bibi yake hakuendesha gari yake.
“Maisha
yangu yamebadilika! Kila mtu alikuwa akinijua kwa kuvaa vizuri. Lakini sasa
hivi navaa kawaida! Hamna muda wa shopping! Hakuna muda wakwenda salon kama
zamani! Hebu angalieni kucha zangu jamani! Zipo hivi zaidi ya …” “Ni jumamosi
mbili tu zimepita Maya.” Bibi yake akajaribu kumkumbusha.
“Sasa
wewe unafikiri ni kawaida!? Nani anakaa na kucha za aina moja zaidi ya majuma
mawili? Siendi club! Na unajua nini?” Akaangalia
kule alipokuwa amekaa kaka yake. Akapunguza sauti, akamsogelea bibi yake pale
mezani.
Ofisi
ya Maya ilikuwa upande wa pili wa upande zilipokuwepo ofisi ya Net na bibi yao.
Ofisi yake ilikuwa nusu imetengeneza nusu na aluminium nzito, juu ndio kioo. “Kana
kwamba haitoshi ile deadline ya mwisho wa mwezi, amesogeza imekuwa week hii.
Namaanisha hii tuliyo nayo sasa hivi!” Akamtolea macho bibi yake.
“Hivi
unajua zilikuwa zimemebaki siku ngapi hii week iishe kwa usalama nikiwa na
furaha?” Maya akaendelea kulalamika. “Leo
ni jumatano, Maya.” Bibi yake akajaribu
kumkumbusha taratibu. “Exactly! Ndivyo ilivyotakiwa iwe kwa watu wote. Na
ijumaa jioni niende na marafiki zangu club, jumamosi niende salon. Lakini
unajua imebidi ratiba ya juma zima ibadilike Nana! Niwaambie rafiki zangu
siwezi kwenda nao club, na jumamosi hatuwezi kutoka. Kwa sababu ‘Mr Boss’.’
Akanyanyua vidole vyake viwili kumkejeli kaka yake.
“Amesema
akiingia hapa ofisini jumatatu ijayo, kazi aliyonipa iwe imekamilika! Isipokuwa
imekamilika, inamaa…” “Umeshindwa kufanya.”
Bibi yake akamalizia. “There you go Nana! Na unajua kama nimeshindwa
mimi kufanya amesema atafanya nini?” “Atampa mtu anayeweza kufanya.” Bibi yake
akajibu taratibu tu.
“No
Nana! ANAAJIRI mtu anayeweza kuifanya. Na amesema hana bajeti yakulipa
wafanyakazi wawili kwa jukumu moja. Sasa unajua ni nini kitatokea kwangu?”
“Utakuwa na muda wakutosha kufanya shopping zako, kwenda saloni na club na
marafiki zako.” Tunda alikuwa anasikia kucheka vile anavyolalamika na bibi yake
kumjibu taratibu tu.
“No
Nana. Nooo. Amesema itabidi nimpishe huyo mtu kwenye ile ofisi. Ili atumie meza
yangu, kompyuta yangu, kiti changu, kufanya kazi niliyoshindwa.” “Lakini
itakusaidia kupata muda wa kutosha kufanya mambo yako.” Maya akavuta kiti
akakaa. “Amesema itabidi amlipe mshahara wangu. Wangu Nana! Hivi unanielewa?
Inamaana nitakuwa siingizi tena pesa.
“Kila
mtu aliyepinga akinikejeli kwamba siwezi kutulia kazini, Vic akiwa mmoja wapo,
watasema wapo sahihi. Mimi sio mtu wakutulia nakufanya jambo lakueleweka. Mimi
sio smart. Na sitaki kuwapa faida. Zaidi Vic. God I hate the girl!” “Hate is a
strong word, Maya.” “Ghhhhhh.” Akanguruma kwa hasira.
“Then I DON”T like
her. Simpendi yule kiumbe kupita kila kitu hapa duniani. Kama Net akinifukuza
kazi hapa, watapata sababu yakunisema. Nitakua gumzo mtandaoni tena! Na siwezi
kuwapa sababu.” Akasimama huku ameweka uso wa huzuni.
Tunda
alikuwa akimsikiliza huku akicheka taratibu. Hapo alipokuwa alikuwa amependeza
sana. Kila kitu alichoweka mwilini mwake, kuanzia juu mpaka chini kilikuwa
kizuri na cha thamani. Alipendeza, ungependa kumwangalia. Lakini alilalamika kuwa
anaonekana kama msichana mkulima au mfuga ngurue. Kucha zake mbaya. Wakati
zilikuwa nzuri tu.
Wakamuona
anatuma ujumbe, kisha akarudi kukaa. “Imebidi kumwambia yule dada anayenitengeneza
kucha na wa nywele, kuwa sitaweza kwenda jumamosi hii. Maisha yangu
yameharibika Nana!” Akaanza kulalamika tena. “Labda uende tu saluni, halafu
jumatatu utazungumza na Net.” “WHAT!?” Akashtuka Maya kama bibi yake anataka
kumponza vibaya sana.
“Wewe
si unamjua huwa hanipi nafasi yakuongea? Anachotaka ni kazi yake. Labda…” Akaanza
kumchekea bibi yake kama aliyepata wazo. Akajisogeza karibu. “Pengine wewe, my
sweet and wounderful Nana, uzungumze naye. Wewe huwa anakusikiliza.” “Oooh!
Nimwambie kuwa Maya hataweza kufanya kazi, kwa kuwa anaenda club ijumaa, na
jumamosi inabidi akatengenezwe kucha na nywele ili jioni atoke na marafiki zake
tena.” “Usiongee kwa kejeli Nana! Nisaidie. Nikifanikiwa weekend hii,
nakuahidi, weekend ile nyingine, nitatulia kazini.”
“Sawa
kabisa. Hilo wazo zuri. Sasa kwa kuwa tatizo la Net ni kazi ifanyike. Sasa wewe
tafuta mtu utakayemlipa kwa weekend hii unapukuwa club. Mlete hapa kesho. Mimi
nitampeleka kwa Net. Nitazungumza naye.” Maya akatulia kama anayefikiria.
“Mimi
ndio nitamlipa?” “Si atafanya majukumu yako!?” Bibi yake akamuuliza taratibu tu.
“Kwa nini usimwambie Net aidhinishe malipo yake?” “Kwani wewe alikwambia nini?”
“Can’t remember.” Mpaka Tunda akacheka kwa sauti vile Maya alivyosema hakumbuki
alichoambiwa na kaka yake.
“Maya!
Si umetoka kusema kuwa amesema hana bajeti ya kuongeza mfanyakazi mwingine?” Bibi
yake akamkumbusha. “Oooh yeah!” Akajidai kukumbuka. “Kwa hiyo utazungumza na
Net kama nikimtafuta huyo mtu?” “Kabisa. Wewe acha funguo za ofisi hapa na
password ya kompyuta yako, pamoja na palipo ya huyo mtu. Nitamkabidhi Net.”
Maya akabadilika kabisa. Akapooza.
“Itakuaje
awe mzuri hapa kazini kuliko mimi? Hudhani Net anaweza kumpa majukumu yangu
moja kwa moja?” “Atakutafutia majukumu mengine ambayo hayatakufunga sana.”
“Unawezaje kusema hivyo Nana, jamani!? Sasa hapa upo upande gani?” “Wako Maya.
Na itakusaidia kupata majukumu rahisi, na utakuwa huru kufanya mambo yako.”
“Sasa
si unajua wazi atanihamishia kwenye ofisi zile za wafanyakazi wote na mshahara
atapunguza!?” “Lakini utakuwa na muda wakutosha kufanya mambo yako? Club,
saluni na dinner na rafiki zako.” Akaendelea bibi Cote. Taratibu tu.
“Hata
yeye alikwambia Maya. Mshahara mkubwa, unakuja na majukumu makubwa. Alikwambia
mapema kabisa. Anakupa ofisi, bili ya simu itakuwa juu ya kampuni, na mshahara
mzuri lakini anataka kuona matokeo. Alikwambia hatawekeza sehemu ambayo
hatapata faida.” Bibi yake akaendelea taratibu tu.
“Alikupa
thamani ya kile chumba unachotumia sasa hivi. Matarajio yake. Sasa kama
umeshindwa mwambie tu. Atatafuta mtu mwingine ambay…” “No nononooo!
Sijashindwa. Na wala usimwambie hivyo. Mimi naweza kufanya kazi zangu zote.
Kwanza nimeshakuwa mkubwa. Mambo ya club nimeacha. Halafu saluni naweza
kuahirisha nikaenda siku ambayo sina mambo mengi. Sio lazima jumamosi.” Maya
akaanza kutoa mipango mipya kama sio yeye. Akakanusha mambo yote. Akaacha
kulalamika kabisa. Bibi yake na Tunda wakabaki wakimsikiliza.
Mara
akaingia Net. “Nilikuwa namwambia bibi jinsi ulivyoniamini na majukumu mengi na
mazito.” Net akamtizama, maana aliingia tu, Maya akamdaka akionyesha wasiwasi
kidogo usoni. Kama anayejihami.
“Ila
sijalalamika. Nimemwambia Nana, jumamosi wakati wewe unakuja kazini, na mimi
nitakuja. Mpaka inafika jumamosi jioni, nitakuwa nimekamilisha kila kitu.
Jumatatu ukiingia kazini utakuta kila kitu kipo tayari.” “Good!” Akajibu kaka yake kwa kifupi tu.
Akamsogelea
Tunda, akainama, akambusu midomoni kwa muda kidogo. Akageuza kiti alichokuwa
amekalia Tunda pale mbele ya meza ya bibi yake, akamgeuzia upande wake. Akapiga
magoti mbele yake. “Vipi?” Akamuuliza. “Safi tu, nilikuwa naonyeshwa kazi.”
Tunda akajibu.
“Nilikuwa
pia namwambia Tunda, asione kama maisha ni mapweke sana huku. Kufungiwa ndani
tokea anafika. Ningekuwa sina kazi jumamosi, ningemtoa dinner, kwenye hoteli
nzuri sana.” Maya akaingilia.
“Pamoja
na wale rafiki zako walevi?” Net akamuuliza huku akipapasa tumbo la mkewe na
kulibusu. Maya akababaika kidogo. Kaka yake alikuwa amempa mgongo. “Sio wale.”
“Unarafiki gani ambaye sio mlevi?” Net akamuuli taratibu tu, kisha akabusu
tumbo la mkewe tena.
“Kama
sio walevi wa madawa ya kulevya, basi pombe kali na wavuta sigara. Na kama
umesahau, Tunda ni mjamzito. Moshi wowote wa sigara na madawa yenu ya kulevya,
utamwathiri Cote na mama yake.” Kimya. “Umenielewa Maya?” Net akasimama na
kumgeukia Maya. “Siwezi kumpeleka huko.” “Na wala usifikirie. Kama wewe unataka
kwenda, nenda. Ila ujue wazi, watakurudisha rehab.” Net akaendelea huku
akimwangalia Maya kwa ukali.
“Na
safari hii ukirudi tena rehab, ujue umepoteza uaminifu wako wote. Hutakaa
kufanya kazi hapa tena. Itakuwa ni juu
yako wewe na Nana. Umenielewa Maya?” Maya alionekana ameshaingiwa hofu
yakupitiliza.
“Mbona
mimi nimeacha kabisa? Nimekuahidi nitatulia. Ndio maana unaniona mpaka sasa
hivi nipo hapa.” “Kwa nini unarudia maisha ya club?” “Sijarudia.” “Maya?” Kaka
yake akamwita kwa ukali kama akimuonya, usinidanganye. Maya akababaika sana.
“Nilitaka
kwenda tu kusalimia rafiki zangu. Sio club kama zamani.” Maya akajibu kwa hofu
huku akimtizama kaka yake. “Sponsor wako alikwambia nini?” Net akamuuliza. Maya
akatulia akijidai anafikiria. “Maya?” Net akamwita kama asipoteze muda amjibu.
“Kuhusu nini?” “MAYA?” Net akamwita
kwa ukali, akiwa ameshabadilika mpaka Maya akarudi nyuma huku akimtizama bibi
yake.
“Alisema
nikae mbali na club na kundi zima la marafiki niliokuwa nikitumia nao madawa ya
kulevya wakati ule na wakanifanya nirudie tena.” Tunda alishtuka kidogo.
Hakujua kama Maya alitumia madawa yakulevya.
“Na
sasa hivi unataka kufanya nini? Tena unataka umpeleke na mke wangu!” “Sio kwa nia mbaya Net. Am so sorry.” Akaanza
kulia. “Sitaki
kurudi tena rehab.” “Then stay away from all clubs and your friends.
Unaweza kutafuta marafiki wengine, ukatafuta kitu kingine chakufanya na
ukafurahia maisha tu. Tafadhali badilika Maya.” “Nimebadilika
Net. Nakuahidi nimebadilika. Muulize Nana.” Maya akamsogelea bibi yake
akitaka utetezi.
“Mwambie Nana. Nana ndio amekuwa rafiki yangu. Sinywi hata wine.
Nakuhakikishia Net. Hata ulipoondoka, nilikuwa naenda saluni na kurudi
nyumbani. Mwambie Nana.” Hapo Maya
alikuwa akilia kwa hofu. Akiongea huku akimwangalia bibi yake akitaka utetezi kwa
Net.
“Unajitahidi
Maya. Hata mimi nakupongeza. Sasa jitahidi kuepuka vishawishi. Weka akili zako
sehemu sahihi. Hutarudi tena rehab.” Bibi yake akamtia moyo. “I love you Net!” Mpaka Tunda akamuhurumia.
Alionekana Net alimbadilikia. Mahusiano aliyowaacha nayo mara ya mwisho sio
haya. Maya alimuogopa sana tofauti na zamani walipoishi pamoja Arusha.
Tunda
akamtizama Net kama anayetaka apokee ujumbe fulani. Net akamtizama kidogo
Tunda, akamgeukia Maya. “Am so sorry Net.”
Maya akaanza. “And I love you so much.”
Kakaongea kwa upendo huku akilia kwa hofu kama anayebembelezea undugu.
Net
akavuta pumzi kwa nguvu huku akimwangalia. “I love you too Maya. Najua unajua.
Nisingekutaka kitu ambacho najua huna uwezo nacho. Nakuhimiza kwa kuwa najua
unao uwezo mkubwa sana. Ndio maana
unapokuwa na muda mwingi usio na matumizi, unaanza kufanya maamuzi mabaya.
Unafanya kazi nzuri sana. Umetushangaza mimi na Nana. Sikutaka kukwambia
kwanza, mpaka baada ya mwisho wa mwezi. Lakini unafanya kazi nzuri.” Net
akajirudi kidogo.
“Kuna
moja ya mtu ambaye ulikuwa ukimfuatilia. Mteja. Amempigia simu Nana. Amekusifia
sana. Kwako alikukatalia. Lakini alikuwa akikuchezea tu akili. Ni wateja wetu
wa zamani. Walifilisika. Wakafunga bishara yao. Alikuwa kimwambia Nana, ndio
wameanza upya. Wewe ndio umewatafuta. Hakuna hata aliyekutuma. Mimi na Nana,
tukahisi ni kuwa ulipitia wateja wa zamani waliokuwa wakiingizia kampuni faida,
ukawapigia. Si ndio?” Maya akacheka huku akijifuta machozi.
“Unaona
sasa? Hiyo akili bila madawa ya kulevya, inafanya kazi vizuri sana.” “Net!” “Yes Maya. Mbali na wale marafiki zako, na
ulevi, wewe ni msichana mwenye akili sana. Una uwezo mkubwa wakufikiria na
kufanya mambo. Umepata nafasi nyingine, na naomba iwe ya mwisho. Usirudie
tena.” “Sitarudia. Kwa
hiyo wamekuwa wateja wapya?” Net na bibi yao wakacheka.
“Wanaanza
biashara, na sisi ndio tutakuwa tukiwasambazia bidhaa zao sehemu zote. Na hiyo
ni wewe umefanya. Hata Nana amekiri kuwa aliwasahau. Lakini wewe umewasaka
mpaka umewapata. Nikafurahi sana. Sasa nashangaa unataka kurudia tena kule ilikotugharimu
kukutoa! Mbaya zaidi na mke wangu! No
Maya.” “Am so sorry Net. Nakuahidi sitarudia tena. Nakuahidi. Nisamehe.”
Net akamsogelea akambusu kisha akamkumbatia.
“Jumamosi
tutakuja wote kazini.” Maya aliongea akiwa amekumbatiwa na kaka yake. Net akacheka.
“Na uhitaji kukaa hapa kazini muda mrefu kama mimi. Jumamosi unaweza kujipangia
masaa machache kama alivyokuwa akifanya Nana, kisha unaendelea na mambo yako.
Shopping au saluni.” Maya akacheka.
“Basi
kama ni hivyo sihitaji kuahirisha saluni. Nitawaambia nitakwenda mchana.” Bibi
yake akacheka, “Hutafuti tena mtu..” “Shhhhh! Nana!?” Maya alishtuka sana
akaruka pale alipokuwa amekumbatiwa na kaka yake akaenda kumnyamazisha bibi
yake. Hakutaka Net asikie.
“Nimebadilika.
Sasa hivi ni Maya Cote. Cote huwa tunafanya kazi kwa bidii, na tunaishi kwa
kufikiria.” Wote wakacheka. “Twende Tunda.” Net akamshika mkono mkewe,
wakaondoka.
Net ampa Tunda historia ya Maya hapo nchini.
Wakati
wapo njiani ikabidi Tunda kuuliza. “Kwani Maya alishatumia dawa za kulevya?”
“Pale alipo, hawezi kuajiriwa popote. Yupo kwenye mitandao yote ya sheria kuwa
ni binti mlevi, mwizi, kahaba na kila sifa mbaya unayoweza kufikiria. Hata
wakati ule alipokuja Tanzania, ukakutana naye mara ya kwanza, tukaishi naye
Arusha, mama ndiye aliyelazimisha aletwe kule kwa muda. Alikuwa ametoka tu
rehab, na ni kama alikuwa na hatari ya kurudia tena madawa ya kulevya.” Tunda
akashangaa sana.
“Unakumbuka
alimaliza tu high school akawa hataki kwenda chuo?” “Uliniambia.” “Basi kazi
yake ilikuwa hiyo. Wanaume na madawa ya kulevya. Gari anayoendesha sasa hivi,
ni yake. Tumekataa kumnunulia gari nyingine, kwa kuwa gari ya kwanza aliyokuwa
amepewa na babu na Nana kama zawadi ya birthday yake alipofikisha miaka 16, alipata
nayo ajali mbaya sana.” Tunda akamgeukia Net aliyekuwa akiendesha.
“Alikuwa
yeye na boyfriend wake. Wote wamelewa. Nikikwambia ni gari ya thamani, niamini
ilikuwa ni ya thamani. Walimnunulia kwa pesa taslimu. Wakaigonga vibaya sana.
Yeye alipata michubuko tu, mwenzake alilazwa karibia mwezi. Ilikuwa mbaya sana.
Maana walinasa kama chini ya daraja. Waokoaji walipata shida sana kuwatoa.
Ulikuwa uokoaji zaidi ya masaa 12. Kila chombo cha habari hapa nchini
kiliwatangaza wao. Walikuwa wakionyeshwa jinsi wanavyohangaika kuwatoa kwenye
gari bila madhara.” Net akaendelea.
“Manesi,
madaktari, polisi, watu wa zima moto, walikaa hapo eneo la ajali kuanzia huo
usiku wamejulikana wamepata ajali, wakiwahudumia, mpaka kesho yake jioni, ndipo
wakafanikiwa kuwatoa hapo kwenye gari.”
“Ilibidi
huyo mwenzake aanzishiwe matibabu hapo hapo kwenye eneo la ajali wakiwa bado
wamenasa ndani ya hilo gari, chini ya hilo daraja. Alipasuka vibaya sana,
ikabidi kushonwa na kuongezewa damu hapohapo wakati juhudi za kuwatoa zikiendelea.
Sidhani kama alikuja kutembea tena yule kijana.” “Net!” Tunda akashangaa sana.
“Ilikuwa
mbaya sana Tunda. Mbaya zaidi ni mtoto anayetoka kwenye familia ya Cote. Hakuna
mtu aliacha kututangaza. Papa na Nana walikaa hapo eneo la tukio muda wote wakisubiria
atolewe. Akatoka hapo anamikwaruzo tu. Nafikiri na alivunjika mkono.”
“Kwa
ile kashfa, ndio akakubali kurudi rehab. Alipotoka hapo, akatulia kidogo, mama
akasema apelekwe tena Tanzania. Ndio wakati ule ukakutana naye wewe, akiwa
ametulia kidogo. Ukamshauri arudi shule, ndio akarudi huku. Akasoma miaka 3,
akamaliza shahada yake vizuri tu.”
“Hatujakaa
sawa, akapata mwanaume mwingine aliyekuwa akitumia madawa ya kulevya,
akamrudisha tena huko huko.” “Net!” Tunda akashangaa. “Maya amesumbua sana. Anajulikana
kila mahali. Kila mtu anamfahamu kuwa ni binti asiye na maadili na haaminiki.”
“Ikawaje tena?” Tunda akauliza. “Ipi sasa? Hii ya baada ya shahada au kabla?”
“Mhhh!
Hata sijui niulize ipi. Maana alinisimulia juu ya kadi aliyokuibia, ndio maana humuamini
na kadi yako.” “Alinitenda vibaya! Niliumia kupita kiasi. Na mbaya zaidi mimi
mwenzie pesa yangu huwa napata kwa kufanya kazi sana.” Net akaendelea.
“Kuna
kipindi mpaka nilikuwa nikiendesha trucks za babu. Kupeleka mizigo mbali ili kukusanya
pesa. Wakati ule hawaajiri watu ofisini, ila madereva tu. Na mimi nilikuwa bado
nipo chuo. Kwa hiyo kila ninapokuwa likizo, nikija kuomba kazi kwa papa,
unakuta hana nafasi ya ofisini. Lakini upande wa madereva, maana huko ndio mara
nyingi kunakuwa na upungufu wa madereva. Kwa hiyo babu alikuwa akiniambia kama
nataka kazi, basi niendeshe lori kusambaza mizigo.” Net akacheka.
“Ni
ngumu sana hasa kipindi cha baridi. Wakati mwingine unakuwa unalala kwenye
barafu usiku kucha. Labda gari imeharibika au unasubiria mzigo sehemu ili urudi
nao huku. Hapo nafanya kwa juhudi huku nikijenga kule Tanzania. Na sikutaka
msaada hata wa tofali moja. Nilipokwenda kumpeleka papa kwenye ile nyumba,
alilia Tunda. Hakuamini!”
“Ninachotaka
kukwambia ni kuwa, japokuwa tulizaliwa kwenye pesa, lakini papa alinifundisha
kupata pesa kwa jasho langu. Sasa hangaika yote hiyo, Maya akapotea. Baada ya
siku ya 5, ndio tukaanza kupatwa na wasiwasi. Kwa sababu huwa akipotea ni siku
3, ya 4 anarudi.” “Subiri kwanza Net. Kuwa hiyo ndio ilikuwa tabia yake?” Tunda
akauliza.
“Hiyo
ya kupotea?” Net akauliza. “Eeeh!”
“Kabisa. Akishakusanya pesa. Maana huwa alikuwa akipewa pesa kila baada ya
majuma mawili. Anakusanya pesa, anapotea na wanaume zake. Zikiisha, anarudi. Na
usifikiri anaenda kupotea sehemu za kimasikini? Anaenda kujifungia kwenye
mahoteli ya maana. Wanakula unga huko, akiishiwa yeye na huyo mwanaume wake wa
wakati huo, anarudi.” Tunda akashangaa sana.
“Sasa tukashangaa siku
ya 5 inaisha, harudi. Babu na bibi wakasema kuna kitu hakipo sawa. Babu akasema
kila mtu aangalie kadi zake. Nikakuta kadi yangu ya akiba haipo. Nikakumbuka
nilimtuma akamnunulie Nana zawadi, hakurudisha. Nikaangalia kwenye salio. Tunda
nililia kama mtoto mdogo.”
“Ndio
ikabidi babu atume watu wakamtafute usiku huo huo. Sijui alipata mwanaume
tapeli wa kiasi gani! Akamsaidia kuhamisha dola laki moja, kutoka kwenye
akaunti yangu, akajiwekea kwenye akaunti yake.” “Mungu wangu Net!” Tunda
alishtuka sana.
“Acha
Tunda. Ni akiba niliyokuwa nikiweka tokea nina miaka 14, nilipoanza kazi
ofisini kwa Papa. Ananipa kazi, ananilipa. Haya, nikiendesha malori yake, akawa
ananilipa pia. Sasa ukumbuke nilikuwa sina matumizi. Nakula na kulala bure.
Gari yangu ya kwanza pia Papa alininunulia. Kwa hiyo kila pesa niliyokuwa
nikipata, natunza. Labda matumizi kidogo sana.”
“Basi.
Akamnunulia gari huyo mwanaume. Gari ya dolla elfu 45. Akamlipia kutoka kwenye
hiyo pesa yangu. Ndio wakaanza starehe. Baada ya siku mbili mbele, yaani ya 7.
Ndio waliotumwa kumtafuta, wakampata kwa kuangalia ni wapi mara ya mwisho kadi
yake imetumika, maana hapo ikabidi Papa afunge kabisa ile akaunti yangu,
akaniambia nifungue nyingine, kwa kuwa yule mwanaume wa Maya wameshaijua.”
“Walimfunga?” Tunda akauliza.
“Hakuwa
na kosa la kushtakiwa. Pesa zilitoka kwenye akaunti ya Nethaniel Cote, kwenda
kwa Maya Cote. Haya, gari amenunuliwa zawadi na mpenzi wake. Na lipo kwa jina
lake yeye huyo kijana. Anakosa gani la kumshitaki? Mbaya zaidi, walikutwa wapo
hotelini wote wapo high. Wamekula madawa, hawajitambui. Ukiita polisi, inamaana
unamtia matatizoni huyo Maya.” “Mungu wangu!” Tunda akaendelea kushangaa.
“Akarudishwa
nyumbani. Hapo kila mtu anajihami na pochi yake. Papa na Nana wanafunga chumba
chao wakiondoka. Mimi ndio alikuwa akiniogopa, hataki hata nimsogelee. Alikuwa
anamfuata Papa mpaka chooni! Sababu ya madawa, akaanza kuuza vitu vyake.”
“Jamani!” Tunda akasikitika.
“Wanaume
wakawa wanampenda. Kazuri, halafu katoto ka Cote. Kule kuwa naye tu, ni
kujipatia sifa mitandaoni. Moja, pili wananufaika. Hakajui uchoyo. Mtu
akimlilia shida tu, anasaidia.”
“Fujo
zikaanza. Wanamg’ang’ania. Hakuna anayekubali kuachwa na Maya. Mwanaume huyu
akijua ameachwa yupo na mwanaume mwingine, hakubali. Picha zake za ngono
zikaanza kuzagaa mitandaoni. Wanamtaka. Akikataa kurudiana nao, wanamchafua kwa
picha au video wanazokuwa wamemchukua kipindi amelewa hajitambui.” “Net!” Tunda
akaumia sana.
“We acha tu. Basi nayo
ikawa fujo. Kila kukicha, Maya yupo mtandaoni akifanya mapenzi na mwanaume huyu
au yule. Mara wakiwa club au kwenye gari, ilimradi ni fujo tupu.” “Maskini
Maya!” Tunda akajikuta akimuhurumia.
“Ilikuwa
mbaya sana. Na yeye hapo hawezi kutulia tena, sababu ya madawa. Akifungiwa
mlango, anatoroka. Papa na Nana wanapokuwa wakienda kazini, wanakuwa wakimuacha
ndani, wanamwambia Carter asimruhusu atoke. Carter anakuja kuwapigia simu
kuwaambia hayupo, na hajui saa ngapi ameruka dirisha.” “Kwenye lile jumba
anaruka dirisha!?” Tunda akashangaa maana hiyo nyumba ina madirisha marefu sana
kutoka chini.
“Madawa!
Hapo hajali jinsi atakavyoumia. Ilimradi atoke tu akapate madawa. Akahangaika
hivyo ndio mpaka akapata ajali, akakubali kwenda rehab. Akatoka akiwa ametulia,
ndio akaja Tanzania. Kipindi kile mkakutana naye kwa mara ya kwanza.” Tunda
alibaki na mshangao.
“Sasa
alipomaliza chuo, safari hii ya pili. Akampata huyo jamaa niliyekwambia naye
akamrudisha kulekule. Walianza vizuri. Tukajua wataoana. Maana alikuwa ametulia
kweli Maya. Ila kazi akawa hapati sababu ya sifa mbaya. Hakutaka kufanya kazi
na Nana. Alijua kanuni ya pale ni kazi tu. Hakuna kucheza. Akahangaika kutafuta
kazi bila mafanikio.” “Sasa kwa nini hamkumsaidia na jina hilo la Cote?” Tunda
akauliza.
“Huku
Tunda sio kama kule Tanzania. Ukishakuwa na makosa yanayokupelekea kufungwa tu.
Au ukaingia kwenye mkosa ukaingizwa kwenye mitandao ya usalama, umejiharibia
kabisa. Kuna kitu kinaitwa background check. Unafanyiwa na mwajiri kabla hujaajiriwa.
Ili wajue wanamwajiri mtu wa namna gani.”
“Sasa
kwa Maya, ilikuwa hata haiitajiki background check. Alijulikana kuwa ni mwizi,
anatumia madawa ya kulevya, haaminiki, na mengine mengi. Sasa ni nani
atamwajiri?” Tunda kimya. “Na papa naye hakutaka aweke jina lake popote asije
akaharibu huko, akaharibia Cote wote! Wakamuacha tu. Maana Nana alisema kama
kweli amekusudia kubadilika, angeomba kazi pale. Kuwakwepa, inamaana
hajakusudia kutulia.”
“Wakamwacha
ahangaike mwenyewe, huku wakijiambia, akikwama, atarudi kuwaomba wao msaada, na
hapo watajua kuwa ametulia. Papa alikuwa akifanya kazi pale, huku akiwafikiria
mpaka hawa kina Cote. Alisema ni kampuni ya kizazi hadi kizazi. Hakutaka mtoto
mmoja aliyekusudia kutotulia, aje aharibie wenzake. Kwa hiyo wakamwacha tu.”
Tunda akashangaa mipango ya hiyo familia.
“Na
kweli, baada ya muda, akarudia tena madawa. Akaanza taratibu. Akizidiwa harudi
nyumbani. Analala huko huko anasema labda usiku huo atalala kwa huyo mchumba.
Haya, akaendelea hivyo hivyo.”
“Subiri
kwanza Net, inamaana alikuwa akiruhusiwa kulala kwa mwanaume wake?” “Tunda!
Labda hujaelewa juu ya Maya. Ilikuwa ni bora hivyo anajulikana yupo na mwanaume
mmoja, kuliko vile alivyokuwa hajulikani yupo na mwanaume gani na wapi!” Tunda akastaajabu
sana.
“Huyo
jamaa mwenyewe mwanzoni alikuja kumtambulisha kwa kina Papa, akaonekana ni
kijana mzuri tu, tena mwenye maadili. Kidogo ikawa afadhali. Kwamba anajulikana
yupo na mwanaume mmoja tu. Halafu wakati huo Papa alishaanza kuumwa. Hakuna
anayefikiria chochote ila ugonjwa wa Papa. Akawa huru na huyo kijana, Nana
anauguza.” “Jamani Maya wangu!” Tunda akamsikitikia.
“Haya,
uhuru ukaongezeka. Hana kazi, ila pesa anayo. Nana na Papa walikuwa wakimpa
pesa za kujikimu wakati akitafuta kazi. Akazidisha madawa, akaanza kuaga kuwa
anasafiri labda siku tatu au nne. Kumbe yupo nyumbani kwa huyo jamaa wanatumia
hayo madawa.”
“Sasa
mbaya zaidi, safari hii akawa amepata mwanaume ambaye na yeye alikuwa na pesa
kidogo. Halafu kama mtu mzima hivi, hana mambo ya kitoto kama vijana wengine
kujiweka mitandaoni. Mambo yakawa yanaenda kimya kimya, hakuna anayejua. Maya
haishiwi hovyo wala haibi. Akiishiwa yeye pesa, yule kijana ananunua yeye hayo
madawa.”
“Wakaendelea
hivyo mpaka Papa akaja kuzidiwa, akafa. Mimi na mama tukaja kuzika. Hakuna
anayejua kama amerudia tabia zake. Msafi tu. Tulipoondoka sasa. Akabaki Nana
akiomboleza, yeye ndio akapata uhuru mkubwa sasa. Hakuna wakumuuliza wala
kumgundua. “Ni kama hapakuwa na mtu tena anayemfuatilia. Hata Nana alipokuwa
naye nyumbani, hakuwa na muda. Ni kama kifo cha Papa kilimsumbua sana Nana. Ni
mpenzi wake waliyekuwa kwenye ndoa ya zaidi ya miaka 65. Tokea Nana ni binti
mdogo, anasema walianzana akiwa na miaka 14 tu, mpaka akaja kumuoa na ndio
kifo.” “Maskini!” Tunda akamuhurumia bibi Cote.
“Sasa
siku moja Nana akaja kugutuka, Maya hayupo! Akili ndio ikamrudia. Akamuuliza
Carter. Carter akamwambia alimsikia akimuaga kuwa atasafiri na boyfriend wake
kwa siku tatu. Nana akasema akashtuka kidogo. Hiyo ilikuwa siku ya 8 tokea
aondoke. Ndio Nana akaanza kutuma watu wapeleleze. Kumbe alikuwa jela.
Alikamatwa na huyo kijana wanafanya mapenzi kwenye gari, pembeni ya barabara,
wamelewa hata hawajitambui.” “Net!” Tunda akashangaa sana.
“Kweli!
Huyo polisi aliyewakamata, alimwambia Nana ilikuwa ni heri vile alivyowachukua
kuliko angewaachia. Wangepata ajali mbaya sana. Wanasema walikuwa hata hawajitambui.
Walipimwa, wakakutwa ni cocaine. Maya akaogopa kupiga simu nyumbani. Akasema
yeye yupo tayari kufungwa. Ila Nana na mimi tusiambiwe. Basi. Ndipo hao watu
waliokuwa wametumwa na Nana wakaja kumpa hizo taarifa.” “Atakuwa aliogopa!” Tunda
akaongeza.
“Kabisa.
Na kipindi hicho nilikuwa Tanzania, ikabidi nirudi nianze kufuatilia kesi yake.
Logan akamtetea kuwa alilevya. Yeye hakuwa na hayo madawa. Mahakama ikataka
dhamana ya dolla milioni moja kwa ajili yake. Kwa kuwa tayari alikuwa na makosa
mengi yanayofanana na hayo. Kuanzia ana miaka 17 mpaka hapo.” Tunda hakuwa akiamini.
“Ndio
Nana akasema hiyo pesa ilipwe, Maya atolewe. Lakini mimi na Nana tukamfuata
akiwa huko huko jela amefungwa, tukampa masharti. Nikamwambia hiyo pesa itatolewa kwa masharti yafuatayo. Arudi
rehab asafishwe kabisa au kutibiwa. Akitoka, atafue kazi itakayomsaidia kulipia
gharama zote, ya hiyo rehab na gh arama
za mwanasheria atakayemtetea kwenye kesi yake. Akakubali haraka sana. Maana
alisema akihukumiwa kufungwa atakufa jela.”
“Basi.
Ndio ikabidi sasa tugharamie gharama zake za rehab na hiyo kesi ambayo
ilinguruma Tunda. Hakuna jinsi nikakwambia ukaelewa. Tulichafuliwa kupita
kiasi.” “Poleni Net.” “Na hapo ukumbuke Papa ndio amekufa amebaki Nana.
Magazeti yakawa yanaandika kuwa ndio mwisho wa kizazi cha Cote.” “Jamani! Kwa
nini sasa?” “Hiyo pesa iliyokuwa ikidaiwa ya mahakama Tunda! Nyingi mno. Halafu
ilibidi kutafuta mwanasheria wa hali ya juu ili ashinde kesi ya Maya ambayo
hapakuwa na uwezekano wa kushinda.” “Net!” Tunda akashangaa.
“Ni
Maya. Kumbuka alikuwa ana makosa kama hayo yanayofahamika kila mahali. Wazazi
wengine, rafiki tu wakaribu wakawa wanasema ni heri Maya afungwe pengine
akitoka atakuwa amebadilika, anaharibu vijana wao. Kuna wazazi walikuwa
wakisema Maya alishawatoa vijana wao mashuleni na kuwafundisha madawa ya
kulenya.” “Jamani!”
“Ilikuwa
mbaya sana. Lakini Mungu akasaidia. Ni kweli pesa ilitoka, lakini Maya
akashinda kesi. Alikuwa akitolewa rehab, anapelekwa mahakamani. Mpaka akashinda
kesi na kutoka rehab. Ndio pale unamuona anafanya kazi kubwa, malipo madogo.” “Net!”
Tunda akashangaa.
“Unafikiri
namtania? Ameshamaliza kulipa kampuni gharama zake za rehab. Sasa hivi analipa
gharama za mwanasheria. Kesi yake ilichukua karibia mwaka mzima. Ikafutwa. Yote
hiyo ilikuwa gharama ya kampuni. Sasa ndio analipia.” “Mmmh!” Tunda akachoka
kabisa.
“Pale
alipo hakuna sehemu yeyote wanaweza kumuajiri, wala hana ujanja wakutolipa.”
“Unanuonaje lakini?” “Anajitahidi. Na tunamfanyia makusudi kumpa kazi nyingi
ili atulie. Tunaamini kadiri siku zinavyozidi kwenda. Tukimpa ukweli wa maisha.
Anaelewa, na kutulia. Papa alimfanya aishi bila kufikiria. Anapewa kila kitu na
alikuwa anamkingia kifua. Hakuwahi kukua kwa Papa. Mpaka leo analia msiba wa
Papa.” “Maskini Maya wangu!”
“Vile
unavyomuona sasa hivi. Hana tofauti na wewe hapa nchini. Anajifunza maisha
mapya kabisa ambayo hakuwahi hata kufikiria anaweza kuja kuishi. Zaidi akijua
hayupo Papa. Papa alikuwa mkali kwa kila mtu, kasoro Maya. Alikuwa anamfanya
kama mtoto wa miaka 5. Sasa kuja kuona ameangukia kwangu! Ni maisha ambayo hakuwahi
hata kufikiria kama atakuja kuishi.” Walikuwa wameshafika nyumbani. Wameegesha
gari nje wakiendelea kuzungumza.
Jumamosi ya Bibi Cote na
Tunda.
Jumamosi
hiyo Net aliamka akiwa na ahadi yakuwahi kurudi kutoka kazini. “Wewe utakuwa na
Nana?” “Amesema anataka twende wote tukafanye manicure na pedicure.” “Safi.
Najua mtapata muda wa mazungumzo pia. Naomba jaribu kumzoea. Ana mambo mengi
mazuri ambayo najua ukikaa naye, utanufaika sana.” Tunda akacheka kidogo kama
anayefikiria.
“Vipi?”
“Namuona anajitahidi kweli kuwa karibu na mimi, lakini naona kuna kama ukuta
kati yetu!” “Ndio maana nakuomba ujitahidi. Kuwa huru. Usimuogope.” “Najitahidi
Net. Kumbuka ni wewe na mama Penny tu ndio mmekuwa watu wakuwa karibu na mimi.
Mnanielewa na kunichukulia vile nilivyo. Mmenibeba zaidi na nilivyowahi
kufikiria. Sijui mahusiano ya watu wengine yanakuaje!” “Mbona Maya umemzoea?” Tunda
akacheka.
“Wewe
unamuona Maya anasubiri kuzoelewa? Akitoka tu kazini, anakuja kujilaza hapa
kwenye kitanda pembeni yangu mpaka akusikie nje ndio anakimbia kutoka hapa.
Ananifuata mpaka chooni! Hasubiri hata nimkaribishe au nimjibu. Atapiga stori
zake hapo weee. Mpaka akusikie wewe ndio anakimbia.” Net akacheka.
“Naomba
mpe nafasi na Nana.” “Nitajitahidi. Sasa nani atalipia?” “Halafu inabidi twende
wote benki jumatatu.” “Kufanya nini?” “Kufungua akaunti yako ya hapa uwe na
kadi yako.” Tunda akanyamaza. Net akarudi pale kitandani alipokuwa amelala
Tunda. Alikuwa anamalizia kuvaa aende kazini.
Akambusu.
“Unawaza nini?” “Hamna kitu.” Tunda akajibu. Net akabusu tena, na tena. Akaanza
kumpapasa. “Utachelewa kazini Net!” Net akacheka huku akimbusu shingoni na
mikono ikimpapasa. “Huko unakokwenda, mwisho wake nitakubaka!” Net alicheka
sana. Akasimama.
“Nataka
nikirudi, unibake.” Tunda na yeye akaanza kucheka. “Net!” “Nani hataki kubakwa
na mkewe? Tena Tunda! Mimi nibake tu.” Tunda akazidi kucheka. “Nana atalipia.
Halafu nimefikiria, naona jumatano wakati tunatoka kliniki ndio twende benki.”
“Sawa. Uwe na wakati mzuri kazini.” “Na wewe ukawe na wakati mzuri huko.”
Akambusu, nakutoka.
Net
alipotoka saa 11:30 asubuhi hiyo, akapitiwa tena na usingizi mpaka kwenye saa
tatu na nusu haja ndogo ilipomuamsha tena. Ikabidi tu aamke na kuoga kabisa. Kwenye
saa nne hivi akatoka. Moja kwa moja mezani. Akakuta Gino alishamtengenezea uji
na vyakula vingine vipo hapo mezani. Lakini Gino mwenyewe hayupo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jumamosi
ilikuwa siku ambayo karibu wote wanachelewa kuamka kasoro Net ambaye kuanzia
jumatatu mpaka jumamosi anatoka hapo nyumbani saa 12 kamili au kasoro, alfajiri
ili saa 12 na nusu au na robo awe amefika ofisini kwake. Inategemea ametoka
nyumbani muda gani.
Wakiagana
kwa muda mrefu na mkewe asubuhi hiyo basi ujue Net atakuwepo ofisini kwake saa
12:30. Kama ni mazoezi tu na kupata kifungua kinywa pamoja, wakati mwingine saa
12:15 au 12 kamili atakuwa ameshawasili ofisini.
Maya
yeye siku za jumamosi huondoka hapo nyumbani mida ya saa mbili na nusu ili saa
tatu kamili awe ameshafika ofisini kwake. Ratiba yake na bibi yake iliendana
kasoro siku hizo za jumamosi alizoamua bibi huyo kutoenda kazini.
Mara
nyingi siku za jumatatu mpaka jumamosi hawakuwa wakipata kifungua kinywa pamoja,
ila jumapili. Kwa kuwa mara nyingi Maya na bibi yake walikwenda kazini muda
unaofanana, wao walipata kifungua kinywa pamoja. Saa moja na nusu asubuhi wao
wanakuwepo mezani wakati Net na Tunda wanakuwa walishapita hapo mezani mapema
sana.
Gino
alikuwa akifika hapo alfajiri ya saa 11, ili kuhakikisha Net anapata kifungua
kinywa kabla ya kwenda kazini. Zaidi smoothie ambayo humtengenezea mara baada
ya mazoezi. Ndipo anakwenda kuoga na kuja kupata kifungua kinywa rasmi.
Mara
nyingi akitoka hapo kwa mara ya pili baada ya mazoezi na kunywa smoothie,
wakati anapata sasa kifungua kinywa rasmi, anakuwa na mkewe. Tunda atakaa naye
hapo wakati anapata kifungua kinywa na yeye anakula kwa mara ya kwanza. Anarudi
kulala, akiamka kwenye saa nne tena, lazima anywe uji.
Kasoro
siku za jumamosi ambapo Net huwa hapati kifungua kinywa kikubwa. Akinywa tu smoothie
baada ya mazoezi, basi. Anakwenda kazini, na kurudi nyumbani mchana kwa ajili
ya mlo mkubwa. Jumamosi alifanya kazi nusu siku.
Mara
nyingi vitu wanavyokula asubuhi huwa havibadiliki sana. Ni kama Gino
alishawajulia kila mmoja anachokula mida ya asubuhi na jioni alikuwa na ratiba
ya nini kipikwe kwa wote. Kwa hiyo ilikuwa ukifika mezani, Gino anatoka jikoni nakuja
kukuhudumia kwa kile unachohitaji.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati
anakaa ili ale, Ms Emily akamsogelea pale mezani. “Ms Cote yupo kwenye chumba
chakusomea. Amesema ukiwa tayari umfuate huko.” Tunda akaangalia saa, akajua
kwa muda ule atakuwa alishaamka na kupata kifungua kinywa na Maya alishaondoka
kwenda kazini.
“Asante.
Wewe umeshakula?” Tunda akamuuliza Ms Emily kabla hajaondoka. Akababaika kidogo
na tabasamu la kinyenyekevu usoni. Kwa kuwa haikuwa kwenye ratiba kuwa
anatakiwa kula akiwa pale kazini na wala hakuna mtu wakuwauliza wafanyakazi
kama wamekula.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ulikuwa
utaratibu mgeni kwao ambao Tunda alianzisha. Akibaki nao pale nyumbani mara baada
ya Gino naye kuondoka asubuhi akiwa ameshamtayarishia na yeye chakula chake,
Tunda alitaka na wao wale. Tena wale sio kwa kujificha. Wawe huru, wachukue
muda wa mapumziko wa kula. Wote wawili, Ms Emily na Carter.
Tena
wakati mwingine aliwashangaza alipokuwa akiwaita wale pamoja mezani au
kuwafuata kula nao jikoni huku akiwaongelesha hili na lile.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Kaa
ule kwanza. Mimi nitakunywa tu uji. Hivyo vitu vingine alivyoandaa Gino ni
vingi sana. Jipakulie ule, umwambie na Carter atafute muda apate kifungua
kinywa. Mimi nitamfuata Nana hukohuko alipo.” Ms Emily akatoa tabasamu la
shukurani. “Asante Tunda.” Tunda akacheka.
Alijua
tu atakuwa hajala sababu bibi Cote siku hiyo alikuwepo nyumbani. Alishawajua
wanamuogopa sana, na wanaongeza nidhamu wakiwepo wao. Lakini yeye alitaka
kuondoa huo mpaka kati yao. Tunda akajinyanyua pale na tumbo lake na kikombe
kikubwa cha uji mkonono, akaelekea alipoambiwa bibi Cote yupo. Alimuacha Ms.
Emily akila.
Yeye
hakuwa akifuata sheria kama wao. Kila kitu kufanyika sehemu sahihi kwa wakati
sahihi. Akaendelea kujivuta huku akinywa uji wake taratibu. Akijua wazi
alitakiwa kulia chakula mezani, hata huo uji asiingie nao chumba cha kusomea.
Tunda hakujali.
Alimkuta
yule bibi akisoma kitabu. “Unasoma nini?” Tunda akamuuliza wakati anaingia.
Bibi Cote akacheka kidogo na kukigeuza kile kitabu. “Morning devotional.”
Akajibu kisha akavua miwani na kumtizama. “Mbona unakikombe cha uji mkononi?”
“Nimeambiwa uko huku. Nikaona nije kukaa na wewe. Sitaki kukaa peke yangu.”
Yule bibi akacheka kidogo.
“Lakini
wewe ni mkimya sana Tunda!” “Sio sana. Hivi unavyoniona, ndivyo baba yangu
alivyo. Halafu pia nilikuwa, nikiwa sijazungukwa na watu au mtu ambaye alikuwa
karibu yangu. Nilikuzwa kwenye mazingira ambayo hayakuwa rafiki kabisa.
Kunyamaza ndio ilikuwa afadhali yangu. Nafikiri ndio sababu. Net ndiye mtu wa
kwanza kukaa chini na kutoa muda wake na kuweza kunisikiliza. Nafikiri ndiye
binadamu pekee anayenifahami zaidi kuliko hata wazazi wangu au mtu mwingine
yeyote. Kwa hiyo ndio maana nipo hivi. Endelea tu kosoma. Mimi sitakusumbua.
Nilitaka tu kukaa sehemu ambayo kuna mtu.” “Nilishamaliza. Nilikuwa natafakari
tu.” Tunda akakaa.
“Unajisikiaje?”
“Vizuri. Naona sasa hivi ndio nafurahia zaidi ujauzito wangu. Sijui daktari
alinipa nini! Sina kichefu chefu tena! Sijatapika muda mrefu!” “Afadhali.”
Tunda akanywa tena uji wake.
Kisha
akamuuliza. “Maya alishaondoka? Leo hajapita chumbani kwetu.” “Mapema sana.
Yeye ndio ameniamsha. Alikuja kuvalia chumbani kwangu.” Tunda akaanza kucheka. “Maya!
Ni waina yake! Lakini katika yote, huwa namshukuru Mungu kutupa Maya.
Ananipenda sana na hataki nimtizame kama amekuwa. Anataka abaki vilevile Maya
mtoto!” Akaongeza bibi Cote, wakacheka.
“Ila
ana upendo sana!” Akamuona bibi Cote anacheka. “Nini?” Tunda akamuuliza baada
ya kumuona amecheka. “Akupende yeye. Asipokupenda Maya, hutatamani kukaa sehemu
alipo. Wewe utakuja kumuona akikutana na watu asio wapenda yeye. Hutaamini kama
ni Maya huyu.” Tunda akacheka kama anayefikiria.
“Kama
Vic?” Tunda akatupa swali. Akamuona bibi Cote ameshtuka kidogo. Kisha
akajibaraguza. Hamu yakupata habari za Vic ikamjia akajiweka sawa akimtizama
ili ampe kwa ufupi habari za Vic.
Ikabidi
bibi Cote acheke na kuona amzungumzie tu Vic. “Ukitaka kumuudhi Maya. Au
kumbadilisha mudi yake, mtaje Vic, au mlete Vic humu ndani. Anakuwa kama
anapatwa na wazimu.” “Kwa nini? Walishawahi kuwa marafiki?” Tunda akauliza tena.
“Kwa
kiasi fulani japo hawakuwa karibu sana. Ila mambo ya Maya yalipobadilika.
Alipoanza tabia zake mbaya, anaamini Vic ndiye anayemsambazia habari mbaya kwa
watu ili kila mtu amuone sio binti wa kuaminika.” Tunda akakunja uso kidogo.
“Kwani
wanalingana? Au kwa nini Vic afanye hivyo?” Tunda akauliza tena taratibu. Bibi
cote akafikiria na kucheka kidogo. “Haya ninayokwambia, hujasikia kutoka
kwangu.” Tunda akacheka. “Sawa.” Tunda akakubali ili apate umbea wa uzunguni.
“Vic
ni umri wa Net. Na yeye ni mjukuu wa familia moja ambayo walikuwa marafiki zetu
sana. Lakini wao wazee wao, yaani bibi na babu ambao ndio walikuwa rafiki zetu
wa karibu sana, walishafariki. Bibi yake Vic, alikuwa best friend wangu wa muda
mrefu sana.” Akaendelea. “Vic ni mtoto wa pekee, anaishi na wazazi wake, ambao
nao walizaliwa sisi tukiwaona. Ni kama watoto wetu. Vic na Net walikuwa pamoja.
Kadiri walivyokuwa wakikua, Vic alitambulika kama mpenzi au mwanamke
atakayeolewa na Net.” Kiroho kikaanza kumdunda Tunda.
“Wakaendelea
hivyo wakisoma na kufanya kila kitu pamoja. Lakini wakaanza kutofautiana. Vic
akageuka kuwa ‘DIVA’.” Bibi Cote aliongea hapo kwa kejeli kidogo akinyanyua na
vidole viwili juu aliposema Diva.
“Ukweli
ni binti mzuri sana. Na yeye anajua hilo. Kutokana na uwezo wa nyumbani kwao,
hata makuzi aliyolelewa, ni kama mtoto wa mfamle. Ikawa tofauti kwa Net. Babu
yake Net alimkuza Net katika kutumika, sio kutumikiwa.” Yule bibi akatulia. “Wakaanza
kujiona tofauti, japo Vic anampenda sana Net. Nikisema sana, yupo kama mwehu
kwa Net. Anampenda kupita nitakavyokueleza hapa, ukaelewa. Asikuhisi wala
kukuona unamtizama Net kwa vile asivyopenda yeye, atakufuata tu na kukuonya
ukae mbali na Net. Linapofika swala la Net, anakuwa kama amechanganyikiwa na
hawezi kujisaidia.” Tunda akatulia tu akisikiliza.
“Wakaendelea
hivyo mpaka wakamaliza high school. Vic akijitangazia yeye ndio atakuwa mke wa
Net, wakati huku nyumbani Net alikuwa akisema, haoni maisha kati yake na Vic.
Ni watu wawili tofauti. Papa yake Net akamwambia nilazima amwambie Vic ili
ajue. Vic anajua kuganda! Kupita kiasi. Swala au jambo la kuwa mbali na Net,
halipo kwenye msamiati wake. Hajui kulielewa wala kulikubali.”
“Kingine,
anapenda kutawala kila mtu na kila kitu. Sasa akakutana na Maya. Na yeye Maya
kadiri alivyokuwa anakua anataka ajaliwe na kila mtu na atambuliwe na kila mtu.
Yakaanza mashindano kati ya Vic na Maya. Maya akisema anataka muda na kaka
yake, basi Vic asiingilie. Muda wa Net ambao anakua hana kazi ni siku za
jumamosi jioni na jumapili. Ndio muda huohuo Maya anapanga na kaka yake mipango
yao yakuwa pamoja. Na Vic naye anataka aonekane na Net mtaani.” Tunda akamuona
anacheka na kutingisha kichwa.
“Nini?”
“Ilikuwa fujo hapa! Wakianza kugombana, mpaka Papa yao aingilie kati. Maya
anamsemea Vic hili na Vic naye anamsemea Maya hili. Hapo Net amekaa
anawasikiliza. Wote wamekutana ni wazuri. Wanakosoana sasa kwa hili na lile.
Haya, Vic anaondoka. Mshindi Maya. Mnapumzika kidogo. Mara linaibuka jingine.
Maya anakuja kulalamika labda alikuwa sehemu, gari yake ameegesha nje, ametoka
amekuta imewekwa pancha, akashindwa kuondoka, Vic amemfanyia kivyo. Akiulizwa
kwa nini anahisi ni Vic, basi atasema Vic alipita hilo eneo itakuwa ni yeye
tu.”
“Haya
mara mko tu hapa nyumbani mnamuona Vic anakuja akilia, labda gari yake
imevunjwa kioo makusudi au imechanwa tairi na Maya. Na ni zile gari za pesa
nyingi sana. Kitu kidogo tu kwenye hiyo gari ni gharama kweli! Haya, ukimtafuta
Maya, unamkuta huko nyuma anaogelea. Ukimuuliza Vic, anakwambia Maya ni muongo,
alipoharibu gari yake ndipo akakimbilia nyumbani. Ikawa fujo hapa, visasi
haviishi.” Bibi Cote akakumbuka kitu kingine akacheka sana.
Tunda
naye akacheka. “Siku nyingine tena.” Yule bibi akazidi kucheka. “Ooh my goodness,
Maya! She is something else!” “Alifanya nini tena?” Yule bibi alicheka.
Akacheka tena.
“Kuna
sehemu Vic alikuwa akipenda sana akifika hapa, anakaa hapo halafu anaanza
kutuma wafanyakazi wa humu ndani wamtumikie kwa hili na lile.” “Subiri kwanza
Nana, kwani yeye huwa anakuja hapa wakati wowote!?” Tunda akauliza.
“Nakwambia
amekua sisi tukimuona. Hapa nyumbani ni kama kwao tu. Amekua pamoja na Net
tokea hawajaanza shule. Walikuwa wanne. Na wale vijana wawili waliokuja
Tanzania. Humu ndani wanaingia mchana na usiku. Walikuwa wakisomea humu ndani
na wazazi walipapenda hapa sababu ya maadili ya Net. Na vile babu yake
alivyoweza kumudu kumtawala Net na Net kufuata kila kitu anachoambiwa. Ile
iliwavutia wazazi wengi sana.”
“Kwa
hiyo mtoto yeyote akijulikana yupo kwa Cote, kukawa hamna shida. Na hapa kukawa
na mafunzo mengi. Kwa hiyo kila wakija, walikuwa wakijifunza na Net. Walikuwa
wakifundishwa lugha mbali mbali, michezo, kutumia vifaa vya mziki. Kwa hiyo
hapa ikawa sehemu wanayopenda kuja mpaka leo. Sema kumetulia sababu tuliwaambia
upo na unahitaji utulivu. Wakuache kwanza mpaka tutakapowaalika tena rasmi.”
Tunda akajisikia vizuri.
“Asante
Nana. Kweli nilihitaji kupumzika. Nashukuru kujali.” Nana akacheka kidogo. “Karibu.
Sasa turudi kwa Maya na Vic.” “Ehe!” “Siku hiyo akamsikia Carter anazungumza
naye getini akitaka afunguliwe get ili aingie. Maya akakimbilia kwenye kile
kama kibembea pale ukiingia mlango mkubwa, kuelekea sebuleni. Akalegeza nuts
mbili kwa haraka. Sasa Vic alipokuja akampita Carter mlangoni bila salamu wala
heshima kama kawaida yake Vic. Na yeye Carter alimuona Maya akiharibu ile
bembea lakini hakumwambia Vic makusudi. Akajua kitakachompata.” Tunda akaanza
kucheka na yeye kama mazuri.
“Sasa
si Vic alimpita pale mlangoni bila salamu wala heshima, na yeye Carter
akanyamaza kimya. Kama kawaida yake Vic, akamwita Ms. Emily amletee juisi ya
nanasi. Ndio juisi anayopenda sana kila akija humu ndani. Gino huwa
anachanganya na vitu vingine, inakuwa nzuri sana, hutawahi kunywa popote aina
ile ya juisi anayotengeneza Gino. Na hajawahi kumwambia mtu huwa anatengeneza
vipi. Ni siri yake.”
“Hata
mimi huwa naipenda.” “Basi, ile utaipata humu ndani tu. Sasa kila alipokuwa
akiingia humu ndani Vic, anamwita Emily amletee glasi moja, kabla hata hajakaa
akiwa anamsubiria Net, waende kule nyuma wakacheze tenesi. Emily aliposikia
jina lake likiitwa na Vic, bila kupoteza muda, akammiminia glasi ya juisi.
Akampelekea.” Yule bibi akacheka tena na tena.
“Sasa
alipoletewa juisi, ile anakaa chini kwenye lile bembea huku amemtuma Carter
akamwite Net, si akaanguka! Wakaanza kucheka kwa pamoja. Carter, Maya na
Emily.” “Jamani! Sasa kwa nini Carter
asimwambie.” “Wakati na wao shida yao ni aanguke!” Wote wakacheka.
“Carter
anampenda sana Maya. Sana. Na hamkosei sababu yakumtetea. Anamtetea kwa kila
kitu. Basi, ile juisi si unajua inakuwa kama nyekundu hivi?” “Nahisi Gino
anachanganya na Berries.” “Hata sisi tunahisi hivyo hivyo. Sasa Net anasogea
pale, na Vic ndio anaanguka, miguu juu, glasi kushoto. Jamani Vic alilia!”
“Maya
acha aanze kucheka! Halafu kumbe alikuwa anamchukua video. Akamtumia hapohapo
video yake huku mwenzie akilia. Sasa Net anashangaa Vic analia, halafu Carter,
Emily na Maya wanacheka sana. Kumbe wote walijua mtego anaotegewa Vic.” “Sasa
nyinyi mlikuwa wapi?” Tunda akauliza.
“Chumbani!
Ndio tulikuwa tumetoka kazini. Wote. Kasoro Maya ndio alikuwa hapa. Ndio
ilikuwa siku yao, Net na Vic yakucheza tenesi. Ndio alikuwa amekuja wakacheze.
Vic akamuonyesha ile video Net, huku akilia kuwa Maya amemfanyia makusudi.”
“Maya
alipoona hivyo, akakimbilia chumbani kwetu. Mgongoni kwa Papa. Net akaingia
amekasirika. Ndio akaelezea vile alivyoambiwa na Vic. Maya akasema Vic
nimuongo, yeye alikuwa anajichukua video, akaacha simu yake kwenye meza ya
karibu na lile bembea, bila kuzima kamera. Kwa hiyo ndio ikachukua lile tukio
la kuanguka kwa Vic. Kama hatumwamini, aitwe Carter.” Tunda alikuwa akicheka
sana.
“Sasa
Carter alivokuja?” Tunda akauliza huku akicheka. “Carter kuja, akasema lile
bembea lilikuwa na matatizo. Ameshapigia simu fundi waje walitengeneze.
Akaulizwa kwa nini hakumwambia Vic, akasema Vic aliingia na maagizo ya haraka.
Akimtaka yeye Carter akamwite Net kwa haraka, na Emily akalete juisi haraka.
Sababu ya haraka, akasahau kumwambia. Hapo Maya akawa amepona. Ameshikilia
kiuno cha Papa, hataki hata babu yake asogee hatua moja. Anaongea na Net huku
amejificha nyuma ya babu yake.” Tunda alicheka mpaka machozi.
“Maya!”
“Ila wewe alikupenda tokea siku ya kwanza anakuona. Hakuacha kukusifia. Na
kukupenda kukaongezeka pale mama yao alipoonyesha hakupendi.” “Kwa nini tena!?”
“Ili tu kumkera mama yake zaidi. Ukitaka kumsikia anakuwa mkali Maya kwa mama
yake, basi awe kinyume na maamuzi ya Net kuwa na wewe. Hapo anakuwa mkali bila
woga. Sasa turudi kwa Maya na Vic.” “Ehe!” Tunda akataka waendelee.
“Mimi
ni kiongozi wa foundation moja hivi ya wanawake tuliianzisha hapa nchini. Sasa
lazima kuwe na mrithi wangu. Iwe mtoto wa kike au mkwe. Sasa Vic akatangaza kuwa Maya hawezi kuchukua
hicho cheo, au kukalia kiti changu. Kwa sababu kile kiti kinakaliwa na wanawake
smart, kama yeye mke wa Net, sio Maya.” “Kwa nini isiwe mama Cote? Yaani mama
yao kina Maya?” Yule bibi akafikiria kidogo.
“Nitakwambia
habari za Ritha. Ila kwa kifupi tu, ni kama Ritha alitoka mapema sana kwenye
picha, alipotaka kurudi baada ya kujua alichokimbia ni kitu kikubwa sana,
amejipunja, nilikuwa nimeshamfungia milango yote. Nikahakikisha namwachia
mlango mmoja tu wakurudi kwetu, watoto wake. Lakini napo..” Akasita kidogo.
“Anyway,
tuendelee kwa Maya na Vic kwanza. Vic akawa anatafuta makosa na udhaifu wowote
ule wa Maya, na kutangaza hadharani ili watu wajue kuwa Maya hawezi kuja
kukalia kiti changu. Au kama kushawishi uma kuwa Maya hana uwezo wa kubeba
madaraka ya kile kiti. Akawa anamfuatilia sana Maya. Maya alipoangukia kwenye
madawa ya kulevya, ndipo Vic akapata jukwaa. Kila siku ni habari za Maya
mitandaoni. Maya hajui anazipataje. Anahisi pia baadhi ya wanaume alikuwa
akiwalipa yeye ili wampe madawa. Akishalewa, basi wamfanyie uchafu, wachukue
video.” “Haiwezekani!” Tunda akashtuka sana.
“Sijui
Tunda! Ila jinsi Maya anavyonieleza, anasema alipoamua kubadilika, wakati
anamaliza chuo, huyo kijana akaanza kumfuatilia. Anasema akivuta kumbukumbu ni
kama nikijana ambaye alishakuwa na taarifa zake. Anajua ni nini anataka na kwa
wakati gani. Na akawa yeye ndio anamuhudumia Maya. Haihitaji pesa ya Maya kama
wanaume wengine. Ndio maana ilituchukua muda mrefu kuja kugundua kama Maya
amerudia madawa. Maana alikuwa akienda kumfungia huko, anampa madawa tu na
kumfanyia mambo mabaya bila Maya mwenyewe kujua. Sasa kwa mtu kama Maya ambaye
alishakuwa mtumiaji, haitaji nguvu nyingi kumrudisha nyuma.” Tunda aliumia
sana.
“Kwa
sababu ni kweli Maya alitulia sana. Akabadilika. Kwa hiyo yule mwanaume akamjia
na nia yakumuoa kabisa. Akawa anamuonyesha vile ambavyo watakuwa na maisha
mazuri. Watoto wao. Na watakavyoendesha maisha yao bila shida kwa kuwa na yeye
anao uwezo.” “Jamani! Kwani nyinyi hamkumuona huyo kijana?” Tunda akauliza kwa
uchungu.
“Tulimfahamu.
Alimleta mpaka hapa kwa babu yake. Tena babu yake alikuwa ameshaanza kuumwa.
Lakini kwa ajili yake, alitoka siku hiyo chumbani, tukapata naye chakula cha
jioni na huyo kijana. Ukweli alionekana ni kijana aliyetulia. Anaongea mambo
sahihi kama aliyejifunza ni kitu gani tunataka kusikia kutoka kwake. Na
ukumbuke hapo Maya alikuwa ndio ametulia. Anamalizia chuo, aanze kazi. Kila mtu
alijua Maya amebadilika, amekuwa binti mkubwa sasa na yeye alishahojiwa kwenye
vyombo vya habari, akakiri ulikuwa ni utoto, na marafiki wabaya ndio
walimuingiza kwenye madawa ya kulevya. Ameamua sasa kutulia. Kwa hiyo moja kwa
moja, yeye ndio angekuja kuchukua cheo changu au angekalia kiti changu.” Tunda
akaumia sana.
“Kwani
Nana, hicho kiti chako kina faida gani?” Ikabidi tu Tunda aulize. “Oooh honey! Usitake
nianze kutaja.” Yule bibi akakaa sawa. “Kwanza ujue ni foundation yenye
mamilioni ya pesa. Kuwa president, au raisi wa hiyo foundation, ni unajulikana
na watu wakubwa wa nchi nzima. Nianzie tu hapa Canada. Inamaana hakuna mlango
unaotaka ufunguliwe, usifunguliwe. Si unakumbuka Viza yako?” Akamuuliza Tunda.
“Nakumbuka!
Mimi mpaka nikashangaa!” “Basi, ndio nguvu ya hicho kiti na jina la Cote, of course!”
Wakacheka maana yule bibi aliongea kwa kujivuna kidogo wakati anasema Cote. “Basi
ndio hivyo. Kina nguvu kubwa sana na kinajulikana, kwa kuwa tunagusa maisha ya
mtoto wa kike moja kwa moja au mwanamke kwa jumla. Tunasaidia wale watoto wanao
bakwa majumbani. Waliopitia kwenye biashara za kulazimshwa kwenye ukahaba.
Nikisema kusaidia, naamisha kuanzia kuwatoa kwenye hayo mazingira, kusomesha,
na kuhakikisha wanakuwa na ujuzi wa kujitegemea wao wenyewe.”
“Haya,
kwa upande wa wanawake, tunawafikia wajane walioachwa kwenye mazingira magumu.
Wanawake walioachika na kubaki bila msaada. Sisi ndio tunawasaidia kuwapa kila
aina ya msaada unaohitajika kwa wakati huo. Iwe msaada wa matibabu, kisheria,
chakula mpaka malazi. Na tukikupitisha kuwa unahitaji msaada wetu, inamaana
maisha yako hayatakuwa kama yalivyokuwa. Tutahakikisha unasimama kwa miguu
yako, tena unasimama vizuri. Hatuanzi jambo na kuliacha katikati. Labda mlengwa
mwenyewe ashindwe. Hapo hatuna jinsi.” Hapo Tunda akawa amefunguliwa macho.
Akakumbuka maneno ya Ritha.
“Sasa
taasisi kama hiyo, kila mtu anataka kuwekeza. Wanasiasa wanapotaka kuingia
madarakani, basi wataweka pesa zao hapo. Kuonyesha jamii kuwa anajali wanawake.
Makanisa pia wanawekeza kwenye hiyo taasisi yetu pia. Matajiri wenye nia nzuri
na wanaotaka kujitangaza kwa jamii, pia wanaweka pesa zao hapo.”
“Bado
mimi mwenyewe huwa kila mwaka nafanya tafrija yakuchangisha pesa. Hapo napo
huwa makampuni mengi huwa wanachangia sana.” “Nani mwanzilishi? Najua mpo na
wenzio. Lakini lilikuwa wazo la nani?”
Akauliza Tunda.
“Nilianzisha
mimi baada ya Mungu kutufungulia milango ya pesa, mimi na mume wangu. Cote
aliamua kuniunga mkono kwa kuwa ni kitu nilimwambia lazima nije nikifanye Mungu
akija kunifanikisha. Tulinunua eneo kubwa sana. Hapa ni padogo. Tukaanza
kujenga. Mimi na Cote tu. Mwanzoni hakutaka kuomba msaada. Akasema lazima
kisimame kwanza, ili watu wote wajue na kuelewa kama ni kitu changu, na watoto
wangu ili wasije kunibadilikia baadaye.” Akamuona ametulia. Akaina kama
anayefikiria.
“Cote
alinipenda, kuliko nitakavyokwambia. Alifanya chochote kwa ajili yangu na
kunipa chochote ninachotaka. Mpaka nilikuwa nikiogopa kulalamika mbele yake. Alikuwa
akinisikia tu naongelea kitu kuwa nakipenda, ujue kama sio siku hiyohiyo basi
ujue baada ya muda mfupi sana, kitakuwa changu. Atafanya kazi mchana na usiku
kuhakikisha nakipata hicho kitu mpaka nilikuwa namuhurumia. Tena tokea tupo
watoto.” “Pole Nana.” Tunda akamuhurumia.
“Asante.
Lakini nitammisi sana Cote! Sana. Tulianzana nikiwa mdogo mno. Yeye ndio alikuwa
kimbilio langu. Kila nilipokuwa na uchungu, nilikuwa nakimbilia nyumbani kwao,
hata kama anakuwa anafanya kazi na baba yake, anaacha ananichukua, atanipeleka
mahali, atakaa na mimi mpaka natulia.”
“Na
kwa kuwa baba yake alitaka awe kama hivi Net, alikuwa akimfundisha sana kazi.
Wakati wote ungemkuta Cote yupo nyumbani kwao na kazi. Basi akawa akiniita
nifanye nao kazi. Ili tu niwe naye karibu. Na ndivyo ilivyokuwa mpaka yule mzee
akaja akafariki, na Cote naye. Lakini tulifanya kazi sisi watatu kwa miaka
mingi sana.” “Na mama yake?” Tunda akauliza.
“Mama yake alifariki
wakati Cote yupo na miaka 12. Na yule mzee hakuja kuoa tena! Hata tulipokuja kufanikiwa
sana na yeye alibaki hivyo hivyo. Alishindwa kupata mwanamke anayefanana na
mama yake Cote. Tukawa tukiishi hapa watatu tu mpaka tukampata CJ, baba yake
Net.”
“Anyways,
hiyo ni habari ya wakati mwingine. Sasa baada ya kusajili hiyo taasisi na
kuandika katiba mpya ndipo sasa tukaanza kuitangaza. Hapo nilikuwa tayari
nimeshaanza kusaidia baadhi ya mabinti waliokuwa wamefungiwa mahali, wakitumiwa
na watu kwa biashara ya ngono. Wao hawanufaiki kwa chochote, ila hao watu
waliokuwa wakiwaingiza nchini kwa siri. Tena walikuwa mabinti wakutokea nchi
mbali mbali ulimwenguni zaidi Mexico.”
“Sasa
kile kitendo cha mimi kutetea binti wakutoka nchi mbali mbali ulimwenguni tena
wageni kabisa hapa nchini, waliokuwa wakija kutafuta maisha na kuangukia kwenye
hiyo mikono ya hao watu wabaya, waliokuwa wakiwaingiza kwenye biashara haramu
ya ngono! Ilivuma kwa haraka sana na hiyo taasisi kujulikana.”
“Maana
walikuwa wakifanya hivi. Ili kuwafunga na kuwamiliki hao wasichana wadogo,
waliohakikisha ni warembo sana, wanaokuwa wanawaingiza hapa nchini kwa siri au
kuwatafuta kwa kuzingatia umri na urembo, wakishajithibitishia labda sio wazawa
wa hapa nchini au binti ambaye hana familia ya kueleweka ili asije kutafutwa na
kuishia kuwaharibia biashara yao. Wanahakikisha ni binti walio na shida ya maisha
au wamekuja hapa nchini kutafuta.”
“Basi,
wakishampata binti wa namna hiyo, mwenye hivyo vigezo, cha kwanza kabisa, kumpa
madawa ya kulevya.” “Nana!” Tunda akashangaa kwa kuumia. “Ni wajanja sana. Mmoja
wa hao mabinti ambaye alikuwa kama kiongozi wao, alisema kila binti ambaye
alikuwa akiingia kwenye hiyo nyumba ambayo wanawapa hifadhi wote, siku ya
kwanza kabisa wakiwaingiza hao mabinti kwenye hiyo nyumba yao, wanawachoma
sindano ambayo inaanza kuwapa kiu ya madawa. Na wanafanya hivyo makusudi.”
“Kisha
wanamuacha huyo binti anateseka kama siku mbili hivi, halafu wanampa madawa ya
kulevya sasa. Anajisikia vizuri siku ya kwanza na ya pili. Kisha wanamnyima
tena. Ujue hapo wameshafanikiwa kumfanya mtumwa wao kwa madawa.” “Jamani!”
Tunda akahuzunika.
“Ukumbuke
huyu binti hapo alipo hana pakwenda. Wamempa malazi kwenye nyumba yao.
Wakishajiridhisha kuwa hawezi kuishi tena bila madawa, ndipo wanamwingiza
kazini sasa. Wanampa mavazi yathamani sana ambayo anavaa wakati wanaenda kumuuza
usiku huo ili watengeneze pesa nyingi. Huku wakiwatisha nakuwaambia wasipoenda
kutumika huko vizuri na mteja akawasifia, hawatawapa madawa ya siku hiyo.”
“Jamani!” Tunda akazidi kuumia. Angalau yeye alitumiwa na pesa iliingia kwake.
Hakuna aliyemlazimisha. Alijua ugumu wa hiyo biashara. Akaumia zaidi.
“Basi,
ikawa ikiwalazimu kwenda kutumika, wanarudi kufungiwa kwa malipo ya madawa ya
kulevya. Wakiwapatia wateja, wanawavalisha vizuri, nakuwapeleka kama ni kwenye
mahoteli makubwa, au kwenye masherehe ya vijana, au majumba ya watu. Wanatumiwa
huko kutokana na malipo ya hao watu, kisha wanarudishwa tena ndani wao ndio
wanalipwa.”
“Sasa
mimi niliposikia, nikafanyia uchunguzi, nikaenda kuvamia hiyo sehemu na polisi.
Tuliwakuta na hali mbaya, halafu wengi wao wapo nchini kinyume cha sheria. Mimi
nikawaambia wale polisi nitawachukua wote kwa kuwa ninayo sehemu ya kuwatunza
na ninao uwezo wa kuwatibu mpaka wapone.”
“Wao
wakataka kuwarudisha kwenye nchi zao. Mimi nikapinga sana. Nikawaambia kwanza
mimi ndio niliwagundua hao mabinti, wakati serikali ilifumbia macho, pili
nikawaambia kibinadamu tu, wale ni watoto wa watu. Walikuja nchini kutafuta
maisha, hawawezi kuwarudisha kwa mama zao wakiwa na hali ile.”
“Nilipambana
kufa na kupona. Na hapo nilikuwa nina jeuri kwa kuwa nilikuwa na sehemu ya
kuwahifadhi na pesa. Nikawaambia serikali waniachie mimi hao mabinti, sihitaji
chochote kutoka kwao. Nikawaambia nitawatibu na kuwarudisha shule. Wakikosea
ndipo wawarudishe. Sasa ikawa ni habari kubwa sana iliyoenea karibu ulimwenguni
kote. Nchi walizotoka wale mabinti wakawa wakiniunga mkono, na nikapata
uungwaji mkono na wanawake wakubwa sana ulimwenguni.”
“Ikageuka
jambo la kisiasa sasa. Chombo cha kupigania haki za binadamu kikaingilia kati.
Na mimi huwa sijui jibu la hapana.” Tunda akacheka. Akakumbuka Maya na Net
walimwambia hivyo. “Waliniambia!” Tunda aliongea huku akicheka. “Hao
waliokwambia wala hawakukosea. Nikitaka jambo langu! Huwa jibu la hapana
haliwezi kukubaliwa akili mwangu. Nitapambana kufa na kupona.” Tunda akacheka
huku akimwangalia.
“Basi,
kwenye hiyo harakati nikiwa nahangaika na hao mabinti, vyombo vya habari
havikuacha kunitafuta nakujua nilipofikia. Na ndipo watu sasa wakaanza kujitokeza
kwenye kutaka kusaidia kwa namna yeyote ile. Wengine pesa, wengine taasisi za vitengo
vya kusaidia watu kutoka kwenye madawa ya kulevya. Wanasheria! Ikawa misaada ya
kila namna inaingia kila kona. Nje na ndani ya nchi ili tu kuniunga mkono.”
“Ndio
mpaka sasa ipo hiyo sehemu. Nimehakikisha panabaki kuwa pazuri. Kuna majengo ya
kisasa. Utakuja kupaona.” Tunda akawa amejibiwa maswali mengi sana. Heshima kwa
huyo bibi ikaongezeka na maswali juu yake kwa hiyo familia yakaongezeka pia.
Akajikuta
amepotelea mawazoni mbele ya huyo bibi, akijumlisha na kuongeza kutokana na
kashfa za Ritha juu yake ya kwa nini ameolewa na kukubaliwa na huyo bibi! Akakumbuka
mengi aliyosema Ritha kwa kumkashifu zaidi siku ya tafrija ya kuchumbiwa kwake
na Net nchini Tanzania na huyo bibi kumtangaza kama ndiye mrithi wake. Hapo yakaanza
kuleta maana. Ukweli ulikuwa mkubwa, japo aliongea akiwa na hasira kwake.
Akangundua
yule bibi alikuwa ametulia tu akimtizama. “Ni majengo ya nini?” Tunda akauliza
na kuficha kile kilichokuwa kikiendelea mawazoni. “Yakuishi watu kwa muda
wakati wanatafuta pakwenda. Unakuta ni mama mjane labda anawatoto, amewajia na
kuwalilia shida. Sasa na matapeli ni wengi. Kabla yakumpa msaada, lazima
kumchunguza. Lakini ukumbuke wakati huo yupo na watoto, hana pakuishi. Lazima
umpe hifadhi yeye na watoto wake. Na mkijiridhisha mkaamua kumsaidia. Huwa
tunapenda wajipatie ujuzi fulani, ili tunapowasaidia kuwapa makazi, baada ya
muda fulani, waweze kujitegemea wenyewe, wasirudi kuwa tegemezi tena.” Tunda
akarudishwa mawazoni. Akakumbuka maisha yake.
“Ni
kitu kizuri na ni pakubwa sana. Tutakuja kwenda siku moja ili ukapaone.
Uangalie mambo jinsi yanavyoendeshwa. Labda utaelewa ni kwa nini Vic
anapataka.” Bibi Cote akamtoa mawazoni, Tunda akacheka na kuinama kama anayefikiria tena. Safari hii
akakumbuka vile Net alivyomwambia watafanya mambo kama hayo. Asimame, ili aje
asaidie wanawake waliopita kwenye maisha kama yake. Akaanza kuunganisha hili na
lile. Akajua labda ndio alikuwa akimtayarisha. Akanyanyua uso, akamtizama yule
bibi. Macho yakagongana. Yule bibi akacheka.
“Nashuku.
Narudia tena, NASHUKU, Vic alitaka kumuharibu Maya makusudi ili ashindwe kuchukua
yale majukumu. Kwa kuwa ndio kipindi nilikuwa nimetangaza nataka kupumzika.
Hapo nilikuwa bado sijamaliza kuomboleza. Nilimuuguza Cote kwa muda mrefu sana.
Lakini bado sikuwa tayari aniache.”
“Kifo
chake kikawa ni kama kifo cha gafla kwangu wakati madaktari walishaniambia muda
uliokuwa umebaki. Niliumia sana. Nikawa nikijua pengine Maya atanisaidia
kuendesha kule. Na yeye akarudia ulevi. Haya, Net naye akawa sio mtu wakuoa.
Kwa Vic ikashindikana, Chloe naye akashindwa. Nilipoona vile, nikaona nikae tu
kwanza mwenyewe.” Tunda akafikiria kidogo. Kisha akaamua kuuliza.
“Vic
alijua kama Net ameanza mahusiano na Chloe?” “Ndiyo. Net alihakikisha anafahamu
ili aliheshimu hilo na aelewe kuwa hatakaa amuoe.” “Vic alilichukuliaje?” Bibi
Cote akafikiria kidogo.
“Nisikilize Tunda. Net
si myumbishwaji. Kitendo cha kukuchagua wewe tu, ujue tayari unao ulinzi mkubwa
sana, ambao cha kwanza, Vic lazima atakuangalia kwa hofu. Net anaheshimika sana
kwenye jamii na anajulikana kwa maamuzi mazuri. Kwa kukuoa tu wewe na sio wao,
tayari wamekuogopa na wanakutizama kwa jicho la tofauti sana.” Tunda akainama.
“Na
mimi nipo hapa. Vic ananiogopa sana kwa kuwa ananijua huwa sipendi ujinga. Kwa
wewe kuishi hapa ndani, kwenye hii nyumba iliyokuwa ndoto ya mabinti wengi, halafu
na mimi nipo hapa, pia hicho kinawaogopesha zaidi. Ndio maana unaona pametulia
kabisa.” “Uliniambia uliwaambia kwamba nipo nahitaji kupumzika. Labda ndio
maana wametulia.” “Wangesumbua sana mitandaoni.” “Mitandaoni!” Tunda akawa hajaelewa.
“Hivi
umemsahau Maya?” Tunda akacheka. “Anakazi ya kukutangaza huko mtandaoni, kama
kuwasuta tu au kuwaumiza roho. Kila mtu atakuwa anawaza lake lakini hawathubutu
kusema sababu umeolewa na Net, na wanajua unaishi hapa. Lazima wanakuogopa
sana. Nilitaka upate nguvu, niandae tafrija fupi ili niwaalike, wakutambue
kabla Cote, hajazaliwa.” Tunda akavuta pumzi kwa nguvu.
“Utakuwa
sawa tu. Usiogope. Umepata mume mzuri sana. Atasimama na wewe katika kila hatua
yamaisha yako. Usigope kabisa. Nenda kajitayarishe tutoke kabla Net hajarudi na
kutukuta hapa.” Tunda akacheka huku akisimama.
Historia ya Ritha.
Wakiwa njiani bibi
Cote akaanza. “Usinielewe vibaya, lakini nataka kukwambia jambo ambalo
hatukuwahi kuwaambia watoto wa Ritha.” Tunda akamgeukia. Walikaa kiti cha nyuma
kwenye gari hiyo safi, nzuri, nyeusi kwa nje, lakini kila kitu ndani kilikuwa
cheupe na kinavutia.
Kwanza ilikuwa Bullet
proof. Hata mtu akipiga risasi, haiingii ndani. Ni gari aina ya ‘Luxury Mercedes
Benz’. Ndio ilikuwa gari ya huyo bibi. Ilitangaza
utajiri mtupu. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Tunda kupanda hiyo gari. Akabaki
akishangaa vile yule dereva alivyobadilisha vitu kadhaa mlangoni na dirishani
mara baada ya wao kupanda na kufunga milango. Bibi Cote alifunguliwa mlango,
ndipo akapanda.
Akaona vioo vya
madirisha ni kama vilipanda na kushuka vingine. Kukarekebishiwa hiki na kile
ndipo dereva ambaye pia ndio mlinzi wa huyo bibi, akaondoa gari. Ndipo hapo
huyo bibi akamtoa kwenye kushangaa. Akajiweka sawa ili kumsikiliza hapo nyuma
walipokuwa wamekaa pamoja.
“Nia yangu, nataka kukwambia mambo ya msingi
ambayo nikija kukuacha, au hata sasa hivi, usiwe na maswali. Na pia nataka ujue
kuwa, kuwa mama Cote, kunakuja na majukumu mengi, na kila uamuzi unaochukua,
chukua ukiwa unawafikiria wajukuu wa huyo Cote hapo tumboni. Iwe ni zaidi ya
hisia zako za wakati huo.” Tunda akashtuka kidogo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mambo ya uzunguni yanazidi kupamba moto, na Tunda
akiona wameweka imani kubwa sana kwake kana kwamba hawamjui hata kwa kusikia
tu! Ritha naye amefanya nini? Usikose muendelezo wa uzunguni...
0 comments: