Story

My Past - Sehemu ya 10.

Wednesday, June 07, 2017 naomimwakanyamale 0 Comments


E
li alikuwa na hasira sana na wale wanawake pamoja na shemeji yake Diva. “Nitawatandika makofi nyinyi wanawake, mpaka niwaharibu sura. Nani asiyekuwa na aibu kati yenu na Bella? Leo ndio mmesikia kama mama ndio alikuwa mgonjwa? Mmekuja kumsanifu mama yetu na maneno machafu hapa!”  “Kwani mimi sikuja kumuona hospitalini? Kila mtu anamajukumu yake. Mtu akija kukuona pia unashukuru kwamba anakuthamini.” “Diva nikinyanyuka hapa nitakuchapa makofi mbele ya mumeo! Naomba nyamaza na kama huwezi, nyanyuka nenda kwenu.” “Jaribu uone. Pombe tu.” Diva alimkejeli Eli.
“Sasa si heri mimi pombe nakunywa kwa pesa yangu, kuliko wewe mpaka uhongwe ndio upate pesa!” “Mzee Mwasha mkataze mwanao. Muone anavyomtukana Diva.” Mama Diva aliingilia. “Mbona umenyamaza? Wewe si jeuri? Nimekuvumilia sana Diva. Nilitaka kukutunzia heshima yako, lakini tokea umdharau mama yangu naona hustahili heshima kabisa. Na kwa taarifa yako kama umeshindwa kumuheshimu JJ, fanya hivyo mkiwa nyinyi wawili, kwenu, sio mbele yetu. Unatudhalilisha sisi. JJ ni kaka yetu, anaheshimiwa humu ndani kama Mzee Mwasha. Unapomjibu utakavyo mbele yetu, ni kutudhalilisha sisi wote hapa.” “Nani amekwambia simuheshimu JJ? Ulitaka nimlambe miguu ndio ujue namuheshimu kaka yenu?” “Ndivyo unavyowafanyia mabwana zako?” “Bwana gani?” “Unafikiri mimi sikujui kama wewe ni malaya hapa mjini?” “Malaya!? Umenifumania?” Diva aliuliza. “Unataka mpaka nikufumanie ndio nijue unalala na bosi wako? Umemwambia mumeo hicho cheo umepandaje?” Kila mtu alipooza gafla.
“Mimi naona twende, haya mambo yatamchanganya tu Mama Mwasha wakati mgonjwa.” Mama Danny alitaka waondoke. “Tena na wewe tulia kimya. Sasa hivi ndio unatambua ugonjwa wa mama? Mmbea mkubwa wewe, unahamisha maneno nyumba hii unapeleka nyumba ile. Mbona husemi mambo ya mumeo kama kazaa na muuza baa?” Mama Danny alishtuka sana. “Muone alivyotoa mimacho. Ulikuwa hujui? Sasa subiri UKIMWI unakujia. Maana mumeo nakunywa naye, na kazi yake kubwa kulala na kila msichana anayemkubali pale baa.” “Eli naomba unyamze.” “Wambea sana mama hawa. Tena wanafiki. Wanajidai wao na watoto wao ndio watakatifu sana.”  Wote walinyamaza.
Eli akamgeukia Diva. “ Diva vipi jeuri yako?” “Unaongea nini Eli?” JJ akauliza. “Mkeo anagongwa na bosi wake. Na ndio maana anakudharau na ndio jeuri yake yote ipo hapo. Kama huamini na anabisha, nitampigia simu aje sasa hivi, hapa hapa mbele yenu huyo Jamaa aliyekuwa anatakiwa apate hicho cheo cha mkeo, lakini bosi mtu akamdhulumu hicho cheo, akampa hawara yake, huyo Diva mkeo halafu yeye akamuhamisha kitengo. Jamaa akakasirika, akaamua kuacha kazi. Kama wewe mwanamke, bisha tena nilete uthibitisho. Maana Jamaa anawafuatilia sana na ana uthibitisho wa kila kitu. Anajua nyumba ya wageni, yaani hoteli mnayokutania, siku zenu hizo za jumamosi mnazodanganya mpo kazini kumbe mmejifungia huko, mpaka mida yenu mnayokutana na huyo Bosi wako. Na picha zenu zote pia anazo mkiwa huko hotelini. Bisha tu, nimwabie anitumie zile picha sasa hivi au yeye mwenyewe aje. Mimi nimezikuta Bar akiwa na marafiki zake wakifanya mipango ya kuwaangamiza wewe na Bosi wako. Watu walimpa hiyo akili, akawa anawafuatilia kwa karibu na walimpa ushauri wa vitu gani vya ushahidi awe navyo ili aje awashitaki kwenye kikao chakufunga mwaka, cha mabosi wenu wote. Na kwa taarifa yako Diva, hata ofisini kwenu wamekuchoka. Wamemsaidia jamaa kumpa copy za madai yenu yote mliyokuwa mkikusanya kwa muhasibu wenu, na pesa zote anazoidhinisha Bosi wako za malipo mnayojidai mnalipana kwakufanya kazi overtime siku za jumamosi, kumbe mnakuwa mpo sehemu zenu mnafanya uchafu wenu. Vyote hivyo anavyo. Kuanzia tarehe, muda na sehemu pamoja na madai yote mliyolipwa ofisini siku na tarehe zilezile na muda mliojifanya mnafanya kazi kumbe mnafanya starehe. Ongeza neno, nimwambie atume sasa hivi hapa na nimpe ruhusa awashitaki, maana mimi ndio nilimpooza kwa heshima ya JJ, nimemtafutia kazi sehemu nyingine na kumlipa pesa kama kumtuliza, lasivyo ungekuwa pabaya sana wewe Diva, na hakuna ofisi wangekupokea kwa umalaya wako, ubadhilifu wa mali za uma, na kingine kutumia rushwa ya ngono kupanda cheo.” JJ alinyamaza.
“Na wewe Mama Banda, toa sura yako humu ndani, hata wewe mwizi wa waume za watu, kama mmeo anavyolala na wafanyakazi wenu wa ndani. Nguvu yakumsema Bella na Mzee Masha mnaitoa wapi nyinyi?” “Eli jiangalie wewe mtoto. Kwanza muongo. Banda anajiheshimu wala sio Malaya.” Eli alianza kucheka sana. “Wewe mama unataka kuingia aibu wewe! Ngojeni kwanza nikalete mwiko jikoni, wakati Mama Banda unaendelea kuongea. Mtaumbuka leo nyinyi, hamtakaa mkanyage hapa.” Eli alienda jikoni akarudi na mwiko wa kusongea ugali.
“Sasa mnisikilize kwa makini, kila mmoja nampa dozi yake, lakini marufuku kupigana humu ndani. Nawapa dozi zenu, mtaenda kumezea huko nje. Nikiona mtu ananyanyuka kuanza kutaka kuleta fujo humu ndani kwetu wakati mama yangu mgonjwa nawachapa wote, tena usoni. Mmejileta wenyewe, na kuanza kujidai mnamuumbua Bella. Sasa naendelea na wewe Mama Banda unayesema wewe mtakatifu, hujalala na Mzee Mwanga?” Kila mtu alishtuka. Mama Mwanga akasimama. “Unasemaje wewe Eli?” “Kaa chini na wewe. Unashtuka nini? Si umuulize huyo rafiki yako?” “Huwezi kuwa unanifanyia hivyo Mama Banda. Si ndio?”  Eli akaanza kucheka.
“Waone sura zao. Mbona wote mmetulia?” “Wewe Mama Banda?” Mama Mwanga akamwita kwa hasira sana. “Sauti hiyo, Mama Mwanga. Nikikusogelea hapo, utanitambua mimi ni nani. Nendeni kwenu mkasutane vizuri. Sio hapa kwetu. Hapa mnapewa dozi tu, mtaenda kuugulia maumivu nje ya hilo geti. Nyinyi si mnajidai kumdharau mama yangu? Leo mtatoka jasho la damu.” “Wewe Mama Banda ndio wakunifanyia hivyo mimi?” “Nikipindi kile cha matatizo na mumeo, ukaondoka nyumbani kwako.” Mama Banda alijibu kwa sura ya aibu.
“Wenzako wanajua kuwa unatembea na dereva wa mumeo? Maana tunakunywa naye kule baa kwa pesa unazo muhonga za mumeo. Anayasema yote.” Eli alimgeukia Mama Mwandri. Wote walimgeukia Mama Mwandri. “Kumbe mashoga zako hawajui?” Eli alinza kucheka huku anapiga makofi. “Mngejiona sura zenu! Kama sio nyinyi mliongia humu ndani kwa dharau. Halafu hapo kati yenu sijamuona hata mmoja wenu ambaye Masha angemtaka angemkataa. Ni hivyo mwenyewe hajawataka hata mmoja wenu hapo, kamtaka Bella, roho na wivu vinawauma.” Wote walikuwa wamenyamaza kimya.
“Mbona hambishi tena? Mmetosheka na dozi au niendelee na wewe Mama Banda ili uondoke hapa na yako na mumeo?” “Eli! Eli!” Mama yake akamwita. “Naomba niangalie mimi Eli.” Mama yake alimsisitiza, Eli akamgeukia mama yake. “Naomba unyamaze, inatosha.” “Wamezidi hawa mama. Tena ndio hawa hawa wanaomsema na Elvin. Sasa...” “Hapana Eli. Naomba unyamaze.”  Eli alitulia kidogo. “Sawa mama. Lakini nipe kama dakika moja niwamalizie.” “Hapana Eli.” “Basi mama. Mumshukuru Mama Mwasha. Nilitaka kuhamia kwa watoto wenu mnaowaabudu. Kutwa mnawatoa mimba halafu…” “Eli?”  “Basi mama. Haya tokeni nje, naona muda wenu wa kumuona mgonjwa umeisha. Na mkamwambie Mama Masha, mke mwenzake yupo hapa, anafanya kazi alizoshindwa kuzifanya cha mdomo Diva. Haya simameni haraka kabla sijawasogelea hapo.” Wote wakasimama.
“Diva, naomba nisikukute nyumbani, wala usiguse watoto wangu hata mmoja.” JJ aliongeza. “Nitaenda wapi?” “Wewe mjinga nini? Swali gani hilo? Naomba nisikukute nyumbani, mpaka nitakapo kutafuta.” “Basi naondoka na watoto.” “Nitakunyonga Diva! Naomba uondoke.” Diva alitoka. Elvin akasimama akaenda kumshika Bella mkono pale alipokuwa amebaki amesimama. “Twende Bella.” Elvin naye alitokea mlango wa jikoni akiwa amemshika Bella mkono.
“Nimeharibu nini Mama?” Eli kama kawaida yake alimgeukia mama. “Sana Eli mwanangu.” “Daah! Kumbe heri ningenyamaza pale pale uliponiambia, eeh?” Kama sio yeye, Eli alirudi kuwa mnyenyekevu sana.  “Ndiyo Eli. Uwe unanisikiliza. Ona umeharibu ndoa ya kaka yako.” “Hiyo ndoa ilishakufa muda mrefu sana mama, wala usimlaumu Eli. Heshima hakuna, mwanamke anadharau kama nini! Haridhiki kwa kila ninachompa! Haambiliki! Mwache aende, nipumzike.” “Hizo ni hasira JJ. Tulia ufikirie vizuri.”  Mzee Mwasha aliyekuwa kimya muda wote aliongeza. “Kila siku unaniambia hivyohivyo baba. Mbona habadiliki?” JJ aliuliza kwa hasira. “Hujui shida ninazopata na Diva, baba. Na mimi nimechoka, mwache aende kwa huyo bwana wake na mimi nipumzike.” JJ alikuwa akimfuata baba yake na kumuomba ushauri juu ya ndoa yake kila wakati bila mama yake kujua.
**********************************
Elvin alimtoa Bella nje upande wa jikoni. Bella alikaa kwenye ngazi na kuanza kulia sana. Alilia kwa kwikwi kwa muda, mwisho akasimama. “Naomba nirudishe nyumbani Elvin.” “Unaondoka na mama?” “Hapana bwana Elvin. Mama hatataka kuniona tena.” “Ndivyo alivyokwambia?” “Nakaaje tena na mama wakati nimekuwa na mahusiano na mume wa rafiki yake?” “Muone! Ujanja wote umekuishia.” “Bwana Vin!” “Wewe ulitegemea ingekuwa siri daima?” “Najua watu wangejua, lakini si kwa namna hiyo.” “Wewe unafikiri mama hakuwa akijua?” Bella alishtuka sana. Mpaka machozi yakakauka gafla.
“Unafikiri mama alikuwa akijua kabla ya hapo?” Elvin akacheka tena huku akimtizama Bella. “Usicheke bwana Elvin. Nani alimwambia baba na mama?” “Irene.” Bella aliweka mikono kichwani. “Elvin! Lini?” “Mama aliniambia nilipotoka tu Arusha. Unakumbuka siku tunarudi kutoka Arusha, tukamkuta Irene, baba na mama, pale mapokezi?” “Nakumbuka.” “Basi ndio siku aliyokuwa amekwenda kuongea na wazazi wangu juu ya mahusiano yako na Mzee Masha.” Bella alikaa chini. “Sasa ukamwambiaje mama?” “Nikamwambia nafahamu, na ulishaniambia.” Bella alikaa kimya.
“Usiwaogope wazazi wangu Bella. Ni waelewa sana, na maadamu hayo ni maisha yako ya nyuma, hawawezi kukuhukumu.” “Uwiii!” Bella alikuwa kwenye mshtuko sana. “Yaani muda wote nipo nao, kumbe wanajua maisha yangu ya nyuma!? Wanajua nilishaishi na yule baba, wanaju…” “We Bella! Hebu acha hizo bwana! Ndio inatakiwa kukuongezea ujasiri, kujua kuwa wanakufahamu vizuri na bado wanakupenda na kukuheshimu. Acha kuchanganyikiwa bwana.” “Mimi naona nirudi nyumbani nikatulie kidogo.” “Sasa hapa unamkimbia nani?” “Sijui. Labda nikapumue kidogo.” Elvin alianza kumcheka tena.
“Si tumekupa chumba? Nenda ukapumulie huko.” “Nawatizamaje tena ndugu zako?” “Kama ulivyokuwa ukiwatizama zamani. Acha woga Bella bwana. Huwezi kuepuka hilo. Ni kweli ni maisha uliyoishi na Mzee Masha, mume wa mtu na ni kama baba yako. Yatakuja mambo mengi tu, ni wewe kujiandaa jinsi ya kuyakabili. Nakuaminia Bella. Utaweza. Kama uliweza kutoka mikononi mwa Mzee Masha, anayeogopewa na kila mtu, na umeweza kusimama mpaka sasa hivi, ujue wewe ni jasiri na hutashindwa chochote kitakacho kukabili. Usiogope.” “Asante Elvin.” Bella alitulia kidogo.
“Mama amekuomba uende naye India.” “Kweli bwana. Nilishasahau. Ningependa kwenda Elvin, lakini namfikiria Ric. Wanafunga shule majuma machache yajayo, nani atamfuata, atakaa wapi, na nani? Hajiwezi Ric kwa lolote. Kama unavyomuona, atakuwa akicheza game tu, nikirudi nitamkuta amekufa.” Elvin alicheka kidogo. “Mimi nitakuwa naye Bella.” “Kweli?” “Nafikiria wakipanga hiyo siku ya nyinyi kwenda India, kabla hawajafunga shule, twende mpaka shuleni, ukamuage, halafu shule zikifunga nitaenda kumchukua tuje tuishi naye hapa mpaka utakapo rudi. Na nitakuwa nikienda naye kazini kila siku ili kutoa mawazo yake kwenye michezo.” “Hapo utakuwa umetatua tatizo kubwa sana.” “Kwa hiyo utaenda na mama?” Bella alibaki akifikiria kidogo.
“Bella!” “Nitaenda lakini sasa hivi namuogopa sio kama zamani.” “Huna haja ya kuogopa Bella. Tena ndio mtapata muda mzuri wakufahamiana zaidi.” “Nitaenda Elvin. Na kazini sasa?” “Mshahara wako utalipwa kama kawaida.” “Simaanishi mshahara bwana, namaanisha kazi. Unawaza pesa tu.” Bella aliinama na kuchota maji yaliyokuwepo kwenye ndoo, kwa mikono yake yote miwili, akamwagia Elvin.
“Umeanza Bella!” Bella alianza kucheka huku akisogea mbali kidogo ya Elvin. “Hakuna umbali utakao kwenda, nikashindwa kukufikia, nikulipize. Heri usogee karibu, nikulipizie yaishe.” Bella alikuwa akicheka sana. “Ujue Elvin kulipiza ni dhambi wewe!” “Njoo Bella.” “Hapana Elvin, jifunze kusamehe.” Bella na Elvin walianza kukimbizana wakimwagiana maji pale nje, huku wakicheka na kupiga sana kelele. Waliokuwepo ndani wakashtuka sana, ikabidi watoke. Waliwakuta wote wamelowana. Kaka zake Elvin na baba yao wote walibaki wakiwaangalia Elvin na Bella. “Elvin ndio ameanza.” Bella alijitetea kwa kumnyoshea Elvin kidole. Akajivuta nyuma kidogo ya Elvin kama kujificha, akainama. Mwasha na wanae walibaki wakishangaa. “Bella! Mama anakuita ndani.” Mzee Mwasha aliamua kuvunja ukimya maana wote walikuwa bado wanamshangaa Elvin, waliyejua ni kijana mtaratibu sana.
**********************************
Hawakuwahi kumuona Elvin akifanya mambo ya kitoto vile. Yeye alikuwa mzuri sana wakupangilia mambo na nimtekelezaji. Kila mtu pale nyumbani kwao, alipenda kumtumia yeye. Ukiwa na jambo lolote lile, hata kama limekaa vibaya, ukimkabidhi Elvin, atalipangilia na atalifuatilia kwa makini sana bila kukata tamaa mpaka kitokee kitu kizuri. Ndio maana hata walipoona baba yao akisumbuka na biashara zake, magonjwa ya moyo hayaishi sababu ya wasiwasi, walimuomba Elvin aingilie kati kumsaidia baba yao. Kipindi cha mwanzoni ilibidi kaka zake wasaidie kulipa mshahara wa Elvin, wakati akifufua biashara ya baba yao. Mwishowe Elvin aliwaandikia ndugu zake matatizo aliyoyaona yanaendelea kwenye kampuni ya baba yao, na jinsi ya kuyatatua. Walichangishana pesa ndugu hao, Elvin akaziba nyufa zote na kurudisha uhai kwenye kampuni ya Mzee Mwasha. Akaongezeka na Bella ambaye alileta maarifa mapya yaliyoongeza faida kubwa sana kwenye hiyo kampuni.
**********************************
Bella aliishi nao hapo ndani akimuhudumia mama yao bila shida wala kinyaa huku akimfariji na kumtania ili kumfanya asijisikie vibaya kila anapojichafua. Walimtegemea kwa kila jambo juu ya afya ya mama yao. Kila aliyetaka kujua mambo yanayomuhusu Mama Mwasha, aliulizwa Bella. Akageuka kuwa mtu muhimu sana kati ya wanaume hao watano. Taratibu Bella akaanza utundu kwa kila mmoja wao pale ndani. Akawa mcheshi sana akichekesha kila mtu pale kwenye nyumba ya Mzee Mwasha, zaidi Eli aliyemuokoa katikati ya kuaibishwa, ndiye walizidi kuwa karibu. Walimpenda sana na akili zake za kitoto na vile asivyojali mambo madogo madogo. Ni binti ambaye alikuwa rahisi sana kuishi naye tofauti na alivyoonekana.
 “Mimi nina sumbuliwa na hili swali Bella.” Eli alianza siku hiyo wakati wapo na Bella jikoni. Lakini wengine wote, mpaka wazazi wao walikuwa upande wa sebleni wakiwasikiliza. “Hivi wewe Bella, uliwezaje kuishi na Mzee Masha na akili hizo za kitoto hivyo!?” “Yule baba ni shetani mkamilifu. Alikuwa ananipiga karibu kuniua. Muulize Elvin. Hataki utani na mtu.” “Sasa ulikuwa unaishije nae?” “Daah! Hata sijui jamani! Unafikiri nilikuwa nacheka hivi? Hamna. Nilikuwa nalia sana, mchana na usiku nilikuwa nalia namkumbuka mama yangu, mpaka nilipompata Elvin. Nikamsimulia maisha ninayoishi, ndio akanipa ushauri jinsi ya kujikomboa.” “Kujikomboa tena? Mimi nilijua alikuwa mpenzi wako.” “Hivi we Eli ujue mimi ni mtoto sana na niliambiwa na mama yangu nisubiri mambo ya wanaume. Sasa yule baba mtu mzima vile kwa nini awe mpenzi wangu!” “Si sababu ya pesa? Yule baba anapesa sana.” “Sasa hizo pesa zake ndio zilitaka kunitoa roho. Alikuwa akinitesa sana. Muulize Elvin.” “Sasa ilikuaje mpaka mkawa wapenzi.” “Ujue sitakusimuli wewe, kama unasema yule baba ni mpenzi wangu!” “Basi mumeo.” “Naondoka Eli.” “Njoo Bella wangu unisimulie. Ujue mimi ndio nitakuoa?” “Aka. Sitaki.”  “Unamtaka Elvin?” Eli aliuliza. Bella akacheka sana.
“Elvin! Hahahahaha. Elvin ni ‘my BFF’ unajua BFF?” “Best Friend Forever?” Eli aliuliza. “Ewaa. Basi ndio mimi na Elvin.” “Humpendi?” “Si ndio maana nakwambia ni my BFF. Hata kama akija kuoa bado tutabaki kuwa marafiki. Sifikirii hata kuolewa kesho. Nitabaki na Mama Mwasha wangu tu.” “Hutaki Elvin akuoe?” Bella alicheka tena. “Wewe naona hujamjua Elvin vizuri. Elvin anajiheshimu sana, halafu ananijua mimi kuliko mtu yeyote hapa duniani. Hata hiyo nafasi aliyonipa yakuwa rafiki yake tu nashukuru Mungu. Elvin anastahili msichana mzuri, aliyetulia sio kama mimi nimepita kwenye maisha mabaya sana. Sitaki hata kufikiria swala la ndoa, Eli. Sitaki hata kufikiria mwanaume.” Bella alipooza sana. “Mungu ameniokoa kwenye hatari ya kifo, huko sirudi tena. Inatosha. Alinitesa na kunidhalilisha sana yule baba. Mpaka nikikumbuka hata kama nipo usingizini, nikiamka nakuta mto umelowa kwa machozi.” “Pole Bella. Alikufanyaje? Au ilikuaje mpaka ukaishia mikononi mwake?” Bella alifuta machozi.
“Usilie bwana.” “Si unamjua Zera yule mwanae?” “Namfahamu sana. Mapepee.” Bella alicheka huku akifuta machozi. “Alikuwa rafiki yangu sana. Sasa baada ya mama yetu kufariki, tulipata shida sana. Nikaamua kwenda kwao kuomba msaada. Nikamkuta yeye Zera na mama yake. Nikawaelezea jinsi tulivyo na shida na kuomba msaada wa aina yeyote ile. Wakatufukuza nyumbani kwao. Basi tukaondoka, wakati tupo njiani ndio dereva wao, akatufuata akasema ameambiwa aje atuchukue. Mimi nikajua ni mama yake Zera amebadili mawazo, akatuonea hurua, ndio amemtuma aje atuchukue. Akatupeleka hotelini, akatuletea pesa, na kutuambia tule kitu chochote tunachotaka. Tusiwe na wasiwasi. Kumbe ndio ulikuwa mwanzo wetu wa matatizo.” “Kwa nini hukuuliza tokea mwanzo?” “Niliuliza Eli. Tena kabla sijapanda kwenye lile gari siku ya kwanza. Yule dereva akasema, ‘wewe si unataka msaada? Basi ndio unapewa msaada’. Sasa mimi nikajua ni Mama Masha tu. Kwa kuwa ndiye niliyekuwa nikiongea naye pale nyumbani kwake, Mzee Masha mwenyewe alikuja wakati tunamalizia mazungumzo. Hata nilipofukuzwa, hakuchangia hata neno. Nikajua hata hakuwa ametusikiliza. Kumbe lile libaba, lilikuwa linafurahia vile mkewe alivyotufukuza ili liwe na mimi. Alinitesa Eli wewe, we acha tu.” “Pole Bella. Pole sana.” “Yaani hata vidonda alivyoniachia moyoni havijapona na sijui kama vitakuja kupona tena maishani. Sijui.” Bella alikaa kimya kwa muda.
“Unajua isingekuwa Elvin, mpaka sasa hivi ningekuwa nikiteseka kwa yule baba? Nilikuwa nina hela kweli. Nilikuwa naendesha gari hiyo, sijui niya mamilioni mangapi! Lakini nilikuwa sina raha hata kidogo. Akianza kunipaga, hataacha mpaka nizimie ndio ananiacha au aone ninakaribia kufa.” “Sasa alikuwa anakupiga kwa nini?” “Wivu. Tena wivu usio hata na maana. Akipiga simu usipopokea kwa wakati, ananipiga. Yaani sababu za kijinga tu.” “Kwani ulikuwa na mwanaume mwingine?” “Eli wewe jamani!?” Bella alishangaa sana.
“Hivi unajua nina miaka mingapi? Kuna jinsi mama yangu alinilea, naona ndio amenifanya nichelewe kukua akili za wanaume. Nakwambia sikuwa hata nawazo la wanaume. Kwanza shuguli ya yule baba! Huwezi kufikiria hata mwanaume mwingine. Jamani sijawahi ona baba mkorofi kama yule! Siku ya kwanza kulala na mimi, niliumwa sana Eli. Sitakaa nisahau. Halafu wala hakunipa pole, akaenda kuniacha kwa…” Bella aliangalia kulia na kushoto. “Wapi?” “Nyumbani kwa Eno. Ili anitibu.” Eli alishtuka sana.
“Eno huyu Eno Mwasha?” “Usiseme kwa nguvu sasa, wewe ukoje?” “Eno!?”  “Ndiyo. Eno huyuhuyu kaka yako anayeishi Dubai.” “Kwa nini sasa?” “Nilizimia wewe Eli. Nahisi na mshtuko pia ulichangia.” “Kwa hiyo mnafahamiana na Eno.” “Nilikuwa na hasira siku ile, sikuongea na mtu hata mmoja, tena na Elvin alikuwepo hapo nyumbani kwa Eno. Wewe huoni namuogopa sana kaka Eno? Nashindwa hata kumtizama muda mrefu?” Bella aliendelea kunong’ona. Eli alianza kucheka. “Eno mtu poa sana. Hana neno.” “Mmmh! Sasa sijui Mzee Masha alimwambia nini? Maana aliniwekea mpaka damu. Ndio maana namuogopa.” “Haiwezekani Bella!” “Kweli. Nilipoteza fahamu tukiwa hotelini damu zikinivuja. Nikaja kuzinduka nyumbani kwa Eno na dripu ya damu mkononi. Eno akanitibu mpaka nikapata nguvu, tukarudi hotelini.” “Maskini Bella! Kumbe kweli ulikuwa mtoto.” “Masha ndio alinikomaza!” Akafyoza nakumfanya Eli acheke sana. Waliendelea kuongea wawili pale jikoni.
“Ngoja nikamchokoze Elvin halafu nimsingizie kwa baba yeye ndio ameanza.” Bella aliaga. “Mwache bwana, tuendelee kuongea.” “Unapenda stori wewe! Mimi nina hamu yakumchokoza Elvin. Hata hivyo nimechoka kuongea.” Eli akacheka. “Hivi wewe Bella, utakuja kukua kweli!?” Bella alicheka na yeye. “Mimi mtu mzima mwenzio. Ngoja nikamwangalie Mama Mwasha kipenzi changu ndio nimchokoze Elvin. Hivi nilikujibu kuhusu Vin?” “Kuhusu nini?” “Kama hukumbuki basi.” “Njoo bwana Bella, mbona hivyo?” “Sasa mtu mwenyewe unasahu maswali yako mwenyewe! Vin huwa hasau mambo.” Bella alikasirika usoni na kukunja mikono yake kifuani kama katoto kadogo kakavuta mdomo.
“Nakumbuka bwana. Si nilikuuliza kama unampenda na unataka akuoe? Ukanizungusha na maneno mengii, hata sijajua jibu ni lipi. Si ndio hivyo?” “Sasa je? Unawezaje kusahau maswali muhimu kama hayo?” “Sijasahau bwana. Kwa hiyo unampenda na unataka yeye ndio akuoe?” “Kama unaniwekea majibu mdomoni, basi sikujibu naondoka.” “Usiondoke bwana Bella, si unijibu?” “Sitaki. Kwanza wewe mwenyewe ulisahau, unaonyesha sio maswali ya muhimu.” “Njoo Bella.” “Sitaki naenda zangu kwa Vin!” Bella aliondoka huku Eli akiendelea kumwangalia na kucheka.
**********************************
Ilikuwa lazima chakula cha usiku Bella na Elvin wale pamoja. Elvin alikuwa akienda kazini asubuhi nakumuacha Bella na mama yake nyumbani. “Sasa wewe Bella, utakaa na njaa mpaka saa ngapi? Heri ule tu. Elvin anaweza kuchelewa sana leo, si ndio wanafunga mwezi?” “Akirudi halafu akakuta nimeshakula, hatakula tena. Labda nimpelekee chakula hukohuko kazini.” “Mmh!” Mama Mwasha aliguna. “Wewe shida yako uende tu ukamchokoze mwenzio.” Bella alicheka. “Ulijuaje mama? Nataka nikamuone sura yake ilivyo sasa hivi. Atakuwa kama ndio mwisho wa dunia! Na wale watu wa idara ya wamasoko walivyo wakorofi! Wanakuwa hawamalizi kazi zao mpaka mwisho wa mwezi. Basi Elvin anapooza huyo!” “Nenda kamsadie basi.” Bella alifurahi sana. Aliruka pale alipokuwa amekaa pembeni ya Mzee Mwasha, nakuanza kucheza. Mzee Mwasha na mkewe, wakaanza kucheka.
“Hivi Bella wewe utakuja kukua kweli?” “Wewe mama subiri. Nikifika tu nitakupigia picha zake nikutumie umuone alivyopooza mwanao.” “Umsaidie bwana Bella, usimchokoze.” “Kama ndio hivyo haina haja hata ya kwenda.” Akarudi kukaa. “Basi kidogo tu halafu mfanye kazi, muwahi kurudi.” “Yess.” Bella alikimbia chumbani kwake kwenda kubadili nguo, baada ya muda mfupi alitoka chumbani. “Mama! Wewe ukiwa na shida yeyote unipigie simu, nitarudi haraka sana.” “Asante Bella mwanangu.” Bella akatoka.
**********************************
Ilikuwa ngumu Bella na Elvin kuachana kwa muda mrefu. Wakati mwingine Bella alimtembelea Elvin kazini, kisha wanatafuta sehemu ya kwenda kula pamoja au Elvin alirudi nyumbani kwa ajili ya chakula cha mchana. Walipopata tarehe ya kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu ya Mama Mwasha, ilimlazimu Bella kwenda kumuaga mdogo wake. “Tutaenda wote Bella.” “Afadhali. Lakini itabidi kukata tiketi ya asubuhi turudi usiku, tusimuache mama bila mtu. Naona jana hakulala vizuri.” “Basi nitaenda kuangalia tiketi za kwenda na kurudi siku hiyo hiyo.” Bella na Elvin waliondoka na ndege ya asubuhi sana kuelekea jijini Arusha.
Walipotua tu, walikwenda moja kwa moja shuleni kwa kina Eric. Wakapata muda mzuri sana naye. “Kwa hiyo nitakuwa naishi kwa kina Elvin?” “Kwa muda mpaka nitakapo rudi.” Eric akanyamaza. Bella wakaangaliana na Elvin. “Kwani hutaki kuishi kwa kina Elvin?” “Nataka, lakini nataka na wewe uwepo Bella. Nilikuwa na hamu na wewe kweli. Ngoja nikuletee barua nilizokuwa nimekuandikia.” Eric alikimbia bwenini kwao, akarudi na barua nyingi sana alizokuwa amemwandikia dada yake.
“Ulinisahau Bella!” Eric aliongea kwa uchungu sana. “Hapana Ric. Unajua siwezi kukusahau hata iweje. Mambo yalibadilika. Sikuwa na…” Bella alifuta machozi. “Nakupenda sana Ric. Nahangaika kwa ajili yako. Siwezi kukusahau hata iweje. Halafu unajua nini?” “Nini?” “Nimekutafutia shule ya palepale Dar, tuwe tunaishi wote.” Eric alifurahi sana. “Kwa hiyo hakuna kutengana tena?” “Hakuna. Safari hii ukirudi nyumbani, ndio basi.” “Nyumbani au hotelini?” Bella hakuwa ameenda kwa mdogo wake tokea alipoachana na Mzee Mwasha. “Sasa hivi tuna nyumbani kwetu Eric. Sio pakubwa, lakini ni kwetu.” Eric alimkumbatia dada yake. “Asante Bella. Najua unahangaika sana. Asante.” “Lakini Ric, mbona ni kama ulionekana unapapenda sana hapa?” “Kwa kuwa uliniahidi ukikaa sawa, utakuja kunichukua. Kwa hiyo ndio maana ikabidi niwe mvumilivu ili nisikutie wasiwasi.” “Miaka yote hiyo! Kwa nini hukuniambia? Mimi nilijua unapafurahia hapa.” “Hapana Bella. Mimi nataka kuishi na wewe. Sitaki kuishi huku peke yangu.” Bella alimkumbatia Eric. “Basi Ric, kuanzia sasa hivi tutakuwa wote.” “Sema kuanzia siku utakayorudi kutoka India.” “Naamini sitakaa sana, mama akitibiwa tu, tutarudi.” “Atapona?” Eric aliuliza kwa wasiwasi. “Tunaamini Mungu, atapona Ric.” Elvin alijibu. “Mungu asaidie huyu mama wa sasa hivi apone, asimchukue kama mama yetu. Sinilikwambia mama yetu hakupona?” “Uliniambia Ric.” “Alikufa. Hakupona.” Bella aliinama akijaribu kuzuia machozi. “Ukifunga tu shule, nitakuja kukuchukua Ric. Usiwe na wasiwasi.” “Asante Elvin.” Eric alishukuru.
 “Safari ya India.”
Usiku wa kuamkia siku ya kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu ya Mama Mwasha, ulikuwa mgumu sana kwa Elvin na Bella. Wote hawakuwa na furaha hata kidogo. Elvin aliwahi sana kutoka kazini wakabaki wamekaa kwenye meza ya kulia chakula. Hapakuwa na utani mwingi sana usiku huo, kila mtu alijua Bella aliyezoea kumchokoza kila mtu ana tatizo. “Vipi Bella mwanangu.” Mzee Mwasha alimfuata mezani akamuuliza. “Natamani ningekuwa na begi kubwa nikamuweka Elvin humo ndani, tukaenda naye.” Wote walicheka. “Muone alivyo mchokozi! Na huko utajifunza kutulia, utakuwa huna mtu wakumchokoza.” “Nitapooza sana.” Bella alifikiria kidogo. “Eti baba nikikuletea mchumba wa kihindi si utampokea?” Mzee Mwasha alicheka sana. “Unataka kuolewa na Muhindi, mwanangu?” “Utafanyaje sasa, kama ndio tunahamia hukohuko?” “Tunawaombea Mungu mambo yaende sawa, muwahi kurudi.” “Kama tukikaa sana utakuja kutuona baba?” Bella aliuliza kwa upendo sana. “Nitajitahidi kuja kuwaona Bella. Na tutakuwa tukiongea kila siku.” Bella alionekana kufurahia. Alijawa upendo wa kitoto lakini uliomfanya kila mtu karibu naye ajisikie vizuri.
**********************************
Watoto wote wa Mzee Mwasha walimpenda sana mama yao na kuonyesha kumjali mama yao kuliko baba yao. Sasa Bella alipokuja pale alijisogeza karibu sana na Mzee Mwasha. Japokuwa Mzee Mwasha alikuwa Mzee mpole sana na mwenye hekima, lakini Bella alimfanya acheke kila wakati. Popote alipoenda alimletea Mzee Mwasha zawadi hata ya pipi. Na alijisahau kabisa kumwita Mzee Mwasha, akageuka kuwa baba kila wakati. Kila alipomuona ametulia, alimfuata na kumwambia wajipige picha wakiwa wamekaa hivi au vile, wakati mwingine alimfundisha kucheza games za simu yake mwenyewe Mzee Mwasha. Alikuwa akimcheka vile Mzee Mwasha alivyokuwa na simu nzuri, lakini aliitumia kupiga na kupokea simu tu. Ali download games nyingi sana na kucheza naye kwenye simu huku akimwambia washindane. Wakati wote alipenda kukaa pembeni ya miguu ya Mwasha kama wanaangalia kitu kwenye luninga.
**********************************
 Eno alishaondoka kurudi kazini nchini Dubai lakini aliahidi kuwafuata nchini India endapo mama yake atafanyiwa upasuaji huko. “Namimi nitakuja Bella kama mtakaa muda mrefu huko, usilie bwana. Nitaenda kumfuata Ric, tutakuja kuishi naye hapa. Umesikia?” Bella alitingisha kichwa. Alishindwa kabisa kuongea wakiwa uwanjani hapo wakisubiri muda wa ndege ufike waondoke. Mzee Mwasha alimkumbatia. “Utakuwa sawa Bella, usiwe na wasiwasi. Kama Elvin alivyosema, kama mtakaa huko kwa muda mrefu tutakuja kuwatembelea. Cha muhimu umuangalie mama, umesikia?” Bella alitingisha kichwa huku akilia na kutoa tabasamu la kuwafariji wakati yeye mwenyewe alionekana akiwa hana furaha.
Tangia ampate Elvin, akamsaidia kumtoa mikononi mwa Mzee Masha, hawakuwahi kutengana. Na walishazoeana kupita kiasi. Kila wakati walikuwa wote na kula wote kila siku usiku. “Sasa nikirudi nisipomkuta Elvin?” Bella alimuuliza Mzee Mwasha huku akilia. Mzee Mwasha akacheka. “Hana pa kwenda huyu. Utamkuta tu.” Eli aliendelea kucheka. “Sasa wewe unafikiri huyu Elvin atakwenda wapi?” Alimuuliza Bella. “Sijui mimi!” Elvin alimvuta kutoka kwa baba yake, akamshika mkono akasogea naye pembeni.
“Niangalie Bella.” Bella alikuwa akilia sana. “Naogopa Elvin.” “Usiogope, nitakuwa nakupigia simu kila siku usiku kabla ya kulala, halafu majuma mawili yakipita bado hamjarudi, nitakuja kuwaangalia. Sawa?” “Usipokuja?” “Nimeshawahi kukuahidi kitu halafu nikashindwa kufanya?” Bella alitabasamu, akatingisha kichwa kukataa. “Basi ujue nitakupigia simu kila siku na nitakuja kama mkikaa zaidi ya majuma mawili. Naomba utulie, naamini kila kitu kitaenda sawa. Umesikia?” Bella alitingisha kichwa. “Hapana Bella, nataka uitikie.” Bella alicheka. “Nimeelewa bwana, wewe ukoje?” Elvin akacheka. “Haya twende tukanunue maji unywe, wakati mnasubiri kuondoka.” Bella alitulia kabisa kidogo akaanza kuongea na watu wengine mpaka muda wa kuingia kwenye ndege ulipofika.
Alienda kumkumbatia Eli na kumbusu shavuni. “Uhakikishe Vin, anakula. Sio unachelewa kurudi nyumbani. Unanisikia wewe Eli?” Eli alicheka. “Sawa mama.” Akambusu tena kisha akamsogelea Mzee Mwasha. “Ubaki salama baba yangu, eeh!” “Na nyinyi msafiri salama. Tunawaombea Bella. Kila kitu kitakuwa sawa.” “Upone kabisa baba.” Bella aliongeza. “Si unaniombea?” Mzee Mwasha alimuuliza. “Tunakuombea mimi na Elvin kila siku. Na amesema atakuwa ananipigia simu kila siku usiku kabla sijalala, kwa hiyo tutaendelea kukuombea.” Mzee Mwasha akatabasamu. “Asante mwanangu. Na ujue tunakutegemea huko. Uwe unatujulisha kila kitu kinachoendelea.” “Usiwe na wasiwasi baba. Nitakuwa karibu sana na mama, na nitahakikisha kila wakati anafuraha.” Akamkumbatia tena Mzee Mwasha na kumbusu, kisha akamsogelea Elvin. “Umeniahidi utakuja Vin.” “Yakizidi majuma mawili Bella. Kumbuka nitakuwa na Ric.” “Oooh! Nimesahau. Basi wewe baki na Ric, mimi nitakuwa na mama, usiwe na wasiwasi.” Elvin alicheka. “Nakupendea hapo tu Bella. Unaakili nzuri sana. Lakini tutaongea, wala usiwe na wasiwasi. Baada ya majuma mawili tu tutakuwa wote au hata muda huo unaweza usifike.” Bella alitabasamu na kumkumbatia Elvin kwa nguvu. Alilia kidogo hapo kwa Elvin, akaondoka huku akilia.
Safarini kuelekea nchini India.
Wakiwa njiani kuelekea nchini India, Bella alikaa karibu na daktari Mtanzania ambaye alichaguliwa kwenda nchini India kusomea zaidi mambo ya moyo. Bella alifurahi sana. Alimuelezea kinachomsibu Mama Mwasha na kwamba wanakwenda huko kwa ajili ya matibabu zaidi. “Lakini hatuna mwenyeji huko.” “Ndio mmepata mwenyeji wa kwanza.” Bella alicheka. “Ndio wewe?” “Mungu anakutanisha watu kwa sababu.” “Umeishi nchini India kwa muda gani?” Bella alihoji. “Miaka miwili sasa, lakini nipo tayari kurudi nyumbani, nimebakisha mwaka mmoja tu?” “Kwani wewe ulikuwa daktari wa nini kabla ya kwenda huko nchini India?” “Unawajua ‘Physician’?” “Wale wanaotibu kila kitu?” Bella alijibu kwa kuuliza swali. “Ewaaa. Au unaweza kusema wale ambao wanakuwa hawajasomea bado kitu fulani maalumu au wenzetu wanasema ambao bado hawaja ‘specialize’ kwenye kitu fulani. Sasa mimi nilipata hii nafasi ya kuja kusomea mambo ya moyo, nikaona heri nije mapema tu kabla sijaanzisha familia.” “Kwa hiyo mpaka sasa bado huna mke wala watoto!?” Bella alishangaa sana huku akimkazia macho kumwangalia vizuri, yule daktari alicheka.
“Ndio natafuta sasa hivi, ili angalau tupate muda wa mwaka mmoja wa mahusiano kabla ya hatujafunga ndoa. Nikimaliza tu shule yangu ya huko India, nitaoa.” Bella alianza maswali yake. “Sasa huyo mchumba unamtafutia wapi?” “Popote tu nitakapompata. Mungu anaweza kukutanisha na mwenzi wako mahali popote pale.” “Sasa utajuaje kama huyu ndio mke wangu wakati unakutana na wasichana wengi sana?” Yule daktari akacheka. “Sio kila ninaekutana naye navutiwa naye.” “Sasa mpaka sasa hivi umeshakutana na wangapi walio kuvutia?” “Unamaswali wewe?” “Nataka kujua, ili na mimi nikifika umri wa kutafuta mume wangu nianze kuangalia wanao nivutia.” “Bado huna mchumba?” “Wewe!!” Bella alishtuka sana nakujiweka vizuri, akamgeukia huku ametoa macho na kushika moyo wake.
 “Mbona unashtuka?” “Hivi wewe unajua mimi nina umri gani?” “Sijui. Kwani una umri gani?” “Mimi ni mtoto mdogo sana wewe! Sitakiwi hata kuzungumzia mambo hayo.” Yule daktari alicheka sana. “Kweli tena.” “Wenzako wanaolewa wakiwa na umri kama wako.” “Hao wanaharaka.” Bella alijibu. “Wewe huna haraka?” “Kwanza lazima unijibu swali langu ndio na mimi nitakujibu.” “Swali gani?” “Vin huwa hasahau.” Bella alijibu na kumchanganya kidogo yule daktari.
“Nimekuuliza umeshakutana na wasichana wangapi ukavutiwa nao? Na vitu gani vinavyokuvutia kwa msichana? Nataka kujua nikiona unaongea vitu vya maana, nitaiga.” “Si umesema wewe haupo tayari?” “Sio kwa ajili yangu na wewe! Ni kwa ajili ya Vin. Nataka nikikutana naye nijidai mimi ndio mtaalamu wa hayo mambo, nimfundishe. Akiniuliza umejuaje, namwambia nimejua tu na nitamwambia afuate ushauri wangu.” “Viini ni nani?” “Haitwi hivyo bwana! Usiharibu jina lake. Anaitwa Vin!” “Si ndivyo nilivyosema?” “Kama huwezi kusema Vin, basi sema Elvin, ndio jina lake lote.” “Ooh! Kumbe ni Elvin!” “Umejitahidi kidogo. Angalau hivyo.” Yule daktari akacheka.
“Unajua Elvin ananiona mimi nina akili za kitoto sana? Sasa wewe nimwagie shule yote ili nikikutana naye, nimpe darasa la nguvu. Na usianze kuniambia mambo yasiyo na maana. Kwa kuwa Elvin ana akili sana yakufikiria. Kama ni kitu chakijinga anajua tu huu ni ujinga.” “Kwani huyo Elvin ni nani?” Ilikuwa ni kama amefunguliwa mdomo mpaka yule daktari alijuta kumuuliza Elvin ni nani. “Wewe humfahamu Elvin Mwasha!?” Bella aliuliza kwa kushangaa sana tena kwa sauti ya juu. “Simfahamu.” “Basi wewe ni mgeni pale Dar. Umekuja Dar mwaka gani?” “Nimezaliwa Dar, Bella.” “Na bado humfahamu Elvin!?” “Simfahamu.” “Elvin Mwasha! Hujawahi kusikia hilo jina?” Bella aliendelea kuuliza kwa kushangaa zaidi kana kwamba yule daktari amesema hamfahamu Raisi wa Tanzania. “Hapana Bella.” “Basi Elvin ni..” Bella aliongea habari za Elvin tu mpaka wanafika nchini India. Alimwaga sifa za Elvin tu. Akilala akiamka anamshika bega yule daktari kumshtua ili amuelezee habari za Elvin. “Unajua Elvin amesema tukikaa huku zaidi ya majuma mawili atakuja kututembelea?” “Sijui Bella.” “Basi atakuja. Elvin akiahidi kitu, lazima anakitimiza. Elvin….” Bella aliongea na kuongea mpaka walipotua uwanja wa ndege wa kimataifa wa Indira Gandhi katika mji wa New Delhi.
“Mbona unaondoka wakati umesema wewe ndio mwenyeji wetu!?” Bella alitoa macho baada yakuona yule daktari anaondoka kimya kimya bila kuaga. “Nitawatafuta.” “Wewe ni muongo. Husemi kweli. Utatutafutaje wakati hata namba yetu ya simu hauna. Elvin alisema…” “Naomba tupumzike habari za Elvin tafadhali sana Bella. Please.” Yule daktari alimkatisha kabla hajaanza tena habari za Evin, alionyesha kuchoshwa sana.
“Si nataka kukwambia Elvin alisema mtu muongo ni hatari sana! Kwani ulifikiri nataka kusema nini!?” “Basi naomba namba yenu ya simu, nikitulia nitawatafuta.” Yule daktari alitaka kujirudi. “Hatutaki tena!” Bella alikataa kwa kupandisha mabega huku amekunja uso na mikono yake. Yule daktari akaanza kucheka. “Hivi wewe Bella una miaka mingapi?” “Mingi yakujua kuwa ulikuwa unatukimbia na wewe sio mtu mzuri. Unaona kabisa sisi niwageni hapa nchini. Nimekwambia mama yangu ni mgonjwa, hatuna pakwenda, wewe unasomea mambo ya moyo ambayo mama yangu anasumbuliwa nayo, halafu ni mwenyeji hapa nchini, badala utusaidie, unatukimbia!!” Mama Mwasha na yule nesi walikuwa wakimsikiliza Bella muda wote tokea kwenye ndege mpaka pale uwanjani jinsi anavyoongea na yule daktari. Mama Mwasha alikuwa ameshakalishwa kwenye kigari cha kusukumia wagonjwa, ‘wheelchair’ ameinama anacheka kimya kimya.
“Haya, samahani Bella.” Bella akacheka. “Nimekusamehe. Kwa hiyo utatuchukua utuweke nyumbani kwako?” Yule daktari alicheka huku akimtizama Bella. “Kwani nyinyi mlikuwa mkienda wapi?” “Hotelini halafu kesho ndio twende kwenye hospitali ya yaa.. yaaa…” Bella alisahau jina la hospitali waliyokuwa wakienda. “Ngoja nisome. Nimeiandika kwenye simu yangu.” Bella alitaka kutoa simu, akairudisha “Lakini naona hamna haja ya haya yote. Hamna sababu ya sisi kuhangaika wakati tumepata mwenyeji wetu, tena Mtanzania mwenzetu halafu ushakaa huku zaidi ya miaka miwili, daktari wa mambo ya moyo! Wewe utatusaidia. Au?” Yule daktari aliendelea kucheka. “Nitawasaidia Bella.” Bella alifurahi sana. “Sasa njoo nikutambulishe kwa mama yangu.” Bella aliwatambulisha vizuri. “Nimefurahi kukufahamu mama.” “Asante mwanangu.” Yule daktari aliwachukua mpaka nyumbani kwake.
Alikuwa amepangisha vyumba vitatu yeye na wasichana wengine wawili ambao na wao ni Watanzania waliokuwa wakisomea mambo ya IT nchini India lakini Bella alikuja kugundua hakuna hata mmoja wao aliyekuwa akisoma kati yao, zaidi ya kustarehe na kula pesa za baba zao nchini hapo. Walipewa chumba kimoja, wakaingiza mizigo yao yote ndani ya chumba hicho.
“Bella wewe!” Mama Mwasha alianza kucheka mara alipoingia mle ndani ya kile chumba. Naye Bella akaanza kucheka na kumnong’oneza, “Alitaka kutukimbia.” “Ulimchosha na habari za Elvin.” Bella alifikiria kidogo. “Njia nzima unamzungumzia Elvin tu, unafikiri atajisikiaje?” “Sasa yeye alitaka tuzungumzie nini? Wakati mimi simfahamu na yeye hanifahamu, sasa si heri tuzungumze habari za Elvin!” Mama Mwasha alitingisha kichwa. “Kweli kazi hapa ninayo.” Bella alicheka. “Unataka ulale kidogo? Eti mama yangu?” “Nijinyooshe kidogo. Mgongo umechoka.” “Basi lala, wakati mimi nakutafutia chakula.”
**********************************
Baada yakupata msaada wa yule daktari, waliamua kumrudisha yule nesi. Bella alisema anaweza kumuhudumia Mama Mwasha yeye mwenyewe. Waliona ni jambo zuri, kwani walipunguza msongamano kwenye nyumba ya watu, na gharama pia. Yule daktari aligeuka kuwa msaada mkubwa sana. Walishirikiana na Bella kumpeleka Mama Mwasha hospitali na kufanyiwa vipimo kwa upya kwa muda mfupi sana, tena bila shida kwakuwa yule daktari alifahamiana na Madaktari bingwa waliokuwa kwenye kitengo hicho cha moyo. Kwa hiyo hawakupata shida hata kidogo. Na Bella alihakikisha anamganda yule daktari kwa kadiri ya uwezo wake kuhakikisha wanapata huduma ya haraka ili wasiendelee kukaa pale nchini India kwa muda mrefu.
Mji huo aliokuwepo Bella na Mama Mwasha huko nchini India wapo masaa mawili na nusu tu mbele ya Tanzania, na kwa Dubai ambapo Eno alikuwepo ilikuwa ni nyuma ya Lisaa tu kwa India, kitu kilichorahisisha mawasiliano kati yao. Walipiga simu kila wakati kujua linaloendelea nchini India. Masikio na akili ya familia hiyo ya Mwasha, vyote vilikuwa nchini India kwa Bella, wakifuatilia hali ya mama huyo kwa karibu sana. Kila wakati Bella alikuwa na kazi ya kuwatuliza wanaume hao watano akiwemo Mzee Mwasha, akiwaambia mama Mwasha anaendelea vizuri.
**********************************
“Sasa saa hizi watakuwa wameenda wapi mama jamani!? Nilikwambia uwe unamwangalia Bella. Bado anaakili za kitoto, huyo daktari asije.., yaani aka…” Elvin alipiga simu kuwasalimia, lakini aliambiwa Bella ametoka na daktari. “Unawasiwasi wa bure Elvin mwanangu. Huyo Bella anaweza kujiangalia yeye mwenyewe. Huyo daktari mwenyewe analala hoi kwa usumbufu wa Bella.” “Kwani mnaishi na huyo daktari kwenye nyumba moja? Nilifikiri anawasaidia tu na nyinyi mnaishi hotelini! Kwani pesa haikutosha? Kwa nini sasa mama na wewe umekubali kuishi na huyo daktari jamani! Kwa hiyo wameshakuwa na mahusiano ya karibu kiasi cha kwamba Bella ndio amemzoea hivyo? Na yeye anamtania?” “Elvin? We Elvin! Unajua hata hujaniuliza hali yangu naona unaulizia habari za Bella tu na huyo daktari tokea ulipopiga simu?” “Samahani mama. Nahofia asije akamchezea Bella. Bella….” “Unarudi kule kule. Hatuwezi kuongea jambo jingine mbali na Bella? Eti Elvin mwanangu?” “Basi mama. Unaendeleaje?” Mama Mwasha akaanza kucheka.
Unacheka nini sasa mama jamani? Namuhofia sana Bella. Lakini tuendelee na hali yako. Wamekwambiaje?” “Nahitajika upasuaji, lakini siunajua wenzetu huku hawakuchani kwa nje? Watatoboa tundu kidogo, wataningiizia tu vimirija na kurekebisha kila kitu.” “Sasa itabidi tuje.” Elvin alishtuka kidogo. “Wamesema tusiwe na wasiwasi kabisa. Ni kitu cha muda mfupi. Ila itabidi nilale hapo hospitalini kwa siku mbili kuniangalia kisha wataniruhusu. Halafu baada ya siku tano natakiwa kurudi kumuona dokta.” “Mbona wanawaweka sana hivyo!?” “We Elvin!? Hivi unajua hata week moja hatujamaliza tokea tuje huku? Sidhani hata week mbili tutamaliza huku. Naomba uwe mvumilivu.” “Sio kwa ajili yangu mama, ni kwa ajili yako.” Mama Mwasha alijua kabisa anayehofiwa ni Bella na huyo daktari. Wivu ulishaanza kumsumbua Elvin na mama yake alijua.
“Mimi nipo kwenye matibabu Elvin, usiwe na wasiwasi.” “Sawa. Naomba akirudi Bella mwambie anipigie.” “Si ni usiku sana huko? Ungelala mtaongea kesho.” Mama yake alimchokoza Elvin. “Hapana mama, kwanza nyinyi ndio mpo mbele masaa mawili na nusu, nashangaa kwa nini mpaka sasa hivi hajarudi nyumbani! Naomba akirudi mwambie anipigie nitasubiri.” “Haya baba. Usiku mwema.” Elvin akakata simu.
**********************************
Mama Mwasha alifanyiwa matibabu mazuri sana. Daktari aliyekuwa akimuhudumia alipoona anaendelea vizuri, waliruhusiwa moja kwa moja. Walimshukuru sana yule daktari kwa kuwatunza pale nyumbani kwao, wakaanza kupanga safari ya kurudi nyumbani. “Heri turudi tu mama. Naona Elvin anawasiwasi kweli na wewe.  Kila wakati anapiga simu.” Mama Mwasha alicheka tu. Kila alipokuwa akimsikiliza Bella na Elvin, aliwaona wamejawa mapenzi mazito sana ndani yao, lakini Bella alijawa na utoto mwingi. “Ni kweli Bella.” Walikata tiketi ya kurudi, kisha Bella akampigia Elvin simu kumpa taarifa za kurudi kwao nyumbani.
“Sasa kwa nini hamjakata tiketi yakuondoka kesho Bella?” “Huyu dokta amesema amepata za kuondoka baada ya kesho kutwa.” Elvin alizidi kuchukia. “Mimi naenda kuzibadilisha.” “Hamna haja Elvin.” “Kwa nini? Au unafurahia kuishi na huyo daktari huko?” “Vin jamani! Naepuka usumbufu kwako.” “Kwangu sio usumbufu, nataka mrudi nyumbani Bella.” “Tutarudi. Hata hivyo itamsaidia mama kupata muda wa kupumzika zaidi.” “Nimeongea na mama, amepona Bella. Wewe ndio unataka kukaa huko. Umeshaanza kumpenda huyo daktari?” “Hapana Elvin jamani! Basi nenda kabadilishe hiyo tiketi tuondoke kesho. Kwanza mimi mwenyewe nina hamu ya kukuona Vin.” “Mbona sasa hutaki kurudi nyumbani?” “Nataka, lakini si ndio nilikuwa nikimuuguza mama? Nikwambie kitu?” “Nini?” “Nimekununulia zawadi nzuri. Najua utapenda. Nilimuomba huyu daktari anizungushe madukani mpaka usiku kukutafutia zawadi wewe Vin.” Elvin alitulia kidogo.
“Umekasirika Vin?” “Hapana, asante kwa zawadi. Na mimi ninahamu na wewe Bella. Nataka urudi nyumbani.” “Basi nenda kabadilishe tiketi kama utapata ya siku ya karibuni. Nitafurahi sana kukuona Elvin.” “Ukirudi nimepanga tutaenda mapumzikoni na Ric.” Bella akafurahia hilo wazo. “Wapi?” “Ni Siri. Utapaona ukifika huko.” Mama Mwasha alikuwa akiwasikiliza Bella na Elvin wakati wakiongea. Ulikuwa ni wakati wa usiku wamelala kitanda kimoja na Bella. Waliongea kwa muda mrefu Bella akicheka taratibu huku akimpa maneno mazuri Elvin, mpaka akatulia.
Uwanja wa Ndege wakimsubiri Mama Mwasha & Bella.
Familia hiyo ya Mwasha wote walikuwa uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere, mapema sana wakimsubiri mama yao na Bella wawasili kutoka nchini India. Vilijaa vicheko na utani pale uwanjani kwani na Eno naye alikuwa amefika siku hiyo hiyo kutoka nchini Dubai. Wakati wamesimama wakiongea ndugu hao, Diva naye akawasogelea na kujaribu kusalimia kila mmoja kwa kumpa mkono kama sio yeye. JJ aliingiza mikono yake yote miwili mfukoni na kubaki akimwangalia huku Diva amebaki amemnyooshea mkono. “Nakusalimia tu JJ.” “Unataka kushikwa na wanaume wangapi wewe? Kwaza unataka nini hapa?” JJ alimuuliza kwa ukali kidogo, huku baba yake na wadogo zake wakiwa kimya wamegeukia pembeni. “Niliwasikia baba na mama wakiongea jana usiku kuwa Mama Mwasha anarudi leo.” Diva alijibu kwa upole. “Kwa hiyo!?” JJ aliuliza kama akimshangaa. “Ndio na mimi nimekuja JJ?” “Umesikia swali langu lakutokea mwanzo au unataka kuharibu hali ya hewa hapa?” Diva alitulia kidogo. “Nia yangu ni nzuri JJ. Nataka kumsalimia mama na kujua anaendeleaje.” “Acha kunifanya mimi mtoto mdogo wewe! Si ulikuwa unakataa tusimpeleke kutibiwa? Ameugua akihitaji msaada wako ukashindwa hata kuwa mnafiki kidogo tu! Sasa hivi unasema nini? Ondoka Diva.” Diva alitulia. “Diva!” “Nimebadilika JJ.” “Unataka nini kwangu wewe?” “Naomba kurudi nyumbani.” “Utalia Diva wewe! Ondoka.” “Naomba basi kuja kuona watoto.” “Huyo bwana wako hazai?” “Nimeshaacha mambo hayo JJ. Sasa hivi nimetulia.” “Ujue unawazimu Diva wewe! Hata mwezi haujaisha, unasema umetulia? Ondoka Diva usitafute matatizo wewe.” “Kweli nimebadilika JJ. Na kazi kule nimeacha kabisa, natafuta kwengine.” “Kwengine au bwana mwingine? Ondoka Diva. Tafadhali usiendelee kuniudhi.” “Basi JJ.” Diva akatulia. “Ondoka sasa.” “Naomba basi nimsubirie mama nimuombe yeye msamaha.” “Ondoka Diva.” “Basi naomba umruhuhusu Mlinzi anifungulie geti pale nyumbani angalau niwaone watoto wakati wewe upo kazini kama hutaki kuniona tena.” “Na safari hii ukirudi tena pale nyumbani, kitakachokupata usinilaumu. Nimebadili kampuni ya ulinzi. Vitu vyako vyote nimevipeleka kwenu. Huna ulichobakiza pale kwangu. Nakushauri usirudi tena.” “Na watoto?” “Ulikuja kwangu na watoto?” “JJ jamani!” “Nenda kanishitaki mahakamani. Vyombo vya sheria si vipo? Nenda kadai haki yako mahakamani kama kuna unachokidai kwangu. Usinitafute tena.” Diva alianza kulia.
“Ondoka Diva. Usiharibu zaidi ya ulivyoharibu. Mama anafika sasa hivi, sitaki akute hii hali hapa. Kama umeshindwa kuniheshimu, naomba umuheshimu mama yangu.” “Nakuheshimu JJ.” “Basi ondoka.” “Uliniambia utanitafuta JJ. Basi nasubiri. Mimi nitakuwa nyumbani.” “Uwe unaishi nyumbani kwenu, au uamue kuolewa tena, au kuzunguka na mabwana zako, hainihusu tena.” “Nimebadilika JJ.” “Ondoka Diva.” Diva alianza kuondoka akasimama. “Naomba unisalimie watoto.” JJ akageuka kumpa mgongo, hakutaka kuendelea kuongea naye tena, Diva alivyoona vile akaondoka.
**********************************
Hakuwahi kumuona JJ wa vile tangia wanaoana. Alishazoea kumkosea na yeye JJ ndiye aliyeomba msamaha na akitaka yaishe. Diva aliishi na JJ kwa kiburi sana. Alishtuka kuona siku zinazidi kwenda bila JJ kumtafuta na huko shuleni pia aliwaambia Diva haruhusiwi kusogelea watoto. Na kwa kuwa hata huko shuleni kwa wanae hakuwa akielewana na mwalimu hata mmoja, haikumsumbua JJ kumdhibiti. Walimu walifanya kama walivyoagizwa na JJ. Kwanza JJ ndiye aliyekuwa akihangaika na mambo ya shule ya watoto wake. Sio Diva. Yeye alifika pale kukosoa hiki au kile. Akilalamikia hiki juu ya wanae au kile, mpaka alifahamika pale shuleni.
**********************************
Baada ya muda kidogo walishangaa kuona wale kina mama na waume zao pamoja na watoto wao wamefika pale uwanjani pia. Mwasha aliwasalimia wazee wenzake, na kuwashukuru kwa kufika pale. Walikuwa na maua mengi sana, kama kumpa Mama Mwasha pole kwa kuugua. Ndege ilitua uwanjani hapo na kushangaa Mama Mwasha akitembea bila hata kushikwa mkono na mtu. Kila mtu alikuwa akishangaa jinsi alivyonekana na uzima mkubwa tofauti alipokuwa anaondoka. Bella alimkimbilia Elvin na kumkumbatia kwa muda mrefu sana akilia. “Nimefurahi kukuona Bella.” “Nilikuwa na hamu na wewe, Vin!” “Hunishindi mimi.” Waliendelea kuongea huku wamekumbatiana. Hakuna ambaye hakuwaona jinsi walivyokuwa wamekumbatiana kwa mapenzi mazito. Irene alibaki ameinama. Eric alifurahi sana kumuona dada yake. Bella alimkumbatia Eric kwa furaha sana. “Miss you Bella.” “Me too.” Bella alisalimia kila mtu huku amemkumbatia mdogo wake na kumbusu kila wakati.
Kila mtu alimpa maua Mama Mwasha, akabaki amebeba maua mengi sana. “Haya maua anastahili kupewa Bella jamani. Alikuwa halali huyu mtoto kwa kunihudumia. Sio kipindi nipo hapa Tanzania tu ambapo watu walikuwa wakinionea kinyaa, sababu ya kujisaidia hovyo, lakini hata nilipokuwa naye India. Bella amenitunza huyu mtoto! Mungu na yeye atamlipa. Tumeondoka pale hospitalini madaktari wote wanatufahamu majina sababu ya Bella. Alikuwa hatulii akiona hali yangu sio nzuri, au kama madaktari wakitoa maelezo ambayo hatujaelewa. Bella alikuwa akifuatilia mpaka tutakaporidhika. Namshukuru Mungu kwa ajili ya Bella. Sikuzaa mtoto wa kike, lakini naona Mungu ametuletea Bella, amekuwa kama mtoto wangu niliyemzaa.” Mama Mwasha alimwaga sifa za Bella palepale uwanjani mbele ya marafiki zake wote, wanae na Mumewe.
“Asante sana Bella.” Watoto wote wa Mama Mwasha walimsogelea Bella na kumpa mkono. Mzee Mwasha alimkumbatia Bella. “Sasa unahitaji kwenda mapumzikoni.” Bella akacheka. “Umeona baba eeh?” Bella aliuliza huku akicheka. “Mimi nitampeleka Bella.” Eli alichokoza. “Elvin ameshaandaa mpaka sehemu ya kwenda, kwa hiyo Elvin ndio atawapeleka Bella na Ric wakapumzike.” “Watu mnanipinga! Basi na mimi naandaa sehemu yangu ya kwenda na Bella, wakirudi tu na sisi tutaenda. Au unasemaje Bella?” Wote walianza kucheka. Taratibu walimuona Irene, anaondoka na kurudi kwenye gari, akifuatwa na marafiki zake nyuma. Wale wakina mama na waume zao pia waliaga, nakuwaacha pale uwanjani Mzee Mwasha na familia yake wakitaniana na kucheka. Walirudi nyumbani wakiwa na furaha sana.
**********************************
Walialikwa watu baadhi jioni hiyo, kwa ajili ya tafrija ndogo ya kumshukuru Mungu kwa ajili ya kupona kwa Mama Mwasha.  “Kama wageni wanakuja usiku, naomba mimi nikalale kidogo. Lakini nina maongezi na Elvin kidogo. Unifuate chumbani ukishamalizana na Bella.” “Sawa mama.” Wote walikuwa wakijishugulisha kwa maandalizi ya tafrija ya usiku huo. Kasoro Elvin, Eric na Bella walikuwa wakiongea na kucheka. Kila mmoja kati ya watoto hao wakiume wa Mama Mwasha walijua kazi zao, kwa hiyo waligawana na kufanya kazi bila tatizo. “Basi na mimi naenda kulala.” “Twende wote Bella.” Eric na yeye akasimama. “Unataka kulala?” “Nitakuwa nacheza game pale pale kitandani utakapokuwa umelala wewe. Nina hamu na wewe Bella.” Bella akacheka. “Haya twende na mimi nina hamu na wewe Ric. Nimekuletea zawadi.” “Game nyingine tena?” Bella na Erica waliendelea kuongea huku wakiongozana chumbani, ndipo Elvin alipoenda kuongea na mama yake.
**********************************
Elvin alimkuta baba yake chumbani kwao. “Funga mlango kabisa.” Elvin alishtuka kidogo. “Kwema mama?” “Kwema lakini kuna kitu nataka nikwambie.”  Elvin alimwangalia baba yake na mama yake, wote aliwaona hawana sura za furaha. Elvin aliogopa kidogo. “Kaa hapo kwenye kochi.” “Mbona unanitisha mama! Kuna nini?” Mama Mwasha alitulia kidogo. “Unajua kama Bella ni mjamzito?” Elvin alistuka sana. “Hapana.” “Tena ana mimba kubwa tu.” “Yeye ndio amekwambia?” “Ndio maana nakwambia wewe Elvin. Bella hajielewi kabisa. Anaweza akanilalamikia kidogo tu juu ya anavyojisikia, lakini hajui kama ni mimba. Yaani kwa kifupi Bella hajielewi hata kidogo. Nilitaka kumwambia wakati tupo India, nikaona anaweza kuchanganyikiwa na wewe haupo wakumtuliza. Nikaamua nimwache,  nije  nikwambie wewe unayemuwezea, ili utafute jinsi ya kuongea naye.” Elvin aliinama. “Mungu wangu!” Elvin alisikika akiwaza kwa sauti.
“Kwani mbali na Mzee Masha, alishakuwa na mwanaume mwingine?” Mama Mwasha akauliza. “Hapana. Bella hakuwahi kuwa na mwanaume kabla na baada ya Mzee Masha.” Elvin alitulia kidogo. “Mungu wangu!” Elvin aliendelea kulalamika.
Mzee Mwasha aliamua kuingilia kati. “Elvin! Nimemueleza mama juu ya nia yako yakutaka kumchumbia Bella. Na kwamba hata pete ulishanunua ulitaka usiku wa leo kwenye tafrija ndio umvishe. Sasa baada yakujua hilo, tunataka kujua msimamo wako bado utaendelea na swala la uchumba?” “Mungu Wangu!” Elvin alisimama akiwa ameweka mikono kichwani akionyesha kuchanganyikiwa zaidi.
**********************************
Harakati zote za kuandaa pete ya gharama sana kwa ajili ya  kumchumbia Bella, zinaingia dosari kwa taarifa za ujauzito wake. Tena mtoto wa Masha! 
Je, Nini Kitaendelea? Bado Elvin atachumbia au ndio basi tena? 
Masha atafanyaje akisikia Bella ni mjamzito? 
Ulimwengu je?
Usikose muendelezo kujua kitakacho Jiri kwa Bella na ndoa ya JJ pia.

0 comments: