Story

My Past - Sehemu ya 11

Wednesday, June 14, 2017 naomimwakanyamale 0 Comments

W
azazi wake walibaki wakimwangalia jinsi anavyozunguka pale chumbani wakijua wazi. “Jipe muda wa kufikiria zaidi Elvin. Ndoa sio kitu cha kukimbilia.” Mwasha alijaribu kutupia neno. “Bella ni mke wangu baba. Nilishakueleza kila kitu. Na kuwa mjamzito hakubadilishi chochote. Ila ni kweli namuhurumia sana. Alikuwa amefurahia sana kuachana na Mzee Masha. Leo akija kujua amebeba mtoto wake! Nahisi atachanganyikiwa.” “Sasa nashauri mpe muda wa kupumzika, usimwambie kitu chochote kwanza. Amehangaika sana kuniuguza huyu mtoto. Alikuwa halali, mpaka nilikuwa nikimuhurumia. Ngoja apate muda wakupumzika, akili yake ikishatulia ndio umwambie swala la ujauzito. Ukishaona jinsi alivyolipokea, ndipo uendelee na maswala ya uchumba. Lakini naomba upate muda wakufikiria Elvin. Ujue mtaanza maisha ya ndoa na Bella, akiwa na mtoto ambaye sio wako!” “Nampenda Bella, mama. Hayo ni matokeo ya maisha aliyoishi zamani. Nilazima mimi ndio niwe mume wa Bella. Nitachanganyikiwa nikija kuona anaolewa na mtu mwingine.” Mama Mwasha alicheka kidogo. “Haya Elvin, sisi tunakuombea. Tunaamini mawazo yako.” Elvin alifikiria kidogo. “Asanteni kwa ushauri wenu na kumpokea Bella na Eric. Asanteni sana. Na nitafanya kama mlivyonishauri.” “Na mimi itabidi nimtafute Mzee Masha nizungumze naye, kabla hamjarudi, nijue ni jinsi gani atamsaidia Bella na huyo mtoto. Asibaki akilea mwenyewe.” “Ni kweli baba. Na kwa kuwa Mzee Masha anakuheshimu sana, najua mtaelewana tu.” Elvin alitoka lakini akiwa amechanganyikiwa.
atagairi baada ya kusikia Bella ni mjamzito

********************************************

Ni kweli Bella alikuwa akiendelea kunenepa. Kwa kuwa akili zake zilikuwa kwa Mama Mwasha hakupata muda wakujifikiria hata kidogo. Alilala, akaamka ilishakuwa jioni. Aliingia bafuni kuoga, akarudi kwenye sanduku lake alilokuwa ameliacha hapo nyumbani, akaanza kutafuta nguo ya kuvaa kwenye tafrija. “Elvin! Elvin!” Walimsikia akimwita Elvin akiwa chumbani kwake, wakajua ameamka. Elvin akagonga na kuingia. Alimkuta amejifunga kitenge cha Mama Mwasha na amekasirika sana. “Vipi?” “Nguo zote hazinienei, nitavaa nini?” “Umejaribu zote.” “Ndiyo. Hazinienei, zinabana na sitaki kubanwa hata kidogo leo.” “Pole. Unataka niende kule kwako nikakuletee nguo zingine?” “Nitashukuru sana. Basi nalala tena kidogo wakati nakusubiria. Najisikia mwili unachoka. Tokea nipo India. Nilimwambia mama, akasema labda kwa kuwa silali vizuri usiku.” “Labda. Basi lala, nikirudi nitakuamsha.” “Lakini njaa pia inauma sana, Elvin.” “Ngoja nikakuletee chakula. JJ ameshaivisha.” Bella alitabasamu. “Asante Vin.” Elvin alirudisha tabasamu na kutoka.

Baada ya muda mfupi akarudi na sahani ya chakula. Bella alikivamia kile chakula, akaanza kukila bila kupumzika, Elvin alibaki akimshangaa. “Nenda basi ukaniletee nguo. Ujue sina nguo kabisa.” “Haya. Sitachelewa. Nitarudi sasa hivi.” Elvin alimtoa headphone Eric masikioni. “Twende unisindikize.” “Subiri kidogo Elvin, namalizia.” “Hapana Ric. Nenda bwana na Elvin sasa hivi mkaniletee nguo.” “Namalizia kidogo Bella.” “Eric wewe!” “Basi Bella. Ngoja niende.” Bella aliinamia sahani yake na kuendelea kula bila kuongeza neno.

Elvin na Eric walirudi na nguo zote za Bella. Wakamkuta amelala kama aliyekufa. “Bella! Bella! Amka wageni wameshaanza kufika.” “Nataka kulala kidogo Elvin. Nipe kama dakika kumi nitaamka.” “Nakupa dakika 20 nyingine Bella, nikirudi nilazima utoke hapo kitandani.” Kabla hajamaliza kuongea, alimsikia Bella akihema kuashiria alishapotelea usingizini. Elvin alisimama pale akimwangalia kwa muda. Akamfunika shuka vizuri, akabaki amekaa pembeni yake akimtazama. Bella alikuwa mzuri sana. Alijaliwa sura nzuri, ya kuvutia kuangalia. Elvin alicheka kidogo, kila akikumbuka visa vya Bella aliendelea kucheka. Alikuwa akimsubiri kwa hamu sana, ili waongee na wataniane lakini Bella alirudi mchovu na mtulivu sana. Alikaa pale akifikiria zaidi ya nusu saa.

 “Bella! Bella!” Bella alishtuka. “Nilikuwa na hamu na wewe kweli!” “Hata mimi Elvin.” “Sasa mbona huamki tukaongea?” “Pole. Nilikuwa nimechoka. Basi navaa sasa hivi nakuja. Umesikia?” “Usichelewe basi.” Kabla Elvin hajasimama ili atoke, mlango ulifunguliwa. “Nyinyi mbona hamtoki?” Eno akauliza. “Nilipitiwa na usingizi. Nakuja sasa hivi.” Bella alijibu, akasimama na kuanza kutafuta nguo. Eno alitoka na kuwaacha pale chumbani, Eric akiwa amepotelea kwenye michezo yake. “Hivi huyu alikuwa anafanya kitu kingine au ni hizi game tu?” “Nilikuwa nikienda nae kazini kuanzia asubuhi mpaka usiku. Alikuwa anachoka mpaka namuhurumia.” “Afadhali.” Bella alianza kutafuta nguo.

 “Mbona umeleta nguo zote?” “Si tunaishi wote hapa?” “Elvin wewe! Natakiwa turudi nyumbani kwetu, maisha mengine yaendelee. Hatuwezi kuhamia hapa moja kwa moja.” “Kwa nini?” “Elvin jamani!” “Niambie Bella, kwa nini hutaki tuishi hapa pamoja?” “Unajua hatuwezi Elvin. Hapa ni nyumbani kwa wazazi wako. Mimi nipo na Ric, hatuwezi kuhamia tu hapa. Si sawa.” “Kwa hiyo kama hapa ingekuwa ni nyumbani kwangu, je?” “Halafu ukanitaka tuishi wote?” Bella na yeye akauliza. “Ndiyo. Ungekubali?” “Haraka sana tena bila hata kufikiria mara mbili. Ningehamisha vitu vyangu vyote mpaka vijiko.” Elvin akacheka. 

“Basi utanifanya niharakishe kumalizia ile nyumba kwa haraka sana.” “Kwa hiyo ikiisha utatuchukua mimi na Ric?” “Haraka sana.” Bella alianza kucheka. “Usije kumaliza kujenga ukatukimbia sisi halafu ukahamia na watu wengine!” “Nishawahi kukuahidi kitu halafu sijatimiza Bella?” Bella akacheka tena. “Hujawahi Elvin.” “Basi tuwe wavumilivu. Nikimaliza tu kujenga, tunahamia wote. Tutakuwa tukiishi wote Bella. Si hauta nikimbia?” Bella alifurahi sana. “Nikikimbia, tunakimbia wote. Mimi, wewe na Eric. Ric akioa tunabaki mimi na wewe tu, Vin. Ni sawa?” Elvin alikuwa akicheka kwa furaha. “Kabisa. Lakini tukae wote hapa kidogo, usikimbilie kurudi kule kwako. Kwanza naona Ric ameshapazoea hapa.” “Ameniambia, na kila nikimwambia itabidi tuondoke turudi kwetu ananizungusha na maneno mengii. Mara nisubirie mpaka shule zifungue, mara hiki. Anaonekana amepafurahia sana hapa. Ric anapenda watu. Anatamani kuishi kwenye nyumba ya watu wengi sio sisi wenyewe wawili tu.” Mlango ulifunguliwa tena. “Bella njoo nikutambulishe kwa Mchungaji wetu.” Mama Mwasha aliingia. “Natafuta nguo mama. Nguo zote zinabana. Sijui ni sababu ya kula sana? Kila saa nasikia njaa. Hapa sina nguo ya kuvaa hata moja, mama yangu!” Bella aliendelea kulalamika.

“Ngoja nikusaidie kutafuta nguo, Bella. Mpe muda mfupi tu mama. Atakuja kusalimia wageni.” Elvin aliingilia maongezi yao na kuinama kwenye sanduku la Bella na kuanza kumtolea nguo za kujaribisha. “Inabidi kwenda kununua nguo nyingine kesho.” “Kweli Elvin, kuliko hii shida tunayopata.” Mwishowe alipata gauni kubwa kidogo, lilikuwa limechanua kuanzia chini ya kifua. Lilimkaa vizuri sana. “Umependeza sana.” Bella akacheka. “Asante. Na nimelipenda hili gauni halijanibana hata kidogo. Lakini njaa inauma tena, Elvin.” “Ndio tutoke ukale.”

Elvin na Bella walitoka pale chumbani na kuelekea jikoni kula. Baada ya kula tena, Bella alitoka kusalimiana na wageni. Hakuna aliyemuona Bella akatosheka kumwangalia binti huyo. Cheko ilimtawala usoni wakati wote nakumfanya kila anaye ongea naye asichoke wala kujisikia vibaya. Na usiku ule waliufanya ukawa ni usiku maalumu kwa Bella. Watoto wa Mama Mwasha walikuwa wamemwandalia zawadi nzuri sana, kama kumshukuru lakini walijua usiku huo ndio mdogo wao angemvalisha pete ya uchumba pia. Bella alikuwa akitoa machozi ya furaha. “Na tumekuandalia sehemu maalumu ya kwenda kupumzika kabla yakurudi kazini. Elvin na Eric watakusindikiza.” JJ alitangaza mbele za wageni wote waliokuwa wamefika mahali pale. “Asanteni sana jamani. Lakini sijui niseme nini? Sikuwa nimejiandaa. Na wala msinge hangaika kwa kiasi hiki jamani! Mama Mwasha ni mama yangu.” Watu walikunywa na kula, lakini Irene na wenzake hawakuacha kunong’ona, huku rafiki wa Mama Mwasha na wao wakiongea kivyao.

Hakikumsumbua sana Mama Mwasha juu ya minong’ono na jicho la husuda kwa Bella. Kwanza alijua ni wivu ndio unaowasumbua. Uzuri wa Bella, ulikuwa sio wakufichika, na wema wake haukuwa wakinafika. Hata alipocheka, alionekana ni mwanadamu mwenye moyo mzuri kutokea moyoni. Hakuwa ameficha hila ndani yake. Tafrija iliisha, kila mtu akaondoka, wakabaki wao kama familia wakiongea na kucheka.

********************************************
“Sasa jamani, Bella akishatoka mapumzikoni na Elvin na sisi tunaenda mapumzikoni mwezi mzima. Njoo kwanza hapa kwenye meza ya chakula tuongee mambo yetu ya familia yetu.” Eli alianza kumchokoza tena. “Wewe na nani?” Bella alimuuliza. Eli akaenda kumshika mkono pale alipokuwa amekaa sebleni na kumvutia mezani. “Si wewe na mimi!” Bella alianza kucheka bila kunyamaza mpaka machozi na kufanya wengine waanze kucheka pia. “Sasa unacheka nini wewe Bella?” “Nacheka mambo mengi sana.” “Nini?” “Ujue wewe Eli una utani mbaya sana? Kwanza sitaki mwenyewe!” “Kwa nini?” “Namtaka Vin.” “Sasa safari hii si unakwenda na Vini, halafu ukirudi ndio tunaenda sisi!” “Kwanza haitwi hivyo. Unaharibu jina lake mwenyewe. Mimi naenda kulala, nimechoka. Twende Vin unisindikize.” “Ngoja mimi nikusindikize Bella wangu.” “Akuuu! Naenda zangu na Vin. Wewe mchokozi sana Eli.” Bella alipandisha mabega yake yote kukataa. 

“Mimi na wewe Bella?” “Mmmh!” Bella aliguna, kisha akaanza kucheka tena. “Ila ujue Eli mimi nakupenda sana? Nilikuwa nakukumbuka nacheka mwenyewe.” “Najua kama unanipenda Bella. Huwezi kuishi bila mimi.” “Sasa usianze kujisifia. Kama ndio hivyo nafuta urafiki na wewe, siongei na wewe tena.” “Nina uhakika huwezi Bella.” Bella alisimama akaanza kuondoka kimya kimya kumfuata Elvin. “Aaaah! Ndio umeanza kuninunia? Njoo Bella wangu bwana.” “Sitaki tena. Twende Vin.” Alienda kumfuata Elvin alipokuwa amekaa, akamshika mkono. “Usiku mwema Bella. Uniote mimi eeh!” Eli alimchokoza tena. Akarudi na kumbusu shavuni kimya kimya akaondoka. “Bwana Bella ananipenda jamani! Hawezi kulala bila kunibusu!” Bella akarudi akamfuta pale alipombusu. “Nimechukua busu langu.” Kila mtu alianza kucheka. “Mjinga wewe!” Bella akarudi kumshika Elvin mkono wakaondoka.

 “Elvin aweka ahadi ya Maisha kwa ndugu hao wawili”
Elvin, Bella na Eric waliondoka asubuhi na mapema wakielekea mapumzikoni. Elvin aliwapitisha kwenye nyumba yake. Wakapata muda wakuzunguka eneo zima, huku Elvin akimtaka Bella ushauri. Nini kiongezwe, nini kiwekwe wapi. Bella naye alimpa ramani nzuri sana ya bustani, na kumpongeza Elvin kwa ujenzi wa hiyo nyumba. “Ric! Unajua kuwa hapa ndio patakuwa kwetu?” Elvin alimgeukia Eric. “Unamaanisha nyumbani kwetu pamoja na mimi na Bella?” “Ndiyo.” Elvin alijibu. “Kweli Elvin?” Eric aliuliza akionyesha mashaka. “Huniamini?” “Nakuamini, lakini nilidhani unanitania.” Eric aliongeza. “Sikutanii Ric. Hapa ndipo patakuwa nyumbani kwetu.” Eric alitulia kidogo. Bella hakuwa ameelewa. Alitegemea mdogo wake afurahie. “Vip Ric?” Bella alimshika begani. “Hujapapenda?” “Naogopa Bella. Huwa wanabadilika.” “Sio Elvin. Elvin hajawahi kutuahidi kitu halafu akashindwa kutimiza.” Bella alimuhurumia mdogo wake. “Siwezi kuwageuka Eric. Na sina sababu yakufanya hivyo. Tuombe Mungu ili iishe haraka, tuhamie. Kwanza tutakuwa tukija wote huku wakati wanamalizia kujenga, ili na wewe utoe mawazo yako.” Eric alicheka bila ya kujibu kitu. “Asante Vin.” Bella aliamua kushukuru kwa ahadi aliyokuwa amepewa. “Mimi ndio nitakuwa na furaha zaidi, mkija kuishi na mimi hapa. Mmeniongezea shauku ya kumaliza mapema.” Walizunguka pale kwa muda, kisha wakaamua waendelee na safari yao.

********************************************

Wote walitoka pale wakiwa na furaha sana. Eric na Bella walikuwa wakiimba njia nzima, Elvin dereva akiwa anawasikiliza ndugu hao. Walifika Bagamoyo, mazingira ya hoteli yalimfurahisha sana Bella kitu kilichomfanya na Elvin afurahi. Kwa Eric yeye hakuwa na neno, ilimradi yupo na dada yake, hakujali alipo. “Nataka kuogelea kabla jua halijaisha, Bella.” Eric alipenda sana kuogelea. “Subiri tutaenda kuogelea wote.” Walipopata chakula cha mchana, wote walielekea kuogelea kwenye pool sio baharini. Walishinda huko wakila na kunywa mpaka ilipofika jioni. “Nimechoka nataka nikalale kidogo, Elvin.” “Basi nitakuletea chakula cha usiku chumbani.” Bella aliondoka akaenda kulala akawaacha Elvin na Eric pale pale.

Usiku Elvin na Ric walienda kumgongea Bella chumbani kwake. Bella alikuwa na chumba chake, Elvin na Eric na wao walikuwa na chumba chao. “Naomba hata nusu saa nyingine, Elvin. Nitaamka kula hicho chakula.” Bella hakutaka kutoka kitandani. “Hapana Bella. Amka ule, ukishiba ndio utalala vizuri.” Bella alikaa na kuanza kula. “Bella!” Eric aliita. “Kesho naomba tukaogelee baharini.” “Wewe huchoki kuogelea!? Leo tumeshinda kwenye maji siku nzima!” “Bella please!” “Sawa, samaki. Kesho tukiamka tunahamia baharini.” Eric akacheka. “Unaniita samaki?” “Kwa kuwa huchoki kukaa majini.” Eric alipanda kwenye kitanda cha dada yake, akaanza kuruka ruka. “Shuka bwana Ric, utanifanya nitapike.” “Miss you Bella. Unalala tu, hujapata muda na mimi hata kidogo!” Eric aliacha kuruka ruka, akabaki akiendelea kuongea naye huku bado akiwa kitandani kwake amepiga magoni, amemuegemea mabegani huku akimchungulia usoni. 

 “Na mimi pia ninahamu na wewe, Ric. Najua nimerudi na uchovu mwingi. Nikiamka kesho nitakuwa na nguvu, tutapata muda wakutosha. Umenisikia?” “Hope so.” Eric alionyesha kutokuridhika. “Promise Ric. Tutapata muda kesho. Tutacheza mpaka unikimbie.” “Wewe ndio huwa unakimbia ukishindwa, Bella. Sio mimi.” “Riccc!!!” “Muulize Elvin. Hukukimbia siku ile?” “I was tired.” Bella alijibu. “Hicho ndio kisingizio chako kila siku, Bella.” Elvin alikuwa akicheka tu.  “FINE. Tutaona kesho.” Bella alijibu kwa ujasiri. “Si umemsikia mwenyewe Elvin? Kesho akisema amechoka, hakuna kumruhusu kurudi kulala. Mpaka nimfunge magoli yakueleweka ndia ataruhusiwa kuja kulala.” “Usije kulia tu, hiyo kesho.” “Sawa Bella.” “Basi narudi kulala, ili kesho niamke na nguvu.” Bella alijirudisha kitandani. Alikuwa na uchovu usioisha. 

“Wakati wewe unalala sisi tutakuwa tukiangalia tv hapahapa chumbani kwako.” Elvin alijirusha na yeye kwenye kochi. “Tucheze game Elvin.” “Umeanza Ric. Kwani huwezi kuwa kama watu wengine? Unacheza game kila wakati!” Bella aliwaingilia. “Leo sijacheza hata kidogo Bella.” “Sitaki kuwaingilia. Mimi naenda kupiga mswaki nilale. Nyinyi endeleeni kufanya chochote mnachotaka.” “Ila umeniahidi kuogelea bahari kesho.” “Nakumbuka Ric. Na tutaenda kuanzia asubuhi mpaka usiku. Mimi nikiamka tu, nitaelekea baharini, mnifuate huko.” Eric alienda akambusu dada yake. Bella akaenda kupiga mswaki, akarudi kujitupa kitandani kulala.

********************************************

Aliamka ilishakuwa asubuhi, kumepambazuka. Hakuamini kama alilala kwa kiasi kile. Akaangaza macho yake kulia na kushoto hakumkuta Eric wala Elvin. Alijisikia ameamka na nguvu mpya.  Akakumbuka ahadi aliyomuahidi Eric. Alivaa nguo za kuogelea, akachukua taulo lake akatoka kuelekea chumbani kwa kina Elvin. Alipoona wamelala. Alirudi chumbani kwake, akaandika ujumbe mfupi kwenye kikaratasi akaenda kukitumbukiza chini ya mlango wao, yeye akaelekea baharini asubuhi hiyo kuogelea ili mdogo wake amkute huko baharini, aridhike.

 “Mkasa Mwingine Mkubwa wa Bella"
Kwa kuwa Elvin na Eric walichelewa sana kulala, waliamka mida ya saa nne. Wakati anaelekea bafuni, Elvin aliona kile kikaratasi.
Nimetangulia baharini kuogelea. 
EnaBella!

Elvin alifanya haraka akabadili nguo, akaamua kumuacha Eric aendelee kulala, yeye akamfuata Bella ili wapate muda wa peke yao kabla Eric hajaamka. Alipofika baharini akakuta malapa ya Bella na taulo lake mchangani, lakini Bella hakuwepo. Alirudi sehemu wanapouzia chakula kumuangalia kama yupo, kwa kuwa alihisi labda alisikia njaa akaamua kwenda kula kwanza ndipo arudi kuogelea, lakini Bella hakuwepo. Elvin alizunguka ile hoteli kama mara tatu, vyooni na mabafuni bila kumuona Bella. Hofu ikaanza kumuingia.

Akarudi baharini kumtizama tena, lakini hakuwepo. Mwishowe akaamua kujitosa majini na kuanza kumsaka. Aliogelea zaidi ya nusu saa, tena chini sana ya bahari akimsaka Bella bila mafanikio. “Mungu wangu Bella wangu!” Elvin alianza kuongea peke yake. Mwishowe akaanza kukimbia kila mahali akimwita mpaka wahudumu na wageni wengine walipojua kuna tatizo. Elvin aliwaambia Bella amepotea, labda amezama. Uongozi wa hoteli uliwatuma waokoji humo baharini kumsaka Bella, huku wengine wakitembea pembeni ya ufukwe kumtafuta. Elvin alikuwa kama amechanganyikiwa.

Aliamua kumpigia baba yake simu. “Vipi mbona unalia?” “Bella amepotea baba. Nitafanya nini?” “Amepotelea wapi?” Elvin alisimulia huku akilia sana. “Nampigia simu JJ, tunakuja sasa hivi kusaidia kumtafuta.” “Msichelewe baba, nahisi nachanganyikiwa.” “Naomba utulie Elvin. Eric yuko wapi?” “Mungu wangu Eric!” Elvin akakata simu na kukimbilia chumbani alipomuacha Eric amelala. Alimkuta Eric bado amelala kama aliyekufa kwa uchovu wakucheza game usiku kucha. Elvin alipumua, akafunga tena mlango nakutoka.

Akaamua kupiga tena simu. “Baba mbona hamjafika bado?” “Elvin, unajua ndio tumetoka kuzungumza sasa hivi, na wewe upo Bagamoyo?” “Kwa hiyo unakuja au? Mbona kama hamjali?” Elvin alianza kulalamika huku akigomba sana. “Tunajali Elvin. Hapa wote tupo njiani tunakuja.” “Samahani baba, nahisi nimepaniki.” “Pole sana. Tunakuja.” “Asante baba. Naomba msichelewe.” Akakata tena simu.

Baada ya muda alifika Mwasha na familia yake. Kabla hajamaliza kuelezea ndugu zake kilichotokea, walishangaa kuona Masha na yeye anaingia na magari ya polisi na mbwa wa polisi kumsaka Bella. Hoteli ilijaa polisi na waokoaji wa majini. Walirudi tena baharini, huku wakiwa wamegawana kumsaka Bella. Pesa ya Masha ilikuwa ikiongea kwa nguvu sana siku hiyo. Aliahidi kwa kutoa hundi pale pale ya pesa nyingi sana, tena kwa kuwaonyesha, kwa atakayefanikiwa kumpata Bella siku hiyo. “Ukiniletea Bella hapa, hii pesa ni yako bila maswali.” Masha aliongeza. Walijitosa watu baharini bila kufikiria. Bella alisakwa baharini na nchi kavu.

Kelele za mahali pale zilimuamsha Eric aliyekuwa amelala. Kwani alisikia jina la dada yake likiitwa kwa kipaza sauti. Alishtuka sana na kukimbilia nje, ndipo alipokuta Hoteli hiyo imefurika watu. Raia kwa Polisi. Alipoambiwa dada yake amepotea, na yeye alijitupa majini kumsaka. Eric alikuwa akilia kama amekatwa kidole. Mpaka kufika usiku huo alikuwa amekaukiwa sana. “Isingekuwa mimi kumlazimisha Bella kwenda kuogelea jana, labda asingepotea.” Eric aliendelea kujilaumu. “Sio kosa lako Eric.” Mzee Mwasha alijaribu kumfariji.

Usiku huo, wote walilala pale pale hotelini. Watu walipiga kambi ufukweni. Masha alinunua vyakula kwa kila aliyekuwepo pale akisaidia kumtafuta Bella. Walijaa vijana wengi sana pale hotelini, wakubwa kwa wadogo waliitana kutoka mtaani wakihangaika baharini kumpata Bella ili wapate pesa ya Masha na kula chakula cha bure kilichokuwa kikigawiwa usiku kucha. Walikuwa wakipishana baharini usiku kucha huku jina la Bella likiitwa bila kupumzika.

Wote walilala, lakini sio Masha, kitu kilichomshangaza kila mtu. Alikuwa kwenye simu usiku kucha akiongea na watu mbali mbali. Polisi kutoka Dar, walizidi kumiminika hotelini hapo na wote waliletwa na Masha. Yaliletwa maboti ya uokoaji, yakaanza kuzunguka humo baharini usiku kucha. Elvin na yeye aliamka asubuhi sana na kurudi baharini. Aliogelea kwa masaa mengi, juu na chini sana ya maji akimtafuta Bella. Alitoka akiwa amechoka. Akaanza kuita Bella, mpaka watu wangine waliamka. Walikuta amepiga magoti ufukweni akiita huku akilia sana. Elvin alikuwa kama amechanganyikiwa.

“Nahisi Bella hayupo huko majini, wamemteka nyara!” Mzee Masha alifikiria kwa nguvu na kufanya kila mtu afikirie. “Nani atamteka nyara Bella jamani?” Elvin aliuliza. “Kama angekuwa amepotelea majini, mpaka sasa hivi tungekuwa tumeshauona mwili wake.” Masha alikuwa akiongea huku akifikiria. “Bella hana maadui. Na alienda kuogelea asubuhi sana. Huyo aliyemteka nyara angekuwa amefika huku saa ngapi?” Elvin aliendelea kuhoji. “Ngoja na mimi niwapigie simu watu baadhi kujua kama ameonekana mahali.” Masha akasogea pembeni kuwasiliana na watu wake.

 “Jinsi Masha alivyopokea taarifa za ujauzito wa Bella.”
Mzee Masha alipoambiwa habari za ujauzito wa Bella, alimshangaza mpaka Mzee Mwasha kwa furaha aliyokuwa nayo. Alizipokea zile habari vizuri sana na kumuahidi Mzee Mwasha kumtunza Bella na mtoto. Hapo hapo alimpigia simu wakili wake kuwa nyumba ya Kunduchi beach ibadilishwe jina kutoka kwa mwanae Junior iandikwe jina la Enabella. Na kuahidi kumpa Mzee Mwasha kiwango fulani cha pesa kila mwisho wa mwezi ili kuhakikisha Bella anatunzwa vizuri. Mzee Mwasha alihisi Mzee Masha hakuwa amefikiria vizuri, kwani alizipokea zile taarifa kwa urahisi sana tofauti na alivyotegemea. Mzee Mwasha alimuomba Masha yeye aondoke pale kwake ili ampe muda wakufikiria kabla hajaendelea kuahidi mambo mengi zaidi. Lakini Masha alimwambia, zile ni habari ambazo hakutegemea kuzikia mpaka anaingia kaburini. Akamwambia yeye ni kama malaika Gabrieli aliyekuwa ametumwa na Mungu, kumwambia Mariamu atazaa wakati alikuwa bikira. Mzee Mwasha hakumuelewa, kwani Masha tayari alikuwa na watoto wawili.

********************************************

Ndoa ya Mzee Masha ni kama ilishafikia ukingoni. Kwani habari za Bella,  Irene alihakikisha anamfikishia Junior mpenzi wake wa siri na Zera, hukohuko waliko. Baada ya watoto wake kujua walikasirika sana, hawakutaka hata kuongea na baba yao tena. Alipokuwa akienda kuwatembelea Uholanzi, wale watoto waliondoka nyumbani kwa muda wote waliokuwa wakijua baba yao yupo nyumbani. Heshima iliwaishia kabisa kwa baba yao. Kile kitendo kilimkera sana Masha akawaahidi kuwa watamrudia kwa magoti, kwani ile jeuri waliyokuwa nayo na heshima waliyoweka mtaani, na kwenye mabaa ni pesa yake. Na kwa kuwa alikuwa na hasira na mama yao zaidi, aliahidi kuwakomoa vibaya sana.

********************************************

Upweke ulishamuandama Masha. Uholanzi akawa haendi tena, na Bella alishamkimbia. Akabakia na maisha yakutafuta pesa tu. Na kwa kuwa hakuwa na asili ya kupenda wanawake, hata hivyo alianza kusumbuliwa na pressure sababu ya matatizo ya familia yake, hakutaka kutafuta mwanamke mwingine tena. Akabaki akibuni miradi kila leo ili kupoteza mawazo huko. Akawa akiingiza pesa kila mahali lakini bila furaha. Sasa kuja kupata taarifa kuwa Bella amebeba mtoto wake, kwake ilikuwa faraja kubwa sana.

********************************************

Kwa kuwa uchunguzi wa siri kubwa sana aliyokuwa akifuatilia kwa muda mrefu juu ya mkewe na watoto wake ulikuwa umekamilika, Masha akaamua ahamishe urithi aliokuwa amempa mwanae Junior kwa huyo mtoto wa Bella, ambaye hata hakuwa amezaliwa. Siku ile ile alipopata taarifa ya ujauzito wa Bella, akampigia simu huyo wakili wake, akamtajia vitu vya kubadilisha kutoka kwa Junior kwenda kwa mtoto wa Bella, kisha akaondoka pale nyumbani kwake kwenda kuweka saini kwa huyo wakili, kuhakikisha hakuna atakayebadilisha tena. Na hakutaka kufanya siri, mbele ya familia yake waliokuwa na wao wamerudi Tanzania kwa likizo, aliongea na wakili wake pale pale sebleni, akijua popote walipo huko vyumbani watamsikia tu.

Na kuanzia leo, haparuhusiwi sherehe ya namna yeyote humu ndani. Kwanza hii nyumba ni ya kwangu, nimejenga kwa jasho langu, wote mmenikuta na mali zangu, hakuna wakunizuia kuongea nitakavyo na kupanga mipango yangu nitakavyo.” Mzee Masha alizidi kuongea kwa hasira.  “Hamna shukurani kabisa nyinyi watoto kama mama yenu. Na nitawaonyesha kama mimi ndiye mwenye mali. Nitamgawia huyo mwanangu anayekuja mali zangu zote. Mbaki mmenuna nyinyi na mama yenu. Nione mwisho wenu ni nini. Na magari yangu yote nitayauza, muone jinsi wenzenu wanaotembea na miguu vile wanavyofaida. Na nikitoka hapa, napitia benki kufunga akaunti zenu nyinyi wote mpaka ya mama yenu, nichukue pesa yangu. Niwabakishie mshahara wa mama yenu, ili muonje maisha kama ya watoto wenzenu wanaoishi na mishahara ya wazazi wao tu. Hamna adabu kabisa.” Mzee Masha alitoka na kuwaacha wanae na mama yao wakiwa wamesogea karibu na alipokuwa amekaa hapo sebleni wakisikiliza sheria mpya.

********************************************

Bella alitafutwa kwa zaidi ya mwezi mchana na usiku bila mafanikio. Kwa mara ya kwanza Mzee Mwasha na Mzee Masha waliweza kufanya kazi kwa karibu na makubaliano makubwa wakati wakutafutwa kwa Bella. Baada ya muda mrefu sana kupita, walikubaliana kuwa Bella alichukuliwa na mawimbi makali sana, na labda mwili wake uliliwa na smaki au ulitupwa nchi za jirani kwani hata vijana wa Masha, walisema hawakusikia tetesi zozote mtaani kama alitekwa nyara. Na huko pia Masha alimwaga pesa akitaka Bella atafutwe na yeyote atakayeleta habari kuwa anawajua waliomteka, napo pia aliahidi pesa nyingi sana. Kwa hiyo sio polisi tu walioingia kazini kumsaka Bella, hata vijana wa mtaani walipeleleza angalau kupata fununu. Wale wote aliowahisi Masha, aliweka ulinzi mkali sana wafuatiliwe, bila mafanikio yeyote yale. Walipojiridhisha kuwa ni kweli Bella hatapatikana tena, walifanya ibada ndogo kama kumbukumbu yake, watu wakaomboleza na kutawanyika.

********************************************

Eric alikuwa na hali mbaya sana. Hakuacha kutoka pale nyumbani na kwenda kumtafuta dada yake. “Bella hawezi kuwa amekufa. Namjua Bella, hawezi kuniacha. Mama aliniambia nitabaki na Bella.” Eric alikuwa akiongea hivyo kila wakati huku akilia na kumtangazia kila mtu kuwa dada yake yupo hai mahali, wasikate tamaa yakumtafuta. Hakukubaliana kabisa na wazo lakumfanyia Bella ibada na watu kukubali amefariki. Alipinga kwa machozi. “Msimkatie tamaa Bella jamani! Atakuwa yupo sehemu anahitaji msaada wetu. Lazima tuendelee kumtafuta.” Wakati mwingine alitoroka pale nyumbani akiwa peke yake na kwenda baharini kumtafuta dada yake mpaka usiku.

 Ikawa hivyo hivyo hata shule zilipofunguliwa. Alikuwa akitoroka shuleni na kwenda baharini kumsaka dada yake. Matokeo yake shuleni yakawa mabovu sana. Mara kwa mara Mzee Mwasha aliitwa shuleni kuzungumzia maendeleo yake, kwani Mzee Mwasha ndio alibaki kuwa kama baba wa Eric, kwani hali ya Elvin ilikuwa mbaya zaidi. Hakuacha kumuombolezea Bella. Ilikuwa ngumu kuamini kama  kweli Bella ndio amefariki. Alishinda kazini akifanya kazi, kuanzia asubuhi mpaka usiku sana bila kula, ila siku za weekend alirudi Bagamoyo kwenda kumtafuta Bella. Siku zilizidi kwenda lakini wao wawili maisha yalishindwa kuendelea kabisa. Waliendelea kumsaka Bella kana kwamba ndio ameondoka jana yake.

“Eric!”
Siku moja Eric alishushwa shuleni na Elvin asubuhi hiyo, alipoona tu Elvin ameondoka, hakuingia hata ndani ya geti la shule, akageuza hapo hapo na kuelekea baharini kumtafuta Bella. Mzee Mwasha alifika shuleni hapo jioni yake kumchukua Eric, lakini akaambiwa hakufika shuleni siku hiyo. Eric naye alianza kutafutwa mchana na usiku, baada ya siku tatu mwili wake uliokotwa ufukweni akiwa amevimba sana, huku  macho yake yakiwa yameliwa na samaki, hatizamiki. Ni habari iliyokuwa imeenea sana kwenye vyombo vya habari. Iliwasikitisha watu wengi. Kisa chake kuwa alikufa akiwa anamtafuta dada yake baharini ndicho kilichowaumiza wengi. Watu kutoka sehemu mbali mbali walifurika kanisani siku ya kuaga mwili wake, Eric alizikwa nyuma ya nyumba ya Mzee Mwasha. Ulikuwa ni wakati wa majonzi sana kwa familia hiyo.

********************************************

Elvin alikuwa kwenye wakati mgumu sana kuliko mtu yeyote kati yao. Hakuwa akilala usiku wala mchana. Ilikuwa ni miezi 19 iliyojaa hekaheka na simanzi kubwa sana kwa Elvin, hali yake haikuwa nzuri hata kidogo. Mwishowe kaka zake wakaamua ahame kabisa pale Dar na kwenda kuishi na kaka yake Eno nchini Dubai. Eno alimpeleka Elvin kwa washauri mbalimbali kuongea naye. Baada ya kama miezi mitano ya matibabu na kuongea na wataalamu yaani kufanyiwa ‘counseling’, ndipo angalau Elvin alirudi kwenye hali yake ya kawaida. Akarudi nchini akionekana angalau anaweza kufanya kitu kingine kikaeleweka. Hapo ilikuwa ni baada ya kama miaka miwili tokea kupotea kwa Bella. Elvin alirudi kazini kama kawaida. Mambo mengi yalikuwa yamebadilika lakini alifurahi kukuta baadhi ya sura alizokuwa akizifahamu.

“Revange/Kisasi.”
Elvin alirudia maisha yake ya kawaida, asijue mkasa mkubwa uliokuwa ukimsubiri. Bila wao wawili kujua, mahusiano yao, na mahusiano waliyokuwa nayo kabla ya wao wawili, yalitengeneza adui wasiojua kusamehe. Na wote waliapa kutopumzika mpaka walipe kisasi. Swali la kifo cha Bella kilikuwa kipi, kama alitekwa au kufia majini likiwa halijajibiwa, njama kubwa sana za kuangamiza familia ya Mwasha wakihesabiwa kama wasaliti katika jamii zilikuwa zikiwasubiria pia. Zilipangwa njama nyingi sana kuumiza familia hiyo waliyosema wanajidai wacha Mungu na wenye umoja kumbe ni wasaliti wakubwa. Kila mmoja kwenye familia ya Mwasha alikuwa na kosa lake lililowapa sababu tosha yakulipizwa kisasi. Kuanzia Mwasha mwenyewe mpaka Elvin walikuwa na makosa walioona ni lazima waangamize familia hiyo kabisa.

Walitafuta kila njia jinsi yakuwatesa kwanza ndipo kuwamaliza, lakini walianza kukata tamaa. Kwanza walianza na Eli waliedhani ni cha pombe wakidhani itakuwa rahisi sana kumwingilia yeye ili kumaliza familia hiyo lakini walishindwa. JJ aliyekuwa ametengana na mkewe na yeye alibaki kulea wanae, mama yake na kazi tu. Hakuonekana mahali popote na yeyote. Eno ndiye alikuwa mbali sana na jamii tokea zamani. Kwanza hata kuongea kwa Eno ilikuwa shida zaidi ya salamu au kucheka basi. Wengine walisema anadharau sana, lakini alikuwa na haiba ya ukimya kupita hata Mwasha baba yao. Hakujulikana kama anamsichana au ana matatizo. Aliporudi Elvin kutoka nchini Dubai, walifurahi sana. Mipango ikaanza upyaa.

********************************************

Walimtafuta binti wa kazi za ndani waliyejua ametulia na mwenye dhiki sana. Wakamuuliza kama anashida na pesa na anataka pesa ya haraka. Yule binti alieleza matatizo ya kwao yote. Akaanza kupewa ahadi nyingi sana kwa kuambiwa anapewa kazi. “Tutakupa sehemu ya kuishi wewe na familia yako hapa mjini. Yaani tutaenda kuwachukua wazazi wako kutoka kijijini na kuwaleta hapa mjini. Huna haja yakufanya kazi za ndani tena, tutakuwa tunakulipa mshahara kila mwezi, kwa mwaka mzima. Lakini ndani ya huo mwaka uwe umefanya kazi tutakayokuwa tumekupa.” “Kazi gani?” Yule binti akauliza. “Kwanza wewe ni bikra?” Yule binti alishtuka kidogo. “Sijawahi kuwa na mwanaume.”  Alijibu kwa aibu kidogo kwani walikuwa wamemzunguka na wote walionekana wanataka matokeo mazuri na pesa sio tatizo. “Wewe utatufaa.” Waliangaliana na kucheka. 

“Jina lake nani tena?” Mwingine akauliza. “Happiness.” Akajibu. “Unakwenda kanisani?” “Ndiyo.” “Sasa sisi tunataka mlokole.” “Mmmh! Sisi kwetu hatuamini hayo mambo, tena baba yangu ndio kabisaa.” Yule binti alisita. “Sasa mnataka pesa au hamtaki?” “Tunataka. Tena mama anasumbuliwa na mgongo kweli! Alikujaga hapa mjini akaambiwa anatakiwa upasuaji, lakini tulishindwa pesa.” “Basi atatibiwa buree. Kaongee nao, waambie atatibiwa na watu wakanisani kama watakubali kubadili dini na tutawapa nyumba yakuishi huku mjini.” “Sasa mbona kazi yenyewe hamniambii!” “Kwanza tunataka kujua kama watakubali kuingia kwenye kanisa la walokole. Na wala sio kwa muda mrefu. Ukijitahidi kufanya kazi yako kwa haraka, utakuwa huru kuishi vile utakavyo, lakini wakati huo utakuwa umeshakuwa tajiri.” Yule binti alikunja uso na tabasamu usoni.

“Ni kazi gani hiyo?” Happiness akauliza kwa shauku huku na wasiwasi kidogo. “Maana kama ni madawa ya kulevya, hiyo sitaki.” “Nani amekwambia madawa ya kulevya wanafanya mabikra?” Walimuuliza kwa ukali kidogo nakumfanya Happy atulie na kufikiria. Wakamtolea picha, Happiness akabaki amekodolea macho ile picha. “Huyu ndio nani?” Aliuliza Happiness kwa sauti yake nzuri ya upole. “Anaitwa Elvin. Huyo ndiye atakupa utajiri wote.” Happiness hakuwa ameelewa. “Sasa ni hivi Happiness, kazi yako kubwa nikuhakikisha huyu kaka anakuoa.” Happiness alishtuka sana. 

“Kaka mwenyewe yupo hivi, atanikubali mimi!?” “Huo nimuonekano tu, usiogope. Sisi tutakuwa tunakufundisha kila kitu kutokana na tabia zake, mpaka akuoe. Hiyo sauti yako, na ukiingia kwenye dini yao, utampata tu. Tutakupa udhaifu wake, na nguvu yake ilipo ili isiwe shida kumwingia. Cha kwanza rudi kijijini, ongea na familia yako. Waambie umepata watu ni walokole, wapo tayari kuwasaidia. Kwanza kumtibu mama yako na kuwapa makazi hapa mjini, lakini sharti lao, nikuwa wanaenda kanisani jumapili na katikati ya wiki.” “Kwani huko kijijini wanafanya kazi gani?” Mwingine akamuuliza Happiness. “Wakulima.” “Basi waambie hapa mjini kazi yao itakuwa ni kwenda kanisani tu, sisi tutawatunza kwa mwaka mzima.” “Sasa na huo mwaka ukiisha?” Happiness akauliza. “Ndipo inapokuja jukumu lako la pili.” Happiness alijiweka sawa, maana mpaka hapo hakuwa ametajiwa kitu kigumu sana kitakachopingana na utajiri unao mjia.

“Huyo kijana tunayekuonyesha, kwao wanapesa. Tunataka zote ziwe zako. Kikubwa na chamuhimu, ukazane uolewe naye, mengine yote, tuachie sisi tutakutajirisha. Ila kwa masharti haya, uingie kwenye ndoa ukijua upo kazini, sio mapenzi na utusikilize sisi kila tutakachokwambia. Usiwahi kumwambia mtu yeyote juu ya huu mkutano wa leo, wala hutakiwi kutujua zaidi ya hivi. Tutakupa simu na pesa za kuanza kujikimu. Ukirudi tu nyumbani leo, ukaache kazi, urudi kwenu ukaanze kazi yakuwashawishi wazazi wako kuingia kwenye ulokole.” Alitolewa simu nzuri ya kisasa na kukabidhiwa pesa zilizomtoa macho Happiness. 
“Unafikiri utaweza?” Akiwa amechanganyikiwa kwa kulala masikini na kuamka tajiri, Happiness alikubali kila kitu. Hakuwahi kushika milioni moja tokea anazaliwa tena hasa kipindi hiki kila mtanzania analia shida! Hata bosi wake alishaacha kumlipa mshahara, akabaki akiishi pale akihofia  kurudi kijijini kwa ugumu wa maisha. Hata hivyo bosi mwenyewe alikuwa akimvumilia sana Happiness. Alikuwa mchafu na mvivu sana. Alibaki amekodoa macho akiwa ameshika simu yake na kitita cha pesa. “Hii ndio namba utakayopiga siku mtakayokuwa mnahamia mjini na familia yako.” Happiness alifurahi sana, akarudi kwa bosi wake, akaaga kuwa mama yake amezidiwa kijijini amepigiwa simu na baba yake, nilazima aondoke asubuhi yake.

Happiness na wazazi wake waanza kazi rasmi kwa ajili ya kuangamiza familia ya Mwasha.

Tofauti na alivyotarajia, hakutumia nguvu nyingi sana kushawishi familia yake. Baada yakusikia mkewe atatibiwa bure, na wanahamia mjini kuishi na binti yao aliyepata ajira itakayoweza kufanya waweze kuishi bila kazi ila kwenda kanisani tu, walifungasha mizigo yao haraka sana, na kurudi na Happiness mjini siku inayofuata. Walipewa nyumba ndogo ya uwani katika nyumba hiyo ya wapangaji wengi, nakuambiwa matibabu ya mama yake yataanza mara watakapoona wamechukua hatua ya pili. Kuanza kwenda kanisani na kuaminisha kuwa wameokoka.

Hilo nalo halikuwa tatizo. Familia hiyo ilihamia kwenye kanisa alilokuwa akiabudu Mzee Mwasha na familia yake. Nakuanza kuwa washirika wa kweli pale. Happiness alikuwa binti wa kuigwa. Aljitoa kwa hali ya juu pale kanisani. Alianza kufahamika na kila mtu huku akisifiwa ni binti mwenye juhudi. Hakukosa kwenye usafi wa pale kanisani, siku za maombi hakukosekana, kwenye mkesha pia alikuwepo yeye na mama yake kuanzia mkesha unaanza mpaka asubuhi. Mama yake aliingia kwenye kundi la kina mama, na yeye kwenye kundi la vijana. Happiness alijaliwa sauti ya upole na ndogo sana. Hakuna jinsi angeongea ukachoka kumsikiliza.

Kwa kuwa Mama Mwasha alikuwa ndiye mwenyekiti wa kundi la kina mama, alishazipata sifa za Happiness. Urafiki kati ya mama yake Happiness na Mama Mwasha haukuchelewa. Happiness alimwambia mama yake ajitahidi sana kuwa karibu na yule mama. Na kweli, alijisogeza mpaka mama Mwasha akamuweka karibu. Waliongozana kwenye kutembelea wagonjwa mahospitalini na kuona watoto yatima. Ukaribu ukazidi, hata alipokuwa akifanyiwa upasuaji katika kitengo cha MOI katika hospitali ya Taifa Muhimbili, akidhaminiwa na adui za Mwasha, Mama Mwasha ndiye aliyekuwa akimuuguza mama huyo kwa karibu sana. Alipika kila chakula akimsaidia Happiness kumuuguza mama yake mpaka alipopona.

“Sasa umeona jinsi tulivyomsaidia mama yako mpaka akapona? Kinachofuata ni kuhakikisha unaajiriwa kwenye kampuni yao kina Mwasha.” Walimpigia simu Happiness usiku huo akiwa anajiandaa kwenda kulala. “Kweli ni rahisi. Hawana shida. Sasa nitafanyaje mpaka niajiriwe?” Happiness akahoji. “Kwa kuwa umefanikiwa kumsogeza mama yako karibu sana na Mama Mwasha, na hiyo familia wanamsikiliza sana mama yao, mwambie mama yako akuombee kazi.” Nalo hilo halikusumbua hata kidogo. Mama yake Happiness alipomwambia Mama Mwasha uhitaji wa kazi, Happiness akaanza kazi mara moja kwenye Kampuni ya Mwasha na ndipo sasa akaanza kuwa karibu na Elvin.

********************************************
Baada ya Mzee Mwasha kujiridhisha kuwa Elvin yupo sawa na akili ipo kazini, alimwachia tena majukumu ya pale ofisini na yeye kubaki mshauri tu. Ulikuwa wakati ambao maadui zao  hawakutaka kuulazia damu. Walimfundisha Happiness kufanya kila awezalo kuwa karibu na Elvin. Walimfundisha kumjali yeye kama Elvin kwanza. Happiness akaingia kazini. Kumjali Elvin kwa karibu. Alihakikisa Elvin anakula milo yote kila awapo kazini. Taratibu Mama Mwasha akaanza kumkaribisha na nyumbani kwake, kufanya ukaribu zaidi. Urafiki kati ya familia ya mama yake Happiness na Happiness ukanoga kwa mama Mwasha. Salamu za hapa na pale kila siku, Happiness akiulizia ni aina gani ya vyakula vidogo vidogo anapenda Elvin ili awe anampelekea kazini. Hilo likampendeza na kumvutia zaidi mama Mwasha. Kwa kiziwanda wake tena! Mungu ampe nini kama sio Happiness? Hata hivyo Happiness hakuwa na mapungufu makubwa yakumfanya mtu aliyekusudia kuoa ashindwe kumuoa. Ubora uliongezeka kwa kuwa alikuwa mcha Mungu sana, mpole na mnyenyekevu.

Ugumu aliokumbana nao na kuwambia adui za Mwasha anakaribia kukata tamaa, ni Elvin mwenyewe. Alishakubalika kwa Mama Mwasha. Alimpenda sana Happiness. Na Happiness akaanza kujiuza kwa upande wa Elvin. Kila alipokuwa akiongea na mama Mwasha, hakuacha kumsifia Elvin kwa hili au lile. Utendaji kazi wake ofisini, utulivu na nidhamu. Alionyesha wazi kuwa anampenda na kumuheshimu Elvin. Kujalia ndio kulizi. Kila mama Mwasha alipotaka kujua maendeleo ya mwanae hapo kazini, basi Happiness ndiye akawa mtu sahihi. Kwa muda mfupi sana, Happiness akaweza kujaa kwenye maisha na upande mzuri wa mama Mwasha. Katika vipimo vyake, Happiness alishampitisha.

Swala la elimu yake haikumsumbua kabisa Mama Mwasha, alijiambia anachotaka ni mke mwema kama Happiness kwa mwanae Elvin. Akaanza kusambaza kwa juhudi zote sifa za Happiness mpaka kwa Mzee Mwasha ili kutengeneza njia rahisi pale kwake ili Happiness akubalike. Kanisani ndipo walipoimba sifa zake zaidi mpaka wazee wakanisa walikuwa wakimtolea mfano Happiness. Kuanzia mchungaji mpaka washirika wengine walimpenda na kumsifia, lakini Elvin ndio alikuwa tatizo ni kama hakuwa akiona kitu. Japokuwa alimuheshimu sana lakini hakuwahi kumfikiria upande wa mapenzi hata kidogo. Kila alipojaribu kumsogelea, alimsimulia habari za marehemu Enabella na Eric. Jinsi alivyokuwa mcheshi na mwingi wa upendo.

********************************************

Siku zilizidi kwenda lakini maongezi yao makubwa yalikuwa ni Enabella tu. “Hata wewe ungempenda tu Bella. Alikuwa ni binti mzuri sana. Mungu alimpendelea kila kitu kizuri. Huwezi kuchoka kumtizama Bella. Iwe usiku au mchana, awe macho au amelala, Bella alivutia kumwangalia. Alinifanya nicheke kila wakati. Hakuwa na sifa za upole hata kidogo, alikuwa muongeaji sana, lakini wakati wote Bella alipoongea mtu yeyote aliyekuwa karibu yake alijisikia vizuri. Hachoshi kuangalia. Akicheka utatamani asiache. Sitakaa nimsahau Bella.” “Pole sana Elvin.” “Na kinachoniumiza zaidi, amekufa nikiwa nataka kumchumbia. Nilikuonyesha pete yake?” “Zaidi ya mara kumi.” Elvin alicheka kidogo.

“Ninatembea nayo hapa.” Akaitoa tena ile pete nakuivaa kwenye kidole chake kidogo. “Tulikuwa tumekwenda mapumzikoni, hukohuko ndipo alipopotea Bella wangu. Natamani ningeendelea na mipango yangu ya mwanzoni. Nilipanga siku aliyokuwa amerudi kutoka nchini India ndiyo siku nilitaka nimuombe awe mke wangu, lakini mama alinishauri nisubiri kwani alikuwa ni mjamzito na yeye mwenyewe hakuwa akijua.” “Mimba ilikuwa ni yako!?” Happy alishtuka kidogo. “Hapana. Hapana kabisa. Ni habari ndefu. Lakini ilikuwa sio yangu.” “Kwa hiyo ulikuwa tayari kumuoa hivyo hivyo?” “Bella alikuwa ni mke wangu, hilo halikuwa na ubishi. Umeshawahi kujua moyoni na kujua, halafu ukaelewa kwamba huyu mtu ni wako? Hata kama mazingira yote yanakataa, lakini wewe unajua huyu ni mtu wangu tu!” “Ndiyo.” Happy akajibu. “Basi ndivyo ilivyokuwa kwa Bella. Nilijua na ninajua Bella angekuwa mke wangu hata iweje.” Elvin aliuliza bila kutarajia jibu la ‘ndiyo’ kutoka kwa Happiness. 

Alitulia kidogo na kukumbuka jibu la Happiness. “Hivi ulijibu ndiyo?” Happy akacheka. “Na mimi nimepitia huko.” “Sasa iweje mpaka leo hujaolewa naye?” Elvin aliuliza kwa mshangao mkubwa sana. “Kwa kuwa mwenzangu hakuwahi kuniangalia mimi kama mke. Hakuwahi kunipenda kimapenzi.” “Lazima huyo mtu anatatizo. Wewe ni msichana mzuri sana Happiness, umetulia na unaweza kumfanya mwanaume yeyote awe na furaha.” Happy alicheka kwa huzuni kidogo. “Sio kwake. Nimejitahidi kwa kila njia lakini hakuwahi kunipenda.” “Unajua Happiness, wapo watu wengine wanahitaji kufunguliwa macho. Kwa nini usimwambie?” “Unafikiri ni sawa kwa mwanamke kumfuata mwanaume?” “Mimi sioni tatizo, lakini sijui wengine.” “Kuna hofu ya kukataliwa pia.” “Mimi nakushauri uende tu Happiness. Hakuna jibu latofauti utakalopewa mbali ya ndiyo au hapana. Na itakurahisishia kuendelea na maisha yako mengine, kuliko kuendelea kumsubiri mtu ambaye pengine na yeye anakupenda sana, ila ameshindwa au anachelewa kuchukua hatua, au hana mpango kabisa na wewe. Nakushauri chukua hatua Happiness. Wewe ni dada mzuri sana, una haki zote zakuwa kwenye nyumba yako, na mume na watoto wenu wakifaidi upendo wako. Nakushauri usichelewe.” Happiness alitabasamu kisha akanyamaza.

Ilikuwa ni siku ya jumapili baada ya ibada, Mama Mwasha alimkaribisha Happiness kwa ajili ya chakula cha mchana pale nyumbani kwao. Na baada ya kula, Mama Mwasha alitoka na mumewe, kama kuwapa nafasi ya mazungumzo pale pale nyumbani kwao. Nia yake ni kuhakikisha Elvin anafunguka macho na kuweza kumpenda Happiness. Na kwa kuwa alishajua jinsi Happiness anavyompenda mwanae, akamshauri asipoteze muda. Atumie muda huo kumwambia Elvin ukweli. Lakini ni kama alimuachia nafasi Elvin yakumtangaza Enabella. Alimsimulia kwa kurudia rudia mpaka Happiness akaishiwa nguvu.

Ilipofika jioni Mzee Mwasha na mkewe walirudi nyumbani na Mama Mwasha akaomba yeye ndio amrudishe Happiness nyumbani kwao. Lakini lengo ilikuwa ni kupata naye muda wa maongezi wakiwa njiani. “Vipi umeweza kumwambia chochote?” “Sijui kama nimuoji wa leo wala kesho mama. Bado anakumbukumbu za Enabella, hawezi kuongea chochote isipokuwa Bella. Sio kazini, si nyumbani. Anarudia habari za Bella tu. Nimejaribu mama, lakini nimeshindwa.” Mama Mwasha alifikiria kidogo. “Ngoja nikwambie ukweli Happiness. Enabella ni msichana aliyeacha pengo ambalo hakuna mwanadamu anayeweza kuliziba mioyoni mwetu wote, hata wewe usijaribu kuziba pengo la Bella. Hutaweza. Kuwa wewe kama wewe. Bella ameshaondoka, na Elvin ni lazima aoe, na jinsi ninavyokuona, wewe ndiye msichana utakaye mfaa Elvin.” “Sidhani mama. Naona sina nafasi kwenye moyo wa Elvin kabisa.” Happiness alishafika mwisho.

“Labda kama uliyoniambia tokea mwanzoni hayakuwa na ukweli. Upendo una nguvu sana Happiness.” “Sasa nitafanyaje mama?” “Kama uliweza kunifuata mimi na kuniambia, kwa nini usimwambie na Elvin mwenyewe? Hapatakuwa na jibu la tofauti zaidi ya ndiyo au hapana. Na itakusaidia wewe kuendelea na maisha mengine Mungu aliyokukusudia. Ni kweli Bella na Elvin walipendana sana, lakini haitamzuia Elvin kuendelea na maisha mengine. Sijui umeelewa?” “Nimeelewa mama.” Bila kujijua, Mama Mwasha aliendelea kumpa moyo Happiness adui mkubwa sana katika maisha yao, na alimpa mbinu nyingi za kuweza kufanikisha lengo la kuolewa na mwanae. Njia nzima aliongea naye kwa hekima sana akimtia moyo nakumuomba asikate tamaa mpaka alipomfikisha nyumbani kwa wazazi wake, akaongea habari za kawaida sana na wazazi wa Happiness ambao walikuwa wameshakuwa karibu sana, mwishowe akaaga na kuondoka.

********************************************

Kama kawaida yake, ilikuwa lazima kutoa ripoti ya maendeleo ya kazi aliyopewa, lasivyo aliambiwa akishindwa watafukuzwa pale kwenye ile nyumba na kurudishwa kijijini. Happiness alitoka nje ili kupiga simu baada yakuhakikisha ndugu zake na wapangaji wote wamelala. Hakuwa akijua jina hata la mmoja wao lakini alipewa namba ambayo aliambiwa huyo mtu ndiye atakayeendelea kuwa akimpa maelekezo. Alieleza kila kitu na ushauri alioshauriwa na mama Mwasha na Elvin mwenyewe. “Lakini labda mnipe njia nyingine jamani. Nimeshindwa kwa Elvin.” Happiness alijitetea. “Labda kama useme umeshindwa kuishi mjini, na unataka kurudia hali yako ya umasikini. Na itabidi utulipe pesa yetu ya kodi tuliyolipia hiyo nyumba mnayoishi sasa hivi na uturudishie pesa zetu zote. Na itabidi uiche ile kazi kwa Mwasha.” “Hee! Si ni kazi aliyonitafutia mama yangu!?” “Usijisahau kabisa Happiness. Sisi ndio tunakupa ramani ya kipi ufanye. Unatembea juu ya ramani yetu. Mbona hukutoka kule ulikokuwa ukifanya kazi za ndani na kwenda kuajiriwa ofisini?” Happiness alipooza gafla. Usijisahau na kuweka kiburi. Tutayafanya maisha yako yawe magumu sana hapa mjini. Kina Mwasha wataujua ukweli wote juu yenu na mtafukuzwa kila mahali. Si kanisani, si hapo kwenye hiyo kazi. Wale watu wanaroho mbaya sana na hawataki wasaliti. Wakijua kuwa ulikuwa na hila tokea mwanzo, na si kweli upo kama hivyo ulivyojionyesha kwao, utajuta. Utakuwa umejitengenezea adui wawili. Wao na sisi. Na kundi letu huwa hatukubali kushindwa.” Wakaendelea kumtisha.

 “Nasisitiza, ili usisahau, upo kwenye maisha yao sasa hivi kwa sababu sisi tumekuvalisha hilo vazi la utakatifu na tumekuwezesha kifedha. Wale watu sio wakukaribisha watu kwenye maisha yao hovyohovyo. Na ninakuahakikishia Happiness, tukikuacha wewe hata siku moja tu, watakugundua kuwa sio mlokole na wewe ni mjinga mjinga tu wa kijijini.” Happiness kimya. “Na tunakupunguzia muda. Naona unaanza kulewa pesa yetu. Tumekuvalisha na kukulisha vizuri wewe na familia yako hapa mjini, unaanza kujifananisha na watu wa hadhi hiyo. Sasa ndani ya miezi 6, uwe umeolewa na Elvin. Kitakachopata familia yako, usimlaumu mtu.” Simu ikakatwa na kumuacha Happiness akishangaa. Hapakuwa na kubembelezwa tena, ni vitisho.

********************************************

Lilikuwa ni jaribu na mtihani mkubwa sana aliokuwa amepewa Happiness na hao Waajiri wake, kwani Elvin hakuacha kurudia habari za Bella bila kuchoka. Kila wakati kazi zilipokuwa zikisuasua, watu wakiwa hawafanyi kazi vizuri, alimkumbuka Bella. “Bwana Bella alikuwa mchapakazi yule mtoto sio mchezo! Alikuwa analala hapa ofisini, kuhakikisha kazi zimekamilika. Halafu umeona hii biashara ndogo inayotuingizia sana faida kuliko hata hii kubwa?” Elvin aliuliza. “Ni wazo la Bella. Alikuwa na akili yakufikiria, sijawahi ona. Na nijasiri kama simba. Haogopi kujaribu kitu chochote. Na yeye ndiye aliyenifundisha msemo wa ‘Hakuna haja yakuogopa kusogelea mlango wowote ule. Kwani matokeo yake ni mawili tu, Kufunguka au kutokufunguka’.Bella sio mchezo.” Happy alisikiliza na kuamua kuondoka ofisini kwa Elvin kwani alikuwa amemletea chai ya saa kumi. “Asante sana Happy.” Happy alitabasamu. “Karibu.” Akatoka.

Siku zilizidi kwenda Happiness akitafuta jinsi yakumwambia Elvin lakini alishindwa. Waajiri wake walimwambia Happiness, kadiri anavyochelewa ndivyo anavyompa nafasi Elvin yakumfikiria msichana mwingine mbali na yeye. Walimwambia anaweza kushuhudia Elvin akioa mwanamke mwingine, kama yeye akishindwa kumwambia ukweli na hapo ndipo atakapoona hasira zao kwa kukubali kazi ambayo anashindwa kufanya. “Nimefanya kila mlichotaka. Kama Elvin mwenyewe hataki mimi nifanyaje? Kwanza nimechoka kumbembeleza na mimi nina mpenzi wangu nataka nimlete mjini tufunge ndoa. Msinibabaishe. Kama ni nyumba yenu na pesa mnayonipa, sina shida navyo tena. Hamkunikuta nalala njaa au nalala nje.” Happiness na yeye akakata simu.


 Onyo kwa Happiness.

Happiness akaamua aachane kabisa na wale watu. Akaacha kupokea simu zao kabisa. Zilipita siku mbili tu, siku ya tatu akiwa anatoka kazini alipigiwa simu na wazazi wake kuwa kaka yake amekimbizwa hospitalini kwani amekamatwa na vibaka wamempiga sana na ameumia. Kaka huyo alikuwa anatoka kwenye shuguli zake wakati anakaribia na nyumbani kwao, lilimsogelea gari, wakashuka vijana asiowafahamu, wakiwa wameficha nyuso zao, walimpiga sana, na kumuacha akiwa anavuja damu. Waliondoka na gari yao, lakini alishindwa hata kusoma namba za gari kwa maumivu na giza lilikuwa limeanza kuingia. 

Happiness alikuwa dada mkubwa nyumbani kwao, baada ya kaka yake waliyekuwa wamepishana kama mwaka tu, na yeye hakuwa amesoma kabisa, aliishi kijijini na wazazi wake pamoja na wadogo zao wawili wakike na wakiume, mpaka walipokuja mjini, huyo kaka mtu alianza shuguli ndogo ndogo kama kuongeza kipato pale nyumbani.

Akiwa amepigwa sana bila hata kupokonywa kitu chochote, ndipo alipowapigia simu nyumbani kwao wamfuate hapo alipokuwa kwani alisema hawezi hata kutembea. Wazazi wake walimfuata na kumkimbiza hospitalini. Mtaa mzima ulijua juu ya sakata hilo na kuwaogopesha sana. Cha ajabu ni kule kutoibiwa kitu chochote. Walijua wazi ni mambo ya vijana, kulipizana kisasi. Labda alitembea na mwanamke wa mtu.

Ilibidi Happiness abadilishe daladala. Kutoka ile aliyokuwa amepanda wanzoni yakumfikisha nyumbani, akashuka na kupanda yakumpeleka hospitalini. Kabla hajaonana na ndugu zake hospitalini hapo, simu yake ikaingia ujumbe. 
“Hayo ni matokeo ya kusahau fadhila. Ulikubali kazi, lazima ulete matokeo yatakayo turidhisha. Ukitoka hospitalini upige simu lasivyo kitakachotokea tena, hutakaa ukasahau.” 

Macho yalimtoka Happiness akaamua kupiga simu pale pale na kuomba msamaha. Sasa kinachofuata ni wewe kuongea na Elvin kama mama yake alivyokushauri. Na tumia mbinu zote za kike kuhakikisha mnafunga ndoa. Unasikia Happiness?” “Ndiyo.” “Kumbuka na simu uliyoshika sasa hivi au unayotumia, pia ni ya kwetu. Usisahau matumizi yake, ukaishia kuonyesha ufahari tu. Tunauwezo wakufika popote na kwa yeyote. Huna utakapotushitaki tusijue na kukufuata wewe na familia yako.” Simu ikakatwa. Happiness alibaki akifuta machozi huku hofu imemjaa.

Pale pale akaamua kumtumia ujumbe Elvin siku hiyo ya ijumaa akiwa hata bado hajaonana na kaka yake aliyeambiwa ni mgonjwa sana. ‘Kama utapata nafasi, naomba tuonane kesho tafadhali sana Elvin.’ Ule ujumbe ulionekana umefika lakini haukujibiwa usiku kucha. Happiness alishindwa hata kuongea na mtu yeyote pale hospitalini, tumbo lilikuwa likimuuma sana kwa wasiwasi.

‘Nilijua tu hawezi kukubali. Nitafanyaje?’ Happiness aliendelea kuwaza. Baada ya kaka yake kuangaliwa na kuonekana ni madonda tu ya nje tu na hakuna popote kwenye madhara zaidi, aliruhusiwa usiku huo, wakarudi nyumbani. Wengine walilala lakini Happiness alibaki akisubiria majibu kutoka kwa Elvin. Alijuta na kuendelea kujuta. Palipambazuka, ikawa asubuhi mpaka ilipofika mchana hapakuwa na jibu lolote. Happiness alijifungia chumbani kwake akilia sana. Mama yake na ndugu zake walimuhurumia sana Happiness, lakini hawakuwa na jinsi ya kumsaidia kwani wao walijua upande mmoja tu wa stori, wakidhani ni mapenzi pekee yanayomliza, kumbe alishaanza kutishiwa maisha. Aliona madonda ya kaka yake, akajua hao watu hawatashindwa kuua.

‘Labda kwa kuwa mimi sio mweupe. Hata umbile lenyewe halivutii. Elvin amenidharau sana. Ameshindwa hata kunipenda hata kidogo jamani! Nimejitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu. Basi hata angerudisha ujumbe wakuniambia hataweza kukutana kuliko dharau aliyonifanyia! Hakika atakuja kulipa matatizo aliyomsababishia kaka yangu.’ Happiness alianza kujenga chuki kwa Elvin. Alikuwa akiwaza huku akilia kwa hofu.

Kila wakati alihakikisha simu yake ipo na chaji yakutosha na haijazimika ili Waajiri wake wakimtafuta wampate na Elvin pia asimkose kama ataamua kumtafuta. Alisubiri simu hiyo ya Elvin huku akijaribu kuwatuliza Waajiri wake, kuwa lazima atafanikisha swala la Elvin, wasiwe na wasiwasi, anaomba muda zaidi. ‘Umebakisha siku chache sana Happiness ili tufikie muafaka na wewe. Mnaonekana mkiendelea kunufaika na maisha tunayowapa bila sisi wenyewe kupata tunachogaramia. Baada ya muda mfupi kuanzia sasa, kama hakutakuwa na matokeo tunayotarajia, tutakuja kuwatoa hapo kama mbwa, na kumrudisha mama yako kuwa kiwete kabisa. Tutafungua huo mshono wa upasuaji aliofanyiwa kwa garama zetu, tutatoa hivyo vyuma mgongoni bila hata ganzi, na wewe utapewa adhabu yako.’ Ujumbe huo ulizidi kumtisha Happiness. Hata maji yalishindwa kupita kooni kwa Happiness. Alishinda chumbani kwake akilia tu.
********************************************

Mpaka ilipofika jioni ndipo alipoona Elvin anampigia simu. Happy aliruka kutoka pale alipokuwa amelala akainyakuwa simu yake. “Hallow!” Happy alianza. “Samahani sana Happiness, niliacha simu kazini tokea jana. Yaani hapa ndio nimeifuata na kukuta ujumbe wako. Sijui nimechelewa au bado tunaweza kukutana tu? Najua muda umekwenda sana, naweza kukufuata hata hapo nyumbani.” Happiness hakuamini masikio yake. “Kama haitakuwa usumbufu kwako.” “Hamna usumbufu kabisa. Basi nitakuwepo hapo nyumbani muda si mrefu.” “Karibu sana.” Hapakuwa na jinsi Happiness angeeleza furaha yake mtu mwingine akaelewa. Alikuwa akiruka ruka huku machozi yakimtoka kwa furaha. Alijiambia atatumia huo muda ipasavyo.

Elvin alifika nyumbani kwao, akiwa na wasiwasi sana na muda, asijue furaha waliyonayo hata wazazi wake Happiness. Hata wazazi wa Happy walimpenda sana Elvin, wakatamani kama angalau wangekuwa na uwezo kidogo sio fukara vile, labda Elvin angempenda mtoto wao, bila kujua mipango inayoendelea. Na wale Waajiri wa Happiness walihakikisha hawana pesa nyingi sana ili kumtia shauku Happiness yakutengeneza pesa zaidi. Kwa hiyo alipoajiriwa kwenye ofisi ya Mwasha, wakaacha kumlipa na kumsisitiza ajitahidi kuolewa nakuanza kufaidi pesa za Mwasha yeye mwenyewe kama mke wa Elvin mpaka watakapompa ramani nyingine.

Elvin alikuwa ni kijana mwenye tabia ya kiugwana. “Samahanini sana najua nimekuja muda mbaya, lakini nahitaji kuongea na Happiness.” “Hamna shida kabisa mwanangu. Msubiri kidogo, nikamwite.” Alimkuta Mama na baba yake Happiness barazani. Mama yake, alisimama na kuingia ndani. Aligonga kwa muda ndipo Happiness alipofungua. Alishtuka sana kuona uso wa mtoto wake. Alikuwa amevimba sana macho na nimekundu kwa kulia. Mama yake alibaki akimwangalia kwa kumuhurumia sana mwanae, kwani alikuwa amejifungia humo chumbani siku nzima bila kutoka. Hakuwa amekula kitu chochote siku nzima. “Elvin amekuja, anakuulizia wewe.” Happiness alitabasamu, wazi alionekana ni habari alizokuwa akizisubiria kwa muda mrefu. “Nakuja sasa hivi.” Happiness alijibu kwa upole, mama yake akataka kuondoka. “Mama!” Happiness alimwita, mama yake akageuka. “Samahani niliposhindwa kukufungulia mlango asubuhi na nikawa mkali sana kwa kila mtu. Nilikuwa kwenye wakati mgumu sana.” “Pole sana Happy. Jitahidi uwahi kutoka huko chumbani, usimuweke sana mwenzio.” “Sitakawia.” Happiness alijaribu kunawa uso mara kadhaa ili kuwa sawa, lakini bado macho yalikuwa yamevimba sana.

Akaamua kutoka vilevile. Elvin alishtuka sana alipomuona, akasimama. “Vipi Happiness? Mzima?” Happy alijaribu kutoa tabasamu la kinyonge lakini Elvin alijua kuna kitu hakipo sawa. “Tunaweza kutoka kidogo tukazungumze?” Elvin aliuliza kiustarabu sana. Happiness aliitikia kwa kichwa huku machozi yakimtoka. “Najua muda umekwenda wazazi wangu, lakini naomba nitoke na Happiness kidogo, sitachelewa kumrudisha.” Elvin aliomba ruhusa. “Bila shaka.” Baba yake akajibu. “Twende Happy.” Elvin aliongoza njia mpaka kwenye gari yake, akamfungulia mlango, Happy alipopanda akaufunga mlango wa gari.

Elvin na Happiness.
“Umeshakula?” Happy alitingisha kichwa kukataa. “Basi twende tukatafute mahali tule wakati tunaongea.” Elvin aliondoa gari. “Vipi lakini? Mbona unalia?” Kama aliyekuwa ameambiwa aanze kulia. Happiness aliendelea kulia kwa kwikwi sana, kitu kilichomtia wasiwasi Elvin. Alishakaa na wasichana waongeaji, Irene na Bella, lakini Happiness alikuwa msichana mkimya sana. Elvin alisimamisha gari nje ya sehemu aliyotaka wakale akamgeukia Happiness. “Niambie nini kimekuudhi Happiness! Ni kazini?” “Nilijua umepuuzia ujumbe wangu Elvin.” Elvin alijisikia vibaya sana. 

“Sijui nini kilitokea jana, nikaacha simu kazini. Na sina matumizi sana na hii simu zaidi ya mambo ya kikazi, kwa hiyo nilipofika nyumbani nikagundua nimeiacha ofisini, sikuwa na wasiwasi kabisa, nikijua hakuna wakunitafuta siku hizi za jumamosi na jumapili. Nimelala karibia siku nzima ya leo, yaani nimeamka ndio nikaamua kuifuata ofisini, ndipo nikakutana na ujumbe wako, na hapohapo nikakupigia. Naomba unisamehe sana. Sina sababu ya kukupuuza Happiness. Unajua ninavyokuheshimu. Naomba uniwie radhi.” Happiness alitulia kidogo. “Sio kwamba ni kosa, ila mimi mwenyewe nilijidharau sana, kuona nimekutumia ujumbe halafu hukujibu.” “Daah! Huna sababu yakujidharau Happiness, ni bahati mbaya tu imetokea. Twende tukale kwanza, ndipo tuzungumze.” Walishuka kwenye gari wakaingia kwenye huo mgahawa na kila mmoja aliagiza chakula alichokipenda.

Haikuwa kawaida ya Happiness kwenda kwenye migahawa ya maana kiasi hicho, kutokana na uwezo wake. Lakini sio Elvin mtoto aliyezaliwa kwenye maendeleo na kuzungukwa na watoto wa matajiri wa pale mjini. Akaja kukutana na Bella mtoto wa viwango vya juu. Kwa hiyo kimaisha Elvin na Happiness hawakuwa sawa hata kidogo. Hata nyumba waliyokuwa wamepangiwa ilikuwa ni nyumba ya kawaida sana pale jijini.

“Bella alikuwa akipenda sana chakula cha hapa.” Elvin alivunja ukimywa. “Tulikuwa tukipenda sana kuja naye hapa. Tulikuwa tukikaa au niseme kujificha kona ile palee, kwa kuwa Bella alikuwa anaweza kukufanya ukacheka mpaka ukaingia aibu. Kwa hiyo kila tulipokuwa tukija hapa, tulikuwa tunajificha pale, ili afanye fujo zake zote na mtu asituone.” Elvin alikuwa akiongea na tabasamu kubwa huku akivuta hisia zilizoonekana kumfurahisha sana moyoni. Alishangaa kumuona Happiness siku hiyo amenyamaza kabisa bila kuchangia neno lolote. Elvin akaamua anyamaze kidogo lakini akakumbuka kitu kingine. “Unajua Bella…” “Samahani Elvin.” Happiness alimkatiza Elvin. “Naomba na mimi unipe muda wako hata dakika tano tu, unisikilize kidogo.” Elvin alitulia kidogo na kumwangalia Hapiness kwa makini.  “Namaanisha kunisikiliza na mimi, na kunipa dakika hata moja ya Bella kati ya muda wote unao mpa hapa duniani.” Elvin alibadilika sana usoni. 

“Najua unampenda sana Bella, na hakuna mwanamke anayeweza kuchukua nafasi yake kwenye moyo wako, lakini naomba unipe nafasi na mimi. Japo kidogo tu Elvin. Nimekuwa nikikusubiri kwa muda mrefu sana. Tokea nilipokuona kanisani, nilibaki kumwambia Mungu yeye anayejua ni kiasi gani nakupenda, akutunze kwa ajili yangu. Nimemshukuru Mungu kunipa kazi kwenye kampuni yenu, nikaona tupo karibu, lakini kila nilipojisogeza kwako ili nipate nafasi angalau machoni kwako tu, imeshindikana. Imenilazimu nikwambie tu ili ujue ni kiasi gani nakupenda na ninakusubiri ili siku moja uje kuwa mume wangu.” Elvin alikuwa kama amechomwa sindano ya ganzi ya mwili mzima.

Ni kama ulimwengu ulisimama kwa muda, akaanza kukumbuka maongezi yake na Happy juu ya mwanaume anayempenda. Akili yake ikafunguliwa gafla akaanza kuona juhudi alizokuwa akizifanya kwake. Alimuhurumia sana, kwani yeye hakuwa hata na wazo la mahusiano ya kimapenzi kwake.

“Nakupenda Elvin.” Happiness alirudia, Elvin alikuwa kama ameshtuliwa kutoka usingizini. “Kwanza nikuombe radhi Happiness. Sikuwahi hata mara moja kukupuuza au niseme kukudharau. Akili yangu haikuwahi hata kukufikiria upande wa mapenzi. Na sio kwa sababu nyingine yeyote, lakini nafikiri ni heshima niliyokuwa nayo kwako. Wakati wote nimekuona kama dada yangu, tena mwenye tabia nzuri sana. Hakuna msichana aliyeteka akili zangu kama Bella. Amefanikiwa kuingia katika kila kiungo changu. Siwezi kulala au haiwezi kupita hata dakika moja bila kumfikiria Bella. Ndio maana imekuwa ngumu sana hata kurudiana na Irene. Irene amejirudi sana, amekuwa msichana mzuri kitabia, lakini hata aliponiomba turudiane nilimkatalia kabisa kwa kuwa sikutaka kuja kumuumiza baadaye. Bado nahitaji muda kuweza kuyafuta maisha niliyoishi na Bella. Yalikuwa ni mafupi lakini yameathiri maisha yangu kuliko nitakavyoweza kuongea. Namuuliza Mungu, ni kwa nini alinikutanisha na Bella halafu akamchukua! Ni swali linalonisumbua sana. Nimekaa na wewe Happiness, wewe ni msichana mzuri sana, unahitaji mwanaume atakayekupenda na kukuenzi, sio mimi hata kidogo.” Elvin aliendelea.
“Nakuhakikishia mimi sipo kwenye nafasi ya kuwa mume bora kwa sasa hivi, kwa msichana yeyote yule hata awaje isipokuwa Bella.” “Kwa hiyo hata akirudi leo utamuoa?” “Bila kupoteza hata siku moja mbele. Nitampokea kwa mikono miwili na kumkimbiza kanisani nikafunge naye ndoa haraka sana. Ndivyo hali yangu ilivyo mbaya kwa sasa. Sijui unanielewa? Natamani kama ningekuwa hata na nafasi kidogo tu moyoni mwangu Happiness, ningekwambia sawa, labda ukinipa muda nitajitahidi kuwa mume anayefaa kwenye maisha yako. Lakini najihisi kama nimeoa, nina mke tayari ambaye ni Enabella. Kuwa na msichana mwingine au hata kufikiria kuoa ni kama namuolea Bella mke wa pili. Nipo kwenye kifungo kigumu sana Happiness. Sitaki uingie huko. Sitafurahi kuja kukuona ukiamka pembeni yangu ukiwa huna furaha na mimi ndio nimeku sababisha. Sitaruhusu hilo litokee.” Happiness aliishiwa nguvu. Akatamani aondoke muda huo huo lakini akakumbuka uhai wa ndugu zake unamtegemea yeye na juhudi zake siku hiyo. Akaamua azidi kupambana.

“Nakupenda sana Elvin, nakuomba nipe nafasi. Naweza nisiwe kama Bella, lakini nakuahidi nitakuwa na wewe katika kila hali utakayokuwa ukipitia. Nipe nafasi. Nikishindwa, mimi mwenyewe nitaondoka.” Elvin alibaki akimwangalia Happiness jinsi anavyoongea kwa hisia kali. Elvin alivuta pumzi ndefu, kisha akaweka mikono kichwani. “Naomba nipe muda nifikirie Happiness. Tafadhali. Sikuwa na wazo la kuja kuoa kabisa. Yaani leo ni kama unataka kuanzisha safari mpya kabisa katika maisha yangu ambayo sikuwa nimeitarajia hata kidogo. Tafadhali nipe muda.” “Nitaendelea kukusubiri Elvin, huku nikikuombea. Nakuahidi kukupenda na kukutunza daima. Nitakuwa na wewe katika kipindi hichi kigumu unachopitia. Naomba uniamini nakupenda.” Elvin alibaki akimwangalia Happiness na mikono yake kichwani. Gafla alisimama akaanza kuzunguka pale mgahawani, Happiness akimtizama. 

Baada ya kuzunguka kidogo, akamuona anaelekea chooni. Akatoka akionyesha wazi aliosha uso. Hakurudi hata kukaa tena. Akaweka pesa chini ya glasi yake ya juisi iliyokuwa imefika nusu, akamgeukia Happiness. “Samahani Happiness, tunaweza kuondoka?” Wazi alionekana alikuwa kwenye wakati mgumu sana. Ni kama aliyepigiwa kengele na kutakiwa aamke, na yeye hakuwa tayari kuamka kabisa.

Elvin alikuwa ni kijana aliyeishi maneno yake. Mwaminifu sana na mcha Mungu. Hali ya kuwa na mwanamke mwingine ni kama usaliti mkubwa sana kwa Bella ambaye ameshakufa muda mrefu sana uliopita, lakini yeye alikuwa na ndoa na Bella ya milele. Alimrudisha Happiness mpaka nyumbani kwao, njia nzima hakuongea kitu. Happy alimuona jinsi alivyoshtuka, ni kama aliyepewa habari za msiba. Happy aliona azidi kukazia maneno ili hata wakiachana, akamfikirie na yeye pia. Kabla ya kushuka Happy aliamua aongee naye kidogo. “Elvin, sijakwambia unioe kesho wala kesho kutwa. Nilitaka ujue na mimi nipo, nakupenda kwa dhati na ninakusubiri uje kuwa mume wangu. Namaanisha kila ninalo kwambia. Nakupenda sana na nina endelea kukusubiri.” Happy aliongea kwa upole kama kawaida yake. 

“Hiyo siku utakayokuwa tayari kuoa, nilitaka unifikirie mimi.” Elvin alibaki akimwangalia. Alipoona kimya, Happy aliamua kushuka kwenye gari. Elvin alimwita, na yeye akashuka. “Samahani sana Happiness. Nashukuru kuniambia, wala hujakosea kabisa. Lakini…” Elvin alishusha pumzi kwa nguvu sana na kuanza kuangalia kulia na kushoto kana kwamba ulimwengu wote unamuangukia yeye. “Daah! Sikutegemea kabisa. Nipo kwenye hali mbaya sana sasa hivi. Zimeibuka hisia ambazo nilijitahidi kuzizika kwa muda mrefu sana. Naomba nikapumzike.” “Samahani sana Elvin, sikukusudia kukuumiza.” “Hapana na wala hujaniumiza. Nahisi mimi nina matatizo Hapiness. Wewe umefanya jambo zuri sana, na ninakupongeza. Asante sana kwa upendo wako, lakini…. Daah! Hapana Happy nitakusumbua sana. Hutafurahia maisha ukiwa na mimi. Sitaki kuja kukuumiza. Nataka niendelee kukuona ukiwa na furaha wakati wote. Ndani yangu sipo kama hivi unavyoniona nje au sipo kama watu wanavyonifikiria nipo. Ni kama nilikufa na Bella. Nipo hovyo kweli! Natamani kama tungekutana kwenye mazingira tofauti, kabla ya Bella, au kabla ya hivi nilivyo sasa. Nakuthamini sana Happy, sitaki kukuumiza. Hapana Happiness. Sitaweza kabisa kuwa na wewe au mwanamke mwingine. Samahani sana.” Elvin aliingia ndani, akashukuru wazazi wa Happiness akaondoka.

********************************************

Njia nzima machozi yalikuwa yakimtoka Elvin. ‘Huu utakuwa usaliti kwa Bella kabisa.’ Elvin alirudi moja kwa moja mpaka nyumbani kwao, alifunguliwa geti na mlinzi, akaegesha gari yake sehemu yake, akabaki amekaa ndani ya gari huku ameweka mikono kichwani. ‘Kwa nini ulimchukua Bella?’ Elvin aliendelea kumuuliza Mungu wake. ‘Kwa nini ulimleta kwangu wakati ulijua kabisa ungemchukua? Unajua ni kiasi gani nampenda Bella, bado ulimchukua yeye na mdogo wake. Unanitesa bila sababu. Nilikukosea nini wewe Mungu? Nimejitahidi kuwa mwaminifu kwako tokea utoto wangu, kwa nini unanilipa magumu hivi?’ Elvin alikaa mle ndani ya gari akilia kwa muda mrefu sana huku akimuuliza maswali Mungu wake.

Wazazi wake walisikia wakati geti linafunguliwa, na wakajua ni yeye tu kwani huo haukuwa muda wa Eli kurudi nyumbani. Baada ya kusubiri kwa muda mrefu na kuona haingii ndani, mama yake akaamua kutoka nje kumwangalia. Alisogea mpaka kwenye mlango wake akamkuta mwanae yupo kwenye hali mbaya sana. Alizikumbuka siku zile akimuombolezea Bella. Akafungua mlango wake wa gari, “Twende ukapumzike Elvin.” Elvin alikausha machozi usoni mwake, akatoka ndani ya gari. Alikwenda chumbani kwake moja kwa moja akapanda kitandani, huku mama yake akimfuata nyuma. Na yeye aliingia akajilaza palepale kitandani kwake.

********************************************

*Bella ametoweka. Hakuna anayejua alipo, lakini walisha fanya kumbukumbu yake na kukubaliana na kifo chake, huku mdogo wake naye akiwa amekufa akijilaumu kusababisha kifo cha dada yake. 
Je, Nini kilimpata Bella? Swali lililoshindwa kujibiwa na kila mtu, hata pesa ya Masha imeshindwa kujibu swali hilo.
*Familia ya Mwasha ipo mtegoni. Nia ni kulipizwa kisasi kwa garama yeyote ile. Unafikiri chanzo ni
v  Eli… aliyetoa siri za watu wote wakagombana na Diva kuachika. Au
v  JJ…aliyeshindwa kumsamehe Diva, na kumzuia hata kuwa karibu na watoto wake, viumbe anavyo vithamini  na kuvipenda sana Diva kwenye maisha yake. Au ni
v  Mwasha na Mkewe…Kwa usaliti kwa Mama Masha au Irene, kwa kumpokea Bella, mke mwenzao. Au ni
v  Elvin… Aliyemkataa Irene hata baada ya kifo cha Bella, Irene alirudi kwa magoti na kumsihi Elvin warudiane, lakini pia alimkataa.
Je, Nani adui ya Familia hiyo wacha Mungu!?

Wakiwa wametulia, maisha yakiendelea, wakijua ipo amani japo wamempoteza Bella na Eric, kumbe wapo watu wasio lala wala kusinzia kwa ajili ya kuwaaangamiza kila mmoja wao, tena kwa garama kubwa sana.

Usikose Sehemu ya 12.

Itaendelea kwenye website za mtazamohalisi.com

0 comments: