Story
iku hiyo ndipo walipoziona
pande zote za Masha waziwazi. Alifika kwenye mgahawa huo mdogo, ambapo
aliwakuta wenzake wote wamekaa nje, wakiwa wameagizia vinywaji vyao. Wote
walikunywa vinywaji visivyo na kileo, kwa sababu Mzee Mwasha alikuwepo.
Hakuna aliyethubutu kunywa pombe mbele ya Mzee Mwasha. Wote walimuheshimu sana
huyo mzee. Masha kama aliyehisi walichomuitia wazee wenzake, alivuta kiti,
akakaa bila kuonyesha tabasamu usoni. Hata muhudumu wao aliyezoea kuwahudumia
kila wawapo hapo, alipomuuliza kwa tabasamu ni kinywaji gani angependa kunywa,
alikataa, akabaki akiwangaalia, akitaka waongee haraka kwani anaharaka kuna
mahali anataka kuwahi mahali.
My Past - Sehemu ya 4.
S
|
iku hiyo ndipo walipoziona
pande zote za Masha waziwazi. Alifika kwenye mgahawa huo mdogo, ambapo
aliwakuta wenzake wote wamekaa nje, wakiwa wameagizia vinywaji vyao. Wote
walikunywa vinywaji visivyo na kileo, kwa sababu Mzee Mwasha alikuwepo.
Hakuna aliyethubutu kunywa pombe mbele ya Mzee Mwasha. Wote walimuheshimu sana
huyo mzee. Masha kama aliyehisi walichomuitia wazee wenzake, alivuta kiti,
akakaa bila kuonyesha tabasamu usoni. Hata muhudumu wao aliyezoea kuwahudumia
kila wawapo hapo, alipomuuliza kwa tabasamu ni kinywaji gani angependa kunywa,
alikataa, akabaki akiwangaalia, akitaka waongee haraka kwani anaharaka kuna
mahali anataka kuwahi mahali.
Mmoja wao, alianza kwa
hofu kidogo, ndipo wenzake wakaingilia kama kuchangia ili kuongeza nguvu kwa
Masha aliyekuwa akiendelea kubadilika kila sekunde waliyokuwa wakipokezana kumuonya.
Kama aliyejua, Mzee Mwasha alibaki kimya akimtizama Masha anavyobadilika rangi
ya mwili wake. Alitulia kimya akiwatizama wenzake wakimjia juu Masha, huku
akitamani kuwashtua na kuwaomba wapunguze jazba kidogo. Mapigo ya moyo ya Masha
yaliongezeka, akawa mwekundu usoni, akiwaka kama moto.
“Mmemaliza?” Masha aliyekuwa kimya
muda wote akiwasikiliza aliwauliza. “Kwa
kweli umetudhalilisha sana Masha. Wote tunaonekana hatuna maana.” Mmoja wao
alimalizia akanyamaza. “Naomba mniambie tofauti yangu mimi
na nyinyi ni ipi! Au leo ndio mnataka kuonyesha ulimwengu kuwa nyinyi ni
wakamilifu sana kuliko mimi? Au kwa kuwa nyinyi hamkubahatika kupata wanawake
wa nje waliotulia? Mimi sihangaiki na wanawake wengi kama nyinyi. Wewe Danny
nguvu ya kunisema mimi unaitoa wapi wakati unalala na wauza bar kila leo? Na
wewe Mwandri, sio wewe uliyezaa na sekretari wako ukamdanganya mkeo mtoto sio
wako? Wewe Banda ndio mchafu wakupindukia, au unafikiri hatujui tabia yako ya
kulala na wasichana wako wa kazi? Wewe mwenyewe ulinifuata ukiniomba nikusaidie
pesa ya kumuhonga yule msichana wako wa kazi aondoke pale nyumbani kabla mkeo
hajajua kama umempa mimba. Na wewe
Tomeo, nashauri ukapime UKIMWI, maana kila leo unaambukizwa magonjwa ya zinaa
na watoto wa chuo.” Masha
alianza kutaja dhambi ya kila mmoja wao.
“Hivi
leo nguvu yakuniweka kikao mnaitoa wapi nyinyi!? Anyooshe mkono hata mmoja wenu
aliyemkamilifu hapa na aliyekuwa na mwanamke mmoja tu. Mmekaa kunifuatilia mimi
na maisha yangu wakati na nyinyi ndoa zetu zimewashinda! Angalau aongee Mzee
Mwasha peke yake, ndio naweza kumsikiliza, lakini sio nyinyi, wapuuzi wakubwa.
Tena Danny nakudai pesa yangu. Jumatatu nikute risiti ya benki ofisini kwangu.
Kuonyesha umelipa yote. Narudia pesa yangu yote, Danny. Kadhalika na Banda vile
vile. Jumatatu nataka pesa yangu iwe benki. Sasa msifanye hivyo, ndipo
mtanitambua mimi ni nani. Narudia tena, PESA YANGU YOTE NINAYO WADAI, ninaitaka
kamili ifikapo siku ya Jumatatu.” Masha alikuwa akimgeukia mmoja baada ya mwingine.
Akamgeukia tena Mwandri,
akiwa amemkazia macho. “Lile ombi lako, nimefikiria naona
sitaweza kukusaidia. Na wewe Mzee Nyami, naona Banda yupo sahihi, haukopesheki.
Ameniambia huwa hulipagi madeni ya watu na sio mtu mzuri kufanya na wewe
biashara, ile tenda nampa yule jamaa wa kihindi, nafikiri ataifanya vizuri
kuliko wewe.”
Mzee Nyami alimgeukia Banda, aliyekuwa amenywea
kabisa. “Mzee Mwasha wewe
tutaongea kwa wakati wetu. Siwezi kuzungumza na wewe mbele ya hawa wapuuzi.”
Mzee Masha alitulia tena akiwatizama machoni kwa muda.
“Kuna
mwenye nyongeza? Au mlitaka kikao kingine kifanyike na wake zetu wakiwepo?” Aliuliza
kwa jeuri sana na kubaki akiwatizama machoni. “Kama hamna nyongeza, naomba niwahi kwenye majukumu yangu mengine,
niwaache nyinyi wasomi mkiongea na kupanga mambo yenu yakisomi.” Mzee Masha akasimama. “Na kama mnafikiria kuniondoa kwenye chama, naomba mpitie katiba vizuri
kwa ajili ya malipo yangu.” Aliwacheka kidogo,
akatingisha kichwa kisha akaondoka. Wote walikuwa kimya kabisa, hakuna hata
aliyejaribu kuongeza na kumtizama mwenzake machoni. Waliondoka hapo kila mmoja
na njia yake. Mzee Masha alirudi kwa Bella, akatulia kimya.
***********************************************
Bella aliendelea kutulia na kumtunza mdogo wake
kwa maadili yote, kama alivyolelewa na mama yake. Hakuwahi kujua kama dada yake
ananyumba wala kama anaishi na mwanaume yeyote. Alipokuwa akifunga shule,
walirudi kuishi pamoja kwenye ileile hoteli waliyokuwa wakiishi mwanzoni, pale
walipopelekwa na dereva wa Zera, Kasimu. Bella alisafiri na mdogo wake nchi na
sehemu tofauti tofauti kipindi cha likizo yake, lakini Mzee Masha akiwepo
kwenye ndege nyingine. Kama ni hotelini, walichukua vyumba viwili tofauti,
ambacho Bella alilala na Mzee Masha na Eric alilala peke yake. Lakini Bella
alihakikisha Eric hakutani na Mzee Masha hata kidogo endapo wanakuwa naye
safarini. Ni sharti alilokuwa amemuwekea Mzee Masha, naye hakuwa na shida
kabisa na hilo, ilimradi kila safari wanakuwa pamoja na kuhakikisha Bella
analala kitanda anacholala yeye. Amani ilikuwepo.
Kwa kuwa Eric alikuwa na msingi mzuri wa shule,
alijikuta haendani na darasa la sita alilotakiwa kuwepo katika shule hiyo.
Walipokuwa wakifanya mtihani wa darasa la saba, na yeye alipewa namba na
kufanya mtihani huo. Alifaulu vizuri, na kuendelea kidato cha kwanza katika
shule ileile. Kwa hiyo Eric alirushwa darasa moja, kitu kilichomfurahisha zaidi
Bella. Alijitahidi sana katika masomo na michezo. Alikuwa akitegemewa na shule
yao, upande wa mpira wa kikapu. Alikwenda mikoa mbali mbali kushindana na
alipokuwa nyumbani, Bella alimtafutia mwalimu wake binafsi wakumfundisha mchezo
huo. Eric alianza kutoka nje ya nchi kwenda kushindana hasa mpira wa kikapu.
Mat naye hakuwa mbali kwenye malezi yake, walimuheshimu kama kaka yao, na Mzee
Masha alimkubali Mat kuwa ndiye ndugu wa pekee wa Enabella na Eric, sio mtu
mwingine.
***********************************************
Mama Masha alibakiwa na njia moja tu ya watoto
wake hao wawili kama kinga yake. Kwani hakuna aliyeweza kumkalisha mumewe
kuongea naye ili kuweza kunusuru ndoa yake. Alijua ni jinsi gani Mzee Masha alivyopenda
watoto wake, kwa hiyo akaendeleza tabia ya kurudi nao Tanzania hata kama watoto
hawapo likizo. Walirudi wote pale mama yao alipojisikia ili kumfanya Mzee Masha
akose muda na Bella awe analala nyumbani au angalau awe anapata naye muda, hata
wakuzungumza jambo lolote. Kwani alipokuwa akirudi peke yake nyumbani, Masha
hakuwa akionana naye kabisa. Hata kama atamfuata ofisini, Masha alimjibu kwa
kifupi na kuondoka na kumuacha mama huyo ofisini kwake yeye Masha. Akiwa
hajakasirika, alikuwa akimuacha na maelezo. Wakati mwingine alimuacha pale pale
ofisini kwake na kumwambia anakwenda sehemu fulani ana kikao na anaweza
asimuone tena mpaka anapoondoka nchini. Lakini kila anapokuwa na watoto nyumbani, hapakuwa na uongo wakuwaeleza
watoto wake, au sababu ya kuwaambia wanae kuwa hataweza kulala au kuwepo
nyumbani wakati na wao ndio wamerudi nyumbani kwa ajili yake.
Watoto wenyewe walikuwa wakikubaliana na wazo la
mama yao la wao ndio wawe wanarudi nyumbani Tanzania kumuona baba yao, kwani
Mzee Masha alipunguza sana safari za kwenda kuiona familia yake. Alikuwa akitoa
udhuru wa mara kwa mara, kwamba hataweza kwenda kuwatembelea nchini Uholanzi.
Mama Masha alimtumia mwanae Zera, ambaye ndio kipenzi cha baba yake, kumfanya
awe bize na familia, na kushindwa kurudi kwa Bella. Na kweli Zera alifanikiwa
kumbana baba yake.
***********************************************
Likizo moja kubwa ya kina Zera, walirudi na mama
yao pia akiwa amechukua likizo, wakarudi Tanzania kwa mapumziko hayo. Zera alimganda
baba yake ipasavyo. Alimfuata baba yake kila mahali, akimwambia baba yake ni
jinsi gani alivyokuwa akitamani likizo hiyo ifike, ili arudi nchini ili awe naye.
Walisafiri kama familia kwenda kwenye vivutio mbalimbali hapo hapo nchini.
Wakati wote Zera alikuwa na baba yake. Na kwa kuwa kipindi cha nyuma alikuwa
akienda naye mpaka ofisini kwake, hata aliposema anataka kwenda ofisini, Zera
alimuomba awe anaenda naye. Zera ni mtoto aliyekuwa na malezi yakudekezwa
vibaya. Masha alikuwa mkali kwa kila mtu, lakini si Zera. Walipendana na baba
yake, na alipewa kila anachotaka. Hakuwahi kutaka kitu asipewe. Kwa hiyo mama
yake alimtumia vizuri sana.
Kilikuwa kipindi kigumu sana kwa Mzee Masha.
Hata mawasiliano na Bella yakawa yashida sana. Alikuwa kimwili na familia yake,
lakini mawazo yalikuwa kwa Bella wakati wote. Kila akikumbuka uzuri wa Bella,
mambo anayomfanyiwa na umri ule mdogo alionao, alijua lazima Bella atamtafutia
msaidizi. ‘Bella ni mtundu mtundu sana wa mambo ya kompyuta. Anaweza kuchezea
zile kamera pale nyumbani, nisijue ameingia nani pale, au anawasiliana na nani. Watanichukulia
yule mtoto!’ Mzee Masha alikuwa akiwaza usiku huo akiwa amelala na
mkewe, kwenye hoteli hiyo ya watalii Serena Safari Lodge Ngorongoro.
Vyumba vyao vilikuwa karibu karibu sana wao na
watoto wao, hakuna jinsi wangegombana hotelini hapo, watoto wao wasiwasikie, au
wasijue. Kwa hiyo Mzee Masha ilimbidi awe mpole ili kutunza heshima kwa watoto
wake. Wakati huo akiwaza juu ya Bella, huku mkewe naye akiwaza jinsi ya kumbana
ili aachane kabisa na hiyo nyumba ndogo yake, ambayo bado hakuwa akijua kama ni
Bella.
Mwishowe akapata wazo. “Nimemuandikia barua raisi kutaka kuacha kazi.” Mama Masha
alimgeukia mumewe. Mzee Masha alikaribia kuchanganyikiwa. “Kwa nini unaacha kazi?” “Nimeamua
kurudi kukaa nyumbani, ili tusaidiane mambo ya hapa.” “Umechanganyikiwa nini!? Na shule za watoto? Junior ndio amekubali
kusoma, ameingia chuo sasa hivi, huko hana makundi mabaya, unataka umrudishe
tena huku ili iweje? Utakuwa unawazungusha hao watoto mpaka lini? Wewe mwenyewe
uliitaka hiyo kazi, ukasema ndio zilikuwa ndoto zako, umechukua watoto wote,
sasa hivi tena unataka kurudi! Acha kuchanganya watoto.” “Hiyo kazi sio muhimu kama ndoa yetu, Masha.
Najaribu nione kama naweza kunusuru hii ndoa.” “Aliyekwambia hii ndoa ipo
matatizoni ni nani? Wewe ndio unakuza matatizo. Kama ingekuwa kuna tatizo,
ningekuwa nimelala hapa na wewe?” “Kama hakuna tatizo, mbona hata hujanigusa
tokea nimerudi? Ni muda gani tangia tumefanya tendo la ndoa mimi na wewe, Masha?
Unakumbuka mara ya mwisho niliporudi nyumbani, tukawa mimi na wewe tu? Ulikuwa
unaniacha usiku kitandani, unaondoka bila kuaga. Wakati mwingine ulikuwa
unarudi na wakati mwingine nilikuwa nikiondoka nchini bila hata kukuona tena.
Nikikupigia simu kuomba tuonane ili tuagane, unaniambia niondoke tu utakuja
kutuona, lakini unaishia kutoa udhuru. Kweli huoni kama kuna tatizo?" “Kwa hiyo unafikiria hayo yote yatabadilika
kwa wewe kuacha kazi na kurudi kukaa nyumbani? Kama sio upumbavu huo ni nini?
Unajiangalia wewe tu, umefikiria watoto lakini?” “Nitarudi na Zera, Junior atabaki hukohuko amalizie chuo.” “Umuache Junior
kule bila ungalizi wowote, eti kwa kuwa wewe unataka kuja kulala na mimi! Acha
upumbavu Matha.” “Sio kulala na wewe tu, Masha.” “Sasa ni nini kama sio akili mbovu hiyo? Huwezi kumuacha Junior huko.
Nenda kesho ukaongee na huyo bosi wako umwambie umebadili mawazo, unataka
kurudi kazini.” “Sitafanya hivyo Masha, mpaka utakapo nihakikishia kuwa
utamuacha huyo msichana uliye naye, na
uniahidi mbele ya watoto kuwa tutakaporudi safari hii nyumbani, Dar, likizo
ikiisha, tutarudi wote Uholanzi ukakae na sisi kwa muda, halafu utakuwa unakuja
kututembelea mara kwa mara. La sivyo
ni heri kuwaambia watoto ukweli kwamba umepata mwanamke mwingine, ambaye
umeamua utuache sisi ili uishi naye huyo mwanamke.” Mzee Masha alishtuka
sana. Mama Masha alivyoona hivyo, alifurahi sana, akajua ameshampata mumewe.
Akasimama na kuanza kubadili nguo zake. Alianza
kuvua nguo za kulalia na kutoa nguo zake za kawaida, akaanza kuvaa. “Kwa nini unabadili nguo? Unaenda wapi?”
Mzee Masha alikaa. “Mapokezi.” Mama
Masha alijibu kwa kifupi huku akivaa viatu vyake. “Kufanya nini usiku huu?” “Kuchukua chumba kingine, ili kukupa nafasi
ya kufikiria. Hata hivyo nakaa humu ndani nafanya nini?” Kama Mshale Mzee
Masha alikimbia mlangoni.
“Hivi
wewe ukoje, Matha? Unafikiria kweli wewe au unataka kusambaratisha hii familia?
Umefikiria watoto lakini? Unafikiri Zera ataelewaje?” “Hivi hayo maswali
unaniuliza mimi au unajiuliza wewe, Masha? Kama ungekuwa unafikiria hata mmoja
wetu, kati yetu, usingefanya unayoyafanya.” “Hebu rudi bwana! Acha
ujinga. Unataka kuchanganya watoto tu.” “Hawawezi kuchanganyikiwa, watajua
ukweli halisi wa maisha uliyoyachagua.” Mzee Masha alibaki mlangoni akiwaza
kama usiku ule ndio iwe kweli ndio mwisho wa ile ndoa, na yeye atoe siri
aliyokuwa ameificha ya mkewe, au anyamaze mpaka atakapokamilisha uchunguzi wake
na kuwa na uhakika na kila kitu, ndipo awaambie watoto na kuwapa sababu ya
kuachana.
Alibaki akifikiria huku akiumia roho, mwishowe
akakubali yaishe kwa usiku huo. “Hebu
acha ukorofi, rudi tulale.” “Hapana Masha. Umenitesa na kunidhalilisha vyakutosha.
Kila mtu ananicheka! Kwa nini hutaki watoto wajue ukweli?” Mama Masha alijidai akilia baada yakuona amefanikiwa kumbana
mumewe kwenye kona. Ni kweli alifanikiwa kumbana vizuri sana usiku ule. Alimuona
vile Masha alivyotulia, akajua amemkamata vizuri sana, bila kujua mumewe ana akili
sana. Bado alikuwa akimtengenezea kosa lakueleweka, ili hata akimwambia
anamuacha ashindwe kwenda kudai mali mahakamani. Hakutaka siku atakayompa mkewe
talaka, asipate hata shilingi yake. Alimjua jinsi mkewe alivyo na akili.
Alimpangia mipango yote kwa tahadhari sana, huku akichunguza kila kitu, na
kukusanya ushahidi wakutosha.
Mama Masha alibaki amesimama huku akilia. “Naomba
nipishe nikalale.” “Huo ni ukorofi, Matha. Umesema nifikirie. Hata
dakika tano hazijapita unaondoka! Wewe vipi?” Mara walisikia mlango unagongwa. “Unaona sasa?” Mzee Masha alistuka sana. “Hebu nenda bafuni, watoto wasikukute hivyo.” Mzee Masha
alinong’ona. “Hey mama! Is everything
okay?” Walimsikia Zera akiongea mlangoni. Wote walinyamaza kimya. “Mjibu sasa?” Mama Masha alimfokea Mzee
Masha. “Yes babygirl.” Mzee Masha alijibu. “Can I talk to Mama?” Zera aliuliza,
lakini kulikuwa kimya ndani. “Dad?”
Walimsikia Junior naye kipenzi cha mama yake akiingilia maongezi baada yakuona
kimya ndani ya chumba cha wazazi wao. “Sure!”
Mzee Masha alijibu huku akibabaika, na mkewe akimtizama. Alibaki amesimama mlangoni
bila kufungua mlango. “Dad?” “Am here
Son!” “Can we talk to mama, please?”
Junior alirudia tena, lakini safari hii alisikika akimaanisha. “Yes, why not?” Masha alijibu. “Open the door, then!” Zera naye akaongeza
wakiwa wanashangaa ni kwa nini baba yao hafungui mlango.
Ilibidi Masha afungue mlango, watoto wakaingia
wakiwa na nguo zao zakulalia. Wote walishangaa kumuona mama yao amevaa nguo
ambazo sio za kulalia na ameshika pochi yake. Junior akamsogelea. “Unaenda wapi usiku huu!?” Mama yao
alibaki kimya. Junior alimgeukia baba yake. “Where
is she going, Dad!?” “Mama yenu haendi mahali popote.” Mzee Masha
alijibu kwa kifupi. “Nyinyi rudini
mkalale. Kila kitu kipo sawa.” “Unauhakika dady?” “Kabisa. Hakuna mahali mama
yenu anaenda. Kila kitu kipo sawa kabisa.” “Sidhani dady.” Junior aliongea
akionyesha mashaka usoni.
“Nilimuona juzi tukiwa nyumbani, mama alikuwa akilia sana chumbani
kwenu. Nilifunga mlango taratibu nikamuacha. Mama amebadilika, hana furaha kama
zamani. What did you do to her?” Junior alimuuliza baba yake. “Na usitudanganye dady. Maana huu ni usiku,
na anaonekana anataka kuondoka, tena peke yake. Umemfukuza?” “Hapana. Hapana
kabisa. Wewe unajua siwezi kumfukuza mama yenu.” “So what’s going on daddy?”
Zera kipenzi cha baba yake aliuliza. “Kwa
sababu hata sasa analia.” Zera aliongeza. Junior alimsogelea mama yake. “Kuna nini mama? Unataka twende wote
chumbani kwangu ukatulie kidogo? Kama unataka kwenda mahali nitakusindikiza,
siwezi nikakuacha ukazunguka peke yako usiku.” Junior alijaribu kuongea na mama
yake kwa upendo akimbembeleza.
“Daddy?” Zera aliita kwa hasira kidogo. “Umemfanya nini mama? Unajua jinsi mama alivyo. She has been always
there for all of us, including you dady. Hajawahi kutuacha wakati wowote ule. Ana
kazi nyingi sana kule Uholanzi. Lakini
anajitahidi kuhudhuruia shuleni kwangu kila anapoitwa au ninapomuhitaji.
Hajawahi kukosa shuleni kwangu au kwenye michezo yangu. Lakini wewe umekuwa
ukiniambia huwezi kuja. Unakumbuka nilikwambia nimechaguliwa kuingia kwenye
kundi la waogeleaji natakiwa kwenda kwenye shindano katika mji wa Brussells,
nikakuomba uje, ili twende ukaone ninavyoogelea? Ukaniambia una kazi nyingi
hutaweza kuja. Mama alikuwa na mkutano mahali, lakini akaahirisha, akasafiri na
mimi. Nilitegemea hata ungenipigia simu uniulize iliendaje, lakini hukuonyesha
kujali hata kidogo.” Zera akaanza kulia.
“Nilishinda.
Kila mtu alinipongeza kasoro wewe, daddy. Nimeingia kwenye timu kubwa sana kule
kwenye ile nchi, na wamesema nikijitahidi zaidi naweza kuingia kwa washindanaji
watakao enda kwenye mashindano ya kombe la dunia. Haunijali tena siku hizi.
Hujui naendeleaje, hujui naishije tena. Unakumbuka wakati tunaishi hapa, wewe
ndio ulikuwa unanipeleka kwenda kujifunza kuogelea? Sasa hivi hujali tena! Na
mama amekuwa na kazi ya kukutetea kwa kila jambo. Kila tukimlalamikia juu yako
anatuambia unakazi nyingi. Lakini tunataka utuambie ukweli daddy.” Mzee Masha alibaki kimya kabisa. “What’s going on
daddy? Tell us the truth.”
Kumbe Zera alikuwa na
uchungu mkubwa sana moyoni mwake. Alipata muda wakutoa dukuduku lake.
“Twende mama ukapumzike.” Junior alitaka kuondoka na mama yake, baada ya
kuona baba yake amebaki kimya anashindwa kujibu. “Ngoja kwanza Junior. Huwezi kuondoka na mama yako. Tulipishana tu
kidogo. Nilikosea, na ninaomba msamaha kwenu wote. Kazi zilikuwa nyingi, naona
nimelemewa. Likizo yenu itakapoisha, tutarudi wote Uholanzi, nitakaa na nyinyi
kwa muda ndipo nitarudi huku. Sitamuachia tena mama yenu majukumu yote ya
kuwalea. Zera, naomba unisamehe, na hongera sana. I am alywas proud of you,
sweatheart. Don’t you ever forgert that. Come here.” Alimkumbatia Zera. “Umenisamehe?” Mzee Masha alimuuliza
Zera. Akiwa na tabasamu, Zera alitingisha kichwa. Walibaki kimya kwa muda, kila
mtu akiwaza lake.
“Mkapumzike sasa. Tutaongea vizuri kesho.” Mzee Masha alivunja
ukimya. “Thanks dad!” Junior
alishukuru. “I mean it. Najua unaacha
kazi zako nyingi ili uwe na sisi, na wakati wote umejitahidi kuweka mazingira
ya sisi kujisikia tuna wazazi wanao tupenda na kutujali. Umejenga familia moja
na yenye nguvu. Asante sana.” Junior akamsogelea baba yake na kumpa mkono.
Yale maneno ya Junior yalikuwa ni hukumu kubwa sana moyoni kwa Mzee Masha,
lakini hakujua chakufanya, na Bella yupo nyumbani akimsubiri. “You are welcome Son!” Mzee Masha
alijibu kwa kifupi tu, huku akifikiria.
Junior alimsogelea mama
yake akambusu. “I love you mama.” “I know
Junior.” Mama Masha alitabasamu. “Ulale
sasa, kesho nitakusindikiza unakotaka kwenda, lakini sio usiku huu.” Mama
Masha alicheka kidogo. “Okay.” Zera
alimbusu mama yake na baba yake kila mmoja akarudi kulala chumbani kwake. Mzee
Masha alirudi kukaa kwenye kochi akifikiria. Mama Masha aliingia bafuni akarudi
na kupanda kitandani akiwa na furaha zote, kwa kuokoa ndoa yake. Nikweli ndoano
aliyoitupa safari hii, ilimkamata Masha vizuri sana. Alijua hawezi kubadilika
tena, kwani ameshaahidi mbele ya wanae.
Mzee Masha aliiangalia simu yake kama anayetaka
kuitumia. ‘Bella!’ Mzee Masha aliendelea kuwaza huku akikuna
kichwa. Kila alipojaribu kubadili mawazo, alimuona Bella akiwa amelala peke
yake akimsubiri. Umbile la Bella liliendelea kumsumbua akilini mwake. Alichukua
simu, akataka kutoka nje kumpigia Bella aliyejua kumliwaza wakati wote, lakini
alisita mlangoni. Alifikiria kutupilia mbali shutuma juu ya mkewe, ili angalau asimpoteze na Zera, lakini
alijua lazima afanye maamuzi yakumuacha Bella kwanza kama anataka familia yake.
Akabaki akiwaza pale mlangoni.
Mwishowe aliamua atulie
kwanza, ajipe muda wakufikiri, huku akijikumbusha vile Bella alivyotulia. ‘Bella
atanisubiri tu. Natakiwa kujipanga upya.’ Aliendelea kuwaza. Akaamua
kuzima ile simu na kurudi kulala kitandani, mkewe alikuwa akimsikiliza kila
anachofanya. Alifurahi sana alivyomuona hajatoka, na kuamua kurudi kulala.
Alijivuta taratibu pembeni ya kitanda, mbali kidogo na Mzee Masha. Mzee Masha
alivuta shuka vizuri, akamfunika mkewe.
“Asante.” Mama Masha akashukuru kwa sauti ya chini kidogo. “Nilijua umeshalala.” “Ndio nataka
kulala.” Mzee Masha alijilaza vizuri, huku akitamani mambo yake na mkewe
yangekuwa kama zamani, angalau angefanya naye mapenzi usiku ule, lakini akili
yake ilishavurugika, mkewe alimchanganya sana. Moyo wake ulishindwa kabisa
kumpokea tena mkewe.
Kadiri siku zilivyokuwa zikidizidi
kwenda tokea agundue ubaya wake na kushindwa kuzungumza naye au kumuuliza juu
ya ubaya huo aliougundua, ndivyo alivyozidi kuwa mbali na mkewe kihisia.
Alijikuna akimkinahi gafla. Hataki hata amguse. Kushiriki naye kitanda kimoja
tu, ile kujua yupo pembeni yake usiku kucha, ikaanza kuwa ngumu pia. Akaanza
kumkwepa kitandani au chumbani. Ikawa kama wanapeana zamu kuingia kwenye chumba
chao. Akimuona mkewe anaingia hapo chumbani, yeye alitoka kwa haraka kama
aliyefukuzwa. Lakini watoto walimbana usiku huo, hakuwa na jinsi. Masha
aliendelea kuwaza huku akimtizama mkewe aliyekwisha kupitiwa na usingizi.
***********************************************
Mambo yalikuwa yamemfika
shingoni Mzee Masha, familia anaitaka na Bella asingekubali kumuachia hata
iweje. Usingizi uligoma kuja kabisa. Bella ni kitu cha thamani ambacho wakati wote
amekiri hakijawahi kumtokea maishani mwake. ‘Labda nipunguze muda na Bella ili nipate muda na familia yangu.
Nikimuacha mke wangu ndio nimempoteza Zera pia. Hatanisamehe akija kujua kama
ninaishi na Bella. Inabidi kuacha kuonekana na Bella kila mahali. Nitamfanyaje
Bella? Yaani nimuache Bella hapa nchini halafu nikaishi Uholanzi! Haiwezekani hata kidogo. Niende naye?
Haiwezekani, anakaribia mitihani. Watanipora Bella hapa mjini.’ Mzee
Masha alikesha akiwaza. Alimuonya Bella asimpigie simu hata iweje, yeye ndiye
atakuwa akipiga. Kwa hiyo Bella wala hakuwa akimpigia.
Siku inayofuata ilikuwa
ni siku ya familia tu. Wote walikubaliana kuzima simu na kuziacha hotelini ili
wapate muda wa peke yao, wakati wanazunguka mbugani. Kwa hiyo kwa siku nzima
Mzee Masha hakuwa ameongea na Bella, na jioni waliporudi hotelini, waliweka
movie nzuri sana chumbani kwa Zera, wakawa wanaangalia wote. Hakupata mwanya
wakutoka na kwenda kupiga simu, na walipoingia chumbani kulala ndipo mkewe naye
akaanza kumkaba na maneno mengi na mipango mingi ya watoto hasa Zera. ‘Bella wangu jamani…’ Mzee Masha
aliendelea kuwaza. ‘Sijui ana hali
gani!?’ Walikaa huko siku nne ndipo waliporudi nyumbani.
Hapakuwa na mawasiliano yoyote kati yake na Bella.
Walipofika tu nyumbani,
kutokea uwanja wa ndege, Mzee Masha aliaga akisema anataka kwenda kazini. “Tunaweza kuongozana wote Dad?” Junior
aliuliza. “Naenda mara moja tu na kurudi,
sitachukua muda mrefu, kuna kitu nataka kuangalia.” Junior alikunja uso. “Unanikwepa?” “Nooo. Kwa nini unafikiri
hivyo?” “Nauliza tu.” “Hapana kabisa Junior, nilifikiri utakuwa umechoka,
nilitaka upumzike halafu kesho ndio tungeweza kwenda wote.” Junior alibaki
akimwangalia kwa kumsuta. “Lakini kama
unataka kwenda, tunaweza kwenda wote tu Junior.” “Hapana, naona kama leo sio siku nzuri kwako, ya kwenda na mimi. Wewe
nenda tu. Tutakwenda wote wakati mwingine.” Junior aliondoka kwenda
chumbani kwake, Zera akafuata, na Mama yao akaondoka, wakamuacha Mzee Masha
peke yake sebleni. Alikaa pale kwa muda, akaamua kutoka nje kupiga simu kwa
Bella badala ya kwenda.
***********************************************
Yalikuwa ni mapumziko ambayo Bella alikuwa
akiyatamani kwa siku nyingi sana lakini hakuyapata. Kuwa mbali na Mzee Masha,
au hata kutosikia sauti yake, yalikuwa mapumziko makubwa sana kwake. Aliweza
kulala vizuri na kujisomea bila shida yeyote. Alikuwa amejilaza wakati Mzee
Masha akimpigia simu. “Umelala na
nani?” Hiyo ndio ilikuwa salamu yake mara baada ya
Bella kupokea simu. “Nipo peke yangu T. Mzima?” “Ulikwenda wapi na wapi?” “Mbali na chuoni,
sijakwenda popote, nilikuwa hapahapa nyumbani nikijiandaa na mitihani. Kwani
wamekwambia wameniona wapi?” Mzee Masha akanyamaza kwa muda. “Vipi T? Mzima?”
“Mzima, mambo yamekuwa mengi tu.” “Utakuja kuniona leo?” “Nitakuja kukuchukua
kesho nikupeleke chuoni.” “Tupo karibia na mitihani T, ratiba imebadilika.
Wakati mwingine walimu wanaingia darasani na wakati mwingine hawaji. Kama huyo
wa kesho asubuhi amesema hatakuja, na kipindi kingine ni mchana.” Mzee Masha akanyamaza. “T!”
“Nipo.” “Utakuja asubuhi au hiyo mchana?” “Nimekwambia nitakuja Bella. Una
wasiwasi gani? Au unataka kwenda kwa wanaume zako?” Bella akanyamaza.
“Unanyamaza
kwa kuwa unajua naongea ukweli? Nimeondoka siku tano tu, umeshaanza kurukaruka
na wanaume wengine!” “Tafadhali T, naomba tusianze kugombana kwa vitu visivyo
vya kweli. Umeniacha kwa siku zote hizo, bila hata kunipigia simu au hata
kunitumia ujumbe kunijulia hali yangu, uko na mkeo. Sijalalamika, wala sijatoka
humu ndani zaidi ya kwenda chuoni. Badala tuongee vizuri, au hata kujua hali
yangu, unanipigia simu na kuanzisha ugomvi! Kwa nini unanifanyia hivyo?” Mzee Masha alinyamaza kwa muda. “Nitakuona
kesho Bella.” Mzee Masha aliongea kwa
aibu, na kukata simu. Akarudi ndani, akakuta mkewe na wanae wote wapo jikoni. ‘Daah!
Watoto wote wameungana na mama yao! Nisipoangalia hata Zera nitampoteza.’ Mzee Masha aliwaza wakati akiingia
jikoni kuungana na familia yake.
“Mkasa wa Bella.”
Siku inayofuata Mzee
Masha alishindwa kutoka kabisa nyumbani. Aliingia chooni na kumtumia ujumbe
Bella, aache gari nyumbani, dereva atakwenda kumchukua ampeleke chuoni, halafu
yeye atakwenda kumfuata. Bella hakuwa na neno. Alijibu kwa kifupi tu ‘Sawa.’ Akiwa amekaa darasani
ameinamia kompyuta yake anajisomea, alimsogelea kijana mmoja aliyekuwa ameanza
naye chuo tokea mwaka wa kwanza. Wote walidhani Bella hawafahamu, lakini Bella
alishawasoma tabia zao wote, na alikuwa akiwafahamu vizuri sana, kila mmoja kwa
jina na tabia.
Yule kijana alimjua ni
mstaarabu. “Samahani Enabella, naomba
uniazime simu yako.” Bella alinyanyua macho na kumtizama kwa muda, huku
darasa zima likitaka kusikia Bella anajibu nini. Hapakuwa na mwalimu darasani,
kwani hata mwalimu aliyeahidi angekuja, hakuja. Kwa hiyo Bella alibaki pale
darasani akimsubiria Mzee Masha aje amchukue kama alivyoahidi. Bella alibaki
akimtizama na macho yake makubwa na yakurembua. “Ni kitu cha msingi sana dada yangu, nisingekuomba. Nimeshaomba watu
kadhaa wa hapa darasani, wanisaidie lakini simu zao hazina hela.” Bila ya
kujibu, Bella aliingiza mkono mfukoni akatoa simu na kumkabidhi yule kaka.
Alitoka nayo nje, baada ya muda akarudi na kumrudishia Bella simu yake. “Asante.” Alishukuru lakini Bella
hakujibu kitu, alipokea simu yake na kuirudisha mfukoni.
Bella alingalia saa,
akaona muda wa kuja kuchukuliwa umefika, akanza kukusanya vitu vyake atoke.
Wakati anakusanya vitu vyake arudishe kwenye begi lake, ujumbe uliingia kwenye
simu. ‘Bado
nipo kwenye kikoa. Hata hivyo hali yangu ya kifedha sio nzuri kwa sasa.’ Bella aliposoma vile
akamuhurumia sana Mzee Masha. ‘Labda
ndio maana amepotea kwa kuwa hana pesa!?’ Bella aliwaza akaamua
kumjibu. ‘Usijali
mpenzi wangu juu ya pesa, mbona mimi bado ninazo? Tutatumia za kwangu.
Nakusubiri kwa hamu.’ Alipomaliza kujibu, akarudisha ile simu kwenye mkoba wake, kwa
bahati mbaya ikabonyeza sehemu ya ‘silence’ kuzima sauti. Bella akijua
Mzee Masha atachelewa, akarudisha vitu vyake mezani na kufungua kompyuta yake
na kuanza kujisomea tena.
Mzee Masha alifika nje
ya chuo na kumpigia simu Bella kama kawaida yake, lakini Bella hakupokea kwa
kuwa haikuwa na sauti, kwa hiyo hakusikia. Na Bella naye hakuwa na wasiwasi
wakuitazama simu yake, kwani alijua kama Mzee Masha angefika pale angempigia simu
ili atoke. Akabaki amekaa akijisomea.
Mzee Masha alimpigia
simu tena na tena lakini Bella hakupokea. Hasira zikaanza kumpanda Mzee Masha,
kwani hata kufika pale, alitumia uongo mwingi sana, ili kuwatoroka wanae. Bella
alipoona muda unazidi kwenda bila Mzee Masha kufika na njaa ilikuwa ikimuuma
sana, akaamua amtumie ujumbe, kumtaarifu atachukua taksii kurudi nyumbani. Na atakapo
pata muda amfuate nyumbani waongee zaidi. Kutoa simu yake, akakuta Mzee Masha
alimpigia simu zaidi ya mara kumi na ilishapita nusu saa. Bella alianza
kubabaika.
Akachukua vitu vyake
harakaharaka na kukutoka darasani kumuangalia Mzee Masha kwani aliogopa kupiga
simu kama alivyokuwa amemuonya. Bella aliangalia kulia na kushoto, hakuona gari
la Mzee Masha. Kwa kuwa wasiwasi ulishamwingia, akachukua taksii kurudi
nyumbani, akijua wazi Masha atakuwa ameshaondoka kwani huwa hapendi kusubiri.
Alifika nyumbani lakini
Mzee Masha hakuwepo. Alibaki na wasiwasi sana. Alikaa akimsubiria Mzee Masha
apige tena, lakini hakupiga. Akaamua kuingia bafuni aoge. Akiwa bafuni kwake
anaoga akasikia mtu ameingia chumbani kwake. “T! Ni wewe T?” Bella alipoona kimya, akaamua ajifunge taulo atoke
akaangalie. Alimkuta Mzee Masha amesimama anaangalia simu yake. Bella alisogea
karibu. “Pole nimekuta umenipigia sana,
simu ilikuwa kwenye ‘silence’ ndani ya mfuko wa kompyuta.” Bella alipigwa
kibao cha nguvu akaangukia kitandani. Kabla taarifa hazijamfikia kichwani na
kuelewa kinachoendelea, Mzee Masha alichomoa mkanda wa suruali yake, nakuanza
kumchapa nao Bella kama anaua nyoka.
“Unataka kuniua na pesa zangu? Nimeondoka hata siku saba
hazijaisha, umeshatafuta wanaume wakuwahonga pesa zangu! Unachotafuta ni nini
wewe Bella!? Unataka nikupe nini ili uridhike?” Mzee Masha aliendelea
kumpiga Bella, bila kupumzika. “Unanidanganya
upo chuoni, kumbe umetoka kwenda kwa wanaume zako! Nimekufuata mpaka darasani
kwako, wakaniambia uliondoka muda mrefu. Nitakuuwa Bella. Huwezi kuja kuniua na
UKIMWI. Ulitumia kondom na huyo mwanaume?” Mzee Masha alikuwa akiongea huku
akimpiga Bella.
“Nitakuuwa Bella, niambie ukweli. Ulikuwa ukitumia kondom?” Aliendelea kumpiga Bella
kwa hasira sana. Alimnyanyua pale kitandani akiwa uchi kabisa, na kuanza
kumchapa makofi, tena ya usoni. Bella alikuwa akilia sana. Hakuwa akielewa ni nini
Mzee Masha anaongea. Alimrusha kitandani kwa nguvu, nakuanza kumkaba. “Nilikwambia nikikufumania nitakuuwa Bella.
Kwa nini umenisaliti?” Alikuwa amemkalia Bella huku amemkaba kooni. Bella
alitapatapa, mpaka akapoteza fahamu.
Alizinduka akiwa
hospitalini. Bella alikuwa amevimba mwili mzima, hata usoni hakuwa akitizamika.
Alijitahidi kuangaza macho, lakini alishindwa, alibaki akigugumia maumivu.
Alipitiwa na usingizi mpaka kesho yake. Dereva alikuja, akamwambia ametumwa
amrudishe nyumbani. Aliporudi nyumbani, alikuta walinzi wamebadilishwa, na gari
alilokuwa amepewa halipo. Dereva alimsaidia kumuingiza ndani, kwani hakuwa
akiweza kutembea vizuri. Alijaribu kutafuta simu yake, lakini haikuwepo. Mzee Masha
alichukua gari yake, simu na kompyuta pia. Bella alipanda kitandani kwa shida
sana, akapitiwa na usingizi tena. Aliingia yule dereva chumbani kwake. “Amka unywe dawa Bella.” Bella
alijaribu kukaa lakini alishindwa. Alikuwa na maumivu makali sana. Yule dereva
alimnywesha zile dawa, akarudi kulala. “Nitakuletea
chakula baadaye.” Bella hakujibu.
Alipoamka hakukuta kadi
ya benki hata moja kwenye pochi yake na aligundua wafanyakazi wote
walishafukuzwa kazi, yupo pale peke yake. Bella alianza kulia sana. Aliendelea
kuuguzwa na yule dereva, na nesi aliyekuwa akija kumsafisha vidonda. Tena nesi
huyo alikuwa akisimamiwa na yule dereva. Hakuruhusiwa kuongea na Bella kitu
chochote isipokuwa kumtibu na kuondoka. Hakuweza kutoka mle ndani, kwa maumivu,
lakini hata hivyo dereva aliambiwa haruhusiwi kumpeleka Bella popote, kila kitu
ataletewa akiwa palepale nyumbani. Getini ndio waliambiwa mtu anayeruhusiwa
kuingia na kutoka ni yule dereva tu, tena akiwa peke yake labda awe anamleta
yule nesi.
Aliuguzwa na yule dereva
mpaka alipopata nafuu. Alikuwa akilia kila alipokumbuka juhudi zake shuleni, na
kuambulia sifuri. Kwani kipindi chote cha mitihani, Bella alikuwa amefungiwa
ndani, hakufanya mtihani hata mmoja. Hakuweza kuwasiliana na Mat, kwani hakuwa
na simu wala kompyuta. Alibaki akilia mchana na usiku, bila kujua cha kufanya.
Na shule yake ndio ilikuwa imekwisha, kwani hakufanya mtihani hata mmoja.
***********************************************
Baada ya majuma mawili
kupita Mzee Masha alirudi. Bella alipomuona anaingia mlangoni, alikimbilia
chumbani kwake nakufunga mlango kwa ndani. “Nitavunja
mlango Bella. Toka.” Bella alisogea mbali kabisa na mlango akakaa chini nakuanza
kulia. “Bella?” Mzee Masha aliendelea
kuita huku akigonga kwa nguvu sana. “Nakupa
dakika moja uwe umefungua huo mlango, Bella. Lasivyo kitakachompata mdogo wako,
usinilaumu.” Bella alivyosikia vile, alisimama kama mshale, akakimbilia
haraka mlangoni nakufungua, kisha akarudi nyuma huku akilia sana.
“Kwa nini umenisaliti Bella?” Bella hakuweza kujibu,
alikuwa akilia sana kwa uchungu. Aliona anaadhibiwa bila sababu na alijua hata
akijitetea vipi hawezi kufanikiwa kubadili mawazo ya Mzee Masha. Aliendelea
kulia kama amefiwa. “Nitakuumiza tena Bella.
Nataka unijibu. Kwanza njoo hapa karibu.” Bella alikataa kusogea,
aliendelea kulia. “Nikikusogelea hapo
Bella! Nimekwambia sogea karibu na mimi.” Bella alisogea hatua chache
akasimama. “Nimekwambia hapa nilipo.”
Mzee Masha aliendelea kugomba. Bella alisogea huku ameficha uso wake. “Sasa nataka unitajie jina la huyo mwanaume
wako, anaitwa nani? Maana nimempigia simu, haipatikaniki tena.” “Mungu wangu ni shahidi. Sina mwanaume mimi?” Mzee Masha alimchapa
Bella kibao cha nguvu akaangukia kitandani.
“Unanidanganya? Heri uniambie ukweli. Nitakuuwa Bella.” Mzee Masha alitoa
bastola na kumnyooshe Bella. “Leo ndio
mwisho wangu mimi na wewe Bella. Heri tufe wote. Huwezi kunisaliti.” Bella
alificha uso wake akisubiri kifo chake. Moyoni alifurahi sana kujua siku hiyo
ndio mwisho wa maisha yake, angalau akapumzike.
Gafla picha ya Eric
akiwa peke yake anahangaika mtaani akiomba chakula, ilimjia. Bella alishtuka
sana. Alikumbuka akifa, Eric atapata sana shida. Aligeuka kwa haraka sana. “Naomba usiniue T. Tafadhali mpenzi wangu, naomba unisamehe.” Mzee Masha alishapanda
kitandani. “Nisamehe T. Kwa
chochote nilichofanya, naomba msamaha. Sitarudia tena.” Bella alijisogeza karibu na kumkumbatia. “Tafadhali T.” Alijikuta akimng’ang’ania Bella bila kumuachia.
Ni kama aliyekuwa na uchu, na hamu naye sana. Aliweka kila kitu pembeni na
kuendelea kumng’ang’ania binti huyo kwa muda mrefu kitandani hapo akifanya naye
mapenzi kama aliyepagawa. Alipojiridhisha, Mzee Masha aliamka, na kuondoka bila
kuaga.
***********************************************
Baada ya siku mbili tena
kupita, Mzee Masha alirudi nakumkuta Bella amejikunja kitandani amelala, mida
ya mchana. Alikaa kitandani, Bella alifungua amcho na kumwangalia. “Nimepata muda wa kufikia, nimefikia maamuzi
haya. Kwa kuwa umenisaliti, siwezi kukuamini tena. Na kwakua umekataa kifo,
utaishi kwa masharti yangu. Hutarudi tena kusoma, utakaa humu humu ndani mpaka
nitakapo jua kitu gani ufanye.” Bella hakuwa na pesa hata kidogo, alijua
mdogo wake atafukuzwa shule. Na alijua akianzisha mambo ya pesa, ndio
ataanzisha ugomvi mkubwa zaidi. “Naomba unisamehe T.
Samahani kwa kukudhi.” Bella aliongea kwa upole sana akijaribu kujinyenyekeza. Mzee Masha
akasimama, akaondoka bila yakujibu kitu.
***********************************************
Bella alibaki akilia
sana mpaka usiku Mzee Masha aliporudi. Alimuona akiingia bafuni kuoga bila
yakumsemesha. Alipomaliza, akapanda kitandani. Bella alitamani asiguswe usiku ule.
Moyo wake ulijawa uchungu sana na hasira. Alitamani kama angekuwa na uwezo wa
kumuua yule Mzee, ili apumzike. Lakini alibaki ametulia pale kitandani akiwaza,
mwishowe alikumbuka ni kwa nini yupo pale.
Akamgeukia. “Pole na kazi, T.” Aliongea kwa sauti ya
upendo sana huku akizuia machozi. “Unanichanganya
Bella. Nashindwa hata kufikiria. Hata kazi zinanishinda.” Bella alianza
kulia taratibu, alijua mwisho wa yale yote ni nini kinafuata, lakini hakuwa na
jinsi, ilikuwa lazima atumikie kifungo chake. “Pole
na samahani, Masha.” Bella aliongea kwa kujishusha sana. “Lakini
T, sikuwa….” Alishangaa amevamiwa tena kama swala. Masha alimkumbatia na
kumbusu kila mahali kana kwamba walikuwa kwenye mazungumzo mazuri sana.
Ilimbidi Bella atoe ushirikiano, kumfanya atulie.
Kesho yake mzee Masha hakutoka
mle ndani, walibaki kitandani na Bella, mpaka usiku. Bella alipoona ametulia na
amerudi kwenye hali yake, aliona ndio muda muafaka wakuchezesha karata zake. “T!” Mzee Masha alimwangalia. “Hivi unajua ninakupenda, na siwezi kuwa
na mwanaume mwingine?” “Yule uliyekuwa mkiwasiliana naye ni nani?” “Sielewi T.
Na wala sijui nini unaongelea. Hakuna mtu nimewahi kuwasiliana naye kwa kutumia
simu yangu ila wewe tu, mpenzi wangu.” “Usinidanganye
Bella. Nachukia uongo. Heri uniambie kweli.” “Mungu wangu ni shahidi, T. Kwanza
unasema umekuta ujumbe gani kwenye simu yangu?” Mzee Masha alisimama na
kuifuata simu ya Bella kwenye gari yake.
“Hii hapa simu yako. Tena jumbe zote zipo. Ujumbe wa huyo mwanaume
wako aliokuandikia na wako uliomjibu.” Bella alichukua ile simu na kuangalia ujumbe. “Mbona hizi zote nilikuwa nimekuandikia wewe
T. Nilipopata huu ujumbe wa kwanza, nikakuonea huruma, nikajua labda ndio
sababu ulipotea muda mrefu bila kunitafuta kwa kuwa hukuwa na pesa. Ndio maana hapa
nikakujibu kuwa ile akaunti yangu nyingine ina hela, usiwe na wasiwasi.
Nimeandika huu ujumbe, nikijua nawasiliana na wewe, sikuwa hata na wazo la
kusoma namba, kwa kuwa hakuna mtu anayeifahamu hii namba yangu T, na wala
sijawahi kumpa mtu namba yangu ya simu. Mungu wangu ni shahidi. Naomba niamini
mpenzi.” Bella alimwangalia Mzee Masha aliyekuwa kimya, na wote
wakiwa wamejilaza kitandani.
“Lakini T, kama hii namba siyo yako, itakuwa ni namba ya nani?” Bella aliuliza. “Sijui.” “Nakuomba mpenzi wangu, kesho
twende kwenye kampuni ya simu tukajaribu kuulizia mwenye hii namba.” Kidogo
Masha akaanza kumwamini Bella. “Najua una
mambo mengi yakufanya T, lakini naomba tukatafute ukweli. Sipendi tuishi bila
kuaminiana, na sipendi kukuudhi. Najua umetusaidia sana T. Bila wewe sisi
tusingekuwa hapa.” Bella aliamua kuanza kumpamba Mzee Masha. “Umenipeleka nchi na sehemu mbalimbali. Ona
nyumba uliyoninunulia! Nguo na vitu vyote hivi vya thamani. Nisingependa uishie
kuumia, T. Naomba tutafute ukweli ili na wewe urudi kuniamini mpenzi wangu.”
Bella alikuwa na ulimi wakubadili akili za Masha, nakumlainisha kabisa. Kila
alipokuwa akifika mikononi mwa Bella, alisahau kabisa kama ana mke na watoto.
“Unauhakika humfahamu mwenye hii namba, Bella?” “Kwa nini tusiende
kesho kutafuta ukweli, T? Tafadhali mpenzi wangu, naomba twende. Tukamuulizie
mpaka tumpate. Nakupenda T, siwezi kukusaliti.” Mzee Masha alizidi
kuchanganyikiwa na maneno yale mazuri. Alimvuta karibu yake, akamkumbatia. “Nilikuwa mpweke ulivyoondoka. Ulinisahau?”
“Unajua siwezi kukusahau Bella. Nilifungwa na mambo mengi.” “Kweli T? Ulitingwa
mpaka ukashindwa hata kunitumia ujumbe!?” Bella alikuwa akiongea na Mzee
Masha huku akimtizama na macho yake ambayo wakati wote yalimfanya Mzee Masha
aliwazike. Alitabasamu na kumbusu Bella. “Unajua
kunichanganya Bella, wewe?” Bella alicheka na kujilaza kifuani kwake. “Kesho tutaenda kujua ukweli.” “Asante T.”
***********************************************
Kesho yake Mzee Masha
alishindwa kumuachia kabisa Bella, waliishia kujifungia tu chumbani huku
wakimtuma dereva awaletee chakula. Bella alibaki akijiuliza kama kweli Mzee
Masha amesahu kabisa kipigo alichompiga!? Alimuona vile anavyomfurahia,
nakukataa kumwachia kabisa. Alikuwa ni kama mtu aliyekuwa na hamu naye sana.
Hakutaka Bella awe mbali naye hata kidogo. Alimfuata humo ndani, popote Bella
alipokwenda, Masha naye alikuwa nyuma yake.
Japokuwa alijua kabisa,
anatumia mwili wake kujiridhisha, lakini hakuwa akielewa kabisa, kama amenyimwa
ubinadamu kwa kiasi hicho. ‘Anawezaje kunipiga vile, na kujifanya kama
hakuna kilichokuwa kimetokea? Atakuja kuniua huyu Mzee siku moja!’
Bella aliwaza huku akitoa
tabasamu, wakiwa jikoni akimwandalia matunda. ‘Lakini lazima nimvumilie, mpaka mdogo wangu atakapofika sehemu ya
kuweza kujitegemea.’ Bella aliendelea kuwaza. Kila Mzee Masha
alipomwangalia, alimpa tabasamu. “Nakuchanganyia
matunda yote kwa pamoja. Kama unavyopenda.” “Twende nayo chumbani, tutakula
wote.” Masha alijibu huku akirudisha macho yake kwenye simu ya Bella,
aliyokuwa ameishikilia muda wote alipokuwa amemfuata hapo jikoni.
“Nimefurahi tumepata wote muda. Nilikuwa na hamu na wewe kweli T!
Usiwe unanisahahu hivyo bwana.” “Mimi ndio nilikuwa nasikia kuchananyikiwa.
Huoni nimeshindwa kabisa kutoka kitandani.” Bella akacheka. “Nimekuona. Lakini ni kweli tulihitaji huu
muda. Imekuwa muda mrefu kweli!” Hakuna jinsi mtu angemwambia Mzee Masha
kama anadanganywa, akakubali. Kila Bella alipokuwa akiongea naye, ni kama akili
yake iliacha kufanya kazi kabisa.
Alikuwa amefungwa kwenye
mahusiano ya wanawake wawili ambao wote ilikuwa ngumu kuwaacha. Mkewe alishapoteza
sifa zote moyoni mwake. Kila alipojaribu kumlinganisha na Bella, alijiambia ni
kama mchana na usiku. Lakini alijua akimuacha mkewe, ndio atakuwa amepoteza
familia nzima, mpaka Zera. Kila alipofikiria kumuacha Bella, na kurudi kutulia
kwa mkewe, ilikuwa ni kama kujinyima usingizi maishani mwake. Bella alikuwa ni
kila kitu. Alikuwa mzuri kwake kwa kila kitu. Alibaki akihangaika asijue chakufanya.
“Masha apata ukweli juu ya
Bella.”
Walishindwa kutoka siku
ile. Masha alisema kila kitu kitasubiri siku ile, anataka kupata muda naye. Kesho
yake, waliamka mida ya saa nne, wakaingia kuoga wote, wakatoka. Bella alijitahidi
kujipendezesha sana. Mzee Masha alitamani kuahirisha safari, ili abaki tena na
Bella, lakini Bella alimbembeleza lazima waende wakamtafute mwenye hiyo simu.
Walipofika kwenye ofisi za mtandao wa namba hiyo ya simu, Mzee Masha alipewa
jina kamili la mmiliki, tena aliambiwa ni mojawapo ya namba zilizokuwa
zimenunuliwa na kampuni fulani, maalumu kwa ajili ya wafanyakazi wao.
“Naomba twende T, tukaonane na huyo mtu.” Mzee Masha alimshangaa
sana Bella. “Tafadhali mpenzi wangu.”
Bado Bella na Mzee Masha walikuwa wamekaa mbele ya meza ya muhudumu.
Aliwatizama kwa hofu. Lakini na yeye alijua Bella alichompendea mtu mzima vile,
ni pesa tu. Alisikia kukereka lakini ilimbidi kuwavumilia na kuwapa tabasamu,
Masha na Bella. “Eti T?” “Kama unaona
hivyo ni sawa.” Wakatoka pale.
Waliongozana mpaka
kwenye kampuni ya yule mtu, kwa bahati nzuri walimkuta na ndio alikuwa meneja
wa pale. Alikuwa ni baba mtu mzima kidogo. Aliwakaribisha ofisini kwake. “Karibuni sana.” Wote wawili walikaa mbele ya meza yake. “Asante. Tunataka kukuuliza kitu.” Mzee
Masha alianza. “Unaifahamu hii namba?”
“Ndiyo. Ni ya kwangu, natumia hapa ofisini.” “Unamfahamu Bella?” “Bella!?”
Yule baba alikunja uso na kuuliza. “Au
Enabella?” Bella alidakia, na kuongeza kama kumsaidia Masha, katika swali
lake. “Hapana. Kwani kuna nini?”
Bella na Mzee Masha wakaangaliana.
“Muonyeshe zile jumbe zote.” Bella aliongea kwa
sauti ya chini kidogo, huku akimwangalia Mzee Masha. “Siku hii hapa, ulituma ujumbe kwenda kwenye simu hii hapa.” Yule
bwana alichukua simu ya Bella, akaanza kusoma ule ujumbe. “Nakumbuka. Huu ujumbe nilikuwa namtumia mtoto wa kaka yangu. Alinipigia
simu kwa kupitia hii namba, akifuatilia pesa alizokuwa ameniomba kwa ajili ya
kulipia ada ya shule yake. Anasomea mambo ya kompyuta. Sasa nilikuwa kwenye kikao,
nikaamua kumjibu kwa kumwandikia ujumbe. Lakini majibu yake, sikuyaelewa
kabisa. Nilifuta ule ujumbe muda ule ule, kuhofia mke wangu asije akaukuta
kwenye simu yangu.” Mzee Masha alionekana kupooza kidogo.
Akachukua simu ya Bella
na kufungua upande wa ‘outbox.’ Akamuonyesha. “Alikujibu hivi?” Mzee Masha alimuuliza. “Eheeee! Hivyo hivyo. Kwa kweli nilishtuka sana.” Machozi yalianza
kumtoka Bella. “Samahani sana. Mimi ndio niliandika hivyo, lakini sikujua kama
nawasiliana na wewe. Huyo mtoto wa kaka yako, aliniomba simu apige.
Aliponirudishia nikairudisha mfukoni bila kuangalia namba. Sasa ulipotuma
ujumbe, kwa kuwa sina mtu ambaye anaifahamu hiyo namba isipokuwa mpenzi wangu,
sikujisumbua kusoma namba, nikajibu tu, nikijua nawasiliana na mpenzi wangu.
Samahani sana.” “Bila shaka binti.
Hapakuharibika neno. Nilifuta huo ujumbe palepale ulipoingia. Si unajua maswala
ya ndoa Mzee mwenzangu?” Alimgeukia Mzee Masha. “Unaweza
kubomoa ndoa yako kwa ujumbe mmoja tu uliongia kwa sekunde, kisha ikakuchukua
miaka mingi sana kuja kurudisha ndoa yako katika hali nzuri. Tena nilihakikisha
na ‘Block’ kufungia hiyo simu yako isiwahi kunipigia wala kutuma ujumbe tena.” Yule
mtu alionekana muungwana sana. Aliongea huku akicheka kirafiki. “Asante sana kwa muda wako ndugu. Uwe na
kazi njema.” Mzee Masha aliaga na kutoka kimyakimya, huku Bella akiomba
Mungu awe amemuelewa yule baba, na amuache yeye, arudi kwenye ndoa yake.
***********************************************
Walirudi kwenye gari,
Mzee Masha akiwa kimya kabisa. Bella alitegemea hata kuombwa msamaha wakupigwa
bila kosa, lakini alishangaa kuona mpaka wanafika nyumbani Mzee Masha haongei
kitu. Alipiga simu mahali ili gari ya Bella irudishwe, na kumkabidhi simu yake.
Baada ya muda mfupi Bella alirudishiwa kila kitu chake, lakini Bella hakutaka
tena. Gafla alianza kukinahiwa na vitu vya Masha, aliyemuona katili kupita
shetani.
‘Lazima nianze kujitegemea. Huyu baba
ananinyanyasa sababu ya mapesa anayotumia kwangu na mdogo wangu.’ Bella aliwaza akiwa
bafuni anajaza maji kwenye jakuzi. Alimwagia ile chumvi yenye marashi ndani ya
yale maji yakatengeneza harufu nzuri sana iliyofanya chumba kizima kinukie
vizuri. Akavua nguo zote hukohuko bafuni, akatoka kumfuata mzee Masha chumbani.
“Tumezunguka sana T, twende tukaoge.”
Bella aliinama, akamvua viatu, na nguo zote wakaelekea bafuni.
Baada yakujisuuza, Masha
aliingia kwenye maji aliyokuwa ametengeneza Bella. “Maji yana joto zuri.” Mzee Masha alisifia. Bella alitabasamu tu,
huku akifikiria ni jinsi gani atakavyomuingia Masha siku ile ili amruhusu ombi
lake. Alijua ile siku ndio yakutupia ndoano yake, kwani ni kweli alimkosea, ila
alishindwa kumomba tu msamaha, kwa hiyo alijua ile ni siku ya kuomba chochote
na kupewa.
“Nimekurudishia gari yako, umeona?” Masha alivunja ukimya. “Asante mpenzi wangu. Lakini kwa nini tusiwe tunatumia gari moja tu?
Tuwe tunatoka wote, wakati unaenda kazini na mimi unishushe kazini kwangu.”
Mzee Masha alimgeukia Bella, kwani Bella alikuwa amekaa nyuma ya mgongo wake
akimmwagia maji taratibu kama kucheza. “Kazini!?”
“Ndiyo. Nataka kuanza kazi T. Nifanyie
kazi kile nilichosomea.” “Daah! Nimesababisha hukufanya mitihani yako.” “Hamna
neno, T. Maadamu nilisoma, ninao ujuzi. Naomba nisaidie kutafuta tu kazi
popote, nitarudia kusoma kidogo wakati nafanya kazi kisha nitafanya mitihani.
Tena natamani tuwe tunafanya kazi sehemu moja, ili tuwe tunakuwa wote wakati
wote.” Bella alikuwa akimchokoza tu.
Alijua haiwezekani. Mzee
Masha asingeruhusu Bella afike ofisini kwake kwani mara nyingi watoto wake huwa
wanapendelea kwenda na baba yao huko, hata Bella alishakuwa kwenye ofisi za
Mzee Masha mara nyingi tu akiwa na Zera na kaka yake Zera. “Kwa sasa hamna nafasi ya kazi kwenye ofisi zangu zote. Ila namfahamu
mtu mzuri sana, ana ofisi yake. Anaweza kukuajiri bila shida. Kwanza nimewekeza
sana kwenye kampuni yake na kwenye elimu ya watoto wake. Nafikiri ni wakati
mwafaka na yeye anatakiwa kulipa fadhila.” Bella alitamani kurukaruka
kwenye yale maji. “Asante T. Nakushukuru
mpenzi wangu.” “Kwa hiyo gari hutaki?” “Sioni sababu T. Naomba tuwe
tunaongozana kama zamani. Kama wewe utakuwa na mambo mengi, basi dereva atakuwa
ananifuata. Najua itakupunguzia wasiwasi.” Mzee Masha alifurahi sana,
alizidi kumwamini Bella, ambaye alianza kujiwekea mikakati ya kujitoa mikononi
mwa Mzee Masha taratibu.
“Bella kwenye usaili!”
Baada ya kama siku tatu hivi,
Mzee Masha alimpigia simu Bella mida ya jioni wakati yeye yupo kazini, na Bella
yupo nyumbani. Alimwambia dereva atamfuata anatakiwa kwenye usaili. Kama
kawaida yake alivaa vizuri, akapendeza. Dereva alimfuata wakaongozana mpaka
kwenye hiyo ofisi. Ilikuwa ni ofisi kubwa tofauti na alivyotegemea Bella.
Ilikuwa na idara mbili kubwa, masoko na watunza fedha. Upande wa uongozi au
utawala, alikuwa ni Mmiliki mwenyewe akisaidiana na familia yake.
Alifika mapokezi akapewa
kiti na dada aliyemkuta pale, naye alikuwa mrembo tu na alionekana anaijua kazi
yake. “Ungehitaji kinywaji chochote
wakati unasubiri?” Alimuuliza Bella.
“Hapana, asante.” Bella alijibu na kujiweka sawa kitini. Baada ya muda simu
ya mezani kwa yule sekretari iliita, akajibu ‘Sawa.’ Kisha akakata simu na kumgeukia Bella. “Naona wapo tayari kwa ajili yako. Ingia kwenye hii ofisi.” “Asante.”
Bella alijibu na kusimama.
Alifungua mlango
taratibu kisha akaingia. Alikutana na watu wawili waliokuwa wakimsubiri ndani
ya ofisi hiyo. Mmoja alikuwa mtu mzima sana, Bella alimwangalia kidogo, akajua
yule ni wakumpa shikamoo. Akasogea kwenye meza kubwa aliyokuwa amekaa akampa
mkono, “Shikamoo.” Yule mzee
aliitikia, kisha akamgeukia kijana mwengine aliyekuwa ameinamia faili pembeni
ya hiyo meza kubwa alimuona ni kijana, alisogea karibu zaidi akanyoosha mkono, “Habari ya…” Macho yake yakagongana na
Elvin. Bella alishtuka sana, akabaki akimtizama Elvin na Elvin alibaki
akimtizama Bella. Yule Mzee alibaki akiwatizama wote wawili kwa zamu. “Mnafahamiana?” “Hapana.” Elvin alijibu
kwa haraka sana huku akibabaika, lakini mtu mzima hadanganywi kirahisi.
Alipoona Bella ameinama na kurudisha mkono wake taratibu, alijua lipo jambo
kati yao. “Karibu kiti.” Bella
alikaribishwa kiti na yule Mzee.
Bella alirudi nyuma
taratibu huku akiwaza, asijue aondoke tu pale, au afanyaje. Alikaa na kubaki
ameinama akichezea pochi yake taratibu. “Naitwa
Mwasha, ndio mmiliki wa hii kampuni.
Huyu ni kijana wangu, anaitwa Elvin, ndiye anayenisaidia sana katika mambo ya
uongozi hapa. Karibu sana.” “Asante.” Bella alijibu huku ameinama. Kimya
kilipita kwa muda, kisha Mzee Mwasha akaamua kuvunja ukimya
tena. “Labda ungeanza kwa
kujitambulisha.” Bella alitulia kwa muda kama anayejishauri, kama aendelee
na usahili au aondoke tu. Wote walikuwa kimya wakimsubiri.
Alikohoa kidogo kama
kusafisha koo, lakini bado alikuwa hajaamua kama aendelee na ule usahili au
aondoke. ‘Nikiondoka, nitamwambia nini Mzee Masha? Nimwambie siwezi kufanya kazi
na Elvin, kwa kuwa ananijua? Mzee Masha atakuwa aliwaambia nini siku ile
nilipozimia kule Dubai? Ananifahamu kama nani kwa Mzee Masha? Hapa
nikujidhalilisha tu, heri niondoke.’ Bella aliendelea kuwaza wakati
akisubiriwa ajitambulishe. Na wote walikuwa kimya wakimsubiri aseme kitu.
“Ungependa tukuletee kitu chochote cha kunywa?” Mzee Mwasha aliuliza
kiustarabu sana. “Hapana, asante.” “Basi
tunakusubiri, utakapokuwa tayari tunaweza kuendelea.” Alionekana ni Mzee
muungwana sana. Alikuwa mtulivu, hata sura yake ilionyesha ni mtu muungwana.
***********************************************
Haya.... Uso
kwa Uso na Elvin aliyemuuguza nchini Dubai. Akitafuta njia ya kujiokoa kwenye
mateso makali sana ya Masha, anakutana na kipingamizi Elvin aliyemshuhudia
nchini Dubai akiwa na Masha. Wazi alionyesha kuvuja damu kwa madhara fulani.
Elvin alimuelewaje kule? Ataweza kufanya naye kazi?
Usikose kuwa na
Bella, katika kipindi hichi kigumu cha maisha anachopitia akiwa peke yake bila
mshauri au faraja. Atafanya nini?
JE, WEWE UNGEKUWA ENABELLA, UNGEFANYA NINI? NA KWA NINI? USIACHE KUTOA
MAONI YAKO HAPO CHINI.
Ooh!I like this story coz it inspire me to have self confidence keep it up the author
ReplyDelete