Story

My Past - Sehemu Ya 5.

Wednesday, May 03, 2017 naomimwakanyamale 0 Comments


W
akati Bella anajitahidi kutulia, kwa mbali masikio yake yalianza kusikia mziki wa taratibu sana, alihisi ni nyimbo za kumuabudu Mungu kwa lugha ya kingereza. Mawazo ya Bella yalianza kutulia sehemu moja na kufikiria mahali alipokuwa amesikia zile nyimbo. Akakumbuka ni kwenye gari lao. Mat alikuwa akipenda sana kuziweka kwenye gari ambalo ilikuwa taksii. Kumbukumbu zikamjia Bella, kuwa anajukumu la Eric, na lazima ajikomboe kwenye mikono ya Masha. Akajua ile kazi inaweza kuwa msaada kwake. Ikabidi kuanza kutulia na kurudisha mawazo pale, akanyanyua uso kwa mara ya kwanza, akakuta bado wakimwangalia.
“Naitwa Enabella.” Aliongea kwa sauti ya chini kidogo, lakini ilisikika. Mzee Mwasha akatoa tabasamu. “Ndio umeshamaliza utambulisho wako?” Bella alifikiria kidogo akaamua kurudia tena. “Naitwa Enabella. Lakini wamezoea kuniita Bella.” Alitulia kidogo kisha akaongeza. “Nina elimu ya ‘IT’. Lakini Sina cheti chochote, ila nilisoma kwa miaka miwili, ninao utaalamu kidogo.” “Kwa nini huna vyeti?” Elvin akamuuliza. Bella alifikiria kidogo, akainama kwa muda kisha akaendelea. “Nilipata matatizo yaliyonisababishia kutofanya mitihani. Lakini nilihudhuria madarasa yote, nilipata elimu kama wengine, kasoro ile week ya mwisho ya mitihani ndipo sikuweza kuhudhuria chuoni kufanya mitihani yangu ya mwisho.” “Ulimaliza mwaka gani? Au ulitakiwa kumaliza mwaka gani?” Elvin aliendelea kuhoji. “Mwaka huu mwezi wa tano.” Bella alijibu.
“Una umri gani Enabella?” Mzee Mwasha akamuuliza. “Miaka 20 sasa.”  Walinyamaza kidogo wakaangaliana. Wasiwasi ukamwingia Bella. “Lakini naweza kujituma.” Bella aliongeza kwa unyenyekevu sana. “Sijui kama unajua hii kampuni inahusika na nini!?”  Elvin alihoji. “Sifahamu.” “Tunaagiza mabomba kutoka South Africa na kuyauza hapa nchini na nchi za Africa Mashariki. Sasa kwa taaluma uliyonayo unafikiri unaweza kufanya kazi gani hapa?” Elvin aliuliza tena. Bella alifikiria umuhimu wa ile kazi kwake na kwa mdogo wake, ilimlazimu kufikiria harakaharaka sana.
 “Labda niulize swali.” Bella alikaa vizuri. “Karibu.” Elvin akajibu. “Mnatumia mfumo gani katika kuendesha biashara zenu hapa ofisini kwenu? Nikimaanisha mnatumia kompyuta au mnaandika kwenye vitabu tu?” “Tupo kwenye mabadiliko sasa. Kutoka kwenye mfumo huo wazamani wa kuandika na kuingiza kazi zote kwenye kompyuta. Kuna mtaalamu huwa anakuja kila mwishoni mwa juma kuifanya hiyo kazi.” Elvin alijibu.
“Naweza kuwasaidia.” Bella alijibu huku akiwaangalia wote kwa zamu. “Mkinipa mimi hiyo kazi, nitaomba muda kidogo kupitia kazi zenu zote, nakujua mnachofanya, ndipo nitakapoweza kuwasaidia kutengeneza mfumo ambao ni rahisi kwa wafanyakazi wenu wote, na nyinyi wenyewe, na pengine naweza nikatoa ushauri pia.” Bella aliwatizama tena usoni kila mmoja wao. Ujasiri ulirudi, akaonekana akijieleza kwa uhakika.
“Nikielewa kazi zenu, yaani nikafahamu hii kampuni na jinsi mnavyofanya kazi, hamtakuwa na haja yakunifuatilia kila mara. Nina uwezo wakujituma mwenyewe, na kufanya kazi vizuri.” Bella aliongezea. Mzee Mwasha alionyesha tabasamu usoni lililompa tumaini Bella.
“Unataka kuanza kazi lini?”  Elvin akahoji. “Wakati wowote mtakao nihitaji, nitakuwa tayari. Sina kitu ninafanya kwa sasa, nipo tu nyumbani.” Elvin alitulia kidogo. “Kwa hiyo hata tukikuita kesho, unaweza kuanza kazi.” “Ndiyo.” Bella akajibu. “Unatarajia mshahara wa kiasi gani?” Elvin alimuuliza. Japokuwa alihitaji sana hiyo kazi, lakini hakuwa amejua hata watu huwa wanalipwa mishahara kiasi gani. Alishazoeshwa kupewa mahela na Mzee Masha. Akaogopa kabisa kutaja mshahara wake. Alibaki kimya akifikiria. Na upande wa waajiri wake, walimuona Bella ni wa garama sana. Kuanzia mavazi yake, yeye mwenyewe alivyojiweka na kujiuza pale kwenye usahili, kidogo walibabaika. Chumba kizima kilijaa harufu ya manukato yake.
“Eti Enabella?” Mzee Mwasha aliuliza. “Sifahamu huwa wanalipaje mishahara. Sijawahi kuajiriwa.” Bella alijibu kwa upole kidogo. Wote walinyamaza kimya. “Au nianze kwanza kazi, halafu mnilipe kwa utendaji wangu?” Bella alitoa wazo huku akiuliza, baada yakuona kumezuka ukimya. “Huyo mtu anayekuja kila mwisho wa week kutusaidia kazi, tunamlipa pesa nyingi sana, tena anakuja mara moja kwa week tu. Kwa hiyo kama utaweza kufanya anachofanya, utakuwa umetusaidia sana kukata matumizi, na kuanzia hapo tutajua kiasi gani cha kukulipa.” “Sawa.” Bella akakubali bila shida.
“Ulitaka kuja kuanza kazi siku hiyo anayokuja yeye ili uone anachofanya?” Elvin akamuuliza tena. “Naomba kama naweza kuanza kabla ya kukutana na yeye, nianze tu. Ili nielewe jinsi mnavyofanya kazi zenu nyinyi kwanza. Sio lazima mkanilipa, hii itakuwa kwa manufaa yangu mimi mwenyewe, halafu atakapokuja huyo mtu, akiwa anafanya hizo kazi, nitakuwa angalau nina uelewa ni kitu gani anafanya au anatakiwa kufanya.” Bella aliweka msisitizo. “Wazo zuri sana Enabella. Besi unaweza kuanza kesho.” “Nije saa ngapi?” Bella akauliza. “Kuanzia saa 12:30 asubuhi ofisi zinakuwa wazi. Mimi ninakuwepo.” Elvin akajibu. “Hapo itakuwa mapema sana. Sitaweza. Labda kuanzia saa nne asubuhi nitakuwa nimefika.” Wote walimwangalia kwa mshangao kisha Mzee Mwasha akacheka kidogo. “Au nitakuwa nimechelewa sana?” Bella akauliza kwa upole.
“Asubuhi huwa nachelewa sana kuamka. Lakini saa nne naweza kujitahidi kuwa nimefika.” Bella aliongea kama mtoto ambaye hana majukumu yanayomkabili. Alipoona wote wapo kimya, aliingiwa na hofu. “Lakini pia naweza kufika saa 12:30 asubuhi, au muda wowote mtakao nipangia, nitakuja.” Bella aliongea kwa upole kidogo, akijirudi. “Hamna shida. Wewe njoo huo muda utakao weza.” “Asanteni sana.” Bella alishukuru. “Karibu sana Enabella. Kesho utakapofika, tutakuzungusha humu ndani na kukutambulisha kwa watu.” “Sawa.” Bella alijibu kwa kifupi na kusimama. “Nitarudi kesho.” “Karibu sana.” Mzee Mwasha alisimama na kumpa mkono lakini Elvin alirudisha macho yake kwenye faili na kuendelea kuandika. Bella akatoka. Bado dereva alikuwa akimsubiri nje ya ofisi hizo. Alimrudisha nyumbani akiwa amefurahi sana.
*********************************************
Alimkuta Mzee Masha akimsubiri. Alimuelezea kila kitu. “Nilikuwa naogopa kweli.” “Wasingeweza kukunyima kazi.” “Kwani uliwaambia mimi ni nani kwako?” Bella aliuliza lakini alimuona Mzee Masha amebadilika sura, akaogopa. “Wewe si ulitaka kazi?” “Ndiyo T. Na ninakushukuru.” Bella alishaingiwa na hofu, alijibu kwa kujinyenyekeza sana, ili usiku ule usiwe mbaya kwake. Walikaa kimya kwa muda, kisha Bella akaamua kuaga akawahi kulala. “Nataka niwahi kulala, ili kesho niamke mapema niwahi kazini.” “Hata kazi yenyewe hujaanza umeanza kuniona mimi mzigo!? Unaniachaje hapa sebleni peke yangu? Ndio maana wanaume wengine hawataki wake zao wafanye kazi.” Bella alijirudisha kukaa pembeni ya Mzee Masha taratibu. “Nitakusubiri T.” Mzee Masha alimwangalia kwa muda na kurudisha macho yake kwenye tv. Bella aliumia sana moyoni, lakini hakuwa na jinsi. Ni lazima afanye kila anachoambiwa. Alijikuta wanalala saa nne ya usiku.

 “Bella aanza kazi.”
Bella aliamka asubuhi na mapema akiwa na furaha sana moyoni. Ni kama aliyekuwa akianza maisha mapya. Alimuacha Mzee Masha kitandani, akaingia kuoga na kutoka kuandaa kifungua kinywa. Alirudi chumbani kumuamsha Mzee Masha, wakapata kifungua kinywa kwa pamoja, Mzee Masha akaanza kumng’ang’ania tena. “Nitachelewa kazini T. Kwa nini tusiendelee jioni tukirudi?” Mzee Masha alimchapa kibao kwa nguvu. “Kazi nimekutafutia mwenyewe, halafu unasema nini? Yaani hiki ninachotaka kufanya sasa hivi ni ujinga? Sikiliza Bella, kazi yako ya kwanza ni hapa nyumbani, na huko kazini ni ya pili. Umenielewa.” “Ndiyo.” Bella alijibu huku ameshika shavu lake lililokuwa likiwaka moto kwa kibao cha nguvu alichokuwa amepigwa.
“Nikukute chumbani ukinisubiri.” Mzee Masha alimuamuru Bella. Huku akilia, Bella alirudi chumbani akavua nguo zote akapanda kitandani na kujifunika shuka. Alikaa pale akimsubiri Mzee Masha, aliyekuwa akiangalia taarifa ya habari ya CNN, asubuhi hiyo. Baada ya kama dakika 45, ndipo alipoingia chumbani. Alikaa na Bella hapo kitandani karibu lisaa lizima. Alipomaliza, Bella alisimama kwenda bafuni. Alikaa bafuni akilia sana, mpaka alipomsikia Mzee Masha akiingia bafuni, akanyamaza.
“Hata ukiingia kazini saa nne, hakuna atakayekufukuza kazi. Jiandae, dereva yupo nje anakusubiri.” Mzee Masha alikuwa amesimama ndani ya bafu hilo akiongea na Bella. “Unanisikia lakini?” “Ndiyo, nimesikia.” Bella alioga harakaharaka, akarudi chumbani kuvaa nguo zake tena. “Uwe na siku njema T.” Bella aliaga. “Asante.” Bella aliingia kwenye gari, lakini alishindwa kujizuia. Aliinama nakuanza kulia sana. Alilia mpaka dereva alipomwambia wamefika. Alishindwa kushuka kwenye gari, kwa wakati ule. Alibaki akilia kwa muda, mpaka alipotulia. Kwa bahati mbaya, macho yalishakuwa mekundu sana, hata rangi ya sura yake ilikuwa imebadilika. “Asante.” Bella alimshukuru dereva, akashuka kuingia ofisini.
*********************************************
Alimkuta sekretari kwenye meza yake. “Nimeambiwa ukifika uende kwenye ofisi ya Elvin. Ni ule mlango wa pili kulia.”  “Asante.” Bella alishukuru na kuondoka. Kabla hajaingia ofisini kwa Elvin alijitahidi kuvuta pumzi mara kadhaa, ndipo alipogonga mlango wake. “Samahani nimechelewa.” Bella aliwahi kabla ya salamu. Ilishakuwa saa nne asubuhi. “Karibu.” Bella hakutaka kabisa kumwangalia machoni. “Karibu kiti ukae.” Bella alikaa mbele ya meza ya Elvin, huku ameinama. Walikaa kimya kwa muda, Elvin akimwangalia Bella, na Bella akiwa bado ameinama.
“Kitu cha kwanza ulitakiwa kufanya ilikuwa ni kusalimiana au kufahamiana na wafanyakazi wengine. Lakini muda huu, wengi wameshatoka, watarudi jioni.” Bella alinyamaza. Elvin alisimama na kutoa maji ya kunywa kwenye friji ndogo iliyokuwepo hapo ofisini. Akayafungua na kuyaweka mbele ya Bella. “Karibu maji.” “Asante.” Bella alijibu kwa sauti ya chini bila hata kumtizama. “Sio wafanyakazi wote wanafika saa 12:30 asubuhi. Ni wale watu wanaofanya stoo, na madereva. Mizigo huwa inafika hapa asubuhi sana, na wanao safirisha nchi za jirani pia, huwa wanapenda kuondoka alfajiri sana. Huwa napenda kuwepo hapa ili nisimamie mimi mwenyewe. Lakini wafanyakazi wengine, wanatakiwa saa mbili kamili wawe wamefika hapa, ofisini.” Bella alinyamaza, akifikiria kama kweli ataweza kufika pale katika mida hiyo. Alijua anajukumu la Mzee Masha, ambalo hawezi kulikwepa. Alibaki kimya akifikiria chakufanya.
“Sidhani kama nitaweza kuwa nafika hapa kwa muda huo.” Bella alijikaza na kumwangalia Elvin. Elvin alibaki akimwangalia jinsi macho yake yalivyo mekundu na yalishavimba kidogo. “Ungependa kuanza kazi kesho? Unaweza kurudi nyumbani ukapumzika mpaka kesho.” Bella alibaki akifikiria. Alijua maisha yake hayawezi kubadilika kwa siku moja au kwa kujionea huruma pale. “Hapana. Naomba nianze tu leo. Nitajitahidi kuwa namaliza kazi zote utakazokuwa unanipangia siku hiyo kabla sijaondoka. Hata kama nitafika kwa kuchelewa, nitajitahidi kumaliza kazi zangu zote. Sitalaza kiporo.” “Ni sawa tu. Kipo choo humuhumu ndani ya hii ofisi.” Akimaanisha aingie akaoshe uso. Bella alielewa. Akasimama na kuingia chooni. Aliloweka uso wake kwenye viganja vyake vilivyokuwa na maji ya baridi, mpaka alipotulia kabisa. Akajikausha, nakutoka. “Asante.” “Karibu. Sasa twende ukaanzie upande wa stoo. Huko utakutana na mtu ambaye ndiye anapokea mizigo yote na kugawa kila siku. Ni kijana mzuri sana, atakuelekeza vizuri tu.” Waliongozana mpaka upande wa stoo.
*********************************************
 Ni kweli, yule kijana aliyekutana naye kule stoo alikuwa ni mnyenyekevu lakini mcheshi sana. Alifahamika kwa jina la ‘Joo’. Alimkaribisha Bella. Bella alianza siku yake vibaya sana, hakuwa na furaha hata kidogo. Lakini hakutaka matatizo yake yaingilie kazi yake. Alijitahidi kuelewa kila alichoelekezwa na kuuliza maswali machache, baada ya muda akawa ameshaelewa kila kitu na kugundua matatizo mengi sana pale. Bella alikuwa na kidaftari chake, akawa anaandika kila kitu.
“Naenda kula dada Enabella. Utataka tuongozane.” “Hapana. Mimi sitatoka. Naomba tu mimi niendelee na kile ulichokuwa ukikifanya wewe, ili ukirudi tuwe tumepunguza kazi.” “Sawa.” Joo alimuacha Bella akiwa amemuelekeza kitu cha kufanya. Alikuwa na mrundikano wa kazi nyingi sana, za miezi mingi iliyopita. Bella alishangaa wanawezaje kufunga mahesabu ya siku au hata mwezi kama huyu mtu wa stoo anakuwa hajakamilisha kazi yake. Alibaki pale kwenye ofisi ya stoo akifaya kazi bila hata kunyanyuka. Alifurahia ile kazi, kwani kwa mara ya kwanza aliweza kupata kitu chakufanya na kufikiria mbali na Mzee Masha. Alibaki akiandika kwa muda, na kupangilia ile kazi vizuri sana.
“Pata mapumziko, ule kidogo.” Elvin alikuwa amemletea chakula. “Sitaweza kula. Asante.” Bella alimgeukia. “Kwa nini?” “Tumbo langu limejaa sana gesi. Siwezi kuingiza kitu chochote humo ndani. Itakuwa ni kama nina jiadhibu zaidi. Asante sana.” Bella aligeuka na kuendelea kuandika. “Vipi unaonaje kazi ya hapa?” Bella akatulia kidogo. “Naruhusiwa kutoa maoni yangu? Najua ni mgeni kabisa, lakini..” Bella alisita. “Sema tu.” “Nimeona mnaviporo vingi sana. Na ninahisi pia inachangiwa na mfumo wa utendaji kazi wenu, unamuia vigumu Joo kumaliza kazi kwa wakati. Kwa nini msitumie kompyuta, mkanunua program ambayo Joo, akiwa anajaza hapa, hata kama muhasimu akitaka kufunga mahesabu yake wakati wowote anaona kilichopo stoo, bila kuzungusha hizi vocha? Kwa namna hii ni rahisi sana kupotea. Hata wewe mwenyewe itakurahisishia kujua nini unacho stoo na nini hauna. Na unatakiwa kuagiza kwa wakati gani. Sijui unanielewa? Yaani mnaweka utaratibu ambao wahusika wanaweza kuona kila kitu wanachokitaka, wakiwa kwenye kompyuta zao, ofisini kwao. Tena kwa urahisi na haraka. Joo anakuwa hana kazi yakuzunguka maofisini na vocha zote hizi. Najua nimeongea sana, lakini sijui umenielewa?” Elvin alibaki akimtizama Bella kwa muda.
“Kama kitu kama hicho unachoeleza kinawezekana, kwa nini huyu mtu tunayemlipa kila anapokuja, hajatushauri hivyo?” Bella hakutaka kuingilia, akaamua kunyamaza. “Wewe unafahamu hizo program?” “Nafahamu baadhi. Naweza nikashauri, kisha mkaangalia bei zake.” Bella aliongea mambo mengi kama msomi sana na kama mtu mwenye uelewa mkubwa sana.
“Umejifunza wapi mambo yote hayo?” Bella alitabasamu kidogo. “Chuo kikuu cha Youtube.” “Youtube! Hii hii youtube?” Bella alicheka kidogo. “Ndiyo. Si unajua huko kunapatikana kila kitu. Na mimi ndio natumia sana kujifunza mambo mengi. Najikuta sina kazi au kitu chakufanya, kwa hiyo natumia muda mwingi sana kwenye kompyuta. Na nina penda sana mambo ya biashara. Kwa hiyo nikaamua kujifunza hii IT kwa upande wa biashara.” “Asante sana Enabella. Ngoja nitaongea na Mzee tuone tunafanya nini.” “Sawa.” Bella alijibu na kugeukia mezani, kuendelea na kazi. Alimuacha Elvin bado amesimama akimtizama.
Bella aliendelea na kazi siku hiyo bila kupumzika mpaka jioni alipoondoka. Huku nyuma alimwacha Joo na mshangao. Kazi alizokuwa anashindwa kumaliza kwa siku, Bella alimaliza zote, na kuanza kushambulia viporo vya nyuma.
*********************************************
Muda wa kuingia kwake kazini haukuwa ukieleweka. Wakati mwingine alifika kazini saa nne, wakati mwingine saa tano. Na mara nyingi kila anapoingia kazini alionekana hana furaha. Alitambulishwa kwa wafanyakazi wote, lakini kama kawaida ya Bella, hakutaka mazoea na mtu yeyote yule. Zaidi ya salamu hakutaka kuzungumzia mambo mengine mbali na kazi. Alisikia wanawake wa pale wakimsema vibaya, nalo halikumsumbua hata kidogo, alishazoea. Alichapa kazi bila kuchoka. Kila anapoingia kazini, ni kweli alifanya kilichompeleka pale.
Sifa zake zilimfikia Mzee Mwasha kutoka kwa wafanyakazi wengine, hasa wakiume. Mzee Mwasha alimwita Bella ofisini kwake. Bella alihofia sana, alijua ni sababu ya kuchelewa kuingia kazini. Alipokaa tu mbele ya meza ya Mwasha, Bella alianza kuongea. “Najua nachelewa sana kuingia kazini, lakini najitahidi kumaliza kazi zangu zote kwa wakati. Kwa wakati huu siwezi kuahidi kuwahi, kuna mambo yamenifunga. Naombeni mnivumilie.” Mzee Mwasha alitabasamu. “Sio hilo nililokuitia, Enabella. Nilitaka kukupongeza kwa utendaji kazi wako.” Bella alipumua kidogo, nakujiweka sawa. Elvin alikuwa akimwangalia.
“Asante. Sijui mmefikia wapi kwenye swala la kubadili mfumo mzima wa utendaji kazi. Niliongea kidogo na na na na…” Bella alishindwa kabisa kutamka jina na Elvin, akaamua kunyamaza kama aliyepatwa na kigugumizi cha gafla. “Tumezungumzia kidogo, lakini inaonekana ni gharama sana. Inabidi kusubiri.” Mzee Mwasha aliamua kujibu. “Nina pendekezo.” Bella aliongea huku akiwa na wasiwasi kama ni sawa kutoa maoni yake. “Karibu Bella. Ujisikie huru tu kutoa maoni yako, usiwe na wasiwasi.” Bella alitabasamu kidogo huku akiendelea kumwangalia Mwasha, aliyekuwa akizungumza naye tokea mwanzo, kwani Elvin alikuwa kimya kabisa, akimtizama. “Nafahamu kabisa kuwa hayo mapendekezo niliyotoa hayakuwa kwenye budget yenu, na ninajua hizo ‘Accounting programs/systems’ zina gharama sana. Lakini nilipokuwa nikifanya kazi kwenye kitengo chenu cha uhasibu, nimeona pesa mnayomlipa huyu mtu anayekuja kuwafanyia kazi mara moja kwa week ni nyingi sana, halafu hata kama akiwafanyia kazi bado anawaacha kwenye matatizo vile vile, na anafanya kazi kwenye kitengo kimoja tu, na kila ninapoangalia, haonekani kama atamaliza kazi anayotakiwa kufanya kwenye hizi siku za karibuni.” Bella akawatizama tena.
“Naomba msinielewe vibaya, sina nia yakumuharibia, lakini nilikuwa ninapendekezo. Naomba mimi nigharamie hiyo program, tuiweke nakuijaribisha kama itawafaa. Naomba tuipe miezi miwili ya majaribio. Mkiona inawarahisishia kazi, na mngependa kuitumia, basi tutaibakisha, na mtanilipa hiyo pesa taratibu na kwa wakati mtakao amua nyinyi, lakini kama mtaona ni kitu ambacho hamkihitaji, nitachukua, na kuuza kwa watu wengine.” Mzee Mwasha na Elvin walibaki wametoa macho. “Sio lazima mkaamua sasa hivi, mnaweza kupata muda wakufikiria zaidi, kisha mtanijulisha.” Bado kimya kilikuwa kimetanda pale ofisini kwa Mwasha.
*********************************************
Msingi wa elimu waliyopewa na mama yao, na mazingira waliyokulia, shuleni na hata mtaani, uliwajenga vizuri sana Bella na mdogo wake. Walifundishwa kuongea mawazo yao, hasa pale wanapoona yanamanufaa. Na walijituma bila hofu. Kitu kilichompelekea hata Eric kupendwa sana shuleni. Mzee Masha ndiye aliyekuwa akimkandamiza sana Bella na kushindwa kuongea kabisa. Alimnyanyasa binti huyo na kumuonyesha wazi kuwa mawazo yake pekee Masha, ndio yataongoza mapenzi yao, si vinginevyo. Lakini tangia afike hapo, alikuwa akifurahia sana anachokifanya. Nikama aliingizwa kwenye anga zake. Hakuona mipaka, alikuwa akielea na kufanya kazi kwa moyo mmoja, tofauti na wafanyakazi aliowakuta pale. Wengi walikuwa na malalamiko na niwazembe. Hakuna aliyefurahia kazi yake.
Bella alijitahidi kuwa nao mbali kwa kadiri ya uwezo wake.  Walikuwa na maswali mengi sana wanayoulizana juu ya Bella bila kupata jibu. Kila siku aliingia na mavazi ya thamani sana, na kila alipopita, utajua tu Bella amepita. Hakuwahi kuwajibu maswali yanayomuhusu yeye binafsi. Kama akiona ni swali nje ya kazi, alikaa kimya na kuendelea na shuguli zake. Walijaribu siku za mwanzoni kumshawishi mambo mengi ili ajiunge nao, lakini Bella hakutaka kabisa.
“Hapa ofisini, wanawake tunakikundi chetu cha kusaidiana. Kuna kiingilio. Na huwa tunakopeshana. Unataka kujiunga?” Mama mmoja mtumzima kidogo alimfuata Bella kujaribu kumshawishi. “Kukiwa na tatizo lolote ambalo mnataka nichangie, usisite kunishirikisha. Nitachanga.” Bella alijibu kwa kifupi na kugeukia kompyuta yake kuendelea na kazi aliyokuwa akifanya. Alisikia wafanyakazi wengine wakicheka nyuma yake, lakini hakugeuka. Kwa hiyo wote walimuelewa hivyo na baadaye wakabaki kuheshimu maamuzi yake. Yeye ndiye alikuwa mdogo kuliko wote pale ofisini, lakini ndiye aliyeonekana kujielewa kuliko wote.
*********************************************
Alipowaona bado wako kimya hawampi jibu lolote, Bella alisimama. Naomba mniruhusu, nina kazi nataka nimalizie kabla sijaondoka. “Subiri kwanza Enabella.” Elvin alimuwahi. “Umesema unaweza kutuwekea hiyo program?” “Ndiyo.” “Kwa kuiweka tu, utatudai kiasi gani?” Bella alikunja uso kidogo. “Hapana siwezi kudai. Si mmenipa ajira kama wafanyakazi wengine au bado hamjafikiria kuniajiri?” “Tutakuajiri Bella.” Elvin alijibu kwa upole kidogo. “Basi itakuwa ni moja ya majukumu yangu hapa kazini na mtanilipa mwisho wa mwezi mshahara kama wafanyakazi wengine.” Bella alijibu kwa heshima kidogo. “Au nimekosea?” “Hapana. Tulipenda kujua, ili tunapokubaliana tuwe tunajua tunajiingiza kwenye nini.” Mzee Mwasha alijibu. Kwa wakati ule, pesa kwa Bella haikuwa tatizo hata kidogo. Alikuwa na pesa za kuchezea kutoka kwa Mzee Masha, lakini ile kazi kwake ilikuwa zaidi ya ajira. Ni sehemu pekee aliweza kujiona na yeye ni mwanadamu wa kawaida, na aliweza kufikiria mambo mengine mbali na Mzee Masha. Hata hivyo alitaka kutengeneza pesa za tofauti na zile za Mzee Masha alizoona nizamkosi kwenye maisha yake.
“Unaweza kuileta lini hiyo program?” Elvin alihoji. “Hata kesho. Ninayo tayari nyumbani. Niliinunua muda mrefu kidogo, nikawa nafanyia majaribio nikiwa nyumbani. Naamini itawasaidia. Naomba na nyinyi muijaribishe, naamini mtaipenda na kuwafaa.” Bella alikuwa akiongea kwa kujiamini, lakini taratibu sana na kwa unyenyekevu. “Asante sana Enabella. Nafikiri sio vibaya tukianza mara moja.” Bella alionyesha furaha usoni. “Nitaileta kesho. Asanteni.” Bella alitoka na kuwaacha Elvin na baba yake ofisini kwa Mzee Mwasha.
*********************************************
Bella aliendelea kufanya kazi kwa bidi sana, bila kuchoka wala kulalamika. Aliweka ile program kwenye ile kampuni, wengi waliisifia isipokuwa baadhi ya wasichana aliowakuta pale, walisema ni ngumu kutumia. Siku moja Bella aliwahi sana kazini kwa kuwa alitaka kumalizia kazi aliyoacha kwenye ofisi ya masoko kabla muda wa kazi haujafika, saa mbili. Kwa hiyo kwa mara ya kwanza aliweza  kuhudhuria  kikao cha wafanyazi wote pale ofisini.
Wengine walianza kulalamikia ule utendaji mpya wa kazi, wakisema ni ngumu na upo kwa lugha ngumu ya kingereza. Joo alisifia na kusema imemrahisishia kazi. “Wewe Joo hebu nyamaza. Unasifia kwa kuwa alikusaidia kufanya kazi zako zote! Hapo ulipo huna kazi yeyote. Sisi tunaviporo vya miaka. Mpaka tuje tumalize kuingiza huko kwenye kompyuta itatuchukua muda mrefu sana.” Msichana mmoja aliongea. “Kwanza hata mambo ya kompyuta yenyewe hatuyajui! Heri turudi kwenye kuandika kwenye daftari.” Mwingine aliongeza. “Kingereza chenyewe shida!” Mwingine aliongeza na wenzake wote wakacheka.
Elvin alishajua wanafanya kusudi, na wivu unachangia. Wakati wote walikuwa wakimlalamikia Elvin wakati Bella hayupo, kuwa Bella anakiburi, hawezi kusalimia watu na kwa nini yeye anaruhusiwa kuingia ofisini kwa muda anaotaka yeye sio muda wa kawaida kama wao!
Mzee Mwasha na yeye hakuwa akija kazini asubuhi. Mara nyingi aliingia ofisini mida ya mchana. Kwa hiyo hakuwepo kwenye hicho kikao, ni Elvin ndiye alikuwa akiongoza karibia kila kitu, kasoro kwenye maamuzi fulani fulani, bado Mwasha, baba yake ndiye ilibidi aidhinishe.
Naelewa jinsi ilivyokuwa ngumu kupokea kitu kipya, hasa kama ulishazoea au kama ulikuwa na utaratibu ambao ulishauzoea. Lakini kama mkijipa muda, naamini mtazoea na kufurahia. Naomba hizo kazi zote za nyuma, mniachie mimi nitazifanya. Nyinyi muendelee kuingiza hizi za sasa, ili zisiwacheleweshe. Na atakaye kwama kwa lolote, naomba asisite kuniambia, nitasaidia. Hata kama utahitaji tuwe wote ofisini kwako, nitahamia hapo kwa muda, kuhakikisha nakuelekeza mpaka unaelewa, na viporo vyenu vya nyuma nitavifanyia kazi kwa wakati wangu ili nisiwabugudhi wakati wa kazi.” Hapo Bella aliwafunga midomo na kuwafanya wakose cha kulalamika tena.
Elvin alikuwa akifurahi sana moyoni. Ilikuwa ni kama Bella ameletwa na Mungu kumsaidia. Kwani baba yake alianza kuugua, lakini hawakutaka kuwaambia watu, kwa hiyo Elvin aliachiwa majukumu mengi sana pale ofisini, yakiwepo hayo ya malalamiko. Walikuwa wakimlalamikia kupita kiasi, na walikuwa wakimchosha asijue atawasaidiaje. Hakuna kitu kizuri ambacho wangeweza kukipokea bila shida. Baba yake, alikuwa akiajiri watu ambao wanashida na pesa. Hakuwa akiangalia vigezo hata kidogo. Ilimradi ukimlilia shida, basi anakupa ajira. Kwa hiyo Elvin aliachiwa ofisi kwenye mazingira magumu sana. Alizungukwa na watu ambao walikuwa mzigo, hawakuwa na sifa za kazi wanazofanya na hawakuwa tayari kujifunza. Akaamua na yeye afanye kazi bora liende. Sasa kuja kukutana na Bella, ilikuwa kama gari ambalo limeongezwa mafuta na kufanyiwa matengenezo na kupata dereva mzuri.
****************************************************
Alirudi nyumbani akiwa na furaha, kwa ajili ya maendeleo ya kazi yake. Aliona mambo yanavyokwenda vizuri pale ofisini kwake. Na kweli ile program ilikuwa sahihi kabisa. Dereva alimrudisha, lakini alimwambia Masha yupo tayari nyumbani, anamsubiri. Aliingia chumbani alipokuwepo Masha na tabasamu kubwa usoni. “Pole na kazi, T.” “Nasafiri Bella, nataka utulie. Umenisikia?”  Bella alibaki amesimama akimtizama Masha aliyempokea kwa mkwara. “Nauliza umenisikia?” “Nimesikia T. Sina mahali pa kwenda isipokuwa kazini tu. Siwezi kufanya ujinga wakati wewe umeniamini. Naomba usiwe na wasiwasi T. Nitakusubiri.” “Nikisikia tu unafanya mambo ya ajabu huku nyuma, sitakusamehe.” Bella alibaki kimya.
 “Unanisikia Bella?” “Nimesikia. Kwani utakaa siku ngapi?” “Unataka kujua ili ujipange kufanya madudu yako huku nyuma? Nitarudi nitakapo rudi.” Bella alizidi kuumia. ‘Nimfanyie nini huyu baba jamani? Nimefanya kila kitu anachotaka, lakini bado ameshindwa kuniamini.’ Bella aliwaza wakati Mzee Masha akizidi kumtishia maisha yake, endapo atakuwa na mwanaume mwingine.
“Na kesho nataka ubaki nyumbani, kwa ajili ya kuagana.” “Siwezi T. Nina kazi ambayo nilazima niifanye kesho. Tafadhali mpenzi wangu. Acha niende hata masaa machache tu, nitawahi kurudi.” “Unasemaje Bella!?” Mzee Masha alisimama akamvuta karibu. Bella alianza kutetemeka, huku analia. “Umeanza ujeuri? Ushapata mwanaume anayekudanganya huko?” “Hapana T. Unajua siwezi kuwa na mwanaume mwingine ila wewe. Siwezi kukusaliti.” Bella alikuwa akilia sana. “Naomba usinipige, Masha. Tafadhali sana.” Mzee Masha alimsukuma.
“Kazi zitasubiri, lakini sio mimi. Huogopi hata kidogo! Mimi namiliki biashara zaidi ya mbili hapa mjini, nakwambia kesho naacha kazi zangu ili niwe na wewe, halafu wewe kwa kazi hiyo moja ya kompyuta tu, tena ya watu, ndio unaniambia eti huwezi kuacha kwenda kazini kwa siku moja! Na nikuone kesho unatoa mguu wako humu ndani. Nitakufungia humu ndani mpaka nitakapo rudi. Umenielewa Bella?” “Nimeelewa T. Kesho sitakwenda kazini, nitabaki na wewe.” Bella alikuwa kitetemeka kwa hofu huku akiendelea kulia.
*********************************************
Na kweli, kesho yake Bella hakutokea kazini wakati ni siku ambayo alitakiwa kumsaidia mhasibu kufunga mahesabu ya mwezi. Alitamani kupiga simu kumueleza Elvin kuwa hatafika kazini, lakini asingethubutu hata kuonekana ameshika simu. Ilikuwa ni marufuku kushika simu au kompyuta yake kama Mzee Masha yupo nyumbani. Alibaki akimtumikia Mzee Masha vile atakavyo, kwa siku nzima.
Usiku alimsaidia kufungasha, tayari kwa safari siku inayofuata ambayo ndio hiyo aliyokosa kazini. Ilikuwa ni zaidi ya mwezi hajaenda kuangalia familia yake. Alikuwa akiondoka na ndege ya KLM ya usiku huo wa saa tano. Bella alimsindikiza mpaka uwanja wa ndege, akiwa na dereva. Walimsubiri mpaka ndege ilipoondoka ndipo dereva alipomrudisha nyumbani.
Kitu cha kwanza alichofanya aliwasha simu yake na kumpigia Elvin. “Samahani, nimekuamsha?” “Hamna shida. Ndio usingizi ulikuwa unanichukua. Nilikuwa ofisini muda wote najaribu kuona kama naweza kuwasaidia kufunga mahesabu.” “Pole sana. Samahani nilishindwa kufika, na nikashindwa kukutaarifu mapema.” Elvin alinyamaza. “Mlifanikiwa kufunga mahesabu yote ya mwezi?” “Tumeshindwa Enabella. Hakuna mwenye utaalamu huo, ila wewe.” “Samahani sana. Kesho naweza kumaliza.” “Kesho ni Jumamosi Bella. Watu hawafanyi kazi pale ofisini.” “Mimi naweza kwenda. Naomba kama inawezekana kesho niende nikajaribu kuona kama naweza kumalizia hiyo kazi.” “Peke yako? Maana nawajua wale kina mama, hawawezi kukubali kuja ofisini siku ya kesho.” “Nitafanya peke yangu, halafu jumatatu mkija ofisini nitawaelekeza nilichofanya.” “Saa ngapi unataka kwenda ili nije kukufungulia? Maana mimi ndio ninakaa na funguo za pale.” “Naomba wewe uniambie muda utakaoona sio usumbufu. Mimi nina nafasi kesho siku nzima, hata ukiniambia saa 12 asubuhi nitafika.” “Kwa kuwa nimechelewa kulala na nimechoka, naomba iwe saa mbili, ili na mimi nipumzike kidogo.” “Sawa kabisa. Utanikuta nakusubiri.”  Palizuka kimya kwa muda. “Hey Enabella!” “Bado nipo.” Bella aliitika. “Naomba kama hutaweza kufika hiyo kesho, unijulishe mapema, usiniache nakusubiri.” Bella alijisikia vibaya sana. “Nimeelewa.” Bella alijibu kinyonge sana. Alijua Elvin amekasirika kwa kutotokea kazini. Alisikia simu imekatwa.
Haraka sana Bella alijitupa kitandani huku akitokwa na machozi ya furaha, akifurahia uhuru wa usiku huo. Alilala kama mtoto mchanga kwa uchovu. Aliamka kwa kuchelewa kidogo, kwa hiyo hakupata muda wa kunywa chai na hakutaka kumchelewesha Elvin.
Alivaa harakaharaka na kutoka. Akiwa njiani alituma ujumbe, ‘Nipo njiani.’ Baada ya muda mfupi aliona Elvin amejibu. ‘Nilishafika.’ Bella aliogopa kidogo akaangalia muda ilishakuwa saa mbili na robo.  Alijitahidi kuongeza mwendo ili asizidi kuchelewa.
*********************************************
Alimkuta Elvin ofisini kwake. “Samahani kwa kuchelewa.” Elvin alimwangalia, “Ni afadhali umekuja, kuliko kutokutokea kabisa.” Bella alijua wazi Elvin bado amekasirika. “Jana nili…,” Bella alijua hata akimpa sababu hawezi kuelewa, na hayamuhusu, akaamua aache kujitetea, aombe msamaha tu. “Samahani kwa kutokutokea jana, na kushindwa kuwasiliana.” “Ulikuwa ukikumbuka kama tulikuwa tukikutegemea wewe?” “Ndiyo. Lakini nilishindwa.” “Hata kutuma ujumbe!?” Bella alinyamaza. Alitamani kama Elvin angeelewa hata kidogo mazingira yake, labda asinge laumu.
“Hii ni kazi Bella. Unapoahidi kufanya jambo, jitahidi kukamilisha. Kwa sasa wote tunakutegemea wewe. Naomba usisahau hilo. Watu wengi walikwama jana bila msaada. Na hukutoa taarifa yeyote, tukabaki tunasubiri mpaka jioni, kwa kuwa pia huna muda maalumu unaoingia kazini. Unakuja unapojisikia wewe.” Elvin alionekana amekasirika sana lakini alijitahidi kuongea kiuungwana kidogo. Bella alikuwa bado amesimama mlangoni.
Alisogea karibu na meza ya Elvin, akavuta kiti, akakaa. “Elvin!” Bella alianza kwa kuita jina lake. “Kumbe unanifahamu jina langu!?” Elvin aliuliza kwa kumshangaa. “Maana tangia unaanza hii kazi, sijawahi kusikia ukitamka jina langu hata mara moja. Mpaka nikawa na wasiwasi labda hatukukupa utambulisho wakutosha! Lakini baadaye nikakumbuka, nilishajitambulisha wakati tulipokutana Dubai, tena hata kule hukuonyesha kama ulinisikia. Sasa sijui umeamua kunipuuza au vipi? Eti Bella?” Bella alinyamaza akiwa bado ameinama, akiwaza amwambie nini Elvin bosi wake. “Basi, ofisi zote nilishafungua. Ukihitaji kitu chochote, nitakuwa hapa ofisini kwangu.”
“Maisha yangu hayatabiriki Elvin, nipo katika wakati mgumu sana. Hakuna jinsi nikaeleza ukanielewa. Nimejawa hofu, ni kama natembea na kifo mgongoni mwangu. Nashindwa hata kuahidi chochote. Siwezi hata nikakuahidi kama nitabadilika, katika mapungufu yote ambayo umeshayaona kwangu, kwa kuwa hata sijui kama baada ya dakika moja ijayo nitakuwa hai au la. Nataamani kukuahidi kama siku nyingine nikishindwa kuja nitakutaarifu au nikuahidi nitakuwa nakuja kazini kila siku muda fulani, nashindwa Elvin. sio kwa sababu ninakudharau, au sithamini hii kazi. Hapana. Naomba kukuhakikishia, naipenda kazi yangu na ninaihitaji sana. Na ndio maana kila ninapopata nafasi ya kufanya kitu, nakifanya wakati uleule kwa akili zangu zote na moyo wangu wote, kana kwamba hakuna kesho. Tafadhali naomba univumilie. Nitajitahidi kufanya hii kazi kwa kadiri ya uwezo wangu, na ninakuahidi kukukamilishia ripoti mapema iwezekanavyo. Kama kila mtu atakuwa ameweka vocha zake kwenye kompyuta, nitahakikisha jumatatu unaikuta ripoti kwenye email yako kabla hujaanza kazi.” Elvin alikuwa kama amepigwa na bumbuazi. Alibaki kimya kwa muda.
“Naomba univumilie.” Bella akarudia tena huku akifuta machozi. “Sawa. Mimi nitakuwa hapa ofisini. Ukihitaji kitu chochote uniambie.” Bella alifikiria kidogo huku akijaribu kutulia. Alijikausha machozi yote, akamwangalia. “Kwa nini usingeenda kupumzika tu, halafu ukarudi baadaye? Kuliko kukaa tu hapa ofisini. Najua unakuwa na kazi nyingi sana kwa juma zima na siku ya leo ndio siku yako yamapumziko. Nenda tu. Kama nina maswali nitakujulisha kwa simu.” “Unauhakika? Maana ni kweli nimechoka.” “Kabisa. Wewe funga tu milango yote, ili mtu yeyote asije niingilia humu ndani.” “Basi ngoja nikalale kidogo, halafu nitarudi baadaye.” “Sawa.” Bella alitoka na kuingia ofisi ya muhasibu, akaanza kufanya kazi.
Alikaa hapo ofisini akiandaa hiyo ripoti siku nzima. Alishangaa jinsi walivyotawanya vocha, kana kwamba walitaka kumkomoa yeye. Lakini Bella akajitahidi kuzikusanya na kuzipangilia vizuri kwa tarehe na kuendelea kuziingiza kwenye kompyuta.
*********************************************
Ilipofika mchana Elvin alirudi na msichana wake. “Vipi? Mambo yanaelekea?” Elvin akauliza. “Kuna matumaini. Nahitaji muda zaidi.” Bella alizungusha kichwa kumwangalia Elvin. “Ungepumzika kidogo angalau ukale.” “Nitakula baadaye.” Bella alisikia mtu mwingine akiongea kutokea kwenye ofisi ya Elvin. “Hey Elvin, njaa inauma bwana.”  “Nakuja sasa hivi.” Elvin alijibu na kumgeukia tena Bella. “Kwa hiyo umegoma kula?” Kabla Bella hajajibu akasogea yule dada. “Mambo!” alimsalimia Bella. “Safi tu.” Bella alijibu kwa kifupi, kukazuka ukimya.
“Huyu anaitwa Irene. Irene huyu anaitwa Bella ndiye anayetusaidia kwenye maswala ya IT.” “Mbona yeye utambulisho wake mrefu wangu ni Irene tu?” Irene aliongea kwa kulalamika huku akimwangalia Elvin. “Unamaanisha nini Irene?” “Wewe kweli ndio wakuniuliza hivyo Elvin au kuna kitu unaficha?” “Naficha nini tena? Sina ninachoficha.” Irene aliondoka kwa hasira. “Samahani Bella. Nitarudi baada ya muda kidogo.” Bella aligeukia kompyuta yake na kuendelea na kazi zake.
Baada ya muda kidogo, Elvin alirudi akiwa amemshika mkono Irene. “Samahani Bella, naomba nimalize utambulisho.” Bella aligeuka tena akionekana ana sura ya kazi, kama asiyetaka usumbufu. “Huyu anaitwa Irene, ni girlfriend wangu.” “Tunakaribia kuvuka huko bwana, tunakaribia uchumba.” Irene aliongeza huku anatoa tabasamu. “Oookayyy!” Bella aliitikia huku akiwatizama kwa kushangaa kidogo. Hakuona ulazima wa utambulisho wote ule, ni kama alikuwa akiwataarifu, ‘hayanihusu’. Ukimya ulitanda kidogo, Bella akiwasubiri kama kuna lanyongeza, alipoona wote wanababaika aliona awe muungwana kidogo, “Nafikiri natakiwa kuwapa hongera, ni sawa?” “Ndiyo. Maana ni hatua kubwa sana katika maisha. Kila mwanamke angetamani kuwa na mwanaume kama Elvin.” Irene alijibu kwa kujivuna kidogo. “Hongera.” Bella alijibu kwa kifupi. “Asante.” Bella aliwatizama tena kama vile akitaka kuuliza, kuna la nyongeza? Alipoona Irene anacheka tu, Bella aligeukia kompyuta yake, akaendelea na kazi zake, akasikia wanaondoka.
 “Umefurahi sasa?” Bella alimsikia Elvin akimuuliza Irene. “Sasa je? Nilidhani unanitosa mchana kweupe!” Wote walicheka, akawasikia wakifunga mlango mkubwa wa kuingilia hapo ofisini. Bella alirudisha mawazo yake kwenye kazi yake.
Alikaa pale ofisini peke yake, mpaka ilipofika jioni ndipo Elvin alirudi tena. “Unataka kufunga ofisi sasa hivi?” Bella aliuliza pale Elvin alipoingia pale ofisini. “Nakusikiliza tu wewe, hata ukitaka kukesha leo, hamna shida, na hivi nililala mchana. Sina neno.” “Basi naomba tena muda kidogo. Kama unamahali unataka kwenda, ungeenda tu, halafu nikimaliza nitakupigia.” “Hamna neno. Nitakuwa ofisini kwangu.” Bella hakupoteza muda aligeukia kompyuta yake tena na kuendelea na kazi.
Aliifanya ile kazi bila kuchoka mpaka ilipofika usiku kabisa. “Kunywa angalau maji Bella.” Elvin alirudi tena kwenye ofisi aliyokuwepo Bella. “Ndio nakutumia ripoti sasa hivi. Nimeshamaliza.” “Daah! Kweli wewe kichwa!” Bella alitabasamu huku akiangalia kompyuta yake, akiendelea na kazi aliyokuwa anafanya.
Bado Elvin alikuwa amemsimamia pale pale ofisini. “Nikuulize kitu Elvin?” “Uliza tu.”“Hii faida unayopata hapa sasa hivi, inalingana na matarajio yako?” “Hii ni kampuni ya baba, Bella. Na mimi nimeajiriwa kama watu wengine. Kuna mambo natamani kubadilisha lakini nashindwa. Lengo la baba kwenye hii kampuni si kutengeneza pesa peke yake, anataka iwe msaada kwa watu wengine pia. Ndio maana unakutana na watu wengi humu ndani ambao hawana hata vigezo vya kazi zao.” “Nimekuelewa. Lakini sasa hivi wewe ndio upo kumsaidia kuendeleza. Nia ya baba ni nzuri, nafikiri ndio maana hata mimi mwenyewe nipo hapa leo, japokuwa sina vyeti. Naona tumsaidie kuongeza faida.” Elvin alivuta kiti akakaa.
“Kwa kufanyaje?” “Naomba tuongee jumatatu kama Mungu akitupa uzima, sasa hivi nimechoka, nataka nikapumzike kidogo.” “Ni kweli. Umefanya kazi siku nzima bila kupumzika tutaongea jumatatu kama utakuja.” Bella alitabasamu. “Naamini nitakuja.” Bella alifikiria kidogo. “Unafikiri ni sawa kama nikichukua baadhi ya kazi nikafanyie nyumbani.” “Nini tena?” “Kuna kazi kubwa sana za nyuma, ambazo wamebakisha watu wa masoko. Nataka kesho nizifanyie kazi.” “Huwendi kanisani?” Bella alikunja uso. “Kanisani!?” “Ndiyo. Kuabudu.” “Hapana. Huwa siendagi kanisani. Siku za jumapili nakuwepo tu nyumbani, ndio maana nataka nikafanyie kazi nyumbani.” Elvin alibaki akimshangaa Bella jinsi alivyojitoa kwenye ile kazi. “Ni sawa tu. Wewe endelea.” Elvin alimpa ruhusa. Aliingia kwenye ofisi za watu wamasoko, akakusanya kazi zote za nyuma, akapakiza kwenye gari yake, akaondoka.
*********************************************
Siku ambazo Mzee Masha hakuwepo nyumbani, Bella alizitumia vizuri sana. Alikuwa akiamka asubuhi sana kuwahi kazini, na kurekebisha kazi za kila kitengo. Maneno yalianza kupungua, ikabaki heshima tu. Maana mwanzo walifanya mbinu nyingi kumuharibia kwenye uongozi, lakini baadaye walikuja kujiona ni kujisumbua wenyewe. Akili na mawazo ya Bella yalikuwa kwenye kazi tu, hakutaka kujichanganya kabisa pale ofisini. Palipokuwa na mgonjwa, misiba, sherehe, na wakachangisha, Bella hakuacha kuchanga. Alipokuwa akisikia mtu anashida yeyote, japokuwa hatataka kujua kwa undani, aliweka pesa kidogo kwenye bahasha, na kutafuta muda ambao huyo mtu yupo peke yake na kumkabidhi. Wanawake wa pale ndani hawakuacha kutupiana maneno au kusemana, na Bella alikuwa akiwasikia, lakini kila penye masengenyo, au ugomvi, Bella alijitahidi kuondoka. Aliwaonyesha wazi, hataki mahusiano, nje ya kazi. Walimuelewa kwa haraka sana, na wakaanza kumpenda. Alipewa ofisi yake kitu kilicho mfurahisha zaidi.
Aliitengeneza hiyo ofisi na kuipamba vizuri sana. Mezani kwake aliweka picha kubwa ya Eric, akawa akiiangalia kila wakati. Alipamba na maua mazuri pembezoni mwa ofisi yake. Kila kona aliweka vyungu hivyo vya maua, juu ya stuli nzuri sana. Vilionekana ni vyungu na stuli za thamani kweli. Yote hiyo ilikuwa pesa yake. Akatandika zulia zuri la thamani pia. Ungependa kuwepo kwenye ofisi hiyo ya Bella.
Kwa kuwa kulikuwa na wafanyakazi wengi ambao Bella aliona hawana kazi pale ofisini, na wanalipwa mshahara, Bella alimpa Elvin mawazo ya kuongeza biashara nyingine, ambayo hata wale ambao hawakusoma ingewafaa na kuwaanzishia kitengo chao, kwa kutumia jina hilohilo la kampuni lakini biashara nyingine.
Kwa kuwa Mzee Mwasha alipotea pale ofisini, Elvin alimfanya Bella kuwa mshauri wake mkubwa. Hakuna kitu ambacho alikifanya bila ushauri wa Bella. Kidogo wakaanza kuwa karibu. Angalau waliweza kusalimiana na kuulizana hali. Ile hali ya kazi tu kati yao ikaanza kupungua. Elvin aliweza kuingia ofisini kwa Bella na kutoa salamu tu na Bella asishangae. Mtu mwingine ambaye hakuwa na tatizo kuingia ofisini kwa Bella alikuwa Joo. Joo aliingia kufanya utani wa hapa na pale, na watu wote walianza kujua Joo ndiye mtu pekee anayeweza kumfanya Bella acheke au aache kazi zake na kumsikiliza yeye, hata akiwa anaongea vitu visivyo na maana. Alikuwa na utundu wa namna yake, uliokuwa ukimfurahisha Bella. Japokuwa hakuwa akiongea sana, lakini alikuwa akimsikiliza na kumfanya acheke.
 “Mkasa mwingine wakusikitisha wa Bella.”
Wakati mambo ndio yanakwenda vizuri, Bella ndio amepata heshima pale ofisini, Mzee Masha naye akarudi kutoka uholanzi. Aliingia na ndege ya Emirates saa nane mchana. Moja kwa moja nyumbani kwa Bella. Aliamua kulala huku akimsubiri Bella ajue ni saa ngapi huwa anarudi nyumbani. Siku hiyo ilikuwa siku ya mvua, usafiri ulikuwa washida sana jijini Dar. Joo akamuomba Bella amsogeze karibu na daladala za Kariakoo ambazo alijua lazima zitakuwepo kwa muda huo, kituo cha Posta Mpya.
Kwa kuwa hakuwa na kitu kinachomuwahisha nyumbani, na walimaliza kazi mapema, Bella alikubali. Hata hivyo alimpenda Joo, alimfanya asahau shida zote na awe na furaha. Njia nzima Joo alikuwa akipiga yeye stori za mtaani kwao uswahilini. Bella alikuwa akicheka sana, akikumbukia maisha ya Kigogo alipokuwa akiishi na Mat, dereva wao. Kulikuwa na foleni kubwa sana, lakini Bella hakujali. Walipoona hakuna daladala za Kariakoo, akaamua amsogeze mpaka  Tazara, ambako alijua lazima kwa wakati ule asingekosa daladala.
Walitoka Posta mpya kuelekea Tazara huku mvua ikinyesha sana, na walikutana na foleni kubwa njiani, lakini Bella hakujali. Aliendelea kusikiliza porojo za Joo huku akicheka. Hakuwa na wasiwasi kabisa, kwani alijua hakuna wakumuuliza, na hakuna anayejali, kwani hata dereva wa Mzee Masha na yeye alikuwa likizo, kwa hiyo Bella akawa hana wasiwasi kabisa. Alimshusha Joo kituoni Tazara, akaanza safari ya kurudi nyumbani kwake, akiwa amejawa furaha, anaimba na kucheka peke yake.
Alifika nyumbani kwao kama saa nne za usiku akiwa amechoka sana. Alipoingia tu alimkuta Mzee Masha amekaa sebleni. Bella alibaki ameduwaa mlangoni bila salamu yeyote. Alitamani arudi alipotoka. Alijua kipigo kinachofuata pale sio cha kawaida. Mzee Masha hakuwa mtu wakusikiliza hata kidogo, kwa hiyo alijua kujitetea ni kujiongezea matatizo. Bella alibaki akimwangalia huku anatetemeka. Alikuwa amelowa kidogo, sababu ya kutembea alipokuwa ameegesha gari lake mpaka ndani. Mbaya zaidi Mzee Masha alikuwa hawezi kukaa sehemu yenye joto. Kwa hiyo mara zote kila awapo nyumbani aliwasha AC, upande wa baridi na wakati wote nyumba yao ilikuwa na baridi kali sana. Alianza kusikia ile baridi mpaka kwenye mifupa. Bella alibaki akitetemeka huku akimwangalia Mzee Masha. Hakuna jinsi angemwambia Mzee Masha alitoka kumpeleka Joo kituoni Tazara akapona. Alijua kifo chake ndio kimefika. Alimkumbuka Eric mdogo wake, machozi yalianza kumtoka.
“Umetoka wapi Bella? Na usinidanganye, kwa kuwa nimepiga simu ofisini kwako nimeambiwa ulitoka kazini tokea saa kumi na mbili.” Bella alibaki akilia. Mzee Masha alisimama na kumsogelea. “UNATOKA WAPI?” Bella alipata kibao cha nguvu, akamvuta mpaka chumbani. “Walinzi wameniambia, week zile za mwanzoni nilipoondoka tu, ulikuwa ukitoka alfajiri sana, na kurudi usiku sana. Ulikuwa ukienda wapi Bella? Unataka kuniua? Unanitia aibu pale kwa Mzee Mwasha, wanaona nimewapelekea Malaya. Wewe ni zaidi ya mbwa Bella. Nimejitahidi kukuridhisha kwa kila kitu lakini hutosheki!” Bella alipigwa usiku huo, kupita kiasi.
“Niambie ulipokuwa Bella, hakika nitakuua leo.” “Hata nikikwambia hutaniamini.” Bella akiwa anatokwa na damu mdomoni, tena ametupwa sakafuni, alijibu. “Kwa nini hauniuwi tu, T. Kwa nini huchukui bastola yako ukaniua na mimi nipumzike. Nimechoka T, umenipiga zaidi ya lisaa, na bado hujatosheka. Naomba unimalize tu, ili upumzike. Lakini nakuhakikishia, sijatoka sehemu mbaya, na hata nikikwambia hutaniamini.” Bella alikuwa akilia sana. “Niuwe tafadhali. Huna cha kupoteza. Najua unauwezo wakupata mtoto mwingine kama mimi ambaye atakuridhisha. Kwa nini usiniue tu, ukaendelea na maisha yako, kuliko hivyo unavyoishi kwa wasiwasi. Huniamini kwa lolote, umenigeuza kuwa ngoma, huni thamini. Unanionea. Unaninyanyasa vile unavyotaka. Unatumia mwili wangu bila shukurani.” Mzee Masha alimsogelea tena.
“Nimekwambia usithubutu kunipiga tena, Mzee Masha. Inatosha. Leo ndio iwe mwisho wako, naomba tumalizane. Niue yaishe. Niue T. Ukitoka kwa mkeo na hasira zako, unakuja kunimalizia mimi, unanipiga kila siku bila kosa. Watoto wako wakikuudhi, au wakikujibu vibaya, au wakigoma kuendelea na masomo, unakuja kunipiga mimi.” Bella aliendelea kulia. “Unashangaa nini? Unafikiri ni wewe tu mwenye uwezo wakurikodi simu yangu? Hata mimi narikodi simu yako.” “Unasemaje Bella?” “Nimekwambia na mimi na rikodi simu yako. Huwezi kuja kuniua na UKIMWI, T. Lazima nijue tupo wanawake wangapi.” “Kwa hiyo unanifuatilia?” “Ndiyo.” Bella alijibu kwa hasira sana.
“Usinisogelee T. Nimechoka, kama hutaniua leo, naomba uniache. Kila watoto wako wakikukorofisha au mkeo akikukorofisha, unageuka kuwa kama mnyama kwangu na kunifanya utakavyo. Kama sio kunitafutia sababu ya kunipiga, basi utanibaka siku nzima. Nimekuwa jalala lako! Unanitumia kumwaga huzuni zako, hasira zako na kila kitu kibaya kwenye maisha yako, mimi ndio umenifanya sehemu yakutupia. Na bado hunithamini. Sidhani hata kama umewahi kumpiga mkeo kama unavyonipiga mimi. Sidhani hata kama umewahi kuheshimiwa na kutunzwa kama ninavyokufanyia mimi, lakini bado unanifanyia ukatili wakupita kiasi na Mungu atakulipa T. Ipo siku atakulipa kwa mabaya yote unayonifanyia. Kama sio wewe basi Zera naye atapita nilipopita mimi na wewe ukiona sio ukiwa umekufa. Utajua mateso ninayoishi nayo.” Bella alikuwa amejawa na uchungu sana. Aliinama akawa analia sana huku damu zikimwagika sakafuni, hata yeye mwenyewe hakuwa akijua zinatokea wapi. Mzee Masha aliondoka usiku huo bila kuongeza kitu wala kumpiga tena.
*********************************************
Kwa maumivu makali aliyonayo, Bella alishindwa hata kusimama, alilala pale pale chini mpaka asubuhi. Aliamka akiwa na maumivu makali sana. Mwili wote ulikuwa umevimba. Alitambaa mpaka sebleni ilipokuwa imedondoshwa pochi yake na simu yake ya mkononi. Akapiga simu getini kuita mlinzi. Mlinzi alipokuja alimuomba msaada wakumbeba mpaka kwenye gari yake. Mlinzi akaja kwa haraka, akambeba mpaka kwenye gari huku akilia sana maumivu.
Safari hii aliamua kwenda hospitalini yeye mwenyewe, kwani alikuwa na maumivu makali sana, hasa kwenye mbavu. Alihisi kule kupigwa mateke kwa muda mrefu, amevunjwa mbavu. Bella alipandishwa kwenye gari akiwa na lengo la kwenda hospitalini. Alijua kama kawaida yake, Mzee Masha akishampiga vile, huwa anapotea hata mwezi.
Bella aliendesha mpaka alipofika Mwenge, akaanza kuona giza. Akaamua akate kona aingie njia ya kiwanda cha Cocacola ambapo hakuna magari mengi, akaliegesha gari pembeni kabisa ya barabara. Alikaa pale akisubiri ajisikie vizuri ili aendelee na safari yake, lakini alishindwa kuona tena, ilikuwa giza kabisa, wakati ilikuwa ni asubuhi jua limechomoza, akaamua kumpigia simu Elvin. Alibonyeza simu yake, akatamka jina la Elvin, aliposikia simu yake imetamka jina la Elvin, akaamuru simu hiyo kumpigia Elvin. Simu yake ilikuwa na uwezo wa kufanya chochote kwa kuamrishwa kwa sauti bila ya Bella kubonyeza sehemu.
“Bella!” “Nisaidie Elvin.” Bella alikuwa akisikika kwa shida sana, kwani alikuwa akilia na yupo kwenye maumivu makali sana. “Uko wapi?” “Kiwanda cha C..” Bella alishindwa kuongea. “Bella! Bella!” Elvin alizidi kupanic. “Uko wapi Bella?” Bella alikuwa akimsikia Elvin kwa mbaliii. Akajikaza ili kumpa maelekezo yakueleweka. “Mwenge, karibu na kiwanda cha Coc..” Alishindwa kumalizia. Akapoteza fahamu kabisa. “Bella! Bella!” Elvin aliendelea kuita kwa hofu, bila majibu upande wa pili.
Baadaye sana alisikia kwa mbali mtu akiongea, na kumpima pressure yake. Bella alijua yupo hospitalini, akajaribu kufunga macho lakini akashindwa. “Maumivu. Nasikia maumivu makali sana.” “Wamesema watakuchoma sindano ya maumivu sasa hivi. Pole Bella.” Aliposikia sauti ya Elvin, alijua yupo salama. Akapotelea usingizini huku anagugumia maumivu.
Alishtuka tena akiwa amelazwa kwenye kitanda cha hospitalini. Alitaka kugeuka lakini alishindwa kabisa, maumivu yalikuwa makali. Alitaka kuongea, lakini mdomo ulikuwa kama umewekwa gundi, Bella alianza kulia tena kwa kulalamika. Elvin alisimama alipoona anajaribu kufungua macho. “Jicho hilo la kulia, lilipasuka kidogo hapo kwenye nyusi, Bella. Wamekushona. Ndio maana inakuwia ngumu kufungua macho. Na mdomo umevimba sana sababu umepasuka pia. Usijaribu kufungua utajitonesha. Wamekutundikia dripu ya maji ili kukupa nguvu na wamekuwekea dawa kwenye hayo maji, ili kuzuia kuvuja kwa damu kwa ndani. Wamegundua jana usiku kuwa ulikuwa unavujia damu ndani kwenye mbavu za upande wakulia. Pia  mbili zimevunjika. Wameweza kusimamisha hiyo damu. Lakini usigeuke, utajitonesha zaidi.” Bella alifunga macho huku machozi yakimtoka, alilia kidogo kisha akapotelea usingizini tena.
Alikuwa chumba cha wagonjwa mahututi, na alipoteza fahamu kwa siku mbili mfululizo. Walijaribu vipimo vingi, kwani hali yake ilikuwa ikizidi kuwa mbaya. Ndipo ilipobidi kufanyiwa vipimo vya mwili mzima, wakagundua anavujia damu kwa ndani. Elvin alishindwa kuondoka kabisa pale hospitalini. Alijilaumu sana kuto muuliza Bella siku ile wakati wanazungumza, na Bella alimwambi kuwa anatembea na kifo mgongoni.
‘Hasira zilinifanya nishindwe kumsaidia Bella. Labda alikuwa anahitaji msaada wangu. Ni mara ya pili hii Mungu anamleta kwenye maisha yangu. Na mara zote anakuwa kwenye shida, na nimeshindwa kumsaidia. Kwanza Dubai, Bella alikuwa akilia sana, tena kwa uchungu, na tena hapa! Nimeshindwa kumsaidia kabisa Bella.’ Elvin aliendelea kujilaumu sana moyoni mwake. Alikaa naye pale hospitalini asijue ampigie simu nani. Kwani simu ya Bella ilikuwa haina jina hata moja, zaidi ya namba yake tu, ambayo ilionyesha ndio aliyopiga kabla hajapoteza fahamu. Hapakuwa na namba nyingine yeyote. Ilikuwa kama simu mpya kabisa, kitu kilichomshangaza Elvin.
Baada ya kulala kwa muda mrefu, kwa mbali tena, akasikia watu wakizungumza. “Kapumzike Elvin, mimi nitakuwa naye hapa.” “Siwezi kuondoka mama.” “Wewe umesikia madaktari wamesema huyu sio mtu wakuzinduka leo wala kesho, mpaka hiyo damu iingie mwilini vyakutosha. Nenda kalale kidogo, halafu ukiamka umtafute na Irene. Mwenzako anawasiwasi sana na wewe Elvin. Ni siku ya tano hii hujamtafuta. Mpaka wazazi wake wanatupigia simu kukuulizia. Wanawasiwasi kama umebadili mawazo.” “Waambie sijabadili mawazo hata kidogo mama. Lakini nahitaji muda kidogo. Nilishamuahidi Irene nitamuoa, na nitafanya hivyo. Sina sababu ya kutokufanya hivyo, wewe unanijua mama.” “Kwa nini wewe mwenyewe usimpigie Irene ukazungumza naye?” “Wewe unamjua Irene, mama. Atataka aje tukae nae hapa, huku akilalamika. Itakuwa vurugu tupu hapa. Wewe tafuta jinsi ya kuzungumza nao, mama yangu. Bella akipata nafuu, tutaendelea na mambo ya uchumba kama tulivyopanga.” “Pete ulishachukua?” Mama Mwasha alimuhoji mwanae. “Nilishalipia mama. Nitaenda kuichukua, au mwambie baba akanichukulie.” Kumbe Bella alizimia tena siku mbili zilizopita, ndipo wakagundua ile damu waliyodhani wameidhibiti hawakuwa wamefanikiwa, kwa hiyo aliishiwa damu. Wakafanikiwa kumfanyia upasuaji, wakamsafisha, na kumuunganisha mirija hiyo ya damu, akawekewa damu nyingine. Hali yake ilikuwa mbaya sana. Ilikuwa ngumu kumtizama Bella mara mbili. Alivimba uso sana. Mwili mzima ulijaa alama za mikanda ya suruali. Wazi alionyesha alipigwa vibaya sana.
Bella akarudi kulala. Lakini akiwa kwenye usingizi mzito Bella alisikia Eric akimwita, ndio maana akashtuka. “Ric! Riccc!” Bella alianza kumwita mdogo wake. Elvin alisimama kwa haraka. “Unajisikiaje?” “Ric!” Elvin alikumbuka jina la Eric, akajua ndiyo huyo Bella anamtaja kwa kifupi. Kwani ni picha ya Eric pekee ndiyo ilipamba ofisi ya Bella. “Upo hospitalini Bella.” Bella alianza kulia huku anaongea kitu. Elvin aliinama kutaka kumsikiliza. “Sikusikii Bella. Pumzika tutaongea baadaye.” Bella alitingisha kichwa kukataa. Elvin alisogeza masikio karibu na mdomo wa Bella uliokuwa bado umevimba. Alimsikia Bella akitaja namba, Elvin aliziandika zile namba akagundua ni za simu. Naomba umpigie simu huyo mtu, tena naomba utumie simu yako, usimwambie kabisa nilipo, mwambie akamwangalie Ric.” Baada ya muda mrefu sana, ndipo Elvin aliweza kuunganisha maneno, akaelewa ujumbe mzima. “Sawa nitafanya hivyo.” Bella alirudi kulala tena.
Alikuwa akilala tu kwa muda wa majuma mawili mfululizo. Baada ya siku kumi na nne ndipo angalau Bella aliweza hata kunyanyua mkono. “Vipi?” “Najisikia vizuri leo.” Elvin alikuwepo pale hospitalini peke yake akimuuguza Bella. “Pole sana.” Bella alianza kulia. “Pole Bella.” “Asante. Ric?” “Nilipiga ile namba ya simu uliyonipa. Nikakutana na mtu anaitwa Mat, akasema atakwenda kumwangalia Ric shuleni. Nilipopiga siku inayofuata, akasema yupo Arusha, lakini Ric wamekwenda Nairobi kwenye michezo.” Bella alifurahi sana. “Asante Elvin.” Machozi yalikuwa yakimtoka Bella. “Karibu.” Elvin alibaki akimwangalia Bella, hakujua chakusema. “Utapona Bella. Ulibahatisha kupata madaktari wazuri sana. Wamekuwa wakikuhangaikia usiku na mchana bila kuchoka. Na mimi nimekuwa nikikuombea.” “Asante.” Mara mlango ukafunguliwa. Waliingia wazazi wa Elvin.
Sifa za Bella zilishafika kwenye familia ya Mzee Mwasha. Jinsi alivyobadilisha ile kampuni na jinsi alivyojitoa kufanya kazi bila kudai malipo ya ziada. Kila mmoja wao aliona anajukumu lakumsaidia Bella. “Pole sana mama. Pole.” Mzee Mwasha alisogea kitandani kwa Bella. “Asante.” Bella alijibu taratibu lakini waliweza kuelewa. “Unajisikiaje?” Mama Mwasha naye akauliza. “Sasa hivi maumivu sio makali sana.” Machozi yalikuwa yakimtoka Bella taratibu pembeni ya macho yake. “Utapona mama. Umesikia? Utapona. Tunakuombea, na kabla yakuondoka hapa, tutaomba pamoja. Mungu atakusaidia.” Bella alitingisha kichwa. Mzee Mwasha akaomba atoke nje na Elvin. Wakatoka na kumuacha Mama Mwasha na Bella.
*********************************************
 “Lazima umpigie simu Irene sasa hivi, na urudi nyumbani ukamuone. Kila siku anakuja nyumbani kukuulizia. Anawasiwasi kwamba umebadili mawazo. Watu wote sasa hivi wameingiwa na wasiwasi Elvin. Huwezi kuanzisha jambo na kuliacha katikati. Umenielewa?” “Ndiyo baba.” “Sisi tutakuwa hapa na Bella, mpaka utakaporudi. Umenielewa? Rudi nyumbani, pumzika, ndipo urudi hapa. Hata kama ni usiku, sisi tutakuwepo hapa. Hata sisi tunamjali Bella. Hatuwezi kumuacha hapa peke yake, mpaka ndugu zake watakapofika. Unanielewa?” “Nimeelewa baba. Basi ngoja nikamuage.” Mzee Mwasha alimpisha. Elvin akarudi kwa Bella.
“Hey Bella!” Bella akafungua macho. “Nitarudi baadaye.” Bella alijitahidi kutoa mkono wake ndani ya shuka na kumpa Elvin. “Asante sana Elvin. Nakushukuru.” “Nitarudi. Sitakawia.” Bella alitingisha kichwa huku machozi yakimtoka. Elvin alisimama akimtizama Bella kwa muda, mpaka baba yake alipomwita tena. “Elvin!” Alishtuka kidogo, akachukua funguo za gari lake, akaondoka. Bella alirudi kulala.
Aliamka usiku akamkuta Mzee Mwasha na mkewe bado wamekaa wakimwangalia. “Unajisikiaje?” “Vizuri kabisa. Leo ni tarehe ngapi?” Bella aliuliza. Alipotajiwa, alifikiria kidogo, akashtuka sana. “Imeshakuwa zaidi ya siku kumi na nne tokea niwe hapa!?” “Ndiyo.” “Nataka kuondoka hapa. Siwezi kuendelea kukaa hapa hospitalini.” Bella alionyesha kupanic sana. “Lazima niondoke sasa hivi.” Bella alianza kulia, gafla mlango ukafunguliwa. “Mbona analia?” Alikuwa ni Elvin. “Mama?” “Ndio ameshtuka kutoka usingizini sasa hivi, analia anataka kuondoka.” Elvin akamsogelea Bella. “Hey Bella! Bella? Niangalie.” Bella alizidi kulia.
“Hali yako bado sio nzuri. Lazima usubiri madaktari wakuhudumie.” “Huwezi kuelewa Elvin, lakini ni lazima niondoke. Nimeshapona, nitaendelea kunywa dawa nikiwa nyumbani.” “Umejiona lakini Bella?” “Hii ni kawaida Elvin, nimeshazoea. Nitakuwa sawa. Naomba ukaongee nao, hizo dawa wanazonipa waniandikie vidonge, niondoke sasa hivi, siwezi kuendelea kukaa hapa hata zaidi ya dakika kumi. Tafadhalini. Lazima niondoke, sasa hivi.” “Ni usiku sana Bella. Kwa nini usisubiri kesho?” “Unaniahidi kesho utazungumza nao waniruhusu?” “Nitaongea na daktari.” Bella alitulia kidogo.
“Wazazi wako wako wapi Bella?” Mzee Mwasha aliuliza. Baada ya muda mrefu sana Bella akajibu. “Tulikuwa tukilelewa na mama, lakani alifariki.” “Ndugu zako wako wapi?” Hapo Bella hakujibu kabisa alikaa kimya mpaka Mzee Mwasha na mkewe walipoaga na kumuacha Elvin akiendelea kuuguza. Wakati Elvin anawasindikiza wazazi wake, Bella alijitahidi mpaka akaweza kukaa. Alianza kujichomoa kila mpira uliopo kwenye mwili wake. Alichomoa mpaka dripu ya maji.
Akasimama kwenda chooni. Alijiangalia jinsi alivyovimba, na kuwekwa bendeji usoni. Bella akaanza kutoa taratibu. Japokuwa uso ulikuwa umevimba, lakini Bella hakushtuka hata kidogo, alishazoea ile hali. Taratibu aliosha uso wake, na maji huku akisikia maumivu lakini pia hakushtuka. Yale maumivu ya sasa hayafikii hata nusu ya maumivu aliyokwisha wahi kujisikia. Elvin alirudi, akashtuka sana. Alimsikia anaoga bafuni.
Maji kutoka kwenye dripu yalikuwa yanamwagika sakafuni, na waya zote zilizokuwa zimewekwa mwilini mwake, kuangalia mapigo ya moyo, na mipira ya kumsaidia kuhema, vyote vilikuwa vimezagaa sakafuni pia. Elvin alimwita nesi, wakasafisha, na kubaki wakimsubiria Bella, waliyedhani ni mgonjwa mahututi, atoke bafuni. Hakuna aliyeamini alipotoka bila bandeji yoyote mwilini mwake.
Elvin alimuwahi kumshika mkono ili asianguke. “Ona Bella! Bado hujapata nguvu.” “Ni kwakuwa sijala chakula, nimekuwa nikiishi kwa maji tu.” “Mbona umetoa kila kitu?” “Hizo bandage zitanichelewesha kupona vidonda na sihitaji maji mwilini kwa njia ya sindano. Nitakula na kunywa maji kama kawaida. Lazima niondoke Elvin. Tafadhali naomba usinizuie.” “Lakini bado wewe ni mgonjwa, Bella.” “Hapana, mimi sio mgonjwa, nimepona. Huu uvimbe ni kawaida tu. Utaisha taratibu. Naomba chakula nile.” Yule nesi na Elvin walikuwa hawamuelewi Bella.
 “Simu yangu iko wapi?” Bella akauliza. “Iliishiwa chaji ikazima.” “No no no nooo. Naomba niazimie chaja haraka unichajie Elvin, tafadhali. Lazima hiyo simu iwake, sasa hivi.” Elvin hakuwa akielewa, lakini alitoka na baada ya muda akarudi na chaja. Aliweka ile simu kwenye umeme hata dakika tano hazikuisha, akaiwasha. “Mbona unaniogopesha Bella.” “Samahani Elvin, hata nikikwambia hutaelewa. Ni lazima nifanye mawasiliano.” Na kweli Elvin hakuwa akielewa.
Bella alipiga simu kwa Mat. “Shikamoo kaka.” “Hujambo Bella?” “Sijambo kaka. Ulienda kumfuata Ric? Maana shule zimefungwa.” “Nilipoenda wakaniambia alishachukuliwa. Ulimtuma nani?” “No no no nooo.” Bella alizidi kupaniki. “Bella?” “Kwaheri kaka, nitakupigia baadaye.” Bella alikata simu.
“Naomba pochi yangu.” Bella alimgeukia Elvin aliyekuwa haelewi. Alitoa wallet yake, akavuta kitabu cha hundi. Akaweka saini kwenye hiyo hundi, bila kuandika kiasi, kisha akamkabidhi Elvin. “Naomba unisaidie kitu kimoja cha mwisho bila kuuliza swali.” Elvin alibaki akimwangalia Bella. “Tafadhali Elvin.” “Unataka nini Bella?” “Uhakikishe wanakuandikia dawa zote ninazotakiwa kunywa, uninunulie. Mimi nitazifuata ofisini. Na hii hundi, utaandika gharama zote watakazokuwa wananidai hapa hospitalini, kisha uwalipe. Lazima niondoke sasa hivi Elvin.” “Sikuelewi Bella.” “Nilikuomba usiniulize swali. Naomba unisaidie tu.” “Lakini wewe bado ni mgonjwa Bella, utatokaje hapa!?” Bella alimpa tabasamu lakumridhisha. “Unaona ile hali uliyonikuta nayo? Ilishanitokea kama hivyo, nilikaa nikijiuguza mwenyewe nyumbani mpaka nikapona. Usiwe na wasiwasi Elvin, mimi nimeshapona. Nitakuja ofisini baada ya siku chache sana. Naomba nisaidie nguo zangu nivae.” Bila kupoteza muda, Bella alianza kubadili nguo zake, pale pale bila hata kufikiria, ikabidi Elvin ageuke.
Alishika viatu vyake mkononi na pochi. “Naomba unisindikize mpaka kwenye gari yangu tafadhali.” “Au mimi nikupeleke?” Elvin akauliza. “NOOOOO.” Bella alikataa kwa nguvu zote na kumshangaza zaidi Elvin. “Lakini asante. Usiwe na wasiwasi. Mimi nitafika salama tu.” Elvin akiwa haelewi chochote, alimsindikiza Bella kwenye gari yake, Bella akaondoka.
*********************************************
* Je Ni nini kinachomuwahisha Bella? Na Wapi anawahi? Nani amemchukua Eric kutoka shuleni?
* Uchumba wa Elvin nao umeanza kuingiliwa na Mikasa ya Bella

Mambo ndio kwanzaaaaa yanaanza, Elvin akiwa ndio anaingizwa kwenye mkasa wa maisha ya Bella, ambayo Mzee Masha hataki hata kuhisi kiumbe kingine kwenye maisha ya ENABELLA.
Ni nini kitaendelea?

USIKOSE SEHEMU YA 6.

0 comments: