Story

My Past - Sehemu ya 4.

Saturday, April 29, 2017 naomimwakanyamale 1 Comments



S
iku hiyo ndipo walipoziona pande zote za Masha waziwazi. Alifika kwenye mgahawa huo mdogo, ambapo aliwakuta wenzake wote wamekaa nje, wakiwa wameagizia vinywaji vyao. Wote walikunywa vinywaji visivyo na kileo, kwa sababu Mzee Mwasha alikuwepo. Hakuna aliyethubutu kunywa pombe mbele ya Mzee Mwasha. Wote walimuheshimu sana huyo mzee. Masha kama aliyehisi walichomuitia wazee wenzake, alivuta kiti, akakaa bila kuonyesha tabasamu usoni. Hata muhudumu wao aliyezoea kuwahudumia kila wawapo hapo, alipomuuliza kwa tabasamu ni kinywaji gani angependa kunywa, alikataa, akabaki akiwangaalia, akitaka waongee haraka kwani anaharaka kuna mahali anataka kuwahi mahali.
Mmoja wao, alianza kwa hofu kidogo, ndipo wenzake wakaingilia kama kuchangia ili kuongeza nguvu kwa Masha aliyekuwa akiendelea kubadilika kila sekunde waliyokuwa wakipokezana kumuonya. Kama aliyejua, Mzee Mwasha alibaki kimya akimtizama Masha anavyobadilika rangi ya mwili wake. Alitulia kimya akiwatizama wenzake wakimjia juu Masha, huku akitamani kuwashtua na kuwaomba wapunguze jazba kidogo. Mapigo ya moyo ya Masha yaliongezeka, akawa mwekundu usoni, akiwaka kama moto.
“Mmemaliza?” Masha aliyekuwa kimya muda wote akiwasikiliza aliwauliza. “Kwa kweli umetudhalilisha sana Masha. Wote tunaonekana hatuna maana.” Mmoja wao alimalizia akanyamaza. “Naomba mniambie tofauti yangu mimi na nyinyi ni ipi! Au leo ndio mnataka kuonyesha ulimwengu kuwa nyinyi ni wakamilifu sana kuliko mimi? Au kwa kuwa nyinyi hamkubahatika kupata wanawake wa nje waliotulia? Mimi sihangaiki na wanawake wengi kama nyinyi. Wewe Danny nguvu ya kunisema mimi unaitoa wapi wakati unalala na wauza bar kila leo? Na wewe Mwandri, sio wewe uliyezaa na sekretari wako ukamdanganya mkeo mtoto sio wako? Wewe Banda ndio mchafu wakupindukia, au unafikiri hatujui tabia yako ya kulala na wasichana wako wa kazi? Wewe mwenyewe ulinifuata ukiniomba nikusaidie pesa ya kumuhonga yule msichana wako wa kazi aondoke pale nyumbani kabla mkeo hajajua kama umempa mimba.  Na wewe Tomeo, nashauri ukapime UKIMWI, maana kila leo unaambukizwa magonjwa ya zinaa na watoto wa chuo.” Masha alianza kutaja dhambi ya kila mmoja wao.
“Hivi leo nguvu yakuniweka kikao mnaitoa wapi nyinyi!? Anyooshe mkono hata mmoja wenu aliyemkamilifu hapa na aliyekuwa na mwanamke mmoja tu. Mmekaa kunifuatilia mimi na maisha yangu wakati na nyinyi ndoa zetu zimewashinda! Angalau aongee Mzee Mwasha peke yake, ndio naweza kumsikiliza, lakini sio nyinyi, wapuuzi wakubwa. Tena Danny nakudai pesa yangu. Jumatatu nikute risiti ya benki ofisini kwangu. Kuonyesha umelipa yote. Narudia pesa yangu yote, Danny. Kadhalika na Banda vile vile. Jumatatu nataka pesa yangu iwe benki. Sasa msifanye hivyo, ndipo mtanitambua mimi ni nani. Narudia tena, PESA YANGU YOTE NINAYO WADAI, ninaitaka kamili ifikapo siku ya Jumatatu.” Masha alikuwa akimgeukia mmoja baada ya mwingine.
Akamgeukia tena Mwandri, akiwa amemkazia macho. “Lile ombi lako, nimefikiria naona sitaweza kukusaidia. Na wewe Mzee Nyami, naona Banda yupo sahihi, haukopesheki. Ameniambia huwa hulipagi madeni ya watu na sio mtu mzuri kufanya na wewe biashara, ile tenda nampa yule jamaa wa kihindi, nafikiri ataifanya vizuri kuliko wewe.” Mzee Nyami alimgeukia Banda, aliyekuwa amenywea kabisa. “Mzee Mwasha wewe tutaongea kwa wakati wetu. Siwezi kuzungumza na wewe mbele ya hawa wapuuzi.” Mzee Masha alitulia tena akiwatizama machoni kwa muda.
“Kuna mwenye nyongeza? Au mlitaka kikao kingine kifanyike na wake zetu wakiwepo?” Aliuliza kwa jeuri sana na kubaki akiwatizama machoni. “Kama hamna nyongeza, naomba niwahi kwenye majukumu yangu mengine, niwaache nyinyi wasomi mkiongea na kupanga mambo yenu yakisomi.” Mzee Masha akasimama. “Na kama mnafikiria kuniondoa kwenye chama, naomba mpitie katiba vizuri kwa ajili ya malipo yangu.” Aliwacheka kidogo, akatingisha kichwa kisha akaondoka. Wote walikuwa kimya kabisa, hakuna hata aliyejaribu kuongeza na kumtizama mwenzake machoni. Waliondoka hapo kila mmoja na njia yake. Mzee Masha alirudi kwa Bella, akatulia kimya.

***********************************************

Bella aliendelea kutulia na kumtunza mdogo wake kwa maadili yote, kama alivyolelewa na mama yake. Hakuwahi kujua kama dada yake ananyumba wala kama anaishi na mwanaume yeyote. Alipokuwa akifunga shule, walirudi kuishi pamoja kwenye ileile hoteli waliyokuwa wakiishi mwanzoni, pale walipopelekwa na dereva wa Zera, Kasimu. Bella alisafiri na mdogo wake nchi na sehemu tofauti tofauti kipindi cha likizo yake, lakini Mzee Masha akiwepo kwenye ndege nyingine. Kama ni hotelini, walichukua vyumba viwili tofauti, ambacho Bella alilala na Mzee Masha na Eric alilala peke yake. Lakini Bella alihakikisha Eric hakutani na Mzee Masha hata kidogo endapo wanakuwa naye safarini. Ni sharti alilokuwa amemuwekea Mzee Masha, naye hakuwa na shida kabisa na hilo, ilimradi kila safari wanakuwa pamoja na kuhakikisha Bella analala kitanda anacholala yeye. Amani ilikuwepo.
Kwa kuwa Eric alikuwa na msingi mzuri wa shule, alijikuta haendani na darasa la sita alilotakiwa kuwepo katika shule hiyo. Walipokuwa wakifanya mtihani wa darasa la saba, na yeye alipewa namba na kufanya mtihani huo. Alifaulu vizuri, na kuendelea kidato cha kwanza katika shule ileile. Kwa hiyo Eric alirushwa darasa moja, kitu kilichomfurahisha zaidi Bella. Alijitahidi sana katika masomo na michezo. Alikuwa akitegemewa na shule yao, upande wa mpira wa kikapu. Alikwenda mikoa mbali mbali kushindana na alipokuwa nyumbani, Bella alimtafutia mwalimu wake binafsi wakumfundisha mchezo huo. Eric alianza kutoka nje ya nchi kwenda kushindana hasa mpira wa kikapu. Mat naye hakuwa mbali kwenye malezi yake, walimuheshimu kama kaka yao, na Mzee Masha alimkubali Mat kuwa ndiye ndugu wa pekee wa Enabella na Eric, sio mtu mwingine.

***********************************************

Mama Masha alibakiwa na njia moja tu ya watoto wake hao wawili kama kinga yake. Kwani hakuna aliyeweza kumkalisha mumewe kuongea naye ili kuweza kunusuru ndoa yake. Alijua ni jinsi gani Mzee Masha alivyopenda watoto wake, kwa hiyo akaendeleza tabia ya kurudi nao Tanzania hata kama watoto hawapo likizo. Walirudi wote pale mama yao alipojisikia ili kumfanya Mzee Masha akose muda na Bella awe analala nyumbani au angalau awe anapata naye muda, hata wakuzungumza jambo lolote. Kwani alipokuwa akirudi peke yake nyumbani, Masha hakuwa akionana naye kabisa. Hata kama atamfuata ofisini, Masha alimjibu kwa kifupi na kuondoka na kumuacha mama huyo ofisini kwake yeye Masha. Akiwa hajakasirika, alikuwa akimuacha na maelezo. Wakati mwingine alimuacha pale pale ofisini kwake na kumwambia anakwenda sehemu fulani ana kikao na anaweza asimuone tena mpaka anapoondoka nchini. Lakini kila anapokuwa na watoto  nyumbani, hapakuwa na uongo wakuwaeleza watoto wake, au sababu ya kuwaambia wanae kuwa hataweza kulala au kuwepo nyumbani wakati na wao ndio wamerudi nyumbani kwa ajili yake.
Watoto wenyewe walikuwa wakikubaliana na wazo la mama yao la wao ndio wawe wanarudi nyumbani Tanzania kumuona baba yao, kwani Mzee Masha alipunguza sana safari za kwenda kuiona familia yake. Alikuwa akitoa udhuru wa mara kwa mara, kwamba hataweza kwenda kuwatembelea nchini Uholanzi. Mama Masha alimtumia mwanae Zera, ambaye ndio kipenzi cha baba yake, kumfanya awe bize na familia, na kushindwa kurudi kwa Bella. Na kweli Zera alifanikiwa kumbana baba yake.
***********************************************

Likizo moja kubwa ya kina Zera, walirudi na mama yao pia akiwa amechukua likizo, wakarudi Tanzania kwa mapumziko hayo. Zera alimganda baba yake ipasavyo. Alimfuata baba yake kila mahali, akimwambia baba yake ni jinsi gani alivyokuwa akitamani likizo hiyo ifike, ili arudi nchini ili awe naye. Walisafiri kama familia kwenda kwenye vivutio mbalimbali hapo hapo nchini. Wakati wote Zera alikuwa na baba yake. Na kwa kuwa kipindi cha nyuma alikuwa akienda naye mpaka ofisini kwake, hata aliposema anataka kwenda ofisini, Zera alimuomba awe anaenda naye. Zera ni mtoto aliyekuwa na malezi yakudekezwa vibaya. Masha alikuwa mkali kwa kila mtu, lakini si Zera. Walipendana na baba yake, na alipewa kila anachotaka. Hakuwahi kutaka kitu asipewe. Kwa hiyo mama yake alimtumia vizuri sana.
Kilikuwa kipindi kigumu sana kwa Mzee Masha. Hata mawasiliano na Bella yakawa yashida sana. Alikuwa kimwili na familia yake, lakini mawazo yalikuwa kwa Bella wakati wote. Kila akikumbuka uzuri wa Bella, mambo anayomfanyiwa na umri ule mdogo alionao, alijua lazima Bella atamtafutia msaidizi. ‘Bella ni mtundu mtundu sana wa mambo ya kompyuta. Anaweza kuchezea zile kamera pale nyumbani, nisijue ameingia nani pale, au anawasiliana na nani. Watanichukulia yule mtoto!’ Mzee Masha alikuwa akiwaza usiku huo akiwa amelala na mkewe, kwenye hoteli hiyo ya watalii Serena Safari Lodge Ngorongoro.
Vyumba vyao vilikuwa karibu karibu sana wao na watoto wao, hakuna jinsi wangegombana hotelini hapo, watoto wao wasiwasikie, au wasijue. Kwa hiyo Mzee Masha ilimbidi awe mpole ili kutunza heshima kwa watoto wake. Wakati huo akiwaza juu ya Bella, huku mkewe naye akiwaza jinsi ya kumbana ili aachane kabisa na hiyo nyumba ndogo yake, ambayo bado hakuwa akijua kama ni Bella.
Mwishowe akapata wazo. “Nimemuandikia barua raisi kutaka kuacha kazi.” Mama Masha alimgeukia mumewe. Mzee Masha alikaribia kuchanganyikiwa. “Kwa nini unaacha kazi?” “Nimeamua kurudi kukaa nyumbani, ili tusaidiane mambo ya hapa.” “Umechanganyikiwa nini!? Na shule za watoto? Junior ndio amekubali kusoma, ameingia chuo sasa hivi, huko hana makundi mabaya, unataka umrudishe tena huku ili iweje? Utakuwa unawazungusha hao watoto mpaka lini? Wewe mwenyewe uliitaka hiyo kazi, ukasema ndio zilikuwa ndoto zako, umechukua watoto wote, sasa hivi tena unataka kurudi! Acha kuchanganya watoto.” “Hiyo kazi sio muhimu kama ndoa yetu, Masha. Najaribu nione kama naweza kunusuru hii ndoa.” “Aliyekwambia hii ndoa ipo matatizoni ni nani? Wewe ndio unakuza matatizo. Kama ingekuwa kuna tatizo, ningekuwa nimelala hapa na wewe?” “Kama hakuna tatizo, mbona hata hujanigusa tokea nimerudi? Ni muda gani tangia tumefanya tendo la ndoa mimi na wewe, Masha? Unakumbuka mara ya mwisho niliporudi nyumbani, tukawa mimi na wewe tu? Ulikuwa unaniacha usiku kitandani, unaondoka bila kuaga. Wakati mwingine ulikuwa unarudi na wakati mwingine nilikuwa nikiondoka nchini bila hata kukuona tena. Nikikupigia simu kuomba tuonane ili tuagane, unaniambia niondoke tu utakuja kutuona, lakini unaishia kutoa udhuru. Kweli huoni kama kuna tatizo?" “Kwa hiyo unafikiria hayo yote yatabadilika kwa wewe kuacha kazi na kurudi kukaa nyumbani? Kama sio upumbavu huo ni nini? Unajiangalia wewe tu, umefikiria watoto lakini?” “Nitarudi na Zera, Junior atabaki hukohuko amalizie chuo.” “Umuache Junior kule bila ungalizi wowote, eti kwa kuwa wewe unataka kuja kulala na mimi! Acha upumbavu Matha.” “Sio kulala na wewe tu, Masha.” “Sasa ni nini kama sio akili mbovu hiyo? Huwezi kumuacha Junior huko. Nenda kesho ukaongee na huyo bosi wako umwambie umebadili mawazo, unataka kurudi kazini.” “Sitafanya hivyo Masha, mpaka utakapo nihakikishia kuwa utamuacha huyo msichana uliye naye, na uniahidi mbele ya watoto kuwa tutakaporudi safari hii nyumbani, Dar, likizo ikiisha, tutarudi wote Uholanzi ukakae na sisi kwa muda, halafu utakuwa unakuja kututembelea mara kwa mara. La sivyo ni heri kuwaambia watoto ukweli kwamba umepata mwanamke mwingine, ambaye umeamua utuache sisi ili uishi naye huyo mwanamke.” Mzee Masha alishtuka sana. Mama Masha alivyoona hivyo, alifurahi sana, akajua ameshampata mumewe.
Akasimama na kuanza kubadili nguo zake. Alianza kuvua nguo za kulalia na kutoa nguo zake za kawaida, akaanza kuvaa. “Kwa nini unabadili nguo? Unaenda wapi?” Mzee Masha alikaa. “Mapokezi.” Mama Masha alijibu kwa kifupi huku akivaa viatu vyake. “Kufanya nini usiku huu?” “Kuchukua chumba kingine, ili kukupa nafasi ya kufikiria. Hata hivyo nakaa humu ndani nafanya nini?” Kama Mshale Mzee Masha alikimbia mlangoni.
“Hivi wewe ukoje, Matha? Unafikiria kweli wewe au unataka kusambaratisha hii familia? Umefikiria watoto lakini? Unafikiri Zera ataelewaje?” “Hivi hayo maswali unaniuliza mimi au unajiuliza wewe, Masha? Kama ungekuwa unafikiria hata mmoja wetu, kati yetu, usingefanya unayoyafanya.” “Hebu rudi bwana! Acha ujinga. Unataka kuchanganya watoto tu.” “Hawawezi kuchanganyikiwa, watajua ukweli halisi wa maisha uliyoyachagua.” Mzee Masha alibaki mlangoni akiwaza kama usiku ule ndio iwe kweli ndio mwisho wa ile ndoa, na yeye atoe siri aliyokuwa ameificha ya mkewe, au anyamaze mpaka atakapokamilisha uchunguzi wake na kuwa na uhakika na kila kitu, ndipo awaambie watoto na kuwapa sababu ya kuachana.
Alibaki akifikiria huku akiumia roho, mwishowe akakubali yaishe kwa usiku huo. “Hebu acha ukorofi, rudi tulale.” “Hapana Masha. Umenitesa na kunidhalilisha vyakutosha. Kila mtu ananicheka! Kwa nini hutaki watoto wajue ukweli?” Mama Masha alijidai akilia baada yakuona amefanikiwa kumbana mumewe kwenye kona. Ni kweli alifanikiwa kumbana vizuri sana usiku ule. Alimuona vile Masha alivyotulia, akajua amemkamata vizuri sana, bila kujua mumewe ana akili sana. Bado alikuwa akimtengenezea kosa lakueleweka, ili hata akimwambia anamuacha ashindwe kwenda kudai mali mahakamani. Hakutaka siku atakayompa mkewe talaka, asipate hata shilingi yake. Alimjua jinsi mkewe alivyo na akili. Alimpangia mipango yote kwa tahadhari sana, huku akichunguza kila kitu, na kukusanya ushahidi wakutosha.
Mama Masha alibaki amesimama huku akilia. “Naomba nipishe nikalale.” “Huo ni ukorofi, Matha. Umesema nifikirie. Hata dakika tano hazijapita unaondoka! Wewe vipi?” Mara walisikia mlango unagongwa. “Unaona sasa?” Mzee Masha alistuka sana. “Hebu nenda bafuni, watoto wasikukute hivyo.” Mzee Masha alinong’ona. “Hey mama! Is everything okay?” Walimsikia Zera akiongea mlangoni. Wote walinyamaza kimya. “Mjibu sasa?” Mama Masha alimfokea Mzee Masha. “Yes babygirl.” Mzee Masha alijibu. “Can I talk to Mama?” Zera aliuliza, lakini kulikuwa kimya ndani. “Dad?” Walimsikia Junior naye kipenzi cha mama yake akiingilia maongezi baada yakuona kimya ndani ya chumba cha wazazi wao. “Sure!” Mzee Masha alijibu huku akibabaika, na mkewe akimtizama. Alibaki amesimama mlangoni bila kufungua mlango. “Dad?” “Am here Son!” “Can we talk to mama, please?” Junior alirudia tena, lakini safari hii alisikika akimaanisha. “Yes, why not?” Masha alijibu. “Open the door, then!” Zera naye akaongeza wakiwa wanashangaa ni kwa nini baba yao hafungui mlango.
Ilibidi Masha afungue mlango, watoto wakaingia wakiwa na nguo zao zakulalia. Wote walishangaa kumuona mama yao amevaa nguo ambazo sio za kulalia na ameshika pochi yake. Junior akamsogelea. “Unaenda wapi usiku huu!?” Mama yao alibaki kimya. Junior alimgeukia baba yake. “Where is she going, Dad!?”  “Mama yenu haendi mahali popote.” Mzee Masha alijibu kwa kifupi. “Nyinyi rudini mkalale. Kila kitu kipo sawa.” “Unauhakika dady?” “Kabisa. Hakuna mahali mama yenu anaenda. Kila kitu kipo sawa kabisa.” “Sidhani dady.” Junior aliongea akionyesha mashaka usoni.
“Nilimuona juzi tukiwa nyumbani, mama alikuwa akilia sana chumbani kwenu. Nilifunga mlango taratibu nikamuacha. Mama amebadilika, hana furaha kama zamani. What did you do to her?” Junior alimuuliza baba yake. “Na usitudanganye dady. Maana huu ni usiku, na anaonekana anataka kuondoka, tena peke yake. Umemfukuza?” “Hapana. Hapana kabisa. Wewe unajua siwezi kumfukuza mama yenu.” “So what’s going on daddy?” Zera kipenzi cha baba yake aliuliza. “Kwa sababu hata sasa analia.” Zera aliongeza. Junior alimsogelea mama yake. “Kuna nini mama? Unataka twende wote chumbani kwangu ukatulie kidogo? Kama unataka kwenda mahali nitakusindikiza, siwezi nikakuacha ukazunguka peke yako usiku.” Junior alijaribu kuongea na mama yake kwa upendo akimbembeleza.
“Daddy?” Zera aliita kwa hasira kidogo. “Umemfanya nini mama? Unajua jinsi mama alivyo. She has been always there for all of us, including you dady. Hajawahi kutuacha wakati wowote ule. Ana kazi nyingi sana kule Uholanzi. Lakini anajitahidi kuhudhuruia shuleni kwangu kila anapoitwa au ninapomuhitaji. Hajawahi kukosa shuleni kwangu au kwenye michezo yangu. Lakini wewe umekuwa ukiniambia huwezi kuja. Unakumbuka nilikwambia nimechaguliwa kuingia kwenye kundi la waogeleaji natakiwa kwenda kwenye shindano katika mji wa Brussells, nikakuomba uje, ili twende ukaone ninavyoogelea? Ukaniambia una kazi nyingi hutaweza kuja. Mama alikuwa na mkutano mahali, lakini akaahirisha, akasafiri na mimi. Nilitegemea hata ungenipigia simu uniulize iliendaje, lakini hukuonyesha kujali hata kidogo.” Zera akaanza kulia.
“Nilishinda. Kila mtu alinipongeza kasoro wewe, daddy. Nimeingia kwenye timu kubwa sana kule kwenye ile nchi, na wamesema nikijitahidi zaidi naweza kuingia kwa washindanaji watakao enda kwenye mashindano ya kombe la dunia. Haunijali tena siku hizi. Hujui naendeleaje, hujui naishije tena. Unakumbuka wakati tunaishi hapa, wewe ndio ulikuwa unanipeleka kwenda kujifunza kuogelea? Sasa hivi hujali tena! Na mama amekuwa na kazi ya kukutetea kwa kila jambo. Kila tukimlalamikia juu yako anatuambia unakazi nyingi. Lakini tunataka utuambie ukweli daddy.” Mzee Masha alibaki kimya kabisa.  “What’s going on daddy? Tell us the truth.” Kumbe Zera alikuwa na uchungu mkubwa sana moyoni mwake. Alipata muda wakutoa dukuduku lake.
“Twende mama ukapumzike.” Junior alitaka kuondoka na mama yake, baada ya kuona baba yake amebaki kimya anashindwa kujibu. “Ngoja kwanza Junior. Huwezi kuondoka na mama yako. Tulipishana tu kidogo. Nilikosea, na ninaomba msamaha kwenu wote. Kazi zilikuwa nyingi, naona nimelemewa. Likizo yenu itakapoisha, tutarudi wote Uholanzi, nitakaa na nyinyi kwa muda ndipo nitarudi huku. Sitamuachia tena mama yenu majukumu yote ya kuwalea. Zera, naomba unisamehe, na hongera sana. I am alywas proud of you, sweatheart. Don’t you ever forgert that. Come here.” Alimkumbatia Zera. “Umenisamehe?” Mzee Masha alimuuliza Zera. Akiwa na tabasamu, Zera alitingisha kichwa. Walibaki kimya kwa muda, kila mtu akiwaza lake.
“Mkapumzike sasa. Tutaongea vizuri kesho.” Mzee Masha alivunja ukimya. “Thanks dad!” Junior alishukuru. “I mean it. Najua unaacha kazi zako nyingi ili uwe na sisi, na wakati wote umejitahidi kuweka mazingira ya sisi kujisikia tuna wazazi wanao tupenda na kutujali. Umejenga familia moja na yenye nguvu. Asante sana.” Junior akamsogelea baba yake na kumpa mkono. Yale maneno ya Junior yalikuwa ni hukumu kubwa sana moyoni kwa Mzee Masha, lakini hakujua chakufanya, na Bella yupo nyumbani akimsubiri. “You are welcome Son!” Mzee Masha alijibu kwa kifupi tu, huku akifikiria.
Junior alimsogelea mama yake akambusu. “I love you mama.” “I know Junior.” Mama Masha alitabasamu. “Ulale sasa, kesho nitakusindikiza unakotaka kwenda, lakini sio usiku huu.” Mama Masha alicheka kidogo. “Okay.” Zera alimbusu mama yake na baba yake kila mmoja akarudi kulala chumbani kwake. Mzee Masha alirudi kukaa kwenye kochi akifikiria. Mama Masha aliingia bafuni akarudi na kupanda kitandani akiwa na furaha zote, kwa kuokoa ndoa yake. Nikweli ndoano aliyoitupa safari hii, ilimkamata Masha vizuri sana. Alijua hawezi kubadilika tena, kwani ameshaahidi mbele ya wanae.
Mzee Masha aliiangalia simu yake kama anayetaka kuitumia. ‘Bella!’ Mzee Masha aliendelea kuwaza huku akikuna kichwa. Kila alipojaribu kubadili mawazo, alimuona Bella akiwa amelala peke yake akimsubiri. Umbile la Bella liliendelea kumsumbua akilini mwake. Alichukua simu, akataka kutoka nje kumpigia Bella aliyejua kumliwaza wakati wote, lakini alisita mlangoni. Alifikiria kutupilia mbali shutuma juu ya mkewe, ili angalau asimpoteze na Zera, lakini alijua lazima afanye maamuzi yakumuacha Bella kwanza kama anataka familia yake. Akabaki akiwaza pale mlangoni.
Mwishowe aliamua atulie kwanza, ajipe muda wakufikiri, huku akijikumbusha vile Bella alivyotulia. ‘Bella atanisubiri tu. Natakiwa kujipanga upya.’ Aliendelea kuwaza. Akaamua kuzima ile simu na kurudi kulala kitandani, mkewe alikuwa akimsikiliza kila anachofanya. Alifurahi sana alivyomuona hajatoka, na kuamua kurudi kulala. Alijivuta taratibu pembeni ya kitanda, mbali kidogo na Mzee Masha. Mzee Masha alivuta shuka vizuri, akamfunika mkewe. “Asante.” Mama Masha akashukuru kwa sauti ya chini kidogo. “Nilijua umeshalala.” “Ndio nataka kulala.” Mzee Masha alijilaza vizuri, huku akitamani mambo yake na mkewe yangekuwa kama zamani, angalau angefanya naye mapenzi usiku ule, lakini akili yake ilishavurugika, mkewe alimchanganya sana. Moyo wake ulishindwa kabisa kumpokea tena mkewe.
Kadiri siku zilivyokuwa zikidizidi kwenda tokea agundue ubaya wake na kushindwa kuzungumza naye au kumuuliza juu ya ubaya huo aliougundua, ndivyo alivyozidi kuwa mbali na mkewe kihisia. Alijikuna akimkinahi gafla. Hataki hata amguse. Kushiriki naye kitanda kimoja tu, ile kujua yupo pembeni yake usiku kucha, ikaanza kuwa ngumu pia. Akaanza kumkwepa kitandani au chumbani. Ikawa kama wanapeana zamu kuingia kwenye chumba chao. Akimuona mkewe anaingia hapo chumbani, yeye alitoka kwa haraka kama aliyefukuzwa. Lakini watoto walimbana usiku huo, hakuwa na jinsi. Masha aliendelea kuwaza huku akimtizama mkewe aliyekwisha kupitiwa na usingizi.

***********************************************

Mambo yalikuwa yamemfika shingoni Mzee Masha, familia anaitaka na Bella asingekubali kumuachia hata iweje. Usingizi uligoma kuja kabisa. Bella ni kitu cha thamani ambacho wakati wote amekiri hakijawahi kumtokea maishani mwake. ‘Labda nipunguze muda na Bella ili nipate muda na familia yangu. Nikimuacha mke wangu ndio nimempoteza Zera pia. Hatanisamehe akija kujua kama ninaishi na Bella. Inabidi kuacha kuonekana na Bella kila mahali. Nitamfanyaje Bella? Yaani nimuache Bella hapa nchini halafu nikaishi Uholanzi! Haiwezekani hata kidogo. Niende naye? Haiwezekani, anakaribia mitihani. Watanipora Bella hapa mjini.Mzee Masha alikesha akiwaza. Alimuonya Bella asimpigie simu hata iweje, yeye ndiye atakuwa akipiga. Kwa hiyo Bella wala hakuwa akimpigia.
Siku inayofuata ilikuwa ni siku ya familia tu. Wote walikubaliana kuzima simu na kuziacha hotelini ili wapate muda wa peke yao, wakati wanazunguka mbugani. Kwa hiyo kwa siku nzima Mzee Masha hakuwa ameongea na Bella, na jioni waliporudi hotelini, waliweka movie nzuri sana chumbani kwa Zera, wakawa wanaangalia wote. Hakupata mwanya wakutoka na kwenda kupiga simu, na walipoingia chumbani kulala ndipo mkewe naye akaanza kumkaba na maneno mengi na mipango mingi ya watoto hasa Zera. ‘Bella wangu jamani…’ Mzee Masha aliendelea kuwaza. ‘Sijui ana hali gani!?’  Walikaa huko siku nne ndipo waliporudi nyumbani. Hapakuwa na mawasiliano yoyote kati yake na Bella.
Walipofika tu nyumbani, kutokea uwanja wa ndege, Mzee Masha aliaga akisema anataka kwenda kazini. “Tunaweza kuongozana wote Dad?” Junior aliuliza. “Naenda mara moja tu na kurudi, sitachukua muda mrefu, kuna kitu nataka kuangalia.” Junior alikunja uso. “Unanikwepa?” “Nooo. Kwa nini unafikiri hivyo?” “Nauliza tu.” “Hapana kabisa Junior, nilifikiri utakuwa umechoka, nilitaka upumzike halafu kesho ndio tungeweza kwenda wote.” Junior alibaki akimwangalia kwa kumsuta. “Lakini kama unataka kwenda, tunaweza kwenda wote tu Junior.” “Hapana, naona kama leo sio siku nzuri kwako, ya kwenda na mimi. Wewe nenda tu. Tutakwenda wote wakati mwingine.” Junior aliondoka kwenda chumbani kwake, Zera akafuata, na Mama yao akaondoka, wakamuacha Mzee Masha peke yake sebleni. Alikaa pale kwa muda, akaamua kutoka nje kupiga simu kwa Bella badala ya kwenda.
***********************************************

Yalikuwa ni mapumziko ambayo Bella alikuwa akiyatamani kwa siku nyingi sana lakini hakuyapata. Kuwa mbali na Mzee Masha, au hata kutosikia sauti yake, yalikuwa mapumziko makubwa sana kwake. Aliweza kulala vizuri na kujisomea bila shida yeyote. Alikuwa amejilaza wakati Mzee Masha akimpigia simu. “Umelala na nani?” Hiyo ndio ilikuwa salamu yake mara baada ya Bella kupokea simu. “Nipo peke yangu T. Mzima?” “Ulikwenda wapi na wapi?” “Mbali na chuoni, sijakwenda popote, nilikuwa hapahapa nyumbani nikijiandaa na mitihani. Kwani wamekwambia wameniona wapi?” Mzee Masha akanyamaza kwa muda. “Vipi T? Mzima?” “Mzima, mambo yamekuwa mengi tu.” “Utakuja kuniona leo?” “Nitakuja kukuchukua kesho nikupeleke chuoni.” “Tupo karibia na mitihani T, ratiba imebadilika. Wakati mwingine walimu wanaingia darasani na wakati mwingine hawaji. Kama huyo wa kesho asubuhi amesema hatakuja, na kipindi kingine ni mchana.” Mzee Masha akanyamaza. “T!” “Nipo.” “Utakuja asubuhi au hiyo mchana?” “Nimekwambia nitakuja Bella. Una wasiwasi gani? Au unataka kwenda kwa wanaume zako?” Bella akanyamaza.
“Unanyamaza kwa kuwa unajua naongea ukweli? Nimeondoka siku tano tu, umeshaanza kurukaruka na wanaume wengine!” “Tafadhali T, naomba tusianze kugombana kwa vitu visivyo vya kweli. Umeniacha kwa siku zote hizo, bila hata kunipigia simu au hata kunitumia ujumbe kunijulia hali yangu, uko na mkeo. Sijalalamika, wala sijatoka humu ndani zaidi ya kwenda chuoni. Badala tuongee vizuri, au hata kujua hali yangu, unanipigia simu na kuanzisha ugomvi! Kwa nini unanifanyia hivyo?” Mzee Masha alinyamaza kwa muda. “Nitakuona kesho Bella.” Mzee Masha aliongea kwa aibu, na kukata simu. Akarudi ndani, akakuta mkewe na wanae wote wapo jikoni. ‘Daah! Watoto wote wameungana na mama yao! Nisipoangalia hata Zera nitampoteza.’ Mzee Masha aliwaza wakati akiingia jikoni kuungana na familia yake.
 “Mkasa wa Bella.”
Siku inayofuata Mzee Masha alishindwa kutoka kabisa nyumbani. Aliingia chooni na kumtumia ujumbe Bella, aache gari nyumbani, dereva atakwenda kumchukua ampeleke chuoni, halafu yeye atakwenda kumfuata. Bella hakuwa na neno. Alijibu kwa kifupi tu ‘Sawa.’ Akiwa amekaa darasani ameinamia kompyuta yake anajisomea, alimsogelea kijana mmoja aliyekuwa ameanza naye chuo tokea mwaka wa kwanza. Wote walidhani Bella hawafahamu, lakini Bella alishawasoma tabia zao wote, na alikuwa akiwafahamu vizuri sana, kila mmoja kwa jina na tabia.
Yule kijana alimjua ni mstaarabu. “Samahani Enabella, naomba uniazime simu yako.” Bella alinyanyua macho na kumtizama kwa muda, huku darasa zima likitaka kusikia Bella anajibu nini. Hapakuwa na mwalimu darasani, kwani hata mwalimu aliyeahidi angekuja, hakuja. Kwa hiyo Bella alibaki pale darasani akimsubiria Mzee Masha aje amchukue kama alivyoahidi. Bella alibaki akimtizama na macho yake makubwa na yakurembua. “Ni kitu cha msingi sana dada yangu, nisingekuomba. Nimeshaomba watu kadhaa wa hapa darasani, wanisaidie lakini simu zao hazina hela.” Bila ya kujibu, Bella aliingiza mkono mfukoni akatoa simu na kumkabidhi yule kaka. Alitoka nayo nje, baada ya muda akarudi na kumrudishia Bella simu yake. “Asante.” Alishukuru lakini Bella hakujibu kitu, alipokea simu yake na kuirudisha mfukoni.
Bella alingalia saa, akaona muda wa kuja kuchukuliwa umefika, akanza kukusanya vitu vyake atoke. Wakati anakusanya vitu vyake arudishe kwenye begi lake, ujumbe uliingia kwenye simu. ‘Bado nipo kwenye kikoa. Hata hivyo hali yangu ya kifedha sio nzuri kwa sasa.’ Bella aliposoma vile akamuhurumia sana Mzee Masha. ‘Labda ndio maana amepotea kwa kuwa hana pesa!?’ Bella aliwaza akaamua kumjibu. ‘Usijali mpenzi wangu juu ya pesa, mbona mimi bado ninazo? Tutatumia za kwangu. Nakusubiri kwa hamu.’ Alipomaliza kujibu, akarudisha ile simu kwenye mkoba wake, kwa bahati mbaya ikabonyeza sehemu ya ‘silence’ kuzima sauti. Bella akijua Mzee Masha atachelewa, akarudisha vitu vyake mezani na kufungua kompyuta yake na kuanza kujisomea tena.
Mzee Masha alifika nje ya chuo na kumpigia simu Bella kama kawaida yake, lakini Bella hakupokea kwa kuwa haikuwa na sauti, kwa hiyo hakusikia. Na Bella naye hakuwa na wasiwasi wakuitazama simu yake, kwani alijua kama Mzee Masha angefika pale angempigia simu ili atoke. Akabaki amekaa akijisomea.
Mzee Masha alimpigia simu tena na tena lakini Bella hakupokea. Hasira zikaanza kumpanda Mzee Masha, kwani hata kufika pale, alitumia uongo mwingi sana, ili kuwatoroka wanae. Bella alipoona muda unazidi kwenda bila Mzee Masha kufika na njaa ilikuwa ikimuuma sana, akaamua amtumie ujumbe, kumtaarifu atachukua taksii kurudi nyumbani. Na atakapo pata muda amfuate nyumbani waongee zaidi. Kutoa simu yake, akakuta Mzee Masha alimpigia simu zaidi ya mara kumi na ilishapita nusu saa. Bella alianza kubabaika.
Akachukua vitu vyake harakaharaka na kukutoka darasani kumuangalia Mzee Masha kwani aliogopa kupiga simu kama alivyokuwa amemuonya. Bella aliangalia kulia na kushoto, hakuona gari la Mzee Masha. Kwa kuwa wasiwasi ulishamwingia, akachukua taksii kurudi nyumbani, akijua wazi Masha atakuwa ameshaondoka kwani huwa hapendi kusubiri.
Alifika nyumbani lakini Mzee Masha hakuwepo. Alibaki na wasiwasi sana. Alikaa akimsubiria Mzee Masha apige tena, lakini hakupiga. Akaamua kuingia bafuni aoge. Akiwa bafuni kwake anaoga akasikia mtu ameingia chumbani kwake. “T! Ni wewe T?” Bella alipoona kimya, akaamua ajifunge taulo atoke akaangalie. Alimkuta Mzee Masha amesimama anaangalia simu yake. Bella alisogea karibu. “Pole nimekuta umenipigia sana, simu ilikuwa kwenye ‘silence’ ndani ya mfuko wa kompyuta.” Bella alipigwa kibao cha nguvu akaangukia kitandani. Kabla taarifa hazijamfikia kichwani na kuelewa kinachoendelea, Mzee Masha alichomoa mkanda wa suruali yake, nakuanza kumchapa nao Bella kama anaua nyoka.
“Unataka kuniua na pesa zangu? Nimeondoka hata siku saba hazijaisha, umeshatafuta wanaume wakuwahonga pesa zangu! Unachotafuta ni nini wewe Bella!? Unataka nikupe nini ili uridhike?” Mzee Masha aliendelea kumpiga Bella, bila kupumzika. “Unanidanganya upo chuoni, kumbe umetoka kwenda kwa wanaume zako! Nimekufuata mpaka darasani kwako, wakaniambia uliondoka muda mrefu. Nitakuuwa Bella. Huwezi kuja kuniua na UKIMWI. Ulitumia kondom na huyo mwanaume?” Mzee Masha alikuwa akiongea huku akimpiga Bella.
“Nitakuuwa Bella, niambie ukweli. Ulikuwa ukitumia kondom?” Aliendelea kumpiga Bella kwa hasira sana. Alimnyanyua pale kitandani akiwa uchi kabisa, na kuanza kumchapa makofi, tena ya usoni. Bella alikuwa akilia sana. Hakuwa akielewa ni nini Mzee Masha anaongea. Alimrusha kitandani kwa nguvu, nakuanza kumkaba. “Nilikwambia nikikufumania nitakuuwa Bella. Kwa nini umenisaliti?” Alikuwa amemkalia Bella huku amemkaba kooni. Bella alitapatapa, mpaka akapoteza fahamu.
Alizinduka akiwa hospitalini. Bella alikuwa amevimba mwili mzima, hata usoni hakuwa akitizamika. Alijitahidi kuangaza macho, lakini alishindwa, alibaki akigugumia maumivu. Alipitiwa na usingizi mpaka kesho yake. Dereva alikuja, akamwambia ametumwa amrudishe nyumbani. Aliporudi nyumbani, alikuta walinzi wamebadilishwa, na gari alilokuwa amepewa halipo. Dereva alimsaidia kumuingiza ndani, kwani hakuwa akiweza kutembea vizuri. Alijaribu kutafuta simu yake, lakini haikuwepo. Mzee Masha alichukua gari yake, simu na kompyuta pia. Bella alipanda kitandani kwa shida sana, akapitiwa na usingizi tena. Aliingia yule dereva chumbani kwake. “Amka unywe dawa Bella.”  Bella alijaribu kukaa lakini alishindwa. Alikuwa na maumivu makali sana. Yule dereva alimnywesha zile dawa, akarudi kulala. “Nitakuletea chakula baadaye.” Bella hakujibu.
Alipoamka hakukuta kadi ya benki hata moja kwenye pochi yake na aligundua wafanyakazi wote walishafukuzwa kazi, yupo pale peke yake. Bella alianza kulia sana. Aliendelea kuuguzwa na yule dereva, na nesi aliyekuwa akija kumsafisha vidonda. Tena nesi huyo alikuwa akisimamiwa na yule dereva. Hakuruhusiwa kuongea na Bella kitu chochote isipokuwa kumtibu na kuondoka. Hakuweza kutoka mle ndani, kwa maumivu, lakini hata hivyo dereva aliambiwa haruhusiwi kumpeleka Bella popote, kila kitu ataletewa akiwa palepale nyumbani. Getini ndio waliambiwa mtu anayeruhusiwa kuingia na kutoka ni yule dereva tu, tena akiwa peke yake labda awe anamleta yule nesi.
Aliuguzwa na yule dereva mpaka alipopata nafuu. Alikuwa akilia kila alipokumbuka juhudi zake shuleni, na kuambulia sifuri. Kwani kipindi chote cha mitihani, Bella alikuwa amefungiwa ndani, hakufanya mtihani hata mmoja. Hakuweza kuwasiliana na Mat, kwani hakuwa na simu wala kompyuta. Alibaki akilia mchana na usiku, bila kujua cha kufanya. Na shule yake ndio ilikuwa imekwisha, kwani hakufanya mtihani hata mmoja.

***********************************************

Baada ya majuma mawili kupita Mzee Masha alirudi. Bella alipomuona anaingia mlangoni, alikimbilia chumbani kwake nakufunga mlango kwa ndani. “Nitavunja mlango Bella. Toka.” Bella alisogea mbali kabisa na mlango akakaa chini nakuanza kulia. “Bella?” Mzee Masha aliendelea kuita huku akigonga kwa nguvu sana. “Nakupa dakika moja uwe umefungua huo mlango, Bella. Lasivyo kitakachompata mdogo wako, usinilaumu.” Bella alivyosikia vile, alisimama kama mshale, akakimbilia haraka mlangoni nakufungua, kisha akarudi nyuma huku akilia sana.
 “Kwa nini umenisaliti Bella?” Bella hakuweza kujibu, alikuwa akilia sana kwa uchungu. Aliona anaadhibiwa bila sababu na alijua hata akijitetea vipi hawezi kufanikiwa kubadili mawazo ya Mzee Masha. Aliendelea kulia kama amefiwa. “Nitakuumiza tena Bella. Nataka unijibu. Kwanza njoo hapa karibu.” Bella alikataa kusogea, aliendelea kulia. “Nikikusogelea hapo Bella! Nimekwambia sogea karibu na mimi.” Bella alisogea hatua chache akasimama. “Nimekwambia hapa nilipo.” Mzee Masha aliendelea kugomba. Bella alisogea huku ameficha uso wake. “Sasa nataka unitajie jina la huyo mwanaume wako, anaitwa nani? Maana nimempigia simu, haipatikaniki tena.” “Mungu wangu ni shahidi. Sina mwanaume mimi?” Mzee Masha alimchapa Bella kibao cha nguvu akaangukia kitandani.
“Unanidanganya? Heri uniambie ukweli. Nitakuuwa Bella.” Mzee Masha alitoa bastola na kumnyooshe Bella. “Leo ndio mwisho wangu mimi na wewe Bella. Heri tufe wote. Huwezi kunisaliti.” Bella alificha uso wake akisubiri kifo chake. Moyoni alifurahi sana kujua siku hiyo ndio mwisho wa maisha yake, angalau akapumzike.
Gafla picha ya Eric akiwa peke yake anahangaika mtaani akiomba chakula, ilimjia. Bella alishtuka sana. Alikumbuka akifa, Eric atapata sana shida. Aligeuka kwa haraka sana. “Naomba usiniue T. Tafadhali mpenzi wangu, naomba unisamehe.” Mzee Masha alishapanda kitandani. “Nisamehe T. Kwa chochote nilichofanya, naomba msamaha. Sitarudia tena.” Bella alijisogeza karibu na kumkumbatia. “Tafadhali T.” Alijikuta akimng’ang’ania Bella bila kumuachia. Ni kama aliyekuwa na uchu, na hamu naye sana. Aliweka kila kitu pembeni na kuendelea kumng’ang’ania binti huyo kwa muda mrefu kitandani hapo akifanya naye mapenzi kama aliyepagawa. Alipojiridhisha, Mzee Masha aliamka, na kuondoka bila kuaga.
***********************************************

Baada ya siku mbili tena kupita, Mzee Masha alirudi nakumkuta Bella amejikunja kitandani amelala, mida ya mchana. Alikaa kitandani, Bella alifungua amcho na kumwangalia. “Nimepata muda wa kufikia, nimefikia maamuzi haya. Kwa kuwa umenisaliti, siwezi kukuamini tena. Na kwakua umekataa kifo, utaishi kwa masharti yangu. Hutarudi tena kusoma, utakaa humu humu ndani mpaka nitakapo jua kitu gani ufanye.” Bella hakuwa na pesa hata kidogo, alijua mdogo wake atafukuzwa shule. Na alijua akianzisha mambo ya pesa, ndio ataanzisha ugomvi mkubwa zaidi. “Naomba unisamehe T. Samahani kwa kukudhi.” Bella aliongea kwa upole sana akijaribu kujinyenyekeza. Mzee Masha akasimama, akaondoka bila yakujibu kitu.

***********************************************

 Bella alibaki akilia sana mpaka usiku Mzee Masha aliporudi. Alimuona akiingia bafuni kuoga bila yakumsemesha. Alipomaliza, akapanda kitandani. Bella alitamani asiguswe usiku ule. Moyo wake ulijawa uchungu sana na hasira. Alitamani kama angekuwa na uwezo wa kumuua yule Mzee, ili apumzike. Lakini alibaki ametulia pale kitandani akiwaza, mwishowe alikumbuka ni kwa nini yupo pale.
Akamgeukia. “Pole na kazi, T.” Aliongea kwa sauti ya upendo sana huku akizuia machozi. “Unanichanganya Bella. Nashindwa hata kufikiria. Hata kazi zinanishinda.” Bella alianza kulia taratibu, alijua mwisho wa yale yote ni nini kinafuata, lakini hakuwa na jinsi, ilikuwa lazima atumikie kifungo chake. “Pole na samahani, Masha.” Bella aliongea kwa kujishusha sana. “Lakini T, sikuwa….” Alishangaa amevamiwa tena kama swala. Masha alimkumbatia na kumbusu kila mahali kana kwamba walikuwa kwenye mazungumzo mazuri sana. Ilimbidi Bella atoe ushirikiano, kumfanya atulie.  
Kesho yake mzee Masha hakutoka mle ndani, walibaki kitandani na Bella, mpaka usiku. Bella alipoona ametulia na amerudi kwenye hali yake, aliona ndio muda muafaka wakuchezesha karata zake. “T!” Mzee Masha alimwangalia. “Hivi unajua ninakupenda, na siwezi kuwa na mwanaume mwingine?” “Yule uliyekuwa mkiwasiliana naye ni nani?” “Sielewi T. Na wala sijui nini unaongelea. Hakuna mtu nimewahi kuwasiliana naye kwa kutumia simu yangu ila wewe tu, mpenzi wangu.” “Usinidanganye Bella. Nachukia uongo. Heri uniambie kweli.” “Mungu wangu ni shahidi, T. Kwanza unasema umekuta ujumbe gani kwenye simu yangu?” Mzee Masha alisimama na kuifuata simu ya Bella kwenye gari yake.
“Hii hapa simu yako. Tena jumbe zote zipo. Ujumbe wa huyo mwanaume wako aliokuandikia na wako uliomjibu.” Bella alichukua ile simu na kuangalia ujumbe. “Mbona hizi zote nilikuwa nimekuandikia wewe T. Nilipopata huu ujumbe wa kwanza, nikakuonea huruma, nikajua labda ndio sababu ulipotea muda mrefu bila kunitafuta kwa kuwa hukuwa na pesa. Ndio maana hapa nikakujibu kuwa ile akaunti yangu nyingine ina hela, usiwe na wasiwasi. Nimeandika huu ujumbe, nikijua nawasiliana na wewe, sikuwa hata na wazo la kusoma namba, kwa kuwa hakuna mtu anayeifahamu hii namba yangu T, na wala sijawahi kumpa mtu namba yangu ya simu. Mungu wangu ni shahidi. Naomba niamini mpenzi.”  Bella alimwangalia Mzee Masha aliyekuwa kimya, na wote wakiwa wamejilaza kitandani.
“Lakini T, kama hii namba siyo yako, itakuwa ni namba ya nani?” Bella aliuliza. “Sijui.” “Nakuomba mpenzi wangu, kesho twende kwenye kampuni ya simu tukajaribu kuulizia mwenye hii namba.” Kidogo Masha akaanza kumwamini Bella. “Najua una mambo mengi yakufanya T, lakini naomba tukatafute ukweli. Sipendi tuishi bila kuaminiana, na sipendi kukuudhi. Najua umetusaidia sana T. Bila wewe sisi tusingekuwa hapa.” Bella aliamua kuanza kumpamba Mzee Masha. “Umenipeleka nchi na sehemu mbalimbali. Ona nyumba uliyoninunulia! Nguo na vitu vyote hivi vya thamani. Nisingependa uishie kuumia, T. Naomba tutafute ukweli ili na wewe urudi kuniamini mpenzi wangu.” Bella alikuwa na ulimi wakubadili akili za Masha, nakumlainisha kabisa. Kila alipokuwa akifika mikononi mwa Bella, alisahau kabisa kama ana mke na watoto.
“Unauhakika humfahamu mwenye hii namba, Bella?” “Kwa nini tusiende kesho kutafuta ukweli, T? Tafadhali mpenzi wangu, naomba twende. Tukamuulizie mpaka tumpate. Nakupenda T, siwezi kukusaliti.” Mzee Masha alizidi kuchanganyikiwa na maneno yale mazuri. Alimvuta karibu yake, akamkumbatia. “Nilikuwa mpweke ulivyoondoka. Ulinisahau?” “Unajua siwezi kukusahau Bella. Nilifungwa na mambo mengi.” “Kweli T? Ulitingwa mpaka ukashindwa hata kunitumia ujumbe!?” Bella alikuwa akiongea na Mzee Masha huku akimtizama na macho yake ambayo wakati wote yalimfanya Mzee Masha aliwazike. Alitabasamu na kumbusu Bella. “Unajua kunichanganya Bella, wewe?” Bella alicheka na kujilaza kifuani kwake. “Kesho tutaenda kujua ukweli.” “Asante T.” 

***********************************************

Kesho yake Mzee Masha alishindwa kumuachia kabisa Bella, waliishia kujifungia tu chumbani huku wakimtuma dereva awaletee chakula. Bella alibaki akijiuliza kama kweli Mzee Masha amesahu kabisa kipigo alichompiga!? Alimuona vile anavyomfurahia, nakukataa kumwachia kabisa. Alikuwa ni kama mtu aliyekuwa na hamu naye sana. Hakutaka Bella awe mbali naye hata kidogo. Alimfuata humo ndani, popote Bella alipokwenda, Masha naye alikuwa nyuma yake.
Japokuwa alijua kabisa, anatumia mwili wake kujiridhisha, lakini hakuwa akielewa kabisa, kama amenyimwa ubinadamu kwa kiasi hicho. ‘Anawezaje kunipiga vile, na kujifanya kama hakuna kilichokuwa kimetokea? Atakuja kuniua huyu Mzee siku moja!’ Bella aliwaza huku akitoa tabasamu, wakiwa jikoni akimwandalia matunda. ‘Lakini lazima nimvumilie, mpaka mdogo wangu atakapofika sehemu ya kuweza kujitegemea. Bella aliendelea kuwaza. Kila Mzee Masha alipomwangalia, alimpa tabasamu. “Nakuchanganyia matunda yote kwa pamoja. Kama unavyopenda.” “Twende nayo chumbani, tutakula wote.” Masha alijibu huku akirudisha macho yake kwenye simu ya Bella, aliyokuwa ameishikilia muda wote alipokuwa amemfuata hapo jikoni.
“Nimefurahi tumepata wote muda. Nilikuwa na hamu na wewe kweli T! Usiwe unanisahahu hivyo bwana.” “Mimi ndio nilikuwa nasikia kuchananyikiwa. Huoni nimeshindwa kabisa kutoka kitandani.” Bella akacheka. “Nimekuona. Lakini ni kweli tulihitaji huu muda. Imekuwa muda mrefu kweli!” Hakuna jinsi mtu angemwambia Mzee Masha kama anadanganywa, akakubali. Kila Bella alipokuwa akiongea naye, ni kama akili yake iliacha kufanya kazi kabisa.
Alikuwa amefungwa kwenye mahusiano ya wanawake wawili ambao wote ilikuwa ngumu kuwaacha. Mkewe alishapoteza sifa zote moyoni mwake. Kila alipojaribu kumlinganisha na Bella, alijiambia ni kama mchana na usiku. Lakini alijua akimuacha mkewe, ndio atakuwa amepoteza familia nzima, mpaka Zera. Kila alipofikiria kumuacha Bella, na kurudi kutulia kwa mkewe, ilikuwa ni kama kujinyima usingizi maishani mwake. Bella alikuwa ni kila kitu. Alikuwa mzuri kwake kwa kila kitu. Alibaki akihangaika asijue chakufanya.
 “Masha apata ukweli juu ya Bella.”
Walishindwa kutoka siku ile. Masha alisema kila kitu kitasubiri siku ile, anataka kupata muda naye. Kesho yake, waliamka mida ya saa nne, wakaingia kuoga wote, wakatoka. Bella alijitahidi kujipendezesha sana. Mzee Masha alitamani kuahirisha safari, ili abaki tena na Bella, lakini Bella alimbembeleza lazima waende wakamtafute mwenye hiyo simu. Walipofika kwenye ofisi za mtandao wa namba hiyo ya simu, Mzee Masha alipewa jina kamili la mmiliki, tena aliambiwa ni mojawapo ya namba zilizokuwa zimenunuliwa na kampuni fulani, maalumu kwa ajili ya wafanyakazi wao.
“Naomba twende T, tukaonane na huyo mtu.” Mzee Masha alimshangaa sana Bella. “Tafadhali mpenzi wangu.” Bado Bella na Mzee Masha walikuwa wamekaa mbele ya meza ya muhudumu. Aliwatizama kwa hofu. Lakini na yeye alijua Bella alichompendea mtu mzima vile, ni pesa tu. Alisikia kukereka lakini ilimbidi kuwavumilia na kuwapa tabasamu, Masha na Bella. “Eti T?” “Kama unaona hivyo ni sawa.” Wakatoka pale.
Waliongozana mpaka kwenye kampuni ya yule mtu, kwa bahati nzuri walimkuta na ndio alikuwa meneja wa pale. Alikuwa ni baba mtu mzima kidogo. Aliwakaribisha ofisini kwake. “Karibuni sana.”  Wote wawili walikaa mbele ya meza yake. “Asante. Tunataka kukuuliza kitu.” Mzee Masha alianza. “Unaifahamu hii namba?” “Ndiyo. Ni ya kwangu, natumia hapa ofisini.” “Unamfahamu Bella?”  “Bella!?” Yule baba alikunja uso na kuuliza. “Au Enabella?” Bella alidakia, na kuongeza kama kumsaidia Masha, katika swali lake. “Hapana. Kwani kuna nini?” Bella na Mzee Masha wakaangaliana.
“Muonyeshe zile jumbe zote.” Bella aliongea kwa sauti ya chini kidogo, huku akimwangalia Mzee Masha. “Siku hii hapa, ulituma ujumbe kwenda kwenye simu hii hapa.” Yule bwana alichukua simu ya Bella, akaanza kusoma ule ujumbe. “Nakumbuka. Huu ujumbe nilikuwa namtumia mtoto wa kaka yangu. Alinipigia simu kwa kupitia hii namba, akifuatilia pesa alizokuwa ameniomba kwa ajili ya kulipia ada ya shule yake. Anasomea mambo ya kompyuta. Sasa nilikuwa kwenye kikao, nikaamua kumjibu kwa kumwandikia ujumbe. Lakini majibu yake, sikuyaelewa kabisa. Nilifuta ule ujumbe muda ule ule, kuhofia mke wangu asije akaukuta kwenye simu yangu.” Mzee Masha alionekana kupooza kidogo.
Akachukua simu ya Bella na kufungua upande wa ‘outbox.’ Akamuonyesha. “Alikujibu hivi?” Mzee Masha alimuuliza. “Eheeee! Hivyo hivyo. Kwa kweli nilishtuka sana.” Machozi yalianza kumtoka Bella. Samahani sana. Mimi ndio niliandika hivyo, lakini sikujua kama nawasiliana na wewe. Huyo mtoto wa kaka yako, aliniomba simu apige. Aliponirudishia nikairudisha mfukoni bila kuangalia namba. Sasa ulipotuma ujumbe, kwa kuwa sina mtu ambaye anaifahamu hiyo namba isipokuwa mpenzi wangu, sikujisumbua kusoma namba, nikajibu tu, nikijua nawasiliana na mpenzi wangu. Samahani sana.” “Bila shaka binti. Hapakuharibika neno. Nilifuta huo ujumbe palepale ulipoingia. Si unajua maswala ya ndoa Mzee mwenzangu?” Alimgeukia Mzee Masha. “Unaweza kubomoa ndoa yako kwa ujumbe mmoja tu uliongia kwa sekunde, kisha ikakuchukua miaka mingi sana kuja kurudisha ndoa yako katika hali nzuri. Tena nilihakikisha na ‘Block’ kufungia hiyo simu yako isiwahi kunipigia wala kutuma ujumbe tena.” Yule mtu alionekana muungwana sana. Aliongea huku akicheka kirafiki. “Asante sana kwa muda wako ndugu. Uwe na kazi njema.” Mzee Masha aliaga na kutoka kimyakimya, huku Bella akiomba Mungu awe amemuelewa yule baba, na amuache yeye, arudi kwenye ndoa yake.
***********************************************

Walirudi kwenye gari, Mzee Masha akiwa kimya kabisa. Bella alitegemea hata kuombwa msamaha wakupigwa bila kosa, lakini alishangaa kuona mpaka wanafika nyumbani Mzee Masha haongei kitu. Alipiga simu mahali ili gari ya Bella irudishwe, na kumkabidhi simu yake. Baada ya muda mfupi Bella alirudishiwa kila kitu chake, lakini Bella hakutaka tena. Gafla alianza kukinahiwa na vitu vya Masha, aliyemuona katili kupita shetani.
‘Lazima nianze kujitegemea. Huyu baba ananinyanyasa sababu ya mapesa anayotumia kwangu na mdogo wangu.’  Bella aliwaza akiwa bafuni anajaza maji kwenye jakuzi. Alimwagia ile chumvi yenye marashi ndani ya yale maji yakatengeneza harufu nzuri sana iliyofanya chumba kizima kinukie vizuri. Akavua nguo zote hukohuko bafuni, akatoka kumfuata mzee Masha chumbani. “Tumezunguka sana T, twende tukaoge.” Bella aliinama, akamvua viatu, na nguo zote wakaelekea bafuni.
Baada yakujisuuza, Masha aliingia kwenye maji aliyokuwa ametengeneza Bella. “Maji yana joto zuri.” Mzee Masha alisifia. Bella alitabasamu tu, huku akifikiria ni jinsi gani atakavyomuingia Masha siku ile ili amruhusu ombi lake. Alijua ile siku ndio yakutupia ndoano yake, kwani ni kweli alimkosea, ila alishindwa kumomba tu msamaha, kwa hiyo alijua ile ni siku ya kuomba chochote na kupewa.
“Nimekurudishia gari yako, umeona?”  Masha alivunja ukimya. “Asante mpenzi wangu. Lakini kwa nini tusiwe tunatumia gari moja tu? Tuwe tunatoka wote, wakati unaenda kazini na mimi unishushe kazini kwangu.” Mzee Masha alimgeukia Bella, kwani Bella alikuwa amekaa nyuma ya mgongo wake akimmwagia maji taratibu kama kucheza. “Kazini!?” “Ndiyo. Nataka kuanza kazi T. Nifanyie kazi kile nilichosomea.” “Daah! Nimesababisha hukufanya mitihani yako.” “Hamna neno, T. Maadamu nilisoma, ninao ujuzi. Naomba nisaidie kutafuta tu kazi popote, nitarudia kusoma kidogo wakati nafanya kazi kisha nitafanya mitihani. Tena natamani tuwe tunafanya kazi sehemu moja, ili tuwe tunakuwa wote wakati wote.” Bella alikuwa akimchokoza tu.
Alijua haiwezekani. Mzee Masha asingeruhusu Bella afike ofisini kwake kwani mara nyingi watoto wake huwa wanapendelea kwenda na baba yao huko, hata Bella alishakuwa kwenye ofisi za Mzee Masha mara nyingi tu akiwa na Zera na kaka yake Zera. “Kwa sasa hamna nafasi ya kazi kwenye ofisi zangu zote. Ila namfahamu mtu mzuri sana, ana ofisi yake. Anaweza kukuajiri bila shida. Kwanza nimewekeza sana kwenye kampuni yake na kwenye elimu ya watoto wake. Nafikiri ni wakati mwafaka na yeye anatakiwa kulipa fadhila.” Bella alitamani kurukaruka kwenye yale maji. “Asante T. Nakushukuru mpenzi wangu.” “Kwa hiyo gari hutaki?” “Sioni sababu T. Naomba tuwe tunaongozana kama zamani. Kama wewe utakuwa na mambo mengi, basi dereva atakuwa ananifuata. Najua itakupunguzia wasiwasi.” Mzee Masha alifurahi sana, alizidi kumwamini Bella, ambaye alianza kujiwekea mikakati ya kujitoa mikononi mwa Mzee Masha taratibu.

 “Bella kwenye usaili!”
Baada ya kama siku tatu hivi, Mzee Masha alimpigia simu Bella mida ya jioni wakati yeye yupo kazini, na Bella yupo nyumbani. Alimwambia dereva atamfuata anatakiwa kwenye usaili. Kama kawaida yake alivaa vizuri, akapendeza. Dereva alimfuata wakaongozana mpaka kwenye hiyo ofisi. Ilikuwa ni ofisi kubwa tofauti na alivyotegemea Bella. Ilikuwa na idara mbili kubwa, masoko na watunza fedha. Upande wa uongozi au utawala, alikuwa ni Mmiliki mwenyewe akisaidiana na familia yake.
Alifika mapokezi akapewa kiti na dada aliyemkuta pale, naye alikuwa mrembo tu na alionekana anaijua kazi yake. “Ungehitaji kinywaji chochote wakati unasubiri?” Alimuuliza Bella. “Hapana, asante.” Bella alijibu na kujiweka sawa kitini. Baada ya muda simu ya mezani kwa yule sekretari iliita, akajibu ‘Sawa.’ Kisha akakata simu na kumgeukia Bella. “Naona wapo tayari kwa ajili yako. Ingia kwenye hii ofisi.” “Asante.” Bella alijibu na kusimama.
Alifungua mlango taratibu kisha akaingia. Alikutana na watu wawili waliokuwa wakimsubiri ndani ya ofisi hiyo. Mmoja alikuwa mtu mzima sana, Bella alimwangalia kidogo, akajua yule ni wakumpa shikamoo. Akasogea kwenye meza kubwa aliyokuwa amekaa akampa mkono, “Shikamoo.” Yule mzee aliitikia, kisha akamgeukia kijana mwengine aliyekuwa ameinamia faili pembeni ya hiyo meza kubwa alimuona ni kijana, alisogea karibu zaidi akanyoosha mkono, “Habari ya…” Macho yake yakagongana na Elvin. Bella alishtuka sana, akabaki akimtizama Elvin na Elvin alibaki akimtizama Bella. Yule Mzee alibaki akiwatizama wote wawili kwa zamu. “Mnafahamiana?” “Hapana.” Elvin alijibu kwa haraka sana huku akibabaika, lakini mtu mzima hadanganywi kirahisi. Alipoona Bella ameinama na kurudisha mkono wake taratibu, alijua lipo jambo kati yao. “Karibu kiti.” Bella alikaribishwa kiti  na yule Mzee.
Bella alirudi nyuma taratibu huku akiwaza, asijue aondoke tu pale, au afanyaje. Alikaa na kubaki ameinama akichezea pochi yake taratibu. “Naitwa Mwasha, ndio mmiliki wa hii kampuni. Huyu ni kijana wangu, anaitwa Elvin, ndiye anayenisaidia sana katika mambo ya uongozi hapa. Karibu sana.” “Asante.” Bella alijibu huku ameinama. Kimya kilipita kwa muda, kisha Mzee Mwasha akaamua kuvunja ukimya tena. “Labda ungeanza kwa kujitambulisha.” Bella alitulia kwa muda kama anayejishauri, kama aendelee na usahili au aondoke tu. Wote walikuwa kimya wakimsubiri.
Alikohoa kidogo kama kusafisha koo, lakini bado alikuwa hajaamua kama aendelee na ule usahili au aondoke. ‘Nikiondoka, nitamwambia nini Mzee Masha? Nimwambie siwezi kufanya kazi na Elvin, kwa kuwa ananijua? Mzee Masha atakuwa aliwaambia nini siku ile nilipozimia kule Dubai? Ananifahamu kama nani kwa Mzee Masha? Hapa nikujidhalilisha tu, heri niondoke.’ Bella aliendelea kuwaza wakati akisubiriwa ajitambulishe. Na wote walikuwa kimya wakimsubiri aseme kitu.
“Ungependa tukuletee kitu chochote cha kunywa?” Mzee Mwasha aliuliza kiustarabu sana. “Hapana, asante.” “Basi tunakusubiri, utakapokuwa tayari tunaweza kuendelea.” Alionekana ni Mzee muungwana sana. Alikuwa mtulivu, hata sura yake ilionyesha ni mtu muungwana.
***********************************************

Haya.... Uso kwa Uso na Elvin aliyemuuguza nchini Dubai. Akitafuta njia ya kujiokoa kwenye mateso makali sana ya Masha, anakutana na kipingamizi Elvin aliyemshuhudia nchini Dubai akiwa na Masha. Wazi alionyesha kuvuja damu kwa madhara fulani. Elvin alimuelewaje kule? Ataweza kufanya naye kazi?

Usikose kuwa na Bella, katika kipindi hichi kigumu cha maisha anachopitia akiwa peke yake bila mshauri au faraja. Atafanya nini?

JE, WEWE UNGEKUWA ENABELLA, UNGEFANYA NINI? NA KWA NINI? USIACHE KUTOA MAONI YAKO HAPO CHINI.

1 comment:

  1. Ooh!I like this story coz it inspire me to have self confidence keep it up the author

    ReplyDelete