Nilipotea! Part 4 - Sehemu ya C
Tunda
alicheka sana vile Net alivyomtizama, akajua ameropoka akamuuliza swali
kubadili mazungumzo. “Sasa nyinyi mkamshaurije huyo Gabriel na mkewe?” “Waliitwa
na wachungaji na wazee wakanisa. Wakasikilizwa na kupewa ushauri. Lakini Gab
akasisitiza anachotaka ni talaka, akuoe wewe.” “Sio mimi. Amuoe Nancy ambaye
alishaondoka.” Tunda alijaribu kumrekebisha Net huku akiendelea kucheka.
“Mimi
naona nikuchukue tu twende wote ndio akili yangu itatulia. Nikikuacha hapa
naweza kuchanganyikiwa huko bure! Kwa jinsi unavyomfahamu Gabriel na yeye
anavyo kulilia! Mimi naona twende tu.” Tunda alizidi kucheka. “Anamfahamu
Nancy. Hamjui Tunda hata kidogo. Net wangu ndiye anayemjua Tunda mwenyewe.”
“Wewe ni poze tu!” “Mimi na wewe Net?” “Bado kabisa Tunda. Naona mpaka nikuoe.”
Tunda alizidi kucheka.
“Sasa
kuna jambo la mwisho linalonisumbua. Maana sasa hivi inabidi nikwambie kila
kitu ili ujue.” Tunda akatulia.
“Si na
mimi sasa hivi unanifahamu kama Gabriel?” Tunda akaanza kucheka tena. “Ujue
uache kujifananisha na Gabriel wewe Net! Yule sio na wala hatakaa akawa
mpinzani wako hata siku moja.” “Kweli Tunda?” “Kabisa. Wewe wala usimsikilize
Gab. Na wala usimuwekee mazingira yakumuonyesha unawasiwasi au mpo wapinzani.
Yeye anamjua Nancy, wewe unammiliki Tunda.” Net akacheka.
“Haya
Tunda.” “Kweli Net. Mimi sikupambi. Hakuna jinsi ikatokea nikarudiana na
Gabriel tena. Yale ni maisha ninayojutia kuyaishi. Wala sifurahii hapa na
kutamani kurudi. Yote niliyafanya kwake ili kufikia pesa yake. Sasa wewe
unafikiri bila kuwa vile, angefikia kuniachia kadi za benki na cheki?” Net
alibaki akimtizama. “Ilikuwa lazima niwe kinyume kabisa na alivyo Bethy ili
kufanikisha malengo yangu. Nancy alikuwa tapeli wa mapenzi. Acha hata kufikiria
hilo, ni kama unanirudisha huko. Naomba sisi tuendelee na yetu Net.” Tunda
akamtuliza.
“Unajua
tukisita sita na kuwasikiliza wanachoongea juu yetu, tutajikuta tunakwama
kwenye njia mbili na hatutaweza kwenda mbele. Tunaishi nyuma, na utashindwa
kunisaidia kama ulivyoniahidi kunisaidia kuishi maisha haya. Tutajikuta
tunaishi nyuma na sasa. Mbele hatuendelei. Tafadhali usiyumbishwe Net. Wewe
ndio nguzo yangu. Ukianza kuangalia nyuma na kusikiliza watu kama Gab, ujue
utanipoteza na mimi. Tafadhali Net, tulia.” Net akavuta nguvu kwa nguvu na
kukaa wima.
Tunda
akasimama na kwenda kumbusu shavuni. “Nakupenda Net.” Akamnong’oneza sikioni.
Net akacheka akionekana ametulia. Akamshika vizuri, akambusu mdomoni kwa muda
tu. Net akiwa amekaa, Tunda amemuinamia. Akambusu tena na tena. Tunda
akafurahia. Maana alilipata busu kama hilo mara ya mwisho ilikuwa jumapili. “Nakupenda
Tunda.” “Nashukuru Net. Nikwawambie siri yangu ndipo tuendelee na mipango
yetu?” Tunda akarudi kukaa.
“Niambie.”
“Nimekuwa na Gab na wanaume wengine wengi tu. Lakini katika yote niliyofanya,
nilitunza busu langu.” Net akashangaa kidogo. “Kwamba ulikuwa hubusu midomo
au!?” “Hata mmoja.” Net akakunja uso. “Hata Gabriel!?” Net akauliza kama
asiyeamini. “Hata yeye.” “Sadiki!?”
Akaendelea kuhoji kwa mshangao zaidi. Tunda akatingisha kichwa kukataa. “Kwa
nini!?” Tunda akacheka kidogo.
“Nilijua
watu wote wananitumia tu. Hakuna anayenipenda mimi kama mimi Tunda. Na mimi
nilijua nawaibia. Nikaogopa kwenye huo wizi, nisije nika fall in love, au
niseme nikapenda halafu nikaja kukimbiwa. Namaanisha ni kitu nilichokuwa nimejiwekea
makusudi ili kujikumbusha kila wakati ni nini nafanya ili nisipitilize na
kuumia kihisia na kiafya. Sijui unanielewa?” Tunda akamuuliza Net.
“Gabriel
ni mmoja wa walio jaribu sana kunishawishi katika hilo lakini hapo nilichora
mstari hata kwake Gab. Nilikataa kabisa. Nilitaka siku nitakapo kubali kumbusu
mtu mdomoni, iwe nimefika mwisho wa kila kitu. Iwe ni ishara kuwa nimejiachia
kwake kwa asilimia zote. Yaani kwa mara ya kwanza niwe nimejifunga kwa huyo mtu
ambaye atanikubali mimi Tunda. Ni wewe Net. Nimekubali kujifunga kwako kwa ile
garama kubwa ambayo umelipa kwangu. Sina jinsi nitakuwa na furaha na mtu
mwingine isipokuwa wewe. Kwako sijifichi. Kwa hiyo naomba uwe na uhakika na
mapenzi yangu. Nakuahidi nitatulia kwako tu.” Ilimgusa sana Net.
“Nashukuru
Tunda.” “Hii nimekwambia makusudi pengine itakusaidia kwa upande mmoja na yale
yanayokukabili sasa hivi kwa Gab. Tafadhali usije wahi kujifananisha naye.
Tupange mipango yetu au upange mipango yetu bila kutishwa na yeyote juu yangu.
Nakupenda nikiwa nahitaji mapenzi tu kwako, sio pesa zako Net. Nakuhitaji wewe
Net.” “Hilo najua Tunda. Ila uliloniambia ni kweli limeniongezea ujasiri.”
Tunda akacheka.
“Basi
tuendelee na mipango yetu.” “Nyumba niliyonayo nimeshakusimulia. Nimejenga kwa
pesa yangu, lakini kwa kuwa mimi sio mzawa, imenibidi kuiweka chini ya jina la
kampuni ya mama. Hati inaonyesha ni ya kampuni ya mama na ninayo. Sasa naomba
nikuuzie ili ikitokea mama anataka kuninyang’anya niwe nimeshauza nyumba
yangu.” “Hapana Net! Sio kwa jina langu mimi. Unataka mama yako aje aniue!?
Hapana Net.” Tunda alikataa kabisa.
“Nisikilize
Tunda. Tanzania ni nyumbani, lazima kurudi. Tukirudi tutaishi wapi? Nataka
ibakie kwa jina lako ili tuwe na kwetu hata hapa.” “Uwiii Net! Unataka
kuniingiza matatizoni wewe!” “Sina jinsi. Sina mtu ninayemuamini ambaye najua
hatakuja kunibadilikia baadaye. Watu wanabadilika Tunda. Na mimi shida yangu
sio pesa, ni ile nyumba. Nilishaona watoto wangu wakicheza mle ndani.
Nilishaona jinsi tunavyoishi mle ndani. Sitaki siku moja mama aje aiuze kwa
hasira au waje wamfilisi na kuichukua nyumba yangu.” “Unahisi wanaweza kuja
kumfilisi?” Tunda akauliza.
“Mama
ameruhusu hasira zimtawale hataki kufikiria. Ile kampuni anasahau kuwa
namsaidia kuiendesha kwa asilimia kubwa sana. Nina uhakika itachukua muda mfupi
sana kuharibikiwa baada ya kunifukuza mimi kama alivyokufanyia wewe Arusha.
Nimeona hapa kuna watu wachache sana wachapakazi, wanaojituma na waaminifu.
Kumpata mtu wa hivyo kwenye kampuni yako! Akakufanyia kazi nzuri, sio kitu
rahisi. Unaweza kumpata mchapakazi, lakini baadaye anaingiwa tamaa, anaanza
kuiba. Mama hilo analisahau wakati limeshamtokea.” Net akaendelea.
“Na kwa
maneno aliyozungumza jana, najua atatekeleza nia yake kwa haraka.” “Nia gani?”
Tunda akaendelea kuuliza kutaka kujua kila kitu. “Aliongea kwa kuropoka sababu
ya hasira kuwa, anaweza kunipokonya kibali cha mimi kuishi hapa nchini.” “Hivi
anao huo uwezo!?” “Kabisa. Kumbuka kisheria yeye ndiye anayeonyesha ananiweka
hapa nchini. Kwamba ni mwajiri wake. Ni kiasi cha kunifukuza kazi kwa maandishi
na kuniripoti kuwa amenifukuza kazi, basi. Itanilazimu kuondoka ili niwe mbali
na wewe.” Tunda akanyamaza.
“Ndio
ujue changamoto zinazotukabili na wewe usaidie sio kulinda nafsi yako.”
“Ninavyojitahidi kujiweka mbali na hizo mali ambazo mama yako anazonihubiria
kila akiiona sura yangu!” “Kwa hiyo na wewe unataka tuwe na ndoa kama ya
Gabriel na Bethy?” “Hapana Net.” “Sasa mbona hutaki hata nikusaidie hata
shilingi wakati umeshasikia ninazo pesa.” Tunda akaanza kucheka.
“Kumbe
kweli unazo pesa?” “Sasa wewe unafikiri kwa nini mama anahangaika hivyo?” Tunda
alizidi kucheka. “Lakini wakati wote wewe umekuwa kunionyesha kwa vitendo vile
unavyofanya kazi kwa bidii Net. Sijawahi kukutana na wewe popote kama haupo
kikazi. Mimi nikajua ndivyo unavyoingiza pesa yako. Kwa jasho lako.”
“Nisikilize Tunda. Ni kweli nimekuzwa kwenye mazingira ya kitajiri sana. Lakini
kila pesa ninayomiliki, babu alihakikisha tokea napata akili yangu, naifanyia
kazi.” Tunda akatulia.
“Hajawahi
kunipa pesa kama kunipa tu. Hata nilipokuwa na shida, alinipa kazi ndipo
ananilipa. Nakiri wakati mdogo alikuwa ananipa kazi zisizoendana na malipo,
lakini nimekuja kuelewa alikuwa akinifundisha. Nimekuja kukua hivyo hivyo.
Hakuna pesa kwenye akaunti yangu ambayo sio jasho langu. Kufanya kazi kwa bidii
ndicho ninachojua tokea mtoto. Na mimi sio kama Maya. Ukimwangalia Maya na
mimi, unaweza kufikiri tumelelewa na watu wawili tofauti. Lakini ni watu hao
hao.”
“Maya
alikuwa akipewa pesa ya matumizi kila week, na akitaka nyingine anapewa bila
kuulizwa swali. Lakini sio mimi. Kwanza babu alinikuza kutoomba pesa ila kazi
ili kupata pesa. Kwa kifupi ninazo pesa kwa kufanya kazi. Nikiwa hapa Tanzania,
namfanyia mama kwenye kampuni yake. Nikiwa Canada, nafanya kazi kwenye kampuni
ya Cote ya Canada, na huko pia nalipwa.” “Basi ndio maana naona kama wewe
unaweza kufanya kazi kwa bidii ukapata pesa, basi na mimi nifanye.” Net
akacheka.
“Sasa
wewe sio mimi. Mimi mwenzio pesa yangu ni yangu tu. Haiombwi na ndugu yeyote
labda niamue kumnunulia mtu zawadi. Nina uhakika nina kazi nyingi
zinazoniingizia pesa nyingi kuliko wewe. Nikikaa pale ofisini, nakuwa nafanya
kazi mbili au tatu kwa wakati mmoja na zote ninalipwa.” “Kivipi?” Tunda
akauliza.
“Kampuni
ya Cote hapa nchini ni ya mama. Cote ya Canada ni ya bibi na babu. Imesambaa
nchi na miji mingi sana. Babu alihakikisha nafundishwa lugha tano muhimu tokea
mtoto. Nina uwezo wakuziongea hizo lugha, na hii ya kiswahili, kama mzawa.”
“Net!” Tunda akashangaa. Net akacheka.
“Nilifundishwa
Tunda.” “Lakini na wewe unayo akili.” “Nikipaji. Babu alikuwa anasema hivyo.
Unajua kuna watu wanakipaji cha lugha tu. Uwezo wakuongea lugha nyingi bila
shida. Na pia kufundishwa. Sasa turudi kwenye swali lako.” Tunda akacheka.
“Babu
naye alikuwa akizungumza lugha nyingi sana. Yule hata ukimtupa kwenye kijiji
chochocte hapa Tanzania, angeweza kuongea kilugha chao.” Tunda akacheka. “Na
wewe unajua kilugha gani?” Net akacheka. “Nimekupita mbali sana kwenye kilugha
Tunda. Nikianza hapa! Utaona aibu unaweza kufikiri wewe ndio mgeni, mimi
mzawa.” “No way! Kilugha gani unazungumza Net?” Tunda akabisha kwa
mshangao. Maana aliuliza akijua wazi Net hajui kilugha chochote kutoka kabila
lolote Tanzania.
“Wewe si
unakijua kipogolo?” Tunda akaanza kucheka. “Net unanitania!” “Kama
unabisha, ongea neno la kipogolo kisha
nitakwambia maana.” Tunda hakuamini. “Net! Kwanza kwa nini Kipogolo?” “Kwa
ajili yako.” Tunda akakunja uso kama ambaye hajaelewa. “Unakumbuka uliniambia
ulikuja mjini ulikuwa hujui kuzungumza kiswahili ila kipogolo tu?” “Net!” Net
akacheka sana.
“Sasa
huwa nina mtindo wa kuchangamsha akili. Just for fun. Kujichangamsha tu. Hilo
neno la ‘kipogolo’ likanisumbua sana. Nikaona
isiwe shida. Sekretari wa mama ni mtu wa huko huko. Nikaanza kumwambia
anifundishe. Na nikamuomba aniandikie maana ya maneno 100 kwa kipogolo.
Nikamwandikia hayo maneno 100 kwa
kingereza na kiswahili, na kumuomba aandike hayo maneno kwa kipogolo.
Nikayaweza hayo 100 mpaka na jinsi ya kuweka ulimi. Nikaongeza mengine 100.
Kisha nikaanza kutengeneza sentensi. Yeye mwenyewe hakuamini. Akabaki kutoa
macho kama wewe.” Tunda akashangaa sana.
“Kweli
sikufahamu Net.” Net akacheka tena. “Turudi swali lako la mwanzoni, kisha
tuendelee na mambo yetu. Kwa hiyo. Kama nilivyokwambia, hiyo kampuni ya Cote
huko Canada, inayo matawi mengi tu, nchi mbali mbali. Sasa huwa nafanya kazi
kwenye upande wa mawasiliano na masoko. Nikiwa nimekaa hapa, nakuwa pia
mfanyakazi wao. Nawasiliana kwenye hizo nchi Papa au tuseme Nana anazokuwa
ananichagulie nifanye mwenzi huo. Matawi yake. Nafanya kazi nao kwa simu, na
kompyuta. Namtafutia na bibi masoko kama hivi mama. Namtumia hizo kazi,
nalipwa.” Tunda akabaki ametoa macho.
“Kwa
hiyo ndio hivyo ninavyoingiza pesa. Usijifananishe na mimi. Kubali nikusaidie
kila unapohitaji msaada. Umenielewa?” “Sasa hivi nimekuelewa Net. Lakini acha
nifanye kidogo. Na mimi nijione naweza kufanya kitu hapa duniani. Wewe umenifundisha.
Mungu amenipa uwezo, naona nitumike kidogo. Nakuahidi nikikwama kabisa
nitakwambia.” Net akacheka.
“Kweli
Net. Niamini bado sijakwama. Najua unasema ni msemo ninaokwambia kila wakati.
Lakini ni kweli sijakwama. Kila kitu kinachonikabili. Wazazi na mimi mwenyewe,
vipo ndani ya uwezo wangu. Na ninataka kujiona ni mimi ndiye nimefanya.”
“Nimekuelewa Tunda. Ila na mimi naomba niongezeke kwenye orodha ya wanaotaka
msaada wako. Fikiria jinsi yakunisaidia mimi na wanangu, wewe kama mama wa
familia.” Tunda akacheka sana.
“Haya
Nethaniel Cote, baba watoto wangu, at your service.” Net akacheka sana. “Nyumba
unauza kwa kiasi gani? Mwenzio sina hela ya kununua nyumba sasa hivi. Kodi tu
yenyewe inanitoa jasho!” “Wala usijali. Hiyo pesa itakuwa ya makaratasi tu.
Hunipi pesa yeyote ile. Ninachofanya ni kukumilikisha wewe. Kutoka Cote Ltd
kuwa Tunda.” “Natamani ingekuwa Tunda Cote tayari!” Net alicheka sana.
“Ndio
twende Canada tukafunge ndoa.” “Kwa nini tusifunge hapa ndio twende?” “Hapa
kuna sheria nyingi Tunda. Mpaka itangazwe na kusiwe na vipingamizi.” “Na tayari
tuna vipingamizi tena vya msingi sana!” Tunda akaongeza. “Umeona eeh! Naona
sasa unaelewa ninakopitia.” Net na Tunda walizungumza wakiweka mipango yao.
Mpaka wakafikia mwafaka.
Kwa mara
ya kwanza walitoka pale wakiwa wapo ukurasa mmoja. Kama watu wenye mipango inayo fanana. Wanania
mamoja kama wanaotaka kujenga familia yao kiukweli. Na kwa mara ya kwanza, Net
alijifungua kwa Tunda, Tunda akamfahamu japo kwa kiasi. Akaweza kumfariji na
kama kawaida ya Tunda, Mungu alimpa na yeye lugha ya ushawishi na alikuwa na
uwezo wa kufikiria kwa haraka. Ndivyo alivyoweza kuwatapeli kina Gabriel,
Kinny, Mbawala na wengine wengi. Sasa akampanga na Net. Akatoka pale kama
Nathaniel Cote wa zamani sio anayetishwa na mama yake na Gabriel.
Mipango Kabambe Yaanza.
Tunda Kwa Mama yake.
T |
unda alitoka pale akiwa
ameshakubali kuwa maisha yake sio Tanzania tena, kwa hiyo akaanza kujiandaa
kuacha familia yake vizuri. Na Net hivyo hivyo ila walikubaliana wasiwaambie
watu kwanza. Tunda alirudi hotelini kwa mama yake akamwambia aende naye akamuonyeshe
kitu. Alitoka hapo na wadogo zake, mpaka ofisini kwake. Mama yake alishangaa
maendeleo ya mwanae. “Hongera Tunda.” “Asante mama. Unapenda niwe nakuchukua
kwenda kupamba? Nitakulipa.” Mama yake akacheka.
“Kweli.”
“Nitashukuru Tunda. Sina pesa kabisa. Nitaanza hata kukusaidia kusafisha.”
Wakacheka.
“Mimi
mwenyewe nilifundishwa hivyo hivyo. Utaweza tu na utafurahia. Lakini inabidi
kutafuta pakuishi mama. Yule mwanasheria ambaye nimekwambia nitakupeleka kwake
amesema mambo ya kesi huwa yanachukua muda. Lazima kina Tom warudi shule. Na
pale nilipowakuta, mlipokuwa mkiishi na baba yao, sio mazingira mazuri kwao
kuendelea na masomo.” “Naelewa Tunda. Lakini hata sijui nafanyaje! Unajua kazi
nilifukuzwa?” “Kwa nini!?” Akasita
kumwambia ukweli Tunda.
Tunda
akaona asilazimishie kujua yasiyo muhusu, yeye afanye anachoweza. “Sababu ya
wizi.” Tom akadakia, wote wakamgeukia Tom. Tunda akakunja uso na kumgeukia mama
yake. “Na wewe walikusingizia!?” Akahisi wazazi wake wote wamepata tatizo
linalofanana. “Mambo yalikuwa magumu sana. Nilianza kuchukua madawa, na
kuwauzia watu. Hasa ya usingizi. Wakanitega na kunikamata. Hivi ninavyokwambia
nimefukuzwa kwa barua kutoka wizarani. Niliponea kufungwa. Nimejiharibia,
hakuna ninakoweza kuajirika tena kwa kazi hii ya uuguzi.” “Pole.”
“Mambo
yalikuwa magumu sana. Lakini najua sikutakiwa kuiba.” Tunda hakuwahi kumuona
mama yake akiwa mnyenyekevu vile. Alijirudi kama sio yeye. “Basi biashara
itakusaidia.” Wakazungumza hapo na mama yake, akimuonyesha anachofanya.
Kwa Net.
N |
et yeye akaondoka pale akiwa
amejawa furaha na ujasiri. Mambo yalikuwa yanakwenda vizuri kwa upande wake na
Tunda. Wapo ukurasa mmoja. Walishakubaliana waendelee na mipango yao,
wasiwajali mama Cote na Gabriel.
Kimya
kimya bila kumshirikisha yoyote akaanza kushugulikia karatasi ambazo alijua
Tunda angehitaji kuombea Visa ya Canada. Na kutafuta ushauri wa kisheria jinsi
anavyoweza kumkabidhisha Tunda ile nyumba kisheria na kuhakikisha hakuna mtu
anayeweza kumnyang’anya tena. Ibakie kwa jina la Tunda tu. Siku hiyo hakurudi
ofisini. Akawa na hekaheka nyingi karibia siku nzima.
Ijumaa.
K |
ila mmoja alikuwa kwenye
mikakati yake kwa nafasi yake. Net na Tunda kivyao, kukamilisha yao ambayo ni
wao tu wawili walikuwa wakiyajua. Na Ritha naye akawa kwenye mikakati yake,
akiwatumia wanandoa hao. Gabriel na mkewe. Ritha kama kawaida yake. Alishawasoma
wote wawili. Gab na Bethy. Akajua udhaifu wa wanandoa hao. Akawapigia mahesabu.
Akawapanga vizuri akabadili utaratibu. Akaamua awe anakutana na wana ndoa hao
tofauti tofauti na kila mmoja alifanya nao makubaliano tofauti tofauti. Akiwa
na Bethy lengo ni kumuangamiza kabisa Tunda, lakini anapokuwa na Gabriel lengo
linakuwa ni kumtenganisha Net na Tunda. Kote, yeye ndiye alinufaika bila
wengine kujua.
Net
alijitahidi kumkamilishia Tunda vitu vyote ambavyo walitakiwa kuwa navyo ili
kuhakikisha Tunda anapata Visa ya Canada. Ilikuwa ni siku ya ijumaa ambapo
walikutana jioni nyumbani kwa Tunda ili kuanza kutuma maombi hayo ya Visa
kwenye ubalozi wa Canada. Simu ya Tunda iliyokuwa karibu na Net, ikaanza kuita.
Net akaichukua ili kumpa. Akashtuka kuona namba ya mama yake. “Nini?” Tunda
akauliza baada yakumuona Net ameshtuka. Net yeye ndiye aliyekuwa akijaza kwenye
laptop yake, kumuombea Tunda Visa, online. “Mama huyu!” Tunda akakunja uso.“Amepata
wapi namba yangu!?” Tunda akauliza. “Pokea tumsikilize.” Net akashauri.
Tunda
akapokea na kubonyeza kwenye speaker ili na Net asikie. “Upo sehemu tunayoweza kuzungumza?” “Ndiyo. Shikamoo.” “Upo peke yako?”
Mama Cote akauliza. “Ndiyo sababu uliyonipigia simu?” Tunda
akamuhoji akimtaka asimpotezee muda. “Hapana. Naona ni
kama tumeanza vibaya Tunda. Nataka amani na wewe. Net ni mtoto wangu najua na
wewe utakuwa kwenye familia. Lazima tuwe pamoja na tupatane.” Tunda
alibaki kimya akimsikiliza. “Upo Tunda?” “Nipo na
ninakusikiliza.” “Ndio nilikuwa nataka nikukaribishe kwa chakula cha mchana,
pale Paz city. Tupate muda wa kuzungumza.” Net akakunja uso.
“Lini na saa ngapi?” “Kesho, saa saba mchana.” “Kesho ndio siku
yangu kubwa ya kazi. Kuanzia asubuhi mpaka usiku.” Tunda
akajibu. “Jumapili je?” Mama Cote akauliza. “Nakuwa kanisani.” “Ukitoka kanisani, je?” “Nitazungumza na
Net, kisha nitakujulisha.” “Sio kila jambo letu tunalofanya mimi na wewe, Net
ajue! Kuna mambo ya wanawake yanayotuhusu sisi tu. Wala Net haihitaji kujua.”
Mama Cote alizungumza kirafiki. “Naomba nikujibu baadaye
kama nitaweza kwa siku hiyo ya jumapili
au tufanye wakati mwingine. Asante na usiku mwema.” Tunda akakata.
“Kuna
jambo linaendelea Tunda. Kuna mtego tu. Kama kweli mama angekuwa na nia ya
kutaka amani na wewe, kwanza asingeficha kukutana kwenu, na angekualika
nyumbani kwake alipo Nana. Mara ya mwisho alikuwa akigomba na Nana alijua kuna
tatizo. Na anajua kabisa vile Nana anavyonipenda na kuniheshimu. Hajawahi hata
kunipazia sauti mbele yake. Kama angetaka kulisawazisha hilo, angeanzia alipo
Nana ambako ameharibu.”
“Kwa
kuwa Nana alishtuka sana, alipotoka na kumkuta mama akinifokea, mimi nimetulia
tu. Alitaka kujua tatizo ni nini, lakini sikutaka kuharibu zaidi, ila najua
Maya atakuwa ameshaanza kuhisi. Alishangaa siku ile ya kukuvalisha pete vile
ulivyoondoka bila kuaga na kutokurudi tena pale wakati bado yeye Nana yupo.
Tena akiwa amekuonyesha amekukubali!” Tunda akajua aliharibu kuondoka bila
kuaga. Ila akaona anyamaze tu, Net aendelee.
“Na Nana
aliposema wakati namrudisha Canada na wewe twende wote, mama alikataa mbele
yetu wote bila kufikiria kitu kilichoamsha maswali kwa Nana na Maya, wakimuhoji
ni kwa nini hataki wewe ufike nyumbani, Canada! Akatoa sababu ambazo hata bibi
alijua anadanganya maana alimuuliza maswali ambayo hakuwa na utetezi mzuri. Liko
jambo Tunda. Na sijui ni nini anataka?” Net alibadilika mpaka sura.
“Nitafanyaje
Net? Naogopa. Akija kunidhuru je?” “Na mimi hilo ndilo linalonitia wasiwasi.
Mama amefika pabaya. Na sasa hivi atafanya chochote ili kushinda. Mbaya zaidi,
sidhani kama atafurahia matunda ya anachopanda sasa hivi. Huwa namjua kuwa
anahasira sana. Sasa najiuliza hiyo hasira ikimwisha, akajikuta katikati ya huo
uharibifu, sijui atajitoaje!? Hakika sijui! Mimi nimemuonya sana. Na mbaya
zaidi ameingia kwenye ndoa ya Gabriel, anawachanganya wale watu, nahisi mwisho
wake hautakuwa mzuri.” Net aliendelea kulalamika.
“Turudi
kwangu Net. Nifanyaje?” “Nenda. Lakini usiende peke yako. Muombe mama Penny
akusindikize. Ila usimwambie mama kama utakwenda na mama Penny. Ashtukie tu unafika
pale na mama Penny. Na mimi nitakuwa karibu. Kwa lolote watakalopanga
kukufanyia, niwepo karibu.” “Hapo sawa.” Wakakubaliana.
Tunda
akampigia simu mama Penny. Akamuelezea kwa kifupi, na hofu yake na Net juu ya
kikao hicho, mama Penny akakubali kumsindikiza. Akamtumia ujumbe mama Cote kuwa
itakuwa jioni ya saa 9 sio saa saba mchana. Mama Cote akakubali. Net na Tunda
wakatuma yale maombi ya Tunda kwenye ubalozi wa Canada, wakabaki wakipanga
mipango yao.
Jumapili!
N |
et alikwenda kumchukua Tunda
nyumbani kwake wakaenda naye ibadani, kanisani kwa kina mama Penny. Walikaa
pamoja. Baada ya ibada wao walikwenda kukaa kwenye gari wakimsubiria mama Penny
amalize mambo yake pale kanisani, waongozane na Tunda. “Nilitamani kwenda kwa
baba leo.” Tunda alianza baada ya muda mfupi kuingia kwenye gari. “Kama ukiwahi
kumaliza, tunaweza kwenda.” Tunda akamtizama Net.
“Vipi?”
“Nina wasiwasi Net. Naomba chochote kikinipata, usiache kumfuatilia baba yangu
na kuhakikisha anatolewa jela.” “Tunda!” “Kweli Net. Chochote kinaweza kutokea.
Nililala nikiwaza. Mama Cote nimempokonya watu wawili muhimu sana kwenye maisha
yake. Nakumbuka chuki aliyokuwa nayo tulipokuwa Arusha! Ile ilikuwa kwa mchumba
wake tu. Sasa, sasa hivi itakuwa zaidi kwa kuwa nimeingia kwenye familia yake
yote. Maya na bibi pia wanaonekana wapo upande wangu. Hawezi kukubali hivi
hivi.” Net akanyamaza.
“Au
usiende?” Hofu ikawa imeshamwingia Net. “Siwezi kuacha kutokwenda. Ikiwa ni
kweli anataka amani je? Nitakuwa nimekimbia kitu cha msingi sana kwetu.” Net
kimya. “Tunamuhitaji Net. Hatuwezi kumpuuza. Katika lolote lile analotaka
kufanya, nia nikulinda kilicho chake.” Net kimya, alimjua mama yake.
Tunda
naye akanyamaza mpaka mama Penny alipokuja kuwagongea kioo. “Mbona mpo kama mko
msibani!?” Wote wakacheka. “Twende Tunda.” Mama Penny akaelekea kwenye gari
yake. Tunda akambusu shavuni Net na kutaka kuondoka. Net akamuwahi tena kupata
busu la mdomoni. Akambusu kwa muda kidogo, akamuachia midomo lakini akabaki
amemshilia pale pale pembeni ya shingo alipokuwa amemshika wakati akimbusu.
“Nakupenda
Tunda. Na nina kuombea.” Angalau Tunda akatabasamu.“Asante Net. Na mimi
ukumbuke nakupenda.” “Siwezi kusahau Tunda. Asante.” Tunda akampa busu la juu ya midomo, akashuka
kwenye gari ya Net, akaingia kwenye gari ya mama Penny. Wakaondoka, Net akiwafuata nyuma kwa gari yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Acha
wasiwasi wewe Tunda!” “Sijui mama Penny, moyo wangu umekosa amani kabisa!” “Sasa
mimi si nipo na Net naye amesema hatakuwa mbali?” Tunda akavuta pumzi mara
kadhaa na kuzishusha. Wakatulia hapo garini. Mama Penny akaendesha moja kwa
moja mpaka Paz City. Kwa kuwa ilikuwa siku ya jumapili, hamna magari mengi
barabarani, iliwachukua muda mfupi kufika. Akaegesha gari, wote wawili wakashuka.
Akajaribu
kumchokoza kidogo, Tunda akaanza kucheka huku wanaingia ndani. Kuingia tu,
akawaona mama Cote na Bethy wamekaa wakimsubiria. Wote walionekana kushtuka.
Kicheko cha Tunda kiliisha gafla baada yakumkuta na Bethy aliyekuwa ameonyeshwa
picha zake na Gabriel na yeye yupo pale. Moja kwa moja akajua lipo jambo. Na
mama Cote naye aliduwaa wazi baada yakumuona mama Penny.
Wakatembea
mpaka kufikia meza. “Karibuni.” Bethy yeye akajikaza kuvunja ukimya maana yeye
Ritha ni kama alibaki ameduaa tu. “Naona umeamua kuleta mtu mwingine!” Ritha
akajikuta anaropoka. “Huyu ni mama
Penny, ni dada yangu. Sidhani kama anashida kuwepo kwenye kikao chetu chakuleta
amani, kama ambavyo na Bethy yupo hapa.” Tunda akamjibu taratibu tu.
“Kumbe
mnafahamiana na Bethy?” Ritha akauliza kwa mshangao. “Ataacha kunifahamu vipi
wakati alikuwa mke mwenzangu?” Bethy akajibu. “Ulikuwa mke mwenza na Nancy,
wala sio Tunda. Na Nancy alishaondoka muda mrefu sana, anayeishi sasa hivi ni
Tunda.” Tunda akajibu bila kubabaika au
kuonyesha hofu. “Akijakurudi Nancy tena itakuaje?” Akauliza Ritha. Tunda
akacheka. “Nilijua tu kama hukuwa na nia ya amani mama Cote. Ila kwa kuwa
nimeshafika mpaka hapa, naomba uniambie ulichoniitia.” “Ni mazungumzo tu ili
kuwekana sawa. Una wasiwasi gani?” “Sina wasiwasi wowote.” Tunda akajibu.
“Basi
niseme haraka.” Ritha akaongeza. Tunda akanyamaza akabaki akimtizama, muhudumu
akafika. “Naona wageni wenu wamefika. Mpo tayari kuagiza vinywaji sasa?”
Muhudumu akauliza na tabasamu akimtizama mama Cote na Bethy. “Naomba red wine.”
Bethy akamwambia muhudumu. “Kama tukipata chupa ya champaign ingetufaa. Isio na
kileo lakini. Tunataka kusherehekea. Lete na glass 3.” “Mimi sitakunywa champ…”
Tunda akataka kukataa, Ritha akamuwahi kwa swali la kejeli. “Hutaki
kusherehekea kumilikishwa nyumba ya Cote?” Kimya.
Tunda
akajua tayari yule mama ameshajua. “Ulifikiri itakuwa siri mpaka lini?” Ritha
akauliza huku akicheka wazi akionekana na maumivu moyoni. “Ulifikiri sitajua
kama umeshaanza kuchukua mali zangu?” Akauliza tena. Tunda na mama Penny kimya.
“Hakuna kitu cha Cote kinaendelea hapa mjini, mimi nisijue. Umefanikiwa kuingia
kwenye akili za Net, kwa akili kubwa sana, kuliko shule aliyosoma yeye! Tena
umehakikisha umefanya mambo yako kisomi sana, hakuna penye swali, wala utata.
Sasa hivi wewe ndio mmiliki halali wa nyumba ya Net, iliyokuwa ipo chini ya
kampuni yangu. Alikwambia hayo yote?” Tunda kimya.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akakumbuka siku ya alhamisi Net
alipomfuata ofisini na makaratasi kutoka kwa mwanasheria akimuomba aweke saini
kwenye hizo fomu, ili kukamilisha utaratibu wa kumiliki hiyo nyumba na kutuma
maombi ya kubadili jina lililopo kwenye hati. Kutoka Cote, kuwa Tunda. Net
alimwambia ameshakamilisha kila kitu. Na baada ya yeye kuweka saini tu, ile
nyumba ni yake kihalali, na akampa milioni 3 taslimu, kisha akamuomba yeye
Tunda, amwandikie hundi ya milioni tatu kama malipo ya kununua nyumba kwa kina
Cote.
Akiwa na wasiwasi, bila amani, huku Net
akimsisitiza kuwa ile nyumba ni jasho lake, hawezi kuacha ikapotea bure, Tunda
alisaini. Akaandika na hundi ya milioni 3 tu, inayoonyesha jina la mlipaji kuwa
ni yeye Tunda, akamkabidhi Net. Net aliondoka akimwambia yeye mwenyewe
atamalizia kila kitu.
Akasahau
hata kumuuliza iliendaje. Alhamisi jioni yake hakumuona Net, alimtoa bibi yake
na Maya kwa chakula cha jioni. Ijumaa walikutana wakiwa na lengo lakutuma
maombi ya Visa. Kila mtu akili ikazama huko kwenye kuhakikisha hawakosei kutuma
hayo maombi. Tunda akimsaidia kumpa Net baadhi ya taarifa zinazomuhusu yeye
tokea anazaliwa, Net anazijaza kwenye kwenye hizo fomu za maombi, mtandaoni.
Ndipo simu ya mama Cote ikaingia kumtaka wakutane. Mambo yakavurugana. Net
akaondoka kwenda kulala kwa makubaliano ataenda kumsaidia mpenzi wake kupamba
siku inayofuata jumamosi.
Tunda
aliamka siku ya jumamosi akiwa na mawazo ya kazi na hofu yakukutana na Ritha
hiyo siku ya jumapili. Alianzia hotelini alikokuwepo mama yake na wadogo zake.
Akamchukua mama yake. Ilikuwa saa 11 asubuhi ya siku hiyo ya jumamosi wakati
Tunda alipowasili ukumbini na mama yake ili waanze kupamba. Net hakuchelewa, na
vijana wa kazi nao hawakuchelewa. Wakaanza kazi. Kufika saa tano asubuhi,
wakawa wamemaliza ukumbi wa kwanza, kwenda wa pili.
Kwa
kuwa kazi zilikuwa mbili tu jumamosi hiyo, wakaambiana wapumzike kidogo,
wakutane saa 6 na nusu kwenye ukumbi mwingine. Mama yake aliondoka kwenda
kukutana na dalali, Tunda na Net wakaelekea ukumbi mwingine. Tunda alirudi
nyumbani saa mbili usiku akiwa hoi, hata wazo la kuuliza juu mipango ya Net na
nyumba yake hakuwa nalo ila wasiwasi wa kukutana na mama Cote kesho yake ndio
uliokuwa umebaki.
Makubaliano
na mama yake ilikuwa ni atafute chumba hata kimoja, aishi hapo kwa muda wakati
anafuatilia mambo ya mali zake na mumewe. Tunda alimuahidi kumlipia kodi ya
mwaka mzima, wakati anatafuta kitu chakumwingizia kipato na wadogo zake warudi
shule. Aneti alishaanza kupata nafuu kubwa tu. Hapo ndipo mama Cote ndio
anamkumbusha maswala ya hiyo nyumba ambayo hata hawakuwa wameongea itakuje
baada ya nyumba hiyo kuwa yake kihalali.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Kwa
hiyo nyumba ishakuwa yako kihalali sasa! Bado tu hati, ni nini kinafuata Tunda?
Hebu tuambie.” Ritha akamtoa Tunda mawazoni.
“Hilo swali ni la msingi sana. Lakini hata sijafikiria kinachofuata.”
Tunda alijibu ukweli wa mambo, lakini wao wakachukulia wanabezwa. “Labda
kuhamisha kampuni yako mama Cote iwe kwa jina lake.” Bethy akaongenza kwa
kejeli. “Hapana. Mnafanya biashara ambazo sina nia wala mpango wa kuzifanya.
Kwa hiyo katika hilo usiwe na wasiwasi. Mimi nipo na Net, wala nyinyi msiwe na
wasiwasi na vyenu.” Tunda akajibu akiwa ametulia tu.
“Ni
kweli. Una haja gani yakufanya kazi wakati pesa yote ninayoitolea jasho na
niliyoitolea jasho inaingia mfukoni mwako?” Ritha akaongeza. “Mama Penny,
naomba twende dada yangu. Naona kikao kimeisha.” Tunda akasukuma kiti nyuma,
akasimama. “Huyo ndio mlinzi wako?” Bethy akauliza kwa kejeli. “Kama ulivyo
wewe kwa mama Cote.” Akajibu Tunda, wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alipoingia
tu kwenye gari, mama Penny akampigia simu Net na mumewe akawaomba warudi
kanisani wakazungumze. Hakuna aliyekataa. Tunda akamuona mama Penny
amebadilika. Lakini hakutaka kumuuliza. Akanyamaza tu, alijua ataongea tu. Mama
Penny hawezi kuweka jambo moyoni. Akaamua ampe muda ayapange maneno yake mpaka
atakapokuwa tayari kuongea ambapo pengine itakuwa kwenye hicho kikao.
Wakaendesha kimya kimya mpaka kanisani.
Wakamkuta
na mchungaji naye ndio anashuka kwenye gari yake. “Njaa inaniuma mama! ”
Mchungaji akamlalamikia mkewe. “Wote hatujala baba Penny. Pole. Lakini hili ni
la muhimu. Umewarudisha kina Penny?” “Ndio nimeingia tu ndani na wewe ukapiga
kunitaka nirudi hapa, kwema?” “Twende tukazungumzie ofisini.” Net naye akafika,
wote wakaingia ofisini.
“Ni nini
kinaendelea Tunda na Net!?” Mama Penny akauliza. “Labda ufafanue zaidi mama
Penny.” Net akaongea kiungwana. “Tuanzie swala la nyumba. Ni nyumba gani
anayolalamikia mama yako?” Net akaeleza kwa kifupi mwanzo mpaka mwisho na
kumuacha mama Penny na mumewe wametoa macho.
“Nia ni
nzuri Net, lakini huoni kama unamwingiza mwenzio matatizoni?” Mchungaji
akauliza. Net kimya. Mchungaji akaendelea. “Kwa historia ya Tunda, na hiki
ulichokifanya wewe, watu wote watajua nia ya Tunda kwako ni kweli ni mali.”
“Sina jinsi baba Penny. Sina namna nyingine. Tunda atakuwa mke wangu. Hiyo
nyumba ikiwa chini ya Tunda, nitakuwa sijapoteza.” Net akaendelea kutetea
lakini akaona kila mtu kimya. Wazi usoni walionyesha kutoridhika. Tunda alibaki
ameinama tu.
“Jamani,
hiyo nyumba ni jasho langu. Nimetengeneza kwa jasho langu mimi bila msaada hata
shilingi kutoka kwa mtu yeyote yule na Mungu wangu ni shahidi. Sio nyumba ya
ajabu sana, lakini ni yangu. Nimeijenga mchana na usiku, kwa kujinyima. Kwa
maombi mpaka nikamaliza. Siwezi kuruhusu hasira ya mama ikafanya ipotee bure.”
Net akaendelea kuweka utetezi wake.
“Babu
mwenyewe kabla ya kufariki alitaka kunisaidia kwa kuwekeza pesa, lakini
nilikataa. Ile nyumba nimejenga nikiwa mwanafunzi, huku nikiwafanyia kazi babu
na Nana. Niliwaambia msaada ninaotaka kutoka kwao, ni kazi. Wakaniajiri kwenye
kampuni yao. Nilikuwa nikifanya kazi huku nasoma, ili tu nijenge kitu changu
kisichokuwa na mkono wa mtu. Sikatai kuwa mama ndiye alihusika kunitafutia
kiwanja.”
“Sijui
alifanyaje kukipata, ila pia nilikilipia mimi mwenyewe kwa pesa niliyoipata kwa
kufanya kazi. Kuanzia msingi mpaka vigae, ni pesa yangu. Hakika siwezi kuruhusu
ikapotea bure. Babu alishawahi kuja kabla hata hajaanza kuugua na kuiona.
Natamani mngeona furaha iliyokuwepo usoni mwake baada yakuiona ile nyumba.
Alijivunia sana na ikawa ni kitu anachojisifia kwa wenzake mpaka anakufa.”
“Babu
alikuwa na mtoto mmoja tu, ambaye ni baba yangu. Baba naye akafariki na kuniacha
mimi nikilelewa na babu. Babu naye alizaliwa peke yake. Mimi na Maya ndio ukoo
kwa babu. Alinilea mimi na Maya kama watoto sio wajukuu. Chochote nilichofanya,
kilimgusa babu moja kwa moja. Ile kuona nimebadili udogo kuwa jengo vile, kwake
ni kitu amekisema mpaka anaingia kaburini anasimulia mpaka madaktari na manesi
waliokuwa wakimtibu, tena kwa kurudia rudia.”
“Alikuwa
akiwaambia kuwa, ‘Net amejenga nyumba kutoka kwenye msingi. Amebadili vumbi
kuwa jengo, msitu kuwa mahali pamakazi.’ Ndio usemi babu yangu alisema na
kujivunia mpaka kifo chake. Leo niache mtu baki tu aje aishi kwenye ile nyumba!
Hapana jamani. Ni garama ambayo nimemuomba Tunda anisaidie kulipa ili hiyo
nyumba ibaki kuwa yetu na watoto wetu.” Hata Tunda hakujua kwa mapana kiasi
hicho.
Yeye
Tunda alijua ni nyumba tu ambayo inamuhangaisha mtoto huyo wa kizungu.
Alishatamani kumwambia wajenge kwenye kiwanja chake nyumba kama ile, lakini
kumbe nyumba yenyewe ina historia nzito sana kwa Net. “That’s my legacy!
Tafadhali naomba mnielewe.” Net alimalizia hivyo akiweka msisitizo, nakuwaacha
wote wanavuta pumzi kwa nguvu.
“Mimi
narudia pale pale Net. Nia ni nzuri. Lakini unamwingiza au tuseme unahalalisha
vita inayoendelea kwa Tunda.” “Ningefanyaje baba Penny? Rafiki au familia ya
pekee mbali na mama yangu ninayoifahamu na ambao nipo karibu nao ni ya Gabriel
ambaye kama tulivyowaambia, ndio wako kinyume nasi kwa sasa. Nikisema niende
kwa wazazi wake Gabriel ndio nitakuwa naharibu kabisa. Gabriel ni zaidi ya
alumasi kwa mama yake. Hakuna mtu mkamilifu hapa duniani kama Gabriel kwa mama
yake.”
“Ni vile
tu yule mama si mtu wa mbele mbele kwenye mambo, najua hili ambalo Gabriel
analalamika nalo, atakuwa anajua kabisa, na kunilaumu. Kwa kuwa ninauhakika ni
sisi tu ndio tulikuwa hatujui kama Gabriel anamatatizo ya ndoa, lakini si yule
mama. Anamjua mwanae kwa kumtizama tu. Furaha ya Gabriel ndio ya yule mama.
Hajui kusema hapana kwa Gabriel, mpaka baba yake alikuwa akihofia atamuharibu.
Kwa kifupi nilikuwa sina wa kumkimbilia ila Tunda.” Kimya.
“Tunda
amesema unamrudisha bibi yako Canada. Ukumbuke utamuacha hapa peke yake. Na kwa
baya lolote litakalompata Tunda, ujue limeathiri watu wanne wanao mtegemea kwa
karibu sana Tunda.” “Naelewa mama Penny. Nimeshaongea na bibi, amekubali arudi
tu na Maya. Sisi tumfuate tutakapokuwa tayari. Japo alitoa ushauri mgumu
kidogo. Najua kwa desturi ya hapa ni ngumu. Sikumjibu ndio au hapana,
nilinyamaza kwa kuwa nilijua haiwezekani.” “Ni nini?” Tunda akauliza. Net
akabaki kama anafikiria.
“Net?”
Tunda akauliza tena kwa upole. Akamshika mkono. “Ni ushauri gani bibi amekupa?”
“Nilimweleza kwa kifupi, kwa kuwa yeye pia anajua ni kwa nini nipo hapa na
ninaishi hapa kwa kibali cha kazi. Akashauri kwa kuwa mambo ya kanisani
yanaweza kuchukua muda mrefu kabla ya ndoa, akatoa ushauri nimuoe Tunda
mahakamani, tukitulia ndio tufanye kanisani. Lakini nika..” “Sawa.” Tunda
akakubali kwa haraka bila hata Net kumaliza. Net hakutegemea.
Wote
wakamgeukia Tunda. “Tunda!” Mchungaji na mkewe wakajikuta wakimshangaa kwa
pamoja. Tunda akamgeukia Net vizuri. “Nisikilize Net. Kama itakusaidia kwenye
mambo yako yakuwa hapa Tanzania bila shida na maswala mengine kama hiyo nyumba.
Angalau ikijulikana ipo kwa jina langu, na mimi ni mkeo, itapunguza maswali na
makali ya hilo jambo. Tufanye tu hivyo.” Kimya.
“Kwani
ndoa ni nini?” Tunda akamgeukia mchungaji na mkewe. “Binafsi nina amani. Ndoa
ni makubaliano ya mume na mke. Kama mimi na wewe tumekubaliana, sidhani kama
kuna shida.” Net akaongeza akionekana kulifurahia hilo. Mama Penny na mumewe
wakaangaliana.
“Kweli
safari hii tumejaribiwa pabaya!” Baba Penny alisikika Tunda akacheka. “Mimi
naombeni mfikirie baba Penny. Hii ndoa yetu mtatangaza lakini wote tunajua
mtagonga tu mwamba, hamtafika popote. Mimi na Net wote tuna vipingamizi ambavyo
hatuwezi kukwepa. Watawapinga kwenye kila tangazo na kila eneo. Na wote
watakuwa na sababu zakueleweka.” “Nakushukuru Tunda.” Net akamgeukia na
kumbusu. Furaha ikawajaa gafla.
“Naomba
msubiri kwanza.” Mama Penny akawakatiza. “Hivi wewe Tunda unajua harusi za
mahakamani?” Akamuuliza Tunda. “Kwanza ujue ni ndoa halali tu, hakuna watu
zaidi yenu na mashahidi. Huwezi kutokea pale na mashela kama maharusi wengine
na kelele za vigelegele. Ni kimya kimya!” “Lakini Net si atakuwepo?” Tunda
akauliza.
“Tunda!
Naomba ufikirie.” “Baba Penny, najua maisha niliyoishi, najua nilipo na
ninapokwenda. Hakuna mwanaume atakuja kunipenda na kuniheshimu ila Net.
Sitakubali apande ndege, hata kwa ahadi ya kurudi, bila kunioa. Iwe kanisani,
iwe mahakamani. Sijali. Na kama Net mwenyewe anaona nisawa, nataka ndoa.”
Ilikuwa faraja kubwa sana kwa Net.
“Binafsi
itanirahisishia mambo mengi sana. Hata ukaaji wangu hapa nchini, hautakuwa wa
shida kama hivi sasa ambavyo nahangaika kuombewa vibali vya kazi kila wakati,
na zaidi sasa hivi inavyojulikana nafanya kazi chini ya kampuni ya mama, ambaye
ndio ananitishia . Najua ni garama kubwa analipa Tunda, lakini sina jinsi.”
“Mimi nipo tayari Net. Naombeni baraka zenu mama Penny na mchungaji. Tafadhali
sana. Nawahitaji sasa hivi kuliko mtakavyofikiria.” “Mmmh! Kazi ipo!” Alisikika
mama Penny. Tunda na Net wakabaki wakiwaangalia kwa zamu.
“Labda
ni hivyo pia ambavyo hata bado hatujaitangaza kanisani. Lasivyo watu
wasingeelewa. Kutoa harusi kanisani kupeleka mahakamani!” “Sio hivyo tu baba
Penny, na sisi ndio wasimamizi!” Akaongeza mama Penny. “Tutabariki kanisani
mambo yakitulia. Hata Nana amesema hivyo. Nana mwenyewe alikuwa anategemea
harusi kubwa ya kanisani, lakini hatuna jinsi. Amesema tutafanya tena nyingine.
Nawaomba mtusaidie mama Penny. Tafadhali.” “Lini?” Akauliza mchungaji.
Net
akamgeukia Tunda. “Wewe ulitaka iwe lini?” Tunda akamuuliza Net. “Utajali
tukifanya kabla ya bibi kuondoka?” “Inamaana iwe week hii inayoanza kesho!?”
Tunda akauliza kwa kushtuka kidogo. “Unafikiri itawezekana?” Net akauliza tena,
Tunda akamgeukia mama Penny. Mama Penny akavuta pumzi kwa nguvu. Akarudi kumtizama
Net. Akajiweka tena sawa kama anayefikiria.
“Maswala
ya mahari! Unaelewa mambo ya mahari Net?” Mchungaji akamuuliza Net. “Sidhani
kama nilazima.” Akawahi kujibu Tunda. “Hapana Tunda. Baba yupo hai. Lazima
kumuuliza yeye.” “Sawa. Nitakwenda kuzungumza naye mimi mwenyewe na kumwambia
nia yangu yakutaka tufunge ndoa kwa haraka. Akitoka, atashuhudia harusi yetu ya
kanisani.” “Hapo sawa.” Mchungaji akaridhika.
“Sasa
mtatusimamia au kwa kuwa ni ya mahakamani hamtaki tena.” Mama Penny
wakaangaliana na mumewe. “Msibadili mawazo bwana!” Tunda akabembeleza. “Ni
hivyo nakupenda tu Tunda, lakini…” Tunda akaanza kucheka. “Unacheka nini wakati
mnatuingiza matatizoni?” “Heri niwe na wewe matatizoni mama Penny, naona
nitashinda kuliko niwe peke yangu.” Mchungaji na Net wakacheka. “Unaakili mbovu
wewe!” “Kweli tena mama Penny. Sasa unafikiri nitafanyaje?” “Haya, nendeni
mkapange mambo yenu mkiwa mmetulia, halafu kesho mtatujulisha.” Net na Tunda
wakashukuru, nakutoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakiwa
njiani Net akampigia simu mmoja wa mwanasheria ambaye wanamtumia sana kwenye
mambo ya kampuni yao kumuomba muongozo. Yule mwanasheria akampa namba ya simu
ya mtu ambaye alijua anaweza kumsaidia kumpa taratibu zote. Alipompigia tu
simu, akapokea bila kuchelewa. Moja kwa
moja Net akamweleza nia yao yakutaka kuoana. Akamwambia kuwa yeye hakuwa mzawa,
lakini alitaka kufunga ndoa ambayo itatambulika kimataifa.
Akamwambia
inawezekana kabisa, lakini kwa kuwa yeye hakuwa raia wa Tanzania, ili kufunga
ndoa nchini anatakia kwanza kuwa na ‘Certificate of No
impediment’ , kutoka nchini kwao. Ili kuonyesha kuwa hujawahi kuoa
kabla. Na iambatanishwe na cheti chake cha kuzaliwa. Aliendelea kuwaeleza pia
lazima kwenda kwenye ofisi za Msajili wa ndoa ili kujaza fomu ambazo utalipia
pesa. Kisha ndipo waombe cheti cha ndoa maalumu kinachoweza kufahamika
kimataifa ambacho watalipia pesa zaidi kwa kuwa watajaza fomu tofauti na zile
za kuombea cheti cha kawaida cha ndoa.
Aliwaambia watakapofika pale waombe fomu
zinazojulikana kama RGM 111, kwa ajili ya ‘International Certificate of Marriege’. Kwa hiyo
akamwambia lazima akienda kwenye ofisi hizo za msajili wa ndoa, awe na copy ya
passport yake, na hiyo Certificate of No Imediment, atakayokuwa ameipata kutoka nchini kwao, na
picha mbili za passport size. Kisha unasubiri siku 21 ili kama kuna mtu
anakipingamizi chochote aweze kufika na kuweza kuwasiliana na ofisi hizo.
Tunda na
Net wakaangaliana. Maana Net aliweka kwenye speaker kwa hiyo Tunda alikuwa
akisikiliza. “Mmmh!” Tunda akaguna. “Hakuna jinsi
yakufupisha hayo mambo yote?” Net akauliza. “Upo
uwezekano wakufupisha hizo siku 21.” Net na Tunda wakajiweka sawa
kusikiliza. “Mnaweza kuomba kwenye hizo hizo ofisi,
lakini itabidi kulipia zaidi.” “Hamna shida.”
Net alijibu kwa haraka sana.
“Okay. Basi mtakapofika pale, muombe ‘Special Marriage License’. Mtakapomaliza kujaza hizo fomu na kulipia
garama zake, mtapewa cheti chenu, kisha mnaweza kufunga hiyo ndoa popote
mnapotaka ambapo Msajili wa ndoa akawafuata mtakapo lakini itabidi kugaramia
zaidi. Mtalipia na usafiri wake pia. Na kama mtataka mfungie pale pale, mnaweza
kuulizia kwa siku yenu mtakayokuwa mmepanga kama wanaweza kuwafungisha. Lakini
mjue itakuwa siku na muda wa kazi.” Yule mwanasheria akaendelea.
“Siku yakufungishwa hiyo ndoa nilazima kuwepo na mashahidi
wasiopungua wawili. Haijalishi kama ni wa zawa au sio wazawa wa nchi. Lakini ni
lazima kuwepo na hao mashahidi. Baada ya kufunga ndoa, ndipo mtakapo ka bidhiwa
vyeti viwili vya ndoa.” Yule mwanasheria akawa amemaliza.
“Sasa na
hiyo ‘Certificate of No impediment’ utaipata wapi Net? Hayo sio mambo ya
leo wala kesho. Hiyo kitu ishakuwa ngumu.” “Naomba tusikate tamaa mapema
Tunda.” Bado yule wakili alikuwa akiwasikiliza.
“Lakini kila kitu kinawezekana.” Wakamsikia yule
mwanasheria akionea. Wote wakatulia. “Mnanisikiliza?”
“Tupo.” Net akaitika. “Njooni kesho ofisini,
tutazungumza zaidi. Naweza kuwasaidia hata ijumaa mkafunga ndoa.” Hiyo
ikawa habari njema sana kwao. Wakaagana kwa makubaliano wakutane kesho yake.
Jumatatu.
Net
alifika ofisini kwa Tunda kumchukua, wakaelekea mpaka kwenye ofisi ya
mwanasheria waliyezungumza naye siku iliyopita. Aliwakaribisha kwa kuchangamka.
Akawaambia wakimlipa vizuri atawaandalia kila kitu. Watakachohitajika kupeleka
pale ni copy ya passport ya Net, na picha zao, basi. Yeye atawafanyia kila
kitu. Hilo nalo likawa jambo jema sana. Wakapanga mipango yao na kuwa ijumaa
ndio harusi.
Net
na Tunda walitoka pale wakiwa wamejawa cheko. Hawakuwa wakiamini kile
kinachotaka kuwatokea. Kutoka kusubiri siku 21 ndipo waoane mpaka kuweza
kufunga ndoa yao ndani ya week! Mungu awape nini! Wakampigia simu mama Penny
wakamweleza kila kitu na kumtaka asimwambie mtu yeyote. Tunda alimwambia
anamfuata ili wakatafute nguo zao na kina Penny watakao simamia, halafu Net
atamtafuta mchungaji wapange mipango yao, lakini ijumaa harusi. Vilijaa vicheko
tu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Vipi
sasa mama Cote?” Tunda akamuuliza Net. “Huyo nitamtaarifu siku yenyewe ya
harusi, nikiwa nimehakikisha wewe upo sehemu ya tukio, na mfungishaji yupo.”
“Net!” “Kweli Tunda. Nashindwa kabisa kumuamini mama kwa sasa, hasa katika
hili. Lolote laweza kutokea.” “Bibi yako?” “Nana nitamwambia. Na hivi anataka
niondoke naye jumamosi, itakuwa sababu nzuri sana. Atajua nipo kwenye honeymoon
na mke wangu.” Tunda akacheka, asiamini kama ijumaa atakuwa mke wa Net.
“Siamini
Net!” “Mimi mwenyewe siamini! Naona siku zinachelewa. Nawahi kuchukua passport
yangu, nikatoe copy, nipige picha nimpelekee leo leo. Naomba na wewe
usinicheleweshe Tunda.” “Mimi naona twende tukapige picha, ukae nazo tu.
Ukienda kumpelekea hivyo vitu, umpelekee kila kitu kwa pamoja.” Wakakubaliana.
Maandalizi
ya Harusi ya
Net
& Tunda.
H |
iyo week ikajaa hekaheka kweli
kwa Net, Tunda, mama Penny na familia yake ili kuweza kukamilisha kila kitu kwa
wakati. Mama Penny yeye alikuwa atafute wapambaji, mtu wa vyakula na vinywaji
pamoja na keki. Tunda alikuwa na kazi zake za kupamba juma hilo, ambazo
alishawakubalia watu, asingeweza kuahirisha tena. Katikati ya juma alimwambia
mama Penny atapamba mwenyewe, ila jumamosi ndio kazi zote akamuhamishia mama
Penny akijua yeye atakuwa kwenye fungate.
Ikawa
tena kuna shuguli nyingine yakutafuta nguo ya harusi itakayompendeza yeye
kwanza kama bibi harusi, na wasimamizi wake, ndani ya siku hizo hizo chache. Na
juma hilo hilo tena alitakiwa kuhama pale alipokuwa akiishi, kuhamisha baadhi
ya vitu vyake kwa mama Penny. Kukajaa heka heka, hata safari ya kwenda kwa
shangazi yake ya kuwaringishia Net, na kujua yaliyojiri baada ya kuwatumia
picha za fumanizi la mjomba wake ikasaulika.
Mama
Cote akashangaa haulizwi chochote. Net anafika kazini asubuhi kama kawaida,
mchana anatoka kwa lisaa au zaidi, kisha anarudi kazini kama kawaida. Salamu
kama kawaida. Hakuna tofauti hata hapakuwa na hasira usoni kwa Net. Ritha
alikumbuka maneno makali na kashfa aliyomtupia Net. Akakumbuka ugomvi aliouacha
kati yake na Bethy, lakini hakuuliza chochote! Na kitendo cha Tunda kufika
kwenye miahadi yao na mama Penny, wazi mama yake alijua Net anajua. ‘Lakini ni nini kinaendelea?’ Mama Cote
akaendelea kujiuliza.
Alitegemea
Maya kugeuka kisirani mara baada ya kusikiliza akimgombesha kaka yake, lakini
akashangaa na yeye ametulia tu. Bibi Cote naye kama vile alivyokuwa akishangaa
siku ya ugomvi, kuashiria hakuwa anaelewa maneno yale makali yaliyokuwa
yakimtoka Ritha kwa kijana wao, basi akaendelea kujidai kama haelewi chochote
na kama amepuuza. Hakuulizia lolote. Akaendelea kuzunguka kwenye sehemu
wanazouza vitu vya asili yeye na Maya, wakinunua zawadi. Wakati mwingine Net
aliwatoa. Basi pakatulia.
Jumatano.
Bibi
Cote kwa Tunda.
N |
et alikuwa amemwambia Tunda kuwa
bibi yake anataka kuzungumza naye. Siku nzima Tunda hakuwa na raha. Tumbo
lilikuwa likimuuma, alishindwa hata kutulia kwa wasiwasi. Alikuwa na kazi ya
kupamba ukumbi wa tamasha. Alipamba zaidi ya alivyolipwa kwa wasiwasi. Net
alimwambia atamfikisha huyo bibi nyumbani kwake mida ya saa 12 jioni ili awahi
kurudi kumchukua kwa kwenda kulala. Tunda aliwahi kurudi nyumbani kwake, ili
kupika chakula chakumkaribisha huyo bibi. Mama Penny alikuwa kwenye simu muda
wote akimtuliza.
Kama
kawaida ya Net, hakuchelewa. Kumi na mbili kamili, anagonga mlango akiwa na
bibi yake na Maya. Net alianza kucheka pale Tunda alipofungua mlango. “Sasa
unacheka nini bwana? Pisha mlangoni wageni waingie.” “Unaonekana una hali mbaya
kweli bibi harusi wangu. Ndoa ipo kweli?” Tunda akacheka na kumsukuma Net
pembeni kidogo, akampa mkono Maya, na kumkumbatia. Maya akaingia ndani,
akamsogelea bibi Net. “Net aliniambia unajua shikamoo.” Tunda alimwambia bibi
Cote na tabasamu la wasiwasi usoni. “Najua.” Akajibu yule bibi wa kizungu kwa
kiswahili na kumshtua sana Tunda. “Sasa ukimsema huyo, ujue anasikia.” Net
akaongeza na kuingia ndani akawaacha Tunda na bibi yake hapo nje wakishangaana.
“Shikamoo.”
Tunda akasalimia. “Marahaba Tunda.” Aliitika vizuri tu, kwa kiswahili chenye
lafudhi ya kigeni kisha akaendelea kuzungumza kwa kingereza. “Nina swali kabla
hatujaingia ndani.” Moyo wa Tunda ulipasuka. “Huyu bibi anataka kuniuliza nini tena!?” Kwa haraka Tunda
akajiuliza huku akimeza mate. “Karibu.” Tunda akajibu kwa upole, na wasiwasi
usoni. Akaangalia mlango kama anayetamani Net atoke ili amsaidie kwenye kujibu
hilo swali.
“Funga
huo mlango vizuri.” Alimwambia Tunda kwa lugha ya kingereza fasaha na chepesi
tu. Tunda akafunga na kurudi pale pale alipokuwa amesimama na bibi Cote. “Hataki Net asikie!?” Tunda alizidi
kupatwa na wasiwasi.
Alikuwa
bibi wa kizungu bila kuchanganya hata kidogo. Alionekana ni mwanamke aliyesoma.
Na kwa kuwa hakuwepo Net wala Maya, hakuweka ile sura yake ya utani. Akavaa
sura ya kimama, yenye jukumu kwa kijana wake. Hakuwa na umbile kubwa. Alikuwa
na mwili wa kiasi unaonekana unafanyiwa juhudi za makusudi, kutunzwa vizuri,
japo usoni alionekana umri umeshakwenda, ila ipo neema yakifedha.
“Why
Net?” Akauliza swali la moja kwa moja, nakumuacha Tunda ametoa macho. “Umenielewa?”
“Ndiyo.” Tunda akajibu kwa upole kama anayetafuta sehemu yakuanzia kujibu swali
hilo fupi tu. “Kwa nini iwe Net?” Akarudia swali lake tena, bila maneno mengi.
Lakini kwa muonekano wa yule bibi, hakuwa mtu wakudanganyika au kupewa majibu
mepesi.
Tunda
akabaki ametulia tu kama anayefikiria, akiwa ameinama. “Ninakuuliza hivyo kwa
makusudi kwa ile garama anayotaka kulipa Net kwa ajili yako. Wewe unaonekana ni
binti mzuri kabisa. Hilo halina swali. Nikiwa na maana kuwa, unaweza kuolewa na
mtu yeyote unayemtaka. Najua kwa sehemu pale alipo kwa sasa Gabriel juu yako,
lakini umeamua kuolewa na Net. Sasa swali langu nataka kujua, ni kwa nini
umemchagua Net, wakati ulishakuwa na mahusiano na Gabriel, na yeye anaonekana
bado anakupenda na anakuhitaji?” Bibi Cote akaendelea taratibu tu akimuelewesha
Tunda ili ampe majibu yatakayomridhisha.
“Kwa
sababu kama ni pesa.” Akatoa kijitabu cha hundi kwenye mkoba aliokuwa amebeba.
Tunda aliweza kujua aina ya ule mkoba. Ni wa Gucci ile ya bei kubwa. “Naweza
kukulipa bila ya yeyote yule kujua. Nitajie tu kiasi unachotaka, nitakupa bila
kukuuliza mara mbili ili umuache Net.” Yule bibi akaendelea, lakini Tunda
akabaki kama amepigwa na bumbuwazi. “Na wala usifikiri huu ni mtego. Sikutegi
ni kutaka kurahisisha mambo tu.” Yule bibi akaongeza.
“Labda hujajua pale alipo Net. Hajawahi kuwa
na tatizo na yeyote mpaka ulipokuja kwenye maisha yake. Alikuwa ni kijana
mwenye furaha na amani na kila mtu mpaka alipotokea Tunda kwenye maisha yake.
Ndipo kila kitu cha Net kimebadilika. Sasa hivi hayupo kwenye maelewano na mama
yake sababu yako. Sasa kama wewe upo kwa ajili ya pesa tu, naweza kukulipa pesa
yeyote unayotaka ili tu, tuachane kwa amani na Net aendelee na maisha yake.”
Yule bibi akamkazia macho Tunda.
“Hata
mimi natamani ingekuwa ni pesa tu, pengine hata kwangu ingekuwa rahisi.” Tunda
akaanza taratibu huku akimtizama bibi Cote. “Kwa sababu ya Net, hata mimi
maisha yangu yamebadilika. Sivyo kama nilivyokuwa zamani. Kabla sijaamua
kutulia kwa Mungu, hata baada ya kutulia kwa Mungu, Net amebadili maisha yangu.
Ile amani na utulivu niliyokuwa nayo siku chache kabla Net hajaja na kuniambia
alikuwa ananipenda anataka anioe, imeisha kabisa. Niliweza kurudisha heshima
kwenye jamii, na watu wakamtizama Tunda ambaye ametulia kanisani, lakini sasa
hivi nalipa garama kubwa sana ambayo hailipiki kwa pesa, kwa kuwa kwenye
mahusiano tu na Net.” Tunda akaendelea.
“Nimejitengenezea
maadui ambao sikuwa hata nikifikiria kama wanaweza kuwa adui. Mbaya zaidi wanatokea
kanisani ambako mimi kumenisaidia kunipa heshima. Na sikuwa nimejiandaa wala
sikuwa nimetegemea.” Tunda akacheka kidogo, kisha akaendelea.
“Nilikuwa
nikimwambia mtu fulani aliyekuwa akinilalamikia ni kwa nini sikuwa nimemwambia
kabla kama yupo mtu kama Net kwenye maisha yangu, nimekuja kumshtukiza tu baada
ya Net kutokea! Nikamjibu kuwa hata mimi sikujua kama Net yupo, japo alikuwepo.
Nakwambia kweli Ms Cote, siku chache zilizopita, kama ungeniambia kama Net
anaweza kunipenda na kutaka niwe mke wake, nisingekubali wala kudhania.”
“Hakika
sikuwahi kumfikiria japo nilishaishi naye kwa kipindi fulani, Arusha. Tena
tulikuwa karibu sana tu, lakini hata sikujua kama anazo hisia zozote za
kimapenzi kwangu na wala mawazo yangu hayakuwahi kumfikiria Net kuja kunipenda
niwe mke wake. Hata kama dunia nzima tungebaki mimi na Net tu, pia nisingeweza
hata kudhania kama Net, anayenifahamu Tunda mimi angeweza kunichagua na
kunitaka niwe mke wake. Bado siamini.” Tunda akaendelea.
“Kipindi
Net ananifuata kunitaka nije niwe mke wake, nilikuwa nina kijana ambaye alitaka
kunioa kama hivi Net. Yeye naweza kusema anauwezo, sio kama Net ninayesikia
kutoka kwa mama yake kuwa anapesa. Naweza kusema yule kijana alikuwa na pesa,
zakuzishuhudia. Za Net nazisikia tu kutoka kwenu. Hatuongelei pesa za Net
tukiwa naye. Hapa naishi kwa jasho langu. Anyways, turudi kwenye jambo la
muhimu. Yule kijana alikuwa akiitwa Julius. Na sio kwamba ni yeye tu aliyetaka
kunioa, ila yeye ndiye anayefanana na Gabriel ambaye nimeshawahi kuchezea pesa
yake, lakini nilishindwa kusema ndiyo kwao, hata Gabriel kwa sasa nimemwambia
hapana, kwa kuwa hawamfahamu Tunda hata kidogo. Ni Net tu ndiye anayenifahamu.
Angalia kiganja chako cha mkono.” Tunda alimwambia bibi Cote.
Yule
bibi akaangalia. “Huo mkono unapokuwa mchafu si unauosha?” Tunda akamuuliza
bibi Cote, kimya. “Unapokuwa mkavu si unaupaka mafuta?” Tunda akamuuliza tena. “Kwani
huo mkono huwa unaongea na wewe mpaka unaufanyia hayo yote?” Kimya. “Jibu ni
hapana. Uwe umechafuka kwa bahati mbaya au makusudi, huwa unauosha. Uwe mkavu
wakati wa baridi au joto. Usiku au mchana, huwa unajua na kuupaka mafuta zaidi
ya mara moja na huwa huchoki wala hakuna mahali unakolalamikia jinsi
unavyouhangaikia huo mkono na kutamani ukatwe.” Tunda akaendelea.
“Hivyo
ndivyo Tunda huyu aliyesimama na wewe hapa, ndivyo nilivyo mkono kwa Net.
Ananifahamu, ananisafisha na hajawahi kuchoka kuyasaka yale mazuri yaliyopo
ndani yangu na kuyatoa nje yale ambayo hakuna mwanadamu ambaye amewahi kuyaona,
hata mama yangu mzazi alishindwa, ila Net ameweza. Kwa kunisifia, na kunihimiza
niyaishi. Sijawahi kuwa mchafu kwa Net kiasi chakushindwa kunisafisha.” Tunda
akaanza kutokwa na machozi.
“Gabriel alishakuwa na mahusiano na Nancy, aliyekuwa akiishi
hapa, akitumia huu mwili wangu kama mpenzi wake. Tunda ambaye alijigeuza Nancy
alimtumikia Gabriel mchana na usiku bila kuchoka, lakini Gabriel alimuacha
Nancy akiwa anamlilia hana pakwenda. Ilikuwa usiku. Mvua ikimnyeshea. Net.
Nathaniel Cote..” Tunda akakwama kwa muda. Akajaribu kutulia.
Akafuta machozi mbele ya yule bibi.
“Usiku
ule, nikiwa nimeachwa peke yangu. Pengine kila mtu angefurahia kupatwa na kile
kilichokuwa kikinipata kwa wakati ule. Wakifurahia nisulubishwe kwa maisha
mabaya niliyokuwa nikiishi wakati ule. Lakini Net hakunihukumu. Alimchukua
Nancy, akijua wazi yupo Tunda ndani ya huyo Nancy, akamhifadhi usiku ule,
akanilisha, akanilipia madeni ya wakati ule, akanipeleka kanisani. Alihakikisha
kila aina ya Nancy, na wengine ndani yangu, wanaondoka ili tu, Tunda aliyemjua
Net, ambaye hata mimi sikujua kama Tunda anaweza kuwa hivi, ila Net.
Alihakikisha anawatoa kina Nancy wote, na kumbakiza Tunda huyu.” Tunda
akaendelea.
“Mwanamke
anayemtaka sasa hivi Gabriel, hayupo. Mungu alimtoa na kumbakisha Tunda mbaye
ni Net tu anamfahamu na kumjua, na bado anampenda. Kwa mwanaume yeyote yule
anayekuja sasa hivi, akimtaka Tunda, halafu akaja kujua habari za kina Nancy
ambao walishaishi zamani kwenye mwili wa Tunda, hakuna anayeweza kunitizama
kama Net, Ms Cote. HAKUNA. Nalijua hilo kwa hakika kwani hata Julius alipojua
historia yangu ya nyuma, alishindwa kunitizama kama zamani, ila Net.”
“Nimekula
na kuichezea pesa ya Gabriel kuliko Net. Ila sijawahi kulala usingizi mzuri,
kama ninaoupata sasa hivi ambapo nipo na Net, nikifanya kazi kwa bidii
kujiingizia kipato kwa jasho langu. Na ndio maana kwa sasa hivi ambapo Mungu
amenipa uwezo wakutengeneza pesa mimi mwenyewe, hata sihitaji pesa ya Net. Net
alinisaidia kunitoa kwenye madeni, akanipa akili ya kuzitafuta pesa. Sasa hivi
sina shida na pesa yako, wala pesa ya mama yake, au hata yeye Net mwenyewe. Isipokuwa
Net mwenyewe. Mimi namtaka Net.” Tunda akaendelea taratibu tu kama kawaida
yake.
“Nitakudanganya
nikikwambia eti habari za Net kuwa na pesa nyingi eti sio habari njema kwangu.
Nitakudanganya. Nimeishi kwenye shida, na ni kweli nimejiapia sitaolewa na
mwanaume ambaye hana pesa au akili ya maendeleo, labda awe Net. Net atanioa
hata kama ni masikini ila mapenzi yatanitosha. Nitakuwa radhi hata kumuweka
ndani nimlishe kama mtoto mdogo, lakini sio mwanaume mwingine. Nimeteseka sana
maishani. Sitaki kuja kuanza kupata tena shida nikiwa na umri huu. Hapana.
Sitaki kurudi nyuma labda na Net. Sasa nikisikia kuwa anazo pesa, nafurahia
naona ni kweli Mungu amekusudia kunipumzisha.” Tunda akamuona yule bibi
anatabasamu.
“Net
ameniambia umenitayarishia chakula cha kitanzania. Naona nipo tayari kula.”
Tunda akacheka huku anavuta pumzi kwa nguvu mpaka akainama kwa kushika magoti
yake. Hata yeye hakujua ni wapi aliupata ule ujasiri wakuzungumza na yule bibi.
Tena kwa kingereza kizuri tu. Akamsikia yule bibi anacheka. Akajua anacheka
vile alivyofanya mbele yake bila kutarajia. Tunda akasimama na kumwangalia na
tabasamu la ushindi. “Karibu ndani.” Tunda akamkaribisha na kumfungulia mlango,
wakaingia.
Kwa
muonekano wa bibi yake tu, akajua mambo yalienda vizuri na amempenda Tunda.
Hakuna aliyeondoka. Wote walikaa jioni hiyo hapo kwa Tunda, vicheko vikaanza.
Ile sura ya yule bibi alipokuwa na Tunda nje, sio hii aliyokuwa nayo alipokuwa
na Net pamoja na Maya, hapo ndani. Tunda akaamini ni kweli anawapenda na
kuwadekeza hao watoto.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wasiwasi
ulikuwa umemwingia huyo bibi baada yakugundua ugomvi mkubwa uliokuwepo kati ya
Net na mama yake. Japokuwa alimfahamu Ritha, lakini hakutaka kumpuuza. Akaona
na yeye apate muda na Tunda kabla hajaolewa na Net na kuingia kwenye familia
yake. Kwa kuwa yule bibi alikuwa msomi, na kazi zake nyingi anakutana na watu
aina tofauti tofauti.
Alijua
kwa kukaa na Tunda kwa muda mfupi tu, atamjua kama ni mkweli au la. Na kweli,
kwa muda mfupi sana aliozungumza na Tunda, akajua moyo wake. Si kwa yale tu
maneno, lakini aliweza kusoma mpaka moyo wake. Hiyo nayo ni karama yake ambayo
Mungu alimjalia huyo bibi na kufanikiwa kufanya anachokifanya huko kwao na ulimwenguni.
Alhamisi.
Tunda
kwa baba yake.
S |
iku ya alhamis Tunda akaamua
kwenda kwa baba yake kabla ya siku ya harusi. Alishatoka hospitalini. Alilazwa
siku tatu tu, akarudishwa gerezani. Ilibidi kuomba kibali maalumu kumuona kwani
haikuwa siku ya kutembelea wafungwa. Alikwenda na mwanasheria wake akamsaidia
kumuombea, alipofanikiwa, yeye akaondoka na kumuacha Tunda akimsubiria baba
yake hapo.
“Unajisikiaje?”
“Nashukuru angalau. Japo bado mwili hauna nguvu. Kuna dawa bado natumia.”
“Pole baba.” “Asante. Nakushukuru sana
Tunda mwanangu. Naona mwanasheria uliyenitafutia anahangaika kweli! Najua
inakugarimu.” “Nahangaika utoke baba. Hata yeye anasema anaona atafanikiwa.
Ameanza upelelezi wa chinichini, anasema ameshapata watu wawili ambao
walimwambia ni mpango walikufanyia pale ofisini ili utolewe. Wanasema
walipokuwa wakitaka upitishe malipo yao kama ni ya uongo, ulikuwa ukiwakatalia
ndio maana walikubambikizia receipt ya uongo, wao wakala pesa, uonekane wewe
ndio uliiba. Sasa anasema anataka kumtega mmoja wao. Amrikodi, ndipo awapelekee
wale wenye kampuni wajue ubaya wa wafanyakazi wao. Na anasema wakikubali kufuta
tu kesi, anafungua ya madai ili ulipwe fidia zote.”
“Ameniambia
na mimi hivyo hivyo. Ila amenisisitiza wakinilipa na kuniomba nirudi kazini,
nisikubali.” Tunda akashangaa kidogo. “Kwa nini tena?” “Anasema hakuna mtu
anafuraia kuingia hasara. Kwa kunilipa mimi fidia, nikuwaingiza wao hasara.
Sasa kuja kurudi tena pale, wanaweza kunitega kokote. Amenishauri nianze
kufikiria kujiajiri.” Baba Chale yaani baba yake Tunda akacheka kidogo kama anayefikiria.
“Nini?”
Tunda akamuuliza. “Anajiamini huyo! Anasema hajawahi kushindwa kesi. Kwa hiyo
anasisitiza niendelee kufikiria biashara yakufanya, pesa inakuja.” Tunda
akacheka kidogo. “Kuwa na imani baba.” “Aaaha!” “Nini? Usikate tamaa.”
“Tusubiri tuone.” Akajibu kama anayefikiria. “Najuta kuacha kazi wizarani
nakuhamia kampuni ya watu binafsi. Najuta mengi tu.” “Pole baba. Naamini kila
kitu kitakuwa sawa. Anza kufikiria chakufanya baada ya kutoka hapa.” Wakatulia
kidogo.
“Naolewa
kesho.” “Net ameniambia. Mbona huna furaha sasa?” Baba yake akamuuliza. “Kwanza
wameshakulipa mahari?” Baba yake akaanza
kucheka. “Au umesamehe mahari?” “Huko kukupenda tu ni mahari tosha. Ningepata
wapi mtu wa kukupenda hivyo? Nimemwambia ahakikishe tu anakuheshimu.” Tunda
akajifuta machozi. “Net ananipenda sana, baba.”
“Sasa tatizo liko wapi!?” Baba yake akamuuliza.
“Kuna
kitu nilikuwa sijakwambia baba na hata Net siku ya kwanza kuja naye hapa
aligusia, lakini najua hukuwa umeelewa vizuri.” “Juu ya nini tena?” Baba yake
akauliza. “Kipindi kile uliponiacha hospitalini
nikiwa mgonjwa, ndio wakakufunga. Nikatoka lakini nikashindwa kuja kukuona, ni
kwa kuwa nilikuwa nakuogopa.” Baba yake akakunja uso.
“Kwa
nini!?” “Nilikuwa nikiishi maisha mabaya sana. Nilijua ungeniona tu, na vile
nilivyokuwa nimefanikiwa, ungeniuliza maswali ambayo ningeshindwa kukujibu, na
mimi sikutaka kukudanganya.” Baba yake kimya. Akainama kama anayefikiria. “Niliishi maisha machafu sana baba. Nilionekana
nimefanikiwa kwa nje, lakini hayakuwa maisha mazuri mpaka Net aliponitoa huko
nakunipeleka kanisani. Huko nako nikapona roho, lakini imekua ndio chanzo cha
matatizo yangu.” Baba yake akawa haelewi.
“Kanisani
tena!?” Akamuuliza. “Ilibidi kutubu dhambi zangu. Nilikuwa na mashetani
ambayo mengine yaliongea uchafu waliokuwa wakinitumia niufanye, mengine
nilikiri mwenyewe. Nilikuwa nimefika mwisho baba. Nilikuwa nimechoka. Nikajua
nimepata sehemu yakutoa matatizo yangu. Lakini hata Net aliniambia pale ni
sehemu sahihi naweza kuongea chochote. Sasa kama nilivyokwambia. Nilikuwa
nimefika mwisho, nataka kupumzika. Na kama unavyojua, uliniacha peke yangu
nikiwa nimefungiwa milango na ndugu wote. Nikajikuta nakiri kila kitu.” “Hukukosea
Tunda. Ulifanya vizuri kukiri kanisani. Si ndio umepata msaada sasa?
Nakupongeza.” Baba yake alijaribu kumsifia.
“Na mimi
ndivyo nilivyofikiria baba. Lakini imekuwa tofauti. Badala yake nimekuwa ni
kama nimetengeneza mwiba wakunichoma. Moja ya wanaume niliokwisha kuwa na
mahusiano nao, alitaka kumuoa mama yake Net.” Baba yake alishtuka mpaka Tunda
akamuona. Tunda akainama. “Net anafahamu hilo!?”
“Anafahamu baba. Na mwingine alikuwa rafiki kipenzi, kama ndugu kwa Net.”
Tunda akaendelea huku anafuta machozi.
“Siku nimeenda kukiri pale kanisani, huyo baba aliyekuwa amuoe
mama yake Net, alikuwepo na mama yake Net alikuwepo. Net hakuwa akijua kama
mama yake alitaka kuolewa na yule mzee. Na mimi nilipaniki nilipomkuta yule
mzee pale ofisini kwa mchungaji. Kwa kuwa nilitaka kuanza maisha mapya, Net
akaniambia amenipeleka pale kwa watu wacha Mungu, nafika pale nakutana na yule
Mzee, nilipaniki sana. Mbele yao, nikapaniki. Nikamwambia Net mbona anataka
kunirudisha kule kule kubaya? Mimi sikujua kama yule mzee ni wa kanisani. Maana
alishawahi kunilipa mara mbili japo kanisani alisema ni mara moja tu. Basi,
ndio uadui umeanza. Mama yake Net hanitaki kabisa.” “Na Net
mwenyewe!?” Baba yake akiwa kwenye mshangao, akauliza.
“Huna
utakachomwambia Net juu yangu, mbali ya kunioa mkaelewana baba. Na hivi
ninavyokwambia sio kwamba alisikia siku nakiri kanisani! Alishanifumania zaidi
ya mara tatu. Hata huyo rafiki yake, anaitwa Gabriel, alishanifumania naye.
Mimi mwenyewe sikuwahi kujua kama Net anaweza kuja kunifikiria mimi kama
mwanamke wakuoa.” Yule baba alivuta pumzi kwa nguvu, akatulia kidogo.
“Utafanyaje?”
Mwishowe akamuuliza. “Sijui baba. Ila ninachojua kesho naolewa naye. Japo ni
kwenye mazingira hatarishi sana. Mama yake anatafuta kila mbinu yakuniangamiza.
Hataki hata kuniona, na ametengeneza watu ambao wanatugeuka. Huyo Gabriel,
amemgeka Net, anamtisha kuwa asinioe kwa kuwa mimi ni mwanamke wake na bado
ananipenda ni kama amempokonya mkewe.” Tunda alimuelezea baba yake kila kitu
bila kumfisha mpaka maswala ya nyumba.
Alimuacha
baba yake haelewi huyo Net anatakaje bado kumuoa binti yake. Tunda aliondoka
akiwa amempa baba yake habari chungu na tamu. Tamu kwa kuwa anajua Net
anampenda kwa dhati. Chungu akiwaza mwisho wake ni nini!? Maana anaingia kwenye
ndoa akiwa na vita na mwanamke mwenye jina kubwa na pesa hapo nchini. Mbaya zaidi,
ni mama yake Net, na ndiye anayemuweka Net mjini
Ijumaa.
Harusi ya Net na Tunda.
S |
iku hiyo Tunda aliamkia saluni
akiwa na mama Penny pamoja na watoto wake. Mama yake alifika hapo saluni
akitokea hotelini akiwa na Aneti. Wote Tunda alitaka watengenezwe. Tunda mpenda
nywele, alishashonewa nywele nzuri sana siku iliyopita kabla ya kwenda kwa baba
yake. Siku hiyo ilikuwa kupambwa tu, na ile nywele kutengenezwa muundo wa
kuweza kubeba shela na maua. Net, mchungaji na Tom walikuwa saluni yao.
Kulikuwa na hekaheka wakitaka kumaliza mapema, ili harusi ifungwe mapema kabla
ya giza kuingia. Bibi Cote alikuwa akiondoka kesho yake, yeye na Maya kurudi
nchini Canada.
Mama
Penny na baadhi ya vijana wa pale kanisani, walishapamba nje ya nyumba ya Net,
ambako kwa wakati huo kisheria ilikuwa nyumbani kwa Tunda. Hawakutaka kufunga
hiyo ndoa kokote ila hapo. Mama Penny alikuwa ameshamsaidia Net kutafuta
wapishi wazuri na waliahidi kuja na vinywaji. Na akawataka wafike hapo mapema
tu. Wakakubaliana na mama Penny. Net alishamkabidhi mama Penny pesa yote bila
maswali. Akabaki mama Penny kufanya mipango yote. Yeye peke yake akipiga simu
huku na kule. Mpaka inafika ijumaa, mama Penny akiwa saluni bado alikuwa kwenye
simu akihakikisha jambo haliharibiki. Alitulia mida ya saa 9 mchana wakiwa bado
wapo saluni, alipopata simu kuwa watu wa chakula, vinywaji, Dj na keki wameshafika
nyumbani kwa Tunda na Net.
Hapo
mama Penny akawa amebakisha kumpelekea Net mke tu. Na Net naye akawa ametulia
kuona kila kitu kinaenda sawa mpaka muda huo. Na yule mwanasheria
aliwahakikishia kila kitu kitakuwa sawa, wakalipia garama zote za mtu wakufika
pale kufungisha hiyo ndoa yao. Na kweli na yeye akafika kwa wakati.
Kama
kawaida Tunda hakujikosea. Alivaa shela nyeupee, kama asiyemjua mwanaume.
Akatengenezwa vizuri, na ile rangi yake ya weusi, usingechoka kupiga
vigelegele. Japokuwa walikuwa wachache lakini palitengenezwa kupendezea
wachache hao. Hakutaka kuhusisha watu wa kanisani kabisa. Wao walikuwa
wachungaji, halafu ndoa inafanyika nyumbani na ni ya serikali! Wanawaambiaje
watu? Hata hivyo walifanya kwa kuwa ni Tunda. Na alishamwingia mama Penny mpaka
rohoni.
Mama
Penny alimuona Tunda kama mdogo wake wakuzaliwa na rafiki haswa. Penny hakuacha
kujisifia. Furaha yake ilitimia pale alipoambiwa ataanza kuingia yeye na mdogo
wake pamoja na Aneti. “Wataniona mimi kabla ya aunt Tunda.” Hakuacha kujisifia.
Net, Tom
na Mchungaji walishafika hapo kutokea saluni. Bibi Cote na Maya walikuwepo hapo
nyumbani kwa Net mapema tu. Wakati Tunda anakaribia na hapo nyumbani ndipo Net
akampigia simu mama yake kumtaka afike nyumbani kwake. Akiwa na mshangao kwani
hawakuwa wakizungumza mbali ya salamu. Akakubali kufika. Lakini akitaka kujua
kuna nini na kama ni mazungumzo kwa nini wasizungumzie tu ofisini, Net
akamwambia anamuomba afike nyumbani kwake, hatamuweka muda mrefu.
Gari
hiyo ya Limousine iliyokuwa imembeba bibi harusi na wasimamizi wake pamoja na
mama yake Tunda, iliwasili nyumbani hapo saa 10 kamili jioni. Net alimpigia
simu mama Penny akimuomba wasubiri kwenye gari mpaka atakapowaambia washuke.
Mama Penny akashangaa ni kwa nini wasubiri nje!
Mama Cote
alifika nyumbani kwa Net bila kuchelewa. Akashangaa kukuta shamrashamra na
nyimbo za taratibu zikipigwa na pameandaliwa kama kwenye sherehe. Net akamfuata
pale alipoegesha gari. “Ni nini kinaendelea?” “Tunaweza kuzungumza pale kwenye
meza aliyokaa bibi?” “No.” Yule mama alikataa bila kupepesa macho. “Niambie ni
nini kinaendelea Net?” “Leo, namuoa Tunda.” Mama Cote alibaki akimtizama mwanae
kwa sekunde kadhaa bila kujibu kitu.
“Nampenda
Tunda, mama. Na nilikwambia lazima nimuoe.” “Kwa shida zote nilizopata na wewe
Net, leo, sasa hivi ndio unaniambia unaoa!? Unaniambia kama
mpitaji tu? Unanitoa ofisini kuja kwenye harusi yako!?” Net alimuona vile mama
yake alivyobadilika. Alipandisha hasira mpaka midomo ilikuwa inacheza.
Ritha amtangazia Vita iliyo ramsi Mwanae, Siku ya harusi yake.
“Unanidharau mimi Net!? Unapanga
mipango yako na bibi yako mimi nakuwa kama mtu wa kando tu?” “Naomba utulie
mama. Hii mipango nimepanga mimi mwenyewe. Bibi hausiki.” “Na yeye bibi yako
umetoka kumpigia simu sasa hivi?” Mama yake akauliza akionekana amekasirika
kupita kiasi.
“Mama!”
Net alitaka kumshika, mama Cote akarudi nyuma. “Niambie ukweli Net. Na yeye
bibi yako ndio anajua leo kama unamuoa Tunda, mwanamke malaya huyo, aliyetembea
na kama baba yako na kaka yako pia!?” “Anajua mama. Maya alikusikia ukiwa
unagomba siku ile. Tuliposhindwa kumjibu ni nini tunaongea, akaja kumuuliza
Maya kesho yake, ndipo Maya akamwambia kile alichokusikia ukisema. Akaja
kuniuliza kama ni kweli juu ya Tunda. Ni kamwambia ni kweli.” “Kwa hiyo yeye
anaona ni sawa umuoe malaya yule!?” Mama Cote akauliza.
“Kwanza
nakusihi mama yangu, usimtukane Tunda. Masaa machache sana, anakuwa mke wangu,
yaani mwili mmoja na mimi. Pili, Nana anaamini kwenye kukosa na kusamehewa
dhambi. Nakuomba..” “Kwa hiki ulichonifanyia leo, ni kunikana hadharani mbele
za watu. Umemchagua Tunda, dhidi yangu. Umemthamini bibi yako anayekupa mali
zao, umenidharau mimi mama yako niliyekubeba tumboni miezi 9, na
kukunyonyesha.” “Mama!” Net akaishiwa nguvu.
“Sasa
kuanzia leo, utakapofanyika mwili mmoja na Tunda tu, sahau kabisa kama mimi ni
mama yako. Nisikuone nyumbani kwangu wala ofisini.” “Mama Please!” Net
alishakuwa mwekundu akatamani kulia. “Sikutanii Net. Ukimuoa tu Tunda. Leo au
kesho, ujue wazi wewe sio mtoto wangu tena. Usiwahi kuja kuniita mama tena
maishani. Hata ukisikia mimi nimekufa leo, usije kwenye mazishi yangu. Usisogee
kwenye chochote nilichokitafuta kwa jasho langu. Wewe sio mwajiriwa wangu.”
Ritha alikuwa akitetemeka kwa hasira. Akaendelea.
“Yaani
kwa kifupi nataka ujue, tokea siku ulipouza mali ya kampuni yangu kwa Tunda,
yaani hii nyumba, ulijifukuzisha kazi, na ujue wazi, umefanya kosa kisheria.”
“Hii nyumba ni yangu mama. Nipo huru kufanya ninachotaka.” Net alimshangaa mama
yake.
“Ilikuwa
kwa jina gani?” Mama yake akamuuliza huku amemtolea macho. “Cote LTD kwa
kuwa..” “Exactly! Ilikuwa chini yangu. Mali yangu kisheria, wewe ni mfanyakazi
wangu. Umeuza mali ya kampuni kwa mwanamke wako. Wewe ni mwizi. Nimekuleta
nchini kama mfanyakazi, umeniibia. Ujue ninapoondoka hapa, nakwenda kukushitaki
kwa watu wa usalama na uhamiaji. Kitakachokupata, ndipo utajua mimi ni nani! Na
ukumbuke nilikuonya. Usinijaribu. Kama unadhani nakutania, muoe huyo malaya.”
“Mama! Nimejenga hii nyumba kwa
pesa yangu, ni jasho langu!” Bibi Cote akasogea. “Kuna nini?” Bibi Cote
akauliza. “Na umwambie bibi yako, kuanzia leo, asinitafute tena, na jina lenu
namwachia Tunda. Nitabadilisha jina la kampuni yangu nirudishe la baba yangu.
Mwambie mtoto wake hakuniokota. Alinikuta Canada sababu baba yangu alinilipia
pesa yakuishi huko. Mizigo yake yote itamfuata hapa kwenye hii nyumba
mliyoniibia. Na umwambie Maya, ana siku ya leo tu kuchagua. Awe mtoto wangu, au
anikane kama wewe utakavyonikana leo, endapo utamuoa Tunda. Uamuzi ni wako.
Tunda au mimi.” Mama Cote akamalizia kwa lugha ya kiswahili, akapanda gari
yake, akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Net maji yamezidi
unga. Je, anamwaga ili asonge ugali? Usikose mwendelezo. Vita yake ndio inaanza
rasmi endapo anamuoa Tunda. Usikose muendelezo kujua kama ameamua kusuka au
kunyoa! Kama Tunda alivyompokonya ndoa yake kwa kutembea na mwanaume wake,
ndivyo anavyotaka kumpokonya na yeye ndoa. Yupo garini, ameshapambwa, anasubiri
harusi. Je, ndoa ipo? Usipitwe.
0 comments: