NILIPOTEA! PART 6 - SEHEMU YA ‘D’.
Bibi Cote akaendelea. “Ritha aliletwa hapa nchini na mume wake, japo anatangazia watu ni baba yake ndiye aliyemletea.” “Mume wake, yaani unamaanisha baba yake Net?” Tunda akauliza akitegemea jibu la ndiyo. “Hapana. Ritha aliolewa akiwa kwao. Akaletwa hapa nchini na mume wake aliyekuwa mwanafunzi.” Tunda akashangaa mpaka akageuka kabisa.
“Sasa
aina ya Visa ambayo alikuwa amepewa mume wake, ilikuwa huwezi kubadilisha. Kwa
kuwa mumewe aliletwa na serekali ya Tanzania. Aje achukue ujuzi fulani, kisha
arudi kwao akatumikie serikali yake. Kwa hiyo palikuwa hakuna jinsi
yakubadilisha aina hiyo ya Viza ili kuwawezesha kuishi hapa, ila kurudi nchini
kwao, wakabadilishie Viza hiyo huko ndipo kama wanataka kurudi, warudi na ndipo
wangeweza kufanya kazi huku.”
“Waliishi
hapa kwa muda wa miaka 3. Wakitafuta jinsi yakuishi hapa moja kwa moja. Lakini
wakashindwa kabisa. Ninavyosikia, japo Ritha alikataa kukiri, Ritha akamshauri
mumewe waachane. Ili Ritha atafute mwanaume ambaye ni raia wa hapa, aolewe.
Akishatengeneza mazingira mazuri. Akafanikiwa kuwa raia, amwache huyo raia
kisha arudi kwa mumewe.” Tunda akashangaa sana.
“Basi.
Wakaachana kisheria kabisa. Kwa kuwa tayari Ritha alikua ameingia kwenye system
za hapa kama mke wa huyo jamaa. Kwa hiyo wakapeana talaka kabisa kwa
mwanasheria.” Yule bibi akatulia kidogo.
Kisha
akaendelea. “Ndio katika mawindo yake, nafikiri ndipo akampata CJ. Mtoto wangu
wapekee! Bila kujua, CJ akiwa amempenda sana Ritha akatangaza ndoa kwa haraka.
Nashuku na ujanja/mipango ya Ritha pia ilichangia kumfanya CJ atangaze ndoa kwa
haraka. Baba yake akamsihi sana Junior, apate muda wakumchunguza Ritha, lakini
yeye akafikiri sisi hatumpendi Ritha sababu ni mweusi. Baba yake akaona
tusimpoteze kwa mwanamke mgeni. Ikaandaliwa harusi. Sasa tukamuuliza CJ, mbona
ndugu zake Ritha hawaji? Ni kama akasema Ritha ni mtoto yatima au alikuwa na
matatizo ya kifamilia. Ndugu ni kama walimtelekeza. Sababu zinazofana na hizo.
Basi. Ikafungwa harusi, wakaenda mapumzikoni, akarudi na ujauzito wa Net.
Hapakuwa na shida.”
“Mwaka
huo ukaisha wakiwa na mtoto mmoja. Net. Net alipofikisha miaka 3 tukaanza
kupata fununu kuwa mume wa Ritha alifika polisi, akidai mke wake. Cote
akashtuka sana. Yeye mwenyewe ikabidi kwenda polisi kufuatilia.” Tunda akabaki
akishangaa.
“Hapakuwa
na mashitaka yeyote yaliyoandikishwa. Tukanyamaza kwa muda. Lakini kile kitu
kikawa kinamsumbua sana Cote. Siku moja wakati tupo mezani tunakula, Cote
akamuuliza Ritha swali la moja kwa moja kama alishawahi kuolewa. Ritha hakutoa
jibu la moja kwa moja. Akatuzungusha kwa majibu yenye hekima. Ritha anaakili
sana. Anaakili ya kufikiria kwa haraka
na anajua kutunga hoja. Basi. Hiyo siku ikaisha.”
“Baada
ya miezi miwili akaaga anakwenda kusalimia wazazi Tanzania. Kila mtu
akashangaa, mpaka mumewe. Kwa nini imekuwa ghafla wakati ni kama alisema hana
ndugu au niyatima? Hapo napo akatoa majibu ambayo yakamfanya aruhusiwe. Junior
alipotaka waongozane na mtoto, akaweka kipingamizi kabisa. Akasema aende yeye,
akaandae mazingira, kisha safari nyingine waongozane.”
“Hapo
alikuwa ameshamaliza shahada yake ya kwanza. Uzuri alikuwa na akili nzuri za
darasani na alijua kutumia fulsa vizuri. Alipoolewa tu, akanza shule. Na tumbo
lake, alikuwa akienda shule. Huyo Net ni kama nilimlea mimi mwenyewe tokea
anazaliwa. Mama yake hakutaka kusubiri. Kwa hiyo alikuwa anamwacha Net tokea
mchanga kabisa. Anaacha na maziwa. Basi mimi na wafanyakazi ndio tukamkuza huyo
Net. Yeye anaondoka asubuhi kurudi ni jioni.”
“Basi.
Baada ya kama mwezi, akarudi nyumbani na mpango wakusoma shahada ya pili.
Hatujakaa sawa, akarudi shule. Pesa ipo na usafiri upo, hakukuwa na shida.
Lakini safari hii akatafuta na kazi kitu kilicho tushangaza! Kazi ya nini
wakati hapa pana pesa? Nikajaribu kumsihi ili atulie, iwe ni shule na mtoto.
Akasema kwao kuna matatizo, anataka kusaidia. Nikazungumza na Cote, tukaanza
kumlipa. Pesa yake binafsi ambayo haihusiani na mumewe, wala haulizwi maswali.”
“Basi,
maisha yakaendelea. Yupo busy na maisha yake na sisi tukimsaidia kumlea Net.
Tukaja kusikia baadaye kuwa alikuja kumrudisha yule mume wake wa kwanza kutoka
Tanzania. Akampangia sehemu yakuishi.” “Nana!” Tunda akshtuka sana. Kweli.
Subiri usikie yote.” Tunda akakaa sawa akajua mambo ni mazito. “Basi, Net
alipofikisha miaka 5, kwenye hekaheka hiyo ya shule ya mama yake na ratiba
zake, Ritha akashika mimba ya Maya. Lakini akalalamika sana kuwa kwa wakati ule
hakuwa tayari kuwa na mtoto, sababu masomo ni magumu na lazima amalize.
Alipoonyesha nia yakutaka kutoa mtoto, CJ akamsihi sana asitoe mtoto wake.
Akamwambia amzalie tu huyo mtoto, yeye atalea mwenyewe.” “Nana!” Tunda akazidi
kushangaa.
“Usimuone
Ritha vile. Anamsimamo, na hana aibu wala hofu kwa yeyote. Zikaanza fujo,
kulalamika juu ya hiyo mimba. Mara alalamikie hiki au kile. Ilimradi tu hataki
huyo mtoto. Mwishoe CJ akamwambia akimtoa mtoto wake, ataenda kumshitaki.”
“Yaani walifikia hapo!?” Tunda akashangaa sana na kuuliza.
“Oooh
yeah! Anamipango yake ambayo mimba imeingilia. Ikawa ile mimba ni tatizo sasa.
Wakasumbuana wee, akakubali kumzaa huyo Maya. Alipojifungua tu, ikawa ndio
amepona matatizo yake. Sidhani hata kama alimnyonyesha Maya. Ratiba zake zikawa
ngumu kweli! Mara akahamia hosteli kabisa ili awe sawa kimasomo. Akasema kipindi
hicho cha miezi 9 ya ujauzito kimemrudisha nyuma kimasomo. Na kelele za mtoto
pia, hataweza kumaliza chuo na yeye amebakisha mwaka mmoja, kwa hiyo akaondoka
nyumbani.” “Subiri kwanza Nana! Inamaana akamuacha mtoto mchanga!?” Tunda
akauliza kwa kuumia sana.
“Why
not? Si CJ alimwambia anachotaka ni mtoto tu, atalea mwenyewe? Sasa ni kama
kazi yake imeisha. Ameshambebea mtoto na kumzaa salama, maisha yake
yanaendelea!” Tunda akabaki ameduaa. “Ikabidi sasa CJ apunguze kazi. Akahama
ofisini, kazi zake baadhi akawa akifanyia nyumbani. Akawa nyumbani muda wote akilea
watoto wake kama mama. Hakutaka amwache zaidi Maya ambaye alikuwa ndio
amezaliwa tu, mikononi kwa wafanyakazi tu.”
“Tukamtafutia
nanny wakumsaidia. Tukapata mwanamke mtu mzima kidogo zaidi ya yule
tuliyekuletea wewe ukamkataa.” Tunda akacheka kidogo bila kutaka kujibu. “Alikuwa
mama mzuri sana. Lakini na yeye alifariki kama miaka 14 iliyopita. Alimpenda
Maya kama mtoto wake. Sasa yeye ndiye aliyekuwa akisaidiana na CJ kuwalea Maya
na Net, na sisi tukisaidia pia, lakini mwanzoni sisi ilikuwa sio sana, kwa kuwa
CJ alijaa kwenye maisha ya wanae, hakubakisha pengo mpaka alipoanza kuugua.”
Akamuona ametulia kama anafikiria.
“Pole
Nana.” Tunda akamtoa kwenye mawazo ili aendelee kupata udaku wa uzunguni. “CJ
alipenda sana watoto wake! Hakutaka yeyote alemewe na watoto wake au mtu aone
watoto wake ni mzigo. Alikaa hapa nyumbani akimlea Maya kama mama
aliyejifungua.” “Mmmh!” Tunda akajikuta anaguna. “Mimi ninavyomsubiri mwanangu
kwa hamu! Naona nitakuwa simuweki chini.” Bibi Cote akacheka. “Hutaki mtu
amguse?” “Kidogo tu Nana, halafu mnirudishie mwanangu. Sio tena na nyinyi
mumng’ang’anie kama hivi Maya anavyompigia mahesabu!” “Na amesema anatunza
likizo zake mpaka Cote azaliwe.” “Ndicho anacho nitangazia kila siku.”
Wakacheka.
“Ehe
Nana!” “Basi, pakatulia. Junior yupo busy na watoto wake kuanzia asubuhi mpaka
usiku, mama yao shule. Hakuna aliyewaingilia. Mimi na Cote tukawa kimya. Net
alipoanza shule, yeye mwenyewe akawa dereva wa Net. Asubuhi anampeleka mtoto
wake shule, mchana anamrudisha kwa ajili ya ratiba za Net za jioni hapo
nyumbani. Net alijengewa ratiba tokea mtoto. Babu yake na baba yake
walihakikisha tokea mtoto anajielewa yeye ni nani. Na tukabahatisha akawa
msikivu kweli. Net hakusumbua kabisa.”
“Maisha
yakaendelea, lakini Ritha na mumewe wakawa ni kama hawaishi pamoja. Baadaye
tukamwambia CJ, sio sawa hivyo wanavyoishi. Lazima mkewe arudi, au yeye amfuate
ili wakaishi pamoja kama familia. Watoto wasikue bila mama. Sijui wakaelewana
vipi, tukaona CJ anahamisha mizigo yake na mkewe na watoto. Wakahamia kwenye
apartment. Kile kitu kikatuuma sana. CJ ni mwanangu wa pekee Tunda. Leo anaacha
nyumba nzuri, anakwenda kuishi kwenye apartment ya vyumba vidogo vitatu! Hata
sijui aliyejenga ni nani, nani anaishi karibu naye! Hapana. Moyo ukakosa raha
kabisa.”
“Ndio
baba yake akamwambia lazima anunue nyumba kwa ajili yake na watoto. Yale sio
mazingira salama kwake na watoto. Akampa na pesa, Junior akanunua nyumba nzuri
tu. Nikamtafutia wataalamu wakaenda kupatengeneza vizuri, wakajaza vifaa vya
kisasa, ndio wakahamia hapo na familia yake. Hapo nikaweza hata kulala usiku
nikijua mwanangu na yeye amelala pazuri.” Tunda akamcheka kidogo.
“Nilikuwa
siwezi kulala. Usiku kucha natembea pale ndani. Namwambia Cote siwezi kulala
humu ndani wakati mwanangu analala pabaya! Hapana. Hapo nilishindwa. Kwanza
ndio ilikuwa mara ya kwanza anaondoka nyumbani tokea anazaliwa. Shule zote
mpaka chuo, mwanangu alikuwa akisoma na kurudi nyumbani kwa mama yake. Ilikuwa
wakati wowote ninapomtaka, namuweka mikononi! Wakati mwingine nilikuwa natoka
kazini, namtoroka Cote namfuata mpaka shule angalau kumuona tu na kumbusu,
wakati tumeachana asubuhi!” “Nana! Unamfuata shuleni wakati asubuhi mliachana?”
Tunda akauliza.
“Na
jioni nitamuona tukirudi nyumbani!” Akajibu na kumfanya Tunda acheke huku
akimwangalia yule mama aliyeonekana mjasiri kama simba kumbe ana soft sport
kubwa ya namna hiyo! “Sasa eti leo anaondoka pale ndani na watoto wawili! Anakwenda
kujibana sehemu wanayoishi watu zaidi ya 1000, tena siwajui! Nilikuwa sipati
usingizi.” Tunda akaendelea kucheka taratibu.
“Mlikuwa
karibu naye eeh?” “Hivi unavyomuona Maya, ndivyo alivyokuwa CJ kwangu. Wakati
wote atataka kuniona. Hakuona aibu hata alivyokuwa mkubwa, mbele ya wenzake eti
na mimi nambusu na kumkumbatia muda mrefu hadharani! Hakuona aibu. Kwanza
alipenda.” Tunda akacheka.
“Alinifuata
popote na nikiwa na yeyote yule kuomba ni mbusu tu. Nilikuwa najisikia vizuri
sana. Net yupo kama babu yake. Sio mtoto wa kudekeza au hana muda wakuwekwa
mikononi muda mrefu. Akili yake imejaa mipango ambayo lazima aitimize kwa
wakati, kama babu yake. Na alikuwa hivyo tokea mtoto. Utafikiri yeye ndio
alizaliwa na mimi na Cote na si CJ. Ila CJ wangu? Oooh Tunda, hakuwahi kukua
kwangu mpaka namzika.” “Pole Nana.” Akacheka kwa unyonge kama anayevuta
kumbukumbu.
“Kilikuwa
kipindi kigumu sana kwangu alipoondoka na watoto? Hata kula yangu ilikuwa
shida. CJ mwenyewe alikuwa na kazi yakunituliza, lakini nilikuwa nakaribia
kuchanganyikiwa, mpaka walipohamia kwenye nyumba niliyoridhika kuwa inamstahili.”
Akatulia tena kidogo. “Anyways, Maya
alipofikisha miaka 3, akamwanzisha day care na yeye CJ akarudi kazini sasa.
Tukawa wote. Ofisi ile uliyomkuta Maya, ambayo alikuwa Net, ndiyo ilikuwa ofisi
ya baba yao.”
“Baba
yake CJ alipomshauri amshauri Ritha afanye kazi kwenye kampuni yetu, hapakuwa
na jibu la maana. Ila Ritha akawa kama anatukwepa hivi. Maswala ya watoto ikawa
ni CJ. Kazi kidogo na watoto. Wakati mwingine Maya akawa anarudi pale nyumbani
tunakuwa naye pamoja na yule nanny wake akitusaidia kumlea. Wakati mwingine
yeye na kaka yake walikuwa wakiletwa hapa ijumaa, baba yao anakuja kuondoka nao
siku ya jumapili ambayo ilikuwa lazima siku za jumapili tukutane kama familia
na kuwa pamoja mpaka jioni. Na hapo ndipo CJ alipokuwa akiondoka na watoto
wake, au kama Maya akigoma kuondoka jumapili basi asubuhi ya jumatatu mimi na
Cote wakati tunakwenda kazini, basi tunawashusha wote shule, ikawa inategemea
na CJ mwenyewe au Maya.”
“Taratibu
kadiri walivyokuwa wakikua, Net na Maya wakazoelea pale nyumbani. Wakawa muda
wakurudi kwao ukifika, wanagoma kuondoka, wanataka kubaki hapa na sisi. Tena
kwa kulia haswa. Ikabidi CJ awe anawaacha. Hapo na mimi ndio ikabidi kupunguza
kazi nikaanza kuwalea ili CJ asiwe na wasiwasi na watoto wake.” “Mama yao?”
Yule bibi akakunja uso kama anayefikiria.
“Ni
ngumu sana kumuelewa Ritha. Sijui nikwambie nini! Alikuwa yupo kama hayupo.
Hapakuwa na ugomvi. Wala huwezi kusema kulikuwa na matatizo ya ndoa. Ila ni
mwanamke ambaye niseme alipenda kujitegemea na asiingiliwe hata kwa maswali.
Alifanya kile anachokipenda yeye.”
“Maya
alipofikisha miaka 7, Net 12 karibu 13, baba yao akaanza kupata matatizo ya
figo. Akaugua, akifanyiwa matibabu ya hali ya juu. Tulihangaika kwa kila namna,
ili tu apone. Nilitumia pesa Tunda! Sina jinsi yakueleza. Uhai ungekuwa
unanunuliwa, hakika wa CJ ningeununua kwa pesa yeyote ile.” “Pole Nana.” Tunda
akamuhurumia. “Asante. Sasa hapo ndipo jukumu la watoto likawa sasa kwangu na
Cote ili kumsaidia Junior ajiuguze. Wakati mwingine matibabu yalikuwa
yakimfanya dhaifu sana. Hakuwa hata akiweza kujisaidia yeye mwenyewe. Tukamtafutia
nesi ambaye akawa akimuuguza hukohuko nyumbani kwao. Anafika hapo asubuhi,
anaondoka jioni akiwa amemuacha kitandani.”
“Sasa
katika mahangaiko hayo yote yakuuguza na kulea, tukaja kupata fununu juu ya
mumewe Ritha sasa. Kuwa anatutafuta ili azungumze na sisi. Cote akampigia simu
Ritha, akamwita nyumbani. Akamuomba amueleze ukweli. Kama kawaida ya Ritha,
mpaka Cote anamruhusu, hakuwa ametoa jibu la maana.” “Mmmh!” Tunda akashangaa
kidogo. Akatamani aulize ila akaona aendelee kusikiliza.
“CJ
alifika kipindi hajiwezi kabisa. Kila kitu ni wakufanyiwa. Nikamwambia Cote, ni
aidha mimi nihame humu ndani, au CJ arudi.” “Saasa uende wapi?” “Nikaishi na
mwanangu Tunda! Nilikuwa siwezi hata kuhema vizuri,
eti nipo pale nyumbani, najua kuna mwanamke mwingine ananilelea mtoto wangu!
Nilimwambia Cote nitakufa hata kabla ya CJ. Nikamwambia aniletee mtoto wangu
niuguze mwenyewe” Akajifuta machozi.
“Pole
Nana.” “Yaani nimemaliza tu kuongea hivyo, Cote
akaondoka bila kujibu. Baada ya muda, naona gari ya wagonjwa inaniletea
mwanangu na mizigo yake. Nililia Tunda, sikuamini.” Tunda alimuhurumia
yule bibi. Hapo ndipo akaona roho ya umama ndani yake.
Akajifuta machozi,
akaendelea. “Pole Nana.” “Asante. Basi. Nikaacha kila kitu. Akili ikawa kwa CJ
na watoto wake tu pale ndani. Nikisaidiwa na manesi pamoja na yule Nanny wa
watoto.” “Na Ritha?” Tunda akauliza. “Hapo hata akili ya mwanadamu mwingine
ilikuwepo? Sikujali mtu, wala kitu, mimi niliyekuwa namtaka ni mtoto wangu.
Nimeletewa, basi. Sasa nafikiri alipojua kama CJ atafariki, akapanga mambo yake
vizuri, akarudi kuishi pale ndani. Mimi nilishangaa tu Ritha mwenyewe amerudi
pale ndani na mizigo yake na yeye anasaidia kumuuguza CJ. Wala sikumuuliza.
Kimya. Mimi nikaendelea na kuuguza na watoto.”
“Baada
ya muda, eti CJ akiwa vile vile mgonjwa ananiambia wameamua kuuza ile nyumba.
Anaona familia yake irudi kuishi pale. Nikajumlisha kichwani na kutoa, sikujibu
kitu. Ila baada ya muda mfupi sana ile nyumba ikauzwa. Sikuuliza kitu. Mimi na
Cote tukanyamaza kuleta amani kwa CJ ambaye ni mgonjwa.”
“Tukaendelea
kumuuguza bila kuuliza lolote juu ya pesa zilizopatikana baada ya kuuzwa ile
nyumba. Hapo tulikuwa tumeshajua kuwa, hatapona mpaka apate figo mpya. Maana
ile ya kwake walishindwa kuitibu. Akawekwa kwenye orodha ya wanaosubiri figo
kama itapatikana huko hospitalini kuwa kama ikipatikana figo inayoendana na
yeye, basi apewe. Akawa anaendelea na matibabu huku akisubiria figo. Akiwa
kwenye kusubiri, Mungu akamchukua mtoto mmoja tu aliyekuwa amenipa.” Tunda
akamuona amebadilika mpaka rangi.
“Pole
Nana.” “He was my sweetheart. Alinipenda kupita nitakavyokueleza. Nakwambia
hivi anavyoniganda Maya, ndivyo alivyokuwa baba yake. Alikuwa na moyo wa
tofauti! Anyways, baada tu yakuzika, Ritha akaaga.” “Tena!?” Tunda akashangaa
sana. “Yeap. Akasema anataka kuondoka kwa kuwa aliyekuwa akimuweka pale ni CJ
na CJ ameondoka. Tukamuuliza swala la watoto, akasema wanaweza tu kubaki na
sisi. Tukashtuka sana. Watoto wadogo, anataka kuwaacha! Cote akajaribu
kumwambia yeye ni kama Junior pale nyumbani. Anaomba abaki angalau mpaka watoto
wake wafikishe miaka 18, akasema yeye yupo na kama watoto watataka kumtembelea,
waende kwake. Atakuwepo hapa nchini kwa muda.” Tunda akatoa macho.
“Nana
wewe! Akaondoka?!” “Nakwambia kama utani. Akachukua vitu vyake vyote, akaondoka.”
Bibi Cote akaguna. “Mwezi ukaisha. Kimya. Mwezi wa pili, kimya. Cote akatuma
watu wakamtafute wajue alipo. Wakarudi nakutuambia anaishi na mtu. Cote akiwa
na hasira sana, akamfuata alipoambiwa anaishi. Ilikuwa apartment tu. Akamkuta
yule mwanamme, Ritha hayupo. Cote akajitambulisha. Yule mwanaume ndio
akamueleza Cote mwanzo mpaka mwisho na kwamba wapo kwenye kutaka kubariki ndoa
yao. Cote akamuuliza kama anajua kama anawatoto. Yule mwanaume akamwambia
anajua, na ilikuwa moja ya mipango yao. Cote akaondoka akiwa amemuachia ujumbe
kuwa Ritha amtafute ili wazungumzie mirathi. Kumbuka hapo alikuwa na ile pesa
ya nyumba waliyokuwa wameuza na mumewe.” “Lakini pesa si zilikuwa za Papa?” Akauliza
Tunda.
“Kumbe
unafuatilia vizuri!” Bibi Cote akashangaa akili ya Tunda. Akafurahi kuwa
hakumpoteza na Tunda yupo makini. “Sasa ukumbuke bado alikuwa analipwa pia na
ile pesa ya wakati ule kabla mumewe hajafa. Basi, baada ya wiki moja akaja
ofisini. Cote akawa ameshaandaa makaratasi ya adoption. Kwamba anawataka wale
watoto, Net na Maya wawe wetu moja kwa moja. Tulijiandaa sana tukijua pengine
tutapata shida. Labda atatusumbua.” Akamuona anacheka kwa kusikitika.
“Ikawaje?”
“Huwezi amini, Cote alimwambia anataka kumuachia pesa yote, na ataendelea
kumlipa kwa makubaliano ya wale watoto, wawe wetu kihalali. Hakutaka kupoteza
muda wala kuuliza swali, akasaini kila kitu, akasimama.” “Nana!” Tunda
akashangaa sana. “Kabisa. Sasa mimi nikamuwahi. Nikamwambia, nataka wale watoto
wamtambue yeye kama mama yao japo sisi ndio tutakao watunza. Nikamuomba awe
anakuja kuwatembelea angalau mara moja kwa week. Apate nao muda, sisi wenyewe
tutagharamia usafari zake. Kuwa tunamtuma dereva awe anakwenda kumchukua na
kumrudisha. Akakubali bila shida. Na kweli, akawa anakuja hata mara mbili kwa
week. Anakaa na watoto wake, anaondoka.”
“Baada
ya miaka miwili kupita, tukamuona anakuja siku hiyo na nia yakutaka kulala.
Cote hakumsemesha, wala mimi sikumuuliza. Akalala siku ya kwanza na ya pili.
Akajirudi kama sio yeye Ritha. Siku ya tatu, tukapatwa na wasiwasi. Cote
mwenyewe ikabidi aende kule alipokuwa akiishi kujua kulikoni.”
“Moja
kwa moja akaenda kwenye lease office. Yaani ofisi ya wanapokodisha hizo
apartment kujua kulikoni. Akaambiwa na uongozi kuwa, mwanaume aliyekuwa akiishi
naye, alimkimbia na kila kitu. Yaani siku tatu zilizopita, Ritha alirudi kutoka
kazini, hakukuta hata kijiko. Na mbaya zaidi, yule mwanaume alimuibia baadhi ya
pesa na kama alimwaribia na kazini.” “Nana!” Tunda akazidi kushangaa.
“Yeap.
Cote akarudi nyumbani akanieleza. Nikamshauri tumuache tuone mwisho wake.
Akakaa hapa kama mwezi. Akiwa ametulia. Mama mwema kwa watoto wake. Hilo
likatufurahisha.” “Kwa nini haukutaka kumuuliza!?” Tunda akauliza kwa mshangao.
“Unakumbuka Cote alimwambia pale ni kwao kama Junior? Sasa amerudi nyumbani,
unamuuliza tena?” Tunda akanyamaza.
“Basi.
Maisha yake yakaendelea, baada ya miezi sita, akaaga tena kuwa ameamua kurudi
kuishi Tanzania.” “Haiwezekani! Tena!?” “Hapakuwa na jinsi yakumzuia Ritha
anapotaka jambo lake. Huwa anataarifu na anakuwa haweki nafasi ya kushauri.
Sasa kwa kuwa Cote alitaka asiue undugu, akamuomba atakapofika kwao, atafute
kiwanja, tujenge sehemu ambayo hata watoto watakapotaka kwenda, wawe na nyumba.
Hilo akalifurahia sana. Alipofika tu huko, baada ya kama mwezi tu, akawa
amepata kiwanja. Akili na mawazo ya Cote yakawa huko. Ikajengewa ile nyumba,
ndani ya mwaka ikawa imekamilika kila kitu. Cote akaandikishana naye kuwa ile
ni nyumba ya Net na Maya, lakini yeye ni msimamizi mpaka wakue au alipe kila
pesa aliyowekeza pale. Sawa.”
“Akarudi
tena na wazo la biashara. Anataka pesa. Cote akampa kwa makubaliano awe analipa
kidogo kidogo kama hivi Net anavyomfanyia dada yake.” Tunda akacheka kidogo. “Si
nilikwambia ni roho ya babu yake? Yaani hivi unavyomuona Net, na mume wangu
alikuwa hivyo hivyo mpaka tabia. Ila Cote alikuwa mkali sana ambaye hawezi
kujificha. Angalau Net anaweza kuficha makucha, ila sio Cote. Pale kazini
wanamjua Net. Mkali na hawezi kuvumilii uzembe wa aina yeyote .” Tunda akacheka
huku akimfikiria mumewe.
“Basi,
ikaonekana ni mkopo ambao lazima alipe. Wakaandikishana mpaka kwa mwanasheria.
Akapewa pesa, akaanza biashara. Lakini yote hayo, hatukuwaambia watoto wake.
Hata mumewe hatukutaka kumwambia.” “Kwa nini!?” “Tunda! Alikuwa mtoto wa pekee! Akawa mgonjwa
sana. Hatukutaka afe akijua amesalitiwa au anasalitiwa. Kwa hiyo habari zote za
mume wa Ritha, tulikubaliana tuzifiche, sisi tusimwambie. Afe kwa amani. Sasa
kama yeye mwenyewe alijua akaamua kuzinyamazia, sijui. Ila hakusikia kutoka
kwetu.” “Ehe!” Tunda akataka aendelee.
“Basi,
Net ndio alikuwa akikubali kwenda kwa mama yake mara kwa mara. Maya alilelewa
na baba yake na mimi. Alipokufa baba yake, mimi na babu yake ndio tukawa kama
wazazi wake. Kumwambia atuache hapa aende Tanzania, alikuwa akilia sana. Hataki
kabisa.” “Labda kwa kuwa hawakuwahi kuwa na mahusiano ya karibu na mama yake!”
“Kabisa. Sidhani hata kama alimnyonyesha!” Hicho akakirudia tena huyo bibi kwa
uchungu. “Kwa hiyo kwake akawa mgeni, hata walipokuwa wakiishi pale nyumbani na
mama yake, alikuwa akinifuata mimi, hataki kuwa na mama yake karibu.”
“Ila
Net alikuwa mkubwa kidogo na kama nilivyokwambia. Net alikomaa akiwa bado
mdogo. Walikuwa wakizungumza na Net kama mtu mzima, tokea mtoto. Kwa hiyo
alikuwa na akili ya kumtambua mama yake. Ila si Maya. Maya hakuwahi kuwa na
mama yake karibu. Nafikiri madawa ya kulevya ndiyo yalimfanya aende kwa mama
yake. Tena ilikuwa kama adhabu, kumtoa hapa na kumpeleka kule ili akajifikirie.
Kwa hiyo hayo ndio yakawa mahusiano ya Ritha na watoto wake.”
“Sasa
kitendo cha Net amekuwa mkubwa, anatakiwa aanze kazi hapa, halafu mama yake
anamng’ang’ania kule, kilimuudhi sana Cote.” “Haikuwa sawa.” “Kabisa. Cote aliona
anavuna sehemu ambayo hakutaka hata kupanda! Na sisi hatukutaka kuweka fitina
kati yao kwakuwa tulijiona tunakuwa wazee, tutaondoka na kuwaacha hapa duniani.
Tukajiambia ni afadhali wabakie na mama yao kuliko wapoteza baba na waje
watupoteze na sisi. Wajikute wamebaki peke yao bila ndugu na tumeua mahusiano
na mama yao! Kwa hiyo ndio hivyo.” Tunda akavuta pumzi kwa nguvu. Akajiegemeza
kwenye kiti akafikiria kwa muda.
Kisha
akamgeukia bibi Cote. “Ni kweli maamuzi mengi mlifanya sio kwa hisia, maana
nirahisi kukasirika nakuchukua hatua kutokana na hasira. Kama mimi yule mama
amenitenda vibaya sana. Sijui kama unajua?” “Nafahamu sana.” Bibi Cote akajibu.
“Na ilinibidi safari hii niwe mkali sana kwake. Hakuamini. Nilikwenda na Logan
nikiwa nimejiandaa kumshitaki na kumfilisi vibaya sana. Nilimwambia akibisha
tu, nampokonya mali zote nakupa wewe.” “Nana!?” Tunda akashtuka sana nakujiweka
sawa.
“Kabisa
Tunda. Sikumwambia hata Net. Lakini nilijiapia kumtenda ipasavyo. Nilikuwa
nimekasirika nakaribia kupasuka. Hivi unajua nilimuuguza Net kwa majuma mawili,
amebanwa mbavu sababu ya kumsafirisha kama mfungwa!” “Alinisimulia Net.” “Aliniudhi
mpaka akanifanya nikumbuke mambo mengi sana. Nikakaribia kumfilisi kabisa.
Nilimbemba bila kuchoka, halafu anamgeuka Net hivyo! Nilikasirika sana.” Tunda
akafikiria kidogo.
“Sasa
hivi unajua alipo?” Tunda akauliza. “Alitumia akili. Nilipokwenda mara ya
mwisho nikamsainisha kwa masharti yakumsamehe pesa yote ilimradi asikuingilie
wewe na Net. Awaache kabisa na afute kesi zote alizokushutumu. Na masharti
mengine ambayo nilimwambia akiyatimiza hayo yote na kujiridhisha, hata akitaka
abadilishe jina la kampuni na nyumba, sitamzuuliza.”
“Baada
ya mwezi tu, alipotimiza kila sharti nililompa, akatuma karatasi,
nikamsainishia kuwa nimemkabidhi kila kitu. Kwa hiyo nyumba na kampuni vyote
vikawa kwa jina lake. Nasikia ameuza kila kitu, kasoro ile nyumba. Nasikia
amerudi huku.” Tunda akashtuka sana.
“Wala
usiogope. Huku hawezi kukufanya chochote. Hana huo uwezo hata kidogo. Na yeye
anajua hilo, hatathubutu kukusogelea.” “Unajuaje Nana? Ritha anaakili na uwezo
mkubwa wakushawishi watu wawe upande wake. Hukusikia alichowafanya Gabriel na
mkewe?” Tunda akauliza kwa wasiwasi. “Kwa sababu mimi nimekwambia, basi usiwe
na wasiwasi. Halafu alifanikiwa kwa Gabriel na mkewe kwa kuwa tayari walikuwa
na ugomvi. Hawakuwa kitu kimoja ndio maana ilikuwa rahisi kwa Ritha kuwatumia
kufanya ubaya wake.”
“Nimeishi
na Ritha. Nimeona kazi zake na ujanja wake. Aliweza kumgeuza Net akawa upande
wake. Hatukutaka kumtenganisha Net na mama yake kwa kumwambia mabaya ya mama
yake. Lakini Mungu alikuja kumfungua macho Net, kwa machozi. Yuko makini sana
sasa hivi na amaeshajua linapokuja swala la pesa, mama yake anaweza kufanya
chochote.” Bibi Cote akafikiria kidogo.
“Kwa
mara ya kwanza, Net alikaa akapata muda wakufikiria na kukumbuka yeye mwenyewe
mambo mengi tokea mtoto mpaka mama yake anamfukuza Tanzania, akauliza kama
alishawahi kuwapenda na kuwahesabu wao kama watoto wake kabisa?” “Ukamwambia
nini?” “Tunda! Hata iweje, Ritha ni mama yao. Siwezi kuwaacha Net na Maya
wakiwa na taarifa mbaya za mama yao, tena kutoka kwangu! Kama sisi mabaya ya
Ritha yalitufikia hapa, na wao siku moja watakuja kumjua tu mama yao.”
“Huwezi
kuingilia mahusiano ya mama na mtoto, hata siku moja. Na wewe nakuonya. Ukitaka
Net awe upande wako siku zote, usiwe adui wa mama yake kwa maneno machafu au
kupanga na Net mipango ya kuwa kinyume na mama yake. Utaona jinsi vita yako
itakavyokuwa rahisi. Net mwenyewe atapigana vita yako, kwa kuwa ameshajua
udhaifu wa mama yake, na anajua anakuonea. Hawezi kukubali. Atafanya kila
awezalo kukulinda wakati wewe umetulia tu.” Tunda akaridhika.
“Net
anakupenda sana. Hawezi kuruhusu chochote kutoka kwa yeyote kikupate. Usiogope
kabisa. Na kuhusu Vic, usiwahi kumuonyesha unamuogopa.” Hapo napo Tunda
akajiweka sawa.
Juu ya Vic.
Bibi
Cote akaanza kama anafikiria kidogo. “Tabia ya Vic ipo hivi, anapenda kuwa juu
ya kila mtu na kila kitu. Na anataka kila mtu alitambue hilo. Atakachofanya
chakwanza ni kukuonyesha yeye ni bora kuliko wewe. Atakuonyesha anamipango
mikubwa au alikuwa na mipango mikubwa sana. Asikutishe kwa lolote. Yeye ni
mtoto aliyezaliwa akiona mambo yanafanyika. Anaangalia na kujua mambo kwa macho
tu sio kuyatenda. Juhudi kubwa inawekwa na wazazi wake, yeye ni mmaliziaji tu.
Sijui kama unanielewa?” Tunda akatulia akisikiliza.
“Vic
hayajui maisha kwa ujumla wake. Anajua maisha aliyoishi yeye tu. Watu
wakimuhangaikia kuanzia wazazi na watu wanaomzunguka. Nikikwambia ni ‘Diva’,
ujue ni Diva kweli! Utakuja kumuona. Anaongea kama mtu muelewa sana. Anatoa
mipango ya umakinifu sana, lakini hajui na hana uwezo wakutekeleza. Kwa kuwa
amezoea kuamuru na vitu, vinakuja. Anaamuru pesa iingie kwenye akaunti yake,
bila kujua inatoka wapi, au huyo mtu anafanya nini kuingiza pesa kwenye mifuko
yake.”
“Hiyo
pia imechangiwa na wazazi wake. Anapotaka juisi kutoka kwa mfanyakazi yeyote
yule, hataomba. Ataamuru juisi ifike mbele yake bila kujali juhudi zilizotumika
kufanya ile juisi imfikie mkononi. Na wakati wote anaonyesha kwa juhudi zake
zote kuwa hakuna mtu anayefikia kiwango chake. Anaamini ni yeye tu, lakini ni
kwa kuwa anastawi kwenye juhudi za mtu au watu fulani.”
“Net
aliposema hatamuoa, wengi walishangaa sana. Kwa kuwa ni kama wamekua kwenye
mazingira yanayoendana. Kwamba wana historia za pesa nyingi. Namaanisha
wametoka kwenye utajiri. Halafu Vic ni mzuri kwa viwango vingi alivyowaaminisha
watu, lakini hatoi ruksa wala mwanya wa kusikiliza mtu yeyote, hata wazazi wake.”
Tunda akaendelea kusikiliza.
“Na
ni mjanja sana. Anazungukwa na wasichana wengine wawili. Wapo kama vijakazi
wake. Nilishawasikia mimi mwenyewe wakilalamika. Hawakujua kama mimi nipo
nawasikiliza. Kuwa Vic ni mjanja na mbabe. Anachukua mawazo yao na kutangaza
kama ni yake. Hilo ndilo hata Net alimgundua. Hana kila kitu, lakini
analazimishia watu wajue yeye ni kila kitu. Na ndipo ugomvi wake na Maya ulipo.
Maya anamdharau kwa wazi kabisa, kitu ambacho kinamuuma sana, na ndio maana na
yeye alimtenda kwa makusudi ili kuhakikisha yeye ndio anabaki juu. Hawezi na
haruhusu mpinzani kwa namna yeyote ile.”
“Lakini
wewe kuwa naye makini kuanzia mwanzo kabisa. Atakapokuonyesha anamfahamu sana
Net, na kutaka kukuonyesha pale kwetu na yeye anauhuru wakufanya anachotaka kwa
kuwa alikuwa pale tokea mwanzo, muonyeshe kwa wazi na mapema sana kuwa wewe
ndio incharge, yaani wewe ndio kiongozi pale kwa sasa. Unanielewa?” “Nana!!
Sijamaliza hata…” “Stop right there.” Bibi Cote akamkata kwa haraka.
“Utakapomfungulia
Vic mlango hata kidogo leo, utamkuta chumbani kwako. Hajui mipaka, hajui
hapana, hajui wapi atawale na wapi asitawale. Atajaa kwenye ndoa yako, atataka
kukufundisha hili na lile, ilimradi watu wote wajue kuwa anakusaidia. Na wewe
si kitu. Na akifanikiwa hilo nalo, hatakuacha. Atakufanya kama Maya. Kuanzia
mwanzo, lazima umuonyeshe pale ni kwako sasa hivi. Yeye ni mgeni ambaye
atafika, utakapomkaribisha wewe sio Net. Na Net naye umuweke sawa tokea
mwanzo.” Akaendelea.
“Ulimwengu
huu mnaoishi sasa hivi, utatawaliwa na wenye nguvu, hekima na mipango.
Kikipungua hata kimoja, watakutawala na kukurudisha jela kwa haraka sana kama
alivyofanya Ritha.” Hapo Tunda akakaa sawa. “Sasa hivi unaanza kuwa mama. Toka huko uliko,
vaa roho ya Simba, King of the Jungle. Hapo ndipo utaweza kuwa salama na
kutawala ufalme wako. Lasivyo jumuia inayotuzunguka sasa hivi, watakusumbua
sana. Kwanza sababu ya rangi ya ngozi yako, pili historia yako ya nyuma. Make
your past as a present precious gift.” Tunda akamgeukia kwa mshangao.
“Hivi
unajua maisha yangu ya nyuma!?” “Najua kama ulishaishi kwa ukahaba. Najua. Na
ninajua hiyo ndio sababu kubwa ya kuwekwa jela. Nafahamu vizuri tu. Usingeweza
kuishi kwenye ile nyumba na sisi bila kukuchunguza vizuri na kukufahamu.” Tunda
akapoa. “Nilifanya kosa kwa Ritha, sikutaka kurudia kosa.” Tunda akaishiwa
nguvu kabisa. Akageukia pembeni
“Lakini!”
Tunda akamgeukia tena. “Ukifanya maisha uliyoishi zamani kuwa siri, kitu cha
aibu, watatumia huo udhaifu wako vibaya sana kuliko utakavyofikiria. Ritha
alilijua hilo, sitaki kukukumbusha kule alikokupeleka. Mungu alikusaidia
umelipa deni yako, sasa hakikisha inakuwa ndio shule na nguvu yako kubwa kwa
kila anayekuzunguka. Lasivyo miezi yote sita uliyokaa jela itakuwa bure. Unanielewa?”
Tunda akafuta machozi.
“Hayo
machozi yaishie kwangu na kwa Net tu. Usiruhusu hata Maya ayaone. Uongelee
maisha yako kwa ujasiri. Kule ulikotoka, ulikopitishwa na madhara yake, kisha
tumia kwa faida ya wengine na watoto wako. Maana watakuja tu kuambiwa. Hutaki
waje wateseke kwa maisha uliyoishi nyuma.”
Juu ya
Taasisi Anayotaka kuachiwa.
Tunda
akaongeza umakini ili kuweka kichwani hayo mazito mengi aliyokuwa akimwagiwa na
bibi huyo aliyeonyesha kukumkubali yeye kama Tunda. Aliona ni shule ambayo
hawezi kuzembea hata kidogo. Zaidi kutoka kwa bibi wa aina hiyo! Akajiweka
vizuri.
“Nilikwambia
ninaongoza chama cha wasomi na wenye pesa. Wengi wa wale kina mama, wanataka
kuongoza kwenye maono ambayo hawajui chanzo chake. Nilikwambia mimi nilikuwa
mwanzilishi. Nilianza mimi na Cote. Lakini kulikuwa na sababu. Hakuna mtu
anayeweza kumfikiria mwenye njaa, kama haijui njaa. Sijui kama unanielewa Tunda?”
Tunda akajiweka sawa.
“Sikuanzisha
ile taasisi kwa sababu mimi ni mwanamke! Hapana. Kwa sababu nilishapitia
wanakopita wengi wa wale wanawake wanakopitia sasa hivi.” Tunda akakunja uso
kama asiyeamini. “Najua kuishi na baba
mlevi anayepiga mke. Najua kuishi na mama aliyepigwa usiku kucha, na asubuhi
inamlazimu kuamka, kuwataarisha nyinyi muende shule, tena akiwa na tabasamu
usoni ili muende shule na furaha.”
“Najua
kwenda shule nikiwa na njaa. Najua kufungiwa ndani kutokwenda shule. Najua
kupigwa mpaka kuzimia bila kosa. Najua kutokuwa nacho, na kuwa nacho. Najua
wanachopitia wale wanawake, au mtoto wa kike, kwa kuishi. Sio kusoma au
kusimuliwa kama Vic na wale wanawake wengine wanaovaa alumasi zakupewa na
wanaume zao. Unanielewa Tunda?” Tunda akaongeza umakini na kumtizama yule bibi
kwa jicho la pili.
“Ukiniona
mimi navaa alumasi, ni kwa kuwa nimeifanyia kazi, nikaitolea jasho na ninaistahili.
Iwe ilitoka kwa Cote au nilijinunulia mimi mwenyewe. Vitu vyote ninavyomiliki
ni kwa kuwa nilivihangaikia kwa kutokulala. Tukiwa mimi na Cote. Kwa shida
sana. Ninapoandika muongozo wa kitu gani kifanyike kwenye ile taasisi kumsaidia
mtoto wa kike, sio kwa sababu inanibidi mimi kama kiongozi! Hata kidogo.
Naandika kwa kile nilichopitia, na ndio maana imedumu kwa muda mrefu sana na
bado ipo.”
“Ninapokwambia
nina shida ya billion moja kwa ajili ya ile taasisi. Na lazima niipate mwaka
huu, ni lazima nitaipata. Hata kama wote watasema ni kubwa sana, hatuwezi. Mimi
najua nilazima niipate. Kwa kuwa kwanza najua madhara ya kutoipata ile pesa.
Inamaana yupo mwanamke mmoja na watoto wake, wataendelea kupitia alikopita mama
yangu na sisi, mpaka kifo.” Tunda akashtuka sana. “Au, inamaana kuna binti wadogo sana, wataendelea kufanyiwa
biashara za ukahaba kwa kuwa ninasikiliza wanaokula vizuri, wanao endesha
maisha yao yakifahari kuniambia haiwezekani! Sio mimi na wananifahamu.”
“Nakwambia
hivi, mimi ninapokwambia ninahitaji kiasi fulani cha pesa, hakuna atakayesimama
mbele yangu akanizuia kutoipata hiyo pesa. Hakuna mlango nitagonga wasifungue.
Hata ikinilazimu kukaa nje ya huo mlango mpaka nikutane na muhusika. Hakuna
malkia nitashindwa kumfikia na kumuomba hiyo pesa. Kwa kuwa najua uharaka wa
hiyo pesa na umuhimu wake. Sitakula wala kunywa, mpaka hiyo pesa yote ipatikane
kwa muda ninaopanga mimi. Sio kwa sababu nataka watu wanione au wanisifie,
hapana. Ni kwa kuwa najua umuhimu wa ile pesa. Sijui kama unanielewa?” Tunda
akavuta pumzi kwa nguvu.
“Sasa
hivi nakuelewa Nana.” Bibi cote akaridhika. “Haiitajiki shahada mbili au tatu za
elimu kumsaidia mwanamke mwenye shida! Ila inahitajika kuelewa alipo kwa wakati
ule wenye shida, na atakapokuwa kama utamsaidia. Ndio maana unaona mpaka leo
nimeshindwa kustaafu au kumuachia mtu majukumu yangu, kwa kuwa sijaona
anayeweza. Hakuna anayeweza kuvua viatu, akapiga magoti mbele ya tajiri, kuomba
chakula cha mama au mwanamke aliye na matatizo isipokuwa anayejua njaa.
Aliyeshiba, atakwambia nikujidhalilisha. Inabidi kuomba appointment.”
“Matajiri
hawana muda wakupoteza. Utaomba appointment leo, ukifanikiwa sana kumshawishi
mtunza kalenda wake, utapewa tarehe ya mbali sana, tena hiyo ni bahati. Lakini
hata kumpata mtunza kalenda wake ni kama umemuona Mungu.” “Sasa wewe
unafanyaje?” Tunda akauliza. “Nikishajua unayopesa ninayoitaka. Hata nusu yake.
Natafuta wapi unakuwa na kwa wakati gani. Hata kama unalindwa kama raisi,
nitakufuata tu. Hiyo fujo itakayotokea getini kwako, lazima utataka niingie
ndani. Sitaharibu kitu, ila sitaondoka hapo mpaka nikuone.” Tunda akaanza
kucheka.
“Nana!”
Tunda akamshangaa huku akicheka. “Wananifahamu sehemu nyingi sana. Na kwa kuwa
pesa yao naifanyia kitu chamaana, sasa hivi hakuna mlango ninaotaka ufunguliwe,
ukashindwa kufunguliwa. Nishatolewa kwenye magazeti nimepiga magoti huku na
kule nikiomba msaada kwa machozi.”
“Historia
yangu ya mateso ya utotoni imegeuka kuwa baraka. Sikuona haya kusema mateso
yangu na kueleza umuhimu wa kumsaidia mtoto wa kike. Utakwenda kupaona, utajua
ni kwa nini nasema hivyo. Ni anayejua njaa tu, ndiye anayeweza kumkumbuka aliye
na njaa. Sio elimu nzuri au ujuaji wa kula na kisu na uma! Sisemi kuwa navyo ni
vibaya, lakini hivyo sio vigezo pekee vinavyohitajika.” Hapo angalau Tunda
akatulia.
“Ritha
alikuwa na shahada tatu nzuri na zakuheshimika kwenye jamii. Lakini kwa kuwa alishindwa
hata kutunza watoto aliozaa yeye mwenyewe, na mwanaume mmoja tu. Nilihakikisha
anaelewa yeye sio mrithi wangu na wala hatakuwa mtawala hapa. Kwa kitendo
chakupokea pesa kwa kuuza watoto wake, kiliniuma kama nawazaa wale watoto mimi
mwenyewe labor.” Hapo hata Tunda akakubaliana naye.
“Huwezi
ukanikuta mimi nazungumza kwa muda mrefu na Vic. Hata mara moja, na yeye
amenijua hivyo. Kwa kuwa najua moyo wake. Najua kiwango alichopo au
anachojiweka, mimi sipo na wala sitaki kuwa huko. Heshima ninayompa Ms Emily
leo, ndiyo ninayompa Logan mwanasheria wangu, ila naweka mipaka tu. Ni kwakuwa
nilishawahi kuwa kama Ms Emily au hata mama yangu alitamani kuwa kama Ms Emily
lakini hakubahatika.”
“Nafasi
au kazi anayofanya Emily mfanyakazi wangu wa ndani, inatamaniwa na wengi sana,
na hawajabahatika. Emily amesomesha watoto wake wote na kusaidia wazazi wake
wakiwa wagonjwa mpaka akawazika kwa kazi yake hiihii ya nyumbani kwangu. Sasa unawezaje
kusema ni mtu duni? Unawezaje kumdharau mtu kama huyo ambaye akiamka asubuhi,
watu zaidi ya watano wanasema asante Mungu? Ni kwa kuwa mtu hafahamu na hajui.
Ila wewe umeweza.” Tunda akashtuka kidogo.
“Nafahamu
kila kitu kinachoendelea mle ndani.” Bibi Cote akacheka. “Hakuna kitu
kinaendelea pale ndani, nisijue. Najua mahusiano yako na Emily, Gino na Carter.
Najua huwa unamsaidia Emily kazi ili awahi kuondoka kurudi nyumbani kwake.
Najua kama unasaidia jikoni na unapenda kumchokoza Gino.” Tunda akacheka.
“Gino
anaakili za kitoto na anapenda kujifunza Kiswahili.” “Kwa kuwa na wewe umemuonyesha
unamthamini. Inawezekana wala hakuwa na lengo lakujifunza Kiswahili. Lakini ule
uthamani unaouweka kwake, na kumwambia awahi kuondoka, mara tu akimaliza
kunitayarishia mimi na Maya, asikusubirie wewe mpaka ukiamka. Utajihudumia na
kumalizia pale jikoni mara ukiamka, usifikiri ni kitu kidogo!” “Eeeh!” Tunda
hakuwa akielewa anachomfanyia Gino. Yeye aliona kawaida tu.
“Kwanza
ujue kazi yake ya asubuhi inatakiwa kuisha pale anapokuhudumia wewe na kuacha
meza na jiko safi. Sasa kwa kumwambia asikusubiri, inamsaidia kuwahi kwenda
kufanya kazi kwenye hoteli nyingine.” Tunda akashangaa kidogo. “Anapika huko
chakula cha mchana, ndipo jioni anarudi tena pale kutupikia sisi. Na vile
unavyomwambia akipika aondoke tu, wewe mwenyewe utaandaa meza, ameniambia
imemsaidia kuongeza kazi ya tatu. Usifikiri ni kitu kidogo!” Tunda akabaki kimya
akifikiria.
“Umekaa
hapa mwezi mmoja unakwenda wa pili tu, lakini umegusa maisha ya watu. Gino
anasomesha dada zake huko nchini kwao. Kwa kumsaidia hivyo, kunamuongezea kipato.”
Tunda akajisikia vizuri. “Haya, kitendo cha kuhakikisha Emily na Carter
wanakula na kushiba, kwanza hawakutegemea.” “Nana wewe! Nani anakwambia bwana?”
Bibi cote akacheka.
“Nakwambia
hakuna kitu kinaendelea mle ndani mimi nisijue. Mahusiano niliyonayo na wale
wafanyakazi si ya kikazi tu na si ya siku moja! Maya alizaliwa Carter na Emily
wakiwepo. Wale ni kama watoto wao. Nafikiri Carter alikuwepo hata kabla ya Net
kuzaliwa. Yeah. Alikuwepo. Ila Emily ndiye alikuja Net akiwa ameshazaliwa na Maya
akiwa analelewa na huyo mama niliyekwambia alifariki, Emily akiendelea kufanya
anachofanya sasa hivi. Kwa hiyo wamefanyika watu wa pale. Pale ni nyumbani pia.
Lakini hapakuwepo mtu wa kuwafikiria hivyo kama wewe unavyowafanyia.” Tunda
akabaki akifikiria.
“Nilipoomba
kuzungumza na wewe Tanzania. Haikuwa kwa ajili ya Net.” Bibi Cote akaendelea na
kumfanya Tunda arudishe mawazo pale. “Ilikuwa ni kwa ajili yangu mwenyewe kwa
kuwa hata ungejibu vinginevyo ambavyo nisingependezwa navyo na bado Net
angesema anataka kukuoa wewe, ungeolewa tu.” Tunda akacheka kidogo.
“Lakini
mimi mwenyewe niliridhishwa na wewe. Nikajiambia wewe ndiye ninayekutaka hapa.
Swali likawa unakujaje huku nakuacha watu wanaokutegemea kule? Maana Net
alikataa kabisa kukuonyesha mali zinazomzunguka huku. Na hata kwa kichache alichokuonyesha
anacho, ulikataa kukitumia.” Tunda akashangaa kidogo. “Alijuaje?” Akajiuliza.
“Mara
nyingi tulipokuwa Tanzania kila tulipokuwa tukitolewa na Net, nilikuwa nikimuuliza
mbona hauji naye, alikuwa akiniambia unafanya kazi mpaka usiku sana, unatafuta
pesa yakumtoa baba yako jela au unatafuta pesa yakujilipia kodi. Wewe mwenyewe!
Kwa jasho lako! Kwa maisha uliyoishi, ulikuwa na sababu zote zakuwa tegemezi,
lakini ulipambana, ukijua umuhimu wakusaidia mtu mwingine. Sasa huyo ndiye mtu
ninayemtaka mimi.” Tunda akajisikia vizuri.
“Na
ndio maana nilikuja mimi mwenyewe Tanzania huhakikisha Ritha hakugusi tena. Na
nilipoambiwa umekubali kulipa gharama ya makosa yako, kwa kukaa jela! Oooh my!”
Yule bibi akacheka nakutingisha kichwa. “Nilipiga magoti pembeni ya ofisi
yangu, nikamshukuru Mungu kukuleta kwenye maisha yangu. Lakini sikumwambia Net,
kwa kuwa yeye alikuwa anakazi ya kulia tu.” Tunda akacheka huku akijifuta
machozi.
“Mimi
nikaendelea kufurahia moyoni. Nikajua Mungu anataka kunipumzisha.” Tunda akakumbuka
mambo mengi na mipango ambayo Net alikuwa akimwambia afanye naye baadaye,
akajua ndio hayo anayozungumzia huyo bibi sasa hivi. Net aliongea kwa mafumbo
lakini hapo ikawa kama huyo bibi anajibu mafumbo yote.
“Lakini naogopa sana Nana. Unafikiri nitaweza kweli? Sijasoma
kabisa. Halafu mwenzio kushika hata hii mimba ni muujiza mkubwa sana. Sijui
kama unajua?” Akamuona kama
anafikiria kidogo, kisha Tunda akaendelea baada ya kutulia.
“Nitakuja
kukusimulia wakati mwingine. Ila kwa huu muujiza wa Mungu kunibariki na hii
mimba tu, nimemuomba Net anipe muda wakulea kwanza. Nitamsaidia majukumu
mengine baadaye. Lakini sasa hivi aniache nilee watoto wangu kwanza. Nakwambia
hivi ili ujue sina mpango wakurudi shule sasa hivi. Nitafanyaje?” Bibi Cote
akacheka kidogo. “Ndio maana mimi nipo
na wewe sasa hivi. Usiwe na wasiwasi. Umechagua kitu kizuri. Tulia kwanza na
watoto ambao Mungu atakubariki. Na sisi tutakusaidia tu, usiogope. Na
nimeshakwambia huhitaji shule kukuwezesha kufanya ninachofanya. Ila umakini na
mipango. Pesa ya Cote na ile taasisi ndio itakusaidia kukupatia wasomi. Sijui
kama unanielewa?” Tunda akajiweka sawa.
“Angalia
wapi na nani unamuhitaji, unaajiri. Mimi sikusomea sheria. Lakini ninaye Logan.
Sijui kupika hata kidogo, lakini napenda kula vizuri, ndio maana ninaye Gino.”
Tunda akacheka. “Ni kweli hujui kupika Nana!?” “Hata kidogo. Na wote wananijua.
Tulipoona na Cote ndiye aliyekuwa akipika. Na ndio kitu wananitania mpaka leo.
Sijui kupika na wala sipendi hata kupita jikoni.” Tunda alicheka sana.
“Ndio
maana huingii jikoni?” “Sina nitakachokifanya huko, halafu pia ni sehemu
inayonikumbusha kifo cha mama yangu.” “Pole Nana.” Akamuona anafikiria. Muda
mrefu tu dereva alikuwa ameshawafikisha salon, ameegesha gari. Kimya. Wao
wanaendelea kuzungumza. “Twende tuingie ndani. Tuwahi kurudi nyumbani. Jumamosi
jioni na jumapili ni muda na familia. Karibu sana Net anatoka kazini.” Tunda
akafikiria kidogo.
“Natamani
tuendelee kuzungumza Nana! Ujue mimi sikupata malezi kabisa. Yaani sasa hivi ni
Net na mama Penny ndio wananisaidia. Na ndio maana lazima nizungumze na mama Penny
kila siku. Ananielekeza mambo mengi. Nakuwa ni kama naishi naye nyumba moja.”
Bibi Cote akacheka.
“Wewe
usiogope. Sidhani kama Mungu atanichukua karibuni, ni mpaka akuone wewe upo
tayari. Tutapata muda mzuri tu wakuelekezana. Sasa hivi fikiria jinsi ya
kupendeza kwenye sherehe ya ukaribisho wako. Na siku hiyo ndipo nitatangaza
siku ya baby shower.” Tunda akacheka. “Sawa.” Wakashuka na kuingia saluni.
Party ya kukaribishwa Rasmi Tunda
Norfolk, Ontario, Canada.
Norfolk ilikuwa ni kama kijiji kilichokuwa
kipo ufukweni. Zilikuwa familia za watu walioishi hapo muda mrefu. Wakazi wa
hapo walijuana kwa vizazi na vizazi. Nyumba ya kina Net ilikuwa mwisho kabisa
wa huo mji, na mipaka yao imeingia mpaka ndani ya hilo ziwa Erie. Walikuwa na
boti za kisasa zimeegeshwa kwenye ziwa hilo upande wa nyuma ya nyumba yao.
Moja
ya kumbukumbu alizonazo Net, ni kwenda na babu yake kuvua samaki siku za
jumamosi au siku awapo likizo. Mzee Cote alikuwa akimchukua Net na kwenda naye
kuvua samaki. Ni kitu alikuwa akipenda sana Net tokea mdogo na enzi za uhai wa
baba yake pia alipokuwa mdogo. Alikuwa akimsimulia Tunda vile wakati mwingine, wao
watatu walivyokuwa wakitoka pale na boti na kwenda kuvua samaki na kukaa huko
mpaka jioni. Alijifunza kuvua samaki akiwa bado mdogo tu. Ndio kitu alichokuwa
akipenda kufanya na baba yake pamoja na babu yake.
Familia
hiyo ya Cote pia ilikuwa na eneo lao la biashara kwenye bandari ndogo ya ziwa
hilo. Ambapo walikuwa wakisafirisha watalii kwenye ziwa hilo lililobeba
historia nyingi. Watalii walipokwenda kutembelea mji huo, walipenda kutalii
kwenye ziwa hilo ambapo kina Cote pia waliwekeza boti za kisasa zakutosha. Na
vyote hivyo viliachwa chini ya uangalizi wa Net.
Baada
yakuonyeshwa utajiri wote ule, Tunda akaelewa ni kwa nini Net alifurahia
alipojua Tunda ana mimba ya mtoto wa kiume. Alimwambia Tunda, kwao hawakuwa na
uzao mkubwa. Baba yake alizaliwa peke yake. Kwa babu yake walizaliwa wanaume
wawili tu. Cote ambaye ndio babu yake Net na kaka mtu ambaye naye alifariki
zamani sana alipokuwa vitani. Na wao wakazaliwa na Ritha. Wawili tu. Net na
Maya. Kwa hiyo akamwambia hata kama Tunda ataishia hapo, lakini angalau
anauhakika wa mrithi wake.
Ni
kweli walikuwa na eneo kubwa sana kuzunguka hiyo nyumba ya kihistoria. Kuanzia
getini mpaka kwenye hiyo nyumba, ilijipanga miti mingi sana kutengeneza
barabara ya kuzunguka uwanja wa mbele wa hiyo nyumba. Napo hapo mbele kulikuwa
na bwawa zuri lililokuwa likimiminika maji kwa muundo tofauti fofauti kutokana
bomba la katikati linavyozunguka. Majani na maua kuzunguka eneo zima, vilikuwa
nadhifu sana. Ungependa kuangalia au kukaa hapo. Kulipangiliwa vizuri sana.
Kasoro
Tunda alifika hapo kilikuwa ni kipindi cha baridi kuanza. Na kikawa kibaya
zaidi kwake yeye muoga wa baridi. Alipenda kusimama madirishani, akichungulia
nje. Labda awe na Net azunguke naye kidogo kisha warudi ndani. Tunda hakuwa
akiamini kama na yeye anaishi humo ndani. Macho na nafsi yake havikuwahi
kushiba thamani za humo ndani.
Ilikuwa
ni familia iliyojulikana kwa utajiri mkubwa na harakati za huyo bibi mgombania
haki za wanawake. Kila mtu alijua mke wa Net ndio atakula mema ya nchi na pengine
ndiye atakalia kiti cha bibi Cote. Kwa hiyo kila mtu alikuwa akimsubiria huyo
mke wa Net kwa hamu sana. Maya alishadharaulika kwenye jamii sababu ya tabia
zake za madawa ya kulevya na wanaume waliokuwa wakifuja pesa ya Cote kupitia
yeye Maya. Hata huko kutulia kwa safari hii, walishaambizana ni kwa muda tu. Wengi
walimtarajia kuja kumuona tena mtaani na madawa ya kulevya.
Tunda
alishatafuta nywele yakuvaa siku hiyo. Aliagiza human hair ya Indian Remmy.
Ilikuwa ni ya pesa yakutosha. Akatafuta saluni za watu weusi kwenye mji wa
jirani, akaenda kutengenezwa mbali kidogo na hapo kwa kuwa eneo hilo wengi
walijaa weupe. Nguo zake Maya ndio aliyeenda naye kutafuta.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilikuwa
siku ya jumamosi jioni ndipo bibi Cote alipotaka watu wafike nyumbani kwake.
Kulikuwa na ukumbi mkubwa na wathamani sana kwenye jumba hilo. Kama kawaida
walikuja watu wakupamba. Tunda alikwenda kuangalia ujuzi wa hapo pia. Akatoa
maelekezo namarekebisho, mpaka akaridhika, akatoka kurudi chumbani kupumzika
wakati anasubiria muda wa tafrija na Net arudi kutoka kazini.
Mkasa wa Kwanza wa Tunda
&Vic.
Tunda alingia na kujilaza kitandani,
akapitiwa na usingizi. Alishtuliwa na binti mrembo sana. Tunda akashtuka na
kukaa. “Wewe ni nani unayeingia chumbani kwangu bila ruhusa!?” Tunda akamuuliza
kwa mshangao. “Vic!” Tunda akakunja uso kwa hasira. Kwanza alimuamsha kutoka
usingizini. Pili ameingia chumbani kwake bila hodi! “Wewe ndiye mfanyakazi mpya
niliyeletewa?” Tunda alimfanyia makusudi, akijua wazi ni Vic aliyeambiwa habari
zake. “OooHoo! Noowo!” Vic akashtuka sana akijiangalia juu mpaka chini.
“Mimi
ni Vic! Vic!” Tunda akakunja uso. “Natakiwa kukufahamu!?” Tunda akamuuliza kama
anayeonyesha kupotezewa muda. “Mimi ndiye nilikuwa mpenzi wa Net.” Vic akajibu
kwa jeuri. “Oooh kumbe jina lako jingine ni Vic? Sikujua!” “Kwani wewe
unafahamu jina gani!?” “Chloe.” Tunda akamjibu huku akimtizama.
“Mimi
sio Chloe! Inamaana hakuna mtu aliyekwambia kama kuna Vic? Chloe hana hadhi
kama yangu! Ni watofauti kabisa. Mimi nimekuwa na Net tokea..” “Subiri kwanza.
Nyamaza kabisa. Huwa sipendi watu wanaongea sana. Sipendi kelele.” “Unamaanisha
nini?” “Nimekwambia unyamaze. Unaongea sana. Just hush and listen.” “Kwa nini
nikusikilize wewe?” Vic akauliza kwa
dharau huku akimtizama Tunda juu mpaka chini.
“Swali
zuri sana. Cha kwanza, umesimama ndani ya chumba changu na mume wangu. Umeingia
bila kubisha hodi. Hiyo ni dharau kubwa sana ambayo leo iwe mwanzo na mwisho.”
“Nilikuwa nikikilalia mimi hicho kitanda.” “Mbona umeshindwa kuendelea
kukilalia mpaka leo?” Tunda akamkazia macho. Vic akababaika.
“Umeshindwa,
na huna hadhi hiyo ndio maana mimi nipo hapa. Sasa nakuonya. Leo iwe mwisho
kuingia kwenye hiki chumba. Usithubutu kurudia tena.” “Utanifanya nini
nikirudia.” “Leo ndio itakuwa mwisho wako wakuingia kwenye hii nyumba na pale
getini. Kama unabisha, toka pale kwenye huu mlango, kisha rudi tena hapa ndani.
Nitakuonyesha mimi ndio Tunda Cote, mke wa Nathaniel Cote. Nijaribu tu kwa
hilo, nitakuonyesha. Na ninakuahidi, sijui nani tena!..” “Jina langu ni Vic.
Kila mtu ananifahamu.” “Kasoro mimi. Na hakuna aliyenitajia wewe kwa kuwa
hawakuoni kama ni wa muhimu humu ndani. Haya, toka kabla hujatolewa hapa na
askari.” Kimya.
Tunda
akasogea mlangoni. “Baada ya sekunde 30, nikishamaliza kukupa haya maelekezo,
uwe umetoka hapa. Na uende ukakae sehemu husika kama waalikwa wengine.
Nisisikie unazunguka humu ndani wala kutoa maagizo yeyote kwa mtu wa humu
ndani. Nenda ukapate huduma kama waalikwa wengine. Sio kwa Ms Emily wala Carter.”
Tunda akaendelea. “Kama ulilala na kucheza humu ndani, ujue ni wakati huo. Sasa
hivi Net ameoa, na anafamilia. Ukishindwa, ondoka kabisa. Maana sio lazima wewe
kuwepo kwenye tafrija.” Uzuri lugha nayo ilikuwa si ya kubabaisha kwa Tunda.
Akaongea kwa kujiamini mbele ya Vic, kama alivyofundishwa na bibi Cote.
“Haya
toka lasivyo baada ya sekunde 30 kuanzia sasa, nitaufunga huu mlango, nitakao
wafungulia ni askari tu watakao kutoa hapa na kukupeleka kituo cha polisi kwa
kosa la kuvamia chumba na nyumba yangu. Haya toka.” Vic akatoka pale alipokuwa
amesimama akaanza kusogelea mlango.
Mara
Maya akaingia huku akicheka sana nakumpiga picha Vic. Maya alikuwa akicheka kwa
sauti ya kukera! “Nitakutag picha zako facebook. Mungu amekuletea kiboko yako
Vic.” Maya aliendelea kumcheka mbele ya uso wake. “Wala simuogopi. Alinikuta
humu ndani.” “Wapi!? Wapi!?” Maya akaendelea kucheka. “Aibu zako Vic. Leo
umeingia aibu ya miaka! Buuuuu!” Maya akaanza kum buuu.
“Na
kwa taarifa yako, hawezi kunifukuza mimi.” “Si amekwambia ubaki hapa ndani
baada ya sekunde 30 anaita polisi? Kama kweli wewe jeuri mbona unaongelea hapo
nje? Ingia humu ndani ubishane na mimi uone jeuri ya mke wa Nethaniel Cote!
Mmiliki wa mali ya Cote. The one and Only. Tunda. Baem!” Akajigongeshea ngumi mikononi
mwake.
Yeye
aliingia ndani, Vic akawa ametoka nje ya mlango. Tunda amesimama mlangoni
anamsikiliza Maya, cha uchokozi. Akaendelea kumzomea kwa sauti huku akimcheka.
Ni kama naye Vic alikuwa ameshikwa na kibumbuazi. Kuondoka haondoki amebaki
amesimama. Amebadilika rangi akawa mwekunduuu. Alikuwa amependeza sana. Hata
Tunda aliona huo uzuri wake.
Wakati
Maya akiendelea kumzomea na kumkejeli, mara wakashtukia Net amesimama pale.
Maya akanyamaza kwa haraka akakimbilia nyuma ya Tunda. “Ni nini kinaendelea?” Akauliza
Net akiwa amekunja uso, anamtizama Vic. Akaanza kulia Vic. “Wamenidhalilisha.” Akaongea Vic kwa kujiliza
mbele ya Net. “Yeye ndio amemdhalilisha Tunda.” Akadakia Maya akiwa mgongoni
kwa Tunda, tena kishabiki. Ikabidi Net amgeukie yeye.
Akaanza
Maya. Pale pale mgongoni kwa Tunda. “Amemdhalilisha vibaya sana Tunda tena kwa
sauti ya juu mpaka ikabidi mimi nije kuangalia kulikoni kumbe ni Vic! Cha
kwanza na kibaya sana, ameingia chumbani kwenu Tunda akiwa amelala. Mimi
mwenyewe na Nana tulikuja tukataka kumsalimia Tunda, Nana akasema tumuache
alale kwa kuwa Carter alimpigia simu Nana kuwa Tunda anafanya sana kazi kule
ukumbini, Nana ampigie simu amwambie akapumzike. Sasa eti sisi tumemuacha Tunda
apumzike, yeye akamuamsha!” Net akakunja uso.
“Maya
anadanganya.” Akakanusha Vic. “Sasa kama huniamini mimi, muulize Tunda kama Vic
hajamuamsha na kumwambia kwamba hicho kitanda alicholalia yeye Tunda, alikuwa
akikilalia na wewe. Muulize Tunda.” Net alishtuka mpaka akawa mwekundu. “Umechanganyikiwa
wewe Vic?” Net akamsogelea na kumuuliza kwa ukali. “Na wala hajamwambia hivyo
tu.” Maya akaendelea kuchongea kishabiki.
“Amemwambia
Tunda mlikuwa mkifanya mapenzi hapo usiku kuc..” “Maya! Maya! Come out. NOW!”
Bibi yake akaja na yeye akamuwahi Maya.
Alijua Maya atazidi kuharibu. “Muongo,
sijasema hivyo.” Vic akabisha. “Nimekurikodi. Kama unabisha narusha sasa
hivi hewani naandika ‘Net alikuwa akikutumia tu lakini….”
Bibi Cote akaingia kwa haraka. Akamvuta Maya nje kwa kumshika mkono. Maya
akaanza kucheka wakati anatolewa pale.
Tunda
akafunga mlango kwa nguvu. Wakabaki wamesimama nje ya mlango Net na Vic. “Unashida
gani Vic? Kwa nini unataka kumvuruga Tunda?” “Maya
anadanganya Net. Ananisingizia.” “Nani amekwambia unaruhusiwa kuingia
chumbani kwangu na mke wangu?” “Nilikuja kumsalimia
tu.” “Hapana Vic. Lazima uheshimu hii nyumba. Sio kama zamani. Mimi
nimeoa, na ninampenda sana mke wangu. Unanielewa?” Vic akasikika akilia.
“Iwe
mwisho kuingia upande huu. Na ninaomba uwe kama wageni wengine. Ufike hapa nyumbani
pale unapokaribishwa na uishie sebuleni. Tafadhali sana.” Tunda akaondoka pale
akaelekea bafuni kuoga. Akajiridhisha na hilo onyo. Alitoka na kumkuta Net
ameinama pembeni ya kochi ameshindwa hata kukaa.
“Pole
na kazi.” Tunda akasalimia. Akanyanyua uso. Ulikuwa mwekundu na mishipa
imesimama kichwani. Tunda akamsogelea akiwa amejifunga taulo, akakaa pembeni
yake kwenye kochi. “Samahani sana Tunda. Usije kufikiri nilikuwa nikiishi
maisha yakihuni zamani. Vic nilikuwa naye pamoja. Hapa ilikuwa kama nyumbani
kwao. Wakati mwingine wazazi wake walipokuwa wakisafiri, walikuwa wakimuacha
hapa.” “Kama mpenzi wako au kama mtoto wa hapa?” Tunda akauliza.
Net
akanyamaza kidogo. Tunda akataka kusimama, akamshika mkono. “Vyote. Wengi
walijua yeye ndio angekuwa mke wangu.” “Wewe ulijua kama na yeye ndivyo
anavyojua?” “Ndiyo.” “Kwa hiyo ulimpa sababu gani yakubadili mawazo? Maana
mlikuwa mkilala naye hapa. Unasema tokea watoto. Iweje ghafla nafasi yake
aichukue mtu mwingine?” “Usiseme nafasi yake. Nani aliitamka kama hii ni nafasi
yake?” “Wewe kwa kufanya naye mapenzi humu ndani na kumtangaza kwa watu kama ni
msichana wako.” “Hiyo ilikuwa zamani sana Tunda. Hata kabla ya Chloe.”
“Net!
Ni sababu gani uliyompa?” “Kwanza alinisaliti. Alifanya mapenzi na mtu
mwingine.” “Yaani hiyo ndio ikawa sababu ya kuachana!?” Tunda akauliza kwa
mshangao. Net akatulia kidogo. “We Net? Inamaana hiyo ndio sababu?” “Sasa
ingekuwa nini kingine?” “Usinichezee akili Net. Mimi sio mtoto mdogo.” “Mungu
wangu ni shahidi.” Net akawa akijitetea kwa hofu hakutaka kuharibu siku hiyo
maalumu kwa historia ya hiyo familia.
“We
Net! Wapenzi wanakoseana. Hasira zikiisha wanarudiana. Wewe ulinikuta mara
ngapi na wanaume tofauti tofauti ukaishia kunioa? Kama ulinioa ukiwa na hasira
na mpenzi wako, hasira ikikuishia ukaamua kurudiana? Naomba usinipotezee muda
Net. Nishahangaika kwenye maisha. Sitaki uje uniumize. Na nilishakwambia,
nitakosa kila kitu isipokuwa wewe. Sijaja hapa kufuata mali ambazo kwanza hata
sikujua kama unazo. Nimekufuata wewe. Sasa hasira zakusalitiwa zikikuisha!?” Tunda
akambadilikia Net.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wageni wamaana, wakumbwa wa nchi na mji huo, vyombo vya habari
wanakaribia kujaza ukumbi kwa ajili ya utambulisho rasmi Mrs Cote/Tunda ambaye
Vic ameshamtibua. Wanandoa hao wapo chumbani, je nini kitaendelea? Usiache kujua
mikasa mizito mbeleni. Kama Vic aliweza kumudhuru Maya ili ampishe enzini,
atamfanya nini Tunda aliyemfukuza kwa kumdhalilisha vibaya hivyo! Usipitwe....
0 comments: